Search This Blog

Monday, 24 October 2022

FEDHEHA - 3

 http://pseudepigraphas.blogspot.com/2019/12/fedheha.html

    Simulizi : Fedheha

    Sehemu Ya Tatu (3)







    Aliendelea kutafuna nyama taratibu huku akishushia na bia baridi ya Kilimanjaro. Pembeni alikuwa amekaa na binti mrembo ambaye hawakuendana kabisa kiumri. Mara mojamoja aliupeleka mkono wake kunako kifua na kumpapasa mrembo yule. Kama ungebahatika kumuona pale alipokaa basi usingemtambua alikuwa na nani. Ni sauti yake tu ndiyo ingemfanya mtu aliyemzoea afahamu kuwa alikuwa Mjomba Masharubu.

    Siku kadhaa zilikuwa zimepita toka afanye kazi maalum iliyokuwa mbele yake, kama kawaida mkuu wake alimpa likizo isiyokuwa na muda maalum hadi pale atakapomuhitaji kwa kazi maalum.

    “Vipi dear mbona uko kimya sana.”

    Alisikika yule binti alikuwa amekubuhu kwenye mambo ambayo yalimzidi umri.

    “Usijali, hii ndio aina ya furaha yangu au unapenda kukaa na mtu mwongeaji.”

    “Inuka basi mi nataka tukacheze.” Aliongea huku akibana pua.

    “Mi nataka tukalale unasemaje?”

    “Wewe tu, lakini si tulishakubaliana bei ya kukesha?”

    “Kwani tutakuwa hatulali mpaka asubuhi,Usijali nitakupa hata zaidi ya ile.”

    “Ndio maana nakupenda dear, kwanza siku nyingi sijapata mwanaume wa kuninywesha na kunilisha kama wewe. Yaani leo nimeeinjoi si mchezo.” Aliendelea kubwabwaja binti yule ambae umri wake haukuzidi miaka kumi na sita.

    “Twende nyuma huku kuna guest.”

    “Unataka nilale Gesti za shilingi elfu tatu?”

    “Sasa wapi dear.” Pombe ilikuwa inafanya kazi yake na kumfanya aondokewe kabisa na aibu.

    Kabla hajamjibu simu yake ya mkononi ikaanza kuita. Aliitazama namba ile ngeni akataka kuipuuza lakini akashtuka baada ya kuona ni namba ambayo alikuwa anaifahamu sana.

    “Hallow nani mwenzangu.”

    “James naongea, nimekamilisha kazi yako nahitaji malipo yangu.” Sauti hiyo ilipenya kama kitu chenye ncha kali kwenye moyo wake.

    “Makabi?”

    “Ndiyo mimi.” Akashusha pumzi na kuganda dakika kadhaa bila kuongea chochote.

    “Ina maana…”

    “Niko hai.”

    “Ulipona?”

    “Sio nilipona nimepona.” Sauti ya upande wa pili ilimtia hofu.

    “Ok, nimekuelewa bwana Makabi uko wapi kwa sasa?”

    “Palepale uliponikabidhi ile kazi.” Kwa mara nyingine akajikuta akiingiwa na hofu na kumsahau kabisa kiumbe ambaye alikuwa amekaa naye muda huo.

    “Ok naomba unisubiri hapo hapo usiondoke sawa?”

    “Sawa mkuu nakusubiri.” Akakata simu.

    Akajishika kichwa dakika kadhaa kabla ya kuanza kupiga namba nyingine.

    “Hallow mr. Moyo.”

    “Ndiyo kaka nikusaidie nini?”

    “Una kazi?”

    “Sina.”
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kuna Bwege anatakiwa kuharakishiwa safari unaweza kunisaidia?”

    “Ni bwege kweli, nisijiandae kwa msako wa mbuzi kumbe ni chui.”

    “Acha woga bwana, nikisema bwege namaanisha kile ninachozungumza au siku hizi hatuaminiani? We fanya hiyo kazi mshiko tukutane palepale.”

    “Poa Kamanda wangu nakuaminia sana.”

    “Sasa subiri, nitakutumia maelekezo kwa meseji wapi uende maana muda huu yuko nyumbani kwake ananisubiri.”



    ***

    Baada ya kugundua kuwa kifo alichosababisha kilikuwa cha Muheshimiwa Makamu wa Rais aliamua kuishi kwa tahadhari, hata pale alipokuwa anaongea na yule mtu anayejiita Mjomba Masharubu kuwa anahitaji pesa zake bado hakumwamini. Hili ndilo lililosababisha kumsubiri kwa hadhari kubwa. Akili yake haikumtuma kuwa anaweza kuzipata kiulaini pesa hizo. Alihisi jela ikinukia tena , hakuiona hata dalili ya msamaha wa Rais kama ule alioupata, tena safari hii alihisi kitanzi kikiwa mbele yake.

    Muda ulizidi kuyoyoma, kadri saa zilivyozidi kusogea ndivyo alivyozidi kuandamwa na hisia za hatari. Alijishangaa kuona amezidiwa na hofu.

    ‘Si bure!’ Aliwaza huku akiinuka pale alipokaa na kwenda nje, aliamua kujificha nyuma ya ndoo ya maua. Dakika chache baadae akasikia mchakato wa mtu aliyekuwa anatembea taratibu. Moyo wake ukazidi kupiga kwa kasi huku akitiririkwa na jasho kwa wingi.

    Mtu akaibuka kama kivuli kwa mwendo uleule wa taratibu. Aliendelea kukitazama kivuli kile hadi kilipofika usawa wa mlango ambako kulikuwa na mwanga hafifu wa mshumaa ambao ulitoka nje. Akashusha pumzi, baada ya kugundua kuwa yule ni mpenzi wake Tamasha.

    “Dear, dear… uko wapi?” Aliita Tamasha.

    James baada ya kujishauri kwa dakika kadhaa akaamua kujiondoa pale kichakani na kumfuatilia Tamasha.

    Sekunde chache tu wakati anainuka akaibuka mtu mwingine ambaye kama Tamasha naye huyu alionekana kama kivuli. Tofauti ya huyu na Tamasha ni kwamba alikuwa anatembea kwa tahadhari kama mtu anayevizia windo lake lisishituke. Hofu ambayo ilianza kutoweka ikajirudia tena safari hii akaanza kutetemeka. Alihisi meno yake yakigongana kwa hofu na baridi iliyotokana na woga. Tumbo pia lilimfanya mngurumo huku akihisi kubanwa na haja ndogo,alijihisi kama mtu ambaye amebanwa na pumzi.

    Yule mtu alitembea kwa mwendo ule ule wa kunyata hadi alipofika mlangoni. Akasita kidogo na kujibanza pembeni ya mlango. James akapatwa na mshituko mkubwa zaidi baada ya kumuona yule mtu akichomoa kisu kutoka kwenye ala ambayo ilikuwa karibu na mfuko wa kulia wa suruali yake. Akaingia ndani na kuurudisha mlango kwa nguvu.

    “Maskini Tamasha.” Aliongea kwa sauti ndogo huku akiinuka pale kichakani na kuliendea tofali ambalo lilikuwa sentimita chache kutoka pale alipojificha.

    Hisia za woga zilianza kumtoka na badala yake akatawaliwa na ujasiri mkubwa. Akavua kandambili na kukimbia kwa kasi akisimamia vidole vyake. Alipofika mlangoni akasimama na kutega sikio.

    “Sema haraka yuko wapi huyu mbwa wako.” Alifoka yule jamaa.

    Tamasha hakutoa jibu lolote zaidi ya kilio cha kwikwi.

    James alishindwa kuelewa yule jamaa kasimama upande gani wa mlango jambo lililosababisha ugumu wa dhamira yake ya kumshambulia kipande kile cha tofali.

    “Kwa kuwa hutaki kusema basi nitaanza na wewe halafu atafuata malaya wako.”

    “Mmmmmm!” Iliksikika sauti ya mtu aliyezibwa mdomo.

    Hakutaka kujiuliza tena akausukuma mlango na kujitoma ndani kwa kasi, kitendo hicho kilimshtua yule adui na kumfanya akose umakini. Kabla hajaamua nini cha kufanya akashtukia kipande cha tofali kikitua katikati ya uso wake, akayumba na kuanguka pembe ya kushoto ya sebule. Damu zilikuwa zinachuruzika kutoka usoni, akaanza kutapatapa hatimaye akakata roho.

    “Mungu wangu,Umeua dear .Kuna nini kinaendelea?” Aliuliza Tamasha.

    “Kwanza tumuondoe huyu mshenzi hapa mambo mengine baadae.”

    “Tutampeleka wapi?”

    “Nafikiri ni bora tuchimbe shimo hapo uani kisha tumfukie.”

    “Dear kwanini usitoe taarifa Polisi?”

    “Polisi? We unawajua polisi au unaongea tu! Kama unataka kujitia matatizoni hebu toa taarifa ndio utajua sheria za nchi yetu jinsi zilivyo.”

    “Kwanza niambie huyu mtu ni nani?”

    “Dear huyu mimi simjui, ninachofahamu ni kuwa katumwa na mjomba ni mambo mazito nitakusimulia kila kitu lakini kwanza tufanye hiyo kazi.”

    “Jembe tutalitoa wapi?”

    “Hapa tuna chepe na vipande vya chuma, vitatusaidia kuifanya kazi hiyo.”

    “Lakini mi nataka kuondoka dear.”

    “Unaweza kuondoka lakini ukumbuke kuwa nimeua kwa ajili yako, nilikuwa na fursa nzuri ya kutoroka lakini mapenzi yangu kwako ndiyo yaliyosababisha yote haya.”

    “Nisamehe dear, kweli leo ninge kufa.”

    “Hivyo hutakiwi kuondoka mpaka tumaleze jukumu hili kwa ukamilifu.”



    ***

    “Dakika tano za kunilipua kwa kosa lipi?” Aliuliza Taisamo huku akijaribu kuvuta muda na kutafuta fursa ya kujiokoa.

    Wakati huohuo akamuona dokta akiinuka kutoka pale alipokaa.

    “Kaa chini dokta, kinywa chako lazima kikuponze umeonekana huwezi kutunza siri zilibaki sekunde chache ungemtaja Mkuu.” Alifoka yule mtu.

    Ghafla, taa zote zikazimika. Ni wakati huo ambao Taisamo alijikuta akiwapongeza na kuwashukuru Tanesco kwa kuleta mgao wa umeme. Alitumia nukta hiyohiyo kujirusha pembeni na ni wakati huohuo ndipo aliposikia mlipuko wa bastola. Mlipuko huo ulileta patashika hata kwa nyumba za jirani ambao wengi walikimbilia kule ulikotoka mlipuko. Hii ndiyo tabia ya Watanzania ya kupenda kukimbilia tukio hata kama ni la hatari.





    Ikafuata milipuko minne ambayo iliwatawanya watu kadhaa ambao walikimbilia nyumbani kwa dokta kushuhudia nini kimetokea. Taisamo akasikia mlango unafunguliwa, akajua jamaa anakimbia. Naye akatoka mbio ili kumfuatilia huyo jamaa ambaye hakubahatika kumuona sura.

    TKD 2341. Alizisoma namba za gari lile ambazo zilisomeka kwa tabu kisha akaziandika kwenye simu.

    Akarudi ndani haraka na kuwasha tochi yake ndogo. Dokta alikuwa anagaragara sakafuni ndipo alipobaini kuwa kuna risasi zilikuwa zimempata dokta.

    “Dokta, dokta……”

    “Nenda kijana siwezi kupona.” Aliongea kwa ufasaha dokta ambaye alikuwa anavuja damu begani na kifuani.

    “Wacha nikuwahishe hospitali.”

    “No… Aaaa.. Nend… aaa ofis..kwangu …. Fung..ua kabat….. kuna rip..ya mauaji na chupa… yeny…

    Usss…..” Hakuweza kumaliza kauli yake akakilaza kichwa chini na kutoa macho.

    Alikuwa amekufa.

    Dakika chache baadae vikaanza kusikika ving’ora vya gari za polisi. Luteni Taisamo akaitumia nafasi hiyo kuchomoka ndani kwa kasi. Alikuwa na bahati kwani sekunde chache baadae nyumba ikazungukwa na Polisi ambao walikuwa wanamulika kurunzi kuzunguka eneo lile.

    Baada ya kuhakikisha kuwa yuko katika eneo ambalo macho ya Polisi hayawezi kumfikia akaanza kutembea taratibu hadi kituo cha teksi. Alikuwa anasikia njaa lakini maelekezo ya dokta juu ya faili la mauaji yalimfanya apuuze kula.

    “Nifikishe Muhimbili.” Aliongea baada ya kuingia kwenye teksi iliyokuwa kwenye foleni.

    “Poa mkubwa.” Alijibu dereva wa teksi.



    ***

    “Haya sasa nieleze yaliyokusibu maana juzi nimekuja mchana we haupo, usiku pia haukuwepo jambo la kushangaza zaidi muda mwingi ulikuwa umezima simu.”

    “Dear haya yote yamesababishwa na mjomba, si unamkumbuka yule mjomba aliyekuja ile siku niliyochelewa kurudi?”

    “Ndiyo, sasa yeye anahusika vipi?”

    James akamsimulia Tamasha kila kitu kilichotokea.

    “James, ina maana wewe ndiye uliyemuua makamu wa Rais?” Aliuliza Tamasha kwa hamaki huku akiwa ameyatoa macho kwa mshangao.

    “Sina uhakika Tamasha.”

    “Huna uhakika vipi wakati umeshaeleza kila kitu hapa!”

    “Sina uhakika kwa sababu hofu ilinifanya niigonge vibaya ile gari yaani tofauti na vile nilivyoelekezwa na sikuona uwezekano wa Muheshimiwa kupoteza maisha.”

    “Mbona vyombo vyote vya habari vimeandika kuwa alikufa kutokana na ajali ya gari?”

    “Unaviamini vyombo vyetu vya habari?”

    “Unataka kuniambia waandishi ni waongo?”

    “Sina maana hiyo Tamasha mpenzi, kwa sheria za nchi yetu mwandishi hana ubavu wa kuandika kila anachokiona au kukiamini yeye kuwa ni sahihi.”

    “Una maana gani?”

    “Waandishi hawako huru kuandika itakiwavyo hususani wanapogusa maslahi fulani.”

    “Huoni kama umejitia matatizoni kwa kukubali jukumu hilo?”

    “Nisingekubali ningeuwawa.”

    “Mtu mmoja tu anakutisha James?”

    “Uwe unafikiria Tamasha mpenzi, yule mtu ana jeuri ya pesa na sina uhakika ni nani yuko nyuma yake pia ndiye aliyefanya mpango nikatolewa gerezani kwa msamaha wa Rais!”

    “Unahisi kuwa kuna watu wako nyuma yake?”

    “Sio kwamba ninahisi, kuna watu wazito sana nyuma yake.”

    “lipi linalokufanya uamini hivyo?’

    “Lile gari nilipewa wiki moja kabla lakini nimeweza kuzunguka nalo bila kukamatwa, kila trafiki aliyekuwa analiona alikuwa analiheshimu sana, yaani ilikuwa kama kuna trafiki maalumu ambao wanafahamiana na Mjomba wamepangwa barabarani.”

    “Sasa utafanyaje ili kujinusuru maana naona kama mjomba alikusudia nawe pia ufe lakini Mungu kakunusuru.”

    “Ni kweli Tamasha na hapa inabidi niondoke, nahitaji kuishi kwa kujificha mpaka mambo yatakapopoa.”

    “Usithubutu kuendelea kudai zile pesa mpenzi.”

    “Dear, siwezi kukubali. Nimeingia gerezani, naishi maisha magumu hawezi kunifanya bwege hata kama ni komando, nitapambana naye mpaka tone la mwisho lakini pesa yangu atalipa tu vinginevyo niwe nimekufa.”

    “Hilo halitakusaidia mpenzi, uhai ni muhimu kwako kuliko chochote. Pesa zinatafutwa lakini si uhai.”

    “Una maneno mazuri mpenzi, lakini ninaomba kitu kimoja tu kutoka kwako. Kwa yote uliyoyasikia na utakayoyasikia naomba mdomo wako uweke super glue.”

    “Sawa mimi niko tayari lakini hiyo mipango yako naona unatafuta kifo.”

    “Dear, maisha yangu yamegubikwa na mikosi kwa hiyo sina cha kupoteza zaidi yako. Nimekaa gerezani kwa kosa ambalo si langu, sasa umefika wakati wa kuingia gerezani kihalali.”

    “Kwa hiyo umeamua kulitafuta gereza kwa nguvu zote?”

    “Sina maana hiyo mpenzi, natafuta haki yangu ambayo imepotea, napigania haki yangu ambayo watu wachache walioko madarakani wameimiliki.”

    “Huoni kama na wewe unahusika kupoteza haki za watu kwa kudhamiria kumuua Muheshimiwa?”

    “Kweli mwanzo nilikuwa na mawazo hayo, lakini nilipokutanisha macho yangu na sura yake iliyojaa upole na busara moyo wangu ukasita na ndio maana nikamuhurumia na kuligonga gari lake ubavuni.”

    “Sasa ni nani kamuua?”

    “Hicho ni kitendawili kingine dear, nashindwa kuamini kama alikufa kwa ajali ile.”

    “Kwa hiyo utaishi wapi?”

    “Hii nyumba nitapangisha, yaani kesho nitaanza kuongea na madalali.”

    “Na huyu uliyemuua hapa atakapoanza kutafutwa itakuwaje?”

    “Nitamfahamisha mjomba kuwa mtu wake nimemuua.”

    “Huoni kuwa utakuwa unahatarisha maisha yako.”

    “Hapana, nafikiri itasaidia kumtia hofu.”



    ***

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa amekaa kwa saa moja na nusu akimsubiri Moyo ili ampe ujira wa kazi yake. Muda ulizidi kuyoyoma huku akiwa na chupa kubwa ya maji . Hakuhitaji kinywaji chochote kabla hajamuona moyo. Kadri muda ulivyozidi kusonga mbele ndivyo fikra za kumpigia simu zilivyochukua nafasi. Hakuwa na hata chembe ya wasiwasi kuwa Moyo ataifanya vema kazi hiyo.

    Akaamua kupiga simu ili afahamu wapi aliko moyo.

    “Vipi we moyo unanikalisha muda wote hapa nakusubiri?”

    “Salimia kwanza Masharubu, Moyo yuko kuzimu saa hizi.” Sauti iliyojaa kejeli ikajibu kutoka upande wa pili.

    “Nani wewe?”

    “ Mpwao hapa James Makabi, kumbe wewe ndio ulimtuma Moyo aje kunipatia malipo yangu?” Dakika kadhaa zilipita bila Masharubu kuongea chochote, kwa mara ya kwanza katika maisha yake alijihisi kutetemeka kwa hofu. Hakuelewa ni jinsi gani Moyo ameweza kudhibitiwa na Makabi.

    “Ongea Mkuu mbona uko kimya?” Ilisisitiza sauti ya Makabi kwenye simu.

    “Ok, shida yako nini?”

    “Usiwe Bwege Masharubu, wewe ni mtu mzima unasahau kabisa tulikubaliana kitu gani?”

    “Hukukamilisha ile kazi kama ulivyoagizwa.”

    “Kwa hiyo uko tayari nikatoe taarifa kwenye vyombo vya usalama?”

    “Naamini hutafika huko kabla risasi haijapenya kwenye kichwa chako.”

    “Kwa taarifa yako nimeshaandaa taarifa ya kuifikisha kwenye vyombo vya habari na pia vya usalama.”

    “Halafu utawaambia nani anahusika?”

    “Wewe.”

    “Mimi?”

    “Ndiyo wewe.”

    “Mimi nani?”

    “Wewe Mjomba Masharubu.”

    “Una uhakika kuwa Mjomba Masharubu ni jina langu?”

    “Sina uhakika.”

    “Kama huna uhakika huoni kuwa utaonekana mwehu.”

    “Masharubu kazi uliyonipa ilikuwa kubwa na pia nilihisi kuwa lolote linaweza kutokea na ndio maana nilikupiga picha mara tatu kwa kutumia simu yangu ya kiganjani bila yawewe mwenyewe kufahamu. Sawa jina umeongopa na picha je?”

    Mjomba akahisi tumbo likinguruma kwa hofu. Alianza kuwa na mtazamo mpya juu ya adui yake huyo, kwa mara ya kwa alianza kujiona amefeli katika mkakati wake wa mauaji.

    “Mbona uko kimya Mjomba?”

    “We uko wapi?”

    “Unataka kuja au kutuma mjumbe mwingine.”

    “Nitakuja mwenyewe.”

    “Na pesa zangu?”

    “Ndiyo.” Alijibu kisha akakata simu. Alijihisi kama mtu anayevuta kisu na mwenzake huku yeye akiwa ameshika makali. Hofu yake ilitokana hasa na mazingira ya ajali ile, halikuwa jambo la kawaida kwake kuona mtu akinusurika kwenye ajali kama ile vinginevyo huyo mtu si wa kawaida.

    ‘James Makabi ni nani?’ Alijikuta akijiuliza swali ambalo lilimtisha.

    “Pumbavu, nitamuua kwa mkono wangu.” Aliwaza huku akiinuka kwenye kiti cha pale baa. Woga uliondoka na nafasi yake ikachukuliwa na hasira, siku nyingi alikuwa hajaua kwa mkono wake, alijikuta akitamani kufanya hivyo kwa James Makabi. ‘Mshenzi atanitambua’ aliongea chinichini huku akimalizia kwa tusi la sehemu nyeti.



    ***

    Nesi Belinda alikuwa anajaribu kupiga simu bila mafanikio, simu ilikuwa inaita lakini haikupokelewa. Kulikuwa na dharura ambayo ilimuhitaji dokta Kilonzo kuja kuitatua. Ilikuwa ni kawaida yao inapotokea dharura kama hiyo kuitwa madaktari maalum ambao walikuwa zamu.

    “Hallow Anna, njoo unisaidie najaribu kumpigia dokta lakini hapokei simu na leo ni zamu yake.” Aliongea huku akionesha kuwa na hasira. Hakumuona mtu aliyesimama nyuma yake.

    “Na inavyoonekana alikuwa hapa ofisini muda mfupi uliopita maana huku kwenye chumba chake amepekuapekua vitu na hata kabati lake amesahau kufunga.” Akakata simu huku akisonya kwa hasira.

    Ghafla akasikia sauti kutoka nyuma yake.

    “Hutomuona tena dokta.” Akashtuka na kugeuka, hapo ndipo alipokutanisha macho yake na Taisamo.

    “Wewe…….” Alishtuka na kutaka kupiga kelele kwa hamaki kabla Taisamo hajamuonya kwa ishara ya kuweka kidole mdomoni. “Shhhhiiiiiiiiiiiiiiiiiiii, Naomba unisikilize kwa makini nesi, hivi ninavyozungumza Dokta kapigwa risasi na watu wasiofahamika nyumbani kwake Tabata, kuna matatizo mazito sana yamejitokeza hivyo naomba ushirikiano wako.”

    “Wewe ni nani?” Aliuliza Nesi huku akiwa ametoa macho kwa hofu. Usiwe na hofu, mimi ni askari maalum ambaye nimekuja kufanya kazi muhimu. Dokta kabla ya kifo chake aliniagiza kuja kuchukua nakala ya ripoti ya muheshimiwa Makamu wa Raisi pia alitaja kitu kama chupa sijaelewa bado kuna uhusiano gani kati ya hiyo ripoti na chupa.”

    “Maskini dokta, sasa ni nani kafungua kabati lake wakati funguo anazo mwenyewe?”

    “Inaonekana hao waliomuua ndio wamekuja kufungua, naomba unisaidie kama naweza kupata hiyo ripoti.”

    “Mimi nilikuwepo wakati mwili wa muheshimiwa unafanyiwa uchunguzi, zimetolewa risasi mbili mwilini mwake ambazo alizihifadhi kwenye chupa maalum ambayo iko pamoja na ripoti, lakini mimi nilizuiwa kuzungumza chochote na dokta alisema kufanya hivyo ni hatari kwa usalama wangu.”

    “Kuna yeyote mwingine anayefahamu kuwa ulikuwepo wakati wa uchunguzi?”

    “Sio kwamba nilikuwa chumba cha uchunguzi huko sikuruhusiwa, siku hiyo nilikuwa zamu ndipo dokta alipokuja na kunionesha risasi mbili ambazo zimetolewa kwenye mwili wa Muheshimiwa, siku ya pili akaniambia mambo ni mazito kile alichonieleza basi nisimueleze yeyote na lau kama angejua basi hata kunidokeza asingenidokeza akanisimulia mambo mengi ambayo yalinitetemesha na kunionya nisithubutu kuzungumza kwa yeyote.”

    “Ok, haya uliyonieleza hakikisha unakuwa msiri kama ulivyoelezwa na dokta vinginevyo ni hatari kwa maisha yako. Ok sasa naomba unionesha kabati lake ambalo anahifadhi vitu muhimu, halafu tupange muda wa kukutana ili tuweze kuongea hayo mengine .”



    “Kabati ni hilo lililofunguliwa na hilo faili na chupa ya risasi zilizotolewa mwilini ziko chini kabisa, faili lina jalada la rangi nyekundu.”

    Taisamo akaanza kulitafuta lile faili lakini hakuliona ingawa alikuwa na bahati ya kuiona ile chupa ambayo ilisadikiwa kuwa na hizo risasi zilizotolewa katika mwili wa muheshimiwa.

    “Ok, inaonesha wameshachukua hilo faili. Kikubwa nitahitaji maelezo kutoka kwako kama ulivyonieleza, kutokana na wakati tulio nao hatuwezi kuongelea hapa hayo mambo naomba upange sehemu ya kukutana.”

    “Sawa lakini tumefahamiana juujuu sana mimi naitwa Belinda Kagaruki naishi Kinyerezi mtaa wa Kifuru, nyumba no.23, mjumbe wangu anaitwa mzee Mvula, nafahamika sana hapo.”

    “Umepanga au ni nyumba yako?”

    “Ni nyumba yangu.”

    “Hongera sana.”

    “ahsante.”

    “Nesi nashukuru kwa maelezo yako mazuri mimi utanifahamu zaidi muda huo tutakaokutana, naondoka kumbuka kuwa msiri kama nilivyokueleza la sivyo utakuwa una hatarisha maisha yako.”

    “Dokta amekufa!” Nesi alijikuta akiongea kwa sauti ya chini wakati Taisamo anaondoka ndani ya ofisi ile.



    ***

    “Sasa umepata faida gani baada ya kumtisha Mjomba?” Aliuliza Tamasha kwa sauti ya kulaumu kwa kitendo kilichofanywa na James cha kumpigia simu Mjomba Masharubu.

    “Tamasha, mimi ni mwanaume nimeumbwa ili kuja kupambana. Sasa huu ndio wakati hasa wa kuonesha uanaume wangu.”

    “Sawa dear lakini tambua kuwa nyuma yako kuna mwanamke ambaye anakutegemea na pengine kitu usichokifahamu ni kuwa nina kiumbe chako tumboni unafikiri tutaishije bila wewe pale utakapokuwa umeuwawa?”

    “Kwani mimi tu ndio ninayestahili kufa? Hata yeye anaweza kufa kwani huu ni mchezo ambao hauna mwenyewe yeyote anaweza kushinda.” Aliendelea kushikilia msimamo wake.

    “Umepatwa na nini dear mbona umebadilika sana?”

    “Nina hasira na mambo mengi, hao hao walionisababishia kifungo ndio walioniachia huru, eti msamaha wakati kosa lilikuwa la waziri. Alipita upande si wake akasababisha ajali na bado mzigo wote wa vifo vile nikabebeshwa mimi, walewale watu wake wamekuja kunitoa ili wanitie kwenye msukosuko mwingine kisha waniue, safari hii ama zangu ama zao.”

    “Unajiapiza bure kwa hasira wenzio wana silaha wewe una nini?”

    “Akili pia ni silaha.”

    “Kuwa makini dear kumbuka hasira ni hasara.”

    “Sawa, unaweza kuwa sahihi lakini mbona nimepata hasara kabla ya hizo hasira, naomba unielewe Tamasha mpenzi kamwe sitorudi nyuma, nitakutii kwa lolote katika mapenzi yetu lakini si hili la kuachana na hawa jamaa kwani hata nikiachana nao bado watakuwa wananiwinda tu.”



    ***

    Siku ya tatu toka auwawe dokta Kilonzo, Furaha ilikuwa inarindima kwenye nafsi ya Taisamo, hakuwa na wasiwasi tena kuwa ataupata ukweli kwa nesi Belinda. Alishangaa kuona kazi aliyoifikiria kuwa ngumu hatimaye inaelekea ukingoni, alihisi kuwa nesi atawataja hao wahusika jambo litakalosababisha kazi yake kufikia ukingoni na jukumu litakalobaki kuwa mikononi mwa polisi.

    Chochote alichokuwa anawaza kikakatishwa na muito wa simu yake ya kiganjani.

    “Hallow mia moja hamsini(150)?”

    “Ndiyo.”

    “Umefanya nini sasa?”

    “Kwani vipi?”

    “Kwanini umemuua dokta Kilonzo?”

    “Mimi nimemuua dokta?”

    “Ndiyo kuna ushahidi wa kutosha kuwa umemuua wakati unajua wazi mission yako ilikuwa ni kupeleleza wauaji na sababu za mauaji hayo.” Sauti ya kike ya mtu aliyejiita Rose iliongea kwa kufoka.

    “Unatakiwa kuonana na Wakuu palepale ulipokutana nao mara ya mwisho ukiwa na sababu za kuridhisha za kutopelekwa kwenye mahakama ya kijeshi Courtmarshall , kwani ushahidi wa mauaji uliyofanya umeshafika mbele ya vyombo husika.”

    “Saa ngapi natakiwa kuonana na hao wakuu?”

    “Saa sita na nusu (6.30) usiku huu.” Simu ikakatwa.

    Akainua mkono wake wa kushoto na kutazama saa, ilikuwa yapata saa mbili kasorobo. Alianza kuchanganyikiwa na wepesi ambao alihisi ulianza kutoweka.

    Wazo la haraka alilolipata ni kumuona nesi Belinda ili aweze kuwa na maelezo ya kutosha atakapokutana na wakuu wake wa kazi.

    Alishika tama Dakika kadhaa huku akitafakari nini cha kufanya kisha akainuka na kufungua droo lililokuwa upande wa kichwa wa kitanda chake ambako aliweka fedha na vitu vingine vidogo vidogo. Akapatwa na mshtuko baada ya kukuta bahasha ya kaki yenye ukubwa wa A5.

    Nini tena? Alijiuliza kwa mshtuko kwani hakuwa na kumbukumbu ya kuweka bahasha ndani ya kabati hilo. Alipoiangalia bahasha aliifahamu vema, ilikuwa na muhuri wa gazeti la THIS MONTH, asingeweza kuusahau muhuri huo kwani ni yeye mwenyewe ndiye aliyeutengeneza kisha akaujaribisha kwenye bahasha hiyo. Kilichomshangaza ni jinsi bahasha hiyo ilivyofika ndani tena kwenye droo la kitanda chake. Huu ni wakati ambao alijua wazi kuwa alitakiwa kutuliza akili yake kwani mambo yalikuwa yanabadilika ghafla.

    Huku mikono yake ikitetemeka akafungua ile bahasha ili aweze kuona kilichomo. Ulikuwa ni mchomo mkali wa mshtuko na mshangao kwa pamoja, Kazi iliyofanywa na mtu mahiri tena mtaalamu ilikuwa mbele ya macho yake. Ndiyo ni picha lakini hazikuwa picha zilizopigwa na kamera ya kawaida. Picha ya kwanza ilikuwa ni ile iliyomuonesha akiwa ameelekeza bastola kwa dokta kilonzo huku picha ya pili ambayo ilimshangaza zaidi ni ile iliyopigwa wakati akimuuliza maswali dokta Kilonzo wakati yuko mahututi. Kilichomshangaza katika picha hiyo ni jinsi ilivyoweza kuonekana vizuri licha ya kiza ambacho kilitawala eneo hilo. Ni kamera ya kijasusi tu ndiyo ingeweza kufanya kazi kama hiyo kwa ufanisi mkubwa kiasi hicho.

    ‘Kwanini umemuua dokta Kilonzo?’ Swali la Rose lilijirudia na kumjengea taswira ya kutisha ya jinsi atakavyosimama mbele ya wakuu wake wa kazi.

    Aliifahamu vema mahakama ya kijeshi, ni mahakama ambayo haikuwa na mchezo wala huruma.

    Aliitazama tena saa yake ya mkononi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Saa 2.12.” Alijisemea kwa sauti ndogo huku akichukua ile bahasha na kuiweka begi lake lenye Ngamizi pakato ‘Laptop’. Mtu wa kwanza kumtilia mashaka alikuwa Mwalimu Suzy mpangaji mwenzie. Alianza kuhisi kuwa huenda Suzy alimfuatilia ile siku aliyomfuata dokta.

    Alikuwa na wasiwasi na Suzy kwani licha kifo cha dokta ambaye siku chache zilizopita alionekana kuwa mtu wake wa karibu bado hakuonesha huzuni. Hili sio tu lilimshangaza bali pia lilimchanganya, hata hivyo upande mwingine aliilaumu nafsi yake kwa kuanza kumfikiria vibaya yule dada ambaye alikuwa na kila dalili ya upole.

    “Lazima nionane na nesi kabla ya wale wakuu” Aliwaza. Huku akifanya maandalizi ya kuelekea nyumbani kwa nesi Belinda.



    ***

    Baada ya kuhangaika kwa dakika kadhaa na kuuliza kwa watu kama watatu alifanikiwa kuiona nyumba namba 23 iliyopo mtaa wa kinyerezi eneo la kifuru. Nyumba hiyo ilikuwa imezungukwa na nyumba kadhaa ambazo ujenzi wake ulikuwa haujakamilika, baadhi ya nyumba hizo tayari zilikuwa zimeshahamiwa bila shaka na watu waliochoshwa na maisha ya kupanga. Nyumba nyingine zilikuwa zinaendelezwa ujenzi wake.

    Nyumba ya Belinda ilikuwa imejengwa kwa mtindo maarufu wa ‘L’ huku ile sehemu iliyotakiwa kuwa na nyumba kubwa ikiwa na mchanga na kokoto ambazo zilionesha kukaa hapo zaidi ya miaka miwili. Kulikuwa na kila dalili ya ujenzi wa nyumba hiyo kwenda kwa mwendo wa kinyonga bila shaka kutokana na maslahi madogo ya manesi ambayo hayakulingana na ukubwa wa majukumu yao.

    Nyumba nyingi za eneo hili zilikuwa hazijavutiwa umeme. Taisamo alishuhudia kupitia nyufa za mlango mwanga ambao alihisi kuwa ni wa kibatari. “ngo,ngo,ngo” Aligonga mlango kwa dakika kadhaa huku akilakiwa na ukimya.

    Akaamua kupiga namba ya yule Muuguzi. Hapo akapokelewa na wimbo wa taarabu ambao bila shaka ulikuwa unatoka katika simu ya nesi Belinda huko ndani. Akaamua kuvuta subira huku roho yake ikimtuma kuwa labda nesi yuko na mwanaume huko ndani.

    Ni wazo hilo ndilo lililomfanya asogee upande wa dirisha ambako alihisi kuwa ni upande wa chumba cha kulala ili aweze kusikia angalau mihemo ya mahaba. Bado ukimya uliendelea kutawala. Aliamua kuerudi tena mlangoni na kuendelea na zoezi la kugonga.

    Hatimaye alijikuta akichoshwa na zoezi lile na kuamua kujaribu kufungua mlango, mlango ukafunguka. Akaanza kupatwa na hisia kali ambazo zilisababisha msisimko wa mwili, vinyweleo vikasimama na hisia za woga zikamtawala.

    Mapigo ya moyo wake yalianza kwenda kasi pale alipoona vitu vikiwa vimetawanywa hovyo pale sebuleni, akaona kitu kingine ambacho kilimshtua zaidi na kuvuta hisia zake, akatazama nyuma, kushoto kisha kulia hakumuona yeyote, akachomoa bastola yake aina ya SIG P 228 yenye kiwambo cha kuzuia sauti. Kwa mwendo wa kinyonga huku akiwa na hisia kali za hatari mithili ya mtu anayetembea kwenye kichaka chenye nyoka wengi wenye sumu kali. Hali hiyo iliwahi kumtokea walipokuwa kwenye zoezi maalumu la kutegua mabomu yaliyoachwa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Angola. Asingeweza kuisahau siku hiyo ambayo waliingia ukanda wenye mabomu mengi zaidi ambayo yalitegwa ardhini. Alikumbuka vema kauli ya Meja mstaafu Silvester Rutakinikwa,

    “Ukanda tulioingia ni wa hatari, tumeshafanya uzembe wa kuingia eneo hili bila kulifahamu vizuri hivyo kutoka ni hatari na kuendelea kubaki ni hatari jambo la muhimu tuombe Mungu huku tukiendelea na zoezi letu.” Aliongea Meja katika zoezi hillo lililoshirikisha wanajeshi kumi na sita wanne kutoka Tanzania ambao walikuwa wakiongozwa na mtaalamu wa silaha ambaye alitegemewa sana hata na jeshi la umoja wa mataifa meja Rutakinikwa ambaye aliongozana na askari watatu ambao walitolewa maalumu na jeshi ili kuja kupata mafunzo kwani Meja alikuwa anakaribia kustaafu.

    Pia walikuwepo wanajeshi wanne kutoka Msumbiji ambao waliongozwa na Kapteni Saimon Chavara, huku wale wanne wa angola wakiwa chini ya Luteni kanali Jonas Dosantos pia walikuwepo wanne kutoka kenya ambao walikuwa chini ya Meja Frank Omondi. Hata hivyo kutokana na umahiri wa meja Rutakinikwa ambaye alisomea taaluma ya silaha mbalimbali kutoka vyuo vya kijeshi vya China, Urusi, Marekani, Cuba na Israel walifanikiwa kutoka salama eneo hilo la hatari.

    Taisamo akapandishwa cheo baada ya zoezi hilo kutoka koplo mdogo ‘lance corporal’ na kuwa Koplo kamili, pia akajikuta akihamishiwa kitengo cha Interejensia yaani Millitary Inteligency akapangiwa UNIT ya 12 ambayo ilikuwa na jina la Snake ikiongozwa na Meja Mwaikambo. Akapewa namba ya utambulisho ya 150, huko alipandishwa vyeo na kujikuta akiwa Luteni. Kikazi alikuwa anafahamika kama Taisamo kwa waliomfahamu kama Taisamo, lakini kikazi zaidi alifahamika kama 150, toka aingie kwenye kitengo hicho alikuwa hajawahi kufanya kazi yoyote kubwa zaidi ya upelelezi wa kawaida wa kukusanya habari hususani kutoka katika makundi ya wanajeshi wenzao, pia hakupewa uzito wowote wa umahiri katika kitengo hicho nyeti zaidi ya kuchukuliwa kama mtu ambaye yuko kwenye mafunzo zaidi. Hii ndiyo sababu alipopewa jukumu la kufuatilia mauaji ya Makamu wa Raisi alipatwa na mshtuko kutokana na udogo wa nafasi na uwezo wake. Alitegemea zaidi kazi hiyo kuongozwa na Kapteni,meja au Luteni kanali.





    Wakati kumbukumbu ya yote haya ikijirudia kichwani mwake bado alikuwa ameikamata barabara bastola yake yenye kiwambo cha kuzuia sauti. Licha ya mwanga hafifu wa mshumaa ambao ulikuwa juu ya stuli ambayo haikukumbwa na zahama ya kuangushwa kama stuli na viti vingine, aliweza kuyaona vema matone ya damu ambayo yalishaanza kuganda.

    Akapiga hatua huku umakini na hisia za hatari zikiongezeka. Akatembea kufuata yalikoelekea matone ya damu, alikuwa anajihisi wazi kukifuata kifo lakini hakutaka kurudi nyuma.

    Alipoangalia mlango wa kuingilia chumbani ulikuwa umefunguliwa kidogo sana kana kwamba kuna mtu alikuwa anataka kuchungulia kinachoendelea sebuleni. Alipotazama chini ili kujua kilichozuia mlango ule kujifunga au kufungwa moja kwa moja akajikuta akipatwa na mshituko.

    “My God!” Alitokwa na neno hilo huku macho akiwa ameyaelekeza pale sakafuni.



    ***

    Alishajenga mazoea ya kukusanya magazeti yote ya asubuhi na yale ya jioni na kisha kuanza kupitia moja baada ya jingine ifikapo saa mbili na nusu usiku. Hakuwa na tabia ya kupuuza gazeti lolote, hata yale yaliyoitwa magazeti pendwa au ya udaku hakuacha kuyasoma. Sio kwamba alipenda kusoma habari za wasanii na vituko zilizoandikwa kwenye magazeti hayo ambayo watanzania wengi hupenda kuyasoma, kilichosababisha ni kanuni yake ya kutopuuza na kudharau habari yoyote. Hii ilikuwa ni sehemu ya majukumu yake ya kazi ambayo alijipangia mwenyewe ingawa kimsingi idara ilichagua watu maalum wa kufanya kazi hizo.

    Mara nyingi alijiuliza kilichowavutia watanzania kusoma magazeti hayo ambayo wengi huyaita ya udaku, lakini mwishowe alipata jibu kuwa watanzania wamechoshwa na habari za siasa zao ambazo mara nyingi zimekuwa zikiwapa msongo wa mawazo. Siasa ambazo hazina matumaini ya kuleta ukombozi wa kweli kiuchumi na kijamii. Ni siasa hizo ambazo ziliwafanya watanzania watumie muda mwingi kwenye mambo ya kuwaburudisha kwani walikuwa wanakatishwa tamaa.

    Mfano mzuri ni magazeti ya siku hiyo ambayo mengi yalikuwa na vichwa vya habari vyenye kuleta hasira kwa mtanzania. Moja ya magazeti hayo lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema KILA MTANZANIA ANADAIWA DOLA LAKI NNE, hiyo ilikuwa imeandikwa kwenye gazeti la chama KIKULACHO, pia alisoma habari nyingine kwenye gazeti lingine lilikuwa na kichwa cha habari, MABILIONI YA WATANZANIA YATUMIKA KUNUNUA MAGARI MABOVU YA SERIKALI akaiona nyingine ambayo bila shaka ilikuwa ni ya kutia hasira kwa mtanzania SERIKALI YAJIANDAA KUTOKOMEZA UMASKINI KATIKA MPANGO WA MIAKA 250 IJAYO.

    Habari hizi zote bila kujali ni za uchumi, kijamii au vyovyote vile watanzania waliziweka kwenye kundi moja la habari za siasa, muda wao wa kuumiza kichwa kwa habari hizi ulikuwa umekwisha na walichohitaji wao ilikuwa ni burudani tu ili nafsi zao ziweze kutulia. Hii ndio sababu pekee iliyosababisha vijana wengi wa kitanzania kupenda magazeti hayo ambayo yaliwarudishia furaha yao iliyopokonywa na viongozi wabovu wenye uchu wa madaraka na pesa za wavuja jasho, viongozi ambao msamiati uliwapamba kwa kuwapa jina lililojengwa kitafsida zaidi yaani MAFISADI lakini ukweli ukibaki kuwa ni WEZI, MATAPELI au MAJAMBAZI na kama si kuogopa hatua za kisheria ilifaa pia kuitwa WASHENZI.

    Muheshimiwa Wahuva Kilale mkurugenzi wa Usalama wa Taifa aliyaangalia haya kwa jicho la upofu, sio kwamba hakutambua kwamba mambo yanaenda sivyo ndivyo isipokuwa hata yeye ameingia madarakani kwa njia hizohizo zisizokuwa rasmi. Unaweza kufikiri ‘CV’ yake ndiyo iliyomuingiza madarakani, la hasha! Yeye alikuwa ni mume wa rafiki wa mke wa Rais, kwa mgongo huo naye akawa rafiki wa Rais, kuanzia wakati wa kampeni akawa mstari wa mbele kupambana ili muheshimiwa aingie madarakani, yeye ndiye alikuwa kiunganishi na wahariri wa vyombo vya habari ambao walipokea pesa nyingi ili kulisafisha jina la muheshimiwa na kumfanya aingie Ikulu.

    Miezi michache baada ya muheshimiwa kuingia Ikulu ndipo akapata zawadi hiyo ya ukurugenzi. Tatizo lililojitokeza ni Idara hiyo nyeti kutoendeshwa kitaalamu, badala ya kuwa na jicho kali la kuwatazama wanasiasa idara hiyo ikajikuta ikiwa inatazamwa kwa jicho kali na wanasiasa. Ikabadilika na kuwa idara maalumu kwa ajili ya usalama wa viongozi maalumu kwa maslahi maalumu. Jicho la kawaida haliwezi kuilaumu idara hii kwa kufikiri inafanya kazi yake sawasawa, jicho linaloona mbali pekee ndilo lingeweza kuyaona makosa ya idara hiyo ambayo yamejenga uzio wa kutotaka kufuatiliwa na kulaumiwa. Lakini kimsingi ilistahili lawama kubwa sana kwani ilitakiwa kujikita hata katika mambo ya kiuchumi na kiteknolojia. Ujasusi ambao hufanywa na nchi kama china, pakistani na nyingi zilizoendelea si wa kiusalama tu, nchi hizi zina ujasusi maalumu wa kiuchumi ‘Economic Inteligency’ na aina nyingine za ujasusi ambazo ni kwa manufaa ya nchi. Lakini hii ya kwetu inaonekana zaidi kwenye ‘Politician security service inteligency’.

    Akiwa amezungukwa na magazeti hayo ambayo alianza kuyapitia kwa kusoma vichwa habari, mara simu yake ya mkononi ikaanza kuita.

    Akaitazama namba ya mpigaji.

    “Halow, habari Mr. Masharubu.”

    “Habari mbaya mkuu.”

    “Vipi kila kitu si kimeenda vema?”

    “Hapana kuna makosa yalijitokeza, yule mtu ambaye nilimtumia kusababisha ajali bado yuko hai na ameshaanza kusumbua, si hivyo tu inaonesha kuna mtu ndani ya system anafuatilia kadhia hii kwa umakini mkubwa sana na amepiga hatua kubwa kiasi kwani ameweza kumfikia hata Dokta na kusababisha tumfunge mdomo, Sijajua ni nani miongoni mwetu umempa kazi hii kwani anajiita Mwandishi wa habari lakini ana kila dalili za ukachero ingawa anaonesha hayuko makini na si mzuri sana au ni mgeni wa kazi.”

    Akatulia dakika kadhaa bila kujibu.

    “Ok, huyo dereva anataka nini?”

    “Anataka pesa zake milioni mia mbili na hamsini, shamba na gari ambavyo tulimuahidi ili aweze kutunza siri.”

    “Unayo picha yake?”

    “Ninayo mzee.”

    “Ok scan hiyo picha kisha uitume kwenye email yangu haraka, mia mbili hamsini milioni atazikosa na badala yake anastahili zaidi risasi ya kichwa au kitanzi. Nipe habari za huyo mwingine.”

    “Huyo mwingine haeleweki vizuri tumejaribu kufuatilia mfanyakazi mwenye jina lake katika gazeti la THIS MONTH tumegundua kuwa mfanyakazi mwenye jina hilo amekufa siku nyingi, jambo la kutatanisha zaidi kuna mtu mwingine ameonekana kufuatilia nyendo zake yaani inatatanisha mkuu si mchezo yaani anawindwa tena na mtu ambaye si wa kwetu.”

    “Huyo mfuatilieni taratibu na kwa umakini isije kuwa kuna msaliti miongoni mwetu nahitaji habari na picha zake kabla hatujajua nini cha kufanya.”

    Simu ikakatwa.



    ***



    Simu yake ikaanza kuita dakika chache baada ya kumaliza maongezi na mkurugenzi.

    “Ndiyo Makabi unasemaje?” Aliuliza baada ya kuitambua namba ya mpigaji.

    “Pesa zangu Masharubu, una masaa 48 tu, la sivyo nitaanika kila kitu hadharani.”

    “Ok lakini nilishafika nyumbani kwako na nimekuta bango, nyumba inapangishwa unategemea ningekupatia vipi huo mzigo wako?”

    “Mimi sio mpumbavu Masharubu, ninachotaka ni fedha zangu na jinsi ya kukutana unatakiwa kupokea maelekezo kutoka kwangu.”

    “Ok, unatakaje sasa.”

    “Nafasi ninayokupa ni ya kuchagua muda tu ndani ya hayo masaa 48, nataka uniambie ni saa ngapi naweza kuzipata hizo fedha?”

    “Saa nne na nusu asubuhi, kesho.”

    “Una uhakika?”

    “Ndiyo.” Sauti ilijibu kwa utulivu uliomtia hofu muulizaji.

    “Ok, nitakusubiri Buguruni sheli njoo na begi langu la pesa sitaki tena ujanja Masharubu.”

    “Mbona ni eneo la wazi sana huoni kuwa ni hatari kukabidhiana pesa eneo hilo.”

    “Masharubu usitake kuzungusha maneno, wewe ni hatari kuliko hilo eneo niletee pesa zikiwa kwenye begi na si briefcase mimi ndo nitajua cha kufanya.”

    “Sawa Kijana tukutane hiyo kesho.” Alimaliza huku uso wake ukifanya matuta ya hasira yaliyoufanya uso wake utishe kama simba anayejiandaa kushambulia.

    ***

    Anaitwa Mary, umri wake unakadiriwa kufikia miaka 25, alitoka Iringa kuja kufanya kazi jijini Dar es salaam, aliahidiwa mambo mengi sana na mwajiri wake aliyemleta. Maskini hakujua kuwa anakuja kuwa mtumwa wa ngono. Mwajiri wake alimtumikisha kwa biashara hiyo inayovunja heshima na utu kwa miaka kadhaa kabla hajaamua kuachana nae na kuifanya biashara hiyo yeye mwenyewe.

    Amekuwa ni mzoefu kwenye biashara hiyo kwani kwa miaka 11 amekuwa ndani ya biashara hiyo ya kuuza mwili kwa pesa kidogo. Alianza akiwa na miaka 14 tu, yaani muda mfupi baada ya kumaliza darasa la saba. Uzoefu huo umemfanya akutane na watu mbalimbali wenye tabia za aina tofauti tofauti, ni biashara hiyo ambayo mara moja moja imemfanya ajikute akiwa chini ya himaya ya majambazi ambao walimshirikisha katika baadhi ya kazi zao hususani za uporaji wa magari. Pia amewahi kushiriki matukio kadhaa ya kijambazi akitumika kama chambo kwa wanaume dhaifu ambao hukosa umakini pale wanapokuwa mbele ya Mwanamke mrembo wa sura kama Mary. Ni aina ya wanaume ambao hata wanapofanya biashara huweza kukosa umakini kwa sauti au manukato ya warembo ambao huwa ni wateja wao. Mfano mzuri ni wale wanaouza magenge ya nyanya ambao hujikuta wakiongeza zaidi na zaidi pale binti anapomlewesha kwa uzuri au mbwembwe zingine ambazo wakati mwingine hufanywa makusudi.

    Sio siri alikuwa ameumbika, Uso wa duara ambao ulibeba pua iliyochongoka kama ya msomali ulimfanya mwanaume kumtazama mara mbilimbili, macho yake makubwa ambayo yalikaribia kuwa ya duara yangeweza kubadilisha mapigo ya moyo ya mwanaume yeyote anayetazamwa. Macho hayo pia yangeweza kubadilisha hata mapigo ya moyo ya mwanamke mwingine ambaye angeyatazama kwa wivu. Kifua chake kilibeba matiti ambayo yalisimama vema kwa msaada wa sidiria, kifua chake kilikuwa ni sababu ya uchokozi kwa wanaume wenye uchu.

    Jumapili hii wateja walikuwa wamepungua sana ndipo alipojikuta akikabiliana na mteja ambaye alionekana kuwa tofauti kidogo. Hisia zilimtuma kuwa ni wateja wake wale wa hatari ambao mara nyingi humtumia kwenye mambo mazito.

    “Sema basi si unatafuna maneno, unajua unavyonizingua nakuwa sikuelewi?”

    James Makabi hakuwa na papara bado alihitaji utulivu na umakini kuongea na mwanamke huyo ambaye alizipata simulizi zake kutoka kwa madereva wenzake ambao alikuwa nao kituo kimoja cha daladala.

    “Haraka ya nini, si tuingie huko ndani tuongee?”

    “Kunitoa tu hapa na kunipeleka ndani mkono mtupu sio ishu.”

    “Nani kakwambia ni mikono mitupu?”

    “Aah, maana ushaanza mara maongezi kidogo na wewe, sijui nini, hii ni sehemu ya kazi na sio kutongozana. Hapa ni biashara yaani kazi tu!” Aliendelea kubwabwaja Mary huku akimalizia kipande cha sigara ambacho kilikuwa mdomoni mwake.





    James hakujishugulisha kutazama kitu ambacho kilikuwa kigumu kuita kaptura au kichupi cha jinzi kilichovaliwa na mrembo huyo. Ni kivazi hicho ambacho kiliruhusu maeneo nyeti ya kahaba huyo kuwa nje. Ni kana kwamba kilienda kuziba sehemu nyeti zaidi na kuacha maeneo mengine ambayo ni nyeti kubaki nje. Mapaja yake yaliyojaa vizuri ndiyo yaliyomfanya apate wateja wengi kuliko wenzake.

    “Mary, punguza kubwabwaja kwani tunataka kuongea ishu ya mamilioni.”

    Kauli hiyo ilimtuliza Mary ambaye alishazoea kubwabwaja ovyo.

    “Mamilioni. Duh, mchizi wangu sio ishu ya kuuzana hiyo?” Aliuliza huku akikaa vizuri na kukunja miguu kwa mtindo wa nne pale kitandani.

    “Ni kazi ndogo sana unatakiwa kufanya.”

    “Halafu malipo.”

    “Milioni kumi, ukifanikiwa.”

    “Nikishindwa.”

    “Sote tutakuwa tumekosa.”

    “Enhe nipe mchoro.”

    “Utatakiwa kusimama hapo Buguruni sheli, Jamaa atakuja na begi lenye noti. Atakukabidhi kisha utafuata maelekezo nitakayokupa.”

    “Hivyo tu?”

    “Ndiyo.”

    “Halafu milioni kumi? Sio tunauzana kweli mchizi wangu.”

    “Hatuuzani, kuna biashara ya unga tumeifanya, na huo ndio utaratibu wangu wa kupokea pesa.”

    “Mbona huna dalili ya kuwa Zungu wewe?”

    “Unataka dalili ipi?”

    “Huna harufu ya pesa mchizi.”

    “Nilikuwa gerezani, nimetoka miezi michache iliyopita unatarajia nini?”

    “Ok, nimekuelewa mchizi, lini sasa hilo dili?”

    “Kesho saa nne na nusu.”

    “Poa niache na ya kiroba basi mchizi.” Aliongea kwa sauti iliyojaa dalili ya ulevi lakini akionesha wazi kuelewa mazungumzo yao.

    Akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti tatu za shilingi elfu kumikumi.

    “Dah, poa mchizi wangu, ngoja nipate kiroba nitulize kichwa maana mchongo huu si mchezo.”

    Makabi akaondoka kwenye kile chumba na kufuata uchochoro mdogo ambao unatokea kituo cha magari cha Temeke Hospitali. Alikuwa na uhakika wa kufanikisha mpango wake kwa asilimia kubwa zaidi bila kudhurika.



    ***

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miguu ya mtu ambaye mwili wake ulikuwa chumbani ilikuwa imetokea mlangoni na kumfanya Taisamo kuingiwa na Mashaka. Licha ya kuwa aliikamata Bastola yake vizuri, alijikuta akiongeza nguvu za vidole vyake kuikamata silaha hiyo hatari kwa nguvu zaidi kwa hofu ya kumponyoka au kupokonywa na adui aliyeko karibu.

    Hisia zilizidi kumtuma kuwa adui yuko karibu pale alipokuwa anausukuma mlango taratibu ili kujionea kilichojiri huko chumbani. Hali ya machugachuga ilikuwa imemtawala na kujikuta akiwa kwenye matarajio ya kushuhudia mkono wake wenye bastola ukipigwa teke na adui ambaye hakujua alikuwa amejificha eneo gani humo ndani.Aliamua kuchuchumaa na kuingia chumbani kwa staili ya kinyonga zaidi. Alishituka aliposikia kitu kama matone ya maji kikidondoka pale alipokaa, alipotazama vizuri zaidi ndipo alipogundua kuwa kwa dakika chache alikuwa amelowa kwa jasho mwili mzima, jasho lililizidi kiasi cha kudondoka kama matone ya maji.

    Aliamua kuusukuma mlango kwa nguvu na kujirusha ndani kwa. Akatulia kwa sekunde chache huku akitarajia risasi kupenya mwilini mwake kutoka kwa adui ambaye alitarajia kuwa angeibuka kama mzuka. Akili ya kivita iliyafanya macho yake kuwa na nguvu ya ziada. Giza jepesi ambalo lilipunguzwa ukali na mwanga hafifu wa mshumaa ulioko sebuleni lilimuwezesha kuona mwili wa mtu uliolala mlangoni, ndio mwili uleule ambao aliweza kuuona wakati anaingia.

    Akautazama kwa makini ule mwili, haukuwa wa nesi Belinda. Ulikuwa ni mshangao mwingine. Aliyeko mlangoni ni nani kama si Belinda? Ni mzima au amekufa? Mfululizo wa maswali ya haraka ulikuwa unapita katika kichwa chake. Hakukuwa na dalili ya adui kama alivyofikiri. Akarudi sebuleni haraka na kuchukua ule mshumaa ili aweze kuona vizuri kule chumbani.

    Hakuwa daktari lakini alikuwa na uelewa mkubwa wa kujua kama mtu yuko hai au amekufa bila ya kuchunguza mapigo ya moyo, hilo ndilo lililomfanya kwa kutumia mwanga wa mshumaa kutambua kuwa yupo kwenye chumba chenye maiti mbili. Alichanganyikiwa, mtu aliyemtegemea kuwa angalau angempa mwanga juu ya kifo cha makamu wa Rais alikuwa ameuwawa.

    Aliutazama mwili wa Belinda akagundua kuwa alichomwa kisu na kisha kumalizwa kwa mikono yenye nguvu ambayo ilimaliza kazi kwa ustadi mkubwa kwa kuvunja shingo yake. Hali jinsi ilivyo aligundua kuwa Belinda alipokea kipigo akiwa sebuleni, kipigo hicho kilimfanya atokwe na damu hivyo akaamua kukimbilia au akaburuzwa kwenda chumbani. Yule aliyelala sakafuni alikuwa binti mdogo mwenye umri kati ya miaka kumi na tano na kumi na sita. Huyu alionekana kufa kwa sababu ya vita ya tembo ambayo huteketeza hata panzi walioko karibu, ni wazi hakuwa sehemu ya mpango wa muuaji. Hili ndio jibu lililopita haraka katika kichwa cha Taisamo baada ya kuutazama mwili wa binti huyo ambao hakuwa na shaka kuwa uliuwawa kwa pigo moja kali la kareti.

    Aliyarudisha macho kitandani, akautazama kwa masikitiko mwili wa Belinda. Alijikuta akishikwa na uchungu huku kitu kigumu kama donge kikitambaa shingoni kwake. Akiwa ameukodolea macho mwili huo akakiona kipande kidogo cha karatasi ambacho kilikuwa kimeandikwa kwa wino wa kijani.

    ......U mwandishi hodari wa kunusa kila mahali lakini u mjinga

    Kwa kukitafuta kifo chako kwa nguvu zote. Tafadhali acha kufuatilia

    Habari za MKUU, hii ni nafasi ya upendeleo ambayo hajapewa yeyote

    Aliyejaribu kunusa mambo haya zaidi yako.

    Alikitia kipande kile cha karatasi katika mfuko wa shati kisha akapiga hatua za haraka kuelekea mlango. Akatoka mle chumbani huku akiwa ametawaliwa na hasira, alijikuta akitamani zaidi kukutana na adui yake hasa huyo mkuu kuliko ilivyokuwa hapo kabla. Alijihisi hatia kwa kifo cha Belinda na yule msichana ambaye alihisi kuwa ni mfanyakazi wake wa ndani ‘House girl’.

    Kuna nini na nani nyuma ya pazia? Lilikuwa swali lingine ambalo lilipita kwenye kichwa cha Taisamo. Ni mtandao gani unaojaribu kunusa kila alipopita? Ni nani kaweza kumpiga picha katika eneo la tukio? Kwanini hakummaliza muda huohuo, kwani badala ya kitufe cha kupigia picha si angetumia tu kifyatulio cha bastola na kummaliza kwa risasi moja tu ya kichwa? Maswali hayo yalimzidishia hofu na kumfanya ajione kama mtu anayeoga kwenye bafu yene ukuta wa kioo ambao haukuzuia mpita njia kumuona.

    Ni nani huyu mkuu na nini lengo lake? Hilo lilikuwa swali jipya ambalo lilianza kukitawala kichwa chake na kumtisha pia.

    ***



    Jumatatu saa 4.30 simu ya James Makabi iliita kwa sekunde chache kabla ya kupokelewa.

    “Niko eneo la tukio.”

    “Sikuoni.”

    “ Unaiona hiyo Rav4 nyeusi inayowekwa mafuta?”

    “Ndiyo nimeiona.” Alijibu James akiwa na uhakika kuwa alikuwa anazungumza na Mjomba Masharubu.

    “Ok, we uko wapi?”

    “Mzigo wangu unao?”

    “Niko kamili uko wapi? unapoteza muda kijana.”

    “Rudi nyuma, fuata barabara ya Mandela upande wa kulia ambako hupita watembea kwa miguu.”

    “Mpaka wapi?”

    “Utaiona karakana inayoranda mbao. Nimesimama karibu na lango.”

    Mjomba akapiga jina linguine kwenye simu yake.

    “Fuata Lumumba Road Kama unaenda Tabata Matumbi, upande wa kulia kuna karakana angalia nani anaongea na simu.” Akakata simu na kupiga tena namba ya James.

    “Nimefika bado uko hapo karibu na lango la karakana?”

    “Ndiyo niko karibu na lango si umebeba begi la fedha?” Simu ikakatwa bila kujibiwa swali hilo kisha ile namba iliyopigwa kabla ikapigwa tena.

    “Vipi umemuona mtu anayeongea na simu?” Baada ya simu kukatwa akakunja uso kwa hasira.

    “Mbona unaleta usumbufu uko wapi wewe?”

    “Angalia hapo karibu na lango kuna mwanamke amevaa hijabu nyeusi naomba umkabidi huyo fedha zote.”

    “Shiiit....” alichukia Masharubu huku akisindikiza hasira zake kwa tusi zito la hifadhini.

    Akiwa na hasira kali akatembea kwa kasi akiwa na begi lake mkononi.



    ***

    James Makabi alifika eneo la tukio sa 3.00 yaani saa moja na nusu kabla. Alikuwa amempa Mary maelekezo muhimu jinsi ya kuja kupokea fedha hizo. Akili zake zilifanya kazi haraka na hisia za kuwa Masharubu ni mtu hatari ndizo zilizotawala kichwa chake, alipofika eneo hilo la Buguruni sheli akavuka barabara na kukaa upande wa pili ambako kulikuwa na madereva wengi wa magari madogo madogo ambayo yalitumika kubebea mizigo. Akajiunga na madereva wa eneo hilo kwani alifahamiana na wawili kati yao. Hata wale ambao hakufahamiana nao bado hakuwa mgeni kwao kwani walishakutana mara kadhaa na kupelekea kutambuana kwa sura.

    Simu yake ilipoanza kuita akajitenga kidogo na eneo lile. Aliweza kumuona vema Mjomba Masharubu akiteremka kutoka kwenye Rav4 nyeusi.

    Baada ya mawasiliano ya dakika kadhaa na makubaliano yao ndipo alipomuona Masharubu akirudi kwenye gari na kuchukua Begi la fedha. Alitabasamu. Tabasamu lililochanganyika na hofu ingawa pia alikuwa na hisia za ushindi ndani yake.

    Kwenye hisia zake aliweza kujenga nyumba nzuri ya kisasa ambayo ilikuwa na mabanda ya kufugia kuku wa mayai na wale wa nyama. Bustani nzuri ya maua ambayo ilikuwa inamwagiliwa na Tamasha akisaidiwa na mfanyakazi binti wa miaka kumi na minne ilikuwa inapendeza na kuvutia.

    Yote haya yalipita kwenye akili zake baada ya kuliona begi lile ambalo aliamini kuwa lilikuwa na fedha.

    “Mia mbili Hamsini milioni!” Alijikuta akitamka kwa sauti ambayo alijisikia mwenyewe.

    “Eee bwana kuna mshikaji namfuatilia hapo mbele.” Alisikika Makabi akimuaga mmoja wa wenyeji wake pale kijiweni.

    “Poa kamanda.” Alijibu rafiki yake huyo wa siku nyingi.

    Akavuka barabara haraka na kwenda kusimama kituo cha daladala zinazoelekea Tabata, Ubungo na Mwenge. Bado Masharubu alikuwa hajapotea kwenye macho yake.

    Wakati huohuo aliweza kumuona Masharubu akiongea na simu. Kidogo akaanza kuingiwa na mashaka, alitamani sana kujua nini anaongea katika wakati ule nyeti na wa hatari. Umbali uliyawezesha macho kufika aliko Masharubu na kumuona anachokifanya lakini uliyanyima fursa masikio yake kusikia alichokuwa anaongea.

    “Usalama upo kweli?” Alijiuliza.

    Aliweza kumuona Mary akiwa amesimama kwa umakini kabisa wakati Masharubu anamuendea. Muda huohuo Makabi akampigia simu.

    “Ni huyo mrefu mwenye suti nyeupe, tai nyekundu na kofia ya pama.”

    “Poa mchizi.” Alijibu Mary ambaye alikuwa amevaa headphone upande mmoja wa sikio lake.”

    Hakujua walikuwa wanaongea nini lakini alimshuhudia Masharubu akikabidhi begi lile la fedha kwa Mary. Kabla hajaondoka Mary akafungua kidogo zipu ya begi na kuchungulia, akatikisa kichwa kukubali. Muda huo huo akamuona Masharubu akirushia kitu fulani ambacho kutokana na umbali hakuweza kukifahamu ndani ya lile begi. Hakujali sana alichoona muhimu ni kitendo cha Mary kutikisa kichwa kwa ishara yakukubali huku akitabasamu.





    Hakujali kuwa zitakuwa zimetimia zote milioni mia mbili hamsini, muhimu kwake ni kuwa hizo fedha zilikuwa nyingi hata akiamua kutoroka zitatosha.

    Ndoto za maisha mazuri zilikuwa zimejikita kwenye nafsi yake. Akili yake ilitawaliwa na harufu ya noti. Alijihisi akikaza mipira kadhaa ya kufungia noti ‘ruberband’’, furaha iliyochanganyika na hofu ilikuwa inarindima kwenye nafsi yake.

    Wakati Mjomba Masharubu anaondoka eneo la makabidhiano ndipo Makabi aliposhuhudia kitendo ambacho hakukielewa. Mary alitimuka kwa kasi sana na kujitoma kwenye Toyota Corola nyeupe ambayo iliegeshwa karibu na eneo la makabidhiano. Kilichomshtua Makabi ni kuwa ile Corolla ilikuwa nje ya mpango wao. Hisia za kuibiwa na yule mwanamke zikachukua nafasi yake. Wakati akiwa amepigwa na butwaa ghafla akashuhudia tukio lingine la kutisha. Hakuamini macho yake kuwa mambo haya yote yalikuwa yanafanyika ndani ya muda mfupi kwa kasi ya aina yake.

    Watu walipiga mayowe na kutawanyika ovyo, ni wakati huo ambao Makabi alijikuta akituliza akili yake kwa kiwango cha hali ya juu na kuyatazama matukio yaliyokuwa yanatokea pale kama filamu fulani ya kusisimua. Alitazama kila upande kuanzia kwa watu waliokuwa wanakimbia ovyo mpaka eneo la tukio. Watu walikuwa kwenye taharuki kubwa.

    Kama si kila mtu kuwa katika hekaheka za kuokoa nafsi yake basi Makabi angekuwa anamshangaza kila mtu kwa hali ya utulivu na ujasiri aliokuwa nao kwenye mazingira magumu kama yale. Hakuwa peke yake, pamoja na tukio hilo la kutisha aliweza kumuona Mjomba Masharubu akiingia kwenye gari kwa utulivu mkubwa kana kwamba hakuna tukio linaloendelea.



    ***

    Ilikuwa saa 4.45, Taisamo alifika nyumbani akiwa amechoka sana. Hakuwa na wazo la kulala pale nyumbani. Akachagua nguo chache na kuziweka kwenye kibegi kidogo ambacho kilifanana na ‘briefcase’ Baada ya kuhakikisha kuwa amekamilisha zoezi hilo fupi akatoka na kufunga mlango wa chumba chake. Alitazama chumba chake kana kwamba anakiambia kwaheri. Akaanza kupiga hatua za haraka kuondoka.

    “Mbona hatuagani?”

    Alishitushwa na sauti ya teacher Suzy ambaye alikuwa nyuma yake.

    “Umekuwa adimu Suzy, huonekani.” Alijitetea Taisamo.

    “Nimefiwa na mume wa Shangazi yangu, anaitwa Dokta Kilonzo hivi ninavyokuambia najiandaa kwenda huko msibani mazishi yatachelewa kidogo kwani mwili wake unafanyiwa uchunguzi na madaktari.”

    Kidogo Taisamo akapatwa na mshituko kwa kauli hiyo, akahisi kama imezungumzwa kwa kukusudiwa. Akainua macho yake na kumtazama Suzy. Hayakubeba huzuni ya mfiwa, yalikuwa yameficha kitu cha ziada ambacho kiliufanya moyo wa Taisamo ulipuke kwa mshituko. Alikuwa anatazamana na macho yaleyale, hayakuwa macho ya kawaida, macho ambayo yalificha kitu zaidi ya huzuni. Kisasi? Alishituka baada ya kujiuliza swali hilo. Askari? Hapana, alikataa haraka sana. Mwandishi? Hapana alishanieleza mapema kuwa yeye ni mwalimu.

    Alishangaa kujikuta akitazamana na macho ya Suzy yasiyo ya kawaida. Halafu mbona kama sura yake sio ngeni sana? Alijiuliza. Sekunde chache zilipita akiwa amekodoleana macho na binti huyo mrembo ambaye aligeuka kuwa kitisho kwa wakati huo.

    “Suzy, pole sana kwa msiba. Nilikuwa na mengi ya kuongea na wewe lakini nimepata dharura ya safari ya kikazi ambayo itanichukua siku mbili au tatu. Nina mengi ya kuzungumza na wewe tutaonana nikirudi.” Alimaliza Taisamo huku akionesha wazi kuwa na haraka.

    “Ok, basi niachie hata namba ya simu.” Alibembeleza Suzy.

    Taisamo akataka kuchomoa business card inayomtambulisha kuwa mwandishi wa habari lakini akasita akaamua kuiandika namba hiyo kwenye kipande cha karatasi na kumpatia.

    “Kwa heri Suzy.” Aliaga huku akiwa ameshapiga hatua kadhaa.

    Hakuwa na jibu la kumpa Jenerali, hakuwa na jibu la kumpa Luteni Jenerali. Alikuwa na mambo mawili tu ya kufanya, kutoroka na kujificha huku akitafutwa kila kona na mkono mrefu wa serikali au kutafuta ukweli kwa gharama yoyote ili aweze kujitoa kwenye tuhuma hizo.

    Njia ya pili ilimsisimua na kumvutia zaidi, kuutafuta ukweli ambao alishaonywa kuwa ni kukitafuta kifo chake mwenyewe. Alijua wazi kuwa ili kuupata ukweli hakutakiwa tena kufuata mpango wa ofisi huku akifuatiliwa kila analolifanya na mtu anayeitwa Rose. Alijihisi kumchukia Rose kwani alipenda afanye kazi kwa uhuru zaidi na sio kila dakika kuulizwa hatua aliyofikia.

    Dakika arobaini na tano baadae alikuwa eneo la Mtoni kwa Azizi Ali, ndani ya chumba kimoja dhaifu katika nyumba ya kulala wageni ambayo haikuwa na umaarufu zaidi ya kujulikana zaidi kwa wapenda ngono na makahaba.

    Akiwa na tafakari nzito juu ya matukio yanayomtokea ndipo simu yake ikaanza kuita, ilikuwa ni miongoni mwa namba ambazo zilikuwa zinamkera sana.

    “150, Rose hapa naomba kukukumbusha kuwa wakuu wanakuhitaji, imebaki saa moja tu, hakikisha unakuwa na ushahidi wa kutosha kwani leo huenda ukakamatwa na Millitary police(MP) kwa uzembe katika kazi na kusababisha mauaji ya daktari pamoja na nesi ambayo inasemekana umemuua saa chache zilizopita.”

    Alikuwa kama aliyepigwa na shoti ya umeme baada ya kusikia taarifa hizo za kifo cha nesi saa chache zilizopita. Alizidi kuchanganyikiwa kwani alihisi kutembea na mtu asiyemuona. Sasa alikuwa na kitu zaidi ya mshangao, nini? Woga! Hakupenda kuruhusu woga kwenye kazi, alitafakari na kuona huu ni wakati wa Liwalo na liwe. Akiwa bado ameing’ang’ania simu yake akajikuta akitoa jibu ambalo hata mwenyewe alijishangaa.

    “Rose, please tell your boss .MISSION CANCELLED. (Rose mwambie mkuu wako mpango umefutwa”

    “150!”

    “Dont call me 150 or Liutenant (Usiniite 150 au Luteni), napenda nibaki kuwa Taisamo.”

    “Una maana gani?”

    “Nimeacha kazi.”

    “what?”

    “Hujanielewa? kila kitu kimeharibika mwanamke, mpango umefeli nahisi kuna msaliti hapo kati maisha yangu yako mashakani.”

    “Unaonaje ukifikisha hayo madai yako kwa Jenerali?”

    “Mwanamke, usinitafutie balaa. Kwaheri.”

    “Usiniite kwa dharau kiasi hicho mimi ni mkuu wako wa kazi.”

    “No, ulikuwa mkuu wangu, kwaheri.” Simu ikakatwa.

    Alijihisi hatia ndani ya nafsi yake lakini akajikuta hana uwezo wa kukabiliana na maswali ya Wazee wale wawili ambao wako katika nafasi za juu za kiutawala ndani ya jeshi. Alizifahamu vizuri taratibu na sheria za kijeshi ambazo huwa kali kama pilipili machoni pindi unapofanya kosa alilolifanya yeye. Alijua kwa taratibu za jeshi lazima atafutwe kutokana na kuwa na baadhi ya vifaa vyao kama vile silaha na fedha. Aliwaza kitu ambacho alitakiwa kukifanya haraka. Alijua nini aanze nacho kesho.

    Ukweli ni kwamba alikuwa amechanganyikiwa, kwani dakika chache zilizopita alikuwa akiota heshima na pengine kupandishwa cheo lakini ghafla upepo umebadilika amejikuta akielekea kudhalilika na pengine kuingia gerezani kutokana na mtego ambao hajui nani kautega na kwa lengo gani. Sasa anatakiwa kujibu maswali ambayo kama atashindwa lazima apelekwe kwenye mahakama ya kijeshi. Alishangaa kuona mambo haya yakitokea kama ndoto.



    ***

    Ilikuwa yapata saa 1.30,ndio kwanza Enerst Bigambo Meneja wa Benki ya NMB tawi la kariakoo alikuwa anakaa kwenye kiti. Ulikuwa ni utaratibu wa matawi mengi ya benki hiyo kuanza kazi zao za ndani kuanzia muda huo hadi saa 2.30 ambapo utaratibu wa kawaida wa kibenki wa kuhudumia wateja huanza.

    Akiwa amevutiwa na tukio la kusisimua la ujambazi lililotokea Buguruni Sheli, alikuwa ni mmoja miongoni mwa wafanyakazi wa benki hiyo ambao walikuwa wamesimamisha utaratibu wa kawaida wa kazi kwa nukta chache na kuelekeza macho yao kwenye tukio hilo ambalo lilikuwa linatangazwa na kuonyeshwa na moja ya vituo vya Runinga.

    Dakika chache baada ya kumalizika kwa taarifa hiyo simu yake ya mkononi ikaanza kuita.

    “Bosi, kuna mtu anaomba kuonana na wewe mara moja.” Ilikuwa ni sauti ya Miriam katibu muhutasi wake.

    “Ananihitaji kibinafsi au.......”

    “Kikazi Bosi.”

    “Miriam, mbona unakuwa kama mgeni unashindwa kumueleza taratibu za kazi?”

    “Nimemueleza kila kitu akanitisha akaniambia mambo yakiharibika nitakuwa Responsible kwani ana kazi muhimu ambayo haitakiwi kusubiri muda wa kawaida kuonana na Meneja.”

    “Dah, we si unajua wateja jinsi walivyo wasumbufu wakiwa na haraka zao mruhusu.”

    Sekunde chache baadae mlango wa ofisi yake ukafunguliwa na mtu ambaye kabla ya kukaribishwa alikaa kwenye kiti kilichoelekeana na kile cha meneja.

    “Habari yako Meneja.”

    “Nzuri, ndugu yangu, sijui nikusaidie nini maana umekuja mapema mno.” Aliongea meneja huku akilazimisha kicheko ili kuficha karaha yake kwa tukio hilo.

    “Nina haraka, ninahitaji pesa kama milioni thelathini kutoka kwenye akaunti yangu.”

    “Lakini muda wetu wa.........”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana meneja kuna mambo mengine huwa ni ya dharura, mimi nafanya kazi muhimu ambayo inanitaka ndani ya dakika kumi na tano niwe nimeshachukua fedha na kuianza.”

    Meneja alianza kuonesha hasira kidogo na kutaka kugeuka mbogo kwa mteja. Mteja alilifahamu hilo na kwa haraka akatoa kitambulisho chake. Kisha yakafuata maelezo mafupi.

    “Luteni JWTZ!” Alishangaa meneja huku akikitazama kwa umakini kitambulisho kile na kuridhika kuwa kilikuwa chenyewe hasa.

    “Kuna kazi muhimu sana inatakiwa kukamilishwa ndani ya muda mfupi ujao kama utashindwa kunisaidia ina maana utakuwa ni mmoja wa waliochangia kushindwa kwa kazi hiyo.” Hata kama asingetoa maelezo hayo, kile kitmbulisho kilitosha kumfanya meneja kubadili msimamo wake kwani alifahamu anaongea na nani. Muda huo huo akabonyeza namba fulani kwenye simu yake ya mezani.

    “Hallow Frank, namleta kwako mteja wetu Alex Taisamo...... naomba umsaidie kutoa fedha anazohitaji kutoka kwenye akaunti yake.”

    “Nenda kwa cashier namba 3 hapo chini utasaidiwa, pole kwa usumbufu bwana Taisamo.”

    “Ahasante mkuu usijali.....”







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog