*********************************************************************************
Simulizi :Balaa !
Sehemu Ya Kwanza (1)
“Mahabusu na Wafungwa simamaaaaa, kofiaaaaaa towaa! Selo salama kabisa Bwana mkubwa , tupo tayari kwa mafungio. Tunafungiwa mahabusu mia mbili , na wafungwa watano, jumla miambili na tano, Selo namba Mbili mkuu”
Ilikuwa ni sauti ya Nyapala wa Kimahabusu, katika Gereza la Mahabusu la Segerea, akiwainua mahabusu waliokuwa wamekaa kitako, wakiwa katika mistari ya watu kumikumi, huku wakiwa vidari wazi, yaani wamevua shati na fulana zao, tayari kwa kufungiwa ndani ya Selo, muda huo ikiwa ni saa kumi alasiri juu ya alama!!!
Askari Magereza, mwenye zamu yake ya kufungia, akiwa na askari wenzake wengine wapatao kumi, alikuwa makini na kifimbo chake, akiwahesabu wale mahabusu, waliokuwa wakiingia ndani ya Selo, kwa mwendo wa mbio, mmoja baada ya mwengine, hadi mtu wa mwisho kuingia ndani ya Selo ile, ambae ni Nyapala wa Kifungwa aliposema kwa sauti, akithibitisha ile hesabu, aliyoitoa Nyapala wa Kimahabusu! “Hapa salama kabisa bwana mkubwa, tunafungiwa wafungwa watano, na mahabusu mia mbili, jumla mia mbili na tano, selo namba mbili bwana mkubwa!”
Baada ya kuingia ndani, ya Selo ile, ambayo imepewa uwezo wa kulala watu wasiyozidi hamsini, lakini wanalazwa Mahabusu hadi mia tatu, kutegemea na wingi wa wahalifu, hasa kipindi cha sikukuu, na mwisho wa mwaka!
Askari magereza, aliifunga kufuli nje ya mlango wa Selo ile, kisha akaja askari mwingine kuhakikisha , kama kufuli ile imefungwa sawasawa!
Askari wale walifungia kwa utaratibu ule, hadi walipomaliza kufungia Selo namba tisa, ambayo ndiyo ya mwisho kufungiwa katika upande ule wa Rumande wing, katika Gereza lile.
Ndani ya Selo ile namba mbili, maarufu kwa jina la ‘Spear’, ambayo ndiyo imepangwa mahususi kwa ajili ya kuchukua Mahabusu wageni, ambao kwamba huwa ndiyo mara yao ya kwanza, kuingia gerezani. Hivyo Selo ile ndiyo pekee iliyoteuliwa na Afisa usalama, ili wageni wa jela kupewa maelekezo na taratibu za kuishi ndani ya Gereza!
Alisimama kijana mmoja, aliekuwa na cheo cha askari Selo, na kupiga makofi. (ASKARI SELO NI MSAIDIZI WA NYAPALA NDANI YA SELO ) Na mara kimya kikatawala Selo nzima! Hiyo ndiyo taratibu ya kutaka utulivu, watu wanyamaze ili itolewe taarifa ndani ya Selo.
Na baada ya utulivu kupatikana, Yule Askari Selo akasema. “Oyaa sikia hiyoo. Kama wewe unajijuwa umeingia leo ndani ya Gereza, au uliwahi kuingia ukatoka na leo umerudi tena, twende mbele kule ukapate maelekezo. Sasa wewe kaa usitoke mbele, halafu uyakanyage uone hapa unapigwa Salala, kisha kwa Meja nakupigisha Rungu nyingi! Na humu utaita taa hadi ishuke chini ikufate” (SALALA) alikuwa anamaanisha kofi la mgongo, linalopigwa kwa mikono miwili, kwa Mahabusu aliekosa kufata taratibu!. (Kuita taa, ni kusimama wima kisha unanyoosha mikono yako juu usawa wa taa ilipo unafumba na kufumbua vidole vyako mithili unamwita mtu kwa ishara ya mkono!)
Mahabusu arubaini waliinuka, na kuenda mbele, ili kupata maelekezo kwa Yule msaidizi wa Nyapala au Askari Selo, kama anavyopenda kuitwa hivyo!
Walipokuwa wote wamekaa na Selo, ikiwa katika utulivu, yule askari Selo, alianza kwa kuwajulia hali wale wageni! “Habari zenu wezi?!” Na wale wageni ambao siyo wote walioingizwa gerezani kwa kosa la wizi, lakini waliitikia kwa pamoja “Poa Mwizi!”
Kisha Yule Askari Selo, akaendelea. “Sema nini, humu ndani ya Selo tunataka heshima, tuwaheshimu viongozi wetu kwani wao ndiyo jicho la askari Magereza. Askari wao wamelala majumbani kwao, sisi tumefungiwa humu ndani kama kuku!” Yule Askari Selo alikuwa akizungumza huku akiwatazama, wale Mahabusu wenzake waliokuwa wamekaa mbele yake ili kutambua kama walikuwa wanamuelewa sawasawa! Baada ya kuridhika kuwa wanamsikiliza akaendelea. “Humu ndani ya Selo yetu namba mbili, tuna viongozi ambao mnatakiwa muwafahamu, ambao wanastahili heshima! Ambao ni Nyapala wa kimaabusu, na Nyapala wa Kifungwa. Mkisha pewa maelekezo mtaoneshwa mahali walipo ili muwatambue.”
Yule askari Selo alisimama kidogo, kisha akaendelea. “Pia tuna kiongozi mwengine mwenye cheo cha Bwana Afya humu ndani ya Selo. Yeye ndiye anaetugawia maji ya kunywa humu. Kwani bila ya yeye kuwepo na kugawa maji katika utaratibu, tungeweza kugombea na asiye na nguvu asingeweza kudiriki kunywa maji! Pia yupo kiongozi mwengine mwenye cheo cha Kilina, yeye anahakikisha vyoo vinakuwa safi, na kwa kuwa maji ni tatizo katika Gereza letu la Segerea, ukisha kwenda haja kubwa, kuna fimbo pale pembeni tunaiita mchokocho. Unatakiwa baada ya kwenda haja kubwa, utapiga mchokocho, kwa maana ya kuponda kinyesi chako, hadi kilainike kiwe uji, ili uweze kutumia maji machache kuondosha kinyesi. Sasa wewe nenda kanye kisha usipige mchokocho uone utakachofanywa! Humu ndiyo mwana ukome jeuri uache kwenu!”
Yule askari Selo alisimama kidogo kuzungumza, kwani alisikia minong’ono ikizidi na kufanya kelele kutoka kwa baadhi ya mahabusu wenyeji, waliokuwa hawana habari kabisa kama wapo jela, walikuwa wakiongea na kucheka kama hawana kesi zinazowakabili! Mara makofi yalipigwa na Nyapala wa Selo, na ghafla Selo yote ikawa kimya kama hakukuwa na watu mle ndani ya Selo! Kisha Yule Nyapala akazungumza kwa ukali.
“Oyaa sema nini mnazingua bwana, wenzenu wanaelekezwa kaeni kimya, nyie mmeshakuwa vijelajela, mnakwenda na kurudi humu nje hamna maisha hamkai, siyo mnatupigia kelele bwana, sasa nateuwa Kihelehele akamate kesi, sasa wewe kaidi, halafu ukamatwe na Kihelehele unapiga kelele uletwe kwangu uone, wewe ndiyo utakuwa funzo kwa wenzako mimi nimeletwa na kesi yangu humu, sikuja na mtu!”
Nyapala baada ya kusema maneno yale, akamteuwa mtu mmoja wakuitwa Dubwi Santana, ambae katika jela na Selo ile, aliaminika kuwa mnaa sana! Akapewa kazi yakuwa Kihelehele akamate kesi! Dubwi Santana alisimama akazungumza.
“Santana hapa, nishapewa rungu na Nyapala, kuanzia sasa hakuna kuzungumza hakuna kumokee! (KUMOKEE NI KUVUTA IWE BANGE AU SIGARA) Hapa ni mwendo wa kimya hadi Nyapala atengue cheo changu, bwanabwana wewe unaejifanya unanijua, ukataka kuniletea shobo, mbona nitakuzingua, mie nuksi halafu sijasingiziwa! Mie ni mwizi na nje naiba kweli yaani wazazi wangu wenyewe hivi mie kuwa huku wao wanaombea nisitoke sasa wewe zingua uone mbona nitakukomesha, kwanza mie sina ndugu humu nimekuja peke yangu na kesi zangu! Askari Selo endelea kuwapa maelekezo hao mafresh huku hakuna Briman wala Blue yeyote atakaezingua hawa ni wanyonge tu, wanaranda nje siyo humu hawa wachumba tu!!!”
Baada ya Dubwi Santana kupiga mikwala mingi, Selo ikarejea katika utulivu mkubwa. Na yule askari Selo Baada yakuona wale mahabusu wageni walikuwa wapo makini kumsikiliza, akawataka wale mahabusu kila mmoja akifika kwa Nyapala wa Selo ataje kesi yake kama alivyosomewa mahakamani, pia ataje mahakama ilipo kesi yake, na jina la Muheshimiwa Hakimu wake, aliemsomea shitaka.
“Oyaa hapa usiseme nimesingiziwa, taja kesi yako kama ulivyosomewa mahakamani, kesho mtapoitwa kwa ajili ya kuandikisha urithi, utaulizwa kesi yako na askari magereza. Sasa wewe ukisema umesingiziwa kesi, utachezea rungu hadi magoti yajae maji hayo tumeelewana?”
Yule askari Selo, alizungumza huku akimalizia kwa swali. Na wale mahabusu wageni ‘Fresh case’ wote kwa pamoja wakaitikia kwa pamoja “ndiyooo.”
Yule askari Selo, alimfata Nyapala wa Kimahabusu, na kumwambia. “Kiongozi wezi wapo tayari kwa kukuona, nimeshawapa maelekezo, hivyo nawaleta waje wakutambue na wewe uwatambue!” Yule Nyapala wa Selo namba mbili, alimuashiria askari Selo wake, awalete wale wageni ili azungumze nao. Na mara moja ikatendeka hivyo wale Mahabusu wageni, wakawa wanatazamana uso kwa uso na Nyapala wa Selo.
“Habari zenu?” Nyapala wa Selo aliwasalimia wale wageni wa Jela, na baada yakuitikiwa akaendelea kusema. “Poleni sana ndugu zangu, nawasihi mfate taratibu za gereza, mtatoka salama bila kupigwa hata kofi, lakini kama mtakaidi yale mliyoelekezwa, mtaumia kwa vipigo na kupata ulemavu wa Rungu za askari Magereza. Mkiwa humu ndani gerezani, ondoweni kabisa mawazo ya wake na wachumba wenu mliowaacha nje! Hao mkiwafikiria sana mtaumiza nafsi zenu bure. Kwani huku unatakiwa ufikirie kesi yako iliyokuleta humu tu acheni kabisa kuwaza vitu ambavyo vitawaletea msongo wa mawazo. Jela kajengewa binaadam na hata wale ambao sasa hivi wapo nje wakiwa raia wema na huru, nao pia ni mahabusu na wafungwa watarajiwa! Kwani wanaweza siku yoyote wakaletwa gerezani bila kukusudia! Kwani siyo wote tuliyopo humu kama ni waalifu kweli, wengine wameletwa kwa bahati mbaya tu!”
Alinyamaza kusema yule Nyapala akitaka kufahamu kama anaeleweka. Baada yakuona anasikilizwa barabara, akawataka wale Mahabusu wataje kesi zinazowakabili kama walivyosomewa mahakamani na Hakimu. “Nataka mnitajie majina yenu kamili, kesi zinazowakabili na mahakama uliyosomewa kesi hiyo.” Wale mahabusu wageni, mmoja baada ya mwengine, walikuwa wakitekeleza agizo lile, hadi kufikia kwa mtu wa Arobaini alipojitambulisha.
“Mimi naitwa Athumani Dobe, Mahakama yangu ni mahakama ya mkoa Kisutu, Kesi yangu ni Mauaji, Nashitakiwa kwa kumuua Mauwa binti Simba Makupa, hakimu wangu ni ……..!!!” Athumani Dobe hakuweza kutaja jina la Hakimu wake, kwani uchungu ulimjaa moyoni, donge likamsugua na machozi yakamtiririka mashavuni mwake, kilio cha kwikwi kikamshika hatimae akalia kwa sauti iliyohuzunisha kuisikiliza! Akazama katika lindi la mawazo. Ama kweli mtu mzima ukimuona analia, basi ujue kuna jambo! Ni kweli.
*******
ZANZIBAR MWAKA 2006.
Upepo mkali ulikuwa ukivuma kutoka kusini kuelekea kaskazini, watu wa pwani huita pepo za Kusi. Mji wa Unguja ulikuwa safi na upepo ule ulikuwa ni burudani kwa watalii wengi waliokuwa katika Bandari ya Unguja kuelekea katika mji wa Dar es salaam. Wasafiri wengi walikuwa katika hekaheka za kusafiri, katika muda ule wa Alasiri.
Boti ya Sea Express, ilikuwa inapakia mizigo kabla ya kupakia abiria waliokuwa wamesheheni pale Bandarini, wakiwa na wahaka wa safari.
“Wale abiria wenye tiketi wanaosafiri na boti yetu ya Sea Express, kuelekea D’salaam mnaombwa kupanda chomboni, muda wa safari umekaribia.” Sauti ya kike ya mfanyakazi wa Boti ya Sea Xpress, ilisikika katika kipaza sauti na msururu wa abiria ulielekea katika boti ile kwa ukaguzi na kupanda chomboni.
Saa kumi kamili boti ile ilifunga milango yake, na safari ya kuelekea katika Jiji la Dar es salaam ikaanza.
“Kaka yangu samahani, naomba hilo jarida nisome, kwani kuna hadithi naifatilia humo yaani sitaki kuikosa.” Ilikuwa ni sauti ya Abiria mmoja mwanamke, aliekuwa amekaa karibu kabisa na Abiria mwenzake mwanaume, huku boti ikiwa imeanza safari, ikiitafuta Chumbe kuelekea bandari salama!
“Ohoo haina shida soma tu mimi nitaangalia filamu katika video pale, kwani hii filamu ya KABIKUSH KABIGHAM, naipenda sana hilo jarida mie nitasoma nyumbani.” Alijibu Yule abiria wa kiume huku akimkabidhi lile jarida la Ndoto.
Muhudumu wa Boti ile, alikuwa akipita na mifuko ya plastiki akigawa ndani ya boti ile, kwani bahari ilichafuka na wale abiria ambao siyo wenyeji wa bahari, wanaweza kutapika sana! Hivyo ilikuwa rasmi mifuko ile kwa kutapikia. Alipofika katika usawa wa Yule dada aliekuwa akisoma lile jarida la Ndoto, Yule abiria wa kiume alimchukulia Yule dada mfuko, yaani alichukua mifuko miwili! Kwani yule dada alikuwa amekazana macho yake katika jarida lile, hakuwa na habari ya mifuko.
Boti ile ilishika kasi, kuitafuta bandari ya jiji la Dar es salaam maarufu ikijulikana kwa jina la Bandari salama. Mwendo kasi wa boti, wimbi kali na upepo wa Kusi uliokuwa ukivuma kwa kasi kubwa, uliitesa sana Boti ile, kiasi ilisukwasukwa na wimbi kubwa, kiasi ikatibua matumbo ya wasafiri, na wale wageni wa bahari, mara wakaanza kuhisi kichefuchefu, vilio kwa watoto vikasikika. Yule dada aliekuwa akisoma jarida aliacha kusoma, akawa amejiinamia hasemi, mdomo wake ulijaa mate, tumbo lilitibuka na akahisi kutapika. Yule abiria wa kiume alimpa mfuko mmoja wa plastiki ili atapikie mle, na kweli alitapika hadi nyongo! Ule mfuko ulijaa, na Yule abiria wa kiume akampa ule mfuko mwengine, nayeye akaenda kuutupa chooni ule mfuko uliojaa matapishi ya Yule dada!
Baada ya kama saa moja na nusu, wakiwa wamebakisha nusu saa kufunga gati, katika Bandari salama, Jiji la Dar es salaam lilikuwa linaonekana kwa karibu, wakiwa maeneo ya kunduchi. Yule dada sasa akiwa ametulia na bahari ikiwa imetulia, akamuomba Yule kaka simu yake ya mkononi. “Kaka yangu samahani, naomba niazime simu yako nitume ujumbe sehemu.” Yule kaka bila kinyongo, alimkabidhi simu ile huku nae akimwambia. “Piga kabisa tu, kwani simu hiyo ina pesa za kutosha humo!” Yule dada huku akitabasamu akamjibu.
“Asante sana ila ujumbe tu mimi unanitosha.” Baada yakusema maneno yale aliandika ujumbe wake, kisha akautuma alipoukusudia, majibu yakarudi kuwa ujumbe ule umefika ulipokusudiwa, kisha akaufuta ujumbe ule katika simu ile, kule kwenye sehemu ya kutuma ujumbe, pia akafuta na ule ujumbe uluorudi kuonesha kuwa ujumbe ule umefika, na alipomrejeshea simu yake Yule kaka, kukawa hakuna ujumbe uliobakia katika simu ile!
“Samahani dada naomba tufahamiane, Mimi naitwa Athumani Dobe, nakaa Mwananyamala Komakoma, mwenzangu unaitwa nani?” Yule dada huku akitabasamu kwa aibu, nae akajitambulisha. Mimi naitwa Mauwa Bint Simba Makupa, nakaa Mtaa wa Swahili Kariakoo, upande ule wa pili kama unaelekea Muhimbili.” Alijibu Mauwa huku akiwa hamtizami usomi Athumani Dobe.
“Ahaa asante sana bi Mauwa, Unguja kwa nani wako?” Athumani Dobe, alimuuliza swali lingine na Mauwa akamjibu.
“Kule ni Kwa Baba yangu Mdogo anaeitwa Haruna Makupa, nimekwenda kuna kitu kuchukua, na nilienda juzi leo ndiyo narudi, mimi makazi yangu ya kudumu ni Dar es salaam.” Alizungumza Mauwa katika utulivu mkubwa. “Je nikitaka kukutafuta nakupataje?” Athumani Dobe alianza kurusha ndoana yake, akakutana na Samaki mbishi! “Mmmh mimi kwetu geti kali, yaani mimi ni ndani, ndani na mie sina muda hata wa kwenda sokoni! Mungu akipenda kama hivi tulivyoonana, basi naamini tutakutana tena!” Mauwa alimjibu Athumani, huku akimkabidhi lile jarida lake la Ndoto, pia akitoa shukurani kwa kusoma.
Athumani Dobe, alilichukua lile jarida akalitumbukiza katika mfuko wake wa safari, wakawa wanazungumza haya na yale, hatimae wakafika salama katika Bandari salama, na abiriria wakawa wanajiandaa kushuka, hayo yakiwa ni majira ya sasa kumi na mbili Magharibi. Athumani Dobe, akamuuliza Mauwa. “Naweza kukusindikiza kwenu?” Mauwa akamjibu. “Asante sana, ila Baba atakuwa yupo nje ananisubiri na gari yake usijali, siku nyingine!”
Katika kiti cha tatu, kutoka alipokuwa amekaa Mauwa Simba Makupa, alikuwepo bwana mmoja akiwasiliana na simu mara kwa mara kwa ujumbe mfupi, huku akiwa macho yake hayampotezi Mauwa Simba, pia akimfatilia kwa karibu sana mazungumzo yake na Athumani Dobe!
Chombo kilifunga gati, na abiria wakaanza kuteremka kutoka mle kwenye Boti, Athumani Dobe akaagana na Mauwa Simba, akashika njia, kujiunga na abiria wengine waliokuwa katika foleni ndefu yakutoka nje ya Bandari. Dakika kumi baadae Athumani Dobe, alikuwa pale stendi ya basi ya posta ya zamani, akisubiri gari za Mwananyamala.
Wakati ule wa jioni gari zilikuwa zinasumbua sana, katika mji wa Dar kwani lilipoonekana basi, watu waliminyana, na wengine walidiriki kupandia kwenye madirisha, ili kuwahi viti vya kukaa!
Gari linalofanya safari zake, Mwananyamala Stesheni, lilisimama na abiria wakajazana hadi mlango ukawa haufungi, Athumani Dobe, akiwa ni miongoni mwa abiria waliosimama ndani ya basi lile, safari ya Mwananyamala ikaanza na kutokana na foleni kubwa waliyokutana nayo, iliwachukua saa mbili hadi Athumani Dobe, kuteremka katika kituo cha Komakoma, na kuelekea kwake jirani na kituo cha basi katika upande huu alioshukia, akiwa anaishi katika nyumba za kota.
Saa tatu kamili ya usiku Athumani Dobe, akiwa na mke wake Siyawezi Binti Gonga, wakiwa wamekaa katika meza ya chakula wakipata chakula cha usiku, mara simu ya Athumani Dobe, ikaanza kuita kwa fujo. Athumani aliichukua simu yake akaitazama namba iliyopiga, akaiona ni namba ngeni! Akaipokea simu ile “Halow?” Simu ile mpigaji wake alikuwa ni mwanamke, alikuwa akiongea kwa jazba kubwa. “Sina haja na halow yako, nakwambia hivi, huyo Malaya mwenzio mruhusu arudi nyumbani, tena haraka!” Simu ile ilikatwa baada ya maneno yale.
Simu ya Athumani Dobe, ilikuwa na sauti kubwa, hivyo maneno yale yaliyosemwa na mwanamke Yule katika simu, yalipenya katika masikio ya mke wa Athumani Dobe, bi Siyawezi mwana wa Gonga, yakatibua nyumba ya wivu, yakapandisha presha, yakaondosha hamu ya kula, akaweka kijiko chini chakula kikamtumbukia nyongo akamkabili mumewe! “Haya bwana, huyo Malaya mwenzio unaetakiwa umruhusu arudi kwao, ndiyo nani?” Siyawezi Binti Gonga, alimtupia swali la wivu mumewe!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Athumani Dobe, akiwa amekasirishwa na maneno yale katika simu, alisonya msonyo mrefu, kisha akamwambia mkewe. “Hii namba iliyonipigia ni ngeni, nahisi amekosea namba. Ila watu wengine siyo wastaarabu, mtu hanijui kisha ananiita Malaya, mie ndiyo nimerudi safari, na hapa nipo na wewe mke wangu, haya huyo Malaya mwenzangu yupi huyo?!” Athumani alimjibu mkewe, lakini alikuwa akitwanga maji kwenye kinu!
“Athumani usinifanye mie mtoto mdogo tafadhali! Wewe mtu hakujui atakwambiaje maneno hayo, ilihali uliposema halow, ameisikia sauti yako?” Bi Siyawezi aliwapandisha wazaramo kichwani, ikawa kauvuta mdomo hatizamiki, jicho kalitoa hasira zimemjaa! Ama kama Mwenyezi Mungu, kuna watu amewapa wivu, basi Siyawezi binti Gonga, atakuwa amepewa wivu kwa kiasi kikubwa sana!
Athumani akamwambia mkewe. “Simu yangu hiyo hapo namba iliyopiga inaonekana chukua uipige ili ujiridhishe, labda utaamini haya nikwambiayo!”
Wakiwa katika kujibizana hivyo mara simu ya Athumani ikaita tena, kwa namba ileile. Siyawezi kama kipanga aliinyakuwa ile simu, kisha akamwambia mumewe huku akimuonesha simu ile. “Namba hii ndiyo iliyokupigia awali?” Athumani aliitazama simu yake, akatikisa kichwa kuashiria kuafiki kuwa ndiyo ile namba iliyompigia muda mfupi uliyopita. Tena safari hii alidhani kuwa Yule mpigaji amegundua kuwa alipiga simu kimakosa, na sasa anapiga tena ili kumuomba radhi, haraka akamwambia mkewe “Pokea hiyo simu na Loud speaker, akimaanisha aweke spika kwa sauti ya juu zaidi.
Ama ngoma ilikuwa imempata Kenge, lazima aingie nayo mtoni! Siyawezi aliipokea simu ile, kisha akapandisha spika kwa sauti ya juu, ila hakusema neno yeye alikuwa anasikiliza maneno yanavyokwenda! Mle kwenye simu sauti ileile ikasema ikimkusudia mwenye simu ile! “Nakuonya mara ya mwisho kijana, mimi ni mama yake Mauwa mruhusu mwenzio arudi nyumbani, kwani baba yake anamsubiri pale jirani na Avalon Cinema, hadi saa hizi Mauwa hajaonana na baba yake, nakupitia simu yako Mauwa alinijulisha mie kwa ujumbe kuwa karibu mngeteremka bandarini kutoka kwenye boti ikitokea Unguja!” Simu ile ilikatika, na Athumani Dobe, alipatwa na fadhaa ya mwaka! Kwani jina la Mauwa, alimkumbuka vizuri yule dada aliepanda nae ndani ya boti, sura yake ilimjia machoni pake! Haraka alikurupuka ili ajibu kuwa kweli Mauwa alimuomba simu, lakini hakushuka nae, lakini alichelewa kwani simu ile ilikatika!
Kazi sasa ikawa kwa Siyawezi Mtoto wa Gonga, mjukuu wa Wivu! “Asante bwana Athumani, wewe ndiyo kidume halisi nimekubali, na mie ndiyo mlinzi wa hiki kibanda cha NHC (National Housing Corporation). Mwanzo ulinambia namba hii imekosea kukupigia wewe, sasa mbona ulivyosikia jina la Mauwa umekurupuka? Nambie ukweli Athumani unamjua Mauwa humjuwi?” Siyawezi alikuwa mbogo, sasa akiwa amesimama ameinuka kwenye kiti. Athumani alikuwa amejiinamia kwa tafakuri nzito, kutokana na taarifa ya Mauwa kutokufika nyumbani kwao, hadi usiku ule. “Mke wangu naomba unielewe, hebu punguza wahaka na wivu. Kweli huyo Mauwa mie nilipanda nae ndani ya Boti, tukakaa hivi na hivi. Kweli aliniomba simu yangu ili atume ujumbe, namie kama msamalia mwema nikampa simu yangu. Yeye alituma ujumbe wake ingawa sikutambua alimtumia nani, na kamueleza nini! Mimi nimeteremka pale bandarini saa kumi na mbili na robo, sikuwa tena na habari na Mauwa!” Athumani alimjibu mkewe, lakini alikuwa kama anaezungumza kiarabu kwa wangoni!
“Mtumeee nafa Siyawezi mie, nishahusudika mwaka huu! Eee umempa simu yako, mmekaa pamoja kutoka Unguja hadi Dar es salaam? Athumani ushamtongoza mtoto wa watu, si ajabu na umeshamzini, kwani kurudi hapa ulikawia siyo kawaida, hata hizo foleni si kihivyo! Sasa naona umenogewa na hayo Mauwa, hadi ukayaficha haya sasa wenyewe wanayataka Mauwa yao, kayatowe Athumani nakwambia! Mwanaume huridhiki na mkeo ukwale umekujaa!” Sasa pumu zilipata mkohowaji, Siyawezi alikuwa anazungumza huku kashika kiuno! Alikuwa akiranda huku na huko katika sebule ile.
Athumani alimtizama mkewe, kwa kuwa anamfahamu kwa wingi wa wivu hakumfanya kitu, zaidi aliiomba simu yake ili aipige ile namba nakutoa ufafanuzi, lakini hata alipopewa simu ile alijaribu kuipiga simu ile, lakini majibu yalikuwa “SIMU UNAYOPIGA KWA SASA HAIPATIKANI, TAFADHALI JARIBU TENA BAADAE!” Athumani alichoka choko, alichoka nyayo hadi utosi! Njaa ikatoweka, uchovu wa safari ukarudi kwao, akawa anahisi Balaa, likimyemelea!
Athumani kila akijaribu kuipiga simu ile bado jibu lile likawa linaendelea kutoka katika simu yake, ikamthibitikia kuwa simu ile itakuwa imezimika chaji, aidha mwenye simu ameizima labda kukataa kusumbuliwa na mumewe juu ya mtoto wao Mauwa! Alifikiri sana akakosa jibu la maana lakutoa kwa wazazi wa Mauwa. Akahisi labda Mauwa amesharudi, na Yule mama yake, sasa anaona haya kwa maneno yake. Basi akashukuru mungu kwa yote, akanawa mkono wake, hakuendelea kula tena japo alipiga vijiko visivyozidi kumi, kabla ile Balaa haijaingia katika nyumba yake!
Siyawezi Bint Gonga, alikuwa amefura anakaribia kupasuka, aliwacha vyombo vimezagaa pale mezani, akaenda chumbani akapanda kitandani kulala huku akiwa amenuna kuliko maelezo! Athumani alipokwenda kuweka ubavu kitandani kwake na mkewe, Mauwa akabadilisha kichwa chake! Yaani walilala mzungu wanne hadi kunapambazuka, hakuna mtu aliethubutu kumgusa mwenzie! Athumani alilala doro.
*******
DAR ES SALAAM 2006.
Katika maegesho ya magari ya Avalon Cinema, Mzee Simba Makupa, alikuwa ameegesha gari yake aina ya Peogot 504. Macho yake yakiwa yamezama kutazama abiria waliokuwa wakishuka kutoka katika boti ile ya jioni, kutoka Unguja boti ya Sea Xpress. Watu walikuwa wengi sana jioni ile, hivyo alikuwa makini kumsubiri Binti yake aliemtuma Zanzibar, kufata kitu muhimu sana kwa upande wake! Mauwa Bint Simba Makupa. Lakini hadi Magharibi inapinduka nakuingia wakati wa Isha, Mauwa hakupandisha huku juu Avalon Cinema! Mzee Simba Makupa ilipofika saa tatu usiku, akaanza kumsumbua mkewe Bi Zaituni, kuhusu taarifa ya mwanae kushuka na Boti ile! Na mkewe alimjibu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Haya ndiyo madhara yakutokuwa na simu mtoto , kila siku nakwambia simu muhimu wewe unasema simu atapata kwa mumewe! Ona sasa tunavyopata tabu, je Mauwa angelikuwa na simu, huoni kama ingekuwa rahisi kujua alipo? Na sie wasiwasi usingekuwepo ila sasa tunawekwa roho juu kama moto wa kifuu! Mie alinitumia ujumbe katika simu ya mtu kuwa anakaribia kushuka, na nilipoitazama namba ya simu ile usajili wake, mwenye simu huyo ni mwanaume, anaeitwa Athumani Dobe, isije ikawa amemrubuni mwanetu, na kuwa nae!” Mama Mauwa alimwambia mumewe hali halisi ilivyokuwa! “Hebu nitumie namba ya huyo bwana aliyoitumia, kwani haiwezekani kuwa mtu akupe simu yake wakati humfahamu!” Simba Makupa, baba yake Mauwa aliitaka namba ya simu ya Athumani Dobe, na mkewe akamtumia namba ile!
Mzee Simba Makupa, alipopewa namba ile hakusubiri tena, aliwasha gari yake huku mapigo ya moyo yakimuenda mbio, akasogea katika kituo cha polisi cha kati, na kushitaki kutoroshwa mwanae na Bwana aliejulikana kwa jina la Athumani Dobe. Askari walifungua jalada, Bwana Simba Makupa akapewa RB, na kuambiwa polisi watashirikiana na yeye katika kuhakikisha Mauwa anapatikana. Bwana Simba akaondoka huku akijiapiza moyoni mwake kuwa ole wake huyo Bwana, aliekuwa na mwanawe Mauwa! Bwana Simba Makupa hadi anafika nyumbani kwake saa nne ya usiku, alipomuuliza mkewe mama Mauwa kama mwanawe amesharudi, bado jibu lilikuwa baya sana kutoka kwa mkewe!
“Wallahi huyu mtoto anatueleleza kwani hadi sasa hajarudi, nahii siyo kawaida yake kabisa, huyo mwanaume anaeniharibia mwanangu, mbona apite juu asipite chini, lakini kama anapita chini, wallahi naapa nitalia nae!” Mama Mauwa alimjibu mumewe huku hasira zikimtawala katika nafsi yake.
*******
*******
Athumani Dobe, aliamka akiwa na mawazo tele, akatafakari kwa kina yale yaliyojiri kutoka kwa Mauwa, akapiga moyo konde, na kuendelea na hamsini zake! Alikwenda kujimwagia maji, kisha akapata kifungua kinywa.
Athumani Dobe, alikuwa ni mtu wa makamo, siyo kijana wala siyo mzee. Alikuwa akifanya biashara ya kuuza bidhaa zilizotumika, alikuwa akisafiri sana Zanzibar kwa kufata Majokofu na Tv zilizokwisha tumika, alikuwa na duka lake Magomeni mikumi nyuma ya Hotel ya Travatine, likiwa mkabala na Barabara ya Kawawa. Unguja alikwenda kufunga mzigo, kwani bei ya bidhaa ile anayoifata kule kisiwani ni nafuu sana ukilinganisha na bei za Dar es salaam. Siku ile ndiyo mzigo wake ungepakiwa katika Jahazi na kuletwa Dar es salaam na wakala wake aliyopo Unguja. Hivyo yeye angeupata siku ya pili asubuhi na mapema.
Siku ile aliamua kushinda nyumbani ili kumpoza mkewe anaempenda sana, bi Siyawezi Binti Gonga. Alikuwa akimsemesha mkewe, lakini alipata majibu ya mkato, ila hakukoma aliendelea kujipendekeza kwa mkewe, hadi mchana akafanikiwa kumlegeza kidogo mkewe, kwani waliweza kula chakula pamoja, na hiyo kwa Athumani akaiona ni hatua kubwa aliyopiga!
Mnamo majira ya saa tisa alasiri, Athumani alitoa simu yake, ili ampigie wakala wake kujua kama mzigo umeshapakiwa katika chombo, simu yake ikawa haitoki! Akajaribu kutuma ujumbe katika simu ya mkewe, na ujumbe pia ukawa hauendi, akashangaa sana! Akachukua simu ya mkewe akaipiga simu yake, lakini pia ikawa haiingii simu katika simu ile! Sasa ndipo akajiridhisha kuwa simu yake, haitoi wala haiingizi simu yoyote, halikadhalika ujumbe ulikuwa hautoki pia ulikuwa hauingii! Akapagawa sana kuona hali ile. Kupitia simu ya mkewe alipiga simu huduma kwa wateja, na baada ya muda simu ile ikapokelewa.
“Naitwa Rose mary Isinika, huduma kwa wateja naongea na nani na unapiga simu kutoka wapi?” Yule muhudumu wa kampuni ya simu, alimuitikia Athumani Dobe. “Naitwa Athumani Dobe, napiga simu kutoka Mwananyamala.” Alijibu Athumani Dobe. “Hii unayotumia ndiyo namba yako?” Rose Mary Isinika alimsaili Athumani Dobe. “Hapana hiyo ni namba ya mke wangu, mie simu yangu haitoki kabisa, wala kuingia, situmi meseji, wala situmiwi!” Athumani alimwambia huduma kwa wateja. “Ahaa nitajie namba yako tafadhali, ili niweze kukusaidia.” Athumani Dobe, alimtajia namba zake akasubirishwa katika line.
“Athumani Dobe, samahani kwa kusubiri muda mrefu, nilikuwa nalishughulikia tatizo lako, sasa kilichotokea hapa, ni tatizo la kimtandao tu na hilo ni tatizo lililo ndani ya uwezo wetu, ni mabadiliko ya kubadilisha mtandao kutoka Zein kuhamia Airtel, njoo na simu yako hapa makao makuu Moroco, ili tuweze kukurekebishia tatizo lako, na kwa kuwa tatizo lililokupata limesababishwa na mitambo yetu, tutakupa muda wa maongezi wa Tsh 10,000/ kama kiondosha usumbufu. Ila usisahau kuja na kitambulisho. Ukifika niulize Rose Mary Isinika. Je? Una tatizo lingine Athumani nikusaidie?!”
Yule muhudumu wa huduma kwa wateja, alimpa maelezo ya kiufundi Athumani, pia akamalizia na swali. “Hapana sina tatizo lingine zaidi ya hilo, nakuja sasa hivi huko makao makuu, kwani nina simu muhimu za mizigo yangu, nashindwa kumpata wakala wangu!” Alijibu Athumani. “Asante kwa kuendelea kutumia mtandao wa Airtel.” Alimaliza Yule muhudumu wa huduma kwa wateja, kisha akakata simu, na Athumani akajiandaa kwenda makao makuu ya Airtel.
Nusu saa baadae, Athumani Dobe alikuwa katika ofisi za Airtel makao makuu pale Moroco, makutano ya Barabara ya Ally Hassani Mwinyi, na Kawawa. “Samahani namuulizia dada Rose Mary Isinika.” Athumani Dobe alimuuliza dada mmoja aliekuwa akiwahudumia wateja. “Yule palee ndiyo Rose.” Yule dada alimjibu akamuoneshea mtu aliekuwa anamuhitaji, kisha yeye akawa anaendelea kuwahudumia wateja waliokuwa mbele yake. Athumani Dobe alimfata Yule dada aliekuwa akimuhitaji na alipomfikia akajitambulisha kwake. “Naitwa Athumani Dobe, naongea na Rose Mary Isinika?” Athumani Dobe alijitambulisha lakini pia alimtupia swali ili kujiridhisha, kama anaeongea nae ndiye mtu aliekuwa anamuhitaji. “Naam mie ndiye Rose, karibu Athumani.” Yule dada aliongea huku akimwemwesa, na Athumani Dobe, akaushuhudia mwanya wa Rose, uso wake wa tabasamu na rangi yake ya weupe wa asili, nywele zake laini alizozibana kwa nyuma, sketi iliyombana ilikuwa imeuchora mwili wake, nakuudhihirisha urembo wake.
“Asante kwa kukuona dada Rose, niliongea na wewe wastani wa saa moja nyuma, kuhusu tatizo la simu yangu kutokutoka wala kuingia, ndiyo nimekuja kama ulivyonitaka nifanye hivyo.” Athumani Dobe, alizungumza kwa kujiamini. “Nakukumbuka Athumani Dobe, je umekuja na kitambulisho na simu yako?” Rose alimuuliza Athumani.
“Naam nimekuja navyo vitu hivyo hivi hapa.” Athumani Dobe alijibu huku akitoa kitambulisho chake cha kupigia kura, na simu yake akamkabidhi.
Rose alivipokea vitu vile, akamuelekeza Athumani, kusubiri katika kiti, kisha yeye akainuka na kupanda ghorofa ya kwanza akaingia ndani katika ofisi ya meneja masoko. Athumani Dobe alimtizama Rose alivyompa mgongo, akashuhudia miguu minene, iliyokuwa ikionekana hadi juu ya mapaja, kutokana na sketi fupi aliyoivaa. Alikuwa na makalio ya wastani, alitanuka kwenye nyonga, umbo lake likachora namba nane! Alikuwa na umbo la kimiss. Rose Mary Isinika, alistahili kuwa hudumia wateja, kwani alikuwa mrembo na mcheshi.
Athumani alikuwa akiangalia ofisi ile, akashuhudia vioo ambavyo huwezi kuona ndani ya ofisi nyingine. Aliipenda namna ilivyopangwa pale huduma kwa wateja, kiyoyozi kikali kilikuwa kinaleta baridi kiasi utakawia kutoka nje kwenye joto kali la jiji la Dar es salaam. Watu walikuwa wengi wenye shida mbalimbali za kimtandao, pia wapo waliokwenda kununua simu na wapo waliokwenda kununua moderm, ilimradi kila mtu alikuwa na shida zake katika ofisi ile. Mara mlango ulifunguliwa, na Rose akatoka katika ofisi ile akaenda katika kiti chake.
“Athumani Dobe, samahani nimekuweka sana, nimeshalitatua tatizo lako hebu jaribu kupiga simu yako.” Rose huku akitabasamu alimwambia Athumani na kumkabidhi simu yake ila kitambulisho chake hakuwa nacho!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Athumani Dobe, alimpigia mkewe na simu ya mkewe ikaita na kupokelewa, nae akamfahamisha kwamba simu yake imeshapona huvyo hana muda mrefu atakwenda nyumbani kwake, kisha akakata simu. “Asante dada Rose, kweli imekubali sasa.” Athumani alimwambia Rose huku akifurahi.
“Asante kwa kushukuru kaka, sasa naomba unifate nikupeleke kwa meneja ili akakupe salio lako na kitambulisho chako.” Rose alisema huku akiinuka na kuongoza katika ngazi wakapanda ghorofa ya kwanza wakaingia ndani ya ile ofisi aliyoingia awali Rose, na Athumani Dobe aliunga tela nyuma akamfata Rose na kuingia katika ofisi ile pana, ambayo kiyoyozi chake ni kikali zaidi, kiasi muda mchache alioingia Athumani katika ofisi ile, alianza kuhisi baridi likimuingia hadi kwenye mapafu!
Athumani Dobe, akimfata Rose aliweza kushuhudia katika vile vioo kila kitu kilichokuwa kikiendelea kule chini alipokuwa mwanzo, katika ofisi za huduma kwa wateja. Sasa yeye akiwa ndani akawa anaona nje ya ofisi ile! Ila wale waliokuwa nje ya ofisi ile, kule chini walikuwa hawawezi kuambua kitu.
Athumani alipiga hatua kama kumi mbele, akasikia sauti ya kiume kutoka nyuma yake ikisema. “Upo chini ya ulinzi!” Athumani akawa hakuelewa, alitaka kupiga hatua nyingine, akaisikia tena sauti ile kwa karibu zaidi. “Upo chini ya ulinzi, kwa kosa la mauwaji ya Mauwa Simba Makupa!” Athumani aliposikia maneno yale, mwili wake ukapata ganzi, nguvu zikamuishia akasimama kutembea kwani miguu yake ilikuwa haina nguvu ya kutembea tena. Pamoja na baridi kali lililokuwa mle ndani, Athumani alikuwa akitokwa na jasho! Alimshuhudia Rose akiingia katika chumba kimoja kilichoandikwa meneja masoko, wala asigeuke nyuma kumtazama!
Athumani Dobe, aligeuka nyuma kule kulikokuwa kukisikika sauti, akashuhudia midomo miwili ya Bastola ikikokiwa, tayari kwa kutumika! “Naitwa Staf Sajenti Kubuta, tulia hivyo hivyo sitosita kutumia hii silaha kama utaleta ubishi!” Yule askari alikuwa akisema maneno yale huku akiwa hatanii hata kidogo. Athumani Dobe akatii amri, akanyoosha mikono yake juu. Yule askari mwengine alichukua pingu akaizungusha mikono ya Athumani Dobe kwa nyuma akamfunga nazo! Kisha wakamchukua na kushuka nae chini wakapita nae palepale alipoingilia! Walipofika pale kwenye meza aliyokuwa akifanyia kazi Rose, Athumani Dobe alimshuhudia kijana wa kiume, akiendelea na kazi hana habari na kitu kilichotokea wala hakushughulika kuwatazama! Athumani Dobe akatolewa nje, akapakiwa katika gari aina ya Toyota Noah, akapelekwa katika kituo cha polisi cha kati kwa mahojiano zaidi.
*****
Mnamo majira ya saa kumi na moja na nusu Alasiri, Siyawezi alikuwa amekaa keshatukana matusi yote anayoyajua na asiyoyajua, amevimba kwa hasira, hasa akizingatia kwamba mumewe alimpigia simu, akimjulisha kuwa tayari simu yake imeshatengemaa, na kwamba hana muda mrefu angerudi nyumbani kwake, sasa anawekwa na lipi, kama hakwenda kwa Mauwa? Wivu ulimtafuna vidonda vya tumbo akavihisi vinamuuma, presha akahisi inashuka kila analolipanga likawa halipangiki! Maneno yakamuishia, kwani keshaipiga simu ya mumewe takribani mara kumi, lakini simu yake ikawa haipokelewi, kama kuna jambo lililomuumiza na kumuudhi basi lilikuwa ni hilo! “Yaani Athumani huyo Mauwa ndiyo anamfanya asipokee simu yangu, basi alale hukohuko mie Siyawezi haya Abadan asilan khaa?! Bwana huyu nimfanyie nini mimi lakini ambacho sijamfanyia?! Bwana ninamsinga kwa wiki mara mbili, kwenye mwili wangu kitu gani sijampa Siyawezi mie? Najikusuru mtoto wa kizaramu nimridhishe bwana huyu, kumbe vile nasomea maiti naondoka na ujaka wangu! Hivi huyo Mauwa anampa nini cha maana hasa ambacho mie sina?! Ama kweli nimeamini mwana wa mwenzio ni mkubwa mwenzio! Tena mwana wa mwenzio kizuka, akizuka zuka nae!” Siyawezi alimaliza maneno, aliongea peke yake kwa hasira sana yaani kifupi alikuwa kachanganyikiwa! Ama kweli jambo usilolijua, ni kama usiku wa kiza!
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siyawezi akiwa katika msongo wa mawazo tele, mara akasikia mlango ukigongwa! Akajisemea moyoni kuwa huyu bwana sasa ndiyo kakumbuka nyumbani. Akiwa bado amekaa kitini akapaza sauti huku akiwa amenuna “Ingia mlango uwazi huo!” Alisema maneno yale huku akikitumbulia macho kitasa cha mlango kikizungushwa na kufunguliwa. Mlango ukafunguka Siyawezi akamuona Mumewe Athumani, sura ameiinamisha chini, nayeye akageuka kwa haraka akampa mgongo akaanza kutapika maneno!
“Mchafu mkubwa wewe, sitaki hata kukuona mbele ya macho yangu, unanitia kichefuchefu rudi kwa huyo Malaya mwenzako Mauwa uliemficha, toka Athumani nakwambia!” Mauwa alisema maneno yale na mara akashangaa pale aliposikia sauti nyingine asiyoifahamu!
“Kumbe na wewe unamfahamu mke mwenzako Mauwa?!” Siyawezi aligeuka kule ilipotokea sauti nyuma yake usawa wa mlango, huku akimjibu yule mtu aliekuwa na mwenzake wakiwa wamekuja pamoja na mumewe!
“Mauwa ataishia kufichwa Guest huko, aolewe atawahi atadandia, kapata bahati kapelekwa Unguja lakini kupata ndoa hathubutu! Labda mie siyo Siyawezi Binti Gonga. Hivi unanijua au unanisikia tu? Haa chezea mie wewe?!” Siyawezi kwa kubwatuka maneno yale, aliwafurahisha sana wale askari waliokuwa wamevaa kiraia. Lakini akimshindilia msumari wa moto mumewe! Athumani Dobe alimtazama kwa chuki mkewe kwa kuropoka kwake, akawa hana jinsi kwani alikuwa yupo chini ya ulinzi, ijapokuwa pale alikuwa hajavishwa pingu!
“Kumbe na wewe pia unajua kwamba Mumeo alisafiri na Mauwa kwenda Unguja? Sasa sisi tumemleta ni jamaa zake, tumekuja kukupa taarifa kwamba huyu bwana ndiyo anakwenda kuoa hivi!” Staf Sajenti Kubuta, alimchimba Yule mwanamke lakini pia akitaka kupata zaidi taarifa, hasa baada yakugundua kuwa mwanamke yule ni kiropo na mwenye wivu uliopindukia!
“Kwenda kuoa huyo hawezi, kwani ili aoe mke mwengine awe huyo Mauwa au yeyote awae, itabidi kwanza niachwe mie! Na kwa kuwa Athumani bado hajanipa talaka, nasema hawezi kuoa hata iweje kama mie bado ni mke wake! Mie ndiye Siyawezi, basi kama lilivyo jina langu pia mitala mie Siyawezi!!!” Mke wa Athumani alikuwa akisema maneno yale huku akijipiga kifua chake!
“Ok tunashukuru kwa msimamo wako, sasa sisi ni askari kutoka katika kikosi maalum, hivi tunavyozungumza na wewe, Mauwa Simba Makupa yupo katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, akiwa tayari ni maiti! Mwili wake umeokotwa leo saa moja asubuhi ukiwa hauna uhai, katika fukwe ya bahari ya hindi pale katika makutano ya barabara ya Chimara na barabara ya Ocean. Hapa tumekuja kuna vitu kuvihakikisha kwa mujibu wa maelezo ya mumeo, ila na wewe pia tutaondoka sote kuelekea kituoni, ili ukatoe maelezo yako kadiri ujuavyo uhusiano wa Mauwa na mumeo!” Staf Sajenti Kubuta alisema maneno yale pia akitowa kitambulisho na kumuonesha Siyawezi Binti Gonga.
Hakika ilikuwa ni hamaniko kuu, Siyawezi alichoka akawa hana nguvu, hana ujuba wa maneno tena, alichoweza kufanya kwa wakati ule ni kukaa kitako! Mate yalimkauka, midomo ikamcheza kamasi zikamvuja akaishiwa pozi, akajibweteka chini bwete, kwa tabu sana akabahatika kusema wallahi hili ni Balaa!
Staf Sajenti Kubuta, alimuuliza Athumani nyumba ya mjumbe ilipo nae akamuelekeza. Akatoka nje ya nyumba ile akamfata mjumbe wa nyumba kumi, huku nyuma akamuacha Sajenti Magane, akiwachunga mtu na mkewe na nje katika gari waliyokuja nayo, Coplo uzegeni alikuwa nyuma ya usukani! Baada ya kama dakika kumi hivi, Staf Sajent Kubuta aliingia tena katika nyumba ile akiwa na mjumbe wa nyumba kumi aliefahamika kwa jina la Mtubwi.
“Samahani ndugu mjumbe, tumekusumbua kidogo sie kama nilivyokufahamisha kule kwako, tumekuja kuhakikisha kitu Fulani kwa mtuhumiwa Athumani Dobe, hivyo tungependa na wewe uwe shahidi katika hilo!” Staf Sajenti Kubuta alimwambia Yule mjumbe, na yule mjumbe akawa hana pingamizi!
“Athumani Dobe, tukiwa katika mahojiano na wewe kituoni, ulituambia kwamba Mauwa ulimpa Jarida la Ndoto akasoma, je? Tunaweza kuliona hilo jarida?! Staf Sajenti Kubuta alimtupia swali Athumani Dobe, aliekuwa hana raha, hana amani! Na hapo ndipo Siyawezi akafunguka mdomo kwa mara nyingine! “Athumani mlipeana na jarida?! Mbona mie hukuniambia hilo?” Athumani hakumjibu, badala yake alimuonesha yule askari mfuko wake wa safari kuwa jarida la Ndoto, lilikuwa humo. Staf Sajenti Kubuta, aliuchukuwa ule mfuko wa safari wa Athumani, akaufungua na hakika akalitoa jarida la Ndoto, alipolifungua jarida lile, tikiti ya Boti ya Sea Xpress, ilipeperuka ikadondoka chini, na watu wote watano waliokuwa ndani ya nyumba ile waliiona! Staf Sajenti Kubuta aliiokota tikiti ile, na kuifungua ndani hakuyaamini macho yake, akamuonesha Sajent Magane, naye akawa anamtizama Athumani kwa jicho la chuki! Mjumbe akasema. “Jamani mbona hicho kikaratasi mnaoneshana nyie wenyewe, kisha mnakaa kimya, sasa mie kazi yangu hapa ni nini? Kama nimeitwa hapa kama shahidi, ningetaka nishirikishwe katika kila kitu!” Staf Sajenti Kubuta, aliposikia malalamiko ya mjumbe, akampa ile tikiti, lakini pia akamtaka aisome jina la tikiti ile kwa sauti! Mjumbe aliishika ile tikiti akaisoma. “Mauwa Simba Makupa, kutoka Znz kwenda Dsm…..!” Mjumbe hakutaja tarehe kwani Siyawezi aliingiza maneno ya masikitiko katikati yake!
“Laa haula walaa kuwata illa billah, hee Athumani, ulimkatia na Tikti huyo marehemu?! Askari wale japo pale kulikuwa na jambo lakusikitisha, lakini walicheka kwa maneno yale na Sajenti Magane akamwambia mke wa Athumani dobe.
“Hakumkatia tikiti marehemu, alimkatia tikiti Mauwa, kwani jana alikuwa mzima wakati mumeo anatokanae Unguja! Ila Mauwa hakurudi kwao, hadi leo asubuhi tulipopigiwa simu na wasamalia wema, mnamo majira ya saa moja asubuhi, ndipo tulipofika eneo la tukio, tukakuta maiti!” Yule askari alifafanua, na Siyawezi akadakia. “Sasa kama maiti ya huyo Mauwa mmeitwa saa moja asubuhi, huyu bwana tangu saa tatu ya usiku, nipo nae hapa nyumbani na leo ugali wa mchana nimekula nae, yaani hajatoka tangu arudi safari, huyo Mauwa kamuuwa saa ngapi?” Siyawezi alisema huku akimtizama mumewe aliejikunyata kama mtu aliemwagiwa maji ya baridi!
“Hayo na mengine mengi, utakwenda kuelezea kituoni kama mumeo ulikuwa nae tangu arudi safari, na kila kitu ukijuacho juu ya Mauwa Simba, hapa tulikuja kujiridhisha juu ya jarida la Ndoto, kwani katika maelezo ya mumeo, alisema hili jarida ndilo chanzo cha yeye kuzungumza na kuwa karibu na Mauwa, nasi tumekuja kupata ukweli wa jarida, tunaikuta na tikiti ya Mauwa! Kwa hiyo hatuna shaka hata kidogo kuwa Athumani alikuwa na Mauwa! Kwa hiyo tunachunguza, baada ya upelelezi kukamilika tutajua nani aliemuua Mauwa, na kwa sababu gani!” Alihitimisha Staf Sajenti Kubuta, na walipotoka wakatoka wote mle ndani, wao wanne wakapanda ile gari aina ya Toyota Noah Nyeupe, yenye namba za kiraia, wakaelekea kituo cha polisi cha kati! Walipofika pale, Siyawezi alilala mahabusu, asubuhi siku ya pili alitoa maelezo yake, akahojiwa ipasavyo, na jioni ya siku hiyo akaachiwa huru, akiambiwa akihitajika ataitwa mara moja! Ila mumewe Athumani Dobe, alipelekwa katika mahakama ya mkoa Kisutu, akasomewa shitaka la mauwaji, hakutakiwa kujibu chochote kwani mahakama ile ya mkoa, ilikuwa haina uwezo wakusikiliza kesi za mauwaji. Hivyo ilipangwa tarehe nyingine baada ya wiki mbili ili ikatajwe tena, akapelekwa mahabusu katika gereza la mahabusu la Segerea!
*******
“Acha kulia mwanaume, huo ndiyo uanaume kwani matatizo kaumbiwa mwanaadamu! Wewe hukuuwa umeletwa huku kupisha upelelezi tu, utatoka ila kwa kesi hiyo ndugu yangu utasaga buja sana hapa Jela yaani miaka itakatika! Mie nina kesi ya mauwaji huu namaliza mwaka wa tano nipo jela nasota bado sijahukumiwa”
Nyapala wa Selo ile alimnyamazisha Athumani Dobe, aliekuwa akilia huzuni na simanzi ikimtawala. “Sawa nimewasikia kesi zenu, na mahakama zilizopo. Sasa kesho mkisikia odeli anapita akitangaza wale freshi wote kaba mbele, basi mjue nyie ndiyo mnaohitajika. Msikae mkaonana na jamaa zenu waliokuwa huku siku nyingi mkajisahau kwa maongezi, yule odeli akikufata kuita tena jina lako, ujue huko unakwenda kuchezea rungu nyingi za magoti tumeelewana?” (Odeli, ni mtumishi ndani ya gereza, ambae anaweza kuwa mfungwa au mahabusu)
Nyapala wa Selo ile namba mbili, aliwauliza wale mahabusu wageni kama wamemuelewa, na hata walipomjibu kwamba wamemuelewa aliendelea kuwaeleza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ngugu zangu jela hakuna kaburi! Wote tuliopo humu tukifa, wanatakiwa ndugu zetu waende hospitali kuchukua maiti zetu! Ndiyo maana kuna utaratibu wa kuandikishwa urithi. Huu urithi nataka muelewe siyo urithi wa mali zako laa! Ni urithi wa mwili wako mara ukiwa maiti na wewe upo humu gerezani, unatakiwa askari magereza wajue waende wapi walipo ndugu zako, kama utakavyoandikisha katika urithi wako sawa?!” Nyapala aliuliza na wale mahabusu wageni wote wakajibu “Sawaaa!” Yule Nyapala aliwapa maelekezo na taratibu za kuandika urithi, na wakaoneshwa viongozi wengine na Askari Selo, na ilipofika saa tatu kamili usiku, Nyapala alipiga makofi, mahabusu wote wakakaa kimya, akawaeleza.
”Oyaaa haya twende ubavu hapo, muda wakulala umefika huo. Unao usingizi huna lala ubavu! Magereza yote Tanzania saa hizi ndiyo muda wao wa kulala, kila mtu ameshapangwa sehemu yake ya kulala, sitaki kusikia tena minong’ono, wala sauti za radio twende ubavu hapo!” Nyapala alimalisa na Askari Selo akatia msisitizo.
“Oyaaa umesikia hiyooo, sauti ya serikali ishasema wote twende ubavu hapo, wote mliokuwa chooni mkivuta tokeni huko sitaki kuona mtu saa hizi kwani, Magereza yote makubwa Tanzania, Isanga Dodoma, Butimba Mwanza, Kiwila Mbeya, Kigongoni Bagamoyo, Mtego wa Simba, Maweni Tanga, Kitai Ruvuma, Ukonga, Keko, wote saa hizi wanalala, haya na hapa twende ubavu hapo!”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment