Search This Blog

Thursday 27 October 2022

ANGA LA WASHENZI (1) - 5

 











    Simulizi : Anga La Washenzi (1)

    Sehemu Ya Tano (5)





    ***



    Klak! Klak! - Klak! Klak! Kitasa kikalia pasipo mlango kufunguka. Jona akajaribu kuupush kwa uzito wake, akashindwa. Mlango ulikuwa mgumu na mzito.



    Basi akarudi nyuma na kuukita teke, ukavunjika! Akazama ndani ya chumba hiki cha Eliakimu na kuanza kupekuapekua kwa macho yake.



    Kitanda kilikuwa hovyo. Na kulikuwa kuna nguo kadhaa juu yake. Kabati la nguo lilikuwa limefungwa nusu, dirisha nalo likiwa limesukumwa kidogo.



    Haraka Jona akatazama droo za kitanda. Akazisogelea na kujaribu kuzifungua kama zipo wazi. Akaona zimefungwa. Akapata tumaini.



    Akachukua ufunguo kule alipoelekezwa na Nade kisha akafungua droo hizo. Ndani akakuta mafaili kadhaa, akayapekua kwa haraka haraka na kuyakusanya. Akatoka ndani ya chumba.



    Kushika korido, akakutana uso kwa uso na Alphonce aliyekuwa amesimama mlangoni.



    "Habari yako?" Alphonce akasalimu kinafki. Kisha akatabasamu na kuuliza:



    "Nimekushtua, unh?"



    Jona akasonga mpaka sebuleni akitembea kwa kujiamini.



    "Kivuli changu kitawezaje kunishtua?" Akauliza akisimama. Kati yao kulikuwa na hatua kama nne tu zikiwatenganisha. "Najua umekuwa kivuli changu ukinifuata kila ninapoenda. Nakutarajia kila ninapotoa mguu."



    Kukawa kimya kidogo wakitazamana kwa macho ya tahadhari. Alphonce akatazama mkono wa Jona, kisha akayarudisha macho yake usoni mwa mwanaume huyo.



    "Umekuja kufanya nini hapa?" Akauliza.



    "Hiyo si kazi yako," akajibu Jona.



    "Nani amekuruhusu kuja hapa?" Alphonce akauliza tena. "Hii kesi haikuwa yako bali ya inspekta Faridi."



    "Najua," Jona akajibu. "Hii kesi ni yangu pia kwani nami nahusika ... actually, nimewasiliana pia na Faridi juu ya hili."



    Kukawa tena kimya. Akili zao zilikuwa zinaongea mengi kuliko midomo.



    "Kwahiyo basi, ungeniwia radhi ukanipisha niende zangu," Jona akapendekeza. Alphonce akamtazama mwanaume huyo kwa kuminya macho kisha akamtaka amkabidhi kile alichokuwa amekishika mkononi.



    "Kwanini nikukabidhi? Wewe unahusika na kesi hii?"



    Alphonce hakujibu hayo, badala yake akaendelea kumsisitizia Jona amkabidhi yale mafaili. Na sasa akamtishia endapo asipifanya anachokitaka.



    Jona akacheka.



    "Unadhani unaweza ukanifanya kitu?" Akamuuliza. "Ni mara ngapi umejaribu kuniua ukashindwa?"



    Alphonce akabinjua lips zake asiseme kitu.



    "Au unadhani sifahamu hilo? Ukamuua na mfanyakazi mwenzangu pia ... yote nayafahamu. Usidhani mimi ni mjinga, Alphonce. Nangoja muda wangu ufike," Jona alisema kwa sauti makini akiwa amezamisha mkono wake wa kushoto mfukoni.



    Alphonce akaguna kidharau.



    "Wakati gani huo Jona? Unadhani unaweza ukapigana na ukuta?" Kisha akacheka. "Kutaka kujua vingi, kulimuua paka. Kwanini usicheze kwa mujibu wa ala ya muziki?"



    Akaongezea:



    "Jona, hakuna mtu aliye upande wako. Tambua hilo. Unatakiwa kubaki jeshini, lakini acha kufuata nyayo za wakubwa zako, ikiwemo mimi kwani kamwe hautafanikiwa!"



    Jona hakusema kitu ila moyoni alikuwa anapasuka.



    "Uliacha jeshi, mbona umerudi? Kwa mwerevu angejifunzia hapo."



    Jona akasaga meno. Alikabwa na hasira kali, lakini akipambana asiionyeshe. Bado kuna kitu alikuwa anakitaka toka kwa Alphonce.



    "Mliteketeza familia yangu, mkaharibu kila kitu changu. Niliwakosea nini?"



    Alphonce akacheka. "Nimeshakueleza, Jona. Na ukiendeleza ukaidi, mkono huu ulioteketeza familia yako, utakuteketeza na wewe pia!"



    "Nani alikutuma, Alphonce?" Jona akauliza. Macho yake yalikuwa mekundu kama bendera.



    "Sina muda wa kuzoza tena, Jona," Alphonce akamjibu. Kisha akamuamuru:

    "Nipe hayo mafaili au niyachukue kwanguvu?"



    Jona akayaweka mafaili mezani.



    "Haya hapa. Chukua."



    Alphonce akatabasamu kwa dharau.



    "Nilikuwa naingoja sana hii nafasi," akasema akivua koti lake la suti. "Leo nitakufunda adabu na kuheshimu wakubwa zako."



    "Unaonaje tukitoka nje?" Jona akapendekeza. Alphonce kwa majivuno akaufungua mlango na kutangulia kumbini. Akakunja ngumi na kusimama sawia kwa ajili ya mpambano.



    Jona akamtazama mwanaume huyu kwa macho ya kina. Akamkagua kuanzia juu mpaka chini kisha akasema na moyo wake.



    Akakunja ngumi, akatanua miguu kupata balansi. Basi haraka Alphonce akamvamia. Akarusha ngumi tano kwa wepesi mno na kwa hasira!



    Vuup! - vup! vuup! - vup!



    Kinyume na mwili wake ulivyo, alikuwa mwepesi kwenye kufanya maamuzi na kujifyatua. Alikuwa ana haja ya kumpiga Jona kuliko Jona alivyokuwa na haja ya kumpiga yeye.



    Alikuwa anatumia nguvu nyingi kushambulia. Lakini mdhaifu kwenye kujikinga, Jona akatambua dhaifu hilo. Lakini hakuwa na haja ya kumuua Alphonce. Hakudhani kama mwanaume huyo anastahili kufa kwa haraka.



    Hakustahili kabisa!



    Mwanaume huyu alistahili kifo cha taratibu taratibu. Mwanaume huyu alistahili mateso ya kufanya kifo kionekane ni ahueni.



    Mwanaume huyu alistahili ahisi angalau robo ya maumivu aliyoyapata mkewe na mtoto wake ndani ya moto mkubwa wa kuteketeza!



    "Shit!" Alphonce akalaani. Alikuwa sasa ametimiza idadi za ngumi ishirini pasipo kufanikiwa hata moja! Na wala Jona hakuanza kumshambulia.



    Akabadilisha mtindo. Sasa akawa anamshambulia Jona kwa mateke zaidi na ngumi za kushtukiza. Hapa sasa akafanikiwa kumtwanga Jona ngumi moja ya shavu iliyompepesa!



    Akatema damu na kujipangusa na mgongo wa kiganja. Akaghafirika mno. Akasahau agano lake juu ya Alphonce, akaanza kumshambulia mithili ya nyuki waliotibuliwa mzingani!



    Akapangua ngumi za Alphonce kwa mateke. Na kwa kasi ya radi, kabla Alphonce hajafikisha ngumi juu ya mwili wake, yeye akawa ameshampachika mwanaume huyo mateke matatu!



    Alphonce alikuwa mwepesi, ila Jona alikuwa mithili ya umeme. Alikuwa anatambua nyendo za Alphonce kabla hajaamua hata kuzitekeleza.



    Alphonce akagugumia maumivu akiwa chini. Kifua kilikuwa kinamuwaka moto. Alimtazama Jona kwa ghadhabu kisha akajikakamua kunyanyuka arudi kwenye pambano.



    Akakimbia kumfuata Jona, lakini kabla hajafanya shambulizi lolote, akastaajabu Jona amefyeka miguu yake na yupo hewani kimo cha ndama!



    Hajakaa vema, akashindiliwa teke la tumbo lililombamizisha sakafuni na kumcheusha damu lita moja!



    Akatulia kwa muda chini. Alikuwa hajielewi kwa maumivu makali aliyoyapata. Kichwa kilikuwa kinamgonga, tumbo lilikuwa linamvuta! Alihisi kiuno pia kimeteguka.



    Akamtazama Jona, akamwona mwanaume huyo akiwa amesimama mkono wake wa kushoto upo mfukoni. Akamuuliza;



    "Umemaliza?" kisha akacheka akionyesha kinywa chake kilichokuwa chekundu kwa damu. "Wewe mshenzi tu! Mshenzi tu kwangu. Unasikia?"



    Jona hakujibu kitu. Alikuwa anamtazama na macho yake mekundu.



    "Bado nakumbuka vizuri siku ile," Alphonce akajinasibu. "Mkeo alikuwa anapiga yowe kukuita. Mwanao alikuwa analia kwa namna moto ulivyokuwa unamtafuna!"



    Akacheka.



    "Ilikuwa ni siku maridadi sana! ... siku maridadi sana. Sitaisahau. Ilikuwa ni siku niliyolipiza kisasi changu cha kwanza dhidi yako. Ilikuwa ni siku niliyokufanya nawe uhisi kile nilichopitia mimi kwa kunipokonya nafasi niliyokuwa nayo jeshini.



    Ulinifanya nidharaulike sana. Kila mtu alikuona na kukusifu wewe. Kila mtu alikuona shujaa. Kila mtu akanisahau mimi ni nani. Juhudi zangu zote jeshini zikawa ni bure!"



    Akatemea damu pembeni.



    "Nilikuchukia sana, na hata sasa pia. Ulinipokonya kile nilichokuwa nacho, lakini ..." akaangua kicheko. "Wewe nimekupokonya zaidi!"



    Akacheka tena.



    "Bado mimi ni mshindi Jona! Bado mimi ni mshindi!"



    Jona akachuruza chozi. Akakunja ngumi yake kwa hasira. Moyo wake ulikuwa unavuja damu. Alimkumbuka mkewe. Alimkumbuka mwanae.



    Akasaga meno. Mishipa ya damu ikamsimama kichwani.



    "Na hata sasa mimi bado ni mshindi!" Alphonce akaropoka akisimama kwa tabu. Akamjongea Jona apate kurusha tena turufu lake la pambano.



    Lakini katika namna ambayo hakuielewa ilitokeaje, akastaajabu kujikuta yupo chini! Kitu pekee alichokuwa anakumbuka, ni kusikia kitu kama upepo ukipita masikioni mwake.



    Lakini zaidi hakuweza kuusogeza mwili hata kidole! Ni macho tu ndiyo yalikuwa yanasonga huku na kule.



    Hakuuhisi mwili wake kabisa.



    "Jona!" Akaita. "Jona! Jona umenifanya nini? Umenifanya nini Jona?"



    Jona akamtazama pasipo kusema kitu. Macho yake yote yalikuwa yanatiririsha machozi.



    "Nisaidie tafadhali!" Alphonce akaomba. Jona akampa mgongo na kwenda zake ndani. Akachukua mafaili yake na kuondoka akimwacha Alphonce anapiga kelele sakafuni.



    **



    Saa nne usiku...



    Kwa mbali muziki laini ulikuwa unaita. Mazingira yalikuwa yametulia kwahiyo basi ungeweza kusikia vizuri sauti tamu ya kukwaruza ya Michael Bolton akiimba kibao chake matata cha Soul Provider cha mnamo mwaka 1989.



    Juu ya kochi, alikuwa ameketi Jona akiwa kifua wazi na kibukta chepesi cha kulalia. Juu ya meza ilikuwa imekaa chupa kubwa ya kinywaji kikali, kando yake kulikuwa kuna yale mafaili aliyoyatoa kwa Eliakimu.



    Akanyanyua chupa yake ya kinywaji na kuipeleka mdomoni, akagigida mafundo mawili makubwa. Akiwa amekunja uso, akarejesha chupa hiyo mezani akiisoma jina lake.



    _Bacardi 151_



    Kwenye lebo yake ya kiasi cha ulevi kilikuwa na alcohol 75.5%! Haikuwa mchezo kabisa!



    Jona alikinunua kinywaji hiki maana aliona anakihitaji kwa usiku huo. Huwa anakunywa vinywaji vikali ila siku hiyo alihitaji kikali zaidi na zaidi maana alihisi anaweza akashindwa kulala.



    Kila saa alipokuwa anatulia alikuwa anasikia maneno ya kebehi ya Alphonce kuhusu familia yake. Kila aliposikia sauti hiyo, akamkumbuka mkewe. Akamkumbuka mtoto wake kuliko kawaida.



    Huwa anawakumbuka, lakini leo hii ilikuwa ni kana kwamba ametoka kushuhudia jengo lake likiwa linateketea. Alphonce alimkumbusha kwa kina. Alikitifua kidonda kilichojenga gamba.



    Akashindwa hata kupekua mafaili yale, akabaki anakunywa tu. Baada ya kuongeza mafundo matatu tu ya Bacardi, kichwa kikashindwa kuendeleza kazi, fahamu zikakata, akajimwagia kochini!



    Jinamizi lililokuwa linamtesa, leo likarudi kwa nguvu zote.



    Saa tatu asubuhi, SPACE BUTTON.



    Kulikuwa bize kama ilivyo ada. Watu walikuwa wanatazama vioo vya tarakilishi zao huku vidole vikitwangatwanga 'keyboard'. Watu hawa kwa idadi walikuwa nane, hakukuwa na mwanamke hata mmoja.



    Mazingira yalikuwa tulivu ukiachana na sauti za keyboard. Hakukuonekana kama kuna shida yoyote, wala kama inaweza kubashiriwa kwa hapo mbeleni.



    Hali ya hewa ilikuwa baridi, viyoyozi vilikuwa moto. Kuna baadhi yao wakawa wanavuta vikamasi na huku pua zao zikiwa nyekundu kwa kuzifikichafikicha mara kwa mara.



    Pengine baridi lilikuwa kali kuliko siku zingine. Mmoja akapaza sauti kumuita Moderator na kumtaka apunguze kasi ya viyoyozi hivyo la sivyo watakufa.



    Kidogo zogo likatokea hapa watu wakiunga mkono hoja hiyo. Ni kama vile walikuwa wanamngojea 'shujaa' ajitokeze kusemea hilo jambo wapate kum 'mback-up'. Kinyume kabisa na taratibu ndani ya chumba cha SPACE BUTTON watu wakaruruma na kuzoza. Haikuwa inaruhusiwa kufanya hivi.



    Moderator alitii haja yao akapunguza kasi ya viyoyozi, kazi zikaendelea tena kwa ukimya. Lakini miongoni mwa watu hao waliopaza sauti zao kuhusu ukali wa viyoyozi, si Marwa wala Panky aliyekuwapo.



    Wao walikuwa kimya. Wao walikuwa wakiendelea na kazi zao kana kwamba hakuna kilichojiri, hakuna walichosikia.



    Zikapita dakika tano watu wakiendelea na kazi. Kama ilivyo ada ndani ya SPACE BUTTON ni keyboard tu ndiyo zikawa zinasikika. Ilipohitimu dakika ya sita, mara taratibu viyoyozi vikaanza kurudi kwa kasi.



    Baridi likawa jingi, watu wakaanza kupata shida. Ni kana kwamba walipelekwa kwenye kilele cha mlima mrefu mno.



    Wakaanza kulalamika tena, mada hii Moderator alikuwa ametoka kidogo. Wakazoza na kuzoza, Moderator aliporudi akastaajabishwa na hali hiyo ya 'soko'. Kabla hajafoka kukemea na kutoa vitisho, akatambua baridi lilikuwa limeongezeka maradufu.



    Haraka akatazama tarakilishi yake. Akabofya keyboard mara kadhaa. Akapiga ngumi mezani kisha akatoka ndani. Bila shaka alikuwa anaenda kuangazia mitambo kama ina hitilafu.



    Kiwizi, Marwa akamtazama Panky, akatabasamu, alafu akarudisha uso wake kwenye tarakilishi.



    "Nimefanikisha!" Ujumbe ukaingia kwenye tarakilishi ya Panky kwa kutumia jina la M-spy.



    Panky akatabasamu. Akamtazama Marwa kiwizi, alafu akachapa haraka kumjibu.



    PANKY: Sure? (Hakika?)

    M-SPY: Yah sure. (Ndio hakika).

    PANKY: How did you do that man? (Umewezaje jamaa?)

    M-SPY: Aaanh! Maswali gani hayo? Nataka nitazame kama naweza pata chochote kwenye mashine yake. Nipe muda kidogo.



    Marwa akaanza kuitembelea tarakilishi ya Moderator kwa kutumia ya kwake. Alikuwa anafanya hayo kwa wepesi kwani hakuwa na muda wa kutosha, na usalama ulikuwa finyu mno.



    Alijua endapo Moderator angepata muda wa kutulia kwenye mashine yake, angezijua njama zake. Kwahiyo alitakiwa kutumia fursa hiyo upesi kabla mwanaume huyo hajarejea kitini.



    Dakika mbili tu, Moderator akawasili. Tayari hali ya hewa ilikuwa imetulia. Akatazama wafanyakazi wake akikagua tarakilishi zao kwa macho, kisha akaketi. Akashusha pumzi ndefu.



    Akakagua tarakilishi yake akijiuliza nini shida. Akakagua kila kitu, hakuona tabu. Akakagua na tarakilishi za wafanyakazi wake kwa kutumia ya kwake, kote akaona wakifanya kazi zao.



    Akajilazimsha kuamini tatizo lile la viyoyozi litakuwa ni la mitambo.



    PANKY: Umefanikiwa?

    M-SPY: Kiasi chake. Bado nahitaji kuingia tena kwenye mashine yake kuna kitu sijamalizia.

    PANKY: Utaingiaje? Amesharejea. Ataongeza uangalifu sasa hivi kuliko mwanzoni.

    M-SPY: Najua. Natazamia namna nitakavyofanya jambo hili kwa usalama.

    PANKY: Be careful. (Kuwa makini)

    Kukawa kimya kidogo kwa dakika nne, Ujumbe wa Marwa uka 'pop-up' kwenye kioo cha tarakilishi ya Panky.

    M-SPY: Nimepata wazo.



    Akamshirikisha wazo hilo Panky, naye akalikubali. Ikapita dakika moja, mara Panky akadondoka chini akihangaika kuhema kana kwamba koo lake la hewa limesiliba! Mbavu zikamsimama. Mishipa ikamchomoza. Macho akayatoa huku shingo ikishupaa.



    Watu wakapigwa na butwaa. Wakaamini Panky atakuwa ameathiriwa na mabadiliko yale ya hewa yaliyokuwa yanatokea ndani ya chumba hicho hapo nyuma.



    Haraka wanaume watatu wakafanya kumsaidia wakiwa pamoja na Moderator. Wakampeleka kupata huduma huko nje. Sasa Marwa akatimiza adhma yake upesi.



    Baadae wakati wa kupata chakula cha mchana, wakaketi meza moja na Panky kuteta. Walihakikisha hakuna mtu aliyekuwa anawasikia, na wapo salama.



    "Panky, kwanini hukuwa muigizaji?" Marwa akatania. "Unajua ulintisha aisee. Nikadhani huenda kweli umepata tatizo! Ilinihitaji roho ngumu kweli kukupuuzia."



    Panky akatabasamu.



    "Sikujua kama nina kipaji hicho, nitalifanyia mazingatio ... anyway, umefanikisha?" Panky akauliza.



    Marwa akameza tonge kwanza. Akatikisa kichwa.



    "Ndio, nimefanikiwa. Nadhani nimepata kila tunachokihitaji."



    Panky akatabasamu. Lakini mara kiganja kikagusa bega lake, akageuka na kukutana na uso wa Moderator.



    "Njoo," Moderator akamwambia kwa lafudhi ya ki Mandarin, kisha akaenda zake. Marwa akamtazama Panky kwa hofu. Moyo wake ulikuwa unakimbia kwa kasi. Alimshika mkono Panky akamwomba awafikishie taarifa familia yake endapo hatofanikiwa kutoka hai.



    Kwa haraka pia akamwambia Panky taarifa alizozipata atakazikuta chini ya keyboard karatasini, kisha akaenda zake.



    Panky akabaki na mawazo. Vipi kama Marwa amegundilikana? Hakupata hamu ya kula tena. Kifua chake kilikuwa kimejawa hofu. Je, watatambua hata kuumwa kwake kulikuwa ni mpango? Akajiuliza.



    Alihisi mwili wake umekuwa wa baridi.



    Mara kengele ya kurejea kazini ikalia, wote wakanyanyuka toka kantini na kurejea ndani ya SPACE BUTTON. Marwa hakuwapo kwenye kiti chake. Akamtazama na pale kwa Moderator, hakumwona, si yeye wala Moderator.



    Basi haraka akanyanyuka na kwenda sehemu ya Marwa, akavuta droo ya keyboard na kutazama kwa chini, akaona kikaratasi kidogo cheupe. Akakibeba na kurudi sehemu yake upesi.



    Hakukitazama kikaratasi hicho, alikiweka mfukoni na kuendelea na kazi yake lakini kila saa akawa anatazama kama atamuo
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/na Marwa ama Moderator.



    Baada ya kama nusu saa, Moderator akarejea ila Marwa hakuonekana. Hapo sasa Panky akapoteza matumaini. Akahisi kweli pengine Marwa ameuawa.



    Hakuweza kufanya kazi vizuri kabisa. Kichwani hakukuwa na maelewano kabisa, alikuwa anamuwaza Marwa. Mpaka unafika muda wa kuondoka kazini, Marwa hakuonekana popote pale!



    Panky akakosa amani.



    "Kuna shida?" Moderator akamuuliza Panky aliyekuwa amebaki mwenyewe kitini. Chumba kizima cha SPACE BUTTON kilikuwa cheupe.



    Panky akashtuka sana. Hakuweza kutazamana macho na Moderator. Alizama fikirani na hata hakuwa anawaza kama mule ndani kaachwa na Moderator pekee.



    Akaweweseka,



    "Hamna shida! -hamna!"



    "Sasa mbona upo hapa mpaka muda huu?"



    Akakosa jibu. Akatazama kushoto na kulia kwake, hakukuwa na mtu yeyote. Akazima tarakilishi yake na kusimama.



    Pasipo kuaga akaenda zake. Moderator akamtazama mpaka mwisho mwanaume huyo akiishilia.



    Alipotoka ndani ya jengo hilo, asiamini, akaongeza kasi mpaka kituo cha mabasi. Akashangaa hakuitwa. Akaketi hapo kituoni akitazama barabara, labda anaweza kumwona Marwa.



    Akaketi kwa muda mrefu hapo pasipo matunda. Akaamua kupanda zake gari arudi nyumbani. Sasa akawa anafikiria ni kwa namna gani awataarifu wazazi wake Marwa juu ya mtoto wao.



    Kwahiyo kama Marwa akiuawa, wazazi wake wataendelea kupewa antidote? Ama ndiyo wataachwa wajifie maana hawana tena umuhimu?



    Alilaza kichwa chake juu ya kioo cha dirisha akiwaza.



    Watakuwa wamemuuaje Marwa? Na kama kweli wamegundua alidukua tarakilishi ya Moderator, hawatamdadisi kujua kwanini amefanya hivyo? Je, Marwa atawatoa chambo?



    Yalikuwa ni mawazo baada ya mawazo. Shukrani tairi la gari lilizama kwenye kabonde kadogo barabarani gari likayumba, Panky akajigonga na kurudi fahamuni. Akatambua alikuwa anakaribia kupitishwa kituo!



    "Shushaa! Shusha hapo!" Aliropoka akisimama. Mfukoni akatoa simu na pesa yake akijongea kwenda mbele kushuka. Mara ujumbe ukaingia.



    Haraka akausoma.



    'Mbona hujaningoja? Upo wapi?' Ilikuwa ni ujumbe toka kwa Marwa. Akajikuta anapiga yowe la ushindi. Akampatia konda shilingi alfu mbili na wala chenji hakuchukua.



    "Oh no keep change, una mawazo mengi itakufariji weekend!" Alisema kisha akiondoka kibingwa.



    Alicheka. Alihisi kifua chake kimekuwa chepesi.



    Marwa yupo hai!



    ***

    Saa kumi jioni, Jangwani Sea breeze.



    Akiwa amevalia gauni fupi jeusi lililombana na chini viatu vyekundu vyenye kisigino kirefu Miranda alitazama huku na kule baada ya kuingia kwenye hoteli hii ya wastani.



    Alikuwa kapendeza na anavutia japokuwa usoni hakuwa amejipara. Alibaki kiasili.



    Nywele zake ndefu za bandia zilikuwa zinarukia huku na kule akipepesa kichwa. Mara akamwona mke wake Boka akiwa ameketi kwa juu, kwenye ghorofa moja iliyokuwepo hapo. Akapandisha ngazi kuelekea huko juu kumkuta.



    "Usiniambie nimechelewa?" Akasema Miranda kwa tabasamu huku akiketi. Mke wa Boka alikuwa ametulia kitini ndani ya vazi la kitenge. Mezani kulikuwa kuna chupa ya soda ya Cocacola.



    "Wala hujachelewa, karibu," akasema Mama huyu. Macho yake mekundu yalikuwa yameingia kwa ndani.



    Wakasilimiana. Miranda akatazama huku na huko kisha akauliza:



    "Hao wazungu wako wapi? Hawajafika bado?"



    Mke wa Boka akamtazama kwa sekunde tano, alafu akamjibu:



    "Hamna mzungu yoyote anayekuja hapa. Hamna wageni wowote toka nje. Nimekuita hapa uje uonane na mimi!'



    "Serious?" Miranda akatahamaki.



    "Yes, serious," mama akajibu akijitengenezea kitini.



    Miranda akaanza kuhisi jambo. Kwa kiasi akawa na hofu moyoni. Aliukagua uso wa mke wa Boka vema, akajua kitumbua kitakuwa kimeingia mchanga.



    Akapanga kukana kila jambo hapa endapo ataulizwa kuhusu Boka.



    "Miranda, umeanza lini mawasiliano na mume wangu?"



    Nilijua tu, Miranda akasemea kifuani. Mawazo yake yalikuwa sahihi. Kitumbua kimeingia mchanga.



    "Mawasiliano ya kivipi, mam?" Akauliza kana kwamba hajui kinachoendelea. Mke wa Boka akamjuza anajua kila kitu na hivyo basi asijaribu kumdanganya hata kidogo.



    Anajua amekuwa akikutana na mumewe na pia wana mahusiano kati yao hadi kupanga mikakati ya kusafiri pamoja na hata ndoa.



    Miranda akabaki amestaajabu. Sasa rangi zake zilikuwa wazi, hakujua kipi cha kusema zaidi ya kuwa kimya na kutazama chini.



    "Sikujua kama wewe ni mbweha kiasi hiki!" Mke wa Boka akateta akisaga meno. "Najua humpendi Boka, unataka tu pesa zake ama kumtumia. Unajua nimetoka naye wapi?"



    Miranda hakusema kitu.



    "Nakuuliza wewe, unajua nimetoka naye wapi?" Mama akasisitizia swali kwa sauti ya kufoka. Bado Miranda alikuwa kimya anatazama chini.



    "Nakuuliza wewe malaya una ..." Mama akanyanyua chupa ya soda na kumrushia Miranda kwanguvu. "...jua nimetoka naye wapi?"



    Ajabu, Miranda akaidaka chupa hiyo kana kwamba kitenesi kisha akaiweka mezani. Akamtazama mke wa Boka na kumwonyeshea ishara ya kidole kikicheza.



    "Usijaribu tena huo ujinga."



    Mke wa Boka akastaajabu. Mwanamke wa aina gani huyu? Asiseme kitu, Miranda akanyanyuka na kwenda zake mke wa Boka akimtazama.



    Punde kwenye siti ile aliyokuwa amekaa Miranda, akaja kuketi mwanamke mwingine mnene mweupe. Naye alikuwa amevalia kitenge kama kile cha mke wa Boka, sare.



    Huyu alikuwa ni rafiki yake mke wa Boka na walikuja naye hapo tukioni lakini wakatengana muda mfupi kabla Miranda hajawasili eneoni.



    "Vipi shoga?" Mwanamke huyo akauliza kwa hamu. "Mbona ameondoka anatamba kiasi kile?"



    Mke wa Boka akaminya lips zake. Hakutaka kusema kitu. Alisimama na kumwambia shoga yake waende zao.



    Wakajipaki kwenye gari na kuanza safari.



    "Niambie basi, Adela. Umeniita mwenyewe hapa alafu unaninyamazia, ndo nini?" Shoga akalalama.



    "Hamna kitu nilichomfanya," akajibu mke wa Boka kisha akang'ata lips yake karibia kuichana. "Amenionyeshea dharau kubwa sana. Lazima nimfunde adabu!" Akabamiza usukani.



    "Lazima nimfunze adabu! Hawezi akanifanyia dharau kiasi kile malaya mbwa yule!"



    Macho yake yakaanza kulowana. Hata shoga yake akaogopa kumwongelesha, akaomba tu safari yao iwe salama maana dereva hakuwa sawa hata kidogo.



    "Nitaona kama na risasi utaweza kuidaka!" Akasema mke wa Boka kwa ghadhabu.



    ---



    Baada ya robo saa...



    Miranda ndani ya gari kwenye foleni la mataa.



    'The woman will spoil the food. She has already known all of our moves' (Mwanamke atatuharibia chakula. Ameshajua nyendo zetu zote) Miranda aliutuma ujumbe kwa BC.



    'What woman? His wife?' (Mwanamke gani? Mkewe?) Ujumbe wa BC ukauliza.



    'Yes, it's her.' (Ndio, ni yeye) Miranda akajibu.



    'Then take care of her immediately!' (Basi mzingatie mara moja!)



    'Thanks' (Ahsante) Miranda akatuma ujumbe huo akitabasamu.



    ***

    Saa mbili asubuhi kwa ofisi ya Kamanda wa polisi mkoa ..



    "Umeambiwa uingie," alisema mwanamke mmoja polisi aliyetoka ndani ya ofisi ya Kamanda. Mwanamke huyu alikuwa amevalia suti ya kike rangi ya kahawia na alikuwa anamwongelesha Jona.



    Jona akamshukuru na kisha akanyanyuka kuzama ndani, akamkuta Kamanda akiwa anasoma gazeti lake kama ilivyo ada nyakati hizi za asubuhi. Akampa heshima yake na kuketi.



    "Nimekuja mkuu."



    "Karibu," akajibu Kamanda na kama vile hakuwa anajua kama kuna mtu hapo, akaendelea kusoma gazeti lake. Akamkalisha Jona kwa muda wa dakika sita kukiwa kimya.



    "Aaannh!" Akafunga gazeti akizinduka. "Ndo umefika enh?" Akauliza kipuuzi. Jona hakusema jambo. Kamanda akatazama saa yake ya mkononi na kisha simu yake.



    Alikuwa anamngoja Alphonce. Mpaka muda huo mwanaume huyo hakuwa ameripoti eneoni. Sasa atamruhusuje Jona akaendelee na kazi wakati mwanaume huyo wa kumfuatilia hajawasili?



    "Em ngoja kidogo."



    Akanyanyua simu yake kupiga. Simu ikaita na kuita pasipo kupokelewa. Akasonya akitikisa kichwa.



    _Ananijaribu huyu_ akasema kifuani mwake. Ina maana hakunielewa nilichomwambia? Sasa dharau inavuka mipaka.



    Hakuwa na namna akamruhusu Jona aende zake akimuagiza amuitie afande Holombe mara moja pindi atakapotoka nje. Jona akatimiza agizo. Mwanaume mrefu mweusi akaingia ndani ya ofisi ya Kamanda na kusimama kwa ukakamavu.



    Kamanda akamuagiza akamfuatilie Jona popote pale atakapokwenda. Jicho lake lisibanduke kumuacha abadani.



    "Ukishindwa, usirudi hapa," Kamanda akatoa kitisho. Holombe akaenda zake kutimiza agizo. Akatoka nje ya ofisi hiyo akiangaza kumtafuta Jona, mara akasikia kiganja begani kugeuka akakutana na mlengwa wake.



    "Bila shaka unanitafuta mimi," Jona akajinasibu. Holombe akatabasamu. Akajaribu kukanusha lakini uso wake ukimsaliti.



    "Usijali, najua umepewa agizo na kamanda. Ila tu kiukweli, hutaweza kunifuatilia Holombe."



    "Umejuaje jina langu?"



    "Nadhani ungejiuliza kwanza nimejuaje kama umetumwa unifuatilie ... anyway, naitwa inspekta Jona. Nisingependa kukuchosha, tutakuwa pamoja, lakini itakapofikia mahali nitakuacha."



    "Lakini mkuu ka--" kabla Holombe hajamalizia, Jona alikuwa tayari yupo mbele hatua nne. Hakuongea tena.

    --

    Saa nne kasoro robo, Aga khan hospital...



    "Karibu," daktari alimwambia Jona huku akitazama tarakilishi yake. Jona pasipo kupoteza muda akamtaka ampashe maendeleo ya mgonjwa wake, Nade, na kama kuna uwezekano wa kuonana naye.



    Hapa sasa daktari akamtazama Jona akiacha kila shughuli yake. Akamwambia Nade amefariki. Jona akashangazwa. Hakutegemea kabisa kupokea habari hizo kwani alimwona Nade akiwa tayari amesharudi kwenye hali yake.



    Vipi sasa kufa huku ghafla?



    Daktari asimpe Jona maelezo ya kutosha, akasisitizia tu amefariki na mwili wake umeshahifadhiwa mochwari.



    "Inaonekana alikuwa ana internal damage iliyokawia kupona na hatimaye kuathiri organ zingine za mwili." Daktari akapandisha mabega yake na kumalizia: "Kifo ni kwa kila mmoja."



    Jona akahisi kuna jambo halipo sawa hapa, na hakuwahi kuwa na shaka na akili yake pindi awazapo hivyo. Akamwagiza daktari aongozane naye kwenda kuutazama mwili wa Nade huko mochwari.



    "Hapana. Nimeba --"



    "Sasa hivi!" Jona akaamuru akimtazama daktari kwa macho ya simba. Daktari akahofu. Akanyanyuka na kutii amri, Jona akapata kukagua mwili wa Nade.



    Punde akagundua jambo.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Ameuawa," akasema kwa kujiamini. Alitomasa tomasa shingo ya marehemu Nade akagundua misuli yake ilikuwa imetapanywa, na koo lake lilikuwa lina ufa.



    Akamtazama daktari na kumwambia:



    "Ameuawa kwa Manual strangulation. Ulikuwa unajua hilo, sio?"



    Manual strangulation ni nini? Tendo hili kwa jina lingine hujilikana kama throttling. Ni kitendo cha kuminya shingo ya mlengwa kwa presha kubwa mpaka kupelekea kupoteza fahamu ama kufa kabisa.



    Daktari akashtuka kusikia habari hizo. Akabanwa na kigugumizi.



    "Unataka kuniambia ulikuwa hulifahamu hili ama ulikuwa unanificha?" Jona akamuuliza. Hakuwa yule Jona umjuaye, alikuwa sasa anatisha. Endapo mtoto amgemtazama, basi angekunywa bilauri lote la uji kwa kauli moja.



    "Nani kamuua?"



    "Sijui nani kamuua!"



    "Nani alikuwa wa mwisho kuingia ndani ya chumba chake?



    Daktari akababaika. Jona akamlamba kofi moja zito. Daktari akapepesuka kama kapitiwa kimbunga.



    "Alikuwa ni yule ... alikuwa yule askari mwingine!" Daktari akaropoka akisugua shavu lake lililozabwa.



    "Sasa naenda kukutia ndani kwa kushirikiana na muuaji!" Jona akafoka. Akamwamuru daktari aongoze mpaka chumba cha kusimamia CCTV kamera zilizopo hospitali. Walipofika huko Jona akataka kuchukua tape (tepu) inayomuonyesha Alphonce akitoka katika chumba cha Nade.



    Ajabu tape hiyo haikuwapo. Wale wasimamizi wakamwambia Alphonce aliwapokonya. Akaishiwa nguvu. Akatoka hospitali na kwenda kantini akiwa ameketi na Holombe. Kwa muda akawa kimya. Hakuagiza hata chakula, isipokuwa Holombe pekee. Mara akachomoa simu yake mfukoni na kupiga, akaibinyia sikioni.



    Alikuwa anampigia yule polisi aliyempatia kazi ya kumlinda Miranda. Punde polisi huyo akapokea na kumweleza Jona kuwa alipewa oda toka kwa mkubwa wake aache kazi hiyo mara moja na kureja kituoni. Ni kwa muda sasa hakuwapo hapo.



    Na ni kweli, Jona akajilaumu kutotambua jambo hilo mapema. Ilikuwaje akapitiwa na uzembe kama huo.



    "Ni nani huyo?" Akauliza.



    "Inspekta Alphonce," akajibiwa. Akakata simu na kuiweka mfukoni. Akaagiza maji makubwa akawa anakunywa akiwa anawazua.



    Sasa ilikuwa wazi Alphonce alikuwa anajaribu kuficha jambo. Kumuua Nade na kung'ang'ania mafaili aliyoyapata kwa Eliakimu vilithibitisha hayo. Lakini vikathibitisha zaidi kuwa Alphonce hakuwa polisi safi. Kwa namna moja ama nyingine atakuwa anahusika na genge la Sheng, BC au pia wakina Nyokaa.



    Kuna haja ya kumfikisha mbele ya dola? Akajiuliza. Akatafakari na kubaini hana haja hiyo. Moja, Alphonce alikuwa tayari ni nusu mfu. Atamwacha afe taratibu tu kuonja ladha ya madhalimu yote aliyoyafanya. Pili, inawezekana kabisa kufanya jambo hilo kukawa ni mbio za sakafuni. Alphonce alishasema hapo awali, anajua kulamba mkono wa wakubwa. Je watamwacha aangamie?



    Haikuingia akilini mwa Jona.



    Lakini vipi kama kibao kikaja kugeuzwa kwake? Napo akajiuliza. Ila hakuwa na hofu sana kwani alikuwa na ushahidi wa kumfanya awe salama.



    Simu yake ilikuwa ina sauti za Alphonce alizozirekodi kipindi mwanaume huyo akiwa anaropoka. Kumbe alipokuwa ameweka mkono wake mfukoni alikuwa akifanya kazi hiyo.



    Na kama haitoshi, alikuwa ana nyaraka za Eliakimu mkononi.



    Akashusha pumzi ndefu. Mara ujumbe ukaingia simuni.





    Akautazama, ulikuwa umetoka kwa Panky. Alikuwa anamhitaji afike kwa Marwa mara moja wapate kujadili kile walichokipata. Pasipo kupoteza muda akalipia maji yake na kisha kwenda zake.



    "Samahani sitakuhitaji huku," alimwambia Holombe aliyenyanyuka upesi aongozane naye. Holombe akaketi na kumtazama Jona akiyoyoma.



    Ndani ya dakika kadhaa akawa amefika nyumbani kwa Marwa na kuwakuta vijana wake wakiwa wanamngoja mezani.



    "Tumefanikiwa," Marwa akamwambia akitabasamu. Jona naye akajikuta anatabasamu pia.



    "Nini mmepata?" Akauliza.



    "Kuna links mbili ambazo zinaenda kwa majina ya BIRD 002 na BIRD 003. Zimekuwa ni link ambazo zinatumiwa sana kuwasiliana na link ya SPACE BUTTON ambayo bila shaka itakuwa ndiyo BIRD 001. Kwahiyo tunaamini kabisa hizi links ni mojawapo ya wale ndege wa mawasiliano."



    Kwa Jona jambo hili likaleta mashiko. Na lilithibitishwa na majina ambayo links hizo zilipewa, BIRD yaani kumaanisha ndege. Na kwenye ile picha ni ndege ndiyo walitumika kama ishara.



    "Kwahiyo mpaka sasa hizo links mbili kutimiza tano ndizo zimekuwa kitendawili. Hatujajua zipo wapi na zitakuwa zinafanya kazi gani," Panky akaeleza.



    "Hamna shida," Jona akawatoa hofu. "Naamini kwenye hizi tulizonazo zinaweza kutusaidia kung'amua hizo zilizobaki."



    Marwa akamueleza wame 'trace' links hizo mbili na wamegundua mojawapo inapatikana Dodoma na nyingine ikiwa Nairobi, Kenya. Na zaidi ya hapo wamefanikiwa kupata jumbe kadhaa zilizokuwa zinatumwa toka upande mmoja kwenda mwingine.



    Jona akavutiwa na habari hizo. Akawapongeza kwa kazi kubwa waliyofanya. Lakini kama haitoshi, Marwa akamwambia zaidi. Bado wanaweza kuzama kwenye links hizo hata sasa, na kudukua mawasiliano hayo kwa kutumia 'unknown mode'.



    Basi kwa haraka Jona akataka kushuhudia jambo hilo. Marwa akazama kwenye links hizo na kuanza kukagua taarifa wakianza na ile ya Dodoma. Huko wakakuta mambo makubwa yaliyowashangaza mno.



    Kuna kambi ndogo ya Sheng ndani ya manispaa ya Dodoma. Na kambi hiyo kazi yake ni kupokea maagizo toka kambi kubwa iliyopo Dar es salaam, kuyatekeleza na pia kutuma taarifa kuja kambi kuu juu ya kinachoendelea bungeni.



    Kambi hii ya Dodoma ilikuwa inafahamu kila kitu kinachojadiliwa na kitakachojadiliwa bungeni. Ilikuwa inajua maamuzi yote yanayoafikiwa huko na mipango yote ya serikali.



    Lakini haswa katika namna zinavyowagusa Wachina. Haswa namna zinavyowaathiri wao katika nchi na ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati.



    Kambi hiyo ilikuwa inahusika na mauaji ya wabunge na viongozi wote wa serikali waliokuwa kikwazo kwa matakwa ya Wachina kwa kutoa taarifa za viongozi hao kisha kikosi cha wauaji kinaagizwa toka kambi kubwa.



    Kwa ufupi tu,



    Sheng hakuwa tu genge hatari. La hasha! Alikuwa pia ni jasusi wa kiuchumi. Alikuwa ni mtu anayehakikisha maslahi na matakwa ya Wachina yanatimia!



    Kwenye kila mkataba wanaopata Wachina aidha kwenye ukandarasi, ama shughuli yoyote ya kiuchumi nchini, Sheng alikuwa na kivuli ama mkono wake hapo. Kwa kifupi alikuwa anaisambaza dola ya kichina kusini mwa jangwa la Sahara, akianzia Afrika Mashariki na kati.



    Na kwa kufanya hivyo, Sheng anakuwa chini ya serikali ya China. Analindwa na mkono wa serikali hiyo na kupewa nafasi maalum mbele ya macho yao. Anafadhiliwa kifedha, anasikilizwa na kupewa mazingatio ya juu.



    Hakufanya haya kwa bahati mbaya ama kwa sababu za faida ya mbuzi, la hasha, bali kujenga ngome itakayomfanya kuwa salama kiuchumi yeye na koo yake.



    Sasa akiingiza ama kutoa mizigo nchini China ama Tanzania, anapewa 'badge' ya serikali. Anatumia nafasi hiyo kunufaika kwa kupitishia magendo yake. Anatumia nafasi hiyo kujijenga na kuwa tajiri mkubwa mno. Kuifanya koo yake kuwa 'dons'.



    "Hii ishu ni kubwa," akasema Jona. "Ni mtandao mpana mno ambao una nguvu, yatupasa kuwa waangalifu sana. Lakini kwa wakati huo tukipanga namna ya kuangusha mipango hii kama daudi alivyofanya kwa Goliath."



    "Tupo pamoja na wewe katika kila namna," Marwa akamueleza na kumpa moyo.



    "Knowledge is power," (Ufahamu ni nguvu,) Jona akaongezea. "Hatuwezi kupigana na mtandao kama huu kwa ngumi. Lazima uwe na taarifa za kutosha kwanza. Ujue unapiga wapi na kwanini.



    Sasa basi kutambua base hizi ya Dar, Dodoma na Nairobi, hakutoshi kabisa. Impact yake ni ndogo sana kwani kazi zake ni kusafirisha taarifa haswa haswa huku mtendaji mkuu akiwa kambi kuu ya Dar.



    Tunahitaji kujua yale mawimbi matatu. Yale mafiga matatu ya ulinzi. Hayo tukikabiliana nayo na kuyamudu, Sheng atakuwa mdhaifu. Sasa tutafanya vile tunavyotaka."



    Lakini pia akatoa agizo la kuyatunza yale yote waliyoyapata kama ushahidi. Ni muhimu mno. Na hata pale watakapotaka kuyafunua mambo hayo hadharani basi watatuma hizo taarifa kwa vyombo husika kwa kutumia 'anonymous profile'.



    Isijulikane nani ametuma taarifa hizo, wala wapi zimetokea kwasababu kuu mbili. Mosi, kwa usalama wao wakiwa wanaendelea na kazi zao kama kawaida, na pili wapate fursa ya kutambua hatua zitakazochukuliwa juu ya taarifa zao, kama ni kitu kitakachopokelewa ama kufichwa kwanguvu.





    ***



    Saa tano usiku, maeneo ya Msasani.



    Sasha akatazama nyuma yake hatua kadhaa baada ya kuacha geti. Hakukuwa na mtu. Akatembea upesi kulifuata gari aina ya Nissan Murano nyeusi, akafungua mlango na kuzama ndani akiketi siti za mbele kabisa.



    Mwanamke huyu alikuwa amevalia dira jekundu, kichwani nywele zikiwa timu.Ndani ya gari kulikuwa kuna wanaume wawili vijana wa Sheng: Nigaa na Mombo, Nigaa akiwa ameukamatia usukani na huku mwenziwe akiwa ameketi viti vya nyuma.



    "Vipi umefanikiwa?" Nigaa akauliza.



    "Bado naskilizia," Sasha akajibu. "Ila uhakika upo lazima tu ntapata nafasi."



    Kukawa kimya.



    "Nadhani unajua cha kufanya, Sasha. Na jambo hili liwe siri hata dada yako Sarah asilifahamu hata kidogo. Na ujue kabisa hakuna nafasi ya wewe kushindwa kwenye hili. Ukishindwa, utaenda kumsalimu Bite mapema sana," Nigaa akaeleza. Kukawa kimya.



    Hakukuwa na maelezo mengine, Sasha akashuka garini, gari likaondoka.



    ****

    Mwanamke huyo akalitazama gari hilo likiishia alafu akarudi zake ndani na kujiweka kochini akiwaza kwa dakika kadhaa.



    Alikuwa mtegoni haswa. Mtego wa kifo na uhai. Mtego unukao mauti. Mtego unaosaka pumzi yake kwa vumba.



    Sasha masikini mimi ... akajisemea mwenyewe kifuani. Alidhani kukimbilia mkoani kungenusuru roho yake dhidi ya mkono wa mauti uliommaliza Mudy kumbe alikuwa amekosea. Alikuwa tayari kwenye rada.



    Pasipo kuelewa ni kwa namna gani ilitokea, aliwekwa kati na kupewa fursa ya kuchagua mambo mawili mikononi mwake. Mosi, abakiziwe uhai lakini kwa kuenenda namna watakavyo, au pili wammalize mara moja na kumtupia mtoni akawe chakula cha mamba.



    Akajawa na hofu sana.



    "Kwani mnataka nini kwangu?" Akauliza akitetemeka. Mbele yake walikuwa wamesimama wanaume wawili waliovalia suti nyeusi, tai nyekundu na vinyago vyeusi.



    Wakamwambia wanafahamu kuwa dada yake Sara sasa anaishi na Kinoo chini ya paa moja. Hivyo basi hitaji lao ni moja tu, afanye afanyavyo, kwa juu ama chini, sukari au chumvi, aingie ndani ya genge la BC.



    Huko watamuelekeza cha kufanya. Endapo akifanya inavyotakiwa kufanya basi atafaidika kwa kiasi kubwa, na akikaidi ama kuvujisha siri hiyo hatabaki salama.



    Tangu siku hiyo akawa anapewa fedha ya kujikimu. Makazi ya kukaa na kila huduma aitakayo.



    Lakini ni nini vitu hivi pale unapokosa amani ya moyo?



    Sarah hakuwa anajua kama dada yake anaishi makazi haya mapya. Hakuwa anajua kama anaishi maisha mazuri anayoyatamani hata yeye. Muda wote huo alikuwa akidhani dadaye anateseka na kazi hana. Basi akazidi kumpatia presha Kinoo kukamilisha muamala wa Sasha.



    Akiwa kifuani mwa Kinoo, Sarah alikuwa ananung'una kupitia puani akimbembeleza mbaba huyo kwa sauti tamu. Alikuwa anamchezea kidevu wakati Kinoo akipapasapapasa tumbo la mwananmke huyo lililokuwa limemhifadhi mtoto wake.



    **



    Majira ya asubuhi...



    Kwa wale watu ambao wakiamka, hata kabla ya kuswaki na kunawa uso, kazi yao ya kwanza ni kuzama na kupekua mitandaoni, walikuwa wa kwanza kupata habari hii.



    Ilikuwa imesambaa mitandaoni na kuzua gumzo kidogo miongoni mwa wachangiaji. Polisi akutwa akiwa hajielewi, amepooza viungo kwenye nyumba ya marehemu Eliakimu.



    Picha zikamwonyesha Alphonce akiwa amelala chini sakafuni mdomo wazi jua kali likiwa linamchapa.



    Taarifa hizo zikaeleza zaidi kuwa polisi huyo amepelekwa hospitali na uchunguzi zaidi unaendelea.



    Nini kimemkumba polisi huyu ndani ya nyumba ya marehemu? Alikuwa akifanya nini hapo? Maswali hayo yakashika vinywa vya wanamitandao. Mmoja wao alikuwa Glady!



    Alikuwa anatoa macho asiamini kama yule anayemwona pichani ni mtu anayemfahamu. Akajiuliza kila saa, si yule jamaa huyu? Akaendelea kukagua kwa kushuka chini na chini kwa kufyagia kioo chake cha simu kwa kidole chake gumba.



    Alipotazama picha kadhaa akaamini kweli ndiye anayemuwaza huyu. Alikuwa kweli ni yule mwanaume. Basi akajikuta anatabasamu.



    Hakuishia hapo, akacheka kabisa.



    "Amepata kiboko yake!" Akajisemea kifuani. Upesi akakumbuka simu ya mwanaume huyo, akaitazama na kuanza kuwaza yale yaliyomo ndani ya simu hiyo.



    Kwahiyo ndiyo hatopata tena ile pesa? Akawaza.



    Hapana. Akakataa. Sasa ndiyo itakuwa rahisi kwake kuipata, akawaza. Ndio! Akakubali na nafsi yake.



    Kama Alphonce amepooza basi hataweza kumfanya jambo. Hataweza kumdhuru. Akatabasamu. Na hivyo basi atahakikisha anapata mawasiliano na mwanaume huyo kisha amweleze ana siri yake mkononi, amfanyie muamala wa pesa. Tena si kidogo, muamala mzito. Muamala wa kutikisa akaunti.



    Na hivi jambo la mwanaume huyo lilikuwa limeshashika moto mitandaoni. Lilikuwa maarufu na lililosomba hisia za watu wengi. Basi palikuwa na 'ka-mtaji'.



    Glady aliendelea kuwaza na kichwa chake kibovu.



    Ama kweli, kufa kuna kufaana ndaniye.

    **

    Muhimbili hospital, Dar es salaam.



    "Mnaweza mkanipatia faragha kidogo?" Alisema Kamanda kwa sauti ya chini. Punde daktari na nesi wakawapisha ndani ya chumba.



    Alphonce alikuwa amelala juu ya kitanda akitazama dari. Alikuwa amefunikwa na shuka jeupe lenye chapa ya MSD.



    "Vipi, nini kimetokea Alphonce?" Kamanda akauliza. "Usiniaminishe eti umedondoka tu na kuwa hivyo kama ulivyowaambia hao wengine. Najua kuna kitu. Nani amekufanya hivi?"



    Kamanda akaketi kitandani akimtazama Alphonce kwa kustaajabishwa na maswali hayo.



    Alphonce akasafisha kwanza koo lake. Akawa kimya kidogo akipangilia cha kunena. Akamtazama Kamanda kwa macho yake mekundu alafu kwa ufupi akamjibu:



    "Ni Jona."



    Kamanda akatoa macho.



    "Kwanini akakufanya hivi?" Akauliza. Alphonce asitake kuweka mambo bayana, akadanganya kuwa Jona aligundua kwamba anamfuatilia, hivyo akamshambulia vibaya mno.



    Kamanda akashangazwa na maelezo hayo. Kwanini Jona afanye hivyo? Akamuuliza alimkuta Jona akifanya nini ndani ya nyumba ya Eliakimu?



    "Alikuwa anafanya search," Alphonce akamjibu. "Nilimkuta akiwa amebebelea vitu kadhaa mkononi mwake na nilipomtaka anionyeshe hakuwa radhi kabisa. Akanikemea kwanini namfuatilia. Ghafla akanishambulia kabla sijajipanga, nikajikuta chini sijiwezi."



    Kamanda akaguna. Habari hii ilimpa tahamaki. Aliunganisha doti siku ile walipoenda nyumbani kwa Eliakimu na kukuta ushahidi wa Jona kuwapo hapo mapema kabla ya kifo cha mheshimiwa.



    Baadae wakaambiwa Jona alienda kutupwa kufuatia kupigwa risasi na Eliakimu. Hapa Kamanda akakubaliana na nafsi yake kwamba Jona ana la kuficha kwenye hili. Ni wazi alikuwa na mahusiano na Eliakimu.



    "Kamanda, Jona si wa kumpa nafasi tena. Ni wa kumalizwa haraka iwezekanavyo. La sivyo atatupa shida kwani ameshafahamu yote tuliyomtendea," Alphonce akaongezea.



    "Amefahamuje hayo?" Kamanda akashtuka kuuliza.



    "Sijajua ameyafahamuje. Ila anafahamu kwani ameniambia mwenyewe kwa kinywa chake."



    Kamanda akahisi tumbo linakoroga. Amani ikampotea. Akasimama na kushika kiuno chake akizunguka ndani ya chumba.



    Akapiga kiganja chake kwa ngumi zisizo na idadi. Pasipo kuaga, akatoka ndani ya chumba alicholazwa Alphonce.



    Kichwa chake kilikuwa kimeelemewa mawazo. Na hasira kwa pamoja. Akaenda ofisini kwake na kujilaza kwenye kiti chake. Akaendelea kuwaza akizunguka na kiti kila upande.



    Mwishowe akaamua kumpigia simu Jona na kumtaka aje ofisini kwake mara moja. Jona akapokea wito. Akamwahidi ndani ya muda mfupi atakuwa hapo.



    Kamanda akatoa bunduki yake kwenye droo na kuikoki, kwa lolote litakalotokea, kisha akairudisha na kuliacha droo wazi iwe rahisi kuifikia silaha hiyo punde atakapoihitaji.



    Akangoja kidogo kabla ya Jona kufika ofisini akiwa amevalia tisheti nyeupe plain na suruali ya kadeti rangi nyeusi. Mgongoni alikuwa amevalia begi. Wakasilimiana, Kamanda akaenda kwenye lengo la wito wake pasipo kupoteza muda. Akamsomea Jona mashtaka ya kumtendea ndivyo sivyo Alphonce akiwa kazini kutimiza maagizo yake.



    Kinyume na Alphonce alivyotaka, Kamanda akampatia Jona nafasi ya kujieleza. Na wakati huo Kamanda akiwa anajaribu kwa kiasi kikubwa kutunza mihemko yake asimwonyeshe Jona.



    Na kwa wakati huo huo mkono wake ukiwa karibu drooni kwa lolote litakalotokea.



    "Mkuu, sikumshambulia Alphonce kwasababu ya kumzuia kutimiza majukumu yake bali yeye kutimiza yaliyo yangu."



    "Yapi hayo?" Kamanda akamkatisha. "Hujui ile kesi ipo mikononi mwa Faridi?"



    "Nafahamu. Si kwamba nimeamua kuibeba kesi hiyo, la hasha. Nafanya haya Faridi akiwa ana ufahamu na kinachoendelea. Nafanya haya kwakuwa nilihusishwa kwenye jaribio la mauaji na marehemu Eliakimu. Sidhani kama ni vibaya kufuatilia sababu iliyomfanya mheshimiwa akajaribu kuniua. Haswa baada ya kutimiza kazi yake aliyonipatia kwa uweledi mkubwa," Jona akajieleza.



    "Kazi gani hiyo? Na ulikuwa mna mahusiano gani na Mheshimiwa?" Kamanda akauliza.



    "Hapo nyuma Eliakimu alikuwa akintafuta nimsaidie baadhi ya kazi zake akiamini historia yangu ya kazi na utendaji wangu. Ikumbukwe sikuwa jeshini kwa muda huo. Na malengo yake ya kuntafuta hayakuwa mengine bali mawili akiahidi kunilipa pesa nzuri. Moja, kumtafuta mkewe, nikalifanikisha. Na pili, kumtafuta mfanyakazi wake aliyetekwa, nalo nikalifanikisha.



    Lakini nikiwa nafanya kazi hizi, nikagundua Eliakimu hakuwa mtu safi. Alikuwa anajihusisha na biashara kadhaa za magendo zilizopelekea mkewe na hata mfanyakazi wake kutekwa.



    Nikiwa nataka kufahamu hayo, siku nampeleka mfanyakazi wake kwake ajabu barabarani nikashambuliwa kwa risasi na vijana kadhaa waliokuwa ndani ya prado nyeusi. Tukafanikiwa kutoka hai isipokuwa dereva.



    Nilipowasili kwa Eliakimu nikahitaji kusikia maelezo yake juu ya shutuma zangu. Lakini sikupata maelezo hayo, badala yake akanipiga risasi na kwenda kunitupa porini pamoja na maiti ya dereva yule aliyefia njiani," Jona akaweka kituo kisha akaendelea:



    "Na hilo ndiyo likawa sumbuko langu tangu hapo. Kwanini Eliakimu aliniua ilhali nilitenda kazi zake? Nini anaficha?



    Ni kheri nikasikia mfanyakazi wake, aitwaye Nade, alinusurika kifo katika jaribio la kuuawa yeye na bosi wake, Eliakimu, ambayo najua wazi wahusika watakuwa ni wale waliomteka mfanyakazi huyo. Nikaona ni busara kwenda kumtembelea kwani atanipatia majibu ya maswali yangu..."



    Baada ya hapo Jona akamweleza Kamanda namna gani Alphonce alivyohusika kwenye mauaji ya mfanyakazi huyo na hata baadae kutaka kumpokonya nyaraka alizozipata kwenye nyumba ya Eliakimu.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipofikia hapo Jona akatoa nyaraka hizo begini na kuziweka mezani. Alafu akaendelea na maongezi yake huku Kamanda akiwa anapitiapitia nyaraka hizo kwa macho ya wepesi apate kuzimaliza amsikilize Jona vema.



    "Sikukubali kumpatia nyaraka hizo kwani sikuona kama ni sahihi. Nilitaka kumkabidhi Faridi anayehusika na kesi hii lakini hakuwa radhi, sikufahamu kwanini lakini baadae nikaja kugundua kumbe naye alikuwa anahusika na madili batili pamoja na bwana Eliakimu na zile zilikuwa ni juhudi za kuhakikisha jambo hilo linabaki kuwa siri.



    Kipindi anataka kunipokonya nyaraka hizo, akawa anasema maneno haya,"



    Jona akacheza sauti ya Alphonce aliyoirekodi. Kamanda akiwa ametoa macho akaskiza sauti hiyo huku moyo wake ukimdunda mithili ya trekta linalopambana na ardhi ngumu ya shamba.



    Mpaka sauti hiyo inakoma, hakusikia kuhusishwa kwake moja kwa moja. Akashusha pumzi ndefu na akajawa na hasira sana juu ya Alphonce. Hakutegemea kama mwanaume huyo angeenda kuropoka upuuzi wa namna hiyo kwa Jona.



    Akatikisa kichwa kwa masikitiko akilaza mgongo wake kitini. Akatazama feni, pangaboi, likizunguka akichambua nini cha kufanya kwa dakika kadhaa. Akaona mwanya wa kumwangushia msala huu bwana Alphonce wakati yeye akijinadi kuwa safi.



    Na kwakuwa hakuhusika na bwana Eliakimu kwa namna yoyote ile, hili halikuwa gumu kwake kulitenda.



    "Alphonce! Alphonce!" Kamanda akabamiza ngumi nzito mezani. "Sikutarajia kama ungekuwa na wivu wa kijinga kiasi hiki!"



    Akaendelea kumshtumu Alphonce hewani akimlaani kwanini wivu wake wa kipuuzi unamuingiza kwenye mauaji yake aliyoyatenda kwa mkono wake mwenyewe.



    Akakana kabisa kuhusika na mauaji ya familia ya Jona akisema yeye si 'mkuu' huyo anayetamkwa sautini. Hiyo ilikuwa ni janja tu ya Alphonce kujisafisha na kutakatisha matendo yake ya kidhalimu.



    Mwishowe,



    "Nakuomba haya mambo ya Alphonce yaishie hapa Jona, niachie mimi nitamshughulikia huyo fisadi wa maadili! ... unaweza kwenda."



    Jona akaenda zake akimwacha Kamanda kichwa kinamuuma kwa mawazo.



    Alichambua kila alilolisikia na kuambiwa. Kwa akili yake akaona Alphonce sasa ni tishio kwake kuliko Jona. Mwanaume huyo si tu kwamba atafanya ijulikane alitia mkono kwenye mauaji ya familia ya Jona, ambacho ni uhalisia, bali atamfanya aonekane alikuwa anashirikiana naye kwenye biashara zake za kidhalimu azifanyazo kwa kofia ya polisi.



    Kitu ambacho si uhalisia!



    Kwa kujilinganisha na Alphonce akajiona yeye ni mtu safi. Na kuwa safi zaidi alitakiwa kufanya namna.



    Ipi hiyo?



    Akaweka simu sikioni na kuongea maneno machache.



    "Kericho, fika ofisini kwangu mara moja."



    Ndani ya dakika chache akaja hapo mwanaume mrefu mzito maji ya kunde ndani ya kaunda suti.



    **



    Saa moja asubuhi ...



    "Ameshaondoka," mke wa Boka aliongea na simu. Haikupita hata lisaa kamili tangu mumewe amuage kwenda kazini. Mama huyu alikuwa ameketi sebuleni akiwa amevalia khanga kifuani.



    "Ndio ebu njoo shoga angu maana hapa sielewi kitu yani! ... yani nahisi kuchanganyikiwa ... njoo bana ... kwani hajatoka? ... mida gani? ... basi nakuja mimi ... sawa nikukute hapo ndani ya robo saa."



    Akaacha simu yake na kwenda kujiandaa. Hakupata hata kifungua kinywa. Ndani ya muda mfupi, akawa ameshavalia batiki lake lililomkaa vema. Akajipaki kwenye gari na kuanza safari.



    ***

    Saa nne asubuhi ...



    "Samahani, Mheshimiwa," sauti ya kike ilimfanya Boka abandue macho yake kwenye karatasi kadhaa alizokuwa anazipitia. Alikuwa ni sekretari wake, bi Salma, mwanamke mnene aliyevalia shati jeupe, sketi ndefu nyeusi na hijabu ya pinki.



    "Kuna barua yako hapa."



    "Toka wapi?"



    "TFF."



    "Ooh niwekee hapo," akaonyeshea mezani kwa kichwa kisha akaendelea na kazi yake. Bila shaka alikuwa ametingwa. Hii ilikuwa ni miongoni mwa siku zake alizo bize.



    Alilenga kufanya kazi pasipo kupumzika mpaka majira ya chakula cha mchana amalizie kila kiporo mezani. Lakini hakufanikiwa kwenye hilo. Kwani muda si mrefu akapata taarifa mkewe amefariki kwenye ajali mbaya ya gari iliyotokea maeneo ya Makumbusho.



    Akachanganyikiwa!



    Akafanya kwenda hospitali alipoambiwa mkewe amekimbiziwa, huko kweli akathibitisha mwanamke huyo amefariki. Mwili wake uliokuwa umeharibika vibaya ulikuwa umeshalazwa mochwari.



    Lakini asiamini, akaenda mpaka kuutazama mwili huo mochwari, labda unaweza ukawa si wa mkewe, wameufananisha! Huenda akawa ni mtu mwingine aliyetumia gari la mkewe. Ndio. Inawezekana. Ama kuna mtu aliyeliiba hilo gari na kukimbia nalo, hatimaye akapata ajali!



    Alitengeneza kila picha kichwani akijaribu kumnusuru mkewe. Aligeuza kila taarifa aliyoambiwa ili tu amuokoe mkewe kifikra lakini haikubadilisha ukweli. Alikuwa ndiye yeye. Hakuweza kurudisha mikono ya muda nyuma.



    Mwili uliokuwa umelala kwenye jokofu za mochwari haukuwa wa mwingine isipokuwa wa mwanamke aliyemzalia watoto.



    Haukuwa unatamanika hata kidogo. Paji la uso lilikuwa limechanika. Amevunjikavunjika. Boka akashindwa kujizuia kutoa machozi.



    "Alikuwa na mwenzake ndani ya gari. Yeye amenusurika kifo, lakini yu hoi hajiwezi. Taarifa alizozitoa kabla hajaenda kupoteza fahamu ni kwamba walikuwa wanafuatiliwa kwa muda mrefu kabla ajali hiyo haijatokea.



    Kwahiyo kwa namna moja ama nyingine hii haikuwa ajali bali tukio lililopangwa," alisema polisi aliyepewa jukumu la upelelezi, kwa jina inspekta Geof.



    "Sasa kama ni hivyo, mnangoja nini kumtia nguvuni huyo mshenzi?!" Boka akafoka kwa hasira. "Au sio kazi yenu hiyo?"



    Inspekta akamsihi apunguze jazba, mambo hayapelekwi mrama kiasi hiko. Tukio ni kubwa na linahitaji utulivu mkubwa kumbaini mhusika, la sivyo wataishia kuwabambikia watu kesi.



    Lakini akamuahidi kwa dhati jambo hilo halitachukua muda kukaa bayana. Amuamini. Akaendaze.



    Akamuacha Boka hospitalini akiwa ameshikilia kichwa kwa mawazo. Ni nani amuue mkewe? Kwasababu gani haswa? Alijiumiza zaidi na hayo maswali asiyokuwa na majibu. Akaishia kuvuja machozi, zaidi akapandwa na hasira maradufu.



    **



    Kwenye vioo vya simu ... whatsapp App.



    'Umehakikisha amekufa?'



    Typing...



    'Ndio, nimefika hospitali kama mwandishi wa habari. Yupo mochwari.'



    Typing...



    'Na mazingira ya ajali?'



    Typing...



    'Hamna mtu anaweza jua. Nimefanya kiustadi.'

    Typing...



    'Nimepata taarifa hakuwa mwenyewe ndani ya gari'



    'Ndio alikuwa na mwanamke mwingine yeye hajafa yupo ICU'



    Typing ... ikaacha ... typing tena ...



    'Una uhakika huyo mwanamke uliyemwacha hai hakukuona?'



    'Tukio lilitokea kwa kasi sana hakuniona'



    Typing ...



    'Kama huna uhakika ni kheri ukammaliza. Hatuna muda wa kusumbuana na polisi'



    Typing ...



    'Nakuhakikishia hakuna haja hiyo'



    'Ok. Stay low. Njoo tuonane.'



    Tap ... Offline ...



    Moja wa mtu huyu anayechat alikuwa ndani ya basi la mwendokasi. Akazamisha simu mfukoni. Alikuwa amevalia suruali ya kitambaa rangi ya kijivu na viatu vyeusi ving'aavyo.



    **



    Muhimbili hospital, Dar.



    Mlango ulifunguliwa taratibu akaingia mwanaume ndani ya shati jeupe na suruali nyeusi. Akamtazama Alphonce kitandani, akamwona akiwa amelala.



    Huu haukuwa muda wa kutazama wagonjwa. Hakuwa amepewa ruhusa wala kuonana na mtu yeyote yule kabla hajaingia humu ndani.



    Alikuwa ni Kericho. Mwanaume mzito mwenye rangi maji ya kunde. Macho yake yalikagua chumba upesi kisha akamsogelea Alphonce na kumbana pumzi kwa mikono yake mipana iliyoshamiri mishipa ya damu.



    Alphonce aliyepooza angefanya nini kuukomboa uhai wake? Kericho akatekeleza zoezi lake kwa wepesi sana. Alimuacha Alphonce baada ya kusikia mlio wa kuashiria mapigo ya moyo yamekata.



    Hakutoka hata jasho. Alphonce akawa amekufa.



    Akatoka ndani ya chumba hicho upesi. Kama alivyoingia, hakuna aliyemuona. Akayeya zake.



    "Fagio limevunjika," akasema akibinyia simu sikioni.



    "Nilikwambia," sauti ikamjibu toka simuni. "Haya leta nilione."



    Kericho akakata simu akiiweka Muhimbili mgongoni mwake. Akajipakia kwenye taksi na moja kwa moja akaelekea Mbweni. Akashukia barabarani na kumkabidhi dereva pesa yake alafu akatembea kwa mwendo wa dakika sita kabla hajazama ndani ya nyumba fulani kubwa ambayo bado haikuwa imemaliziwa kupauliwa.



    Humo akakutana na Kamanda akiwa amevalia sare ya traksuti nyeusi.



    "Umehakikisha kila kitu kipo sawa?"



    "Kila kitu kipo kwa mstari," akasema Kericho akitabasamu. Kamanda naye akatabasamu kujibu.



    "Safi sana. Nilikuamini ndo' mana nikakupatia hiyo kazi."



    Lakini ikatokea upesi sana, Kericho akaona chepeo na jembe kwa umbali wa hatua kadhaa nyuma ya Kamanda. Kabla hajauliza, akajikuta amedidimiziwa kisu tumboni mara tatu!



    Chop! Chop! Chop! Akadondoka chini akimimina damu lukuki.





    "Hakuna siri ya watu wawili Kericho," Kamanda akasema akimtazama Kericho akijifia.



    Kericho akamnyooshea kidole Kamanda mkono wake mmoja ukiwa tumboni umemezwa na damu. Macho yake yalikuwa mekundu. Akatamani kusema jambo lakini hakuweza. Akamtazama Kamanda mpaka roho yake inaacha mwili.



    "Kwaheri afande," Kamanda akamfunika macho kisha akachimba shimo na kuufukia mwili wa Kericho humo.



    Akakung'utia jasho pembeni alafu akaendea gari lake na kujipakia, akayeya.



    Njiani ...



    "Ndio, mheshimiwa," akasema akibinyia simu sikioni kwa mkono wake wa kushoto wakati wa kuume ukishikilia usukani.



    "Ndio, nimesikia mheshimiwa pole sana kwakweli ... yah! Ndo nipo njiani nakuja ... usijali, nitakuwa hapo muda si mrefu."



    Akakata simu.



    Nusu saa baadae akawa ameshafika hospitali, yu ndani ya sare, anateta na Boka juu ya ajali ya mkewe. Akampatia Boka pole za kutosha baada ya kumpa kumbatio na mkono wa kheri.



    "Nakuhakikishia, mheshimiwa, lazima atakamatwa!" Kamanda akasema kwa sura ya msisitizo. "Atatafutwa kokote alipo. In fact, nina wapelelezi wazuri sana hawataniangusha."



    Boka akashukuru.



    "Lakini nashangazwa sana, bora ingekuwa mimi ningesema nina maadui wa kisiasa. Lakini kwa mke wangu, mke wangu, ana makosa gani?" Boka akateta kwa uchungu.



    "Huwezi jua, Mheshimiwa. Hata hao maadui wako wewe wanaweza wakatumia njia hiyo," Kamanda akamueleza kisha akamuuliza: "kuna yeyote unayemshuku kwenye hili?"



    Boka akafikiria kidogo. Akabinua mdomo wake akitikisa kichwa.



    "Sidhani." Akafikiri tena. "Sidhani kwakweli."



    "Tuliza kichwa," Kamanda akamsihi. "Najua kwa sasa unafikiri mengi lakini baadae utatengemaa kimawazo. Nijulishe."



    "Sawa, nitakubarisha. Ahsante."



    Wakaachana. Baadae kwenye vyombo vya habari majira ya usiku, Kamanda akanguruma akiongelea kifo cha mke wake Boka na inspekta Alphonce.



    Kwa upande wa mke wa Boka akasema uchunguzi unaendelea huku akisisitiza watu waache kusambaza maneno yasiyothibitishwa huko mitandaoni, waache polisi wafanye kazi yao. Kwa upande wa Alphonce akasema mwanaume huyo amefariki kwasababu za kiafya.



    "Shit!" Jona akalaani. Alikuwa anatazama taarifa ya habari akimwangalia mkuu wake wa kazi. Yeye pekee ndo alikuwa anajua mwanaume huyo anaongopa juu ya Alphonce.



    Aliamini Kamanda ndiye kamuua mdhalimu huyo. Hakuna mwingine.



    Ila hakujali.



    'Acha wafu wazikane wenyewe.'



    Punde simu yake ikaita. Alikuwa ni Kamanda. Akajiuliza anataka nini? Alipopokea Kamanda akamuuliza kama amesikia ya Boka.



    "Ndiyo nimetoka kuona kwenye habari," Jona akajibu.



    "Ok," Kamanda akaitikia. "Sasa hiyo kazi nimekupatia uifanye. Nataka huyo muuaji apatikane. Sawa?"



    Kimya.



    "Sawa?"



    "Sawa, mkuu!"



    **

    "Utaonana na Inspekta Geof, atakupatia alipofikia."



    Baada ya hapo Kamanda akampatia Jona namna ya kumpata Inspekta Geof, alafu akakata simu.



    Jona akaweka simu yake kando na kuanza kuitafakari simu hiyo ya Kamanda. Akatafakari na kazi aliyopewa. Hakuwa na kitu kichwani na hakuwahi kujisumbua na Boka.



    Ndio alikuwa anajua mwanaume huyo ni waziri ila hakuwahi kumfuatilia wala kuwa shabiki wake. Kwanini mkewe auliwe? Akabinua mdomo.



    "Huwezi jua ya wanasiasa!" Akajipa pumziko kwa kauli hiyo kisha akapuuzia. Lakini hakudumu muda mrefu, akili yake ikamrudisha tena kwenye hilo tukio.



    Vipi kama haya yakawa ni mwendelezo wa mauaji ya watu mashuhuri na maarufu kama ilivyokuwa hapo nyuma? Akawaza.



    Inawezekana Boka akawa ameingia kwenye Anga lile la Washenzi? Alifikiri sana lakini akajitahidi tena kupuuzia apumzishe kichwa.



    Aliamini atakapokutana na Geof atajua wapi pa kuanza kutia mguu wake. Akanyanyuka na kujipatia chakula akishushia na juisi ya embe.



    Kabla hajalala akaamua kushika kitabu kikubwa cha riwaya apate kupitia kurasa kadhaa kuhadaa kichwa alale. Alikuwa anasoma riwaya iitwayo THE BIG SLEEP cha mnamo mwaka 1939 kilichoandikwa na mwandishi nguli Raymond Chandler.



    Riwaya hii ilikuwa ni ya mambo ya kijasusi. Ndivyo ambavyo Jona anapenda kuvipitia pale apatapo muda. Vitabu vya kufikirisha akili. Vitabu vya kuchemsha ubongo na kupanua mawazo.



    Mbali na hiki cha Raymond Chandler, pia kwenye maktaba yake kulikuwa na vitabu vingine maarufu vya kijasusi vilivyoandikwa kwa mkono mtamu na akili zilizopevuka.



    Kuvianisha kadhaa vilikuwa kama: THE HOUND OF THE BASKERVILLES cha mwaka 1902 kikiandikwa na Arthur C Doyle, THE MOONSTONE cha mwaka 1868 kikiandikwa na Wilkie Collins na cha bwana Dashiel Hammett kiitwacho THE MALTESE FALCON cha mwaka 1930.



    Ingawa vitabu hivi vilikuwa vya kale, ila vilikuwa na thamani ya kusomwa tena na tena. Haswa kwa watu wa kariba ya Jona, wapendao kudadisi, kufuatilia na kupembua.



    Kweli, baada ya muda wa dakika kadhaa Jona akiwa amesogeza karatasi kama kumi hivi, akaanza kusinzia. Mwishowe akalala kabisa.



    Leo akawa anauendea usiku pasipo kutumia kilevi. Akalala kwa muda wa nusu saa tu, kabla hajakurupushwa na simu. Akalalama sana.



    Alikuwa ameshapotelea usingizini. Alikuwa anafahamu ni namna gani atahangaika kupata nafasi hiyo tena. Na kwa mawazo yake yote alijua Kamanda ndiye aliyemtafuta.



    Akasonya akiivuta simu na kuitazama. Alikuwa ni Marwa! Akawaza anataka nini muda huo? Akapokea simu.



    "Yes,Marwa ... niko poa, wewe? ... yah nlikuwa nshalala ... bila samahani ... sasa hivi? ..." Jona akatazama saa kwenye simu, ilikuwa saa tatu usiku na dakika kichele, akairudishia simu sikioni. "Ok, basi nakuja."



    Punde akanyanyuka na kuvaa, akaenda zake.



    Akiwa njiani kwenda huko, sie twende huku ...



    "Kwahiyo umeamuaje sasa?" Aliuliza shoga yake Glady akimtazama mwenzake kwa macho ya mtindio wa urembo. Mwanamke huyu hakuwa mwingine bali yule aliyebananishwa siku ile na Alphonce ndani ya gari, akajichafua na mkojo.



    Alikuwa amevalia tight nyekundu na blauzi nyeusi isiyo na mikono. Kandokando yake bibie Glady alikuwa bado amevalia taulo anajikwatua kabla ya kwenda kazini.



    "Sasa shoga yangu, niamue nini sasa hapo unadhani?" Akauliza Glady akipaka wanja. "Mtu mwenyewe ndo ashakufa hivyo. Sasa mimi si kaniachia mzigo tu hapa!"



    Kukawa kimya kidogo. Glady akauvunja:



    "Yani mimi hapa ndipo ninapokereka na maisha. Unajikinga na UKIMWI eeeeenh miaka nenda rudi kutumia marambo alafu unakuja kuuawa au kufa ka siku ka moja tu!"



    Akasonya.



    "Ila mwanamke wewe una bahati sana!" Shoga akamwambia. "Yule jamaa kama asingekufa alikuwa anakuua wewe nakwambia!"



    "Aanzie wapi?" Glady akajivuna akipakaa rangi ya mdomo. "Kama alishindwa nilivyokuwa naye chumbani angeniwezea wapi?"



    "Haya, bana! Mie sina neno. Niuzie basi hii simu," Shoga akapendekeza akiitazama simu ya marehemu Alphonce.



    "Ishia hapo hapo!" Glady akamkemea. "Huoni choo ukapita?"



    "Sasa shosti ya nini na mtu mwenyewe keshajiendea kwa mola wake? We sema hapa nikupatie laki moja unipe!"



    "Fala kweli wewe. Laki moja unampa nani labda? Umeona simu ya laki moja hiyo?" Akamtazama Shoga yake. "Eti?"



    "Unataka shingapi sasa?"



    "Sitaki chochote we bwana we!" Akasema Glady akimalizia kujipara. Akajipulizia marashi na kujiveka nguo, gauni jeusi la lawama mtaani.



    Akaketi kitandani.



    "Hiyo simu itanipa pesa zaidi ya hiyo, tena mara kumi yake!"



    "Wapi sasa?"



    "Tatizo wewe akili yako tope. Nishapata wazo hapa mwenzako. Wazo la kupiga pesa ya maana niache kuuza uchi."



    "Wewe hata upate milioni utauza tu. Iko damuni!"



    "Ebu skiza nyoko wewe n'kupe mawazo ya maana, acha kuongea mashudu. Hizo picha zilizokuwepo humo ni pesa. Cha kufanya tunawatafuta wanaohusika na picha hizo tunawaambia watoe pesa tukae na siri, la sivyo mambo kweupee mitandaoni."



    "Mh! Wakikataa?"



    "Unaona sasa? Tatizo lako wewe unadhani kila mtu ananuka shida kama wewe. Watu wana pesa zao bwana. Unadhan mke wa mbunge, au mke wa waziri atakubali picha zake za uchi zisambazwe?"



    Shoga kimya.



    "Ohoo!" Glady akasimama. "Ngoja nkuonyeshe nitakavyotajirika mbele ya macho yako."



    Akavaa viatu akamtaka mwenzake anyanyuke waende.



    **



    Baada tu ya kuketi, Marwa akamwambia usiku huo umekuwa wa kipekee kwani kuna mambo kadhaa muhimu amepata kuyadukua toka kwenye zile links, akaona si mbaya akamshirikisha kwenye taarifa.



    Jona akakaa tenge apate kusikia. Marwa akiwa amemsogezea tarakilishi yake, akamwonyesha Jona jumbe kadhaa toka katika hizi pande. Hazikuwa na maana sana, ila moja.



    Jona akatabasamu. Ujumbe huu ulikuwa umeanishwa kama ifuatavyo:



    *From : Second Wave, Nairobi.*



    *To: First Wave, Dar.*



    *Content: Help for an ambush for killing and framing*



    *Place: Karen and Langata.*



    *Aim: Kamau Githeri and Wachuku Otieno.*



    *Time: immediately!*



    Ujumbe huo ukawapa mawili, mosi wakatambua 'nguvu moja ya bahari' ipo Dar na ya pili ipo Nairobi. Hii kumaanisha huko kuna matawi ya ulinzi yanayolinda kisiwa. Je, ya tatu itakuwa Dodoma? Hawakuwa na uhakika bali makisio.



    Lakini pili na zito zaidi ni mpango wa kuuawa kwa viongozi wa kiserikali wa huko Kenya, bwana Kamau na Wachuku. Na si kuwaua tu, bali kufanya pia 'framing'.



    Framing ni nini? Kwa kifupi ni zoezi la kutengeneza ushahidi wa uongo dhidi ya mtu asiye na makosa (an innocent person) ili aonekane mkosefu mbele ya watu ama mahakama, ama kote.



    Njia hii imekuwa ikitumika sana ulimwenguni na kuwatia watu hatiani kwa makosa ambayo hawajatenda. Kwa ustadi jambo linatengenezwa na kuhusanishwa na fulani huku mtendaji akibaki salama.



    Na mtendaji huyu hufanya hivi kwakuwa huyo aliyemfanyia jambo na huyo anayesingiziwa kitaalamu kuwa yeye ndiye ametenda hilo jambo wakiwa wote ni maadui zake.



    "Sasa tunafanyaje?" Akauliza Marwa.



    "Inabidi tutoe taarifa kwa vyombo vya usalama vya Kenya," Jona akashauri.



    "Kwa namna gani?" Marwa akauliza.



    Hapo Jona akasita kidogo. Alifahamu jambo hilo litampatia shida kupata 'access'. Akafikiria sana namna ya kufanya, lakini kila njia aliyoipata haikumridhisha kwa umakini wake.



    Mwishowe Marwa akamuuliza kama viongozi hao wana nyadhifa ya ubunge pia?



    "Ndio," Jona akajibu. "Vipi kuna wazo umepata?"



    "Haswa!" Marwa akamshauri waingie kwenye tovuti ya bunge la Kenya kisha kule wakapekue orodha ya wabunge na taarifa zao.



    Jona akaafiki hilo wazo, wakazama mtandaoni na isipite muda wakawapata walengwa wao wanaowatafuta. Wakatazama 'additional info' wakapata akaunti ya barua pepe ya Kamau Githeri lakini kwa Wachuku Otieno wakaambulia patupu!



    "Sasa ukimtumia barua pepe, haitachukua muda, ikakawia, mwishowe akauawa?" Jona akauliza.



    Marwa akamtoa hofu, akamwambia atatuma barua pepe hiyo kwa njia ya kirusi bandia. Kama kawaida itafika kwa mlengwa, na kama huko atakuwa ameweka anti-virus itakuwa bora zaidi kwani itapiga kelele kumshtua.



    Hivyo akasoma kwa wakati! Na kwa wakati huo bado simu yake ikibakia salama.



    Jona akapenda hilo wazo. Na kwa upande wa Wachuku Otieno?



    "Acha tuwasiliane na karani wa bunge kwa hizi namba walizozianisha kwenye tovuti," Marwa akapendekeza.



    "Huoni itaweka taarifa zetu wazi tukitumia namba zetu binafsi?" Jona akauliza.



    "Hapana," Marwa akamjibu. Akamwambia wataweka 'chip' kwenye mashine yake alafu atafanya kautundu wapige kwa 'private number'.



    Wakafanya hivyo, ila hawakufanikiwa kumpata karani. Mwishowe wakaamua kutuma ujumbe wa kumtaarifu wakitumai atausoma kwasababu ya zile 'missed calls'.



    ***



    Walipomaliza kazi hiyo wakatulia sasa na kufanya mambo mengine. Marwa akampata kumkaribisha Jona vitafunwa vya kusogezea muda huku wakipiga soga za hapa na pale.



    "Umeonana na Panky leo?" Jona akauliza.



    "Kiasi chake," Marwa akajibu akitafuna. "Ilikuwa ni asubuhi tukasalimiana na kuteta mambo kadhaa kabla hatujaachana."



    "Kuachanaje?" Jona akastaajabu. "Hamfanyi kazi sehemu moja?"



    Marwa akameza kwanza kabla ya kutia neno.



    "Asubuhi nilipoongea naye aliniambia wanataka kumbadilisha kitengo, wamtoe SPACE BUTTON."



    "Wampeleke wapi?" Jona akauliza.



    Marwa akapandisha mabega. "Sijajua. Hatukuwa na muda wa kuongea naye sana kabla hatujaachana."



    Jona akawaza kidogo.



    "Haiwezekani wakawa wametambua na kuyatilia shaka mahusiano yenu?"



    "Sidhani!" Marwa akawahi kujibu. "Huwa ni taratibu yao kubadilisha watu vitengo kila baada ya muda fulani. Ila ni kwa mara chache sana hutokea kwa SPACE BUTTON."



    "Sasa mbona imetokea kwa Panky?"



    Marwa akabinua mdomo. "Sijajua lakini nadhani ni kwasababu ya kifo cha mmoja wa wafanyakazi wa kitengo cha uhasibu kilichotokea hivi karibuni. Panky atakuwa amepelekwa huko kukaimu nafasi yake."



    "Kwanini Panky, si mwingine?" Jona akaendelea kuuliza maswali.



    "Unanifanya nijihisi nipo kituoni," Marwa akasema na kucheka. Jona naye akacheka.



    "Anyways, kwa hisia zangu Panky atakuwa amehamishiwa huko kwasababu ya hali ya hewa. Ofisi ya huyo marehemu haikuwa na kiyoyozi kwasababu alikuwa na tatizo la asthma," Marwa akadadavua.



    "Kwani Panky ana asthma?"



    Marwa akacheka.



    "Hana, ila aliigiza anayo. Imemgharimu sasa."



    "Huyo marehemu ulijuaje ana asthma?"



    "Ni mmojawapo wa wafanyakazi wa muda mrefu sana, actually nilimkuta akiwa hapo. Watu hawa wazamani wengi nawafahamu."



    Jona akaridhika na maelezo haya Marwa. Lakini akapata wazo hapa, kama kweli Panky atakuwa amehamishiwa kwenye hiyo ofisi aliyosema Marwa, hamna namna akapata kuwatambua wanaume watakaotumwa Nairobi kusaidia Second wave?



    "Kivipi?" Marwa akamuuliza Jona baada ya mwanaume huyo kumshirikisha wazo hilo.



    "Watu hao hawaweza wakatumwa pasipo kupewa fedha za usafiri, makazi na kujikimu. Pesa zinatoka wapi?"



    "Kwa mhasibu!" Marwa akajibu kisha akatabasamu. "Kweli inawezekana."



    Hii ilikuwa hatua tamu sana kwa Jona kuwang'amua baadhi ya wahusika wa 'the first wave' na kisha kuwashughulikia.



    Wakafanya mpango wa kumtafuta Panky lakini simu ikaita pasipo mafanikio.



    "Ana mke, anaweza akawa anahudumia nyumba," Marwa akapendekeza wasitishe zoezi hilo. Jona akamsihi kesho asubuhi atakapokutana naye ahakikishe anamuuliza na kufanya namna.



    Marwa akamtoa shaka Jona.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakapumzika sasa Marwa akimsihi Jona alale nyumbani kwake kwani muda umeshaenda.



    ***



    Saa nne asubuhi ...



    Gari Rav4 rangi ya damu ya mzee ilikuwa imepaki pembeni kidogo mwa njia itumiwayo na daladala kuingia ndani ya kituo cha daladala cha Makumbusho.



    Ndani ya gari hiyo alikuwamo Inspketa Geof na Jona wakibadilishana ndimi. Geof alikuwa akimweleza Jona yale aliyoyapata toka kwenye ajali ya mke wa Boka, Jona naye akiuliza maswali kadhaa.



    "Gari lilitokea kwa kasi huku stendi, Chaser nyeupe, ikikwepa daladala kwa pupa. Ilipofika hapo kwenye maungio ya barabara ya lami, ikasogea kidogo na kuibamiza gari ya marehemu kwa upande wa dereva! Kisha ikayoyoma," Geof alielezea hayo akitumia mikono yake kuonyeshea uhalisa wa matukio na mahali yalipotukia.



    Akamweleza pia Jona kuhusu shoga wa mke wa Boka aliyelazwa hospitali kisha akamkabidhi Jona faili lake.



    "Mpaka hapo tutakuwa tumemalizana," alihitimisha Geof.



    "Nashukuru sana," akasema Jona. "Ila nina ombi dogo kwako."



    "Karibu."



    "Nisaidie kunisogeza kwa Boka mara moja."



    Geof akamtimizia haja yake. Jona akashuka mbele ya nyumba ya Boka na kuzama ndani.



    Kulikuwa kuna watu kadhaa. Turubai limefungwa likitoa kivuli kwa viti kadhaa vya plastiki vilivyozagaa.



    Akafanya mpango wa Kuonana wa Boka. Haikupita muda mrefu akawa ameketi kando na mwanaume huyo. Akajitambulisha yeye ni nani, ametoka wapi na hapo anafanya nini.



    "Ooh! Nilikuwa natarajia ujio wako," akasema Boka. "Kamanda alinambia atanibadilishia mpelelezi. Bila shaka wewe anakuamini."



    Jona akajibu kwa tabasamu kisha akaanza kutekeleza kazi yake. Akamuuliza Boka maswali kadhaa, na kati ya hayo taarifa iliyokamata sikio lake ilikuwa ni hii.



    "Siku hizi mbili au tatu za mwishoni, hakuwa sawa. Hakutaka kuongea na mimi na wala hakunieleza nini tatizo hata nilipojaribu kumuomba."



    Jona akahisi hapa patakuwa chemchem yake ya mfanikio.



    "Haukuwa umemkwaza au kugombana kwasababu yoyote ile?"



    "Hapana. Hatukuwa na ugomvi japo niliona amebadilika ghafla. Lakini sijui, labda nilikuwa nimemuuzi, ila hakunambia."



    Jona alipotoka hapo akazuru pia kazini kwa mwanamke huyo, huko akakutana na mkurugenzi msaidizi, bwana Liundi akiwa hae hae anataka kutoka aende msibani.



    Akamwomba muda kidogo watete.



    "Imekuwa ni ghafla mno, amefariki akiwa kwenye projekti kubwa ambayo ingejenga jina la Tanzania na hadhi yake kwa ujumla," alielezea bwana Liundi.



    Jona akataka kujua zaidi kuhusu projekti hiyo. Liundi akaeleza kinaga ubaga, akitoa mpaka na mpango kazi na hata hatua waliyokuwa wamefikia kwenye kusambaza vipodozi vyao vya kiasili nchini Kenya.



    Wakiwa humo wanaelezeana, Jona akastaajabu kuona picha ya Miranda! Aliitazama picha hiyo kwa umakini kisha akauliza:



    "Huyu ni nani?"



    "Aaahm ... alikuwa kama patna wa mama kwenye hii projekti."



    "Tangu lini alianza kufanya kazi na mama na unafahamu walijuanaje?"



    Liundi akajibu swali la kwanza ila la pili akashindwa. Hakujua Miranda alikutana wapi na aliyekuwa bosi wake.



    "Nitakichukua hiki kipeperushi," akasema Jona.



    "Hamna shida, viko vingi waweza chukua," Liundi akamtoa shaka. Jona akaaga.



    Sasa kichwani akawa anamuwaza Miranda tu. Imani yake yote ilimwangukia mwanamke huyo maana anamjua vema. Alijikuta anakubaliana na nafsi yake kabisa kuwa mwanamke huyo atakuwa mtuhumiwa wake wa kwanza!



    Anahitaji kumtafuta haraka iwezekanavyo.



    Akampigia simu, ikaita mara mbili kabla haijapokelewa.



    "Unaongea na --"



    "Jona!" Sauti ya Miranda ikamkatiza.



    "Ndio, Jona hapa, nina shida na wewe haraka iwezekanavyo."



    "Nini shida Jona? Mbona upesi hivyo? Ni mambo ya ile picha?"



    "Hapana! Ni kuhusu ajali ya mke wa mheshimiwa!"



    "Ooh! My God. Jona, I didn't do it. Honestly!" (Ooh! Mungu wangu. Jona, sijalifanya hilo. Ukweli kabisa!)





    ****



    Jona akamtaka waonane kesho kwa ajili ya maongezi zaidi. Akakata simu na kuendelea kuwaza. Kuna yeyote zaidi Miranda?



    Aliamini hata kama kuna yeyote zaidi ya Miranda basi njia ya kumpata mtu huyo ni kwa kupitia Miranda tu. Atampatia namna ya kupiga hatua hiyo.



    Akatulia baada ya muda kidogo, akampigia simu Marwa. Simu ikaita pasipo matokeo. Akagundua Marwa atakuwa yupo kazini kwa muda huo, hivyo ni ngumu kupokea!



    Akaachana naye avute subira mpaka majira ya mchana, aotee muda mwanaume huyo atakuwa akipata chakula cha mchana.



    Muda ukasonga.



    Kwenye majira ya mchana, saa saba na robo, Marwa akawa kantini akipata chakula. Alikuwa ameketi mwenyewe akijitenga kidogo na wenzake. Na kwakuwa Marwa hakuwa amezoeana na yeyote, basi hakuna aliyemuwazia.



    Lakini mwanaume huyo alikuwa anamngoja Panky. Alitegemea atakuja kula na hivyo basi waketi pamoja kwa hapo pembeni.



    Muda ukasonga kidogo mpaka majira ya saa saba na dakika ishirini na tano, Panky akaonekana akichukua chakula. Akatazama huku na kule pa kukaa, Marwa akanyoosha mkono amwone, Panky akaenda huko.



    "Nilikuwa nakungoja muda wote huo."



    "Aanh! Kuna kazi kidogo nilikuwa nazimalizia. Yani huko waliponipeleka ni kama mwehu, kazi kazi kila saa simu tu!"



    "Wamekupeleka wapi kwani?"



    "Uhasibu na mawasiliano."



    Vile vile kama Marwa alivyokuwa anawaza. Ni ngumu sana kwa Sheng kuajiri mtu mpya kwani inakuwa ngumu sana kwa mtu huyo kujua na kuufuata utaratibu wa kazi chini yake hivyo hupendelea kutoa mtu huku na kumweka pale, kama haitaathiri.



    "Ila huko hamna kiyoyozi," Marwa akatania. Wakacheka. Wakawa kimya kidogo wakitafuna.



    "Sasa kuna kazi ya kufanya," Marwa akaingizia. Kabla hajaendelea simu ikaita, alikuwa ni Jona.



    "Yah! Ndo nipo naye ... poa, baadae."



    Akaweka simu mezani, na kumwambia Panky maagizo toka kwa Jona. Nini anatakiwa kufanya akirejea ofisini kwake.



    "Hope tumeelewana!" Marwa akamalizia.



    "Usijali, nitalifanyia kazi. Na nadhani hao watu watakuwa wameshaondoka. Taarifa zao zitakuwepo kule kimalipo. Nitatazama."



    Wakamalizia kula, wakarejea kazini. Panky akaanza kukagua nyaraka za risiti na taarifa kadhaa kwenye tarakilishi, pesa zilizotoka hivi karibuni.



    Akanoti pembeni na kumtumia ujumbe Marwa kwa kuhofu baadae anaweza akakawia kutoka hivyo hatokutana naye. Alipotuma ujumbe huo, akaendelea na kazi yake kama kawaida.



    Lakini baada ya muda kidogo, akaja kuitwa.



    "Unahitajika ofisini kwa mkuu," alisema mwanaume mmoja akisimama mbele ya Panky.



    "Mimi?"



    Japo hakujua anaitiwa nini, moyo wake ukaanza kumtwanga. Alipaliwa na hofu. Kuitwa na mkuu halikuwa jambo dogo hata kidogo.



    "Ndio, wewe!" Akasema mleta wito.



    "Sawa, nakuja," Panky akajibu.



    "Nakungoja twende," mleta wito akamsihi.



    "Kwani lazima twende wote?"



    "Ndio! Nimeambiwa nikupeleke."



    Hapa Panky akazidi kupata hofu. Ina maana wanahisi anaweza kukimbia? Akaacha kazi zake na kuongozana na mwanaume huyo mpaka ofisini mwa Sheng. Alipofika, yule aliyemsindikiza akaagizwa angoje nje.



    "Panky," Sheng akaita huku akitazama karatasi kadhaa juu ya kashelf kake kadogo ka kioo juu ya meza.



    "Naam, mkuu!" Sheng akaitikia. Mikono yake ilikuwa inatetemeka na kujawa jasho.



    Sheng akamuuliza juu ya kazi aliyompatia hapo kitambo ya kummaliza Jona. Panky kusikia hivyo akaishiwa nguvu! Sasa akajua mwisho wake umewadia.



    Sheng akiongea kwa lafudh yake ya kimandarin, akamwambia Panky kwamba siri yake isingeweza kudumu kwa muda. Alimpatia kazi na kwa kumdharau hakuitenda, akaja kumlaghai.



    Na kwa asili ya uongo wake, inaonyesha ana mahusiano na Jona kwani mwanaume huyo alihama mara moja baada ya yeye kuja kusema amemmaliza.



    Panky akalia kuomba msamaha. Hakuwa na lingine sasa la kufanya zaidi ya hilo. Akalia abakiziwe uhai wake. Atakuwa mtiifu kwa Sheng na hatorudia tena kufanya kosa.



    Lakini kwa Sheng hayo yote yalikuwa makelele. Hakumwelewa Panky hata kidogo. Akafungua droo yake na kuchomoa binduki ndogo, akaitazama ina risasi ngapi.



    Nne.



    Akaikoki na kumwonyeshea Panky mdomo wa bunduki kwenye paji lake la uso.



    "Nina mke na watoto wananitegemea. Pia wazazi huko kijijini. Tafadhali bakiza uhai wangu!" Panky akawaga machozi.



    Sheng akabofya kitufe cha bunduki mara nne! Chuma zikatoboa kichwa cha Panky na kumlaza chini akiwa mfu!



    Baada ya risasi hizo, yule mwanaume aliyeambiwa angoje nje, akaingia ndani na kubeba mwili wa Panky.





    **





    "Sasa? Si naweza nikatoka?" Akauliza Miriam. Sasa alikuwa ameboreka zaidi kiafya. Alikuwa anawasiliana na mama aliyempokea ambaye alikuwa mlangoni akitazama huko nje.



    Ni majira ya jioni sasa. Jua lilikuwa linaelekea kuzama. Na siku hii Miriam aliona inafaa kwake kutoroka.



    Tayari mtoto alishaenda kukagua huko nje mpaka barabarani. Akarejesha taarifa kwamba kupo salama.



    "Ndio, njoo," mama akamruhusu, Miriam akatoka mpaka huko nje, akamkumbatia mwenyeji wake kumuaga akimshukuru sana. Na akamuahidi atarudi kuja kumshukuru siku moja.



    "Bado hutaki nikusindikize?" Akauliza mama mwenyeji.



    "Hapana, hatari niliyokuweka kwa muda wote huo inatosha. Acha hili nipambane mwenyewe."



    Miriam akaanza kutembea akitazama chini. Kulikuwa na kaumbali kutoka hapo mpaka kituoni. Alikazana kutembea mkononi akiwa amebebelea kamfuko. Na mwili wake ukiwa umehifadhiwa ndani ya dira chakavu alilopewa na mwenyeji wake.



    Akiwa amekaribia kituoni, kuna mtu mmoja akamuita.



    "We mwanamke!"



    Hakugeuka. Akakazana kutembea. Sauti ikamuita tena, we mwanamke we mwanamke. Ila hakugeuka abadani.



    Akahisi anafuatwa. Watu walikuwa wengi kiasi chake hivyo kidogo akawa hana woga. Akatembea kwa kasi mpaka akafika kituoni kungoja basi.



    "Napanda hilo linalokuja!" Akajisema kifuani. "Hata kama limejaa vipi."



    Akatazama kushoto na kulia kwake, watu wote walikuwa wametulia, lakini akamwona mwanaume aliyemtilia shaka. Mwanaume huyu alikuwa amevalia shati jeusi, mweupe kwa rangi mwenye macho mekundu.



    Naye huyu mwanaume akamtazama Miriam, wakakutana macho kwa macho. Moyo wa Miriam ukadunda kwa kasi.



    Akatazama barabara. Gari alilokuwa analingojea lilikuwa limekaribia kufika. Akaendelea kuapia moyoni kwamba lazima alipande gari hilo, hata iweje.



    Gari likasimama, yalikuwa ni yale mabasi ya zamani sana. Lilikuwa linamwaga moshi mzito mweusi ambao ukiujumlisha na vumbi la barabara, basi kupata mafua ama matatizo ya kifua ilikuwa haiepukiki.



    "Arusha town hiyo!" Konda akapaza sauti. Lakini gari lilikuwa limejaa mno. Hakukuwa hata na pa kukanyaga sembuse pa kusimama.



    Lakini wanaume wawili wakaliwahi, ikiwemo na Miriam watatu, wakang'ang'ana kulidandia. Wanaume wakafanikiwa, Miriam akaambiwa na konda angoje lijalo, hataweza.



    Hakuwa namna akangoja. Akatazama mahali alipomuona mwanaume yule aliyekuwa anamtilia shaka, hakumwona!



    Akajiuliza kaenda wapi? Akaangaza macho huku na kule lakini kabla hajamaliza msako wake wa macho, ghafla akasikia sauti ya gari lingine laja.



    Akajiweka sawia kung'ang'ana. Sasa gari liliposimama akawa wa kwanza kufika mlangoni, akazama ndani!



    Japo alikuwa amebanwa haswa, hakujali. Alichotaka ni kutoka tu eneo hilo. Lakini kuna jambo.



    Kuna jambo ambalo hakuwa analifahamu.



    Nyuma yake alikuwa amesimama mwanaume yule aliyekuwa anamtilia hofu. Kumbe naye aligombania gari hilo na kuzama humo ndani.



    Miriam alikuja kufahamu hilo baadae baada ya kukaribia Arusha town! Lakini ajabu ni kwamba, hakuelewa kuna nini ama nini kilifanyika, akajikuta anapoteza fahamu.



    "Ni dada yangu, anaumwa!" Miriam alisikia sauti ya mwanaume ikisema huku yeye akipotelea kwa kudhoofu.



    Alihisi kabisa sauti hii itakuwa ni ya mwanaume yule aliyemtilia mashaka, lakini hakuweza hata kupayuka wala kujikomboa.



    Pap! Akawa gizani kamili asijue kinachoendelea.



    **

    Akaja kupata fahamu baada ya muda asioujua. Alikuwa begani mwa mwanaume aliyekuwa anatembea kwa miguu akipiga hatua kubwakubwa.



    Alipoangaza kumtazama mwanaume huyo akagundua ndiye yule aliyekuwa anamtilia mashaka. Sasa afanyaje?



    Akaangaza kushoto na kulia, akayaona mazingira batili. Haya hayakuwa mazingira ya Arusha town. Palikuwa pakavu mno, majani yaliyokauka, barabara ngumu iliyojawa vumbi na mawe.



    Oh my God! Sasa akatambua alikuwa anarejeshwa kwa Nyokaa.



    Hapana! Akasema nafsini. Kamwe sirudi huko nikiwa hai, labda mfu. Lakini atajinasuaje? Ni wazi asingeweza kupimana ubavu na yule jibaba!



    Akaazimia kutafuta namna. Kweli, penye nia pana njia, muda mfupi akaipata ya kwake. Aliona alama ya bunduki kiunoni mwa mwanaume aliyembeba. Ilikuwa ni bunduki ndogo iliyofunikwa na shati alilolivaa.



    Akawaza kuikwapua imuokoe. Japo hakuwa anajua namna ya kuitumia, itamtisha adui yake mwishowe akapata upenyo.



    Ndio, hiyo ilikuwa ni njia yake sahihi kwani njia ya kwanza aliyoifikiria ya kupiga yowe kali isingemsaidia kwa muda huo. Mahali walipokuwa wanapita hapakuwa na ishara ya mtu kabisa.



    Angejichomesha.



    Sasa, moyo wake ukiwa unaenda mbio, akaanza kuhesabu. Akifika tatu, anasita. Akifika tatu, anasita kwa woga.



    'I have to do this! Miriam you have to!' (Inanibidi nifanye hivi! Miriam inakubidi!) akajisemea kifuani.



    Akafunga macho kwanguvu, akahesabu, ilipofika tatu akavuta shati la yule mwanaume upesi na kuchomoa bunduki. Akamwekea kichwani.



    "Nishushe haraka kabla sijakumaliza!" Akaamuru. Yule mwanaume akamshusha akasimama mwenyewe.



    "Ulidhani utanipeleka huko nilipotoka?" Akauliza kwa kiburi. "Umekosea sana. Utaenda mwenyewe."



    Akamwamuru mwanaume huyo ageuke nyuma na akimbie kwa nguvu zake zote. Akihesabu mpaka tatu asimwone, la sivyo atamfyatulia risasi.



    Miriam hakuwahi kuua maisha yake yote. Tukio la kumuua binadamu mwenzake lilikuwa ni zaidi ya mtihani. Yeye mwenyewe kifuani mwake alikuwa anafahamu hawezi kulifanya.



    Lakini katika namna ya ajabu, mwanaume yule akiwa amenyooshewa mdomo wa bunduki, hakutii agizo alilopewa. Badala yake hata mikono aliyokuwa ameiweka juu akaishusha na kisha akatabasamu.



    "Nimesema geuka ukimbie kuokoa uhai wako. Umechoka maisha unh?" Miriam akafoka.



    Yule mwanaume akacheka. Kisha akamsogelea.



    "Simama hapo hapo! ... nimesema simama!" Miriam alifoka lakini mwanaume yule hakutii, akafyatua bunduki, ajabu hakikutoka kitu. Akafyatua tena na tena, hola!



    Mwanaume yule akampokonya bunduki hiyo.



    "Ukitaka kushoot, unakoki kwanza bunduki, sawa?" Akamwambia Miriam huku akikoki bunduki kisha akamwamuru: "Haya sasa geuka twende!"

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miriam akanyong'onyea. Akapoteza matumaini ya kutoroka. Lakini akaapia moyoni mwake hatokuwa radhi kurejeshwa tena kule alipotokea.



    Labda tu awe maiti.



    "Nimekwambia geuka twende!" Akarudia mwanaume akitoa macho ya kutisha lakini Miriam akaendelea kusimama kana kwamba hajasikia.



    Kuonyesha hana mchezo, mwanaume akapiga risasi kandokando ya Miriam kisha akarudia sentensi yake akimtaka Miriam waende.



    "Siendi, niue!" Miriam akamwambia pasi na hofu. Kabla mwanaume huyo hajafanya kitu akasikia sauti nyuma yake, kilikuwa ni kishindo cha mtu kwa mbali.



    Haraka akageuka kutazama. Kweli alikuwa ni mama aliyekuwa amebebelea ndoo ya maji kichwani. Mama huyo alikuwa ametoa macho ya mshangao akiwatazama.



    Mwanaume akamgeuzia bunduki na kufyatua risasi moja, heri ikamkosa, mama akadondosha ndoo na kukimbia kama mwehu akipiga ukunga.



    Mwanaume huyo alimpogeukia Miriam akakutana na jiwe la uso! Akadondoka chini akiacha bunduki. Akamwaga damu za kutosha akilalama kwa maumivu makali.



    Miriam akaokota bunduki.



    "Tatizo nikikuacha, bado utanisumbua!"



    Akafyatua bunduki pasipo kumtazama mlengwa wake. Hata alipomaliza kumfyatulia hakumtazama akaondoka zake. Alikuwa anaogopa. Alijua ameshamuua mwanaume huyo.



    Kumbe hizo risasi zote zilipiga chini!



    ***



    "Honestly I thank God, kwanza shukrani ziende kwake. Na pia kwa huyo malaika aliyemtuma kuniokoa," alinguruma bwana Kamau Githeri kwenye televisheni ya KTN wasaa wa taarifa ya habari.



    "Unaweza kutuambia ilikuwaje hasa?" Akauliza ripota. Kwa wakati huo maandishi yaliyokuwepo chini ya video yakisomeka kama ifuatavyo:



    'MHESHIMIWA K. GITHERI APONA CHUPUCHUPU YA KUCHUNGULIA KABURI'



    "Ni ujhumbe tu nilipongeaga kwa email," akaeleza mheshimiwa Githeri. "ukinitell kwamba nipo about kuwa ambushed na wauajhi. I didn't ignore it, nikatake steps along with my family immediately!"



    Wakaonyesha walinzi wa nyumba ya bwana Githeri, wawili, wote walikuwa wameuawa pamoja na mbwa wao.



    "Unadhani ni kwanini walitaka kukuua?" Akauliza ripota.



    "I think ni haya tu issues za politics, nothing more," akajibu mheshimiwa. "Furthermore, nisingependa kuongea sana. Shauri yangu iko kwa polisi hands as we talk."



    Baada ya hapo KTN wakaonyesha na upande wa pili wa mheshimiwa Otieno. Hapa kichwa cha habari kikabadilika na kusomeka ifuatavyo:



    'HON. OTIENO AMIMINIWA RISASI KUUAWA'



    Wakahojiwa baadhi ya mashahidi wa tukio hilo na mhusika mmoja wa familia akieleza namna walivyoguswa na msiba huo kwa ndani.



    Hata mhusika huyo wa familia hakuweza kueleza kwa muda mrefu, akakabwa na kilio, mahojiano yakakatishwa.



    Habari ikaendelea kurushwa. Sasa wakihamia kwa viongozi wa bunge wameupokeaje msiba huo na mashambulizi hayo ya ghafla ndani ya siku moja huku mojawapo likizaa matunda.



    Spika akanena kulaani tukio hilo akisema linatishia uhuru wa bunge kama mhimili muhimu wa serikali kufanya kazi yake. Lakini zaidi akatupa lawama za waziwazi kwa karani wa bunge ambaye alipuuzia ujumbe aliotumiwa na msamaria mwema kuhusu shambulizi hilo.



    "Somehow, he is responsible for such act!" (Kwa namna fulani, anawajibika na tukio hilo!)



    Baada ya hapo ripota akasema uchunguzi wa kipolisi unaendelea, habari hiyo ikapita zikiendelea zingine.



    "Shit!" Sheng akasaga meno. "How is this possible?" (Linawezekanaje hili?)



    Alikuwa ameketi sebuleni akikodolea televisheni yake kubwa iliyomeza ukuta. Akatetemeka kwa hasira.



    Ni nani aliyetuma taarifa za kutaka kuuawa viongozi hao? Ni swali lililomnyima raha. Hakuweza kukaa nalo kifuani akanyanyua simu yake ya mkononi akapiga.



    Akaagiza watu wote wa vitengo vya mawasiliano pamoja na heads wa WAVES zote wafike ofisini kwake kesho asubuhi na mapema.



    Wanapokuja wahakikishe wana maelezo yanayojitosheleza. La sivyo wataingia hai na kutoka wafu!



    **



    "Dada, una mgeni," mfanyakazi alimtaarifu Miranda.



    "Nani huyo?" Miranda akauliza kwa hasira. Alikuwa ameketi kitandani kwake akiperuzi kwa kutumia tarakilishi yake mpakato. Mwilini ana gauni la kulalia.



    Majira ni saa nne usiku.



    "Simjui mimi. Ni mzungu!" Akajibu dada wa kazi. Miranda akashtuka. Moja kwa moja akawaza atakuwa ni BC.



    Lakini mbona hakunipa taarifa?



    Akanyanyuka upesi na kwenda sebuleni. Kweli akamkuta BC ndani ya suti kama ilivyo ada. Akamkaribisha na kusalimiana.



    Pasipo kupoteza muda BC akamuuliza:



    "Are you the one who did it?" (Wewe ndiye uliyelifanya?)



    Miranda akatikisa kichwa.



    "I didn't do it," (sijalifanya) akajibu kwa msisitizo.



    BC akashusha pumzi ndefu maana sasa alikuwa amechanganyikiwa. Kama si Miranda aliyetekeleza lile agizo, basi ni nani mwingine?



    Hofu ilimuingia ukute wamezamishwa mtegoni na 'wajanja' kisha waumie huku wakiwanufaisha wengine. Lakini hao 'wajanja' ni wakina nani?



    BC akamuuliza Miranda yeye alikuwa amepangaje kummaliza yule mwanamke. Miranda akasema hakuwazia njia ya ajali kabisa kwani ni risk sana. Aliwazia kumtwanga tu risasi akiigiza jambazi ili kufinya ulimwengu wa kipepelezi.



    Sasa sio tu kwamba walikuwa kwenye rada za polisi, kama vile Miranda alivyosema kuwa anatafutwa na inspekta Jona, bali pia walikuwa na kazi ya kumng'amua mtu aliyewazidi hatua na kulifanya hilo akilenga kuwa 'frame' wakamatwe.



    BC akamuaga Miranda na kisha akaenda zake. Alimwachia Miranda kazi ya kufanya, ashirikiane na Jona hatua kwa hatua kumjua mtu huyo. Lakini kwa wakati huo akijiweka safi, mwenye mikono isiyo na hatia.



    Usiku huo kwa Miranda ukawa mgumu haswa. Alijaribu kuchambua kila mazingira aliyoyapitia kuangaza kama kuna mahali alifanya kauzembe, hakupata!



    Huu mtihani ulikuwa mgumu sana.



    Lakini mwanamke huyu alisahau jambo moja. Jambo moja lililomtia kwenye mtego wa ngiri. Hakufahamu, aidha tuseme alisahau kuwa ni yeye aliyefanya akajazwa kwenye rada ya adui.



    Adui huyu ni mwerevu mno. Hakurupuki na hubonyeza kitufe pale anapoona anatakiwa sasa kufanya hivyo.



    Unakumbuka kipindi kile Miranda alipojionyesha runingani akiwa na mke wa Boka akitambulishwa kama balozi wa kampuni hiyo ya urembo na vipodozi na akinadi bidhaa za kampuni hiyo?



    Basi kama wakumbuka, mipango miwili ilianzia hapo, mosi ya kumsaka Miranda, pili, kuimaliza kabisa kampuni ya mama huyu.



    Lakini yote hayo yatekelezwe katika njia 'laini'. Mama afe, Miranda afe pia ama akafie jela.



    Kila Miranda alipokutana na Boka, hakujua anatazamwa na kufuatiliwa. Na ijapokuwa wanaomfuatilia hawakujua nini Boka na Miranda walikuwa wanaongea, kiutuzima, ukubwa dawa, wakang'amua watu hao wapo kwenye mahusiano.



    Sasa kuna nini tena hapo?



    Miranda akawa anatafutwa ajae kiganjani. Kwenda kuonana na mke wa Boka hotelini na kugombana huko, kote kulikuwa kunatazamwa.



    Sasa je kuna sehemu gani ya kumaliza mchezo kama hii? Endapo tukimmaliza mke wa Boka, polisi watamalizana na Miranda. As simple as that!



    Hakikisha mke anakufa, shoga yake anabaki kutoa ushahidi. Shoga huyu lazima atamtuhumu Miranda kwani alikuwapo wakati zogo latukia.



    Unadhani atamhisi nani mwingine? Ni Miranda anataka kumuua mke ili abakie na mume wa mtu!



    Miranda alikuwa ana fumbo hili kubwa kulifumbua. Yeye pamoja na Jona.



    **



    Majira ya saa nne asubuhi.



    "Uliona wakati akiitwa?" Jona akamuuliza Marwa. Mezani kulikuwa kuna vikombe viwili vya chai. Vikombe hivi vilikuwa vimejaa lakini chai ikiwa imeshapoa. Tangu viwekwe hapo mezani havikuguswa.



    "Sikuona akiitwa," alijibu Marwa. "Tuliachana vizuri tu kila mtu akaenda kufanya kazi yake. Baadae tulipotoka, sikumwona. Nikajua atakuwa ametingwa kwani aliniambia anaweza akawa yupo tight. Kumbe ndo' alikuwa ashauawa!"



    Hizi habari zilikuwa ngumu sana kwa Jona. Alijaribu kujilazimisha aziamini lakini kichwa chake kikagoma kabisa. Kwanini Panky ameuawa?



    "Marwa, inabidi uwe makini sana," Jona akashauri. "Hatuwezi jua pengine Panky ameuawa kwasababu za kipelelezi ambao unaweza ukakuweka hatarini nawe pia."



    Marwa akanyamaza. Alikuwa anatazama chini uso wake ukimezwa na hofu. Aliogopa sana. Kifo cha Panky kilimshtua na kumkumbusha kuwa hayupo salama abadani.



    Aliwaza mtu atakayefuata kuuawa atakuwa ni yeye. Si mwingne. Mawazo hayo yakamfanya asimsikilize kabisa Jona alichokuwa anaongea.



    Jona akamtikisa.



    "Marwa, tupo pamoja!" Marwa akashusha pumzi ndefu alafu akanyaka simu yake mezani na kumkabidhi Jona.



    "Alinitumia ujumbe muda mfupi baada ha kuachana toka kula. Akiniambia hao ndo' watu waliotumiwa pesa muda si mrefu kwa ajili ya malazi, chakula na makazi nchini Kenya."



    Jona akatazama majina hayo, akamuuliza Marwa kama anawafahamu hao watu, anaweza kumsaidia angalau kwa picha.



    Marwa akazama ndani ya tarakilishi yake, punde akapata picha na kumwonyesha. Jona akatumia simu yake kudaka picha hizo na kuzitunza.



    Watu hao walikuwa ni Lee na wenzake watatu: Devi, Nigaa na Mombo.



    "Ahsante sana," Jona akashukuru. Marwa akamtazama mwanaume huyo na kumwambia pasi na chembe ya masikhara.



    "Hapo ndiyo utakuwa mwisho wa kukusaidia. I am out!"



    Jona akaduwaa.



    "Una maanisha nini Marwa?"



    Marwa pasipo kupepesa macho akamwambia hataki tena ushirika. Mpaka hapo alichokifanya inatosha. Anaomba asihusishwe kwa njia yoyote ile tena!



    "It is enough. I cant take this risk anymore!" (Inatosha. Siwezi kubeba hii hatari zaidi!)



    Haikujalisha Jona aliongea nini, Marwa hakutaka sikia. Alimtaka aende na amwache na maisha yake kama alivyomkuta.



    Ni bora maisha yake ya awali kuliko haya ya sasa ambayo anaweza akakosa vyote. Kheri sasa anapata kimoja, wazazi wake kuwa hai. Inatosha!



    Marwa alikuwa ame 'panik'. Alikuwa pia na hasira ndaniye ambayo ilizidi kujionyesha kadiri alivyokuwa anaongea.



    Jona akaona huo si wasaa wa busara kwake kukaa hapo, akaondoka zake.



    **



    Aliegemea kiti cha taksi akiendelea kuwaza. Alifahamu fika kwa mawazo haya kama angelipanda daladala angepitishwa kituo. Application yake ya UBER ikamsaidia kupata usafiri chap!



    Alimfikiria Panky na kisha Marwa. Marwa na kisha Panky. Akaja kubanduliwa toka kwenye mawazo hayo na mlio wa simu. Alikuwa ni Kamanda.



    "Umefikia wapi?"



    "Bado naendelea na upepelezi, mkuu. Nitakufahamisha, sipo maeneo mazuri."



    Simu ikakata. Sasa Jona akatazama mandhari ya nje ya gari. Akapata kuwaza kidogo kuhusu kesi ya mke wake Boka, akapata wazo.



    Alikuwa anaelekea hospitali kuonana na rafiki wa mke wa Boka kisha aende kwa Miranda. Lakini akaona ni vema apite kwa Boka kisha aende mawasiliano.



    Akapita huko, akachukua simu na namba ya simu ya marehemu kisha akaelekea mawasiliano ambapo alifanya utaratibu wa kupata mawasiliano ya mwisho na marehemu, akaenda kumalizia utaratibu wake huo TIGO.



    Akachapiwa jumbe zote na hata akapata 'access' ya 'recorded calls' za mwisho. Yote hayo yaliwezekana pasipo kuchukua muda sana kwa kujieleza anayahitaji kiupelelezi.



    Napo kwa wakati huo ...



    Mlio wa risasi ukasikika mara mbili toka ofisini mwa Sheng.



    Tah! - tah!



    Mlango ukafunguliwa ikatolewa maiti ya mtu mwenye asili ya China! Wanaume wawili walimbebelea wakielekea upande wa kushoto mwa jengo.



    Marehemu huyu alikuwa ni Moderator! Moderator wa SPACE BUTTON. Tayari roho yake ilishanyofolewa na mkono wa Sheng baada ya kubainika ni yeye ndiye alifanya uzembe.



    "I want that traitor alive!" (Namtaka huyo msaliti akiwa hai!) Sheng alisikika akifoka ndani ya ofisi kisha akabamiza meza.



    Mara wanaume kadhaa wakatoka ndani. Wakaendelea kuteta kadiri walivyokuwa wanasonga mbali na ofisi ya mkuu.



    Sasa wazi, Marwa alikuwa hatiani!



    Hati ya hatiani. Uzembe mdogo hauruhusiwi ndani ya ANGA LA WASHENZI - ANGA LA WAUAJI. Ndani ya dakika chache tu kipindi cha usiku, Marwa baada ya kufanya kazi ya udukuzi, akasahau ku 'log-out'.



    Hakujua alisahau na maisha yake hapo, haraka akatambuliwa. Uangalizi ulikuwa mkubwa sana haswa baada ya kubainika kuwa mawasiliano yao yalidukuliwa na kupelekea zoezi la kuokolewa kwa walengwa.



    Haraka alipojulikana, akajazwa kwenye GPS na haraka tena akajulikana makazi yake yalipo. Haya makazi yalikuwa ya nani? - Marwa! Toka SPACE BUTTON - BIRD ONE.



    Moderator angeachwaje hai?



    **



    "Miranda, kila kitu kinakuonyeshea ni wewe," Jona alisema baada ya kunywa maji mafundo kadhaa.



    Miranda akasonya akitikisa kichwa.



    "Jona, I swear to God. Sijafanya hicho kitu kabisa kabisa!"



    "Sasa tatizo ni kwamba inabidi uthibitishe hilo. Si kwa maneno tu," Jona akasema akimtazama Miranda kana kwamba mwalimu amtazamavyo mwanafunzi mtoro.



    Miranda akashika kichwa chake na kukikuna kwanguvu.



    "Pengine ni maadui zangu," Miranda akajitetea kidhaifu. "Huwezi jua?"



    Hata mwenyewe alijiona anaongea kitu ambacho haki 'make sense'. Jona alikunywa maji tena alafu akamtazama. Akamuuliza ni lini walianza ile projekti ya kupeleka bidhaa zao Kenya.



    Miranda baada ya kufikiria kidogo, akasema anakumbuka ilikuwa ni punde tu baada ya majadiliano na makubaliano yaliyofanyika nchini Kenya kuwa bidhaa toka nchi za Afrika Mashariki zipewe kipaumbele sokoni, zipunguziwe makato na kufanyiwa wepesi.



    Mke wa Boka akaona hiyo ni fursa adhimu kwake kulivamia soko hilo la vipodozi na urembo.



    Baada ya maelezo hayo, Jona akamuaga Miranda aende zake lakini akimuahidi atakuwa anamtembelea mara kwa mara.



    "Naamini hautaufanya uhuni wako," alimwonya akiwa ameushikilia mlango.



    **



    Saa saba usiku ...



    Gari jeusi lilisimama kwa mbali hivyo halikuonekana vema ni la aina gani. Wakashuka wanaume wawili waliovalia suti nyeusi, tai nyekundu na vinyago vyeusi.



    Wanaume hawa walikuwa wakakamavu wakitembea kwa haraka, wazi wakienda kutenda tukio.



    Kutokana na giza lililokuwepo na pia mavazi yao, ilikuwa ngumu kuwatambua. Waliufikia ukuta mmoja akatumika kama ngazi mwenzake kukwea mpaka juu, alafu naye aliye juu akamvuta mwenzake wakaingia ndani.



    Hakuna hata chembe ya kelele iliyotokea hapa. Na yote haya yalifanyika ndani ya sekunde tu, wala si dakika, kuthibitisha kwamba wanaume hawa walikuwa wana mafunzo.



    Walitumia waya kufungulia kufuli za milango, na kwa upande wa magrili, kabla hawajafungua walimiminia mafuta viungoni, basi yakafunguka pasi na tone la makelele!



    Mpaka wanafika kitandani mwa Marwa, walikuwa wametumia dakika mbili tu tangu walipotoka kwenye usafiri wao!



    Wakamwamsha Marwa kwa kumpiga na kitako cha bunduki kisha wakamtaka aongozane nao kimya kimya!



    "Sasa jifanye mjanja uone kilichomfanya fisi awe na miguu mifupi!



    Marwa akatetemeka sana. Jasho likamiminika kama nusu ndoo. Alihisi kila aina ya haja. Aliona roho inamtoka mbele yake na hana cha kufanya!



    Akasimama na kuswagwa alekee nje.



    Kufika huko kabla hawajatoka, wakasikia sauti ya mluzi! Wanaume watekaji wakaangaza kushoto na kulia, hawakuona mtu!



    Wakatazamana.



    Sauti ya mluzi ikalia tena, mara hii ikifuatisha melodi za muziki.



    ***



    Watekaji wakachanganyikiwa. Ni nani huyo anawafanyia mchezo? Wakaangaza tena wasifanikiwe. Wakawa wamepigwa na bumbuwazi.



    Wakatishia kumuua Marwa endapo huyo apigaye mluzi hatajitokeza mwenyewe. Lakini kinyume na matarajio, mpiga mluzi hakujitokeza!



    Na sasa hivi badala ya kupiga mluzi akaongea:



    "Najua hamuwezi kumuua. Kama mngelikuwa mmepanga hivyo, msingelikuwa na haja ya kumtoa nje."



    Kisha kukawa kimya kidogo.



    Kutazama huku na kule, ghafla akatokea mwanaume hewani! Alikuwa ni Jona. Hamaki kutazama, bunduki ikapigwa teke na kisha Jona akajifichia kwenye mwili wa mwanaume mtekaji.



    Risasi mbili zikatupwa! Mwanaume mtekaji alimpiga mwenzake kwa pupa na kumuua. Jona akamrusha yule mtekaji marehemu kwa mwenziwe, akamdaka, ikawa kosa.



    Kabla hajafanya jambo, Jona akawa amemchapa teke zito, kinyago na bunduki zikarukia kando. Kuja kukaa sawa, tayari ashawekwa chini ya ulinzi.



    "Tulia kama maji mtungini!" Jona akamwamuru. Wakamfunga mikono na miguu na kisha kinywa!



    Baada ya muda mfupi wakatoka wanaume wawili nje ya uzio. Walikuwa wamevalia suti na vinyago. Wakatembea kwenda kufuata lile gari lililowaleta watekaji.



    Walipolifikia wakamuweka dereva chini ya ulinzi na kumwamuru asogeze gari lake kwa nyumba ya Marwa. Naye wakamfunga miguu na mikono na kinywa, wakampakia na yule marehemu kwenye gari wakawapeleka kituoni.



    "Nitakuja kuwahoji mwenyewe," Jona alitoa maelezo kwa polisi kisha wakitumia lile gari la wavamizi, wakayeya.



    Marehemu akapelekwa mochwari.



    Lakini bado kichwani mwa Marwa kulikuwa na maswali. Jona aliwezaje kufika pale nyumbani kwake kumuokoa? Alijuaje kama wavamizi watakuja kummaliza usiku huo?



    Kusema ukweli alimwona Jona kama malaika kwani alishajua amekwisha usiku huo. Kitendo cha mwanaume huyo kutokea na kumwokoa, kulikuwa ni muujiza. Bado hakuamini!



    "Ahsante sana, Jona," akashukuru.



    "Usijali," Jona akamjibu akitazama mbele. "Ni kazi yangu."



    Kukawa kimya kidogo.



    "Najua una maswali kichwani," Jona akasema akili ya Marwa. " unawaza nilifikaje pale kwako kwa muda muafaka kiasi kile. Ila tambua nilikuwa nakuwaza. Sikuweza kulala nyumbani kwangu kwa amani kabisa. Na akili yangu iliniaminisha haupo salama. Kama Panky ameuawa, basi nawe lazima utakuwa kwenye rada zao."



    Baada ya kusema hayo, Marwa akaomba msamaha kwa Jona. Alitenda kosa kumfukuza kiasi kile na hata amemsaliti kwenye mapambano.



    Jona akamwambia asijali, sasa watazame ya mbele. Amelenga kumfundisha mwanaume huyo sanaa ya mapambano, martial arts, ikapate kumsadia kujilinda kwani atahitaji sana mafunzo hayo kwa kipindi hicho.



    Marwa akaridhia. Wakaenda nyumbani kwa Jona na kupumzika. Lakini Marwa hakulala kabisa kwa woga. Alihisi wale majamaa wanaweza kurudi tena kumuua.



    Kila aliposikia sauti ya kitu akakurupuka na kuangaza. Alipomtazama Jona yeye alikuwa tayari anakoroma baada ya kunywa vinywaji vyake vikali.



    Kama haitoshi Marwa alikuwa anawafikiria na wazazi wake. Yeye amenusurika kifo lakini vipi wazazi wake ambao wanategemea kupata antidote toka kwa Sheng? Wataishije?



    Ina maana atawaona baba na mama yake wakifa huku hana cha kufanya? Akakosa amani.



    Akajigeuza huku na huko. Akajibaraguza kitandani lakini hakupata usingizi kabisa. Akaona kuna haja ya kupumbaza kichwa.



    Akanyanyuka na kumalizia kinywaji alichobakiza Jona chupani. Kilikuwa ni kinywaji kikali mno na yeye hakuwa mzoefu wa hayo mambo kabisa.



    Sasa hakuchukua dakika akalala usingizi ambao hajawahi kuupata tangu azaliwe. Kama mfu!



    Alikuja kuamka saa tatu asubuhi kichwa kikiwa kinamgonga haswa. Kumtazama Jona, hakuwepo! Alishaondoka akimwachia maelekezo kwa njia ya maandishi,



    Aikute supu jikoni.



    ***



    Saa ya ukutani ilikuwa inasema ni saa tano asubuhi hivi sasa. Jona hakuwa mtu wa kukaa ofisini mara kwa mara, ila leo hii huu muda ulimkuta akiwa kwenye kiti nyuma ya meza iliyobebelea tarakilishi.



    Kuna mambo kadhaa alikuwa anayapitia haswa kuhusu kesi ya ajali ya mke wake Boka. Alikuwa anachambua maelezo ya Miranda akaona kuna kitu mule ndani yake.



    Kuna jambo la kulifuatilia!



    Mojawapo ya kanuni ya upelelezi ni kwamba kila kitu mbele yako ni mtuhumiwa katika namna yake. Hutakiwi kupuuza chochote kile, wala kukidharau. Kwani yeyote anaweza kufanya lolote kwasababu yoyote.



    Jona akazama mtandaoni na kuangazia yale ambayo Miranda alikuwa anayasema kuwa mke wa Boka alianza kupeleka bidhaa zake nchini Kenya baada ya kuona hali ni shwari huko kisera.



    Alipopekua kwenye vyanzo mbalimbali akaja gundua kuwa jambo hilo lilikuwa ni 'hot issue' huko nchini Kenya. Ambapo lilizua mjadala mkubwa miongoni mwa wachangiaji, hoja ikiwa kwamba soko la Kenya sasa limefurika bidhaa toka China.



    Bidhaa za wazawa zimekuwa hafifu mno na kwasababu za ulimbukeni na unafuu mkubwa ambao unawekwa kwenye bidhaa za China, basi bidhaa za wazawa zimekosa soko, si wakulima wala wafanyabiashara wanaohema kwa unafuu.



    Sasa mswada uliletwa bungeni kuangazia namna ya kukabili na kubadili hali hii, miswada hii ikiletwa na wabunge wa chama pinzani ambao kwa jina walikuwa ni waheshimiwa Kamau Githeri na W.Otieno.



    Sasa haya majina yakamshangaza Jona! Yalikuwa ndio wale waheshimiwa waliolengwa kuuawa. Kumbe kulengwa kwao ilikuwa ni kwasababu ha hili jambo! Sasa akajua.



    Kwa kupitia mswada wao waliouleta bungeni, sheria sasa ikatungwa kuweka mipaka kwa bidhaa za nchini China na huku zikiongezewa kodi na makato ili wazawa na hata wale wafanyabiashara toka nchi Afrika Mashariki wapate ahueni.



    Alarm ikaita kichwani mwa Jona! Sasa hapa kulikuwa na harufu ya jambo.



    "Hata ukitazama vema, most of Chinese products zimekuwa zikiwaharibu wanawake zetu. Sasa wabadilika rangi kama chameleons hata their shapes zimekuwa awkward. Why cant we allow our natural products to take over and ban these Chinese takataka?" Hii ilikuwa mojawapo ya kauli aliyoitoa marehemu W. Otieno punde baada ya kutoka kwenye mzozo mkali bungeni.



    Sasa Jona akapata picha kamili. Hivi vitu vilikuwa vina mahusiano, tena ya kindakindaki! Kilichomuua mke wa Boka, hakuwa Miranda bali wachina ambao walimchukulia kama tishio kwa bishara yao ya vipodozi nchini Kenya!



    Jona akatafuta clips za video ndani ya mtandao wa YOU TUBE zikionyesha hotuba za waheshimiwa Kamau Githeri na W. Otieno kupinga udhalimu wa China kwenye kudhoofisha uchumi wao wa ndani, baada ya hapo akazipakua pia na video za marehemu mke wa Boka.



    Kama haitoshi akapakua na vielelezo kadhaa toka mtandaoni na kuviprint akiviweka kwenye faili. Sasa akijumuisha na vile alivyovipata kwa link kwa msaada wa Marwa, alikuwa kwenye hatua njema kabisa.



    Rrrrrrrrnnng! Simu ikaita. Akaipokea na kuiweka sikioni. Kamanda.



    "Nakuja, mkuu," akasema kwa ufupi simu ikakata. Akanyanyuka na kwenda kuonana na Kamanda ofisini kwake.



    "Umefikia wapi?" Lilikuwa swali la kwanza la Kamanda.



    Jona akamweleza namna gani anavyowashuku wachina kuhusika na kifo cha mke wa Boka, haswa kwasababu za kibiashara huko nchini Kenya. Watu hao wakilenga kummaliza mwanamke huyo ili kuendelea kutawala soko la bidhaa zao za urembo na vipodozi.



    Kamanda akashusha pumzi ndefu. Alielewa kila ambacho Jona alieleza lakini ugumu unakuja hapa, kwa kesi hiyo kutimia, wanahitaji msaada toka jeshi la polisi la Kenya kwenye upelelezi na 'confirmation'. Mahusiano baina ya nchi hizi mbili kwa hapa karibuni yamedidimia, itawawia vigumu kutekeleza hilo.



    "Lakini Jona, bado hii simulizi yako inahitaji ushahidi zaidi," akasema Kamanda. "Utathibitisha vipi muuaji huyo alitumwa na Wachina? pili, mauaji ya viongozi hao wa Kenya hatuwezi kuyatolea tamko bali mamlaka zao za ndani, tutawasemeaje wameuawa na wachina?"



    Jona akamwomba Kamanda ampatie muda zaidi, atatafutia ufumbuzi kila swala lililopo mezani. Kwa muda huo akaomba aende ubalozi wa China kwa ajili ya mahojiano.



    "Utaenda kuwauliza nini huko? Huoni utateteresha mahusiano baina yetu na wao?" Kamanda akapata hofu.



    "Usijali, Kamanda," akasema Jona. "Najua namna ya kuenenda."



    Jona akatoka ofisini.



    Sasa ilikuwa ni majira ya saa saba ya mchana. Akaona ni kheri kama angelipata kitu tumboni. Akasonga kantini na kujipatia chakula.



    Akiwa hapo mara ujumbe ukaingia ndani ya simu yake toka kwa namba mpya. Akaufungua:



    'Habari, Jona. Ni Miriam hapa. Tafadhali naweza kuonana na wewe?"



    "Miriam?" Jona akatahamaki. Badala ya kujibu ujumbe huo akaamua kupiga simu. Ikapokelewa na sauti ya kike, akajitambulisha ni Miriam, mke wa marehemu Eliakimu.



    "Upo wapi?" Jona akauliza.



    "Nipo kwa shangazi yangu Kimara," akajibu Miriam.



    "Sawa, basi nitafanya mpango tuonane jioni."



    Simu ikakatwa.



    "Miriam!" Jona akajisemea wenyewe. Alikiri ana maswali kadhaa ya kumuuliza mwanamke huyo, kwa upande wa Eliakimu na hata pia wakina Nyokaa.



    Aliamini atapata taarifa za maana toka kwa mwanamke huyo akawatie nguvuni wadhalimu.



    Alipomaliza kula akalipia na kunyookea ubalozi wa China. Humo ndani hakumkuta balozi bali msaidizi wake. Wakateta kwa lisaa limoja kabla Jona hajatoka ndani ya jengo hilo.



    Kitendo cha kutoka tu, ikachukua dakika mbili, Sheng akaarifiwa juu ya ujio wa Jona. Na shuku zake zote alizozileta ubalozini!



    ***



    MWISHO WA SEASON 1,



    - JE SHENG ATAMFANYA NINI JONA?



    - MARWA ATAPATA MBADALA WA TIBA YA WAZAZI WAKE?



    - MIRIAM ANAMTAKIA NINI JONA?



    - JONA ATAWEZA VITA HII MWENYEWE?



    - MAJIBU YAPO MSIMU WA PILI! SEASON 2 YA ANGA LA WASHENZI

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





0 comments:

Post a Comment

Blog