Search This Blog

Thursday, 27 October 2022

MVUVI BRUNO (BRUNO THE FISHERMAN) - 1

 







    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Mvuvi Bruno (Bruno The Fisherman)

    Sehemu Ya Kwanza  (1)



    Bruno The Fisherman (Mvuvi Bruno)

    Hali ya hewa angani ilibadilika ghafla, jua kali lililokuwa likiwaka lilifunikwa na mawingu mazito ya kijivu yaliyokuwa yametanda angani. Kwa jinsi hali ilivyokuwa ikionekana, kila mmoja aliamini kwamba mvua kubwa ingekwenda kunyesha.

    Mawimbi makubwa kiasi yalianza kupiga kwa nguvu ufukweni, kila mtu aliyekuwa akiiona hali hiyo aliogopa na kuona kwamba siku hiyo mvua hiyo ingekuwa kubwa kuliko hata zile ambazo ziliwahi kunyesha katika Kijiji cha Guolduvai kilichokuwa nchini Kenya pembezoni mwa bahari ya Hindi.

    Watu waliokuwa wakiogelea, wakatoka majini na kuelekea nyumbani kwao, kila mmoja alionekana kuwa na hofu kwani hali iliyokuwa ikionekana siku hiyo ilikuwa ni ya hatari tupu.

    Wavuvi waliokuwa wakivua samaki kama kawaida yao kwa nyakati za mchana, haraka sana wakaanza kurudisha mitumbwi yao kijijini kwani kwa kuwa walikuwa wakitumia mitumbwi ambayo haikuwa na nguvu ya kupambana na mawimbi makubwa, wakahisi kabisa kwamba kama mvua hiyo kubwa ingewakuta baharini basi hali ingekuwa mbaya zaidi.

    Wakati kila mtu akiogopa mvua kubwa iliyokuwa ikitarajiwa kunyesha, kijana masikini, aliyevalia fulana iliyokuwa imechanika ambayo kwa mbele iliandikwa 50 Cent huku ikiwa na picha kubwa ya mwanamuziki huyo alikuwa amesimama katika kichaka kilichokuwa kijijini hapo huku akiangalia huku na kule.

    Kwa muonekano wake tu haikuwa kazi kubwa kugundua kama kijana huyo alikuwa masikini wa kutupwa. Mbali na fulana yake hiyo iliyoonekana kuchakaa, chini alivalia pensi, kandambili zilizokuwa tofauti huku nywele zake zikiwa timtim.

    Kijana huyu aliitwa Bruno. Alikuwa kijana mkimya kijijini hapo, alimheshimu kila mtu aliyekuwa akiishi mahali hapo. Hakuwa mtu aliyekuwa na furaha, maisha yalimpiga, wazazi wake ambao walifariki miaka miwili iliyopita kwa kuzama na mtumbwi uliokuwa ukielekea Mombasa hawakumuachia kitu, alikuwa mikono mitupu huku akiendelea kufanya kazi ya uvuvi katika bahari ya Hindi.

    Alisimama mahali hapo huku macho yake yakiendelea kuangalia huku na kule. Hakuonekana kuogopa mvua kubwa iliyokuwa ikitarajiwa kunyesha, kile alichokuwa akikitaka ni kuongea na msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati, Sharifa ambaye alimwambia kwamba angefika mahali hapo muda si mrefu.

    Mpaka mvua kubwa inaanza kunyesha bado msichana huyo hakuwa ametokeza. Mvua iliyoambatana na upepo mkali ilimnyeshea lakini hakukubali kuondoka, aliendelea kusubiri mahali pale mpaka alipomuona msichana huyo akija kutoka kule kijijini huku akikimbia.

    Uso wake ukajawa na tabasamu, kumuona Sharifa mahali hapo ndiyo lilikuwa lengo lake. Kila alipomwangalia, uzuri wa msichana huyo ulikichanganya kichwa chake. Sharifa akamsogelea mpaka pale alipokuwa, kama alivyokuwa Bruno, hata naye alikuwa amelowanishwa na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha.

    Sharifa alipomfikia Bruno, akamsogelea, akamkumbatia na kuangaliana pasipo kuzungumza kitu chochote kile. Bruno alikuwa na mambo mengi ya kuzungumza na msichana huyo aliyekuwa amesuka mabutu kichwani mwake na viatu vyake ya chachacha vikiwa miguuni mwake.

    “Nimekusubiri sana!” alisema Bruno huku akimwangalia Sharifa, walipokuwa wamesimama, bado mvua kubwa iliendelea kuwanyeshea.

    “Pole sana! Nimechelewa kidogo lakini sidhani kama umekasirika,” alisema Sharifa kwa sauti ndogo huku akimwangalia mpenzi wake huyo kwa jicho lililoonyesha mahaba yote kwake.

    “Hakuna! Siwezi kukasirika! Ulizungumza na wazazi wako?” aliuliza Bruno.

    “Ndiyo! Nilizungumza nao, waliniambia vilevile.”

    “Kwamba?”

    “Hawataki kuona nikisimama na kuongea nawe. Kiukweli wanakuchukia, wanasema kwamba huna kitu, utanilisha nini? Utanipa nini? Huna chochote kile,” alisema Sharifa huku akimwangalia Bruno ambaye nguvu zilimuisha baada ya kuambiwa hivyo.

    Moyo wake ulikuwa na hasira tele, alimpenda sana Sharifa lakini kipingamizi kikubwa kilikuwa ni nyumbani kwa msichana huyo. Hakukubalika kwa sababu tu alikuwa masikini, wazazi wa msichana huyo walimchukia kupita kawaida.

    Sharifa alikuwa mzuri wa sura, alipendwa na kila mtu kijijini hapo, wanaume walimfuatilia, tena wale waliokuwa na mitumbwi yao ambao kila siku walipata pesa nyingi baada ya kuvua samaki.

    Wote hao, Sharifa hakuwakubali, kwake, moyo wake ulikuwa kwa mtu mmoja tu, Bruno ambaye alikuwa masikini wa kutupwa. Alichokuwa akikiangalia Sharifa hakikuwa pesa wala mali, hakuangalia mambo mengine zaidi ya mapenzi. Aliamini kwamba penzi lilikuwa kila kitu, hata kama Bruno hakuwa na kitu lakini aliamini kwamba angeweza kumpa furaha aliyokuwa akiihitaji.

    “Niambie tufanye nini! Sitaki kuolewa na mtu yeyote, ninataka kuolewa na wewe tu. Niambie Bruno unataka tufanye nini?” aliuliza Sharifa huku akitokwa na machozi yaliyokuwa yakitiririka mashavuni mwake ila ilikuwa vigumu kuyaona kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.

    “Sijui tufanye nini! Labda unipe muda wa kujifikiria!”

    “Hatuna muda! Sema tufanye nini! Au tutoroke?”

    “Tutoroke?”

    “Ndiyo!”

    “Kwenda wapi?”

    “Popote pale. Nitahitaji kuwa nawe, sitaki kuona nikikukosa. Bruno, ninakupenda sana, wewe ndiye kila kitu katika maisha yangu, siwezi kuishi bila wewe,” alisema Sharifa, hapohapo akamkumbatia tena Bruno.

    “Sharifa! Sina pesa, sina kitu chochote kile. Nipo mtupu kama unavyoniona, hata tukitoroka, itakuwaje huko tutakapokwenda?” aliuliza bruno.

    “Vyovyote itakavyokuwa. Naomba tutoroke. Sitaki kukupoteza,” alisema Sharifa.

    Kwa jinsi alivyoonekana, Sharifa alikuwa tayari kutoroka mahali hapo. Moyo wake ulichoka na alihitaji kuendelea kuishi na mpenzi wake huyo. Hakutaka kubaki kijijini pale, wazazi wake walikataa yeye kuolewa na Bruno kwa kuwa tu alikuwa masikini. Hilo lilimuumiza mno na kitu alichokuwa amekifikiria ni kutoroka kijijini hapo.

    Kwa Bruno ilikuwa ngumu kukubaliana naye. Hakuwa na kitu, kilichomuumiza kichwa si kutoroka kijijini hapo bali ni maisha baada ya kutoroka. Alimwambia wazi Sharifa kwamba huo haukuwa uamuzi mzuri, walitakiwa kubaki hapohapo kijijini huku wakiamini kwamba kuna siku maisha yangekuwa kama wanavyotaka yawe.

    “Hatutakiwi kutoroka. Kama tatizo ni pesa, tutatafuta pesa, tutakuwa na pesa na kufanikiwa. Sharifa! Sitaki nikupoteze, kama kweli wazazi wako wanasema siwezi kukuoa kwa sababu sina pesa. Nitatafuta pesa tu, tena kwa nguvu zote,” alisema Bruno huku akimwangalia mpenzi wake huyo.

    Japokuwa ilikuwa vigumu kumshawishi msichana huyo lakini mwisho wa siku wakakubaliana kwamba hakukuwa na sababu ya kutoroka zaidi ya Bruno kupambana mpaka kuhakikisha kwamba anapata pesa na kumuoa msichana huyo.

    Walizungumza kwa dakika kadhaa, walipomaliza, Sharifa akaondoka kurudi nyumbani kwao. Huku nyuma Bruno alichanganyikiwa, bado hakufahamu ni kitu gani alitakiwa kufanya.

    Hali iliyokuwa ikiendelea ilimtisha mno, hakutamani kuona akimkosa msichana huyo kisa tu hakuwa na pesa. Alitaka kupambana mpaka kuhakikisha anapata pesa na kumchukua msichana huyo.

    Maisha yaliendelea, kama kawaida kila siku alikuwa akiondoka kuelekea baharini na rafiki yake, Abdul huku wakiwa kwenye mtumbwi wao. Huko, hasa nyakati za usiku walikuwa wakivua samaki na kwenda kuwauza kijijini kwao.

    Abdul alikuwa akifahamu kila kitu. Huyo ndiye alikuwa rafiki yake wa karibu, walipendana na kupeana siri ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake. Abdul alimuonea huruma Bruno, alijua ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alimpenda Sharifa, alijitahidi kufanya kila liwezekanalo kwa msichana huyo lakini bado wazazi wake hawakutaka kabisa kumuona binti yao akiwa na kijana masikini kama yeye.

    “Ila kuna siku nitapata pesa tu na kumuoa Sharifa,” alisema Bruno huku akimwangalia rafiki yake huyo, wakati huo walikuwa kwenye mtumbwi wao, chemli ilikuwa ikiwaka, walikuwa wakielekea mbali kabisa na bahari.

    “Unahisi utafanikiwa kwa kupitia hawa samaki?” aliuliza Abdul.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Inawezekana! Pia nitaanza kuangalia mpango wa kuelekea mjini Nairobi kwenda kuuza huko. Abdul, hujui ni kwa kiasi gani nampenda Sharifa,” alisema Bruno.

    “Najua. Unampenda sana. Ila hili suala la wazazi wake linaniumiza sana kichwa,” alisema Abdul.

    “Najua! Ila nitapambana tu!”

    Walikuwa wakipiga stori huku wakiwa safarini kuvua. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao ya kila siku. Walivua usiku kucha, walipigwa na maji, walipigwa na baridi na asubuhi walirudi kijijini huku wakiwa na samaki wa kuwauza kwa siku mbili.

    Mtu wa kwanza kabisa aliyekuwa akiwapokea na kuwasaidia kutoa samaki kwenye mtumbwi alikuwa Sharifa. Alikatazwa kuwa karibu na Bruno lakini hilo halikumfanya kumsaidia kazi hiyo. Wazazi wake walisema sana lakini hakutaka kusikia, alijitoa kwa kila kitu, kama kupigwa kwa ajili hiyo, alipigwa leo na kesho kama kawaida alifanya vilevile.

    “Pole sana mpenzi,” alisema Sharifa huku akimsogelea Bruno alipokuwa. Alionekana kuwa hoi.

    “Ahsante sana!”

    Wakawachukua samaki, wakamuita dalali na kwenda kutafuta wateja huku wakiwa wamekwishaelewana naye kabisa. Wakaondoka mahali hapo na kwenda nyumbani kwake, katika nyumba ya nyasi, ndani kitanda cha teremka tukaze na kutulia hapo.

    Walibaki wakiwa wameshikana mikono, waliangaliana kwa bashasha huku kila mmoja akionekana kuwa na hamu na mwenzake. Sharifa akaanza uchokozi kwa kukichezea kifua cha Bruno aliyekuwanaye kitandani hapo.

    “Ushaanza...” alisema Bruno huku akitoa tabasamu pana.

    “Kwani kuna tatizo mpenzi?” aliuliza msichana huyo, hapohapo akaanza kumvua fulana Bruno.

    Huku tayari akiwa amekwishavuliwa fulana yake, mara wakaanza kusikia sauti ya Adul kutoka nje ikimuita.

    “Bruno...Bruno fungua mlango...” ilisikika sauti ya Abdul.

    Wote wakashtuka, haraka sana Bruno akafungua mlango na kumwangalia rafiki yake huyo. Alikuwa akihema kwa nguvu, akamuuliza tatizo lilikuwa nini.

    “Mzee Jumanne anakuja na panga. Kimbia! Anakuja kukumaliza,” alisema Abdul. Bruno alivyosikia hivyo tu, haraka sana akachukua fulana yake lakini hata kabla hajatoka tu ndani ya kijumba chake cha nyasi, mzee huyo akatokea na kusimama mlangoni. Jasho lilikuwa likimtoka, alionekana kuvimba kwa hasira, mwili ulikuwa ukimtetemeka.

    Kitandani pale, alimuona binti yake akiwa amekaa, hasira zikamzidi zaidi, akalishikilia vizuri panga lake tayari kwa mashambulizi. Bruno aligundua hilo, akaona kabisa kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake kwani kwa jinsi mzee huyo alivyoonekana, hakuwa na masihara hata kidogo.



    Mzee Jumanne alisimama mbali kidogo na nyumba yake, macho yake yalikuwa yakiangalia baharini namna mitumbwi ilivyokuwa ikiingia kijijini hapo baada ya wavuvi kutoka kuvua samaki. Moyo wake ulikuwa na hasira kali, alimchukia Bruno, kati ya watu wote aliotokea kuwafahamu maishani mwake, mwanaume huyo alikuwa mtu wa kwanza kumchukia kwa chuki kubwa moyoni mwake.

    Alimchukua binti yake, hakupendezwa na jambo hilo kwa sababu tu alikuwa kijana masikini ambaye alikuwa na uhakika kwamba angempeleka mtoto wake kwenye mzigo mzito wa umasikini kitu ambacho hakuwa radhi kukiona kikitokea.

    Alimkataza Sharifa kuwa na Bruno lakini binti huyo hakutaka kukubali hata mara moja, alimwambia baba yake wazi kwamba kuachana na Bruno lilikuwa jambo lisilowezekana hata kidogo na alikuwa tayari hata kufa lakini si kumwacha mwanaume huyo.

    Maneno hayo yalimchoma mno mzee Jumanne kiasi kwamba akaona kitu pekee cha kumfanya binti yake aachane na Bruno kilikuwa ni kumuua mwanaume huyo tu. Hakuogopa, alikuwa tayari kukaa gerezani hata kifungo cha maisha lakini si kuvumilia kumuona Bruno akiendelea kuvuta pumzi ya dunia na binti yake aliyekuwa akipendwa na wanaume wengi.

    Sharifa alimpenda sana Bruno, hakuwa radhi kuona akichukuliwa na mwanaume mwingine, katika maisha yake kila siku alimwambia wazi kwamba ilikuwa ni bora kufa lakini si kuona akiingia kwenye mapenzi na mwanaume mwingine.

    Mzee Jumanne alijaribu kwa nguvu zote kuwaleta wanaume waliokuwa na pesa kwa lengo la kumchukua binti yake lakini wote hao walishindwa kuuteka moyo wa binti huyo, kwake, hakukuwa na kitu kilichokuwa na thamani zaidi ya moyo wake kwa Bruno.

    Mzee Jumanne alipanga siku hiyo kuwa ya mwisho kumuonya binti yake kutembea na Bruno, alikuwa na uamuzi mmoja tu kichwani mwake, kumuua mwanaume huyo na yeye kuondoka zake hapo kijijini.

    Alitulia pembeni kabisa mwa bahari, macho yake hayakuacha kuangalia kule ambapo mitumbwi ilikuwa ikiingia. Alitulia, alimuona binti yake, Sharifa akiwa karibu na bahari, macho ya msichana huyo yalikuwa yakiangalia baharini.

    Alijua kabisa kwamba Sharifa alikuwa akimsubiri Bruno ili ampokee na kuondoka naye. Wala hazikupita dakika nyingi, mtumbwi wa Bruno ukaanza kuonekana kwa mbali, alijitahidi kujizuia kwani tayari hasira zilikuwa zimempanda na hata panga alilokuwa amelishika lilikuwa likitetemeka kwa kuwa mkono wake ulikuwa ukitetemeka kwa hasira.

    Akamuona Bruno akiteremka, akamuacha rafiki yake, Abdul na yeye kuondoka na binti yake. Moyo wake ukachoma, hasira zikampanda, akajipa nguvu kwamba alitakiwa kusubiri mpaka watakapoondoka na kwenda huko walipotaka kwenda.

    Baada ya dakika tano, naye akatoka mahali pale alipokuwa na kuanza kwenda nyumbani kwa Bruno ambapo aliamini kwamba binti yake alikuwa humo.

    Abdul alimuona mzee Jumanne, hakutaka kuchelewa, akaanza kukimbia kuelekea kwa Bruno kwa lengo la kumwambia kwamba mzee huyo alikuwa njiani akija na panga.

    Wakati Bruno akijiandaa kukimbia, tayari mzee huyo alikuwa amekwishafika ndani ya kibanda kile huku akiwa na panga lake mkononi.

    Bruno akabaki akitetemeka, alishikwa na hofu, kwa jinsi mzee Jumanne alivyokuwa akionekana ilionyesha kabisa alikuwa na hasira kali na kama asingefanya harakati za kukimbia mahali hapo basi angeweza hata kumkatakata kwa panga.

    Hakukuwa na sehemu ya kukimbilia, alitakiwa kupitia palepale mlangoni aliposimama mzee huyo. Alijua kuwa kwa nguvu alizokuwanazo mzee Jumanne asingeweza kumzuia hata kidogo. Hakutaka kujiuliza sana, hapohapo akamvamia kwa kasi, wote wakadondoka, haraka sana Bruno akasimama na kuanza kukimbia. Mzee Jumanne hakutaka kukubali, akasimama na kuanza kumkimbiza kwa panga.

    Ulionekana kama mchezo au filamu fulani hivi. Bruno alikuwa akikimbia kwa kasi kubwa kwani alijua dhahiri kwamba kama angesimama basi angeweza kukatwakatwa na lile panga. Akaongeza kasi zaidi, kasi ambayo mzee Jumanne hakuweza kumfikia hata kidogo.

    Mzee huyo akasimama, akashika kiuno huku akihema kama mbwa, macho yake yalikuwa yakimwangalia Bruno aliyezidi kukimbia kuelekea mtaani.

    Watu wote waliokuwa wakifuatilia tukio lile walishangaa na wengine kucheka kabisa. Walifurahishwa na jinsi mzee Jumanne alivyoinama na kushika magoti, panga lilikuwa chini huku akihema kwa nguvu.

    Bruno aliendelea kukimbia mpaka alipofika sehemu ambayo alihisi kwamba ilikuwa salama, akasimama na kupumzika. Hakujua ni mahali gani alitakiwa kwenda, alitulia huku akiangalia kila kona kuona kama mzee huyo alikuwa akija au la.

    Maumivu aliyokuwanayo moyoni mwake hayakuelezeka hata kidogo. Aliumia kuona akimpenda msichana ambaye wazazi wake walimchukia kwa sababu tu ya umasikini aliokuwanao.

    Siku hiyo hakurudi nyumbani, aliondoka na kuelekea nyumbani kwa rafiki yake, James ambapo akakaa huko na kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea.

    Hakutaka kurudi nyumbani kwake kwani alijua kwamba piga ua mzee Jumanne ilikuwa ni lazima kurudi nyumbani hapo kumtafuta. Alikaa huko kwa siku hiyo na baadaye kuonana na Abdul na kutaka kusikia kilichotokea.

    “Sharifa alipigwa sana na baba yake,” alisema Abdul huku akionekana kuumizwa na kile kilichotokea.

    “Acha masihara!”

    “Yule mzee anapiga. Angemuua bila watu kumpoza,” alisema Abdul.

    “Daah!”

    “Ila ana msimamo mno. Alipigwa na kupigwa lakini bado alimwambia baba yake kwamba anakupenda na kamwe asingeweza kukuacha, yaani kila mtu alikuwa akishangaa,” alisema Abdul.

    Moyo wa Bruno ukauma zaidi, kitendo cha kuambiwa kwamba mpenzi wake alipigwa mno na baba yake kisa yeye, kiliuvuruga kabisa moyo wake kwani miongoni mwa vitu ambavyo hakutaka kabisa kuona vikitokea ni kuliona chozi la mpenzi wake.

    Japokuwa alikuwa nje ya nyumba yake lakini aliendelea kufanya kazi ya uvuvi kama kawaida. Kila siku jioni aliondoka na mtumbwi wa mvuvi mwenzake, James ambapo walikwenda mpaka baharini ambapo huko walikutana na Abdul na kisha kuingia kwenye mtumbwi wake na kwenda kuvua kama kawaida.

    Akawa akiishi kwa namna hiyo, hata alipokuwa akirudi, alipofika njiani kabisa alikuwa akikutana na akina James, anaingia kwenye mtumbwi wao na kurudi.

    Alifanya hivyo kwa wiki nzima. Mzee Jumanne hakuwa akijua kilichokuwa kikiendelea, alichoamini ni kwamba Bruno alikuwa amekimbia baada ya kumkosakosa kumkata kwa panga kama alivyokuwa amepanga.

    Wakati akijipa uhakika kwamba mwanaume huyo alikuwa amekimbia akapata maneno kwamba Bruno alikuwa akiendelea na shughuli zake za uvuvi kama kawaida.

    “Anafanyaje?” alimuuliza mvuvi mmoja aliyekuwa akiusimamia mitumbwi yake.

    “Watu wanasema kwamba anaonekana sana tu akivua,” alisema kijana huyo na kuanza kumwambia jinsi Bruno alivyokuwa akiingia baharini.

    Hilo lilitosha kabisa kumwambia kwamba Bruno aliendelea kuwepo kijijini hapo, alichokifanya ni kumtafuta James na kumwambia kwamba alitaka kufanya naye kazi moja kwa malipo makubwa ambayo asingeamini.

    “Kazi gani?” aliuliza James.

    “Umuue Bruno!”

    “Nimuue Bruno?”

    “Ndiyo!”

    “Nitamuuaje?”

    “Utamchukua kama unavyomchukuaga kwenda baharini, ukifika huko, mtupe baharini!” alisema mzee huyo.

    “Mmh!”

    “Unaogopa?”

    “Hapana! Ila si ataweza kuogelea, sasa akifika nchi kavu itakuwaje?” aliuliza.

    “Hakikisha siku ya tukio hauonani na huyo Abdul. Mnaondoka naye kwenda mbali kabisa, sehemu ambayo hata mkimtosa baharini, hawezi kupona,” alisema mzee huyo.

    “Hakuna shida. Kwa hiyo vipi kuhusu mfuko?”

    “Nawapeni elfu ishirini!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sawa.”

    Hilo halikuwa tatizo, akachukua shilingi elfu ishirini ya Kenya ambayo ilikuwa ni zaidi ya laki nne kwa shilingi ya Tanzania na kumpa.

    “Basi sawa. Hiyo kazi inafanyika usiku wa leo. Hutoweza kumuona tena,” alisema James.

    “Sawa. Nitashukuru sana!” alisema mzee Jumanne na kuondoka huku moyo wake ukiwa na furaha tele.



    James alikuwa na furaha, hakuamini kama mzee Jumanne angetoa kiasi kikubwa cha pesa kwa kazi ndogo namna ile. Pesa alizopewa kwa upande wake zilikuwa nyingi mno kiasi cha kufanya utekelezaji haraka sana.

    Huyo Bruno aliyeambiwa amuue wala hakuwa ndugu yake, urafiki wao ulikuwa wa juujuu tu. Hakuona kama kulikuwa na tatizo lolote lile, kwake, kazi hiyo ilikuwa ni ya kutekeleza haraka sana pasipo kujiuliza.

    Akamwambia mwenzake aliyeitwa Kitula kwamba walitakiwa kufanya kazi ile huku pesa ile wangegawana. Maisha yao walijitahidi kufanya kazi kwa bidii mno, usiku na mchana kwa lengo la kupata pesa, leo huu, pesa ilikuja yenyewe na ni utekelezaji tu ndiyo uliokuwa ukitakiwa kufanyika.

    Walichokifanya ni kukubaliana kuifanya kazi ile kwa usiku wa siku hiyo kwa kumchukua Bruno na kuondoka naye mpaka mbali kabisa ambapo huko wangemtosa ndani ya maji na wao kuendelea na kazi yao ya uvuvi.

    Ilipofika jioni, kama kawaida wakamchukua Bruno na kuondoka naye. Hawakutaka kuonekana tofauti, walikuwa wacheshi vilevile, tabasamu yalitawala nyusoni mwao kiasi kwamba Bruno hakuona tatizo lolote lile wala kuhisi kwamba siku hiyo watu hao walitaka kumfanyia kitu kibaya.

    Wakaondoka mpaka mbali kabisa. Siku hiyo hali ilionekana kuwa tofauti na siku nyingine, kulikuwa na mawimbi mengi yaliyokuwa yakipiga hali iliyoonyesha kwamba bahari ingechafuka baada ya muda mchache. Waliendelea kupiga stori kama kawaida huku James na Kitula wakijifikiria ni kwa jinsi gani wangeweza kumtupa Bruno ndani ya maji na kuondoka zao.

    Siku hiyo hawakutaka kwenda upande wa Mashariki kama ilivyokuwa siku nyingine, waliondoka na kwenda upande wa Kaskazini ambapo waliamini kwamba wasingeweza kukutana na Abdul.

    Mtumbwi ulikwenda kwa umbali kama wa kilometa ishirini ndipo wakafika sehemu ambayo ilikuwa na kina kirefu mpaka zaidi ya mita elfu tatu. Waliona sehemu hiyo kuwa sahihi kwa kufanyia ule umafia waliotaka kufanya.

    Mpaka kufika hapo tayari Bruno alionekana kuwa na hofu, akahisi kabisa kulikuwa na kitu kilichotaka kutokea. Walikuwa wamekwenda kwa umbali mrefu sana pasipo kukutana na Abdul. Haikuwa kawaida, alijua kabisa kwamba kwa umbali fulani hivi walikuwa wakikutana na Abdul na kuingia katika mtumbwi wake lakini kwa siku hiyo mambo yalionekana kuwa tofauti kabisa.

    “Jamani! Huku tumekuja wapi?’ aliuliza Bruno huku akiwaangalia kwa uso uliokuwa na hofu nzito.

    “Baharini! Abdul mbona haonekani leo?” alijibu James na kujiuliza, yeye mwenyewe akajifanya hajui.

    Walizidi kwenda mbele kabisa, walipoona kwamba wamefika sehemu ambayo ni nzuri, hapohapo wakamgeukia Bruno na kuanza kumwangalia. Muonekano wao ulibadilika, hawakuwa kama wale ambao aliwazoea kipindi cha nyuma, walibadilika na kuwa watu wenye muonekano mwingine kabisa.

    Hilo likamtia hofu Bruno na kuhisi kwamba kulikuwa na kitu kilichotaka kutokea. Hata kabla hajafanya kitu chochote kile, wakamsogelea, wakamshika kinguvu na kumtosa baharini.

    Bruno alishangaa, hakujua sababu ya watu hao kufanya hivyo. Akabaki akielea ndani ya maji huku akiwaona James na Kitula wakiondoka mahali hapo na mtumbwi wao.

    Aliwaita, aliwaomba msaada lakini hakukuwa na mtu aliyerudi, wote waliondoka na mtumbwi huku wakipiga kasia ya nguvu kuondoka mahali hapo.

    Hilo lilimuuma, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, hakuamini kama watu wale ambao kila siku alikuwa akiwaamini ndiyo waliokuwa wamemfanyia kitu kama kile.

    Hakutaka kukata tamaa, ilikuwa ni usiku sana, bahari ilitisha, mawimbi makubwa yalikuwa yakipiga kwa nguvu. Alipiga kelele lakini hakukuwa na msaada wowote ule. Kutokana na giza zito lililokuwa mahali hapo ilikuwa vigumu kuona hata hatua saba kutoka pale alipokuwa.

    Alijua kabisa kwamba siku hiyo ndiyo ungekuwa mwisho wake, alipiga mbizi mpaka mikono ikachoka na kubaki akiwa amekata tamaa kabisa. Alitulia hapo, wakati mwingine alizama, akaibuka na kuendelea kuelea juu ya maji tu.

    Muda ulizidi kwenda, kikafika kipindi bahari ikaanza kuchafuka, mawimbi makubwa yakaanza kupiga. Akapiga kelele lakini bado hakukuwa na mtu aliyetokea na kumpa msaada wowote ule. Alikuwa peke yake baharini, alipoangalia pande zote, hakukuwa na msaada wowote ule kitu kilichomfanya kuhisi kwamba siku hiyo ndiyo ungekuwa mwisho wake.

    “Mungu nisaidie,” alisema huku akiwa amekata tamaa.

    Alimuomba Mungu sana lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yale. Mawimbi yalimpeleka huku na kule, alizamishwa na kuibuliwa, alikunywa maji mengi, alijitahidi kujiokoa lakini akashindwa kabisa mpaka kufikia hatua akajiweka tayari kwa kufa.

    Alimkumbuka mpenzi wake, Sharifa, hakuamini kama huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kumuona msichana huyo mrembo. Yaani kitendo cha kuchukuliwa na kuelekea baharini kilimaanisha kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.

    “Sharifa mpenzi! Ninakufa pasipo kukuona. Bebi! Ninakufa,” alisema Bruno kwa uchungu mkubwa.

    Mawimbi yaliendelea kupiga, alikosa nguvu na baada ya dakika kadhaa, akaanza kuzama, alijitahidi kuibuka juu lakini ilishindikana kabisa, baada ya dakika tatu, mwili ukaishiwa nguvu, macho yakaanza kuwa mazito na hatimaye yakaanza kufumba, alijitahidi kujitingisha ili kuona kama alikuwa hai, akashindwa kabisa. Giza likaendelea kujaa machoni mwake na hakujua ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo.

    ***

    Abdul alikuwa ndani ya mtumbwi wake, macho yake hayakutulia, yalikuwa yakiangalia huku na kule ili kuona kama mtumbwi wa akina James ungefika mahali hapo au la.

    Mitumbwi mingi ilikuwa ikipita mahali hapo, aliitolea macho kuona kama ilikuwa ni mtumbwi wa akina James lakini haikuwa huo. Moyo wake ulikuwa na hofu tele, kwa jinsi bahari ile ilivyokuwa imechafuka ilionyesha kabisa kwamba hali haikuwa nzuri hata mara moja.

    Hakwenda kuvua, alikuwa akisubiri, dakika zilizidi kwenda mbele kama kawaida huku akiendelea kuwasubiri watu hao lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alitokea mahali hapo.

    Alihisi kwamba kulikuwa na tatizo, akajua kulikuwa na mchezo uliokuwa umefanyika ambao uliwafanya watu hao kuchelewa namna hiyo. Hakukata tamaa, aliendelea kusubiri mpaka ulipofika usiku mkubwa ambapo akaamua kuondoka zake huku akiwa na maswali mengi juu ya nini kilichokuwa kimetokea.

    Asubuhi ilipofika, alirudi kijijini kama kawaida. Alitaka kuonana na akina James, alitaka kujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka watu hao kutokukutana nao usiku uliopita.

    Wakati akiwa ameweka mtumbwi wake pembezoni mwa bahari na kuufunga, kwa mbali akauona mtumbwi wa akina James ukija kule alipokuwa. Haraka sana akawafuata huku akiwa na shauku ya kutaka kufahamu ni kitu gani kilitokea.

    Alipowafikia tu na kuuwaangalia usoni, akabaini kwamba kulikuwa na tatizo lililokuwa limetokea kwani nyuso zao zilionekana kuwa tofauti na siku nyingine, zilikuwa ni sura zenye majonzi tele.

    “Msiniambie kama kuna jambo baya limetokea,” alisema hata kabla ya salamu.

    Wanaume hao hawakujibu, walibaki wakimwangalia tu huku kila mmoja akiwa kimya. Ukimya wao ukazidi kudhihirisha kwamba kulikuwa na jambo baya lililokuwa limetokea. Akawauliza kwa mara ya pili ambapo James akaanza kumwambia kwamba Bruno alikufa baharini.

    “Alikufa baharini?” aliuliza Abdul kwa mshtuko.

    “Ndiyo! Bahari ilichafuka, si uliona?”

    “Ndiyo!”

    “Mtumbwi ukapelekwa huku na kule na hatimaye ukapinduka. Tulijaribu kuogelea, tukaupindua na kuuweka sawa. Yeye alishindwa kuungana nasi, akapelekwa na maji, tulimuita lakini hakutumuona te...” alisema James hata kabla hajamaliza sentensi yake, akanyamza, machozi ya kinafiki yakaanza kujikusanya na kutiririka mashavuni mwake.

    Abdul hakuamini alichokuwa amekisikia, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, aliwaangalia akina James, maneno aliyokuwa akiambiwa yalionekana kama si katika ulimwengu halisi uliokuwa ukitokea, alihisi kwamba yupo ndotoni ambapo baada ya dakika kadhaa angeamka na kujikuta akiwa kitandani.

    Hakujua ni kwa jinsi gani alitakiwa kumwambia Sharifa. Msichana huyo alikuwa akimpenda Bruno kupita kawaida, kitendo cha kumfuata na kumwambia kwamba mpenzi wake, Bruno alikufa baharini aliona kabisa angesababisha maumivu makali moyoni mwa msichana huyo.

    Hakutaka kabisa kumfuata na kumwambia ukweli lakini baada ya kujifikiria sana, hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kumtafuta Sharifa na kumwambia juu ya kile kilichotokea.

    Hakumwambia moja kwa moja kwamba alikufa baharini, alimwambia kama alivyoambiwa kwamba bahari ilichafuka, alitumbukia ndani ya maji na kupotelea huko kitu kilichomaanisha kwamba mwanaume huyo alikufa humo baharini.

    “Brunoooo...” Sharifa alijikuta akiita, akaufumba mdomo wake kwa viganja vyake na kuanza kulia kwa maumivu makali.

    Hakukuwa na kitu kilichotokea kumuumiza kama kitu hicho, kifo cha mpenzi wake kilikuwa na maumivu makali hata zaidi ya ambavyo wangekufa wazazi wake wote wawili. Alilia kwa sauti kiasi kwamba mpaka watu wengine wakabaki wakishangaa.

    Akaelekea chumbani kwake, hakunyamaza, aliendelea kulia mfululizo mpaka mafua yakampata. Alisikia kitu chenya ncha kali kikiuchoma moyo wake, maumivu aliyokuwa akiyasikia kipindi hicho hayakusimulika hata kidogo.

    Wakati Sharifa akiwa analia, upande wa pili baba yake baada ya kupewa taarifa kwamba Bruno alikuwa amekufa baharini moyo wake ukawa na furaha, hakuamini alichokisikia, alitabasamu na kumpongeza James kwa kazi nzuri aliyokuwa ameifanya.

    “Amekufa kweli?” aliuliza.

    “Ndiyo! Usiku bahari ilichafuka sana, mawimbi makubwa, yaani sikuwahi kuona hali kama ile tangu nizaliwe. Kwenye mawimbi hayohayo, mbali kabisa na bahari, tukamtosa majini, ataponaje hapo,” alisema James na wote kuangua kicheko.

    Kwao ilikuwa ni furaha tele, hakukuwa na mtu aliyehuzunika, mioyo yao ilikuwa na furaha kwamba hatimaye walikuwa wamefanikiwa kummaliza mwanaume huyo aliyeonekana kuwa mwiba mkali moyoni mwa mzee Jumanne.

    Hicho ndicho kilikuwa kipindi kibaya kwa Sharifa, kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, moyo wake ulichoma, kila siku asubuhi alipokuwa akiamka alikwenda mpaka ufukweni na kusimama karibu kabisa na bahari na kuanza kuyaangalia maji.

    Hakuamini kama bahari hiyo ndiyo iliyommeza mpenzi wake aliyempenda kwa mapenzi ya dhati. Kifo cha Bruno kilisikika kila kona, kila mtu alimuonea huruma msichana huyo kwani mapenzi aliyokuwanayo moyoni mwake yalikuwa makubwa mno.

    Wengi hawakutaka kukutana naye kwani kwa jinsi alivyokuwa na huzuni, kila aliyekutana naye alikuwa akilia, Sharifa alisikitisha kupita kawaida.

    Wiki ya kwanza ikakatika, ya pili, ya tatu mpaka mwezi. Bado mwili wa Bruno haukupatikana. Alichokifanya Sharifa ni kwenda kuchimba kaburi kisha kuzizika nguo za mpenzi wake, Bruno kama ishara ya kumzika mwanaume huyo.

    “Nitakupenda maisha yangu yote hata kama umekufa. Siwezi kuolewa, siwezi kuwa na mwanaume mwingine tena,” alisema Sharifa huku akiwa kwenye kaburi hilo la mpenzi wake ambapo ndani yake kulikuwa na nguo tu.



    Biashara ya madawa ya kulevya iliyokuwa imeshamiri duniani kote ilianza kuyumba. Kila mtu aliyekuwa akiifanya biashara hiyo alishangaa, mizigo mingi ilikuwa ikikamatwa, watu waliokuwa wakisafirisha ambao walijulikana zaidi kama punda walikamatwa na kufungwa gerezani huku wakipewa mateso makubwa.

    Marekani iliamua kuingia kazini, haikutaka kuona biashara hiyo ikiendelea kufanyika kwa kuwa watu waliokuwa wakiathiriwa zaidi walikuwa vijana ambao ndiyo walikuwa nguvu kazi ya taifa.

    Iliingia kazini rasmi, wasafirishaji waliokuwa wakipitia mipakani walikuwa wakikamatwa, Wamexico ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kusafirisha madawa na kuingiza nchini humo walikamatwa na kufungwa gerezani tena huku wakipewa mateso makali.

    Hali ilitisha, biashara iliyumba kupita kawaida. Wamarekani walichukiwa kwa kuwa walijifanya kimbelembele kuhakikisha kwamba wanazilaghai serikali za nchi nyingine kuhakikisha biashara hiyo inapotea haraka sana vinginevyo nchi ambayo ingepuuzia ingetolewa katika Umoja wa Mataifa.

    Hilo ndilo lililozifanya nchi nyingine kuwa makini na kutumia nguvu kubwa katika kuhakikisha wanatokomeza biashara hiyo iliyokuwa ikiwatesa sana vijana waliokuwa wakitumia. Ndani ya miezi sita tu, biashara ililala kwa kiasi kikubwa sana kiasi kwamba kila mmoja akahisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa biashara hiyo haramu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa waliokuwa wakifanya biashara hiyo walikuwa Samuel Maxwell aliyekuwa na umri wa miaka hamsini na mbili na Richard Todd aliyekuwa na miaka hamsini na nane.

    Wawili hao walikuwa mabilionea wakubwa nchini Marekani, Todd alikuwa na utajiri wa dola bilioni ishirini na nne ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni arobaini na nane huku Maxwell akiwa na utajiri wa dola bilioni ishirini ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni arobaini.

    Japokuwa walikuwa na biashara nyingi zilizokuwa zikiwaingizia pesa lakini biashara kubwa zaidi ambayo iliwafanya utajiri wao kukua kila siku ni biashara ya madawa ya kulevya waliyokuwa wakiifanya.

    Waliuziana madawa, walifanya biashara kama ndugu, walipendana kiasi kwamba mpaka mabilionea wengine wakashangaa kwani hawakuwahi kuwaona mabilionea ambao walikuwa wakishirikiana vizuri katika biashara zao kama wawili hao.

    Wakati Marekani ilipoanza kuleta figisufigisu katika biashara hiyo ndipo wawili hao wakatokea kugombana na kuonana kama paka na panya na chanzo kikubwa kikiwa ni biashara hiyohiyo ya madawa ya kulevya.

    Wakati watu wakihitaji sana madawa hayo na Todd kujiona kwamba hana kitu, haraka sana akawasiliana na Maxwell na kumwambia kuhusu mkakati wake ambao angeufanya kuhakikisha anapata mzigo na kuupeleka barani Afrika ambapo kulikuwa na uhitaji mkubwa wa madawa hayo.

    Maxwell hakuona kama kulikuwa na tatizo, alimwamini Todd, walikuwa wakifanya biashara hiyo kwa miaka mingi. Akampa mzigo wa dola bilioni mbili kwa lengo la kuupeleka Afrika na kufanya biashara hiyo na kumpelekea pesa zake.

    Todd akachukua mzigo na kwenda nao Afrika. Hakutaka kumwamini mtu yeyote, alitaka kuusafirisha yeye kama yeye na kuufikisha nchini Msumbiji salama kabisa. Akawasambazia watu wake na kuondoka zake.

    Alitegemea kupata pesa zake baada ya wiki mbili ambapo biashara hiyo ingekuwa imefanyika kikamilifu lakini kitu cha kushangaza kabisa, mpaka wiki mbili zinakatika bado hakuwa amepata pesa hizo alizoambiwa kwamba angepata.

    Kuwaamini watu wengine kukamgharimu, alikuwa akiwasiliana nao kwenye simu lakini bado watu hao hawakuwa wakipokea, hilo lilimchosha sana, lilimfanya kufadhaika kwa kuwa mzigo ule haukuwa wake, alikopeshwa na kuahidi kulipa pesa hizo mara baada ya biashara kufanyika.

    Waafrika wakamuingiza choo cha kike, hawakumlipa pesa zake. Kila siku Maxwell alikuwa akimpigia simu na kumwambia kuhusu pesa zake, hakujua ni kitu gani alitakiwa kumwambia kwani kama angemwambia ukweli kuwa hakuwa amelipwa, angeonekana tapeli na muongo mkubwa.

    Baada ya kukatika mwezi, Maxwell akachoka kufuatilia, japokuwa walikuwa marafiki lakini kwenye ishu ya pesa akaamua kuuweka urafiki pembeni na kuanza kumdai kibabe.

    Hilo halikumshangaza Todd, alijua dhahiri kwamba kuna siku kitu kama hicho kingetokea, alichomwambia ni kuendelea kusubiri kwani bado aliendelea kuwakumbusha watu hao kuhusu pesa zake.

    Akili yake ikavurugika, miezi miwili bila kulipwa kukamfanya kupaniki na hivyo kupanga kusafiri mpaka nchini Msumbiji kwa lengo la kwenda kuwaambia watu wake wamlipe.

    Wakati yeye akipanga kusafiri kwenda huko, Maxwell hakutaka kumuacha, aliona kabisa kwamba alikuwa akienda kutapeliwa. Hakuangalia tena urafiki, hakuangalia ni kwa kipindi gani walikuwa pamoja, alichokifanya ni kutuma watu kwenda kumteka, wamtese sana na awahamishie kiasi cha pesa alichokuwa akidaiwa katika akaunti yake.

    Vijana wakaondoka mpaka nchini Msumbiji. Walipofika, wakamwambia Todd kwamba aandae meli ambayo hapo ingewachukua mpaka Nigeria ambapo huko ndipo walipopanga kufanya mauaji hayo.

    Hilo halikuwa tatizo kwani kabla ya wao kwenda huko, tayari meli yake ya mizigo ilikuwa imeandaliwa kwa kufanya kazi hiyo na kipindi hicho ilikuwa ikitoka Afrika Kusini. Ilipofika, wakaambiwa kwamba imefika na hivyo kilichotakiwa kufanywa ni utendaji kazi kuhakikisha kwamba wanampata mwanaume huyo.

    “Mtafuteni mtu anayeitwa Robson Mautinho, huyo ndiye mtu aliyepewa mzigo huo, hakikisheni mwanaume huyo anapatikana,” ilisikika sauti ya Maxwell kwenye simu.

    Hilo ndilo lililofanyika, kumpata mwanaume huyo halikuwa jambo gumu kwa kuwa alijulikana kutokana na utajiri wake mkubwa. Walipoonana naye, hawakutaka kumficha, walimwambia kuhusu mpango wao wa kummaliza mwanaume huyo.

    Kwa Mautinho ilikuwa habari njema kwake, alikuwa akidaiwa pesa nyingi na hakuwa na mpango wa kuumlipa mzee Todd hivyo alivyoambiwa kwamba watu hao walikuwa na mpango wa kumteka, kwake ilikuwa ni furaha tele kwani kama wangemuua ilimaanisha kuwa asingesumbuliwa tena na mwanaume huyo.

    “Hakuna tatizo. Ameniambia kwamba kesho atakuja tuzungumze,” alisema Mautinho.

    “Basi sawa. Waambie vijana wako wamteke, wamfunge sehemu na tutakuja kumchukua mtu wetu,” alisema kijana mmoja aliyeitwa Phillip.

    “Sawa.”

    Hilo ndilo lililofanyika, siku iliyofuata, wakati mzee Todd amefika mahali hapo, akaanza kuzungumza na Mautinho na baada ya kumaliza mazungumzo, akajikuta akizungukwa na vijana wa mwanaume huyo, cha kwanza kilikuwa ni kuwaua walinzi wake aliokwenda naye na yeye kufunikwa uso wake na kitambaa kilichokuwa na umbo la kikapu.

    Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alijaribu kuuliza lakini mwanaume huyo hakumwambia kitu chochote kile. Akaamrisha apelekwe kwenye chumba kimoja cha giza na kuhifadhiwa humo.

    Alichanganyikiwa, alijiona kugeukiwa, akilini mwake hakuhisi kabisa kama Maxwell ndiye aliyefanya hivyo, alichoamini ni kwamba Mautinho ndiye aliyeamua kuucheza mchezo ule ili amtapeli pesa zake alizokuwa akimdai.

    Usiku mzima alikuwa akilia tu, moyo wake ulimuuma mno, akahisi kabisa kwamba watu hao walikuwa wakitaka kumuua. Kufa kwake halikuwa tatizo, ila tatizo lilikuwa ni kuiga familia yake tu.

    Alikuwa na mke aliyeitwa Juddie na mtoto wake wa kike aliyeitwa Martha. Kwake, kufa pasipo kuiaga familia yake alihisi ni maumivu mazito mno.

    Katika chumba alichokuwa amewekwa, hakikuonekana kuwa kizuri hata kidogo. Kilikuwa kichafu kilichokuwa na harufu ya damu. Hakupigwa, hakufanywa lolote lile lakini kukaa ndani ya chumba kile kulimfanya kuhisi mateso makubwa kupita kawaida.

    Ilipofika usiku, mlango ukafunguliwa na wanaume wawili kuingia, wakamchukua huku wakiwa wamemfunga kitambaa machoni na kuondoka naye. Hakujua alipokuwa akipelekwa ila alijua kwamba hakukuwa sehemu nzuri na kwa katika kipindi hicho ilikuwa ni lazima kuuawa.

    Aliingizwa ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Baada ya dakika kadhaa, akashushwa na kupelekwa sehemu huku akiwa ameshikwa na watu wawili kushoto na kulia.

    Akapelekwa sehemu iliyokuwa na ngazi na kuanza kupandishwa. Mlango ukafunguliwa na kuingizwa ndani ya chumba kimoja na kuwekwa humo.

    Hapo, kwa mbali alisikia kelele za watu wakicheka huku wengine wakigongesheana glasi, kwa jinsi vicheko vilivyokuuwa vikisikika ilionyesha kabisa kwamba walikuwa kwenye maisha ya raha kupita kawaida.

    Baada ya dakika kadhaa, honi ikaanza kupigwa, haikuwa ya gari wala treni, aliposikia vizuri ilikuwa ni honi ya meli, hapo akagundua kwamba alikuwa ndani ya meli ambayo hakujua ilikuwa ikielekea wapi, ndani ya dakika chache akaisikia ikianza kuondoka mahali hapo.

    Alichokifanya ni kutoa kitambaa kile usoni mwake. Chumba kilikuwa na mwanga hafifu, alibaki akiangalia huku na kule, hakujua mlango ulikuwa mahali gani. Akasimama na kuanza kuzunguka huku na kule, bahati nzuri kwake akagusa kitu ambacho alijua kabisa kilikuwa ni kama kitasa cha kufungua mlango wa kutokea ndani ya chumba hicho.

    Humo ndipo alipotakiwa kukaa mpaka atakapofikishwa mbali kabisa, Nigeria ambapo alitakiwa kuuawa. Hakujua mahali alipokuwa, na wala hakujua mahali ambapo meli hiyo ilipokuwa ikielekea.

    “Mungu naomba uniokoe! Naomba uniokoe Mungu,” alisema mzee Todd ndani ya chumba kile. Moyo wake uliogopa na muda wowote ule alihisi kwamba angeuawa na watu waliokuwa wamemchukua.



    Maisha ya Sharifa yalibadilika na kuwa kama mtu aliyekumbwa na msiba mzito. Hakuwa na furaha, maisha yake aliyaona kuwa na giza kubwa mbele yake, moyo wake uliuma na kuuma, alilia usiku na mchana lakini machozi yake hayakuweza kumrudisha Bruno katika upeo wa macho yake.

    Kila siku ilikuwa ni lazima kwenda kwenye kaburi la mpenzi wake na kukaa huko, alikuwa mtu wa kulia huku muda mwingi akimlaumu baba yake kwamba ndiye aliyesababisha hayo yote.

    Bruno kutokuwa na pesa, kikabadilisha kila kitu, maisha yake yakaonekana kuwa si lolote na hata yule mpenzi aliyekuwa akimpenda aliambiwa aachane naye.

    Yote aliyokuwa akiyakumbuka yaliuumiza moyo wake, Sharifa aliumia kupita kawaida. Wakati mwingine alimuuliza Mungu kwamba kwa nini alizaliwa na baba yake, alitamani hata angezaliwa na mtu mwingine ambaye angemsapoti katika uhusiano wake na Bruno.

    Hakutaka kula, alikuwa kwenye maombolezo mazito. Mzee Jumanne hakujali, alichokuwa akikiangalia ni kuona mtoto wake akiachana na Bruno ambaye tayari muda huo alihesabika kama marehemu.

    Siku zikakatika, baada ya miezi mitatu, nyumbani kwa mzee Jumanne kukatokea ugeni kutoka jijini Nairobi, ugeni wa mzee Mohammed Olioh na ulifika hapo kwa kuwa walitaka kuzungumza mambo mengi kuhusu watoto wao.

    Mzee Olioh alikuwa mtu mwenye pesa zake jijini Nairobi. Alimiliki mabasi kadhaa yaliyokuwa yakifanya safari zake kwenda Tanzania, Uganda na mengine kwenda mpaka Rwanda. Alikuwa na pesa nyingi, aliheshimika kupita kawaida.

    Maishani mwake alibahatika kupata mtoto mmoja tu, aliyeitwa Rahman ambaye kipindi hicho alikuwa nchini Marekani akisomea sheria katika Chuo cha Kikuu cha Mississippi.

    Kipindi hicho Rahman alikuwa akijiandaa kurudi kutoka chuoni na kitu kimoja alichohitaji ni kutafutiwa mwanamke wa kuishi naye. Mtu ambaye alikuja kichwani mwa mzee Olioh ni msichana Sharifa aliyekuwa akiishi katika Kijiji cha Guolduvai kilichokuwa pembeni mwa bahari ya Hindi.

    Alimfahamu msichana huyo, alikuwa mrembo na baba yake alikuwa na heshima kubwa huko alipokuwa akiishi. Alichokifanya ni kuondoka na kuelekea huko. Alipofika, akaonana naye na kuanza kuzungumza naye.

    Alimwambia ukweli kuhusu mtoto wake aliyekuwa akitarajiwa kurudi nchini Kenya. Mzee Jumanne alipoambiwa hivyo, alishtuka, hakuamini kama mzee huyo angemfuata na kumwambia kitu kama hicho.

    Kumshawishi mtoto wake halikuwa tatizo, aliamini kwamba angekubaliana naye kwa sababu mtu aliyekuwa akimpenda, Bruno wakati huo alikuwa marehemu. Akamwambia mzee Olioh kwamba hakutakiwa kuhofia kitu chochote kwani yeye kama mzazi angezungumza na Sharifa na bila shaka msichana huyo angekubaliana naye.

    Mzee Olioh akaondoka kurudi jijini Nairobi huku akiwa na mategemeo mengi kwamba Sharifa angekubali na hivyo kuolewa na kijana wake.

    Huku nyuma, mzee Jumanne alikuwa na kazi kubwa ya kuzungumza na binti yake. Alijua kabisa kwamba alikuwa kwenye maumivu makali lakini hakutaka kuona akimkataa Rahman, ilikuwa ni lazima akubali kwa kuwa alitoka katika familia iliyokuwa na pesa.

    Sharifa alipoambiwa, akashtuka, hakuamini kama baba yake alifikia hatua ya kumtafutia mwanaume wa kumuoa. Hilo lilimuumiza mno moyoni mwake na bila kificho alimwambia baba yake kwamba hawezi kuolewa na mwanaume huyo.

    “Ila ana pesa! Anasoma Marekani!” alisema mzee Jumanne.

    “Siwezi kuolewa. Siwezi kuolewa na mwanaume yeyote baba,” alisema Sharifa huku akimwangalia baba yake.

    “Huoni kama umri unakwenda tu binti yangu?”

    “Kama unaona umri unakwenda, ungemkubali Bruno anioe, umeona amekufa ndiyo unakuja na kuniambia kwamba umri unakwenda. Kwa taarifa yako siolewi,” alisema Sharifa huku akimwangalia baba yake.

    Huo haukuwa muda wa kuogopa tena, alimwambia baba yake wazi kwamba hakutaka kuolewa na mwanaume huyo. Mzee Jumanne hakusema kitu, akakubaliana na mtoto wake na kuondoka.

    Alikwenda mpaka chumbani kwake, alivimba kwa hasira, hakuamini kama Sharifa angekataa kufanya kile alichotaka akifanye. Yeye ndiye alikuwa mzazi, sasa kwa nini amkatalie kuolewa na mwanaume aliyekuwa akimtaka?

    “Nitatumia mabavu kama mzazi! Si anakataa kwa hiari, sasa ataolewa kwa lazima,” alisema mzee Jumanne,.

    Alichokifanya ni kumpigia simu mzee Olioh na kumwambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari, alizungumza na binti yake na kukubaliana naye na hivyo walitakiwa kupanga tarehe ya kufunga ndoa kijijini hapo.

    Haraka sana mzee huyo alipoambiwa hivyo, akampigia simu kijana wake nchini Marekani na kumwambia kile kilichojiri kwamba msichana waliyekuwa wamemchagulia alikubali kuolewa naye na hivyo alitakiwa kurudi Kenya haraka sana mara baada ya kumaliza mitihani.

    “Amekubali?” aliuliza.

    “Ndiyo! Haikuwa kazi kubwa.”

    “Ila ni binti mzuri?”

    “Niamini! Siwezi kumchagulia kijana wangu binti mbaya! Ni mzuri kama mama yako alivyokuwa kijana,” alisema mzee Jumanne na kuanza kucheka.

    “Sawa. Nilindieni mke wangu! Nikija tu ni ndoa na kuendelea kufanya mambo yangu,” alisikika Rahman.

    “Sawa. Hakuna shida.”

    ***

    Safari baharini ilikuwa ikiendelea, mabaharia walikuwa wamelala kwa kuwa usiku mzima walikuwa wamekunywa pombe kali. Ndani ya meli hiyo iliyokuwa na watu kumi na sita ni watu wawili tu ndiyo ambao hawakuwa wamelala, nahodha, mzee Sam Maskovich na mzee Todd aliyekuwa katika chumba alichohifadhiwa.

    Meli iliendelea kukata mawimbi, hapo walipokuwa, hakukuwa na nchi kavu yoyote iliyokuwa ikionekana. Meli ilikuwa katikati ya bahari ikiendelea na safari yake.

    Macho ya Maskovich yalikuwa mbele kabisa, alikuwa akiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Alichoka mno lakini hakuwa tayari kulala, yeye ndiye alikuwa kila kitu katika safari hiyo.

    Wakati akiendesha meli hiyo, pembeni kulikuwa na chupa ya pombe ambayo ndiyo ilikuwa ikimuweka sawa kila alipokuwa akisikia usingizi. Muda ulizidi kwenda mbele mpaka pale alipokiona kitu kikiendelea juu ya maji.

    Hakujua ni kitu gani, haraka sana akachukua darubini na kuanza kuangalia kwa karibu, alichokiona ni mwanaume akiwa anaelea juu ya maji. Alishtuka, hakujua ni kitu gani kilikuwa kimeendelea mpaka mwanaume huyo kuwa hapo.

    Alichokifanya ni kuwaamsha wenzake na kuwaambia kile kiliichokuwa kikiendelea. Wote wakaamka na kuangalia mbele, kweli walimuona mwanaume akiwa anaelea juu ya maji.

    “Chukueni boya,” alisema mzee Maskovich.

    Boya moja la duara lililofungwa kamba ngumu likachukuliwa na kutupwa baharini, mwanaume mmoja naye akajitosa baharini na kuanza kumfuata mtu huyo kule alipokuuwa.

    Alipomfikia, akamshika na kuwaambia wenzake wavute boya kitu ambacho kilifanyika kwa haraka sana. Mtu aliyekuwa kwenye maji akaokolewa na kuwekwa ndani ya meli, alikuwa Bruno ambaye hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo.

    Tumbo lake lilikuwa kubwa, alikunywa maji mengi, ngozi yake ilikuwa laini sana huku ikiwa inateleza kutokana na muda mwingi kuwa ndani ya maji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Huduma ya kwanza kabisa waliyompa ni kumlaza kifudifudi na kuanza kuukandamiza mgongo wake kwa lengo la kuyatoa maji aliyokuwa amekunywa. Hiyo ilisaidia kwani baada ya kukandamizwa mara kadhaa, maji yakaanza kutoka, walipohakikisha kwamba wamemaliza, wakamchukua na kumpeleka kitandani kupumzika.

    Kila mmoja alikuwa na maswali mengi, walijiuliza kuhusu mwanaume huyo, alikuwa nani na alikuwa akifanya nini mpaka kuwa baharini hapo. Wengi wakahisi kwamba inawezekana alikuwa kwenye meli na wenzake na meli kuzama.

    Wakaangalia mahali pale ili kuona kama wangeweza kuwaona watu wengine lakini hawakufanikiwa. Walipomaliza kumpa huduma ya kwanza, wakamchukua na kumpeleka katika chumba alichokuwemo mzee Todd na kumuacha humo.

    Mzee huyo alishtuka, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alimwangalia kijana aliyekuwa ameletwa, hakuwa na fahamu, alionekana kuwa kwenye hali mbaya kwani hata kwa jinsi ngozi yake ilivyokuwa, ilionyesha alikuwa kwenye mateso makali ya kupigwa baridi.

    Akamsogelea pale chini alipokuwa na kuyasikiliza mapigo ya moyo wake, yalikuwa yakidunda kwa mbali sana hali iliyomfanya kugundua kwamba mwanaume huyo alikuwa hai.

    “Kwa nini wamemleta humu? Naye ni mateka au?’ alijiuliza mzee huyo huku akimwangalia Bruno aliyekuwa hapo chini.

    Hiyo ilikuwa siku ya kwanza, hakurudiwa na fahamu japokuwa alionekana kuwa hai. Vijana wa meli hiyo walikuwa wakiingia mara kwa mara ndani na kumwangalia kama alikuwa ameamka au la. Kila walipoingia, bado Bruno alionekana kuwa vilevile kama alivyokuwa kipindi cha nyuma.

    Walimuokoa kutoka baharini lakini baada ya kuona kwamba amechukua muda mrefu pasipo kurudiwa na fahamu, wakajadiliana ni kitu gani wafanye, wakakubaliana kwamba wamtupe baharini kwani tayari alionekana kuwa mzigo.

    “Tumtupe? Hakuna! Siwezi kukubaliana na kitu hicho,” alisema mzee Maskovich huku akiwaangalia watu hao.

    “Lakini amekufa!”

    “Bado mapigo yake ya moyo yanadunda.”

    “Lakini haamki! Inawezekana ndiyo hatua zake za mwisho kuishi ndani ya dunia hii,” alisema mwingine.

    “Hata kama. Tusubiri, kama kweli yeye ni wa kufa, atakufa na sisi kumtupa. Tumemuokoa, hebu tufanyeni lolote kuionyesha dunia kwamba tuna upendo wa ajabu,” alisema nahodha huyo maneno ambayo yaliingia kichwani mwa kila mtu.

    Siku nyingine ilipoingia ndipo Bruno akarudiwa na fahamu, akaanza kuwa kuyafumbua macho yake na kuangalia huku na kule. Alishangaa, alikumbuka kwamba mara ya mwisho alikuwa ndani ya bahari huku mawimbi yakimpeleka huku na kule na hatimaye kuzama, ila kilichotokea baada ya hapo, hakukijua.

    ”Nipo wapi?” lilikuwa swali la kwanza kabisa alilouliza mara baada ya kufumua macho na kumuona mwanaume mmoja akiwa amekaa pembeni yake.

    “Who the hell are you?” (wewe ni nani?) aliuliza mzee Todd. Aliposikia hivyo tu akajua kwamba mtu huyo alikuwa Mzungu, hivyo naye alitakiwa kuongea Kiingereza japokuwa kwa elimu yake ya kidato cha nne hakuwa akiifahamu vizuri.

    “Bruno!” alijibu huku akijitahidi kujinyanyua kutoka pale alipokuwa.

    “Bruno?”

    “Help me! I’m hungry...give me food, pleaseee...” (nisaidie! Nina njaa, naomba chakula tafadhali) alisema Bruno.

    “Want some food huh?” (unataka chakula huh?)

    “Yeah! Help me! Hunger is killing me,” (ndiyo! Nisaidie! Njaa inaniua) alisema Bruno huku akimwangalia mzee huyo kwa jicho lililokuwa la huruma kupita kawaida.

    Alichokifanya mzee huyo ni kusimama na kisha kuanza kupiga mlango kwa nguvu huku akiita kwa sauti. Hiyo ilisaidia, baada ya sekunde chache, mlango ukafunguliwa na kijana mmoja ambaye baada ya kuingia tu akamwambia kwamba kijana yule alizinduka na alikuwa na njaa kali.

    “Nakuja!”

    Kijana yule akaondoka, kule alipokwenda, akawaambia wenzake, vijana wanne wakaelekea kule huku wakiwa na chakula, walipofika, wakampa na Bruno kuanza kula kwa pupa kwani alihisi kama asingekula ndiyo ungekuwa mwisho wake.

    “Want some more?” (unataka kingine?)

    “Yeah!”

    Akaletewa, alikula na kula, baadaye akapelekewa soda na kunywa. Kidogo tumbo lake likapata nafuu na nguvu kuanza kurudi upya. Aliwaangalia vijana waliokuwa wamesimama mbele yake, hakujua ni wakina nani na hakujua ni kitu gani kilitokea.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Vijana hao wakamnyanyua na kuondoka naye mpaka kwa wenzao, wakamuweka kati na kuanza kumuuliza sababu ya kuwa baharini. Hakutaka kuficha, alisimulia kila kitu, historia yake iliwakera watu wote kwa sababu kuchukiwa kwa mtu kisa umasikini kilikuwa kitu kibaya sana.

    “Pole sana! Kwa hiyo huna pa kwenda?”

    “Sina! Kama mtaweza, naomba mnirudishe!” alisema Bruno.









    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog