Sehemu Ya Tatu (3)
Jacob hakujua ni muda gani mkono wake ulikuwa umefika kichwani kwa Merina na kuanza kuchezea nywele zake. Merina kwa upande wake hakushangazwa na kitendo hicho hivyo hakuweka upinzani wowote. Wakati mkono wa kushoto ukiwa unachezea nywele zake ule wa kulia ulitoa kitambaa na kuanza kufuta machozi yaliyokuwa usoni kwa Merina.
Ghafula Merina alijinasua toka kifuani na mikononi kwa Jacob na kusimamia wima huku akimuangalia. Kisha kwa sauti iliyojaa uchungu akasema “ Jacob, taarifa za ujio wako nilikuwa nimepewa na mzee Edson ambaye kwa sasa ni marehemu pia. Mzee Edson na baba yangu jaji Mark Gordón walikuwa ni marafiki sana. Hivyo tangu kutokea kwa kifo cha baba yangu mzee Gordón, mzee Edson alinichukua kama sehemu ya kunifanya nipumzike. Nilimweleza mzee Edson juu ya uamuzi wangu wa kuwatafuta wauaji wa baba yangu. Ndipo kwa kuzingatia uwezo uliokuwa umeonyeshwa na wauaji mzee Edson akanishauri kuwa ingekuwa hatari sana kama ningeendesha operesheni hii peke yangu. Ndipo akaamua anieleze juu ya wasifu wako, alishangaa pale nilipomwambia kuwa nilikuwa nakufahamu na kuwa umewahi kukaa nyumbani wakati ulipokuwa Ubelgiji katika shughuli zako hizi hizi za upelelezi.
Baba alikuwa ameshawahi kunieleza juu ya sifa zako na vilevile nimekuwa nikizisikia sehemu mbalimbali hivyo nilifurahi niliposikia kuwa jana jioni ulikuwa umeingia Arusha ili kushughulikia suala hili. Lengo la mzee Edson kuja kukuchukua asubuhi hii ilikuwa ni kutukutanisha kwani alihofia kuwa yawezekana ukawa umenisahau. Nashukuru kusikia kuwa unanikumbuka bado, hii inathibitisha ni jinsi gani ulivyo na kiwango cha juu cha kumbukumbu.
Jacob, najua kuja kwako hapa umefanya siri kubwa na hukutaka mtu yeyote ajue. Lakini naomba unifanye kuwa mshirika wako katika kazi hii ili niweze kumlipizia kisasi marehemu mpenzi baba yangu na rafiki yake mzee Edson aliyeuawa kikatili asubuhi hii kama ulivyoshuhudia”. Merina Alipofika hapo kwa mara nyingine tena akajiegemeza kifuani kwa Jacob huku machozi yakimtoka kwa kasi. Huruma, chuki na hasira viliutawala moyo na akili ya Jacob kwa wakati mmoja.
Alijikuta akimvuta Merina na kumkumbatia zaidi. “bila shaka tutakuwa pamoja kwani jambo kama hilo si la kumkatalia mtu. Ila kabla hatujaanza ningependa tuwe na maongezi zaidi. Kwani naamini kuwa unaweza kuwa unajua mazingira ya ndani zaidi kabla na baada ya kifo cha baba yako na mzee Edson. Hivyo ningependa unipe japo kidogo ila hatutatumia hapa kwa maongezi hayo” Jacob alisema huku akimwachia. Uso wa Merina ulionyesha furaha fulani, bila shaka ni kule kusikia kuwa angeshirikiana na Jacob katika msako wa kuwasaka wauaji wa baba yake jaji Mark Gordón.
“Gari unayotumia ilikuwa unatumia hata kabla ya kifo cha baba yako? Jacob alimwuliza Merina wakati alipokuwa akielekea alipokuwa ameacha gari alilokuwa amekuja nalo.
“Hapana gari hii nimeikodisha ili kutofuatiliwa kwa urahisi na watu wabaya, mengine mengi nitakuelea baadaye ila kwa sasa sidhani kama gari hiyo ina madhara yoyote” Merina alisema huku akianza kuelekea alipokuwa amepaki gari aliyokuwa amekuja nayo. Tayari Jacob alikuwa ameshamrudishia Merina bastola yake.
Kila mmoja alitumia gari aliyokuwa amekuja nayo huku porini. Ilibidi Jacob atangulie maana hakuwa amemwambia Merina ni wapi wangeelekea baada ya hapo.
Safari ya kurudi mjini ilianza huku kichwani mwa Jacob kukiwa na maswali mengi, lakini wakati huohuo akiwa na furaha ya kukutana na Merina tena akiwa ni mtu aliyekamili katika fani. Jambo moja alianza kulihisi juu ya huyu msichana tangu pale alipomwona kwa mara ya kwanza. Hakujua hali hii ingeishia vipi na wapi maana inasemekana kuwa inapomshika mtu huwa haijifichi. Wengine huifananisha na kikohozi kama alivyoimba mwanamuziki Fresh Jumbe. Mbegu haichagui pa kupandwa, ndiyo yalivyo mapenzi.
Oldongei Hotel ndiyo ulikuwa mwisho wa safari ya Jacob na msichana Merina toka porini walikokuwa. Hoteli hii iko nje kidogo ya mji wa Arusha. Jacob aliichagua sehemu hii kwa vile ni tulivu kwa ajili ya maongezi kati yake na msichana huyo.
Baada ya kuwa ameshaegesha gari sehemu ya kuegeshea aliteremka na kumsubiri Merina ambaye ndiyo kwanza alikuwa anaingia ndani ya eneo la hotel hiyo. Merina Aliposhuka Jacob alianza kutembea huku akiwa anachagua sehemu ya kukaa.
Hoteli hii ilikuwa na sehemu mbili zilizotumiwa na wateja wake kwa kukaa. Kulikuwa na sehemu ya ndani na sehemu ya nje. Jacob alionelea ilikuwa vizuri wakae nje ambapo wangekuwa huru na salama zaidi katika maongezi yao. Hivyo alichagua sehemu iliyokuwa imejitenga hapo nje na kumwonyesha Merina ishara ya kumtaka wakakae hapo. Merina alionekana kuridhia na kufurahia sehemu iliyokuwa imeichaguliwa na Jacob.
Muda mfupi tu mara baada ya kuwa wamekaa mhudumu wa hotelini hapo alifika na kuomba awahudumie walichopendelea. “hey bibie, lady’s first, agiza kisha nami nitachagua”. Jacob alisema huku macho yake yakiwa yamekazwa usoni kwa Merina.
“ Hilo ni kati ya maneno ninayoyachukia sana” Alisema Merina huku akimwangalia Jacob, bila shaka ni kuona kuwa angepokeaje neno hilo.
“Kwa nini hulipendi, kwani wewe ukiwa msichana hupendi kupewa nafasi ya kwanza? Jacob aliuliza huku akionyesha kuvutiwa na kauli hiyo ya Merina. .
“Hali ingekuwa kama maana halisi ya neno ilivyo nisingechukia, lakini tatizo ni kuwa neno ‘msichana kwanza’ au ‘Ladies first’ huwa mnapenda kulitumia maeneo kama haya madogo madogo tu”. Alisema Merina ambaye sasa alitabasamu na kuacha moyo wa Jacob ukilipuka. Ingawa Jacob mwenyewe hakujua ni kwa nini tabasamu la Merina lilikuwa likiufanya moyo wake kupata taabu kiasi hicho.
“ Eti dada, naomba unisaidie kidogo kunifahamisha. Je meneja na mhasibu wa hoteli hii ni Wanawake? Merina alimwuliza dada aliyekuja ili kutuhudumia na ambaye wakati huu ilibidi asimame na kusikiliza mdaharo usio rasmi uliokuwa ukiendelea.
“Wote ni wanaume, ila sisi wahudumu wengi ndiyo wanawake” Alijibu huyo dada mhudumu huku sauti yake ikionyesha dhahiri kumuunga mkono Merina.
“Sasa wewe unadhani kuwa kati ya hawa wahudumu walioko hapa hakuna wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo? Aliuliza Merina katika sauti ya kusuta. Kabla Jacob hajajibu yule dada muhudumu akadakia. “aah wapi kuna wahudumu wengi tu hapa wamesoma kuliko huyo meneja na mhasibu, lakini kwa vile wao ni wanaume wanaheshimiwa zaidi” alisema dada huyo kwa sauti ya juu kidogo.
“ Dada angalia usimseme meneja na mimi nikiwepo. Hujui kuwa yule ni ndugu yangu? Nitamwambia, shauri yako” Alipoona Amezidiwa na hawa wasichana, Jacob akaona amtishe huyo muhudumu. Alionekana kutishika.
“Naomba uniletee ugali na samaki mbichi aina ya sato” Merina aliagiza kisha akatupia jicho kwa Jacob.
“ Kwa nini unaagiza mbichi badala ya aliyepikwa? Hapa sio Sokoni hivyo ni vema ukaagiza aliyepikwa na sio mbichi” Jacob alisema hivyo makusudi huku akimwangalia Merina usoni. Merina aliangua kicheko na hapo mwanya wake mdogo uliweza kuonekana. Jacob alikuwa anataka Merina acheke. Aligwaya pale alipogundua kuwa Merina alipokuwa akicheka uzuri wake uliongezeka maradufu.
“Mie niletee utumbo wa kuku wa kienyeji na supu yake” Hatimaye Jacob aliagiza na kumpa yule dada fursa ya kuondoka ili kufuata aliyokuwa ameagizwa.
“Naomba tuachane na hayo na tuangalie mambo makubwa yaliyoko mbele yetu na ambayo yanatuhitaji ili kuyapatia ufumbuzi” Mara moja Jacob alibadilisha maongezi na sura yake, wakati huo huo sura ya Merina ilibadilika pia.
“ Ila nashukuru kuwa na mtu kama wewe kwani kazi hii bila shaka itakuwa nzuri kama vile ulivyo” Alisema Merina kisha akaendele. “ Siku chahe kabla ya kifo cha baba yangu aliniita na kuniambia jambo” Mara hii Merina naye akawa amebadili maongezi. Kama mtu aliyejua kuwa Jacob alikuwa anahitaji nini waongee wakati huo. Alianza kuongea juu ya mazingira kabla na baada ya kifo cha baba yake. Hapo Jacob akatambua kuwa msichana huyu alikuwa na ufahamu wa juu sana.
“ Aliniambia kuwa alikuwa amepokea simu ya vitisho toka kwa watu asiowafahamu. Katika simu hiyo aliambiwa kuwa alikuwa amejiingiza katika jambo ambalo limegusa ‘Ndevu nyeupe’ za ‘bosi’ ambazo huwa haziguswi hovyo na kwa hiyo adhabu yake ingekuwa ni kifo. Baba anasema alimwuliza mpigaji wa simu hiyo amwambie jambo gani alilokuwa ameingilia. Ndipo pasipo kusita aliabiwa kuwa kitendo ha yeye kushiriki katika kutunga muundo wa mkataba wa amani ya nchi kadhaa alikuwa amegusa ‘ndevu nyeupe’ za ‘bosi’ moja kwa moja.
Alipouliza kuwa alikuwa amegusaje hizo ‘Ndevu nyeupe’ na kuwa ‘bosi’ anayesemwa hapo ni nani, anasema simu ilikatwa. Hivyo akawa anajiuliza huyo bosi ni nani na hizo Ndevu nyeupe ndio nini. Siku hiyo jioni alipokuja Nyumbani alionekana kuwa mnyonge sana. Hayo yalitokea wakati ilikuwa ni siku moja tu imepita tangu pale nilipokuwa nimerudi toka Costa Rica, ambapo nilikuwa nimeenda kuongezea utaalamu zaidi katika judo. Hivyo nilipomwuliza baba ili aniambie sababu ya yeye kuwa mnyonge ndipo akanisimulia hayo.
Nilimshauri atoe taarifa kwenye vyombo vya usalama ili aongezewe ulinzi. Wakati huo huo nikawa nimepanga kuanza kuufuatilia mienendo ya baba kwa karibu ili niweze kubaini kama kuna mtu aliyekuwa anamfuatilia. Hivyo mchana wa siku iliyofuata ndio nilikuwa nimepanga kuanza kuufuatilia nyedo za baba kwa siri ili kumlinda. Jambo la kusikitisha ni kuwa mauaji yake yalifanyika mchana kabla hata sijafanya lolote.
Inaniuma sana kuona kuwa baba alitumia pesa zake nyingi kwa kunipeleka vyuo maarufu vya kujifunzia utaalamu wa kujihami na kupambana lakini amefariki pasipo mimi kuweza kumsaidia. Kibaya zaidi ni kuwa alinitaarifu juu ya tisho hilo lakini nikachelewa kumpa msaada. Najiona kama msaliti kwa kushindwa kuokoa maisha ya baba yangu”. Alipofika hapo machozi yakaanza kumlengalenga tena. Wakati huohuo yule dada muhudumu akawa ameleta chakula walichokuwa wameagiza. Merina alifanikiwa kuficha hali aliyokuwa nayo machoni kwa yule muhudumu ambaye mara baada ya kuhudumia aliondoka.
“ Merina kumbuka kuwa ndio maana tuko mahali hapa na katika hali kama hii hivyo unahitajika kuvumilia ili tushirikiane kuwasaka wauaji hao” Jacob alisema huku akisogeza kiti chake jirani na alipokuwa Merina.
“ Nashindwa kuvumilia Jacob, unajua inauma sana. Baba yangu alikuwa akinipenda sana, bila shaka kabla hajauawa alilitaja jina langu katika hali ya kuomba msaada” alisema Merina huku akifuta machozi.
“ Pole sana Merina najua ni namna gani inauma lakini jikaze tufanye kazi. Kwani ni nini kinakufanya uamini kuwa baba yako alilitaja jina lako wakati alipokuwa akielekea kuuawa? Alimbembeleza Merina na wakati huohuo akiachia swali.
“ Jacob, kifo cha mzee Edson kwa kiasi kikubwa kimechangiwa na mimi” Alisema kisha akamwangalia Jacob usoni.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa nini unasema hivyo? Jacob aliuliza
“Siku moja baada ya mazishi ya baba yangu mama yangu alipokea simu. Kama kawaida mpigaji wa simu hiyo hakujulikana. Simu hiyo ilimtaarifu mama kuwa mtu ambaye angafuata kuuawa alikuwa ni mimi. Mama alipouliza sababu ya wao kutaka kuniua mimi alijibiwa kuwa mimi nilikuwa nimetajwa na baba kuwa kwa vyovyote ningewapata wauaji na kumlipizia kisasi. Hivyo inaonyesha kuwa baba ilikuwa akinitaja wakati alipokuwa akiuawa. Bila shaka aliamini kuwa kama ningekuwepo ningemsaidia na kweli ningefanya hivyo, lakini nasikitika kuwa sikuwepo”. Alipofika hapo aliangalia juu kana kwamba anakumbuka kitu.
“ Naapa kuwa nisingekubali baba yangu afe mbele ya macho yangu na hata hivyo ninaapa kuwa watu hawa lazima wataiona hii Arusha ndogo sana kwa kazi watakayokabiliana nayo toka kwangu. Nitapambana mpaka nitakapohakikisha mtu wa mwisho ambaye wao wanamwita kwa jina la ‘Bosi’ yuko mikononi mwangu. Na pia hizo ‘Ndevu nyeupe’ lazima zikatwe na sio kuguswa. Zitakatwa pale nitakapohakikisha kuwa mkataba wa amani unafanyika na kunakuwa na amani ya kudumu eneo hili”. Merina aliongea maneno haya kana kwamba yuko mahakamani na ameambiwa kula kiapo. Lakini bado Jacob alitaka kujua uhusiano wa Merina na kifo cha mzee Edson.
“Eeh kuna uhusiano gani kati ya kifo cha mzee Edson na wewe? Jacob aliuliza
“Mama alipopokea kitisho toka kwa hao wafuasi wa ‘bosi’ juu ya maisha yangu alinishauri kuwa siku iliyofuata tupande ndege tuhame Tanzania na kwenda kuishi Ubelgiji ambako pia tuna makazi na tunatambulika kama raia wa nchi hiyo. Sikukubaliana na wazo hilo la mama. Nilikuwa na hamu ya kujilipizia kisasi kwa ajili ya baba yangu na wakati huohuo kuhakikisha kuwa lile lililosababisha baba kuuawa linafanyika. Mama alishikilia msimamo wake, hofu ilikuwa imemjaa. Kweli siku iliyofuata alipanda ndege na kwenda zake Ubelgiji. Mimi Nilionelea niende nikaishi kwa mzee Edson ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa baba na ambaye amekuwa karibu sana nasi tungu tupate msiba wa baba. Kwenda kuishi kwake ilikuwa ni siri kubwa. Nilipanga kuamua kufanya operesheni yote ya kisasi nikiwa hapo kwa mzee Edson. Sikuona kuwa ni vema kufanya mambo haya bila kumwambia huyo mzee juu ya azma yangu hiyo.
Nilipomwambia ndipo akaniambia juu ya wewe na kuwa ingefaa uje ili tushirikiane katika kazi hii ya kumsaka ‘Bosi’ ambaye hataki ‘Ndevu zake nyeupe’ ziguswe. Ninaamini kuwa wauaji walikuwa wamepata taarifa juu ya kuwepo kwangu nyumbani kwa mzee Edson, na hivyo wakajua kuwa wenda nimeshamsimulia habari kuwahusu wao. Maana wao wanaamini kuwa ninuja kila kitu kuhusu wao, wakati mimi Sijui lolote.
Wamemuua mzee Edson wakidhani kuwa ana habari zao, na najua wako mbioni kunitafuta. Ndiyo maana tangu ameuawa hii asubuhi nimeamua kutojihusisha kwa namna yoyote na mazishi yake na sitapenda mtu yeyote ajue niko wapi. Inaniuma kutokuwa karibu na familia ya yule mzee wakati mgumu kama huu. Sijui wataniweka katika fungu gani, lakini kwa usalama wangu na lengo nililonalo ni lazima niishi maisha kama haya sasa. Nadhani mpaka hapo haitakuwa na swali jingine la kuniuliza? Merina alimaliza maelezo yake ya kusisimua huku akimuachia swali Jacob. Kabla Jacob hajasema kama alikuwa na swali jingine au la, alikuwa amekumbuka kuwa ni dakika kadhaa sasa zilikuwa zimepita tangu waletewe chakula na hawakuwa wameanza kula.
“Wakati nafikiria ni maelezo gani mengine ningehitaji toka kwako, naomba tupate chakula tusije tukakosa hata nguvu za kuanzia kupambana na hao jamaa” Jacob alisema hayo huku akianza kushambulia utumbo wa kuku na supu yake. Merina naye alianza kula ugali na samaki taratibu huku akionyesha wazi kutokuwa na hamu ya kula.
Baada ya chakula Merina aliagiza juisi Wote wakaanza kunywa.
“Merina kwa hisia zako na baada ya kutafakari kwa undani tangu kifo cha baba yako na mzee Edson asubuhi ya leo, unahisi huyu ‘bosi’ anaweza kuwa ni nani? Jacob aliuliza kwa pozi.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“nimejaribu sana kufikiria lakini nimeshindwa kujua huyu mtu ni nani.” Alijubu Merina huku akimuangalia Jacob kwa jicho kali.
“Sawa kwa sasa naomba ukapumzike jioni muda wa saa kumi na moja tukutane hapa ili nikwambie mikakati ya kazi yetu hii. Na wewe ukienda huko hebu tafakari ni namna gani tunaweza kutekeleza kazi hii iliyoko mbele yetu. Ila kabla hatujaachana naomba unipe ramani ya ilipo nyumba ya marehemu mzee Edson”. Jacob alisema hivyo wakati wakiwa tayari kwa kusimamia.
“Mzee Edson alikuwa anaishi maeneo ya Njiro. Nyumba yake iko mkabala na kiwanda cha Temdo. Kwa vile kwa sasa kuna msiba na mzee huyu alikuwa maarufu kama ujuavyo basi ukifika bila shaka utapatambua tu. Ila kama unataka kwenda inabidi uwe makini sana Jacob”. Namna Merina alivyotamka ile sentensi yake ya mwisho sauti yake iliashiria kitu fulani ambacho hata hivyo Jacob hakuweza kubainisha sawasawa.
Wote walisimama na kupeana mikono kama ishara kuwa sasa walikuwa shirika. Merina alipoanza kutembea kuelekea ilipokuwa gari yake, Jacob alibaki amesimama huku macho yake yakiwa yanamsindikiza Merina.
“Farasi uliyempanda hakutishi mwondoko” Jacob alijisemea huku akiwa bado anamsindikiza Merina kwa macho. Merina alipokaribia kwenye gari aligeuka ghafula na kuangalia huku alikokuwa Jacob, alipokuta kuwa Jacob alikuwa anamwangalia alikonyeza kidogo a kuingia ndani ya gari. Kidogo Jacob amwambie asubiri waende wote lakini akaona si vema.
“Kazi ni namna ya kumpanda tu huyo Farasi, baada ya hapo hatishii tena kwa mwondoko wake” Jacob alisema huku akiwa anaelekea kwenye gari yake.
Baada ya hapo, Jacob naye aliingia ndani ya gari yake tayari kwa safari ya kwenda Njiro Nyumbani kwa marehemu mzee Edson. Aliamua kufanya hivyo ili kuona kilichokuwa kikiendelea mahali pale.
Wakati Anafika 'keep left' ya Naazi tayari ilikuwa ni saa tisa alasiri. Akili yake ilikuwa ikiwaza mambo mengi sana wakati huo.
* * *
Ilipogonga saa tisa na robo tayari Jacob alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wakimiminika kwenda nyumbani kwa mzee Edson. Alikuwa ameshaegesha gari lake mbali kidogo toka ilipo nyumba hiyo. Alitembea taratibu kuelekea ilipo nyumba hiyo.
Alipofika alionyeshwa mahali pa kukaa kama ilivyokuwa kwa wageni wengine. Japo yeye alikuwa tofauti na wageni wengine kutokana na malengo yaliyokuwa yamemleta mahali hapo. Alijua kuwa walikuwepo waliokuwa kama yeye kwa kuwa na malengo mengi yaliyowaleta hapo. Moja kati ya watu aliowahisi kuwa wangekuwa hapo ni wauaji wa mzee Edson. Kwa vyovyote wangekuja kuangalia hali ya mambo ilivyokuwa.
Alikuwa ametulia tuli mahali alipokuwa amechagua kukaa. Ndungu na jamaa wa karibu wa mzee Edson walikuwa wakitoa vilio vya uchungu kiasi kuwa hata kama ulikuwa umekuja mahali pale bila tarajio la kutoa machozi yangekutoka tu. Majonzi yalionekana wazi kwenye kila sura iliyokuwepo mahali hapa. Jacob kwa upande wake aliivaa sura hiyo huku macho yake yakiwa yanamuhakiki kila aliyekuwa akiingia mahali hapo.
Dakika moja.. mbili… kumi… kumi na tano tayari watu walikuwa wameshajaa. Kadiri muda ulivyokuwa ukikimbia na watu kuongezeka Mpelelezi Jacob Mtata alijikuta akiingiwa na hali fulani ya hasira. Hali hii ilikuja pale macho na ubongo wa Jacob ulipoanza kupoteza umiliki wa kuweza kumwona na kumchunguza kila aliyekuwepo mahali hapo.
Ili kushinda hilo Jacob akajikuta ameshachagua watu kadhaa ambao aliamua kuwaangalia kwa ziada. Sababu zilizomfanya kuwatenga watu hawa na kuwapa upendeleo huu maalumu zilikuwa za kikachero na kitaalamu zaidi
Baada ya muda alikuwa amebakiwa na mtu mmoja tu kati ya wale aliokuwa ameamua kuwafuatilia hapa msibani. Si kwamba wengine walikuwa wameondoka la hasha ila sababu kubwa hasa ni kuwa hawa wengine hakuwaona na ‘uzuri’ aliokuwa anautaka. Huyu aliyempa upendeleo zaidi alikuwa na ‘sifa’ moja iliyomvutia.
Katika uso wake alikuwa amebeba kitu zaidi ya huzuni na majonzi. Inamaanisha alikuwa na zaidi ya huzuni na majonzi. Jacob alijikuta akitaka kujua kile cha ziada kilikuwa ni nini. Hivyo kwa chati sana akawa anamfuatilia kwa makini na kuyasoma mawazo yake. Alionekana kama mtu ambaye alikuwa kwenye vita. Lakini vita yake ilikuwa tofauti na vita unayoifahamu wewe. Vita yake ilikuwa baina yake yeye na nafsi yake mwenyewe. Ndiyo! Hakuwa na raha, si kwa sababu ya msiba bali kwa sababu ya vita hiyo iliyokuwa ikiendelea ndani yake.
Dakika kumi baadaye kijana huyo alisimama na kuanza kupiga hatua kuelekea nje. Jacob alipoangalia saa yake akagundua kuwa muda wa kukutana na Merina kule walikokuwa wameagana kukutana ulikuwa umekaribia. Hivyo akaona ulikuwa ni wakati mzuri wa yeye kuondoka huku akiwa anaangalia huyu kijana angeelekea wapi.
Alitoka nje huku kwa makini akiangalia kama kuna macho yalikuwa yakimfuata kwa namna asiyoitaka. Naam wakati anapotelea kwenye geti kubwa la kutokea nje alitupa jicho nyuma na kukutana na macho mengi yaliyokuwa yakimwangalia, lakini kuna jicho moja lililokuwa likimwangalia kwa mtindo ambao yeye Jacob huwa haupendi. Kwa bahati mbaya hakupata nafasi ya kuiona sura iliyokuwa imebeba jicho hilo. Hivyo alipofika nje kama mtu aliyekuwa amesahau kitu alirudi mpaka alipokuwa amekaa na kujifanya kuangaza angaza kama mtu aliyepoteza kitu. Wakati huo wote lengo lake ilikuwa ni kumwangalia mtu aliyetoa lile jicho wakati alipokuwa akitoka muda mfupi uliopita. Aliyetiliwa mashaka alikuwa ni mzee mmoja mwenye upara uliokuwa uking’aa sana. Aliporidhika na kuhakikisha kuwa sura ya mtu huyo ilikuwa imehifadhiwa vizuri kwenye kumbukumbu zake alitoka, safari hii bila kugeuka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipofika nje alimkuta yule kijana aliyempa upendeleo wa kumfuatilia akiwa amesimama huku akiwa ameegemea gari aina ya Toyota Carina. Alipokuwa amefika usawa wake Jacob alimpita kana kwamba alikuwa hajamwona na wala hakuwa anafuatilia lolote juu yake. Alipokuwa ametembea kama hatua kumi na tano hivi kuelekea ilipokuwa gari yake, Jacob alisikia mlango wa gari ukibamizwa. Hakugeuka alijua fika kuwa angekuwa ni yule kijana ambaye alionekana kuzidiwa na mawazo. Kwa chati sana Jacob aliongeza mwendo kuliendea gari lake.
Alipoingia ndani ya gari na kuliwasha hakuliondoa ili kuruhusu gari aina ya Toyota Carina iliyokuwa inakuja ipite kwanza. Ilikuwa ni ya yule kijana, bila shaka alikuwa akielekea mjini. Jacob alijiona mwenye bahati, kwani hii ilimpa fursa ya kuongozana naye. Kwa hadhari kubwa aliingia barabarani na kuanza kuelekea mjini huku akilini akiwa na nia ya kujua yule kijana angeishia wapi.
Mpaka wanafika mzunguko yalipo majengo ya kumbukumbu ya azimio la Arusha Jacob hakuwa anajua wanaelekea wapi na huyu mtu. Kwa namna alivyokuwa amemfuatilia isingekuwa rahisi kwake kujua kuwa kuna mtu kama Jacob alikuwa anamfuatilia. Walishika barabara ya makongoro na kunyoosha, alipofika jirani na uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abed aliwasha taa za kupunguza mwendo na baadaye aliwasha ile za kuashiria kuwa anakata kulia. Aliingi barabara ya Colenel Middlenton, alipita makutano ya Stadium Road na Celenel Middlenton kwa mwendo wa taratibu kidogo kama mtu aliyekuwa akitarajia kusimama jirani. Naam, Alipokaribia kuwa mkabala na Annex Hotel by night alipunguza mwendo zaidi na kuwasha taa za kuashiria kuwa alikuwa anaingia hotelini hapo. Aliingia wakati Jacob akapitiliza na kwenda kupaki mbele kidogo upande wa kushoto wa barabara hii ambapo kulikuwa na duka la vitabu Kimahama.
Kabla hajashuka Jacob aliangalia saa yake ilikuwa imebaki kama dakika kumi ili kufika muda wa miadi kati yake na Merina. Aliangaza huku na huko kisha akatelemka na kuanza kutembea haraka kuelekea ulipokuwa mlango mkubwa wa kuingilia Annex hoteli. Alingia kwa tahadhali kubwa huku akiwa hajui angejuaje alipokuwa huyo jamaa yake.
Alipofika sehemu iliyokuwa na watu waliokuwa wakinywa mara akamwona jamaa yake aliyekuwa akimfuatilia akiwa kasimama na jamaa mmoja, bila shaka walikuwa akiongea kitu. Huyu mwenzie tofauti na yule aliyekuja na Jacob hapo hotelini alipomwona tu akaanza kutembea kama anayetoka nje kupitia alipokuwa anaingilia Jacob, huku akimwacha yule jamaa aliyekuja naye akianza kupanda ngazi za kuingilia chumbani.
Huyu mwenzie Alipofika usawa wa Jacob akageuka ghafula kama aliyesahau kitu “Rich hebu subiri kidogo” alisema kumwita yule aliyekuwa akielekea chumbani. Mara moja Jacob akajua kumbe mtu aliyekuwa akimfuatilia alikuwa akiitwa Rich. Rich mwenyewe ambaye alikatiza safari yake ya kupanda juu, alionyesha kutofurahishwa na kitendo cha jina lake kuitwa hadharani. Lakini aliificha hali hii. Tayari Jacob alikuwa ameshatafuta sehemu na kukaa. Alisubiri mpaka hawa jamaa walipomaliza maongezi yao. Rich alianza kupanda ngazi kama alivyokuwa akataka kufanya awali, ilionyesha kuwa chumba chake kilikuwa kwenye orofa za juu.
Jacob alifikiria namna ambavyo angeweza kukifikia chumba cha Rich. Alisimama na kwenda mapokezi. “ Samahani dada naomba kuulizia chumba cha mwenyeji wangu” Alisema kwa dada huyu wa mapokezi huku macho yake yakiusoma uso wa dada huyo
“Anaitwa nani? Aliniuliza
“Anaitwa Rich” Jacob alisema huku macho yake yakizidi kutompa nafasi ya kuangalia pembeni huyo dada. Aliweza kuona uso wake ulivyobadilika mara baada ya kulitaja jina la Rich. Ghafula kama mtu aliyekumbuka kitu, dada huyo alibadilika na kutabasamu, tabasamu la ushawishi fulani.
“Yuko chumba namba 125 ghorofani” Alisema kisha akainama kama anayeangalia kitu. Jacob alitambua hilo lakini hakutilia maanani zaidi japo alipenda kufanya hivyo. Aliziparamia ngazi za kuelekea vyumba vilivyoko ghorofa za juu kwa mwendo wa wastani. Lakini akiwa anajiwa na hisia za hatari kadiri alivyokuwa akipanda. Alipofika sehemu ya ghorofa ya kwanza alipapasa sehemu aliyokuwa ameweka bastola yake, alipoona iko sawa alianza kupanda ngazi za kuelekea ghorofa ya pili.
Wakati akiwa ameshamaliza robo ya ngazi za kuelekea ghorofa ya pili, nywele zilimsimama. Mbele yake alikuwa yule jamaa aliyekuwa amemwangalia kwa mtindo asioutaka wakati anatoka nyumbani kwa mzee Edson. Yule jamaa alipomwona Jacob alijifanya kutokuwa na habari kabisa na yeye. Jacob kwa upande wake pamoja na kuwa alishahisi kitu lakini hakuonyesha hali yoyote tofauti wakati wanapishana. Baadaye vilisikika vishindo vyake akishuka ngazi kwa kasi zaidi. Jacob alipata hamu ya kumjua zaidi huyu jamaa lakini hakuwa na nafasi kwa sasa kwani kipaombele ilikuwa ni kwa Rich.
Tayari alikuwa ameshafika ilipokuwa korido iliyokuwa ikivigawa vyumba vilivyokuwa kwenye eneo hili la ghorofa ya pili. Baada ya kuangaza kwa muda kidogo alifanikiwa kukipata chumba namba 125. Alipofika mlangoni alitoa bastola yake na kuugonga mlango taratibu. Alipokelewa na kimya. Aligonga tena na tena mpaka pale alipoamua kujikaribisha mwenyewe. Jacob alishangaa……….
Jacob alishangaa kukuta kuwa mwenyeji aliyetarajia amkaribishe alikuwa amelala kitandani. Kulala si jambo lililomshangaza, kilichomshangaza ni muda mfupi uliotumiwa na Rich mpaka akapitiwa na usingizi mzito kiasi cha kushindwa kusikia mlango ulipogongwa. Kwa staili ya aina yake alijaribu kumwamsha ili aweze kuongea naye kama alivyokuwa amekusudia. Lakini jitihada zake zote hazikufaa kitu. Baada ya kuangalia huku na huko chumbani humo aliamua kwenda kumwamsha kwa karibu zaidi. Hapo ndipo Jacob alishikwa na mshangao uliostahili. Juu ya kitanda hicho hakuwepo Rich aliyekuwa amepanda huko muda mfupi uliopita bali alikuwepo marehemu Rich.Maiti yake yalikuwa yamefunikwa vizuri kama mtu aliyekuwa amelala. Apoifunua vizuri maiti hiyo macho yake yaligota kwenye mpini wa kisu uliokuwa unaning’inia juu ya kifua cha Rich. Mpini wa kisu hicho ulikuwa umezungushiwa karatasi moja nyeupe. Jacob alipoiangalia vizuri karatasi hiyo akatambua kuwa ilikuwa imeandikiwa. Akaichukua ili aisome maandishi yaliyokuwepo. Kabla hajaisoma aliifunua zaidi ile maiti ili kuona sehemu zaidi ya mwili wake. Jacob alitabasamu baada ya macho yake kutua kwenye tumo la maiti huyo. Sehemu ya tumboni ilikuwa na alama ambayo ilitokana na kukanyagwa na hivyo kuacha alama ya kiatu. Alama hiyo ilikuwa ya Sungura aliyefumba macho. Ilionyesha kuwa muuaji alitaka alama hiyo ionekana, kwani inaonyesha alikanyaga dimbwi la damu kisha akakanyaga tumboni kwa marehemu na hivyo kuacha alama hiyo.
“The Fuse – Max, hii kazi ya Max” Jacob alijisemea huku macho yake sasa akiyahamishia kwenye karatasi aliyokuwa ameshika. Moyo wake ulipiga kwa kasi pale alipoyasoma maandishi yaliyokuwa yameweka ujumbe kwenye karatasi hiyo. Si kwa sababu ya hofu bali hasira na kumbu kumbu zilizomjia kutokana na ujumbe huo. Ujumbe wenyewe ulikuwa hivi; Jacob na kimada wako Merina pokeeni salamu toka kwa ‘Bosi’ mwenye ‘ndevu nyeupe’ anawakumbusha kuwa ndevu zake huwa haziguswi na hazijawahi kuguswa”.
Mwili wa marehemu Rich ulionyesha kuwa alikuwa ameuawa dakika chache zilizopita. Mara moja akili na mawazo ya Jacob akayapeleka kwa yule jamaa ambaye alikuwa amepishana naye kwenye ngazi wakati akipanda kuja chumbani kwa Rich. Alijua ili kumfikia Max ilikuwa ni lazima kumpata yule mtu kwanza.
Kwa siku hiyo alikuwa amekutana na jamaa huyo mara mbili. Ya kwanza Jacob aliliona jicho lake wakati anatoka nyumbani kwa mzee Edson, ya pili ni dakika chache zilizopita wakati akipanda ngazi za hoteli hii.
Jambo moja lilimtatiza Jacob ni kuwa yule jamaa alimwacha kwa mzee Edson akiwa hana dalili zozote za kutoka, sasa ilikuwaje akakutana naye eti anashuka ngazi za majengo haya. Pili hakujua ni kwa nini aliamua kumuua Rich.
Pamoja na maswali kuwa mengi kuliko majibu, lakini jambo moja alilibaini kuwa watu hawa walikuwa hatari kuliko hatari yenyewe. Bila shaka alijua kuwa Jacob anamfuatilia Rich hivyo akaamua kumwahi kabla Jacob hajamwahi. “Lakini alinijuaje? Jacob alijiuliza pasipo kupata jibu la swali hilo. Ila aliamini kuwa kwa baadaye angekuwa nalo.
Alipoangalia saa yake ilionyesha kuwa zilikuwa zimepita dakika kumi tangu kupita muda waliokuwa wameahidiana kukutana na Merina. Alipekua chumba hicho bila kuambulia lolote la maana. Jacob akaonelea amwahi Merina, ambaye angeweza kupata wasiwasi kwa kutomuona akitokezea katika muda waliokubaliana. Alikifunga chumba na kuanza kushuka ngazi.
Alipofika mapokezi ndipo alipopata wazo la kumwangalia yule msichana wa mapokezi ambaye vitendo vyake pia vilionyesha kuwa kuna jambo lisilo la kawaida alilokuwa akilijua.
Jacob alipotupia macho sehemu ya mapokezi hakumwona yule msichana. Hapo likamjia wazo jingine, wazo la kwenda pale mapokezi na kuangalia ni nini yule msichana alikuwa akiangalia wakati alipomwuliza juu ya Rich. Alitembea taratibu mpaka sehemu hiyo ya mapokezi. Wakati Jacob anakaribia ilipokuwa meza ya mapokezi ndipo macho yake yalipogongana na alama ya soli ya kiatu yenye alama ya Sungura aliyefumba macho ikiwa sakafuni jirani na meza ya mapokezi.
“Max!!!! Jacob alinong’ona huku akiongeza tahadhari na kuuweka mwili wake katika hali ya wepesi tayari kwa lolote.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kabla hajaamua kufanya lolote alichungulia ili kuona isije ikawa yule msichana yuko ameinama. Macho ya Jacob yalishikwa na mshituko mwingine, hakuamini alichokuwa akikiona. Mwili wa msichana yule ulikuwa umelala sakafuni huku dimbwi la damu likiwa limeuzunguka. Damu ilikuwa bado ikitililika kuashilia kuwa ni sekunde chache tu zilizopita mauaji haya yalikuwa yamefanyika. Jacob aligeuka kuangalia kama kuna mtu alikuwa akimfuatilia. Watu wota eneo hilo walionekana kuwa wako katika mambo yao, hii inaonyesha muuaji alikuwa akitumia utaalamu wa hali ya juu katika kutoa roho za viumbe hawa. Kwa vile alishajua kuwa watu hawa walikuwa bado hawajapokea amri ya kumuua toka kwa huyo mkubwa wao wamwitae ‘Bosi’ ambaye Jacob hakuwa na hakika kama Max ndiye ‘Bosi’ au kulikuwa na mwingine.
Hivyo aliingia hiyo sehemu ambayo hukaa mtu wa mapokezi na kuanza kuangalia angalia. Kwa mara nyingine tena macho yake yalikutana na karatasi yenye ujumbe kama ule aliokuwa amekutana nao kwenye chumba cha Rich. Alipopekua zaidi ndipo alipoona kitu alichokuwa akihisi kukikuta ndani ya sehemu hii. Kitu hicho ni picha yake. Ndipo alipotambua ni kwa nini wakati alipomwuliza yule dada juu ya Richard aliinama na kuangalia sehemu kwanza. Kumbe alikuwa anafanya uhakika wa sura ya Jacob. Inaonyesha alikuwa ameelekezwa na mtu juu ya ujio wake.
Lakini bado aliendelea kuvutiwa na jinsi muuaji huyu alivyo na uwezo wa kutabiri na kufikiri kwa ziada, kwani alikuwa ameshahisi kuwa wenda Jacob alihisi kitu kwa msichana huyu na kwa yale ambayo angeyakuta kule chumbani kwa Rich angepata hamu ya kumuhoji dada huyo, hivyo akawa amemuwahi tena kabla Jacob hajafika.
Aliichua picha yake na kuiweka mfukoni. Badala ya kutokea sehemu ya kawaida akaona ni vema apoteze nyayo zake ambazo kwa sasa kulikuwa na kila ishara kuwa ziko mikononi mwa adui. Hivyo alipita mlango nyuma uliokuwa kwenye hicho kijichumba ambacho hukaa mtu wa mapokezi. Mlango huo ulimleta mpaka sehemu iliyokuwa na chumba kikubwa tu. Hapo alikutana na mlango mwingine ambao alipopita alijikuta yuko chooni. Chooni humo kulikuwa na milango miwili. Alichungulia nje kwa kupitia dirishani ili kuona kama angepita hapo na kutokezea nje. Naam aliweza kuiona miti iliyoashiria kuwa ulikuwa ni sehemu ya ua wa hotel hii kwa upande wa mashariki. Aliujaribu mlango na kukuta umefungwa. Kwa mchezo kidogo tu na huo mlango tayari akawa nje. Hapo aliruka ukuta na kutokezea mtaa wa pili ambapo kulikuwa na wauza viatu vya mtumba wengi.
* * *
Max na kundi la vijana wapatao watano wao waliendelea kusubiri nje ya hoteli hiyo ya Annex by night. Walikuwa na hakika kuwa mpelelezi waliyekuwa wakimtafuta sana, Jacob Matata lazima angetoka kwa kupitia mlango huo wa kawaida. Walikuwa wameshaandaa vijana wenye shabaha kwa ajili ya kummaliza Jacob.
Kama walivyokuwa wamefikiria, kitisho walichokuwa wametoa pamoja na mauaji waliyokuwa wameyafanya yalisababisha jambo. Jambo hilo walikuwa wakiombea litokee na lilikuwa limetoke. Wakuu wengi wa usalama wa nchi za ukanda huu walikuwa wametuma wapelelezi wao ili kuona ni nini kilikuwa kikiendelea katika jiji hili la Arusha.
Max kwa kushirikiana na kundi la vijana wake makomandoo na maninja walikuwa wmeshafanikiwa kuua na kukamata baadhi ya wapelelezi hao. Hii ingepelekea wao kupata fedha nyingi kama malipo toka kwa mabwana zao huko Ulaya ambao ndiyo walikuwa wamewaamuru kuwamaliza wapelelezi hao kwanza.
Kuna wapelelezi wachache ambao bado walionekana kuwa kikwazo kwa kazi yao hiyo ya awali. Mpelelezi Jacob Matata alikuwa mmoja wao. Kwani licha ya kupata taarifa za ujio wake na sehemu ambayo angefikia lakini watu hawa kila walipotaka kumtia mkononi Jacob aliwaponyoka katika njia za kutatanisha. Kwanza ilikuwa ni siku ile aliyofika tu Arusha, Max alituma watu kumpokea. Kweli walifanikiwa kumwona na kulifuatilia gari lililokuwa limembeba. Cha kushangaza ni namna dereva wa gari alilopanda alivyofanikiwa kuwapoteza.
Pamoja na kuwapoteza, lakini kwa kutumia vijana wake aliokuwa amewatapanya mji mzima alifanikiwa kujua kuwa mpelelezi Jacob Matata alikuwa amefikia Mlimani hoteli. Hapo alituma watu ili kummaliza usiku huo. Taarifa za kuwa Jacob hakuwepo na chumba kilikuwa wazi zilimshangaza pia.
Taarifa za Jacob kulala Paradiso hoteli zilimfikia Max asubuhi hii. Hapo alituma watu kumsubiri nje ya hoteli hiyo ili kummaliza. Walisubiri atoke lakini hawakumwona, kwani kwa kutumia vifaa alivyokuwa ameletewa na yule mzee dereva Jacob alikuwa ameshabadilisha sura. Hivyo jamaa kuona hivyo hasira zao wakamalizia kwa mzee Edson ambaye naye alikuwa hotelini pale akimsubiri Jacob Matata.
Max alipata taarifa za Jacob kwenda nyumbani kwa Mzee Edson kule Njiro. Hapo akamtumia Richard kama chambo ili kuweza kupata Jacob. Kweli Richard alifanikiwakuigiza kiasi kuwa alifanikiwa kuteka hisia za mpelelezi Jacob Matata. Lengo ilikuwa ni Jacob aanze kumfuatilia Richard.
Hivyo wakati Richard na Jacob wanatoka na kuanza kufuatana kuja hapo Annex hoteli, Max na vijana kadhaa waliwatangulia. Wakaenda kumsubiri Richard chumbani kwake namba 125 ghorofa ya pili. Ndiye aliyemwua Richard na kuwahi kutoka.
Sasa walikuwa wakisubiri Jacob atoke ndani yo hoteli hiyo ili wammalize. Hawakuwa wanajua kuwa Jacob alikuwa ameshatoka nje ya hoteli hiyo kwakutumia njia za panya. Waliendelea kusubiri wakiwa tayari kwa mapambano.
Jacob Mwenyewe aliyekuwa akisubiriwa, mara baada ya kuwa ameshafanikiwa kutoka hotelini hapo alitembea kwa miguu mpaka alipofika hoteli 77 na kukodi taxi. Alifanya hivyo akijua fika kuwa gari alilokuja nalo lingekuwa limeshawekewa mtu wa kuufuatilia.
“Nipeleke Oldongei Hotel haraka” Jacob alisema huku akijikung’uta kwa vile nywele zake zilichafuka wakati alipokuwa akiruka ule ukuta wa miti.
“Shilingi elfu nne tu baba angu” aliongea dereva huyo katika rafudhi ya kichaga. Jacob hakumjibu. Akaondoa gari.
Alipofika alikuta Merina kishasubiri sana na kuanza kuingiwa na wasiwasi. Alipomwona kidogo amkumbatie kwa furaha lakini akajiziuia. Baada ya kuwa ameketi Jacob alimsimulia yote yaliyokuwa yametokea. Pia hakusita kumpa salamu toka kwa ‘Bosi’.
“Wamejuaje? Merina Aliuliza huku akionekana kutotishwa kabisa na salamu toka kwa ‘Bosi’
“Hilo ni swali ambalo mimi na wewe kwa sasa hakuna anayeweza kuwa na majibu muafaka, ila ili kufikia jibu sahihi kazi ya ziada inatakiwa. Maana adui zetu wanaoneka wametujua haraka wakati sisi hatuwajui kabisa. Kwa hali hii itakuwa ngumu sana kwetu kufanya kazi. Kwani kama wamediriki kumpa yule msichana wa mapokezi picha yangu hawatasita kuwapa vijana wao wote picha kama hiyo na kuwaamuru kunisaka popote”Jacob alisema huku akiziangalia mboni za macho ya Merina.
“ Kwa hiyo unashauri vipi maana hakuna namna ya kufanya zaidi ya kupambana nao. Katu hatuwezi kuwakimbia”. Alisema Merina katika hali ya kuweka wazi msimamo wake na kujitoa mhanga katika kasheshe hili.
“Kwa sasa nina imani kuwa watakuwa wameshasambaza vijana wao karibuni hoteli zote na sehemu zote muhimu ambazo wanahisi mimi na wewe tunaweza kuwa au kutembelea. Hatuwaogopi, lakini tatizo ni kuwa wao kila mara ndiyo watakuwa wanakuwa wa kwanza kutuona na kulenga mashambulizi na sisi tutakuwa tunawatambua pale tu mashambulizi ya yanaposhindwa. Hii ni kujihatarishia maisha katika mazingira ya kijinga sana. Hivyo kuna mahali itabidi tukalale usiku huu. Huko tutatengeneza sura za bandia na kesho tutakuwa watu wengine kabisa. Hii itatuwezesha kuwasaka hawa watu huku wao wakiwa hawatujui kama sisi tusivyo wajua hii ndiyo itakuwa fair game ” Merina alikuwa akiyasikiliza maongezi na mipango ya Jacob kwa makini. Hakuwa na hata moja la kupinga.
* * *
Saa mbili za usiku tayari Jacob na Merina walikuwa ndani ya nyumba moja ya wastani nje kidogo ya jiji la Arusha. Wote walikuwa sebuleni wakiangalia televisheni na kuzungumza hili na lile. Upande mwingine wa chumba kulikuwa n mzee mmoja aliyeonyesha dhahiri kuwa alikuwa amezama katika kazi aliyokuwa akiifanya.
Mzee huyo ndiye mmiliki wa nyumba hii. Ndiye yule aliyempokea Jacob Matata wakati alipofika Arusha. Huyu ndiye aliyekuwa amekabidhiwa jukumu la kuwa msaidizi wa Jacob kwa muda wote wa operesheni hii. Jacob alivyouona upepo wa mambo aliamua kumtafuta mzee huyu ili awatafutie sehemu salama ya kulala usiku huo ambao walikuwa na hakika kuwa adui alikuwa ametanda kona zote kuwatafuta.
Pamoja na kutaka sehemu salama ya kupumzika, lakini Jacob pia alimpa mzee huyo kazi ya kuwatengenezea sura bandia ili kesho yake waonekane watu wengine mbele ya macho ya adui.
Baada ya mvutano kidogo hatimaye ilikubaliwa kuwa Jacob na Merina walale vyumba tofauti. Mzee huyo ndiye aliyeonekana hasa kuwa na msimamo huo. Baada ya kupata chakula cha usiku huo walikaa katika hali ya kupanga hili na lile. Usiku ulipozidi sana Merina alikuwa wa kwanza kuaga kuwa anaenda kulala baada ya usingizi kuwa umemlemea.
Baada ya Merina kwenda kulala, yule mzee alimwambia Jacob kuwa kulikuwa na maagizo toka Dar es salaam makao makuu ya upelelezi ya ‘Ofisi Fukuzi’. Aliposema hivyo, mzee huyo aliingia ndani na kutoka na vifaa fulani. Akaanza kuviunganisha kama mtu aliyekuwa akifanya mchezo fulani. Baaya muda fulani mlio kama wa redio ulisikika. “Ok sasa chukua uende nayo chumbani kwako maana mkurugenzi, Bi. Anita anahitaji kuongea na wewe” Alisema mzee huyo huku akikabidhi vifaa hivyo kwa Jacob ambaye alivipokea na kuelekea navyo chumbani.
“Pamoja na hayo uliyofikia lakini unatakiwa kuwa makini zaidi Jacob,maana mji huo kwa sasa uko katika patashika kubwa. Nimepata taarifa toka kwa wakuu wa usalama wa nchi kadhaa wa eneo hili kuwa walikuwa wametuma wapelelezi wao Arusha, lakini la kushangaza ni kuwa wapelelezi hao wameuawa kikatili sana. Hivyo wewe ni miongoni mwa wapelelezi ambao nchi hizi kwa sasa zinawategemea ili kufichua nini kinaendelea ndani ya mji huo. Silaha zinazotumika kuwaua wapelelezi hao ni za kisasa mno kiasi inatisha sana. Jambo lingine linalo tushangaza ni namna watu hawa wanakuwa wepesi kupata taarifa juu ya nyie wapelelezi wetu. Hivyo sishangai kusikia kuwa walikuwa wameshajua kuwa upo Arusha……………” Hiyo ilikuwa ni sehemu ya maelezo ya mkurugenzi wa ofisi pekuzi Bi. Anita kwa mpelelezi Jacob Matata. Muda wote huo Jacob alikuwa kimya akisikiliza maelezo hayo ya Bi. Anita. Baada ya kutoa malezo yake Jacob alifunga hicho kifaa na kwenda zake kulala.
* * *
Wakati huohuo ambao Jacob alikuwa anaongea na Bi. Anita mkuu wa ofisi pekuzi, upande mwingine mambo yalikuwa yamepamba moto. Max kiongozi wa genge lililokuwa na kazi ya kufanya unyama wa kutisha ndani ya jiji la Arusha alikuwa ameshikilia simu yake. Hapa alikuwa na hasira iliyochanganyika na aibu. Hii ni baada ya kuwa wameachwa kwenye mataa na mpelelezi Jacob Matata pale hoteli ya Annex. Wakati huo alikuwa ndani ya chumba mojawapo ya vyumba katika jumba moja la kifahari ambalo walikuwa wamepewa kufanyia kazi zao.
“kwa hiyo unasema kuwa kesho hatakuwa Jacob yule tuliyemzoea, atakuwa katika sura ya bandia? Alidadisi Max mara baada ya kupata taarifa za Jacob kubadilisha sura yake toka kwa moja ya watu wa karibu na Jacob.
Asubuhi ya siku iliyofuata wote waliamka mapema sana. Jacob aliwahi zaidi na kufanya mazoezi, kisha akaenda kumwamsha Merina.
Walipomaliza kupata kifungua kinywa, kila mmoja wao alichagua sura ambayo angeivaa. Waliporidhika na jinsi kila mmoja wao alivyokuwa amejibadirisha walitoka tayari kwa safari ya kurudi mjini ambapo alikuwa wakipaona kuwa ndiyo uwanja wa mapambano.
“Jacob kuwa makini na nguo ulizovaa nina mashaka nazo!! yule mzee alimwambia Jacob wakati wakiagana. Jacob alimwelewa maana hiyo ilikuwa ni lugha ya kikachero zaidi.
“Itabidi chakula cha mchana tukale pale hotel ya annex. Bila shaka tunaweza kupata lolote pale. Maana mlengwa wetu wa kwanza atakuwa ni yule jamaa ‘kipara’. Bila shaka anajua mambo mengi katika Patashika hili”. Jacob alisema huku akimwangalia Merina kupitia kwenye kioo cha mbele. Walikuwa ndani ya gari kuelekea mjini.
Walipoingia ndani ya hotel hiyo ya Annex ambayo imefanyiwa uarabati mkubwa siku za karibuni walionekana kama watu wa makamu ambao walikuwa kama mtu na mke wake. Hotel hii ni ya kawaida tu. Walipita na kwenda kuchagua sehemu ambayo wangeweza kuwaona kila waliokuwa wakiingia na kutoka katika hotel hii. Waliagiza chakula na kuanza kula huku kila mmoja akiwa makini katika kuchunguza nyendo za kila aliyekuwa akiingia katika hotel hii. Eneo hili na hotel yote kwa ujumla ilikuwa na watu wengi tofauti na nilivyotarajia. Jacob alidhani kuwa vifo vile vya mkupuo na kinyama ambavyo anajua fika vilikuwa vimefanywa na ‘mzee mwenye kipara, vingesababisha watu waogope hotel hiyo. Lakini inonyesha huduma nzuri za hotel ndizo zilizowafanya watu washindwe kujizuia kuja kujiburudisha na kupumzika mahali hapo.
Walimaliza kula, wakaongea wakachoka, wakapanga mambo mbalimbali wakamaliza lakini si mzee mwenye kipara wala yeyote wa kuhisiwa aliyeingia ndani ya hotel hii. Wote walioingia walionekana kuwa na shughuli zao za kawaida tu.
“Nadhani ni muda muafaka wa kuangalia ni wapi tupange vyumba kwa ajili ya makazi yetu hapa Arusha. Hatuwezi kutumia vile vyumba tulivyokuwa tunatumia awali kwani bila shaka kutakuwa na watu wanaosubiri ili kutumaliza nasi hatuwajui. Ila kwa vile sasa hatuko katika sura zile walizokuwa wanazifahamu tunaweza kufanya kazi kwa urahisi zaidi”. Jacob ailisema kwa tuo.
“sawa ila safari hii sitapenda kuwa hoteli tofauti na wewe, tukitofautiana vyumba tu haitakuwa mbaya sana…”
“haitakuwa mbaya sana ila itakuwa mbaya kidogo? Jacob ailimdakiza Merina kabla hajamaliza kauli yake. Badala ya kujibu Alitabasamu, tabasamu la nusu aibu nusu mwitikio.
“sawa bibie hata kama utataka tutumie kitanda kimoja haitakuwa mbaya, mie sina tatizo ni wewe tu. Sasa unapendekeza hoteli gani itafaa kukuhifadhi mrembo kama wewe na wakati huohuo nisinyang’anywe na wajanja wa mji huu? Jacob ailisema huku mkono wake ukichezea ule wa Merina juu ya meza waliyokuwa wameizunguka. Merina hakujibu kitu bali alimwangalia Jacob kwa macho ya nusu kukaribisha nusu kuuliza, lakini Jacob hakufanikiwa kupambanua kati ya mambo hayo mawili pale aliposema “Ok Jacob ni wakati mzuri wa kwenda, nafikiri Moivalo hoteli itafaa sana kukuhifadhi mbabe kama wewe”
Kwa njia tofauti tofauti wote walichukua vyumba katika hoteli ya Moivalo. Hoteli hii iko nje kabisa ya mji wa Arusha. Chumba cha Jacob kilikuwa upande wa kaskazini wakati kile cha Merina upande wa kusini. Baada ya kila mmoja kupanga chumba chake kata mtindo alioutaka walikutana ndani ya chumba cha Jacob.
“ Mie naona tuanze upelelezi wetu usiku wa leo kwa kuzungukia kwenye kumbi mbalimbali za starehe. Bila shaka tunaweza kupata harufu ambayo inaweza kutufikisha jirani na watu tunaowatafuta”. Merina ambaye wakati huu alikuwa amekaa kwenye moja ya makochi yaliyokuwa ndani ya chumba hicho alitoa mapendekezo yake.
“Hata mimi nilikuwa nafikiria hivyo, kwa vile hatuna sehemu ambayo tunaweza kumpata yule ‘mzee mwenye kipara, basi ni vema tukajaribu kumwinda katika sehemu ulizozitaja”. Jacob alisema na wote wakakubaliana na mpango huo. Hivyo Merina akaelekea chumbani kwake kwa maandalizi tayari kwa lolote usiku huo.
Saa mbili ya usiku iliwakuta wako ndani ya gari wakielekea Club Triple A, waliadhimia waanzie hapo. Walipofika waliingia ndani na kutafuta sehemu ya kukaa. Safari hii Jacob na Merina walionekana vijana walioneemeka. Hata kama angekuja mmoja wa wazazi wao asingeweza kuwatambua. Ukumbi ulikuwa umefurika watu wa rika mbali mbali japo vijana walionekana kuwa wengi zaidi.
Macho ya Jacob na yale ya Merina yalikuwa katika kazi ya kuchunguza na kutofautisha watu mbalimbali katika ukumbi huu ambao ni moja ya kumbi nzuri na za kisasi katika mji wa Arusha.
Wakati mambo yakiwa ndiyo kwanza yanapamba moto, mara Jacob akamwambia Merina “naomba nikuache kidogo baada ya kama dakika kumi nitakuwa hapa” alimwaga Merina huku akiinuka bila kumpa nafasi ya kuuliza alikokuwa anaelekea.
Alitoka nje ya ukumbi na kuingia ndani ya gari tayari kwa kuondoka. Aliiondoa gari kwa kasi. Mpaka alipofika barabara ya sokoine ndipo alipokumbuka kupapasa bastola yake. Alifanya hivyo kwani aliona hisia za hatari zikizidi kumnyemelea.
Aliendelea na uhuru road huyo akazunguka ‘keep left’ ya nazi na kuchua barabara ya nyerere tayari akawa anaikaribia Impala hotel. Japo lengo lake ilikuwa ni kuingia Paradiso Hoteli, lakini hakusimama hapo. Alipitiliza kama anataka kwenda AICC majengo, hapo mbele kabla hajafika daraja la Bethel alikata kulia na kuingia kituo cha kunyweshea mafuta. Alijifanya kana kwamba alikuwa na shida ya mafuta. Mhudumu alipomaliza kuweka kiasi alichokuwa amemwambia alitaka kuondoka, hapo ndipo akamwita.
“ Hallo nahitaji kuacha gari langu hapa kwa dakika kadhaa”. Kabla hajajibu Jacob aliongeza “ Kuna Shilingi elfu tatu kwa kuniangalizia kwa muda huo”. Hapo uso wake ulibadilika tofauti na hapo hawali. “Sawa kaka‘angu ila jitahidi kwa maana hapa hairuhusiwi kupaki magari ofyo ofyo” Alijibu jamaa huyo katika lafudhi ya kichaga. Alisogeza gari pembeni na kuiegesha hapo.
Alishuka, baada ya kuhakikisha kuwa milango yote ilikuwa imefungwa sawasawa alianza kupiga hatua kurudi Paradiso hoteli ambayo alikuwa ameipita umbali mdogo toka ilipo gereji hii. Hii ndiyo ile hoteli aliyofikia kwa mara ya kwanza juzi alipofika Arusha. Hakulala hapo kwa sababu alizozijua yeye, japo alichukua chumba hapo.
Aliingia ndani ya hoteli hiyo bila wasiwasi wowote kama ilivyokuwa kwa wateja wengine. Huku akijua fika kuwa hata angekutana na mtu yeyote anayemfahamu sana asingeweza kumtambua, Jacob alianza kutembea ndani ya maeneo mbalimbali ya hoteli hiyo. Baada ya kuwa amezunguka kwa muda mrefu bila kupata lolote, ndipo akaamua aende kutembelea chumba alichokuwa amepanga. Bado alikuwa na funguo za chumba hicho. Lakini aliamua kutembelea chumba hiki kwa mtindo wa aina yake. Kwa vyovyote vile alihisi kuwa kutakuwa na watu waliopewa kazi ya kufuatilia na kuona pindi akiingia na kutoka chumbani humo.
Alienda mapokezi. “Anti naomba uniletee vinywaji na nyama choma chumba namba 98, funguo hizi hapa nenda ukaniwekee mie nitavikuta”. Jacob alisema huku akimkabidhi mhudumu huyo funguo za chumba. Baada ya kumkabidhi Jacob alijifanya kana kwamba anatoka nje.
Alienda kubana mahali ili kutoa nafasi kwa muhudumu huyo aende kumpelekea vitu alivyoagiza. Alisubiri muhudumu huyo aanze kwenda. Mpaka pale alipomwona akipanda juu ndipo naye alipoanza kumfuatilia kwa makini na hadhali.
Kwa namna ya uficho na ujuzi mkubwa aliweza kufuatana na yule kijana mpaka pale alipoingia ndani ya kilichokuwa chumba chake kabla ya kifo cha mzee Edson. Alikuwa umbali wa kama hatua ishirini na tano hivi toka mlangoni. Kwa jinsi alivyokuwa yeyote asingeweza kudhani alikuwa anaelekea wapi. Hakuwa katika safari ya kupanda juu wala kushuka chini, hakuwa ametulia wala hakuwa na purukushani. Alikuwa katika staili aliyoijua mwenyewe na ambayo si rahisi kuielezea.
Alikaa katika hali hiyo ili kuona kama kuna mtu ambaye angewashwa kuona yule muhudumu akiingia mle ndani. Muda ulipita bila kuona ishara yoyote ya mtu aliyekuwa akifuatilia chumba kile. Baada ya kusubiri kwa muda mrefu na huku usiku ukizidi kupamba, akakata shauri asogee karibu zaidi na mlango wa chumba.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kama mtu anayetafuta chumba na asiyekuwa mwenyeji hapo ndani, mpelelezi Jacob alianza kupiga hatua taratibu kuelekea ulipokuwa mlango wa chumba hicho. Hakuwa amepiga hata hatua tatu mara akasikia vishindo vya mtu akija nyuma yake. Haraka sana akageuka kwa chati ili kuona ni nani aliyekuwa anakuja upande huo. Macho yake yaligongana na mama mmoja nadhifu. Kwa mwonekano alionekana kuwa ni mmoja wa wateja wa hoteli hii tena asiye na hatari yoyote. Hivyo Jacob Matata aliendelea na hatua zake za taratibu wakati huo mama yule alikuwa akipishana naye. Alionekana kuwa mgeni kwa jinsi alivyokuwa akiangalia namba za kila mlango.
Jambo moja Jacob Matata hakuwa na hakika nalo, nalo ni juu ya yule muhudumu. Hakumbuki kumwona wakati alipotoka ndani ya chumba alichokuwa amemwagiza vinywaji na nyama choma. Kutoka na mawazo yake kuwa katika umakini wa hali ya juu, hakutoa nafasi kwa kumbukumbu zake kutunza taarifa za kutoka ama kutokutoka kwa yule muhudumu.
Alipofika usawa wa mlango wa chumba chake hicho, kama kawaida alijifanya kana kwamba anaangalia namba ya mlango wa chumba hicho. Masikio, macho na ufahamu wake vilikuwa katika kutaka kujua kama kulikuwa na mtu ndani. Baada ya kusikiliza kwa makini, haikuonekana dalili yoyote ya kuwamo mtu mle ndani. Hakuingia, alipitiliza mpaka upande mwingine wa vyumba vya upande huo. Alipohakiki kuwa hakukuwa na mtu aliyekuwa akimfuatilia, alirudi kwa haraka na kwenda moja kwa moja kuingia ndani ya chumba.
Kichefuchefu, huruma, na hasira vilimshika kwa pamoja mara baada ya kuwa ameingia ndani ya chumba hicho. Aliyoyakuta ndani ndiyo yaliyomfanya kuwa hivyo. Mle chumbani kulikuwa na mwili wa yule mhudumu aliyekuwa amekuja kuleta chakula. Alikuwa ameuawa kikatili kiasi cha kutisha. Damu ilikuwa bado ikichuruzika katika majeraha ambayo yalikuwa yameshaichukua roho yake muda mfupi ulipita.
Haraka haraka Jacob akajaribu kufikiri huyu muuaji alikuwa amepitia wapi. Kwani tangu huyo muhudumu alipoingia ndani ya chumba hicho yeye Jacob alikuwa eneo hilo.Hakuna mtu yeyote aliyekuwa amepita kuja kwenye vyumba hivi zaidi ya yule mama nadhifu. Wakati bado anajiuliza maswali hayo, ndipo macho yeka yalipoiona kamba iliyokuwa imefungwa dirishani. Alisogea mpaka karibu na dirisha la chumba hicho.
Sehemu ndogo ya dirisha hilo ilikuwa imebomolewa, na kamba ilikuwa imefungwa kwenye moja ya nondo za dirisha hilo. Kamba hiyo ilikuwa ndefu sana, Jacob alipochungulia ili kuona ilipokuwa imeishia alibaini kuwa ilikuwa imefika chini kabisa ya jengo hilo la hoteli ya paradiso.
Hakuona umuhimu wowote wa kuendelea kuwepo ndani ya chumba hicho ambacho kilikuwa kina kila aina ya harufu ya mauti. Kwa makini sana alitoka na kuanza kunyata mpaka alipofikia mlango wa kutokea eneo hili. Alijipenyeza kwenye kona moja na kutokezea upande mwingine, hapo badala ya kutokezea mapokezi alipita kwa nyuma na kutokezea upande kulipokuwa na wanawake wengi na wanaume wachache. Hawa walionekana kukazana katika kazi ya mapishi, bila shaka hapa ndipo ilipokuwa sehemu ya jiko. Bila kuonyesha wasiwasi wowote Jacob alipita eneo hilo na kuingia sehemu iliyokuwa imeandikwa kuashilia kuwa ndipo palipokuwa na vyoo.
Alijifanya anaingia chooni, kisha akapitia mlango wa nyuma na kutoka nje. Alisimama sehemu fulani kana kwamba alikuwa anasubiri mtu. Alikuwa ameshangazwa na jinsi hawa jamaa vibaraka wa ‘bosi mwenye ndevu nyeupe’ wasivyokuwa na woga katika swala zima la kutoa roho za watu. Kuna kitu kilikuwa kinamjia katika akili yake kumuhusu yule mama aliyepita. Mazingira ya kifo cha huyu muhudumu yalionyesha wazi kuwa yule mama nadhifu alikuwa amehusika. Nitamwona wapi? Hilo ndilo swali ambalo lilimfanya akose raha.
Alitembea taratibu mpaka alipotoka ndani ya hua wa hoteli hiyo. Hapo nje aliangaza macho huku na huko. Kisha akaanza kutembea kuelekea kwenye gereji ambapo alikuwa ameegesha gari yake.
Alipofika ndani ya gari Jacob alionelea ampigie simu Merina ili kumwambia kuwa asingerudi wakati huo, na kuwa aendelee kuangalia kama kuna lolote ambalo angeona linawafaa katika shughuli yao. Hakumwambia alikokuwa amekusudia kwenda, maelezo kuwa angetamtaarifu yote wakati atakapokuwa amerudi.
Mara baada ya kuwa ameshamlipa yule mlinzi hela yake aliwasha gari moto na kuondoka. Alishika barabara ya Njiro tayari kwa safari ya kuelekea nyumbani kwa marehemu mzee Edson. Kwa vile msiba bado ulikuwa unaendelea Jacob alitarajia kukuta watu wengi. Hakuwa na jambo jingine la kufanya usiku huo zaidi ya kazi ya kunusanusa.
Alifika nyumbani kwa marehemu mzee Edson majira ya saa nne usiku. Kama alivyotarajia watu walikuwa bado ni wengi. Bia zilikuwa zikinyweka huku mchezo wa karata ukiwa umeshamiri. Alitafuta sehemu ya kukaa. Alipotulia macho yake yakaanza kazi ya kumtafuta mtu mmoja tu naye si mwingine ila mzee kipara.
Alikaa hapo kwa muda kama wa saa moja na nusu. Saa tano na dakika arobaini na tano usiku, akawa amekata shauri kuondoka. Wakati anasimama ili kuondoka, macho yake yaligongana na sura fulani. Kwa usiri mpelelezi Jacob alimwangalia huyu mtu, alikuwa ni yule mama nadhifu aliyempita karibu na mlango wa chumba chake muda mfupi kabla ya mauaji ya yule muhudumu wa Paradiso hoteli.
Mama huyo alionekana kuwa mwenyeji sana hapo msibani, kwani mara kwa mara alikuwa akiingia ndani na kutoka. Mara chache alionekana akiangaza macho yake hapa na pale. Kwa mtu wa kawaida tu asingeweza kuona dosari yoyote kwa mama huyu. Lakini macho ya mtu kama Jacob yaliyokuwa yakimwangalia kwa kuibia yaliweza kuona dosari katika macho ya huyu mama. Japo alionekana kuwa mchangamfu kwa wageni lakini bado hakuweza kuficha wasiwasi aliokuwa nao. Hii ilidhihirika wakati fulani simu yake ya mkononi ilipoita. Alikimbia na kuelekea upande wa nyuma wa nyumba ili kupokea simu hiyo. Sehemu aliyokuwa amesimama ilikuwa karibu kabisa na ilipokuwa choo iliyokuwa ikitumiwa na wanaume.
Kwa haraka lakini si kwa kiasi cha mtu kugundua Jacob alisimama na kuanza kuelekea kilipokuwa choo hicho. Hata wakati anampita mama huyo hakumshitukia bali aliendelea na maongezi yake kama kawaida.
“Najua kuwa ‘mtakatifu wa kuzimu’ atakuwa anataka habari kamili juu ya hazina hiyo, hivyo mtumie taarifa ‘bosi mwenye ndevu nyeupe’ kuwa ‘malaika wa giza’ amesema wamesharudi na kufikia kesho atakuwa ameshatupa ramani ya kuifikia hazina. Asiwe na wasiwasi kwani ‘malaika wa giza’ amefanikiwa kwa kiasi kikubwa” Alisema huyo mama kumweleza mtu wa upande wa pili. Baada ya kumsikiliza mtu wa upande wa pili, mama huyo akasema tena. “ Mwambie sisi tupo hakuna wa kugusa ndevu zake, na najua kwa kazi hii ‘matakatifu wa kuzimu’ atatupandishia dau” Alipofika hapo alicheka na kukata simu.
Sasa Jacob Matata aliona wasiwasi wake juu ya huyo mama ulikuwa sahihi. Kwani moja kati ya majina yao ya siri aliyokuwa akiyataja hayakuwa mageni kwake.Huyu mtu aliyemtaja kwa jina la ‘bosi mwenye ndevu nyeupe’ Jacob alikuwa ameshapata barua mbili za vitisho toka kwake.
Mtu huyu ndiye aliyejitaja kuwa alikuwa nyuma ya mauaji ya Rich na dada wa mapokezi katika hoteli ya Annex. Kwa madai yake anasema alifanya hivyo ili kumfikishia salamu mpelelezi Jacob Matata.
Lakini kuna majina mawili mapya aliyoyasikia Jacob. Hakuwa anajua kuhusu ‘Mtakatifu wa kuzimu’ na ‘malaika wa giza’. Kwa jinsi inavyoonyesha huyu wanayemwita ‘mtakatifu wa kuzimu’ ndiye bosi wao, ndiyo maana wanasema bosi mwenye ndevu nyeupe anataka taarifa ya kumpa mtakatifu wa kuzimu.
Mpaka alipohakikisha kuwa huyo mama alikuwa ameondoka hapo nje, Jacob alitoka chooni ambamo hata hivyo hakuwa amejisaidia, lengo lake halikuwa hilo. Huku akijifanya kutengeneza suruali yake alitoka chooni na kurudi sehemu aliyokuwa amekaa hawali. Alianza kufikiria namna ambavyo angeweza kupata nafasi ya kumuhoji huyu mama.
Mara simu yake ya mkononi iliita.
“Nani na una nini? Jacob liuliza
“ Merina, vipi mbona kimya? Ulijibu upande wa pili ambapo alikuwa ni Merina
“ Nafikiri tutaonana kesho maana wakati huu kuna kitu nafuatilia” Jacob alijibu katika sauti iliyoonyesha kuwa hakuwa tayari kwa maongezi zaidi.
“ Sawa lakini ningependa kampani yako usiku huu” Merina alisema katika hali ya mzaha, lakini alikuwa akimaanisha.
“Hamna taabu kama nitawahi basi nitafika wakati wowote” Jacob alisema huku kwa mbali akifurahia mwaliko huo wa Merina. Aliiweka simu mfukoni na kuendelea kukaa katika hali ile ya utulivu.
Muda kidogo yule mama akiwa akiwa amebeba mkoba wake, alitokeza. Alionekana kama mtu aliyekuwa anataka kutoka. Macho ya wasiwasi yalikuwa bado yako usoni kwake. Jacob alikata shauri afuatane naye ili kujua ni wapi alikuwa akielekea.
Alimwacha mpaka alipotoka ndipo na yeye akaingia ndani ya gari na kuanza kumfuata.
Safari yao iliishia Moivalo hoteli. Jacoba alijikuta anakuwa na hamu ya kujua ni nini kilikuwa kimemleta huyu mama hotelini hapa usiku huu. Hii ilitokana na kuwa hoteli hii ndiyo ambayo yeye Jacob na Merina walikuwa wamechukua vyumba. Jacob alijua kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa Merina angekuwa ndani amejipumzisha.
Mara moja akahisi labda watu hawa wamejua juu ya kuwepo kwao katika hoteli hii. Kama ndivyo basi hii ilimaanisha kuwa kuna mtu wa karibu sana anayewapa habari kuwahusu. Hapo tena Jacob akakumbuka ushauri wa yule dereva mzee kuwa anatakiwa kukagua mavazi yake.
Kwanza alitaka kumtaarifu Merina juu ya ugeni huo lakini alisita. Kwa vile hakuwa na uhakika wa yote aliyokuwa akifikiria, aliamua kuacha ili asimtie kiwewe mrembo huyo ambaye bila shaka alikuwa akimsubiri chumbani.
Wakati huu tayari Jacob alikuwa amesimama sehemu ya uficho kidogo ili kuweza kuona chochote ambacho kingefanywa na yule mama nadhifu.
Alipotoka ndani ya gari alisimama nje huku akiwa ameegemea gari hiyo kwa mbele. Alitoa simu na kuanza kuongea maneno ambayo hata hivyo Jacob hakuweza kuyasikia kwa vile mama huyo alikuwa akiongea kwa sauti ya chini na Jacob alikuwa mbali kidogo. Baada ya kumaliza kuongea na simu, mama huyo alitulia tuli kana kwamba kuna mtu au kitu alikuwa anasubiri.
“Hizi kazi zetu hizi hukufanya mtu kuwa kama kichaa kwa kufuatilia watu usiojua undani wao” Mara Jacob alikumbuka maneno ya mmoja wa waalimu wake wa saikolojia katika mambo ya ujasusi. “Pia inabidi uwe mvumilivu ili kupata unachokitarajia toka kwa yule unayemfuatilia. Maana haraka inaweza kukufanya usipate unachotaka na wakati huohuo kuhatarisha maisha zaidi” Falsafa hiyo ya mwalimu wake huyo ilimfanya Jacob aendelee kubana mahali hapo huku mbu wakizidi kimsheherekea.
Baadaye alitokezea jamaa mmoja ambaye alikwenda mpaka alipokuwa amesimama yule mama nadhifu. Watu katika eneo la nje la hoteli hii walikuwa wameanza kupungua. Wengi walikuwa wameondoka ama kwenda kulala kwa waliokuwa wamekodi vyumba katika hoteli hii au makwao kwa wenyeji wa mji.
Yule jamaa alipofika kwa mama nadhifu waliongea kwa sauti za kunong’ona. Baadaye yule jamaa aligeuka na kuanza kuelekea ndani ya hoteli, hapo Jacob alipata fursa ya kuiona sura yake. Haikuwa sura ngeni, alikuwa ni yule mzee mwenye kipara. Mara moja Jacob akajua kazi ipo akahisi hatari. Maana mara zote ambazo amebahatika kukutana na mzee huyo, lazima roho ya mtu iondoke. Alikuwa ni mtoa roho mzuri sana.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment