Search This Blog

Thursday 27 October 2022

ANGA LA WASHENZI (2) - 3

 











    Simulizi : Anga La Washenzi (2)

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Usiku wa saa nne ...



    Simu iliita, ila Sarah alihofia kuipokea. Alikuwa kitandani pamoja na Kinoo, na ni dada yake ndiye aliyekuwa anapiga.



    Akamtazama Kinoo, hakuwa anatikisika. Alimpatia mgongo akitazama ukutani. Ila naye hakuwa amelala. Na alisikia simu hiyo ikiita. Lakini hakusema wala kufanya kitu.



    Sarah akakata simu. Kisha akatulia kwanza asiseme jambo kwa kama dakika mbili akisikilizia pengine Kinoo atafanya jambo. Hakufanya!



    Basi akafungua simu yake na kwenda moja kwa moja upande wa ujumbe. Akaandika kwa haraka akitumia vidole vyake vyepesi kumwonya Sasha asimpigie muda huo kwani yupo na Kinoo.



    Kisha akatuma tena ujumbe wa pili kumuuliza anataka nini usiku wote huo?



    Akangoja kwa sekunde tano ujumbe kuingia. Sasha akianzia mbali kwa kumuuliza nini kinakawiza zoezi lao la kuungwa kundini. Je watu wao wametingwa na kazi gani?



    Sarah akasonya, kisha kwa pupa akabofya kioo cha simu kumwambia dadaye mbona hilo alishamwambia kuwa hajui, na Kinoo amekuwa mgumu kujipambanua?



    Sasa Sasha akaenda kwenye lengo lake, akamwomba dada yake amweleze makazi ya watu wanaohusika na Kinoo. Sarah akamwambia kuhusu Miranda tu, maana ndipo anapopafahamu. Kisha asipoteze muda akamuaga dada yake na kuzima simu kabisa.



    Akalala baada ya kuchoma dakika kadhaa akiwaza nini Sasha amepanga kufanya. Akapotelea kabisa usingizini.



    Ila Kinoo bado alikuwa macho! Alivuta tena dakika kadhaa alafu akavuta simu ya Sarah na kuiwasha. Akatia nywila na kubonyeza OK. Simu ikakataa kufunguka.



    Akajaribu tena kuweka nywila, akabonyeza OK, majibu yaleyale, simu imegoma! Kumbe Sarah alibadilisha nywila ya simu yake. Kinoo akalalama. Akairejesha simu alipoikuta kisha akaendelea kuwaza.



    Ni nini mwanamke huyu alikuwa anafanya nyuma ya mgongo wake? Tena yeye na dada yake?



    Haki alipata shaka. Na aliona alichukulie hatua hilo.



    Ila atawahi kabla ya madhara kutokea? Hili ni la mimi na wewe kujiuliza.



    **



    Saa moja kasoro asubuhi...



    Baada ya kupata kifungua kinywa, Lee alienda kukutana na Nieng, Shifoo Nieng, aliyekuwa ametulia ndani ya bustani aki-meditate kama afanyavyo kila siku kuanzia majira ya saa kumi na moja alfajiri.



    Alipofika hapo, akatulia na kungoja. Alishaambiwa zoezi hilo la Nieng huwa linakoma saa moja kamili hivyo alijua hatakaa hapo kwa muda mrefu kungoja.



    Hakukosea, muda si mrefu akaungana na Nieng ambaye alimtaka waende kufanyia maongezi yao ndani. Ofisi yake ilikuwa imekaa mbele ya dojo, ndani hakukuwa na kiti wala meza, bali mito midogo chini ambayo ndiyo hutumika kama kiti.



    Wakaketi humo katika mtindo wakaao wanafunzi wa sanaa ya mapambano ndani ya dojo kisha maongezi yakachukua nafasi. Nieng akaanza kwa kumuuliza Lee kwanini alimuua Chong Pyong.



    Lee akaeleza kila kitu. Hakuhusika na kumuua Chong Pyong. Amesingiziwa tu akiwa katika harakati za kumtafuta Chen Zi.



    Nieng akastaajabu kusikia Chen Zi. Akamuuliza Lee ana mahusiano gani na Chen Zi? Lee akalaghai kuwa ni rafiki. Alihofia kusema kuhusu nyaraka ile aliyokuja kuitafuta.



    Basi Nieng akamwambia Lee kuwa Chen Zi aliuawa na familia ya Li. Wala hakuwa amezidisha madawa kama inavyosemekana. Na sababu kubwa iliyopelekea Chen Zi kuuawa ni kuhisiwa ana mahusiano na Wu family.



    Nieng akaenda mbali akamwambia Lee kuwa kuna mengi sana yanatukia ndani ya China, watu kuuawa na wengine kupotea. Familia ya Li imekuwa yenye nguvu mno hapa karibuni, na kama wasipofanya jitihada basi wataifutilia mbali kabisa familia ya Wu.



    Mpaka hivyo wanapoongea, tayari wameshapokonywa jiji la Hongkong. Na hata Shanghai imekuwa matatani. Haitachukua pia muda mrefu kuwa chini ya Li, kama vile Beijing.



    Ajabu ni kwamba, japo familia ya Wu inaungwa mkono na serikali, bado tu Li wanawasumbua. Inasadikika kuna baadhi ya vibaraka ndani ya serikali, na wao wamekuwa wakitoa taarifa zote kwa Li family.



    Sasa kuwadhibiti inabidi liwe kipaumbele chao kikubwa. Kuna baadhi ya viongozi inabidi wauawe, kuna baadhi ya watu inabidi wapotezwe.



    Japo wanawajua watu hao, bado kazi imekuwa ngumu! Ila Nieng akaendelea kwa kusema sasa amepata matumaini. Anaamini Lee atakuwa mwarobaini wa tatizo hilo.



    Anaamini kwenye uwezo wake, atamkabidhi jeshi na orodha ya watu wa kuwamaliza.



    Kwa Lee halikuwa gumu hilo. Akaliafiki. Ila shida kidogo ilikuja pale alipoambiwa mtu wa kwanza wa kummaliza.



    Alikuwa ni makamu wa raisi!



    Nieng akamwambia Lee kuwa makamu huyo wa raisi ndiye kikwazo cha kwanza katika mambo yao. Yeye ndiye amekuwa kibaraka wa Li family kinyume kabisa na serikali ilivyo. Amekuwa akichukua taarifa na mipango yao yote na kuifikisha mezani mwa familia ya Li.



    Yeye ndiye ambaye amekuwa kiungo kikubwa cha Wu family kudhoofika ndani ya nchi na hata huko ulimwenguni.



    Lee alitakiwa kummaliza mwanaume huyo pasi na simile hata kidogo. Ahakikishe habaki na uhai na hata kama kutakuwa na uwezekano basi familia yake nayo itokomee kisibaki kitu.



    Hiyo itakuwa salamu mwanana kabisa kwa familia ya Li. Na kwa namna iliyo kubwa itawapa kimuhemuhe na joto miilini.



    Ila Nieng akaenda mbele zaidi kwa kumwambia Lee kuwa kazi hiyo haitakuwa nyepesi kabisa maana makami huyo mbali tu na kulindwa na serikali kama afisa mkubwa, pia analindwa na ulinzi binafsi unaopewa nguvu na familia ya Li.



    Inabidi awe makini sana. Ahakikishe hakuna kosa lolote linalotokea.



    Basi Lee baada ya kupewa maelekezo hayo pamoja pia na anwani ya makazi ya makamu wa raisi akaenda kuonana na watu atakaofanya nao kazi. Walikuwa wengi mno, kadiri kama watu alfu mbili wenye mafunzo.



    Ila kwasababu alitaka wanaume waliokomaa kimafunzo ili kazi ikawe rahisi na kwa ufanisi, basi akafanya 'interview' kidogo akisaidiwa na Nieng, wanaume wale wakapewa fursa ya kupambana wenyewe kwa wenyewe, mwishowe Lee akachagua watu watano wa kazi.



    Akawataka waonane baadae usiku kwa ajili ya kuyapanga. Yeye akatoka kwenda kukagua makazi yale ya makamu wa raisi ambayo alikuwa amelenga kufanya tukio kesho yake.



    Ilikuwa ni umbali uliomgharimu masaa maana kiongozi huyo alikuwa anakaa Beijing na si Hongkong. Alipofika huko akatumia tu macho yake kuchambua eneo, kwa dakika kumi, kisha akayeya.



    Baadae usiku kama alivyopanga miadi akakutana na wale watu wake watano wa kazi, akaanza kuwapanga namna ya kuenenda. Ila wakiwa maongezini, shifoo Nieng akaingilia kwa kumhitaji Lee dakika chache.



    Akamweleza kuwa mambo yamebadikika. Amepata taarifa kuwa kiongozi huyo hayupo nchini, amesafiri kikazi kwenda Mongolia, nchi jirani na China kwa upande wa kusini. Hivyo basi inabidi aende huko kufanya kazi, na pia itakuwa wepesi zaidi kwa maana ulinzi wake utakuwa hafifu.



    Basi kwa maelezo hayo, Lee akaona ni kheri akaenda mwenyewe kutekeleza hiyo kazi. Ila Nieng akamwambia kuwa taarifa juu ya wapi anakaa huko Mongolia, haijapata. Ni jukumu la Lee sasa kuitafuta atakapokuwa huko.



    Kumbuka ilikuwa usiku. Lee akiwa peke yake baada ya maongezi hayo alijikuta anaugawa muda wake wa kupumzika kwa kufuatilia mitandaoni ziara ya kiongozi huyo huko Mongolia.



    Akagundua alienda kufungua balozi yao huko na pia miradi kadhaa. Kwa makadirio akaona kiongozi huyo atadumu ndani ya nchi hiyo kwa siku zisizozidi mbili. Hivyo basi kesho anatakiwa kumaliza kila kitu.



    Atatumia njia za vichochoro kuzama ndani ya Mongolia, mosi kwasababu ya usalama. Anaenda kufanya mauaji huko, hakutaka kubakiza harufu yoyote maana endapo akitumia njia rasmi anaweza akatiliwa shaka na hata atakapotafutwa ikawa rahisi kupatikana.



    Pili, hakuwa na nyaraka stahiki.



    **



    Baada ya Miriam kukaa nje kwa muda mrefu, shangazi yake alimfuata na kumjulia hali. Alikuwa na uso uliopooza na macho yanayohakisi mawazo kichwani.



    Shangazi akamuwekea mkono begani na kumuuliza kama ni lile lile ndilo linalomtatiza. Miriam akatikisa kichwa kuafiki. Alikuwa anamuwaza Jona.



    Hapa siku za karibuni hakuwa na furaha hata chembe maana hakuonana na mwanaume huyo. Na zile taarifa za kuhusishwa na kumuua Kamanda na pia tena kutoroka jela, zilimtia kimuhemuhe sana.



    Alikuwa anahofia sana maisha ya Jona. Aliona si mtu anayestahili hayo anayoyapitia kwa namna alivyo mtu wa kujali. Na hata pasipo kusita, kwa moyo wake wote, alikuwa anaamini Jona hakuhusika na mauaji ya Kamanda kwa namna yoyote ile. Japo hakuwa anajua kuna mchezo gani nyuma ya pazia.



    Anajiuliza sana Jona yupo wapi. Na ana hofu kama mwanaume huyo atakuwa mzima wa afya kwani kama ingelikuwa yu mzima, anaamini angelikuja kumtembelea na kumjulia hali.



    Ila hofu haijengi.



    Hofu yanyima kula hata kunywa. Yanyima amani. Na hichi ndicho Shangazi yake alikuwa anamweleza. Kuendelea kuwaza namna ile hakutamfanyia chochote chema zaidi ya kumuumiza.



    Akamsihi waende ndani. Na kama chambo kitaungua, basi watasikia tu harufu. Kama Mungu alivyomlinda yeye alipokuwa mikononi mwa wale wadhalimu, basi ndivyo atakavyomlinda na Jona kama vile wanavyomwombea kila uchwao.



    Wakaenda ndani.



    Basi kama ni kheri hii ilikuwa ya asubuhi. Kwenye majira ya saa mbili asubuhi mlango ukagongwa shangazi akaenda kufungua. Akamkuta Marwa mlangoni.



    Akapatwa na hofu. Hakuwa anamtambua mtu huyo. Akiwa amekunja sura akamuuliza Marwa nini anataka, Marwa akamtaka kwanza amwambie kama hapo ni makazi ya Miriam. Alipomjibu akamweleza kuwa ametumwa na Jona kufikisha salamu.



    Basi shangazi akamruhusu Marwa kuingia ndani na kumkutanisha na Miriam. Akamweleza kuwa Jona anamsalimu sana. Alikuwa hoi na pindi alipopata ahueni akamuulizia na kumwelekeza aje kumwona.



    Miriam akafurahi sana. Akataka kumwona Jona ila Marwa akamwambia haitawezekana kwa sasa. Na ahakikishe hilo jambo linakuwa siri kupita kiasi. Jona atakuja kumtembelea yeye mwenyewe atakapotengemaa.



    Marwa hakukaa sana, akaaga aende zake. Ila Miriam akamtaka angoje kwanza. Akaingia ndani na kutoka na karatasi na peni, akaandika ujumbe na kumkabidhi Marwa ampelekee Jona. Akamsisitizia sana ujumbe huo ufike mikononi mwa Jona.



    Marwa akamuahidi. Kisha sasa akaenda zake.



    **



    Saa tatu usiku ...



    Jona alitabasamu punde aliposoma ujumbe wa Miriam. Hakika ulimgusa moyo wake na kumpa ahueni sasa ya kuwa mwanamke huyo ni mzima wa afya maana alikuwa anahofia huenda wakina Nyokaa wakawa wamefanya jambo kumdhuru.



    Bado hakuwa na afya tenge, ila angalau kwa siku moja ya kutumia antidote, aliweza kutazama, kutambua na hata kunena. Pia kujisogeza huku na pale japo kichovu.



    Alifurahi sana kumwona Marwa ni mzima. Kila saa alikuwa anamkumbatia kwa kutoamini. Alimshukuru pia na Miranda kwa kazi waliyofanya. Hata kabla hajaelezwa alikuwa anafahamu ni kazi kubwa imefanyika mpaka yeye kuwa pale.



    Ila kutokana na hali yake bado kuwa si nzuri, Miranda na Marwa hawakuona kama ni muda sahihi wa kuanza kumchanganya mwanaume huyo mapema yote hiyo. Bado alikuwa anastahili kupumzika, tena sana.



    Ndo maana hata huu ujumbe wake alikuja kuusoma saa hizi japo uliletwa kwa muda mrefu sana maana ndo muda aliofungua macho.



    Marwa akamletea chakula na kisha akakaa naye kwa muda kidogo wakiteta. Akamuuliza kuhusu Miriam. Jona akamweleza kwa ufupi.



    Marwa hakutaka kumpeleleza sana. Akatoa vyombo na aliporejea akamkuta Jona amekwisha lala. Antidote zilikuwa zinamchosha.



    Basi akakaa pembeni yake na kuchukua ile karatasi ya Miriam na kuisoma. Akajikuta anatabasamu. Miriam alikuwa ana hamu sana ya kumwona Jona. Na akiapa siku hiyo itakuwa ya furaha sana kwake.



    Marwa akaikunja vema hiyo karatasi, kisha akaiweka chini ya mto wa Jona. Akatoka chumbani.



    Ila siku hii bado haikuwa imekwisha. Ndiyo kwanza ilikuwa imeanza. Kabla ya jua la kesho kuchomoza, kuna misheni mbili kubwa zilikuwa zinatakiwa kumalizika.



    Mosi, Sarah kutambua kama Jona anaishi kwa Miranda. Na pili, Lee kummaliza makamu wa raisi ndani ya nchi ya Mongolia.



    Litakalojiri, si mimi wala wewe anayejua. Ila ni wazi kiti kilikuwa cha moto.



    Basi na muda ukasonga kama ilivyo ada. Ilipogonga saa nne ya usiku, mtu mmoja akazama ndani ya jengo la Miranda. Mwanaume huyu alikuwa amevalia suti nyeusi na barakoa nyeusi usoni.



    Ni ajabu mtu kuvaa suti katika kazi kama hizi. Mtu huyu alijibana nyuma ya ukuta, akatazama usalama. Kulikuwa ni kimya na sebuleni alikuwa amekaa Miranda na Marwa wakitazama televisheni.



    Huku vyumbani kote kulikuwa gizani. Na kule getini mlinzi alikuwa amejilaza kwenye kiti chake akichokonoa meno. Hakuwa anajua kinachoendelea.



    Mwanaume yule mwenye barakoa akajongea dirisha la kwanza, akachungulia. Akatoka hapo akaizunguka nyumba kwa nyuma, kisha akatazama tena dirisha lingine.



    Mara akasikia sauti ya kitu kikitembea. Akajibania kwenye ukuta kwanguvu, mkono wake wa kuume akiushikizia kiunoni ambapo aliweka silaha, bunduki ndogo.



    Alipotulia hapo kwa sekunde nne, akagundua hamna hatari yoyote. Basi akaendeea tena lile dirisha na kuchungulia. Chumba hicho ndicho alalacho Marwa. Tayari ameshatazama anacholala Miranda, na anacholala Jona, ila hakugundua kitu. Kulikuwa na giza na pupa zake hazikumfanya akaona jambo zaidi tu ya mwili uliofunikwa nusu shuka.



    Basi alipotoka tena hapo akawa amebakiza sehemu moja tu. Matumaini yake yote yakawepo hapo kuwa ndiyo itakuwa mahali penye kitu wanachokitaka.



    Ila hakujua chumba hicho kilikuwa ni cha mfanyakazi wa ndani. Na msichana huyo hakuwa amelala. Ni muda mfupi ametoka kuoga na kumbe ndiye yeye ambaye vishindo vyake vilisikika hapo kabla.



    Basi bwana yule mwenye barakoa, akachungulia. Akameona mwanamke huyu akijifuta. Napo akagundua si penyewe. Ila sasa akashindwa kutoka hapo upesi. Macho yake yaliganda kwenye mwili wa mwanamke ulio uchi.



    Japo ilikiwa ni giza, akatumbua macho aambulie chochote kitu.



    Akachukua hapo kama sekunde sita, msichana akagundua jambo. Akageuza shingo yake kutazama dirishani, mwanaume yule mwenye barakoa akajificha upesi.



    Hakufanikiwa kumwona.



    Mwanaume yule akanyata na kurudi kule alipojibania mara ya kwanza alipozama ndani. Akatulia hapo kwa sekunde kama nne tena, kisha akaanza kurejea zoezi lake kwa mara nyingine ili ahakiki kabla hajaondoka na jibu la mtu wanayemtafuta hayupo hapo.



    Akapitia dirisha la kwanza. Salama salmin. Akiwa kwenye dirisha la pili, akasikia vishindo vikubwa! Haraka akajivuta na kujibana kwenye kona ya mbele.



    Alisimama hapo kwa tahadhari sana. Na vishindo vile alivyosikia havikukoma, vikaendelea kujita kumfuata. Akatambua wazi kuwa ajaye ni mlinzi.



    Sasa zoezi likawa linaendea kubadilika. Hakutaka kuacha alama yoyote hapa ila ikaanza kuonekana itashindikana maana endapo mlinzi huyu akimwona, basi hatoweza kumwacha hai.



    Vishindo vikaendelea kusonga. Miguu hii ya mlinzi ilikuwa inaburuza haswa. Sijui alijifunzia wapi ulinzi huyu bwana. Alipiga hatua nne zaidi, na hamaki akajikuta mikononi mwa mvamizi!



    Kilichosikika hapo ni mtu akigugumia tu, na mlinzi akawa amemaliza habari yake. Akatuliwa chini taratibu na yule jamaa sasa akawa yupo huru zaidi. Sasa akatazamia madirisha yaliyobakia.



    Akanyata na kunyata. Akatazama lile dirisha la chumba anacholala Jona, hapo akasita kidogo. Akajiwa na fikra. Kamaa kule sebuleni yupo mwanaume na mwanamke, na kile chumba kingine yupo mwanamke, hichi yupo nani?



    Kabla hajaacha dirisha hili, akachomoa kurunzi yake ndogo na kumulika ndani. Mwanga wa kurunzi hii ulikuwa mdogo, kaduara kake ka mwanga kalikuwa chenye ukubwa wa sarafu ya mia mbili.



    Akaangaza usoni mwa mtu yule aliyekuwa amelala, akagundua ni Jona! Akajikuta anatabasamu.



    Ila sasa alivyo mjinga, asiondoke akataka kwenda kwenye lile dirisha la msichana wa kazi akatazame tena. Basi akanyata na kufika hapo, akachungulia. Hakumwona mwanamke.



    Akazubaa hapo kwa sekunde kama tano akiangazaangaza maana ilikuwa giza. Ila punde akasikia sauti ya mguu ukiburuza. Akaangaza upesi. Kidogo akatokea mtu konani, alikuwa ni Miranda!



    Mwanaume yule mwenye barakoa akatupa risasi mbili. Miranda akawahi kujificha ila alikuwa tayari amejeruhiwa. Bega lake la kushoto lilikuwa linachuruza damu!



    Bwana yule mvamizi asipoteze muda akadaka ukuta na kurukia nje. Miranda naye akajaribu, ila maumivu ya mkono yakampatia shida. Japo alifanikiwa, ila hakuwa ndani ya muda. Kwa mbali akaona gari likiyoyoma kwa kasi!



    Akarudi zake ndani. Sebuleni akamkuta msichana wa kazi ma Marwa. Haraka wakampatia huduma ya kwanza kwa kumtia dawa ma kumfunika jeraha. Uzuri risasi haikupenya ndani, bali iliparaza bega na kwenda zake.



    Wakiwa wanampatia huduma hiyo, msichana wa kazi akaeleza namna alivyotilia shaka kwamba kuna mtu nje. Na zaidi hisia zake hizo zikathibitishwa na sauti ya mguno. Kumbe ndo ile iliyokuwa ya mlinzi.



    Hapo Miranda akapata maswali. Ni nani yule mtu na alikuwa anafanya nini. Kwa akili ya kawaida, baada ya kujadili, wakagundua watakuwa ni watu wa Sheng. Na hapo walikuja sababu ya kumtafuta Jona ndiyo maana walikuwa wanapeleleza dirishani.



    Sasa wakapata shaka. Kama watu hao watakuwa wamegundua kuwa Jona yupo hapo, watafanya nini?



    **



    Ngo! Ngo! Ngo!



    Shao akafungua mlango. Uso kwa uso akakutana na kijakazi wake aliyevalia suti. Akamkaribisha ndani na wakaketi sebuleni. Kijakazi yule akampa mrejesho wa kazi waliyotoka kufanya.



    Amemwona Jona, yupo mikononi mwa kijakazi wa BC. Ila akaeleza pia ameonekana alipokuwa akifanya kazi hiyo. Hapo Shao akaghafirika!



    Akalalama kazi imeharibika kwani watu hao watachukua tahadhari kutokana na tukio hilo. Hapo hamna kazi yoyote iliyofanyika!



    Akamtaka kijakazi huyo aende zake amwache mwenyewe afikirie cha kufanya. Kijakazi akaenda zake. Shao akafikiri sana. Mwishowe akaona sasa cha kufanya ni kuanza kupanga mipango ya kuwashambulia wakina BC maana ameshajua Jona yupo mikononi mwao.



    Akawaza kama kazi hiyo anapaswa kumshirikisha Sheng, akaona haina haja. Ataifanya na kuimaliza mwenyewe.



    **



    Hakuwa amepumzika siku hii nzima. Kutwa allikuwa kwenye safari, na hata usiku huu hakuwa mtu wa kupumzika bali yupo kazini.



    Tayari Lee ameshazama ndani ya Mongolia, kitambo tu. Na tayari alishasonga eneoni ambapo anatakiwa kufanya tukio. Eneo ambapo makamu wa raisi wa China yupo kimalazi.



    Eneo hilo lilikuwa linalindwa na watu lukuki hapo nje. Na pia huko ndani walikuwa watu kadhaa wakienda huku na kule.



    Lee akatoa hadubini na kupekua eneo hilo kila pande. Alikuwa umbali wa kama kilomita mbili na nusu. Aliporidhika na alichokipata kwa hadubini, akairejesha begini alafu akavalia barakoa.



    Mwanaume akazama kazini.





    Ni mwendo wa dakika chache kuwasili ndani ya eneo la tukio kwa namna alivyokuwa anatembea. Alitulia kidogo na kuangaza, eneo lilikuwa linalindwa haswa. Akapiga hesabu kama anaweza kufanikiwa kuingia ndani pasipo kuleta taharuki.



    Ilikuwa ngumu. Kila mahali palitapaka walinzi na taa nazo zilikuwa zinaharabu mahesabu. Ilikuwa ngumu kujibanza ukiwapo ndani.



    Basi akawa mvumilivu kidogo, akatazama wale walinzi wanaozunguka kwa nje na kutambua mienendo yao. Akasogelea mti uliokuwapo karibu, akakwea kwa haraka alafu akapekua tena mazingira.



    Akavuta subra. Kisha kidogo akatoa kakifaa kwenye mkoba wake, kakitu kama kafilimbi rangi nyeusi, akakiweka mdomoni na kukipuliza kwanguvu. Ndani yake kulikuwa na kakipini kadogo chembamba.



    Kaliruka na kumkita mlinzi mmoja shingoni kwa usahihi wa hali ya juu! Yule mlinzi akaguna akikunja sura. Kabla hajanyofoa kapini hako shingoni, akajikuta amedondoka chini na kupoteza fahamu!



    Lee akataka kurukia ndani, ila akawahi kusita. Alimwona mlinzi mwingine akija upande ule aliokuwa amelala mwenzake chini. Akafika na kustaajabu. Haraka Akaweka kidole chake sikioni akiminyia kufanya mawasiliano na wenziwe.



    Ila kabla hajafungua kinywa, chap! Kipini kikamchoma na yeye shingoni, akadondoka chini baada ya sekunde mbili tu!



    Sasa Lee akajitupia ndani, akafikia kwa kujituliza na sarakasi. Kisha upesi akaikusanyia miili ya wale watu ukutani, akaifunika na shuka jeusi alilotoa begini, ikaonekana kama kamlima fulani kadogo.



    Alafu haraka akasonga akifuata mlango akichomoa kapini fulani ambacho alifungulia kitasa na kuzama ndani.



    Kulikuwa kimya.



    Alitulia kwa sekunde kama nne akiwaza namna ya kufanya na pia akiskizia huko nje kama wamebashiri lolote. Zilipokwisha sekunde hizo nne, akajongea taratibu.



    Ndani kulikuwa na mwanga lakini ilikuwa ngumu kubashiri kama watu wamelala ama lah maana palikuwa kimya na kwa wakati huohuo taa zikiwa zinawaka kila eneo.



    Kazi ikawa kwa Lee kutambua ni wapi alipo mtu anayemlenga. Hapa alihitaji kuwa mwangalifu na msikivu mno. Alipotulia kwa sekunde kama tatu, kazi ikawa nyepesi kuliko alivyodhani.



    Alisikia sauti ya mtu bafuni akisafisha koo. Bila shaka akamtambua kama ndiye mlengwa wake. Basi akanyata kufuata bafu. Akatulia hapo kidogo, kama baada ya dakika hivi, mlango wa bafu ukafunguliwa.



    Akatoka bwana mmoja wa kichina, ana kiwaraza hafifu na mwili wake umemomonyoka kizee. Basi haraka Lee akamminya bwana huyo na kumweka ndani ya uwezo wake. Hata kelele hakuwa anaweza kupiga!



    Ila alipomtazama ... alipomtazama akagundua hakuwa makamu wa raisi! Akastaajabu. Basi akiwa amemminya bwana huyo, akamuuliza yeye ni nani? Na makamu wa raisi yupo wapi?



    Bwana yule akiwa amebanwa na hofu kuu, na akiwa amebanww mbavu katika namna ambayo hawezi kuongea kwanguvu, akasema yeye ni msaidizi wa makamu, ila akasema hajui makamu alipo!



    Lee akaghafirika maana alijua wazi bwana huyo anaongopa. Ni lazima tu atakuwa anajua mlengwa wake alipo. Akamminya zaidi, ila bwana yule hakuwa tayari kusema!



    Lee akamziraisha alafu akamlaza chini, akaenda kukagua vyumbani. Akatazama chumba cha kwanza, humo akakuta wanawake wawili wembamba wakiwa wamelala. Ina maana wanawake hawa walikuwapo hapo kumhudumia msaidizi yule wa makamu au makamu mwenyewe.



    Lee akaenda chumba cha pili. Taa ilikuwa inawaka ndani, huenda makamu akawa hajalala, akawaza. Basi cha kufanya akagonga mlanga mara mbili na kuskizia.



    Akasikia sauti nzito ikimwamuru aingie ndani. Akafungua mlango na kuzama. Kutazama, uso kwa uso na mlengwa wake! Alikuwa mwanaume mwembamba mwenye makadirio ya miaka sitini ya mwishoni ama sabini za mwanzoni.



    Usoni alikuwa amevalia miwani ya macho. Nywele zimekuwa kama za kahawia kwa mvi za mbali. Alikuwa amevalia kaushi nyeupe na bukta fupi. Amekalia kakiti kadogo kalichopakana na meza ya saizi yake. Juu ya meza hiyo ndogo kulikuwa kuna karatasi kadhaa nyeupe, na diary yenye kava gumu jeusi.



    Basi ile kutazamana, bwana makamu akapatwa na woga sana! Akatazama kando upesi kama mtu atafutaye silaha, ila upesi akatupiwa pini shingoni, akanyeta. Punde akaanza kuona mbilimbili, mara kichwa puh mezani!



    Lee akafunga mlango na kumsogelea. Akakusanya kila kitu chake na kisha akatengua shingo kumfanya mfu! Akatoka na kwenda kumkuta yule bwana aliyemziraisha. Naye hakumwacha salama, akamtengua shingo kumfanya mfu!



    Sasa akabakia na kazi ya kutoka mule ndani. Pengine inaweza ikawa kazi kubwa kuliko kuingia, akatazama kushoto na kulia, wakapita walinzi wawili. Alipoona mazingira murua, akatoka chap kwenda ukutani.



    Ila alipofika na kabla hajatoka, mlinzi mmoja akamwona! Akagutuka. Haraka mlinzi akachomoa bunduki yake ndogo na kuifyatua risasi mara mbili! Ila bahati haikuwa kwake, haikumpata mlengwa!



    Lee akachumpa nje na kuanza kukimbia kwa kasi. Wale walinzi nao wakajikusanya na kumkimbiza Lee ambaye alikimbilia huko msituni.



    Walitoka hapo kama wanaume kumi. Wote wakiwa wamebebelea silaha. Ila hawakufua dafu msituni humo Lee akafanikiwa kuwapotea na kwenda zake salama salmini.



    Alikuwa ameegesha pikipiki kubwa mahali, akaiwasilia na kuitia moto, safari ikashika hatamu. Hakutaka hata kubaki Mongolia kabisa, alikuwa amelenga siku hiyohiyo kutoboa mpaka China.



    Kazi aliyotumwa alikwisha itekeleza. Tena kwa ustadi mkubwa.



    Haikuwa hata na haja ya kuitangaza kwani jua likipanda kesho yake tayari habari zitakuwa zimeshasambazwa na vyombo vya habari kuwa makamu wa raisi na msaidizi wake wameuawa huko nchini Mongolia na mtu asiyejulikana!



    **



    Saa tatu asubuhi ...



    Shao alikuwa na kikao kifupi na vijakazi wake kumi. Walikuwa katika mpango mkakati wa kufanya jambo, tena kubwa na lenye madhara.



    Vijakazi wote walikuwa tuli wakimsikiliza mkuu wao, na yeye Shao akatumia huo mwanya kueleza kinagaubaga jambo la kufanyika. Naam. Hakutaka muda upotezwe, bali uhai wa adui.



    Alichotaka ni kuletewa kichwa tu. Haijalishi risasi ngapi zitatumika ila jambo litekelezeke, yupo tayari kugharamia kila risasi kugharamia kila risasi itakayopotea kwenye uwanja wa vita.



    Basi na wasipoteze muda, kikao kikafungwa na wakaahidiana kukutana tena hapo majira ya saa sita usiku.



    **



    Saa tatu usiku ...



    Gari aina ya Subaru iliyobebelea wanaume watano ilisimama na kuzimwa kabisa. Wanaume hao wakateta kidogo kisha wakatoka wote garini isipokuwa dereva.



    Wote hawa walikuwa wamevalia mavazi meusi na kofia za soksi kichwani. Na hata kwa kuwatazama upesi ungeligundua walikuwa wamefichilia silaha za moto.



    Wanaume hawa wakatokomea dereva akiwatazama mpaka wanaishilia. Walikunja kona kama mbili kufika mahali walipokuwa wanaelekea.

    Wakaruka ukuta, na kuzama ndani.



    Kulikuwa ni makazi ya Miranda!



    Kimya.



    Wakagawana pande. Wakachomoa na silaha zao kuziweka vema viganjani kwa ajili ya kazi. Wawili wakaendea kibanda cha mlinzi, kutazama hamna mtu.



    Kwa ukimya wa hali ya juu, wakasonga kuufuata mlango. Na wale wa nyuma na wao wakasonga mlango wa ziada. Wakatulia hapo.



    Ndani taa zilikuwa zimewashwa. Na sauti moja ya kike ilikuwa inasikika kwa mbali kuashiria kuna mtu humo.



    Basi wale wavamizi, wakahesabu mpaka tatu, wakazama ndani kwa kuvunja mlango kwa mateke yao mazito.



    Wakaangaza huku na kule. Hamna kitu! Ila bado ile sauti ya kike ilikuwa inasikika.



    **



    Wakatazamana kwa duwazo. Kisha wakiwa wamebebelea silaha zao, wakasonga kwenda mavyumbani. Wakapekua kivita, hawakuona kitu! Ila mule chumbani sauti ilipokuwa inatokea, wakaukuta mdoli kitandani.



    Aaagh!



    Mdoli ulikuwa umerekodiwa na kuachwa hapo ucheze wenyewe. Wote wakakusanyika na kuutazama mdoli huo. Ulikuwa ni wa kike, nywele ndefu za kupendeza na macho makubwa yenye nyusi ndefu.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nyuma ya mgongo wake alikua ana kitu fulani kigumu. Wakamfunua nguo na kumtazama. Ilikuwa spika! Basi bwana yule aliyemshikilia mdoli huyo akasonya na kumminya huyo mdoli kwa mkono wake mpana.



    Yule mdoli akasinyaa na kuvunjika. Ila baada tu ya sekunde nne, wakaanza kukohoa mno. Kumbe yule mdoli alitoa hewa fulani na hiyo hewa kwa upesi ikasambaa ndani ya kile chumba.



    Hao mabwana wakakohoa sana. Wakatoka ndani ya chumba wakiwa wanajikokota wakipaliwa na kikohozi. Hata macho yakawa mekundu kwa kukohoa!



    Hawakupata wanachokitaka, na zaidi wakapata matatizo. Walijikokota mpaka kwenye gari yao wakazama ndani. Wakaendelea kukohoa sana kiasi cha kushindwa kuongea.



    Baada ya dakika kama kumi, bado wakiwa hapohapo hawajaenda popote, angalau wakapata ahueni. Wakamweleza yule dereva kuwa mule ndani hamna mtu! Hawajamwona yoyote yule na huenda kabisa likawa tego. Walengwa wao watakuwa waligutuka mapema kuwa watakuja kuwatembelea.



    Basi dereva akaleta ubishi. Akawauliza kama kweli walipekua vema. Wale mabwana wakasema walitazama kila eneo na walichokiambulia ni mdoli tu kitandani ukiwa umerekodiwa sauti!



    Sasa kukawa hamna namna. Ikabidi waende zao, wale mabwana wakiendelea kukohoa sana na sana.



    **



    Basi zikapita kama dakika chache. Ndio, ni chache si nyingi, Miranda na Marwa wakawa wamezama ndani ya jengo lao ambalo lilitoka kupekuliwa muda si mrefu.



    Walifika katika kile chumba, kile ambacho kilikuwa na mdoli, Miranda akamwokota yule mdoli chini akitabasamu. Akamtazama Marwa na kumwambia kwamba mpango wao umeitika. Kile walichokipanga kimezaa matunda.



    Wasipoteze muda, wakaondoka hapo isijulikane wameenda wapi.



    **



    Baada ya mlango kuita mara moja tu, Shao akafungua na kukutana na kikohozi cha watumishi wake. Hata ndani hakuwakaribisha akawauliza kwa pupa imekuwaje?



    Wakamweleza ya kuwa kule hawajapata kitu chochote, zaidi wameambulia maradhi! Shao afanye nini zaidi ya kukasirika?



    Alikasirika mno, akang'ata meno yake na sasa akaridhia na akili yake kwamba maadui zao watakuwa walishatambua kuwa watatembelewa.



    Sasa afanyaje? Akajiuliza. Akawataka wale watu waende zao wamwache afikiri na kupanga lingine. Asubuhi na mapema atawajuza namna ya kufanya.



    Basi wale wajakazi wakaenda zao.



    ***



    Hali haikuwa nzuri kabisa kwa usiku huu mzima. Wale mabwana wanne walikohoa sana na hawakupata nafasi haya ya kufumba macho kufurahia lepe la usingizi.



    Walikohoa mno. Kadiri muda ulivyokuwa unasonga ndivyo walivyozidi kukohoa, mwishowe wakakosa pumzi na kujifia!



    Yani kama vile mchezo. Mpaka jua linachomoza kesho asubuhi yake, watu hao wakawa wamekauka kaukau!



    Maiti zao zilikakamaa kama mibuyu! Shao akapewa taarifa na akaenda kuwaona kabla hawajawazika. Akatahamaki na akasihi mwili mmoja ubakizwe kama sample watazame ni nini kiliwakumba.



    Baadae walipofanya hivyo, wakagundua kuwa watu hao walikuwa wamevuta hewa mbaya ya ukaa. Mapafu hayo yalikuwa meusi kama mkaa na koo lao la hewa lilikuwa limetobokatoboka!



    Hapa Shao akatambua kuwa hata wale wakina BC wako vema kwenye 'chemical weapon'. Ilimpasa awe makini zaidi.



    Ila kama kuna kitu ambacho alikuwa anaridhia na nafsi yake ni kwamba hajashindwa vita.



    Bado ana uwezo wa kumpata na kummaliza Jona. Cha kufanya ni kuja tena na mpango mwingine. Na sasa anatakiwa kutumia sana maabara kumaliza kazi yake.



    **



    Majira ya kumi na moja jioni ...



    Shao alizama maabara na kuvalia mavazi yake ya kazi. Koti jeupe na maski ya kubana pua na mdomo, pia na glovu za mikononi kujilinda.



    Akatumia kama masaa matatu akiwa humo maabara. Alikuwa peke yake. Na macho na mikono yake ikafanya kazi barabara kuitikiwa wito akili yake. Alichukua hiki akachanganya na kile, kile akachanganya na hiki na mwishowe akajikuta anapata kimiminika cha kijani iliyokolea.



    Akakitikisa na kukitazama kikiwa ndani ya tube. Kukihakiki, akatwaa panya watatu wakubwa, na mmoja wao akamminyia kemikali hiyo mwilini akitumia bomba la sindano.



    Yule panya akadumu kwa sekunde moja, mara akaanza kutapatapa akimimina damu. Na isichukuwe muda akafa! Ila hata baada ya kufa, Shao hakumtoa, badala yake akaendelea kuwatazama wale panya mpaka zilizopohitimu dakika tatu.



    Hakuona mabadiliko! Akasonya. Si hicho alichokuwa anataka. Basi akamtoa panya yule aliyekufa kisha akawabakiza wale wawili.



    Akarudi tena kwenye 'experiment' zake na baada ya punde akawa amepata mchanganyiko mwingine ambao ulikuwa ni wa kijani kupitiliza hata kuelekea kuwa nyeusi!



    Akaifyonza na bomba la sindano na kumdunga panya mmoja, kisha akatulia na kuangaza.



    Yule panya akadumu kwa sekunde tano tu, na tofauti na yule wa kwanza, huyu hakutapatapa kabisa, alidondoka chini ghafla baada ya moyo kusimama!



    Ila Shao hakumtoa na badala yake akaendelea kumtazama panya huyo. Na kama vile dakika moja, yule panya mwingine ambaye hakuwa amedungwa kemikali, akaanza kudhoofu! Alianza kuyumba kama chombo kiendacho mrama, na mara akadondoka na kufa!



    Shao akatabasamu. Sasa alikuwa amepata anachokitaka.



    **



    Majira ya saa mbili usiku ..



    Kwa huku nje kulikuwa kumetulia tuli. Ni hatua tu nzito za walinzi hapa na pale ndizo zilikuwa zinasikika.



    Ni hapa karibu na ofisi ya Sheng.



    Taa za ndani ya ofisi zilikuwa zimezimwa kuashiria hakuna mtu humo ndani. Ila ...



    Ni kama vile ungetulia vema ungesikia sauti za watu kwa mbali. Labda ungewaza ni masikio yako ila ndani ya muda mfupi sauti ya kitasa ilijita, na mlango ukafunguliwa kistaarabu akatoka bwana mmoja aliyekuwa amevalia nguo nyeusi kama walinzi wengine wazungukao eneoni.



    Bwana huyo alitoka kwa tahadhari, na baada ya punde akanyanyua miguu yake kutokomea.



    Lakini ...



    Huyu bwana hakuwa mgeni machoni petu. Kama kumbukumbu zi vema, huyu bwana ni mmoja wa wale wateuzi kumi wa bwana Shao kwa ajili ya kazi yake. Sasa nini alikuwa anafanya ofisini kwa Sheng tena wakiwa kizani?



    Vilevile taa ikiwa haijawashwa, mule ndani ya ofisi ya Sheng, simu ya mezani ikanyakuliwa na kupachikwa sikioni kisha punde sauti ya Bwana Sheng ikauliza kama aongeaye naye ni makao polisi.



    Baada ya hapo, akatoa taarifa ya kwamba Jona anashikiliwa na mwingereza bwana Brown Curtis hivyo wakafanye msako kwenye nyumba yake haraka iwezekanavyo!



    Aliposema hayo akapachika simu mezani. Tulipata kutambua hilo kwa sauti, kisha akaketi na kusema kwa lugha ya kichina, acha tuone nani atakayekuwa ndege wa alfajiri.



    **

    Ni nini alimaanisha bwana huyu? Ni nini anadhamiria kufanya na mbona jambo hili hakumshirikisha Shao? Kwanini alifanyia maongezi haya ndani ya kiza?



    Pengine unawaza hali ya Jona na wenzake ukasahau kujiuliza maswali hayo.



    Basi siku hii ikaenda. Kesho yake majira ya asubuhi tu, Shao akaamkia ndani ya maabara. Akachukua ile kemikali yake aliyoitengeneza jana yake na akaanza kuifanyia taratibu kuigeuza kuwa katika mfumo wa hewa.



    Alifanya zoezi hilo kwa muda wa masaa matatu, kumbuka alikuwa yu mwenyewe, na hatimaye alipogeuza kemikali hiyo kuwa hewa, akaijaribisha kwa panya aliowatoa kwenye hifadhi yake, na punde tu panya hao, watatu kwa idadi, walipovuta hewa ya kemikali hiyo wakafa pasipo kuomba maji!



    Shao akatabasamu. Kazi ilikuwa kufyonza tu hewa hiyo na kuiswekwa kwenye kontena zake maalum.



    Aliazimia kemikali hiyo kutumika usiku wa siku hiyo. Kwa matarajio yote aliamini itamletea matunda anayoyataka.



    **



    Saa tano asubuhi ...



    Gari, defenda kama yalivyozoeleka kuitwa, ya polisi ilitua mbele ya geti na honi ikapigwa mara nne, geti likafunguliwa na gari likazama ndani.



    Lilikuwa limebebelea askari wanaume watano kwa nyuma, na wawili upande wa dereva ambao wao walikuwa wamevalia nguo za raia. Gari hili liliposimama tu, askari wale wakashuka upesi.



    Watatu miongoni mwao walikuwa wamebebelea bunduki na mmoja ameshikilia redio koo mkono wa kuume.



    Kibarazani alikuwa amesimama BC akishangazwa na ujio huu. Alikuwa amevalia gauni la bafuni alilolifungia vema kiunoni. Alidaka kiuno chake akijiuliza maswali kichwani, punde askari wakamfikia na kumweka chini ya ulinzi, na wakamweleza haja yao kuwa ni kufanyia upekuzi eneo hilo lote maana wanahisi litakuwa linahifadhi mtu wanayemtafuta.



    BC akashangaa na hata akawaambia kwamba hamna mtu wanayemhitaji humo. Pia hawana haki ya kumweka chini ya ulinzi kama madai yao hayajathibitishwa.



    Pia akawasihi wangoje ampigie na kuongea na mwanasheria wake kwanza.



    Madai yake yote hayo yakapuuzwa, askari hawakumzingatia hata kidogo. Wakamweka chini ya ulinzi na kumtia pinguni kisha wakaanza kufanya upekuzi hadidi.



    Wakapekuwa kila pande ya nyumba na wakagundua kuwa mwanaume huyo alikuwa na baadhi ya kemikali maabarani mwake. Ila hawakufanikiwa kumpata yeyote yule. Hata yule waliyekuwa wanamdhania yumo.



    Basi wakambeba BC na pia wakawasilisha kemikali zake zote walizozitoa maabara na kuzipeleka moja kwa moja kwenye ofisi ya mkemia mkuu kwa ajili ya uchunguzi na maelezo zaidi ya kitaalamu.



    Bwana yule mzungu akaswekwa rumande.



    Na kama haitoshi, kamanda wa mkoa akaitisha 'press conference' kuwaambia waandishi na wananchi nini kimetokea. Lengo kuu hapa lilikuwa ni kufanya jeshi lionekane 'linashughulika', halijashindwa na kila kitu kipo kwenye 'mikono yao.'



    Hivyo japo hawakumpata Jona, bado kutangaza kwenye vyombo vya habari ilikuwa ni turufu! Hata bwana Sheng hili jambo lilimpendeza machoni.



    Na baadae kwenye majira ya jioni, bwana huyo wa kichina akaenda kuonana na Kamanda mkuu. Akamweleza kuwa bwana huyo wa kizungu waliyemtia kizuizini anajua fika wapi alipo Jona. Wanachotakiwa kufanya ni kumbana mpaka aseme.



    Kamanda akamwambia aondoe shaka, atalisimamia hilo kwa nguvu zake zote. Ila akamsisitizia tena kuwa jambo lao liwe la siri, hata wenzake hawatakiwi kulijua.



    Kamanda akamtoa hofu. Na Sheng hakukaa sana, akaenda zake kurudi makaoni.



    **



    Baadae majira ya usiku ...



    Hodi iligonga mara mbili kwenye makazi ya Sheng. Alipopokea hodi hiyo, akazama ndani Bwana Shao aliyekuwa amevalia suti ya traki rangi nyeusi. Akaketi na kumwambia Sheng juu ya habari zile za polisi kumvamia na kumkamata BC.



    Akaeleza namna alivyoshangazwa na habari hiyo maana walikuwa katika mpango. Ila akamuuliza bwana Sheng kama amehusika kwa vyovyote na hiyo oparasheni.



    Sheng akakataa, na hata akasema aliwaza pengine ni yeye, yaani bwana Shao, ndiye aliyefanya hilo.



    Basi baada ya kwenda tofauti kimaudhui, Shao akamuuliza Sheng kuhusu hilo jambo. Ni nini msimamo wao kwenye hili? Watafanya nini sasa?



    Sheng akatikisa kichwa kwanza alafu akamwambia Shao kuwa yeye ahusiki na wala hatahusika na chochote kile kwani kila kitu alimkabidhi yeye.



    Na hata akamkumbusha kuhusu ile HATI yao ya kifo. Shao akashangazwa. Asiseme kitu, akaaga na kwenda zake!



    **



    majira ya saa tano asubuhi ...



    Mwanaume mzungu aitwaye Henry Marshall alifika kituoni akiwa amebebelea briefcase nyeusi na pia amevalia suti nyeusi iliyomkaa vema mwilini.



    Mwanaume huyu alikuwa ni mwenye nywele rangi ya 'brown'. Macho yenye kiini cheusi. Mwili wake ulikuwa mwembamba na wenye nishati ya kutosha. Alikuwa anatembea kwa ukakamavu. Na macho yake ndani ya miwani nyeupe ya macho, yalikuwa yanaangazaangaza huku na kule.



    Akajitambulisha kwa jina na pia dhumuni lake kuwapo hapo. Yeye ni mwanasheria wa Bwana Brown Curtis. Amekuja hapo kwa dhumuni la kumtetea mteja wake.



    Na bwana huyo akawachachafya askari hao akiwaambia wamekiuka sheria kwa kumsweka ndani mteja wake kwa mashauri yasiyo na uthibitisho na hata pasipo kuongea naye kama mwanasheria.



    Japo bwana Henry alijieleza vema kutokana na nafasi yake, wale askari hawakutaka kumwelewa kabisa. Hata kuonana na Brown Curtis hakuruhusiwa. Basi akaenda zake akisema atalipeleka shauri hilo mahakamani.



    Na ana uhakika atashinda, na hilo shauri litaigharimu serikali pesa kubwa!



    Hakuwa anatania. Alikuwa ni mwanasheria wa hadhi yake toka Uingereza. Tena anayefahamu vema sheria nje na ndani. Aliapa kulifanyia kazi jambo hili kuonyesha thamani ya pesa anayolipwa na mteja wake.



    **



    Saa nane mchana ...



    Simu iliita kwa muda mfupi tu, Kinoo akapokea na kuiweka sikioni. Alikuwa ni Miranda anampigia na tayari alikuwa anajua mwanamke huyo anataka kuongelea nini.



    Nalo si jingine bali swala la BC. Akapokea simu na kuteta. Miranda akamtaka waonane haraka iwezekanavyo kupanga namna ya kufanya kwa ajili ya bosi wao.



    Ikachukua kama nusu saa tu, wakawa wamekutana na kujiweka ndani ya gari kunena mawili matatu. Basi Miranda akamwambia Kinoo kuwa inabidi aende kumtembelea BC kule kituoni maana yeye wanaweza kumhisi kwa namna moja ama nyingine kuwa anahusika na Jona kwani alishawahi kufika huko mara kadhaa.



    Ila Kinoo naye akasita, akaeleza hofu yake. Vipi kama naye akikamatwa? Miranda akamsihi hamna muda wa kuhofu, na hawana machaguzi mengine zaidi ya kutenda.



    Na hapo anapoteta naye, tayari ashafikisha habari za Brown Curtis makao makuu, hivyo wanaweza wakatumwa mawakala hivi karibuni.



    Basi Kinoo akaridhia, ataenda kuonana na BC kesho asubuhi na mapema. Ila akamuuliza Miranda, vipi kuhusu bwana yule, Jona? Wapi alipo na anaendeleaje?



    **





    Katika namna ya ajabu, Miranda akasita kumweleza Kinoo juu ya maswali hayo. Akamtaka aende akajiandae na yeye aende zake maana kuna eneo anapitia.



    Kinoo akashuka toka garini na kisha akasimama akishuhudia gari la binti huyo likitokomea.



    Ila kuna jambo lilimjia kichwani. Ni kama radi jambo hilo lilikuja upesi. Akawaza namna ambavyo Miranda amekuwa kama mtu wa 'kumtenga' siku hizi.



    Amekuwa si wa kumshirikisha na wala kumhitaji kama ilivyokuwa huko nyuma. Kwa namna moja ama nyingine alipata wivu wa kiume. Aliona kama vile Jona na mwenzake Marwa wametenganisha familia yake.



    Nafasi yake imezibwa na hao watu.



    Akawaza.



    Kama hali ipo hivyo na huyo Jona bado yupo kitandani, vipi akiamka na kurejea kwenye hali yake? Atakuwa na nafasi hata robo?



    Alihofia.



    Aliwaza akiwa anatembea kurejea nyumbani kwake. Alipofika ndipo mawazo hayo yakaenda zake na kuacha nafasi ya kuwaza mengine. Ya mkewe.



    Hakuwa amemkuta hapo nyumbani na hakuwa anajua wapi kaenda. Akalalama yaani kutoka kidogo tu naye keshafungua mlango!



    "Mwanamke huyu!" Akatikisa kichwa. Akanyakua simu na kumpigia. Nayo ikaita mara tatu pasipo majibu. Akasonya na kujiongelesha mwenyewe.



    "Sijui nimfanye nini. Na hivi ana ujauzito, basi keshapata sababu haswa!"



    Akalalama na kulalama. Hata kama angelitukana isingelisaidia kwani mtuhumiwa hakuwapo wala hakuwa anasikia, wala kujali.



    **



    "Kama nilivyokuambia, kumbe yule muuaji alikuwapo huko," alisema Sasha kisha akashushia na juisi. Akamtazama dada yake, Sarah, na kuendelea kumwambia,



    "Wewe umekaa siku zote hizo, umekalia pesa dada yangu. Ina maana hujui kama donge nono lilitangazwa kwa mtu atakayetoa taarifa zitazosaidia upatikanaji wake?"



    Sarah akapandisha mabega akisema hana habari kabisa. Na hata kama angelikuwa na habari asingelifanya lolote kwani hakuwa anajua kama wakina Kinoo wamemuhifadhi jamaa huyo.



    Basi Sarah akaendelea kumpasha habari. Akamwambia taarifa zake zilishafika polisi na hata walipoenda kumsaka, hawakumwona, tayari wameshamuamisha!



    "Sasa dada yangu, nataka tupige hela kama wehu! Najua wewe utakuwa unajua wapi alipo. Tumbua basi tupige hizo milioni kisha twende zetu Ibiza huko mbali na ulimwengu."



    Sarah akatikisa kichwa. Akatazama kinywaji chake mezani, juisi ya embe, ambayo haikuwa imeguswa kabisa, kisha akasema:



    "Sasha, sijui niwe nakuambia vipi? Mimi sijui kabisa. Sijuuui kwa herufi kubwa!"



    Sasha akatikisa kichwa chake na kuminya mdomo.



    "Yani wewe unakuwa kama sio dada yangu yani. Mbona unakuwa zoba zoba wewe bana! Unashindwaje kujua na wakati unaishi na yule mwanaume?"



    "Sasha!" Sarah akaita kwa tahadhari. "Nakuapia kwa Mungu wangu, yule mwanaume muda si mrefu atahisi huu mchezo tunaoufanya. Kabisa nakwambia. Ndipo anapoelekea."



    Sasha akapeleka mdomo wake pembeni. "Uoga wako tu huo! Unadhani atakufanya nini na umebeba mimba yake? ... hana ujanja wowote."



    Sarah hakusema kitu. Akajaribu kunywa kinywaji chake ila hakikupanda. Alipokunywa fundo moja tu, akarejesha glasi chini. Akasema,



    "Naomba niende."



    "Nimekuudhi?" Sasha akajishuku.



    "Hapana," Sarah akajibu. "Naona tu muda umeenda. Nahisi yule bwana atakuwa amerejea nyumbani isije kuwa nongwa bure."



    "Ok!" Sasha akasema na kisha akanywa fundo za nguvu kumalizia juisi yake mezani, alafu akanyanyuka.



    "Twende nikusindikize."



    Akampeleka Sasha hatua kadhaa akiendelea kumshawishi afanye kazi yake ya kupeleleza alipo Jona. Sarah akaahidi kulifanyia kazi, ila si kwa haraka hivyo. Akajikweza kwenye gari na kuondoka zake.



    Sasha akatoa simu yake ya mkononi na kupiga. Akaongea na huyo wa kuongea naye kwenye simu ya kwamba ameshapiga hatua moja. Wavute subira kuona matokeo yake, kisha akakata simu.



    **



    Kesho yake, majira ya saa nne, central ...



    "Nimekuja kuonana na mfanyakazi mwenzangu," alisema Kinoo akimtazama askari machoni pasi na woga. Askari akamtazama kwa jicho la uchovu wa kebehi na kumuuliza,



    "Nani huyo mfanyakazi mwenzako?"



    "Yule mzungu aliy ..."



    "Yule jambazi!" Askari akaropoka.



    "Hapana, si jambazi," Kinoo akamtetea.



    "Ni nani basi?" Askari akauliza. "Mtu anayemficha jambazi ni nani kama sio na yeye ni jambazi?"



    "Afande, hakuwa amemficha yeyote. Sidhani kama mtu huyo mnayemwongelea alionekana kwenye jengo lake baada ya msako mlioufanya."



    "Kijana," askari akamnyooshea kidole Kinoo. "Usitufundishe kazi, sawa?"



    Kinoo kimya.



    "Sawaa? ... kwanza nenda zako kabla sijakuweka ndani na wewe. Wewe mwenyewe unaonekana jambaka tu. Ebu nenda bwana! ... Nenda, husikii!?"



    Kinoo akashusha pumzi na kisha akageuka aende zake. Akatwaa simu mfukoni na kumpigia Miranda.



    "Wamenikatalia kuonana naye."



    "Kwanini?"



    "Sijajua."



    "It's ok. Naona wameamua hivyo. Na itakuwa ni agizo wanatekeleza. Sasa achana nao, tutafanya njia nyingine."



    "Ipi hiyo?" Kinoo akatazama nyuma yake kisha akarudisha macho mbele. "Usinambie ni kama ile tuliyofanya mara ya kwanza? Kwa sasa haitawezekana. Ulinzi umekuwa mkali kupita kiasi!"



    "Hapana, si njia hiyo bali nyingine ya kidiplomasia zaidi. Anyways, tutaongea baadae."



    Miranda akakata simu.



    **



    Simu ya mezani ya bwana Sheng iliita, akainyofoa toka kwenye kitako chake na kuiweka sikioni. Alikuwa ni kamanda akimpigia majira haya ya jioni.



    "Mkuu, naomba mambo yataenda kombo," alisema Kamanda simuni.



    "Una maanisha nini?" Sheng akauliza akikunja ndita.



    "Naona hili swala la bwana Brown litatoka nje ya mikono yangu."



    "Kivipi?"



    "Mahakama imeamuru aachiliwe. Amekamatwa kinyume na taratibu!"



    "You can't be serious!"



    "Sure! Na si hivyo tu, hata waziri wa sekta hii amenipigia simu na kuniagiza nitende kama nilivyoambiwa maana hili swala limeanza kuvuta hisia za kimataifa, haswa Uingereza juu ya namna raia wake alivyokuwa treated offensively!"



    Sheng akashusha pumzi, kisha akauliza, "na vipi kuhusu zile kemikali? Hauwezi ukapata chochote huko?"



    "Hamna kitu. Hata tukipeleka mahakamani, hatutashinda. Tutashindwa kutetea hoja zetu na mwishowe itaonekana kuna dhamira binafsi katika hili!"



    Sheng akakosa cha kunena. Akiwa anatetemeka mkono akapachika simu yake ya mezani kwenye kitako chake na kisha akalaza kichwa kochini akiwaza.



    Alihisi kuchanganyikiwa.



    **



    Saa mbili usiku ...



    Bwana Henry Marshall alimfikisha BC nyumbani kwake alafu akaingia ndani na kuteta kidogo kuhusu swala lake, akimtoa hofu kabisa kwani kila kitu kipo sawa mikononi mwake.



    BC akamshukuru sana, na akamtakia usiku mwema akapumzike maana amefanya kazi nzito siku hiyo. Bwana huyo akaenda zake.



    BC akaenda kukoga na kisha akavaa vema. Akafungua jokofu lake la kuteua chupa moja ya kinywaji. Alikuwa ana kiu nacho haswa. Akafungua na kunywa kwa mtindo wa tarumbeta mpaka pale alipobakiza robo chupa ndiyo akaenda nayo mezani.



    Akanywa taratibu akitafakari. Akawaza lile tukio la yeye kukamatwa, na akakubaliana na akili yake kuwa tayari wakina Sheng watakuwa wanafahamu kuwa Jona yupo mikononi mwake.



    Hii ilikuwa ni vita. Na yeye kuachiwa huru na polisi si kwamba ndiyo ilikuwa imekoma, bali ndiyo inaanza.



    Amejipangaje kupambana? Alikuna kichwa chake. Lazima Sheng atakuja na njia nyingine baada ya hii. Itamgharimu kiasi gani kumsimamisha Jona asimame mwenyewe?



    Alikuwa amechoka sana. Hata hakuwaza vema, akamalizia kinywaji chake na kwenda kulala. Kesho yake asubuhi na mapema akamwita Miranda aje nyumbani.



    Ila alipokata simu hiyo, akapewa taarifa kuwa bwana Henry Marshall amefariki dunia.



    **

    Jambo hili likageuza maisha yake haraka, juu chini chini juu! Hata akasimama apate kuzisikia vema. Hakuamini kabisa. Na hata huyo mtu aliyempa taarifa akamwona mwehu.



    Akakata simu. Ila punde kidogo ndipo akagundua kuwa jambo hilo ni kweli baada ya kumpigia simu Henry Marshall na kuita pasipo majibu, alafu akaona mtandaoni habari za mwanasheria wake.



    Ajabu iliyoje hii! Alihisi mwili mzima umekuwa wa baridiii, ila kichwa kinawaka moto haswa!



    Gari la Henry lilikuwa zima kabisa, isipokuwa kioo tu cha mbele ndicho kilipasuliwa na risasi zilizomwagwa kama njugu kumpasua na kumtoboa Bwana Henry, akalala pasipo msaada.



    Suti yake imefyonza damu mpaka ikashiba na kuchuruza nyinginezo. Uso wake umeshindiliwa risasi tatu hivyo kufanya ugumu kidogo kutambulika!



    Hakika hizi zilikuwa habari mbaya sana kwa Bwana Brown. Hakuwahi kupata habari hizi hapa karibuni isipokuwa hii. Alijikuta anapata hasira sana. Tena sana, hata akahisi hataweza kuendesha gari.



    Akamwita kijakazi wake na kumpatia funguo ampeleke eneo la tukio.



    Alipofika huko akakuta gari la bwana Henry likiwa linakusanywa na gari 'breakdowns' na mwili wake ushapelekwa hospitali.



    Akawasiliana na baadhi ya watu wake na wakaliongelea jambo hilo kwa kukubaliana kupeleka maiti nchini Uingereza ikazikiwe huko.



    Na wakakubaliana baadae majira ya usiku wakutane wapate kuteta jambo.



    **



    Baadae majira ya saa nne usiku, nyumbani kwa Brown Curtis.



    Wanaume watatu walikuwa wamekalia sebuleni. Wawili walikuwa ni sura ngeni machoni na mmoja wao alikuwa ni Brown Curtis (BC). Wote walikuwa wamevalia suti nyeusi, si muda mrefu walikuwa wametoka kwenye makazi ya muda ya marehemu bwana Henry Marshall.



    Wanaume hawa wageni inakuwa vema na rahisi kuwatofautisha kwa rangi za nywele zao. Mmoja nywele zake zilikuwa nyeusi ti, aitwa McKnight na mwingine alikuwa na nywele 'blonde', aitwa Woodman.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Pengine majina yao si ya muhimu sana maana hatutahangaika nayo sana katika simulizi hii, ila kwa hapa wana umuhimu fulani.



    Basi wakiwa wanateta hapo, BC akionekana waziwazi kuwa ana hasira na anajua fika aliyetenda jambo hilo la kidhalimu, akasema anahitaji watu kadhaa wa 'kazi'.



    Na watu hao waagizwe toka Uingereza mara moja pasipo kupoteza muda hata punje!



    Ila mabwana wale wakawa wastaarabu kidogo, "slow down, Brown," alisema yule mwenye nywele nyeusi. "Our government will respond on this, we don't need to rush in!"



    Brown akatikisa kichwa. "No! It is enough. I am done with this and now my patience is gone! I want to end things immediately! Enough is enough!"



    Hakutaka kusikia wala kungoja namna Uingereza itakavyochukua hatua. Alitaka hatua achukue mwenyewe mkononi.



    Siku zote hakuwa mtu aliyekuwa amepanga wala kudhamiria kummaliza Sheng. Ila kwa sasa hilo ndilo litakuwa lengo lake la kwanza kabisa!



    Sheng aende kaburini!



    Basi mabwana wale wengine wawili, kwa kuona sikio hili lilikuwa la kufa, wakaafikiana naye na kumwahidi kumuunga mkono. Watatimiza kile bwana huyo anataka.



    ***



    Kesho, saa sita mchana.



    Hodi ilibishwa na kabla Sheng hajatia neno akastaajabu mlango unafunguliwa, anazama Kamanda mkuu!



    Uso wake haukuwa katika pumziko. Mweusi kuliko kawaida. Alikuwa amevalia nguo za kiraia, shati ya kitenge na suruali nyeusi ya kitambaa, na kichwa chake akikihifadhi ndani ya kofia 'cowboy' rangi ya kahawia.



    Akaketi na kumuuliza Sheng, "ni nini umefanya?"



    Sheng akatabasamu, alafu akajisukuma na kiti kwenda mpaka ukutani. Akaweka viganja vyake tumboni na kumtazama Kamanda kana kwamba mama wa kambo anavyomtazama mtoto wa mumewe akiwa anaongopa.



    Akauliza, "kwani kuna nini Kamanda?"



    "Sheng!" Kamanda akatahamaki. "Ina maana hujui ulichokifanya? Kulikuwa kuna haja gani ya kummaliza yule mwanasheria?"



    Kimya kidogo.



    " ... na nilishakwambia Sheng. Nilishakwambia. Waziri aliniambia hili jambo linaweza kuleta utata sana na serikali ya Uingereza. Tuachane nalo tu, tuangazie namna zingine. Hujataka kunisikia kabisaaaa, ndugu!



    Huoni umeiingiza serikali yetu matatani. Dunia nzima watalichukuliaje hili tukio? Si wataona Bwana Henry kauawa na serikali! Na mimi nikiambiwa nipeleleze huoni nitaingia matatizoni!"



    Sheng akashusha pumzi ndefu puani kisha akarembua macho na kuyakodoa.



    "Kamanda, dharau kwangu zina mipaka," akasema kwa sauti ya wastani. "Zile zilikuwa ni dharau. Kuna muda a king has to remind fools that he is a king!"



    Kamanda akasikitika sana. Akakunja ndita na kumweleza bwana Sheng,



    "Umekosea sana na uniweka kwenye wakati mgumu mno. Bila shaka mimi na wewe tumemalizana, hatudaiani. Kwa hivyo, naomba kila mtu sasa ashunghulike na mambo yake. Pesa zako zinanuka, Sheng!"



    Kamanda akasimama kwa kiburi. Akafungua mlango na kwenda zake. Sheng akatabasamu, kisha akacheka.



    Ikapita dakika tatu, mlango ukagongwa tena. Na kama ilivyokuwa awali, kabla Sheng hajasema kitu, mlango ukafunguliwa. Akajiuliza kuna nini leo?



    Kutazama akamwona Shao.



    Bwana huyo aliketi pasipo kusalimu. Akakunja nne akimtazama Sheng na kisha akamuuliza,



    "Ni wewe ndiye uliyewaita polisi kwa bwana yule?" Aliongea kiswahili kilichonyooka. Bila shaka alifanyia mazoezi maswali haya kwa msaada wa wale watu wake.



    "Unasema nini wewe?" Sheng akauliza.



    "Unajua ninachokiongelea, Sheng. Unajua kila kitu, na nashangazwa nia yako ni nini?"



    Wakatazamana kwa sekunde mbili.



    "Shao, kama umeshindwa kazi yako, usitafute mlango wa kutokea, sawa?"



    "Sijashindwa," Shao akasema kwa kujiamini. "Ila wewe unataka nishindwe. Nimeligundua hilo. Sijajua utafaidika na nini katika hili. But its ok. Kama unataka kunimaliza, nimekuja. Niue."



    Sheng akatabasamu. Akatikisa kichwa chake mara mbili alafu akamtazama Shao.



    "Sina shida ya kukuua. Na kama nitakuua basi ni kwa mujibu wa makubaliano tuliyoweka mimi na wewe. Si vinginevyo, Shao ... kama hutojali, naomba unipishe nina kazi nyingi za kufanya."



    Kabla Shao hajaamka toka kitini akamtazama kwanza Sheng na macho yanayoongea husda, kisha akanyanyuka na kwenda zake.



    **



    Baadae, majira ya saa tano usiku..



    Kwa umbali wa kama hatua nane hivi za mtu mzima, kuna mtu alikuwa amejificha hapo akitazama mlango wa ofisi ya Sheng.



    Kuna kitu alikuwa anakingoja hapo. Na ni kama muda ulikuwa unasogea kuendea hilo tukio.

    Mazingira yalikuwa kimya haswa.



    Zikapita dakika tano, mara mlango wa ofisi ya Sheng ukafunguliwa akatoka mwanaume mmoja aliyekuwa amevalia nguo nyeusi.



    Mwanaume huyu alikuwa ndiye yule. Bila shaka unamkumbuka. Miongoni mwa wale 'vijakazi' kumi wa bwana Shao.



    Mwanaume huyo alitazama huku na kule, kule na kule kisha akashika njia kujiendea. Ila hakuwa anajua kuwa leo zilikuwa zimetimia zile arobaini zake.



    Akiwa anatembea, hana hili wala lile, akajikuta amedakwa shingo. Kabla hajashangaa, akatenguliwa kuvunjwa!



    Akadondoka chini mfu.



    Aliyemuua akamtemea mate na kusema, "tangulia kuzimu sisi twaja."



    Kisha akaenda zake.



    Baada ya dakika kadhaa, maiti hiyo ikagundulikana na taarif akafikishiwa Sheng.



    ***





    Ilikuwaje? Hilo ndilo lilikuwa swali la kwanza la Sheng. Mwanaume huyo alikuwa ametoka kumjulia hali hivi punde na sasa amekufa? Alishangazwa.



    Akawaita walinzi na kuwaliza nini kilijiri. Wote hawakuwa wanajua. Swala hili likamtia hofu Sheng. Huenda mwanaume huyo kauliwa na Shao? Aliwaza. Na kama kweli anachokiwaza ndicho, ina maana Shao atakuwa anafahamu kuwa anamzunguka?



    Akashusha pumzi ya mawazo. Pasipo kulifanya jambo hilo kuwa la hadhara, akamzika mtu huyo kisiri na kisha akaendelea kutafakari. Sasa hakuwa na daraja la kumfanya ajue kinachondelea kwa Shao. Hawezi kukaa hivi. Lazima afanye namna.



    Akiwa anawaza hivyo, kule upande wa Shao nao wakiwa wamekutana katika usiku huu huu wakawa wanapanga mipango yao. Kuna mwanaume mmoja alikuwa amesimama mbele na ndiye huyo aliyetoka kumuua yule mwanaume aliyetoka kwa Sheng. Ungeweza kumtambua mtu huyo kwa nguo alizokuwa amevaa.



    “Tuwe makini sana,” alisema Shao. “na zaidi ya kuwa makini tuwe na uahirikiano. Najua Sheng atamfuata mwinginewe ili awe anajua ninachokipaga na kukifanya. Na itakuwa ngumu kwenu kukataa, cha kufanya kubali ila utoe taarifa kwangu nami nitakuwa nakuelekeza namna ya kuenenda."



    Baada ya Shao kusema hayo, akawataka waende zao na kumwacha peke yake. Vijakazi hao wakatii.



    **



    Ni asubuhi, katika makazi yasiyojulikana...



    Marwa akamkalisha Jona kitako akitabasamu. Jona alikuwa anavuja jasho jingi na Marwa akitiririka kiasi. Wote walikuwa wamevalia nguo nyepesi chini traki rangi ya bluu zinazofanana.



    “Sasa hivi inabidi uwe unafanya kila siku!" Alisema Marwa akimtazama Jona. Angalau afya yake ilikuwa imeanza kurejea. Macho yanaonekana ila bado akiwa mdhaifu kiasi.



    Angalau sasa, tunaweza tukasema hivyo kwani hakuwa hivyo hapo awali. Na mtu aliyemwona ingemuwia vigumu kuamini kama mwanaume huyo angelikuja kusimamia miguu yake siku moja.



    Alitabasamu na kumwambia Marwa, “Dah! Si mchezo." Akafuta jasho kwa kiganja chake. Alikuwa anahema kwanguvu.



    “Ila unajitahidi sana!" Akasema Marwa. “sikutegemea leo kama ungefanya mazoezi kiasi kile. Hata Miranda akija nikamweleza hataamini!"



    Jona akatabasamu. “Nataka kurudi kwenye hali yangu kwa udi na uvumba."



    “Naona kwakweli," Marwa akabinua mdomo. “hautachukua hata juma moja kila kiungo kitakuwa sawa mwilini. Uanze yale mambo yako yale!"



    Wakacheka.



    “Ila Jona," Marwa akataka kuchokoza mada. “unamwona yule mwanamke?"



    “Nani? Miranda?"



    “ndio!"



    “kafanyaje?"



    “mwanamke hafai yule! Mamamama! Anapigana kama kazaliwa ulingoni. Yani daaah!"



    Jona akacheka. Marwa akaendelea kulonga, “ila hakuzidi wewe, bana. Nakuaminia kamanda wangu. Si bure wakina Sheng wanakesha kukutafuta. Wanajua wewe jembe."



    “umeanza sasa, Marwa. Mimi nimechoka hapa sina hata nguvu ya kunena. Naomba nikaoge tutaongea zaidi najua una mengi ya kunambia maana mengi yametokea kipindi sipo ulimwengu huu."



    Jona akajiendea kukoga. Alipomaliza akajifuta vema na aliporejea sebuleni akamkuta Marwa akiwa pamoja na Miranda. Mwanamke huyo alikuwa amevalia shati na suruali nyeusi ya jeans. Alipomwona Jona alitabasamu toka moyoni.



    “naona umepona sasa!"



    Jona akatabasamu na kuketi kitini. Akatet kidogo na Miranda kuhusu hali yake na maendeleo yake yakamtia hamasa Miranda. Alifurahi sana kumwona Jona anarejea kwenye hali yake.



    Walipomaliza maongezi hayo, Miranda akatazamana na Marwa katika namna fulani ya kuwasiliana kisha Marwa akasafisha koo na kusema;



    “Jona, kwakuwa sasa angalau umerejea kwenye hali yako, tunaona ni muda muafaka kukushirikisha jambo."



    Marwa akaweka kituo baada ya kusema hayo. Alafu akamtazama tena Miranda kabla hajaendelea.



    “sidhani kama nina haja ya kusema sana juu ya namna gani Miranda na mkuu wake, bwana Brown, walivyotusadia mpaka sasa. Hilo liko wazi. Ila sasa, kuna jambo, ama naweza kusema mkataba wa maneno ambao kwa namna moja kubwa kwasababu ya kuhitaji msaada, niliuingia mimi pamoja na mr. Brown.



    Bwana huyo alinisihi sana kuwa atakusaidia sana kwa kadiri ya uwezo wake, nawe unaweza ukaona. Ila akaniambia kwamba atahitaji umrudishie fadhila kiasi kidogo."



    Hapa Marwa akasita kidogo. Akamtazama Miranda na kisha akaendelea.



    “sasa bwana Brown anataka uwe mtumishi wake. Ni hilo tu ndi..."



    “haitawezekana!" Jona akamkatisha Marwa. Akasema kuwa hilo jambo kamwe halitatokea japo anashukuru sana kwa msaada aliopatiwa.



    “siwezi kufanya kazi chini ya BC. Haitakaa itokee hata siku moja hata kwa dau gani!"



    Miranda akashusha pumzi ndefu alafu akatia neno, “Jona, naomba ulifikirie hili swala kwa mapana zaidi. Ni bwana Brown pekee ndiye aliyekuokota wakati wengine wakiwa wamekitekeleza. Tafadhali fikiri mara mbili."



    Jona akatikisa kichwa. “Marwa, Miranda, huo ndiyo msimamo wangu na hautabadilishwa na chochote kile. Siwezi kufanya kazi na bwana Brown kwa sababu yoyote ile! Ila..."



    Akanyamaza kwanza akitazama chini. Akakunja ngumi.



    “lazima wale wote walionilaza chini walipe kwa gharama yoyote ile. Wamenitesa mno na kuharibu maisha yangu. Kamwe sitawaacha salama. Iwe kwa kunuka ama kunukia. Nitawasaka kama mbwa mwenye njaa na nitawaua kwa mkono wangu nwenyewe pasipo na tone la huruma.



    Niliapa kwa Mungu wangu. Siku nitakayotoka kwenye mateso yale itakuwa kiama chao hakika. Sitabakiza hata mmoja. Na kila ninapokumbuka hilo, napata nguvu ya kufanya mazoezi zaidi niwe kamili."



    Jona akisema haya, machozi yakamjaa machoni. Alikuwa anaongea kwa uchungu mno na kwa hisia kali. Aliminya ngumi yake mpaka akahisi maumivu.



    Alisimama na kwenda zake chumbani pasipo kuaga.



    “sasa tunafanyaje?" Akauliza Marwa akimtazama Miranda.



    “sijui kwakweli!" Miranda akatikisa kichwa. “naona mambo yanakuwa magumu zaidi."



    “kabisa! Ila hata mimi nililihisi hili jambo. Halijanishangaza kabisa. Ni asilimia ndogo sana niliihifadhi kuwa Jona ataridhia hili jambo. Kichwa chake anakijua mwenyewe."



    Kukawa kimya kidogo. Miranda akanyanyuka na kumwambia Marwa,“acha nikapumzike kidogo. Baadae nitaenda kuonana na Bwana Brown "



    “utamwambia nini?" Marwa akauliza upesi.



    “nimwambie nini zaidi ya nilichoambiwa na Jona," akasema akienda zake. Marwa akaachwa akiwa na hofu. Aliona kabisa mambo yanapoeleka si kwema. Ila afanye nini sasa?



    Alihisi tumbo linavuruga. Hakutaka kuona kazi yote ile waliyoifanya inageuka kuwa vumbi.



    **



    Saa mbili usiku ...



    Ndege kubwa ya kampuni ya BRITISH AIRWAYS ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius K. Nyerere. Ndege hiyo ikatema watu kadhaa ikiwemo wanaume kumi na mbili waliovalia suti nyeusi kali na wamebebelea mikoba mikononi.



    Wanaume hawa waingereza kw utaifa, walikuwa wametokea jiji la London na hapa nchini walikuwa wamekuja kwa agizo la bwana Brown Curtis.



    Walitoka nje ya uwanja, wakapokelewa na Bwana Brown mwenyewe ambaye alikuja na gari kubwa la kuwatosha wote, Noah nyeupe yenye vioo vyeusi. Wakajitweka humo na safari ikaanza ya kuelekea nyumbani kwa bwana Brown.



    Pasipo kupoteza muda baada ya kuwasili, BC akawaeleza kuwa wamekuja nchini kwa kazi moja, kummaliza Sheng na utawala wake hapa nchini.



    Lakini kwakuwa watu ha walikuwa wamechoshwa na uchovu wa safari, bwana Brown akawataka wapumzike kisha kesho itakapofika watayajenga na kuyapanga vema.



    Basi wanaume hao kumi na wawili wakaenda kukoga wafanye mpango wa kupumzika. Hawakuwa watu wa soga nyingi, bali matendo. Miili yao ilikuwa imejengeka kimazoezi na macho yao yalionyesha kweli wao ni watu wa kazi.



    Wakiwa wanajishughulisha huko, Miranda akafika nyumbani kwa BC. Akaelezwa juu ya ujio wa hao watu na hata wakaitwa na kutambulishwa kwa mwanamke huyo. Baada ya hapo, Miranda akasema lengo la ujio wake.



    “Jona doesn't want to join with us."



    BC akatabasamu. Sigara yake iliyokuwa kwenye kisosi ilikuwa haijazima, akainyakua na kuifyonza.



    “ok, he's chosen death over life. He wil pay!"



    Akafyonza tena sigara. “in fact I dont need him anymore. The men are already here, I know they will do the work effectively. But I won't leave Jona alive. He must die!"

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miranda hakusema kitu. Alikuwa anamtazama tu BC akivuta sigara na kunena.



    “did you hear me? He must die. And you are the one who's gonna do it."



    Miranda akatahamaki, “me!"



    “yes, you!" BC akabweka. “kill him!" Alisema akiwa ametoa macho. Akasisitiza zaidi, Jona auawe. Na isichukue hata siku mbili awe amemletea kichwa cha mwanaume huyo mfukoni!



    **



    Jambo hili lilikuwa si jepesi hata kidogo. Miranda alienda zake akiwaza mno namna gani atalitekeleza. Yaani ina maana kazi yote ile waliyoifanya, wakahatarisha na uhai wao, ni bure!



    Alikosa usingizi. Hata alimtazama Jona kwa macho ya maswali hata wenzake wakajua hayuko sawa.



    “vipi hujapenda chakula?" Marwa akauliza. Alijua wazi shida si chakula. Alitafuta pa kuanzia tu.



    Miranda akatabasamu kiuongo alafu akaguna. Akasema, “hamna bana. Chakula ni kitamu sana tu."



    Akakaa kimya kidogo. Alafu akaendelea. Hakuwa anamtazama mtu bali chakula chake.



    “kuna mambo flani tu nawaza. It's not a big deal!"



    “ni kuhusu Mr. Brown?" Jona akauliza akimtazama mwanamke huyo ambaye hakutaka kumtazama. Aliendelea kuangushia macho yake kwenye sahani yenye chakula alichopika Marwa. Wali na njegere.



    “hapana," Miranda akatikisa kichwa. “si kuhusu yeye. Ni mambo mengine tu yananitatiza. Ila kama nilivyosema ..." Hapa akawatazama upesi. “it's not a big deal, guys. Msijali!"



    Kukawa kimya kidogo. Sauti za sahani na kijiko zikivuma, na kwa mbali watu wakitafuna.



    Kama dakika mbili hivi, Jona akauliza, “bila shaka ulienda kuonana na BC. Anasemaje kuhusu taarifa yangu?"



    Miranda akangoja atafune na kumeza kwanza. Ila pia awaze cha kusema kichwani.



    Akasema, “sikufanikiwa kuonana na BC. Alikuwa ametoka hivyo sijapata kujua msimamo wake kwenye hili. Japo najua litamkwaza kwa kiasi kikubwa."



    Jona akanyamaza. Aliendelea kutafuna na baada ya muda kidogo, Miranda akanyanyuka na kuwaaga anaenda kulala.



    “Unadhani yupo sawa?" Marwa akauliza punde baada ya kusikia Miranda akifunga mlango.



    “hayupo sawa," akajibu Jona. “na ni kwasababu ya BC."



    “BC?"



    Jona akatikisa kichwa kuafiki. “japo hakutuaga, atakuwa alikwenda kwa BC. Na bila shaka alichomwambia ndicho kinamnyima raha. Najua BC hatakubali kwa urahisi kile nilichokisema."



    Ila akapuuzia.



    “tule bana," akamwambia Marwa. “kila kitu kitajulikana kutokana na muda. Hatuna haja ya kuhofia sana mwisho tukapoteza appetite ya kula chakula kitamu kama hiki!"



    Ila kiuhalisia Jona hakuwa ‘amelipotezea' hili jambo. Na tangu hapa alifahamu fika kuwa inabidi awe makini zaidi maana lolote linaweza kutokea.



    **



    Saa tano asubuhi ... Shanghai, China.



    Katika asubuhi hii, Lee alikuwa yupo katika chumba fulani ndani ya ghorofa refu katika jiji la Shanghai. Ndani ya chumba hichi, kitandani kulikuwa kuna begi jeusi na kuna bunduki moja ndefu, yenye kiwamba chembamba cha kumezea sauti.



    Na juu kidogo ya bunduki hiyo kulikuwa kuna kifaa cha kumwekea mlengwa ‘targetini'. Kioo cha ku-zoom. Hapo mtu anapojaa kiooni na mlengaji akabofya kitufe, basi tunahesabu ashakuwa mfu!



    Bunduki hii, Lee aliipa jina la ‘Death lullaby' kumaanisha wimbo mzuri wa kubembelezea kifo. Wimbo huu unapopigwa basi lazima mpigiwaji alewe na afe kifo kitamu kisicho na maumivu.



    Na hicho ndicho ambacho Lee amekuja kukifanya hapa Shanghai. Amekuja kumletea mtu wimbo wa kifo. Mtu huyo aitwa bwana Chow, balozi wa Umoja wa mataifa.



    Alishapata taarifa kuwa mtu huyo yupo katika hoteli hii maarufu. Yani si hii ambay Lee yupo bali ile ambayo anaitazama tangu saa kumi na mbili asubuhi.



    Katika hoteli hiyo chumba namba mia thelathini, bwana Chow alikuwa amechukua hifadhi na ndani alikuwa na mwanamke kahaba. Hivyo basi ujio wake hapo hotelini ulikuwa ni wa faragha, hata mwanamke huyo alikuja hapo kama mteja mwingine tu, na chumba akalipia kabisa.



    Yote hayo kwasababu ya kutotengeneza ombwe la siri kuvuja. Na pale mlangoni kulikuwa kumesimama wanaume wawili walinzi. Wamevalia suti nyeusi wakisimama kama masanamu.



    Basi baada ya kungoja sana, hatimaye Lee anapata anachokitaka. Anamwona mwanamke yule kahaba akielekea ndani ya bafu akiwa amefunga taulo kifuani.



    Haraka anazamisha jicho lake kwenye kioo cha lenzi na kumweka mwanamke huyo tagetini. Ila si yeye anamtaka, lah! Alifahamu tu kama mwanamke huyo anaelekea bafuni basi nyuma yake atakuwapo bwana Chow.



    Na kweli. Bwana huyo akiwa amevalia taulo kiunoni naye alitokezea kwenye kamwanya kadogo kiooni akielekea bafuni. Alipita kwa kasi sana. Lee alitaka kubofya kitufe cha bunduki, ila akawahi kujizuia.



    Akatulia kwanza. Akaona ni vema akavuta subra kwani endapo akitupa risasi na ikamkosa bwana huyo basi atakuwa amefanya kosa kubwa sana. Na itamgharimu muda na pesa kumpata tena bwana huyo kimyani.



    Akashusha pumzi ndefu alafu akaendelea kukaa tenge kungoja. Hapa hakutaka hata mbu amsumbue. Ni kazi iliyohitaji uangalifu wa hali ya juu. Ana sekunde kama tatu tu za kufanya hilo tukio kwani kamwanya kadogo kalicho dirishani kangechukua sekunde tatu tu mtu kukapita asionekane tena.



    Kwa hivyo, japo hakujua Bwana Chow atatoka muda gani bafuni, alilazimika kukaa tayari muda wote kwa jicho lake kuwa kiooni na kidole chake kupapasa kitufe tayari kwa ajili ya tukio.



    Moja ... Mbili ... Tatu ... Nne ... Alikuwa anavuta pumzi akiwa ametulia katika hali ya juu. Ni pumzi yake tu ndiyo iliyosikika. Zaidi ya hapo hakuna kitu. Hata yale magari yaliyokuwa yanakatiza huko chini yakipiga honi ama kunguruma, hayakuwa yanasikika!



    Lee hakuwa anayasikia.



    Basi baada ya kungoja kama mwendo wa dakika ishirini na kitu hivi, mlango wa bafuni ukafunguka. Binti akatoka kutangulia. Lee akakaza kidole kwenye kitufe cha bunduki.



    Sekunde mbili mbele, akatoka bwana Chow. Mlengwa. Akapiga hatua mbili tu kufika kwenye kale kamwanya ka dirisha. Alipofika hapo hakunyanyua hata mguu, Lee akafyatua risasi, ikatoboa paji la uso la bwana Chow.



    Asipige hata kelele, akadondoka chini mfu. Yule mwanamke kahaba akapaza kelele za hofu kwanguvu! Wale walinzi wawili wakazama ndani. Mmoja akamtazama bwana Chow, mwingine akaangaza macho yake dirishani. Akaona tobo la risasi!



    Akapaza sauti, ni mdunguaji! Basi wale wanaume wakatoka na kuanza kukimbilia kule kwenye jengo alilokuwa Lee.



    Hata kabla hawajatoka ndani ya hoteli yao walikuwa tayari wameshachelewa sana. Kwani Lee ‘alishayeya' muda mrefu ndani ya sekunde kumi tu baada ya tukio.



    Alitumia kamba kutoka katika dirisha la chumba chake hivyo akapotea ndani ya eneo hilo pasipo hata mapokezi kujua.



    Sasa akawa ametimiza mtu wa sita kumuua kwa mkono wake. Kwenye orodha alibakiza watu wawili tu ambao kimahesabu alipangia kuwamaliza msibani.



    Yaani watakapohudhuria msiba wa bwana Chow.



    **



    Saa kumi na mbili jioni ..



    BREAKING NEWS!



    Sauti nzito ilivuma redioni. Kisha ikatafsiri, habari zilizotufikia hivi punde... Baada ya hapo sauti ya kike ikadakia ikisema,



    ‘kamanda mkuu wa polisi nchini, amekutwa mfu nyumbani kwake baada ya kusemekana amevamiwa na watu wasiojulikana ambao walimshindilia risasi nane kifuani mwake kabla hawajaondoka katika namna ya ajabu. Habari zaidi itawafikia majira ya saa mbili usiku.'



    Taarifa hiyo ikasambaa kwa upesi sana ndani ya jiji na ndani ya nchi. Ikazidi kuzua tafrani na hofu kwa wananchi kwani hata lile la mauaji ya Kamanda wa mkoa halikuwa limepatiwa ufumbuzi.



    Ni nani aliyemuua Kamanda mkuu? Je ni yule yule aliyemmaliza Kamanda mkoa?



    Na basi katika namna ambayo ilileta hoja nzito, serikali ya Uingereza ikahusishwa kwenye hili ikihesabiwa huenda ikawa ni kisasi cha kifo cha bwana Henry Marshall na ukamatwaji wa mtu wao, yaani Bwana Brown Curtis.



    Ila hayo yote hayakuwa sahihi, kwani aliyemuua Kamanda huyo alikuwa ni bwana Sheng. Sasa yupo ofisini kwake na habari alishazipata.



    Kamanda ilibidi afe tu, hakukuwa na namna. Ilibidi afe kwani anajua siri za Sheng na alijitoa mkondoni. Atabaki vipi hai?



    Sheng akazima redio baada ya taarifa hiyo na kwa kujipongeza, akachomoa mvinyo kwenye jokofu akajimiminia na kupiga mafundo kadhaa.



    Na akiwa hapo anakunywa, mara mlango wake ukagongwa. Akameza kwanza kinywaji kisha ndio akaruhusu mgongaji azame ndani ...



    Bwana huyo mlangoni alikuwa anahema kwanguvu mpaka Sheng alisikia akiwa ndani. Na kwa kujihami alishavuta droo yake yenye silaha...



    ***



    “we've finished!" Alisema bwana mzungu akimtazama bwana Brown aliyekuwa amekaa kitini. Walikuwa wamesimama wanaume watatu waliovalia suti, warefu na wenye miili mipana.



    Wanaume hawa ni miongoni mwa wale waliotoka Uingereza wakija hapa nchini kutenda kazi. Na sasa walikuwa wameshaifanya. Wapo hapa krejesha ripoti.



    “are you sure about that?" Brown Curtis aliuliza akijitengenezea kitini. Hata sigara aliacha kuvuta akawatazama watu wake kwa makini.



    “yes, we are sure," akasema mwanaume mwingine. “his head's swallowed ten of our bullets!"



    Bwana Brown akacheka sana mpaka akakohoa. Hakuamini kama bwana Sheng angekufa kwa urahisi hivyo. Alicheka na kulaani sana. Ila pia akawapongeza vijana wake kwa kuwamiminia kinywaji kwenye glasi.



    Basi wakanywa sana na hata wakapiga soga ndefu kuhusu Uingereza. Ila ikafikia mahali bwana Brown akawaambia, “there is one simple task I want you to do."



    Wale wanaume wakampatia masikio. Bwana huyo akawaeleza juu ya Jona. Anataka mwanaume huyo afe kwani aliyempatia hiyo kazi haamini kama ataitekeleza.



    Pia akawasihi, “if the woman trouble you, jus kill her."





    Wale wanaume wakabeba maagizo hayo na kwasababu usiku ulikuwa umeingia, wakaenda kupumzika wakilenga kufanya kazi hiyo kesho na huku wakitaka kazi nyingine itafutwe mapema kwani hiyo waliyopewa haitawia hata dakika.



    Basi BC akafurahishwa na hilo. Huu usiku wake ukawa mwororo kabisa. Alivuta sigara mpaka akajichokea. Pia akanywa kwa raha zake kamili.



    **



    Saa saba usiku ...



    Japo Shao hakuwa kwenye mipango yake, jambo hili la kuuawa kwake kulimshtua haswa bwana Sheng. Inakuwaje adui anaingia ndani na kummaliza mtu kama Shao?



    Adui huyo ni nani na anajiamini kiasi gani hivyo?Na ni kweli alikuwa amemlenga Shao ama yeye?



    Akiwa amesimama kandokando ya kaburi la Sheng ambalo lilikua limetoka kuchimbwa muda si mrefu, aliwaza sana. Hata siku hiyo hakuwa na hasira kama kawaida yake.



    Alikuwa ametulia na kwa kumtazama tu alionekana kumezwa na lindi kubwa la mawazo. Macho yake yalikuwa mekundu, lips kavu na uso wa njano.



    Mwili wa Shao ukazama ndani ya ardhi na kisha ukafukiwa upesi. Yote hayo Sheng akitazama ila asione chochote kwani alikuwa mbali haswa.



    Hata kila kitu kilipokamilika, ilibidi Sheng ashtuliwe kwamba kila kitu kimekwisha na sasa akapumzike.



    Wakati huo walinzi wakiwa wanatetemeka kwa hofu. Walijua Sheng atawamaliza kwa kile anachokiita uzembe.



    Ila kinyume kabisa na mawazo yao, Sheng hakutia neno. Na kwa ukimya kabisa akajigeukia na kwendaze. Akajiweka kitini sebuleni na kuendelea kuwaza sana.



    Alikosa amani na raha kabisa. Alijitathmini namna mambo yalivyoenda hapa karibuni. Pasipo kutarajia akajikuta anatoa chozi. Chozi la simba.



    Aling'ata meno yake kwanguvu akimeza mate yaliyokuwa na ladha ya klorokwini.



    Mara hodi ikagonga. Hajasema kitu, mtu akazama ndani. Alikuwa ni mwanaume yule aliyekuja kumpasha habari ya kifo cha Sheng. Mwanaume mrefu aliyevalia tisheti nyepesi nyeupe na suruali ya kadeti rangi nyeusi.



    Alikaa kitini na kumtazana Sheng kwa sekunde kadhaa kabla hajashusha pumzi ndefu na kuanza kuteta. Ni kama vile Sheng hakuwa anajali anachosema kwani alikuwa anatazama pembeni kwa umakini.



    Ila masikio yake yalikuwa yanadaka kila jambo hapa. Yalikuwa makini kuliko kawaida.



    “Wauaji walikuwa ni wazungu. Waliruka ndani na kuwamaliza walinzi takribani nane kabla hawajafika nyumbani kwa Shao. Ni watu wenye ujuzi wa hali ya juu. Walikuwa ni watatu ila walifanya tukio hilo kwa muda mfupi.



    Na japo waliua watu wengi, ilifanyika ndani ya muda mchache mno kiasi cha kutokujulikana! Na baada tu ya kummaliza Shao waliondoka zao. Hatujajua walitumia usafiri gani kwani hawakubakiza alama yoyote ile.



    Na hatujajua kwanini wamemuua Shao. Na walilenga haswa kummaliza yeye kwani walimnyookea na kummaliza na kisha wakapotea!"



    Sheng akafikicha pua yake pasipo kusema jambo. Akamtazama kijakazi wake huyo na kumwonyeshea ishara ya kichwa akimtaka aende, naye kijakazi akaenda zake kumpatia faragha.



    Sheng akaendelea kuwaza. Na baada ya muda ndipo akafungua kinywa na kusema neno moja, “Brown!"



    Kisha hakusema tena neno lingine lolote mpaka usiku huu unaishilia zake.



    **



    Saa nane usiku...



    Tap! Sauti ya chupa ililia baada ya kugonga meza. Kinoo akanguruma kama simba kupooza koo lake kwa pombe kali aliyogida.



    Akapiga kichwa chake kofi na kukitikisa kisha akamtazama mkewe, bibie Sarah. Macho ya mwanaume huyu yalikuwa mekundu haswa yakirembua.



    Kwenye sebule yao mezani kulikuwa kuna ‘bapa' mbili na kopo kubwa la juisi ya embe. Juisi hii ilikuwa ni ya Sarah na bapa hizi zilikuwa ni za Kinoo. Tayari alishamaliza moja, hii ya pili ilikuwa nusu sasa.



    Tayari Kinoo alishachanganya waya kichwani. Hakuwa sawa na alikwishalegea, ila kwa upande wa Sarah bado alikuwa ngangari. Japo macho yake yalikuwa mekundu kwa usingizi, alikuwa anajitahidi ‘kukaza'.



    Kuna lengo alitaka litimie. Hakutaka kulaza jahazi.



    “kwahiyo wewe sasa umeamuaje? Umekubali kirahisi hivyo?" Akauliza akimkuna Kinoo kidevu.



    “ah-ah! Mimi sio bwege unajua!" Kinoo akajitapa kilevi. “mimi natazama tu. Najua watazama kwenye anga zangu tuuu ... Mimi," akajipigapiga kifua. “mimi ndiyo Kinoo wa Kunikavu! Kisiki walichoshindwa wakata mkaaa!"



    Aliposema hayo akatulia kama mtu aliyepitiwa na usingizi.



    “ila mume wangu mi' n'na wazo," Sarah akateta akichezea kifua cha Kinoo. “wewe sasa hivi si waekutenga, wanakuona hufai, huna mana! ... Unaonaje na sisi tukamwaga mboga kabisa!"



    Kinoo akaguna kwa mbali kuitikia. Sarah akaendelea kunena,



    “Unaonaje tukatoa taarifa za yule jamaa, tukapiga mpunga mrefu tukafanya yetu mbele kwa mbele huko. Nani atajua?"



    Kinoo akagunia kooni, “mmmmhhh!" Kisha akapambana kufungua macho yake ya kilevi. Akamtazama mkewe.



    Sarah akaendelea kunena, “usiwe kama boya, watu washakuchoka, shika lako tembea mbele. Utakuja kujuta baadae nakwambia."



    Kinoo akanyaka kwanza chupa ya kileo, akanyonya mafundo kadhaa kana kwamba anakunywa juisi. Kisha akaiweka chupa mezani na kusema, “tatizo nini unajua .. Sijajua wapi walipomweka huyo bwege!" Akakohoa kidogo na kusema, “ila ngoja..." Akayoosha kidole juu.



    “nitafanya mchongo mmoja, mmoja tu, nitajua kila kitu alafu kama mbwai na iwe mbwai tu," akajivuna kilevi kisha akanyanyua tena kilevi na kupiga fundo kadhaa, sasa akamaliza na yeye akalala papo hapo.



    **



    Saa tano asubuhi ...



    “Kino! Kino!" Sauti ya kike ilisikika kwa mbali ikiita. “we Kino, amka bana simu yako inaita!"



    Kinoo akaufinyanga uso wake na kuangaza. Kichwa kilikuwa kinamgonga haswa, alijilaza palepale kitini kwa usiku huo mzima.



    Macho mekundu na mwili wa kichovu.



    Kabla hajasema kitu Sarah akamkabidhi simu inayoita mkononi. Kutazama akaona ni Miranda. Akapokea na kuiweka sikioni.



    “... Nipo home! ... Saa hii? ... Kuna ishu gani? ... Basi nipe kama robo saa ..."



    Simu ikakatwa.



    “kuna nini?" Sarah akawahi kuuliza. Kinoo akajikusanya na kunyanyuka zake. Alisema maneno kadhaa tu, “mambo yameharibika huko!" Kisha akayeya zake.



    Sarah akapaza sauti kumkubushia kile walichoongea usiku wake.



    “usisahau basi ile ishuu!"



    Kinoo akafungua geti na kwenda zake. Sijui kama alisikia ama alipuuzia.



    **



    Saa nane mchana ...



    “I think there is something for you, boss," alisema jamaa mmoja wa wale wanaume wa kazi toka Uingereza. Mkononi alikuwa amebebelea mfuko mkubwa mweusi wa rambo. Macho yake yalikuwa yanamtazama BC aliyekuwa ameketi kwenye kiti cha mbao bustanini.



    “what is that?" BC akauliza kabla hajapokea mfuko huo.



    “I don't know. Somebody on a bike delivered it," alisema bwana yule wa kizungu. Bado mkononi akiwa ameshikilia mfuko huo.



    “we have scanned it. It is not a bomb."



    “Open it," BC akaagiza.



    Bwana yule aliyeleta mzigo akauweka chini na kuufungua. Ndani akakuta kichwa cha binadamu!



    Kichwa hiki kilikuwa cha bwana Graham, bwana aliyeenda zake asubuhi ya siku hii kwenda kutimiza agizo la Bwana Brown la kummaliza Miranda na Jona.



    Kwenye mdomo wake alikuwa ana karatasi yenye ujumbe.



    **Bwana Brown akatahamaki haswa kuona haya. La haula! Akatoa karatasi hiyo mdomoni mwa kile kichwa cha bwana Graham na kukisoma.



    ‘Don't you ever do that again!' Kikaratasi kiliandikwa vivyo. Bwana Brown akakichanachana kwa hasira akiwa amepaliwa na ghadhabu kuu kifuani mwake.



    Akang'ata meno na kutazama huku na kule. Mbili haikuwa inakaa wala tatu haikuwa inasogea. Alikasirika mno na akawaza mawazo kadhaa kichwani mwake. Nani aliyemuua Graham?



    Jona asingeweza kufanya haya, aliamini hilo. Wala si yule rafiki yake, yaani Marwa. Hakuwa na uwezo huo wa kumwangusha mtu kama Graham.



    Hapa ni Miranda pekee.



    Kichwa hiki na huu ujumbe anamaanisha nini? Bwana Brown aliwaza. Ina maana Miranda amekaidi maagizo yake? Ina maana ...



    Ina maana Miranda ameamua kumkingia kifua Jona?



    Bwana Brown akajikuta anatabasamu katika haya. Alimtuma kijakazi wake amletee sigara yake kubwa na alipoitia kinywani akainyonya kwanguvu na kutema moshi kando.



    Alivuta sigara hii kama kichaa. Nadhani unajua huwa anafanya hivi akiwa kwenye hali gani. Alipovuta sigara mbili na kuzimaliza ndiyo angalau kichwa chake sasa kikatulia.



    Akawaza na kukubaliana mambo kadhaa na kichwa chake. Ahitaji tena kufanya kazi na WASWAHILI. Sasa kazi zake atazifanya na waingereza wenzake tu.



    “where is Randon? Call him for me!" Aliagiza kwa mdomo wake mkavu utemao moshi. Punde kidogo kijana mrefu, mwili mpana ndani ya suti kana kwamba mwanasheria mahakamani, akawasili.



    Akasimama kwa ukakamavu akimtazama bwana Brown.



    “from today, you will be my assistant supervisor. You will monitor your colleagues and make sure all things are under control," alisema Bwana Brown kisha akamtaka mwanaume huyo awaite wenzake wote hapo.



    Akalitekeleza hilo na ndani ya muda mfupi, wakawasili na bwana Brown akawaambia juu ya uteuzi wake. Wote wakaafiki.



    Sasa bwana Brown akampatia kazi bwana Randon. Kazi yake ya kwanza. Yeye pamoja na wenzake wawili, hivyo jumla watatu.



    Kazi hiyo ikiwa ni kummaliza Jona na Miranda. Hakuwapa hata muda wa kujivuta. Akaagiza ndani ya masaa matano kazi iwe imekwisha!



    **



    Saa kumi jioni ...



    Gari la Miranda, Range rover sport, ilitua mbele ya nyumba ya Kinoo, bwana huyo akashuka wakaagana na kisha akaenda zake ndani.



    Hakumkuta mkewe, ila punde akawasili akiwa amebebelea mfuko mweusi wa rambo. Alisema ametokea sokoni.



    Na alipoketi akamuuliza kuhusu ile gari kama ni ya Miranda. Alipojibu ndiyo. Akamuuliza, “umefanikisha ile ishu?"



    “ishu gani?" Kinoo akatoa macho.



    “naweee! Ina maana tuliyoongea jana umeshayasahau?" Sarah akatahamaki.



    “nini tuliongea jana?" Kinoo akauliza. Sarah akasonya na kisha akanyanyuka na kujiendea zake pasipo kusema kitu. Kinoo akabaki akiduwaa.



    Akawaza kidogo kabla hajashusha pumzi ndefu na kwenda zake kujinywea maji. Akarejea sebuleni kisha akatulia kwa muda kidogo. Hapa akakumbuka ‘ujinga' alioufanya jana usiku wa manane pamoja na mkewe.



    Akatikisa kichwa chake na kuzama zaidi kwenye mawazo. Akawaza sana hatma yake na maisha haya. Akafikiria kile Miranda alichomwitia, kuwa ameamua kuachana na Bwana Brown na anamtaka wafungue ukurasa mpya wa maisha yao.



    Akawaza sana na mwisho wa siku hakuona anga nyeupe kabisa. Maisha yalikuwa yanaelekea kuyumba. Kila kitu BC ndiye anatia mkono, leo wakiwa ‘yatima' mambo yataenda?



    Ni wazi yatachukua muda. Na hata zaidi, roho zao zitakuwa rehani kwani vipi kama bwana Brown akiazimia kuwasaka na kuwamaliza?



    Akashusha pumzi.



    “Sarah!" Akaita akiwa amelaza kichwa chake kitini. Mkewe akaja pasipo kuitika.



    “mke wangu, nimefikiria kuhusu lile jambo tuliloliongea jana usiku, na nimeona lile wazo lako ni vema. Mambo hayapo kwenye mstari na huenda tukicheza tukakosa yote haya."



    Sarah akatabasamu. Bado hakutia neno.



    “nimeshapata ninachokitaka," alisema Kinoo. “nimeshajua wapi wanapoelekea pia kuweka makazi yao mapya. So kilichobakia hapa ni kutoa tu siri hiyo tupate cash tufanye mambo mengine. Ikiwezekana tuondoke kabisa katika mji huu!"



    Hapa sasa Sarah akafungua kinywa, “hayo ndiyo maamuzi ya kiume sasa?"



    Akamkumbatia mumewe kwa furaha.



    “Shetani akikosa namna, humtuma mwanamke."



    ***



    Saa kumi na mbili jioni kuelekea saa moja usiku ...



    Gari aina ya Toyota Prado nyeusi ilitoka kwenye makazi ya bwana Brown Curtis ikiwa katika mwendo wa wastani.



    Gari hiyo ilivuma na barabara kwa dakika tano, ikafika mahali pa kona ili kuishika barabara iliyonyooka kwenda mpaka huko kuitafuta town.



    Ilipokata kona hii ... Mambo yakabadilika haraka mno! Badala ya kukutana uso kwa uso na barabara, gari hii ya bwana Brown ikakutana uso kwa uso na kifo!



    Ni katika namna ya ajabu. Mbele limesimama gari, Subaru, ikiwa imetanua mbawa zake kama mwewe anayetaka kupaa. Na kwenye mbawa hizo walikuwa wamesimama wanaume sita kwa ujumla. Kumbuka ni hatua chache tu toka kwenye kona.



    Wanaume hawa kila mmoja alikuwa amebebelea bunduki aina ya short machine gun (SMG) ambazo zimejawa na risasi za kutosha. Na tayari zimesha-kokiwa kwa ajili ya kazi.



    Ee bwana weh!



    Baada ya kitendo kilichochukua sekunde tatu tu cha gari la Bwana Brown kuchomoza, ikaanza kunyesha mvua za risasi haswa. Gari liliminiwa ‘njugu' za kutosha. Kioo kilikuwa nyang'anyang'a. Uso wote wa gari uliharibika vibaya mno.



    Kioo kilikuwa chekundu kwa damu.



    Gari lilitulia likifuka moshi.



    Hakukuwa na alama ya uhai.



    Wale wanaume baada ya hili tukio lililodumu kwa dakika tano tu, wakajitweka ndani ya gari lao na katika zile mbio uzionazo runingani kwenye mashindano, wakatimka!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ***



    “Good job. Are you sure he was in?" Sheng aliuliza.



    “hapana. Tulichokifanya ni kumiminia tu risasi gari lake katika namna ambayo haitamwacha salama yeyote aliye ndani."



    Si haba kwa Sheng. Aliwapongeza vijana wake kwa kufanya kazi hiyo vema, mengine atayaona kwenye taarifa ya habari.



    Ila kabla hajawaruhusu vijana hao waondoke, simu yake ya mezani ikaita. Akapokea na kuiweka sikioni.



    “yes ... Serious? ... Tell me the address ... Ok!"



    Alipokata simu akatabasamu na kuwatazama vijana wake wa kazi. Akawaambia kuna kazi ya kufanya imepatikana. Na kazi hii haitakiwi kulala hata kidogo.



    Akawatajia eneo ambalo inabidi wakafanye tukio. Na kazi hiyo ni kummaliza Jona na Miranda! Taarifa imeshatolewa juu ya wapi wanapopatikana.



    Basi vijana wale wakiongozwa na ‘waskaji' wake Lee, wakapokea agizo hilo na kuahidi kulitekeleza. Bwana Sheng akawaahidi endapo watatekeleza kazi hiyo, kila mmoja atapata kiasi cha milioni hamsini taslimu!



    Pesa shetani. Nani asingetaka mambo haya?



    ***



    Usiku wa saa tano ...



    Usiku wa saa sita ...



    Sheng alitazama saa yake. Ilikuwa vema haimdanganyi. Akachukua mvinyo na kuumiminia kweye glasi. Akagida na kuumaliza wote kabla hajamiminia tena glasini.



    Akapiga simu. Iliita. Haikupokelewa. Akaendelea kunywa zake kinywaji. Baada ya punde chache, akasikia hodi mlangoni. Akasimama upesi na kuendea mlango.



    Alipofungua alikutana na sura ngeni. Zaidi akakutana na mdomo wa bunduki.



    Macho yakamtoka pima. Asiseme kitu akaamriwa,



    “get on your seat!"



    Basi akajongea kwenye kiti chake na kuketi. Uso umejawa na hofu na macho yamejawa na maulizo.



    Mwanaume huyu aliyemnyooshea bunduki hakuonyesha kama ana utani. Alikuwa amekuja hapa kwa ajili ya kutenda kazi tu.



    Alikuwa ni mzungu.



    Alikuwa ndani ya suti.



    Alikuwa ni bwana Brown!



    “you can't kill me you Asian bastard!" Bwana Brown alibweka. “you are so fucking young to me. You are jus' nothing, nobody to me!" Bwana Brown aliwaka. Macho yake yalikuwa makali na mdomo wake anaupindisha.



    Ila bwana huyu hakuonekana mzima. Hakuwa mzima. Upande wake wa kushoto ulikuwa unavuja damu iliyochuruzika mpaka kidevuni. Jicho lake la upande huohuo lilikuwa jekundu.



    Suti yake ilikuwa chafu. Na hata shati lake jeupe lilikuwa lina mabaki ya damu ya moto kabisa. Na ungemtazama vema mkono wake wa kuume huu uliobebela bunduki, nao ulikuwa unachuruza damu. Kwa chini matone yalikuwa yanadondoka dondoka.



    Na hata huu mwendo wake haukuwa wa yule bwana Brown tumjuaye.



    “now who's laughing at last, you bitch!" Bwana Brown alisema aking'ata meno. “I ask you, who's laughing now??" Akapaza sauti akifoka.



    Bwana Sheng alikuwa kimya akimtazama. Bila shaka bwana huyu alikuwa ana jambo analifikiri kichwani. Alitakiwa kuwa mwangalifu mno hapa maana bwana Brown alikuwa ameweka kidole chake kwenye kifyatuo cha risasi.



    Akihema tu, risasi inapasua kichwa ama kifua chake na kumpeleka jehanamu mara moja!



    “All over England know me!" Bwana Brown aliendelea kunguruma. Chumba kizima alikuwa anasikika yeye tu. Ungejiuliza je wale walinzi wa bwana Sheng wanaojaa eneo hilo, wako wapi muda huo!



    “I am an abandoned rock. But look! Here I am still standing. I am on top of the hill and nobody can fall me down!"



    Bwana Brown aliposema hayo, akafuta pua yake kwa mgongo wa kiganja cha mkono wa kushoto kisha akatoa neno lake la mwisho.



    “now I am done talking. Send my wishes to hell!" Akafyatua risasi!



    Click!



    Click! Click! Hakuna kitu! Akaitazama bunduki ... Click!



    Haraka Sheng akajitupa na kufyatua miguu yake kupiga mkono wa bwana Brown wenye bunduki na kisha katika upesi akamkita na teke la kifua lililomwangusha Bwana Brown chini!

    Kisha akacheka.

    “who's laughing now?" Akauliza kwa kebehi. Bwana Brown akajikusanya na kunyanyuka. Akajipanga kupambana.

    Ila asingeweza. Alikuwa amechoka. Alikuwa hajiwezi. Alikuwa ana majeraha.





    Alijaribu kutupa shambulio la ngumi, ila kwa Sheng akaona mchekechea. Akamlamba bwana huyo mateke mawili tu, akadondoka chini akiwa mfu!



    Ni baada ya punde tu maiti ya bwana Brown ikaanza kumwaga damu kuchafua sakafu.



    “send my wishes to hell," bwana Sheng alinung'una akiwa amebinua mdomo kisha akaendea jokofu lake na kutoa kinywaji. Akakiminia kwenye glasi na kuketi kitini.



    Haki alikuwa ana haja ya kusherehekea kwa maana aliponea chupuchupu haswaa kutolewa roho. Alijipongeza kwa mafundo manne ya kinywaji kisha akashusha pumzi ndefu na kuegesha kichwa kitini.



    Akawaza kama angelikuwa ameuawa. Hakuna mtu aliyekuja kichwani mwake isipokuwa mkewe na mtoto wake. Aliwaza sana vipi kama leo ingekuwa ndiyo mwisho wa pumzi yake?



    Akaona kuna haja ya kuwasiliana na mkewe na mwanae ambao wote wapo China, Beijing. Ila asingeweza kuwapigia simu muda huo. Na ubaya ni kwamba asingeweza hata kuacha ujumbe wakapelekewa kwani familia yake hii ilikuwa ni ya siri.



    Hakuna mfanyakazi wake yeyote aliyekuwa anayeijua kwani ilikuwa ni mwiko haswa! Viongozi wote wa juu wa familia hii ya Wu hawakutakiwa kuwa na familia kabisa. Na yote haya ni sababu ya kutotoa mwanya wa udhaifu.



    Endapo kiongozi akiwa na familia, maadui watapata fursa ya kumkamata kwa urahisi wakitumia mke na watoto kama chambo.



    Ngo! Ngo! Ngo!



    “Mkuu!" Sauti ilisikika mlangoni na kumtoa Sheng kwenye kawimbi ka mawazo kalichokuwa kamemchukua. Hakuitikia, alingoja asikie tena sauti hiyo na alipohakikisha anaifahamu, akaendea mlango na kuufungua.



    Alikuwa ni kijakazi wake



    “Upo salama, mkuu?"



    “Ulikuwa wapi mpaka maadui wanafika kwenye makazi yangu??" Sheng akafoka.



    “mkuu umesahau kuwa uliniagiza?"



    “vipi wenzako wamesharudi?"



    “hapana, bado hawajarudi."



    “umefanya nao mawasiliano yoyote?"



    “hapana! Sijawatafuta tangu walipoondoka. Kwani hawajakupigia?"



    “hapana. Hawajanipigia."



    Sheng akaangaza macho yake huku na kule, hakuona watu. Alistaajabu akauliza walinzi wako wapi. Yule bwana aliyemjia akamwambia wengi wao wameuawa. Maiti zao zinazagaa huko mazingirani.



    Ina maana Bwana Brown ndiye aliyewamaliza hao wote?



    “kuna maiti mbili pia za wazungu!" Akaeleza kijakazi yule akionyeshea uelekeo. Basi akiongozana na bwana Sheng, wakaenda huko.



    ***



    Asubuhi ya saa mbili ... Kwa mbali redio ya simu inanguruma ...



    “ulifanikiwa?" Akauliza Sarah akimtazama mumewe. “maana hata hukunambia namna mambo yalivyoenda."



    “yah!" Akasema Kinoo kisha akadaka kikombe cha chai na kunywa fundo moja. “nilifanikiwa. Niliwapata nikawapasha habari."



    “sasa?"



    “nasikilizia. Walinambia watan'tafuta wakithibitisha kama habari hizo ni za kweli."



    “watathibitishaje sasa?"



    “si wataenda kumkamata huko! Huoni redio ipo on hapa nataka nisikie kila kitu."



    Sarah akaguna.



    “vipi kama wakimkamata alafu wasikupe hiyo pesa?"



    “hawawezi bana."



    “unajuaje? Wakikuzunguka na kwenda zao?"



    “Sarah, unaweza ukaniacha nikanywa chai basi?"



    “chai gani? - Hii ya rangi? Si tujadili vya maana lakini Kinoo?"



    “ningoje basi nimalize! Kwani nachukua mwaka hapa!"



    Kabla Sarah hajatia neno, mara sauti ikasikika redioni kutangaza habari zilizowasili hivi punde. Wote wakajikuta wananyamaza kusikiliza kwa umakini.



    “maiti sita za wanaume pamoja na bunduki nne zimekutwa kandokando ya mto Msimbazi na kusababisha taharuki kwa wakazi wa karibu na maeneo hayo. Mpaka sasa maiti hizo hazijatambulika, na uchunguzi unaendelea."



    Habari ikakata. Kinoo akatazamana na Sarah.



    “wanaweza wakawa wakina Miranda au?" Kinoo aliuliza kana kwamba kuna mtu mwenye majibu. Haraka akanyakua simu yake na kupiga, ikaita mara mbili na kupokelewa na sauti ya kike.



    “halo Miranda! ... Vipi? Unaendeleaje? ... Safi, upo salama? ... Kabisa? ... Umesikia hiyo habari ya watu waliokutwa mtoni? ... Poa, sawa!"



    Alipokata simu akanyanyuka na kuacha chai.



    “wapi sasa? Umejua ni wakina nani?" Sarah aliuliza. Kinoo hakujibu, akazama chumbani na baada ya dakika moja akatoka akiwa amebadili nguo ya juu, amevalia kibodi cheusi.



    “baadae!" Akamuaga mkewe. “tutaongea vizuri baadae!"



    Alikuwa kwenye haraka haswa.



    ***



    Majira ya jioni ya saa moja ...



    Habari hii ya maiti mtoni ikiwa imesambaa na kukamata jiji na nchi zima, Sarah aliipata mwanya wa kuifaidi kwa kupitia mitandao ya kijamii ambayo haikuwa nyuma kabisa kwa mfululizo wa picha na vimaelezo vya hapa na pale.



    Alipekua kila picha aliyoiona mtandaoni na akasoma kila neno lililoandikwa. Kila mtu akaeleza yake na kusimulia katika namna yake, ila kwa upande wa Sarah bado hakupata alichokuwa anahitaji.



    Japo alipekuwa picha zile zote, hakuona sura ya Jona. Hii ikampa maswali kidogo, ina maana Jona atakuwa hajakamatwa na polisi? Na wale watu waliouawa, watakuwa wanahusika naye kwa namna yoyote ile?



    Akiwa mawazoni, mlango unagongwa. Anaacha simu na kwenda anamkuta mwanaue aliyevalia helmet akiwa amebebelea mfuko mweusi.



    “mzigo wako nimetumwa kukuletea."



    Sarah alipoupokea, mwanaume huyo hakukaa, akaenda zake. Sarah akaketi kitini na kufungua mzigo huo.



    ***



    Akakuta boksi kubwa jeupe. Akalifungua na ndani akakuta rundo kubwa la pesa zilizo katika mfumo wa dola za kimarekani. Akatabasamu, na mwishowe akaangua kabisa kicheko.



    Alifurahi mno kuona pesa hizo. Alihisi moyo wake unamwenda mbio, haraka akanyanyuka na kuzipeleka chumbani. Akajifungia huko, na kuhesabu kibunda kimoja baada ya kingine.



    Hakuwa anajua ni kiasi gani cha pesa hicho ila alifahamu ni pesa nyingi. Nyingi za kuweza kutia mtu kiburi. Ila akiwa anatazama pesa hizo, akaona na kipande cha kikaratasi.



    Haraka akakichomoa na kukisoma maana kilikuwa na ujumbe.



    ‘Habari yako ilikuwa ya kweli, ila hatujafanikiwa kumpata mlengwa. Tunatumai utakuwa na taarifa zaidi. Kila taarifa itakuwa na thamani ya pesa hizi.' Baada ya maelezo hayo, ikaandikwa namba ya simu kwa chini. Namba mbili.



    Basi Sarah akajikuta anataka pesa zaidi. Alitamani Kinoo arejee nyumbani upesi ampashe habari hizi na kumtia hamasa.



    Ila wakati huu anamngoja mumewe, acha sisi tujifikirishe kidogo. Mtu huyu aliyemletea hizi pesa ametumwa na nani? Bila shaka ni Sheng. Na mwanaume huyo tayari ameshapokea taarifa za kuuawa na kutupwa kwa vijakazi wake huko mtoni.



    Na hata zaidi ameshatambua kuwa taarifa hizo za Jona na Miranda zimetoka kwa nani kwa kupitia Sasha. Bwana huyu anajua atapata zaidi mambo ya Jona kwa kumtumia mwanaume huyu.



    Na mara hii akipata taarifa, ataingia mwenyewe uwanjani kucheza mziki ambao vijana wamefeli.



    Simu ikaita. Sarah akapokea baada ya kuitazama kiooni na kujua ni ya dada yake, Sasha.



    “Hallow!"



    “mambo?" Sauti ya Sasha ilisikika vizuri kwenye simu.



    “fresh. Vipi wewe?"



    “niko poa. Vipi upo mahali salama?"



    “yah! Niko fresh."



    “jamaa yupo wapi?"



    “ametoka kidogo. Ila nadhani anakaribia kuja."



    “vipi umepokea mzigo wowote?"



    “yah! Nimepokea eenh!"



    “poa. Nitakutafuta baadae au kesho. Uwe karibu na simu yako, sawa?"



    “Poa!"



    Simu ikakata.



    **



    Majira ya saa mbili kasoro usiku ... Mahali fulani tulivu ...



    “Kwahiyo sasa mtafanyaje?" Aliuliza Kinoo. “maana maisha yenu yamekuwa kama swala."



    Miranda akashusha pumzi ndefu, alafu akanywa kinywaji chake ndani ya glasi, juisi ya dhabibu, kisha akasema;



    “Tutazama kipi cha kufanya. Jona anarejea wa kasi kwenye hali yake na nadhani njia nyepesi sasa ya kuwa salama ni kwa kum-face adui yetu badala ya kumkimbia."



    Akanywa kwanza kinywaji kisha akaendelea na maneno, “kadiri tunavyokimbia ndivyo anavyozidi kutuwinda. Hakuna mahali tutakayokuwa salama. Ila kwa sasa hatutaweza kwenda kukabiliana naye.



    Nadhani tunahitaji siku kama tatu au nne hivi za kujipanga na Jona kuwa sawia kabisa."



    “sasa kwa muda wa hizo siku, mtakuwa mnakaa wapi?" Kinoo akauliza.



    “hatuwezi tukapata mahali pa kudumu. Tutajiegesha hotelini kwa siku hizo. Ntakupa habari ni wapi tutakapokuwa punde tu ntakapopapata."



    “Sawa."



    Kinoo akatazama saa yake ya mkononi. Muda wa kuondoka ulikuwa umekaribia. Ila kabla hajaaga akamuuliza Miranda,



    “umepata habari zozote za BC?"



    “hapana," Miranda akajibu na kisha akauliza, “vipi kuna mpya yoyote?"



    “hapana. Ila auhisi anaweza pia akawa amehusika kuleta hao watu kuwavamia?"



    “hapana. Watu waliotumwa walikuwa ni wanaume weusi. Endapo wangekuwa ni wazungu basi ningemshuku bwana Brown moja kwa moja. Na hivi tangu wazungu hao wamekuja, sidhani kama atakuwa anatukumbuka."



    Kinoo akatazama tena saa yake kisha akasimama. Sasa akaaga na kwenda zake. Baada ya dakika tatu Kinoo hakuonekana, Miranda akanyanyua simu yake na kupiga.



    **



    Majira ya saa nne usiku ...



    “Hallow!" Bwana Sheng alipaza sauti akiongea na simu yake. Alikuwa ameketi sebuleni mwa nyumba, amekunja zake nne. Amevalia nguo nyepesi za kulalia.



    “umepata ujumbe wangu? ... Ok, nakusikiliza ... Sawa, hamna shida, tukubaliane tu, nadhani unajua ninachotaka ... Sawa, basi tutafanya vilevile si ndio? ... Sawa."



    Simu ilipokatika, akapiga na kusema maneno machache tu kisha akakata. Baada ya muda kidogo wakaja wanaume wawili vijakazi wa Sheng. Wakasalimu na kuketi kitini kusikiza wito.



    “kesho tutakuwa kazini. Nimeshapata taarifa nyingine ya makazi ya Jona. Jiandaeni maana muda wowote nitawataka twende huko! Muwataarifu na wenzenu sita."



    Baada ya kusema hayo, wale vijakazi wakaenda zao. Bwana Sheng akabakia hapo sebuleni akinywa taratibu kinywaji chake na akiwaza kwa mbali.



    Punde kidogo simu yake ikaita, alipotazama akaona ni mkewe toka Beijing. Akashangaa kuona amempigia majira haya. Akapokea na kuibandika simu sikioni.



    Mkewe alikuwa amemkumbuka na anamuulizia ni lini atarudi China kumwona kwani hata mtoto amekuwa akisumbua sana. Hata shule haendi anakesha akilia anataka kumwona baba.



    Kwa sauti ya upole kabisa, bwana Sheng akaongea. Akamwahidi mkewe kuja kumwona pindi atakapomaliza kazi fulani kubwa mbele yake.



    Japo mwanamke hakumwamini, alimsisitizia zaidi. Lazima aje kuwaona muda mfupi tu baada ya kumaliza kazi hiyo. Kisha simu ikakatwa.



    **



    Majira ya saa saba mchana ...



    Limousine nyeusi ilingia ndani ya uwanja wa hoteli. Dereva akashuka na kufungua mlango wa nyuma akatoka mwanaume fulani mweusi aliyevalia suti rangi ya kijivu.



    Mwanaume huyu alikuwa mrefu, na kichwa chake hakikuwa na nywele. Suti yake ilimkaa vema na kwa kumtazama upesi ungesema ni mtu fulani mkubwa taasisi fulani.



    Mdomoni alikuwa ana sigara kubwa na kwenye mkono wake wa kushoto alivalia saa ya dhahabu.



    Mwanaume huyo, akiwa anapiga hatua za kikakamavu, akaendea mapokezi na kujitambulisha anaitwa bwana Lorenzo Kagula, anahitaji mapumziko kwa muda wa siku tatu hotelini hapo.



    Basi mhudumu, mdada fulani mweupe aliyevalia sare, akiitwa Lidia Kombo kwa mujibu wa kibandiko kifuani mwake, akatazama orodha ya vyumba na kisha akampatia bwana huyo chumba namba 114.



    “Samahani, unaweza ukanibadilishia. Nishawahi kuja hapa na sikupenda hiko chumba. Unaweza ukanitazamia chumba namba sabini na kitu hivi?"



    “usijali," akasema mhudumu kisha akatupia macho yake kwenye orodha tarakilishini, baada ya punde akasema,

    “aaahm ... Kuna chumba namba 74!"





    “si mbaya"



    Bwana huyo akalipia na akageuka aende baada ya kukabidhiwa ufunguo. Na kwasababu alisema ni mwenyeji basi hakuhitaji kusindikizwa.



    Ila upesi akarejea kwa mhudumu na kumwambia,





    “samahani, dada. Kuna wageni wangu pia ningependa wafikie hapa. Vipi kuna vyumba vya kutosha?"



    “pasipo shaka," akasema mhudumu kwa tabasamu. Basi bwana Lorenzo akaenda zake akipiga mluzi.



    Baada ya kama dakika kumi na tano, gari aina murrano nayo ikaja hapo hotelini, wakashuka wanaume watatu waliobebelea briefcase. Waliingia ndani ya hoteli na kisha wakauliza kuhusu ujio wa bwana Lorenzo hapo hotelini.



    Walipohakikisha yupo, wakaweka oda ya vyumba.



    “naomba utupatie chumba namba 75 au 76 ili tuwe karibu naye. Ni mwenzetu."



    Yule dada mhudumu akasikitika akiwaambia vyumba hivyo vina watu, kwa kuwasaidia akawatafutia na kuwapatia vya namba 80 na 86.



    Basi wakalipia na kwenda zao wakisindikizwa na mhudumu mpaka milangoni. Mhudumu akaenda zake akiwakabidhi funguo.



    Wote wakaingia chumba namba 80, na baada ya dakika chache wakatoka na kwenda kwenye kile chumba cha Lorenzo. Mmoja akasema,



    “vile vyumba viina watu. Bila shaka watakuwamo humo kama tulivyopewa maelezo."





    Bwana Lorenzo akatikisa kichwa kisha akasema, “ila ni vema tukahakiki, usiku tumalize zoezi. Si umekuja na vile vitu nilivyokuambia?"



    “ndio."



    Mmoja wa wale mabwana waliokuja ‘kumcheki' Lorenzo akafungua briefcase. Ndani kulikuwa na nguo, sare zinazofanana na za wahudumu wa hoteli.



    Bwana huyo akazivaa na kufanana vilevile na wahudumu, kisha akatoka ndani kuendea mlango wa chumba namba 75.



    Alipofika hapo akabisha hodi.



    “mhudumuu!" Akapaza na sauti.



    ***

    Baada ya muda kidogo mlango ukafunguka, akachungulia mwanamke mmoja mweupe mwenye nywele mtindo wa afro.



    “Samahani, nimekuja kuchukua mataulo," alisema bwana huyu aliyekuja hapa kwa kujidai mhudumu.



    Yule dada akatazama ndani kisha akarudisha uso wake kwa huyo mhudumu na kumwambia,



    “mataulo si mmeshachukua? Au mwayabadilisha mara ngapi kwa siku?"



    Huyu bwana akatabasamu alafu akaomba radhi na kusema, “kama yameshachukuliwa hamna shida, kuna tatizo lingine lolote?"



    Dada yule akatikisa kichwa kisha akafunga mlango na mhudumu yule akaenda zake. Alirejea kule alipowaacha wenzake na kuwaambia yale aliyoyakuta huko.



    “ina maana hawatakuwapo?" Akauliza yule mwanaume aliyejinasibu kwa jina la Lorenzo Kagula.



    “hapana!" Akasema mwanaume mwingine. “tusikate tamaa kiuwepesi hivyo! Kwani kufungua mlango mtu mwingine kunazuia mlengwa watu kuwepo ndani?"



    Basi wakakubaliana kwamba inabidi wafanye vivyo hivyo alimradi misheni yao ikamilike. Inabidi tu wavute muda na kisha baadae, majira ya usiku, wakakague vyumba vyote viwili ambavyo wamepewa taarifa kuwa vinawahifadhi watu wao.



    Basi Lorenzo akampigia simu mkuu na kumpa mrejesho wa kinachoendelea. Na kwasababu za kuvutia muda, wakaagiza vinywaji vikali kupooza makoo yao.



    Wakanywa na kujilaza.



    Baadae wakati giza likiwa limeingia, ni majira ya saa mbili usiku, bwana Lorenzo akashtuka na kutazama saa yake ya mkononi.



    Kichwa kilikuwa kinamgonga kwa mbali. Wenzake wote walikuwa wote walikuwa wamejilaza hoi. Akataka kuwaamsha ila akasita. Muda wa misheni bado haukuwa umefika.



    Basi kurejea usingizini, akapiga tena kinywaji, chupa nzima yeye mwenyewe. Hapo akalala kama mfu wa kale. Hata mwivi angeweza kumnyanyua na kuiba godoro kisha akamrudisha na asisikie lolote lile!



    Masaa yakaenda. Ilipohitimu majira ya saa sita kasoro usiku, mmoja wao, yule aliyeigiza mhudumu, akaamka. Akawakurupua wenzake na wote wakaamka isipokuwa Lorenzo.



    Walijitahidi sana kumwamsha ila wapi. Hata kama angeamka asingeweza kufanya kitu kwa hali aliyomo. Basi ikabidi wale wengine wapange kufanya tukio pasipo yeye maana isingewezekana misheni hiyo kutokufanyika siku hiyo.



    Na hapo tayari Lorenzo, ambaye yupo hoi hajiwezi, alikuwa ameshamwambia bwana Sheng kuwa misheni hiyo ipo chini ya uwezo wao, haina haja ya yeye kusumbuka.



    Basi mabwana hawa wakaweka kila kitu sawa. Walikuwa na bunduki mbili zilizojaa risasi. Wakavalia na nguo nyeusi za kazi isipokuwa mmoja ambaye alitumwa akatazame usalama kwanza.



    Bwana huyo akatoka na kwenda, baada ya dakika kadhaa akarejea na kuwaambia kila kitu kipo sawa. Basi akavalia sare za wahudumu na kisha wakaenda huko chumbani wanapohisi watu wao wapo.



    Yule bwana aliyevalia sare akagonga hodi na kusema, “mhudumuu!" Kisha akangoja.



    Kimya.



    Akagonga tena na kupaza sauti ya kujitambulisha kuwa mhudumu, ila napo ikawa kimya. Akawatazama wenzake. Ni kama vile waliwasiliana kwa macho, bwana ‘mhudumu' akarudia tena kugonga.



    Napo bado kimya. Ila kwa ndani taa ilikuwa inawaka na hili ndilo liliwapa imani kuwa kuna watu ndani.



    Wakatazamana.



    Mmoja wao aliyekuwepo nyuma, akachomoa kitu mfukoni kisha akachokonoa kitasa. Sauti ikasikika tas-tas! Na alipobinya kitasa, mlango ukaitika kwa kufunguka.



    Hawakuingia kwanza, wakangoja kuskiza. Kama sekunde tano hivi, kisha yule bwana mhudumu akazama ndani.



    Na mara wenzake punde wakazama ndani.



    Wakatazama huku na kule. Hakukuwa na mtu. Wakapekua chumba kizima, kila kona, hakukuwa na kitu!



    Basi wasipoteze muda, wakatoka na kwenda kile chumba kingine, cha pili yake. Huko hawakupoteza muda kama ilivyokuwa kwenye hiki cha kwanza, wakachokonoa kitasa na kuzama ndani.



    Kulikuwa ni kiza. Waliwasha taa na kuangaza. Hamna kitu! Wakasaka kila kona, hakukuwa na kitu! Hapa wakatazamana kwa butwaa.



    Iliwezekanaje hili? Au taarifa walizopewa hazikuwa sahihi? Ilibidi wajiulize mara mbilimbili. Wakatoka chumbani mule na kurejea chumbani mwao.



    Wakamkuta bado Lorenzo amelala. Hawakuhangaika naye, wakateka simu na kupiga kwa mkuu wao kumweleza yaliyojiri.



    “ndio, namba ni hizohizo! ... Hamna mtu mkuu, saa zile mara ya kwanza kulikuwa kuna kabinti flani hivi. Sasa hivi hata naye hayupo maana hata tungempata yeye kwa namna moja angeweza kuwa na majibu ... Ndio, mkuu ... Sawa."



    Simu ikakata.



    “anasemaje?"



    “turudi makaoni!"



    “saa hii?"



    “ndio."



    “na hii mishe vipi?"



    “amesema huenda taarifa sio sahihi au watakuwa wameshashtukia. Anampigia mtu aliyempa taarifa kwa maongezi zaidi."



    Wapoelezana hayo, wakaanza kujipanga waende zao. Walipotia kila kitu kwenye begi, wakamwamsha Lorenzo. Bado hakuamka.



    Walimpigapiga makofi na kumvutavuta lakini bado haikusaidia. Ila wakiwa katika huo mchakato, mmoja wao akaona kama rangi nyekundu shukani.



    Kutazama vema, damu! Wakamgeuza Lorenzo aliyekuwa amelala kifudifudi, wakagundua mwanaume huyo alikuwa ameuawa! Tumbo lake lilikuwa limejawa na damu ambayo bado ilikuwa ya moto kabisa!



    Kutazama vema zaidi, alikuwa ana jeraha la kisu, matundu matatu tumboni! Wakapata kitendawili. Nani aliyemuua Lorenzo ndani ya muda mfupi ambao walitoka?



    Hapa wakajikuta wanaamini kuwa walengwa wao walikuwapo mulemule ndani ya hoteli. Na si tu kuwapo bali pia walikuwa wanawafuatilia kiasi cha kujua kuwa wametoka na wakaenda kummaliza Lorenzo!



    Haraka wakatoka nje na kuanza kuangaza huku na huko. Na hapa wakashirikiana na walinzi wa hoteli baada ya kuwapa taarifa, msako ukafanyika kote hotelini.



    Na hata baadae wakapitia taarifa za watu wote waliokuwamo humo ndani ya hoteli ili wapate kubaini nani hakuwapo au aliyetoka hivi karibuni.



    Wakagundua kuna watu wawili tu waliotoka, nao wote wakiwa ni wanaume, kwa majina Zebedayo na Derick, wakiwa ni wakazi wa chumba namba 200.



    Zaidi ya hapo hakuna kingine kilichopatikana.



    Mabwana wale wakampigia simu mkuu wao na kumweleza habari hizo ambazo zilimshangaza na kumghafirisha sana.



    Ila mchezo huu ulianzia wapi na ulifanyikaje?



    Ni hivi, wakati mhudumu yule feki wa kwanza kabisa alipokuja kwenye chumba walichokuwa wanakishuku kuwa kina watu wao, akamkuta mwanamke mgeni hapo, ndipo mambo yalipoanza kuchanganyia.



    Kwanza, mhudumu huyu hakuwa na kibango cha jina lake kama ilivyo kwa wahudumu wote hapa hotelini. Pili, japo sare yake ilijitahidi sana kufanana na za wahudumu wa pale, bado zilikuwa na kasoro kidogo kwenye ukoleaji wa rangi.



    Na tatu, kuja kuulizia taulo kwa majira yale, tena ikiwa tayari yashabadilishwa asubuhi, kulileta shaka. Basi mwanamke huyo aliyempokea, akafikisha taarifa kwa mtu aliyemwomba afanye hivyo kwani alitegemea kutakuwa kuna ugeni mahali hapo.



    Na alipotoa taarifa hiyo tu, mwanamke huyo akaondoka zake maana alishamaliza kazi.



    Baada ya hapo, mengine yote yakawa historia. Mwindaji akawindwa kwa ustadi.



    **



    Saa tano asubuhi ...



    Hodi sasa ilikuwa inagongwa kama fujo mno mlangoni. Hata Kinoo aliyekuwa amelala usingizi wa mfu akaamka. Akghafirika akipaza sauti yake nzito kuuliza kwa kufoka.



    Hakujibiwa.



    Akatazama kando, mkewe hakuwapo. Kichwa nacho kilikuwa kinamuuma sana. Alipata hata tabu kusimama. Alijikongoja mpaka sebuleni akitaka kuelekea mlangoni, ila mezani akaona unga fulani mweupe.



    Akaujongea na kuutazama. Akaubinyia kwenye kidole chake na kunusa. Akapata shaka. Kabla hajauendea mlango, akaenda jikoni. Akarudi tena chumbani. Akagundua nguo za mkewe hazikuwapo!



    Mwanamke ametoroka? Alijiuliza. Ina maana jana usiku alintilia dawa kwenye kinywaji? Akawehuka. Akili yake ikamtuma moja kwa moja kwenye pesa. Tazama pesa kama zipo!



    Akatazama, hola! Patupu!



    Akahisi miguu imemwishia nguvu. Akahisi mwili umekuwa wa baridi kama barafu. Akahisi haja zote kwa mpigo!



    Bam! Bam! Bam! Mlango ukabamizwa tena na tena.



    ***





    Akajikakamua na kuuendea. Alipofungua akakutana na mwanadada Miranda. Moyo wake ukapiga fundo kubwa, ila akajitahidi kubana hisia.



    "Miranda!" akaigiza kutahamaki. "mbona bila taarifa mama?"



    Miranda hakujibu. Akazama ndani na kwenda kuketi kitini. Akakunja nne.



    "Habari yako?"



    "Salama," akajibu Miranda na kisha akauliza, "vipi wewe?"



    "Mimi niko poa tu," akasema Kinoo. Ila kiuhalisia hakuwa salama. Hata uso wake ulimsaliti. Alijawa na hofu. Na kwa namna fulani alikuwa anasutwa roho.



    Akajichekesha.



    "karibu bana. Naona Leo umeamua kun'tembelea!"



    "Kinoo," Miranda akait kisha akamtazama mwanaum hiyo machoni na kumuuliza, "mkeo yupo wapi?"



    Kinoo akatazama kando na kando kisha akasema, "sijui ameenda wapi. Ametoka kidogo."



    "Una uhakika?"



    "yah! Hayupo ndani. Vipi kwani kuna shida yoyote?"



    "Hamna shida kwangu. Ila shida ipo kwako."



    "shida gani?"



    Miranda hakusema kitu. Akabaki akimtazama Kinoo kwa sekunde kadhaa. Akatazama chini na kisha akashusha pumzi ndefu.



    "Kinoo," akauvunja ukimya kwa kuita. "Kama isingalikuwa wewe ni jamaa yangu niliyetoka nawe mbali, hata sasa ningekuwa nishakumaliza. Sijui ni nini kimekukalia kichwani mpaka ukadiriki kututoa sadaka kiasi hiki."



    Kinoo akakunja sura kwa mkanganyiko.



    "Sijakuelewa. Ni nini unamaanisha?"



    "Unajua kila ninachokisema hapa, Kinoo. Wewe si mgeni hata kidogo. Unajua ulichokitenda na kama nakusingizia, nitazame unambie haujui."



    Kinoo akatazama chini.



    Kukawa kimya kwa sekunde kadhaa.



    "Ni yule mwanamke, sio?" Miranda akauliza. Kabla hajapewa jibu, akaendelea kunena, "tangu alipoingia mwenye maisha yako nilijua vitu havitakuwa kama vilivyokuwa hapo awali. Nilifahamu fika, na ndiyo maana hata kukushirikisha tena kwenye mambo yangu nilisitisha."



    Akanyamaza. Kinoo bado alikuwa anatazama chini.



    "sasa yupo wapi hiyo mwanamke? unajua hata alipo hivi sasa? ila mimi nipo hapa. Nipo hapa kama nilivyokuwapo tangu nyuma. Je kama ningaliuawa, nani angalikuwa nawe hapa?"



    Kinoo hakusema kitu. Ila macho yake yalianza kuwa mekundu.



    "Hata pesa si hajakuachia?" Miranda akaendelea kunena. "Amekuacha kama alivyokukuta ... Nimeshangaa sana ni kwa namna gani alivyokufanya mjinga. Ulikuwaje mjinga kiasi hiki ndugu?"



    Kimya. Miranda akasimama.



    "Nakutakia maisha mema," akasema na kwendaze kuelekea mlango, ila Kinoo akamdaka mkono na kumsihi akae. Sasa macho yake yalikuwa mekundu zaidi.



    "Miranda," akaita. "Nisamehe sana. Nastahili kuadhibiwa vikali. Siku zote umekuwa mkarimu na kama dada kwangu ila nikachagua kukuangamiza. Nimekabwa na hayà, hata uwepo wangu ni unafki mtupu.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tafadhali, naomba uniangamize. Nami nimeridhia kwa hali zote."



    "Sina haja ya kukuua, Kinoo," Miranda akajisemea. "Nina damu nyingi za kuziangamiza ila yako si mojawapo. Niliona tu tuachane kwa amani. Kila mtu akawa na maisha yake. Inatosha."



    Ila Kinoo bado hakuwa radhi kumruhusu Miranda aende zake. Akiwa amemng'ang'ania mkono akamsisitiza amsamehe. Na yupo tayari kufanya lolote lile kama nauli ya msamaha wake."



    Baada ya hiyo kauli, Miranda akaketi na kusema,



    "Kuna kazi ya kufanya. Upo tayari?"



    **



    Saa nane mchana ...



    "Kwahiyo una mpango gani na hiyo mimba?" Aliuliza Sasha kisha akapooza koo lake na kinywaji kikali.



    Walikuwa wameketi sebuleni. Nyumba hii ni kubwa na ya kupendeza. Samani zake pia ni za gharama kubwa.



    "Sijui nafanyaje!" Akasema Sarah. Alikuwa amejilaza kiuchovu kochini. "Siwezi kusema niitoe. Ni kubwa sasa. Ni hatari!"



    Sasha akanyamaza kwanza. Akajinywea mafundo mawili kisha akasema, "kwahiyo utaubeba huo mzigo mpaka lini?"



    Sarah akabinua mdomo. "Mpaka pale nitakapoutua. Hamna namna."



    "You are not serious!" Sasha akang'aka. "Alafu huyo mtoto unakuja kumwambia baba yake nani?"



    "Amekufa."



    Sasha akacheka.



    "Anyway, inabidi ufanye namna. Mimi sijaona haja ya kubeba mzigo huo. Na kuhusu ukubwa wa mimba, sio shida. Madaktari wapo, wazuri tu ninaowaamini. Nakupa muda wa kufikiri, utanambia. Sawa?"



    Sarah hakujibu. Alitazama zake kando. Sasha akanywa mafundo kadhaa na kumaliza chupa yake, ndipo Sarah akanena, "kwahiyo itakuwaje kuhusu Kinoo?"



    "Itakuwaje?" Sasha akatahamaki. "Itakuwaje nini? Haitakuwa kitu."



    "Kwahiyo atabaki hai?"



    "Aaahm yah! Atabaki hai ndio. Ila kwa muda."



    "Unamaanisha nini kwa muda?"



    Sasha akanyamaza kana kwamba hakusikia. Sarah akarudia kuuliza, "una maanisha nini? Mtamuua?"



    "Bado unampenda? Mbona unajali sana?"



    Sarah hakujibu. Macho yaliyomtazama dada yake yalionyesha anataka majibu na si maswali.



    "Ana nafasi moja tu ya kujitetea. Kama asipotoa taarifa yenye kuzaa matunda hivi sasa, nadhani Sheng atamuangamiza."



    "Ila taarifa anazotoa ni sahihi!" Sarah akang'aka.



    "Sijakataa. Ila hazizai matunda. Na Sheng anawaza kuwa huenda akitoa taarifa huwapasha pia na wenzake!"



    "Hapana. Hafanyi hivyo!"



    "Sijabisha, Sarah. Ila ndivyo ambavyo nimekwambia kuhusu Sheng."



    Kukawa kimya kidogo.





    "Ole wako umwambie Kinoo haya n'lokwambia," Sasha akatahadhari.



    **



    Saa nne usiku ...



    "Una uhakika?" Aliuliza Sheng akiongea na simu.



    "Ndio, nina uhakika. Na mara hii sitataka pesa yako mpaka pale utakapohakikisha maneno yangu."





    "Sawa. Tutawasiliana." Sheng akakata simu.



    Baada ya kama lisaa limoja akawa na wajakazi wake kumi na mbili. Wakajiweka kwenye chombo cha usafiri na kwenda zao.



    Wakanyookea eneo fulani mbele ya hoteli. Tutaita eneo hili hoteli ila haikuwa na hadhi hiyo, ila ilizidi hadhi ya guest house au lodge.



    Hapo baada ya kukaa ndani ya gari kwa muda kidogo, wakatoka wanaume wanne na kuzama ndani ya hoteli.



    Punde kidogo sauti za bunduki zikavuma! Wanaume wengine watatu wakatoka garini na kuzama ndani. Milio mingine ikavuma. Kisha kukawa kimya.



    Sasa kwenye gari wakawa wamebakia wajakazi watatu tu pamoja na Sheng. Hawakuwa wanaelewa nini kinaendelea ndani. Na Sheng, kwa kuhisi kuna jambo halipo sawa, akawazuia watumishi wake wasiende tena ndani.



    Wakangoja hapo kwa muda kidogo. Lakini katika hali ya ajabu, mara hoteli nzima ikazima taa na kuwa kiza!



    Na mwanga uliporejea, Sheng akashuhudia watu wakiwa wamesimama mbele ya gari! Na watu hao walikuwa wamebebelea bunduki kubwa mikononi mwao, wakiwanyooshea!



    "Shuka upesi garini!" Amri ikasikika. Sheng akatazamana na watumishi wake. Hakuwa tayari kutii amri ya yeyote. Basi wale wafanyakazi, katika namna ya kipekee, wakamziba Sheng, kisha mwanaume huyo wa kichina, akasukuma gia na kukanyaga mafuta kwa pupa!



    Gari likamchupa kuwafuata wale watu waliowanyooshea bunduki. Na kabla watu wale hawajanusuru roho zao, wakagongwa na kusinywa!



    Sheng akaangua kicheko. Na kama haitoshi, akarudisha tena gari na kuwasinya tena aliowagonga.



    Kisha akashuka na kuwatazama. Usoni mwake alikuwa na tabasamu.



    "Hakuna mtu wa kupambana na ..." kabla hajamalizia kauli yake hiyo, akakaukiwa na maneno ghafla baada ya kugundua aliowaua ni miongoni mwa wafanyakazi wake.



    Lakini iliwezekanaje hili?



    Hakujua kumbe wafanyakazi wake hao walikuwa wametolewa mhanga. Viunoni walikuwa wamefungiwa mabomu na hata bunduki walizokuwa wamebebelea hazikuwa na risasi hata moja.



    Kabla hajafanya jambo, akashangaa kuona alama ya kitaa chekundu cha bunduki kikiwa kifuani mwake. Na kisha akaamriwa na mtu ambaye hakumwona,



    "Weka mikono yako juu!"



    ***



    Haraka akaweka mikono yake juu kutii amri.



    Dakika ... watu wakamveka kinyago cheusi akawa gizani. Akapakizwa ndani ya gari ambalo hakulifahamu, safari ikaanza kwenda mahali ambapo hapafahamu.



    Kama mwendo wa lisaa limoja. Akashushwa ndani ya eneo fulani hivi, kiwanda ambacho kimetekelezwa. Akaingizwa ndani ya chumba fulani na kuvuliwa kinyago.



    Hakuwa anaona kitu maana kulikuwa ni giza totoro. Dirisha moja lililo juu kabisa halikutosha kuingiza mwanga kabisa ndani kwahiyo watu hawaonani.



    Baada ya kutupiwa humo, mlango ukafungwa na kukawa kimya kwa kama dakika tatu, hakuna kinachofanyika.



    Baadae kidogo, Bwana Sheng anasikika akijikusanya na anajinyanyua. Anaangaza huku na kule kisha anapaza sauti kuita,



    "Heeeey!" Kimya. Ni mwagwi tu wa sauti ndiyo ulimjibu. Akarudia kuita na kuita, ila ni bure. Hakukuwa na kitu. Na hata alidhani hakuna mtu anayemsikiliza.



    Akanyamaza. Ila baada ya kama dakika mbili hivi, mlango ukafunguliwa. Vikasikika vitu fulani vikidondoka kang!-kang! Na kisha mlango ukafungwa.



    Sheng akaita, hakuna aliyemjibu wala kuhangaika naye. Punde baada ya muda hewa ikaanza kuwa nzito. Akawa anahangaika kuhema.



    Hakuchukua muda mrefu, akajihisi mdhaifu na hatimaye akapoteza fahamu.



    Kama vile watu wale waliotupia vile vitu ndani walikuwa wanahesabu muda kwani punde walikuja kufungua mlango na nyuso zao zilikuwa zimefunikwa na vinyago vya kuzuia gesi.



    Wakamtazama bwana Sheng wakitumia kurunzi. Wakamwona amelala hajiwezi. Wakatazamana na kutikisiana vichwa. Wakamjongea, na kumnyanyua.



    Wakatoka naye ndani wakielekea kusikojulikana.



    **



    Beijing, mishale ya saa tano asubuhi ...



    Baada ya kufanya kazi yake vema, kumaliza wale wote waliopo orodhani, sasa Lee alikuwa ndani ya jiji la Beijing kwa dhumuni la kuonana na afisa fulani wa serikali kwa ajili ya kujadili vitu kadhaa.



    Mezani alikuwa ameweka glasi yenye mvinyo. Ila hakuwa anahangaika nayo sana, bali simu yake ambayo alikuwa anaandika text na kutuma.



    Anapokea na kutuma. Baada ya muda kidogo, simu yake ikazima charge. Akalaani. Akaiweka simu yake mezani na sasa akahamishia mawazo yake kwenye glasi yake ya mvinyo.



    Akanywa mafundo matatu alafu akatazama nje ya kioo. Huko nje watu walikuwa bize kila mtu akihangaika na yake. Watu walikuwa wanapita huku na kule. Kila mmoja na yake.



    Hapa bwana Lee akapata wazo. Alimwona mzee fulani akikatiza akiwa amebeba briefcase mkononi. Akaitazama briefcase yake na kuinyakua kuiweka mezani.



    Akafungua na humo ndani akatoa diary fulani ambayo alilenga asome kusogezea muda. Diary hii ilikuwa ni ile ambayo aliitwaa toka kwa makamu wa raisi aliyemmaliza kule nchini Mongolia.



    Aliperuzi diary hiyo kwa muda kidogo. Kuna kitu kikavutia macho yake. Akatazama kwa umakini, ila kabla hajakata kiu chake, akahisi kiganja begani mwake. Kugeuka akakutana uso kwa uso na afisa yule aliyekuwa anamngojea.



    Afisa huyo akatabasamu pasipo kusema kitu. Akampatia Lee ishara ya kichwa kisha akatangulia kwenda zake. Lee akalipia kinywaji chake kisha akamfuata afisa huyo.



    Mpaka nje kulikuwa kuna gari limesimama, Lee akajiweka na safari ikang'oa nanga.



    Ila afisa yule alikuwa mtu mkimya sana. Gari lilitembea kwa takribani robo saa na hakutia neno lolote.



    Alikuwa anatazama nje ya gari na alionekana mtu aliyetingwa na mawazo kiasi. Lee alimtazama afisa huyu, na hakuona kama kuna haja ya yeye kusumbuana naye.



    Akatulia tuli akiangaza huko nje. Ila baada ya muda kidogo afisa huyo akamwongelesha akitaka kumjua Lee kwa undani.



    Lee hakujiweka wazi sana. Hakuona sababu ya yeye kufanya hivyo, basi akawa anamjibu afisa huyu kwa ufupi tu.



    Afisa huyu kama mtu aliyegundua hilo, akaacha kusumbuana na Lee. Akanyamaza kama alivyofanya hapo awali. Safari ikaendelea.



    Baada ya kama dakika ishirini, wakiwa wameacha jiji la Beijing kwa kiasi kidogo, gari ikasimama na kujiegesha pembeni. Kisha dereva pasipo kupewa maelezo yoyote, akaizima gari na kutulia tuli.



    Yule afisa akafungua briefcase yake na kutoa karatasi kadhaa. Akamkabidhi Lee pasipo kusema jambo.



    Naye Lee akatoa karatasi kadhaa kwenye briefcase yake na kumpatia afisa huyo kisha wakapeana mkono.



    Ila kabla Lee hajatoka ndani ya gari hilo, afisa huyu alipomaliza kukagua karatasi alizopewa kwa haraka, akamsihi Lee kwa maneno machache sana. Awe makini.



    Kabla Lee hajatia neno, mlango wa upande wake ukafunguka. Akaenda nje na gari la afisa likatimka akilishuhudia.



    Akatazama mwanzo na mwisho wa barabara. Kulikuwa kuna safari ndefu ya kuelekea jijini Beijing. Hakika alihitaji usafiri.



    Ila kwanini afisa yule alimtupia mbali huko? Aliwaza. Alikokotoa kichwani akajikuta akiamini pengine ni sababu za kiusalama.



    Angalau mawazo hayo yakampa unafuu. Ila akawaza tena, kama ni sababu za usalama, je ni sahihi kwake kutelekezwa eneo kama hilo akiwa na nyaraka muhimu na nyeti hivyo?



    Aliendelea kuwaza akijongea. Alitembea kwa mwendo wa dakika kumi, na mara ghafla akasikia sauti ya breki kali! Akashtuka na kutazama kando yake. Akaona gari aina ya Ford ranger nyeusi. Ilikuwa imeshusha vioo na ndani yake walikuwa wanaume kadhaa.



    Kabla hajawajua wanaume hao ni wakina nani, wapo wangapi, akastaajabu wakitoa mitutu ya bunduki na kumwonyeshea.



    Wakamimina risasi kadhaa. Zikatoboa na kujeruhi mwili wa Lee vibaya! Akadondoka chini kama mzigo asiyeonyesha dalili za uhai.



    Wanaume wawili wakashuka toka kwenye lile gari, wakampoka Lee briefcase yake na kisha wakatimka zao kwa kasi wakirudi kule walipotokea, yaani kule mbali na jiji.



    Baada ya muda asioujua. Akiwa gizani, Lee anasikia sauti za watu. Anakakamaa na kufungua kope za macho yake. Anamwona mwanamke mmoja na wanaume wawili. Anataka kusimama, anashindwa.



    Watu wale wakamtaka atulie kwani amejeruhiwa vibaya. Akajitazama, tumbo lake lilikuwa limejawa damu. Alihisi maumivu makali sana.



    Hakudumu tena muda mrefu, akapoteza fahamu.



    **





    Saa nne usiku, nchini ...



    Mlango ulifunguliwa, Bwana Sheng akaingizwa ndani ya chumba chake akiwa hajiwezi kwa lolote. Alibwagwa chini na kisha mlango ukafungwa.



    Watu hawa waliomleta walikuwa ni wanaume wawili waliovalia suti nyeusi na vinyago usoni. Vinyago vya kuzuia gesi yenye sumu hivyo nyuso zao hazikuwa zinaonekana haswa ni wakina nani.



    Walikuwa wanatembea kwa ukakamavu. Miili mirefu na yenye nguvu.



    Baada ya kuufunga mlango waliondoka zao wakielekea upande wa kulia wa mahali alipohifadhiwa bwana Sheng. Baada ya mwendo wa dakika tano, wakavua vile vinyago vyao na punde wakawa wametoka ndani ya eneo hili.



    Huko nje napo palikuwa kiza, hivyo hawakuonekana vema watu hawa. Walijipaki kwenye gari, cadillac nyeusi, wakatimka.



    Kule chumbani, kizani, baada ya dakika tatu tangu gari lile litimke, Bwana Sheng alianza kugugumia. Na mara akakohoa kama mara sita kabla ya kunyamaza na eneo zima likawa kimya kana kwamba ni chini ya shimo.



    Akataka kuita, ila akashindwa. Kifua kilikuwa kinambana haswa. Akaishia kuvuta kamasi.



    ***





    "We are eagerly waiting for your command, sir," sauti ilisikika toka garini. Punde gari likasimama na wanaume watatu wakashuka.



    Gari hii lilikuwa ni ile cadilac nyeusi iliyotoka kule kwenye kiwanda kilichotelekezwa. Hivyo basi tuna kila sababu ya kuamini kuwa, wanaume hawa ndiyo wale waliomtia Sheng mikononi.



    Walikuwa ni wazungu. Watu wanaoonekana wamestaarabika kabisa. Ila kwa yale matendo yao machache tulioyaona, inatosha kuwaweka kwenye kundi la wauaji maarifa.



    Wauaji maarifa ni watu stadi wenye uwezo wa kupanga tukio la kuua kwa fomula za kisayansi. Yaani wakammaliza mtu na kubakishwa maswali mengi sana kwa washuhudiaji ama wapelelezi juu ya namna gani wametekeleza hilo.



    Kama wewe ulivyobaki hapo ukiwa hutambui ni kwa namna gani watu hawa wamefanikiwa kumtia kimyani bwana Sheng. Na hata pengine ungeweza kushupaza shingo kuwa watekaji si hawa, maana hawakuwapo mafikirioni.



    Hawa ni wauaji wasomi. Wamekaa darasani kufundishwa namna ya kuua, kuteka na hata kutesa. Kila kitu chaenda kimahesabu.



    Na punde tu unapoona jambo linatokea kwa bahati, basi kwa upande wao hapo ndipo mambo yalipoenda kombo maana hawaamini kwenye bahati, bali nguvu za akili na miili yao.



    Kwa jina la pamoja waliitwa 'the intellect instinct'. Na wapo watano tu kwa idadi. Nguo zao ni suti tu, na pengine ungeweza kuwatofautisha na wengine kwa ua dogo jekundu wanalolipachika kifuani upande wa kushoto.



    Waliposhukia ilikuwa ni ndani ya nyumba maridadi sana. Si kubwa, bali ya wastani na rangi zake za kupendeza. Ni kama jengo la vyumba vinne ama vitatu mbali na jiko, choo bafu na stoo.



    Hapa nje kwenye uwanja wa kuegeshea magari, kulikuwa kuna cadillac nyingine nyeusi imetulia.



    Wanaume hawa watatu wa kizungu wakaingia ndani na kujumuika na wenzao wawili ambao walikuwa sebuleni wakihangaika na tarakilishi.



    Na mmoja wao wale waliozama ndani alikuwa anaendelea kuongea na simu hata alipozama ndani na kuketi.



    "Yes it does ... I think tomorrow I'll be very sure, sir ... no any reason for that ... ok, thanks."



    Simu ikakata.



    ***



    Saa tisa jioni ...



    "Mara ya ngapi sasa?" Aliuliza Miranda akitazama bahari. Upepo ulikuwa unapuliza haswa na fukwe ilikuwa na watu wachache kwasababu haikuwa mwisho wa wiki.



    Mwanamke huyu alikuwa amevalia tisheti nyeusi, na suruali ya jeans. Unaweza ukasema kama ilivyo ada yake. Miguuni alikuwa peku akikanyaga mchanga na kuoga maji ya bahari.



    Kwa mbali kidogo, alikuwa amepaki gari lake. Ni kama umbali wa hatua ishirini na tatu au na nne hivi. Na hapa alipokuwa amesimama, kando yake alikuwepo mwanaume, Kinoo.



    Kifua chake kilikuwa kimebanwa na kibodi cheusi na suruali yake ya kadeti rangi ya udongo ilikuwa imeminya mapaja yake manene.



    “Kutakuwa na tatizo gani?” akauliza Miranda. Bado alikuwa anatazama bahari, na kabla Kinoo hajajibu, akaendelea kwa kusema, “Nahisi kuna tatizo hapa. Tena si dogo. Ni jambo la muda tu tatizo hili kuwa bayana. Haya matukio yaliyotukia hapa karibuni, yanafikirisha.”



    “Ni kweli. Huenda kwenye ile …” Kinoo hakumaliza hiyo kauli, wakasikia sauti kubwa ya mluzi toka upande ule ilipo gari la Miranda. Wote wakatazama na kumwona Marwa huko. Akawafanyia ishara ya kuwaita.



    “Nadhani nina kitu kwa ajili yenu!”



    Wakajongea huko. Ndani ya gari alikuwapo Marwa pamoja na Jona. Wote walikuwa wamevalia mashati meupe na suruali za jeans, zikitofautiana rangi tu, bluu na nyeusi.



    “Nadhani tulikuwa sahihi kwenye lile jambo. Ni wazi Sheng atakuwa ametekwa, ama amehifadhiwa mahali,” alisema Marwa ambaye mbele yake, juu ya dashboard, kulikuwa na tarakilishi iliyounganishwa na mtandao.



    “Mmejuaje?” akauliza Miranda.



    “Hapa karibuni mtandao wa wachina hawa, haujawa katika namna nzuri kiulinzi na hata kiutendaji. Nimeweza kuzama tena katika mtandao wao na kudukua taarifa ambazo zinakiri upoteaji wa bwana Sheng, lakini zaidi tumefanikiwa kupata code itakayotusaidia kumtia kimyani.



    Ni hivi, kila kiongozi mkubwa wa wachina hawa ana jina lake la siri ‘code name’ ambalo humtambulisha popote pale kwenye himaya yao. Na tulipolipata hilo jina, tumefanikiwa kuli-trace kwa kuongezea baadhi ya taarifa, satellite ikatuonyesha wapi yupo!”



    “Imewezekanaje katika namba hiyo?” Kinoo akauliza.



    “Imewezekana kwasababu hiyo ‘code name’ si jina tu ambalo mlengwa hupewa, bali pia ni chip ambayo hushindiliwa ndani ya mwili wake ambayo itasaidia upatikanaji wake popote pale atakapopotea, ama kutokujulikana yupo wapi.”



    “Kama ni hivyo, kwanini wafuasi wake hawajampata na kumwokoa mpaka sasa?” Miranda akatia shaka.



    “Kwasababu taarifa ya kupotea kwa Sheng haijafiikishwa makao makuu, China,” Jona akajibu. “Ni huko makao makuu pekee ndipo kwenye ‘wing’ kubwa ya kimtandao ambayo hu-monitor wings zote za familia na koo ya Wu.”



    “Mbona nyie mkaweza mkazipata taarifa hizo?” Kinoo akauliza.



    “Kwasababu ni sisi,” Marwa akajibu kiwepesi na kisha akatazamana na Jona na kujikuta wanacheka.



    “Ok, guys, sasa tunafanyaje?” Miranda akauliza. “Kuna haja ya kwenda huko kumkomboa Sheng?”



    “Hapana,” Jona akajibu. “Endapo tukifanya hivyo, ni wazi kuna mambo fulani tutakayoyakosea majibu. Kwanza, ni kwanini chamber ya Sheng hawajatuma taarifa huko China juu ya hili? Ni kipi wamepanga kufanya? Alafu, ni nani anayehusika na utekaji huu? Na amepanga kufanya nini na Sheng?



    Maana kama wangelikuwa na lengo la kumuua, wangelifanya hivyo toka pale hotelini.



    Kuna mengi ya kujifunza hapa. Watu wale waliomteka Sheng, si wa kawaida. Haiwezekani kwa yale yote yaliyotukia, hakuna hata shahidi wala maelezo yoyote yaliyotolewa mpaka sasa.



    Hatujui wamejipangaje. Hatujui ni wakina nani. Kumjua adui yako ni nusu na robo ya kumshinda. Inabidi tuwe wapole hapa, ama twaweza kuzamisha mguu kwenye kisima chenye maji meusi.”



    “Jona!” Miranda akaita. “Twende kwa Mr Brown!”



    “Are you serious?” Kinoo akawahi kuuliza akitoa macho.



    “Yes, I am totally serious!” Miranda akajibu. Na kabla hajamngoja yeyote aseme jambo akakalia kiti cha dereva, akatia moto, safari ikaanza.





    ***



    Baada ya honi ya gari kupigwa mara mbili, geti dogo linafunguliwa kidogo. Mwanaume mmoja mzungu anachungulia nje na kukagua usafiri kwa macho akitumia sekunde tatu, kisha anatupa swali,



    “Who are you?”



    “Mr. Brown associates!” Miranda akajibu. Yule bwana mzungu akatoka vema getini, alikuwa amebebelea bunduki kubwa mkononi.



    “How can I prove that?”



    “Kit-kat is the play of the cat, pat it before cut it out of its curiosity. Then hat it and give it to a big fat rat,” Miranda akasema maneno hayo upesi, basi bwana yule wa kizungu akaridhia, akafungua sasa geti kamili wageni wakazama ndani.



    Baada ya dakika chache wakawa wameketi sebuleni, na kuwakarimu wageni, akawepo bwana mmoja mzungu pamoja nao. Bwana huyo ni mtu wa pili aliyekuwapo hapa, mbali na yule aliyewafungulia mlango.



    “We are here to see Mr. Brown,” akasema Miranda kwa kujiamini.



    “I am sorry,” Bwana yule mwenyeji akasema akitikisa kichwa, “Mr Brown is not here anymore. He was killed.”



    “Killed?” Miranda akatahamaki.



    “Yes, and that’s all I can tell. He was killed. So he’s no more.”



    “Who killed him?”



    “Madam,” bwana yule akaita akimtazama Miranda kwa macho dhalili, “I said that was all I can tell. He was killed. Enough. We are done here. The business with him is over.”



    Basi Miranda na wenzake wakawa hawana lingine la kusema hapa, wakaondoka zao.



    “Sheng amemuua Brown,” Miranda akasema akiwa anatazama mbele waendako.



    “So waliyemteka Sheng watakuwa ni watu wa Mr Brown?” Marwa akauliza.



    “Nadhani,” Miranda akajibu. Alisimamisha gari kwenye foleni, akaweka kiwiko kwenye dirisha na kucha mdomoni akifikiri.



    “Ila mbona bwana yule hakutaka kusema zaidi? Ina maana hawakuamini?” Jona akauliza.



    “Pengine wanaweza wakawa hawaniamini, ila pengine pia hata na wao wanaweza wakawa hawafahamu linaloendelea.”



    “Unamaanisha nini kusema hivyo?” Jona akaendelea kueleza. Na kwa macho yake ya kijanja ndani ya miwani akaona mikono ya Miranda ikiwa inatetemeka kwa mbali. Na hata uso wake ukiwa umejawa na mashaka.



    “Ni bora wakawa hawaniamini,” Miranda akajibu, “Kuliko wakawa hawajui linaloendelea.”



    Akavuta hewa na kusema, “Kama hawajui linaloendelea, basi kazi itakuwa kubwa sana kuliko tunavyowaza. Kazi kubwa kuliko tunavyoweza kuwaza, kwani watakuwa wametumwa watu wa kikosi kingine kuja kumaliza kazi.”



    “Ni tofauti na wale?” Jona akauliza.



    “Ni tofauti kama ardhi na mbingu,” Miranda akateta. “Na sasa ndo’ napoanza kupata majibu, kwa mujibu wa lile tukio, watakuwa ni watu hao ndiyo wamelifanya, hawa watu wa siri ambao inawezekana hata wenzao hawajui kama wapo nchini.”



    “Kuna haja ya kuhofia kuhusu hilo?” Jona akauliza.



    “Ipo!” Miranda akajibu akimtazama. “Jona, watu hawa ni wachawi.”



    “Wachawi? - Kivipi? Unamaanisha nini?”





    ***

    Miranda akanyamaza kwanza. Foleni likaruhusiwa kwendaze, basi akatia gari moto wakaendelea na safari. Baada ya kutembea kwa dakika tatu, bado akionekana mtu anayebughudhiwa na mawazo, akasema:



    “Kuna kipindi Mr Brown alinieleza kidogo juu ya watu hawa. Tulikuwa tunaongelea mambo yetu tukiwa tumetoka kufanya kazi fulani hivi kubwa. Siku hiyo nilimfurahisha sana kwa utendaji wangu wa kazi, akaniambia kama nikiendelea hivyo hivyo, basi siku moja angalinipeleka Uingereza.



    Huko nitapata mafunzo zaidi na kama nikifuzu basi nitakuwa HS, yaani Headquarter Servant. Nitapata kila ninachokitaka, na nitafanya kazi mataifa mbalimbali kutimiza adhma ya kundi.



    Sikuweza kumuuliza sana kwani alikuwa amelewa, na hata yale maongezi yake kwa namna moja ama nyingine nilidhani yanachochewa na pombe, hivyo sikuzingatia sana. Lakini kwa sasa naona yalikuwa na mantiki ndani yake.



    Na zile simulizi alizokuwa ananipa, hazikuwa za uongo wala kutiwa chumvi. Alikuwa anasema ukweli.”



    “Ni simulizi gani hizo alikuwa anakupa?” Jona akataka kujua.



    “Alikuwa anaongea kwa kujivuna na kucheka mara kwa mara. Ni wazi alikuwa anapendezwa na simulizi hizo. Alijipambanua akinieleza ni namna gani vijana hao wamekuwa wakifanya kazi kwa ufanisi, na hata akan’tolea mifano kedekede ya watu mashuhuri na maarufu waliouawa na hao watu mpaka sasa hakuna aliyekamatwa.



    Anyways, sitamaliza kama tukiongelea haya. Ila yatupasa kuwa makini sana.”



    Baada ya lisaa limoja na nusu, wakawa wamewasili kwenye nyumba fulani yenye ghorofa moja. Wakazama ndani na walipoketi wakajihudumia glasi glasi za juisi na maongezi yakaendelea.



    “As long as hawa watu hawaonekani ku-pose threat, Inabidi tungoje kwanza ni kitu gani kundi la Sheng litafanya,” alisema Jona alipoweka glasi mezani. “Hatua yao ndiyo itatupa mwanga sisi tufanye nini.”



    Marwa akaguna na kisha akatia neno, “Mimi kuna kitu nahisi. Kwa akili yangu yote na kwa moyo wangu wote, siamini kama watu hawa, kama Miranda alivyowaongelea, watahusika na Sheng pekee kisha wakajiondokea zao. Nahisi mbali na hili la Sheng, kuna la ziada.



    Na hapo ndipo ndipo utata utakapotokea.”



    Jona akabinua mdomo, “Inawezekana unalolinena ni kweli. Si la kulipuuza hata kidogo. Kama kuna uwezekano, inabidi kufuatilia nyendo zao hatua kwa hatua.”



    **



    Saa nane usiku …



    “Tunaenda siku nyingine sasa, naona kuna haja ya kuchukua hatua,” alisema jamaa mmoja mweusi. Macho yake yalikuwa yanamtazama mwanaume wa kichina aliyekuwa ameketi kwenye kiti kirefui akinywa whiskey.



    Mwanaume huyu wa kichina alikuwa ndiye yule aliyekuwa akiwasimamia wakina Marwa walipokuwa kwenye kitengo cha SPACE BUTTON. Sasa ndiye yeye amekuwa mkuu baada ya Sheng kutoonekana.



    Alikunywa tena fundo moja la whiskey kisha akamtazama mwanaume huyo aliyempa taarifa, akamwambia kwa sauti yake nyembamba yenye lafudhi ya ki-mandarin,



    “That’s none of your business. Najua cha kufanya na ni kwa muda gani nifanye. So can you please get away from my face?”



    Mwanaume yule aliyemfikishia taarifa akageuka aende zake, ila huyu bwana wa kichina akamwita na kumwambia,



    “Ole wako ufanye kitu ambacho sijakwambia,” alisema akiwa anarembua kilevi. “Nitakuambia nini cha kufanya. Usidhani mimi ni chizi, I am not crazy. I am not craaazy, ok?”



    Mwanaume yule mweusi akaenda zake akimwacha huyu bwana wa kichina hapa anaendelea kunywa. Baada ya kama dakika tano, bwana huyu akamalizia kinywaji chake, akanyanyuka na kujikokota kwenda ndani.



    Alipofika akajitupia kitandani akitabasamu. Akatazama simu yake. Akabofyabofya kutazama akaunti yake ya benki, mara punde ujumbe ukaingia kumwambia ana shilingi milioni mia nane taslimu. Akatabasamu na kukumbatia simu yake.



    Alikuwa ana furaha sana. Huu ulikuwa ni muda wake. Na akiwa anaamini kabisa kuwa bwana Sheng hatarudi akiwa hai, basi aliazimia kujiweka sawa kabla mambo hayajarudi kwenye mstari.



    Simu ikaita.



    Akaitazama akikunja sura. Akajiuliza kwa sekunde kadhaa kisha akapokea na kuiweka sikioni. Alikuwa ni wakala toka makao makuu, Hong Kong, China.. Na alibashiri bwana huyo atakuwa amempigia kumuuliza kuhusu Sheng.



    Maongezi yao yakadumu kwa muda wa dakika kumi. Na kama alivyobashiri, mada ilikuwa Sheng kwani hajatuma mrejesho wa maendeleo kwa muda wa ‘masiku’ sasa. Na bwana huyo akaenda mbele kwa kuuliza sababu zinazomfanya bwana Sheng kutokuwapo eneo la kazi kwa siku zote hizo.



    Kumbe walishatazama kwenye ‘tracing’ zao wakabaini kwa siku zote hizo ambazo bwana Sheng hajawasilisha mrejesho wa kazi, hakuwapo eneo la kazi.



    Basi kwa maswali hayo, huyu bwana wa kichina akashindwa kuficha. Ikabidi sasa aweke bayana kuwa Sheng hayupo eneo la kazi, na hawafahamu wapi alipo.



    Basi haikuwa taabu, bwana yule aliyewapigia simu akasema anatuma taarifa za location aliyopo Sheng, na kufikia kesho majira kama hayo apewe ‘feedback’.



    “****!” Bwana huyu wa kichina akalaani. Sasa mipango yake ilikuwa imeharibika. Usiku wake uligeuka kuwa wa maruwani ghafla na hata pombe zilizokuwa zimemwingia kichwani, zikapotea!



    Akabaki akiwaza nini cha kufanya.





    **



    Saa nne na robo asubuhi …



    “He is weak enough!” aliongea mwanaume wa kizungu, mmoja wa kundi la ‘intellect instinct’ akiwa ndani ya eneo lile la kiwanda kilichotelekezwa.



    Mwanaume huyu alikuwa ametoka ndani ya chumba kile walichomhifadhi bwana Sheng. Na hapa akiwa anaongea alikuwa ametia mkono wake wa kuume mfukoni, yu ndani ya suti nyeusi matata.



    “We have already done each and everything. It’s just a matter of time for us to interrogate and kill him … we need at least eight final hours ... ok. I’ll be in touch.”



    Bwana huyo akakata simu, akageuka arejee kule chumbani, ila alipopiga hatua nne, akasikia kama sauti ya mlio wa gari. Haraka akasimama na kutulia tuli kuhakikisha kama alichokisikia ni kweli.



    Hakusikia tena sauti yoyote, ila akawa tayari ana shaka. Badala ya kwenda kule chumbani akatembea kwa ustadi kwenda nje ya kiwanda. Alipofika mlangoni, akajibana mahali na kutazama nje.



    Hakuona kitu.



    Ila akiwa amejiweka kwenye mazingira ya utulivu mkubwa, masikio yake yakampa taarifa kuwa kuna jambo halipo sawa. Akanyanyua mkono wake wa kuume na kuongea kwenye saa yake kwa sauti ya chini,



    “Alert.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kisha akachomoa bunduki yake ndogo na kuikamata vema mkononi. Baada ya kama dakika mbili za utulivu, akasikia sauti ya kitu cha chuma kikidondoka chini. Sauti ilitokea upande wake wa kushoto.





    **







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog