Search This Blog

Monday 24 October 2022

DHIHAKA - 1

 

    IMEANDIKWA NA : BEKA MFAUME



    *********************************************************************************





    Simulizi : Dhihaka

    Sehemu Ya Kwanza (1)







    ALIISHIA kidato cha sita. Mara baada ya kushindwa kujiunga na masomo ya elimu ya juu, aliamua kujiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF). Alikuwa akizipenda kazi za kijeshi na hasa zenye sulubu akiamini kujiunga kwake jeshini kungemwezesha kuwa komandoo. Lakini aliiona ndoto yake ya kuwa komandoo ikishindwa kutimia baada ya kushindwa mafunzo ya awali ya kufuzu ukuruta. Kwanza ulikuwa ni ugumu wa mafunzo yenyewe ambayo yalikuwa magumu kiasi cha kumtia hofu ya kuipoteza roho yake. Lakini cha pili, ni kunyanyaswa na viongozi waliokuwa wakimsimamia mafunzo kwa kumpa adhabu ngumu zilizoandamana na kauli za kuudhi ambazo alishindwa kuzivumilia. Akaamua kuasi jeshi na kurudi uraiani.

    Aliitwa Badi Mohamed.

    Baada ya kurudi uraiani alifanyiwa mpango wa ajira, akapata kazi kwenye hoteli ya kimataifa yenye hadhi ya nyota tano kwa kuajiriwa huku akipewa mafunzo ya uhudumu wa vyakula na vinywaji. Akawa mahiri kwenye kazi hiyo na kupandishwa cheo cha uongozi wa kati wa kuwasimamia wahudumu wenzake. Kufanya kazi kwake hotelini kukambadilisha tabia, akawa anahusudu mambo ya kizungu.

    Akazidi kubadilika kwa kuwa mtanashati zaidi na kupenda kufuatilia mambo ya dunia kupitia Mitandao ya Kijamii. Upeo wake wa akili ukazidi kupanuka, lakini pia akapendwa na wakubwa zake kutokana na kuimudu vyema kazi yake na utanashati aliokuwanao. Hatimaye akahamishiwa Idara ya Mapokezi.

    Kuhamishiwa idara hiyo mpya kukayabadilisha maisha yake. Ghafla akaonekana kuwa na uwezo wa kipesa, lakini hakuna aliyejua alizipataje! Wafanyakazi wenzake, kila mmoja akawa na maelezo yake. Wapo waliomtuhumu kuwa alifanya njama za kuingia chumba cha mgeni wakati mwenyewe hayupo na kuitumia nafasi hiyo kuiba pesa nyingi za kigeni. Lakini pia, kuna waliomtuhumu alikuwa akiuza mihadarati kwa wageni na ndiyo sababu ya kuwa na pesa hizo. Kwa upande wake, Badi hakuwa tayari kuzungumzia masuala yake ya kipesa.

    Akipewa sifa ya kuzungumza lugha ya Kiingereza cha ufasaha chenye maringo kana kwamba aliwahi kuishi nchi za nje, Badi akajifunza na lugha ya Kifaransa ambayo nayo akaimudu kuizungumza kwa ufasaha. Hatimaye akawa anazungumza na Kijerumani cha kuombea maji alichojifunza kupitia kwenye kamusi. Akionekana kuwa mwenye kipaji cha kujua lugha tofauti, Badi alipandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Idara ya Mapokezi.

    Akiwa ni mrefu wa futi tano na nusu, jamali wa sura na mwenye haiba ya mvuto kwa wanawake, mwili wa Badi uliumbika kimichezo na alikuwa na nguvu za mikono. Suti zake za kazini zilikuwa zikimpendeza kwa wakati wote azivaapo ikiwa ni nyeusi au ya bluu yenye kiza na kufuatiwa na shati jeupe na tai nyeusi. Wakati mwingine baadhi ya wageni walikuwa wakighafilika kwa kumdhania ndiye meneja wa hoteli.

    Mvuto wake uliwavutia hata baadhi ya wageni weupe wanawake waliopanga kwenye hoteli hiyo huku wafanyakazi wenzake, hasa wasichana wenye kuupenda ulimbwende, wakifurahia kuwa naye karibu wakati wote na wengine wakijileta kimapenzi. Baadhi akawa anatembea nao.

    Jina la Badi Mohamed likawa jina maarufu hotelini hapo, hata mhudumu wa bustani alikuwa akilijua. Badi hakuwa mjivuni, lakini aliitwa mjivuni. Alizungumza na kutaniana na wafanyakazi wa ngazi zote kwa kupiga nao stori za kishabiki hasa zilizohusu mpira wa miguu. Pamoja na kujiweka kwenye hali hiyo, bado baadhi ya wafanyakazi wenzake hasa wanaume, walijengwa na wivu kumwona akipapatikiwa mno na wafanyakazi wa kike!
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Badi alianza kujenga nyumba kwa siri, hakutaka wakubwa zake wajue. Haikuwa nyumba kubwa sana, lakini ilikuwa ya kisasa iliyosanifiwa kiujenzi na kuijaza samani za kifahari. Hatimaye akanunua gari dogo ambalo awali alikuwa akiogopa kwenda nalo kazini kwa vigezo vilivyofanana wakati akijenga nyumba. Lakini hatimaye akawa anakwenda nalo.



    ***



    MAISHA yake yalianza kuingiwa na kivuli baada ya kundi la wanafunzi waliomaliza mafunzo ya hoteli kuletwa hapo kwa ajili ya kupata uzoefu wa kazi. Siku ya kwanza kundi hilo lilipoingia, Badi alikuwa amepata ruhusa maalum ya kutatua matatizo yake binafsi. Kundi hilo lililokuwa na mchanganyiko wa wanawake na wanaume wote wakiwa ni vijana wa umri usiozidi miaka ishirini na mitano, walisambazwa kwenye idara tofauti hotelini humo kulingana na fani walizosomea. Mmoja kati ya wanafunzi hao aliitwa Hija Nurdin aliyekuwa akisomea ‘Utawala.’

    Alianza na Idara ya Restaurant. Ujio wake ukawa gumzo hotelini hapo kwa sababu moja tu, aliumbika! Kwa kila aliyemwona alimuweka msichana huyo kuwa ni wa daraja la juu. Wengi wakamhisi kuwa ni mtoto wa kizito.

    Mvuto wa msichana huyo ulikuwa ukionekana tangu akiwa mbali wakati akitembea, na kila aliyemwona hakukawia kuvuta subira ili amwangalie kwa karibu. Sura yake ilimfanya aonekane kama Mnyarwanda wakati hakuwa na nasaba nao. Uvumi ukasambazwa na baadhi ya wafanyakazi kwa kumwelezea kuwa, baba yake ni mfanyabiashara tajiri, lakini wengine wakidai alikuwa akimiliki kiwanda. Ilimradi uzuri wake uliwazuzua na kumtukuza pasipo doa.

    Katika siku za mwanzoni baadhi ya wafanyakazi wa kiume walianza kujipanga kumtongoza kwa staili tofauti. Wapo walioomba namba yake ya simu, wengine wakitaka kujua anapoishi na wengine wakijitokeza kwa wasifu wa ujivuni. Yeye akawa anacheka au kutabasamu kwa sababu alizijua fikra zao.

    Mtu wa kwanza kuonekana amefanikiwa kujenga naye ukaribu ni Meneja Msaidizi wa Vyakula na Vinywaji anayeitwa Nicolaus Semi. Wengi walimwita Nico. Pamoja na kuwa ni meneja, lakini pia ndiye aliyekuwa bosi wake wa idara. Huyu katika wiki ya kwanza alionekana kuzungumza naye kwenye maeneo yaliyotilia shaka mazungumzo yao. Wakati mwingine walionekana wakiwa ofisini peke yao, lakini pia uonekanaji wao ulitafsiriwa kuwa, hata waliyokuwa wakizungumza, walikuwa wakizungumza mapenzi! Ikakubalika Nico ndiye mwenye nafasi kubwa ya kumpata Hija! Baadhi ya wafanyakazi wa kiume ikawauma kwa wivu, wakiamini Nico alikuwa akitumia umeneja wake kuwazidi kete!

    Wengi walikuwa wakimwelewa kuwa anapenda wanawake. Mfanyakazi yeyote wa kike ambaye ni mzuri alitongozwa na huyu jamaa. Wapo aliofanikiwa kuwapata, wengine walipatikana kwa woga wa kufukuzwa kazi na wengine kwa kutaka sifa kuwa, wanatembea na meneja. Lakini pia, wapo waliomkataa. Hawa akawajengea chuki! Ingawa alikuwa ni meneja aliyekwenda shule, lakini katika masuala ya wanawake alionekana ni mjinga fulani!

    Akiwa anatumia madaraka yake kwa kumwita Hija aende ofisini kwake na kuchukua muda mrefu kuzungumza naye, sehemu kubwa ya mazungumzo yake yakawa hayana tija. Muda mwingi alikuwa akizunguka na maswali ya kijinga kama vile kutaka kujua kwao kukoje, kwa nini ameamua kupenda kufanya kazi hotelini, baba yake ni nani, wako wangapi kwenye familia yao, anapenda nini, lakini pia kuna siku alimuuliza kama ana rafiki wa kiume!

    Wafanyakazi waliokuwa wameshaanza kumtongoza msichana huyo wakaanza kujiengua baada ya kujua ‘meneja’ anafukuzia! Uwanja ukawa wa Nico. Ghafla ikaanza kuvumishwa kuwa, Meneja Nico na msichana Hija mambo yao yako poa!



    ****



    WAKATI hayo yakiendelea Badi aliripoti kazini baada ya kumaliza siku alizopewa ruhusa. Alikaribishwa na sifa za uwepo wa mwanafunzi mpya anayeitwa Hija! Sifa yake ikaleta mirindimo ya tamthiliya isiyoisha ladha masikioni mwake. Badi akatamani kumwona msichana huyo mwenye kupewa sifa lukuki. Bahati mbaya wakawa wanapishana zamu kwa wiki hiyo. Hija akawa anaingia alasiri, Badi kwa kuwa ni kiongozi akawa anaingia zamu ya asubuhi kila siku. Badi akakosa kumwona Hija wiki hiyo!

    Kama vile ulikuwa ni mchezo fulani wa kuigiza, kwa upande wa Hija naye alikuwa akilisikia jina la Badi likitajwa kwa kutukuzwa kwa sifa mbalimbali tena na wasichana wenzake. Hija naye akawa na hamu ya kumwona Badi!

    Baada ya wiki moja, watu hao wawili wakaingia zamu ya asubuhi na siku hiyohiyo wakakutana kwa mara ya kwanza ana kwa ana!

    Ilikuwa saa tatu na nusu asubuhi Badi alipokwenda mgahawani kwa ajili ya kustafutahi. Mgahawa huo ndiko Hija alikokuwa amepangiwa kuanzia kufanya kazi. Mgahawa huo ndio unaotumika kwa wageni kwa ajili ya chakula kwa kuanzia chai ya asubuhi hadi mlo wa jioni. Wafanyakazi wa hotelini hawakuruhusiwa kuutumia, isipokuwa kwa baadhi ya viongozi wachache wa hoteli, Badi akiwa mmoja aliyeruhusiwa. Wafanyakazi wengine wote walikuwa na kantini yao.

    Badi alipoingia humo mgahawani akaziona sura ngeni za wafanyakazi wa kike wakiwa na wenyeji wao, lakini akavutiwa na mmojawao. Moja kwa moja akajua ndiye msichana anayezungumziwa! Kweli bomba! alikiri.

    Hija alimwona Badi akiingia mgahawani, akadhani ni mgeni aliyepanga hotelini humo. Akamwangalia mtu huyo mrefu aliyevaa suti iliyompendeza akija taratibu. Kwa kanuni za huduma za hoteli, mgeni anayeingia mgahawani anatakiwa akaribishwe na mfanyakazi na amwelekeze mahali pa kukaa. Hija akachepuka kutaka kulifanya hilo.

    Akiwa naye amependezwa na sare za kazi alizovaa, blauzi ya njano iliyovaliwa na kizibau cha kijani na sketi fupi ya rangi ya buluu, akamfuata Badi kwa ajili ya kumkaribisha. Lakini wakati akimpita mfanyakazi mwenzake wa kike ambaye ni mwenyeji, akamshitua kwa kumwambia, “Huyo ni staff!” akimaanisha ni mfanyakazi wa hotelini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hija akasitisha kwenda kumpokea Badi. Akasimama pembeni mwa aliposimama mwenzake. Wote kwa pamoja wakawa wanamwangalia Badi alivyokuwa akiingia.

    “Vicky hujambo?” Badi alimsalimia msichana aliyesimama na Hija.

    “Sijambo kaka Badi. Shikamoo,” msichana aliyeitwa kwa jina la Vicky alijibu.

    Mungu wangu! Hija alishtuka. Huyu ndiye Badi mwenyewe! Handsome! aliwaza. Kuanzia hapo ikawa kama aliyeambiwa achukue jukumu la kumsaili Badi kwa macho.

    Badi aliitikia amkizi alilopewa na Vicky huku akimwangalia Hija.

    “Shikamoo!” Hija alijikuta akimwamkia Badi kwa kumgeza Vicky kutoa shikamoo.

    “Marahaba,” Badi aliitikia shikamoo ya Hija, kisha alimwangalia Vicky. “Huyu ni mgeni?” alimuuliza.

    “Ndiyo,” Vicky alijibu.

    “Ni mwanafunzi?”

    “Ndiyo.”

    “Anaitwaje?”

    “Hija.”

    Badi akamwangalia Hija. “Karibu,” alimwambia Hija.

    “Ahsante,” Hija alijibu.

    “Umetokea chuo gani?”

    Hija akakitaja chuo alichotoka.

    “Ni chuo kizuri,” Badi alisema. “Lakini nasikia ni ghali!”

    “Kiasi!” Hija alijibu kupoza makali.

    “Una muda tokea umekuja?”

    “Naingia wiki ya pili.”

    “Kwa muda huo utakuwa umeshaanza kujuajua ku-serve?”

    “Kidogo,” Hija alijibu na kutengeneza tabasamu la aibu.

    “Njoo uni-serve niweze kuku-recommend,” Badi alisema na kwenda kukaa kwenye meza.

    Hija na Vicky wakaangaliana machoni.

    “Nenda kam-serve!” Vicky alisema.

    “Siyo mkorofi?” Hija aliuliza.

    “Hana ukorofi.”

    Mara Badi alipokaa kitini, kiongozi wa wahudumu akaenda kwenye meza hiyo. Akataka kuchukua maagizo ya chakula atakachoagiza Badi.

    “Namtaka huyu mwanafunzi anayekuja achukue oda yangu na kisha anipe huduma yeye mwenyewe!” Badi alisema.

    Yule kiongozi akageuka, akamwangalia Hija aliyekuwa akija mezani. Kisha akaurudisha uso wake na kumwangalia Badi huku akitabasamu. “Bosi unatafuta ugomvi na Meneja Nico!” alionya.

    Badi akataka kutamka neno, lakini akasita baada ya kumwona Hija amewasili.

    Kiongozi wa wahudumu alimkabidhi Hija kitabu cha kuandikia oda. “Si unajua namna ya kuchukua oda na kuandika?” alimuuliza Hija.

    Hija akabetua kichwa kukubali. Akakiandaa kitabu huku kalamu ikiwa mkononi kuandika. Akamwangalia Badi.

    “Utapenda kula nini asubuhi hii?” Hija alimuuliza Badi.

    Badi akauinua uso wake na kumwangalia Hija. “Niulize kwa Kiingereza,” alisema.

    Hija akatabasamu, kisha akauliza kwa Kiingereza.

    “Nitaanza na mixed fruit, juice na black coffee, kisha, fried egg sun side up, sweet beans, sausages na fresh slice tomatoes. Umenipata?” Badi aliongea kwa kuchanganya Kiswahili na Kingereza.

    Hija akatabasamu. “Nimekupata!” alijibu. Akaiandika oda na kutaka kuondoka. Badi akamzuia!

    Hija akamwangalia Badi kwa kushangaa.

    “Unatakiwa umuulize mgeni mayai yake yapikweje, yawe welldone? Au medium rhea?”

    Hija akamwangalia Badi kwa macho yaliyotulia. Akauliza swali alilotakiwa aulize.

    “Rhea!” Badi alijibu.

    Hija akaenda jikoni. Baada ya muda alirudi akiwa na baadhi ya vyakula alivyoagizwa na Badi. Akamhudumia hadi mwisho.

    Ukawa mwanzo kwa watu hao kuwa karibu.

    Ikawa kila anayemwona mwenzake anatabasamu. Hija akaendelea kutoa shikamoo, Badi akaendelea kuitikia kwa uchangamfu. Ingawa walikuwa hawaonani mara kwa mara, lakini kila walipokutana, macho yao yalizungumza kimyakimya. Na kama wakionana zaidi ya mara moja, Hija aliishia kufanya tabasamu lililorudishiwa na Badi.



    ***



    UVUMI wa kuwa Meneja Nico na Hija wapo katika uhusiano unaohusishwa na mapenzi, uzagaaji wa uvumi huo ulimfurahisha Nico. Ulimfanya ajione ni kidume na huku baadhi wakimpongeza kwa kauli za kiushikaji kama vile, ‘Mzee tunakuona na kitu kipya!’ au ‘Mzee pale umelenga!’ na mengine mengi ya kumsifia. Kauli hizo zikawa zinamvimbisha kichwa kila anamopita na kujipa taswira ya kujiona ana mvuto kwa wanawake.

    Lakini upande wa pili alikuwa akihuzunika. Alihuzunika kwa sababu ya ukweli uliokuwa umejifunika; alikuwa bado hajafanikiwa kumpata msichana huyo! Ilikuwa ni tofauti kama ilivyodhaniwa na wafanyakazi. Akawa anahofia ukweli huo usije ukagunduliwa. Hilo likawa linamsumbua.

    Hija naye hakutaka kuliweka wazi jambo hilo kwa sababu baada ya wafanyakazi kuhisi kuwa ana uhusiano wa mapenzi na Nico kutokana na ukaribu uliopo kati yao, uvumi huo akaamini ungemsaidia kumuweka kwenye mazingira salama ya kumwezesha kupata alama nzuri katika cheti atakachotoka nacho baada ya kumaliza mafunzo yake. Ingawa hakuwa na mpango wowote wa kuanzisha uhusiano wa mapenzi na Nico, lakini kuligundua hilo kukamfanya asipoteze muda wake kuukanusha uvumi huo!

    Idara ya Chakula na Vinywaji huhusisha maeneo matatu. Kuanzia jiko, mgahawa na baa. Wafanyakazi wa idara hizi wana ukaribu kutokana na kazi zao kutegemeana. Kwa uzoefu huo, wafanyakazi wa idara hizo hujenga urafiki wa kikazi wenye kutaniana, kupiga stori na hata kutongozana. Matukio ya aina hiyo yakawa ni ya kawaida. Lakini uvumi wa kuwa Nico ana uhusiano wa mapenzi na Hija, ukaanza kuleta taswira tofauti. Nico alianza kusumbuliwa na wivu kila alipomwona Hija amesimama na mfanyakazi wa kiume wakipiga stori!

    Nico kila alipokuwa akiliona tukio hilo, akawa anazuga kama hakuliona. Lakini baadaye hupiga simu na kuwalaumu viongozi wa idara ambazo watu wake aliwaona wakipiga stori na Hija kwa kuwashutumu kuwa, wanaachia watu wao kupiga soga wakati wa kazi! Lakini pia akawa anatishia kuwahamisha idara endapo watashindwa kuwasimamia watu wao!

    Baadhi ya wafanyakazi wakaanza kumkwepa Hija kuwa naye karibu, na wengine wakimkabili kwa kumwambia wazi kuwa, wanaogopa kuhamishwa idara!



    ***



    BADI alianza kuziona mapema dalili za kuwa angempata Hija kimapenzi. Macho ya Hija yalikuwa yakimpa ishara zote kuwa milango iko wazi kwake. Lakini Badi alijikuta akishikwa na kigugumizi kwa kuhofia asije akaliingilia na kuliharibu penzi la Nico ambaye alishaonyesha wivu kwa baadhi ya wafanyakazi. Lakini pamoja na kuingiwa na kigugumizi hicho, alikiri nafsi yake ilikuwa ikiteketea kila alipomwona msichana huyo.

    Badi na Nico walikuwa ni marafiki wa kikazi. Mara nyingi walikutana wakati wakiwa wamekwenda kula chakula, huko hukaa pamoja na kupiga soga tofauti za hapa na pale, au wakati mwingine walikuwa wakikutana kwenye vikao vya Wakuu wa Idara na kushirikiana kubadilishana mawazo. Lakini kati yao, hakukuwa na hata mmoja aliyekuwa akimzungumzia mwenzake mambo yake binafsi. Kutokana na mitazamo yao tofauti, Nico hakuwahi kumzungumzia Badi kuhusu uhusiano wake na Hija. Pamoja na Nico kutouzungumzia kwa Badi uhusiano wake huo, lakini kila mmoja alikuwa akijua uhusiano huo ulikuwa ukijulikana. Kwa mtazamo huo, Nico akatarajia Badi angeuheshimu uhusiano huo kwa kutouingilia kwa njia moja au nyingine. Badi akawa anajitahidi kumkwepa Hija kadri alivyoweza, lakini ndani ya moyo wake kukawa na msukumo uliokuwa ukimlazimisha awe karibu na msichana huyo!

    Siku zote Badi alimchukulia Nico kama mshamba fulani na yeye akijiona wa mjini zaidi. Na alikuwa akishangaa huku akijiuliza, ilikuwaje Hija akamkubali mtu kama Nico? Alimwona mjinga huyo kuwa ni mwenye wivu wa kibwege na mshamba wa wanawake. Pamoja na kujitahidi asije akagombana na meneja wake kuhusu msichana huyo, Badi alizidi kuingiwa na hofu alipogundua kuwa, kadri alivyokuwa akimkwepa Hija asiwe karibu naye, ndivyo Hija alivyozidi kujisogeza zaidi kwake!

    Ikawa asubuhi moja, Badi yupo kazini, simu ya ndani ya hoteli iliyopo kwenye meza ya mapokezi ikaita. Ikapokewa na msichana aliyepo kwenye idara hiyo. Baada ya kuipokea na kuzungumza maneno machache, akamwangalia Badi, kisha akasema “Yupo.”

    Akaitoa simu sikioni na kumnyooshea mkono Badi kumpa simu huku akisema, “Bosi simu yako!”

    Badi akaichukua simu mikononi mwa msichana huyo na kuiweka sikioni. “Helloh, it’s me Badi,” alisema.

    “Hija naongea!” sauti ya kike kutoka kwenye simu ilisema kwa utulivu na kujiamini.

    Badi akajikuta akiangalia pembeni yake kama kungekuwa na mfanyakazi aliyekuwa karibu yake. “Oh, ni wewe? Unasemaje bibie?” alisema kwa maringo na kwa sauti yenye mawimbi ya kuonyesha kupenda.

    “Nina zawadi yako, nikuletee?”

    Badi akahisi mapigo ya moyo yakimwenda mbio ghafla. “Why not?” alisema na kuonekana kujizuia asichanganyikiwe baada ya ombi alilopewa kulitambua lililenga kwenye penzi!

    Aliirudisha simu kwenye kitako chake na kuzubaa. Akaonekana kuhama kiakili. Ghafla akakurupuka na kwenda kuinamia meza na kuanza kuandika mambo yanayohusu kazi huku akili yake ikiwa makini na ujio wa Hija.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hija akatokea kwenye mlango wenye korido inayoelekea kwenye mgahawa. Akakatiza kwenye ukumbi mkubwa unaopendeza wa ‘lounge’ uliokaa kimataifa ambao kwenye dari kulikuwa na miali hafifu iliyochomoza kutoka kwenye taa zilizokuwa ndani ya vishimo. Akiwa kwenye sare za kazi zilizompendeza na mkononi amekamata mfuko mdogo wa karatasi, Hija alionekana kutembea kwa kasi kuelekea kwenye meza ya mapokezi huku baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye meza hiyo wakimwangalia.

    Kwa kuwa alijua mgeni huyo ni wake, Badi alijisogeza na kwenda kusimama mwishoni mwa meza hiyo ili mazungumzo kati yao yawe ya faragha. Akafanya tabasamu wakati Hija alipomkaribia kuelekea aliposimama.

    Badi akatarajia Hija angechukua japo sehemu ya dakika kusalimiana kabla hajasema kilichomleta, lakini haikuwa hivyo. Hija hakusalimia. Alifika na kumpa Badi mfuko aliokuwa ameukamata. Badi akaupokea.

    “Zawadi yako!” Hija alisema, kisha bila ya kusubiri kujibiwa na Badi, aligeuza na kuondoka!

    Badi akaganda ameshangaa, akamwangalia Hija aliyekuwa akirudi alikotoka kwa mwendo uleule wa kasi. Akauangalia mfuko aliopewa, akazichomoa pini zilizofungia mfuko na kuangalia ndani. Akaliona tunda aina ya tufaa au apple kama wengine wanavyoliita na lilikuwa moja! Badi akatabasamu peke yake huku sura yake ikiwa bado inaangalia ndani ya mfuko, kisha akawaangalia wafanyakazi wenzake waliokuwepo mezani, mmoja wa kike na mwingine wa kiume. Wote wakawa wanamwangalia.

    Ilianza kama dhihaka!



    *****



    KILA kitu kikawa wazi! Tatizo likawa Nico! Itakuwaje akijua? Badi alijiuliza. Hakujiuliza kwa ajili ya kuendelea kumwepuka Hija, safari hii msukumo wa kumkabili binti huyo ulimjia kwa nguvu, lakini hofu yake ikawa kwa Nico, asije akajua! Tunda hilo lilimchanganya akili, aliamini kuletewa kama zawadi ilikuwa ni dalili ya kupendwa. Moyo wake ukawa unamshauri kutoiachia bahati hiyo! Tunda hilo lilimfanya awe kama aliyesukumiwa msukule, akili yake ikaingia kwenye utumwa wa kulifikiria tukio hilo kutwa nzima ya siku hiyo.

    Alirudi nyumbani akiwa amelibeba tunda hilo kwenye mfuko uleule ambao ulinukia manukato ya kike yaliyotawala hadi ndani ya gari lake. Hakujua kama yalitokana na mikono ya Hija kuacha harufu hiyo kwenye mfuko huo au alipulizia manukato hayo ndani ya mfuko kama ishara ya kuonyesha mapenzi aliyokuwa nayo kwake?

    Aliingia kwenye sebule yake nzuri iliyosheheni samani za kupendeza ndani ya nyumba yake aliyokuwa akiishi na mdogo wake. Akakaa kwenye moja ya sofa zake nzuri. Akalitoa tunda alilopewa na Hija kutoka kwenye mfuko na kuliangalia kama kitu kigeni kwake. Uso wake ukafanya tabasamu alipokuwa akiirudisha kumbukumbu ya kumwona Hija akikatiza kwenye ukumbi wa mapokezi hadi alivyomwachia tunda hilo na kisha kurudi zake! Alitamani kumbukumbu hiyo ingekuwa kwenye hifadhi ya santuri ya dvd awe anaiangalia kila ambapo angeihitaji.

    Zawadi yako! aliikumbuka sauti ya Hija ilivyomwambia wakati akimpa tunda hilo. Ikajirudia kama mwangwi uliotokana na ala ya muziki mtamu kwenye ubongo wake. Akataka kujilaumu kwa nini kabla ya kutoka kazini asingewasiliana naye na kumwomba namba yake ya simu. Lakini akatambua kusingekuwa na mazingira ya aina hiyo kwa pale kazini baada ya kumwazia Nico. Alihofu kama angemwomba namba yake ya simu halafu ikatokea mmoja wa wafanyakazi akasikia au kulijua jambo hilo, taarifa zingemfikia Nico! Na angekuwa ameuwasha moto na mjinga huyo!

    Kwa mara ya kwanza Badi alitamani angekuwa anapajua nyumbani anakoishi Hija, huko ndiko kungekuwa sehemu ya kuonana kwao, lakini pia kungekuwa ni sehemu ambako wangepanga mipango ya kumfanya aje hapo nyumbani bila ya Nico kujua. Akajihisi unyonge kwa kukosa fursa hizo, mojawapo ikiwa ni simu ambayo kwa muda huo hapo sebuleni alipokuwepo angekuwa anazungumza naye. Badi akaitamani siku imalizike haraka ili siku inayofuata aende kazini akaonane tena na Hija.

    Kwenye nafsi yake akaingiwa na hisia kuwa, kumwona tena Hija ni kupata utulivu wa moyo wake!

    Akalitoa tunda alilopewa kutoka kwenye mfuko na kuliangalia tena kana kwamba kuliona aina ya tunda hilo ilikuwa ni mara yake ya kwanza. Nalo pia likawa linanukia manukato! Badi akalimega mdomoni bila ya kuliosha huku manukato yakiendelea kumliwaza. Akakitafuna taratibu kipande alichokimega na alipokuwa akitafuna, hisia zikawa zinamfanya ajihisi kama vile alikuwa akimfaidi Hija!



    ***



    BADI aliingia kazini asubuhi, akafanya kazi huku akitamani muda wa kunywa chai uwadie ili aende mgahawani ambako angemkuta Hija. Aliwaona baadhi ya wahudumu wa kike waliokatiza mara chache eneo la ukumbi wa mapokezi waliokuwa kwenye majukumu ya kikazi kwa shida tofauti huku sare za kazi walizovaa zikimkumbusha kumwona Hija.

    Muda wa kunywa chai kwa viongozi ukawadia ambao ulikuwa ni saa nne. Akahisi moyo ukifunguka kwenye amani wakati alipokuwa akienda kuipata huduma hiyo. Akapanga atakapofika mgahawani asionyeshe hali yoyote ya kwamba yuko karibu na Hija, alijua kufanya kwake hivyo kungemfanya Hija naye aigize igizo hilo.

    Badi aliwasili kwenye mgahawa na kuwakuta baadhi ya viongozi wenzake wakiwa wametangulia kufika. Naye akajiunga nao na kuagiza alivyohitaji asubuhi hiyo. Mazungumzo kati yake na viongozi wenzake yakawa yameshamiri kwa kuzungumza mambo tofauti huku wakiendelea na unywaji wa chai na baadhi ya waliotangulia kufika wakawa wanaondoka kurudi maeneo yao ya kazi.

    Pamoja na mazungumzo yao kushamiri na Badi mwenyewe akiwa ni mchangiaji, lakini muda wote alikuwa akifuatilia mienendo ya wahudumu waliopo humo mgahawani. Akaiona kasoro. Hija alikuwa haonekani! Kutomwona Hija kukamfanya ajikute akiinywa chai bila ya hamasa. Alikuwa na uhakika Hija asubuhi hiyo hakuwepo kazini! Ushawishi wa kutaka kumuuliza mhudumu wa kike aliyekuwa akimhudumia ukawa unamsukuma ili amuulize kuhusu kutokuwepo kwa Hija.

    Akajionya kwa mara nyingine kwamba, kitendo chochote cha kuonyesha yuko karibu na Hija kingeweza kumuweka kwenye msuguano na Nico!

    Badi aliondoka bila ya kumuuliza mhudumu yeyote, aliondoka akiwa mnyonge huku akijiuliza maswali kadhaa yaliyohusu kutokuja kwa Hija kazini. Lakini kwa upande wa pili alijipa matumaini huenda angekuwa na zamu ya mchana kwa siku hiyo. Pamoja na kujipa matumaini, lakini kitendo cha kukosa taarifa za uhakika kuhusu kutoonekana kwa Hija kulimkosesha amani.

    Shughuli za kazi zikiwa zimembana na kulisahau suala la Hija angalau kwa muda, Badi alimwona mhudumu wa kike kutoka mgahawani akikatiza eneo la ‘lounge’ akielekea kwenye lifti. Akampungia mkono na kumwita. Akawahi kumfuata msichana huyo aliyekuwa ameanza kuelekea eneo la mapokezi kuitikia wito.

    “Kuna mgeni alimuulizia Hija hapa reception, nikamwambia aje restaurant, alikuja?” Badi alidanganya.

    “Mwanamume?”

    Ili asimuweke msichana huyo kwenye tashwishi ya kudhani huenda ni mambo ya mapenzi, Badi alijibu, “Mwanamke!”

    Kwa haraka lakini kwa uhakika, msichana huyo alijibu, “Mi’ sijamwona!”

    “Lakini Hija yupo?” Badi aliitimiza dhamira yake.

    “Hija leo hakuja!”

    “Yuko off?”

    “Mh, leo siyo off yake, sijui ana matatizo gani.”

    “Ok,” Badi alisema na kumshukuru mhudumu huyo wa kike na kuondoka. Akawa na uhakika Hija ana matatizo! Anaumwa? alijiuliza. Hakupata jibu. Hali ya unyonge ikamrudia tena.





    Ukawa mwanzo wa kugundua kwamba, Hija ameanza kuwa muhimu kwake!



    ***



    ASILIMIA kubwa ya wafanyakazi wanaofanya kazi idara ya mgahawa walikuwa ni watu wake wa karibu kutokana na kufanya kazi katika idara hiyo wakati wa nyuma. Ingawa alikuwa na ukaribu nao, lakini haukuwa ukaribu wa kujuana katika mambo yao ya ndani. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza Badi alijikuta kwa siku hiyo kutaka kuutumia ukaribu huo ili aweze kuzipata taarifa sahihi za Hija. Alikuwa akikabiliwa na shida mbili ambazo aliziona ni muhimu kwa siku hiyo; kuipata namba ya simu ya Hija, au anakokaa Hija! Na alikuwa akijua eneo pekee ambako angeweza kutatuliwa shida yake hiyo ni kwa wafanyakazi wanaofanyia Idara ya Restaurant.

    Akampigia hesabu kijana mmoja ambaye alimwona ni mjanja fulani. Akaamini kufanya kazi kwake pamoja na Hija kungemwezesha kwa njia moja au nyingine kujua baadhi ya mambo yanayomhusu Hija. Akampigia simu, akamwomba atakapomaliza zamu waonane.

    Ilipofika alasiri wakaonana.

    “Seif naomba uniambie ukweli,” Badi alisema huku akimwangalia kijana huyo anayeitwa kwa jina la Seif. “Ni kweli Nico anatembea na Hija?”

    Ingawa hakuonyesha kwa uwazi, lakini Seif alionekana kushtushwa na swali hilo. “Ina maana hujui?” aliuliza.

    “Ndiyo maana nimekuuliza!”

    “Mbona liko wazi!”

    “Kwamba?”

    “Hija ni demu wa Nico!” Seif alisema kwa kauli iliyosisitiza.

    Kauli hiyo ikamwumiza Badi na kuhisi wivu ukimwingia.

    “Vipi, ulikuwa unamwania?” Seif aliuliza.

    Ingawa ni swali alilotarajia kuulizwa, lakini kutokana na jibu alilojibiwa, akili yake ikashindwa kujiandaa kulijibu swali hilo kwa ufasaha. “Hapana!” alijibu kwa kifupi na haraka.

    Seif akamwangalia Badi kwa mtazamo wenye shaka. “Kwa nini umemuulizia?” aliuliza.

    Safari hii akili ya Badi ikajenga utulivu. “Anataka kuolewa na jamaa yangu,” alidanganya.

    “We si unawajua mademu? Tamaa! Huku anataka na kule anataka!”

    “Na wao pia wanasema hivyohivyo kuwa wanaume wana tamaa,” Badi alisema na kuendelea, “Sasa sikiliza, kuna kamchezo nataka nikacheze. Unaijua namba yake ya simu?”

    “Nani? Hija?”

    “Ndiyo.”

    “Namba yake ningekuwa nayo, lakini si unajua yule bwege baada ya kuingiza vitisho vyake nikaamua kumpotezea! Lakini ilikuwa anipe namba yake!”

    “Unamzungumzia nani?”

    “Si huyu demu ndiye unayemuulizia?”

    “Ndiyo.”

    “Sasa?” Seif aliuliza kama anayeshushua. “We ulifikiri namzungumzia nani?”

    “Nina maana bwege gani unayemzungumzia?”

    “Nico! Yule si bwege tu! Unajua mi’ yule demu nilikuwa naye beneti kichizi, sijui alinizimia?” aliposema hivyo alitingisha kichwa kusikitika huku akijiinamia kama vile anajutia kumkosa kwake. “Nikataka kumwomba namba yake ya simu, yule bwege si ndiyo akanibamba napiga naye stori! Basi akaniwakia kiroho mbaya na kun’tolea mimacho mwanangu…Haa! je, kama angenikuta napiga denda? Nadhani hata kibarua chenyewe kingeniotea nyasi siku hiyohiyo!”

    “Lakini kwao unakujua?”

    “Yule demu?”

    “Ndiyo.”

    “Nakujua wapi? Mi’ jamaa baada ya kuniyeyusha na mikwara yake mbuzi, nikaamua kupotezea kiaina! Basi mpaka leo mi’ na yule demu huwa tunapeana hai tu, hatuna stori!”

    Juhudi za Badi zikaishia hapo!

    Aliporudi nyumbani, Badi aliingia chumbani kwake na kuufuata mfuko uliotiwa tunda alilopewa na Hija ambao aliuhifadhi, akauweka karibu na pua yake, akaisikia harufu ya manukato na kuirudisha kumbukumbu ya tukio la kupewa tunda hilo.

    Zawadi yako! sauti ya Hija ilimrudia masikioni. Kutomwona kwake kwa siku hiyo, ikawa kama vile hajamwona kwa miezi kadhaa. Amepata matatizo gani hadi leo hakuja kazini? alijiuliza.

    Hija hakuonekana kazini kwa siku tatu nzima!



    ***

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    KILA mmoja aliugulia kivyake kwa kutomwona Hija! Nico naye alikuwa kama aliyechanganyikiwa. Kwa muda wa siku hizo tatu alikuwa akijaribu kumpigia simu binti huyo bila ya mafanikio ya kumpata. Akaanza kutumia nguvu ya madaraka yake kwa kuwauliza wasimamizi wa kazi wa idara ya mgahawa kama walikuwa na taarifa zozote zilizohusu kutokuja kazini. Wote wakampa jibu moja, kuwa hata nao hawana taarifa kutoka kwake!

    Kutompata Hija kwenye simu kulimnyima Nico mawasiliano na binti huyo, kwani hata naye kama ilivyokuwa Badi, alikuwa hakujui anakoishi Hija. Nico akajaribu kuwauliza baadhi ya wanafunzi wenzake ambao walitoka chuo kimoja kujiunga na hoteli hiyo kama yupo anayepajua kwake. Wengi wao wakasema, wanachojua ni kwamba, Hija anaishi Tabata, lakini hakukuwa na aliyekuwa akijua ni eneo gani la Tabata alilokuwa akiishi.

    Kama ilivyokuwa kwa Nico, hali hiyo ya sintofahamu ya kutoonekana kwa Hija, iliendelea kumsumbua Badi. Yeye alihofia huenda Hija ameacha kazi bila ya kumjulisha mtu yeyote. Hisia hizo zilimwingiza kwenye woga wa kumkosa msichana huyo ambaye tayari alikiri kuwa amempenda. Hakujua angemwona wapi au angemtafutia mahali gani kama ni kweli angekuwa ameacha kazi! Akamwona tena Seif, akamwelezea mshangao wake wa kutoonekana kwa Hija, Seif naye akamwambia hata kwenye idara wanayofanya kazi pamoja, hakuna hata mmoja anayejua kwa nini Hija haji kazini.

    Badi akaingiwa na dhana huenda Nico angekuwa anajua kwa nini Hija haji kazini, lakini asingeweza kwenda kumuuliza. Kwa kutambua asingeweza kumuuliza Nico, Badi aliamua kubaki kimya huku akiugulia kwa kutomwona Hija kazini, lakini pia, akiteketea kwa wivu akiamini Nico ndiye pekee aliyekuwa akiujua ukimya wa Hija wa kutoonekana kazini!

    Siku ya nne Hija alionekana kazini! Nico na Badi kila mtu akataka kuonana naye ili amlalamikie kwa kitendo chake cha kupotea bila ya kumjulisha udhuru uliompata. Urahisi wa kuonana na Hija hapo kazini ukaangukia kwa Nico. Yeye alitumia madaraka yake ya umeneja kwa kupiga simu Idara ya Restaurant baada ya kumwona Hija kwa mbali. Akatoa agizo kuwa aje ofisini kwake.

    Hija akapewa maagizo hayo na kuyaitikia kwa kuutii wito huo. Akaenda.

    “Sweetie,” Nico alimwambia Hija. Alipenda kumwita kwa jina hilo wanapokuwa wawili. “Kisheria, kutoonekana kazini kwa siku tatu mfululizo ni sawa na kujifuta kazi mwenyewe,” alisema kwa upole ikiwa ni tofauti na uhalisia pale kiongozi anapotoa onyo la aina hiyo kwa mtu wake wa chini. “Kitendo cha kutokuja kazini bila ya maelezo naomba usikirudie tena sweetie, hata kama upo hapa kwa mafunzo. Unapokuwa kazini fuata sheria za kazi, vinginevyo utanipa lawama kutoka kwa wafanyakazi kuwa nakulinda.”

    Pamoja na Hija kujitetea kuwa alisafiri kutokana na ugonjwa wa mjomba wake anayeishi Morogoro, lakini hatima ya yote ilibidi aombe msamaha na kuahidi asingekirudia kitendo cha aina hiyo. Nico akawa ameijua sababu iliyomfanya Hija asije kazini kwa siku tatu!

    Shughuli ikawa kwa Badi! Yeye siku hiyo alijua kuwa Hija ameripoti kazini. Akataka kujua kwa nini hakuonekana kwa siku tatu, lakini yeye ikawa tofauti na mwenzake; ikawa si kupiga simu tu, Badi alihofia hata kumtuma mtu wa kumwitia Hija. Hofu yake ilikuwa asije akawekewa dhana ya kuwa, na yeye alikuwa yupo kwenye juhudi za kumtongoza msichana huyo. Akapanga asubuhi hiyo atakapokwenda kunywa chai, afanye kila mbinu ya kuweza kumpa ujumbe kuwa, anahitaji kuonana naye!

    Ilipofika saa nne, muda ambao viongozi huenda kustafutahi, Badi akaamua kuzuga kwa kujifanya ana shughuli nyingi za kikazi ili muda usogee, ili atakapokwenda akute viongozi wenzake wawe wamekwishaondoka.

    Zilipita dakika ishirini tangu muda wa kustafutahi ulipoanza, ndipo Badi alipokwenda. Kama alivyopanga, aliwakuta karibu viongozi wote wakiwa wameondoka. Akapewa huduma ya kifungua kinywa, lakini akili yote ikiwa ipo kwa Hija. Hata hivyo alishangaa baada ya kujiona akielekea kumaliza mlo huo wa asubuhi akiwa hajamwona Hija! Akajipa imani huenda binti huyo amepata wito wa asili uliomlazimisha kwenda kuuitikia msalani. Akataka kujizidishia dakika chache za kuwepo hapo mgahawani, lakini muda wa kuwepo hapo kisheria ulikuwa umekwishamalizika. Akajipa angalizo endapo ataonekana na Meneja Mkuu akiwa bado yuko hapo kungeweza kumletea matatizo. Akaamua kuondoka!

    Alipokuwa akijiondoa kwenye meza, akapishana na mhudumu wa kike ambaye naye ni mwanafunzi kama alivyo Hija.

    “Nakumbuka kama nilimwona Hija leo?” Badi alimuuliza msichana huyo.

    “Yupo, lakini ameitwa na Meneja Nico muda mrefu, nadhani bado yuko ofisini kwake.”

    Kauli hiyo ikamkera Badi, ikamwuma njia nzima wakati akirudi sehemu yake ya kazi. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuanza kumwonea wivu Nico, lakini pia hisia za kumchukia nazo zikawa zinamwandama. Tukio hilo liliendelea kumtesa, likamharibia siku na kumwondoa kwenye ari ya kufanya kazi. Ilikuwa kama ndiyo kwanza alikuwa akitambua kuwa, Nico alikuwa akiyatumia madaraka yake ya kazi kumdhibiti Hija kimapenzi.

    Ilipofika saa nane na dakika arobaini na tano alasiri, Badi alijua muda huo ulikuwa ukitumiwa na wafanyakazi wengi walioingia zamu ya asubuhi kujiandaa kwa kubadilisha nguo kwa ajili ya kutoka na kuwapisha wafanyakazi wengine wanaoingia zamu ya mchana. Akaiona hiyo ndiyo nafasi pekee iliyobaki ya kuweza kulazimisha kuonana na Hija. Akainua simu ya kazini na kupiga Idara ya Restaurant.

    Simu ikapokewa.

    “Mwambie Hija anahitajiwa mapokezi!” Badi alisema, akidhamiria simu hiyo ionekane kuwa ni ya kikazi zaidi.

    Sekunde hiyohiyo akamsikia mtu aliyeipokea simu akisema kwa sauti ya juu kumwambia mfanyakazi mwingine, “Mwambie Hija anaitwa mapokezi!”

    “Bosi, ameshaambiwa!” aliyepokea simu alimwambia Badi

    “Shukrani,” Badi alisema na kukata simu.

    Kitendo cha kupiga simu hiyo na kuhakikishiwa kuwa Hija alikuwa njiani akija, kikaanza kumkosesha amani. Kila alichokuwa akikifanya akawa hakimalizi. Mara ashike kile, aache hiki, wakati mwingine kuitengeneza tai yake vizuri ili Hija atakapokuja amkute yuko smati huku akiendelea kufanya mambo mengine yaliyomfanya akose utulivu.

    Hija akafika mapokezi.

    Badi akaamua asiuchezee muda huo alioupata kwa blah blah zisizo na mpango. Alikuwa akimhofia Nico asije akatokea na kumkuta anazungumza na Hija. Akajisogeza kando ili asiwe karibu na wafanyakazi wenzake.

    “Nataka kuwasiliana na wewe,” Badi alisema kwa haraka. “Niachie namba yako ya simu!”

    “Nitakutumia kwenye simu,” Hija alisema na kutaka kuondoka.

    “Namba yangu ya simu unaijua?”

    Hija akatengeneza tabasamu zuri huku akimwangalia Badi, kisha akaziinua juu nyusi zake kukubali bila ya kutamka neno. Akaondoka.

    Badi akaganda akiwa amepigwa butwaa huku akimwangalia Hija akiondoka.

    Nani aliyempa namba yangu ya simu? Swali hilo nalo likawa sehemu nyingine iliyomwongezea usumbufu!



    ***



    KUIPATA namba ya simu ya Hija kukawa ni faraja kubwa kwake. Akajiona kama aliyepewa silaha maalum ya kumwezesha kupambana na Nico. Siku hiyohiyo akiwa amepitia baa baada ya kutoka kazini, akampigia simu Hija.

    “Uko wapi?” Badi aliuliza baada ya simu yake kupokewa.

    “Niko njiani narudi nyumbani,” Hija alijibu kwa utulivu.

    “Nataka kukuona!” Badi alisema wakati mhudumu akimhudumia bia yake ya kwanza.

    “Kesho nitakuja kazini, tutaonana!”

    “Nataka kukuona leo!”

    “Leo?” Hija aliuliza kwa sauti iliyojaa mshangao.

    “Ndiyo!”

    “Si nimekwambia naelekea nyumbani?”

    “Nyumbani ni wapi?”

    “Tabata.”

    Umbali wa kutoka alipokuwepo hadi Tabata, na kisha kutoka Tabata hadi nyumbani kwake Tegeta ulimchanganya. Alikuwa na uhakika kwa muda huo wa jioni na foleni za magari zilizopo Dar, angepoteza mafuta mengi ya gari lake kwa kusota kwenda na kurudi. Uamuzi wa kutaka kuonana naye kwa siku hiyo akauondoa!

    Akamkubalia waonane kesho.

    Siku ya pili asubuhi wakiwa kazini, Badi aliamua kutumia simu ya kazini kuwahi kumpigia Hija. Aliogopa kufuatwa hapo mapokezi. Alikuwa bado hajaliweka bayana angalizo lake kwa Hija kuwa, mwonekano wao wa pamoja usiwe unafanyika hadharani wakiwa hapo hotelini. Aliamini kauli hiyo ingesaidia kumhadharisha Hija na kumfanya asijipe uhuru wa kuonyesha ukaribu uliopo kati yao mbele ya wafanyakazi wengine.

    “Zaina,” Badi alimwita msichana anayefanya naye kwenye idara hiyo ya mapokezi.

    Zaina aliitikia na kumwangalia Badi.

    “Nipigie simu restaurant, uniulizie Hija. Ukimpata, nipe simu niongee naye.”

    “Sawa bosi,” Zaina alijibu. Kisha aliuinua mkonga wa simu usiokuwa na waya inayotumika kwa mawasiliano ya humo hotelini, akabonyeza namba za restaurant.

    “Naomba kuongea na Hija,” Badi alimsikia Zaina akisema kwenye simu.

    Kimya kikapita.

    “Bosi,” Zaina aliita huku akimwangalia Badi. “Ongea naye!” alisema.

    Badi aliuchukua mkonga wa simu kutoka kwa Zaina na kuelekea pembeni mwa meza ndefu ya mapokezi. “Hija,” alisema kwenye simu huku akitembea.

    “Bee!” Hija aliitikia.

    Uitikiaji wa Hija ukamjulisha Badi kuwa, Hija alikuwa bado hajajua ni nani anayezungumza naye. “Badi nazungumza,” alisema.

    “Ah, shikamoo!”

    “Marahaba. Sikiliza Hija,” Badi alisema moja kwa moja, hakutaka kupoteza muda. “Unaifahamu hoteli ya RM iliyopo Mwenge?”

    “Naijua!” Hija alijibu kwa kifupi.

    “Utanikuta pale.”

    “Saa ngapi?”

    “Ukitoka tu kazini, njoo moja kwa moja utanikuta.”

    “Ina maana utatangulia kutoka?”

    “Ndiyo maana yake!”

    “Sawa.”

    “Kitu kingine,” Badi aliongeza. “Tusifanye mazoea ya kuzungumza kazini, au kuonyesha hali yoyote kuwa tuna ukaribu, sawa?”

    “Sawa.”

    “Kwa hiyo baadaye.”

    Badi alikata mawasiliano na kuurudisha mkonga wa simu.

    Ilikuwa rahisi kama aliyemsukuma mlevi!





    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    HIJA alimkuta Badi kwenye Hoteli ya RM kama walivyoahidiana. Kila kitu kilikuwa wazi kwao huku kila mmoja akijua kuwa, ahadi hiyo ya kukutana kwao ilimaanisha kitu kimoja; walikuwa wakianzisha uhusiano wa mapenzi kati yao!

    “Nico akijua tuko pamoja, anaweza akaua mtu!” Badi alimwambia Hija na kutabasamu.

    “Kila mtu akiwa na mimi anaongelea kumwogopa Nico, kwani mnafikiri mimi na Nico tukoje?” Hija alilalamika.

    “Mpenzi wako!”

    Hija aliangua kicheko kidogo na kusikitika. “Sijui kwa nini wafanyakazi wote wanafikiria hivyo!”

    “Unataka kusema tunakosea?”

    “Tena sana!”

    Badi akazubaa, akamwangalia Hija aliyekuwa akiinua glasi yake yenye bia na kuinywa kidogo.

    “Kama angekuwa ni mpenzi wangu, sidhani kama ningekubali mimi na wewe tuonane hapa!” Hija alisema. “Au una jambo jingine uliloniitia huku zaidi ya love story?”

    “Unamaanisha nini?”

    “Najua unanitaka kimapenzi na ndicho ulichoniitia! Vinginevyo usingemtaja Nico!”

    Wote wakaangaliana machoni.

    “Kwa hiyo Nico sio..?” Badi akasita.

    “Huamini?”

    “Ni vigumu kuamini!”

    “Kwa hiyo unataka kumwibia?”

    “Nimejipanga hivyo!”

    “Ni kujipa mwenyewe wakati mgumu!”

    “Tuachane na Nico,” Badi alisema kwa utulivu. “Nataka ukapajue nyumbani kwangu.”

    “Unaishi wapi?”

    “Tegeta.”

    “Kwa leo haitowezekana, fanya siku utakayokuwa off.”

    “Haimaanishi kama na wewe utakuwa off?”

    “Nitajipa mwenyewe!” Hija alisema kwa kujiamini.

    “Ina maana hutokwenda kazini?”

    “Nimekuja kujifunza kazi, silipwi mshahara. Hata nisipoonekana kwa siku moja, sina hasara yoyote nitakayoitia hoteli.”

    “Unaonaje siku yangu ya off tukionana hapahapa?”

    “Saa ngapi?”

    “Saa nne asubuhi?”

    “Poa.”

    Badi akamtajia Hija siku atakayopumzika.

    Hija alipomaliza bia yake ya kwanza, akaaga.

    Badi akashangaa. “Mbona mapema?” aliuliza.

    “Narudi nyumbani!”

    “Kwani unaishi na nani?”

    “Na wazazi wangu.”

    “Ongeza japo bia nyingine, kisha nitakusindikiza.”

    “Hapana, ahsante. Nitapanda basi.”

    “Dah!” Badi alisema akiwa kwenye mshangao.

    “Vipi?”

    “Hivi unavyoondoka!”

    “Si narudi nyumbani?”

    “Najua!”

    “Sasa kinachokushangaza ni kipi?”

    Badi alimwangalia Hija, kisha akatabasamu. “Nimefurahi kampani yako,” alisema.

    “Hata mimi nimefurahi.”

    “Tutaonana kesho kazini.”

    Ikawa zamu ya Hija kumwangalia Badi. “Salamu inaruhusiwa?” aliuliza.

    “Kwa nini unaniuliza hivyo?”

    “Si umenionya tukiwa kazini…”

    “Agh!” Badi alimkatisha Hija. Si unawajua wapambe…”

    “Ndiyo maana nakuuliza, salamu inaruhusiwa?” Hija naye alimkatisha Badi.

    Badi akajichekesha mwenyewe. “Salamu haina ubaya!” alisema.

    “Basi poa.”

    Hija akainuka kutoka mezani.

    “Na mimi narudi zangu nyumbani!” Badi alisema ghafla na kuimalizia glasi yake yenye bia kwa kuinywa kwa mkupuo. Akasimama. “Nitakuchukulia teksi,” alimwambia Hija.

    “Sawa.”



    4



    SIKU ya ahadi ikiwa haijawadia, wote wawili walianzisha tabia waliyokuwa hawajawahi kufanyiana. Kila mmoja alionekana kuzingatia onyo walilopeana la kutoonyesha ukaribu wao wanapokuwa kazini. Wakawa wanalitekeleza kwa staili ya kila wanapokutana, kila mmoja akawa anajikausha mbele ya mwenzake. Wakati mwingine macho yao yalipokuwa yakigongana, wote wakawa wanafanya tabasamu la kificho. Ikawa ni aina ya dhihaka waliyokuwa wanafanyiana.

    Mawasiliano yao yakaendelea kufanyika kwa kuonana hoteli ya RM kila jioni baada ya kutoka kazini kwa siku mbili. Na kila walipoachana, Badi alikuwa akimkodishia Hija teksi ya kumrudisha nyumbani. Lakini ilipofika siku moja kabla ya kuwadia siku yao ya ahadi, Badi akaugeuza utaratibu wa kumkodishia Hija teksi.

    “Leo nitakupeleka,” Badi alimwambia Hija.

    “Sawa,” Hija alisema bila ya kuonyesha mshangao wowote.

    Ikawa ni mara ya kwanza kwa Hija kupanda gari la Badi. Ndani ya gari wakiwa kwenye foleni wakielekea Tabata, ubaridi wa kiyoyozi uliokuwemo ndani ya gari hilo uliendana na muziki wa taratibu uliosikika kwa sauti ndogo ukipigwa na wanamuziki maarufu duniani. Zote zilikuwa nyimbo za mapenzi zenye midundo ya taratibu yenye hisia kali zikiwa na tenzi zenye maneno yanayosihi, kusisitiza, kulaumu au kubembeleza. Baadhi ya nyimbo hizo zikaonekana kumkamata Hija ambaye aliongozana nazo kwa kuimba kwa sauti ndogo.

    “R&B zako ni nzuri mno!” Hija alikiri huku akionekana kuendelea kutekwa na wimbo uliokuwa ukiendelea kusikika.

    “Thanks,” Badi aliipokea sifa hiyo kwa sauti hafifu.

    Kiza kiliwakuta barabarani kutokana na foleni. Baada ya kumwelekeza Badi njia za kumfikisha nyumbani kwao, hatimaye Hija alisema, “Simama hapo kwenye mwembe!”

    Badi alisimamisha gari alipoelekezwa.

    “Nyumba yetu ni ile inayotuangalia yenye geti jeusi,” Hija alimwambia Badi.

    “Nyumba yenu ni nzuri,” Badi alisema huku akiendelea kuiangalia nyumba aliyoonyeshwa.

    “Thanks.”

    Kimya kikapita kati yao.

    “Kwa hiyo?” Hija aliuliza na kuonekana kujiandaa kutoka kwenye gari.

    “Unakumbuka kama kesho ndiyo ahadi yako ya kwenda kupaona nyumbani?” Badi aliuliza.

    “Najua.”

    “Hakuna mabadiliko yoyote?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yakiwepo nitakujulisha!”

    “Jitahidi yasiwepo.”

    “Dharura haizuiwi kwa jitihada!”

    “Basi tumwombe Mungu kusitokee mabadiliko yoyote.”

    “Mbona kama unazungumzia upande wangu tu, ina maana wewe huwezi kutokewa na dharura yoyote?”

    Badi akafanya kicheko na kuuegemea usukani kwa mikono yake miwili huku akimwangalia Hija ndani ya kiza kidogo kilichokuwemo ndani ya gari.

    “Mimi nina imani hakutatokea dharura,” Badi alisema.

    Hija hakujibu.

    Badi akajiinua kutoka kwenye usukani, badala ya kujiweka sawa kwenye kiti alichokaa, akaelemea upande aliokaa Hija. Ikawa kama Hija alikuwa akisubiri. Wote wawili wakajikuta wakinyonyana ndimi zao kwa hisia kali.

    “Kesho?” Badi alisema baada ya kujiondoa kumkumbatia Hija.

    “Sawa,” Hija alisema huku akiufungua mlango wa gari.



    ***



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog