Simulizi : Mkimbizi
Sehemu Ya Tano (5)
“Lakini sio mchezo Kamishna Vata! Ni kweli huyu mtu anayejiita Martin Lundi ameniteka na hivi niongeavyo wanafanaya bidii ya kunimezesha vidonge vya...”
“Sasa mbona unaongea na simu...wao wako wapi?”
“John Vata naomba unielewe! Hapa nimefanikiwa kumdhibiti nesi anayenisimamia humu ndani ya wodi,naomba unisaidie kabla yule mtu anayejiita Martin Lundi na yule daktari mwingine hawajanikuta humu ndani!” Nilimjibu kwa kiherehere huku nikibubujikwa machozi.
“Kwa mwenendo wa tabia uliyoonesha kwangu Tigga, inaniwia vigumu sana kukuamini.”
“Tafadhali naomba uniamini Kamishna na unisaidie! Please!” Nilimwambia na hapo hapo niliangua kilio. Nililia kwenye simu, nikimlilia John Vata aje anisaidie. Huwezi kuamini.
“Okay..Okay! Sasa...unaweza kujua hapo ulipo ni wapi?” Aliniuliza kwa sauti ya upole lakini iliyojaa uharaka ulioonesha kuwa alikuwa amelitilia umuhimu ombi langu. Sikujua niko wapi, na nikamweleza hivyo huku nikipeleka macho kule mlangoni. Bado kulionekana shwari.
“Okay, Tigga. Unaweza kuchungulia dirishani na kuniambia hiyo hospitali iko jirani na jengo au eneo gani?” Aliniuliza, nami nilimjibu kuwa niliweza na kuivuta ile simu kuliendea dirisha, lakini waya wa ile simu ulikuwa mfupi. Nilimwambia asubiri na nikaiweka sakafuni ile simu na kukimbilia dirishani. Niliangaza nje lakini kulikuwa kuna ukuta mrefu tu ulioizunguka ile nyumba, na nje ya ukuta ule kulikuwa kuna miti mirefu ya mi-Ashok, ambayo ilinizuia kuona kitu chochote nje ya ukuta wa ile hospitali.
“Shit!” Nililaani jambo lile na kuangaza mle ndani kwa fadhaa. Hakukuwa na dirisha jingine zaidi ya lile. Nilirudi kwenye simu na kumueleza Kamishna Msaidizi John Vata.
John Vata alionekana kutilia mashaka jibu lile.
“Dah! Sasa...Lakini Tigga, are you sure about all this? Isn’t this one of your tricks?” (...una uhakika na yote haya unayonieleza? Je hii si moja kati ya laghai zako?)
“Oooh Kamishna Vata! Mimi sina laghai zozote! Ninachokuambia ni kweli tupu! Naomba ujaribu kuniamini, kwani kama wakifanikiwa kunivuruga akili, hata wewe hutaweza kufanyia kazi ushahidi nitakaokupa kuhusiana na mauaji ya kule msituni...na wauaji wa kweli watabaki wakitembea tu mitaani na bila shaka kuua tena na tena. Is that what you want?” (...Je, hilo ndilo unalotaka litokee?)
“Of Course not! Lakini wewe umekuwa na tabia ya kunichengachenga sana kila nilipokuwa nikikutaka ujitokeze...sasa leo ghafla unanitafuta eti nije kukusaidia, halafu wewe mwenyewe hujui uko wapi! Unategemea mimi nielewe vipi?” John Vata aliniuliza kwa sauti ya utulivu mkubwa, nami nikajua kuwa alikuwa amechukia.
Nilizidi kuogopa.
“Please Kamishna Vata. Hatuna muda wa kubishana...tayari niko kwenye wakati mgumu bila ya hizo shutuma zako. Wewe ni afisa wa jeshi la polisi, tena wa ngazi ya juu kabisa. Nimekuletea ombi langu la kuomba msaada wa kuokoa maisha yangu. Sasa hata kama huniamini, naomba tu utimize wajibu wako kama afisa wa usalama...hata sio lazima uje wewe mwenyewe. Unaweza hata kutuma askari walio chini yako waje wanisaidie, kwa sababu najua kuwa hawa watu wabaya wakifanikiwa kujua wanachokitaka kutoka kwangu...they will kill me!” (...wataniua!) Nilimjibu kwa kirefu huku nikitiririkwa na machozi.
“Kwa hiyo unataka kuniambia nini Tigga?” Aliniuliza kwa utulivu mkubwa sana, nami nikajua amezidi kuchukia, lakini sikujali. Shit! Yeye ni afisa wa polisi, na ni wajibu wake kunilinda mimi kama raia, hata kama hanipendi au hataki.
“Wakiniua, damu yangu itakuwa mikononi mwako John Vata!” Nilimwambia kwa hasira.
“Unanitishia?” John Vata aliniuliza kwa hasira. Niliamua kurudi chini.
“Nakuomba Kamishna John Vata! Nakuomba unisaidie. Kwa sasa sina mtu yeyote wa kunisaidia hapa duniani isipokuwa wewe...niamini tafadhali!” Nililia huku nikimbembeleza yule afisa wa polisi ambaye hapo mwanzo sikuweza kumuamini kabisa. Kimya kilitawala kutoka upande wa John Vata.
“Kamishna? Bado upo...? hatuna muda, nisaidie tafadhali!”
“Okay...lakini nitakusaidiaje Tigga? Hatujui uko wapi! Hatujui ni watu gani waliokuteka...”
“Wewe ni askari John Vata! Tafuta namna ya kunisaidia...mimi akili yangu inashindwa hata kufikiri sawasawa sasa!” Nilibwabwaja huku nikilia.
“Okay...nimeshaipata namba yako. Nitakupigia. Just...you wait right there!” (...wewe subiri tu hapo hapo!)
“Lakini muda sasa, Kamishna...!” Nilimwambia kwa kiherehere, lakini alikuwa ameshakata simu.
Kilichofuata kilikuwa ni kipindi kigumu miongoni mwa nyakati ngumu nilizowahi kukabiliana nazo maishani mwangu. Niliona kuwa Kamishna John Vata aliamua kunitosa katika swala lile. Vije aseme nisubiri anipigie simu katika mazingira kama yale? Ana mpango gani? Vije itakuwa iwapo ataamua kupiga simu ile wakati wale wauaji wamo mle ndani? Na kwa nini apige simu? Swala lile lilikuwa halihitaji simu! Lilihitaji askari kuvamia ile hospitali na kufanya msako wa wodi mpaka wodi hadi wanikute na wanitoe mle ndani na kuwaweka chini ya ulinzi wahudumu wote wa ile hospitali na viongozi wao, akiwemo Martin Lundi muongo. Sasa yeye anasema nisubiri anipigie simu...huyu ni Kamishna kweli au naye ndio wale makamishna wa kubebwa bebwa tu?(Nilisonya).
Siwezi kukaa tu kiwete wete hapa nikisubiri Kamishna wa Polisi aitwaye John Vata anipigie simu!
Nilikurupuka mpaka pale mlangoni na kujaribu kuufungua lakini ulikuwa umefungwa kwa funguo, na nje ya ule mlango wa kioo niligundua kwa mara ya kwanza kuwa kulikuwa kuna mlango mwingine wa chuma. Nilitoa sauti ya ghadhabu, kisha nikarudi kwa yule nesi aliyelala pale sakafuni. Nilianza kumpekua mwili wake nikitafuta funguo za ile milango. Nilikuta funguo mbili zilizobanwa pamoja ndani ya sidiria yake.
“Yes!” Nilijisemea kwa ushindi na kurudi tena pale mlangoni na kuanza kuingiza moja ya zile funguo kwenye tundu ya funguo pale mlangoni, lakini nilibaki nikiwa nimeduwaa.
Kile kitasa kilikuwa na tundu mbili zilizofanana za kuingizia funguo! Nilitazama zile funguo zilizokuwa mkononi mwangu. Zilikuwa ni funguo aina mbili tofauti! Nini maana yake hii? Niliingiza funguo moja ikagoma, nilipojaribu nyingine ikakubali kufungua kitasa cha moja kati ya zile tundu mbili. Ile nyingine ikagoma kabisa kuingia kwenye ile tundu nyingine. Nilijaribu kufungua ule mlango, lakini hata haukutikisika. Mungu wangu! Sasa nitafanyaje? Nilihamanika kuliko kawaida. Nilichungulia kule kwenye ule mlango mwingine wa chuma, nao nikaona kuwa ulikuwa na tundu mbili za kuingizia funguo.
“Pumbavu! Sasa hii ndio nini...?” Nilifoka kwa hasira, huku nikielewa ile hali iliyojitokeza. Ilimaanisha kuwa nesi Tamala alikuwa na ufunguo mmoja tu kwa kila mlango, na ili aweze kufungua ile milango, ilibidi na mtu mwingine, aidha yule daktari mtu mzima au Martin Lundi muongo, naye afungue kwa funguo nyingine katika zile tundu za pili zilizokuwa katika kila mlango. Hii ilinionesha ni jinsi gani Martin Lundi muongo alivyodhamiria kutofanya makosa kabisa katika kuupata ule mkanda wenye ushahidi dhidi yao kutoka kwangu. Na kwa kufanya hivyo alikuwa amenizidi kete kwa mara nyingine tena.
“Aaah! Jamani! Sasa...sasa...” Nililia kwa uchungu na maneno yakanikaba kooni, sikuweza hata kuendelea kusema. Nilirudi tena kwa yule nesi na kumpekua upya, lakini hakukuwa na funguo nyingine. Nikaenda kule nyuma ya ile pazia na kupekua kwenye droo za ile meza iliyokuwako kule lakini nako hakukuwa na kitu. Nilikuwa nimenasa.
Sasa nifanye nini?
Nilirudi na kumtazama yule nesi aliyelala pale sakafuni. Niliona alikuwa akipumua kwa taabu sana, na nikaona kuwa kwa pale alipokuwa ameangukia, mtu yeyote akichungulia tu kwenye ule mlango wa kioo angeweza kumuona moja kwa moja. Nilianza kumuinua na kumburuzia pale kitandani, lakini alikuwa mzito sana kwangu. Nilikiendea kile kitanda na kufyatua vizuio maalum kutoka kwenye matairi yaliyokuwa kwenye miguu ya kile kitanda na kukisukumia pale alipokuwa ameangukia yule mwanamke. Kwa taabu sana nilifanikiwa kumlaza chali pale kitandani. Nilimfunga kwa ile mikanda maalum iliyokuwa kwenye kile kitanda na kumfunika kwa shuka mpaka usoni, nikiacha sehemu ya pua tu ili asikose hewa. Nilisimama kando ya kile kitanda nikimtazama huku nikitweta.
Na wewe uonje adha uliyokuwa ukinitia! (Nilimsonya)
Nilirudi kuchungulia kwenye kioo cha ule mlango. Kote kulikuwa kimya kabisa. Hakukuwa hata na pirika pirika za kawaida katika mahospitali. Hii hospitali gani? Kwanza ni hospitali kweli hii? Nilishitushwa kutoka kwenye mawazo yale na mlio mkali wa simu. Niliruka huku nikiropoka yowe la mshituko na kuikimbiia ile simu huku nikihisi kuwa ule mlio ungeweza kuwashitua watu wote waliokuwemo ndani ya jengo lile, hususan Martin Lundi muongo. Ilikuwa inaita muito wake wa tatu wakati nilipoifikia na kuikwapua.
“Hello...?” Nilisikia sauti ya John Vata ikiongea upande wa pili wa ile simu na kwa mara ya pili katika siku ile niliuhisi moyo wangu ukiyeyuka kwa faraja.
“Kamishna! Oh, Kamishna umenipigia kweli? Ahsante sana! Yaani nilikuwa...”
“Tulia Tigga, nilikuwa nataka kuhakikisha hiyo namba kama inakuja hapo unaposema kuwa upo. Endelea kusubiri.”
“Kamishna No! Usiniache....” Alikuwa ameshakata simu.
Nilijiona kuwa ninaelekea kupata wazimu. Hapo hapo nilianza kuipiga ile namba yake. Iliita mara kadhaa kisha ikakatwa bila kupokelewa.
“Shit! Shit! Shit!” Niliipiga tena ile namba, lakini safari hii ikawa imefungwa. Nilijibwaga sakafuni na kuagua kilio cha uchungu na kukata tamaa.
John Vata, una mpango gani na mimi? Kwa nini unanifanya hivi?
Nilikaa kule nyuma ya pazia kwa muda mrefu nikibubujikwa na machozi. Na hata machozi yaliponikauka, niliendelea kukaa kule nyuma ya pazia nikisubiri ujio wa yule daktari na hatima yangu, kwani nilikuwa na hakika kabisa yule daktari alikuwa na uwezo wa kuingia mle ndani bila hata ya kuhitaji funguo za nesi Tamala.
Baada ya muda ambao sikuweza kujua ulikuwa mrefu kiasi gani, nilisikia ule mlango ukifunguliwa. Nilihamanika na kuanza kutapa tapa nikiangaza huku na huko katika lile eneo nililokuwa nimejibanza. Nilikamata kisu kikubwa na kikali sana cha upasuaji kilichokua miongoni mwa vingi vilivyotapakaa juu ya meza iliyokuwa nyuma ya ile pazia. Huku Moyo ukinipiga kwa kasi sana nilichungulia kutokea kule nyuma ya pazia na niliona mlango ukifunguka na yule daktari mtu mzima akiingia mle ndani, macho yake yakienda moja kwa moja pale kitandani ambapo mwili wa nesi Tamala ulikuwa umefungwa na ile mikanda maalum naye akiwa hana fahamu, kisha akageukia ule upande kilipokuwa kiti cha nesi Tamala, na niliona uso wake ukitoa mikunjo ya mshangao.
“Eeee...Tamala! Tamala...?” Yule daktari aliita kwa sauti ya chini huku akianza kupiga hatua kuelekea ule upande niliokuwapo. Nilijizatiti nikiwa nimekishika kile kisu kwa mikono yangu yote miwili huku moyo ukinipiga kwa nguvu na woga ukinielemea.
Sasa nitamfanya nini na hiki kisu...nitamchoma kweli au...?
Alizidi kukaribia. “Nesi Tamala? Uko chooni...?”
Alitokeza nyuma ya ile pazia nami niliruka huku nikipiga ukelele wa mashambulizi, mikono yangu iliyokamata kile kisu ikiwa imeinuliwa juu tayari kuteremsha pigo la hatari. Yule daktari alitoa pumzi ya mshituko na hapo hapo aligeuka, na aliponiona uso wake uliingiwa na woga mkubwa. Haraka sana alijigeuza na kunikwepa, lakini wakati huo huo akiipiga ile mikono yangu kwa mikono yake yenye nguvu na kunisukuma pembeni. Ingawa alionekana mtu mzima, yule mtu alikuwa na nguvu za ajabu, kwani nguvu ya msukumo wake ilinitupa mbali naye kama unyoya. Nilipepesuka na kujipigiza ukutani huku nikitoa yowe la woga. Niliteleza na ule ukuta na kujibwaga sakafuni nikiwa nimekalia matako na kuinua uso wangu kwa woga kumtazama yule daktari.
Nilibaki nikiwa nimepigwa na butwaa nilipomuona yule daktari mtu mzima akiwa amesimama kishujaa ilhali kile kisu kirefu kilichokuwa mikononi mwangu kikiwa mikononi mwake. Sijui kilitokaje mikononi mwangu na kuhamia kwake, lakini nilijua kuwa katika ile sekunde aliyoipangusa mikono yangu kama unyoya, alinipokonya kile kisu kitaalamu sana!
“That was very foolish Tigga!(Huo ulikuwa ni ujinga mkubwa sana Tigga!). Ningeweza kukuua bure!” Alinikemea nami nilibaki nikiwa nimejikunyata pale sakafuni nikimtazama kwa woga mkubwa, akilini mwangu nikiamini kabisa maneno yake, kwani kama yule mtu ameweza kufanya kitendo cha haraka na ajabu namna ile, hakika asingeshindwa kuniua. Nilimeza funda la mate na kujaribu kujiinua kutoka pale sakafuni lakini yule daktari alipiga hatua moja kubwa na kuninyooshea kile kisu huku akinikemea tena kwa ukali.
“Kaa chini!”
Nilikaa huku nikitoa mguno wa woga. Yule Daktari alinitazama kwa mshangao uliochanganyika na hasira, macho yake yakielekea pale kitandani alipolala nesi Tamala na kunirudia.
“Umefanya nini we’ mtoto, umefanya nini?” Aliniuliza kwa hasira. Sikumjibu, badala yake niliendelea kumtazama kwa woga, moyo ukinienda mbio. Alimtazama nesi Tamala aliyelala pale kitandani bila fahamu. Alitukana tusi zito sana la nguoni, kisha alitikisa kichwa kwa kuchanganyikiwa na kunigeukia.
“Nijibu wewe binti! Ni nini ulichofanya na utarajia ufanywe nini sasa baada ya hapo eenh?” Aliendelea kunikemea, nami nikaamua kujitutumua na kuinuka taratibu kutoka pale sakafuni, nikimtazama kwa jeuri.
“Unajua ulichofanya wewe binti? Unajua...?
“Ndio! Ndio!” Nilimjibu kwa jazba, kisha nikaendelea. “Nimemshindilia huyo nesi wenu vidonge zaidi ya kumi vya ile midawa mliyokuwa mnatarajia mimi niibugie! Now do you have a problem with that?”(Sasa wewe una tatizo lolote juu ya hilo?)
Nilisikia sauti kwanza, halafu ndio nikaelewa kuwa nilikuwa nimezabwa kofi kali la shavu na yule daktari lililonipeleka na kunibamiza ukutani. Yaani sikupata hata nafasi ya kupiga yowe.
“Don’t talk to me like that young lady!(Usinijibu namna hiyo bi mdogo!) Hujui ni kitu gani ulichofanya wewe! Huyu mama anaweza kufa! Vidonge kumi? Oh, My God, wamekutoa wapi we’ mwanamke?” Alinikema huku akimnyooshea nesi Tamala. Nilijishika shavu langu huku nikihisi machozi yakinichonyota na shavu likinifukuta.
“Oh, Yeah? Kwa hiyo mimi kufa ni sawa, ila huyo mama hapo si sawa, sivyo?” Nilimkemea huku nikibubujikwa na machozi.
“Ningekuwa na nia ya kukuua usingekuwa ukibishana na mimi hapa sasa hivi binti! Nia si kukuua, na ndio maana hukupewa vidonge kumi kwa mpigo mwanamke!”
“Sikutakiwa kupewa kidonge hata kimoja, Dokta! Na wala sikutakiwa kuwa hapa sasa hivi, Okay? Sasa kama wewe ungekuwa Daktari anayejali maadili ya kazi yake, usingeshiriki kabisa katika zoezi lote hili!” Nilimjibu kwa hasira. Yale maneno yalionekana kumchoma sana yule daktari mtu mzima. Alinitazama na kujaribu kusema neno, akaghairi. Akamgeukia yule nesi aliyelala pale kitandani, kisha akanigeukia.
“Hujui ulisemalo na wala huwezi kuelewa. Sasa Wagga akija hapa sijui itakuwaje...”
“Wagga...?”
Yule daktari alitikisa kichwa kwa masikitiko bila kusema neno. Nilibaki nikimtazama kwa utashi wa kupata habari zaidi.
“Wagga...ni nani? Ndio yule mtu unayemuogopa sana anayelazimisha nilishwe hizo dawa...?” Nilimuuliza.
“Kelele!” Alinikemea kwa hasira huku akininyooshea kile kisu kilichokuwa mkononi mwake.
“Don’t Move!”
Wote tuligeukia kule mlangoni ilipotokea ile sauti nyingine ambayo kwangu haikuwa ngeni. Kamishna Msaidizi John Vata alikuwa amesimama ndani ya kile chumba akiwa amekamata bastola mkononi mwake nami sikuamini kabisa macho yangu! Alikuwa amevaa suruali nyeusi na fulana nyeusi ya mikono mirefu. Miguuni alikuwa amevaa viatu vyeusi vya buti vilivyokuwa na soli za mpira. Yaani kumuona vile alivyokuwa akitusogelea taratibu huku akiwa amemuelekezea bastola yule daktari ilikuwa ni kama ndoto kwangu. Kwa mara ya tatu katika siku ile John Vata aliuyeyusha moyo wangu kwa faraja isiyo kifani. Chozi la furaha lilinitoka.
“Kamishna!” Nilipiga kelele huku nikikimbilia ule upande aliokuwepo na kumuacha yule daktari mtu mzima akiwa ameduwaa, akimtazama Kamishna John Vata kwa mshangao huku akiangusha kile kisu sakafuni. “Oooh Kamishna umekuja kuniokoa! Hukuniacha! Umewezaje kuigundua sehemu hii...? Oh! Mungu wangu...” Niliropoka kwa sauti iliyozongwa na kitetemeshi cha furaha.
“Namba ya simu. Nilifuatilia kumbukumbu za ile namba ya simu uliyotumia kunipigia huko Kampuni ya simu. Nikapata anuani kamili ya sehemu ilipo hii nyumba, utashangaa kutambua kuwa hii nyumba si hospitali wala nini!” John Vata alinijibu taratibu huku akiwa amemkazia macho na kuendelea kumnyooshea bastola yule daktari aliyekuwa ameduwaa, na alivyokuwa akiongea na kumtazama, niliona kuwa John Vata alikuwa amemtambua.
“Dokta Kashushu?” Alimwita huku akimsogelea taratibu, nikihisi mshangao katika sauti yake.
“U...unanifahamu mimi?” Yule Daktari alimuuliza kwa kitetemeshi huku akiinua mikono yake juu kujisalimisha.
“Yeah...Nakufahamu wewe ni nani! Wewe ni daktari bingwa wa magonjwa ya akili nchini baada ya kustaafu kwa Dokta Martin Lundi. Mimi ni Kamishna Msaidizi wa Polisi John Vata na kuanzia sasa uko chini ya ulinzi!” John Vata alimjibu kwa sauti ya utulivu sana, nami nikajua kuwa alikuwa amechukia kwa kiasi kikubwa. Nilimtazama yule daktari mtu mzima kwa mshangao.
Dokta Kashushu! Yaani kumbe huyu mtu ni Daktari bingwa wa magonjwa ya akili!Sasa inakuwaje akina Martin Lundi...Wagga...kama mwenyewe alivyomwita wakawa na uwezo wa kumshurutisha mambo kama haya namna hii?
Bila kusubiri zaidi Kamishna Msaidizi John Vata alichomoa pingu kutoka kwenye mfuko wa suruali yake na kunikabidhi, akiniamrisha nikamfunge zile pingu yule daktari. Nilimuendea yule daktari ambaye alikuwa amefadhaika ghafla na kuwa mnyonge sana. John Vata alikisogelea kile kitanda na kufunua ile shuka iliyomfunika nesi Tamala usoni huku bado bastola yake ikiwa imemuelekea Dokta Kashushu, nami nilimkamata mkono mmoja yule daktari na kumfunga ile pingu.
“Umenikatisha tamaa kabisa Dokta Kashushu! Sikutegemea kabisa kukuta mtu kama wewe sehemu kama hii!” John Vata alisema kwa uchungu, nami niliukamata mkono wa pili wa yule daktari ili niufunge sehemu ya pili ya ile pingu.
“I am not the bad guy Commissioner!” (Mimi sio mtu mbaya unayemtafuta Kamishna!) Dokta Kashushu alimjibu kwa upole huku akitia msisitizo maneno yake kwa mikono, na ule mkono wake wa pili nilioushika ukanitoka.
“Alaa! I had no idea! (Sikujua!) Wewe ni mtu mzuri sana, ulichofanya ni kumteka tu nyara huyu binti na kumtishia kwa kisu na kumfanyia vitu gani tu vingine, au sio?” John Vata alimjibu kwa kebehi iliyochanganyika na hasira. Niliuchukua tena ule mkono wa yule dokta kwa ajili ya kuufunga pingu.
“You don’t understand Commissioner...” (Wewe huelewi Kamishna..)
“Na ndio maana nakuweka chini ya ulinzi ili tukaeleweshane vizuri huko mbele ya safari...” John Vata alimkemea kwa hasira huku akichungulia kule nyuma ya ile pazia, ilhali bado akiwa amemuelekezea Dokta Kashushu bastola yake, lakini yule dokta hakuwa na dalili ya kutoa kipingamizi chochote. Mimi nilikuwa nimeugeuzia mgongo mlango na yule daktari alikuwa akielekea kule mlangoni, wakati Kamishna Msaidizi John Vata alikuwa amemuelekea Dokta Kashushu na akitembeza macho mle ndani.
Mambo yote yalitokea haraka sana.
Ghafla nilisikia kishindo kikubwa kikitokea nyuma yangu, na wakati huo huo nilimuona Dokta Kashushu akitoa macho akitazama kule mlangoni nami nikaanza kugeuka, lakini hapo hapo yule daktari bingwa aliuchomoa mkono wake kutoka kwenye himaya yangu na kunisukumia mgongoni kwake kwa mkono wake huku yeye akijisukuma mbele na akipiga kelele.
“Wagga Noooooo!”
Hapo hapo nilisikia milipuko mfululizo ya bastola na Dokta Kashushu akinikumba kwa nguvu na sote tukasambaratika sakafuni huku akitoa yowe la uchungu. Nilimsikia John Vata ikitoa ukelele wa ghadhabu nami nikajigeuza haraka pale sakafuni kushuhudia kilichokuwa kikitokea huku nikipiga kelele kwa woga. Na hata pale nilipogeuka, nilimuona yule mtu niliyekuwa nikimtambua kwa jina la Martin Lundi akiwa anamimina risasi kwa bastola mbili zilizokuwa mikononi mwake kuelekea kule alipokuwapo Kamishna Vata, na katika nukta ile nilipolitia lile tukio akilini mwangu, nilimuona John Vata akikisukuma kwa nguvu kile kitanda alicholalia nesi Tamala na kumbabatiza nacho Martin Lundi ukutani, ambaye alitoa yowe la maumivu huku bastola moja ikimtoka mkononi. Muda huo huo John Vata alirukia juu ya kile kitanda na akiwa amesimama juu ya kile kitanda bila kujali kama alikuwa akimkanyaga nesi Tamala, aliipiga teke bastola iliyobaki mkononi mwa yule muuaji muongo nayo ikatupwa pembeni, na hapo hapo Martin Lundi alimdaka mguu na kumvuta kwa nguvu. Wote wawili walipiga mweleka mzito hadi sakafuni, bastola ikimtoka John Vata mkononi. Wakati yote haya yakitokea nilikuwa nikipiga kelele kama mwehu, huku nikimsikia Dokta Kashushu akigumia kwa uchungu.
Nilimgeukia Dokta Kashushu aliyekuwa akigaragara sakafuni na kuona alikuwa amepigwa risasi ya bega la kulia na damu nyingi ilikuwa imemtapaka eneo la kifuani na begani mwake.
Ile risasi ilikuwa inipate mimi, na Dokta Kashushu alikuwa akijaribu kuniokoa na badala yake ikampata yeye!
“Oh, Dokta Kashushu! Umeni...yaani umepigwa kwa ajili yangu...!” Nilibwabaja huku nikijaribu kumsaidia kujiweka sawa pale sakafuni.
“Sikutaka mtu yeyote afe... na we’ unajua hilo! I am just sorry that things got out ofhand!” (Nasikitika tu kuwa mambo yamevurugika!).
“Aaah, Pole sana Dokta Kashushu..lakini kwa nini ulilazimika kushirikiana na Martin Lundi...?”
“Sio Martin Lundi yule! Dokta Martin Lundi ni mtu mzuri na aliyejitolea sehemu kubwa ya umri na ujuzi wake kwa ajili ya taifa hili! Huyu mshenzi sio Martin Lundi! Yeye ni Wagga Maingo! And he is a very bad guy!”(Na ni mtu mbaya sana!) Dokta Kashushu aliongea kwa hasira huku akiuma meno kwa maumivu ya jeraha lile, nyuma yangu purukushani za mpambano baina ya John Vata na Wagga Maingo ulikuwa ukiendelea.
Hii ilikuwa ni taarifa mpya kwangu. Kumbe yule muuaji anaitwa Wagga Maingo! “Sasa...sasa lile tukio la kule msituni lilikuwa linahusu nini Dokta...” Nilimuuliza yule daktari kwa kiherehere, lakini alinibadilishia mazungumzo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sijui lolote juu ya hilo...Chana hii fulana msichana...tuangalie! Nadhani risasi imepita kwenye nyama, haikupiga mfupa...” Yule daktari bingwa aliongea kwa taabu, na wala hakuonesha kutilia maanani maneno yangu. Nyuma yangu niliendelea kusikia vishindo na mikiki mikiki ya mapambano baina ya John Vata na yule muuaji aliyeitwa Wagga Maingo, ambaye hapo mwanzo nilikuwa nikimtambua kama Dokta Martin Lundi. Hali hii ilinichanganya sana. Niligeuka na kutazama kilichokuwa kikiendelea nyuma yangu, na nilimuona John Vata akimshindilia Wagga teke la kifuani lililompeleka yule muuaji hadi ukutani ambapo alijibamiza kwa nguvu, yowe la uchungu likimtoka na niliona uso wake tayari ulikuwa umeshachakazwa kwa kipigo, kwani ulikuwa umetapakaa damu na umevimba. Mungu wangu John vata ni mtu hatari namna hii? Na hata pale nilipokuwa nikipitiwa na wazo lile, John Vata alimrukia kwa teke la kushindilia ili ambabatize zaidi pale ukutani, lakini Wagga aliwahi kujitupa pembeni na John Vata akautimba ukuta badala yake. Hapo hapo Wagga alimchota ngwara ule mguu wake uliobakia na Kamishna John Vata akaenda chini mzima mzima. Oh, Mungu wangu... Wagga alimrukia pale chini na kuanza kumkaba na hapo hapo Dokta Kashushu akanipigia kelele kwa hasira.
“Hebu chana hii fulana msichana, ebbo!”
Nilikurupuka na kujitahidi kuichana ile fulana nikashindwa. Nikachukua kile kisu kilichotupwa pale sakafuni na yule daktari na kuirarua ile fulana yake na kutazama lile jeraha. Ni kweli risasi ilikuwa imepita kwenye msuli wa bega lake na kutokea upande wa pili, ikiacha tundu baya lililokuwa likivuja damu iliyoniogopesha. Huku akitweta na kuuma meno kwa uchungu, Dokta Kashushu aliniagiza nikachukue vichupa vyote vya dawa nitakavyovikuta kwenye droo ya meza iliyokuwa nyuma ya ile pazia maalum iliyoigawa ile sehemu ya mwisho ya kile chumba, pamoja na bomba la sindano. Huku nikiwa bado nasumbuliwa akili yangu na mpambano baina ya Wagga Maingo na John Vata, nilifuata maagizo yake na kurudi pale alipokuwapo na vichupa vipatavyo vinne vya dawa ambazo sikuzitambua na kuviweka sakafuni kando ya Dokta Kashushu. Wakati huo nilimuona John Vata akimtupa pembeni Wagga Maingo na kujiinua kutoka pale chini walipokuwa wakigaragarazana. Wagga Maingo alijiinua haraka lakini John Vata alimwahi kwa teke kali la uso. Yowe lilimtoka Wagga Maingo naye akajipigiza kwenye kitanda alicholalia nesi Tamala na kupepesuka huku akijitahidi kusimama wima. John Vata hakumpa nafasi. Alimrukia teke jingine lililompata chini ya kidevu ambalo lilimrusha nyuma mzima mzima, sehemu ya nyuma ya magoti yake ikijipigiza kwenye kile kitanda naye akapinduka na kile kitanda mpaka sakafuni kwa kishindo kikubwa. John Vata alikuwa kama mbogo aliyejeruhiwa. Alikiruka kile kitanda na kumshukia Wagga Maingo kifuani aliyekuwa akijiinua kwa taabu kutoka pale sakafuni alipoangukia kwa miguu yake yote miwili.
“Msichana!” Dokta Kashushu aliniita kwa hasira, nami nikashituka na kumgeukia. “Hebu nisaidie hapa, huoni nashindwa...?” Alikuwa anajaribu kuweka dawa kwenye bomba la sindano bila mafanikio kwani mkono wake wa kulia ulikuwa hauwezi kufanya kazi kabisa. Nilichukua kichupa kimoja kati ya vile vilivyokuwa pale sakafuni na kuvuta dawa iliyokuwamo mle ndani kwenye lile bomba la sindano nikifuata maelekezo ya Dokta Kashushu kwamba ile dawa ijae kwenye lile bomba hadi kwenye namba tano iliyoandikwa nje ya lile bomba.
“Choma hiyo sindano kando ya hicho kidonda!” Aliniambia.
“Mimi?”
“Sasa kuna nani mwingine hapa? Hebu fanya upesi!”
Niliinua ile sindano na Dokta Kashushu alinizuia kwa mkono wake wa kushoto na kuitazama ile dawa iliyokuwa ndani ya lile bomba la sindano kwa makini.
“Umeitoa wapi hii dawa wewe?” Aliniuliza kwa wasiwasi mkubwa. Nilimshangaa, kwani sikuelewa maana ya swali lile, lakini aliniuliza tena. Nilimwonesha kile kichupa kilichokuwa na ile dawa. Dokta Kashushu alitikisa kichwa kwa fadhaa na woga.
“Si...sio hii wewe! Hii dawa ni hatari sana!” Aliniambia huku akiusukumia pembeni mkono wangu taratibu, na kunionesha kichupa kingine kilichokuwa pale sakafuni.
“Dawa ninayohitaji ni hii, fanya haraka!”Aliniambia. Niliweka pembeni lile bomba la sindano na kuchukkua kile kichupa kingine, ambacho ingawa hapo mwanzo nilikiona ni sawa na vile vingine, lakini kilikuwa tofauti kabisa. Niliinuka haraka na kwenda tena kuchukua bomba jingine la sindano huku kwa mara ya kwanza ikiniingia akilini kuwa mle ndani kulikuwa kimya, purukushani za John Vata na Wagga Maingo zilikuwa zimekwisha.
John Vata alikuwa amesimama akiwa amejishika kiuno, akimtazama yule mtu aliyenipa taabu sana maishani, aliyejitia kujiita Martin Lundi, ambaye sasa nimembaini kuwa anaitwa Wagga Maingo. Alikuwa amejitawanya sakafuni akiwa hana fahamu, kipondo alichopokea kutoka kwa John Vata kilikuwa si cha mchezo.
“Bastard!” John Vata alisema kwa hasira kumuambia yule muuaji aliyezirai pale sakafuni na moyoni mwangu nilifarijika kupita kiasi. Nilitaka kumsemesha yule afisa wa polisi kijana lakini kwa mara nyingine Dokta Kashushu alinihimiza.
Niliweka ile dawa nyingine niliyoelekezwa kwa kufuata kipimo kile kile na kumchoma yule daktari kwenye eneo alilonielekeza kando ya lile jeraha. Yule daktari alijiegemeza ukutani na kuonekana kama aliyepoteza fahamu nami nikamgeukia John Vata, ambaye alikuwa akimfungua nesi Tamala kutoka kwenye ile mikanda iliyombana pale kitandani. Wakati huu alikuwa ameshaamka, lakini alikuwa ameduwaa tu akitumbua macho ukutani, akionekana wazi kuwa akili yake ilikuwa imezimika.
Mungu wangu! Nimefanya nini sasa...?
“Tuondoke haraka eneo hili!” John Vata alisema baada ya kumfungua yule nesi aliyerukwa akili na kumwacha akiwa amejilaza sakafuni naye kuiendea ile simu na kuanza kupiga kituo cha polisi kuwaarifu juu ya tukio lile, akiwapa maelekezo jinsi ya kufika pale.
Kitendo kilichofuatia kilikuwa ni cha haraka na si mimi wala Kamishna Msaidizi John Vata aliyekitarajia. Wagga Maingo alikurupuka kutoka pale chini na kukikwapua kile kisu kikali cha upasuaji kilichokuwa kimetupwa sakafuni hapo awali na kumuendea John Vata kwa kasi.
. Wote tulisikia vishindo vya miguu yake kwa wakati mmoja na nilipoona jambo alilokuwa anataka kulifanya, nilibaki nikiwa mdomo wazi. John Vata aligeuka haraka na kuona Wagga Maingo akimwendea kasi ilhali kile kisu kikiwa kimeinuliwa juu kwa mkono wake wa kulia, akiwa amekenua meno na amekunja uso kwa ghadhabu. Kwa pale alipokuwapo sikuona ni jinsi gani John Vata angeweza kujiokoa, lakini alifanya jambo ambalo hata Wagga Maingo hakulitarajia.
John Vata alitupa chini ile simu na haraka sana aliruka hatua moja kubwa kumuendea yule muuaji na hivyo kumfaya awe karibu zaidi naye kuliko yule muuaji alivyotarajia na ili aweze kumchoma kile kisu, ilimbidi yeye arudi nyuma kidogo, lakini hakukuwa na muda wa kufanya hivyo, matokeo yake alijaribu kushusha kile kisu kwa nguvu ili abahatishe tu kumchoma John Vata kwa ukaribu ule ule, na hapo John Vata aliwahi kuinua mikono yake na kumkamata ule mkono wenye kisu kwa mkono mmoja ilhali kwa mkono wake mwingine akiukamata mkono mwingine wa yule muuaji.
Na hapo ndipo nilipopata nafasi ya kupiga kelele.
Wale wanaume walikuwa wakishindana nguvu, Wagga Maingo akitaka kukishindilia kile kisu kwenye mwili wa John Vata, na John akishindana naye katika hilo. Walijibamiza ukutani huku wakitoa miguno na bado wakiwa wameshikana vile vile. John Vata alimgeuza Wagga Maingo na kumbamiza ukutani, lakini ilioneka Wagga alikuwa amekishika vizuri kile kisu. Nilikuwa nikiwazunguka huku nikipiga kelele hovyo, na wakati nikifanya hivyo, niliweza kuona kwa kihoro kuwa John Vata alikuwa anaelekea kushindwa kuendelea kuishikilia ile mikono ya Wagga Maingo kwa muda mrefu kutokana na jasho lililokuwa limetapakaa mikononi mwa yule muuaji na kufanya vidole vyake viteleze. Kwa pale walipokuwa wameshikana, nilikuwa nauona uso wa Wagga Maingo aliyebanwa ukutani, John Vata alikuwa amenigeuzia mgongo wake, na niliona uso wa Wagga Maingo ukitoa lile tabasamu lake baya la ushindi.
Bloody fool!
Nilimtupia jicho Dokta Kashushu pale chini alipokuwa amelala na nikaona bado hajitambui. Sikufikiri wala kusubiri zaidi. Nilikurupuka na kunyakua lile bomba la sindano nililotaka kumchoma Dokta Kashushu kwa makosa hapo mwanzo na kuwaendea kwa kasi pale walipokuwa wakivutana. Wagga Maingo alitumbua macho kwa woga alipoona nawaendea kwa kasi nikiwa nimeinua juu lile bomba la sindano yenye ile dawa ambayo Dokta Kashushu aliniambia kuwa ni hatari sana, lakini kwa kuwa alikuwa ameshikwa na John Vata hakuwa na la kufanya, na badala yake alianza kunipigia kelele.
“Tigga Noooooo! Noooooo! Aaaaaaaaaagh....”
Nilipitisha mkono wangu wa kushoto ubavuni kwa John Vata na kumkamata Wagga Maingo kiuno, kisha kwa nguvu zangu zote niliishindilia ile sindano kifuani kwa yule muuaji, na kuishindilia ile dawa mwilini mwake.
“Ayyyaaaa Tiggaaaaa! You Bitch!(Malaya we!)....Aiiii....” Wagga Maingo alipiga kelele huku akifurukuta ilhali mimi na John Vata tukiwa tumemshika na kumbana kwa nguvu, mimi nikiwa nimekandamiza kifua changu mgongoni kwa John Vata ambaye aliendelea kuikata ile mikono ya yule muuaji muongo. Tulitazamana na yule muuaji wakati akihangaika kushindana na ile dawa na wakati huo huo akijaribu kujikwamua kutoka mikononi mwetu bila mafanikio.
“Tulia wewe! Bastard...! John Vata alimkemea kwa sauti ya kugumia, lakini yule muuaji alikuwa na mimi tu. Alinitazama kwa macho ya hasira na kunitukana tusi zito la nguoni.
“Mwenyewe, Wagga Maingo! Na wewe uonje ladha ya ufidhuli wako!” Nilimjibu kwa hasira huku nikijisikia furaha isiyo kifani moyoni mwangu kwa kumfikisha pale yule mtu aliyenisumbua na kunifitinisha na watu wangu wa karibu.
Nilizidi kumkandamiza kifuani na ile sindano hata baada ya ile dawa yote kuuingia mwili wake. Alijitutumua kwa nguvu sana na ile sindano ikakatikia mwilini kwake, lakini niliendelea kumkandamiza ukutani kwa mkono wangu wa kulia huku ule wa kushoto bado ukiwa umemkamata kiuno. Alipiga yowe kubwa la uchungu na kukata tamaa na niliona uso wake ukimbadilika na kuingiwa na woga mkubwa. Chozi lilimbubujika Wagga Maingo na niliona akianza kuishiwa na nguvu.
Kisu kilimtoka mkononi na ghafla alikuwa mzito sana. Macho yalimrembuka na povu likaanza kumtoka kinywani huku akitoa sauti za mikoromo, miguu ikamlegea na akaangusha kichwa kifuani kwake.
Wagga Maingo, zamani Martin Lundi, alipoteza fahamu.
Nilimwachia na kurudi nyuma huku John Vata akimlaza chini taratibu nami nikitazama hali ile kwa hali ya kutoamini.
Nimemweza Wagga Maingo! Nimemtoa machozi Wagga Maingo! Atie adabu, pumbavu zake...kama ataishi!
John Vata alinigeukia.
“Safi sana Tigga...safi sanna!” Alinipongeza kwa kitendo changu cha kumshindilia yule muuaji kwa ile sindano na kummaliza nguvu.
“Mi’ nakushukuru wewe afande, kwa kuja kuniokoa...”
“Whaaa...? Aaauw! Nini kimetokea...?” Dokta Kashushu alizinduka na kuuliza huku akiangaza mle ndani. Tulimtazama lakini hatukuona umuhimu wa kumjibu, naye akabaki akiwa ameduwaa tu. John Vata alinigeukia.
“Sasa tukubaliane hapa hapa. Utanitoroka tena au nikutie pingu na wewe? “ Aliniuliza huku akimfunga Wagga Maingo pingu miguuni na mikononi.
“No! No afande! Sina tena sababu ya kukutoroka! Mi’ nitakuwa bega kwa bega na wewe...nahitaji sana msaada wako.”
“Vizuri. Sasa tufanye hima tuondoke, maana niko peke yangu na sina hakika iwapo wenzao hawa watu hawako mbali na hapa...”John Vata aliongea huku akimuinua Dokta Kashushu, nami nikamuuliza vipi alikuja peke yake.
“Nilitaka kuchunguza eneo lenyewe kwanza...bado nilikuwa na mashaka na maelezo yako, na nilipolifikia eneo hili na kuona kuwa nyumba yenyewe haikuwa hata na dalili ya uhai, nikaamua kuingia kupeleleza...ndio nikawakuta na Dokta Kashushu.” Alinijibu.
Tulitoka mle ndani tukiwa tumembeba Dokta Kashushu aliyeonekana kuishiwa nguvu. Na nilipotoka kule nje niligundua kuwa ni kweli ile nyumba haikuwa Hospitali, badala yake ni kile chumba kimoja tu nilichokuwa nimefungiwa ndicho kilichotengenezwa kionekane kama wodi ya hospitali. Ilikuwa ni nyumba ya kawaida sana iliyokuwa maeneo ya Reagent Estate jijini. Kiza kilikuwa kimeingia na lile eneo, kama kawaida yake, lilikuwa kimya, hata baada ya milio ya bastola. Tuliiendea gari aina ya Land Rover Discovery aliyokuja nayo John Vata na kumweka Dokta Kashushu katika kiti cha nyuma cha ile gari. John Vata aliniagiza nibaki na Dokta Kashushu pale kwenye gari naye akakimbia kurudi tena mle ndani kumchukua Wagga Maingo na ghafla, muda mfupi baada ya John Vata kuingia mle ndani, tulisikia mlio wa bastola na muda huo huo mlipuko mkubwa ulilitikisa jiji na ile nyumba ikalipuka moto mkubwa.
“Jooohn!” Nilipiga kelele kwa kihoro na kuanza kutimua mbio kukimbilia kule kwenye ile nyumba, lakini Dokta Kashushu alinikamata kiuno na kunizuia.
“Usiende huko Mwanamke! Huna utakachofanya...ni hatari!’
“No!No! John Vata! Lazima tukamsaidie!”
“Huna cha kumsaidia hapo! Hilo ni bomu. Lets go!(Tuondoke!)” Dokta Kashushu alinikemea nami nikajitutumua ili aniachie, na hapo hapo nilishuhudia kioo cha dirisha la ile Landrover Discovery kikipasuka sambamba na mlio wa bunduki. Dokta Kashushu alinirukia na kunikandamiza chini huku akipiga kelele.
“Tunashambuliwa kwa risasi...Take cover!(Jifiche!)”
Nilipiga kelele kwa kuchanganyikiwa, na nikiwa nimekandamizwa na Dokta Kashushu pale chini nilisikia mlio mwingine wa bunduki na mchanga ukatifuka hatua chache kutoka pale tulipokuwa tumejilaza na Dokta Kashushu alijiingiza chini ya uvungu wa ile gari huku akinihimiza nami nifanye hivyo hivyo. Nilipeleka macho kule nilipohisi kuwa zile risasi zilikuwa zikitokea huku nikijisokomeza chini ya lile gari na nikipiga mayowe. Na hapo, kwa kusaidiwa na mwanga uliotokana na ule moto uliokuwa ukiwaka kutoka kwenye ile nyumba, nilimuona mwanamke mwembamba na mfupi akiwa amevaa joho la kike kama la baibui hivi, ambalo lilikuwa wazi sehemu ya mbele na kuonesha suruali na fulana ya mikono mirefu na kichwani akiwa amejitanda mtandio uliofunika sura yake yote na kuacha sehemu ya macho tu, akitutupia risasi kwa bunduki fupi aliyoishika kwa mikono yake yote miwili.
“Aah! Ndio yule mwanamke...!” Nilipiga kelele wakati akilini mwangu nikikumbuka maelezo juu ya yule mwanamke aliyeenda kuonana na hayati Dick Bwasha kule benki baada ya mimi kutoka.
Yule mwanamke alikuwa amesimama kwenye pikipiki kubwa, na katika ile sehemu ya mbele ya ile pikipiki, karibu na tanki la mafuta, niliuona mwili wa Wagga Maingo ukiwa umelazwa kifudi fudi kwenye ile pikipiki, sehemu ya juu ya mwili wake ikiwa upande mmoja wa ile pikipiki, na sehemu ya miguu yake ikiwa upande mwingine.
Mambo yote haya niliyaona ndani ya sekunde moja tu na hapo hapo tukatupiwa risasi nyingine na nikapata mshituko mkubwa niliposikia mlipuko wa bastola karibu na sikio langu. Dokta Kashushu alikuwa anajibu mashambulizi kwa kutumia bastola aliyokuwa ameishika kwa mkono wake wa kushoto.
“Wanataka kuniua mimi! Lakini siuawi kibwege...nitapambana!” Alikuwa akisema huku akifyatua risasi mfululizo kumuelekea yule mwanamke, na kwa mbali nilianza kusikia ving’ora vya gari za polisi. Yule mwanamke alitia moto pikipiki yake na kutokomea kwa kasi kutoka eneo lile akiwa ameubeba mwili wa muuaji Wagga Maingo kwenye ile pikipiki yake.
“Twen’zetu!” Dokta Kashushu aliniambia huku akitoka uvunguni mwa ile gari na kuanza kutimua mbio kukiendea kichochoro cha jirani.
“No! John Vata...”
“Huna unachoweza kufanya kumuokoa yule, mwanamke...! Bila shaka amekufa!” Aliniambia huku akizidi kukimbia kwa taabu. Nilibaki nikiwa nimeduwaa, nikiiangalia ile nyumba ikiteketea na kuona kuwa hakuna hata dalili ya John Vata kutokea. Na ving’ora vya polisi vilizidi kukaribia na baadhi ya majirani wa eneo lile wakianza kutoka nje ya nyumba zao.
Oh, My God...sasa...
Sikujishauri zaidi. Nilitoka mbio kumfuata Dokta Kashushu huku nikilia kwa sauti na bila ya kujua naye atanifikisha wapi, ilhali moyoni nikiwa nimeumia kupita kiasi, nikishindana na nafsi yangu juu ya kukubali ukweli kuwa Kamishna Msaidizi John Vata amefariki katika mlipuko ule.
Kwa ajili ya kuja kuniokoa mimi...
Kichochoro alichoingia Dokta Kashushu kilitokea kwenye mtaa uliokuwa nyuma ya ile nyumba iliyokuwa ikiwaka moto, na nilikuta yule dokta akihangaika kufungua mlango wa gari ndogo ambayo niliihisi kuwa ni Toyota Mark II nyeusi, au buluu. Nilipomfikia aliniuliza iwapo nilikuwa najua kuendesha gari huku akinikabidhi ufunguo na kuniambia nifungue mlango wa ile gari. Haraka bila ya kujisumbua kumjibu nilifungua mlango wa ile gari na kujitumbukiza ndani huku nikimfungulia na yeye mlango wa abiria, naye akjitupa ndani.
“Tunaenda wapi sasa?” Nilimuuliza yule dokta huku nikiiondoa ile gari kwa kasi kutoka eneo lile.
“Endesha kwa mwendo wa kawaida! Vinginevyo tutaanza kufukuzwa na mapolisi sasa hivi! Just Relax...Okay?” Dokta Kashushu alinikemea, kisha alinielekeza njia za vichochoroni ambazo zilitufikisha eneo la Drive Inn, kisha tukakamata barabara ya Kawawa hadi Magomeni Mapipa, hapo akaniambia nielekee maeneo ya feri.
“Dokta Kashushu...ni nini kinaendelea hapa? Wagga Maingo anataka nini hasa?” Nilimuuliza yule daktari bingwa huku nikiendesha ile gari na nikitiririkwa na machozi. Badaya ya kunijibu, yule dokta alikuwa akijifunga kidonda chake kwa kipande cha fulana yake huku akigumia kwa maumivu. Kisha alitoa simu na kuanza kuongea na mtu ambaye nilielewa kuwa ni mkewe.
“Rukia! Rukia nisikilize kwa makini...limetokea! Nimeshagundulika...we have to go! Kama bado uko na msimamo wako basi mchukue mtoto na begi letu uondoke sasa hivi!’ Aliongea kwa kiherehere, nami nikazidi kujawa na udadisi na kutoelewa.
“Muondoke kwenda wapi dokta? Na mimi itakuwaje...”
“Ndio, Rukia! Acha kila kitu kama kilivyo. Ukichelewa wanaweze kukuta hapo, tukutane kwenye boti sasa hivi! Utanikuta...”
“Dokta Kashushu! Mbona sielewi?”
“Si kazi yako! Lakini labda nitakuelezea kiasi cha kukuwezesha kuelewa, na labda ukishaelewa na wewe utaamua kuondoka kama mimi!” Dokta Kashushu alinikemea, kisha akaendelea kuongea na simu yake.
“Niko na mtu ananiuliza maswali tu hapa...ah, fanya hima Rukia! Okay!” Alimaliza kuongea na simu na kuirudisha ile simu mfukoni mwake.
“Dokta Kashushu...ni nini kinaendelea? Mimi sielewi...!” Nilimwambia huku nikiendelea kuendesha ile gari nzuri.
“Nitakueleza Tigga. Na Labda nikishakueleza utaweza kuelewa kwa nini nililazimika kufanya mambo yale niliyokuwa nikikufanyia ingawa hata wewe uliona kuwa sikuwa nikipendelea kufanya vile...lakini...I had no choice (Sikuwa na la kufanya). Na sasa, maisha yangu hapa nchini yamefikia mwisho. I have to be on the run again(Yanipasa nianze kukimbia tena)” Dokta Kashushu aliniambia kwa upole huku akigumia kwa maumivu, nami nikazidi kushangaa.
“Uanze kukimbia tena? Ni nini kilichotokea Dokta...Oh, Mungu wangu, mbona mnanichanganya hivi?”
Hapo Dokta Kashushu alianza kunieleza mambo yaliyopelekea hata yeye na mimi tukakutana katika mazingira yale, na kufikia hatua ile ya kukimbia pamoja baada ya ule mlipuko uliopoteza maisha ya Kamishna Msaidizi John Vata.
--
“Miaka kadhaa iliyopita, nilikuwa daktari wa rais wa Burundi. Ingawa fani yangu ilikuwa ni magonjwa ya akili, niliteuliwa kuwa daktari mkuu wa rais na baadhi ya majukumu yangu ilikuwa ni kuhakikisha kuwa rais na familia yake wanapatiwa matibabu yanayofaa ndani na nje ya nchi...” Dokta Kashushu alianza kunielezea kisa chake nami nikabaki nimepigwa na butwaa, kwani kama alikuwa daktari wa rais wa Burundi, vije awe Tanzania hivisasa?
“Sasa kwa nini uliteuliwa wewe wakati fani yako ilikuwa tofauti?’ Nilimuuliza.
“Sio siri Tigga...kwa wakati ule ilikuwa kila anayechukua madaraka anawaweka watu anaowaamini...na hilo nadhani ndilo tatizo kubwa la siasa za Afrika ya kati...” Dokta Kashushu alinijibu. Kisha akaendelea.
“Nilikuwa na mke wangu na watoto wawili niliowapenda sana...kama utakumbuka, kwa miaka mingi hali ya kisiasa ya Burundi haikuwa shwari. Kulikuwa kuna vikundi vilivyokuwa vikipingana na serikali, vikundi ambavyo vilikuwa vinapata msaada kutoka vikundi vya upinzani vya nchi za jirani hasa Rwanda, ambako uhasama wa kikabila ulikuwa umekithiri...”
Tulikuwa tunakaribia eneo la pwani na Dokta Kashushu alinielekeza niegeshe gari kando ya barabara katika eneo la kituo cha mabasi cha posta ya zamani, kisha tukaanza kutembea kwa miguu hadi kwenye eneo jirani na chuo cha ubaharia.
Wakati tukielekea eneo lile Dokta Kashushu aliendelea kunielezea huku bado akionekana kuwa na wasiwasi sana juu ya usalama wa mkewe.
“Siku moja nilitembelewa na watu nisiowafahamu ofisini kwangu, ambao walinitaka nifanye mambo kama yale niliyokuwa nikikufanyia wewe kule kwenye ile nyumba kwa mashinikizo ya Wagga Maingo...ila wao walinitaka nimfanyie rais....”
“Whaaat?” Nilishitushwa na taarifa ile na kumgeukia yule Dokta kwa mshangao.
“Mmmnh! Ndivyo walivyonitaka na nadhani unaweza kukisia ni jinsi gani nivyoshituka juu ya ombi lao hilo. Niliwakatalia katakata na kutishia kuwaripoti serikalini.”
“Lakini...kwa nini walitaka kitu kama hicho...”
“Walitaka kunitumia kumtia rais wazimu...kisha asiwe tena na uwezo wa kuongoza nchi... wenyewe walidai kuwa hiyo ilikuwa ni njia pekee ya amani ya kumtoa rais madarakani bila kumwaga damu...( alicheka kwa dharau na kutikisa kichwa kwa masikitiko) Yaani lilikuwa ni jambo la kipumbavu nililowahi kulisikia maishani mwangu”
Eh...jamani! Haya mapya kuliko!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pale jirani na kile chuo cha ubaharia kulikuwa na geti dogo ambalo lilitokea kwenye ngazi ndefu za mbao na chuma zilizokuwa zikiteremka pwani, eneo ambalo zamani ilikuwa inaegeshwa boti kubwa ya kwenda Zanzibar iliyoitwa MS SEPIDEH. Dokta Kashushu alijitambulisha kwa mlinzi wa pale getini ambaye alionekana kumtambua vizuri na kumuambia kuwa tulikuwa tunaelekea kwenye boti lake huko chini, na kwamba mkewe atafika muda mfupi ujao. Tuliteremka zile ngazi huku nikimuuliza kuwa alikuwa anamiliki boti. Aliafiki kwa kichwa bila kuonesha kujali juu ya swala lile.
“Baada ya wale watu ambao baadaye nilikuja kuelewa kuwa walikuwa ni wawakilishi wa kundi moja la upinzani lililokuwa likiendesha vita vya msituni dhini ya majeshi ya serikali kuona kuwa nimezidi kuwa mkaidi katika kutekeleza matakwa yao, walianza vitisho kuwa nikithubutu tu kutoa taarifa serikalini, wataiteketeza familia yangu yote! Nilikuwa kwenye wakati mgumu sana Tigga, na nilipoendelea na msimamo wangu, waliwateka mke na watoto wangu. Wakinishinikiza nimfanyie rais vile wao walivyotaka, kwani ni mimi pekee ndiye niliyeidhinisha dawa aina yoyote anayopewa rais iwapo atakuwa mgonjwa, na jambo ambalo ulimwengu haukulijua ni kwamba kwa wakati ule rais alikuwa akisumbulia na ugonjwa wa kisukari ambao ulimlazimu awe anameza vidonge maalum kila mara. Nilichotakiwa kufanya ni kumchanganyia dawa zangu za kumharibu akili pamoja na zile dawa za kisukari.”
“Dokta Kashushu haya mambo unayonieleza ni mazito sana! Inawezekana vipi mambo kama haya?” Nilimuuliza kwa msahangao. Yule Dokta alitikisa kichwa kwa masikitiko.
“Ninachokueleza Tigga ni kweli kimetokea. Hatimaye nilimweleza rais ukweli wa jambo lote, na kujiuzulu nafasi yangu ya utabibu wa rais. Rais alianzisha msako mkali wa kuwasaka mke na watoto wangu waliotekwa na wale watu ambao niliwajua kwa sura lakini sikuyajua majina yao. Kitendo hicho kiliwaudhi sana wale watu na siku moja baada ya kujiuzulu nafasi yangu, miili ya mke na watoto wangu ilikutwa kando ya msitu mmoja wakiwa wameuawa...” Aliniambia kwa huzuni nami nikahuzunika pamoja naye.
“Siku ile ile wale watu walinitumia wauaji nyumbani kwangu kuja kuniangamiza. Lakini jambo walilosahau ni kwamba mimi nilisomea shahada yangu ya udaktari huko Urusi, ambapo pamoja na shahada hiyo nilisomea pia mbinu za kijasusi na mapambano, kwani wakati huo urusi ndio ilikuwa inaendekeza zile siasa zake za ujamaa na ilikuwa ikisomesha waafrika wengi bure na kuwatumia katika propaganda zake za kijamaa. Niliwateketeza wale wauaji wawili na kuiacha nyumba yangu ikiteketea kwa moto, nami nikakimbia ile nchi Tigga. Nchi yangu niliyozaliwa na kukulia. Nilikuwa nimeficha pesa nyingi nje ya nchi, hivyo haikuwa taabu kwangu kutoroka nchini. Na kuanzia hapo nikawa mkimbizi Tigga. Huku nyuma nikasikia ndege iliyokuwa imembeba rais wetu na yule wa Rwanda ilianguka na kuwaua wote, lakini nilijua kuwa ni lile kundi lililokuwa likinitaka nimharibu akili rais ndilo lilihusika na kuanguka kwa ndege ile.” Dokta Kashushu alimalizia maelezo yake taratibu. Tuliingia kwenye ile boti yake ambayo kwa kweli ilikuwa kubwa na ghali sana. Aliniambia kuwa alikuwa ameiandaa ile boti kwa ajili ya tukio kama hili, ingawa huwa anakuja na mkewe mara kwa mara na kuiendesha hadi katikati ya bahari, siku nyingine wakiishi kwenye ile boti kwa siku mbili au tatu kabla ya kurudi tena nyumbani kwao Mbezi bichi.
Dokta Kashushu aliniambia kuwa alikimbilia Senegal. Baadaye alimtambua mmoja wa wale watu waliomfuta na kumshurutisha kumharibu akili rais akiwa miongoni mwa mawaziri wapya wa Rwanda, nchi ambayo ilikuwa ikishirikiana na waasi waliokuwa wakiipinga serikali ya Burundi. Kisha uchunguzi wa kifo cha rais wa Burundi na yule wa Rwanda ulianza, kwamba ile ndege haikuanguka kwa hitilafu za kawaida, bali huenda ikawa ilitunguliwa. Hapo wale watu wakaanza kumsaka tena ili kummaliza, kwani walijua ni yeye tu ndiye anayeweza kuwatambua wale watu waliomfuata na kumshurutisha kumharibu akili rais. Walimuibukia Senegal. Akafanikiwa kuwatoroka na kwenda Botswana. Huko nako akaondoka baada ya miaka miwili na miaka sita iliyopita akaingia Tanzania kwa pasipoti ya bandia aliyomtambulisha kuwa yeye ni Mtanzania aliyejulikana kwa Jina la Dokta Mohammed Kashushu. Hapa alianza maisha mapya na alioa mwanamke aliyekuwa yatima, kwani alijua kuwa wale watu bado walikuwa wakimsaka na hakupenda kabisa kujihusisha na mwanamke mwenye familia. Akiwa Tanzania, yule mtu aliyemtambua kuwa ni mmoja wa wale waliokwenda kumshurutisha kufanya mambo ya ajabu kwa marehemu rais wa Burundi, ambaye baadaye alikuwa miongoni mwa mawaziri wapya wa Rwanda baada ya mauaji ya halaiki, alionekana kwenye Televisheni akiwa ni mmoja kati ya watu waliokamatwa na kuletwa kwenye mahakama ya kimataifa dhidi ya mauaji ya halaiki ya Rwanda na Burundi iliyopo Arusha, Tanzania. Kufikia hapo alianza kuona mashaka juu ya usalama na amani yake nchini Tanzania, hivyo alimweleza ukweli mkewe mtanzania. Mkewe huyo aliamua kuwa pamoja naye popote atakapoenda, na ndio maana tukawa pale tukimsubiri mkewe ili atoroke naye.
Haya maelezo yalikuwa mapya sana kwangu na nikaanza kufikiria upya mkasa wote ule. Nilikumbuka kusoma habari za mahakama ya kimataifa dhidi ya mauaji ya halaiki ya Rwanda na Burundi. Nilikumbuka kusoma habari juu ya mtanzania kuteuliwa kuwa jaji wa mahakama hiyo...
“Lakini Dokta Kashushu, ilikuwaje ukapata nafasi ya kufanya kazi hapa nchini kwani vyeti vyako vya shule, hizo digrii zako, zilikuwa zinakuonesha wewe kama Dokta Kashushu? Kwani hilo ndilo jina ulilokuwa ukilitumia wakati unasoma?” Nilimuuliza.
“Hapana Tigga. Ukumbuke kuwa nilikuwa na pesa nyingi. Nilipata digrii zangu Urusi. Lakini pia nilitengeneza vyeti vya digrii hiyo hiyo kutoka vyuo vingine viwili vya nchi za magharibi, kimoja Finland na kingine kutoka chuo kidogo sana kisichojulikana kabisa kilichokuwa nchini Austria. Hiki cheti cha Austria kilinitambulisha kwa jina la Mohammed Kashushu kutoka Tanzania. Na hiki ndicho cheti ninachokitumia hapa Tanzania. Kwa hiyo ingawa fani niliyosomea ni ya kweli kabisa kama inavyoonekana kwenye cheti, jina lililo kwenye cheti na chuo ambacho kinaonekana kwenye cheti kuwa nimesomea si vya kweli. Chuo cha kweli nilichosomea kiko Urusi na katika cheti cha chuo kile kuna jina langu halisi, ambalo siwezi kukutajia kwa sababu ambazo nadhani unazielewa kufikia sasa.” Dokta Kashushu alinifafanulia. Haya mambo kwangu yalizidi kuwa mazito.
“Sasa ina maana kuwa wale watu waliokuwa wakikusakama tangu Burundi, Senegal na Botswana ndio hawa akina Wagga Maingo?” Nilimuuliza Dokta Kashushu kwa mshangao, huku nikianza kupata hofu kubwa juu ya huu mkasa mzima ulioniangukia.
“Hapana...huenda hawa wakawa na uhusiano na wale, lakini sio wale walionifuata kule Burundi. Kilichotokea hapa Tanzania, ambapo kama ulivyoelewa, nilikuwa nikiishi kwa amani sana, lakini kama Burundi, siku nne tu zilizopita yule mtu niliyekuja kumtambua kama Wagga Maingo aliniijia ofisini kwangu na kuniambia kuwa anajua kuwa mimi si mtanzania na ninaishi kwa hati bandia, na nimepewa nafasi nzuri sana katika nchi hii iliyoniwezesha kuishi kwa raha. Na akanitaka nimfanyie kazi yake, ambayo nikiifanya bila matatizo, wataendelea kunitunzia siri yangu na kuniacha niendelee kuishi kwa amani hapa nchini...kinyume na hapo, wao wangepiga simu idara ya uhamiaji na maisha yangu yangesambaratika.”
“Oh, Mungu wangu...!”
“Ndio Tigga. Nilikuwa na wakati mgumu. Na wakati huu umri wangu umesogea, sikuwa tena na uwezo wa kujiingiza kwenye mikiki-mikiki kama hapo mwanzo. Kwa hiyo sikuwa na la kufanya, nikakubaliana na sharti lao, ingawa sikuwa na uhakika kuwa huu ndio ungekuwa mwisho...nadhani sasa unaelewa ni kwa nini nililazimika kufanya vile Tigga, na nataraji utapata nafasi katika moyo wako kunisamehe kwa hili....” Dokta Kashushu alimalizia huku akinitazama kwa huzuni. Sikuwa na la kusema. Nilibaki nikiwa nimeduwaa.
“Kwa hiyo hujui hawa watu...akina Wagga Maingo walikuwa wanataka nini hasa?” Nilimuuliza.
“Hapana. Ila nakuhakikishia kuwa hawa watu ni wabaya sana. Sasa kama wana uhusiano na lile kundi lililofanya mambo ya kule Burundi miaka ile, basi nchi yenu sasa iko hatarini, na kwa kuwa wewe unaonekana kuwa na kitu wanachokitaka, nakushauri na wewe ukimbie mdogo wangu. Hapa hapakufai tena. Ukiwapa wanachokitaka, sina shaka kuwa wataiangamiza nchi yenu...wataitia kwenye balaa fulani tu! Hawa ni watu wanaopenda kuvuruga amani ndani ya nchi Tigga...kwa namna fulani ili wao wawe na maisha mazuri, ni wajibu kusiwe na amani.Kama kuna amani si mahala pao...ndio maana nakushauri kuwa ukimbie Tigga...ukipenda tunaweza kukuchukua pamoja nasi...nitakupatia pasipoti ya nchi yoyote uitakayo ukakae huko...”
“Hapana! Hapana Dokta Kashushu...mimi hapa ndio kwetu! Nina ndugu na jamaa zangu hapa, siwezi kuwaacha...” Nilimjibu kwa hamasa. Na hapo mkewe akafika. Walikumbatiana kwa upendo huku yule dada, ambaye alikuwa kijana zaidi ya Dokta Kashushu, akibubujikwa na machozi. Alimtazama mumewe kwa upendo na huruma, kisha macho yake yakaangukia kwenye pingu iliyokuwa ikining’inia kwenye mkono wake wa kushoto na kumuuliza kwa woga kulikoni.
“Ni hadithi ndefu...nitakuelezea baadaye...” Dokta Kashushu alimjibu. Mkewe akaanza kumchunguza ule mkono uliojeruhiwa kwa risasi lakini Dokta Kashushu alimtoa wasi wasi kuwa halikuwa tatizo kubwa. Yule dada alikuwa amehamanika vibaya sana. Walikuwa na mtoto wa kike aliyapata miaka minne ambaye naye alikuwa akilia kwa kumuona tu mama yake akilia. Dokta Kashushu alinitazama huku akiwa amemkumbatia mkewe.
“Sisi hatuna muda wa kupoteza Tigga...inatupasa tuanze safari mara moja. Una hakika hutaki kuambatana nasi?” Aliniuliza. Nillimtazama yule Dokta mtu mzima kwa muda huku nikimhurumia kwa mikasa iliyompata. Nilitamani kuwa pamoja naye, lakini akilini mwangu nilikuwa na mambo mengi niliyotaka kuyafanyia kazi nikiwa hapa hapa nchini. Nilitaka kujua sababu ya yule mtu kuuawa kule msituni, nilitaka kumjua ni nani yule mtu kigulu aliyekuwa na akina Wagga Maingo kule msituni, nilitaka kujua nini hatma ya yule dada askari aliyekuwa akishirikiana na akina Wagga Maingo...nilitaka kujua juu ya yule mwanamke mwenye hijab, aliyetuvurumishia risasi na ambaye nadhani ndiye aliyehusika na kifo cha Dick Bwasha...na hatma ya John Vata.Masikini John...iliniwia vigumu sana kuamini kuwa amefariki.
“Mimi nitabaki hapa hapa Dokta Kashushu...hata kama nitauawa, ni bora nifie nchini kwangu.” Nilimjibu taratibu. Yule Dokta alinitazama kwa muda, kisha akafungua begi alilokuja nalo mkewe na kutoa funguo zipatazo tatu zilizokuwa zimefungwa pamoja na kunikabidhi.
“Basi nakuomba uchukue hizi funguo za nyumba yangu nyingine Tigga. Hakuna mtu yeyote anayeijua nyumba hii, na nimeaindikisha kwa jina la huyu binti yangu.Unaweza ukahitaji maficho...nadhani huko kutakufaa kwani nina imani ukiwa kule hutagundulika kirahisi...na vitu vyote utakavyovikuta humo ni mali yako kuanzia leo...hiyo ni namna yangu ya kukusaidia katika mtihani huu Tigga...”
“Ah! Dokta Kashushu...siwezi kukubali jambo kama hilo...mkeo....?” Nilimwambia yule Dokta huku nikimtazama mkewe. Yule mwanamke mwenye sura ya kuvutia na mwili uliojigawa vizuri aliniambia kuwa nisikatae amana ile. Kwani hata yeye hatarudi tena hapa nchini. Nilipokea kwa mikono iliyojaa kitetemeshi.
“Sa...sasa ni wapi huko, yaani nitapajuaje....?” Niliwauliza. Dokta Kashushu alimwambia mkewe anichoree ramani ya eneo ilipo ile nyumba na akanitajia maeneo ya kuulizia ili nifike hapo, halafu akatoa picha ya ile nyumba na kunikabidhi. Ilikuwa ni nyumba ndogo ambayo ilikuwa bado haijamaliziwa sawasawa kujengwa kwa maana kuwa haikuwa imepigwa plasta kwa nje, ingawa ilikuwa imeezekwa kwa vigae na ilikuwa imewekwa madirisha na milango na ilikuwa imewekewa “grill” madirishani na milangoni.
“Ahsante sana Dokta...na Mrs. Kashushu... Mungu awajaalie huko mwendako.” Niliwashukuru, na Dokta Kashushu alimwambia mkewe aandike barua ya kunitambulisha kwa mlinzi wao, akiniambia kuwa mkewe ndiye aliyekuwa akijulikana sana na yule mlinzi kuliko hata yeye. Yule dada aliandika na kusaini ile barua kisha akanikabidhi. Kisha yeye alinitoa nje ya ile boti nami nikateremka na kusimama kwenye ukingo wa bahari juu ya baraza. Dokta Kashushu alinitazama na kuniuliza.
“Yule mwanamke aliyekuwa akitutupia risasi...unamfahamu? Ulionekana kuwa uliwahi kukutana naye hapo mwanzo...”
“Aaah! Yule...hapana, ila kuna mtu aliuawa, na ikasemekana kuwa mtu wa mwisho kuonana naye alikuwa ni mwanamke aliyevaa baibui...hivyo nikahisi labda ni yeye. Kwani vipi?”
“Umeshawahi kumsikia mtu aitwaye ‘The Virus’?” Aliniuliza. Nikamjibu hapana, na kumuuliza huyo ni nani.
“Ni muuaji wa kukodiwa...kama Carlos the Jackal, kama uliwahi kumsikia, lakini yeye anajiita The Virus...yaani Kirusi...huwa anafanya kazi zake Afrika. Nadhani ndiye yule aliyekuwa akitushambulia pale...”
“Ah, lakini yule alikuwa mwanamke...!” Nilimjibu kwa hamasa.
“Ndio maana nakwambia hivyo...kwa sababu inasemekana kuwa huyo The Virus, ni mwanamke!” Dokta Kashushu alinijibu. Nilibaki mdomo wazi.
Muuaji wa kukodiwa! Tanzania hii? Hapana hii sasa imekuwa kazi kubwa!
“Kila la kheri Tigga, we have to go now (yatupasa twende sasa)” Aliniambia nami nikampungia mkono. Dokta Kashushu aliingia kwenye boti lake, na muda ule ile boti ikaanza kuondoka kwa mwendo mdogo.
Nilisimama pale nikilitazama lile boti likiondoka mpaka likapotea kwenye upeo wa macho yangu.
Goodbye Dokta Mohammed Kashushu....Mwenyezi Mungu akulinde huko uendako...
Usiku ule ule nilirudi Uno Trabajo Bar nikiwa taabani. Nililiacha gari la Dokta Kashushu pale pale lilipokuwa limepaki, ingawa yule Dokta aliacha ufunguo ndani ya ile gari. Nilijua kuwa ile gari ilikuwa inajulikana na wale wauaji na hivyo sikutaka kabisa kulitumia. Akili yangu ilikuwa imechoka vibaya sana na nilikuwa nimejawa na simanzi kutokana na hatima ya John Vata. Kwangu ilikuwa ni ngumu sana kuamini kuwa yule afisa wa polisi kijana alikuwa amefariki. Nilipofika Uno Trabajo, Kachiki alinijia juu kwa mara nyingine kutokana na kupotea kwangu kazini kwa siku tatu mfululizo.
“Hivi Nuru una matatizo gani wewe! Unajua kuwa tayari umeshajifukuzisha kazi?” Kachiki aliniuliza kwa ukali tukiwa chumbani kwake, chumba changu tayari alishapewa msichana mwingine aliyepatikana kujaza nafasi yangu, na begi langu lilikuwa limehifadhiwa chumbani kwa Kachiki.
“Usijali Kachiki... ni hadithi ndefu...” Nilimjibu kwa unyonge.
“Nisijali gani? Nataka kujua ni nini kilichokufanya upotee namna hii!”Kachiki alinikemea huku akiwa amenishikia kiuno.
“Nilipata buzi...na kesho nahamia kwake, naomba leo tu nilale chumbani kwako, we’ si uko zamu mpaka karibu na alfajiri?” Nilimjibu kwa upole huku nikijishughulisha kupanga nguo zangu vizuri kwenye begi langu. Kachiki alinitazama kwa hasira, kisha akatoa mguno wa kukereka, halafu akatoka nje kwa hasira huku akilaani tabia ya akina dada kufanywa mabwege na wanaume “wasio na mpango hata kidogo”.
Nilienda kujimwagia maji na kurudi ndani huku nikiwa na mashaka makubwa na akili yangu. Madawa niliyomiminiwa mwilini na Dokta Kashushu kwa shinikizo la Wagga Maingo bado yalinitia wasiwasi. Sikuwa na uhakika kuwa kile kiasi kidogo kilichouingia mwili wangu hakitakuwa na madhara katika akili yangu. Usiku ule nilikaa kitandani kwa Kachiki na kuanza kuandika matukio ya mkasa wote huu ulionitokea mpaka kufikia siku ile, tangu nilipoanza safari ya kwenda Manyoni na mambo yote yaliyotokea baada ya hapo. Sikulala mpaka nilipohakikisha kuwa nimeyaweka kwenye maandishi matukio yote yaliyonitokea. Na nikaazimia kuendelea kuandika kila kitakachonitokea baada ya hapo mpaka nitakapoishia…au mpaka akili yangu itakapozimikia.
Labda siku moja kuna mtu atakuja kuyaona maelezo yangu haya na kusaidia kuielewesha jamii juu ya mambo haya na shutuma zilizotupwa dhidi yangu.
Ilinijia wazi kichwani mwangu kuwa bila John Vata, safari yangu kuelekea mwisho wa kisa hiki ilikuwa imebaki fupi sana…sikuwa tena na mategemeo ya kupata majibu ya maswali yaliyokuwa yakikisumbua kichwa changu tangu mkasa huu uanze kunikuta.
Wakati nilipopata nafasi ya kuweka ubavu kitandani, majogoo yalikuwa yakiwika huko nje. Na hata hivyo, sikupata hata lepe la usingizi. Badala yake nilijilaza kitandani na kubaki nikibubujikwa na machozi mfululizo, nikimlilia John Vata na kuijutia nafsi yangu. Moyo uliniuma kuliko kiasi. Akilini mwangu nikimfikiria yule askari kijana niliyekuwa nikimpa wakati mgumu kila alipojaribu kunishawishi nijitokeze ili anisaidie nami nimsaidie. Na pamoja na yote hayo, bado alijitolea kuja kuniokoa nilipokuwa nimenasa pasina ujanja wa kujiokoa.
Na sasa hayupo tena duniani…Mungu wangu!
Nilimfikiria Dokta Kashushu na mambo aliyonieleza juu ya watu ambao anahisi kuwa akina Wagga Maingo wanashirikiana nao. Nilimhurumia yule Dokta mtu mzima. Ilionekana kuwa maisha yake yalikuwa yamezingirwa na majonzi zaidi ya furaha, na sasa ataendelea kukimbia tu…Mungu amsaidie apate amani huko aendako. Yeye na mkewe na mwana wao. Lakini mimi siwezi kuwa mkimbizi milele…lazima nilifikishe mwisho swala hili. Lakini peke yangu nitaweza kweli?
Nilimfikiria yule mwanamke hatari aliyevaa hijab na kutushambulia kwa risasi mfululizo. The Virus…sikuwa na shaka kabisa kuwa yeye ndiye aliyemuua Dick Bwasha, na sasa nilikuwa na hakika kabisa kuwa ndiye mtu anayewajibika na kifo cha John Vata.
Oh, Mungu wangu! Laiti John Vata angekuwepo…!
Nililia! Nililia sana usiku ule. Nilimlilia John Vata. Nililia kwa uchungu na huzuni na hasira. Uchungu kutokana na kifo cha John Vata, huzuni juu ya maisha ya Dokta Kashushu na ambayo ndiyo yalielekea kunikuta na mimi, na hasira dhidi ya yule mwanamke baradhuli anayejiita The Virus…
Hatimaye nilipitiwa na usingizi mwepesi, lakini tayari kulikuwa kumepambazuka. Asubuhi ile niliagana na rafiki yangu Kachiki na kuondoka na begi langu begani kutoka katika ile baa ya Uno Trabajo ambayo ilinihifadhi kwa zile siku chache nilizokuwa nahitaji sehemu ya kujificha jijini. Mfukoni mwangu nilikuwa na ile ramani niliyochorewa na mke wa Dokta Kashushu ambayo ingenifikisha kwenye ile nyumba niliyoruhusiwa kuitumia na yule Dokta aliyezungukwa na huzuni maishani mwake. Sikuwa na pa kwenda na kwa kweli nilihitaji sehemu pweke. Nilipanda basi la Gongo La Mboto – Ubungo na safari ya kuelekea Kimara kwenye nyumba niliyoachiwa na Dokta Kashushu ikaanza. Kabla lile basi halijaanza safari niliwahi kununua magazeti kadhaa ya siku ile na kuanza kuyasoma kwa kiherehere, nikitarajia kuona habari za tukio la usiku uliopita kule Regent Estate. Habari za mlipuko wa bomu lililoteketeza nyumba huko maeneo ya Regent zilitawala vichwa vya habari katika magazeti mengi siku ile. Nilisoma gazeti mojawapo lililokuwa limeandika habari ile kwa mara ya tatu na kubaki nikiwa nimeduwaa. Habari ilieleza kuwa mlipuko ulitokana na bomu la mkono na kwamba miili ya watu wawili ilikutwa ikiwa imeteketea katika moto uliotokana na mlipuko ule. Mmoja kati ya miili ile ulikuwa ni wa mwanamke, ambaye sikuwa na shaka kuwa alikuwa ni nesi Tamala, na mwili wa pili haukuweza kutambulika kabisa.
Habari ziliendelea kupasha kuwa mara baada ya mlipuko ule kulizuka mapambano ya kutupiana risasi katika eneo lile baina ya makundi mawili yasiyojulikana na kwamba muda mfupi kabla ya polisi kufika eneo la tukio, mtu mmoja alionekana akitokomea kutoka eneo lile kwa pikipiki, wakati watu wengine wawili, mwanamke na mwanamume walionekana wakikimbia kutoka eneo la tukio na polisi wanaendelea na msako dhidi ya watu hao.
Mbona Kamishna John Vata hajatajwa kabisa katika habari ile?
Nini maana yake hii?
Ndio kusema ule mwili mwingine uliokuwa umeteketea kwa moto mle ndani ni wa John Vata? Inawezekana kweli? Hapana…It can’t be! (Haiwezekani!).
Oh, My God…sio John Vata tafadhali…John Vata hakustahili kufa kabisa Mungu wangu…
Lakini…mbona habari ile haikuelezea lolote juu ya gari ya Kamishna Msaidizi John Vata lililokuwa katika eneo la tukio? Kwa nini haikuandikwa habari juu ya simu iliyopigwa na Kamishna Msaidizi John Vata kutoka kwenye ile nyumba kwenda kituo cha polisi, bila shaka cha Oysterbay, kuwajulisha juu ya hujuma iliyokuwa ikifanyika ndani ya nyumba ile na kuwaelekeza namna ya kufika pale? Niliguna peke yangu na kutazama nje ya dirisha wakati lile basi likisafiri kwa kasi kuelekea Ubungo.
Angalau safari hii sikutajwa kuhusika au kushukiwa kuhusika na tukio lile. Lakini bado nilibaki na maswali mengi kichwani, na ikanijia kuwa maisha yangu sasa yalikuwa yamechukua uelekeo wa kwenda hatua tatu mbele na kurudi hatua tano nyuma.
Mungu nisaidie tafadhali...
--
Ubungo niliunganisha basi la Kimara ambalo kwa mujibu wa maelekezo ya mke wa Dokta Kashushu, nilitakiwa niteremkie kituo cha Suca, kisha nifuate ramani hadi eneo la ndani kidogo kutoka kituoni ambapo kulikuwa kuna bwawa kubwa. Ile nyumba niliyotakiwa kwenda ilikuwa kwenye kiji-mwinuko kidogo kando ya lile bwawa. Alinihakikishia kabisa kuwa nikilifikia lile bwawa tu sitapotea kabisa. Sikuwa nimewahi kufika maeneo ya Kimara hata siku moja maishani mwangu zaidi ya kupita tu kwa gari au basi nikiwa safarini kuelekea nje ya mkoa wa Dar es Salaam. Lile basi liliishia Kimara mwisho, na nilipomuuliza kondakta juu ya kituo cha Suca, aliniambia kuwa nilitakiwa nipande basi la Mbezi au Kibamba ndio niteremkie kituo hicho, kwani kile kituo kilikua mbele zaidi, na lile basi lilikuwa limefika mwisho wa safari. Sikubabaika. Niliwaendea madereva wa teksi bubu waliojazana pale kituoni na kuwauliza. Nilipowatajia bwawa tu wote walidai kuwa wanaifahamu sehemu ile, nami nikamkodi mmoja wao ili anipeleke. Tuliingia barabara ya zamani ya Morogoro na baada ya mwendo mfupi tuliingia ndani zaidi nami nikaanza kupata wasiwasi, lakini baada ya kuteremka kibonde kidogo na kupandisha mwinuko mmoja mkali kidogo, tuliteremka bonde jingine na mbele yangu nililiona bwawa kubwa. Yule dereva wa teksi aliniambia kuwa tumeshafika na akataka nimuoneshe ni nyumba gani hasa niliyotaka kwenda. Niliangaza kidogo na kweli kabisa, niliiona ile nyumba ikiwa kwenye kiji-mwinuko kidogo hatua kadhaa kando ya lile bwawa. Nilimwonesha yule dereva nyumba moja iliyokuwa jirani na pale tuliposimama huku nikiteremka na kumlipa pesa. Niliweka begi langu begani na kuiendea ile nyumba ambayo haikuwa ile niliyoitambua kuwa ni ya Dokta Kashushu huku yule dereva akihangaika kugeuza gari yake ili arudi kituoni kwake, nami nikabisha hodi kwenye ile nyumba. Mlango ulifunguliwa na binti ambaye nilihisi kuwa ni msaidizi wa ndani wa nyumba ile, na wakati huo yule dereva alikuwa ameshageuza gari yake na kuanza kuondoka. Nilimgeukia na tukapungiana mikono kuagana, kisha nikamgeukia yule binti aliyefungua mlango. Nilimtaka radhi na kumuomba maji ya kunywa. Hii ilikuwa ni njia ya kumpoteza yule dereva wa teksi ili aelewe kuwa safari yangu iliishia kwenye ile nyumba, sikutaka ajue kuwa nilikuwa naenda kwenye ile nyumba iliyokuwa juu ya kilima kando ya bwawa. Nilikunywa maji na kumshukuru yule binti, kisha nikaiendea ile nyumba ya Dokta Kashushu huku moyo ukinidunda kwa nguvu. Nisingeshangaa kabisa kama ningefika kwenye ile nyumba na kukuta mfuasi wa Wagga Maingo akinisubiri.
Maisha yangu sasa yalikuwa yamefikia hatua ya kuwa na wasiwasi kiasi hicho.
Nilimkuta mlinzi wa nyumba ile akilima-lima kwenye eneo la ile nyumba, ambayo kando yake kulikuwa na nyumba nyingine ndogo, kama banda la uani, ambalo nilielewa kuwa ilikuwa ndio nyumba ya yule mlinzi. Baada ya kusalimiana naye yule mlinzi aliyekuwa na asili ya kigogo, nilimpatia ile barua iliyoandikwa na mke wa Dokta Kashushu aliyeitwa Rukia huku nikijitambulisha kuwa mimi ni mdogo wa yule dada, kwani ndivyo ambavyo ile barua ya mke wa Dokta Kashushu ilivyonitambulisha. Kwamba mimi ni mdogo wake na kuanzia wakati ule nitakuwa nikiishi pale na yeye alitakiwa anipe ushirikiano wa kutosha. Kwa mujibu wa barua ile, yule dada alimfahamisha yule mlinzi kuwa yeye alikuwa anasafiri kwenda masomoni nje ya nchi na hivyo mimi ndiye nitakuwa naishi kwenye ile nyumba kwa muda wote ule amabao yeye hatakuweppo, ambao hakutaja ni muda gani. Yule mlinzi alinitazama kwa mashaka kidogo baada ya kusoma ile barua, lakini nilipotoa zile funguo za nyumba hakuwa tena na kipingamizi na alianza kuninyenyekea kwa heshima, akitambua kuwa sasa mimi ndio nilikuwa muajiri wake. Niliingia kwenye ile nyumba na kuanza kuikagua haraka haraka. Kwa hakika ilikuwa ni nyumba nzuri ya vyumba vitatu, sebule, sehemu ya kulia chakula na bafu na choo. Na kwenye chumba kikubwa cha kulala, Master bedroom, kulikuwa kuna bafu na choo humo humo ndani.
Kama jinsi ilivyokuwa nyumbani kwa Kelvin...
Lakini zaidi ya kitanda kimoja na godoro ambavyo bado havikuwa vimefungwa ipasavyo, hakukuwa na kitu kingine chochote mle ndani.
Sasa kwa nini Dokta Kashushu aliniambia kuwa vitu vyote nitakavyovikuta mle ndani ni mali yangu? Alimaanisha hiki kitanda...au...?
Niligundua kuwa mlango wa nyuma wa ile nyumba ulikuwa umefungwa kwa ndani na funguo zake zilikuwa zikining’inia kwenye tundu ya funguo ya mlango ule kwa ndani. Nilizitazama zile funguo tatu nilizopewa na Dokta Kashushu, ambapo moja ilifungua lile geti la chuma lililokuwa kwenye mlango wa mbele wa nyumba ile na ya pili ilifungua mlango wenyewe. Ile ya tatu ilikuwa tofauti sana na funguo za nyumba. Ilikuwa kama...lakini haileti maana...sasa kwa nini Dokta Kashushu alinipa ule ufunguo?
Nilitoka nje na kuitazama ile nyumba kwa umakini. Ilikuwa imejengwa kwenye mwinuko, na ile sehemu iliyokuwa imeinuka ilitumika kujengea gereji ya gari ambayo iliifanya ile nyumba ionekane kama ya ghorofa moja, ilhali ile sehemu ya chini ndipo kulipokuwa na ile gereji. Nilirudi ndani na kufungua mlango uliokuwa kando ya ule wa kuingilia bafuni na kuteremka ngazi zilizonifikisha kwenye ile gereji ambayo ilikuwa ina kiza kidogo. Nilipapasa ukutani na kuwasha taa na hapo nikatoa pumzi ya mshangao.
Kwenye ile gereji kulikuwa kuna gari ndogo ambayo ilikuwa imefunikwa kwa turubai maalum lililoificha kabisa. Niliisogelea ile gari na kulifunua lile turubai na pale nilibaki nikiwa nimesimama nikiitazama ile gari mpya na ya kifahari sana. Niliizunguka ile gari huku nikiitamani kwa uzuri wake. Ilikuwa ni gari aina ya Mitsubishi Diamante, ya rangi nyeusi metallic yenye vioo vya tinted. Ilikuwa mpya kabisa na hata namba ilikuwa haina. Sikuamini macho yangu na nikautazama tena ule ufunguo wa tatu uliokuwa pamoja na zile funguo mbili za nyumba ile nilizopewa na Dokta Kashushu, na nikatoa mguno wa mshangao na furaha kwani haikuwa na shaka kabisa kuwa ile funguo ilikuwa ni ya ile gari. Nilifungua mlango wa ile gari na kuipiga stati kwa kutumia ule ufunguo, na ile gari ilinguruma na kuwaka mara moja. Kwenye kiti cha nyuma cha ile gari kulikuwa kuna vibao vya namba za ile gari, ambazo zilikuwa ni mpya na za kisasa. Nilifungua sehemu ambayo madereva wengi hapa kwetu hutumia kuwekea kadi za gari pale mbele (Glove Compartment) na nikakuta kadi ya ile gari, ikiwa katika jina la mke wa Dokta Kashushu.
Rukia bint Mkiwa.
Nilikumbuka maneno ya Dokta Kashushu wakati akinikabidhi zile funguo.
“...na vitu vyote utakavyovikuta humo ni mali yako kuanzia leo...hiyo ni namna yangu ya kukusaidia katika mtihani huu Tigga...”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Oh, Dokta Kashushu...yaani, Oh, Mungu wangu, yaani umeniachia hii gari?” Nilijisemea mwenyewe huku nikiizunguka na kuipapasa ile gari kwa kutoamini.
Duh! Dokta Kashushu! Wewe ni mtu wa aina gani lakini...? Ahsante sana huko uliko...!
Nilifurahi sana na kwa muda nilisahau matatizo yangu. Kwani kuwa na usafiri kungenirahisishia sana mienendo yangu iliyobakia katika kutafuta ukweli wa matukio haya ya ajabu yanayonikabili. Niliiacha ile gari ikiunguruma mle gereji nami nikarudi ndani ya ile nyumba na kuanza kufanya usafi. Kisha nilirudi na kuizima ile gari na kumuomba yule mlinzi wangu aje tusaidiane kukifunga kile kitanda kama inavyotakiwa.
Wakati tukifanya ile kazi nilikuwa nikimtupia maswali mbalimbali juu ya yule mke wa Dokta Kashushu ambaye yeye ndiye alimtambua kuwa ndiye mwenye nyumba, na nikagundua kuwa yule dada alimwambia yule mlinzi kuwa hakuwa na mume na alikuwa akijishughulisha na biashara zake binafsi ambazo hata yule mlinzi aliyeitwa Thonya hakuzijua. Naye alijaribu kunihoji juu ya maisha yangu na nikamwambia kuwa nimekuwa nikiishi Namibia kwa miaka mingi, na sasa nimerejea nchini kufanya kazi katika kampuni niliyokuwa nikiifanyia kazi huko Namibia, ambayo imefungua ofisi hapa nchini.
Alipotaka kujua jina langu nilimwambia kuwa nilikuwa naitwa Nuru bint Mkiwa.
Baada ya kumaliza shughuli hiyo nilioga na kujibwaga kitandani. Muda mfupi baadaye nilipitiwa na usingizi mzito, hasa kutokana na kwamba usiku uliopita sikulala vizuri.
--
Nilipoamka ilikuwa jioni na njaa ilikuwa ikiniuma sana. Nilibandika vile vibao vya namba kwenye ile gari na kutoka nayo nikimwambia Thonya kuwa nilikuwa naenda mjini mara moja. Niliingia kwenye kituo cha mafuta cha Suca na kuifanyia huduma muhimu (service) ile gari, kwani nilijua kuwa haikuwa imetembea kwa muda mrefu. Na wakati wale wataalamu wa kile kituo cha mafuta wakiifanyia marekebisho ya muhimu ile gari, nilikiendea kibanda cha simu kilichokuwa jirani na kupiga simu ile namba ya Kamishna Msaidizi John Vata. Ile simu haikuita kabisa, yaani ilikuwa kimya kabisa na moyo wangu ulizama kwenye simanzi. Bado iliniwia vigumu sana kuamini kuwa John Vata alikuwa amefikwa na umauti namna ile. Nilimpigia simu dada yangu Koku.
“Tigga? My God, uko wapi wewe...? Tuna wasiwasi sana juu yako! Yaani...hujajisalimisha kwa Kamishna Vata mpaka sasa? Sasa unadhani utaendelea kukimbia hovyo jijini mpaka lini mdogo wangu...mambo yametokea huku na hatujui uko wapi...!”
“Kamishna Vata...hajawasiliana na wewe...?” Nilimuuliza kwa wasiwasi.
“No! Angalau sio katika siku za hapa karibuni. Kuna wakati alinifuata ofisini na kuniambia kuwa ulikuwa ukimpa taabu...kwamba unampigia simu halafu hutaki kujitokeza...what’s the matter with you Tigga?”(...una tatizo gani Tigga?). Koku aliniuliza kwa hasira.
“Aaah, Koku...huu sio muda wa kulaumiana. Ni mambo gani hayo yaliyotokea tena...?”
“Kelvin is dead Tigga...(Kelvin amekufa Tigga)”
“Ke-Whaat? Mungu wangu, sasa...” Niliropoka kwa mshituko na nikahisi mbingu zikinishukia na pumzi zikinibana. Kelvin amekufa? Oh, Mungu wangu...kwanza John Vata...na sasa Kelvin...?
“Li...lini Koku? Amefariki lini...”
“Juzi. Hospitali. Na tumemzika mchana huu wa leo. Inasikitisha sana Tigga...ndugu zake, mama yake...wana simanzi kubwa, nao walitarajia wewe ungekuwepo kwenye mazishi, ingawa wanajua kuwa umekumbwa na matatizo...Kelvin aliwaeleza kwa kiasi fulani, nami nikawathibitishia.” Koku alinijibu haraka haraka. Ilinijia kumbukumbu ya Kelvin akiwa amelala sakafuni chumbani kwake huku akivuja damu. Akiniambia niondoke eneo lile kabla wale wauaji hawajanikuta. Na kuniomba samahani kwa kutoniamini hapo mwanzo. Niliumia sana na nikajitahidi kuzuia machozi yasinibubujike.
“Tigga...? Upo?” Koku aliniuliza kwenye simu.
“Ndiyo Koku nipo...hii habari imenishitua sana. Amezikwa wapi...?”
“Makaburi ya Kinondoni...Kulikuwa kuna askari kibao Tigga...na nadhani walikuwa wakikuvizia wewe. Ndio maana nakuambia kuwa jitahidi ujisalimishe kwa Kamishna Vata...he is the only one who can help you now Tigga (...kwa sasa ni yeye pekee ndiye anayeweza kukusaidia Tigga)” Koku aliniambia na moyo wangu uliumia kupita kiasi
“Kamishna Vata amekufa Koku...tulikuwa wote, ukatokea mlipuko...he is deadtoo...!(naye amekufa vile vile...!)”Nilimjibu kwa uchungu huku nikitoa mguno wa kilio.
“Whaaat?” Koku aliuliza kwenye simu nami sikuweza kuendelea na mjadala ule mchungu, nilikata simu na kurudi haraka kwenye gari yangu mpya. Niliendesha gari bila uelekeo maalum huku nikibubujikwa na machozi. Sikupenda kumkatia simu dada yangu namna ile lakini sikuwa na uwezo wa kuendelea kuongea naye hata neno moja zaidi baada ya habari zile.
Kelvin amekufa. John Vata amekufa. Moyo uliniuma na sikujua ni kipi kati ya vifo vile viwili kilichonisikitisha zaidi. Kelvin alishindwa kuniamini na nikamchukia kwa hilo, nikavunja uchumba wangu naye, lakini hakutakiwa kufa...na aligundua mapema kuwa alinikosea, ndio maana aliniomba msamaha na kunishauri niondoke haraka na nimuache yeye akiwa anavuja damu sakafuni.
John Vata alijitolea kuja kunisaidia hata baada ya kumpa taabu sana na kumfanyia vituko na kumjibu majibu ya mkato...na kwa kufanya hivyo akakutana na kifo...
...kwa sababu inaelekea kuwa kila unapopita unaacha kifo au vifo nyuma yako...
Maneno ya John Vata. Na inaelekea kuwa ni ya kweli tupu!
Oh, Mungu wangu...
Nilikuwa nikiendesha gari huku nikilia peke yangu. Njaa iliyokuwa ikiniuma iliyeyuka yenyewe na wala sikujisikia tena hamu ya kula kitu chochote. Na ilinijia akilini kuwa mambo yote haya, machungu yote haya, ni kwa sababu ya kushuhudia lile tukio la kutisha la kule msituni...na fitna za yule muongo aitwaye Wagga Maingo, natumai ile sindano niliyomchoma itakuwa imemuondoa duniani kufikia sasa.
Hatimaye niliishia kuegesha gari yangu kando ya bahari ya Hindi eneo la Ocean Road na kubaki mle ndani nikitazama bahari huku nikisononeka peke yangu juu ya misiba ile iliyoniangukia kwa kishindo. Sasa niliuona kabisa mwisho wangu ukinikaribia kwani sikuwa na shaka kabisa kuwa yule mwanamke mwenye hijab...The Virus...ataniua.
Salama yangu ni kuendelea kuushikilia ule mkanda wa video wenye ushahidi dhidi ya akina Wagga Maingo na yule kigulu aliyekuwa nao kule msituni.
Kwanza yule kigulu ni nani? Kwa nini sijamuona tena tangu siku ile kule msituni?
Lakini swali kubwa kabisa lililokuwa likiusakama ubongo wangu sasa ni kwamba baada ya kifo cha John Vata, niupeleke kwa nani sasa ule mkanda?
Baada ya kuzubaa pale pwani kwa muda bila ya kupata uamuzi wa kufaa, niliamua kurudi kwenye makazi yangu mapya Kimara, na ndipo nilipopita tena kwenye ile barabara ambayo kando yake ilikuwako ile kasino maarufu jijini, La Dreamer, na nilipoiona tu sikufikiri zaidi. Nilitafuta sehemu muafaka nikaegesha gari yangu mpya kwenye maegesho ya ile kasino iliyoificha kasino nyingine ndani yake na kuingia mle ndani kwa mara nyingine tena. Huku moyo ukinipiga haraka haraka, nilipitiliza moja kwa moja hadi kwenye ule mlango wa vioo na kupanda lifti kuelekea kule ilipokuwa ile kasino iliyoitwa The Rickshaw. Niliteremka kutoka kwenye lifti na kujikuta tena kwenye ile korido ya vioo na ile hisia ya kuwa nimo ndani ya boksi kubwa la kioo ilinijia tena. Mlangoni niliwaona wale mabaunsa wawili nami niliwapita na kuingia ndani ya ile kasino niliyokuwa na hamu sana ya kuiingia tangu siku ile nilipoigundua. The Rickshaw ilikuwa tofauti sana na ile kasino ya kule chini, kwani hapa niliona wazi kuwa kulikuwa kuna mambo makubwa zaidi. Kwanza hakukuwa na mwanga wa kutosha, ambao nadhani uliwekwa vile kusudi ili kuficha mambo yaliyokuwa yakifanyika mle ndani,kwamba kila mtu awe huru kufanya lake bila kuwa na shaka ya kuonwa na wengine. Nilifinya macho na kuangaza mle ndani na baada ya muda, macho yangu yalizoea ule mwanga wa mle ndani na kwa kihoro kikubwa nilishuhudia wahudumu wa mle ndani wakiwa wamevaa nusu uchi! Yaani kama unavyoona kwenye makasino ya kule ulaya kwenye filamu. Walikuwa wamevaa vijikaptura vya jeans vifupi sana vilivyokatwa kama chupi, na sidiria za kitambaa cha jeans lakini chepesi zaidi. Kwa vile viji-kaptura walivyovaa akina dada wale, karibu nusu nzima ya makalio yao ilikuwa nje! Kivazi kingine kilichokuwa miilini mwao wahudumu wale baada ya hivyo nilivyovitaja ni viatu virefu. Wote walikuwa na shepu nzuri na za kuvutia. Sikuamini macho yangu.
Ina maana hivi ndivyo akina Kachiki wanavyovalishwa wakija kutoa huduma humu ndani?
Niliangaza mle ndani kwa muda, kisha nikaamua kwenda kuketi kwenye moja ya viti virefu vilivyokuwa kaunta, nikiacha meza na viti zilizokuwa kwenye ukumbi mkubwa uliokuwa umetapakaa wateja kadhaa waliokuja kujistarehesha mle ndani, na kuanza kuangaza mle ndani kwa utulivu, ingawa moyoni nilikuwa na wasiwasi mkubwa, kwani sikujua nitagundua nini humu ndani ambacho Mr.Q alitaka nikigundue. Kwa hakika TheRickshaw ilikuwa ni kasino ghali kuliko ile ya kule chini. Hili nililiona mara moja kutokana na watu waliokuwemo mle ndani. Wengi wao walikuwa ni watu wenye asili ya kihindi, kiarabu na wazungu, ingawa kulikuwa na watu weusi wachache. Kulikuwa kuna wanaocheza pool, kamari za kila aina na kwenye kona moja ya ule ukumbi kulikuwa kuna steji ambapo akina mama wawili walikuwa wakicheza muziki wa vyombo vitupu uliokuwa ukisikika kutoka kwenye spika zilizokuwemo mle ndani, na muziki uliokuwa ukitoka kwenye spika zile ulikuwa ni ambao nimewahi kuusikia kabla, lakini huu ulikuwa ni wa vyombo vitupu. Mhudumu wa kaunta aliniuliza nilihitaji kinywaji gani, nami bila kusita nikaagiza Red Bull. Niliwekewa kile kinywaji mbele yangu juu ya kaunta nami nikaendelea kuangaza mle ndani kwa udadisi wa hali ya juu.Macho yangu yalirudi kule kwenye steji walipokuwa wakicheza wale akina mama wawili, au niseme ilikuwa ni miji-mama. Walikuwa wakicheza ule wimbo wa sasambu-sasambu huku wakisasambua nguo zao moja moja na niliona walikuwa wamepata watazamaji wengi waliokuwa wakishangilia na kupiga mbinja kila kiwalo kilipotolewa huku wakitupa mapesa kule stejini ili kuwashawishi wale akina mama waendelee kutoa nguo zao na kuwaonesha miili yao. Nilibaki nikiwa nimeduwaa. Mambo waliyokuwa wakiyafanya wale akina mama ni sawa kabisa na yale ambayo huwa tunayaona kwenye “Kitchen Party”,cha ajabu hapa yalikuwa yanafanywa mbele ya midume ya kizungu, kihindi, kiarabu na baadhi ya waswahili. Nilitupa macho yangu upande mwingine wa ile kasino na nikaona kuwa kulikuwa kuna milango ya mninga iliyokuwa imejipanga katika upande ule, ambayo nilidhani ilikuwa ikifungukia kwenye vyumba. Na hata pale nilipokuwa nikiitazama ile milango, mmoja ulifunguliwa na mwanamme mmoja wa kiarabu alitoka na mwanadada mmoja wa kiswahili ambaye sikuhitaji kabisa kuambiwa kuwa alikuwa changudoa. Na kwa jinsi walivyokuwa wameshikana, sikuwa na shaka kuwa walikuwa wametoka kufanya ngono.
Mungu wangu! Yaani kuna danguro humu humu!
Na muda mfupi baadaye, jamaa mmoja wa kiswahili aliyekuwa akinyonyana na kupapasana na binti mwingine kwenye meza waliyokuwa wamekaa kwenye ule ukumbi, aliinuka na kuongozana na yule binti kuelekea kwenye vile vyumba.
“Uko peke yako?” Nilishitushwa na sauti ya kiume ya yule mhudumu wa kaunta aliyeniuliza huku akipangusa kaunta kwa kitambaa. Nilimtazama kwa muda na kumjibu kwa kichwa kuwa nilikuwa peke yangu.
“Ni nini unachokitaka hapa? Wanawake huwa hawaji peke yao hapa...” Aliniambia bila kunitazama huku akiendelea kupangusa kaunta yake kwa kitambaa.
“Kuna mtu namsubiri...tuna miadi tukutane hapa...kwani hairuhusiwi?” Nilimjibu na kumuuliza hapo hapo. Yule bwana alibetua mabega yake tu na kuendelea na shughuli zake bila kuongea zaidi. Sikuelewa nini maana ya kitendo kile, lakini nilielewa kuwa sikutakiwa nikae pale peke yangu kwa muda mrefu. Tayari nilikuwa nimeshaanza kuleta wasiwasi ndani ya nyumba. Nilivuta bakuli kubwa lililokuwa limejaa korosho na kuanza kuzitupia kinywani mwangu taratibu huku nikishushia kwa Red Bull yangu.
Nifanye nini sasa?
Muda huo aliingia mwanamume mmoja ndani ya ule ukumbi na kuketi kwenye kiti cha tatu kutoka kile nilichokalia nami sikumtilia maanani, nikiendelea kuangaza mle ndani, lakini baada ya muda niligundua kuwa yule mtu aliyeingia alikuwa akinitazama sana. Nilimgeukia kumtazama naye akaamua kutazama saa yake, kisha akainuka na bilauri yake ya kinywaji na kwenda kuketi kwenye meza iliyokuwa katikati ya ule ukumbi na kuanza kuangalia ile sasambu-sasambu iliyokuwa ikiendelea kule kwenye steji, sasa hivi ile miji-mama ikiwa imebaki na vibikini tu wakiwa wamejifunika vitambaa laini sana vilivyoonesha kila kitu, na ukumbi wote sasa ulikuwa ukizizima kwa vifijo na hoi hoi, wale mashabiki wakiwashawishi wale akina mama watoe kabisa zile nguo zilizobakia miilini mwao, nao wakitishia kuvua na kuvaa tena.
Nilimtazama yule jamaa aliyeingia mle ndani kwa makini. Alikuwa mwembamba na mfupi, rangi yake maji ya kunde, nywele za shombe, na alikuwa amevaa miwani myeusi usoni kwake. Sasa miwani myeusi ya nini humu ndani?
Ni nani huyu? Mbona ameonesha udadisi sana kwangu? Ni kwamba amenitamani tu kama kawaida ya matamanio ya wanaume, au kuna kitu kingine...?
Niliwatazama wale akina mama wenye maumbo makubwa yaliyojazia wakifanya yale mambo ya aibu na nikajihisi kudhalilika kusiko kifani. Na wakati nikiwatazama, nilipatwa na mshituko mkubwa sana na moyo ukaanza kunienda mbio. Niliteremka kwenye kile kiti kirefu na kusogea katikati ya ule ukumbi na kuwatazama kwa makini wale akina mama. Hususan mmoja kati yao, kwani ilinijia akilini mwangu kuwa nilishawahi kumwona sehemu kabla ya pale na akili yangu ilikuwa ikizunguka kujaribu kutafuta ni wapi hasa nilipomuona.
Nina hakika nimewahi kumuona huyu mwanamke sehemu...ni wapi...?
Na hata pale wazo hilo lilipokuwa likipita kichwani mwangu, yule mwanamke aliinama na kuwatazama wale wanaume wa makabila mchanganyiko huku akiwa ameinua makalio yake kuelekea ukutani na wale watu walikuwa wakimpigia kelele kumshawishi awageuzie wao, na yule mwanamke aliwatolea tabasamu fulani la tash-wishi, huku akiwa amerembua macho kwa namna ya kuchokoza hisia za wanaume. Na hapo ikanijia.
Lile tabasamu! Nimeshaliona mahali...
Oh, My God! Nilikumbuka! Nilikumbuka nilimuona wapi yule mwanamke na moyo wangu uliingia baridi na nikaanza kurudi pale kaunta nilipokuwa nimekaa hapo awali taratibu huku akili ikinitembea.
Yule mwanamke alikuwa ni mmoja kati ya ile mijimama miwili iliyokuwa kwenye picha niliyooneshwa na marehemu Dick Bwasha ofisini kwake siku ambayo baadaye alikutwa akiwa amefariki!
Ni yeye! Ni lile tabasami ndilo lililokuwa kwenye sura yake wakati anapigwa ile picha akiwa na mwenzake wote wakiwa utupu kabisa kitandani pamoja na yule meneja wa benki aliyekuwa mwingi wa jeuri na dharau.
Ah! Sasa nimemkuta “live” hapa The Rickshaw! Ama kwa hakika Mr. Q alijua kuwa hapa ndipo kwenye majibu ya maswali yangu. Nilimtazama yule mwanamke mwingine aliyekuwa akisasambua na yule niliyemtambua pale stejini, lakini yule hakuwa yule aliyekuwa kwenye ile picha niliyooneshwa na Dick Bwasha marehemu.
Na muda huo taa za pale ukumbini walipokuwa wakicheza wale akina mama zilizimika na nikashuhudia zile bikini zilizokuwa zimevaliwa na ile mijimama zikitupwa kule walipokuwa wamekaa wale wanaume waliokuwa wakiwashangalia. Ile midume ilizigombea zile bikini kama mijibwa inayogombea nofu la nyama, huku waliobahatika kuzitia mikononi mwao wakizibusu na kushangilia. Aibu iliyoje hii!
Taa zilipowashwa tena kule stejini, wale akina mama walikuwa wametoweka, wakiacha miguno na hoi hoi kutoka kwa wale wanaume waliojazana kushuhudia mchezo wao ule mchafu. Nilichoka! Yaani haya mambo ndio yako hivi! Niliagiza Red Bull nyingine na kubaki nikiangaza huku na huko mle ndani huku akili ikinitembea. Watakuwa wameenda wapi wale akina mama? Ni lazima niongee na yule mwanamke. Nimuulize kuhusika kwake na tafrani yote hii inayonikabili.
Lakini kaenda wapi sasa?
Niliinuka na kuelekea sehemu iliyokuwa na vyoo vya akina mama ndani ya ile kasino ambayo sikupata taabu kuiona, nikiwa na matarajio kuwa huko ndiko ningewakuta wale akina mama. Haswa yule mmoja niliyemtambua kutoka kwenye picha ya Dick Bwasha.
Kule chooni sikukuta mtu. Nilirudi tena kwenye kiti nilichokuwa nimekalia hapo mwanzo huku akili ikinizunguka.Kapotelea wapi tena?
Bila shaka kutakuwa kuna chumba cha kubadilishia nguo sehemu fulani mle ndani, naye atakuwa huko. Niliamua kuendelea kusubiri pale pale nikiamini kuwa mlango wa kutokea mle ndani ni ule ule mmoja tu.
Wakati nikisubiri huku nikinyonya Red Bull na kuendelea kuangaza mle ndani, nilipata mshituko wa hali ya juu baada ya kumuona yule jamaa mwenye nywele za shombe aliyevaa miwani ambaye hapo mwanzo nilimtilia mashaka kwa kunitazama sana akinyonyana ndimi na mwanaume mwingine aliyenyoa upara ambaye sikuweza kujua kwa urahisi iwapo alikuwa mmbantu au muasia kutokana na mwanga hafifu wa eneo lile.
Khah! Hii sasa dharau hii! Yaani...Ah!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yaani sikuamini, na nikahisi kichefuchefu kuona midume mizima ikifanya mambo ya aibu namna ile. Na hata pale nilipokuwa nikistaajabia tukio lile, nilishuhudia yule jamaa mwenye upara akimpapasa yule shombe kama kwamba alikuwa mwanamke!.
Heh! Yaani kumbe huyu jamaa shoga! Mmnh! Mbona makubwa!
Nilimgeukia yule mhudumu wa pale kaunta ili nimuulize juu ya maajabu yale, lakini wakati huo huo nikamuona yule mama niliyekuwa nikimvizia akitokea sehemu nyuma ya ile steji waliyokuwa wakichezea na mwenzake na kuja pale kaunta. Alikuwa amevaa suruali ya skin tight iliyoonesha shepu yake kubwa ambayo sikuwa na shaka ilikuwa ikiwapagawisha wanaume kwa kadiri alivyotaka, na juu alikuwa amevaa shati fupi lililoishia juu kidogo ya kiuno chake ilhali mikono ya shati lile ikiiishia chini kidogo ya viwiko vyake. Chini alikuwa amevaa viatu vya chini kama vile vyangu vya kamba nilivyonunua mtumbani kule Manyoni katika hatua za mwanzo kabisa za mkasa huu , na kwapani kwake alikuwa amefumbata mkoba mzuri sana wa kike. Nilimkodolea macho yule mwanamke mtu mzima na nikastaajabia kitendo cha mama kama yule kujihusisha na mambo kama yale, hasa nikiikumbuka ile picha aliyopiga akiwa na Dick Bwasha. Alipita pale kaunta na kumsalimia yule mhudumu huku akimtolea tabasamu zuri sana na kuelekea kwenye mlango wa kutokea nje ya ule ukumbi wa starehe uliojaa madhambi. Bila kufikiri wala kujishauri nilimlipa yule mhudumu pesa yake na kuinuka kumfuata.
“Vipi, uliyekuwa ukimsubiri ameshafika? Au kakugandisha?” Yule mhudumu aliniuliza kwa kejeli. Niligeuka kumtazama na hapo nilimuona yule mwanamke mwingine aliyekuwa akifanya mambo ya unyago na yule mama pale stejini akitokea kule alipotokea mwenzake akiwa ameambatana na mwanaume wa kihindi ambaye alikuwa amemshika kiuno huku wakichezeana kwa mahaba, nami badala ya kumjibu yule mhudumu, nilimbetulia mabega kama jinsi yeye alivyonibetulia hapo mwanzo na kutoka nje ya ule ukumbi kumfuata yule mama.
Nilimuwahi kwenye lifti na nikajikuta nikiwa naye ndani ya ile lifti wakati ikiteremka kutoka kwenye ghorofa ya juu ya lile jengo lililohifadhi zile kasino mbili. Nilimtazama na kujikohoza kidogo kisha nikamsalimia kwa kumpa shikamoo. Yule mama alitabasamu na kuitikia salamu yangu. Nilimtazama naye alikuwa akinitazama huku akiwa amefanya tabasamu dogo.
“Anti...samahani. Nilikuwa na shida na wewe...sijui tunaweza kuongea kidogo...?” Nilimuuliza kwa mashaka. Yule mama alicheka.
“No, no, no....una shida na mimi Anti? Hapana, mi’ huwa sifanyi wanawake bwana! Kama unataka wanawake sema nitakuonesha wasagaji kibao hapo juu, lakini itabidi unilipe!” Yule mama aliniambia huku akicheka nami nikabaki mdomo wazi.
“Eti? Hapana Anti! Sio hivyo, sina nia hiyo, Loh!” Nilimjibu kwa kihoro huku nikimtazama kwa mshangao.
Mmnh! Yaani mambo ya The Rickshaw ni ufirauni mtupu! Sasa na mimi kwa kuja huku tayari nimeonekana ni miongoni mwao! Eh, Mungu wangu nisamehe mja wako! Mbona n’nazidi kutumbukia kwenye mambo ya ajabu?.
Ile lifti ilifika chini na yule mama alitoka na kuanza kuelekea kwenye ule mlango uliotokea kwenye ile kasino nyingine ya chini nami nikamfuata.
“Sasa ulikuwa na nia gani binti! Hii The Rickshaw bwana! Hakuna kinachotafutwa humu zaidi ya hilo...we vipi?” Alinisemesha bila kunitazama huku akiendelea na safari yake. Nilimshika mkono na kumsihi anisikilize. Aliuchomoa mkono wake na kunitazama kwa macho ya kuuliza.
“Anti, naomba dakika chache tu za muda wako. Labda tukae kidogo hapa tupate kinywaji...nina tatizo kidogo tu ambalo nadhani wewe utaweza kunisaidia...please!” Nilimwambia kwa kumsihi. Alinitazama kwa muda, kisha bila ya kusema neno alichagua meza iliyokuwa karibu pale kwenye ile kasino ya chini na tukaketi.
“Sema. Una shida gani, na sema upesi kwani sina muda wa kupoteza.” Aliniambia.
“Anti, ninaamini nimepata kukuona mahali. Na nilipokuona ulikuwa na mtu fulani. Nina hitaji taarifa za huyo mtu niliyekuona naye.” Nilimwambia kwa upole huku nikijiuliza iwapo ile ilikuwa ni njia nzuri ya kuanzisha mazungumzo na yule mama ambaye kila nilipomtazama, neno “shangingi” lilikuwa likipita kichwani mwangu. Alinitazama kwa namna ya kutoelewa.
“Sema kitu kinachoeleweka binti! Uliniona mahali, sasa mahali hapo ni wapi? Mimi natembea sehemu nyingi bwana!” Aliniambia kwa kukereka. Hapo mhudumu alifika, nikamwambia aagize atakacho.
“Castle ya kopo...mbili. Huyu atalipa!” Alimuagiza huku akinioneshea kidole, nami nikaafikiana naye kwa kichwa huku nikijiuliza kwa nini ameagiza Castle mbili. Mimi sikutaka kuagiza chochote.
“Actually, ni picha ambayo ulikuwa umepiga..ukiwa na mwenzako na mtu mwingine...” Nilianza kumuelezea, lakini hapo yule mama aliangua kicheko kikubwa sana. Nikashangaa ni nini kinachomchekesha, lakini kabla sijamuuliza alinijibu.
“Ah! We’ binti kweli juha. Mimi kupigwa picha ndio kazi yangu bwana! Nimepiga picha nyingi sana ambazo chache zinaonekana hapa nchini, lakini nyingi zinauzwa nje ya nchi na ninajipatia pesa nzuri tu. Hata mikanda ya video ipo niliyopiga. Sasa wewe kuona picha ndio inakuwa ajabu? Hiyo ni kazi yangu bwana!”
“No Anti. Sioni ajabu. Ila picha yenyewe...picha yenyewe ilikuwa ya utupu! Na ilikuonesha wewe na mwanamke mwingine mkiwa na mwanaume mmoja kitandani...sasa ni huyo mwanaume ndiye ninayetafuta habari zake.”
“Binti, kupiga picha za utupu kama unavyoziita, ni miongoni mwa kazi zangu. Si umeona mambo niliyokuwa nikiyafanya mle ndani sasa hivi? Nayo ni kazi yangu, na ndio inayoniweka mjini. Na wala sioni haya juu ya hilo. Sasa kuhusu huyo mtu niliyepiga naye picha, kama ni mumeo basi si swala langu. Ni yeye mwenyewe ndiye aliyeona kuwa anahitaji huduma ya watu kama sisi, kwani nina uhakika kabisa kuwa mambo tunayoweza kumfanyia watu kama sisi wewe usingeweza kumfanyia asilani!” Alinijibu kwa jeuri na muda huo vinywaji vilifika. Alifungua kopo moja la Castle na wakati huo huo akatumbukiza kwenye mkoba wake lile kopo la pili.
“Hapana Anti, yule si mume wangu, ila kuna mali alinidhulumu nami nilikuwa namtafuta kwa hilo...unadhani unaweza kunisaidia?” Nilimuuliza.
“Kwanza ni nani? Mimi hata sina kumbukumbu ya huyo mtu unayemsema wala hiyo picha unayoisema. Ninachojua ni kwamba mimi nikiambiwa na bosi wangu kwenda kumhudumia mteja naenda, nikirudi nachukua posho yangu naondoka. Sina haja kabisa ya kujua mteja ni nani au anatoka wapi!Ndio utaratibu tuliopangiana na bosi wetu!”
“Ah, sasa ina maana humfahamu mtu aitwaye Dick Bwasha?” Nilimuuliza huku nikimtazama kwa makini, nikijua kuwa Dick Bwasha ameshakufa na kwamba kama alikuwa anamfahamu, bila shaka angejua kuwa ameshakufa. Na kwa vyovyote angesema neno au angefanya jambo la kunijulisha kuwa alikuwa akimfahamu yule mtu.
Yule mama alitikisa kichwa kumaanisha kuwa hamfahamu huku akinywa kinywaji chake. Na wala haikuonesha kuwa alikuwa akimfahamu Dick Bwasha. Yaani kwake lile jina halikuwa likimaanisha chochote. Hii ilinipoteza muelekeo na sikujua niendelee vipi.
“Kwa hiyo sasa... bosi wako ndiye anayekuunganisha na hao wateja? Kwa hiyo ndiye aliyekuunganisha na Dick Bwasha?” Nilimuuliza. Aliafiki tena kwa kichwa kabla ya kuongea. “Nd’o maana’ake! Sasa kama huyo mtu uliyeniona naye kwenye picha alikuwa ndio huyo Dick-nani-sijui, au nani, hiyo mi’ sijui, lakini huo ndio utaratibu. Na naona nimekuwa nikikuongelea tu mambo yangu bila ya sababu ya msingi. Nashukuru kwa kinywaji na sasa naomba niende!”
Hakuonesha dalili ya kuondoka. Bado alikuwa akibugia ile bia niliyomnunulia.
“Hapana Anti! Naomba nikuulize swali la mwisho! Ni muhimu sana...!” Nilimwambia lakini alitikisa kichwa vikali kukana swala lile.
“Kama lingekuwa ni muhimu ningeona angalau elfu kumi mkononi mwako sasa hivi. Hapo ningeamini kuwa kweli ni muhimu! Sasa wewe hivi hivi tu...” Yule mama alisema kijanja huku akijitia kukusanya mkoba wake tayari kwa kuondoka. Nilijua alitaka nimpe pesa ili anipe ushirikiano zaidi.
Pumbavu!
Mara moja mkononi mwangu kukawa kuna noti ya elfu kumi, na nikamtupia swali.
“Sasa...huyo bosi wako ni nani...na nitampata wapi?” Nilimuuliza. Aliikodolea macho ile pesa.
“Aaa, sasa kwa hilo siwezi kukuambia! Sio taratibu...kama ungekuwa unamtafuta kwa biashara ningekuambia, lakini ni wazi sababu zako si za kibiashara...” Alinijibu kwa mashaka. Nilimwambia kuwa ndio maana kuna ile pesa mkononi mwangu, ili anitajie bosi wake ni nani, ingawa ni kinyume cha utaratibu. Alikaa kimya kwa muda, na nikaona alikuwa akijishauri kichwani mwake. Moyo ulianza kunienda mbio kwani nilijua kuwa akinitajia, huenda nikawa nimemjua mtu atakayenikurubisha kwenye chimbuko la lile genge la akina Wagga Maingo na yule mshirika wao hayati Dick Bwasha.
“Anti, nijibu tafadhali! Bado zipo nyingi huku nilipotoa hii noti...” Nilimwambia huku nikiongeza noti ya shilingi elfu tano mkononi mwangu. Yule mama alizikodolea macho zile noti zilizokuwa mkononi mwangu.
“Ni nani huyo bosi wako? Naahidi kuwa sitakutaja kuwa ni wewe ndiye uliyenitajia!” Nilizidi kumshawishi.
Alizichukua zile pesa taratibu kutoka mkononi mwangu, lakini nilizing’ang’ania naye akashindwa kuzichukua. Tulitazamani tukiwa tumeshikilia zile pesa, kila mmoja akijaribu kuvutia kwake. Huku akinitazama kwa makini yule mama aliniambia.
“Okay binti, umetaka jina la bosi wangu nami nitakutajia. Nipe hizo pesa kwanza!”
Nilimtazama kwa muda, kisha bila kusema neno niliziachia zile pesa naye akazizamisha ndani ya mkoba wake. Tukabaki tukitazamana.
“Utahitaji kuongea na The Bastard...yeye ndiye bosi.” Alinijibu na nikapata mlipuko mkubwa wa moyo na hapo hapo ukaanza kunienda mbio.
“Eti Whaat?The Bastard...?” Niliropoka huku nikimkodolea macho yule mwanamke mtu mzima mwenye kupiga picha za utupu na kucheza unyago kwenye kasino. Nini maana yake hii? Yaani The Bastard ni mtu anayeishi? Ni jina la mtu? Ina maana yule mtu aliyeuawa na Macho ya Nyoka kule porini aliposema “Find The Bastard” alikuwa anamaanisha kuwa nimtafute mtu aitwaye The Bastrad!
Oh, My God...This is unbelievable!( hii ni ngumu kuamini!).
“He! We’ binti vipi? Mbona hivyo...?” Yule mama alinishitua kutoka kwenye mawazo yangu huku akinisukuma mikono yangu na ni hapo ndipo nilipogundua kuwa nilikuwa nimemkamata mabega kwa nguvu.
“Oh, Oh...samahani! Samahani...nilikuwa...nilikuwa...nime...umesema The Bastard ndiyo bosi wako? Ni nani yeye? Na nitampataje? Yuko wapi? Oh, My God! Nitamjuaje?” Nilibwabwaja kwa papara huku nikijitahidi kumzuia yule mama asiondoke, naye akiwa tayari ameshainuka na akipachika mkoba wake begani na akinitazama kama kwamba nilikuwa mwehu, au juha kama mwenyewe alivyoniita hapo awali.
“Binti. Mimi sijui wewe ni nani na kwa nini unamtafuta huyo Dick –nani-sijui. Umetaka kujua bosi wangu ni nani nimekutajia, na hapo ndipo biashara yetu ilipoishia.Mimi naondoka na nikiondoka hapa nitakuwa sijawahi kuonana na wewe hata siku moja, na wala wewe hujaonana na mimi hata siku moja. Kama kuna mtu aliyekutajia kuwa bosi wetu ni The Bastard basi mtu huyo sio mimi! Sawa?” Aliniambia na kutoka nje ya ile kasino, akiniacha nikiwa nimepigwa na butwaa pale kwenye ile meza. Nilipopata ufahamu, tayari yule mama alikuwa ameshatoka nje. Nilikurupuka kumfuata, lakini yule mhudumu alinisimamisha akidai pesa yake. Nilimpa noti ya shilingi elfu kumi na kumwabia kuwa nitarudi kuchukua chenji yangu na kuwahi kule nje alipopotelea yule mama. Nilimkuta akiongea na dereva wa teksi.
“Samahani Anti, lakini bado ninahitaji taarifa zaidi. Huyu The Bastard...hana jina jingine? Ni wapi anapofanyia shughuli zake?” Nilimuuliza. Yule mama alinitazama, na bila kunijibu aliingia ndani ya ile teksi, kisha alinijibu huku akinitazama kupitia dirisha la ile teksi.
“We’ binti mbona unakuwa juha hivi? Nimekwambia hilo ndilo jina lake! Na hiyo ndio ofisi yake!” Aliioneshea ile kasino kwa kichwa chake, kisha akamgeukia dereva wa teksi.”Lets Go!(Twende zetu!)”
Nilibaki nikiwa nimesimama pale nje ya ile kasino nikiishuhudia ile teksi ikiondoka eneo lile nikiwa sina la kufanya.
The Bastard ni jina la mtu!
Muda wote nimekuwa nikiamini kuwa Mr. Q aliposema yale maneno yaliyomaanisha nimtafute “The Bastard” alikuwa akimaanisha kuwa nimtafute yule mwanaharamu Wagga Maingo na wenzake ili niwafikishe mbele ya sheria.
Kumbe alikuwa anamaanisha mtu maalum! Mtu ambaye ndiye alikuwa akiendesha ile biashara ya ufuska na uhuni ndani ya ile Kasino iliyoitwa The Rickshaw.
Nimekuwa nikitafuta majibu ya tukio lile la kule msituni kwa muda mrefu. Na tangu mwanzo wa kizaazaa hiki niliambiwa na Mr. Q kuwa majibu nitayapata The Rickshaw, na leo ndio nimeambiwa kuwa The Bastard, ambaye ndiye alikuwa na majibu ya maswali yangu yuko ndani ya hii kasino The Rickshaw.
Lazima leo nipate majibu. Lakini nilijua kuwa huenda huu ukawa ndio mwisho wa safari yangu ya kutafuta ukweli juu ya mambo haya yaliyonikuta. Aidha niwafichue madhalimu waliofanya mauaji kule msituni, au wao waniangamize. Woga mkubwa ulinikumba na nikaanza kulitazama lile jengo lililokuwa na ile kasino The Rickshaw kwa mtazamo mpya.
I wish John Vata was here (Natamani John Vata angekuwepo).
Kwa vyovyote lazima nirudi tena mle ndani, hata kama ndio litakuwa jambo la mwisho kulifanya hapa duniani. Nilimfikiria dada yangu Koku na mama yangu.
Eh, Mungu wangu, huenda nisiwaone tena baada ya kuingia tena ndani ya hii kasino.
Na hata sijapata nafasi ya kwenda angalau kumwombea dua Kelvin kaburini kwake...
Nilivuka barabara na kukiendea kibanda cha simu kilichokuwa hatua chache upande wa pili wa ile kasino na kumpigia tena simu dada yangu. Alipopokea ile simu na kunitambua alianza kunifokea na kunilaumu kwa kumkatia simu wakati tulikuwa tukiongea mambo mazito namna ile. Nilimtaka radhi kuwa sikuweza kabisa kuendelea kuongelea mambo yale ya kuhuzunisha.
“Nilienda kumuulizia John Vata makao makuu ya polisi, lakini hakuna nililoelezwa, na nikashindwa kuwauliza iwapo ni kweli amefariki kwani ningejitia kwenye matatizo...” Koku alinieleza.
“John Vata amekufa Koku, mimi nilikuwepo wakati tukio lililopelekea kifo chake lilipotokea! Lakini hilo silo nililokupigia Koku...” Nilimjibu kisha nikamwomba anielekeze sehemu ambapo Kelvin alizikwa pale kwenye makaburi ya Kinondoni. Koku alinielekeza kisha akaniuliza nilikuwa nataka kufanya nini.
“Koku, naomba ujue kuwa mimi nakupenda sana dada yangu, na mama pia. Nimegundua sehemu ambayo nadhani ndio chimbuko la mkasa wote huu ulionikuta na sasa nataka kwenda. Huenda nisitoke salama huko niendako Koku...”
“Usiende Tigga! Achana na mambo hayo.Bora ujisalimishe polisi...” Koku alidakia kwa wasiwasi.
“Hapana Koku, wewe huelewi.Hili jambo ni zito na linawahusu wengi na siwezi kwenda kichwa kichwa kwa kila askari na kumueleza. Kama nitatoka salama huko niendako, nina nia ya kwenda kumwombea dua Kelvin, lakini kama nitatokewa na jambo lolote Koku, naomba ukaniombee kwa Kelvin kwa niaba yangu na ujue kuwa ninawapenda sana...wewe na mama...”
Koku alianza kulia.
“Kwa nini unaniambia mambo hayo mdogo wangu...?”
“Na kama nitatokewa na jambo lolote, nakuomba sana uchukue ile Televisheni yangu kule nyumbani kwangu. Nataka iwe yako Koku. Ina matatizo kidogo, lakini ukifungua kule nyuma, kuna kiji-waya kidogo huwa kinalegea. Ukikikaza itafanya kazi kama kawaida. Nakuomba sana Koku!” Nilimwambia bila ya kujali maneno yake. Koku alishindwa kunielewa na alizidi kulia kwa sauti.
“Kwa nini unanifanyia hivi mdogo wangu lakini...?” Alilalama.
“Zingatia maelezo yangu Koku! Televisheni iwe yako! Mimi yanipasa niende sasa. Kama nitatoka salama, ujue nitakuwa nimejikomboa kutoka kwenye mkasa huu, na nitakupigia simu kukufahamisha. Ila siku ya leo ikipita, na kesho ikapita bila kupata simu kutoka kwangu, basi ujue ndio...ndio...ukumbuke kuwa nawapenda sana...na uzingatie maelekezo yangu!” Nilimwabia nami nikihisi donge kubwa likinikaba kooni. Sasa Koku alikuwa akilia kwa kwikwi.
“Tigga...Tigga...”
“Koku, Kwa heri. Niombee kwa Mungu, na zingatia maelekezo yangu!”
Nilikata simu. Nilishusha pumzi ndefu, kisha nilijipa moyo na kuvuka tena barabara na kuelekea kule ilipokuwa ile kasino La Dreamer. Ndani yake kukiwa na ile kasino The Rickshaw.
Na mtu aitwaye The Bastard.
Niliingia ndani ya ile kasino na kuchukua chenji yangu kutoka kwa yule mhudumu wa La Dreamer. Kisha nilipanda tena ile lifti na kurudi ndani ya The Rickshaw.
Come what may.
Liwalo na liwe.
--
Nilipotokea tu kwenye ile korido ya vioo niliona wale mabaunsa wakitazamana na kujizatiti vizuri zaidi pale mlangoni. Mara moja nilijua kuwa sikuwa nikihitajika tena mle ndani, nilishajionesha kuwa si miongoni mwao. Nilisita kidogo pale kwenye korido nisijue nichukue uamuzi gani, lakini muda huo nikamuona binti moja akitokea mwisho kabisa wa ile korido, kushoto kwangu ambapo siku ile nilipokuja kwa mara ya mwanzo kabisa niliona kuwa kulikuwa kuna ngazi zilizokuwa zikielekea juu zaidi ya lile jengo. Bila kufikiri zaidi nilikunja na kuelekea kule alipokuwa akitokea yule binti ambaye alikuwa akihesabu pesa huku akitembea kwa mikogo. Nilimtazama kwa makini huku nikienda kule alipokuwa akitokea na nikamkumbuka kuwa ni yule binti wa kiswahili niliyemuona akiingia kwenye vile vyumba nilivyohisi kuwa ni vya kufanyia ngono mle The Rickshaw akiwa na mwanamume wa kiswahili.
Nilipomfikia karibu niliona yule binti akinitazama kutoka chini mpaka utosini na kunishusha, kisha akabetua midomo yake kwa dharau. Nilimtazama kwa mshangao.
Inahusu nini tena? Kwa nini ananitazama namna hii? Sikuelewa, na sikujali. Mwisho wa ile korido nilikunja kulia na kuzifikia zile ngazi. Nilizipanda taratibu huku nikijitahidi nisigeuke nyuma kutazama iwapo wale mabaunsa walikuwa wakinifuata. Mwisho wa zile ngazi nilikuta mlango mzito wa mninga ambao ulikuwa umezatitiwa na geti la chuma mbele yake. Ule mlango ulikuwa ukiingia kwenye nyumba ndogo iliyokuwa juu ya ile kasino ya The Rickshaw, yaani Penthouse. Kwa uelewa wangu mara nyingi nyumba za aina hii huwa hazina vyumba vingi. Nilisimama nje ya ule mlango nikijishauri nifanye nini huku nikigeuka nyuma kutazama iwapo wale mabaunsa walikuwa wameamua kunifuata, na nikaona nilikuwa peke yangu. Lile geti la chuma lilikuwa wazi. Niliujaribu ule mlango nao ulifunguka bila taabu. Sidhani kama nina haja ya kukuambia ni jinsi gani moyo wangu ulivyokuwa ukipiga kufikia hapa, lakini ndani kabisa ya moyo wangu kulikuwa kuna msukumo uliokuwa ukinizuia kabisa kurudi nyuma.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapa ndipo nilipoambiwa kuwa majibu yatapatikana, na sikuwa na namna nyingine ya kuyapata majibu hayo bila mimi mwenyewe kujitosa. Niliingia ndani.
Nilijikuta nikiwa ndani ya sebule moja nzuri sana, kuta zake zikiwa zimepambwa na mapicha ya akina dada wa kila kabila wakiwa utupu katika mitindo mbalimbali. Hewa ndani ya sebule ile ilikuwa ikipozwa kwa kiyoyozi mwanana. Zulia lililotandikwa sakafuni lilikuwa zuri na ghali sana.
Chumba chote kilikuwa kikinukia harufu ya manukato fulani ambayo sikuweza kuyajua mara moja, lakini ilikuwa ni harufu iliyoleta hisia fulani ya mapenzi. Yaani hata mimi niliyekuwa kwenye matatizo mazito kama haya niliyonayo nilipata hisia hiyo, sasa sijui kwa mtu anayekuja hapa kwa nia ya kutafuta burudisho la mapenzi. Muziki laini wenye mahadhi ya kiarabu ulikuwa ukisikika kutoka kwenye spika zilizokuwa zimening’inizwa kwenye kila kona ya chumba kile kwa juu. Kufikia hapa tayari nilikuwa nimeshapata hisia kuwa hapa ndipo haswa mahala nilipotakiwa kuja, kwani kulionekana wazi kuwa ndipo mipango yote ya ngono za kule ndani ya kasino ilipokuwa ikifanyikia. Kulikuwa kuna masofa mazuri sana pale sebuleni nami nilianza kutembea mle ndani kwa hatua zisizo na uhakika huku nikijikohoza ili kama kuna mtu anisikie na kuja kunisikiliza shida yangu.
Kulia kwangu kulikuwa kuna mlango mwingine ambao sikuwa na shaka kuwa ulikuwa ukiingia chumbani. Mlango ule ulikuwa wazi na pazia laini ilikuwa ikidhibiti macho ya mtu aliye sebuleni kuona kilichokuwa kikitendeka ndani.
“Karibu mrembo, karibu! Pita ndani!”
Sauti ya kike ilinikaribisha kwa pozi za madaha ya hali ya juu na nikashituka kusikia ile sauti ikitokea kule chumbani. Niliangaza huku na huko mle ndani lakini nilikuwa peke yangu.
Sasa huyo mtu wa huko ndani amenionaje?
Sikuwa nimetegemea kukuta mwanamke humu ndani, lakini mara baada ya kuisikia ile sauti, nilijua kuwa kwa mazingira ya pale ni mwanamke pekee ndiye ambaye nilitakiwa nimtarajie humu ndani. Niliusogelea ule mlango wa kile chumba taratibu huku moyoni nikiwa nimejawa na woga juu ya nitakayokutana nayo humo ndani.
Je, huyu mwanamke atanitajia The Bastard ni nani?
Niliingia chumbani. Na nikabaki nikiwa nimepigwa na butwaa.
Kilikuwa ni chumba kipana sana, na katikati ya chumba kile kulikuwa kuna kitanda kikubwa kiasi cha kuwa zaidi ya futi sita kwa sita. Upande mmoja wa chumba kile pamoja na dari lake vilikuwa ni kioo kitupu, kiasi kwamba kama ukilala chali pale kitandani utakuwa ukijiona kutokea kwenye dari la chumba kile. Upande wa pili kulikuwa kuna mlango wa kioo kizito ambao sikuwa na shaka kuwa ulikuwa ukielekea chooni. Upande mwingine wa kile chumba, kulikuwa kuna kabati kubwa kabisa la nguo lililotambaa upana wote wa chumba kile, na kutoka chini hadi juu. Na kwa ule upande ambao mlango ulikuwako, kando ya ule mlango, kulikuwa kuna meza kubwa na safi ya kiofisi ambayo juu yake kulikuwa kuna viji-runinga vidogo vipatavyo vinne au vitano hivi, na kiti kizuri cha kiofisi kikiwa nyuma ya ile meza. Hapo nilielewa kuwa yule mwanamke aliweza kuona kila kilichokuwa kikitendeka pale sebuleni kwake kupitia kwenye moja ya zile runinga, na ndio maana aliweza kuniona nikiwa pale sebuleni kabla mimi sijamuona.
Nilizungusha macho yangu mle ndani. Zaidi ya kuonesha matukio ya pale sebuleni, pia zile runinga zilikuwa nikionesha matukio mbali mbali yaliyokuwa yakitokea kule ndani ya ile kasino The Rickshaw, kwani niliweza kuiona ile steji waliyokuwa wakichezea michezo ya ajabu wale wanawake wawili muda mfupi uliopita, sasa hivi kukiwa kuna binti mmoja akitumbuiza kwa kuimba wimbo ambao sikuuelewa. Zile runinga nyingine zilikuwa zikionesha matukio ya aibu kabisa ya watu wakifanya ngono bila shaka ndani ya vile vyumba nilivyoviona kule ndani ya ile kasino. Yote haya niliyaona ndani ya mkupuo mmoja tu wa kuzungusha macho yangu mle ndani.
Lakini yote haya hayakunifanya nipigwe na butwaa kama jinsi nilivyopigwa na butwaa na kile nilichokiona pale juu ya kitanda.
Mimi ni mwanamke na ninajiamini sana kwa jinsi nilivyoumbika. Ninaamini kuwa Mwenyezi Mungu ameniumba mrembo wa kuvutia, nina shepu nzuri tu na ninajua kuwa huwa inawapagawisha wanaume ipasavyo.
Lakini huyu kiumbe aliyelala pale kitandani akinitazama huku akiwa ameshikilia sigara kwa pozi za hali ya juu kwa mkono wake mmoja alikuwa ni zaidi ya mrembo. Alikuwa amejilaza kitandani ilhali akiwa ameegemeza uzito wa mwili wake kwenye kiwiko cha mkono wake mmoja wakati ule mwingine ukiwa umeshikilia sigara, na alikuwa akinitazama huku mdomo wake ukiwa umefanya tabasamu dogo na akinitazama kwa macho ya kutegea, kama kwamba alijua fika kuwa nitababaishwa sana na urembo wake, naye alikuwa anataka kuona ni kwa kiasi gani nitakuwa nimebabaishwa.
Na sio siri, nilibabaishwa vilivyo. Na mimi ni mwanamke mwenzake...
Miguu yake mirefu ilikuwa imejazia kwa namna ambayo ningeweza kuamni kuwa labda huyu alipewa nafasi ya kujichagulia mwenyewe miguu yake iwe namna gani na Muumba, halafu naye hakufanya makosa katika hilo. Ngozi yake nyororo ilikuwa na rangi ya weusi ulioelekea kwenye kahawia na nywele zake ndefu zilikuwa nyeusi na za kuvutia. Macho yake sasa! Ama kwa hakika huyu mwanamke ameumbika na nilibaki nikimkodolea nisijue la kusema, huku akilini mwangu nikimkumbuka yule mwanamke niliyewahi kusikia tu simulizi za urembo wake hapo zamani, Cleopatra.
Mungu wangu! Huyu ni mtu au jini....?
“Nimeumbika eenh?” Yule mwanamke aliniuliza kwa maskhara huku akiinuka kutoka kitandani na kusimama mbele yangu na akinitazama kwa makini, mdomo wake ukifanya tabasamu dogo la kupendeza. Alikuwa amevaa nguo ndefu iliyotoka shingoni hadi chini kabisa miguuni mwake, na hapo niliona kuwa alikuwa amejaaliwa shepu ya ajabu. Makalio yake makubwa yalikuwa yamejikamata vizuri sana mwilini kwake na hips zake zilikuwa zimejizungusha kwa namna ya kuvutia haswa. Ile nguo aliyovaa ilikuwa imetengenezwa kwa kitambaa cha mfano wa chandarua, na chini ya nguo ile hakuwa amevaa kitu chochote! Hata pale nilipokuwa nimesimama, niliziona chuchu za matiti yake ya wastani ambayo nilijua wasichana wengi walikuwa wakitamani kuwa nayo.
“Sa...sam...mahani Anti, Shika...moo!” Nilijitahidi kusema kitu na kuishia kumpa shikamoo, kwani pamoja na urembo wake ule uliotukuka, yule mwanamke alikuwa na umri mkubwa kuliko mimi, na nilimhisi kuwa kati ya miaka thelathini na saba au na nane, lakini bado hajafikia miaka Arobaini. Na bado alikuwa na mvuto wa hali ya juu!
Yule mwanamke alicheka sana na hapo hapo alinisogelea na kunitazama mwili mzima huku akinizunguka. Alinikamata makalio yangu na kuyatomasa-tomasa nami nilijisogeza mbali naye huku nikiingiwa na woga mkubwa. Lakini yule mwanamke alizidi kunichumguza kwa makini na kunikamata matiti yangu nami nikalazimika kurudi nyuma huku nikijiziba matiti yangu.
“Anti vipi...?”
Alinitazama na kuvuta sigara yake kwa utulivu, kisha akanipulizia moshi mwingi usoni kabla ya kunijibu.
“Vipi kivipi mrembo? Kwani si umekuja kutafuta kazi? Nitakwambia neno moja tu kuwa na wewe si mbaya hata kidogo.Unafaa. Na hapa nikikutazama tu tayari nimeshaona wateja kama saba hivi ambao nikikupeleka kwao tutafanya biashara nzuri sana na wewe utanufaika...what’s your name (Jina lako nani?)” Yule mwanamke aliongea taratibu nami nikashikwa na kihoro.
“Kazi...?” Nilimuuliza, halafu hapo hapo nilielewa. Yule mwanamke alikuwa akidhani kuwa nimeenda pale kuomba kazi ya ukahaba. Je, yeye ndiye mtendaji wa TheBastard? Haraka sana nilidakia.”Oh,kazi...ndiyo lakini....” Mungu wangu nifanye kazi ya ukahaba mimi?
“Lakini nini? Hujiamini...? Usiwe na wasiwasi, hapa utatulia tu. Jina lako nani?”
“Ti...Nuru. Naitwa Nuru...lakini wewe ni nani? Nataka kuongea na muhusika mkuu. Mwenyewe hasa....” Nilimjibu huku nikiwa sina hakika iwapo huu mwelekeo niliochukua ulikuwa sahihi. Yule mwanamke aliangua kicheko kikubwa na kujibwaga kitandani. Alikuwa ana kicheko kizuri.
“Mnnh! Kwanza hilo jina si la kweli. Kwani kama lingekuwa la kweli usingesita. Labda jina lako ni Tina au Tindikali au kitu chochote kinachoanzia na Ti, lakini sio Nuru. Lakini hilo si tatizo, kwa sasa nitaenda na jina hilo hilo.” Aliniambia huku akitabasamu. Nilijiona mjinga sana, lakini sikuwa na ujanja.
“Sawa...lakini nataka kuonana na mwenyewe...yaani muhusika mkuu...”
“Mimi ndio mwenyewe. Mimi ndiyo muhusika mkuu na wala usiwe na wasi wasi wowote. Mimi ndiyo Kemirembe Wairema!” Alinijibu kwa utaratibu lakini kwa msisitizo, nami nikabaki nikimtazama nisijue niseme nini. Alinitazama kwa macho ya kuuliza.
“Hujawahi kunisikia?” Aliniuliza nami nikamjibu kwa kichwa kuwa sijawahi kumsikia.
“Basi mimi ndio Kemirembe Wairema a.k.a PCD...Principal ChanguDoa, Mkuu wa Machangu Doa jijini, a.k.a The Bastard...”
Nilihisi chumba kikididimia nami nikididimia pamoja nacho. Moyo ulinilipuka na akili ilinifa ganzi, nikahisi kama niko ndotoni. Yule mwanamke alikuwa akiendelea kuongea maneno mengine lakini inaelekea usikivu wangu ulikomea pale pale kwenye lile neno “The Bastard” alilolitamka na sikusikia chochote alikichosema baada ya neno lile.
“YOU ARE THE BASTARD....??” Nilibwata kumuuliza huku nikiwa nimemkodolea macho na nikimnyooshea kidole. Mambo yakiwa hayapangiki kabisa akilini mwangu. Sasa huyu mwanamke muongoza danguro ndani ya kasino hapa mjini atahusika vipi na mauaji ya kule msituni hata yule mtu aliyeuawa anisisitizie nimtafute kiasi kile?
This is too much!(Hii sasa imezidi!).
Yule mwanamke aliuona mshituko wangu juu ya lile neno ambalo yeye alijitambulisha kuwa ni jina lake na hapo akawa makini kuliko kawaida.
“The one and only pretty one(Ni mimi pekee mrembo). Ni nini hasa kilichokuleta hapa we’ binti, kwani naanza kuhisi kuwa ujio wako ni zaidi ya jinsi nilivyodhani mimi hapo mwanzo.” Alijibu kwa ukali na kuachana kabisa na maskhara. Na hata alipokunja sura kwa hasira yule mwanamke alizidi kuonekna mrembo.
“We..wewe...ndiye The Bastard...? Jina lako...unaitwa The Bastard...?” Nilimuuliza taratibu huku nikimkodolea macho. Akilini mwangu ilinijia ile taswira ya yule mtu aliyeuawa kule msituni niliyempachika jina la Mr.Q akinisisitizia kwa taabu kuwa nimtafute mtu aitwaye The Bastard...
“Watakuua...wacha nijaribu kukusaidia”
“I don’t care...you go find the bastard!”
Na hata sikumuelewa. Kwa wakati ule nilielewa alikuwa akimaanisha kitu tofauti kabisa. Mungu wangu...
Yule mwanamke alinitazama kwa muda mrefu, kisha alinijibu taratibu.
“Ndiyo. Mimi ndiye The Bastard... and what exactly brought you here?(...na ni nini hasa kilichokuleta hapa?)”
Oh, My God...! Oh, My God...
“MR. Q”
x.
S
ekunde kadhaa zilipita bila ya mimi kujua nifanye nini. Bila shaka miguu iliniishia nguvu, kwani nilipokuja kupata akili ya kuamua nifanye nini, nilikuwa nimeketi kwenye kile kitanda kikubwa nikimtazama yule mwanamke mzuri aliyejinadi kuwa yeye ni The Bastard. Na katika sekunde zile nilizokuwa kama nimepigwa bumbuwazi, yule mwanamke alikuwa amewahi kufunga mlango wa kile chumba naye akawa amenishikia bastola huku akiwa ameketi kwenye kile kiti chake kilichokuwa mbele ya ile meza iliyokuwa na runinga kadhaa huku akiwa amekunja nne.
“Wewe ni nani na unataka nini hapa?” Yule mwanamke aliniuliza tena alipoona kuwa nilikuwa nikimkodolea macho bila ya kusema neno. Nilimtazama na akilini yakanijia yale matukio ya kutisha ya kule msituni.Nilikumbuka matukio ya ndani ya ofisi ya mkuu wa wilaya kule Manyoni na hapo woga wangu ukawekwa pembeni na badala yake hasira kubwa ilinitawala.
“Nataka majibu...na nimekuwa nikikusaka kwa muda mrefu ili unipe majibu na maelezo...Bastard!” Nilimjibu kwa hasira huku nikilitilia mkazo lile neno “Bastard”. Yule mwanamke alinitazama kwa mshangao.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Majibu? Majibu ya nini? Maelezo juu ya nini? We’ mtoto mwehu? Yaani we’ umekuja kwenye anga zangu halafu unajitia jeuri? Kwa jinsi hali ilivyo ni kwamba wewe ndiye unayetakiwa kutoa maelezo na si mie!” Alinikemea kwa hasira, lakini bado sura yake haikupoteza ule urembo wake.
“Come on The Bastard, unajua ni nini ninachozungumzia. Nataka kujua ni nini kilichotokea kule msituni...” Nilimkemea huku nikionesha kukerwa kwa hali ya juu na majibu yake, lakini yule mwanamke alizidi kunishangaa.
“Mbona sikuelewi wewe mtoto? Kama una wazimu...na huelekei kuwa una wazimu... nitakuitia mabaunsa sasa hivi waje wakutupe nje. Lakini kama una sababu za msingi za kunijia humu ndani na kuanza kunisemea mambo nisiyoyaelewa, basi nakuomba uziseme hizo sababu haraka sana kabla sijachukua uamuzi mwingine. Mimi nina kazi za kufanya hapa...” Aliniambia kwa ukali.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment