Search This Blog

Tuesday, 20 December 2022

KWA AJILI YENU WANANGU, NITAMWAGA DAMU - 3

  




Simulizi: Kwa Ajili Yenu Wanangu, Nitamwaga Damu 

Sehemu Ya Tatu (3)



"Hofu yako ya nini ilhali hela ipo tutakwenda kuwatembelea huko huko."

Jasmine alimjibu baada ya kupora simu kwa Jackline ili amsalimu Shamimu.


"Haaa dada Jasmine nawe uko hapo? Shikamoo!"


"Marahaba mdogo wangu, niko hapa ninachokuomba komaa ufikie ndoto zako ili siku moja ukawakomboe Wanalupa."


"Asante kwa maombi yako dada yangu."

Shamimu alishukuru. Baada ya mazungumzo ya hapa na pale waliachana na Shamimu kisha kumsimulia Daktari Abbas kile ambacho kilitokea kule Clayton Hotel usiku uliopita.


"Humu ndani wenyewe."

Dorice aliita pale mlangoni.


"Aaah fundi pole na kazi tulikutelekeza peke yako."

Jackline alimkaribisha.


"Wala usijali dada yangu kazi nimeshaimaliza naona mimi niwakimbie."

Dorice aliwaaga wenyeji wake baada ya kumaliza kazi ya kupachika kioo kwenye dirisha ambalo lilipata dhoruba kutoka kwa Roberto.


"Nakushukuru sana dada Dorice kwa kazi yako naona ubora umerejea na pia kama hutojali nitaomba nikutoe."

Daktari Abbas alimshukuru Dorice kisha akampa ofa ya kumtoa.


"Wala usijali nimeshawataarifu ofisini na bila shaka inawezekana gari liko nje linanisubiri."

Hivyo waliagana na kuachana naye kisha kurejea kwenye mazungumzo ya kilichokuwa kimewatokea na muda huo Roberto alikuwa akiifuatilia namba ya Mackdone kwenye Brain Hub' yake kutaka kujua nini anakifanya, alipatwa na mshangao kidogo.


" Hee njooni muone hapa anachopanga kukifanya panya wa kienyeji huyu."

Ilibidi awaite waje wajionee wenyewe kile alichokiona.


"Saa moja na nusu lililopita mmiliki wa namba +267-****01 aliwasiliana na mmiliki wa namba +27-****99 na +27-****76"

Baada ya kusoma ujumbe uliorekodi muda na namba alizofanya nazo mawasiliano ilibidi wazifuatilie na kugundua yeye Mackdone alikuwa Botswana huku aliowasiliana nao wakiwa Afrika ya Kusini.


"Si mmeona hapa moja kwa moja hawa aliokuwa akiwasiliana nao inawezekana ndio wako na Bi Elizabeth hapa kuna uwezekano wa mimi kuelekea huko huko Afrika ya Kusini kuujua undani wa huyu mtu aitwaye Mackdone."

Roberto aliongea akiifunga laptop yake huku akimuangalia Daktari Abbas ambaye alikuwa akiongea jambo.


" Vipi usalama wako au nikupe na kijana wangu Mahmoud? "

Daktari Abbas aliuliza.


" Hapana mimi naona Mahmoud ataongozana na wewe unapowapeleka watoto Australia huku dada zangu wakisalia hapa na Botswana kuhakikisha hakuna kinachoharibika."

Roberto alimjibu na kutoa ushauri wake juu shughuli iliyo mbele yao ambao kila mmoja aliukubali. Hivyo hawakuwa na la kusubiri zaidi ya kuelekea shuleni kuwafuata wakina Natalie kwa kuwa taarifa zote za uhamisho zilikuwa zimekamilika.


JE KUNA NINI KINAKUJA MBELE?




Maandalizi yalianza kwenye familia ya Daktari Abbas ambapo mgawanyo wa majukumu ulipangwa ikiwa ni pamoja na watoto kufuatwa kule shuleni huku wengine wakianza maandalizi ya safari katika hili Roberto alikuwa anafuatilia kwa ukaribu zaidi nyendo zote za Mackdone pale Botswana. Hofu na mashaka iliitawala familia hii hasa Daktari Abbas ambaye hakuwahi kukutana na misukosuko kama zaidi ya kuiona tu na zaidi kujitoa kwa kusaidia tu lakini haikuwa moja kwa moja yeye kama yeye kuingia mzima mzima na kuacha shughuli zake ambazo alikuwa akizifanya mara moja moja. Kuna alimuhofia zaidi mke wake Jackline ambaye siku zote hakuwa tayari kuona haki yake ikiporwa kirahisi na hilo alishindwa kulizuia kabisa.


"Mume wangu sisi ngoja tuelekee shuleni kuwachukua watoto nafikiri wewe na Roberto mtakuwa na la kufanya."

Jackline alimtaarifu mume wake juu ya wao kuelekea shuleni St. Petro Schools kuwachukua wakina Nathan.


"Haina shida ngoja sisi tukakutane na Mahmoud tujue cha kufanya maana mwenzenu kichwa kinaniuma balaa."

Daktari Abbas alijibu.


"Basi sawa, Jasmine tuondoke zetu ili tuwahi kurudi si unajua tena."

Jackline alimwambia Jasmine na kuondoka zao.

Wakiwa njiani kuelekea St. Petro Schools Jackline aliona apitie kituo cha mafuta ili kuongeza kwenye gari baada ya kuona mshale unaelekea sehemu asiyoipenda hivyo waliingia pale kituoni na kushuka garini na kwenda kumuelekeza mhudumu kiasi anachokihitaji lakini wakati huo huo Jasmine alikuwa bize kuiangalia 'site mirror' ya upande wake haikujulikana alikuwa anaangalia nini. Jackline baada ya kufanya malipo alirudi kwenye gari akafunga mkanda na kuondoka zake lakini Jasmine yeye macho yalikuwa kwenye 'site mirror' ambako ni kama kuna kitu alikuwa anakifuatilia pasipo kumjulisha Jackline lakini Jackline ni kama alishtukia jambo lile.


"Jasmine mbona hubandui macho kwenye 'site mirror' kulikoni?"

Jackline aliona amuulize tu ili kujua.


"We twende nitakwambia tu."

Jasmine alimjibu kifupi huku macho akiwa kayang'ang'aniza pale pale na baada ya mwendo kidogo alimtaka asimamishe gari kwanza na Jackline hakuwa na pingamizi akasimama. Baada ya kusimama Jasmine alishuka na kwenda mbele ya gari na kuinama kama vile kuna kitu alikuwa anakikagua hivi kisha aliinuka na kutoa simu yake akawa kama vile anataka kupiga hivi mara kuna gari iliwapita kwa mwendo wa kasi sana na kumfanya Jasmine kutabasamu akarudi kwenye gari na kumtaka Jackline asiende mwendo mkali.


"Kuna nini?"

Jackline alimuuliza.


"Gari lililotupita muda si mrefu limekuwa nyuma yetu toka tunaingia barabara kuu hivyo nina hofu nalo."


"Kwamba tuko kwenye anga za adui?"

Jackline alimuuliza tena Jasmine.


"Nahisi hivyo lakini jambo muhimu ni kuingia sehemu tulipaki gari na kuchukua Taxi ili kuwapoteza maboya."

Jackline alicheka sana baada ya kupewa mbinu hiyo aliyoitoa Jasmine.


"Wewe hilo likichwa ni hatari aisee."

Jackline alimtania Jasmine huku akishuka kwenye gari mara baada ya kuipaki kando ya barabara. Waliposhuka wote walitoa triangles na kuziweka mbele na nyuma kisha wakasimamisha Taxi iliyokuwa ikipita na kuondoka zao.


"Lazima wafanye kazi ya kulilinda gari pale wakati sisi tukikamilisha zoezi letu."

Jasmine alimwambia Jackline.


"Wanatakiwa wafanye kazi ziada kutufuatilia sisi siyo wanaingia kichwa kichwa tu."

Jackline aliunga mkono hoja ile wakati huo wakikaribia viwanja vya shule ya St. Petro Schools kama walijua vile lile gari waliliona limesimama mita zaidi ya mia mbili kutoka kwenye njia ya kuchepuka hivyo kuwafanya wakina Jackline kubonyezana. Walimtaka dereva Taxi awasubiri kisha wao wakashuka na kuingia ndani ya shule huko walifuata taratibu zote kama zilivyoelekezwa na mamlaka husika kisha wakawa wanatoka,lakini wakiwa koridoni kuliendea lango kuu la kutokea uwanjani kabla ya kulifikia geti la nje kupitia madirisha ya koridoni waliweza kuwaona watu zaidi ya wanne pamoja na yule dereva Taxi wakiwa wanaoneshana kwa vidole mle ndani.


"Subiri kwanza ina maana ile haikuwa Taxi?"

Jackline alimuuliza mwenzake.


"Kivipi Jackline?"


"Hebu cheki kule nje."

Jackline alimuonesha Jasmine kupitia dirishani kuona kilichokuwa kule nje.


"Mackdone si mtu wa kawaida, moja kwa moja hawa ni watu wake."

Jasmine aliongea baada ya kuwaona na muda huu walikuwa wanakuja ndani hivyo haraka sana ikabidi warudi ndani kwenye ofisi za shule ile kutafuta msaada wa kujificha kutoka kwa wenyeji.


"Mama kuna nini tena?"

Nathan aliuliza baada ya kuona wakishikwa mikono na kurudi ndani huku wakikimbia.


"Acha maswali mwanangu wewe kimbia kwanza mengine utayajua baadaye."

Jackline alimjibu.


"Kama mnawahofia watu kuna mlango wa dharura huku nyuma."

Natalie aliwaambia huku akiwaonesha huo uchochoro wa kuelekea kwenye lango hilo la dharura. Wakati huo wakikimbia hivyo wanafunzi wengine walikuwa wakiwashangaa tu wakiwa hawajui nini kinaendelea. Kupitia ule mlango walifanikiwa kutoka na kukimbilia kwenye matenki ya kuhifadhia maji pale shuleni, kama vile walikuwa wenyeji waliufuata ukuta ili wapande juu.


"Tumechemka aisee ukuta huu ni mrefu sana."

Jasmine aliongea baada ya kuuangalia urefu wa ule ukuta na kumkatisha tamaa kabisa.


"Ni kweli kabisa lakini lakini bado tunatakiwa kuangalia namna nyingine."

Jackline aliongea huku akiwaacha na kuelekea upande mwingine huku watoto wakiwa migongoni muda huo kwani moja kwa moja hali haikuwa shwari kwani kutokana na wanafunzi kuwashangaa walipokuwa wakikimbia walijua wataambiwa tu walikoingia.


" Hapa panafaa sasa."

Jackline alijisemea baada ya kufanikiwa kuikuta ngazi ndogo iliyokuwa imeegeshwa kwenye tenki mojawapo na kuiweka kwenye ukuta tayari kwa kupanda.


"Huku haraka wewe."

Jackline alimwambia Jasmine huku yeye akiwa kaanza kupanda na baada ya kufika juu alimsubiri kwanza Jasmine naye afike juu kisha waivute ile ngazi na kuihamishia upande wa pili. Walifanikiwa kuihamishia upande wa pili kisha walishuka na baada ya kufika chini tu waliiangusha chini kisha wao wakakimbia. Na kweli kama waliota hivi kwani dakika chache baada ya kuondoka eneo lile wale watu walifika eneo lile bastola mikononi na kuishia kushika viuno tu kutokana na ukuta ulivyokuwa mrefu. Ilibidi warudi haraka kule nje waweze kuwawahi kabla hawajalifikia gari lao lakini wenzao hesabu zilikuwa nyingine kabisa kwani wao walichukua Bajaj na kuishia zao.


"Siamini macho yangu kama tumesalimika kutoka kwa panya wale."

Jasmine aliongea huku akifuta jasho usoni kwa kutumia sweta lake.


"Yaani wewe acha tu maana hapa bega langu halina kazi huku Natalie huku mbegi daa, hivi wametuoteaje hawa?"

Jackline alimuuliza Jasmine kama vile anajua chochote wakati walikuwa pamoja.


"Endesha Bajaj acha umbea unasikiliza nini wewe?"

Jackline alimwambia dereva Bajaj aliyekuwa akiendesha huku akiwaangalia wakina Jackline.


"Samahani dada zangu si kosa langu ni masikio tu haya lakini mbona sifahamu chochote?"

Alijitetea dereva Bajaj huyo ambaye walikwenda naye mpaka mtaa mmoja hivi ambao ni maarufu kwa pombe za kienyeji huko walimlipa chake dereva huyo na kuachana naye na baada ya kutembea kidogo ndipo walichukua taxi ambayo iliwafikisha nyumbani kwao salama lakini miili ikiwa haina kazi kwani lilikuwa ni tukio la bila kutarajia.

Walikutana na wakina Roberto nao wakiwa kwenye kikao cha mkakati kati yao na Thomas pamoja na yule kijana ambaye ni dalali wa nyumba, mashamba na viwanja.


"Waooo wanangu...."

Daktari Abbas aliinuka na kuwalaki watoto wake.


"Waooo baba wenzako leo ilikuwa tufe."

Natalie hakutaka kusubiri akaona amwambie kilichowakuta.


"Ni kweli shemeji?"

Daktari Abbas alimuuliza Jasmine.


"Yaani acha tu shemeji, wewe angalia nje hakuna gari tumelitelekeza huko njiani."

Jasmine alimjibu.


"Mmelitelekeza njiani gari? Haiwezekani hata kidogo ngoja."

Roberto aliuliza na kisha kuinuka na kuelekea chumbani kwake na baada ya muda alirejea na kuwataka wakina Mahmoud wamfuate hivyo hakukuwa na mjadala walitoka na kuchukua gari la Daktari Abbas ambalo dakika kadhaa zilizopita liliendeshwa na Roberto hivyo funguo alikuwa nazo mkononi.


"Dada Jackline ni sehemu gani huyo?"

Roberto alimuuliza.


"Eneo silifahamu jina lakini ni barabarani tu tumelipaki mtaliona au tuongozane?"

Jackline alishindwa kulitambua eneo hivyo akataka kuongozana nao.


JE NINI KITAENDELEA?


USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA YA KIGONGO HIKI.




Kikosi cha watu wanne ambao ni Roberto, Mahmoud, Thomas na dalali ambaye jina lake halisi ni Nolan waliekea eneo ambalo gari lilitelekezwa na wakina Jackline baada ya kuhisi walikuwa wanafuatiliwa nyuma na watu ambao hawakuwa wazuri kwao na hivyo kuamua kuingia kwenye taxi ambayo walijua wamewaweza wale watu kumbe hiyo taxi nayo ilikuwa ni ya wale wale.


"Jamani naomba niulize kidogo hivi hao watu kwanini waliwafukuzia wakina Jasmine?"

Nolan aliwauliza wenzake ambao aliamini wanaweza kumuondolea utata huo.


"Ndiyo kwanza umeianza hii kazi bwana Nolan ni mapema sana kujua hili kwani ni stori ndefu sana ambayo inaweza kuchukua hata mwezi mzima kukusimulia hivyo cha kufanya ni kutulia tu kwani kadri tunavyoendelea na majukumu wewe mwenyewe utakuwa unapata majibu ya maswali yako."

Roberto alimjibu Nolan akiwa nyuma ya usukani.


" Punguza mwendo Robbie nadhani gari ndiyo lile pale mbele kama sijakosea."

Mahmoud alimwambia Roberto kupunguza mwendo baada ya kuliona gari kwa mbele. Baada ya kujiridhisha kuwa ni lenyewe waliona wasifike lile eneo kwani hawajui maadui zao wamechukua hatua gani juu yao hivyo waliona wasimame huku waliko na kisha kwenda lile eneo kupitia vichochoroni na wengine wataendelea na gari na kulipita kisha kwenda kusimama mbele kabisa ya gari hilo ambapo walikuwa ni Roberto na Nolan huku Mahmoud akishuka na Thomas.


"Kuwa makini mdogo wangu usiende kichwa kichwa ni hatari huku unaweza usirudi nyumbani na roho yako ohhhooo."

Mahmoud alimtahadharisha Thomas ambaye alikuwa anajiendea tu bila tahadhari yoyote.


"Niambiage kaka haya mambo wapi na wapi mimi mtoto wa kitaa?"

Thomas alijitetea.


"Nimekuelewa Thomas songa mbele kupitia njia hii na mimi ngoja nipitie huku tukutane mbele kwa usalama wetu."

Mahmoud alimwelekeza Thomas.


"Sawa mkuu."

Thomas alimjibu.

Walisonga mbele na kisha kukutana na wakina Roberto ambao nao walipita njia nyingine na kukutana kisha kuanza kulisogelea gari kwa tahadhari kubwa visu na bastola zikiwa mikononi. Walitokwa macho mara baada ya kulifikia gari ambalo lilikuwa limechakazwa kwa risasi kwenye tairi pamoja vioo.


"Wamefanya yao tayari."

Roberto aliongea akiwa amelifikia gari na kuchungulia ndani ya gari na kugundua limeharibiwa mfumo mzima hivyo haliwezi kutembea zaidi ya kubebwa.


"Hatuna la kufanya watu wangu zaidi kuondoka eneo hili kwani kilichotuleta hakina maana kwetu tena kama mnavyoona."

Mahmoud aliongeza kwa kuwaambia wenzake ambapo walikubaliana na kuondoka zao.


"Lakini hebu ngoja kwanza."

Roberto aliwaambia wasubiri huku akitoa simu mfukoni ambayo alipiga.


"Vipi Roberto kwema?"

Jackline aliuliza baada ya kupokea.


"Tumefanikiwa kulikuta gari lakini halitamaniki wamelifanyia unyama hatari tairi zote nne hazina upepo huku vioo vimemwagika chini."

Alimweleza.


"Wanaharamu hao yaani gari langu waliligeuza sehemu ya range? Haina shida leo wameshinda wao kwa hiyo tunafanyaje hapo?"

Jackline aliishia kuuliza wanafanyaje ili kulinusuru.


"Mwambie shemeji aongee na watu wa Gereji waje walichukue na kulifanyia kazi"


"Basi sawa Roberto lakini poleni kwa usumbufu."


"Wala usijali dada."

Roberto alimjibu na kukata simu kisha akawaambia wanaweza kuondoka lakini wakati Mahmoud ameinama kufunga vizuri kamba za raba yake kuna mtu alimuona akikimbia kutoka eneo la karibu na pale walipokuwa wao.


"Nifuateni."

Aliongea hayo na kutimua mbio hivyo hakukuwa na maswali zaidi ya kumfuata alikokuwa anakwenda. Walikimbia kwenye vichochoro vya eneo lile kuhakikisha wanamdhibiti mtu yule.


"Piteni kwenye uchochoro huo kuna mtu alikuwa anatuvizia aliponiona tu akatimua mbio."

Mahmoud akawaambia wenzake hivyo wakatawanyika kumzungukia na kama bahati walipofika eneo la wazi waliweza kumuona akitimua mbio na kuingia kwenye jengo moja ambalo lilikuwa halijamalizika vizuri.


" Kaingia pale kwenye jengo lile hivyo tunazama ndani kupitia madirishani lakini kuweni makini."

Roberto aliwataarifu wenzake hivyo haraka sana walimzungukia pande zote kama vile alijua kwani wakati wenzake wamepita pande zao kuingia ndani yeye Roberto alizunguka nyuma kabisa na kubana chini ya madirisha bastola mkononi. Mara yule kijana aliruka dirisha ili atokomee porini lakini bahati haikuwa kwake alipotua tu chini alikutana na risasi ya mguu.


"Mamaaaaaa mguu wangu...."

Alipiga kelele huku akienda chini. Roberto hakumsikiliza makelele yake zaidi alimsogelea karibu na kuchuchumaa.


"Unaitwa nani? Umetoka wapi? Kwanini ulikuwa unatukimbia?"

Roberto alimmiminia maswali mfululizo kijana huyo.


"Naomba unisamehe kaka nilikuwa siwakimbii ninyi....."

Kabla hajajibu vizuri alikutana na teke la mgongoni kutoka kwa Mahmoud ambalo lilimrambisha vumbi.


"Hii sura si ngeni hata kidogo, hebu niambie unaitwa nani au nikuulize unanikumbuka?"

Mahmoud alimvamia na maswali.


"Mimi sikukumbuki kaka labda umenifananisha."

Alimjibu huku akijivuta nyuma kidogo, lakini Mahmoud akajua anamchezea akamfuata na kumkanyaga sehemu aliyopigwa risasi na Roberto.


"Ngoja niongee jamani mnaniumiza."

Alijitetea.


"Ongea haraka kabla hatujalibadili jina lako."

Roberto alimsisitiza huku akiwa kamuwekea bastola kichwani kuonesha hawakuwa na mzaha naye hata kidogo.


"Mimi naitwa Hamza ni mfanyabiashara wa matunda."

Alijitambulisha na kumfanya Mahmoud kucheka kinafiki.


"Kwa hiyo umeachana na biashara yako na kuamua kumtumikia Bi Elizabeth siyo?"

Alimuuliza.


"Hapana kaka siyo hivyo, siku kadhaa nyuma nilipokea ujumbe wa vitisho kutoka kwa mtu nisiyemfahamu akinitaka kuzifanyia kazi oda zake tofauti na hapo ataniua."

Hamza alijitetea.


"Una uhakika unachokisema?"

Mahmoud alimuuliza.


"Ndiyo kaka na hivi jana alinitumia ujumbe akinitaka kukutana na vijana ambao anataka nifanye nao kazi lakini sikujua ni kazi gani kumbe ilikuwa ni ya kuwateka watoto wa Daktari Abbas."

Maelezo ya Hamza yaliwachanganya wakina Roberto kwani hesabu za kuwatoa watoto wale pale shuleni ilifanywa ndani na hakukuwa na mtu mwingine zaidi yao wenyewe.


" Wewe hebu sema vizuri taarifa za watoto kufuatwa mlizitoa wapi?"

Roberto alimuuliza.


" Tulizipata kutoka nyumbani kwa Daktari Abbas."

Hamza alimjibu.


"Kivipi?"

Mahmoud alimuuliza huku akiwa kambana shingo.


"Tulitega kifaa cha kunasa mawimbi ya sauti mlangoni kwake."

Hamza aliendelea kuwashangaza.


"Ni nani ambaye mlimtuma kukiweka hicho kunasa mawimbi ya sauti?"

Roberto alipandwa na hasira kwani alijua mambo yao mengi yamenaswa na hawa wakina Hamza hivyo alimshindilia ngumi nzito ya shavuni.


"Mackdone ni mtu hat...hata..riii sana na hu...hu.wa hawaachi salama watu wanao.....wanaomuingilia kwenye mapito yake."

Aliongea kwa tabu kidogo baada ya kupokea ngumi ya shavu kutoka kwa Roberto.


"Hatuhitaji ngonjera zako hapa, hujasema ni nani alifika kuweka hicho kifaa?"

Roberto alirudia kumuuliza swali lile lile.


"Tulifika pale siku moja na kumkuta mrembo mmoja akitoka mle ndani tukamsimamisha na kumuuliza iwapo ni mwenyeji mle ndani akatujibu kuwa yeye ni fundi na amefika kuchukua vipimo vya dirisha, tulifurahi sana tukamuomba atufanyie kazi yetu kwa malipo mazuri ya shilingi milioni sita. Mwanzo alikataa lakini baada ya kumpa kile kifaa na kumuelekeza kitu cha kufanya akakubali kwani aliona ni kazi ndogo yaani kukipachika tu kuendelea na mishe zake."

Roberto na Mahmoud walianza kumshambulia Hamza kwa mateke ya tumbo na kichwa mpaka pale simu yake ilipoita mfukoni kwake, ndipo Mahmoud alipoichomoa na kuiweka sauti ya juu na kumkabidhi aongee na mke wake ambaye ndiye aliyepiga.


" Naam mke wangu."

Aliongea baada ya kupokea.


"Hivi mume wangu mbona sikuelewi lakini? Ni siku ya ngapi haupo nyumbani?"

Maswali ya mke wake yalimfanya ababaike kidogo na kuwaangalia wakina Mahmoud.


"Unashangaa nini hapa mjibu mkeo huko."

Thomas alimwambia huku akiwaangalia wakina Roberto kama watamfokea.


"Mke wangu nitarudi hivi karibuni, matunda ya safari hii yalikuwa ya ushindani sana na ndiyo maana nimechukua muda mrefu."

Hamza alidanganya.


"Kwanini hukuniambia kama siku zote na mbaya zaidi ulinizimia na simu kabisa, mume wangu jidai mjuaji lakini jua hakuna siri chini ya jua."

Mke wake alimwambia na kumkatia simu akabaki ametoa macho kwa alichoambiwa.


"Brother kumbe ndiyo kazi zako hizi halafu unatuambia kuwa ulipokea oda ya vitisho siyo?"

Roberto alimuuliza huku akimshindilia risasi nyingine pale pale kwenye jeraha.


"Naombeni mnisamehe ndugu zangu watu wa Bi Elizabeth ndiyo walionishawishi kuingia kwenye kazi hii ambayo hata mke wangu hajui kama naifanya."

Hamza aliendelea kujitetea, lakini walichokifanya walimchukua na kuondoka naye kuelekea kwa Daktari Abbas ili akahojiwe na timu nzima.


" Inuka hapo haraka."

Mahmoud alimtaka asimame japo alishindwa kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia kutoka kwenye jeraha aliloshindiliwa risasi mbili hapo hapo.


"Naombeni msiniue jamani nilishawishiwa na hela tu kama mnavyojua maisha yetu Waafrika yalivyo magumu."

Hamza aliendelea kuomba msamaha kwa wakina Mahmoud.


"Inuka haraka na hakuna wa kukusaidia utatembea tu mpaka kwenye gari, unakopelekwa ni wapi siyo jukumu lako kujua."

Roberto alisisitiza huku akimnyanyua juu.

Walimuinua na kuanza kumburuza kuelekea kwenye gari lakini Roberto aliichukua simu ya Hamza na kumtumia ujumbe mfupi Mackdone baada ya kuikuta namba yake ambayo aliihifadhi kwa jina la 'Don'


" BOSS NIMEPATWA NA TATIZO."

Kisha alimtumia na baada ya muda mfupi alipiga simu ambayo hakuipokea zaidi ya kuiangalia tu na ilipokata akamtumia ujumbe tena.


"NAOMBA MSAADA WAKO, WAMENIKAMATA VIJANA NISIOWAFAHAMU."

Roberto alimtumia tena ujumbe huo kisha akaizima simu na kuiweka mfukoni. Safari iliendelea na hatimaye walifika garini wakapanda na kuondoka kuelekea nyumbani kwa Jackline.


"BABY USINIFANYIE HIVYO KWANINI LAKINI? INA MAANA HAKUNA UGOMVI KWENYE MAHUSIANO KWELI?"

Ulikuwa ni ujumbe ambao ulitumwa na mpenzi wake Titiana ambaye siku kadhaa nyuma walikwaruzana na kupelekea kutowasiliana kwa muda wa siku kadhaa.


"NIPE SIKU KAMA TATU HIVI NITAKUTAFUTA KWA SASA NIACHE KWANZA."

Alimjibu kwa kifupi hakutaka maelezo marefu. Baada ya muda wa dakika kadhaa alijibiwa tena.


"SAWA KIPENZI LAKINI ELEWA ZILIKUWA HASIRA TU MIMI BADO NAKUPENDA ROBERTO."

Titiana hakuona sababu ya kujizuia zaidi ya kumueleza kilichomfanya kumkwaza siku ile kuwa ilikuwa ni hasira tu na si kingine kitu kilichomfanya Roberto atabasamu baada ya kuusoma na kisha kuiweka mfukoni simu na muda huo walikuwa wanawasili kwa Daktari Abbas.


UTAMU WA MUWA ULE MPAKA FUNDO LAKE.



Geti lilifunguliwa na kuliruhusu gari la wakina Roberto kuingia. Baada ya kulipaki sehemu ya maegesho walishuka kisha kumuamuru Hamza kushuka chini. Kwa kujivuta vuta alishuka huku jasho likiwa limeuvamia mwili wake kuashiria hofu ya uhai wake.


"Sasa naanza kuunganisha doti zangu ambazo zinaelekea kunipatia kitu kizima."

Jackline aliongea baada ya kuwaona wakimshusha Hamza ambaye alimtambua.


"Kwanini dada Jackline?"

Roberto alimuuliza.


"Huyu kijana ukimuangalia haraka haraka huwezi kufikiria kuwa anaweza kufanya mambo ya kipuuzi kama haya. Hebu tueleze unamtumikia nani?"

Jackline alimuuliza Hamza.


"Naombeni mnisamehe ndugu zangu najua nimewakosea sana kwa kitendo cha kusababisha hasara kwenye gari lenu."

Hamza alijitetea.


"Unafikiri ni hivyo tu?"

Jasmine alimsogelea akiwa kashikilia waya mkononi.


"Najua ninyi hamuwezi kuwa roho mbaya kiasi hicho, okoeni maisha yangu."

Hamza aliendelea kujitetea japokuwa sura zilizokuwa mbele yake hakuna hata moja ambayo ilionesha chembe ya huruma kwake.


"Umeulizwa unamtumikia nani?" Hayo mengine yako chini yetu sisi kukuhurumia au kukutoa sadaka."

Mahmoud alirudia swali akiwa kamshika mdomo.


" Niwe muwazi tu jamani, mimi ni mfanyakazi wa Bi Elizabeth pamoja na Mackdone nikihudumu kitengo maalum (Undercover) majukumu yangu yakiwa ni kumfuatilia yeyote ambaye nakuwa nimepewa maelekezo yake."

Hamza aliongea.


"Tunajua kuwa Bi Elizabeth hayuko nchini baada ya kutoroshwa, unaweza kutuambia yuko wapi? Na vipi kuhusu wale vijana wake wa kule Namport?"

Mahmoud alimuuliza tena swali na safari hii alimshika kabali ya suruali na kuanza kumvuta kuelekea sehemu aliyoelekezwa na Daktari Abbas kwa ujumbe wa simu kwani muda huo yeye hakutokea pale nje alikuwa ndani akiwaangalia kupitia dirishani.


"Bi Elizabeth yuko Afrika ya Kusini kwa matibabu lakini kutokana na tatizo lake kuwa kubwa wako kwenye mchakato wa kumpeleka Australia huku vijana wake wa Namport wakifa wote kwenye ajali ambayo waliipata na kusababisha Bi Elizabeth kuwa kwenye hali aliyo nayo."

Hamza aliendelea kufunguka.


" Dawa ya sumu ni sumu huyu mnamfanyia mahojiano yote hayo ya nini ikiwa kawaeleza kazi aliyokuwa akiifanya hii ina maana tayari mchakato wetu wa safari alishauuza..... "

Kabla Jackline hajamaliza Hamza alimkatisha.


" Dada hapana sijui chochote kile kuhusu hiyo safari yenu."


"Utaongea tu Hamza walikuwepo watata kama wewe lakini moto waliupata sembuse wewe?"

Jackline alimwambia wakiwa wanaingia naye kwenye chumba kilicho pembeni ya jengo lao. Huko walimkarisha kwenye kiti cha waya kisha wakamfunga mikono na miguu kwa kutumia waya uliokuwa ukining'ia kwenye kiti. Baada ya kuona kila kiko sawa swichi ya umeme iliwashwa na kwakuwa nguvu ya umeme ilikuwa chini Hamza hakuonesha dalili yoyote ya hofu. Daktari Abbas baada ya kuona kazi imefika ya kumuadhibu Hamza yeye alitoka na kuingia kwenye gari akaondoka zake huku akiacha ujumbe kwenye simu ya Mahmoud.


"Hakikisheni anaongea kila kitu na iwapo ataendelea kuleta jeuri nijulishe nimletee kiboko yao."

Baada ya kuusoma ujumbe ule Mahmoud alitabasamu kwanza kisha akaiweka mfukoni simu na kisha kumfuata Hamza ambaye alikuwa akipata suluba nyepesi kutoka kwa Roberto huku Jackline na Jasmine wakiwa nje kibanda hicho wakibadilishana mawazo na Thomas pamoja na dalali.


"Brother niachie kidogo huyu panya nimlishe chakula."

Mahmoud alimwambia Roberto na kumfuata Hamza na kumkaba shingo.


"Ni bora ukaongea yote maana unachokwenda kukutana nacho utajuta.

Mahmoud alimwambia huku akimtemea mate machoni, Hamza hakuweza kuyatoa kutokana na mikono yake kufungwa kwenye kiti hivyo kuishia kumuangalia tu Mahmoud.


" Niangalie hivyo hivyo tu muda si mrefu utanifananisha na izrael mtoa roho."

Mahmoud aliendelea kumtisha huku akiifuata swichi ya umeme ambayo aliipandisha mpaka kwenye alama nyekundu. Kelele alizopiga Hamza zilimshtua kila mmoja mle ndani kwani muda wote alikuwa akitoa mlio wa chini lakini safari hii uvumilivu ulimshinda.


" Haa...ha..hak...haki ya..... Mungu te....tena sijui chochote mtaniua bure."

Hamza alijitetea kwa shida kwa safari hii kile kiti kilianza kuwa chekundu.


"Usalama wako ni kuongea mambo yote uliyofanya na Mackdone pamoja na Bi Elizabeth."

Roberto alimwambia akiwa kamuinamia pale kitini.

Kitu cha ajabu alimtemea mate usoni na kuanza kucheka kwa nguvu.


"Unafikiri ni rahisi kupata unachokitaka? Haiwezi kutokea hiyo mnaweza kuniua tu."

Maneno ya Hamza yaliwafanya kutazamana usoni huku wakina Jackline wakiingia ndani baada ya kumsikia Hamza akicheka.


"Zima umeme Mahmoud, ikiwa kiti kimefikia hatua ya kuwa chekundu lakini anasema hivyo. Haina haja mtoeni hapo kisha nitamuonesha kuwa yeye bado sana hajafikia ukomavu wa hivyo."

Jackline alimuamuru Mahmoud kumtoa kwenye kiti. Baada ya kuzima umeme walimfuata na kumtoa kitini ambapo sehemu zilizokuwa zimepitiwa na nyaya kuchora drafti ya vidonda huku suruali na t-shirt vikiwa havitamaniki hata kidogo. Walitoka na kumuacha mle ndani kisha wakaufunga mlango kwa nje.


"Saizi ni usiku, muda mzuri kuifanya kazi yetu. Si kagoma kuongea huyo paka dawa yake ni kumletea panya tu."

Jackline aliwaambia wenzake pale nje.


"Tunaomba ufafanuzi."

Mahmoud alimtaka aifafanue kauli yake.


"Tumfuate mke wake na pia tumtafute yule kinyago aliyeuza ramani kwao akijidai fundi aluminum."

Jackline aliwafafanulia kisha wakagawana makundi mawili moja likiwa la Jackline mwenyewe ambalo lilielekea kwa Dorice na kundi jingine likielekea nyumbani kwa Hamza huku pale nyumbani mlinzi akiachiwa jukumu la kuhakikisha hakuna mtu anayeingia kwa namna yoyote ile.


***


Mackdone aliwasili salama nchini Afrika ya Kusini na kuelekea moja kwa moja Victoria hospitali kukutana na Leon kujua taratibu za uandaaji nyaraka kwa ajili ya mgonjwa wake zimefikia wapi. Mtu wa kwanza kukutana alikuwa ni mrembo Vivian ambaye ukikutana naye kwa mara ya kwanza na kutoambiwa tabia yake unaweza uza mpaka nyumba ya urithi ilmradi tu uwe naye hata usiku mmoja, alikuwa kaumbika lakini kama alivyokuwa mrembo wa kuvutia na ndivyo hivyo hivyo alivyokuwa mchafu wa tabia kwani ungetamani kuendelea kumfuatilia kujua kama ni kweli anaweza kuwa Mafia kiasi hicho.


"Bosi ncha moja ya kamba yetu imekatwa tunafanyaje?"

Vivian alimpa taarifa ambayo aliielewa maana yake.


"Nisubiri kwanza nionane na Daktari Leon."

Mackdone alimjibu huku akimpiga mgongoni na kuingia ndani. Alimkuta Daktari Leon akiwa anaongea na simu hivyo akaketi kitini kumsubiri amalizane na simu kisha wayajenge.


"Naam kaka, lete habari sasa!"

Daktari Leon alianza baada ya kukata simu.


"Nikwambie nini mdogo wangu zaidi ya kujua umefikia wapi kwenye maandalizi ya nyaraka za mgonjwa wangu."

Mackdone alimjibu.


"Mgonjwa hali yake wala haijabadilika iko vile vile na kuhusu documents ziko tayari kinachosubiriwa hapa ni kugongwa mhuri tu."

Daktari Leon alimwambia huku akimuonesha zile nyaraka zilizoandaliwa.


"Ziko vizuri sana kumbe ninaposubiri huo mhuri ngoja na mimi nishughulikie mchakato wa usafiri."

Mackdone aliongea huku akiinuka kitini na kuzirudisha nyaraka kwa Daktari Leon. Na baada ya kuagana Mackdone alitoka na kumfuata Vivian.


"Enhh sasa nikusikilize."

Mackdone alimwambia Vivy.


"Bosi kama ambavyo nilikwambia kuwa mtu wetu kadakwa na maadui."

Vivy alirudia kutoa maelezo.


"Hilo achana nalo ujinga wake umemponza huyo ila cha kufanya ni kuhakikisha tunamdaka mke wake kabla hawajamshika naye ili tumlinde na kumpa mafunzo yetu na iwapo yatamuingia atachagua mwenyewe kuungana nasi au la, na vipi kuhusu aliokuwa nao Hamza?"

Mackdone aliuliza.


" Wako salama na hivi tunavyoongea wako njiani kuelekea sehemu waliyompeleka Hamza kuhakikisha anaokolewa na hao wajinga."

Vivian alimjibu Mackdone kitu ambacho alionekana kufurahishwa nacho kwani alitingisha kichwa.


" Vizuri waambie wawe makini zaidi kwani najua tukifanikiwa kuwateka wale watoto kabla Bi Elizabeth hajazinduka itakuwa furaha sana akizinduka na kukutana na zawadi ambayo naamini itamfungulia ukurasa mpya wa maisha yake."

Mackdone alimwelekeza Vivian huku akitoa simu yake mfukoni ambayo iliingiza ujumbe.


" NADHANI UMEONA UACHANE NA BIASHARA ZAKO NA KUJIINGIZA KWENYE LIGI YETU SIYO? JIANDAE MKUBWA."

Aliusoma ujumbe huo ambao haukuwa na utambulisho wa mtumaji.


"Sijui ni nani huyu anayenifuatilia nyendo zangu?"

Mackdone aliongea akiendelea kuishangaa ile jumbe.


"Nani huyo?"

Vivy aliuliza huku akimsogelea Bosi wake ili aoneshwe huo ujumbe lakini Mackdone aliupuuzia ujumbe huo.


"Achana naye najua atanasa muda si mrefu."

Mackdone aliongea akiiweka simu mfukoni na kumgeukia Vivian ambaye ndiye kiongozi Mkuu wa kundi lake la siri liitwalo 'THE SHADOW' ambalo hulitumia kufanya uhalifu mbalimbali ndani na nje ya Afrika ya Kusini hasa maeneo yenye vivutio vya kitalii.


" Vivian hakikisha Mob yako inakuwa imara kila wakati kwani najua hao Vikaragosi wanaweza kufanya lolote mara baada ya kumdaka Hamza na ndiyo maana nahitaji kuiona sura ya mke wake hapa."

Mackdone aliongea hayo huku akiondoka na kumuacha Vivian akimjibu kwa kichwa.


" Mmefika wapi? "

Lilikuwa swali la Vivian kwa watu wake mara baada ya kuachana na Mackdone.


" Tumeshafika kwenye nyumba yao hapa tunakagua sehemu ambayo tunaweza kupita na kuingia ndani bila kushtukiwa na yeyote."

Alijibiwa na mtu aliyekuwa upande wa pili akionekana kuwa na msaidizi wake.


"Vizuri kuweni makini maana hao watu siyo wa kawaida."

Vivian aliwatahadharisha.


"Usihofu tulishachukua tahadhari mapema sana kwani tumefika mapema na kuwashuhudia wakitoka hivyo tunajaribu kuona ni wangapi waliosalia ndani."

Alijibiwa.


"Sawa, mkifanikiwa kutoka hapo salama hakikisheni mnaelekea kwake huyo Hamza mkambebe mke wake kuna mpango juu yake."


"Sawa kiongozi."

Aliyekuwa akiongea naye alimjibu kisha Vivian akakata simu na kurejea ndani kumchungulia Bi Elizabeth kwani kwa kipindi hiki ambacho kikosi chake kilikuwa kazini suala la ulinzi lilibaki mikononi mwake yeye hivyo hakuwa tayari kuona anaiharibu kazi aliyoachiwa na Bosi wake kutokana na uaminifu aliojijengea kwa Mackdone hakuwa tayari kuona unasambaratika kwa njia yoyote ile.


JE NINI KITAENDELEA?



THE SHADOW waliingia ndani jengo la Daktari Abbas kupitia ukuta wa nyuma ambako waliruka na baada ya kuingia kitu cha kwanza walihakikisha wanamteka mlinzi ambaye ndiye atawaonesha aliko mtu wao. Vijana wawili kati ya wanne walimvizia mlinzi ambaye alikuwa katulia na silaha yake mkononi macho yakiwa getini kuhakikisha usalama ni asilimia mia moja. Mara alisikia mluzi umepigwa nyuma yake haraka akageuka kuangalia ni nani aliyepiga wakati pale nyumbani yuko peke yake hakuona mtu yeyote akapuuzia lakini mara akahisi kitu cha baridi kikimgusa sikioni.


"Tulia hivyo hivyo usilete jeuri ambayo itakupeleka kuzimu, tumeelewana?"

Sauti hiyo ilimwambia mlinzi Thadei ambaye alikuwa kaloa kwa mkojo uliokuwa ukibubujika kwenye suruali lake kama chemchem.


"Sawa sa.....sa....sawa."

Alijbu kwa hofu.


"Achia silaha yako taratibu kisha ongoza alikohifadhiwa mtu wetu najua kuwa unakufahamu."

Aliamrishwa na mtu huyo.


"Sifahamu lolote lile ila ni kama alihifadhiwa kwenye kijumba kile pale."

Alimjibu huku akionesha kiliko kile kijumba na hivyo yule mtu akawaambia wenzake wakifuate kile kijumba wakafanye ukaguzi mara moja huku yeye akisalia pale na mlinzi ili kama kawadanganya aweze kumshughulikia mara moja.

Baada ya kufika kwenye kijumba kile waliweza kumuona na hivyo mmoja wao alirudi kwa kiongozi wao na kumpa taarifa, wakamchukua mlinzi na kwenda naye mpaka kule na kumpa kazi ya kuvunja mlango.


"Wewe si ndiyo mlinzi wa jengo hili? Haya haraka vunja mlango huu."

Hakuwa na la kujibu zaidi ya kuanza kuuvunja kwani alipoangalia nyuma ule mdomo wa bunduki ulimgusa tena kuashiria kuwa bado wanakitafuta kifo chake. Alitumia nguvu nyingi sana kuuvunja mlango na hatimaye alifanikiwa na bila kutarajia alishtukia yuko ndani ya kile kijumba baada ya kutandikwa teke na yule kiongozi wa 'The Shadow' na kisha wao nao wakaingia ndani. Haraka sana walimfuata Hamza ambaye wakati huo alikuwa kazrai hajitambui hata kidogo.


"Mbebeni haraka hatuna muda wa kupoteza humu."

Kiongozi wao aliwaamrisha hivyo wakamchukua na kutoka naye nje ya kile kijumba huku nyuma yule kiongozi wao alimchukua Thadei na kumkarisha kwenye kile kiti kisha akamfunga na zile nyaya mwili mzima kama ambavyo alifanywa Hamza na baada ya kujiridhisha aliwasha swichi ya umeme kisha yeye akatoka zake nje na kuwakuta wenzake wakimsubiri.


"Kifuatacho Bosi?"

Mmoja wa vijana wa kundi hili la 'The Shadow' alimuuliza.


"Tunaelekea ndani ya nyumba kuhakikisha tunawachomoa watoto wao na kuondoka nao mara moja."

Baada ya kusema hivyo waliondoka na kulifuata lango la kuingia ndani ya nyumba hiyo lakini kitu walichokutana nacho hawakuamini kwani kitendo cha kuugusa tu mlango taa za ulinzi za jengo hili ziliwaka na kulifanya eneo lote kuwa kama mchana huku ving'ora vya ulinzi vikilia kwa fujo.


"Tuondokeni hili eneo haraka washenzi hawa wameiunganisha nyumba yao na system ya ulinzi ya jeshi la ulinzi hivyo muda si mrefu askari wanaweza kuwa hapa."

Kiongozi wao aliwaambia na hivyo walimfuata Hamza pale chini na kumbeba kisha kuondoka naye kupitia mlangoni.

Waliondoka kwa kasi na kuelekea nyumbani kwa Hamza ili kumchukua mke wa Hamza kwa usalama zaidi, lakini baada ya kufika walikutana na milango ikiwa wazi ikiwaita tu na hata walipoingia ndani walikuta sebule imevurugika hovyo hovyo na ndani hakukuwa na dalili yoyote ya kuwemo mtu,walitafuta kila kona na kila chumba hawakuweza kumkuta.


"Kazi imekuwa pevu kiongozi."

Alimpigia simu Vivian kumpa taarifa ya walichokutana nacho.


"Kivipi?"

Vivian alimuuliza kijana wake.


"Hamza tumefanikiwa kumchukua japo hali yake ni mbaya lakini upande wa watoto tumechemka kwani kuna ulinzi mkali wa kielektroniki hivyo tumetoka mkuku bila kugeuka nyuma maajabu mengine mke wa Hamza ni kama vile katekwa kwani nyumba yake imevurugwa sana."

Alieleza Kijana wake.


"Ondokeni hapo haraka si salama kwenu."

Vivian aliwataka kuondoka eneo hilo kwani alihisi kunaweza tokea janga kubwa kwao.


***


Mahmoud, Thomas na Jasmine walikuwa wa kwanza kuwasili nyumbani kwa Jackline wakiwa wamemtia mkononi mke wa Hamza Bi Aisha. Kitu kilichowashangaza ni kitendo cha kulikuta geti wazi na Thadei hayupo lindoni na pili zilikuwa ni zile taa pamoja na king'ora wakajua kuwa hakuna usalama hivyo moja kwa moja wakasambaa kulizunguka jengo kuangalia kuna tatizo gani, lakini Jasmine akiwa sambamba na mke wa Hamza yeye akili yake ilimtuma aelekee kwenye kijumba ambacho alihifadhiwa Hamza na baada ya kuingia alikutana na kituko.


"Heee huyu si Thadei?"

Alihamaki Jasmine na kuifuata swichi ambayo aliizima na kwenda kumtoa pale ambapo hali yake ilikuwa mbaya sana kwani alikuwa hajitambui.


"Njooni huku Mahmoud, wamemchukua mtu wao na kulipiza kwa Thadei."

Walikuja na kumbeba Thadei kisha wakamuingiza ndani na kuanza kumpatia huduma ya kwanza wakati akisubiri huduma kamili.


"Huku hali si shwari wametuvamia na kumchukua mtu wao Hamza kisha kumfunga Thadei kwenye kile kiti na kuwasha swichi kisha wao kuondoka hivyo hali ya Thadei si nzuri."

Jasmine alimpigia simu Daktari Abbas ambaye toka alipoondoka haikufahamika kaelekea wapi.


" Nakuja sasa hivi vipi watoto wako salama? "

Daktari Abbas alimjibu na kuulizia watoto wake.


" Wako salama lakini tumewakuta juu ya ceiling board wametulia."

Jasmine alimjibu huku akicheka kutokana na kitendo cha wakina Nathan kukimbilia chumba cha juu ambacho huwezi kujua kama hujaelekezwa kwani chumba hicho kiko ndani ya chumba cha kulala watoto huko kuna swichi ambayo ukiibonyeza tu kuna ngazi inashuka kisha unapanda na baada ya kufika juu tu kuna swichi nyingine ambayo ukiibonyeza tu ile ngazi inapanda juu na kujifunga na lile eneo ukiliangalia huwezi kujua kama kuna mlango wa kuendea juu.


"Watoto wa nyoka ni nyoka shemeji."

Daktari Abbas alimjibu kwa ufupi.

Jasmine alitoka nje na kumchukua mke wa Hamza na kumuingiza kwenye chumba cha ziada na kumfungia huko kisha alirejea kuungana na wenzake kumpa huduma ya kwanza mlinzi. Wakiwa wanaendelea mara Daktari Abbas aliingia na kumchukua Thadei mpaka kwenye jengo dogo la mjini hapo ambalo hulitumia kwa wagonjwa wake wa dharura na kuanza kumhudumia. Usiku ulikuwa umesonga lakini wakina Jackline walikuwa hawajarejea kutoka kwenye windo lao na kuleta hofu kwa wenzao, ikabidi Jasmine amtafute hewani.


"Vipi bado tu?"

Jasmine alimuuliza baada ya kupokea simu.


"Huku mambo ni magumu kuna gari tulimvizia kutoka ofisini kwake mpaka anaingia kwenye gari tukajua anaelekea kwake kumbe akawa ameunga na mtu wake kwenye Bata hivi tuko hapa 'African Power' tunamvizia anakunywa."

Jackline alimweleza.


"Kweli mna kazi asipotoka itakuwaje? Huku hali si shwari jamaa walivamia na kumfanya kitu mbaya Thadei kwenye kiti cha umeme hivi shemeji yuko kuhangaika naye na wakati huo huo Hamza walifanikiwa kuondoka naye na yote hayo yamefanyika wakati tumeondoka."

Jasmine alimsimulia Jackline.


" Kuna uwezekano wa kupona na vipi wanangu wamesalimika?"

Jackline alionesha hofu kwa watoto wake.


" Tusubiri majibu ya Daktari Abbas na kuhusu watoto wewe mwenyewe unawafahamu walikimbilia chumba cha juu."

Jasmine alimjibu.


"Mungu mkubwa, ngoja nitakupigia tayari Roberto kawafuata pale pale walipokaa ngoja nikampe sapoti."

Jackline alikata simu na kumfanya Jasmine naye kurudi ndani kuwaandalia chochote wakina Natalie japo muda ulikuwa umekwenda sana.


"NAJUA WEWE NI MKE WA DAKTARI ABBAS MTU MAARUFU HAPA NAMIBIA KUTOKANA NA TAALUMA YAKE YA U DAKTARI HILO HALINA UBISHI HATA CHEMBE LAKINI NINACHOMSIKITIKIA NI KUKUOA MNYAMA KAMA WEWE SIJUI ALIWAZA MARA MBILI MBILI? KWA KUWA KAINGIA MWENYEWE AJIANDAE KUPATA PIGO AMBALO HAJI KUSAHAU MAISHANI."

Ujumbe huu ulimshtua Jackline baada ya kuusoma na alipoangalia namba ya mtumaji ilikuwa ngeni hivyo akajua huyo ni Mackdone hakuna mwingine, akatafakari kwa muda kisha akaona amjibu.


" NAJUA WEWE NI KIDUME UNAONAJE MIMI NA WEWE TUKUTANE SEHEMU TUPATE KAWAHA KULIKO KUTISHIANA?"


Na baada ya kutuma ujumbe huo aliiweka simu mfukoni na kuwasogelea wakina Roberto walipokuwa.


"Kaka sisi hatuna shida na wewe hivyo ukimya wako ndiyo uhai wako hivyo tunaomba msimame taratibu na kuongoza nje bila vurugu tambueni kuwa chochote mtakachofanya kinyume na maelekezo yetu kitagharimu uhai wenu."

Roberto aliwaambia huku akiwaonesha bastola iliyokuwa kiunoni kwake. Dorice na mtu wake waliishiwa pozi wakaangalia kama wanaweza kupata msaada eneo lakini walichelewa kwani Jackline alifika na kumsogelea mpaka sikioni Dorice na kumnong'oneza.


"RAMANI ULIYOIUZA KWA MAADUI TUMEIKAMATA NA SASA NI ZAMU YAKO."

Aliongea hayo na kumtandika kibao cha usoni kilichompeleka mpaka chini asijue cha kufanya.


"Sister mbona vurugu....?"

Yule kijana aliyekuwa na Dorice alijutia kufungua kinywa chake kwani alikutana na teke kutoka kwa Jackline lililotua barabara mdomoni na kumfanya kutema damu pamoja na meno mawili.


"Unasemaje wewe?"

Kijana yule baada ya kupokea teke lile akajua kuwa aliyemtandika si mtu wa kawaida hivyo hata kujibu swali aliloulizwa alishindwa zaidi ya kutikisa kichwa kuashiria kuwa hana swali.


"Inuka haraka ongozeni nje."

Waliamrishwa na hivyo walitii na kuongoza nje ambako walimkuta dalali aliyeachana na kazi yake iliyokuwa ikimuweka mjini na kuungana na Mahmoud na hii ni baada ya kupata msaada wa kuokolewa kutoka mikononi mwa watu wa Mackdone.


" Panda kwenye gari haraka."

Waliamrishwa kuingia kwenye gari na mara baada ya kupanda tu yule kijana dalali akiwa nyuma ya usukani aling'oa gari na kuondoka zao kutoka eneo hilo. Wakiwa njiani mara Jackline alipokea ujumbe mwingine.


"UKIONA SIJAKUTIA MIKONONI MWANGU NDANI YA SIKU CHACHE HIZI UJUE KUWA NITAKUWA NIMEKUGUSA SEHEMU NYINGINE AMBAYO HIYO HAUKO TAYARI MTU YEYOTE AIGUSE. JIANDAE MAMA NA PIA MWAMBIE DAKTARI NDANI YA SIKU HIZI MBILI NITAMTEMBELEA NYUMBANI AU KAZINI KWAKE."

Aliusoma ujumbe ule ambao alionekana kama kuupotezea hivi lakini aliumiza kichwa sana ni namna gani amdake mtu huyo.


JE NINI KITAENDELEA KWENYE MCHEZO HUU?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA KUJUA KITAKACHOJIRI.





Waliondoka na watu wao mpaka kwenye pori moja lililo nje ya mji ambako waliwafunga kwenye miti kisha Jackline akavua mkanda na kuanza kuwachapa sehemu mbalimbali za miili. Mikanda iliendelea hasa kwa Dorice ambaye alikuwa mgumu kuongea pamoja kichapo chote alichopewa.


"Mrembo unaonekana wewe ni sugu sana ee?"

Roberto alimuuliza huku akichezea kinyundo mkononi kama kawaida yake.


"Niseme kuhusu nini ninyi si mmeamua kunisulubisha endeleeni mpaka mchoke."

Dorice aliongea kwa kujiamini kabisa kama vile hajaguswa.


"Unasemaje wewe? Yaani waendelee kutushambulia? Kwa hiyo unayafurahia haya mateso siyo?"

Yule kijana ambaye walidakwa pamoja aliona amuulize Dorice.


"Kelele wewe mshenzi unaongea nini mimi nilijua niko na kidume kumbe sifuri kabisa."

Dorice alimwambia kwa ukali na kumfanya kijana yule kuwa mpole.


"Lakini kwanini tufanyiwe haya mpenzi si unieleze?"

Aliendelea kuuliza huku Jackline na Roberto wakitabasamu baada ya kubaini kuwa kijana kaingizwa mkenge kwa kupenda maganda ya ndizi ambayo yamemchana msamba.


"Tunaweza kuanza dada mbishi."

Roberto alimwambia Dorice na kumgonga na kile nyundo kwenye kidole gumba cha mguuni.


"Aaaaaahhhhh aachaaaa unaniumizaaaa......"

Dorice alipiga kelele baada ya kinyundo kutua kwenye dole gumba la mguu wa kulia.


"Ni kitu kimoja tu dada mbishi, tuambie wewe ni nani?"

Roberto alimwambia Dorice huku akiishusha nyingine. Lakini hakuna alichoongea zaidi ya kuendelea kupiga makelele ambayo yalimchefua Roberto aliyeamua kuanza kugonga vidole vya miguuni bila kutulia. Hali ile ilimfanya Dorice kulia sana na kuomba aache ili awaeleze.


"Tunakusikiliza fundi."

Jackline alimwambia baada ya Roberto kuacha kumgonga vidole vyake ambavyo muda huo vilikuwa vikitoa damu.


"Si uongee kama kuna kitu umewafanyia mpenzi?"

Mpenzi wake alimwambia Dorice.


"Kelele wewe mwanaharamu wakati unatumia ulijua mimi nimezitoa wapi? Kama ulivyokuwa unaburudika na hapa tuendelee kuburudika pamoja."

Dorice alimjibu mpenzi wake ambaye alionekana kumtegemea yeye pasipo kujua mpenzi wake anajishughulisha na nini.


"Laiti kama ningejua ulizitoa wapi thubutu Dorice usingeniona najuta kukufahamu."

Alilalamika sana huyu kijana kitu ambacho kilimfanya Dorice kumsonya.


"Acheni hizo drama' zenu hapa tunakusikiliza wewe fundi uchwara."

Jackline alimkumbusha Dorice.


"Kwani nimewaambia nitafanya nini hapa nikumbusheni."

Dorice aliongea kauli ambayo aliwachefua kiasi cha Roberto kumfuata na kumtandika ngumi ya tumboni na kisha kumuuliza.


"Umesemaje mrembo?"


"Acha utemi kwenye mwili laini huu unajua nimetumia pesa ngapi kuung'arisha? Na kama wewe ni mtemi hebu fanya kitu kimoja kama unajiamini fungua hizi kamba kisha tuzipige kavu kavu."

Dorice aliendelea kuwakera kiasi kwamba Jackline aliiangalia saa kisha akamfuata na kumfungua kamba. Dorice katika kuwaonesha kuwa yeye ni nani aliruka kavu kama nne kisha akajiweka sawa tayari kwa mpambano, Jackline aliurusha mkanda kwa Roberto kisha akamfuata Dorice aliyekuwa kajitanua kama Pakapori anayejiandaa kumparua mtu. Lakini kabla Jackline hajafanya chochote alirukiwa na Dorice kisha kugongwa na kiwiko begani kiasi cha kumpeleka chini huku akiyasikilizia maumivu ya mkono. Dorice alitabasamu baada ya kumuona Jackline akigugumia kwa maumivu pale chini hivyo alimfuata tena ili kwenda kumuongeza pigo jingine, alichelewa kwani alishtukia Jackline yuko katikati ya miguu yake na kwa kasi ya ajabu alijipindua na kumbwaga chini Dorice ambaye aliangukia mkono wa kushoto na kuutegua.


"Aaaaaghh mwanaharamu wewe ndiyo umenifanya nini?"

Dorice alimuuliza Jackline ambaye hakujibu kitu chochote zaidi ya kumfuata na kumkanyaga kwenye vile vidonda alivyogongwa na Roberto.


"Mamaaaaa......"

Alipiga kelele.


"Uko tayari kuongea?"

Jackline alimuuliza huku akichomoa bastola yake kiunoni.


"Fanya chochote nimesema lakini hapa hupati chochote shetani wewe."

Majibu ya Dorice yalimfanya Jackline kufyatua risasi moja ambayo ilikwenda pale pale kwenye kidole gumba chenye kidonda na kukitawanya hali hiyo ilimtisha sana mpenzi wake ambaye alikuwa pale kwenye mti akiwa bado kafungwa kamba huku pembeni yake akiwepo Roberto.


"Mnatufanyia nini jamani kama mmepanga kutuua si mtuue tu kuliko michezo mnayotufanyia."

Mpenzi wake Dorice uzalendo ulimshinda akajikuta akilopoka maneno hayo ambayo hakujua kama yatamgharimu.


"Kwani wewe umepata kichapo chochote?"

Roberto alimuuliza huku akiwa ameshamgonga na kinyundo kichwani.


"Ha...ha...haa..paaaana."


"Kelele za nini sasa?"

Roberto alimuuliza.


"La...laki...ni mimi sina kosa lolote naomba mniachie niondoke mama yangu atakuwa ananitafuta."

Kijana yule aliomboleza kwa Roberto ambaye alitaka kumshindilia nyundo nyingine lakini aliishusha baada ya kumuona kijana wa watu akilia mpaka kamasi.


"Mmezidi kutaka maisha mazuri kwa jasho la wengine sasa angalia unavyotoa kamasi."

Roberto alimwambia.


"Sikujua kaka yangu naujutia ulimbukeni wangu."

Roberto alichokifanya ni kumfungulia yule kijana na kumwambia anataka kumuacha lakini kwa sharti moja tu la kumfanya Dorice aongee yeye ni nani na kwanini aliwadanganya.


"Mpenzi hebu waeleze wewe ni nani hujui kukaa kimya kwako kunawapandisha hasira watu hawa."

Maneno ya mpenzi wake ni kama yalimpandisha mashetani Dorice ambaye aliinuka pale chini na hali yake ile ile na kwenda kumkaba shingoni kwa nguvu kiasi cha kumfanya kijana wa watu kushindwa kupumua vizuri, hali ile ilimfanya Roberto kufika na kumsukuma pembeni Jackline na kumpiga teke la mbavu Dorice ambalo lilikwenda kumtupa pembeni na kumfanya kijana yule kama kichaa kuinuka na kuanza kukimbia hovyo hovyo kitu ambacho wakina Jackline hawakumjali zaidi ya kumfuata Dorice na kuanza kumpiga kwa mikanda na kile kinyundo kiasi cha Dorice kuomba msamaha na kuwaambia yuko tayari kuongea.


"Nafasi ya mwisho hii anza mara moja."

Jackline alimwambia huku akimsindikiza kwa teke jingine la mbavu ambalo lilimfanya aanze kulia kwa nguvu lakini kama umeme alitulia akafuta machozi.


"Naitwa Nawane Gabathusi ni mzaliwa wa Gaborone Botswana mimi kazi yangu kubwa ni mmoja wa ma'Undercover' wa siri wa Mackdone nisiye na mipaka."


"Kwa hiyo wewe siyo fundi kama ulivyojitambulisha?"

Jackline alimuuliza.


"Hapana mimi naweza shughuli nyingi sana nilizojifunzia nchini Israel kwa miaka zaidi ya saba."

Majibu yale yalimfanya Jackline kupumua kwa nguvu huku akimtazama Dorice kwa hasira.


"Tulia hapo unafikiri unaweza kutoroka hapa."

Dalali ambaye muda wote alikuwa kwenye gari alimkamata yule kijana aliyetaka kukimbia na kumrudisha kwa wakina Jackline.


"Lakini kaka mimi niliachiwa...."

Kabla hajamaliza aliulizwa.


"Unasemaje wewe?"

Roberto alimuuliza huku akiwa kashikilia kile kinyundo na yule kijana baada ya kukiangalia akajua kazi imehamia kwake.


"Hapana kaka sirudiii tena."

Alijitetea huku akiwa chini anagalagala.


"Sogea kwa mpenzi wako kule haraka."

Roberto alimuamrisha huku akimtishia kumtandika teke,kwa hofu ya kupigwa tena na Dorice hivyo alisogea pembeni kidogo na kutulia huku Dorice akimuangalia kwa hasira.


"Hivyo mimi naweza kufanya lolote lile nikiamua na ndiyo maana niliweza kudukua mawasiliano ya Daktari Abbas wakati akifanya mawasiliano na dada mmoja aitwaye Dorice kutoka City aluminum na baada ya kuyadukua niliweza kumtraki anakoishi huyo Dorice na kwenda kumuua kisha nikaichukua kazi yake mimi ili kulifanikisha zoezi langu. Na mimi ndiye niliyekuwa nafuatilia nyendo zenu Jackline na Daktari Abbas ili siku nikiamua kufanya chochote iwe rahisi kwangu na hata wakati mmekuja kunivizia pale niliujua mchezo mzima ndiyo maana nilijirahisisha ili akili yenu iwe kwangu huku mikakati yetu ya kumsagirisha Bi Elizabeth iende kama tulivyopanga."

Dorice aliongea huku akiwaangalia wakina Jackline ambao waliishiwa nguvu na kubaki wamemtolea macho tu.


" Kwa hiyo unataka kusema kuwa Bi Elizabeth ameshasafirishwa... "

Roberto alimuuliza.


" Unauliza nini sasa wewe si ndiyo ulidukua mfumo wetu wa mawasiliano kupitia kwa Bosi Mackdone na sisi tukakujaza......"

Hakumalizia sentensi yake alichota vumbi kwa mkono wa kulia kwa shida hivyo hivyo na kuwatimulia machoni baada ya kuona wamejisahau baada ya kutazamana kama vile walikuwa wanapeana ishara. Walibaki pale wakijifuta vumbi kwenye macho yao na kuja kuangalia pale hawakuona mtu na walipogeuka kumuangalia Dalali hawakumuona wakatazamana wakapeana ishara na kutawanyika.


***


Safari ilikuwa njema kwao kwani walifika salama pasipokuwa na upinzani wowote ule kutoka kwa maadui wao. Vivian kwa kushirikiana madaktari wa nje wa Hospitali ya St. Mathew ya jijini Canberra ambao ni mji Mkuu wa nchi ya Australia walimchukua Bi Elizabeth na kumpeleka chumba maalum tayari kwa kuanza matibabu ya tatizo lake ambalo limempelekea mpaka sasa kuwa kwenye hiyo koma.


"Tunaziomba hizo nyaraka tuweze kuzipitia japo kila kitu tulikipata kupitia email yetu."

Daktari Mkuu wa kitengo kile amwambia Daktari muuguzi aliyeongozana na mgonjwa ambaye alilitoa lile faili na kumkabidhi Daktari. Wakati huo Vivian alitoka nje kuongea na simu ambayo alipigiwa na Mackdone.


" Naam Mkuu."

Vivian aliitikia baada ya kupokea simu.


"Vipi mmeshafika?"

Mackdone aliuliza.


"Tumefika Bosi na muda huu wako kumsajili ili taratibu nyingine zianze."

Vivian alimjibu Mkuu wake.


"Vizuri, hakikisha kuwa haukai mbali naye kwa sababu wakina Jackline wameshapata ramani ya hiyo Hospitali, na kizuri zaidi ni kwamba Chawa wetu amefanikiwa kuwatoroka watekaji wake na hivi ninavyoongea tayari anapangua miti kuinusuru roho yake japo najua hawamuwezi yule."

Mackdone alimsimulia Vivian juu ya kilichotokea kwa Nawane Gabathusi maarufu kwa jina NAGA ambalo ni kifupi cha jina lake na la baba yake.


" Mkuu jitahidi kumnusuru kabla hawajamfikia si unaufahamu umuhimu wa NAGA kwetu."

Vivian alimtaka Mkuu wake afanye jitihada za kumuokoa.


"Usihofu tayari panya watoto wako eneo hilo wanamfuatilia kwa msaada na pia nilikuwa najifikiria kumsafirisha Hamza kuelekea Hospitali moja ya nchini Tanzania inayopatikana Nyanda za Juu Kusini katika mkoa wa Njombe ambayo inamilikiwa na Kanisa la KKKT."


"Mkuu huko si ndiyo inasemekana huyo Jackline ndiyo kwao itakuwa salama kweli?"

Vivian alionesha hofu.


"Vivy acha uoga kwani wewe unayafahamu mazingira yote ya Afrika ya Kusini na Botswana?"

Mackdone alimuuliza swali ambalo lilimfanya Vivian kujiona mjinga.


"Nimekuelewa Mkuu wangu kumbe fanya hivyo kikosi kazi kirejee majukumuni kama zamani, sorry Mkuu naona nahitajika huku ndani."

Vivian alimwambia Mackdone baada ya kumuona Daktari waliyeongozana naye akimpa ishara ya kumwita.


JE NINI KITAKWENDA KUTOKEA?





Jackline na kikosi chake walipambana kuwatafuta Dorice (Nawane Gabathusi) na mpenzi wake ndani ya msitu ule bila mafanikio kiasi cha kushindwa kuendelea, walirudi mpaka walikokuwa wameegesha gari lao.


"Mungu wangu........"

Jackline alitokwa na maneno hayo baada ya kulishuhudia gari lao likiteketea kwa moto.


"Kwa hiyo washenzi hawa bado wako msituni humu humu hawajaondoka."

Jackline aliongea kwa hasira akiyasaga meno yake. Roberto alichukua simu yake na kutafuta namba aliyokuwa akiihitaji na kuipiga.


"Shemeji bado tuko porini huku kuna janga limetupata."

Roberto aliongea baada ya Daktari Abbas kupokea simu.


"Janga gani hilo Roberto?"

Daktari Abbas alimuuliza Roberto baada ya kupokea simu.


"Mateka wetu wametutoroka tumewatafuta mpaka giza hili limeingia tunarudi kwenye gari wamelipiga moto."

Roberto alitoa maelezo.


"Unasemaje?"

Daktari Abbas aliuliza.


"Kama nilivyokueleza hivyo waambie wakina Jasmine na Mahmoud watufuate kwenye msitu huu wa Motsepe."

Roberto alipomaliza kutoa maelezo yake hakusubiria jibu alikata simu na kuwafukuzia wakina Jackline ambao hawakuweza kumsubiri, aliwakuta na kuungana nao. Msitu ulikuwa umetulia sana ilikuwa ni milio ya wadudu waliokuwa wakihangaikia malalo huku giza nalo liliendelea kuchukua nafasi kwa kasi na kuwafanya kutoa simu zao na kuwasha tochi.


"Tunatakiwa tuwahi maana nimewaambia watufuate tusije potezana na giza hili."

Roberto aliwaambia.


"Ni kweli kabisa, jamani ee hebu twende mbele turudi nyuma wenzangu mnaamini hawa mbuzi wameshatoka ndani ya por...."

Kabla Jackline hajamalizia sentensi yake mara waliweza kuiona miale ya taa za gari kwa mbali hiyo ikawapa imani kuwa wamekaribia barabarani.


" Kwamba tumeikaribia barabara? "

Jackline alihamisha mada na kuingia kwenye mada ya barabara.


" Bila shaka lakini nikionacho mimi tunatakiwa kuzima tochi zetu si mnajua mpaka muda huu hatujui adui wetu yuko wapi."

Roberto alitoa pendekezo ambalo liliungwa mkono na wenzake ambapo bila kuchelewa tochi zilizimwa na safari hii walianza kukimbia mdogo mdogo. Lakini wakiwa kwenye mchakamchaka huo mara ilikuja gari kwa kasi na kusimama mbele yao kama mita mia moja hivi hivyo kuwafanya kujificha kwanza.


"Watakuwa wakina Jasmine hao."

Aliongea Roberto huku akitaka kujitokeza barabarani lakini Jackline alimzuia pale chini.


"Subiri kwanza kama ni wenyewe watatujulisha kwa simu."

Jackline alimsihi Roberto asifanye kile alichotaka kukifanya.

Alimsikiliza kisha akatulia pale huku wakiendelea kulifuatilia lile gari ambalo muda huo lilisimama mita hizo kutoka pale walipokuwa ndipo waliposhangaa kuona ni kama kuna watu wanapanda.


" Buuuuushiiiiiiiit........!! Kenge hawa ndiyo wanatoroshwa?"

Jackline alipiga kelele mara baada ya kuwaona watu waliokuwa wanawatafuta wakipanda kwenye lile gari ndipo akaona ajaribu bahati yake kwa kuichomoa bastola yake na kulifyatulia risasi lile gari huku wakiinuka na kuanza kulifukuzia. Hakuna walichoambulia kwani gari lile liliondoka kasi na kuwaacha kwenye mduao usio na kipimo.


"Huyu binti tunatakiwa tumpate kwa namna yoyote ile vinginevyo itatuletea shida kwani kwa maelezo yake ni kwamba wameshatuzunguka wanasubiri muda ufike wafanye yao."

Jackline aliongea huku akiwa kashika kiuno akilifuatilia lile gari ambalo lilikuwa likipotea mbele ya macho yao.


"Hebu ngoja kwanza."

Jackline aliongea huku akiichukua simu yake na kuanza kutafuta namba ambayo aliipiga.


"Mdogo wangu Shamimu najua mitihani mmeanza ratiba ikoje kama kuna nafasi ndani ya wiki hii jitahidi uje mara moja uwachukue wakina Natalie ukae nao huko huko Urusi."

Jackline aliongea hayo kwenye simu baada ya Shamimu kupokea.


"Dada naona nina nafasi ya siku mbili tu ndani ya wiki hii ambazo ni Jumamosi na Jumapili hivyo nilikuwa nashauri kuwa wakina Natalie wasafirishwe mpaka Gaborone Botswana hapo watasafiri kwa ndege ya 'Gaborone Finest Airline' ambayo wana huduma ya kusafirisha watoto kwa uangalizi wa hali ya juu sana, sijui unalionaje hilo."

Shamimu alimjibu dada yake.


" Okay ngoja tufanye mchakato wa kuwaandaa maana leo si Ijumaa walau Jumapili wawe wamefika huko kwani usalama wao ni mdogo na pia nina mashaka na njia ya kuelekea Botswana lakini nitaivuka tu mdogo wangu usijali."

Jackline alimwambia Shamimu kuonesha kuwa kakubaliana naye.


" Basi dada yangu nikutakie usiku mwema."

Shamimu aliagana na dada yake kisha akampigia mume wake ili kulijadili hili suala la watoto wao kutokana na hofu waliyonayo ya kuwapeleka Australia ambako wanahisi wanaweza kuwatoa sadaka kwa Bi Elizabeth.


"Nimeongea na Shamimu kuwa aandae mazingira kule Urusi ya kuishi na wakina Natalie kwa kipindi hiki au hata siku mbili wakati tunaangalia shule nzuri ya kuwapeleka pale pale Urusi."

Jackline alimfafanulia mume wake.


"Hakuna shida kwa hiyo tutawasafirishaje mpaka wafike huko au utaongozana nao?"

Daktari Abbas alimuuliza.


"Hapana wewe kwa kuongozana na Mahmoud utawasindikiza mpaka Gaborone Botswana lakini kwa magari tofauti."

Jackline alimjibu.


"Hakuna tatizo katika hilo mke wangu nitafanya kwa mapenzi yangu kwa wanangu sitaki wapatwe na tatizo lolote na ikiwezekana tutaianza safari kesho. Mko sehemu gani muda huu maana wakina Jasmine wameondoka muda mrefu."


"Okay basi ngoja nimpigie maana mpaka sasa hawajafika."

Jackline aliongea hilo na kukata simu ya mume wake na kuitafuta namba ya Jasmine.


"Mmekwama wapi?"

Jackline alimuuliza Jasmine.


"Tumefika kwenye huu msitu lakini tumeshindwa tuelekee wapi nikajaribu kukutafuta namba ilikuwa bize."

Jasmine alimjibu.


"Okay sisi tuko barabarani kabisa uelekeo wa mashariki ambako mtaliona daraja kabla ya kulifikia mtatuona."

Jackline alitoa maelekezo ya kuwafikisha mahali walipo ambapo muda huo giza lilikuwa ni totoro hakuna kiumbe aliyekuwa akipiga kelele kulikuwa kimyaa sana na baada ya dakika kadhaa waliona mwanga kutokea magharibi wakajua ni wenyewe hivyo wakajiandaa. Na kweli lile gari lilikuja taratibu sehemu hiyo na hivyo kumfanya Jackline kuipiga namba ya Jasmine ili kujua kama ni wenyewe.


"Mmefika."

Jackline aliongea baada ya Jasmine kuipokea simu na Jackline kuuona mwanga wa simu ndani ya gari. Walijitokeza mbele ya gari na kuanza kulifuata na baada ya kusimama walijongea mpaka pale na kuwakuta wakina Jasmine wakishuka.


"Poleni sana ndugu zangu msijutie kumpoteza adui yetu shukuruni Mungu mmepona na pia mmepata nafasi ya kumfahamu adui vizuri."

Jasmine aliwaambia wakina Jackline ambao walikuwa wamepoa siyo kawaida yao kwa mpango wanaoupanga kushindwa.


"Ni kweli kabisa Jasmine na kupitia pori hili ndiyo nimegundua kuwa adui yetu ana nguvu kuliko sisi, hebu njooni huku tuongee kwanza."

Jackline alimjibu Jasmine na kuwaita pembeni yeye Jasmine pamoja na Roberto na Mahmoud.


"Tunaianza vita rasmi kwani kulingana na maelezo ya mwanaharamu yule wamejipanga hivyo nilichoamua ni kuwapeleka wanangu Urusi kwa kutumia ndege ya Gaborone inayoondoka usiku pale Botswana kuelekea Urusi."

Jackline aliwaelezea wenzake.


"Kwa kuwa hili eneo limetulia sana tumalize mpango wetu hapa hapa mnaonaje?"

Jasmine alitoa pendekezo ambalo kila mmoja alikubaliana naye.


"Mchakato utakavyokuwa ndugu zangu kesho mume wangu ataondoka na wanangu kuelekea Botswana ambako huko atakwea pipa jioni kuongozana na watoto japo sijamwambia nilichomwambia ni kuwasindikiza mpaka Gaborone ambako wao wataondoka peke yao lakini mchakato wa kuhakikisha naye anaingia kwenye ndege ni wa Mahmoud kumshawishi kwani nawe utaongozana naye akiingia kingi tu utarejea haraka kuungana nasi katika maandalizi ya kuelekea nchini Australia kuhakikisha tunamtia mikononi Bi Elizabeth maana yeye ndiye mwenge wa chezo hili huku nyuma watabaki Thomas na Dalali ambaye nambatiza jina la Dala wao watahakikisha kazi yao ni kutupa kila kinachofanyika na maadui wetu baada ya kupewa maelekezo ya namna ya kuitumia BRAIN HUB."

Jackline alitoa maelezo marefu ambayo kila mmoja alikubaliana nayo.


" Jamani nafanya hii kuwa siri kwa sababu mume wangu ni mbishi sana hivyo nimeona tumtoroke hata wewe Mahmoud hautakiwi kumwambia hiki kwani lengo akifika tu Urusi nitamwambia asiondoke kwanza kwa tahadhari."

Jackline alisisitiza kitu ambacho kila mmoja alikubaliana nacho na kisha waliingia kwenye gari na wataondoka eneo lile kurejea nyumbani. Walifika nyumbani na muda huo ilishakuwa alfajiri tayari hivyo moja kwa moja wakaelekea alikohifadhiwa Bi Aisha na kuanza kumhoji anajua nini kumhusu mume wake. Lakini yeye alieleza kile akijuacho kumhusu mume wake.


"Mume wangu Hamza ninayemfahamu mimi ni mfanyabiashara wa matunda ikiwa ni biashara ambayo kaanza kuifanya hata kabla ya kunioa mimi zaidi ya hapo sifahamu chochote."

Bi Aisha alieleza.


"Na hayo matunda alikuwa akiyafuata wapi maana naambiwa huwa mnayauza jumla na reja reja."

Roberto alimtwanga swali jingine.


"Ni kweli huwa tunayauza jumla na reja reja na alikokuwa akiyachukua ni kutoka vijijini."

Alimjibu.


"Unaweza kutuambia alikuwa anachukua muda gani huko vijijini?"

Jackline alimtupia swali jingine.


"Kiukweli alikuwa akichukua mpaka wiki au wiki mbili kulingana na msimu wenyewe."

Majibu ya Bi Aisha yaliwafanya kubaini kitu hivyo waliitana nje wakina Jackline kujadili kidogo.


"Tunatakiwa kwenda nyumbani kwake tunaweza kubaini kitu kwani hata hiyo biashara ilikuwa ni geresha tu mke wake asijue."

Jackline aliwaambia wenzake.


"Ni kweli tusichukue muda."

Jasmine aliwaambia na hivyo walimchukua Bi Aisha na kuondoka naye kuelekea kwake.

Baada ya kufika waliingia ndani na huko walianza kuipekua nyumba hiyo kwenye kila kona na vyumba.


"Hakuna chumba ambacho ni stoo ambayo mara nyingi alikuwa akiingia yeye tu?"

Mahmoud alichezwa na machale akaona amuulize Bi Aisha.


"Kipo ngoja nikachukue funguo chumbani ili tukifungue."

Aliwajibu na kuingia chumbani kwake ambako alirudisha mlango na kuubana. Huku nje pekua pekua iliendelea kuhakikisha wanapata kitu kinachoweza kuwasaidia. Mahmoud yeye aliitazama saa yake na kubaini ni dakika kumi zimepita toka Bi Aisha aingie chumbani.


"Chumba si ni cha kwake? Hiyo funguo si anaifahamu inapohifadhiwa iweje achukue muda wote huu?"

Mahmoud aliona amfuate akajue kulikoni. Alipofika mlangoni aligonga mlango mara kadhaa lakini haukufunguliwa. Aliita na kuita lakini wapi hivyo akaona awaite wenzake ambapo waliamua kuuvunja mlango.


" Whaaaaaaat.............. "

Mahmoud alitaharuki baada ya kuingia chumbani humo.


UNAFIKIRI WAMEKUTANA NA NINI CHUMBANI HUMO?



Taharuki ya Mahmoud iliwatoa wakina Jackline walikokuwa wakipekua pekua na kumfuata kule chumbani kujua nini kimemshangaza, walipoingia mle chumbani nao walichokutana nacho kiliwaacha midomo wazi huku kila mmoja akimtumbulia macho mwenzake.


"Bi Aishaaaa kwanini sasa?"

Yalikuwa ni maneno ya Jasmine mara baada ya kuuona mwili wa Bi Aisha ukining'inia. Alikuwa ameshajinyonga kwa kutumia mtandio wake ambao aliufunga kwenye mkono wa feni kubwa (panga boi) iliyokuwa mle chumbani kwao.


"Huyu Mackdone si mtu wa kawaida hata kidogo nahisi makampuni anayoyamiliki ni kivuli chake tu lakini yeye ni mtu mwingine hatari sana, hebu angalia namna huyu mwanadada namna ambavyo alikuwa akijieleza si kila mmoja wetu alimuamini?"

Jackline aliwauliza wenzake wakiwa wanauangalia mwili wake pale juu.


" Mpaka sasa nina wasiwasi na usalama wa watu wetu wa karibu."

Roberto aliongea akitoka mle chumbani.


" Hivi unaweza kubaini kwanini Bi Aisha kajinyonga?"

Jasmine alimuuliza Mahmoud ambaye aliishiwa nguvu na kuamua kutulia zake dirishani akiangalia nje huku akivuta sigara na mkono mmoja ukiwa unachezea nywele zake.


"Hakuna kingine huyu naye hakuwa mtu wa kawaida na kuhusu aliyotueleza hakuna lenye ukweli hata moja ukweli kakimbia nao na kutuachia fumbo kubwa ambalo ufumbuzi wake ni kumtafuta mtu aitwaye Mackdone peke yake na si vinginevyo."

Mahmoud alieleza kile alichokihisi kutoka kwenye tukio la Bi Aisha kajinyonga.


" Hatuna cha kusubiri hapa jamani tuondokeni."

Roberto aliwaambia wenzake waliokuwa kama wamepigwa bumbuwazi hawajui wafanye nini.


" Na vipi kuhusu kuushusha mwili wa marehemu?"

Jasmine aliuliza.


"Jasmine acha kujiongezea majukumu yasiyokuhusu si kapanda mwenyewe na hii nyumba si ni ya kwake? Atajua mwenyewe."

Roberto alimjibu Jasmine akitoka nje. Walitoka kwenye ile nyumba na kuuacha mwili wa Bi Aisha ambaye aliamua kupoteza maisha yake kuliko kutoa siri za kundi lao la 'The Shadow' ambalo linaongozwa na mtu hatari sana ambaye huwa akipanga kitu lazima kiwe. Waliingia kwenye gari tayari kwa kuondoka.


"Thadei katuacha."

Ujumbe mfupi uliingia kwenye simu ya Jackline kutoka kwa mume wake Daktari Abbas na baada ya kuusoma Jackline alianza kukuna kichwa huku akitaka kuongea kitu hivi lakini alijizuia na kuongeza spidi ya gari kitendo ambacho kiliwashangaza wenzake.


" Jackline mwendo huo angalia."

Mahmoud alimwambia baada ya kumkosa muendesha pikipiki.


"Niko makini sana wala usihofu mbona hapa nimebeep tu muungwana?"

Jackline alimjibu huku akiendelea kupishanisha miguu pale kutoka kwenye moto na kuhamia kwenye breki huku Roberto yeye akitabasamu kwani Jackline anamfahanu vizuri kwenye upande huo wa kulenga madaraja. Na baada ya muda fulani walikuwa nyumbani, walipoingia ndani ya geti tu Jackline alilipaki gari na kushuka na moja kwa moja aliongoza walikokuwa wakina Thomas.


"Nimeupigania uhai wake lakini haikusaidia kwani mwili wake ulikuwa umeshambuliwa sana na umeme hivyo katuacha."

Daktari Abbas aliwaambia.


"Mume wangu hatuna muda wa kupoteza anza maandalizi naingia ndani kuwaandaa watoto kwa safari."

Daktari Abbas alimuangalia mke wake akataka kuuliza kitu lakini akaona akae tu kimya. Lakini hali ile ilishuhudiwa na Jasmine aliyekuwa karibu yake huku Jackline akiwa keshaondoka kuingia ndani.


" Shemeji, hali si shwari hivi unaweza kuamini kuwa Bi Aisha katukimbia akiwa mikononi mwetu?"


"Kivipi shemeji?"

Daktari Abbas alimuuliza Jasmine huku akivua miwani yake.


"Tumefika pale tukaanza kuipekua nyumba yao huku naye akitupa ushirikiano lakini mara akabadili mawazo na kumdanganya Mahmoud kuwa ngoja akachukue ufunguo si akaruhusiwa, kwani alirejea mapema? Thubutuuu hakutokea kwa wakati mpaka pale ambapo Mahmoud aliposhtukia na kuamua kumfuatilia huko huko chumbani na ndipo alipomkuta akiwa kajinyonga."

Jasmine alimsimulia mkasa mzima.


" Kwanini sasa kachukua uamuzi huo? "

Daktari Abbas alimtupia swali jingine.


" Inavyoonekana wana kiapo kikali kutoka kwenye kundi lao hawako tayari kutoa siri kwa mtu yeyote hivyo wako tayari kupoteza maisha."

Roberto aliingilia kati na kumuelezea kile anachokihisi kutokana na kifo cha Bi Aisha.

Maelezo ya Jasmine na Roberto yalimchanganya Daktari Abbas aingie kwenye dimbwi la mawazo kwani hakujua nini tatizo na kama wanamefikia hatua hiyo ina maana hakuna usalama hata kidogo.


"Mpaka hapo kila tunachokifanya na kukipanga kiko mikononi mwa maadui itakuwaje sasa kwa upande wangu kutokana na jina nililolitengeneza kwa muda mrefu na kufahamika kwa kila kona mpaka kwa watoto wadogo itakuwaje siku ambayo wataiona sura yangu kwenye kurasa za mbele za magazeti? Si itakuwa aibu hii?"

Akiwa kaliegemea gari huku mawazo hayo yakipita kichwani kwake hakuweza kupata jibu la haraka hivyo aliamua kumfuata mke wake ndani alikokuwa akiwaandaa watoto wake.


" Tayari mke wangu? "

Alimuuliza mke wake.


" Ndiyo namalizia kuyafunga mabegi yao."

Jackline alimjibu akiendelea kufunga zipu ya begi moja.


"Mke wangu mabegi yote hayo ya nini kumbuka wanakwenda shule na si kwenye maonesho huko."

Daktari Abbas alimwambia mke wake mara baa ya kuona kawafungashia mabegi matatu ya nguo.


"Hebu niache niwaandae wanangu haijalishi wanakwenda shule au kwenye maonesho ninachotaka ni furaha ya wanangu sitaki wafike huko wakaanze kutaabika bure."

Jackline alimjibu mume wake ambaye hakuendelea kukaa chumbani humo kwa watoto wake akatoka na kuelekea chumbani kwao.


" Lazima nifanye kitu hapa kabla mambo hayajaharibika, eenh ngoja nimcheki kaka yangu Daktari Hans Murray niweze kumuomba msaada wa kiushauri."

Daktari Abbas alikuwa kalala chali pale kitandani akiwaza juu ya yale yanayotokea ambayo yeye hakuyatarajia kwa wakati huo ambao aliamini kila kitu kiko sawa.


" Wapi maeneo kaka yangu?"

Daktari Abbas alimuuliza Daktari Hans baada ya kuipokea simu yake.


"Muda huu niko kazini, umepatwa na nini Abbas kwanini uulize swali ambalo majibu unayajua?"

Daktari Hans alimuuliza baada ya kuona anaulizwa swali ambalo halikuwa na mantiki yoyote.


"Nisamehe kaka yangu siko sawa hata kidogo nakuja sasa hivi kuna kitu nataka unisaidie kaka."

Daktari Abbas alimwambia Daktari Hans ambaye hakuwa na pingamizi.


"Okay sawa utanikuta."

Daktari Hans alimjibu.

Na kweli Abbas aliinuka koti mkononi akatoka na kuelekea Makambi Hospital kukutana na Daktari Hans.


"Wapi sasa mume wangu muda huu wakati unatakiwa uianze saa? Umetazama saa kweli?"

Swali lile lilimfanya Daktari Abbas kuigeuza saa mkononi na kuiangalia ndipo aliposhangaa baada kuona ni saa tano na anatakiwa awe Gaborone ifikapo saa kumi na mbili jioni.


"Nisamehe mke wangu sikuangalia muda nikajua bado sana kumbe nilidanganywa na hili jua ambalo linawaka kama vile bado mapema sana."

Daktari Abbas alijiona mjinga mbele ya mke wake na hivyo akamshika mkono na kurejea ndani ambako maandalizi ya mwisho mwisho yalifanyika kisha walitoka na kupakia mabegi kwenye gari.


" Mahmoud uko tayari kwa safari?"

Jackline alimuuliza Mahmoud.


" Madam kama unionavyo niko tayari kila saa na kila dakika."

Mahmoud alimjibu.


"Usisahau tulichoongea jana kule msituni ni muhimu sana."

Jasmine alimkumbusha Mahmoud.


"Siwezi kusahau hata kidogo....."

Kabla hajamaliza alikatishwa na sauti ya Daktari Abbas.


"Tunaweza kuondoka sasa kamanda wangu Mahmoud."


"Bila shaka Bosi."

Mahmoud alimjibu Daktari Abbas na kisha alimfuata na kumpokea briefcase na kuiweka kwenye siti mbele akageuka kumruhusu aweze kuingia kwenye gari.


"Mahmoud hiyo briefcase kaa nayo huko nyuma na huku mbele wakae wanangu bwana."

Daktari Abbas hakuwa tayari kukaa mbali na watoto wake.


"Bila tatizo mkuu limepita hilo."

Mahmoud alimjibu huku akiitoa briefcase na kuihamishia siti ya nyuma kuwapisha Nathan na Natalie.


"Bye byeee mama tutakukumbuka sana."

Nathan alimwambia mama yake huku akimkumbatia na wakati huo ndugu yake Natalie alikuwa akilia tu kwani hakutaka kutengana na mama yake kabisa.


"Wanangu nitawakumbuka sana lakini nawaahidi kuwa ndani ya siku chache tutakutana huko huko kuna vitu vichache ninavikamilisha."

Jackline aliongea huku akibubujikwa machozi.


"Acha kuwapa uchuro watoto unalia nini sasa?"

Jasmine alikuja akamuondoa Jackline na kumpeleka kando kidogo baada ya kuona kuwang'ang'ania kisha Roberto aliwapandisha kwenye gari kisha liliondoka na kuwaacha kama vile wanaomboleza msiba.


"Huo mwili wa Thadei hakikisheni mnaupeleka sehemu ambayo hamtaonwa na mtu kisha mtautupa huko."

Ulikuwa ni ujumbe ambao Daktari Abbas aliutuma kwa Roberto. Baada ya Roberto kuusoma aliwapa ishara wakina Thomas na kumuacha Jasmine akimpeleka Jackline ndani kwani alikuwa akiendelea kulia.


" Sasa sijui itakuwaje kwa waajiri wake? "

Roberto alijiuliza wakiwa wanautoa ndani mwili wake Thadei na kuuingiza kwenye gari.


"Kaka mimi nina wazo kama litafaa tulifanyie kazi."

Aliongea Dala.


"Lipi hilo Dala?"

Thomas aliuliza.


"Tumchukue na kwenda kumtelekeza mtaani huko ambako kutakuwa hakuna watu wanaotutazama kisha tutatoa taarifa kwenye kampuni yake."

Dala alitoa wazo lake ambalo kila mmoja pale alikubaliana nalo hivyo waliingia kwenye gari na kuondoka zao kuelekea mtaani, hawakwenda mbali sana walipofika kama mtaa wa nne hivi walipunguza mwendo kisha wakausukumia nje mwili wa marehemu Thadei kisha wakaondoka kasi kusonga mbele kabla hawajaonwa.


"Kweli wewe ni dalali nimekuaminia maana naambiwaga kuwa Madalali ni waongo sana sasa namshangaa dalali wetu aliyeasi kazi yake namna alivyokuwa na plani za kazi."

Roberto aliongea huku akigonga baada ya kufanikiwa kuutupa mwili wa Thadei pasipo kuonwa na mtu yeyote yule.


" Ukitaka kunukia vizuri unatakiwa kukaa karibu na manukato hata kama hujajipulizia utanukia tu na hata mimi kukaa tu kidogo na ninyi nimeanza kujiona Komandoo John."

Maneno ya Dala kama alivyobatizwa kwa kulikatisha jina la Dalali kwani hawakutaka utambulisho wake upotee yaliwachekesha sana mle ndani ya gari kiasi kwamba ilibidi Roberto asimamishe gari kuhofia ajali.


" Mbona mmeondoka bila taarifa yoyote ile? Mmeelekea wapi na mwili wa marehemu Thadei?"

Ulikuwa ni ujumbe wa Jasmine na baada ya Roberto kuusoma alimpigia.


"Wala hakuna haja ya kuwa na mashaka yoyote yale tumemtupa mtaani na hivi ndiyo nataka niwapigie waajiri wake kuwajulisha kuwa mtu wao katoweka lindoni bila taarifa."

Roberto alimjulisha Jasmine baada ya kupokea simu.


"Okay vizuri sana Roberto hilo ni bonge la plani aisee."

Jasmine alimjibu kisha akakata simu. Lakini wakati anaiweka simu mfukoni kuna gari lilikuwa linakuja taratibu nyuma yao na baada ya kuliona akalitilia mashaka kidogo ikabidi Roberto aongeze mwendo alitimua vumbi hilo kutokana na barabara ambayo waliipita lakini alipoangalia kwenye site mirror' yake aliliona lile gari nalo likiwa limechanganya vile vile. Hofu ikamuingia ikabidi akunje kuingia barabara ya pembeni ili aone kama itawafuata na huko.


"Ni nani huyu mbona anatufuatilia tu mpaka huku?"

Roberto aliuliza baada ya kuona limewafuata mpaka kule walikoingia.


NI NANI HUYO ANAYEWAFUATILIA?


DAKTARI ABBAS ATAFANIKIWA SAFARI YAKE?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.





Baada ya kuona lile gari limeendelea kuwafuatilia mpaka nje ya barabara waliamua kujiandaa kukabiliana na walio kwenye gari hilo na kutokana na kile walichokifanya muda mfupi uliopita cha kuutelekeza mwili wa mlinzi Thadei aliyekufa muda mfupi uliopita kutokana na majeraha ya shoti ya umeme. Walitulia ili kuona ni nani hao kutoka kwenye hilo gari hivyo hawakutoka ndani ya gari.


"Watakuwa wakina nani hawa? Naona nao wamesimama nyuma yetu."

Thomas aliongea wakati akiishuhudia ile gari ikisimama.


"Hebu tusubiri tuone maana kuendelea kuwakimbia haina maana cha kufanya kila mmoja ajiandae kwa lolote linalokwenda kutokea muda huu."

Roberto aliwaambia wenzake huku akiikagua bastola yake pamoja na kisu chake ambacho huwa hakiachi popote anapokuwa. Wakiwa pale mara walimuona mmoja wa watu waliokuwa ndani ya gari lile akishuka na kuwafuata.


" Mmh ni nani huyu?"

Roberto aliuliza swali huku akimuangalia kupitia site mirror' na alipomuangalia vizuri mkononi aliweza kuiona bastola hivyo akabaini hakuna usalama.


"Jiandaeni kwa mpambano lakini ninyi mtasalia humu garini na mimi nakwenda kumkabili msifanye lolote mpaka mtakapoona nalivua koti haraka mtakuja kwa mpambano, nimeeleweka?"

Roberto aliwaelekeza wakina Thomas ambao hawakuwahi kukutana na changamoto kama hiyo kwenye maisha yao. Kisha alishuka bastola ikiwa kwenye koti lake.


" Hapo hapo usisogeze hatua yako mbele tofauti na hapo utakuwa haki yangu."

Mtu huyo alimtahadharisha Roberto kutofanya lolote, akasimama na kumsubiri mtu huyo afanye kile alichokuwa kapanga kukifanya kwake. Mtu yule ambaye hakufahamika jina lake alimsogelea Roberto.


" Mikono juu kijana na wala usifanye chochote cha kunitia wazimu."

Aliendelea kumtisha Roberto huku akimsogelea na alipomkaribia alianza kumkagua mifukoni lakini alipoupeleka mkono kwenye mfuko wa koti uliokuwa na bastola Roberto alimpiga kiwiko cha kichwa na kabla mtu yule hajafanya chochote Roberto alikwenda hewani na kumtandika teke la mbavu lililompeleka chini mtu yule huku bastola yake ikiruka hatua kadhaa pembeni ambayo aliifuata huku akiwa kamnyooshea bastola mtu yule pale chini. Aliifikia na kuichukua na wakati anamrudia ndipo alipoisikia sauti kutoka nyuma yake.


"Kijana unaonekana ni mbobezi kwenye shughuli kama hizi siyo? Ukifanya kingine juu ya mtu huyo nakusambaratisha." Aliongea hayo mtu huyo aliyekuwa kwenye gari na kuja baada ya kumshuhudia mwenzake akishughulikiwa.

Roberto akiwa pale chini amemuinamia mtu yule alipotaka kumnyanyua juu aliweza kumuona mtu huyo naona alivyosimama hivyo haraka sana alimvuta mtu yule na kumuweka mbele yake kama kinga huku akiwa kamuelekezea kichwani bastola.

"Nadhani unanielewa sasa, chagua moja kuweka chini hiyo bastola yako au nimsambaratishe huyu kijana wako pamoja na wewe."

Roberto alimtishia yule mtu ambaye alikuwa kamshikia bastola ambayo aliamua kuiweka chini kisha akainua mikono juu.


"Kwa kutumia mguu wako ipige teke hiyo bastola ije kwangu."

Roberto alimwambia yule mtu.

Na bila kupinga aliweza kuipiga teke ile bastola yake na kumfanya Roberto kuwapa ishara wakina Thomas wakashuka na kuja kuichukua ile bastola.


"Sogea mbele hatua kumi kisha piga magoti yako."

Roberto alimuamrisha.

Baada ya kusogea hatua hizo alipiga magoti ambapo Roberto alimsukumizia mwenzake aliyekuwa kamshikilia.


"Mnaweza kueleza shida yenu sasa."

Roberto aliwapa fursa watu hao kueleza kilichowafanya wawafukuzie mpaka eneo hilo.


"Naitwa Daktari Hans Murray ni Mkurugenzi Mkuu na Mmiliki wa Hospitali ya Makambi hapa Windhoek. Mtanisamehe kama nimekosea lakini nilikuwa nikiwafukuzia mara baada ya kupita pale njiapanda ya kuelekea Hospitalini kwangu na kuwaona watu tofauti na ninayemfahamu mwenye hii gari. Na mbaya zaidi hapatikani kwenye simu yake toka nilipowasiliana naye masaa mawili yaliyopita."

Daktari Hans alijitambulisha na kueleza kile ambacho kilimsukuma kuwafukuzia. Utambulisho wa Daktari Hans ukamfanya Roberto kumkumbuka japo ni miaka zaidi ya mitano toka walipokutana lakini sura yake ni ile ile na aliweza kuifahamu zaidi mara baada ya Daktari Hans kuvua kofia yake.


"Oohh sorry Daktari nakuomba uinuke hapo chini pamoja na huyo mtu wako mimi naitwa Roberto ni familia ya Jackline Joachim nafikiri umenikumbuka?"

Roberto alijitambulisha na kuomba radhi kwa kilichotokea.


"Roberto yupi yule aliyekuwa kundi moja na wakina Jackline na Jasmine kipindi kile mnapambana na Nafiwe?"

Daktari Hans aliuliza kwa kuvuta picha ya nyuma.


"Ndiyo mimi Daktari, naomba unisamehe kwa kilichotokea."

Roberto aliomba msamaha tena huku wakisaidiana kumpandisha kwenye gari la Daktari Hans mtu yule aliyekuwa na Daktari alimshambulia.


"Wala msijali hii ni kawaida kwa mtu aliye kamili katika kujihami na adui."

Daktari Hans alimjibu Roberto ambaye alitoa bastola zile na kumkabidhi Daktari kisha akamvuta pembeni.


"Rafiki yako kaelekea Gaborone kuiwahi ndege ya jioni inayoelekea Urusi."

Roberto alimwambia.


"Urusi? Kufanya nini? Mbona hajanieleza."

Daktari Hans alishangaa kuisikia taarifa hiyo.


"Bila shaka ni kutokana na kuchanganyikiwa kwani masaa hayo hayo mawili yaliyopita mke wake Jackline alipokea ujumbe kutoka kwa watu wasiojulikana kuwa wajiandae kupokea taarifa mbaya kutoka kwa watu wa karibu wanaowapenda, hivyo hapo hapo ikawa kama vile wametandikwa risasi ya hofu ndiyo wakafanya mawasiliano na mdogo wa Jackline anayesoma huko Urusi afanye maandalizi ya kuwapokea watoto pamoja na shemeji huku sisi tukisalia kujibu shambulizi lolote kutoka kwa watu hao na ndiyo maana tulipoliona gari lenu tukajua ni wenyewe tusamehe Daktari unaweza kuongozana nasi maana Jackline analia tu baada ya watoto wake kuondoka."

Roberto alimaliza kuelezea.


" Poleni sana Roberto hiki kitu nilikitarajia sana hasa baada ya Bi Elizabeth kutowapenda wakina Jasmine toka wafike kwake na kupelekea familia yake kuuawa da poleni sana nitakuja baadaye kwa sasa nina kikao na bodi ya Wakurugenzi wa Hospitali yangu."

Daktari Hans aliwaambia huku akipeana mikono ya kutakiana heri kisha waliachana na kila mmoja kuingia kwenye gari lake.


" Ni nani yule kaka? "

Thomas aliuliza wakiwa wanaribia nyumbani.


" Anaitwa Hans Murray ni rafiki mkubwa wa Abbas Mukesh na wote ni madaktari na wamiliki wa Hospitali na kitendo cha kutufukuzia walijua tumeliiba gari la rafiki yake."

Roberto alimjibu Thomas.


" Aisee basi wanapendana sana angekuwa mwingine angejali?"

Thomas aliuliza tena.


" Kwenye Ulimwengu huu ninaoufahamu mimi? Labda mwingine."

Roberto alimjibu huku akilipaki gari.

Baada ya kupaki walishuka na kuingia ndani.


" Mbona mmechukua muda mrefu kiasi hicho? "

Jackline aliwauliza walipoingia na kuketi.


" Acha tu, si yakatukuta ya mwanakuli-find' mwanakuli-get'? "

Roberto alimjibu huku akinywa maji yaliyoletwa na Jasmine.


"Kivipi?"

Jackline alitaka kujua zaidi.


"Tukiwa tumeshautupa ule mwili barabarani huko mtaani tukawa tunarudi si ndiyo tukaliona gari likija kasi baada ya kuliona tukaongeza kasi lakini kila tulivyojaribu kuliacha wapi hili hapa ikabidi tuache barabara na kuingia zile za mtaani nako tukafuatwa si ndiyo nikajitoa fahamu na kusimamisha wakajileta kwanini nisimshughulikie aibu yake sasa kumbe ni mtu wa Daktari Hans aliyekuwa kasalia kwenye gari bwana walihisi tumeiba gari lakini tumeyamaliza kisha tukaachana nao ila kaahidi kuja kukuona baadaye."

Roberto alieleza kwa kirefu.


" Aisee poleni sana kwa hilo."

Jackline aliwapa pole.


"Poleni sana jamani kikubwa hakukuwa na baya watu wangu."

Jasmine aliwapa pole kisha akawakaribisha mezani kwa chakula kabla hawajaiendea meza kwa ajili ya kuchora ramani ya kazi.


sultanuwezo.com:

***


Baada ya Oparesheni iliyochukua masaa takribani kumi hatimaye ulikamilika na kisha Bi Elizabeth alihamishiwa kwenye chumba maalum ambacho kilikuwa na uangalizi mkali wa madaktari wakishirikiana na Vivian, hakuna aliyeruhusiwa kuukaribia mlango wa chumba hicho bila kuwa na kibali kutoka kwa wahusika.


"Nini kinaendelea hapo?"

Mackdone alimuuliza Vivian baada ya kupokea simu yake.


"Oparesheni imekamilika na hivi ninavyoongea na wewe ameshaingizwa kwenye chumba maalum kama ambavyo uliomba Mkuu."

Vivian alimjulisha Mackdone.


"Vizuri sana Vivy, kinachotakiwa kuzingatiwa kwa sasa asiruhusiwe mtu yeyote ambaye si mhusika wa hapo kuingia kumuona Bi Elizabeth."

Mackdone alikazia maagizo yake ya awali.


"Kama ulivyoagiza Bosi hakuna kukiukwa labda ningeomba kuongezewa ulinzi walau tuwe wanne hivi."

Vivian aliomba kuongezewa ulinzi pale Hospitali.


"Kuhusu hilo ondoa shaka kabisa na mimi nilikuwa nalifikiria na kwa kuwa umepita kwenye wazo langu maana yake ni muhimu ngoja niwasiliane Daktari Leon tujue anatusaidiaje maana yeye anafahamiana na madaktari wa huko."


"Sawa Bosi nimekuelewa ngoja na mimi nimpange Daktari mmoja ambaye kaingia kwenye anga zangu."

Vivian alimjibu Bosi wake.


"Na wewe umeanza mambo yako!! Fanya yote lakini kazi kwanza tofauti na hapo unanifahamu."

Mackdone alimjibu na kumkumbusha kilichompeleka kule Australia ni nini kisha alikata simu na kumuacha Vivian akilitafakari neno la mwisho.


"Bosi mimi ni binadamu na ukiondoa yote hayo ni binti mrembo ambaye kuna vitu vya msingi ninavyovihitaji hasa mapenzi. Nakuahidi kuifanya kazi yako vizuri."

Vivian alijisemesha mwenyewe pale nje ya Hospitali. Lakini akiwa pale nje akiiweka simu yake mfukoni mara aliliona gari fulani hivi jeusi aina ya Buno Race ambalo lilisimama kwa muda mita chache kutoka alipokuwa na alipogeuka kuliangalia liliondoka kasi.


"Amaa kulikoni tena? Mbona lilisimama na limeondoka kwa kasi hiyo?"

Vivian alijiuliza juu ya gari hilo ambalo lilitokomea kusikojulikana.

Haraka sana alikimbia kuingia kule alikolazwa Bi Elizabeth kujua kama kuna usalama. Na baada ya kufika alikutana na Muuguzi akiwa na kifuko cha nylon kisha akamkabidhi Vivian.


" Dada Vivian mzigo wako huu nimekabidhiwa na dada mmoja ambaye kafika hapa na kudai wewe ni rafiki yake."

Muuguzi huyo alimjulisha Vivian na kumkabidhi kifuko hicho.


"Kasema ni rafiki yangu? Wa wapi?"

Vivian aliuliza huku akiondoka sehemu hiyo kujitenga na yule Muuguzi huku akikifungua kile kimfuko.


"Whaaaaaaat.....!!!!"

Vivian alipigwa na butwaa mara baada ya kukutana na risasi moja iliyofungwa vizuri kwenye kitambaa cheupe chenye tone la damu huku kukiwa na ujumbe uliomduwaza.


"MIMI NI RAFIKI YAKO VIVIAN JE UNGEPENDA KUNIJUA? WALA USIHOFU NITAKUJA HIVI KARIBUNI KIKUBWA NITUNZIE HUO MZIGO WANGU."

Ujumbe huo ulimpandisha joto na kujikuta akitoa kitambaa mfukoni na kujifuta jasho ambalo liliuvamia uso wake.


"Hii ina maana gani? Na huyu ni nani aliyenitumia hiki kifuko chenye risasi?"

Vivian alijiuliza maswali ambayo hakuyapatia jibu ikabidi achukue simu na kumpigia Mackdone.


"Kuna jipya Vivy?"

Mackdone alimuuliza baada ya kuipokea simu yake.


"Naweza kusema ndiyo."

Vivian alimjibu.


"Niambie fundi wangu."

Mackdone alimtaka amueleze.


"Kuna kitu kigeni kimenipata hapa Bosi."

Vivian alianza kumuelezea.


"Kitu gani hicho?"


"Wakati nimetoka kuongea na wewe kuna gari jeusi lilikuwa limesimama likinifuatilia na nilipogeuka liliondoka kasi nikahisi kitu ikabidi nirudi ndani haraka ile nafika nikakutana na mhudumu aliyekuwa na kifuko cha nylon na akanikabidhi na kunijulisha kuwa kapewa na binti mmoja aliyejitambulisha kama ni rafiki yangu. Ikabidi nikifungue kifuko hicho Bosi wangu nilichokutana nacho humo ni risasi moja iliyofungwa kwenye kitambaa cheupe chenye tone la damu huku kukiwa na ujumbe uliosema kuwa nikitaka kumjua nisijali atakuja muda wowote kikubwa nimtunzie zawadi aliyoniachia."

Vivian alimweleza Bosi wake.


"Zawadi ya risasi? Ina maana wameng'amua ulipo?"

Mackdone aliuliza swali hilo na kuondoka hewani na kumuacha Vivian akiwa kashikiria simu yake akihisi labda atarudi hewani tena.


JE NI NINI KINAKWENDA KUTOKEA HUKO?




Baada ya kutoka hewani Mackdone alitafakari kwa muda juu ya huyo mtu aliyeiacha kifuko chenye ishara ya hatari kwa Vivian. Aliipitia taarifa ya awali ambayo ilionesha kundi la Jackline bado liko Afrika hivyo kuwahusisha na tukio hilo ilikuwa ni ngumu sana. Mackdone aliwaza sana lakini aliamua kubonyeza vitufe vya simu yake.


"Uko wapi pepe wangu Nawane?"

Ulikuwa ni ujumbe alioutuma kwa Nawane Gabathusi ambaye anajulikana kwa jina feki la Dorice.


"Mida hii niko mitaa ya Millbrook hapa hapa Windhoek."

Nawane alimjibu Mackdone.


"Una hatari wewe yaani pamoja na kilichokukuta bado uko ndani ya Windhoek? Mimi nilijua uko maeneo ya Gaborone?"

Mackdone alimuuliza Nawane.


"Wamenitia wazimu hawa mijusi hivyo nimeamua kupiga kambi hapa hapa na nina uhakika hawawezi kujua lolote kunihusu kwa sasa."

Nawane alimjibu Bosi wake kwa kujiamini.


"Na yule chizi wako vipi?"


"Niko naye japo alitaka kunikimbia lakini nikawa nimeiona hiyo nilichokifanya Bosi nimeamua kumpa mafunzo ya kujiamini na kwa sasa anaenda vizuri."

Nawane alimpa Mkuu majibu ya kutia moyo.


"Nafurahi kusikia hivyo pepe langu, sasa kuna tatizo kwa Vivian kule Australia."

Mackdone alimueleza Nawane juu ya kilichotokea pale Hospitali masaa machache yaliyopita.


"Tatizo gani hilo Bosi?"

Nawane alimuuliza Mackdone.


"Kuna mtu kajitokeza pale Hospitali ameweka tishio baada ya kumuachia kifuko chenye risasi moja iliyofungwa kwa kitambaa cheupe chenye tone la damu na inavyoonekana mtu huyu anamfahamu vizuri Vivian kwani kwenye kile kikaratasi kamtaja jina kabisa."

Mackdone alimweleza Nawane kwa kirefu.


" Atakuwa ni nani huyo aliyefanya hivyo? "

Nawane aliuliza.


" Ndicho ninachojiuliza na mimi kwani ninyi wenyewe mliniambia kuwa hakuna yeyote ambaye amesafiri kutoka nje ya nchi sasa iweje? "

Mackdone alimuuliza Nawane ambaye alichanganyikiwa baada ya kuisikia taarifa hii.


"Bosi nipe muda nilifuatilie hili nitakujulisha."

Nawane aliona amuage Bosi wake kwa staili hiyo.


"Fanya Nawane si unajua nitakachowafanya ikiwa Bi Elizabeth atapata tatizo lolote?"

Mackdone alimuuliza.


"Najua mkuu wacha nianze kazi yangu."

Nawane alimjibu na kukata simu.

Mackdone aliiweka simu mfukoni akaingia kwenye gari na kuelekea sehemu moja maarufu sana kwa vinywaji vikali ndani ya mji wa Pretoria ijulikanayo kama 'SAFAYA POINT' ambalo limekuwa maarufu sana kutokana na kukusanya watu wengi kutoka pande mbalimbali ndani na nje ya Botswana.


"Mrembo habari yako?"

Mackdone alimsabahi mhudumu aliyefika mezani kwake kutaka kujua mteja wake anahitaji kinywaji gani aweze kumhudumia.


"Nzuri kaka, shikamoo!"

Mhudumu yule alimsalimu.


"Shikamoo ndiyo mtaa gani bwana unakuwa kama vile siyo mtoto wa kileo? Mimi niko poa na ndiyo maana niko hapa muda huu."

Alimjibu huku akiupeleka mkono wake kwenye kifua cha mhudumu huyo ambaye hakufurahishwa na kitendo hicho akautoa mkono wa Mackdone.


"Kaka samahani naomba nikuhudumie."

Mhudumu huyo alimwambia.


"Sasa unawaka nini huduma ninayoitaka si ndiyo hiyo?"

Mackdone alimfokea yule mhudumu kama vile alichokifanya kilikuwa sahihi.


"Huduma gani unayoitaka hapa?"

Mhudumu huyo alimuuliza.


"Nahitaji ninachokiona mbele ya macho yangu kilicho mbali ya macho yangu hicho ni haramu."

Mackdone alimjibu huku akiitoa sigara yake mfukoni na kuiwasha. Kauli ile ilimfanya mhudumu yule kutoa msonyo mkali na kuondoka zake.


"Hee Mrembo wewee mbona hufanani na hiyo tabia ya kuwapiga mabusu bubu wanaume si ungesogea karibu unipe romantic kiss? Hebu mcheki na lile tege lake hovyoo."

Aliongea hayo huku akiusindikiza kwa macho ule moshi alioupuliza hewani.


"Halafu kanaongea ongea tu utumbo wake hakajui kanajibishana na nani we kaache nitakabadilishia jina sasa hivi."

Mackdone aliendelea kuongea peke yake huku akiwatazama watu waliokuwa meza za jirani yake wakiendeleza furaha zao,baada ya kuwaangalia kwa muda alicheka sana kiasi cha kuwafanya waliokuwa karibu kugeuka kumtazama kitu ambacho yeye hakujali.


" Vipi mmevutiwa na burudani yangu ee si na ninyi mna burudani yenu? Waafrika bwana vitu vidogo tu mnataka kuvunja shingo je ningefanya yangu hapa mngefanyaje si mngezimia hapa."

Aliongea hayo na kutoa simu yake ambayo ilitoa mlio wa ujumbe kuingia.


" Bosi tuliingia kitambo nchini Tanzania na muda huu tuko katika mkoa wa Njombe sehemu moja inayofahamika kama Wanging'ombe na kwa mujibu wa wenyeji tulioongea nao hapa barabarani wanasema tuna masaa yapatayo sita mpaka kufika Hospitali ya St. Consolata Ikonda. Hivyo tunaomba msaada wa hela kidogo kwani Taxi ambayo tumeichukua tulikubaliana itufikishe Njombe mjini."

Baada ya kuusoma ujumbe huo Mackdone aliangalia huku na kule kisha akainuka na kutoka mpaka kwenye gari lake na kumpigia kijana wake aliyemtumia ujumbe.


" Ndiyo Bosi. "

Kijana huyo aliongea baada ya kuipokea simu ya Mackdone.


" Kwa hiyo kutoka Songwe Airport mpaka Njombe kawaambia mumpatie kiasi gani?"

Mackdone aliuliza.


"Katuambia dola mia tatu."

Alimjibu.


"Hebu mpatie simu huyo taxi driver' niongee naye mwenyewe maana ninyi naona kama ugeni unawazuzua hivi."


"Sawa Bosi, suka ongea na mkurugenzi wetu."

Alimjibu na kumpatia simu dereva ambaye alikuwa bize na usukani huku masikioni akiwa katupia earphones akiliwazwa na muziki baada ya wateja wake kumgomea kuachia muziki wa kwenye gari wakidai mgonjwa wao haitaji makelele yoyote hivyo akaona isiwe kesi akachukua earphones zake na kuendeleza burudani.


"Ndiyo kiongozi nakusikiliza."

Dereva alianza mara baada ya kukabidhiwa simu.


"Dola mia tatu mbona nyingi sana kijana wangu?"

Mackdone alimuuliza dereva Taxi juu ya kiwango alichowawekea vijana wake.


"Kwani wewe ulitaka kiasi gani? Unaifahamu bei ya mafuta? Na vipi kuhusu umbali kati ya Mbeya na Njombe?"

Badala ya kumjibu swali yeye alimtupia maswali mfululizo ambayo yalimuacha mdomo wazi bwana Mackdone.


"Ebwana ee kumbe ni kweli kile ambacho nilikisikia?"

Mackdone alishangaa.


"Kuhusu nini kiongozi mbona unanichanganya."

Dereva huyo aliendelea kumtupia maswali.


"Niliambiwa kuwa watanzania wanautambulisho wao ambao ni tofauti na Taifa jingine lolote kuwa ukimuuliza swali tu unakuwa kama vile umetupia unjiti wenye moto kwenye tanki la petroli kwani badala ya kujibu swali aliloulizwa yeye atakurudishia maswali mfululizo ambayo usipokuwa makini nayo utashindwa kujua uanzie wapi kujibu."

Mackdone ilibidi aanze kutoa simulizi.


" Kiongozi kumbuka naendesha gari na nina mgonjwa wako humu hivyo ni bora ukienda kwenye pointi yako moja kwa moja."

Dereva Taxi huyo ambaye hakuwa tayari kuendelea kusikiliza ngonjera za Mackdone aliona amkatishe.


"Sasa tufanye hivi dereva, nitakupa kiasi cha dola elfu moja ambazo zitakuwa ni gharama za awali za kuikodi taxi kwa kipindi chote cha matibabu ya mgonjwa wetu nikimaanisha kuwa gari lako litatumika kwa shughuli za hapa na pale kwa kipindi hicho."

Mackdone aliona amuoneshe kuwa yeye ni nani kwa vitendo kitu ambacho kilimshangaza sana dereva huyo kwani kilikuwa ni kiwango kikubwa sana kukishika kwa wakati huo kwani yeye alihisi hiyo dola mia tatu kawapiga kumbe alijidanganya mwenyewe.


" Nimekuelewa mkuu hilo limepita sina tatizo niamini katika hilo na bila shaka vijana wako watafurahia safari hii kwani nitawapeleka popote pale."

Dereva Taxi alichanganyikiwa na kujikuta akiongea vitu ambavyo havieleweki kwani alisema atawapeleka popote sijui kwa gharama za nani? Hatujui.


" Vizuri mpatie simu Henry. "

Mackdone aliona amkatishe na kumtaka amkabidhi simu kijana wake Henry.


" Huyo keshaingia kwenye hamsini zetu niachieni mimi kikubwa endeleeni kuyasoma mazingira tu kitakachofuata nitawaelekeza si gari liko vizuri?"

Mackdone ambaye kila siku anaifikiria faida kwa kila anachokifanya alimjulisha Henry mkakati wake japo kwa fumbo.


" Mashine ni bomba mbaya Mkuu inatembea hiyo usipime kwanza ilivyo tu ni kama imenunuliwa leo."

Henry alimjibu Mackdone kiaina ili dereva asishtukie kile ambacho Bosi wake alitaka kukijua.


"Ana wasiwasi na hii mashine? Mwambie mtambo huu ni mpya kabisa una miezi tisa toka umetoka ardhi ya Malkia Elizabeth chezea Toyota Buno XJ 600?"

Dereva Taxi alirukia kujibu baada ya kusikia kama vile wateja wake wana mashaka na usafiri wake ndipo alipousifia bila kujua kama Henry alishaiweka loudspeaker ili Bosi wake asikie mwenyewe namna anavyolinasibu gari lake.


"Henry safari njema mkifika nijulisheni nimemsikia panya huyo muache achekelee dola za Mackdone."

Mackdone alihitimisha na kukata simu na kisha kuiweka simu pembeni na kufunga mkanda na kuondoka zake.


****


"Kama ulivyoagiza kipenzi nimefika na kumkabidhi muuguzi kile kifuko na nikatoka zangu lakini nikiwa naondoka nilimuona huyo mwanamke anayesifika kuwa ni mtata japo sikuuona kwa mtazamo wa mbali alikuwa akiongea na simu."

Titiana alimjulisha Roberto baada ya kufanikisha zoezi ambalo alipewa.


" Vizuri hakukuona? "

Roberto aliuliza.


" Sina uhakika mpenzi kama aliniona lakini hata kama aliniona haitasaidia niko vizuri kwenye kila hatua."

Titiana alimjibu.


" Okay vizuri hata sisi tuko njiani kuelekea Namport ambako tunakwenda kuongeza vitendea kazi tayari kwa safari ya kuelekea Afrika ya Kusini lakini tukipiga kambi kwanza Botswana."

Roberto alimuelekeza mpenzi wake Titiana ambaye tayari yuko Australia kwa kazi maalum.


" Jackline au Jasmine wakiniuliza juu yako? "

Titiana alimuuliza Roberto juu ya wakina Jackline ambao waliwachezea sinema ili waifanye kazi yao kwa ufasaha bila kuingiliwa.


"Kama ambavyo nilikwambia hakuna kilichobadilika mpenzi."

Roberto alikazia kauli yake.


"Roberto hizo simu gani zisizoisha? Ni nani unayeongea naye kwa muda wote huo?"

Jasmine alifika kumfuata Roberto ambaye alikuwa kajisahau kama anasubiriwa yeye ili waianze safari yao.


"Kuna dogo mmoja kule kazini kwangu Brazil alikuwa ananipa taarifa ya kiutendaji kwani niliomba afanye hivyo kila baada ya miezi miwili."

Roberto alimdanganya Jasmine wakiwa njiani kuelekea kwenye gari.


"Nimekumbuka Roberto hivi mgogoro wenu na Titiana mliumaliza?"

Jasmine alimuuliza Roberto.


"Achana naye huyo mjinga siku akiona mashetani yamemuisha atanitafuta mwenyewe kwa sasa sina muda naye."

Roberto alimjibu Jasmine kama vile hawaelewani kabisa na mpenzi wake.


"Haiwezekani hiyo ngoja niongee naye wifi yangu hilo ni pepo Roberto."

Jasmine aliongea huku akitoa simu yake mfukoni na kuanza kuitafuta namba ya Titiana.


"Achana naye kwanza bwana tufanye kazi iliyo mbele yetu."

Roberto alimkataza Jasmine asimpigie Titiana.


"Acha upuuzi huo Roberto kazi gani wakati ndiyo tuko njiani hebu Jasmine mpigie Titi wetu maana hata mimi nimemkumbuka."

Jackline aliungana na Jasmine kutaka kuongea na Titiana ambaye Roberto alitaka wasimpigie lakini undani aliujua mwenyewe na mpenzi wake.


" My wifi huyo niambie."

Jasmine aliongea hayo mara baada ya Titiana kupokea simu.


" Ninalo basi my wifi."

Titiana alimjibu.


"Ndiyo nini kutukaushia wenzako kiasi hicho?"

Jackline alimuuliza wakati simu ikiwa kwenye loudspeaker.


"Naombeni mnisamehe jamani zilikuwa ni hasira tu za mtu mwingine zikajumuishwa na kwenu, naombeni mnisamehe waungwana."

Titiana aliwajibu kwa sauti ya huzuni kama vile kweli kuna ugomvi kati yake na Roberto unaloendelea. Na hilo wakina Jackline waliliamini kwani Roberto wanamjua vizuri akisimamia misimamo yake.


JE NINI KITAENDELEA?




Wakati wanaongea na Titiana macho yalikuwa kwa Roberto ambaye muda huo alikuwa akicheza gemu tu huku earphones zikiwa masikioni akijidai hataki kusikia yaliyokuwa yakiendelea baina yao. Jackline akashindwa kujizuia akaona amchokoze.


"Roberto hebu tuambie kitu kimoja kwanini unamchukia Titiana? Ni kosa lile lile au kuna jambo ambalo hatulifahamu?"

Lakini Roberto kama vile hakusikia chochote aliendelea kutikisa kichwa tu kitu hicho kilimkwaza Jasmine ambaye alizivuta zile earphones.


"Kaka unaboa sana ujue? Kwanini unaulizwa swali hujibu au tunajipendekeza kwenye mahusiano yenu? Acha hizo mambo bwana na kama hauko tayari kuwa naye mwambie tu siyo umetulia eti unasubiri mpaka upigiwe simu hiyo siyo poa kabisa kuwa mwanaume kamili."

Maneno ya Jasmine yalimfanya Roberto aangue kicheko kutokana na vile Jasmine alivyokuwa akiongea kwa sauti ya kibezi wakati hiyo siyo sauti yake.


" Unacheka? Tuko siriazi hapa twambie unaongea naye au hutaki?"

Jackline aliingilia huku akiendelea kulenga madaraja.


"Nitaongea naye wala msijali ndege wa kwangu kwanini nimshikie manati? Muda ukifika mtafurahi wenyewe."

Roberto aliwajibu huku akilizima gemu na kuipiga namba ya Jessica.


"Mzima wewe?"

Jessica alijibu baada ya kupokea simu.


"Mbona kimya hivyo?"

Roberto alimuuliza.


"Hapana Roberto wala siyo hivyo nilikuwa bize kidogo na mitihani kwa sasa nimemaliza kuna vitu vichache nakamilisha hapa chuoni kisha ndani ya siku tatu nitakuwa Australia kuungana na Titiana ambaye alitangulia kama wiki moja iliyopita ila kaniambia siwaambie kama tutakuwa kule."


"Kwanini sasa?"

Roberto aliuliza kama vile hajui kinachoendelea na kwa kuwa alikuwa anatumia earphones alienda upande wa ujumbe akamuandikia Titiana.


"Msisitize Jessica asiwaambie wakina Jackline juu ya uwepo wenu Australia maana naona tayari kanipigia mimi huku ananiambia juu ya safari ya huko."

Kisha akaendelea na stori.


"Hebu mpeleleze kakuitia nini tujue?"

Roberto alimwambia kwa kumtega.


"Poa Roberto hebu nimuulize enhhh kama mchawi vile kaja hewani wacha niongee naye nimsikie anasemaje?"

Jessica alimwambia Roberto na kukata simu.


"Nafikiri tayari tumeshafika ndani ya Namport hivyo kabla ya kuingia katikati ya mji tubadili mavazi kisha safari iendelee."

Jackline aliwaambia wenzake.


"Hakuna haja ya kubadilisha mavazi na ukizingatia tayari ni jioni lakini nisiwazuie ninyi badilisheni mimi nawasubiri hapa hapa."

Roberto aliwagomea akabakia kwenye gari na wakina Jackline kushuka.


"Basi sawa tukukute mara moja."

Jasmine alimjibu wakishuka kwenye gari.

Lakini Jackline aliangalia nyuma walikotoka na kuduwaa kidogo kitu kilichomshangaza Jasmine aliyekuwa akiweka sawa raba zake.


"Vipi mbona umeduwaa kuna nini?"

Jasmine alimuuliza.


"Mhh hakuna kitu ila kinachonishangaza kuna gari lilikuwa nyuma yetu kwa takribani saa moja hivi nikiongeza mwendo nalo linafanya hivyo nikipunguza nalo ni hivyo hivyo sasa tumesimama nalo silioni bila shaka limesimama sehemu, hivyo nina hofu tunafuatiliwa."

Jackline alimwambia Jasmine.


" Kweli?"

Jasmine alimuuliza.


" Siwezi yatilia mashaka macho yangu nina uhakika nayo."

Jackline alimhakikishia.


" Tunafanyaje sasa? "

Jasmine alimuuliza tena. Lakini Roberto aliyekuwa bize na simu yake alishangaa kuona wakina Jackline wakiwa wanaongea pale chini alitaka kushuka lakini akasita kidogo baada ya kuhisi kuwa wameamua kubadilishia pale pale karibia na gari kwa kuhofia vichaka vya eneo hilo.


"Roberto, we Roberto!"

Jackline aliita baada ya kuchungulia mlangoni.


"Naam tayari?"

Aliitika Roberto kama vile katoka kwenye usingizi mzito.


"Sikia ondoa gari taratibu huku macho yako yakicheza na site mirrors' kuna kitu tumekishtukia."

Jackline alimwambia.


"Na ninyi?"

Roberto aliuliza.


"Tunabaki kulichunguza gari hilo kisha tutaungana nawe baadaye."

Jackline alimjibu huku akimfuata Jasmine kwenye kichaka alichojificha na kumuacha Roberto akiwa hajui afanye lipi lakini aliondoka kama alivyoelekezwa.

Kama walivyokuwa wameshtukia jambo hilo ni kweli kuna gari lilijitokeza na kuja eneo lile.


" Tunafanyaje hapa?"

Jasmine alimuuliza Jackline.


"Hatuna uhakika ni wakina nani lakini tunatakiwa kushambulia matairi na wasipotii tutafanya shambulizi kwenye vioo vya mbele."

Jackline alimjibu huku akiitega vizuri bastola yake hivyo Jasmine naye hakuwa na chaguo jingine naye akafanya hivyo hivyo.


"Pyuuuuuu Pyuuuuuu......."

Matairi yalianza kupiga kelele za kutoa upepo kitendo kilichowafanya wenye gari wapate hofu na kusimama kujua kulikoni kwani wakina Jackline walitumia viwambo vya kuzuia sauti.


"Tumekanyaga nini mbona tairi halina upepo kabisa?"

Mmoja wa wale vijana aliuliza baada ya kushuka na kulikagua tairi la mbele.


"Si hilo tu hata hili la nyuma nalo liko hivyo hivyo au kuna kitu kilitegwa hapa nini maana hili eneo si ndiyo walisimama wale wanaharamu?"

Mwingine naye alishangaa kuona na la nyuma halina upepo. Hivyo ikabidi wachukue tochi na kuanza kumulika walikotoka kuona kama wanaweza ona chochote kile walichokikanyaga.

Kitendo cha kuanza kumulika kurudi nyuma kiliwaibua wakina Jackline kutoka walikokuwa wamejificha na kuja mpaka kwenye gari hilo na kuingia siti za nyuma na kutulia.

Walimulika maeneo yote lakini hawakuona chochote hivyo waliamua kupotezea.


"Twenzetu itakuwa hizo tairi zilifungwa za masafa mafupi na kosa ambalo tulilifanya ni kutopitia kwenye checkup' sijui tutafanyaje?"

Mmoja alitoa majibu ya kile kilichotokea.


"Ushenzi na ujinga wa hali ya juu sana angalia sasa Wanahizaya wameshapotea sijui tutawakutia wapi sasa?"

Mwingine aliyeonekana ni kiongozi wa safari ile alichukizwa na kilichotokea na kuamua kupiga simu.


"Kipenzi mambo yamekuwa magumu huku."

Aliongea baada ya simu yake kupokelewa upande wa pili.


"Magumu kivipi msinipe taarifa mbaya hapa?"

Upande wa pili uliuliza.


"Kuna sehemu karibu na mji tumepata hitilafu tairi moja la mbele na la nyuma yameishiwa upepo kwa pamoja sijui nini kimetokea?"

Alimjibu.


"Ilikuwaje mpaka ikawa hivyo?"

Upande wa pili uliendelea kuuliza kama vile haukuwa tayari kwa majibu yaliyotolewa.


"Tukiwa tunawafuatilia kwa mbali mara walisimama ikabidi nasi tusimame kujua wanataka kufanya nini na baada ya dakika kadhaa waliondoka nasi tukaendelea kuwafuatilia lakini cha ajabu tulipofika eneo ambalo walisimama ndiyo likatokea lililotokea?"

Alimjibu.


" Ondokeni hilo eneo haraka wamewashambulia kwa risasi zisizokuwa na mlio."


"Unasemaje mpenzi?"

Yule kijana aliuliza huku akiangalia huku na kule kuona kama anaweza kuona chochote na muda huo simu ilishakatwa akaiangalia kama itaita haikuwa hivyo akaamua kuiweka mfukoni.


"Oya kwa maelezo ya Nawane tumeshambuliwa tunatakiwa kuondoka eneo hili hivyo hivyo mpaka town ambako tutabadilisha matairi yote na natengeneza mengine ambayo yatajitokeza."

Aliyekuwa akiongea na simu alimwambia mwenzake na kuingia kwenye gari na mwenzake naye akafanya hivyo hivyo kisha wakafunga milango na kuwasha gari, mara simu ya yule dereva iliingiza ujumbe mfupi akaitoa na kuusoma.


" Kuweni makini hao ni watu hatari sana kabla ya kuingia kwenye gari kagueni kwanza."

Baada ya kuusoma ujumbe ule alimwangalia mwenzake ili amjulishe lakini kabla hajafanya chochote kile vitu vya baridi vilikuwa shingoni mwao.


"Mko mikononi mwetu sisi hivyo mtafanya kile tu ambacho tutawaamuru sisi na si vinginevyo, sawa?"

Jasmine aliwaambia huku akijiinua kwenye kiti.


"Sawa."

Dereva alimjibu.


"Vizuri, watu waungwana siku zote huwa hawakutani na majanga kwa sababu ni waelewa hivyo tunaamini hata ninyi ni wa kundi hilo. Taratibu elekeeni nje."

Jasmine aliwaambia hivyo huku Jackline akiwa tayari nje na huku akiwa kawanyooshea bastola kupitia dirishani kisha akawafungulia mlango na kuwataka kupitia mlango mmoja wote. Hawakuwa na chaguo zaidi ya kushuka chini kutii amri.


" Vizuri sana sasa tulieni hivyo kama kama mmepigwa shindano za ganzi miguuni."

Aliongea Jasmine huku Jackline akiwasogelea kwa tahadhari na kuanza kuwatoa vitu vilivyokuwa mifukoni mwao. Kila kitu kilitolewa kisha wakawapiga pingu mikononi.


"Roberto njoo tunakusubiri hapa mara moja."

Jackline alimpigia Roberto ambaye baada ya muda kidogo alikuja.


"Haya changanyeni hayo makongoro yenu kwenye gari haraka."

Jasmine aliwaamrisha huku akiwagonga kwenye mabega.


"Wapi hiyo?"

Roberto aliuliza.


"Ni safari ya gofu la kifo kule Gezra."

Jackline aliongea huku akiipekua simu aliyoichukua kwa kwa yule dereva. Roberto hakuwa na jingine alijua huko Gezra kuna nini kinakwenda kutokea.


"Okey vizuri kumbe wewe ndiye uliyetukimbia siku ile ukiwa pamoja na yule mshenzi wako ambaye ulisema hujui chochote kumhusu wewe ulimchukulia kama mpenzi wako kumbe ulicheza picha siyo?"

Aliuliza baada ya kukutana na picha mbalimbali zake huyo kijana akiwa na mpenzi wake Nawane na kilichomtisha zaidi Jackline ni baada ya kukutana na picha zao wenyewe kuanzia Jasmine, Roberto, Daktari Abbas, Daktari Hans, watoto wao, Thomas, Dalali na Mahmoud.


"Hapana dada sisi tulijua ninyi ni wale watu waliovamia kituo chetu cha mafuta pale Windhoek kumbe tuliwafananisha tu."

Alijitetea yule kijana.


"Vizuri tutaongea lugha moja tukifika mwisho wa safari."

Jackline hakutaka makuu alikubaliana naye huku akimkabidhi Jasmine ile simu ili aziangalie zile picha.


"Haaaaaaa......"

Jasmine alipigwa na mshangao baada ya kujiona akiwa ni miongoni mwa zile picha, alipotaka kuongea kitu Jackline alimkanyaga mguuni na kumfanya kutulia.


***


Titiana aliingia hotelini na moja kwa moja aliongoza chumbani kwake na kuichukua laptop yake ambayo aliiwasha na moja kwa moja aliingia sehemu iliyoandikwa 'E-connect' na kuifungua ilipofunguka tu aliisearch device' ambayo aliibandika kwenye mlango wa kuingia alimolazwa Bi Elizabeth na ikakubali.


"Waoooo... Hapana chezea mimi weweee !"

Alijisemea hivyo mara baada ya kumuona Vivian akiwa katulia pale mlangoni akichezea simu yake pasipo kujua kama ameshajaa kwenye tageti ya Titiana. Hivyo Titiana akiwa mwenye furaha aliinuka na kwenda kuchukua kinywaji kwenye friji ambayo iko ndani ya chumba chake kisha alirudi na kuketi huku macho yakiwa kwenye ile video.


"Ngoja nimpigie kwanza nimtoe kwenye wazo analolifikiria."

Titiana alisema hivyo baada ya kumuona Vivian akitaka kupiga simu hivi mara anaahirisha hivyo Titiana akajua kuna kitu anataka kukifanya lakini kabla hajafanya hivyo akaona ampigie mtu wake wa kazi ambaye amemuweka pale Hospitali maalum kwa ajili ya kumpanga Vivian mpaka akubali kuwa na mahusiano naye huyu jamaa si mwingine bali ni Daktari Yakoub.


"Niambie mtu wangu mchakato umeuanza?"

Titiana alimuuliza baada ya simu yake kupokelewa.


"Subiri majibu muda si mrefu kwani nimeshamchukua tayari niko naye kwenye Restaurant ya Hospitali nampigisha mavyakula si unajua mambo haya yanakwenda kwa hatua."

Daktari Yakoub alimjibu Titiana ambaye alitabasamu tu.


"Na kweli unajua nini Daktari kwa kuwa tumeanza kuiteka akili yake taratibu haina haja kuwa na papara tusije mkosa bure kwa haraka zetu."

Titiana alimjibu.


"Ndiyo hivyo mkubwa wa kazi kumbe ngoja mimi nirudi asije shitukia mchezo."

Daktari alimwambia Titiana.


"Bila shaka wewe rudi kampe mtoto roho inapenda."

Titiana alimjibu na kuikata simu kisha akaigongesha kwenye meno yake huku akiendelea kuifuatilia ile video ya Vivian pale mlangoni.


"Daktari Yakoub siku zako ziko mkononi mwangu zinahesabika kama mshale wa saa unaeezaje kunidanganya hivyo? Hapana siyo bure kuna kitu hapa."

Titiana alinyanyua glasi ya wine na kupiga funda tatu mfululizo kwa alihisi Daktari Yakoub kuna mchezo anamchezea kwani Vivian alikuwa akimuona pale mlangoni lakini yeye anasema yuko naye. Baada ya kutulia aliona hapana ngoja amjulishe Roberto.


" Baby, Huyu chizi ni kama kuna mchezo anataka kuucheza kwani nimempigia kutaka kujua kafikia wapi? Ananiambia yuko naye Restaurant wakipata chakula huku akiendelea kumvuta kwake taratibu wakati mimi namuona katulia kwenye mlango wa mgonjwa, baby hebu ngoja kwanza..... "

Alimkatia simu Roberto na kuyarudisha macho kwenye laptop ambayo ilimuonesha Daktari Yakoub kwa kushirikiana na wauguzi wawili akiwapo yule ambaye alimkabidhi kifuko wakisaidiana kumtoa mgonjwa kutoka kwenye chumba kile.


" Whaaaaaaaaaat.........? Noooo Daktari Yakoub huwezi cheza na akili yangu hata kidogo na kwa kuwa umeamua kucheza na akili yangu endelea sina haraka na wewe umeingia mwenyewe mzima mzima."

Titiana aliongea hayo huku akiifunga laptop yake kisha akachukua simu na kumtumia ujumbe Roberto.


"Baby dili limekuwa dirisha."

Kisha akaitupa kitandani simu yake na kutoka zake chumbani humo na kuelekea nje ili kupunga upepo kwani alihisi kama vile kichwa kinakwenda kupasuka kwa kuchemka.


"Kwanini Daktari Yakoub amenifanyia haya? Hivi kajua kama kapiga hodi kuzimu?"

Titiana alijiuliza maswali hayo huku akiwa anauangalia mji kutoka juu ghorofani.


NINI KITAENDELEA?



Titiana aliondoka usiku huo huo na kuelekea St. Mathew Hospital kuhakikisha kama kweli Bi Elizabeth katoroshwa na mtu ambaye alimuamini sana. Aliingia ndani ya gari lake na kuondoka japo baridi lilikuwa kali usiku huo yeye hakujali kwani baada ya kuingia ndani ya gari lake la kifahari aina ya Buno Race lenye rangi nyeusi ya kung'aa aliondoka kwa mwendo mkali kama vile anaingia kwenye mashindano ya magari.


"Daktari Yakoub nataka nikuoneshe mimi ni nani? Huwezi kunifanyia mchezo wa kitoto kama huo."

Titiana aliongea peke yake huku macho yakiwa mbele kuhakikisha kuwa hafanyi kosa linaloweza kumletea tatizo la kiusalama, na baada ya kufika kwenye ardhi ya Hospitali ya St. Mathew kama kilometa tano hivi kutoka hospitalini alipunguza mwendo na kuachana na barabara iendayo hospitalini na kuingia msituni. Huko alishuka kwenye gari na kulifunga milango na vioo vyake vizuri kisha akarejea barabarani na kutembea kwa miguu kuelekea ilipo Hospitali, akiwa mita chache kuifikia Hospitali alichukua simu yake na kuitracki namba ya Daktari Yakoub ili ajue yuko wapi muda huo na kama bahati vile ilionesha yuko ndani eneo la Hospitali hivyo moja kwa moja akampigia.


"Habari ya muda dada Tiana!"

Daktari Yakoub alimsabahi Titiana mara baada ya kupokea simu.


"Uko wapi muda huu Daktari?"

Titiana alimuuliza.


"Muda huu ndiyo nafika nyumbani maana nimechoka sana na shughuli za leo si unajua tena kazi zetu hizi."

Daktari Yakoub alimjibu Titiana.


"Okay vizuri Daktari mimi mwenyewe nimejilaza hapa usingizi hakuna nimeangalia Televisheni mpaka nimechoka nikaona nikujulie hali."

Titiana alimdanganya Daktari Yakoub.


"Pole sana ningekuwa karibu na hapo Hotelini ningekupa kampani dada yangu."

Daktari Yakoub ambaye hakujua kinachoendelea usiku huo alijiachia kwenye simu akimpatia matumaini mtu ambaye hamfahamu undani wake.


"Asante sana Daktari, lakini vipi kuhusu mchakato wako na Vivian mmeishiana vipi?"

Alimtega kwa swali.


"Vivian hawezi kuruka kwangu dada Tiana kwani tumeshapangana naye kuwa kesho natoka naye kidogo nje ya mji lengo langu ni kutaka anizoee ili muda ukifika tufanye yetu."

Daktari Yakoub alimjibu Titiana ambaye muda huo alikuwa akiiangalia simu yake kuona anayeongea naye yuko upande gani na alipojiridhisha vizuri aliko Daktari Yakoub alitabasamu kwa dharau.


" Vizuri kumbe wacha mimi nilale tutawasiliana kesho mapema na usisahau kunipa taarifa ya mgonjwa wetu."

Titiana alimjibu kisha akamkatia simu na kuiweka mfukoni kisha akaongeza mwendo kuelekea Hospitalini ambako aliongoza moja kwa moja mpaka kilipo chumba ambacho alilazwa Bi Elizabeth.


" Samahani nesi sijui unanikumbuka vizuri? "

Titiana alimuuliza nesi ambaye alimkabidhi kifuko ambacho alimtaka amkabidhi Vivian.


"Nakukumbuka vizuri sana madam."

Nesi yule alijibu huku akiwa anatetemeka kwani hakutarajia kuonana na mtu huyo kwa wakati huo eneo lile la Hospitali.


"Vipi hakutarajia kuniona hapa muda huu mbona unatetemeka nesi wangu?"

Titiana alimuuliza mara baada ya kuona kaangusha pleti iliyokuwa na vifaa vya kazi ambavyo alitoka navyo wodini.


"Hapana dada nafikiri ni kwa ajili ya hii baridi tu."

Nesi alimjibu.


"Okay vizuri, naomba uniambie Vivian yuko wapi?"

Titiana alimuuliza akimsogelea taratibu.


"Nilikuwa wodini sijui yuko wapi kwani nilimuacha hapa nje."

Nesi alimjibu.


"Naweza kumuona mgonjwa wake?"

Titiana alimuuliza Nesi kwa kumnong'oneza sikioni.


"Hapana hauwezi kumuona kwani muda huu kuna madaktari wanamshughulikia hivyo ni ngumu kumuona dada tafadhali."

Nesi alimkatalia katakata.


"Wewe si umetoka wodi jingine? Unajuaje kama bado wapo? Na kwanini Vivian asiwepo mahali hapa? Naomba unifuate huku."

Titiana alimtupia maswali Nesi ambaye alikuwa akitetemeka tu muda huo.


"Nipeleke kwanza vifaa ofisini."

Nesi alimjibu Titiana.


"Umechelewa dada yangu huwezi kufanya hivyo kabla sijakupa tiba ya uongo wako na pia ukikutana na Vivian mpe salamu zangu."

Titiana alimfuata alipokuwa kasimama Nesi na kumkita kisu cha kifuani kisha akamkamata na kumvutia nyuma ya jengo lile. Huko alimkamata ulimi wake Nesi na kuukata kisha akamshikisha mkononi pamoja na kisu kisha yeye akaondoka kupitia kule kule alikoingilia pasipo walinzi kumuona. Lakini wakati akiuruka ukuta aliangukia sehemu iliyokuwa na majani makavu ambayo yalirundikwa na hivyo kutoa mlio ambao uliwashtua walinzi wa geti la nyuma na kuigeuzia taa upande ule kuona kilichotoa mlio ni kitu gani. Titiana alitulia kimya ndani ya yale majani kuukwepa mwanga wa ile taa mpaka utoke sehemu ile. Lakini wakati huo huo walinzi wengine walifika eneo lile na kuanza kuchunguza.


"Itakuwa ni nini?"

Mmoja wa walinzi aliuliza.


"Halafu nilishawaambia ninyi madogo kuwa mkiona kaka yenu nimesinzia kidogo heshima basi, sasa angalia mmeniamsha kwa lipi hapa?"

Mlinzi mwingine aliwalaumu wenzake kwa kitendo cha kumuamsha na alipokuwa akiongea hayo alijiachia na kukaa kwenye yale majani.


" Acha kutulaumu brother hii ni kazi yako hujaajiriwa kulala hapa na kama ukitaka hivyo acha kazi ulale hadi mwakani, sisi wenzako tumesikia kabisa mlio wa haya majani kama vile yamekanyagwa na kitu."

Alijibiwa na mlinzi mwingine aliyekuwa akiendelea kumulika maeneo ya karibu na pale.


" Umeona sasa kumbe haya ndiyo yalikanyagwa? Au mmesahau kuwa mitaa hii ya huku nyuma ina miumbwa mingi? "

Yule mlinzi aliyekuwa akilalamika kwa kuamshwa alichoka kabisa baada ya kusikia maelezo ya mwenzao akainuka na kuondoka zake na kuwaacha wenzake pale. Kwa upande wa Titiana hali ilikuwa tete kwani sehemu aliyokuwa kajificha haikuwa mbali na pale walipokuwa walinzi hivyo presha ilikuwa ikipanda kwa kasi na kushuka kwa kasi. Muda wote alikuwa akisali waondoke kabla hawajashtukia kwani hofu yake ilikuwa ni kikohozi ambacho mara nyingi katika mazingira kama hujitokeza kama vile kimetumwa hasa ukizingatia eneo lile lilikuwa chafu sana. Na bahati ikawa kwake kwani wale walinzi waliondoka kurudi getini wakati huo taa ya ulinzi nayo ilihama upande ule. Hakufanya kosa kwa staili ya kuviringika kama gurudumu alipotea eneo lile huku walinzi kurudi mbio tena baada ya kusikia michakacho ya majani yale makavu.


"Angalieni hapa jamani."

Mlinzi mmoja aliwaita wenzake na kuwaonesha majani yaliyosambaa kutoka kwenye lundo lile na kusambaa.


"Lazima hapa kulikuwa na mtu."

Mlinzi mwingine aliwaambia wenzake.


"Yaani hawa vibaka hawakomi kabisa yaani pamoja na kumuua mwenzao wiki iliyopita wamerudi tena?"

Mlinzi mwingine aliongea akiyamulika majani yale yaliyotapakaa kutoka kwenye ule mkusanyo.

Wakati huo Titiana alikuwa amefanikiwa kuondoka sehemu hiyo na alishalifikia gari lake kule porini ambapo aliingia huku akiwa hoi.


" Da yaani wangenikamata mbwa wale sijui ingekuwaje Titiana mie."

Aliongea huku akizivua gloves' zilizokuwa mikononi na kuzirushia siti ya nyuma na kisha akaliwasha na kuondoka zake eneo.


***


Waliwasili ndani ya Majengo ya Gezra na baada ya kuwasili waliwataka wale vijana kushuka kwenye gari na kuelekea ndani ya magofu yale.


"Haya shukeni mmefika kwenye makazi yenu ya muda mpaka pale mtakapoachiwa."

Jackline aliwaambia huku akiwasukuma kuelekea ndani.


"Haraka bwana ingieni ndani mnajivutavuta nini kwani tuliwaita?"

Roberto aliongea akiwaongoza ndani.


"Jamani tunaomba msitufanye chochote kile kibaya."

Kijana mmojawapo alitoa utetezi wake mbele ya wakina Jackline.


"Tena nina hasira na wewe mwanaharamu ungejua usingepanua hata hilo domo lako, najua muda mfupi ujao utaongea tu."

Jackline alimjibu yule kijana ambaye alikuwa akiomba msamaha kwani ndiye yule aliyewatoroka kule porini akiwa na Nawane kisha kulichoma moto gari.


" Lakini mimi sihusiki ndugu zangu kwa lolote huyu rafiki yangu alinichukua nimsindikize huku lakini hakusema tunafuata nini."

Mwenzake alijitetea. Lakini maneno yake hayakuwa msaada wowote kwake kwani alikutana na ngumi ya mgongoni kutoka kwa Jasmine iliyotua vilivyo mgongoni na kumpeleka chini kama gunia la pamba.


" Unaongea nini wewee? Yaani huoni aibu kuendelea kutudanganya unafikiri sisi watoto wadogo eee safari tutaona njia mtakayoitumia kutoroka hapa nyaaambafu."

Jackline aliongeza huku akiikunjua kamba ambayo alikuwa akiiandaa kwa ajili ya kuwafungia.


"Kile chumba cha katikati kitawafaa sana maana nimekichunguza na kugundua kuwa kuna wadudu ambao no rafiki wakubwa wa binadamu."

Roberto aliwaambia baada ya kuingia.


" Wadudu gani hao tena na wewe? "

Jasmine alimuuliza Roberto.


" Si siafu hao yaani ni wengi balaa kiasi kwamba hawa vidume wenzangu wakiwekwa kule wataongea bila wenyewe bila kuulizwa."

Roberto alielezea huku akimsaidia Jackline kukunjua kamba huku Jasmine akiwa kawakalia karibu wale vijana.


"Huko kutawafaa najua kufikia asubuhi watakuwa wamenona."

Jackline alichombeza. Lakini wakiwa wanaendelea na maandalizi mara simu ya Roberto iliita na Roberto alipoitoa simu na kuiangalia kujua mpigaji ni nani alitoka nje huku akiwa kaipokea tayari.


"Niambie."

Roberto alianza mara baada ya kufika nje.


"Nilikuwa St. Mathew Hospital kidogo ninaswe na walinzi Mungu mkubwa kanisaidia."

Titiana alimwambia Roberto.


"Uko poa lakini?"

Roberto alimuuliza mara baada ya kuelezwa kilichompata kule Hospitalini.


"Niko poa wangu nilikwenda kutaka kumuadhibu Daktari lakini nikaona niwape taarifa kwa kumuua yule Nesi aliyeshirikiana nao kumtoa Bi Elizabeth."

Titiana alimwelezea Roberto.


"Haitakuwa hatari kwako mpenzi, na hujajua kapelekwa wapi?"

Roberto aliuliza.


"Wala Usijali nitakuwa salama tu na uzuri kesho Jessica ataungana nami yaani ni full mtanange na kuhusu alikofichwa itafahamika mara baada ya kumdaka Daktari Yakoub."

Titiana alimtoa hofu.


"Kumbe vizuri, muwe makini ngoja nirudi ndani wasije nishtukia wakina Jackline."


"Okay poa usiku mwema mpenzi nimekumiss sana."

Titiana alionesha hisia zake pamoja na kuwa kwenye shughuli ambayo ni hatari.


"Hata mimi mpaka naumwa mpenzi wangu, ila muda si mrefu tutakuwa hapo."

Roberto alimjibu mpenzi wake kisha alikata simu na kurejea ndani kuungana na wakina Jackline kuwashughulikia mateka wao waliowanasa walipokuwa wakifuatiliwa.


JE NINI KITAENDELEA?





Aliingia ndani na moja kwa moja akaanza kuwafunga kamba za miguu na mikono kisha akawaingiza kwenye chumba ambacho alisema kina siafu wa kutosha na humo aliwaacha na kutoka bila kusahau kufunga mlango.


"Narudi baada ya dakika sifuri kwa sasa pigeni na kubadilishana mawazo na hao wananzengo."

Roberto aliwaambia akiwa anatoka nje.


"Brother tunaomba ututoe humu tutakufa jamani hawa wadudu si wa kawaida, tuko tayari kutoa ushirikiano kwa mnalolitaka."

Mmoja wa wale vijana aliongea dakika chache tu baada ya kuachwa mle ndani. Lakini Roberto aliishia kuwasikiliza tu kisha alitabasamu na kuondoka zake kuwafuata waliko wakina Jackline waliokuwa wakibadilishana mawazo.


" Kulikoni huko ndani? "

Jasmine alimuuliza Roberto.


"Tukae kidogo kila kitu kitakuwa sawa kwani mmoja keshaanza kutokwa na maneno."

Roberto alimjibu.


"Hivi mnafikiri hawa Vilubwada wanaweza kutupatia tunachokitafuta?"

Jackline aliwauliza wenzake.


"Japo sina uhakika lakini najua itasaidia kidogo."

Roberto alijibu huku akicheka kutokana na makelele yaliyokuwa yakipigwa na wale vijana mle ndani.


"Hivi hao wadudu siyo hatari kweli?"

Jasmine aliuliza huku akiondoka pale kuelekea ndani.

Swali lile la Jasmine liliwafanya na wakina Jackline nao kuondoka pale na kurudi ndani kwa ajili ya kuwashughulikia sasa.


"Haya sasa ni muda wenu wa kukikwepa kifo."

Jackline aliongea wakati wakiwachomoa ndani ya chumba ambacho kilikuwa kimetapakaa siafu.

Lakini wakiwa wanawavuta wale vijana kutoka ndani wakiwa hoi kwa mng'ato wa siafu mara simu ya Jackline iliita na alipojaribu kuangalia mpigaji ni nani alibaini kuwa ni mdogo wake Shamimu hivyo alitoka nje na kupokea.


"Kwema mdogo wangu?"

Jackline alianza baada ya kuipokea simu.


"Ni kwema tu dada, vipi za huko?"

Shamimu alimjibu.


"Enhh lete maneno mdogo wangu."

Jackline alimtaka aongee kile alichotaka kusema.


"Hivi ndiyo nimetoka kwenye mtihani wa mwisho bila shaka sasa nitaweza kukaa na wanangu japo ni pasua kichwa hasa Natalie lakini tutaenda sawa tu uzuri najua udhaifu wake. Lakini dada ulisema kuwa wameondoka mbona kimya? Au ulinidanganya?"

Shamimu aliongea kitu kilichomshangaza Jackline.


" Unasemaje Shamimu? "

Jackline aliuliza huku akitoa simu nyingine mfukoni.


" Ndiyo hivyo dada hawajafika bado au shemeji aliamua kubadili mawazo akiwa njiani? "

Shamimu alimjibu na kumuuliza swali jingine dada yake Jackline.


"Hebu ngoja kwanza mdogo wangu."

Jackline alimtaka mdogo wake asubiri kwanza, hivyo alikata simu na kuelekea kuitafuta namba ya mume wake kwenye ile simu nyingine na kisha kumpigia.


"Mmmhhh kuna nini hapa, mbona hapatikani wakati masaa kadhaa yaliyopita nimeongea naye?"

Jackline alijiuliza baada ya kuona mume wake hapatikani hewani. Alimtafuta tena na tena lakini hali haikubadilika hakupatikana hewani.


"Jackline mbona unaongea peke yako Kulikoni?"

Jasmine alikuja na kumkuta Jackline akiongea peke yake huku akienda upande huu na kurudi upande ule.


"Jasmine nahisi kuna tatizo limetokea hapa."

Jackline alimjibu.


"Wapi humo ndani?"

Jasmine alimuuliza huku akionesha jengo lile la Gezra.


"Dogo Shamimu anadai Daktari Abbas hajawasili Urusi na nimejaribu kumtafuta hewani lakini hapatikani."

Jackline alimjibu huku akichora chora chini.


"Hebu jutulize kwanza Jackline tulifuatilie inawezekana kuna sehemu wako na mtandao unasumbua si unajua tena hizi ndege zetu zinakuwaga na mapito mengi?"

Jasmine alimtia moyo Jackline ambaye muda huo alionekana kuchanganyikiwa juu ya kile kilichotokea. Hivyo Jasmine alimchukua Jackline na kurudi naye ndani ambako Roberto alikuwa akiendelea kuwabana wale vijana.


" Hakuna sababu ya kuendelea kupoteza muda na hao wanaharamu dawa yao ni hii tu."

Jackline alitoa bastola na kuwaelekezea wale vijana huku akitokwa na machozi.


"Noooo Jackline usifanye hivyo hawa wanatakiwa waongee kwanza."

Jasmine alimzuia Jackline asifanye kitendo hicho.


"Waongee nini hawa wakati inafahamika fika wametumwa na yule Dorice feki, kazi iliyo mbele yetu ni kumtafuta huyu Chaupele."

Jackline aliongea huku akiwa tayari kaziachia risasi mfululizo zilizowapata vilivyo wale vijana maeneo ya vifuani.


"Kwendeni kuzimu huko tuwabembeleze kama wakina nani ninyi?"

Jackline alikuwa kavurugwa kiasi kwamba hakuna hata mmoja kati ya Jasmine na Roberto aliyeweza kumzuia.


"Sa..sa...waa si..si tuna....ku...faaa laki...ni majibu utaya....."

Yule kijana aliyekuwa kiongozi na mpenzi wake Nawane aliongea maneno hayo ambayo alishindwa kuyamalizia akakata roho.


"Jackline hasira ni hasara umeona sasa kaishia njiani na kama tungewabana lazima wangesema unafikiri tunafanyaje sasa?"

Roberto aliona amwambie tu ukweli wake Jackline.

Lakini ni kama alikumbuka kitu hivi kwani aliingiza mkono kwenye jaketi lake na kuitoa simu mojawapo kati ya mbili za wale marehemu na kuanza kuzikagua na ikawa kama bahati kwani alipoiwasha tu kwanza akakutana na ujumbe ambao ni kama uliingia muda si mrefu.


"Ni aje? Mbona kimya hamjawapata?"

Baada ya kuusoma ujumbe ule Roberto alifurahi sana akamfuata Jasmine na kumuonesha huku Jackline akiwa anachezea chezea bastola yake baada ya kumaliza kazi yake.


"Tunaitumiaje hii jumbe?"

Roberto alimuuliza Jasmine.


"Hebu lete hiyo simu."

Jasmine aliongea na kuichukua simu mkononi mwa Roberto.


"Tulikuwa kwenye mchapano mkali lakini tumewadhibiti tayari tuko hapa kwenye magofu ya makumbusho ya Gezra tumewapiga pini."

Jasmine alimtumia Nawane ujumbe ule lakini cha ajabu majibu yakaja kinyume na matarajio yake.


"Mmh kwenye Mob yetu hakuna mtu anayeweza kuandika ujumbe kama huo, mmedanganya."

Wakati Jasmine na Roberto wakiwa wanaupitia ujumbe ule mara simu iliita.


"Mbona huongei sasa wewe si mjuaji? Jiandae baada ya hawa Kenge kuwa mizoga ni zamu yako Nawane."

Roberto alimtisha Nawane.


"Sikiliza wewe usimtishe mtu usiyemjua na kwa taarifa yenu mnakwenda kuzilipia hizo damu za watu wangu."

Nawane alijibu mashambulizi.


"Usitutishe kwa lolote wewe na ninakuahidi kukuua kwa mkono wangu labda ninalifikiria lisiwe kweli."

Jackline alimnyang'anya simu Roberto na kuongea naye Nawane.


"Nakuona una hofu eee...."

Kabla hajamaliza kuongea Nawane Jackline alimkatia simu.


"Anasemaje huyo?"

Jasmine alimuuliza.


"Hapa tuondokeni haraka nina wasiwasi mkubwa kuwa hawa washenzi wamewateka wakina Abbas."

Jackline aliongea huku akiiweka bastola mfukoni.


"Tunaelekea wapi sasa?"

Jasmine alimuuliza.


"Tunatakiwa kuelekea Gaborone tutaingia barabara ya kaskazini ambayo ni fupi kuingia Botswana."

Jackline alimjibu huku akiwaongoza kutoka nje ambako waliingia kwenye gari na kuondoka.


"Hiyo namba icheki tuone kwenye system tujue aliwasiliana na nani ndani ya masaa kadhaa."

Roberto aliandika ujumbe pasipo kuonwa na yeyote kati yao na kumtumia Jessica.


"Kumbuka tulivyoongea hii kimya kimya."

Roberto alimsisitiza Jessica.


"Wala usihofu Roberto na sisi huku tuko kuichora ramani ya namna ya kuingia nyumbani kwa Daktari Yakoub. Kifo cha Nesi kimewavuruga pale Hospitalini kila mmoja akiongea lake huku walinzi wa zamu wakiwa wameshadakwa."

Jessica ambaye tayari alikuwa Australia kuungana Titiana alimweleza Roberto kinachoendelea pale St. Mathew Hospital.


" Na ninyi mko hapo hapo? "

Roberto alimuuliza Jessica.


" Tuogope nini tuko hapa hapa Hospitali tumejichanganya na waombolezaji wengine huko tukijaribu kumuangalia Vivian."

Jessica aliendelea kumjibu Roberto kwa kujiamini kabisa.


"Okay sawa kuweni makini si mnajua tuko kwenye wakati mgumu kila kona tumezungukwa na maadui kikubwa ifanyie kazi hiyo namba muda huu."

Roberto aliona apunguze maelezo kwa Jessica.


"Bila shaka Robbie muda si mrefu nakupa jibu maana muda huu tuko kwenye Restaurant ya Hospitali."

Jessica alimjibu kisha Roberto akairudisha simu yake mfukoni.

Kumbe muda wote huo akichati na Jessica alikuwa akifuatiliwa na Jasmine japo hakujua anachati na nani.


" Mbona bize na simu halafu tabasamu kuuubwa au ndo tayari umepata totoz? "

Jasmine alimuuliza Roberto ambaye alimkatalia.


"Totoz ya nini Jasmine hapa kuna chizi langu lilikuwa linanichekesha hapa."

Roberto alimjibu.


"Tupitie hapa kwanza pale 'Holiday Corner' tupate chochote na kubeba chakula kingine sababu tutakapoingia porini itatuchukua takribani masaa kumi bila kukutana na nyumba yoyote."

Jackline aliwaambia wenzake juu ya hiyo safari yao.


"Duuu hatari sana lakini kwetu haitusumbui hiyo hali lakini wacha tuongeze nguvu hapa kwanza."

Jasmine alimjibu.

Hivyo waliacha barabara kuu na kuingia kwenye Mgahawa huo ambao uko njiapanda ya kuelekea Botswana kupitia mashambani tofauti na ile barabara kuu ambayo walihofia kuipita.


" Nimeshawapata wale wote aliowasiliana nao, wa kwanza ni Mackdone ambaye kawasiliana naye kama dakika ishirini zilizopita na mwingine ni Vivian ambaye huyu waliwasiliana dakika kumi na tano zilizopita. Na mwisho kuna namba nyingine ambayo sijaijua vizuri ila iko ndani ya Botswana kwenye mji wa Gaborone."

Jessica alimjulisha Roberto.


" Basi sawa kwa kuwa tuko njiani kuelekea huko nitakujulisha tukifika Shem lake."

Jessica alimjibu.

Kwa namna moja Roberto alifurahi sana baada ya kupata taarifa ile aliwaangalia wakina Jackline waliokuwa wakiingia ndani ya Mgahawa huku Jackline akiwa anatembea kwa kujivuta tu. Na wakiwa wameshachukua nafasi zao kwenye moja ya meza mara simu ya Jackline iliita.


"Haloo."

Alipokea


"Naongea na Jackline?"

Upande wa pili uliuliza.


"Ndiyo mwenyewe, wewe ni nani tahadhari?"

Jackline alimuuliza mpigaji.


"Jina langu sio lazima, ila kuna......"

Kabla hajamaliza kueleza mara simu ilikata na alipoangalia tatizo ni nini alibaini kuwa ni mtandao.


"Mungu wangu maeneo mengine bwana sijui yakoje?"

Jackline alijilaumu.


"Kuna nini Jackline?"

Jasmine alimuuliza baada ya kuona analalamika.


"Kuna mtu kanipigia simu na anauliza jina ambalo kalitaja mwenyewe inavyoonekana kuna kitu ambacho si cha kawaida."

Jackline alimjibu Jasmine huku akiinuka kutoka nje.


"Sasa unakwenda wapi Jackline?"

Jasmine alimuuliza baada ya kuona anatoka nje kasi.


"Nakuja ninyi agizeni na anzeni kula."

Alimjibu huku akikaza mwendo kwenda nje ambako haikufahamika anakwenda kufanya nini.


NI KITU GANI KINAKWENDA KUTOKEA?




Baada ya kutoka aliitafuta ile namba iliyompigia akiwa ndani na hii ilikuja alipoupata mtandao. Japo haukuwa vizuri aliendelea kutembea akiwa kainyoosha simu juu kuhakikisha mtandao haupotei na wakati huo huo simu ikiwa katika sauti ya juu.


"Haya ndiyo yanayoitwa maajabu, huyu si kanipigia muda si mrefu sasa iweje asipatikane tena?"

Jackline alijisemesha mara baada ya kutopatikana ile namba.


"Dawa yake ndogo huyu Kibwengo anafikiri anaweza kucheza na akili yangu?"

Aliongea mwenyewe huku akitafuta namba ya mtu mwingine ambaye alijua atamuondolea tatizo lake.


"Habari ya huko Jessica?"

Alianza mara baada ya Jessica kupokea simu yake.


"Huku kwema dada Jackline vipi huko kuna usalama?"

Jessica alimuuliza.


"Naweza sema kuna usalama lakini si asilimia mia moja kwani shemeji yako hapatikani hewani toka jana usiku na kama nilikueleza alikuwa safarini kuelekea Urusi kuwapeleka watoto lakini Shamimu kanishtua alfajiri kwamba hawajafika si ndiyo ikabidi nimtafute hewani kwenye namba zake zote lakini hapatikani mbaya zaidi hata Mahmoud naye hapatikani. Kinachonishangaza ni hiyo namba niliyotumia imenipigia kwa kunitaja jina kisha akapotea hewani nilipoangalia ilikuwa mtandao, namtafuta muda huu hapatikani hivyo naomba uitafute kwenye system pamoja na namba za Mahmoud pamoja na Daktari Abbas."

Jackline alimfafanulia Jessica juu ya kilichotokea kwa familia yake pamoja na mtu aliyempigia simu.


" Kwanza pole sana dada yangu Jackline na pili nakuahidi kuwa ndani ya muda mfupi tutayanasa mawasiliano yao. Nina uhakika tunakwenda kuwapata."

Jessica alimhakikishia Jackline kuwa hilo litafanyika kwa muda muafaka.


"Nitashukuru sana ndugu yangu kwani akili yangu haifanyi kazi kwa kutowapata wanangu wewe mwenyewe unafahamu namna ninavyowapenda mapacha wangu."

Jackline aliendelea kumsisitiza Jessica huku machozi yakimtoka.


"Hakuna haja ya kulia Jackline hili ni letu sote na nina uhakika tutafanikiwa."

Jessica alimpa uhakika katika hilo.


"Nitashukuru sana iwapo hili litafanikiwa Jessica nikutakie majukumu mema na sisi tuko njiani kuelekea Gaborone Botswana ambako tunahisi kuna ngome ya maadui wetu."

Jackline alimwambia Jessica.


"Aisee nami niwatakie safari njema ili mnalokwenda kulifuatilia likalete mafanikio."

Jessica alimtakia safari njema kisha akakata simu.

Jackline alisalia pale nje akiwa mwenye mawazo mengi kwani alishindwa hata kurudi ndani kuungana na wenzake badala yake alielekea lilikokuwa gari lao.


" Ikitokea kuna mtu au watu watakuwa wamehusika katika hili wajiandae sitonyamaza haki ya Mungu."

Jackline alijisemea akikunjua kiti na kujilaza ndani ya gari.

Wakina Roberto walipoona hatokei waliamua kumfuata nje na baada ya kuangalia huku na kule hawakumuona na ndipo waliporudi kwenye gari na kumkuta akiwa kalala usingizi.


" Tuna jukumu la kuhakikisha hiki kiumbe hakifanyi lolote baya maana naona kitendo cha kutoipata familia yake hewani kimemchanganya sana."

Roberto alimwambia Jasmine mara baada ya kumkuta kwenye gari akiwa kalala fofofo huku akiwa kasahau hata kufunga mlango.


" Masikini Jackline wangu namuonea huruma sana lakini najua muda si mrefu atarudisha furaha yake."

Jasmine alimjibu huku akimtingisha Jackline aamke. Lakini wakati wakimuamsha mara simu ya Roberto iliita.


"Naam injinia."

Roberto aliitika mara baada ya kupokea simu ya Mahmoud.


"Uko wapi Roberto?"

Mahmoud alimuuliza.


"Tunaelekea mpakani mwa Botswana na Namibia kwani vipi?"

Roberto alimuuliza.


"Naomba unisikilize kwanza, hapa nilipo sipafahamu kiukweli lakini ni kijijini sana niko na watoto lakini aliko Daktari Abbas sifahamu."

Mahmoud alimwambia.


"Inakuwaje sasa?"

Roberto alimuuliza.


"Tulikuwa kupata chakula kwenye Restaurant iliyo pale uwanja wa ndege wa Gaborone mara umeme ulikata ghafla na muda huo Daktari Abbas yeye alitoka kuelekea maliwatoni hivyo kwa kutosubiri inakuwaje niliwabeba watoto na kuondoka. Lakini nikiwa nimefika nje huku giza likiwa limetanda kila sehemu nilisikia sauti nyuma yangu ikisema 'Mmezembeaje mpaka wamewatoroka' niliposikia hivyo nikajua moja kwa moja sisi tulikuwa ndiyo walengwa hivyo nikajificha kwenye moja ya magari yaliyokuwa pale kwenye maegesho uzuri dereva wa ile gari hakuwa mbali nikamwambia anakimbize mpaka nje ya mji ambako nilimwambia aniache baada ya kuziona taa nikajua ni makazi ya watu."

Mahmoud aliongea kwa kirefu juu ya kilichomkuta yeye na watoto wa Jackline.


" Mungu wangu kwa...... "

Kabla Roberto hajamalizia kuongea alichotaka kuongea mara Jackline alimfuata na kumnyang'anya simu.


" Kuna nini na wewe ni nani? "

Jackline alimuuliza kwani hakujua ni nani aliyekuwa akiongea na Roberto lakini hakujibiwa badala yake alikatiwa simu kitu kilichomkasilisha sana Jackline.


"Hebu niambie Roberto huyu ni nani uliyekuwa ukiongea naye maana macho yako tu yalionesha haikuwa ya kawaida, ongea!!!"

Jackline alimuuliza Roberto huku akiwa kamkunja kabali.


"Jackline huko umekwenda mbali sana kwanini umkunje hivyo Roberto kakukosea nini si ungesubiri mwisho wa simu ataongea nini."

Jasmine alimwambia akiwa kamvuta huku Roberto akiwa katoa macho kwani ilikuwa ni kabali maridhawa.


"Ok okay haya tuambie sasa?"

Jackline alikubali na huku akiwa anataka Roberto aongee kile alichoambiwa kwenye simu.


"Jamani eee ni hivi aliyempigia simu ni Mahmoud...."

Jackline alipolisikia jina hilo hakutaka kusubiri aendelee kusimulia.


"Mahmoud?"

Jackline alimuuliza.


"Yes mwenyewe."

Roberto alimjibu.


"Anasemaje?"

Jasmine alimuuliza tena.


"Kifupi alichokizungumza Mahmoud ni kwamba yuko porini na watoto lakini hafahamu ni wapi alipo ila ni kijijini sana."

Roberto alimjibu.


"Eee Mungu wangu asante kwa muujiza huu, na vipi kuhusu Daktari Abbas?"

Jackline alimshukuru Mungu akiwa anaelekea chini kusujudu na kisha akamuulizia mume wake.

0 comments:

Post a Comment

Blog