Simulizi : Wimbo Wa Gaidi
Sehemu Ya Pili (2)
Saa moja baadaye helikopta ilitua pembezoni mwa jiji la Islamabad, na mara baada ya Imraan na kundi lake kuteremka,rubani aliirusha tena ile helikopta na kutokomea angani.
Imraan aliwaongoza wenzake kimya kimya, wakikata mitaa kadhaa kabla ya kutokea kwenye kituo cha teksi. Walionekana kama wenyeji watatu tu waliokuwa na mgeni wao mmoja wa kiafrika wakitoka kwenye moja ya sehemu kadhaa za starehe, ambazo kwa mazingira ya nchi ile zilikuwa ni za siri sana.
"Okay makomredi...mimi naelekea kwangu sasa. Ninyi mtarudi kwenye mahoteli yenu na kukipambazuka mtoweke nchi hii...si tiketi na pasipoti zenu viko sawa?" Imraan aliwaambia na kuwauliza wenzake.
"Yah...tuko vizuri..."Mmoja alijibu.
"Okay..tutawanyike. Ikiwa kutatokea kazi nyingine ninajua nitawasiliana vipi na nyie..."
"Kuna kazi tena na dalali wako wa madili keshadunguliwa kule?" Mwenzake mmoja alimuuliza.
Imraan akafyatua kicheko kifupi, kisha akamjibu, "Kufa ndio sehemu kuu ya kazi yetu kaka…ndio maana hata kama mmoja wetu angeuawa leo hii, bado hela yake ingetumwa tu kwenye akaunti yake, familia yake ikanufaika. Kafa yeye...sio harakati, bwana. Atawekwa mwingine wa kusimamia mambo haya badala yake...na atanitafuta tu muda ukifika..." Alimjibu.
Kila mmoja akachukua teksi yake na kuelekea kwenye hoteli aliyofikia. Imraan alimuelekeza dereva wa teksi yake amrejeshe nyumbani kwake...ambako alipaacha kwa siku kadhaa alipokuwa ameenda kwenye misheni ile ya hatari.
________________
CNN ndio walikwa wa mwanzo kutangaza juu ya shambulizi lile kubwa kabisa la ndege zisizo na rubani dhidi ya ngome kuu ya wataleban iliyokuwa kilomita saba kutoka kwenye kile kijiji cha Dargah Mandi.
Kupitia taarifa ile, dunia ilihabarishwa kuwa kiongozi mkuu wa wataleban ndani ya Waziristan alikuwa ameuawa pamoja na wafuasi wake wengi wakiwemo wale wa Al-Qaida waliokuwa wamehifadhiwa kwenye ngome ile.
Aidha, CNN ilihabarisha kuwa katika kampeni ile ya mashambulizi iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya jeshi la marekani na lile la Pakistani, jeshi la shirikisho lilifanikiwa kumtia mbaroni gaidi muhimu aliyehusika katika ulipuaji mabomu ubalozi wa Marekani nchini Tanzania mwaka 98, aliyekuwa akisakwa sana, Nouman bin Fattawi...lakini helikopta aliyokuwa akisafirishwa nayo kutoka Pakistani ilidunguliwa na vikosi vya wapiganaji wasiojulikana na yeye pamoja na watu wengine saba waliuawa. Mpaka muda habari ile inarushwa hewani, hakukuwa na kundi lolote lilojinadi kuhusika na udunguliwaji wa helikopta ile. Habari hii ilidakwa na vyombo vingine vya habari na kusambaa dunia nzima.
Ni habari iliyoleta kizaazaa kikubwa nchini Tanzania...
___________________
Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam, Tanzania. Wiki moja baadaye:
Umma wa watu ulikuwa umefurika kwenye makaburi ya kisutu. Muda ulikuwa ni saa kumi za alasiri. Ufurikaji wa umma makaburini pale haukutokana na kwamba kulikuwa kuna mtu maarufu aliyekuwa akizikwa siku ile, La Hasha. Mfuriko ule ulitokana na ukweli kwamba kulikuwa kuna marehemua watano waliokuwa wakizikwa siku na wakati ule, na hivyo kulikuwa kuna makundi matano ya ukubwa tofauti kwenye makaburi matano yaliyochimbwa sehemu tofauti ndani ya uzio wa eneo lile la makaburi maarufu jijini.
Ni kutokana na ujumla wa makundi yale matano yenye ukubwa tofauti kuwa ndani ya eneo lile kwa wakati mmoja, ndipo taswira ya umma wa watu kufurika ilipopatikana makaburini pale.
Nje ya uzio wa makaburi yale magari mengi yalikuwa yameegeshwa pande zote za barabara finyu, kiasi kwamba ilikuwa ni shida kwa magari mengine kupita tu pale barabarani, wachilia mbali kupishana.
Kwenye kaburi lililochimbwa pembeni kabisa ya eneo lile la makaburi, upande wa kushoto mara baada ya kuingia kwenye geti la makaburi yale, kulikuwa kuna kundi la wastani la wanandugu waliokuwa wakimzika mpendwa wao, wakiongozwa na sheikh aliyekuwa mjuzi katika taratibu za kuendesha maziko. Lilikuwa ni kundi lenye huzuni kwa kuondokewa na ndugu na jamaa yao ambaye hata hivyo wamekuwa mbali naye kwa muda mrefu, siku zote hizo kabla ya umauti kumkuta mpendwa wao, wakiwa wamegubikwa mashaka mazito juu ya hatma yake…mpaka habari zilipowafika kuwa hatimaye mpendwa wao alikuwa ameuawa kwenye kifo kibaya kabisa, huko ughaibuni.
Walikuwa wamekusanyika kumzika Nouman Fattawi.
Kaka, mwana, mjomba, rafiki, mpenzi…na kwa wengine, ndugu yao katika imani.
Hata hivyo, hawa wote walikuwa ni sehemu moja tu ya wale waliokuwapo kwenye mazishi ya Nouman Fattawi siku ile.
Pamoja nao walikuwepo wana usalama wa taifa, ambao walikuwa pale kushuhudia maziko ya gaidi aliyekuwa akisakwa na wamarekani kwa udi na uvumba, akihusishwa na ulipuaji wa ubalozi wa marekani jijini Dar miaka kumi na minane iliyopita… na pia kuwatazama kwa makini wote waliokuwa wamefika kwenye mazishi ya mtu yule hatari sana kuwahi kutokea kwenye historia ya Tanzania tangu vita dhidi ya kile kilichokuja kunadiwa na kutambulika kama “ugaidi” inadiwe duniani. Na ni kutokana na kulijua au kulitarajia hilo ndio maana hata kundi lililokuwa kwenye maziko ya Nouman Fattawi jioni ile pale kisutu ndilo lilikuwa dogo kuliko yale mengine manne yaliyokuwa pale makaburini siku ile.
Ni nani anayetaka kuhusishwa na gaidi?
Hakuna…isipokuwa kama ni ndugu wa damu au wa karibu sana…au ambaye yuko bega kwa bega na harakati za marehemu kiasi kwamba hajali iwapo na yeye atahusishwa na harakati hizo.
Na ni hawa wa mwisho ndio ambao wanausalama waliojipenyeza kwenye maziko yale, wakiwa wamejivika kanzu na vibaraghashia ili kufanana na waombolezaji halisi wa tukio lile, ndio waliokuwa wakijaribu kuwabaini kwenye mkusanyiko ule. Walitaraji kupata cha kuwaongoza kwenye azma yao ile kutoka kwenye mawaidha ya mwisho yatakayotolewa na yule shekhe atakapomaliza kuongoza maziko yale.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lakini pia walikuwepo watendaji wa shirika la ujasusi la marekani, C.I.A., ambao nao walikuwa ni weusi kama wengine pale kaburini, wakiwa wamejivika mavazi muafaka kwa tukio lile, na ambao pia walijua namna ya kuitikia dua zilizokuwa zikielekezwa na shekhe mazikoni pale. Lengo lao lilikuwa ni kujithibitishia kuwa kweli gaidi waliyekuwa wamemtamani kwa miaka mingi, hakika alikuwa amezamishwa ndani ya tumbo la ardhi jijini Dar…ili watakapopeleka ripoti huko kwenye makao yao makuu kule Langley, Virginia, wawe na ushahidi wa dhahiri kabisa kwa kile walichokishuhudia. Lakini vilevile, uwepo wao pale ulikuwa na lengo la kujaribu kuona iwapo kutakuwa kuna atakayepandwa na jazba pale makaburini na kubwabwaja kulipiza kisasi kwa wamarekani kwa kifo cha yule mshirika wao…au kuona yeyote ambaye angeelekea kuwa alikuwa akishirikiana na marehemu kwa namna moja au nyingine.
_________________
Maziko yaliendelea kama ilivyotakiwa. Kutokana na namna mwili wa marehemu ulivyoharibika, ulizikwa kwa shida sana, kilichozikwa kikiwa ni mabaki yaliyopatikana ya mwili wake. Baada ya mwili kuingizwa kaburini na kuzikwa, shekhe alitoa mawaidha kwa wafiwa kuwa wawe wastahamilivu, na kuwa Nouman Fattawi alikuwa ameshakunywa kifo chake kutoka kwenye gilasi ya umauti, ambayo sote hapa duniani tumeahidiwa kunyweshwa baada ya muda fulani…hivyo wote waliobakia pamoja na yeye mwenyewe walikuwa wana gilasi zao zinazowasubiri.
“Siku gani…saa ngapi…mahala gani na sisi tutaletewa gilasi zetu za umauti haijulikani. Mwenzetu kapelekewa gilasi yake Pakistani, lakini huenda kuna miongoni mwetu ambaye ya kwake inamsubiri hapo morogoro road akiwa njiani kutoka hapa mazikoni…basi na tushike ibada ndugu zangu, tumrejee mola wetu na tuchukulie kifo cha ndugu yetu, mpendwa wetu, mwana imani mwenzetu, raia mwezetu huyu…kuwa ni ukumbusho kwetu sisi tuliobaki…”
Shekhe alimalizia. Akapiga “Fat-ha”, kisha akaomba dua ndefu kwa lugha ya kiarabu. Watu wakaitikia dua. Alipomaliza akaruhusu watu kutawanyika kwa maelezo kuwa wanafamilia wamesema kuwa hakutakuwa na matanga nyumbani kwao. Hakuongelea hata neno moja kuhusu ugaidi wa Nouman Fattawi wala namna alivyokufa.
Maziko yakaisha.
Watu wakatawanyika.
Wanausalama wa taifa na wenzao wa C.I.A. wakaambulia kunufaika na mawaidha tu ya shekhe kwenye maziko yale.
Kutokea chini ya mti uliokuwa hatua kadhaa kutoka kwenye kaburi la jirani ambako napo maziko mengine yalikuwa yakiendelea, mtu mmoja mrefu aliyevaa suruali nyeupe ya kitambaa chepesi, viatu vyeusi vya ngozi bila ya soksi na shati jeupe la mikono mirefu ambalo hakulichomekea, wala hakuwa amelifunga vifungo kiasi cha kuionesha fulana nyepesi nyeusi aliyoivaa chini ya shati lile, alikuwa akifuatilia kwa makini sana kile kilichokuwa kikiendelea sio pale kwenye yale maziko aliyokuwa amesimama karibu nayo, bali kule kwenye maziko ya gaidi Nouman Fattawi.
Usoni alikuwa amevaa miwani ya jua iliyoficha macho yake, na kichwani alikuwa amevaa barghashia moja ghali sana. Kwa pale alipokuwa amesimama kando ya mti, uso wake ulikuwa umeelekea pale kwenye yale yaliyokuwa yakiendelea kwenye maziko yaliyokuwa jirani na ule mti aliokuwa amesimama chini yake, miongoni mwa wazikaji wengine, lakini macho yake yaliyokuwa nyuma ya miwani ile myeusi, na masikio yake vilikuwa kule kwenye kilichokuwa kikifanyika kwenye kaburi la Nouman Fattawi.
Na sasa alibaki pale pale chini ya mti wakati akiwatazama watu waliokwenda kumzika Nouman wakitawanyika, ilhali wale waliokuwa wakimzika marehemu wa kwenye kaburi alilokuwa amesimama kando yake, wakimalizia kumfukia yule marehemu wao pale kaburini.
Alibaki akiwa amesimama pale pale chini ya mti hata pale wale watu waliokuwa wakimzika yule marehemu mwingine walipomaliza na kutawanyika…
__________________________
Kiasi cha kama saa moja na nusu baada ya watu wote kutawanyika pale makaburini, kaburi la marehemu Nouman Fattawi likapata mgeni. Jua lilikuwa limeshazama na mwanga ulikuwa unatowekea kutoka kwenye hafifu kwenda kwenye kiza, na umbile la mtu likafika pale kaburini kama mzuka tu na kusimama wima upande ambapo miguu ya marehemu aliyelala chini ya tuta lile la udongo ingekuwapo.
Kutokea pale chini ya mti alipokuwa amechutama baada ya kuwa ameshasimama kwa zaidi ya saa tatu, tangu wakati mwili wa Fattawi unaletwa, unazikwa na kuachwa peke yake pale chini ya udongo, mtu mrefu aliyekuwa amevaa nguo nyeupe alimakinika vilivyo, huku akijibanza zaidi nyuma ya mti ule. Alijifuta machozi yaliyokuwa yakimtiririka na kukaza macho kukitazama kile kiumbe kilichokuwa kimesimama pale mbele ya kaburi la hayati Nouman.
Kutokea pale nyuma ya mti, jamaa alibaini vitu viwili. Kwanza yule mtu alikuwa ana umbo dogo…halafu, kutokana na mavazi yake, alikuwa ni wa jinsia ya kike.
Umakini wake ukapanda daraja.
Yule mwanamke alikuwa amevaa vazi la dera lenye rangi iliyojificha, aidha buluu au kahawia…au nyeusi… hakuweza kujua kwa urahisi kutokea pale alipokuwa. Alikuwa amesimama wima hali mikono yake akiwa ameishika pamoja kwa mbele, chini kidogo ya kitovu chake, na kichwa chake akiwa amekiinamisha kwa mbele kama anayeomba dua fulani kwa marehemu yule.
Jamaa alizidi kumfuatilia huku kwa wakati huo huo akitembeza macho huku na huko ili kuona iwapo yule mwanamama alikuwa amekuja na watu wengine pale makaburini muda ule. Hakuona mtu mwingine yeyote.
Kisha, ghafla kama alivyoibuka, yule mwanamke aligeuka na kuondoka pale kaburini kwa mwendo wa haraka.
Jamaa akajichomoa nyuma ya mti na kuanza kumfuata kwa mwendo wa tahadhari. Nje ya uzio wa makaburi yale mwanadada alikunja kulia na kutembea kwa mwendo mfupi kabla hajalifikia gari dogo ambalo jamaa hakuweza kulitambua mara moja lilikuwa ni la muundo gani, na dakika moja baadaye lile gari likaondoka eneo lile kwa mwendo mdogo.
Bila kujishauri zaidi, jamaa akafungua mnyororo uliokuwa umeifunga pikipiki yake aina ya boxer aliyokuwa ameipaki pale nje, na kuiingiza barabarani, akilifuata lile gari.
Baada ya kulifuata lile gari kwa muda, likikata mitaa kadhaa wa kadhaa ya jiji, hatimaye lile gari ambalo sasa alibaini kuwa lilikuwa ni Toyota Duet, liliashiria kukata kona kuingia kwenye jengo la hoteli moja nzuri sana ya ghorofa tano iliyokuwa maeneo ya sinza. Jamaa alipitiliza na pikipiki yake hadi kwenye maegesho yaliyokuwa nje ya hoteli ile, akamkabidhi mlinzi wa kimasai pale kwenye maegesho yale, na kuelekea kwenye lango kuu la hoteli ile, akiliona lile gari la yule dada bado likiwa pale nje ya geti la hoteli ile likisubiri geti lifunguliwe ili liingie.
Jamaa akapitiliza hadi sehemu ya mapokezi ya hoteli ile na kukuta watu kadhaa wakijiandikisha pale. Akaketi kwenye moja ya makochi ya pale mapokezi akiwa makini sana.
Dakika chache baadaye alimuona yule mwanamke mwenye umbo dogo akiingia mle hotelini na kupita moja kwa hadi kaunta ya mapokezi.
“Naomba ufunguo wangu dada…namba mia tatu na saba…” Dada alipaaza sauti kumwambia binti wa mapokezi. Binti alimkabidhi ule ufunguo na mwanadada akaongoza kwenye lifti iliyompandisha huko juu.
Jamaa akakunja uso. Hakuwa amepata kumuona yule dada hata siku moja hapo kabla, na wala ile sauti yake haikumletea kumbukumbu yoyote.
Lakini jambo moja lilimfunukia wazi wazi akilini mwake, na ndilo lililomfanya akinje uso.
Yule mwanamke aliitaja namba ya chumba chake kwa sauti makusudi…kwa faida yake yeye…ili yeye ajue kuwa yule dada yuko kwenye chumba namba mia tatu na saba.
Kwa nini?
Ina maana yule dada alijua kuwa yeye angekuwepo pale makaburini muda ule? Na alijua kuwa alikuwa akimfuata kwa pikipiki muda wote? Kama ndivyo…ni kwa nini basi?
Kwanza anahusika vipi na Nouman Fattawi yule dada?
Akili ilimuwamba mtu mwenye nguo nyeupe, au mzee wa chini ya mti.
Hatua gani ifuate sasa?
Jamaa alijiuliza akiwa ametulia kwenye kochi la pale mapokezi. Jibu lilijileta kwake dakika tano baadaye.
___________
Sehemu nyingine ya jiji, mzee Fattawi, baba wa hayati Nouman alikuwa kwenye wakati mgumu sana. Vijana waliombeba kwa gari lao wakati wakitokea makaburini akiamini kwa ni miongoni mwa waombolezaji kwenye msiba ule wa mwanaye aliyemkosa kwa miaka mingi, walikuwa wakimuongelesha maneno ambayo hakuwa akiyaelewa.
“Mzee…tunajua kuwa uko kwenye msiba mzito…sisi pia tuna masikitiko na kifo hiki. Letu kwako ni moja tu…elewa kuwa mwanao amekufa kishujaa, hivyo asitokee mtu yeyote akaja kukuletea habari za kuwa eti alikuwa gaidi…yeye amekufa kwenye njia iliyo sahihi. Na tuko wengine pamoja naye kwenye njia hiyo hiyo aliyoenda yeye…” Mmoja wao alimwambia. Mzee akapagawa.
“Wanangu…mbona siwaelewi? Mimi Nouman nilishamzika miaka zaidi ya kumi iliyopita! Nilimzika moyoni mwangu. Sikuwahi kuonana naye tangu nimeanza kusikia hizo habari za eti naye ni gaidi. Nilishahojiwa na watu wa kila aina mimi…na wote jibu langu limekuwa ni hili hili…sitambui swala la mwanangu kuwa gaidi na siamini…sio Nouman…sasa mmeshamuua, haitoshi kuwafanya muiache nafsi yake ipumzike jamani? Hebu nishusheni hapa! Nishusheni haraka tena!” Mzee alifoka.
Bila kuongea zaidi, jamaa walipaki gari kando ya barabara na kumteremshia njiani, nao wakatia moto gari lao na kutoweka.
Mzee wa watu akabaki akilia kwa uchungu peke yake barabarani…
_______________
Akiwa pale mapokezi, jamaa aliona watu wawili wenye asili ya kiajemi wakiingia mle hotelini huku wakiangaza macho huku na huko, wakiwa na mabegi yao ya safari. Muonekano wa watu wale mara moja ulimjuza kuwa hawakuwa wenyeji, lakini pia hawakuwa wema. Hakusubiri zaidi.
Aliinuka na kuziendea ngazi za miguu na kuzikwea haraka hadi ghorofa ya tatu. Huko akaanza kukisaka chumba namba mia tatu na saba. Alipokifikia alisimama nje ya mlango wa chumba kile na kutazama huku na huko, akaona korido ilikuwa tupu. Akajaribu kusikiliza iwapo kulikuwa kuna mienendo yoyote nyuma ya mlango wa chumba kile. Kulikuwa kimya kabisa.
Akajaribu kushika kitasa cha mlango ule, na ajabu mlango ukajisukuma ndani kirahisi kabisa.
Kengele za hatari zikaanza kugonga kichwani mwake. Akili ikamwambia ageuze pale pale, aondoke. Lakini udadisi ukamwambia vinginevyo. Akausukuma zaidi ule mlango na kujidhihirishia chumba kilichokuwa kimegubikwa na kiza. Haraka akaingia ndani na kuusukuma taratibu ule mlango nyuma yake na kuufunga. Alianza kutafuta kitasa cha kuwashia taa kando ya mlango ule wakati ghafla taa ya mezani ulipowaka moja kwa moja mbele yake. Alihemka huku akijisogeza pembeni kwa hamaniko, akitafuta pa kujificha.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tulia hivyo hivyo…!” Sauti nzito ilimkoromea, na hapo hapo ndipo alipomuona mtu mmoja aliyekuwa ameketi kwenye kochi lililokuwa upande wa pili wa chumba kile. Kutokea pale alipokuwa, aliweza kuona miguu tu iliyokuwa imekunjwa nne, na juu ya goti la mmoja kati ya miguu ile kulikuwa kuna mkono ulioshika bastola kubwa, ambayo ilikuwa imemuelekea yeye.
Duh!
Ule mwanga wa ile taa ulikuwa ukimmulika usoni, na hivyo hakuweza kumuona vizuri yule mtu mwenye bastola. Aligwaya kidogo.
“Weka mikono yako sehemu ambayo nitaiona kwa urahisi, na usifanye utundu wowote hapo!” Sauti ilimkoromea tena, na jamaa akahisi moyo ukimlipuka.
Ile sauti!
Alishapata kuisikia kabla…
Akasikia mchakacho hafifu jirani na pale alipokuwa amesimama, na ghafla, kabla hajaweza kugeuka vizuri kutazama kule ambako mchakacho ule ulitokea, akapigwa kwa nguvu na kitu kizito kichwani.
Mguno hafifu ukamtoka, naye akaenda chini bila kupenda…kiza kikatanda mbele ya uso wake…
No way!
Kwa namna isiyotarajiwa alijiachia kwenda chini na hapo hapo akalikwapua kwa nguvu sana zulia refu na jembamba lililokuwa limetandikwa pale juu ya sakafu ya marumaru ya chumba kile, likitambaa kutokea pale mlangoni hadi pale kwenye kiti alichokalia yule mtu mwenye bastola, na kubingirika nalo sakafuni.
Kile kiti kilichokuwa juu ya lile zulia kilipinduka pamoja na yule jamaa aliyekuwa amekikalia, ambaye aliachia mgutuko wa kutotarajia huku akienda chini na bastola yake. Jamaa hakuhangaika naye bali alijizungusha zaidi pale chini akiunyooshea mguu wake kule alipohisi kuwa pigo la kichwa lilipotokea, lakini akaambulia patupu, kwani mtu aliyempiga lile pigo aliwahi kuruka juu na ngwara yake ikapita patupu.
Pale pale chini akajigaragaza kufuata kule miguu ya mtu mwenye bastola ilipokuwa na kumkumba vibaya yule jamaa. Wote wawili wakajibabatiza kwenye kiti alichokuwa amekalia yule jamaa hapo awali.
Jamaa akawahi kujiinua lakini akakutana na teke zito la ubavu kutokea nyuma yake. Akagumia huku kwa pembe ya jicho lake akimuona yule mtu mwenye bastola akiinuka ilhali bado ile bastola yake ikiwa mkononi mwake. Jamaa akachanganya miguu huku akijirusha nyuma kana kwamba alikuwa akicheza dansi isiyojulikana, kisha kwa namna ya ajabu mguu wale ukafyatuka kama kofi kali la mkono na kuipangusa vibaya ile bastola kutoka mkononi mwa yule jamaa.
Heh!
Hapo mshirika wa yule mtu mwenye bastola alimrushi teke jingine kali sana, na kwa mara nyingine mzee wa chini ya mti alijigeuza kwa wepesi wa ajabu mithili ya mtu aliyekuwa akicheza dansi, na pigo la yule mwanadada mwenye umbo dogo likapotea, naye akayumba kibwege na kujikuta akiwa amedhibitiwa kwa namna ambayo wala hakuielewa.
“Basi inatosha nyinyi…ebbo!” Jamaa alibwata, na yule mtu aliyekuwa ameshika bastola hapo awali alibaki akiwa amepiga mduwao usiosemeka pale alipomshuhudia yule jamaa akiwa amemkaba kabali kali sana yule mwanadada huku akiwa amemuwekea kisu kooni.
E bwana we!
Walitazamana.
“Tulia mzee…huhitaji kabisa kuanzisha mambo haya na mimi nakwambia…nielezeni ni nini kinaendelea hapa?” Mzee wa chini ya mti alisaili huku akiwa amemkazia macho makali sana yule bwana aliyekuwa na bastola hapo awali.
Jamaa alikuwa akimtazama kwa makini na kutoamini.
“Oh…okaayy…tulia basi…tulikuwa tunataka kuongea tu…!” Yule bwana alisema kwa mashaka huku akiwa ametawanya mikono yake kuonesha kuwa hakuwa na silaha yoyote mikononi mwake muda ule.
“Hivi ndivyo mnavyoongea na watu?” Mzee wa chini ya mti akasaili.
“Sasa unaniachia au huniachii wewe?” Yule dada naye alikoroma kwa hasira. Jamaa alimpapasa mwilini haraka kwa ule ule mkono wake ulioshika kisu huku bado akiwa amemkaba.
“Toa hiyo bastola uloificha pajani…taratbu sana, kisha tuongee!” Jamaa alimkoromea yule dada.
“Dah!” Dada alinywea na kutekeleza kwa kupitisha mkono ndani ya ile nguo iliyoonekana kuwa kama dera, lakini kumbe ikiwa ni suruali iliyoshonwa kwa mtimbo wa bwanga pana aliyoivaa chini ya blauzi ya kitambaa kile kile cha ile suruali, ambayo ilishonwa kwa mtindo wa namna madera yanavyoshonwa, ila yenyewe ikiishia sehemu baina ya kiuno chake na magoti yake.
Akaitupia sakafuni ile bastola.
Jamaa akamsukuma mbele kwa nguvu kumuendea yule bwana na wale washirika wawili wakapamiana vibaya. Walipojiweka sawa, jamaa alikuwa ameketi kitandani mle ndani huku akiwa amewanyooshea ile ile bastola iliyokuwa kwenye uvungu wa paja la yule mwanadada, ilhali kile kisu alichokuwa nacho hapo awali hakikuwepo tena mkononi mwake.
Loh!
Walikodoleana macho.
“Anzeni maongezi!” Jamaa alisema kwa ukali.
________________
“Ulikuwa unatafuta nini pale makaburini wewe?” Bwana aliyekuwa na bastola hapo awali alimuuliza.
“Hatuendi hivyo…utambulisho kwanza…sauti yako naijua, lakini sura yako hainiletei kumbukumbu yoyote…ni nani wewe?” Jamaa alisaili.
Swali lake lilionekana kumzidishia udadisi mkubwa yule bwana, aliyepata umri wa kama miaka hamsini au hamsini na miwili hivi.
“Hunikumbuki?”
“Sikujui! Ila sauti yako…? Sauti yako si ngeni kabisa masikioni mwangu…ni nani wewe? Na huyu dada…ni nani? Mnanitakia nini?”
“Mnh! This is interesting…kwamba hunikumbuki kabisa ila sauti yangu unaikumbuka?” Babu alisaili tena.
“Hebu acha mambo ya kis…nge hapa wewee! Mi nakuuliza maswali unajitia kukomaa na hilo la kuwa sikukumbuki? Nimekwambia sikujui na nataka nipate maelezo ya mchezo huu haraka sana!” Jamaa alimjia juu.
“Ondoka hapa jijini wewe, usiwe mjinga! Hutakiwi kuwepo hapa na wala hukutakiwa kuwepo kule makaburini leo hii…!” Yule dada alidakia kwa hasira.
“Excuse me…na wewe ni nani tena?” Jamaa alihoji zaidi.
“Okay Grey, nadhani tunahitaji kuwekana sawa kwanza hapa…” Yule mtu mzima alisema, na jamaa akaonekana kumakinika baada ya kusikia akitajwa kwa jina lake.
“Unalijua jina langu?”
“Na zaidi ya hapo…tutulie, tuwekane sawa…” Mzee alimjibu.
“Sawa…anza maelezo.”
“Naitwa Benson Kanga…”
“Jina geni masikioni kwangu hilo…”
“Si ajabu kuwa hivyo, lakini ridhika tu kuwa hilo ndio jina langu na niko upande wako.”
“Mnh, sasa kama mko upande wangu…kwa nini hamkunijia kistaarabu zaidi?”
“Ni ngumu kidogo kuelezea…ila tu ni kwamba baada ya kifo cha Nouman Fattawi…na mchango wako hadi kufikia kwenye kifo kile, hukutakiwa kabisa kuonekana popote pale ambapo japo mzuka tu wa Nouman ungekuwepo. Uwepo wako pale makaburini leo ulikuwa unahatarisha sana swala hili. Watu wengine watapoteza maisha yao bure…” Mtu aliyenadi kuwa ni Benson Kanga alimwambia.
Yule mtu aliyetambuliwa na Benson kwa jina la Brey alimung’unya midomo kwa namna iliyoonesha kuwa alimuelewa sana, ingawa kama angewepo mtu mwingine anayewasikiliza wakati ule ambaye si katika wao, hakika asingeelewa kitu.
“Ni kweli, lakini ilikuwa ni muhimu kujihakikishia kuwa ni kweli Nouman Fattawi amezikwa, Benson.”
“Haikuwa lazima uwepo pale makaburini ili kupata uhakika wa hilo. Mimi kazi yangu ni kuhakikisha kuwa swala zima la Nouman Fattawi linabakia kuwa limezikwa. Nouman Fattawi anatakiwa asahaulike kabisa kwenye uso wa dunia…uwepo wako jijini na hususan pale makaburini leo hii hausidii sana kwenye hilo.” Benson Kanga alimwambia.
“Kwa hiyo mliniona nikiwa pale makaburini?”
“Tulikuhisi kuwa ni wewe pale ulipoingia makaburini ila hatukuwa na uhakika…umebadilika sana katika miaka michache ya hapa kati, Brey…lakini baada ya maziko hatukukuona ukitoka…tukapata wasiwasi. Ndio ikabidi nimtume msaidizi wangu arudi pale kukuchomoa mle makaburini”
“Mlijua kuwa nimo mle?”
“Ndio jibu pekee lililopatikana Brey…tumeona mtu anayeshabihiana na wewe akiingia kisha akatupotea mle mle makaburini. Tukaweka kambi kwenye milango yote miwili ya kutokea nje ya makaburi, na bado hatukukuoana ukitoka…ikabidi tubahatishe kwa njia ile. Na imesaidia…”
Brey Jabba alitikisa kichwa.
“Hivyo ndivyo ilivyokuwa…ilibidi tujihakikishie kuwa ni wewe kweli, ndio maana ikabidi tujihami kwa bastola namna ile pale ulipoingia humu ndani…”
“Nimeelewa.”
“Basi sasa fanya utoweke hapa jijini…ukae mbali sana na jiji...huo ndio ulikuwa utaratibu. Hatutaki ya Fattawi yaje yakukute…kazi yako umeifanya kwa hiyo sasa nenda ukaanze maisha mapya nje ya jiji. Tayari umeshaandaliwa pa kwenda…natakiwa nihakikishe umefika huko na nikuache huko. Sahau kila kitu kuhusu kazi uliyoifanya kwenye swala la Nouman Fattawi!” Benson alimwambia.
“Nadhani mmechelewa…” Brey Jabba alimjibu.
“Ukimaanisha nini?”
“Kuna watu nimewaona wakiingia hapa hoteini…kama dakika tano baada ya huyu msaidizi wako kuingia…wamenitia mashaka sana.”
Wenyeji wake wote wawili wakamakinika.
“Unamaanisha nini…? Ni watu gani?”
“Wana asili ya asia wale jamaa…kimuonekano tu ni kama wapakistani, au wa-afghanistan…lakini sio waarabu. Hii hoteli iko sinza, sidhani kama watu kama wale ni wa kuja kukaa hoteli ya sinza...wangekaa angalau kariakoo huko au katikati ya jiji…” Brey Jabba alisema.
Benson aliguna.
“Unamaanisha nini?”
“Kwamba wao, kama mimi, waliweza kumfuata huyu msaidizi wako kutoka huko alipokuwa hadi hapa…”
“No! Hilo haliwezekani! Nilikuwa makini sana…” Mwanadada alimaka, na kuendelea, “…mbona wewe nilikuona wakati unanifuata na nilikuacha kwa kuwa nilitaka uje hapa!”
“Sawa. Ulimakinika na mimi…hukuweza kumakinika na wale wengine…jamaa wamo humu hotelini nawaambia.” Brey Jabba alisema.
“Lazima tutoweka hapa…sasa hivi!” Benson alisema huku akiinuka. Akaganda kwenye hatua zake pale wote mle ndani waliposikia mlango wa kile chumba walichokuwamo ukabishwa hodi kutokea nje.
Wakatazamana, wakiwa kimya, macho yakiwatembea.
Hodi ikabishwa kwa mara ya pili, kwa nguvu zaidi.
“Wamefika.” Brey Jabba alisema kwa utulivu wa kuogopesha…
“Oh, Shit!” Benson Kanga alilaani huku akijibingirisha sakafuni, akaikwapua ile bastola yake iliyokuwa imetupwa pale sakafuni baada ya kupigwa teke kutoka mkononi mwake na Brey, na kujipanza ukutani huku akiwa ameielekezea ile bastola yake kule mlangoni kwa mikono yake yote miwili.
Muda huo huo Brey akamrushia yule dada mwenye umbo dogo ile bastola aliyompokonya hapo awali. Dada akaidaka kizoefu mikononi mwake, na hapo hapo akajitupa nyuma ya kitanda, akabaki akiwa ameinyooshea ile bastola kule kule mlangoni kwa mikono yake yote miwili kutokea chini ya tendegu la kitanda kile, mwenyewe akiwa katikati ya tendegu lile na ukuta wa chumba kile.
Mlango ukabishwa tena kwa nguvu zaidi pasina mtu aliyekuwa kule nje kusema lolote kutambulisha uwepo wake au nia ya kubisha kwake mlangoni pale.
Brey Jabba aliwaashiria wale washirika wawili aliokurupushana nao mle ndani dakika kadhaa tu zilizopita kuwa watulie, huku kwa mkupuo mmoja akiunyofoa waya wa pasi iliyokuwa mle chumbani kutoka kwenye kichwa cha pasi ile, akiiacha ile sehemu inayochomekwa kwenye soketi ukutani ikiwa kama itakiwavyo. Haraka mno alizisonga nyaya za umeme wa pasi ile kwenye kitasa cha chuma cha mlango ule huku bado ule waya ukiwa umechomekwa kwenye soketi iliyokuwa ukutani kando ya mlango.
Akaiwasha ile swichi ya umeme, kisha hapo hapo akaitumia ile pasi kupasua kitufe cha kengele ya dharura ya moto kilichokuwa mle chumbani, na hapo hapo ving’ora viikaanza kurindima kwa fujo mle hotelini, kama kwamba kulikuwa kuna moto, naye akajirusha upande wa pili wa mlango ule na kujibanza.
Kizaazaa!
Kutokea kule nje, mtu alikamata kitasa cha mlango ule na hapo hapo ukelele wa mshituko na maumivu vikasikika baada ya mtu yule kupigwa shoti kali za umeme huku akijibamiza pale mlangoni, mayowe na vishindo vya wapangaji wengine vikasikika huko nje kutokana na ving’ora vile vya tahadhari ya moto.
Mlango ulisukumika ndani kwa nguvu na mtu mmoja akabwagika kwa kishindo mle ndani na kubaki akitetemeka mithili ya mwenye kifafa. Kabla ya yeyote kati ya waliokuwa mle ndani hajatabahi, mtu wa pili alijitupa mle ndani kutokea kule nje huku akimimina risasi za mfululizo pasina milipuko yoyote kusikika. Benson Kanga alipiga ukelele, Brey Jabba akatupa teke kali lililokuwa likimuendea shingoni yule jamaa wa pili lakini ni muda huo huo ambapo yule mvamizi aliinama kwa lengo la kumchukua yule mwenzake pale chini huku kwa mkono mmoja akiendelea kumwaga marisasi pande zote mle ndani, ilhali kwa mkono mwingine akiikamata sehemu ya mkanda wa suruali ya yule mwenzake aliyebwagika kifudifudi pale sakafuni na kuanza kumvutia nje.
Teke la Brey likasalimiana na hewa.
Bastola ya Benson Kanga ililipuka mara moja, na ya mara pili.
Brey aliruka kutoka pale kando ya mlago na kuipiga teke ile bastola kutoka mkononi kwa yule mvamizi, nayo ikatupwa pembeni.
Jamaa alimgeukia kwa kiwiko kikali lakini Brey alijizungusha kama anayecheza dansi aina ya “waltz”, kiwiko cha mvamizi nachi kikasalimiana na hewa, na Brey akaikamata sehemu ya mbele ya koti la yule jamaa na kumvuta mbele kwa nguvu huku akimuinulia goti lake kwa lengo la kuubabatiza uso wa yule mvamizi kwenye goti lake, lakini jamaa akawahi kuweka mikono yake kuukinga uso wake. Brey akamshushia kiwiko kwa nguvu nyuma ya shingo na jamaa akasukumwa chini kama mlevi, lakini hapo hapo akaibinukia bastola yake iliyokuwa pale chini, akaikwapua na mlipuko wa tatu bastola ukasikika mle ndani.
Jamaa akaachia yowe la maumivu huku akiitupa ile bastola aliyoinyakua na kujishika upande wa kichwa chake, damu ikimchuruzika kutoka sikioni, na hapo yule dada mweye umbo dogo alijiinua mzima mzima kutoka kule nyuma ya kitanda na kumtupia risasi ya pili yule mvamizi. Lakini yule mwenzake naye akawa amezinduka na kumsukumia kile kitanda kwa miguu yake, akambabatiza nacho ukutani, na risari ya yule binti ikaenda hewani na kuchimba dari sanjari na mlipuko wa nne wa bastola mle ndani.
Mvamizi wa pili alimrukia Brey mzima mzima, lakini kwa mara nyingine Brey akijigeuza mithili ya wale “El Matador”, wanaocheza mchezo wa ng’ombe wa kule Hispania, na kumpisha kistadi yule mvamizi ambaye alipitiliza kama ng’ombe kweli, na kujipigiza vibaya ukutani kando ya mlango na kusambaratika sakafuni.
Brey aliunguruma kama simba na kumgeukia yule mtu wa kwanza aliyepigwa shoti ya umeme hapo mwanzo, lakini jamaa naye alikuwa ameshajiinua na akaruka kwa hatua moja hadi kitandani, akadunda na kurudi tena sakafuni, akitua nyuma ya Brey. Brey alijigeuza kwa wepesi wa ajabu huku akichanganya miguu, lakini yule jamaa hakuwa tena na kasi, ari wala nguvu ya kuendelea na mapambano. Alimkumba mwenzake kutoka pale kando ya mlango na kutoka naye mbio nje ya chumba kile, wakijichanganya na watu wengine waliokuwa wakiishia pale kwenye korido wakikimbilia ghorofa za chini za hoteli ile.
Brey akawatukania mama zao wale wavamizi kwa hasira na kuwageukia wale wenzake mle ndani huku akiufunga mlango wa chumba chao kwa kisigino cha mguu wake.
Akabaki ameduwaa.
__________________http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwenye eneo la mapokezi la hoteli ile taharuki ilikuwa imetawala. Meneja na watendaji wake walikuwa wakijitahidi kuwatuliza wateja wao waliopanga kwenye hoteli ile, ilhali wafanyakazi wanaohusika na maswala ya umeme kwenye lile jengo wakijaribu kutafuta hitilafu ilikuwa imetokea wapi, Imani ikiwa ni kwamba ni hitilafu ya umeme ndio iliyosababisha vingo’ora vile vya tahadhari ya moto.
Katikati ya sintofahamu iliyoshamiri katika eneo lile, watu wawili wenye asili ya kiajemi walichomoza kutokea kwenye ngazi za kuteremka kwa miguu na kufika pale mapokezi, kila mmoja akiwa na begi la wastani mkononi. Waliangaza huku na huko, kisha, huku nyuso zao wakiwa wamezifunika kwa miwani za jua ingawa muda ulikuwa ni usiku, walitoka nje ya hoteli ile huku wakiwa wamenuna, mmoja kati yao akichechemea kwa taabu sana. Waliingia kwenye gari lao aina ya Range Rover na kuondoka eneo lile kwa kasi.
Mle garini, yule aliyekuwa kwenye kiti cha abiria alikuwa ameshikilia kiganja chake kilichobabuka baada ya kunyanyaswa na shoti ya umeme mkali pale alipojaribu kushika kitasa cha mlango wa chumba namba mia tatu na saba kwenye ile hoteli.
“Who the hell was that guy?” Alifoka kwa hasira huku akiupapasa mkono wake uliobabuka, akimaanisha kuwa anataka kujua kuwa yule mtu waliyekabiliana naye mle ndani alikuwa nani.
“Nadhani ndiye hasa tuliyemkusudia…ila ametuzidi mahesabu kidogo tu, mjukuu wa ibilisi yule!” Mwenzake alimjibu kwa hasira huku akiendesha gari lile kwa kasi, kuelekea maeneo ya katikati ya jiji.
“Ulipata kumuona sura yake vizuri…ndiye yeye kweli?” Mwenzake alihoji.
“Taarifa zetu zimetuongoza moja kwa moja mpaka pale alipokuwa…tatizo ni wale watu aliokuwa nao mle ndani…ni kina nani wale?” Mwenzake alisema na kuuliza kwa utulivu wa ghadhabu.
“Wale sio ishu Mukri…kazi yetu ni yule jamaa…na tumeshapoteza nafasi moja…”
“Shaka ondoa patna…” Mukri alimjibu mwenzake huku akiendesha gari kwa utulivu, na kuendelea, “…leo kanusurika, lakini kila siku sio leo…tutakapokutana naye tena ndio utakuwa mwisho wake…”
Yule mwenzake alisonya kwa hasira.
“Lazima tumzime huyu mtu tutoweke hapa…viza yetu ni ya miezi mitatu tu hapa Tanzania…sina nia ya kumalizia miezi yote mitatu kwenye nchi hii aisee!” Jamaa aliyebabuka mkono alisema.
Mwenzake aliuma midomo kwa ghadhabu, lakini hakujibu kitu.
_________________
Benson Kanga alikuwa ametawanyika sakafuni akiwa amekodoa macho kwa mshangao wa kudumu, damu ikimchuruzika kutoka sehemu ya kifua chake ilhali ile bastola yake ikiwa bado mkononi mwake.
“Nooo, Benson, NOOOH!” Dada mwenye umbo dogo alipiga ukelele huku akimkimbilia yule mwenzake kutokea ubavuni kwa kile kitanda alichokuwa amebabatizwa nacho hapo awali.
Brey Jabba aliitazama ile hali, na mara moja akajua kuwa hakukuwa na la kufanya kuhusu yule mtu aliyejitambulisha kwake kwa jina la Benson Kanga.
Yule dada alimtikisa Benson kwa nguvu huku akilia, lakini uhai ulikuwa umeshamtoka yule bwana.
“Amekufa huyo…tuondoke hapa haraka sana…” Brey alimwambia kwa kuhimiza.
“No! Hatuwezi kumuacha hapa! Haiwezekani…” Dada alikuja juu.
“Okay, endelea kumsubiri tu hapo hapo…mimi sikutwi na wanausalama nikiwa na maiti humu ndani bi mdogo…kwa heri!” Brey alimjibu huku akigeuka. Alifungua mlango na kuchungulia nje. Korido ilikuwa tupu.
“Huwezi kuniacha humu namna hii wewe!” Dada alimaka. Brey akamgeukia na kurudi ndani, akiufunga tena mlango.
“Look, bibie…sikujui…hunijui…nilikuwa naelekea kujuana nawe zaidi lakini naona hujui tunapambana na watu wa aina gani…naondoka!” Alimkoromea.
“Una uhakika sikujui mimi wewe?” Binti alimkoromea.
“Sio ishu…wako wengi wanaonijua zaidi ya wewe…na nimejuana na wengi kabla ya wewe…nijuali ni kwamba nahitaji kuendelea kuishi, na kukaa hapa hadi kukutwa na wanausalama au wambea wengine wa kawaida hakutanihakikishia uhai wangu…tuondoke hapa mwanamama…hatuna tunaloweza kulifanya kuhusu Kanga kwa sasa!” Brey alimwambia.
***Makubwa!
Mwanadada aliinuka na kujifuta machozi.
“Okay…tunaenda wapi sasa?” Alimuuliza.
Badala ya kumjibu, Brey aliuendea ule mwili na kuusachi haraka haraka. Akatoa pochi ya yule mtu iliyokuwa na vitambulisho kadhaa pamoja na kisu kilichokuwa kimefutikwa kiunoni kwa yule marehemu. Aliinuka na kuvishindilia mfukoni mwake vile vitu.
“Tutajua mbele ya safari….twen’zetu!” Alimjibu huku akiongoza na kufungua mlango. Baada ya kuchungulia nje kidogo, alitoka nje bila ya kugeuka. Binti akamfuata nyuma kwa mwendo wa haraka.
Brey aliongoza usawa wa sehemu ya kujisaidia, akijipenyeza miongoni mwa wananchi waliorundikana pale mapokezi.Mwanadada akamfuata kule kule na walipofika sehemu ambapo ilibidi wagawane njia kila mmoja aelekee kwenye maliwato ya jinsia inayomhusu, Brey alimgeukia.
"Una sehemu ya kwenda kutoka hapa?" Alimuuliza.
"Nyu...nyumbani kwangu tu sasa..."
"No...usiende nyumbani...tafuta nyumba ya wageni leo...kama una mume utajua namna ya kujieleza....mi ntakufuata nyuma kwa pikipiki..." Alimjibu haraka na kugeuza kurudi kule mapokezi, ambako alikuta watu wakielekezwa kutoka nje ya hoteli ile. Bila kujali kuwa yule dada alikuwa akimfuata au la, alitoka moja kwa moja nje ya geti la hoteli ile, na dakika tano baadaye aliliona gari la yule dada nalo likitoka nje ya geti lile. Akaanza kulifuata kwa nyuma akiwa kwenye pikipiki yake.Mwendo wa kama saa moja baadaye dada aliingiza gari kwenye maegesho ya magari ya kulipia yaliyokuwa kwenye ofisi ya chama tawala maeneo ya Kigogo. Brey naye akaifunga kwa mnyororo pikipiki yake kwenye moja ya nguzo za zege kwenye jengo la ofisi ile, wakamlipa mlinzi ipaswavyo kisha wakatoka kwa miguu nje ya uzio wa eneo lile la kulazia magari.
"Nini kinaendelea...?" Brey alihoji huku akimfuata yule dada aliyekuwa akitembea kwa mwendo wa haraka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Tunaenda gesti...si ndivyo ulivyotaka?" Alijibiwa.
"Vipi kuhusu mumeo...?"
"Si kazi yako!" Alijibiwa tena.
Akapiga kimya na kuendelea kumfuata huku akiwa makini sana na kila waliyekuwa wanapishana naye humo njiani.
______________________
Dakika chache baada ya watu wote kutolewa nje ya hoteli ile, gari la kikosi maalum cha usalama lilifika pale hotelini kwa makeke na askari sita waliteremka na kuingia ndani ya hoteli ile. Meneja alihamanika. Hakuwa amepiga simu kuita wana usalama wowote hadi kufikia muda ule na alikuwa akiuliza kwa wahka ni nini ilikuwa azma ya ujio wa wale askari pale.
"Watu wote wabaki nje...tunahitaji kufanya uchunguzi ndani ya jengo hili!" Kiongozi wa wale askari waliovalia nguo maalum za makabiliano zilizotisha alisema kwa mamlaka.
"Kwa...kwa vipi? Hapa palilia king'ora tu kilichoashiria kulikuwa kuna moto jengoni...lakini sasa tunaamini kuwa ilikuwa ni bahati mbaya tu...hakuna moto wowote...na..." Meneja alitoa maelezo.
"Mnataka kusema kuwa hamkusikia milipuko ya bastola humu ndani?" Yule askari alihoji zaidi, na meneja akahamanika.
"Ah..kuna mipuko ilisikika wakati na ving'ora vinaendelea kulia...lakini...tulidhani ni sehemu ya hitilafu iliyosababisha moto...kumbe ni bastola? Mungu wangu! Sasa...?" Meneja alibwabwaja kwa woga.
"Okay...kwa hiyo hamna mlilogundua mpaka sasa..?"
"Hakuna...ndio tulikuwa tunaendelea..."
"Basi wote subirini nje...!" Yule askari aliamuru, na meneja kwa woga mkubwa akatii...akiwaona wale askari wakipanda lifti ilhali wengine wakipanda kwa miguu...mmoja wao akiwa na fuko kubwa sana jeusi la plastiki ngumu.
Hakuelewa.
Na alizidi kutoelewa pale wale askari walipotoka kule ndani, nusu saa baadaye, wakiwa wamebeba furushi kubwa na refu kwenye lile fuko ambalo awali lilionekana tupu. Ilikuwa ni kama kwamba kulikuwa kuna mwili wa binadamu kwenye like fuko.
"Heh! Ni...ni nini hicho...?" Meneja alihoji kwa wahka.
Kiongozi wa wale askari alimkamata bega na kumvutia pembeni wakati wale wenzake wakiuingiza kwenye lile gari lao aina ya Land Rover lililokuwa mwenye muundo wa pick-up bila kumjali.
"Hakuna tatizo lolote...rudisha wateja wako hotelini wakalale..." Alimwambia.
"Aaah! Inawezekanaje hii? Na vipi kuhusu hiyo milipuko ya bastola mliyosema? Mmegundua nini bwana?" Meneja alisaili.
"Inaelekea ilitokea nje ya jengo hili...lakini kuna chumba kimoja kimeathiriwa kwa risasi...ila hakuna tatizo lolote..." Jamaa lilimjibu.
"Na...ule...ule mwili vipi?" Meneja alihoji huku akioneshea kule kwenye gari. Jamaa lilimuacha na kuingia kwenye gari sehemu ya mbele, kando ya dereva.
"Mwili gani?" Alimuuliza huku gari liking'oa taratibu na kuchanganganya kasi kutoka eneo lile.
Meneja alibaki "gaa".
________________________
“Okay, sasa hebu tuwekane sawa…pale hotelini ulisajili chumba wewe…? Au Benson? Maana nimekuona ukijinadi kwa herufi kubwa sana pale kuwa upewe ufunguo wa chumba chako, namba mia tatu na saba…ina maana wale wahudumu wa hoteli wote wamekuona sura yako na yumkini ya Benson…” Brey alianza mara baada ya kuwa wamejifungia chumbani.
Walikuwa wamepanga chumba kwenye nyumba ya wageni ya hadhi ya wastani iliyojificha maeneo ya kule kule Kigogo.
“Una wasiwasi kuwa wakiukuta mwili wa Benson mle chumbani maaskari wataanza kunisaka sio?” Mwanadada alimuuliza huku akiwa amekunja sura kwa tafakuri, maswala ya kumlilia Benson yalikuwa yameisha, ingawa macho bado yalikuwa yamemuwiva na yamemvimba.
“Ndio maana yake…tatizo linalotuandama peke yake ni kubwa, sasa ikija kuingiliana na swala la maaskari tena, itakuwa…”
“Hakuna askari atakayefuatilia swala hili.” Dada alimkatisha. Brey akamuinulia nyusi kwa kuuliza.
“Ukimaanisha nini? Yaani wale wahudumu wa hoteli wakute maiti mle chumbani, halafu wasiitarifu polisi?”
“Kama kila kitu kitaenda sawa hawatakuta mwili wala damu mle chumbani…” Mwanadada alijibu, na Brey aliyejijengea tabia ya kutoshitushwa na mambo kirahisi akatumbua macho kwa mshangao.
“Ongea zaidi mwanadada…sijaelewa hapo!” Alimwambia.
Mwanadada akaguna, na kutazama pembeni, kisha akamgeukia.
“Nilipokuwa kwenye gari nilipiga simu moja…na nikawaeleza watu tunaofanya nao kazi juu ya kilichotokea…wataendea kumchukua Benson bila tamasha yoyote pale…na hakuna maswali yatakayoulizwa…sitasakwa mimi wala wewe kuhusika na kifo kile…”
Ikawa zamu ya Brey kuguna sasa. Akabaki akitikisa kichwa huku akimung’unya midomo, akiieneza akilini mwake taarifa ile.
“Kwa hiyo nyie ni akina nani…yaani ni taasisi gani ya dola, au usalama, au ujasusi, au chochote kinachofana na hivyo?” Hatimaye alimuuliza.
Kwa mara ya kwanza mwanadada akatabasamu.
“Kuna kichekesho chochote hapo?” Brey alimuuliza.
Tabasamu likazidi kuwa pana.
“Hapana…ni namna tu ulivyouliza hilo swali ndio iliyonifanya nitabasamu…”
“Na sasa kwa kuwa swali limeshakuchekesha, naomba jibu…”
“Sisi ni akina nani sio muhimu…muhimu ni wewe kuondoka hapa jijini haraka sana…ili wengine tuendelee na maisha yetu.” Dada alimjibu kwa kiburi.
Brey akamkata jicho.
“Okay, tutalipatia ufumbuzi tu hilo naamini…haya, wewe ni nani?”
“Hilo ndo uloliacha…”
“Enh?”
“Naitwa Sandra…na niko upande wako…”
“Sawa Sandra nimefurahi kukufahamu…tupange mikakati sasa. Natakiwa niondoke vipi hapa jijini?”
“Kila kitu kilikuwa kimeandaliwa na Benson…itanibidi nikafuatilie kesho kwa wenzangu, na kisha nije nikupe maelekezo…na mpaka hiyo kesho, hutatoka nje ya chumba hiki…”
“Unawasahau wale wahindi koko waliotuibukia kule hotelini? Tunajipanga vipi kuhakikisha kuwa hawatuibukii tena?”
“Sina namna ya kuhakikisha hilo, lakini nadhani ukiwa umejificha huku haitakuwa rahisi wao kukuona…yumkini pale walitubahatisha kutoka makaburini…na baada ya kuwakurupusha namna ile kule hotelini, itawachukua muda kuja kutushitukia tena mahala tulipo…ndio maana wewe inabidi utoweke haraka kabla hawajakushitukia tena…”
“Okay, na iwe hivyo basi!” Brey alisema, ilhali bado akiwa ana kiu ya kujua zaidi.
Haikuwa…
Mukri, yule mvamizi aliyebabuliwa na shoti za umeme pale alipojaribu kufungua mlango wa chumba namba mia tatu na saba kwenye ile hoteli iliyokuwa kule Sinza, alisonya kwa mara bila shaka ya saba usiku ule. Alibaki akimtazama mwenzake akimalizia kujibadika plasta sikioni kwa msaada wa kioo kilichokuwa kwenye chumba cha yule mwenzake.
Walikuwa kwenye nyumba ya kupanga maeneo ya Kariakoo, nyumba ya ghorofa nne zilizogawanywa kwa fleti kadhaa za kujitegemea kwa ajili ya kupangishwa. Wengi wa wapangaji wenzao kwenye jengo lile walikuwa ni raia wa kichina waliokuwa nchini kwa kuendesha biashara mbali mbali jijini hususan eneo lile la Kariakoo. Wao walikuwa wamepanga fleti moja yenye vyumba viwili ndani ya jengo lile. Kwa kuwa mwenyewe nyumba alikuwa raia wa Pakistani aliyeishi nchini miaka mingi, iliwawia rahisi wao kupata mawasiliano yake tangu wakiwa Pakistani, na kuweza kupata uhakika wa vyumba ndani ya nyumba ile tangu wakiwa kule kwao. Hili lilikuwa zuri sana kwao kwani liliwapunguza ulazima wa kuacha taarifa zao kwenye hoteli ambayo vinginevyo ingebidi wafikie, pamoja na kuwa pasi walizotumia kusafiria hata hivyo zilikuwa bandia.
“Si unajua hiyo haisaidii kitu, eenh?” Mwenzake alimwambia huku akigeuka kutoka pale mbele ya kioo na kumtazama. Huyu alikuwa mrefu kama Mukri, lakini sio mwembamba kama yule mwenzake. Yeye alikuwa amejengeka kimazoezi zaidi.
“Hii ilipaswa iwe ni kazi ya kuingia na kutoka tu Jarraar, sasa ona jinsi tulivyofanywa. Nusura yule mwanamke akulipue bichwa hilo kwa risasi pale! Na mimi…? Ona jinsi walivyonifanya mkono wagu!” Mukri alilalama.
Jaraar Bakhtiyaar alimtazama mwenzake pale kwenye mkono alipotoka kumfunga plasta maalum baada ya kuwa amempaka dawa kutoka kwenye mkoba wake wa safari ambao daima huwa haukosi dawa mbali mbali za dharura.
“Bado naamini kuwa ni swala la kuingia na kutoka tu hili Mukri…tumeingia humu siku ngapi…? Nne tu, right? Ndani ya siku nne tumeweza kumnasa mlengwa wetu…sidhani kuwa baada ya hapa atakuwa na siku zaidi ya mbili za kupumua huyu…tumeshafanya kazi ngapi ngumu zaidi ya hii?” Alimjibu mwenzake na kumuacha na swali.
“Oh yeah…nadhani hii kazi tuliidharau baada ya kusikia kuwa jamaa mwenyewe ni mtanzania…”
“Yap, hilo ni hakika…”
“Funzo kubwa sana hili…mtu mpaka akiletwa kwetu maana yake si wa kumdharau hata kidogo huyo…hata kama ni mtanzania!” Mukri alisema kwa hasira.
“Kabisa, aisee…”
“Na kibaya zaidi…yeye yuko kwenye uwanja wa nyumbani hapa…siye tuko ugenini…” Mukri aliendelea.
“Aaah Mukri…tumeua watu wenye ulinzi katikati ya miji mikuu kama Paris, New York na Nairobi…tumemundoa mlengwa mwenye mabodigadi wengi tu katikati ya Syria…huyu hawezi kuwa kikwazo kwetu eti kwa kuwa yuko kwao bwana! ”
“Hapana muuaji wangu…huko kote ulipopataja tulishawahi kufika mara kadhaa kabla ya hizo kazi tulizozifanikisha huko…hii nchi ndio mara yetu ya kwanza kuikanyaga hii…hilo linatukwaza kiasi!”
“Pamoja na hivyo…bado naona kuwa pia tulimchukulia poa huyu bwege tangu mwanzo, lakini sasa haitatokea ten…” Jarraar alisema, lakini Mukri alimkatisha.
“Huyu ni zaidi ya hayo yote…nilipokuwa pale chini niliona jinsi alivyokuwa anapambana nawe Jarraar…kabla yule mwanamke mshenzi hajataka kukulipua kichwa kwa bastola nami nikawahi kumpoteza lengo kwa kumsukumia kitanda…”
“Na…?”
“Akh! Jamaa amepata mafunzo maalum yule aisee…na ana kitu cha ziada juu ya hayo mafunzo…”
“Kitu gani sasa…?”
“Mnh! We hukuweza kuona maana ulikuwa umemakinika kukabiliana naye tu, lakini jamaa ana kitu nahisi ni cha peke yake aisee…namna anavyochezesha miguu yake na kuzunguka kwama mcheza dansi…? Ile hufundishwi popote aisee…yaani n’na hamu hasa ya kukutana naye tena mtwana yule!” Mukri alisema.
Jarraar alikunja uso.
“Mnh, atakuwa amefunzwa wapi basi yule…? Tanzania…? Inawezekana kweli?” Alisema kama anayejiwazia mwenyewe.
“No, way! Sio Tanzania…”
“Wapi sasa…?”
Mukri aliguna.
“Jiulize ni nani aliyetupa tenda ya kumuangamiza huyu mtu…nadhani hapo utapata jibu kuwa hakika yule jamaa hakupata mafunzo yale Tanzania….” Hatimaye alimjibu.
Jarraar alizidi kukunja uso pale jibu lilipojitengeneza kichwani mwake.
“Aise!” Ndilo neno pekee lililomjia akilini muda ule. Ukimya ukatanda baina yao.
“So nini kinafuata…? Unahitaji kulala? Upumzishe mkono wako?” Hatimaye Jarraar alimuuliza mwenzake.
Mukri alikunja na kukunjua vidole vya mkono wake wa kushoto vilivyobandikwa plasta.
“N’talalaje wakati risasi bado haijatua kwenye dango?” Mukri alimjibu kwa swali.
Jarraar Bakhtiyar aliachia tabasamu baya.
“Ndio ninachokupendea patna!” Alimwambia huku akitoa aina ya simu pana kutoka kwenye mfuko wa suruali yake…
____________________
Sauti ya mhemo hafifu wa mtu aliye usingizini ilisikika. Ulikuwa ni usiku mkubwa, na karibu watu wote ndani ya nyumba ile walikuwa wamelala. Mukri alisimama nje ya mlango ambao alikuwa ana uhakika kuwa ndimo windo lake lilikuwamo. Aligeuka nyuma na kumuona Jarraar akimsukumia binti wa mapokezi chini ya meza baada ya kumpoteza fahamu kwa kabali kali, tayari wakiwa wameshamzimisha mlinzi mmoja wa kimasai huko nje na kumsukumia chini ya uvungu wa moja kati ya magari machache yaliyokuwa pale nje.
Taa moja ya balbu ndio ilikuwa inasambaza mwanga hafifu kwenye korido fupi ya nyumba ile ya wageni, na sasa Jarraar alikuwa amemfikia pale nje ya chumba ambacho waliamini kuwa mlengwa wao alikuwamo, akiwa amening’iniza bunduki mgongoni, na ameshika bastola mkononi. Ile sauti ya mkoromo hafifu kutoka nyuma ya mlango ule iliwaambia kuwa kazi yao safari hii ilikuwa inaelekea kuwa rahisi.
Walipeana ishara, kisha Mukri akaweka mdomo wa bastola yake iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti kwenye sehemu ambayo loki ya kitasa ilikuwa inakutana na ubao wa fremu ya mlango ule na kuifyatulia risasi mbili za haraka haraka. Mlango ukaachia kwa sauti kali ya kuvunjika kwa ubao mkavu, na hapo hapo Jarraar akajitupa ndani huku akibingirika, macho yake yakiwa kitandani ambapo aliona mtu akiwa amelala…
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
________________
Ile sauti kali ya ubao wa mlango ukitawanyika vibaya ilimshitua mlalaji pale kitandani na bila kufikiri, kama kwamba ni kwa mazoea, alijitupa chini huku akigumia kwa mshituko, risasi mfululizo zikimiminika kitandani pale, na kule alipoangukia mlalaji hakuweza kujizuia tena bali alichia ukelele wa woga.
Muda huo Mukri naye alizama ndani na kuruka hadi pale kitandani, kisha akajitupia upande wa pili wa kitanda kile na kumuona mtu wao akiwa amegaragara sakafuni upande wa pili wa kile kitanda.
“Tulia!” Mukri alifoka, na hapo hapo Jarraar alikisukuma pembeni kwa fujo kile kitanda huku sasa akiwa ameielekeza ile bunduki yake fupi aina ya “assault rifle” AR-15, iliyounganishwa na tochi kali kwenye mtutu wake.
“No, jamani…please!” Sauti ya woga kutoka kwa mlengwa wao iliwafikia kutoka pale chini ya kitanda, na hapo hapo tochi kali kutoka kwenye bunduki ya Jarrar ikawaka, sanjari na miguno ya mshangao kutoka kwake na kwa Mukri.
Sandra alikuwa amelala sakafuni huku akiwa ameinua mikono kuomba suluhu, macho yakiwa yamemtoka pima, hali akiwa na chupi tu…
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment