Search This Blog

Monday, 24 October 2022

NI ZAMU YAKO KUFA - 1

 

    IMEANDIKWA NA : JAPHET NYANG’ORO SUDI



    *********************************************************************************







    Simulizi : Ni Zamu Yako Kufa

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Katika riwaya hii safari ya mpelelezi Jacob Matata inaanzia pale anapoitwa na bosi wake ili kwenda Arusha kufuatilia tetesi za kuwepo kwa silaha za hatari katika jiji hilo. Jacob Matata alihisi kuwa ilikuwa ni safari ya hatari, lakini hakudhani kuwa ingekuwa ni hatari kiasi hicho.

    Alipoweka tu mguu wake katika jiji hilo alipokelewa na harufu ya tofauti, si ile ya ubaridi wa Arusha bali ya Mauti. Hivyo kila hatua aliyokuwa akijaribu kupiga ilizidi kumsogeza jirani zaidi na kifo. Mbaya zaidi ni pale alipoambiwa kuwa “NI ZAMU YAKO KUFA”. Hapo ndipo Jacob Matata ilimbidi kupambana na genge la kutisha na lililosheheni sumu ya mauti.

    Hali ya ujanja, ujasusi wa hali ya juu, utaalamu wa kupigana na utumiaji wa silaha inatawala huku pande zote zikihitaji ushindi.

    Sasa endelea nayo

    * * *

    Alhamisi ya Julai 16, 2009 majira ya saa kumi na mbili kamili asubuhi, wakati ambapo hali ya baridi kali ilikuwa imehanikiza mji wa Arusha, gari aina ya Landcruser V8 ilipiga breki mbele ya lango la kuingilia hospitali kuu ya mkoa wa Arusha, Mt. Meru Hospitali. Mlinzi aliyekuwa zamu ya kufunga na kufungua lango kuu la kuingilia eneo la hospitali hii aliingalia gari hiyo kwa sekunde kadhaa huku akiwa bado amejikunyata kwa sababu ya baridi kali. Hakusubiri kuambiwa kuwa alitakiwa kufungua lango la kuingilia katika uwanja wa mbele ya hospitali hiyo, akafanya akafungua mlango huku akitetemeka kwa baridi. Gari iliungurumishwa hadi sehemu ya kuegeshea magari. Haukupita muda mrefu milango yote minne ya gari hilo ilifunguliwa. Lakini zikapita dakika kadhaa bila mtu yeyote kuteremka toka garini. Baadaye kila sehemu ya mlango mguu mmoja ulitelemshwa na kuruhusiwa kukanyaga ardhi ya eneo hilo. Macho ya mlinzi huyu yaliendelea kuwafuatilia wageni hao kwa makini, hakuwa na uhakika kama walihitaji matibabu au walikuwa wamekuja kutembelea mgonjwa. Lakini hili wazo la kuwa watu hao walikuwa wamekuja kutembelea mgonjwa alitaka kulifuta pale alipokumbuka kuwa muda wa kutembelea wagonjwa ulikuwa bado haujawadia. Lakini alipotanabahi kuwa katika nchi yetu hii sheria na taratibu huwekwa kwa ajili ya watu wa kawaida na wasio na vyeo wala fedha alirudia wazo lake la awali kuwa huenda walikuwa wamekuja kuona mgonjwa. Hadhi ya gari na namba zake vilimfanya aamini kuwa gari ile ilikuwa imebeba mkubwa au familia ya mkubwa. “Anayetaka usawa mwisho wake uchawi na sheria hutungwa na wenye madaraka, huvunjwa na wenye madaraka na wenye fedha na hutafsiriwa barabara na kutekelezwa na wasio na lolote” Alijiwazia mlinzi yule huku akiendelea kupambana na baridi kali iliyokuwa ikiachiwa toka kwenye safu za Mlima Meru ambao asubuhi hii ulikuwa ukitabasamu kuelekea uso wa mji wa Arusha.

    Vitendo vilivyofuatia viliuacha wazi mdomo wa yule mlinzi, bila ridhaa yake. Sekunde ya kwanza watu wanne walitoka ndani ya gari kwa wakati mmoja kutokea kila mlango wa gari huku wote wakiwa na Bastola mikononi mwao huku pia Bunduki za kisasa zikiwa zinaning’inia migongoni mwao. Sekunde ya pili aliona hao watu wakitembea kuelekea katika sehemu kulipokuwa na Valanda iliyoishia vilipo vyumba vya wodi za wagonjwa. Jinsi watu hao walivyokuwa wakitembea kwa haraka na hatua zao kufanana alilinganisha na wale mashujaa wa kwenye sinema za mapigano. Walipiga hatua ndefu zilizofanana, walikuwa na makoti marefu yaliyofunika hadi magotini huku hatua zao zikienda kwa pamoja. Vitendo vyao vilifanyika kwa kasi, bila wasi wasi. Walionekana ni watu waliojua nini walikuwa wanafanya. Jamaa watatu walizama ndani ya wodi ya wagonjwa huku mmoja alibaki analinda eneo la nje. Mlinzi kuona hivyo alisisimkwa na kujikuta akipata hamu ya kuona kile jamaa hao walikusudia kufanya. Wazo la kutoa taarifa sehemu husika juu ya ujio wa wale watu lilikuwa mbali kabisa na ufahamu wake, japo aliweza kuhisi hatari kutokana na matendo na vile jamaa hao walivyokuwa wamebeba silaha. Lakini hamu ya kuangalia ile sinema ilimjaa hakutaka kuishia kwenye utangulizi tu ambao alikuwa ameshauona hadi dakika hiyo.

    Kwa hatua za haraka alinyata kupitia upande mwingine ili achungulie kilichokuwa kikiendelea pale wodini. Alifanikiwa kufika mahali dirisha la wodi lilipokuwa lakini hakuweza kuchungulia ndani kwani ghafula alisikia ubaridi wa ajabu ukijipenyeza katika shingo yake, ambao alishindwa kupambanua kama ulikuwa umeandamana na uzito au wepesi, lakini aliweza kuhisi tu nguvu zikimwisha mwilini na kuhisi ngiza totoro limetanda machoni mwake. Nukta chache baadaye alihisi kama mwili wake unatengana naye huku yeye menyewe akiwa anapokelewa giza kama mtu aliyetumbukia kwenye shimo lenye moshi mzito lisilokuwa na mwisho.



    * * *



    Saa tatu na dakika saba asubuhi ya siku hiyo hiyo, yaani inamaana masaa mawili na dakika thelathini na saba baadaye baada ya wale watu kuwa wameingia hospitali ya mkoa wa Arusha, Polisi, wataalamu wa afya, viongozi wa Serikali na wanausalama wengine walikuwa wamekusanyika katika hospitali hiyo hiyo. Lakini safari hii hali ya hewa eneo hilo la hospitali ikiwa imeshabadilika kabisa. Sauti za watu waliokuwa wakitoa vilio vya uchungu zilisikika sambamba na zile za askari Polisi waliokuwa wakijitahidi kuuzuia umati wa watu waliokuwa wakitaka kuingia ndani ya eneo la hospitali. Habari za mauaji ya kutisha zilikuwa zimeshazagaa mji mzima wa Arusha. Hali ilikuwa ya kutisha na kusikitisha eneo hilo.

    “Afande inawezeka wakawa wamemwagiwa Tindikali hawa. We huoni jinsi nyuso zao zilivyokuwa kama kibande cha mkate uliooza na kufunikwa na ule ukungu mweusi” Askari huyu alijaribu kumnong’oneza mkuu wake wa kazi, ambaye hata hivyo hakujibu lolote.

    “Afande Mwita, hebu wasiliana na mkuu wa FFU atuletee kikosi cha ziada ili kuzuia hilo kundi la watu wanaotaka kuingia humu ndani. Lazima wataalamu wamalize kazi yao ndipo ndugu wa marehemu wataruhusiwa kuja kuona marehemu wao” Inspekta Sogoyo alimwamuru mmoja wa vijana wake.

    “Sawa afande” Askari mkusudiwa alijibu na kumalizia kwa saluti

    “Afande! Sauti iliita toka upande mwingine. Inspekta Sogoyo akageuka, nyuma yake upande wa kushoto, macho yake madogo kama ya mchina lakini yanawaka yamtazamapo mtu yakamkazia askari aliyeita. Askari huyu alikuwa amesimama jirani kabisa na mlango wa wodi hii ambayo wakati huu ilikuwa imejaa Madaktari wa Hospitali hiyo ya mkoa ambao walikuwa wakisaidiana na Madaktari waliokuwa wamekuja toka AICC hospitali na ile ya Seliani. Wote walikuwa wameunganisha nguvu katika kutafuta chanzo cha vifo vya wagonjwa ambao waliuawa na watu wasiojulika na kwa namna isiyojulikana.

    “Mtaalamu anasema yule mlinzi hana jeraha lolote, ila inaoneka alibanwa na kitu kama mkono shingoni kwa upande wa nyuma wa shingo” Askari yule alieleza

    “Una maana gani unaposema kitu kama mkono? Inspekta Sogoyo alihoji

    “Anasema kuna alama za vidole, lakini haamini kama nguvu iliyotumika kuivunja shingo ya yule mlinzi kwa kuiminya inaweza kuwa ya mkono tu, kwani kiganja cha binadamu hakiwezi kuwa na nguvu ya namna hiyo!!! Yule askari alijibu huku akijitahidi kupambana na macho ya Inspekta Sogoyo ambayo yalikuwa madogo kama ya mchina lakini makali sana yakuangaliapo.

    “Okay, nitahitaji kusoma taarifa yake ya maandishi hapo baadaye. Kwa sasa mwili wake uhifadhiwe vema” Inspekta Sogoyo alijibu huku akitupia macho yake sehemu ya nje. Kwa kupitia dirishani aliweza kuona umati wa watu ambao ulikuwa ukisukumana na FFU ambao tayari walikuwa wameanza kutumia nguvu kuutuliza.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Oooooophs” Daktari mmoja alisema huku akiwa anavua vifaa alivyokuwa amevaa wakati akiwa anazichunguza maiti.

    “Hii inatisha sana!!!!! Hatimaye daktari huyo alisema katika hali ya kushusha pumzi huku uso wake ukiwa umeelekea juu na macho yake kukazwa darini. Wengine walitulia na kusubiri kusikia atasema nini.

    “Baada ya kupima na kuchukua sehemu ya mwili wa mmoja wa maiti hizi, madaktari wote tuliopo hapa tumefanya uchunguzi wa kina na tumegundua kuwa watu hawa wameuawa kwa chemikali. Ila kinachotushangaza ni kuwa imekuwa ngumu kujua ni kemikali ya aina gani. Maana inaoneka kuwa waathirika ngozi zao nilipokea kitu kama hewa lakini iliyo na unyevunyevu kama ile itokayo kwenye chupa ya perfume, lakini baadae kuna aina Fulani ya wadudu wadogo sana ambao wameweza kuoneka kwenye hii Microscope ijulikanayo kama STEHM, baada ya Microscope nyingine kushindwa, wameoneka. Wadudu hao wameshambulia mapafu na mishipa midogo ya fahamu na kuwaangamiza waathirika ndani ya masaa machache mno….”

    “Dokta, unajua unachoongea ni silaha ambazo huwa tunaziona kwenye sinema tu, au kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa mataifa yenye nguvu Duniani yanazimiliki. Sasa kuongelea suala kama hilo hapa Africa, tena kutumika kwa wagonjwa wasiojiweza sipati mwanga wa jambo hili kama laweza kuwa kweli…” Inspekta Sogoyo aliingilia maelezo ya yule Daktari. Lakini na yeye akakatishwa

    “Sikiliza Inspekta Sogoyo, siongei hivi ili wewe ukubali au ukatae, hapa nachoongea ni hali halisi ambayo sisi kama wataalamu tumeiona kwenye maiti hizi. Na hii ndiyo taarifa yetu kama wataalamu, sasa ni juu yenu kama vyombo vya usalama kuikubali au kuikataa” Daktari yule alisema, huku akionyesha kukereka na jinsi Inspekta Sogoyo alivyokuwa amesema.



    * * *

    Saa saba na dakika saba mchana wa Alhamisi ile ile Arusha ilikuwa kama ilivyokuwa asubuhi. Baridi kali ambayo sasa ilikuwa ikisaidiwa na manyunyu membamba kama steel wire ilikuwa imejiachia kwenye kila kona ya Arusha, jua lilikuwa limejificha kwenye mawingu mazito ambayo yalifanikiwa vyema kuiua miale yake isilifikie ardhi ya mji huo. Lakini pamoja na hali kuwa hivyo, kijasho chembamba kilikuwa kimestawi kwenye paji la uso wa Inspekta Sogoyo. Yalikuwa yamepita masaa kadhaa tangu alipokuwa ametoka Hospitali ya mkoa kushuhudia yale mauaji ya kutisha, ya kinyama. Alikuwa ameshasambaza vijana wake katika maeneo mbali mbali ya Arusha ili kunusa na ikiwezekana kumtia nguvuni yeyote aliyekuwa amehusika na unyama ule. Siku hii pia akaamuru kuwa taarifa yoyote kuhusiana na tukio la asubuhi iende moja kwa moja kwake kwa maamuzi ya haraka. Hivyo basi hiyo saa saba na dakika saba mchana Inspekta Sogoyo akiwa ofisini kwake, simu yake ya kiganjani iliita.

    “Inspekta Sogoyo hapa” Alipokea

    “Koploa Sahani hapa, naongea tokea maeneo ya Sakina huku jirani na Radio Habari Maalum. Kuna mauaji yametokea, nimona nikutaarifu kwa sababu namna majeraha ya maiti hii yalivyo hayana tofauti hata kidogo na yale ya zile maiti kule Hospitali ya mkoa. Hivyo nafikiri yeyote aliyafanya unyama huu hapa atakuwa ni yule yule aliyefanya pale hospitalini…” Maelezo ya Koplo Sahani yalikatizwa na swali la Sogoyo.

    “Wewe umepataje taarifa za mauaji hayo?

    “Nilipigiwa simu na raia mmoja akaniambia kuwa ameona hii maiti”

    “Huyo raia amepata wapi namba yako?

    “Sijui. Sikumuuliza afande.!!! Labda nimuulize sasa hivi maa….” Koplo Sahani alijieleza lakini akakatizwa tena

    “Huyo raia anaitwa nani? Sogoyo alihoji tena

    “Hakujitambulisha jina” Sahani alijibu

    “Nipe namba yake nimpigie. Nitumie namba yake kwa ujumbe mfupi sasa hivi. Fanya taratibu zote za kuichukua na kuhifadhi hiyo maiti.” Inspekta Sogoyo alisema na kukata simu.

    “Kuna simu nitapiga sasa hivi, nataka kujua mmiliki wake ni nani na uifuatilie kujua eneo ambalo hiyo simu itapokelewa. Nikimaliza tu kuongea nahitaji taarifa haraka” Inspekta Sogoyo alitoa maelekezo kwa aliyekuwa upande wa pili wa simu, hii ilikuwa simu nyingine baada ya kukata ile aliyoongea na Koplo Sahani.

    “Baraka weka gari tayari na vijana wa kutosha kwa ajili ya oparesheni, inawezekana muda wa dakika chache zijazo tukajua mtu wetu yuko wapi” Inspekta aliongea na simu hii ya tatu, kabla hajampigia mtu aliyekuwa ametoa taarifa za mauji kwa Koplo Sahani. Baadaye aliingiza namba aliyokuwa ametumiwa na Koplo Sahani, alisogeza dole gumba kwenye kitufe cha kijani, akakiminya. Akapeleka simu sikioni tayari kwa kuongea na yeyote ambaye angepokea.

    “Namba ya simu unayopiga haipatikani kwa sasa, tafadhali……” Hakutaka kumalizia kusikiliza, aliikata na kuitua chini ile simu kwa fujo.

    “Shiiiit!!! Ilimtoka Inspekta Sogoyo. Alinyakua tena ile simu, akatafuta namba fulani kisha akaminya kitufe cha kijani.

    “Yule mtu wetu hapatikani hivyo habari ya kujua yuko wapi haitowezekana kwa sasa. Nachotaka ufanye ni kuniambia mmiliki wa hiyo namba ya simu na alikuwa meneo gani wakati anampigia Koplo Sahani” Inspekta Sogoyo aliamuru na kukata simu bila kungoja maelezo mengine. Aliibwaga chini tena ile simu, muda wote huo alikuwa amesimama. Alitembea hadi dirishani, aliyaruhusu macho yake kusafiri upande wa pili wa jengo alilokuwemo, yakatua kwenye ofisi za ukusanyaji wa mapato mkoa wa Arusha. Ilikuwa wazi usoni kwa Inspekta Sogoyo kuwa hakuwa na amani hata kidogo. Atakuwaje na amani wakati kuna mtu anafanya mauji ovyo ovyo bila kujulikana chanzo wala sababu. Simu aliyokuwa ameicha mezani ilianza kupiga kelele. Kidogo akimbie, alienda haraka akainyakua na kuiweka sikioni.

    “Inspekta kuna mauaji mengine tena yametokea, Koplo Sahani ameuwawa katika mtindo ule ule wa tukio la asubuhi na mchana huu….”

    “Uko wapi?

    “Niko eneo la tukio afande”

    “Eneo la tukio halina jina au utambulisho? Inspekta alifoka

    “Hapa kwenye daraja la mto Arusha jirani na New Arusha Hotel, kabla hujafika mzunguko wa Naaz”

    “Nakuja hapo sasa hivi”Sogoyo alisema huku akiparamia ngazi kushuka chini. Ofisi ya Inspekta Sogoyo iko orofa ya pili katika majengo hayo ya Polisi.





    Dakika tano baadaye Inspekta Sogoyo alikuwa ameungana na askari wengine waliokuwa eneo la tukio.

    “Wewe umesema Koplo Sahani kauwawa mbona hukusema kuwa kuna mtu mwingine kauwawa? Inspekta alimtupia swali Koplo Maganga bila ya kumwangalia usoni, kwani macho ya Inspekta yalikuwa yametuama kwanye maiti mbili zilizokuwa mbele yake. Maiti moja ilikuwa ya Koplo Sahani na nyingine ya raia mmoja, mwanume ambaye alionekana kuwa umri wa kati ya mtu mzima na kijana.

    “Kuna lolote la haja ambalo mmeweza baini hapa? Inspekta Sogoyo alihoji huku macho yake yakiwa bado kwenye zile maiti kama mwanzo .

    “Hakuna lolote la maana” Koplo Maganga alijibu

    “Lisilo la maana je? Aliuliza safari hii macho yake madogo kama ya mchina yakiwa yanamwangalia Maganga.

    “Tumekuta mchoro wa Sungura kwenye kiganja cha Koplo Sogoyo, sasa tumeshindwa kuelewa kuwa alijichora mwenyewe au kachorwa na muuaji!!!

    “Uko wapi huo mchoro?

    “No no no no don’t ever try that, usiguse hata kidogo” Sogoyo alifoka mara baada ya kumuona Koplo Maganga anataka kushika kiganja cha maiti ya Koplo Sanani.

    “Kwa mujibu wa ripoti ya madaktari, muuaji anatumia silaha ya kibaologia kwa hivyo ni hatari sana kugusa gusa chochote kwa sasa bila kuwa na kinga, ndiyo maana uchukuaji na utunzaji wa hizi maiti unafanywa na wao wenyewe Madaktari” Inspekta Sogoyo alifafanua.

    “Okay, nimeona” Hatimaye Inspekta Sogoyo alisema baada ya Koplo Maganga kutumia kijiti kufunua kiganja cha mkono wa maiti ya Koplo Sahani.

    “Hili ni balaa, ila kwa njia yoyote ile lazima huyu mnyama apatikane. Hatuwezi kuendelea kushuhudia huu upuuzi” Maneno yalimtoka Inspekta Sogoyo.

    “Bila shaka na wewe utakuwa umepigiwa na mtu usiyemjua kukupa taarifa za mauaji haya?

    “Ndiyo afande. Ila miye nilifanikiwa kumuuliza jina, hakunijibu akakata simu? Koplo Maganga alisema huku akiwa anaifunika maiti ya Koplo Sahani.

    “Sasa wewe mbona umeleta shuka moja wakati unajua kuna maiti wawili hapa? Inspekta Sogoyo alimuuliza askari mmoja aliyekuwa ameleta shuka ya kufunikia maiti wakati wakisubiri madaktari wafike kwa ajili ya upimaji na ubebaji wa zile maiti.

    “Au unadhani kuna ngazi tofauti ya hadhi ya ubinadamu kati ya askari na raia wa kawaida? Wote ni raia, tena nilitegemea ungemfunika raia wa kawaida ambaye tuna jukumu la kumlinda. Ni aibu kwa askari aliyepewa mafunzo kuuawa pamoja raia wa kawaida” Alisema Inspekta Sogoyo, huku askari kadhaa waliokuwa eneo hilo wakiwa wanaangaliana.

    “Kama hamna shuka ya ziada, hiyo shuka itumieni kufunika hiyo maiti ya raia wa kawaida” Sogoyo aliamuru hukua akiwa anatembea kutoka kwenye bonde la mto. Sehemu iliyotokea mauaji hayo iko upande wa nyuma wa duka la matairi na vipuri vya magari liitwalo Michellin. Upande wa pili ukivuka barabara juu ya daraja hilo ndipo ilipo hoteli ya New Arusha.

    Inspeka Sogoyo alikuwa ameshafika upande wa juu wa bonde hilo sambamba na ukuta wa Michellin, gafula akaropoka.

    “Sungura, sasa nimekumbuka!!!! Kwa nini Koplo Sahani alijichora Sungura” Alikimbia kurudi kule chini bondeni.

    “Hebu tuone hiyo picha ya Sungura iliyoko kwenye kiganja cha Koplo Sahani” Alisema alipozifikia zile maiti. Kwa vile maiti ya Koplo Sahani ilikuwa haijafunikwa, kwa kutumia kijiti kama awali walikipanua kiganja cha Koplo Sahani. Macho ya askari kadhaa yakawa yanauangalia ule mchoro. Ulionyesha wazi kuwa Sungura alyechorwa alikuwa amefumba macho.

    “Okay, mtakumbuka kuwa kule hospitali, alama za viatu vya mtu anayesadikiwa kuwa ni muuaji zilikuwa na picha ya Sungura, mauji ya pili pia yalionyesha unyayo wa kiatu kilichokuwa na picha ya Sungura. Kuna kitu hapa lazima. Ila isiwe shida maana uzuri wa nyavu siku zote ni matundu yake. Samaki anaweza jiona anapita, atashangaa tu mifupa yake imebana” Alisema Inspekta huku akitembea taratibu kwa mwendo wa mtu aliyevaa nguo ya ndani ambayo ni mbichi.



    * * *

    Dakika ishirini baadaye ilikuwa imefika saa Kumi na moja kasoro dakika sita jioni ya siku hiyo hiyo ya Alhamisi Julai 16, 2009, Inspekta Sogoyo alikuwa na jalada jipya kabisa ambalo lilikuwa limebeba karatasi kadhaa. Vituko na mauaji yaliyokuwa yameanza kutokea asubuhi hiyo walikuwa wameshayafungulia jalada. Jalada hilo kwa sasa lilikuwa na ripoti za madaktari kuhusu matoke ya vipimo ya maiti waliokuwa wamekufa mpaka wakati huo. Pia kulikuwa na taarifa za Polisi kuelezea matukio yalivyotokea na ushahidi mbali mbali uliokuwa umepatikana mpaka muda huo.

    Kwa mujibu wa kitengo cha habari na mawasiliano cha jeshi la Polisi mkoa, ilionyesha kuwa mpigaji wa simu aliyewapigia Koplo Sahani na Koplo Maganga alikuwa ni mmoja japo alitumia namba tofauti. Lakini pia iligundulika kuwa mpigaji wa simu, mara zote aliwapigia Polisi akiwa ama jirani sana na eneo la tukio au katika eneo la tukio kabisa.

    “Sungura akiwa amefumba macho, maana yake hajalala, yuko macho na makini kabisa kwa lolote” Inspekta alijisemea katika hali ya kutafuta sababu hasa ya Koplo Sahani kujichora picha ya Sungura akiwa amefumba macho! Inspekta Sogoyo alihisi jasho likiyatekenya makwapa yake japo kulikuwa na hali ya baridi kali. Akatoa kitambaa mfukoni na kufuta paji lake la uso ambapo kulikuwa na ile jasho nyembamba ya baridi. Jasho ambayo inamudu kuipenya ngozi ya baridi kutokana na msukumo mkubwa wa damu unaofanyika ndani ya mwili inayoletelezwa na muhusika kutingwa na mawazo mengi!!!!

    “Ama kweli ukiamua kuuza utumbo basi usiogope kufuatwa na Inzi” Sogoyo alijisemea huku bado akiwa anatajaribu kutafakari nini maana ya Sungura aliyefumba macho. Aliinua mkonga wa simu ya mezani iliyokuwa upande wa kushoto wa meza yake. Alibonyeza namba kadhaa, ambazo hakuhitaji kuangalia mahali kwani inaonyesha alikuwa nazo kichwani.

    “Ndiyo mzee Edson. Habari za siku mzee wangu? Inspekta Sogoyo alisalimia baada ya simu kupokelewa upande wa pili.

    * * *



    Kati ya sehemu zilizojengeka vema katika jiji la Arusha basi ni upande wa nyuma ya mlima kilipo chuo utawala cha nchi za Kusini na Mashariki ya Afrika – ESAMI. Ukifika eneo hilo utatamani kushinda hapo ukiangalia nyumba za kifahari ambazo zimeoteshwa kama uyoga. Maeneo hayo ndipo anapoishi mtu ambaye Inspekta Sogoyo alikuwa amempigia simu. Mtu mwenyewe anaitwa Edson Kinyaro. Wakati simu iliyopigwa na Inspekta Sogoyo inaingia, Edson Kinyaro alikuwa amepumzika nyumbani. Umri wa miaka Sitini na Tisa na hali ya hewa ya Arusha siku hiyo ilikuwa ni sababu tosha ya kumfanya ajikunyate kwenye jiko lake la Dohani akiwa anaota moto.

    “Vipi kijana, mbona sauti yako inaonyesha kuna jambo limekukalia vibaya? Mzee Edson alihoji baada ya kupokea simu ya Inspekta Sogoyo

    “Kwani hujasikia mzee? Inspekta Sogoyo alihojihttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimesikia, lakini si ndiyo kazi yako kijana. Yasipokuwepo hayo na uhalali wa wewe kuwekwa juu ya kikosi cha askari kadhaa walio na dhana na vifaa unakuwa batili” Edson alisema, huku macho yake yakiwa yanang’aa. Alishahisi kuwa kuna jambo kubwa la kiufundi linamtatiza Inspekta Sogoyo. Inspekta Sogoyo hakuwa mgeni kwake, aliujua ujasiri na ushupavu wa Sogoyo, binafsi alimwona kama mmoja wa vijana ambao jeshi la Polisi linafaa kujivunia kuwa nao. Lakini kumsikia Inspekta Sogoyo anaongea kwa sauti ya namna hii, ilimtia shaka Edson Kinyaro.

    “Inspekta, najua kuna mauaji yametokea asubuhi na bado yanaendelea kutokea. Raia wanauwa, askari wanauwa, lakini hizo ni changamoto za kazi, na kutatua masuala kama hayo ndiyo kunakupa uzoefu na promosheni kazini. Sisemi tuombee majanga yatokee ili watu mpate uzoefu wa kazi na kupandishwa vyeo baada ya kuyatatua, la hasha, ila wakati ule tunawafundisha tulikuwa tunawaandaa kwa mambo kama haya” Mzee Edson alisema huku akiwa anajitengeneza vema pale alipokuwa amekaa.

    “Sikiliza mzee wangu, nahitaji kuongea na wewe maana kuna kitu ambacho nahisi unaweza nisaidia ili kutatua. Siyo kuwa naogopa shida, unanijua vema, inapokuja suala la kutetea raia, niko tayari kuifuata mauti ilipo na kupambana nayo. Ila kuna kitendawili ambacho najua kinahitaji siku nyingi kukitegua ila kwa ufundi ulionao na uzoefu wako najua waweza kuwa na walau mwanga juu ya hiki kitendawili….”

    “Kitendawili gani tena hicho Sogoyo? Miye nimeshatundika viatu aisee sitaki tena kuingia kwenye hayo mambo, tena mambo yenyewe ya kipolisi. Kumbuka sikuwahi kuwa Polisi, muda wangu wote nimefanya kazi kwenye Usalama wa taifa kama CID” Edson alijitetea

    “Nakuja tuongee, sitakuchukulia muda wako mwingi…nadhani waelewa kuna mambo hatuwezi ongea kwenye simu….SUNGURA ALIYEFUMBA MACHO Mzee wangu, ndiyo kitendawili chenyewe. Haya naja sasa hivi” Inspekta alisema kwa kushusha pumzi nyingi kwenye kiwambo cha kupokelea sauti cha ule mkono wa simu.

    “Haaaaaaaaah toba, Sungura aliyefumba macho!!!!!!! Hapo kazi ipo haya njoo unisimulie nisikie” Simu ilikatwa.

    Dakika tano baadaye, gari ya Inspekta Sogoyo ilikuwa inaegeshwa kwenye uwa wa ndani wa nyumba ya Edson Kinyaro.

    “Karibu kijana, keti kitini” Edson Kinyaro alikaribisha baada ya Inspekta Sogoyo kuwa ameingia ndani.

    “Asante mze, naona wajibanika tu motoni hapo”

    “Nitafanyaje mwanangu, hii hali ya hewa na umri huu basi inakuwa shida kweli kweli!!!

    “Ila una mwili mzuri sana Mzee Edson, unajua mtu akiangalia mwili wako hawezi amini kuwa unabeba miaka uliyonayo. Unaoneka mtu wa kati ya miaka arobaini na tano hadi hamsini hivi”

    “Aaaaah nashukuru, ila tofauti naiona kwenye uwiano wa akili na vitendo. Akili bado inauwezo wa kuwaza kwa kasi lakini mwili unashindwa kuendana na kasi ya akili, hapo ndipo najua miye siyo yule Kinyaro ambaye watu walikuwa wakihangaika kuonana na miye miaka ile nikiwa kazini”

    “Aaah ha ha ha ha” Wote walicheka

    “Ndiyo niambie kijana, kuna nini kinakusibu?

    “Aaaah mzee wangu si unajua Visima vya kale havifukiwi! Inspekta Sogoyo alisema huku akikunjua karatasi fulani nyeupe.

    “Kuna hii picha” Inspekta Sogoyo sasa alisema huku akikabidhi karatasi iliyokuwa na mchoro.

    “Leo asubuhi baada ya mauaji ya pale hospitalini, kati ya alama ambazo vijana wangu waliweza kuzipata eneo la tukio ni alama ya soli ya kiatu. Alama hii ilipatika eneo ambalo ulikutwa mwili wa mlinzi wa hospitali. Lakini pia alama hii ya viatu iliishia sehemu ambayo gari lililokuwa limebeba wauaji lilikuwa limeegeshwa. Alama hii pia imekutwa sehemu ambayo tuliukuta mwili wa raia aliyeuwawa mchana wa leo hii hii kule maeneo ya Sakina. Alama hii hii tumeikuta tena sehemu ambayo tumezikuta maiti za Koplo Sahani na raia mwingine waliouawa alasiri hii. Kilichonifanya nitilie maanani alama hii ya Sungura aliyefumba macho ni pale tulipokuta Koplo Sahani ambaye pia ameuawa alikuwa ameichora alama hii kwenye kiganja chake cha mkono” Alipofia hapo, Inspekta Sogoyo alivuta pumzi, huku akiwa anaminya minya vidole vyake. Muda wote huo, Edson Kanyaro alikuwa ameshaiweka pembeni ile karatasi akawa anamsikiliza Inspekta Sogoyo, bila kumuangalia macho yao wote yalikuwa yameelekezwa kwenye moto.

    “Nimejaribu kuunganisha hii picha na tukio lolote au taarifa yoyote lakini sijafanikiwa. Kwa taarifa nilizo nazo hakuna kampuni ambayo inatengeneza viatu vyenye soli yenye picha ya Sungura. Hivyo kuna uwezokano mkubwa kuwa picha hii ni maalumu na inatambulisha kitu fulani. Na inawezekana inabeba ujumbe Fulani toka kwa yeyote aliye nyuma ya matukio haya” Inspekta Sogoyo alizidi kueleza kwa tuo kama mtu ajielezaye mbele ya Daktari.

    “Nimefikiria mtu anayeweza kunipa mwanga wa hili suala, nikapata majina mawili. Moja ni wewe na jingine ni mkuu wa usalama wa taifa aliyeko sasa baada ya wewe kustaafu. Mkuu aliyeko sasa ni mtu mwenye majivuni makubwa hivyo sijawa huru kumuomba ushauri wake, nimekimbilia kwako” Sogoyo alisema huku akiwa anamwangalia Edson kwa upande wa kulia. Mzee Edson hakujibu kitu, aliinuka toka kitini na kuelekea chumbani. Baada ya kama dakika tano alirejea.

    “Mzee naona hujabadilika kabisa, tabia zako bado ni zile zile kama wakati ule ukiwa kitengoni” Sogoyo alisema baada ya mzee Edson kuwa amerejea toka chumbani. Alikuwa kimya tena kwa muda bila kusema neno.

    “Sogoyo, mtu anayefanya haya mauaji ni moja kati ya watu waliokuwa vijana wangu wa kutegemewa katika idara ya Usalama wa Taifa miaka ile. Lakini kwa sababu ya tamaa ya pesa aliasi na kukimbilia Zaire ya wakati huo ambayo sasa ni Congo DRC. Kutokana na uwezo wake na ufundi wa kupigana na mambo ya kijasusi, Raisi wa wakati ule, Mobutu Sseseko alimchukua na kumfanya kuwa miongoni mwa watu wake wa siri.” Hatimaye Edson alisema safari hii akiwa anamwangalia Sogoyo machoni.

    “Vijana wanne kati ya watano niliokuwa nao, walikuwa wanapenda kutumia alama ya wanyama kama utambulisho wao. Kijana mmoja tu hakuwa anatumia utambulisho kama huo. Nasikitika kusema kuwa vijana wengine wawili walikuja kutoweka baadaye, hadi leo hii haijulikani wako wapi. Hatujui kama wamekufa au wako hai. Mmoja aliyekuwa anatumia alama ya Paka aina ya Amazon yaani Amazon Cat [Soma Kitabu cha riwaya ya Heka Heka utamwona huyu] yeye alipoenda kwenye mafunzo ya juu zaidi hakurudi na wala hatukuwa na taarifa zake hadi alipoibuka mwaka jana katika kile kisa cha kusisimua HEKA HEKA. Nadhani unaelewa namwongelea nani? Mzee Edson alimkazia macho Sogoyo.

    “Unamwongelea yule Jasusi aliyeuwawa mwaka jana katika lile tukio la kuiba meno ya Tembo?

    “Ndiyo huyo huyo” Edson aliitikia

    “Ndiyo, sikuwa namjua kabla ila baada ya kuuwawa na Jacob Matata, ndiyo nikajua kuwa alikuwa naitwa Ben au Kiroboto!!!! Inspekta Sogoyo alisema.

    “Basi huyo pia alikuwa kijana wangu japo alipokwenda kwenye mafunzo ya mwisho hakurudi tena Tanzania na wala sikuwa na taarifa zake. Kwa hiyo kati ya hawa watatu waliotoweka na ambao hatujui kama wamekufa au la mmoja alikuwa anapenda sana kutumia alama ya Sungura aliyefumba macho kama alama yake. Bila shaka unaelewa sifa za Sungura; akiwa amefumba macho ina maana hajalala, na macho yakiwa yamefumbuliwa ina maana amelala. Sungura anajiamini kwa mbio fupifupi na haoni shida kuwa jirani na adui maana anajiamini kwa chenga. Hizo ndiyo zilikuwa sifa za huyo kijana wangu. Yeye alikuwa hamkwepi adui hata siku moja, alikuwa akiwasaka na kuwafuata hadui katika himaya zao. Kijana huyu alikuwa mjanja kupindukia, kama Sungura. Kwa hii alama na vitendo vilivyokwisha fanyika, nina hakika kabisa kuwa huyu kichaa yuko hapa mjini. Na kama yuko hapa mjini basi kazi ipo kweli kweli. Inabidi ujipange sawa sawa Sogoyo…..”

    “Jina lake halisi anaitwa nani? Inspekta Sogoyo aliuliza





    “Mtu akishaondoka kwenye timu na tukawa tunajua ni mtu hatari sana, jina lake linabaki kuwa kitu cha siri ambacho kitafia vifuani mwa wanaojua. Tunafanya hivi ili hata ikitokea akafanya madhambi nchi nyingine hatutaki wamuhusishe na sisi. Huwa tunaharibu jina lake katika kumbukumbu zote ambazo limewahi kuwepo. Hivyo jibu naloweza kukupa ni…sijui jina lake halisi”

    “Kwa hiyo kati ya vijana wako safi watano hakuna hata mmoja aliyebaki kuwa msafi? Inspekta Sogoyo alihoji huku akishusha pumzi.

    “Aliyemuua Kiroboto mwaka jana yeye ndiye pekee aliyebaki upande wa serikali japo si rahisi kumpata maana hajihusishi na serikali moja kwa moja, mmoja atakuwa ndiyo huyu ambaye unatakiwa ukabiliane naye hapa Arusha sasa, wengine wawili sijui wako wapi na sijui majina yao kama nilivyokuambia. Mmoja ndiyo aliuawa mwaka jana” Edson alisema huku akijinyoosha na kisha kumimina kahawa kwenye kikombe.

    “Haina shida nadhani tunaweza kabiliana naye tu, tutamshinda tu. Nikimpata nitamfikishia salamu zako kabla sijaweka risasi ya mwisho kwenye kichwa chake. Maana mijitu kama hiyo ukiipata unaua pale pale halafu unaandaa sababu safi za kuhalalisha kitendo chako” Inspekta Sogoyo aliongea kwa sauti ya jazba kidogo.

    “Naomba Mungu mumpate, na kama kweli ukimpata mfikishie salamu kama ulivyosema. Ila najua haitakuwa kazi rahisi, kumbuka hapa mnapambana na mtu mwenye uwezo wa kumaliza kikosi cha jeshi la watu Mia moja yeye peke yake. Ninaposema vijana safi namaanisha walikuwa vijana safi, ambao Nyerere mwenyewe alikuwa anaelewa kuwa ana watu kama hao….”

    “Sasa mzee Edson naona unanitisha sasa” Sogoyo alifoka.

    “Sikutishi, nakuambia hali halisi, kumjua mpinzani wako inasemekana ni nusu ya ushindi. Nakuambia hivi ili ujue namna ya kupambana na huyu mtu. Hata miye najuta kwa nini niliwaacha hai hawa vijana, nadhani kuwaacha hai lilikuwa ni kosa la kifundi ambalo madhara yake nayaona sasa” Mzee Edson aliongea kwa unyonge na sauti ya kusononeka.

    “Tutampata tuu, wala usijali. Miye Sogoyo. Nina timu ya vijana safi ambao kwa pamoja tunaweza utifua mjiu huu juu chini hadi mtu wako apatikane. Labda akimbie mji mambo yakishamkalia vibaya, la, nitakuletea kichwa chake hapa utoe salamu za mwisho!!!!

    Inspekta Sogoyo alisema huku akiwa anainuka tayari kwa kuondoka.

    “Nani wa kukimbia? Edson aliuliza kwa sauti ya chini

    “Huyo mtu wako” Sogoyo alisemahttp://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Inspekta, kuwa makini kijana wangu, unaingia kupambana na fundi hasa” Edson alisema, kisha akaongeza.

    “Yule ni mtu ambaye kama anakutaka hata wewe anaweza kukufuata kituoni, ukiwa umezungukwa na askari wako”

    “Inaonekana wamfagilia sana huyo mtu wako!!! Sogoyo alisema kwa sauti ya mashaka kidogo.

    “Sogoyo, usipoteze moyo wa mapambano, wakati mambo yanapokuwa magumu ndipo tunapoweza kuwatambua watu wagumu pia. Nakutakia mafanikio katika kazi yako, ila kuwa makini sana kwa kila ufanyalo kuanzia sasa” Mzee Edson Kinyaro alisema kisha wakapeana mikono kama ishara ya kuagana.

    “Je, wahitaji kubaki na hii karatasi? Sogoyo aliuliza

    “Hapana, kwenye kazi zetu tulikuwa hatupendi kukaa na ushahidi bila sababu” Mzee Edson alisema huku akiwa anaifinyanga ile karatasi yenye mchoro wa Sungura aliyefumba macho, akaitupia kwenye moto.

    Ilikuwa inagota saa moja kasoro dakika sita jioni wakati ambapo Inspekta Sogoyo alipokuwa akiondoka nyumbani kwa Edson Kinyaro, mkuu wa zamani wa idara ya usalama wa Taifa.

    Sogoyo alipoondoka, Edson alijibwaga kwenye moja ya sofa zilizokuwa pale sebuleni, huku akionekana mwingi wa mawazo.

    “Shiiiit, Max amekuja Tanzania kutafuta nini!!!!!! Edson alijikuta akiwaza kwa sauti. “Mbona hatari sana, kuna jambo kubwa linaendelea hapa Arusha, Max hawezi kuja Arusha hivi hivi. Mshenzi huyu huwa akianza kuua huwa inakuwa nghumu sana kupata namna ya kumzuia, any way dawa yake ni moja tu……!!!!! Edson aliendelea kuwaza kwa sauti huku safari hii akiwa anajizoa zoa toka pale kwenye sofa alipokuwa amejibwaga hapo awali.

    “Ama kweli, hata kama mavi ya kale hayanuki lakini bado ni najisi” Alijisemea mzee Edson huku akinyanyua kikombe cha kahawa.



    * * *

    Inspekta Sogoyo aliendesha gari taratibu wakati akiwa anapita eneo la Nane Nane jirani na kiwanda kilichokufa cha General Tyres. Kwa jinsi alivyokuwa amekaa nyuma ya usukani ungeweza dhani ni mtu mwenye raha zake anaelekea sehemu za burudani kuiridhisha nafsi yake. Akili yake ilikuwa akiwaza mambo mengi wakati simu yake ya mkononi ilipoiita.

    “Sogoyo hana naongea”

    “Afande kumetokea mauaji tena, safari hii watu watatu wameawa, wanne ni Koplo Maganga” Upande wa pili ulisema.

    “Taarifa yoyote ya kutusogeza kwa muuaji? Inspekta Sogoyo alihoji huku akiingiza gia kuliamuru gari liongeze mwendo.

    “Hakuna ila ni ajabu sana kwa vile mauji ya safari hii yamefanyika jirani sana na zilipo ofisi zetu afande. Huyu muuaji sijui anajiamini nini, amediriki kufanya mauaji pembezoni mwa majengo ya ofisi za Polisi!!!!!!???? Upande wa pili ulisema kwa sauti ya mshangao iliyochanganyika na mfadhaiko.

    “Moto wa makaratasi hauwaki ukakesha, ngoja tuone” Inspekta Sogoyo alisema huku akipangua gia nyingine kwa fujo na kuacha gari ikilalamika na kuongeza mwendo zaidi. Hata alipofika kwenye tuta la pale relini kwenye mchepuko wa kwenda zilipo kotazi za NSSF Njiro wala hakupunguza mwendo. Alipita kiwanda cha Pepsi Njiro akiwa kwende mwendo wa Mia moja na ishirini.



    * * *



    “Unamwona afande wako huyo anapita, nadhani kishapewa taarifa za mapigo mengine. Namuhurumia anaweza vua nguo huyo. Hajui kuwa anacheza na maji yaliyomzidi kimo na ufundi wa kuyaogelea. Ha ha ha ha Nyani hurukia miti yote,lakin sio wa miba” Jamaa huyu alisema kwa majivuni baada ya wao kuiona gari ya Inspekta Sogoyo ikiwa inapita hapo maeneo ya Nane Nane. Walikuwa ndani ya moja ya vyumba vya biashara eneo hilo ambalo linatazamana na kiwanda cha Fibre Board, wote walimwona Inspekta Sogoyo wakati anapita kuelekea nyumbani kwa Edson Kinyaro. Kwa hofu kwamba Inspekta Sogoyo atajua ukweli kuhusu Max, mmoja alipendekeza wammalize kwa kulipua gari ya Inspekta Sogoyo atakapopita wakati akienda kwa Edsoni Kinyaro. Lakini Max alikataa hilo wazo.

    “Najua mzee Edson hawezi kumpa askari Polisi taarifa zozote za siri. Sababu ni nyingi lakini pia anajua wazi kuwa Inspekta hawezi kukabiliana na mimi hata akija na jeshi lake zima. Hivyo kumpa jina langu na hata sura yangu anajua fika atakuwa anasaidia kufanya mauaji badala ya kutatua tatizo” Max alisema huku akiendelea kusafisha bastola yake ambayo alikuwa ameisambaza mezani vipande vipande. Baada ya maelezo hayo wenzake wanne aliokuwa nao kwenye chumba hicho walibaki kimya wakimuangalia.

    “Haina shida, najua namna tutakavyomchukua Inspekta Sogoyo” Max aliwaondoa wasi wasi wenzie.



    Max ama The Fuse kama mzee Edson alivyosema, alikuwa mmoja wa vijana watano waliofuzu mafunzo ya juu kabisa ya ufundi wa kupigana na ujasusi. Utakuwa sawa kapisa kama kwa sasa ungeweza kumwita the world class assassin. Max mwenyewe hujifariji siku zote kwa kusema kuwa; kuna tofauti ndogo sana kati ya malaika na shetani. Mwanzo wote walikuwa malaika, wakati wengine wakibaki malaika hawa wengine wakataka kuwa malaika huru na hivyo jina lao likabadirika kuwa shetani. Kwa vile hawako katika sharia za Mungu. Malaika anaweza kuwa Shetani ila shetani hawezi kuwa malaika wa Mungu tena. Hiyo ndiyo tofauti ya wapelelezi (Spies) na wauaji (Assassin). Hakujutia kitendo chake cha kuasi kwani kwa mtazamo wake kimemfanya kuwa huru na kutumia ufundi wake kwa kiwango cha juu zaidi.

    Tangu alipoasi miaka ile, Max alitumia muda mwingi akiwa nchini Zaire na kuwa moja kati ya vifaa vya karibu vya mkono wa kushoto, si wa kulia, wa kushoto wa Raisi wa wakati huo Mobutu Ssseseko. Tangu kufa kwa Mobutu hadi miaka ya karibuni Max alikuwa ameshashuhudia mambo mengi ana mabadiliko mengi sana nchini Congo DRC ambalo ni jina jipya iliyobatizwa nchi hiyo. Kwa muda wote huo ameweza kujifunza kuwa ujasusi ndiyo huongoza nchi, kuchagua maraisi na hata kubadili majina ya nchi. Japo wengi huamini kuwa nchi huongozwa na Raisi na Katiba ambayo hupewa uhai na Bunge, lakini uzoefu wake unamwambia kuwa kila nchi ina kitengo cha ujasusi na hivyo ndiyo huliongoza taifa na kumwambia Raisi nini cha kufanya. Mwaka 1971 alishuhudia jinsi Joseph Désiré Mobutu alivyobadili jina lake kuwa Mobutu Sese Seko hakuishia hapo tu, kwa sababu zile zile za kijasusi zilizomfanya abadili jina lake mwenyewe mwaka huo huo akalazimika kubadili jina la nchi toka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuiita Zaire. Hapo akaridhika na kuiendesha nchi. Lakini pia jenerali Kabila alipoichkua nchi mwaka 1997 kwa sababu zile zile za kijasusi akaamua kurudisha jina la awali na sasa haiitwi tena Zaire bali Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.



    Na sasa Max yuko Tanzania, Arusha, kwa kazi maalum kama mwenyewe anavyosema.

    “Najua afande kisha changanyikiwa hadi sasa. Nyie endeleeni na shughuli nyingine na kupata muda wa kupumzika. Kazi tuliyofanya hadi sasa inaridhisha sana. Nitawapa taarifa wakubwa kuwa tumeshaanza kuitingisha Arusha, lakini najua hata kabla sijawapatia watakuwa wameshaanza kuzipata kupitia vyombo vya habari. Kwa sasa macho yangu na masikio yangu mawili nayaelekeza kwa Mzee Edson Kinyaro. Najua atakuwa ameshajua kuwa niko hapa mjini kutokana na alama fulani ambayo nimekuwa nikiiacha katika maeneo ya tukio. Katika wapelelezi wote tunaotakiwa kuwaua, kazi kubwa itakuwa namna ya kumuua Jacob Matata. This is my old friend, work mate na pia mwalimu wetu ni mmoja. Ila najua namzidi uzoefu, yeye ameendelea kuwa malaika wakati miye ni shetani sasa. Najua Edson anajua kama kuna mtu wa kuweza kunidhibiti miye kwa lolote nililokusudia kufanya, japo hajui ni nini nataka kufanya, basi mtu huyo ni Jacob Matata. Hatutakiwi kuwauwa Inspekta Sogoyo na Edson Kinyaro kwa sasa. Inspekta Sogoyo tunamwacha hai ili aendelee kueneza habari zetu. Edson tunamwacha ili atusaidie kupata nyendo za Jacob Matata. Akishatuletea tu Jacob Matata basi tunammaliza Edson na Matata pamoja. Nadhani hadi hapo tutakuwa tumemaliza kazi kwa awamu ya kwanza” Max alielezea, wakati huu alikuwa ameshamaliza kusafisha bastola yake.







    * * *

    Siku iliyofuata yaani Ijumaa ya Julai 17, 2009 majira ya jioni, tetesi ya kwanza ilipomfikia Jacob Matata hakushtuka sana kwa sababu hakuipa uzito, kwani aliyeitoa hakumwamini vilivyo. Jambo jingine ni kwamba isingekuwa busara kwa mpelelezi wa hadhi kama yake kuamini mara moja maneno ya kijiweni. Mkusanyiko wa vijana mtaani usio rasmi kwa ajili ya kusimuliana mambo mbalimbali ya kila siku, wenyewe huuita Kijiwe. Kijiwe kilichotumiwa na vijana hawa kilikuwa maeneo ya Kinondoni-Mkwajuni pembezoni mwa baa moja maarufu sana eneo hilo iitwayo Ufipa Bar. Hapo ndipo Jacob alipohakikisha kuwa anajichanganya na vijana hao ili kupata habari mbalimbali zihusuzo vijana na jamii kwa ujumla.

    Pamoja na kuwa alikuwa ni mtu mwenye majukumu mengi na muhimu, Jacob Matata bado alikuwa akiamini jambo moja, nalo ni kuwa; kama unataka kutatua matatizo yanayoikabili jamii basi huna budi uwe na muda wa kukaa na jamii hiyo. Aliamini kuwa fimbo ya mbali haiuwi nyoka. Nadhalia hii ndiyo iliyomfanya atenge muda wake kwenda kukaa kijiweni kila apatapo nafasi mida ya jioni. Japo alionekana kuwa na ufahamu wa juu kuliko wao, lakini vijana wenzie hawakusita kumshirikisha na kujadili mambo kadha wa kadha pamoja naye. Hawakukosekana waliomtilia shaka juu ya uamuzi wake wa kujichanganya pamoja nao. Sababu kuu ni kwa vile vijana wengi wenye hadhi kama yake hawakuwa na desturi ya kukaa kijiweni hapo. Wamekuwa wakijitenga na jamii ya chini kwa kigezo kuwa kukuaa nayo wala haikuongezei kitu chochote – Hwana mawazo. Huku wakisahau kuwa ustawi wao hao vijana wanaojiita wameendelea kwa kiasi kikubwa unategemea utengemavu wa hawa vijana wa kijiweni. Pia Jacob aliamini kuwa kama vijana walio elimika na kuafikiwa kimaisha wakijitenga na wale ambao hawako vema je nani atawasaidia hawa ambao bado hawajatoka, hata kimawazo tu.

    “Ee bwana ee hii nchi imevamiwa”. Alianza Idrisa kijana ambaye alikuwa maarufu kwa michapo ambayo isingekuwa rahisi wenzie kuipata. Alisita kidogo wakati Jacob alipowasili kijiweni hapo na kuwasalimia wote kabla hajachukua jiwe lililokuwa pembeni na kutia kitako.

    “Eee, kwani vipi mshikaji Idrisa?” Mmoja alidadisi katika hali ya kumtaka Idrisa aendelee.

    “Kuna skendo moja nimeipata inashangaza”. Alitulia kidogo. “Nasikia kuna watu fulani kutoka mamtoni wameingia hapa nchini wakiwa na silaha za maangamizi, silaha hizo ni za vijidudu ambazo huwa mnasikia zinatengenezwa huko mamtoni. Sasa jamaa wamekuja nazo huku ili kuzifanyia majaribio...” Alisema Idrisa huku akiomba aongezewe kahawa katika kikombe chake.

    “Hiyo haiwezekani, we unafikiri hii nchi haina ulinzi? Isitoshe silaha hizo ni hatari sana, ikipigwa kama hapa inaweza kumaliza nchi nyingi sana kwa muda mfupi” mmoja alipinga huku wengine wakitingisha vichwa kama ishara ya kuafikiana na huyu aliyepinga.

    “Jamani tusimpinge Idrisa kwani hatuwezi kujua mchapo huu kautoa wapi. Kwani we Idrisa hii skendo umeipata wapi? Hatimaye Jacob aliingilia huku akiwa na hamu ya kujua huyu kijana alikuwa amepata wapi taarifa hizo za kusisimua.

    Weee braza Sam, achana nao hawa, jana nilimsikia baba akiwa anaongelea mambo haya…” Katika kijiwe hiki Jacob alijitambulisha kwa jina la Sam.

    “Idrisa acha, hata kama dingi yako ni kigogo serikalini lakini mara nyingine unataka kutufunga kamba kwa kisingizio cha - baba yako kasema”. Huyu aliyeonekana kuwa kinyume na Idrisa alipinga tena.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa hiyo hao jamaa wako hapa hapa mjini au kwingineko? Jacob Aliuliza

    “inasemekana wameenda mji mwingine, nahisi wameona hapa jijini itakuwa rahisi kushitukiwa” Kwa jinsi Idrisa alivyokuwa akielezea ilikuwa wazi kuwa mchapo huo hakuwa ameubuni, japo wenzake wote walionekana kutokuwa na imani naye hata kidogo. Jacob kwa upande wake hakuyabeza wala kuyapa uzito mkubwa maelezo hayo.

    Baada ya hayo zilifuata stori za hapa na pale ambazo Jacob hakuona kama angeendelea kuzipa muda wa kusikiliza, aliondoka zake baada ya kuwa amelipa bili yote ya kahawa kwa wote waliokuwa hapo. Vijana kijiweni walifurahi baada ya kulipiwa na Jacob, hii ilikuwa moja ya sababu za wao kumpenda sana pale kijiweni.



    * * *

    Siku iliyofuata yaani Julai 18, 2009, tetesi hizo zililifikia tena sikio lake, safari hii ziliupekenya Moyo wake na kumweka katika hali tofauti. Jacob Matata alipata taarifa rasmi. Ilikuwa ni siku moja tu tangu alipopata tetesi toka kwa Idrisa pale kijiweni maeneo ya Ufipa Bar.

    Siku hii akiwa ofisini kwake alipokea simu toka kwa mkurugenzi wa Ofisi Fukuzi, Bi. Anita. Simu hii ilikuwa ni ya wito wa haraka ambapo Jacob alihitajika ofisini kwa mkurugenzi huyo. Alipofika ofisini kwa Bi. Anita alimkuta akimsubiri. Bi. Anita alikuwa katika suti nyeusi ya kike iliyomfanya apendezeshe ofisi hiyo. Alipomwona Jacob akiingia alitabasamu na kujitengeneza vizuri kitini.

    "Keti Jacob" Alisema huku akitoa karatasi fulani toka katika uvungu wa meza yake.

    “Asante” Jacob alisema huku akivuta kiti kabla ya kuketi.

    “Nimekuita hapa kufuatia dharura iliyojitokeza”. Bi. Anita alirekebisha sauti yake, kisha akaendelea

    “Siku chache zilizopita kumekuwa na taarifa kuwa kuna kundi la watu ambalo limeingia Nchini kwa siri. Kundi hilo limeingia likiwa na silaha na inaaminika kuwa silaha hizo ni za nchi za magharibi. Watu hawa wametumwa na Nchi hizo kwa lengo la kuzifanyia majaribio. Haijulikani kwa nini watu hawa wameamua kuja kuzifanyia majaribio hapa nchini wakati kwa kawaida watu hawa hufanya majaribio baharini, misituni na sehemu zinazofanana na hizo. Uhakika uliopo na jambo la kusikitisha ni kuwa, silaha hizo hazitafanyiwa majaribio kwenye mojawapo ya misitu, mbuga, au maeneo wazi yaliyopo hapa nchini. Bali wanataka kufanya majaribio kwa kutumia viumbe hai – raia wa Tanzania. Kwa kuona kuwa maisha ya watu wetu hayana thamani sawa na yale ya watu wao, nchi hizo zilizoendelea zimeona kuwa majaribio haya yatakuwa ya mafanikio kama yakifanyika kwetu. Habari zisizo rasmi zinadai kuwa watu hao tayari wapo Arusha. Bila shaka wameuchagua mji huo kwa kuanza kufanya kazi yao.

    Inawezekana umeshasikia jinsi walivyouawa wale madaktari sita, askari kumi na moja, na vichaa saba huko Arusha ndani ya siku chache hizi. Ni baada ya watu hao kwenda kwenye Hospital ya mkoa wa Arusha Mount Meru na kutumia silaha hizo hatari. Kama ujuavyo mji wa Arusha hivi karibuni utakuwa mwenyeji wa mkutano mmoja muhimu, lakini watu wasiojulikana wamesambaza barua za kutishia mkutano huo. Leo asubuhi nimepokea taarifa toka kwa mheshimiwa kunitaka kuhakikisha kuwa watu hao wanapatikana haraka iwezekanavyo.

    Kama ujuavyo hii ndiyo ofisi inayotegemewa kwa maswala yaliyoshindikana na nyeti kama haya. Bila shaka unamjua vema Mheshimiwa kwa jinsi alivyo, asingependa kuona watu wakizidi kuteketea, huku kukiwa na tishio la silaha hatari kama ambazo inasemekana watu hao wanazo. Pia itakuwa aibu sana kama mkutano uliopangwa kufanyika hautafanyika kwa sababu ya vitisho toka kwa wahuni kama hao…..”

    “Lakini kuna hakika gani kuwa jamaa walioingia na silaha ndiyo hao hao waliotishia mkutano? Jacob aliuliza katika hali ya kuunganisha mambo

    “Haijawahi tokea watu kutishia mkutano wa kimataifa katika nchi hii. Hii ni mara ya kwanza na imetokea wakati watu hao wameingia nchini na wameshafanya mauaji ya kutisha. Hivyo kwa akili ya kawaida sana, wamehusishwa moja kwa moja na vitisho vilivyotolewa. Lakini ushahidi wazi kabisa ni kuwa mmoja kati ya askari waliouawa jana, pembeni ya maiti yake pia ulikutwa ujumbe wa kutishia mkutano. Kutokana na kazi waliyoifanya juzi katika hospitali ya mkoa walipokwenda, imethibitika kuwa watu hao wamekuja na silaha za kisasa. Si hivyo tu bali imethibitika pia kuwa wanauwezo wa hali ya juu katika mapigano. Binafsi kilichonishangaza ni kitendo cha watu hawa kutaka kuingilia na kuvuruga mkutano muhimu huu uliopangwa kufanyika kwenye moja ya miji yetu siku chache zijazo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mtazamo wangu katika suala hili ni kwamba kuna jambo limefichika juu ya watu hao wanaodaiwa kuingia nchini na ambao tayari wameshaanza kufanya ukatili wa kutisha. Ninahisi kuna jambo jingine zaidi ya lile la kutaka kufanyia majaribio silaha zao. Kwa nini waamue kufika kipindi ambacho mkutano huu umekusudiwa kufanywa na waingie moja kwa moja nchini mwetu na si kwingineko katika bara hili la Africa….” Kabla hajaendelea alikatizwa na swali la Jacob.

    “Bosi kwani silaha hizo ni za aina gani mpaka waamue kuja kufanyia hapa nchini na si kwao. Na je watu hao ni waafrika au wazungu? Jacob aliuliza huku amekaza macho yake yakitazamana na yale ya Bi. Anita.

    “Watu walioingia hapa nchini si wazungu ni waafrika ambao bila shaka wametumika kama vibaraka wa wazungu. Kwa vile silaha hizo ni za hatari sana, ndio maana waliozitengeneza wameogopa kuzifanyia majaribio huko kwao. Kwani taarifa tulizonazo toka Arusha kwa wataalamu wetu zinasema ni silaha za kibaiolojia ambazo huathiri kabisa mfumo mzima wa mwili wa binadamu.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog