Search This Blog

Friday, 28 October 2022

BONDIA - 5

 









    Simulizi : Bondia

    Sehemu Ya Tano (5)





    ***

    Kapten Deusdelity Macha aliteremka kutoka kwenye gari la jeshi na kutembea kiaskari kuuelekea mlango wa nyumba yake. Upande wa pili wa barabara, Roman alijiinua kutoka kwenye benchi alililokuwa amekalia lililokuwa mbele ya kibanda cha mkaanga chipsi na kumfuata taratibu. Usoni alikuwa amevaa miwani ya jua na ndani ya kifua chake alikuwa akihisi mfukuto wa ghadhabu wakati akimtazama Deus akifungua mlango wa nyumba yake na kuanza kuingia ndani.

    “Hallo Deus...!” Aliita taratibu, sasa akiwa hatua si zaidi ya tano kutoka mlangoni kwa Deus. Deus aligeuka, na mara tu alipomuona uso ulimbadilika na kusajili mshituko mkubwa sana.

    “Roh...Roman!” Alisema kwa kitetemeshi na kubaki akimtazama.

    Walitazamana.

    “Un...nataka nini...umekuja lini...?” Deus alijikuta akiuliza bila kufikiri. Roman alibaki akimtazama, chuki isiyo kifani ikijijenga moyoni mwake.

    “Rachel is dead Deus.”

    Deus alitazama chini.

    “Na...naomba uende Roman...nasikitika kwa msiba uliotokea, lakini...”

    “Sijakuona msibani hata kidogo Deus...sasa najiuliza, kwa mtu ambaye ndiye niliyekukabidhi mdogo wangu wakati naondoka nchini, kwa nini usitokee msibani?” Roman alimwambia kwa sauti ya utulivu. Deus alianza kufunga mlango, akimuacha Roman nje. Haraka sana Roman aliweka kiatu chake mlangoni na kuuzuia ule mlangokufunga. Deus aliinua uso wake na kumtazama Roman kwa mshangao.

    “Toka bwana!” Alisema huku akimsukuma kwa ule mlango. Roman hakutetereka.

    “Umemuua Rachel Deus....”

    “No! Amejiua mwenyewe Roman, na naomba usinilaumu kwa hilo...mi’ sikuwa na nia mbaya kwake, nilimpenda kikweli kabisa, lakini...”

    Hapo Roman alishindwa kuzuia ghadhabu zake. Aliukamata mlango kwa nguvu na kumsukumia ndani Deus huku naye akimfuata nyuma yake.

    “Kelele wewe! Ulimpenda mdogo wangu wewe? Mi’ nilikukabidhi ili umrubuni na kumtelekeza?” Alimfokea huku akimsukuma kwa mikono yake yote miwili kifuani. Hapo hapo Deus alimtandika ngumi kali ya uso, na Roman akayumba hadi ukutani huku akiachia mguno wa maumivu. Deus aligeuka na kukimbilia ndani zaidi ya nyumba yake na kujifungia chumbani kwake, ambako alienda moja kwa moja hadi kwenye simu iliyokuwa kando ya kitanda chake.

    “Hallo Polisi? Mimi ni kapteni Desudelity Macha! Nahitaji msaada haraka sana nimevamiwa nyumbani kwangu...haraka!”

    Nyuma yake Roman alikuwa akibamiza mlango wa kile chumba.

    “Fungua mwanaharamu, fungua!” Roman alifoka huku akiubamiza mlango ule kwa hasira.

    “Ondoka Roman, ondoka! Mi’ nimeita polisi...yatakayokukuta tusilaumiane!” Deus alimpgia kelele kutokea chumbani kwake.

    “Umemuua mdogo wangu Deus! Nimekukabidhi nikiamini kuwa u-binaadamu kumbe ni shetani usiye haya?”

    “Sikudhamiria Roman! Hebu ondoka upesi Roman...ondoka nyumbani kwangu!”

    Roman alipandwa na ghadhabu. Alirudi nyuma na kuurukia kwa nguvu ule mlango. Lakini ule mlango ulikuwa mgumu sana naye aliishia kuanguka chini kwa kishindo.

    “N’takuua mwanaharamu! N’takuua kama ulivyomuua mdogo wangu shenzi wee!” Roman alipiga kelele kwa hasira. Nje ya nyumba ile majirani walisikia mayowe na wakaanza kukimbilia kwenye ile nyumba kujua kulikoni. Roman aliubamiza mlango kwa nguvu bila mafanikio. Alitoka mbio na kuingia jikoni. Akachukua chupa ya mafuta ya taa na kuitupia pale mlangoni, chupa ikapasuka na mafuta ya taa yakiilowesha pazia iliyokuwa imetundikwa mbele ya ule mlango.

    Akaliwasha moto lile pazia.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Utatoka humo ndani paka we! Utatoka! Kama hutoki basi utaangamia humo humo ndani kwa moto baradhuli mkubwa we!” Alimtupia maneno ya ghadhabu. Moto ukapamba kwa kasi, mlango ukaanza kuugua, moshi ukatanda kila mahali. Kule chumbani Deus alianza kukohoa kwa taabu, moshi ukimuelemea. “Roman! Roman...acha ujinga...acha...” Alipayuka kwa taabu.

    Sasa moto ulikuwa umetawala mlango wote, na bila kufikiri Roman aliurukia ule mlango na kupita nao mzima mzima mpaka ndani, huku nyuma akisikia mayowe ya majirani na ving’ora vya magari ya polisi.

    Deus alimshitukia Roman akitua ndani ya chumba kile kwa kishindo. Alijitupa pembeni na kujaribu kumzunguka Roman ili akimbilie nje ya ya chumba kile, lakini Roman alimrukia na kumdaka kiuno na wote wawili wakaenda chini. Deus alimsukumia Roman teke lililomtupa pembeni. Wote waliinuka kwa wakati mmoja na Roman akamsukumia konde kali la uso, lakini Deus aliliona, akabonyea likapita hewani naye akamtandika ngumi nzito ya tumbo. Roman aliguna kwa maumivu na hasira huku akiyumba. Sasa ule moto uliokuwa mlangoni alitambaa mpaka ndani na kupamba kwenye shuka la kitanda.

    Roman akamrukia Deus mzima mzima na kumshidilia kichwa cha mwamba wa pua, na Deus alipelekwa mpaka ukutani, akiachia kilio cha maumivu huku akijishika pua iliyokuwa ikibubujika damu. Roman alimuendea na kumchapa konde kali la mbavu na Deus alijipinda huku akigumia kwa uchungu. Roman akamshindilia konde jingine la ubavu wa pili, Roman akajipindia upande wa pili. Roman akampa konde jingine zito la tumbo, Deus akajipinda kwa mbele. Roman akamkamata kichwa na kumsihdilia kwa goti usoni na Deus alienda chini kama mzigo. Sasa chumba chote kilikuwa kimetanda moto, kitanda chote kilikuwa kikiwaka moto, na ndimi za moto ule zilirukia kwenye pazia za madirisha, nayo yakashika moto.

    “Acha Roman...acha!” Deus alikuwa akibwabwaja huku akijitahidi kuinuka. Sasa Roman alikuwa amepandwa wazimu wa ghadhabu. Alimdaka ukosi wa gwanda lake la jeshi na kumuinua, kisha akamshindilia kichwa kingine kilichotua sawia mdomoni.

    Deus alichia yowe kubwa huku akienda tena chini.

    “Umemuua mdogo wangu, Deus! Umemuua mdogo wagu halafu unaniambia nitoke nyumbani kwako? Nyama we, sasa nawe utaenda kuzimu kunakokustahili!”

    “Roman, I am sorry...! Nisa...me...he...brother!” Deus alibwabwaja, lakini Roman alikuwa ameshapanda mzuka wa kulipa kisasi. Huku wakiwa wamezongwa na moshi kila upande, alimkamata na kuunyofoa kwa nguvu mkanda wa gwanda la kijeshi alilokuwa amelivaa Deus na kumzingira nao shingoni.

    “Roman Nooookkhhhh!” Deus alipiga kelele lakini hapo hapo Roman alianza kumkaba kwa kutumia ule mkanda, akimkata mayowe yake na kumuacha akikoroma.

    “Utamfuata Rachel alipo ili ukamuombe msamaha nyau we!” Roman alisema huku akitweta na akizidi kumkaba kwa ule mkanda. Macho yalimtoka pima Deus, alianza kutupa mikono huku na huko, akijitahidi kufurukuta bila mafanikio kutoka kwenye kifo dhahiri kilichokuwa mbele yake.

    “Polisi! Jisalimishe sasa hivi!” Sauti kali ya kiaskari ilifoka kutokea mlangoni. Roman aliinua macho yake yaliyowiva kwa ghadhabu na moshi uliotanda mle ndani, na aliona kivuli cha mtu akiwa amesimama pale mlangoni.

    “Sijisalimishi mimi! Naua! Namuua bazazi huyu! Niacheni nimmalize halafu nanyi mkaninyonge!” Aifoka huku akizidi kumkaba. Mara hiyo mlio wa bastola ulisikika, na kabla hajatanabahi, Roman alishuhudia kiumbe kikijitupa mle ndani na kujibiringisha sakafuni, kisha akajikuta akiwa amewekewa kabali shingoni kwake na mdomo wa bastola ukiwa umekandamizwa kwenye upande wa kichwa chake.

    “Uko chini ya ulinzi mwanaume! Muachie huyo mtu sasa hivi, ama si hivyo napasua bichwa lako kwa risasi!”

    Ilikuwa ni sauti kali ya kike.

    Roman alizidi kumkaba Deus kwa ule mkanda, pua zikimtutumka, akitweta kwa ghadhabu.

    “Niue nami nakufa naye afande!” Alisema kwa hasira, kisha akamalizia, “...huyu mwanaharamu kasabaisha kifo cha mdogo wangu gaddemitt, afande!”

    “Utakufa wewe kwanza, naye utamuacha akitapatapa kutafuta pumzi, lakini akiwa hai. Muachie huyo askari sasa hivi!” Fatma, wakati huo akiwa koplo, alisema kwa msisitizo, bastola yake ikiwa kichwani kwa Roman. Na hata alipokuwa akisikia maneno yale, Roman alishuhudia askari wengine watatu wakivamia mle ndani, bunduki aina ya SMG zikiwa mikononi mwao, zote zikiwa zimemuelekea yeye, huku moto ukizidi kupamba mle ndani. Alihema kwa pumzi za haraka haraka, na huku bado akizidi kumkaba Deus kwa ule mkanda, alisogeza mdomo wake sikioni kwa yule rafiki yake aliyebadilika na kuwa adui yake mkubwa, na kumnong’oneza kwa sauti nzito ya kongofya.

    “Umeokolewa na askari safari hii Deus, lakini ujue kuwa bado kifo chako kiko mikononi mwangu...I will kill you one day Deus...that’s a promise (nitakuua tu siku moja Deus...nakuahidi hilo)!” Kwisha kusema hivyo, alimsukuma mbele kwa nguvu, akimuacha Deus akisambaratika ovyo sakafuni, naye akijikuta akisukwasukwa kwa nguvu na wale askari, mikono yake ikivutwa nyuma na akipachikwa pingu.

    “Ita gari la kuzima moto hapa...upesi!” Koplo Fatma alibwata huku akimburura Roman nje ya kile chumba kilichokuwa kikiwaka moto mtindo mmoja. Nje ya nyumba ile kundi la watu waliojaa udadisi lilikuwa limetanda, wengi kati yao wakiwa ni majirani wa Deus pale mtaani. Akiwa ndani ya gari la polisi kabla ya kuondolewa eneo lile, Roman aliiona nyumba ya Deusdelity Macha, ikiteketea kwa moto kuanzia ule upande kilipokuwa chumba chake cha kulala kuelekea nyuma ya nyumba ile.

    Kate alikuwa ni miongoni mwa majirani waliojazana pale nje siku ile, wakimshuhudia Roman akiingizwa kwenye gari la polisi akiwa na pingu mikononi, na jirani yao Deus akiingizwa kwenye gari jingine la polisi huku akivujwa damu. Na wakati akimtazama yule mtu aliyempa kipigo cha haja jirani yao, Kate hakutegemea kabisa kuwa kiasi cha miaka miwili baadaye angekutana na mtu yule uso kwa uso...



    ***



    Roman alishitakiwa kwa kosa la shambulio baya na kusababisha hasara ya mamilioni baada ya kuiteketeza nyumba ya Deus kwa moto. Aliwekwa rumande wakati Deus na jamhuri wakiandaa ushahidi wa kumtia hatiani kwa kosa lile zito alilotuhumiwa kwalo. Mark alijitahidi kumtafutia dhamana, lakini haikuwezekana. Roman alionekana ni mtu hatari sana kuachiwa huru mitaani hivyo aliwekwa ndani. Mara moja Mark Tonto alitafuta wakili wa kumtetea.

    Kesi iliendeshwa kwa miezi mitatu, Koplo Fatma akiongoza upande wa upelelezi. Na ni katika miezi mitatu ile, ndipo Koplo Fatma alipopata kuufahamu kwa undani uhasama uliojengeka baina ya Roman na Deus. Lakini mambo mabaya ndio kwanza yalikuwa yanaanza kwa Roman. Kutokana na kuhusishwa na kesi ya kiraia, Roman alijikuta akisimamishwa kazi jeshini, wakuu wake wa kazi wakiweka wazi kuwa iwapo atapatikana na hatia, basi na ajira yake jeshini nayo itakuwa imekwisha.

    Kesi ya Deusdelity Macha dhidi ya Roman Kogga ilivutia watu wengi hususan majirani wa Kapten Deusdelity Macha walioshuhudia siku ile Roman alipotiwa nguvuni baada ya kumporomoshea kipigo Deus na kuiteketeza nyumba yake kwa moto. Miongoni mwa wale waliokuwa wakiifuatilia kesi ile kwa karibu sana kila ilipotajwa alikuwamo Kate, jirani wa Deus. Na ni katika kuendelea kwa kesi ile, ndipo mambo yote ya jinsi Deus alivyomrubuni Rachel, mdogo wa rafikiye Roman yalipoweka hadharani, Sada akitoa ushahidi wa matukio yote hayo. Siri ya Deus ikawa wazi kwa majirani na wakuu wake wa kazi pia. Hata hivyo, upande wa mashitaka ulifanya kazi nzuri ya kuusambaratisha ushahidi wa Sada kuwa hauna vithibitisho na badala yake ulikuwa ni simulizi tu miongoni mwa masimulizi ya kubuni. Aidha, upande wa mashitaka, uliweza kutumia historia ya nyuma baina ya Roman na Deus kuonesha kuwa Roman alikuwa na chuki binafsi na Deus kwa muda mrefu, pale muendesha mashitaka wa serikali alipompandisha Deus kizimbani kutoa ushuhuda wa jinsi Roman alipompiga kwa nguvu wakati wakifanya mazoezi ya ndondi wakiwa michezoni jeshini, na kumvunja taya. Kwa jinsi Deus alivyoielezea hali ile, ilionekana kama kwamba wakati walitakiwa wapigane kimichezo, Roman aliingia ulingoni kwa lengo la makusudi la kumuumiza. Ushahidi huu ulimuweka Roman kwenye wakati mgumu sana pale ulipooanishwa na lile tukio la kumvamia Deus nyumbani kwake, kumpiga na hatimaye kumchomea moto nyumba yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwisho wa kesi, mahakama ilimtia Roman hatiani. Hukumu ikawa ni kifungo cha miaka miwili pamoja na kumfidia Deus kwa hasara aliyomsababishia alipomteketezea nyumba yake kwa moto. Hivyo alitakiwa atumikie kifungo, na baada ya kifungo, alipe fidia ya ile nyumba aliyoiteketeza.Au atekeleze yote mawili kwa pamoja, lolote litakalokuwa rahisi zaidi.

    Muda wote wakati hakimu akimsomea hukumu ile, Roman alikuwa amemkazia macho Deus huku akiwa ameuma midomo yake kwa hasira. Baada ya kusomewa hukumu yake Roman alitiwa pingu pale pale mahakamani, na Koplo Fatma akisaidiwa na askari wengine watatu walimuongoza kuelekea chumba cha mahabusu pale mahakamani ili asubiri gari la kumpeleka gerezani, na wakati akiongozwa kutoka pale kwenye chumba cha mahakama, Roman alipitishwa karibu na alipokuwa amesimama Deus na muedesha mashitaka wake. Roman alisimama na kumtazama kwa muda mrefu yule adui yake, kisha kwa sauti iliyojaa utulivu mkubwa alimwambia;

    “Mimi nakwenda gerezani Deus. Lakini nataka nikuhakikishie kuwa miaka miwili si mingi...nitatoka. Na nikitoka, nakuja kukuua Deus, hilo ni hakika kabisa!”

    Ilikuwa ni kauli ya kuogofya kuliko zote ambazo Deus alipata kuzisikia. Na wakati akiongea maneno yale, sauti na macho yake vyote vilionesha kuwa Roman alikuwa amedhamiria kulitekeleza lile alilokuwa akilisema. Kwa muda karibu mahakama yote ilikuwa kimya kabisa. Watu walitazamana, kila mmoja aliyesikia kauli ile asijue achukue hatua gani. Deus alibaki akimtazama Roman kwa woga uliokithiri, akishindwa kusema lolote.

    “Twende Roman...acha mambo hayo sasa!” Koplo Fatma alimwambia huku akimsukuma mbele. Roman alimgeukia na kumtazama kwa jicho kali sana, kisha bila ya kusema neno, aligeuka na kuelekea kule alipokuwa akiongozwa.

    Kutoka kwenye kona moja ya mahakama ile, Mark Tonto na Sada walikuwa wakimtazama Roman akiondolewa eneo lile huku wakibubujikwa na machozi.

    Kwa hukumu ile, Roman Kogga akawa amepoteza rasmi kazi yake jeshini...



    ***



    Wiki mbili baada ya hukumu, wakili wa Roman alifanikiwa kufikia muafaka na wakili wa Deus, wa namna ya kumfidia hasara ya kumuunguzia nyumba yake. Ilikubaliwa kuwa nyumba ya Roman aliyoachiwa urithi na wazazi wake iuzwe kwa usimamizi wa mahakama, na pesa zitakazopatikana zilipe gharama za ukarabati wa nyumba ya Deus.

    Swala likafikiwa muafaka.

    Hivyo, ndani ya muda mfupi sana, Roman alipoteza mdogo wake wa damu, kazi yake iliyokuwa ikimpatia riziki hapa duniani, na nyumba yake ya urithi. Na yote ni sababu ya mtu mmoja tu...Deusdelity Macha.



    ***

    Miezi miwili baadaye, Mark Tonto alienda kumtembelea kule gerezani.

    “Mark...” Roman alimsalimu rafiki yake huku akitabasamu. Mark Tonto alifanya jitihada za hali ya juu kujizuia asiangue kilio. “Roman...vipi hali yako bwana...?” Alimuuliza kupitia kwenye dirisha la wavu lililowatenganisha. “Sio mbaya...nahesabu siku tu...” Roman alimwambia. Mark aliuma midomo na kutikisa kichwa.

    “Jamaa yetu ameacha kazi...ametoa notisi ya saa ishirini na nne...” Mark alimwambia. Roman alimtazama kwa macho ya kuuliza. “Deus...amecha kazi?”

    “Yap! Taarifa nilizozipata zinasema kuwa jeshi lilikuwa linajiandaa kumuachisha kazi kutokana na mazingira ya kujihusisha kwake na kifo cha Rachel...inasemekana ingawa mahakama haikumtia hatiani kwa kuwa hakushitakiwa kwa kifo kile, tayari alikuwa ameshalitia doa jeshi...”

    “Kwa hiyo yeye akawahi kujitia kuacha kazi kabla hajafukuzwa?”

    Mark akaafiki kwa kichwa. Roman akatikisa kichwa kwa masikitiko, uso wake ukionesha kukereka na tabia ile.

    “Na sasa ameingia kwenye ngumi za kulipwa...eti ameamua kuwa professional boxer...” Mark alisema kwa dharau. Lakini Roman alikuwa akimtazama kwa makini, ilhali akionekana kuwa na mawazo mazito, akili yake ikiichambua kwa kasi sana habari ile iliyoletwa na Mark.

    “Unasema kaamua kuwa bondia...wa kulipwa?” Roman alimuuliza tena kwa sauti iliyojaa udadisi. Mark alimtazama kwa mshangao kidogo. “Ndio...kwa nini?”

    Roman alikaa kimya kwa muda, akiwa kwenye mawazo mazito.

    “Okay, naomba kuanzia sasa unikusanyie habari zake zote.Najua atakuwa anaandikwa sana magazetini, naomba unikusanyie makala zote...nitakapotoka nitataka kuziona...” Hatimaye alisema. Mark akamtazama kwa muda.

    “Kwa nini unataka habari zake...kuna kitu hujaniweka wazi Roman?”

    “Usijali. Naomba unifanyie hivyo nikuombavyo Mark...na...mengine nitakueleza kadiri siku zinavyokwenda. Kuna wazo limepita kichwani mwangu, ila nahitaji kulichekecha vizuri kwanza...kisha nitakueleza...” Roman alimjibu. Mark Tonto alimtazama yule rafiki na mwanafunzi wake kwa muda, kabla ya kukubaliana naye.

    “Okay, Roman...unajua nitafanya lolote kwa ajili yako...”

    “Thanks buddy!”

    Hiyo ilikuwa ni kiasi cha miaka miwili na miezi kadhaa iliyopita...



    ******



    Siku mbili baada ya ujio wa Inspekta Fatma pale nyumbani kwake Bagamoyo, Roman, alipanda ndege kuelekea visiwa vya ushelisheli kwa ajili ya maandalizi ya pambano lake na Deusdelity Macha. Pamoja naye walikuwako Kate, Mark na Dan Dihenga. Ilikuwa ni miezi mitatu ya mazoezi mazito kwa Roman kuliko wakati wowote maishani mwake tangu aanze kucheza ndondi. Wakati wote akiwa kwenye mazoezi yake kule ushelisheli, huku nyumbani matangazo ya redio, televisheni na hata magazeti, yalizidi kulinadi pambano lile lililokuwa likisubiriwa kwa hamu. Kambi za ushabiki baina ya mabondia wale wawili zilizidi kukua, watu wakiwekeana madau makubwa na madogo. Vipindi maalum vya michezo viliwasiliana naye moja kwa moja kwa simu akiwa kule ushelisheli na kumhoji juu ya maandalizi yake kwa mpambano ule wa kihistoria, kama jinsi alivyokuwa akihojiwa Deus aliyekuwa Tanzania.

    Kila bondia alikuwa akijigamba kumuonesha kazi mwenzake.

    Na kwa upande mwingine, wadhamini wao pia walikuwa wakiwatumia mabondia wale kushindanisha biashara zao. Picha za Roman akiwa ushelisheli akiongea kwa simu ya kampuni iliyomdhamini zilionekana kwenye matangazo ya televisheni na magazeti, na wakati huo huo, picha za Deus akizinadi huduma za simu za kampuni inayomdhamini nazo zilionekana kwenye televisheni, magazeti na mabango ya barabarani. Ndani ya miezi mitatu ile, Roman Kogga na Deusdelity Macha, walikuwa watu maarufu sana miongoni mwa watanzania na duniani kote.Lakini ukweli ulibaki kuwa mshindi wa pambano lao, ndiye ambaye angekuwa maarufu zaidi ya mwenzie.

    Hatimaye siku ya pambano iliwadia. Pambano lilipangwa kufanyikia kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ***



    Roman, Kate na Mark waliingia nchini saa nne asubuhi siku moja kabla ya pambano. Dan Dihenga alitangulia siku moja kabla yao ili kufanya maandalizi ya muhimu. Akiwa uwanja wa ndege, kundi la waandishi wa habari lilimzonga Roman kwa maswali juu ya matarajio yake katika pambano lililokuwa mbele yake.

    “Kama nilivyosema kule Kairo, pambano la kesho ni la kusherehekea kukabidhiwa kwangu ule mkanda niliounyakua kule Kairo...kwa hiyo nawaomba watanzania waje kwa wingi kushuhudia nikikabidhiwa mkanda wangu hiyo kesho. Ahsanteni sana.” Roman aliwajibu waandishi huku akipigwa picha za magazeti, televisheni na kurekodiwa na wanahabari wa vyombo mbalimbali vya redio. Kwisha kusema hivyo, Dihenga alimuongoza Roman na msafara wake kwenye gari la kifahari alilowaandalia na kuondoka eneo lile. Siku ile Dan hakuwapeleka Bagamoyo, badala yake msafara wao uliishia kwenye hoteli ya kifahari ya Movenpick, jijini.

    “Leo tutalala hapa Roman...” Dan alisema, “...na tutaondokea hapa kwenda ukumbini hiyo kesho.”

    “Wow! Yaani tayari mmeshaanza kunipa huduma za kibingwa? Safi sana!” Roman alisema huku akitabasamu, na wote walicheka.

    “Hizo ni fadhila za wafadhili wetu Roman...kwa hiyo hatuhitaji kuwaangusha kesho, au sio?” Dan alimwambia.

    “Ah, kuangushwa kesho ni lazima, hakuna ujanja...” Roman alijibu akiwa hana utani hata kidogo. Wote waliokuwemo mle ndani walimshangaa.

    “Ati...?” Mark Tonto aliuliza kwa mshangao.

    “Nini...?” Dan alimaka, wakati Kate akimtazama Roman kwa macho yaliyojaa maswali.

    “...ila tu atakayeanguka hiyo kesho ni Deus!” Roman alimalizia kauli yake huku bado akiwa makini sana. Pumzi za ahueni ziliwashuka wenzake aliokuwa nao mle chumbani, Mark akiangua kicheko kikubwa.

    “Ah, Roman ulitupa ugonjwa wa moyo kidogo pale...”

    “Mwenye ugonjwa wa moyo saa hizi ni Deus tu...” Roman alimjibu.

    Saa sita mchana siku ile walienda kwenye zoezi la kupima uzito kwenye ukumbi wa habari maelezo. Waandishi wa habari kutoka katika kila chombo cha habari nchini na nje ya nchi walikusanyika. Mabondia wote wawili walifika na makocha na ma-paromota wao. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili na miezi kadhaa, Roman alikutana tena uso kwa uso na hasimu wake Deusdelity Macha. Walipoonana tu, mabondia wale walisogeleana na kutunishiana vifua huku wakitazamana usoni kwa ghadhabu, wapiga picha za televisheni na magazeti wakipiga picha tukio lile kwa bashasha.

    “Nilipata ujumbe wako kutoka kwa Inspekta Fatma, Roman...na nilimwambia kuwa nitakujibu ulingoni siku ya tukio...na sasa siku imewadia!” Deus alimwambia kwa sauti iliyojaa uchokozi. Roman alibaki akimtazama kwa ghadhabu, akiwa amebetua midomo yake kwa kukereka, lakini hakumjibu kitu.

    “Vipi, leo huna la kusema Roman? Hakuna macho ya watu ya kukupa kiburi cha kuropoka utumbo wako?” Deus alimsaili kichokozi. Roman alizidi kumtazama kwa ghadhabu, sasa midomo ikimcheza kwa hasira, misuli ikiwa imememtutumka, mishipa ya shingo ikiwa imemsimama.

    “Nilipokuwa napelekwa gerezani nilikuahidi jambo Deus...” Hatimaye Roman alimjibu kwa sauti iliyojaa ghadhabu na dhamira halisi, “...kesho nitakutimizia hiyo ahadi, kwa hiyo usiniharakishe...vumilia kidogo tu, ahadi itatimia!”

    Uso wa Deus ulimbadilika, na akafunua kinywa kutaka kusema kitu, lakini muda huo huo walinda usalama wakaja kuwatenganisha.

    Zoezi la kupimana uzito lilipokamilika, waandishi wa habari waliwahoji wale mabondia kwa muda, na Deus akajigamba kuwa yeye ndiye bingwa na ataendelea kuwa bingwa baada ya pambano lake na Roman.

    Kwa upande wake Roman alirudia ile ile kauli yake aliyoitoa kule Kairo, na pale uwanja wa ndege wa JK Nyerere. Alikuwa anaenda ukumbini kuchukua mkanda wake alioushinda kule Kairo.

    Magazeti yakaandika, redio an televisheni zikanadi, na homa ya ushabiki juu ya nani atamshinda mwenzake kati ya Roman Kogga na Deusdelity Macha ilipanda mara dufu...



    ***



    ***

    Ulingo wa kimataifa ulitengenezwa ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee jijini. Ukumbi ule ulibadilika kwa kupambwa kimataifa. Watazamaji na majaji walioteuliwa na shirikisho la ndondi duniani walikuwa wameshaingia ukumbini saa kumi na mbili za jioni. Mapambano kadhaa ya utangulizi,au exhibition, yalifanyika, lakini ilikuwa wazi kuwa wote waliofurika ukumbini usiku ule walikuwa wamekuja kushudia pambano kati ya bingwa wa dunia Desudelity Macha, na mpinzani wake mkubwa kabisa, Roman Kogga.

    Ndipo muda ulipowadia, ukumbi ukiwa umejaa wahka, mtangazaji maarufu alipanda ulingoni na kutangaza kuwa muda wa pambano kuu la usiku ule, au main card, ulikuwa umewadia. Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi na vifijo.

    Mwamuzi wa pambano lile kutoka Caracas, Venezuela, alipanda ulingoni na kuwaita mabondia. Ndipo kwa mbwembwe za hali ya juu, mtangazaji alianza kwa kumuita mpinzani, Roman Kogga ulingoni. Roman aliingia ukumbini kutokea mwenye chumba cha mapumziko akiwa kidari wazi na chini amevaa bukta yake nyeusi ikiwa na mkanda mpana kiunoni, jina lake la kwanza likiwa limeandikwa kwenye mkanda wa bukta ile kwa maadishi makubwa ya rangi nyeupe. Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi wakati alipokuwa akikimbia kibondia kuelekea ulingoni akisindikizwa na second wake, ambaye pia ndio alikuwa kocha wake, Mark Tonto. Roman alipanda ulingoni na kukimbia huku na huko, akitupa ngumi hewani kwa kasi ya ajabu kisha akajipigapiga kifuani na kuinua ngumi yake juu kwa ishara ya ushindi. Ukumbi ulipagawa kwa vifijo. Kwenye viti vya watazamaji, Dan Dihenga alimgeukia Kate kwa jazba.

    “That’s my boxer! Leo ndio Deus atajuta kunisaliti mwanaharamu!” Alimwambia. Kate alibaki akitazama kwa wasiwasi. “Naomba mungu amsaidie Roman ashinde Dan...naomba sana!”

    “Ooh! Atashinda tu Kate...atashinda..tena kwa kishindo!”

    Kule ulingoni, mtangazaji alimnadi bingwa Deus“deadly” Macha, na muda huo Deus naye alitoka chumbani kwake na kuelekea pale ulingoni, akiwa kifua wazi, na chini akiwa ameva bukta nyekundu, jina lake likiwa limeandikwa kwa maadishi makubwa meusi kwenye mkanda mpana wa bukta ile, mkanda wake wa ubingwa wa dunia akiwa ameuning’iniza begani kwake. Ukumbi ulimpokea kwa shangwe na mayowe mengi, naye akawa anatembea taratibu kuelekea ulingoni akisindikizwa na kocha wake huku akiwa ameinua juu ngumi yake.

    Lakini ilionekana wazi kuwa Deus alikuwa anaenda ulingoni kama ng’ombe anayepelekwa machinjoni. Hakuonesha bashasha ambayo mashabiki wake waliitarajia.

    Alipanda ulingoni, na hapo alibadilika ghafla. Alianza kurukaruka huku na huko, na kutupa ngumi za haraka haraka hewani huku ukumbi ukimshangilia kwa jazba, kisha akageuka kila upande wa ulingo akiuonesha juu ule mkanda wake aliokuwa anaushikilia.

    Baada ya kila bondia kufanya majigambo yake ulingoni, mwamuzi aliwatuliza na kuwaita ili kuwapa nasaha za maadili ya pambano. Kisha kila bondia akarudi kwenye kona yake.Mwamuzi aliwaita kati ya ulingo na wale wapinzani wawili wakaziacha kona zao na kwenda kusimamiana kibondia katika ile pozi ya honour stance, wakisubiri amri ya kuanza pambano.Hatimaye kengele ya kuanza pambano ikagongwa, na mwamuzi akaruhusu pambano.

    Deus alianza raundi ya kwanza kwa kasi. Akimshambulia Roman kwa ngumi za haraka haraka na zenye uzito wa kumpeleka mtu chini, lakini Roman alikuwa mtulivu, akimkwepa na kumtandika ngumi za kudokoa na mara moja moja akimtupia ngumi kali za ghafla ambazo hazikuleta madhara yoyote kwa Deus. Na sekunde chache kabla ya raundi ya kwanza kuisha, mabondia wale wawili walijikuta wakiwa wamekumbatiana.

    “Umemuua mdogo wangu Deus...sasa leo ndio nami nakutimizia ahadi niliyokupa siku ile nilipokuwa napelekwa gerezani, mshenzi we!” Roman alimnong’oneza kwa hasira. Deus alifurukuta kujichomoa mikononi mwa Roman, lakini Roman alizidi kumbana mpaka refa alipokuja kuwatenganisha. Wote walirudi kwenye kona zao na kuanza kurudiana tena kwa pambano wakati kengele ya kumaliza raundi ilipogonga.

    “Unamchezea Roman!” Mark alimkemea Roman wakati wa mapumziko. Roman alibaki akimkodolea macho yaliyojaa vitisho Deus, ambaye alibaki akimtupia macho huku akitweta kutokea kule kwenye kona yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nampiga taratibu...mpaka ajute kujiingiza kwenye ndondi!” Roman alimjibu kocha wake na kuinuka kurudi ulingoni baada ya kengele ya raundi ya pili kugongwa.

    Raudi ya pili, Deus aliingia kwa kasi kali zaidi, sasa akionesha hasira za wazi wakati Roman alikuwa mtulivu zaidi, akimtupia makonde ya kushtukiza huku akimcheka mpinzani wake. Lilikuwa ni pambano kali, na kwa dakika moja nzima, Deus alimbana Roman kwenye kona na kumvurumishia makonde makali ya mfululizo huku ukumbi ukirindima kwa hoi hoi, lakini Roman alifanikiwa kuyakwepa masumbwi yale akiwa pale pale kwenye kona, mengine akiyakinga na machache yakimpata, ndipo akiwa pale pale kwenye kona alipojikunja na kujikunjua kwa sumbwi kali la upper cut lililojikita sawia kidevuni kwa Deus na kumyumbisha vibaya, naye akajichomoa kutoka kwenye ile kona na kurudi kati kati ya ulingo. Lakini sasa Deus alikuwa ameshapata matumaini ya kumuangusha mpinzani wake hivyo akamuendea tena kwa kasi, Roman akampisha kidogo na wakati huo huo akimzungushia ngumi ya kushoto, Deus aliiona na kujikinga haraka, na kushitukia akipokea cross nzito ya mkono wa kulia lililotua sawia kwenye upande wa uso wake. Deus aliyumba mpaka kwenye kamba na ukumbi ulichangamka kwa vifijo.

    Roman alibaki akirukaruka katikati ya ulingo akimsubiri mpinzani wake, ingawa ile ilikuwa ni nafasi nzuri ya kumbana Deus pale kwenye kamba na kumsulubu atakavyo. Deus alirudi kwa hasira na kujaribu kumtupia makonde ya nguvu. Roman alimpisha tena kidogo na kumtandika konde la tumbo, na Deus alijikunja huku akimkumbatia Roman.

    “Unamkumbuka Rachel Deus...?” Roman alimnong’oneza wakiwa wamekumbatiana pale ukumbini. Deus alijikurupusha kujinasua kutoka mikononi mwa Roman, wazi kuwa yale maneno ya Roman yalikuwa yakimchanganya, na Roman alitumia nafasi hiyo kumuachia ghafla na hapo hapo akampa upper-cut nyingine ya kulia iliyotua tena kidevuni. Deus alitupwa nyuma na kuangukia goti pale ulingoni. Ukumbi ulilipuka kwa shangwe, na Roman alikuwa anamuendea wakati kengele ya kumaliza raundi ulipogonga, na ukumbi ukaachia mguno wa fadhaa.

    Pambano liliendelea kwa raundi nyingine mbili, na waliposhikana tena kwenye raundi ya tano, Roman alimnong’oneza, “Unakumbuka jinsi nilivyokuvunja taya Deus...? Unakumbuka jinsi nilivyoua mabondia wawili ulingoni...?” Deus alipiga ukelele za hasira na kumsukuma nyuma kwa nguvu Roman. Mara moja refa aliingilia kati na kuweka nidhamu pale ulingoni. Deus alibaki akimkodolea macho ya ghadhabu Roman huku akitweta, wakati Roman akimtazama huku akimcheka. Sasa Deus alionekana wazi kuwa alikuwa akipigana huku akiwa makini sana na ngumi ya kushoto ya Roman, lakini kufikia raundi ya saba, mabondia wote walionekana kama kwamba walikuwa wametoshana nguvu. Lakini ilipofikia raundi ya nane, Roman aliingia na mtindo tofauti kabisa wa upiganaji.

    Badala ya kusimama kwa mtindo aliokuwa akiutumia tangu mwanzo wa pambano wa orthodox, yaani kusimamia kulia, ambao ndio ungempa nafasi nzuri zaidi ya kumpiga mpinzani wake kwa mkono wa kushoto, yeye sasa alitumia mtindo wa kusimamia kushoto, yaani southpaw.

    Deus alichanganyikiwa, kwani kwa kutumia msimamo huu, Roman hangeweza kutupa konde la kushoto. Deus akahisi Roman amejisahau, na kuingia kwa makonde ya nguvu na ya mfululizo. Katikati ya raundi ile, ghafla bila ya Deus kutaraji, Roman alirudisha tena mtindo wa orthodox na kumtupia konde kali la kushoto lililomkosa kichwani Deus kwa umbali mdogo sana. Deus akajibu kwa konde la kulia la mtindo wa jab, lililompata Roman tumboni. Roman akayumba, Deus akaingia mzima mzima kwa sumbwi la cross, ambalo linapigwa kwa karibu huku mpigaji akienda na mwili wake wote kwa mpinzani wake. Roman alikuwa ametarajia jambo hili, hivyo alijikunja huku akilalia kulia na kumpisha na wakati huo huo akijikunjua huku akiachia right hook iliyotua upande wa kushoto wa kichwa wa Deus, Deus aliyumba, na hapo hapo Roman akalalia kushoto na kujikunjua haraka huku akiachia left hook iliyompata Deus upande wa kulia wa kichwa.

    Deus akapoteza mwelekeo, sasa Roman alikuwa upande wake wa kushoto na sio mbele yake tena, ukumbi ulikuwa umepagawa kwa shangwe. Deus akageuka haraka kushoto kwake, lakini Roman akaruka hatua moja mbele na kumtupia ngumi sita za mfululizo za usoni kwa mtindo wa one-two, yaani kulia na kushoto kama mara tatu hivi, kila ngumi iliyoingia ilikuwa ikipokelewa na ukelele wa pamoja kutoka kwa watazamaji. Deus akayumba nyuma na kuangukia kwenye kamba, Roman aliingia pale pale kwenye kamba kwa upper cut ya kulia, na kwenye nukta ya mwisho kabisa akabadili mkono na kumshindilia Deus kwa upper cut ya kushoto iliyompata sawia kidevuni, na hapo Roman aliona macho ya Deus yakipinduka, weusi wa mboni ukipotelea ndani ya macho, na bila kusubiri zaidi alimmalizia na hook ya kulia iliyompata Deus kichwani na kumpeleka moja kwa moja sakafuni kama mzigo.

    E bwana we!

    Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi, Dan Dihenga na Kate waliruka wima na kushangilia huku wakikumbatiana, Mark Tonto akifuatilia kwa makini wakati Roman akirudi kwenye kona yake na mwamuzi akianza kumhesabia Deus.

    Huku nje ya ukumbi, Inspekta Fatma akiwa katika mavazi ya fulana na suruali ya jeans na kofia yake ya kepu kichwani alijipenyeza hadi kwa kocha wa Deus.

    “Simamisha pambano hili...simamisha sasa hivi kocha uokoe maisha ya bondia wako!” Alimwambia kwa wahka huku akimvuta mkono. Kocha wa Deus alimgeukia kwa mshangao.

    “Khah, we’ mwanamke vipi...? Hebu toka hapa...!”

    “No! Mimi ni afisa wa polisi na najua kinachoelekea kutokea...”

    “Hebu toka hapa, ebbo!” Kocha alimkemea na kugeukia kule ulingoni. Wakati askari wa usalama pale ukumbini walipokuja kumvuta kando Inspekta Fatma.

    Kule ulingoni Deus aliwahi kusimama ilipofikia nne na kujiweka tayari kwa pambano. Refa alimuuliza iwapo yuko sawa, akaafiki kwa kichwa, akamuwekea vidole viwili mbele ya uso wake na kumuuliza anaona vingapi, Deus akamjibu anaona viwili, refa akaruhusu pambano liendelee.Kutokea upande wa pili wa ulingo Mark Tonto, Kate na Dihenga waliona kile kilichokuwa kikitokea baina ya Inspekta Fatma na kocha wa Deus, ingawa hawakuweza kuelewa ni kwa nini kilikuwa kinaongelewa.

    Sasa ukumbi ulikuwa hauna utulivu hata kidogo. Deus aliingia kwa kasi ya ajabu, akiwa na ghadhabu za kupelekwa chini na mpinzani wake wakati Roman akiwa amedhamiria kumaliza mchezo na kumuweka Deus mahala pake. Deus alikuja na ngumi ndefu-ndefu za mfululizo, na kwa muda walikuwa wakizungukana bila ya madhara kwa yeyote, wakati ghafla sana Roman alipomuendea kwa kasi mpinzani wake na kusita kama kwamba alikuwa amejigonga miguu na kupoteza uelekeo, akijikunja kutokea kwenye magoti kama anayetaka kuanguka. Deus aliiona nafasi ile na hakuifanyia ajizi. Alimuendea kwa left hook iliyobeba nguvu zake zote, na hapo, bila kutarajiwa, Roman aliruka mbele huku bado ameinama, na kujiinua wima akiwa moja kwa mojambele ya Deus.

    Deus akajikuta yuko karibu sana na Roman kiasi cha kutoweza kumpiga kama alivyokusudia, haraka alijitahidi kurudi nyuma lakini alikuwa amechelewa kwani alikuwa ameingia kwenye mtego wa Roman kama inzi aingiavyo kwenye utando wa buibui, na wakati alipojiinua wima namna ile, Roman aliinuka na upper cutnzito ya kulia na hapo hapo akaifuatishia na upper cut nyingine ya kushoto. Yaani ilikuwa ni one-two ya upper cut! Si mabondia wengi wanaoweza kupiga namna ile, mara lipigwapo pigo la namna ile, basi huwa ni pigo la kumaliza mchezo.

    Ukumbi ulipayuka kwa mayowe, wakati kwa mara nyingine katika raundi ile, Deus alipojiona akinyong’onyezwa nguvu za magoti na mikono kwa mapigo ya Roman. Roman alimuona mpinzani wake akilegea, na ndipo kwa nguvu zake zote, alipomshushia konde la mkono wake wa kushoto kwa mtindo wa left hook. Deus aliiona ngumi ikimwendea kakini hakuwa na nguvu tena ya kuikwepa wala kujikinga. Ngumi ilimpata Deus juu kidogo ya sikio na kumpeleka kiubavu-ubavu mpaka chini, akisambaratika sakafuni na kubiringika vibaya.

    Ukumbi uliachia shangwe za ajabu...

    “Kwisha kazi bloody kenges! Roman kamaliza mchezo bloody bastard!” Dihenga akamgeukia Kate na kumwambia kwa bashasha.

    Lakini kwa namna ambayo haikutegemewa,Deus alijiinua haraka na kusimama, akayumba kinyuma-nyuma na kusimamia kamba. Mashabiki wake waliamsha hoi hoi za kumtia moyo, wakitaja jina lake kwa pamoja. Deeee-us...deadly! Deeee-us...deadly! Deee-us...deadly....

    Inspekta Fatma alimfuata kocha wa Deus kwa mara nyingine.



    “Inabidi usimamishe hili pambano sasa hivi kocha! Please...!” Alimwambia kwa jazba. Lakini kocha alikuwa makini na kile kilichokuwa kikiendelea kule ulingoni.

    “No! Anaendelea na pambano bado mwanamke! Hebu tok...”

    Fatma alilikwapua taulo jeupe kutoka mabegani kwa yule kocha na kurukia kamba za ule ulingo huku akilitupia ndani ya ulingo lile taulo.

    “No Dan...look...!” Kate alipayuka huku akioneshea kule ulingoni, ambako Inspekta Fatma akiwa ameshikilia kamba za ulingo huku akipayuka maneno ya wahka.

    Mwamuzi alishangaa kuona taulo likitupiwa ulingoni na mtu asiye kocha wa yeyote kati ya wale mabondia wawili. Ukumbi mzima uliachia mguno wa fadhaa uliofuatiwa na kelele za kuchanganyikiwa. Roman alimtazama yule askari mtukutu kwa hasira, wakati Deus akimgeukia kwa mchanganyiko wa mshangao na kutoelewa.

    “Achana na hili jambo Deus! Huwezi kushinda hili pambano...okoa maisha yako!” Inspekta Fatma alimpigia kelele yule bondia aliyeelemewa. Hapohapo Fatma akamgeukia Roman.

    “Haina haja ya kuendelea na pambano Roman, tayari umeshaonesha uwezo wako...achana na visasi!”

    “Toa nje huyo mwanamke!’ Mwamuzi alipiga kelele wakati askari wa jeshi la polisi waliokuwa kwenye sare rasmi za kazi wakimkamata Fatma na kumvuta kutoka ulingoni Fatma alizing’ang’ania zile kamba huku akipiga kelele.

    “No, niacheni! Deus achana na pambano hili tafadhali! Kubali kushindwa tu...there is no way utashinda hili pambano! Mwenzio hakuja ulingoni kwa nia ya mchezo kama wote hapa wanavyodhani, nawe walijua hilo! Get out now wakati bado uko hai Deus...PLEASE!”

    Deus alimtazama yule mwanadada akitolewa pale kwenye kingo za ulingo huku akitweta. Alimgeukia Roman aliyekuwa amesimama katika ile honour stance akisubiri uamuzi kutoka kwake huku akimtazama kwa macho ya ghadhabu iliyokithiri.

    “Achana na hili jambo Deus! Huwezi kushinda hili pambano...okoa maisha yako!” Inspekta Fatma alimpigia kelele yule bondia aliyeelemewa. Hapohapo Fatma akamgeukia Roman.

    “Haina haja ya kuendelea na pambano Roman, tayari umeshaonesha uwezo wako...achana na visasi!”

    “Toa nje huyo mwanamke!’ Mwamuzi alipiga kelele wakati askari wa jeshi la polisi waliokuwa kwenye sare rasmi za kazi wakimkamata Fatma na kumvuta kutoka ulingoni Fatma alizing’ang’ania zile kamba huku akipiga kelele.

    “No, niacheni! Deus achana na pambano hili tafadhali! Kubali kushindwa tu...there is no way utashinda hili pambano! Mwenzio hakuja ulingoni kwa nia ya mchezo kama wote hapa wanavyodhani, nawe walijua hilo! Get out now wakati bado uko hai Deus...PLEASE!”

    Deus alimtazama yule mwanadada akitolewa pale kwenye kingo za ulingo huku akitweta. Alimgeukia Roman aliyekuwa amesimama katika ile honour stance akisubiri uamuzi kutoka kwake huku akimtazama kwa macho ya ghadhabu iliyokithiri.

    “Yuko sahihi Deus! Kubali kushindwa...huu mkanda hauna thamani ya maisha yako!” Alimwambia, na akaona Deus akikunja uso kwa ghadhabu maradufu.

    Kule nje kocha wa Deus alikuwa akiruka huku na huko kwa hasira, akipinga kitendo cha yule mwanadada kurusha taulo ndani ya ukumbi bila ya ridhaa yake. Kule kwenye meza ya majaji nako kulikuwa kuna mtafaruku mkubwa, baadhi wakisema pambano liendelee wakati wengine wakishauri lisimamishwe.

    Huku ulingoni, Deus alilitazama lile taulo lililokuwa mbele yake pale chini, kisha kwa mguu wake wa kulia alilisukumia nje ya ulingo na kusima katika ile honour stance tayari kuendelea na pambano huku akimtazama Roman kwa ghadhabu.

    “Sikuja hapa kushindwa Roman! Kama unadhani maisha ni bora zaidi ya mkanda, jitoe wewe kwenye pambano!” Alimwambia kwa hasira, na Romana akaona kuwa yule jamaa alikuwa amedhamiria.

    Ukumbi uliamka kwa hoi hoi mpya, wakati Inspekta Fatma akijishika kichwa na kuangukia magoni sakafuni huku akitazama kile kilichokuwa kikitokea kule ulingoni kwa fadhaa kubwa.

    Kabla mwamuzi hajapitisha uamuzi, Deus alijiengemeza kwenye kamba na kuziacha zimsukume mbele kwa kasi naye akaenda mzima mzima huku akiachia ukelele wa ghadhabu ilhali akimsukumia Roman konde la mkono wa kulia.

    Roman alimuona Deus akimjia na ngumi ya mkono wa kulia huku miguu ikimuishia nguvu, na ndipo aliporuka mbele haraka kumfuata mpinzani wake yule bazazi, mkono wake wa kushoto ukiwa juu kabisa hewani, kisha akaushusha na kuuzungusha kutokea chini na kumshindilia konde zito sana kwenye upande wa kichwa chake chini kidogo ya jicho lake la kulia.

    Deus alienda chini kama mzigo, kinga ya meno iliyokuwa kinywani mwake ikimtoka na kusambaratika mpaka nje ya ulingo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Roman alirudi nyuma na kusimama kwenye kona ya neutral, akiiacha kona yake, huku akimtazama mpinzani wake kwa makini. Deus alijiinua na kubaki akiwa amepiga magoti na ameshika sakafu kwa mikono yake, akajiinua wima, akayumba kulia na kushoto, kisha akaenda chini mzima mzima na kuanguka chali kwa kishindo.

    Ukumbi ulilipuka kwa shangwe na hoi hoi zisizo kifani. Roman alibaki akimtazama mpinzani wake akiwa ametulia chali pale sakafuni, damu ikimtoka puani na mdomoni. Mwamuzi alimsogelea Deus na kuanza kumhesabia na ilipofika tano bila ya Deus kutikisika, watazamaji nao wakawa wanahesabu pamoja naye.

    “SITA...SABA...NANE...TISA...KUMIIIIII....!”

    Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi na nderemo, jina la Roman likitamkwa kila kona ya ukumbi ule. Mwamuzi ulimuinua Roman mkono juu kumtangaza mshindi, na mara baada ya kufanya hivyo alimgeukia Deus aliyelala pale chini, kisha akawaashiria wahudumu walete machela.

    Roman alibaki akiwa anatweta huku ameinua juu mkono wake wa kushoto kwa ishara ya ushindi huku akimtazama adui yake aliyelala pale chini. Machozi yalikuwa yakimtiririka na alikuwa akigeuka huku na huko akiwa akiwatafuta Dan, Mark na Kate, lakini kwa namna ya ajabu alikuwa hawaoni.

    Sasa ulingo ulikuwa umevamiwa na baadhi ya watu wa kambi ya Deus walioenda kumtazama mtu wao aliyelala taabani pale chini. Walimvua glovu na mikono yake ikabaki na zile bandeji mabondia wanazozifunga mikononi mwao kabla ya kuvaa glovu za kupigania.

    Macho ya Roman yakaangukia kwa Inspekta Fatma aliyekuwa amepiga magoti nje ya ulingo huku akimtazama kwa fadhaa na masikitiko makubwa.

    Walitazamana...

    Huku nyuma Deus alijaribu kujiinua lakini alishindwa. Watu wachache walikuwa wamemzonga pale chini lakini bado akili yake iligoma kabisa kukubali kuwa alikuwa amebwagwa chini na Roman. Aligeuza uso wake uliomvimba na kumuona Roman akiranda kibabe pale ulingoni huku akiwa ameinua juu mkono wake, na ghadhabu zikamzonga. Alihisi maumivu yasiyo ya kawaida kichwani...ndani ya kichwa chake, na kwa mara ya kwanza akabaini kuwa amekuwa akisikia mvumo mzito masikioni mwake tangu alipojigundua kuwa alikuwa ameagushwa chini na Roman.

    Ina maana huu ndio mwisho wangu kweli?

    Alijisukuma na kuinuka kwa kujishikilia kwenye kamba za pale ulingoni na baadhi ya watu wake wakamsaidia kuinuka.

    Nimevuliwa ubingwa na Roman!

    “Tulia tu Deus, tulia. Pambano limeisha hili...tumeshindwa kaka!” Mmoja wa watu wa kambi yake alimwambia, bila ya kujua kuwa Deus hakuwa akisikia lolote zaidi ya ule mvumo mzito masikioni mwake.

    Alijishikilia kwenye stuli iliyowekwa pale kwenye kona yake kwa ajili ya kupumzikia mwisho wa raundi, na hata pale alipojishikilia kwenye stuli ile, aliona tone la damu nzito kutoka puani kwake likiangukia pale kwenye ile stuli.

    Yaani Roman ndio amenifanya hivi kweli?

    Aligeuka kule alipokuwa Roman na kuona kuwa alikuwa hatua chache kutoka pale alipokuwa, akiwa amemgeuzia mgongo na amezibwa kidogo na watu. Kwa nguvu alizobakiwa nazo zilizosukumwa na ghadhabu ya hali ya juu aliikwapua ile stuli na kuwasukuma wale watu waliomkinga Roman huku akimwendea kwa hasira...

    Roman alikuwa anaanza kuhamisha macho yake kutoka kwa Inspekta Fatma ili awasake akina Kate, wakati alipoona uso wa yule Inspekta ukibadilika na kuwa wa taharuki, macho yakimtumbuka na kinywa kikimtanuka bila ya sauti kumtoka. Pamoja na badiliko lile alilolishuhudia katika uso wa Inspekta Fatma alisikia sauti ya Kate ikiita kwa wahka kutoka nyuma yake.

    “Roomaaaaaan!”

    Wito wa Kate ulikuja nukta moja tu kabla ya ule wa Inspekta Fatma ambaye hapo naye alipiga ukelele wa hamaniko huku akimuoneshea kwa mkono wake nyuma yake.

    “Angaliaaaaaaa!”

    Haraka Roman aligeuka nyuma yake...

    La Haula!

    Alijikuta uso kwa uso na Deus aliyekuwa amefinyanga uso kwa ghadhabu huku akiwa ameinua juu ile stuli kwa mkono wake wa kulia, na aliona wazi kuwa ile stuli ilikuwa inamshukia kichwani...

    Deus hakuwa akisikia mayowe ya watu waliokuwa wakipiga kelele kutahadharisha juu ya kile alichokuwa akikifanya, na aliishusha kwa nguvu sana ile stuli kichwani kwa Roman aliyekuwa ameegemea kamba pale ulingoni bila ya namna yoyote ya kujiokoa...

    Kate, Dan na Mark Tonto waliokuwa upande wa pili wa ulingo waliachia vilio vya fadhaa huku wakishuhudia kiwetewete kilichokuwa kinatokea.

    Bila ya kuhama hata kidogo kutoka pale alipokuwa amesimama, Roman alijipindua kutokea kiunoni kwenda juu na kulalia kulia kwake huku akiwa ameegemea kamba za ulingo, na pigo baya la Deus likakikosa kichwa chale na kumpunyua kidogo juu kidogo ya unyusi wake wa kushoto, na hapohapo, bila ya kufikiri wala kupanga, Roman akajigeuza kulalia kushoto huku sumbwi lake la kushoto likichomoka kwa nguvu yenye msukumo wa ajabu na kumshindilia Deus kwa upper cut nzito sana iliyojikita sawia chini ya kidevu na kumnyanyua hewani mzima mzima kabla ya kumbwaga tena sakafuni kama mgomba.

    E Bwana we!

    Ukumbi sasa ulilipuka kwa yowe moja kubwa la pamoja, ambalo halikuwa la kushangilia bali na la mshituko, au mastaajabu, au mshangao.

    Kisha kimya kikatanda ukumbi mzima wakati Kate, Dan na Mark wakivamia ulingo na kwenda kumzingira Roman aliyebaki akiwa ameegemea kamba huku mikono yake ameiinua kibondia katika ile honour stance, tayari kuendelea na pambano kama lipo.

    Kate alishindwa kujizuia na kumkumbatia Roman pale pale ulingoni. Roman naye akamkumbatia huku ukweli wa kile kilichotokea pale ukimfunukia wazi akilini mwake.

    “Oh, Roman! Alitaka kukuua yule Roman!” Kate alibwabwaja, na Roman ahakuwa na jibu, kwani alihisi donge kubwa likimkaba kooni.

    Watu wengine pamoja na watoaji huduma ya kwanza walimkibilia Deus aliyekuwa amelala chali pale kwenye sakafu ya ulingo ule huku damu ikitambaa taratibu pale sakafuni kutokea sehemu kwenye kichwa cgake. Wale wahudumu wa huduma ya kwanza waliweka machela kando ya Deus pale ulingoni na kumchunguza kwa muda, kisha mmoja akamgeukia mwamuzi kwa macho yaliyohamanika.

    “Amekufa huyu refa!” Alisema kwa wahka mkubwa.

    Mwamuzi alibaki akiwa amekodoa macho.

    Roman aliyeisikia kauli ile alifumba macho huku akimeza funda kubwa la mate kondoa donge lililomkaa kooni.

    “Nimelipiza kifo chako Rachel...sasa unaweza kutulia kwa amani huko uliko mdogo wangu...rest in peace.” Alinong’ona peke yake huku akiwa amemkumbatia Kate kwa mkono mmoja, ilhali kwa ule mwingine akiwa amenyoosha ngumi yake juu, jina lake likitajwa kwa shangwe ukumbi wote ule.

    Rooman...Koooga! Rooman...Kooogga! Roooman...Kooogga!

    Hatua chahe pale ulingoni, Mark Tonto alikuwa akimtazama yule rafiki yake aliyetimiza azma aliyojiwekea tangu akiwa gerezani, na hakuweza kuzuia machozi kumtiririka. Moja kwa moja alikutana na macho ya Inspekta Fatma aliyekuwa akimtazama kwa macho yenye mchanganyiko wa fadhaa na kutoamini, naye akakwepesha macho yake na kujichanganya na akina Dihenga na Kate, pamoja na kundi la mashabiki waliovamia ulingo na kumbeba Roman juu juu.

    Roman aliinua juu ngumi yake huku akibubujikwa na machozi.

    “Nimelipiza kifo chako Rachel...nimelipiza...kama nilivyokuahidi!” Alijisemea mwenyewe wakati akimshuhudia bingwa wa zamani Deusdelity Macha akitolewa ulingoni akiwa kwenye machela.

    Saa moja baadaye dunia na umma wa watanzania walitangaziwa kuwa bondia Deusdelity Macha alifariki dunia akiwa ulingoni baada ya kupigwa na mpinzani wake wakati akitetea ubingwa wake wa dunia katika uzito wa Super Middle, dhidi ya bingwa mpya wa dunia wa uzito ule, Roman Kogga.



    ***

    Kaburi lilikuwa limejengewa vizuri kwa marumaru ghali, na msalaba uliokuwa kwenye kichwa cha naburi lile ulikuwa umesimama wima, nao ukiwa umetengenezwa kwa marumaru. Kwenye kichwa cha kaburi lile, kibati cha shaba kilichojengewa pale kaburini na kuwekea kioo juu yake kilimnadi wazi yule marehemu aliyelala usingizi wa milele ndani ya kaburi lile.



    Rachel Kogga

    Dada uliyependwa kwa dhati.

    Uliishi, ukadhulumiwa, ukalipiziwa.

    Pumzika kwa amani.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Chini ya maneno yale, paliandikwa tarehe ambayo marehemu Rachel Kogga alizaliwa na ile ambayo aliiaga dunia .



    *

    MWISHO



    TOA MAONI YAKO…….











0 comments:

Post a Comment

Blog