Search This Blog

Tuesday, 20 December 2022

KWA AJILI YENU WANANGU, NITAMWAGA DAMU - 2

  




Simulizi: Kwa Ajili Yenu Wanangu, Nitamwaga Damu 

Sehemu Ya Pili (2)



"Si mwingine ni mtu wako Mackie."

Upande wa pili ulijibu.


"Enhh unasemaje Mackdone?"

Bi Elizabeth alimuuliza baada ya kumjua mpigaji.


"Nilitaka kukuuliza kama fedha iko tayari kwenye akaunti yako."


"Nashukuru sana Mackie imeingia, sijui nikushukuru vipi?"

Bi Elizabeth alimjibu.


"Wala usijali furaha yako tu kwangu ni shukrani tosha, cha msingi ni matumizi mazuri ya fedha hizo maana ni nyingi sana na pia leo niko hapa Namibia tuna mkutano wa wafanyabiashara Kusini mwa Afrika ambao utafanyika hapa, hivyo natakiwa kukutana na wewe kabla ya kuelekea huko."

Mackdone alimweleza Bi Elizabeth ambaye alishangaa kusikia kuwa yuko ndani ya Namibia.


" Maajabu, kwa hiyo uko mji gani? "


" Niko Windhoek."


"Windhoek?"

Bi Elizabeth aliuliza baada ya kuusikia mji huo wenye historia ya kipekee kwenye maisha yake ya jela.


"Mbona unashangaa tena?"

Mackdone alimuuliza.


"Hapana, nilijua uko hapa Namport?"

Bi Elizabeth alimjibu kwa swali.


"Wala usihofu kuhusu hilo nafikiri baada ya mkutano wetu nitakuja huko huko Namport."


"Hayo ndiyo maneno Mackie, basi utanijulisha ukiwa tayari."


"Okey sawa basi baadaye."

Mackie alimuaga Bi Elizabeth na kukata simu na safari yao ikaendelea.


***


Daktari Abbas na mkewe walijiandaa na safari ya kuelekea kwenye mkutano wa wafanyabiashara huku Daktari Abbas ambaye ni mmiliki wa hospitali ya King's Medicare Centre na mkewe akiwa kama mfanyabiashara mpya ambaye ni mmoja wa waalikwa kwenye mkutano akiwa ni mmoja wa wamiliki wa Kiwanda cha vinywaji kiitwacho AFRICANA DRINKING chenye makao makuu yake nchini Marekani huku wamiliki wengine ni Jessica na Jasmine. Kiwanda hiki kimejipatia umaarufu mkubwa duniani ndani ya muda mfupi kutokana na ubora wa bidhaa zao ambazo ni Vinywaji baridi vya Tabasamu ambavyo havina kilevi japo vina harufu ya kilevi hivyo kumfanya hata yule ambaye ni mtumiaji wa pombe kukichangamkia kinywaji ambacho kwa Afrika kinapatikana kwenye nchi za Tanzania, Kenya na Madagascar huku Namibia wakiwa njiani kukiruhusu mara baada ya mkutano huo ambao mmiliki wake atatumia kama daraja la kuitangaza bidhaa yao. Na baada ya kufika waliingia na kuketi sehemu yao na kwa kuwa muda ulishafika mkutano ulianza rasmi. Lakini wakati mkutano ukiwa umeanza kama dakika tatu hivi aliingia mtu mmoja mtanashati sana ambaye alionekana ni maarufu kwani hata mwenyekiti pale mbele alisitisha mazungumzo na kumwita mbele mtu huyo ambaye alikuwa akitembea kwa madaha na kumuonesha sehemu ya kuketi.


"Samahani jamani aliyeingia hapa ni mfanyabiashara mwenzetu aitwaye Mackdone kachelewa kidogo."

Maelezo ya mwenyekiti yalimshangaza kila mmoja mle ndani kwani walikuwa ndiyo wako kwenye mchakato wa kuanza kutambulishana iweje yeye Mackdone atambulishwe kabla.


" Unajua mwenyekiti hana ujanja kwa yule jamaa kwani biashara zake zote zinapewa sapoti na Mackdone hivyo muda mwingine hujikuta anachanganyikiwa akidhani kila mmoja ni mdhaminiwa wa Mackdone."

Alisikika jamaa mmoja aliyekuwa karibu na pale alipoketi wakina Jackline alikuwa akimsimulia mwenzake. Ndipo Jackline alipomtazama mume wake na kumpa ishara kuwa anatoka nje mara moja. Jackline baada ya kutoka nje alitoa simu yake na kumpigia Jasmine.


"Jamani hatuna haja ya kuleta bidhaa yetu ya TABASAMU hapa Namibia na Afrika ya Kusini."


"Kwanini Jackline?"

Jasmine alimuuliza.


"Tukiwa ndiyo tunaanza tu kikao chetu si kaingia Mackdone?"


"Mackdone?"

Jasmine aliuliza.


"Ndiyo Jasmine kaja kwa mikogo ya hatari ndugu yangu, ni kweli jamaa ni mtanashati japo umri umekwenda lakini hivyo vyote haviufichi uso wake wa kikatili."

Jackline aliendelea kumsimulia Jasmine.


"Sasa ni kipi ambacho kimekufanya useme kuwa hatutakiwi kuleta bidhaa zetu kwenye nchi hizo?"

Jasmine alimtupia swali.


"Ni namna alivyotetemekewa na watu humo ndani yaani baada ya kuingia tu kila mtu utafikiri kamuona Mungu hivyo kwa hali hiyo anaweza kutuharibia biashara yetu hasa baada ya kubaini ni sisi wamiliki wake."


"Hilo nalo ni neno."

Jasmine alimjibu.


"Mimi nina wazo juu ya mtu huyu."

Jackline alimwambia Jasmine.


"Wazo gani hilo?"


"Huyu tumtafutie mwanamke ambaye atamshawishi waingie kwenye uhusiano na akiingia tu ndiyo hapo hapo tutakapo muangusha chini na kufanya yetu."


"Hilo ni bonge la wazo na bahati yake Bi Elizabeth ananifahamu ningemuijia mimi mwenyewe."

Jibu la Jasmine liliwafanya wote kucheka.


"Hapana hiyo Jasmine, Bi Elizabeth kwa sasa anatakiwa atutafute kwa tochi kwanza."

Mara simu ya Jasmine ilisubirishwa na kuingia ya Roberto.


"Nambie dada yangu."


"Ninalo basi Roberto."

Jackline alimjibu Roberto.


"Enhh umefikia wapi kwenye suala la wajomba zangu kuhama huko?"

Roberto alikwenda moja kwa moja kwenye lengo lake.


"Nilishamueleza mume wangu japo hakutoa jibu mara baada ya taarifa ya kupotea Mahmoud kuichanganya akili yake."


"Enhh imeishia wapi hiyo ya Mahmoud kutekwa?"


"Si unamfahamu yule acha si alijiokoa na kukimbia."


"Afadhali maana angetuweka roho juu juu, lakini dada msisitize shemeji katika hilo kwani hali si shwari kabisa."

Roberto alimsisitiza.


"Wala usijali mdogo wangu hata leo hii hii nitamwambia kisha nitakupa mrejesho wake."


"Ok siku njema wape HI siku ambayo utawatembelea shuleni kwao wajomba zangu."


"Bila shaka kabisa."

Jackline alikata simu ya Roberto na kurejea kwa Jasmine.


"Kwa hiyo cha kufanya tushirikiane kumtafuta huyu mwanamke ambaye atasafiri mpaka Afrika ya Kusini kwa ajili ya mwanaharamu Mackdone."

Jackline aliendeleza agenda.


"Sawa ndugu yangu, ulikuwa unaongea na nani?"

Jasmine alimuuliza Jackline baada ya kuona kasubirishwa.


"Nani mwingine bwana si ni Roberto kaishikiria issue ya wakina Natalie kuhama."


"Hiyo hata mimi ninaiunga mkono wanatakiwa kuhama mara moja kabla hawajatutoa machozi."


"Nimewaelewa ndugu zangu."

Jackline alijibu kwa mkato na kumfuatilia Mackdone aliyetoka nje huku akiongea na simu ambayo ilikuwa ni kwa ukali kidogo.


UNAFIKIRIA NINI KATIKA HATUA HII?




Mackdone alikuwa akiongea kwa vitendo mara mkono mfukoni mara aunyoshe mbele kuonesha msisitizo wa jambo fulani huku sauti ikiwa ni ya ukali. Akiwa amezama kwenye simu hakujua hata kama kuna mtu yuko nyuma yake anayafuatilia mazungumzo yake, Jackline alikuwa kajificha kwenye kimti cha maua karibu kabisa na Mackdone akimfuatilia mazungumzo yake ambayo hakujua alikuwa akiwasiliana na nani.


"Ni nani aliyeingilia mfumo wetu? Na kwa sababu gani afanye hivyo?"

Ni miongoni mwa maswali ambayo Jackline aliyasikia kutoka kwa Mackdone akiuliza hivyo kwa mtu aliyekuwa akiongea naye kwenye simu.


"Nawapa masaa mawili niwe nimepewa majibu yanayofurahisha na si vinginevyo."

Mackdone aliongea hivyo na kukata simu kisha akabakia ameishika tu huku akienda kulia mara kushoto kama vile alikuwa akihakiki jambo pale chini kisha alirudi ndani na kumuacha Jackline ambaye alihisi kitu na hapo hapo akaishika simu yake kutaka kupiga namba fulani lakini ghafla ukaingia ujumbe.


"Dada Jackline unaweza kuamini kuwa nimeingia kwenye mfumo wa Mackdone na kuhamisha documents' muhimu zote?"

Jackline alibaki mdomo wazi baada ya kusoma ujumbe ule na pale pale ndipo alipobaini ndiyo ile simu ya Mackdone. Hapo hapo akaona kama vile uhondo haujanoga vizuri akaona ampigie tu ili kupata ladha kamili.


" We Roberto ikoje? "

Lilikuwa ni swali baada ya Roberto kupokea simu.


"Ndiyo hivyo dada nimefanikiwa kuingia na kuchota kama vile yangu."

Roberto alimjibu kwa sauti ya kujiamini kabisa.


"Kuna jipya?"

Jackline alimuuliza.


"Ndiyo, huyu Mackdone ni mfanyabiashara mkubwa ndiyo lakini kuna mengine yaliyojificha nyuma ya pazia."


"Kivipi Roberto?"


"Hapa nikiangalia kuna mengi nayaona kama vile kufadhili vikundi vya kijambazi huko Afrika ya Kusini na pia ana kundi lake mwenyewe linaloitwa THE SHADOW ambalo hulitumia kuteka kwenye mabenki pamoja na maeneo mengine tofauti tofauti na kwa kupitia kundi hili ndiyo Mackdone kapanda juu kwa utajiri."

Roberto alieleza.


" Mhhh kwa hiyo tunafanyaje?"

Jackline alimuuliza.


" Nadhani nipate muda wa kuendelea kumfuatilia huyu mtu kisha tutajua ni kipi tufanye ila tu ni kuwa makini na mtu huyu."

Roberto alitoa tahadhali kwa Jackline.


" Nimemsikia kwa masikio yangu akiwafokea watu wake kwa kuuliza ni nani aliyeingilia mfumo wake na baada ya simu hiyo alionekana kutokuwa sawa kiakili."


"Achana naye dada na ikiwezekana hata huo mkutano achana nao kwani atakapofahamu uwepo wako lazima atafanya jambo."

Roberto alimjibu na kukata simu yake na kumfanya Jackline kumtumia ujumbe mume wake kuwa hataweza kuingia ndani hivyo watakutana nyumbani.


"BABY NATANGULIA NYUMBANI, SIWEZI KURUDI HUMO NDANI TENA KUNA KITU HAKIJAKAA SAWA MUME WANGU."


Jackline aliondoka eneo hilo mara moja na kuelekea sehemu ya maegesho ya Taxi na kuita kisha akampa maelekezo ya anakoelekea na safari ikaanza.


Wakiwa njiani aliweza kumuona Hamza akiongea na simu kando ya barabara hivyo bila kungoja alimwamuru dereva Taxi amuache hapo kuna mtu anataka kuonana naye, hakuwa na pingamizi lolote akaipaki taxi pembeni kisha Jackline akashuka na kumlipa chake dereva kuachana naye. Lakini kitu cha ajabu kidogo hakuweza kumuona tena Hamza eneo hilo aliangaza huku na kule lakini wapi hakumuona.


"Kwamba nilimfananisha au mbona hizi ni kama vile nguvu za giza?"

Jackline alijiuliza baada ya kutomuona mtu ambaye alidhamiria kumfuata, akaona isiwe shida moja kwa moja akaongoza mpaka kwenye soko ambalo alimuona kwa mara ya mwisho Hamza akiamini kuwa anaweza kumkuta huko. Aliingia mpaka ndani ya soko na kuanza kumtafuta Hamza kila kona ya soko. Alimtafuta sana lakini hakuweza kumuona hicho kilimchanganya sana Jackline kwa mtu aliyemuona dakika sifuri lakini kapotea kama upepo.


"Atakuwa kaenda wapi?"

Jackline alijiuliza.


Na alipojiridhisha kutomuona Hamza aliamua kuondoka zake eneo hilo alitoka na kuchukua Taxi iliyompeleka mpaka kwake.


***


Bi Elizabeth aliwataka vijana wake waelekee Hospitali ya KING'S MEDICARE CENTRE kumtafuta mtu mmoja aitwaye Daktari Abbas ambaye alipatiwa taarifa kuwa huyu ndiye aliyemuoa Jackline.


"Huyu Daktari Abbas lazima afuatwe kule kule hospitalini kwake atueleze anafahamu nini kuhusiana na mkewe."

Bi Elizabeth aliwaambia vijana wake.


"Hapana mama hapa cha kufanya ni kutafuta tatizo ambalo litatufanya sisi kukutana naye moja kwa moja na kama hakuna ujue itakuwa ngumu kumuona maana ni mtu mkubwa yule."

David Orlando alitoa ushauri.


"Kwa hiyo unataka kusema nini David?"

Bi Elizabeth alimuuliza.


"Hebu tusiende huko kwanza mimi nafikiri tuelekee Windhoek ambako ndiyo kwenye chanzo kumbuka Jackline inasemekana anaishi huko hivyo ndani ya siku kadhaa tutajua anaishi wapi."


"Umenikumbusha David kule anaishi kijana wangu Hamza nadhani kupitia yeye kuna taarifa tutazipata ambazo zitatusaidia kwenye mpango wetu."

Bi Elizabeth alimuunga mkono kijana wake David. Hivyo waliingia kwenye gari tayari kwa safari ya kuelekea Windhoek ambako waliamini watamnasa Jackline lakini mara simu ya Bi Elizabeth iliita na kisha aliipokea.


" Hivi ndiyo tunatoka kwenye kikao yaani mpaka kichwa kinauma."

Mackdone alianza baada ya Bi Elizabeth kupokea simu.


"Pole sana lakini kwa kuwa kilikuwa ni cha faida siyo mbaya hata kama umechoka."

Bi Elizabeth alimjibu.


"Ni kweli kilikuwa na manufaa makubwa sana kwani siku zote mimi huangalia ni mshindani gani kaingia ulingoni."


"Enhh ukishamuona inakuwaje?"

Bi Elizabeth alimuuliza.


"Naingia ulingoni kuhakikisha namshusha chini na siyo chini tu bali nampeleka sifuri kabisa chezea Mackdone wewe."

Mackdone aliendelea kujisifia mbele ya Bi Elizabeth.


"Mmhh basi wewe kiboko mtu wangu, kwa hiyo unakuja?"

Bi Elizabeth aliona aachane na stori ambayo haimuhusu akaona aende kwenye pointi yake.


"Ndiyo lazima nije au ulitakaje?"

Mackdone alimuuliza.


"Kama vipi tutakutana huko huko niko njiani naja."


"Afadhali utakuwa umenisaidia sana."

Mackdone alimjibu na kuikata simu na hivyo kutoa nafasi kwa Bi Elizabeth na wenzake kushika njia kuelekea Windhoek hakika waliidhamiria safari ambayo walijua lazima ingeleta matokeo mazuri kwenye kazi yao hiyo. Wakiwa ndani ya msitu maarufu wa Bendamigha mvua kubwa ilianza kunyesha na haikuwa ya mchezo ilikuwa mvua kubwa sana iliyoambatana na upepo pamoja na mawe na kuwafanya kushindwa kuona mbele vizuri kwani gari lao lilikuwa la wazi nyuma, lakini pamoja na hali hii David hakutaka kusimama yeye aliendelea kupambana nalo kuhakikisha wanavuka eneo.


"Kwanini tusisimame ikate kwanza?"

Bi Elizabeth aliuliza baada ya kuona hata njia haionekani mbele.


"Hapana mama tutaendelea taratibu eneo hili linatisha sana hivyo hatuwezi kusubiri."

David Orlando alimjibu Bi Elizabeth huku akiendelea kupambana na usukani lakini akiwa anamalizia kumjibu Bi Elizabeth swali lake alishtukia mlio mkubwa mbele yake na baada hapo hakuna alichokiona.


JE NINI KIMETOKEA?




Ilikuwa ni ajali mbaya sana ambayo ilihusisha gari la mizigo na gari hii ndogo ya wakina Elizabeth ambazo ziligongana uso kwa uso na kupelekea gari ya wakina Elizabeth kuwa nyakanyaka huku lile gari la mizigo lenyewe likiharibika zaidi mbele na pia milango yote miwili iling'oka na kusababisha dereva na kondakta wake kurushwa nje. Hakika ilitisha sana kwa kila aliyefika eneo hili na kushuhudia kilichotokea hapa na sababu kubwa ya kutokea ajali hii ilikuwa ni mwendo mkali kwa magari yote mawili na kingine kilikuwa ni mvua kubwa ambayo iliambatana na upepo mkali na kusababisha madereva kutoona mbele vizuri.


"Hivi kwenye gari kubwa kulikuwa na watu wangapi?"

Mkuu wa kitengo cha uokozi kutoka mji wa Windhoek alikuwa akimuuliza mfanyakazi wake mmoja wakati zoezi la uokozi likiendelea.


"Hakuna wengine zaidi ya wale wawili ambao tumewakuta chini kwani tumepekuwa ndani ya gari pamoja na maeneo ya jirani na gari hatukuweza kuona chochote."

Mkuu wa kitengo cha Uokozi alijibiwa na mfanyakazi wake.


"Vizuri kumbe wapakieni wale wagonjwa na miili yote kwenye 'Ambulance' lengwa tuokoe muda."


Moja kwa moja miili ya marehemu ilipakiwa kwenye Ambulance tayari kwa kupelekwa sehemu husika huku wagonjwa wakikimbizwa Hospitali kwa matibabu kwani hali zao hazikuwa nzuri.

Vyombo vya habari vya ndani na nje ya Namibia vilielekeza macho yao kwenye tukio hili kwani lilikuwa ni tukio ambalo halikuwahi kutokea kwa muda mrefu kutokana na ubora wa miundombinu yake hivyo walitaka kujua nini kimesababisha ajali hiyo kutokea japo walihisi mvua kubwa ambayo ilinyesha usiku huo ndiyo sababu lakini hawakutaka kuamini hivyo walitaka mamlaka husika ziwape majibu huku vyombo vya kimataifa vikitaka kuitumia ajali hiyo kuichafua Namibia.

Hivyo walichukua picha na video fupi tayari kuandika makala ambazo zitakuwa na vichwa tofauti tofauti kulingana na chombo husika. Mahututi baadhi walikimbizwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya jiji hilo tayari kwa kuanza matibabu na wengine walipelekwa Makambi Hospital kwa Daktari Hans Murray, hospitali hii husifika kwa huduma bora zaidi ambazo hufanywa na wataalam wake kutoka Ujerumani kwa viwango vya juu zaidi.


"Aisee habari ya siku mbili tatu?"

Daktari Hans alimsalimu rafiki yake ambaye unaweza kusema ni zaidi ya ndugu Daktari Abbas.


"Kwema kabisa kaka, naona umebanwa na majukumu mpaka ulishindwa kuhudhuria kikao cha wafanyabiashara."

Daktari Abbas alimjibu.


"Nilituma mwakilishi wangu mimi kuna shughuli nilikuwa naimalizia hapa nyumbani kwangu, lakini kila kitu kilikwenda kama kilivyotarajiwa."


"Ni kweli kabisa kaka japo kuna mtu anaitwa Mackdone anatupeleka kama atakavyo vile sijui ni lini tutajitoa kwenye utumwa huu?"

Daktari Abbas alimjibu huku akimuelezea dukuduku lake juu ya Mackdone.


"Labda wewe lakini mimi kwa upande wangu hawezi kuniumiza kichwa hata kidogo mtu kama yule kwani mimi ni mtaalam ambaye naweza kumfanyia kitu mbaya muda wowote ule."


"Athubutu kaka kwa ukorofi wa Mackdone hawezi kukuacha salama hata kidogo."


"Abbas hebu tuachane na stori za pimbi huyo hapa kuna habari mbaya sana."


"Habari mbaya?"

Daktari Abbas aliuliza kwa mshtuko kidogo.


"Ndiyo, kuna ajali mbaya imetokea nje kidogo ya mji kwa kuhusisha gari ndogo na lile la mizigo, OK naambiwa iko live' hebu washa TV kama uko sehemu nzuri."


"Ok okay ngoja niicheki nitakupigia kaka."

Daktari Abbas alijibu na kuamka kitandani.


"Kuna nini mume wangu?"

Jackline alimuuliza mume wake baada ya kuona anaelekea sebuleni akiwa kashikilia t-shirt mkononi.


"Subiri kwanza."

Daktari Abbas alimjibu mke wake akiiwasha TV.


"ZILIZOTUFIKIA HIVI PUNDE....,

watu watatu waliokuwa kwenye gari ndogo wamefariki wakiwa njiani kuelekea hospitalini huku wengine watatu akiwemo mwanamke mmoja wa makamo hali zao zikiwa mbaya sana na inasemekana hao wawili ni wale waliokuwa kwenye gari kubwa.

TUTAENDELEA KUWAPA TAARIFA HIZI KILA ZINAPOTUFIKIA..... "

Daktari Abbas hakuona sababu ya kuendelea kuangalia taarifa hiyo akamgeukia mke wake.


" Shemeji yako ana vituko sana mke wangu yaani kanitoa kitandani mkukumkuku taarifa yenyewe ndiyo hii? "


" Sasa unaiona ni ya kawaida hakuna roho za watu zilizokatishwa hapo? "

Jackline alimuuliza mume wake.


" Wapo watatu na wengine hawajitambui."

Daktari Abbas alijibu huku akirejea chumbani kwa ajili ya maandalizi ya kuelekea kazini. Lakini mke wake ni kama alitaka kumweleza kitu hivi akaahirisha na kuketi kitini huku akiangusha pumzi kubwa kuonesha kuna jambo linamtatiza kichwani.


" Hivi yule kijana alinipoteaje pale? Au Shushushu genge la kiharifu nini?" Alijiuliza maswali hayo huku akizima TV ambayo alihisi kama vile inamzingua tu.


"Nitamnasa tu jana kashinda yeye."

Alijipa jibu yeye mwenyewe huku akiongoza chumbani alikokuwa mume wake.


"Vipi ushaamua ni nchi gani tunawahamishia wanetu?"

Jackline alimtupia swali mume wake.


"Mambo mengi mke wangu nilisahau, unaonaje twende pale Livingston Square tukawape kazi wale vijana wa worldeducationlink.com waifanye kazi hii maana wao wameifanya kazi hii kwa muda mrefu sana wanaweza kutusaidia katika hili."

Daktari Abbas alimjibu mke wake.


" Hapo naungana na wewe, basi tufanye fasta tuelekee huko, tulikamilishe suala hili mapema kabla wanetu hawajapatwa na majanga."

Jackline alikubaliana na mume wake katika hili hivyo naye akaingia kujiandaa.


"Dada una habari? Nasikia Bi Elizabeth yuko hoi hospitali."


Ni ujumbe ambao uliingia kwenye simu ya Jackline huku yeye akiwa kuoga lakini jumbe hiyo ilionwa na mume wake aliyekuwa akijifunga tai yake mbele ya kioo na kumfanya kutaka kujua zaidi hivyo alichokifanya alitoa simu yake na kutoka nje ambako alimtafuta Daktari Hans na kumpigia.


"Kaka hivi una taarifa zozote za ajali hiyo? Mimi ni kama vile niko gizani hivi."


"Ninazo Abbas kwani Hospitali yangu imepokea wagonjwa wawili ambao ni mwanamke wa makamo hivi na kijana mmoja. Huku mmoja akipelekwa hospitali ya Rufaa.

Daktari Hans alimjibu.


" Hakukuwa na watu waliokufa pale pale eneo la ajali? Au achana nayo kwani si habari hiyo..."


"Una maanisha nini kusema si habari mdogo wangu ni hivi waliofia pale pale ni watu wawili wote wa kiume hivyo ukichanganya na hawa wapya waliofia njiani tunakuwa na marehemu watano."

Daktari Hans alimjibu Abbas ambaye alionekana kuingiwa na jambo fulani hivi kichwani akaikata simu ya Hans na kumpigia Mahmoud ambaye kwa wakati huo alikuwa keshaungana na wakina Thomas aliowaokoa na kuwaeleza kile kinachokwenda kufanywa na Bi Elizabeth na kuona njia pekee ya kuwa huru ni kumsapoti Mahmoud.


"Elekeeni Makambi Hospital kuna majeruhi wa ajali ya gari fuatilieni mnipe taarifa mapema."


"Sawa Mkuu ndani ya masaa mawili tutakuwa hapo."

Mahmoud alimjibu.


"OK sawa Mahmoud msifanye kosa."

Daktari Abbas alisisitiza.


"Bila shaka." Simu ilikatwa na kumfanya Daktari Abbas kurejea ndani ambako alimkuta mke wake akiwa kajishika shavu akiusoma ujumbe ule.


"Mume wangu miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo ni Bi Elizabeth."


"Bi Elizabeth? Alikuwa akielekea wapi?"

Daktari Abbas aliuliza kama vile hajui chochote kile wakati tayari alishapiga chabo la maana.


"Wala sijui, na sijui kalazwa hospitali gani?"

Jackline naye aliuliza.


"Kwa mujibu wa vyanzo vya habari inasemekana wagonjwa wote wako kwenye Hospitali mbili tu ambazo ni Makambi kwa shemeji yako pamoja na ile ya serikali."

Daktari Abbas alijibu akiwa hajui taarifa hizo zitapokelewa vipi na Jackline ambaye aliinuka bila kusubiri maelezo ya mwisho ya mume wake moja kwa moja aliifuata gari.


" Wapi sasa mke wangu? "

Daktari Abbas alimuuliza mke wake baada ya kumkimbilia.


" Naelekea Makambi muda huu."


"Haitakuwa hatari huko mke wangu kwanini usisubiri kwanza?"

Mume wake alimsihi.


"Hakuna la kusubiri hapo mume wangu natakiwa nielekee huko nikafanye mpango na shemeji yangu."

Jackline alimjibu mume wake aliyekuwa bado pale chini na kisha alimuacha kama alivyosimama na hali hiyo ilimchanganya Daktari Abbas akajua huko hakuna usalama wowote kwani mke wake anamfahamu vizuri kwa sasa hivyo haraka sana akaingia kwenye gari lake na kuanza kumfukuzia.


"NIKO NJIANI SHEMEJI YANGU, NAOMBA TUONANE HOSPITALINI KWAKO."

Ni ujumbe aliomtumia Daktari Hans kisha akampigia Roberto kutaka kujua taarifa hii ameipata wapi.


"Umejuaje kama Bi Elizabeth ni miongoni mwa manusura wa ajali?"


"Taarifa zao zimetapakaa kila kona za Dunia huku blog moja ya nchini hapo Namibia imeandika taarifa ambayo si nzuri kwa upande wa Bi Elizabeth."

Roberto alimjibu Jackline.


"Kivipi?"


"Imeandikwa hivi 'Mfungwa aliyetoroka jela hivi karibuni apata ajali mbaya ya gari."


"Mhh ndiyo hivyo?"


"Ndiyo dada."


"Ok baadaye nitakucheki niko naendesha gari."

Alimjibu hivyo na kukata simu bila shaka taarifa hii ilimchanganya zaidi kwani alijua moja kwa moja Bi Elizabeth atakuwa mikononi mwa jeshi la ulinzi kwa vyovyote vile hivyo alikanyaga mafuta kuhakikisha anafika mapema walau ajue iwapo kachukuliwa ama bado ili amnyakue yeye.


JE, NINI KITAKWENDA KUTOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.



Jackline aliendesha Harrier yake kama vile yuko mashindanoni maana si kwa spidi ile ilikuwa hatari sana kwani kila aliyepishana naye ilikuwa lazima ageuke na kwa wenye magari waliiangalia gari ya Jackline kupitia 'site mirror' hii ilikuwa ni siku ambayo Jackline aliipania kwa asilimia zote na baada ya kulifikia geti la Makambi Hospital alilizungusha na kulipaki nje ya geti na kushuka. Baada ya kushuka kitu cha kwanza ilikuwa ni kuchungulia ndani ili kujua kuna kipi ambacho kingemzuia yeye kuifanya kazi yake na kilichofuata alitoa simu yake na kumcheki mwamba wa kike auaminiao sana ambaye ni Jasmine.


"Nimeshafika hapa Makambi nimeshatelemka garini kifuatacho ni umafia tu huko ndani, tegeni masikio yenu na usisahau kuwajulisha makamanda wote."

Jackline alimjulisha Jasmine uwepo wake Makambi.


"Da kweli umelipania game but be careful."

Jasmine alimtahadharisha Jackline.

Jackline macho yakiwa getini alikata simu baada ya kuona geti linafunguliwa huku king'ora kikipigwa na kisha ilitoka gari nyeupe ikiwa imewasha taa zote za mbele na king'ora kikiendelea kupigwa, lilikuwa ni gari la wagonjwa kutoka kampuni binafsi ambayo Jackline alijaribu kusoma jina lake ubavuni lakini alichelewa kwani ilipita kasi sana na kuacha vumbi tu pale getini hivyo kushindwa kufanya chochote zaidi ya kusonga mbele na kulifikia geti, mlinzi aliweza kumruhusu baada ya kujua ni mgeni wa bosi wake Daktari Hans angeweza kumsitisha kuingia kutokana na muda wa kuona wagonjwa kupita kwani ilikuwa ni saa nane na nusu mchana hivyo ilikuwa ni lazima busara zitumike ili kuingia ndani.


"Karibu shemeji yangu mwenyewe."

Daktari Hans alimkaribisha Jackline ambaye aliona aingie moja kwa moja ofisini kwake.


"Asante shemeji yangu za siku mbili tatu?"


"Mungu ni mwema tunaendelea kuvuta pumzi ya bure kabisa."

Daktari Hans alimjibu.


"Ni kweli kuna wakati huwa nawaza sana juu ya Ukuu wa Mungu huwa sipati majibu ya moja kwa moja fikiria iwapo angeamua kutulipisha kwa kila mvuto wa hewa hii ni wangapi wangeweza kuishi?"

Jackline alimtupia swali Daktari Hans ambaye muda huo alikuwa anaandika vitu fulani kwenye kitabu chake pale mezani.


" Yaani Shemeji Tumuache tu Mungu aitwe Mungu inatosha hebu fikiria kama hawa wapendwa jana tu walikuwa na mipango mingi ya kifamilia lakini mwisho wa siku hatunao tena."


"Enhh shemeji hilo ndilo limenileta hapa."

Jackline alishapata pa kuanzia.


"Kivipi shemeji kwani kuna mgonjwa unayemfahamu?"

Daktari Hans alimuuliza.


"Hapana shemeji ila kuna mtu ambaye nahisi si mtu mzuri kwangu ni miongoni mwa walioletwa hapa kwako kama sikosei."


"Ni mgonjwa gani huyo maana hapa waliokuwepo hai ni wawili tu ambao ni Kijana mmoja pamoja na mama mmoja ambaye jina lake ni Elizabeth Mackey na hawa wote wamechukuliwa na jeshi la Polisi kuna taarifa kuwa huyu mama alitoroka jela miezi kadhaa nyuma hivyo wamemchukua na kumhamishia kwenye Hospitali ya jeshi chini ya uangalizi wao wenyewe na hivyo huyu mwingine wameona naye waondoke naye kwa uchunguzi zaidi."

Maelezo ya Daktari Hans yalimwingia sana Jackline ambaye alimsikiliza huku akichambua moja baada ya nyingine kwani kilichomchanganya zaidi ni kwanini jeshi hilo litumie gari la wagonjwa kutoka Kampuni binafsi? Lilikuwa ni swali ambalo hakumuuliza Hans alibaki nalo kichwani.


"Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa kwenye magari yote mawili kulikuwa na watu sita?"

Jackline aliona apotezee kwa kuuliza swali hili.


"Mhh ni kweli kabisa inasemekana gari dogo lilikuwa na abiria wanne ambao hawa wote wamefariki na kubakia mmoja ambaye ni huyu mama huku wawili wakiwa ni abiria kutoka kwenye gari la mizigo huko nako kasalia mmoja ambaye ni huyu kijana ambaye mwanzoni alikuwa hospitali ya Rufaa."


"Aisee mpaka hapo shemeji sina la kuongeza zaidi nikuache maana nilijua kuwa nitamkuta huyu mama hapa nifanye naye mahojiano kutaka kujua nilichokisikia kina mashiko?"


"Pole sana shemeji yangu kwa hilo, lakini nikuahidi kuwa hata mimi nitajaribu kulifuatilia kwa ukaribu zaidi kujua kwanini alitoroka."

Daktari Hans alimuahidi shemeji yake Jackline ambaye aliaga na kutoka huku jasho likimtoka kwani alishahisi kuna mchezo umechezeka hapo.


"Polisi wamemchukua? Haiwezekani kwanza kwanini watumie gari la kampuni kumtoa hapa? Na pili kwanini wambebe na mtu ambaye hausiki na utoro wa Bi Elizabeth."

Jackline aliendelea kujiuliza maswali ambayo aliyapa uzito wa kutosha.


"Hao askari ni wenyewe lakini kuna mtu nyuma yao si bure."

Aliendelea kuwaza na muda huu alikuwa akifungua mlango wa gari ambapo aliingia na kuondoka zake lakini kando kidogo kulikuwa na gari ambalo lilisimama na baada ya Jackline kuondoka nalo lilishika njia kumfuatilia na hakuwa mwingine bali Daktari Abbas ambaye hakutaka kujionesha zaidi alimtaka Mahmoud afanye haraka ili yeye ndiye acheze na Jackline na yeye arejee kazini.


"Umefika wapi mwana? Naona huko ndani mambo si shwari kwani Jackline katoka akiongea peke yake hivyo wewe utakwenda kuonana na mlinzi ambaye utatumia mbinu zako za kivita kumchimba maana mimi kwa sasa sitaki nionane na jamaa yangu Daktari Hans."


"Kama kawaida Mkuu wangu hivi ndiyo tumeshaingia mjini wewe endelea kumfuatilia kisha baada ya kupata majibu ya maswali yetu nitakuja huko."


"Ok sawa kazi njema."

Daktari Abbas alimjibu na kukata simu na kuendelea kucheza na usukani.


Kuhakikisha kwamba hachezi mbali na Jackline ambaye kwanza aliamua kuelekea eneo la ajali akajionee mwenyewe na baada ya saa moja kasoro Jackline aliwasili eneo hilo na kukutana na damu tu ambazo zilikuwa zimetapakaa eneo lile lakini hakukuwa na gari lolote kwani yalishavutwa kwa usalama zaidi. Lakini Jackline yeye hakujali sana pamoja na kwamba ilikuwa ni magaharibi yeye alishuka kwenye gari na kulisogelea eneo na kulikagua kwa ukaribu japo hakuambulia chochote kitu na hivyo kuamua kuondoka zake na baada ya dakika kadhaa alisimamisha gari na kuchukua simu yake kisha kumpigia Jasmine.


"Hakieleweki ndugu yangu kuna faulo imefanyika hakuna mgonjwa pale lakini mashaka yangu ni ile Ambulance iliyotoka kasi pale Hospitali, nina uhakika huyu Mackdone anahusika katika hili."

Jackline alianza baada ya Jasmine kupokea simu yake.


"Kwani Daktari Hans anasemaje katika hili?"

Jasmine alimuuliza.


"Mhh yeye si kaingizwa mkenge kwani waliofika pale ni askari kabisa wakiwa vielelezo vyote lakini swali ni moja kwanini hawakutumia Ambulance ya serikali?"

Jackline alisimamia hapo.


"Hapo kuna jambo mtu wangu na ninachokiona mimi ngoja niwasiliane na Roberto tuanze maandalizi ya safari siku ya kesho baadaye Jessica na Titiana watafuata kwani Jessica anamalizia mitihani yake ya chuo."

Jasmine aliamua.


"Kweli kabisa Jasmine fanyeni hivyo maana hapa kuna bomu litatulipukia."


"Haina shida ngoja nifanye mawasiliano na shujaa Roberto."


"Nimekupata Jasmine."

Jackline alikubali na kukata simu kisha akagonga mikono kwenye usukani kuashiria hasira. Roberto amekuwa mwema kwao kutokana na mafanikio aliyoyapata baada ya kuwasaidia awamu ya kwanza na kulipwa hela za kutosha na hivyo kuachana na maisha yake ya awali ambayo yalitegemea uhalifu mpaka pale alipokutana wakina Jackline.

Lilikuwa tayari ni giza na kulifanya eneo hilo kuwa kimya sana hivyo ilibidi aondoke mahali lakini kilichomshangaza ni baada ya kuona gari mbele yake likiwa linaondoka hapo akagundua kuwa kuna mtu alikuwa anamfuatilia hivyo haraka ikabidi ale naye sahani moja hivyo akaanza kumfuatilia. Alimfukuzia kwa nyuma taratibu akihakikisha hamuachi mbali mtu huyo.


"Atakuwa nani huyu ambaye anacheza na nyendo zangu."

Jackline alijiuliza.

Na baada ya kulifuatilia sana alilifikia gari lile na kulipita kwa kasi na kwenda kulizuia kwa mbele kisha akashuka bastola mkononi na wala hakuchekewa akainyoosha usawa wa dereva kupitia kwenye kioo cha mbele.


" Shuka mwenyewe taratibu mikono ikiwa juu kwa usalama wako."

Jackline alipaza sauti na kama alivyotaka ndivyo ilivyokuwa kwani dereva yule alishuka na kunyoosha mikono juu, hapo Jackline alimsogelea karibu na kutaka kumshikisha adabu lakini alichokutana nacho kilimchosha na kuamua kurusha ngumi tatu mfululizo zilizokwenda mpaka kwenye uso wa mtu yule.


"Mshenzi wewe angalia nyakati za kunivizia nitausambaza ubongo wako mume wangu."

Jackline aliongea kwa hasira huku machozi yakimmwagika.


"Nisamehe mke wangu nilifanya hivi baada ya kunipita sehemu moja hivi ukiwa kasi nikaona hakuna usalama huku na mimi nikaingia kwenye gari kukufukuzia."

Daktari Abbas alijitetea.


"Enhh ningefyatua risasi?"

Jackline alimuuliza akiwa kamtolea macho huku kamkwida kabali ya shingo.


"Yaishe mke wangu."

Aliomba msamaha na hapo Jackline alimuachia na kurejea kwenye gari lake bila kuongea lolote zaidi ya kuangusha machozi na Daktari Abbas naye akiingia kwenye gari lake na safari ikaanza.


"BI ELIZABETH KACHUKULIWA NA MTU MMOJA ALIYEJULIKANA KWA JINA LA MACKDONE AMBAYE NI MFANYABIASHARA MAARUFU KUTOKA AFRIKA YA KUSINI NA HIVI NINAVYOTUMA UJUMBE HUU WAKO NJIANI KUELEKEA AFRIKA YA KUSINI NA HII IKIWA NI KUUKWEPA MKONO WA SHERIA."

Ulikuwa ni ujumbe ambao uliingia kwenye simu Jackline lakini mtumaji akiwa kaficha utambulisho wake. Na baada ya kuisoma jumbe hiyo alicheka sana kwani mwenye mchezo huo mara nyingi huwa Roberto na alijua si mwingine bali ni yeye tu. Hivyo Jackline akaona njia pekee ni kumpandia hewani.


"Lete stori Roberto."

Jackline alianza baada ya simu yake kupokelewa.


"Sina stori dada yangu."


"Mhh kweli?"

Jackline alimuuliza


"Kweli kabisa zaidi ya mazungumzo tuliyofanya na Jasmine ya kuianza safari siku ya kesho jioni baada ya yeye kutoka Brazil na kuja hapa Marekani ambapo tutaianzia safari yetu."

Roberto alifafanua.


" Mimi sina neno mdogo wangu nawasubiri tu kwa hamu tulianzishe si umeambiwa kuwa Bi Elizabeth katoroshwa Hospitali?"


" Nimeambiwa dada ila nakusihi usifanye chochote kwa sasa wewe tulia mpaka tufike kwanza."


"Sawa Roberto, nikutakie usiku mwema."

Jackline alimtakia usiku mwema.

Alikata simu na kuendelea na safari yake lakini hakuacha kuufikiria huu ujumbe ambao alijua umetumwa na Roberto lakini siyo.


"Ni nani sasa huyu ambaye anaucheza mchezo huu?"

Alijiuliza Jackline bila ya kuwa na majibu sahihi kwani mtumaji huficha utambulisho wake na kwanini afanye hivyo kama ana nia nzuri.


MIMI SINA MAJIBU LABDA WEWE MSOMAJI ZAIDI TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA INAWEZEKANA TUTAPATA JIBU.





Baada ya kufanikiwa kumtorosha Bi Elizabeth kwa kutumia usafiri wa Helicopter yake ambayo aliipaki nje kidogo ya mji wa Windhoek mtu mzima Mackdone alikuwa katulia nje ya Hotel ya Clayton iliyo jijini Windhoek, hapa alikuwa katulia chini ya mwamvuli mmoja mkubwa miongoni mwa mitano ambayo inaipamba Hotel hii yenye hadhi ya nyota tano akiwa anapitisha macho yake kwenye kompyuta yake mpakato huku mdomoni akivuta sigara aina ya volta ambayo inazalishwa nchini Afrika ya Kusini na sifa ya sigara hii inasemekana ni kuchangamsha mwili huku wengine wakidai kuwa hii ni bangi iliyotengenezwa maalum kwa ajili ya watu maarufu pamoja na matajiri tu huku ikiwa inauzwa ghali sana. Paketi yenye sigara sita inauzwa dola mia mbili, lakini kwa mtu kama Mackdone suala la pesa si tatizo. Akiwa anaendelea kupitia taarifa za mbalimbali za masoko ya fedha duniani mara simu yake iliita na baada ya kuangalia mpigaji ni nani aliweza kumfahamu akaipokea.


"Ongea Vivian."

Mackdone aliongea mara baada ya kupokea.


"Bosi ndiyo tumetua hapa Hospitali."

Vivian alimweleza Mackdone.


"Vizuri sana Vivian na vipi kuhusu wale askari waliowaleta hao wagonjwa?"


"Kama ambavyo uliagiza mkuu tumetekeleza agizo lako."

Alijibu Vivian.


"Inapendeza Vivy kikubwa kama hamkuacha ushahidi."

Mackdone alitaka kujua zaidi.


"Hata mifupa yao hawataiona popote Mkuu kazi yetu si unaijua?"

Vivy alimuuliza Mackdone ambaye sura yake ilipambwa na tabasamu pana baada ya kupokea taarifa ile.


"Hapo tu ndiyo nakupendeaga Vivy safi sana, naomba niunganishe na Daktari Leon hapo mara moja. Huyu Leon ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Victoria ambayo inamilikiwa na mfanyabiashara Stewart ambaye ni rafiki mkubwa wa Mackdone.


" Nini kimetokea huko au ndiyo umesababisha nini?"

Leon alimuuliza baada ya kupokea simu kutoka kwa Vivy.


"Ha ha ha ha Leon unauliza nini sasa wakati unamjua vizuri kabisa kaka yako."


"Nakujua ndiyo maana nikataka kujua kilichowatokea hawa wagonjwa wako."

Daktari Leon alimjibu Mackdone.


"Naomba anza kuwashughulikia kwanza mengine tutaongea mdogo wangu nikirejea hapo."

Mackdone aliongea kwa kujiamini sana na kwa kuwa Leon anamjua vizuri hakuwa na la kuongeza zaidi ya kukubaliana naye na kisha kumrejeshea simu Vivy ambaye alikuwa katulia pembeni.


" Naam Mkuu."

Vivy aliitikia baada ya kuichukua simu kwa Daktari Leon na kuiona haijakatwa.


"Hakikisha hakuna kimburu yoyote anayeingia hapo kufuatilia chochote sijui nimesomeka?"

Mackdone alimpa maagizo Vivian huku akitaka kujua kama ameeleweka.


"Nimekupata bosi wangu hakuna litakaloharibika hapa."

Vivy alimjibu.


"Vizuri nikuache uendelee na majukumu yako na kuhusu utaratibu wa ulinzi hapo uko mikononi mwako mwenyewe hao wengine ni wako."


"Sawa Mkuu."

Vivian alijibu na kukata simu kitu ambacho kilitoa nafasi kwa Mackdone kuinua glasi ya mvinyo na kuiweka mdomoni kama ishara ya ushindi kwake. Aliitua ikiwa tupu akaongeza na kunywa tena kisha akainuka pale alipokuwa na kuingia ndani ambako aliongoza kwenye chumba chake na huko akijitupa kitandani huku akiendelea kuvuta sigara yake na macho yakiwa kwenye taa ya ua iliyokuwa ikiwaka na kuzima kitendo ambacho kilimfanya Mackdone kutoa tabasamu bila shaka ilimburudisha sana ile taa.


***


Ndani ya ndege ya 'Panama Airways' walitulia watu wawili ambao walionekana kuwa na furaha sana bila shaka ni baada ya kufanikiwa kuianza safari yao nao si wengine bali ni Roberto na Jasmine wakielekea nchini Namibia kuungana na Jackline kwenye oparesheni ya kumdhibiti Bi Elizabeth ambaye waliamini ni kirusi kwao. Panama Airways ni kampuni maarufu sana ya usafirishaji kutoka nchini Marekani ikiwa tayari inafanya kazi kwenye mataifa yote makubwa duniani. Na ndiyo maana haikuwa kazi ngumu kwa Jasmine na Roberto kulichagua shirika hili kwenye safari yao ya kuelekea barani Afrika katika nchi ya Namibia.


"Kwa mara nyingine ndani ya Namibia, unakumbuka nini dada Jasmine?"

Roberto alimuuliza swali Jasmine huku akiangalia nje ya ndege kuushuhudia uzuri wa bara la Afrika kwani tayari wameanza kuvuta hewa ya bara hili ambalo limebarikiwa sana na mwenyezi Mungu kwani ni kitu gani ambacho utakitaja hakipatikani kwenye ardhi au anga la bara hili.


"Kiukweli kuna mengi nayakumbuka mdogo wangu lakini kubwa kuliko yote ni lile la kuokolewa na familia ya mzee Jerome ndani ya bahari tukiwa hatujitambui acha tu Mungu aendelee kuwapa pumziko la milele."

Jasmine alimjibu Roberto huku akifuta machozi kwa kitambaa chake cheupe.


" Ni kweli kabisa dada yangu mimi mwenyewe hilo liliniliza sana hasa baada ya kuambiwa kuwa mmeuawa na kutupwa baharini lakini kwa uwezo wake Allah bado mko hai na maisha yanaendelea."

Roberto aliguswa na simulizi ya Jasmine na kuamua kumliwaza kwa maneno ya faraja. Na wakati huo huo ndege ilikuwa ndiyo imeatamia njia ndani ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Windhoek kuchukua nafasi yake ya kusimama. Na baada ya dakika kadhaa ndege iliweza kusimama na hivyo kuweza kutoa nafasi kwa abiria wake kushuka. Walishuka watu wote kutoka kwenye ndege ile na hatimaye walihitimisha Jasmine na Roberto ambao walihesabu ngazi kuelekea chini ambako waliweza kukutana na Jackline ambaye aliongozana na mume wake Daktari Abbas waliokuwa wakiwasubiri kwenye eneo la kusubiria wageni wanaowasili hakika ilikuwa ni furaha ya ajabu kwa ndugu hawa kukutana uso kwa uso baada ya kuachana kwa miaka kadhaa nyuma Jackline akirudi Tanzania kwa ajili ya kutanua mizizi ya makampuni yao wanayoyaongoza na kuyasimamia.


"Waooo ndugu zangu sikutegemea kukutana nanyi siku ya leo maana Jasmine tunajuana wenyewe."

Jackline alianza.


"Kwa taarifa yako safari hii niliipania sana ila kuna jitu lilitaka kuitia doa sema tu ilikuwa bahati yake."

Jasmine aliongea hayo huku akimuangalia Roberto aliyekuwa akirekebisha earphones zake za simu.


"Asijishaue huyo wala mimi nihusiki kwa lolote kikubwa tumewasili salama ndani ya Namibia."

Roberto alijibu baada ya kuona Jasmine anataka amgeuze mbuzi wa kafala. Baada ya utani wa hapa na pale waliweza kuingia kwenye gari na safari ya kuelekea nyumbani ilianza.


" Shemeji zangu karibuni tena kwa mara nyingine nchini kwetu Namibia."

Daktari Abbas aliwakaribisha wageni wao huku akiwa macho pima mbele kuhakikisha kuwa hasababishi ajali kwani ndiye alikuwa dereva huku Jackline na ndugu zake wakiendelea na utani wao wa hapa na pale.

Muda huo huo Jackline kama kawaida yake aliifungua simu yake upande wa whatsApp na kulifuata group lao na kuandika.


"Wanajeshi kamili."

Aliandika maneno hayo ambayo yaliambatana na picha ya pamoja ambayo ilikuwa kama kuwatamanisha wakina Jessica na Titiana.


"Haa ndiyo nini bila taarifa?"

Titiana aliandika baada kuiona ile picha.


"Jamani acheni basi kututamanisha wenzenu tunaweza toroka mitihani eti."

Jessica aliandika huku akiambatanisha na viimoji vya kulia.


"Kuleni kwa macho wenzenu kama muonavyo."

Jackline aliendelea kuwatamanisha kwani alitupia picha nyingine tena.


"Sawa tu nawashukuru kwa mlilonifanyia, sawa tu Roberto."

Titiana aliendelea kulalamika kwa inavyoonekana Roberto alimtoroka bila kumpa taarifa.


"Mhh Titiana wifi yangu kuna nini mbona hivyo?"

Jackline aliona aulize.


"Haina haja wifi si ndiyo mlipanga hivyo nashukuru sana hata hivyo mimi si ndugu yenu na sina umuhimu wowote kwenu."

Titiana aliwatwisha zigo la lawama wote.


"Roberto umefanya nini sasa?"

Jessica aliuliza naye.


"Jamani ee naombeni huyo niachieni tukitulia nitaongea naye, kwani kama mjuavyo yuko kwenye mitihani lakini kama ningemweleza tu kuhusu safari hii angeachana na mitihani na kuungana nasi jambo ambalo sikutaka litokee..."

Wakati Roberto akifafanua sababu ya kutomuaga mara Titiana kuonesha kuwa hakufurahishwa kabisa na kilichofanywa alileft group.


" Hee jamani kaleft."

Jasmine alishangaa.


" Roberto umekosea bwana katika hili."

Jessica aliandika.


" Nakubali ndiyo lakini ni kwa manufaa yake mwenyewe ila msijali masaa machache yajayo mtamuona kundini niachieni hili tuendelee na mengine."

Roberto aliomba kuachiwa hili sababu Titiana ni wake atamalizana naye tu na atarejea tena kundini hivyo walikubaliana kumuachia Roberto hilo alimalize na muda huu walikuwa wanawasili nyumbani kwa Jackline.


JE NI NINI KINAKWENDA KUTOKEA?





Gari ilitia nanga getini kumruhusu mlinzi aweze kufungua geti baada ya kupigiwa honi. Mlinzi alifungua na kisha gari lilijongea ndani taratibu kuelekea kwenye egesho lake. Wageni walishuka kwenye gari na kuongozwa ndani na Jackline huku mume wake akisalia kushusha mizigo iliyokuwa kwenye buti.


"Ndugu zangu karibuni sana sana na jisikieni nyumbani kabisa."

Jackline aliwakaribisha wageni wake.


"Wala usijali ndugu yetu sisi ndiyo tumetua hapa Windhoek na kama ujuavyo sisi huwa tukitua hatunaga mbwembwe ni kazi kwa kwenda mbele."

Roberto alimjibu Jackline huku akitoka nje baada ya simu aliyokuwa kaipiga kupokelewa upande wa pili.


"Unasemaje Roberto?"

Titiana alimuuliza baada ya kuipokea tu.


"Mbona unaniuliza swali la mwendo kasi hivyo au bado una hasira?"

Roberto alimuuliza baada ya kukutana na swali ambalo hakulitarajia kutoka kwa mpenzi wake.


"Hata kama nina hasira unaumia nini wewe?"

Titiana alimpiga na swali jingine badala ya kujibu swali aliloulizwa.


"Sikutegemea kwa unayoniambia wewe ungenipa walau dakika moja nikueleze kile ambacho nilikifikiria mpaka kuondoka bila kukuaga."

Roberto alianza kumuingia Titiana.


"Nikwambie kitu mpenzi wangu?"

Titiana alimuuliza Roberto.


"Uliza kipenzi uko huru kabisa katika hilo."

Roberto alimruhusu.


"Hivi kwa akili zako za juu juu unafikiri mimi ni mtoto mdogo eeh? Wewe ulichotakiwa kukifanya ni kunijulisha kisha usikie mimi nitasema nini lakini siyo tu umetoka huko oohhh Titiana ningemwambia angetaka kulazimisha kuondoka nasi kwamba mimi ni hayawani fulani nisiyejitambua niiache 'future' yangu nifuate ujinga siyo?"

Titiana alimshushia maswali na tuhuma za kutosha ambazo zilimfanya Roberto kushindwa afanye nini kwenye hilo kwani alijiona yeye ndiyo kakosea.


" Titiana naomba radhi katika hilo nimekosea."

Ilibidi aombe radhi hakuwa na jinsi hata kidogo.


" Tulia kwanza wewe nikupe vidonge vyako, nilichojifunza kutoka kwako ni kwamba safari ile ambayo niliambatana nawe na kuahirisha masomo yangu kumbe mwenzangu hukufurahishwa hata kidogo. Hivyo kutokana na hilo naomba kukufahamisha kuwa kujikombakomba nimekoma siwezi kurudia tena Roberto."

Titiana alipomalizia kumsigina vizuri Roberto alimkatia simu pamoja na kuwa aliombwa msamaha. Hivyo Roberto akaona isiwe tabu akampigia tena lakini ajabu ni kwamba hakupatikana tena hewani kwa tafsiri rahisi kuwa alimzimia kabisa simu hakutaka usumbufu. Kitendo cha kuzimiwa simu kilimuudhi sana Roberto.


"Shiiiit amenizimia simu?"

Roberto alijiuliza swali na kwa hasira alirusha ngumi ambayo ilikwenda kutua kwenye kioo cha dirisha ambacho kilitawanyika vipande vipande na kuwashtua wote waliokuwa ndani na kutoka nje haraka ambako walimkuta Roberto pale varandani akiwa kashikiria fremu ya aluminium huku mkono wa kushoto ukitoa damu na walipomuangalia vizuri walibaini kuwa alikuwa akilia.


"Nini kimekukuta Robbie?"

Daktari Abbas alimuuliza baada ya kukuta vipande vya kioo vikiwa vimesambaa chini huku damu inamtoka mkononi. Jackline aliangaza huku na kule kama kuna mtu aliyefanya tukio hilo lakini hakuona mtu hivyo akarudi kuungana na wenzake waliokuwa wanajaribu kumuuliza kilichomsibu japo hakujibu chochote zaidi ya kumwaga tu machozi.


"Sasa kaka yangu usipotueleza na kuendelea kulia itasaidia nini? Tueleze ni nini kimetokea tujue tunakusaidiaje."

Jackline alimsogelea Roberto na kumsihi awaambie kuna nini kimetokea mara baada ya kuona wenzake wamechemka lakini hata kwake hali ikawa vile vile kitendo hicho kikampa wazo Daktari Abbas ambaye aliona amshike mkono na kumsogeza pembeni mpaka kwenye kijumba kidogo kilicho karibu na egesho la magari na kumtaka aketi kwenye kiti kisha yeye akaingia ndani huku Jackline na Jasmine wakisalia pale kufanya usafi kwa kuondoa vipande vya vioo. Daktari Abbas alirudi akiwa na kisanduku cha huduma ya kwanza na kuketi karibu na Roberto kisha akaanza kumfanyia huduma ya kwanza.


"Pole sana Robbie utakuwa sawa muda si mrefu kwani dawa hii hufanya kazi vizuri na haina madhara kiafya."

Daktari Abbas alimwambia Roberto ambaye aliitikia kwa kutikisa kichwa tu huku akivuta kamasi. Daktari yeye aliendelea na huduma wala hakungoja kujibiwa na hata baada ya kumaliza kumhudumia aliinuka na kuchukua kisanduku chake.


" Samahani shemeji kwa kilichotokea pale ni hasira tu hakuna shambulio lolote lililotokea kwangu."

Roberto aliona auvunje ukimya kwa kumueleza Daktari Abbas ambaye hakutaka kumhoji kwa alichoelezwa zaidi ya kurudi kitini na kutua chini kiboksi chake na kisha kumshika bega.


" Wala usijali Robbie ila tu jaribu kuidhibiti hasira yako."

Kisha akainuka na kuondoka zake huku akimuacha Roberto aliyekuwa kainama huku akiiangalia bandeji aliyofungwa mkononi.


"Baba Natalie kaongea chochote?"

Jackline alimuuliza mume wake.


"Nafikiri tumpe muda apumzike kwanza ili atafakari kwa kina kilichotokea bila shaka ataongea tu mwenyewe wala hatuhitaji kumbana kihivyooo."

Majibu ya mumewe aliyaelewa kwani ni ya kitaalamu sana na ukizingatia mume wake ni tabibu alihisi kabaini kitu hivyo aliona hakuna haja ya kuendelea kuhoji zaidi ya kurudi ndani kuendelea na maandalizi ya chakula. Daktari Abbas yeye aliingia ndani ambako alirejesha kisanduku kile cha huduma ya kwanza kisha alitoka na kuwafuata wakina Jackline kule jikoni.


"Mimi niwaache tafadhali natakiwa kuelekea Namport mganga mkuu kanijulisha kuwa kuna dharura hivyo natakiwa kuwahi."

Aliongea hayo huku akimpa mkono Jasmine na kisha akamfuata Jackline ambaye alimkumbatia.


"Nikutakie safari njema na majukumu mema ukifika salama."

Jackline alimtakia safari njema mume wake.


"Shemeji."

Jasmine aliita na baada ya kugeuka kumuangalia.


"Safari njema ee na kuwa makini barabarani maana hatumjui adui yetu vizuri."

Jasmine alimtakia safari njema na kumtahadharisha na njiani pia lakini vile vile aliamua kumuita walipokuwa wamekumbatiana na Jackline kuliepusha pepo mahaba ambalo lilitaka kuwaingia mbele yake.


" Nawahakikishia kuwa nitakuwa salama."

Aliwajibu na kutoka zake mpaka alipokuwa Roberto ambaye muda huu alikuwa akiongea na simu huku sura yake ikionekana kuchangamka kidogo.


"Subiri kwanza nitakucheki nipe dakika sifuri."

Roberto aliongea na kuikata simu kisha akamgeukia Daktari Abbas aliyekuwa kasimama pembeni yake.


"Robbie niwaache, kazini kwangu kumetokea dharura hivyo nahitajika mara moja."

Daktari Abbas alimjulisha Roberto ambaye alipata hofu kidogo.


"Kweli shemeji au umechukizwa kwa kilichotokea? Naomba usiondoke ni hasira tu ambazo zilinishika nikashindwa kuzizuia."

Roberto yeye alichukulia tofauti dharura ile akahisi mwenyeji wake kachukia.


"Wala si hivyo Robbie hakuna cha kunikasirisha katika hili lililotokea kwani mimi ni mwanasaikolojia hivyo hayo yote nayafahamu na ndiyo maana nilikuachia ushauri ambao unatakiwa kuufanyia kazi. Kule kazini huwa nikiipokea simu ya mezani tu huwa siulizi najuaga tayari kuna mgonjwa wa oparesheni hivyo kuwa na amani tu."

Daktari Abbas alimuondoa hofu Roberto ambaye alionesha hofu kwamba labda yeye ndiyo tatizo la Daktari Abbas kuondoka muda huo ambao ilikuwa ni jioni kabisa.


" Nimekuelewa shemeji yangu nikutakie safari njema na kazi njema."

Waliagana na Daktari Abbas kuingia kwenye gari na kuondoka huku Roberto akitoka mle bandani na kuingia ndani walikokuwa wakina Jackline.


"Enhh mwapika pishi gani huku jikoni maana dada zangu na kupika wapi na wapi?"

Roberto aliwauliza mara baada ya kuingia jikoni ambako walikuwepo wakina Jackline. Wakina Jackline walitazamana kwanza kabla kujibu na kila mmoja akabinua tu mabega.


"Chezea ndoa wewe lazima ujue kupika hata kwa mangumi."

Jackline alimjibu huku akimuonesha sehemu ya kuketi.


"Ila kwa upande wangu sijui hata itakuwaje siku hiyo na ndiyo maana najitahidi kujua kila kipengele cha jikoni kila kukicha ili nisije ipua boko na kutia aibu."

Jasmine aliona aeleze ukweli wake uliopelekea wote mle jikoni kucheka.


"Wala msijali mwalimu wenu wa mapishi nimefika niulizeni chochote nitawaelekeza kwa utuo ila sharti lazima liwe swali linalohusiana na chai na si vinginevyo kwa nyongeza liwe linalohusu ugali wa dona."

Maelezo ya mwalimu wa mapishi bwana Roberto yaliwafanya kulipuka tena kwa vicheko bila shaka kwa upande wa Jackline hii 'combination' aliikumbuka sana.


"Sawa mwalimu wa mapishi mimi nina swali langu moja tu."

Jasmine alianza kuuliza.


"Karibu mwanafunzi kwa swali lako usijali."

Roberto alimruhusu aulize.


"Asante swali langu linasema hivi ni kwanini tulipokukuta pale varandani ulikuwa unalia huku mkono unatoa damu na sakafu ikiwa imechafuka sana?"

Jasmine alimuuliza swali ambalo lilimfanya Roberto kucheka sana.


"Unajua mbwembwe zote za barabara huishia kituoni na wewe umerukaruka wee lakini nilishajua ni wapi unakwenda kuangukia haya bwana sikiliza jibu la swali lako kwa makini."


"Tunasikiliza wote humu."

Jackline alidakia.


"Ok sawa vyovyote vile, kilichopelekea haya yote kutokea ilikuwa ni majibu ya hovyo ya Titiana na kibaya zaidi kilichonichefua ni kitendo cha kunizimia simu wakati mimi nikiwa kwenye laini niliumia sana nikajikuta nikirusha ngumi ambayo kama ingemkuta sijui ingekuwaje vile na mimi nilijua naupiga ukuta lakini mlio wa vioo ulinishtua kwani sikutarajia kabisa, naomba dada Jackline pamoja na shemeji yangu Abbas Mukesh mnisamehe kwa hasara niliyoisababisha haikuwa dhamira yangu kabisa na kama wasemavyo waswahili 'Hasira ni Hasara' kweli kabisa nimejionea mwenyewe. Dada Jackline niko ta.... "

Kabla hajamalizia kuelezea Jackline alimkatisha.


" Kwanza kabisa nikupe pole kwa lililokutokea lakini pili naomba nikuhakikishie kuwa hakuna hasara uliyoiingiza hapa kila kitu kiko sawa Roberto na kuhusu mpenzi wako Titiana hilo tuachie sisi wanawake wenzake sawa mdogo wangu?"

Jackline alihitimisha kwa kumpigapiga mgongoni.


" Asante mwalimu kwa maelezo mazuri ambayo yameeleweka vizuri sana."

Jasmine yeye aliundeleza utani wake kama ambavyo aliuanza mwanzo.


" Nashukuru mwanafunzi kwa kuelewa haraka somo langu."

Roberto alipigilia kwenye utani ule ule huku akimrushia punje za mchele waliokuwa wakichambua.


" Niliingiwa sana na hofu kumbe....."

Kabla hajamalizia maelezo yake Jasmine mara kengele ililia kuashiria kuwa kuna mgeni nje walitazamana usoni wote kisha Roberto ambaye hakusubiri kuelekezwa alienda kuufungua mlango.


"Samahani kaka yangu naitwa Dorice ni fundi kutoka 'City Alluminium Co. Limited tumepokea maelekezo ya kazi kutoka kwa Daktari Abbas."

Alijieleza yule dada aliyefika pale, na hivyo Roberto kumkaribisha ndani ili akaongee na mwenyeji wake.


"Ni mgeni wako naomba umsikilize."

Roberto alimwambia Jackline.


"Karibu dada yangu naomba nikusaidie tafadhali."


"Asante naitwa Dorice ni fundi kutoka 'City Alluminium Co Limited' tumepokea simu kutoka kwa Daktari Abbas kuwa nifike hapa kuna kazi."

Dorice alijitambulisha kwa Jackline tena kama alivyofanya kwa Roberto.


JE NINI KINAKWENDA KUTOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA KUJUA KINACHOKWENDA KUTOKEA.




Fundi aliyefika nyumbani kwa Jackline kwa maelezo kutoka kwa Daktari Abbas alikaribishwa na kuelezwa namna dirisha hilo linavyotakiwa kuwa ili lisiweze kutofautiana na mengine. Baada ya maelekezo hayo Dorice aliianza kazi yake mara kwenye lile dirisha kwa kuchukua vipimo ili kesho yake iwe kazi rahisi na ukizingatia muda nao ulikuwa umekimbia sana kwani kigiza kilikuwa kimeanza.


"Nashukuru nimefanikiwa kupata vipimo naomba mimi niwaache tutakutana siku ya kesho panapo majaliwa."

Dorice aliwaaga wenyeji wake.


"Karibu tena fundi."

Jackline alimkaribisha kwa wakati mwingine.


"Asante na niwatakie usiku mwema."

Aliaga na kuondoka.

Na kwa kuwa chakula kilikuwa tayari wenyewe waliketi kula.


"Leo nitakula sana chakula kwani ni muda mrefu sana tangia tuketi pamoja kama familia."

Roberto alianzisha mazungumzo akiwa amekiinamia chakula.


"Kwanza wee acha tu hata hao wanaoviziaga makombo watatusamehe kwani hakuna kinachokwenda kutupwa hapa kila kitu kilicho mezani ni hitaji muhimu sana la tumbo."

Jasmine naye alimuunga mkono Roberto huku Jackline yeye alikuwa akitabasamu tu.


"Mimi sina neno yangu macho tu kwenye ligi hii."

Jackline aliona asibaki kimya.

Baada ya kula na kila kitu kuwa sawa Roberto aliingia chumbani kwake na baada ya dakika dakika kadhaa alirejea akiwa na laptop ambayo aliiwasha na baada ya kufunguka aliingia kwenye programu moja matata ambayo akiingiza namba yako ya simu tu itaonesha kila kitu kinachofanywa na namba hiyo kuanzia mazungumzo mpaka jumbe fupi zote na hata kama ikiwa imefungwa programu hiyo taarifa zote hujiihifadhi na ukiifungua tu unazikuta 'unread sms' na 'recorded voices' programu hii maarufu inajulikana kwa jina la BRAIN HUB imekuwa ikitumiwa sana na Jessica pamoja na Roberto kila wanapopewa kazi za kundi. Aliketi na kuangalia kama kuna mpya yoyote lakini hakupata na hivyo kuwageukia wakina Jackline.


"Hivi hakuna mtu ambaye anaweza kutupa taarifa za Bi Elizabeth za hivi karibuni au hata kupata namba yake ya simu anayoitumia kwa sasa."

Roberto alimuuliza Jackline kama kuna uwezekano wa kupata anachokihitaji.


"Mhh umenikumbusha Robbie kuna watu wawili ambao wanaweza kutusaidia katika hili kama tutashindwa yupo wa tatu ambaye huyu sina uhakika naye sana."

Jackline alimjibu Roberto.


"Ni nani kati ya hao tuanze naye muda huu hatuna muda wa kupoteza."

Baada ya kuulizwa swali hilo aliinuka na kwenda chumbani ambako alichukua simu yake na kumtafuta Mahmoud.


"Ndiyo nini sasa shemeji yake?"

Jackline alianza kwa swali la utani baada ya simu kupokewa upande wa pili.


"Aaah shemeji yake mwenyewe huyo hebu nijuze tuone."

Mahmoud alimjibu.


"Unafikiri kuna lolote basi shemeji yangu? Zaidi nilitaka kujua kama umeweza kuyaotea mawasiliano ya Bi Elizabeth au Mackdone."


"Mhh ya Bi Elizabeth nilipata kwa Thomas si unajua ninaye kwa sasa? Lakini Mackdone sijaipata lakini tuendelee kuitafuta."

Mahmoud alimjibu.


"Ok kama inawezekana nitumie hiyo ya Bi Elizabeth kisha nyingine hiyo tuipe muda."

Jackline alimueleza.


"Dakika sifuri shemeji."

Mahmoud alimjibu.

Haikuchukua muda ile namba ikawa imetumwa na hapo hapo akakabidhiwa Roberto ambaye aliichukua na kuijaribu kwanza kama iko hewani.


"Haipatikani, lakini ngoja kwanza kama imezimwa nitajua."

Aliongea Roberto na kuiingiza kwenye programu yake na baada ya kuhakikisha kila kiko sawa aliizima laptop yake na kuirudisha chumbani kisha alirejea na kuungana na ndugu zake waliokuwa bize kuseti nywele zao.


" Hivi hatutoki usiku huu? "

Roberto aliwauliza.


"Itawezekana vipi kuisubiri asubuhi tukiwa humu ndani?"

Jasmine alimjibu Roberto.


"Kwa hiyo nifanye maandalizi siyo?"

Roberto aliuliza.


"Unauliza majibu mdogo wangu."

Jackline alimjibu huku akijiangalia kwenye kioo kikubwa kilichokuwa pale sebuleni. Hivyo kila mmoja alizama chumbani kwake kwa maandalizi na baada ya dakika chache walitoka na kuingia kwenye gari lao pale nje.


"Sasa tutaondoka mpaka mjini kisha mimi mtanishusha nitapanda taxi ambayo itakuwa nyuma yenu kikubwa nifahamu tunaelekea kiwanja gani."

Roberto aliwapa maelekezo ambayo walijua maana yake hivyo hakukuwa na la kujadili zaidi kulipitisha na kuondoka.


"Ni kiwanja gani kizuri hapa Windhoek?"

Jasmine alimuuliza Jackline.


"Kiwanja cha kijanja ambacho kila mtu hupenda kufika hasa mida ya usiku ni ndani ya Clayton Hotel, hii ni hotel ambayo ina hadhi ya nyota tano ndiyo hata wageni huipenda sana kwani hata huduma zake ni za kiwango cha kimataifa."

Jackline aliwaelekeza wenzake namna Clayton Hotel ilivyo.


" Kwa maelezo hayo hatuna chaguo jingine zaidi ya kuelekea hapo."

Jasmine alimuunga mkono Jackline kuelekea Clayton kitu ambacho Roberto hakuweza kupinga na walipofika katikati ya mji Jackline alisimamisha gari na Roberto akashuka na kuwaruhusu kuondoka na yeye akatembea kwa hatua kadhaa na kuifikia taxi iliyokuwa miongoni mwa taxi zilizopaki eneo lile lililokuwa na bango kubwa lililosomeka WE DRIVE IN TOWN na kuingia ndani.


"Tafadhali nikimbize Clayton Hotel."

Roberto alimpa maelekezo dereva huyo ambaye baada ya kufunga mkanda aliiondoa gari yake.


"Ni kiasi gani mpaka hapo?"

Roberto alimuuliza.


"Hatuna bei mkubwa tunachaji shilingi elfu ishirini kwa safari za ndani ya mji haijalishi unakwenda wapi ndani ya mji."

Dereva wa taxi alimjibu Roberto ambaye hakutaka kuendelea kubishana naye ilibidi akubaliane naye. Waliwasili Clayton Hotel ambapo Roberto alimlipa ujira wake dereva yule kisha akaongoza mpaka ndani ya Hoteli hii ambayo kweli ilionekana kuwa ni bab'kubwa Roberto mwenyewe aliikubali. Alipoingia mpaka ndani aliona kuna ukumbi wa nje ukiwa umechangamka sana akaona isiwe tabu ngoja naye ajichanganye huko, alitoa simu na kuwatumia ujumbe wakina Jackline.


"Niko eneo la burudani huku nje kwenye ili eneo la wazi."

Kisha akaiweka akaiweka mfukoni akachukua nafasi yake na kuketi sehemu iliyokuwa wazi. Alipoangalia mbele alibaini kulikuwa na shindano la kucheza ngoma za asili.


"Waooo hii ndiyo kitu naipendaga katika maisha yangu."

Roberto alifurahi sana kuona hii kitu akaitoa simu na kuwatumia tena ujumbe wakina Jackline.


"Mko wapi ninyi mnaukosa uhondo huku."

Baada ya kuutuma kwa Jackline ulijibiwa haraka sana.


"Nani akose shindano kama hili hata sisi tuko humu humu tuko karibu kabisa na jukwaa hili chezea sisi wewe?"

Alipousoma alitabasamu kisha akaiweka mfukoni simu yake na kuagiza maji.


***


Mackdone baada ya kunywa sana wine kule chumbani kwake aliona muda huu anaweza kushuka chini kuangalia kuna nini mpaka kelele zinapigwa kiasi hicho hivyo alikuja na kuingia kwenye ukumbi huu wa wazi na kuketi sehemu iliyokuwa na siti tatu kisha akamwita Mhudumu wa mle ndani.


"Habari yako mrembo?"

Alimsabahi yule mhudumu.


"Mimi siyo mrembo naomba kukuhudumia."

Mhudumu yule alimjibu kwa mkato kwa namna alivyokuwa hakutaka kujuana na watu hovyo.


"Mbona uko hivyo mrembo au umekatwa malipo yako ya siku nini?"

Mackdone aliendelea kumchimba binti wa watu.


"Mzee kuwa muelewa basi kwani hata kama ni kweli inakuhusu nini wewe?"

Mhudumu yule alionekana kukerwa na maneno ya Mackdone akaamua kuondoka.


"Unakwenda wapi mrembo? Binti mrembo kama wewe hustahili hata kidogo kukasirika na kuzira unatakiwa kukaa karibu na maua yanayonukia ili na wewe unukie vile vile au?"

Alimzuia kwa kumshika mkono kisha akatoa burungutu la noti ambalo alimkabidhi Mhudumu yule.


" Hee wewe Mzee umechanganyikiwa nini hela zote hizi ni za nini? "

Mhudumu alijikuta akiuliza swali ambalo liliwafanya hata waliokuwa karibu kugeuza vichwa vyao kujua kulikoni kwani aliongea kwa sauti ya juu.


"Unauliza? Unauliza kweli? Naanza kuamini kuwa wewe ni bushgirl okay hiyo hela nimelipia hizi siti zote tatu hapa hivyo sihitaji mtu mwingine karibu yangu mpaka nitakapoondoka humu ndani nyingine utaniletea wine chenji unaweza kuitupa si hauhitaji hela wewe? "

Mackdone aliongea kwa madaha kama kawaida yake huku akisimana kujiweka sawa.


" Sikiliza Mzee viti humu ndani havilipiwi na pia hatuuzi pombe hizo zinapatikana kule juu mzee."

Mhudumu alimjibu Mackdone.


" Aahh nimegundua wewe hunitaki wacha niondoke zangu siwezi kaa na watu wasiojitambua."

Mackdone aliinuka na kuondoka zake baada ya kuona lugha gongana na yule mhudumu.


" Na hela zako hizi?"

Mhudumu alimuuliza baada ya kumfuata.


"Utaniletea chumbani kwangu kama huzitaki."

Alimjibu huku akiondoka na kumuacha mhudumu huyo akiwa anamsindikiza kwa macho. Aliona hakuna haja ya kuendelea kubishana naye mzee huyo hivyo alizichukua zile hela na kuziweka kwenye pochi yake kisha akaangalia kushoto na kulia kama kuna anayemuangalia kisha akaondoka lakini wakati hayo yote yanaendelea Roberto alishuhudia mwanzo mpaka mwisho kwani kiti chake kilikuwa ni cha nne kutoka pale alipokuwa amekaa Mackdone hivyo aliweza kusikia kila kitu kutoka kwa Mackdone na mhudumu akapenda kumfahamu mzee huyo ambaye hela si tatizo kwake, akaamua kumfuata yule mhudumu kule alikoingia alimfuatilia kwa mbali na kubaini kuwa alikuwa anaingia chooni hivyo akajificha kumsubiri. Akiwa pale mara wakatokea vijana wengine watatu ambao waliingia mle ndani na kuongoza upande viliko vyoo hivyo Roberto akajua kuna jambo akajificha vizuri ili asionwe akawa anausoma mchezo ule.


"Huku hakuna noma yoyote kaeni sawa."

Mmoja wao aliyekuwa pale nje aliwajulisha wenzake.


"Ok sawa lakini kuna yule mwamba aliyekuwa mbele yetu yuko wapi?"

Mwingine aliuliza.


"Wa nini huyo mlevi hapa tunaingia humo humo chooni tunachukua chetu kisha tunasepa zetu na huyo fala akijipendekeza tu tunamsafisha na yeye."

Mwingine aliongea kisha wakausogelea mlango ule alioingia yule mhudumu upande wa vyoo vya kike wakaangalia kulia na kushoto kisha wakajiandaa kuusukuma lakini kabla hawajafanya hivyo mlango ulifunguliwa na yule mhudumu alitoka. Hawakuweza kusubiri walimvamia na kumziba mdomo ili asipige kelele.


"Ile soltepu iko wapi tumpige gundi mdomoni?"

Mwenzao aliuliza.


"Mbane hivyo hivyo soltepu ya nini kwani tunaondoka naye hapa atupe chetu tumuache."

Aliongea huyu mwingine ambaye alionekana kuwa na kisu huku hawa wengine wakiwa hawana chochote kile mkononi. Kama upepo Roberto alitokea na kumtandika teke la mkono uliokuwa na kisu na kupelekea kuanguka chini, alipotaka kukiwahi kile kisu alikutana na teke la kidevu lililopeleka chini huku akitema damu. Wenzake kuona vile wakaona isiwe tabu wakamuachia mhudumu na kutimua mbio wakimuacha mwenzao.


"Simama haraka wewe si ni kidume mpenda vya bure."

Roberto alimwambia yule kijana aliyekuwa akivuja tu damu pale chini.


"Naomba nisamehe kaka yangu mbona hatujamuumiza eti dada tumekuumiza?"

Yule kijana aliona aombe tu radhi kwa Roberto ambaye alikuwa katulia tu akimsubiri ainuke pale. Wala maneno yale hayakumuingia Roberto hata kidogo na alichokifanya alimfuata pale chini na kumtandika mateke ya mbavu mfululizo huku yule dada akiwa kajikunja kwenye kona huku kaziba macho yake asione anachofanyiwa yule kibaka.


"Inuka na utoke humu ndani haraka kabla sijakumalizia."

Roberto alimwamuru baada ya kuridhika kwa alichomfanyia. Kwa shida sana aliinuka na kukimbia huku akiyumba yumba, Roberto alimfuata yule mhudumu pale kwenye kona.


"Pole dada hujaumizwa kweli?"

Alimuuliza lakini yule dada hakujibu zaidi ya kujikunja kwenye kona huku akijificha macho yake.


"Tafadhali dada yangu mimi si mtu mbaya kwako nimefanya hivyo baada ya kuwashuhudia wakiwa wamekukunja wakati nataka kuingia chooni."

Aliona amtoe hofu dada wa watu ambaye alijua na yeye anataka kumdhulu ili achukue kitita cha fedha.


"Nashukuru kwa msaada wako kaka yangu, kwa inavyoonekana wewe ni mgeni hapa Windhoek."

Mhudumu alimshukuru sana Roberto ambaye pia alimshangaa.


"Kwanini unauliza hivyo?"

Roberto alitaka kujua.


"Huku ukivamiwa na magenge au vibaka tu wakija wengine kukusaidia usifikiri umepona wale inakuwa ni fursa wao tena kujinufaisha kifupi mwenye nguvu ndiye anaondoka na bingo."

Maelezo ya mhudumu yalimshangaza kidogo Roberto ambaye alitulia kumsikiliza wakati huo yule mhudumu alikuwa akiifungua pochi yake ambayo aliiweka kwenye mfuko wa koti la sare ya hotel akitaka kutoa hela.


" Unataka kufanya nini sasa?"

Roberto alimuuliza.


"Nisiposhukuru nitakuwa sina busara chukua kidogo hiki kaka yangu."

Alimwambia huku akimkabidhi hela Roberto ambaye alikataa kupokea.


"Sikiliza dada sihitaji hela kwa msaada nilioutoa ila tu kwa mawasiliano zaidi na mimi kadi yangu hii hapa."

Roberto alimweleza dhumuni la kutopokea ile hela kisha akamkabidhi kadi yenye mawasiliano yake na kuondoka zake huku akimuacha mhudumu kaduwaa pale pale alipokuwa.


HIVI UNAONA NINI HUKO MBELE?



Aliingia pale ukumbini na kuwafuata wakina Jackline walipokuwa wamekaa kutazama shindano ambalo lilikuwa limefikia ukingoni na muda huo aliyekuwa akisubiriwa alikuwa ni jaji mkuu wa shindano hilo ambaye alipewa jukumu la kumtangaza mshindi. Wakina Jackline walikuwa bize na shindano wala walikuwa hawajui kilichokuwa kinaendelea upande wa pili na ndipo walipomuona Roberto akikaa pembeni yao.


"Yaani mwenzenu hapa ningepewa jukumu la kumtangaza mshindi sijui ingekuwaje maana kila aliyepanda jukwaani alikuwa ni zaidi ya yule wa awali sijui kwa upande wenu."

Jasmine aliongelea shindano hilo ambalo liliwakonga nyoyo zao usiku huo.


"Mimi nitakuwa muongo tu maana dakika mbili macho jukwaani dakika nne usingizi ila yote kwa yote lilikuwa ni bonge la burudani kupata kutokea."

Jackline aliona aongee ukweli tu kwani hakulifaidi vizuri shindano hilo kutokana na usingizi ambao hajaupata kwa siku kadhaa.


" Mhhh yaani wewe dada Jackline nakufananisha na wale mashabiki kindakindaki wa vilabu vikubwa kwa kule kwetu mfano Boka Junior au Vasco Da Gama unamkuta kaingia kwenye vibandaumiza kuangalia mpira akiwa humo yeye ni kuupiga usingizi tu sasa asikie ukumbi umelipuka kwa shangwe na yeye bila hata kuuliza ni timu gani imefunga naye huyo gooooooaal' anapokuja kuangalia vizuri kumbe timu yake ndiyo iliyofungwa."


"Tafadhali dogo nitake radhi yaani mimi ndiyo unifananishe na huyo shabiki maboga kweli?"

Jackline alitania na wote wakaanza kucheka.


"Hebu tuachane na hayo naombeni mnifuate mara moja."

Roberto aliongea huku akiinuka na kutoka nje na kuwaacha wakina Jackline wakiwa hawaelewi kuna nini huko anachowaitia.


"Kuna nini huko tenaaa?"

Jasmine aliuliza kwani hakutaka kukosa kumshuhudia mshindi anayekwenda kutangazwa.


"Mimi mwe ni kama wewe tu hebu twende si unamfahamu dogo tukichelewa?"

Jackline alimjibu Jasmine huku akiinuka kumfuata Roberto nje na Jasmine hakuwa na jinsi ilibidi ainuke kuwafuata.


"Kuna nini tena?"

Jasmine aliuliza baada kufika nje.


"Jamani mwenzenu sijashuhudia chochote humo ndani nilikuwa bize na uchunguzi wangu."


"Wa nini huo?"

Jackline alimuuliza.


"Nikiwa nimekaa naangalia shindano kuna mtu wa makamo kiasi alikuja na kukaa siti kama ya nne kutoka nilipokuwa akamwita mhudumu na kuanza kumchimba chimba huku akimpa mihela lundo lakini mhudumu alionekana kutoshobokea mbwembwe za mtu huo ambaye aliamua kuondoka zake na kumuacha mhudumu akiwa hajui afanye nini hivyo aliona aingie chooni kwanza kwa ajili ya kujiweka sawa ndipo, sikucheza mbali na mwanamwali nikamfuata huko huko chooni lakini kabla sijafanya yangu si wakatokea wahuni ambao walitaka kumpora zile hela."


"Ikawaje sasa Roberto mbona unatupa presha wenzako?"

Jackline alimuuliza.


"Unafikiri nini kilitokea? Niliingia ulingoni kumsaidia na hilo lilifanikiwa."

Alimaliza Roberto.


"Yuko wapi huyo mhudumu kwa sasa na vipi kuhusu mzee ulifanikiwa kumfahamu?"

Jackline alimuuliza maswali mfululizo.


"Mhudumu ni yule pale anayeongea simu na kuhusu huyo mzee sina ninachokifahamu lakini kupitia yule mhudumu nitamfahamu tu."

Roberto alimjibu na wakati huo huo simu yake iliita na alipoangalia mpigaji ni nani aliona ni namba mpya hivyo aliipokea.


"Haloo."

Alianza mara baada ya kuipokea.


"Haloo bila shaka naongea na Roberto Cruise?"

Upande wa pili uliuliza.


"Bila shaka nani mwenzangu?"

Roberto aliuliza huku akimuangalia yule mhudumu pale mlangoni ambaye simu ilikuwa sikioni hivyo moja kwa moja akajua ni yeye tu.


"Naomba tuonane hapa nje kwenye maegesho ya magari tafadhali kama hujaondoka hapo utanifahamu."

Upande wa pili ulipomaliza kuongea ulikata simu na kumuacha acha Roberto akiwa bado na simu sikioni. Kisha aliitoa na kuwageukia wakina Jackline.


"Naombeni dakika mbili tafadhali msitoke hapa."

Aliwaaga.


"Unakwenda wapi tena?"

Jasmine alimuuliza lakini Jackline alimziba mdomo kuwa atulie kwanza wakati huo Roberto alishaondoka na kuelekea kwenye makutano na huyo aliyempigia simu. Alipofika kwenye maegesho hakuhangaika sana kwani kulikuwa na mtu mmoja tu na ambaye alimfahamu kwa mavazi yake akiwa kaegemea gari moja ndogo hivi aina ya Vitz nyeusi.

Alipomkaribia aliipiga namba ile na alipoangalia kwa yule mtu mbele yake aliona akiiangalia simu ambayo ilikuwa ikiita hivyo akaikata na kumpa nafasi yule mrembo kugeuka nyuma.


"Ooh ndiye uliyenipigia muda huu?"

Yule mhudumu alimuuliza kama kumtega wakati aliona jina la mpigaji.


"Ndiyo ni mimi, nimekuja mara moja kukusikiliza wenzangu wale pale wananisubiri."

Roberto alianza kwa kutoa sababu zake kama gia ya kumuingia yule mhudumu.


"Okey Robbie mimi mwenyewe sitapenda kukuchukulia muda wako, uliponiacha kule chooni nikajikuta kama vile moyo wangu hauna amani hivi nikahisi kuna deni bado nadaiwa na wewe."

Mhudumu yule alianza kueleza sababu ya kumpigia.


"Ondoa shaka juu yangu mimi kama ambavyo nilikueleza nilijitoa kukupa msaada ambao si wa malipo naomba unielewe dada yangu."

Roberto alisimamia msimamo wake ule ule.


"Nimekuelewa kaka Robbie, naomba unisaidie kitu."


"Kitu gani hicho?"

Roberto alimuuliza.


"Shifti yangu ni ya mpaka asubuhi hapa kazini hivyo siuoni usalama wa hizi hela zangu hivyo naomba nikukabidhi ukae nazo mpaka kesho ndipo nitazichukua."

Mhudumu alimueleza shida yake.


"Mhh kwenye hilo ondoa shaka hakuna atakaye kuibia nakuhakikishia kabisa."

Roberto alimjibu huku akimshika mkono uliokuwa na zile hela kumzuia asimpe.


"Unarahisisha Robbie hivi kwa mfano kesho tukionana au kukupigia simu kwamba nimeibiwa zile hela utajisikiaje ilhali ulijitoa kwa ajili ya hizo."

Swali lile lilimfanya Roberto kuwa mpole kidogo ni kama lilimuingia kwani hakuwa na jibu la kumpa yule mhudumu.

Akajikuta akizipokea zile hela ambazo zilikuwa vile vile kwenye pochi ya yule mhudumu ambaye aliitoa tu simu mle kwenye pochi.


" Umeniamini vipi mrembo mtu ambaye hunijui na hujawahi kuniona popote pale nikiondoka nazo itakuwaje?"

Roberto alimuuliza.


"Utakuwa umeamua na kukuamini ni mara baada ya kunisaidia kutoka kwa wale vibaka. Wewe Roberto ni mgeni hapa mjini huwajui vibaka wa hapa?"


"Ok asante kwa kuniamini lakini pamoja na yote sikufahamu jina lako?"

Roberto aliona amuulize jina.


"Kila kitu kiko humo humo."

Alimjibu na kuondoka zake huku akimuacha Roberto akimshangaa. Aliifungua ile pochi kuhakikisha asije uziwa mbuzi kwenye gunia ndipo aliziona pamoja na kadi ya mawasiliano iliyokuwa na jina la Grace Goka hapo hapo alichukua simu na kumpigia.


" Mambo Grace?"


"Umefurahi sasa kunifahamu?"


"Kama unavyofikiri."

Roberto alimjibu.


"Poa bwana nikutakie usiku mwema kesho ukiwa free utanijulisha maana kuanzia asubuhi mpaka jioni nitakuwepo tu kazini ni usiku."

Grace alimjibu.


"Poa bwana salamu kwa shemeji."

Grace hakujibu kitu zaidi ya kukata simu bila shaka hakutarajia kusikia alichoambiwa na Roberto.

Hivyo Roberto aliondoka na kuwafuata wakina Jackline walipokuwa.


"Woyo woyo Roberto na mchepuko wakeee, yaani mpaka pochi yake umeachiwa? Roberto umenishinda."

Jasmine alimpokea na dongo kavu lenye vumbi la kutosha.


"Mhh kwa mazingira hayo Titiana analo na atajutia maamuzi yake. Kwa hiyo umechukua na vitu vyake kwamba unakwenda kulala kwake au...."

Kabla Jackline hajamaliza alikatishwa na Roberto.


"Hebu acheni basi kutoa hukumu tangulizi si msubiri niwape udambwidambwi huu kuliko kutengeneza stori yenu?"

Majibu ya Roberto yaliwafanya wakina Jackline kukanyagana miguu na kutulia.


"Tunakusikiliza kaka yetu mwenyewe."

Jasmine alimpamba.


"Naombeni tuondoke mahali hapa kwa sasa na kuhusu hii pochi wala msiijaji vibaya humu ndani ndiyo kuna zile hela nilizowaambia muda mfupi uliopita."


"Kwanini akupe wewe sasa?"

Jackline alimuuliza akiwa anaingia kwenye gari.


"Kaomba hivyo kuhofia usalama wake ukizingatia kuwa kazini anakesha mpaka asubuhi hivyo akaomba nimhifadhie japo nilimkatalia akakomaa kwa kuniambia nimezipigania mpaka zimesalimika itakuwaje nikisikia kuwa zimeibwa hivyo nikawa sina jinsi na mkumbuke nina kazi naye huyu hivyo sikutaka kumuudhi."

Roberto alieleza kwa kirefu.


" Kwa hapo sawa."

Jasmine aliyekuwa pembeni kwa Jackline aliyekuwa anaendesha gari alimjibu.


" Mpaka hapa kazi yetu inakwenda kuwa rahisi kidogo kwani hawa panya tutakwenda kuwatia mikononi mwetu mara moja."

Roberto aliongea kwa kujiamini.


"Mungu akawe mbele yetu kwa kila hatua maana maadui zetu ni wapya hatuwajui hata chembe."

Jackline alimjibu.


Walifika nyumbani na kuingia ndani ambako Jackline alikwenda kulipaki gari wakati huo Jasmine akiwa anafungua mlango baada ya kushuka.


"Mungu ni mwema tumefika salama."

Jackline aliwaambia wenzake wakiwa sebuleni.


"Ni muda wa chakula huu."

Jasmine aliongea huku akifunua vyombo vyenye chakula mezani.


"Wewe kula tu mimi sina hamu ya chakula naenda zangu kulala tutaonana kesho kikubwa kumbukeni safari yetu ya kwanza itakuwa ni shuleni nikaonane na wajomba zangu."

Roberto aliwaambia akiingia chumbani kwake.


"Hilo limepita hata mimi mwenyewe nimewamisi wanangu."

Jackline alimjibu huku akiungana na Jasmine mezani. Na wao mara baada ya chakula walikwenda kulala.

Baada ya kupambazuka Roberto aliamka na kutoka nje ambako alianza kufanya mazoezi ya viungo kwenye eneo ambalo lilikuwa na vifaa vichache vya kufanyia mazoezi kwenye kijumba cha wazi hata wakina Jackline walipoamka na kumuona mle nao waliungana naye kwenye mazoezi ambayo yalichukua kama saa moja na nusu mpaka saa moja ambapo kila mmoja alikwenda kuoga baada ya kuoga Jackline aliingia kuandaa kifungua kinywa huku Roberto akiwa mbele ya laptop yake tayari kwa kuiingiza namba ya Grace kwenye application maalum ili ajui aliwasiliana na anawasiliana na nani. Lakini akaona kwanza muda huo ampigie kumuuliza kama anaweza kuwa na namba ya yule mzee aliyempa hela.

Hivyo akaichukua simu yake na kuiwasha na mara baada ya kuwaka aliangalia kama kulikuwa na namba zozote zilizomtafuta muda huo au kabla. Alipigwa na butwaa baada ya kukutana namba ya Grace ikiwa imemtafuta zaidi ya mara kumi na sita.


"Mmhh alitaka kujua nini mbona mara nyingi hivyo? Lakini yuko sahihi mihela hii ni mingi hata ningekuwa ni mimi hofu lazima."

Alijisemesha mwenyewe huku akipitia namba nyingine na mojawapo ilikuwa ni ya Jessica ambaye alimtafuta mara mbili hivi.


"Wao Jessica bora yako uliyenitafuta hata hiyo mara mbili chizi wako yeye kauchuna tu na mimi sina muda."Aliichukua simu na kuitupa pembeni na kusogeza laptop yake ili aendelee na mambo mengine. Lakini akili nyingine ikamwambia amtafute Grace kujua alitaka kusema nini.


" Samahani mtumiaji unayemtafuta kwa sasa hayuko hewani tafadhali acha ujumbe wa sauti."

Hakumpata hewani Grace na alipoiangalia vizuri simu yake aliona bado kuna jumbe ambazo hakuzisoma akaona azisome.


"Jamani karibieni mezani kifungua kinywa kiko tayari."

Alikuwa ni Jackline akiwakaribisha mezani.


"Nakuja dada."

Roberto alimjibu na kuiweka simu kando na kutoka kuelekea chumba cha chakula.


"Dada uko fasta kwenye mambo ya jiko?"

Roberto alitania.


"Hii kwa sasa nimeshaizoea kama utaratibu wangu hasa siku za kwenda kuwaona watoto wangu huwa lazima niwaandalie chakula si unajua tena?"

Jackline alimjibu.


"Ni kweli kabisa hata ningekuwa mimi lazima kuwapa furaha wanangu."

Jasmine naye alichagiza kwe hoja hiyo ya Roberto.

Walipata chakula pale kisha Roberto akashukuru na kuinuka.


"Jamani mimi niko chumbani kuna mambo nayaweka sawa mtandaoni lakini kuna jipya ambalo sijalielewa hebu ngoja kwanza."

Alitoka na kuelekea chumbani kwake na kisha alirejea simu ikiwa sikioni.


"Bado hapatikani tu."

Aliongea akiwa anaitoa simu sikioni.


"Nani huyo hapatikani?"

Jackline alimuuliza Roberto aliyeonekana kama kuchanganywa na kitu.


"Grace simpati hewani toka nilipoanza kumpigia na kinachonishangaza ni kuzikuta jumbe zake za kunikosa hewani zaidi ya mara kumi na sita."


"Zaidi ya mara kumi na......"

Kabla hajamaliza alikatishwa na kengele ya mlango ambapo Jackline hakuona sababu ya kuendelea kusubiri akaenda kuufungua mlango.


"Naitwa Thadei Zombe ni mlinzi wa zamu hapa kwako kwa mwezi huu kutoka Kampuni ya ulinzi ya Global Security Company."

Alijitambulisha yule mlinzi.


"Kweli mambo ni mengi yaani mpaka nilishindwa kuwasiliana na mlinzi aliyemaliza?"


"Wala usihofu kwa hilo."

Mlinzi alimjibu.


"Ok sawa geti mikononi mwako Thadei."

Jackline alimkaribisha rasmi mlinzi hiyo kuianza kazi yake ya mwezi mzima. Kisha jackl alirejea ndani.


"Atakuwa kapatwa na nini Grace? "

Jackline aliuliza akiwa mlangoni tu.


" Yaani wala sijui kilichompata ni nini huko."

Roberto alimjibu huku akipitia jumbe zilizokuwa kwenye simu yake.


" KAKA ROBERTO NAKUSHUKURU KWA WEMA WAKO KWANGU LAKINI NA.."

Ujumbe ule ambao ulitoka kwa Grace ulimchanganya Roberto.


"Hebu someni huu ujumbe na ninyi mnaweza kuuelewa."

Roberto aliongea hayo akiwakabidhi simu wakina Jackline na Jasmine.


"Nooo kuna jambo limempata huyu hebu twendeni pale Clayton Hotel tunaweza kupata chochote."

Jasmine aliongea baada ya kuusoma vizuri.

Waliinuka kila mmoja akibeba kilicho chake na kutoka nje mkuku mkuku kuelekea lilipokuwa gari.


"Thadei tunarudi muda si mrefu kuna dharura imetokea kazini."

Jackline alimjulisha mlinzi akiwa anawafungulia mlango.


"Sawa bosi."

Mlinzi alijibu.

Walitoka haraka kuelekea Clayton Hotel ambako walihisi wanaweza kupata chochote kutoka kwa watumishi wa Hotel.

Walifika pale Clayton Hotel na kukuta watu wengi wakiwa nje ya lango la kuingia pale Hotelini. Na Jackline alipotaka kuingia ndani alizuiwa na mlinzi.


"Huko ndani kuna mauaji yametokea hivyo hakuna anayeruhusiwa kuingia kwa sasa mpaka kwa kibali maalum."

Mlinzi aliwajulisha.


"Ni nani aliyeuawa na ni nani aliyefanya unyama huu?"

Jackline alimtupia swali mlinzi.


"Sijui kama utakuwa unamfahamu ni mhudumu wa Hotel hii anaitwa Grace kauawa na mtu asiyejulikana kwenye moja ya vyumba vya kulala wageni hivyo polisi wanafuatilia ni nani aliyekuwa mteja wa chumba hicho kwa siku ya jana."

Mlinzi alitoa maelezo marefu ambayo wakina Jackline hawakuyahitaji kwa wakati huo jina pekee ndiyo liliwatoa jasho na miili kuishiwa nguvu.


" Maskini Grace wa watu."

Roberto alijisemesha mwenyewe akiwa kashika kichwa.


JE NINI KITATOKEA?





Jackline aliwaita wakina Roberto pembeni kujadili kilichotokea, na muda huo gari la wagonjwa lilikuwa ndiyo linaingia ndani kwa ajili ya kuubeba mwili wa Grace ambao ulikuwa bado mle chumbani.


"Hapa mnafikiri mhusika anaweza kuwa nani?"

Jackline aliwauliza wenzake.


"Mimi kwa upande wangu nina mashaka na yule mzee wa jana aliyemuachia pesa."

Roberto aliongea kile anachokihisi kwenye tukio hilo.


"Sijui hata niseme nini kwani kila kitu kilikuwa ni simulizi kutoka kwa Roberto hivyo hata kilichotokea hapa nahisi simulizi bado inaendelea hivyo bado naendelea kuunganisha nukta ambazo baadaye zinaweza kunipa kitu."

Jasmine alishindwa aongee nini kwa kuwa hakumjua vizuri Grace.


" Hili tukio limesikitisha sana japo sikuweza kumuona macho kwa macho Grace."

Jackline aliongea hayo akimuangalia Roberto aliyekuwa akitokwa na macbozi huku macho yakiwa kule ndani ya Hotel. Kitu kilichowaacha midomo wazi wakina Jackline ni baada ya kumuona Roberto akichukua kitambulisho na kukivaa kisha akatoa kijitabu kidogo kama kinotbook hivi na kuondoka kuelekea kule ndani.


"Kaka unaelekea wapi?"

Mlinzi alimuuliza Roberto ambaye alitaka kupita kuingia ndani.


"Unauliza nini tena kwani kitambulisho hakiongei?"

Roberto alimuuliza mlinzi.


"Sawa lakini unatakiwa unipe ufafanuzi kaka."

Mlinzi aliendelea kumkalia shingoni Roberto.


"Labda nikuulize swali humo ndani hakuna waandishi wa habari?"

Roberto aliona amuulize mlinzi huku akimpita na kuingia ndani na kumuacha mlinzi akiwa anatabasamu tu. Kule ndani Afisa Upelelezi aliwaambia waandishi wa habari kuwa mwili wa marehemu umekutwa umetobolewa sana kwa visu.


" Na inavyoonekana muuaji alidhamiria kuyatekeleza mauaji haya."

Afisa Upelelezi wa Polisi aliwaambia waandishi wa habari. Na hivyo kuibua maswali kutoka kwa waandishi wa habari wakitaka kujua zaidi juu ya tukio hilo na mtu wa kwanza kupata nafasi ya kuuliza swali hakuwa mwingine bali ni Roberto.


" Kwa jina naitwa Robbie wa Uwezoblog ambayo ni International blog swali langu ni dogo tu Afisa."

Alijitambulisha Roberto.


"Uliza swali lako Robbie."

Afisa Upelelezi alimruhusu Roberto kuuliza swali.


"Wakati tukio linatokea wafanyakazi na walinzi wa Hotel hii ambayo ni ya Nyota tano kabisa walikuwa wapi? Na huyo muuaji aliwezaje kuingia ndani na kutekeleza mauaji yake na kutoka bila kuonwa na mtu yoyote yule na mwisho kabisa Kamera za ulinzi zinasemaje? Yangu ni hayo naomba majibu tafadhali."

Roberto alihitimisha na kutulia kusubiri majibu kutoka Afisa.


" Naomba niwajibu kwa ufupi kabisa kwa nahitajika ofisini, kila kitu kinakwenda vizuri kwani tayari tumepata sehemu ya uchunguzi wetu ambayo ni picha mjongeo kutoka kwenye Kamera za ulinzi lakini pia mawasiliano ambayo yalifanyika ndani ya simu ya marehemu kabla ya kufikwa na umauti... "

Majibu ya Afisa huyu wa Polisi yalimpa kiwewe kidogo Roberto akatoa simu mfukoni.


" Ndiyo ndiyo bosi hapa bado niko Clayton Hotel namalizia kukusanya taarifa kisha nakuja."

Roberto aliongea hayo huku akitoka pale hatua moja baada ya nyingine kulitafuta geti liliko kwani alihisi kuendelea kubaki pale simu yake ingeweza kunaswa na alipolifikia gari tu.


" Ondoa gari fasta eneo hili si salama kwangu."

Roberto aliongea huku akiingia ndani ya gari, wakina Jackline hawakuwa na la kuhoji zaidi ya kuondoka huku Roberto yeye akiifungua simu yake na kuchomoa chipu yake kisha akairusha nje ya gari simu yake.


"Nini sasa mbona unatupa simu tena?"

Jasmine alimuuliza Roberto ambaye alikuwa akitokwa jasho kama vile katoka kufanya mazoezi ya viungo.


"Nitawaambia tukifika nyumbani hapa siyo sehemu yake ndugu zangu."

Roberto alijibu kwa kifupi kitu kilichowashangaza wakina Jasmine na hivyo ilibidi wawe kimya huku Jackline yeye alikuwa akimuangalia Roberto kwa kuibia kupitia 'Upper Mirror' ni kama alikuwa na maswali mengi sana ya kumuuliza Roberto lakini alijizuia mpaka wafike nyumbani. Walifika nyumbani kwao na kuingia ndani huku Jackline akipaki gari sehemu ya maegesho kisha akamfuata mlinzi wake Thadei.


"Habari Thadei, kuna jipya?"


"Hakuna jipya lolote zaidi ya dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Dorice ambaye ni fundi ndiye alikuja nikamwambia sijaachiwa taarifa zake hivyo aliondoka na kuahidi kurudi mchana."

Thadei alimjulisha Jackline.


" Ok namfahamu huyo kuna kazi tuliahidiana naye aifanye siyo mbaya akiwahi atanikuta."

Jackline alimjibu na kuondoka zake kuelekea ndani. Alipofika ndani alimkuta Jasmine akinywa juisi.


" Roberto yuko chumbani kwake? "

Jackline alimuuliza.


"Yuko huko sijui kuna nini anakifanya."

Jasmine alimjibu na kuendelea kunywa juisi yake.

Hivyo alimuacha Jasmine na kumfuata Roberto chumbani kwake ambako alimkuta akiwa katulia na laptop yake.


"Niambie brother?"

Jackline alimuanza Roberto.


"Dada acha tu kuna kitu nakiweka sawa hapa na kama nisingeingia kule ndani inawezekana ningedakwa pale pale tulipokuwa."


"Kwanini Roberto?"

Jackline aliendelea kumuuliza.


"Nikiwa mle ndani kama mwandishi wa habari niliuliza swali la kiuchunguzi ambalo walijibu kuwa kuna vitu wamebaini moja ni video mjongeo kutoka kwenye kamera za ulinzi na pia kuna namba ambazo zilifanya mawasiliano ya mwisho na marehemu wanazifuatilia."

Roberto alitoa maelezo ambayo yalimchanganya Jackline.


" Mungu wangu, so itakuwaje? "

Alimuuliza.


" Chezea mimi dada nishakiruka kihunzi hicho kwani tayari nimeshahamisha namba za muhimu kwenye chipu yangu ambayo huwa siitumii mara kwa mara na kisha kuitupa chooni chipu hivyo kunipata wasubiri sana."

Roberto alimjibu akiwa kwenye tabasamu kubwa na macho yakiwa kwenye laptop yake.


" Hivi ulipataje wazo la kuingia mle ndani kama mwandishi wa habari? "

Jasmine alimuuliza baada ya kuungana nao chumbani kwa Roberto.


" Si wazo tu kifupi mimi ni mwandishi wa habari nimesomea kabisa na nina miliki blog yangu ambayo inaitwa uwezoblog huwa nikitulia napandisha habari mbalimbali kutoka kila kona ya miji mikubwa duniani ambako kuna waandishi wangu wa habari na ni hao hao huwa nawatumia kwenye siri zangu mbalimbali, au umesahau nilipokupa background ya Mackdone?"

Roberto aliwapa jibu ambalo liliwashangaza sana wakina Jasmine kwani hii ilikuwa ni habari mpya kwao.


" Wewe ni kiboko."

Jackline alimwambia huku akimpiga bega Roberto.


" Na tayari nimeyanasa mawasiliano ya Grace na yule muuaji wake."

Roberto aliwapa habari njema.


"Umepataje na pia umejuaje kama ni yeye?"

Jackline alimuuliza.


"Angalieni hapa." aliwaonesha kitu kwenye ile application' anayoitumiaga kuwana watu.


"Muda huu hapa kama mnakumbuka ni pale ambapo Grace alikuwa anaongea na simu ninyi mkaniuliza yuko wapi na mimi nikawaonesha alipokuwa akiongea na simu na mara akanihitaji tukutane kwenye maegesho ya magari ambapo alinikabidhi hela zake, hapo nahisi tayari mtu huyo alikuwa kamtishia hivyo aliingia hofu japo hakusema kwangu. Na hapa ni mawasiliano ya mwisho ya mtu huyo kabla ya kufanya alichokifanya."

Roberto alitoa maelekezo kupitia application yake.


" Tutamjuaje huyu muuaji? "

Jackline alimuuliza.


" Kazi ndogo hiyo dada Jackline hebu ichukue namba hiyo na iingize kwenye hicho kiboksi cha kulia kwako kisha bonyeza batani ya kijani."

Jackline alifuata maelekezo ya Roberto akafanya kama alivyoambiwa na baada ya kubonyeza kitufe cha kijani ulikuja wasifu wa mmiliki wa namba ile.


" Haa mbona siamini ninachokiona hapa huyu si Mackdone? "

Jackline akiwa kashika mdomo wake aliuliza kitu ambacho jibu lake analiona pale kwenye laptop ya Roberto. Na hapo hapo Roberto akaipiga ile namba kupitia application ile na baada ya dakika sifuri upande wa pili ulipokea simu.


" Haloo.. "

Roberto alianza.


"Nani anaongea?"

Mackdone alimuuliza.


"Unaongea na Hilbert mwandishi wa habari kutoka blog ya kimataifa iitwayo uwezoblog."

Roberto alidanganya utambulisho wake.


"Ndiyo bwana mwandishi nikusaidie nini na kwanini umeficha utambulisho wako?"

Mackdone alimuuliza baada ya kuona kwenye simu yake limekuja jina lililosomeka 'Unknown number' halafu anaambiwa ni blogger.


"Usihofu mkuu, mfumo wetu umetengenezwa hivyo kwa sababu za kiusalama."

Roberto alimjibu.


"Vizuri kwa hiyo kuna kipi unahitaji nikusaidie?"

Mackdone alimuuliza.


"Kwanza napenda kukupongeza kwa uimara wako katika kuendeleza makampuni yako hasa kampuni ambayo inafanya kazi kama yangu ya 'Kwazulu Media' ambayo inaisimamia televisheni ya 'Big Television na Bigfm Radio."


"Nashukuru sana Hilbert kwa hiyo ungependa kufanya kazi na sisi?"

Mackdone alimuuliza Roberto ambaye lengo lake lilishatimia hivyo kumkatia simu Mackdone kabla ya kujibiwa.


"Kwa kweli wewe ni kichomi Roberto ndiyo nini kufanya hivyo?"

Jackline alimuuliza Roberto.


"Kaingia mkenge mwenyewe hebu angalia hapo chini ya kitufe cha kijani."

Roberto alimwambia Jackline kuangalia hiyo sehemu na baada ya kuangalia alishangaa kuona umbali kati ya mpokeaji simu na mpiga simu ni kilometa mia sita huku mji aliopo Mackdone uko ndani ya Botswana.


" Kwa hiyo kajiona kafichama mwenyewe maskini Mackdone umekwisha sasa."

Jackline aliongea na kutaka kutoka lakini Roberto alimzuia.


"Hatuwezi kufanya chochote kwa sasa mpaka umewatoa wanao nchini kisha tutaianza kazi yetu rasmi."

Jackline hakuwa na chaguo zaidi ya kukubali huku Jasmine akimuunga mkono Roberto.

Wakiwa wanajiandaa kutoka humo chumbani kwa Roberto mara simu ya Jackline iliita.


NI NANI ALIYEPIGA SIMU?





"Hebu niambie Vivian anaendeleaje mgonjwa?"

Mackdone alimpigia simu Vivian kujua hali ya Bi Elizabeth.


"Bosi kiukweli bado maana hata fahamu bado hazijamrejea."

Vivy alimjibu


"Ok vizuri, kumbe ngoja niongee na Daktari kujua ikoje ili ikiwezekana nimbadilishie Hospitali. Maana kuna kazi za kufanya mnatakiwa kuzianza mara moja."

Mackdone alimwambia Vivy na kukata simu kisha akampigia Daktari Leon ambaye ndiye anamhudumia Bi Elizabeth ndani ya Hospital ya Victoria.


" Kaka Mackdone."

Daktari Leon alianza mara baada ya kupokea simu.


" Leon kwa kipindi hiki bila shaka utakuwa unajua maana ya simu zangu."

Mackdone alimjibu Daktari Leon.


"Najua, kifupi mgonjwa wako bado yuko kwenye koma tatizo lake ni kubwa sana kaka."

Daktari Leon alimjulisha Mackdone ambaye hakuzitegemea taarifa hizi hata kidogo kwa kuwa Hospitali hii anaiamini sana.


"Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa hawezi kuinuka tena mgonjwa wangu?"

Mackdone alimuuliza.


"Kuinuka anaweza iwapo tu utamsafirisha mpaka 'St. Matthew Hospital' iliyoko Australia."


"Australia tena?"

Mackdone alimuuliza kwa mshangao baada ya kutajiwa nchi hiyo.


"Ndiyo hiyo ndiyo Hospitali pekee ambayo itamshughulikia Bi Elizabeth kwa tatizo lake kichwa kaka Mackdone."

Maelezo ya Daktari yalimchanganya kidogo Mackdone lakini mwisho wa siku alimuelewa na kukubaliana naye hivyo alikata simu na kisha aliingia mtandaoni kuiangalia hiyo Hospitali ya St. Matthew na huduma zitolewazo hapo.


" Waoo inaweza kumsaidia Bi Elizabeth hii Hospitali ngoja nifanye maandalizi."

Alijisemea huku akiondoka mtandaoni na kuinuka kuyafuata maji baridi kwenye friji iliyo mle ndani ya chumba chake. Baada ya tukio la Clayton Hotel, Mackdone alikimbilia Gaborone nchini Botswana katika Hoteli ya Apple.

Anayafakamia maji kama vile anafukuzwa na baada ya kumaliza alitoka nje ili kuanza kushughulikia safari ya Bi Elizabeth na alipofika nje aliona watu wakiwa wamemzunguka muuza magazeti aliyekuwa anapita nje ya Hotel hiyo, hakuona sababu ya kuangalia kwa mbali akaona naye asogee aone kuna taarifa gani mpya kiasi cha kuwakusanya watu. Alipofika alikutana na maandishi makubwa ya rangi nyeusi yaliyosomeka 'AUAWA KIKATILI HOTELINI' maneno hayo yalimshtua kidogo ikabidi asogee karibu ili aiangalie picha ya marehemu ili aone kama ni yule anayemfahamu.


"Buuu Shiiiit....... Huyu si yule mshenzi wa Clayton Hotel?"

Hakuona sababu ya kuendelea kuwepo eneo lile maana yaliyokuwa yakiongelewa pale hakuyategemea hata kidogo.


"Masikini dada Grace kaondoka na ndoto zake hivi hivi?"

Kijana mmoja aliongea akiwa kalishikilia gazeti lile, hapo Mackdone hakuona sababu ya kusubiri akamfuata yule kijana na kumuuliza.


"Vipi unamfahamu huyu dada?"

Mackdone aliuliza.


"Sana, huyu dada ni mwenyeji wa hapa Gaborone alikuwa ni mama lishe maarufu hapa mjini na miaka mitatu iliyopita alishiriki mashindano ya 'Miss Matata' yaliyolenga kumpata mrembo mwenye kipaji zaidi ya kimoja yakiandaliwa na Clayton Hotels zilizopo hapa na kule Namibia na yeye kuibuka mshindi. Clayton walimuajiri pamoja na kumpa zawadi zake na kumhamishia Namibia, da inauma sana."

Kijana huyo alihitimisha kwa kuanza kutokwa na machozi kitu ambacho kilimfanya Mackdone kutosubiri zaidi aliondoka zake huku akitoa simu yake na kupiga sehemu.


" Njoo hapa Gaborone natakiwa kuondoka mara na sitakiwi kupanda usafiri wa umma."

Baada ya kuagiza alikata simu na kuangalia huku na kule kisha akaingia kwenye Bajaj.


***


"Habari my wifi wa mie."

Jackline alianza kwa kumsalimu baada ya kupokea simu ya Titiana.


"Ninalo basi wifi yangu? Vipi mnaendeleaje huko na pilika?"

Titiana alimjibu.


"Mungu anasaidia tunaendelea vizuri wifi yangu. Ndiyo ukafanya nini kwa kaka yangu?"

Jackline aliona amuanzie kabla hajasahau.


"Nimefanya nini mimi wifi?"


"Kwamba hujui ulichokifanya?"

Jackline alimuuliza.


"Wifi unanilaumu mimi badala ya Roberto aliyenitoroka kweli?"

Titiana alimuuliza.


"Kwa hiyo umefurahi kuona mpenzi wako hana furaha siyo? Halafu akikubwaga na kuanza mahusiano mapya uanze kulialia hapa."

Jackline hakutaka kumuacha alimpa za uso.


"Na ndiyo maana nikakupigia simu wifi Jackline ili unisaidie kuniombea msamaha kwake."


"Sitaki mimi kama ulivyolianzisha limalize mwenyewe wifi ninyi ni wapenzi sitaki niingilie mapema."

Jackline alikataa na kumtaka ampigie Roberto moja kwa moja.


"Basi sawa nitampigia baadaye kidogo."

Titiana alihitimisha na kukata simu baada ya kuona njia aliyotaka kuitumia imekuwa ngumu huku Jackline akimpa ishara Roberto ya ushindi.


"Kashindwa kujizuia kapiga, akikupigia hiyo baadaye mkazie kwanza kisha mlegezee kama unaingia kama unatoka hivi au unasemaje?"

Jackline alimwambia Roberto.


"Hebu acheni kulishana ujinga bwana mtu mpaka kapiga simu maana yake kajutia na ukizingatia kosa lilikuwa kwetu."

Jasmine alipingana na kauli ya Jackline kitu ambacho kilimfanya Roberto kutabasamu kidogo kisha akawatoa wasiwasi.


"Msihofu nitamalizana naye tu bila shaka yoyote."

Roberto akiwa anawajibu mara mlango uligongwa na baada Jasmine kwenda kuufungua alikuwa ni Dorice kutoka City Aluminum.


"Karibu ndani Dorice."


"Nashukuru unafikiri niingie ndani naona mniruhusu nianze kazi yangu maana jana nilifika nikaambiwa mna dharura."

Dorice alimjibu Jasmine ambaye alimwita Jackline akutane na mgeni wake, lakini wakati huo huo Daktari Abbas naye aliwasili.


"Na Bosi naona ndiyo anaingia."

Dorice aliongea akiwa anaelekea kwenye kazi akiwa na Jackline.


"Si unajua shughuli zake tena."

Jackline alimjibu.


"Ni kweli kabisa dada."

Dorice aliongeza huku akipiga magoti kuanza kazi.


"Pole fundi."

Daktari Abbas akifika.


"Ndiyo nafika hivi kama dakika sifuri tumepishana."


"Ohh kumbe wewe endelea na kazi yake ngoja tukuache."

Daktari Abbas alimjibu huku akimshika mkono Jackline kuelekea ndani.


"Pole na majukumu mume wangu."

Jackline alimwambia mume wake.


"Nashukuru mke wangu japo zimepamba moto safari maana si kwa ajali zile kila siku wagonjwa wa ajali za barabarani tu lakini nikaona nije mara moja baada ya kupata email kutoka kwa wale jamaa wa worldeducationlink.com kuwa nafasi imepatikana kutoka kwenye moja ya shule zinazofanya vizuri kwa sasa."


"Shule gani hiyo?"

Jackline alimuuliza akimvua koti mume wake.


"Nimeambiwa inaitwa Australia Montessori School (AMS) na kama jina lilivyo inapatikana huko huko Australia sikuishia hapo ilibidi niigoogle kuijua vizuri, aaah ni bonge la shule mke wangu."

Daktari Abbas aliisifia hiyo shule.


"Kwa hiyo tunakwenda kutengana na mapacha?"

Jasmine aliongea huku akimtazama Jackline ambaye humwambii kitu kwa watoto wake Natalie na Nathan.


"Kwa usalama wao niko tayari kuwapeleka kokote kule duniani kikubwa wawe hai tu basi."

Jackline alimjibu Jasmine huku akifuta machozi kwa pembe ya kanga aliyokuwa kajifunga.


"Kumbe tujiandaeni tuelekee shuleni kwao tukawaone bwana au mnasemaje?"

Jasmine aliwauliza wenzake.


"Ni kweli hiyo shule ya Australia Montessori School (AMS) ni shule kubwa sana aisee nilikuwa naipitia hapa imepata tuzo mbalimbali za kimataifa kwa taaluma bora na pia inapatikana ndani ya mji Canberra ambao ni mji Mkuu wa nchi ya Australia. Hakika wajomba wangu watafaidi sana aise."

Roberto aliendelea kuichimba hii shule wanayotakiwa kupelekwa Natalie na Nathan.


" Mungu asaidie wafike salama tu bila kupatwa na chochote."

Daktari Abbas aliongea hayo akiiangalia saa yake.

Mara simu ya Jackline iliita na alipoangalia mpigaji ni nani alibaini ni mdogo wake Shamimu ambaye ni mtoto wa baba mdogo Mzee Fikirini akaipokea.


" Shikamoo dada yangu."


"Marahaba mdogo wangu habari za siku, vipi kitabu?"

Jackline alimwitikia na kutaka kujua anaendeleaje kimasomo.


"Nashukuru Mungu naendelea vizuri na hivi kuanzia mwezi ujao tunaanza paper' la mwisho."

Shamimu alimjulisha dada yake kinachoendelea chuoni kwake. Shamimu alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Mount Gregory cha nchini Urusi akichukua degree ya Masoko na Utawala huku dada yake Jackline akiwa ndiye anayemlipia kila kitu. Pamoja na kuwa walikuwa ni watoto wa baba yake mdogo pamoja na kaka yake Athuman huku yeye Jackline akiwa ni mtoto pekee wa mzee Joachim hakuwatelekeza alikuwa nao bega kwa bega huku Athuman akisimamia Kampuni ya Usafiri pale jijini Mbeya inayojumuisha Bajaj na Daladala.


"Mdogo wangu hongera sana na ninaomba Mungu asikuache mpaka mwisho ufikie malengo yako."

Jackline alimpongeza mdogo wake.


"Nashukuru sana dada vipi wanangu wanaendeleaje hapo?"

Shamimu alimuuliza.


"Wanaendelea vizuri kabisa na hivi muda wowote wanapanda pipa kuelekea nchini Australia kwa masomo tumepata shule kule ambayo inatoa taaluma na malezi bora kabisa."

Jackline alimjibu.


"Jamani kwa hiyo nitakaporudi sitaweza kukutana nao?"

Shamimu alimuuliza dada yake.

0 comments:

Post a Comment

Blog