Sehemu Ya Nne (4)
* * *
Baada ya kuachana na Husna, Justin aliondoka na picha iliyomwonyesha kuwa, kuuawa kwa Himidu na Ali Othman ni mauaji yaliyofanyika kutokana na sababu za kisiasa. Wote wawili ndio waliotarajiwa kushika nafasi mbili za uongozi wa juu baada ya rais aliye madarakani kumaliza kipindi chake cha utawala.
Pamoja na kuwa na uhakika huo, lakini bado alikuwa akijiuliza, ni nani aliyekuwa nyuma ya mauaji hayo? Anaweza akawa ni rais? Akaziangalia baadhi ya sababu na kuziona kuwa zinaweza kumuweka rais katika nafasi ya kuhusika na mauaji hayo na moja ya sababu yenye nguvu ni kutoridhika na watu hao wote wawili kwa mmoja wao kumkasimu madaraka ya urais pale atakapomaliza kipindi chake cha urais. Ingawa ilieleweka kuwa, hakukuwa na utawala wa kiimla wa rais kumwachia madaraka mtu ampendaye na badala yake ni kuwa, kila mwanachama wa chama tawala mwenye sifa za kugombea urais anaweza akaingia kwenye kinyang’anyiro hicho na itategemea na kampeni atakazoweza kuzipiga ili aingie kwenye fainali za ugombeaji huo na hatimaye kuwa rais. Lakini Justin akachukulia kuwa, huenda rais aliwaona watu hao wawili ndiyo waliokuwa na nguvu za ushawishi wa kuwezesha kuupata urais na alihofia nguvu zao za ushawishi zisije zikafikia mahali akashindwa kuzidhibiti. Hiyo ndiyo sababu kubwa aliyoiamini Justin kuwa, hilo linaweza likamuhusisha rais na mauaji ya mawaziri wake hao! Na kama ingekuwa ni hivyo, ni nani angeweza kumwonyeshea kidole rais aliye madarakani na kumwambia, ‘Wewe rais umeua!’ au ni nani angeweza kuipeleka ripoti ya uchunguzi kwa bosi wake ambayo ina maelezo ya kumnyooshea kidole rais?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kujiuliza maswali hayo, Justin akaona kuwa, hakukuwa na sababu ya kuandika ripoti kama hiyo endapo angegundua kama ukweli utabakia kuwa hivyo, badala yake angemwendea IGP na kumweleza kwa mdomo kile alichokigundua na nini kifanyike angemwachia mwenyewe IGP. Yeye angeahidi kwa kumuhakikishia kuwa, ataufunga mdomo wake daima kuhusu ugunduzi wake huo!
Lakini kabla ya kufikia kumwona IGP na kumpa taarifa hizo, Justin alijionya kwamba, anachotakiwa kukifanya kwa sasa hivi ni kuendelee na uchunguzi wake ili kupata asilimia mia moja ya ushahidi na kujiridhisha nao kabla ya kumwona IGP na moja ya eneo analopaswa kuhangaika nalo ni kumtafuta mwuaji aliyeyafanya mauaji hayo. Lakini pamoja na kuvutwa na hisia kuwa, Ikulu inaweza ikahusika na mauaji ya mawaziri hao wawili, Justin bado alikuwa na mashaka na watu wengine wawili ambao nao wanaweza wakahusika na mauaji ya mawaziri hao. Watu aliowaona kuwa wangeweza kuhusika na mauaji hayo ni Omar Sharif na mwenzake Raphael Kibaha! Hawa aliwaona nao wangeweza kuhusika na vifo hivyo kwa sababu zile alizoziona kwa rais! Kuwa, Omar Sharif na Raphael Kibaha hawakuridhika kwa wenzao hao kuchukua madaraka na wao wakawa chini yao pamoja na kwamba walikwisha kubaliana katika kuachiana nafasi ya kugombea urais na wengine wabaki kama wapiga debe. Picha hiyo ikamwonyesha kuwa, Himidu na Ali Othman ndiyo walikuwa na nguvu ya kisiasa, nguvu ambazo ama zilimwogopesha rais au ziliwaogopesha hawa wenzao wawili. Ni nani mwuaji aliyetumika kuifanya kazi hiyo? Justin alijiuliza na kuamua kukifanyia kazi kitendawili hicho.
*****
Muda uliotumika kuuawa kwa Himidu na Ali Othman ndiyo alioutilia maanani Justin. Wote waliuawa usiku, ikiwa na maana waliuawa wakati dunia ikiwa na kiza na kumaanisha kuwa, mwuaji ni mtu anayependa kutumia kiza ili kufanikisha mauaji yake. Kwa nini? Justin alijiuliza. Mauaji yote ya usiku humpa nafasi mwuaji kupata mwanya mzuri wa kumfuatilia mtu anayetaka kumwua bila ya kuonekana au kugundulika kwa urahisi! alijijibu swali lake. Pia, humpa nafasi mwuaji kuweza kutoroka kwa ulaini na kupotea bila ya kuonekana, lakini pia, muda wa usiku ni rahisi kutumiwa na mwuaji kujificha kumsubiri adui yake bila ya kuonekana na kumfanyia shambulizi la ghafla bila ya kumpa nafasi ya kujitetea. Picha hiyo akamuhusisha nayo mwuaji ambaye aliamini alikuwa ni mmoja aliyewaua Himidu na Ali Othman kuwa ni mwuaji anayependa kukitumia kiza kufanya mauaji.
Atakuwa alitumia usafiri uliokuwa ukimsubiri kutorokea nao mara baada ya kufanya mauaji? Justin alijiuliza. Akajaribu kuiweka picha ya mwuaji huyo kwa ukamilifu. Picha ya kwanza aliyoipata ni kumwona mwuaji huyo hakuwa kibaka aliyekodiwa kwenda kuwaua mawaziri hao. Ikulu haiwezi kumkodi kibaka! Alijiambia. Kama Ikulu iko nyuma ya mauaji haya ni wazi mwuaji ni mwenye taaluma itakayomuhusisha na taasisi yoyote ya ulinzi ya serikali ambayo imemruhusu kuwa na matumizi ya silaha kama sehemu ya kazi yake akiwa ni mtu anayeijua itifaki. Huwezi kutumwa kwenda kumwua mtu maarufu halafu ukawa mpayukaji! Justin aliwaza. Kwa hiyo mwuaji hawezi kutoka nje ya taasisi hizo! Mwuaji lazima awe ni mtu maalumu aliyefuatiliwa tabia zake kabla ya kupewa kazi hiyo, na watu waliomfuatilia lazima nao wawe ni watu wenye kuaminika kwa kula kiapo, ikiwa na maana kuwa, hata wao wangemtafuta mtu watakayemlisha kiapo, mtu ambaye wamemwona anakubalika baada ya kuziangalia sifa zake, mtu maalumu!
Picha hiyo ikampa mwanga Justin kuwa, mwuaji alikuwa akitumia usafiri wa kumuwezesha kuweza kuifanya kazi yake kwa utulivu kwa kuweza kuwafuatilia watu aliotaka kuwaua! Akaanza kuyakariri maelezo ya jalada la uchunguzi wa mauaji ya Himidu na kumwonyesha kuwa, Himidu aliuawa akiwa ndani kwenye uwanja wa mbele wa nyumba hiyo iliyozungukwa na ukuta. Kwa hiyo mwuaji hakuwa kwenye gari wakati alipofyetua risasi kumpiga Himidu! aliwaza. Justin akaona ulikuwepo uwezekano wa mwuaji kuliegesha gari sehemu na kuliacha wakati akienda kufanya mauaji na baada ya kuua ndipo alipolirudia gari lake na kuondoka nalo. Kwa mzunguko huo, mwuaji atakuwa aliliegesha gari lake sehemu ambayo alikuwa na uhakika lisingeweza kutiliwa mashaka. Justin akajikuta anahitajika kuchukua hatua mbili muhimu. Hatua ya kwanza ni kuwasiliana na IGP ili awezeshwe kuyapata maelezo ya mazingira ya kifo cha Ali Othman kilivyokuwa ndipo aende kwenye hatua ya pili ambayo ni kwenda kuyaangalia mazingira ya maeneo yaliyotumika kuuawa kwa mawaziri hao.
Aliwasiliana na IGP saa moja baadaye na kumweleza shida yake. IGP hakuwa na jinsi, ni yeye ndiye aliyemtaka Justin aifanye kazi hiyo kwa siri na ikawa ni wajibu wake kumlinda ili asionekane yuko kwenye kujihusisha kwa kina na uchunguzi wa vifo vya mawaziri hao wawili. Kwa kuwa mara ya kwanza alimwagiza Justin kulichukua jalada la uchunguzi wa kifo cha Himidu kwenye kituo cha polisi cha Oysterbay, mara hii hakutaka Justin aonekane tena akifuatilia jalada la uchunguzi wa kifo cha Ali Othman.
“Nitamtuma mtu akanichukulie maelezo unayoyataka,” IGP alisema. “Yakiwa tayari nitakutaarifu uje uyachukue.”
“Nashukuru mkuu,” Justin alisema na kukata simu.
* * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku ya pili, Justin akiwa tayari ameyapata maelezo yaliyoelezea mazingira aliyouawa Ali Othman alijikuta akirejewa na wazo la kwenda nyumbani kwa Ali Othman ili kufanya mahojiano japo machache na mke wa mheshimiwa huyo kama alivyokuwa amefanya na mke wa Himidu. Lakini wakati alivyokuwa akifikiria hivyo, akaisikia kengele ya hatari ikipiga kichwani mwake baada ya kugundua kuwa, mchezo huo wa kuwafuata wake wa marehemu hao unaweza ukamuweka mahali pabaya. Hofu hiyo ilimjia baada ya kujipa hadhari kuwa, endapo mauaji hayo yatakuwa yamesimamiwa na Ikulu basi hata yeye anaweza akayapoteza maisha yake endapo atagunduliwa kuwa, yupo kwenye mwelekeo wa kugundua ukweli huo! IGP atakuwa aliliona hilo na ndiyo sababu ya kunitumia kwa siri? Justin alijiuliza. Kwa dakika kadhaa alijikuta akiwa ndani ya usumbufu wa kusumbuliwa na fikra hizo. Natakiwa niwe mwangalifu na hatua zangu! alijionya. Wazo la kwenda kumwona mke wa Ali Othman akalifuta!
Usiku, muda uliozidi saa mbili, Justin alikwenda kwenye mtaa anaoishi Husna na kwenda kulisimamisha gari lake kwenye sehemu kunakouzwa chipsi ambako mkabala kulikuwa na baa iliyokuwa na wateja waliokuwa hawakujaa sana, wala hawakupungua sana. Wengi wa wateja hao walikuwa wamekaa kwenye meza zilizokuwa uwanjani ambako miti ya mwarobaini ilikuwepo na kuleta mandhari yenye kiza. Justin hakufanya haraka ya kushuka kutoka kwenye gari lake, alitulia ndani kwa dakika kadhaa na kuona hakuna watu waliolipatiliza gari lake tokea alivyolisimamisha isipokuwa wanawake wachache walioonekana ni viruka njia ambao macho yao yalimwangalia yeye na kuonyesha kuwa tayari kumfuata endapo angewaita.
Justin aliteremka kutoka kwenye gari na kuangaza macho yake pande zote wakati akiufunga mlango, hakutaka kushangaa na kuwapa picha wakazi na wenyeji wa eneo hilo kuwa yeye ni mgeni. Hakuelekea kwenye chipsi wala kwenye baa, badala yake akalivinjari eneo hilo kwa makini. Hatua chache kutoka kwenye baa akaliona eneo linalolaza magari kwa malipo kisha, akaiendea nyumba ya Husna ilipo. Akapita karibu na ukuta bila ya kuingia ndani, lakini aliweza kuyapitisha macho na kuona mpaka ndani kwa kupitia kwenye matundu ya nakshi yaliyojengewa kwenye ukuta huo na kuliona gari dogo likiwa limeegeshwa kwa ndani. Akalitarajia kuwa ni gari la Husna pamoja na kwamba hakuwahi kuliona gari lake kabla. Justin aliipita nyumba ya Husna na kuyaangalia mazingira yaliyoizunguka nyumba hiyo. Mkabala na nyumba hiyo kulikuwa na nyumba iliyokuwa ikijengwa ambayo haijamalizika na moja kwa moja, Justin akauona urahisi alioupata mwuaji wakati akimsubiri Himidu atoke ambako angeweza kumwona kupitia matundu ya ukutani. Justin alikwenda kwenye nyumba hiyo inayojengwa na kuujaribu mlinganisho wake wa urahisi alioupata mwuaji kumsubiri Himidu. Alipofika hapo ndipo alipoupata uhakika kuwa, mwuaji alimsubiri Himidu akiwa hapo na aliweza kulitumia boma hilo kwa saa nyingi kabla ya Himidu hajatoka kutokana na boma lenyewe kuachwa pweke.
Kwa upande wa pili, Justin aliamini mwuaji hakulitumia eneo la mbele la boma hilo kuliegesha gari lake, kwani angefanya hivyo ni wazi gari lake lingetiliwa mashaka kwa kuegeshwa kwenye boma hilo lisilokaliwa na watu na wenyeji wangetaka kujua sababu ya kuegeshwa hapo na pengine baadaye ushahidi wa kuwepo gari hilo kabla ya mauaji ungemuweka mwuaji kwenye wakati mgumu. Picha nyingine aliyoijenga Justin ni kumwona mwuaji akiwa kwenye boma hilo alivyoweza kumwona Himidu akitoka nyumbani kwa Husna na mwuaji kuitumia nafasi ya usiku mwingi kupata urahisi wa kuvuka kwenda upande wa pili wa barabara iliko nyumba ya Husna na kulitumia moja ya matundu ya nakshi yaliyopo kwenye ukuta huo na kumfyetulia risasi Himidu bila ya kuonekana na wakazi na kuweza kutoroka bila ya kupata kipingamizi chochote na kurudi sehemu alipoliegesha gari lake na kukimbia. Ni wapi atakapokuwa aliliegesha gari lake? alijiuliza. Justin aliziona sehemu tatu ndizo zilikuwa na uwezakano kwa mwuaji kuliegesha gari lake na kuja kwenye boma kumsubiri Himidu, sehemu hizo ni pale panapouzwa chips ambako ndipo lilipo gari lake, sehemu nyingine ni kwenye ile baa. Hata hivyo, sehemu hizo mbili alizitilia mashaka kama kweli mwuaji angeweza kuliacha gari lake mpaka kwenye muda wa saa saba na zaidi za usiku huku akiamini sehemu hizo mbili zingekuwa tayari wamefunga biashara zao kwa muda huo. Mwuaji hakuwa mjinga kiasi hicho! Justin aliwaza tena. Picha aliyoiona hapo ni kuwa kwa vyovyote mwuaji atakuwa aliitumia sehemu ya kulazia magari kwa malipo kwenda kuliegesha gari lake na kuwaahidi walinzi kuwa angerudi baadaye na kukubali kutoa malipo ya usiku mzima kwa muda huo mfupi wa kuliweka gari lake hapo na nafasi hiyo kutumiwa na walinzi kuyaingiza malipo hayo mifukoni mwao bila ya kuliandikisha gari hilo kwenye daftari kama sheria zao zinavyowataka wafanye.
Wazo la kuwafuata walinzi hao lilimjia, lakini matumaini ya kupata ushirikiano kutoka kwao aliuona utakuwa ni mdogo kutokana na dhana yake ya kuwatilia shaka kitendo chao cha kutia mfukoni malipo hayo hata kama yalikuwa ni madogo, lakini yangeweza kuwagharimu kama yangegundulika na tajiri yao yasingetoa nafasi kwao kumpa ushirikiano. Hilo tu lingetosha kuwafanya wakatae katakata kuwepo kwa tukio hilo sembuse kukosekana ushahidi! Kitu kingine ambacho kilizidi kumvunja nguvu Justin ni ule muda uliokwisha kupita tokea kitendo hicho kifanyike; ulikwishapita muda mrefu. Pamoja na kwamba kupita kwa muda mrefu si kigezo cha polisi kutofanya upelelezi, lakini ni mazingira ya kuwahusisha walinzi hao kuwa ndani ya wizi wa malipo hayo ndiyo yatakayowalazimisha asiupate ushirikiano kutoka kwao. Wazo hilo likamuweka kwenye njia panda ya kutokuwa na uamuzi wa ama awafuate muda huo au asiwafuate kwa muda huo kwa hofu ya kutopata ushirikiano na kuupoteza muda wake. Justin akaamua kwa usiku huo awaweke kiporo na endapo atafikia mahali na kuuhitaji ushahidi wao ndipo atakapowafuata kuwahoji na kama itabidi kuwaweka mahabusu hatosita kufanya hivyo na suala la msalie mtume halitakuwepo na atahakikisha wanakiri kwa kuwepo tukio hilo!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Justin alirudi kwenye gari lake, akaliwasha na kuondoka nalo bila ya kuzungumza na yeyote kwenye eneo hilo.
* * *
Siku iliyofuata, muda ule ule kama alioutumia siku iliyopita kwenda mtaa wenye nyumba anayoishi Husna ndiyo muda alioutumia kuwasili mtaa wenye nyumba aliyokuwa akiishi mheshimiwa Ali Othman.
Akiwa anaupita kwa mwendo wa taratibu akiwa ndani ya gari lake, Justin aliyaangalia mazingira ya mtaa huo na kugundua kuwa, isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kuliegesha gari lake kwa kuliacha barabarani kwenye maeneo hayo bila ya kutiliwa mashaka, ilikuwa ni tofauti na mtaa anaoishi Husna. Tofauti ya maeneo anaoishi Husna ambayo ni ya Kinondoni ni kuwa na mchanganyiko wa watu wenye kipato cha juu na kipato cha chini, wakati maeneo yenye makazi ya Ali Othman na eneo zima la Mbezi ya Africana halikuwa eneo la walala hoi. Kwa kipindi hicho cha usiku alichokuwa akivinjari kwenye mitaa hiyo ya Mbezi ya Africana, aliweza kuiona tofauti nyingine iliyozidisha tofauti kati ya maeneo hayo. Tofauti hiyo ni kutowaona watu wakitembea hovyo barabarani kama ilivyo mitaa ya Kinondoni. Mtaa wote na mitaa mingine ya huko aliyoipita ilikuwa kimya na mitupu kiasi kwamba, kama hutokuwa mwenyeji na maeneo hayo, basi unaweza ukatembea huku ukitawaliwa na uwoga wa kuwa peke yako. Kitu mbadala ambacho Justin aliweza kukutana nacho ni magari aliyokuwa akipishana nayo yaliyokuwa kwenye mwendo mdogo kutokana na hali halisi ya barabara za huko ambazo hazikuwa na lami. Hali hiyo ndiyo iliyomfanya aamini kuwa, endapo gari lolote litaachwa nje barabarani lingetiliwa mashaka kwa sababu nyumba zote za huko zilikuwa na maeneo ya ndani ya kuegesha gari zaidi ya moja. Kwa hiyo kuegeshwa kwa gari lolote barabarani na kuachwa kwa muda mrefu, kungetoa picha mbili. Ya kwanza, ni kwa wenyeji kujiuliza, inakuwaje gari hilo likageshwa barabarani na lisiingizwe ndani ya nyumba? Swali kama hilo huleta mashaka kwa mkazi wowote wa huko na hasa akiliona halina mtu. Kwa mtazamo huo ni rahisi mtu kuikariri namba ya usajili wa gari na muundo wa aina ya gari na pengine kuweza hata kukariri alama yoyote itakayoweza kumfanya akiliona tena alikumbuke! Picha ya pili, wangeweza kuliwekea mashaka kuwa, huenda lingekuwa limeharibika na kila mtu angependa kuliangalia kwa makini na kumwangalia mmiliki wake kama angekuwa ni mmoja wa majirani anayejulikana ili apewe msaada. Lakini kitendo cha kutoonekana kwa mmiliki wake, hicho nacho kingekuwa ni kigezo kwa wenyeji kulitilia mashaka na endapo kutatokea tukio lolote la kiuhalifu, inakuwa rahisi kwa wenyeji kutoa ushahidi wa kuliona gari lililokuwa limeegeshwa barabarani endapo watahojiwa na polisi. Justin akaamini, mwuaji mwenye akili kama anayemtafuta asingeweza kuufanya uzembe kama huo wa kuliacha gari lake barabarani!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mzunguko huo wa mawazo aliokuwa akijaribu kupanga na kupangua, ukawa umemuweka kwenye eneo moja tu la uwezekano; uwezekano wa mwuaji kuitumia sehemu moja tu ya kuliegesha gari lake ambayo lisingeweza kuwekewa mashaka na wenyeji, nayo ni kwenye baa iliyokuwa mita chache kutoka nyumbani kwa Ali Othman! Justin aliiona sehemu hiyo ni sehemu pekee ambayo ingeweza kutumika kama kichaka kwa mwuaji kuliegesha gari lake kwa kulichanganya na mengine bila ya kutiliwa mashaka! Alisimama jirani na nyumba ya Ali Othman na kuteremka, akalivinjari eneo hilo na kusaidiwa kuliona vizuri kutokana na mwanga wa taa za magari machache yaliyokuwa yakipita eneo hilo. Kutokana na eneo la hapo lilivyokuwa, Justin akatilia mashaka kama mwuaji aliweza kumsubiri mheshimiwa Ali Othman arudi nyumbani kwake kwa kuvinjari na kuzubaa zubaa kama hapo anavyozubaa yeye. Kwa vyovyote mwuaji alikuwa amejificha wakati akisubiri! Justin aliwaza. Eneo hilo halikuwa na sehemu ya kujificha kwa urahisi, na moja kwa moja fikra za Justin zikaangukia kwenye kidaraja kilichokuwa mkabala na nyumba ya Ali Othman na kuiweka dhana kuwa, kidaraja hicho ndicho alichokitumia mwuaji kujificha!
Baada ya kuridhika na hesabu zake za kujumlisha na kutoa, hatimaye alienda kwenye baa hiyo ya jirani na hapo. Nje ya baa hiyo ndogo kulikuwa na magari yapatayo sita au saba na kumwona mlinzi wa kimasai amesimama akiwa ameegemea moja ya magari hayo ambayo yote yalikuwa madogo. Alipoteremka alijikuta akiangaliwa na mmasai huyo mpaka alivyoingia. Ndani, kwenye uwanja wa baa hiyo ambayo haikuwa na shamra shamra zozote za kufunguliwa mziki kama baa nyingine, hapa palikuwa na ukimya kama vile umeingia kwenye hoteli kubwa za kitalii. Watu waliokuwemo humo hawakupishana kwa idadi na magari yaliyokuwa nje na kumpa picha halisi Justin kuwa, baa hiyo haikuwekwa hapo kibiashara kwa lengo la kuendeshea maisha ya mtu, bali ilikuwepo kama sehemu ya kutuliza akili baada ya presha za kazi za siku nzima na pia, kama sehemu ya kujenga udhibiti mwingine wa akili kwa kunywa bia mbili tatu kabla hujafika nyumbani na kukutana na gubu za baadhi ya wake wanaosubiri waume zao wafike nyumbani na kuanza tafrani nyingine.
Baadhi ya watu wawili watatu waliokuwemo humo waliinua vichwa kivivu na kumwangalia mara moja Justin aliyeingia kisha, waliendelea na mazungumzo yao ya kimya kimya, wengine wao hawakupata shida kabisa ya kumwangalia. Justin hakupata tabu kutafuta mahali pa kukaa, aliendea meza moja kati ya meza chache zilizomo humo na kukaa. Mara ya kwanza alikuwa na wasiwasi huenda sehemu hiyo kulikuwa na huduma ya kujihudumia mwenyewe, lakini mara akamwona mhudumu wa kiume aliyekuwa nyuma ya kaunta kwenye kaunta iliyokuwa na mteja mmoja akiufungua mlango mdogo na kutoka kwa kuinama, akaja alipokaa.
Akiwa ameagiza bia na kuletewa, Justin alijaribu kujiuliza kama endapo ni kweli mwuaji aliweza kuliegesha gari lake nje ya baa hiyo na kama aliingia humo ndani na kuagiza kinywaji kabla ya kwenda kukamilisha mauaji. Hakupata jibu la swali hilo na asingeweza kumwuliza mtu yeyote kwa hapo! Kwa upande mmoja alijipa imani kuwa, mwuaji atakuwa aliiegesha gari nje kisha ndipo alipokwenda kuua. Sawa, tufanye hivyo! Justin alijiambia. Kinachofuata? Swali hilo likamfanya ajione kama aliyefika mwisho wa njia aliyokuwa akiifuata. Alijiona akiwa hakuna alichokigundua zaidi ya kupata dhana ya mienendo iliyotumiwa na mwuaji kabla ya kufanya mauaji yake kwa Himidu na Ali Othman! Ilikuwa ni hatua muhimu kiupelelezi kuzitambua angalau nyendo zilizotumika na mwuaji, Justin alijisemea moyoni. Lakini kuzijua nyendo hakumaanishi kumjua mwuaji. IGP alimtaka amtafute mwuaji na siyo nyendo zilizotumiwa na mwuaji kuyatekeleza mauaji!
Fikra za kutaka kuwafuata walinzi wa magari wa kule Kinondoni B zilianza kumshawishi awafuate, ilikuwa ni sehemu pekee ya matumaini yaliyobaki ya kumuwezesha angalau kujua mtu anayemtafuta yukoje. Aliamini hao ndiyo watu pekee ambao walifanikiwa kumwona mwuaji na kuzungumza naye na pia kuliona gari lake. Wao ndio wangempa picha ya umbile la mwuaji huyo alivyo na kutoa namba za usajili wa gari na aina ya gari. Hata hivyo, hofu ya walinzi hao kukataa kukubali kuwa walionana na mtu huyo ilitawala kwenye nafsi yake, alijua wasingekubali kirahisi na alijua ili kuwafanya waseme ukweli ni kutumia njia ya vitisho dhidi yao.
Justin aliimaliza kuinywa bia aliyokuwa ameiagiza na kujikuta akishindwa kuagiza nyingine ya pili baada ya kuona uwepo wake wa kuwepo hapo ni sawa na kupoteza muda. Alihitajika kwenda kuwaona walinzi hao usiku huo. Akajiuliza kama kulikuwa na umuhimu wa kupita kituo kidogo cha polisi kilichoko maeneo ya Kinondoni, ajitambulishe na kuomba apatiwe msaada wa polisi wawili ambao angeongozana nao mpaka kwa walinzi hao na kuwahoji akiwa nao. Aliamini kuwa, endapo angeenda kama yeye mwenyewe na nguo zake za uraiani kamwe wasingemwelewa hata kama angewaonyesha kitambulisho chake cha uaskari. Isitoshe, uendaji wa aina hiyo ungewapa nafasi walinzi hao kumtilia mashaka pengine amewaendea kwa ajili ya kutaka kidogo kutoka kwao na hatimaye kutupiana maneno ambayo yangewavuta watu wengine na kibao kumgeukia. Lakini aliamini, endapo angewachukua askari kutoka kituoni na akaenda nao, kuonekana kwa sare za askari atakaowachukua ungekuwa ni mjeledi tosha wa kuwaogopesha pindi atakapoanza kuwahoji kwa vitisho na huenda wakakiri kuonana na mtu huyo.
Justin alimwita kijana aliyemhudumia na kumlipa malipo ya bia moja aliyokunywa kisha akaondoka na kulifuata gari lake. Alipoingia ndani ya gari na kabla hajaufunga mlango, mlinzi wa Kimasai akamjia.
“Rafiki unaondoka?” Mmasai aliuliza.
“Ndiyo rafiki,” Justin alijibu na kuufunga mlango wa gari.
“Niachia pesa ya soda, rafiki.”
Justin hakutaka kuendelea kuzungumza naye, akili yake ilikwisha kuwa Kinondoni B kwa walinzi wa magari. Alitoa kiasi kidogo cha pesa na kumpa mmasai ambaye alipokea.
“Wewe ni mgeni hapa?” Mmasai aliuliza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa nini unaniuliza hivyo?” Justin aliuliza na wakati huo huo akiliwasha gari lake.
“Sijawahi kuiona sura yako hapa.”
“Kesho nitakuja tena,” Justin alisema ili apate nafasi ya kuondoka. Baada ya kusema hivyo akaliondoa gari na kumwacha mmasai akiondoka kama vile hakuwa alizungumza na mtu.
Justin alifanikiwa kufika kwenye kituo kidogo cha polisi na kujitambulisha kisha, aliomba askari wawili na kwenda nao kwenye eneo la kulaza magari ambako waliwakuta walinzi wote wakiwa na hekaheka ya kulizunguka lindo lao. Justin na wale askari wawili wakamfuata mlinzi aliyekuwa amekaa juu ya meza iliyokuwa na daftari kubwa la kuandika magari yanayolazwa hapo. Yule mlinzi kuwaona askari polisi wawili wakiwa na raia wakimjia, akajikuta akiwa makini kuwaangalia.
“Karibuni,” mlinzi alisema bila ya kuteremka kutoka juu ya meza.
Justin alijitambulisha na kuwatambulisha wale askari aliokuja nao bila ya kuwataja majina pamoja na kwamba walipokuwa ndani ya gari wakija hapo waliweza kujitambulisha majina yao kwake.
“Tuna maswali tunataka kukuuliza,” Justin alimwambia yule mlinzi.
“Sawa. Karibuni,” mlinzi alijibu.
“Ni nani anayeandikisha magari yanayokuja kulala hapa?”
“Ni mimi,” mlinzi alisema na kumwangalia Justin kwa makini.
“Huna mwingine unayeshirikiana naye?
“Nikiwepo kazini, mimi hiyo ndio kazi yangu.”
“Kwa hiyo unakuja kila siku?”
“Ndiyo.”
“Una muda gani kwenye kazi yako?”
“Sasa hivi nina mwaka wa tatu.”
Justin akaanza kwa kutaja tarehe na siku aliyouawa Himidu, lakini hakulitaja jina la Himidu wala kulitaja tukio lililotokea siku hiyo. Kisha akauliza, “Siku hii ulikuwepo kazini?”
Mlinzi akajaribu kufikiri kwa kichwa, lakini akajipa hadhari ya kutojiingiza kichwa kichwa kwa kukubali. Akalichukua daftari lililokuwa kando yake na kulipakata kwenye mapaja yake na kuanza kuitafuta tarehe aliyoulizwa. Hatimaye aliifikia kurasa yenye tarehe hiyo na kusema, “Nilikuwepo kazini.”
“Siku hii kabla ya saa saba usiku, kuna mtu alikuja kulileta gari lake hapa kwa ajili ya ulinzi mfupi, kisha baadaye alirudi na kulichukua. Unalikumbuka tukio hilo?”
Mlinzi hakujibu haraka. Alionekana kufikiri kisha akasema, “Nakumbuka alishawahi kunijia mtu kwa shida hiyo na kweli nilimruhusu aliweke gari lake na baadaye alirudi na kulichukua. Na nakumbuka nilimpa daftari akajiandikisha. Ngoja niangalieni ni nani aliyekuwa ameliweka gari kwa muda mfupi siku hiyo,” baada ya kusema hivyo, akaurudisha uso wake kwenye daftari na kuanza kukagua kwa msaada wa kidole chake. Hatimaye kidole chake kilisimama kwenye jina na kusema, “Huyu hapa! Nakumbuka nilimwandika, wateja wa namna hii wa kuja kuweka magari yao kwa muda mfupi ni nadra sana kutokea na tuko makini nao sana na ndiyo maana imekuwa rahisi kwangu kumkumbuka.”
Justin hakuamini kama ingekuwa rahisi hivyo, ilikuwa ni tofauti na fikra zake za awali. “Anaitwaje?” aliuliza.
“Anaitwa…” Mlinzi alisema kwa kuvuta matamshi huku akiwa ameliinamia daftari. “S. Ramadhani,” alimalizia na kumwonyesha Justin lilipo jina hilo kwenye daftari.
Justin aliangalia na kuoa ni kweli limeandikwa jina hilo na kuangalia sehemu iliyoandikwa aina ya gari na kuona ni Toyota Corolla pamoja na namba zake za usajili ambazo alizinukuu kwa kuziandika. “Jina aliandika mwenyewe au alikutajia na ukaandika?” aliuliza.
“Kila kitu alijaza mwenyewe, huo ndio utaratibu wetu.”
“Kwa hiyo mteja akishajiandika huwa hamna chochote mnachohakikisha kwa macho yenu zaidi ya maandishi aliyoyaandika?”
“Kuna baadhi ya vitu huwa tunavihakikisha kabla hajaondoka. Kwa mfano namba za gari, kama ana tairi la akiba pamoja na jeki na pia kama taa zake zote ni nzima, vitu kama hivyo.”
“Kuna mapungufu uliyoyaona?”
“Hakukuwa na mapungufu.”
“Hapa ameandika ni Toyota Corolla, Corolla ya aina gani?”
“Limited toleo la mwanzo.”
“Unaweza ukalitambua endapo ukiliona tena?”
“Sina hakika, lakini nakumbuka ilikuwa na nembo ya timu ya Liverpool kwenye kioo chake cha nyuma. Naikumbuka nembo hiyo kwa sababu siku hiyo timu hiyo ilichukua ubingwa wa FA kwa kuifunga Manchester ambayo ni timu ninayoipenda. Moja ya kitu ambacho kilinikera ni kuiona gari hiyo ikiwa na nembo hiyo iliyoniongezea machungu. Ninaweza kuitambua kama nikiiona tena, lakini siwezi kukuahidi hilo.”
“Nani alimkabidhi gari lake wakati alivyorudi?”
“Ni mimi mwenyewe.”
“Alikuwa kwenye hali gani?”
“Alikuwa kwenye hali ya kawaida, nadhani alikuwa ametoka kwa mwanamke?”
“Nini kilichokufanya umdhanie hivyo?”
“Unadhani ni nini kilichomfanya kuja kulificha gari lake hapa kama si kwenda kwa mwanamke? Pengine hakutaka gari lake lionekane eneo la sehemu alipokwenda.”
“Inawezekana alihofia kuliacha gari lake sehemu isiyo na usalama na kuogopa kuibiwa.”
“Gari lake halina sifa ya kumshawishi mwizi wa magari asumbuke kuliiba.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Ni gari kuukuu.”
“Ulivyokuwa ukizungumza naye, lafidhi yake ilionyesha ni Mtanzania?”
Mlinzi akavuta fikra kwa sekunde chache. “Ndiyo, alikuwa ni Mtanzania!” alijibu kwa uhakika.
“Ukimwona tena unaweza ukamkumbuka?”
“Sina uhakika. Labda hapo nitakapomwona. Samahani, naweza nikakuuliza?”
“Uliza.”
“Amefanya nini?”
“Ni mapema mno kukwambia. Nadhani tutarudi tena kuomba msaada wako mwingine tukihitajika kufanya hivyo. Unaweza ukaniachia jina lako?”
Mlinzi akalitaja jina lake.
“Tunashukuru kwa msaada wako,” Justin alisema na kumpa mkono wa kuagana mlinzi huyo.
Justin akashukuru angalau siku yake haikuishia bure, ilikuwa ni siku iliyompeleka hatua za kuridhisha kidogo. Aliwaacha wale polisi wawili kituoni kwao na yeye mwenyewe kurudi nyumbani huku akipanga asubuhi atakapofika ofisini, kitu cha kwanza kukifanya ni kuonana na IGP kabla hajafanya chochote.
* * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Asubuhi, Justin aliwahi kwenda ofisini kwa IGP kabla ya mkuu wake huyo hajakwenda kuhudhuria kikao cha kila siku asubuhi cha kuonana na maofisa wa polisi kwa kutathimini matukio ya usalama ya saa ishirini na nne zilizopita yanayohusu nchi nzima. Alimkuta IGP akiongea na simu na wakati huohuo kikombe cha kahawa nyeusi inayofuka moshi kikiwa juu ya meza. Inno alitoa ishara ya kumkaribisha Justin kwenye kiti kwa kuupunga mkono wake huku akiendelea kuzungumza na simu. Justin alikaa kwenye kiti na kumsubiri mkuu wake amalize kuongea kwenye simu.
“Karibu Justin,” Inno alisema baada ya kumaliza kuzungumza kwenye simu.
“Nashukuru mkuu,” Justin alisema na kuamkia. “Kuna matukio niliyoyagundua ambayo yananitia wasiwasi huenda mwuaji alihusika nayo kabla ya kufanya mauaji kwa kila tukio,” alisema na kuanza kumweleza kwa kirefu Inno huku akijaribu kuzungumza hatua kwa hatua ili awe na uhakika kuwa, maelezo yake yaonyeshe hatua alizokuwa amekwenda nazo zilete ushawishi kwa mkuu wake kuwa, kazi inayofanyika inatia moyo.
Hatimaye Justin alikamilisha maelezo yake kwa kusema, “Namba ya gari lake ni hii hapa. Lakini kabla ya kuanza kuwapa askari wa usalama barabarani, nadhani kuna ulazima wa kuchunguza usajili wa namba hizo ili tuweze kumjua mmiliki halali wa kwanza wa gari hilo. Pengine mtuhumiwa wetu anaweza akawa ameliiba kabla ya kufanya mauaji au pengine gari hilo linaweza likawa limepitia kwenye mikono ya watu zaidi ya mmoja kabla halijamfikia yeye ama kwa kulinunua au kwa mazingira yoyote.”
Akiwa ameonyesha kuridhika na maelezo ya Justin, Inno alisema, “Nitamjulisha mkuu wa kitengo cha kompyuta kinachoweka kumbukumbu za usajili wa magari yote nchini ili akupe msaada wa kile utakachokitaka kutoka kwake, mimi sasa hivi nahitajika kwenye kikao. Nenda kamwone kisha, utanipa taarifa zote.”
Wakaagana.
Shughuli ya kuchunguza usajili wa namba alizokuwanazo Justin ulichukua dakika chache kutoa matokeo kwenye kompyuta ambayo ilionyesha kuwa, namba hizo za usajili zilikuwa ni namba za trekta lililosajiliwa miaka ishirini iliyopita na mmiliki wake ambaye kwa kipindi hicho cha usajili alikuwa akiishi kijiji cha Isimani, mkoani Iringa!
Baada ya kuyapata matokeo hayo, Justin aliondoka na kurudi ofisini kwake. Matokeo hayo aliyoyapata yalimuweka kwenye uelewa wa kuwa, sasa yupo kwenye kumfuatilia mwuaji halisi aliyehusika na mauaji ya Himidu kutokana na kitendo hicho cha kutumia namba ya trekta kwa kuiweka kwenye gari yake. Kutumika kwa namba hizo pia, kukamuweka kwenye kutoliamini jina lililoandikishwa na mtu huyo wakati akilikabidhi gari kwa walinzi. Inawezekana likawa si jina lake halali! Justin aliwaza. Kama aliweza kuweka namba bandia kwenye gari lake, atashindwaje kujiandikisha kwa jina la bandia? Pamoja na kuziwekea mashaka nyendo za mtu huyo, lakini kwa upande wa pili, Justin alikuwa na uhakika mwuaji huyo alitumia gari hilo la Toyota Corolla Limited kumpeleka kwenye eneo alilokuwepo Himidu! Corolla yenye nembo ya Liverpool! aliwaza huku akiyakumbuka maelezo ya mlinzi. Hilo ndilo gari la kulitafuta! Lakini wazo la pili lililoingia akilini mwake likamuweka kwenye njia panda; wazo la kuamini kuwa, mwuaji hatakuwa mpumbavu wa kuendelea kuziacha namba hizo za bandia kubaki kwenye gari hilo na kutembea nazo. Mwuaji angetumia namba nyingine badala ya zile na kuuona ugumu wa kulikamata gari hilo ikiwa hakuna namba zake maalumu zilizonukuliwa kutokana na magari ya aina hiyo ambayo yamejazana jijini Dar es Salaam, isitoshe pia, yapo magari lukuki ya aina hiyo yaliyobandikwa nembo za Liverpool kwenye vioo vyake vya nyuma!
Akiwa bado amejikita kwenye kutafakari, Justin akajikuta akijiuliza kama mwuaji atakuwa pia alilitumia gari hilo hilo la Toyota Corolla kwenda kumwua mheshimiwa Ali Othman. Endapo angeweza kulijua hilo, kungeweza kumpa picha kama mwuaji anatumia gari hilo hilo au zaidi ya moja wakati akienda kuhitimisha mauaji yake. Mashaka yake akayaweka kwenye ile baa yenye mlinzi wa kimasai kuwa, inawezekana ikawa ilitumika na mwuaji kwa kuliegesha gari lake hapo na kisha kwenda kwa miguu mpaka nyumbani kwa Ali Othman na kumsubiri arejee. Akikariri jalada linaloendelea kutumika kuchunguza mauaji ya mheshimiwa huyo ambalo linasomeka kuwa, dereva aliyekuwa akimwendesha Ali Othman hakuwa aliliona gari lolote likiwa limesimama barabarani jirani na nyumbani kwa mheshimiwa wakati akimpeleka, zaidi ya kuyaona magari yaliyokuwa yameegeshwa nje ya baa. Hilo ndilo lililokuwa likimtia imani Justin kuwa, mwuaji alilitumia eneo hilo kuliegesha gari lake kabla ya kwenda kumwua Ali Othman. Nani atakuwa aliliona gari lake? Swali hilo likamkumbusha kuhusu mlinzi wa kimasai, na hapo hapo kulikumbuka swali aliloulizwa na mlinzi huyo kama yeye ni mgeni kufika kwenye baa hiyo! Kama mwuaji atakuwa si mwenyeji wa kufika kwenye baa hiyo, ina maana hata yule mlinzi atakuwa alimgundua kuwa ni mgeni kama alivyoonekana yeye? Justin alijiuliza. Au mwuaji si mgeni na ile baa kama alivyokuwa yeye? Na ikiwa si mgeni kama alivyokuwa yeye, ina maana hata yule mmasai hatomwekea kumbukumbu mwuaji kwa kuliacha gari lake pale na kisha kuondoka kwa mguu kutokana na wenyeji wake kwenye baa hiyo? Inawezekana likawa tukio ambalo si muhimu kwa mmasai kuliwekea kumbukumbu? Maswali ya kujiuliza yalikuwa mengi kuliko kupata majibu, na alijua kukaa kwake hapo ofisini kusingesaidia kutatua tatizo hilo la kutaka kujua kama mwuaji alilitumia gari hilo hilo kumfikisha eneo la Mbezi Africana kabla ya kufanya mauaji! Nahitajika kulifuatilia jambo hili, aliwaza. Lakini kwa muda huo alihofu usingekuwa mwafaka wa kwenda kumwona mmasai kwa kuhofia kutokuwepo kazini kwa mlinzi huyo. Justin akajipa subira kwa kusubiri usiku uingie kisha, ndio aende Mbezi Africana.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dakika chache zilizofuata akapata taarifa kuwa, IGP alishamaliza kikao na amerudi ofisini. Akajiandaa kumwendea kwa ajili ya kumpa taarifa mpya zilizojiri za kuwa, namba iliyotumika ni ya trekta iliyosajiliwa miaka ishirini iliyopita na nini anachotarajia kukifanya. Isitoshe, akapanga kuitumia nafasi hiyo kumfahamisha kuwa, ilibaki wiki moja ili aweze kufunga ndoa!
* * *
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment