Simulizi : Bondia
Sehemu Ya Tatu (3)
Baada ya lile pambano lake na mzungu kutoka Hungary, Macha alipambana na bondia kutoka Afrika ya Kusini mjini Johannesburg, ambako alimtawanya taya msauzi huyo na kuondoka mshindi. Sifa za bondia “Deus-deadly” Macha sasa zilikuwa zimeenea duniani kote, na Tanzania ikawa moja ya nchi za kutazamika katika ulimwengu wa ndondi.
Kwenye faili kulikuwa kuna habari juu ya mzozo baina ya Deus na promota wake, mzozo ambao kwa mujibu habari za magazeti, ulitokana na Deus kutoridhika na mapambano anayoandaliwa na promota wake huyo. Mwisho wa habari ile ilielezwa kuwa Deus alivunja mkataba na promota huyo na kujiunga na promota mwingine ambaye alionekana kuwa na mtazamao wa maendeleo zaidi kwa Deus kuliko yule promota wake wa awali aliyemtoa jeshini. (Roman alitikisa kichwa tena kwa masikitko, kisha akendelea kusoma).
Ndipo, miezi sita baada ya lile tukio la kutishiana baina yake na yule bingwa wa dunia wa wakati ule, promota mpya wa Deus alipokubali pambano baina ya bondia wake na bingwa yule, pambano likiwa ni la kugombea mkanda ule wa dunia. Kufikia hapa Roman alikuwa anasoma kwa hamasa, akiwa amejawa udadisi wa kujua kilichojiri kwenye pambano lile baina ya Bondia Deusdelity Macha na yule bingwa wa dunia wa wakati ule...
Lilikuwa ni pambano lililotangazwa na kunadiwa sana, na siku ya tukio ukumbi ulifurika kuliko ilivyowahi kutokea. Kengele ya kuanza pambano ilipogongwa, wapinzani wale waliendeana kwa bashasha na azma ya pambano la kukata na shoka. Na hapa ndipo Deus alipoonesha kuwa kweli yeye alikuwa muuaji kwani kufikia raundi ya kumi na moja bingwa wa dunia aliyekuwa akitetea ubingwa wake alikuwa ameshavunjwa mwamba wa pua na akitokwa damu kama maji.
Refa alilazimika kusimamisha pambano na Deus akatawazwa ubingwa wa dunia katika uzito wa Super Middle kwa Technical Knock Out.
Picha ya mwisho ndani ya faili lile ilimuonesha Deus akimvugumizia konde la kulia katikati ya uso mpinzani wake, ngumi ambayo ndiyo iliyomvunja mwamba wa pua na kumvua ubingwa. Hii ilikuwa ni miezi sita iliyopita...
Roman alishusha pumzi ndefu huku akilifunika lile faili. Aliketi kwa muda mrefu pale kwenye kiti akiwa amejawa na tafakuri nzito, kisha akainuka na kutoka nje. Alienda kuketi kwenye kona moja ndani ya ile baa iliyokuwa nje ya ile klabu na kuagiza kinywaji. Uso wake ulikuwa umekunjamana kwa mawazo mazito. Muda mfupi baadaye, Makongoro “Mark Tonto” Tondolo aliingia eneo lile na kuanza kuelekea kule kwenye klabu yake ya ndondi. Roman alimpigia mbinja, na Mark alipogeuka, alimpungua mkono.
“Haya niambie nini kilitokea jana Roman...Inspekta Fatma alikuibukia hadi huku?” Mark alisema huku akiketi kwenye kiti mbele ya Roman. Roman aliita muhudumu na Mark akaagiza kinywaji.
“Bora ingekua Inspekta Fatma Mark, angalau yeye najua ni nini kinachomsumbua”
“Ama! Ni nani kumbe?”
Roman akamsimulia juu ya tukio baina yake na yule mwanadada aliyejitambulisha kwa jina la Kate. Mark alichanganyikiwa.
“Mnh!Kate? Kate huyu wa wapi? Na alikuwa anataka nini hasa?” Alijikuta akiuliza maswali ambayo tayari Roman alishajiuliza. Roman alimbetulia mabega na kubaki akimtazama tu. Kimya kilichukua nafasi baina yao kwa muda, kisha Mark akaongea.
“Okay, sasa unadhani tufanyaje juu ya hii hali?”
“Tusifanye kitu...tuendelee na mipango yetu kama tulivyopanga.”
“Khah! Sasa na huyu Kate...?”
“Kate hatuzuii kufanya lolote. Yeye atakuja tena tu, na safari hiyo hatonitoka kirahisi...” Roman alisema kwa utulivu. Lakini Mark hakuwa na utulivu hata kidogo katika swala lile.
“Hii ni mbaya sana Roman...mbaya sana!” Alisema kwa hamasa. Roman alibaki akimtazama akiwa kimya. “Sasa unajuaje iwapo huyu...huyu...Kate, si askari aliyetumwa na Inspekta Fatma Roman? Unajua huyu Fatma mi’ hanipi amani kabisa?” Alizidi kusema kwa wasiwasi. Roman alimtazama yule rafiki yake wa makamu na kumpiga ngumi ya maskhara begani.
“Relax kocha, okay? Haitusaidii kuumiza kichwa kwa jambo ambalo hatuna hakika nalo kwa sasa bwana. Lolote ambalo yule dada alikuwa analitaka kwangu, hakulipata, hivyo lazima atarudi tena, na hapo ndipo tutajua. Kwa sasa tunaendelea na mambo yetu kama kawaida.” Alimwambia kwa kirefu. Mark alimtazama kwa muda, kisha huku bado uso wake ukiwa makini, alimwambia; “Tutaendelea na mipango yetu kama kawaida, lakini hatutakiwi ku-relax hata kidogo juu ya swala la huyu Kate, Roman...mpaka tujue ni nini hasa anataka kutoka kwako, okay?”
“Okay, kocha wangu...”
Kimya kilichukua nafasi kwa muda wakati watu wale wawili wakiendelea kunywa vinywaji vyao, kila mmoja akiwa na mawazo yake.
“Kesho ndio mnaanza mechi za kugombea ubingwa wa wilaya, sio?” Hatimaye Roman aliuliza.
“Yeah Roman. Naona vijana wako katika hali na ari nzuri, natumai tutashinda tu...”
Kimya kilitawala tena.
“Jina langu limo kwenye orodha ya mabondia waliosajiliwa kwenye timu yako?” Roman aliuliza tena.
“Kama tulivyopanga Roman. Nilikusajili tangu wakati uko gerezani, na kama bado una nia ya kuendelea na azma uliyoweka, basi nawe utapanda ulingoni pindi ukiwa tayari...”
“Azma iko pale pale Makongoro. Ila itabidi vijana wako wafanye kazi ya kuvuka katika ngazi hii ya wilaya, mimi nitaingia kwenye ngazi ya mkoa...nahitaji mazoezi zaidi...” Roman alimjibu, kisha akaendelea, “...unadhani wanaweza kutuvusha?”
“Ninajua kuwa wanaweza kutuvusha...” Mark alijibu kwa kujiamini.
****
Kwa wiki mbili mfululizo baada ya siku ile, Roman alijishughulisha katika mazoezi mazito sana ya ndondi. Akikimbia umbali mrefu kila alfajiri na kurudi kwenye ile klabu yao ya ndondi kwa ajili ya mazoezi zaidi ya viungo na ya ulingoni chini ya usimamizi makini wa kocha wake wa muda mrefu, Mark Tonto. Timu yao ya ndondi haikufanikiwa kuchukua ubingwa wa wilaya, lakini ilifanikiwa kusonga hadi ngazi ya mkoa kwa kutoka washindi wa pili katika ngazi ile ya wilaya. Na katika wiki mbili zile, pamoja na kuweka umakini wa hali ya juu kila alipokuwa, Roman hakuonana tena na Kate wala Inspekta Fatma.
Mazoezi yaliendelea kwa nguvu, na kadiri alivyokuwa akiendelea na mazoezi, ndivyo alivyozidi kujihisi akirudia kwenye uwezo wake wa ngumi aliokuwa nao hapo awali...kabla hajapigwa marufuku kushiriki katika mchezo ule aliokuwa akiupenda sana, na kujikuta akikaa nje na ulingo kwa miaka mingi, miwili kati ya hiyo akiwa gerezani.
Kadiri siku zilivyosogea, ndivyo alivyozidi kuhisi msisimko wa ajabu wakati utashi wa mchezo ule ukimtambaa ndani ya mishipa yake ya damu. Mchezo wa ngumi...ndondi...mchezo wa mabondia. Naye sasa alikuwa anajiandaa kuingia tena ulingoni kushiriki mchezo ule.
Wengi walikuwa wakishiriki mchezo ule kwa ajili ya kutaka sifa na umaarufu, wakati wengine walikuwa wakishiriki kwa ajili ya pesa tu, ilhali wengine ilikuwa ni kwa ajili ya pesa na umaarufu na sifa. Na wachache miongoni mwa mabondia walikuwa wakishiriki mchezo ule kwa upenzi tu wa michezo kama ilivyokuwa kwake kabla hajapigwa marufuku... na kabla ya kifungo chake.
Lakini safari hii Roman alikuwa anarudi ulingoni kwa ajili ya kutimiza azma. Azma ya hatari. Azma iliyokuwa ikifumfukuta moyoni kwa miaka miwili. Azma iliyogubikwa usiri mkubwa.
***
Roman alikuwa akikimbia huku akitupa ngumi mbele yake na kuruka huku na huko kibondia kando ya barabara. Alikuwa amevaa suruali ya mazoezi na fulana nchinjo ya mazoezi ambayo ilikuwa na kofia iliyofunika kichwa chake. Usoni alikuwa amevaa miwani maalum ya kumkinga na upepo na vumbi. Mark Tonto alikuwa akimfuta nyuma taratibu akiwa kwenye baiskeli. Walikuwa kwenye mazoezi makali, ikiwa ni siku tatu tu kabla ya kuanza kwa mashindano ya ndondi za ridhaa kugombea ubingwa wa mkoa, safari hii Roman naye akiwa miongoni mwa mabondia wa Kawe Boxing Club watakaopanda ulingoni.
Wakiwa katika harakati zao zile za mazoezi, hawakuitilia maanani kabisa Toyota Prado short chasis yenye rangi ya metallic iliyokuwa imeegeshwa kando ya barabara ile waliyozoea kuitumia kila asubuhi kwa ajili ya mazoezi yao makali.
Ndani ya ile gari, Master D na Kate walikuwa wakiwatazama kwa utulivu wawili wale wakiendelea na mazoezi yao. Kate alimtazama yule jamaa aliyetoka gerezani siku kadhaa zilizopita jinsi akitupa masumbwi hewani namna ile huku akiranda kulia na kushoto kistadi wakati akikimbia kando ya ile barabara, na uso wake ukafanya tabasamu dogo.
“Enhe? Nini kinafuata sasa Master D?” Alimuuliza yule mtu mzima aliyekuwa naye ndani ile gari huku bado akiwaangalia akina Roman. Ilikuwa ni zamu ya Dan kuachia tabasamu dogo, kisha akaliondoa gari kando ya barabara, akawapita akina Roman na kuondoka eneo lile.
“Kinachofuata ni kukabiliana na Roman sasa...nadhani mambo yanaenda kama tutakavyo...” Master D alimjibu.
“Okay...lini sasa?” Kate alihoji.
“Soon...very soon...(muda mfupi sana ujao) mrembo wangu!”
***
Mashindano ya ndondi kugombea ubingwa wa mkoa wa Dar es Salaam yalichukua muda wa wiki tatu. Katika wiki ya kwanza Kawe boxing club ilipandisha mabondia wanne ulingoni, watatu wakishinda na mmoja akipoteza pambano. Roman alikuwa miongoni mwa watatu walioshinda kwa kumuangusha mpinzani wake katika raundi pili tu ya pambano, na hapo hapo kujipatia mashabiki kwa jinsi alivyokuwa akipigana.
Wakiwa mazoezini ndani ya ile klabu yao mwisho wa ile wiki ya kwanza,Roman alipata ugeni asioutarajia. Siku hiyo alikuwa ulingoni akipigana na bondia mwenzake ikiwa ni sehemu ya mazoezi, mkufunzi wao Mark Tonto akiwa kama muamuzi na wakati huo huo akitoa mafunzo. Mabondia wengine wa timu ile ya ndondi walikuwa nje ya ulingo wakifuatilia pambano lile la mazoezi kwa makini, wote sasa wakiwa wamemkubali Roman kama mwenzao na kama bondia mwenye uwezo mkubwa miongoni mwao.
Yule bondia alikuwa akimjia kwa ngumi kali za mfululizo, na Roman alikuwa akiruka huku na kule, akitupatupa miguu yake mbele na nyuma kiufundi huku akimsogezea uso mpinzani wake na kuurudisha nyuma kila jamaa alipojaribu kumtupia konde, hoi hoi na vifijo vikirindima kutoka kwa mabondia wenzao waliokuwa nje ya ulingo. Jamaa alikuwa akimjia kwa kasi, Roman aliyumba kushoto na kubonyea kidogo huku akimsogelea, wakati jamaa alipotupa konde kali la kushoto lililopita hewani, na Roman aliibuka na upper cut iliyotua sawia kidevuni kwa mpinzani wake na kumpeleka chini kama mzigo.
Shangwe ziliibuka kutoka kwa mabondia wenzao, wakati Roman akimsaidia bondia mwenzake kuinuka kutoka pale chini.
“Pole partner...sikuipa nguvu zangu zote hata hivyo...kwa hiyo hutadhurika sana!” Alimwambia yule bondia huku akimsaidia kusimama.
“Sasa huo ndio upiganaji Roman!” Mark alisema kwa hamasa huku akiwasogelea wale wapiganaji wake, na kumgeukia yule kijana aliyepelekwa chini kwa konde la Roman, “...na ule si upiganaji! We’ umenaswa kwenye mtego wa Roman, Chumbi... anakuchezeshea uso nawe unautamani uso, unasahau kujikinga...” Mark alikuwa akisema, lakini hapo macho yake yaliangukia nje ya ulingo, na kutulia huko kwa muda, sentensi yake ikibaki ikielea hewani. Alimtupia jicho la haraka Roman, na kuyarudisha tena macho yake kule nje ya ulingo. Roman aligeuka kufuata ulelekeo wa macho ya Mark, kama jinsi ambavyo na wale mabondia wengine walikuwepo pale walivyofanya.
Inspekta Fatma alikuwa amesimama nyuma kabisa ya ule ukmbi wao wa mazoezi, akiwa amevaa mavazi yake ya kiaskari, kofia yake akiwa ameikumbatia chini ya kwapa lake la kushoto. Kwa mkono wake wa kulia alikuwa ameshika fimbo yake ya kiaskari ambayo alikuwa akiipiga-piga taratibu kwenye tumbo la kiganja chake cha kushoto. Uso wake uliokuwa umefunikwa kwa miwani myeusi ulikuwa ukimtazama Roman moja kwa moja kule ulingoni.
“Sasa huyu anataka nini tena hapa?” Mark Tonto alisema kwa sauti ya chini huku akimtazama yule askari wa kike. Roman alimuacha Chumbi na kuusogelea ukingo wa ule ulingo na kusimama akiwa ameshika kamba ya ulingo ule huku akimtazama Inspekta Fatma. Walibaki wakitazamana kwa muda, kisha Inspekta Fatma aliweka kofia yake kichwani taratibu, na bila ya kusema neno lolote, aligeuka na kuondoka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hivyo tu!
Roman na Mark walitazamana, lakini hakuna yeyote kati yao aliyesema neno, kisha Mark akawageukia wale mabondia wake.
“Alrigh, alright, alright, Hey! Haya tunaendelea, tumeshaona jinsi Roman na Chumbi walivyojifua...sasa nataka niwaone Dulla na Kibwe ulingoni...” Alisema huku akipiga makofi kuwahamasisha wachezaji wake.
Roman aliteremka ulingoni, na taratibu aliondoka eneo lile kuelekea ofisini kwa Mark, ambako ndiko kilikuwa chumba chake cha kulala. Uso wake ulikuwa umekunjamana kwa tafakuri nzito.
“Sasa ndio nini vile?” Mark Tonto alimuuliza Roman saa moja baadaye wakiwa wamekaa kwenye ile baa iliyokuwa nje ya klabu yao ya ndondi pale Kawe, kisha akaendelea, “...yule askari ana maana gani kuja hapa na kuondoka bila kusema neno?”
Roman aliuma mdomo wake kwa hasira. “Alikuwa anajaribu kunipa ujumbe Mark...”
“Ujumbe gani sasa?”
“Kwamba bado ananifuatilia na kwamba nisisahau onyo alilonipa siku ile nilipotoka gerezani.”
Mark alitikisa kichwa kwa mastaajabu. “Ama hakika huyu mwanamke majinuni...sasa tufanyaje Roman?”
“Sisi tunaendelea na harakati zetu kama kawaida, hakuna kinachobadilika.Hii mikwara ya Inspekta Fatma hainitishi hata kidogo mimi.”
Wiki ya pili ya mashindano ya ubingwa wa mkoa wa ndondi za ridhaa, Kawe boxing club ilipoteza bondia mmoja, na Roman na Chumbi wakasonga mbele kwenye fainali, safari hii Roman akimuangusha mpinzani wake katika dakika ya kwanza tu ya raundi ya nne na ya mwisho. Lilikuwa ni pambano lililojaa hoi hoi na nderemo kwa jinsi Roman alivyokuwa akimchezea yule mpinzani wake, na hatimaye kumuangusha kwenye ile raundi ya mwisho. Sasa Roman alikuwa ni miongoni mwa mabondia wenye mashabiki wengi kabisa katika mashindano yale. Jioni ile Mark aliandaa sherehe fupi pamoja na mabondia wake kuwapongeza Roman na Chumbi kwa kufikia fainali ambayo ingefanyika katika wiki ifuatayo. Wakiwa katikati ya sherehe zao pale kwenye ile baa iliyokuwa nje ya klabu yao, Mark alinunua gazeti la jioni lililokuwa likipitishwa na mchuuzi pale baa na kumuonesha Roman habari iliyokuwa kwenye ukurasa wa michezo wa gazeti lile.
Deus wa mauaji kukabiliana na Mswazi.
Kichwa cha habari ile kilinadi, na mara moja Roman akawa makini na habari ile, ambayo ilieleza kuwa bingwa wa dunia wa uzito wa Super Middle Deus “deadly” Macha alikuwa akitarajia kuzipiga na bondia kutoka Swaziland katika pambano la kimataifa kutetea ubingwa wake alioupata miezi sita iliyopita. Pambano lile lilipangwa kufanyika mwisho wa wiki ile, siku ya jumamosi katika ukumbi wa PTA jijini.
Habari ile ilileta mjadala baina ya wale mabondia wa ile timu ya Kawe, baadhi ya wale mabondia wakimsifia Deus jinsi alivyo mahiri katika masumbwi, na jinsi alivyokuwa akiwaangusha wapinzani wake, wengine wakitamani siku moja kuwa kama yeye.
Roman na Mark Tonto walitulia kimya akiwasikiliza wale vijana wakimjadili Deus.
“Okay boys, mnaonaje sote tukienda kushuhudia pambano hilo jumamosi hii, eenh?” Hatimaye Mark aliuliza.
Mayowe na shangwe vililipuka kutoka kwa vijana wale, wakiiafiki hoja ile ya Mark kwa mbinja na hoi hoi, wengine wakirukaruka huku wakitupa ngumi hewani na kucheza kibondia kufurahia swala lile.
“Aaah, acheni fujo sasa, ebbo!” Mark aliwaasa wale vijana wake kwa ukali huku akiona wateja wengine pale baa wakionekana kuwashangaa na kukereka kwa mayowe yale.
Roman aliinuka na kuondoka na lile gazeti kuelekea chumbani kwake bila ya kuaga. Mwili ulikuwa ukimtetemeka kwa mchanganyiko wa hamasa na jazba.
***
Siku ya pambano ukumbi wa PTA ulifurika mashabiki wa kitaifa na kimataifa. Baada ya mapambano ya utangulizi hatimaye ulifika wakati ambao hasa watu wote waliofurika pale walikuwa wakiusubiri. Bondia kutoka Swaziland alipanda ulingoni akisindikizwa na kocha na wapambe wake wachache, shangwe kidogo zilisikika,lakini zaidi ilikuwa ni sauti za kuzomea kutoka kwa mashabiki wa Deus. Kisha akaingia Deus mwenyewe akiongozana na kocha na promota wake pamoja na msururu wa wapambe, muziki wa bongo flava maalum wa kumsindikiza ukirindima kutoka kwenye maspika makubwa yaliyotandazwa kila kona ya ukumbi ule, mayowe, vifijo na mbinja vilirindima kila upande, na kadiri zile shangwe zilivyozidi, ndivyo Roman, akiwa miongoni mwa watazamaji waliohudhuria pambano lile pamoja na mabondia wenzake wa Kawe Boxing Club na kocha wao Mark Tonto, alivyoweza kusikia muitiko wa pamoja kutoka pale ukumbini.
“Deus...Deadly...Deus...Deadly...Deus...Deadly...!”
Roman alitulia kimya akitazama kila tukio kwa makini, na kengele ya kuanza pambano ilipogongwa, alishuhudia jinsi Deus akimsulubu mpinzani wake kutoka uswazi kwa namna ambayo ilimfanya aelewe ni kwa nini alifikia hatua ya kuitwa “Deus wa mauaji”. Mswazi alienda chini mara mbili, kwenye raudi ya nne na ya tisa, na alipoenda chini kwa mara ya tatu kwenye raundi ya kumi hakuinuka tena. Kwisha kazi. Deus alikuwa amefanya “mauaji’ kwa mara nyingine.
Ukumbi ulipagawa kwa vifijo. Mashabiki walijaribu kuvamia ulingo, kabla ya kutulizwa na Deus akatangazwa mshindi rasmi. Hapo ukumbi ulilipuka upya, Deus aliinuliwa juu huku akizungusha ngumi hewani kushangalia ushindi wake. Roman alisimama na kuanza kusogea karibu na ule ulingo, Mark Tonto akiwa sambamba naye.
“Vipi Roman...” Mark aliuliza.
“Nataka nimuone vizuri...” Roman alijibu huku akijisukuma mbele na kusimama hatua chache kando ya ule ulingo, akiwa amefumbata mikono kifuani kwake akimtazama yule bingwa wa dunia mtanzania akifurahia ushindi wake. Na ndipo ghafla, katika kuzunguka kwake huku na huko akishangilia ushindi wake ilhali uso wake ukiwa na tabasamu pana, macho ya “Deusdeadly” Macha yalipoangukia kwa Roman akiwa amesimama kando ya ule ulingo akimtazama.
Walionana...uso kwa uso.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ghafla uso wa bingwa wa dunia Deus ulibadilika, na lile tabasamu likafutika, nafasi yake ikichukuliwa na mshangao, kisha kitu kama woga mkubwa, na haraka ule woga ukachukuliwa na ghadhabu. Alijikurupusha na kuteremka kutoka mabegani kwa yule shabiki aliyekuwa amembeba. Katika kufanya hivyo,aliinamisha kichwa chake kuangalia asianguke, na wakati alivyofanya vile, Roman aliweza kumuona Inspekta Fatma akiwa upande wa pili wa ule ulingo.
Yule askari hakuwa akiangalia yale yaliyokuwa yakitendeka ndani ya ule ulingo, bali alikuwa akimtazama Roman kutokea kule alipokuwa amesimama!
“Shit! Inspekta Fatma!” Roman alinong’ona kwa hasira na kujirudisha nyuma akijichanganya kwenye umati wa mashabiki waliokuwepo pale.
“Wapi...wapi?” Mark Tonto alinong’ona kwa wahka, lakini Roman alimshika mkono na kumvutia kule alipokuwa akitowekea, akizidi kujichanganya katikati ya kundi la watu.
“Deusdeadly” Macha, bingwa anayeendelea kutamba na mkanda wake wa dunia katika uzito wa Super Middle, alitoka mbio hadi kwenye ukingo wa ulingo katika ule upande ambao alimuona Roman akiwa amesimama hapo awali, na kuangaza macho yake yaliyojaa wahka eneo lile.
Patupu! Roman hakuwepo!
Badala yake aliona kundi la mashabiki tu wakimshagilia na kumpungia mikono huku nyuso zao zikiwa zimejawa tabasamu. Deus hakuwatilia maanani. Alikuwa akimtafuta Roman katika kundi lile lakini hakumuona tena. Aligeukia upande wa pili wa ulingo ule hali ikawa vilevile, aliranda huku na huko ndani ya ulingo ule akijaribu kumtafuta tena Roman, lakini Roman hakuonekana kabisa machoni mwake. Ilikuwa kama kwamba yule aliyemuona hakuwa Roman bali ni taswira tu iliyojijenga kichwani mwake!
Kwenye kona moja ya ukumbi ule, Master D alimgeukia Kate na kumwambia huku akiinuka kutoka kwenye kiti chake.
“Okay, tunaweza kwenda sasa mrembo wangu...tumeona mengi kwa leo au sivyo?”
“Sana anko...sana tu. Si umeona jinsi uso wake ulivyohamanika alipomuaona Roman? E bwana we! Leo mbona tumeona mambo!” Kate alisema huku naye akiinuka.
*****
Roman alikuwa akikimbia kando ya barabara asubuhi huku akitupa-tupa ngumi hewani mbele yake kama kawaida yake. Asubuhi hii alikuwa peke yake. Ilikuwa ni asubuhi ya siku ya pili baada ya lile pambano la Deus na mswazi. Yeye pambano lake lilikuwa siku ile jioni, ambapo angepanda ulingoni na bondia kutoka timu ya wilaya ya Ilala, kugombea ubingwa wa mkoa katika ndondi za ridhaa. Alikuwa akikimbia katika upande wa barabara ambao ulimuwezesha kuona magari yaliyokuwa yakimjia mbele yake. Hata hivyo alfajiri ile barabara ile haikuwa na magari mengi, na ndio maana alipenda kukimbia alfajiri. Mbele yake, kiasi cha mita ishirini hivi, gari aina ya Toyota Prado Short Chasis Metallic lilikuwa limeegeshwa kando ya barabara likiwa limeelekea kule alipokuwa akielekea yeye, lakini upande wa pili wa barabara. Kutokea nyuma yake alisikia mvumo wa gari likielekea kule alipokuwa akikimbilia yeye, lakini hakutilia maanani, alikuwa akiendelea na mazoezi yake tu kama kawaida.
Mvumo wa lile gari lililokuwa likitokea nyuma yake uliongezeka na akahisi kama lile gari lilikuwa likiongeza kasi, na hata wakati wazo lile lilipokuwa likipita kichwani mwake, aliona mlango wa ile Prado iliyokuwa imeegeshwa mbele yake, ambayo sasa ilikuwa umbali wa kama mita tano tu kutoka pale alipokuwa, ukifunguka ghafla na mtu mmoja aliyekuwa amevaa suruali na fulana ya mazoezi akiruka nje na kumpungia mikono kwa wahka huku akipiga kelele, na hapo hapo alilisikia lile gari liliyokuwa nyuma yake likimkaribia huku likizidisha kasi.
Oh, my God! Nagongwa...!
Bila ya kugeuka nyuma, Roman alizidisha kasi ya mbio na hapo hapo alijirusha kwa nguvu kulia kwake na kuangukia kwenye kichaka kilichokuwa kando ya ile barabara. Muda huo huo aliliona gari ndogo likimpita kwa kasi sana usawa wa pale alipokuwa akikimbilia sekunde moja tu iliyopita, alijibiringisha na kusimama wima akilitazama lile gari likiyumba kidogo baada ya kumkosa na kurudi barabarani, likimkosakosa na yule mtu aliyeruka kutoka kwenye ile Prado, ambaye alijirusha upande wa pili wa gari lake lile gari lililomkosa kumgonga likitokomea kwa kasi eneo lile. Yaani lile gari ilihama kutoka upande wake na kumfuata kule alipokuwapo!
Tusi zito lilimtoka Roman, na kutimua mbio kukimbilia pale kwenye ile Prado na kuzunguka upande wa pili huku akitweta. Moyo ulimlipuka na kujikuta akibwata huku akiwa amekodoa macho.
“Wewe!!”
Kate alikuwa amekaa chini kando ya lile gari huku akiwa amejishika mguu wake.
“Unajua kwenye pochi yangu kulikuwa kuna hela mle?” Kate alimwambia huku akitabasamu, ingawa alionekana kama kwamba alikuwa kwenye maumivu makali.
“Ama?” Roman alimshangaa yule binti na kubaki akimkodolea macho, kisha akamtupia swali, “Unasemaje wewe?”
“Jamaa zako walikuwa wanataka kukugonga wale! Na kwa kasi ile wangekuua tu!” Kate alisema tena, akipuuzia lile swali la Roman. Roman alizidi kuchanganyikiwa.
“Jamaa zangu? We’ umewaona waliokuwa kwenye lile gari?”
“Kulikuwa kuna watu wawili, ila sijawaona sura...walikuwa wamekudhamiria wewe haswa!”
“Sasa we’ ulikuwa unafanya nini huku. Na usiniambie kuwa ulikuwa unanitafuta mimi tena!” Roman alimwambia kwa jazba.
“Ndio haswa. Nilikuwa nakuvizia wewe. Na ni bora nilivyofanya hivyo kwani nimekuokoa, kwani kama si mimi kukupigia kelele za kukutahadharisha jamaa wangekugonga wale!”
“Mnh! Kweli...ahsante sana. Lakini...kwa nini ulikuwa unanivizia huku saa hizi?”
“Si nikudai pesa zangu!” Kate alimjibu kwa maskhara huku bado akiwa amefinya uso kwa maumivu. Roman alibaki akimtazama kwa mastaajabu. “We’ unafanya maskhara kwenye kila kitu, eenh?Hebu inuka hapo unieleze vizuri ni nini kinachoendelea hapa?”
“Siwezi...nadhani nimetegua mguu! Nisaidie tafadhali...!” Kate alimwambia huku uso wake ukionesha kuwa alikuwa kwenye maumivu makali. Roman alimsaidia kuinuka, na alipojaribu kutembea tu yule msichana aliachia kiyowe kidogo cha maumivu na kuanza kuanguka tena chini, lakini Roman aliwahi kumdaka kiuno.
“Dah! Nimeumia sana...naomba unisaidie kuingia kwenye gari...” Kate alisema kwa uchungu. Roman alimsaidia na kumuweka nyuma ya usukani.
“Oh, Roman samahani, lakini itabidi uniendeshe, mimi sitaweza, kwani mguu niutumiao kuendeshea ndio ulioumia...” Kate alisema akiwa kwenye maumivu makali. Roman alimtazama yule dada kwa muda na akaona kuwa hakuwa akifanya maskhara.
“Sasa unajuaje kama mi’ naweza kuendesha?” Alimuuliza.
“Oh, come on Roman, mi najua mengi juu yako bwana, kwa hiyo najua kwamba unaweza kuendesha gari...hebu nisaidie tafdhali, nipeleke nyumbani!”
“Nikikusaidia utanieleza kinachokufanya unifuate-fuate namna hii?”
“Of course nitakueleza...leo nd’o nilikuwa nataka tupange siku ya kuonana, lakini ndio yametokea haya...twende tafadhali!” Kate alimjibu huku akijisukumia kwenye kiti cha abiria kule mbele. Roman aliangaza huku na huko, kisha akaingia nyuma ya usukani na kuliondoa lile gari kutoka eneo lile. Njiani Roman alijaribu kuwaza juu ya tukio lile la kukoswa kugongwa, lakini hakuweza kuwaza kitu cha msingi juu ya tukio lile kwani Kate alikuwa akimuongelesha.
“Inaelekea una maadui wengi Roman...mpaka wengine wanataka kukugonga na magari!”
“Hilo halinipi taabu.Linalonipa taabu ni wewe uko upande gani Kate, na unataka nini kwangu?”
“Mnhu! Kuhusu mimi usiwe na taabu. Mi’ niko upande wako, na nd’o maana nikakupigia kelele nilipoona kuwa lile gari lilikuwa linaelekea kukugonga...”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Na ndo maana siku ile ukaja kupekua ofisini kwetu na kunitoroka?” Roman alidakia. Kate alicheka.
“Siku ile ulinishtukiza Roman, sikuwa na namna zaidi ya kukutoroka...I am so sorry...” Kate alimjibu, na kuendelea, “...lakini pesa zangu nazitaka ujue, nilijua siku tukikutana n’takudai tu!”
“Pesa zako zipo na wala sijazitumia, ila sinazo hapa. Sasa je unaweza kuniambia ni nini unachotaka kwangu Kate...kama hilo ni jina lako kweli?”
“Okay...kwanza Kate ni jina langu kweli...kama jinsi Roman lilivyo jina lako la kweli. Na pili...ninachotaka kutoka kwako ni muda wako tu...kuna mtu nataka nikukutanishe naye Roman. Ni muhimu sana kwako na kwake pia!” Kate alimjibu, safari hii uso wake ukiwa umepoteza kabisa maskhara.
“Ni nani huyo unayetaka nikutane naye? Na ana nini ambacho ni muhimu kwangu na kwake?”
“Mimi kazi yangu ni kukutanisha naye tu Roman. Najua leo una pambano la ngumi jioni, unaonaje tukija kuonana nawe baada ya pambano leo usiku pale kwenye ile baa ya pale kwenye klabu yenu?” Kate alisema. Roman alitikisa kichwa kwa mastaajabu.
“Inaelekea unajua mambo mengi juu yangu Kate...why?”
“Labda leo usiku utajua, nikimleta huyo mtu anayetaka kukutana nawe.” Kate alimjibu.
Baada ya hapo Roman hakuongea tena. Aliendesha kimya mpaka alipomfikisha Kate nyumbani kwake. Kate alipomkaribisha ndani hakukubali.
“Sasa utarudi vipi? Ngoja basi nikupe pesa ya teksi...” Kate alimwambia.
“Usijali...n’tarudi kwa mbio tu...si unajua bado nilikua mazoezini?” Roman alimjibu. Kate alichanganyikiwa kidogo, lakini Roman hakumpa muda wa kuongea zaidi. Aliruka nyuma hatua mbili, akageuka, na kuanza kukimbia kimazoezi kurejea kwenye klabu yake ya ndondi.
“Basi sisi tutakuja huko leo usiku, okay?” Kate alimpigia kelele. Roman alimpungia mkono bila ya kugeuka wala kupunguza kasi...
***
Jioni le Roman alipanda ulingoni akiwa na ghadhabu kubwa, ghadhabu ambayo alikuwa ameielekeza kwa yule mtu asiye sura aliyetaka kumgonga makusudi asubuhi ile.
“Nakupa asilimia tisini na tisa Deus anahusika na tukio hilo Roman!” Mark alisema baada ya Roman kumsimulia tukio lile asubuhi ya siku ile.
“Kwa nini unasema hivyo Mark...? Angeweza kuwa mtu mwingine yoyote...” Roman aliuliza, ingawa hata yeye alikuwa na hisia kama alizokuwa nazo Mark.
“Acha hizo Roman! Huyu ni yeye tu! Kwanza jiulize...iweje siku zote jambo hili lisitokee lije kutokea leo baada ya yeye kukuona kwa mara ya kwanza tangu urudi uraiani? Ni yeye bloody swine...ni yeye!” Mark alimjibu kwa jazba.
Ghadhabu zake zilimuishia mpinzani wake pale ulingoni jioni ile, kwani kwa mara ya kwanza tangu arudi tena kwenye ngumi za ridhaa, Roman alitupa makonde mazito kabisa yaliyosukumwa na ghadhabu iliyokuwa ikimchemka mwili mzima. Alisukuma makonde ya nguvu na hasira kiasi kwamba katika raundi ya kwanza tu alishamdondosha chini mpinzani wake mara mbili, na alipomdondosha mara ya tatu katika raundi ile, muamuzi akatangaza Technical Knock-Out, na Roman akaipatia timu yake ya Kawe Boxing Club ubingwa wa wilaya!
Ndani ya dakika tatu tu!
Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi na vifijo, mabondia wenzake walivamia ulingo kwa furaha, naye akajikuta akiinuliwa juu juu, akiwa ameinua juu ngumi kuashiria ushindi wake ilhali sura yake bado ikiwa imefura kwa hasira...
***
“Hongera kwa kunyakua ubingwa Roman...hakika leo umepigana kwa namna tofauti kabisa na mapambano yako yaliyopita...” Dan Dihenga alimwambia mara baada ya kutambulishana na kusalimiana jioni ile.
“Oh, ahsante...kwani ni mapambano yangu gani mengine uliyowahi kuyaona?” Roman alimjibu na kumuuliza huku akimtupia jicho Mark Tonto aliyekuwa pamoja nao pale kwenye meza iliyokuwa kweye kona kabisa ya ile baa iliyokuwa nje ya klabu yao ya ndondi.
“Oh, tumekuwa tukihudhuria mapambano yako yote Roman...” . Master D alimjibu huku akitabsamu, na kuendelea, “...na nd’o maana nakwambia leo umepigana kwa namna tofauti kabisa na mapambano yako yote hayo niliyowahi kuyashuhudia.”
“Mnhu! Ukiniuliza mimi n’takwambia kuwa leo amepigana kwa ghadhabu zaidi kuliko vinginevyo!” Kate alisema huku akimtazama Roman kwa macho ya uchokozi. Muda ulikuwa ni saa mbili za usiku. Kate na Master D walifika pale klabuni kiasi cha saa moja na nusu za jioni na kutulia pale kwenye baa kwa muda, wakisikia shangwe na hoi hoi zilizokuwa zikirindima pale kwenye ile klabu ya ndondi ya akina Roman mpaka wale mabondia wengne walipoondoka na kuwaacha Roman na Mark Tonto pale klabuni. Ndipo Kate, huku akichechemea,alipokwenda kuwabishia hodi na kuwaarifu kuwa walikuwa wameshafika. Ndipo wapojumuika nao pale kwenye ile meza waliyokuwa wamekalia.
“Okay, mnaonaje mkitueleza dhamira ya ujio wenu?” Mark Tonto aliuliza huku akiielekeza kauli yake kwa Master D. Roman alitikisa kichwa kuafiki kauli ya Mark.
“Sawa kabisa...” Dan alisema na kujiweka sawa, kisha akaendelea, “...kama nilivyojitambulisha hapo awali, mi’ naitwa Dan Dihenga...na huyu ni mpwa wangu Kate...”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Na kama nilivyosema hapo awali, jina lako si geni masikioni mwangu Mr. Dihenga...” Mark alisema.
“Yeah, na kama ungekumbuka ni katika mazingira gani ulipata kulisikia jina langu, moja kwa moja ungejua dhima ya ujio wetu huu...”
“Sasa unaonaje ukituweka wazi Mr. Dihenga, maana mi’ nahitaji kujipumzisha...” Roman, bingwa mpya wa ngumi za ridhaa wa uzito wa Super Middle kwa mkoa wa Dar es Salaam, alisema.
“Very well Roman. Nitaenda moja kwa moja kwenye swala lililo kichwani mwangu...” Master D alisema na kumtazama Roman kwa muda, kisha akamgeukia Mark Tonto, na kumrudia tena Roman, “...nataka nikuingize kwenye ndondi za kulipwa Roman...nataka niwe promota wako...”
Moyo ulimpasuka Roman kwa kauli ile, na akafinya macho kidogo kwa umakini huku akimtazama yule mtu aliyeketi mbele yake, kisha akamtupia jicho Mark, moyo ukimwenda mbio. Hapo hapo Dan akamgeukia Mark haraka.
“Eenh, sina nia ya kukuvua nafasi yako kwa Roman Mark...la hasha, najua wewe ndiye umekuwa promota na kocha wake, lakini...”
“Nimeshakukumbuka sasa!” Mark alisema kwa hamasa, akimwangalia kwa mtazamo mpya yule mtu huku akimuoneshea kidole. Dan Dihenga alimuinulia nyusi na kutamtazama kama kwamba akimwambia “alaa?”
“Wewe ni Dan Dihenga!” Mark alisema huku bado akiwa na hali ya mshangao. Roman aliachia mguno huku akimtazama Dan kwa makini.
“Hilo hata mimi nalijua Mr. Tondolo...” Master D alimjibu huku akitabasamu, lakini Mark alikuwa kama kwamba hajamsikia, akaendelea,“Wewe ni promota mkubwa wa ndondi nchini...!”
Master D alibetua mabega yake tu bila ya kusema neno. Bado Mark alikuwa akimtazama kwa ule ung’amuzi mpya uliomshukia baada ya kumkumbuka yule mtu.
“Wewe...wewe...ndiye promota wa zamani wa Deusdelity Macha!” Mark alimalizia, na hata pale alipomalizia kauli ile, Roman alitoa mguno mkubwa wa mshangao na kumtumbulia macho yule jamaa aliye mbele yao, na kumtupia jicho Kate, ambaye alimtawanyia tabasamu pana ambalo kama kwamba lilikuwa likimwambia “...sasa ulikuwa unatarajia nini?”
“There you are!” Dan Dihenga alisema huku akitupa mikono hewani kumaanisha kuwa sasa Mark alikuwa amesema hasa kilichokuwa ndicho.
Kimya kilichukua nafasi wakati wale watu wakitazamana, kila mmoja akiuweka sawa akilini mwake ufahamu ule mpya uliotokana na ung’amuzi wa uhalisia wa Dan Dihenga.
“Kwa nini?” Hatimaye Roman aliuliza taratibu.
“Ndio kazi yangu Roman!” Dan alimjibu, na kuendelea, “Mimi kama promota wa ndondi, ni kazi yangu kutafuta mabondia wazuri na kuwapromoti katika mchezo huu mpaka wafikie mafanikio yanayohitajika kwao, kwangu na kwa mchezo huu wa ndondi hapa nchini na duniani kote. Hiyo ndio azma yangu kubwa katika ku-promoti ndondi...”
“Kwa nini umtake Roman...?” Mark aliuliza. Dan alimtazama kama kwamba alikuwa ameuliza swali la kijinga.
“Roman ni bondia mzuri! Promota yeyote ajuaye kazi yake akimuona tu Roman apiganavyo, hatosita kum-promoti. Nami ni promota nijuaye kazi yangu Mr. Tondolo...naijua vizuri sana!” Alimjibu. Muda wote huu Kate alikuwa kimya tu akifuatilia mazungumzo yale.
“Come on Mr. Dihenga! Kuna mabondia wengi tu wazuri hapa nchini ambao wana uwezo wa kufanya makubwa kama watapata promota kama wewe. Unataka kuniambia kuwa hao wote hukuwaona ila Roman tu?” Mark alimuuliza kwa hamasa. Dihenga alimtazama, kisha akamtupia macho Roman.
“Jibu swali bwana Dihenga...why me...and why now?” Roman alimsisitizia swali la Mark, akimaanisha kwa nini amteue yeye na kwa nini amteue wakati ule. Dan aliachia cheko hafifu na kutikisa kichwa kwa mastaajabu.
“Mbona napata picha kama kwamba mnaniona adui ndugu zangu?” Hatimaye aliuliza.
“Nadhani hapo mwanzo ulisema kuwa utaenda moja kwa moja kwenye swala lililo kichwani mwako Mr. Dihenga, sasa mbona tena unaaza kusua-sua? Nimesema mapema kuwa mi’ nataka kwenda kujipumzisha. Kwa hiyo kama mtaniwia radhi ndugu zangu, mi’ naenda kulala!” Roman alisema na kuanza kuinuka. Haraka sana Kate ulimdaka mkono na kumzuia.
“Hatuendi hivyo mzee!” Alimwambia huku akimtazama usoni. Roman alibaki akimtazama yule binti kwa mshangao, na kabla hajauliza Kate akamwambia, “Hapa huondoki mpaka unirejeshee pesa zangu!”
“Ati nini wewe?” Roman alimaka huku akiuchomoa mkono wake kwa nguvu kutoka kwenye himaya ya yule binti.
“Achana na Kate Roman, tuongee mambo ya maana. Kaa kitini tafadhali!” Dan alimwambia kwa utulivu. Roman alimtazama Kate kwa muda, kisha akamgeukia Dan.
“Nimekuuliza swali jepesi sana Mr. Dihenga...why me? Umeshindwa kujibu kwa hiyo mi’ naona...”
“Kwa sababu ni wewe pekee ndiye unayeweza kumvua ubingwa Deusdelity Macha, Roman!” Dan Dihenga alimkatisha kwa kumjibu kwa utulivu ilhali bado akimtazama moja kwa moja usoni.
“Atii???” Mark Tonto alimaka huku akiinuka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia, wakati huo huo, Roman akajikuta akiketi kitini huku akiacha kinywa wazi na akimtazama yule mtu kama kwamba ndio kwanza alikuwa anamuona.
“Ndio!” Dihenga alithibitisha jibu lake huku akimtulizia macho Mark kwa muda kkabla ya kuyarudisha tena kwa Roman.
“Ni kweli kuwa kuna mabondia wengi wazuri hapa nchini. Lakini nakuhakikishia kuwa hakuna hata mmoja kati yao anayeweza kumuangusha Deus...” Dihenga aliendelea kutetea hoja yake. Mark na Roman walitazamana. Wazi hili halikuwa kabisa miongoni mwa matarajio yao.
“Isipokuwa wewe Roman!” Dan alimalizia huku akimuoneshea kidole Roman.
Kimya kilichukua nafasi kwenye ile meza.
“Kwa nini unataka Deus aangushwe Mr. Dihenga?” Hatimaye Mark alimuuliza, ingawa tayari jibu alikuwa nalo. Dan Dihenga alibadilika kidogo, uso wake ukionesha ghadhabu yenye kufukuta.
“Mimi ndiye niliyemfikisha mahala pa kutambulika kimataifa kwenye ndondi mshenzi yule...lakini akathubutu kunigeuka na kunitolea kebehi na kashfa. Nataka nimuoneshe kuwa kama mimi ndiye niliyemfikisha hapo alipo mpaka hao anaowaona ndio mapromota wanaomfaa wakamuona, basi mimi ndiye nitakayemporomosha!” Dan Dihenga alisema.
“Na unataka kunitumia mimi katika hicho kisasi chako binafsi?” Roman alimuuliza.
“Hapana Roman. Mimi na wewe tunahitajiana katika kumfikisha Deus mahala panapomstahili...”
“Nini kinachokufanya uamini kuwa mi’ nataka kushirikiana nawe katika hilo?” Roman aliuliza. Dan alitabasamu kidogo.
“Najua mengi juu yako na Deus, Roman...mengi. Hivyo najua kuwa kwa namna moja au nyingine nawe unahitaji kumfikisha Deus mahala panapomsatahili...na pale alipo sasa sipo panapomstahili. Sote twalijua hilo!”
Duh! Roman na Mark walichoka.
“Unaelewa nini juu yangu na Deus wewe?” Roman alikuja juu. Dan hakufanya haraka kumjibu. Badala yake alimuita mhudumu na kumuomba bili ya vinywaji waliyoagiza pale mezani. Alipewa bili naye akalipa.
“Najua kiasi cha kutosha kunihakikishia kuwa mimi na wewe hivi sasa tuna lengo moja kuhusu Deus, nalo ni kumtia adabu. Sababu zetu za kutaka kufanya hivyo zinaweza kuwa tofauti, lakini hakika lengo letu laweza kuwa moja...na...naamini sote tunahitajiana katika hili!” Dan alimjibu baada ya yule mhudumu kuondoka.
“Si kweli. Sikuhitaji...hatuhitaji mtu yeyote. Tunajitosheleza kama tulivyo. Naona mkutano huu umekwisha!” Roman alisema.
“Kwa hiyo hukatai kuwa nawe una kisasi na Deus?”
“Sijui unaongelea nini...” Roman alianza, lakini Dan Dihenga alimkatisha.
“Wazee, hilo ndilo nililokuja nalo kwenu. Kitu ninachosema ni kwamba iwapo tutakubaliana, mimi nataka niwe promota wako katika ngumi za kulipwa. Nitakulipa pesa nzuri, nitakupatia vifaa vyote na mahitaji yote muhimu kwa professional boxer, nitakupatia nyumba nzuri ya kuishi, na nitakupa nafasi ya kuuchukua ubingwa ulio mikononi mwa Deus mbabaishaji hivi sasa...” akamgeukia Mark Tonto, “...na kwako, nitakuajiri kama kocha wa bondia wangu Roman, na nitakulipa kwa kadiri ya makubaliano tutakayoafikiana...ambayo nakuhakikishia kuwa yatakuwa ni makubaliano mazuri sana Mark. Wewe ni kocha mzuri, na najua kuwa unajua upiganaji wa mabondia wote wawili hawa.” Alimalizia na kubaki akiwatazama wale watu wawili wenye azma ya siri. Si Roman wala Mark aliyeongea, hivyo Dan akamalizia, “Hiyo ndiyo kete yangu kwenu. Naomba muifikirie kwa makini sana, na baada ya siku tatu nitamtuma mpwa wangu kuja kupata jibu lenu la mwisho. Kama bado hamtakubaliana nami basi nitawaacha na hamsini zenu nami nitaendelea na hamsini zangu. Usiku mwema!”
Dan na Kate waliinuka kwa pamoja na kuanza kuondoka, wakiwaacha Roman na Mark wakiwa vinywa wazi.
“Kate!” Roman aliita. Kate na Dan walisimama na kugeuka. Roman alitoa ile pochi ya yule dada ambayo ilikuwa mfukoni mwake muda wote, na kuiweka juu ya meza huku akimtazama kwa hasira. Kwisha kufanya hivyo alimuashiria Mark na kwa pamoja waliinuka na kuondoka, ile pochi ikibaki pale mezani. Kate aliirudia pochi yake kwa mwendo wa kuchechemea...
***
Usiku ule Roman na Mark walichelewa sana kulala. Walibaki pale ofisini wakijadili juu ya ule ujio wa promota Dan Dihenga kwa undani. Hofu kubwa ya Roman ilikuwa ni iwapo Dan alikuwa ametumwa na Deus aje kumchimba undani wake, au iwapo atakuwa ametumwa na Inspekta Fatma.
“Kwa hayo yote mawili mimi nakataa Roman. Ni kweli kuwa Dan Dihenga ni promota wa ndondi, na ni kweli kuwa alikuwa promota wa Deus...na ni kweli kuwa Deus alimsaliti...hivyo ana kila sababu ya kuwa na kinyongo naye.” Mark alisema.
“Kwa hiyo...?”
“Kwa hiyo hawezi kuwa kibaraka wa Deus...yule mtu ana kinyongo kikubwa na Deus...si umesoma makala nilizokukusanyia kwenye lile faili? Walifikia hadi hatua ya kutaka kupelekana mahakamani bwana!”
“Ni kweli...na sasa nakumbuka kuwa hata jina lake nililisoma kwenye lile faili...” Roman aliafiki, kisha hapo hapo akauliza, “...na vipi kuhusu Inspekta Fatma...hawezi kumtumia?”
“Kwa lengo gani? Hali ilivyo, Dihenga ndiye ambaye anaweza kuwa kwenye nafasi ya kumtumia Inspekta Fatma na si vinginevyo. Nadhani nia ya Dihenga ni hiyo hiyo aliyotueleza...anataka akupromoti wewe ili umnyang’anye Deus ubingwa...hiyo ni njia yake ya kumlipizia kisasi. Swala ni je, sisi...wewe...uko tayari kushirikiana naye?”
Kimya kilitawala, kisha Roman akarudia tena kauli ambayo tayari alikuwa ameshaitumia zaidi ya mara tatu mle ndani tangu akina Kate waondoke.
“Lakini...inaelekea hawa akina Kate wanajua sana habari zangu...hii mimi hainipi amani kabisa Mark!”
“Sasa basi ni bora tuwe nao sambamba Roman...!” Mark alisema.
“Ili?”
“Ili tuweze kujua ni nini hasa wajuacho kuhusu wewe... na sisi tuweze kuwajua wao zaidi...nadhani tukubaliane na wazo la Mr. Dihenga Roman. Kwani sisi hatutapoteza lolote zaidi ya kunufaika...kwanza tutaweza kutimiza azma yetu, pili tutaweza kuitimiza azma hiyo katika mazingira yaliyo bora zaidi...sasa hivi Roman huna kipato chochote, kujiunga na Dihenga kutakupatia makazi bora, vifaa bora zaidi vya mazoezi, na pesa nzuri...nami pia nitanufaika kama kocha wako. Hii ni nafasi nzuri kwetu Roman...ni sawa na nyota ya jaha!” Mark alisema na kubaki akimtazama Roman kwa muda, kisha akamalizia kwa sauti ya chini, “Hiyo ni kama bado una nia ya kuendelea na ile azma yako Roman.”
“Azma iko pale pale Mark...iko pale pale!” Roman alimjibu haraka bila hata ya kusita.
“Basi na tukubaliane na ofa ya Dihenga...we have nothing to lose (hatuna cha kupoteza) kwa hii ofa Roman!” Mark alimwambia. Siku tatu baadaye, Kate alifuata jibu.
“Mwambie Dihenga tumekubali...no problem!” Roman alimwambia bila kupoteza muda. Hii ilikuwa ni taarifa tamu sana kwa Kate na Dan Dihenga.
*****
Maisha ya Roman yalibadilika ghafla. Dan alitimiza kila aliloahidi. Kwa kuhofia jaribio jingine la kumuua Roman, Dan alimhamishia Roman Bagamoyo, ambako alimpangia nyumba ndogo lakini nzuri na yenye kujitosheleza. Mark Tonto kama kocha wake alilazimika awe anaishi baina ya Bagamoyo na Dar. Kila siku akifanya safari za Bagamoyo asubuhi na kurudi jioni, baadhi ya siku akilala huko huko. Huko kazi ilikuwa ni moja tu, nayo ilikuwa ni mazoezi makali. Dan alimpatia Roman vifaa vyote muhimu vya mazoezi, na pale kwenye nyumba aliyompangia alimtengea chumba maalum cha mazoezi (Gym) ambacho kilikuwa na kila kitu.
Kwa miezi mitatu mfululizo Roman alijichimbia Bagamoyo akijijenga kibondia. Mark Tonto alikuwa naye muda wote huo ingawa siku nyingine alikuwa akirejea Dar kuwa na familia yake. Kate na Dan nao walikuwa wakimtembelea na kumtazama akifanya mazoezi, wakitumia sehemu ya muda wao kutazama mapambano ya Deusdelity Macha kwenye mikanda ya video. Na katika miezi mitatu ile, Roman na Kate waliondokea kujenga ukaribu, na hata siku nyingine Kate alikuwa akienda kule Bagamoyo peke yake na kukutana na Roman, wakitembea pwani na kuongea mambo mengi na kujuana zaidi.
Ndani ya miezi mitatu ile, hakuonana kabisa na Inspekta Fatma, isipokuwa siku moja tu alipoletewa salamu na Mark kuwa Inspekta Fatma alifika pale kwenye klabu yao ya Kawe na kumuulizia. Kwa kuwa hata wale mabondia wa Mark pale klabuni hawakujua Roman alipo, hawakuwa na msaada wowote kwake.
Roman aliendelea na mazoezi yake, na Dan hakuishia hapo katika kumjenga zaidi. Pamoja na kuwa na Mark kama kocha, pia alimletea makocha kutoka nje ya nchi ambao walikuja kumuongezea mbinu zaidi za ndondi, ikiwa ni pamoja na namna ya kubadili namna ya upiganaji akiwa ulingoni kutokana na aina ya upiganaji wa mpinzani wake.
Na baada ya miezi hii mitatu ya mazoezi makali na ya nguvu, Roman alikuwa tayari kuingia katika ulingo wa ndondi za kulipwa, kama professional boxer.
***
Dan Dihenga alimuandalia Roman pambano lake la kwanza kama bondia wa kulipwa mwezi mmoja baada ya Roman kujinadi kuwa yuko tayari kuingia rasmi ulingoni, ambapo alimpatia mpinzani kutoka afrika kusini. Katika pambano hili Roman alikuwa na nafasi ya kujivunia milioni tano za kitanzania akishinda, na milioni mbili akishindwa. Dan hakutaka kulinadi sana pambano hili kwenye vyombo vya habari, na waliondoka kimya kimya kwenda Afrika Kusini, msafara wao ukimjumuisha Dan, Roman, Mark, Kate na tabibu mmoja. Pamoja nao alikuwamo mwandishi wa habari mmoja. Mark alimuuliza Dan sababu ya kutolinadi ipasavyo pambano lile la kwanza la Roman.
“Roman hahitaji kunadiwa Mark...Roman atajinadi mwenyewe baada ya kufanya mauaji huko sauzi...we’ subiri tu, utaona!” Dan alimjibu wakiwa angani kuelekea Johannesburg. Usiku wa pambano jijini Johannesburg, Roman alitoa kipigo cha mbwa mwizi kwa mwenyeji wake, na mnamo raundi ya nane, kocha wa mpinzani wake alilazimika kutupa taulo ulingoni kumnusuru bondia wake!
Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi kutoka kwa watanzania wachache waishio Afrika Kusini waliokuwapo pale ukumbini, Roman akiinuliwa juu juu na watanzania wale. Ilikuwa ni furaha isiyo kifani kwa kambi ya Roman kule ugenini. Mara moja habari zilirudi nyumbani, mwandishi wa habari aliyesafiri na akina Roman akituma habari nyumbani usiku ule ule kwa simu, na akituma picha kadhaa za jinsi Roman alivyokuwa akimsulubu mwenyeji wake kwa mtandao wa intaneti. Usiku ule ulikuwa ni usiku wa tafrija kwa kambi ya Roman jijini Johannesburg. Walirejea Tanzania siku iliyofuata, na kukuta habari za pambano la Roman nchini Afrika kusini zikiwa zimetapakaa jijini,na waandishi zaidi wa habari wakiwasubiri uwanja wa ndege. Na ndipo hapa ambapo Dan Dihenga alimpomnadi Roman kuwa ndiye bondia wake mpya. Waandishi walimtupia maswali kadhaa naye kama promota mzoefu alitumia nafasi hiyo kumnadi vizuri sana bondia wake. Alipohojiwa na waandishi juu ya ushindi wake ule, Roman alisema kwa utulivu kabisa kuwa ushindi ule haukuwa ajabu kwake, kwani alijua kuwa atashinda. Ndipo mwandishi mmoja alipomtupia swali Dan.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Bwana Dihenga, je ndio unataka kutuambia kuwa Roman amekuja kuchukua nafasi ya Deusdelity Macha, bondia wako wa zamani na ambaye ndiye bingwa wa dunia hivi sasa?”
Bila ya kusita, Dan Dihenga alimjibu yule muandishi, “Nijuavyo mimi Roman ni bondia bora kuliko bondia mwingine yeyote hapa nchini katika uzito wake...hivyo siwezi kusema kuwa kaja kuchukua nafasi ya mtu yeyote hapa, labda tu niseme kuwa amekuja kuchukua nafasi yake inayomstahili!”
“Una maana gani kwa kauli hiyo bwana Dihenga?” Waandishi kadhaa walimrukia kwa swali hilo. Dan hakujibu kitu zaidi ya hapo. Alimuongoza bondia wake kwenye gari na kuondoka eneo lile, akiwaacha wale waandishi wakijijazia majibu yao wenyewe. Habari ya pambano lake la afrika kusini ilimfanya Roman awe gumzo kwa wengi nchini.
Lakini pia ilimrejesha tena Inspekta Fatma katika maisha yake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment