Sehemu Ya Nne (4)
***
HASSANI mdogo wake Badi ndiye aliyekuwa wa kwanza kumkuta Badi akiwa amelala sakafuni huku akiendelea kutokwa na damu kichwani.
“Kaka!” Hassani aliita baada ya kuingiwa na mshtuko wa kumwona Badi amelala sakafuni. Moja kwa moja akatambua kaka yake amekufa!
Akapiga goti na kumwinua Badi huku akimtingisha, lakini alipokiona kichwa cha kaka yake kikiangukia nyuma kuonyesha kuwa shingo yake haikuwa na mhimili wa kujizuia na wakati huohuo hakukuwa na dalili zozote zinazoonyeshwa na Badi kuwa yupo hai, Hassani alijikuta akianza kuchanganyikiwa. Akamrudisha kaka yake sakafuni kwa haraka kidogo lakini kwa uangalifu, kisha aliinuka na kukimbilia barabarani kuangalia kama kungekuwa na jirani yeyote aliyejitokeza au mpita njia. Akawaona wanaume wawili ambao hakuwatambua vizuri wakiongozana na Hija kwa mwendo wa kasi kuelekea alikosimama.
“Hassani vipi?” mmoja wa watu alimuuliza Hassani baada ya kukamribia.
Hassani akawaona vizuri, walikuwa ni majirani zao, akamwona mmoja akiwa amekamata bastola mkononi.
“Wamemuua kaka!” Hassani alisema kwa sauti inayokaribia kulia.
“Mungu wangu!” Hija alikuwa wa kwanza kutaharuki.
Wale wanaume wawili wakaangaliana usoni.
“Yuko wapi?” mmoja aliuliza.
“Amelala pale chini karibu na gari,” Hassani alisema huku akitangulia kuelekea kwenye gari.
Hija aliyeonekana kupatwa na baridi ya ghafla, akiwa na watu aliokuja nao, walimfuata Hassani huku akionekana kushikwa na kihoro.
Walimkuta Badi palepale alipoachwa na Hassani akiwa hatikisiki. Pembeni mwa kichwa chake kulionekana dimbwi la damu na koti lake jeupe likiwa limezagaa mabaka na michirizi ya damu.
Hija alijikamata kichwa, akaanza kupaza sauti ya kulia huku akitamka maneno ya kuombuleza.
“Siwezi kukuzuia kulia,” mmoja wa wale majirani alimwambia Hija. “Lakini ukilia kwa sauti kubwa utawaleta watu na kuwajaza pasipo na sababu za msingi. Nakuomba ukae ndani ya gari na uishushe chini sauti yako!”
Hija akaelewa, akaingia ndani ya gari kwenye kiti cha nyuma, akaupakata uso wake kwenye mapaja na kuuziba na viganja vyake. Akaendelea kulia, lakini kwa sauti ndogo tofauti na awali. Hata hivyo, kwikwi alizokuwa akiziibua zilisikika kwa uwazi.
Mmoja wa wale majirani wawili alipiga magoti kandoni alipolala Badi, akauinua mkono wa Badi na kuviminyisha vidole vyake viwili katikati ya kiganja na mkono kusikilizia mapigo ya damu, akaushusha mkono huo, kisha akavigusisha vidole kandoni mwa shingo ya Badi kwa kuviweka kwenye mshipa mkubwa kusikilizia mapigo ya damu huku akiangaliwa na Hassani pamoja na yule jirani mwingine. Akasimama na kumwacha Badi palepale sakafuni.
“Yuko hai!” alisema yule mtu aliyekuwa akimkagua Badi. “Tumwahisheni hospitali!”
****
KWA muda wa siku tatu Badi alipoteza fahamu, alisaidiwa kupumua kwa mashine akiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Taarifa za kuvamiwa kwake zilizagaa hotelini anakofanya kazi na kuzungumzwa kwa hisia tofauti na uelewa uliotofautiana. Pamoja na dosari hizo za kulielezea tukio hilo, hakuna hata mmoja aliyeingiwa na fikra huenda Nico alikuwa nyuma ya mkasa huo!
Wazazi wake Badi, ndugu na rafiki zake na baadhi ya wafanyakazi wenzake kwa muda wa siku tatu mfululizo waliishia kusimama kitandani na kumwangalia Badi bila ya kusema naye! Badi akiwa pale kitandani alionekana kama mfu aliyevishwa kifaa cha kupumulia huku kichwani akiwa na bandeji zilizozagaa damu. Baadhi ya waliokwenda kumwona walianza kumtabiria asingepona na walikuwa wakitarajia kupewa taarifa ya kifo chake wakati wowote!
Siku ya nne Badi alionekana na muuguzi akiuchezesha mkono wake. Hali hiyo ikamfanya muuguzi aweke subira kutaka kuhakikisha kama alichokiona kilikuwa sahihi. Mkono wa Badi ukashtuka tena, safari hii ukafanya hatua kwa kuusogeza kidogo. Muuguzi akamfuata daktari na kumpa taarifa hizo.
Siku ya tano Badi aliondolewa kifaa cha kumsaidia kupumua baada ya kuonekana hayupo tena kwenye hali iliyokuwa ikihatarisha maisha yake. Ili kumwondolea usumbufu ambao angeupata kutoka kwa watu watakaokuja kumwona, daktari akaruhusu idadi ndogo ya watu kumwona.
Taarifa za kupigwa na kujeruhiwa kwa Badi zilimfikia Nico. Ingawa alitarajia tukio hilo lingetokea wakati wowote, lakini kamwe hakutarajia kipigo hicho kingemfikisha Badi kwenye hali ya kuwa nusu mfu. Taarifa hizo za kuwa Badi ana hali mbaya na amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi huku madaktari wakipigania kuokoa uhai wake, zilimuweka Nico kwenye taharuki. Sikuwaagiza wamfanyie hivi! alijiambia kwenye nafsi yake. Taharuki hiyo ikamlazimisha ampigie simu Chaza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Chaza ndiyo mmefanya nini?” Nico alisema kwenye simu kwa sauti iliyoonekana kufoka zaidi kuliko kuuliza.
“Kwani vipi?” Chaza aliuliza taratibu.
“Sikuagiza mkamuue!” Nico aliendelea kufoka. “Nilitaka mumfanyizie kiaina kama kumpa fundisho. Lakini kilichofanyika ni tofauti. Nyie mmetaka kumuua! Hivyo ndivyo nilivyoagiza?”
“Jamaa yako alileta ujuaji wa kujifanya anajua kupigana, ikabidi atulizwe. Hata hivyo kilichotokea ni bahati mbaya mjomba, hakuna aliyekusudia kumuua. Anaendeleaje?”
Nico hakujibu. Aligundua sauti ya Chaza haikuwa na chembe ya kujali!
“Mjomba!” Chaza aliita kwenye simu kutaka kujua kama Nico bado yuko hewani.
“Mlivyofanya sikupendezwa nacho!” Nico alisema kuonyesha hakuwa kwenye kukaribisha masihara.
“Hizi ni ajali ya kikazi mjomba, usifikirie tu kuumia kwa jamaa, lakini pia fikiria jamaa zangu wangekamatwa na kuuawa kwa kipigo au kuchomwa moto? Hivyo ni vitu vidogo havipaswi sana kuvimaindi.”
“Kupigwa hadi kuuawa kwa jamaa zako kusingeibua upelelezi wa polisi, wangechukuliwa ni majambazi na hakuna jamii inayohani msiba wa jambazi. Lakini ujue kama Badi atafariki, basi ujue polisi wataingia kwenye upelelezi ambao unaweza ukatishia usalama wetu. Nikimaanisha mimi na wewe!”
“Jamaa wamenihakikishia hakuna ushahidi waliouacha nyuma yao. Kwa hiyo mjomba hakuna kitakachoharibika.”
“Tuombe Mungu jamaa apate nafuu,” Nico alisema, safari hii sauti yake ikionyesha kunyongea.
“Kwa hiyo mjomba kiporo cha kumalizia vipi? Jamaa wameshaanza kukiulizia.”
“Kwa nini tusisubiri hadi jamaa apate nafuu?”
“Hawatanielewa!”
“Aa, wasilete ujinga!” Nico alibwata. “Lazima uwafahamishe kuwa, endapo jamaa atakufa, mjini hapatakalika! Kutafutwa na polisi ni ishu nyingine!”
“Hizo ni stori mjomba, jamaa hawaelewi stori!”
“Unamaanisha nini?”
“Usipowalipa hela yao watakushughulikia mjomba. Hawana utu!”
“Kwani wananijua?”
“Wataanzia na mimi!”
“Unataka kuniambia nini?”
“Nisipokulengesha kwao, hasira zao zitamalizikia kwangu. Naomba ufikirie tena uamuzi wako!”
“Unamaanisha utanitaja?”
“Kumbe nifanyeje? Kila mtu anayapenda maisha! We wamalizie kiporo chao tuangalie ustaarabu mwingine!”
Kimya cha sekunde chache kilipita, kisha Nico akarudi tena hewani na kusema, “Nitazileta!”
“Lini?”
“Una akaunti kwenye mtandao wako?”
“Ndiyo ninayo,” Chaza alisema na kuutaja mtandao wenye akaunti yake ya pesa.
“Nitakutumia baadaye.”
“Usichelewe mjomba.”
Nico hakujibu, alikuwa ameshakata simu!
***
SIKU ya sita, Badi akiwa amerejewa na fahamu kikamilifu, alitolewa kutoka kwenye wodi mahututi na kupelekwa kwenye wodi ya kulipia ambako watu waliruhusiwa moja kwa moja kwenda kumwona. Lakini muda mfupi kabla ya watu kuruhusiwa kwenda kuwaona wagonjwa, askari wawili waliovalia kiraia walimwendea Badi kitandani kwa mahojiano.
“Unazikumbuka sura zao?” moja ya maswali waliyomuuliza, hilo lilikuwa mojawapo.
“Kati ya wawili niliopambana nao ana kwa ana, nadhani mmojawao naweza nikamkumbuka endapo nitamwona tena,” Badi alijibu.
“Lakini kwa sasa huwajui?”
“Siwajui.”
“Kwa hisia zako, unadhani walikuvamia kwa kutaka kukuibia gari?”
“Walivyonivamia walionekana kunipania mimi mwenyewe, sina uhakika kama lengo lao lilikuwa ni kunidhibiti kabla ya kuniibia au walikuwa na lengo jingine.”
“Basi tutaomba ushirikiano wako wakati tukiendelea kulichunguza tukio hili. Usisite kuripoti kituoni endapo utafanikiwa kumwona yeyote kati yao. Lakini pia, tunaweza tukakuita kituoni wakati wowote tutakapokuhitaji. Hawa watu huwa tunawakamata mara kwa mara, unaweza kuitwa kwa ajili ya gwaride la kuwatambua.”
“Niiteni wakati wowote, nitakuwa tayari kuja,” Badi alisema na kuagana na askari hao.
Siku iliyofuata, Nico akawa mmoja wa watu waliokwenda kumwona hospitali! Ujio wa Nico ukaonekana kama ni uthibitisho uliowathibitishia Badi na Hija kwamba mtu huyo hakuwa tena na kinyongo kwao. Ujio wake ukamfanya Badi amweleze Nico kwa kirefu kuhusu tukio lilivyotokea.
“Unawafahamu waliokufanyia hivi?” Nico aliuliza baada ya kuelezwa.
“Siwajui,” Badi alijibu.
“Lakini ukiwaona unaweza ukawakumbuka?”
“Wawili kati yao naweza nikawakumbuka, hasa mmoja huyo ndiye nilimwona vizuri. Jamaa alionekana kama teja!”
Akiwa mtulivu, lakini mwenye kuingiwa hofu na kauli hiyo ya Badi, Nico akauliza, “Polisi wamekwambiaje?”
“Wanaendelea na uchunguzi, wamenitaka yeyote nitakayemwona kati ya watu walionishambulia, nisisite kutoa taarifa kwao.”
Nico akataka kuuliza swali jingine, lakini akajishtukia kuwa anaweza akashtukiwa. Akaacha kuuliza habari za kuvamiwa kwa Badi.
“Lakini sasa hivi kiafya unajisikiaje?” Nico aliuliza.
“Kwa kweli namshukuru Mungu, naendelea vizuri.”
“Daktari alikufanyia uchunguzi?”
“Wamenichunguza. Fuvu liko salama na wala sina mvujo wowote wa damu wa ndani kwa ndani. Nadhani ni habari njema.”
“Yah, ni habari njema,” Nico aliitikia kisha alimwangalia Hija aliyekuwa kando ya Badi. “Una bahati hawakukushambulia, vinginevyo usingeipata nafasi ya kukimbia na kupiga kelele. Na sijui ingekuwaje kama na wewe wangekushambulia?”
“Wangekuwa wamekwishaondoka na gari!” Hija alijibu.
“Sidhani kama walikuwa wakilihitaji gari,” Badi alisahihisha kauli ya Hija. “Waliondoka pale wakiwa tayari wamenifletisha, Hija naye alikuwa ameshawatoroka na kukimbia, wakabakiwa na gari lililokuwa likinguruma. Nakumbuka nilipokwenda kufungua geti nilikuwa sikulizima. Nadhani hiyo ingekuwa nafasi nzuri ya kuliiba, lakini hawakufanya hivyo. Nadhani walikuwa na lengo jingine, si kuiba gari!”
Kauli hiyo ya Badi ikamshtua Nico.
“Unadhani walikuwa na lengo gani?” Nico aliuliza huku akijaribu kuyakwepesha macho yake yasikutane na macho ya Badi.
“Sijui, lakini nina hakika walikuwa hawalihitaji gari langu!”
Uso wa Nico ukanywea, lakini hakuna kati yao alioushtukia.
Nusu saa baadaye, Nico akiwa kwenye gari la kazini analolitumia alimpigia simu Chaza.
“Jamaa anasema anazikumbuka sura za watu wawili waliomshambulia, na hasa mmoja! Hii inaweza ikawa hatari kwetu!” Nico alisema kwenye simu.
“Alikuelekeza walivyo?”
“Mmoja ndiye anayemkumbuka vizuri, anasema anaonekana kama ni teja. Kwa hiyo mjomba fanya kitu kimoja, fuatilia ni nani huyo anayeonekana kama teja.”
“Nitakwenda kuwauliza,” Chaza alizungumza katika hali ya kawaida, sauti yake haikuwa na taharuki kama aliyokuwanayo Nico, lakini pia haikuonyesha msisitizo wa kitu alichokuwa akiahidi.
Nico akainasa hali hiyo. “Chaza!” aliita kwa sauti iliyokuwa kavu. “Nadhani huioni hatari ya kitendo cha Badi kuzikariri sura za watu wawili waliomshambulia, hasa huyo mmoja. Nataka ujue, endapo mmoja akikamatwa, na sisi tumekwisha! Wote walioshiriki watakamatwa, wewe mwenyewe utakamatwa, hali kadhalika na mimi sitopona!”
“Hata wakikamatwa, kwani mimi nilishiriki kumshambulia? Au wewe ulishiriki kumshambulia? Woga wa nini mjomba?”
“Watakutaja! Na utakapokamatwa, utanitaja!”
Chaza akafanya kicheko cha nguvu kilichomtia karaha Nico.
“Watu niliowatumia sikuwaokota barabarani,” Chaza alisema. “Ni wazoefu wa shughuli hizi. Endapo watakamatwa, haitakuwa mara yao ya kwanza. Mikong’oto ya polisi imeshatutia usugu. Kutotajana ni sehemu ya kiapo kwetu, haitatokea tukatajana! Kwa hiyo mjomba, hata mimi ni sehemu ya mmoja aliyekula kiapo hicho, sitokutaja!”
“Kwa hiyo unanihakikishia hakutakuwa na matatizo kwangu?”
“Mjomba kula kuku zako!”
Kwa sehemu fulani Nico akapata ahueni ingawa bado mashaka yaliendelea kumzunguka. “Sawa mjomba,” alisema. “Kukiwa na lolote nitakufahamisha, lakini na wewe usisite kusikilizia.”
“Hofu ondoa!”
Wakaagana kwenye simu.
*
Kibusta! Chaza aliwaza mara baada ya kumaliza kuzungumza na Nico kwenye simu. Aliirudisha simu taratibu mfukoni mwa suruali. Akili yake haikuwa tena iko sawa, mazungumzo aliyotoka kuyafanya na Nico yalimsumbua. Hadhari iliyotolewa na Nico, sasa alikuwa akiiona dhahiri. Mtu mwenye mwonekano wa kiteja aliyetajwa na Nico katika watu aliowapeleka kumshambulia Badi, alikuwa na hakika angekuwa ni Kibusta!
Kibusta pekee ndiye aliyekuwa mbwia unga kwenye kundi hilo la watu wanne, lakini hata mwonekano wake ulikuwa ukimwonyesha kuwa ni teja! Alikuwa na uhakika endapo Kibusta atakamatwa, basi mtu huyo asingesita kumtaja! Kibusta hakuwa mtu wa kazi kama walivyokuwa wenzake na kukamatwa kwake si tu angemtaja yeye peke yake, lakini kungesababisha awataje wote alioshirikiana nao kumshambulia Badi!
Ni yeye ndiye aliyetoa wazo la kutaka Kibusta awemo kwenye mpango huo. Kwa upande fulani, Chaza akawa kama anayejutia wazo lake la kumwingiza mtu huyo. Umuhimu wa Kibusta kuwepo kwenye mpango huo sasa aliuona haukuwa wa lazima ingawa awali aliona kulikuwa na umuhimu wa kuwepo kwake. Kibusta alipangwa kuifanya shughuli ya kumlawiti Badi!
Kutofanyika kwa shughuli iliyompeleka Kibusta ikawa kama iliyomzindua kuwa mtu huyo hakuwa na umuhimu wowote katika zoezi hilo. Badala yake, ameanza kuwa mwiba kwao! Alimjua vizuri Kibusta kuwa ni mpiga debe kwenye vituo vya daladala hasa Kituo cha Studio Kinondoni, lakini pia alikuwa kibaka mzuri wa simu za abiria na hata pochi. Sifa nyingine aliyokuwa akipewa ni ile ya kupenda kuwalawiti wanaume wenzake. Sifa hiyo ndiyo iliyomshawishi kumwingiza kwenye mpango huo baada ya Nico kutaka Badi afanyiwe kitendo cha kulawitiwa!
Akiwa bado kwenye lindi la kumfikiria Kibusta, Chaza alikiri alifanya kosa kubwa kumshirikisha mtu huyo. Utumiaji wa dawa za kulevya unaotumiwa na Kibusta ingekuwa ni kigezo kikubwa cha kumshawishi kutomshirikisha mtu wa aina hiyo. Lakini hakufanya hivyo! Akamruhusu aende! Sasa mtu huyo amekuwa tishio kwake kwa sababu kuu moja; Kibusta ni mwoga wa polisi!
Sifa hiyo ya mwisho ndiyo iliyompa wakati mgumu. Alijua kukamatwa kwa Kibusta kungekuwa ni janga kwao! Hakutaka kujiwekea mjadala, alifahamu wazi kwamba, endapo Badi atakuwa aliikariri sura ya Kibusta na ikatokea akamwona na kumripoti polisi, timu nzima, akiwemo yeye mwenyewe wangekamatwa!
Palepale akatumbukiza mkono mfukoni na kuitoa simu. Akampigia mmoja wa watu wake aliowatuma kwenda kumshambulia Badi.
“Yule jamaa mliyemshambulia anadai kuzikariri sura za watu wawili. Kwani ni nani aliyekabiliana naye ana kwa ana wakati mkimpiga?” Chaza alisema kwenye simu.
“Wa kwanza kupambana naye alikuwa teja wako uliyetuletea, mwingine Tito…”
“Duh!” Chaza alidakia. “Kwa Tito sijali, yeye ni mtu wa kuhadharishwa, tatizo ni huyu jamaa yangu, akidakwa na polisi atatutaja wote!”
“Wewe habari hizo amekwambia nani?”
“Mtu aliyenipa tenda.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwani jamaa aliyepigwa anamjua Tito au huyo teja wako?”
“Hawajui wote, lakini anadai akiwaona anaweza akawakumbuka.”
“Si mpaka tudakwe na polisi? Kwa fununu gani polisi walizokuwanazo hadi watukamate? Labda huyo mbwia unga wako! Na anakujua wewe zaidi kuliko sisi. Ni wazi akikamatwa, atakutaja!”
“Basi nitacheki naye,” Chaza alisema na kukata simu.
Limeshakuwa tatizo! Chaza aliwaza. Kabla ya kuzungumza na Nico alikuwa na safari ya kwenda Kitongoji cha Mwenge kwa shughuli zake na alikuwa hakupanga kupandia basi la daladala kwenye Kituo cha Studio, lakini kutokana na taharuki iliyompata baada ya taarifa kuwa Kibusta ni mmoja wa aliokaririwa sura na Badi, Chaza akaamua kubadilisha mwelekeo. Aliamua aende kwenye Kituo cha Studio kwa ajili ya kumwona Kibusta na akishamaliziana naye ndiyo apandie basi hapohapo kuelekea Mwenge.
Alimkuta Kibusta akienda sambamba na daladala linalokwenda Masaki lililokuwa likiwasili kituoni hapo na kuanza kulipigia debe kabla hata halijasimama. Chaza akamdaka kwa kumshika kwapani.
Kitendo hicho kilimshtua Kibusta aliyekuwa hakumwona Chaza. Akataka kumng’akia kwa kumwona anataka kumkosesha riziki yake ya kupiga debe kwenye basi hilo huku akihofia kuwahiwa na wenzake kuichukua nafasi ya kulipigia debe. Alichowahi kukifanya ni kuufyetua mkono wake uliokamatwa na kutaka kuachia tusi zito. Lakini alipomwona ni Chaza, akanywea!
Vibaka wengi wa vituoni walikuwa wakimhofia Chaza. Walimjua kuwa ni mtoto wa kihuni na mkorofi. Ingawa hakuwa mbwia unga wala kuwa kibaka kama wao, lakini biashara walizokuwa wakifanya naye za kumuuzia simu walizokuwa wakiwaibia abiria au watu wengine wa mitaani, kuliwafanya wamjue vizuri mtu huyo.
Chaza alikuwa mzoefu wa ngumi za mitaani. Hakuwa mtu wa kuzinguliwa, na moja kati ya kesi isiyosahaulika na kusambaa kwenye vilinge vya wavuta unga ni kesi iliyowahusu vibaka waliotaka kumgeuzia kibao baada ya kupatana nao akawauzie simu kwa bei waliyoelewana. Chaza akaifanya kazi hiyo na kuzipeleka pesa zilizokuwa kwenye makubaliano yao baada ya kuziuza simu walizomkabidhi. Wakazikataa pesa walizoletewa na kudai zaidi. Mzozo huo ukawasababishia kupigiana mikwara huku vibaka wakimtishia kutoa maisha yake kama hataongeza pesa. Kwenye ugomvi huo, vibaka wakamtishia kumchoma na bisibisi. Kilichotokea hapo ni Chaza kuanza kuwasambaratisha na kipigo. Hatimaye baada ya kuwasambaratisha, hata zile pesa alizokusudia kuwapa awali, nazo hakuwapa!
Sifa za Chaza kupigana zikakamata hatamu kuanzia siku hiyo!
Matukio ya aina hiyo na mengineyo yaliyomhusisha na vibaka hao wa vituoni, vikawafanya wote wamtambue Chaza kuwa ni mtoto wa kihuni mwenzao asiyependa kuzinguliwa! Na hiyo ndiyo ikawa sababu ya Kibusta kunywea baada ya kumwona Chaza!
“Ah, Chaza!” Kibusta alisema na kufanya tabasamu la kutengeneza huku akiuondoa kwa haraka uso uliokuwa umeanza kujenga hamaki iliyotokana na kuzuiwa kwenda kuipigia debe daladala.
Hakuwa akimdai chochote Chaza, alikwishalipwa pesa zake mara tu baada ya shambulizi la kupigwa kwa Badi kufanyika ingawa alichokusudiwa akakifanye, hakikufanyika! Akajiuliza, mtu huyo anataka nini kwake wakati walishamaliziana?
“Njoo huku!” Chaza alisema kwa sauti ya kuamrisha.
Kibusta akatii. Akamfuata Chaza huku vibaka wengine wakiliangalia tukio hilo kwa fikra zilizopishana. Wengi walihisi Kibusta alikwishalikoroga kwa Chaza, lakini kila mmoja akaogopa kufuatilia kwa kuhofia Chaza asije akawabadilikia.
“Naona kimenuka!” vibaka walibonyezana kiaina na wakati huohuo wakizikoromisha sauti zao kupigia debe madaladala yaliyokuwepo kituoni.
“Polisi wanakutafuta!” Chaza alimwambia Kibusta.
Sura ya Kibusta ikataharuki, kisha ikanywea kama mtu aliyelitambua kosa lake. Palepale akaonekana kuchanganyikiwa.
“Yameshakuwa hivi!” Kibusta alisema kwa unyonge huku akiutazamisha chini uso wake mikono ikiwa kiunoni.
“Potea nje ya mji haraka sana!” Chaza alimwambia.
“Niende wapi?” Kibusta alihoji bila ya kuinua uso wake. Alikuwa bado akiangalia chini.
“Kwenu! Kijijini kwenu ni wapi?”
“Nitaendaje kuishi kijijini, usawa wenyewe kama huu?”
“Kumbe? Unataka polisi wakukamatie mjini? Au kukamatiwa mjini unaona ndiyo dili?”
“Kwa hiyo, hata nikienda kijijini bado watanikamata!”
“Polisi wa Dar hawahangaiki na watu wa sampuli zenu mnapokimbilia vijijini. Kwanza wanafurahi wanaposikia mmejichimbia maeneo ya huko. Labda uwe umeua! Ukiua mwanangu halafu ujichimbie huko, lazima watakuja kukuchomoa. Lakini kwa vikesi vidogovidogo kama hivi, hawapotezi muda wao kukufuateni ushenzini.”
“Mimi kijijini sirudi!” Kibusta alisema na kuonyesha kupuuzia.
“Eti nini?” Chaza aliuliza huku sura yake ikiwa imebadilika ghafla.
“We’ mwenyewe si unayajua maisha ya kijijini?”
“Hakuna kubwia! Au siyo?”
“Ah..,” Kibusta hakuendelea.
“Kibusta sikiliza!” Chaza alisema kwa hamaki. “Polisi wakikukamata, kisha unitaje, nitakuua!”
“Nani akutaje? Ah, mwanangu vipi?”
Chaza akamwangalia Kibusta kwa jazba. “Ninachokwambia ondoka hapa mjini!” alisema. “Kama hutaki mi’ n’takuondoa! Nitahakikisha popote pale n’takapokuona nakubamiza hadi mwenyewe utalikimbia jiji!”
“Sasa huo uonevu! Au kwa sababu unajua mi” mnyonge wako?”
“Kwani we’ ukipotea kwa muda hadi mambo yakipoa kuna ubaya gani? Usilete mzaha, n’takubamiza kweli!”
Kibusta akanywea, lakini hakujibu.
“Mi’ nd’o n’shakwambia!” Chaza alionya. “Nikikuona kituoni nakubamiza!” Baada ya kusema hivyo akaondoka.
Kibusta alisimama palepale alipoachwa akiwa amejiinamia, kisha akamwangalia Chaza aliyekuwa akipotea kwa kasi kwenye kundi la abiria na kulikimbilia basi linalokwenda Mwenge.
Baada ya basi alilopanda Chaza kuondoka, Kibusta alirudi kituoni na kuendelea kupiga debe. Nusu saa baadaye, akapotea kituoni.
Tokea siku hiyo hakuonekana tena!
***
AKIWA bado yuko wodini akiuguza majeraha, Badi alishangaa alipomwona Hija akiwasili hospitalini hapo akiwa na watu wawili wa makamo, mmoja mwanamume na mwingine mwanamke.
“Badi,” Hija alisema akiwa amekaa kwenye ncha ya kitanda alicholalia Badi. “Hawa ni wazazi wangu, huyu baba’angu na huyu mama yangu.”
Lilikuwa shambulizi la ghafla ambalo Badi hakulitarajia. Akaupokea utambulisho huo kwa unyenyekevu na kufanya tabasamu la upendo. “Karibuni,” alisema. “Hija hakuniambia kama angewaleta.”
“Nadhani alitaka ujio wetu uwe surprise kwako,” mama yake Hija alisema.
Kikatoka kicheko kifupi kutoka kwa Badi, lakini Hija alitabasamu.
“Za nyumbani?” Badi alihoji.
“Tupo wazima, pole sana,” mama yake Hija alisema na kuchukua nafasi hiyo kumhoji Badi kuhusu alivyoshambuliwa.
Badi akalielezea tukio zima lilivyokuwa hadi kujikuta akiwa hospitali.
“Pole sana,” safari hii baba yake Hija alisema baada ya kuusikiliza mkasa huo.
Ujio wa wazazi wa Hija ulikuwa faraja kwa Badi baada ya kuona amekubalika na upande wa pili hadi kuja kumwona hospitali. Tukio hilo likawa changamoto nyingine ndani ya penzi lake na Hija. Akapanga na yeye akamtambulishe rasmi Hija kwa wazee wake pindi atakapotoka hospitali.
Siku iliyofuata, Hija alikuja na wasichana watatu ambao Badi alikuwa hajawahi kuonana nao. Wote walikuwa wamevaa mavazi ya gharama na kuwa vivutio kwa waliopishana nao. Walipendeza na walionekana kuishi maisha ya anasa. Mmojawao alikuwa ameshika funguo ya gari kama manjonjo ya kuonyesha anamiliki usafiri. Alionekana kuwa na umri uliowazidi wenzake, na yeyote angewaona asingesita kutambua kuwa, wanaume wanaowahudumia wasichana hao ni watu wenye pesa, wengine wakiwaita, mapedeshzee!
Mara tu walipofika na kusimama kando ya kitanda alicholalia Badi, eneo lote likatawaliwa na harufu ya manukato ya bei ya gharama.
“Badi waone shoga zangu,” Hija alimwambia Badi. “Huyu ndiye dada yetu anaitwa Fina na hawa wengine, huyu ni Ester na huyu Mahadia.”
Wote wakampa mkono Badi na kumalizia kwa kumpa pole.
“Jamani,” Hija aliwageukia shoga zake. “Huyu ndiyo mzee mwenyewe! Yule mliyekuwa mkimsikia…Badi, Badi!” kisha akacheka na kujiinamia kama anayeona aibu. “Basi ndiye huyu, mwoneni vizuri!”
Kuzungukwa na wasichana wazuri kama hao na wageni wengine waliokuwepo, kulimfanya Badi ajisikie ufahari wa kiuanamume.
Wasichana hao wakiwa na Hija waliteka mazungumzo kutokana na uchangamfu wao. Kwa muda mfupi wakajenga ukaribu wa haraka na Badi aliyekuwa akifurahia maongezi yao yaliyokichangamsha chumba chake. Walikaa hadi muda wa kuangalia wagonjwa ulipomalizika.
Hija pekee ndiye aliyeagana na Badi kwa kubusana papi za midomo, kisha akaondoka na shoga zake.
****
BADI alitolewa hospitali na kuzidishiwa mapumziko ya kikazi kwa wiki moja zaidi. Kwa wiki hiyo yote, Hija alihamia nyumbani kwa Badi kuzifanya huduma zote za kupika na usafi. Kuhamia kwa Hija nyumbani kwa Badi kuliwezesha wazazi wake Badi wamjue Hija na nafasi hiyo ikachukuliwa na Badi kumtambulisha Hija.
“Baba,” Badi alisema huku akimwangalia baba yake, kisha aligeuka na kumwangalia mama yake. “Mama,” alisema. “Huyu ni mwenzangu anaitwa Hija. Ndiye ninayetarajia kumwoa.”
Utambulisho huo ukaleta mahojiano mafupi kati ya wazazi wake Badi na Hija. Kwanza walifurahi kusikia kijana wao amefikia uamuzi wa kutaka kuoa na wakaitumia nafasi hiyo kumhoji Hija ni mwenyeji wa wapi, wazazi wake ni nani, anaishi wapi na mengine ya hapa na pale. Maswali ambayo Hija aliyajibu kwa ufasaha na kujiamini.
Mara tu wazazi wake Badi walipoondoka, Hija akamkabili Badi.
“Unanitangazia uchumba kabla hata hujazungumza na mimi?” Hija alimuuliza Badi.
“Wewe mbona ulinitangazia uchumba kwa yule uliyedai ni mjomba wako? Ulizungumza na mimi?”
“Kwa hiyo ulinizungumzia ili kuhalalisha uwepo wangu hapa nyumbani?”
“Ukimaanisha?”
“Pengine ulishindwa kuwaambia mimi ni rafiki yako, ukaona bora uweke uzito wa uchumba.”
“Nilikuwa nikimaanisha hivyo!”
“Kwamba unataka kunioa?” Hija aliuliza na kuonyesha aina ya mshangao.
“Ndiyo dhamira yangu!”
Hija akaduwaa kwa sekunde chache. “Sidhani kama ulistahili kulihalalisha hilo kabla ya kupata ridhaa yangu,” alisema.
“Kwa hiyo unataka kuniambia nini Hija? Usiniambie nilifanya kosa kuwaambia hivyo? Sitarajii baadaye niwaambie kuwa hakutakuwepo ndoa kati yetu!”
Hija akaduwaa kwa mara nyingine na kumwangalia Badi, safari hii alizidisha sekunde kuliko alivyoduwaa awali. Akashusha pumzi na kumwangalia tena Badi. “Unataka kunioa Badi?” aliuliza kama vile kulikuwa na kitu anakificha.
Ikawa zamu ya Badi kuduwaa. “Kwani vipi?” aliuliza.
“Nilipanga kutoolewa hivi karibuni!”
“Kwa hiyo nilichowaambia wazazi nilikosea?”
“Sina uhakika.”
“Huna uhakika na lipi?”
“Si nimekwambia nilikuwa sina mpango wa kuolewa hivi karibuni.”
“Kwa hiyo unasemaje?”
Hija hakujibu!
Badi akajikuna kichwani kwa uangalifu kuepuka kujitonesha vidonda. Kwa mtazamo wa mbali akaonekana kuchanganywa na ukimya wa Hija. “Sasa nitawaambia nini wazazi?” Badi alinung’unika kama kwamba Hija alikwishamhakikishia kuwa hataki kuolewa.
Hija akainua macho, akamwangalia Badi. Kuna kitu kilichokuwa kikisomeka kwenye macho yake ambacho Badi hakukiona. Alikuwa kama akimshangaa Badi.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unaonaje suala hili tukilizungumza siku nyingine?” Hija aliuliza.
“Nina nia ya kweli ya kutaka kukuoa!” Badi alisisitiza.
“Najua!” Hija alijibu kifupi bila ya kumwangalia Badi usoni.
“Niruhusu nikuoe!”
Hija akawa kama aliyeshtuka na kumwangalia Badi, lakini hakujibu!
Kitendo hicho kikaanza kumkera Badi. “Kwani tatizo liko wapi?” aliuliza.
Sekunde kadhaa zilipita, kisha Hija alisema, “Sawa!”
Badi akainua macho kumwangalia Hija kama vile alitatizwa na jibu hilo. “Unamaanisha nini?” aliuliza.
“Si umesema unataka kunioa?”
“Ndiyo.”
“Nimekwambia sawa. Au ulitaka nikwambie nini?”
Badi akashusha pumzi. “Lakini usione kama nimekulazimisha,” alisema.
“Sasa hayo ni yako!”
“Nitakwenda kujitambulisha kwa wazazi wako,” Badi alisema kutaka kuishusha presha ya Hija.
“Nilishakutambulisha ukiwa hospitali, usiende kufanya kichekesho Badi.”
“Duh! Kweli bwana!” Badi alisema na kujichekesha ambako hakukupokewa na Hija.
Hija akaonekana kujenga umakini usoni kama aliyekuwa akiisaili akili ya Badi. Akawa amejenga utulivu, hakufurahi wala hakununa.
“Vipi?” Badi aliuliza kama aliyejishtukia.
“Poa,” Hija alijibu kwa utulivu huku akiendelea kumwangalia Badi kwa ukimya uleule wa kutofurahi wala kununa.
Taswira hiyo ikampa wakati mgumu Badi.
“Nitamtuma mshenga!” Badi alisema na kuonekana kama aliyekuwa akijaribu kutaka kuweka mambo sawa, lakini akiwa hajui ni kipi hasa alichokuwa akitaka kukiweka sawa.
Uangaliaji wa Hija katika hali ile ya utulivu uliendelea kumchanganya. Ukamfanya ajituhumu kuwa, kulikuwa na maeneo ndani ya maongezi yake huenda aliyavurunda.
“Utamtuma nani awe mshenga wako?” Hija aliuliza, safari hii kwa utulivu zaidi.
“Rajabu,” Badi alijibu na kumwangalia Hija. Alipomwona Hija hakujibu, akajikuta akijiongelesha zaidi. “Au unamwonaje?” aliuliza.
Hija akatengeneza tabasamu linalosafiri kwenye tasnifu iliyokwishamsaili Badi ya kumwona anahangaika na maelezo.
“Jamani!” Hija alisema kwa sauti ya kumshangaa Badi, sauti yenye udhibiti wa kujiamini na kiburi cha kujua anapendwa. “Usinichekeshe,” aliendelea. “Ulitaka nikujibu nini? Kwamba hafai, mpeleke mwingine?”
“Basi nitamtuma Rajabu.”
Hija hakujibu!
Badi akajiuliza, anakosea wapi kwenye kujieleza?
***
RAJABU aliyemzidi umri Badi kwa zaidi ya miaka mitano, ndiye aliyekuwa rafiki mkubwa wa Badi. Kuchaguliwa kwake na Badi awe mshenga hakukumshangaza Hija. Hija aliujua urafiki wao ulivyokuwa wa karibu na alikuwa akimwamkia shemeji yake huyo kwa kumpa heshima ya ‘shikamoo’ kutokana na umri wa Rajabu.
Ukaribu wao uliwafanya watoke pamoja mara kwa mara kwenda kwenye majumba ya starehe wakati mwingine akiwepo na mke wa Rajabu. Fursa hiyo ya kutoka pamoja ilimuweka Hija kuyajua baadhi ya mambo yanayomhusu Rajabu. Alimjua Rajabu kuwa sio mtu wa dhiki. Alikuwa hababaishwi na vijisenti mbuzi vya kuendesha maisha yake kwa mfumo anaoutaka. Lakini pia, aligundua jamaa huyo ilikuwa aghalabu kumwona amezidiwa na ulevi. Ilikuwa hata anywe vipi pombe, si bia si pombe kali, alikuwa hayumbi au kupoteza mhimili wa akili au wa kuzungumza. Kwake alimwona kama mtu wa ajabu!
Kwa upande wa Rajabu, alikuwa ni mtu aliyependa kujenga umakini wakati wote, lakini pia alikuwa mwerevu wa kushtukia mambo. Ingawa kulikuwa na ukweli wenye shaka aliokuwa akiuona kutoka kwa Hija kuwa alikuwa akimpenda Badi, lakini kwa upande wa pili aligundua Hija hakuwa mwanamke wa kuishi maisha ya kuolewa. Alimwona ni msichana aliyekuwa hajawa tayari kujenga utulivu wa kutulizwa nyumbani kutokana na maisha ya ndoa, lakini pia alionyesha shaka ya uaminifu wa kuwa na mwanamume mmoja! Alimwona ni msichana anayejiona ni mzuri na anayeudekeza uzuri wake kwa kuamini wanaume wengi wenye uwezo wa kipesa walikuwa wakimpapatikia. Kwa imani hiyo, Rajabu akaamini, Hija ni mwanamke anayependa kuwa juu ya mwanamume, akitaka asikilizwe kila anachokitaka kwa sababu aliamini, uzuri wake ulimpa fursa ya kumpiga chini mwanamume! Na sio yeye kupigwa chini!
Lakini kwa upande wa pili, Rajabu alimwona Badi akiwa mwenye hofu ya kuachwa na Hija, na Hija alikuwa akiitumia nafasi hiyo kudeka kimapenzi kwa Badi. Mbinu hiyo ikampa turufu ya kumdhibiti Badi. Akiwa anawaangalia wawili hao kwa mtazamo wake, Rajabu alimtambua Hija kuwa pindi anapotaka jambo lake litimizwe na Badi, alianzisha tabia iliyokuwa inamkera; tabia ya kununa! Mbinu hiyo kila ilipotumiwa na Hija, Rajabu alimwonea huruma rafiki yake jinsi alivyokuwa akihangaika kutaka kumridhisha Hija na wakati mwingine kumbembeleza pasipo na sababu yoyote ya kueleweka!
“Inakuwaje wewe mwanamke anakuendesha kibwegebwege?” siku moja Rajabu alimng’akia Badi. Lakini Badi aliishia kutabasamu na kukanusha kuwa, alikuwa haendeshwi!
Akiwa yupo katika jitihada za kumuweka sawa rafiki yake ili asiwe anapandwa kichwani na Hija, ghafla Badi akamjia na hoja nzito ambayo kamwe hakuitarajia!
“Nataka uwe mshenga wangu kwa Hija!” Badi alimwambia Rajabu.
Rajabu akashtuka kama aliyeambiwa alikuwa akitafutwa na polisi! Akapata kigugumizi cha sekunde kadhaa. Uso wake ukapigwa na butwaa. Hakuamini!
“Una…unataka kumuoa Hija?” Rajabu aliuliza kama vile aliambiwa kitu cha ajabu.
“Bwana nimeamua kumwoa,” Badi alisema huku akionyesha kutokuwa na hatia na kile alichokizungumza.
“Ulishazungumza naye?” Rajabu aliuliza huku akiamini Badi angekuwa hajazungumza na Hija kwa kuamini, Hija asingelikubali wazo hilo.
“Ndiyo,” Badi alijibu.
“Na amekubali?”
“Ndiyo.”
Rajabu akanywea, lakini pia kichwa kilimwuma! “Sidhani kama umeshamjua vizuri Hija hadi ufikie uamuzi kama huo,” alisema.
“Sasa Rajabu, unataka nimjue vipi zaidi ya hivi ninavyomjua?” Badi alijitetea.
“Naona bado mapema kuchukua uamuzi huo. Angalau ungekuwa naye japo kwa mwaka mmoja kisha ndipo ungeamua hivyo.”
“Kwa hiyo umekubali?”
“Kukubali nini?”
“Kuwa mshenga wangu.”
Badala ya kujibu swali aliloulizwa, Rajabu akauliza, “Unatarajia shughuli hiyo ifanyike lini?”
“Wakati wowote kuanzia sasa.”
“Aisee!” Rajabu alisema kisha hakuendelea.
“Kwa hiyo umekubali?”
Rajabu akamwangalia Badi usoni. Akataka kumwambia, mwanamke unayetaka kumwoa hafai! Lakini nafsi yake ikamwonya kuwa, watu wa aina hiyo wanaweza kwenda kwa mhusika na kuyaropoka maonyo uliyoyatoa.
“Ukiwa tayari niambie!” Rajabu alisema huku sauti yake ikionekana kutolishabikia jambo hilo.
***
BADI alirudi kazini na kuanza kazi huku Hija akishindwa kurudi tena kazini baada ya kuenguliwa kwenye nafasi ya mafunzo kutokana na kutoonekana kazini pasipo na sababu za msingi.
Kutokuwepo tena kazini, Hija na Badi wakawa wanaonana nyumbani kwa Badi au wakati mwingine Badi humfuata Hija ama nyumbani kwao au kwenye duka kubwa la nguo linalomilikiwa na Fina. Huko Badi alikuwa akipokewa kwa bashasha zote wakati akimfuata Hija. Ester na Mahadia waliokuwa wauzaji kwenye duka hilo pamoja na Fina mwenyewe walikuwa wakimpokea kwa bashasha na kuhamia kwenye baa iliyokuwa jirani na kuanza kunywa.
Awali, Badi alikuwa akitumia kinywaji cha bia kihifadhiwacho kwenye chupa kubwa za bia, lakini baada ya kuanza kuwa karibu na shoga zake Hija, wakawa wanambeza kwa kumwambia hadhi yake haifanani na bia anayokunywa! Akatakiwa awe anakunywa bia zinazotengenezwa nje zenye ujazo mdogo wa kwenye chupa, lakini huuzwa kwa bei ya juu. Badi akabadilishwa. Ukawa mwanzo wa kudhibitiwa na kundi hilo!
Dalili za Badi kugubikwa na kivuli kinachoongozwa na Hija akishirikiana na shoga zake hasa Fina, kilishika kasi baada ya Badi kutangaza nia ya kumwoa Hija.
Ilikuwa baada ya Rajabu kupeleka posa kwa wazazi wake Hija, posa ikarudi na majibu ya kukubaliwa, taratibu maalum za sherehe zikachukua nafasi yake. Fina kwa kutumia marafiki zake wengine wenye mwonekano kama wake, wakamwandalia kikao shoga yao Hija kwa ajili ya kumfanyia sherehe ambayo wenyewe waliita, ‘Ngoma ya Jikoni.’
Vikao vya harusi navyo vikaanza rasmi. Wazazi wa pande zote mbili wakaanzisha vikao. Kwa upande wa Hija kukawa na vikao vya maandalizi ya ‘Usiku wa Hija,’ na upande wa wazazi wa Badi kwa kushirikiana na marafiki wa Badi wakaandaa vikao vya sherehe za harusi.
Kundi la shoga zake Hija kwa kuelewa wamemuweka Badi kiganjani, wakamwomba wafanyie vikao vyao kwenye nyumbani yake. Badi akakubali bila ya kushauriana na mtu yeyote. Vikao hivyo vikawa vinajenga taswira ya matumizi ya matanuzi kila kilipofanyika. Karamu ya vinywaji na vitafunwa vikawa sehemu ya kuendeshea kikao huku wenye kuhudhuria wakishindana kwa uvaaji wa vito vya thamani na baadhi wakionyeshana uvaaji wa nguo fupi. Wengi wao, kama hawakuja na magari yao, basi walikuja kwa usafiri wa kukodisha.
Kauli za kimipasho, majigambo na kushushuana kukifuatiwa na makofi ya kuunga mkono hoja au hata kwa vigelegele vilisikika kutoka ndani ya nyumba hiyo.Vikao hivyo vya nyumbani kwa Badi vikaleta taswira kuwa, safari hii Badi amepatikana!
***
SIKU ya harusi, sherehe ilifana mno. Ndoa ilifungwa nyumbani kwa wazazi wake Hija baada ya mshuko wa sala ya adhuhuri. Siku ya pili ambayo ilikuwa ni Jumamosi, sherehe ya kuwapongeza maharusi ilifanyika kwenye ukumbi maarufu. Chakula kilikuwa kingi na kizuri, vinywaji hasa bia, watu wakajinywea na kuviacha, ikawa sehemu ya sifa iliyosherehesha sherehe hiyo kwa vigelegele na nderemo.
Kwa mara ya kwanza wakati sherehe zilipokuwa zikiendelea ndani ya ukumbi, Badi akatambua ukweli ambao hakuwahi kuambiwa na Hija. Baba wa Hija ambaye alikuwa akimtambua, hakuwa baba yake mzazi! Alikuwa ni baba mlezi aliyemlea Hija tokea udogoni baada ya baba yake kuachana na mama yake. Usiku huo, baba yake mzazi Hija alihudhuria harusi hiyo na wakati alipopewa nafasi ya kuzungumza ndipo alipotambulishwa kuwa, ndiye baba mzazi wa Hija! Badi akapata mshtuko. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kumwona mzee huyo!
Fungate ilifanyika Bagamoyo. Huko walifikia kwenye hoteli ya kitalii iliyoko ufukoni mwa bahari na kukaa kwa siku nne. Kwa siku zote hizo, Hija hakuonekana kuguswa na suala lililojitokeza harusini kuhusiana na baba yake huyo mzazi. Hakulizungumza kwa Badi wala kuonyesha dalili kuwa angelilizungumza! Kwa upande wa Badi, jambo hilo la kutoelezwa likawa linampa usumbufu wa kujiuliza, kwa nini Hija hajawahi kumweleza kuwa baba aliyekuwa akiishi naye hakuwa baba yake mzazi? Pamoja na kujiuliza huko, lakini kamwe hakudiriki kumuuliza mkewe!
*
Akiwa amerudi tena kazini baada ya fungate, Nico aliitumia nafasi hiyo kumpongeza Badi kwa kuwa bwana harusi. Na katika hali isiyotarajiwa, Nico akamwalika Badi na mkewe chakula cha usiku hapo hotelini.
“Itabidi kwanza niongee na mwenzangu,” Badi alimjibu Nico.
Nico akatabasamu. “Poa, mkiwa tayari utanifahamisha,” alisema.
Hayakuwa mazungumzo marefu kati yao, lakini pia, Badi hakuutilia maanani mwaliko huo. Alipofika nyumbani akamgusia Hija kuhusu mwaliko alioutoa Nico.
“Achana na bwege yule!” Hija alijibu kwa mkato na kuonyesha kutotaka kulizungumzia suala hilo.
Badi akatii. Hakuligusia tena suala hilo!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ingawa kwa siku za mwanzoni Badi alipata tabu kila alipoonana na Nico kutokana na kukosa kutoa jibu la mwaliko aliopewa, lakini hatimaye alijikuta akipata faraja baada ya kumwona Nico kutomkumbushia jambo hilo. Hatimaye mwaliko huo ukafa kifo cha kimyakimya.
Maisha yao mapya ya ndoa yakamlazimisha Badi kuajiri msichana wa kazi kwa ajili ya kumsaidia Hija kazi za ndani, lakini badala ya kuonekana Hija amepata msaada, ikawa kama ndiyo imetoa mwanya kwake wa kuaga mara kwa mara na wakati mwingine bila ya kuaga, akawa anakwenda kwa shoga zake. Ikawa siyo jambo la ajabu Badi kurudi nyumbani akitokea kazini na kutomkuta Hija. Maisha yao ya kuwa ndani ya ndoa, yakaendelea kama watu waliokuwa hawajaoana!
Awali, Badi hakuitilia maanani tabia hiyo kwa kuamini Hija angeiacha baada ya kuyaelewa majukumu mapya yanayomkabili ya kuwa ni mke wa mtu. Lakini wazo hilo likaonekana lipo kwa Badi pekee! Hija hakuonekana kuutilia maanani umuhimu huo wa kujiona ni mke wa nyumbani na wala kuwa
Katika uvumilivu wake kwa mkewe, siku moja Badi alichelewa kurudi nyumbani baada ya kutingwa na kazi zilizomfanya achelewe kurudi, akarudi usiku. Muda mwingi alioutumia kazini ulimfanya arudi nyumbani akiwa na hamu nako huku akitamani kuwa karibu na mkewe.
Lakini ile kuingia tu nyumbani, dalili za kutokuwepo mkewe zikaonekana! Palepale unyonge ukamwingia.
“Mama yuko wapi?” Badi alimuuliza msichana wa kazi baada ya kuhakikisha Hija hayupo.
“Hajarudi,” msichana wa kazi aliyeitwa Helena alijibu.
“Kwani amekwenda wapi?”
“Sijui.”
“Alitoka saa ngapi?”
“Mchana baada ya kumaliza kula.”
Badi alijikuna kisogoni kisha aliingia chumbani kwake. Kitendo cha mkewe kuwa na uhuru wa kuondoka nyumbani wakati wowote kilianza kumgusa kwa undani kwa mara ya kwanza. Anaondokaje bila ya kuniarifu? alijiuliza. Kuchelewa kurudi kwa mkewe kwa siku hiyo hadi muda huo, tena bila hata kumwambia yuko wapi kulimchanganya. Alikuwa na uhakika hakukuwa na dharura yoyote iliyomtokea, kwa sababu taarifa za kuwa angechelewa kurudi nyumbani akitokea kazini alimfahamisha mapema, lakini pamoja na kumfahamisha huko, Hija hakumwambia kama angetoka na badala yake ameichukua nafasi hiyo ya kuchelewa kurudi kuitumia kwenda kwa shoga zake kunywa! Tukio hilo likampa hadhari mpya. Aliuona uhuru anaomwachia Hija unamfanya yeye ndiye awe mtawala wa nyumba. Akijipa angalizo kuwa yeye ndiye mtawala wa humo ndani, hapaswi kuiachia hali hiyo iendelee!
Ghafla akamsikia mdogo wake, Hassani akizungumza na Helena sebuleni, akataka amwite chumbani kutaka kumzungumzia suala la Hija, lakini akaghairi. Akaiangalia saa yake, ilikuwa saa tatu na nusu usiku! Ilimwuma kuona hadi muda huo Hija alikuwa hajarudi! Hakuiona mantiki ya mkewe akijijua kuwa yuko peke yake huko aliko, lakini bado akawa anachelewa kurudi nyumbani.
Taswira ya kumwona Hija akiwa na shoga zake wamekaa baa ikajiunda. Ilikuwa ni tabia iliyojengwa na Fina ambapo mara nyingi anapomaliza shughuli yake ya kuuza duka na kufunga, hupenda kuhamia kwenye hiyo baa iliyokuwa jirani na duka lake na alipenda kuwachukua shoga zake kuwa nao, mmojawao akiwa ni Hija! Badi alikiri tabia hiyo ndiyo imemsababishia mkewe kutotulia nyumbani, tabia aliyokuwa nayo kabla hajamuoa. Lakini pia ilimpa wakati mgumu yeye mwenyewe Badi kwa kuwa alikwishamzoesha kumfuata huko na kumchukua mara kwa mara.
Alikuwa bado yupo kwenye taswira ya kumwona mkewe akiwa na kundi hilo la shoga zake kwenye baa hiyo ambayo ni maarufu, inayopendwa kutumiwa na wanaume wenye vipato vya juu, huku baadhi yao aliwajua kwa kupewa utambulisho na Fina na wakati mwingine na mkewe mwenyewe. Taswira hiyo ikamwonyesha mkewe amechanganyika na makundi ya wanaume usiku huo, kwa mara ya kwanza ilimpeleka mbali zaidi.
Kama vile ni mara yake ya kwanza kuanza kutambua kuwa ushoga uliopo kati ya Hija na shoga zake hao unaanza kuhatarisha ndoa yake, hali ya kutokuwa na imani na mizunguko ya mkewe ikaanza kuwa saratani kwenye akili yake kwa usiku huo!
Kabla ya kumuoa Hija, Badi alikuwa mshiriki wa genge hilo la kina Fina kwa kunywa nao pombe kwenye baa hiyo huku yeye mwenyewe akitambulika kama mteja hai wa hiyo baa. Tabia hiyo aliendelea nayo hata baada ya kumuoa Hija kwa kuamini kuwa, kama angeamua kuiacha ghafla tabia hiyo kwa kutokwenda huko, lakini pia akamzuia mkewe naye asiende, asingeeleweka hasa na Fina ambaye alitoa mchango mkubwa wa kuifanikisha harusi yao iliyokuwa gumzo! Ilikuwa ni kama sehemu ya kumshukuru Fina kwa kuwa naye karibu.
Ikiwa ni mara yake ya kwanza kuanza kuchanganyikiwa kikamilifu na kundi hilo linaloongozwa na Fina, Badi alikumbuka alivyotaka kumshirikisha Rajabu kwenye genge hilo kwa kwenda kumtambulisha, lakini baada ya kwenda mara kadhaa kujumuika nao, Rajabu akashtuka kuwa yuko hatarini kusukumiziwa mmoja wa shoga zake Fina ili awe bibi yake! Akamwonya Badi kuwa, kundi hilo halifai! Na halimfai hata kwa yeye pamoja na Hija kwa sababu lipo kwa ajili ya kuchukua wanaume za watu. Lakini pia, aina ya wanaume wenyewe wanaotembea nao, ni wale wasiojiheshimu na wanaweza kuwachanganya shoga zake Hija na Hija mwenyewe! Badi akakumbuka jinsi alivyoupuuza ushauri wa rafiki yake huyo!
Akiwa ametawaliwa na hofu kutoka kwa wanaume hao ambao ndio wanunuzi wakubwa wa vinywaji, Badi alikiri ni kweli baadhi ya wanaume hao walikuwa wapo kwenye ndoa zao, lakini walionekana kupenda zaidi huduma za kikahaba zitolewazo na kundi hilo la Fina. Alikubali kuwa, wasichana hao ni wajanja wenye uwezo wa kuwadhibiti wanaume za watu kimahaba kwa kuwafanyia kila kitu wanachokitaka! Fikra hizo zikamkumbusha mahaba aliyokuwa akipewa na Hija katika siku za awali za kuonana kwao! Akakumbuka yalivyompeleka puta, na bado yalikuwa yakimpeleka puta! Na sasa ni mkewe!
Wakati akiyafikiri hayo, Badi alikuwa amesimama chumbani kwake karibu na sofa dogo lililomo humo chumbani. Alipokuwa akiyafikiria mahaba hayo anayopewa na mkewe, hisia za wivu zikapenya kwenye moyo wake baada ya dhana kumwingia kuwa, huenda mahaba hayo kuna mwingine anayepewa! Akahisi kuishiwa nguvu, akakaa kwenye kochi kwa kujiachia kama vile alikosa mhimili wa kusimama!
Machale ya kuwa anachezwa shere na mkewe yakamjia! Safari za mara kwa mara za Hija kuaga anakwenda kwa Fina au wakati mwingine akiaga anakwenda kwao kuwasalimia wazazi wake, akaziona ni kama fursa iliyokuwa ikitumika kwenda kuonana na mabwana zake!
Fikra hizo zikamfanya Badi aifikirie milumbesa ya nguo za kifahari na vito vya thamani, manukato na vipodozi vya bei za juu na viatu vya kumwaga alivyonavyo Hija, tokea hajamuoa na baada ya kumuoa.
Lazima kuwe na mtu anayempa huduma hizo! aliwaza.
Ingawa awali kabla ya kumuoa alikuwa na dhana kuwa Hija angekuwa na bwana, lakini wazo hilo halikumpa usumbufu baada ya kujiona ni yeye ndiye anayefanya mapinduzi dhidi ya mtu mwenye kuingia gharama hizo. Na baada ya kukubali kuolewa, Badi akaamini, Hija angeachana na bwana huyo!
Kichwa chake kikiwa kimejikita kwenye tafakuri nzito, Badi alijiona akikiri ndani ya nafsi yake kuwa, alikuwa na safari ndefu ya kumtoa Hija kwenye mikono ya huyo anayemshuku kuwa ni bwana wake! Kwa mara ya kwanza mshawasha wa kutaka kumjua mwanamume huyo ni nani, ulimwingia!
Wivu ulimwumiza, lakini upendo kwa mkewe nao ukawa unachukua nafasi yake kiasi kwamba hakutaka kukubali kama Hija alikuwa mhuni! Nafsi yake ilikiri bila ya ubishi kuwa anampenda mkewe, na akakiri zaidi anampenda kwa uzuri wake na mahaba anayopewa! Na wivu ukaendelea kumwumiza alipoyafikiria mahaba hayo ndiyo aliyokuwa akipewa huyo jamaa!
Dalili za kuchanganyikiwa zikiwa zinaelekea kushika hatamu, Badi alisimama ghafla kutoka kwenye kochi alilokuwa amekalia. Akatoa simu yake mfukoni na kumpigia mkewe. Akaisikia simu ya Hija ikiita, lakini baada ya kuita kwa muda mfupi, simu ikakatwa! Yuko na bwana wake! fikra zake zikalenga huko.
Akaamua kupiga tena, safari hii kwa jazba zaidi. Akaisikia inaita tena. Baada ya miito michache, simu ikawa kimya, akawa na uhakika ilikuwa imepokewa, lakini mpokeaji alikuwa kimya.
“Haloh!” Badi alisema kwa hasira na kuhisi damu ikimchemka.
“Nipo getini, nifungulie!” sauti ya Hija isiyokuwa na chembe ya hatia ilisema kwa utulivu kwenye simu.
Jazba iliyokuwa imempanda Badi, ikamshuka. Kujua mkewe amerudi kulimpa afueni, lakini chembechembe za hasira zilikuwa bado zikitawala kwenye akili yake. Akatoka mwenyewe chumbani na kwenda kufungua geti.
Badi alisimama kando ya geti huku akiacha nafasi mkewe apite. Alikuwa bado amenuna na kuufanya uso wake utune. Hakusema lolote kwa mkewe alivyokuwa akiingia!
Hija alimwangalia Badi moja kwa moja usoni wakati akipita.
“Vipi mwenzetu?” Hija aliuliza kwa sauti ya kujiamini. “Ndivyo ulivyotakiwa uwe unamkaribisha mkeo kwa kununa?”
“Tutaongea ndani!” Badi alisema kwa mkato akiwa bado amenuna.
Hija akafanya tabasamu lililoubinua kidogo mdomo wake na kuingia ndani. Wakaongozana kimyakimya hadi chumbani. Walipoingia, Badi akaufunga mlango kwa ishara ya kuashiria kuwa kuna kesi ya kuzungumzwa ingawa mlango huo ilikuwa ni kawaida kuwa umefungwa wakati wote. Badi akatarajia Hija angesimama au kukaa akisubiri kusomewa risala. Lakini msichana huyo hakufanya hivyo! Kama vile hakuna mtu mwingine zaidi yake humo chumbani, akiwa ameuelekeza mgongo wake upande aliokaa Badi, Hija alizivua nguo zake moja baada ya nyingine huku akiangaliwa na Badi aliyekuwa akiendelea kuvimba kwa hasira.
“Hivi wewe unaondokaje nyumbani bila ya kumuaga mumeo ni wapi unakwenda?” Badi alikosa subira na sauti yake ilionyesha himaya ya kiutawala.
Kimya kifupi kilipita kati yao. Kisha kama vile Hija alijiwa na hisia kuwa kimya hicho kinamsubiri yeye akivunje, aliugeuza uso wake na kumwangalia Badi kwa macho yanayopendeza lakini yasiyokusudiwa kumpendezesha Badi. “Unazungumza na miye?” aliuliza.
Kama lingekuwa ni bomu, tayari lingeshakuwa vipandevipande kwa kutawanyika. Badi alihisi kichwa chake kama kinachotaka kulipuka kwa hasira! Alikuwa na uhakika Hija alimsikia alichozungumza, na alikuwa na uhakika alikuwa akionyeshwa dharau!
“Unataka kuniambia hukunisikia?” Badi aliuliza huku akitaka uso wake uonekane kuwa hayupo kwenye mzaha.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kama ningekusikia, ningekuuliza hivyo?” Hija aliuliza kwa kiburi.
“Yaani mimi nakuuliza, halafu tena unanijibu jeuri?” Badi alionekana kupoteza mhimili wa udhibiti wa hasira.
Akiwa amevaa khanga moja nyepesi aliyoifungia kifuani ikionyesha chupi pekee iliyokuwa ndani ya mwili wake, Hija alimgeukia Badi kikamilifu na kuangaliana kighadhabu.
“Jeuri yangu iko wapi?” Hija aliuliza. “We’ kama una jambo lako sema! Maana tokea nimekuja, sikuelewi! Umekuwa huna salamu, sura umeivimbisha kama vile…” akanyamaza na kuyatuliza macho yake usoni kwa Badi. “Au unadhani nimetoka wapi? Kwa bwana?”
Swali aliloulizwa Badi ndilo lililokuwa kiini cha hasira aliyokuwanayo, lakini pia ilikuwa ni hoja yake msingi aliyokusudia kumhoji Hija! Hata hivyo, kuulizwa kwa swali hilo ni kama vile Hija alimuwahi. Ikawa kama vile Hija aliyasoma mawazo yake! Badi akajiona kama aliyebanwa kwenye kona ya ulingo wa kupigana ngumi.
Ni kweli alitaka kujua Hija alikuwa wapi kama siyo kwa bwana! Lakini swali aliloulizwa asingekubali limwingize kwenye mtego wa kukubali; kufanya hivyo kungehalalisha fikra za Hija za kumwona kuwa alikuwa akilia wivu! Likamchanganya Badi!
Ghafla akaupata mwanya wa kutoka! Angeitumia sababu ya pombe ambayo harufu yake ilisikika kutoka kinywani kwa Hija ingawa hakuonekana kulewa, lakini alikuwa na uhakika akili ya mkewe ilikuwa ikielea kwenye ulevi.
“Ina maana kilichokutoa hapa nyumbani bila ya kuaga, ni kwa ajili ya kwenda kulewa?” Badi aliuliza.
Hija akaganda kidogo huku akiendelea kumwangalia Badi. Ilikuwa kama vile swali aliloulizwa alikuwa hakujiandaa nalo.
“Unanikasirikia kwa sababu ya kukurudia nyumbani nikiwa nimekunywa? Au..?” aliuliza.
Badi akagundua Hija yupo kwenye kutaka kuzungusha maneno ili apate mwanya wa kulijibu swali hilo vizuri. Akaminya palepale, “Nakuuliza hicho ndicho kilichokutoa nyumbani bila ya kuniarifu?” safari hii sauti yake alitaka Hija aione ni yenye dalili ya ugomvi.
“Hicho ndicho kilichokuudhi?” Hija aliuliza kwa dharau.
Badi akasimama kama kisiki. “Unanijaribu?” lilikuwa onyo!
Kama vile hakutishwa na onyo hilo, Hija alimwangalia Badi kwa macho yaliyotulia. “Unataka kunipiga?” aliuliza kama vile akiulizia jambo la kawaida.
“Ukinilazimisha, nitakupiga kweli!” uso na sauti zilimwonyesha Badi alikuwa yupo kwenye nyuzi joto za hasira kwa kiwango cha juu.
“Usithubutu!” Hija alionya.
“Eti nini?” Badi aliuliza huku akionekana kupoteza mhimili wa kujizuia.
“Umetaka mwenyewe kunioa? Sasa nini? Umenikuta nikiwa sina ngeu babu ehh! Kama nakushindwa niache, dini yetu inakupa nafasi ya kunipa talaka! Mambo ya kupigwa aah, aah, sijayazoea!”
Ulikuwa mjeledi tosha uliomchapa Badi. Kauli hiyo ya mkewe ikawa kama imemjeruhi na kummaliza nguvu. Akaganda kama aliyekuwa akishangaa kukabiliana na kiumbe asichokijua kilichomtokea ghafla. Wakatazamana jicho kwa jicho na Hija kama watu waliokuwa maadui waliokutana bila ya kutarajia!
“Hija unaniambia kauli hiyo?” Badi aliuliza huku sauti yake ikisikilizika kwenye lawama zaidi kuliko kuonya.
uku sauti yake ikisikilizika kwenye lawama zaidi kuliko kuonya.
“Unataka nikwambieje Badi?” Hija alisema akiwa amegeuka ghafla na kuonekana siye yule sekunde chache alikuwa akijibu kwa jeuri na kujiamini. Sauti yake ilikuwa imetulia yenye ushawishi wa kumwonyesha Badi kuwa alikuwa akizungumza na mtu wake wa karibu. Alishakigeuza kibao, aliamua kucheza na akili ya Badi. Yeye ndiye akawa wa kumlalamikia Badi! “Wewe mwenzangu ndiye uliyeanza kunipokea kwa hasira,” alizicheza karata zake. “Ile tu kuniona, uso huo umekuvimba! Najua nimeondoka bila ya kukuaga, hilo nakubali ni kosa, lakini siyo kwa njia ya kunipokea kama ulivyonipokea Badi,” sauti yake ilionyesha kutaka kulia. “Mimi ni mkeo, nichukue taratibu hadi chumbani, kisha uniulize, haya mke wangu ulikuwa wapi hadi saa hizi? Umeondoka hukusema, na umerudi ukiwa umekunywa! Hayo ndiyo maswali ya kuniuliza mume wangu, kisha nisubiri nitakujibu nini! Lakini sivyo! Wewe ghadhabu tu na kutaka kunipiga…tutafika kweli Badi?”
Ikawa sawa na kiinimacho kilichomwingia Badi. Ikaonekana ameshushuliwa yeye, akanywea na kuitumbukiza mikono kwenye mifuko ya suruali. Akaanza kuzunguka humo chumbani, akaenda na kurudi kama aliyekuwa akitafuta mahali pa kuanzia huku akiangaliwa na Hija.
“Ulikuwa wapi?” Badi aliuliza. Hakuwa mkali tena!
“Nilikuwa na da’ Fina, tena walitarajia ungekuja,” Hija alizidi kuzishusha presha za Badi.
“Si nilikuarifu kama ningechelewa kurudi nyumbani?”
“Nilitarajia ungenipigia simu kabla hujarudi nyumbani, ningekujulisha unifuate kwa da’ Fina.”
“Kwa nini hukuniarifu kama unakwenda huko?”
“Nilijua ungenipigia simu. Lengo langu nilitaka unipitie turudi pamoja nyumbani. Baada ya kuona kimya, nikahisi umechukia. Nimeamua kurudi peke yangu Badi! Sasa ningefanya nini?”
“Baada ya kuniona kimya kwa nini usinipigie simu?”
“Nimpigie simu mtu aliyechukia? Si kila mtu angejua nilikuwa nagombana na mume wangu kwenye simu!”
Kimya kikapita kati yao, ikaonekana kama Badi ameishiwa hoja.
“Kwa nini hukunifuata?” Hija akaimalizia karata yake ya mwisho baada ya kugundua Badi ameishiwa hoja.
“Ningekufuata vipi wakati nimechelewa kutoka kazini?”
“Baada ya kufika nyumbani ukanikosa, kwa nini usinipigie simu kujua niko wapi?”
“Si nilikuwa ndiyo nakupigia, ukanijibu uko getini?”
Akijua ameishaishusha presha ya Badi, huku akionyesha kutaka kufanya shughuli nyingine, Hija alisema, “Mume wangu uwe na subira usiiweke hasira mbele…” akaishia kwa kumwonya Badi ambaye alijenga utulivu na sakata lao kuishia kwa kila mtu kwenda kuoga.
Wote wakiwa wamebadili nguo baada ya kuoga, walikwenda mezani kwa ajili ya chakula cha usiku.
Usiku wakiwa wamelala kiubavu-ubavu, wote wakielekea upande mmoja wakizungumza maongezi ya hapa na pale ya kitandani yanayovutia usingizi, kabla ya kupitiwa na usingizi, Badi alilikamata bega la Hija na kulivutia kwake kwa lengo la kumgeuza ili wachezeane kabla ya kuingia kwenye hitimisho la tendo la ndoa.
Hija akalitambua kusudio la Badi, palepale akafyetua kiwiko cha mkono wake kikampiga Badi ubavuni!
“Sijisikii vizuri!” Hija alisema bila ya kugeuka.
Badi akaacha kulivuta bega la Hija, lakini mkono wake ukaendelea kuganda kwenye bega hilo. Akazubaa kwa sekunde chache, kisha kwa unyonge, aliuondoa mkono begani kwa Hija. Akajilaza chali kama mtu aliyechoka. Akatulia ndani ya kiza huku akiangalia juu kwa sekunde kadhaa. Akazama kwenye fikra za peke yake, kisha akajigeuza taratibu, akapeana mgongo na Hija. Ukawa mwisho wa maongezi yao usiku huo!
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Badi kunyimwa unyumba tokea alivyofunga ndoa na Hija!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment