Search This Blog

Monday 24 October 2022

MKIMBIZI - 4

 

    Simulizi : Mkimbizi

    Sehemu Ya Nne (4)





    “What did you expect Tigga(Ulitegemea nini Tigga)? Yule ni daktari, mtaalamu...ananieleza mambo kama hayo unategemea nitaacha kumuamini?

    “Yule sio mtaalamu lolote ni muuaji mkubwa! Nimeshuhudia kwa macho yangu akishirikiana na wenzake wawili kumtesa mtu na hatimaye kumuua!” Nilimkatisha Aulelia kwa jazba. Niliona Aulelia akichanganyikiwa, asijue iwapo aniamini au ndio aamini kuwa kweli mimi ni mwehu, kwani kwake Martin Lundi ni mtaalamu na mimi nasema ni muuaji.

    “How could you believe him Aulelia? We’ unanijua mimi!”

    “Sikumuamini wala sikumbishia Tigga! Nilichomuambia ni kuwa ni mimi ndiye nitakayeamua iwapo ni kweli Tigga ana wazimu au vinginevyo pale nitakapomuona kwa macho yangu mwenyewe! Ndivyo nilivyomwambia Tigga!” Alinijibu na kutazama pembeni huku akifuta machozi. Na hivyo ndivyo nilivyotegemea Aulelia angelichukulia swala lile.

    “Sasa kama ulikuwa na mtazamo huo kwa nini ulinifanya vile pale tulipokutana?” Nilimuuliza.

    “Habari zako zilizagaa kwenye magazeti Tigga, na hazikuwa habari nzuri. Halafu nikaanza kupokea meseji za simu...” Aliniambia

    “Meseji za simu? What has that got to do with any of this?” Nilimuuliza kwa mshangao na kutoelewa, nikitaka kujua hizo meseji za simu zinahusika vipi na habari zile tulizokuwa tukiziongelea. Aulelia alinitazama kwa muda kisha akageuka pembeni na kutoa simu yake ya kiganjani kutoka kwenye mfuko wa koti lake la suti alilokuwa amevaa. Alibofya bofya kwa muda kwenye ile simu kisha alinikabidhi bila ya kusema neno. Niliipokea ile simu huku nikimtazama kwa macho ya kuuliza, lakini Aulelia aligeuka pembeni.

    Niliitazama ile simu nikaona Aulelia alikuwa ameniwekea sehemu iliyoonesha ujumbe mfupi wa simu, nami nikaanza kuusoma. Ulikuwa ni ujumbe mbaya wa vitisho vikali sana, na matusi mazito ya nguoni ambao uliishia hivi:

    Nina hamu na damu yako! Najisikia kukuua na kuutafuna moyo wako. Ole wako nikutie mikononi malaya mkubwa we!

    Nilishangazwa na ujumbe ule na nikainua uso kumtazama Aulelia, nikaona alikuwa akinitazama kwa makini.

    “Aulelia! Ni nini hii? Huu ujumbe umetoka wapi? Unahusu nini? Una ugomvi na huyu mtu? Ni nani huyu?” Nilimuuza lakini alizidi kunitazama kwa muda kisha alinijibu.

    “Tazama mtumaji wa hiyo meseji ni nani” Nilimtazama kwa mshangao, lakini nilitekeleza na kwa kihoro kikubwa nikaona kuwa ule ujumbe ulikuwa umetumwa kutoka kwenye simu yangu!

    Niliiweka kwenye kochi ile simu na kusimama nikimtazama Aulelia kwa mshangao mkubwa.

    “Si..si..sikutuma mimi ujumbe huu!” Nilimwambia huku nikiinyooshea kidole ile simu. Aulelia alizidi kunitazama bila ya kusema neno. “Simu yangu ilipotea kule msituni...na hadi hivi niongeavyo sina simu! Nina hakika akina Martin Lundi waliichukua! Si nilikuambia? Hao ni watu wabaya sana!” Niliendelea kujieleza, lakini Aulelia aliichukua ile simu na kubofya tena kabla hajanikabidhi kwa mara nyingine. Niliipokea huku nikimtazama kwa mashaka na kusoma ujumbe mwingine uliotumwa kwa Aulelia kutoka kwenye simu yangu.

    Nimeshaua watu wengi na sasa najisikia kuutafuna moyo wako! Kaa chonjo, nakuja kukumaliza! Changudoa mkubwa we!

    Nilichoka! Mara moja nilielewa kuwa ile ilikuwa ni njama ya Dokta Lundi ya kutaka kunifarakanisha na watu wangu wa karibu ambao walielekea kuniamini. Na bila shaka yoyote nilielewa sababu ya Aulelia kufanya mambo aliyofanya siku ile nilipokutana naye pale katikati ya jiji. Machozi yalinibubujika bila kituo huku nikitikisa kichwa kwa masikitiko.

    “Pole sana Aulelia, lakini mimi siye niliyetuma hizi meseji rafiki yangu. Why should I ? Ni wazi hii ni mbinu ya Dokta Lundi kutaka kunifanya mimi nionekane kichaa kwako!” Nilimwambia rafiki yangu huku nikitokwa na machozi.

    “Ni kweli Tigga. Niliamini kuwa umepata wazimu baada ya kuanza kupata hizo meseji kutoka kwako...lakini nadhani sasa naelewa kilichotokea. Kama unachosema ni kweli...”

    “Tangu lini nikaanza tabia ya uongo? Ninachokuambia ni kweli. Hawa watu wanataka kunichafua ili kila mtu apoteze imani na mimi...wewe ulitumiwa hizi meseji ili uamini kuwa mimi ni mwehu na upoteze kabisa imani na mimi! “

    Aulelia aliniambia kuwa zile meseji zilikaribia kumtia yeye wazimu. Mara nyingine alikuwa akipigiwa simu usiku wa manane kwa ile simu yangu na akipokea hakuna anayeongea. Akanionesha ujumbe mwingine ambao ndio ulionichanganya zaidi.

    Unatembea na mchumba wangu. Sasa nimegundua. Nimemuanza yeye halafu nakujia wewe! Nitainywa damu yako bila kuichemsha, Kimburu we!

    Nilibaki mdomo wazi.

    “Siku iliyofuata nilipata habari za mkasa uliomkuta Kelvin pale nyumbani kwake. Nilichanganyikiwa!” Aulelia aliniambia kwa huzuni.

    Sikuwa na la kusema. Angalau nilikuwa nimeelewa ni nini kilichotokea kwa rafiki yangu Aulelia. Nilijenga chuki kubwa kwa yule mtu aliyejiita Martin Lundi, kwani mambo aliyokuwa akinifanyia yalikuwa hayavumiliki.

    Tulikumbatiana na rafiki yangu Aulelia na kuombana radhi.

    Nilimuelezea juu ya mkasa ulionikuta kule msituni kwa ufupi sana.Ingawa aliniomba sana niendelee kujificha pale kwake mpaka hapo mambo yatakapopoa, sikukubali. Nilimwambia kuwa ilikuwa ni salama zaidi kwake kama akiendelea kuwa mbali nami kwa kipindi hiki cha matatizo.

    Nilichukua begi langu na kuagana na rafiki yangu Aulelia, nikimuacha akibubujikwa na machozi. Angalau nilikuwa nimefumbua ukweli fulani katika kitendawili hiki kilichonizunguka.



    --



    Nilikutana na Kachiki kwa bahati mbaya sana. Na nilipokutana naye sikuwa na hata chembe ya wazo kuwa yeye ndiye ambaye angenifunua macho kuhusu kile kitendawili cha pili nilichoachiwa na Mr.Q, The Rickshaw.

    Niliondoka nyumbani kwa Aulelia pale Kijitonyama nikiwa mwingi wa furaha kuwa angalau nilikuwa nimefanikiwa kuzishinda fitna za Dokta Martin Lundi na kurudisha maelewano mazuri na rafiki yangu Aulelia. Aidha, nilikuwa nimefanikiwa kugundua njia aliyotumia yule mtu muongo,mfitinishaji na muuaji katika kunifarakanisha na watu wangu wa karibu, kama Aulelia.

    Ndio maana walichukua simu yangu kule msituni!

    Nilipanda basi la Kariakoo kutokea Mwenge nikiwa na nia ya kutafuta hoteli itakayoniridhisha katikati ya jiji na kuanza kupanga mikakati mipya ya kukabiliana na akina Martin Lundi, nikiwa na nia ya kutafuta namna ya kujisalimisha kwenye vyombo vya dola nikiwa na ule ushahidi wangu. Nilidhani kuwa kufikia sasa wale wabaya wangu walishajua kuwa huwa najificha kwenye nyumba za wageni zilizojiegesha nje kabisa ya jiji. Sasa mimi niliamua kuhamia kwenye hoteli na katikati ya jiji. Swala la pesa bado lilikuwa kikwazo, kwani nilijua elfu hamsini nilizoongezewa na dada yangu Koku, zingetosha kwa malazi ya siku nne tu hotelini. Nikiongezea na pesa zangu zilizobakia, labda ningeweza kuishi kwa siku tano zaidi. Baada ya hapo nisingekuwa na ujanja.

    Lakini bado nilikuwa na jukumu la kukamilisha kazi niliyoachiwa na Mr. Q, na siwezi kuishi vema na nafsi yangu kama sijawafikisha kwenye mikono ya sheria wale wauaji wengine waliomfikisha yule mtu kwenye mauti dhalili kama yale kule msituni. Mauti yasiyo na maziko ya kueleweka na bila jamaa zake kujua kuwa amefikwa na mauti.

    Hivyo nilikuwa naomba Mungu anisaidie katika wiki mbili ambazo nitaweza kuishi hotelini niwe nimetimiza azma yangu ya kumlipizia kisasi yule mtu na kuwafikisha kwenye sheria akina Martin Lundi.

    Labda kufikia muda huo nitakuwa nimeshawasambaratisha akina Martin Lundi, au nikawa nimepata namna ya kujisalimisha kwenye mikono halali ya sheria na kuukabidhi ule mkanda wenye ushahidi katika mikono salama.

    Lakini nitaweza?

    Nikiwa nimezama kwenye mawazo yangu haya, ndipo niliposhitushwa na kelele za mabishano ndani ya daladala baina ya kondakta na dada mmoja aliyekuwa akidai kuwa ameibiwa pesa zake na hivyo hakuwa na nauli. Kutokana na mavazi yake yaliyoleta hisia kuwa alikuwa changudoa, hata abiria waliokuwamo mle ndani walianza kumshutumu na kumtetea kondakta kiasi yule dada alianza kuangua kilio. Basi nilijitolea kumlipia na safari ikaendelea kwa amani. Lakini nilipoteremka Kariakoo, yule dada alinifuata tena na kuniomba nimsaidie mia hamsini nyingine ili aendelee na safari yake ya Gongo la Mboto, kwani ni kweli kuwa alikuwa ameibiwa pesa zake zote.

    Nikiwa na mashaka kuwa huenda yule dada alikuwa ni changudoa tu wa mjini anayetaka kunifanya bwege kwa kujitolea kwangu kumlipia nauli hapo mwanzo, nilianza kumhoji juu ya safari yake huku nikiendelea kutembea kuelekea kwenye maeneo niliyohisi yanaweza kuwa na hoteli ilhali yule dada akinifuata.

    Ni hapo ndipo nilipogundua kuwa alikuwa anaitwa Kachiki, na kwamba alikuwa akifanya kazi ya uhudumu katika baa moja iliyoitwa Uno Trabajo iliyoko maeneo ya Gongo La Mboto. Nilikumbuka kuwa alipandia basi la Kariakoo maeneo ya Makumbusho, na nilipomuuliza kuwa ndipo alipokuwa akiishi, alinifahamisha kuwa yeye na wenzake wanaofanya kazi katika ile baa huwa wanalala palepale baa kwani mmiliki wa baa ile alikuwa amewajengea vyumba vya kulala, ila alienda kule Makumbusho kumfuatilia mwenzao ambaye aliondoka kazini siku mbili zilizopita na hakurejea, ambapo alipomkuta aligundua kuwa alikuwa ameamua kuacha kazi kienyeji tu kwani alikuwa amepata bwana wa kumweka ndani, kisha akaendelea kulaani tabia ile ya yule mwenzake ya kuamini wanaume wa mpito kiasi cha kuamua kuacha kazi, lakini kufikia hapa nikawa makini sana na ile taarifa yake.

    “Mnapewa na malazi hapo hapo?” Nilimuuliza.

    “Tena kila mtu na chumba chake bwana! Chakula tunakula hapo hapo, hata ukilipwa mshahara mdogo kuna tatizo gani? Kwa maisha ya hapa mjini Anti mtu ukipata pa kuweka ubavu bila kulipia kodi unataka nini tena zaidi?” Kachiki alisema kwa hamasa, nami nikawa nimeanza kulizungusha lile jambo kichwani mwangu.

    Akina Martin Lundi sasa hivi lazima watakuwa wananitafuta kwenye nyumba za wageni, na muda si mrefu msako wao utahamia kwenye mahoteli. Muda si muda watanikamata, kama jinsi walivyoniibukia kule Kigamboni. Na pesa zilikuwa zinaniishia kwa kasi sana. Lakini hata siku moja wale watu wabaya hawatafikiria kunitafuta kwenye mabaa, labda nikutane nao kwa bahati mbaya tu wakiwa kwenye manywaji, jambo ambalo uwezekano wake ni moja kati ya mia moja.

    Nilifanikiwa kumshawishi Kachiki anipeleke huko kwenye hiyo baa aliyokuwa akifanyia kazi na aniunganishie hicho kibarua alichokiacha huyo rafiki yake. Alinishangaa kupita kiasi, hakuamini kabisa kuwa mtu kama mimi naweza kuwa na shida ya kibarua tena cha hovyo kama jinsi yeye alivyokiona kama kile. Ilibidi niseme uongo wa kukata na shoka lakini nilifanikiwa, kwani nilimwambia kuwa pale nilikuwa naenda kutafuta nyumba ya wageni nilale kwani nilikuwa nimelaghaiwa na mwanaume aliyeniweka ndani kinyumba baada ya kunitorosha kwetu Kisiju, lakini sasa amepata bibi mwingine na ameamua kunitelekeza kwenye nyumba ya kupanga kwa wiki nzima bila taarifa wala matumizi yoyote. Nikimpigia simu anasema yuko bize. Nikaamua kuondoka lakini baada ya kuuona mji, sikuwa tena na haja ya kurudi kwetu Kisiju.

    Kachiki aliipokea ile hadithi yangu ya uongo kwa masikitiko makubwa hasa akiioanisha na lile tukio la yule rafiki yake aliyetoka kumfuatilia kule maeneo ya Makumbusho. Moja kwa moja alikubali kunipeleka kwenye ile baa aliyokuwa akifanyia kazi kuchukua nafasi ya huyo mwenzao aliyeacha kazi kama namna ya yeye kulipa fadhila yangu.

    Ingawa kwa wakati ule niliona kuwa ile ilikuwa ni njia ya kujipatia mahala pa kujihifadhi kwa muda na wakati huo huo kujipatia kipato kidogo, lakini umuhimu wa uamuzi wangu wa kumsaidia yule dada na hatimaye kuamua kwenda kuomba kibarua kwenye ile baa aliyokuwa akifanyia kazi nilikuja kuuona baadaye.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    --



    Uno Trabajo ilikuwa ni baa ya aina yake. Ilikuwa ni vigumu sana kuamini kuwa kule Gongo la Mboto kuliweza kuwa na baa kama ile, kwani ilikuwa katika kiwango cha kimataifa kabisa. Na kama alivyonieleza Kachiki, mmiliki wa ile baa aliwawekea wahudumu wake mazingira mazuri sana ya kazi, kwani pamoja na kuwapatia vyumba vya kulala nyuma ya ile baa, pia aliwapatia mahitaji kama sabuni, dawa za meno na matibabu.

    Siku ile ile nilipata kibarua cha uhudumu wa baa kwa mshahara wa shilingi elfu ishirini kwa mwezi pamoja na mahitaji yote hayo muhimu,kwangu la msingi likiwa ni malazi na zile elfu ishirini. Nilipelekwa kwenye chumba changu kidogo lakini kisafi cha kuridhisha tu, kilichokuwa na kitanda kidogo cha futi tatu na mashuka yenye lebo ya ile baa.

    Nilijifungia mle chumbani na kuanza kuweka vitu vyangu kwa mpangilio nilioutaka. Nilitoa lile burungutu la pesa nilizopewa na Koku na kuanza kuzipanga vizuri pamoja na pesa nyingine nilizokuwa nazo, na wakati nafanya hivyo niliona kitu kama kadi ndogo ikidondoka kutoka kwenye lile burungutu nililopewa na dada yangu. Niliiokota na kugundua kuwa ilikuwa ni kadi ya anuani, ambayo dada yangu aliifumbata pamoja na zile pesa wakati ananipa nami bila kuangalia nilizishindilia mfukoni mwangu pale hospitali ya wilaya ya Temeke. Niliisoma ile kadi na moyo ulinilipuka na kuanza kunienda mbio kwani ile kadi ilikuwa imeandikwa ifuatavyo:



    John Vata

    Assistant Commissioner of Police

    Special Op.



    Chini ya maelezo hayo zilifuatia namba za simu za waya, za kiganjani, anuani ya posta na anuani ya barua pepe. Nilikaa kitandani taratibu huku nikiendelea kuitazama ile kadi bila ya kuamini, nikijua wazi kuwa Koku alikuwa ameniwekea ile kadi makusudi, na kwa maana hiyo, lile jina nililoliona kwenye ile kadi ndilo lilikuwa la yule afisa wa polisi anayekata ndevu katika mtindo wa Timberland.

    “Mungu wangu! Kumbe pale ofisini nilikuwa naongea na Kamishna msaidizi wa polisi!”

    Nilijisemea mwenyewe na kutazama tena lile jina lililoandikwa kwenye ile kadi.

    John Vata.





    Sikuwa nimepata kulisikia lile jina mahala popote kabla ya pale. Nilijikuta nikitikisa kichwa na kutabasamu nikistaajabia werevu wa dada yangu Koku, kwani nilijua kuwa alikuwa amefanya vile kusudi kwa sababu alitaka nijisalimishe kwa yule askari ambaye alimuona kuwa ni mstaarabu.

    Lakini mimi naweza kukuamini John Vata?

    Na kwa nini afisa mkubwa kama yule afuatilie swala lile yeye mwenyewe? Mtu mwenye wadhifa kama ule alitakiwa atume vijana wake wafuatilie, kisha yeye aletewe taarifa tu ya maendeleo. Vije aingie yeye mwenyewe kwenye upelelezi na hata kufikia hatua ya kupambana na muuaji kama Macho ya Nyoka namna ile?

    Nilifikiria sana juu ya jambo lile, kisha nikapitisha uamuzi.

    Baada ya kuweka vitu vyangu katika utaratibu nilioutaka mle ndani, nilitoka na kufunga mlango wa chumba changu kwa nje na kumfuata Kachiki aliyekuwa amejilaza chumbani mwake. Nilimuuliza ni muda gani tulikuwa tunaanza kazi akaniambia kuwa ni saa tisa mchana watu wakianza kutoka maofisini, ingawa kwa muda ule huduma ilikuwa ikitolewa lakini hakukuwa na wateja wengi hivyo tuliweza kupumzika tu na kwamba kuna zamu maalum huwa zinapangwa kwa kuhudumia muda ule wa kabla ya saa tisa. Basi nilitoka nikimuambia kuwa nilikuwa naenda kununua nguo za mitumba kwani niliona kuwa nguo zangu za kushindia zilikuwa haziendani kabisa na mazingira yale.

    “Kweli shoga, maanake hizo suti zako na mazingira haya hata si mwake!” Kisha tukacheka nami nikatoka, nikiwa na ule mkanda wangu wa video ndani ya sidiria yangu. Nilienda mpaka Kariakoo, huko nikatafuta kibanda cha simu na kuipiga ile namba ya simu ya kiganjani ya Kamishna Msaidizi wa polisi John Vata na kuisikiliza ikiita huku moyo ukinienda mbio.

    “John Vata!” Sauti niliyoikumbuka kuwa ni ya yule afisa wa polisi aliyenikamata pale ofisini kabla ya Macho ya Nyoka kutokea ilipokea ile simu.

    “Tigga Mumba!”

    Kimya kilitanda kwa muda, nikisikia yule afisa akihema upande wa pili wa ile simu.

    “Uko wapi? Nahitaji kuongea na wewe...na ukumbuke kuwa bado uko chini ya ulinzi na...”

    “Mimi ndiye niliyekupigia afande hivyo naomba unisikilize!”

    “Unatakiwa ujisalimishe ndio uongee hayo unayotaka kuongea, sio kwenye simu namna hii...okay, unasemaje?”

    “Niko tayari kujisalimisha afande, lakini nataka kwanza umtafute na umweke chini ya ulinzi mtu aitwaye Martin Lundi...Dokta Martin Lundi. Nitakapothibitisha kuwa huyo mtu

    amewekwa chini ya ulinzi mimi nitajitokeza mahala popote utakapotaka, na nitakuja na ushahidi wa kukuonesha kuwa huyo ndiye mtu unayetakiwa umsake na sio mimi. Tena nisikie na nione kwenye vyombo vya habari kuwa amekamatwa...magazeti, redio na televisheni...sio uniletee stori tu kuwa...”

    “Tigga...”

    “Sikiliza bwana! Sio uniletee habari tu kuwa tayari amekamatwa bila mimi kuona ushahidi wa hilo. Bila hivyo sijitokezi ng’o!”



    “Tigga, unafanya kosa kubwa. Ujue sisi hatushindwi kukutia mikononi, ni swala la muda tu. Na ujue kwamba sifanyi kazi kwa kupewa mashinikizo na watu wanaokimbia mikono ya sheria. Lakini nakuhakikishia kuwa hata usipojitokeza, mimi nitaendelea kukuwinda mpaka n’takutia mikononi tu...”

    “Na ujue kuwa unaweza kuendelea kuniwinda na kujigamba namna hiyo kwa sababu mimi niliokoa maisha yako kutoka kwenye kifo kilichokuwa mikononi mwa yule muuaji aliyetaka kuniteka pale ofisini kwetu siku ile. Usisahau hilo kabisa!” Nilimjibu kwa hasira. John Vata alikuwa kimya kwa muda na nikahisi alikuwa amechomwa na ukweli wa maneno yangu.

    “Sasa utafanya ninavyokuambia au hutafanya?” Nilimuuliza baada ya kuona amekuwa kimya kwa muda mrefu.

    “Sitoweza kumkamata Dr. Martin Lundi kwa kusikiliza uzushi wako tu mwanamke, na kama huna la msingi kata simu na usubiri jinsi nitakavyokutia mbaroni!” Alinijibu kwa ile sauti yake ya utulivu mkubwa usioendana kabisa na mazingira ya mjadala ule, kwani pale alitakiwa awe mkali lakini yeye alikuwa mpole sana.

    Kama jinsi alivyomjibu Macho ya Nyoka kwa upole wa hali ya juu kabla hajamshambulia kwa teke lililoipangusa bastola kutoka mikononi mwa yule muuaji.

    Hapo nilijua kuwa John Vata alikuwa mtu hatari sana kupambana naye kwani anapochukia huwa anakuwa mpole. Nilianza kuogopa.

    “Kwa nini unawahi kunishutumu kuwa ninazusha kabla hujafanya uchunguzi?”

    “Martin Lundi unayemsema ni daktari bingwa wa magonjwa ya akili wa muda mrefu. Ni mzee wa miaka sabini na tano, na sasa ni mstaafu anayesumbuliwa na maradhi ya kiharusi. Anaishi kwenye nyumba aliyojenga shambani kwake Kibaha, hivyo hawezi kuwa ndiye mtu unayemsema wewe kuwa eti alikuwa na wauaji wengine huko porini, ambaye aliendesha helikopta baada ya mauaji ya kule msituni na kuwa ndiye anayekuwinda kwa nia ya kukuangamiza. Kwa hiyo kata huo upuuzi na ujisalimishe mara moja!”

    Nilibaki mdomo wazi. Huyu askari ameyajuaje yote haya nami sijawasilisha maelezo yoyote kwenye vyombo vya dola? Yaani yule mtu sio Martin Lundi?

    “We’ binti upo? Sema ulipo ili nije tuonane, sisi wawili tu.Nadhani tunaweza kusaidiana katika hili.”

    Bado nilikuwa nimepigwa bumbuwazi.

    “Um...Umejuaje yote hayo? Yule mtu sio Martin Lundi? Ina maana na nyie mlikuwa mnajua juu yake? Au na wewe ni mwenzao?”

    “Habari zote hizo zilikuwa kwenye maelezo yako uliyoandika kwa muajiri wako pale ofisini. Ulitakiwa na mwajiri wako uandike yale maelezo kwa maelekezo yangu. Na baada ya kupata maelezo yale nilianza kuyafuatilia na ndio nikagundua hayo juu ya huyo Martin Lundi wako uliyemtaja kwenye maelezo yako.”

    Nilikata simu.

    Nilihisi dunia ikizunguka nami nikizunguka pamoja nayo. This is impossible!

    Kwa hakika nilichanganyikiwa.

    Nililipa pesa za muda nilioongea na kuondoka eneo lile haraka. Kwa mara nyingine tena Martin Lundi alikuwa amenizidi kete.

    Alitumia jina la uongo lakini la mtaalamu wa kweli wa magonjwa ya akili, aliyestaafu kazi muda mrefu.

    Ama kwa hakika yule ni Martin Lundi muongo!

    Sasa kama Dokta Martin Lundi halisi ni mzee wa miaka sabini na tano na mgonjwa wa kiharusi, yule mtu aliyekuwa kule msituni anayejiita Dokta Martin Lundi ni nani?

    Nilitazama saa yangu nikaona saa tisa ilikuwa inakaribia sana, na bado nilikuwa sijanunua hizo nguo nilizodai kuwa naenda kununua. Lakini nilijua nilipanga kulitatua vipi tatizo hilo, hivyo nikakamata teksi na kwa mara ya kwanza tangu niingie jijini kutoka kule Manyoni kilipoanzia hiki kizaazaa, nilimwamrisha dereva anipeleke nyumbani kwangu nilipopanga pale Upanga kwenye nyumba ya msajili.

    Nilipanda ngazi kuelekea kwenye nyumba yangu iliyokuwa katika ghorofa ya pili ya jengo lile la msajili huku moyo ukinidunda na nikiwa makini sana. Wengi wa wapangaji wenzangu katika jumba lile walikuwa ni wahindi ambao sikuwa na mazoea nao, hivyo sikuwa na wasiwasi wa ule umbea wa mitaa yetu ya uswahilini, ambapo baada ya habari zangu kutangazwa kwenye redio na magazeti, muda huu ningekuwa natumbuliwa macho ya udaku na bila shaka baadhi ya majirani wangeanza kupiga simu polisi kuwaarifu kuwa nilikuwa nimerudi nyumbani kwangu.

    Geti langu lilikuwa limefungwa vilevile kama nilivyoliacha.

    Nilipanda kwenye ule mlango wa chuma uliozatiti usalama mbele ya mlango wangu wa mbele na kufungua tungi la kioo lilitakiwa liwe linaifunika taa iliyokuwa mbele ya mlango wangu ambalo ndani yake hakukuwa na taa yoyote hivyo lilibaki limefungwa pale kwenye dari kama urembo tu. Nililitoa lile tungi na kutumbukiza mkono wangu ndani yake nikatoa funguo zangu za nyumba, kisha nikalifunga tena pale kwenye dari.

    Hii ilikuwa ni sehemu yangu ya kuficha funguo zangu miaka yote, na zaidi ya dada yangu Koku, hakuna mtu yeyote mwingine aliyeijua. Niliingia na kujifungia kwa ndani. Niliitazama nyumba yangu kwa upendo mkubwa kwani nilikuwa nimeipamba kwa namna nilivyotaka, na ilikuwa vile vile. Bila kupoteza muda nilienda moja kwa moja hadi kwenye runinga yangu iliyokuwapo pale sebuleni na kuigeuza kule nyuma...



    --



    Baada ya muda niliingia chumbani na kuchagua baadhi ya nguo zangu za kushindia ambazo niliona zingeendana na mazingira ya kule kwenye kibarua changu kipya na kuziweka kwenye mfuko wa nailoni nilioupata mle ndani. Niliiangalia nyumba yangu kwa mara ya mwisho na kufungua mlango ili niondoke,na hapo hapo nilisimama ghafla nikipatwa na mshituko mkubwa.

    Nilikuwa natazamana uso kwa uso na yule askari wa kike niliyemtoroka kule kwenye ile nyumba ya wageni ya Kigamboni, safari hii akiwa katika mavazi yake ya kiaskari.

    Niliguna kwa mshituko huku mfuko wangu wa nguo ukinidondoka na hapo hapo yule dada alinisukumia ndani kwa nguvu naye akaingia na kuufunga ule mlango kwa ndani.

    Nilijiinua taratibu kutoka sakafuni nilipoangukia baada ya kusukumwa na yule dada na kumtazama kwa macho ya woga na wasiwasi mkubwa huku nikijiuliza ni jinsi gani alijua kuwa nitakuwa pale muda ule.

    “Unaenda mahali Tigga?” Aliniuliza huku akinisogelea taratibu hali macho yake yakionesha ghadhabu za hali ya juu. Sikuweza kukusanya nguvu za kumjibu.

    “Au ulidhani utaweza kutukimbia milele? Tulijua tu kuwa utakuja hapa kwako, kama tulivyojua kuwa ungekwenda kule ofisini kwako...ingawa kule ulitupotezea mwenzetu mmoja lakini bado tuko wengi na ni hatari kuliko hata yule uliyesababisha auawe.” Aliniambia kwa jeuri.

    “Toka nyumbani kwangu! Huwezi kunitish-“ Nilianza kumkemea lakini yule dada alinirukia na kunichapa kofi kali la uso lililotawanya maumivu uso mzima. Kabla sijajua nijibu vipi pigo lile alinishindilia ngumi kama nne hivi za haraka haraka zilizotua bila mpangilio kuanzia kichwani hadi tumboni. Nilijibwaga kwenye moja ya masofa yaliyokuwa pale sebuleni nikitweta kwa mapigo yale. Yule dada alinijia kasi na kunikwida shati langu huku akiniinua na kunibamiza ukutani kabla ya kunishindilia ngumi nyingine ya tumbo. Niliguna kwa maumivu na nikahisi fahamu zikinihama. Huku nikiingiwa na wazo iweje mwanamke mwenzangu aninyanyase namna ile.

    “Nilikuambia kuwa utajuta Tigga! Sasa wakati ndio umefika-“ Alisema kwa hasira lakini hapo nami nikawa nimezinduka kwani nilimtwanga kichwa cha uso naye akayumba pembeni huku akilalama kwa maumivu na akiniachia. Nilimuendea mbio nikamshindilia teke la tumbo huku nikimtukana naye akajipinda kwa uchungu. Sikuishia hapo, nikamtupia teke jingine lililokuwa linauendea uso wake, lakini alinidaka mguu wangu na kunitupa kwa nguvu nami nikajibwaga sakafuni nikipigiza kichwa changu kwenye upande wa sofa mojawapo mle ndani.

    Kabla sijainuka yule askari alinijia na kuniwekea bastola usoni na kunikemea kwa hasira.

    “Where is the tape Tigga?”

    Badala ya kumjibu nilimtemea mate usoni naye akanichapa kofi kali la uso.Kisha alilichana shati langu kwa hasira kiasi cha kuniacha nikiwa na sidiria tu, na kutumia kipande cha shati langu kujifutia yale mate.

    “Usinichezee mimi wewe! Lete huo mkanda!”

    “Kwani kule gesti mlipochana chana mito na kuvuruga chumba kizima hamkuupata?” Nilimuuliza kwa jeuri. Akanipiga kichwani kwa kitako cha ile bastola yake na nikahisi maumivu makali.

    “Na bahati yako hukuichukua ile simu tuliyokuachia kule gesti, kwani ungeichukua tungeweza kukufuata kila ulipoenda kwa kutumia mionzi maalum tuliyoitegesha kwenye ile simu.” (Akasonya).

    “Hivi nyie mnadhani mimi ni mwehu kweli kama mlivyonipakazia?” Nilimuuliza kwa kujitutumua huku moyoni nikistaajabia jinsi wale watu walivyokuwa makini na maovu yao.

    “Usilete ujeuri usio na msingi Tigga, nipe huo mkanda sasa hivi!”

    “Nilishawaambia kuwa mkanda uko kwa wakili wangu! Kwa hiyo mimi mkanda sina jamani mbona mnanisumbua hivi?” Nilimuuliza kwa jazba. Alinichapa kofi jingine kali sana.

    “Wacha uongo!”

    “Sasa si uniue tu basi halafu uone jinsi mkanda utakavyooneshwa kwenye vyombo vya habari na wakili wangu?”

    Yule dada alichanganyikiwa, alinitazama kwa hasira halafu akatazama pembeni. Nilimtazama kwa makini, nikaona kuwa kushindwa kwake kuupata ule mkanda kulikuwa kunamchanganya sana. Alinigeukia kwa hasira na kuanza kunipekua mwilini, akiutafuta ule mkanda. Alichana chana nguo zangu kwa hasira hadi ile sidiria yangu na kuniacha matiti nje.

    Mkanda haukuwepo.

    “Sasa hii ndio nini lakini wewe? Hivi ni kipengele gani cha neno ‘sina mkanda’ ambacho kinakuwia vigumu kuelewa?” Nilimuuliza huku nikishindana naye katika kunipekua kwake. Nilipoona hanisikii nilimpiga kofi la uso na alinisukumia kwenye sofa lilikuwapo pale sebuleni na kunibana juu ya sofa lile huku akiniwekea mdomo wa ile bastola yake usoni na kunitazama kwa macho makali na ya hasira huku akihema kwa ghadhabu. Kwa mara nyingine niliona kuwa yule dada alikuwa tayari kunilipua kwa ile bastola kama si kuhofia kuukosa kabisa ule mkanda wa video anaoutaka kwa kila hali. Yaani kwake kama kwamba kuupata ule mkanda lilikuwa ni jukumu binafsi.

    Kwa nini?

    “Hivi ilikuwaje hata askari mzuri kama wewe ukajihusisha na watu wabaya kama wale lakini?” Nilimuuliza yule dada nikiwa nimebanwa pale kwenye sofa.

    “Si kazi yako kujua! Toa huo mkanda Tigga ama si hivyo mi’ n’takuua kweli!”

    “Huwezi kuniua wewe!” Nilimbishia kwa jeuri huku nikimtazama usoni. Alianza kunisemesha kitu lakini hapo hapo nilijiinua kwa nguvu na kumsukumiza pembeni nami niliukikimbilia mlango ili nitoke mbio nimuache mle ndani, lakini alinirukia na kunidaka miguu na wote tukapiga mwereka mzito. Alinibana pale sakafuni na kuirudisha bastola yake kwenye mkoba wake uliokuwa ukining’inia kiunoni na kuanza kunishindilia mangumi na makofi mengi huku akinitukana na kunikemea kuwa alikuwa anautaka ule mkanda. Nilijitahidi kupambana naye lakini alinielemea vibaya sana na nikahisi nguvu zikiniishia.Nilijitutumua kwa nguvu zangu zote na kufanikiwa kumbwaga pembeni nami nikajiinua kujaribu kukimbia lakini alinirushia teke lililonisukima hadi kwenye friji langu lililokuwepo mle ndani nami nikaanguka tena sakafuni ilhali lile friji likifunguka na kuangusha chupa za maji ambazo zilipasuka na kumwaga maji sakafuni pamoja na baadhi ya vyakula vilivyokuwamo ndani ya ile friji. Maji ya baridi yakinimwagikia na kutapakaa mle ndani. Nilianguka chini nikiwa nimeishiwa nguvu kabisa.





    Yule askari wa kike aliniacha nikitweta pale sakafuni naye akauendea ule mfuko wangu wa nailoni niliokuwa nikijiandaa kutoka nao na kuanza kuupekua kwa vurugu, akitafuta ule mkanda wa video, bila ya kujali kuwa alikuwa amepiga magoti kwenye dimbwi la maji yaliyomwagika kutoka kwenye chupa zilizopasuka kutoka kwenye friji langu.

    Nilipeleka mkono wangu na kukamata waya wa pasi uliokuwa umechomekwa kwenye swichi ya umeme ukutani hali ncha yake ya pili ikiwa kwenye pasi. Ile pasi ilikuwa imelegea sehemu ule waya ulipokuwa ukiingia kwenye ile pasi na mara kadhaa huwa inanitetemesha wakati nikiitumia. Niliung’oa ule waya kutoka kwenye ile pasi na huku nikiwa nimeushika hali zile ncha za kupitisha umeme zimetokeza nje, niliwasha ile swichi ya umeme na kuutupia ule waya pale kwenye lile dimbwi la maji hali mimi mwenyewe nikirukia juu ya kochi.

    Yule dada alipigwa na shoti kubwa ya umeme ambayo hata mimi ilinitisha. Alitetemeshwa vibaya sana na ingawa alipanua kinywa kwa maumivu na kupiga ukelele, hakuna hata sauti iliyotoka. Alitupwa na ule umeme na kujipigiza kwenye mguu wa meza na kubaki akitupatupa miguu na mikono pale sakafuni. Nilikimbia na kuizima ile swichi na kubaki nikimtazama yule dada.

    Alikuwa amenyooka kama gogo pale sakafuni akiwa ametoa macho bila ya fahamu.

    Bila ya kujali iwapo nilikuwa nimemuua yule askari au la, nilikusanya vitu vyangu haraka haraka na kubadilisha zile nguo zangu zilizoraruriwa na yule askari mbaya. Nilijifuta uso wangu kwa nguo zile na wakati huo huo nilibadili na kuvaa nguo katika zile nilizochagua kwa ajili ya kwenda nazo kule Gongo la Mboto. Kisha nilimburura yule askari mpaka nje ya mlango wa nyumba yangu na kuangaza huku na huko.

    Kama jinsi nilivyotarajia, hakukua na mtu. Muda kama ule pale kwetu huwa kunakuwa kimya sana. Nilifunga mlango wangu kwa ufunguo na kumalizia kwa kulifunga na lile geti langu la chuma na kuuficha ule ufunguo wangu mahala pale pale pa kila siku.

    Niliuruka mwili wa yule askari na kuondoka haraka eneo lile. Nje ya lile jengo nilikodi teksi na kumwamrisha dereva anipeleke sokoni kariakoo. Huko nilimpigia tena simu yule afisa wa polisi aliyeitwa John Vata.

    “John Vata.”

    “Tigga...” Nilisema huku nikihema na kuangaza huku na kule.

    “Tigga! Sasa mbona unakata simu kabla hatujamaliza kuongea? Uko wapi?”

    “Sikiliza afande. Sasa hivi kuna askari mwenzenu ametaka kuniua nyumbani kwangu, na kama utawahi utamkuta pale nje ya nyumba yangu akiwa aidha hana fahamu au amekufa. Najua kufikia sasa utakuwa unapafahamu nyumbani kwangu.”

    “Ndio, Upanga,...nilishafika lakini nyumba ilikuwa imefungwa..”

    “Wahi eneo hilo upesi. Huyo askari ndiye atakayekupa undani wa mambo yote haya, na yuko upande wa yule mtu anayejiita Martin Lundi. Mi’ n’takupigia tena kesho..”

    “No Tigga! Usikate! Nataka...”

    Nilikata simu na kukodi teksi nyingine niliyoiamrisha inipeleke moja kwa moja hadi Uno Trabajo Bar kule Gongo la Mboto.

    Nikiwa kwenye kiti cha nyuma ndani ya ile teksi, mwili wote ulianza kunitetemeka na woga usio kifani ulinitawala.

    --

    Usiku ule sikulala vizuri. Kwanza kutokana na kazi za uhudumu wa baa ambazo sikuwa nimepata kuzifanya hata siku moja, na sikutarajia kuwa ingefika siku ningelazimika kufanya kazi kama ile. Kachiki alinijia juu sana kwa kuchelewa kwangu lakini halikuwa jambo lililoleta matatizo makubwa kutoka kwenye uongozi wa ile baa. Nilipopata nafasi ya kuweka ubavu kitandani ilikuwa saa nane za usiku na badala ya kulala nilikuwa nikisumbuliwa na wazo la yule askari wa kike mshirika wa mtu anayejiita Martin Lundi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Itakuwaje iwapo nitakuwa nimemuua? Je, yule mtu niliyetarajia anisaidie, Kamishna Msaidizi wa polisi John Vata atanielewa? Yaani huku kupambana na hawa wauaji kunanifanya na mimi sasa niwe muuaji? Kwa hiyo ndio tayari maisha yangu yamebadilika sasa, na sijui kama yatawezakurudi katika ile hali ya zamani...

    Mawazo kama hayo yalinisumbua sana usiku ule na kulipokucha tu niliamka na kusubiri kupambazuke ili nikampigie simu John Vata nipate kujua hatma ya yule mwanadada, na mustak-bali wangu baada ya hapo.

    “Yeah Hallow!”

    “Eem-ah...Tigga hapa...”

    “Sikiliza we’ binti, hivi unajua unaongea na kufanya mchezo na nani? Kwa nini hutaki kufanya...”

    “Ulimkuta yule askari pale kwangu?”

    “Unajua kuwa hakukuwa na mtu pale kwako, ndio maana nakuuliza kuwa unajua unafanya mchezo na nani?”

    “Hakukuwa na mtu? Yaani hukumkuta nje ya mlango wangu?” Nilimuuliza huku nikifarijika moyoni kuwa kumbe yule dada hakufa. Ina maana alizinduka na kufanikiwa kuondoka kabla Kamishna Msaidizi John Vata hajamkuta.

    “Hakukuwa na mtu na nyumba ilikuwa imefungwa vilevile!”

    “Aaah....sasa basi...”

    “Sasa mchezo basi! Hili swala la kusema kuna askari mwenzetu anashirikiana na huyo mtu anayejiita Martin Lundi sio la masihara, na nitahitaji uthibitishe hilo kwa ushahidi usiopingika, la si hivyo n’takutia kwenye matata mazito zaidi ya haya ambayo unayo hivi sasa!”

    “Kwa hiyo huniamini Kamishna?”

    “Siwezi kukuamini mpaka ujitokeze na nisikie maelezo yako!”

    “Sasa basi nakutaka umweke chini ya ulinzi mtu aitwaye Dick Bwasha. Ni meneja wa tawi la benki moja hapa jijini. Huyu naye ni mmoja wa hao watu waliofanya mauaji kule msituni...”

    “Tulishapitia mchezo huo na sasa hatuuchezi tena! Jitokeze utueleze unalojua juu ya watu wote hao ndipo sisi tutaamua iwapo tuwaweke chini ya ulinzi au la...”

    Nilitaka sana kujitokeza kwake na kupata msaada na ulinzi kutoka kwake, lakini bado ilikuwa vigumu kwangu kumuamini moja kwa moja kwani kumbukumbu ya mambo yaliyonikuta mpaka sasa bado haikuniruhusu kuamini mtu yeyote kirahisi kama jinsi yule afisa wa polisi mtanashati alivyotaka.

    “Fanya hivyo afande nami nitajitokeza. Nataka ujionee mwenyewe kuwa ni kweli hao watu ninaokutajia wapo, kisha tutaongea kwa undani zaidi na nitakupa vithibitisho vya kutosha.”

    John Vata alibaki kimya kwa muda, kisha akauliza Dick Bwasha ni meneja wa tawi gani la benki nami nikamtajia, na kumsisitizia kuwa utaratibu ulikuwa ni ule ule. Nataka nihakikishe kwa yakini kabisa kuwa ni kweli huyo mtu amekamatwa.

    “Kwa nini unafanya hivi wewe mwanamke?”

    “Nataka kujua iwapo ninaweza kukuamini.”

    “Unaitilia mashaka serikali?”

    “Hata hao walionitumbukiza kwenye balaa hili nao walidai kuwa ni serikali.”

    “Ni kina nani hao?”

    “Kwa kweli sijui, ila ninachojua ni kwamba huyo mtu aliyejiita Martin Lundi ni mmoja wa viongozi wao na huyo Dick Bwasha niliyekutajia hivi punde ni mmoja wa vibaraka wao...mkamate Dick Bwasha afande, huenda akakufikisha kwa Martin Lundi muongo, nami nitajitokeza.” Nilimjibu na Kamishna Msaidiza John Vata alikaa kimya kwa muda kabla ya kuongea tena.

    “We’ unanipigia simu kila unapotaka. Sasa mimi nikikuhitaji nitakupataje?”

    “Nadhani ulisema kuwa utaniwinda mpaka utanitia mbaroni, sasa imekuwaje tena?” Nilimjibu na kukakata simu kabla hajaongea zaidi.

    Nilirudi Uno Trabajo Bar na kuchapa usingizi mzito.

    --

    Baada ya kusubiri kusikia habari za kukamatwa kwa Dick Bwasha kwa siku mbili bila mafanikio nilimpigia tena simu Kamishna Msaidizi John Vata. Nikiwa nimejawa ghadhabu kutokana na kutotekelezwa kwa maagizo yangu, nilijitambulisha kwake na kuanza kumshutumu juu ya swala la kutokamatwa kwa yule meneja wa benki anayeshirikiana na kundi la Martin Lundi muongo, naye kwa utulivu mkubwa alinipa jibu ambalo sikulitarajia na lililonishitua kupita kiasi.

    “Dick Bwasha is dead, Tigga!”

    “Dick Bwasha is d-whaaaat?” Nilimuuliza kwa mshangao mkubwa.

    “Huyo mtu uliyenielekeza nikamkamate kuwa ni mshirika wa mtu anayejiita Martin Lundi amekufa. Sasa nataka ujitokeze utoe maelezo juu ya mambo haya Tigga kwa sababu inaelekea kuwa kila unapopita unaacha kifo au vifo nyuma yako...halafu unasema mtu aitwaye Martin Lundi ndio muuaji!” John Vata aliniambia kwa upole wa hali ya juu, na nikajua kuwa alikuwa ameghadhibika kupita kiasi.

    Ina maana sasa naonekana kuwa namsingizia tu huyu mtu aitwaye Martin Lundi, ambaye kiutaratibu ni kwamba hayupo kwani Martin Lundi halisi ni mstaafu wa miaka sabini na tano.

    Sikujua niseme nini, nilipigwa na butwaa.

    Kwa mara nyingine tena Martin Lundi muongo alikuwa amenizidi kete!

    Hivi ni siri gani hiyo waliyonayo hawa watu ambayo njia pekee ya kuificha ni kifo?

    “Tigga? Bado upo?”

    “Yeah...lakini...Dick Bwasha? It can’t be! How...I mean... amekufaje?”

    “Nadhani wewe ndiye unaweza kutueleza kwa ufasaha juu ya hilo Tigga, sasa aidha ujitokeze mara moja au uache kabisa kunipigia simu namna hii. Mimi ni Kamishna msaidizi wa polisi, sio mtu wa kufanyiwa mchezo namna hii!”

    Niliogopa!

    “Sifanyi mchezo afande! Lakini...lakini hizi taarifa zinanitatanisha! Itakuwaje Dick Bwasha Afe? Na kwa nini unasema kuwa mimi ninaweza kuwaeleza kwa ufasaha juu ya kifo chake?” Nilikuwa nakaribia kuangua kilio kwenye simu.

    “Wewe ndiye unasemekana kuwa ni mtu wa mwisho kuonana naye kabla hajakutwa akiwa amekufa ofisini mwake siku chache zilizopita, na mezani kwake kulikuwa kuna fomu uliyoijaza ya kuchukulia pesa pale benki...”

    Haya makubwa sasa!

    “Niliondoka nikimwacha Dick Bwasha akiwa hai na jeuri kuliko kawaida afande! Kuna kitu kingine kimetokea baada ya mimi kutoka mle ofisini mwake...umewauliza vizuri wale wahudumu wa ile benki afande?” Nilipayuka kwa kihoro huku nikiogopa ile hali iliyokuwa ikijitokeza, na badala ya kunijibu John Vata alikata simu.

    Khah! Yaani yule afisa wa polisi amenikatia simu! Sikuamini masikio yangu.

    Ina maana ameniona kuwa mimi ni muongo na bila shaka muuaji na ninataka kumchezea kwa sababu zangu binafsi.

    Oh! Mungu wangu hii ni mbaya sana! Hii ni mbaya sana!

    Nilimpigia tena, lakini ile simu ilibaki ikiita tu bila kupokelewa hadi ikakatika yenyewe, nami nikazidi kuhamanika. Nikapiga tena, nayo ikawa inaita tu bila kupokelewa.

    Please John Vata, pokea simu tafadhali!

    Hatimaye ile simu ikakatika, na nilipopiga tena ile simu ikawa imefungwa.

    Oh! My God! Nitafanyaje sasa...

    Niliondoka nikiwa niliyevurugikiwa na niliyehamanika kupita kiasi. Nilienda moja kwa moja hadi kwenye mgahawa uliokuwa jirani na ile benki niliyohifadhia pesa zangu. Niliketi kwenye kiti kilichokuwa kwenye kona na kuelekea mlangoni ambapo niliweza kumuona kila aliyeingia na kuagiza chipsi kwa kuku na kusubiri kwa kufyonza juisi taratibu. Nilisubiri huku moyo ukinienda mbio na woga usio kifani ukinifanya nishindwe hata kuinua ile glasi ya juisi. Muda si mrefu niliona baadhi ya wafanyakazi wa ile benki wakianza kuingia mle mgahawani kupata mlo wa mchana nami nikawa makini sana nao. Hatimaye nilimuona yule dada niliyezoeana naye pale benki akiingia nami nikahama na juisi yangu hadi kwenye meza aliyoketi na kuketi mbele yake.

    Tulitazamana.

    “Ti...Unafanya nini hapa?” Aliniuliza kwa wasiwasi na kuanza kuangaza huku na huko ndani ya ule mgahawa.

    “Nahitaji kuongea na wewe mara moja na naomba unisikilize kwanza halafu unijibu maswali yangu. Sina muda mrefu, itanilazimu niondoke mahala hapa.” Nilimwambia haraka, na kumtupia swali kabla hajasema neno lolote. “Ni kweli kuwa meneja Dick Bwasha amefariki?” Yule dada aliafiki kwa kichwa huku bado akionekana kuwa amepigwa na butwaa na ujio wangu.

    “Amekufa lini na amekufaje?”

    Yule dada alinitazama kwa muda kisha akameza funda kubwa la mate.

    “Amekufa siku ile ulipokuja kujaribu kuchukua pesa pale benki...” Alinijibu na kuendelea kunitazama kwa mashaka. Niliendelea kumtazama nikitarajia maelezo zaidi kutoka kwake. “Tulichoambiwa ni kwamba amepatwa na mshituko wa moyo...stroke...amekutwa akiwa ameegemea kiti chake kama kwamba amelala.” Yule dada alinijibu huku akinitazama kwa mashaka nami nikiwa nimemkazia macho kwa umakini.

    “Ninasemekana kuwa mimi ndiye nilikuwa mtu wa mwisho kuonana naye na polisi wananishutumu kwa kifo chake...unajua nini kuhusu swala hilo?” Nilimuuliza nikiwa makini sana. Akanieleza kuwa naye ndivyo alivyokuwa anajua na kwamba baada ya kuhojiwa na polisi amegundua kuwa kumbe nilikuwa nikitafutwa kwa mauaji ya kutisha tangu siku ile niliyokwenda pale benki na kujaribu kuchukua pesa kutoka kwenye akaunti yangu. Jambo alilodai kuwa nusura limtie na yeye kwenye matatizo kwa kushirikiana nami wakati akijua kuwa nilikuwa natafutwa kwa mauaji, ingawa ukweli ni kwamba yeye hakuwa akijua lolote juu ya hilo kwa wakati ule.

    “Hayo yote sio ya kweli Anti, ila ni hadithi ndefu, muda hatuna na hapa sio mahala pake. Ni nani hasa aliyetoa hiyo taarifa kwa polisi kuwa mimi ndiye nilikuwa wa mwisho kuonana na meneja Dick Bwasha? Na kuna uhakika gani juu ya hilo?”

    “Mimi nilikuacha naye mle ofisini, kisha ikaja amri kuwa asiruhusiwe mtu yeyote kuonana na meneja kwa siku ile...”

    “Kwa hiyo wewe ndiye uliyewaeleza polisi kuwa mimi ndiye nilikuwa wa mwisho kuonana na Dick Bwasha?” Nilimuuliza kwa mshangao.

    “Mi’ nilikuacha na Dick Bwasha ofisini, sijakuona ukitoka! Sasa ulitarajia niwaeleze nini polisi?” Yule dada aliniambia kwa msisitizo. Nilitaka kumtupia swali iwapo aliweza kuona kila aliyeingia na kutoka benki wakati akiwa anahudumia wateja, lakini niliona akipepesa macho kwa mashaka, kama kwamba hana imani na kauli yake.





    Nilimkazia macho na kumsaili zaidi iwapo alikuwa na uhakika na maneno yake, akilini mwangu nikianza kupata mashaka iwapo naye hajarubuniwa na yule muongo ajiitaye Martin Lundi.

    “Lakini walipokuja Agnes alikuwa ameshaondoka...na mi’ sikukumbuka kuwa siku iliyofuatia alikuwa anaanza likizo...” Yule dada alisema kwa wasiwasi, kama kwa kujitetea. Sikumuelewa, na nilipomuuliza zaidi aliniambia kuwa Agnes alikuwa ni yule dada mwingine aliyekuja kuniita na kunipeleka kule ofisini kwa Dick Bwasha na kutuacha naye mle ofisini. Yeye alikuwa ni sekretari wa meneja Dick Bwasha.

    “Ah! Lakini nilipotoka Agnes alikuwepo pale kwenye meza yake nje ya ofisi ya Dick Bwasha!” Nilimwambia kwa msisitizo. Yule dada aliangalia pembeni, asijibu kitu.

    “Sasa Agnes yuko wapi? Aliongea na polisi? Naye aliwaeleza nini?” Nilimuuliza kwa hamasa kubwa.

    “Agnes hakuwepo wakati askari walipofika, siku ya tukio aliondoka mapema kwa sababu kesho yake alikuwa anaanza likizo...” Aliniambia. Nilimtazama kwa huzuni iliyochanganyika na mshangao. Yule dada aliona huzuni usoni mwangu, na aliendelea haraka. “ Mi’ niligundua kuwa kuna mwanamke mwingine aliyeingia ofisini kwa Dick Bwasha baada ya wewe kutoka nilipoongea na Agnes kwa simu akiwa nyumbani kwake kumpasha habari za kifo cha Dick, lakini wakati huo nilikuwa nimeshaongea na polisi...”

    “Yaani kumbe kuna mwanamke mwingine aliye....” Nilidakia kwa mshangao.

    “Kwa mujibu wa maelezo ya Agnes. Alikuja mwanamke aliyevaa baibui na hijab kama mzanzibari, akinukia manukato ya udi kama jinsi akina mama wa kizanzibari wanavyonukia....” Aliniambia nami nikawa nimezidiwa na jazba, nikadakia.

    “Huyo mwanamke alionana na Dick Bwasha?”

    “Aliomba kuonana naye lakini Agnes alimwambia kuwa meneja haonani na mtu yeyote. Yule dada alitoa simu yake ya kiganjani na kumpigia Dick palepale. Dick alitoka na kumkaribisha ndani yeye mwenyewe.”

    “Kwa hiyo mpaka hapo tu Dick alikuwa hai baada ya mimi kuondoka siku ile...”

    “Sasa mimi hayo sikuyajua wakati naongea na wale askari! Na kutokana na mshituko wa tukio lile, hakuna aliyekumbuka juu ya Agnes kwa kipindi kile!”

    “Okay...nini kilitokea baada ya yule dada wa kizanzibari kuingia ofisini kwa Dick Bwasha?”

    “Kwa mujibu wa maelezo ya Agnes, alikaa huko ndani kwa muda, kisha alitoka na kumuambia Agnes kuwa meneja amesema kuwa asisumbuliwe tena. Ni baada ya huyo dada kuondoka ndipo Agnes alipoenda kuchukua barua yake ya likizo na kuondoka kimya kimya bila kumuaga bosi. Kilichofuata ni wale wafagizi kumkuta Dick akiwa amekufa ofisini mwake. Muda huo benki ilikuwa imeshafungwa kwa siku ile kwa wateja na tulikuwa tumebaki sisi tu...”

    Hizi taarifa zilikuwa kali sana na nisingeweza kuziacha hivi hivi tu bila kuzifanyia kazi.

    “Sasa rafiki yangu mimi nazidi kuhisiwa uuaji huko na wewe unakaa na taarifa kama hizi?”

    “Sasa mi’ sikujua nifanye nini baada ya hapo...na jambo hilo limekuwa likinitisha sana...”

    Nilichukua simu yake ya mkononi na kuanza kupiga namba ya John Vata. Yule dada aliniuliza nilikuwa nafanya nini, nami nikamwambia kuwa nawapigia polisi ili wajue juu ya taarifa ile. Ingawa alijitahidi kupinga jambo lile, lakini sikujali. John Vata alipopokea ile simu nilijitambulisha na kumweleza juu ya ile taarifa kwa kifupi.

    “We’ unajuaje mambo haya? Au bado unaendeleza mchezo wako wa kunitania? Nakuhakikishia kuwa....”

    “Niko na huyo dada hapa niongeapo. Inaonekana hao vijana wako waliokuja kuchunguza juu ya kifo cha Dick Bwasha hawakuwa makini. Ndio maana hata mimi sina imani nao sana.”

    “Nipe huyo dada niongee naye sasa hivi!”

    “Sasa wewe ndio umpigie au umtembelee hapa benki, hii ni simu yake na tunammalizia dola zake!” Nilimjibu na kukata simu. Yule dada alikuwa ameogopa pasina kiasi, na alikuwa akilengwalengwa na machozi.

    “Oh! Mungu wangu. Sasa itakuwaje...si nitaingia kwenye matatizo mimi?” Aliniuliza kwa wasiwasi mkubwa.

    “Waeleze kama ulivyonieleza mimi. Usifiche chochote. Hutakuwa kwenye matatizo.” Nilimjibu na hapo hapo simu yake ikaanza kuita. Yule dada alishituka na kuruka kama aliyetekenywa kwenye mbavu na kuitazama ile simu ikiita kwa woga mkubwa.

    “Pokea simu na uongee Anti...” Nilimwambia na nilipoona anazidi kuigwaya ile simu, niliipokea. Nilisikia sauti ya John Vata ikiongea nami nilimkabidhi yule dada ile simu. Aliiweka sikioni taratibu huku uso wake ukiwa na woga mkubwa. Niliondoka eneo lile haraka nikimwacha yule dada akiongea na Kamishna Msaidizi John Vata.



    --



    Ni nani tena huyu mwanamke mwenye kuvaa baibui na kunukia udi?

    Je, naye ni miongoni mwa wafuasi wa Martin Lundi muongo?(niliendelea kumwita hivyo kwa sababu sasa sikujua nimwite nani). Na kama ni mfuasi wa yule muuaji muongo, kwa nini amuue Dick Bwasha? Mimi sikuamini kabisa maelezo ya kuwa Dick Bwasha kafa kwa mlipuko wa moyo. Hilo kwangu nililiona ni uongo mtupu. Sikuwa na shaka kabisa kuwa wale akina Martin Lundi walikuwa wamemuua, kwamba walikuwa na namna za kumuua mtu kwa njia yoyote waitakayo. Nilikumbuka maelezo ya Koku juu ya mambo waliyomfanyia Kelvin, na sasa hawezi hata kuongea na inaelekea anakufa taratibu.

    Ila kilichonishinda kuelewa ni kwa nini wamuue Dick Bwasha!

    Au ndio adhabu yake kwa kushindwa kuuchukua ule mkanda wa video kutoka kwangu? Lakini kama ni hivyo mbona yule dada askari ameshindwa kuupata ule mkanda mara kadhaa na hajauawa?

    Nilikuwa nimejilaza kitandani chumbani mwangu pale Uno Trabajo Bar nikitafakari mambo yaliyotokea siku ile.

    “Yaani tayari Kamishna Msaidizi John Vata alishaniweka kwenye shutuma za kuhusika na kifo cha Dick Bwasha!” (Niliguna). Nilifikiria hali ingekuwaje kama nisingechukua jukumu la kumuendea yule dada wa pale benki na kuanza kumsaili juu ya kifo cha yule mtu jeuri aliyeitwa Dick Bwasha.

    Na sasa huyu mwanamke anayevaa baibui....http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilikumbuka maneno ya yule dada askari wakati aliponishtukiza pale nyumbani kwangu Upanga.

    ...ingawa kule ulitupotezea mwenzetu mmoja lakini bado tuko wengi na ni hatari kuliko hata yule uliyesababisha auawe.

    Je, na huyu mwanamke mwenye baibui ndio miongoni mwa hao wenzao wengi na hatari kuliko yule muuaji niliyemwita Macho ya Nyoka?

    Niliamua kwenda kumpigia tena simu Kamishna Msaidizi John Vata. Sikuwa na ujanja.

    Nikiwa bado nasumbuliwa na haya mawazo, nilishitushwa na kishindo cha Kachiki aliyeingia chumbani mwangu kwa pupa akiwa amejawa hamasa kubwa.

    “Nini wewe!” Nilimaka nikiwa nimeshituka sana.

    “Mshikaji kuna dili la kwenda The Rickshaw, si mchezo!” Aliniambia huku akiwa ametoa macho na uso wake ukiwa umejawa matarajio makubwa.

    The Rickshaw!

    Niliinuka kutoka kitandani nikiwa makini mno na kumtazama kwa macho ya wasiwasi na kutoelewa.

    “Umesema The Rickshaw?” Nilimuuliza nikiwa wima na nikimsogelea taratibu, akilini mwangu nikianza kumhisi kuwa kumbe na yeye anahusika na wale akina Martin Lundi.

    “Yes! The Rickshaw mwanangu! Yiiiii-Hhaaa!” Alinijibu na kushangalia huku akiruka juu. Nilimkamata mabega kwa nguvu na kumkalisha kitandani.

    “We’ unajua nini kuhusu hili neno The Rickshaw, eenh? Niambie upesi Kachiki na usinidanganye!” Nilimwambia kwa ukali huku nikimtikisa na moyo ukinienda mbio, akilini mwangu ikinijia picha ya yule mtu aliyeuawa kule msituni akinitamkia lile neno wakati akitapatapa katika dakika zake za mwisho za uhai wake.

    Sasa leo Kachiki ananiambia kirahisi tu eti kuna dili la kwenda The Rickshaw! Tena kwa bashasha na furaha kubwa namna hii!.

    Yaani mimi nililihusisha lile neno na kifo, tena kifo cha kutisha kilichoambatana na vifo vya watu wengine wasio na hatia, yeye analizungumzia kwa bashasha namna hii!

    Nilihisi msisimko usio kifani.

    Kachiki alinitazama kwa wasiwasi na mshangao kutokana na jinsi nilivyombadilikia ghafla baada ya kusikia neno lile.

    “Aaah! Niachie bwana! Mbona hivyo?” Aliniambia huku akinikunjia uso na akiitoa mikono yangu kutoka mabegani mwake. Niliona kuwa nilikuwa nimekurupuka kwa jazba kubwa bila sababu, Kachiki angeshindwa kunielewesha juu ya neno lile kwa mtindo ule. Nilijitahidi kutulia na kumweleza kwa upole ingawa moyoni sikuwa na upole wowote.

    “Samahani Kachiki, lakini nimekuwa nikiitafuta sehemu hiyo iitwayo The Rickshaw kwa muda mrefu bila mafanikio. Sasa leo unaponiambia kuna dili la kwenda The Rickshaw nimepatwa na kiherehere kikubwa...”

    Kachiki alinicheka kwa kebehi.

    “Huwezi kupajua The Rickshaw hivi hivi tu Nuru!(Yeye ananifahamu kwa jina la Nuru Bint Shaweji) Huko huwa tunapelekwa tu na tunajikuta tumefika, lakini wewe mwenyewe ukitaka kujiendea tu hivi hivi huwezi kufika...mpaka upelekwe.” Alinijibu nami nikazidi kuvurugikiwa kwa jibu lile.

    Mbona inakuwa kama simulizi ya Alfu lela-u-lela? Vije nifike kwa kupelekwa tu na hata nikitaka kwenda mwenyewe nisipajue?

    “Kachiki, huwa mnapelekwa? Mnapelekwa na nani? Na kwa nini kwenda huko kuwe ni “dili”? Kuna nini hapa Kachiki? Mbona sielewi?”

    Kachiki alinicheka, kabla ya kujaribu kunifafanulia.

    “Inasemekana Mzee Kazimoja ana hisa katika hiyo The Rickshaw, na mara moja moja...”

    “Mzee Kazimoja? Ndio nani huyo tena Kachiki? Mbona unanichanganya?”

    “Aaah Nuru nawe! Mzee Kazimoja si ndio mwenye hii baa tunayofanyia kazi? Sijakuambia?”

    Nilibaki kinywa wazi. Sikuwa nimetilia maanani kumjua mmiliki wa ile baa hapo mwanzo, na hata nilipoanza kazi, sikuwa nimeonana na huyo mmiliki bali nilionana na muangalizi tu wa ile baa aliyekabidhiwa majukumu hayo. Lakini hapo pia nilipata jibu la swali langu, kwa sababu tangu niliposikia jina la ile baa, nililiona kuwa si la kawaida, kwani kwa lugha ya kihispania, neno “Uno Trabajo” lilimaanisha “Kazi Moja” kwa kiswahili. Kumbe yule mmiliki alikuwa ameiita baa ile kwa kufuatisha jina lake kwa lugha ya kihispania.

    “Enhe, umesema Mzee Kazimoja ana hisa The Rickshaw...The Rickshaw ni nini?”

    “Ndio...”

    Kachiki alinieleza mambo ambayo sikuyatarajia kabisa, na kama nisingekutana naye na kuja kwenye hii baa, hakika nisingeyajua asilani!

    Aliniambia kuwa The Rickshaw ilikuwa ni kasino moja ya hali ya juu sana jijini. Huko kuna kila aina ya starehe, kuanzia kamari hadi biashara ya ngono. Mara moja moja huwa wanakuja wafanyabiashara kutoka nchi mbali mbali za magharibi kwa ajili ya kujistarehesha katika ile kasino, na pindi wajapo hao wafanyabiashara, baadhi ya wahudumu wa ile baa ya Uno Trabajo huwa wanateuliwa na kupelekwa The Rickshaw kusaidia katika kutoa huduma kwani wahudumu wa huko huwa hawatoshi katika nyakati kama hizo. Na ni hapo ndipo kwenda huko inapokuwa dili, kwani wale wafanyabiashara wa kizungu huwa wanatoa bakshishi nyingi na kama ikiwa bahati yako unaweza kuchukuliwa na kuburudika na mmoja wao na kujipatia pesa nyingi. Kwa maelezo ya Kachiki, kuna mwenzao mmoja alifikia hatua ya kuchukuliwa kabisa na mmoja wa hao wafanya biashara na kwenda naye ulaya na mpaka muda ule alikuwa bado yuko huko.

    Lakini kama hiyo haitoshi, mara tu wakirudi kutoka huko huwa wanapewa malipo maalum na uongozi wa ile baa ya Uno Trabajo, malipo ambayo hufikia kiasi cha laki mbili hadi tatu.

    Hii taarifa ilikuwa mpya sana kwangu. Na hapo hapo niliamua kuwa ni lazima nifike huko The Rickshaw. Hii ilikuwa ni nafasi ambayo nisingeweza kuiachia hata kidogo.

    “Mimi naujua sana mji wa Dar, Kachiki, lakini mbona hata siku moja sijawahi kuiona hiyo kasino iitwayo The Rickshaw?” Nilimuuliza.

    “Sasa hapo ndipo hata mimi nilipochemsha, kwani mara ya kwanza nilipopelekwa huko, kesho yake nilitembela karibu mji mzima nikijaribu kuitafuta ile kasino ili nikatafute namna ya kuhamia huko moja kwa moja. Sikuiona kabisa Nuru. Na si mimi tu, hata wenzangu pia walijaribu lakini wapi!” Aliniambia kwa masikitiko.

    Sikumuelewa.

    “Lakini si mlipelekwa? Kwa nini sasa mshindwe kupajua baada ya hapo?”

    “Tunapelekwa tukiwa kwenye gari kama ki-hiace hivi, ambalo huwa halina madirisha kabisa, lina kiyoyozi cha nguvu humo ndani. Hivyo huwa hatujui tunapelekwa wapi, na tukifika huko, ile gari huingia mpaka ndani, tukiteremka huwa tayari tuko ndani. Tunaona tu neno “The Rickshaw” mle ndani. Na mtindo huwa ni huo huo wakati wa kurudi. Tunateremkia kwenye mlango wa kuingizia vinywaji nyuma ya baa na kuingia ndani moja kwa moja” Kachiki alinieleza kwa kirefu.

    Nilichoka!

    Kwa vyovyote huko The Rickshaw kulikuwa kuna mambo mengi yasiyo sawa, ndio maana hata wale wahudumu wanaopelekwa huko walitakiwa wafike tu humo ndani bila ya kujua njia ya kufikia huko.

    Kuna nini huko?

    Ndio maana hata Mr. Q alikuwa amesisitiza sana eneo lile, ina maana alijua kuwa huko kuna jambo lisilo sawa...na huenda ndio lililosababisha kifo chake.

    Je, huko ndio makao makuu ya lile kundi la akina Martin Lundi muongo?

    “Sasa lini mnakwenda huko?” Nilimuuliza Kachiki kwa upole. Alinijibu kuwa siku iliyofuatia ndio walitakiwa wapelekwe The Rickshaw.

    “Na mimi naweza kwenda? Nataka kwenda huko nami nikajionee!” Nilimwambia huku moyo ukinidunda, nikijua kuwa jibu lake ndilo lingekuwa mwanzo wa majibu mengi yaliyokizunguka kisa hiki cha kutisha kilichonizunguka. Kachiki alinicheka.

    “Wewe huwezi kwenda Nuru. Lazima uelewe kuwa hata sisi tunaopelekwa huko kwanza huwa tunasisitiziwa kuwa tutakayoyaona huko ni siri na tunatakiwa tuyaache huko huko! Halafu tunachukuliwa wale tu tuliokuwa hapa baa kwa muda mrefu, wewe bado mgeni huwezi kuchukuliwa bwana!”

    Akili ilinizunguka. Nifanyeje sasa? Nilizidi kumhoji Kachiki juu ya ile kasino iliyoitwa The Rickshaw lakini kufikia hapo alikuwa amechoka kujibu maswali yangu na kuamua kucheza muziki kwa furaha akisubiria hiyo siku ya kupelekwa huko The Rickshaw kasino. Nilimtazama kwa kukata tamaa, kisha nikamfukuza chumbani kwangu, nikimwambia nataka kulala.

    “Usikonde shoga, nikirudi keshokutwa nitakukatia na wewe kidogo dogo, si unajua tena?” Aliniambia wakati akitoka. Nilimsukuma nje na kufunga mlango wangu.

    Mungu wangu! Kumbe The Rickshaw ni kasino ya hapa hapa jijini!

    Ee Mr. Q, ni kipi ulichokiona huko The Rickshaw hata ikabidi uuawe?





    Nilishindwa kulala. Nilikuwa nikizunguka mle ndani nikiwaza juu ya ile Kasino ya maajabu iitwayo The Rickshaw. Iko wapi? Kuna nini huko? Nitafikaje? Ina uhusiano gani na yale mauaji ya kule msituni na wale wauaji akina Martin Lundi muongo?.

    Vyovyote iwavyo, nitahakikisha kuwa na mimi naingia kwenye huo msafara wa kwenda huko The Rickshaw hiyo kesho! Nilidhamiria.

    Na nilisahau kabisa kumpigia simu Kamishna Msaidizi John Vata.



    viii.

    G

    ari nyeusi isiyo na madirisha aina ya Nissan Serena Mini-Bus iliyokuwa imewabeba wasichana wanne wahudumu wa ile baa ya Uno Trabajo akiwemo Kachiki, ilitoka nje ya ua wa ile baa na kuingia barabarani. Nikiwa ndani ya teksi bubu iliyokuwa imepaki upande wa pili wa barabara nilimwamrisha dereva wa ile teksi aifuate ile gari mpaka itakapoishia. Ile teksi iliingia barabarani nyuma ya ile Nissan Serena ikiacha gari moja baina yetu.

    Safari ya kuelekea The Rickshaw ilikuwa imeanza nami moyo ulikuwa ukinienda mbio kwa hamasa ya kuona mwisho wa safari ile ungenifumbulia kitu gani katika msukosuko huu ulioniangukia.

    Awali nilitoka nje ya ile baa nikiwa nimevaa suruali yangu ya jeans iliyoukamata mwili wangu vizuri na fulana nyeupe nikiwa nimebeba mfuko wa nailoni. Niliwaaga wenzangu pale baa kuwa nilikuwa naenda kwa fundi cherehani kushona baadhi ya nguo zangu zilizochanika, nikiwaacha Kachiki na wale wasichana wengine watatu wakisubiri ile gari iliyotarajiwa kuwapeleka huko The Rickshaw, ambapo walitaarifiwa kuwa ingefika mnamo saa tisa za mchana. Nilipotoka na ule mfuko wangu nilipanda daladala na kuteremka kituo kimoja baada ya kile nilichopandia na kuelekea moja kwa moja hadi kwenye choo cha kulipia kilichokuwa karibu na kile kituo. Nilipotoka nilikuwa nimeongezea shati jekundu la mikono mirefu la kitambaa kizito cha drafti-drafti juu ya ile fulana, kichwani nilikuwa nimevaa kofia ya kapelo na usoni nikiwa nimevaa ile miwani yangu ya jua. Niliikodi ile teksi na kurudi nayo mpaka pale Uno Trabajo Bar na kumuambia dereva aegeshe upande wa pili wa barabara. Wakati tukisubiri huku nikiwa makini kuangalia kila gari iliyotoka kule baa, nilimweleza yule dereva kuwa nilikuwa namvizia mpenzi wangu ambaye nilishabonyezwa kuwa alikuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa wahudumu wa ile baa, nami nilikuwa nataka niwafuatilie mpaka watakapoishia ili niwafumanie.

    Yule dereva aliniuliza swali moja tu; nilikuwa na pesa ya kutosha?

    Nilitoa elfu kumi na kumkabidhi, nikimwahidi nyongeza pindi tutakapofika mwisho wa safari yetu naye akaona kuwa ile pesa haikutosheleza.

    Tuliifuata ile gari wakati ikikata mitaa ya jiji kwa ustadi mkubwa, yule dereva akiamini kuwa ilikuwa ni gari ya mpenzi wangu iliyombeba mhudumu wa ile baa ya Uno Trabajo anayehusiana naye kimapenzi. Lakini kadiri tulivyoendelea kuifuata ile gari, niliona kuwa tulikuwa tukizunguka tu katika mitaa mbali mbali ya jijini bila ya uelekeo maalum, na nikaanza kupata mashaka kuwa huenda wale watu waliokuwa kwenye ile gari walikuwa wametugundua na kuamua kutuzungusha tu mjini ili watupoteze.

    “Hawa jamaa zako vipi Anti, au wanatuchezesha...” Dereva naye alianza kupata wasiwasi lakini nilimkatisha.

    “Endesha gari Anko! Kazi yako ni kuwafuata tu mpaka watakapoishia!”

    “Sawa, lakini hii misele inakuwa mingi sasa! Tusije tukaanza kupigizana kelele kuhusu kulipana hapa, Oh-hoo!”

    Bila ya kuongea nilitoa elfu tano na kumkabidhi. Jamaa aliipokea na kuendelea kuendesha bila kelele zaidi. Wakati tukiendelea kuifuata ile gari ikizunguka mitaani, nilipata wazo lililonielewesha ni kwa nini akina Kachiki, ingawa walishapelekwa mara kadhaa, bado walishindwa kujua ni wapi ilipo ile kasino ya The Rickshaw, kwani ilinijia akilini kuwa wale watu hawakuwa wametugundua, bali walikuwa wakiwazungusha hovyo mjini wale wasichana kabla ya kuwapeleka kulipokusudiwa ili wapoteze kabisa uelekeo wa safari yao ili wasiweze kurudi tena.

    Kwa nini?

    Sikupata jibu lakini hii ilizidi kunihamasisha kuwa uamuzi wangu wa kuifuata ile gari waliyopanda akina Kachiki ulikuwa wa busara sana, na kwamba Mr. Q alikuwa na sababu za msingi za kunisisitizia juu ya hiyo The Rickshaw kwani hapana shaka kabisa kuwa alijua kwamba The Rickshaw ndiko ambapo ningepata majibu ya kitendawili chote kilicholizunguka lile tukio la kutisha la kule msituni. Tuliendelea kuifuatilia safari ya ile Nissan Serena iliyokuwa mbele yetu, sasa hivi kukiwa kuna magari mawili baina yetu.

    Baada ya kuzunguka bila uelekeo unaoeleweka kwa muda, ile gari iliingia maeneo ya katikati ya jiji, maeneo ambayo nilikuwa nimeyazoea sana na kwenda moja kwa moja hadi nje ya geti la nyuma la kasino maarufu jijini, Casino La Dreamer, na kupiga honi mara mbili. Tulisimamisha gari yetu hatua kadhaa nyuma, upande wa pili wa barabara nami nikawa natazama kinachoendelea kule kwenye lile geti huku maswali mengi yakianza kujijenga kichwani mwangu.

    Casino La Dreamer ilikuwa ni sehemu maarufu tu ya starehe jijini na hakuna mwenyeji wa jiji hili lililojaa kila aina ya starehe asiyeijua kasino ile.

    Sasa vije akina Kachiki waseme walikuwa wakipelekwa The Rickshaw wakati kumbe walikuwa wakiletwa Casino La Dreamer?

    “Ee bwana ee...jamaa kamleta mtoto kasino! Si mchezo babaake...” Yule dereva alisema kwa kushabikia ile hali huku akinitupia jicho la pembeni na kukatisha mawazo yangu.

    “Na sasa jasho litamtoka. Bado unahitaji pesa zaidi? Nimekupa elfu kumi na tano ukumbuke!.” Nilimwambia yule dereva huku nikishuhudia ile gari iliyowabeba akina Kachiki ikiingia ndani ya lile geti la nyuma la Casino La Dreamer, na lile geti likifungwa nyuma yake. Yule dereva alidai aongezwe elfu kumi zaidi, lakini baada ya mabishano mafupi, nilimuongezea shilingi elfu tatu na kuagana naye.

    Kwa nini ile gari iliishia CasinoLa Dreamer? Hii kasino mimi nilikuwa nikiijua sana, kwani ingawa sikuwa nimewahi kuingia humo ndani hata siku moja, nilikuwa nikiiona mara kwa mara nilipokuwa katika pita pita zangu za mjini na hata katika matangazo mbali mbali ya barabarani na kwenye vyombo vya habari, hasa televisheni.

    Lakini Casino La Dreamer sio The Rickshaw!

    Sasa kwa nini akina Kachiki wasipelekwe huko The Rickshaw na badala yake waletwe hapa kwenye hii kasino?

    Nilijipa moyo na kuingia ndani ya ile kasino, ikiwa ndio mara yangu ya kwanza kuingia katika kasino tangu nizaliwe. Niliangaza huku na huko kwa chati na kutafuta meza iliyokuwa pembeni na kuketi. Niliagiza kinywaji na chakula cha makaroni, huku moyoni nikiumia sana baada ya kutajiwa ile bei ya vyakula vile, na wakati nikisubiri nilianza kuangaza mle ndani. Hakukuwa na watu wengi, na niliona wengi wa waliokuwamo mle ndani walikuwa wakijishughulisha na michezo mbali mbali ya kamari, pool na kunywa pombe. Wengine walikuwa wamepakatana na mabinti waliokuwa nusu uchi, wakinyonyana ndimi na kufanya mambo ya aibu bila haya;na wala hakuna aliyeonekana kushangazwa na hali ile isipokuwa mimi.

    Ni nini kinaendelea hapa? Wako wapi akina Kachiki?

    Nilianza kula chakula changu taratibu sana, huku nikitembeza macho mle ndani kujaribu kuona iwapo kuna kitu chochote cha kuniwezesha kuelewa kinachoendelea mle ndani kuhusiana na tukio nililolishuhudia kule msituni siku kadhaa zilizopita, kwani kwa vyovyote ile sehemu iitwayo The Rickshaw ilikuwa na umuhimu mkubwa sana kwa yule mtu aliyeuawa kule msituni kiasi cha kuisisitizia sana kabla ya kifo chake. Sasa kama hii kasino iitwayo La Dreamer ilikuwa na uhusiano wowote na The Rickshaw, lazima kuwe na kitu cha kuniwezesha kujua...

    Lakini ni kitu gani?

    Mazingira yalionekana shwari kabisa. Hakukuwa na dalili ya hao wafanyabiashara kutoka nchi za magharibi, wala akina Kachiki...kulikoni?

    Nilimwita mhudumu na kumuuliza uelekeo wa chooni. Aliponielekeza niliinuka na kuanza kuelekea usawa wa chooni huku nikiangaza kwa chati mle ndani nikijaribu kutafuta namna ya kuwaona akina Kachiki. Kabla ya kuvifikia vyoo, kulia kwangu niliona milango mipana ya kioo kisichoruhusu kuona upande wa pili, yaani tinted. Bila kujishauri zaidi na huku moyo ukinipiga kwa nguvu, niliacha ule uelekeo wa vyooni na kujaribu kusukuma ile milango, ambayo ilifunguka nami nilijitoma ndani haraka na kujikuta nikiwa kwenye korido fupi iliyokuwa na hewa safi ya viyoyozi visivyoonekana. Nilisimama kwenye ile korido na kuangaza mazingira niliyokuwamo. Kulia kwangu, hatua chache mbele yangu, kulikuwa na milango ya lifti za kupanda kwenye ghorofa ya juu, na hatua chache mbele zaidi, upande wa kushoto, kulikuwa kuna mlango mwingine mpana uliokuwa na kioo katika nusu yake ya juu ilhali nusu yake ya chini ikiwa ni mbao safi ya mninga. Niliunyatia ule mlango na kuchungulia kwenye kile kioo na kugundua kuwa ulikuwa ni mlango uliotokea jikoni, ambapo niliona wapishi wengi wake kwa waume wakiwa wamezama katika mapishi mbali mbali. Nilirudi hadi kwenye ile milango ya lifti na kubonyeza kitufe kimoja na pekee kilichokuwa kando ya ile milango nayo ikafunguka. Niliingia ndani ya ile lifti huku moyo ukiwa unanipiga kwa wasiwasi na ile milango ikajifunga. Ndani ya ile lifti nilibonyeza kitufe cha kwenda juu na ile lifti ilianza kupanda taratibu. Kufikia hapa moyo ulikuwa ukikimbia kwa kasi isiyo ya kawaida na ingawa kulikuwa kuna kiyoyozi cha nguvu ndani ya ile lifti, nilihisi jasho likinitoka.

    Hatimaye ile lifti ilifika mwisho wa safari yake na ile milango ikafunguka nami nikatoka nje kwa mashaka, na kwa hakika sikuwa nimejiandaa kabisa na kile kilichokuwa kikinisubiri nje ya ile lifti.

    Hatua zipatazo kumi na tano mbele yangu kulikuwa kuna lango kubwa lililonakshiwa kwa mbao na vioo kwa namna ya kupendeza kabisa, na juu yake kukiwa na maandishi yaliyowaka taa, herufi zake zikiwa zimerembwa kwa mtindo wa kuvutia nami nikabaki nikilitazama lile neno lililoandikwa juu ya mlango ule huku taa za rangi mbali mbali zikitembea ndani ya herufi zake.

    THE RICKSHAW.

    “Oh, My God...” Nilibaki nikiwa nimepigwa na butwaa huku nikiingiwa na msisimko mkubwa uliotokana na ufumbuzi wa fumbo lile la The Rickshaw nililoachiwa na Mr.Q, na uficho ulioizunguka sehemu hii kama jinsi nilivyoelezwa na Kachiki.

    The Rickshaw ni kasino ndani ya kasino!

    Niliangaza taratibu katika lile eneo nililokuwa nimeibukia. Sehemu yote ilikuwa na ukuta wa kioo, nami nilikuwa nimesimama kwenye korido pana iliyozungukwa na vioo kila upande, hadi kwenye dari. Kila nilipogeuka nilijiona mimi mwenyewe, na kiasi niliinigiwa na woga kutokana na hali ile. Ni kama nilikuwa ndani ya boksi la kioo. Sakafu ya ile korido ilikuwa ni ya marumaru, yaani ceramic tiles, na kushoto kwangu, mwisho wa ile korido kulikuwa kuna ngazi zilizoelekea juu ya jengo lile.

    “Hakuna huduma leo Anti!” Nilishitushwa na sauti nzito ya kiume na kwa mara ya kwanza niliwatilia maanani wale mabaunsa wawili waliokuwa wamesimama kila upande wa lile lango kubwa la kuingilia ndani ya ile sehemu ya starehe iliyoitwa The Rickshaw.

    Ingawa niliwaona wale watu wenye miraba minne wakiwa wametunisha vifua mbele ya ule mlango tangu nilipoteremka kutoka kwenye lifti, lakini akili yangu ilichotwa moja kwa moja na lile neno The Rickshaw lililokuwa juu ya ule mlango na yale mazingira ya vioo ya eneo lile kiasi kwamba sikuwatilia maanani kabisa.

    Nilijikohoza kwa aibu na kuwauliza kulikoni leo kuwe hakuna huduma huku nikiwasogelea taratibu

    “Leo ukumbi umekodiwa kwa siku nzima…labda uje kesho….” Mmoja wa wale mabaunsa aliniambia huku akisimama mbele ya ule mlango kunizuia nisijaribu kujipenyeza humo ndani. Moja kwa moja nilielewa kuwa huduma ilikuwa imefungwa kutokana na ule ugeni maalum wa wafanyabiashara kutoka nchi za mbali ambao akina Kachiki waliletwa kuja kuwahudumia. Nilijikohoza tena kwa kukosa jambo la kufanya na kumtazama kwa hofu yule baunsa na kujaribu kumuambia kitu lakini nilikosa la kusema. Nilirudi nyuma taratibu huku nikiwatazama wale watu kwa woga, huku nao wakinitazama kijeuri, kama kwamba walikuwa wakinitegea nibishane nao ili wanioneshe madhara ya kubishana na misuli yao.

    Nilibonyeza kitufe, milango ya lifti ikafunguka nami nikaingia ndani. Niliendelea kutazamana na wale mabaunsa wakiwa mbele ya ule mlango wa The Rickshaw hadi ile milango ya lifti ilipojifunga nami nikateremshwa kule chini kwenye lile eneo la CasinoLa Dreamer.

    Kwa nini ile kasino nyingine iitwayo The Rickshaw isitangazwe hadharani kama jinsi ilivyokuwa ikitangazwa ile kasino La Dreamer ambamo ndani yake ndio ilikuwamo ile kasino iliyoitwa The Rickshaw?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilitoka kwenye ile milango ya kioo na kukata kushoto haraka, nikijitia ndio nilikuwa natokea chooni, na kurudi kuketi mezani kwangu. Moyo ulikuwa ukinipiga kwa nguvu sana.

    Ee, Mungu wangu! Yaani nimeigundua The Rickshaw!

    Sikuamini, na kwa mara nyingine nilishukuru uamuzi wangu wa kumsaidia Kachiki siku nilipokutana naye kwa mara ya kwanza na kuomba kuambatana naye hadi kule Uno Trabajo Bar.

    Ningeigundulia wapi The Rickshaw kwa jinsi ilivyokuwa imefichwa namna ile! Yaani ningezunguka mji mzima na ningeambulia patupu. Lakini sasa nilikuwa nimepagundua.

    Hapana shaka pale ndio kwenye majibu yote ya mkasa huu niliotumbukizwa bila ya ridhaa yangu.

    “Haya Mr.Q, nimeshafika The Rickshaw, ni kitu gani sasa ulichotaka nikione humu ndani?” Nilijinong’onea mwenyewe huku nikiendelea kushika shika chakula changu na nikiangaza-angaza mle ndani, nikitegemea kumuona yule muuaji muongo anayejiita Martin Lundi au yeyote katika wale wafuasi wake.

    Lakini sikumuona yeyote kati yao.





    Baada ya kuzubaa mle ndani kwa muda, niliamua kuondoka. Nilijua kwa kuwa nimeshaigundua The Rickshaw ilipo, niliweza kurudi tena wakati wowote, jambo ambalo nilidhamiria kulifanya siku iliyofuata tu na kuendelea na uchunguzi wangu wa kutafuta majibu ya maswali yaliyotokana na lile tukio la msituni. Nililipia chakula na kinywaji changu na kutoka nje ya ile kasino na kuanza kukata mitaa kutafuta uelekeo wa kurudi Uno Trabajo Bar, huku kichwani mwangu nikiwa natafakari mtirirko wa matukio yaliyopelekea hadi mimi kulazimika kuitafuta ile kasino iliyoitwa The Rickshaw na kufanikiwa kuibaini. Mr. Q alikuwa ameniachia ile namba ambayo mpaka sasa sikuwa nimeweza kuing’amua ilikuwa inahusu nini, na lile neno The Rickshaw ambalo leo hii nimehakikisha kuwa ni jina la kasino iliyojificha ndani ya kasino nyingine katikati ya jiji. Sasa nilikuwa na kitendawili cha neno “Key”, neno lililotamkwa na yule marehemu aliyeuawa na marehemu Macho ya Nyoka kule msituni, likimaanisha “ufunguo”. Kwa kadiri mambo yalivyojitokeza hivi sasa, nilidhani kuwa yule mtu aliyeuawa kule msituni alikuwa akimaanisha kuwa nikiigundua The Rickshaw, nitakuwa nimepata ufunguo (key) wa ufumbuzi wa kile kizaazaa nilichokishuhudia kule msituni, ufunguo ambao ungeniwezesha kumtia mbaroni yule mwanaharamu aliyejiita Martin Lundi na wenzake. Nilidhani hivi ndivyo Mr.Q alivyomaanisha alipokuwa akinitajia yale maneno na kuniambia “find the bastard”, akimaanisha kuwa nimtafute mwanaharamu Martin Lundi muongo.

    Nilikuwa nimefika eneo la posta mpya nikielekea kwenye kituo cha mabasi ya Gongo la Mboto, akilini mwangu bado nikiwa nimejawa na mawazo juu ya hatua ya kuchukua baada ya kuigundua ile kasino iliyoitwa The Rickshaw.

    Sasa kitendawili pekee kilichobakia ni ile namba ambayo hapo mwanzo nilidhani kuwa ni ya simu na kugundua kuwa haikuwa hivyo.

    Huyo “The Bastard” nilikuwa nimeshamjua, tatizo lilikuwa ni kumtia mbaroni tu. Na wakati nikiwa napishana na wimbi la watu waliokuwa wakipita na hamsini zao katika sehemu ile ya jiji iliyokuwa na msongamano mkubwa wa watu siku zote, nilifikiri kuwa ule ulikuwa ni wakati muafaka wa kumtafuta Kamishna Msaidizi John Vata na kujitokeza kwake nikiwa na zile taarifa muhimu dhidi ya kundi la akina Martin Lundi. Kwa vyovyote yeye angekuwa na namna nzuri ya kuingia The Rickshaw na kuvumbua kilichokuwemo.

    Ghafla nilisikia nikichomwa na kitu kama sindano kwenye ubavu wangu wa kulia na hapo hapo nilihisi maumivu makali na mwili wangu ukinifa ganzi kutokea kiunoni kuelekea chini. Nilijishika eneo lililochomwa huku nikitoa yowe la uchungu na kuangaza huku na huko nikimtafuta aliyenichoma, lakini watu walikuwa wengi sana, na kila mtu alionekana akiwa na hamsini zake.

    Au nimeumwa na nyuki…?

    Nilihisi kichwa kikiniwia chepesi na miguu ilianza kugongana, ilhali kizunguzungu kikinigubika ghafla.

    Imekuwaje tena Mungu wangu?

    Nilitazama watu niliokuwa nikipishana nao huku nikijitahidi kutembea, lakini niliona watu wote sasa walikuwa wakitembea taratibu sana…kiminyato…kama kwenye slow motion ya kwenye sinema, na sura zao zikibadilika na kuwa za kutisha sana.

    Naingiwa na wazimu au…?

    Nilimpamia mama mmoja mnene sana naye akanigeukia kwa hasira na kunikemea, lakini sikusikia lolote katika maneno aliyokuwa akiniambia na badala yake nilisikia mvumo mzito masikioni mwangu na niliona midomo ya yule mama mnene sana ikifunguka na kufumba taratibu sana na meno yake yakiwa makubwa kupita kawaida ya meno ya binadamu.

    Jamani…! Ni nini tena hii…?

    Nilianza kuyumba huku nikiwatazama watu usoni, nikiona sura zao zikibadilika na kuwa kama za wanyama wa ajabu-ajabu. Mtu alinipamia kwa nyuma nami nikampamia mtu mwingine aliyenisukuma pembeni huku naye akitoa maneno ya kukereka na kitendo kile, lakini sikusikia neno lolote. Kwa mbali niliwaona makondakta wa madaladala na wapiga debe wakipanua midomo yao kwa nguvu na wakipiga kelele nyingi huku mishipa ya shingo zao ikiwatutumka ilhali macho yao yakiwa mekundu na makubwa sana. Lakini sikusikia sauti yoyote kutoka vinywani mwao. Ilikuwa ni taswira ya kutisha sana.

    Mungu wangu…what is happening?(Ni nini kinatokea?)

    Nilianza kusikia kichefuchefu na miguu ikiishiwa nguvu kabisa.Nilijiona nikianguka mzima mzima na sikuwa na lolote nililoweza kufanya kujiokoa. Nilipiga kelele kuomba msaada lakini hata sauti yangu sikuisikia. Nilijaribu kujizuia kuanguka kwa kujiegemeza kwenye meza ya mmoja wa wauza peremende waliokuwa pale kando ya kituo cha mabasi. Ile meza ilipinduka nami nilipiga mwereka mzito pamoja nayo mpaka chini. Hapo ndipo nilipoanza kusikia mayowe na sauti za wapita njia. Nilibaki nikiwa nimelala chali kando ya barabara nikitweta na nikiona maluweluwe matupu mbele ya macho yangu na mwili wangu ukiunguzwa na joto la jua lililoikaanga ile ardhi.

    “Bila shaka ana kifafa! Mpeni nafasi! Apate hewa!”

    Macho yalianza kuniwia mazito na nikaona watu wawili wawili wakiwa wameniinamia.

    “Ana njaa huyo...mjini hapa, usimuone mrembo...”

    Oh, Mungu wangu! Lazima niinuke..niondoke...nikampigie simu John Vata...

    Nilijaribu kujiinua lakini mwili uliniwia mzito sana na nilihisi pumzi zikiniishia, watu walinizingira, na nikahisi mikono mingi ikinishikashika mwilini.

    Wananiibia sasa…vibaka wananiibia! Wanajitia kunisaidia lakini wananiibia…wananiibia…

    “Nipisheni! Nipisheni, mimi ni daktari...naweza kumsaidia!”

    Naijua hii sauti! Naijua hii sauti... ni nani...?

    “Jamani bahati kuna dokta...mpisheni, mpisheni...”

    Nilijaribu kujiinua lakini nilishindwa na koo likaanza kunikauka. Niliona watu wakisogea pembeni na kuniacha peke yangu.

    Jamani nisaidieni mwenzenu! Msiniache...!

    “Jamani mimi ni daktari...I am a Doctor...naomba nimuangalie...tafuta gari haraka!”

    Ile sauti! Ile sauti! Oh. My God...

    Macho yalizidi kuniwia mazito, lakini nijitahidi kuyafumbua huku moyo ukinienda mbio kuliko kawaida.

    Lazima nimuone mwenye hii sauti! Namjua! Ni nani...

    Kwa kihoro nilimuona yule mtu anayejiita Martin Lundi akipiga goti kando yangu na kuniinamia wakati watu wote waliokuwa wamenizunguka hapo mwanzo wakikaa pembeni kumpisha.

    Oh! Mungu wangu!

    Nilijaribu kupiga kelele lakini sauti haikutoka. Niliinua mkono wangu na kumtandika kofi zito la uso, lakini hiyo ilikuwa mawazoni mwangu tu, kwani hata mkono wangu sikuweza kuuinua. Nilimuona Martin Lundi muongo akinitazama kwa makini, kama jinsi ambavyo daktari angeweza kumtazama mgonjwa katika mazingira kama yale, ingawa macho yake yalionesha mng’ao wa ushindi ambao watu wote waliokuwapo pale hawakuweza kuuelewa isipokuwa mimi.

    Nilimtemea mate kwa ghadhabu, lakini niliambulia kujimwagia udenda mzito uliotiririka mashavuni mwangu na kumwagika mchangani kila upande wa shingo yangu.

    Get away from me you bloody bastard!(Kaa mbali na mimi ewe muuaji mwanaharamu!)

    Nilibaki nikimtazama yule mtu ajiitaye Martin Lundi kwa kukata tamaa huku nikishindana na macho yangu yaliyokuwa yanataka kufumba nami nikiyalazimisha yaendelee kutazama, lakini yaliniwia mazito kupita kiasi.

    Martin Lundi aliniwekea mkono kwenye upande wa shingo yangu na kunifunua macho yangu kitaalamu.

    Eti alikuwa akinichunguza kitabibu!

    “Kaa mbali na mimi muuaji mkubwa we! Niache! Niache!” Lakini hizo kelele zote zilikuwa akilini mwangu tu, hakuna hata sauti moja iliyotoka kinywani mwangu. Mdomo uliniwia mzito kupita kawaida.

    Oh! Mungu wangu, wameshanichoma sindano ya sumu...

    Kisha kote kukawa kiza.



    “THE BASTARD"



    H

    ix.



    arufu kali ya dawa ilizivamia pua zangu, nami nikajaribu kufumbua macho nikishindana na usingizi mzito. Mwanga mkali ulinipiga usoni na nikajikuta nikifumba tena macho yangu na nikaelewa kuwa nilikuwa nimelala chali kitandani, lakini sikujua nilikuwa wapi. Nilifumbua tena macho taratibu, na huku nikishindana na ule mwanga mkali wa taa uliokuwa ukinipiga usoni nilianza kuangaza yale mazingira niliyokuwamo na mara moja nilijua kuwa nilikuwa hospitali.

    Nimefikaje hapa?

    Sikuwa na kumbukumbu yoyote ya uhakika juu ya matukio yaliyopelekea mimi kuwa mahala pale, ila nilikuwa na kumbukumbu za mbali sana...kama ukungu tu, juu ya yaliyotokea. Moja kwa moja mbele yangu kulikuwa na mlango wa kioo kizito. Niligeuka taratibu kushoto kwangu huku nikisikia maumivu mwili mzima. Kulikuwa kuna ukuta uliopakwa rangi nyeupe na kalenda ikining’inia pale ukutani. Ile kalenda ilikuwa ikionesha kuwa ule ulikuwa ni mwezi wa julai mwaka 1999.

    Nilikunja uso.

    Eh! Hii nini sasa? Mwaka 99! Kwani huu si mwaka...mwaka...mwaka gani...! Mungu wangu, yaani nimesahau huu ni mwaka gani?

    Niligeuza kichwa kulia kwangu ambako niliona mitambo kadhaa ya kitabibu, kitanda kirefu cha kufanyia uchunguzi wagonjwa na kando ya ule mlango kulikuwa kuna kabati refu lililojengewa ukutani ambalo milango yake ilikuwa imefungwa. Macho yangu yaliangukia tena pale mlangoni na kutokea pale nilipokuwa nimelala, niliweza kuona maandishi yaliyoandikwa kwa nje ya kioo cha mlango ule, ambayo yalisomeka kutokea kulia kwenda kushoto. Nilifinya macho na kujaribu kuyasoma yale maandishi kwa taabu, na nilipofanikiwa niliuhisi mwili wangu wote ukiingia baridi na moyo ukianza kunipiga kwa nguvu.

    PSYCHIATRIC WARD 4

    Psychiatric Ward?

    Wodi ya wagonjwa wa akili!

    Yaani niko kwenye wodi ya wagonjwa wa akili? Nini maana yake hii?

    Na hapo hapo ilinijia taswira ya yule mama mkuu wa wilaya ya Manyoni akiniambia kuwa mimi nilikuwa mgonjwa wa akili.

    “Wewe ni mgonjwa Sylvia…Paranoid Schizophrenia ni ugonjwa hatari sana, unaweza kuwaua wenzako bila kujijua halafu ukaamini kuwa watu walikuja kuwaua na wewe ukafanikiwa kutoroka…vitu hivi vipo…”

    Eh, Mungu wangu! Sasa...

    Kichwa kilianza kunigonga na ghafla niliuhisi ulimi wangu ukiwa mkavu kama msasa. Nilijaribu kwa mara nyingine kukumbuka matukio yaliyopelekea mimi kujikuta mle ndani lakini lile neno lililokuwa limeandikwa pale kwenye kioo cha ule mlango lilizidi kuikamata akili yangu.

    Psychiatric Ward!

    Ina maana mimi ni kichaa?

    Kichwa changu kilikuwa kinazongwa na vitu vingi kwa wakati mmoja na hakuna hata kimoja katika hivyo kilichokuwa kimekamilika. Vitu vyote vilikuwa nusu-nusu.

    Nikiwa nimeingiwa na woga mkubwa, nilijiinua kwenye kitanda kile na kuzungusha kichwa changu kulia zaidi ili nizidi kuona zaidi vilivyomo mle ndani na ndipo nilipomuona.

    Mwanamke wa makamu aliyekuwa amevaa sare za nesi wa hospitali alikuwa amekaa kwenye kiti kilichokuwa kwenye kona ya chumba kile akisoma kitabu. Nilimtazama kwa wasiwasi, lakini yeye alikuwa amezama kwenye kitabu chake, akidhani bado nimelala.

    Ni nani tena huwa anavaa nguo kama hizi...?

    Nilimtazama yule mwanamke. Kifuani alikuwa amening’iniza simu nzuri ya kiganjani iliyokuwa ikining’inia kutoka kwenye kamba maalum iliyopitishwa shingoni mwake. Niliitazama ile simu, kisha nikageukia kule ukutani kwenye ile kalenda.

    “Nitoe humu ndani upesi!” Nilimwambia yule mwanamke kwa sauti iliyokoroma na ingawa nilikuwa nimedhamiria kumkaripia, lakini ilitoka kwa udhaifu sana. Yule mwanamke alishituka na kuweka kitabu chake juu ya meza iliyokuwa kando ya kiti alichokuwa amekalia na kuja kando ya kitanda nilichokuwa nimelalia huku akitabasamu.

    “Hatimaye ameamka! Unajisikiaje sasa kisura wangu?” Aliniuliza kwa sauti ya kuliwaza kama kwamba alikuwa anaongea na mtoto mdogo. Nilimtazama kwa mshangao. Sikuwa nimewahi kumuona hata siku moja kabla ya pale.

    “Wewe ni nani...niko wapi hapa?” Nilimuuliza kwa wasiwasi.

    “Mimi ni nesi...niite nesi Tamala...na hapa uko hospitali...Nellie Nightingale Memorial Hospital”

    Sikuwa nimepata kuisikia hii hospitali hata siku moja na wala sikujali.

    Kwa nini akili haizingatii mambo?

    Niliitazama tena ile simu yake na kupeleka macho yangu kwenye ile kalenda, ambayo ilikuwa bado mpya.

    “Leo ni siku gani...” Nilimuuliza taratibu, alisita kidogo.

    “Emm...Alhamisi. Tarehe kumi na mbili Julai...”

    “Mwaka gani...?”

    “1999...Lakini usijitese kwa mawazo mengi...ni mbaya kwa afya yako.Unahitaji utulie...upumzike.” Yule mwanamke alinijibu haraka. Nilishindwa kuelewa, nikaigeukia tena ile simu yake. Nikakitazama na kile kitabu alichokuwa akisoma kilichokuwa juu ya meza kando ya kiti alichokuwa amekalia hapo mwanzo.

    Mbona sielewi? Kuna kitu hakipo sawa hapa. Lakini ni nini? Na kwa nini najiona kama...kama...mjinga?

    “Hii hospitali...Iko wapi? Na nimefikaje hapa?”

    “Hapa hapa Dar es Salaam. Ulianguka njiani, wasamaria wema wakakuleta...lakini unahitaji upumzike Sylvia.Unahitaji kunywa dawa yako sasa....”

    “Whaaat? Sylvia? Mimi sio Sylvia! Nani kakupa hilo jina? Mimi ni....mimi ni....” Oh, Mungu wangu mbona jina langu silijui? Wamenifanya nini hawa watu?

    “Hapana binti, wewe ni Sylvia, ndio maana nakuambia kuwa unahitaji dawa na kila kitu kitakuwa sawa....”

    Nilipata mlipuko mwingine wa kumbukumbu kichwani mwangu, safari hii nikiwa kule ofisini kwa mkuu wa wilaya na yule mwanamume aliyevaa mavazi ya kitabibu akinisogelea huku akitabasamu.

    “Hallo Sylvia, unajisikiaje leo?”

    Nilipiga ukelele mkubwa sana wa woga na hasira, kwani matukio yote yaliyotokea kule msituni hadi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya yalinirudia akilini mwangu haraka haraka na kuishia na sura ya yule mwanaume aliyekuwa amevaa mavazi ya kitabibu akinitolea tabasamu baya na la kuogofya.

    “Waongo wakubwa! Wabaya sana nyinyi...! Nitoe humu ndani haraka sana! Nitoe! Nitoe! Nittt-toeeeeeeeeeeee!”

    Nilijiinua kwa nguvu kutoka pale kitandani na kujaribu kuteremka lakini nilishindwa. Mikanda maalum iliyokuwa imefungwa kwenye kile kitanda ilikuwa imepita chini ya makwapa yangu na kubana kifua na sehemu ya mapaja yangu, na kadiri nilivyokuwa nikijikukurusha pale kitandani ndivyo ilivyozidi kujikaza na kunibana zaidi pale kitandani.

    Ni nani yule mwanaume mwenye koti la kitabibu aliyeniita kwa jina la Sylvia? Nalijua jina lake, lakini kwa nini halinijii?

    “Tulia Sylvia, utajiumiza bure kisura wangu! Tulia nikupe dawa! Usipotulia nitakuchoma sindano, lakini ukitulia nitakupa dawa ya vidonge tu umeze umesikia?” Nesi Tamala aliniambia kwa ukali nami nikabaki nikimtazama, nikishangaa kujisikia hamu kubwa sana ya kuangua kicheko.

    Sasa kwa nini nicheke? Hii si hali ya kuchekesha! Nimekuwaje mimi?

    Nilianza kububujikwa na machozi huku nikimtazama yule nesi kwa kukata tamaa.

    Oh! Mungu wangu, sasa nimekuwa mwehu...http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





    “Ooo, sasa usilie kisura wangu eeenh....usilie anti utapona tu!” Nesi Tamala alinisemesha kwa kubembeleza huku akiwa ameshika bomba la sindano, tayari kunichoma. Niliitazama kwa woga ile sindano na nilihisi mwili ukinisisimka.

    “Kwa...kwani ninaumwa nini nesi?” Nilimuuliza huku nikilia. Yule mwanamke alinitazama kwa muda kisha akaniambia kuwa nilikuwa ninaumwa sana. Nilikuwa ninaumwa sana kichwani.

    “Una ugonjwa ndani ya kichwa chako Sylvia....ndio maana inabidi upatiwe hii dawa.”

    “Lakini...lakini mimi sio Sylvia! Mimi ni...mimi ni....” Oh, Mungu wangu, jina langu ni nani tena? “Mimi ni....sio Sylvia!”

    “Sasa kama sio Sylvia, jina lako ni nani basi?” Nesi Tamala aliniuliza taratibu huku akizidi kuiandaa ile sindano. Badala ya kumjibu, nilibaki nikiikodolea macho ile sindano.

    “Naomba usinichome sindano tafadhali mama! Naomba usinichome sindano...” Nilibwabwaja kama mtoto huku nikilia. Eh! Mungu wangu, mambo gani tena haya! Mbona najiona nakuwa mjinga-mjinga tu?

    Nesi Tamala alinitazama, kisha aliweka pembeni ile sindano na kutoa dawa za vidonge kutoka kwenye kichupa cheupe cha plastiki.

    “Okay Sylvia...kwa kuwa umekuwa mpole nitakupa vidonge....”

    “Mimi sio Sylvia! Kwa nini mnapenda kuniita hivyo?”

    “Kwa sababu ndio jina lako, Sylvia!”

    Nilishituka na kutazama kule mlangoni ilipotokea ile sauti nzito iliyonijibu kwa ukali. Na muda nilipomtazama tu yule mtu aliyenijibu akiingia mle ndani, nilipatwa na mlipuko mwingine wa kumbukumbu ya tukio lililotokea kabla ya kujikuta ndani ya ile hospitali.



    Niliyumba na kupiga mweleka mzito barabarani, kisha nikasikia mayowe ya watu wengi, kila mtu akisema neno lake. Nikiona yule mtu akipiga goti kando yangu na kunishika shingoni, kisha akafunua macho yangu. Nikijaribu kumtemea mate na kuishia kujibubujia udenda. Kisha kiza kizito kilitanda...



    Nilihamanika kuliko kawaida. Nilimgeukia yule nesi aliyekuwamo mle ndani kutaka msaada wake, lakini hapo hapo akili yangu ilikuwa kama iliyosimama. Nilibaki nikimkodolea yule nesi uso wake ukionesha woga mkubwa kwa yule mtu aliyeingia, na hiyo ilinikumbusha nesi mwingine aliyenitazama kwa woga kama ule...ni nani...?Lini...? Nilianza kumgeukia tena yule mwanaume aliyeingia na hapo nilipatwa na mlipuko mwingine wa kumbukumbu. Nilimuona dada yangu Koku akiwa katika mavazi kama ya yule nesi akinitazama kwa woga mkubwa sana kama ule niliouona usoni kwa yule nesi, akinisemesha kwa wasiwasi mkubwa.

    “Huelewi Tigga. Hawa watu wamo humu hospitalini!”

    Na hapo nilikumbuka.

    Tigga! Jina langu ni Tigga...sio Sylvia!

    Nilijiinua kwa nguvu kutoka pale kitandani nikijaribu kumrukia yule mtu kwa hasira huku nikimpigia kelele za ghadhabu.

    “Wewe! Nimekumbuka! Mimi ni Tigga! Tigga Mumba...sio Sylvia, na wewe ni muuaji! Toka! Ondoka machoni mwangu! Usinisogelee! Muuaji!”

    Martin Lundi muongo alishituka sana na nilishuhudia uso ukimbadilika na kwa muda hatua zake zilisita, kisha akajikaza na kunisogelea pale kando ya kitanda na kunitazama kwa ghadhabu bila ya kusema neno. Nami nilimrudishia mtazamo wa ghadhabu huku nikijitutumua nikijaribu kujiinua kutoka pale kitandani ilhali ile mikanda maalum iliyonibana pale kitandani ikizidi kukaza na kunibana zaidi.

    “You are crazy Sylvia, and you know it!” Aliniambia kwa hasira, akimaanisha kuwa mimi nilikuwa kichaa na kwamba na mimi mwenyewe nilikuwa najua juu hilo, akizidi kuniita lile jina alilonibatiza kienyeji.

    “I am not!” Nilimbishia kwa jeuri, kuwa sikuwa mwendawazimu.

    “Then you soon will be, unless you give us what we want!” Alinijibu kwa jeuri, akimaanisha kuwa kama sikuwa na wazimu, basi nitakuwa na wazimu muda si mrefu, labda niwape walichokuwa wakikitaka.

    Nilimkodolea macho kwa mshangao lakini kabla sijasema neno, mtu mwingine aliingia mle ndani, akiwa na mavazi ya kitabibu.

    “Ni nini kinaendela hapa?” Aliuliza taratibu huku akisogea pale kando ya kitanda nilichokuwa nimelazwa. Huyu alikuwa mtu wa makamo, lakini aliyeonekana kujiweka katika afya nzuri na haikuwa na shaka kuwa alikuwa ni daktari. Alikuwa amevaa koti jeupe la kitabibu juu ya fulana nyeusi na suruali ya jeans. Martin Lundi muongo alimgeukia yule daktari na kumkemea kwa ukali.

    “Naona dawa zako hazifanyi kazi inavyotakiwa Dokta!”

    Yule daktari badala ya kumjibu aliniinamia na kuanza kuniuliza juu ya hali yangu. Nilimtazama kwa jeuri na kutazama pembeni bila kumjibu. Martin Lundi muongo alimkemea tena yule daktari.

    “You said the medication will make her docile enough to tell us everything!” (Ulisema hizo dawa zitampumbaza na kumfanya awe mtiifu kiasi cha kutueleza kila kitu!) “Lakini bado akili yake inaonekana makini!”

    Yule daktari alimgeukia Martin Lundi muongo na kumjibu taratibu, huku nikigundua kitetemeshi katika sauti yake.

    “Yes, but I said after three days of medication. This is only the first day!” (Ndio, lakini nilisema baada ya kutumia dawa kwa siku tatu. Hii ndio siku ya kwanza!)

    Eh! Ni nini kinatokea hapa?

    “Nilishasema kuwa siwezi kusubiri muda wote huo! Nataka...”

    “Then I can’t help you! Unless you want the poor girl to go completely mad...or even die!”

    (Basi siwezi kukusaidia! Isipokuwa kama unataka huyu msichana awe mwehu kabisa...au hata afe!) Yule daktari alimkatisha Martin Lundi kwa ukali nami nikaingiwa woga mkubwa kwani yale maneno yalinielewesha kilichokuwa kikiendelea pale.

    “Baada ya kupata ninachokitaka, hilo ndilo hasa ninalotaka litokee!” Martin Lundi muongo alijibu kwa hasira. Alienda kusimama nyuma ya dirisha na kukaa kimya kwa muda, kisha alimrudia yule daktari kwa mwendo wa haraka.

    “Nakuambia nataka matokeo baada ya siku mbili, na usijitie kunitolea ukali mimi kwa sababu unajua ni nini ninachoweza kukufanyia na kukuharibia maisha yako! Don’t you ever forget that I can destroy your comfortable life by a single telephone call!” Alimwambia kwa sauti iliyojaa vitisho na hasira huku akimtomasa kwa kidole chake cha shahada kifuani, akimaanisha kwa yale maneno ya kimombo kuwa yule daktari asisahau hata siku moja kuwa yeye (Martin Lundi) anaweza kuyaharibu maisha yake mazuri kwa kupiga simu moja tu. Yule daktari alitahayari na kuingiwa na woga, lakini alijitahidi kujitutumua na kumjibu yule muuaji muongo.

    “Na wewe usiingilie kazi yangu, kwani ujio wako unaingilia utendaji kazi wa dawa zangu. Huyu binti anakutambua na inaonekana taswira yako imejishindilia sana akilini mwake, hivyo ni vyema ukawa mbali naye kwa muda wote huo wa matibabu...”

    Martin Lundi muongo alimtazama kwa hasira yule bwana, kisha akanitazama kwa hasira na alimjibu yule daktari huku bado akiendelea kunitazama mimi kwa ghadhabu.

    “Okay Dokta! Nitafanya hivyo lakini nitakuwa humu humu ndani ya jengo! Kwani nimemuandalia mateso makali huyu dada baada ya kukamua taarifa zote nizitakazo kutoka kwake. Sasa ole wako baada ya siku mbili hizo dawa zisifanye kazi!” Kisha alitoka kwa hasira na kuniacha nikiwa na nesi Tamala na yule daktari aliyeshurutishwa kunipa dawa za kunichanganya akili na kunipumbaza.

    Niliogopa kupita kawaida.

    Yule dokta alimuuliza yule nesi iwapo alinipa dawa baada ya kuamka, akajibiwa kuwa ndio nilikuwa katika hatua ya kupewa hizo dawa wakati Martin Lundi alipoingia mle ndani. Yule daktari alitikisa kichwa kwa masikitiko bila ya kusema neno na kuanza kunichunguza mapigo ya moyo wangu kwa vipimo maalum vilivyokuwemo mle ndani huku akiniuliza maswali kuhusu jina langu, la mama yangu, umri wangu na kadhalika. Kwa maswali yake yote hayo sikutoa jibu hata moja. Hatimaye alimwambia yule nesi ampe sindano anichome. Hapo nilianza kujitutumua nikipinga ile hali.

    “Mnataka kunivuruga akili yangu! Kwa nini?” Nilimuuliza kwa uchungu.

    “Tulia binti, wala haitauma...” Alinijibu bila kunitazama. Niliona kuwa hakuwa akipenda kufanya jambo lile lakini ilikuwa wazi kuwa Martin Lundi alikuwa amemshurutisha kufanya vile kwa shinikizo fulani ambalo kama lingejulikana sehemu fulani, basi yule daktari angeingia matatani.

    “Samahani binti...itauma kidogo tu halafu kila kitu kitakuwa shwari.” Aliniambia kwa upole huku akinichoma sindano.

    “Unaonekana hupendi hii hali dokta...sasa kwa nini unafanya mambo haya?” Nilimuuliza huku nikiuma meno kutokana na uchungu wa sindano. Hakunijibu, badala yake alimgeukia yule nesi na kumpa maelekezo ya kunipa vidonge vitatu kila nitakapoamka kwa siku mbili zilizofuatia.

    “Akiwa anaonesha upinzani ndio achomwe sindano, kwa sababu sindano ndio inafanya kazi haraka kuliko vidonge, ingawa zote zina nguvu sawa. Ila sindano zinaacha alama nyingi mwilini kiasi cha kuweza kuleta matatizo iwapo utafanyika uchunguzi baadaye.” Alimwambia yule nesi kwa sauti ya chini, nami nilimsikia kwa mbali. Nikianza kusikia macho yakiniwia mazito na masikio yakivuma.

    Oh, Mungu wangu...jaalia hizi dawa zisifanye kazi...

    Lakini niliona kuwa zilianza kufanya kazi nami nikaanza kujihisi hamu ya kuangua kicheko na kulia kwa wakati mmoja.

    Oh, My God!

    Nilimgeukia yule nesi na nikamuona akiyeyuka mbele ya macho yangu na kuwa mvuke. Nilitaka kupiga kelele lakini niliona mdomo wangu ukiwa mzito sana. Nilimtazama yule daktari aliyekuwa amesimama akinitazama na nikamuona akirefuka na kuwa mrefu sana. Nilitaka kupiga mayowe, lakini sasa niliuhisi ulimi wangu ukivimba na kujaa kinywa chote. Mama njoo unisaidie mwanao...nakufa....

    Kiza kilitanda na kote kukawa kimya.

    --



    Nilipoamka sikuweza kujua kama ilikuwa usiku au mchana, kwani muda wote mle ndani kulikuwa kunawaka taa. Nilizungusha macho yangu huku nikihisi kichwa kikiniuma, lakini nikiwa na hisia kuwa kichwa changu kilikuwa kitupu kabisa! Yaani hakuna kitu chochote ndani ya ubongo wangu. Sijui inakuwaje hivyo, lakini kwa hakika hivyo ndivyo nilivyojihisi. Nilikuwa nimevalishwa gauni refu la kijani, kama yale ya hospitali,lakini lenyewe halikuwa limeandikwa jina la ile hospitali kama nilivyotajiwa na yule nesi, ambaye sikuwa na shaka kabisa kuwa alikuwa ni mfuasi wa yule mtu ajiitaye Martin Lundi. Nilitazama kule kwenye kabati refu lililokuwa ukutani kando ya mlango, nikahisi kuwa nguo zangu zilikuwa ndani ya kabati lile. Nilibaki kimya pale kitandani kwa muda mrefu na taratibu nilianza kuhisi akili yangu ikianza kufanya kazi. Nilikumbuka maagizo ya yule daktari aliyenichoma sindano kabla sijazama kwenye dimbwi la kiza kizito kuwa yule nesi anipe vidonge vitatu kila nitakapoamka kwa muda wa siku mbili mfululizo.

    Kwa maana hiyo akili yangu haitapata muda wa kutulia na kufanya kazi sawasawa.

    Niligeuka taratibu kule alipokuwa ameketi yule nesi akisoma kitabu chake, na kwa mara ya kwanza nikagundua kuwa yule nesi alikuwa amekaa mbele ya pazia maalum la hospitali, yale ambayo kama mtu akiwa anatakiwa kuchomwa sindano au kupatiwa tiba itakayomlazimu atoe baadhi ya nguo zake, huwa yanavutwa tu na kutoa faragha kwa mgonjwa na daktari. Hapo awali sikugundua hilo kutokana na rangi nyeupe ya lile pazia maalum kufanana sana na ile ya kuta za chumba kile.

    Hawa watu walikuwa wameamua kunivuruga akili yangu kwa haya madawa yao, ambayo waliamini kuwa baada ya siku tatu yatanifanya nishindwe kabisa kubishana nao na badala yake nitawaeleza kila walilotaka...hasa juu ya ule mkanda wa video. Nilikuwa na hakika kabisa kuwa wakifanikiwa katika azma yao hiyo wataniua. Au wataniacha nikiwa mwehu kabisa, kama jinsi nilivyomsikia yule daktari akimuelezea Martin Lundi muongo juu ya athari ya zile dawa iwapo hazitawekwa kwa vipimo maalum.

    Martin Lundi muongo angependa sana hali hiyo itokee, kwani ingenifanya kweli nionekane mwenda-wazimu na kwamba ndiye niliyefanya yale mauaji kule msituni, na hapo hakuna hata mtu mmoja ambaye angenisikiliza.

    Mungu wangu!Hawa watu mbona wabaya hivi!

    Nilimtazama nesi Tamala, nikaona alikuwa amekaa kwenye kile kiti chake akiwa anasoma kile kitabu chake cha hadithi, na kando yake juu ya meza kulikuwa na bilauri yenye soda ilhali kando ya ile bilauri kukiwa na chupa ya mirinda iliyokuwa imebakiwa na robo ya soda ndani yake.

    Nilifinya macho na kukitazama tena kile kitabu.

    Kilikuwa ni kitabu kipya kabisa cha Danielle Steel, ambaye hata mimi hupenda sana kusoma vitabu vyake.

    Lakini kile kitabu ni cha karibuni sana na hakikutungwa mwaka 99!

    Ndio maana nilikuwa nashindwa kuelewa juu ya ile kalenda ya mwaka 99 kuwamo mle ndani na yule nesi kuniambia kuwa ule ulikuwa ni mwaka 1999.

    Shit! Mwaka 1999 mimi ndio nilikuwa naanza masomo Chuo Kikuu...!

    Hata ile simu iliyokuwa ikining’inia shingoni kwa yule nesi haikuwa toleo la mwaka 99, kwani kwa kadiri nilivyoelewa, mwaka 99 simu aina ya Nokia 2100 ilikuwa bado haijatengenezwa.

    Hawa watu wanataka kunifanya kichaa...ee mwenyezi mungu nisaidie kiumbe wako!

    Kwa mara nyingine tena nilistaajabia umakini wa akina Martin Lundi katika kupanga maasi yao. Sasa nilielewa kabisa kuwa kuwekwa kwa ile kalenda mle ndani, na wale watu kuniita kwa jina lisilokuwa langu, ilikuwa ni mbinu yao ya kuzidi kunichanganya na kunivuruga akili. Mvurugiko huu ukichanganywa na hizi dawa wanazonishindilia akilini mwangu kwa hakika ungenifanya nishindwe kabisa kuelewa ukweli ni upi na uongo ni upi, hata nikiambiwa kuwa jina langu lilikuwa ni Jennifer Lopez mimi ningeamini tu, wachilia mbali hiyo kuambiwa kuwa eti mimi ni Sylvia vitu gani tu sijui huko...!(Nilisonya)

    Bila shaka nesi Tamala alisikia jinsi nilivyosonya, naye akashusha kitabu chake na kuniangalia kwa makini.





    “Njaa...” Nilimwambia yule nesi kwa sauti iliyokoroma naye alinijia haraka na kuanza kunisemesha kinafiki kama kwamba ni nesi anayejali afya yangu, nami nikamnyamazia tu. Aliniandalia chakula ambacho nilikishambulia kwa nguvu kwani hakika njaa ilikuwa ikiniuma.

    “Saa ngapi...?” Nilimuuliza. Alingalia saa kwenye simu yake na kuniarifu kuwa muda ulikuwa ni saa sita usiku. Nilijaribu kupiga hesabu kuona iwapo ilikuwa ni sawa au alikuwa akinidanganya. Sikupata jibu la haraka, na mara hiyo nesi Tamala akaniletea vidonge vitatu nimeze. Nilivipokea bila ubishi na kuvitupia kinywani mwangu huku nikipokea bilauri ya maji kutoka kwa yule nesi. Nilikunywa yale maji na kumrejeshea ile bilauri nami nikajilaza kitandani huku nikifumba macho. Nilisikia hatua za yule nesi zikielekea mezani kurudisha ile bilauri nami nikafumbua macho kumtazama na nilipoona amenigeuzia mgongo kuelekea kule kwenye meza, nilivitoa haraka sana vile vidonge kutoka chini ya ulimi na kuvitemea kiganjani mwangu. Nesi Tamala aliweka ile bilauri na kunigeukia, nami nikamtazama huku nikipeleka mkono wangu na kuviweka vile vidonge chini ya mto niliolalia bila yeye kuelewa kilichofanyika.

    “Kulala sasa binti! Au unataka sindano?” Alinisemesha kama anayeongea na mgonjwa wa akili, nami nikamtukana tusi kali la nguoni kisha nikatema mate sakafuni kwa hasira. Yule nesi alitabasamu akiamini kuwa zile dawa zilikuwa zimeanza kufanya kazi, wakati mimi nilikuwa nimemtukana kwa dhati hasa kwani alinikera kupita kiasi na nilitema mate ili nisimeze mabaki ya zile dawa nilizokuwa nimezificha chini ya ulimi wangu.

    Nilijilaza tena kitandani na kufumba macho, nikijitahidi kutafuta usingizi huku moyo ukinidunda, nikijua kuwa yule mtu anayejiita Martin Lundi alikuwamo ndani ya jengo lile, akisubiri kuja kunihoji baada ya zile dawa kufanya kazi...baada ya siku mbili.

    Lazima nitoroke hapa kabla ya muda huo!

    Nilibaki nikiwa nimejilaza pale kitandani huku nikiwa nimefumba macho kwa muda mrefu, nikijaribu kutafakari namna ya kujikwamua kutoka katika mtego ule. Kitu kilichonikosesha amani katika hali ile ni ile mikanda maalum iliyonibana pale kitandani,kwani nikiwa nimetulia haisumbui lakini muda nikianza kujikurupusha tu inakaza na kunibana kabisa pale kitandani.

    Nitajitoaje hapa?

    Hatimaye nilipitiwa na usingizi.



    --



    Asubuhi baada ya kunipatia chai, na yule nesi alinipa tena vidonge vitatu vya ile dawa. Nilifanikiwa kutumia mbinu ile ile ya kuvificha chini ya ulimi na kupitisha maji juu ya ulimi wangu na kuyameza nikiacha zile dawa chini ya ulimi bila yule nesi kugundua. Muda mfupi baadaye yule daktari alikuja na kunifanyia uchunguzi katika mapigo yangu ya moyo, na kuniwekea kipimo maalum kichwani huku akisikiliza mienendo ya ubongo wangu kwa kuweka visikilizio maalum masikioni mwake. Moyo ulikuwa ukinienda mbio sana kwani nilijua kuwa yule mtaalam atagundua kuwa sikuwa nimemeza dawa yoyote tangu alipoondoka siku iliyopita. Nilimuona akikunja uso kwa kutafakari matokeo ya uchunguzi wake.

    “You are very resistant young lady(U-msichana mbishi sana)...itabidi nikuongezee dozi, ingawa nisingependa kabisa kufanya hivyo.” Alisema kwa sauti ya chini kuniambia, akimaanisha kuwa mwili wangu ulikuwa unatoa upinzani mkubwa kwa zile dawa, hivyo itabidi aniongezee dozi. Niliona wazi kuwa alikuwa akijisemea mwenyewe, kwani kwa uelewa wake, mimi nisingeweza kuelewa chochote katika yale aliyoyasema.

    We’ ongeza dozi kadiri utakavyo, lakini ujue mi’ simezi hata kidonge kimoja katika hizo dawa zako!

    Nilizidi kumtazama tu bila ya kusema neno. Yule daktari alinitazama kwa muda mrefu.

    “Kwa nini usiwape tu hicho wanachotaka msichana? Inaweza kukupunguzia matatizo mengi tu!” Aliniambia kwa upole huku akiamini kuwa ingawa nilikuwa nikimtazama, akili yangu ilikuwa haielewi chochote katika maneno yale. Yaani ilikuwa kama anaendelea kujisemea mwenyewe.

    Oh, Yeah? Una hakika kuwa kaburini huwa hakuna matatizo? Unadhani Martin Lundi ataniachia nitembee huru mitaani baada ya kumpatia hicho anachotaka?

    Badala ya kumjibu nilifumba macho na kugeuza uso pembeni, nikimsikia yule daktari akimwambia yule nesi kuwa nikiamka aongeze kidonge kimoja katika dozi zangu zilizobaki.

    Sawa. Vyote hivyo vitaenda chini ya mto.

    Yule dokta alitoka na kutuacha na nesi Tamala nami nikajitia nimelala, lakini akili yangu ilikuwa ikifanya kazi haraka sana. Nilijua kuwa ni lazima nitoke mle ndani, lakini kila nilipojaribu kutafuta namna ya kutoka nilishindwa kupata jibu. Nilijiuliza iwapo ile hospitali ilikuwa na yule mhudumu mmoja tu na daktari wake, kwani nilitegemea kuona manesi wakibadilishana, lakini tangu nimekuja nilikuwa na nesi yule yule na hata pale nilipokuwa nimejilaza kitandani nikimtupia jicho la wizi, yule nesi hakuwa na dalili za kuondoka. Je, hana mume na watoto? Kwa nini asirudi kwa familia yake na kumuachia nesi mwingine akae na mimi?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kupata mlo wa mchana, nilimuomba yule nesi anipeleke chooni, nikitarajia kutolewa nje ya chumba kile, lakini badala yake, yule nesi alinifungua kutoka pale kitandani na kunipeleka nyuma ya lile pazia maalum, kama yale yanayopatikana katika mahospitali mengi, ambako huko kulikuwa kuna mlango mwingine wa kioo na kando ya mlango ule kulikuwa kuna meza iliyokuwa na vifaa vingi vya upasuaji pamoja na chupa kadhaa za dawa. Lakini kilichoyavutia macho yangu zaidi ilikuwa ni simu iliyokuwa juu ya ile meza pamoja na vile vitu vingine. Nesi Tamala aliniingiza chooni na kunisimamia wakati nikijisaidia, kisha alinirudisha tena kitandani na kunifunga na ile mikanda, lakini wakati huu nilishajua ni jinsi gani ya kuifungua bila ile mikanda kunibana zaidi.

    Alinipa vidonge vinne nami nikatumia ujanja ule ule na kuvificha chini ya mto, kisha nikajilaza kitandani wakati nesi Tamala akifungua soda nyingine ya mirinda na kuanza kusoma kitabu chake.

    Nilipokisia kuwa muda ulikuwa umefikia saa kumi na moja za jioni nilijitia kuamka. Nesi Tamala kuona hivyo alinishindilia tena vidonge vingine vinne, nami nikavificha chini ya mto. Nilikuwa nimepata muda wa kutafakari mustak-bali wangu kwani nilijua kuwa Martin Lundi angenijia siku iliyofuata kupata majibu ya maswali yake, akiamini kuwa zile dawa zitakuwa zimenilevya na kunipumbaza kiasi cha kum-miminia majibu kwa kila swali atakaloniuliza, kubwa likiwa ni wapi nilipouficha ule mkanda wa video.

    Sasa ole wake yule daktari atakapokuta kuwa zile dawa hazijafanya kazi ipasavyo, na nilitamani sana kuona jinsi nesi Tamala atakavyohamanika pindi ikigundulika kuwa kumbe sikuwa nikimeza vile vidonge alivyokuwa akinipa.

    Lakini la muhimu kuliko vyote lilikuwa ni namna ya kutoka mle ndani.

    Nilimuomba tena yule nesi anipeleke chooni, naye alinifungua kutoka pale kitandani huku akinisimanga kwa tabia yangu ya kubugia “mimaji mingi” wakati wa kumeza dawa halafu naanza kumsumbua kwenda chooni kila mara.

    Nilikuwa natembea kwa taabu kidogo ili kumfanya nesi Tamala aone kuwa nilikuwa nayumba kutokana na dawa nilizomeza, naye alinishika mkono kuniongoza chooni. Tulipofika usawa wa ile meza yake ambapo alikuwa ameweka kile kitabu chake na bilauri yake ya soda, niliachia mkojo ukinipita hadi sakafuni na kujitia kushangaa kibwege huku nikiinama kuangalia jinsi nilivyojikojolea.

    “Aaaah! Unaona sasa! Yaani umeshindwa kujikaza we binti...?” Nesi Tamala alinikemea kwa kero huku naye akiinama kutazama jinsi nilivyojikojolea. Na huo ndio wasaa niliokuwa nikiusubiri, kwani haraka sana nilitumbukiza vidonge vyote nilivyovitoa chini ya mto wangu, ambavyo muda wote nilikuwa nimevifumbata kwenye kiganja cha mkono wangu, ndani ya ile bilauri yake ya soda.

    “Hebu sogea huko sasa! Na ukianza kunipa kazi za kupiga-piga deki humu tutakorofishana sasa hivi!” Alinikemea huku akinisogeza pembeni nami nikabaki nikiwa namtazama tu, nikijitia bwege niliyepumbazwa na madawa aliyokuwa akinimezesha, moyoni nikiombea asiinuke kabla zile dawa hazijayeyuka vizuri ndani ya ile soda yake.

    “Kubwa zima kazi kujikojolea tu...kama mtoto bwana! Sasa bado kujinyea tu!” Alizidi kunikemea kwa hasira nami nilishindwa kujizuia, nikaanza kumcheka huku moyoni nikiona raha kumsumbua namna ile. Alinitupia jicho la hasira kwa muda, lakini hiyo ilinifanya nizidi kumcheka, naye akaona kuwa tayari nilikuwa nimesharukwa na akili kutokana na zile dawa.

    “Lione kwanza, na utabaki hivyo hivyo! Hebu vua hilo gauni huko nikutafutie jingine!” Alinikemea huku akifuta ile mikojo kwa ufagio maalum wa kupigia deki. Niliacha kucheka na kuanza kuvua lile gauni taratibu bila ya kusema neno, safari hii nikijitahidi kujifanya bwege kadiri nilivyoweza huku moyo ukinienda mbio sana, kwani vile vidonge vilikuwa vinakawia kuyeyuka.

    Itakuwaje iwapo atagundua nilichokifanya?

    Nesi Tamala aliweka pembeni lile fagio na kwenda moja kwa moja hadi kwenye lile kabati la nguo la ukutani na kulifungua nami nilitumia muda aliokuwa amenigeuzia mgongo kuichukua ile bilauri yake ya soda na kuitikisa kidogo ili vile vidonge viyeyuke haraka. Nesi Tamala aligeuka kutoka kule kabatini akiwa na gauni jingine kama lile wakati nikirudisha mkono wangu baada ya kuitikisa ile bilauri. Aliona kitendo cha mkono wangu na alianza kupata wasiwasi, akinitazama usoni na kunitazama mkononi mwangu, akidhani kuwa nilikuwa nimechukua kitu fulani kutoka pale mezani, nami hapo hapo nilijitia kuingiwa na kizunguzungu na kujiyumbisha huku nikirembua macho kama ninayetaka kupiga mwereka nikipeleka ule mkono alioutilia mashaka kwenye paji langu la uso. Haraka sana alinikimbilia na kunidaka, kisha akaniburuza hadi kitandani huku mimi nikiwa nimejilegeza kabisa. Huku akigumia kwa taabu, yule nesi alinivika lile gauni jingine na kunilaza kitandani, ambapo nilijitia kupitiwa na usingizi moja kwa moja, huku nikisikilizia jinsi hatua zake zilivyokuwa zikitembea mle ndani na kwenda tena hadi pale kabatini kwani nilisikia milango ya lile kabati ikifungwa, kisha nikasikia hatua zake zikitembea na kusikia mlango wa kule chooni ukifunguliwa na maji yakitiririka kutoka bombani.

    Kaa basi unywe hiyo soda!

    Moyo ulikuwa ukinipiga kwa nguvu sana na nilitamani kufumbua macho nimtazame harakati zake, lakini nilijilazimisha kujitia nimelala ili yule nesi asiwe na shaka kabisa. Hatimaye nilisikia hatua za yule nesi zikiishia pale kwenye kiti chake naye akijibwaga juu yake. Kimya kilitawala ndani ya kile chumba. Nilifumbua jicho kwa chati na kumuona nesi Tamala akiwa kwenye kiti chake akisoma kitabu ilhali ile bilauri yake ya Mirinda ikiwa pale pale juu ya meza.

    Hebu kunywa hiyo soda basi we’ mwanamke!

    Nililala nikimchungulia namna ile kwa muda mrefu, lakini ilionekana kama kwamba yule nesi alikuwa amesahau kabisa juu ya ile soda. Nikaanza kupata wasiwasi, kwani nilijua kuwa muda wowote yule daktari angekuja kuangalia maendeleo yangu na huenda yule nesi akaona kuwa ile soda imekaa sana na kuimwaga.

    Nilipokuwa nimekata tamaa kabisa, Nesi Tamala aliinua ile bilauri na kubugia soda yote iliyobaki na kuijaza tena ile bilauri kwa kumimina kiasi cha soda kilichokuwa kimebaki kwenye chupa. Aliiweka ile bilauri mezani naye akarudia kusoma kitabu chake, akiachia mbwewe kubwa. Nilishusha pumzi za faraja na kujilaza kimya nikisubiri matokeo, kwani nilijua jinsi zile dawa zilivyokuwa zikifanya kazi, lakini kwa idadi ya vile vidonge nilivyommiminia yule nesi, sikujua nitarajie kitu gani.

    Nesi Tamala alikuwa amebugia zaidi ya vidonge kumi kwa mpigo!

    Nilibaki nikiwa nimelala pale kitandani nikimkodolea yule mwanamke aliyebugia vidonge vingi vya kupumbaza akili huku nikikumbuka maneno ya yule daktari alipokuwa akimuelezea madhara ya kutumia zile dawa kinyume na maelekezo.

    ... Unless you want the poor girl to go completely mad...or even die! (...Isipokuwa kama unataka huyu msichana awe mwehu kabisa...au hata afe!).

    Mungu wangu! Anaweza kufa huyu mama...

    Mara yule nesi aliinuka ghafla, kitabu kikimtoka mikononi na kuanza kumanga manga mle mdani bila uelekeo maalum. Alitumbua macho na kuanza kukoroma huku akinitazama kwa macho ya woga, akijishika koo na kuanza kuyumba huku akinijia pale kitandani nilipokuwa nimelala nikimkodolea macho kwa woga huku moyo ukinienda mbio.

    “We..we! Umeni...fanya ni-ni?” Alinikemea kwa taabu huku akizidi kunisogelea, miguu yake ikigongana na povu likianza kumtoka kinywani. Alipiga yowe kubwa huku akinitumbulia macho na akinyoosha mbele mikono yake yote miwili kuielekeza pale nilipokuwa nimelala.

    Oh! My God, anakuja kunikaba sasa! Na mimi nimefungwa hapa kitandani...amewehuka nini ?

    Nilianza kuhangaika kujifungua lakini mikono ilikuwa ikitetemeka vibaya sana, na ghafla nilimuona nesi Tamala akisimama wima na kukauka kama gogo huku akiwa ametumbua macho akitazama moja kwa moja kule ukutani kulipokuwa na kalenda ya mwaka 1999. Kwa jinsi alivyokuwa ametumbua yale macho,ni wazi alikuwa haoni chochote. Kisha alijibwaga mzima mzima sakafuni kwa kishindo kikubwa.

    Kimya kilitawala.

    Nilibaki nikiwa pale kitandani kwa muda mfupi tu, kisha nilijikurupusha kutoka kwenye ile mikanda na kuliendea lile kabati lililokuwa ukutani, nikiuruka mwili uliokauka wa yule nesi pale sakafuni. Nilitoa nguo zangu na kuanza kuzivaa haraka haraka. Kisha nilikimbia kule nyuma ya pazia na kuikamata ile simu na bila kufikiri zaidi, nilianza kuipiga namba ya John Vata huku mikono ikinitetemeka na moyo ukinienda mbio.

    “John Vata!” Niliisikia sauti yake ikijibu simu upande wa pili na moyo wangu uliyeyuka kwa faraja.

    “Oh! Kamishna! Oh...thank God! Msaada Kamishna!. Nisaidie! Niko matatani... nimetekwa!” Nilipayuka haraka haraka kwenye ile simu huku nikipeleka macho kwa yule nesi aliyelala pale sakafuni bila fahamu.

    “Nani...Tigga...?”

    “Ndio Kamishna..ni mimi Tigga. Wameniteka! Na sasa wananilisha dawa za kunivuruga akili ili nichanganyikiwe! Oh! Mungu wangu sijui nitafanyaje...

    “Tigga, hebu tulia kwan...”

    “Naomba uje uniokoe Kamishna! Naogopa sana...mambo haya ni magumu sana kwangu...”

    “Hebu tulia basi, ebbo!Ni nani waliokuteka na uko wapi?” John Vata alinikemea, nikajilazimisha kutulia na kuongea kwa utulivu.

    “Nimetekwa na nimeletwa kwenye hospitali fulani...Nightingale Memorial Hospital...sijui iko wapi...”

    “Hakuna hospitali ya jina hilo hapa jijini. Ni nani waliokuteka, unawafahamu?”

    “Martin Lundi! Na mwenzake daktari...”

    “Tigga! Tulishapitia huo mchezo wa Martin Lundi! Nimeshakwambia kuwa Dr. Martin Lundi ni mzee wa miaka sabini na nilikwambia uache kabisa kunifanyia mchezo mimi...”





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog