Search This Blog

Monday 24 October 2022

MKIMBIZI - 2

 

    Simulizi : Mkimbizi

    Sehemu Ya Pili (2)







    Kelvin alikuwa amepanga chumba kimoja kilichoingiliana na bafu yaani master bedroom, na sebule, huko maeneo ya sinza. Aliingia chumbani kwake kutokea bafuni alipokuwa akioga,akiwa na bukta tu. Alikuwa ameinamisha kichwa chake akijifuta maji kwa taulo, na alipoinua kichwa alitoa mguno mkubwa wa mshituko, macho yakimtoka pima. Akarudi mbio kule bafuni, lakini aliteleza na kupiga mweleka. Aliinuka haraka na kubaki akiwa ameegemea ukuta huku akinitumbulia macho ya woga mkubwa kabisa.

    Aka!

    Nilipoingia nilipita moja kwa moja chumbani kama kawaida yangu, ambapo niliposikia maji yakimwagika bafuni, nikajua alikuwa anaoga. Nikaamua kumsubiri pale chumbani.

    Niliinuka haraka na kumsogelea.

    “Kelvin! Kelvin! It’s me...Tigga...” Nilimwambia huku nikizidi kumsogelea.

    “Tigga...?” Kelvin aliuliza kwa mshangao huku akinitazama kama kwamba hajawahi kuniona hata siku moja.

    ”Ni wewe? Mbona hivyo...?”

    “Ndiyo Kev...ni mimi...” Nilimjibu, halafu nikakumbuka jinsi nilivyojishindilia miwanja na nguo nilizovaa. Nilitoa kile kilemba nilichokuwa nimejifunga kichwani na rasta zangu zikamwagika kichwani kama zinavyotakiwa. Nikavua jaketi langu la mtumba na kubaki na lile gauni refu. Kelvin alinitazama na nikaona kuwa sasa amenitambua vizuri. Lakini bado alionekana kuwa na mashaka.

     Ni nini tena?

    “Oh! Tigga! Umerudi?” Alisema na kubaki akiwa amesimama pale pale alipokuwa huku akinitazama kwa namna ya ajabu. “U..umeingiaje...?”

    “Mlango ulikuwa wazi Kev, niligonga sikupata jibu...nikaingia.” Nilimjibu huku nikimtazama mchumba wangu kwa makini. Niliona kuwa hakuwa na furaha kuniona kama nilivyotarajia, na nikashindwa kuelewa ni kwa sababu gani.

    “Sasa...huo wanja...?” Aliuliza kwa mshangao. Nilijikuta nikitabasamu pamoja na matatizo yangu.

    “Oh! Huu? Ni hadithi ndefu Kev...naomba niingie bafuni kwanza.” Nilimwambia huku nikielekea kule alipokuwapo ambapo ndio bafuni. Kelvin alisogea pembeni kwa woga kunipisha, na alikuwa akinitazama kwa namna ya ajabu.

    Ni nini kinatokea hapa?

    Nilisita.Nilijikuta nikirudi na kuuchukua ule mfuko wangu wa nailoni uliokuwa na lile begi langu niliouacha juu ya kitanda na kwenda nao bafuni huku nami nikimtazama Kelvin kwa mshangao.

    Nilitumia muda mrefu kuliko kawaida yangu kule bafuni, na nilipotoka nilikuwa nikijisikia murua zaidi. Kelvin, akiwa ameshavaa suruali yake ya mazoezi na fulana mchinjo, alikuwa amesimama nyuma ya dirisha akimalizia kuongea na simu. Aligeuka nilipoingia na kuja kuketi kitandani, akiitupia simu yake pembeni yake pale kitandani na kunitazama. Kwa kawaida huwa naweka baadhi ya nguo zangu pale kwa Kelvin kwani mara kwa mara huwa tunalala wote pale kwake. Hivyo nilibadili nguo na kuvaa suruali yangu ya jeans na kiji-top changu chekundu kilichoishia juu kidogo ya kitovu, na juu yake nikamalizia na koti la jeans. Nilipojitazama kwenye kioo nilijiona kuwa kweli nilikuwa nimerudi kuwa Tigga Mumba ninayejijua na ambaye Kev, kama nilivyozoea kumwita kwa mkato, alimzoea.

    Lakini bado nilikuwa na wasiwasi mkubwa, sikuwa na amani kabisa. Na nilikuwa na wasiwasi kuwa baada ya mambo niliyoyaona na niliyoyafanya kule Manyoni, maisha yangu hayatakuwa kama zamani tena. Nilihisi joto sana. Niliiendea swichi ya kuwashia feni lililokuwa likining’inia darini mle ndani ili nipate upepo, lakini Kelvin alinishtua kwa kunipigia kelele.

    “No Tigga! Usiwashe!”

    Nilishituka! Niliruka nyuma na kusimama nikimkodolea macho Kelvin kwa mshangao.

    “Ni nini? Nataka kuwasha feni...”

    “Ina shoti hiyo Tigga. Yaani ukifyatua tu hiyo swichi, taa zote zinazimika nyumba nzima. Mpaka waje wapande juu ya dari huko sijui wachokonoe vitu gani ndio iwake.”

    “Ah! Umenishitua! Tangu lini?” Nilimuuliza huku bado moyo ukinienda mbio.

    “Leo ni ya nne. Yaani nyumba yote inakuwa kiza Tigga. Kuanzia huko kwa mwenye nyumba hadi huku kwangu. Na mpaka waje huku kwangu wapande huko juu wachokonoe ndio uwake.”

    Nilishusha pumzi na kubaki nikiwa nimesimama katikati ya kile chumba.

    Kelvin alinitazama kwa wasiwasi.

    “Tigga, uko...okay...mbona umekuja kiajabu ajabu?” Aliniuliza. Nilimtazama kwa muda mpenzi wangu yule.

    Kwani ni kitu gani tena mpenzi? Leo hakuna busu kama kawaida, hakuna kukumbatiana kama kawaida, hakuna kunisifia jinsi nilivyotoka bomba,angalau baada ya kutoka bafuni, kama kawaida yako...why?

    Lakini sikumuuliza maswali hayo yaliyopita kichwani mwangu, bali nilibaki nikimtazama tu. Nilitamani nimfuate pale kitandani alipokuwa ameketi nimkumbatie, nipate liwazo nililolihitaji sana wakati ule. Lakini sikufanya hivyo.Sikujua nianzie wapi. Niliketi kando yake pale kitandani na kumgeukia.

    “Kiajabu vipi Kev?”

    “Nguo ulizovaa...wanja...what’s happening? Umenitisha sana.”

    “Hukunitambua?”

    “Aah, hapana...ila, ndio... kwanza sikukutambua...” Alijibu na kunitazama, kisha akatazama pembeni.

    Hapana Kev, ulinitambua, ila uliniogopa sana tu. Kwa nini?

    “Mnh! Kelvin, nimekutwa na matatizo makubwa na ya kutisha...” Nilimwambia huku nikimtazama kwa makini.

    “Ni matatizo gani mpenzi...kwa jinsi ulivyokuja, ni dhahiri kuna tatizo. What happened?” Kelvin aliniuliza huku akinitazama kwa mashaka.

    Nikamuelezea mambo yote yaliyotokea kule msituni, na yaliyotokea kule kwa mkuu wa wilaya hadi jinsi nilivyofanikiwa kutoroka na kulazimika kusafiri mpaka Dar nikiwa nimejipaka wanja kishamba namna ile na nikiwa nimevaa nguo zilizokuwa bado zinanuka harufu ya mitumba na ambazo hazikuwa katika mtindo wangu wa mavazi kabisa.

    Nilimueleza kwa sababu nilikuwa nataka nipate mtu japo mmoja atakayeniamini. Kwa namna fulani hilo kwangu lilikuwa ni jambo la muhimu sana. Katika mazingira ya kawaida, Kelvin angekuwa ni mtu wa kwanza ambaye ningetegemea aniamini katika hili, ukitoa mama yangu na dada yangu. Lakini mazingira hayakuwa ya kawaida.

    Muda wote niliokuwa nikimuelezea matukio yale ambayo mimi niliamini kuwa ni ya kutisha na yaliyoweza kumtisha na kumshitua yeyote nitakayemsimulia, Kelvin alikuwa amejiinamia akichezea vidole vyake akitazama sakafu. Na baada ya kumaliza maelezo yangu, bado Kelvin alikuwa amejiinamia akichezea vidole vyake akitazama sakafu.

    “Pole sana Tigga...” Hatimaye aliinua uso wake na kuniambia, lakini bado alionekana kuwa alikuwa anaficha kitu fulani.

    Nilimtazama na kuitikia pole yake kwa kichwa huku nikiuma mdomo wangu kwa uchungu. Kelvin alikuwa ananificha kitu. Nilitazama pembeni. Kitu kikubwa kilichonishangaza ni kwamba hata nilipomueleza Kelvin kuwa nilikuwa nimepiga picha za video tukio la kuuawa kwa yule mtu asiye na jina kule msituni, bado hakuonesha udadisi wa kutaka kuona ushahidi ule. Kwa nini?

    Machozi yalianza kunitoka taratibu. Nilikimbilia kwa mkuu wa wilaya nikitegemea msaada, matokeo yake nikakutana na balaa jingine kubwa zaidi, kwani liliashiria kuwa huenda kuwa mimi ndiye niliyeua. Sasa nimekimbilia kwa mpenzi wangu...mchumba wangu, nikitegemea kueleweka na kuliwazwa na kupewa msaada wa mawazo jinsi ya kukabiliana na balaa hili.Lakini nako nakuta mazingira tofauti.

    Eeh! Mungu wangu...

    “That’s all you can say Kelvin?” Nilimuuliza kwa uchungu huku bado nikitazama pembeni, nikimaanisha kuwa baada ya kusikia mambo yaliyonikuta, hana la kusema zaidi ya kuniambia pole sana.

    Kelvin aliinuka na kuja kuchutama mbele yangu, akiweka mikono yake juu ya mapaja yangu. Niliinamisha kichwa changu na kumtazama.

    “Tigga my dear,najua ni vigumu sana kwako kuelewa, lakini...lakini...unahitaji msaada wa kitaalamu Tigga...” Aliniambia kwa upole.

    “Say Whaat!” Niliropoka kwa mshangao huku nikisimama na kumtazama Kelvin kama kwamba alikuwa kichaa.

    “Ndio Tigga, unahitaji matibabu...na kama unajali mapenzi na maisha yetu pamoja, nakuomba sana ukubali kupatiwa matibabu...” Kelvin aliniambia kwa upole huku akinitazama usoni.

    Hii ni kali zaidi!

    Uchungu niliousikia ulikuwa hauna kifani. Akili yangu ilikuwa kama iliyokufa ganzi. Nilimtazama Kelvin kwa mshangao, na sikuweza kummaliza.

    “Na wewe pia Kelvin? Yaani na wewe huniamini? Hata baada ya kusikia matatizo yaliyonipata bado unadiriki kuniambia kuwa nahitaji matibabu? Nitibiwe nini sasa Kelvin?” Nilimuuliza kwa jazba huku nikitiririkwa na machozi.

    “Tigga...”

    “Kelvin! Yaani...Kelvin! Unataka kuniambia kuwa unaamini mimi ni mgonjwa wa akili...? Kwamba nimewaua wenzangu wote kule msituni na...na...Ooh! My God! Hii haiwezekani, hii haiwezekani kabisa!” Nilishindwa kuendelea na maneno yangu yalinikwama kooni. Moyo uliniuma. Yaani ilikuwa kama kuna ndoana iliyounasa moyo wangu na ikiuvuta kwa nguvu. Nilimtazama yule mtu niliyempenda kwa moyo wangu wote kiasi cha kufunga naye uchumba, na nilishindwa kuelewa ni nini kimetokea.

    “Tigga jaribu kuelewa...naelewa kuwa kwako hili ni jambo gumu kulielewa, lakini...”

    “Unaweka mapenzi na maisha yetu pamoja at ransom Kelvin kwa ajili ya kutosheleza imani kuwa mimi nina wazimu kweli?” Nilimkatisha kwa uchungu, nikimaanisha kuwa anaweka mazingira ya maisha yetu pamoja kutegemeana na kukubali kwangu kufanyiwa hayo matibabu ya ugonjwa wa akili nisiokuwa nao.

    “Tigga...”

    “Unachoniambia Kelvin ni kuwa unaamini kwamba mimi, Tigga, mchumba wako, nina ugonjwa wa akili, sio?”

    “Tigga dear, ingawa hilo linaonekana ni jambo baya, lakini hilo ndio jambo pekee linaloleta maana, mchumba!”

    “Hah! Wait a minute Kelvin,” Nilimwambia na kumkazia macho huku nikishusha sauti na kumuuliza, “unataka kuniambia kuwa mimi kuwa mgonjwa wa akili ndio jambo linaloleta maana?”

    “Ndio Tigga! Otherwise haitaleta maana hata kidogo! Mambo uliyoyafanya huko Manyoni kwa mkuu wa wilaya...Tigga ninayemjua mimi hawezi kufanya mambo kama yale!” Kelvin alinijibu kwa jazba iliyochanganyika na wasiwasi.

    “Aakh! Pale nilikuwa under pressure Kelvin! Nilikuwa najaribu kuokoa maisha yangu!” Nilimjibu kwa jazba nikisisitiza kuwa nilifanya mambo yale kwa sababu nilikuwa kwenye shinikizo kubwa la kujaribu kuokoa maisha yangu.

    “And that is the problem Man! Paranoid Schizoprenia is all about uncontrolled pressures Tigga!” Kelvin alijibu kwa hamasa huku akisisitiza maneno yake kwa mikono, akimaanisha kuwa ule ugonjwa unaosemekana kuwa ninao unahusiana na kushindwa kudhibiti mashinikizo. Nilichoka! Kelvin alionekana kuamini kila alilokuwa akilisema. Kama jinsi yule mkuu wa wilaya alivyoonekana kuamini kila aliloelezwa na yule dokta wa uongo.

    ”We’ unajua nini kuhusu hiyo Paranoid Schizo...Schizo...shit Kelvin! You can’t be serious! Wale watu walikuwa wanasema mimi naitwa Sylvia-vitu gani-tu-sijui huko, halafu unaniambia nidhibiti mashinikizo!” Nilimfokea Kelvin kwa hasira. Alinitazama kwa huzuni, alijaribu kusema neno akaghairi. Alitupa mikono yake juu kwa kukata tamaa na kwenda kusimama nyuma ya dirisha. Alijishika kichwa kwa mikono yake yote miwili na kurudi tena hadi pale alipokuwa amesimama hapo mwanzo. Alinitazama, akataka kuongea tena akaghairi. Akaenda kuketi kwenye kochi moja na pekee lililokuwamo mle chumbani na kujiinamia akiwa amejishika kichwa.

    Nilimtazama kwa muda mrefu huku moyo ukiniuma sana.

    “Why do you believe them so, Kelvin?” Hatimaye nilimuuliza kwa sauti ya kunong’ona iliyojaa majonzi na kukata tamaa, kwa nini alikuwa akiwaamini wale watu waliozusha kuwa mimi ni mgonjwa wa akili kwa kiasi kile. Kelvin aliinua uso wake na kunitazama kwa muda.

    “You wanna know why?” Aliniuliza huku akiinuka na kwenda kwenye kabati la nguo na kutoa karatasi moja kutoka kwenye droo ndogo ya kabati lile. “This is why!” Aliniambia huku akinikabidhi ile karatasi. Nilimtazama kwa mshangao na kuipokea ile karatasi kwa mikono ya kutetemeka. Kelvin alirudi na kuketi kwenye lile kochi na kujiinamia kama alivyokuwa hapo mwanzo.

    Nilianza kuisoma ile karatasi.

    Akili ilinizunguka. Nilimtazama Kelvin kwa mshangao na kuisoma tena ile karatasi.

    Sasa huu ni mchezo!

    Ile karatasi ilikuwa ni ile ile niliyopewa na mkuu wa wilaya kule Manyoni. Ikiwa na kivuli cha sura yangu kwenye kona yake ya kulia, na yale maelezo ya uongo yaliyokuwa yakielezea jinsi nilivyokuwa mtu hatari kutokana na ule ugonjwa wa akili niliosingiziwa. Yaani ilikuwa ni karatasi ile ile isipokuwa kitu kimoja tu.

    Wakati ile karatasi niliyoiona kule kwa mkuu wa wilaya ilikuwa ikinitambulisha kwa jina la Sylvia-nani-sijui huko, hii niliyopewa na Kelvin hivi sasa ilikuwa ikinitambulisha kwa jina langu halisi, yaani Tigga Mumba!

    Hii ni nini sasa jamani...hawa jamaa wanataka kunichanganya akili yangu nini?

    Kwa kweli nilizidi kuchanganyikiwa. Sikuelewa kabisa ni nini maana ya jambo lile. Lakini nadhani lililonichanganya zaidi ni vipi ile karatasi ilifika kwa Kelvin. Kelvin anahusika vipi na sakata hili la ajabu. Nilipagawa kabisa!

    Nilimtazama Kelvin kwa muda bila ya kujua niseme nini, naye alikuwa akinitazama kama mtu aliyekuwa anasubiri kuona nitafanya nini baada ya kuisoma ile karatasi.

    “K-K-Ke-Kelvin, umeipata wapi hii karatasi?” Nilimuuliza kwa sauti ya kutetemeka. Badala ya kunijibu, Kelvin alibaki akinitazama tu. Nilizidi kuchanganyikiwa.

    “Kelvin, hii taarifa ndio niliyopewa kule kwa mkuu wa wilaya...lakini kule ilikuwa ikinitambulisha kwa jina Sylvia...where did you get this?” Nilimwambia na kumuuliza.

    “Hiyo ni nakala ya karatasi uliyooneshwa kule Manyoni Tigga. Walichosema ni kwamba baada ya kuoneshwa hiyo karatasi, ukaanza kupiga kelele na kudai kuwa wewe ni Sylvia Mwamkonda na sio Tigga Mumba, walipozidi kukusaili ndipo ulipojaribu kumteka mkuu wa wilaya Tigga...walipokushinda nguvu ndipo ulipotoroka na kukimbia...” Kelvin alinijibu huku akinitazama machoni. Nilipigwa na butwaa.

    “Walichosema? Ni kina nani hao waliosema hivyo Kelvin!

    “Polisi...na Dokta Lundi.”

    “Dokta Lundi! Dokta Martin Lundi? Alikuja hapa?”

    “Walikuja ofisini...kisha tukaja wote mpaka hapa, ndio wakanieleza mambo yaliyotokea huko...”

    “Wamekujuaje wewe...?” Nilimuuliza kwa mshangao na kuchanganyikiwa. Kelvin alibetua mabega yake. “Ile ni serikali Tigga...wana njia zao...” Aliniambia. Nilifumbua mdomo, sikujua nataka kusema nini, hivyo nikaufumba. Nilitembea kutoka kona moja ya chumba hadi nyingine na kurudi. Kisha nikakumbuka.

    Ni ile albamu waliyoiba kutoka kwenye mkoba wangu kule msituni!

    Mle ndani kulikuwa kuna picha nyingi tulizopiga pamoja na Kelvin, tukiwa katika mikao ya mapenzi na hata baadhi ya picha tulizopiga wakati wa sherehe yetu ya kufunga uchumba. Na kuna picha kadhaa ambapo Kelvin alikuwa amevaa fulana zilizokuwa na nembo ya kampuni aliyokuwa akifanyia kazi.

    Eh! Mungu wangu! Wamefika hadi huku! Kunitafuta mimi...ili waniue na mimi!

    “Li-lini...?” Niliinua uso wangu na kumuuliza Kelvin huku akili ikinizunguka.

    “Jana Dear...niliwabishia sana Tigga, lakini ushahidi wa maelezo waliyonipa...havipingiki.Ndio maana nakuomba ukubali kufanyiwa matibabu...kwa sababu yote uliyoyafanya si kosa lako...”

    “Sikufanya kitu chochote zaidi ya kuokoa maisha yangu Kelvin! Kwa nini hutaki kuniamini? Wale ni watu wabaya sana Kelvin...yaani wamekuja mpaka hapa halafu wewe bado unawaamini hata baada ya kukuambia kuwa nina ushahidi wa mkanda wa video wa tukio zima la kuuawa kwa yule mtu asiye na jina kule msituni!”
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa mujibu wa maelekezo ya Dokta Lundi, hivyo vyote vinaweza kuwa ni vitu unavyofikiria tu kichwani mwako Tigga, lakini havipo!...kitendo cha kujaribu kumteka nyara mkuu wa wilaya tu kinathibitisha jinsi unavyohitaji msaada wa kitabibu!” Kelvin alizidi kutetea hoja zile za uongo. Na ndio alizidi kunichanganya kabisa.

    “Huo ni uongo na uzushi mkubwa niliopata kuusikia maishani mwangu! Hakuna cha dokta Lundi wala nini...yule mtu ni muuaji, na nakushangaa kuwa unaweza kuamini utumbo kama huo,Kelvin. What’s the matter with you Kev?” Nilimuuliza kwa jazba huku nikimtazama kwa makini, lakini bado Kelvin alionekana kabisa kuwa alikuwa haniamini.

    Kwa hakika haya mambo sasa yalikuwa yanaelekea kunishinda. Ni nini hii? Haiwezekani!

    “Kelvin, ile karatasi niliyoiona Manyoni ilinitambulisha kuwa mimi ni Sylvia Mwamkonda, na ni wao ndio waliokuwa wakiniita mimi Sylvia, nami nikawa nasisitiza kuwa mimi ni Tigga na sio Sylvia! Sasa tena wewe unaniambia eti walikuambia kuwa ni mimi ndio nilikuwa nalikana jina la Tigga na kung’ang’ania jina la Sylvia? This is preposterous Kelvin!” Nilimwambia na hata pale nilipokuwa nikimwambia maneno yale, na jinsi nilivyousoma uso wake alipokuwa akinitazama, wazo lilinijia.

    Ndio maana aliponiona alishituka sana hadi akapiga mweleka! Sio kwa kuwa hakunitambua kutokana na wanja na mavazi niliyovaa, bali kwa hofu kuwa ameingiliwa na mwehu na muuaji...Mungu wangu!





    “Sawa bwana...naona kuwa umeamua kuwaamini hao watu...lakini nakuhakikishia kuwa hiyo karatasi waliyokuonesha imeghushiwa tu. Na ninashangaa kuwa huwezi kuelewa hilo” Nilimwambia kwa unyonge huku akilini nikijaribu kutafuta la kufanya baada ya kujitokeza kwa hali ile.Hata huyu mchumba wangu mwenyewe niliyemtegemea naye ametekwa na laghai za wale wauaji. Nilipiga mwayo. Nilijihisi mchovu na njaa iliniuma. Kelvin alinitazama kwa huruma.

    Sasa kama unanihurumia kwa nini huniamini? Kwa nini hutaki kunisaidia? Au ni kweli nina matatizo ya akili mimi?!

    “Sio hivyo tu Tigga, maelezo ya Dokta Lundi, hiyo karatasi, mambo uliyoyafanya kule kwa mkuu wa wilaya, pamoja na maelezo ya kwenye gazeti...”

    “Gazeti? Gazeti gani? Maelezo gani?” Nilimkatisha kwa jazba. Lakini Kelvin hakunijibu maswali yangu na badala yake aliendelea na maelezo yake.

    “...vyote hivyo vinanifanya nisiamini moja kwa moja kuwa huhitaji msaada wa kitabibu Tigga. Lakini kama huna matatizo hayo yanayosemwa kuwa unayo, njia pekee ya kuthibitisha hivyo ni kufanyiwa uchunguzi wa kitaalam ili kuthibitisha ukweli au uongo wa maelezo yao hayo.” Kelvin alisema.

    “Kitu ambacho hujui Kelvin ni kuwa hao watu sio madaktari, na kwamba hawanitaki kwa uchunguzi bali kwa kuniua ili kuficha ushahidi kuwa kuna mtu aliyewaona wakiua mtu msituni na baadaye kuwaangamiza wenzangu wote kule porini...mi’ siwezi kujipeleka kichwa kichwa tu katika mtego wao wakati nimeshaona mambo wanayoweza kuwafanyia binadamu wenzao bwana!”

    Kelvin aliinuka na kuchukua gazeti lililokuwa juu ya meza kando ya kitanda na kunitupia.

    “Hebu soma hilo gazeti Tigga, mi’ naenda kukuletea chakula, kwani naona kuwa una njaa.” Aliniambia na kuelekea jikoni, ambalo lilikuwa kando ya ile sebule yake. Nililichukua lile gazeti na kupekua kurasa zake haraka haraka nikitafuta habari inayoelekea kuhusiana na maelezo ya Kelvin huku moyo ukinienda mbio. Lilikuwa ni gazeti litokalo kila siku kwa lugha ya kiingereza ambalo katika ukurasa wake wa habari za ndani ya nchi (local news) kulikuwa kuna kichwa cha habari kilichosomeka “Massacre at an expedition site” (Mauaji ya kinyama katika eneo la utafiti)

    Habari iliyofuatia kichwa cha habari kile, ilielezea juu ya kuuawa kwa watafiti wa mambo ya kale wanne na wenyeji wawili katika msitu mmoja huko Manyoni. Iliendelea kuelezea dhumuni la utafiti ule na kuwaorodhesha waliouwa ambao ni wale wenzangu pamoja na majina ya wale wenyeji wawili waliotoka katika ofisi ya mkuu wa wilaya.

    Zaidi ya hapo ilielezea kuwa polisi ilikuwa ikimsaka mwanamke anayejulikana kwa jina la Tigga Mumba, ambaye alikuwa ni mmoja wa watafiti waliouawa na ambaye ametoweka kutoka eneo la utafiti na hajulikani aliko. Habari ilizidi kubainisha kuwa mwanamke huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili ujulikanao kama Paranoid Schizophrenia, ambao inaaminiwa kuwa huenda ndio uliompelekea kuwaua wenzake hao na kutoweka. Habari ile iliendelea kutoa maelezo marefu juu ya ugonjwa ule, huku ukielezea mambo ambayo mtu anayesumbuliwa na ugonjwa huo anaweza kuyafanya, ikiwemo kukana utambulisho wake na kujiamini kuwa ni mtu mwingine kabisa, kumuona kila mtu ni adui anayefaa kuuawa ili kuokoa wananchi wengine na kuamini vitu vingi vya kufikirika. Aidha habari ilendelea kuelezea juu ya tukio la mwanamke mmoja aliyejaribu kumteka nyara mkuu wa wilaya ya Manyoni siku hiyo hiyo ya tukio, na kudokeza kuwa inaaminika kuwa mwanamke huyo ndiye huyo aliyefanya mauaji ya kule msituni, ambaye mwandishi alimsema kuwa ni hatari sana na kuiasa jamii iwe macho na kutoa taarifa katika kituo chochote cha karibu cha polisi mahala popote atakapoonekana.

    Habari ilimalizia kwa kuainisha kuwa iwapo msichana huyo atapatikana na kuthibitika kuwa alikuwa ameathirika na ugonjwa huo wa akili atapatiwa matibabu katika hospitali ya wagonjwa wa akili na hatowajibika kwa matendo aliyofanya akiwa katika ugonjwa huo.

    Nilimaliza kusoma habari ile na kubaki nikiwa nimepigwa na butwaa.

    Ile habari ilikuwa ni uongo mtupu!

    Ilieleza kuwa watu waliouawa kule msituni walikuwa sita na kuwataja majina yao, kitu ambacho si kweli. Kwa uelewa wangu, watu waliouawa ni saba. Mbona hawakumtaja yule mtu asiye na jina? Lakini pia nilielewa ni kwa nini hata Kelvin aliamini maelezo yale, kwani ni wazi kuwa ile habari ilikuwa imeandikwa kwa nia ya kunichafulia kabisa jina na muonekano wangu mbele ya jamii, hasa kwa watu wanaonifahamu na ambao wangeweza kunisikiliza na kuamini upande wa maelezo yangu juu ya mambo niliyoyaona kule porini.

    Kile kipande cha mwisho cha habari ile ndio hasa kilikuwa kikionesha ni jinsi gani habari ile ilivyokuwa ya kupikwa na kupotosha.

    Eti nikigundulika kuwa ni mgonjwa wa akili sitawajibika kwa matendo yangu! (niliguna). Yaani wanachodhani ni kwamba nitajisalimisha mwenyewe na kudai kuwa ni mgonjwa wa akili ili nisiwajibishwe! (nilisonya). Wana wazimu kweli kweli!

    Niliirudia tena ile habari na kuangalia jina la mwandishi wa habari ile.

    Na mwandishi wetu.

    Nilitabasamu kwa huzuni na kutikisa kichwa. Na mwandishi wetu. Nani? Hakuna jina!

    Mungu wangu! Hawa watu wana uwezo namna gani! Yaani wameweza hata kueneza wayatakayo kupitia kwenye gazeti muhimu kama hili!

    Sasa tayari wameshamteka mawazo Kelvin, sijui nitakimbilia kwa nani tena!

    Niliwafikiria mama yangu na dada yangu. Sijui na wao wameshatembelewa na Dokta Lundi? Lakini nilikuwa na imani kuwa hawatamuamini hata kidogo. Nilichukua simu ya Kelvin huku nikisikia mabakuli yakigongana kule jikoni na kuanza kutafuta namba ya mama yangu ambayo nilijua kuwa ilikuwa imehifadhiwa kwenye kumbukumbu za simu ya Kelvin. Ilikuwa ni simu aina ya Nokia ambayo sikuwa na mazoea nayo kwani simu yangu ilikuwa ni aina ya Sony. Nilibonyeza kitufe nilichodhani kitanifikisha kwenye kumbukumbu za namba za simu za watu mbalimbali zilizohifadhiwa kwenye simu ile.

    Call register.

    Siyo hapa! Nilibonyeza tena.

    Missed Calls.

    Akh! Siyo hapa. Nilibonyeza tena ili nirudi kwenye sehemu iliyoonesha namba za simu.

    Received Calls.

    Nilibonyeza tena, bado nikihangaika kurudi kwenye sehemu iliyoonesha namba za simu.

    Dialled Numbers.

    Bado tu! Niliamua kubadilisha kitufe, na kubonyeza kingine. Moyo ulinilipuka na nikazidi kuchanganyikiwa. Kwenye ile simu kulitokea maneno:

    Dialled 1

    Kisha chini yake kulitokea namba ya simu.

    Ilikuwa ni namba ya simu yangu.

    Ilimaanisha kuwa simu ya Kelvin ilitumika kunipigia simu kwenye namba yangu.

    Nilikunja uso kwa kutoelewa. Nilibonyeza sehemu iliyosema Options, halafu nikabonyeza sehemu iliyosema Time of Call. Kwenye simu ilitokea tarehe ilipopigwa ile simu na muda ilipopigwa.

    Ilikuwa ni siku ile ile.

    Na muda ilipopigwa simu ile ulikuwa ni katika wakati ule mimi nilipokuwa bafuni!

    What is this?

    Sikuwa na shaka kuwa simu yangu ilikuwa imechukuliwa na wale wauaji. Sasa vije Kelvin apige namba yangu wakati ule mimi nikiwa naoga bafuni kwake?

    Nikabonyeza kitufe kilichosema Back, na kurudi tena pale ilipokuwa inaonekana namba yangu kama ni namba iliyopigwa na ile simu ya Kelvin.

    Kwa kidole kinachotetemeka kikabonyeza kitufe kinachoashiria kupiga simu na kupeleka simu ile sikioni mwangu taratibu.

    Ilikuwa inaita.

    Nilisikiliza huku moyo ukinipiga sana, na nilikuwa nataka kuikata wakati niliposikia ile simu ikipokelewa upande wa pili!

    “It’s Okay Kelvin, tunakuja. Endelea kumkawiza hapo hapo...” Sauti ya kiume iliyopokea simu yangu iliongea.

    Ilikuwa ni sauti ya Dokta Martin Lundi.

    Nilihisi chumba kikisogea nami nikapepesuka kwa kizunguzungu cha ghafla. Nilijibwaga kitandani na kubaki nikiwa nimekaa nikiikodolea macho ile simu.

    Niliishiwa nguvu kabisa na mwili ulinifa ganzi. Nilielewa ni nini maana ya jambo lile lakini bado iliniwia vigumu sana kuamini.

    Ah! Yaani kumbe muda ule nilipotoka bafuni na kumkuta Kelvin akimalizia kuongea na simu alikuwa akimpigia Martin Lundi aliyekuwa anatumia simu yangu!

    Na wakati huo huo Kelvin aliingia mle chumbani akisukuma kijitoroli cha kuandalia chakula kikiwa na boksi la Kellog’s Corn Flakes, bakuli la kulia pamoja na kijiko na glasi ya maziwa. Ule ulikuwa ni mlo nilioupenda sana na nadhani ndio maana Kelvin aliamua kuniandalia. Niliirudisha pale kitandani ile simu taratibu huku nikimtazama usoni yule mwanamume niliyempenda kwa kiasi kikubwa kabisa.

    Why Kelvin?

    “Kula flakes kwanza, mchumba, halafu ukiona unahitaji kula zaidi itabidi tutoke tukapate mlo wa maana hoteli.” Aliniambia huku akinitupia lile tabasamu lake nililolipenda sana na kuniita kwa jina alilopenda kulitumia akitaka kuonesha upendo.

    Mchumba.

    Nilibaki nikimtazama huku akili ikinizunguka vibaya sana. Yaani nimeacha kwenda kwa mama yangu nimekuja kwake, kumbe yeye...

    Siyo siri, iliniuma sana.

    Mara nilijisikia nimeshiba na hamu yote ya kula ikaniisha. Niliinuka na kusimama nikimtazama Kelvin kwa kutoamini, yeye akijishughulisha kunichanganyia maziwa na zile corn flakes. Na nilipokuwa nikimuangalia nilijikuta nikipandwa na ghadhabu za hali ya juu na midomo ikaanza kunitetemeka. Machozi yalianza kunitiririka bila ya kupenda.

    Inanibidi niondoke haraka kabla sijafanya jambo la kijinga!

    Kelvin alinigeukia na kutaka kusema kitu, bila shaka kunialika ule mlo aliouandaa, lakini alikunja uso kwa mshangao na wasiwasi baada ya kuniona nikimtazama huku nikitiririkwa na machozi.

    “Honey? Mbona unalia...kuna nini tena?” Aliniuliza huku akinisogelea na akionesha kujali kwa hali ya juu. Alijaribu kunishika na kunivutia kwake kuniliwaza na hapo ndipo alipozidi kunikera.

    “Usiniguse Kelvin! Niache!” Nilimfokea kwa hasira. Kelvin alishituka na kushangaa kupita kiasi. Aliruka hatua chache nyuma na kunitazama kwa mshangao, na sura yake ilionesha hofu kubwa, kama jinsi ilivyokuwa pale aliponiona kwa mara ya kwanza mle ndani alipokuwa akitoka bafuni.

    “Tti-Ti-Tigga...ni nini...?” Aliuliza huku akizidi kunitazama kwa mshangao. Sikuweza kumjibu. Nilibaki nikimtazama kwa fadhaa na hasira. Nilichomoa pete ya uchumba iliyokuwa kidoleni kwangu na kumnyooshea mkono wangu ukiwa umekunja ngumi, ile pete ikiwa ndani yake. Kelvin alipokea mkono ule huku bado akiwa na mshangao mkubwa.

    “Ni nini kwani...” Aliuliza huku akifungua kiganja chake na alipoiona ile pete aliinua uso na kunitazama akionekana kuwa hakuelewa kabisa ni nini maana ya tendo lile.

    “Khah! Tigga! Ni vipi...” Aliuliza kwa kuchanganyikiwa.

    “Naondoka Kelvin. Na sitakuwa na haja tena na hiyo pete yako!” Nilimwambia huku nikiuendea ule mfuko wangu wa nailoni. Kelvin alinizuia kwa kunishika mabega na kunigeuza ili tutazamane. “What’s the meaning of this, Tigga?” Alinifokea kwa kimombo akimaanisha kuwa anataka nimueleweshe maana ya kitendo kile. Nilimsukuma kwa nguvu na kumkemea kwa ukali.

    “It means uchumba umekwisha Kelvin, that’s what it means!”

    Alinitazama kwa mshangao mkubwa sana, na hata pale alipokuwa akinitazama, niliweza kuona kuwa kwa hakika sasa nilimthibitishia kuwa nilikuwa mwehu. Paranoid Schizophrenia.

    Potelea mbali!

    “Ah! Tigga, lakini...kwa nini?”

    “Usipoteze muda wangu Kelvin...kwani we’ uko tayari kuoa kichaa?” Nilimuuliza huku nikiuchukua ule mfuko wangu wa nailoni na kutoa ule mkoba wangu uliokuwa ndani yake.

    “Tigga, hebu kaa basi tuongee...huwezi kuvunja uchumba kienyeji namna hii...”

    “Nimeshauvunja Kelvin na niache niende zangu!” Nilimjibu huku nikivaa viatu vyangu vya kamba.

    “Hapana Tigga, huwezi kuondoka saa hizi...hebu ngoja tuelewane.”Aliniambia kwa sauti ya kitetemeshi. Nilimtazama kwa muda, kisha nikachukua mkoba wangu na kuelekea bafuni huku nikimwambia, “Unataka kunikawiza ili rafiki yako Martin Lundi anikute kama alivyokuagiza Kelvin?”

    Kauli hii ilimchanganya vibaya sana. Alinitazama kama kwamba ndio kwanza ananiona. Alijaribu kufungua kinywa akakosa la kusema. Akatupa mikono juu kwa kukosa la kufanya.

    “U-Unasemaje? Kwa nini unasema hivyo...”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilisimama nje ya mlango wa kuingia bafuni na kumtazama kwa muda. Nilisikia uchungu sana kuona kuwa bado alikuwa anajaribu kunidanganya.

    “Umeingiwa na nini Kelvin? Kwa taarifa yako najua kuwa ulimpigia simu Martin Lundi wakati niko bafuni, kwa kutumia simu yangu. Na najua kuwa hivi sasa yuko njiani kuja hapa kunikamata na hatimaye kuniua!” Nilimjibu kwa hasira huku nikimtazama moja kwa moja usoni. Jamaa alihamanika vibaya sana. Kwa hakika aliona kuwa uongo wake umegundulika. Tulitazamana kwa muda, kabla sijamuuliza kwa uchungu.

    “Kwa nini lakini Kelvin?”

    “Nimefanya hivyo kwa faida yako Tigga! Niamini tafadhali!” Alinijibu huku akiniangalia kwa kuomboleza.Nilimtazama kwa dharau na kebehi.

    “Kwa faida yangu?”

    “Ndio Tigga...unahitaji matibabu Tigga, na Dokta Lundi ana nia ya kukutibu mpenzi...”

    “Wakati nimeshakuambia kuwa huyo Dokta Lundi wako ni muongo na muuaji Kelvin? Na wakati nimekuambia kuwa nina ushahidi wa mkanda wa video unaoonesha jinsi alivyoshirikiana na wenzake kumuua mtu kule msituni, na sina shaka kabisa kuwa ndio waliowaua watafiti wenzangu kule porini Kelvin? Eti kwa faida yangu! Unan’chekesha!”

    Nilimkemea kwa hasira. Kelvin alikosa la kusema. Alinitazama kwa kukata tamaa na kuchanganyikiwa, asijue la kusema. Niligeuka kuelekea kule bafuni, lakini Kelvin alinisemesha.

    “Sasa ndio unavunja uchumba Tigga kweli?”

    Nilimgeukia na kutazama kwa dharau ambayo sijawahi kudhani kuwa ningepata kuionesha kwake maishani mwangu.

    “Umesaliti upendo wangu na umesaliti imani yangu kwako Kelvin. Umeamua kumuamini dokta Lundi muongo hata baada ya kusikia maelezo yangu, Kelvin. Na sasa umeshayaweka maisha yangu hatarini kwa upuuzi wako!” Nilimjibu na kugeuka haraka kuingia kule bafuni.

    “Lakini Tigga...”

    “Mimi naondoka Kelvin!” Nilimpigia kelele bila ya kugeuka wakati nikiingia kule bafuni.

    “Ni kweli kabisa Tigga...lakini utaondoka na mimi!”

    Mwili ulinifa ganzi na nilisimama ghafla, kwani ile ilikuwa ni sauti ya dokta Martin Lundi.

    Nilitoka mbio kule bafuni na kurudi pale chumbani kwa Kelvin.

    Dokta Martin Lundi muongo alikuwa amesimama ndani ya chumba kile akiwa na wafuasi wake wengine wawili, tofauti na wale aliokuwa nao kule Manyoni siku mbili zilizopita. Ingawa alikuwa amevaa nguo tofauti, bado juu ya nguo zile alikuwa amevaa lile koti lake refu jeupe lililomfanya aonekane tabibu.

    “Hallow Tigga...” Alinisemesha huku akitabasamu na akinitazama kwa makini. Sikuwa na la kusema. Nilimeza funda kubwa la mate na kutembeza macho yangu mle ndani. Nilikuwa nimenasa. Hakukuwa na namna yoyote ya kutoroka kutoka mle ndani.



     Nilimtazama Kelvin.

    “Ah! Dokta Lundi..umefika hatimaye...” Alisema kumuambia yule mtu aliyejiita Dokta Martin Lundi. Badala ya kumjibu, Dokta Martin Lundi alinikazia macho yake ya kuogofya na kuniuliza.

    “Oke Tigga, ni ushahidi gani huo unaodai kuwa unao?”

    Nilibaki nikimkodolea macho kwa mshangao. Nikamtazama Kelvin, naye alionekana kushangaa tu. Alimtazama yule muuaji aliyeamini kuwa ni tabibu, kisha akanitazama, akamtazama tena yule muuaji.

    “Eeh...dokta, sijui mnatarajia kufanyia wapi hayo matibabu...” Kelvin alimuuliza Martin Lundi muongo kwa mashaka kidogo.

    “Huyo sio daktari Kelvin! Ni muuaji huyo!” Nilibwatuka kwa hasira. Dokta Lundi alitoa tabasamu lake baya kabla ya kusema, “Tigga, Tigga, Tigga...usiwe na wasiwasi, nitakupatia dawa sasa hivi na utajisikia vizuri tu...”

    Ingawa nilikuwa nimejawa na woga usio kifani, nilijikuta nikimbetulia midomo kwa kukereka na kumtupia swali.

    “Kwa hiyo sasa nimekuwa Tigga na sio Sylvia tena, eenh? Hivi unadhani unamlaghai nani hapa wewe?”

    Yule dokta laghai alijitia kutikisa kichwa kwa huzuni huku akinitazama kwa makini. Kelvin alionekana kutoelewa afanye nini. Dokta Lundi alinisogelea taratibu huku wale watu wake wawili wakijizatiti mlangoni ili nisijaribu kutimua mabio. Na kwa hakika nilikua nimekwama. Nilijilazimisha kufikiria jinsi ya kujiokoa sikupata jibu. Niliufikiria ule mkanda wa video na nikajihisi kizunguzungu. Ikiwa watafanikiwa kunipokonya ule ushahidi, basi nimekwisha.

    “Mnh! Paranoid Schizo...” Dokta Lundi alianza kusema uongo wake huku akinisogelea lakini sikumpa nafasi.

    “Toka na uzushi wako hapa! Hakuna cha Paranoid Schizo-nini wala nini hapa! Uongo mtupu! Na wewe unajua hilo! Mimi ni mtu na akili zangu na nimewaona mkiua mtu, na najua kuwa ndio mliowaua wenzangu kule msituni...sasa mnanitaka na mimi kwa kujitia eti madaktari, kwenda zako huko!” Nilimbwatukia kwa kelele huku nikirudi nyuma.

    Dokta Lundi alighadhibika na kunitolea macho. “We’ Tigga...” Alianza kunikemea, lakini nilimkatisha tena.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Utawadanganya hao hao lakini sio mimi...kaa mbali nami!” Nilimwambia huku nikimwoneshea Kelvin aliyekuwa akizidi kushangaa. Sijui ilikuwaje hata nikapendana na jitu bwege kama hili!

    “Tigga ana ushahidi kuwa mliua mtu Dokta...nadhani labda tungehakikisha juu ya hilo kabla hamjamchukua...” Kelvin aliropoka kwa kitetemeshi.

    “Sawa kabisa Kelvin...Tigga, hebu tuoneshe huo ushahidi wako!” Dokta Lundi aliniambia huku akizidi kunisogelea na uso wake ukionesha mashaka, kama kwamba anajishauri iwapo aamini kuwa inawezekana nikawa kweli na kitu kama hicho au la. Nilitazama huku na huko sikuona pa kukimbilia.

    “Ah! Tangu lini mwehu...Paranoid Schizo-nini sijui huko, akawa na ushahidi wa kumtia wasiwasi mtu mwenye akili timamu kama wewe dokta? Mi’ si mwehu bwana? Then why are you so worried about my evidence, eenh?” Nilimuuliza huku nikizidi kurudi nyuma, nikimaanisha kwa nini ushahidi wangu uwatie hofu wakati wanajua kabisa kuwa mimi ni mwehu. Niligota ukutani. Dokta Lundi alitoa amri na kwa hatua moja kubwa mmoja wa wale vibaraka wake alinirukia pale nilipokuwa. Nilipiga yowe huku nikiruka pembeni lakini yule jamaa alikuwa mwepesi. Alinidaka na kunikamata mikono yangu kwa nguvu. Nilimpiga teke la ugoko, akaguna kwa maumivu na kulegeza mikono yangu. Nikamchapa kofi la uso. Kelvin aliropoka neno, Dokta Lundi akamfokea. Yule jamaa alinichapa kofi kali sana la uso lililonipeleka chali kitandani kwa Kelvin na kunigaragaza mpaka upande wa pili wa kitanda, huku mkoba wangu ukianguka sakafuni.

    Nilijiinua huku nikisikia kizunguzungu kutoka nyuma ya kitanda na kujikuta nikikamatwa kwa nguvu na wale wasaidizi wa Martin Lundi ambao waliniinua mzima mzima na kunikalisha kwenye kochi lililokuwa mle ndani. Nilihisi mchirizi wa damu ukinichuruzika kutoka puani kutokana na kofi lile. Nilitoa ulimi wangu kuramba eneo nililohisi kuwa lina damu juu ya mdomo wangu na nikahisi ladha ya chumvi-chumvi.

    “Heey! Sasa mbona mnampiga? Hivi ndivyo mnavyo wahudumia wagonjwa nyie!” Kelvin aliwafokea wale watu na kumtazama Dokta Lundi ambaye alikuwa akinitazama kwa hasira bila ya kusema neno.

    “Dokta! Ongea na watu wako! Hawawezi kumfanya hivi mchumba wangu hata kama ni mgonjwa wa akili...”

    “Mimi sio mchumba wako Kelvin, na wala sio mgonjwa! Haya ndio uliyoyataka, sasa unalalama nini? Kwa nini hukutaka kuniamini tangu mwanzo...”

    “Kelele!” Dokta Lundi alifoka.

    “Ebbo! Yaani mnakuja kunitolea amri nyumbani kwangu? Haiwe....” Kelvin alianza kumaka, lakini Dokta Lundi alimchapa kofi la uso lililompeleka mpaka ukutani.

    “Shut Up!”

    Na hapo hapo mmoja wa wale wasidizi wa Martin Lundi alimrukia na kumkamata mikono kwa nyuma. Ikawa sote tumeshikwa na wale wasaidizi wa Martin Lundi.

    Nilimtazama Kelvin kwa kukata tamaa. Alibaki akitembeza macho huku na huko asijue afanye nini.

    “Unasema ulituona tukiua mtu?” Martin Lundi aliniuliza nikiwa nimebanwa na yule msaidizi wake pale kwenye kiti. Sikumjibu. Alinipiga kofi la shavu lililotia vimulimuli machoni mwangu. Kelvin aliropoka kitu, lakini sikuelewa ni kitu gani. Nilimtazama yule muuaji kwa ghadhabu.

    “Ndio, nimewaona! Wewe pamoja na mwenzako mwenye mguu mbovu na mwingine mwenye macho kama nyoka! Mlikuja na helikopta na wewe ndio ulikuwa ukiendesha, uongo?” Nilimtemea yale maneno kwa hasira. Jamaa alinitazama bila ya kusema neno lakini niliona kuwa uso wake ulibadilika na aliamini kuwa nilikuwa nasema kweli.

    “Uongo?” Nilimuuliza tena. Nilipigwa kofi jingine kali la uso lililotawanya maumivu makali usoni mwangu, na nililia kwa uchungu.Lakini sikukata tamaa.

    “Kwa nini mlimuua yule mtu Lundi? Au na yeye alikataa kukubali kuwa ni mgonjwa wa akili kama mimi?” Nilizidi kumkemea kwa hasira yule muuaji muongo.

    “Hah! Ni kweli hayo maneno Dokta?” Kelvin aliropoka kutoka kule alipokuwa ameshikiliwa na yule kibaraka mwingine. Dokta Lundi alimwendea kwa kasi na kumtamdika ngumi ya uso huku akimkemea.

    “Hebu Nyamaza wewe!”

    Alinirudia pale nilipokuwa nimeshikiliwa kwenye kiti na kuniuliza. “Na unasema kuwa una ushahidi wa tukio hilo?”

    “Kwa hiyo ni kweli?” Kelvin aliuliza kwa kihoro huku akimkodolea macho yule daktari bandia, damu ikimchuruzika kutoka kwenye kona ya mdomo wake.

    “Nina ushahidi wa mkanda wa video!” Nilimtemea tena maneno kwa hasira huku nikimsogezea uso wangu kwa kumsuta. Hapo hapo alibamiza kofi jingine kali la uso na kunidaka koo kabla sijataharuki. Kelvin alijikurupusha kutoka kule alipokuwa ameshikwa lakini niliona kuwa yule mtu aliyemshika alikuwa amemzidi nguvu. Alianza kupiga kelele lakini haraka jamaa alimbana koo na kumzuia kupiga kelele.

    “Nautaka huo ushahidi sasa hivi!” Dokta Lundi muongo aliniambia kwa hasira. Nilimtazama kwa kiburi bila ya kusema neno. Alizidi kunitazama kwa ghadhabu.

    “Au unadanganya wewe? Huna cha ushahidi wala nini...!” Aliniambia huku bado akiwa amenikaba.

    “Mimi sio muongo kama wewe! Lakini kwa kukuridhisha tu, tufanye ninakudanganya na wala sijawaona mkishuhudia wakati bastola ya macho ya nyoka ilipoutoa uhai wa yule mtu kule msituni, na wala sina ushahidi wowote!” Nilimjibu. Dokta Martin Lundi alichanganyikiwa kwa jibu hili. Alinitazama halafu akamgeukia Kelvin, kisha akanitazama tena.

    “We’ unao ushahidi, uko wapi?” Alisema na kuniuliza kwa jazba. Nilimchekea mbele ya uso wake bila ya kumjibu. Yule kibaraka wake alinibamiza kofi la kichwa, na hapo hapo Dokta Lundi aliniinua na kunibamiza ukutani huku akiwa bado amenikaba koo.

    “Tuoneshe huo mkanda sasa hivi!” Alinifokea. Sikumjibu. Alimuamrisha yule msaidizi wake anikamate, naye akaunyakua ule mkoba wangu na kumimina vitu vyote vilivyokuwa ndani yake juu ya kitanda. Aliiona ile video kamera ya Gil. Aliokota kile kisu kidogo nilichonunua kwenye treni na kukitazama, kisha akanitazama.

    “Unatembea na visu mwanamke? Kwa hakika wewe ni muuaji!” Alisema kwa kebehi. Kisha aliichukua ile kamera na kuanza kuitazama taratibu, akiigeuza huku na huko. Moyo ulikuwa ukinidunda vibaya sana na watu wote mle ndani walibaki kimya. Nilimtazama Kelvin na nikaona kuwa alikuwa akiikodolea macho ile kamera kama kwamba ilikuwa ndio tegemeo pekee la kuokoa maisha yake. Muda huu yule jamaa aliyekuwa amemkaba alikuwa amelegeza kabali, naye akaropoka.

    “Kumbe ni kweli...!”

    Akili ilikuwa ikinitembea haraka sana. Niliangaza mle ndani nikitazama uwezekano wa kujiokoa. Ulikuwa mdogo sana.

    Mtu aliyejiita Dokta Martin Lundi alifungua sehemu ya kuingizia mkanda kwenye ile kamera na kutazama ndani yake, na wote mle ndani wakawa wanamtazama yeye.

    Hamna mkanda!

    Aliinua uso wake kwa ghadhabu na kunitazama.

    “Hamna mkanda wa video humu!” Aliniambia kwa ghadhabu.

    “Ulitegemea nini Dokta Martin Lundi?” Nilimuuliza kwa kejeli.

    “Kwa hiyo hamna ushahidi wa mkanda?” Aliniuliza.

    “Sijui, we’ si ndio dokta bwana! Unajua kila kitu. Hadi umeweza kujua kuwa mimi ni mwehu bila hata ya mi’ mwenyewe kujua...” Nilitoa majibu ya kejeli huku akilini nikitafuta namna ya kujiokoa.

    Dokta Lundi alipekua kwenye rundo la vitu vilivyotoka kwenye mkoba wangu akitafuta mkanda wa video asiupate. Alitoa bastola na kunigeukia kwa ghadhabu. Kelvin aliguna kwa woga baada ya kuona ile bastola.

    “Where is the tape?” Aliniuliza kwa hasira. Nilijua pale nikizidisha jeuri yule mtu angeweza kuniua kweli. Njia pekee ilikuwa ni kuendelea kumfanya yeye ahitaji ule mkanda kutoka kwangu.

    “Mkanda ninao na nimeuficha...” Nilipigwa kofi jingine na kujipigiza kisogo changu ukutani. Yowe la uchungu lilinitoka.

    “Umeuficha wapi mwanamke?”

    “Nimeukabidhi kwa wakili, akiwa na melekezo kuwa auwakilishe kwenye vyombo vya dola na vituo vya televisheni iwapo nitashindwa kuwasiliana naye kwa siku mbili mfululizo, au nitakapofikwa na umauti kwa namna yoyote ile.” Nilimjibu kwa kujiamini huku nikimtazama usoni.

    Jamaa alichanganyikiwa.

    “Muongo mkubwa! Where is the tape?” Alibwata akisisitiza nimwambie ni wapi ulipo ule mkanda wa video huku akiniwekea bastola yake kwenye paji la uso.

    “Mimi sio muongo kama wewe! Huo ndio ukweli, kama huamini basi...fanya utakalo!”

    “N’takuua wewe!”

    “Kwani hiyo si ndio kazi yako? Nimeshuhudia kwa macho yangu kule porini, na wakili wangu ameshuhudia hilo kupitia kwenye ule mkanda wa video niliomkabidhi.”

    Kelvin alicharuka.

    “Kumbe nyie ni wauaji! Niacheni! Niacheni!” Alijikurukupusha na kumsukuma yule mtu aliyemkamata. Jamaa alipambana naye kwa muda na kufanikiwa kumbwaga chini na kumbana sakafuni.

    “Hapana. Huo mkanda uko humu humu ndani...” Martin Lundi alisema, na kumgeukia yule kibaraka aliyekuwa amenishika mimi, ”...hebu pekua humu ndani mpaka uupate!” Aliamrisha. Kiza kilikuwa kimeanza kuingia, na yule jamaa aliwasha taa za mle ndani na kuanza kupekua. Alipekua kila mahali huku Kelvin akilalamika akiwa amebanwa sakafuni jinsi vitu vyake vilivyokuwa vikitupwa tupwa hovyo mle ndani. Jamaa alipekua kila mahali. Kabati lilichambuliwa hovyo hovyo, chini ya kitanda, bafuni, akatoka na kuingia jikoni, sebuleni.

    Alirudi bila mafanikio.

    “Mkanda uko wapi we’ binti?” Aliuliza Martin Lundi.

    “Kama nilivyokuambia. Kwa wakili wangu.”

    Alitikisa kichwa kwa masikitiko.

    “Twende kwa wakili wako!” Aliniamrisha.

    “Mnh! We’ unadhani mi’ mwehu kama unavyonipakazia?Itabidi uniue kwanza ndio nikupeleke huko kwa wakili wangu, na ukiniua taarifa zitatapakaa kwenye vyombo vya habari kama mvua!”

    Alinipiga kofi kali la mdomo. Na wakati huo huo Kelvin alipata upenyo, kwani alimtupa pembeni yule jamaa aliyekuwa amembana pale chini na kusimama. Jamaa alijitahidi kumkamata tena lakini Kelvin alimwahi na kumsukumia teke la kifuani lililomtupa ukutani. Kisha akamrukia Dokta Lundi huku akipiga kelele za ghadhabu. Dokta Lundi aligeuka akitanguliza bastola yake, nami niliruka pembeni na kufyatua ile swichi ya kuwashia feni.

    Mlio wa bastola ulivuma ndani ya kile chumba na kiza kikatawala ghafla kikiambatana na yowe la uchungu kutoka kwa Kelvin. Nilijitupa sakafuni na kujibiringishia chini ya kitanda wakati wale wauaji wakipiga kelele za kuchanganyikiwa.

    “Washa taa!” Dokta Lundi alibwata, lakini mmoja wa watu wake alipiga kelele kuwa ni kiza nyumba yote.

    “Pumbavu! Yuko wapi mwanamke!”

    Nilisikia Kelvin alikilia kwa maumivu na nikaingiwa na woga mkubwa. Bila shaka alikuwa amejeruhiwa na bastola ya Dokta Lundi.

    Oh! Mungu, Ni mabalaa mpaka lini sasa?

    Na mara nilisikia kelele kutokea kule nje.

    “Kelvin! Kelvin! Fungua! Sasa mbona umefyatua hiyo swichi tena?”

    Ilikuwa ni sauti kutokea nje ya nyumba! Ndio kitu nilichokuwa nakitarajia. Nikiwa nimejilaza chini ya uvungu nilinyamaza kimya nikisikiliza. Ilikuwa ni heka heka mle ndani wakati wale wauaji wakikimbia hovyo huku na kule.

    “Twendeni! Kuna watu wanakuja...Shit!”

    “Sasa huyu mwanamke?”

    “Tutampata tu...Let’s Go!”

    Nilisikia vishindo vyao vikitoka nje ya chumba, na huko sebuleni nilisikia kelele nyingine, bila shaka walikutana na watu waliokuwa wanaingia sebuleni kwa Kelvin kuja kujaribu kurekebisha hitilafu ya umeme.

    “Heyy! Nyie nani...”

    “Toka!”

    “Yallaaaa! Wezii!”

    “Ohh! Shiit! Let’s Gooooooo!”

    Nilisikia vishindo na mikiki mikiki huko nje, na wakati huo huo Kelvin alizidi kulia mle ndani. Nilitoka kule uvunguni na kumuendea pale niliposikia sauti yake ikitokea.

    “Kelvin! Kelvin...? Vipi?” Nilimsogelea huku nikipapasa kutokana na kiza.

    “Wamenipiga risasi! Nakufa Tigga....sa...sama...hani kwa kuto...kuamini!”

    “Aaaah! Kelvin! Nyamaza ngoja nitafute msaada...”

    “Nenda Tigga! Wata...rudi! Mi’ nakufaaaa!”

    Hii nini tena sasa?

    Nilisikia mlipuko wa bastola huko nje na nikaruka kwa mshituko huku yowe likinitoka. Watu walipiga mayowe huko nje.

    “Nenda Tigga!”

    Nilikurupuka bila ya kujijua. Nilikimbilia kwenye kitanda cha Kelvin na kutoa tochi niliyojua kuwa huwa inakaa kwenye droo ya kando ya kitanda kile. Niliwasha tochi ile na kuvikusanya vitu vyangu haraka haraka na kuvitia kwenye mkoba wangu, pamoja na ile kamera ya Gil. Nilikimbilia bafuni kwa Kelvin na tochi mkononi. Niliichukua sabuni kubwa aina ya Geisha ambayo Kelvin hupenda kuongea na kuitumbukiza kwenye mkoba ule na kutoka mbio. Kelvin alikuwa akigaragara pale sakafuni huku damu ikimvuja ingawa sikuweza kujua jeraha lilikuwa wapi hasa. Huko nje nilisikia gari ikitia moto na kuondoka kwa kasi. Nilimuinamia Kelvin na kutaka kumsemesha, lakini alinihimiza niondoke.

    “Go Tigga...watu watajaa sasa hivi!”

    Na hata aliposema maneno yale, nilianza kusikia ving’ora vya gari ya polisi kwa mbali.

    “Iam so sorry dear!” Nilisema kwa sauti ya chini na kuiacha ile tochi ikiwaka mle ndani kando ya Kelvin nami nikatoka mbio nje ya nyumba ile huku nikitiririkwa na machozi nikiwa na mkoba wangu mgongoni.







    PEKE YANGU



    Nilikurupuka kutoka usingizini huku nikipiga yowe kubwa. Niliketi kitandani na kuangaza huku na huko ndani ya chumba ambacho kilikuwa kigeni kwangu. Jasho lilikuwa likinitoka na koo lilinikauka. Ilikuwa ni ndoto ya kutisha iliyojumuisha matukio ya kuogofya niliyoyaona kule msituni siku si nyingi zilizopita ambayo ilinifanya nikurupuke namna ile kutoka usingizini. Kwa sekunde kadhaa nilizidi kuduwaa pale kitandani bila ya kujua nilikuwa wapi na nilifikaje mahala pale, kisha nikakumbuka. Niliteremka kutoka kitandani na kuelekea juu ya meza iliyokuwamo mle ndani na kuchukua chupa ya maji ya Uhai na kuyabugia kwa pupa. Nilirudi na kuketi kitandani na kuitafakari ile ndoto.

    Niliota matukio ya kule msituni na jinsi nilivyokuwa nikihangaika kuifukuza ile midege iliyokuwa ikiwadonoa wale wenzangu waliouawa kule msituni, na nilipokuwa nikiwafukuza, mmoja wa midege ile alikuwa ameng’ang’ana kuudonoa uso wa bwana Ubwa Mgaya, ila nilipomsogelea, bwana Ubwa Mgaya aligeuka na kuwa Kelvin.

    Oh! Mungu wangu!

    Nilimfikiria Kelvin na moyo ulianza kunipiga kwa nguvu. Sijui ana hali gani huko aliko! Bila shaka atakuwa amekufa, kwani nilimwacha bila msaada wowote...

    Lakini kwa nini hukutaka kuniamini Kelvin?

    Nilipotoka mbio pale nyumbani kwa Kelvin sikuwa na uelekeo maalum na sikujua nilikuwa nakimbilia wapi. Ila kitu kilichonisaidia ni kuwa kule nje kulikuwa kuna mtafaruku mkubwa uliotokana na ule mlipuko wa risasi kutoka kwenye bastola ya wale wauaji niliofanikiwa kuwakurupusha kwa kutawanya kiza katika nyumba ile. Nilitoka mbio kwa muda mfupi na nilipopotelea mtaa wa pili tu nilianza kutembea haraka haraka huku nikilia peke yangu kwa kwikwi. Kiza kilikuwa kimeingia na eneo la sinza ndio lilikuwa linaamka. Watu walikuwa wamejaa katika mabaa mengi yaliyotapakaa eneo lile huku muziki ukisikika kutoka kila kona.

    Nilikuwa nimechanganyikiwa vibaya sana, na nilijaribu kufikiri ni kitu gani nilitakiwa kufanya lakini iliniwia vigumu sana. Akili ilikuwa imekufa ganzi. Nilijilazimisha kuogopa swala la Kelvin kupigwa risasi na wale wauaji, lakini cha ajabu nilijikuta siogopi kabisa. Hisia zote zilikuwa zimekufa ganzi.

    Nilizidi kukata mitaa ya sinza bila ya kujijua hadi nilipojihisi kuchoka. Niliangallia saa yangu ikaniambia muda ulikuwa ni saa tatu kasoro robo za usiku.

    Sasa niende wapi Mungu wangu saa hizi!

    Nilijua kuwa kwa hali iliyofikia, nilitakiwa kuripoti kituo chochote cha polisi kujisalimisha na kupata msaada. Lakini kila nilipokumbuka maelezo ya Kelvin kuwa Dokta Lundi alifika ofisini na hatimaye nyumbani kwake akiwa na askari wa jeshi la polisi, niliingiwa woga na wasiwasi mkubwa iwapo huko nitapata msaada ninaouhitaji. Kwa kadiri nilivyoelewa, pamoja na kuwa nawindwa kwa nguvu sana na wale wauaji wabaya, pia nilikuwa natafutwa na polisi sio tu kwa kile kimuhemuhe nilichozusha kule kwa mkuu wa wilaya, bali pia kama muhusika wa yale mauaji yasiyo na maana kule msituni. Kwenda kituo cha polisi kwa sasa ni sawa na kujipeleka mwenyewe kwa Pilato. Nilidhani kuwa njia salama kwangu ni kwenda kwa mtu mkubwa kabisa katika jeshi la polisi nikiwa na ule ushahidi wangu wa mkanda wa video, vinginevyo ule mkanda unaweza ukapotelea mikononi mwa Dokta Martin Lundi muongo, na huo ndio utakuwa mwisho wangu.

    Sasa niende wapi?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Swala la kwenda nyumbani kwangu halikuwepo kabisa, kwani bila shaka kama wale watu wabaya walikuwa wameamua kunifuatilia kwa nguvu kiasi kile, basi huko ndio wangekuwa wamepiga kambi kabisa.

    Nilifikiria kwenda nyumbani kwa mama yangu Tabata, lakini nilihisi kuwa nako ningemkuta Dokta Lundi na vibaraka wake wakinisubiri. Nilifikiria kwenda kwa mmoja kati ya marafiki zangu wachache, lakini sikulipenda kabisa wazo la kumgongea mtu usiku kama ule na kumpelekea mashaka yangu. Nilikimbilia kwa Kelvin na matokeo nimeyaona, sasa itakuwaje nikienda kwa mmoja wa hao marafiki zangu halafu Dokta Lundi akaniibukia huko huko? Ingawa unaweza kuona kuwa nilikuwa nampa huyu Martin Lundi uwezo mkubwa wa ki-Mungu wa kuweza kunifikia mahala popote niwapo, lakini kwa wakati ule akili yangu ilikuwa imeingiwa na woga mkubwa kabisa. Nilikuwa ni mtu niliyejawa wasiwasi wa hali ya juu.

    Paranoid?

    Niliamua kupitisha usiku ule wa mashaka kwenye nyumba ya wageni, ambamo baada ya kujitahidi kupata usingizi kwa shida, nilijikuta nikikurupushwa na ndoto ile ya kutisha.

    Mwili ulinisisimka.

    Ndani ya masaa sabini na mawili mlolongo mzima wa maisha yangu ulikuwa umebadilika kwa namna ya ajabu kabisa. Ndani ya muda huo, maisha yangu yaliyokuwa yamepambwa na ndoto nzuri sana za mafanikio na matarajio makubwa, yaligeuka na kuwa ndoto moja ya kutisha sana iliyogubikwa mashaka mazito.Ndani ya masaa hayo nilikuwa nimevunja uchumba kama masikhara, na bila shaka mtu aliyekuwa mchumba wangu alikuwa amepoteza maisha.

    Kwa nini?

    It is always the very good times of one’s life that normally turns into one’s very bad times in no time…

    Nilianza kulia upya.

    Nililia kwa unyonge na upweke. Nililia kwa kusikitikia maisha yangu yaliyoharibiwa bila sababu. Niliwalilia wenzangu niliokuwa nao kule msituni, waliouawa bila hatia.

    Nilimlilia Kelvin.

    Nililia sana na kwa muda mrefu. Kisha nilijilaza kitandani, huku nikijihisi mchovu kuliko kawaida.

    Nilipitiwa na usingizi.

    Lakini muda si mrefu baadaye nilishtushwa na vishindo na kelele nje ya chumba changu. Nilikurupuka nikiwa makini ghafla. Nje ya chumba kile nilisikia kelele za watu waliokuwa wakifoka na kushurutisha wapangaji wengine wafungue milango yao. Nilihamanika vibaya sana. Niliangaza huku na huko ndani ya chumba kile nisione pa kukimbilia. Kile chumba kilikuwa ni kama kile cha Kelvin, kikiwa na bafu lake kwa ndani, ila mlango wa kutokea ulikuwa ni mmoja tu. Nilinyakua koti langu la jeans na kulivaa haraka haraka na kuanza kuvuta viatu vyangu kutoka chini ya kitanda huku moyo ukinienda mbio wakati niliposikia mlango wa chumba changu ukigongwa kwa nguvu.

    “Nani?” Niliuliza kwa sauti ya kitetemeshi huku nikihangaika kuvaa viatu.

    “Polisi! Fungua!” Sauti kali ilijibu kutoka nje ya mlango ule na kuamrisha.

    Mungu wangu, nimenyakwa! Nilienda haraka mpaka pale mlangoni, nikiacha kuvaa viatu na kuuliza kwa mashaka.

    “Mnataka nini...?”

    Mlango ulipigwa ngumi kwa nguvu.

    “Hebu fungua mlango mwanamke...!Upesiiii, Ebbo!”

    Nilifungua mlango haraka kwa woga na nilijikuta nikisukumiwa ndani kwa nguvu na askari wawili wakiingia mle ndani, mmoja akiwa mwanamke. Nilirudi nyuma na kubaki nikiwakodolea macho kwa woga. Yule askari wa kiume alipita moja kwa moja hadi kule bafuni na kukagua huku na huko, na kurudi pale chumbani. Yule wa kike aliliendea kabati la nguo la mle ndani na kulifungua. Hakukuta kitu, hivyo akarudi na kusimama mbele yangu.

    “Ni..niwasaidie nini afande...” Niliuliza kwa wasiwasi. Badala ya kunijibu wale askari walikuwa wakinitazama huku nyuso zao zikificha hisia zozote ambazo ningeweza kuzisoma, kisha yule mwanaume aliongea.

    “Uko peke yako humu?”

    “Ndiyo...”

    “Mwanamke peke yako gesti?” Yule mwanamke alidakia. Hili sikulijibu.

    “Wewe ni nani, na kwa nini uko hapa saa hizi?” Yule askari wa kiume aliniuliza. Sikusita, nilitoa jibu hapo hapo.

    “Naitwa Mwajabu, nimelala hapa gesti kwa sababu sina mwenyeji hapa mjini nami ni msafiri...”

    “Ukilala ndio huwa unavaa nguo namna hii? Je ukioga?” Yule askari wa kike aliniuliza.

    “Nimevaa nguo baada ya nyie kuanza kunigongea...ndio maana nilichelewa kufungua mlango.” Nilimjibu.

    “Una kitambulisho?”

    “Sina.” Walitazamana, kisha wakaniamrisha nitoke nje. Huko nilikuta askari wengine wapatao wanne, mmoja kati yao akiwa mwanamke. Wapangaji wengine walikuwa wamesimamishwa nje ya milango ya vyumba vyao, nami nikaamriwa nisimame mbele ya mlango wangu. Nikiwa nimejawa wasiwasi na udadisi, niliwatazama wale wapangaji wengine waliotolewa vyumbani mwao. Wengi wao walikuwa wawili-wawili,yaani mume na mke, na walikuwa wakilalamika kwa kuingiliwa faragha yao, hasa wanaume ambao bila shaka walikuwa pale kwa kujiiba wakisaliti ndoa zao.

    Nilimgeukia yule askari wa kike.

    “Afande kwani kuna nini...mbona mnadhalilisha watu namna hii?”

    “Huu ni msako wa machangudoa...na wewe ni mmoja wao kwa hiyo usijitie kutoelewa hapa!”

    Eh! Kwanza kichaa...Paranoid Schizophrenia...sasa changudoa! Ni nini hiki?

    “Hah! Mi’ sio changudoa...mi’ ni msafiri...”

    “Wasafiri huwa hawakai kwenye viji-gesti vya vichochoroni kama hivi, halafu huwa wanatembea na vitambulisho. Tulia hapo tuelekee kituoni sasa hivi!” Alinijibu yule askari wa kike halafu akawaendea wale askari wengine na kuanza kuwaeleza vitu ambavyo sikuweza kuvielewa huku akinioneshea kidole. Wawili kati ya wale askari niliowakuta pale kwenye korido nje ya chumba changu walinisogelea taratibu huku wakinitazama kwa makini. Kwa namna fulani nilihisi kuwa pale mimi ndio nilikuwa kusudio la msako ule, ila nilishindwa kuelewa ni vipi walijua kuwa nipo kwenye ile gesti, ambayo kwa hakika ilikuwa vichochoroni.Na kama hivyo ndivyo, basi kwa hakika lile kundi la Dokta Martin Lundi lilikuwa hatari sana. Na kama haikuwa njama ya Martin Lundi muongo, basi ilimaanisha kuwa ule ulikuwa ni msako wa polisi kweli, ambao kwa vyovyote mwisho wake ilikuwa ni kupelekwa kituoni tu. Sikuwa na shaka hata kidogo kuwa iwapo nitafikishwa kituoni tu, basi nitakuwa kwenye mashaka mazito.

    Mungu wangu, hivi nitaweza kuondokana na balaa hili mimi?

    “Enhe, msichana, mbona uko hapa gesti peke yako?” Mmoja wa wale askari wengine, mwanaume aliniuliza. Nilitaka nimuulize iwapo hilo lilikuwa ni kosa, lakini kabla sijajibu, yule askari mwingine wa kike alidakia. Nilimhisi kuwa na umri wa kati ya miaka thelathini na tatu au na tano. Alikuwa na sura ya kuvutia, na yale mavazi yake ya kiaskari yalimkaa vizuri sana, hasa suruali yake ambayo ilionesha jinsi alivyojaaliwa makalio mazuri ya kuvutia.

    “Na usituletee habari ya kuwa eti u-msafiri...msafiri huna hata mzigo?”

    Nilibaki nikiwakodolea macho wale askari nisijue la kuwaeleza. Na wakati bado naendelea kushangaa, yule askari mwanamke alinisukumia tena chumbani mwangu na kufunga mlango kwa ndani, akimuacha yule mwenzake kule nje. Bila ya kunitazama alitembeza macho mle chumbani na kuniuliza. “Umesema unaitwa nani?”

    “Mwajabu...”

    Aliliendea kabati la nguo la mle ndani na kulifungua kwa kutumia fimbo yake na kuchungulia ndani bila ya kushika kitu. Hakukuwa na kitu. “Unasema we’ ni msafiri...unatokea wapi na unaelekea wapi?” Aliuliza tena bila ya kunitazama huku akielekea kule bafuni.

    “Natokea Mkuranga...naenda Zanzibar...” Jibu lilinitoka kama kwamba nilikuwa nasema ukweli. Yule askari aliguna na kurudi kando ya kitanda changu. Akiendelea kutonitazama, alilisukuma kwa fimbo yake begi langu dogo lililokuwa pale kitandani, kisha alilichukua na kukung’uta vilivyokuwamo ndani yake pale kitandani.

    “Zanzibar unaenda kufanya nini?” Aliniuliza huku akipekua vile vitu vilivyomwagika pale kitandani. Aliinua ile kamera ya Gil na kuitazama kwa makini.

    “Ku...kununua nguo za biashara...”

    Aliifungua ile kamera sehemu ya kuwekea kaseti na kuchungulia ndani. Ilikuwa tupu. Nilikuwa nikitazama kila kitendo chake kwa makini huku moyo ukinienda mbio. Yule askari wa kike aliiweka kitandani ile kamera, na kuanza kupekua vitu vyangu vingine kwa muda na kwa utaratibu wa hali ya juu. Nilizidi kupata wasiwasi kwani huyu askari alionekana kuwa anajua anachofanya na sio anayebahatisha tu ambaye ningeweza kumlaghai kirahisi. Aliinua tena ile kamera na kuitazama kwa makini, huku akiigeuza huku na huko. Hatimaye aliiweka kitandani na kunitazama usoni kwa mara ya kwanza tangu aingie mle ndani.

    “Oke, sasa mchezo basi Tigga, where is the tape?” Aliniuliza huku akiwa amenikazia macho kiaskari hasa, akimaanisha nimweleze ni wapi ulipo ule mkanda wa video wenye ushahidi wa mauaji ya yule mtu asiye na jina kule msituni.

    Mshituko nilioupata kwa swali lile ulikuwa mkubwa sana. Niliruka kama kwamba nimepigwa kofi na kubaki nikimkodolea macho yule mwanamke aliyevaa mavazi ya kiaskari, kama kwamba nilikuwa nimeona jini.

    Mimi nilijitambulisha kwake kwa jina la Mwajabu, sasa yeye ameniita kwa jina langu halisi na anajua juu ya ule mkanda wa video! Kwa hiyo muda wote ule alikuwa akijua kila kitu!

    Hii ni njama ya Dokta Martin Lundi muongo! Oh, My God! Sasa nitapata wazimu!

    Nilimtazama kwa kihoro yule mwanamke.

    Hii ni babu kubwa! Na huyu naye ni mwenzao?

    “Mbo..mbona sikuelewi Afa...nde?” Nilijitutumua kumuuliza huku nikirudi nyuma kwa woga.

    “Usinitanie mimi wewe! Lete huo mkanda sasa hivi!” Yule askari alinifokea na hapo hapo alinitolea bastola na kuniwekea usoni. Sikumjibu kitu. Nilibaki nikiukodolea macho mdomo wa ile bastola huku moyo ukinienda mbio. Tulibaki tukitazamana kwa muda huku yule askari akinihemea usoni kwa hasira. Alipoona bado namkodolea macho bila kumjibu, alinidaka koo na kunisukumia kitandani.

    “Tunajua kuwa unao huo mkanda...tunautaka...na nakuahidi kuwa tutayafanya maisha yako yawe mabaya sana hapa duniani mpaka utautoa!” Alinifokea kwa sauti ya chini huku akinitomasa puani kwa mdomo wa ile bastola yake.

    Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa hawa watu kujidhihirisha kwangu, nami sikuweza kuiachia nafasi hii, ingawa nilikuwa nimetishika vibaya sana.

    “Kwani nyie ni kina nani? Wewe sio askari...ni mmoja wao!. Mnataka nini kutoka kwangu?”

    “Kauli ya kijinga na swali la kijinga! Mimi sio askari wakati unaniona kuwa ni askari? Unauliza tunataka nini wakati nimekwambia tunautaka huo mkanda! Mjinga sana wewe!”

    “Nyinyi?Nyie ni kina nani?”

    “Si kazi yako kujua.......where is the tape Goddamn it?” Yule askari wa kike alinijibu kwa ghadhabu huku akisisitiza nimpatie ule mkanda wa video. Aliniudhi.

    “Mnh! Mi’ naona wewe ndio mjinga. Sasa nikikupa huo mkanda halafu mimi hatima yangu itakuwa nini?” Nilimuuliza kwa kebehi. Alinibamiza kofi kali sana la ghafla na macho yalinichomachoma kwa machozi machanga. Nikiwa sijawahi kupata kipigo cha aina yoyote ile kwa miaka mingi sana, vipigo nilivyopata siku ile viliniuma sana. Kwanza Dokta Lundi na vibaraka wake, halafu huyu mwanamke mwenye mavazi ya kiaskari.

    “Mi’ n’takuua ukinichezea we’ mtoto, lete huo mkanda...”Alinikemea kwa sauti ya chini huku akinididimizia bastola yake kooni.





    “Sina mimi huo mkanda!...kwani rafiki yako Martin Lundi muongo hajakueleza?”

    Yule askari alisonya kwa hasira na kuikoki bastola yake huku akiididimiza kwa nguvu katikati ya koo langu na kuniambia kwa ghadhabu. “Usicheze na serikali Tigga...sisi tuko kila mahali, huwezi kutukwepa.Salama yako ni kutoa ushirikiano unaohitajika...”

    “No! Wewe sio askari na wala nyie...sijui ni watu gani, lakini nyie sio serikali...serikali haiko hivyo...”

    “The tape Tigga! Nautaka huo mkanda wa video sasa hivi!”

    “Swala hilo nilishalimaliza kwa rafiki yako Martin Lundi muongo...kanda iko kwa wakili wangu!” Nilimkemea huku nikimsogezea uso wangu kwa kiburi. Yule askari alitoa sauti ya kukereka kwa jibu lile na kutaka kusema neno lakini ghadhabu zilimkaba kooni hivyo alibaki akinitumbulia macho kwa hasira, akijaribu kuamua achukue hatua gani badala ya kunilipua kwa ile bastola yake. Tulitazamana, na katika muda ule niliona kuwa yule dada alikuwa tayari kunilipua kwa risasi, kwani jibu langu lilimghadhibisha vibaya sana.Nilishuhudia midomo ikimcheza kwa hasira na macho yakimwiva.

    Nilibaki nikimtazama kwa woga mkubwa na wasiwasi usio kifani. Bado shavu lilikuwa likinichonyota kutokana na kofi lake kali. Tulibaki tukitazamana kwa muda mrefu,hakuna mmoja kati yetu aliyesema neno.

    Na mara yule askari wa kiume aliita kutokea nje ya chumba changu akimhimiza yule mwanadada waondoke nami pamoja na wale wapangaji wengine walioshindwa kujieleza vizuri kule nje kuelekea kituoni.

    “Dakika moja afande!” Yule mwanadada askari alimjibu kwa sauti huku bado akiwa ananitazama usoni kwa macho ya ghadhabu. Hatimaye alishusha pumzi ndefu, na huku akilegeza mdidimizo wa bastola yake shingoni kwangu alinong’ona kwa hasira.

    “Unafanya kosa kubwa sana Tigga, na utajuta kwalo!”

    Kisha alisonya na kuiweka bastola yake kwenye mkoba wake na kuelekea mlangoni kwa mwendo wa haraka akiniacha nikiwa nimeduwaa mle chumbani nikimtazama huku nikijitahidi kumeza mate bila mafanikio. Alipofika mlangoni nilimsikia yule askari wa kiume alimuuliza juu yangu. Yule mwanadada aliyevaa mavazi ya kiaskari alisimama mlangoni na kunitazama kwa muda, kisha akamjibu huku bado akiwa ananitazama.

    “Hana matatizo huyu...ni msafiri anayeelekea Zanzibar. Lets get out of here!” Kisha alifunga mlango taratibu na kutoweka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilibaki nikiwa nimeduwaa.

    Heh! Hawa watu...ni watu gani hawa? Kwa nini wanakuwa na uwezo wa kunifuatilia namna hii? Na vije wanakuwa na namna ya kujiingiza kwenye nyanja za kiserikali namna hii? Hivi yule mwanamke ni askari kweli au bandia?

    Yaani kichwa kilinizunguka kwa maswali hayo kwa muda mrefu nikiwa nimekaa pale kitandani bila ya kupata dalili ya uelewa. Lakini swali kubwa zaidi lililobaki kichwani mwangu lilikuwa moja tu: kwa nini yule dada askari hakunikamata na kunipeleka kituoni?

    Naam. Kwa hakika hili kwangu lilikuwa ni a hundred dollar question, kama wamarekani wanavyopenda kusema. Kwa nini yule dada asinikamate na kuniweka chini ya ulinzi? Kwani baada ya kituko kile, sikuwa na shaka kuwa alikuwa ana taarifa zote za tafrani niliyoizusha na kizaazaa nilichoacha kule Manyoni kwa mkuu wa wilaya.

    Sasa kwa nini ameniacha?

    Kadiri nilivyozidi kujiuliza maswali hayo, ndivyo taratibu nilipoanza kupata mwanga.

    Nilijishawishi kuwa wale watu wanaonisakama hawakuwa wakifanya hivyo ili wanitie kwenye mikono halali ya sheria, bali walikuwa wananitaka kwa sababu yao binafsi, ambayo ni kuupata ule mkanda wenye ushahidi wa madhambi yao niliojinadi kuwa ninao.

    Kitu kingine ambacho kilijitokeza ni kwamba wale watu...watu gani...? walikuwa na uwezo wa kutumia mamlaka za nyanja mbalimbali za kiserikali kwa maslahi yao.

    Sasa hii ilibadilisha lile swali langu la msingi: hawa watu ni akina nani?

    Niliwaza na kuwazua lakini bado niliishia kujiongezea maswali mengi yasiyo na majibu. Lakini kitu kimoja kilibaki akilini mwangu. Ule mkanda wa video ndio ulikuwa salama yangu,kwani nilikuwa na hakika kabisa kuwa wale watu hawashindwi kabisa kuniua, lakini hawatoweza kufanya hivyo mpaka waupate ule mkanda. Kabla ya hapo hawatathubutu kuniua, labda wajithibitishie kuwa hakuna mtu mwingine yeyote anayejua juu ya mambo yaliyomo ndani ya mkanda ule zaidi yangu.Lakini hilo wazo halikunipa amani hata kidogo, hasa nilipomkumbuka yule mtu niliyempachika jina la macho ya nyoka. Yule jamaa ni kichaa, angeweza kuniua wakati wowote, kama jinsi alivyomuua yule mtu asiye na jina kule msituni.

    Nilikumbuka maneno makali ya yule askari wa kike aliyetoka mle chumbani muda si mrefu uliopita.

    “...na nakuahidi kuwa tutayafanya maisha yako yawe mabaya sana hapa duniani mpaka utautoa!”

    Kufikia hapa niliamua kuwa sina ujanja bali niendelee kukimbia tu mpaka nipate mtu nitakayeweza kumuamini na ule mkanda na ambaye ataweza kunisaidia, kwani lile swala sikuwa na uwezo wa kupambana nalo peke yangu.

    Lakini ni nani wa kunisaidia? Na ni nani wa kumuamini?

    Mambo yaliyonikuta kwa Mkuu wa Wilaya na kwa Kelvin yalinifanya nizidi kujiona kuwa bado niko peke yangu, nisiye na kimbilio.

    Na yote hii ni kwa ajili mambo niliyoyaona na ambayo sasa yako kwenye ule mkanda wa video. Sikusubiri zaidi.

    Nilikurupuka ghafla na kuanza kukusanya vitu vyangu vilivyotawanywa hovyo pale kitandani na kuvishindilia kwenye begi langu. Niliichukua ile sabuni aina ya Geisha niliyoichukua bafuni kwa Kelvin na kwa kutumia kile kisu changu kidogo,nilifuatisha mchinjo mwembamba sana nilioukata kuuzunguka mgongo wa ile sabuni wakati nilipokuwa nimejifungia bafuni kwa Kelvin kabIa ya kuanza kuoga, na kuitenganisha ile sabuni kwa ubapa na kubaki na vipande viwili mithili ya silesi mbili za mkate. Katikati ya kila ubapa wa ile sabuni kwa ndani nilikuwa nimechimba kwa kisu kiasi cha kuweza kuzamisha ile kaseti ndogo kabisa ya video. Kwa mikono iliyotetemeka na huku moyo ukinipiga kwa nguvu, niliitoa ile kaseti ambayo hapo awali nilikuwa nimeizungushia nailoni ya sabuni kabla ya kuizamisha kwenye kishimo nilichochimba kwenye moja ya bapa mbili za ile sabuni niliyoikata kistadi na kuibananisha tena kwa maji kidogo na kuuficha ule mchinjo kwa rojo zito la sabuni ile baada ya kuiloweka na kukauka.

    Ile kaseti ilionekana safi na salama, wala haikuonekana kuathirika na kificho kile kilichoiokoa kutoka kuangukia mikononi mwa dokta Martin Lundi na kuendelea kuiokoa tena kutoka kuangukia mikononi mwa yule askari wa kike aliyeahidi kuyafanya maisha yangu yawe mabaya mpaka atakapoitia mkononi ile kaseti.

    Kwa kutaka kuhakikisha, niliingiza kwenye ile kamera ya marehemu Gil na kuirudisha mwanzo kidogo, kisha nikabonyeza sehemu iliyoandikwa “play”.

    Kwenye kile kijiruninga kidogo cha kamera ile, nilimuona tena yule mtu asiye na jina akimg’ang’ania koo macho ya nyoka...

    Niliizima na kutumbukiza ile kamera pamoja na ile kaseti ndani ya mkoba wangu.

    Nilivaa viatu vyangu na kutoka haraka mle ndani bila kujali kuwa ulikuwa usiku.

    Kwa wakati ule jambo la muhimu kwangu lilikuwa ni kuwa mbali na eneo lile kwa kadiri iwezekanavyo.



    --



    Nilipitisha sehemu iliyobaki ya usiku ule Club Billicanas, ambako nilijichimbia kwenye kona pweke ndani ya ukumbi ule na kuduwaa nikiangalia jinsi vijana wenzagu wakijirusha na kufurahi pamoja na wapendwa na marafiki zao. Baada ya kukurupuka kutoka pale kwenye ile gesti, sikuwa na kimbilio lolote la haraka nililoweza kulifikiria kwa wakati ule. Ingawa nilibahatika kupata watanashati kadhaa waliojitokeza kutaka kucheza nami na wengine hata kujaribu kunitongoza, sikuwa na hamu kabisa ya kujipumbaza na furaha zile, hivyo niliwakatalia kistaarabu na kuendelea kukaa kimya peke yangu ndani ya ukumbi ule.

    Akili yangu ilikuwa imepigwa na bumbuwazi kwa jinsi mambo yalivyozidi kuniendea vibaya, kwani nilijiona nikizidi kudidimia katika dimbwi la uadui na tuhuma zisizo na msingi, bila ya matumaini ya kujinasua kutoka katika dimbwi lile. Na ilionekana kuwa kadiri mambo yalivyozidi kusonga mbele, ndivyo ule mtandao dhalimu wa akina Martin Lundi ulivyozidi kupanuka.

    Angalau pale ndani ya ule ukumbi maarufu wa starehe sikuwa na wasiwasi wa kukurupushwa na vibaraka wa yule mtu anayejiita Martin Lundi, au wana usalama ambao nao nilikuwa na imani kuwa walikuwa wakinisaka. Nilikuwa na hakika kabisa kuwa katika mawazo yao wasingetarajia kabisa kwamba katika mazingira kama niliyokuwa nayo ningeweza hata kufikiria kwenda sehemu kama Club Billicanas.

    Na kuanzia hapo niliamua kuwa salama yangu ilitegemea katika kufanya yale ambayo wao hawayatarajii.

    Wao.

    Nilimfikiria yule mwanadada aliyevaa mavazi ya kiaskari aliyeacha kuniweka chini ya ulinzi muda mfupi uliopita...

    Wao ni nani? Who are these people?

    Alfajiri kulipopambazuka nilitoka pamoja na washabiki wengine wa starehe waliokesha pale ukumbini na kuchukua teksi mpaka nyumbani kwa mama yangu Tabata,nyumba ambayo tuliachiwa na marehemu baba yetu.

    Niliondoka pale nyumbani baada ya kuanza kazi na kwenda kupanga nyumba ya msajili maeneo ya Upanga ili niweze kujitegemea, nikimwacha mama na dada yangu wakiishi pale nyumbani. Kwa kuwa naye hakuwa ameolewa, na ajira yake hakikumuwezesha kupanga nyumba na kujitegemea kama mimi, dada yangu aliendelea kuishi na mama pale nyumbani.

    Ilikuwa ni saa kumi na mbili kasoro robo wakati mama aliponifungulia mlango nami nikaingia ndani ya nyumba ile niliyolelewa tangu utoto wangu. Mama alionekana wazi kuwa ameshitushwa na ujio wangu, na mara nilipoingia ndani alifunga mlango haraka na kuniongoza hadi chumbani kwake ambako tulikumbatiana kwa nguvu huku sote tukibubujikwa na machozi kimya kimya. Nilimuuliza iwapo Koku, dada yangu alikuwepo nyumbani. Aliniambia kuwa alikuwa ameshatoka kwenda kazini. Koku alikuwa ni nesi wa hospitali ya wilaya ya Temeke. Nilibaki nikiangaza mle ndani huku nikitokwa na machozi. Kwa namna fulani nilihisi amani kwa kuwepo tu pale nyumbani na mama yangu.

    “Oh! Tigga mwanangu! Ni nini tena kimekukuta mwanangu?” Mama alilalamika kwa sauti ya chini huku akibubujikwa na machozi. Sikuweza kujibu. Sasa nilikuwa nikilia kwa nguvu nikiwa nimemkumbatia mama yangu. Hapa nilikuwa nimepata liwazo nililokuwa nikilihitaji sana tangu nikutane na mtihani huu mgumu kabisa katika maisha yangu.

    “Matatizo makubwa yamenikuta mama...” Nilibwabwaja kwa simanzi.Nilitaka kumueleza juu ya Kelvin, lakini jibu lake lilinishitua.

    “Najua mwanangu...pole sana. Lakini unahitaji kitu cha kula...na mapumziko.”

    “Unajua...?” Nilimuuliza huku nikimtazama kwa mashaka. Tulitazamana, na niliona kuwa alikuwa akinitazama kwa huzuni kubwa...

    “Walikuja hapa...wakanieleza kila kitu...” Alinifafanulia huku akiniketisha kitandani kwake.

    Hapo nilikuwa makini kupita kawaida. Walikuja hapa...wakanieleza kila kitu...

    “Nani walikuja mama? Dokta Lundi? Dokta Martin Lundi alikuja hapa?”

    “Ndio mwanangu...Dokta Lundi alikuja, akanieleza yote yaliyotokea...”

    Nilimtazama mama yangu na nikahisi moyo ukiniisha nguvu. Kwa jinsi mama alivyokuwa akiongea, niliona kuwa lolote ambalo alikuwa ameelezwa na huyu mtu anayejiita Martin Lundi, alikuwa amelielewa vizuri sana na hakuwa na shaka nalo kabisa.

    Eh! Mungu wangu!

    Sikuwa na shaka hata kidogo kuwa Martin Lundi muongo atakuwa ameleta uongo na fitna zake kwa mama yangu, lakini nilikuwa na hakika kabisa kuwa mama asingeweza kumkubalia ule uongo wake kirahisi. Lakini kilichonishangaza ni kuona kuwa mama alikuwa anaongea kama kwamba alikuwa amemuamini! Nilimeza funda la mate, ambayo niliyahisi machungu kuliko kawaida.

    “A...alikuja na polisi...?” Nilimuuliza mama kwa wasiwasi. Mama alinitazama kwa mshangao mkubwa sana. Kama kwamba alikuwa anamshangaa mtu mwenye wazimu.

    “Polisi? Kwa nini aje na polisi? Hapana, alikuja na madaktari wenzake...”

    Nilibaki mdomo wazi. Kwa hiyo hapa hakuja na askari. Ni uongo gani uliotumia kwa mama yangu Martin Lundi?

    “Na akakueleza kila kitu...?”

    “Yes, my love. I am so sorry for you, lakini usiwe na wasiwasi, mama yako hatokuacha peke yako. Na nitahakikisha kila kitu kinakuwa sawasawa.”

    “How, mama? Utahakikishaje kuwa kila kitu kinakuwa sawa...? Kwani umeelezwa nini na Dokta Lundi? Yule ni muongo sana mama, isije ikawa...”

    “Usiwe na wasiwasi mwanangu...mimi nitakuwa na wewe kila hatua mpaka mwisho.”

    Nilichoka!Nilitaka kumuuliza alikuwa anamaanisha nini kwa kauli ile, lakini hakunipa nafasi. Aliinuka kwenda kunitayarishia chai nami nikaingia bafuni na ule mkoba wangu ambako nilioga haraka haraka na kupiga mswaki kwa kutumia kidole na kusukutua kwa dawa ya meno. Niliogopa hata ile kuwaza tu kuwa na mama naye atakuwa amekolezwa ule ujinga wa Dokta Lundi. Nilitaka kuamini kuwa alikuwa upande wangu na aliazimia kunisaidia mpaka mwisho wa mkasa huu.

    Lakini hivyo ndivyo alivyokuwa akimaanisha kwa kauli yake ile?

    Au alikuwa anamaanisha vinginevyo?

    Nilipotoka nilimfuata mama jikoni ambako alikuwa akimalizia kukaanga mayai. Nilikunywa chai kule kule jikoni huku akilini nikiwa najaribu kutafakari ni nini maana ya yale maneno ya mama. Baada ya kunywa ile chai na kushiba kisawasawa, nilianza kujihisi usingizi mzito. Nilikumbuka kuwa sikuwa nimepata muda wa kulala sawasawa tangu niingie hapa jijini kutoka kule Manyoni ambapo balaa lote hili lilipoanzia. Nilijilazimisha kupingana na usingizi ule na kumkabili tena mama yangu.

    “Mama...umesema Dokta Lundi amekueleza kila kitu...amekueleza nini?” Hatimaye nilimuuliza mama yangu. Alinitazama kwa muda, kisha alishusha pumzi kabla ya kunijibu taratibu.

    “Amenieleza kuhusu...kuhusu yaliyotokea kule msituni Tigga. Lakini amenihakikishia kabisa kuwa yote yaliyotokea kule si jukumu lako! Niliogopa sana mwanangu, lakini Dokta Lundi is such a humble man...(ni mtu mkarimu sana...) ameahidi kukusaidia kwa kadiri ya uwezo wake...”

    Mwili ulinifa ganzi na nikahisi ile nyumba ikizunguka. Yaani mama alikuwa anaamini kuwa Dokta Lundi ni mtu mzuri mwenye nia ya kunisaidia!

    Sikuamini.

    “Mama! Unataka kuniambia kuwa umeamini aliyokueleza Dokta Lundi?” Nilimuuliza kwa jazba huku nikiinuka kutoka kwenye kiti nilichokuwa nimekalia na kumsogelea huku nikimtazama kwa makini. Mama alinitazama kwa mashaka huku akijishughulisha kusogeza vile vyombo nilivyokuwa nikilia pale mezani.

    “Sasa kwa nini nisimuamini Tigga mwanangu? Yule ni mtu mwenye nia ya kusai...”

    “Yule ni mtu mwenye nia ya kuniua mama! Na usimruhusu kabisa aje karibu na wewe, atakudhuru! Dokta Martin Lundi ni muuaji mama, na mimi nimemuona kwa macho yangu akishirikiana na wenzake kumtesa na hatimaye kumuua mtu kule msituni.” Nilimkatisha mama yangu kwa hasira.

    Kwa nini watu wanapenda kumuamini Martin Lundi muongo?

    “Hapana Tigga...hayo yote yamo katika fikira zako tu mwanangu...ni kutokana na...”

    “Paranoid Schizophrenia?” Nilimkatisha mama yangu kwa uchungu, kabla hajamalizia ile kauli yake, na kuendelea; ”Hivyo ndivyo Dokta Lundi alivyokueleza mama? Kuwa hayo mambo ni fikira zilizojengeka bila msingi kichwani mwangu kutokana na huo ugonjwa unaosemekana kuwa ninao?”

    “Tigga mwanangu, usiifanye hii hali iwe ngumu kuliko inavyohitajika...”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Nilitoa sauti ya kukata tamaa na kutikisa kichwa kwa masikitiko makubwa.

    “Mama! Hivi kuna historia ya wazimu katika familia yetu? Kuna mtu yeyote...babu au bibi fulani huko nyuma, aidha upande wako au wa baba ambaye alipata kuugua wazimu?” Nilimuuliza kwa jazba. Mama alibaki akinitazama tu huku akivisogeza sogeza vile vyombo bila uelekeo maalum. Lile swali lilionekana kuwa lilimchanganya kidogo na niliona wazi kuwa wazo hilo halijawahi kumpitia kichwani mwake hata kidogo.

    “Ennh, mama, hebu nieleze hilo...sijawahi kusikia hata siku moja...au mlituficha?” Nilizidi kumsukumia maswali.

    “Hakuna Tigga, lakini...”

    “Unaona? Mi’ najua magonjwa kama hayo yana namna ya kurithishwa katika familia, au nakosea?”

    Mama hakunijibu. Niliona alikuwa amechanganyikiwa na nilimwonea huruma sana.

    Nilihisi chuki ya hali ya juu kwa yule mjinga anayejiita Dokta Lundi kwa kutufikisha katika hatua hii mimi na mama yangu. Lakini kwa nini mama asiuone uongo huu? Mimi ni mwanae for God’s sake!

    Nilimsogelea na kumuambia kwa kuomboleza: “Mama. Naomba uniamini mimi mwanao. Dokta Lundi ni muongo tena muongo mkubwa sana! Na wala sidhani kama ni dokta kweli yule. Anachofanya ni kupita akinipakazia uzushi wa ugonjwa huo wa uongo ili kuninyima nafasi ya kusikilizwa na kuaminika mahala popote nitakapokwenda. Na hiyo ni kutokana na mambo niliyoyaona kule msituni na ambayo nina ushahidi usiopingika...ushahidi ambao utamuathiri sana huyo Dokta Lundi na wenzake!”

    Niliona kabisa kuwa hali ile ilikuwa ikimchanganya vibaya sana mama yangu, na nilizidi kumuonea huruma lakini ilibidi nimueleweshe.

    “Mama, mi’ n’na ushahidi wa kuthibitisha kuwa Dokta Lundi si mtu mwema kama anavyotaka wewe umuone...”

    “Amenionesha picha za kule msituni Tigga...watu wameuawa Tigga! Kama kuku...!Inatisha sana!” Alisema kwa sauti ya chini huku akilengwa na machozi.

    “Na akakuambia kuwa ni mimi ndiye niliyewaua wale watu?” Nilimuuliza mama kwa uchungu. Hakunijibu, lakini katika macho yake niliona kuwa nilikuwa nimeuliza jibu. Iliniuma sana.

    “Mama! How can you believe such rubbish?” Nilibwata huku nikitupa mikono yangu hewani,nikimuuliza ni vipi anaweza kuamini upuuzi kama ule, kisha nikaendelea kwa sauti ya chini huku nikisisitiza kauli yangu kwa mikono yangu.

    “Mama...ni yeye pamoja na wenzake watatu ndio waliofanya yale mauaji kule msituni! Na hakuna mtu yeyote anayejua hilo isipokuwa mimi. Huoni kuwa anafanya kusudi kunipakazia ugonjwa huo ili taarifa nitakazotoa dhidi yake na wenzake zitiliwe mashaka na kila mtu? Si unaona jinsi wewe mwenyewe unavyoshindwa kuniamini? Hivi ndivyo anavyotaka, na ndivyo inavyokuwa kila mahali niendapo mama!How can you believe him mama?” Nilimueleza kwa hisia kali huku nikihoji uhalali wa mama yangu kuamini uongo wa Martin Lundi kirahisi namna ile.Na hata pale nilipokuwa nikiongea maneno yale, nilijihisi uchovu na usingizi mzito. Nilipiga mwayo mrefu na kujibwaga tena kwenye kiti. Mama alinisogelea na kunipapasa kichwani.

    “Pole sana Tigga. Unaonekana una usingizi, kwa nini usijipumzishe kidogo halafu tutaongelea hili jambo baadaye?” Aliniambia kwa upole. Na hii ndio tabia ya mama yangu ambayo toka utotoni mwangu nilikuwa siipendi. Akiwa na jambo lake basi yuko radhi mliahirishe kwa muda kuliko kukubaliana na wazo jingine, akitumaini kuwa baada ya muda utakuwa umeelewa “ujinga” wako na kukubaliana na mawazo yake.

    Sasa mimi sina muda wa kupoteza namna hiyo mama!

    Nilimtazama mama yangu kwa kukata tamaa, na mwayo mwingine ukanitoka. Sikuwa nimepata usingizi wa kutosha usiku uliopita. Lakini huu sio wakati kulala!Dokta Lundi akitokea...

    “Tafadhali usimruhusu Dokta Lundi anikamate mama...please!” Nilimwambia kwa sauti ya chini huku nikihisi macho yakiniwia mazito kuliko kawaida.

    “Mi’ nakutakia yaliyo mema kwako mwanangu, na si vinginevyo.” Mama alijibu, lakini kauli ile haikunipa amani hata kidogo.Nilijilazimisha kuinuka na kwenda kujilaza kwenye kochi refu lililokuwa pale sebuleni huku nikiwa nimeukumbatia mkoba wangu. Mama alinishauri nikalale chumbani, lakini sikukubali, nilimwambia kuwa nataka kujipumzisha kwa dakika chache tu.

    Nadhani nilisinzia kwa dakika chache sana, kisha nikahisi nikipambana na usingizi ule mzito, nikijitahidi usinielemee.

    Lazima niamke! Lazima niamke!

    Wazo hilo lilikuwa likinijia tena na tena ilhali usingizi ukizidi kunielemea.Kwa mbali nilisikia sauti ya mama yangu ikinisemesha. Niliinuka ghafla na kutazama kila upande, lakini nilikuwa peke yangu pale sebuleni. Ilikuwa ndoto? Hapana, nilisikia sauti ya mama ikitokea sehemu ndani ya nyumba ile. Alikuwa akiongea na nani? Aliniambia kuwa Koku alikuwa ameshaenda kazini, sasa huyo anayeongea naye ni nani? Niliinuka taratibu na kuelekea kule niliposikia sauti yake ikitokea.

    Nilimkuta akiwa katika chumba cha kulia chakula. Alikuwa amekaa kwenye kiti akiwa amenigeuzia mgongo na alikuwa anaongea na simu, na alikuwa akimbembeleza kitu fulani huyo aliyekuwa akiongea naye. Nilisimama kando ya mlango wa kuingilia kule alipokuwepo na kujaribu kusikiliza maongezi yale huku moyo ukinienda mbio.

    “...nataka nijue ni wapi hayo matibabu yatakapofanyika na mimi nataka niwepo...”

    Usingizi ulinikauka mara moja, nikazidi kusikiliza.

    “...yeye yupo hapa, lakini lazima na mimi niwepo...”

    Moyo ulinilipuka na kuongeza mapigo.

    Mama alikuwa anaongea na Dokta Martin Lundi!

    Nilichanganyikiwa.

    Haraka nilirudi kule sebuleni na kulinyakua lile begi langu dogo. Nilitembea haraka kuelekea mlango wa nyuma wa nyumba ile, na nilipopita tena kwenye ule mlango wa kuingia chumba cha kulia chakula, mama alikuwa ameshamaliza kuongea na simu.

    “U...unaenda wapi Tigga...usingizi umeisha mara hii?” Aliniuliza huku akinisogelea. Moyo uliniuma kuliko kawaida. Sikuweza kumtazama.

    “Na...naenda kulala chumbani...” Nilimjibu bila kumtazama na bila kupunguza mwendo wangu. Mwisho wa korido kabla ya kuufikia mlango wa nyuma wa nyumba ile kulikuwa kuna chumba cha wageni. Nilipokifikia nilisimama nje ya mlango wa chumba kile na kumgeukia mama yangu. Alikuwa amesimama akinitazama.

    “Ennh...naomba uniamshe ifikapo saa saba...” Nilimwambia kwa sauti ya chini huku nikifungua mlango wa kile chumba.

    “Sawa mama...” Alinijibu, kisha akanisogelea kwa hatua za haraka, nami nikamsubiri huku nikitazama sakafuni. Alinikumbatia kidogo na kunibusu kwenye paji la uso.

    “Lala unono mwanangu...yote yatakwisha tu, muamini mama yako.”

    Sikujua nimjibu nini, lakini machozi yalinitiririka nami nikageuza uso wangu ili asione jinsi nilivyoumia.Niliingia ndani ya kile chumba na kusimama nyuma ya mlango kwa ndani nikisikilizia mienendo ya kule nje huku moyo ukinipiga sana. Hakuna kilichotokea, kisha nikasikia maji yakimwagika jikoni na vyombo vikigongana. Nikahisi mama alikuwa akiosha vyombo jikoni.

    No time to waste!

    Nilitoka nje ya chumba kile taratibu na kufungua mlango wa kutokea nyuma ya nyumba ile taratibu mno. Nilitoka nyuma ya nyumba yetu na kuruka michongoma iliyofanya uzio wa kuizunguka nyumba ile na kutokea mtaa wa pili.

    Huku nikitiririkwa na machozi, nilitembea kwa mwendo wa kasi kuelekea nisiKokujua.

    Nilikimbilia kwa Kelvin, nikakutana na usaliti nisioutegemea na roho iliniuma sana. Lakini hili la kukuta usaliti kama ule kwa mama yangu liliniuma zaidi. Sasa nitakimbilia wapi? Kwa nini hawa akina Martin Lundi wanakuwa na uwezo wa kuwarubuni watu mpaka wanafikia hatua ya kunigeuka namna hii?

    Au inawezekana ikawa ni kweli mimi nina huo ugonjwa ninaosemekana kuwa ninao na mambo yote ninayoamini kuwa nimeyaona ni fikara zangu tu zenye maradhi?

    Lakini nilipopapasa begi langu na kuigusa ile kamera ya marehemu Gil, nilipata hakika kuwa niliyoyaona yalikuwa ni kweli tupu.

    Sasa ni nini hii?

    Hata mama yangu! Oh, My God!

    Ama kwa hakika sasa nilikuwa peke yangu, nisiye na kimbilio.

    Ili iweje sasa?

    Nilijua kuwa mama alifanya vile akiwa na imani,kuwa ananisaidia, kwamba anafanya kwa faida yangu.

    Lakini sivyo mama! Martin Lundi ni muongo na muuaji! Nitawezaje kusema hadi niaminike?

    Nilikuwa nikiwaza mambo hayo na mengi mengine huku nikipotelea mitaa ya nyuma kutoka ule uliokuwamo nyumba yetu. Sikuwa na uelekeo maalum, na kwa wakati ule sikujali. Jambo pekee nililojali kwa wakati ule ni kujiweka mbali na mikono ya yule mtu mbaya anayejiita Martin Lundi, na kundi lake.

    Bila ya kujua nilikuwa nimezunguka na kufuata mtaa uliotokea mwanzoni mwa ule mtaa ambao nyumba yetu ilikuwepo. Nikiwa nimesimama mwanzoni mwa mtaa ule, niligeuka kutazama upande ilipokuwepo nyumba yetu ambapo ni katikati ya ule mtaa. Nilishuhudia kwa kihoro magari matatu yakisimama kwa kasi na vishindo nje ya nyumba yetu na watu wakiremka na kukimbilia nyumbani kwetu, huku wengine wakiizingira nyumba ile kwa nje. Nilidhani nilimuona Dokta Lundi miongoni mwao. Lakini kwa umbali ule sikuweza kuwa na uhakika. Niliogeza hatua na kupotea eneo lile nikimwomba Mwenyezi Mungu amsaidie mama yangu.

    iv.



    S

    iwezi kuelezea jinsi nilivyoumizwa na kitendo cha mama yangu kuamua kumuamini yule shetani anayejiita Martin Lundi na kupuuzia kabisa utetezi wangu. Kwa kweli hakuna maneno ambayo ninaweza kuyatumia hata yakatosha kuonesha ni kiasi gani jambo lile lilikuwa limeniumiza, kwani ilikuwa ni kupita kiasi. Ni kweli kuwa pale nilipogundua kuwa Kelvin aliamua kunisaliti kwa yule shetani Martin Lundi hata nilipompa maelezo yangu, niliumia hata nikahisi kama kuna ndoana iliyokuwa ikiuvuta moyo wangu kwa nguvu kubwa; lakini kuumia nilikoumia kutokana na hali iliyotokea pale kwa mama yangu, kulikuwa ni zaidi ya hivyo.

    Lakini sikuwa na la kufanya, lililotokea lilikuwa limetokea, na aliyelifanya ni mama yangu.

    Angalau kwa Kelvin niliweza kuamua kuvunja uchumba na kuachana naye, lakini huyu alikuwa mama yangu! Mama aliyenizaa kwa uchungu mwingi. Sasa vije mtu kama Dokta Lundi akaweza kumrubuni, kumlaghai na kumshawishi hata akaweza kumuamini yeye na akashindwa kuamini maelezo ya mwanae mwenyewe ambaye alipata uchungu usio mfano wakati akimzaa?

    Nilishindwa kuelewa, na nilizidi kuchanganyikiwa iliponibainikia kuwa hata ningefanya nini, nisingeweza kumfuta asiwe mama yangu kama jinsi nilivyoweza kumfuta Kelvin kutoka katika maisha yangu (sijui naye yu hali gani huko aliko). Hivyo nilimwomba Mwenyezi Mungu amnusuru mama yangu na ghadhabu za Dokta Lundi baada ya kufika pale nyumbani na kukuta kuwa nimewatoroka kwa mara nyingine tena, wakati yeye aliwapigia simu na kuwahakikishia kuwa nilikuwepo pale nyumbani.

    Baada ya kuwashuhudia kwa mbali akina Martin Lundi wakiizingira nyumba yetu, nilielekea moja kwa moja kituo cha basi na kupanda basi nililolikuta likipakia abiria pale kituoni bila ya kujali lilikuwa likielekea wapi, lengo likiwa ni kupotea kabisa eneo lile. Na njia nzima wakati basi lile likifanya safari yake ambayo nilikuja kuelewa baadaye kuwa lilikuwa likielekea posta, nilikuwa ni mtu niliyepigwa bumbuwazi. Woga ulinitawala kupita kiasi kwani sasa ilikuwa imenifunukia wazi wazi kichwani mwangu kuwa katika janga hili nilikuwa peke yangu.

    Nilikwangua akili yangu nikijaribu kutafuta ni hatua ipi ifuate lakini niliambulia ukungu tu. Nilifikiria kumfuata dada yangu Koku kazini kwake, lakini nililifuta wazo hilo haraka, kwani nilijua kuwa asingeweza kunisaidia lolote katika mazingira yale. Nilijua iwapo mama ameamua kuchukua msimamo aliouchukua katika swala langu, hakuna shaka kabisa kuwa na yeye atakuwa na mtazamo ule ule.

    Nilidhani kuwa Koku angeweza kusaidia kwa kumbana Dokta Lundi kwa maswali ya kitaalamu juu ya ule ugonjwa anaonipakazia na hatimye kubainisha uongo wake, lakini kama angefanya hivyo, basi hata mama angekuwa na mtazamo tofauti. Lakini pia nilikumbuka kuwa, dada yangu alikuwa ni nesi wa kawaida tu.Yumkini akawa hana uwezo na utaalamu wa kuuelewa ugonjwa ule kama jinsi alivyouelewa Dokta Martin Lundi muongo.

    Sasa nifanye nini...?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliamua kwenda ofisini kwangu, katika jumba la Makumbusho ya Taifa. Huenda huko nikapata baadhi ya majibu ya maswali yangu. Kwani si huko ndipo iliposemekana kuwa ile barua ya uongo iliyopelekwa kwa mkuu wa wilaya ilikuwa imetokea? Sasa niliona kuwa iwapo nilikuwa nashutumiwa kwa mambo yasiyo na msingi, basi ni wajibu juu yangu kutafuta kiini cha shutuma hizo. Shutuma za kuwa nilikuwa mgonjwa wa akili zilikuwa ni nzito na mbaya sana. Nilijua kuwa ile barua ilikuwa imeghushiwa, na hata kule ofisini haijulikani kuwa kulikuwa kuna barua kama ile. Lakini sikuwa na namna ya kujithibishia hilo isipokuwa kwenda ofisini. Aidha nilijua kuwa kwa vyovyote iliniwajibikia kuripoti pale ofisini baada ya kutoka kwenye ile safari iliyozaa balaa niliyotumwa na ofisi. Sikujua ningekutana na nini huko nilipoazimia kwenda, lakini sikuona njia nyingine ya kuanza kutafuta ukweli wa mambo yale ya uongo niliyopakaziwa zaidi ya ile.

    Niliingia ndani ya jengo la ofisi yetu na kuelekea moja kwa moja ofisini kwa afisa utumishi, ambaye ndiye muangalizi wa maswala yote ya wafanyakazi na ajira zao, lakini kabla sijaifikia ofisi yake niliwahiwa kwenye korido na baadhi ya wafanyakazi wenzangu ambao walinizingira kwa maswali kemkem kuhusu matukio ya huko msituni. Wapo walionipa pole, wapo walioulizia ilikuwaje hadi wenzangu wakaangamia kule porini, wengine walikuwa wakiniambia kuwa kwa kujipeleka pale ofisini nilikuwa nimejitia kwenye mtego na kunishauri niondoke haraka, huku wengine wakionesha wazi kuwa walikuwa wakiniogopa. Sikuweza kujibu swali hata moja, kwani yalikuwa yakija bila mpangilio maaluim, nami nilianza kuingiwa na woga na kujuta kwa nini niliamua kwenda pale ofisini. Niligundua kuwa habari zangu zilikuwa zimefika pale ofisini, na kwamba kwa ujumla ilieleweka kuwa Tigga si mtu salama tena kuwa karibu naye. Hili nililibaini kutokana na hali iliyojitokeza pindi nilipoingia pale ofisini, kwani wenzangu walikuwa wakiniuliza maswali yale na kunipa pole huku wakinitazama kwa wasiwasi, na muda wote walikuwa kikundi, hakuna hata mtu mmoja aliyekuwa tayari kukaa na mimi peke yake. Nikiwa nimezingirwa na wale wafayakazi wenzangu pale kwenye korido, nilimuona Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho akitoka ofisini kwake, iliyokuwa kwenye ghorofa ya kwanza, na kuchungulia pale chini nilipokuwa nimezongwa na wafanyakazi wenzangu. Tulitazamana kwa muda, kisha alirudi ofisini kwake na kufunga mlango.

    Hatimaye nilifanikiwa kujichomoa kutoka kwenye lile kundi la wafanyakazi wenzangu na kuingia ofisini kwa afisa utumishi.





    “Heey! Tigga! Karibu mrembo...karibu...” Suleiman Kondo, afisa wetu wa utumishi alinikaribisha huku akiweka chini simu aliyokuwa akiongea nayo muda mfupi kabla ya ujio wangu, naye akiinua mwili wake mkubwa na mzito na kusimama kwa heshima yangu. Hili ni jambo ambalo halijawahi kutokea.Hata siku moja Suleiman hajawahi kunikaribisha kwa kusimama, leo vipi hadi kusimama? Nilitembeza macho haraka mle ndani na kugundua kuwa ile simu aliyokuwa akiongea nayo ilikuwa ni ile niliyoijua kuwa huwa ina mawasiliano ya moja kwa moja na ofisi ya Mkurugeenzi.

    “Nimekuja kuripoti Suleiman...na kuleta taarifa za maafa yaliyotokea huko Manyoni.” Nilimwambia.

    “Oke...karibu na pole sana Tigga. Tumeingiwa na msiba mkubwa...wenzetu wametutoka...what happened out there Tigga?” Suleiman alisema kwa huzuni huku akinitazama usoni, na kunitupia swali akitaka nimweleze ni kipi kilichotokea kule msituni. Sikufanya haraka kumjibu bali akilini mwangu nilikuwa nikijaribu kuisoma hali ya mle ndani iwapo ilikuwa na maslahi nami au bado nilikuwa nakabiliwa na vikwazo kutoka kwa watu wangu. Niliketi kwenye kiti mbele ya meza yake na kwa mara nyingine Suleiman alitaka kujua ni kipi kilichojiri kule Manyoni. Lakini kabla sijamueleza kilichojiri Manyoni, nilimuuliza swali langu la msingi.

    “Suleiman...hivi kuna barua yoyote iliyotoka hapa ofisini kwenda kwa mkuu wa wilaya Manyoni wakati tukiwa kule?”

    Suleiman alionekana kutoelewa maana ya swali lile, lakini niliona kuwa hakuwa akielewa lolote juu ya kuwepo kwa barua hiyo.

    “Si kuna barua iliyotoka hapa ambayo mlipewa kwa ajili ya kuiwasilisha kwa Mkuu wa wilaya baada ya kufika huko?” Alinijibu kwa swali. Nilimjibu kuwa ni kweli, lakini nilikuwa nauliza kuwa iwapo kuna nyingine iliyotumwa kwa fax kutokea pale ofisini kwenda kule kwa mkuu wa wilaya baada ya sisi kufika kule.

    “Hakuna. Ni wapi umepata mawazo hayo, na ni nani aliyeandika barua hiyo?” Alinijibu kwa uhakika kabisa na kunihoji zaidi.

    “Nimeiona hiyo barua kwa mkuu wa wilaya na imesainiwa na Mkurugenzi mwenyewe...nimeiona saini yake kabisa!” Nilimjibu kwa uhakika.

    “Hakuna, haiwezekani. Barua zote za Mkurugenzi huwa nazitayarisha mimi, sekretari wake anazitaipu kwa kompyuta, na yeye anasaini tu...huo ndio utaratibu, na hakuna barua yoyote iliyotoka hapa kwenda Manyoni baada ya nyie kuondoka.” Suleiman alinijibu, nami nilimuelewa kwani huo ndio utaratibu uliokuwepo pale ofisini.

    Kwa hiyo ile barua ya akina Martin Lundi ilikuwa imeghushiwa.

    “Hebu nieleze ni nini hasa kilichotokea huko Manyoni Tigga? Kwa sababu hapa wamekuja wana usalama wakikusaka kuhusiana na mauaji ya wenzetu kule msituni, na tuhuma nyingine za ajabu sana kuwa ulifanya fujo katika ofisi ya mkuu wa wilaya...infact, wamesema kabisa kuwa wewe ni fugitive from justice, sasa hiyo ni hali mbaya sana Tigga, na inatuweka sisi kama waajiri wako katika wakati mgumu sana.”

    Nilimtazama Suleiman kwa muda nisijue nimueleze nini, kwani yale maneno yake yalinitisha sana, ingawa taarifa yake haikuwa ngeni kabisa akilini mwangu.

    Fugitive from Justice Nililitafakari lile neno na mwili ukanisisimka.

    Mkimbizi kutoka katika mikono ya sheria.

    “Naona ni bora nikitoa maelezo ya safari yetu na mambo yaliyotokea kwa Mkurugenzi, Suleiman...nadhani na wewe utahitajika uwepo.” Nilimwambia huku nikiinuka. Suleiman alionekana kusita kidogo, kisha akaafikiana nami, lakini kwa mashaka. Sikuelewa ni kwa nini alisita, ila niliona kuwa sikuhitajika kutumia muda mwingi sana pale ofisini. Baada ya kutoa maelezo yangu niliazimia kuchukua likizo ili nipate muda wa kuzidi kutafuta namna ya kukabiliana na mtihani huu ulionikabili, na kujaribu kutafuta ukweli wa matukio yale ya ajabu.

    Tulipoingia ofisini kwa Mkurugenzi tu nilihisi kuwa nilikuwa nimeingia kwenye matatizo, kwani moja kwa moja niliona kuwa yule mzee wa makamu ambaye tulizoea kumwita “mkuu” tukimaanisha mkuu wa idara, alikuwa ameshadhamiria kunituhumu, bila shaka akiwa na taarifa za mambo niliyofanya kule Manyoni, na zile taarifa potofu zilizotoka kwenye gazeti siku chache zilizopita. Baada ya kumuamkia aliniuliza iwapo ndio siku ile nilikuwa nimeingia kutoka Manyoni, nikamjibu kuwa niliingia jijini jioni ya siku moja iliyopita. Yule mzee ambaye huwa tunamuogopa sana kutokana na mtindo wake wa uongozi ambao ni wa ukali na amri, alimwita katibu muhtasi wake na kuniambia nitoe maelezo ya safari yangu na mambo yote yaliyotokea huko Manyoni, wakati yule katibu muhtasi wake akinukuu maelezo yangu kwenye kompyuta.

    Nilieleza mkasa wote wa safari yetu na mambo yote yaliyotokea kule Manyoni tangu pale nilipoishuhudia ile helikopta ikitua kule msituni, jinsi akina Ibrahima Geresha walivyowekwa chini ya ulinzi na wale watu wabaya ambao mmoja wao hivi sasa nilimjua kwa jina la Martin Lundi. Wote walikuwa kimya kabisa wakisikiliza maelezo yangu, nami nilikuwa makini sana kwa kutoeleza mambo niliyoongea na yule mtu asiye na jina kule msituni wakati wale wauaji walipoondoka na wenzangu.Nikawaelezea jinsi nilivyorudi kule kambini kwetu na kuwakuta wenzangu wakiwa wameuawa na kudonolewa na ile midege mibaya. Hapa nilishindwa kujizuia, na machozi yalinitoka upya, na mara kadhaa nililazimika kushindwa kuendelea na maelezo yangu nikielemewa na kwikwi, na niliona hata yule katibu muhtasi wa kamishna naye alikuwa akitirikwa na machozi. Nilielezea jinsi nilivyolikuta begi langu nje ya hema na jinsi nilivyoweza kufika hadi ofisini kwa mkuu wa wilaya, na mambo yaliyotokea huko.

    Hapa niliona kuwa Kamishna alizidisha umakini, na nikaelezea juu ya ile barua iliyotumwa kwa fax kwa mkuu wa wilaya ikisemekana kuwa imetokea pale ofisini.

    “Hakuna barua ya aina hiyo msichana! Huo ni uzushi sasa!” Hapo Kamishna aliingilia kati kwa ukali. Nilimtazama kwa kutoelewa.

    “Uzushi kivipi mkuu...? Kwamba hiyo barua haikuwepo, au unadhani kuwa mimi ninazusha juu ya kuwepo kwa barua hiyo?” Nilimuuliza kwa mashaka.

    “Uzushi! Hakukuwa na barua ya aina hiyo iliyotoka hapa ofisini kwenda huko kwa Mkuu wa wilaya...labda wewe unataka kutuchanganya tu kwa kuleta hadithi za barua za ajabu ajabu...”

    “Aaah! Mkuu! Ni wewe ndiye uliyesaini ile barua, na sehemu ya maelezo yangu yaliyotolewa kwenye ile barua yalikuwa ni yale yanayoweza kupatikana kwenye faili langu la ajira hapa ofisini!” Nilimjibu kwa jazba, kisha nikaendelea kuwaeleza jinsi nilivyoikana ile barua mbele ya mkuu wa wilaya kuwa ni ya kughushi. “Hakukuwa na barua ya aina hiyo!” Kamishna alizidi kusisitiza, kisha akaendelea, “Unaweza kutuonesha hiyo barua?”

    Nilimjibu kuwa niliiacha pale pale kwa mkuu wa wilaya, na nikamwambia kuwa nina imani itakuwepo kwa mkuu wa wilaya iwapo wataamua kuifuatilia, kwani kule walikuwa wameamini kabisa kuwa ilikuwa imetokea pale ofisini.

    Mkuu alinitazama kwa muda huku nikiona wazi kuwa alikuwa haniamini. Kisha bila ya kusema neno aliniashiria niendelee na maelezo yangu.

    Nilieleza kisa chote hadi kufikia pale nilipoingia ofisini asubuhi ile.

    Baada ya hapo ofisi yote ilibaki kimya. Kamishna alinitazama kwa muda mrefu wakati yule binti aliyekuwa akinukuu maelezo yangu akitoa nakala ya yale maelezo na kumkabidhi. Aliyatazama kwa muda na kunipatia akiniambia niyapitie iwapo yalikuwa ni sawa na nilivyoeleza. Nilisoma maelezo yale yaliyotoka kurasa saba, na kutoa marekebisho machache ambayo yule dada aliyarekebisha kwenye kompyuta yake na kutoa nakala nyingine ambayo ilikuwa sawa.

    Kwa makusudi kabisa nilikuwa nimeacha kuelezea juu kuwepo kwa mkanda wa video uliokuwa na ushahidi wa yale mauaji ya kule msituni.

    Niliweka saini yangu chini ya maelezo yale. Kisha Suleiman Kondo naye alisaini kama shahidi aliyekuwepo wakati nikitoa maelezo yale, na Kamishna mwenyewe. Yule dada aliambiwa arudi ofisini kwake na kuendelea na kazi zake.

    Kilichofuatia ni mahojiano marefu baina yangu na Kamishna ambayo kwa ufupi yalikuwa yanahitaji kuelewa mtazamo wangu juu ya swala lile. Kwa nini yale mauaji yatokee, kwa nini wale wauaji waghushi ile barua iliyokuwa ikinitangazia mimi ule ugonjwa wa akili, kwa nini mkuu wa wilaya alionekana kuwaamini zaidi wale madaktari badala yangu. Sikuwa na majibu ya kuwatosheleza juu ya mengi ya maswali yao, kwani mimi mwenyewe nilikuwa natafuta majibu hayo, ila jibu kubwa nililowapa lilikuwa ni juu ya sababu nilizodhani kuwa ziliwafanya wanipakazie ule ugonjwa wa uongo, kuwa walifanya kusudi kunipakazia ugonjwa huo ili taarifa nitakazotoa dhidi yao na mambo niliyoona wakiyafanya kule msituni zitiliwe mashaka na kila mtu.

    Swali kubwa kabisa aliloniuliza mkuu wangu wa kazi ni kwa nini muda wote tangu mambo yale yalipojitokeza sikuenda kuripoti polisi. Hili kwake lilikuwa ni jambo la muhimu sana, na alishindwa kuelewa kuwa kama sikuwa na matatizo, kwa nini nilishindwa kwenda polisi.

    “Mkuu wale watu tayari walikwishaonesha kuwa wana namna ya kuingiliana na vyombo vya dola kwa maslahi yao! Nilishindwa kwenda polisi kienyeji tu bila ya kuwa na uhakika wa hali nitakayoikuta huko...” Nilijaribu kuwaelewesha lakini niliona kuwa swala lile lilikuwa gumu kueleweka. Sikuweza kuwaeleza kuwa nilishindwa kwenda polisi kwa sababu nilikuwa nahofia usalama wa ule mkanda wa video wenye ushahidi, kuwa huenda ungeangukia mikononi mwa askari mwenye uhusiano na wale wauaji. Kwa usalama wangu, sikuwaeleza kabisa juu ya kuwepo kwa huo mkanda tangu mwanzo, sasa wangeelewa vipi? Ilikuwa ni hali ngumu.

    “Tigga, samahani sana binti, lakini lazima nikueleze kuwa hii taarifa yako ni ngumu sana kuiamini...mimi binafsi naiona kama masimulizi ya filamu ya kubuni tu.” Hatimaye Mkurugenzi aliniambia, na nikaona na afisa utumishi wetu, Suleiman Kondo naye akitikisa kichwa kuafikiana naye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa nifanyeje wakuu wangu? Maana mi’ nimekuja kwenu kwa msaada...” Nilisema huku nikiwatazama kwa zamu. Badala ya kunijibu, Mkurugenzi aliinuka na kuingia chooni, ambacho kilikuwa kimejengwa humo humo ndani ya ofisi yake.

    Kama Masterbedroom ya Kelvin...

    Tulibaki na Suleiman Kondo mle ofisini, nami nikajaribu kumdadisi juu ya hatua iliyopaswa kufuatwa.Lakini Suleiman alionekana kuwa na mashaka sana na kuongea lolote na mimi tukiwa peke yetu. Nilianza kujiuliza kwa nini, lakini mara nilipata jibu na moyo ulinifa ganzi.

    Mkurugenzi alitoka kule chooni na kuingia tena pale ofisini akiwa amefuatiwa na afisa wa jeshi la polisi!

    “Ni wajibu wangu kukukabidhi kwenye mikono ya sheria Tigga, sehemu pekee ambayo nadhani swala lako linaweza kushughulikiwa ipasavyo.” Mkurugenzi aliniambia huku akimtanguliza yule afisa wa polisi.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog