IMEANDIKWA NA : BEKA MFAUME
*********************************************************************************
Simulizi : Siku Ya Utakaso
Sehemu Ya Kwanza (1)
Saa nane hii! Inno alishangaa kuuona muda huo kwenye saa. Alishangaa kwa sababu simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita usiku huo na kumshitua usingizini, ikawa bado inaendelea kuita. Karaha ya kushituliwa kwake usingizini ndiyo iliyomfanya auangalie muda. Akashangaa na kujiuliza, ni nani angekuwa anampigia simu wakati kama huo?
Simu iliyokuwa ikiita ilikuwa ni simu yake maalumu na iliyokuwa imesajiliwa majina ya watu maalumu hasa viongozi wa serikali. Wakati akiinuka na kuunyoosha mkono wake kando ya kitanda kwenye meza ndogo kuichukua, alijikuta akiingiwa na mashaka kuwa, huenda simu inayopigwa, ni simu inayotoka Ikulu. Hakujua ni kwa nini aliingiwa na wasiwasi huo!
“Nani?” mkewe aliyekuwa amelala ubavuni mwake akiwa ameuelekeza mgongo upande aliko mumewe, aliuliza bila ya kusumbuka kujigeuza kumwangalia mumewe.
“Sijui ni nani anayenipigia saa hizi,” Inno alijibu huku akiionyesha fadhaa ya kukatizwa kwa usingizi wake. Wakati huo huo aliichukua miwani yake ya kusomea na kuivaa ili aweze kulisoma jina la mpigaji kabla hajaipokea. Simu ikaacha kuita. Hakuwa na wasiwasi kwa simu hiyo kuacha kuita, alikuwa na uhakika mpigaji angepiga tena.
Ikapigwa tena, Inno akaangalia kwenye kioo cha simu, akaliona jina la Profesa Feza ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani. Kukamshangaza, kulimshangaza kwa sababu pamoja na kwamba Waziri huyo ni mkuu wake wa kazi na pia ni rafiki yake, lakini hakuwa na tabia ya kupiga simu muda kama huo. Moja kwa moja akatabiri kuwa, asingepigiwa simu na Profesa Feza kwa muda huo bila ya kuwa na tatizo, tatizo ambalo alilihisi litakuwa kubwa! Akaipokea simu.
“Ndiyo Mkuu,” Inno alisema kwenye simu.
“Unayo taarifa kuhusu Himidu?” sauti ya Profesa Feza ilisikika kwenye simu. Ilikuwa nzito na iliyoonyesha ametoka usingizini.
Kuna tatizo! Inno aliwaza. “Himidu huyu Waziri wa Miundombinu?” akajikuta akiuliza swali la kipumbavu.
“Kuna Himidu mwingine tunayemjua mimi na wewe zaidi ya huyu?”
“Ana nini?” Inno aliuliza kwa sauti aliyojaribu kuiweka kwenye utulivu.
“Ameuawa usiku huu kwa kupigwa risasi!”
“Mungu wangu! Nani aliyempiga risasi?” Inno aliuliza kwa kihoro, utulivu wa sauti yake ukapotea.
“Hajulikani na bado hajakamatwa. Sasa hivi nafanya utaratibu ili taarifa hizi ziweze kumfikia mheshimiwa Rais. Baada ya hapo nitaelekea hospitali ya Muhimbili iliko maiti ya Himidu. Tukutane huko,” simu ikakatwa.
Inno alishusha kwa nguvu pumzi za mara moja, simu yake ikaita tena. Akadhani ni Profesa Feza anapiga tena, lakini alipoangalia kwenye kioo cha simu likawa siyo jina la Profesa, alikuwa ni Mkuu wa kituo cha polisi Oysterbay. Akaipokea.
“Mkuu, mheshimiwa Himidu ameuawa usiku huu,” sauti kutoka upande wa pili wa simu ilisema.”
“Nimeshazipata taarifa hizo,” Inno alisema kwa utulivu. Kisha akauliza, “Mkewe kishapewa taarifa za kuuawa kwa mumewe?”
“Bado Mkuu, tunaangalia taratibu za kumpelekea taarifa hiyo.”
“Asipigiwe simu. Nitamtuma mtu wa kuzipeleka taarifa hizo kwake.”
“Ndiyo Mkuu.”
“Wewe uko wapi?”
“Tuko njiani kuelekea hospital ya Muhimbili.”
“Una taarifa yoyote inayomuhusu mwuaji?”
“Bado hajapatikana.”
“Tuonane Muhimbili,” Inno alisema na kukata simu. Akainuka mzima mzima kutoka kitandani na kusimama. Simu aliyoiacha kitandani ikaita tena. Akageuka na kuiangalia huku akionekana kujiuliza aidha aipokee au aiache iendelee kuita. Mkewe akamsaidia kumpatia ufumbuzi wa swali lake kwa kuichukua simu hiyo na kunyoosha mkono kumpa. Akaipokea na kuangalia jina la mpigaji, alikuwa ni mmoja wa Makamishina wa polisi wa kanda maalumu. Akajua naye alipiga kwa ajili ya taarifa za mauaji hayo. “Yes, Denyo,” alisema.
“Mkuu, umekwishazipata taarifa…”
“Nimekwishazipata, Denyo. Tuonane Muhimbili ndani ya nusu saa,” Inno alimkatisha mzungumzaji wa kwenye simu kwa kumpa jibu fupi. Akaikata simu yake kisha, akaizima. Alikwishajua simu za aina hiyo zingeandamana kwa mfulululizo usiku huo kutoka kwa watu mbali mbali kutokana na wadhifa alionao wa Inspector General of Police.
“Vipi?” mkewe aliuliza huku akimwangalia mumewe aliyekuwa tayari ameanza kuvua pajama na kujiandaa kuvaa nguo za kutoka.
“Mheshimiwa Himidu ameuawa kwa kupigwa risasi,” Inno alisema. Kisha kwa haraka haraka akaongezea kusema, “Mwuaji bado hajajulikana,” alisema hivyo kumuwahi mkewe kabla hajauliza swali hilo.
“Itanibidi niende nyumbani kwake kumpa pole mkewe,” mkewe Inno alisema na kujiinua kutoka kitandani.
Inno akamwangalia kwa jicho la haraka mkewe na kumshangaa. Ni muda mfupi nimetoka kulizungumzia suala hili, ina maana hakunisikia? alijiuliza. “Subiri mpaka asubuhi,” Inno alisema bila ya kumwangalia mkewe. “Mpaka sasa bado hajapewa taarifa za kifo cha mume wake.
Mkewe Inno akajirudisha taratibu kitandani na kuendelea kumwangalia mumewe aliyekuwa akimaliza kuvaa.
“Tutaonana baadaye,” Inno alisema na kumgusa mkewe kwenye bega kisha, akatoka.
* * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Viongozi wengine wa serikali walikuwa wamekwisha kuwasili na wengine wakiendelea kuwasili wakati IGP Inno alipowasili hospitali ya Muhimbili na moja kwa moja alipelekwa kuiona maiti ya Himidu na kuihakikisha. Ingawa ilikuwa ni usiku mwingi lakini wingi wa watu waliokuwepo hapo na magari yaliyojazana iliweza kuibadilisha hali hiyo na kuufanya muda huo uonekane kama ulikuwa bado ni mapema. Kila kiongozi aliyewasili hapo alipokelewa kwa itifaki iliyozingatiwa kutokana na wadhifa wake. Ukimya uliofanywa na umma uliokuwepo hapo ulionyesha dhahiri hali ya huzuni iliyowakumba. Sura zao zilionyesha majonzi kutoka kwenye vikundi vikundi vilivyokuwa vimejikusanya ambavyo vilionekana kukatisha mazungumzo wanayozungumza kila lilivyowasili gari lenye hadhi na kuonyesha kuwa, aliyewasili ni mkubwa fulani na waliokuwepo kuonyesha udadisi wa kutaka kumjua.
Saa chache baadaye, wakuu wa jeshi la polisi walikutana katika kikao kisicho rasmi kuzungumzia hatua inayofuata ya kuhakikisha mwuaji anapatikana kwa udi na uvumba ili kuonyesha uwezo wa wa umahiri wao kiutendaji.
“Inasemekana mheshimiwa aliuawa wakati akitoka nyumbani kwa kimada wake?” mmoja wa wakuu hao aliuliza.
“Ni kweli,” Mkuu wa kituo cha Oysterbay alisema. “Aliuawa akiwa hatua chache kabla ya kulifikia gari lake. Kimada wake alikuwepo kwenye tukio wakati Himidu akipigwa risasi, lakini alishindwa kumwona mwuaji. Pamoja na kimada wake kupiga kelele za kuita msaada na kujitokeza majirani wachache ambao walijaribu kumtafuta mwuaji, nao hawakuweza kufanikiwa kumwona wala kujua lolote kama mwuaji huyo alikuja na gari au vipi, kama ni mwanamume au mwanamke! Haya ndiyo maelezo niliyoyapata kutoka kwa mmoja wa askari wangu aliyewahi kufika eneo la tukio ambaye alijaribu kuchukua maelezo ya hapa na pale kutoka kwao.”
“Utaifichaje habari hii kwa waandishi wa habari?” Inno aliuliza huku akimwangalia Kamanda wa mkoa wa Kinondoni ambaye ndiye mwenye mkoa uliotokea mauaji na ndiye atakaye wajibika kukutana na waandishi wa habari.
“Kuificha kivipi?” mkuu wa kituo aliuliza.
“Endapo kama watafahamu Himidu alikuwa akitoka kwa kimada wakati alipouawa, ujue kwamba magazeti yote yatatoa umuhimu wa mauaji haya kwa kulipa umuhimu suala la kimada kwenye vichwa vya kurasa za mbele na uzito wa kuuawa kwake ukafuatia baadaye. Kunatakiwa kutolewe maelezo mbadala yasiyomuhusisha na kimada wake.”
“Sitosema aliuawa akitoka kwa kimada wake,” Kamanda wa mkoa wa Kinondoni alisema. “Nitasema aliuawa akiwa kwenye gari lake. Na kama kutatokea yeyote atakayeniuliza kuhusiana na suala la kimada, nitamjibu kuwa, tupo kwenye uchunguzi wa hilo alilouliza. Nitakuwa nimemfunga mdomo.”
“Kulikuwa na minong’ono pale Muhimbili kuwa, wakati Himidu akiuawa hakukuwa na mlipuko wowote wa risasi uliosikika. Ni kweli?” afisa mwingine wa ngazi ya juu wa jeshi la polisi aliuliza.
“Hilo nalo ni kweli,” alijibu mkuu wa kituo cha Oysterbay. “Hakukuwa na mlio wowote wa bunduki. Nadhani mwuaji alitumia kiwambo cha kuzuia mlio kwenye silaha aliyoitumia.”
“Kwa hiyo mwuaji alikusudia kumwua mheshimiwa Himidu. Mnadhani inawezekana ni mauaji yanayohusiana na mambo ya kisiasa?”
“Kwamba ni chama cha upinzani kinaweza kikahusika na mauaji yake?”
“Si lazima kiwe cha upinzani, hata ndani ya chama tawala kunakuwepo upinzani wa kisiasa wa wenyewe kwa wenyewe.”
“Nadhani ni mapema mno kukimbilia kwenye siasa,” IGP alisema. ‘Nina wasiwasi mauaji yake yametokana na mambo ya wivu. Hilo mnalionaje?”
“Lina nafasi yake,” mwingine aliunga mkono. “Upo uwezekano wa kimada wake kuwa na bwana mwingine ambaye amechukizwa kwa kumwona mheshimiwa ameingilia kati kumchukulia mpenzi wake. Inawezekana akaamua kuufanya uamuzi huu kwa ajili ya kulipiza kisasi. Ni vyema tukaanzia na eneo hilo kuanza kumtafuta mwuaji wetu. Kuna haja ya kumchunguza huyu kimada kama alikuwa akitembea na bwana mwingine na wakati huo huo akitembea na mheshimiwa Himidu. Pia, upo uwezekano kwa kimada huyu kumtema hawara au mchumba aliyekuwa naye baada ya kumpata mheshimiwa Himidu na aliyetemwa anaweza akachukua hatua kama hii ya kuua, hivi vyote vinahitajika vichunguzwe. Na hata mimi nimeanza kuingiwa na dhana ya kuwa, mauaji ya mheshimiwa Himidu huenda yametokana na wivu wa mapenzi.”
“Hii ni kazi tutakayowakabidhi vijana wetu waifanye kwa nguvu zote mpaka wampate mwuaji,” IGP Inno alisema na kumwangalia Mkuu wa kituo cha Oysterbay. “Ni vijana wako ndiyo watakayoifanya kazi hii, lakini nataka vijana mahiri wenye kufanya kazi. Unao?”
“Ninao Mkuu,” Mkuu wa kituo cha Oysterbay alikiri.
“Panga timu yako unayoijua itakayoweza kufanya kazi nzuri ili mwuaji apatikane. Nitakupa msaada wowote utakaoutaka ili mradi mwuaji apatikane kwa haraka. Una swali lolote?”
“Sina Mkuu,” Mkuu wa kituo cha Oysterbay alijibu.
“Siyo vibaya hata ukiweka tathimini; unadhani zoezi lako litachukua muda gani mpaka kumpata mwuaji?”
“Nipe kati ya wiki moja mpaka mbili, nadhani kwa muda huo vijana wangu watakuwa wamempata mwuaji.”
IGP Inno akamgeukia kamanda wa kanda ya Kinondoni. “Jiandae kukutana na waandishi wa habari,” alisema. “Hakikisha maelezo yako hayagusi katika unasaba wowote utakaohusisha kifo cha mheshimiwa Himidu na kimada wake.”
“Ndiyo mkuu nimeelewa,” kamanda wa kanda ya Kinondoni alisema.
Kunguru wakiwa wameanza kuitana kuashiria kuwa kumekucha, kikao cha wakuu hao wa jeshi la polisi nacho kikawa kimemalizika huku wote wakimsisitiza Mkuu wa kituo cha Oysterbay ahakikishe anapanga timu nzuri itakayoweza kufanikiwa kumpata mwuaji haraka iwezekanavyo.
Kikosi maalum kilichoundwa kwa ajili ya kumtafuta mwuaji wa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu mheshimiwa Himidu, kiliundwa chini ya uongozi wa kachero aliyejulikana kwa jina la Nunda. Halikuwa jina lake halisi, jina hilo alipewa na wakuu wake wa kazi kutokana na utendaji wake kikazi uliompa sifa ya ukatili wa kuwatesa watuhumiwa mbalimbali walionekana kuwa sugu wa kutokukubali kukiri makosa yao. Ni yeye ndiye mwenye uwezo wa kulazimisha watuhumiwa kukiri makosa wanayotuhumiwa nayo kwa kuwataja wahalifu wenzao au kuonyesha mahali zilikofichwa silaha, baada ya kushindwa kuyavumilia mateso yaliyokuwa yakitolewa na kachero huyo.
Maelekezo ya kwanza aliyopewa Nunda na Mkuu wake wa kituo ni kupeleleza kama aliyekuwa kimada wa mheshimiwa Himidu alikuwa na bwana au mabwana wengine aliokuwa akitembea nao kwa siri wakati akiwa na mheshimiwa Waziri. Hali kadhalika alitakiwa ayachunguze maisha ya kila siku aliyokuwa nayo kimada huyo.
Nunda alilianza zoezi hilo akiwa na timu yake ya watu watano ambao waliwatumia watoa habari wao wa mitaani waliojulikana kwa jina la ‘mainfoma’ waliokuwa wakimfahamu kimada huyo kuwapatia taarifa zake kabla ya Nunda kuanza kufanya mahojiano ya moja kwa moja na kimada huyo aliyeitwa, Husna.
Taarifa za Husna zikawa zimepatikana baada ya siku mbili. Sehemu za mvuto za kwenye taarifa hizo ni kuwa, Husna ana nyumba aliyokuwa akijengewa na mheshimiwa Himidu iliyokuwa kwenye hatua za mwisho za kumalizika. Anamiliki gari dogo la kifahari lenye bei mbaya na ana saluni na duka la vipodozi vyenye bei ghali vilivyopo katikati ya jiji. Kingine kwenye taarifa hiyo ni kuwa, Husna ana akaunti yenye pesa nyingi kwenye benki moja ya kigeni na ana bwana mwingine mwenye ajira ya kawaida ambaye anaishi maisha ya anasa na ni mtanashati wa kuvaa mavazi yenye bei ghali na aliyezidiwa umri na Husna kwa miaka miwili zaidi.
Gharama za maisha ya kijana huyo zimekuwa zikiendeshwa kwa kiasi kikubwa na Husna. Mara nyingi alikuwa akienda kulala nyumbani kwa Husna, nyumba ambayo Husna amepangiwa na marehemu Himidu. Muda ambao ulikuwa ukitumika kwa kijana huyo kwenda kulala ni muda na siku ambazo ama mheshimiwa Himidu akiwa safarini au siku ambazo ratiba zake hazitamfikisha nyumbani kwa Husna. Kijana huyo alijulikana kwa jina Beda ambaye Husna aliwahi kumtambulisha kwa mheshimiwa Himidu kuwa, ni mtoto wa mama yake mdogo.
Kachero Nunda na timu yake waliipiga picha nyumba ya Husna aliyokuwa akijengewa na Himidu, wakapiga picha gari yake na wakafanikiwa kumwona Beda kupitia kwenye picha waliyoonyeshwa na watu waliokuwa wakiwatumia kupata habari ambayo waliipata kutoka kwa mmoja wa marafiki wa Beda. Ripoti hiyo, Nunda akaikabidhi kwa mkuu wake wa kituo pamoja na picha walizopiga.
* * *
Ilikuwa ni jioni, siku moja baada ya mazishi ya mheshimiwa Himidu, Husna akiwa nyumbani kwake amezungukwa na mashoga zake waliokwenda kumpa pole, wote kwa pamoja wakaisikia kengele ya mlango ikiita. Mmoja wa mashoga zake akainuka kwenda kufungua mlango huku akiamini ni mwendelezo wa wageni wanaokuja kumpa pole mwenzao. Lakini mara baada ya kuufungua mlango na kuziona sura za wanaume wawili waliokuwa wamesimama, akatambua kuwa, sura hizo hazikuja kumpa pole Husna. Akashusha pumzi za presha na kusema, “Karibuni.”
“Tumemkuta Husna?” mmoja wa wageni hao wawili aliuliza. Hawakuonyesha kutaka kusalimia.
Kwanza mwanamke huyo aliyekuja kuufungua mlango alitaka kujibu, ‘Yupo.’ Lakini alisita ghafla na kuwaangalia usoni wanaume hao. “Kwani nyie ni akina nani?” aliuliza.
Wanaume wale wakatazamana usoni. Mmoja akawahi kuurudisha uso wake kumwangalia mwanamama aliyekuwa mlangoni. “Mwambie kuna wageni wake,” alisema.
Mwanamama akaonekana kusita. Kisha akasema, “Karibuni ndani.”
“Tunamwihitaji aje hapa,” yule mwingine alisema.
Kauli hiyo ikamzidisha mashaka mwanamke aliyekuwa mlangoni. “Yupo kwenye huzuni ya msiba,” alisema.
“Tunajua,” mmoja wa wale wageni alijibu.
“Kwa hiyo mfiwa atoke aje kuona wageni, siyo wageni waingie kumwona mfiwa?”
Wanaume hao wawili wakaangaliana tena.
“Tutaingia ndani, lakini tutataka kuzungumza naye peke yake,” mmoja wao alisema.
“Kwani nyie ni nani kina baba?”
“Polisi!” mwingine alisema na kutoa kitambulisho na kukionyesha mara moja na hapo hapo kukirudisha mfukoni na kumwangalia machoni mwanamke wanayezungumza naye.
“Karibuni,” mwanamama alisema na kutoa nafasi kwa wageni hao wapite huku yeye mwenyewe akionekana kutawaliwa na hofu iliyomshambulia ghafla usoni mwake.
Aliwaongoza askari hao mpaka eneo la varanda ambako kulikuwa na kundi la akina mama waliokuwa wakimfariji Husna.
“Husna,” mwanamke aliyeingia na wale makachero aliita na kuangalia upande aliokaa Husna. “Wageni wako.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Karibuni,” Husna alisema akiwa ameuinua uso wake kuwaangalia wageni alioambiwa ni wake. Alionekana kutowatambua ujio wao ulikuwa ni wa nini.
“Wanataka kuzungumza na wewe,” mwanamke aliyeingia na hao makachero alisema huku sura yake ikiwa makini. Umakini huo pamoja na kauli aliyoitoa ikawafanya wote waliokuwepo pale wageuke na kuwaangalia wale makachero wawili, nyuso zao zikionyesha dalili zote za kuwatilia mashaka.
“Waje tu hapa,” Husna alisema.
Yule mwanamke aliyeingia na polisi hakufanya ajizi, alikwenda alipokaa Husna na kumwinamia, akamnong’oneza sikioni. Husna akainua uso wake mara moja na kuwaangalia wale makachero wawili kisha, akainuka na kutoka kwenye kundi lililomzunguka. “Karibuni,” alisema. Akawaongoza makachero kuingia nao chumbani.
“Polisi!” yule mwanamke aliyewakaribisha makachero aliliambia kundi lililokuwepo pale kwa sauti ya chini na kufuatiwa na minong’ono iliyoleta udadisi wa tukio.
Minong’ono ilinyamaza ghafla baada ya kumwona Husna na wale makachero wawili wakitoka. Husna alisimama, lakini wale makachero wakaendelea kutoka. Utokaji wao ukawa kivutio kwa wote waliokuwepo pale.
“Mariam,” Husna alimwita mmoja wa akinamama aliyekuwepo pale.
Mwanamke mwenye umbo kubwa lililojaa huku mwilini mwake ukisheheni vito vya dhahabu na michoro ya wino wa piko, aliitikia kwa sauti ya chini na kujiinua kutoka kwenye kochi alilokuwa amekaa na kumwendea Husna huku macho ya wote waliokuwepo pale yakiwa yanawatazama. Wakanong’ona kidogo, mwanamke aliyemwendea Husna akashusha pumzi kubwa za mara moja, ushushaji wa pumzi alioufanya ukatoa ashirio kwa wote kuwa, mambo hayako shwari.
Husna aliingia chumbani mwake akiwa amemuacha Mariam pale varandani. Nafasi ya kutokuwepo wale makachero ikatumiwa na Mariam kwa kuwaambia wenzake, “Wanamchukua Husna!”
“Wanampeleka wapi?” swali hilo likaulizwa kutoka kwa mmoja wao.
“Kituoni!”
“Kwani kafanya nini?” wawili watatu wakauliza.
“Himidu jamani kauawa kwa kupigwa risasi, labda polisi wanataka kuchukua maelezo ya Husna ya jinsi ilivyokuwa,” Mariam alisema kwa nia ya kuwatuliza wenzake.
“Huko ndiko kuisaidia polisi wenyewe wanavyoiita, lakini ukifika huko unaswekwa mahabusu na kubadilishiwa msamiati, ukaitwa mtuhumiwa. Si ajabu tukimwona Husna anapotea hivi hivi!” binti mmoja mzuri wa kuumbika alisema. Pamoja na kuonekana ni binti, lakini alionekana ni gwiji aliyekamilika kishangingi.
Minong’ono ikaanza huku wengine wakilalamikia kitendo hicho. Lakini ilichukua muda mfupi kunyamaza baada ya kumwona Husna akitoka chumbani. Umbeya wa huzuni ukaanza kwa baadhi yao na kujifanya wanasikitishwa na kitendo hicho kinachofanywa na makachero hao huku wengine wakidiriki kuitukana hatua hiyo.
“Twendeni wote!” mmoja wao akatangaza hivyo.
“Hapana!” Husna alisema. “Nadhani kila mmoja anajua kilichotokea, na tukio kama lile haiwezekani lisihusishe polisi. Wanachokitaka polisi kutoka kwangu ni kujua mazingira yalivyokuwa wakati Himidu alivyouawa, si kingine. Msiwe na wasiwasi, niwacheni niende na nitarudi.”
Kauli ya Husna ikawapoza wenzake. Wote kwa pamoja wakamsindikiza kwa kumtoa. Walipofika nje, Husna alimwita kando Mariam. “Endapo kama sitarudi,” Husna alimnong’oneza Mariam. “Nakuomba ulale hapa. Siamini kuiacha nyumba na mlinzi, tena mlinzi mwenyewe nimeanza kumwajiri jana tu baada ya matatizo haya kutokea. Hakikisha jioni atakapokuja akukute, maana funguo moja ya geti anayo yeye.” Baada ya kusema hivyo, Husna akautumbukiza mkono kwenye begi lake na kutoa funguo tano zilizokaa pamoja. “Utakaponifuata kituo cha Oysterbay uje na Bi Hija peke yake, maana wengine wakikuona unaondoka na gari na kujua unanifuata polisi basi kila mmoja atataka kuja.”
Baadaye Husna aliingia kwenye gari la makachero na kushuhudiwa na wenzake waliokuwa wakimtazama kwa sura zenye simanzi.
* * *
Husna alipelekwa moja kwa moja kituo cha Oysterbay na kuongozwa kwenye ofisi ambako walimkuta kachero Nunda akiwa amekaa kwenye kiti kilichokuwa nyuma ya meza pekee iliyomo humo ofisini. Kuwepo kwake ilionekana kama aliyekuwa akimsubiri Husna afikishwe ofisini humo.
“Karibu,” Nunda alimwambia Husna wakati akiingizwa.
“Ahsante,” Husna alisema na kwenda kukaa kwenye kiti cha wageni kilichopo mbele ya meza. Wale makachero wawili waliomleta Husna wao waliishia mlangoni baada ya kumfungulia mlango na kumuacha Husna aingie mwenyewe. Husna aligeuka na kuangalia mlangoni, wale makachero walikuwa wamekwisha kuondoka!
Kachero Nunda, mrefu wa kimo na mwili uliojaa kiasi, alikuwa na sura iliyomwonyesha kuwa ni mkorofi wa kuzaliwa. Sura yake ilikaa kiume zaidi na kupoteza sifa ya uzuri unaoweza kumvutia mwanamke. Macho yake yalikuwa mekundu kwa wakati wote na kudhaniwa ni mvuta bangi mzuri, dhana ambayo ilibakia hivyo hivyo huku kukiwa hakuna hata mmoja aliyemshuhudia akikifanya kitendo hicho. Pamoja na kuijua dhana ambayo wenzake walikuwa wakimtuhumu nayo, Nunda hakuwahi hata mara moja kuikanusha au kuikubali. Siku zote alikuwa ni mwenye tambo za kujisifu kipumbavu kwa kuonyesha kuwa hashindwi na kitu na alipenda sana kujiweka kwenye ujuaji wa kujua mambo kuliko mtu mwingine. Baadhi ya makachero wenzake walitokea kumchukia kwa tabia zake hizo, lakini aliaminika kwa wakuu wake wa kazi hasa katika shughuli za mahojiano na kutesa watuhumiwa
Nunda aliikunja mikono yake na kuigandamiza juu ya meza, akamwangalia Husna. “Pole na matatizo,” alisema.
“Ahsante,” Husna alisema na kujiinamia.
“Husna,” Nunda aliita kwa sauti ya upole. “Tunaomba utusaidie. Wewe ndiye ulikuwa ni mtu wa mwisho kuwa na marehemu mpaka kifo chake kilipomkuta. Mheshimiwa Himidu alipigwa risasi akiwa na wewe, naomba unipe maelezo ya hali ilivyokuwa mpaka marehemu anapigwa risasi.”
“Nilikuwa nikimsindikiza kwenye gari yake wakati akitoka kwangu,” Husna alisema kwa sauti hafifu huku Nunda akimwangalia. “Ghafla nikamsikia mwenzangu akitoa sauti ya maumivu na kuanguka kama aliyesukumwa na kitu. Baada ya kuanguka pale chini nikamwona akiipigapiga miguu yake kama mtu aliyekuwa akikata roho. Mara nikaona damu kwenye shati lake. Mh! Nikaona haya yamekwisha kuwa makubwa. Nikaanza kumwita mwenzangu, akawa kimya! Lakini nikimwangalia usoni namwona akiniangalia, nikasema hapana, hapa kuna namna. Nikapiga kelele za kuita msaada, majirani wakaja na hao ndiyo walionifungua akili kuwa Himidu amepigwa risasi, lakini hawakuniambia kuwa alikwisha kufa…” Husna akaacha kuendelea kuzungumza na kukikita kilio cha kimya kimya.
Nunda aliendelea kumwangalia Husna bila ya kufanya hatua yoyote ya kubembeleza au hata kwa kutoa leso kumkabidhi Husna afute machozi! Badala yake alitulia kimya na kuendelea kumwangalia Husna kama vile mtu aliyekuwa anaangalia runinga. Hatimaye Husna alinyamaza.
“Nyumbani kwako hakuna mlinzi?” Nunda aliuliza baada ya kumwona Husna amenyamaza kulia.
“Kabla ya hapo sikuwa na mlinzi, nimeanza jana kuajiri mlinzi.”
“Wakati mlivyokuwa mkitoka, kulikuwa na mtu au watu nje ya nyumba yako?”
Husna alimwangalia Nunda. “Una maanisha ndani ya uzio wa nyumba au nje ya uzio?” aliuliza.
“Ndani ya uzio.”
“Hakukuwa na mtu yoyote.”
“Lakini nje ya uzio kulikuwa na watu?”
“Kwa muda kama ule isingekuwa rahisi kuwe na watu nje.”
“Ulisikia mlio wowote wa bunduki?”
“Hapana.”
“Ulisikia hatua zozote za mtu kukimbia baada ya mheshimiwa Himidu kuanguka?”
“Hapana.”
“Unadhani ni nani atakayekuwa amempiga risasi mheshimiwa Himidu?”
“Sina ninayemtuhumu kwa hilo.”
“Mheshimiwa Himidu aliwahi kukulalamikia lolote kama vile kukorofishana na mtu au kutofurahiswa na kitu au jambo fulani?”
“Hakuwahi.”
“Turudi kwa upande wako,” Nunda alisema na kujitingisha kidogo. “Mnahusiana vipi na Beda?”
Lilikuwa swali la ghafla lililokuja kama shambulio lisilotarajiwa! Misuli ya sura ya Husna ikakaza na akazubaa kwa sekunde chache kabla ya akili yake kurudi na kumwonya asiendelee kuzubaa. “Ni mdogo wangu,” alisema.
“Kivipi?”
“Mtoto wa mama yangu mdogo.”
“Siyo mpenzi wako?” Nunda aliuliza huku akihakikisha macho yake hayapotezi mwelekeo wa kumwangalia Husna usoni na swali lake kuonekana la utani zaidi.
“Yaani Beda ni mpenzi wangu mimi?” Husna aliuliza huku akimudu kuutengeneza mshangao kwenye sura yake.
“Unanishangaa mimi au unashangaa swali langu?”
“Vyote. Nadhani nilikujibu kuwa ni mdogo wangu, mtoto wa mama yangu mdogo, vipi uniulize kama ni mpenzi wangu?”
“Nipe jina la huyo mama yako mdogo.”
“Bee?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nunda alitingisha kichwa kumsikitikia. “Mama yako mdogo anaitwaje?” alilirudia swali hilo.
“Mama yangu miye?” Husna aliuliza kipumbavu akionyesha kupoteza udhibiti wa akili yake na wakati huo huo akijaribu kutaka kujua ilikolalia akili ya Nunda.
“Sikiliza Husna,” Nunda alisema kwa sauti kavu, iliyoondoka kwenye kuzoeana. “Huwezi ukawa kimada wa kiongozi wa serikali kisha vyombo vya usalama visilitambue jambo hilo. Tunajua kama mheshimiwa Himidu alikuwa akikujengea nyumba, tunajua kama amekununulia gari na hata yale maduka uliyonayo amekuanzishia kwa kukupa mtaji, isitoshe hata nyumba unayokaa amekupangia na samani zote zilizomo mle amekununulia yeye. Na pia tunajua Beda ni bwana wako na ulikuwa ukimdanganya mheshimiwa Himidu kuwa Beda ni mtoto wa mama yako mdogo. Tunajua kuwa, Beda hakuwepo kwenye mazishi ya mheshimiwa Himidu na wala hayupo hapa jijini. Unaweza ukanifahamisha alipo?”
Akili ya Husna ikawaza haraka haraka na kuijua sababu ya Nunda ya kutaka kujua mahali aliko Beda.
“Beda hahusiki na kifo cha Himidu!” Husna alisema ghafla.
“Nakuomba kwa unyenyekevu uniambie mahali aliko Beda!” Sauti ya Nunda ilikuwa kavu na iliyojenga amri. “Vinginevyo nitakuweka mahabusu na kukufungulia mashitaka ya kukuhusisha na mauaji ya mheshimiwa Himidu. Nitakuweka ndani kisha, tutamtafuta Beda na tutamkamata na yeye kumuweka ndani vilevile. Popote atakapojificha, tutamkamata! Fikiria nyote mkiwa ndani kisha, tukawapeleka mahakamani kwa ajili ya kusomewa shitaka lenu la mauaji, baada ya jalada lenu kuhamishwa na kupelekwa Mahakama Kuu tutaiomba mahakama hiyo mwendelee kukaa ndani kwa sababu uchunguzi wetu haujakamilika na mtaendelea kusota mahabusu hata kwa miaka mitano au zaidi bila ya kesi yenu kuzungumzwa. Upo tayari kukaa gerezani kwa muda wote huo kwa ajili ya kumlinda bwana mdogo? Kisa tu anakutosheleza kingono? Unafikiri ni nani atakayehoji kukaa kwenu gerezani wakati sisi tukizidi kuendelea kutoa taarifa kwa Jaji kuwa, ushahidi haujakamilika? Wapo wengi wanaondelea kusota mahabusu kwa utaratibu kama huu!” Nunda alitabasamu na kumwangalia Husna kwa ukimya wa sekunde chache. Kisha akauliza tena, “Beda yuko wapi?”
Husna alikuwa tayari yuko hoi!
“Yuko Tanga,” Husna alisema kwa sauti iliyopwaya huku akiwa ameuiamisha uso wake chini na kuanzisha kilio kingine!
“Onyo jingine,” Nunda alisema akiwa ameendelea kuukaza uso wake akimwangalia Husna. “Endapo nitagundua umempa hadhari Beda kuwa tunamtafuta, nakuhakikishia utajuta na kujiuliza kwa nini Mungu alikupa wasaa ukaonana na kiumbe kama mimi!”
Husna alijilazimisha kuuinua uso wake na kumwangalia Nunda kwa macho yaliyoiva na kuwa mekundu huku yakiwa yamelowana machozi. “Naapa kwa jina la mwenyezi Mungu, baba yangu. Beda siye aliyemwua Himidu!” Husna aliapa.
“Nadhani umelisikia onyo langu!” Nunda alionya.
****
Beda, kijana mtanashati mwenye sura ya kupendeza inayomvutia mwanamke yeyote, akiwa nyumbani kwa wazazi wake mjini Tanga, alikuwa tayari anamalizia kifungua kinywa kwa mkono mmoja kushika kikombe na mkono mwingine akiwa ameshika gazeti. Aliipitia taratibu sehemu ya gazeti aliyokuwa akiisoma na kujikuta akizama tena kwenye fikra nzito, fikra zilizorudishwa tena kutokana na kuisoma habari inayomuhusu mheshimiwa Himidu. Tokea alivyozipata taarifa za kuuawa kwa mheshimiwa Himidu ambazo aliambiwa kwa kupigiwa simu na Husna na zikawa zimemshitusha, habari hizo zikawa kama mwiba uliochoma kwenye nafsi yake. Alijua wazi kuwa, kifo cha mheshimiwa Himidu si kwamba kitakuwa kimeharibu mstakabali mzima wa maisha ya Husna, bali na maisha yake vilevile, kutokana na sehemu kubwa ya utegemezi wake wa kuendeshewa maisha na mwanamke huyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kupewa taarifa hizo za kuuawa kwa mheshimiwa Himidu, Beda akaamtaarifu Husna kuwa, anajiandaa kurudi Dar es Salaam kwa ajili ya mambo mawili. La kwanza, ni kurudi kumpa pole mwenzake na kuwa naye karibu kwa ajili ya kumfariji. La pili, ni kuwahi maziko ya mheshimiwa Himidu. Lakini kinyume na matakwa yake yalivyokuwa, alishangaa pale Husna alivyomkataza na kumuonya kuwa, asirudi Dar es Salaam kwani uonekano wake kwenye mazishi unaweza kuzusha minong’ono ya kuzungumziwa uhusiano wa mapenzi uliopo kati yao. Beda akatii onyo la Husna kwa kuamua kubaki mjini Tanga ambako alikwenda kwa ajili ya kuwatembelea wazazi wake.
Akiwa amemaliza kuisoma sehemu hiyo ya gazeti iliyokuwa ikimzungumzia mheshimiwa Himidu na kujikuta akimfikiria zaidi Husna na kutamani kuwa karibu naye, Beda aliliweka gazeti juu ya meza aliyokuwa akiitumia kunywea chai na kurudi chumbani kwake ambako alijiandaa kwa mavazi na hatimaye alitoka na kwenda kuwaaga wazazi wake kuwa, anakwenda mjini.
Eneo ilipo nyumba ya wazazi wake ni eneo la Chumbageni na halikuwa mbali na mjini. Kutokana na kuwepo umbali huo mdogo, kukamfanya Beda asione umuhimu wowote wa kutafuta usafiri, badala yake akaamua aende mjini kwa miguu. Alitoka nyumbani kwao na kukamata barabara yenye mwelekeo wa alikokuwa anakwenda. Hata hivyo wakati alipokuwa akitoka, alishindwa kulitilia maanani gari dogo lililokuwa limesimama hatua chache jirani na nyumba yao.
Nunda aliyekuwa amekaa kiti cha mbele cha abiria, alimwangalia Beda alivyokuwa akitoka kwenye nyumba ambayo walikuja kuitegeshea tokea saa kumi na mbili ya asubuhi baada ya kuelekezwa na Husna ilipo nyumba hiyo walipokuwa kwenye kituo cha polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam siku moja nyuma. Baada ya kuzipata taarifa hizo, Nunda aliamua kuzifanyia kazi kwa kuichukua timu ya watu wanne na kufanya nayo safari ya kuelekea mjini Tanga!
Wote wanne walimwangalia Beda alivyokuwa akipita kando ya gari walilokuwemo bila ya kuonyesha kuwa, walikuwa wakimwangalia yeye. Baada ya Beda kutembea hatua kadhaa, Nunda akatoa ishara kwa kachero aliyekuwa nyuma ya usukani kuwa, aligeuza gari kwa ajili ya kumfuata Beda anakoelekea.
Dereva aliliwasha gari na kuligeuza, wakamwona Beda akikata kona kuingia mtaa wa pili.
“Muwahi kabla hajatupotea!” Nunda alimwamrisha dereva.
Dereva akafanya kama alivyoambiwa, lakini kutokana na uzoefu wake wa kufuatilia watu kwa aina hiyo, hakuifanya hatua hiyo kwa pupa. Aliligeuza gari kwa mwendo mkali kidogo, mwendo ambao haukumshitua mtu yeyote wakati akiligeuza. Wakamfuata Beda.
Walipomwona Beda akitembea kwenye mtaa waliokata kona, dereva akalipunguza mwendo gari. Wakamsogelea na kumpita kwa hatua chache.
“Simamisha gari!” Nunda alimwamuru dereva bila ya kugeuka kumwangalia Beda. “Tunamshitukiza!” Baada ya kusema hivyo akasubiri gari lisimame. Baada ya gari kusimama, akateremka.
Beda aliliona gari hilo likisimama mbele yake kisha, akauona mlango wa mbele wa upande wa abiria ukifunguliwa na kutokeza mtu ambaye ile kumwona tu, akajua mtu huyo ameteremka hapo kwa ajili ya kutaka kuzungumza na yeye. Akahisi atakuwa na jambo analotaka kumwuliza, akaijenga dhana kuwa, watakuwa wamepotea njia na akajiweka tayari kuulizwa…
‘Polisi!” Nunda alisema ghafla na kumwonyesha Beda kitambulisho. “Tunakuhitaji kituoni bwana Beda. Ingia kwenye gari tuongozane!”
Wakati Beda akiwa amepigwa na mshangao huku akijiuliza wamelijuaje jina lake, hapo hapo akausikia mlango wa nyuma wa gari ukifunguliwa. Akatoka mtu na kuja kusimama nyuma yake. Kabla ya Beda kugeuka kumwangalia, akajihisi akikamatwa kwa kupitishiwa mkono kwa kwenye paja lake, akavutwa kidogo kwa nyuma kisha, akahisi mkono wenye nguvu ukikamata katikati ya shingo na kichogo chake na kuinamishwa ili aingie kwenye gari. Akatii kuingia kwenye gari bila ya kufanya ubishi wowote.
“Nimefanya nini mpaka mnanikamata?” Beda aliuliza akiwa amewekwa katikati ya mtu na mtu kwenye kiti cha nyuma.
“Utajua baada ya kufikishwa kituoni,” Nunda alisema bila ya kugeuka nyuma kumwangalia Beda.
Beda akapelekwa kwenye kituo cha polisi cha Chumbageni cha hapo mjini Tanga kabla ya kusafirishwa kurudishwa Dar es Salaam.
* * *
Alifikishwa Dar es Salaam akiwa amefungwa kitambaa cheusi usoni na kuswekwa kwenye kituo cha polisi cha darajani. Safari yake ilifanywa usiku na yeye mwenyewe hakuwa na uhakika wa anakopelekwa, lakini kadri alivyouona mwendo wa safari ukizidi akahisi anarudishwa Dar es Salaam. Alishatambua kuwa, alikuwa akihusishwa na kifo cha mheshimiwa Himidu kutokana na maelezo ya pale kituo cha Chumbageni baada ya kuwasikia askari wakimzungumza kuwa ni mtuhumiwa wa mauaji ambayo hawakusema ni ya nani. Ilikuwa ni baada ya kuzidisha hesabu za mbili mara mbili kwa kutumia fomula ya kuuawa kwa mheshimiwa Himidu na uhusiano wa mapenzi alionao kati yake na Husna ndiyo ukampatia jawabu hilo.
Akiwa amefungwa pingu mikononi na miguuni, Beda aliteremshwa kutoka kwenye gari huku akiwa bado amefungwa kitambaa cheusi usoni na kutembezwa akiwa ameshikwa na watu wawili kwa mkono wa kushoto na kulia. Wakati akiongozwa asipokujua, aliisikia milio ya gari ya hapa na pale ikipita kwa mwendo wa kasi barabarani na kushindwa kubuni angekuwa yupo wapi. Hatimaye alijihisi akiingizwa kwenye nyumba iliyokuwa na harufu iliyozoeleka kwa nyumba zote za aina hiyo na kujijua kuwa, amefikishwa kwenye kituo cha polisi ambacho alishindwa hata kukibuni ni cha wapi. Aliwasikia watu aliokuwa nao wakisalimiana na watu wengine na moja kwa moja aliwahisi kuwa ni polisi wa kituo hicho. Alizidi kutembezwa kwenye maeneo ambayo alihisi ni kwenye korido na hatimaye akasikia mlango wa chuma ukifunguliwa kwa komeo lililokuwa likitoa kelele na kuingizwa humo na baadaye kuusikia mlango huo ukifungwa nyuma yake na kufuatiwa na kelele za komeo. Alifunguliwa kitambaa alichokuwa amefungwa nacho machoni na macho yake kupata shida ya kupambana na mwanga wa taa kwa sekunde chache. Alijikuta yumo kwenye chumba kidogo chenye dirisha dogo lililokuwa juu ambalo halifikiwi na mtu mwenye kimo cha aina yoyote, lilikuwa ni dirisha lililowekwa kwa ajili ya kupitisha hewa tu. Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kiti kimoja tu ambacho ndicho alichokikalia na hakukuwa na kitu kingine zaidi ya sakafu iliyochakaa kama kilivyo chumba chenyewe. Mbele yake kulikuwa na makachero wawili, mmoja wapo akiwa ni Nunda wakiwa wamesimama na kumwangalia kwa makini.
Sura yake ikiwa imetawaliwa na kihoro cha uwoga, Beda aliwaangalia makachero hao na akajipa ujasiri kwa kuwauliza, “Nina makosa gani niliyoyafanya mpaka nikamatwe na kuletwa huku?”
“Ya kumwua mheshimiwa Himidu,” Nunda alisema. “Nina maswali machache ya kukuuliza, kitu pekee cha kukufanya uwe salama ni kushirikiana nasi, lakini ukijaribu kutuzungusha, hatimaye utakuja kukiri wakati umekwishaumia. Nina imani utakuwa msikivu.” Nunda alinyamaza kutoa nafasi ili maneno yake yamwingie Beda. Kisha akasema, “Ulishirikiana na nani kumwua mheshimiwa Himidu?”
“Naapa mbele ya mwenyezi Mungu mimi siye niliyemwua mheshimiwa Himidu,” Beda alisema.
“Nakuuliza kwa mara ya pili, umeshirikiana na nani kumwua mheshimiwa Himidu?”
“Mimi sijamwua mheshimiwa Himidu jamani,” safari hii sauti ya Beda ilitia huruma zaidi.
“Nakuuliza kwa mara ya tatu na ya mwisho. Tunajua kuwa umemwua mheshimiwa Himidu, sasa tueleze kama ulikuwa peke yako au kuna wenzao ulioshirikiana nao?”
Beda akaikunja sura yake kuonyesha kutaka kulia na kutaka aaminiwe kile anachokijibu. “Kama ningemwua mimi ningesema,” alijitetea huku kichwa akiwa amekiweka upande na uso wake ukiwa umeinuka kumwangalia Nunda. Machozi yalianza kumtoka.
Machozi yake hayakusaidia kuileta huruma kwa makachero hao, kipigo cha mbwa mwizi kikamwanzia usiku huo.
“Usipotaja ulioshirikiana nao kumwua mheshimiwa Himidu, ujue na wewe unakufa!” Nunda alimwonya Beda.
Akiwa taabani kwa kipigo kilichomchukua takribani saa nzima huku sura yake ikiwa na mabonde ya uvimbe kuanzia machoni mpaka mdomoni na sehemu nyingi ya hizo zikimwaga damu, Beda alisota kwa maumivu makali kutoka kwenye miguu yake aliyokuwa akiiburuza. Hakuwa na uhakika nayo kama ilishavunjika kutokana na kipigo alichokuwa akiendelea kukipata. Akajaribu kumwangalia Nunda ambaye hakuwa akimwona vizuri kutokana na uvimbe ulioko machoni na damu nyingi zilizokuwa zikichirizikia juu ya macho yake.
“Sikumwua Himidu afande!” Beda alisema huku akilia na kulazimisha kumwangalia Nunda angalau aonekane hana hatia na aonewe huruma.
Aliendelea kukanusha kuwa, hahusiki kabisa na kumwua mheshimiwa Himidu na akaendelea kukanusha kadri alivyokuwa akipata kipigo ambacho kiliendelezwa ili akubali kuhusika na mauaji hayo. Hatimaye Beda aliachwa akiwa amelala taabani kwenye sakafu huku mikono na miguu ikibaki na pingu alizofungwa.
Taarifa za kuwa Beda hajakiri ziliwafikia maofisa husika na kumtaka Nunda aendelee kumuhoji.
* * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Asubuhi hiyo, Beda alitolewa kwenye chumba hicho na kwenda kufungiwa kwenye chumba chenye kiza cha peke yake na kupewa uji ambao alishindwa kuunywa kutokana na maumivu ya kinywani aliyoyapata na kuchangiwa na hali halisi inayomkuta humo. Alasiri alipelekewa chakula cha aina ya ugali na maharagwe ambacho alishindwa kukila kutokana na kuchanganyikiwa kulikompata.
Kwa hali ya kiza iliyokuwemo humo chumbani, Beda alishindwa kuujua mchana, akabaki na kiza chake mpaka alipousikia mlango wa chuma ukifunguliwa tena. Mara baada ya kufunguliwa akauona mwanga wa taa ulioingia kwa uchache chumbani humo na kumtambulisha kuwa ilishafika usiku asioujua muda wake. Akawaona watu wawili waliovaa kiraia wakiingia na kuwajengea hofu ya kuwa ni askari, watu hao walimkaribia na kumwambia, “Simama!”
Beda alisimama kwa kujizoazoa kwa shida kisha akayumba, siku moja ya kuwekwa mahabusu ilikwisha kuivuruga afya yake na kuonekana kudhofu ghafla. Watu hao walimwendea na kumfungua pingu za mikononi na miguuni, lakini alishangaa alipowaona wakimvua nguo! Tendo hilo likamshitua na kujijengea hofu kuwa amedhamiriwa kufanyiwa kitendo kinachofanywa na mashoga, akajaribu kujitutumua kukataa kuvuliwa nguo zake, lakini pasipo kutarajia kofi la nguvu likamnasa na kumzoa mpaka sakafuni. Makachero hao wawili bila ya kutamka chochote, wakamwendea pale alipoanguka na kumwinua kwa nguvu zote na kumsimamisha wima. Wakaendelea kumvua nguo, safari hii Beda hakuthubutu kuwazuia.
Akiwa yuko uchi wa mnyama, Beda alifungwa kitambaa cheusi machoni na kurudishiwa tena pingu za mikono na miguuni, akatolewa kwenye chumba hicho kwa kutembezwa bila kuona kule anakoelekea. Pamoja na kutokuona kule anakopelekwa, lakini nyayo zake zilizokuwa peku peku zilimpa hisia mwa mle alimokuwa akipita kuwa alikuwa bado yuko ndani ya jengo hilo hilo kutokana na sakafu aliyokuwa akiikanyaga. Baadaye alihadharishwa na watu waliomchukua kuwa, aushushe mguu wake taratibu na alipofanya hivyo, mguu wake ukawa umekanyaga mchanga wenye changarawe na kutambua yuko kwenye kulitoka jenga hilo. Lakini alijikuta akitembea kwa hatua chache na kutakiwa ainue mguu wake, na mara alipofanya hivyo, mguu wake ukagusa bodi la gari na kutambua kuwa ni gari dogo. Akaingizwa humo na kukaa kwenye kiti alichohisi ni cha nyuma kwa kuwekwa kati huku upande wake wa kushoto na kulia kukiwa na askari ambao wote wawili waliyagusisha mabega yao kwenye mabega yake. Akaisikia milango ya gari ikifungwa na gari kuwashwa. Hakujua alikokuwa anapelekwa, hali hiyo ikamfanya asali kimoyomoyo!
Mkanganyiko uliokuwa ukimkumba akilini alishindwa hata kutathimini muda walioutumia baada ya gari kusimama na kutakiwa ateremke. Alitii amri aliyopewa na kupelekwa kwenye jengo lililokuwa na harufu kama ya jengo alilokuwa ametoka, akatambua amehamishiwa kwenye kituo kingine cha polisi. Lakini kwa nini niletwe nikiwa uchi wa mnyama? alijiuliza na kuamua kuiacha hatima yake kwenye mikono ya Mungu!
Alipelekwa kwenye chumba kingine cha mateso usiku huo, akaondolewa kitambaa kilichokuwa usoni mwake na kumwona Nunda aliyekuwa amesimama mbele ya kiti kilichokuwa kitupu na kutakiwa kukaa kwenye kiti hicho kisha, akapewa kalamu na karatasi.
“Andika majina ya watu ulioshirikiana nao kumwua mheshimiwa Himidu,” Nunda alimwambia Beda kisha akarudi hatua moja nyuma.
“Sina,” Beda alisema na kumtazama Nunda kwa macho yaliyojaa uwoga na kutia huruma.
“Kwa hiyo ulimwua ukiwa peke yako?”
“Siyo mimi niliyemwua!”
Makachero wawili waliomleta humo chumbani, wakamfuata Beda na kukifunika gubigubi kichwa na uso wake kwa mfuko mweusi wa nguo na kumtoa kwenye kiti baada ya kumnyang’anya kalamu na karatasi kisha, wakamlaza kichalichali chini ya sakafu. Mmoja wa makachero akaenda kuchukua ndoo ya maji na kuyatiririsha juu ya uso wa Beda na kumwagikia kwa nguvu kwenye uso wake, yakampalia kwa kumwingia puani na mdomoni. Yakaziba pumzi za Beda, Beda akagugumia kwa kuhangaika kuzitafuta pumzi, Nunda akatoa ishara kwa kachero aliyekuwa na ndoo ya maji aache kumwagia Beda.
Akiwa amebanwa kwa kuzikosa pumzi kutokana na maji aliyomwagiwa usoni, Beda alihangaika kwa kuhema kwa nguvu huku akikohoa na kutapatapa kuitafuta hewa. Akiwa anaendelea kuisaka hewa ya kutosha, Nunda alitoa ishara ya kichwa kwa kachero mwenye ndoo amwagie tena maji, Beda.
Maji aliyomwagiwa tena Beda, yalimjia kwa kumshitukiza akiwa kati kati ya kuzitafuta pumzi. Baadhi ya maji akayanywa na kumfanya agumimie kwa kuitafuta hewa, mengine yakamwingia puani na kumuweka kwenye hali ngumu iliyomfanya apaliwe zaidi. Nunda akatoa ishara ya kumzuia kachero mwenzake asiendelee kuyamwaga maji hayo. Beda alionekana kama anakata roho kwa kuitafuta pumzi aliyokuwa haipati, alihangaika kwa kutapatapa hali iliyomfanya Nunda atoe ishara ya Beda ainuliwe haraka. Kwa kuwa ni wazoefu wa kutoa mateso ya aina hiyo, makachero wale wawili wakawa wanakijua wanachotakiwa kukifanya. Mmoja akamwinua Beda kwa kumshika mgongoni na kumkalisha, mwingine naye akawahi kuuvua ule mfuko mweusi kutoka kichwani kwa Beda. Hali hiyo ikamfanya Beda aanze kuipata pumzi kutoka kwenye hewa ya wazi na kuivuta kwa pupa huku macho yakiwa yamemtoka pima na kuendelea kukohoa kikohozi cha kupaliwa huku akitokwa na udenda alioshindwa kuudhibiti, wakati huo huo makachero wote watatu wakimwangalia kwa kumsubiri apate afuheni.
Baada ya kuzipata pumzi zake lakini bado akiendelea kuhema kama mwenye ugonjwa wa pumu, Nunda akatoa ishara ili mateso mengine yafanyike. Beda akachukuliwa mzobemzobe na kupelekwa eneo maalumu lenye umeme wa kutesea watuhumiwa, mikono yake ikainuliwa na kufungwa kwenye mikanda minene iliyotengenezwa kwa nguo yenye kitambaa kizito cha khaki. Hofu ya kusulubiwa tena ikaiteka nafsi yake, akaanza kutweta kwa uwoga, macho yake yakameremeta kuonyesha dalili ya machozi yakiwa njiani, akataka kusema neno, likamshinda kutamka, badala yake akatetemekwa na papi za mdomo kama mtu mwenye kiharusi. Mmoja wa makachero waliokuwemo humo akawa amechukua fimbo ya chuma inayoshitua kwa nguvu ya umeme na kuigusisha mgongoni mwa Beda, misuli yote ya mwili wa Beda ikatikiswa kwa nguvu ya umeme iliyotoka kwenye fimbo hiyo! Beda akahisi roho inamtoka! Akapiga ukelele ambao hajawahi kuupiga kwenye maisha yake! Fimbo ikaondolewa kutoka mwilini mwake.
“Nakiri kumwua mheshimiwa Himidu!” Beda alikiri kwa sauti aliyoitaka iwe ya nguvu, lakini hakufanikiwa kuifanya iwe hivyo kutokana na kuishiwa nguvu, badala yake ikawa sauti hafifu inayotweta ya mtu aliyekuwa akitubu.
Kimya kikajitengeneza humo ndani. Nunda na makachero wenzake wakatazamana.
“Kwa hiyo unakiri kuhusika na kifo chake?” Nunda aliuliza kwa utulivu.
“Ndiyo. Ni mimi niliyemwua mheshimiwa Himidu!” Beda alisema na kuonekana kuisisitiza kauli hiyo huku akiendelea kutweta na kichwa kikiwa kimetangulia mbele ya mikono yake kikining’inia na kulalia upande mmoja.
Nunda akawataka makachero wenzake wamfungue Beda kutoka kwenye mikanda ya umeme. Baada ya kufunguliwa, miguu ya Beda ikashindwa kukibeba kiwiliwili chake na kujikuta akianguka sakafuni. Akainuliwa na kukalishwa kwenye kiti.
Nunda akamwendea Beda na kumpa kalamu na karatasi. “Saini hapa,” alimwambia Beda.
Beda akasaini kisha, akawekeshwa alama ya dole gumba.
Ilipofika asubuhi, Nunda aliiwakilisha taarifa kwa mkuu wake wa kituo kwa kumwonyesha nyaraka aliyoisaini Beda. “Amekiri kuhusika na mauaji ya mheshimiwa Himidu,” alisema.
“Alikiri moja kwa moja?” Mkuu wa kituo alimwuliza Nunda.
“Kwanza alikana kuhusika.”
“Ulimtesa?”
“Ndiyo. Na ndiyo sababu iliyomfanya akiri.”
“Anaweza akawa alikiri kwa ajili ya kuogopa kuendelea kuteswa.”
Nunda hakuijibu kwa haraka hoja ya mkuu wake. Badala yake aliumumunya mdomo wake na kuonyesha kutafakari. “Nina imani amekiri kwa sababu ya kuhusika kwake,” alisema.
“Siwezi kujua kwa sababu ni wewe ndiye uliyemtesa. Hata hivyo chukua maelezo yake kwa kina ili uwe na uhakika kabla hatujampeleka Mahakamani.”
“Hawa watu bila ya kuwatesa hawawezi kusema ukweli mkuu,” Nunda alisema kwa nia ya kutetea mbinu yake ya utesaji.
“Sikupi baraka zangu kwa hilo. Si unajua utesaji haukubaliki katika sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu? Kwa hiyo kama unataka kumtesa mtuhumiwa kwa ajili ya kupata ushahidi hakuna anayelikataa hilo ndani ya uongozi wa jeshi la polisi. Tunachokikataa sisi kama viongozi ni kuhusishwa moja kwa moja kutoa amri ya utesaji kwa watuhumiwa. Sisi kazi yetu ni kuwatetea nyinyi pale mnaposhitakiwa kwa makosa hayo ya utesaji kwa kukanusha kuwa, vituo vyetu vya polisi havihusiki na kuwatesa watuhumiwa. Kwa hiyo kaendelee kufanya mahojiano na mtuhumiwa wako, tunachokihitaji ni kuupata ushahidi kama ni kweli alihusika na mauaji ya mheshimiwa Himidu bila ya kujali ni mbinu zipi zitatumika kufanikiwa kuupata ushahidi huo. Wapo aliokiri kushirikiana nao?”
“Bado hajatuweka sawa kwa hilo.”
“Nendeni kaendeleeni naye.”
* * *
Nyumbani kwa wazazi wake Beda, familia nzima iliamka asubuhi ikiwa imechanganyikiwa. Kutorudi nyumbani kwa Beda usiku uliopita ndiko kulikowafanya waipate taharuki hiyo. Haikuwa kawaida ya Beda kupotea kutwa nzima hadi usiku bila ya kupiga simu kuwajulisha alipo.
Kitu cha kwanza asubuhi hiyo walichokubaliana kukifanya ni baadhi yao waende kituo cha polisi cha Chumbageni kwa ajili ya kuuliza na kuripoti kupotea kwa Beda. Hatua ya pili iliyokusudiwa kufanywa endapo hakutokuwa na taarifa zake kwenye vituo vya polisi basi watalazimika kwenda kumtafuta kwenye eneo jingine muhimu ambalo ni hospitali tofauti za hapo mjini Tanga.
Taarifa za kutoonekana kwa Beda zikazifikia nyumba za jirani na kurudisha majibu kuwa, kuna baadhi ya majirani waliomwona Beda jana asubuhi akiingizwa kwa nguvu kwenye gari na watu wasiojulikana na kuondoka naye. Habari hizo zikaingiza mzuka kwenye familia hiyo, wale ambao awali walichaguliwa ili waende polisi kuulizia habari zake, sasa wakawa na uhakika kuwa, suala la Beda ni la kipolisi na siyo la kihospitali tena! Wakakurupuka kwa mwendo wa kasi na kila aliyewaona walivyokuwa wakitembea barabarani alibaini kuwa, watu hao walikuwa ndani ya taharuki iliyowapata. Walitembea kwa kasi huku wakiachana kwa hatua tofauti kutegemea na uwezo wa hatua za mtu. Kila mmoja alionekana kutaka kusema, ikawa kama zogo walivyokuwa wakizungumza.
Hatimaye walifika kituo cha polisi cha Chumbageni. Kabla ya kukikanyaga kidato cha kwanza cha ngazi cha lango la kuingilia kituoni, wote kwa pamoja wakawa wameipoteza kwa ghafla ile kasi waliyokuwa nayo, sura za kutaharuki na wahka waliokuwa nao vikayeyuka na badala yake kujengwa sura za nidhamu na kuingia kwa taadhima mbele ya kaunta ya polisi na kujikusanya pamoja, wote wakitaka kukisikia kile kitakachozungumzwa na mwenzao mbele ya askari waliowakuta.
Hatimaye mmoja akajieleza baada ya kuulizwa shida iliyokuwa imewaleta.
“Amefunguliwa mashitaka ya mauaji na amepelekwa Dar es Salaam,” askari wa kaunta alimjibu yule aliyekuwa akijieleza.
Kwanza wote waligwaya na jibu alilopewa mwenzao. Wakatazamana nyusoni kama vile walitaka kumjua ni nani mwenye kulijua hilo. Kisha, bila ya kutarajiwa mmoja wao akageuka na kumwangalia askari aliyewajibu. Akasema, “Amemwua nani?”
“Kwa kweli sijui,” alijibu askari. “Nendeni Dar es Salaam mtapewa maelezo yote.”
Zogo dogo likaanza kwa kila mmoja akisema na kuuliza lake. Wapo waliotaka maelezo ya kutaka kujua kwa nini askari huyo asimjue aliyeuawa, wengine walitaka kukijua kituo alichoswekwa ndani Beda huko Dar es Salaam na wengine wakilalamika na kulishutumu jeshi la polisi kwa tabia ya kubambikia makosa wananchi na kushindwa kutoa majibu sahihi…
Hatimaye Mkuu wa kituo alitoka na kulituliza zogo hilo kwa kuwaelekeza namna ya kumfuatilia ndugu yao na wapi pa kupata maelezo yanayohusu mashitaka aliyofunguliwa Beda.
Baadaye taarifa zikasambazwa kwa ndugu na jamaa, kikao kikafanyika na kukubaliana atafutwe wakili wa kulifuatilia suala la Beda. Safari ya kwenda Dar es Salaam ikaandaliwa.
******
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment