Search This Blog

Monday, 24 October 2022

MKONO WA SHETANI - 1

 

    IMEANDIKWA NA : JAPHET NYANG'ORO SUDI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Mkono Wa Shetani

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Si kawaida kwa ndege zifanyazo safari za kimataifa kubadilisha muda wake wa safari au kuchelewa kuanza safari. Sababu ziko nyingi, kuna sababu za kiuchumi, kisheria na utaratibu wa usafiri wa anga. Kiuchumi, ilivyo ni kuwa abiria anapokuwa ameshaingia sehemu ya kusubiria kuingia ndani ya ndege baada ya kuwa ameshakaguliwa na kupewa kibali cha kuingia kwenye ndege yaani boardig pass tayari anahesabika kuwa yuko kwenye ndege. Hivyo ikitokea kuwa shirika la ndege limehairisha safari itabidi shirika hilo kulipia gharama zote za abiria kama vile malazi, chakula na usalama wao wakati wakiwa wanasubiri mudamwingine wa ndege kuondoka. Hivyo ni gharama kubwa kwa shirika kuhairisha safari. Sehemu ile ambayo abiria anasubiri muda wa kuingia kwenye ndege kisheria si eneo la nchi yoyote, ndiyo maana ukiwa eneo hilo vitu vinavyouzwa hapo havina kodi kwa vile hakuna nchi yenye uhalali wa kuendesha sharia zake hapo. Unamkumbuka Yule jasusi wa Marekani Edward Snowden kipindi alipotoa siri za Marekani na akawa anasakwa na Marekani kwa udi na uvumba; alipoona kuwa kila nchi imeshajisalimisha kwa Marekani na iko tayari kumtoa, alikata tiketi ya ndege na kuigia ile sehemu ya kusubiria ndege kuondoka kwenye moja ya viwanja vya ndege nchi ya Urusi kisha akang’ang’ania hapo. Hakukuwa na nchi iliyokuwa na haki ya kumkamata eneo hilo. Kingine kinachosababisha isiwe rahisi kwa shirika la ndege kuhairisha safari yake ni jinsi abiria anavyoweza kungia gharama kubwa kwa kukosa kuunganisha ndege zaidi ya nne mbele ya safari. Utakuta abiria anaondoka New York akitegemea kwenda kubadilisha ndege Amsterdam, kisha anabadilisha ndege nyingine Toronto, sasa akicheleweshwa sehemu ina maana amecheleweshwa kupanda ndege zote zilizo mbele yake. Mwisho wa siku abiria ana haki ya kulidai shirika husika gharama zote zilizotokana na usumbufu huo. Hivyo, si kawaida kwa shirika la ndege kuhairisha au kubadiri muda wake wa safari.

    Lakini siku hii ilibidi iwe hivyo, shirikala ndege la Uingereza ilibidi kuhairisha safari yake. Hii ilitokana na taarifa za kijasusi kuonyesha kuwa kulikuwa na mpango wa shambulio la kigaidi katika moja ya ndege za shirika la ndege la Uingereza. Hali hiyo ilisababisha ndege zote za shirika la ndege la Uingereza kuondoka kwa kuchelewa kwa zaidi ya masaa kumi na moja.



    Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa New York au ukipenda uite John F. Kennedy International Airport, maana najua wewe msomaji wangu ni mchunguzi sana utakwenda kwenye ramani na kugundua kuwa hamna uwanja wa ndege uitwao New York. Haya basi, John F. Kennedy International Airport ulikuwa umejaa watu wengi kama kawaida yake. Kelele za kutua na kuondoka kwa ndege zililijaza eneo hilo. Hiki ni moja kati ya viwanja vikubwa vya ndege Duniani. Ndege toka kona mbali mbali duniani zilikuwa zikitua na kuondoka uwanjani hapo. Kwa wengine ilikuwa ni mwisho wa safari zao, wengine katikati ya safari, huku wengine ikiwa ndiyo mwanzo wa safari. Hii ilipelekea eneo hili kuwa sehemu ya purukushani na hali ya aina yake. Purukushani kwa wale waliofanya sehemu hii kuwa kama sehemu yao ya kazi, kama kuuza vitu na kutoa huduma mbalimbali. Ilikuwa ni sehemu ya pekee kwa wale waliokuwa wakipokea wapendwa wao au kuwaaga wapendwa. Bila kuwasahau waliokuwa hapo kiwanjani katika hali ya kulazimika tu, kama vile wafungwa waliokuwa wakisafirishwa, wagonjwa nakadhalika.

    Upande wa kaskazini mashariki mwa kiwanja hiki kulikuwa sehemu maalumu ambayo walijipumzisha abiria waliokuwa wakisubiri muda wa safari zao. Eneo hilo kulikuwa na migahawa, maduka ya pombe, maduka ya vitu mbali mbali huku mengi yao yakiwa yameandikwa duty freeikimaanisha kuwa vitu vilivyouzwa hapo bei zake hazikujumuisha ushuru. Inaaminika kuwa ukishakuwa sehemu ya kusubiri kuingia ndani ya ndege baada ya kupita ile ya kukaguliwa na kugongewa hati yako ya kusafiri, sehemu hii huwa ni ardhi huru, si sehemu ya nchi yeyote. Ndiyo maana maduka mengi yanayouza vitu maeneo hayo hayaweki kodi kwenye bei za vitu wanavyouza.



    Upande wa kushoto kabisa, ukiwa unaingia ndani ya eneo hili la kusubiri muda wa safari, kuna kijana mmoja alikuwa ametulia tuli utadhani mtu aliyepigwa sindano ya ganzi. Huyu naye alikuwa na yake kiwanjani hapo. Jacob Matata ndilo jina hasa la kijana huyo. Yeye alikuwa ni miongoni mwa maelfu ya abiria waliokuwa wakisubiri muda wa safari zao. Alikuwa anataraji kusafiri kwa ndege ya shirika la ndege la uingereza British Airways toka hapo New York mpaka Tanzania. Safari yao ilikuwa imezuiwa kwa takribani masaa kumi na moja. Ingekuwa ni safari ndefu ya masaa mengi sana, ambayo ingewapitisha vituo vingi kama vile Geneva, Amstardam, Adis Ababa kabla ya kuingia Tanzania.

    Alipofika kiwanjani hapo, Jacob Matata alitafuta sehemu hiyo ambayo hivi sasa amekaa akiwa ametulia tuli akiangalia purukushani za watu. Miwani yake nyeusi usoni, suti nyeusi, shati nyeupe na tai nyeusi vilimfanya aonekane nadhifu sana.

    Pamoja na kuwa mwili wake ulikuwa umetulizana kiasi cha kumridhisha yeyote aliyemtazama, macho yake na akili yake vilikuwa macho. Macho yake aliyapepesa hapa na pale. Hii ilikuwa ndio kawaida ya wapelelezi wa “saizi” yake. Wao hupenda kupima kila wanaloliona mbele yao. Alimwangalia huyu akamwacha akamwangalia yule pia akamwacha, alichunguza gari hii ,ile na nyingine akaziacha. Waweza kudhani kuwa hii ni tabia ya kuchosha, lakini kwao ni jambo la kawaida ambalo halikuwa na gharama yoyote kulifanya. Nadhani ndiyo maana wakaitwa wapelelezi ili kuwatofautisha na watu wengine wa usalama kama vile Polisi wa kawaida, wanajeshi n.k. Ndiyo maana wengine hudiriki kudhani kuwa watu hawa si binadamu wa kawaida, jambo ambalo si kweli. Wao ni binadamu wa kawaida, ila mafunzo yao huwafanya wafanye mambo ambayo si rahisi kufanywa na mtu wa kawaida tu kama wewe.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni katika hali kama hiyo hiyo niliyokueleza, ndipo macho ya mpelelezi Jacob Matata yalipogongana na sura ya mzungu mmoja uwanjani hapo. Robo tatu ya watu waliokuwa kiwanjani hapo walikuwa ni watu weupe. Lakini kwa sababu ambazo mimi na wewe si rahisi kuzijua, Jacob Matata akajikuta anapata hamu ya kufuatilia nyendo za mzungu huyo.

    Alikuwa ni mzungu mwenye umri kati ya miaka arobaini na tano na hamsini. Alikuwa na kipara kilichong’aa, urefu wa wastani na mwili uliojengeka vizuri. Macho yake yalikuwa ni moja ya vitu vilivyomwambia mpelelezi Jacob kuwa huyu mzungu ni tofauti na wazungu wengine aliokuwa akiwaona kiwanjani hapo.

    Mzungu huyo alipiga hatua kadhaa na kuingia sehemu hii ambayo Jacob alikuwa amekaa. Alitembea mpaka alipofika jirani kabisa na alipokuwa ameketi Jacob. Baadae kama mtu aliyekumbuka kitu muhimu , alielekea upande wa kusini mwa sehemu hiyo, huko alifika kwenye duka moja walilokuwa wakiuza vitu mbali mbali. Hapo alinunua stika ya bendera ya Tanzania na kurudi upande ule aliokuwa amekaa Jacob Matata.

    Safari hii alikaa karibu kabisa na alipokuwa Jacob Matata. Aliichukua ile stika ya bendera ya Tanzania na kubandika ubavuni mwa briefcase yake. Hapo Jacob akahisi kuwa yawezekana mtu huyu anaifahamu Tanzania au anaelekea Tanzania. Kwa jinsi alivyokuwa akitembea na kutazama, kama ungekuwa na macho yaliyoenda shule ya hali ya juu ya upelelezi na ujasusi kama ya Jacob Matata, usingepata shida kutambua kuwa yule mzungu kama si kachero basi ni moja kati ya mahalifu ya kimataifa. Hivyo Jacob japo hakumfahamu lakini alijikuta akitaka kumjua huyu jamaa.

    Jacob alipoangalia saa yake, ilimwambia kuwa muda wao wa kuingia ndani ya ndege ulikuwa umefika, kutokana na tangazo walilokuwa wamepewa masaa mawili yaliyopita. Kabla hata hajamalizia vizuri kuangalia saa yake mara tangazo la kuwataka abiria wote waliokuwa na safari ya kuelekea Tanzania kwa ndege ya shirika la ndege la British Airways kuingia ndani ya ndege. Pia katika tangazo hilo shirika liliendelea kuwaomba radhi wateja wake kwa kuchelewa kuondoka kwa takribani masaa kumi na moja kwa sababu za kiusalama. Hii ilimaanisha wangetumia masaa kati ya saba hadi kumi toka New York hadi Amsterdam halafu Amsterdam hadi Addis Ababa ingekuwa takribani masaa kumi kisha toka Addis hadi bandari salama yaani Dar es salaam ni kama masaa mawili na dakika arobaini na mbili hivi, Hivyo inamaanisha wangekuwa kwenye ndege kwa Zaidi ya masaa Zaidi ya Ishirini. Hii inamaanisha kuwa wangefika Dar asubuhi ya siku nyingine, ila kama ndege ingeondoka kwa muda uliopangwa wangefika Dar es salaam usiku japo bado wangetumia masaa yale yale.





    * * *



    Kwa vile alikuwa miongoni mwa abiria waliongia mapema ndani ya ndege, Jacob aliweza kumwona kila abiria aliyekuwa akiingia ndani ya ndege hiyo. Hata wakati yule mzungu aliyekuwa amevutiwa kujua nyendo zake alipokuwa anaingia na kwenda sehemu yake ya kukaa, macho ya Jacob yalimfuatilia kwa usiri mkubwa.

    Hii ni moja ya mambo yaliyomfanya mpelelezi Jacob Matata kuwa tofauti na wapelelezi wengine. Kwani mara nyingi hisia zake zilipomtuma kufuatilia kitu basi alizitii mara moja na kufuatilia kitu hicho na mara nyingi matokeo yake huwa mazuri.

    Ni hisia hizo na sababu ambao nimetangulia kusema kuwa mimi na wewe hatuwezi kujua zilimfanya Jacob apate hamu ya kumfuatilia mzungu yule. Hivyo Jacob akawa ameadhimia kutumia safari hii kama nafasi yake ya kumfuatilia mtu huyu. Yule mtu alikaa kwenye moja ya viti vilivyokuwa mbele ya Jacob upande wa kulia. Hivyo ingekuwa rahisi kwa Jacob kumchunguza mzungu huyo bila yeye mwenyewe kujua. Sehemu aliyokuwa amekaa Jacob ilimwezesha kuona kila kilichofanywa na yule mzungu bila yeye kujua.



    * * *



    Lakini tofauti na mawazo ya Jacob Matata kuwa yule Mzungu hakuwa amemfahamu. Lakini huyo mzungu, Dr. Don alipoingia tu ndani ya ndege na kuiona sura ya Jacob Matata aliifananisha. Aliifananisha na sura ya mtu hatari sana ambaye amepata bahati ya kumfahamu siku za hivi karibuni.

    Alimwona wapi?

    Hilo ndilo swali alilokuwa akijiuliza Dr. Don Keller wakati akiwa anajitengeneza kwenye kiti chake mara baada ya kuwa amekaa.

    Dr. Don Keller ni moja kati ya majasusi ya kutisha ya kizungu. Amekuwa ndani ya fani hiyo kwa muda mrefu. Kwa siri kubwa ameweza kuwahi kufanya kazi na mashirika mbalimbali ya ujasusi duniani bila kujulikana, kwa kuwauzia habari au kutekeleza mauji kwa niaba yao. Mwanzoni mwa miaka ya themanini ndio wakati ambapo Dr. Don alibadili mwelekeo wa utendaji wake na kuingia katika biashara lakini ndani yake akiwa anafanya uharamia wa kutisha.

    Akili yake ilikuwa bado inazunguka kutafuta ni wapi alipoiona sura ya mtu huyo aliyemkuta ndani ya ndege.

    “Ok huyu ndiye Jacob Matata”

    Hatimaye Dr. Don Keller alijisemea kwa sauti ya mtu aliyeona mzimu usiku akiwa anatoka kuiba mke wa mtu huko kijijini, mara tu kumbukumbu zake zilipofanikiwa kuleta taarifa fasaha juu ya mtu aliyeko nyuma yake ndani ya ndege hiyo. Alitupa jicho lake kwa chati na kuhakikisha kuwa kweli anayemwona ni Mpelelezi hatari sana Jacob Matata. Akajikuta akijuta kukutana na mtu kama Jacob Matata katika wakati ambao anatakiwa kutimiza jukumu muhimu kama hili ambalo liko mbele yake.

    “Ndio nilimwona kwenye faili moja la siri siku chache zilizopita” Mawazo yake yalisema kana kwamba anaongea na mtu. Sasa Dr. Don licha ya kukumbuka jina la Jacob , akakumbuka kule alikomwona na kupata habari zake. Pamoja na kuwa alikuwa ameacha kujishughulisha kama jasusi, Dr. Don hakuwa ameacha kufuatilia taarifa mbali mbali za kijasusi. Alipenda kujua taarifa za mashirika makubwa ya kijasusi kama KGB la Urusi , CIA la Marekani, BND la Ujerumani na meningineyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku chache zilizopita wakati akiwa anasoma habari za shirika la kijasusi la Urusi KGB katika tovuti ya kijasusi, ndipo aliposhangaa kukuta taarifa kuwa hatimaye mpelelezi toka Afrika ni miongoni mwa watu wanaoitingisha dunia hivi sasa katika masuala ya upelelezi. Taarifa hiyo ilisema kuwa mpelelezi huyo wa kiafrika ameingia katika orodha ya wapelelezi kumi na tano bora duniani. Picha na jina la mpelelezi huyo havikuwekwa. Taarifa hiyo ilisema kuwa uwezo wa mpelelezi huyo umethibitika hivi karibuni kutokana na kazi aliyokuwa anaifanya huko Mashariki ya kati.

    Kama miezi sita ilikuwa imepita ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa limepokea malalamiko ya Israel ya kuishutumu Urusi kuwa majasusi wa Urusi walikuwa wamehusika katika vifo vya makomandoo kumi na moja wa Isarel ambao maiti zao zilikutwa zinaelea baharini asubuhi moja. Hivyo Israel ikawa imetishia kuwa, kwa vyovyote vile lazima ingelipa kisasi. Urusi kwa upande wake ilisisitiza kutohusika katika jambo hilo, na kuongeza kuwa kitendo chochote cha Israel dhidi ya nchi hiyo ingekuwa ni uchokozi ambao usingevumiliwa.

    Kwa kuzingatia uwezo wa kivita wa nchi zilizokuwa zikizozana, baraza la usalama la umoja wa mataifa likaamua kutafuta ukweli wa mambo juu ya suala hilo ili kusuluhisha. Kwa vile wapelelezi wengi wa baraza hilo walikuwa ama wanaipendelea Urusi au Israel, baraza hilo la usalama likaamua kutafuta kachero ambaye hasingependelea upande wowote. Ndipo hapo jina la mpelelezi huyo kijana toka Afrika lilipopendekezwa. Japo baadhi ya maafisa wa baraza hilo walitilia shaka uteuzi huo kwa kigezo kuwa mwafrika tena toka nchi za Afrika mashariki na kati asingeweza kufanya chochote cha maana wala kufika mbali mbele ya majasusi waliokubuhu huko mashariki ya kati.

    Dunia ilishangaa pale mpelelezi huyo alipoingia ndani ya mashariki ya kati na baada ya siku ishirini na saba tu tayari akawa na taarifa yote iliyoambatana na ushahidi juu ya suala hilo. Nchi husika huko mashariki ya kati zilikiri kuwa haizikujua ni namna gani mpelelezi huyo aliingia na alivyotoka. Ila walichoweza kuona ni alama ya hatua zake kila mara alipokuwa akitoka sehemu. Urusi na Israel walikubaliana na matokeo ya upelelezi wake na kukiri kuwa vidhibiti vilivyokuwa vimetolewa vilikuwa ni sawa.

    Kama mfanya bishara mkubwa ambaye ndani yake kuna ujasusi mkubwa uliojificha, Dr. Bon hakuishia hapo, kwakutumia marafiki na vyanzo mbali mbali vya siri vya habari alianza kutafuta jina la mpelelezi huyo na sura yake. Hapo ndipo akapata taarifa kuwa mpelelezi huyo ni Jacob Matata toka Tanzania.

    Sasa jambo lililomtia kiwewe Dr. Don ni namna gani angeweza kufanya lile alilotakiwa kufanya na Bosi wake, huku akijua fika kuwa macho ya Jacob Matata kwa vyovyote yangeona kilichokuwa kikiendelea.







    ********

    Safari ilikuwa ndefu, tayari walikuwa wameshapitia vituo kadhaa. Mpaka walipokuwa wanakaribia uwanja wa kimataifa wa Addis Ababa nchini Ethiopia, Jacob hakuweza kuona lolote jipya toka kwa mtu wake. Muda wote wa safari, macho ya Jacob Matata hayakumpa nafasi yule mzungu. Abiria wengi walikuwa wameshuka kwenye vituo vya njiani na wengine walikuwa wameingia kujiunga na safari ya hiyo ndege. Dr. Don kwa upande wake alishatambua kuwa Jacob alikuwa ameshuku kitu juu yake. Hivyo ilimbidi kuwa mtulivu na kupanga kwa makini namna ya kutimiza azma yake ndani ya ndege hiyo.

    Hari ya hewa katika anga la Ethiopia haikuwa nzuri. Mawingu mazito yalikuwa yametanda kiasi cha kutisha katika eneo hilo maarufu la Bole ambalo liko kama kilomita 6 au maili 3.7 kusini mwa mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Ndege hii ingekuwa kama zile ndege uchwara, basi ratiba ya kutua hapo ingebadilishwa. Lakini hii ni ndege ya kisasa na yenye nguvu. Hivyo bila kusita rubani ilianza kuishusha ile Ndege taratibu kuelekea upande ulikokuwa uwanja wa Addis Ababa, Bole International Airport. Abiria walikuwa wameshatangaziwa juu ya hali hiyo mbaya, na hivyo kuhimizwa kufunga mikanda. Wakati ndege inakaribia kutua katika kiwanja hicho kulikuwa na mtikisiko mkubwa kiasi cha kuweza kuwafanya watu waoga kusali sala zao za mwisho. Haraka haraka kwa kupitia mwanya huo Dr. Don alipindua macho yake kushoto na kulia kama kinyonga na kubaini kuwa jirani zake wote walikuwa wamepoteza umakini huku wengi wao wakiwa wamefumba macho kwa wasi wasi na wengine wakiwa wanaonyesha ishara ya sala wakiwa wamefumba macho. Alipoangalia nyuma alimwona Jacob akiwa anahangaika na mkanda wa kiti alichokuwa amekikalia. Kwa kasi ya ajabu na umakini mkubwa pasipo purukushani, Dr. Don aliichukua Briefcase yake na kuiweka pale ilipokuwa ya abiria jirani yake kisha akachukua ila ya abiria yule na kuiweka pale ilipokuwa ya Dr. Don hapo awali. Kwa vile abiria wengi walikuwa wameshuka toka kwenye hiyo ndege kwenye vituo vya njiani, kama ilivyokuwa kwa Don, jirani yake naye alikuwa ameweka briefcase yake kwenye kiti jirani na yeye kwa vile hakikuwa na mtu. Hivyo ikawa rahisi kwa Don kunyanyua yake na kuiweka pale ilipokuwa ya jirani yake. Tayari akawa amebadilisha briefcase bila mtu yeyote kujua. Jambo hilo alilifanya kwa kasi ya ajabu na utulivu mkubwa. Baada ya tendo hilo alihakikisha kama kuna mtu aliyekuwa akimwangalia. Alipohakikisha kuwa hakuna mtu, kwani hata Jacob alionekana kuwa hakuwa na taarifa juu ya kile alichokifanya, Dr. Don alijituliza tuli. Gundi hainasi kwenye chupa yake!! Don liwaza huku akikuna upara wake.



    Kama ilivyokuwa tangu walivyoanza safari yao, jicho la Jacob Matata halikumpa nafasi kabisa Don. Uzoefu wake katika mambo ya ujasusi ulimwambia Jacob kuwa magaidi au watu hatari hufanya mambo wakati ambao hutarajii, hivyo njia bora ya kukabiliana nao ni kuwa macho muda wote. Hata wakati Dr. Don anabadilisha zile briefcase jicho la Jacob lilimwona vizuri kabisa, japo isingekuwa rahisi kwa Don kugundua kuwa kuna mtu aliyemwona tena mtu mwenyewe ni Jacob Matata.

    Mpaka wakati huu Jacob Matata hakuwa anamfahamu Dr. Don na pia hakujua ni kwa nini aliamua kubadilisha briefcase yake na ile ya abiria mwenzie katika hali ya kificho namna ile. Jacob alimwangalia yule mtu ambaye briefcase yake ilikuwa imebadilishwa na kutambua kuwa alikuwa amesinzia. Akachungulia dirishani na kuweza kuona Ndege zilivyokuwa zimetapakaa kwenye kiwanja hicho. Kwa upande wa kushoto kwa mbali aliweza kuona majengo ya Ethiopian Aviation Academy.

    Don ni Jasusi aliyeiva, hii ilithibitika pale ndege ilipokuwa tayari imetua kwenye kiwanja cha ndege cha Addis Ababa. Pamoja na kuwa alijua kuwa Jacob Matata hakuwa amemwona akiwa anaichukua ile briefcase, lakini alitumia muda huo kwenda chooni na kuwasiliana na ‘vijana wake wa kazi’ Dar es Salaam.

    “…hakikisha mkija kunipokea mje na hicho kitu nilichowaambia na msisahau kuweka stika ya bendera ya Tanzania ubavuni mwake…” Hayo yalikuwa ni sehemu tu ya maagizo ya Don kwa vijana wake walioko Dar.

    Jambo moja ambalo Jacob alikuwa amegundua ni kuwa mzungu huyo ambaye yeye Jacob hakuwa amefahamu kuwa ndiye Dr. Don Jasusi la kutupa alikuwa amejiandaa kwa tukio hilo. Kwani briefcase yake na ya yule mtu aliyembadilishia zilikuwa zimefanana kila kitu. Cha kushangaza ni ile stika ya bendera ya Tanzania ambayo yule mzungu aliinunua pale New York na kuibandika ubavuni mwa briefcase yake, kwani ile briefcase nyingine pia ilikuwa nayo tena ikiwa imebadikwa upande ule ule. Hivyo isingekuwa rahisi kwa mtu ambaye briefcase yake ilibadilishwa kugundua badiliko katika briefcase nyingine. Hivyo Jacob Matata akaadhimia kufuatilia jambo hili mpaka mwisho. Penye mzoga ndipo wakusanyikapo Tai, Jacob alijisemea. Huku akitengeneza tai yake.



    * * *



    Jacob Matata alikuwa amedhamiria kufuatilia mpaka aone mwisho wa mchezo uliokuwa ukichezwa mbele ya macho yake. Japo mpaka wakati huu hakuwa anamfahamu Dr. Don, pia Jacob Matata aliamini kuwa mzungu huyo hakuwa ana habari juu yake. Hivyo hakuwa na wasiwasi kuwa anajulikana japo alimfuatilia kwa tahadhali zote na ufundi mkubwa.

    Yeye Dr. Don alishahisi kuwa anafuatiliwa na mtu, tena mtu mwenyewe ni hatari kupindukia. Kufuatiliwa na mpelelezi kama Jacob Matata kulimfanya Dr. Don akili yake ifanye kazi haraka sana na awe makini zaidi. Yeye peke yake ndiye aliyekuwa anajua pande zote mbili. Alimfahamu Jacob Matata na wakati huo huo alimfahamu mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa ambaye mpaka wakati huu tayari alikuwa ameshafanikiwa kupora briefcase yake bila Kimisa mwenyewe kuishtukia.

    Tofauti kabisa na wenzie, mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa alionekana ni mwenye furaha muda wote tangu afike kwenye uwanja wa kimataifa wa ndege wa Dar es salaam. Wakati alipokuwa ameshuka toka ndani ya ndege na kulakiwa na maafisa kadhaa wa shirika lake

    Dr. Don na Jacob Matata tayari walikuwa wameshaingia ndani ya magari yao. Kila mmoja sehemu yake. Don aliingia ndani ya gari ambayo alikuwa ameletewa na mmoja wa vijana wake kiwanjani hapo. Jacob Matata alichukua gari yake aliyokuwa ameiacha uwanjani hapo wakati akielekea mashariki ya kati. Alijiweka tayari kufuatilia nini kingetokea baada ya hapo. Alishangazwa sana na mapokezi aliyoyapata Kimisa. Hii ilitokana na kuwa wakati Bwana Kimisa anateuliwa na Rais ili kuwa mkurugenzi wa shirika la JEPA, Jacob Matata alikuwa nje ya nchi kwenye kibarua cha mashariki ya kati. Hivyo hakuwa anamfahamu Makia Kimisa. Gari alilopanda Makia Kimisa lilipoanza kuondoka Jacob alitupia macho kwenye gari ya Don na kuona kuwa ndiyo kwanza ilikuwa inawashwa. Mtikisiko wa gari na taa za pembeni zilizowashwa za gari aliyokuwa Don zilithibisha hayo.



    Don alikuwa amepanga kufuatilia msafara wa Makia Kimisa ili aweze kuona kuwa angeifikia wapi na ile briefcase ya bandia. Gari ya Makia Kimisa iliposhika lami ya barabara kuu ya uwanja wa ndege, gari ya Don ilikuwa ndio inatoka kiwanjani.

    “Kwa ninitusimfutilie mbali halafu kesho tumalize mchezo mzima? Kijana mmoja wa Donalishauri

    “Hapa ninazana ambayo inawza limaliza gari alilopanda Kimisa...” Aliongeza huyo kijana

    “Hapana, Jipu hukamuliwa likiwa limeiva, ukilikamuwa likiwa bado jipu hilo huuma na hujikusanya upya sehemu nyingine ya mwili. Subiri, kila kitu kwa hatua” Don alijibu kwa sauti kama anayejisemea mwenyewe.



    Mpaka wakati gari ya Kimisa imeacha barabara ya Bibi titi, na kuingia zilipo ofisi zake katika majengo ya shirika la JEPA, Makia Kimisa hakuwa ameshitukia lolote lile. Don hakupata taabu sana kuiona gari ya Jacob Matata iliyokuwa ikimfuatilia kwa mbali sana. Baada ya kuona sehemu ambayo Kimisa angefikishia mzigo wake, Dr. alikanyaga mafuta moja kwa moja mpaka alipokaribia eneo la hoteli ya Fortune Inn ambapo alipunguza mwendo na kuingiza gari eneo la kuegeshea magari la hotel hiyo. Muda mfupi baadaye gari alilokuwa amekodi Jacob Matata pia liliegeshwa upande mwingine wa eneo hilo la kuegeshea magari, katika hoteli ya Fortune Inn.

    Dr. Don alikuwa amelitarajia jambo kama hilo, ndio maana alipofika Addis aliwamuru vijana wake waandae briefcase iliyofanana na zile alizofanyia mchezo ndani ya ndege. Hivyo alipoingia ndani ya gari pale alipotelemka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es salaam aliikuta briefcase hiyo ndani ya gari. Kweli zilikuwa zimefanana sana na ile aliyomwibia Makia Kimisa.

    Dr. Don alifungua mlango wa gari na kuufunga baada ya kutoka. Alipiga hatua kama tano hivi toka kwenye gari kisha kama mtu aliyekumbukua kitu alirudi mpaka ndani ya gari na kuchukua ile briefcase moja na kutoka nayo. Baada ya kuwa amefunga mlango wa gari, alipiga hatua za haraka kuelekea bara barani. Alivuka barabara na kuelekea upande mwingine, namna Don alivyokuwa akitembea ungeweza mfananisha na jinsi alivyokuwa akitembea yule gwiji wa soka wa Liberia George Opong Weah.



    Kuona hivyo, Jacob Matata akahisi kuwa Dr. Don ndio alikuwa amekwenda kuifungua briefcase aliyoipora. Hivyo kwa haraka sana alishuka ndani ya gari na kufunga mlango kwa kuubamiza. Akaanza kuelekea kule alikoelekea Dr. Don kwa hatua za kikakamavu. Safari ya Dr. Don iliishia kwenye majengo ya shirika la JEPA. Hapo aliingia moja kwa moja mpaka mapokezi.

    “Habari za kazi? alimsabahi mama mmoja aliyekuwa mapokezi ofisini hapo.

    “Nzuri tu, karibu”

    “Asante”

    “Nikusaidie nini?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naomba kuonana na mkurugenzi kama ana nafasi” aliomba Dr. Don, japo macho yake hayakuonyesha kuwa alikuwa na shida hiyo.

    “Ulikuwa na miadi naye?

    “hapana ila nilikuwa nataka kumwona ili nimpe malalamiko yangu juu ya masuala fulani ya kiutendaji” Dr. Don alidanganya huku akijua fika kuwa hatoruhusiwa kuingia ndani.

    “kwa leo hana nafasi maana ndio kwanza ameingia toka safari, isitoshe siku ya kusikiliza malalamiko binafsi ni mwanzoni mwa kila mwezi. Hivyo si rahisi kumwona leo”. Alisema huyo mama huku akiendelea na upangaji wa mafaili fulani yaliyoonekana kuwa na vumbi. Hata wakati Dr. Don anaweka ile briefcase pale chini , yule mama hakumuona.

    “Haya mie naenda nitajaribu siku nyingine” Dr. Don aliaga na kuanza kuondoka akiiacha briefcase pale chini.

    “Haya karibu tena”

    “Asante” Don aliitikia wakati tayari akiwa usawa wa mwimo wa mlango wa kutokea nje. Hakuwa na muda wa kupoteza. Alitoka nje, akapiga hatua kurudi upande ule aliokuja nao awali. Dr. Don alijua fika kuwa Jacob atakuwa amemfuata pale ofisi ya shirika la JEPA. Hivyo alipofika mbali kidogo aligeuka kuangalia upande ule wa majengo alikotoka, alimwona Jacob Matata ndiyo akiwa anaishilia ndani ya majengo hayo. Alitumia nafasi hiyo kukimbia mpaka Fortune Inn hotel. Alipofika Fortune Inn hotel, Dr. Don alienda mapokezi ambapo aliomba chumba kimoja. Alipewa chumba namba 110 ghorofa ya pili.

    Don alikuwa akicheza karata zake vizuri sana. Yote hayo alifanya ili aweze kumdanganya Jacob Matata na kutoweka. Baada ya kuwa amepata chumba alitoka ili aelekee lilipo gari lake. Alipofika usawa wa mlango alimwona Jacob Matata akiwa ndio amemalizia kuweka kitu ndani ya gari yake. Mara moja akajua mtego wake wa kwanza ulikuwa umenasa, kwani Jacob alikuwa ameichukia ile briefcase aliyoiacha pale shirika la JEPA. Alitambua Jacob atafikiri ndio ile briefcase aliyoiba ndani ya ndege.

    Bila kuonyesha wasiwasi wowote wala kusita, kwa mwendo wa Mbwa dume aliemwona Mbwa ambaye anamzidi nguvu Don alitembea alitembea kwa hara na kifahari mpaka alipokuwa ameegesha gari lake. Alijitoma ndani ya gari na kuitia moto. Muda wote huo Jacob alikuwa ametulia tuli ndani ya gari yake akiwa anamwangalia Don. Don alingia barabara kuu na kukanyaga mafuta. Alirudi Bibi Titi, Morogoro road na kutokomea kwa kasi huku akimwacha Jacob Matata akiwa ameridhika na ile briefcase ya bandia.



    Baada ya kuondoka Don, Jacob Matata alitoka ndani ya gari na kuelekea mapokezi ya hoteli ya Fortune Inn.

    “Habari za kazi binti mzuri” Jacob alisabahi, huku akiminya jicho la kushoto.

    “Nzuri tu nikusaidie nini? Alijibu yule dada huku akitabasamu

    “Nahitaji vyumba viwili vilivyopakana”

    “Umepata, tena una bahati kweli kwani vilikuwa vimebakia vitatu tu”.

    “Mtu kama mimi bahati ndio nyumba kwake, hivyo usihofu. Kwa hiyo naweza kupata vitatu? Jacob alitegeshea na yule binti akajichomeka kwa kusema “Hapana kwa sasa vipo viwili tu kama ulivyoomba awali”

    “Usiniambie kuwa kile cha tatu umemtunzia bwana yako au. Maana mtu chake bwana?!!!

    “Hapana kaka mi sina bwana ila kuna mzungu mmoja amekichukua muda si mrefu uliopita” hili ndio jibu ambalo Jacob Matata alikuwa akilitaka muda wote. “Vilivyobaki ni namba ngapi? Kufuatia swali la Jacob ilimlazimu yule dada kufungua kitabu chake cha orodha ya majina ya wageni na vyumba vyao.

    Kabla hata yule dada hajaangalia vizuri namba ya vyumba ambavyo havina wapangaji, tayari macho ya Jacob yalikuwa yameshaona namba hizo na ile ya yule mzungu.

    “Chumba chako kitakuwa namba 111 na 112” yule dada alimueleza Jacob ambaye baada ya kumaliza kujiandikisha alitoka nje mpaka pale alipokuwa ameengesha gari yake. Alifungua mlango wa gari na kutoa ile briefcase. Aliingia nayo ndani. Akapitia funguo za vyumba vyake na kuparamia ngazi akipanda kuelekea ghorofa ya pili.

    Alianza kuingia chumba namba 111 kisha baadae akaingia namba 112. Humo aliamua kuangalia nini kilikuwa ndani ya ile briefcase. Haikumchukua muda mrefu tayari akawa amefanikiwa kuifungua ile briefcase. Nusura Jacob Matata acheke kutokana na kile alichokiona ndani ya ile briefcase.



     Haikumchukua muda mrefu tayari akawa amefanikiwa kuifungua ile briefcase. Nusura Jacob Matata acheke kutokana na kile alichokiona ndani ya ile briefcase. Briefcase ilkuwa nakipande kikuwa cha mbao ngumu, kati kati ya mbao hiyo kulikuwa na kibakuli ambachokilikuwa kimejaa kinyesi. Kati kati ya hicho kinyesi ilichomekwa karatasi iliyoonekana kuwana maandishi. Jacob Matata alikichukua ile kaatasi huku pua yae ikishindana na harufu ya kinyesi, akakunjua. Kikaratasi hicho kilichokuwa kimeandikwa kwa kalamu ya wino mwekundu katika herufi kubwa zilizosomekaa hivi, JACOB MATATA HONGERA KWA KAZI NJEMA HUKO UTOKAKO, KARIBU TANZANIA, ILA UYAONAYO YAACHE KAMA YALIVYO LA SIVYO……….TUSILAUMIANE. Yalikuwa ni maneno machache sana, ambayo hayakumchukua Jacob hata nusu dakika kuweza kuyamaliza kusoma. Ndio kwa mara ya kwanza tangu ameingia Dar leo, Jacob akalihisi joto la Dar. Kijasho chembamba kiliyatekenya maungo yake. Alitabasamu.

    “Kazi ipo na lazima ifanyike” maneno haya yalitoka kinywani mwa Jacob bila ruhusa yake. Hapo ndipo akagundua kuwa Dr. Don tayari alikuwa ameshagundua kuwa alikuwa anamfuatilia. Mara moja akajua kuwa sasa nyendo zake zilikuwa mikononi mwa adui. Hivyo alikuwa na kazi ya kupoteza nyayo zake zisiwe mikononi mwa adui.

    Wakati huo tayari bastola ilikuwa mkononi, Jacob alifungua mlango wa chumba alichokuwemo kwa hadhali kubwa. Alitelemka na badala ya kutoka nje aliingia chooni, huko kwa kutumia upenyo wa dirisha alipasua eneo kubwa zaidi pasipo kufanya makelele. Kwa kutumia bomba la maji aliweza kutelemka mpaka chini hapo aliruka ukuta na kutokezea mtaa wa pili ambapo safari ya kwenda kwake ilianza.

    “kwanza nikamsalimie Regina mpenzi wangu, mambo mengine baadaye“alijisemea Jacob wakati akiangalia taxi ya kumpeleka kwake. ‘Ukilazimisha ‘King’ utaliwa nyingi’ aliwaza huku akiwa anajitengeneza kwenye kiti baada ya kingia kwenye taxi.



    ***********



    Yalikuwa yameshapita masaa kama kumi hivi, tangu Jacob Matata alipokuwa ametoka katika hoteli ya Fortune Inn. Kutokana na jinsi mambo yalivyokuwa yamejitokeza na jinsi alivyokuwa ameona ujuzi wa adui yake, Jacob Matata alionelea si vema jambo hili akaliweka kiporo. Kwa hivi sasa anaelekea kwenye kile chumba kilichokodiwa na Dr. Don, alikuwa anajaribu aone kama atafanikiwa kumtia mikononi mzungu huyo. Ambaye hata hivyo hakuwa anamfahamu bado. Hakujua ni kitu gani mzungu huyo alikuwa amepora ila hamu ya kutaka kumjua ndiyo iliyokuwa inamsukuma kumfuatilia mzungu yule.



    Akiwa amesaliza hatua kama nne tu toka ulipo mlango ambao juu yake ulikuwa umeandikwa namba 110, Jacob Matata alitupia macho kwenye saa yake ya mkononi. Saa ilimwonyesha kuwa ilikuwa imeshatimia saa nane na dakika kumi usiku wa manane. Tayari alishakuwa nukta chache usawa wa mlango wa chumba namba 110, bastola ikiwa tayari mkononi. Wakati anajiandaa kupiga teke mlango wa chumba, ghafla Jacob akasikia kitu cha baridi kikiigusa shingo yake. Kabla hajatambua ni nini, akasikia sauti nzito ikimwambia, “huna haja ya kuvunja mlango bwana Jacob Matata, karibu ndani!!! Sauti hiyo ilipomaliza kusema tu, mara mlango ukafunguliwa. Ndani kulikuwa na watu watatu ambao walikuwa wameshikilia imara kabisa silaha zao bunduki aina ya AK 47 zote zilikuwa zimelenga kifua cha Jacob.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mpaka hapo Jacob akajua kuwa tayari alikuwa ameshatekwa. Yule aliyekuwa nyuma yake alimwamuru Jacob aingie ndani. Jacob bila ubishi akatii amri. Alipoingia ndani wale vijana watatu waliokuwa ndani wameshikilia bunduki kumuelekea Jacob Matata, ambao muda wote walikuwa kimya walitawanyika na kila mmoja alichukua nafasi yake. Kila kona ya chumba ilikaliwa na mmoja wao. Yule aliyekuwa nyuma ya Jacob ndiye ambayo muda wote alikuwa akitoa amri.

    Jacob alifungwa mikono yake kwa pingu na yule mtu aliyemteka nyara pale nje ya chumba! Tofauti na mategemeo ya Jacob yule mzungu ambaye ndiye Dr. Don hakuwemo ndani ya chumba, kwa namna hawa watu walivyokuwa wakifanya kazi zao, Jacob alitambua kuwa ni wakati mwingine tena ambapo anapambana na kikundi hatari sana.

    Maswali mengi yalikuwa yakifumuka ndani ya kichwa chake. Hawa watu wamemjuaje? Je wanajihusisha na nini? Ile briefcase waliyopora ndani ya ndege ilikuwa na nini? Je yule Mzungu ambaye ndiye hasa amekuja kumtafuta kwenye chumba hiki ni nani na anajihusisha na shughuli gani? Maswali yalikuwa yakija ndani ya kichwa kwa fujo lakini Jacob hakufanikiwa kupata jibu hata moja.

    Mmoja wa wale watu waliomteka, alichukua simu yake ya kiganjani na kubonyeza namba kadhaa kisha akasema, “Tayari”.

    “Mleteni hapa Gardenia Hotel chumba namba….” sauti ya upande wa pili haikusikika vizuri alipofika hapo kutokana na Jacob kupiga chini viatu vyake kwa nguvu na kutoa kelele kubwa, maelekezo ya mwisho hayakusikika vema na huyo kijana kwa hivyo akajikuta anauliza tena.

    “Umesema Gardenia namba 11? “

    “Ndio” ulijibu upande wa pili.

    Aliiweka simu yake mfukoni kisha akamkata Jacob kofi kali la usoni.

    “Haya simama twende, ila ujanja wowote utakuwa umeyamaliza maisha yako mwenyewe” Aliongea huyo jamaa ambaye alionekana kutokuwa na hata punje ndogo ya utani na alijali kazi yake.



    Badala ya kusimama kama alivyoamriwa, Jacob aliendelea kukaa. Kitendo hicho kilimfanya apate kipigo kikali toka kwa huyu jamaa ambaye alikuwa jirani naye. Kwa vile Jacob alikuwa amefungwa pingu hakuwa na namna ya kujitetea, vile vile wale jamaa wengine watatu walikuwa kimya na imara kabisa huku midomo ya bunduki zao ikielekea kila mahali kifua cha Jacob kilipoelekea.

    Ghafla yule jamaa aliyekuwa karibu na Jacob na ambaye alikuwa akimshambulia Jacob aliponyokwa na bastola yake, wakati anataka kuiokota akaanguka chini. Dakika tatu baadaye jamaa wote walikuwa chini.

    Ubishi aliokuwaameufanya Jacob wa kugoma kusimama ulikuwa w makusudi kabisa, kwani wakati ule huyo jamaa alipokuwa akiongea na simu Jacob alipopiga viatu kwa nguvu sakafuni, alikuwa anapasua vichupa vidogo sana ambavyo aliviweka katikati ya viatu vyake kwa chini. Vichupa hivi vilikuwa na ‘gesi’ ya kulewesha. Vichupa hivyo Jacob alikuwa amevipachika kenye kona ya ndani chini ya sole ya kiatuambacho kilikuwa kimetengenezwa maalum kwa huduma hiyo. Kabla ya kuja hapa Jacob alipaka puani dawa maalumu ambayo ingemwezesha kutoathirika na dawa hizo kama angelazimikakuzitumia. Hivyo Jacob alijichelewesha kusimama ili kuruhusu dawa hiyo kufanya kazi. Ili kufanya kazi dawa hiyo ilihitaji kama dakika mbili tu tangu kupasuliwa kwake, ili iweze kumlaza mtu atayekuwa ameivuta hewa yake. Tayari ile dawa ilikuwa imeshaanza kufanya kazi ndiyo maana yule mmoja aliponyokwa na bastola akaanguka kisha akafuatiwana wengine waliosalia.

    Jacob Matata hakutaka kupoteza muda, alijivuta mpaka alipokuwa yule jamaa aliyemfunga pingu, akasogeza mikono yake iliyofungwa mpaka ilipo mifuko yake ya Suruali. Kwa kulazimisha sana Jacob akafanikiwa kuupata ufunguo wa zile pingu toka kwenye moja ya mifuko ya huyo jamaa.

    Haikumchukua muda sana Jacob tayari akawa amesimama humo chumbani. Jacob alionelea kulikuwa na umuhimu wa kuwahi huko Gardenia Hotel. Kwani kutokana na mawasiliano ya simu yaliyokuwa yamefanyika mtu aliyewatuma hawa jamaa atakuwa ameshaenda kumpokea Jacob kama mateka na sio kama Jacob Matata kamili. Jacob alichukua bastola yake ambayo alikuwa amepokonywa na yule mtu aliyekuwa amemteka. Akawalamba risasi mbili mbili za vichwa kila mmoja. Maana ingewachukua muda mpaka wazinduke ili awahoji. Hii ingempa wasiwasi bosi wao ambaye bila shaka angekuwa anawasubiri kule Gardenia Hotel. Jacob aliweza kusikia jina na namba ya chumba cha hotel wakati yule jamaa anarudia ili kuhakiki.



    * * *



    Dakika tano baadaye, mpelelezi Jacob Matata alikuwa ndani ya eneo la hoteli ya Gardenia. Ndio kwanza watu walikuwa wanaanza kupungua ndani ya hoteli hiyo.

    Saa tisa kasoro dakika kumi usiku ni wakati ambapo mpelelezi Jacob Matata alipokuwa usawa wa malango wa chumba namba 11 katika hoteli ya Gardenia. Kwa jinsi alivyokuwa amenyata, isingekuwa rahisi kutambua kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akitembea maeneo hayo.

    Bastola mkononi, Jacob alitega sikio usawa wa kitasa cha mlango, ndani ya chumba kulikuwa kimya kabisa. Mara sauti ya kitabu kilichokuwa kikifunguliwa ilisikika.

    Moja, mbili, tat…, tayari Jacob alikuwa ndani ya chumba mara baada ya teke lake kufanikiwa kufungua mlango.

    Alipotua tu chini, alikaribishwa kwa teke kali toka kwa Dr. Don ambaye hata hivyo hakutegemea ujio wa Jacob katika hali kama hiyo. Hata hivyo hakutaka kupoteza muda kwa kufikiria imekuwaje mpaka Jacob akaja kama mwindaji na si mateka kama yeye Don alivyotarajia. Dr. Don alijua fika kuwa Jacob angependa na alitegemea yeye ashituke kwa hivyo kama kweli angeshituka na kuzubaa basi angekuwa amejimaliza kilaini sana ndani ya mikono ya mtu hatari sana kama Jacob Matata.

    Wakati Jacob anajiweka sawa Dr. Don alipiga gumi tatu mfululizo ambayo hata hivyo Jacob aliiona na kuachilia ngumi kali iliyompata Don shingoni, akayumba. Pamoja na maumivu hayo, Dr. Don aliruka kama ndege na kujipindua kwa teke ambalo kama Jacob asingeliona lisingembakiza hai, kwani Jacob alipolikwepa, lile teke lilitua kwenye kabati la nguo chumbani humo na kuivunja vipande vipande.

    Jacob alitoa kareti tatu mfululizo ambazo hata hivyo Don aliziona zote na kukwepa. Wakati Jacob anajiweka sawa Don alirusha ngumi iliyompata Jacob sawa sawa, wakati Jacob anataka kuanguka Don akamfuata ili ammalize, hapo akapokelewa kwa mapigo manne mfululizo ambayo yalimchanganya kabisa Don na kumfanya aangukie karibu na lilipokuwa dirisha. Jacob alimfuata Don kwa staili ya kunesa. Alipokuwa anamkaribia kufumba na kufumbua Don alikuwa ameshatoweka.

    Kwa namna ya ajabu sana Don alifanikiwa kupitia kwenye dirisha na kutokomea nje.

    “Shit” Jacob akasonya kwa hasira baada ya Dr. Don kutokomea nje. Kutoweka kwa Don katika mazingira yale, Jacob alijihisi kama Mwewe aliyeponyokwa na kifaranga cha kuku!

    Bastola ikiwa mkononi, Jacob alikagua chumba chote bila hata ya kuambulia chochote zaidi ya gazeti la The Business Times likiwa juu ya kitanda. Alitoka mle chumbani na kuelekea nje. Akiwa ndiyo kwanza ameufikia mlango wa kutokea nje sehemu ya mapokezi, kulisikika mlio wa sauti ya gari lililoondolewa kwa kasi. Akili yake ikajua kuwa mtu wake ndiyo alikuwa anatoroka. Hakukuwa na kingine kwa Jacob usiku huo zaidi ya kwenda kwake ili kujipumzisha ukizingatia kuwa hakuwa amepumzika vya kutosha tangu ametoka safari. Pia kesho yake asubuhi alitakiwa kwenda kuripoti ofisini kuwa tayari amesharudi toka safari.





    ******

    “Jacob” ilisikika sauti ya kike ikimwita wakati akikatiza katikati ya kiwanja cha mbele ya majengo ya ‘Ofisi Fukuzi’. Wakati huu alikuwa akitoka eneo alilokuwa ameegesha gari na alikuwa akielekea mlangoni. Kama kawaida alikuwa akipiga hatua zake ndefu za kikakamavu. Jacob Matata aligeuka na kuangalia ni nani aliyemwita.

    “Uzee huo unakupeleka pabaya yaani ndio unafika ofisini” hatimaye Jacob alisema mara baada ya kumwona aliyemwita.

    “Thubutu nifike saa hizi kwani ofisi za baba yangu hizi, au unadhani napenda wanangu wafukuzwe kwa kukosa karo pale nitakapofukuzwa kazi eeh? aliongea mama huyu ambaye alishindwa kuficha furaha yake kwa kumwona Jacob Matata asubuhi hii. Huyo hapo ofisini alijulikana sana kwa jina la mama Wambura.

    “Shikamoo mama” Jacob alimsalimia walipokuwa wamefikiana na kuanza kutembea pamoja kuelekea ndani ya ‘Ofisi Fukuzi’.

    “Marahaba umerudi lini? Nilikuwa nimeshakukumbuka sana” aliuliza mama Wambura huku akimwangalia Jacob usoni kama anayesoma kitu.

    “Jana majira ya saa tano hivi asubuhi” alijibu Jacob.

    “Ooh pole kwa safari na karibu sana. Vipi na hilo jicho linakuuma au ndio umepigwa ngumi? Mama Wambura alikaribisha huku akiachilia swali kuhitimisha uchambuzi wake usoni kwa Jacob. Ni kweli jicho la Jacob lilikuwa jekundu kuliko kawaida. Hii ilitokana na shughuli ya usiku kati yake na Dr. Don.

    “Aaah si unajua tena vya wazungu vina kizungu zungu, nilipokuwa kule nilivamia kwa pupa na matokeao yake ndio haya” Jacob aliongopa huku akiondoka pale walipokuwa wamesimama na mama Wambura.

    Ofisini hapo Jacob alipendwa karibuni na kila mtu. Japo kuna mengi yaliyopelekea hali hii, lakini yaliyowazi ni wasifu wake wa ndani ambao ni ucheshi, ujasiri, ushirikiano na wengine, na sifa zake katika kazi zilipelekea kila mtu kuvutiwa na moja kati ya sifa hizo. Bosi wake na Jacob ambaye ni Bi. Anita alimpenda Jacob kutokana na heshima aliyoiletea ‘Ofisi Fukuzi’ kwa kazi yake nzuri. Vijana wenzie walimpenda kwa vile alipenda kushirikiana nao na kuwapa mbinu mbalimbali za kazi, kwani wengi walipenda kujifunza toka kwake kutokana na mafanikio makubwa katika kazi yao hii ya upelelezi. Hakuwa mchoyo, alishirikiana nao hivyo walimpenda. Mabinti walimpenda kwa mambo mengi lakini mojawapo lililo wazi ni mvuto wa Jacob na sifa zake. Alijua kuishi nao nakushirikiana nao maisha, hakupenda wajisikie wapweke, alishirikiana nao vipawa.

    “Mambo Jacob? Sauti ya Kike ilimsabahi

    “Amanda!!!!!! Nilikumiss sweetie!!! Jacob alisemahuku akimkumbata Amanda

    “Daaaah tangu umeondoka nilikuwa sijakumbatiwa na mtu hapa ofisini mtu wangu!! Amanda alisema huku akimwangalia Jacob machoni.

    “Usijali nimerudi mwenyewe, mwenyewe ushindwe!! Jacob alisema

    “Je Regina wifi yangu hajambo?

    “Mzima wa afya, sikuwepo basi alikuwa hataki kuniachia asubuhi hii ndiyo maana nimechelewa hivi” Jacob alisema

    “Mwache mwaya ale vyake. Ila najua nami utanitoa walua week ijayo!! Amanda alisema

    “Kama wifi yako ataruhusu!! Jacob alisema huku akiminya lile jicho lake la kushoto.

    Baadaye alitembea kuelekea mlango mwingine ndani ya ofisi hizo

    “Shimaoo mkuu” Jacob alisalimia mara baada ya kuingia ofisini kwa mkurugenzi wa ‘Ofisi Fukuzi’ Bi. Anita.

    “Marahaba, karibu uketi” Bi Anita aliitikia huku macho yake yaking’aa kwa furaha.

    “Nimesikia kazi yako”

    “Ndiyo hivyo mkuu”

    “Hongera sana kwa kazi nzuri ambayo licha ya kukuletea sifa wewe binafsi, bali pia imeiletea Tanzania na Bara la Afrika sifa kubwa. Nimepokea taarifa juu ya kazi uliyotumwa kufanya huko mashariki ya kati. Mkuu wa kitengo cha upelelezi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amenitumia taarifa yako, amekumwagia sifa lukuki. Kwa kifupi hawakutegemea kama ungeweza kuifanya na kuimaliza kazi hiyo ngumu kwa muda mfupi kiasi hicho katika ufanisi “alisema Bi.Anita.

    “Asante sana ila sina budi kukushukuru wewe na ofisi yako, kwani ndio mmekuwa chachu ya mafanikio yangu siku zote. Taifa ni lazima lijivunie kuwa na watu kama wewe mkuu” sauti ya Jacob ilimaanisha kile alichokuwa akikisema.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Moja kati ya mambo ambayo humfanya Bi. Anita ampende sana Jacob ni nidhamu yake.

    “Nafikiri kwa kazi hii uliyofanya huko Israel na mashariki ya kati kwa ujumla unaweza kuwa miongoni wa wapelelezi bora kumi. Ngoja tusubiri takwimu yao ya ubora mwaka huu” Mara zote Bi. Anita amekuwa akijisikia fahari kwa ofisi yake kuwa na mtu kama Jacob Matata.

    “Nakupa mapumziko ya wili mbili wakati huo huo ukijiandaa kwa ile kazi ya faili namba ‘HASIDI’ ” alisema Bi. Anita huku akimruhusu Jacob Matata kutoka.

    Ilikuwa yapata saa nne na dakika ishirini na moja wakati mpelelezi Jacob Matata alipokuwa ndani ya gari tayari kwa kuondoka hapo ofisi fukuzi kuelekea nyumbani kwake kwa mapumziko.

    * * *



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog