Search This Blog

Monday, 24 October 2022

SIKU YA UTAKASO - 5

 









    Simulizi : Siku Ya Utakaso

    Sehemu Ya Tano (5)





    Taarifa za kufunga ndoa wiki moja ijayo alizompa IGP aliziona zikiwa zimempa usumbufu mkubwa mkuu wake huyo.

    “Jiandae kufunga ndoa ukiwa ndani ya mazingira ya kikazi,” IGP alisema baada ya kuchukua muda mrefu wa kusuasua kutoa jibu la nini kifanyike kwa wiki hiyo moja iliyobaki. Akaendelea kusema, “Sitopenda uahirishe kufunga ndoa yako kwa ajili ya hii kazi maalumu niliyoikabidhi kwako, lakini pia, sitopenda uahirishe hii kazi maalumu niliyokupa ili ufunge ndoa. Jukumu nililokupa linahusu mustakabali wa nchi! Rais anashangaa, inakuwaje mpaka leo aliyehusika na kumwua mheshimiwa Himidu bado hajakamatwa! Na wakati akiwa hajakamatwa, mauaji mengine ya waziri yanatokea, waziri ambaye ni kiungo muhimu kwa rais! Rais amechanganyikiwa na kuamini mauaji haya huenda yakawa ni ya kisiasa na hofu yake kubwa ameiweka kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu ujao kwa kuamini wanasiasa wanaanza kuitumumua misuli yao kwa kuuana. Ana hofu mauaji mengine yanaweza yakatokea kutokana na kuwa mpaka leo hakujakamatwa waliohusika na mauaji hayo zaidi ya kukamatwa kwa raia ambao baadaye wanaachiwa kwa kukosekana ushahidi! Jambo hili limemtia hofu, na hofu yake kubwa ni kuwa, wauaji wanafahamika, lakini polisi inashindwa kuwakamata kwa sababu ya vigogo wa serikali kujihusisha na njama za mauaji hayo. Ana hofu vigogo hao wanajipanga kuingia madarakani kwa uchaguzi mkuu ujao!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sababu nyingine inayoniweka njia panda ya kukutaka usiahirishe ndoa yako ni kutokana na hali halisi inayoweza kujitokeza kwa askari wenzako, wao watataka kuijua sababu ya wewe kuiahirisha ndoa yako. Endapo nitautoa mwanya huo, basi uwezekano wa kuja kuijua sababu iliyosababisha kuahirishwa kwa ndoa yako utakuwa ni mkubwa na litakuwa jambo la hatari sana. Hatari kwa sababu kama ni kweli vigogo wa serikali wapo nyuma ya mauaji haya, taarifa za kukuhusisha na dhamana ya upelelezi uliyokabidhiwa zitawafikia na hakuna watakaozipeleka taarifa hizo kwao isipokuwa ni hawa hawa vijana wetu ambao watakuwa kwenye malipo ya mlango wa nyuma wa vigogo hao. Na wakizifikisha taarifa hizi kwao, zinaweza zikayaweka maisha yako hatarini kwa sababu wewe si mtu wao! Kwa hiyo ninachokwambia, ikifika siku ya ndoa, nenda kafunge ndoa. Lakini wakati unapofunga ndoa ujielewe kuwa, hakutokuwa na fungate itakayokutoa nje ya Dar es Salaam na wala hutokuwa na wakati wa kujifungia hotelini na mkeo. Ni vyema mkeo asikuelewe kwa kipindi hiki kuliko ukieleweka na wenzako kuwa, umekabidhiwa kazi hii nyeti na maalumu hasa kwa mustakabali wa nchi. Nataka uelewe, kazi uliyopewa inaweza kukupeleka kugundua jinsi vigogo wa serikali na wa chama tawala wanavyojihusisha kuwa nyuma ya mchezo huu mchafu. Ni kazi ambayo haitakiwi uiache njiani kwa ajili ya kufunga ndoa au kwa ajili ya fungate. Kufanya hivyo kunaweza kukawapa nafasi washenzi hawa wakumalize endapo watajua upo katika kuyachunguza mauaji haya!”

    Onyo hilo la IGP lilimuweka Justin katika hali tete ya sintofahamu na fikra zake za awali kuwa, huenda ilikuwa ni Ikulu iliyokuwa nyuma ya mauaji ya mawaziri hao wawili. Lakini kule kumsikia kwake IGP akizungumza kuwa, rais yupo ndani ya hofu huenda baadhi ya vigogo wa serikali na ndani ya chama chake wanajiandaa kuingia madarakani kuiongoza nchi kwa kuwaua baadhi ya viongozi wenzao, hii inadhihirisha kuwa, kuna mgawanyiko ndani ya chama kwa kuwepo makundi mawili yanayogombania madaraka ya nchi na kundi moja limeanza kulimaliza kundi jingine kwa staili ya kuwaua kama sehemu ya zoezi la kusafisha njia!

    Akiwa bado yupo na fikra hizo ambazo zilikuwa zikiendelea kumpa usumbufu wa siku nzima, muda mfupi kabla ya kuingia giza, Justin aliamua kukituliza kichwa chake kwa kwenda kupata bia chache zisizozidi mbili kwenye baa iliyopo njiani wakati akielekea Mbezi ya Africana kwa lengo la kuonana na mlinzi wa kimasai.

    Tokea bia ya kwanza aliyoiagiza na akiwa na bia ya pili, swali alilokuwa akijiuliza kwa wakati wote lilikuwa, nani yupo nyuma ya mauaji ya mawaziri hawa wawili? Ni kweli ni mauaji ya kisiasa? Ni kweli kuna mtafaruku ndani ya serikali na chama tawala katika kugombea madaraka? Ni kweli walio nyuma ya njama hizi za mauaji ni vigogo wenye nguvu kiasi kwamba hata rais ameingiwa na woga? Au rais anazuga ili aonekane hivyo wakati ni yeye mwenyewe ndiye mwuaji? Akiwa haelewi lipi la kushika na lipi la kuacha, Justin akajikuta akilifikiria onyo alilopewa na IGP linalompa hadhari ya maisha yake kuwa hatarini endapo atagundulika kwamba ni yeye ndiye mpelelezi wa kupeleleza mauaji hayo! Endapo ni kweli rais ameonyesha hofu ya wimbi la mfulululizo wa mauaji ya mawaziri wake wawili ni wazi atakuwa alizungumza na IGP na kuiweka hofu hiyo mbele yake. Je, IGP atakuwa alimwambia nini rais baada ya kauli hiyo? Ni wazi atakuwa alimwahidi jambo! Justin aliwaza. Atakuwa alimwahidi nini? Kuwa, mtukufu rais usiwe na wasi wasi, nina kijana wangu mchapa kazi ambaye ana uwezo wa kuwajua walio nyuma ya mauaji haya! Kama atakuwa amemwahidi hivyo, basi hata jina lake litakuwepo kwa rais! Na ikiwa ni hivyo; je, endapo kama rais atakuwa nyuma ya mauaji haya na IGP amekwisha kumpa jina lake, si ataonekana ni kidudu mtu na kutolewa kafara na damu yake kutumiwa kama kitisho kwa wale wote watakaojaribu kupeleleza mauaji haya? Hilo lilimtisha Justin, lakini pia, asingeweza kwenda kulilalamikia kwa IGP, badala yake kama sheria za kijeshi zilivyo, ni kutekeleza amri unayopewa!

    Akiwa katika kutekeleza sheria hizo za kazi, Justin aliirudisha akili yake kwenye kazi na hapo hapo kuyafikiria maisha yake ambayo tayari alikwisha kuyaona yakiwa hataraini! Akaanza kumfikiria mwuaji aliyekwisha kuwaua mawaziri wawili kuwa anaweza kupewa zabuni mpya ya kumwua yeye endapo ni kweli Ikulu itakuwa nyuma ya mauaji hayo au vigogo wa serikali wenye uroho wa madaraka kujihusisha na mauaji hayo watakapomgundua kuwa anajihusisha na upelelezi wa kesi hiyo. Ukitaka kupambana na adui yako, kitu cha kwanza ni kumjua! aliwaza. Kwa wazo hilo akajiona yupo kwenye kumsaka mwuaji aliyetumwa amtafute kwa amri ya mkuu wake wa kazi, lakini pia amejikuta akimsaka mwuaji huyo kama mtu anayeweza kuyaweka maisha yake hatarini. Na kabla hajaingia hatarini, lazima amjue ili ikibidi amuwahi kabla hajawahiwa yeye kama walivyowahiwa Himidu na Ali Othman!

    Baada ya kuimaliza bia yake na giza likiwa linakolea kuingia, Justin aliingia kwenye gari lake na kuelekea Mbezi ya Africana ilipo baa aliyokusudia kufika kwa ajili ya kumwona mlinzi wa kimasai.

    Alifika kwenye baa hiyo na kumkuta mlinzi wa kimasai akiwa ameegemea kwenye ubavu wa moja ya magari aliyokuwa akiyalinda. Mlinzi huyo aliyekuwa amesimama kwa staili ya kuupitisha mguu mmoja juu ya mwenzake akiwa amevaa viatu vya matairi huku lubega lake amelizungushia shingoni na kupozi kwa kuikamata fimbo iliyokuwa mbele yake ambayo aliikita ardhini, alimwangalia Justin tokea alivyotoka kwenye gari lake na kuzidisha ushawishi wa kumwangalia baada ya kumwona akielekea aliposimama.

    “Habari rafiki?” Justin alisema baada ya kusimama akiwa amekabiliana na mlinzi huyo ana kwa ana.

    “Nzuri,” mlinzi alijibu bila ya kutikisika na kuonekana kama sanamu ya kimasai.

    “Unanikumbuka?”

    “Nilikuona hapa jana,” Mmasai alijibu kwa mkato.

    Justin akatafuta njia ya kutaka kuwa karibu naye. “Basi rafiki angalia gari yangu, mimi niko ndani.” Alisema na kuelekea mwelekeo wa kuingia ndani ya baa.

    “Hamna shida,” mlinzi alisema na kumwangalia Justin alivyokuwa akiingia ndani huku akionyesha kutokuwa na dalili ya kuondoka kutoka hapo aliposimama wala kuliangalia gari aliloambiwa.

    Justin alipoingia, safari hii hakukaa kwenye meza ya peke yake, badala yake alikwenda kukaa kaunta na kuagiza bia. Aliinywa bia hiyo kwa lengo la kuvuta muda ili atakapotoka na kuelekea kwenye gari lake, alijua yule mlinzi wa kimasai atamfuata kwa ajili ya kupewa bakshishi na hapo ndipo alipomtega kumnasa mlinzi huyo!

    Alitoka nje ya baa, jambo la kwanza alilolifanya lilikuwa ni kumwangalia mlinzi wa kimasai kutoka sehemu aliyokuwa amemwacha wakati alipowasili. Mlinzi yule hakuwepo! Justin hakujali, hakushangaa wala kuzubaa, akaelekea moja kwa moja mpaka alipokuwa ameiegesha gari yake. Wakati alipokuwa akiufungua mlango wa gari akajiwa na hisia kuwa nyuma yake kuna mtu anayemfuata, akageuka na kumwona mlinzi wa kimasai. Hakujua alitokea upande gani. “Sema rafiki,” alisema.

    “Unakwenda?” Mmasai aliuliza.

    “Ndiyo rafiki,” Justin alisema na wakati huo huo aliutumbukiza mkono mfukoni na kuyaona macho ya mlinzi wa kimasai nayo yakienda sambamba na mwelekeo wa mkono wake.

    “Mbona hukaa sana?”

    Mkono wa Justin ukachomoka na noti ya shillingi elfu kumi kutoka mfukoni. “Nilipita mara moja kumwangalia rafiki yangu kama amefika hapa,” alisema huku akimpa mlinzi huyo ile noti. “Lakini sikumkuta.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mlinzi wa kimasai akasita kuipokea ile noti. “Sina chenji rafiki,” alisema.

    “Chukua tu.”

    “Yote?” Mmasai aliuliza bila ya kuuficha mshangao wake.

    “Chukua yote, wewe ni rafiki yangu.”

    “Nakushukuru rafiki,” Mmasai alisema na kutaka kuondoka.

    “Kama rafiki yangu akija…” Justin alisema kisha, akajifanya kusita huku akizuga kama anayetaka kuingia kwenye gari. “Unamjua rafiki yangu?” alimwuliza Mmasai na kutokuwa na uhakika kama swali lake aliliingiza ilivyotakiwa. Akajilaumu kwa kumchukulia kirahisi mlinzi huyo.

    “Simjui. Yukoje?”

    Swali hilo likampa faraja Justin na kushukuru shillingi elfu kumi yake ilivyomuweka mmasai huyo kwenye unyenyekevu. Vinginevyo, jibu hilo la ‘simjui’ lingetosha kabisa kwa mlinzi huyo kujibu na kuondoka zake.

    “Yeye ni mgeni hapa, sidhani kama unamjua.” Justin alisema.

    “Alishawahi kuja hapa baa?”

    “Alishawahi,” Justin alisema kwa kubahatisha.

    “Kama angekuwa alikuja na gari ningemjua,” mlinzi wa kimasai alisema kwa kujiamini.

    “Huwa unawajua watu wote wanaokuja na gari?” Justin aliuliza na kumwangalia Mmasai kwa umakini. Alihofu Mmasai huyo huenda anajitia ni mjuaji wa kujua kutokana na shillingi elfu kumi aliyompa.

    “Ndiyo!” Mmasai alijibu kwa kujiamini zaidi kuliko mara ya kwanza.

    Justin akaingiwa na wasiwasi zaidi kuhusu Mmasai huyo. “Kwa nini una uhakika huo?” aliuliza.

    “Hii baa, wateja wake ni hao hao kila siku. Wateja wote ni wakazi wa maeneo ya hapa hapa, ndio maana nawajua.”

    Kauli hiyo ya mlinzi ikamfanya Justin awe na wasiwasi na dhana yake kama itakuwa ni ya kweli ya kumuhusisha mwuaji kuwepo kwake hapo muda mfupi kabla hajakwenda kufanya mauaji. Akaamua kubahatisha, “Alishakuja hapa na gari lake kisha, akaja nyumbani kwangu na kusema ameliwacha gari lake hapa. Hukuwahi kumwona mtu aliyeliwacha gari lake hapa na kuelekea huku?” alisema na kuuelekeza mkono wake upande ulipo makazi ya Ali Othman.

    “Ilikuwa usiku?” Mmasai akauliza kwa makini.

    “Ndiyo ilikuwa usiku.”

    “Wewe unakaa huku?” Mmasai aliuliza na kumwangalia Justin usoni kama vile alikuwa akijiuliza; Inakuwaje asimjue!

    “Nimehamia hivi karibuni. Nakaa pale mbele,” Justin alisema na kuelekeza mkono upande ule ule aliouonyooshea mara ya kwanza.

    Kabla ya kuzungumza tena, mlinzi yule alionekana kama aliyekuwa akijaribu kuvuta kumbukumbu. Hatimaye akasema, “Siku za hivi karibuni kama mara mbili au tatu, yuko mtu alikuwa anakuja na gari, alikuwa ni mteja mgeni. Aliingia baa na kunywa bia, lakini mara ya mwisho alipokuja, aliteremka kwenye gari na kunipungia mkono. Mimi nikajua anaingia baa, baadaye nikashangaa kumwona hakuingia, badala yake nikamwona anaelekea huku kwa miguu,” Mmasai alisema na kuelekeza mkono upande wa magharibi ambako Justin alielekeza ndiko anakokaa. “Baadaye alirudi na kuingia kwenye gari lake, nikamfuata ili aniachie hela ya soda. Akaondoka bila ya kunisubiri na kuahidi angerudi, lakini mpaka leo hajarudi. Pengine ni huyo.”

    Justin akajikuta akishindwa kukiamini kilichokuwa kikizungumzwa na mlinzi huyo. “Gari lake unalikumbuka?” aliuliza.

    “Nikiliona nitalikumbuka.”

    “Ni la aina gani? Labda ukiniambia nitaweza kujua kama alikuwa ni yeye kweli.”

    “Unataka kujua jina ya gari?”

    “Ndiyo.”

    “Mimi nitajuaje? Mimi siyo fundi!”

    “Lina rangi gani?”

    “Siikumbuki vizuri sana. Kama likija nitalijua.”

    Justin akataka kumwomba Mmasai ili amwelezee jinsi mtu huyo anavyoonekana na aliisikiaje lafidhi yake ya kiswahili, lakini alisita kufanya hivyo kwa kuhofu kushinikiza maswali mengi ambayo yanaweza yakamshitua mlinzi huyo kuwa, anazungumza na askari.

    “Pengine anaweza akawa ni yeye,” Justin alisema. “Gari lake halikuwa jipya?”

    “Limechakaa chakaa hivi.”

    Justin akacheka huku akiingia ndani ya gari na kusema, “Usiongee hivyo mwenyewe akakusikia…” akaliwasha gari lake na kuondoka.

    Mwuaji anaweza akawa ni mmoja! Justin aliwaza wakati akiliendesha gari lake. Aliwaza hivyo kutokana na utambulishi wa kutambuliwa gari hilo kutokana na uchakavu wake kutoka kwa walinzi wote wawili, lakini alishindwa kuiweka dhana hiyo kwenye uhakika kutokana na mlinzi wa kwanza kutoielezea rangi ya gari na akauona umuhimu wa kurudi tena kwa mlinzi huyo ili akaupate uhakika wa rangi wa gari hilo.





    Alimkuta mlinzi huyo akimwandikisha mteja aliyekuja kulaza gari lake. Mara mlinzi alipomwona Justin akaonyesha kumkumbuka na kumkaribisha.

    “Unaikumbuka rangi ya lile gari?” Justin alimwuliza mlinzi baada ya kubaki peke yao.

    Mlinzi alijaribu kuzivuta kumbukumbu na hatimaye alionyesha uso uliokata tamaa. “Silikumbuki lilikuwa la rangi gani, unajua ni siku nyingi zimeshapita tokea gari hilo lilivyokuja. Hata hivyo nakumbuka halikuwa jeupe ingawa sijaikumbuka rangi iliyokuwa nayo,” alisema.

    “Jaribu kuvuta kumbukumbu vizuri,” Justin alisisitiza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mlinzi akachukua muda kujaribu kukumbuka, hatimaye akaonekana kama kulikuwa na kumbukumbu iliyoanza kumjia. “Ilikuwa kama na rangi nyekundu hivi…kitu kama hicho!” alisema.

    Justin akataka kudadisi jinsi ya mwonekano wa mmiliki wa gari hilo alivyo, lakini hakuona mantiki yake. Kusudio lake la kwanza lilikuwa ni kupatikana kwa gari hilo, alikuwa tayari amekwisha kuwa na mashahidi wawili waliokwisha kumwona mtuhumiwa wake ambao wangeweza kumthibitisha kumwona endapo litafanyika gwaride la utambulisho siku atakayokamatwa. Kuwepo kwa mashahidi hao ilikuwa ni changamoto kwake ya kulitafuta gari ambalo mpaka muda huo aliamini ndilo lililohusika na kumbeba mwuaji kwa matukio yote mawili. Kulipata gari, ndio kumpata mwuaji! Justin aliwaza wakati akiondoka kwenye lindo hilo.



    * * *



    Siku ya pili asubuhi, Justin alikwenda kumwona IGP na kumpa taarifa ya uchunguzi wake.

    “Nina wasiwasi na Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje kuwa, maisha yao yanaweza yakawa hatarini,” Justin alisema.

    “Omar Sharif na Raphael Kibaha?” IGP aliuliza kwa mshangao.

    “Ndiyo, wote hawa ni washiriki wa mtandao wao, Himidu na Ali Othman. Kama ni kweli lengo la mauaji ni kuwamaliza kisiasa, basi hakuna watakao kuwa wanawajua wauaji wa mawaziri hawa wawili isipokuwa ni Omar Sharif na Raphael Kibaha! Na kama itakuwa ni hivyo, basi hata nao nasema, maisha yao yapo hatarini!”

    “Kwa hiyo nao watakuwa wanalijua hilo kuwa, maisha yao yapo hatarini?” IGP aliuliza na macho yake kuonyesha kuingiwa na wasiwasi.

    “Yote mawili yanawezekana, ama wanao wasiwasi huo au kutokuwa nao, itategemea vifo vya wenza wao hao walivyovichukulia. Endapo walivichukulia kuwa ni vya kisiasa; na kama ni hivyo basi watakuwa wanawajua wauaji wa wenzao ni akina nani na hilo moja kwa moja litawapelekea tishio kuwa hata nao wanaweza kufuatilia kuuawa! Lakini kama watakuwa wanashangaa na kujiuliza kwa nini wameuawa, upo uwezekano na wao kuuawa kirahisi kama walivyouawa Himidu na Ali Othman endapo ni kweli mauaji hayo yalikuwa ni ya kisiasa!”

    “Ni kipi kinachokupeleka kusema hivyo?”

    “Moja ya timu iliyokuwa imejipanga kuchukua madaraka katika uchaguzi mkuu ujao na kuonekana mtandao wao ukifanya kazi vizuri ni hawa watu wanne ambao tayari walikuwa na mikutano ya mara kwa mara ya kujiimarisha kabla hata ya kipindi cha kampeni kujulikana kitaanza lini.”

    “Umezipataje habari hizi?”

    “Husna!”

    “Ndio nani?”

    “Aliyekuwa hawara wa Himidu.”

    Inno akatingisha kichwa kukataa. “Nilidhani alikuwa ni mkewe aliyekupa taarifa hizo, kumbe ni hawara! Hawara ana nafasi gani kuyajua mambo ya ndani ya mtu kama Himidu?”

    “Mke wa Himidu ni wale wa aina ya ‘Hewala bwana’ ambao hawana nafasi ya kuyajua mambo binafsi ya mumewe kutokana na kuogopa kupewa talaka endapo atakuwa ni msumbufu wa kudadisi nyendo zake. Mara nyingi nafasi hizo za kuwa mwingi wa udadisi na kujiamini kupita kiasi huchukuliwa na mahawara wenye akili za kumkoroga mtu kimapenzi kwa kutumia uzoefu wao wa ushangingi na hila zao za kingono kumteka mtu wa aina ya Himidu. Husna alimuweka Himidu kwenye kiganja chake na kumfanya Himidu abwabwaje yote yenye mantiki na yasiyo na mantiki alimradi kuthibitisha anammiliki Husna kimapenzi kwa kila hali!”

    “Tuachane na suala la huyo Husna,” IGP alisema. “Turudi kwa Omar Sharif na Raphael Kibaha, kwa nini usiende kuwahoji? Kama kutakuwa na kitu kama hicho unachokizungumza ni dhahiri watakiri, na watakiri kwa sababu kukiri kwao kutawasaidia wapate msaada wa kulindwa na polisi. Isitoshe, kukiri kwao kutatusaidia kuwajua wauaji wa Himidu na Ali Othman.”

    “Haitokuwa rahisi hivyo kama ni kweli mauaji hayo yakiwa yalifanyika kisiasa.”

    “Kwa nini?”

    “Mafia! Mafioso wote sio watu wa kukiri kumtambua adui kwa polisi wakati wakijua ndani ya jeshi la polisi kuna baadhi ya polisi waliopandikizwa na kuwa chini ya malipo ya kundi husika, kufanya hivyo ni kosa na litamgharimu. Litamgharimu kwa kuuawa na pengine sio kutoka kwa adui, inawezekana hata kutoka kwa mtu wake; kwa sababu atakuwa amewashitua maadui na maadui kuichukua nafasi hiyo kujipanga, adhabu ya mtu kama huyo ni kuondolewa maisha yake! Endapo dhana yangu itakuwa ina ukweli, basi si Omar Sharif wala Raphael Kibaha atakayekubali kukiri kuwatambua waliowaua Himidu na Ali Othman. Watakachokifanya ni kukataa ili waonekane na maadui zao hawajui lolote kuhusiana na njama hizo na pale maadui watakaporidhika, ndipo wao huichukua nafasi hiyo kuwafanyia maadui shambulizi la ghafla la kulipiza kisasi.”

    “Unataka kuniambia wao ni mafia?”

    “Wanasiasa wote walioko madarakani ni mafia!”

    “Sasa unataka kuniambia nini? Tusiwahoji kwa sababu ya umafia wao?”

    “Tukawahoji kwa kigezo kipi, Mkuu? Niwaambie kuwa, ni mtandao wao unaoandamwa?”

    Inno hakujibu haraka. Hatimaye akasema, “Wewe una mawazo gani?”

    “Nitamfuata mmoja na nitamwambia kuwa, tumeona maisha yako yapo hatarini kutokana na vyanzo vyetu vya upelelezi. Kwa hiyo nitamshauri awe makini kuziangalia nyendo zake wakati wote. Nitamtahadharisha kuhusu gari tunayoitafuta na kumwomba wakati wowote atakapoiona atoe taarifa kwangu na yeye mwenyewe achukue hadhari ya kujilinda kwani mtu mwenye gari hilo tunamuhisi anaweza akawa ni mtu hatari kwake. Huenda hilo likamsaidia kujiweka kwenye ulinzi wake binafsi na mwuaji asifanikiwe kirahisi kumpata. Isitoshe, inaweza kuturahisishia kumpata mwuaji endapo atawahi kumwona mwuaji kabla ya kudhuriwa na kutuarifu mapema kwa kutuambia mahali alipo na sisi kuchukua nafasi hiyo kwenda kuweka mtego.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa nini tahadhari apewe mmoja? Hatuna uhakika wa kujua ni yupi atakayefuata!”

    “Nilikuwa nina wasiwasi kuwa, endapo wote watapewa taarifa kwa pamoja, wakakutana na kuambiana na wote kupagawa, habari hizi zinaweza zikavuja na kuvifikia vyombo vya habari. Hali hiyo inaweza ikavuruga upelelezi wote kwa sababu hatuna uhakika kama kuna mipango mingine ya kuuawa kwa viongozi, hasa wao. Ni vyema tukampa hadhari mmoja na kumwomba asimwamini mtu yeyote kwa siku za hivi karibuni mpaka hali hiyo itakapokuwa shwari, hii itasaidia kwa mwingine kutojua kinachoendelea kwa mwenzake.”

    “Ni vyema wote wakapewa hadhari hiyo na wote wakaonywa kutomwamini mtu yeyote kwa kipindi hiki,” IGP alisema na kuonyesha kuungana na hoja ya Justin. “Na isisitizwe kwa kila mmoja wao kutomwamini mwenzake yeyote kwa sababu mwenzake huyo huyo anaweza akawa ni adui yake. Hii itasaidia wasiambiane kwa sababu kila mmoja atakuwa hamwamini mwenzake hata kama watakuwa wanawajua kwa pamoja maadui zao wa upande wa pili ni akina nani. Maana kila mmoja itamwingia akilini kuwa, ikifikia kuhadharishwa na polisi, basi itawalazimu kufuata maelekezo na si vinginevyo!”

    Justin akalikubali wazo la mkuu wake na kukabidhiwa jukumu hilo la kwenda kuwaambia kila mmoja kwa wakati wake. Lakini kabla ya kutoka ofisini humo akasema, “Mkuu, nahitaji kuwa na bastola.”

    “Ya nini?”

    “Sijui ni muda gani watauchukua kabla ya mmoja wao kuanza kuliimba onyo hilo kwa mtu mwingine na huyo mwingine akaenda kumwambia mwingine, habari zikavuja na kuwafikia vigogo wa serikali waliopo nyuma ya mauaji haya. Hatimaye ni mimi ndiye nitakayetolewa kafara kwa kujifanya najua kupeleleza mambo. Kumiliki kwangu bastola itakuwa ni njia ya kujilinda endapo mwuaji atapewa tenda ya kuniua!”



    ******



    Tokea awali baada ya vifo vya Himidu na Ali Othman, Omar Sharif alitia wasiwasi kuwa huenda vifo hivyo vilipangwa kwa kudhamiriwa, lakini alishindwa kumuhusisha na yeyote kuhusika na vifo hivyo na pia alishindwa hata kubuni kwa uhakika sababu ya kuuawa kwao. Kuna kipindi alivihusisha na siasa, lakini hilo likamtia mashaka kulikubali kutokana na jinsi mtandao wao ulivyokuwa ukifanya kazi katika kujiandaa kuelekea kwenye kuushika uongozi wa nchi. Kutokana na mtandao wao ulivyo, aliamini kuwa, laiti kungekuwa na mipango yoyote ya kuuawa kwa mmoja wao, habari hiyo ingevuja na kuwafikia kabla ya mauaji yenyewe kufanyika. Vyanzo vyao vya upelelezi vilikuwa na mtandao uliopanuka kuanzia, jeshini, polisi, usalama wa taifa na hata mitaani kiasi kwamba Sharif aliamini visingeshindwa kuzigundua njama hizo. Isitoshe yeye mwenyewe alikwisha kufanya mawasiliano na baadhi ya wahusika wa upelelezi na wakakiri kuwa, hawakuwahi kusikia au kupata tetesi za njama za kuuawa kwa wenzao wawili.

    Akiwa hajui ni njama za kisiasa au ni sababu binafsi zilizowapelekea Himidu na Ali Othman wauawe, Omar Sharif alikutana na Raphael Kibaha pamoja na mtandao wao, kuzungumzia mustakabali wao wa kushika uongozi wa kuongoza nchi katika uchaguzi mkuu ujao. Wakakubaliana kuwa, vifo vya Himidu na Ali Othman havikutokana na uhasama wa kisiasa baada ya duru za kipelelezi kuwahakikishia hivyo. Mkakati ulipangwa upya na wao kubaki kama vinara wakuu, wakachaguliwa wengine kutoka kwenye mtandao wao na kukamata nafasi za wenzao wawili waliouawa na kuhakikisha harakati za kuhakikisha wanaupata uongozi wa nchi unaendelea.

    Lakini siku chache baada ya kuyaweka mambo sawa kwenye mtandao wao, Omar Sharif alijikuta akipata mshituko mwingine baada ya kufuatwa na Justin na kuhadharishwa kuwa, maisha yake yapo hatarini kuuawa! Onyo hilo na mengine ya kumtaka asimuamini mtu yeyote kwa wakati huo na kutakiwa kuwa makini na gari dogo la Toyota Corolla Limited endapo litakuwa linamfuata, vikawa vimemuweka kwenye taharuki iliyomfanya apatwe na shinikizo la damu na kulazwa hospital huku akiwaweka walinzi watatu kumpa ulinzi na amri ya kuwazuia watu kumwona kiholela ikawekwa!

    Baada ya kutoka hospital, Omar Sharif hakumwambia mtu yeyote kuhusiana na onyo alilopewa kwa kuzingatia sharti alilopewa kuwa, asimuamini mtu yeyote kumtaarifu jambo hilo. Hata hivyo, baada ya kutoka hospitali na hatimaye kuona kuwa hakukuwa na dalili zozote za kuandamwa na gari alilohadharishwa nalo na pia kutoonekana mienendo yoyote ya kutilia wasiwasi usalama wake, akawaondoa walinzi wawili wa ziada waliokuwa wakimlinda hospital na kumbakiza mlinzi mmoja ambaye ndiye mlinzi wake wa kila siku. Mlinzi aliyebaki kumlinda ambaye ni mlinzi wake wa kila siku alimtaka alizingatie onyo alilopewa na kumtaka kwa wakati wote wanapokuwa pamoja awe makini kuchunguza kama watakuwa wanafuatiliwa na gari lolote dogo au gari la Toyota Corolla Limited kuukuu lenye nembo ya klabu ya Liverpool kwenye kioo chake cha nyuma na kumwonya kuwa, asipuuzie mwito huo kwani mtu mwenye gari hilo ni mtu hatari na lazima amfahamishe mara moja pindi akiliona!

    Kwa upande wa Raphael Kibaha, yeye onyo hilo alilopewa na mpelelezi Justin, lilimfanya afike mbali zaidi kimaamuzi. Alijizidishia ulinzi wake binafsi na alitumia muda mwingi kubaki ofisini na kila jioni alivyokuwa akirudi nyumbani kwenye msafara wake kulikuwa na gari la walinzi lililokuwa likilifuata gari lake kwa nyuma ambalo dereva wake alikuwa haruhusu gari jingine limkalie mbele yake, na kama ikitokea hivyo alikuwa akihakikisha analipita gari hilo hata ikibidi kwa uendeshaji wa kihuni ili mradi ahakikishe gari la mheshimiwa Raphael Kibaha linakuwa mbele yake! Uamuzi mwingine aliouchukua Raphael baada ya kupewa onyo hilo, alibadilisha wosia aliokuwa ameuandika awali na kumkabidhi mwanasheria wake ili kufariki kwake kusilete misuguano ya kifamilia. Pamoja na kuyafanya hayo, naye kama Omar Sharif, hakumuamini wala kumweleza mtu yeyote kuhusu onyo hilo zaidi ya walinzi wake!





    Ilikuwa ni siku ya ijumaa, siku ambayo Justin aliamka akiwa ni mchovu baada ya hekaheka za usiku uliopita ambako alihudhuria sherehe maalumu ya kuagwa mke wake mtarajiwa. Mara baada ya kutoka kwenye sherehe hiyo, Justin akiwa na baadhi ya ndugu zake na mpambe wake maalumu atakayemsimamia kwenye harusi yake hawakurudi majumbani kwao moja kwa moja, badala yake walikwenda kwenye disco na huko walikunywa na kufurahi na kurudi majumbani kwao majogoo yakiwa yanawika.

    Akiwa na uchovu wa pombe na kukesha, Justin aliamua siku hiyo aitumie kwa ajili ya kupumzika na akili yake kumezwa na tukio analolitarajia kulifanya siku inayofuata, siku ya jumamosi, siku ambayo atafunga ndoa. Pamoja na kwamba kulibaki saa chache ili tukio hilo lifanyike, lakini kwake lilikuwa ni kama tukio linalotarajiwa kufanyika mwaka mmoja ujao! Kwa kuwa alishapanga siku hiyo iwe ya kupumzika, akawa aliishaifanyia maandalizi yake kwa kuchukua chumba cha siku moja kwenye nyumba ya kulala wageni ili akisha amka na kustaftahi ahamie huko kwa ajili ya kuepuka bugudha. Simu yake anayoitumia kwa ajili ya kuwasiliana na watu wa kawaida aliizima, akaiwacha wazi ile yenye majina ya watu muhimu muda mfupi kabla hajahamia kwenye chumba hicho cha nyumba ya kulala wageni.

    Kwa Omar Sharif, siku hiyo ya ijumaa ilikuwa ni siku muhimu kwa ajili ya sala ya adhuhuri kama zilivyo ijumaa nyingine. Akiwa kwenye vazi la kanzu, kofia na koti jeusi, mheshimiwa Omar Sharif akiwa na mlinzi wake waliwasili kwenye msikiti mkubwa ulioko kwenye eneo la Mikocheni B na kupokewa na waumini wenziwe ambao walimpa heshima hiyo kutokana na wadhifa wake wa Uwaziri huku dereva wake akibaki nje akimsubiri akiwa ndani ya gari.

    Ilikuwa baada ya mshuko wa sala hiyo kumalizika, mheshimiwa Omar Sharif aliagana na waumini mbali mbali huku wengine wakiitumia nafasi hiyo kueleza matatizo yanayowazunguka, hatimaye alirudi kwenye gari na kufunguliwa mlango na mlinzi wake. Wakati mlinzi alipokuwa akitaka kujifungulia mlango wake wa nyuma ili aingie kwenye gari, akajikuta akiingiwa na wasiwasi na gari lililokuwa limeegeshwa pembeni ambako ndani ya gari hilo alikuwepo dereva aliyekuwa amekaa nyuma ya usukani akiwa makini kuwaangalia. Kilichomvutia mlinzi kwenye gari hilo ni aina ya gari alilokuwa akiliangalia, lilikuwa limeshabihiana na gari alilohadharishwa nalo, lakini mvuto zaidi ukawa kwa mtu aliyekuwemo kwenye gari hilo kwa jinsi alivyokuwa makini kuwaangalia, akazuga kama hakukiona kitendo hicho.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mlinzi aliingia kwenye gari la mheshimiwa Omar Sharif ambalo ni Land Cruiser la kisasa lionekanalo kuwa ni jipya, akaufunga mlango na kujiegemeza kwenye kiti cha nyuma bila ya kuonyesha ishara yoyote kuwa, kuna gari alilolitilitia wasiwasi. Gari lao lilipoondoka, naye akageuka kitaalamu bila ya kujulikana na kuangalia nyuma. Akaliona gari dogo la Corolla Limited nalo likijitoa kutoka sehemu ilipoegeshwa na kuingia barabarani na kuanza kuwafungia mkia kwa kuwafuata nyuma.

    Mlinzi aliurudisha uso wake na kuangalia mbele bila ya kusema lolote kuhusiana na tukio hilo. Gari lao lilipokata kona na kuingia mtaa mwingine, akageuka tena kwa mbinu ile ile ya kutojulikana kama anaangalia nyuma. Akaliona Corolla nalo likikata kona na kuingia mtaa waliokuwa wao, lakini safari hii likiwa limetanguliwa na magari mawili mbele. Mlinzi akaurudisha uso wake mbele na kutulia bila ya kutamka neno. Pamoja na kwamba alikuwa na uhakika kuibeba bastola iliyojaa risasi iliyokuwa kibindoni mwake, alijikuta akiupeleka mkono wake ilipo silaha hiyo na kuipapasa.

    Gari lao likawa linaelekea mjini, lakini mlinzi huyo akawa amemsikia Omar Sharif akimwambia dereva kuwa wapitie Kinondoni kulikuwa na mtu aliyetaka kwenda kumwona. Kwa kuwa gari lao lilipitia barabara mpya ya Bagamoyo, lilipofika kwenye taa za kuongoza magari likasimama kwa ajili ya kusubiri taa iwaruhusu kukata kona ya kuingia barabara ya Morocco inayoelekea Kinondoni. Walipokuwa wamesimama kuisubiri taa hiyo iwaruhusu, mlinzi aligeuka nyuma na kuiona Corolla ikiwa ni ya tatu kutoka gari yao na ilikuwa imesimama kwenye upande wa barabara wa gari zinazokwenda Kinondoni. Taa ikaruhusu, gari zikaondoka. Kufika mbele gari lao likakata kona kulia eneo la Kinondoni B na kuingia kwenye mitaa ya eneo hilo. Mlinzi aligeuka nyuma, lakini cha ajabu alipoliona gari la Corolla likiwafuata taratibu, mlinzi huyo akashituka, mapigo ya moyo yakaanza kupiga kwa kasi na kujikuta akiukosa utulivu aliokuwa nao awali. Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza tokea aingie jeshi la polisi, kukabiliana na adui mwenye dhamira ya kumwua mtu aliye jirani naye, adui anayehesabiwa kuwa ni mtu hatari! Kisaikolojia, umaarufu wa uhatari wa mwuaji huyo ukawa umemwathiri kiharaka mno mlinzi huyo na kujiona kuwa hata naye anaweza akauawa kama asipokuwa makini na mwuaji huyo ambaye yuko mita chache kutoka alipo!

    Gari lao likapunguza mwendo na kuelekea kando ya barabara ilipo nyumba aliyokusudia kwenda mheshimiwa Omar Sharif.

    “Usisimamishe gari!” mlinzi alibwata ghafla na kuwashitua waliokaa mbele.



    Wa kwanza kugeuka kumwangalia mlinzi huyo alikuwa mheshimiwa Omar Sharif. “Kwa nini?” aliuliza huku swali lake likionyesha kushitushwa na onyo lililotolewa na mlinzi.

    Kabla ya kulijibu swali la Omar Sharif, mlinzi aligeuka nyuma na kuliangalia gari linalowafuata. Akaliona linawakaribia likitaka kuwapita, mlinzi akageuka kwa haraka na kumkabili mheshimiwa Omar. “Lala chini!” alipiga kelele huku mkono wake wa kushoto ukimkandamiza chini mheshimiwa Omar kwenye kiti alichokalia na mkono wake wa kulia ukihangaika kuichomoa bastola yake.

    Omar Sharif akaitii amri ya mlinzi wake kwa kujikunja kwenye kiti huku dereva akihangaika kulikwepa gari la Corolla lililoanza kuwapita kama kwamba alikwisha kupewa onyo dhidi ya gari hilo! Mlinzi akaliona gari la Corolla likiwapita huku dereva aliyemo humo akiwaangalia walivyokuwa wakihangaika. Mlinzi akaduwaa na silaha yake huku yeye na dereva wakishangaa kwa kuliangalia gari hilo likiwapita likiwa limeongeza kasi. Mheshimiwa Omar naye aliinuka kutoka kwenye kiti na moja kwa moja akaliangalia gari hilo lilivyokuwa likitokomea huku akiiona nembo ya timu ya Liverpool iliyokuwa imebandikwa kwenye kioo cha nyuma cha gari hiyo ikimpa utambuzi wa purukushani wa tukio hilo!

    Wote kwa pamoja walikuwa wakitweta na gari lao likiwa limesimama huku nyuso zao zikiendelea kuangalia upande uliotokomea gari la Corolla. Hali ya kutaharuki iliendelea kuwepo kwenye macho yao wakati walipoanza kuwaangalia watu wachache waliokuwepo mtaani hapo ambao nao walikuwa wakiwaangalia.

    “Turudi nyumbani!” Omar Sharif alisema na kujaribu kuutafuta utulivu wa haraka haraka ambao ulionekana kuwa mbali naye. Jasho lilikuwa likimtoka pamoja na kuwa kiyoyozi cha ndani ya gari kilikuwa kikifanya kazi, hali hiyo iliyoonekana kwa mheshimiwa Omar ilianza kuwatia mashaka dereva na mlinzi kuwa, huenda mkuu wao alishapandwa na shinikizo la damu.

    Wakati gari hilo likiwa njiani kuelekea nyumbani kwa mheshimiwa Omar ambako ni eneo la Mikocheni B, kimya cha Omar humo ndani ya gari kiliwafanya na wengine nao waendelee kubaki kimya huku wakisubiri mheshimiwa ndiye aanze kuhoji sakata la tukio lililopita lilikuwaje. Walifika mpaka nyumbani bila ya mheshimiwa Omar kuhoji au kuagiza lolote. Baada ya gari kusimama kwenye uwanja wa kuegesha magari wa nyumbani hapo, mheshimiwa Omar alisema kwa ufupi, “Njooni ndani!” kisha aliteremka kutoka kwenye gari na kuelekea ndani ya nyumba na kuafuatiwa na watu hao wawili.

    “Ulianza kuiona tokea wapi ile gari?” Omar alimwuliza mlinzi wake mara baada ya kuingia ndani. Wote watatu walikuwa wamekaa sebuleni. Kwenye meza kulikuwa na glasi ya maji aliyoiagiza Omar mapema alivyoingia ndani ambayo ilitengeneza umande wa baridi kutokana na maji yaliyokuwemo humo aliyokuwa tayari ameyanywa nusu.

    “Niliiona wakati tukiingia Kinondoni B,” mlinzi alidanganya kwa kuhofia asionekane alizembea kutoa tahadhari ya mapema kama angesema aliliona tokea wakitoka msikitini.

    Omar akamwangalia dereva wake. “Sijawahi kukudokeza lolote kuhusu kutishiwa maisha yangu, ilikuwaje na wewe ukaanza kulikwepa lile gari kama vile ulikuwa unaelewa kinachoendelea?” aliuliza.

    “Niliwahi kumhadharisha,” mlinzi aliwahi kusema kabla ya dereva kujibu. “Alipaswa naye akae kwenye hali ya kujiandaa endapo kutatotekea kitisho cha kuhatarasha maisha yako; na hivi ndivyo alivyofanya baada ya mimi kukutaka ulale chini na yeye muda huo huo akajua kinachoendelea na akaamua kuwajibika kuyaokoa maisha yako kama alivyofanya!”

    Omar aliichukua glasi na kuyanywa maji yaliyobaki. Alipoirudisha glasi kwenye meza akawa hakuuinua uso wake, akabaki amejiinamia na hatimaye kujikuna utosini. Alionekana kutekwa na fikra ambazo hakuonekana kutaka kuzieleza kwa hao aliokuwa nao hapo. Kisha aliichukua simu yake ya mkononi iliyokuwa kando ya glasi na kupiga.



    * * *



    Justin aliamshwa na simu yake iliyokuwa ikiita ambayo ilikuwa kando ya mto aliolalia. Pamoja na kuamshwa na simu hiyo, lakini alionekana kuvutwa zaidi na upande wa kutaka kuendelea kulala kuliko kuipokea simu hiyo. Akaiacha iendelee kuita, lakini ikawa inambugudhi mwenyewe. Akashindwa kuikabili bugudha aipatayo, akajigeuza kivivu na kuichukua simu iliyokuwa ikiendelea kuita. Akaliona jina la mheshimiwa Omar Sharif. Kuliona jina hilo kukamwamsha kikamilifu, akaipokea simu haraka haraka kwa lengo la kuiwahi kabla haijakatika yenyewe.

    “Shikamoo mzee,” alisema baada ya kuipokea.

    “Marahaba Justin,” Omar Sharif alisema kwenye simu. “Mwuaji wangu leo alikaribia kuniua!”

    Justin akajiinua ghafla na kukaa. “Samahani mzee, umesema..?” aliuliza huku akijiweka kwenye umakini wa kusikiliza.

    “Yule mtu wetu mwenye Corolla Limited yenye nembo ya timu ya Liverpool, muda mfupi uliopita alikuwa kwenye jaribio la kutaka kuniua!”

    “Mungu wangu!” Justin alihamanika kwenye simu. “We uko wapi mzee?” aliuliza.

    “Niko nyumbani.”

    “Nakuja sasa hivi,” Justin alisema na kuiondoa shuka iliyokuwa maungoni mwake. Akateremka kwenye kitanda kwa kasi na kuvaa nguo zake kwa haraka haraka kisha, alikwenda kwenye beseni la kupigia mswaki na kunawa uso, akajifuta kwa taulo iliyokuwa pembeni na kuchana nywele.

    Dakika chache baadaye akawa yuko barabarani akiwa ndani ya gari lake akiiminya pedeli ya mafuta kwa mbinyo mkubwa kuelekea nyumbani kwa mheshimiwa Omar. Utulivu aliokusudia awe nao kwa siku hiyo, ukawa umefikia tamati!



    ****http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Jaribio la kuuawa kwa Omar Sharif likaleta sura mpya kwenye vyombo vya usalama na kikao cha wakuu wa vyombo hivyo kikaandaliwa na kujaribu kujikita kwa kina angalau waweze kukijua chanzo cha mauaji yaliyotokea kwa mawaziri wawili na yanayotaka kuendelea kwa mawaziri wengine. Hali halisi ya tukio la kutaka kuuawa kwa Omar Sharif pia, likawa limeweka bayana uwepo wa kachero Justin aliyekuwa amewekwa kwa siri na IGP na kumfanya Inno aeleze kwenye kikao hicho sababu za kumuweka kwake kwa siri.

    Sababu zilizoelezwa na IGP mbele ya viongozi wenzake zikawa zimepata baraka baada ya kuonekana hatua yake hiyo imeleta mafanikio angalau ya kujua kuwa, ni mwuaji mmoja ndiye aliyefanya mauaji hayo na kugundua dhamira yake ya kutaka kuendelea kuua vingozi wengine na ugunduzi huo kusaidia kuyaokoa maisha ya Omar Sharif ambaye alijulishwa uwepo wa maisha yake kuwa hatarini na kupewa hadhari ya gari la Corolla Limited, maonyo ambayo yamefanya kazi na kufanikiwa asiuawe.

    Justin aliitwa kwenye kikao hicho ili kuzieleza fikra zake jinsi aonavyo sababu za mauaji hayo na wengine kutakiwa kuuawa. Justin alikielezea kikao hicho kuhusu hisia zake dhidi ya kundi la Himidu linalotaka kuchukua uongozi wa nchi ndiyo sababu kuu ya mauaji hayo, lakini akashindwa kubainisha ni nani yuko nyuma ya njama hizo. Maelezo yake hayo yakaleta kigugumizi kwa viongozi kukiri ama kutokiri ayasemayo Justin yana ukweli upi.

    Vyanzo vingine vya upelelezi wa uchunguzi wa kifo cha Himidu na Ali Othman ambavyo vilileta ripoti zao bila ya kuwaleta wapelelezi wenyewe kama ilivyokuwa kwa Justin, ripoti zao zikaonyesha kuwa, walikuwa bado hawajamgundua mwuaji wa mauaji hayo na wala kujua sababu za vifo hivyo.

    Kutokana na utata wa baadhi wa vijana wa jeshi polisi kujihusisha kushirikiana na majambazi katika kupashana habari, tatizo ambalo IGP alikiri kuwepo kwa jambo hilo, wakuu hao wa vyombo vya ulinzi, wote kwa pamoja wakakubaliana kuwa, Justin apewe vijana kutoka Usalama wa Taifa kushirikiana naye kuendelea na uchunguzi wa kumtafuta na kumkamata mwuaji huku vijana wa jeshi la polisi nao wakiachiwa waendelee kufanya upelelezi na Mkuu wa Upelelezi nchini moja kwa moja awe analisimamia zoezi hilo kwa upande wa jeshi la polisi; wakati ule upande wa Justin na wenzake ukikabidhiwa moja kwa moja kwa IGP.

    Pamoja na uamuzi huo, kikao pia kikaamua kuzidisha ulinzi kwa mheshimiwa Omar Sharif na Raphael Kibaha kwa kuweka ulinzi wa saa ishirini na nne kwenye nyumba zao na wao wenyewe kutembea na walinzi watatu watokapo nje ya nyumbani, mmoja akiwa amepangiwa kuwepo ndani ya gari linalomchukua mheshimiwa Waziri na wawili wakipangiwa kuwemo kwenye gari litakalokuwa linalifuata nyuma gari la Waziri. Ulinzi huo ukakubalika utolewe kwa kipindi cha miezi sita baada ya hapo kikao kingine cha maamuzi kitafanyika kutathimini kama kutakuwepo na ulazima wa kuendelea kwa ulinzi huo.

    Wote wawili, Omar na Raphael kwa pamoja, pamoja na kupewa ulinzi huo, lakini kwa gharama yao wakajiongezea ulinzi kwenye nyumba zao kwa kuweka nyaya za umeme juu ya ukuta uliozunguka nyumba. Mzunguko mzima wa ulinzi ukawapa faraja.



    * * *





    Kushindwa kumwua Omar Sharif kule Kinondoni B baada ya kumfuatilia tokea asubuhi kulikuwa kumemsonenesha mtu mwenye Corolla Limited. Alikumbuka jinsi alivyoweza kumwandama mheshimiwa huyo tokea akiwa nyumbani kwake na kumfungia mkia hadi Wizarani na kujenga subira ya kumsubiri kwa kukaa nje ya gari na kuzuga kwa kila hali mpaka ilipofika saa tano akamwona tena Waziri huyo akitoka. Baada ya kumwona ametoka, akarudi kwenye gari lake na kuanza tena kumwandama mpaka Msikitini. Huko hakukaa nje kumsubiri Waziri atoke kama ilivyokuwa Wizarani, bali alichokifanya, naye aliingia Msikitini. Akatawadha kwa ajili ya kuchukua udhu kisha, aliingia sehemu ya kufanya ibada na kwenda kusimama msitari wa tatu nyuma kutoka alikokuwa amesimama Omar Sharif ili asije akampotea. Alimwona akisali sala ya sunna, naye vile vile akasali sala ya sunna, baada ya kuisali sala hiyo, naye alikaa kwa ajili ya kusikiliza hotuba ya mawaidha ya sala ya ijumaa yaliyokuwa yakitolewa na Imamu wa Msikiti huku akimwangalia kwa kificho mlinzi wa Omar Sharif ambaye alikaa nyuma ya Omar kuhakikisha usalama wa bosi wake. Hatimaye kwenye muda wa saa saba, sala ya ijumaa ikafanyika. Mara baada ya kumalizika sala hiyo, mtu huyo akawahi kutoka kabla ya Omar na mlinzi wake hawajainuka kutoka. Akarudi kwenye gari lake kumsubiri Omar.

    Alimwona mheshimiwa Omar akitoka huku akifuatwa na mlinzi wake na kuingia kwenye gari lao na kuondoka, naye akaliwasha gari lake na kuanza kuwaandama mpaka Kinondoni B.

    Kutokana na utulivu wa eneo hilo la Kinondoni B ambalo halikuwa na magari mengi wala watu wengi, akajikuta akilifanyia maamuzi ya haraka kuwa ni eneo ambalo lingekuwa zuri kutimiza shambulizi lake, akaomba Mungu gari la mheshimiwa Omar lisimame kwenye nyumba yoyote ya mitaa ya huko kisha, mheshimiwa atoke kwenye gari na kuingia kwenye nyumba hiyo na angeweza kuitumia nafasi hiyo kujipanga kwa kujificha sehemu kumsubiri mheshimiwa atoke kisha amdungue kwa risasi moja tu kama alivyofanya kwa Himidu na Ali Othman halafu atokomee zake kirahisi.

    Lakini wakati akiomba hilo litokee, akaliona gari alilopanda Omar likipunguza mwendo kutaka kusimama kwenye nyumba, mtu huyo akaamini Mungu amelipokea dua lake. Akaamua kulipita gari la mheshimiwa ili aende mbele zaidi kwa ajili ya kuangalia kitakachofanywa baada ya gari hilo kusimama. Akashangaa kuuona mshituko uliowapata akina Omar na wenzake ndani ya gari wakati alivyokaribia kuwapita! Hapo ndipo alipogundua kuwa, njama zake zilikuwa zimegunduliwa!

    Purukushani iliyotokea ndani ya gari ya mheshimiwa Omar wakati akiipita ikawa imemwongezea kumpa picha nyingine kwamba, tayari amegundulika kuwa ni mtu aliyemwua Himidu na Ali Othman. Hali kadhalika akahofu pia, upo uwezekano wa kujulikana kwa njama zake za kutaka kumwua kiongozi mwingine. Kuzinduka kwake huko kukawa kumempa hadhari kuwa, hata naye yuko hatarini kukamatwa!

    Lakini kitu kilichokuwa kikiipa tabu akili yake ni kule kutaka kujua ukubwa wa kutambulika kwake kulivyokuwa. Ametambulika kwa eneo lipi? Wamemtambua kama yeye binafsi na kujulikana sura yake? Au kuna kitu kingine maalumu kilichogundulika na humtambulisha pindi kikionekana? Wazo lake moja kwa moja likaenda kwenye gari analolitumia! Aliamini isingekuwa rahisi kwa mheshimiwa Omar na wenzake waliokuwemo kwenye gari kumtambua akiwa ndani ya gari lake kwa kuiona sura yake wakati walivyokuwa Kinondoni B! Ni wazi watakuwa waliiona gari yangu ndio wakashituka! aliwaza.

    Wazo hilo likampa hatua nyingine iliyomwingiza kwenye mashaka zaidi kwa tathimini aliyokuwa akiendelea kuifanya pale alipoona kuwa, kama ni gari lake ndilo linalotumika kutambulika kwake, basi kwa vyovyote kutakuwa na tahadhari iliyotolewa kwa mheshimiwa Omar au kwa viongozi wote wa juu wa serikali kuhusiana na gari lake hilo na kuamini gari hilo litakuwa linasakwa na askari wa barabarani! Akajiuliza, iliwezekanaje kutembea nalo kwa siku zote lisikamatwe au asikamatwe nalo? Akahisi kuna uzembe ndani ya jeshi hilo wa kutofanikisha kukamatwa kwake kabla hata hajagundua kuwa alikwishajulikana! Alilishangaa zaidi jeshi la polisi kwa yeye kuweza kuitumia nusu ya siku hiyo akizunguka kwa kumfuatilia mheshimiwa Omar Sharif bila ya gari lake kuonekana na askari wa barabarani huku akikumbuka kuwapita hasa katika maunganishi ya barabarani kwenye taa za kuongoza magari; isitoshe ilibaki kidogo tu angefanikiwa kumwua Waziri huyo!

    Tathmini ya mzunguko wote huo ukampa ukurasa wa kuchukua hatua nyingine mpya za kujilinda zaidi na mienendo yake. Awali alikuwa makini na mienendo yake hasa iliyohusiana na gari hilo kwa kutowahi kulifikisha nyumbani kwake tokea alinunue, na kutowahi kumwambia mtu yeyote kuwa anamiliki gari na kutowahi kulilaza gari hilo sehemu moja ya kulazia magari kwa siku mbili mfululizo. Siku zote alikuwa akililaza gari lake sehemu tofauti za kulazia magari na wakati mwingine mbali zaidi na eneo analoishi na kuwa tayari kupata gharama ya kupanda usafiri mwingine wa kumrudisha nyumbani. Lakini kutokana na hofu aliyokuwa nayo ya gari lake hilo kutambulika, mkakati mpya wa kutolitumia kabisa gari lake kwa safari yoyote ili polisi wasije wakautumia mwanya huo kumkamata kirahisi ulihitajika ili gari hilo lisitumike tena kama sehemu ya kumshitua mheshimiwa Omar pindi atakapomwendea tena.

    Lazima nimwue mshenzi huyu! aliapa wakati akipanga mkakati huo na kuirudisha dhamira yake ya kumwua Omar Sharif kwa namna yoyote itakayowezekana kwa kuhakikisha anajiandaa vyema na kusitokee makosa kama yaliyotokea na kuvuruga mpango wake huo…



    * * *



    Nyumba ya mheshimiwa Omar Sharif ilizungukwa na ukuta wenye nyaya za umeme na ilikuwa katikati ya nyumba nyingine za kifahari kwenye eneo la Mikocheni B. Maingilio ya kuingia humo yalikuwa kwenye mlango wenye geti la chuma ambako kulikuwepo na askari wa JKT ambao walibadilishwa kila siku kwa mchana na jioni. Ulinzi huo wa saa ishirini na nne uliwashangaza hata majirani zake na kujiuliza dhamana ya Waziri wa serikali kupewa ulinzi wa aina hiyo ilitoka wapi! Magari yote yaliyoingia yalipekuliwa baada ya mahojiano ya dhati ya kuthibitisha ulazima wa gari kuingia ndani, vinginevyo gari hubaki nje na mwenye gari kuingia kwa miguu. Magari yote yaliyoruhusiwa kuingia ni yale ya Wizarani au yale ambayo wamiliki wake majina yao yalishafikishwa mapema kwa walinzi kuwa, wangefika nyumbani hapo.

    Mwindaji wa Omar Sharif aliyaona mabadiliko hayo ya kiulinzi na kumthibitishia ile dhana yake ya kutambulika ilikuwa ni ya kweli! Kwa kuwa hakuwa na usafiri mwingine baada ya kuacha kulitumia gari lake la Corolla Limited kwa kulificha ndani ya wigo wa nyumbani kwake alikokuwa akiishi peke yake, mwindaji huyo akaanza kutumia utaratibu mwingine wa kufika maeneo ya nyumbani kwa mheshimiwa Omar Sharif kwa kuyapita kwa miguu kama raia yeyote asiye na hatia na kuzuru kwenye ofisi za wizara husika ya mheshimiwa Omar kama mgeni mwingine yeyote, mtu huyo aliweza kuitembelea korido yenye ofisi ya Omar Sharif kwa kiasi cha mara nne bila ya kuwa na wasiwasi wowote wa kushukiwa kutokana na kutokuwa na rekodi ya kihalifu polisi na kugundua kutokuwepo kwa ulinzi thabiti kama ule anaokuwa nao mheshimiwa waziri wakati akiondoka ofisini au ule uliopo nyumbani kwake.

    Watu wote waliokuwa wakiingia kwenye ofisi ya Katibu wake Muhtasi ambayo ilikuwa na watumishi wawili, mmoja mwanamke ambaye ndiye Katibu Muhtasi wa waziri Omar mwenyewe na mwingine mwanamume, waliishia kwenye mlango wenye uwazi wa juu na kuwa kama dirisha ambako walipata huduma za matatizo yao kutoka kwa mfanyakazi huyo wa kiume na hata wale waliokuwa wakija na nyaraka kwa ajili ya kupelekwa kwa mheshimiwa waziri nao waliziacha nyaraka hizo sehemu hiyo na ama kusubiri kushughulikiwa kwa kusubiri kwenye benchi lililokuwa kwenye korido mkabala na mlango huo ama kuondoka kabisa. Pamoja na kuwa na utaratibu huo, lakini mwindaji huyo aliweza kuwaona baadhi ya watu wengine walioonekana kuwa na wajihi wa kibiashara ama wa nyadhifa ya kiserikali wakiwa na mafaili mikononi mwao, wakiingia moja kwa moja na kuwahisi kuwa, walikuwa wakienda kumwona moja kwa moja mheshimiwa Omar Sharif. Mmoja wa watu aliowaona, alikuwa ni mfanyabiashara maarufu mwenye asili ya kiasia aliyeitwa Pal Manjeet!



    * * *



    Kumwona Pal Manjeet kukampa wazo jipya mwindaji huyo na kuanzia wakati huo akaanza kufuatilia habari za mfanyabiashara huyo kwa umakini hasa uhusiano wake na mheshimiwa Omar Sharif.

    Ilimchukua wiki zisizopungua mbili kupata habari zilizotoka kwa watu waliozijua habari za Manjit kwa njia moja au nyingine kama vile wafanyakazi wa benki au wa Mamlaka ya Mapato na wengineo wakati wakiwa kwenye baa wakinywa pamoja. Alichogundua ni kwamba, Manjeet alikuwa ni muhimu kwa Omar Sharif na sehemu kubwa ya urafiki wao ulihusisha dhamana ya uwaziri aliokuwa nao Omar na ufanya biashara wa Manjeet, muungano uliojenga maslahi kati yao. Isitoshe pia, akapata habari za Manjeet kuwa si mtu wa kutulia nchini, mara nyingi alisafiri nje ya nchi. Eneo hilo likawa mtaji kwa mwindaji huyo!

    Ukurasa mpya wa mkakati wake ukawa ni kufuatilia ratiba za kusafiri kwa Manjeet nje ya nchi na wakati mwingine alijikuta akiwavaa kwa ulaghai wa kisanii wafanyakazi wa nyumbani kwa Manjeet wanaoishi uswahilini na hatimaye akabahatika kupata taarifa inayomuhusu Manjeet kuwa, anatarajiwa kusafiri nje ya nchi siku inayofuata asubuhi na mapema na ndege ya Swiss Air kwenda Ujerumani.

    Siku ya pili saa kumi na nusu asubuhi, mwindaji huyo alifika Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere kwa teksi akiwa amevaa suti iliyompendeza na mawani bandia ya macho, akalipa ujira wa teksi kisha akaenda eneo ambalo hutumiwa na abiria wanaoondoka ambao walikwishaanza kujaa. Akaangalia kwa haraka haraka na kutomwona Pal Manjeet, akatafuta sehemu ya kukaa na kuuweka mkoba mweusi wa ofisini kando ya miguu yake na kuupachika mguu mmoja juu ya mwenzake na kulikunjua gazeti alilokuja nalo.

    Hakuweza kulisoma gazeti hilo kutokana na kila wakati kuyaangalia magari yaliyokuwa yakiwasili na kuwateremsha wasafiri, hatimaye gari la kifahari la aina ya BMW Station Wagon liliwasili. Mwindaji akalihisi ni gari litakalokuwa limemleta Manjeet, hakuwa na uhakika kwa nini aliwaza hivyo, lakini aliamini ni kutokana na lile gari kuwa la kifahari lililoendana na hadhi ya Manjeet ndiko kulikomfanya aiweke dhana hiyo. Bashiri yake ikawa ya kweli, Manjeet akateremka kutoka kwenye gari hilo akisindikizwa na mwanamke aliyemdhania angekuwa ni mkewe.

    Manjeet akiwa ameliegesha koti lake mkononi akiwa sambamba na mkewe walipokewa na waasia wengine wawili ambao walitangulia kufika hapo uwanjani kwa ajili ya kumsindikiza. Akiwa anawaangalia kwa kificho, mwindaji alitulia pale pale alipokaa huku akimwona Manjeet akiwa hana dhamira ya kukaa. Akajiuliza, ingekuwaje kama Manjeet angepitia eneo la V.I.P?

    Msururu wa abiria wanaoondoka na ndege ya Swiss Air ulikuwa ukiingia kwa kupita mlango wa abiria wanaosafiri ambao ulianza kupungua na hatimaye Manjeet alijiunga nao na kupotea ndani ya jengo. Mwindaji naye akalikunja gazeti lake huku akiikunjua miguu yake, akainama kuuchukua mkoba wake na kuondoka. Akazunguka upande wa pili ambako alikodi teksi iliyompeleka mjini.

    Saa 2:05 kamili asubuhi ya siku hiyo, baadhi ya wafanyakazi wa Wizarani walionekana wakiingia kwenye geti kuu wengine wakionekana wakizungumza kwa makundi ya watu wawili au watatu na wengine walionekana wakiingia kwa mwendo wa haraka haraka huku wakiwasalimia wafanyakazi wenzao waliokuwa wakiwapita, mwelekeo ulikuwa ni mmoja, wote wakielekea kwenye lango kuu la jengo hilo lenye ghorofa saba. Mmoja aliyekuwa kwenye kundi hilo na kuonekana kuwa na haraka ni mwindaji! Yeye alikuwa ndani ya suti yake nadhifu, mkono mmoja ukiwa umebeba mkoba na mkono mwingine ukiwa ndani ya mfuko wa suruali!

    Aliingia kwenye lifti akiwa na wafanyakazi wa wizara hiyo ambao walikuwa wakizungumza kwa sauti ya juu huku yeye akiwa kimya uso wake ukiangalia juu ya mlango, akiziangalia namba za ghorofa ambazo karibu zote lifti ilikuwa ikisimama na watu kupungua. Lifti ilifika ghorofa ya sita, ghorofa ambayo ndiko iliko ofisi ya mheshimiwa Omar Sharif. Wafanyakazi wa ghorofa hiyo waliteremka, lakini mwindaji hakuteremka. Yeye alikwenda kuteremkia ghorofa ya saba kisha, akatumia ngazi kurudi ghorofa ya sita.

    Korido ya ghorofa ya saba kama ghorofa nyingine za jengo hilo, haikuwa na shughuli zilizoanza kushika kasi kutokana na kutokuwa na wageni wenye shida zao na wizara hiyo, walikuwa bado hawajawasili kwa wingi. Hali hiyo ikajenga ukimya huku wafanyakazi nao wakiendelea kujipanga kwa ajili ya shughuli za siku hiyo.

    Mwindaji alielekea moja kwa moja ilipo ofisi ya Omar ambaye alikuwa na uhakika naye kuwa alikwishawasili. Alikwisha kuliona gari lake likiwa limeegeshwa eneo maalumu ya maegesho ya magari ya wizara kabla hajaingia kwenye jengo hilo. Alifika kwenye mlango wa ofisi ya Katibu Muhtasi wa Waziri unaotoa huduma kwa wageni ambao ulikuwa umefunguliwa sehemu ya juu na kuachwa wa chini ukiwa umefungwa. Hapo alimkuta mtumishi wa kiume aliyekwisha kumwona mara zote alizokuwa akija hapo na kushindwa kupata uhakika kama ni kweli kazi yake ilikuwa ni kutoa huduma kwa wageni au alifundishwa maalumu kuitenda kazi hiyo lakini wakati huo huo akiwa ni mlinzi wa kumlinda mheshimiwa Omar.

    “Karibu,” mtumishi huyo wa kiume alisema.

    “Nataka kumwona mheshimiwa Omar,” mwindaji alisema huku macho yake yakimwangalia mtumishi huyo na wakati huo huo akiyapitisha zaidi na kumwangalia Katibu Muhtasi aliyekuwa kwenye chumba kilichotenganishwa kwa dirisha kubwa la kioo ambaye alikuwa shughulini na kompyuta iliyokuwa usoni mwake.

    “Una ahadi naye?” mtumishi wa kiume aliuliza.

    “Nina maagizo ya mheshimiwa kutoka kwa ndugu Manjeet.”

    “Kama ni Manjeet nenda kamwone yule dada pale,” mtumishi alisema na kunyoosha mkono wake kwa Katibu Muhtasi.

    Mwindaji aliingia ofisini kwa Katibu Muhtasi na kuisikia sauti ya yule mtumishi ikitoka nyuma yake akisema, “Ametumwa na mzee Manjeet!

    “Karibu,” Katibu Muhtasi alisema na kumkabili mgeni aliyeingia kwake.

    “Ahsante,” mwindaji alisema na kusalimia huku akiuweka mkoba wake juu ya meza. “Nimetoka Uwanja wa ndege asubuhi hii kumsindikiza Manjeet,” mwindaji alisema na wakati huo huo akiufungua mkoba wake kwa uangalifu na kutoa bahasha kubwa. “Amenikabidhi hii bahasha ili nimletee mheshimiwa Waziri na ana maagizo ameniambia nimpe mwenyewe.”

    “Ameondoka na Swiss Air?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo,” mwindaji alijibu na kuufunga mkoba wake.

    “Juzi aliniaga kuwa anaondoka leo, kumbe ameshaondoka!”

    “Saa hizi hata huduma za kifungua kinywa watakuwa wanapata au wameshapata.”

    “Lakini mimi sijawahi kukuona! Ulishawahi kuja?” Katibu Muhtasi aliuliza swali la msingi, lakini uso wake haukujenga msingi wa umakini kama swali lake lilivyokuwa.

    “Niliwahi kuja naye mara moja hivi karibuni, lakini nilimsubiri pale kwenye benchi lenu.”

    “Aisii,” Katibu Muhtasi alisema na wakati huo huo akainua simu na hatimaye akasema, “Kuna mgeni wako kutoka kwa mzee Manjeet…Anasema walikuwa pamoja Uwanja wa ndege na ameachiwa maagizo ya kukuletea…” ghafla akakata simu na kumwangalia mgeni wake. “Anasema uende,” alisema.



    ***MWINDAJI amefanikiwa kuifikia na kuingia kimbinu katika ofisi ya waziri Omary…….. nini kitajiri…. Omary hajui hili wala lile…..

    *Kwa nini mwindaji anaua…… na ataua mpaka lini?? Na huyu mwindaji ni nani??



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog