Search This Blog

Monday 24 October 2022

MKIMBIZI - 3

 

    Simulizi : Mkimbizi

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Mate yalinikauka na nikapigwa na butwaa. Nilimtazama kwa mshangao, kisha nikamtazama yule askari na kumgeukia Suleiman Kondo ambaye alinitazama kidogo na kuinamisha kichwa. Nikamgeukia tena yule afisa wa jeshi la polisi.

    “Mkurugenzi...” Nilianza kuongea kwa sauti ya kukwaruza huku moyo ukinipiga vibaya sana na huku nikisimama kutoka kwenye kiti changu.

    Haraka sana yule afisa wa polisi alipiga hatua kubwa na kuwahi kusimama mlangoni akinizuia nisitoke mle ndani.

    Nilikuwa nimenaswa, na hata wazo hilo liliponijia, akili yangu ilienda kwenye ule mkanda wa video uliokuwa ndani ya mkoba wangu uliokuwa ukining’inia begani kwangu.

    “Sina la kukueleza Tigga, na naomba uelewe kuwa hapa natimiza wajibu wangu. Na kwa mujibu wa sheria za kazi, kuazia muda utakaokuwa chini ya ulinzi, ajira yako itasimama mpaka hapo itakapoamuliwa vinginevyo, Suleiman atakupatia barua rasmi kukuarifu juu ya hilo na taratibu nyingine za kisheria.” Mkurugenzi aliniambia kwa upole lakini kwa mkazo usioyumba kabisa.

    “Lakini...lakini...si mmepata maelezo yangu? Kwa nini tena nikamatwe...?”

    “Tigga Mumba?” Yule askari aliongea kwa mara ya kwanza. Nilimgeukia huku macho yakiwa yamenitoka pima. Nilimtazama kwa umakini. Alikuwa amevaa mavazi wanayovaa askari wa ngazi za juu katika jeshi la polisi. Alikuwa mrefu na nilimhisi kuwa alikuwa katika umri wa kati wa ujana.

    Alikuwa na sura ya kuvutia hasa, na tofauti na askari wengi, yeye alikuwa amechonga ndevu zake vizuri katika ile staili ya Timberland ambayo mabrazameni wengi huwa wanaipenda. Sasa askari gani ananyoa ndevu kwa staili ya timberland!

    Hivi huyu ni askari wa kweli au ni miongoni mwa wale wanaomsaidia Martin Lundi moungo?

    Nilimkumbuka yule askari wa kike aliyeacha kunikamata kule gesti usiku uliopita.

    “Mkurugenzi! Hu...huyu si askari wa kweli! Anaweza kuwa miongoni mwao! Usimruhusu anichuku...”

    “Kuanzia sasa nakuweka chini ya ulinzi kwa kosa la kutoroka mikono halali ya sheria ambayo ilikutaka uisaidie polisi katika swala la mauaji yaliyotokea Manyoni.” Yule afisa alinieleza kwa ukakamavu bila ya kujali mapingamizi yangu.

    “Lini? Lini nilitoroka mikono ya sheria? Huo ni uongo! Uongo mkubwa...” Nilibwata huku nikihaha mle ndani ilhali yule askari akiwa amedhibiti njia yangu ya kutorokea.

    “Pia nakuweka chini ya ulinzi kwa kosa la kufanya vurugu zilizomsababishia mkuu wa wilaya ya Manyoni maumivu makali wakati ukiwa katika harakati za kuikimbia mikono ya sheria huko Manyoni.” Aliendelea kunisomea makosa yangu yule afisa wa polisi ambaye kwa hakika nilimuona kuwa ni muongo tu kama wale wengine.

    Miguu iliniisha nguvu nikajikuta nikijibwaga kwenye kiti.

    Yule askari alininyanyua kwa nguvu kutoka pale kwenye kiti na kuniongoza nje ya ofisi ile akiwa amenishika mkono wangu kwa nguvu juu kidogo ya kiwiko changu.

    Oh! Mungu wangu, huu ndio mwisho wangu!

    --

    Yule afisa wa polisi aliniongoza kuniteremsha ngazi kuelekea ghorofa ya chini ambapo ndio kulikuwa na uelekeo wa kutoka nje ya jengo lile. Kwenye ngazi tulipishana na binti mmoja wa kampuni ya ufagizi iitwayo WE KLEEN OFFICE CLEANERS na ambayo ilikuwa mkataba wa kufanya usafi na ufagizi katika ofisi yetu. Nilijionakama niliyekuwa ndotoni na sikuwa na ujanja. Mkono ulionikamata ulikuwa imara na wenye nguvu, na niliongozana na yule askari huku nikijaribu bila mafanikio kuilazimisha akili yangu inishauri ni hatua gani nichukue ili kujikomboa kutoka katika mtego ule.

    Wafanyakazi wenzangu walikuwa wakinichungulia kutoka kwenye milango ya vyumba vyao vya ofisi kwa wasiwasi uliochanganyika na udaku. Nilizungusha macho na kumtazama tena yule askari aliyenikamata. Mimi ni mrefu kuliko wasichana wengi, lakini huyu bwana alikuwa mrefu zaidi kwani niliona kuwa kichwa changu kilikuwa kinaishia juu kidogo ya bega lake. Nilipata harufu ya marashi ghali sana ya kiume ikitokea kwenye mavazi yake ya kiaskari, na hapo nikawa na hakika kabisa kwamba yule mtu hakuwa afisa wa jeshi la polisi kweli, na hata kama alikuwa ni afisa wa kweli, basi alikuwa ni miongoni mwa wafuasi wa Martin Lundi, na si vinginevyo.

    Nifanye nini Mungu wangu!





    Tulipofika mwisho wa zile ngazi tulikata kushoto ambapo aliniongoza kufuata kijikorido kidogo kilichoelekea kwenye mlango mdogo wa dharura ambao ulitokea moja kwa moja kwenye sehemu ya kuegeshea magari ndani ya uzio wa jumba la makumbusho. Mbele yetu, upande wa pili wa ile korido niliona kuna mfanyakazi mwingine wa ile kampuni ya kufanya usafi pale ofisini akiwa ameinama akipiga deki. Kwa pale tulipokuwa, niliweza kuona tu yale maandishi makubwa kwenye mgongo wa fulana yake yaliyokuwa yakiitambulisha ile kampuni ya usafi na ufagizi. Na hata pale tulipochukua uelekeo wa ule mlango mdogo wa dharura, naye aliinuka na kubeba ndoo yake ya maji pamoja na mifagio yake maalum ya kupigia deki na kuelekea kule tulipokuwa tukielekea na kuanza kupiga deki ile korido ndogo tuliyokuwa tukiiendea. Tulizidi kuelekea kule mlangoni huku yule afisa akianza kuchomoa pingu kutoka kwenye mfuko wa suruali, nami nikaingiwa na woga maradufu. Sijawahi kufungwa pingu hata siku moja maishani mwangu, na sio siri, pingu bora uisikie tu watu wakiitaja, lakini kuiona kwa macho inatisha si mchezo. Nilianza kutetemeka huku miguu ikiniwia mizito kuliko kawaida.

    “Tembea vizuri mwanamke...!” Yule afisa alinikemea huku akinivuta mkono wangu kwa mkono wake mmoja hali ule mwingine ukiweka pingu yake sawa. Na hapo hapo wote tulishitushwa na kishindo kikubwa. Yule mfagizi alikuwa akiinua ndoo yake ili kutupisha, lakini ghafla ile ndoo ilimponyoka na kuanguka sakafuni kwa kelele kubwa huku ikimwaga na kurusha maji sehemu yote, akilowanisha miguu ya suruali yangu na ya yule askari.

    Niliruka kwa mshituko huku nikitoa sauti ya woga hali yule afisa wa polisi akiropoka neno la kulaani kitendo kile naye akiruka pembeni bila kuniachia na kutazama jinsi suruali yake ilivyotota maji. Aliinua uso wake kwa hasira na kumtazama yule mfagizi na hapo hapo yeye na mimi wote tuliachia midomo wazi kwa butwaa.

    Macho ya nyoka alikuwa ametupa ile mifagio yake na sasa alikuwa ametuelekezea bastola kubwa iliyotisha huku akiwa amekenua meno kwa ghadhabu. Yule afisa wa polisi alikunja uso kwa hasira na mshangao.Alinigeukia, akaona jinsi nami nilivyohamanika, akamgeukia tena yule mtu mwenye bastola mbele yetu.

    Nilichoka!

    Yaani kumbe muda wote ule nilikuwa nikimtazama macho ya nyoka na sikumjua. Nilipeleka macho kwenye ile fulana nyeupe aliyovaa, ikiwa na maandishi WE KLEEN OFFICE CLEANERS kifuani, na suruali ya jeans nyeusi ambayo ndio sare wanazovaa wale wafanyakazi wa ile kampuni ya usafi na ufagizi.

    Eeh! Hawa watu ni kiboko!

    “Wewe ni nani...na Unataka nini...? Mimi ni afisa wa ngazi ya juu wa polisi, na nakuamuru uweke chini hiyo silaha yako upe...” Yule afisa wa polisi alianza kumuambia yule muuaji huku akiwa ameinua mikono yake usawa wa mabega yake kuonesha kuwa hakuwa na silaha, akiachia ile pingu yake ianguke sakafuni, lakini macho ya nyoka alimkatisha kikatili.

    “Kimya! Sitojali iwapo ni afisa wa ngazi ya mbinguni au ya ardhini! Usipotii maelekezo yangu nakuua sasa hivi!” Alimfokea, na niliona wazi kuwa alikuwa hatanii. Bila kujijua nilijikuta nikijificha mgongoni kwa yule afisa wa jeshi la polisi huku nikijiuliza kuwa iwapo naye alikuwa ni mfuasi wa Martin Lundi, vije tena Macho ya nyoka amtishie bastola? Sikuwa na shaka kabisa kuwa mimi ndiye niliyekuwa nikitakiwa pale, na si yule askari. Nilipata wazo kuwa muda wote Macho ya nyoka alikuwa akinisubiri pale ofisini akijifanya naye ni mfagizi akijua kuwa kuna siku ningetokea. Bahati leo nimetokea na kukutwa na huyu askari, kwani sasa ilinijia wazi kuwa yule mtu alikuwa ni askari wa kweli.

    “Oke...haina haja ya kugombana. Unataka nini...?” Yule askari alimuuliza Macho ya nyoka kwa tahadhari kubwa huku akimtazama usoni.

    “Namtaka huyo mwanamke, na sitaki uniingilie, kwani sitasita kukuua!” Macho ya nyoka alifoka.

    “Hapana! Usimkubalie! Ni muuaji huyo...” Niliropoka kwa jazba huku nikimng’ang’ania mgongoni yule askari.

    “Kelele malaya wee! Kuja hapa! Upesi!” Macho ya nyoka alinikemea huku akiniashiria nimfuate kwa ile bastola yake.

    “Sijui unamtakia nini huyu binti, lakini najua kuwa unafanya kosa kubwa sana. Huyu binti yuko chini ya ulinzi, na we’ unataka kumtorosha...mna uhusiano gani?” Yule afisa alimuuliza taratibu huku nikiuhisi mwili wake ukikakamaa.

    “Sina uhusiano naye wowote! Huyo ni muuaji...namjua sana! Ndiye aliyeua...anataka kuniua!” Nilipayuka kwa jazba kumuambia yule askari huku nikimtazama Macho ya Nyoka kwa hofu kubwa. Nilijaribu kuangaza nyuma yetu kuona iwapo akina Suleiman waliweza kutuona, lakini tulikuwa tumeshapinda kona na hivyo watu wote waliokuwepo kule upande wa vyumba vya ofisi hawakuweza kutuona. Tulikuwa tumejinasa wenyewe kwenye kona ya muuaji.

    “Afande kaa chini! Msichana njoo kwangu haraka!” Macho ya Nyoka aliamrisha huku nikimuona akiukaza ule mkono uliokuwa umeishika bastola hali macho yake ya kuogofya yakitoa mng’ao wa chuki kubwa. Sikuwa na shaka kabisa kuwa tukizidi kubisha tu ataua mtu.

    Huyu ni muuaji wa kuzaliwa hasa...

    Na nilipokuwa nikimtazama, nilipata hisia isiyo shaka kabisa kuwa alikuwa anatafuta sababu tu ya kuua mtu.

    “Mimi chini sikai, Utafanyaje?” Yule askari alimuuliza kwa sauti ya upole sana, kama kwamba alikuwa anaongea jambo la kawaida na mtu asiye hatari, nami nikazidiwa na woga.

    “Hah! Atakuua huyo afande! Atatuua sote...” Niliropoka kwa woga, na hapo nilishitukia kitu kama upepo tu kikipita kwa kasi na bastola ya macho ya nyoka ikisambaratika sakafuni kwa kelele, kwani yule afisa alirusha teke lililoipangusa ile bastola kutoka mkononi mwake kama mzaha. Mimi na Macho ya Nyoka tulijikuta tukizubaa kwa kama sekunde hivi wakati akili zikijaribu kuelewa kilichotokea, kisha Macho ya Nyoka alikurupuka ghafla huku akinguruma kwa ghadhabu kuirukia bastola yake iliyotupwa sakafuni, lakini yule afisa wa polisi alikuwa amejiandaa kwani alimrushia teke la kifua lililomtupa yule muuaji hadi ukutani, naye akajirusha kuiwahi ile bastola ya yule muuaji.

    Macho ya nyoka alijiinua haraka na kujirusha miguuni kwa yule afande kabla hajaifikia ile bastola, na wote wawili wakapiga mwereka mzito pale sakafuni. Sasa na mimi nilizinduka na nikaanza kupiga kelele, nikiwa nimejibanza kwenye kona ya ile korido huku macho yakiwa yamenitoka pima nikishuhudia wale wanaume wakigaragazana sakafuni kila mmoja akijaribu kumzuia mwenzake asiiwahi ile bastola. Kwa pale nilipokuwa nimesimama, niliona kuwa Macho ya Nyoka alikuwa amemlalia juu yule askari huku akinyoosha mkono wake kuiwahi ile bastola, wakati yule askari akiuvuta mkono wa Macho ya Nyoka usiifikie ile bastola. Na wakati huo huo niliona kwa mkono wake mwingine akijaribu kutoa bastola yake iliyokuwa kiunoni mwake, lakini mguu wa Macho ya Nyoka ulikuwa umeubana ule mkono hivyo ilimuwia vigumu kufanikisha lengo lake.

    Hapo ilinijia kumbukumbu ya lile tukio la kule msituni baina ya Macho ya Nyoka na yule mtu asiye na jina. Tukio lililopelekea yule mtu kupoteza maisha yake. Kumbukumbu ile iliniletea woga mkubwa na nikahofia kushuhudia tena tukio kama lile.

    Kwa nini kifo kinifuate kila mahali?

    Nilikurupuka kutoka kwenye kona ya ile korido nilipokuwa nimejibanza na kujaribu kuwaruka wale jamaa ili niiwahi ile bastola, na wakati huo huo yule muuaji alijiinua akijaribu kuinuka na miguu yangu ikampamia kwenye ubavu wake nami nikapiga mwereka mkubwa huku nikiachia yowe la woga. Nilijiinua kwa kupepesuka na kuegemea ukuta huku macho yakinitembea. Macho ya Nyoka alikuwa ameshainuka akiwa ameikamata tena ile bastola yake na sasa ilikuwa ikimuelekea usoni yule askari ambaye alibaki akiwa amepiga goti pale sakafuni huku akitweta, akimtazama kwa hasira. Niliona kuwa alikuwa hana ujanja. Macho ya Nyoka hakutaka kuongea zaidi. Na niliona kuwa alikuwa ameghadhibika kupita kawaida.Akili yake ilikuwa imemuelekea yule askari na kwa muda ule alikuwa hana habari na mimi. Alifyatua kitunza usalama cha ile bastola na uso wake ulimbadilika. Macho ya Nyoka alikuwa ameazimia kuua!

    Huku nikiwa nimetumbua macho na moyo ukinipiga kwa woga niliinyakua ile ndoo ya bati aliyokuwa akipigia deki na kumpiga nayo kichwani kwa nguvu zangu zote huku nikitoa ukelele wa hasira iliyochanganyika na woga. Macho ya Nyoka alitoa mguno hafifu na miguu ikamlegea huku bastola ikimtoka mkononi na damu ikimchuruzika kutoka upande wa kichwa chake pale pigo langu lilipotua. Haraka sana yule afisa wa polisi aliruka na kumshindilia ngumi ya taya iliyopeleka chini mzima mzima, na wakati huo huo kelele za wafanyakazi wenzangu pale ofisini zilinijia huku wengine wakianza kuja eneo lile mbio wakiwa wamejaa udadisi mkubwa.

    Nilibaki nikitazama kwa woga wakati yule afisa wa polisi akimnyanyua Macho ya Nyoka aliyeonekana wazi kuwa amepumbazwa na mapigo yale na kumbandika ile pingu iliyokuwa inifunge mimi mkono mmoja na kumgeuza kwa nguvu kimgongo mgongo ili amfuge na ule mkono wa pili kwa nyuma.

    Hilo lilikuwa kosa.

    Macho ya Nyoka aligeuka na pigo zito ambalo mpaka sasa siwezi kuelewa kama lilikuwa ni ngumi, teke au kiwiko cha mkono. Nilichoona ni yule afisa wa polisi akitoa yowe huku akijipinda kwa maumivu na kupepesuka. Hapo hapo Macho ya Nyoka aliruka na kumtamdika teke la kichwa lililompeleka ukutani kwa kishindo yule askari. Nilipiga kelele na hapo hapo wale wafanyakazi wenzangu pamoja na wale wafanyakazi wengine wa ile kampuni ya usafi walitimua mbio kurudi walipotoka huku kila mmoja akipiga kelele kivyake. Macho ya nyoka aliruka hatua mbili za nyuma nyuma na kunigeukia huku akininyooshea kidole kwa hasira bila ya kusema neno, na katika macho yale, niliona ahadi isiyotamkwa ya kifo cha mateso kutoka kwa Macho ya Nyoka. Kisha aligeuka na kutimua mbio kutoka nje ya jengo lile kutumia ule mlango wa dharura tuliokuwa tukiuelekea hapo awali.

    “Don’t Move!” Yule afisa wa polisi alininyooshea kidole na kuniambia huku akiikwapua ile bastola ya macho ya nyoka na kutoka mbio kumfuata yule muuaji, akimpigia kelele asimame.

    Sikuzubaa. Nililiweka sawa begi langu mgongoni na kutimua mbio kuelekea upande wa lango kuu la kuingilia na kutokea ndani ya jengo lile, nikipuuzia kabisa ile amri ya yule afisa wa polisi. Mazingira yalikuwa hayaeleweki, nami sikuwa tayari kuhatarisha usalama wangu zaidi katika mazingira kama yale. Suleiman Kondo alinipigia kelele nisikimbie lakini sikumjali. Niliendelea kutimua mbio.

    “Mkamateni huyooo!” Suleiman Kondo alipiga kelele na nikaona wafanyakazi wenzangu pamoja na baadhi ya wale wafanyakazi wa ile kampuni ya usafi ambayo Macho ya Nyoka alifanikiwa kujipenyeza ili aweze kunivizia pale ofisini wakitanda mbele yangu na kunizibia njia.

    “Tigga don’t run! Hii ni kwa usalama wako!” Suleiman Kondo alinipigia kelele huku akihangaika kunikimbilia kwa taabu kutokana na mwili wake mzito. Nilipagawa. Niligeuka na kutaka kurudi kule nilipotokea, nako nikakuta kuna baadhi ya wafanyakazi wakiwa wamefanya ukuta. Nilichanganyikiwa, jasho likinivuja na moyo ukinienda kasi kuliko ilivyowahi kutokea. Nilikuwa kama chui aliyezingirwa na wawindaji wenye ghadhabu. Nilimgeukia Suleiman Kondo, nikaona alikuwa ameungana na Mkurugenzi wakinikodolea macho.

    “Tigga! Usifanye tena kosa hilo...uko chini ya ulinzi! Utazidi kujiwekea mazingira mazito!” Suleiman alinipigia kelele. Na hata pale Suleiman alipomalizia kauli yake nilisikia mlipuko mkubwa wa bastola kutokea kule nje ambapo yule afisa wa jeshi la polisi alikuwa akikimbizana na Macho ya Nyoka huku vilio vya woga vikitawala mle ndani kutoka kwa wafanyakazi wenzangu. Sikutaka kusubiri kujua ni nani aliyepigwa risasi kati ya yule askari na yule muuaji niliyempachika jina la Macho ya Nyoka.Nilikwapua mtungi mkubwa wa maua uliokuwa pale kwenye korido kama sehemu ya mapambo ya ofisi na kwa nguvu zangu zote niliutupia kwenye dirisha kubwa la kioo lililokuwa karibu yangu na kulipasua vibaya, likiacha uwazi mpana sehemu iliyokuwa na kioo.

    Kelele zilitawala mle ndani nami nikajitupa nje ya dirisha lile na kuangukia nje ya jengo ambako nilijiinua haraka na kutoka mbio. Nilijipenyeza kwenye uzio wa nyuma ya jengo lile uliofanywa kwa aina ya miti kama michongoma na kutokea kwenye eneo la wazi lililokuwa limetapakaa majani yaliyokuwa yakitunzwa vizuri. Nilizidi kutimua mbio huku akili ikinizunguka bila ya kujua ni kwa nini niliamua kufanya vile na nini ingekuwa matokeo yake.

    Lakini nilichojali ni kuwa mbali na eneo lile ambalo lilishaingia walakini kuhusiana na usalama wangu. Nilikimbia nikijipenyeza kwenye uzio mwingine wa miti na kutokea kwenye mtaa mmoja mfupi na uliokuwa kimya sana. Nilihaha kwa muda, nikiangaza kulia na kushoto, kisha nikachomoka kasi kuelekea kushoto kwangu na kukutana na barabara nyingine ya lami, ambapo pia nilikutana na njia panda. Nilitimua mabio kuelekea kulia huku magari yakinipigia honi na nikisikia msuguano wa tairi za gari wakati zikifunga breki kwa ghafla. Sikugeuka nyuma wala sikupunguza mwendo.Nilikua natoka kasi kweli kweli. Niliibukia katika eneo nililolifahamu ambapo nililiona jengo la Internationa House likiwa kulia kwangu. Nilikunja kushoto kwenye makutano ya ile barabara niliyotoka nayo na ile ya kuelekea kwenye lile jengo la International House na Holiday Inn na kuanza kutembea kwa mwendo wa haraka huku nikikimbia kidogo kidogo, nikichukua uelekeo wa jengo la PPF Tower. Jasho lilikuwa likinitirirka vibaya sana na sina hata haja ya kukuambia jinsi moyo ulivyokuwa ukinipiga.



    Miguu ilikuwa ikinitetemeka na nikahisi maumivu kwenye sehemu ya juu ya mkono wangu wa kulia. Nilipojitazama nikaona kuwa nilikuwa nimejichanja na kipande cha kioo pale niliporuka dirishani. Kioo kilichana mkono wa lile koti langu gumu la jeans na kwa kiasi kikubwa kabisa lile koti lilipunguza makali ya kile kioo na hivyo kupunguza ukubwa wa lile jeraha ambalo lilikuwa likichuruzika damu kidogo, lakini hilo nililiona kuwa ni swala dogo sana. Niliangaza huku na huko, kila mara nikitaraji kusikia mtu akinipigia ukelele kuwa nisimame au akiwapigia kelele wapita njia wengine kuwa wanikamate.

    Nililipita duka la Imalaseko na kuongeza kasi kuelekea barabara kubwa ya Azikiwe. Hatua kadhaa mbele yangu niliona daladala kubwa aina ya Isuzu Journey likisimama kwenye makutano ya ile barabara niliyokuwapo na ile ya Azikiwe kuelekea posta ya zamani, na kondakta akinipigia kelele akiniuliza iwapo nilikuwa ni msafiri. Kwa rangi ya mstari wa lile basi, niliona kuwa lilikuwa ni basi linalofanya safari za Mwananyamala-Posta.Sikufikiri zaidi, nilimpungia mkono anisubiri huku nikiongeza mbio.

    Kwa wakati ule, basi lolote lingekuwa muafaka kwangu. Niliparamia lile basi kwa pupa nalo likaondoka kwa kasi eneo lile kuelekea maeneo ya posta ya zamani, huku yule kondakta akishangilia na kurukaruka mlangoni, nami nikijibwaga kwenye kiti nikitweta huku nikijifuta jasho kwa mkono wa koti langu. Tulipofika eneo la posta ya zamani nilipatwa na kihoro baada ya kuona tukisimamishwa na askari wa usalama barabarani. Niliangaza huku na huko na nikaona magari yote yaliyokuwa pale barabarani yalikuwa yamesimama, yakifanya foleni kubwa. Nilichanganyikiwa vibaya sana. Niliinuka na kutaka kuteremka, lakini konda alinizuia, akiniuliza iwapo nilikuwa nataka kuwalipisha faini ya elfu ishirini kwa kuteremsha abiria sehemu isiyo kituo, tena mbele ya wana usalama. Niliketi kwenye kiti huku akili ikinizunguka.

    Ina maana huu ni msako kwa ajili yangu?

    Nilitoa kichwa nje ya dirisha na kutazama kule mbele tulipokuwa tukielekea. Mwili ulinifa ganzi niliposhuhudia askari wa jeshi la polisi zaidi ya sita wakiwa wameshika bunduki aina ya SMG wakiwa wametanda mbele ya barabara, baina yao wakiwamo askari wa usalama barabarani.

    Nimekwisha!

    Nilimgeukia konda na kumuuliza kwa sauti ambayo nilishindwa kuamini kuwa ni yangu.

    “Ni...ni kitu gani? Kuna nini mbona tumesimamishwa?”

    Konda alinitazama kwa muda kabla ya kuniuliza. “Anti vipi...? Una haraka sana nini?” Nilimtazama kidogo kisha nikapeleka uso wangu pembeni, asije akanishika sura halafu akaja kuniletea matatizo hapo baadaye.

    “Hao ni wenye nchi wanapita dada yangu, eeeh!” Yule konda aliniambia baada ya kuona kuwa sikumjibu hapo awali, kisha akaongezea. “Hii ndio Bongo dadaangu, Ohooo! Namna hii mtu hata umpe nini hakubali kuachia madaraka. We’ watu wote tunasimamishwa ili mkuu apite bwana! Hata ingekuwa mimi siachii ngazi mwanangu!” Abiria waliangua kicheko nami nikabaki nimeduwaa huku nikihisi moyo ukinipiga kwa nguvu.Kwa hakika nilikuwa nimeshikwa na woga mkubwa.

    Kumbe ni msafara wa kiserikali tu!

    Nilishusha pumzi za faraja kwani nilijua kama ule msako ungekuwa kweli ni kwa ajili yangu basi nisingekuwa na namna ya kujiokoa. Muda si mrefu ving’ora vilisikika na msafara mrefu wa magari ya kifahari ambayo hayakuwa na shaka kuwa ni ya serikali ulipita, nasi tukaruhusiwa kuendelea na safari yetu muda mfupi baadaye. Nilitahamaki kuona lile basi likikunja kuelekea maeneo ya feri badala ya kule posta ya zamani kama nilivyotarajia. Kumbe lilikuwa ni basi la Mwananyamala-Kivukoni. Hii ilikuwa ni mbaya kwangu, kwani nilitaka nipotee lile eneo la mjini haraka iwezekanavyo. Sasa hii ya kuelekea Kivukoni tena si ndio ninazidi kujizamisha ndani ya mji kabisa. Nilitaka kumpigia kelele konda aniteremshe, lakini nikachelea kuonekana kituko bila sababu.

    Niliamua kutulia kufuata safari ya lile basi. Potelea mbali.

    Nilipofika Kivukoni niliteremka baada ya kuona lile basi lilikuwa linaendelea kusubiri abiria wajae ndio lianze safari yake ya kuelekea Mwananyamala. Niliamua kutafuta basi lolote litakalonitoa katika yale maeneo ya katikati ya mji na kunirudisha uswahilini ambapo ningeweza kupotea kirahisi, ingawa sikuwa na wazo nielekee wapi hasa. Nilianza kuangaza huku na huko pale kituoni nikitafuta basi lolote ambalo lilikuwa liko tayari kuondoka eneo lile wakati niliposhituka kwa kihoro baada ya kuona umma wa watu ukinijia mbio kama kwamba walikuwa wanamkimbiza mwizi.

    Moyo ulinilipuka na woga ukanitawala.

    Ni nini tena? Wamenijuaje?

    Nilianza kukimbia kidogo kidogo huku akili ikinizunguka kwa woga na mwili ukiniingia baridi.

    Lakini mbona walikuwa wananikimbiza kimya kimya? Au...?

    Na hata pale nilipokuwa nikijitahidi kukimbia kwa wasiwasi na woga mkubwa, nilishuhudia wale watu wakinipita bila hata kunijali na badala yake wakiendelea kutimua mabio kuelekea mbele.

    What is happening...?
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliendelea kukimbia huku nikiangaza huku na huko, nikijaribu kuwatazama wakimbiaji wenzangu kwa mshangao nisijue kinachoendelea, halafu nikaelewa.

    Wanakimbilia pantoni!

    Kama mwehu nami nikakaza msuli na kutimua mbio kwa nguvu zangu zote kuikimbilia ile pantoni. Niliiwahi nikiwa miongoni mwa watu wa mwisho kabisa, na muda si mrefu ile pantoni ikauacha ukingo wa bahari na kuanza safari ya kuelekea Kigamboni. Nilijiegesha kwenye kona moja mle ndani na kujikunyata nikilitazama jiji la Dar es Salaam likirudi nyuma taratibu wakati ile pantoni ikikata maji kuelekea upande wa pili wa bahari ya Hindi.

    Mwili wote ulikuwa ukiniuma na miguu ilikuwa ikinivuta kuliko kawaida. Nikiwa ndani ya pantoni nilitoa kitambaa changu cha kichwa na kujifunga kichwani, nikizificha kabisa zile nywele zangu za rasta.

    Niliteremka upande wa pili wa bahari na kujiunga na msururu mrefu wa wasafiri wenzangu kuelekea katikati ya kitongoji kile cha Kigamboni. Sikuweza kabisa kuiruhusu akili yangu iyatafakari matukio ya asubuhi ile, kwani nilihisi kuwa ningeweza kulipuka wazimu ghafla. Nilipitia kwenye maduka ya pale karibu na kipando cha pantoni na kununua nguo za kubadili kwani zile nguo zangu zilikuwa zimeanza kutoa harufu ya jasho, na pia nilijua kuwa kufikia sasa nilikuwa najulikana nguo nilizovaa, hivyo polisi wangekuwa wanamsaka mwanamke aliyevaa suruali na koti la jeans, kijitopu chekundu kwa ndani, akiwa amesuka nywele katika mtindo wa rasta. Kwa kuwa bado nilikuwa na pesa za kutosha, nilinunua nguo kadhaa za kubadili na kuongeza begi jingine dogo ambamo niliweka zile nguo zangu mpya. Niliingia duka la dawa na kununua dawa ya kidonda, bandeji, mswaki na dawa ya meno.

    Kisha nilikodi teksi na kumuambia dereva anipeleke kwenye nyumba nzuri ya wageni iliyotulia. Alinipeleka kwenye nyumba moja ya wageni ambayo niliafikiana naye kuwa ilikuwa imetulia. Nikijiandikisha kwa jina la Nuru bint Shaweji, nilikodi chumba cha self contained kwa muda wa siku tatu. Kazi yangu nilijiandikisha kama mwanafunzi wa chuo cha elimu ya sayansi ya bahari cha Zanzibar. Sababu ya ujio wangu pale Kigamboni ikiwa ni kuandika juu wa mwenendo wa pwani ya Kigamboni. Maelezo yote haya nilijua kuwa ni upuuzi na uongo mtupu, lakini ilikuwa ni vigumu kwa yule jamaa wa mapokezi, ambaye alionekana kuwa hakwenda shule kiasi cha kuweza kuelewa mambo kama yale, kuyatilia maanani na kuyafuatilia.

    Nilijifungia chumbani kwangu na kuelekea moja kwa moja bafuni ambapo nilioga kwa muda mrefu. Kisha niliosha na kufunga kidonda changu, kabla ya kujibwaga kitandani na kuchapa usingizi mzito.

    v.



    J

    ambazi lauawa na pingu mkononi.

    Kilikuwa ni kichwa cha habari kilichochukua uzito wa juu kabisa katika moja ya magazeti ya kila siku yanayotoka jioni. Moyo ulinilipuka na kuanza kunienda mbio, huku nikishuhudia lile gazeti likitetemeka mikononi mwangu wakati nikikodolea kwa kutoamini kichwa kile cha habari.

    Ilikuwa ni majira ya saa moja za jioni wakati nikiwa napata mlo wa jioni kwenye mgahawa wa ile nyumba ya wageni wakati nilipoona kile kichwa cha habari kutoka kwenye moja ya magazeti yaliyokuwa yakitembezwa na kijana mmoja ndani ya mgahawa ule. Nilinunua haraka lile gazeti huku hamu ya kula ikiniisha. Niliinamia sahani yangu ya chakula na kukichezea chezea kwa muda kile chakula, kisha nikarudi chumbani kwangu upesi na kuanza kuisoma habari ile.

    Macho ya Nyoka ameuawa!

    “Haiwezekani! Haiwezekani auawe kirahisi namna hii! Macho ya Nyoka! Labda ungeniambia Dokta Martin Lundi, ningeweza kuamini, lakini sio Macho ya Nyoka!” Nilikuwa nijisemea peke yangu mle ndani huku nikitikisa kichwa kukana habari ile huku nikiiona kwa macho yangu pale gazetini.

    Hapana bwana, kwangu hilo lilikuwa haliwezekani kabisa. Yule mtu ni muuaji wa kuzaliwa. Yaani yeye ndiye mwenye kazi ya kuua watu, sasa iweje tena yeye ndio auawe kirahisi namna hii?

    Sio Kweli. Hii ni mbinu yao tu ya kutaka kunilaghai ili nijiamini kuwa niko salama halafu wanikamate kirahisi. Macho ya Nyoka ndiye mtu niliyemuhofia kuliko wote miongoni mwa wale wauaji niliowaona kule msituni, na nilishapata hisia kuwa kama sitanusurika na maisha yangu katika kindumbwendubwe hiki, basi ni Macho ya Nyoka ndiye atakeniua. Sasa tena hii habari...hapana si kweli!

    Macho ya Nyoka afe! Sikuamini.

    Lakini gazeti ndivyo lilivyoandika!

    Macho ya Nyoka aliniahidi kifo cha mateso makubwa kwa macho tu na nikaelewa bila shaka yoyote ni nini alikuwa akiniahidi! Yaani hakutamka hata neno moja! Macho tu, na ujumbe ukafika!

    Nilikumbuka yale macho yake jinsi yalivyoniahidi kifo pale aliponitazama kwa chuki huku akininyooshea kidole kabla hajatimua mbio kumkimbia yule afisa wa polisi, pingu ikimning’inia katika mkono mmoja.

    Eti amekufa!

    Nilikumbuka ule mlipuko wa bastola niliosikia ukitokea kule nje walipokuwa wakikimbizana, baada ya yule afisa wa polisi kuniamuru nisiondoke wakati akimfuata mbio yule muuaji. Nami nikaamua kutimua mbio kutoka eneo lile bila ya kujali kelele za Suleiman Kondo kuwa nisikimbie.

    Pamoja na kuona kuwa kile kilichosemekana kutokea kuwa hakiwezekani, sikuweza kujizuia kuisoma ile habari iliyoandikwa gazetini kuhusu tukio lile lililotokea asubuhi ya siku ile pale ofisini kwetu.

    Na hata nilipomaliza kuisoma kwa mara ya pili, bado nilibaki mdomo wazi na kujiuliza iwapo nilitakiwa niiamini au nisiiamini habari ile.

    Kwa mujibu wa gazeti lile, ni kwamba jambazi hilo ambalo bado jina lake halijatambulika, liliuawa katika mapambano na polisi baada ya kufanikisha kutoroka kwa mwanamke ambaye alikuwa ametiwa mbaroni na polisi kuhusiana na mauaji ya kutatanisha ya watafiti wa Idara ya Makumbusho ya Taifa pamoja na watu wengine huko Manyoni.

    Kutokana na maelezo ya gazeti lile, nilielewa kuwa Macho ya Nyoka alipokuwa akikimbizwa na yule askari, aliamua kusimama ili apambane naye, ambapo alitoa bastola (hii itakuwa nyingine, ambayo bila shaka alikuwa nayo – kwani ile bastola yake ndiyo aliyokuwa akiitumia yule askari baada ya kuangushwa chini katika mapambano), lakini kabla hajaitumia, yule askari alimuwahi kwa risasi ya mguu, na alipozidi kujaribu kumtupia risasi ndipo yule askari alipompiga risasi nyingine(sikumbuki kusikia mlipuko wa pili wa bastola, lakini wakati huo mimi ndio nilikuwa nimehamanika nikitafuta namna ya kutokomea kutoka eneo lile) iliyompata kifuani na kumuua.

    Just like that...!Yaani hivi hivi tu!

    Baada ya hapo gazeti lilielezea tena habari za yale mauaji ya kule Manyoni, na kutaja kuwa mwanamke aliyetoroka katika tukio lile bado anatafutwa na polisi na kutaja jina langu halisi, huku likinukuu taarifa ya polisi kuwa mwananchi yeyote atakayemuona au kuwa na habari zozote za mahala anapoweza kupatikana mwanamke huyo, atoe taarifa katika kituo chochote cha polisi kitakachokuwa karibu naye.

    Kwa kuwarahisishia kazi wananchi, wasifu wangu wote ulielezwa gazetini, ikiongezewa na taarifa ya nguo nilizokuwa nimevaa siku ile pamoja na mtindo wa nywele niliokuwa nimeusuka. Nilishukuru mungu kuwa ingawa nilipoingia pale kwenye ile nyumba ya wageni nilikuwa nimevaa zile jeans zangu, nywele zangu za rasta nilikuwa nimezifunga ndani ya kilemba ambacho hadi muda ule nilipokuwa nakula pale kwenye mgahawa bado kilikuwa kichwani mwangu, na nilikuwa nimebadilisha nguo.

    Zaidi ya hapo, picha yangu yenye ukubwa wa pasipoti iliwekwa pale gazetini, picha ambayo sikuwa na shaka ilitoka pale ofisini. Ni picha ambayo niliipiga siku chache baada ya kumaliza masomo yangu Chuo Kikuu, niliyoiwasilisha pale ofisini wakati naanza kazi kwa ajili ya kuwekwa kwenye faili langu binafsi la ajira. Katika picha ile nilikuwa naonekana mdogo zaidi, mwembamba zaidi, na zaidi ya hapo nilikuwa nimekata nywele zangu na kuziacha ndogo ndogo sana, ikiwa si siku nyingi tangu nitoke kwenye msiba wa baba yetu, ambapo kutokana na msiba ule, nilinyoa nywele zote.

    Haikuwa picha ya kunitia shaka sana, lakini niliogopa kupita kiasi, kwani sasa jina langu lilikuwa hadharani, na wajihi wangu ulikuwa gazetini kwa kila mwenye macho kuuona.

    Nitakimbilia wapi sasa?

    Bila hata kufikiri zaidi nililitupa pembeni lile gazeti na kuanza kufumua zile rasta.

    Hivi ni kwa nini haya mambo yanatokea?Ndilo swali lililokuwa likijirudia tena na tena kichwani mwangu tangu nilipoamka kutoka kwenye ule usingizi mzito ndani ya ile nyumba ya wageni. Na baada ya kusoma zile habari za kwenye lile gazeti, nilijikuta nikizidi kujiuliza lile swali. Na kila nilipojiuliza swali lile,nilijikuta nikijiuliza swali jingine kubwa na gumu zaidi. “Kwa nini mambo yale yanikute mimi katika watu wote?”

    Kwa kweli wakati natimua mabio baada ya tukio la pale ofisini, sikuwa na hakika kama nilikuwa nachukua uamuzi wa busara, kwani nilipoyatafakari upya matukio yote yaliyotokea pale ofisini siku ile, nilipata hisia kuwa huenda yule afisa wa jeshi la polisi alikuwa ni askari wa kweli, na kwamba hata kama alikuwa na nia ya kunikamata kwa makosa yale aliyonitamkia pale ofisini kwa Mkurugenzi, kutokea kwa Macho ya Nyoka na matendo yaliyofuatia, kungeweza kabisa kumbadilisha mawazo na labda angeweza kuwa ndiye mtu wa kunisaidia, hasa nikizingatia kuwa yule alikuwa ni afisa wa ngazi ya juu katika jeshi la polisi.

    Lakini kwa wakati ule ningeyajuaje hayo? Ningeweza kuyachezea bahati nasibu maisha yangu? Hapana, bora nilivyokimbia.

    Lakini kila nilipozidi kutafakari tukio la pale ofisini na uamuzi niliochukua, ilinifunukia wazi kuwa sasa nilikuwa naendeshwa na hisia zaidi kuliko kitu kingine chochote. Kuwa ujumla wa matukio yote yaliyonikuta huko nyuma hadi kufikia sasa, umepelekea hisia zangu zote kufikia hatua ambapo zilikuwa zinaanza kutekeleza matendo ya kujihami na kujiokoa kwanza, halafu kutafakari juu ya hatua hizo baadaye. Baada ya matukio ya kule kwa mkuu wa wilaya nilipokimbilia kutafuta msaada, na yale ya kule kwa Kelvin na nyumbani kwa mama yangu, nilikuwa nimejitosheleza fika akilini mwangu kuwa sehemu pekee yenye usalama kwangu ni pale nitakapokuwa peke yangu. Na kwamba kila nitakayemdhania kuwa huenda akawa na msaada kwangu, anaondokea kuwa upande wao.







    Wao.

    Wao ni akina nani?

    Na yule afisa wa polisi naye...

    Macho ya Nyoka alikuwa tayari kabisa kumuua yule askari...sasa amekufa yeye!

    Kwa hakika nilijua kuwa kama sikuchukua uamuzi wa haraka na kumbamiza Macho ya Nyoka na ile ndoo, bila shaka ningeshuhudia yule askari akiuawa mbele ya macho yangu.

    Kadiri nilivyolitafakari tukio lile, nilijishawishi kuwa kwa wakati ule, nilikuwa nimechukua uamuzi wa busara sana kukimbia kutoka eneo lile, kwani kwa mambo niliyoyashuhudia kutoka kwa akina Martin Lundi, isingekuwa ajabu kabisa kukuta kuwa yule askari na Macho ya Nyoka walikuwa kitu kimoja, na walikuwa wanajifanya kutupiana mateke mbele yangu ili nijenge imani kwa yule askari wapate kunichukua kirahisi.

    Lakini sasa nilielewa vinginevyo.

    Kwa hakika yule alikuwa ni askari wa kweli, lakini hata kama ningebaki pale ofisini kama alivyoamrisha, angenielewa na kunisaidia? Au ndio ingekuwa kama yale ya kule kwa Mkuu wa Wilaya?

    Kadiri nilivyoitafakari ile hali huku nikiendelea kuzifumua zile rasta, ilinijia wazi kuwa ingawa kifo cha Macho ya Nyoka kilitakiwa kiwe faraja kwangu, bado hakikuleta unafuu wowote katika hali yangu, kwani bado nilikuwa natafutwa na Dokta Martin Lundi na wenzake waliobaki. Tena sasa baada ya kifo cha mwenzao na kuelezwa gazetini kwa mazingira yaliyopelekea kifo chake, nilikuwa na hakika kabisa kuwa watazidisha bidii za kunisaka kwani nilikuwa na hakika kabisa wao hawakutaka kabisa nitiwe mbaroni na polisi wasio upande wao ili waweze kupata na kupoteza ule ushahidi ambao ulikuwa na madhara makubwa sana kwao. Lakini kama hiyo haitoshi, na polisi nao kwa upande wao walikuwa wanaendelea kunisaka. Sasa sijui kwa nini gazeti liliandika kuwa Macho ya Nyoka alikuwa amekuja kunitorosha, wakati yule afisa aliona wazi kuwa yule muuaji hakuwa na nia ya kunitorosha kwa urafiki baina yetu bali kwa sababu nyingine tu. Vyovyote itakavyokuwa, mbele ya yule afisa wa polisi na jeshin lake, bado nilikuwa mkimbizi kutoka kwenye mikono ya sheria, tena niliyekaidi amri ya kutotoroka niliyopewa na yule afisa wakati akimfukuza yule muuaji.

    Lakini yule afisa wa polisi akiendelea kuniwinda ajue kuwa anaweza kuendelea kuniwinda kwa sababu niliokoa maisha yake...

    Kwa siku mbili mfululizo sikutoka nje ya chumba changu zaidi ya kwenda kula na kurudi tena chumbani. Uzuri wa mambo ni kuwa pale pale kwenye ile nyumba ya wageni kulikuwa kuna sehemu ya mgahawa, hivyo sikupata taabu ya kutembea umbali mrefu kutafuta chakula. Kwangu, hizo zilikuwa ni siku mbili za tathmini ya matukio yote yaliyonitokea na jinsi nitakavyokabiliana nayo.

    Siku yangu ya kuondoka pale kwenye ile nyumba ya wageni, niliongeza siku nyingine tatu, nikidai kuwa nilikuwa bado nina kazi za kuandika. Wakati huu nilikuwa nimeshanunua madaftari na makaratasi pamoja na kalamu kadhaa ili kweli nionekane mwanafunzi niliye kwenye utafiti. Na ili nisijiletee mashaka, nilikuwa nikitoka nje na kwenda kuzubaa pwani iliyokuwa karibu na ile nyumba ya wageni, na mara nyingine nikitembea tu mle mjini. Na mara zote nilizotoka, nilihakikisha kuwa nilikuwa na madaftari yakionekana wazi kwenye mkoba wangu.

    Katika kipindi hiki, nilitumia muda wangu mwingi kadiri nilivyoweza kuangalia televisheni iliyokuwamo mle chumbani, hasa taarifa za habari ili nijue iwapo kuna habari zaidi juu yangu katika vyombo vya habari na kama zipo, zimetolewa kwa mtazamo gani. Aidha nilikuwa nikinunua magazeti kila siku nilipotoka kwenda kupata kiamsha kinywa asubuhi na kuyasoma kwa makini kutafuta habari zozote zilizohusiana na matukio niliyokumbana nayo. Lakini katika siku zilizofuatia, habari zile zilionekana kufifia kabisa.

    Kama mvua iliyonyesha ghafla wakati wa kiangazi, halafu ikapotea na kukiacha kiangazi kiendelee kutawala.



    --



    Ukimya uliotawala baada ya habari ya kuuawa kwa Macho ya Nyoka ulinitia wasiwasi sana. Haikuniingia akilini kabisa kuwa baada ya taarifa kama ile, na taarifa zangu zikiambatana na picha yangu kutolewa gazetini, mambo yawe kimya kiasi kile. Nami nilizidi kuchoka kukaa katika ile hali ya wasiwasi na kujificha nikipita nikijibandika majina yasiyo yangu kwa woga wa kukutwa na watu wa Dokta Lundi au wana usalama.

    Na kadiri nilivyokuwa nikiendelea kujificha katika ile nyumba ya wageni, nilikuwa nazidiwa na hamu na duku duku la kutaka kujua hali ya mama yangu ikoje hasa baada ya kukutana na dokta Lundi siku ile nilipowatoroka pale nyumbani. Nilitamani pia kumpigia simu dada yangu labda angenipa habari zozote lakini nilishindwa kutokana na woga kuwa huenda namba ya simu nitakayotumia ikafuatiliwa na kugundulika kuwa nimepiga kutokea Kigamboni halafu wakaniibukia kule kule Kigamboni. Nilishindwa pia kutafuta habari za Kelvin kwa sababu hiyo hiyo, ingawa naye nilikuwa na shauku kubwa ya kujua ni nini ilikuwa hatima yake.

    “Lakini kwa nini niendelee kuishi maisha haya ya kikimbizi namna hii?” Nilijisemea peke yangu nikiwa chumbani mwangu pale kwenye ile nyumba ya wageni na kusonya kwa hasira na kuchanganyikiwa. Niliinuka kutoka kitandani nilipokuwa nimejilaza na kwenda kusimama nikiegemea ukuta huku nikiwa nimetumbukiza mikono yangu kwenye mifuko ya suruali ya michezo niliyokuwa nimeivaa.

    “Na nitaendelea kuwindwa namna hii mpaka lini?” Nilijisemea tena kwa hasira na kutoa msonyo mkali. Nilitembea mle ndani huku nikiwa nimezamisha mikono yangu mifukoni nikitafakari ile hali niliyokuwa nayo.

    “Halafu kibaya ni kwamba hao wanaoniwinda wananijua fika, lakini mimi siwajui…naona watu wananikimbiza, wanaua watu, wanawarubuni ndugu na jamaa zangu nao wanigeuke…lakini wao ni akina nani hasa sijui!” Niliguna na kujibwaga tena kitandani kwa kukata tamaa.

    Muda ulikuwa ni kama saa kumi na mbili za jioni na kwa mbali nilisikia sauti ya adhana ikiwakumbusha waislamu kwenda msikitini kwa swala ya jioni.

    “Lakini tatizo hasa ni nini…? Kwa nini yale mauaji yalitokea kule msituni? Kwa nini ilikuwa muhimu kwa Dokta Lundi kunipakazia mambo ya uongo namna ile…?”

    Niliinuka na kuliendea begi langu na kuitoa ile kamera ya Gil, na kwa mara ya kwanza tangu nitoke kule Manyoni nilikaa chini na kuutazama upya ule mkanda tangu mwanzo hadi mwisho. Nikilirudia upya lile tukio la kule msituni. Nilipomaliza kutazama yale mambo ya ajabu niliyoyarekodi kule msituni nilijikuta nikibubujikwa na machozi bila kupenda. Lakini pia kulitazama tena lile tukio kuliniletea mwanga mpya katika uelewa wangu wa tukio lile na nikajikuta nikiurudisha tena nyuma ule mkanda na kuuangalia upya kutokea mwanzo hadi mwisho huku nikitafakari matukio mengine yaliyonitokea ambayo hayakuwamo mle kwenye ule mkanda.

    Niligundua kuwa kumbe wale wauaji, akina Martin Lundi, wote walikuwa wamevaa glovu mikononi mwao, kitu ambacho sikuwa nimekiona hapo mwanzo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ina maana walikuwa wamedhamiria kuwa wasiache ushahidi wowote wa kuhusika kwao aidha na kifo cha yule mtu, au tukio zima la pale msituni.

    Nilirudia ile sehemu nilipokuwa naongea na yule mtu asiye na jina kule msituni, ambapo hapa nadhani nilirekodi bila ya kujijua, kwani ile kamera ilikuwa imeelekea ardhini kwenye mchanga, na ilichorekodi kilikuwa ni yale mazungumzo yaliyotokea baina yetu pale mchangani. Na nilipokuwa nikitazama ule mkanda ukionesha michanga tu ya pale alipokuwa amelala yule mtu na sehemu kidogo ya bega na mkono wake, nilikuwa nayasikia upya yale maongezi kutoka kwenye ile kamera.

    “Usiongee! Tulia, nitakusaidia”

    Halafu nilisikia miguno ya yule mtu kisha nikaona zile namba ambazo yule mtu aliziandika mchangani na kunisistizia nizitazame.

    Niliusimamisha ule mkanda na kukimbilia kalamu na kijitabu kidogo kilichokuwa mezani, nikarudi pale nilipoiacha ile kamera na kuinakili ile namba huku moyo ukinienda mbio.

    Nikaendelea kuangalia ule mkanda.

    “Sawa...nimeshaona! Hizi namba ni za nini? Na wewe ni nani...kwa nini wale watu wamekufanya hivi? Umewafanya nini? Ni nani wale?”Ilifuatia sauti ya yule mtu akikohoa kwa taabu, ikifuatiwa na pumzi zake akitweta kama mtu aliyemaliza mbio ndefu.

    “Find the Bastard!”

    “Yes! Usiwe na wasiwasi nitahakikisha wanafikishwa mbele ya sheri...’

    “...at the Rickshaw...!”.

    “Rickshaw? Rickshaw iko wapi ?”

    Niliisimamisha tena ile kaseti na kuandika tena kwenye kijitabu changu:

    Bastard.

    Rickshaw.

    Nikaendelea kuutazama tena ule mkanda.

    Zilifuatia sauti za yule mtu akigumia kwa taabu, nami kumbukumbu zangu zikanionesha picha ya yule mtu alipokuwa akitapatapa huku akitupa kichwa chake huku na huko na nikakumbuka jinsi nilivyopandwa na woga nilipodhani kuwa yule mtu ndio alikuwa anakata roho.

    “Wewe ni nani...ndugu zako ni nani?”

    Niliusimamisha ule mkanda na kuandika kwenye kijitabu changu:

    Wewe ni nani? – No answer. Mr. Who?Mr. Nani? Question Mark! =Mr. Q?

    Nikabonyeza sehemu inayotakiwa na ule mkanda ukaendelea.

    “Get the key....the bastard!”

    “Key…? What key…?”

    Niliisimamisha ile kaseti na kuandika tena kwenye kijitabu changu:

    Key – Ufunguo. ???

    Nikaendelea kuutazama ule mkanda.

    “At the Rickshaw…!”

    “I don’t understand!”

    “Please…Go now!”

    “Lakini bado sijaelewa…nataka kukusaidia! Au hujui Kiswahili…? Can’t you speak Swahili?”

    “Find the bastard!”

    Niliisimamisha tena na kuandika kwenye kijitabu changu:

    Find the Bastard! – Mtafute Mwanaharamu? (M. Lundi&wenzake???)

    Nilibaki kimya kwa muda mrefu huku nikitafakari wakati picha ya siku ile msituni ikinijia akilini na nikakumbuka jinsi yule mtu alivyonitazama huku akitoa kitu kama tabasamu dogo sana baada ya kuniambia yale maneno.

    “Now why did you smile like that Mr. Q, eenh?” Nilijisemea mwenyewe kwa sauti ya chini, nikimuuliza yule marehemu huko aliko kwa nini alitabasamu namna ile baada ya kunieleza maneno yale. Nilikaa nikitafakari kwa muda mrefu sana, huku nikichorachora vitu visivyoeleweka katika kile kijitabu changu. Kisha niliamua kuendelea kuuangalila ule mkanda.

    “Okay...I can speak english....who are you? Who are those people…? Do you have any relatives….? I can help you…I want to help you!”

    “Please Go...watakukuta!”.

    “Watakuua...wacha nijaribu kukusaidia”

    “I don’t care...you go find the bastard!”

    Hapa niliusimamisha tena ule mkanda na kuandika kwenye kijitabu changu:

    Mr.Q hajali kama angeuawa?? Anachojali = Find the Bastard!!!!

    Who is the Bastard? – M. Lundi, Kigulu,Macho ya Nyoka(Dead?) Au kuna kitu kingine?

    Hapa nilitafakari tena kwa muda mrefu, na ingawa sehemu hii yote ya mkanda nilikuwa nimerekodi sauti tu, wakati picha ikionesha michanga tu ya pale mchangani alipokuwa amelala yule mtu asiye na jina(nilishampachika jina la Mr.Q), bado niliikumbuka vizuri sana sura yake ilivyokuwa pale alipomaliza kusema yale maneno na jinsi alivyojitahidi kutabasamu tena halafu akazidiwa na kikohozi kikali na damu ikaanza kumtoka mdomoni. Hapa mkanda ulisimama kabisa kurekodi na hakukuwa na picha wala sauti yoyote, nami nikakumbuka kuwa ni wakati huu ndipo nilipomwinua kichwa chake ili damu isimpalie na kuanza kumfuta ile damu kwa mkono wa shati langu. Nilikumbuka waziwazi kuwa nilipofanya hivi, yule mtu alinishika mkono kwa nguvu na kunitolea macho huku akinisisitizia kuwa niondoke eneo lile haraka kabla wale wauaji hawajanikuta na kuniua.

    Na kweli masikini, nilipoondoka na kumwacha pale, wale wauaji walirudi na kumkuta akiwa anagaa gaa pale mchangani.

    Nililia kwa uchungu baada ya kuona ni jinsi gani yule mtu alivyonisisitiza niokoe maisha yangu ingawa alijua kuwa yeye angekufa muda wowote.

    “Lakini kwa nini uliniita? Hukutaka nikuokoe, bali ulitaka kunieleza kitu…?” Nilimuuliza yule marehemu huko aliko kwa fadhaa huku nikibubujikwa machozi na nikihisi donge kubwa likinikaba kooni.

    “Sasa mbona hukunieleza kitu chochote cha maana, Mr. Q?” Nilimuuliza tena kwa uchungu huku nikibubujikwa na machozi. Nilitazama vitu nilivyoandika kwenye kile kijitabu changu. Hakukuwa na kitu chochote kilichokamilika ambacho kiliniwezesha kujua ni nini yule mtu alitaka kunieleza. Kwa muda mrefu nilibaki nikikodolea macho vitu nilivyoandika kwenye ule ukurasa wa kile kijitabu changu, na bado sikupata jibu la moja kwa moja.



    456718

    Bastard.

    Rickshaw.

    Wewe ni nani? – No answer. Mr. Who? Mr. Nani? Question Mark! = Mr. Q?

    Key – Ufunguo.???

    Find the Bastard! – Mtafute Mwanaharamu?(M. Lundi&wenzake???)

    Mr. Q hajali kama angeuawa?? Anachojali = Find the Bastard!!!!

    Who is the Bastard? – M. Lundi, Kigulu, Macho ya Nyoka (Dead?) Au kuna kitu kingine?



    Nilidhani ningeweza kupata mwelekeo fulani kutoka kwenye ule mlolongo wa vitu nilivyoandika kutoka kwenye kauli za yule mtu aliyeuawa msituni. Nilihitaji kutafakari zaidi.

    Hatimaye niliamua kuendelea kuutazama ule mkanda na nilipofikia katika sehemu ambapo yule mtu niliyembatiza jina la Mr. Q alimrukia Macho ya Nyoka na kuanza kupambana, niliusimamisha tena ule mkanda na kubaki nikikodoa macho kwa mshangao mkubwa huku akili ikinizunguka. Kitu nilichokiona pale, ingawa nilishakiona kwa macho yangu kule msituni, na nikakiona tena kwenye ule mkanda mara ya kwanza, kilinishitua na kuniletea mtazamo mpya kabisa katika swala zima la mkasa huu ulioniangukia.

    Ilikuwa ni vigumu kuamini, lakini ndivyo ilivyoelekea.

    Niliirudisha tena ile sehemu na kuiangalia upya.

    Ni kweli kabisa nilichogundua, na hata pale ugunduzi ule uliponiangukia, nilijikuta nikishikwa na butwaa nisijue la kusema.

    Mr. Q alimrukia Macho ya Nyoka kusudi ili auawe!

    Naam! Ndivyo haswa.

    Nilihisi mwili ukinisisimka na hapo hapo vipele vya baridi vilinitoka mwilini.

    Kwa nini Mr. Q aamue kufanya vile? Kwani bila shaka na yeye alijua kuwa katika wale watu watatu, Macho ya Nyoka ndiye aliyekuwa anaelekea kuua bila hata ya sababu, hivyo akaamua kumpa sababu ya kumuua na ndivyo ilivyotokea!

    Nilifikiria maana ya kitendo hiki huku maswali yakinielemea.

    Kwa nini aamue vile? Kwa nini aamue vile wakati ule, na si wakati wowote kabla ya hapo?

    Kutokana na tukio lile kama jinsi nilivyojikumbusha kwa kuutazama tena ule mkanda, ni kwamba yule mtu aliteswa sana kabla ya kuletwa pale msituni, na kama aliteswa, lazima kuna sababu ya kuteswa huko.

    Nilikumbuka kuwa kuna wakati kabla ya yule mtu kumrukia Macho ya Nyoka na hatimaye kuuawa, alimtemea mate Kigulu ambaye alikuwa akimuuliza kitu fulani, na kisha akamtupia mchanga usoni, na wakati kigulu anajipangusa mchanga, yeye alimrukia Macho ya Nyoka.

    Ambaye wakati huo alikuwa pembeni kabisa tena na bastola yake alikuwa ameiweka mfukoni baada ya kukemewa na wenzake alipokuwa akimtishia Mr. Q kwa bastola ile.

    Hii ilimaanisha kitu kimoja tu...

    Yule mtu alikuwa anawachokoza kusudi ili wamuue!





    Kwa nini?

    Nilikaa muda mrefu nikitafakari juu ya hilo, na hatimaye nilipopata jibu ubaridi ulinitambaa mwilini na kijasho kilinitoka.

    Mr. Q aliamua kufanya vile ili afe kwa sababu alijua kuwa alikuwa amenieleza kila kitu alichotaka na ndio maana akaona afe na siri yake kabla hajaitoa kwa wale wauaji.

    Duh! Si mchezo!

    Jibu lilikuwa katika yale maneno aliyokuwa akiniambia, na si kwingine.

    Nilijikuta nikikirudia kile kijitabu changu na kutazama vile vitu nilivyoviandika kwa umuhimu mpya. Na nilipokuwa nikitazama vile vitu nilivyaondika, nilipitisha uamuzi kuwa sasa muda wa kuendelea kuwindwa na akina Martin Lundi ulikuwa umekwisha. Na badala yake ulikuwa umefika muda wa mimi kuanza kuwawinda wao.

    Windo lawa mwindaji, na mwindaji awa windo.



    --



    Usiku ule sikulala. Sikutaka hata kula.

    Kwa muda mrefu nilikuwa nikiutazama ule mkanda kwa kuurudia tena na tena nikijaribu kutafuta ugunduzi mpya kutoka katika vile nilivyorekodi katika ule mkanda. Mkanda ambao niliurekodi bila kufikiri, in a spur of a moment, lakini sasa umeondokea kuwa muhimu sana katika maisha yangu hasa kutokana na mkasa ulioniangukia.

    Na kila nilipoutazama ule mkanda, hasa ile sehemu ya mwisho, nilizidi kujihakikishia kuwa ugunduzi wangu ulikuwa sahihi, kuwa Mr. Q aliamua kumrukia Macho ya Nyoka kusudi ili auawe. Alifanya hivyo baada ya kuwa amenieleza kila kitu alichotaka kunieleza.

    Ndio maana alikuwa akiniita kwa bidii sana pale alipoachwa peke yake kule msituni.

    Na ndio maana alipokwisha nitajia The Rickshaw na kuniachia ile namba aliyoniandikia pale mchangani, na kunipa maagizo kuhusu The Bastard, alitoa tabasamu la faraja. Kwa wakati ule sikuelewa ni kwa nini alifanya vile, lakini sasa nilielewa ni kwa nini hasa alifanya vile.

    Kila nilipotafakari hali ile, nilizidi kumshangaa na kumwonea huruma yule mtu niliyempachika jina la Mr. Q. Kwa hakika yule mtu alikuwa na ujasiri wa hali ya juu, kwani kwa hali niliyomkuta nayo, haikuwa na shaka kabisa kwangu kuwa alikuwa ameteswa sana kabla ya kuletwa pale msituni ili atoe siri aliyokuwa nayo kwa wale wauaji. Na kwa jinsi mambo yalivyojitokeza pale msituni, ni kwamba hakuwatajia hiyo siri, na ndio maana Macho ya Nyoka aliponaswa na ujanja wa Mr. Q na kumuua, wale wenzake, Martin Lundi muongo na yule Kigulu mwenye jicho la bandia walimkemea na kumfokea sana. Kwani Macho ya Nyoka alikuwa amemsaidia Mr. Q kufa na siri yake.

    Na ilipogundulika kuwa mimi nilikuwepo eneo lile, nikawa windo lao kuu kwa nia ya kutaka kufuta ushahidi wowote kuwa kuna mtu aliwaona wakiwa kule msituni. Lakini ilipowafunukia kuwa niliwaona wakimuua yule mtu, na kwamba nina ushahidi wa tukio lile kwenye mkanda wa video, umuhimu wangu kwao ukaongezeka maradufu.

    Na sasa mimi ninajua mambo aliyokuwa anayajua Mr. Q ambayo wao walishindwa kumlazimisha Mr. Q awatajie pamoja na mateso waliyompa, kwani Mr. Q hakutakiwa kufa kabla ya kuwatajia hilo walilokuwa wakilitaka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Na mimi sikutakiwa kufa mpaka waupate ule mkanda wa video.

    Asubuhi ya siku iliyofuata nilitoka na kuingia tena katikati ya jiji kwa mara ya kwanza tangu nikimbilie kule Kigamboni. Katika mawazo ya wale wauaji, haikuwajia kabisa kuwa ningekimbilia eneo kama lile, na bila shaka walikuwa wamesaka sana jijini na sasa walikuwa wamebaki wamepigwa butwaa, wakijiuliza nimewezaje kuyeyuka kiajabu kama vile. Nilikuwa nimekata nywele zangu katika mtindo wa Bob Cut, ambao ulinifanya nionekane tofauti sana. Na nilikuwa nimevaa suruali nyeusi ya kitambaa laini iliyonikaa vyema, na shati jeusi la kitambaa kizito lililokatwa katika mtindo wa koti, ndani yake nilivaa blauzi nyepesi ya kitamba cheupe, na hivyo kuonekana kuwa nimevaa suti nyeusi, na viatu vyangu vile vile vya kamba vilivyoniwezesha kukimbia kwa urahisi pindi itakapolazimu kufanya hivyo. Nilikamilisha vazi langu kwa kubandika ile miwani yangu ya jua.

    Kwa mtu yeyote ambaye angeonesha hamu ya kutaka kunijua mimi ni nani, basi wazo ambalo angekutana nalo ni kwamba nilikuwa ni wakili miongoni mwa mawakili aidha wa serikali au wa kujitegemea, ambao huwa wanavaa nguo nyeusi na nyeupe kama vile.

    Huku nikiwa nasumbuliwa na wazo kuwa laki zangu nne nilizotoka nazo kule Manyoni sasa zilikuwa zinaniishia kwa kasi, nilisafiri kwa basi mpaka maeneo ya Makongo, huko nilitafuta kibanda cha simu za kulipia na kuanza kujaribu kupiga simu huku moyo ukinienda mbio. Nilianza kuipiga ile namba iliyoandikwa mchangani na Mr. Q kule msituni, kwani mawazo yangu yalinituma kuwa ile ilikuwa ni namba ya simu. Na kama ingekuwa hivyo, basi ilikuwa ni namba ya muhimu sana katika ufumbuzi wa swala hili, kwani nilikumbuka jinsi Mr. Q alivyokuwa akijitahidi kuiandika ile namba kwa taabu pale mchangani, nami nikamdhania kuwa alikuwa amerukwa na akili kutokana na kukaribia kifo. Lakini sasa nilielewa kuwa alikuwa anaelewa anachofanya, na alitaka mimi niione ile namba.

    Nilipiga ile namba kwa mtandao wa Vodacom, lakini nikapata ujumbe kutoka kwenye mtambo kuwa ile namba haikuwapo katika mtandao wao. Nilijaribu tena kwa mtandao mwingine, nako nikapata jibu kama lile. Wasiwasi ulianza kunipanda, na nikajaribu namba ile kwa mtandao wa Celtel, nako mambo yakawa ni yale yale.

    Mungu wangu, sasa itakuwaje?

    Nilichanganyikiwa na nikabaki nikiwa nimeduwaa. Kama ile si namba ya simu, basi itakuwa ni namba ya nini? Nilikuwa na imani kubwa kabisa kuwa ile namba ilikuwa ni chanzo muhimu katika ufumbuzi wa kitendawili chote kilicholizunguka lile tukio la kule msituni. Nilikumbuka kuwa kuna mtandao mwingine wa Zantel.Niliipiga tena ile namba kwa kutumia mtandao wa Zantel, nako jibu likawa ni lile lile.

    Sasa ni nini? Yaani usumbufu wote huu uwe ni bure kweli?

    Nilikuwa nimekwenda kupigia simu kule Makongo nikiwa na matarajio kuwa endapo ile namba ilikuwa ya simu, hasa zile za kiganjani na ina uhusiano na akina Martin Lundi, basi ingekuwa rahisi sana kwa wale wauaji kunifuatilia na kujua kuwa nilikuwa nimepiga simu kutokea Makongo. Hivyo wao wangenisaka kwa nguvu zote maeneo ya Makongo, wakati mimi ningekuwa mafichoni kwangu Kigamboni. Lakini sasa haikuwa hivyo,ile namba haikuwa ya simu.

    Angalau haikuwa namba ya simu ya Kiganjani.

    Nilidhani huenda ikawa ni namba ya simu ya waya ya TTCL, lakini nilikumbuka kuwa namba zote za TTCL hapa jijini zilikuwa na tarakimu saba, na zilipangwa kutokana na eneo. Kwa mfano namba za Tabata anapoishi mama yangu zilikuwa zinaanzia na tarakimu 280xxxx wakati zile za maeneo ya barabara ya Nyerere zilikuwa zikianzia na tarakimu 286xxxx. Lakini ile namba niliyoachiwa na Mr. Q ilikuwa na tarakimu sita, kwa hiyo kama ni hivyo basi ingekuwa ni namba ya mikoani. Sasa ni mkoa gani? Itanibidi nijue namba za utambulisho za mikoa yote ili niweze kuipiga ile namba na huenda nikabahatisha ikaita katika mkoa mmoja.

    Niliondoka eneo lile na kuchukua basi hadi Kariakoo ambapo nilielekea moja kwa moja hadi kwenye kituo cha huduma za wateja cha simu za waya za TTCL. Niliingia ndani ya ile ofisi na kukiendea kimoja kati ya vitabu vingi vya simu vilivyokuwa mle ndani kwa ajili ya kuwasaidia wateja na kufunua ukurasa ulioonesha namba za utambulisho, area code, za mikoa yote ya Tanzania. Niliuchana uke ukurasa kwa uficho mkubwa na kuusokomeza kwenye mfuko wa suruali yangu bila ya kuonwa na mtu yeyote. Kisha niliiendea kaunta ya mle ndani na kununua kadi ya kupigia simu ya thamani ya Shilingi elfu kumi na kutoka nje.

    Kituo changu kilichofuata kilikua ni katika vibanda vya kupigia simu za kadi vilivyokuwa katika eneo la Telephone House, katikati ya jiji, kwani sikutaka kubaki eneo moja kwa zaidi ya nusu saa, kwa kuhofia kukutwa na wale wauaji au wana usalama waliokuwa makini na picha yangu iliyotolewa gazetini siku chache zilizopita.Nilianza kuipiga ile namba kwa kutumia area code za mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.

    “Karibu TTCL.Namba uliyopiga haitumiki. Kwa maelezo ya namba zinazotumika, tafadhali piga namba 1-3-5”

    Ndilo jibu nililoambulia kutoka katika mitambo ya kampuni ya simu katika mikoa yote niliyopiga.

    Nilichanganyikiwa. Niliona kuwa matumaini yangu yote niliyojijengea kutoka kwenye ile namba yakiyeyuka. Kwa unyonge zaidi nilijiondoa eneo lile pasina kuwa na uelekeo maalum. Lakini hatua chache mbele wazo likanijia na nikarudi haraka pale kwenye vile kibanda cha simu za kadi. Nilikumbuka kuwa namba za jijini Dar zilikuwa na tarakimu saba baada ya kubadilishwa kutoka kwenye mfumo wa zamani wa tarakimu sita na tano, ambapo zile zilizokuwa na tarakimu sita, zilibadilishwa kwa kuongezea tarakimu 2 mbele ya ile namba ya zamani. Nikiwa na tumaini jipya nilipiga tena ile namba huku nikitanguliza ile tarakimu 2 , lakini bado nilikutana na ujumbe ule ule kuwa ile ilikuwa ni namba isiyotumika.

    Hapa nilikubali kushindwa. Ile namba haikuwa ya simu.

    Ilikuwa ni namba ya nini?

    Sasa nilikuwa nimebaki na vitu vingine viwili kichwani mwangu:

    The Bastard na The Richshaw.

    Je, baada ya kushindwa kuwawinda akina Martin Lundi kwa kuitumia ile namba, nitaweza kutumia miongozo ile miwili iliyobaki kuniongoza waliko na kwenye siri ya tukio zima la kule msituni?

    Nilidhani kuwa The Bastard halikuwa jambo kubwa sana kwani bila shaka Mr. Q aliposema vile alikuwa akimaanisha Martin Lundi na wenzake, kwani ule walioufanya pale msituni si uanaharamu?

    Ila sasa hii The Rickhaw…

    “Mr. Q, kwa nini umeniachia mtihani mgumu namna hii?” Nilijisemea kwa huzuni huku nikiondoka eneo lile.

    Kutokana na wahka wa kuifuatilia ile namba nikiamni kuwa ni ya simu, nilisahau kabisa kununua magazeti ya siku ile, hivyo nilinunua magazeti na kutafuta hoteli ya karibu ili nipate mlo. Niliyasoma yale magazeti nikiwa pale hotelini huku nikidonoa donoa chakula nilichoagiza. Hakukuwa na habari yoyote katika yale magazeti kuhusiana na mkasa ulionisibu. Habari iliyochukua uzito wa juu kabisa katika magazeti yote yale ilikuwa ni ya kifo cha ghafla cha Jaji mkuu wa mahakama ya kimataifa dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda. Niliisoma habari ile taratibu huku nikiendelea kula chakula changu na akili yangu ikiruka ruka mara kwa mara ikijaribu kutafuta hatua muafaka ya kuchukua baada ya kushindwa kutegua kitendawili cha ile namba niliyoachiwa na Mr. Q. Niligundua kuwa kitu kilichoifanya habari ile ichukue uzito wa juu ni habari iliyoambatana nayo kwamba mtanzania alitarajiwa kushika nafasi yake.

    Hii hata mimi ilinivutia, kuona kuwa jumuiya ya kimataifa imeweza kutupa heshima sio tu ya kuifanya mahakama ile muhimu kuwa na makao yake hapa nchini kwetu, bali pia kutoa nafasi kwa mtanzania kuongoza mahakama hiyo ya kimataifa.

    Kwa mujibu wa maelezo ya magazeti, Mtanzania anayetarajiwa kuchukua nafasi ya Jaji aliyefariki, alikuwa ni kaimu wa jaji huyo raia wa New Zealand aliyekuwa na msimamo mkali dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994.

    Ingawa historia ya mtanzania aliyetarajiwa kuwa jaji mpya wa mahakama ya kimataifa dhidi ya mauaji ya halaiki ya Rwanda ilielezwa kwa kifupi katika magazeti yale,

    sikuifuatilia zaidi kwa sababu hata huyo jaji mwenyewe mtarajiwa nilikuwa sijawahi kumsikia kabla ya hapo.

    Nililipia chakula changu na kuondoka, nikiyaacha yale magazeti pale mezani.

    Nilipotoka tu nje ya ile hoteli nilimuona rafiki yangu mpenzi, Aulelia Mushi, ambaye tulisoma wote chuo kikuu na sasa alikuwa ameajiriwa na shirika la Umoja wa Mataifa la UNDP. Hata baada ya kuanza kazi, tulikuwa tukiendelea kuwasiliana na kukutana mara kwa mara. Lakini tangu nikutane na masahibu haya sikuwa nimeweza kuwasiliana naye hata kidogo, na nilihofia kukimbilia kwake kwa kuhofia kumpelekea akina Martin Lundi huko na kumwachia matatizo. Na nilipomuona akitembea hatua chache mbele yangu, sikuwa na shaka kabisa kuwa alikuwa ni yeye na moyo ulinilipuka kwa furaha kuwa hatimaye nimekutana na mtu wa karibu nitakayeweza kuongea naye.

    Kwa hakika alikuwa ni yeye, na ingawa alikuwa amenitangulia mbele yangu nami nilimuona kutokea mgongoni, nilimjua kwa hakika kabisa kuwa ndiye.

    “Aulelia!” Niliita kwa sauti huku nikiongeza mwendo nimfikie. Aulelia alisimama ghafla na kugeuka baada ya kisikia jina lake na niliona akinitazama kwa mashaka na hatua zake zilisita, kama ambaye haamini kuwa anayemuona ni mimi kweli au ananifananisha huku sura yake ikionesha kitu kama mshituko.

    “Heey! Aulelia! Mambo?” Nilimchangamkia huku nikiongeza hatua kumsogelea na nikinyoosha mikono yangu kumkumbatia kama ilivyo kawaida yetu. Kwa mshangao wa hali ya juu nilimshuhudia Aulelia akiruka nyuma kunikwepa na kunitazama kwa namna ya ajabu. Nilibaki nikimkodolea macho.

    “He! We’ vipi? Mbona sikujui?” Aliniambia huku akinitazama kama kwamba nina wazimu.

    “Hunijui? Ni mimi! Tigga! Yaani inawezekana ukawa umenisahau?” Nilimuuliza kwa mshangao. Aulelia aligeuka na kuanza kuondoka kwa mwendo wa haraka bila ya kunijibu.

    Heh! Hii tena mpya! Huyu ni Aulelia kabisa, sasa vije anasema hanijui?

    Nilimkimbilia na kumshika mkono huku nikimsemesha, nikiwa makini kuwa watu walikuwa wameanza kutushangaa pale barabarani.

    “Aulelia! Wewe si Aulelia wewe? Kwa nini unasema hunijui?” Nilimuuliza huku nikimchungulia usoni kwa makini. Aliuvuta mkono wake kutoka mkononi mwangu na kunikemea.

    “Hebu niache we’ vipi? Mi’ sikujui, naona umenifananisha!” Alisema kwa hasira huku akitazama mbele na akiendelea kutembea haraka. Hakutaka kabisa kunitazama machoni.

    “Kama we’ si Aulelia mbona umegeuka nilipokuita? Kwa nini unafanya hivyo?”

    Yule dada ambaye sasa nilishindwa kumfikiria kuwa ni Aulelia niliyemjua ingawa nilijua fika kuwa ni yeye, alinitazama kwa woga na wasiwasi huku nikiona akilengwa na machozi, kabla ya kunijibu,

    “Mimi ni Aulelia kweli, lakini wewe sikujui! Na naomba usinicheleweshe!” Alinijibu kisha aliondoka kwa mwendo wa haraka akiniacha nikiwa nimepigwa na butwaa.







    Hii ni nini tena?

    Nilimtazama yule mtu ambaye tulikuwa pamoja kwa muda mwingi wakati tukiwa chuoni na nilishindwa kuelewa ni nini maana ya tukio lile. Na hata pale nilipokuwa nikimkodolea macho, nilimshuhudia akifungua mlango wa gari yake aina ya RVR ambayo niliijua fika hadi namba na kuondoka eneo lile kwa kasi. Na wakati gari ile ikinipita kwa kasi, Aulelia alinigeuzia uso wake kunitazama na nikaona alikuwa akibubujikwa na machozi.

    Mungu wangu! Martin Lundi amemfikia na yeye?

    Niliondoka eneo lile nikiwa nimezidi kuchanganyikiwa.Moyo uliniuma vibaya sana kutokana na kitendo alichonifanyia rafiki yangu Aulelia.

    Kwa nini Aulelia, eenh? Why do you have to do this to me?

    Sikuwa na shaka kuwa tabia ya Aulelia niliyoishuhudia muda mfupi uliopita ilitokana na yale mambo yaliyonikuta. Lakini Aulelia ni mtu mwenye uelewa wa hali ya juu, si kawaida yake kufanya kitu kama kile bila ya kuwa na uhakika nacho. Nilikuwa na imani kabisa kuwa hata kama angesikia taarifa kuwa nimekuwa kichaa ninayeua watu hovyo, Aulelia angetaka kuongea na mimi na kuelewa ni yepi hasa yaliyonisibu na kujihakikshia mwenyewe kuwa kweli nimekuwa mwehu, badala ya kunikana moja kwa moja kwa maneno ya kuambiwa tu au ya kusoma magazetini. Lazima kuna kitu zaidi.

    Ni nini? Sikuwa na la kufanya zaidi ya kurejea kwenye eneo langu la maficho kule Kigamboni. Siku yangu ilikuwa imepotea bila mafanikio yoyote.



    --



    Safari yangu kurudi kwenye ile nyumba ya wageni kule Kigamboni ilikuwa kama ndoto. Sikumbuki chochote kilichotokea humo njiani, ila nilijikuta tu nimefika na kupitiliza moja kwa moja chumbani kwangu na kujifungia. Usiku ule nilisumbuliwa zaidi na mawazo juu ya tabia aliyoonesha rafiki yangu kipenzi Aulelia Mushi nilipokutana naye pale mjini. Sikuwa na shaka hata kidogo kuwa yule ni yeye, kwani hata gari aliyoondoka nayo ilikuwa ni ile ambayo mimi niliijua siku zote kuwa ni yake, hata namba za ile gari ni zile zile za gari lake. Nikiwa nimejilaza kitandani nikiwaza juu ya mambo haya, nilisikia wahudumu wa ile nyumba ya wageni wakifungua chumba kilichokuwa kikitazamana na kile nilichokuwa nimepanga na kumkaribisha mpangaji mpya kwenye chumba hicho. Mawazo yangu yalirudi kwa rafiki yangu Aulelia Mushi.

    Sasa kwa nini amefanya vile?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sikupata jibu la kuniliwaza, na nilibaki na uchungu mkubwa moyoni kwani tukio lile lilinikumbusha kuwa bado nilikuwa mkimbizi nisiye na kimbilio, na kwamba sehemu pekee inayonifaa ni pale nitakapokuwa peke yangu.

    Zaidi ya hapo mawazo yangu yalisumbuliwa na tatizo la upungufu wa pesa uliokuwa unaelekea kunikumba. Kwa hali hii nitakimbilia kwa nani anipe pesa? Na bila pesa nilikuwa sina ujanja wa kujiokoa kutoka katika msako wa akina Martin Lundi. Nitakimbilia kwenye nyumba gani ya wageni au hoteli bila ya pesa?Hapo niliamini kuwa hawa akina Martin Lundi walikuwa ni watu hatari sana wanaopangilia mambo yao kwa wigo mpana sana, kwani kwa kunichukulia kikadi changu cha benki, walihakikisha kuwa wamenizibia kabisa mianya ya kujipatia pesa na hivyo kuyafanya maisha yangu kuwa magumu sana. Nilikumbuka maneno ya yule askari wa kike aliyeniibukia kule kwenye nyumba ya wageni maeneo ya sinza:

    ...na nakuahidi kuwa tutayafanya maisha yako yawe mabaya sana hapa duniani mpaka utautoa!

    Na ilielekea kuwa kweli.

    Sijui kwa nini hawakuzichukua na zile pesa taslimu zilizokuwa kwenye begi langu kule msituni, labda kwa kuwa nilikuwa nimezishindilia chini kabisa ndani ya begi lile nao hawakuwa na muda wa kulipekua sana. Na pia hakuna ambaye angetarajia kuwa ningeweza kuwa na pesa kiasi kama kile porini namna ile. Nilikumbuka kuwa marehemu Ibrahim Geresha alichukua pesa kidogo sana, na sehemu kubwa ya posho yake ya safari alimwachia mkewe kwa matumizi ya familia yake. Sasa mimi sikuwa na familia ya kuiachia pesa, hivyo nikaenda nazo msituni.

    Na ndio zilizonisaidia mpaka kufikia hapa. Ingawa bado nilikuwa na pesa za kuniwezesha kujikimu kwa siku kadhaa zijazo, lakini niliona ni bora ningeanza kufanya utaratibu wa kutafuta pesa mapema kabla hazijanikaukia kabisa. Niliikumbuka akaunti yangu kule benki. Nilikuwa na zaidi ya Milioni moja na nusu kwenye ile akaunti, lakini ndio sikuwa na namna ya kuzipata bila ya ile kadi yangu ya benki.

    Njia ya kujitia kuwa kadi imepotea isingenisaidia kwani utaratibu niliujua wazi. Nilitakiwa nitoe ripoti polisi, nipewe RB ya upotevu wa kitambulisho cha benki, ndipo Benki wangeweza kunipatia kadi nyingine. Kinyume na hapo hakukuwa na namna.

    Na swala la kwenda polisi kutoa ripoti ya kupoteza kitambulisho cha benki lilikuwa haliwezekani kabisa, kwani huko kulikuwa ni kujipeleka kwenye mdomo wa mamba, kwani nisingeweza kwenda polisi kwa jina la Nuru Bint Shaweji, nilitakiwa niende kwa jina langu halisi, Tigga Mumba, ambalo ndilo lililokuwa kwenye kadi yangu ya Benki na ambalo linatambulika kule benki.

    Pia ni jina ambalo kufikia sasa sikuwa na shaka kwamba lilikuwa maarufu katika vituo vyote vya polisi sio tu jijini, bali pia hata mikoani.

    Sasa nifanyeje?

    Niliamua kwenda benki siku iliyofuata na kubahatisha kutoa kiasi cha pesa kutoka kwenye akaunti yangu. Namba yangu ya akaunti nilikuwa naikumbuka kwa kichwa, na kulikuwa kuna dada ambaye nilikuwa nimezoeana naye sana pale benki, kwani mara nyingi nikienda kutoa pesa huwa namuachia na yeye bakshishi kidogo, hivyo kila mara niingiapo pale benki huwa akinichangamkia sana.

    Nilitaraji kuwa zile bakshishi nilizokuwa nikizitoa kwa yule dada huenda zikanisaidia kupata pesa bila kulazimika kutoa kitambulisho changu cha benki.

    Baada ya hapo ningemfuatilia rafiki yangu Aulelia Mushi ili nijue kiini cha ile tabia ya ajabu aliyonionesha pale tulipokutana. Huenda ningepata mwanga wa kunikurubisha katika ufumbuzi wa mtihani ulionikuta.

    Kwa muda ule nilisahau kabisa maswala ya The Rickshaw, The Bastard na Key.



    --



    “Eem…Samahani kidogo anti, lakini itabidi nipate kibali cha kukupatia pesa kutoka kwa bosi wangu, si unajua tena…mambo ya procedure?” Yule dada niliyekuwa nimetaraji kuwa angekuwa mwepesi kunielewa pale benki na kunipatia pesa bila usumbufu na vipingamizi aliniambia huku akitabasamu kijinga, uso wake ukionesha wazi kuwa hakupenda kabisa hali ile.

    “Aaah! Ni lazima ufanye hivyo? We’ si unanifahamu anti? Na hiyo ndiyo akaunti yangu…mi’ nakuja hapa benki mara kibao tu kuchukua pesa kwa hiyo akaunti…” Nilimjibu huku nikianza kujutia uamuzi wangu wa kuja hapa benki. Nilikuwa nimecheza bahati nasibu mbaya sana kuja hapa, kwani pia ingewezekana hata hapa benki wakawa na habari zangu na hivyo kunifanya niwe nimejiingiza mwenyewe kwenye mdomo wa Mamba.

    Lakini ningeishi vipi bila pesa?

    “Akaunti iko sawa kabisa Anti, na mi’ nakujua vizuri na sina shaka na wewe…”

    “Sasa tatizo ni nini?” Nilimkatisha kwa swali.

    Nilipofika pale benki nilijaza fomu ya kuchukulia pesa na kufoleni kwenye dirisha alilokuwa yule dada niliyemkusudia tangu siku iliyopita. Aliponiuliza juu ya kadi yangu ya benki nilimwambia kuwa nilikuwa nimeisahau nyumbani kwa mama yangu Morogoro nilipoenda likizo na kwamba nilikuwa nimeagiza mtu aniletee, lakini kwa sasa nilikuwa na shida kubwa sana ya pesa na hivyo nikamwomba anisaidie. Aliniuliza kuwa nilikuwa na uhakika kuwa sijaipoteza nami nikamhakikishia kabisa kuwa nilikuwa nimeisahau pamoja na baadhi vitu vyangu kule Morogoro na nimewasiliana nao wakanithibitishia kuwa ipo na italetwa.

    Nilimuona yule dada akisita huku akijaribu kuamua iwapo adharau procedure kwa muda na anisaidie. Niliona wazi akilini mwake alikuwa akizikumbuka zile bakshishi nilizokuwa nikimkatia kila nilipokuwa nikienda kuchukua pesa pale benki.

    “Naomba unisaidie Anti, Please!” Nilimwambia kwa kuomboleza huku moyo ukinidunda.

    Yule dada alisita kwa muda. Kisha nilimuona akianza kuigonga muhuri ile fomu yangu nami nikabana pumzi, lakini mara aliingia dada mwingine pale kwenye kaunta ya yule dada.

    “Bosi anakuita…sasa hivi!” Alimwambia na kutoka. Yule dada alinitazama na kutabasamu kisha akaniomba radhi na kuelekea sehemu ya ndani ya ile benki ambapo wateja hatukuweza kuona kilichokuwa kikitendeka. Nilibaki nikisubiri pale kwenye foleni huku moyo ukinienda mbio na wasiwasi ukinipanda. Nilisikia manung’uniko ya wateja waliokuwa nyuma yangu, kwani nilikuwa nimetumia muda mrefu na yule dada pale dirishani, lakini sikujali.

    Baada ya muda yule dada aliyekuja kumwita mwenzake alinijia na kuniomba niongozane naye kuelekea sehemu ya ndani alikoelekea yule dada aliyekuwa akinihudumia. Hapo machale yalinicheza na nikataka kutimua mbio, lakini sikuweza kufanya hivyo kwani mlangoni kulikuwa kuna askari mwenye silaha na zaidi ya hapo watu waliojaa mle ndani wangeweza kunikamata kwa urahisi sana.

    “Ku…kuna nini, something wrong?” Nilimuuliza kwa wasiwasi iwapo kulikuwa kuna tatizo lolote huku nikiangaza huku na kule nikijaribu kumtafuta yule dada aliyekuwa akinihudumia hapo mwanzo.

    “Hakuna tatizo la kukutisha dada yangu, ni kuweka taratibu sawa tu. Nifuate tafadhali.” Yule dada alinijibu huku akiongoza njia. Nilihisi mwili ukiniisha nguvu na kwa mara nyingine nilijutia uamuzi wangu wa kuja hapa benki. Nilimfuata yule dada huku nikiwa nimeingiwa na woga wa ajabu, akilini mwangu nikijua fika kuwa huko niendako nilikuwa naenda kukutana tena na yule muuaji muongo, Martin Lundi.

    Niliingizwa kwenye ofisi moja nzuri sana iliyokuwa nyuma ya ukuta wa zile kaunta za kuhudumia wateja na mtu mmoja mrefu na mtanashati sana alikuwa ameketi kwenye kiti kizuri sana nyuma ya meza kubwa na safi. Mlangoni mwa ofisi ile kulikuwa kumeandikwa “Branch Manager” nami moja kwa moja nikaelewa kuwa huyu ndiye alikuwa meneja wa tawi lile la benki. Baada ya kunifikisha ndani ya ile ofisi yule dada aliyenileta aliondoka na kuniacha pamoja na wale niliowakuta mle ndani.

    Nilibaki nikiwa nimesimama kizembe nikisubiri maelekezo, lakini yule bwana tuliyemkuta mle ndani alikuwa akinitazama tu bila ya kusema neno. Yule dada aliyekuwa akinihudumia pale kaunta alikuwa amesimama kando ya ile meza na ile fomu yangu niliyoijaza ilikuwa juu ya meza ya meneja wa tawi. Kibao kidogo kilichokuwa juu ya meza ile kilimtambulisha yule bwana kama Dick Bwasha. Nilipotembeza macho mle ndani, niligundua kuwa kulia kwa meza ya yule meneja wa tawi, kulikuwa kuna vijiruninga vidogo ambavyo vilimwezesha yule meneja kuona kila kilichokuwa kikitendeka kule kwenye kaunta za kuhudumia wateja. Nilimgeukia yule dada aliyekuwa akinihudumia pale kaunta na nikaona alikuwa amebadilika na uso umemsawajika vibaya sana. Alikuwa ametishika vibaya sana, nami nikaanza kugwaya nisijue nitafanyaje. Muda huo yule bwana alimwashiria yule dada atoke nje ya ile ofisi naye aliondoka haraka akiniacha na yule mtu mle ndani. Hatimaye yule meneja wa tawi aliniashiria niketi kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake nami nikatii.

    “Ulikuwa unataka kumfukuzisha kazi yule binti bila ya sababu. Ukisahau kitambulisho chako cha benki unatakiwa urudi ukakifuate ndio uje benki kutoa pesa. Na ukikipoteza, unatoa ripoti polisi, unapewa RB, unakuja hapa, unatengenezewa kadi nyingine kisha unachukua pesa. Huo ndo utaratibu.” Dick Bwasha akiniambia huku akiwa ameninyanyulia nyusi na akinitazama usoni. Uso wake ulikuwa umejaa jeuri na kila alipoongea alibetua midomo yake kama kwamba anasikia kichefuchefu. Hii ilitia dosari kubwa katika utanashati wake. Nilibaki nikimkodolea macho kwa muda kabla sijapata neno la kusema.

    “Lakini nilikuwa nimeomba msaada tu! Nina shida sana ya pesa na kitambulisho nimekisahau nje ya mkoa, nisingeweza kurudi kukifuata wakati nimeshikwa na shida ya dharura.” Nilimjibu huku nikizidi kupata hofu ya kuendelea kubaki na yule mtu mwenye majivuno na kiburi kikubwa kabisa ndani ya chumba kile.

    “Hilo halitawezekana!” Alinijibu kwa mkato huku akinibetuliwa midomo yake mibaya na kuniinulia nyusi zake nene kwa kiburi cha hali ya juu. Nilimtazama kwa muda huku hasira zikinipanda.

    Kwani imekuwaje? Mimi sikuona kama lile lilikuwa ni swala kubwa sana kiasi cha kuanza kujibizana na meneja wa tawi.

    “Lakini kuna pesa zangu kwenye benki yako! Zaidi ya milioni na nusu, sasa unataka kuniambia kuwa siwezi kuchukua kilicho changu kwa vile tu…”

    “Sio kwa utaratibu uliotaka kuutumia. Sisi tuna taratibu zetu bwana!”

    “Sasa kwa nini umeagiza niletwe huku ofisini kwako? Kwa sababu nilitaraji nimeletwa huku ili nipate msaada ambao labda wale wahudumu wa kule kaunta hawana mamlaka nao!” Nilimjibu kwa mshangao. Yule bwana alinitazama kwa kiburi huku akitafuna tafuna kalamu yake na domo lake likifanya tabasamu la kuchukiza.

    “Unataka msaada?” Aliniuliza huku akiendelea kutafuna tafuna kalamu yake na akinitazama kwa macho ya matamanio, na kuendelea; “Itabidi nawe ukubali kusaidia.”

    Alinichefua!

    Yaani huyu bwana alikuwa anataka kutumia nafasi hii kuniletea mzuka wake wa ngono!

    “Sikiliza Mista, nilitegemea tatizo langu lingeeleweka na kupatiwa ufumbuzi kwa taratibu zinazoeleweka. Sioni sababu ya kujirahisi kwako kwa pesa yangu mwenyewe bwana! Kama we’ una mzuka wa ngono si ukatafute machangudoa waliojaa tele huko mitaani!” Nilimkemea kwa hasira, wakati yeye akibaki akinitazama tu huku akiendelea kunichekea akitafuna tafuna kalamu yake.

    Nilizidi kuchukia.

    “Na nitahakikisha kuwa naifunga akaunti yangu na nahamia benki nyingine, Benki gani inakuwa na watendaji wasio na adabu hata kidogo!” Nilimwambia kwa ghadhabu.

    “Mnnhu! Mi’ n’lidhani utaenda polisi kupeleka mashitaka ya unyanyasaji wa kijinsia!” Dick Bwasha aliniambia kwa kebehi huku akinitazama machoni na sura yake ikiendeleza ile cheko yake ya kebehi, na aliposema vile, alitilia msisitizo sana neno “polisi”. Sikumuelewa, tulibaki tukitazamana kwa muda, kisha nikaamua kuondoka eneo lile. Nilipeleka mkono wangu kwa nia ya kuinyakua ile fomu yangu ya kuchukulia pesa iliyokuwa pale mezani huku nikiinuka. Lakini mkono wa Dick Bwasha ulichomoka ghafla na kuukamata mkono wangu, akinizuia nisiichukue ile fomu. Niliruka kwa mshituko huku nikiachia yowe la woga.

    “Not so fast young lady!” Dick Bwasha alinikemea huku naye akisimama kutoka kwenye kiti chake na kunikunjia sura yake kwa ghadhabu, ile cheko yake ya kejeli na mchezo-mchezo ikiyeyuka kabisa usoni mwake, akimaanisha kuwa nisifanye haraka kuondoka.

    “Hey! Niachie!” Nilimwambia kwa hasira huku nikijaribu kuunasua mkono wangu kutoka mkononi mwake. Dick Bwasha alizunguka ile meza kwa wepesi wa ajabu na kuja hadi pale kwenye kiti nilichokuwa nimekalia hapo awali na kunikalisha huku akiniinamia na kunisemea karibu sana na sikio langu.

    “Unataka msaada, n’takusaidia. Lakini na wewe lazima ukubali kunisaidia bibie, unasemaje?”

    Mwili ulinifa ganzi. Huyu bwana ana wazimu au kitu gani?





    “Mista, mimi ni mtu mwenye heshima zangu. Naomba huo upuuzi wako uupeleke kwa wanaoweza kuuvumilia lakini sio kwangu! Naomba niende zangu.” Nilisema kwa utulivu wa hali ya juu huku nikitafuta kitu cha kumbamiza nacho ili niweze kutoka salama mle ndani. Nimekuja kujaribu kuchukua pesa kutoka kwenye akaunti yangu ili niweze kukabiliana na matatizo yangu, badala yake nakutana na mjinga mwenye mawazo ya ngono za kibeberu.

    Haya mambo gani sasa.

    Dick Bwasha alirudi nyuma ya meza yake na kutoa picha kutoka kwenye droo ya meza ile na kuitupia juu ya meza mbele yangu.

    “Ukitazama hiyo picha utagundua kuwa sina shida kabisa na hicho ki----- chako mwanamke!” Aliniambia taratibu huku akinitazama kwa ghadhabu, akizitamka nyeti zangu kama anayetamka takataka fulani tu hivi.

    Sikuamini macho yangu.

    Nilitazama ile picha bila kuishika, ikiwa imelala pale mezani na nilihisi kudharaulika na kudhalilika kusiko kifani. Ile picha ilimuonesha Dick Bwasha akiwa uchi wa mnyama juu ya kitanda. Pamoja naye, ilikuwapo mijimama miwili ambayo nayo ilikuwa kama ilivyozaliwa, hakukuwa na shaka kuwa walikuwa wakifanya nini pale kitandani. Ilikuwa ni picha chafu sana na sikuelewa wale watu waliwezaje kupiga picha kama ile bila ya kuwa na wazimu kidogo. Na pia nilishindwa kabisa kumuelewa yule meneja wa tawi la ile benki niliyoiamini kunitunzia pesa zangu miaka yote ile.

    Niliinua uso kwa mshangao na kumtazama yule jamaa, huku akilini mwangu nikijithibitishia kuwa jamaa hakuwa mzima.

    “Kha! Sasa hii ndio nini?” Nilijikuta Nikimuuliza kwa mshangao huku ile hisia ya kudhalilika kusiko kifani ikizidi kunikolea.

    “Hiyo ni kukuonesha ni jinsi gani mawazo yako yalivyo potofu. Niliposema na wewe inabidi unisaidie sikuwa na maana hiyo iliyojengeka kichwani mwako!” Aliniambia huku akibenua midomo yake kwa kiburi kikubwa kabisa.

    Kwa kweli alinichosha!

    “Sasa…” Nilianza kumuuliza, lakini Dick Bwasha alipiga meza kwa nguvu kwa kiganja chake na kunikatisha.

    “We want the tape Tigga!” Aliniambia kwa sauti ya msisitizo huku akiinua mwili wake na kunisogezea uso karibu sana na wangu, akinitazama kwa macho makali yenye kuogofya, akimaanisha kuwa wanautaka ule mkanda wa video niliokuwa nao.

    Duh! Hii sikuitegemea kabisa, na mshituko nilioupata naona ulikuwa mkubwa kuliko yote niliyowahi kukutana nayo tangu kinyang’anyiro hiki kinikute.

    “Say whaaat!” Niliruka kwa mshituko huku nikiinuka kutoka kwenye kiti nilichokuwa nimekalia na kubaki nikiwa nimemkodolea macho yule mtu aliyekuwa mbele yangu huku nikishindwa kabisa kuuzuia mwili wangu usitetemeke. Dick Bwasha aliendelea kunitazama kwa hasira bila kutetereka.

    “You give us the tape, we give your money back…and more.” Dick Bwasha aliongea taratibu huku akiendelea kunitazama, akimaanisha kuwa wataniruhusu kuchukua pesa zangu na hata na ziada, iwapo nitawapatia ule mkanda wa video wenye ushahidi dhidi ya akina Martin Lundi.

    Niliinua mkono uliokuwa ukitetemeka na kumnyooshea kidole huku macho yakiwa yamenitoka pima.

    “We…wewe…ni mmoja wao!” Nilisema kwa kitetemeshi. Dick Bwasha hakunjibu, badala yake aliketi vizuri kwenye kiti chake na kuirudisha ile picha yake chafu ndani ya droo ya meza yake.

    “Mmoja wa akina nani Tigga?” Aliniuliza huku akiendelea kunitazama kwa makini. Sikuweza kujibu. Nilibaki nikimkodolea macho kwa kihoro.

    Yaani hawa akina Martin Lundi wametanda kila mahali?

    Inawezekana vipi hii lakini? Huyu mtu anahusikaje na swala zima la kule msituni? Mungu wangu! Sasa nitapambana na watu wangapi Tigga mie?

    “Tunautaka huo mkanda Tigga, na tutakupa pesa zote uzitakazo.” Dick Bwasha alinizindua kutoka kwenye yale mawazo ya kuijutia nafsi yangu.

    “Halafu hizo pesa nikazitumie ahera? Nyie ni wauaji! Sina mkanda mie!” Nilimropokea kwa jazba huku nikianza kusota ukutani kuuelekea mlango. Dick Bwasha aliendelea kuketi tu kwenye kiti chake bila hata kutetereka.

    “Huwezi kutukimbia Tigga. Bora ukubali ofa hii. Tulijua tu kuwa utakuja hapa, nami nilikuwa nakusubiri muda wote. Toa mkanda huo halafu tutakusahau na hutatuona tena.”

    “Ooh, Yeah? Sitawaona tena kwa sababu nitakuwa mfu sio?”

    “Tukitaka kukuua Tigga tunakuua tu, wala hilo si tatizo kwetu lakini hilo si lengo letu…”

    “Nyinyi ni akina nani? Mna lengo gani na nchi hii? Maana mnachokifanya kinaelekea kuathiri taifa zima sasa! Haiwezekani muwepo katika kila nyanja muhimu kama hizi halafu muwe na sera kama hizo….”

    “Sio swala la nchi hili mwanamke!” Dick Bwasha alifoka kwa hasira kali kuliko nilivyotarajia, na akabaki akinitazama kwa hasira huku akihema kwa nguvu, kisha akaendelea; “Ni swala dogo tu la mkanda wa video Tigga, sasa sijui kwa nini unataka kulikuza bila sababu!”

    “Khah! Hilo swala dogo limeacha watu wameuawa kama kuku kwenye msituni fulani ndani ya nchi hii, huku mimi nikitangaziwa wazimu!”

    “Wewe ni mgonjwa wa akili Tigga, lazima ukubali hilo. Kuung’ang’ania kwako huo mkanda wa video ni sawa na kichaa kung’ang’ania bunduki. Ataua kila mtu, ndio maana sisi tunataka kukusaidia…”

    Nilibaki nikimkodolea macho kwa mshangao yule jamaa. Hivi hawa jamaa ni kweli wanaamini kuwa mimi ni mwehu? Nilitaka kusema neno nikaghairi, sikuona sababu ya kuendelea kubishana na yule adui juu ya jambo lile.

    “Siwezi kuendelea kusikiliza upuuzi huu. Mi’ naondoka, fanya utakalo!” Nilimwambia huku nikiuendea mlango kwa hatua za haraka.

    “Nenda tu Tigga, na wala sitakuzuia. Lakini ujue kuwa tutayafanya maisha yako yawe magumu sana na utajuta kwa ubishi wako!” Dick Bwasha aliniambia huku akinitazama kwa hasira. Nilitoka nje ya ofisi yake na kupitiliza hadi pale kaunta ambako nilikuta watu wachache wakiwa wamepanga foleni wakiendelea kupata huduma kama kawaida, bila ya kujua mambo yaliyokuwa yakitokea nyuma ya zile kaunta, wala undani wa watendaji wakuu wa benki ile.

    Ni wapi ambapo hawa watu hawapo?

    Nilitoka nje ya ile benki nikipepesuka huku akili ikinizunguka. Nilivuka barabara bila ya kuangalia na nikashtukia nikipigiwa honi huku nikisikia msuguano wa tairi za gari na lami. Niliruka kwa mshituko huku nikikoswakoswa kugongwa na gari iliyokuwa inakuja kwa kasi. Nilichanganyikiwa nakurudi mbio kule nilipotokea, kumbe nako kulikuwa kuna gari nyingine inakuja, nayo ikanipigia honi kubwa huku ikiserereka na kunikwepa.

    Dereva wa ile gari ya pili iliyonikwepa alitoa uso nje ya dirisha lakena kunipigia kelele kwa hasira.

    “Anti umepewa talaka nini?” Kisha akamalizia na tusi zito la nguoni. Nilisikia kelele na mayowe ya watu wakizomea, lakini sikujali.

    Nilizidi kuongeza mwendo, ingawa kwa wakati ule sikujua nilikuwa naenda wapi. Nilikuwa nimechanganyikiwa vibaya sana, na nilijiona kuwa sasa nilikuwa naelekea kabisa kwenye wazimu.

    Nilipopata fahamu kidogo niligundua kuwa nilikuwa nimeshika usawa wa kuelekea kituo cha mabasi ya Kivukoni.

    vi.



    H

    atua chache kutoka kwenye ile nyumba ya wageni niliyokuwa nimepanga kule Kigamboni nilipata na mshituko mwingine ambao sikuutegemea. Nikiwa kimya ndani ya teksi niliyokodi baada ya kuteremka kwenye pantoni baada ya kile kisanga cha kule benki kilichonivuruga akili, nilimuona mwanamke akitoka kwenye ile nyumba ya wageni na kuiendea gari iliyokuwa imepaki upande wa pili wa barabara nje ya nyumba ile. Moyo ulinilipuka na nikaketi wima kwenye kiti cha gari ile na kumtazama kwa makini huku ile tekis niliyoikodi ikizidi kuikaribia ile nyumba ya wageni na ile gari aliyoiendea yule mwanamke.

    Moyo ukinipiga nilimtazama kwa makini yule mwanamke na kihoro kilichoanza kutulia baada ya mshituko nilioupata kule benki kilinirudia upya tena kwa kishindo kikubwa.

    Alikuwa ni yule askari wa kike aliyeniachia kule kwenye nyumba ya wageni ya sinza nilipokimbilia baada ya vurumai iliyotokea nyumbani kwa Kelvin!

    Mwili wote uliingia baridi na nikahisi nikishindwa kupumua vizuri. Nilibaki nikimkodolea macho yule mwanadada, ambaye alikuwa amevaa mavazi ya kiraia na alikuwa akiongea na mtu aliyekuwa ndani ya ile gari iliyokuwa imepaki mbele ya ile nyumba ya wageni, upande wa pili wa barabara. Na muda huo dereva wangu alianza kupunguza mwendo kwani tulikuwa tumeifikia kabisa ile nyumba ya wageni ambapo ndipo nilipomuelekeza anipeleke.

    “Twende mbele tu! Usisimame hapa!” Niliropoka kwa hofu huku nikijishughulisha kutoa pesa kwenye mfuko wa suruali yangu.

    “Lakini Anti, gesti si hii hapa?” Yule dereva aliniuliza kwa mshangao.

    “Endesha bwana! Naenda...naenda saluni kwanza...kule mbele!” Nilimfokea yule dereva kwa kuchanganyikiwa, naye aliipita ile nyumba ya wageni kwa mwendo ule ule wa taratibu huku akinigeukia kwa mshangao. Wakati huo nilijitia kuangusha baadhi ya sarafu na kuinama kuziokota huku nikilaani kitendo kile, lakini nia yangu hasa ilikuwa kuinama ili yule mwanamke asinione wakati gari yetu ikipita pale walipokuwa wamesimama.

    Nikiwa ndani ya ile teksi niligeuka na kupitia kwenye kioo cha nyuma cha ile teksi nilimuona yule mwanamke akiingia ndani ya ile gari nayo ikaondoka eneo lile kwa mwendo wa kasi.

    “Shit!” Nililaani kitendo cha wale wauaji kugundua maficho yangu nikiwa nimechanganyikiwa na kutazama kule tulipokuwa tukielekea.

    “Sasa nini tena Anti? Mbona hivyo?” Yule dereva alilalamika huku akinitazama kwa mshangao, akidhani nilikuwa nimemlaani yeye. Nilimtaka radhi kuwa si yeye niliyemkusudia na kumuambia aniteremshe mbele ya saluni moja ya akina mama, jambo ambalo alilifanya kwa faraja kubwa, kwani bila shaka alishaanza kuona kuwa nilikuwa kichaa.

    “Heh! Sasa nitakimbilia wapi?” Nilijisemea mwenyewe huku nikizubaa nje ya ile saluni na kuelekea kwenye kiosk kimoja kilichokuwa jirani yake na kuketi nikiiangalia ile teksi ikitoweka.

    Bila shaka utakuwa na hisia ni jinsi gani nilivyochanganyikiwa. Yaani baada ya msukosuko wa kule benki na vituko na vitisho vya yule mtu aliyeitwa Dick Bwasha, halafu nafika hapa kwenye maficho yangu nakuta kuwa kumbe yule mwanamke aliyeahidi kuyafanya maisha yangu yawe mabaya kabisa hapa duniani naye alikuwa amekwisha fika.

    Ni wazi kuwa wale wauaji walifika pale kwenye ile nyumba ya wageni kunifuata mimi wakanikosa, sasa wameacha ujumbe gani pale kwenye ile nyumba ya wageni? Jambo la busara kuliko yote kwangu wakati ule lilikuwa ni kutokomea moja kwa moja, nisirudi tena kwenye ile nyumba ya wageni, kwani haikuwa na shaka kuwa ile nyumba sasa si salama tena kwangu, lakini nitafanyaje? Ni lazima niende tu nikajionee mwenyewe kilichoandaliwa kwa ajili yangu na wale wauaji wabaya. Pia kuna vitu vyangu kule kwenye ile nyumba ya wageni ambavyo nisingeweza kuondoka bila kuvichukua.

    Hasa ule mkanda wa video.

    Nilikaa kwa muda mrefu pale kwenye kiosk nikitafakari hatua ya kufanya, lakini kila nilivyotafakari, pamoja na woga ulionikumba katika kuingia tena kwenye ile nyumba ya wageni, sikupata wazo lolote zuri zaidi ya kwenda tu kwenye ile nyumba ya wageni na kukusanya vitu vyangu na kuondoka. Iwapo nitakuta kuwa yule askari wa kike anayeshirikiana na akina Martin Lundi ameacha wenzake wanisubiri, basi nitapambana nao huko huko. Si niliamua kuwa muda wa kuanza kuwawinda ulikuwa umefika? Sasa hii ndiyo ilikuwa nafasi yangu. Nilijipa moyo huku nikijiona kabisa kuwa ujasiri ulikuwa ukinipungua kwa kasi, kwani kasi ya maadui zangu kunizidi kete ilikuwa ni kubwa mno.

    Kwanza Dick Bwasha, halafu yule mwanadada askari...kisha nani tena? (Niliguna).

    Nililipia soda niliyoagiza na kuondoka kuelekea kwenye ile nyumba ya wageni huku nikiomba Mungu anijaalie uwezo wa kukabiliana na mambo nitakayokutana nayo.

    Niliingia ndani ya ile nyumba ya wageni nikiwa na wasiwasi mkubwa. Nilichukua ufunguo wangu pale kaunta nikitarajia kusikia ujumbe wowote wa ajabu ajabu kutoka kwa yule mhudumu lakini haikuwa hivyo. Nilianza kuelekea chumbani kwangu taratibu, lakini nilirudi na kumuuliza yule mhudumu.

    “Nilimuona dada mmoja akitoka huku ndani muda mfupi uliopita...ni nani yule?”

    “Dada mmoja makini hivi mwenye shepu moja bomba sana?” Yule mhudumu aliniuliza, akielezea maumbile ya yule mwanadada. Nilimwambia ndio huyo huyo huku nikikumbuka jinsi hata mimi nilivyoisifia shepu yake siku ile nilipomuona kwa mara ya kwanza alipokuwa amevaa mavazi yake ya kiaskari.

    “Yule ni mpangaji mpya, ameingia jana usiku, yuko na buzi lake chumba namba 16.” Yule mhudumu alinijibu bila ya kuonesha kutiwa wasiwasi na kuuliza kwangu juu ya yule mwanadada.

    “Aaanh! Okay....” Nilimjibu huku nikigeuza na kuanza kuelekea chumbani kwangu huku uso wangu ukiwa umejikunja kwa kutafakari hali ile, kwani chumba namba 16 kilikuwa kinatazamana na chumba changu.

    Na nilikumbuka kuwa usiku uliopita niliwasikia wahudumu wa ile nyumba ya wageni wakimkaribisha kwenye kile chumba yule “mpangaji” mpya, wakati nikiwa nimezongwa na mawazo juu ya kitendo cha rafiki yangu Aulelia Mushi kunikana wazi wazi hadharani na tatizo la pesa lililokuwa likielekea kunikabili.

    Kumbe nilikuwa nimelala nyumba moja na adui yangu!

    ...ameingia jana usiku, yuko na buzi lake chumba namba 16.

    Moja kwa moja nilijua kuwa wale watu watakuwa walinifuata nikitokea mjini siku iliyopita, kwani baada ya kuchanganywa na tabia ya Aulelia, sikuwa makini kabisa wakati narudi huku mafichoni kwangu. Hivyo iliwezekana sana wao kunifuatilia bila mimi kujua.

    Shit!







    Nilifungua chumba changu nikiwa bado nimezongwa na wazo la kuwa wale watu wangeweza kunivamia usiku ule mle ndani na nisingekuwa na njia yoyote ya kujiokoa kwani sikuwa nimejiandaa kwa lolote, nikiwa na imani kabisa kuwa hakukuwa na mtu yeyote aliyejua kuwa nilikuwa nimejificha katika ile nyumba kule Kigamboni. Niliingia chumbani mwangu na kusimama ghafla huku nikitoa mguno wa mshituko mkubwa.

    Chumba changu kilikuwa kimechakuriwa vibaya sana. Yaani ilikuwa ni kazi ya haraka na isiyojali mpangilio uliokuwamo mle ndani kabla. Mashuka yote yalikuwa yametolewa kitandani na kutupwa chini kwenye zulia. Makochi yalikuwa yamepinduliwa juu chini na kuraruriwa kwa ghadhabu, mito na godoro vilikuwa vimechanwa kwa kisu au wembe mkali sana. Kabati la nguo lilikuwa limefunguliwa na kuachwa wazi. Meza ndogo iliyokuwamo mle ndani ilikuwa imelalia ubavu kwenye kona moja ya kile chumba, madaftari na makaratasi yangu vikiwa vimesambaratishwa hovyo sakafuni. Zulia lilikuwa limefunuliwa baadhi ya sehemu na kuachwa likiwa hovyo kabisa.

    Nilitazama mabegi yangu na nikaona kuwa yalikuwa yamepekuliwa kwa umakini wa hali ya juu. Nguo zangu zote zilikuwa zimetawanywa hovyo mle ndani na kutokana na mtawanyo ule wa vitu mle ndani, niliweza kuona hasira za wale waliokuwa wakiifanya hiyo kazi, na nikapata hisia ya hali ambavyo ingekuwa iwapo wangenikuta mimi mwenyewe.

    Nilibaki nikiwa nimeduwaa huku hasira zikinipanda, kwani hakuna kitu kilichinokera kama mtu kuchezea nguo zangu za ndani. Na pale nilipokuwa nimesimama, niliziona nguo zangu za ndani zikiwa zimetupwa tupwa hovyo na hata zile pedi zangu za hedhi zikiwa zimechanwa chanwa kwa visu au viwembe na kutawanywa hovyo mle ndani.

    Nikiilazimisha akili yangu ifanye kazi inavyotakiwa, nilianza kuisaka kamera yangu ambayo nilipoondoka niliiacha ndani ya kile kibegi chagu kidogo, ambacho nilikitumbukiza ndani ya lile begi langu jingine kubwa kidogo nililonunua wakati nilipotia mguu wangu kwa mara ya kwanza pale Kigamboni.

    Niliikuta kamera yangu ikiwa chini ya kitanda, sehemu ya kuwekea mkanda ikiwa wazi.

    Mkanda haukuwemo.

    Nilitoka mbio na kuwaita wahudumu wa ile nyumba na kuwaonesha kituko kile, nikitaka kujua ni nani aliyehusika na tendo lile.

    Kilichofuatia hapo ni vurumai ya hali ya juu, kila mhudumu akidai kuwa yeye hakuhusika na tukio lile. Waliuliza iwapo wakaite polisi, nikawauliza kuwa wanataka hao polisi waje wamkamate nani kati yao, na wote wakagwaya. Nilimuuliza yule mfagizi wa siku ile iwapo alipoingia kufagia chumba changu alikikuta katika hali ile, naye akaeleza kuwa hakikuwa kwenye hali ile na alikisafisha na kutandika kama kawaida na kukifunga, wakati huo mimi nilikuwa nimeshatoka.

    “Ina maana hamkusikia kelele au vishindo vyovyote kutokea humu ndani?” Niliuliza kwa mshangao huku akili ikinichemka. Walinijibu kuwa hawakusikia chochote, na mara nyingi muda wa katikati ya asubuhi wakishafanya usafi wao huwa wanakaa upande wa mbele wa ile nyumba, hivyo inawezekana kabisa wasisikie lolote.

    Niliwauliza iwapo waliwaona wale wapangaji wa chumba namba 16 wakitoka nje muda wowote katika siku ile baada ya mimi kutoka. Wakanijibu kuwa kwa mara ya kwanza wapangaji wa chumba namba 16 walitoka nje ya chumba chao muda mfupi kabla ya mimi kurejea, na kwamba hata usafi chumbani kwao hawakutaka ufanyike, wakidai kuwa walikuwa wanalala na chumba hakikuwa kichafu.

    “Walipotoka muda mfupi uliopita, waliwaaga kuwa ndio wanaondoka moja kwa moja au walisema watarudi?” Niliwauliza, nao wakanijibu kuwa walikuwa wamelipia kwa muda wa siku mbili na kwamba walisema kuwa wangerudi.

    Nilijua kuwa wale watu walikuwa ndio wameondoka na hawatarudi, lakini sikuwaambia hilo.

    “Kwa hiyo Anti…kuna vitu vimeibiwa?” Mmoja wa wale wahudumu aliniuliza. Nilimgeukia kwa hasira na kumuuliza kwa ukali.

    “We’ unaonaje, huu si wizi wa wazi tu?” Halafu nikaanza kuokota vitu vyangu huku nikilaani kwa sauti kuwa nilikuwa nimekaa kwenye nyumba ya wageni isiyo na usalama hata kidogo. Moyoni nilijua kuwa si kosa lao, kwani nilijua kuwa hata ningekuwa kwenye hoteli gani, au nyumba yoyote nyingine ya wageni, ilikuwa ni swala la wale wabaya wangu kujua niko wapi tu, halafu tukio kama lile lingetokea huko huko. Bahati yao mbaya ni kuwa nilikuwa nimeamua kuja kujificha kwenye nyumba yao ya wageni, na wale wabaya wangu wamenigundua. Ingawa walijitetea sana kuwa tukio kama lile halijawahi kabisa kutokea pale kwao, lakini niliamua kuzidi kulaumu ili wasizidi kuniuliza maswali zaidi, kwani kama ingewajia akilini kuwa ule haukuwa wizi bali wale watu walikuwa wakitafuta kitu fulani mle ndani mwangu, lazima wangekimbilia kuita polisi, jambo ambalo sikulitaka kabisa kwa sababu zinazoeleweka.

    Mmoja wa akina dada wahudumu wa mle ndani alianza kunisaidia, lakini nilimzuia na kuwaomba wote wanipishe mle ndani nikiwaambia kuwa nilihitaji kuangalia vitu vyangu vizuri ili nijue ni vitu gani hasa vilivyoibiwa.

    Walitoka huku wakibwabwaja maneno ya kunipa pole na wakiulizana wao kwa wao ni jinsi gani tukio lile liliweza kutokea.

    Nilijifungia mle ndani na kuanza kukusanya vitu vyangu haraka haraka, nikijua kuwa muda wowote wale wauaji wangeweza kurudi na kunitembezea ubabe wao, kwani wakishindwa kuupata ule mkanda kwa njia moja, lazima watatumia nyingine. Kufikia sasa vitisho vimeshindwa, ndio kisa wakaamua kutumia njia hii ya wizi, na iwapo na hii haitafanikiwa, basi kwa vyovyote watatumia ubabe.

    Baada ya kukusanya nguo na baadhi ya vitu vyangu ambavyo havikuathirika na ule upekuzi ambao kwangu niliuona kuwa ni kuingiliwa undani wangu kusikofaa kabisa, nililifungua tena lile begi langu kubwa na kuweka vitu vyangu vilivyonusurika kutoka kwenye upekuzi ule wa fujo, nikiitumbukiza na ile kamera ambayo likuwa imevunjika kidogo kwenye pembe yake moja, bila shaka baada ya kupigizwa chini katika ile pekua pekua yao, nikijua kuwa kama si kile chumba kuwa na zulia zito, basi bila shaka ile kamera ingevunjika vibaya sana.

    Nilipokamilisha hili nilikimbia upesi kule bafuni na kuchukua mswaki na baadhi ya vipodozi vyangu na nilikuwa narudi tena kwenye kile chumba changu cha kulala wakati niliposikia simu ikiita. Nilipagawa, kwani sikuwa na simu na muda wote katika kuokota vitu vyangu mle ndani sikuona kuwa kulikuwa kuna simu.

    Hii ni nini sasa?

    Nilianza kuisaka ile simu nikifuatilia sauti ilipokuwa ikitokea huku moyo ukinipiga na akili ikinitembea kwa kasi sana. Ilikuwaje hata hii simu ikawa humu ndani? Ni kwamba imesahauliwa na wale wavamizi walioondoka muda si mrefu, au wameiacha makusudi ili wanipigie wakitaka kuongea na mimi? Na kama ni hivyo, ina maana walijua kuwa hivi sasa nilikuwamo mle ndani? Au walikuwa wanabahatisha tu?

    Niliikuta simu kwenye ua la plastiki lililokuwamo mle ndani kama sehemu ya mapambo, ambapo simu ile iliwekwa kwenye kopo maalum lililobeba lile ua ambalo lilikuwa limesimamishwa kwenye kona moja ya kile chumba.

    Nilipotoka mle ndani asubuhi ile, lile ua lilikuwa juu ya meza ndogo iliyokuwamo mle ndani, sehemu ambayo lilikuwa likiwekwa siku zote tangu nianze kuishi ndani ya chumba kile.

    Ilikuwa ni ile simu yangu iliyotoweka kule msituni!

    Niliichukua ile simu kwa mikono iliyojaa kitetemeshi na kuangalia namba iliyokuwa ikinipigia.

    Hakukuwa na namba yoyote iliyoonekana kwenye ile simu zaidi ya neno “Private Number Calling”.

    Huyu ni nani?

    Nilizidi kuitazama ile simu kwa mshangao huku moyo ukinipiga kwa nguvu, nikijishauri iwapo niipokee ile simu au vinginevyo.

    Vije iwapo ile simu ilikuwa imepigwa na wale wauaji kwa nia kwamba nikiipokea watajua kuwa nipo mle ndani ili wanivamie?

    Au ni kweli kuwa wameisahau, na huyo alikuwa ni mwenzao akijaribu kuwasiliana nao? Kama ni hivi, basi labda nikiipokea angalau nitaweza kuongea na mmoja wa wabaya wangu na labda nitaweza kumlaghai kuwa mimi ni yule askari wa kike na kuweza kujua sehemu ya mikakati yao.

    Lakini ni kweli ile simu ilikuwa imesahauliwa?

    Kwa nini itokee leo ghafla tu baada ya kupotea muda wote huo?

    Hapana,haikuwa imesahauliwa.

    Niliona wazi kuwa ile simu ilikuwa imewekwa pale kusudi, kama jinsi lile ua lilivyosogezwa kusudi kwenye kona ya chumba kile na si kwa bahati mbaya; kwani kwa uharibifu uliofanywa mle ndani, ningetarajia na lile ua nalo lingekuwa limesambaratishwa vibaya sana.

    Niliitupa kitandani ile simu na muda huo huo ikaacha kuita. Haraka niliinua ile meza iliyokuwa imelalia ubavu mle ndani na kuisimamisha usawa wa feni kubwa lililokuwa likining’inia kwenye dari la mle ndani. Nilikimbilia kule lilipokuwapo kabati la nguo, lakini nilijikwaa kwenye mabegi yangu na kupiga mwereka mzito mle ndani. Nilitoa tusi kubwa na kuinuka, nikachomoa droo ya kabati lile na wakati huo huo ile simu ikaanza kuita tena. Nilirudi na lile droo kubwa la kabati na kulilaza juu ya ile meza. Niliparamia na kusimama juu ya ile droo iliyokuwa juu ya ile meza na kupeleka mikono yangu kwenye moja ya panga tatu za ile feni na kuipapasa sehemu ya mgongo wake iliyokuwa imeelekea kwenye dari.

    Hamna kitu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliizungusha kidogo ile feni na kupapasa pangaboi jingine. Nako hali ikawa kama ile ya mwanzo na nikahisi kitu kikiuchoma moyo wangu na hofu ikanijaa. Niliizungusha tena ile feni na kukamata pangaboi la tatu la ile feni na kupapasa mgongo wake taratibu.

    Vidole vyangu vilipapasa kitu nilichokitarajia.

    Huku nikishusha pumzi ya faraja, niliushika ule mkanda mdogo wa video uliokuwa umeshikiliwa kwenye mgongo wa lile pangaboi kwa utepe wa gundi na kuibandua kutoka kwenye lile pangaboi.

    Niliteremka na kuuweka ule mkanda ndani ya sidiria yangu, nikanyakua begi langu na kutoka haraka nje ya chumba kile nikiiacha ile simu ikiendelea kuita



    “THE RICKSHAW”

    vii.

    K

    oku alinijia juu vibaya sana. Aliponiona tu nimeingia ofisini kwake pale katika hospitali ya wilaya ya Temeke, aliangaza macho huku na huko, kisha aliinuka upesi, akachukua koti jeupe la manesi lililokuwa likining’inia nyuma ya mlango na kunitupia huku akiwa amekunja uso kwa hasira.

    “Vaa hilo koti, upesi!” Aliniambia huku akiwa amekasirika. Nilishangaa, lakini nilifanya kama alivyoniagiza, huku naye akiukwapua mtandio mweusi niliokuwa nimejitanda kichwani mwangu, kisha akanishika mkono na kuniongozea maeneo ya vyoo vya wanawake, wote tukiwa tumevaa yale makoti meupe wanayovaa wahudumu wa hospitali yaliyofika hadi chini kidogo ya magoti, mimi nikiwa na ile miwani yangu ya jua usoni. Kando ya vyoo vya wanawake kulikuwa kuna chumba kimoja kidogo ambacho baadaye nilielewa kuwa kilikuwa kunatumika na manesi wa kike kubadilishia nguo.

    Koku aliniingiza ndani ya chumba kile na kufunga mlango kwa ufunguo.

    “What the matter with you Tigga, eenh? Kwa nini umekuja hapa? Hujui kuwa unajihatarishia maisha yako! Mi’ n’lidhani wewe ni smart kumbe bwege namna hii? Umekuja kufanya nini hapa? Ondoka! Tena ondoka upesi!” Alinikemea mfululizo kwa sauti kali ya kunong’ona huku nikiona kuwa alikuwa amechukia vibaya sana.

    Nilibaki nikimkodolea macho dada yangu nisipate la kumweleza kwa wakati ule. Nilipotoka mbio kule Kigamboni, wazo lililonijia ni kwenda moja kwa moja hadi kazini kwa dada yangu. Sijui ni nini hasa kilichonipeleka kule, lakini nadhani nilihitaji sana kuonana na mtu yeyote kutoka kwenye jamii yangu, na sikuweza tena kwenda nyumbani kwa mama yangu. Pia nilihitaji msaada wa pesa kutoka kwake.

    “Nilihitaji kukuona Koku! Nimekutwa na matatizo makubwa na nimekuwa nikikimbia na kujificha peke yangu kwa muda mrefu...”

    “Na hilo ndio jambo la busara zaidi kwako!” Koku alinikatisha kwa ukali.

    “Najua! Vipi mama, yu hali gani?”

    “Ah! Yuko salama.Hajambo. Lakini amelichukulia vibaya sana swala lako.Linamuumiza.”

    Nilimtazama dada yangu yule, na machozi yalinilengalenga usoni. Koku alikuwa akijitahidi kujikaza asiangue kilio na alipokuwa akinikemea niliona midomo ilikuwa ikimcheza. Tulibaki tukitazamana, kisha akanivuta na kunikumbatia kwa nguvu.

    “Oooh! Tigga, pole sana mdogo wangu. Nimekuwa nikikuogopea sana kwa siku zote hizo ulizokuwa ukihangaika peke yako. Nina hamu sana ya kujua ni kipi kilichokutokea huko porini, lakini hapa mahala si salama kwako.”

    “Ina maana unaamini kuwa mimi si mwehu? Siye niliyeua kule msituni?’ Nilimuuliza huku nikijitoa mikononi mwake na nikipangusa machozi. Koku alinitazama kwa huzuni kwa muda kabla ya kunijibu.

    “Sio siri mdogo wangu, kwanza niliamini kabisa kuwa ulikuwa umefanya hayo mambo ya ajabu. Dr. Lundi ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kujieleza na akaaminika, lakini baadaye nikaja kuelewa kuwa wale si watu wazuri pale walipoanza kunihoji juu yako. Maswali waliyouliza...”

    “Maswali gani?”

    “Ah! Walianza kuuliza maswali ambayo nilidhani wao kama madaktari hawakutakiwa kuuliza. Maswali ambayo yangetakiwa yaulizwe na polisi.Maswali kuhusu mkanda wa video, jinsi nilivyokuelewa tabia zako, marafiki zako...lakini...lakini zaidi ya hapo ni baada ya kuongea na Kelvin...yeye ndiye aliyenihakikishia kuwa wale ni watu wabaya.”

    ”Kelvin? You talked to Kelvin?” Nilimuuliza kwa hamasa, nikaendelea,”Yu hali gani sasa?”

    “Niliongea naye siku kadhaa baada ya lile tukio la pale nyumbani kwake, na hapo ni baada ya Dr. Lundi kuja kututembelea nyumbani na kutueleza juu ya habari zako. Baadaye nilipata habari za masahibu yaliyomkuta Kelvin na nikaenda kumtembelea hospitali ya Muhimbili. Akanieleza kila kitu, japo kwa taabu....”

    “Ameumia sana?”

    “Risasi ilimpata kifuani upande wa kulia, ikatokea mgongoni, na ndio salama yake, kwani ingeingilia upande wa kushoto tungezika.” Koku aliniambia lakini bado alionekana na wasiwasi mkubwa.

    “Maskini Kelvin...sasa anaendeleaje?”

    “Nilipoenda kumuona alikuwa na hali mbaya, lakini alijitahidi sana kunielezea yaliyomkuta na ndipo nilipoelewa kuwa Martin Lundi ni mtu mbaya na kwamba yote aliyotueleza juu yako ni uongo. Siku iliyofuatia tu hali yake ilibadilika ghafla, na sasa yuko chumba cha wagonjwa mahututi na hawezi hata kuongea, ni ajabu kabisa. Nilipoenda tena kumtembelea, Kelvin alishindwa kabisa kuongea, ila aliniashiria nimpe kalamu na karatasi, na nilipompa, kwa mkono uliotetemeka vibaya sana aliniandikia kitu ambacho kilinitisha sana, na kilifanya nisiende tena kumwona pale hospitali mpaka leo.” Koku alinieleza kwa kunong’ona nami nilipata msisimko mpya na moyo ukaanza kunipiga kwa nguvu.





    “Alikuandikia nini Koku?” Nilimuuliza kwa jazba.

    “Dr. Lundi. Ondoka upesi’!” Koku alinijibu.

    Nilibaki mdomo wazi. “Yaani hayo ndio maneno aliyokuandikia?” Nilimuuliza.

    Koku aliafiki kwa kichwa huku akizidi kuonesha wasiwasi mkubwa.

    “Mungu wangu! Ina maana...”

    “Nadhani Dr. Lundi alimfanya kitu kibaya Kelvin pale hospitali Tigga. Nadhani kuna sindano au dawa fulani amempa...inamuua Kelvin taratibu Tigga.” Koku aliniambia kwa huzuni kubwa.

    Nilibaki hoi. Niliegemea ukuta na kujishika paji la uso. Akilini mwangu nilikumbuka wakati yule mtu aliyejiita Martin Lundi akipokea sindano kutoka kwa mmoja wa vibaraka wake kule katika ofisi ya mkuu wa wilaya na kujitia kuangalia kiwango cha dawa kilichowekwa ndani ya bomba la ile sindano.

    Mungu wangu! Haya ni mambo gani sasa?

    Lakini ilileta maana. Kama Kelvin ataishi na kuelezea juu ya tukio zima la kule nyumbani kwake siku ile, ingenitoa kabisa kwenye hizi shutuma za uongo, na wakati huo huo ingemuweka yule mtu anayejiita Dr. Lundi katika wakati mgumu.

    “Kwa hiyo ni nini kilifuatia baada ya hapo?”

    “Baada ya hapo ndio sijaenda tena kwa Kelvin, lakini akina Lundi walianza kunifuata fuata sana hadi hapa kazini, wakitaka kujua iwapo niliogea lolote na Kelvin. Niliwaeleza kuwa Kelvin hakuweza kuongea lolote na mimi, lakini naona hawakuniamini.” Koku alinijibu.

    Hii kali. Sasa na dada yangu tena ametiwa katika mkumbo?

    Nilimuuliza iwapo alimuelezea mama juu ya mambo haya, Koku akaniambia kuwa hakumueleza mama kabisa, kwa sababu mama alionekana kumuamini sana Martin Lundi, hivyo aliamua kumuacha hivyo hivyo.”

    “Umefanya vizuri sana.”

    “Na wewe umefanya kosa kubwa sana kuja hapa. Inabidi uondoke upesi sana.” Koku aliniambia kwa wasiwasi.

    “Kwani bado wanaendelea kukufuata mpaka sasa?” Nilimuuliza. Koku alinishika mabega na kunitazama usoni kwa macho ya kuomboleza.

    “Huelewi Tigga. Hawa watu wamo humu hospitalini!”

    ”Say Whaat?”

    “Ndio Tigga. Watu wapya wamekuwa wakiletwa hapa ofisini kufanya kazi, na mmoja amewekwa moja kwa moja pale kwenye kitengo changu. Yaani kama leo ungewahi kufika kidogo tu ungemkuta na sijui ingekuwaje Tigga. Ondoka na usije tena hapa!” Koku aliniambia kwa jazba. Niliogopa kupita kiasi, na lile jambo nililiona haliwezekani.

    “Sasa...sasa unajuaje kuwa ni miongoni mwao?” Nilimuuliza. Koku alitikisa kichwa kwa masikitiko na kukata tamaa.

    “Yule mtu sio nesi Tigga. Hajui lolote juu ya unesi, kazi yake kukaa tu pale na kupokea simu, can you believe that? Jamaa kazi yake ni kupokea simu tu! Sasa pale kwangu ni ofisi ya maopareta pale?”

    Nilikubaliana na Koku, huku kwa mara nyingine nikikubali kichwani mwangu kuwa hakika ule mtandao wa Dr. Martin Lundi ulikuwa mkali na ulizidi kunizingira. Lazima niondoke haraka iwezekanavyo. Kabla sijaongea neno lolote, Koku aliendelea kunipasha habari.

    “Halafu na polisi nao wakaja na maswali juu yako.” Koku aliniambia kwa upole. Niliinua uso wangu na kumtazama kwa uso uliojaa maswali. Akili yangu ikienda kwa yule mwanadada askari aliyekichambua chumba changu kwa vurugu kubwa kule kwenye ile nyumba ya wageni muda mfupi tu uliopita, akitafuta mkanda wa video wenye ushahidi wa kumuangamiza Martin Lundi na wenzake.

    “Na wao wako upande wa Martin Lundi.” Nilijibu kwa masikitiko huku nikitikisa kichwa.

    “Hapana. Huyu aliyekuja ni polisi hasa, tena anaonekana wa ngazi ya juu tu, kutokana na mavazi yake. Na jinsi wale askari alioongozana nao walivyoonekana kumgwaya.”

    Hapo nikawa makini sana.

    “Yukoje huyo askari?” Nilimuuliza. Koku alimuelezea haraka haraka yule askari aliyemjia na maswali juu yangu, na aliposema kuwa alikuwa amekata ndevu zake katika mtindo wa Timberland, nilipata uhakika kuwa alikuwa ni yule askari niliyemtoroka pale ofisini kwangu, katika jumba la makumbusho.

    “Alitaka nini?” Nilimuuliza.

    Koku akaniambia kuwa yule askari aliwataka yeye na mama yangu waende kuutambua mwili wa mtu ambaye aliuawa akijaribu kunitorosha mimi kutoka mikononi mwa polisi, iwapo waliwahi kuniona naye mtu huyo wakati wowote hapo nyuma na katika mazingira gani.

    “Mlienda? Mlimuona huyo mtu?” Niliuliza huku moyo ukinipiga sana, nikijua kuwa huyo mtu aliyetakiwa akatambuliwe alikuwa ni yule jambazi niliyempachika jina la Macho ya Nyoka.

    “Tulipelekwa mpaka mochuari Muhimbili. Na tukamuona huyo mtu. Ni jambazi hasa, Tigga! Yaani hata katika kifo, unaona kabisa kuwa yule mtu alikuwa muuaji! Yale macho! Mama hakulala.”

    “Kwa hiyo mlinuona kwa macho yenu kuwa amekufa?”

    “Mimi ni nesi Tigga, na najua mtu akifa anakuwaje. Yule mtu alikuwa amekufa! Of course tulimwambia yule askari kuwa hatujawahi kukuona ukiwa na mtu yule hata siku moja, nasi hatukuwa tumepata kumwona yule mtu kabla ya pale kwenye sanduku la barafu la mochuari.”

    “Kumbe kweli Macho ya Nyoka amekufa!” Nilijisemea mwenyewe kwa sauti, na Koku alinikazia macho.

    “Unamjua yule mtu?”

    “Hapana, ila nilikutana naye muda mfupi kabla yule askari hajamuua. Ni mfuasi wa Martin Lundi, na nilimuona kwa macho yangu akiua mtu kule msituni Koku. Ni mtu mbaya sana yule, bora alivyokufa.”

    “Mungu wangu, Tigga!” Koku alistaajabia taarifa ile.

    “Kwa hiyo yule askari akachukua hatua gani baada ya hapo?” Nilimuuliza. Koku aliguna kabla ya kunijibu.

    “Achukue hatua gani nasi tulishamwambia kuwa yule mtu hatujawahi kumuona hata siku moja? Alichofanya ni kutueleza kuwa muda wowote utakapowasiliana na sisi tumjulishe, na tukushauri ujisalimishe. Akatuachia kadi yake yenye namba zake za simu ili tuwasiliane muda wowote tutakapopata habari kuhusu wewe.”

    “Ooo? Kwa hiyo unadhani ni bora nijisalimishe? Au utamjulisha huyo askari kuwa nilikuja kuwasiliana na wewe?” Nilimuuliza dada yangu. Kauli yangu ilionekana kumuumiza sana.

    “Wewe ni mdogo wangu Tigga. Najua mambo mengi yanayosemwa juu yako si ya kweli, na nilimueleza hata yule askari, pamoja na zile habari nilizozipata kutoka kwa Kelvin. Lakini siwezi kukusaliti hata kama ungekuwa umefanya hayo mambo. Lakini nadhani ni bora ujisalimishe Tigga, na katika kufanya hivyo inabidi uwe makini sana unajisalimisha kwa nani. Nadhani yule askari ni mtu safi...anaonekana ana uelewa fulani.” Koku alinieleza kwa kirefu. Niliyatafakari yale maneno ya Koku kwa muda. lngawa nilikubaliana kabisa na ushauri wake, bado nilikuwa na tatizo la kujua ni yupi hasa askari wa kumuendea. Je yule afisa aliyemuua Macho ya Nyoka alielekea kuwa muafaka? Sikuweza kupitisha uamuzi wowote kwa wakati ule, lakini hata mimi nilidhani kuwa labda ningeanza na yule askari katika kutafuta msaada wa kuaminika juu ya swala hili.

    Tulibaki kimya kwa muda, kisha nikamwambia Koku shida yangu.

    “Koku, nahitaji pesa. Unaweza kunipatia kiasi chochote? Nimeishiwa...” Nilimwambia dada yangu. Aliniambia nimsubiri mle mle ndani akanitazamie kwenye pochi yake pale ofisini kwake, kwenye kitengo cha madawa. Alitoka na kurudi muda mfupi baadaye akiwa amebeba maboksi matupu ambayo bila shaka yalikuwa yamewekewa chupa za dawa mbali mbali. Alinikabidhi kiasi cha pesa akiwa amekifumbata mkononi mwake, nami nilizipokea bila kuzihesabu na kuzishindilia mfukoni mwangu.

    “Hiyo ni shilingi elfu hamsini. Samahani sina zaidi ya hapo.” Aliniambia. Nilimshukuru sana na kumwahidi kumlipa iwapo nitatoka salama katika msukosuko ulionikabili. Aliniambia nisijali na kunieleza kuwa yule mtu aliyekuwa akifanya kazi ya kupokea simu pale ofisini kwake ambaye alimhisi kuwa ni mfuasi wa Martin Lundi alikuwa amerudi. Hakukuwa na njia nyingine zaidi ya kutokea nje ya jengo lile isipokuwa kupita pale mbele ya dirisha la ofisi ya Koku. Koku alinibebesha yale maboksi, akitumbukiza lile begi langu ndani ya boksi moja na kuniambia kuwa nitoke nje nikiwa nimebeba yale maboksi na kuyatumia kuficha uso wangu nikipita mbele ya ofisi yake, labda nitafanikiwa kumpita yule mtu bila kutambulika, hasa kutokana na lile koti jeupe nililovaa juu ya nguo zangu. Nilimshukuru dada yangu kwa mara nyingine tena, naye alinikumbatia tena na kuniambia kuwa amefurahi kuniona hata hivyo.

    Nikiwa nimebeba yale maboksi kama mmoja wa manesi wa hospitali ile, nilitembea haraka kuelekea nje ya jengo lile huku nikificha uso wangu nyuma ya yale maboksi. Nilipopita kwenye dirisha la ofisi ya Koku, nilichungulia juu ya uzio wa maboksi niliyokuwa nimeyabeba na kuzungusha macho yangu yaliyofichwa na ile miwani ya jua niliyovaa kuelekea ule upande ambao nilidhani ningeweza kumuona huyo mtu anayekaa kwa kazi ya kupokea simu tu mle ofisini kwa dada yangu.

    Koku alikuwa sahihi.

    Yule mtu alikuwa ni mmoja wa wale vibaraka wawili wa Martin Lundi alioniibukia nao kule ofisini kwa mkuu wa wilaya.

    Nilitoka nje ya jengo huku nikiwa na woga mkubwa, lakini yule mtu hakunitambua wala hakunitilia shaka. Niliyatupa yale maboksi kando ya mapipa ya taka, huku nikitoa begi langu kutoka ndani ya moja yale maboksi. Nyuma ya jengo lile nililivua lile koti jeupe nililovaa juu ya nguo zangu na kulitupa nyuma ya maua.

    Niliangaza kulia na kushoto, kabla ya kuvuka barabara na kutoweka eneo lile huku nikijifariji kuwa angalau nilikuwa nimepata mwanzo mzuri, kwani nilikuwa nimepata taarifa za muhimu sana kutoka kwa dada yangu Koku.

    --

    Saa yangu iliniambia kuwa muda ulikuwa ni saa sita na robo mchana. Nilisimamisha teksi na kumuelekeza dereva anipeleke Kijitonyama, nyumbani kwa aliyekuwa rafiki yangu Aulelia Mushi. Kwa kadiri nilivyoelewa, Aulelia bado alikuwa hajaolewa na alikuwa akiishi peke yake na msichana wa kazi tu. Aulelia alikuwa na tabia ya kurudi nyumbani kula chakula cha mchana na kurudi tena kazini. Nilitaka nimkabili ili nijue nini kiini cha tabia yake ya ajabu, na huenda kwa kufanya hivyo ningepata mwanga mwingine kuhusu wale watu wabaya wanaoniwinda.

    Nilimkuta msichana wake wa kazi ambaye alinikaribisha kwa mashaka huku akinieleza kuwa tajiri yake amemzuia kukaribisha wageni asiowajua. Huyu alikuwa msaidizi tofauti na yule niliyemjua mimi, lakini kwa hapa jijini wasaidizi wa ndani huwa wanabadilika kila mara.Nilimwambia mimi ni dada ya tajiri yake na kwamba nimewasiliana naye kwa simu na kuwa yuko njiani anakuja. Nilikaribishwa sebuleni na kuketi nikisubiri huku moyo ukinipiga kwa nguvu.

    “Samahani Aulelia, lakini ni muhimu kwangu kujua ukweli.” Nilinong’ona huku nikisubiri ujio wa Aulelia. Sikusubiri sana, kwani muda si mrefu nilisikia gari ya Aulelia ikisimama nje ya nyumba na Aulelia aliingia ndani huku akimpigia kelele msaidizi wake aende akashushe mizigo kutoka kwenye gari. Nilisimama kutoka kwenye kochi nililokuwa nimekalia na kumtazama. Aulelia alisimama ghafla na uso ulimbadilika mara moja, ukichukua mtazamo wa woga uliochanganyika na chuki kubwa. Tulitazamana.

    “Toka nyumbani kwangu Tigga! Toka kabla sijakuitia polisi!” Hatimaye Aulelia alinifokea kwa chuki na ghadhabu. Nilimuinulia viganja vya mikono yangu kumwashiria kuwa sikuwa na silaha yoyote na kwamba sikuwa nikitaka shari.

    “Nitaondoka Aulelia, lakini nataka maelezo ya kitendo chako cha kunikana vile mbele ya watu...kumbe unanifahamu kuwa mimi ni Tigga, sasa kwa nini ulisema hunijui?” Nilimuuliza huku nikimsogelea taratibu. Aulelia alinitazama kwa jeuri na kuniinulia kidevu kwa kiburi.

    “Hilo ndilo lililokuleta au kuna jingine?” Aliniuliza. Nilimtazama na sikuamini kama ni yeye kweli anaweza kuniongelesha kwa kiburi namna hii.

    “Aulelia! Ni nini lakini kinatokea? Mimi nimekutwa na matatizo makubwa sana rafiki yangu. Nimeshuhudia maiti za wenzangu zikiwa zimetawanywa kama mizoga ya wadudu tu huko porini, nimekuja hapa mjini kila mtu ananigeuka, kuanzia Kelvin hadi mama yangu....hadi wewe! Sijui ni nini kinatokea...”

    “Kwa hiyo umekuja kunimalizia na mimi? Unataka kutafuna moyo wangu na kunywa damu yangu? Ndicho kilichokuleta?”

    Nilishangaa.

    “Nini? Mbona sikuelewi Aulelia? Ni vitu gani hivyo unaniambia?”

    “Habari zako zote ninazo Tigga, na nakuhakikishia kuwa mimi hutanipata kirahisi...tutapambana!” Na baada ya kusema hivyo Aulelia aliruka kwa wepesi wa ajabu na kuchukua kisu kikubwa kilichokuwa kwenye kabati la vyombo lililokuwa pale sebuleni. Nilishangaa, lakini akili ilianza kufanya kazi haraka haraka. Aulelia alinijia akiwa na kisu mkononi. “Ondoka upesi nyumbani kwangu Tigga, Ondoka na usirudi tena!”

    “Sitaondoka bila majibu Aulelia! Kama utaniua kwa hicho kisu basi uniue tu, lakini mimi sikuja kwa shari kwa sababu ushari si fani yangu, nawe unajua hilo.” Nilimwambia huku nikiwa bado nimemuinulia viganya vyangu na nikimsogelea. Aulelia aliduwaa kwa hatua yangu hii, kwani bila shaka alitaraji ningemjia juu na kujaribu kupambana naye.

    “Tigga n’takuchoma kisu! Toka tafadhali...!”

    “Nichome tu Aulelia! Mimi nimekikwepa kifo mara kadhaa tangu nikutwe na mkasa huu unaouendeleza hapa. Lakini huko nilifanikiwa kukikwepa kifo kwa sababu nilikuwa najua kuwa nilikuwa napambana na adui. Lakini wewe sio adui yangu Aulelia, wewe ni rafiki yangu. Natarajia msaada kutoka kwako na sio mapambano. Kwa hiyo kama unadhani kunichoma kisu ni salama zaidi kwangu Aulelia, nichome tu. Lakini mimi ninachotaka ni majibu tu kutoka kwako.” Nilimwambia kwa utaratibu huku nikizidi kumsogelea.Aulelia hakulitegemea hili na nikaona akitetereka katika msimamo wake na machozi yakimlengalenga.

    “Umeongea na mtu anayejiita Dr. Martin Lundi?” Nilimuuliza kwa upole. Aulelia aliafiki kwa kichwa, na kutazama pembeni.

    “Akakuambia kuwa mimi nina wazimu...Paranoid Schizophrenia?” Aulelia aliafiki tena kwa kichwa na akaketi kwenye kiti, akiachia kisu chake kikianguka sakafuni. Nami niliketi kando yake huku moyo ukinipiga. “Ulimuamini Aulelia? Uliamini kuwa mimi nina wazimu?”







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog