Sehemu Ya Tatu (3)
Walipokuwa sebuleni wakikagua kama kulikuwa na chochote kilichoibwa, Husna akagundua kuwa, kwa hapo sebuleni hakukuwa na chochote cha thamani kilichoibwa. Tukio hilo lilimshangaza, lilimshangaza kwa sababu kulikuwepo na vitu vya thamani vyenye kubebeka kirahisi lakini havikuibwa!
“Nashangaa hakuna chochote kilichoibwa!” Husna alisema huku akiendelea kukagua kwa macho eneo la sebuleni.
“Chumbani kwako hawakuingia?” mlinzi aliuliza.
“Sijafika hata chumbani kwenyewe!”
“Kwa nini usiende kuangalia?”
Husna hakusubiri kumjibu mlinzi hoja yake, aliondoka bila ya kutamka chochote na kuelekea chumbani kwake. Mlinzi naye akamfuata nyuma.
“Mungu wangu!” Husna alisema baada ya kuiona hali iliyokuwemo chumbani kwake. Huko nako kulipanguliwa kwa kila kilichokuwemo humo, hata godoro lilikuwa lipo nusu kitandani, nusu likiwa chini. Hali hiyo ikamfanya awe kama mwehu, akaanza kukagua kila kitu chake alichokithamini. Hatimaye akagundua vyote alivyokuwa amevitilia wasiwasi kuwa vingekuwa rahisi kuibwa, vilikuwa havikuibwa! “Huku nako hakuna kilichoibwa!” alisema bila ya kumwangalia mlinzi.
“Sasa waliingia kufuata nini?” mlinzi aliuliza huku akionyesha kushangazwa na tukio hilo.
“Nashindwa kuelewa!” Husna alisema na hapo hapo macho yake yakakutana na kitabu kinachohifadhi picha kikiwa kipetupwa chini na kilikuwa kimefunguka baadhi ya kurasa zake. Akakiendea na kukichukua na kuanza kukikagua. Alichokigundua ndicho kilichomshangaza. Kurasa zote zilizokuwa zimetolewa picha zilikuwa zimechanwa nailoni yake wakati wa kutolewa picha hizo. Cha ajabu zaidi alichokistajabia ni kugundua kuwa, picha zote zilizokuwa zimetolewa ni picha zilizokuwa zimemuhusu mheshimiwa Himidu! Picha nyingine zilibaki kama zilivyo! Ugunduzi huu ukabakia nafsini mwake bila ya kumwambia mlinzi.
Wakati mlinzi akiwa ametoka, huku nyuma Husna alimpigia simu wakili Feruzi na kumhadithia yaliyomtokea.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Waliokuingilia hawakuwa majambazi,” Feruzi alisema. “Watakuwa ni polisi! Na ndio maana walichukua picha zenye nasaba na Himidu, kama kungekuwa na kingine chenye nasaba na mheshimiwa Himidu nacho wangeweza kukichukua.”
“Kwa nini lakini wananifanyia hivi?” Husna alilalamika.
“Wanataka kuhakikisha hutokuwa na chochote cha kuthibitisha kuwa, Himidu alikuwa ni mpenzi wako. Kwa maana nyingine ni kwamba, lile onyo la kukutaka ukanushe uhusiano wa kimapenzi uliokuwepo kati yako na Himidu liko pale pale pindi habari hizo zikiandikwa na vyombo vya habari. Wanaogopa waandishi wa habari wasije wakapata ushahidi wowote utakaohusisha uhusiano wenu.”
“Kwa nini wahangaike hivi wakati Himidu wanaejaribu kumtetea au kumlinda na hilo amekwishafariki?”
“Kuna tukio lililotokea lililohusu ndoa yake na lipo jingine ambalo linawafanya wakufanyie hivyo. Unataka kuniambia hukuwa ukifahamu kuwa, ndoa yao iliingia mgogoro kwa sababu yako?”
Husna alishusha pumzi na kusema, “Hakuwahi kunidokeza tukio hilo. Atakuwa alinificha.”
“Uhusiano wako na Himidu uligunduliwa na mkewe na kuleta mfarakano mkubwa kwenye ndoa yao. Himidu akawa amekana kuwa na uhusiano na wewe, mkewe akaita Masheikh na baadhi ya viongozi wengine wa chama na serikali ili Himidu ale kiapo cha kuukana uhusiano wake na wewe. Wote walikuja na Himidu akakubali kushika Quran kuapa kuwa, hakuwa na uhusiano wowote wa mapenzi na wewe. Bahati mbaya mmoja kati ya mashuhuda walioshuhudia tukio hilo, baadaye alikihama chama tawala na kujiunga na chama cha upinzani. Hilo ndilo tukio linalowasababisha polisi watumike kuhakikisha hakupatikana ushahidi wowote wenye kuhusisha uhusiano wako na Himidu pindi waandishi wa habari watakapoanza kukufuatilia. Sababu ya pili ni kwamba, mtoto wa kiume wa Himidu amejiandaa kugombea ubunge kwenye jimbo la Kinondoni baada ya kutenguliwa kwa matokeo ya awali na mahakama. Matokeo ambayo yamelifanya jimbo hilo sasa liwe wazi. Kinachohofiwa hapa ni mpinzani wa kutoka chama cha upinzani ndiye anayeonekana kuwa mwiba kwa mtoto wa Himidu, chama hicho cha upinzani ndicho kilichohamiwa na shuhuda aliyemshuhudia Himidu akishika Quran kuukana uhusiano wake na wako.
“Fikiria waandishi wa habari wakizipata habari hizo kutoka kwa huyo mheshimiwa aliyehamia upinzani kisha, wakapata ushahidi wowote kutoka kwako mwenyewe kuwa ni kweli alikuwa ni mpenzi wako au wakapata ushahidi wa picha kutoka kwako itakayothibisha uhusiano huo na kibaya zaidi, Himidu ameuawa akiwa mikononi mwako. Ni wazi kashfa hiyo itatumika kwenye kampeni za kuitia doa familia ya Himidu kuwa, haina uaminifu kuanzia kwenye familia yao wenyewe na isingestahili kupewa dhamana ya kukabidhiwa madaraka ya kuwaongoza watu wengine. Hilo linaweza likawa ni pigo kwa mtoto wa Himidu na chama tawala kukipoteza kiti hicho. Kwa hiyo kinachofanyika hapa ni kuhakikisha kiti hicho lazima kiende kwa mtoto wa Himidu kwa gharama zote au kwa maana nyingine, kiti hicho kiende kwa chama tawala. Hapa kuna mkono wa chama tawala na serikali, Husna. Kuwa makini na maamuzi yako, vinginevyo unaweza ukajikuta kwenye balaa kama lililomkuta Beda. Unajua kama bado wanaamini kuwa, Beda ndiye aliyemwua mheshimiwa Himidu? Wanadhani Beda amemwua Himidu kwa ajili ya wivu wa mapenzi. Kwa sasa hivi jiepushe na lolote linalomuhusu Himidu au Beda. Polisi watakuwa wanakufuatilia na hapo hapo wanajua kuwa, waandishi wa habari nao wapo kwenye kukufuatilia kama mafisi wanaovizia lolote kutoka kwako ili iwe habari kwao.”
“Unataka kuniambia hata kesho nisiusindikize mwili wa Beda kwenda nao Tanga?” Husna aliuliza kwa utulivu.
“Nakushauri usiende, huu siyo wakati wake!”
Husna akaihisi miguu yake ikipoteza nguvu za kukibeba kiwiliwili chake. Lilikuwa pigo jingine la mfulululizo kwake baada ya kumkosa Himidu kwa kuuawa kisha, akakosa kwenda kumzika kwa hofu ya kukushushuliwa msibani. Beda naye kauawa kisha, anaambiwa hata naye asiende kumzika!
Huu ni mwaka wangu wa mikosi! aliwaza na kuanza kulia.
*****
MIEZI MIWILI BAADAYE
Ilimchukua mtu huyu wiki nzima kumfuatilia mtu aliyekuwa akimfuatilia. Akaujua muda wa kurudi nyumbani wa mtu anayemfuatilia na hicho ndicho hasa alichokuwa akitaka kukijua. Alianza kumfuatilia mtu huyo kuanzia muda wa jioni wakati akitoka kazini kwa kulifungia mkia gari lake na kulifuata huku yeye akiwa ndani ya gari lake dogo kuukuu la kijapani aina ya Toyota Corrola.
Hakupata tabu ya kumfuatilia kutokana na foleni ndefu za magari yaliyo barabarani kwa muda huo wa jioni ambayo yalikuwa yakijivuta kwa mwendo wa taratibu na wenye kutia karaha. Foleni za aina hiyo zikawa ni kinga yake ya kutoweza kugunduliwa na mtu aliyekuwa akimfuata kutokana na wingi wa magari ambayo humfanya mtu yeyote asiwe makini na magari yaliyo nyuma yake.
Kwa nini hawa matajiri wanaokaa maeneo ya Mbezi beach, Tegeta na Bunju wasinunue boti ndogo za kisasa ambazo zitakuwa zinawapeleka mjini kila asubuhi na jioni kuwarudisha badala ya kuhangaika na foleni za kuudhi za asubuhi na jioni kila siku? Mtu aliyekuwa kwenye gari la Corrola alijiuliza wakati gari lake likiwa ni la tatu kutoka kwenye gari la aina ya Land Cruiser VX ambalo yumo mtu anayemfuatilia. Aliwashangaa matajiri wanaokaa maeneo hayo kuweza kumiliki mahekalu, biashara zenye kuwaingizia mamilioni ya pesa kwa njia za halali na za ufisadi na wengine kumiliki viwanda vikubwa, wakiwa wanapoteza muda mwingi barabarani kwa ajili ya foleni au kujikarahisha kwa kuamka mapema asubuhi ili kukwepa foleni hizo wakati wangeweza kununua boti na kutumia njia ya bahari kama usafiri wa kwenda ofisini. Gharama pekee za ziada ambazo wangegharamikia ni kutengeneza gati kwa ajili ya boti zao, kuwa na gari mbili, moja ya kuwapeleka mpaka kwenye boti na nyingine ya kuwachukua baada ya kuteremka kutoka kwenye boti.
Wakati akiwa anayawaza hayo, mtu huyo aliliona Land Cruiser likiacha barabara ya Bagomoyo na kuingia kwenye barabara inayoelekea kwenye uwanja wa egesho la magari yanayokwenda duka la Super market huku foleni aliyokuwepo ikijongea taratibu na kutoa nafasi kidogo kwa magari kuongeza kasi ya kufidia nafasi iliyoachwa na Land Cruiser.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mtu aliyekuwa kwenye Corrola aliiangalia saa iliyokuwemo ndani ya gari na ikamwonyesha kuwa ni saa 1: 08. Kiza kilikuwa kimekwishaingia huku baadhi ya magari yakiwa tayari yamewasha taa za barabarani na mengine yakiwa yamewasha taa ndogo za egesho. Foleni ikiwa imesimama, mtu huyo aliliangalia Land Cruiser lilivyokuwa likijiandaa kujiegesha vizuri kwenye egesho la magari lililopo kwenye Super market huku taa zake za nyuma za breki zikiwaka na kuzima kadri lilivyokuwa likijiweka vizuri. Mtu aliyekuwemo kwenye gari alikuwa na uhakika usimamaji kwenye Super market kilikuwa ndio kituo cha mwisho cha gari hilo la Land Cruiser kabla halijaelekea nyumbani. Uhakika wa kulijua hilo aliupata baada ya kulifuatilia gari hilo kwa wiki nzima na kuliona likisimama kwenye duka hilo kwa ununuzi wa bidhaa kiasi cha mara mbili na kisha baada ya hapo huelekea moja wa moja nyumbani.
Kwa kuwa siku hiyo ndio siku aliyodhamiria kuitimiza azma aliyoikusudia kuifanya, mtu huyo hakulisubiri Land Cruiser mpaka litoke dukani hapo kama alivyokuwa akifanya siku za nyuma, badala yake aliendelea kuwepo kwenye msafara wa foleni wa magari na kujongea nao taratibu huku akijaribu kuituliza akili yake kadri alivyoweza na kujipa uhakika kuwa, gari hilo la Land Cruiser halitaweza tena kumpita kabla ya kuwasili eneo ambalo alilipanga kulisimamisha gari lake.
Alipofika njia ya panda ya Africana, aliliingiza gari lake barabara inayoelekea Africana na kwenda nayo barabara hiyo kwa mwendo wa kama kilomita moja na nusu kisha, alikata kona upande wa kushoto na kuiacha barabara ya lami na kuingia barabara isiyo na lami. Sehemu kubwa ya eneo hilo halikuwa na mwanga wa kutosha, mwanga wake ulipatikana kutoka kwenye nyumba za jirani ambazo nazo hazikuwa na mwanga mkali. Kwa ujumla eneo hilo lilikuwa limetawaliwa na kiza chepesi ambalo si rahisi kumgundua mtu aliyekusudia kujificha. Eneo lote lilitawaliwa na nyumba za kifahari zenye kushindana kwa uzuri na ubora huku barabara zake zisizo na lami zikiwa zimejaa nyasi na majani kando kando yake.
Mbele ya alikokuwa akielekea kulikuwa na baa moja ndogo yenye utulivu ambayo ilitumika kama sehemu ya kuonana kwa wakazi wa eneo hilo waliopenda kutoka bila ya kwenda mbali na majumbani kwao kwa ajili ya kuunganika kupata kinywaji na watu wengine. Uwanja wa egesho la magari wa baa hiyo ulikuwa finyu na ikawa ni kawaida baadhi ya magari mengine kuegeshwa kandoni mwa barabara na wateja waliofika hapo. Gari la Corrola lilifika eneo hilo na kwenda kuegeshwa eneo la mbele la kando ya barabara na kujumuika na yaliyokuwepo hapo.
Mtu aliyekuwa akiiendesha Corrola hiyo aliteremka taratibu na kuufunga mlango. Baada ya kuufunga mlango akawa wima aliyenyooka. Hakuwa mrefu wala mfupi, haikuwa rahisi kuuona uso vizuri kutokana na kiza kilichokuwepo pamoja na kwamba hakikuwa cha nguvu. Maungoni mwake alikuwa amevaa shati la cadet lenye rangi ya ugoro na ndani yake akiwa amevaa fulana nyeusi. Suruali yake ilikuwa ya jeans nyeusi na viatu vyake alivyovaa vilikuwa aina ya boot vya rangi nyeusi. Eneo hilo aliloliegesha gari lake halikuwa mbali na nyumba anayoishi mtu aliyekuwa akimfuatilia kwenye gari la Land Cruiser na alikuwa akijua baada ya muda mfupi gari hilo litapita kumpeleka mtu wake nyumbani.
Mlango wake wa gari hakuufunga kwa ufunguo kwa sababu alijua atarudi baada ya muda mfupi. Alivyokuwa akielekea kwenye baa hiyo ambayo eneo lake la baa lilizungushiwa uzio wa miti ya mianzi na kuonyesha dhahiri kuwa haikuwa ni baa ya kudumu, mtu huyo aliyaangaza macho yake kumtafuta mlinzi wa kimasai ambaye kwa kipindi cha wiki moja alichokuwa akimpeleleza mtu wake, aliweza kumshuhudia mlinzi huyo kila alivyokuwa akipita na kuzitumia mara mbili za kusimama kwenye baa hiyo kupata kinywaji cha haraka haraka na kuangalia mazingira yaliyopo hapo pamoja na kuutathimini uwezo wa kiulinzi wa mmasai huyo. Alichokigundua kutoka kwa mmasai ni kuwa, alikuwa na tabia ya kulifuata gari la mteja wakati mteja akitaka kuondoka. Pamoja na kwamba alitaka dhamira yake ionekane kwa wateja wake kuwa, alikuwa akionyesha anamshuhudia mwenye kuondoka na gari ndiye mwenye gari, lakini pia lengo kubwa la mmasai huyo lilikuwa ni kufuata bakshishi kwa wamiliki wa magari hayo baada ya kuwalindia.
Alimwona mmasai huyo akiwa amesimama ng’ambo ya pili ya barabara uso wake akiwa ameuelekeza lilipo gari lake na walipotazamana, mmasai akaupunga mkono wake kumwonyesha kuwa yupo na ameliona gari lake. Naye akampungia mkono na kuzuga kama anayeelekea kwenye baa, akamwona mmasai akiondoka sehemu aliyokuwepo na kutokomea yalipo magari mengine na mgongo wake kuuelekeza kwake. Mtu huyo akaitumia nafasi hiyo kurudi haraka kwenye gari lake bila ya kuonekana na mmasai huku akilivua shati alilokuwa amelivaa. Aliufungua mlango wa gari na kulitupa shati juu ya kiti cha dereva kisha, akafungua dawati la gari na kutoa bastola na kuiswinda sehemu ya nyuma ya suruali yake na kuifunika na fulana aliyokuwa haikuichomekea. Akainama tena na kukirudisha kiwiliwili chake cha juu ndani gari na mkono wake kurudi tena kwenye dawati ambako safari hii alichukua kiwambo cha kuzuia mlio wa bastola na kukitia mfukoni, akaurudisha mlango na kujiondoa kwenye gari. Badala ya kurudi kwenye mwelekeo wa mwanzo wa kuelekea kwenye baa, mtu huyo akaubadilisha mwelekeo kwa kuelekea mbele na kuifuata barabara. Akaangalia nyuma kiasi cha mara tatu kuhakikisha kama kungekuwa na mtu aliyekuwa akimwangalia, licha ya kutokuwepo kwa mtu wa aina hiyo, lakini hata yule mmasai naye alikuwa haonekani.
Sehemu aliyoikusudia kwenda haikuwa mbali na baa aliyokuwa ametoka, ilikuwa ni kwenye nyumba iliyokuwa jirani ambayo ilikaa katikati ya nyumba nyingine na iliyokuwa na kiwanja kikubwa kama zilivyo nyumba zote zilizokuwepo hapo. Nyumba aliyokuwa akiiendea ilizungukwa na ukuta mkubwa uliopakwa rangi ya chungwa, juu ya ukuta huo kulizungushwa nyaya za umeme za kuzuia wezi na kuwepo tangazo la kuhadharisha uwepo wa nyaya hizo. Geti kubwa la kifahari la kuingilia kwenye nyumba hiyo lilitazama upande iliko barabara na kabla ya kuifikia njia inayoingia kwenye geti kulikuwa na kidaraja kilichojengwa juu ya mfereji mdogo uliokuwa umekatiza barabarani.
Akiwa na mavazi meusi yaliopo mwilini mwake ambayo ni fulana na jeans, mtu huyo aliendelea kuambaa kando kando ya barabara kwa mwendo wa nusu anakimbia na nusu anatembea huku akiwa ameinama. Mavazi aliyokuwanayo yalimfanya aonekane kama kivuli kilichokuwa kinasogea chenyewe na kupotea kando ya kidaraja kilichopo jirani na nyumba hiyo. Alipofika kwenye kidaraja hicho alijiachia na kujikita kama aliyeanguka na kukaa na mgongo wake kuegemeza kwenye ukuta wa kidaraja, akatulia kwa sekunde kadhaa na kusikiliza kama kungekuwepo na aina yeyote ya sauti ambayo ingemtia mashaka. Baada ya kuona hali ni shwari, aliitoa bastola aliyokuwa ameiswinda kwenye suruali na kuikamata kwa mkono mmoja.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
**Ni nani mtu huyu??
kisha, akakitoa kiwambo cha kuzuia mlio wa bastola na kukifunga kwenye mdomo wa bastola. Akasubiri!
Mbu walioanza kujikusanya kutokana ujio wake wakaanza kumpa karaha kiasi kwamba subira yake akaiona ni ndefu kadri alivyokuwa akilisubiri gari la Land Cruiser liweze kuwasili. Magari ya hapa na pale yaliyokuwa yakipita juu ya kidaraja hicho kuwarudisha majumbani wamiliki wa nyumba zilizopo eneo hilo nayo yakawa ni eneo jingine lililompa usumbufu kwa kudhani kuwa, huenda moja ya magari hayo likawa ni lile alilokuwa akilisubiri. Hali hiyo ya kumuweka katika dhana hiyo ikawa inamuweka kwenye maandalizi ya kujiweka sawa kwa kufanya shambulizi, lakini anapotanabahi kuwa silo gari analolisubiri hujikuta akijirudisha kwenye mkao wa awali wa kusubiri upya na kuirudia adha ya kutafunwa na mbu!
Ilianza kama magari mengine yalivyokuwa yakipita juu ya kidaraja hicho kwa mtu huyo kujiweka sawa kwa kufanya shambulizi wakati alipokuwa akiziangalia taa za gari iliyokuwa ikija. Akiwa ameanza kufikiria kuwa, huenda hata gari hilo linaweza likawa silo analolisubiri, ndipo akaona taa ya indiketa ikionyesha mwelekeo wa kuingia kwenye geti na mwendo wa gari ukapungua na kuwa mdogo sana. Ndilo lenyewe! aliwaza. Akajiweka vizuri zaidi, akaliona likipita juu ya kidaraja alichokuwepo na macho yake kuangalia upande wa kiti cha mbele cha abiria, akamwona mtu aliyekuwa amekaa upande huo huku kioo cha mlango kikiwa kimefungwa kuonyesha kuwa, kiyoyozi kinatumika. Alikuwa na uhakika asingekuwa mtu mwingine zaidi ya yule aliyekuwa akimfuatilia kwa wiki nzima. Ubavu wa kushoto wa mtu aliyemo ndani ya gari ulikuwa umeelekea kwake kwa kuonekana kuanzia sehemu ya kifua mpaka kichwani. Hakuhitaji sehemu nyingine ya mtu huyo zaidi ya kichwani, huko ndiko alikopanga aielekeze shabaha yake ambayo ingempa uhakika kama italenga sawia kuwa, ingemmaliza mtu wake kwa haraka!
Alivyokuwa akianza kuikaza misuli yake ya kidole kwa kukivuta kiwambo cha kufyetua risasi, akamwona mtu aliyemo ndani ya gari akigeuka na kuangalia nje upande aliko yeye. Mtu aliyekuwa kwenye kidaraja hakusubiri, akafyetua risasi iliyotoa mlio wa kikohozi na risasi hiyo ikaenda moja kwa moja na kuingia katikati ya paji la uso wa mtu aliyekuwemo kwenye gari!
Mwuaji akatoka kwa kasi kutoka kwenye kile kidaraja na kukimbia kama kivuli kurudi alikoiegesha gari yake. Alipoifikia gari yake akamwona mmasai yupo ng’ambo ya pili ya barabara akizungumza na mmiliki wa gari aliyekuwa anataka kuondoka. Akaingia kwenye gari yake na kuirudisha bastola kwenye dawati la gari kisha, kwa haraka haraka akalivaa shati lake na kutulia ndani ya gari bila kuliwasha. Akasubiri mpaka gari alilokuwepo mmasai lilivyoanza kuondoka, naye akaliwasha lake na kuligeuza. Akamwona mmasai akimjia kwa mbele.
“Narudi!” alisema kupitia dirishani bila ya kulisimamisha gari na baada ya kumpita mmasai akaziwasha taa za gari na kuwa nyuma ya gari lililomtangulia, wote wakielekea kwenye barabara kuu ya Africana. Walipoifikia barabara hiyo, gari lililomtangulia lilikata kona upande wa kushoto kuelekea Africana na yeye alikata kona upande wa kulia kuifuata barabara ya Bagamoyo!
* * *
IGP Inno aliitundika taulo kwenye ufito wa chuma uliokuwa karibu na beseni la kupigia mswaki baada ya kujifuta mwilini kukausha maji aliyotoka kuoga na kujiangalia kidogo usoni kutoka kwenye kioo kidogo cha ukutani kilichokuwa juu ya beseni hilo. Alilichukua joho la nyumbani alilokuwa amelitundika mlangoni kabla ya kuoga na kulivaa kisha, akaufunga mkanda wa joho hilo kiunoni mwake. Aliufungua mlango wa maliwatoni na kutoka huku mvuke wa maji ya moto aliyooga nao ukitokeza kutoka humo na kuingia kwenye chumba cha kulala kabla ya kuufunga mlango huo.
Hakuwa na chochote cha kukifanya chumbani humo zaidi ya kujiandaa kwenda kwenye chumba cha mlo ambako mkewe alikuwa akimsubiri kwa ajili ya kupata chakula cha usiku. Usiku huo alikuwa akijisikia njaa na hali hiyo ilimfurahisha kwa sababu alijijua atakula vizuri hasa akizingatia kuwa, chakula kilichoandaliwa kikiwa ni wali uliopikwa kwa kuchanganywa na njegere na kufuatiwa na nyama ya kuku iliyopikwa kwa kutengenezewa mchuzi hafifu uliojaa karoti na pilipili mboga zilizokuwa hazikuivishwa sana. Moja ya sifa mojawapo aliyokuwa akimpendea mkewe ni kujua kupika. Simu yake ya mkononi ikaita, ilikuwa simu ileile yenye majina ya watu maalumu. Hakushangaa ilipokuwa ikiita, kwa muda huo ilikuwa ni jambo la kawaida kuwasiliana na baadhi ya watu hao maalumu kwa jambo moja au jingine. Aliichukua kutoka kitandani alipokuwa ameiacha wakati alipokwenda kuoga, akaliangalia jina la mpigaji. Lilikuwa jina la Mkuu wa kituo cha polisi cha Oysterbay.
“Yes, Madaraka…” Inno alisema huku akielekea mlangoni kwa madhumuni ya kutoka humo chumbani.
“Mkuu,” Madaraka aliita kwa utulivu. “Kuna habari nyingine mbaya,” akasita kwa kutarajia Inno angeuliza ubaya wa habari hiyo. Alipoona Inno naye amekaa kimya akaendelea, “Mheshimiwa Ali Othman ameuawa usiku huu kwa kupigwa risasi, maiti yake ipo hospitali ya Lugalo!”
Inno alihisi kitu kikimkaba kooni, akashindwa kujibu lolote na kujikuta akiganda mlangoni huku mkono wake mmoja ukiwa umekishika kitasa.
“Mkuu,” Madaraka aliita ili kuhakikisha kama mkuu wake bado yuko kwenye simu.
“Nimekusikia, Madaraka. Ameuawa wapi?” Hatimaye Inno alisema.
“Ameuawa nje ya geti la nyumbani kwake akiwa ndani ya gari lake akirudi. Mwuaji bado hajajulikana na nimepeleka makachero eneo la nyumbani kwake kwa uchunguzi zaidi.”
“Unaongea kutoka wapi?”
“Nipo hospitali ya Lugalo.”
“Nakuja,” Inno alisema na kukata simu. Mara tu alipoikata, akaanza kuwapigia simu baadhi ya viongozi aliowaona ni muhimu kupewa habari hizo mapema.
Hakutoka nje kama alivyokuwa amekusudia awali, badala yake alilivua joho lililokuwa mwilini mwake na kuvaa nguo za kiraia kwa ajili ya kutoka. Akiwa tayari kutaka kutoka, mkewe akaingia chumbani humo, akamshangaa kumwona Inno akiwa na mavazi yaliyoashiria kuwa anatoka.
“Vipi?” mkewe aliuliza huku uso wake ukiwa umetawaliwa na mshangao.
“Ali Othman ameuawa!” Inno alijibu kwa mkato.
“Waziri wa Mambo ya Ndani?”
“Ndiyo. Ndio nimepewa taarifa sasa hivi, ameuawa kwa kupigwa risasi akiwa anataka kuingia nyumbani kwake.”
“Jesus! Nani aliyemwua?”
‘Hakuna aliyekwishakamatwa. Maiti yake iko Lugalo, ndiko ninakokwenda.”
“Chakula utakula…”
“Endelea kula, mimi nitakula nikirudi.”
Inno akatoka, njaa aliyokuwa akiisikia awali ikawa imetoweka.
* * *
Ni risasi iliyotolewa kutoka kwenye mwili wa Mheshimiwa Ali Othman ndio iliyowaweka viongozi wa jeshi la polisi na serikali kwenye mshangao. Ilikuwa ni aina ya risasi aliyouliwa nayo Mheshimiwa Himidu!
“Inatupa tafsiri ipi?” mmoja wa wanakamati wa kikao cha kamati ya Ulinzi na Usalama kilichoitishwa ghafla baada ya kugundulika risasi hiyo, aliuliza.
“Inawezekana ikawa ni mwanzo wa kuuliwa kwa viongozi,” Mwenyekiti wa kamati alijibu.
“Kwa nini wauawe?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hilo ndilo lililotufanya tukiitishe kikao hiki,” Mwenyekiti alijibu tena na kumwangalia IGP Inno. “Pengine IGP anaweza akawa na mwanga wa jambo hili.”
IGP Inno alizipekua na kuziweka sawa nyaraka zilizokuwa mezani kama kwamba maelezo aliyokuwa akitaka kuyatoa angebidi kuyanukuu kutoka kwenye nyaraka hizo. Macho ya watu wote waliokuwemo humo yakawa yanamwangalia yeye na yeye akahisi hali hiyo ya kutazamwa kwake.
“Mwenyekiti,” Inno alisema bila ya kuziangalia nyaraka zilizo mbele yake. “Mshituko ulioko kwenu, ndiyo uliotupata sisi pale tulipogundua ni aina moja ya risasi iliyotumika kumwua Mheshimiwa Himidu na Mheshimiwa Ali Othman, na kuonyesha kuwa, bastola iliyotumika ni aina ya Uzi iliyotengenezwa nchini Israel. Ugunduzi wa tukio hili pia, umeifanya ripoti ya awali ya uchunguzi wa kifo cha Mheshimiwa Himidu ionekane haikulenga kwenye shabaha ya kumpata mwuaji halisi wa mauaji yake na hata sababu iliyoonekana kutumika kumwua Mheshimiwa Himidu nayo imedhihirisha kuwa haikuwa ya kweli. Ninachoweza kukizungumza hapa ni kuwa, hata sisi jeshi la polisi tumeanza kujipanga upya kwa kufanya uchunguzi wa kina kujua kama anayefanya mauaji haya ni mtu mmoja au kuna kundi linalofanya mauaji haya kwa viongozi na kwa nini mauaji yaelekezwe kwao.”
“Ripoti ya uchunguzi wa mauaji ya Himidu ilieleza nini?” mjumbe mmoja aliuliza.
“Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mheshimiwa Himidu aliuawa kwa sababu za kimapenzi.” Inno alijibu.
“Fafanua ndugu mjumbe, mapenzi hayo yalihusu nini?” mjumbe alimbana Inno.
Inno akaonyesha kusita na kumwangalia mwenyekiti. “Ripoti iliyokuwemo mle tuliishaipeleka kwa Waziri husika na sidhani kama nitaifanyia haki kuizungumza hapa bila ya kupata kibali cha Waziri aliyekabidhiwa,” alisema.
Mwenyekiti wa kamati aliinamia meza na kujikuna utosini baada ya IGP kumaliza kauli yake. Akauinua uso wake na kumwangalia Inno. “Ndugu mjumbe naona hapa amejikanganya kidogo,” alisema. ‘Kamati hii ina haki ya kufahamishwa lolote linalohusu usalama wa nchi, viongozi na raia zake. Si ajabu hata Mheshimiwa mjumbe unalijua hili, sasa sijui ni kwa nini unakwepesha kwepesha. Kamati inaomba ufafanuzi wa ripoti hiyo!”
IGP Inno akajiona amekwama. “Mheshimiwa Himidu aliuawa wakati akitoka kwa hawara wake,” alisema. “Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa, kulikuwa na mtu mwingine wa pili aliyekuwa akitembea kimapenzi na hawara huyo huyo. Kwa kuwa mtu huyo alikuwa yupo karibu kwenye kuijua mienendo ya Mheshimiwa Himidu inayohusiana na maudhurio yake kwa mpenzi wake huyo, tukamwekea dhana kuhusika na kifo cha Himidu, tukamkamata. Baada ya kukamatwa akakiri kuhusika na kifo cha Mheshimiwa Himidu.”
“Alikiri?” Mwenyekiti aliuliza kwa mshangao.
“Ndiyo alikiri,” Inno alijibu, baada ya kujibu akazikusanya tena nyaraka zake na kuziweka sawa kwa kuzigonga gonga juu ya meza.
“Sidhani kama niliisikia kesi yake ikizungumzwa mahakamani,” Mwenyekiti alisema huku akionyesha mshangao na kuwatazama wajumbe wengine kama kwamba angetokea mmoja na kumpa jibu kabla hajajibiwa na IGP Inno.
“Haikuwahi kuzungumzwa,” Inno alisema.
“Kwa nini?”
“Mshukiwa alifariki kabla ya kesi kuzungumzwa.”
“Alifariki akiwa mahabusu?” Mwenyekiti aliuliza huku akionyesha kupewa jibu analolitarajia.
“Ndiyo. Alifariki kutokana na ugonjwa wa kipindupindu.”
Mwenyekiti akaonekana kukumbuka kitu na hapo hapo akasema, “Hii si ndiyo ile kesi iliyopigiwa kelele na vyombo vya habari kuwa, mtuhumiwa alikufa kutokana na kipigo?”
“Ni hiyo hiyo mwenyekiti, lakini nani asiyewajua waandishi wa habari. Huandika lolote wanaloliwaza kwenye vichwa vyao badala ya kuandika ukweli. Vyombo vya habari vya hapa nchini kazi yao ni kupata umbeya wa mitaani na kwao kuzifanya ni habari na hasa habari hizo zikiwa zinailenga serikali!”
“Sasa ilikuwaje mtuhumiwa awe amekiri mwenyewe kuhusika na mauaji kisha, baadaye mseme alikuwa hahusiki?”
IGP Inno hakujibu.
“Kwa hiyo waandishi wa habari waliandika kweli?”
Kwa mara nyingine Inno akawa hakujibu.
“Ok, tuachane na hilo.” Mwenyekiti alisema na kuonekana kutoungana na hoja ya IGP kuwa vyombo vya habari vinapenda kuvituhumu vyombo vya serikali kwa sababu zisizo na ukweli. “Kwa hiyo sasa hivi ndio mmejipanga upya kupeleleza vifo hivi?”
“Ndiyo Mwenyekiti,” Inno alisema na kuonyesha dhahiri amepata afueni. “Tuna uhakika, kama yupo mwuaji wa mauaji haya au kama ni genge linalojihusisha na mauaji haya, tutawatia mbaroni!”
* * *
* * *
Kila kanda ya mkoa maalumu Kinondoni, Temeke na Ilala zilikusanya makachero na doria zilizohusisha polisi wa miguu na magari, wote kwa pamoja walitawanywa maeneo tofauti ya jiji huku makachero maalumu wanaofahamika kupambana na majambazi nao walijikuta wakifanya safari ya kuonana na majambazi wanaowajua ambao hushirikiana nao katika upashanaji wa habari ulio kwenye mtandao wao usio rasmi ili kupata taarifa kutoka kwao kama kutakuwa na kikundi kilichoingia kutoka nchi jirani watakuwa wanajihusisha na mauaji ya viongozi wa serikali; au endapo hata kama wana uelewa wowote wa kuwa na fununu na watu watakaokuwa wanaendesha vitendo hivyo vya mauaji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Uelewa wa majambazi waliofuatwa uliweka wazi kuwa, walikuwa hawajui ni nani waliohusika au kuhusika na mauaji ya viongozi hao wawili, lakini kutokana na makachero kuhofia kuwa, wangeonekana wanashindwa kuifanya kazi yao kwa kuchelewa kuwabaini kwa haraka mwuaji au wauaji ambao wameiwezesha nchi kuwa kwenye mzizimo wa kutaka wahusika na mauaji wakamatwe, ikawalazimu kuwalazimisha majambazi hao angalau wawatajie hata wale ambao wangekuwa na mashaka nao tu ili waende kuwakamata na kuonekana wapo kwenye kuitenda kazi yao vizuri. Majambazi yakaanza kutaja majina ya hata wale waliokuwa na visa nao binafsi hata kama ni vya kunyang’anyana wanawake…
Hali hiyo ikaleta kizaaza cha ukamataji wa watuhumiwa kwa mtindo wa kimya kimya na kuwekwa mahabusu kwa mahojiano, safari hii wakuu wa vituo wakawa makini vituo vyao havitumiki kuwatesa watuhumiwa kwa kuhofia kuingia kwenye mzozo na vyombo vya habari. Hata hivyo, waandishi wa habari nao wakapata fununu za kuwa, kuna watuhumiwa waliokamatwa kwa kuhusika na mauaji ya mawaziri hao wawili. Wakuu wa vituo vya polisi walipofuatwa na waandishi wa habari kuhojiwa kuhusu ukweli wa matukio hayo, haraka haraka wakazikanusha taarifa hizo, lakini waandishi hao hao walipowaendea makamanda wa kanda maalumu kuwahoji, wao wakajibu kuwa, “Kunapotokea hali kama hiyo ya mauaji hasa ya viongozi, matukio ya ukamataji kwa watuhumiwa ni ya kawaida kwa ajili ya kufanya mahojiano, na wale watakaonekana hawahusiki ni dhahiri wataachiwa,” mmoja alinukuliwa akisema hivyo.
Baadhi ya waliokamatwa walianza kuachiwa kutokana na kutumika nguvu za vigogo kuwatetea, wengine waliachiwa kwa kutoa kitu kidogo pamoja na kwamba hawakuonekana kuhusika na mauaji hayo. Wengine ambao wao walishindwa kutoa kitu kidogo pamoja na kwamba walionekana kutohusika na tuhuma za mauaji, hawa waliunganishiwa kesi za kubambikiwa bila ya maofisa wa ngazi za juu wa polisi kujua ingawa awali walikuwa msitari wa mbele kutangaza kukamatwa kwao kwenye vyombo vya habari na kuahidi haki kutendeka katika mchujo wao. Tukio hilo likaonyesha dhahiri jinsi maofisa wa juu wanavyopenda kuzisikia sauti zao zikisikika kwenye vyombo vya habari kuelezea watuhumiwa wanavyokamatwa na kuahidi kuwatendea haki, lakini mara habari zao zikishatangazwa huwa hakuna hata mmoja anayefuatilia mwisho wa mahabusu hao utakavyokuwa!
****
Kachero justin Rajabu, kachero mwenye wadhifa wa ngazi ya juu ambaye alikabidhiwa ofisi na meza kwenye jengo la Makao Makuu ya Polisi lililopo katikati ya jiji na kujishughulisha na kazi za utawala badala ya zile za mikiki mikiki za kuhangaika mitaani kupambana na kesi za jinai, alikuwa ni mmoja wa makachero aliyekuwa akiifanya kazi yake mitaani kwa uwezo mzuri kabla ya kupelekwa masomoni kujifunza taaluma ya uongozi wa kikachero. Ilimchukua miaka mitatu kuhitimu mafunzo yake akiwa Israel na aliporudi nchini akapelekwa moja kwa moja Makao Makuu ambako alifanya kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kurudishwa tena nchini Israel kwa mafunzo zaidi ya miaka miwili.
Alipomaliza mafunzo yake ya miaka miwili na kurudi nchini, akapangiwa kazi mkoani Dodoma na kufanya kazi katika ofisi ya Mkuu wa upelelezi wa mkoa huo kwa kipindi cha miaka miwili. Baadaye alipandishwa cheo na kurudishwa jijini Dar es Salaam ambako alirudishwa tena Makao Makuu. Sakata la kuuawa kwa mawaziri wawili ndani ya miezi miwili na kutumika aina moja ya risasi ni tukio lililomchanganya IGP Inno na kujikuta akimfikira Justin Rajabu!
Ilikuwa ni asubuhi wakati Justin Rajabu akiwa ofisini, akaletewa mwito wa kuitwa ofisini kwa IGP. Hakushangaa kuitwa ofisini kwa IGP, lilikuwa ni jambo la kawaida hasa akizingatia kuwa, wote walikuwa kwenye jengo moja ingawa ghorofa tofauti. Justin aliripoti mara moja na kumkuta IGP Inno akimsubiri.
“Nataka kukutoa kwenye kiti chako kwa muda Bwana Justin,” Inno alisema huku akimwangalia Justin aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha wageni kilichopo mbele ya meza.
Justin hakuonekana kumwelewa kwa haraka mkuu wake na Inno akalitambua hilo kabla ya Justin mwenyewe kujieleza.
“Sijakuelewa mkuu,” Justin alisema na kufanya tabasamu dogo.
“Nataka nikupe kazi ya kuingia mitaani kwa muda,” baada ya kusema hivyo, Inno akamkumbusha Justin kuhusu mauaji ya kuuawa kwa mawaziri wawili ndani ya miezi miwili na kugundulika kwa risasi zilizotumika kuwa, zilikuwa za aina moja. “Kuna uwezekano mkubwa kwa bastola iliyotumika kumwua Himidu, ndiyo hiyo hiyo iliyotumika kumwua Ali Othman. Isitoshe, bastola iliyotumika ni aina ya Uzi iliyotengenezwa nchini Israel, katika ufuatiliaji wa kitengo cha kutoa kibali kwa watu wanaomiliki bastola hapa nchini, imegundulika hakuna hata mmiliki mmoja mwenye kumiliki bastola ya aina hiyo. Kwa hiyo, hapa kuna mwuaji mmoja aliyefanya mauaji haya akiwa peke yake au kikundi kinachomtumia na huenda mwuaji akatoka nchi jirani kutokana na silaha aliyoitumia, anaweza akatoka nchini Kenya au Uganda ambako ndiko kwenye uwezekano wa kupata bastola za aina hii au hata Burundi. Nataka ukamtafute mwuaji huyu au kikundi hicho!” Inno alimaliza.
“Kuna fununu yoyote uliyoipata inayoeleza sababu za mauaji haya?” Justin aliuliza na kumwangalia Inno usoni.
“Bado. Makachero wanaendelea kufanya uchunguzi wao, huenda wakaambulia mawili matatu. Tunasubiri uchunguzi ukamilike.”
“Kuingia kwangu mimi katika kupeleleza huko, hakutaleta mgongano wa kiupelelezi wakati tayari kuna wapelelezi wengine?”
“Utatumika kama mpelelezi wa kujitegemea.”
“Kuna sababu yoyote ya kuufanya uamuzi huu?”
“Ipo,” IGP alisema na kusita kuendelea. Akaonekana kuvuta fikra kwa sekunde kadhaa. Baadaye akasema, “Mwuaji au wauaji kwa mauaji waliyoyafanya ni dhahiri watakuwa wanazifuatilia nyendo za kashkashi za makachero wetu ambao wengi huwa wanajulikana, kujulikana kwao kutawafanya wauaji au mwuaji kuweza kuwatoroka kwa urahisi makachero wetu na inaweza ikaleta ugumu wa kukamatwa kwao au wakakamatwa watuhumiwa ambao siyo, makosa haya yamekwisha kufanyika sana na kutuletea shida kama jeshi. Kuingia kwako kuwatafuta waliohusika na mauaji ukitokea Makao Makuu kutakupa nafasi ya kutojulikana, kutakupa nafasi ya kuwa makini zaidi kwa sababu uko peke yako na kuweza kuidhibiti mienendo yako na itakuwa rahisi kwako kulifanyia uamuzi tukio lolote litakalokutia mashaka hata kutoka kwa mtu mmoja mmoja. Mwenendo wako wa kupeleleza mauaji haya utakuwa ni wa siri na hautamuhusisha mtu mwingine yeyote zaidi ya wewe na mimi.”
Ikawa ni nafasi ya Justin naye kufikiri, akawa anakisugua kidole chake cha shahada chini ya kidevu chake bila ya kusema lolote huku akiangaliwa na Inno. Hatimaye aliuinua uso wake na kumwangalia IGP Inno kwa macho yaliyotulia. “Unatarajia kutokea kwa mauaji mengine?” aliuliza.
“Kwa kuwa bado sijajua kiini cha sababu cha kuuawa kwa waheshimiwa hawa, siwezi nikalijibu swali lako.”
Justin akajikita tena kwenye kufikiri na kuachiwa afanye tafakuri yake bila ya Inno kumwingilia kwa kumsemesha. Kama alivyofanya awali, hatimaye Justin alikiinua kichwa chake na kumwangalia Inno. “Nimekubali mkuu,” alisema.
“Nadhani utanisaidia,” Inno alisema bila ya kuonyesha uchangamfu wowote usoni mwake.
“Tuangalie itakavyokuwa.”
“Nitaandika agizo kwa mhasibu ili akupe fungu la pesa litakalo kusaidia kuwepo kwako mitaani na nitatoa maelekezo ili kila wiki upate lita arobaini za petroli kutia kwenye gari lako. Kuna msaada mwingine unaouhitaji kutoka kwangu?”
‘Kwa kuwa bado sijaingia mitaani, siwezi nikakujibu hilo. Bado sijajua ugumu utakaokuwepo, kama nikihitaji nitakujulisha.”
“Vyema, Justin,” Inno alisema. “Rudi ofisini kwako wakati nikiwasiliana na mhasibu, fungu la pesa likiwa tayari nitakuita tena ofisini.”
Justin akatoka kimya kimya.
* * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku tatu zilipita bila ya kujua aanzie na wapi, na takriban wiki moja na nusu ilishapita tokea Mheshimiwa Ali Othman auawe. Akiwa amekaa kwenye kochi varandani kwake, Justin ambaye alikuwa akitarajia afunge ndoa na mchumba wake wiki mbili zijazo, kwa mara ya kwanza alijikuta akikosa uhakika endapo ndoa yake ingefanyika kwa tarehe iliyokwishapangwa kutokana na jukumu jipya la kazi alilopewa na mkuu wake. Hakuwa na uhakia kama hilo lingemsababishia akose umakini wa kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi. Pamoja na kuingiwa na mashaka ya kutofanyika kwa ndoa yake kwa tarehe iliyopangwa endapo jukumu la kikazi alilopewa linaweza kuingilia hafla hiyo, Justin alijikuta akijionya kutofanya pupa ya kumwarifu mwenyekiti wa kikao cha harusi kuhusu wasiwasi wake huo. Aliliona hilo lingebaki kuwa ni tatizo ambalo angelipeleka kwa IGP na kumwachia alifanyie maamuzi na baada ya hapo ndio angejua kama kutakuwa na ulazima wa kukutana na mwenyekiti wa kikao na kumjulisha kuahirishwa kwa ndoa.
Akilitafakari jukumu alilopewa la kumtafuta mwuaji, Justin alijiuliza kama makachero wenzake waliopewa jukumu kama hilo wangekuwa wamekwishapata mwanga angalau wa kujua kiini cha sababu ya mauaji hayo ya mawaziri wawili. Alijizuia kujipa nafasi ya kuanza kuvifikiria vifo hivyo kwa kuvihusisha na siasa kwa kuviwekea dhana kuwa, huenda mauaji hayo yakawa yamesukwa na vigogo wa chama tawala kwa ajili ya kata mti panda mti, kumwondoa wasiyemtaka na kumuweka wanayemtaka. Sasa mauaji hayo yatakuwa ni ya nini kama haitokuwa siasa? alijiuliza.
Akaanza kumfikiria mwuaji kama alikuwa ametumwa na watu ambao wako karibu na mawaziri hao, na kama ingekuwa ni hivyo basi kwa vyovyote walikuwa ni watu wanaojuana na walikuwa wakijua sababu ya kuuawa kwao. Kutakuwa na mwingine aliyebaki kwenye orodha ya kuuawa ambaye naye atakuwa anaijua siri hiyo ya kuuawa kwa wenzake? alijiuliza. Naye atakuwa ni mwanasiasa? Naye pia anatarajia kuuawa kama wenzake? Atakuwa ni Waziri kama walivyokuwa wenzake? Tishio la kuuawa kwake linaweza likampeleka polisi na kutoa taarifa ya kutishiwa maisha yake? Kabla ya kuuawa kwa waliouawa, nao walikuwa wakijua kama wangeuawa? Kama walikuwa wakijua, kwa nini wasiripoti polisi? Kuna sababu iliyowazuia kufanya hivyo? Kama ilikuwepo, kwa hiyo hata kama yupo mwingine anayejua sababu ya kuuawa wenzake na yeye akifahamu kuwa atauawa kama wenzake, naye atakuwa anashindwa kuripoti polisi kwa kuirithi sababu iliyowafanya wenzake washindwe kuripoti? Itakuwa ni sababu ipi inayowafanya wasiogope kuuawa lakini wakaogopa kuripoti polisi? Ndipo Justin akapata wazo kichwani mwake, wazo ambalo linahitaji msaada wa IGP kuweza kulifanikisha.
“Mkuu,” Justin alisema kwenye simu baada ya kumpigia IGP. “Nahitaji kuyasoma mafaili ya Himidu na Ali Othman.”
Kimya cha sekunde chache kikapita bila ya IGP kujibu lolote, lakini Justin akawa na uhakika kuwa, IGP alikuwa bado yuko kwenye simu. Naye akanyamaza!
“Niachie nifanye utaratibu,” hatimaye IGP alisema. “Yatakapokuwa tayari nitakutaarifu.”
“Nitashukuru mkuu,” Justin alisema na kukata simu.
Ilikuwa ni jioni wakati Justin alivyopigiwa simu na IGP kufahamishwa kuwa, mafaili hayo yapo tayari na aende kuyasoma Makao Makuu ya Polisi kwa sharti la kutotoka nayo nje ya jengo hilo.
Justin alikabidhiwa mafaili hayo na IGP mwenyewe, naye aliyachukua mpaka ofisini kwake na kuanza shughuli ya kuyasoma. Zoezi hilo lilimchukua mpaka usiku wa saa tano na kuyamaliza kuyasoma. Mara tu alipomaliza kuyasoma ndipo alipougundua uchovu uliokuwa mwilini mwake na macho kuyaona mazito. Alipiga mwayo na kuionyoosha mikono yake kama anayesulubiwa kisha akayachukua mafaili hayo na kuyafungia kwenye meza yake ili asubuhi inayofuata aweze kuyarudisha kwa IGP.
* * *
Asubuhi baada ya kuyakabidhi mafaili kwa Katibu Muhtasi wa IGP, Justin aliomba kuonana na IGP. Akaruhusiwa.
“Mkuu,” Justin alisema baada ya kuingia kwa IGP. “Naweza nikaipata ripoti ya upelelezi wa awali inayohusu kifo cha Himidu?”
“Nenda kituo cha Oysterbay ukamwone mpelelezi anayeitwa Nunda, yeye ndiye mwenye faili hilo. Nitawasiliana na Mkuu wa kituo kumjulisha ujio wako,” Inno alisema.
Baada ya kutoka Makao Makuu, Justin alikwenda moja kwa moja mpaka kituo cha polisi cha Oysterbay na kumkuta Nunda akiwa anamsubiri na faili hilo. Justin alitumia muda mwingine kuipitia ripoti hiyo baada ya kurudi nayo Makao Makuu. Baada ya kuipitia na kuimaliza, alijikuta akiifananisha ripoti hiyo kuwa sawa na bomu lililotegwa ambalo endapo litalipuka linaweza likawafukuzisha kazi baadhi ya maofisa wa polisi na wengine kwenda kutumikia kifungo jela baada ya kuyaona maelezo yaliyomwonyesha mtuhumiwa aliyekamatwa kwa kushukiwa kuhusika na mauaji ya Himidu, aliyeitwa kwa jina la Beda alikuwa amekiri kuhusika na kifo cha Himidu, baadaye mtuhumiwa huyo akawa amefariki kwa ugonjwa wa kipindupindu. Justin akakipongeza kitendo cha usiri wa jeshi la polisi kwa kutotangaza risasi iliyokuwa imemwua Ali Othman ni aina moja ya risasi na iliyomwua Himidu. Alijua endapo taarifa hizo zingefikia vyombo vya habari ni wazi wangezibebea bango na kulazimisha maofisa waliohusika na ukamataji wa mtuhumiwa huyo washitakiwe na lisingekuwa jambo la ajabu kwa taasisi za haki za binadamu kujikuta wakiiburuza kuipeleka kesi hiyo mahakamani.
Baada ya kulirudisha faili lenye ripoti hiyo kituoni Oysterbay na kumkabidhi Nunda, Justin alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Himidu na kumkuta mkewe. Huko alijitambulisha na kukaribishwa.
“Nitakupa usumbufu wa kuutumia muda wako ili unisaidie,” Justin alisema akiwa amekaa kwenye kochi dogo huku akimwangalia aliyekuwa mke wa Himidu ambaye alikuwa amekifunika kichwa chake kwa hijab. Alimkadiria miaka yake ambayo alihisi ni kati arobaini na nane mpaka hamsini. Pamoja na kuwa kwenye umri wa utu uzima, lakini uzuri wa sura yake na siha yake vilimwonyesha kuwa, alikuwa bado anadai. Isitoshe, mwonekano wake ulijidhihirisha kuwa wakati alipokuwa ni msichana wa umri wa miaka ishirini na kitu alikuwa ni moto wa kuotea mbali na kumfanya mtu kama mheshimiwa Himidu ashawishike kumwoa.
“Kwanza naomba samahani kwa kukufanya uyarudishe tena mawazo yako katika kipindi kigumu cha msiba wa marehemu mume wako,” Justin alisema na kuonyesha sura inayodhamiria kuiona huzuni hiyo.
“Usijali,” alisema mwanamke huyo.
“Kifo cha mzee bado kinaleta utata kutokana na alivyouawa na ndiyo maana nimelazimika kuja pamoja na kwamba kulishafanyika uchunguzi na kamata kamata ya awali kwa watu waliokuwa wametuhumiwa, lakini hilo halifanyi tusiendelee kutaka kupata habari zaidi ambazo zitatusaidia na hatimaye kumpata mwuaji halali wa mzee. Kwa hiyo kuja kwangu hapa ni kutaka kupata mawazo yako binafsi kuhusiana na kifo cha mzee.” Justin alinyamaza na kuiacha kauli yake iingie kwa mwenyeji wake.
“Karibu.”
“Ahsante,” Justin alisema na kuinama huku mikono yake akiiegesha juu ya magoti na kumwangalia sawia mke wa Himidu. “Binaadamu huwa tumeumbwa na hisia ambazo huja zenyewe pale kunapotokea tukio la kushitusha na hasa kama linaumiza moyo,” alisema. “Hisia hizo huletwa na kumbukumbu za nyuma ambazo huweka unasaba na tukio halisi lililotokea ambalo kwa njia moja au nyingine hukujenga kwenye mashaka binafsi na kusema moyoni ah, hili jambo lisingetokea kama si kitu fulani. Mara nyingi hisia hizo haziwezi kuchukuliwa kama ushahidi wa thibitisho, lakini kwa upande wa pili, hisia za namna hiyo zinasaidia sana kuwa chanzo cha kuelekea kwenye ukweli wa jambo.” Justin alipofika hapa akayatuliza maelezo yake kwa kunyamaza. Kisha akasema, “Wewe binafsi, baada ya kifo cha mume wako ambacho kilitokana na kupigwa risasi, ni hisia zipi ulizipata ambazo zilikupa sababu ya mashaka uliyonayo na kuhisi ndicho kilichosababisha mumeo auawe?”
Mke wa Himidu aliyatuliza macho yake usoni mwa Justin na kuwa kama aliyekuwa akijaribu kuyasoma mawazo ya kachero huyo. “Nilichukulia hivyo ndivyo alivyoandikiwa hatma yake iishie kwa kuuawa,” alisema kwa utulivu. “Ilikuwa ni ahadi yake, huwezi kupingana na mwenyezi Mungu!”
Mcha Mungu! Justin aliwaza na kutambua kuwa, watu wa aina hiyo huwezi ukawaondoa kwenye imani hiyo ya kuwa, kifo chochote ambacho humfika binaadamu ni ahadi ya Mungu na huwezi kumshawishi vinginevyo kuwa, wakati mwingine uhai wa mtu unaweza kukatishwa na jeuri ya mtu mwingine au kwa uzembe wa kitu fulani.
“Unamjua kijana aliyekamatwa baada ya mauaji ya mzee aliyekuwa akiitwa Beda?” Justin aliuliza.
“Nilimsikia tu baada ya kukamatwa kwake, lakini simjui.”
“Unamjua mwanamke anayeitwa Husna?” Justin aliuliza na kuyaangalia kwa makini macho ya mama huyo ili asiipoteze ishara yoyote itakayotokea machoni mwake.
“Husna ndiye nani?” mke wa Himidu aliuliza na kumwangalia Justin moja kwa moja usoni. Macho yao yakagongana na kumfanya Justin ajiulize, mama huyo alikuwa ni kweli hamjui Husna? Ina maana hajui hata mumewe aliuawa akiwa kwa nani?
“Ah, tuachane na Husna,” Justin alisema na hapo hapo akaunganisha kwa kuuliza, “Siku za uhai wa mzee, aliwahi kukulalamikia kupata upinzani wowote au kuwa na mgogoro ndani ya kazi yake?”
“Hakuna kitu kama hicho,” mke wa Himidu alijibu huku akionyesha utulivu.
“Au hakuwa na tabia ya kukuelezea mambo yake yanayomzunguka kikazi?”
“Huwa tulikuwa tunayazungumza, lakini hilo la kunilalamikia kama kulikuwa na chokochoko iliyokuwa ikimkera, hilo hakuwahi kuniambia. Labda alinificha, huwezi kujua!”
“Aliwahi kuwa na mgogoro wowote uliohusiana na biashara zake binafsi?”
“Sijui.”
“Unajihusisha na biashara zake kwa njia moja au nyingine?”
“Hilo siwezi kukujibu, nadhani ni suala la kibinafsi zaidi. Lakini ninachokijua ni kuwa, hakukuwahi kuwa na mgogoro wowote ndani ya biashara zake.
“Mzunguko wote huo haukufanyi ushangae ni kwa nini mumeo auawe? Pamoja na kuwa na imani, kifo ni ahadi ya Mungu, lakini kifo cha mumeo ni kifo kilichosababishwa na sababu iliyojificha, sababu iliyomfanya mwuaji achukue hatua ya kuja kumwua mumeo na sababu hiyo siyo upendo, bali kwa vyovyote ni uhasama uliokuwepo kati ya mwuaji na mumeo. Huoni kama kifo hiki kimesababishwa na mkono wa binaadamu, huoni kumtumia Mungu katika kifo cha mumeo ni sawa na kumkingia kifua mwuaji? Au unadhani mwuaji atakuwa ni mwenda wazimu wa kukurupuka tu kwa akili yake ya uenda wazimu na kuchukua hatua ya kumwua mumeo kwa ajili ya kujiridhisha uenda wazimu wake?”
Kimya kikapita kati yao huku wakiangaliana.
“Sasa baba unataka mimi nikujibu nini?” hatimaye mke wa Himidu alisema. “Unataka nikwambie namjua mwuaji wa mume wangu wakati simjui? Unataka nikwambie marehemu mume wangu aliwahi kunitaarifu kama alikuwa na migongano wakati si kweli? Unataka nikwambie ni kweli mume wangu aliuawa kwa chuki wakati hata maadui zake siwajui?”
Justin akashindwa kujibu. Akajikuna kichwani na kutambua hakuna atakachoambulia kutoka kwa mama huyo. Akamwona ni mama mwenye uhafidhina wa tabia, mgumu na mwenye msimamo. Akamchukulia kuwa, mama wa aina hiyo akitokea kukataa kutoa ushirikiano kutokana na imani anazoziamini, abadan asingeweza kumbadilisha!
“Nashukuru kwa msaada wako mama,” Justin alisema na kutengeneza tabasamu la hadaa huku akiinuka kutoka kwenye sofa.
“Karibu tena,” mkewe Himidu alisema huku naye akiinuka.
Justin alisindikizwa mpaka mlangoni ambako alipeana mkono wa kwaheri na mwenyeji wake. “Ukiwa na lolote la kunifahamisha nakuomba usisite kufanya hivyo,” alisema huku akijua kuagana kwao hapo ndiyo imetoka!
Akiwa kwenye gari, Justin aliufikiria muda wake alioupoteza kwa mama huyo ambako ameondoka akiwa hana chochote alichofaidika nacho zaidi ya kuzijua tabia za mwenyeji wake huyo. Aliamua kuyaondoa mawazo yake kutoka kwa mama huyo aliyemwona mwenye utata na kufikiria kwenda kwa mke wa aliyekuwa mheshimiwa Ali Othman, lakini kabla ya kujikita kufikiria atakachokwenda kukiuliza kwa mama huyo, Justin alimkumbuka Husna. Alikuwa hamjui mwanamke huyo aliyekuwa amemsoma kwenye jalada la uchunguzi wa mauaji ya mheshimiwa Himidu, lakini taarifa za ripoti hizo zilimfahamisha kuwa, Husna alikuwa ni hawara wa karibu wa mheshimiwa Himidu na ni hawara aliyefaidika kimaslahi kutoka kwa Himidu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alimkuta Husna akiwa kwenye duka lake la nguo akiwa na wanawake wengine ambao ni wasichana waliokaa ki-model, wakiwa ni wasaidizi wake. Hakumjua Husna kwa kumwona, kwanza alipofika ilibidi ajiweke kwa mwonekano kama ni mteja aliyeingia humo kwa kuhofia kutoswa kama angeingia na kumwulizia Husna moja kwa moja, kitendo ambacho kingewaweka kwenye kumwogopa kwa kumwona ni askari anayefuatilia habari za mheshimiwa Himidu. Akiwa kwenye uangaliaji wa vitu vilivyomo humo ndani pamoja na wateja wengine, Justin aliwasikia wasichana hao wasaidizi wakimwita mara kwa mara Husna kwa jina la anti Husna. Hapo Justin akatafuta utaratibu wa kumvizia Husna mpaka alivyokuwa peke yake.
“Samahani da Husna,” Justin alisema baada ya kumfuata Husna kwenye meza kubwa iliyokuwa kama ofisi yake. “Naitwa Justin, natoka makao makuu ya polisi na nimekuja kukuona kwa niaba ya IGP Inno.” Alinyamaza na kumwangalia Husna kuona kauli hiyo ya kulitaja jina la IGP Inno ambaye ni maarufu itakuwa imemwingiaje. Aliamua kulitumia jina la IGP kwa ajili ya kupata urahisi wa ushirikiano baada ya kuingiwa na hisia kuwa, aina ya wanawake kama Husna ni ile aina inayopenda kujulikana na wakubwa wa vyombo vya serikali hasa wakitembea kimapenzi na kigogo wa juu kama alivyokuwa mheshimiwa Himidu, akahisi kuwa anaweza kujuana na hata IGP!
“Karibu kwenye kiti,” Husna alisema akionyesha kuchangamka na kujisikia sifa ya umuhimu wake wa kujuana na wakubwa huku akiuona uzuri wake na hali nzuri ya kifedha aliyonayo kama silaha yake. “Bahati mbaya ofisi yangu ndiyo duka hapo hapo.”
“Unaonaje tukitoka kidogo, tukaenda kwenye mgahawa uliopo karibu? Nina mazungumzo ya siri niliyotumwa nikwambie.” Justin alisema akiwa amemwinamia Husna huku mikono yake akiwa ameiegemeza juu ya meza.
Macho ya Husna yakajiongeza ukubwa baada ya kauli hiyo ya Justin, na Justin akatambua Husna amepata mshituko.
“Mazungumzo yenyewe ni marefu?” Husna aliuliza.
“Ni mafupi. Ni kiasi cha kuiwakilisha meseji na kuongea hapa na pale.”
“Ni Inno aliyekutuma kwangu?”
“Ndiyo.”
Husna akaonyesha kusita. “Sidhani kama nafahamiana naye,” alisema. “Sijawahi kuzungumza naye ana kwa ana kama tunayefahamiana ingawa amekwisha kunikuta si mara moja nikiongea na baadhi ya mabosi wengine pale makao makuu na tukaishia kusalimiana tu.”
“Basi ndiye aliyenipa meseji ya kuja kukuona na ujio wa hapa ni siri, hata mabosi wengine hawajui na hapendi hata wewe umweleze mtu mwingine yeyote.”
Kauli hiyo ikamteka Husna kikamilifu.
“Basi twende mgahawa wa hapo nyuma wa Christoms, nadhani pale patafaa,” Husna alisema.
Mgahawa wa Christoms hufanya biashara ya kuuza ice cream, keki laini, milk shake na kahawa, tatizo la mgahawa huo ni kuwa haukuwa wa walala hoi. Justin na Husna waliingia mgahawani huo na wote wawili waliagiza kahawa na keki ya aina ya swiss roll.
“IGP anakupa pole kwa misiba yote miwili iliyokukuta ya kumpoteza mheshimiwa Himidu na kijana wako Beda,” Justin alisema baada ya kujikuta wametulia humo mgahawani.
“Mwambie ahsante,” Husna alisema na kusita, akaonekana kuwa na mshawasha. “Anajua kama waliomwua Beda ni askari wake?” Hatimaye aliuondoa mshawasha wake kwa kulitamka hilo na sauti yake ilifanya mkwaruzo ulioonyesha ghadhabu iliyojificha.
“Anazifanyia kazi ripoti hizo baada ya kuziona kwenye vyombo vya habari,” Justin alidanganya.
“Ni wao ndio waliyemwua!” Husna aliweka msisitizo.
“Pengine walichanganyikiwa na kifo cha mheshimiwa Himidu na kujikuta wakitumia nguvu zaidi kwa Beda ili kujua kama ni kweli alihusika. Lakini yote haya yasingetokea kama si kuuawa kwa Himidu, waliomwua Himidu ni kama pia ndio waliomwua Beda na hilo ndilo linalomtia hasira IGP, laiti asingeuawa Himidu na Beda naye asingekufa. Kwa hiyo IGP anataka wauaji wa Himidu lazima wapatikane na anaamini mmoja wa kumsaidia katika hilo ni wewe. Hizi ndizo salamu alizonipa,” Justin aliumaliza uwongo wake na kumwangalia husna.
“Anataka mimi nimsaidie kivipi?”
“Anaamini wewe ndiye mwenye kumjua vizuri mheshimiwa Himidu kuliko mtu mwingine yeyote. IGP anasema yeye mwenyewe atakulinda endapo utamsaidia kwa hilo.”
“Kwa hilo lipi?”
“Anasema wewe utakuwa unaujua vizuri uhusiano wake ulivyokuwa na mheshimiwa Ali Othman na ana wasiwasi kuwa, waliomwua Himidu ndiyo waliomwua Ali Othman,” hapa Justin alisita na kuyatuliza macho yake usoni mwa Husna. Kisha akauliza, “IGP anataka kujua uhusiano wa Himidu na Ali Othman ulikuwaje?”
“Walikuwa ni marafiki wazuri na walikuwa wakishirikiana katika mambo mbali mbali, hata wakati mwingine walikuwa wakionana pale nyumbani kwangu.”
“Una maana walikuwa wakiagana kukutana kwako?”
“Ndiyo. Imekwishatokea hivyo zaidi ya mara…kama tatu nne hivi au na zaidi. Kwa kweli nilikuwa sina sababu ya kuhesabu ni mara ngapi!”
“Unajua watu wa aina yao ni watu ambao hawakosi kuwa na maadui, walivyokuwa wakikutana nyumbani kwako ulikwisha kuwasikia wakizungumza lolote kuhusiana na mwelekeo kama huo wa kuwasema maadui zao?”
“Mmm…siwezi nikasema niliwahi kuwasikia wakizungumzia moja kwa moja kuhusu hilo, unajua walipokuwa wakizungumza mambo yao mimi nilikuwa sipendi kuyasikiliza mazungumzo yao. Lakini hata hivyo, mara moja moja nilipokuwa nikiwa na shida na Himidu na kuingilia mazungumzo yao, nilishasikia wakiongea kitu kama hicho.”
“Kuwa wana maadui?”
“Ndiyo.”
“Waliwataja akina nani?”
“Nimekwambia, sikuwasikia wakiwazungumzia moja kwa moja, bali nimewasikia wakizungumza kitu kama hicho. Kwa hiyo ukiniuliza maadui wenyewe ni akina nani, nitashindwa kukujibu kwa sababu sikuwahi kuwasikia wakiwataja kwa majina mbele yangu.”
“Kwa hiyo huna hisia na yeyote kuwa, anaweza akahusika na kifo cha Himidu?”
Husna alitingisha kichwa kukataa. “Sina,” alisema.
“Unataka kuniambia kuwa, hata alivyokamatwa Beda hukuwa na hakika kama angeweza kuhusika na kifo cha Himidu?”
“Beda hakuhusika na kifo cha Himidu,” Husna alisema kwa sauti iliyotulia.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Kwa sababu namjua Beda vizuri sana na zilikuwepo sababu za kumfikiria hivyo.”
“Kama zipi?”
“Ni sababu za kibinafsi ambazo zipaswi kukueleza, isitoshe Beda mwenyewe kishafariki, kwa nini tumzungumzie?”
“Kumbuka hata Himidu amefariki, lakini tunamzungumzia!”
“Maumivu ninayoyapata kuhusu watu hawa wawili yako tofauti.”
“Kama?”
“Bado ni swala langu binafsi.”
Justin akamwangalia Husna bila ya kutamka lolote kisha, alitabasamu.
Kimya kifupi kikapita kati yao. Justin akakivunja kimya hicho kwa kusema, “Ukimwondoa Ali Othman, ni nani mwingine aliyekuwa karibu naye?”
“Omar Sharif,” Husna alijibu.
“Waziri wa Nishati na Madini?”
“Ndiyo.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Naye alikuwa akija kwako?”
“Hakuwahi kufika kwangu hata siku moja.”
“Anakufahamu?”
“Sidhani. Sijawahi kuwa naye pamoja, sijui kama Himidu aliwahi kumweleza lolote kuhusu mimi.”
“Ulijuaje kama alikuwa ni mtu wa karibu na Himidu?”
“Himidu alikuwa akinieleza kuwa, Omar alikuwa ni kati ya watu aliokuwa akiwaamini sana, isitoshe hata na Raphael Kibaha, wote walikuwa ni timu moja. Himidu alikuwa akijigamba kuwa, mmoja kati yao ndio anategemewa kuwa Rais mtarajiwa baada ya huyu wa sasa kumaliza kipindi chake.”
Justin hakushangaa na mnong’ono huo, ulikuwa ni mnong’ono uliokwishaanza kusikika kwa mbali kwa watu waliokuwa kwenye vyombo vya usalama, lakini alijikuta akishituka kwa kupata uhakika huo kutoka kwa mtu ambaye ana sababu zote za kumuamini kwa asilimia mia moja. Taarifa hizo zikamfanya aanze kujenga mashaka kuwa, mauaji ya viongozi hao wawili yanawezekana yakawa yametokana na njama za kisiasa.
“Ni nani waliyekuwa wamempa nafasi kubwa ya kuutwaa urais?” Justin aliuliza.
“Himidu au Ali Othman, endapo mmoja angekuwa ni Rais basi mwingine angekuwa ni Waziri Mkuu.”
“Unadhani ndiyo sababu ya kuuawa kwao?”
“Sijui. Lakini kwa mtazamo mwingine unaweza ukaamini hivyo.”
“Unataka kuniambia ndani ya timu yao walikuwa na mshikamano wa dhati?”
“Nadhani walikuwa hivyo. Mara kwa mara Himidu alikuwa akiniambia kuwa na mikutano na wao.”
“Ni biashara zipi kubwa alizokuwa akizimiliki Himidu kabla ya kifo chake?”
“Biashara zake kubwa alijiweka kuwa na hisa nazo kuliko kuonekana ni mmiliki.”
“Nitajie baadhi.”
Husna akamtajia.
Baada ya hapo mazungumzo yao hayakuchukua muda mrefu, bili ikaletwa na Husna akawa wa kwanza kutoa pesa kutaka kulipa.
“Nitalipa,” Justin alisema na kumzuia mhudumu aliyetaka kuchukua pesa kutoka kwa Husna.
“Kwa nini?” Husna alihamanika. “Wacha nilipe tu!”
“Gharama hii ni yangu mimi. Siku nyingine utalipa wewe,” Justin alisema na wakati huo huo akimlipa mhudumu.
* * *
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment