Search This Blog

Thursday 27 October 2022

ANGA LA WASHENZI (2) - 2

 











    Simulizi : Anga La Washenzi (2)

    Sehemu Ya Pili (2)





    "Kwanini haukunambia siku zote hizo Sasha?" Sarah aliuliza akimtazama dada yake kwa macho ya ndita.



    "Niliogopa," Sasha akajibu. "Ningeanzia wapi na wewe tayari umebeba mimba yao??"



    Sarah akabaki njia panda. Hakuwa na neno la kusema. Sasha akamshika bega na kumuuliza:



    "Utanisaidia?"



    "Hapana!!" Sarah akajibu akisimama. "Nitawezaje kufanikisha hilo?? Mwanangu atatolea wapi baba mwingine kama ikatokea Kinoo akafa??"



    "Ssshhhhh!" Sasha akaweka kidole mdomoni. "Punguza sauti yako, tutasikika!"



    Akatazama dirishani kisha akarudisha macho yake kwa Sarah.



    "Sijasema tumuue yeyote yule, Sarah!"



    "Sasa unadhani hizo taarifa utakazokuwa unapeleka huko zitaishia kwenye nini?" Sarah akamkatiza.



    Hakutaka kumwelewa dada yake hata kidogo. Alitoka zake ndani ya nyumba pasipo kuaga akamwacha Sasha akiwa ameduwaa.



    Akang'ata meno na kukunja ngumi kwanguvu. Mpango wake ulikuwa umefeli!!



    Sasa atafanyaje?? Kichwa chake kilikuwa moto. Hakuna mtu yeyote anayetakiwa kujua siri hiyo ila tayari ashamweleza dada yake.



    Hapa akapata shaka kubwa. Hakuamini kama Sarah atautunza mdomo wake asiseme kitu. Kama tu akiufungua mdomo wake basi kazi itakuwa imekwisha!!



    "Damu nzito kuliko maji," alijipa moyo. Ila kama mambo yasipoenda kama inavyotakiwa, basi hamna budi.



    Hamna budi.



    Itabidi amtoe sadaka dada yake!!



    Aliwaza.



    **



    Usiku mzito, ndani ya chumba chenye giza ...



    Waaaaa!! Jona alimwagiwa maji ya baridi na kuamriwa aamke upesi. Hakujua hapo alipo amefikaje. Alijaribu kufungua macho yake kutazama lakini hakuwa anaona kitu.



    Si tu kwamba kulikuwa ni giza, hakuwa na uwezo wa kuona kabisa mbali na kutokuwa miwani. Hata masikio yake yalikuwa yamepoteza uwezo wake wa kawaida. Pia ngozi yake yake, ilikuwa hafifu kwenye kuhisi.



    Lakini ajabu alipomwagiwa maji hayo ya baridi, alilia kwa maumivu makali ambayo hajawahi kuyapata!!



    Ni kama vile maji hayo yalikuwa na visu ama viwembe. Yalimfanya ang'ate meno kwa ukali wa maumivu yaliyopitiliza. Alihisi amechanjwa chanjwa kila sehemu ya mwili wake iliyoonja maji hayo ya baridi.



    Alihisi maji hayo yameingia mifupani. Yanamtafuna!!



    Japo alikuwa dhaifu, akatapatapa kujinasua. Akahangaika huku na kule lakini hakuweza kufua dafu kwenye kamba ngumu alizokabwa nazo kitini.



    Lakini kama haitoshi, ndani ya chumba hicho kulikuwa na ndoo tatu za maji baridi kabisa. Zote zilikuwa zinamgojea yeye.



    Zinamngoja akileta ukaidi.



    "Mzee, hatuna muda wa kupoteza hapa na wewe. Tunataka kitu kimoja tu. Kiri na sisi tutaenda zetu. Ukileta ujuaji, tutasema na wewe usiku huu mzima."



    Jona alisikia sauti hiyo kwa mbali mno. Hakumjua anayemwongelesha ni nani. Alikuwa amekunja shingo yake kana kwamba kaelemewa na kichwa.



    "Sisemi kitu," akasema kwa kunong'oneza. Mtesi wake akatabasamu kuonekana meno kizani.



    Baada ya hapo Jona akamwagiwa ndoo mbili za maji baridi. Maji haya si kwamba yalimfanya asikie baridi, ila mchanganyiko wake na virusi vilivyomo mwilini mwa Jona, ulizalisha maumivu makali yasiyomithilika!!



    Haikupita muda mrefu, Jona akazima.



    Simu ikapigwa.



    "Hatujafanikiwa, mkuu."



    "Sawasawa," sauti ikatoka simuni. Sauti nzito ya Kamanda mkuu ikiashiria kutoka usingizini. Mwanaume huyo alisafisha koo lake kisha akasema:



    "Sasa tuhamie kwenye njia ya mwisho. Kesho hakikisha mnamteka yule kijana anayemletea chakula kisha mumpatie machaguzi mawili, aidha tumuue huyo kijana ama afanye tunachokitaka."



    **



    Kesho yake, asubuhi ya saa mbili ...



    "Kila kitu kipo tayari," alisema Miranda akimtazama Kinoo kwa jicho la kazi. Kinoo akabinua mdomo wake na kutengua vidole.



    "Basi na kazi itendeke!" Akasema kwa kujiamini akinyanyuka.



    "Hakikisha hakuna kosa hata moja linafanyika," Miranda alisisitiza. "Hii ni kazi ya kufa ama kupona. Kama tukiharibu basi tumetia mchanga kwenye wali wa kula mwaka mzima."



    "Usikonde, bibie," Kinoo akamtoa shaka. "Kila jambo litaenda kama lilivyopangwa. Lakini usisahau ahadi yangu."



    Miranda hakusema kitu, akachomoa simu yake na kupiga. Punde akasema:



    "Nikukute hapo hapo." Alafu akakata simu na kusimama.



    **



    "Bila shaka unakumbuka maelezo?"



    "Ndio."





    Miranda akamshika Marwa mkono wake wa kuume.



    "Hakikisha unafanikiwa," akamsihi. "Hatuna nafasi ya kufanya kosa lolote leo. Aidha kama tunataka kupoteza yote.



    Marwa akatikisa kichwa.



    "Ntajitahidi kadiri ya uwezo wangu."



    Miranda akatabasamu, kisha akanyanyuka na kwendaze.



    **



    Kwenye majira ya saa kumi jioni ...



    Baada ya mlio wa gari huko nje, mara Marwa anafungua geti na kuzama ndani. Mkononi amebebelea hotpot ya chakula. Mwendo wake ni wa ukakamavu na usoni hakuonyesha shaka.



    Ni katika kituo hiki cha kati. Watu walikuwa kadhaa wakiwa wamesimama huku na kule aidha wakingojea watu wao watoke nje ama wakingoja kuingia ndani.



    Kwa haraka haraka Marwa akatazama mazingira hayo alafu akazama ndani. Hakumkuta afande Devi wala koplo Massawe. Alimkuta hapo afande fulani wanne waki wapo bize na kazi za hapa na pale.



    Akaeleza dhumuni lake kumwona Jona na kumpatia chakula. Afande wale wakatazamana kisha mmoja akamwambia haitawezekana.



    "Kwanini?" Marwa akauliza. Afande wale hawakumpa sababu, wakamwambia tu haiwezekani. Kwa ufupi.



    Basi Marwa akatoka zake hapo kaunta na kuelekea kantini akiwaza ni kwa namna gani atafanya. Kwa muda wote aliokuwa pale kaunta roho ilikuwa inamdunda haswa.



    Alikuwa ana kauoga ndani yake. Kama wale polisi wangemtazama vema wangelibaini hilo na huenda wakamtia mashakani.



    Alivuta kiti akaketi. Akachojoa simu yake na kumtumia ujumbe Miranda kumweleza hali iliyopo. Punde Miranda akampigia.



    "Do it," sauti ya kike ilisihi. "You must do it, Marwa. Alafu utatuhabarisha."



    Kabla Marwa hajajieleza sana, mara simu ikakata. Marwa akashusha pumzi ndefu. Moyo ulikuwa unamwenda mbio.



    Jasho kwa mbali lilianza kutambaa usoni mwake.



    "Samahani, naweza nikakusaidia?" Sauti ya mhudumu ilimgutua mawazoni.



    "Naomba maji makubwa," akaagiza na kuendelea kutafakari. Kama bahati akamwona afande Devi. Hapa angalau akajikuta anapata ahueni. Lakini haikutakiwa Devi amwone pale kantini!!



    Kama Devi angelimwona pale kantini basi afande huyo angeishia kuchukua hotpot na kumtaka aende, yeye atasimamia zoezi.



    Hivyo, haraka akanyanyuka na kujificha. Afande Devi hakuketi hapo kantini akateka soda na kulipa kisha akayeya eneo ambalo Marwa aliamini itakuwa ni kule kaunta.



    "Pesa yako hii hapa," alisema Marwa pasipo kumtazama mhudumu. Macho yake yalikuwa yanatazama njia asiwaze hata kama kuna chenji anatakiwa kungoja.



    "Chenji!"



    "Kaa nayo tu," akasema akiondokaze.



    Aliwasili kaunta na kama alivyowaza, afande Devi akawa tayari amejaa pale. Kabla hajamsalimu, mmoja wa wale afande waliomfukuza hapo awali akamtazama na kumfokea:



    "Haukuerewa enh? ... nitakutia sero sasa hivi ukamkute mwenzako huko!!"



    Marwa hakujibu. Alimtazama afande Devi kwa macho ya mhitaji, afande huyo akaingilia kati.



    "Chacha," Devi akaita. "Jamaa 'angu huyu bana."



    Basi Marwa akacheza karata dume hapa hapa. Haraka akafunua chakula chake alichokiweka pale kaunta na kuzuga analalama kuwa chakula ki safi. Hamna tatizo lolote na hata akitakiwa kuonja atafanya hivyo.



    "Huna haja hiyo, ndugu yangu," Afande Devi akamtoa shaka akimwekea mkono begani. "Its ok. Funha tu chakula chako."



    "Hapana!" Akasema Marwa akitikisa kichwa. "Labda ana hofu na hiki chakula. Tazama afande ... nipo hapa kumsaidia tu rafiki yangu."



    Marwa akaigiza mpaka pale alipoona muda ni sahihi kwake kufunga hotpot, zoezi lake la kwanza likawa limefanikiwa. Lakini la pili, kwenda kumpelekea Jona chakula. Kidogo ikawa tabu.



    "Wewe liache tu hapa. Nitalipeleka," alisema Afande Devi akivuta hotpot.



    "Lakini afande, tafadhali naomba ulipeleke saa hii. Najua hajala tangu jana na hata leo nikakawia kuleta chakula. Atakuwa naa njaa sana."



    "Ooh! Sawa," Afande akatikisa kichwa. "Nitafanya hivyo."



    Marwa akaenda zake. Akatoa simu yake mfukoni na kutua ujumbe kwa Miranda.



    'ABC'



    Akimaaanisha mambo matatu yamekwishafanyika. Alipoletea ujumbe wa 'delivery report' akaweka simu mfukoni na kwenda kukaa mbali kidogo na kituo lakini eneo alilohakikisha anapata hewa ya kutosha kwani ni kama alianza kuhisi kichwa kimeanza kuwa kizito.





    **



    Wiu!-Wiu!-Wiu!-Wiu!-Wiu!!



    Ilikuwa sauti kali ya king'ora.



    Mara gari la wagonjwa lililokuwa katika kasi kubwa liliingia ndani ya eneo la kituo na mara wakashuka watu wawili waliovalia sare za kiuguzi. Wakashusha machela harakaharaka na mmoja wao akazama ndani!



    Punde wakatoka na Jona na akiwa amebebwa. Na wasiwe na haraka sana, yule muuguzi aliyebakia nje akaweka sikio lake kifuani. Akachopeka dripu na kumwingiza Jona ndani.



    Alafu kukatisha utepe, muuguzi yule awali akarudi tena ndani na kumtoa afande Devi. Hakuonekana kama mtu anayejielewa. Alikuwa anarembua akikokotwa. Mkono wake wa kuume ulikuwa shingoni mwa muuguzi.



    Naye wakamzamisha ndani na kisha gari likahepa!!



    Hata wale maafande waliokuwepo mlangoni wakiwa wamebaki na butwaa.



    **



    "Habari zilizotufikia hivi punde!" mwanamke mrembo nyuma ya kioo cha televisheni alinguruma kwa sauti yake ya kuvutia watazamaji na wasikilizaji.



    Alikuwa amevalia suti rangi ya damu ya mzee. Na kwa namna alivyokuwa amependeza, ungeliweza kupuuza habari anayoitangaza na badala yake ukamtazama yeye.



    Lakini kwa ukubwa wa habari hii, hakuna ambaye angeweza kudiriki kufanya hivyo. Habari hii iliyowafikia hivi punde ilikuwa ni ya moto!!



    Ya kustaajabisha na kuvuta watu wasonge karibu na vyombo vyao vya habari.



    "Mtuhumiwa nambari moja wa mauaji ya aliyekuwa mkuu wa polisi mkoa, ametoroshwa kituoni na watu wasiojulikana ... watu hao wakiwa wamefika hapo kwa kutumia gari la wagonjwa, walifanikiwa kuondoka na mtuhumiwa huyo pia na polisi mmoja ambapo mpaka sasa haijajulikana wamepelekwa wapi ... tukutane saa mbili usiku kwa habari zaidi."



    Taarifa hiyo ikazua gumzo kubwa haswa jijini. Watu wakapigwa na bumbuwazi na kwa namna wahalifu walivyowazidi akili polisi mpaka kufanikiwa kukwapua mtu tena kituo kikuu!



    Watu waliosikia habari hiyo wakiwa ndani ya madaladala wakapata mada ya kusogezea muda angalau kuwasahaulisha foleni ya kukera nyakati kama hizi.



    Na wale wa mitandaoni wakazisambaza upesi. Si katika namna ya kusikitika bali kushangazwa!!



    **



    "Kamanda siwezi nikakuelewa hata kidogo!" Alifoka Sheng kana kwamba anaongea na mtoto wake. Na kadiri akiwa na hasira basi lafudhi yake ya ki-mandarin inafanya asieleweke kabisa nini anaongea.



    Kila mara Kamanda akawa anamuuliza simuni ni nini anaongea.



    "Ametorokajhe??" Sheng alitoa macho akibamiza meza.



    "No! No! No! I can't understand!"



    Uso wake ulikuwa mwekundu. Jasho jembamba lilikuwa linakatika kwenye paji lake la uso.



    Akatoa agizo:



    "Namtaka! ... I want him kabla siku ya kesho haijakwisha. La sivyo ..." akakata simu na kuibamizia mezani.



    Kutazama mlangoni alikuwa amesimama mdada mchanga wa kichina ndani ya sare, sketi nyeusi na form six nyeupe, akiwa amebebelea trey yenye chupa kubwa ya mvinyo na glasi yake.



    Mdada huyo alikuwa amesimama kwa hofu akimtazama Sheng kwa mashaka. Bila shaka alishaona mambo yametibuka.



    Sheng, kwa hasira, akavuta droo na kutoa bunduki yake ndogo. Pasipo kujiuliza mara mbili, akamtwanga risasi tatu mwanadada huyo, akafa papo hapo!!



    Mwanadada ambaye hakuwa na hatia bali akitimiza tu kazi yake.



    Punde wakaingia wanaume wawili na pasipo kuuliza wakanyanyua maiti na kuipeleka inapotakiwa kuwapo.



    Sheng akabaki akizunguka kitini kwake akiwa na mawazo makali sana. Hakujua namna ya kufanya. Alihisi kichwa chake kimeganda. Amechanganyikiwa. Hakupata cha kufanya japo aliwaza sana.



    Mwishowe akaamua kunyanyua simu na kupiga. Simu ikaita mara mbili kabla ya kupokelewa. Akasemakwa ufupi, nakuhitaji ofisini na punde muda usiende sana hapo ofisini akaingia mwanaume mmoja mwenye asili ya China.



    Alisalimu na kuketi. Mwanaume huyu alikuwa ndiye yule waliyejadiliana na Sheng kipindi kile mpaka kufikia kumpelekea pesa Kamanda mkuu hotelini.



    Alikuwa amevalia suti yake nyeusi. Imemkaa vema japo hakupendeza. Alikaa kitini kwa muda kidogo kabla Sheng hajamwongelesha.



    Kwa muda wote huo Sheng bado alikuwa anawaza tu lakini kitu kisichoeleweka. Unajua namna mtoto mchanga aandikavyo karatasini?? Ndivyo Sheng alivyokuwa anahisi kichwani.



    Yaani vuruguvurugu tupu!



    Baada ya muda kidogo, akanyanyuka na kuendea jokofu. Akatoa maji madogo na kuyanyonya kama ndama afanyavyo ziwa la mamaye. Si kwamba alikuwa anahisi kiu kali, hapana. Alitaka angalau kifua chake kipoe.



    Kwani la sivyo angeweza hata kuchojoa bunduki kwenye droo na kumtwanga mtu aliyemuita mwenyewe hapo.



    Alipokunywa na kumaliza maji hayo, angalau kwa mbali akapata ahueni. Akamweleza yule jamaa, jinale Shao, juu ya kikichotokea. Na hakika hata Shao akapigwa na bumbuwazi zito!



    Ila akatafuta namna ya kukabiiana nalo apate kumshauri mkuu wake ambaye alikuwa amekwama. Kwanza akamtoa hofu juu ya Jona.



    "Women huì dédào ta!" (Tutampata!) Akasema kwa kujiamini.



    "Rúguo women bù yuànyì dehuà, ta huì si de!" (Na kama tusipofanikiwa basi atajifia)

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa minajili kwamba virusi waliomuingizia mwili hawatadumu naye kwa muda mrefu. Kadiri anavyokaa navyo ndivyo watakavyomdhoofisha na mwishowe kufa!!



    "Tamen yongyuan bù zhidào cóng nali dédào jie yào!" (Kamwe hawatajua wapi pa kupata antidote!) Akasema Shao kwa msisitizo. Maneno hayo yakaingia ndani ya kichwa cha Sheng lakini bado hayakumkosha. Akauliza kama antidote ipo ndani ya kambi yao.



    Shao akamjibu ni kiasi kidogo sana kilichopo. Hakiwezi kudumu hata zaidi ya juma moja.



    "Méiyou! Wo yào lìjí mái xià suoyou de jiedú jì!" (Hapana! Nataka antidote zote zifukiwe mara moja!) Sheng akabweka akigongesha kidole chake mezani. Alihofia pengine antidote hizo zinaweza kupatikana na kumsaidia Jona.



    Shao akalipokea hilo agizo na kuapa kulitekeleza. Kisha akamsihi mkuu wake kutumia fedha yake sasa kama chambo cha kumpatia Jona. Aweke matangazo kote mitandaoni akitangaza kutafutwa kwa mwanaume huyo na mtu atakayetoa taarifa zitakazofanikisha upatikanaji wake basi apatiwe donge nono la pesa.



    Sheng akaridhia hilo wazo kwa moyo mkunjufu. Lakini pia akaagiza vijana wake wote wa vitengo vya usalama wakutane naye usiku wa saa nne. Ana mambo kadhaa anataka kujadili nao.



    **



    "Hatujafanikiwa mpaka sasa, mkuu!" Sauti ilivuma kwenye simu ya Kamanda. Alikuwa amesimama koridoni akiwa amevalia taulo. Ameshikilia kiuno chake kipana.



    Si sebuleni wala chumbani kulipokuwa kunakalika. Tumbo lilikuwa joto. Kama kuna kipindi kigumu alichowahi kupitia akiwa kazini, basi ni hiki.



    Mwili ulikuwa unamtetemeka na kila simu iliyokuwa inapigwa alikuwa akiidaka upesi na kuiweka sikioni. Zaidi ya hapo alikuwa mbogo haswa. Hata mkewe na watoto walienda kujifungia ndani baada ya kuona hapakuwa panakalika.



    "Hamjafanikiwa mnafanya nini sasa huko??" Akafoka. "Ni kazi gani mwafanya huko ina maana mmeshindwa kui-trace hiyo ambulance mkajua imeelekea wapi??"



    "Tumefanya hivyo mkuu," sauti ikajitetea simuni. "Tumefuatilia na hata kwenda mpaka hospitali ambayo jina lake lilikuwa ubavuni mwa ambulance hiyo ..."



    "Wakasemaje??" Kamanda akakatiza.



    "Hawaitambui hiyo ambulance! Haipo kwenye orodha ya usafiri wao. It means ilifojiwa tu!"



    "Na namba?? ... hizo plate nu-number je??" Kamanda akauliza upesi.



    "Namba tumezifuatilia, ni za biashara. Gari lilisajiliwa kama daladala ila kuhusu mwenye mali nayo alikwisha fariki muda sana. Hata hili gari halikuwa likifanya kazi hiyo ya daladala kwa muda mrefu hapa jijini kutokana na marufuku ya vyombo vya aina hiyo kufanya kazi hiyo jijini."



    Kamanda akashusha pumzi ndefu kisha akauliza:



    "Sasa mmefanyaje?"



    "Bado tunaendelea na upelelezi mkuu, tutakapopata chochote kitu basi tutakutaarifu."



    Kamanda akakata simu na kurejea sebuleni. Akakaa hapo akiwaza na kuwazua nini afanye. Akiwa hapo, mara simu yake ikaita. Akatazama alikuwa ni Sheng. Akapokea simu na kuiweka sikioni.



    Sheng akampa taarifa ya kumhitaji ofisini kwake majira ya saa nne usiku.



    **



    "This is disgrace to Wu family!" (Hii ni fedheha kwa familia ya Wu!) Sheng aliwaka. Macho yake yalikuwa mekundu. Hakuketi kitini, alihisi hataeleweka. Aliongea kwa hasira na jazba.



    "Siwezi kukubali kudhalilishwa kiasi hiki na kikundi kidogo cha watu. Kamwe!"



    Akatazama kushoto na kulia akipekua rundo la wafanyakazi wake wanaomtazama kwa umakini. Ukumbi ulikuwa kimya. Hata mbu angelikatiza hapo angelisikika.



    Vijana watabe, vijana wa kazi, wachina kwa weusi, walikuwa wametega sikio kumsikiliza mkuu wao. Na wakiwa tayari kubeba agizo lolote lile watakalokabidhiwa.



    "Sasa ni hivi," Sheng akaelekeza kwa mkono. "Kwa sasa kazi zote zitasitishwa. Hakuna kufanya kazi nyingine yoyote isipokuwa moja tu! Kumtafuta Jona popote alipo. Yeyote atakayeleta kichwa chake ofisini kwangu, nitampatia cash shilingi milioni mia nane!



    Zoezi hili lisizidi mwezi mmoja tangu sasa."



    Baada ya hayo akawataka waende. Akabaki na Shao aliyejadiliana naye kwa sekunde kadhaa kabla hajamuuliza kumhusu Lee.



    "Ta zài nali?" (Yuko wapi?)



    Shao akapandisha mabega akisema hana taarifa naye.



    Kabla hawjajadiliana zaidi, kijakazi akaja na kumpasha habari Sheng kuwa ana mgeni. Kamanda mkuu ameshafika ofisini kwake.



    **



    "Nimekuita hapa kwa jambo moja," Sheng alifungua kijikao chake cha dharura. Mbele yake alikuwa ameketi Kamanda mkuu akiwa ndani ya shati la kitenge na suruali nyeusi ya kitambaa.



    "Nahitaji silaha zaidi kwa ajili ya kazi zangu. Nataka unisaidie kwenye hilo."



    "Silaha?" Kamanda akadakia. "Nitakusaidiaje bwana Sheng. Ni ngumu kutoa silaha stock na kukupatia. Itaweza leta suspicions!"



    "No! No! No!" Sheng akatikisa kichwa. "Sihitaji silaha zako. Kuna mzigo mkubwa utafika bandarini ukiwa kwenye meli ya wauguzi wanaokuja kutoa huduma ya matibabu bure hapa nchini. Ndani ya meli hiyo kubwa kuna kontena zangu mbili za silaha. Ninachojitaji wewe ufanye ni kuzipitisha kwa kutumia jina la jeshi. Basi!"



    Kamanda akameza mate.



    "I need them kwa ajili ya kumsaka Jona!" Sheng akamalizia habari.



    **



    Sasa shauri lilikuwa limekatwa na kesi imefikishwa mahakamani. Boka na Miranda wakataarifiwa kuhitajika kituo cha polisi mara moja.



    Ikiwa ni majira ya jioni, Miranda na Boka wakawasili hapo kila mtu akija na usafiri wake lakini ikionyesha bayana kuwa walikuwa na mawasiliano.



    Boka alikuwa ameongozana na mwanasheria wake, Bwana Manyanja Mayanja, ambaye yeye ndiye alikuwa akihusika na kila kitu hapo huku mteja wake akiwa msikilizaji tu.



    Kwa msaada wa mwanasheria bwana Mayanja Mayanja, wakapewa dhamana na zaidi tarehe za kuhudhuria mahakama kwa ajili ya kusikiliza kesi yao.



    "Tutakaposhinda kesi hii, jamhuri italazimika kulipa fidia ya muda na usumbufu na pia kusafisha taswira ya mteja wangu kwa kupitia vyombo vyao vyote vya habari!" Bwana Mayanja Mayanja alinguruma.



    Baada ya hapo wakatoka kituoni, ila kabla hawajakwea kwenye vyombo vyao vya usafiri, mara Miranda akaitwa.



    Alipogeuka akakutana uso kwa uso na Koplo Massawe.





    Moyo wake ukashtuka. Macho ya koplo Massawe yalikuwa yanamtazama kwa yamkini.



    Akageuza shingo yake kumtazama Boka kisha akamsihi amngojee yeye akienda kukutana na koplo Massawe.



    "Habari yako?"



    "Safi, afande."



    Massawe akamtazama Miranda machoni. Miranda naye akajitahidi kuyakaza macho yake. Ila moyo ulikuwa unampwita haswa. Kama koplo Massawe angeligundua hilo, basi angeliweza kumshukumu kindakindaki.



    "Kama nishawahi kukuona hapa, bibie," alisema Massawe kwa uso wa mashaka. "Ndiye wewe?"



    "Mimi?" Miranda akajiwekea kiganja kifuani. Akabinua mdomo wake na kusema: "labda, inawezekana ikawa ni mimi ... kuna kesi yangu nafuatilia hapa kwa inspekta."



    "Oooh!" Massawe akatikisa kichwa. "Basi sawa. Unaweza tu ukaenda."



    Miranda asiamini macho yake, akageuka na kuenda zake. Massawe akamtazama akiyoyoma kichwani akijaribu kukumbuka alipomuonea mwanamke huyo.



    Alikuwa tayari ameshamtilia mashaka akidhani anaweza kuwa na mahusiano na Jona. Na kama angelithibitisha hilo basi Miranda angekuwa na mashtaka ya kujibu. Asingelitoka hapo kituoni kwendaze.



    Ni kama bahati Miranda kuwa na kesi mbadala hapo kituoni. Alichoropokea tundu la sindano.



    **



    Mikono yake ikiwa ndani ya mifuko ya koti la ngozi, Lee alitazama huku na huko kukagua majengo marefu ndani ya Hongkong.



    Macho yake yalikuwa yamezibwa na miwani ya jua. Mdomoni alikuwa ana pipi ndogo ya kijiti akiimung'unya taratibu.



    Kuna kitu alikuwa anatafuta. Mkononi mwake alikuwa ana karatasi ndogo nyeupe yenye 'address' ya kufika mahali anapopataka. Na huko si kwengine bali kumfuatilia Chen Zi!!



    Wamkumbuka mwanaume huyo?? Mwanaume wa mwisho kuwasiliana na kutumiwa nyaraka kwa njia ya mtandao na yule mchina aliyekwiba nyaraka ya siri ya Lee??



    Sasa Lee alikuwa ndani ya Hongkong kumtafuta na hata kumuangamiza kwa mkono wake mwenyewe!! Alifanya yote haya kwa siri kubwa asiwataarifu hata wenzake. Aliona huo ndiyo muda wa kufanya hivyo, la sivyo hatalifanya hilo milele!



    Tangu Jona alipotiwa gerezani, alidhani angeweza kufanya misheni yake hii pasipo kusumbuliwa na Sheng. Hivyo mpaka sasa hakuwa anajua chochote kile kuhusu yaliyotokea kwa Jona.



    Hakuwa anajua kuwa mambo hayapo tena 'under control' bali 'over control'. Anahitajika na kutafutwa na mkuu wake huko nchini!



    Alikuwa anatimiza siku ya tatu akiwa Hongkong. Katika upelelezi wake wa akitumia mtandao wa Facebook alikuwa amepata pa kuanzia kumtafuta na kumpata Chen Zi amtakaye.



    Chen Zi ambaye anadhani anaweza akawa ni shabiki wa mwanamuziki Chen Zi halisi ambaye alikuwa mwanamuziki maarufu chini China aliyeripotiwa kufa kwa kuzidisha dozi ya madawa ya kulevya.



    **



    Ngo! Ngo! Ngo! Lee alibisha hodi kisha akatoa pipi yake mdomoni. Punde akafunguliwa mlango na kikongwe wa kichina aliyemkarimu kwa upole.



    Akazama ndani na kuketi. Akafanya 'survey' kukagua sebule ya bibi huyo. Ilikuwa hafifu na yenye vitu vya kale na haikuchukua muda akagundua kuwa bibi huyo anakaa hapo na binti mdogo anayetunza.



    "Wo zhao chén Zi!" (Namtafuta Chen Zi!) Lee akasema hitaji lake. Yule kikongwe akafikiri kidogo kisha akatikisa kichwa chake.



    Chen Zi yupi unayemuongelea? Akauliza. Lee akafungua simu yake na kumwonyesha kikongwe yule picha aliyoipakua toka kwenye mtandao wa Facebook.



    Kikongwe akavalia miwani na kuitazama picha hiyo kwa ukaribu. Akamuita na yule dada anayekaa naye, akamkabidhi picha hiyo aitazame. Dada akaiangazia na punde akatikisa kichwa.



    "Women bù rènshì ta!" (Hatumjui!)



    Lee akaitazama tena ile picha kisha akairejesha simu yake mfukoni.



    "Ni shì shéi?" (Wewe ni nani?) Akauliza yule kikongwe akimtazama Lee kwa umakini.



    "Wo shì ta de péngyou," (Mimi ni rafiki yake,) Lee akajieleza. "Ta gàosù wo ta zhù zài zhèli." (Aliniambia anaishi hapa.)



    Kikongwe yule akatikisa kichwa. Basi Lee akashukuru na kwenda zake. Kichwani akiwa anawaza pengine mtu huyo aliyechat naye alimlaghai kama ilivyokuwa kwa mtu yule wa mwisho kumfuatilia jana yake.



    Hii ndiyo shida ya Facebook. Watu hata mia wanaweza wakawa wanatumia jina moja. Kwa kupitia mtandao huo, Lee aliwang'amua watu wanne wakitumia jina la Chen Zi na wote wapo China!



    Tayari mmoja ashamwendea na kukuta sipo anapoishi. Alipofuatilia address' aliyopewa na mtu huyo akajikuta anafika nyumbani kwa mwanamke mmoja mjane!



    Na leo amefuatilia address ya mtu mwingine wa pili, ameishia kufika mlangoni mwa kikongwe! Akawaza nini shida. Lakini hakujali sana. Alikuwa ana muda wa kutosha siku hiyo hivyo hivyo atawamalizia na hao wawili aliowabakiza kwenye orodha.



    Akiamini kati ya hao basi mmojawao atakuwa ni Chen Zi anayemtafuta yeye. Moyoni akiwa anaomba nyaraka hiyo isiwe imezagaa ama kufika kwenye mikono ya maadui.





    **



    "Huanyíng!" (Karibu!) Sauti ya kiume ilifika masikioni mwa Lee. Hakupata wasaa wa kuitafakari sauti hiyo, mara mlango ukafunguliwa na mwanaume mwenye umri wa makadirio 40 - 45. Mwanaume huyo alikuwa amekalia 'wheel chair'. Mkono wake wa kushoto ulikuwa umelemaa na mdomo wake ulikuwa umepindia kushoto pia.



    Akamsalimu Lee na kumuuliza ni kwa namna gani atamsaidia. Lee akaeleza haja yake, kumtembelea rafikiye aitwaye Chen Zi.



    Mwanaume yule aliyemkarimu akatahamaki. Hakuwa anamjua mtu huyo. Kwa mujibu wa maelezo yake anaishi na mkewe anayefanya kazi kiwandani, hata simu hana, na huwa yupo bize sana kumhudumia akiwa nyumbani.



    "Wo hen bàoqiàn raoluàn!" (Samahani kwa usumbufu!) Lee akaenda zake. Kichwani akiwaza haya matukio. Ina maana Chen Zi wote aliochat nao wamemlaghai??



    Alitoa simu yake akaitazama. Akairudisha tena mfukoni.



    **



    "Wo bù rènshì ta!" (Simjui!) Alisema mwanamke mwembamba mwenye tumbo kubwa la ujauzito. Alikuwa amesimama mlangoni akimtazama Lee machoni.



    Nywele zake zilikuwa hovyo. Alionyesha kuchoka. Kama si wa kushusha vitu kesho basi keshokutwa haipiti.



    "Wo yigè rén zhù zài zhèli!" (Naishi peke yangu hapa!) Alisema mwanamke huyo mjamzito akizika matumaini yote ya Lee! Sasa rasmi idadi ikawa imetimia ya watu wanne aliochat nao na kati ya wote hao hakuna Chen Zi anayemtafuta.



    Ilimshangaza hili. Lakini ilimshangaza zaidi kwa namna alivyokuwa anakutana na watu wasiojiweza kwenye kila pango alilokwenda kumtafuta Chen Zi.



    Kwanini watu hao walimdanganya kama vile alivyoaminishwa na wenyeji wake?? Kwanini wafanye hivyo ilhali hakuwa ameeleza taarifa zake binafsi, badala yake akitumia picha ya kike??



    Hapa akabishana na akili yake. Ina maana amebumburukiwa?? Hapana! ... kivipi?? Hakuwa ameacha nyayo zozote za kuhisiwa kombo.



    Ila ...



    Akawaza.



    Kuwaomba wanaume hao 'address' zao kutakuwa kuliwapa mashaka?? Yani mwanamke aliyejirahisisha kupita kiasi?? Hapana. Akatikisa kichwa. Sidhani.



    Aliagiza juisi hapo mgahawani. Akatoa simu yake na kuitazama. Haikuwa na ujumbe wowote ule. Akaiweka mezani na kunywa juisi yake taratibu akifikiria namna ya kufanya.



    Punde hapo mgahawani wakaingia wanaume watatu waliovalia nguo nyeusi juu mpaka chini. Walikuwa ni wanaume wenye miili mikubwa, wawili miongoni mwao walikuwa ni wachina, mmoja alikuwa ni mtu mweusi ti.



    Jamaa huyu mweusi hakuwa na nywele hata moja kichwani. Wenzake walikuwa nazo ila chache, kwa mbali.



    Wakakaketi eneo moja. Upande wa kushoto wa Lee kwa umbali wa hatua kama nne hivi za mtu mzima. Nao wakaagiza juisi.



    Ikapita kama dakika tatu wakiwa hapo. Ila walikuwa wanamtazama Lee si mara moja wala mbili, wala tatu.



    Na kuna kitu walikuwa wanateta midomoni mwao kisisikike hata kwa majirani.



    Basi Lee akiwa hapo, hakuwatambua hao watu hata akatoka na kulipia kisha akaenda zake. Lakini wale watu wakatoka nao wakiwa wameacha hata vile walivyoagiza hapo mgahawani. Hao wakaongoza kumfuata Lee kama mkia.



    Lee akapanda gari na kuketi akiwa peke yake nyuma kabisa. Alipoketi akachomoa kitabu fulani kilichokuwapo kwenye vijindoo vidogo vijishikavyo ukuta mwa gari, akakunja nne na kukipitia kitabu hiko kilichokuwa na mambo matamu yaliyovutia.



    Kilikuwa ni kitabu kilichoonyesha mambo kadhaa kadhaa ya kitalii ndani ya China. Maeneo ya kutembelea na vivutio kadhaa ndani ya nchi hiyo. Milima na mabonde. Uoto na utamaduni. Na pasipo kusahau ukuta ule mkuu 'great wall' wa China.



    Lee akavutiwa sana na kitabu hicho, akapanga kutembelea moja ya vivutio vile kwani alikiri kifuani mwake kuwa japo alikuwa yu mchina, hakuwa anajua mambo mengi kuhusu nchi yake, maana amekuwa wa kutembea sana huku na kule.



    Hakutulia nchini mwake tangu alipotwaliwa na familia ya Wu, baada ya hapo akasafiri na kwenda kuishi nchi nyingine kabisa, kwa hivyo amekuwa mgeni katika nchi yake. Na ana hamu ya kujua mambo kadhaa zaidi.



    Kwa muda akatekwa na hicho kitabu, gari likasonga na kusonga. Alifungua kurasa na kurasa akivutiwa na anachokiona. Hata hakujua kama ndani ya gari lile walipanda wale wanaume watatu ambao kwa namna moja ama nyingine walikuwa wanamzingatia.



    Akafika kituoni na kushuka. Akatembea kuelekea jengo fulani lenye urefu wa wastani. Nyuma yake kama hatua kadhaa, wale wanaume nao wakawa wanajongea taratibu kumfuata.



    Lee akapapasa mifuko yake, na mara akatoa kiasi fulani mfukoni mwake na kuzama ndani ya duka moja kubwa 'Mi Hao supermarket', humo akapate kutazama baadhi ya mahitaji yake kabla hajarejea nyumbani.



    Alipozama humo ndani wale wanaume wakasita kuzama. Wao wakaamua kungoja kwa nje. Lee akazurura taratibu ndani ya duka akipitia shelvu moja baada ya nyingine. Hakuwa na haraka. Hakuwa na ratiba nyingine zaidi ya kurejea nyumbani kupumzika, na kwa namna moja ama nyingine mahali pale palimsahaulisha mawazo yake kwa muda kidogo.



    Basi akiwa anautumia muda wake kiasi humo, mara mlinzi aliyekuwa amekaa ndani akatoka nje kwenda kuwakuta wale mabwana kule nje maana aliona wamekaa kwa muda mrefu hapo wasionekane kama wana shughuli yoyote ya maana.



    Na kwa kiasi kimoja ama kingine, mwonekano wao ulizua mashaka. Walionekana wahuni. Si watu wa kuamini. Japo mlinzi alikuwa mwembamba asiye na nguvu, akatumia madaraka yake kuwauliza wanaume wale majabali ni nini walikuwa wanafanya hapo.



    Basi wakatazamana na kisha mmoja akasema, wanamngoja mwenzao aliyeingia humo ndani na maelezo waliyotoa wakamlenga Lee. Basi mlinzi akaachana nao na yeye akazama ndani.



    Moja kwa moja akamwendea Lee na kumuuliza kuhusu hilo. Hapo ndiyo akawa ametibua mambo. Sasa Lee akajua kuna watu. Na kwa kutumia kamera za mapokezi akawaona watu hao. Hakuwa anawatambua. Na kwa kumbukumbu yake hafifu, aliwaona mahali.



    Hakujua ni wapi, ila kama aliwaona, aliwaza.



    Basi akamaliza kuchukua vitu vyake naye akalipa na kutoka nje, hakuwasemeza wale wanaume. Alitaka kuona kama watahangaika naye. Nao hawakusumbuka. Ila wakaunga nyuma kama mkia.



    Lee akatembea akiwa anawaza kichwani mwake namna ya kufanya. Na akiwa anawaza wale watu ni wakina nani. Akaona si busara kwenda nyumbani kwake moja kwa moja. Na hakuwa na haja ya kuwakimbia wale wanaume maana wapo ndani ya uwezo wake kabisa.



    Basi akatafuta kichochoro alipozama humo. Ilikuwa ni kaupenyo kadogo kakuongoza kutokezea upande wa pili ambapo huko kuna bahari kwa kama umbali wa hatua hamsini kwa mbele.



    Njia ilikuwa nyembamba, na kwa wale wanaume majabali iliwawia vigumu kidogo kupita kwa kujinafasi kama walivyokuwa wakifanya barabarani.



    Humo njiani Lee akaona ni mahala pema pa kufanya alichokuwa anawaza kichwani - kuwakabili wale wanaume ambao aliamini kuwa maadui.



    Basi akasimama na kuweka vitu vyake kando. Kisha akakung'uta mikono na kugeuka kuwatazama wale wanaume ambao nao walisimama punde Lee alipofanya hivyo.



    Akawauliza wao ni wakina nani na kwanini wamfuata. Wanaume wale kwa kebehi wakamwambia kabla hawajamfuata, yeye ndiye aliyewafuata. Lee akashangaa.



    Hakuwa anataka kusumbuka sana, akawauliza wanataka nini toka kwake. Wale wanaume wakasema wana maongezi naye, na kama hatojali basi aongozane nao kwenda huko wanapomtaka kuteta.



    Lee akasita. Vipi kama watu hawa wanatafuta mahali pa kummalizia? Kama kweli walikuwa na hitaji basi ni kwanini walikuwa wakimfuata kimya kimya hivyo? Akakataa, akema kama wana hitaji basi walieleze hapo hapo na si vinginevyo.



    Wale wanaume wakatazamana. Na basi akasema kama hakuwa anahitaji kwenda kwa hiyari, basi watamlazimu maana wametumwa vivyo.



    Wakamfuata wakitaka kumnyakua, lakini Lee akajiandaa kwa mapambano. Akajiweka sawa na kuanza kupambana. Alikuwa mwepesi kukwepa na kuutupa mwili tofauti na maadui zake.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Japo ilikuwa pevu, akaimudu ndani ya dakika kadhaa. Alikuwa amechoka kwani wale majamaa walikuwa majabali haswa kwa hivyo kuwalaza chini wakiwa hawajiwezi, haikuwa kazi rahisi hata kidogo.



    Akakusanya vitu vyake na kuondoka. Ikiwa hakuonekana na yeyote yule zaidi ya wale waliobakia hoi sakafuni.



    **



    "We are already here!" Sauti ilivuma garini. Lilikuwa ni gari refu jeusi, Limousine. Dereva akashuka na kwenda kufungua mlango wa nyuma, akatoka mwanaume mfupi mchina aliyevalia suti nyeusi. Mkononi mwake alikuwa ana sigara kubwa iliyokuwa inafuka moshi mwingi. Na macho yake yalikuwa yamefunikwa na miwani meusi.



    Mwanaume huyo akavua miwani na kuangaza huku na huko. Mara akawaona wale wanaume majabali wanne wakiwa wanajikongoja kuja garini. Mwanaume huyo ndani ya suti akawatazama kwa uso wa ghafira, alafu akaingia ndani ya gari na kutulia.



    Wale wanaume nao wakaingia na kisha gari likahepa wasipate hata kuongea. Kwa muda kukawa kimya.



    Baada ya muda wa dakika kadhaa humo katika gari hilo la kifahari, mwanaume yule jabali mwenye rangi nyeusi, akamtazama yule bwana aliyekuja kuwachukua, akamsihi mambo hayakuwa kama vile walivyotaraji.



    Lakini yule bwana hakujali. Mdomo wake aliutumia kuvuta sigara badala ya kuteta. Alikuwa 'bize' uso wake ukitazama mbele, na ubaya miwani yake iliyokuwa imeficha macho, haukutuonyesha wapi au nani anamtazama.



    Hatukupata uhakika kilichoendelea maana baada ya dakika kadhaa hivi, limousine hiyo ikazama ndani ya jengo moja refu hapo Hongkong, likaendea eneo la maegesho ya gari.



    Lakini kitu pekee ambacho tulikuja kupata hakika nacho ni kuwa, wale mabwana, majabali waliogaragazwa na Lee, waliuawa na maiti zao zikafungiwa mawe makubwa na kutupiwa baharini!



    Aliyesalimika akawa ni mmoja tu, yule bwana mweusi. Naye usiku akajikuta kitandani akiwa amefunikwa mdomo wake na karatasi pana. Akainyofoa akilalama kwa maumivu makali.



    Na kwenye ile karatasi kulikuwa kuna ujumbe ulioandikwa kwa wino mweusi kwa lugha ya kichina ukimtaka ahakikishe anampata Lee ndani ya siku mbili tu, la sivyo maisha yake yatakuwa katika rehani kubwa.





    **



    Alipoweka glasi yake ndefu mezani, akakohoa kidogo kisha akamtazama Miranda aliyekuwa amekaa kando. Akamuuliza;



    "How is he now?" (Anaendeleaje sasa?)



    Miranda akanywa kwanza naye kinywaji chake glasini. Ulikuwa ni mvinyo mwekundu. Akagida mafundo matatu, alafu akamtazama Bwana Brown almaarufu, BC, ambaye kama kawaida yake alikuwa ndani ya suti tamu iliyomkaa mwilini. Mguu ameukunja nne, na vidoleni amebebelea sigara kubwa.



    "He is still far from being ok," (Bado hayuko sawa,) Miranda akasema kwa vuli la huzuni, alafu akashusha pumzi ndefu na kuufumbata mdomo wake.



    "We have to get the cure, otherwise he will die in our hands," (inabidi tupate tiba, vinginevyo atafia mikononi mwetu,) Miranda alisema akiwa anamtazama BC kwa kina.



    Kukawa kimya kidogo. Wakinywa na pia BC akivuta sigara yake. Baada ya muda kidogo, BC akaulizia kuhusu antidote iliyoletwa na kijana aliyemfahamu kwa jina la Marwa.



    Alipata kumwona kijana huyo hapo kwa Miranda na kisha akatambulishwa kama mkazi wa eneo moja na Jona.



    "That antidote makes things worse! He almost died the last time I gave it to him!" (Antidote huaribu mambo kabisa! alikaribia kuca nilipompatia mara ya mwisho!") Miranda alitema cheche. Basi BC akanyamaza kidogo. Na kama ilivyo hulka yake akiwa mawazoni, akawa anavuta sana sigara kuliko kunywa.



    Kwa hivyo, Miranda akanyamaza akingojea jibu maana alikuwa ana uhakika bwana huyo atateta baada ya muda fulani.



    Hakuwa amekosea, baada ya muda BC akafungua mdomo wake mkavu kuteta. Akamwambia Miranda, Bwana Sheng atakuwa ametambua kuwa Marwa alikuwa na antidote hivyo akabadili virusi vya kumtilia mwilini.



    Basi wasihangaike sana, yeye anahitaji kiasi kidogo cha mate ya Jona, akienda nyumbani kwake ayafanyie utaratibu wa kuyapembua kwenye maabara yake binafsi wajue cha kufanya.



    "I am sure, after two days he will be dead if he wont be taking antidote." (Nina uhakika baada ya siku mbili atakufa kama hatakuwa anatumia antidote.) Bwana BC akateta. Na huu ulikuwa ukweli mtupu mana Jona alikuwa amekwisha mno, hajiwezi kitandani.



    Kama ungelikuwa na roho nyepesi, machozi yangalikutoka ukimwona.



    Na basi kwa uzito wa swala hilo, hata ule mvinyo aliokuwa anakunywa Miranda hakuwa unasuuza koo lake kabisa. Hakuufurahia maana kichwa chake kilikuwa kimetingwa na mawazo lukuki.



    Basi wasipoteze muda hapo, ndani ya muda mfupi baada ya BC kumaliza sigara yake, Miranda akapata mate ya Jona kwenye kijifaa kidogo cha chupa, na haikuwa ngumu kwake kupata mate hayo kwani Jona alikuwa akiyatiririsha ya kutosha.



    Akamkabidhi BC na bwana huyo akaondoka zake.



    **



    "Nadhani amelala sasa," alisema Marwa akirudishia mlango wa chumba alicholazwa Jona. Mbele yake alikuwa amesimama Miranda akiwa amekumbatia mikono yake, ametazama chini akizimeza lips zake.



    Alikuwa amesimama hapo koridoni maana hakuwa anataka kwenda kumtazama Jona chumbani akihofia kusononeka moyo. Kila alipomwona Jona macho yake yalibadilika rangi kuwa mekundu, na akihisi moyo wamuuma haswa.



    Baada ya kupewa taarifa taarifa hiyo na Marwa, wakaongozana kwenda sebuleni. Na punde alipoketi, simu yake ikaita. Alikuwa ni BC. Akapokea na kuiminyia simu sikioni.



    "I have never seen such a virus like this before!" (Sijawahi kuona kirusi kama hiki hapo kabla!) Sauti ya BC ilinguruma simuni. Miranda akabana pumzi kwa mshangao. Moyo wake ulianza kwenda mbio.



    Akauliza kwa hofu, "So what shall we do??" (Sasa tutafanya nini??)





    ***



    BC akaguna kidogo alafu akasema inabidi wafanye kuipata antidote hiyo kwa namna yoyote maana la sivyo Jona atakufa. Ila kwa kusogezea muda, atampatia antidote mbadala. Hiyo itampatia Jona ahueni ila si ya kudumu!



    Na ubaya ni kwamba kadiri atakavyoendelea kutumia antidote hiyo basi ataishia kuwa kilema hapo baadae kwani si nzuri sana.



    "Send that man to my house. I will give it to him. (Mtume huyo mwanaume nyumbani kwangu. Nitampatia.) BC alihitimisha maongezi yake kisha akakata simu.



    Miranda akateta na Marwa aende kwa BC, akamkabidhi na funguo ya gari kisha maelekezo ya namna ya kufika huko.



    "Usikawie," akamsihi. "Inabidi ulete hiyo antidote upesi Jona apate unafuu."



    Marwa akafichama funguo kiganjani mwake.



    **



    "You are welcome!" BC alimkaribisha Marwa sebuleni. Mwanaume huyo akaketi kwenye sofa zenye nyama na kumtazama Bwana huyo mzungu pasipo kutia neno. Aliamini anajua kilichomleta hapo.



    BC akakung'utia mabaki ya sigara kisosini, kisha akavuta pafu ndefu na kuzima kabisa sigara yake. Akapuliza moshi angani na kumtazama Marwa.



    "So you are the man?" (kwahiyo wewe ndiye mwenyewe?)



    Marwa akatikisa kichwa chake, akasema, "Yes, I am."



    "Ok, so listen to me very carefully," (sawa, sasa niskize kwa umakini,) BC akafungua dibaji yake ya maongezi. Akajitengenezea vema kitini kisha akamtazama Marwa aliyekuwa amemwazima masikio.



    "You have to follow instructions properly. Time and diet. I didn't have time to write them down so I'll just tell you orally!" (Inabidi ufuate maelekezo vema. Muda na mpango kula. Sikuwa na muda wa kuviandika kwahiyo nitakuambia kwa mdomo!)



    Baada ya hapo akamwelekeza Marwa dozi, muda na chakula anachotakiwa kupewa Jona. Marwa akavi- note vyote kichwani pasipo kubakisha hata chembe. Akashukuru, na kuaga. Alikuwa ndani ya upesi. Hakutaka kupoteza hata sekunde.Lakini bwana BC akamtaka avute subira kwanza.



    Kuna jambo anataka kujadili naye kwa ufupi.



    "I know you dont know but I want to let you know, I spend a lot of money on him. And it is clear that I will even spend more and more to get him on his feet. The question is, will I get his loyalty?" (Najua hujui lakini nataka kukujuza, natumia fedha nyingi juu yake. Na ipo wazi kuwa nitatumia zaidi na zaidi kumfanya asimame kwa miguu yake. Swali ni, nitaupata uaminifu wake?)



    Hapa Marwa akasita. Si tu kwamna hakuwa na jibu, bali alihofia kuteta. Hakuwa anajua lililopo kichwani mwa Jona, wala mwa Bwana BC. Hakutaka kutibua mambo mapema hii, akaomba muda kidogo. Itakuwa vema Jona akisema mwenyewe punde atakapopata uwezo wa kutamka.



    Bwana BC akaguna akisafisha koo lake. Akalamba lips zake kavu akimtazama Marwa kwa sekunde kadhaa akiwa kimya.



    "You are his friend. I hope you know him inside out. I adopted him when he was abandoned by the world. When he was no one. So he should be someone under my shadow. Deliver this message to him." (Wewe ni rafiki yake. Natumai unamjua ndani nje. Nilimuokota akiwa ametelekezwa na ulimwengu. Akiwa si mtu. Kwahiyo inabidi awe mtu chini ya kivuli changu. Fikisha huu ujumbe.)



    Marawa akatikisa kichwa kwa kuridhia, alafu akaaga na kwenda zake.





    **





    Akiwa kwenye mataa, akapata kufikiria yale maneno ya BC. Alilaza kichwa chake akitazama 'sight mirror'. Na kwa muda kidogo akawa amesafiri kwenda ulimwengu mwingine. Ulimwengu wa mawazo na fikra.



    Akaumauma midomo yake akijaribu kupembua. Akisikia sauti ya Bwana BC na kwa muda huo akiyaweka maneno yake kwenye mizani na hulka ya Jona.



    Je, Jona ataridhia masharti ya BC? Hili swali lilimuumiza kichwa kidogo. Vipi kama Jona atakaidi na kuamua kufuata njia yake, BC atachukua hatua gani? Naye atakuwa upande gani?



    Mawazo haya yakaonyesha kutokuwa na komo zaidi ya kujiumiza kichwa. Asingeweza kuyapatia majibu kwa muda huo, ila alishindwa kuyafukuza kichwani mwake.



    Alikuja kushtuliwa na honi kali za magari yaliyo nyuma yake maana taa zilisharuhusu na alikuwa bado hajasogeza matairi ya chombo. Haraka akapangua gia na kukanyaga pedeli ya mafuta.



    **



    Tip! Tip! Vidole vilibonyeza vitufe kiooni, mara ujumbe ukaenda na muda si mrefu tiki ikatokea ujumbeni kuashiria ujumbe umefika.



    Lee akaweka simu yake pembeni kisha akajilaza akitazama dari. Muda ulikuwa unazidi kwenda akiwamo Hongkong pasipo mafanikio. Endapo akiendelea kukaa huko, basi Sheng atafahamu hayupo na hata akarudi akawa na wasaa mgumu wa kujieleza.



    Akashusha pumzi ndefu. Akafikiri kidogo na akili yake mtambuka ikamletea majibu. Kidogo akajiona mjinga. Kama kulikuwa kuna njia ya yeye kupata anachokitaka, basi ilikuwa kwa kupitia wale majamaa watatu!



    Akatikisa kichwa chake kwa masikitiko. Kwa akili yake mtambuka wale majamaa watakuwa wana mahusiano na hichi anachokitafuta. Hakuamini kama wanaweza kuwa vibaka wa kawaida tu, wakimtaka akaonane na mkuu wao.



    Huyo mkuu ni nani? Na amemfahamuje ingali hapa Hongkong yeye ni 'mgeni?' Hapa mawazo yakampeleka mbali sana. Hata akaanza kuwatilia mashaka wale watu aliokuwa anawakuta kule majumbani kumtafuta Chen Zi.



    Je, na wao watakuwa wanahusika na wale mabwana watatu?? Akatambua hapa kutakuwa kuna kitu, na kama akipata wasaa basi ana haja ya kuzitazama nyumba zile katika namna ya kipekee. Atagundua jambo.



    Akatazama kesho yake, hakuwa na muda. Alipanga kwenda mahali ambapo marehemu Chen Zi halisi, yule aliyekuwa maarufu nchini, alikuwa akifanyia mazoezi yake. Aliamini huko anaweza akapata lolote jambo likampa mwanga.



    Akaendelea kuyapanga mawazo hayo kichwani mpaka akapitiwa na usingizi.



    **





    "Boss, tumemaliza kazi," alisema mwanaume ndani ya suti nyeusi akimtazama Sheng kitini.



    "Una uhakika mmefukia kila kitu?" Sheng akauliza. Macho yake yalikuwa yanamtazama kijana huyo mjumbe kwa ukali.



    "Ndio, mkuu. Kila kitu tumemiminia shimoni!" Akaapa mjumbe. Uso wake ulikuwa umepooza. Macho yake yamelegea. Na mara akaanza kukohoa kwa pupa mpaka akatoa damu. Akamuaga Sheng kwa ishara kisha akatoka zake.



    Sheng akalaza kichwa chake kitini akifikiria kwa sekunde kadhaa. Punde simu yake ikaita, akainyakua na kuweka sikioni.



    "Sawa, nakuja," alisema kwa ufupi kisha akaiweka simu mezani. Akaendelea kufikiria kwa muda kidogo, na kisha akanyanyua simu yake ya mezani na kulonga, "tazameni hao vijana waliozika hizo antidotes! Kama watakuwa wameanza kubadilika, wawekeni kwenye cages. Ntakuja kuwatazama kesho mapema."



    Alipotoa agizo hilo akasimama na kutoka ofisini.



    **



    Bandarini, usiku wa saa nne ...



    Meli ya kichina inayojinasibu kuja kutoa huduma za afya bure nchini, haswa jijini. Ilikuwa tayari imeshatia nanga. Ndani yake ilikuwa imebeba wafanyakazi alfu moja na mia. Miongoni mwao vikosi vya wanajeshi wa kichina takribani vitatu kila kimoja wapo kikiwa na askari hamsini.



    Ilikiwa ni meli kubwa. Juu yake ikipeperusha bendera ya nchi, na ubavuni ikiwa ina chapa ya msalaba mkubwa rangi nyekundu.



    Gari jeusi, Ford Ranger modeli ya 2016 ikiwa imefunikwa bodi ya nyuma, ikasimama eneoni na punde akashuka Sheng. Kisha wanaume kadhaa watatu wenye asili ya China wakiongozana naye.



    Sheng akatembea kwa ukakamavu akifunga kifungo cha koti lake la suti. Alikuwa anaelekea kule ambapo Meli ilituama. Akiwa ametazama mbele aendako, mara akasikia sauti:



    "Kiongozi," kutazama, akamwona Kamanda mkuu akitokea upande wa gizani. Alikuwa yu mwenyewe akiwa amevalia nguo za kiraia. Akasogea, ila wale wanaume waliokuwa wanaongozana na Sheng wakamzuia.



    Sheng akawaamuru wamwachilie.



    Kamanda akampatia Sheng mkono. Akasema, "nimekuwapo hapa kwa muda."



    Lakini uso wake ulionyesha shaka.



    "Lakini sikuwa nafahamu kuwa si silaha tu umeleta. Umeleta pia na watu na chemicals!" Kamanda akakunja uso akitoa macho. Sheng akasimama na kumtazama.



    "Kamanda," Sheng akaita, "kwani kuna shida nikiongezea kidogo mzigo wangu?"



    Kamanda akabanwa kwanza na kigugumizi. Akatafuta neno la kuongea, akasema, "Hapana bwana Sheng. Lakini nilipaswa kuwa na taarifa rasmi. Namma hii inaweza kututia hatiani!"



    Sheng hakumjibu Kamanda. Akaendelea kutembea akiwa anawaza mambo yake kichwani. Alipofika getini, akasimama na kumtazama Kamanda. Akasema, "ni hatia gani hiyo waizungumzia? Kwani nakulipa kwa kazi gani?"



    Kamanda akataka kujibu, ila Sheng akasimamisha kidole chake kama ishara ya kumtaka asimuingilie. Alafu akaendelea kunena, "fanya kazi yako, Kamanda."



    Kisha akazama getini na ndani ya muda mfupi yakatoka magari mawili makubwa yaliyobebelea kontena rangi za kijani. Zilipotokomea eneoni, Sheng akaonana na Kamanda na kumpatia mkono wa kheri, anataka kwenda zake.



    "Samahani," Kamanda akasafisha koo na kuuliza; "Mmefikia wapi kwenye swala la Jona?" Sheng akamtazama kwa sekunde mbili kisha akamwekea mkono begani.



    "Kamanda, kati yangu nawe, nani wa kumuuliza mwenzake hilo swali?"



    "Aahm pengine unaweza ukawa umepata jambo. Si mbaya kunishirikisha."



    "Sijapata kitu. Na nilidhani hata hilo jambo wewe ndiye utakuwa wa kwanza kuling'amua maana limeshusha hadhi ya jeshi lenu."



    Sheng aliposema hayo, akamwacha Kamanda pasipo kumuaga. Akatembea hatua tano, ila mara akageuka na kumtazama Kamanda. Akasema, "fom today, hilo swala la Jona, niachie mimi, sawa?"



    Kabla Kamanda hajasema jambo, Sheng akageuka na kwenda zake. Kamanda akabaki akimtazama mwanaume huyo anayoyoma.



    Akalaani sana. Aliona amedharaulika. Thamani yake imeshuka. Juzi tu, alikuwa akinywa na Sheng kwa furaha, leo anaongea naye kana kwamba kakijana ka mtaani!



    Akang'ata meno. Punde akajikuta ndani ya gari lake, akatekenya shina la usukani na kutimka eneoni baada ya kuhakikisha kila jambo limeenda sawa.



    Alijua wazi kesho yake vyombo vyote vya habari vitakuwa hapo bandarini. Na hata yeye atakuwapo hapo akiwakilisha jeshi la polisi. Ila akiwa kama mtu asiyejua kinachoendelea hapo. Akiwa ni miongoni mwa wageni rasmi!





    **



    Saa nane usiku ...



    "Kila kitu tayari, unaweza kwenda kupumzika, boss," alisema mwanaume mrefu mweusi, kijakazi wa Sheng. Alikuwa amevalia 'ovaroli' la bluu na kichwani akiwa amejiveka kofia ngumu na usoni amevalia miwani kubwa ya kumkinga macho na mikononi ana glovu ngumu rangi ya njano.



    Sheng na Shao walikuwa wamesimama pamoja wakiwa wametia mikono mifukoni. Macho yao yalikuwa yanatazama magari yale mawili makubwa yaliyotoka bandarini, na watu kadhaa wakiwa wanashughulika hapa na pale kwenye upakuaji.



    Baada ya kijakazi huyo kusema hayo, wanaume hao wa kichina wakaongozana kwenda kutazama kama kila kitu kipo sawa. Wakakuta kontena limebakia tupu, na ndani ya maabara kulikuwa kumesheheni vitu kadha wa kadha.



    Wakatazama maabara ile kwa kitambo kidogo, kisha Sheng akamuuliza Shao, "unadhani vitasaidia?"



    Ni nadra kwao kutumia lugha ya kiswahili katika maongezi yao. Ila Sheng aliamua kufanya hivi maana alitaka kumpa Shao mazoezi zaidi ya kutumia lugha hii. Imekuwa ikimsumbua, na kwakuwa yupo ndani ya nchi itumiayo kiswahili katika maongezi ya kila siku, hakuwa na budi kukifahamu.



    "Nadhani vitasaidia sana," Shao akajibu kwa sauti ya puani. Kama ungelikuwa unamsikia usingelimwelewa kabisa kwa namna anavyoongea. Ila kwa mwenzake Sheng ilikuwa haina shida maana wanashea lugha.



    "Lakini, Shao," Sheng akasema akimtazama mwenzake. "Naona kuna haja ya kuagiza vijana toka China kuja kufanya kazi huku. Hawa vijana wa hapa siwaamini kabisa, haswa ukizingatia Lee sijui alipo.



    Tuna haja ya kutuma maombi nyumbani watukabidhi baadhi ya vijana waliowapika huko kwa mafunzo magumu, waliojawa stadi za mapambano, waje kutusaidia."



    Shao akaminya lips zake nyembamba. Akatoa mkono wake mmoja mfukoni na kufikicha pua yake kidogo kama mtu mwenye mafua.



    "Sishani kama itawezekana kwa shasha," akasema Shao akitikisa kichwa. "Unajhua shasha hivi kule nyumbani kumekuwa na shiida shana. Li wameamka na kuwa ngufu kuba tofauti na mwashoni. Inasemekana wanafadhiliwa na matafa ya magaribi. Wanapambana shana kuhakksha Wu inakufa na waon ku-rise."



    Li ni wakina nani?



    Miaka kadhaa huko nyuma koo ya Li ilikuwa ni moja ya koo ya kawaida sana ndani ya nchi ya China. Hakuna mtu aliyekuwa anaizungumzia wala kuipa uzito kwenye maongezi yao. Ilikuwa ni koo iliyoundwa na wakulima na wafanyabiashara wadogowadogo.



    Na katika kipindi chao, koo hiyo ikashuhudia koo ama familia ya Wu ikipanda kwa kasi sana mbele ya macho yao haswa baada ya kuonekana kuvutia serikali katika namna ambavyo ilikuwa ikiwasaidia kupata na kulinda mikataba ya China. Vilevile ikihakikisha dola ya China inakua kiuchumi kwa kutumia mkono wowote, aidha wa damu ama kitabu!



    Na kwasababu hiyo basi, Wu wakatengewa kitengo maalum ndani ya chemba za serikali. Kitengo ambacho kiliikabidhi koo ya Wu ofisi ya ujasusi wa kiuchumi dunia nzima. Kwa hivyo basi, koo hii ikawa si siri tena ndani ya nchi ya China japo biashara zao zingine zilikuwa haramu kama vile utumwa wa kileo, madawa na utekaji.



    Sasa basi kwa kuitambua hili, nchi za magharibi ambazo hazipo tayari kuona dola zao zinawekwa miguuni na China, zikaamua kufanya jambo kujinasua na kuwadhoofu wachina wajao kwa kasi. Na njia bora waliyoichagua ikiwa ni ile ile ya 'kikulacho ki nguoni'. Wakiwa wanafahamu nguvu ya China ni familia koo ya Wu, basi wao wakaungana na koo ya Li kuhakikisha wanamtokomeza na kumdhoofisha Wu!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Na basi kwasababu Li walitaka umaarufu na pesa (Fame n' money), kwao hili hawakuliona gumu. Wakalipokea wakiwa vichwani wamedhamiria kifuta kiburi cha Wu, na kuirejesha koo ya Li kama koo yenye nguvu zaidi kama ilivyokuwa kabla ya mapinduzi ya nchini China ya mnamo mwaka 1945 mpaka 1950.



    Na sasa, Li wamekuwa wakiitawala Hongkong. Taratibu wakijipanga kutanuka na kwenda kuikabili Wu popote ilipo.



    Je, vipi kuhusu ile nyaraka ya Lee na saga la Chen Zi huko Hongkong??



    Tuurudi kwa Sheng na Shao ...



    Sheng alitikisa kichwa chake. Alikuwa ameelewa nini Shao amemaanisha. Akalaani. Akalaani tena maana aliona ni uzembe umefanyika mpaka kufikia hali kama hiyo ya sasa. Hakuwa anaamini kama Li ingefikia kipindi kuwa tishio na hata sasa Wu ikashindwa kusambaza wapambanaji wake na basi wakabakizwa hukohuko China.



    Akafikiria kidogo na kuona kuna haja ya kwenda huko China. Akakutane na viongozi wake juu na kujadili mambo kadhaa. Lakini Shao akampa tahadhari. Haitakuwa vema kama akienda huko akiwa hajakamilisha kwanza kazi yake ya kumtia Jona mikononi.



    Toa boriti kwenye jicho lako ndipo utazame ya wengine. Sheng akakubali shauri hilo. Punde atakapomalizana tu na Jona, atasafiri kwenda China angalau kwa juma moja tu.



    Na aliamini hilo la kumshughulikia Jona halitachukua muda maana ameshaleta vifaa vya kazi.



    Wakatoka maabara na kwenda kwenye ghala za silaha. Napo wakatazama ingizo jipya na kufurahishwa nalo. Baada ya hapo wakatoka na kwenda kupumzika maana muda ulikuwa umeshaenda sana.





    **



    Asubuhi Redioni ...





    " ... kwa hivyo basi, mimi kama kiongozi mkuu wa mkoa, ningependa kutoa rai kwa wananchi wangu kutumia fursa hii adhimu. Kuanzia majira ya saa mbili asubuhi kesho mpaka majira ya kumi jioni, wafike pale kwenye meli ya kichina ili wapatiwe matibabu na vipimo bure kabisa!



    Hili lamaanisha na kuonyesha namna gani serikali yao inavyowajali, na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata afya bora akaijenge nchi kwa kufanya kazi."





    Ilikuwa sauti ya mkuu wa mkoa.





    **

    Na kweli fursa ikachangamkiwa ipasavyo. Watu wenye matatizo mbalimbali wakajaa kwenye meli na kutibiwa bure kabisa. Lakini changamoto ikizuka kuwa wagonjwa walikuwa wengi mno hata wengine wakarejea majumbani pasipo kupata huduma wanayoihitaji.



    Baadae usiku kwenye televisheni, habari ikaruka na baadhi ya wananchi waliopata huduma wakoipongeza serikali kwa msaada huo toka nje kwa namna ambavyo walipata mapokezi na huduma za kisasa.



    Na hapohapo habarini, kiongozi wa meli hiyo akapata kuongea, pamoja pia na kiongozi mkuu wa mkoa. Wakanena namna uhusiano wao unavyoimarika na kwa namna gani wataendelea kusaidiana zaidi.



    **



    Saa tatu usiku, Hongkong





    Siku yake nzima haikuwa na mafanikio, tunaweza tukasema hivyo kwani kitu alichokuwa amekiendea hakuwa amekipata hata kidogo. Bwana Lee akashusha pumzi, kisha akadaka kiuno. Akatazama saa yake, majira yalikuwa yamemtupa mkono.



    Akawaza kuondoka sasa. Pengine akirudi kesho anaweza kumkuta huyu meneja ahusikaye na uwanja huu uliopo ghorofa ya tatu, ambapo ndipo Chen Zi alikuwa anafanyia mazoezi enzi za uhai wake.



    Na endapo siku hii ikienda bure, itakuwa hasara kubwa sana kwake maana muda unazidi yoyoma. Alijua wazi hatakiwa kupoteza hata sekunde huko Hongkong maana anaweza hitajika na Sheng mara moja akakosekana.



    Akanyanyuka, na kuvaa miwani yake meupe isiyo ya macho bali urembo wa kuficha identity yake. Akachomeka mikono yake mfukoni, kisha akatembea kufuata lifti. Akangoja kidogo, mara ikafunguka na mzee mmoja mfupi mnene mwenye nywele nyeusi na kiwaraza kwa mbali, akatoka kwenye lifti akitembea kwa ukakamavu.



    Lee akamtazama mzee huyu. Alikuwa mwenyewe. Amevalia shati na koti la kizibao lililofumwa na ngozi. Chini alivalia suruali brown ya kadeti na kumalizia na raba.



    Lee akahisi pengine huyu mwanaume ndiye anahusika na uwanja huu. Mavazi yake yaliakisi mtu wa michezo. Basi akaachana na lifti na kumuita huyu Bwana. Hakugeuka, akanyoosha tu mkono wake kumwambia Lee amefunga hilo eneo, na kwa sasa haitaji mteja yeyote.



    Lee akamweleza yeye si mteja, yupo hapo maana ana shida fulani, anaomba amsikize. Yule Bwana akasimama na kumtazama kwa shari. Kisha akamuuliza shida gani hiyo?



    Lee akatabasamu kwanza. Hakutaka kumhofisha bwana huyu. Alijitahidi kuwa rafiki kadiri alivyoweza. Akasema kwa ustaarabu kuwa alipewa taarifa kwamba Chen Zi alikuwa akifanyia mazoezi hapo. Basi kwa namna gani atapata mtu anayefahamiana na huyo jamaa?



    Yule Bwana akadhani pengine Lee ni polisi. Akastaajabu na kumwambia akiwa amekunja uso, ni kwa mara ngapi watakuja hapo kumsumbua na maswali ya mara kwa mara? Amechoka.na hana muda tena. Na basi ndiyo maana ameamua kutokujihusisha tena na mambo ya burudani.



    Lee akatabasamu na kumuahidi hiyo itakuwa mara yake ya mwisho kuja hapo. Hatopenda kumbughudhi, ila kama asipojali amsaidie, naye kwa namna fulani atamfurahisha.



    Aliposema hayo alikuwa akigusa mfuko wake. Yule Bwana akatabasamu. Akakunjua uso wake na kumtazama Lee kisha akampasha habari muhimu.



    Anajua mengi kuhusiana na Chen Zi, ila swala la kifo chake kimekuwa ni utata hata kwake. Lilikuwa la ghafla mno! Kwa mara zote ambazo Chen Zi alikuwa akifanya mazoezi hapo, alikuwa anakatazama hata washirika wake kutumia sigara, ilikuwa ni ajabu kuja kupewa taarifa kuwa amekufa kwa kuzidisha dozi ya madawa!



    Bwana yule akatikisa kichwa. Akatazama chini kwa masikitiko. Alikuw amemkumbuka Chen Zi, si tu kama mteja wakw bali kama mwanae kwa namna alivyokuwa mkarimu.



    Lakini asipoteze muda zaidi, akamwelekeza Lee kumhusu mpiga gitaa wa Chen Zi. Huyo anaitwa Chong Pyong. Ni kijana mfupi aliyetoboa kila sehemu ya uso wake. Tangu Chen Zi alipokufa, alijiunga kwenye bendi moja maarufu Hongkong na Shanghai. Wamekuwa wakipiga muziki wao kwenye hoteli mbalimbali!



    Akamtajia baadhi ya hizo hoteli. Lee akamshukuru kwa kumpatia kiasi fulani cha pesa kisha akaenda zake.



    Basi akashika njia ya kuelekea kituo cha mabasi maana muda bado ulikuwa unaruhusu upatikanaji wake, pia hii itamsaidia kutunza fedha zaidi, kichwani akipanga kutumia taksi wakati wa kurudi tu.



    Baada ya muda mfupi, akawa amefika kwenye moja ya hoteli aliyoambiwa na yule Bwana. Bahati akakuta tangazo likinadi uwepo wa ile bendi aliyoambiwa kuwa ndaniye ndo' yupo Chong Pyong.



    Ikamlazimu alipie kiingilio kikubwa sana kuingia humo maana ilikuwa hoteli ya 'watu wazito'. Akatafuta mahali pa kukaa, na kisha macho yake yakaangaza mbele kwa wale watumbuizaji.



    Hakuchukua muda mrefu, akamwona mlengwa wake kwani kwa kadiri muziki ulivyokuwa unapigwa, Chong Pyong alikuwa anaonekana kwa wepesi maana alijiri mbele kila muda akionyesha umahiri wake kwenye upigaji wa gitaa.



    Sasa Lee akaanza kupanga namna ya kumchomoa bwana huyo apate kuteta naye. Ila siku hiyo ikajiri kama bahati, hakungoja sana, mara muziki ukazima na wale watumbuizaji wakaingia kwenye mtindo wa utofauti kidogo.



    Sasa alisimama mwimbaji nyuma ya kidaka sauti, akaanza kuimba kwa mtindo wa 'akapela' - sauti kavu pasi na vyombo. Bila shaka walikuwa wamelenga wasikilizaji wapate ladha halisi ya sauti tamu toka kwa mwimbaji, lakini pia kuwapa mapumziko wale wengine wapate kuvuta pumzi baada ya kutumbuiza kwa muda.



    Hapo sasa, Lee akamwona Chong Pyong akielekea nyuma ya ukumbi. Akanyanyuka akitazama usalama. Walikuwa wamesimama walinzi kadhaa konani wakiwa wamevalia suti nyeusi na masikio yao yakizibwa na vifaa vya mawasiliano.



    Lee akahesabu idadi yao, sita. Na basi akatambua kuwa walinzi hao watakuwa wanamtazama mienendo yake. Na hakuwa amekosea. Walirusha macho kumtazama, na hatimaye wakamtilia shaka. Haikuruhusiwa mtu kueleka kule nyuma ya ukumbi kama wewe si mhusika.



    Wale walinzi wakawasiliana, kisha mmoja akanyanyua mguu wake mzito kumfuata Lee kule aelekeapo.



    Lee akaongeza mwendo. Na yule mlinzi naye akaongeza mwendo, na akazidi kumtilia Lee shaka. Akapaza sauti kidogo akimtaka Lee asimame hapo hapo alipo. Alijitahidi sauti yake isiwatie hofu wateja wengine waliokuwa wametulia, aidha wakila ama kuburudishwa na sauti tamu ya mtumbuizaji.



    Ila Lee akakaidi. Akaendelea kutembea. Na baada ya muda kidogo, akazama nyuma ya jukwaa. Sekunde tano nyuma, na yule Bwana mlinzi naye akakazamia humo.



    Akaangaza, ila hakumwona Lee! Kwa umbali wa hatua ishirini walikuwapo baadhi ya wale wahusika wa bendi, kwa idadi watu watano, wawili walikuwa wanatazama baadhi ya vifaa, wawili walikuwa wakiteta na mmoja anakunywa maji.



    Mlinzi huyu akapata shaka zaidi juu ya Lee. Akapaza sauti kuwauliza wale wasanii kama wamemwona mtu mgeni humo, wote wakasema hawajui!



    Mlinzi akatazama kushoto kwake, kulikuwa kuna korido ndogo inayoelekea stoo, na 'emergency exit door'. Akawaza pengine Lee atakuwa ameenda huko. Ila kabla hajanyanyua mguu, mara king'ora kikaanza kuita kwanguvu!



    Kilikuwa ni king'ora kinachoashiria moto kuzuka ndani ya hoteli, mara sauti za watu wakipiga mayowe zikaanza kusikika huku na kule, na watu wakaanza kukimbia kama wehu kila mmoja akitaka kunusuru roho yake.



    Hata yule mlinzi akaachana na kumtafuta Lee, akaenda kule kwenye hall kubwa kuhakikisha usalama.



    Ila kiuhalisia hakukuwa na moto. Ni kwamba Lee aliwasha 'lighter' karibu na 'sensor', hivyo ikapeleka taarifa ya moto ambao kumbe aliuzima na kutia lighter mfukoni.



    Hapa kwenye vurumai ya watu, sasa akageuka kuwa chui aliye mawindoni, jicho lake lilimwagukia Chong Pyong lisimwache. Na baada ya muda mfupi akawa amemtia mkononi. Akamzimisha na kutoka naye kwa kupitia emergency door.





    Baada ya muda mfupi Lee akawa amefanikiwa kufika na Chong Pyong mahali alipoweka makazi, akamlaza hapo na kwenda kuoga kuondoa uchovu. Alipomaliza akakumbuka kuwa hakuchukua chakula, akashuka chini kuendea.



    Aliporejea akakuta kitanda kitupu! Chong Pyong hakuwapo. Hamaki kugeuka nyuma, mara kiti kikarushwa kwanguvu kumfuata. Haraka akakwepa, kiti kikakita ukutani na kuvunjika.



    Chong Pyong akajaribu kurusha mateke na ngumi, lakini hakuwa na mafunzo ndani yake, hakuweza kufua dafu kwa Lee, akatulizwa punde na kujikuta sakafuni akiugulia maumivu.



    Akamuuliza Lee yeye ni nani na nini anahitaji kwake? Lee akamwambia ingekuwa busara kama angemuuliza kabla hajaamua kumshambulia. Lakini kwa wakati huo, Chong Pyong akadhani aidha Lee ni afisa wa polisi, na basi kama sio, atakuwa jambazi aliyetumwa amuangamize.



    Basi akaanza kujitetea akijieleza yeye hana makuu na mtu. Anacharaza zake gitaa tu kwa ajili ya kuingizia kipato familia yake na si kingine. Kama haitoshi, akaendelea kubwabwaja kwa hofu, akasema mpaka mengine ambayo Lee hakuwa na haja nayo.



    Kwa maelezo hayo Lew akatambua Chong Pyong alikuwa mtu wa aina gani. Mpenda starehe na anasa. Alafu pia ni mwongomwongo.



    Basi akamtaka anyamaze. Yeye hayupo hapo kwa ajili ya kumdhuru ila ana shida na mtu mmoja tu ambaye anafahamu atakuwa na taarifa zake, naye si mwingine bali Chen Zi!



    Chong Pyong akatoa macho kusikia jina hilo. Kwa sekunde kidogo akatulia akimtazama Lee kwa uso wa maulizo. Akamuuliza Lee yeye ni nani? Lee akamjibu shabiki mpenzi wa Chen Zi. Chong Pyong akamtazama tena kwa sekunde kama tano pasipo kunena kitu.



    Mosi, kuna kitu alikuwa anafahamu. Pili, kuna kitu alikuwa anaogopa. Mara akatikisa kichwa akasema, Chen Zi ni mfu. Hana taarifa zozote juu yake.



    Lee akamdaka shingo na kumbamizia ukutani, alafu akamning'iniza kwa mkono wake mmoja akitazama uso wa Bwana huyo ambao ulijawa na vipuli.



    Akamwambia kwa sauti ya chini, hana masikhara naye. Na hapo walipo ni ghorofa ya kumi, haoni soni kumtupia nje akajifia endapo asiposema anachokihitaji. Tena haraka asimpotezee muda. Ni nini kilimuua Chen Zi?



    Basi bwana yule akiwa amekabwa kwanguvu asiweze hata kuhema, akapambana kunena huku jasho likimchuruza. Lee akamwachia avute hewa akiwa amempatia dakika moja tu kueleza, la sivyo waendelee na zoezi!



    Chong akavuta hewa kwa pupa huku akikagua shingo yake. Baada ya sekunde kadhaa, akamtazama Lee kwa macho yake mekundu. Akameza mate. Akasema hajui kitu. Kitu pekee ajua ni kuwa Chen Zi alizidisha dozi ya madawa ya kulevya.



    Lee akamdaka tena shingo na kumbamiza ukutani! Mara hii hakumkaba, akabadili zoezi, akadaka moja ya kipini puani mwa Chong Pyong, akakinyofoa kwanguvu. Damu zikaruka! Chong Pyong akapiga kelele kali za maumivu.



    Ila Lee hakukoma, wala hakumwongelesha, akadaka kipini kingine kwenye nyusi ya Chong Pyong, nacho akakivuta kwanguvu, damu zikachuruza!



    Chong Pyong akalalama kwa maumivu. Lee, sasa mkono wake ukiwa umejawa damu, akadaka tena kipini kingine cha Chong Pyong, sasa cha mdomoni, Chong Pyong akapaza sauti, nasema! Nasema! Uso wake ukiwa umejawa na damu.



    Lee akamwacha na pasipo kuongeza neno, akamtazama kwa macho yenye kiu na neno. Basi Chong Pyong akavuta kwanza pumzi kisha akasema kuwa Chen Zi hakufa kwa madawa, bali aliuawa na watu wasiojulikana. Akasema anaamini watu hao walikuwa ni wapinzani wake kimuziki.



    Lee akamuuliza, sasa ilikuwaje vyombo vyote vya habari nchini na vya kimataifa vikatangaza kuwa amekufa kwa kuzidisha dozi ya madawa ya kulevya? Chong Pyong akahema kwanza. Kisha akamwambia Lee kuwa huo ni mchezo tu ulipangwa kwani Chen Zi alipewa sumu, na alipopoteza fahamu, wakamvutisha madawa na kuacha baadhi mezani mwake, mpaka mauti kumkuta.



    Lee akashangazwa na hiyo taarifa. Akamuuliza bwana huyu, aliyajuaje hayo, na kwanini hakuchukua hatua kuripoti huo ukweli?



    Chong akabanwa na kigugumizi. Akajitetea alikuwa anaogopa pengine angefanya hivyo, watu hao wangemuwinda na kummaliza. Aliamua kunyamazama kunusuru roho yake.



    Na kitendo cha kwamba alijuaje, alipata kushuhudia hayo yakitukia. Hapa Lee akamuuliza swali jingine, hao wauaji akiwaona ataweza kuwatambua kwa kuwatazama?



    Kabla Chong hajajibu, simu yake ikaita mfukoni. Hapa wakatazamana kwa sekunde kama tatu. Lee akazamisha mkono wake mfukoni mwa Chong na kutoa simu. Ilikuwa ni iphone 8 rangi ya fedha. Akapokea na kuweka 'loud speaker', kisha akamuwekea Chong Pyong mdomoni.



    Sauti iliyotoka simuni ilikuwa ni nzito. Na mara moja ilimuuliza Chong yupo wapi muda huo? Chong akalaghai yu mgahawani. Sauti ikauliza tena wapi amefikia kwenye lile swala la yule jamaa anayemtafuta Chen Zi?



    Hapo Chong Pyong akabanwa na kigugumizi. Alimtazama Lee wakakutana jicho kwa jicho. Lee akamkazia ndita na kumpa ishara aendelee kuongea na simu.



    Chong Pyong akasema bado hajafanikiwa, kisha akakohoa mara tatu. Mara simu ikakata. Lee akaelewa kile kikohozi kilikuwa ni ishara.



    Na sasa akatambua kuwa Chong Pyong alikuwa ana mengi ya kumjuza. Kwa namna moja ama nyingine ni adui anayemtafuta. Akamuamuru ampatie nywila za simu yake. Hili swala likawa gumu kidogo kwa Chong Pyong.



    Lakini baada ya Lee kunyofoa vipini vyake vitatu, akashindwa kustahimili maumivu, akatoa nywila, Lee akafungua simu na kuzama ndani. Akaingia Facebook na kukuta Chong Pyong akitumia jina la Chen Zi!



    Akaelekea kwenye kona ya ujumbe, huko akakuta 'conversation' kati yake na Chong Pyong akiigiza kuwa Chen Zi! Kumbe Chong alikuwa miongoni mwa wale watu ambao Lee aliwaomba anwani na wakampatia kisha Lee alipoitafuta akaishia kujikuta katika nyumba ya yule kikongwe mjane!



    Kama haitoshi, kumbe Chong Pyong alikuwa anawasiliana na wale Chen Zi wengine wote ambao Lee aliwasiliana nao na kisha wakampatia anwani ya uongo!



    Kwanini Chong Pyong anatumia jina la Chen Zi huko Facebook? Kwanini na wenzake wanayatumia majina hayo? Na kwanini walimlaghai?



    Kabla hajapata majibu ya maswali hayo, Lee akaamini kuwa Chong Pyong atakuwa anahusika na mauaji ya Chen Zi halisi, kwa namna moja ama nyingine! Kwanini walimuua? Na hao ma - Chen Zi wengine ni wakina nani?



    Akamkaba Chong Pyong na kumwamuru amueleze kila analolijua, la sivyo atanyofoa roho yake ndani ya sekunde moja tu! Aliminya mishipa ya koo la Chong mpaka mwanaume huyo akatoa ulimi nje, macho yakitumbuka!



    Alipomwachia, akadondoka chini akipapatika kuhema! Lee akamwambia ana sekunde tatu tu za kusema, la sivyo ataendeleza zoezi na mara hii hatalisitisha kamwe mpaka atakapogeuka kuwa mfua



    Mara wakiwa hapo, Lee akasikia vishindo vizito mlangoni mwake. Vilikuwa vya watu waliotoka kukimbia kisha wakasimama ghafula!



    Vishindo hivyo vilipokoma, sauti nzito zikaulizana. Lee akatambua hapo si salama. Ndani ya sekunde tatu mbele, mara mlango ukavunjwa na wanaume watatu majabali wakaingia ndani wakiwa wamebebelea bunduki mikononi. Miongoni mwao alikuwapo yule jabali mweusi aliyepewa agizo la kumtafuta Lee.



    Wakatazama huku na kule, hawakumwona mtu zaidi ya Chong Pyong aliyekuwa amelala chini akihema kama bata. Kutazama dirishani, wakaona li wazi, Lee alikuwa ametoroka kwa kutumia shuka!



    **

    Yule jabali mweusi akaghafirika akipiga ngumi kiganja chake. Haraka akaamuru wenzake washuke kule chini kumtafuta mwanaume huyo wakati yeye akiwa amebaki na Chong Pyong ndani ya chumba.



    Akamuuliza Chong Pyong maswali kadhaa. Ma maelezo yake yakazidi kumtia Lee hatiani na kuthibitisha kuwa si mtu wa kubaki hai hata kidogo.



    Lazima auawe! Maana tayari atakuwa amefahamu siri yao kuwa Chen Zi aliuawa na si kuzidisha madawa kama vile watu wadhaniavyo.



    Lakini pia, wakammaliza na Chong Pyong kwa usalama zaidi. Waliona endapo mtu huyo akiendelea kuwa hai, basi Lee atamtafuta na kupata kila anachokitaka. Kitu ambacho hawakuwa radhi kitokee, hata kidogo!



    Yule jabali mweusi baada ya kutimiza agizo la mkuu wake, kummaliza Chong Pyong, akaamriwa aende polisi na kuripoti hilo tukio katika namna ambayo Lee ataonekana kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo tangu amekuwa mkazi wa hilo eneo ambapo Chong amefia.



    Jabali hilo likatii na kufanya kama alivyoagizwa. Ndani ya muda mfupi, polisi wakafika eneo la tukio, wakapiga picha kadhaa, wakachukua maelezo toka kwa Jabali yule mweusi kama shahidi, kisha wakaondoka na mwili wa Chong Pyong.



    Na kwa msaasa wa kamera za CCTV, zilizokuwako maeneo ya koridoni na huko nje, polisi wakapata picha ya Lee iwasaidie kwenye msako.



    **



    Saa mbili asubuhi ...



    "Vipi? Unaendeleaje?" Marwa alimuuliza Jona aliyekuwapo kitandani akitazama kana kwamba mtu aumizwaye na mwanga mkali.



    Ndani ya chumba walikuwa wenyewe tu, na tayari Marwa alikuwa amembembelezea chai mgonjwa na kufanikiwa kwa kiasi chake. Alikula kidogo akasema ameridhika.



    Kabla Jona hajajibu, alimtazama Marwa kisha akafumba macho yake kwanguvu kama mtu auguliaye maumivu, alafu akasema kwa kunong'ona:



    "Naendelea vizuri."



    Mdomo wake ulikuwa mkavu. Macho yake madhaifu yalikuwa yamezungukwa na duara jeusi kwa mbali. Uso wake ulikuwa umekonda na kudhoofika.



    "Nipo wapi hapa?" Akauliza akijitahidi kuchanua macho yake. Ila akashindwa. Haraka akayaminya na kuyafumba.



    Marwa akamwambia, "Upo kwa Miranda. Unamkumbuka?"



    Jona akakunja ndita kwa mbali, alafu akauliza, "Miranda?"



    "Ndio, Miranda," Marwa akamjibu akimtazama na tabasamu kwa mbali. Jona hakusema tena, akanyamaza.



    Marwa akamtazama kwa muda. Kisha akarudia tena swali, "unamkumbuka?"



    Jona akabaki kimya. Ni kama vile alikuwa amepitiwa na usingizi. Marwa akaondoa vyombo na kumwacha peke yake. Ila muda kidogo akarudi na kumtazama. Bado Jona hakuonyesha dalili ya kuamka.



    Akaketi kitandani na kuendelea kumtazama kwa muda wa dakika tano, akasikia hodi mlangoni na sauti ya kike. Alikuwa ni Miranda. Akanyanyuka kwenda kukutana naye.



    "Vipi hali yake?" Akauliza mwanamke huyo. Marwa akageuza uso kumtazama Jona, kisha akatoka ndani ya chumba na kukifunga.



    "Angalau," akajibu akipandisha mabega. "Ameweza kuongea leo, japo kwa muda mchache ... ile antidote imemsaidia!"



    Marwa akatabasamu kwa mbali, ila Miranda akatazama chini. Marwa akamuuliza, "Vipi?"

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miranda akatikisa kichwa kisha akaongoza mpaka sebuleni. Wakaketi.



    "Ile si antidote ya kumpatia," Miranda akasema kisha akalaza kichwa chake kitini. "Itampa ahueni kwa sasa, kwa kitambo kidogo, ila inabidi atafutiwe antidote ya kudumu. Endapo akiendelea kutumia hii ya sasa, ataishi kupooza mwili."



    Marwa akatoa macho kwa mshangao.



    "Mbona hukuniambia mapema?"



    Miranda akamtazama. "Ingesaidia nini?" Akauliza. Kisha kama mtu aliyejishtukia aidha atakuwa amemkwaza Marwa, akashusha pumzi yake na kunyanyua mkono.



    "I am sorry. I didn't mean to be that rude."



    "Usijali," Marwa akamtoa hofu. "I understand. It's ok."



    "Inabidi tutafute antidote halisi," Miranda akasema. Ila uso wake haukuwa na lepe la matumaini. "Tusipofanya hivyo, tutatibu tatizo moja kwa kuleta jingine."



    "Tutaitafutia wapi sasa?" Marwa akauliza. Mara simu ya Miranda ikaita. Kutazama alikuwa ni BC.



    **



    Saa nne asubuhi ...



    BC alichomoa leso yake mfukoni akijifikicha pua. Mafua yalikuwa yanamsumbua. Aliporudisha leso yake mfukoni akanywa fundo moja kubwa la whisky kisha akamtazama Miranda na Marwa waliokuwa wameketi pembezoni mwake.



    Walikuwa wapo nje ya nyumba ya bwana huyo wa kizungu. Meza mbili zilikuwa mbele yao, ila ya Bwana BC pekee ndiyo ikiwa na kinywaji. Wote walikuwa kimya wakimtazama bwana huyo wa kizungu kwa hamu.



    BC akawatazama kisha akapooza koo lake kwa kunguruma. Akalaza mgongo wake kwenye kiti kidogo cha chuma alichokalia, na kusema kwa sauti kakamavu:



    "We have to prepare for any risk so far. To get the actual antidote won't be an easy task at all!" (Inabidi tujiandae kwa hatari yoyote. Kupata antidote halisi haitakuwa kazi ndogo kabisa!)



    Miranda na Marwa wakaendelea kumtazama kwa umakini. Na sura zao hazikuonyesha kama watu wanaohofia hatari hizo. Bali wana kiu na kupambana nazo. Na Bwana BC aliliona hilo.



    Akanywa fundo moja tena la whisky na kuwaambia haswa lengo lake la kuwaitia hapo.



    "Did you hear about that Chinese ship?" (Mmesikia kuhusu ile meli ya wachina?) Kabla hajajibiwa, akasema, "for sure, it might have brought something huge. And I fear, amongst them, is what we need." (Kwa uhakika, itakuwa imeleta kitu kikubwa. Na nadhani, miongoni mwavyo ni kile tunachokohitaji.)



    Akaweka kituo akitazama chupa yake ya kinywaji chake. Akafikiri kidogo na kuwataka Miranda na Marwa wafanye jambo kuhusu kile kitakachokuwa kimeletwa na ile meli. Kama kutakuwa na namna ya kuingia ndani ya kambi ya Sheng na kisha kupekua.



    "Though it is risky. It worths it." (Japo ni hatari. Ina manufaa.)



    Lakini vipi kama hawataikuta antidote huko? Akauliza Miranda.



    "Then you will surely see something else!" (Basi kwa hakika mtaona kitu kingine!) Akajibu BC. Na kuongezea, "and it will be equally important!" (Na kitakuwa na umuhimu sawa!)



    Lakini pia akawaambia kama njia hiyo haitafanikiwa, basi atawaeleza plan B. Na kwasababu plan A itakuwa haijafanikiwa, basi Plan B itakuwa ndiyo njia pekee iliyobaki na kwa namna yoyote ile iliyopo duniani, lazima itimie!



    **



    Saa nne usiku ...



    "Una hofu?" Miranda aliuliza akimtazama Marwa. Mwanaume huyo alikuwa ameketi kwenye kiti nje ya nyumba akiwa anafikiri na kuyajenga kichwani.



    Akamtazama Miranda na kutikisa kichwa. "Hapana, nipo ok." Ila uso wake ulimsaliti. Alikuwa na hofu. Na tumbo lake lilikuwa linauguza woga.



    Miranda akamsogelea na kuketi karibu yake. Akamwambia, "usijali. It will be ok. Hatutakufa. Tutafanikiwa kutoka hai na salama."



    Lakini kumbukumbu ya Marwa eneo lile haikuwa nzuri. Mara ya mwisho almanusura apate ukilema. Na ni ustadi tu wa Jona ndiyo uliowatoa hai. Hakuwa anaamini kama yeye na Miranda wataweza mudu.



    Miranda akatambua shaka lake hilo.



    "Unadhani siwezi kukulinda?" Akamuuliza akitabasamu.



    Marwa naye akatabasamu, kisha akatazama chini.



    "Hapana. Si hivyo."



    Miranda hakusema kitu. Akamgusa mgongoni na kumtaka akajiandae kwani muda umeshafika.



    Baada ya muda kidogo wakawa tayari wakiwa wamevalia sweta nyeusi zinazobana, suruali nyeusi za kombati na buti. Miranda akajiweka kwenye gari. Ila Marwa akaenda kwanza kumuaga Jona.



    Akamtazama kwa sekunde kama tatu. Hakuonekana kama ana fahamu. Akaketi kitandani na kumshika mkono wake. Akamuita, "Jona." Kisha akasema kwa sauti ya chini, "nakuacha kidogo. Mungu akijaalia tutaonana, tukiwa na dawa mkononi."



    Alipomaliza kusema hayo akaendelea kumtazama Jona kwa muda kidogo. Mlango ukagongwa.



    "Twende, Marwa!"



    Marwa akanyanyuka na kwenda kumkuta Miranda huko nje. Wakakwea garini na kutimka.



    Baada ya robo saa wakawa wamefika karibu na eneo. Miranda akaliegesha gari lake eneo aliloona ni salama, eneo fulani la baa walilolipia kiasi fulani, kisha wakatembea kwenda mahali husika. Wote migongoni mwao walikuwa wamwmevalia vibegi vidogo vyeusi.



    Kwa mwendo wao wa upesi, wakatumia kama dakika kumi tu kuwasili, wakaelekea upande wa kushoto wa jengo na kukwea ukuta baada ya kukata nyaya za umeme, Miranda akisimamia zoezi hilo.



    Kama nyani, Miranda aliudaka ukuta na kisha akamvuta Marwa, wakazama ndani na 'kunyuti' kwa muda kidogo kusoma rada.



    Eneo lilikuwa linalindwa mara mbili ya hapo mwanzo tangu mzigo mpya ulipoletwa na pia tangu antidote ziibwe mara ya kwanza na Jona na Marwa.



    Kwa hivyo walitakiwa kuwa makini sana. Makini zaidi. Na hata Marwa alimkubusha hilo Miranda mbali tu na kumuelekeza ramani ya eneo maana yeye ni mwenyeji.



    Wakaficha nyuso zao na vinyago. Na kisha wakaanza songa taratibu kuelekea upande wao wa kulia. Mahali walipo kulikuwa na vijumba vidogo vidogo visivyokuwa na watu. Ndani humo kulikuwa na majengo majengo kadhaa na kila jengo likiwa na kazi yake. Aidha ghala ama sehemu pa kupumzikia watu au ofisi.



    Eneo lilikuwa kubwa sana! Na lote lilikuwa limezingirwa na uzio. Na kwa makadirio ya haraka, ndani ya eneo hilo kulikuwapo na watu takribani mia mbili hamsini!



    Miongoni mwao wakiwa vijakazi, pamoja na walinzi wanaolinda hapo mchana na jioni. Na kila kijipande cha eneo, kilikuwa na kikosi cha walinzi wake. Na kila kikosi kikiwa na kiongozi wake mkuu.



    Eneo kubwa lilikuwa linamulikwa na mwanga mkali wa taa. Mahali pachache pachache palikuwa na kiza. Na huko ndiko ambako Miranda na Marwa walikuwa wanajiegeshea huku maeneo yale yenye mwanga wakiyakwepa ama kuyapita kwa upesi sana.



    Mpaka kufikia maabara kulikuwa na umbali wa kama nusu na robo ya kilomita. Na hapo katikati walinzi wakiwa wamejaa. Wanarandaranda. Wamebebelea bunduki nzito.



    Basi taratibu. Tazama. Pita. Simama. Tazama tena. Pita. Ngoja. Tazama. Pita. Huo ndiyo ulikuwa mchezo. Wakafanikiwa kupita salama robo kilomita.



    Ila wakiwa wanatafuna tena umbali huo, kuna mlinzi akahisi jambo. Alikuwa ni baba la miraba minne. Amevalia kibodi cheusi kinachobana misuli na suruali ya jeans 'dark blue'. Bwana huyu alihisi msogezo wa vitu nyuma ya kibanda kimoja cha mawasiliano.



    Akasimamisha masikio yake na kukodoa macho. Akashikilia bunduki yake vema mkononi. Akasonga kueleka huko alipopatilia shaka. Akatazama tazama, hakuona kitu. Ila kugeuza shingo, akastaajabu kumkuta mtu amesimama.



    Kunyanyua mkono, akanyakwa, akapokwa silaha. Hajakaa vema, akala teke lililomchana shavu. Mwanamke alikuwa amevalia 'high heels'.



    Akashika shavu lake linalomimina damu. Akakodoa kwa hasira. Akanyanyuka na kujipanga. Kutazama vema akamwona ni mwanamke. Akaguna.



    Basi akarusha ngumi, Miranda akayeya kisha akanyaka mkono huo na kuuviringita kama anauvunja. Mwanaume akabinua mgongo akiugulia, Miranda akamzawadia teke la kifua na kumcheusha damu bwana huyo aliyepepesuka kana kwamba kakumbwa na dhoruba.



    Hajasimama vema, Miranda akazunguka na kutuma mguu wake wa kulia, akakata koo la bwana huyo kwa kisigino cha kiatu chake. Mwanaume akalala chini mauti!



    Damu zinamwagika haswa. Miranda na Marwa wakamficha kwenye kachombingo fulani cha hilo jengo kisha wakaendelea na safari yao.



    Wakakata tena robo kilomita. Wakiwa wanaenda kwa tahadhari kubwa. Simama. Ngoja. Tazama. Tembea. Simama. Ngoja. Tembea.



    Wakafikia mahali ambapo palikuwa kama uwanja. Mahali hapo palikuwa na mwanga mkali. Pia kwa mbali, kule konani ya uwanja, walikuwa wamesimama wanaume watatu wakivuta sigara. Mikononi mwao walikuwa wameshikikia kamba za zilizofunga mbwa shingoni.



    Bahati Miranda na Marwa waliwaona wanaume hao kwa kutumia hadubini. Wakiwa wamejilaza chini wakajadili namna ya kufanya. Na ilikuwa lazima wakatize hapo kuendelea na safari yao kutokana na mahali walipoingilia.



    Miranda akatazama tena na hadubini yake. Kushoto na kulia. Kushoto na kulia. Kwa mbali wakaona kuna walinzi wengine wakiishilia kwenda kaskazini ya mahali walipo.



    "Sasa tunafanyaje?" Marwa akauliza.



    "Tungoje kidogo," Miranda akamjibu macho yake yakiwa ndani ya tundu za hadubini. "Muda si mrefu watamaliza ile sigara wanayoshea. Tutajua watatawanyika ama lah!"



    Basi wakangoja kwa muda wa kama dakika tatu, kweli wale wanaume wakawa wamemaliza kile kipisi walichokuwa wanashea. Mlinzi mmoja akabaki hapo wakati wawili wakitawanyika. Mmoja akaelekea kushoto na mwingine kulia.



    Sasa wakaona huo ndiyo mwanya wa kusonga hapo mataani wakiingiza kuwa kama walinzi, wakitumai kwa umbali ambao yule mlinzi mmoja alipo, itamuwia vigumu kutambua wao ni wavamizi.



    Ila kabla hawajanyanyuka, wakastaajabu sauti nyuma yao, "tulia hivyo hivyo!"



    Marwa akaogopa sana. Moyo wake ukaanza kupiga makasia.



    "Haya ... taratibu! ... nyanyuka mkiwa mmeanika mikono yenu juu!" Akaamuru mwanaume mlinzi aliyekuwa amewanyooshea mdomo wa bunduki.



    Basi wakatii. Wakiwa wananyanyuka, Miranda akaigiza kupaliwa na kikohozi kikali. Mlinzi kutazama, upesi Miranda akakanyaga ukuta kisha akajibidua! Mguu wake wa kushoto ukapiga bunduki, na wa kulia ukachana uso wa bwana mlinzi kama kiwembe! Bwana huyo akapiga yowe kali la kuugulia.



    Aaaaghh!!!



    Mara Miranda akamwamuru afunge mdomo wake upesi akiwa amemnyooshea bunduki. Kisha akamkita na kitako cha bunduki na kumzimisha. Wakamficha na kundelea na safari.



    Ila sauti ile ya mlinzi akigugumia maumivu, haikuwa imeishia kwenye masikio yao. Kuna wengine pia walisikia. Nao walitambua hilo, kwa hivyo walitakiwa kuondoka eneo hilo upesi.



    Wakakatiza ubavuni mwa uwanja wakiwa wanatembea kwa haraka. Mlinzi yule aliyekuwa mbali konani akarusha macho yake kuangaza, ila hakutia shaka sana. Zaidi alitazama wale wenzake wawili kama wamepotelea, kisha akachomoa sigara nyingine mfukoni na kuiwasha. Akaitia mdomoni.



    Akainyonya kwa nguvu na kutema moshi juu kama kiwanda.



    "Sasa, tupite njia hii!" Marwa akamwelekeza Miranda. "Hii ni shortcut. Tutavuka barabara mbili, kisha tutakunja kushoto. Kama hatua hamsini hivi, tutakuwa tumewasili."



    Wakafuata hayo maelekezo. Wakashika barabara nyembamba iliyowakatisha chochoro. Wakaibuka kwenye njia pana. Wakatazama huku na huko. Salama. Wakavuka na kudaka chochoro nyingine. Napo wakapita, wakakutana na njia kubwa. Wakatazama huku na huko. Hawakumwona mtu. Ila kabla hawajapiga hatua, wakasikia kishindo cha mtu.



    Wakasita. Kidogo akakatiza mwanaume mrefu mwenye mwili uliojengeka. Mkononi mwa mwanaume huyo alikuwa ameshikilia kamba ya mbwa. Kabla ya mwanaumr huyo kupita, mbwa akanusa jambo na mara akasimama!



    Akatazamatazama huku na huko akinusanusa. Mara akabweka akiangazia kule kwenye uchochoro! Akawa anavuta kamba akitaka kwenda.



    Mwanaume yuple aliyemshikilia akatazama kule uchochoroni. Kulikuwani giza, hakuona vema. Mbwa akawa anamvutia huko kwanguvu sana. Mwishowe, akaamua kuacha kamba, mbwa akakimbilia huko upesi na kuzama kichochoroni.



    Mwanaume yule akawa amekaa tenge akiwa ameshikilia bunduki yake. Sekunde kama tano, kimya. Hakusikia sauti ya mbwa. Akapata shaka. Akachomoa bunduki yake pajani na kuishika vema. Akaanza jongea kwenda uchochoroni.



    Hatua ya kwanza ... hatua ya pili ... hatua ya tatu ... hatua ya n ... mara akashtuka kumwona mbwa anatoka uchochoroni! Akaruka na kusogea kando. Akamwona mbwa amebebelea mfupa mdomoni. Mara ameulaza chini na kuanza kuulambalamba.



    Hajakaa vema, akasikia kishindo cha mtu upande wake wa kushoto. Kugeuka, akashanga tu ghafla yupo gizani. Hata hakujua katendwa nini. Akadondoka chini puh! Kama gunia la mkaa.



    "Twende!" Miranda akamsihi Marwa kwa sauti ya chini. Mara mwanaume huyo skachomoka alipokuwa amejificha, wakaendelea na safari. Mpaka wakafanikiwa kufika maabara.



    Tatizo ni kwamba, hapo wakakuta walinzi takribani sita! Wote wakiwa wamebebelea bunduki mikononi mwao. Warefu na waliojaza miili kwa misuli minene!



    Marwa akatikisa kichwa. "Hatutoweza, Miranda!"



    Miranda akaminya mdomo wake na kukuna kichwa.



    "Lazima kutakuwa na njia."



    ***



    "Njia gani hiyo na pale waliposimama ndipo kuna mlango?" Marwa akauliza. Miranda hakumjibu, akaendelea kutafakari namna ya kuenenda. Namna ya kuzama mule ndani pasipo kuzuiwa na pande zile za baba.



    Baada ya dakika mbili, akamuuliza Marwa, "Kule nyuma hamna njia ya kuingilia?"



    Marwa akamwambia hakuna, isipokuwa dirisha tu. Miranda akatulia akiendelea kuwaza. Akamtaka Marwa wangoje hapo kwa muda kidogo. Aliamini wale walinzi sita hawatakaa pale kwa muda mrefu.



    Basi wakavuta subira kidogo. Kama dakika kumi hivi, mlinzi mmoja akachoropoka na kuacha wenzake watano. Ila hao walioachwa hawkauonyesha dalili ya kuondoka maana walilaza kabisa miili yao, wakipiga soga za hapa na pale.



    Sasa ikabidi Miranda atafute namna ya kuwaondoa hapo maana la sivyo watakesha. Wanaweza kujikuta wanakaa hapo mpaka mambo yakagutukiwa!



    Akamuuliza Marwa ampatie ramani ya wapi ilipo 'main switch'. Kidogo Marwa akasita. Hakuwa na kumbukumbu nzuri juu ya wapi ilipo 'main switch' kwa hivyo akamtajia mwanamke huyo sehemu tatu, akibashiri mojawapo itakuwa sahihi.



    "Unaenda kufanya nini huko?" Marwa akauliza. Miranda hakujibu, asipoteze muda akamtaka Marwa ajifiche kisha yeye aende huko. Akanyata na kusonga. Akatazama usalama. Akaendea njia yake kwa tahadhari na baada ya muda mfupi akawa amefika kwenye eneo moja ambalo aliambiwa na Marwa.



    Kutazama, hapakuwa penyewe! Akasonya na kuanza kufuata mahali pa pili alipoelekezwa na Marwa. Kwa upesi ila kwa tahadhari akasonga akielekea huko. Kabla hajafika akawaona wanaume wawili wakikatiza. Akajibanza. Wanaume wakapita.



    Akatazama kondo na kondo, kukawa salama. Akashika tena njia na kutembea. Akanyata kama mende ukutani, hakutoa sauti. Kuchungulia, akaona chumba kidogo chenye tahadhari ya umeme. Akashukuru. Hapo ndipo alikuwa anataka.



    Akatazama tena kushoto na kulia. Upesi akatembea kwenda kwenye kichumba hicho. Hapo kwa nje kulikuwa na mwanga kwa hivyo hakutakiwa kukaa hapo kwa muda. Akajaribu kufungua kichumba hicho, mlango ulikuwa umefungwa!



    Haraka akavuta begi lake mgongoni akachomoa chuma chembamba alichokizamisha nyuma ya mlango alafu haraka akautegua mlango. Basi ukafunguka. Akazama ndani na kutulia humo.



    Muda si mrefu, kama sekunde tatu tu kupita tangu Miranda aingie ndani, mlinzi mmoja akatokea akikatiza hapo. Miranda akatulia kimya ndani ya kijichumba. Mlinzi yule kabla hajapita, akasita, aliona mlango ukiwa wazi.



    Akasonga na kuutazama. Akaushika na kuusukuma mbele na nyuma. Na asijiulize sana akaurejeshea mlango ule sawa, kisha akaendelea na safari yake ya lindo.



    Miranda akashusha pumzi ndefu, kisha akachomoa miwani ya mpira na kuiveka machoni. Sasa akawa anaona mule kizani, japo kwa mwanga wa kijani.



    Akafungua kebo ya swichi.



    **



    "Marwa!" Sauti ikanguruma sikioni kwa kupitia kifaa kidogo Marwa alichokichomeka sikioni.



    "Bado wapo hapo?" Sauti ya Miranda ikauliza kifaani.



    "Ndio." Akajibu Marwa kwa kunong'oneza. "Bado wapo, wanne sasa!"



    "Sawa," sauti ya Miranda ikajibu.



    "Unafanya nini huko, Miranda??" Marwa akauliza akishikizia kifaa chake sikioni. Miranda akamwambia, "nakuja!" Kisha akakata mawasiliano. Marwa akahisi umeme utakata muda si mrefu. Akatazama taa akihesabu muda na akiwaza ni nini Miranda anapanga kichwani.



    Ikapita dakika kama tatu, Miranda akawa amefika hapo. Akamwambia Marwa, "tulia, muda si mrefu, ntakwambia cha kufanya!"



    Basi wakatulia hapo, muda si mrefu taa zikaanza kufinyafinya. Wale walinzi wakatazama na kuanza kuulizana. Taa zikazidi kufinyafinya maradufu. Miranda akamtazama Marwa na kumtaka avae miwani yake ya kiza kisha akamkabidhi pini nyembamba na kumpa maelekezo mafupi ya kueleweka juu ya kitu cha kufanya.



    Marwa alipokwisha fanya hivyo tu, taa zote zikazima baada ya mlio mkubwa wa mlipuko. Kukawa kumejawa na kimuhemuhe. Walinzi wale wakatazamana na kisha upesi wakakimbilia kule kwenye mlipuko wakimwacha mlinzi mmoja pale eneoni.



    Na kwakuwa kulikuwa ni kiza na vishindo vya watu vilikuwa vinasikika huku na kule, basi Miranda na Marwa wakasonga eneo la maabara pasipo kugutukiwa upesi. Wakamfikia yule mlinzi, Marwa akakimbilia mlangoni wakati Miranda akimkabili yule bwana mlinzi.



    Hakupoteza naye muda, mitupo yake mitatu ikamlaza mwanaume chali. Anavuja damu. Na pasipo kupoteza muda, akamburuza mwanaume huyo mpaka mlangoni. Marwa alikuwa tayari ameshaufungua mlango. Wakamzamisha ndani kisha wakafunga mlango.



    Haraka Miranda akamweleza fomula ya kemia wanayohitaji kuitazama maabarani humo. Na basi upesi wakaanza kusaka fomula hiyo huku na kule. Maabara ilikuwa imeshona kwa kujaa vitu lukuki hivyo kazi haikuwa nyepesi kutazama huku na kule kutafuta kitu kimoja.



    Wakachoma dakika mbili ... tatu ... nne ... tano ... mpaka kumi na tano, hakuna kitu walipata. Mpaka wakaanza kusikia sauti za walinzi wakisongamana huko nje.



    Huko nje walikuwa wamefika walinzi watatu wakiwa wamebebelea kurunzi kubwa mikononi kupambana na kiza. Walinzi hao wakasimama hapo mbele, mmoja akapanda kibaraza na kutupa miale ya kurunzi ndani ya dirisha la maabara. Akalipeleka kushoto na kulia. Hakuona kitu.



    Miranda na Marwa walikuwa wamejihifadhi chini ya meza wakiwa wamefunikwa na mizigo kadhaa. Wakangoja hapo, kurunzi likapita. Walipoona salama, wakanyanyuka na kuendelea na msako wao walioufanya kimya kimya.



    Ikapita dakika tano, Miranda akaona kitu ndani ya chupa ndogo aina ya 'test tube'. Kutazama vema, akaona kuna seti hapo za chupa hizo zikiwa na vimiminika rangi ya 'pinki' iliyopauka.



    Uzuri alikuwa ni mtu mwenye ujuzi na mambo ya kemikali. Si tu kuwa alisomea mambo hayo darasani akiwa na diploma, bali pia aliyafanyia kazi kwa muda mrefu akiwa na bwana BC.



    Akanong'ona, "Marwa, nahisi ndiyo hizi." Marwa akatazama na kuuliza, "mbona haina badge?"



    "Ndio, ila hii ndiyo rangi yake," Miranda akasema kwa uhakika kisha akageuza begi lake na kutoa vizibo vidogo vya mpira, akaziba midomo ya test tube kisha akatia seti hiyo begini na kuweka begi mgongoni.



    "Tuondoke," Miranda akamsihi Marwa.



    "Tunapitia wapi?"



    Miranda akasimama kidogo na kuangaza nje. Wasingeweza kupitia pale mlangoni. Basi akamwambia Marwa watumie dirisha maana ndiyo njia pekee iliyobakia.



    Kabla Mara hajatia neno, mara Miranda akatambaa kama mende kufuata dirisha la kusini, mbali kabisana mlango. Alipofika hapo, akajaribu kufungua dirisha hilo. Akagundua lipo 'sild', basi akafungua begi lake kwa mkono hata asitazame. Akapapasapapasa na kutoka na chuma fulani kilichojichanua kama mbawa za 'helikopta'.



    Akakinasisha pale dirishani, kisha akaanza kunyongorota mashine ndogo iliyo nyuma ya mbawa hizo. Basi hicho kifaa kikanguruma kidogo, Miranda akatoa mikono upesi, basi zile mbawa za kifaa hicho zikainama na kukuta kioo. Zikazunguka upesi na kabla hazijamaliza kutengeneza tundu, Miranda akakizima na kukinyofoa.



    Akamtazama Marwa na kumpa ishara asogee. Marwa akatii. Ila akamuuliza kuhusu kile kioo. Hakitatoa sauti wakashtukiwa?



    Miranda akatikisa kichwa, kisha akampatia kidude kidogo chekundu alichokitoa mfukoni, na kumwambia, "utakibonyeza ikifika tatu. Sawa?"



    Marwa akapokea agizo. Moja ... mbili ... tatu! Marwa akabonyeza kitufe hicho na hapohapo ikasikika sauti kubwa ya mlipuko. Sauti hiyo kuja kuzima tayari Miranda alishadondosha dirisha zima, wakatoka!



    Sauti za watu zikarindima huku na huko. Watu wakawa wanapishana ama kusimamishana wakijiuliza nini kinatokea humo. Kulizuka hali ya taharuki, na ukizingatia bado mwanga haukuwa umerudi.



    Basi Miranda na Marwa wakatumia fursa hiyo kufika kwenye uzio, wakanyaka na kujitupia nje baada ya Miranda kufanya kazi yake ya kukata nyaya za umeme. Miranda alitua chini katika namna ambayo alihakiki hakuna kitu kitakachovunjika begini. Mkono wake wa kushoto ulishikilia begi akitua kwa kishindo.



    Ila kabla hawajanyanyuka na kuhepa, Miranda akamtaka Marwa atulie hapohapo tuli, la sivyo wangeharibu chakula mwishoni.



    "Shhhhhh!!!" Miranda akampa ishara kisha akakagua eneo zima kwa macho yake mepesi.



    Wakiwa wametulia hapo kwa muda kidogo, wakaona watu kwa mbali wakiwa wanasonga kuzama ndani ya uzio. Na pale getini palikuwa na hekaheka.



    Basi Miranda akamtaka Marwa wabadili njia, nao hawakwenda mbele bali wakarudi nyuma na kufumbukia njia huko. Baada ya muda wa dakika nane, wakawa wamelifikia gari lao. Wakapanda na kulitia moto upesi.



    Hapo Miranda akatabasamu na kucheka. Walikuwa wamekamilisha kazi yao. Hata moyo wake ukawa wa baridi sasa na Marwa akalaza kichwa chake kwenye kiti akitabasamu. Alihisi ametua mzito wa toni kadhaa kichwani. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo.



    Ila kabla hawajaikuta barabara kuu, mara risasi tatu zikalia! Pah! - pah! - pah! Kioo cha nyuma cha gari kikapasuka na kuwa unga.



    Wakawehuka. Kumbe walikuwa wanafuatiliwa! Nyuma yao kulikuwa kuna gari jeusi, Toyota Harrier, imeshusha vioo vya madirisha ya nyuma.



    Miranda akamtazama Marwa. Hawakuongea kitu. Kumbe walikuwa wamekosea sana. Vita bado haikuwa imeisha. Bado refa hakuwa amepuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo.



    Sasa hapo wakawa na zoezi la kukabili lile gari ambalo ndani yake hawakuwa wanajua wapo watu wangapi.



    "Marwa," Miranda akaita. "Inabidi tuwamalize hawa watu wote. Endapo tukiwatorola ila tukawaacha salama, itakuwa rahisi kutufuatilia na kutujua. Wameshalijua gari letu."



    Marwa akataka kuuliza watawamalizaje, ila akaamua tu kunyamazama. Pengine Miranda alikuwa ameshapanga namna ya kufanya. Akawaza.



    Na ni kweli, mwanamke huyo alikuwa tayari ameshayapanga yake kichwani. Alihakikisha hajai kwenye macho na tageti ya adui, na baada ya muda fulani akamwambia Marwa, "shika usukani!"



    Hakurudia mara mbili, akachumpa kwenda nyuma ya gari. Haraka Marwa akalazimika kuudaka usukani na kusonga hapo kwenye kiti cha dereva kwa tahadhari.



    Risasi zikarushwa tena. Zikabangua gari kando na kando. Marwa akawehuka kwa uoga. Akayumbisha gari huku na huko. Ila akamudu na kuliweka sawa tena. Mwendo ulikuwa mkubwa sana.



    Akatazama kwenye 'sight mirror', akamwona Miranda amelala kochini. Hakujua mwanamke huyo anafanya nini maana hakuwa na muda wa kubakiza macho kiooni.



    Baada ya muda kidogo, Miranda akanyanyuka toka kitini, akachungulia kutazama gari linalowafuata. Kisha akarudi tena chini. Sauti ya kukoki bundiki ikaita. Na mara kidogo akanyanyuka na kuchomoa mikono yake nje ya gari kwa kupitia uwazi uliosababishwa na kioo kuvunjwa.



    Mikononi alikuwa amebebelea bunduki fupi, kama vile 'sub-machine gun' ila hizi zilikuwa fupi zaidi, zimechomekwa risasi pomoni.



    Basi akaelekezea mikono yake katika lile gari liwafuatalo na kilichofuatia hapo kikawa kufuru. Alimwaga 'njugu' kama mvua ya masika. Alichokuwa anakifanya ni kupeleka mikono kushoto, kulia. Kulia, kushoto.



    Risasi zikatoka pasipo kupumzisha koo la bunduki. zikachakaza kioo cha gari lile linalowafuata. Zikachomoa uhai wa dereva na mtu aliyekaa naye mbele mara moja wasiombe hata maji!



    Gari likayumba. Likayeya. Mara likapiga kona ya ghafla na kubinuka, likabiringita mara ya kwanza, ya pili, ya tatu, juu kukawa chini!



    Matairi yalizunguka na kukoma. Punde ndani ya gari ikasikika sauti ya mwanaume akikohoa. Kisha akaguguma kidogo kwa maumivu aliyokuwa anayapata. Si kwamba yalikuwa madogo, la hasha, mbavu zilikuwa zimembana. Anachuruza damu. Amevunjikavunjika kuanzia kiunoni kushuka chini.



    Basi mara mlango wa gari hilo ukasukumwa kwanguvu, akatoka mwanaume aliyekuwa amechafuka damu kichwani. Akajivuta na mikono kutoka ndani ya gari. Akatoa mwili mpaka kiuno, kisha akalala hapo akiwa hoi!



    Alilalama sana kwa maumivu makali. Hata kuhema ilikuwa tabu. Alikuwa ndiye mtu pekee aliyesalia kwenye ajali hiyo. Wenzake wote walikuwa wameshakata kauli.



    Akiwa hapo chini, anagugumia, mara akasikia kishindo cha miguu kikimsongea. Akajikakamua na kunong'ona, "nisaidieee ..."



    Mara kishindo cha miguu kikakomea mbele ya kichwa chake. Kutazama akaona kiatu kirefu cha kike, rangi nyeusi. Akakazana kurusha macho yake kutazama juu. Hakuona vema, ila akapata kutambua ni mwanamke waliyekuwa wanamkimbiza. Bunduki yake bado ilikuwa inanuka moto.



    "Nisa ...."



    Hajamalizia kauli, akala risasi tano za kichwa! Sina haja ya kusema kuwa alikufa papo hapo maana unajua kilichotokea. Damu zikamwagika kutengeneza kadimbwi.



    Miranda akachuchumaa na tazama ndani ya gari, akaona kimya. Hama dalili ya uhai. Basi akaondoka zake akirusha miguu upesi.



    Ila hakuridhika. Pengine mule ndani kunaweza kukawa na watu waliopoteza fahamu tu na si maisha. Basi alipokaribia gari lake, akatema tena risasi kadhaa kulenga uvungu wa gari, mara chombo kikalipuka.



    Wakayeya upesi.



    Kukawa kimya ndani ya gari kwa muda wa dakika kumi na, hakuna mtu aliyemwongelesha mwenzake. Ni kama vile walikuwa wanawaza na kuchambua kilichotoka kutokea. Na kama vile bado hawakuwa wanamini kama kazi imekwisha.



    Walifika kwenye makutano ya barabara, Marwa akatazama 'sight mirror' baada ya kusimamisha gari lao kupisha gari kubwa lililobebelea kontena kubwa rangi ya bluu.



    Nyuma yao akaona daladala moja, costa, akashusha macho yake na kumtazama Miranda aliyekuwa amejilaza kitini. Alikuwa anatazama nje akiwaza jambo.



    Hakumwongelesha. Ila baada ya kukanyaga mafuta na kuondoa chombo baada ya gari lile kubwa kukatiza, akamwita mwanamke huyo na kumwambia, "You were amazing! Really amazing! I didn't expect ... oh God!" Marwa akatikisa kichwa na kumalizia, "Nifundishe na mimi!"



    Miranda akatabasamu. Akaguna puani asiseme kitu. Wakafika nyumbani. Miranda akaweka ile set ya test tube mezani.



    "Vipi anaendeleaje?" Marwa akamuuliza dada wa kazi akionyeshea kichwa chake kule chumbani alazwapo Jona.



    "Nahisi yupo sawa," dada akajibu.



    "Hauna uhakika. Hukwenda kumtazama?" Marwa akauliza. Dada akapandisha mabega. "Nilienda kumtazama jioni. Sasa kila nikimtazama naona tu yu vilevile. Sijamtazama tena mpaka muda huu!"



    Marwa akatazamana na Miranda kisha akaelekea chumbani kumwona Jona. Mwanaume huyo alikuwa amekaa vilevile kama alivyomuacha. Akamshika mkono na kumwita. Hakuitika. Ila hakujali, akamtazama kidogo alafu akatabasamu na kusema, "Nimerudi, Jona. Tumefanikiwa kupata antidote."



    Akatabasamu zaidi, na kuendelea kunena kwa sauti ya chini, "haikuwa rahisi hata kidogo. Miranda alikuwa so magnificient. Siamini hata kama sasa nipo na wewe. Nilijua sitakuona tena, ila Mungu si Athumani ..." akanyamaza kidogo. Kuna kitu kilikaba koo lake. Akajaribu kumeza mate kisha akaendelea kunena, "... Mungu ana makusudi nawe. Ana makusudi na sisi. Muda si mrefu utaacha kitanda na mikono yako itafanya kazi iliyozoea."



    Aliposema hayo, akamtazama tena Jona kwa muda kidogo kisha akamuaga. Ila kabla hajatoka ndani ya chumba, akasikia sauti ya Miranda huko sebuleni. Alikuwa anaongea na simu.



    Basi akatoka na mpaka kufika sebuleni akamkuta mwanamke huyo ameshamalizana kuteta na simu. Akaketi na kumtazama. Alikuwa ana uso wa mafikirio. Akamuuliza, "vipi kila kifu kipo sawa?"



    Miranda akashusha pumzi alafu akasema, "nimetoka kuongea na BC. Nimemwelezea kuhusu hii chemical. You know what? Amesema si yenyewe ..."



    Marwa akahisi baridi la ghafla limempitia. Koo limemkauka. Na joints zote za mwili zimeishiwa nguvu.



    Akatoa macho. Ila kabla hajanena, Miranda akamwambia, "ngoja kwanza ..."





    ***

    Miranda akanyanyuka akishika kiuno chake. Akang'ata kidole akifikiria. Kisha akamtazama tena Marwa na kumwambia.



    "I know it can't be!" Akatikisa kichwa. "It can't be kabisa! Lazima hii iwe yenyewe."



    Alikuwa kama mtu aliyewehuka, na Marwa aliogopa kumwongelesha. Akabaki anamtazama aone ataishia wapi. Ila na yeye alikuwa amegawanyika nafsi.



    Alikuwa amejihisi mtupu kabisa. Akifikiria shurba alizopita, tundu la sindano, kisha kazi ikawa bure, anachoka kabisa. Alitamani alie, ila hapana. Hata macho yalikuwa makavu.



    Miranda akaketi kitini. Akashika kichwa. Akatazama zile seti pale mezani kisha akainamisha tena kichwa chini. Hapa Marwa akatambua mwanamke huyu alikuwa ana roho ngumu.



    Haki ingekuwa ni mwanamke mwingine, angeweza kujaza ndoo kwa machozi. Angekuwa tayari ameshanyofoanyofoa nywele zake akisaga meno.



    Pengine alikuwa anaugulia kwa ndani, ila kitendo cha kuweza kubakiza gulio hilo kifuani asilitoe, bado kulimfanya Marwa ashangae.



    "Sasa tunafanya nini?" Marwa akauliza.



    Miranda akashusha pumzi na kukodoa macho. Akaminya lips zake kama apendavyo, alafu akasema kwa sauti ya chini, "tungoje, labda akiziona anaweza kubadili mawazo."



    "Una maanisha BC?" Marwa akauliza. Miranda akatikisa kichwa na kujibu kifupi, "yah!"



    Kukawa kimya kidogo. Punde Miranda akamuita dada wa kazi na kumuagiza amletee maji ya kunywa. Haraka dada huyo akatii agizo, akamletea Miranda jagi kubwa la kioo na glasi kwa pembeni.



    Miranda akafakamia glasi mbili kwa mpigo kana kwamba kilevi, wakati huo Marwa akiwa anamtazama. Angalau akahisi ahueni kifuani mwake.



    Marwa akasafisha koo na kumwambia, "pole. I know how you feel."



    Miranda akatanua lips zake kama mtu anayetabasamu, hakusema kitu.



    "Natumai ile kazi uliyoifanya haitakuwa bure. Naomba Mungu iwe hivyo. Unastahili pongezi sana, ila si bahati kuna muda dunia huwa katili ... si kila saa ipo fair. Na tukio lile linaweza kupita ila kwangu litaacha nyayo maishani mwangu yote. Sitalisahau.



    Si tu kwamba niliona ulivyo mkufunzi kwenye sanaa za mapambano, bali namna ulivyokuwa unahangaika kumrudishia uhai mtu aliye hoi kitandani. It was remarkable!"



    Miranda akaguguma na kusema, "ingekuwa remarkable kama ningefanikiwa. All of that was useless!"



    Kisha akanyanyuka na kwenda zake chumbani. Marwa akabaki peke yake. Akatazama yale maji kwenye jagi kwa sekunde kadhaa kisha akayavuta upande wake.



    Ikapita kama dakika tano. Mara akasikia vishindo vya miguu koridoni. Kutazama akamwona Miranda akiwa amevalia taulo kifuani. Uso wake ulikuwa 'fixed'.



    Akaita, "Marwa." Kisha akaongezea akinena kwa sauti ya chini, "Thanks kwa compliments. Nisamehe kwa maneno yangu."



    Kwa namna moja ama nyingine Miranda alikuwa amejiskia vibaya kumsemesha Marwa vile. Roho ilimsuta.



    Marwa akajibu kwa tabasamu lile nesi ampalo mgonjwa. Miranda akaenda zake na ndani ya muda mfupi Marwa akasikia mtu akijimwagia maji kwa 'shower', naye akaamua kumwagia maji ndani ya mwili wake.



    Akakaa hapo sebuleni kwa muda mpaka akaanza kusinzia. Kwa mujibu wa saa ya ukutani, ilikuwa ni saa tisa usiku.



    Hakujua alikurupushwa na nini, akaamka na kuangaza kisha akajikokota kwenda chumbani alipolazwa Jona, akajimwaga kwa pembeni ya mgonjwa huyo na kuanza kujiongelesha mwenyewe.



    "I am sorry, Jona ... I am so sorry ... bado hatujafanikisha ... hatujafanikiwa."



    Hakunena tena jingine usingizi mzito ukambeba pasi na huruma. Akakoroma kwa uchovu.



    **

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Marwa!" Sauti iliita. Haikuwa sauti ya kike bali ya kiume. Kabla hajaitika, akajaribu kuifikiria ni sauti ya nani, akakosa jibu.



    Ikajirudia tena, "Marwa, amka! ... Marwa!"



    Mara hii alipofikiria kuhusu hii sauti, akagutuka baada ya kupata majibu. Ilikuwa ni sauti ya Jona! ... hapana! ... akakataa ... akatega sikio asikie tena kuhakiki.



    "Marwa!" Sauti ikaita tena. "Marwa!" Ikarudia kuita. Na hapa Marwa akapata kweli uhakika wa kile alichokiwaza. Kweli ilikuwa ni ya Jona.



    Basi kichwa chake kilikuwa kizito sana. Alikuwa bado ana usingizi pomoni kichwani. Ila akapambana kukinyanyua na kufungua macho aone amwitaye.



    Hakuona mtu! Kutazama kando, Jona alikuwa yupo vilevile kama alivyomuacha. Amelala. Dirisha lilikuwa jeupe kuashiria pamekucha.



    Sasa nani alikuwa akiniita? Akawaza. Punde akapata jibu.



    "Marwaa!" Sauti iliita mlangoni. Na sauti hii akaitambua kuwa ni ya Miranda, na si Jona kama alivyokuwa anasikia! Akasonya na kujibandua kitandani. Akaendea mlango.



    "He! Ulikuwa umelala au umekufa?" Miranda akauliza akistaajabu. Alikuwa amevalia gauni refu jeusi lililobana kifua na kumwaga chini. Nywele zake alikuwa amezifichama ndani ya mfuko fulani wa nailoni.



    "Sorry, yani nlikuwa usingizini kweli," Marwa akajitetea.



    "Na mbona ukalala huko kwa mgonjwa badala ya chumba chako?"



    "Aaahm! Unajua nilizidiwa na usingizi, hata huko chumbani nikaona mbali kufika."



    Miranda akaguna, kisha akamwambia ajiandae kwani BC amefika. Itakuwa vema wakiwa wote. Basi Marwa akaenda kuoga na kuosha uso kisha akajivuta sebuleni. Ila usingizi bado ulikuwa unamsumbua. Macho yalikuwa mekundu. Na kichwa kizito sana.



    Alipotazama saa ya ukutani, akaona ni saa nne kasoro asubuhi. Akastaajabu. Si bure Miranda alimuuliza kama amelala ama amekufa.



    Sebuleni alikuwa ameketi BC ndani ya suti ya kijivu na kando yake aliketi Miranda. Mwanamke huyo hakuonyesha dalili ya kuwa na hata lepe la usingizi, hali hii ilimshangaza kidogo Marwa ukizingatia muda waliolala. Ila hakuwa na muda wa kujiuliza sana.



    Mezani kulikuwa kuna seti ya zile test tube Miranda alizozikwapua toka maabara ya Sheng, kwa hivyo ilikuwa rahisi kubashiri mada mezani ilikuwa ni hizo kemikali.



    "They are not the one," (sio zenyewe,) BC alinena akimtazama Marwa. Ilionekana alishateta tayari na Miranda hapo kabla.



    "It seems Sheng did not want to risk. And perhaps, the antidote is not there at all, or it wasnt brought as we thought. But ..." (inaonekana Sheng hakutaka kujiweka hatari. Na pengine, antidote haipo kule kabisa, au haikuletwa kama tulivyowaza. Lakini ...)



    Bwana huyu mzungu akaweka kituo, kisha akakunja nne na kuumwaga mgongo wake kwenye ukuta wa kiti.



    "... In one way or the other, this may be our starting point." (... kwa namna moja ama nyingine, hili linaweza kuwa kianzio chetu.)



    Japo Marwa alikuwa na usingizi kichwani, hakupepesa macho hata kidogo. Alisimamisha masikio yake na kujaribu kukaza macho. Pengine kumsikiliza mzungu akiongea kunahitaji juhudi za ziada kusikia kila analolitamka kwasababu ya ung'ataji wao wa maneno.



    "Though this is not the antidote we want, it can act as a great ingredient we need to make one ... the real one." (Japo hii si antidote tunayoihitaji, inaweza kutumika kama kiungo kikubwa tunachokihitaji kutengeneza yenyewe. Ile ya ukweli.)



    Hapa Marwa akajikuta anatabasamu. Hatimaye ile kazi haikuwa bure, akawaza. Ila kama kuna kitu hakuwa anakijua ni kuwa ndiyo kwanza kazi ilikuwa inaanza! Maana walitakiwa kupata viungo vingine viwili kutimiza antidote inayohitajika kumtibu Jona.



    "So you mean we have to go there again?" (Kwahiyo unamaanisha inabidi turudi tena kule?) Marwa akauliza akiwa na uso wa hofu.



    BC akatikisa kichwa na kusema, "No! Maybe it's somewhere more dangerous than there." (Hapana! Labda ni mahali hatari zaidi kuliko kule.)



    Marwa akamaliza mate.



    "Where is it?" (Ni wapi huko?) Akauliza.



    BC akatazamana na Miranda.





    Kisha wakacheka. Miranda akamtoa hofu Marwa.



    "Anakutania tu. Kuna mahali panapotisha kuliko pa Sheng?"



    "Ni wapi huko anasemea?" Marwa akauliza kwa uso 'serious'. Miranda akatasabamu kwanza, kisha akamwambia, "ni MSD. Medical Store Department."



    "Ghala la dawa la serikali?" Marwa akatahamaki.



    "Ndio," Miranda akamjibu. "Huko ndiko tutapata mojawapo ya dawa tunayoihitaji ili tuichanganye na hii kumtibu Jona."



    Marwa akatulia. Napo haikuwa rahisi.



    "Kama tusipofanikiwa kukipata hiko kitu, basi mambo yatakuwa magumu zaidi. Itatulazimu twende ughaibuni."



    "Sawa," Marwa akatikisa kichwa. "Ni lini tutaenda?"



    "Leo usiku," Miranda akamjibu. "Hatuna muda wa kupoteza, Marwa. Unaona hali ya Jona ilivyo. Sio?"



    Marwa akaafiki. Wakateta kidogo, baada ya muda wakarudi tena kwenye mada yao, mara hii BC akiongea kwa msisitizo.



    Akasema punde dawa hiyo atakapoitengeneza, basi ataitoa kwa awamu na kwa masharti. Anataka kujua kama Jona atakuwa upande wake ama lah! Anahofia kuhangaika 'for nothing'.



    "You two must make sure, he allies. It is the only thing I can afford to hear." (Ninyi wawili lazima mhakikishe, anashirikiana. Ni kitu pekee ninachotaka kukisikia.)



    Miranda akatazamana na Marwa, kisha akarudisha uso wake kwa BC. Akamhakikishia kila jambo litaenda sawa. Hakuna la kutilia shaka. Kwa sasa wazingatie kumkomboa Jona, na kila kijacho kitaangukia panapostahili.



    BC akaafiki akitoa onyo. Hakukaa tena sana, akaaga na kwenda zake.



    **



    "Chai ipo tayari, nakwambia kwa mara nyingine. N'kuletee?" Akauliza Kinoo kwa uso wa kughafirika. Macho yake yalikuwa yanamtazama Sarah aliyejilaza kitandani.



    Ni robo saa sasa tangu amwambia mwanamke huyo kuwa chai ipo mezani, na wala hajasogeza msuli wake hata mmoja. Chai inaelekea kupoa sasa ingali iliandaliwa kwa haraka baada ya mwanamke huyo kulalama njaa.



    "Nimeshakusikia," Sarah akajibu kwa kujivuta. Na badala ya kuamka aende, akajigeuzia upande wa pili.



    Kinoo akatikisa kichwa. Kifuani mwake alijawa na hasira. Aliondoka akaenda zake sebuleni alipoketi na kutazama chai iliyokuwepo mezani. Chapati, mayai manne ya kuchemshwa, soseji tatu, chai ya maziwa.



    Kikombe cha chai hakikuwa kikifuka moshi tena.



    Akasonya. "Tabu zingine bana," akalalama. Akashika tama akiendelea kungoja. Alichoshwa na hizi kero za mwanamke wake, ila hakuweza kuchukua hatua hata moja.



    Lakini cha ziada, hakujua Sarah anateswa pia na msongo wa mawazo juu ya dada yake, Sasha. Alikuwa yu njia panda ya kuchagua aidha asimame na ndugu yake wa damu ama mpenzi, baba wa mtoto wake. Mambo haya yalikuwa magumu. Na hakuweza kuomba ushauri.



    Baada ya muda kusonga, mtu hatoki chumbani, Kinoo akakomba vitu vyake mezani na kuvipeleka jikoni. Akavitumbukiza ndani ya 'microwave' na kuvipasha huku chai akiinywa kama maji.



    Baada ya dakika kadhaa, akavitoa na chai akamimina nyingine, ya moto, alafu akaongozana na vyakula hivyo, vikiwa kwenye trey, mpaka chumbani. Akaviweka kando ya Sarah na kumtaka aamke ale.



    "Kinoo, sijisikii kula."



    "Unamaana gani hujisikii kula?"



    "Nahisi tumbo limejaa."



    "Kwa kitu gani na hujala?"



    Sarah akanyanyuka na kuketi kitako. Akamtazama Kinoo.



    "Muda si mrefu nitakuwa na ugeni. Sasha anakuja. Nadhani nitakula naye."



    Kabla Kinoo hajafunua mdomo wake, hodi ikagongwa huko nje. Wakatazamana na Sarah kisha asiongee kitu, akanyanyuka kuendea mlangoni. Alikuwa ni Sasha. Alivalia blauzi ya zambarau na suruali ya jeans rangi ya bluu iliyokolea rangi.



    Akamsalimu na kumkaribisha ndani. Akaketi sebuleni. Punde Sarah akatoka chumbani na kukutana naye. Walikumbatiana na muda si mrefu wakajumuika kwenye kunywa chai.



    Kinoo akawapa faragha kwa kuaga anaenda dukani.



    "Anakujali sana unh?" Sasha aliuliza kimbea punde Kinoo alipofunga mlango na kupiga hatua kama nne hivi akijiendea.



    Sarah akatabasamu na kuguna. "Kwakweli. Namchosha sana. Ila huu ndiyo muda wa kumsumbua."



    Wakacheka.



    "Hongera sana," Sasha akampongeza. "Wenzako hawapati bahati kama hii!"



    Wakateta maongezi hayo kwa muda wa kama dakika tatu, kisha Sasha akaanza kuelekea kwenye lengo lililomleta hapo.



    "Vipi? Mmefikia wapi kwenye lile swala? Jamaa amefanikisha?"



    "Hapana," Sarah akajibu akitikisa kichwa. "Ameniambia mazingira bado hayajatulia."



    "Mazingira yapi hayo?"



    "Sasha, sifahamu. Muda mwingine akinijibu kama hivyo, nashindwa kuendelea kuuliza sana."



    "Hapana, Sarah!" Sasha akapiga kofi paja lake la kulia. "Unajua nakutegemea wewe. Unataka nife, eti? Upo kwenye nafasi nzuri sana ya kumshawishi. Najua hatotaka kukuudhi ukiwa kwenye hali kama hii."



    Sarah akatikisa kichwa. "Unajua si kazi nyepesi kabisa, sister. Inabidi ufahamu kuwa nikimuuliza sana ama kumshawishi sana, anaweza akahisi kuna jambo. Hufikirii hilo?"



    "Hamna. Unatumia tu akili, Sarah. Laiti, kama isingelikuwa kule makaoni kuna jambo wanalishughulikia kwa sasa, nisingelikuwa hai. Wangeshanimaliza maana muda wangu wa kufanya nililoagizwa, umeshakwisha."



    Sasha akamshika mkono Sarah.



    "Maisha yangu yapo mikononi mwako. Know that. Wewe niingize tu nami nitajua namna ya kuenenda ... na na kuhusu Kinoo, nitafanya kadiri ya uwezo wangu kumweka salama."



    Mara mlango ukafunguliwa akaingia Kinoo. Wakashtuka, ila hawakuteta. Kinoo akapitiliza kwenda chumbani.



    "Unadhani anaweza akawa amesikia?" Sarah akauliza akinong'ona.



    "Hapana," Sasha akajibu. "Tulikuwa tunaongea kwa sauti ya chini. Hawezi akawa amesikia."



    "Una uhakika?"



    "Ndio. Sasa mimi naomba niondoke, tutawasiliana baadae. Ila nakuachia kazi moja, unajua hatujamaliza maongezi yetu, ila hatuna budi kuyakatisha. Mpeleleze na unambie ni nini sasa hivi wanahangaika nacho?"



    "Unamaanisha nini?"



    Sasha akatazama mlango wa chumbani kisha akarudisha macho yake kwa dadaye.



    "Nataka kujua wanahangaikia kitu gani sasa hivi. Lazima kitakuwapo, kimoja ama viwili. Ukivijua, nijuze upesi. Sawa?"



    Sarah hakujibu, Sasha akasimama na kusema kwa sauti. "Niitie basi shemeji nimuage!"



    Sarah akapaza sauti kumwita Kinoo, akafika na Sasha akamuaga, akaenda zake.



    "Sarah," Kinoo akaita muda mfupi baada ya kuketi kitini wakitoka kumsindikiza Sasha. Sarah moyo ukampwita. Alihofu.



    "Kuna kitu unanificha?" Kinoo akauliza. Moyo wa Sarah ukazidi kwenda mbio. Vidole vyake navyo vilianza kutetemeka.



    "Kitu gani nikufiche, Kinoo?" Akauliza akikunja shingo. "Kwanini unawaza hivyo?"



    Kinoo akamtazama Sarah ndani ya kiini cha macho yake kwa sekunde tano asiseme jambo, kisha akanyanyuka na kwenda zake chumbani. Akamwacha Sarah akiwa na mawazo lukuki kichwani.



    Akahisi pengine mwanaume huyo amesikia kile walichokuwa wanaongea. Habari hiyo ikamtisha. Ikamfanya ahofie hata kwenda huko chumbani kukutana naye.



    **



    Saa tatu usiku ...



    "Hatuna muda wa kuzubaisha mambo," alisema Miranda. Walikuwa ndani ya gari pamoja na Marwa. Gari hili lilikuwa dogo, Toyota IST rangi nyeusi.



    "Tunachotakiwa kukifanya ni kufika hapa," akaonyeshea kidole kwenye ramani kubwa aliyoiweka mapajani. "Tutapita njia hii, ni fupi zaidi. Walinzi wapo wanne tu, na hupendelea kukaa maeneo haya ..." Miranda akaonyeshea kidole maeneo matatu kwenye ramani.



    "Na kama ikitokea dharura, basi tutatokea kwa njia ya huku kusini. Ni njia ndefu, ila ina uhakika wa kutoka nje baada ya kukwea makontena yaliyokaribu na kuta."



    Kabla hawajatoka, wakavalia barakoa kuficha sura.



    Lakini waliposonga muda mchache baada ya kutoka kwenye gari waliloliegesha umbali wa kilomita kadhaa toka eneo la tukio, mara likafika gari moja lililotembea kwa mwendo mdogo na kukoma. Halikuwa limewashwa taa.



    Gari hili lilikuwa ni Nissan Patrol rangi nyeupe. Vioo vyake vilikuwa vyeusi usiweze kuona ndani. Punde gari hilo likazimwa na mwanaume mmoja akatoka ndani.



    Akalisogelea lile gari lililowaleta Miranda na Marwa.



    **



    Akalikagua na kisha akarudi kwenye ile Nissan Patrol waliyokuja nayo. Ndani ya muda mfupi wakashuka wanaume wanne, wote walikuwa wamevalia nguo nyeusi kuanzia juu mpaka chini. Nyuso zao hazikuwa za kuvutia, bali kutisha.



    Walikuwa na miili mipana wakionyesha waja wa shari. Na wasiwe na papara, wakaegemea gari lao na kungoja kwanza muda. Mmoja wao, ambaye alikuwa dereva, akatoa simu mfukoni na kupiga.



    Ikaita mara mbili kabla haijapokelewa.



    "Yes, boss. Tumewakuta ... ndio, sawa ... tutahakikisha hatufanyi makosa."



    Kisha akakata simu na kuidumbukiza mfukoni. Alikuwa ni nani huyo aliyeongea naye? Najua bila shaka unadhani ni Sheng. Hujakosea. Ndiye yeye, lakini alijuaje 'move' hii ya Miranda na BC?



    Turudi nyuma kidogo, si mbali sana, bali usiku wa kuamkia leo.



    Baada ya taarifa kufika kwake kuwa wamevamiwa, watu kadhaa wameuawa na pia kusababisha hasara kubwa, Sheng hakufurahishwa kabisa na hili. Alikuwa mwekundu kwa hasira, na kwa mkono wake wa kulia akawamiminia risasi wanaume kumi waliokuwa wanahusika na lindo.



    Ilikuwa awamalizs wote ila jamaa yake akamsihi asifanye hivyo maana itakuwa hasira ya samaki kujitumbukiza mtegoni. Atamaliza nguvu kazi ambayo bado ingemea matunda.



    Lakini haikuwa rahisi hata kidogo kwa Sheng kuwabakizia uhai. Ilibidi mawazo mbadaka yatumike kumshawishi kwamba bado adui anaweza kutiwa mkononi. Hajatokomea kama alivyowaza.



    Kwa kuwa, maadui hao waliowavamia waliiba chemical ndani ya maabara basi ni wazi watakuwa washirika wa Jona wakihaha kumtafutia ahueni. Kwahiyo, moja, Jona yu hai.



    Na basi kama watu hao watakuwa wana ujuzi wa kemia, watatambua kuwa chemical waliyoichukua, haitakuwa suluhisho, bali kipande chake. Kwa hivyo, watataka kukamilisha antidote. Hapo watatafuta kipande kilichokosekana.



    Na kwa mawazo ya haraka, sehemu ya kuipata ni MSD. Watege hapo, watawakamata wahitaji wao. Watu waliowatia hasara kubwa. Watu watakaowasaidia kumpata Jona na kummaliza 'for good'.



    Ila likatoka onyo toka kwenye kinywa cha Sheng. Kama mpango huo hautafanikiwa, kama mpango huo hautamea matunda, basi atamwaga damu za wale wote aliotaka kuwamaliza pasi na simile.



    Hivyo, ndiye wewe uliyetumwa hapa kuhakikisha unafanikisha kazi, ukitambua kuwa roho yako ipo rehani, utafanya mzaha?



    "Itawachukua kama dakika tano tu kufika mahali wanapopataka," alisema Dereva akitazama saa yake ya mkononi. "Kwa makadirio mepesi, baada ya dakika ishirini, inabidi tujiandae. Haijalishi watatokea wapi, ila lazima watarejea kwenye chombo chao cha usafiri."



    Huyo dereva aliponyamaza, alimtazama mmoja wa jamaa aliongozana nao, pasipo kusema neno, jamaa huyo akafungua mlango na kutoa begi jeusi, ndani yake akatoa kifaa fulani cheusi chenye umbo la duara.



    Akasonga karibu na gari la wakina Miranda, akalala chini na kupachika kifaa hicho uvunguni. Alafu akakibonyeza tip! ... tip! Ikasikika sauti kama ya kitu kinachozunguka kwa kasi, kisha ikanyamaza.



    Jamaa huyo akanyanyuka na kurejea garini. Yule dereva akanyoosha mkono wake ndani ya gari, akatoa kifaa kipana mithili ya tablet. Akakibofya bofya mara tatu, mara kiooni ikaonekana ramani, na mahali pale palipokuwa gari la wakina Miranda.



    Kumbe walikuwa wameliwekea 'tracking chip'. Sasa hata gari hilo litakapoenda popote pale wataliona na kulifuatilia vema.



    Ikapita muda kidogo wakakwea gari lao na kusogea mbali kidogo na hilo eneo.





    **



    Ndani ya Bohari ...



    Miranda akatoa ishara ya mkono, Marwa akasimama upesi akimtazama kwa umakini. Mwanamke huyo akachungulia, akaona mwanaume mmoja aliyevalia ovaroli la bluu na kofia, akikatiza.



    Mwanaume huyo alipoyoyoma, Miranda akampa ishara Marwa, wakaendelea kutembea.



    Majengo haya yanayohifadhi dawa, yalikuwa yamepangwa katika mistari kana kwamba bweni. Na kila jengo lilikuwa lina milango miwili, mmoja mbele, mmoja nyuma.



    Miranda alikuwa anafahamu ni jengo gani wanaliendea, walishayavuka mawili, na lile moja kabla ya la mwisho ndilo alilokuwa analitaka.



    Basi wakaendelea kunyata. Walikuwa makini maana si tu walinzi ndiyo waliokuwepo humo, bali pia na baadhi ya wafanyakazi, ambao wengi wao walikuwa wamevalia ovaroli na kinyago cha kuziba pua na mdomo.



    Hawakuwa wengi, ila kikwazo kikubwa kilikuwa ni mataa yaliyokuwa yanamulika huku na kule. Mataa makubwa yenye nguvu ya mwanga.



    "Tutaingia mule ndani," alisema Miranda akinyooshea kidole jengo la mbele. "Nadhani unajua cha kufanya. Kama kawaida, hatuna muda wa kuchomesha!"



    Miranda akachungulia tena, njia ilikuwa nyeupe, akachoropoka haraka akitembea asitoe kelele. Alipofika jengoni, akatazama nyuma. Alikuwa amemwacha Marwa. Upesi akampa ishara ya kumtaka aje.



    Marwa akachungulia, kulikuwa shwari. Akatoka mbio, ila akiwa katikati, akajikwaa na kudondoka chini. Akaguna kwanguvu kwa maumivu maana alidondokea sakafuni.



    Kishindo chake na sauti ya kugugumia, ikamshtua mmoja wa wafanyakazi wa Bohari aliyekuwa amesimama kwa mbali, akiwa kwenye bomba akinawa mikono yake.



    Akatazama na kumwona Marwa akijinyanyua. Akapata shaka. Uso wa Marwa ulikuwa umefunikwa na barakoa. Na hata nguo alizokuwa amevaa, hazikuwa zile za walinzi wala wafanyakazi.



    Basi akasonga karibu na lile jengo, akibeba kila tahadhari pamoja naye. Aliposimamisha masikio yake, akasikia lango likifunguliwa, na pia sauti ya watu wawili wakinong'ona.



    Akapata shaka zaidi. Kwa hofu, asije jitia hatarini zaidi, akachomoka mpaka kwenye kibanda cha walinzi akatoa taarifa kuwa kule ameona wezi, wamevalia barakoa na nguo nyeusi. Wanazama ndani ya ghala pili toka mwisho!



    Ndani ya kibanda hicho cha walinzi, kulikuwa kuna walinzi takribani watatu. Mmoja mwanamke. Mezani kwao kulikuwa kuna bunduki mbili kubwa kuukuu, daftari na virungu viwili.



    "Wana silaha?" Akauliza mlinzi akitoa macho kana kwamba pera.



    "Niliyemwona mikono yake ni tupu," akasema yule mfanyakazi, na pasi kupoteza muda, wakatoka walinzi wawili waliobebelea silaha, wakaongozana na bwana yule aliyewaletea silaha.



    Wakasonga mpaka eneoni.



    Walipofika wakanyamaza na kutumikisha masikio yao. Hawakusikia jambo. Wakatazama mlango, ulikuwa umetenguliwa kufuli. Hapa wakaamini wamevamiwa.



    Basi wakatumia mafunzo yao ya kijeshi, wakazama ndani ya jengo na kutanguliza midomo ya bunduki. Wakaangaza, hawakuona kitu!



    "Wako wapi?" Akauliza mlinzi mmoja akipepesa macho yake makubwa.



    Punde, wakasikia sauti huko nje, ya yule bwana aliyekuja kuwapasha habari,



    "Wale kulee!"



    Basi haraka wakatoka ndani na kwenda huko nje. Yule bwana akawaelekeza, kule mbali kwenye makontena. Ameona kitu huko. Basi walinzi wakakimbilia huko upesi.



    Sekunde tano mbele ...



    "Twende," sauti ya Miranda ikasema kwa kunong'ona. Kumbe hawakuwa kule ambako walidhaniwa wapo. Ulikuwa ni mtego. Walikuwa wapo nyuma ya jengo walilotoka kukwapua walichokifuata, na walitazama wale walinzi wanapoelekea.



    Wakatoka hapo mafichoni, na haraka wakakimbia kwa muda wa sekunde kumi na tano, Miranda akadanda ukuta na kujivuta juu. Akamvuta pia na Marwa wakadondokea nje ya eneo la Bohari!



    Hawakupoteza muda, wakaendea usafiri wao. Wakakwea na kutimka.



    Sekunde kumi mbele ...



    Gizani ndani ya gari, kifaa kikawaka na kuonyesha 'tracking chip' ikiwa inatembea. Dereva akaguna puani. Kisha akasema,



    "Wameshatoka.



    Gari likawashwa na taratibu likaanza kusonga.





    **

    Basi Miranda pamoja na Marwa wakiwa hawana habari yoyote, wakaswaga na chombo chao wakikata mitaa. Na sasa mioyo yao ikiwa misafi maana wameshakamilisha kazi.



    Sasa walikuwa wanatazamia Jona apone, kisha arejee kwenye uwanja wa mapambano. Ni wazi walikuwa wanamhitaji. Ni wazi picha zake enzi za 'uhai' wake zilikuwa zinasumbua akili zao.



    Basi kupunguza kuboreka ndani ya gari, Marwa akanyoosha mkono wake na kuwasha redio kisha akajilaza kitini akikonga moyo kwa nyimbo zilizokuwa zinarushwa.



    Miranda akatabasamu, akamtazama mwanaume huyo na kumuuliza; "ni wapi unakumbuka?"



    Redioni kulikuwa kunarushwa nyimbo za kale ya miaka ta themanini na tisini za mapema.



    "Mbali sanaa!" Marwa akasema akitikisa kichwa. Na huku macho yake akiwa ameyafumba anasikiza muziki kwa hisia.



    "Mbali wapi na wakati wewe ni wa juzi?" Miranda akatania. Marwa akaamka na kumkodolea macho.



    "Wa juzi? Nani wa juzi?" Akauliza.



    "Wewe 'apo wa juzi. Unataka kubisha nini sasa?" Miranda akatamba. "Unamjua mwenye hii gari?"



    Marwa akalaza kichwa kitini kisha akafumba macho akiendelea kula muziki.



    "Si yule jamaa wako wa vibodi?"



    Miranda akacheka. "Sasa huwezi amini yule ni mdogo wangu, tena wa pili!"



    Marwa akaitikia kwa kumridhisha.



    "Nakwamba ukweli. Sikutanii!"



    "Haya, dada. Shikamoo."



    "Ewaa. Marhaba. Sasa umekua."



    "Hivi ..." Marwa akanyanyuka na kuketi vema kitini. "Unataka kunambia tunapeleka gari kwa yule jamaa?"



    "Ndio," Miranda akajibu akitazama mbele. "Umesahau makubaliano yetu?"



    "Aaagh! Nimechoka asee. Kwanini tusimpelekee kesho?"



    "Kesho? Hapana! Siku nyingine hutopewa ukiomba. Tutunze ahadi tuliyoiweka."



    Marwa hakuridhia, ila hakuwa namna. Aliona uvivu kushuka na kuanza kutafuta usafiri mwingine. Kweli lilikuwa ni swala la kuchosha.



    Basi akakaza macho yake saa hii akiwa amegemea kioo. Sijui nini alikuwa anawaza. Macho yake yakatazama 'side mirror' kwa muda mrefu na akili yake ikiwa inawandawanda huku na kule.



    Japo hakuweka mazingatio kiooni, baada ya muda fulani, alitambua jambo. Alitilia shaka kuwa wanafuatwa. Kuna kitu cheupe chaenenda kila wanapokwenda.



    Akakaa vema na kutazama. Akaweka mazingatio. Akatambua kitu hicho cheupe ni gari aina ya Nissan patrol.



    Akasema, "Miranda, ile hadubini yako ipo begini?"



    Miranda akamwambia ndio. Na akauliza anaitakia nini? Marwa hakujibu. Akarukia nyuma na kufungua begi, akatoa hadubini na kuivesha machoni. Akajitengenezea kitini na kubakisha hadubini tu juu. Akatazama.



    Miranda akapata walakini. Akamtazama mwanaume huyo kwa kutumia 'sight mirror' ila hakupata wasaa wa kumzingatia kwa kina maana gari lilikuwa kwenye mwendo.



    Baada ya muda kidogo, Marwa akarejesha hadubini kwenye begi kisha akatazama akiwa na uso wa hofu.



    "Marwa, kuna nini?" Miranda akauliza. Ilikuwa imebakia dakika kama sita tu kuwasili kwa Kinoo. Tayari njia ya vumbi ya kuelekea huko walikuwa wameshaishika.



    Marwa akashusha kwanza pumzi, kisha akamjuza Miranda kuwa wanafuatiliwa na Nissan huko nyuma. Miranda akaangaza, kweli akaliona.



    "Sure?"



    "Yah! Kwa muda mrefu sasa. Ndani kuna wanaume zaidi ya watatu waliovalia mavazi meusi."



    Hapa kichwa cha Miranda kikaanza kuzunguka kama tiara. Nini afanye. Ni wazi sasa endapo akilipaki gari hilo kwa Kinoo, atakuwa ameuza kesi. Na inaweza ikawa huo ndiyo mwisho wao endapo adui wao anatafuta tageti ya kuwamaliza.



    Basi akakanyaga mafuta kwanguvu, gari likaanza kupepea. Akaendesha kama mwehu, ila kwa ustadi na japo njia ni nyembamba.



    Ndani ya muda mrefu akatokea kwenye barabara ya lami, akakata kona kuchubua barabara, akajiweka sawa, akatimka kama kishada. Ndani ya muda mfupi akawa amewapoteza maadui zake.



    Haikujalisha namna gani Marwa alitazama na hadubini, hakuwaona abadani.



    Ila hawakuwa wanajua. Wanaweza kukimbia ila si kujificha. Na maadui zake wakiwa wanatambua hilo, hawakuangaika kukimbizana naye. Kikubwa walichojua ni kwamba tayari Miranda ameshafahamu kuwa wameunga mkia.



    Basi wakiwa wanaendesha gari lao kistaarabu kabisa, wakawa wanatazama kifaa chao namna kikienenda. Mara kinakata kona. Mara kinanyoosha.



    Yule bwana dereva akawaamrisha washike silaha zao vema maana tukio linalofuata huenda likahusisha kutupiana risasi kwani tayari tageti yao imebumburuka. Wale wanaume walipofanya hivyo, basi dereva akaongeza mwendokasi.



    **



    Gari lilitulia tuli na kuzima. Kisha kukawa kimya kana kwamba hamna kitu hapo. Miranda na Marwa wakatazamana. Kisha wakatazama huko nje. Walikuwa wamezingirwa na nyumba zilizotulia kimya na vichaka vya hapa na pale.



    Walidhani wapo eneo salama. Hakukuwa hata na watu waliokuwa wanakatiza. Miranda akamwambia Marwa hapo ni sehemu sahihi kwao kutulia wasome na kutazama mambo yanavyoenenda.



    Endapo kukiwa shwari, basi wanaweza kutoka na kuendelea na safari yao. Na wakitoka hapo, waelekee moja kwa moja nyumbani, si kwa Kinoo tena.



    Basi dakika zikasonga. Hawakusikia wala kuona kitu cha kutilia mashaka. Ila ilipohitimu dakika ya nane. Wakastaajabu watu watano wanasimama wakinyooshea bunduki gari lao!



    Watu hawa walikuwa wamevalia barakoa na nguo nyeusi ti. Miili yao ilikuwa imetuna kwa misuli. Bila shaka walikuwa ndiyo wale jamaa wa Nissan Patrol!



    Kufika hapo waliacha gari lao kwa umbali kisha wakatambaa chini kama nyoka. Ni kuja tu kustaajabu watu wananyanyuka na silaha!



    "Tokeni nje upesi!" Wakaamuru. Miranda akataka fanya ujanja, ila wakamwonya. Wanamwona kila anachofanya. Aweke mikono juu na atoke nje kwa usalama wake kabla hawajamiminia risasi gari likawachakaza na wao waliomo ndani.



    Basi sasa wakina Miranda wakawa hawana ujanja. Wakatoka wakiwa wameanika mikono yao juu. Na kama walivyoamriwa, wakapiga magoti. Wanaume wawili wakazama ndani ya gari lao na kupekua, mmoja wao akatoka na begi la Miranda ambamo humo ndimo kuna dawa waliyotoka iba bohari.



    "Mwisho wenu umewadia. Mlidhani ninyi ni werevu sana, sio?" Akasema jamaa mmoja. Kisha akatazama zile dawa zilizokwapuliwa kule bohari kama uhakiki. Jamaa huyu ni wazi alikuwa ndiye yule dereva.



    Aliporidhika na zile dawa, akazirejesha mkononi mwa aliyemkabidhi kisha akamtazama Miranda na kumwambia,



    "Sasa tutafanya biashara kati yetu nawe. Upo tayari kubadili maisha yako kwa yale ya Jona?"



    Miranda akamuuliza, "una maanisha nini?"



    Basi yule bwana akajibu, "nikabidhi Jona nami nitakuacha na uhai wako."



    Miranda akamtazama Marwa. Marwa akamtikisia kichwa akiwa amekunja uso. Miranda asijali, akarudisha uso wake kwa yule bwana na kusema, "nimekubali!"



    Marwa akapayuka, "Hapana! Hapana, Miranda usifanye hivyo!!"



    Miranda hata hakumtazama. Akarudia kusema kuwa ameridhia.



    "Miranda!" Marwa akaita kwa uchungu. "Mirandaa!" Na mara akazirai.



    "Vipi huyu?" Akauliza yule bwana.



    "Ana matatizo ya kupoteza fahamu akiwa over excited!" Miranda akajibu. Basi mabwana wawili wakambeba Marwa na kumtia garini. Naye Miranda akaamrishwa asimame waelekee huko alipo Jona.



    Wakamtia garini na safari ikaanza. Wakatembea kwa umbali wa kilomita moja, bwana dereva akauliza:



    "Ni wewe ndiye ulimtoa Marwa kituoni?"



    "Ndio, ni mimi." Miranda akajibu na kisha kukaa kimya.



    "Unaonekana mwerevu sana wewe. Na jasiri haswa. Ila umefanya makosa sana maana upande uliopo si sahihi. Hakuna aliyeanzisha vita na Sheng akashinda.'



    Miranda akakaa kimya.



    "Ni nani bosi wako wewe? Na kwanini ulimtoa Jona kituoni?"



    "Sina bosi," Miranda akajibu. "Jona ni rafiki yangu mkubwa, bila shaka hiyo ni sababu ya kumhangaikia."



    Yule bwana dereva akaguna kwa cheko.



    "Unajifanya mjanja sio? ... laiti usingekuwa umeingia makubaliano nami basi ningelikuwa nishakumaliza muda mrefu uliopita. Ila ntaheshimu makubaliano yangu nawe ..."



    Akaendelea kulonga na kulonga, ila sasa Miranda akawa hamsikii tena. Alikuwa amezama fikirani akiwaza mambo kadhaa. La kwanza ikiwa ni namna gani atajinasua.



    Alikuwa amezungukwa na 'mababa'. Na kando yake akiwa amelala Marwa. Kule viti vya mbele walikuwa wamekaa tena wababa wawili.



    Ni wazi mazingira yalikuwa magumu kujikomboa hapa.



    Alipotoka fikirani, akastaajabu kuona tayari wameshafika getini. Gari linasimama.



    "Bila shaka ni hapa bibie?" Akasema dereva.





    Miranda akakosa la kunena. Pasipo kungoja wale wanaume wakashuka toka kwenye gari, dereva akitaka kuwa mtu wa mwisho, abaki garini ili afunge na kuweka kila kitu sawa.



    Kabla Miranda hajashuka akamgusa kidogo Marwa, mara mbili mguuni mwake katika namna ambayo hakuonekana, kisha akasimama kandokando ya mlango akitazama wanaume wale ambao tayari wameshajongea getini, ni yeye tu ndiye anangojewa awafungulie wazame ndani.



    Akakohoa mara mbili, kisha akaanza kujongea. Na kabla hajafika mbali, yule dereva akauliza, "vipi huyu mtu wako?"



    Akimaanisha Marwa. Miranda akabinua mdomo kisha akasema, "nadhani twende tukamtoe kwanza huyo mnayemhitaji kisha tukirejea tutamtoa huyo. Au mwaonaje?"



    Yule dereva akagutuka na jambo. Akiwa bado garini akauliza, "kwanini tusimtoe tukaenda naye kabisa ndani?"



    Miranda akapandisha mabega kupendekeza kwamba lolote ni kheri tu. Kisha akakohoa tena mara tatu na kupigapiga kifua chake kama mtu asikiaye maumivu.



    Wale wajamaa waliokuwa wameshuka, wakajiteua wawili wauendee mwili wa Marwa. Miranda akasimama akitazama kwa makini. Na kwa macho ya wizi, akamtazama mwanaume mmoja aliyekuwa amesimama kando yake.



    Basi katika namna ya ajabu, haraka ya radi, milio miwili risasi ikavuma. Mara wale wajamaa walioenda kumbeba Marwa wakajikuta chini. Na ni ajabu kama walibakiwa na uhai maana walitulia tuli ya maji mtungini!



    Na katika namna hiyo hiyo, yani haraka ya kustaajabisha, Miranda akamsulubu yule jamaa aliyekuwa amesimama naye kwa teke barabara, akajikuta kama mkungu wa ndizi uliochoropoka mgombani! Tih!



    Na mara, "tulia hivyohivyo!"



    Ilikuwa ni sauti ya Marwa. Sura yake ameijaza ndita na akikodoa kutishia amani. Mdomo wa bunduki ameuelekezea kichwani mwa dereva.



    Akampa sisitizo, "ukitingisha hata nywele, basi uhai wako mali yangu!"



    Dereva akaweka mikono juu akiwa amefura. Miranda akarejea ndani ya gari na kisha akachukua bunduki aliyokuwa ameishikilia Marwa. Akambonda dereva na kitako chake, akazirai.



    "Umefanya kazi nzuri sana, Marwa!" Miranda akampongeza. "Umekuwa mwanafunzi mwepesi sana kushika mambo. Najivunia kuwa nawe."



    Basi wasipoteze muda, wakawafungasha wanaume wale ndani ya gari kisha Miranda akamtaka Marwa azame ndani na yeye akamalizane na maadui hao.



    Kazi haikuwa ya kulala! Hawana mahali pa kuhifadhi maiti hizo, na huenda ikaleta kesi. Bila shaka majirani watakuwa wamesikia vishindo vya risasi. Amelenga kuwapeleka mahali salama na kisha ampatie ujumbe murua bwana Sheng.



    "Basi twende wote!" Marwa akabweka. "Ya nini uje kuniacha kwenye tisa na kumi i-karibu?"



    Wasizoze na jamvi, wakakwea na Miranda akatimua chombo mpaka maeneo yapatikanayo makao ya Sheng. Huko akaliweka gari kwenye maegesho yasiyo rasmi, alafu akashuka na kwenda ... baada ya dakika kama tano akarejea na kumwambia Marwa kila kitu kipo sawa japo hakusema alienda kufanya nini.



    Na kabla hawajaliacha gari hilo, mwanamke huyo akaandika baadhi ya maneno kwa 'marker pen' nyekundu kiooni.



    Kisha wakayoyoma eneo hilo.



    **



    Zikapita kama dakika kumi na tano, na jamaa mmoja mrefu mwembamba mwenye asili ya kichina akakatiza eneoni akiwa anavuta sigara kwa hisia.



    Pengine alikuwa anasikia baridi. Sigara yamsaidia kuiondoa. Ila ambacho alikiona sekunde chache mbele yake, nadhani kilimsaidia zaidi kupasha mwili joto.



    Alisita, akatazama. Akapekua na kugundua ile ilikuwa gari ya makaoni. Mbona ipo huku? Akajongea kutazama. Akaangalia na mule ndani. Haki alichokiona kikamfanya aachame, sigara ikadondoka chini.



    **



    "Mkuu, kunaa ... kuna ..." alimwemweta bwana mweusi akijawa na puzo la hofu usoni. Mbele yake alikuwa amesimama bwana Shao, yule jamaa wa karibu na Sheng. Yule jamaa aliyemshawishi Sheng kurusha ndoano kwenye zoezi lingine badala ya kuwamaliza wafanyakazi kwa kuwaua.



    Japo ilikuwa ni usiku mkali, bwana huyu hakuwa amelala. Macho yake yalikuwa meupe na uso wake upo moto.



    Alikuwa ameketi sebuleni. Usiku huu mzima alikuwa anakaa na kungoja kuja kupewa mrejesho wa zoezi aliloliasisi. Akiwa anategemea mambo yataenda bambam.



    Ila kwa namna mtumishi huyu aliyemtoa ndani alivyokuwa anaongea, akaanza kupata shaka. Hata moyo wake ukaanza kuchanganyia kasi.



    Haiwezekani akafeli! Haki Sheng hataelewa.



    "Kuna nini?" Shao akauliza kwa lafudhi yake ya kimandarin. Macho yake madogo alikuwa ameyakodoa.



    Basi mtumishi yule akajikaza na kusema,



    "Kuna ujumbe wako ... kule!"



    Ikachukua dakika tano tu, Shao akawa ameshajua yale yote ya habari za watu walioagizwa. Ya kwamba wameuawa, na wengine wakazimishwa fahamu.



    Na ujumbe akaandikiwa kiooni, "Nenda kaukute ujumbe wako ndani ya kibanda cha mlinzi!"



    Akavuta mafundo mawili ya hewa, na tayari ujumbe huo alioambiwa upo kibandani mwa mlinzi ukawa umewasili mkononi mwake. Kuna mtumishi alikuwa tayari anao mkononi.



    Ulikuwa ni ujumbe wa maneno machache tu ukiwa umeandikwa kwenye kikaratasi kidogo, ukisema, "Tumepata antidote. Mmepata kifo!"



    Shao akaghadhabika haswa. Dharau ya aina gani hii? Ina maana mtu alileta gari hapo, mosi, pili, akazama ndani ya uzio wao na kwenda kwa mlinzi, akaweka karatasi ndani ya droo!



    Alafu ... alafu akatoka salama!



    Shao akajihisi amevuliwa nguo. Na kwa bayana akatambua jambo hili likimfikia Sheng, hakuna atakayekuwa upande salama hata punje! Sheng hana moyo wa kubeba kejeli kiasi hiki! Ni mwepesi wa maamuzi. Ni mwepesi wa kushika hasira.



    Basi bwana Shao akawaita watumishi kumi, akawaagiza wawazike wale watu upesi. Na wale ambao walikuwa amezirai, akawamalizia kwa kuwadunga risasi za kichwa akitumia bunduki yenye kiwamba cha kumeza sauti.



    Akasihi jambo hilo liwe la siri mno. Na akatishia endapo likisikika basi ata-deal na hao watumishi kumi aliowapa kazi. Wahakikishe Sheng hajui lolote lile, na yeye anajua cha kufanya!



    Wakatii agizo.



    Makaburi yakachimbwa, watu wakazikwa kupumzishwa.



    **



    Asubuhi ya saa mbili ...



    "Marwaa!" Sauti nyembamba iliita mlangoni baada ya hodi ya kistaarabu. "Dada anakuita!"



    Marwa akafungua jicho moja na kuangaza. Bado alikuwa ana usingizi pomoni. Kwanini jua linawahi kuchomoza kiasi hiki? Alilalama.



    Hapa karibuni amekuwa akilala robo usiku. Anachoka. Hii haikuwahi kuwa mfumo wa maisha yake hapo kabla. Yeye ni mtu wa kulala mapema, aghalabu huchelewa sana endapo akibanwa na kazi za hapa na pale, tena haizidi saa sita usiku.



    Miranda anawezaje?



    Akajikusanya na kuamka. Akajianda kwa muda mfupi na kisha kwenda sebuleni. Huko akamkuta Bwana BC na Miranda. Sebule nzima ilikuwa imejawa na moshi wa sigara za BC.



    "Pole, naona bado umechoka!" Miranda alimpokea kwa tabasamu. Akashukuru. Akiwa anaketi, naye BC akampongeza kwa kazi aliyoifanya usiku wa kuamkia siku hiyo. Akashukuru tena.



    Basi BC akamwambia kazi imeshakwisha. Ndani ya siku tatu tu, Jona atarejea kwenye hali ya kutia matumaini. Na pasipo kuzidi mwezi, atakuwa amesharejea kuwa Jona kamili.



    Habari hizi zikamfurahisha sana Marwa. Akatabasamu mpaka gegoni. Ila BC akamwonya. Akamkumbusha yale makubaliano ya awali waliyoyaweka.



    Atampatia Jona antidote, ila wataandikishiana makubaliano. Na atakuwa akitoa kidogo kidogo akitazama kama makubaliano yake yataheshimiwa.



    **





    Marwa angelisema nini? Hakuwa na la kusema zaidi ya kuafiki kile ambacho BC alikuwa anamwambia japo ndani ya moyo wake alijawa na hofu. Hakuwa anamwamini kabisa Jona. Alihofia anaweza kiuka vifungu hivyo na kuleta tafrani.



    Misukosuko waliyopitia inatosha. Pengine Jona anaweza akalitambua hilo, alijipa moyo. Basi baada ya muda mfupi BC akaaga na wakaondoka pamoja na Marwa kwa makubaliano kwamba aende kumpatia antidote.



    Walipofika nyumbani kwa BC mwanaume huyo akazama maabara na kufanya kile anachokijua zaidi. Ikamchukua kama robo saa akatoka akiwa amebebelea kemikali ndani ya chupa maalum ya kioo. Akamkabidhi Marwa na kumpa maelekezo.



    Marwa hakupoteza muda, akamuaga na kwenda zake BC akimsisitizia kuwa makini na chupa hiyo iliyobebelea antidote.



    Alipowasili nyumbani, akampatia Jona kiasi alichoelekezwa kisha akajikuta sebuleni pamoja na Miranda.



    Aliketi akiwa ana mawazo kichwani. Miranda alimtazama na kisha kumuuliza, "Marwa, kuna tatizo?"



    Marwa akatikisa kichwa akiminya lips. Hakusema kitu. Miranda akamtazama na kisha akamjongea akiachana na kutazama televisheni.



    Akamwambia, "Najua unachowaza."



    Marwa akamtazama. Bado hakusema kitu.



    "Hata mimi kinanipa hofu kama wewe. Ila natumai kila kitu kitakuwa fresh. Usiwaze sana."



    Marwa akamuuliza, "una uhakika?"



    Akajibu, "Hata kama sina uhakika, ila ya nini kufikiria yajayo ambayo bado hayajafika? Don't worry ..." akamshika Marwa bega. "Kama tumepita kule kwenye bonde la mauti, tutashindwa hapa?"



    Marwa akashusha pumzi. Akauliza, "ila vipi kama Jona hataridhia? BC atammaliza?"



    Miranda akatulia kwanza akiwaza. Kwa kama sekunde tano, akasema, "pengine hiyo inaweza ikawa kazi kubwa kuliko zote tulizozifanya.."



    Miranda akashusha pumzi. "Endapo kama Jona akikataa, tutakuwa njia panda. Tuna kazi ya kumshawishi. Na naamini inawezekana ... yah! Inawezekana."



    Miranda akatabasamu. Naye Marwa akatabasamu.



    "Leo jioni tutatoka out for a dinner. Angalau tukatefresh minds na kujipongeza. Au unasemaje?" Miranda alichombeza. Marwa akajibu kwa kuongeza upana wa tabasamu lake.



    **



    Akiwa anakula chakula cha mchana ndani ya mgahawa mdogo jijini Hongkong, mara akaona askari wawili wakiingia ndani ya mgahawa huo. Mmoja wao alikuwa mrefu, kijana, mwenye nguvu, na wa pili alikuwa mzee kidogo, kofia yake alikuwa ameishikilia mkononi hivyo mvi na uso wake uliochoka ulionekana vema.



    Walinyookea kaunta, wakaskizwa na kisha wakaketi kwa mbali kidogo.



    Wakiwa wanafanya yote haya, Lee alikuwa anawatazama chini ya kofia yake 'kapelo' kwa macho ya kuibiaibia.



    Alikuwa anafahamu anatafutwa na hata huko kwenye vyombo vya habari wamekuwa wakimrusha akihusishwa na kifo cha Chong Pyong, mpiga gitaa maarufu jijini.



    Sasa anaishi kama ndege. Na hata juhudi za kujikomboa kurudi alipotoka zinakuwa ngumu zaidi kwani huko viwanja vya ndege watamtambua na kumweka chini ya ulinzi.



    Basi akaendelea kula, na kwa macho ya kuibia akaendelea kuwatazama wale askari ambao nao muda si mrefu wakaletewa chakula na kuanza kushibisha matumbo wakipiga soga za hapa na pale.



    Akiwa anaelekea kumaliza chakula, mhudumu akaja. Alikuwa ni mama mtu mzima anayejitahidi kujiweka vema. Alikuwa amemletea bili yake ya chakula.



    Akaipokea na kuitazama, kisha akatoa pesa mfukoni na kuiweka mezani. Hakutaka hata kumtazama yule mhudumu usoni.



    Mhudumu akakusanya pesa yake na kushukuru. Akaenda zake. Ila akiwa na shaka juu ya Lee. Kwanini alikuwa ana-behave namna ile? Kwa utaratibu wa kichina, si adabu, haswa ukifanya vivyo kwa mtu mzima.



    Basi yule mhudumu, pasi na kujenga hoja ya kumhisi Lee, akaenda kusema kule kaunta na jikoni namna vijana wanavyobadilika siku za karibuni. Na pasipo kujua basi akaalika macho zaidi kwa Lee. Wakamtazama. Ila hawakujali sana.



    Ilipopita dakika tatu, ndipo kidogo mambo yakaanza kubadilika. Televisheni iliyokuwa imepachikwa ukutani kwa ajili ya kusogezea muda wateja na kuwavutia kwenye eneo hilo dogo, ikarusha matangazo ya kutafutwa kwa Bwana Lee!



    Picha yake ambazo zilikuwa zimedakwa na CCTV nazo zikarushwa, ila napo haikujalisha sana, ni watu wawili ambao walikuwa wamekaa karibu na wale askari ndiyo waliupokea ujumbe huo wa televisheni na kuanza kuujadili.



    Wale askari nao wakaungana nao, wakawa wanne. Na kwasababu eneo hili halikuwa kubwa, basi kila mtu ndani ya mgahawa alisikia vema kilichokuwa kinazungumzwa, akiwamo Lee.



    Napo haikujalisha sana, ila tabu halisi ikaanzia pale ambapo yule mhudumu aliyeenda kuchukua pesa toka kwa Lee kugundua kwa namna moja yule mtu aliyetangazwa kideoni anafanana na Lee!



    Si kwa sura, la! Bali vazi. Lee alikuwa amebadili mavazi yake yote isipokuwa shati lake la ndani ambalo kwa juu alilifunika na koti ambalo hakulifunga zipu.



    Sasa yule mhudumu akaunga taarifa kichwani kwake. Huenda yule kijana amejifunika uso na hataki kutazama watu maana anahofia kugundulika.



    Hakumwambia mwenzake yoyote, taratibu akaenda kwa wale askari, kisha akawatonya akielekezea macho kwa Lee. Lee akagundua hilo.



    Askari wote walitazama upande wake, pamoja na yule mhudumu.



    Akasimama upesi! Kisha akageuka kuuendea mlango kwa kasi. Huku nyuma akasikia sauti ikipaza kwanguvu, ikimwamuru asimame. Hakutii. Akazidi kunyoosha mguu. Akakimbia!



    Wale askari wakatoka nje na kuangaza. Kushoto ... kulia ... kushoto ... wakamwona yule kwa mbali! Yule askari kijana akachomoa filimbi na kuipuliza kwanguvu akimkimbilia Lee.



    Akipiga kelele asimame! Asimame!



    Lee akakimbia kwa kasi sana. Na baada ya punde fupi, akajibana sehemu, kwenye kuta ndogo ya kauchochoro, hapo akabana mpaka na pumzi asisikike.



    Baada ya dakika moja, yule askari akawa amefika eneo hilo. Alikuwa anatembea, anahema kwanguvu, macho yake yanaruka huku na kule kuangaza na kupekua watu.



    Alitilia shaka kiuchochoro, akatupia macho huko, hakuona mtu. Ila kabla hajapita, mara simu ya Lee ikaita mfukoni! Askari akashtuka na kuangaza. Moja kwa moja akahisi mtuhumiwa wake atakuwapo hapo.



    Akajongea akiwa ameshikilia kipochi kidogo cha ngozi kiunoni mwake kilichobebelea bunduki ndogo.



    Alipopiga hatua ya nne, Lee akamuwahi! Hafla! Akampiga ngumi tatu za haraka, askari akapoteza nguvu! Akamchomolea bunduki, na kunyofoa risasi zote kisha akamwachia kasha tupu akiondoka zake kwa mwendo wa wastani.



    Askari akabaki chini akilalama kwa maumivu.



    Lee aliposonga kwa mbali kidogo, akatazama simu yake. Akagundua ni Sheng ndiye alikuwa anampigia. Akastaajabu imewezekanaje? Amepata wapi mawasiliano yake? - ina maana ameshafahamu yuko China?



    Simu ikaita tena. Akasita kupokea. Akajiuliza kwa kama sekunde nne, akakata shauri na kupokea.



    Swali la kwanza, unafanya nini China? Na la pili, kwanini umemuua Chong Pyong?



    Kumbe Sheng alishafahamishwa habari za kutafutwa kwa Lee. Habari zake ambazo zimezagaa ndani ya Hongkong zilishafika mpaka makao ya Wu family, nao wakamjuza Sheng kumhusu mtu wao.



    Sasa Lee akawa njia panda. Mosi, hakuaga. Pili, atasema anafanya nini huko Hongkong? Kufuatilia nyaraka ya Sheng iliyopotea??



    Akajikaza na kulaghai. Akasema amekuja China kusalimia na kujizoeza na mazingira. Ila bwana Sheng hakujali sana hiyo sababu wala hakumpeleleza zaidi, akamwambia kuna kazi anataka kumpatia.



    Na kwakuwa yupo huko China, anaamini ataifanya vema.





    **Lee akatega sikio apate kusikia kazi hiyo, ila pia kwa wakati huo huo akiwa na tahadhari juu ya mazingira yake asije akawa anafuatiliwa na askari.



    Alikuwa anatazama huku na kule. Akatafuta mahali pazuri pa kujishkiza, akatazama chini akifunikwa na kofia. Akaendelea kuteta na simu.



    Basi Sheng akamwambia kuwa huko Hongkong afanye namna, juu ama chini, ahakikishe anaenda makao makuu ya Wu family kukutana na viongozi. Watakuwa na kazi ya kumpatia.



    Lee akapeleleza kuhusu kazi hiyo, ila Sheng hakuwa tayari kumwambia. Akamsisitizia tu aende huko. Maelezo yote atapewa.



    Na kabla hajakata simu akamwambia ahakikishe anafanya kazi hiyo. Na ahakikishe anakwenda kabla siku hiyo haijakoma.



    Yeye ni nani akatae agizo la bosi? Akaweka simu mfukoni na kisha akaanza kufanya utaratibu wa kwenda mahali ambapo ndipo alipokuzwa punde baada ya kuokotwa mtaani.



    Mahali palimpofunza yale yote anayoyajua. Kumpandikiza roho ya unyama, na ujuzi wa kutisha kabisa kabla hajaanza kusafiri kwenda kutenda kazi.



    Ikamchukua masaa matatu na dakika arobaini kuwasili mbele ya geti kubwa lililofunikwa na paa yenye mitindo ya tamaduni za kijenzi za China. Na chini ya paa hiyo, kulikuwa kumening'inizwa kibao cheusi chenye maandishi ya kichina ndani ya rangi ya dhahabu. Yakisomeka kwamba eneo hilo ni milki ya WU DRAGON.



    Lee akatazama sana hapo akikumbuka mbali. Kipindi kile akiwa kijana mdogo zaidi. Akajikuta anatabasamu na kukiri kwamba muda ni upepo. Unakimbia haswa.



    Akiwa hapo, mara sauti ya kichina inapaza. Anatazama sauti hiyo inapotokea na kumwona mwanaume mmoja aliyevalia gauni jeupe za michezo ya mapambano. Kiunoni amefungia mkanda mweusi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Jamaa huyo akamuuliza Lee ni nini anafanya hapo na yeye ni nani? Kabla hata Lee hajajibu, wakatokea tena wanaume watatu toka msituni. Jengo hili lilikuwa limezungukwa na msitu mpana. Na hata Lee akiwa njiani kuja, alikuwa tayari ameshaonekana.



    Watu hawa, wanne kwa idadi, walikuwa kama chambo tu. Wengine zaidi bado walikuwa mafichoni na Lee alilitambua hili. Akatanua mikono yake na kutabasamu.



    Akajitambulisha yeye ni wa Wu familu. Ila wale watu wakatilia mashaka. Wakamtaka athibitishe kauli yake kwa kupambana na mmoja wao maana wanatambuana kwa mitindo na mienendo ya mapigano.



    Basi pambano likazuka, yule jamaa aliyemshtua Lee mwanzoni kabisa akijitolea kupimana ubavu, huku wenzake wakibakia kama watazamaji.



    Wakajitenga bayana, na pambano likaanza! Kijana yule mgeni machoni mwetu, hakuwa haba. Alidumu kwenye ulingo kwa dakika tatu akimpa changamoto kubwa Lee, kwa wepesi wake wa maamuzi na mwili.



    Ila ngoma ya watoto haikeshi, Lee akamtuliza kwa kuisimamisha ngumi yake nzito kandokando ya shavu baada ya kumshambulia kwanguvu mno!



    Yule bwana akatabasamu na kuafiki. Haki Lee ni wa Wu family. Akampatia mkono na kumkaribisha. Ila mara wakashtuliwa na sauti kavu ya kizee ikiwapongeza.



    Kutazama getini hawakuona mtu, bali alikuwapo juu ya ukuta akiwa ameketi kwa kukunja miguu! Ilikuwa ni ajabu kwa namna mtu alivyokaa hapo. Alikuwa ni mzee asiye na nywele kichwani, ila mustachi mwembamba mrefu, na kidevuni ana ndevu nyembamba zilishoshuka mpaka kitovuni. Nywele hizi zote zilikuwa nyeupe kama sufi.



    Alikuwa amevalia joho la mapambano, rangi ya karoti iliyofubaa.



    Kwa jina alikuwa anaitwa Shifoo Nieng, yaani master Nieng. Mkufunzi aliyewalea, na anayewalea vijana wote watokao kwenye 'temple' ya Wu family. Japo ni mzee, kwa makadirio miaka sabini na, ila bado ni mwenye nguvu akitenda kazi yake inavyotakiwa.



    Na kama kuna kitu cha ziada kuhusu yeye, basi ni kumbukumbu. Haikujalisha ametoa vijana mamia kwa mamia, alikuwa ana uwezo wa kuwakumbuka vijana wote kwa sura!



    Hakupata shaka kabisa kumwona Lee. Na alifurahishwa kuona bado kile alichomfundisha kipo ndani yake.



    Akamkaribisha Lee nyumbani.



    **



    Saa nane mchana ... nchini.



    Punde Sheng aliporejea kitini akitoka kwenye jokofu, mlango wake uligongwa mara mbili. Akiwa anatambua ni nani yupo mlangoni, akapaza sauti ya kusafisha koo.



    Mlango ukafunguliwa na Shao akaingia. Kama vile walikuwa wameambizana, walikuwa wamevalia suti ya kijivu wote, ila Sheng yeye alikuwa amechomeka ua dogo jekundu upande wake wa kuume.



    Wakasilimiana, na Sheng asiseme kitu, akamtazama Shao katika namna ambayo Shao alielewa ni nini mwanaume huyo anataka. Si kingine bali taarifa ya ile misheni ya Bohari.



    Shao akasafisha kwanzo koo alafu akakunja nne. Akamwambia Sheng kuwa vijana walienda kutenda kazi waliyotumwa, ila hawakufanikiwa. Hapa kwenye 'hawakufanikiwa' alipaongea kwa sauti ndogo, kisha akamtazama Sheng.



    Akashuhudia Sheng akikunja ndita alafu akajilaza kitini, akibinua mdomo. Shao akabashiri Sheng atakuwa anapapasapapasa droo yake yenye silaha.



    Akajawa na hofu. Moyo wake ulimwenda mbio ila akajitahidi kujikaza. Akaweka mkono wake mezani, akiigiza kujiamini, na kumweleza Sheng kuwa vijana walishindwa kufanya hiyo kazi kwakuwa walengwa wao hawakwenda bohari la dawa kama walivyotarajia.



    Sheng hakusema kitu. Bado uso wake ulikuwa umetindwa na ndita na macho yake ameyafinyanga kuwa madogo zaidi.



    Basi Shao akaendelea kujieleza. Isingeliwezekana tukio kufanyika pasipo watu. Na mwishowe akaomba apewe muda. Atakamilisha kazi.



    Bado Sheng hakusema kitu. Uso wake ulikuwa vilevile. Sasa alikuwa anatisha na usijue nini anawaza kichwani!



    Shao akaendelea kusisitiza ampatie nafasi nyingine. Ila akiwa anaongea, akasikia sauti ya droo ikifunguka. Akanyamaza. Akasema moyoni hayupo radhi kupoteza uhai wake.



    Na kichwani akapiga mahesabu, endapo Sheng akichomoa bunduki, basi atapambania uhai wake mpaka tone la mwisho. Akaweka miguu yake tenge.



    Sheng akauvuta mkono wake na mara juu akaweka faili rangi ya zambarau. Angalau Shao akapata amani. Sheng akafungua lile faili na kisha akatoa wino ndani ya droo. Akaandika jambo, kisha akasukumia faili alipo Shao.



    Akalipokea na kulitazama. Ilikuwa ni HATI YA KIFO. Sheng alikuwa anamtaka atie sahihi kwenye makubaliano ya kumpata Jona, la sivyo atammaliza kwa mkono wake mwenyewe!



    Ila kwanini Sheng alimsitiri Shao? Ni wazi angelikuwa mtu mwingine angelitoka mfu humo ofisini. Kwanini Shao?



    Kwa mara ya kwanza, Sheng alitumia akili dhidi ya hasira. Kumuua Shao kungemuweka matatani na kwa namna iliyo bayana, ingesababisha mgogoro ndani ya familia ya Wu. Hivyo, akataka kuweka mikono yake safi.



    Shao asaini kuridhia.



    Shao akamtazama kwanza Sheng. Wakatazamana kwa kama sekunde tatu, kisha Shao akasema kabla ya kutia sahihi, apewe kwanza kila kinachohitajika kumpata Jona.



    Sheng akamuuliza ni kipi ambacho hana na hali jeshi zima alimkabidhi? Shao akasema bado havitoshi, anahitaji 'access' ya maabara kwa muda wowote ule.



    Hapa kidogo Sheng akasita.







    Akamtazama Shao kwa jicho la shaka na kumuuliza kwanini anataka hilo aliloomba. Shao akamjibu kwa ufupi, amwamini. Sheng akafikiri kidogo kisha akapandisha kichwa chake juu kama ishara ya kuafiki, basi Shao akatia sahihi katika hati ile na kisha akamrudishia Sheng kisha akaaga na kwenda zake.



    Sheng akabaki akifikiri. Hata naye Shao akaenda akifikiri. Alikwazwa na kile kitu. Alifika kwenye makazi yake na kuketi akiwaza haswa. Baada ya muda kidogo akaita vijana wake kumi na kuwaeleza kile kilichotukia.



    Akawaonya na kuwasisitiza ya kwamba sasa misheni ya kumkamata na kumuua Jona si tu ni kazi bali utetezi wa uhai wao. Wafanye kila wakijuacho kuhakikisha wanamtia mkononi.



    Na zaidi akawaambia ana mpango. Ila atawashirikisha muda si mrefu baada ya kukutana na mtu mmoja nyeti kabla siku hiyo haijaisha. Kwa hivyo, akawaambia wale vijakazi wakutane nae majira ya saa nne usiku palepale walipokutania.



    Agizo hilo likapita, watu wakatawanyika. Kwenye majira ya saa mbili usiku, mwanamke mmoja aliyevalia baibui, akaja kwenye makazi ya Shao. Aligonga mlango mara mbili, Shao aliyekuwepo ndani akatazama saa yake ya mkononi, akagundua ndiye mgeni anayemngojea, akatabasamu akinyanyuka. Akauendea mlango na kufungua.



    Alikuwa ni Sasha! Mwanamke huyo akazama ndani na muda si mrefu maongezi ya kiini yakachukua nafasi. Lengo kuu la Shao kumwita hapo mwanamke huyo ni kuwa anaamini kwa namna moja ama nyingine, wakina BC wanaweza wakawa wanahusika na tukio la kukombolewa kwa Jona.



    Japo hakuwa na uhakika, aliona jambo hilo sio la kulipuuzia. Na sasa alikuwa anataka mrejesho wa Sasha amefikia wapi kuomba 'access' ya kuzama ndani ya kundi hilo akitumia mgongo wa dada yake, Sarah.



    Sasha akanywa maji kwanza kupoza koo kisha akamwambia Shao kuwa kazi haikuwa nyepesi hata kidogo. Na kwa namna moja, wakuu wa kitengo hicho wanaonekana kutingwa na kazi kiasi kwamba maombi hayo yamewekwa kwenye mangojeo.



    Hapa Shao akazidi kuamini aidha 'kazi' hizo ambazo zimewatinga zinaweza zikawa zinamhusu Jona. Akang'ata lips zake akitafakari.



    Akanyanyua glasi yake ya kinywaji akanywa mafundo mawili alafu akakuna kidevu chake cheupe.



    Akamwambia Sasha hawana muda wa kupoteza. Inabidi jambo lifanyike kuhakikisha makazi ya watu hao wanaowashuku yanapelelezwa kama yamemuhifadhi Jona. Na kazi hiyo ataifanya yeye, Sasha, kwani atakuwa ana ufahamu wa maeneo hayo.



    Hata alipojitetea hayafahamu, Shao hakumwelewa. Akamsisitizia amtumie dada yake, Sarah, kuyafahamu na kisha afanye kazi hiyo ndani ya siku mbili tu!



    Punde atakapofahamu kuwa Jona amelazwa miongoni mwa majengo hayo, atoe taarifa na wao watalifanyia kazi mara moja!



    Sasha hakukaa, akaenda zake.



    **







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog