Simulizi : Mkono Wa Shetani
Sehemu Ya Tano (5)
Jacob alijaribu kufikiria juu ya hao watu wawili lakini bila majibu.
Kutokana na maongezi yao, ilionekana wazi kuwa katika walinzi hao wote, hakuna aliyejua cha ziada katika yale aliyokuwa akiyatafuta. Hivyo hakuona sababu ya kubakiza mlinzi hata mmoja.
“Eeehe bwana hii mvua balaa maa….” Kabla huyu mlinzi hajamaliza kauli yake alikatizwa na sauti ya mluzi uliopigwa na Jacob.
Wote walikurupuka na kuanza kutoka nje. Risasi zilikuwa zikiwahesabu tu toka kwenye bastola mbili za Jacob. Kila aliyetokeza tu mlangoni alihesabiwa na risasi. Na kila aliyehesabiwa na risasi alienda chini akiwa marehemu.
Aliwafyeka wote. Alipoingia ndani ya banda hakuambulia chochote. Aliwakagua walinzi wote lakini pia hakuambulia chochote zaidi ya simu ya mkononi. Simu hii ilionekana kuwa ndio ya yule aliyekuwa kiongozi wao.
Wakati anamalizia kuiweka mfukoni ile simu, alipigwa teke na mtu aliyeonekana kutoka kwa juu. Kabla hajakaa sawa alipigwa ngumi ya mbavuni na mtu mwingine aliyekuwa nyuma yake. Hakuchelewa zaidi, aliruka na kuangukia upande mwingine wakati wakipiga mapigo mengine ambayo hata hivyo yalikutana na hewa. Kabla hajasimama aliwaona adui zake wakija kwa kasi pale alipokuwa ameangukia baada ya kujirusha. Mara moja akajua ndio wale waliozungumziwa na yule mlinzi ndani ya banda.
Kama kichomi, Jacob alibiringika na kumkumba mmoja. Akasimama haraka huku akiachilia pigo la kasi kwa kutumia kiwiko kwa yule aliyefika. Akazoa judo ambayo yule jamaa aliiona kwa urahisi na kuizuia. Jacob akajua huyu ni mchezaji mzuri.
Akanesa kidogo ili kulipisha pigo la kareti toka kwa jamaa aliyekuwa nyuma yake. Aliponesa yule aliyepiga alikosa stamina baada ya kukuta hewa, hivyo akapitiliza. Sasa wote wakawa upande mmoja anatazamana nao.
Kwa kasi ya radi, Jacob aliruka juu na kuachilia pigo la teke kwenye paji la uso wa mmojawao, kisha wakati mwili wake unaelekea chini Jacob akautumia kama ngazi ya kujigeuzia na kumpiga ngumi yule mwingine na wote wakaenda chini. Mmojawao alijiviringisha kwa ustadi mkubwa na kumkumba Jacob, akaanguka chini kabla pigo la yule mwingine halijampata, Jacob alijisogeza kwa kasi na pigo hilo likampata mwenzie ambaye naye alikuwa chini akijitahidi kuinuka. Pigo alilokwepa Jacob lilipompata yule jamaa mwingine lilimsababishia mauti. Hii ilionyesha kuwa jamaa aliyebaki alikuwa fundi wa kutosha.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hawa jamaa ni moja kati wa wale wapiganaji ambao Dr. Don alikuwa ameletewa na Mr. Peari. Walikuwa ni mafundi kweli. Sasa wakawa wamebaki wawili baada ya yule jamaa mmoja kuuawa na pigo la mwenzie. Yule jamaa alitoa ishara iliyoonyesha kuwa watumie judo tu. Kwa vile huko ndiko kulikuwa nyumbani kwa Jacob, hakuona shida. Hivyo wote wakawa tayari kupambana kwa staili ya judo. Wakati Jacob anajiandaa kuanza mashambulizi alishangaa kuona adui yake akianguka chini. Hakuchelewa, kwa staili ya sarakasi aliruka na kwenda kujibanza kwenye ukuta. Alipomwangalia yule jamaa damu zilikuwa zikimtoka kwenye paji la uso. Ilikuwa ni risasi. Jacob alifikiria ni nani angeweza kufanya kitendo hicho, mara moja ndipo akakumbuka kuwa hakuwa peke yake. Amanda. Akaanza kuangaza huku na huko. Mara eneo lote likajaa mwanga. Umeme ulikuwa amerudi baada ya kuwa umekatika kwa kipindi kirefu. Mara akamwona Amanda anakuja tokea upande wa kulia huku bastola zake mbili zikiwa mkononi. Ni yeye aliyempiga yule jamaa.
“Mbona unanikatili kiasi hicho?” Aliuliza Jacob huku akifutika bastola zake mifukoni.
“Mchezo niliouona unatosha. Sikupenda niendelee kuangalia zaidi maana sijalipia. Ila unatisha. Siku moja uje unifundishe hizo staili ulizokuwa ukitumia,” Amanda alisema, wote wakacheka.
Mvua bado ilikuwa inaendelea kunyesha. Tayari ilikuwa saa saba usiku. Baada ya kukagua maiti zote walianza kukagua jengo na kuangalia uwezekano wa kuingia ndani.
Wakati wakiwa katika zoezi hilo, wote walishitushwa na honi za gari nje ya lango kuu la kuingilia ndani ya majengo hayo ya Afri Afri Mich Co.Ltd. Ilionesha kuna mtu alikuwa anataka kuingia. Honi ilizidi kupigwa. Jacob alikimbia mpaka sehemu waliyokuwa wameficha maiti za wale walinzi, aliichukua maiti ya yule mlinzi. Aliyekuwa kiongozi na kuivua gwanda akalivaa. Baada ya muda mfupi tayari akawa getini kufungua lango.
Gari lilipoingia ndani Dr. Don ndiye aliyekuwa akiendesha.
Alipaki gari, baada ya kushuka alitembea mpaka ulipo mlango wa kuingilia ndani. Mlango ulikuwa umefungwa hivyo badala ya kuingia ndani akawa amesimama kama mtu anayesubiri kitu. Muda mfupi baadaye akageuka na kumwangalia Jacob kana kwamba kuna kitu alikuwa akihitaji toka kwake.
Jacob alijifanya kuhangaika na ufungaji wa geti wakati huo akifikiri nini Dr. Don alikuwa akihitaji. Alitambua kuwa kuna kitu Dr. Don alikuwa akihitaji au alitilia shaka. Kwa hiyo alikuwa amejiandaa tayari kwa lolote maana hakuelewa kama alikuwa ameshagundulika ama la.
Dr. Don alikuwa akisubiri mlinzi aje kufungua lango. Hakujua kuwa mlinzi huyo ni Jacob Matata. Wakati Jacob anamalizia kufunga geti mara akaja mlinzi mmoja aliyekuwa akikimbia kuelekea hapo alipokuwa ameinama, akajua mambo yameharibika. Huyu mlinzi alikuwa amebana wapi? Alijiuliza Jacob. Yule mlinzi alifika alipokuwapo Jacob. Aliinama kana kwamba anataka kumsaidia kufunga geti.
“Funguo za mlango wa ndani kwenye suruali yako,” sauti ya Amanda ilinong’ona. Jacob aliitambua sauti hiyo alijiinua na kuanza kutembea kuelekea ulipo mlango na ambapo Dr. Don alikuwa amesimama.
Wakati akitembea alikuwa akikagua mifuko yake. Alijua kuwa kwa vyovyote kwa vile sare alizochukua ndizo alizokuwa amevaa yule kiongozi wa wale walinzi hivyo funguo zingekuwa ndani ya moja ya mifuko ya suruali hiyo. Kofia aliyovaa ilimwezesha kuificha sura yake kwa macho ya Dr. Don. Hatimaye alizipata funguo kwenye moja ya mifuko ya suruali hizo. Alijiona mwenye bahati.
Kwa jinsi Jacob alivyokuwa akifanya mambo bila wasiwasi na kujiamini, Dr. Don alikuwa bado hajamgundua Jacob. Alifunguliwa mlango na kutokomea ndani. Alionekana kuwa mtu mwenye shida muhimu. Akili yake ilifahamu fika kuwa Jacob alikuwa maiti.
Baada ya kuingia ndani, Jacob alitembea mpaka alipokuwa amesimama Amanda. Amanda alikuwa amebadilika kabisa. Usingeweza kudhani ni msichana kutokana na zile sare za wale walinzi alizokuwa amevaa.
“Mimi nitaingia ndani ya buti ya gari la Dr. Don ila we’ ubaki hapa. Uwasiliane na kijana pale ofisini akuletee gari wakati huu huu ili iwe rahisi kunifuata nitakakokuwa nimefika na Dr. Don.” Jacob alimwambia Amanda ilhali akijiandaa kwenda lilipo gari.
“Hapana, ikitokea akataka kuongea na wewe akiamini ndiye kiongozi wa walinzi itakuwaje? Mimi nashauri niende mimi wewe utafanya taratibu zote huku nyuma,” alishauri Amanda.
“Sawa, haya twende uingie haraka, ila ukifika na kufanikiwa kutoka usifanye jambo lolote zaidi ya kupafahamu mahali anapoishi. Unipigie simu ili nikufuate,” alisema hayo huku tayari akiwa ameshafungua upande wa nyuma wa gari la Dr. Don.
Sehemu hiyo ilikuwa kubwa ya kuweza kutosha hata magunia mawili ya mkaa.
“Kila la heri!” Jacob alisema
“Na wewe pia!” Amanda alijibu.
Jacob alifunga buti na kuondoka.
* * *
Dr. Don alitoka, wakati huo mvua ilikuwa imeshakatika. Alipiga hatua kuelekea lilipo gari, Jacob alielekea getini ili kufungua.
Dr. Don hakuweza kuhisi jambo lolote. Alionekana kuzama kwenye mipango yake.
Geti lilifunguliwa, gari likatoka. Alilisikia likitokomea kusikojulikana. Jacob alifunga geti.
Alitumia muda huo kupiga simu gereji ambayo ilikuwa maalumu kwa shughuli za Ofisi Fukuzi. Ilikuwa ikifanya kazi saa ishirini na nne. Wengi waliijua kama gereji ya kawaida, lakini haikuwa hivyo. Magari mengi yaliyokuwa yakipaki pale yalimilikiwa na Ofisi Fukuzi.
“Tino, niko yalipo majengo ya Afri Afri Mich Co.Ltd, Mtaa wa Samora, lete gari, ulipaki nyumba ya pili toka hapa,” alisema Jacob huku akielekea ulipo mlango wa kuingilia ndani.
Kwa kutumia funguo zake malaya na zile alizozikuta kwenye mfuko wa suruali ya mlinzi, Jacob alikuwa amefanikiwa kuingia ndani.
Hakuambulia lolote katika vyumba vya ghorofa karibuni zote. Ila kilichompa wasiwasi ni ile ghorofa ya pili. Alipofika hapo alikutana na maandishi yaliyoonyesha kuwa ni eneo lililozuiwa kuingia mtu asiyehusika. Maandishi hayo ndiyo yalimfanya apate hamu zaidi ya kutaka kuingia. Lakini hakuweza! Hakuweza kwa vile hakuuona mlango wa kuingilia.
Ukiingia ndani ya ghorofa ya pili ndipo ilipokuwapo ile ofisi ya siri ya Dr. Don. Ilijengwa kitaalamu kiasi kwamba isingekuwa rahisi kwa mtu mwingine kuingia. Mlango wa kuingilia ulikuwa hauonekani. Ilihitaji mtu abonyeze namba fulani zilizokuwa kwenye kona moja ya ukuta karibu na main switch. Aliona umuhimu wa kuingia eneo hilo, ila ilihitaji muda. Muda wa kutafuta sehemu ya kufungulia. Kwa usiku huo aliona afanye jambo hilo kuwa kiporo. Alihitaji kujua Amanda alikuwa amefikia wapi katika safari yake na Dr. Don. Aliyaangalia maeneo hayo kwa makini kama mtu anayekariri kitu fulani.
Alipofika nje, mbele ya jengo hilo kabla ya kutoka lango la nje, alizichukua maiti za walinzi wengine na kuzirundika mbele ya jengo kisha za wale jamaa wawili akaziweka sehemu yake. Alipomaliza alivua magwanda na kubaki na nguo zake.
Akafungua lango kuu na kutoka nje kabla kulifunga nyuma yake. Kwa wakati huu alikuwa akisubiri simu toka kwa Amanda na wakati huohuo aletewe gari na Tino, kijana toka gereji. Kwa mbali kukawa na mwanga wa taa za gari. Tayari alikuwa amefika eneo ambalo gari lao liliteketezwa na shambulio la Dr. Don na vibaraka wake. Jacob akabana sehemu wakati magari mawili yaliyoongozana yaliposogea karibu na eneo hilo.
Gari la kwanza lilipita katika mwendo wa kawaida tu. La pili lilikuwa likiendeshwa taratibu sana. Lile lililokuwa mbele, lilisimama lilipofika umbali fulani hili la nyuma nalo likasimama hata kabla halijalifikia lile la mbele. Mara akashuka mtu toka ndani ya gari hili la nyuma. Jacob akamtambua huyo kuwa ni Tino, kijana toka gereji aliyemwagiza kuleta gari. Alitembea mpaka kwenye gari, wakati amefikia gari lililoachwa, gari lile la mbele lilikuwa ndio limeondoka baada ya Tino kuwa ameingia. Wakati anataka kuingia ndani ya gari ambalo alitambua kuwa ndilo aliloletewa, simu yake ya kiganjani iliita.
“Vipi salama?” aliuliza mara baada ya kusikia sauti ya Amanda.
“Salama tu, njoo Mbezi Beach eneo la Kitwana. Utanikuta Grocery moja inayoitwa Kigoma Ndiyo Kwetu,” Amanda alijibu.
“Nakuja sasa hivi,” Jacob alisema na kukata simu huku akiondoa gari kwa kasi.
Baada ya dakika kama kumi tu, tayari alikuwa amefika eneo aliloambiwa. Sasa akawa anatafuta Kigoma Ndiyo Kwetu Grocery, ambayo aliiona na kusimamisha gari pembeni.
“Ingia twende!” Jacob alisema baada ya Amanda kuwa amesimama kwenye dirisha la mlango wa mbele. Alifikaje Jacob hakujua , ila hakushngaa kwani alijua Amanda ni mtu wa namna gani.
“Anaishi mbali toka hapa?” Jacob aliuliza wakati akiondoa gari.
“Si mbali ni nyumba ya saba toka nyumba ile pale!”
“Ok, twende nyumbani tukabadilishe hizi nguo alafu ndipo turudi kumtembelea mwenyeji wetu Dr. Don,” alisema Jacob huku akiongeza mwendo wa gari. Tayari ilikuwa ni saa nane usiku.
*****
Ilipofika saa nane na nusu usiku simu ya kiganjani ya Dr. Don iliita. Mlio wake ulimshitua Dr. Don ambaye ndio kwanza alikuwa amepitiwa na usingizi.
“Hellow nani?” Dr. Don alipokea simu hiyo kwa swali lilionesha kukerwa na ujio wa simu muda kama huo.
“Shiit!! nakuja sasa hivi. Nitammaliza kwa mkono wangu mwenyewe wa!” Dr.Don alisonya kwa ghadhabu huku akiruka toka kitandani alipokuwa amelala.
Bastola mbili, visu vitatu, mkanda maalumu wa kupigania na video kamera ndogo mfano wa kiberiti ambayo aliiweka mbele ya kofia yake ni baadhi ya vitu alivyochukua. Haraka alifunga milango ya nyumba yake na kukimbia mpaka lilipokuwa gari. Aliingia ndani ya gari na kuling’oa hapo kwa mwendo wa gari liliyobeba mgonjwa mahututi. Alikuwa tayari kwa mapambano. Damu ilikuwa ikikimbia mwilini kwa kasi. Hasira iliyochanganyika na woga vilimfanya amchukie Jacob kwa ukomo wa chuki.
Wakati haya yanatokea kwa Dr. Don, Jacob Matata na Amanda walikuwa karibu kabisa na lango kuu la kuingilia nyumbani kwa Dr. Don. Walimwona vizuri wakati akitoka na kuliondoa gari kwa kasi ya ajabu. Wote walitabasamu baada ya kuona mbinu yao imefanikiwa. Jacob alicheka.
Kwa kutumia simu aliyoipora toka kwa yule mlinzi kule Afri Afri Mich Co.Ltd, Jacob alipiga simu iliyomchanganya Dr. Don. Alipiga simu hiyo akiwa hatua chache toka nyumbani kwa Dr. Don.
“Bosi tumevamiwa na wenzanagu wameuawa.” Ni maneno aliyoyasema Jacob na kukata simu. Maneno hayo yaliyomfanya Dr. Don akurupuke toka kitandani, aliamini kuwa simu hiyo ilipigwa na yule mlinzi aliyemwacha Afri Afri Mich Co.Ltd.
“Tumempata unasemaje? Mara nyingine wataiogopa nchi yetu na kutofanya ushenzi na ujinga kama huu huku wakijua wenye nchi tupo. Ndiyo atajua kuwa, mvaa viatu huvua,” alisema Jacob.
“Mambo yako yanatisha sana, kumbe yale yanayosemwa kuhusu wewe ni kweli,” Amanda alisema huku akionyesha kupagawa na mbinu za Jacob.
“Nataka tukamilishe kazi usiku huu kwa kutega hiki kifaa cha kunasia mazungumzo ndani ya nyumba hii,” Jacob alimwambia Amanda ambaye macho yake yalionesha kila dalili kuwa alikuwa amechoka sana.
Walitawanyika. Walipokutana tayari walikuwa ndani ya sebule ya Dr. Don. Jacob alitoa mkebe fulani ndani yake kulikuwa na vitu vingi kama vifungo na saa moja ya mkononi.
“Hivi vifungo tutaweka sehemu yoyote ambayo tunataka. Kwa kushirikiana na hii saa vinaweza kurekodi mazungumzo sehemu yoyote ambayo Dr. Don atakuwa na moja ya vifungo hivi,” Alisema Jacob huku akimkabidhi Amanda baadhi ya vifungo.
Alichukua viatu vyote vya Dr. Don na kuweka vile vifungo. Kila kiatu na kifungo. Kwa umakini sana alitoboa dari na kuweka ile saa. Walitega vile vifungo kwenye nguo zake lakini sehemu za nguo ambazo isingekuwa rahisi kwake kuvigundua.
Ndani ya dakika kumi na tano tu, tayari walikuwa wameshatega sehemu zote walizoona ni muhimu. Kabla hawajatoka walihakikisha wamefuta kila aina ya alama ambayo ingeonyesha kuwa humo ndani, mliwahi kuwa na mtu.
Jambo moja lililomshangaza Jacob ni jinsi Dr. Don alivyoishi. Hakuwa na mlinzi, mfanyakazi wa ndani, mbwa wala paka. Aliishi peke yake. Kama walivyoingia ndivyo walivyotoka, walikutana ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea nyumbani. Jacob alimpitisha Amanda kwake kisha yeye akaelekea nyumbani kwake. Kazi waliyoifanya iliwaridhisha.
* * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati Jacob na Amanda wanaelekea kujipumzisha, Dr.Don tayari alikuwa ameshafika ndani ya Afri Afri Mich Co.Ltd. ili kuitikia mwito alioamini kuwa ulikuwa umetolewa na mlinzi wake na sio Jacob kama ukweli ulivyo. Alipoangalia eneo hilo la Afri Afri Mich Co.Ltd. hakuhitaji maelezo ya kitaalamu kumwambia kuwa mtu aliyefanya kazi hiyo hakuwa mwingine kwa Tanzania hii zaidi ya Jacob Matata.
Kabla na baada ya kuingia hapo alikuwa tayari kwa kupambana. Lakini kadri dakika zilivyozidi kukatika jambo moja lilianza kumtatiza. Lililomtatiza ni nani apambane naye.
Maiti zilizokusanywa na Jacob? Hapana.
Apambane na jina la Jacob? Hapana.
Alishikilia bastola akaziweka, akachukua visu navyo akaviweka na kuchukua mkanda wake wa kupigania. Kila alichokishika aliona hakifai. Ndipo baadaye alipogundua kuwa tatizo si zana zake za kazi, bali ni kutoonekana kwa adui, Jacob.
“Jitokeze kama wewe mwanamume kweli mbona unajificha!” Maneno yalimtoka bila idhini yake alihisi ubongo wake umechemka, nusura kutoboa fuvu la kichwa chake kwa jambo ambalo hakulijua.
Dr. Don alijihisi ama kupiga karate, ama judo ama mchanganyiko. Hakuona sababu, akajihisi kucheka akashindwa, kulia akashindwa. Akili na roho yake vilijaa hisia za hatari. Aibu na hasira vilifanya makazi kwenye nafsi yake.
Alishusha pumzi ndefu kama mkimbiaji aliyemaliza mashindano ya mbio ndefu. Alihisi aibu kwa kazi iliyofanywa na Jacob. Kama sitampata basi sifai kuitwa mwanamume! Alijaribu kuuzuia ubongo wake usimpe sifa Jacob lakini akashindwa kwani uliachia kila sifa kwenda kwa Jacob.
“Hawa nao!” Alishindwa kujizuia kushangaa, pale alipowaona wale jamaa wawili ambao walipambana na Jacob kwa muda mrefu.
Sifa alizokuwa amepewa na Mr. Peari Robert juu ya watu hao ndizo zilizomfanya ashangae. Chika na Alonzi ni watu ambao kwa kipindi cha kujuana kwao, walikuwa wameshafanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kwenda nao katika matukio ya hatari zaidi. Hivyo, alikuwa anawatambua kama watu waolikuwa wamejaa sumu na kuwa wazoefu wa kushuhudia mauaji na maasi kadha wa kadha yakifanyika.
Hao walikuwa ni Chika na Alonzi. Ni miongoni mwa makomandoo waliotumwa na Mr. Peari Robert ili wamwongezee nguvu Dr.Don. Mwezi mmoja ulikuwa Chika na Alonzi wakiwa katika operesheni kule Congo DRC. Huko walikuwa wameenda kupora madini toka kundi moja la waasi wa Congo DRC. Katika zoezi hilo waliweza kupambana na jeshi la watu wapatao mia mbili na kufanikiwa kulitekeleza na kurudi na almasi ambazo ziliwaingizia pesa nyingi Dr. Don na Mr. Peari. Hisia za woga zilianza kumnyemelea, lakini akazitupilia mbali. Leo ameweza kwa muda mfupi kuwamaliza watu walioteketeza jeshi!
Hakuelewa ni namna gani Jacob aliweza kuponyoka katika shambulio la mabomu walipokuwa ndani ya gari.
Dakika tano zilizofuata alijikuta yupo ndani ya ofisi yake ya siri. Alifungua kabati alipokuwa amesheheneza noti. Noti za dola za Marekani alizoiba. Alipoziona moyo wake ukatulia. Hata hivyo jambo moja, usalama. Kweli zitatoka na kufika Marekani salama? Alifunga kabati na kukiendea kiti, akakaa. Huku mikono yake ikiwa imepakata kichwa chake, macho yake yalikuwa yametua ukutani, ilhali mawazo yake yakiwa maili nyingi toka hapo.
Ilikuwa ni mipango ya kusafirisha hayo maburungutu ya dola kuelekea Marekani. Siku aliyopanga kufanya hivyo ni Jumamosi. Hapa alipo ni usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa.
Saa kumi kamili alfajiri iligonga huku Dr. Don akiwa bado amezama katika kupanga hili na lile. Ujasiri na ushupavu zilikuwa ni moja ya sifa alizokuwa nazo Dr. Don. Pamoja na yote aliyoyafanya Jacob, lakini akili yake ilimwambia Jumamosi ndio siku muafaka ya kutorosha pesa.
Jacob amechachamaa, ulinzi ni mkali nchi nzima macho ya wapelelezi ni mengi. Lakini hapo ndipo watatambua kuwa mimi ndie Dr. Don jasusi niliyefuzu kazi yangu, aliwaza Dr. Don huku picha ya Jacob ikiwa haibanduki kichwani mwake.
Kiganja chake kilinyanyua mkono wa simu iliyokuwa juu ya meza. Aliweka sambamba na sikio lake.
“Chris nakuhitaji sasa hivi. Njoo pamoja na wenzio wote kuna kazi muhimu, yule mdudu Jacob amefanya uharibifu mwingine.”Dr. Don alinguruma na kukata simu.
Chris ni mmoja wa wale makomandoo waliotumwa na Mr. Peari kuja kumsaidia Dr. Don walikuwa watano, lakini sasa wamebakia watatu baada ya wale wawili kuuawa usiku huo hapo Afri Afri Mich Co.Ltd. na mkono wa Jacob. Baada ya dakika saba wote walikuwa wamekusanyika. Walikuwa kwenye moja ya vyumba vilivyopo jengo la chini la ghorofa hizi.
“Nimewaiteni kuwaelezeni kilichotokea,” Dr. Don alianza kuwaeleza.
“…..si walinzi tu waliouawa bali hata Chike na Alonzi wameuawa kwa mkono wa Jacob. Nadhani mnaweza kuona wenyewe ni jinsi gani huyu kiumbe asivyohitaji mzaha hata kidogo. Kwa vyovyote kwa vile ameshapafahamu hapa atahitaji kuja kupekua. Hivyo kama alivyowaangamiza Chike na Alonzi ndani ya jengo hili nataka naye aangamizwe pindi akitia pua yake hapa. Chris utaongoza doria kwenye jengo hili. Steve utamfuatilia Jacob popote alipo ili kummaliza. David utaenda kuwapokea wale wageni asubuhi. Hakikisha umetimiza mpango wetu. Wako watalii kumi, nafikiri habari zote unazo.
Lakini kabla ya kuanza harakati zetu, inabidi tuchukue hiyo ‘mizoga’ ya watu hapo chini na kuipeleka sehemu ambayo itaondoa hatia mikononi mwetu”.
Dr. Don aliamini kuwa kwa jinsi alivyopanga mambo lazima pesa zingeondoka siku ya Jumamosi. Pesa hizo zingewafanya wawe matajiri maisha yao yote mpaka kizazi chao cha nne. Akili yake ilimwambia, Hii ndio fainali. Mambo mawili lazima yafanyike. Pesa zisafirishwe na Jacob lazima auawe!
“Lazima nimuue! Na pia nibaki tajiri!”Dr.Don alijiapiza kimoyomoyo.
Dr. Don alihakikisha kila mpango unafanikiwa. Aliwagawa makomandoo wake watatu kama ifuatavyo. Chris alipangwa kuongoza doria jengo la Afri Afri Mich Co.Ltd. Steve alitakiwa kuhakikisha kuwa anajua nyendo za Jacob na kumpata. David alitakiwa kwenda kuwapokea wale wageni watalii toka Marekani. Akili ya Dr. Don ilishajua kuwa Jacob yuko karibu sana na yeye. Alitarajia jambo moja tu. Kuwahi! Alitambua katika sehemu iliyobaki ya mchezo huu, mshindi ni yule atakayewahi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Leo ikiwa ni Ijumaa, alitarajia kuwa kesho angezituma hizo pesa kwenda Marekani. Mipango yake ilikuwa tayari kwa zoezi hilo. Lakini ilitegemea ni namna gani wangefanikiwa kumdhibiti Jacob.
* * *
Alipoangalia saa yake ilimwonesha kuwa ilikuwa ni saa mbili kasorobo asubuhi. Jacob akatambua kuwa alikuwa amelala kwa takribani saa tatu tangu alipokuwa ametoka nyumbani kwa Dr. Don.
Alikurupuka haraka na kuanza maandalizi. Regina tayari alikuwa ameshaandaa kifungua kinywa. Baada ya kuoga na kupata kifungua kinywa aliliendea kabati na kuanza kuangalia nguo za kuvaa kwa siku hiyo. Siku hiyo ilikuwa na kila ishara ya shari kichwani mwa Jacob. Hivyo pamoja na nguo za kazi alichukua vifaa vingi vya kazi.
Saa nne na nusu ilimkuta Jacob akiwa ameegesha gari lake sehemu ya kuegeshea ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es salaam. Mikononi alikuwa na picha za wazungu wapatao kumi. Picha hizi ndio zile alizozichukua kwa yule meneja wa LIVE VIEW REAL AFRICA, kwa vile kati ya karatasi alizozipata ndani ya bahasha hiyo ilionesha kuwa wale watu wangefika leo na shirika la ndege la Ufaransa. Jacob aliona ni vyema afuatilie nyendo za watalii hao. Alihisi wanaweza kuwa na uhusiano na upotevu wa yale mamilioni ya dola.
Aliangaza macho yake huku na kule kama kuna mtu aliyemfahamu lakini hakuona. Ndege aliyokuwa akiitarajia ilifika saa tano na robo. Abiria waliokuwa ndani ya ndege walipoanza kushuka, Jacob alifanikiwa kuwaona hao watalii wakiwa wanashuka. Walipoteremka wote kumi na kufika sehemu ya kuonana na wenyeji wao, walinyanyua bango lililoandikwa LIVE VIEW REAL AFRICA. Hii ilimaanisha walihitaji mwenyeji wao aje kuwachukua. Mwenyeji wao ndio yule waliyemwandika kwenye bango yaani LIVE VIEW REAL AFRICA.
Macho ya Jacob yalisubiri kuona ni nani angekuja kuwapokea wazungu hao. Mara likaja gari moja. Lilikuwa ni basi dogo maarufu kama kipanya. Liliegeshwa walipokuwapo wazungu hao. Baada ya dereva aliyeendesha gari hilo kujitambulisha na kuonesha vitambulisho vyake, waliingia ndani ya gari. Mizigo yao iliwekwa sehemu ya kubebea mizigo juu ya gari. Alisubiri mpaka gari hilo lilipotoka kabisa kiwanjani hapo ndipo na yeye alipoanza kulifuatilia.
* * *
Kama ilivyokuwa imepangwa na Don, David ndiye aliyekuja kuwachukua wageni hao. Kwa maelekezo ya Dr. Don, David alitakiwa kutoa roho za watalii wote kumi. Alitakiwa kufanya hivyo kwa namna ambayo isingewaingiza mikononi mwa sheria. Njia hiyo ni ajali, hivyo David alitakiwa kupanga ajali ambayo ingewaacha wote walio ndani ya gari wakiwa maiti, huku yeye mwenye akitakiwa kuwa hai. Kwa mtu wa hivi hivi lingekuwa ni zoezi gumu lakini kwa mtu kama David hiyo haikuwa shida kwake.
Jacob alikuwa akilifuatilia gari lililokuwa likiendeshwa na David. Kwa jinsi alivyofuatilia haikuwa rahisi kugundua kuwa kuna mtu alikuwa akilifuatilia.
Tangu Steve alipopewa jukumu la kumfuatilia Jacob hakuchelewa kujua Jacob alikuwa wapi hivyo hata uwanja wa ndege walikuja pamoja naye. Steve alikuwa mjuzi katika kufuatilia nyendo za mtu. Alikuwa ameshatambua kuwa Jacob alikuwa amemfuatilia David na wale wazungu toka Marekani. Ili kutibua mambo, akaona ni heri ammalize kwa kulipua gari la Jacob, kabla Jacob hajajua David alikuwa anataka kufanya nini. Hivyo akawa anatafuta nafasi tu ya kufanya hivyo.
Kama ilivyoamriwa na Ofisi Fukuzi kuwa, Amanda asaidiane na Jacob katika kazi hii, ndivyo ilivyo mchana huu. Amanda hayuko mbali sana toka ilipokuwa gari ya Jacob. Amanda alishahisi kuwa kuna jambo ambalo Jacob anafuatilia. Hata hivyo, Amanda hakutaka kuonyesha kuwa wako wote bali alikuwa akimfuatilia Jacob kwa makini kabisa. Toka lilipokuwa gari la Jacob walikuwa wametenganishwa na magari manne. Ila gari lililokuwa mbele yake na ambalo aliweza kusoma sahani yake la namba ni gari la Steve, ambaye wakati huu alikuwa katika harakati ya kutafuta nafasi ya kummaliza Jacob.
Hamu ya Steve kutaka kummaliza Jacob ikaongezeka. Hivyo akatafuta namna ya kulipita gari la kwanza na la pili na kuacha gari moja tu likiwatenganisha yeye na Jacob.
Kitendo cha Steve kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake kwa namna ya kulazimisha kulimshitua Amanda hivyo na yeye akataka alipite gari lililokuwa mbele yake ili alikaribie gari la Steve. Lakini hakufanikiwa, kwa makini akawa analiangalia gari la Steve na Jacob.
Wakati Steve anainua mtambo wake wa kulipulia ndipo Amanda alipoamini kuwa Jacob yuko hatarini. Lakini kabla hajakata shauri afanye nini, aliona gari la Jacob likichepuka na kuacha barabara ya kuingia gereji iliyokuwa pembeni mwa barabara. Mara moja akatambua kuwa Jacob alitaka kubadilisha gari kwani hiyo ndiyo ile gereji inayomilikiwa na Ofisi Fukuzi.
Hapo Amanda akafurahi na ndipo akajua ni kwa nini Jacob amekuwa hawezekani na maadui zake. Anahisia tena hisia kali. Naye bila kusita akachepuka na kuingia hapo gereji. Wakati huo gari ya Steve na ile ya David zikazidi kwenda.
Kama alivyofikiri Amanda, Jacob alishuka haraka na kuchukua gari lingine. Aliwasha na kuingia barabarani. Amanda naye aliposhuka ndani ya gari alilokuwa nalo akaingia ndani ya gari aliloliacha Jacob naye pia akaingia barabarani. Mchezo ulikuwa unazidi kuwa mtamu.
Kutokana na uzoefu, Steve alijua Jacob aliamua kuacha barabara kwa lengo moja tu. Nalo ni ili kumpoteza kama kuna mtu alikuwa anamfuatilia. Alikuwa na hakika kuwa Jacob angerudi tena na kuendelea kulifuatilia gari la David na wale wazungu.
Wakati gari la Jacob linampita, Steve hakumtambua kwa vile Jacob alikuwa amebadilisha gari. Wakati gari aliloamini kuwa ndani yake alikuwamo Jacob lilipokuwa likipita, Steve hakutaka hata kuangalia ndani kwa kuogopa kumshitua. Amanda akatumia fursa hiyo kumwangalia Steve na kuishika sura yake. Amanda alimpita Steve makusudi maana alijua kinachoendelea.
Amanda alijua kuwa kitendo cha kuwa mbele ya gari la Steve ilimaanisha kulipuliwa. Kwani Steve bado aliamini kuwa Jacob ndiye aliyekuwa akiendesha lile gari ambalo wakati huu linaendeshwa na Amanda. Hivyo muda wote macho ya Amanda yalikuwa kwenye kioo cha kuangalizia nyuma ili kuona Steve alikuwa anafanya nini. Wakati huu alikuwa tayari ameshafungua mlango wa gari.
Wakati wanafika Barabara ya Kawawa kuingia Barabara ya Kilwa, Steve akaona ndio sehemu nzuri ya kummaliza Jacob. Hivyo akatwaa kifaa chake tayari kwa kazi hiyo.
Wakati Steve akijiandaa kufanya hivyo, David alishadhamiria kufanya kitu papohapo. Roho ya uuaji tayari ilishamjaa. Aligeuka na kuwaangalia wazungu aliowabeba. Macho yake yalionesha kama yaliyokuwa yakiwaaga. Aliongeza mwendo kwa ghafula na wakati huohuo akifungua mlango tayari kwa kuruka.
Jacob alishangaa namna lile gari lilivyoongeza mwendo kwa ghafla wakati huo huo kuna Scania kubwa lilikuwa likija tokea upande wa Barabara ya Mandela.
Jacob alishangaa mwendo wa gari hilo.
David akawa tayari kuruka.
Kidole cha Steve kikawa tayari kulipua. Amanda akawa tayari kuruka.
Mambo mawili yalitokea kwa wakati mmoja. Moja ni kitendo cha kugongwa gari lililokuwa limebeba wazungu kumi. Huku dereva wao akiruka kando ya barabara. Pili ni mlipuko wa gari moja dogo huku dereva wake akiwa ametua kando ya barabara baada ya kuruka.
Gari lililodhaniwa kuwa alikuwamo Jacob liliendelea kuteketea baada ya kushambuliwa na Steve. Hakuna aliyekufa kwani Amanda alifanikiwa kuruka sekunde chache kabla gari hilo kulipuka. Alitarajia na aliona wakati Steve akiwa tayari kushambulia.
Wazungu wote kumi walikuwa ni maiti ilhali David akiwa ni majeruhi pembeni mwa barabara. Alifanikiwa kuruka huku akiwaacha wale wazungu wakimaliziwa na Scania ndani ya kipanya.
Macho ya Steve yalifanikiwa kuona mambo mawili tu baada ya kushambulia gari la Amanda. Aliona gari hilo likiteketea kwa moto na wakati huohuo alimwona David akiwa ameangukia pembeni ya barabara. Kwa jinsi alivyotua chini, Steve alijua fika kuwa David atakuwa ameumia na angehitaji msaada. Kwa vile baada ya ajali hiyo magari yote eneo hilo yalikuwa yamesimama, Steve alishuka haraka sana kwenda pale alipotua David kabla watu hawajamwona. Akainama ili amuinue na kumpeleka lilipo gari lake. Lakini kabla hajafanikiwa kufanya hivyo, risasi tatu ziliondoa pumzi ndani ya kifua chake.
* * *
Pamoja na kuiona ajali yenyewe, lakini Jacob alifanikiwa pia kumwona David wakati akiruka. Alipogeuka nyuma kuangalia ule mlipuko mwingine macho yake yalimwona Amanda wakati ndio anatua chini. Alipoangalia gari lililolipuka akaona ndilo lile lake. Mara moja akajua mambo yameiva. Alishuka ili kumwendea David kwanza. Kabla hajafika alishangaa alipomwona Steve akiwa anataka kumwinua. Hapo ndipo akamshindilia zile risasi tatu.
Amanda alitua vizuri chini hakuumia kiasi cha kushindwa kusimama na kutembea. Hivyo aliinuka haraka na kuelekea lilipo gari la Jacob. Aliingia ndani haraka na wakati huo akamwona Jacob anahangaika kumbeba David huku mwili wa Steve ukiwa chini maiti baada ya kupokea risasi tatu toka bastola ya Jacob yenye kiwambo cha kuzuia sauti.
Jacob alifanikiwa kumbeba David ambaye wakati huo alionekana kupoteza fahamu. Alipomfikisha lilipokuwepo gari lake, alishangaa kuona mlango unafunguliwa na Amanda.
“Wewe nawe unatisha!” alisema Jacob huku wakisaidiana kumweka David viti vya nyuma. Jacob alichukua waya zilizokuwa nyuma ya gari na kutumia kumfunga David ili pindi akipata fahamu asije akawaletea kasheshe.
Mambo hayo yote yalikuwa yamefanyika ndani ya dakika mbili na ushei hivi. Kasi na akili ndivyo vilivyotumika sana, huku nguvu ikitumika ilipobidi.
Gari la Zimamoto, Polisi wa Usalama Barabarani na na lile la wagonjwa yalifika kwa nyakati tofauti ila zilizokaribiana sana.
Maiti za wale wazungu zilibebwa na kupelekwa hospitali.
Baada ya kutoka hapo Jacob na Amanda walienda moja kwa moja mpaka Ofisi Fukuzi. Kabla hawajashuka walijaribu kumwangalia David na kukuta bado yuko taabani ilhali damu zikimvuja vibaya. Jacob aliingia ofisini ambapo alikuwa na shida ya kuongea na mkurugenzi wa Ofisi Fukuzi, Bi. Anita. Pamoja na maongezi mengi yaliyofanywa baina yao, Jacob alimwomba Bi. Anita awaambie polisi kutoziwekea ulinzi zile maiti za wale watalii kumi. Wakati huohuo kutofuatilia kwa undani juu ya suala hili ili kumpa yeye nafasi ya kulifuatilia vizuri suala hilo. Bi. Anita alimuahidi Jacob kuwa ahesabu kuwa hilo limeshafanyika na pia akamtaka kuongeza juhudi kwani zilikuwa zimebaki siku mbili tu ambapo ‘Mkubwa’ angehitaji taarifa toka ofisi yao juu ya wizi wa pesa hizo.
* * *
Taarifa za kuuawa kwa wale watalii kumi zilimfikia Dr. Don. Lakini hakupata taarifa za kuuawa kwa makomandoo wake, David na Steve. Mara moja akajua kuwa David alifanikiwa kuwaua wale wazungu. Hilo alilihitaji na kwa hivyo akafurahi. Pia aliposikia gari la Jacob limeteketea kwa moto hapo pia akajua mambo yamekwisha. Jambo moja hakulijua na alitaka kulijua; David na Steve walikuwa wapi? Alinyanyua simu na kuanza kupiga kwa vijana na vibaraka wake mbalimbali ndani ya jiji. Lakini kila jibu lililokuja lilikuwa ni ‘sijui’. Hatimaye aliamua kupiga simu kwa Inspekta wa Polisi Juma Muya ili kuulizia kama ana taarifa za kupatikana kwa vijana wake. “Sijui!” Ndilo lilikuwa jibu la kwanza na kufuatiwa na ahadi kuwa yeye Inspekta Juma Muya angefuatilia na kumtaarifu kama angepata taarifa yoyote.
Polisi hawakuwa na moto wa kufuatilia matukio yaliyotokea. Hii ni baada ya kupokea taarifa toka kwa mkuu wa polisi ambaye aliombwa kufanya hivyo na Bi. Anita, Mkuu wa Ofisi Fukuzi Kitengo cha Idara ya Ujasusi.
Kazi moja tu ilikuwa mbele ya Dr. Don kuhakikisha anajua miili ya wale watalii imehifadhiwa sehemu gani katika Hospitali ya Muhimbili.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pili alihitaji kuwasiliana na Mr. Peari Robert, ili kama Shirika la JEPA la Marekani liliamua kuisafirisha ile miili ya wale watu basi washirikiane katika kufanya hivyo.
Mpaka inafika saa kumi na mbili jioni siku ya Ijumaa, Dr. Don alikuwa ameweka mambo sawa. Alishajua miili ya watalii ilipohifadhiwa. Pia baada ya majadiliano ya muda mrefu, hatimaye Ubalozi wa Marekani na serikali vilikubali kushirikiana na kampuni ya kitalii ya LIVE VIEW REAL AFRICA katika kuisafirisha miili hiyo siku ya Jumamosi. Dr. Don alipokea makubaliano hayo kwa furaha kubwa, cha kufurahisha zaidi ni kusikia kuwa HospNitali ya Muhimbili hapakuwa na polisi waliolinda miili ya watalii hao. Jambo lingine lililomshangaza ni jinsi Jeshi la Polisi lilivyokuwa kimya juu ya tukio hilo kwani alitarajia kampuni yake kusakamwa sana kwa tukio hilo. Lakini alipokumbuka kuwa Jacob ni marehemu hapo akajipa moyo kuwa ndio sababu, maana aliamini wengine hawakuwa na hata hisia juu yake. Hivyo akajua fika kuwa ameshinda vita kirahisi.
Jioni hiyo alipiga simu kumtaarifu Mr. Peari Robert kuwa ajiandae kupokea mamilioni ya dola toka Tanzania siku ya Jumatatu. Mr. Don alimwambia Mr. Peari kuwa pesa hizi zingeondoka Tanzania siku iliyofuata na kufika Marekani Jumatatu. Hakumweleza ni namna gani zitafika.
Ilipofika saa mbili usiku, ulinzi ndani ya eneo la Afri Afri Co Ltd ulikuwa si wa kawaida. Kila mlinzi alionekana makini kabisa na kazi yake. Hakuna aliyezungumza na mwenzie. Dr. Don alikuwa ndani ya ofisi yake ya siri katika ghorofa ya pili ya jengo hili la Afri Afri Co Ltd. Humo alikuwa akipanga maburungutu ya pesa katika mafungu na kuweka katika mifuko ya nailoni. Ilimchukua takribani saa moja na dakika kadhaa mpaka alipomaliza kuweka pesa hizo katika mafungu alivyotaka.
Saa nne usiku siku hiyo ya Ijumaa, Dr. Don aliangalia marundo ya dola hizo na kutabasamu. Alichukua bastola yake na kufutika kiunoni. Akachukua dawa za usingizi na kufutika kiunoni pia. Alichukua kila kitu alichohitaji na kuweka sehemu aliyofikiri ni sawa. Cha mwisho kuchukua ilikuwa ni kibali chake cha kuingilia Hospitali ya Muhimbili usiku huo.
Kama mkurugenzi wa kampuni ya LIVE VIEW REAL AFRICA, alikuwa na kibali maalumu cha kumwezesha kushughulikia miili ya wale watalii. Hii ingemwezesha katika kuhakikisha kuwa mpaka kesho asubuhi miili yote iwe tayari kwa safari ya Marekani kwa ndege maalumu. Alichukua yale maburungutu ya pesa na kuyajaza ndani ya viroba kama yalivyokuwa katika mafungu. Dola katika mafungu! Zilikuwa ni pesa nyingi ambazo kutoweka kwake ni kilio kwa taifa.
Wakati Dr. Don anataka kushika kitasa cha mlango ili kufungua, mambo mawili yalitokea. Alisikia mlio wa bastola na kisha simu yake iliita. Kwa uwezo alionao alijishughulisha na yote mawili. Huku akifikiri juu ya mlio wa bastola alipokea simu.
“Bosi tumevamiwa!” Ilikuwa ni sauti ya Chris ambaye alipewa jukumu la kuongoza ulinzi katika jengo hili.
“Waache vijana wapambane, wewe njoo huku ghorofa ya pili tutoe mizigo Fulani,” Dr. Don alisema kwa sauti ya utulivu huku akiviweka tayari vile viroba alivyokuwa amejaza noti za dola za Marekani. Alikuwa akimhitaji Chris ili amsaidie katika kuzibeba na kuzitoa nje.
Chini kabisa ya jengo hilo mapambano makali yalikuwa yakiendelea. Anga lote lilirindima kwa mlio wa silaha. Jacob alikuwa amebana nyuma ya mashine moja ya kuchanganyia zege, tokea hapo ndio alikuwa akiwahesabu adui kwa risasi. Amanda alikuwa juu ya ukuta wa ghorofa ya pili. Hapo alikuwa akitambaa na kuachia risasi kuelekea chini ambapo walinzi walikuwa wakikimbia ovyo.
Jacob ilibidi aje mahali hapo akiwa amejiandaa. Kilichomshitua Jacob mpaka kufikia uamuzi huo ni taarifa za makubaliano baina ya Ubalozi na Kampuni ya LIVE VIEW REAL AFRICA katika kusafirisha miili ya watalii. Ubalozi uliamini kuwa watalii hao waliuawa katika ajali ya kawaida. Lakini Jacob hakujua hivyo maana macho yake yaliyoona namna watu hao walivyouawa makusudi kwa ushirikiano wa Steve na David ambao wote sasa ni marehemu. Jacob akajua fika kuwa kuna mchezo ‘mchafu’ ulikuwa unaenda kuchezwa usiku huo. Hivyo wakajiandaa kwa operesheni ya kutisha usiku huo. Kabla ya kuja hapo, Jacob alimwambia Bi. Anita awataarifu Polisi kutoingilia mapigano yoyote yatakayotokea pale Afri Afri Co Ltd.
Jacob alikuwa ameweka vijana wa kufuatilia nyendo za Dr. Don nyumbani kwake. Lakini pia kwa kutumia vile vifungo na mashine alivyovitegesha nyumbani kwa Dr. Don aliweza kujua mipango mizima ya Dr. Don na mpaka wakati wanakuja alikuwa na hakika ya kumkuta Dr. Don mahali hapo. Sasa mapigano yalikuwa makali sana hapo Afri Afri Co Ltd. Vijana wengi wa Dr. Don walikuwa ni wajuzi wa kutumia silaha lakini mpaka robo saa inakatika tayari wengi wao walikuwa marehemu.
Wakati Jacob anammalizia mlinzi wa mwisho kwa risasi ya kisogo, ni wakati huo ambapo Dr. Don alikuwa akitoa kiroba cha mwisho na kukirusha upande wa pili wa ukuta wa kuzunguka jengo hilo. Chris alikuwa upande wa pili wa ua wa kuzunguka nyumba hiyo. Dr. Don alikuwa akitoa pesa ndani na kurusha mpaka upande wa nje wa ua unaozunguka jengo hilo, huko Chris alipokea na kukimbia mpaka walipokuwa wameegesha gari aina ya ‘Suzuki turbo’ za mizigo.
Kwa vile Amanda alikuwa kwa juu aliweza kuona wakati kile kiroba cha mwisho kinarushwa. Wakati anasimama ili kuangalia ni nini kilikuwa kinaendelea upande huo, alianguka chini. Dr. Don alimwona Amanda na akatambua kuwa amewaona hivyo alikuwa amemwahi kwa risasi.
Mlio wa risasi kule juu ulimgutua Jacob ambaye kama nyani aliparamia ukuta na kwa kutumia bomba la maji machafu aliweza kufika juu. Hakuchukua muda kumwona Amanda akiwa amelala chini na damu zikimtoka.
Weme.. wameondoka na. na mi… miz…go…. Sa.. pe…sa..” alisema Amanda kwa shida sana mara alipomwona Jacob na kumtambua. Jacob alimchukua Amanda na kumfunga mgongoni kisha akachukua waya wa simu akaukata. Akaufunga hapo juu na kwa kutumia waya huo akateremka mpaka chini huku Amanda akiwa taabani mgongoni mwake.
Alipofika nje alimpigia simu Tino, yule kijana wa gereji ili aje na magari mawili. Moja wamwachie na lingine watumie kumkimbiza Amanda hospitali. Jacob aliona labda wanaweza kuokoa maisha ya Amanda japo matumaini yalikuwa kidogo kwani risasi aliyopigwa ilitua karibu kabisa na sehemu ya moyo.
Dakika tatu baadaye Tino alifika na magari mawili. Moja alikuwa akiendesha mwenyewe na lingine aliendesha kijana mwingine. Walipokagua gari alilokuja nalo Jacob na Amanda hapo kabla walikuta matairi yote yakiwa yametobolewa.
Jacob alijua hakuwa na muda wa kupoteza. Baada ya kuwataarifu polisi juu ya maiti hapo Afri Afri Co Ltd alitia moto kuelekea kusikojulikana huku damu ikimchemka tayari kwa mapambano ya mwisho.
Wakati Jacob anamsubiri Tino amletee gari, ni wakati huo ambapo Dr. Don na Chris walikuwa nje ya lango la kuingilia Hospitali ya Muhimbili. Gari lao lilikuwa limepakia viroba na majeneza yaliyotengenezwa kisasa kabisa. Viroba hivyo vilikuwa vimesheheni noti za dola za Marekani. Majeneza yalikuwa ni kwa ajili ya kuhifadhia miili ya marehemu wale watalii kumi.
Baada ya kuonyesha kibali chake, Dr. Don na Chris waliruhusiwa kuingia ndani. Muda mfupi baadaye wakawa katika harakati za kuweka miili ya marehemu wale katika majeneza waliyokuwa nayo. Haikuwa kazi yao na si utaratibu wao kuhifadhi miili kwenye majeneza, lakini pesa inaweza kupindisha sheria yoyote ile.
Kazi hiyo iliwachukua takribani saa mbili hivi kukamilika. Si kwa sababu ilikuwa ngumu sana, ila kwa sababu kulikuwa na wafanyakazi wachache sana wa kuwasaidia. Hata hivyo wafanyakazi waliokuwapo hawakuruhusiwa kutoa msaada wao katika shughuli hiyo. Dr. Don aliwazuia. Kwa nini aliwazuia? Kwa sababu ya mambo ya siri aliyokuwa akiyafanya.
************
Kitendo cha kuiona asubuhi hii kilimaanisha jambo moja kwa Mkurugenzi wa Ofisi Fukuzi. Ilimaanisha kuwa zilikuwa zimebaki saa kadhaa ili akabidhi kazi kwa rais. Bi. Anita, Mkurugenzi wa Ofisi Fukuzi alijua muda wowote angepokea simu toka ofisi muhimu ya umma kwa rais, kumkumbusha kuwa siku iliyofuata angetakiwa kupeleka hatima ya sakata la wizi wa mamilioni ya dola katika Benki ya DE EURO LINKAGE.
Leo ikiwa ni siku ya Jumamosi, Bi. Anita tayari alikuwa ameshafika ofisini mapema sana. Alitamani kufanya jambo lakini hakuwa na uwezo kwani kazi yote ya sakata la wizi wa pesa aliikabidhi kwa mtu. Mtu mwenyewe ni Jacob Matata ambaye mpaka inagonga saa tatu asubuhi haikujulikana yuko wapi.
Taarifa za kupigwa kwa Amanda zilimchanganya sana Bi. Anita, lakini kilichomchanganya zaidi ni kitendo cha Jacob kutojulikana yuko wapi na wala kutopokea taarifa yoyote toka kwake. Leo ndio siku ambayo Jacob Matata alitakiwa kukabidhi hitimisho la kazi aliyopewa. Kesho Bi. Anita alitakiwa kuiwasilisha taarifa hiyo kwa rais wa nchi.
Eneo lote ndani ya Ofisi Fukuzi lilikuwa kimya kabisa. Hakuna aliyejua ni kasheshe gani ilikuwa imempata Jacob Matata. Wala hakuna aliyejua ni nini itakuwa hatima ya sakata la wizi wa mamilioni ya dola ambalo lilikuwa limedumu kwa takribani wiki nzima sasa. Kila sehemu alikuwa ameshatafutwa lakini hakuna aliyejua kuwa Jacob alikuwa wapi. Mtu wa mwisho kuulizwa alikuwa ni Regina mpenzi wa Jacob, lakini jibu lake lilikuwa ni ‘sijui’.
Saa nne kasoro dakika tatu ni wakati ambapo ngurumo ya simu ilisikika ofisini hapo. Kwanza wakati anaenda kuipokea simu hiyo Bi. Anita hakuwa na hakika ilitoka wapi.
“Unakumbuka pesa ziliibwa saa ngapi? sauti ya rais ilisikika upande wa pili.
“..Aah….tano na robo asubuhi,” Bi. Anita alijibu mara baada ya kuitambua sauti hiyo. Wakati anajibu mlango wa ofisi yake ulifunguliwa. Jacob Matata aliingia. Macho ya Bi. Anita hayakuweza kuficha furaha aliyokuwa nayo.
“Basi nahitaji uniletee taarifa na matokeo kesho muda kama huo ambao pesa hizi ziliibwa.”‘ rais alisema na kukata simu. Bi. Anita aliweka mkonga wa simu chini.
“Leta taarifa Jacob Matata,” Bi. Anita alimwambia Jacob, ambaye bado alikuwa amesimama.
“Aah mama kijana wako naweza kuanguka hivihivi, naomba unikaribishe walao kiti nikae kwanza ndipo uniulize mambo yako yote unayotaka,” alisema Jacob huku akiachilia tabasamu lililoashiria kuwa alikuwa amechoka sana.
“Acha utani Jacob, mambo ni magumu sana. Haya karibu kiti”.
“Asante!” Jacob aliitikia huku akiwa anakaa.
“Habari?” Bi Anita alisema huku akiwa na hamu ya kujua Jacob alikuwa na habari gani juu ya kazi aliyompa.
“Habari sio nzuri, kwani leo sijalala nyumbani, kwa hivyo Regina mpenzi wangu ameumia sana na baridi ya masika hii,” Jacob alisema huku akimwangalia Bi. Anita usoni.
Uso wa Bi. Anita ulibadilika ghafla na kuonesha hasira aliyokuwa nayo, macho yakang’aa zaidi na pua zikapanuka kwa hasira.
“Ninakuonya tena, acha utani, simu niliyopokea sasa hivi inatoka kwa rais, anataka ripoti kesho asubuhi hivyo nategemea unieleze ni nini kinachoendelea katika sakata hili,” Bi. Anita aling’aka.
“Mwambie aje achukue hata sasa hivi kama ana shida nayo sana. Tutamkabidhi mapesa yake na mijizi yake ili aamue kama ni kuyalamba risasi au .….”
Kabla Jacob hajamaliza, Bi. Anita alipiga meza kwa ngumi. “Shit Jacob, tangu lini mie nimekuwa mtani wako?” Bi. Anita alisema huku akisimama na kuanza kuzunguka chumbani humo. Jacob alijua ishara hii. Hii ilimaanisha kuwa Bi. Anita alikuwa amechukia ukomo na wakati wowote angeweza kumlamba risasi bila kujali.
“Nimekuja kukuchukua ili nikakuonyeshe kitu muhimu sana katika sakata hili. Ni imani yangu kuwa kwa sasa tutaongozana na kuelekea sehemu hiyo.”
Jacob alisema hayo huku akiwa anasimama tayari kwa kuondoka.
* * *
Gari aina ya Land Rover 110 lilikuwa limeegeshwa karibu na jengo moja katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa J.K.Nyerere zamani ukiitwa Uwanja wa Kimataifa wa Dar es salaam. Ilikuwa tayari imetimu saa nne na nusu asubuhi. Ndani ya gari hilo kulikuwa na watu saba. Bi. Anita ndiye aliyetimiza idadi hiyo ya watu saba huku waliobaki wakiwa ni vijana wake toka Ofisi Fukuzi. Jacob ndiye aliyeendesha gari mpaka hapo. Wenzie hawakuwa wakijua alikuwa na lengo gani.
“Bosi naomba uvute subira, muda mfupi ujao utajua ni kwa nini nimewaleta hapa,” Jacob alisema baada ya kutambua kuwa wenzie walikuwa wamepigwa bumbuwazi.
Dakika nne baadaye mlio ulioashiria kuwa kuna gari la wagonjwa lilikuwa linakuja ulisikika kiwanjani hapo. Magari matano ya kubeba wagonjwa maarufu kama ‘ambulance’ yaliingia kiwanjani na kufuatiwa na magari mengine matatu. Magari yote katika msafara huo hayakupata kizuizi chochote kuingia sehemu zilipokuwa zimeegesha ndege.
“Kazi imeiva, hapa inahitajika akili. Bosi utakaa pembeni kuangalia ila ukiona tumezidiwa itabidi uingilie kati. Wengine nadhani mmeliona lile gari pale nyuma. Ndani ya lile gari watashuka watu wawili, mmoja ni mzungu na mwingine ni ngozi nyeusi kama sisi. Watu hao ni makomandoo kamili. Inatakiwa asiuawe hata mmoja. Hata hivyo si rahisi kuwapata bila kuwajeruhi. Hivyo ni ruksa kuwajeruhi ila si ruhusa kuwaua,” Jacob alisema huku akitoa bastola zake mbili. Zote zikiwa ni automatic. Wenzake pia hawakuwa na hiari iliwalazimu kushikilia zana zao za kazi.
“Enoce na Jeff mtaenda mpaka upande ule wa ndege ile. Hillary na Agness mtaenda upande ule, mimi na Toni tutaenda usawa huu. Tusiwape nafasi wakishuka tu nitanyanyua mkono na hapo wote tutaanza mashambulizi; tuhakikishe tumewapata hao wawili kwanza kisha mambo mengine yatakuwa safi,” Jacob aliwaagiza na kuwapanga wenzie ambao walishuka toka ndani ya gari.
Muda wote huo Bi. Anita mkuu wa Kitengo cha Ofisi Fukuzi alikuwa kimya kabisa akisikiliza yaliyokuwa yakisemwa na Jacob. Hakuwa anajua Jacob alikuwa na lengo gani, lakini aliamini kuwa kuna jambo muhimu ambalo Jacob alitaka kumwonesha.
“Bosi naomba umtaarifu mkuu wa Polisi, ili askari wengine wa kawaida wasiingilie mapigano haya, maana kuingilia kwao kutarahisisha kazi ya maadui wetu. Mapambano yakiisha tu naomba uje pale yaliposimama yale magari,” Jacob alisema huku akiteremka toka ndani ya gari wenzie tayari walikuwa wameshatawanyika.
Macho ya wapelelezi wote sita wakiongozwa na Jacob yalikuwa yakiangalia gari moja tu. Ukiondoa magari ya ambulance ambayo yalikuwa matano, kulikuwa na magari mengine matatu katika msafara huo. Moja lilimbeba balozi wa nchi moja ya Ulaya chini. lingine lilikuwa limembeba Ofisa wa Ushirikiano wa Kimataifa. La tatu ndio hilo ambalo macho ya wapelelezi wote sita yalikuwa yakiliangalia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Magari yote yalikuwa yamesimama karibu na ndege moja iliyokuwa na alama ya Bendera ya Marekani. Ndege hiyo ilikuwa ndogo tu.
Baada ya milango ya ambulance zote kufunguliwa, majeneza yaliyokuwa na maiti za watalii yalianza kutolewa. Kila gari lilikuwa na majeneza mawili. Majeneza hayo yalikuwa makubwa sana tofauti na yale mengine yaliyozoeleka. Sababu hasa ya ukubwa huo haikujulikana, majeneza hayo ndio yale yaliyokuwa yametengenezwa na Dr. Don.
Gari la tatu milango yake ilifunguliwa. Jacob na wenzie wote walikuwa makini kabisa. Wa kwanza kushuka toka ndani ya gari hilo ambalo watu sita walikuwa wakiliangalia kwa makini alikuwa ni Chris. Huyu ndiye yule komandoo aliyekuwa amepewa jukumu la kuongoza ulinzi katika jengo la Afri Afri Co Ltd. Baada ya kushuka, Chris aliangaza huku na huko kiwanjani hapo. Bila shaka alikuwa anahakikisha kama kulikuwa na noma yoyote. Baada ya kuridhika na ukaguzi wake alitembea taratibu kuelekea ilipokuwa ndege.
Baada ya kama dakika mbili hivi mlango wa lile gari alilokuwa ameshuka Chris ulifunguliwa. Dr. Don alishuka. Alisimama hivi akiangalia huku na huko. Naam, tofauti na Chris yeye aliona kitu! Lakini kabla haja............
MWISHO
0 comments:
Post a Comment