*********************************************************************************
Simulizi : Mtuhumiwa
Sehemu Ya Kwanza (1)
Jambazi hatari linalojishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya huko Marekani ya Kusini limefanikiwa kwa mara nyingine tena kuwatoroka askari wa Kikosi Cha Kupambana na madawa ya kulevya cha Marekani (D.E.A) baada ya askari hao kuizingira kambi yake.
Habari za kuaminika zinaeleza kwamba jambazi hilo, Claudio Zapata, liliwatoroka askari hao baada ya mapambano makali ya kutupiana risasi kati ya kundi lake na wana usalama wa D.E.A. Katika mapambano hayo, askari kadhaa walijeruhiwa na wawili waliuawa. Wafuasi wengi wa jambazi hilo waliuawa na wachache waliokuwa wamejeruhiwa walitiwa mbaroni.
Kutokana na hali hiyo, msako mkali wa kimataifa umeanza dhidi ya jambazi hilo hatari ukiongozwa na askari wa D.E.A
wakishirikiana na wana usalama wa FBI ambapo habari zisizo za uhakika mpaka sasa, zinaeleza kuwa jambazi hilo hivi sasa limejificha ndani ya nchi za Afrika ya mashariki.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania alikaririwa akisema kuwa panahitajika ushirikiano wa karibu sana baina ya Serikali ya nchi yake na nchi za Afrika ya Mashariki kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba jambazi hilo linaweza kuwa ndani ya nchi yoyote miongoni mwa nchi za Afrika ya Mashariki . Chanzo chetu kingine cha habari kimedokeza kuwa tayari wana usalama wa FBI na D.E.A wameshaingia nchini Tanzania, kama jinsi walivyokwishaingia nchini Kenya, Uganda na hata kule Rwanda na Burundi katika harakati za kulisaka...
Disemba 15
Ndege kubwa ya Shirika la ndege la Uholanzi, KLM, ilitua kwa madaha kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (K I A) jijini Arusha. Ilikuwa ni saa nne za usiku, kiasi cha wiki mbili kabla ya sikukuu ya Noeli, na abiria wengi waliokuwa wakiteremka kutoka kwenye ndege ile walikuwa wamejawa bashasha zinazoambatana na maandalizi ya sikukuu ile mashuhuri.
Miongoni mwa abiria wale waliokuwa wakiteremka usiku ule alikuwamo Jaafar “Jeff” Bijhajha, mtu mmoja mrefu aliyejengeka kimichezo, hususan mchezo wa kikapu yaani basketball. Kwa mujibu wa hati zake za kusafiria, huyu jamaa alikuwa ni mwanafunzi wa shahada ya pili katika fani ya udaktari wa meno kutoka kwenye chuo kimoja cha kisichokuwa sana huko Uholanzi. Hati zake hizo pia zilibainisha kuwa mtu huyo alikuwa anaitwa Jaafar H. Bijhajha, mtanzania mzaliwa wa Machame huko Moshi, ingawa kabila lake lilikuwa ni Mfipa.
Iwapo angetokea mtu na kuamua kufuatilia ukweli wa maelezo haya, basi angegundua kuwa maelezo hayo yalikuwa ni kweli tupu kwa maana yalithibitishwa na vyeti vyote halali vinavyotambulika kitaifa.
Jamaa alikuwa amevaa suruali nzito aina ya Jinzi yenye rangi ya buluu na viatu vikubwa vya ngozi nyeusi vinavyofanana na vile vya wapanda milima huko Ulaya. Usoni alikuwa amevaa miwani ya kusomea iliyomletea ile taswira ya kitabibu haswa, na kichwani alikuwa amevaa kofia ya kepu au 'Kapelo' yenye lebo ya “Reebok”. Alikuwa amevaa shati zito la rangi ya buluu la mtindo wa drafti-drafti ambalo alikuwa amelichomekea vizuri sana ndani ya suruali yake. Begani alikuwa amening'iniza begi la wastani aina ya Ruksack.
Hakuwa na mzigo mwingine.
Kutokana na kazi zake, mtu huyu mrefu alilazimika kutumia majina mbalimbali kwa nyakati tofauti kutegemea na kazi anayokabiliana nayo katika wakati husika, na kwa kazi hii iliyomleta hapa Tanzania safari hii (ambapo ukweli ndio nchi yake hasa aliyozaliwa), jina lake lilikuwa ni Jaafar Bijhajha, mwenyewe akipendelea zaidi kujitambulisha kama "Jeff Bijhajha".
Ingawa nia ya safari yake ilikuwa ni Dar es Salaam, mtu huyu mwenye ndevu zilizochongwa vizuri na kufanya umbo la herufi "O" kuuzunguka mdomo wake, alikata tiketi ya kuteremkia Kilimanjaro na ndivyo alivyofanya. Azma yake ilikuwa ni kusafiri kwa basi kutoka Kilimanjaro hadi Dar es Salaam siku iliyofuata.
Ukweli ni kwamba mtu huyu, ambaye kutokana na kazi yake ni nadra sana kutumia jina lake la halali alilopewa na wazazi wake kiasi cha miaka thelathini na minane hivi iliyopita, hakuwa mwanafunzi wala hakuwa akitokea Uholanzi masomoni.
Ingawa hati zake za kusafiria zilionyesha kuwa safari yake ilianzia Uholanzi, ukweli ni kwamba safari yake hii aliianzia Marekani, ambapo alisafiri kwa ndege ya kukodi akitumia jina tofauti na hati tofauti za kusafiria zilizobainisha kuwa alikuwa raia wa marekani mwenye asili ya kiafrika. Alisafiri mpaka Ukraine, ambako siku mbili baadaye, alipanda ndege nyingine hadi uswizi kwa zile zile hati zake za kimarekani. Huko akasafiri tena kwa treni akiwa kama Jeff Bijhajha, mwanafunzi kutoka Tanzania mpaka Uholanzi, ambako alifika mida ya saa mbili na nusu asubuhi, na saa nne na nusu asubuhi ile ile alipanda ile ndege ya KLM kuelekea Tanzania, mkoa wa Kilimanjaro.
Jeff Bijhajha alikuwa amekuja Tanzania kwa kazi maalum, na kama kawaida ya kazi zake zote, ambazo watu wanaomtuma huziita “Operesheni”, ilikuwa ni kazi ya hatari, mashaka na mikiki-mikiki isiyosemeka. Ilikuwa ni kazi ambayo uhakika wa kuikamilisha akiwa hai ni mdogo na matarajio ya kuimaliza akiwa kilema ni makubwa...
Kitabu Cha Kwanza:
JAKA
1
Ni usiku mnene. Kiza ni kizito. Mvua kubwa inanyesha.
Watu wamo vitandani mwao, wamelala. Wengine wakiichukulia mvua inyeshayo huko nje kama chachu ya kujumuika na wapenzi au wanandoa wenzao ndani ya nyumba au vyumba vyao. Wengine ndio hawana habari kabisa na yanayotokea, wala hawajui kama kuna mvua inanyesha huko nje. Wengine wanasikia kwa mbali tu kuwa mvua inanyesha huko nje, hawana haja ya kuacha usingizi wao.
Ni ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Katika kiza hiki kinene na mvua hii kubwa, msichana mmoja yuko matatani. Amelowa mwili mzima kwa mvua na amechoka vibaya sana kutokana na mwendo sio tu mrefu bali pia wa mbio. Sauti imemkauka kwa kupiga kelele za kuomba msaada kwa watu, ambao kichwani mwake anajua kuwa wanamsikia, lakini cha ajabu ni kwamba hakuna hata mmoja anayetoka kwenda kumsaidia!
"Jamani nisaidieni mwenzenu nauawa jamani!" Anajitahidi kupiga tena kelele huku akiendelea kukimbia kwa taabu. Hata hivyo, kelele zake zile hazikusaidia lolote.
Na sasa sauti imemkauka, pumzi zimemjaa, na miguu imemlegea kwa kukimbia. Bila kujitambua anapiga mweleka mzito kwenye tope na maji ya mvua. Akiwa pale topeni anageuka kwa wahka kuangalia alipotokea.
Wabaya wake hawaonekani.
Sijui nao wamechoka na kuamua kumuachia?
Hapana.
Sauti zao zinasikika...vishindo vya miguu yao...wanakimbilia upande ule ule aliopo yeye.
Ni wanaume, hawa wabaya wake, na wana nguvu na nia mbaya sana dhidi yake. Wanapata wanne au watano hivi, mwanadada hakumbuki sawa sawa.
"Oi! Yulee...yule pale chini...! Tumempata mshenzi mkubwa...twende !" Mmoja wao anabwata.
"Aaah! Kaumia...! Katusumbua sana malaya huyu!" Mwingine anadakia kwa ghadhabu.
Msichana anainuka, lakini mwili wote unamuwia mzito.
Kimbia. Kimbia tu..! Utakufa ukiendelea kuzubaa hapo...! Watakuua hao!
Anaisikia sauti yake mwenyewe ikimshinikiza kichwani mwake.
Lakini nguvu za kukimbia zimekwisha. Hawezi tena kutetea maisha yake.
Wacha waje waniue tu sasa...hamna yeyote wa kunisaidia!
Bora ufe huku unajitetea kuliko kufa kibwege...jitahidi...kimbia!
Ile sauti yake inazidi kumsisitizia ndani ya kichwa chake.
Mbio!
Msichana anatimua tena mbio. Kwa taabu na kusuasua kwanza, halafu nguvu zinamrudia na anaongeza kasi. Miguno ya ghadhabu na vishindo vya mbio za wabaya wake vinazidi kurindima masikioni mwake kutokea nyuma yake.
Anaongeza kasi zaidi, huku akilia wazi wazi.
Kwa mbele yake anaona kona inayokata kuingia mtaa wa pili kutoka kwenye ule aliokuwako. Anaongeza kasi kuielekea ile kona. Kwa namna fulani anadhani akiifikia ile kona ataweza kuwapoteza wabaya wake. Lazima aifikie ile kona...lazima aifikie.
Nikiifikia tu ile kona tu nitawapoteza hawa jamaa...labda hawatanipata tena...!
Anajipa moyo.
Pumzi zimemwisha, kichwa kinagonga, miguu inagongana magotini...anataka kuanguka...kona bado iko mbali...
Lazima nifike kwenye kona...lazima niifikie...oh, Mungu wangu, lazima...
Anakata kona.
Anajikuta uso kwa uso na mtu mwingine!
Yowe linamtoka anapojipamia kwa kishindo kifuani kwa yule mtu. Nguvu zinamwishia kabisa! Miguu inamtepweta kutokea magotini na anaanguka chini kama gunia tupu lililoachiwa lisimame lenyewe.
Yule mtu anamdaka kabla hajafika chini. Naye amelowa chapachapa. Mgongoni amebeba begi dogo kama mtu anayesafiri.
Mkojo unampita mwanadada.
"Nisamehe kaka yangu...! Chukua chochote utakacho niachie uhai wangu tu tafadhali!" Analalamika na kuomboleza yule msichana hali akiwa ameshikiliwa mikononi mwa yule mtu ambaye amebaki akiwa amemshikilia huku amepigwa butwaa.
Jamaa hapati muda wa kumjibu lolote yule binti, kwani muda huo anawaona watu wengine wanne wakikunja ile kona na kusimama ghafla. Kisha hapo hapo wanajipanga kuwazunguka na kuwasogelea yeye na yule binti taratibu.
Jamaa anawatazama kwa kutoelewa kinachoendelea, bado akiwa amemshika yule msichana aliyekuwa akitetemeka kama bua la muanzi mikononi mwake. Bila ya kuwasemesha wale watu wanne wanawazingira yule jamaa na yule msichana, na jamaa anawatazama mmoja baada ya mwingine.
Mmoja, bonge la mtu, ana upara na madevu mengi mashavuni hadi kidevuni. Huyu amepiga suti ya kitambaa cha jinzi, yaani koti na suruali. Miguuni alikuwa amevaa viatu mithili ya vile vya jeshi na mkononi ameshika rungu refu na bila shaka, zito. Macho yake yanaonekana kung'aa kizani mithili ya yale ya paka anapokuwa kizani. Ni wazi kuwa huyu si mtu mwema. Alikuwa amesimama mbele yao, kiasi cha kama hatua tano hivi kutoka pale yule jamaa mwenye kibegi mgongoni alipokuwa amesimama na yule binti aliye matatani.
Kulia kwa yule jamaa mwenye kibegi mgongoni walisimama watu wengine wawili. Mmoja, kwa haraka tu, aliweza kumuona kuwa ni mdogo kuliko yule upara. Alikuwa amekata nywele zake zote za pembeni na kuachia kibwenzi tu, ambacho nacho hakikuchanwa. Juu alikuwa amevaa kizibao tu, na chini alikuwa amevaa suruali kama ya Upara ila miguuni alikuwa amevaa viatu vya raba.
Mkono wake wa kulia ulikuwa umening'iniza mnyororo mnene.
Yule mwingine alikuwa mikono mitupu, ila alikuwa na msuli mnene. Mikono yake mikubwa ilikuwa imetulia kiunoni pake, uzito wake ameuegemeza kwenye mguu wake wa kushoto ilhali mguu wake wa kulia akiwa ameutanguliza mbele kidogo kama mtu ambaye yuko tayari kushambulia. Alikuwa amevaa 'fulana mchinjo', au maarufu kama 'Singlet', nyeupe iliyomganda mwilini kutokana na kutota mvua. Suruali yake ilikuwa nyeusi au buluu, haikuwa rahisi kutofautisha.
"Oi! Kama unajali maisha yako bora umwachie 'uyo mwanamke!" Alisema kibabe mtu wa nne ambaye alikuwa kushoto kwa jamaa mwenye kibeki mgongoni. Huyu alikuwa ameshika kisu kikubwa kilichotoa mng'ao hafifu katika kiza kile cha usiku.
Lah!
Jamaa mwenye kibegi mgongoni akaanza kurudi nyuma taratibu huku akimweka mgongoni yule msichana, kwa namna ya kumweka mbali na wale watu wabaya. Huku akitetemeka na kubwabwaja vitu visivyoeleweka kwa urahisi, yule binti aling'ang'ania lile begi la 'mkombozi' wake kwa mgongoni, nae akirudi nyuma ili kuongeza umbali kati yao na watu wale.
"Jamani eeh...mie siwajui na nyie hamnijui. Ila ninachojua ni kuwa huyu msichana siwezi kuwaachia..." Jamaa alijibu kwa sauti ya kutetema.
"Unasemaje wewe !?" Kwa ukali Upara alimfokea, na hapo hapo akamvurumishia rungu lake kwa nguvu. Jamaa akabonyea na pigo likapita hewani na kufanya mvumo kama kwamba feni kubwa ilikuwa ikikata upepo, na hapo yowe kali lilisikika kutoka kwa yule muhuni aliyekuwa na kisu kwani lile rungu lilitua sawia kichwani kwake na kile kisu kikamtoka.
Wakati huo huo jamaa akarusha teke kali lililompata Upara kwenye sehemu zake za siri. Upara aliachia yowe kubwa kwa sauti yake mbaya huku akiinama akiwa amejishika sehemu zake za siri. Bila kupenda alipiga magoti matopeni, akigumia kwa maumivu.
Kwa pembe ya jicho lake jamaa aliona mmoja kati ya wale magangwe wawili waliokuwa kulia kwake akimjia mbio, nae akageuka ili amkabili huku akisikia sauti ya yule binti akipiga kelele kuomba msaada.
Jamaa alichelewa kama sekunde hivi katika kugeuka kwake, kwani alikutana na teke kali la uso kutoka kwa jamaa mwenye fulana mchinjo. Nyota zilimtawala usoni yule 'mkombozi' huku akipepesuka na kujigonga kwenye ukuta wa nyumba iliyokuwa pale karibu yao.
Pamoja na vishindo vyote walivyokuwa wanavitoa, bado hakuna hata mtu mmoja aliyetoka nyumbani kwake kuja kutoa msaada au kuchunguza kulikoni.
Mara hiyo yule mwenye mnyororo naye alituma pigo lake. Jamaa aliwahi kuyumba pembeni kidogo na sauti kali mithili ya mbinja ilipita sikioni mwake, mnyororo ukamkosa.
"AAAARRGHHH!" Aling'aka mwenye mnyororo kwa kuona pigo lake limepotea.
Wakati huo Upara akawa anajizoazoa kutoka pale kwenye tope alipokuwa amedondokea magoti. Jamaa akamuona na kumuwahi kwa teke lingine la nguvu sana lililotua katikait ya uso wake. Yowe jingine kubwa likamtoka Upara huku akienda tena chali matopeni, damu zikiruka kutoka puani kwake.
Jamaa hakumwona yule mtu mwenye misuli jinsi alivyomfikia, ila alishtukia akikandamizwa ngumi nzito sana ya tumbo iliyomlegeza miguu na kumtoa upepo wa ghafla kinywani, na kabla hajakaa sawa akabebeshwa ngumi nyingine nzito ya uso, ambayo ilimsukuma hadi ukutani huku akiachia kilio cha maumivu.
Jamaa alijikuta ameshikwa kwa nguvu kutokea nyuma na hakuweza kufurukuta hata kidogo kwani mikono yenye nguvu ilipenya makwapani mwake na kufanya kabali kali kwa nyuma ya shingo yake.
"Unajifanya bingwa sio?" Yule gangwe aliyekuwa na kisu hapo awali alimuuliza kwa hasira huku akijichua sehemu chini ya jicho lake la kulia kwa kiganja cha mkono wake.
Pale pale Upara alikurupuka kutoka pale chini alipokuwa akigaragara kwenye tope na kumshindilia konde zito la mbavu kwa hasira yule jamaa.
Jamaa aligumia kwa uchungu, na yule binti akaachia kilio sambamba na pigo lile kama kwamba amepigwa yeye.
"Mshenzi sana 'uyu!" Kama kwamba lile pigo lilikuwa halitoshi Upara aliongezea na tusi.
Jamaa alijikunja kwa maumivu huku akihisi nguvu zote zikimhama kama jinsi upepo unavyotoka kwenye puto lililotobolewa. Lakini mikono iliyokuwa imemshikilia ilikuwa imeshiba, hivyo akabaki ananing'inia tu.
"Jamani basi tusameheni..." Yule binti aliomboleza, na kuendelea, "...chukueni herini...bangili...pete...na hata nguo mkitaka mtuvue...maisha yetu tu mtuachie ndugu zetu!"
Jamaa alimgeukia yule binti, na hapo akaona kuwa na yeye pia alikuwa amedhibitiwa vilivyo na yule mtu aliyenyoa panki
"Ee jama ee...tufanye kweli tuishie jama...!" Mmoja wa wale watu wabaya alisema, na hapo Upara alianza kumvua pete za dhahabu yule binti kwa pupa, huku wale wenzake wakianza kulivua lile begi lililokuwa mgongoni kwa yule jamaa aliyeibuka ghafla kwenye uchochoro na kupamiana na yule binti aliyekuwa matatani. Lakini ghafla, kabla hawajafanikiwa kulitoa lile begi kutoka mabegani kwa yule jamaa, mwanga mkali uliwamulika wote pale.
"Mko chini ya ulinzi!" Sauti kali ya ki-askari ilisikika.
Si kizaa zaa hicho!
Wale waporaji wakawabwaga chini mateka wao na kuanza kutimua mbio. Lakini kule walipotaka kukimbilia nako mwanga mwingine mkali ukawamulika. Wakati huo huo yule jamaa aliyejitolea kumtetea yule msichana nae akatoka kasi sana kuelekea upande ambao kwake ulionekana kuwa ni salama. Lakini kabla naye hajafika popote alimulikwa na mwanga mkali usoni. Jamaa hakusimama. Alinyanyua mikono yake kuziba uso wake huku akiendelea kukimbia kuelekea kule kule mwanga ule ulipokuwa unatokea. Alichofanya ni kuikimbilia ngumi moja nzito ya uso, iliyompeleka chali kwenye tope.
Yule binti naye akatimua mbio kuelekea kwenye kona ya kutokea kwenye ule mtaa waliokuja nao, ambako ndiko mwanga wa mwanzo ulipotokea huku akipiga mayowe na kupayuka hovyo.
"Tusaidieni askari...tunauawa...watatuua! Heeeelllpp, for God’s Sake, jamaniii!"
"Tulia kama mlivyo! Tuna bunduki na tutavunja mguu mtu yeyote atakayejaribu kukimbia !" Sauti nyingine ya ki-askari ilifoka.
Wale majambazi wanne wakazingirwa mara moja na yule jamaa mwenye kibegi naye akaletwa na askari mwingine tayari akiwa ameshatiwa pingu. Askari wengine wawili walikuwa katika harakati za kuwatia pingu wale jamaa wanne, wakati askari mwingine alikuwa amemshikilia yule msichana kwa kumzungushia mkono wake mabegani kama ishara ya kumhakikishia usalama.
"Haya ndiyo tanayotu-distabu kira siku!" Mmoja wa wale askari alifoka kwa lafudhi ya ki-kurya huku akimtandika kofi kali la kisogo yule muhuni aliyenyoa panki.
Yule binti alishindwa kustahmili alipoona kuwa na yule jamaa aliyejitahidi kumsaidia naye ametiwa pingu kama wale wahuni.
"Afande huyu kaka sio mwenzao...tulikuwa wote katika balaa la hawa mabazazi...alikuwa akinisaidia huyo..."
"Waaacchaa! Mbona na renyewe ririkuwa rinajitahidi kuikimbia serikali, eenh?" Yule askari mwenye lafudhi ya ki-kurya alimkatisha yule binti kwa ukali.
"Kweli jamani...na yeye angeweza kuuawa na hawa jamaa..." Binti aliendelea kutetea.
"Hayo yote tutayajulia kituoni mama, sawa?" Aliingilia kati yule askari aliyemshika yule binti, ambaye ilionekama kuwa ndiye kiongozi wa doria ile.
Binti hakuwa na kauli zaidi.
Muda wote huo yule jamaa mwenye kibegi alikuwa kimya tu, uso wake akiwa ameuinamisha chini. Yule binti alimsogelea na kumshika bega kama ishara ya kumtoa hofu. Jamaa wala hakuonesha kama ameuhisi mkono wa yule binti begani kwake. Aliendelea kuinamisha uso wake huku akifuata ule msafara uliokuwa ukielekea kwenye Land Rover ya polisi iliyokuwa imepaki mwanzo wa ule mtaa.
Yeye na wale vibaka wanne pamoja na askari watatu waliingia nyuma ya ile gari iliyokuwa katika muundo wa “Pick-up”, ambako kulikuwa kumefunikwa kwa turubai. Yule askari aliyekuwa akiongoza ile doria akaingia sehemu ya mbele ya lile gari, yule binti akiwa katikati yake na dereva.
Safari ya kuelekea kituo cha polisi ikaanza.
Yule jamaa aliyejikuta matatani baada ya kujaribu kumsaidia yule binti aliyekuwa matatani aliendelea kuinamisha uso wake chini huku akiwa kimya.
Mvua iliendelea kunyesha kwa nguvu.
____________________
Walipelekwa kituo cha Polisi cha Oysterbay. Huko wale vibaka waliswekwa rumande bila ya kuulizwa lolote, na yule dada pampja na yule jamaa mwenye kibegi wakaingizwa kwenye ofisi nyingine ndani ya kituo kile na kuamriwa waketi kwenye benchi lililokuwa kwenye kona moja ya ofisi ile. Yule askari aliyekuwa akiongoza ile doria aliwaacha mle ndani pamoja na askari wenzake wawili, naye akatoka nje ya ofisi ile huku akivua koti lake la mvua.
Wale askari wawili waliobaki mle ofisini wakamtaka binti atoe maelezo ya kile kilichotokea kule mtaani, na ndipo binti alipoanza kutoa maelezo yake juu ya matata yaliyompata kutoka kwa wale watu wanne waliokuwa wakimfukuza katika usiku ule wa kiza kinene na mvua kubwa.
Alieleza kuwa yeye alikuwa ni msafiri aliyekuwa akitokea Dodoma kuja kumtembelea mjomba wake ambaye anaishi Mikocheni jijini Dar. Basi lao lilichelewa sana kufika Dar es Salaam kutokana na kuharibikiwa huko njiani kiasi kwamba hawakufika jijini hadi saa tano za usiku. Alichukua teksi kutoka pale stendi ya mkoa kuelekea huko Mikocheni.
"Sasa tulipofika pale Kinondoni Biafra nikaona dereva anasimamisha gari na kudai kuwa limeharibika. Kabla hata sijajua la kufanya, wale jamaa wanne wakavamia na wawili wakaingia kiti cha nyuma nilipokuwa nimekaa na wawili wakabaki nje, lakini mi’ niliwahi kuchomoka na kutoka nje. Wale wawili waliokuwa nje wakanikamata na kunipiga makofi, halafu wakanipora pochi langu na kulirushia mle mle ndani ya gari ambako bado begi langu la safari lilikuwamo. Ndani ya pochi kulikuwa na shilingi zangu elfu themanini, kadi zangu za benki na simu yangu ya mkononi...pamoja vitu vingne vidogo dogo na vijichenji-chenji...”
“Sasa huyu jamaa naye alikuwa wapi muda huo?” Mmoja wa wale askari alimuuliza, akimuoneshea yule jamaa mwenye kibegi.
“Ah, hapo huyu bado hajatokea! Sasa tukiwa pale nje ya gari wakaniamrisha nivue viatu na niwavulie vito vyangu vya dhahabu...nilijua kuwa hata nikiwapa kila kitu nilicho nacho, bado wangeniua tu...au wangenibaka. Ndipo nilipopata upenyo tu nikawachomoka na kuanza kukimbia huku nikiomba msaada bila mafanikio...Dah! Ama hakika Dar si mji wa kuishi. Yaani kelele zote nilizopiga hakuna hata mtu mmoja aliyesema aje kutoa msaada!"
"Sasa na huyu jamaa ulikutana naye vipi?" Yule askari alizidi kuhoji kuhusu yule jamaa mwenye kibegi.
Binti alimgeukia yule jamaa ambaye alikuwa amekaa kwenye benchi huku bado akiwa ameinamisha uso wake chini.
"Huyu kaka naye alikuwa na safari zake tu...tukapamiana pale kwenye kona...(hapo binti alitabasamu kidogo huku akimtazama yule jamaa aliyeendelea kuwa kimya huku akiwa amejiinamia) kwanza nilidhani ni mwenzao. Lakini hawa jamaa waliokuwa wakinikimbiza walipotukuta, wakaanza kututishia maisha sote. Hapo ndipo nikajua kuwa huyu kaka hakuwa upande wao...at least yeye alijitolea kunisaidia, na hapo ndipo ngumi zilipoanza kupigwa mpaka nyie mlipotokea." Binti alieleza kwa kirefu.
Baada ya hapo binti alitoa namba ya simu ya mjomba wake ambaye alimtaja kwa jina la Deogratius Salvatori, jina ambalo yule askari alionesha wazi kuwa si geni masikioni mwake.
Binti akaambiwa asubiri. Alishusha pumzi ndefu na kuketi pale kwenye benchi kando ya yule jamaa na kuanza kumtazama kwa makini zaidi.
Jamaa alikuwa na uso wa duara ambao ulikuwa na ndevu ndogo ndogo zilizochomoza kama jinsi zinavyokuwa kwa mtu ambaye amezoea kuzinyoa halafu akakaa siku kadhaa bila ya kufanya hivyo.
Kuna kitu kingine alichokiona kwa mtu yule ambacho hakuweza kukitambua mara moja...ilikuwa kama mvuto fulani hivi. Na jamaa alionekana kama...kama...msomi fulani hivi...yaani hakustahili kabisa kuwa pale...
Kuna kitu cha kushangaza kuhusu huyu mtu...
Alijiwazia.
Tangu wameingia kwenye mwanga wa mle kituoni yule jamaa hajamuangalia hata kidogo, jambo ambalo si la kawaida kumtokea pindi awapo karibu au akipita mbele ya wanaume. Na alipoulizwa jina lake na wale askari hakutaka kujibu. Askari walipotaka kupekua kibegi chake aliking'ang'ania mpaka walipokichukua kwa nguvu na kumchapa makofi.
Muda huo yule askari aliyekuwa kiongozi wa ile doria iliyowaokoa kutoka mikononi mwa wale wanyang’anyi alirudi mle ofisini akiwa amevua koti lake la mvua, hivyo cheo chake kilionekana kwenye mkono wa shati lake la polisi.
Alikuwa na cheo cha Sajenti.
Alimkazia macho yake madogo na makali yule jamaa, kisha taratibu akamsogelea na kusimama mbele yake. Taratibu yule jamaa akainua uso wake na kumtazama.
Kama angepigwa kofi, basi yule askari asingeruka kama alivyoruka kwa mshtuko baada ya kuiona sura ya yule jamaa.
"Wewe!" Aling'aka kwa sauti huku akimkodolea macho yule jamaa.
Jamaa aliendelea kumtazama tu bila ya kusema neno.
"Unafanya nini hapa wewe?" Alifoka kwa ghadhabu yule Sajenti.
Jamaa akazidi kumtazama tu bila ya kumjibu.
"Naongea na wewe ‘apo...ala! We' si unajua kuwa hutakiwi kuendelea kuwepo hapa mjini wewe...? Tena leo hii hii hukumu imepitishwa...ina maana umepinga hukumu ya mahakama wewe?" Aliendelea kubwata kwa hamaki yule Sajenti huku akiwa amemkazia macho yule jamaa, ambaye aliendelea kumkazia macho tu yule askari bila ya kujisumbua kujibu maswali yake.
Makubwa!
Binti akazidi kushangaa.
Mahakama?
Ina maana huyu mtu naye ni jambazi? Lakini mbona amenisaidia? Lakini...mbona haelekei kuwa anaweza kumdhuru mtu..?
"Naongea na wewe 'apo Jaka...nataka jibu!" Sajenti aliendelea kumsaili kwa hasira yule jamaa.
Jaka?
Ina maana huyu jamaa anaitwa Jaka...hadi polisi wanamjua!
Bila ya kukepua jamaa aliendelea kumuangalia yule askari bila ya kusema neno. Kwa hasira yule Sajenti alimrushia kofi la nguvu yule jamaa, na kwa wepesi usiotarajiwa mkono wa kushoto wa yule jamaa ulichomoka na kuudaka mkono wa yule askari kabla haujaufikia uso wake. Hapo hapo Sajenti akatuma kofi la mkono wa kushoto, nalo pia likadakwa na yule jamaa kwa mkono wake wa kulia huku akiwa amemkazia macho yake yule askari.
"Uuuww...Wwiii! Yaani rinaridaka mikono riserikari! Yaani rinarizuia riserikari risifanye kazi yake!" Alibwaka kwa mori yule askari mwenye lafudhi ya ki-kurya huku akimwendea kwa kasi yule jamaa aliyemkamata mikono yule Sajenti, na mara hiyo hiyo walitoka askari wengine wawili na kumvamia kwa nyuma yule jamaa.
Mateke, ngumi, virungu, mbata, ngwara!
Alimuradi mapigo kemkem yalimuangukia yule jamaa kama mvua.
"Basi...basi inatosha jamani, he!" Msichana aliropoka baada ya kuona kuwa wale askari walikuwa wanaendelea kumpa kipigo cha mbwa mwizi yule jamaa.
Jamaa akaanguka chini akiwa amejishika tumbo, huku amejikunja kwa uchungu, damu zikimtoka mdomoni.
"Wewe mama tulia 'apo! Usitufundishe kazi yetu ofisini kwetu saa hizi, umesikia we’? Tutakulaza ndani na wewe vilevile 'a'afu mjomba'ako aje kupiga kelele 'apa...au unabisha?" Mmoja wa wale askari alimjia juu yule msichana.
Binti naye akamjia juu.
"Kazi yenu? kazi yenu gani? Hii ndiyo kazi yenu hii? Kupiga watu hata wakiwa chini ya ulinzi, eeenh? Au hamjui maana ya human rights nyie? Na kama hamjui basi msidhani na sie hatuzijui bwana...tunazijua kiasi cha kutosha kutujulisha kuwa hii sio sahihi...hii sio sahihi kabbisa! Hii ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binada..."
“Shut Up! ” Yule Sajenti alimkemea yule binti kwa ukali.
Binti akabaki amemkazia macho kwa hasira huku akihema kwa nguvu.
Jamaa alibaki akigaragara pale chini akiugulia kimya kimya.
Kama kwamba yule binti hakuingilia kati hata kidogo, yule Sajenti alimuinamia yule jamaa pale chini na kumbana taya zake kwa mkono wake wa kulia na kumgeuza uso wake ili watazamane.
"Tena una bahati sana wewe...maana ilikuwa unyongwe kabisa! Sasa bora usikie ushauri wangu...na sio watu wengi wanaopata bahati hiyo fala wewe...chukua virago vyako uondoke hapa mjini! Uondoke na usionekane tena! Umenisikia wewe?" Sajenti alimkoromea huku akiwa ameuma meno kwa hasira.
Eh! Kunyongwa tena? Huyu jamaa ni nani kwani?
Binti alizidisha idadi ya viulizo akilini mwake dhidi ya yule jamaa.
“Sasa we’ jitie kiburi halafu uone jinsi kitanzi kinavyounyofoa uhai wako mbovu kutoka mwilini mwako, bwege wewe!” Sajenti alimalizia kumkoromea yule jamaa, kisha akausukuma chini kwa nguvu uso wa yule jamaa na kumpigiza sakafuni kisogo chake. Maumivu makali yalimpata kichwani kwani jamaa alifumba macho kwa uchungu na akashika kichwa chake kwa mikono yake yote miwili, akigaragara huku akiinua juu magoti yake akiwa amelalia mgongo pale sakafuni.
"Ai jamaani...Looh!" Alisikitika kwa simanzi yule msichana.
"Koplo!" Sajenti aliita kwa sauti.
"Afande!"
"Piga simu kwa huyo mjomba’ake aje amchukue huyu mgeni wake hapa...upesi!"
"Yes, Sir!"
Kisha yule Sajenti alimgeukia tena yule jamaa, ambaye sasa alikuwa amekaa chini huku ameegemea ukuta akikohoa huku akitikisa kichwa kwa uchungu na masikitiko. Alimwinamia pale chini na kumtomasa kwa nguvu kifuani kwa kidole chake cha shahada.
"Nakupa nafasi ya mwisho bwana mdogo. Sasa ni saa sita na nusu usiku. Nitakulaza hapa kituoni. Asubuhi nakupatia escort ya kuhakikisha kuwa unatoka nje ya mkoa huu...sasa ole wako urudi tena...utajuta kuzaliwa!"
Baada ya hapo jamaa alibebwa juu juu na kutupwa kwenye chumba cha mahabusu.
Yule binti alibaki akitazama hali ile kwa huzuni kubwa. Alitamani amwambie neno lolote la kumliwaza yule jamaa lakini hakulipata neno wala nafasi ya kufanya hivyo.
Muda wote wakati haya yanatokea, yule jamaa wala hakuwa na habari na yeye. Ni kama kwamba yule binti hakuwepo kabisa katika eneo lile.
2
Jaka ndilo jina la yule jamaa.
Jaka Brown Madega ndio jina lake kamili.
Jioni hii alikuwa amejiinamia nje ya nyumba moja ndogo iliyojengwa kwa tope na kuezekwa kwa bati kama jinsi nyumba nyingi nyingine katika eneo lile zilivyokuwa. Kwa mbali aliweza kusikia muziki wa zamani wa kikongo kutoka kwenye moja kati ya vilabu vingi vya pombe za kienyeji vilivyotawala eneo lile.
Nyumba aliyokuwa amekaa yeye ilikuwa ni ya vyumba viwili na sebule ndogo iliyotawaliwa na vigoda vya kigogo na majamvi. Jiko lilikuwa nyuma ya nyumba hiyo ambako pia ndipo kilipokuwa choo cha shimo, mlango wake ukiwa ni kipande cha gunia. Bafu lilikuwa kando ya choo. Kuta nne ambazo juu hazikuezekwa kitu chochote na uwazi ulioachwa kwenye moja ya kuta zile nne kuwa kama mlango ukiwa umefunikwa kwa kipande cha gunia kwa ajili ya ile faragha ya kibinaadamu pindi muogaji atakapohitaji faragha.
Mbele ya nyumba ile kulijengwa ukuta mdogo wa kozi zipatazo nne hivi kwa kutumia vipande vya matofali ya kuchoma. Ukuta huu ulitokea kwenye kona ya kulia ya nyumba ile na kwenda mbele kama hatua kumi na tano hivi za mtu mzima, kisha ukarudi kuelekea kushoto na kuacha uwazi mdogo usawa wa mlango wa mbele wa nyumba ile, halafu ukaendelea na kukutana na ukuta mwingine uliotokea kona ya kushoto ya nyumba ile.
Ni juu ya ukuta uliotokea kona ya kushoto ya nyumba hii ambapo huyu mtu aitwaye Jaka Brown Madega alikuwa amejiinamia, mgongo wake akiwa ameuegemeza kwenye ukuta wa sebule ya nyumba ile, miguu yake akiwa ameikunja kwa mbele, paji lake la uso akiwa ameliegemeza juu ya magoti yake hali akiwa amekumbatia miguu yake kwa kuzungusha mikono yake chini kidogo ya magoti yake. Alionekana kuwa ni mwenye mawazo mazito.
Ni siku nne sasa zimepita tangu alipopambana na ule mkasa uliotokea katika usiku wa mvua nzito ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Baada ya kulala pale kituoni usiku ule, asubuhi na mapema kabla hata mkuu wa kituo kile hajaingia, yule Sajenti aliyekuwa akiongoza ile doria iliyomkumba usiku ule, ambaye Jaka alimjua kama Sajenti John Vata, alimtoa mahabusu na kumpakia ndani ya ile ile Land Rover iliyowabeba usiku uliopita na kuelekea naye mjini. Safari hii aliyekaa katikati ya Sajenti John Vata na dereva alikuwa ni Jaka. Nyuma ya ile Land Rover alikuwako Koplo mmoja mnene mwenye sura ya kibwege sana ambaye alikuwa na bunduki aina ya SMG aliyoipakata mapajani mwake.
"S'jui kwa ni' n'sikurudishe tena mahakani na kukufungulia shitaka la kukiuka amri ya mahakama wewe!" Alisema Sajenti Vata huku akimtupia Jaka jicho la pembeni.
Jaka hakumjibu kitu. Alibaki kimya tu, akitazama mbele wakati safari ikiendelea.
"Utakwenda mpaka Dodoma na utaripoti kwa Kamanda wa Polisi wa mkoa, yaani RPC, ukiwa na barua yako kutoka mahakamani, sawa?"
Kimya.
Bila kujali kwamba Jaka hakujibu kitu, Vata aliendelea, "Koplo Aporinari atakwenda na wewe mpaka Dodoma na kukukabidhi kwa RPC, kisha yeye atakuja kuripoti huku...hiyo ndio maana ya escort, tumeelewana?"
Kimya.
"Na utatakiwa uripoti kwa RPC kila siku asubuhi na jioni kwa siku zako zote unazotakiwa kuwa huko, najua hilo ulishaelezwa zamani tu, labda utake kuleta tena huo upumbavu wako!"
Hakutarajia jibu lolote kutoka kwa Jaka, ambaye aliendelea kutazama mbele tu bila kujibu lolote. Bila kujali yule Sajenti aligeuka kule nyuma alipokuwa yule Koplo na kupitia kwenye kidirisha kidogo kilichokuwa baina ya upande wa dereva na ule wa nyuma ya gari ile aliita, "Aporinari! "
"Afande!" Aliitikia yule Koplo kule nyuma.
"Amri uliyopewa inasemaje iwapo huyu mfungwa atajaribu kutoroka?"
"Kupiga risasi ya mguu kwanza, halafu kuuliza maswali baadaye afande!" Alibwaka yule Koplo kutokea kule nyuma, isipokuwa tu ile 'risasi' aliitamka kama “rithathi”, na 'maswali' ilisikika kama “mathwali”.
"Nzuri! Endelea Koplo!"
"Yes Sir!"
Ilisikika kama “Yeth-Tthaa.”
Jaka alibaki kimya tu na safari ikaendelea.
Jaka na yule Koplo wakapakiwa kwenye basi la Shabiby lililoondoka saa moja kamili asubuhi ile kuelekea Dodoma. Kwa vile hawakutoa nauli, iliamriwa Jaka asimame na yule askari akapatiwa kiti karibu sana na aliposimamishwa Jaka, SMG yake mkononi. Macho yaliwatoka pima abiria waliokuwa ndani ya basi lile kwani halikuwa jambo la kawaida kuona askari akisafiri na silaha wazi mkononi kwenye basi la abiria.
Kabla basi halijaondoka ndipo Jaka alipofungua kinywa chake. Alimshika mkono Sajenti Vata kwa nguvu na kumwambia, "Sajenti...tafadhali sana naomba ukamwambie mama yangu kuwa niko salama...tafadhali sana Sajenti!"
"Oke, Oke...nitamwambia. Lakini na wewe usifanye tena upuuzi kama huu huko. Miaka mitano sio mingi sana, Okay?"
"Oke...Sir!" Alijibu Jaka akiwa amemkazia macho ya ghadhabu yule Sajenti huku akimtemea lile neno “sir” kwa kejeli na ghadhabu.
_________________
Miaka mitano!
Alikuwa akiwaza Jaka.
Miaka mitano akae mbali na mji aliozaliwa na kukulia! Mji ambao alitegemea kuanzia maisha mara baada ya kumaliza masomo yake! Sasa ndoto zake zote hizo zilikuwa zimekatika...hakuna tena mategemeo ya kurudi na kuishi kama alivyozoea na alivyotarajia.
Roho ilimuuma sana.
Kwa nini dunia inamfanyia hivi? Si bora angekufa tu...?
Lakini haiwezekani...siwezi kufa na kumuacha mama yangu mpenzi peke yake.
Alijirekebisha mawazoni akiwa amejikunja pale juu ya ule ukuta mfupi wa matofali ya kuchoma, muziki wa kizamani wa kikongo ukiendelea kusikika kwa mbali kutokea pale alipokuwa.
Lakini hata sasa, Jaka aliendelea kuwaza, mimi ni sawa na mfu tu...
“Ah! Mimi sina makosa. Sijafanya hilo kosa ambalo Mheshimiwa Jaji, pamoja na madigrii yake yote, na busara zake zote, ameona kuwa nimelifanya kiasi cha kustahili adha hii. Cha ajabu ni kwamba watu wazima na shahada za vyuo vikuu mbalimbali wameshindwa kuelewa kuwa mimi sikufanya kosa lile na kwamba nimesingiziwa tu...!” Sasa alijisemea peke yake kwa sauti.
Laiti ningekuwa na pesa za kutosha ningetafuta wakili mwingine wa binafsi nikakata rufaa...
“Sajenti Vata anasema eti ingefaa ninyongwe kabisa! Bora wangeninyonga basi kuliko kunipa hii adhabu ya kifungo cha nje kama wenyewe walivyoiita (alisonya kwa sauti). Eti nisionekane katika mkoa wa Dar es Salaam kwa muda wa miaka mitano! Na katika miaka mitano hiyo nisipatikane na kosa jingine lolote, vinginevyo adhabu itakuwa kali zaidi na eti huenda ikawa hata kifungo cha maisha! (akasonya).” Alijiogelesha kwa sauti.
Hata mama yangu siruhusiwi kuonana naye isipopkuwa kwa barua tu...kibaya zaidi ni kwamba barua zangu zote lazima zipitie kwa RPC wa hapa Dodoma...naye ana wajibu wa kuzifungua, kuzisoma, na akiona zina mashaka naweza nisizipate kabisa! Maisha gani haya....
Alizidi kuwaza kwa simanzi.
Na kama kweli hao wanasheria waliokabidhiwa hili jukumu la kuhakikisha kuwa haki inatendeka katika jamii walijihakikishia kuwa kweli mimi nimefanya hivyo nilivyotuhumiwa kuwa nimefanya, kwa nini basi wasinipe hizo adhabu wanazosema kuwa ningestahili? Kwa nini wasininyonge moja kwa moja au wasinihukumu hicho kifungo cha maisha? Wanaishia kunipa eti kifungo cha nje ya jiji la Dar kwa miaka mitano! (akawatukania mama zao, akasonya).
Akapiga kimya kingine mawazoni.
“Mnhu! Hapa kuna namna tu...si bure. Laiti wangeamua kunisikiliza na kuyafanyia uchunguzi mambo niliyokuwa nikijaribu kuwaeleza!” Alijisemesha kwa sauti. Yaani kama kuna mtu ambaye angekuwa anamfuatilia wakati ule, hakika angeamini kuwa jamaa alikuwa kwenye hatua za mwanzo za kuingiwa wazimu.
Sasa alikunja uso kwa kuvuta lindi jipya la mawazo, akiinua uso wake juu na kuegemeza kisogo chake ukutani, akinyoosha mguu mmoja pale juu ya ukuta, hali mwingine akibaki kuwa ameukunja kama hapo mwanzo.
Lakini...nahisi kuna kitu fulani ambacho kingeweza kunitoa kwenye janga hili bwana...! Kuna ushahidi fulani hivi...sijui nini...Akh! Tatizo ni kwamba toka misukosuko hii ilipoanza sijapata muda wa kukaa nikafikiri lolote kwa kituo...ilikuwa ni vurumai moja baada ya nyingine. Lakini kwa kweli kuna kitu fulani...kipo tu!
Kwa mbali akilini mwake Jaka alianza kuwa na mashaka iwapo akili yake itaweza kufanya kazi tena kama zamani.
"He! Anko! Mbona umejiinamia hivyo!"
Jaka alishtuka kutoka kwenye mawazo pale juu ya ukuta wa nyumba aliyofikia. Akageuza uso wake kumtazama mtu aliyemsemesha na mara ile ile akatabasamu na macho yake yakatoa nuru yake ya uhai.
"Ah! Anko Mnyaga umerudi..." Jaka alisema huku akitabasamu kwa huzuni kama kwamba hakutaka mtu yeyote amsumbue kutoka kwenye mawazo yake, halafu kama kumfanya yule mtu aliyemwita Anko Mnyaga asiendelee kumuuliza maswali zaidi akaongezea, "Sijajiinamia Anko...eem..nilikuwa napunga upepo tu hapa, kumbe nikaanza kupitiwa na usingizi." Hapo hapo akajua kuwa uongo wake haukufanikiwa.
Yule mtu aliyeitwa Mnyaga alimuangalia kwa sekunde kadhaa, kisha bila ya kusema neno akaondoka kuelekea ndani ya nyumba ile. Mkononi, kama kawaida yake, alikuwa amebeba kapu lake la kuendea "kibaruani" kama mwenyewe alivyozoea kusema.
Jaka alimtazama yule mzee mwenye umri upatao miaka arobaini na minane hivi na ambaye bado alionekana imara na mwenye nguvu, akipotelea ndani ya nyumba ile ya matope.
Alimpenda sana yule mzee...tangu utotoni mwake.
______________________
Jaka hakuwa na ndugu yeyote jijini Dodoma wala mkoa mwingine wowote nchini Tanzania. Ndugu yake hapa duniani alikuwa ni mama yake mzazi tu, ambaye wakati ule alikuwa jijini Dar es Salaam ambako ndiko Jaka alipozaliwa na kukulia.
Baba yake Jaka alifariki zamani sana wakati yeye akiwa bado tumboni mwa mama yake. Mama yake alimwambia kuwa baba yake alikuwa mwanajeshi na alifariki akiwa vitani. Aliwahi kuziona picha za marehemu baba yake akiwa katika mavazi yake ya kijeshi, na akakiri kuwa hakika alifanana sana na baba yake.
Ni wakati huo miaka kadhaa iliyopita wakati Jaka akiwa bado mdogo sana, ndipo mzee Mnyaga, wakati huo akiwa kijana tu, alipoletwa nyumbani kwao huko Lugalo kama msaidizi wa nyumbani. Na kutokea wakati huo Mnyaga akawa mlezi wa Jaka. Mama yake Jaka akienda kazini, mtoto Jaka alibaki nyumbani na Mnyaga. Hata alipoanza shule ya watoto wadogo Mnyaga ndiye aliyekuwa akimpeleka na kumfuata shuleni kila siku ili kumpa mama Jaka muda mzuri wa kuwahi kazini na kufanya mambo mengine ya kikazi bila mtoto Jaka kuwa kipingamizi.
Hali hii ilimfanya mtoto Jaka kumzoea zaidi Mnyaga kuliko hata mama yake, hali ambayo iliendelea mpaka Jaka alipotimiza umri wa miaka saba na kupelekwa kuanza darasa la kwanza katika shule ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, ambako pia ilibidi awe anapelekwa na kufuatwa na Mnyaga. Wakati huu Jaka alikuwa tayari ameshaanza kumwita Mnyaga “Anko Mnyaga”.
Mnyaga aliishi na Jaka pamoja na mama yake kwa utii na uelewano mzuri mno, kwa muda mrefu sana. Hata alipoamua kuacha kazi na kurudi kwao Dodoma, Jaka alikuwa na umri wa miaka ishirini kamili. Lakini huo haukuwa mwisho wa umoja wao. Muda wote ambao Mnyaga alikuwa mbali nao, waliendelea kuwasiliana kwa njia mbali mbali za mawasiliano. Mara kadhaa baada ya mama Jaka kustaafu kazi serikalini na kuanza kujishughulisha na biashara, alikuwa akisafiri kuelekea mikoa ya Mwanza na Shinyanga katika biashara zake kwa basi au treni, Mnyaga alijitahidi sana kufika Stesheni ya treni au kituo cha mabasi pale Dodoma ili kumsalimia na kumpa zawadi ndogo ndogo.
Kwa hiyo walikuwa kama ndugu.
Kutokana na hali hii basi, wakati Jaka alipolazimika kuuhama mji wa Dar es Salaam, mama yake kwa uchungu mwingi alimwambia aende Dodoma na akafikie kwa Anko wake Mnyaga ambaye alikuwa anafanya biashara ya kuuza matunda katika soko kuu la Dodoma. Baada ya kufika Dodoma Jaka hakupata taabu kumpata Mnyaga kwani tayari mawasiliano ya simu yalishafanyika tangu awali. Mnyaga alisikitishwa kwa Jaka kufika pale Dodoma katika mazingira yale. Baada ya Jaka kumueleza yaliyomsibu, akioanisha na maelezo aliyokwishapewa na mama Jaka hapo awali kwa njia ya simu, Mnyaga alisikitika maradufu na machozi yakamtoka kwa uchungu. Ndipo alipomkaribisha Jaka hapo kibandani kwake, katika eneo la Makole pale Dodoma mjini.
Alimuomba asijisikie mnyonge bali ajisikie kuwa yuko nyumbani na asiwe na wasiwasi kabisa kumfahamisha pindi atakapokuwa na tatizo lolote pale Dodoma kwani yeye sasa ni sawa na mzazi wake.
Jaka alimshukuru sana yule mzee na leo ndio siku ya nne tangu akaribishwe pale nyumbani kwa Mnyaga.
"Jaka...mbona hukula kile chakula nilichokuwekea pale mezani mwanangu?" Mnyaga alitoka ndani na kumuuliza. Safari hii Jaka alikuwa amesimama akiangalia barabarani huku mikono yake akiwa ameizamisha ndani ya mifuko ya suruali yake, na mabega yake akiwa ameyainua juu kwa kujikunyata kutokana na baridi kali la pale Dodoma.:
"Sijisikii kula kabisa leo Anko." Jaka alimjibu bila kugeuka, jibu ambalo lilikuwa ni kweli tupu.
"Na lini unategemea kujisikia kula?" Mnyaga alimuuliza huku akimkazia macho kwa ukali. Tangu amefika Jaka amekuwa akikataa kula kwa sababu mbali mbali naye amekuwa akimlazimisha na kumbembeleza ili ale.
"Labda nitakula jioni..."
"Jioni si ndio hii...kuna jioni gani tena?"
"Nilikuwa namaanisha baadae kidogo, Anko."
"Sikiliza Jaka...kula kwako ni muhimu sana hivi sasa. Wewe una mawazo mengi ambayo yanakula sana mwili wako...usipokula chakula utazidi kuihatarisha afya yako na mwisho wake utakufa..."
"Potelea mbali hata nikifa! Kwani kuna tofauti gani tena sasa?" Jaka alidakia kwa sautti ya ukali. Mnyaga hakubabaika. Alimjibu kwa upole huku akimtazama usoni kwa macho makali.
"Sidhani kama mama yako amekuagiza uje huku ili ufe, Jaka."
"Wewe Anko kwako ni rahisi kusema hivyo kwa sababu hayajakukuta yaliyonikuta mimi..."
"Mimi yamenikuta kama jinsi ambavyo mama yako anavyoona yamemkuta...matatizo yako Jaka, ni yetu sote! Cha kufanya ni kusaidiana kuyakabili matatizo haya na sio kuongezeana mengine juu yake!"
Jaka hakuweza tena kuendelea kumjibu yule mzee, kwani alimheshimu sana.
"Samahani Anko...nilikuwa sijui nasema nini..."
"Naelewa Jaka. Huu ni wakati mgumu sana kwako...ila inabidi ukabiliane na hali hii kiume. Unakumbuka nilikwambia nini wakati ule bado uko mdogo? Siku uliporudi shuleni unalia njia nzima baada ya kupigwa na mwenzako?"
Jaka alimtazama yule mzee kwa muda bila ya kusema neno, kisha uso wake ukachanua kwa tabasamu pana.
"Hah! Yaani Anko bado unakumbuka mambo hayo?" Alimuuliza, halafu akacheka sana kwa sauti na Mnyaga nae akacheka huku akimshika mkono na kumuongoza ndani.
"Twende tukale bwana." Alimwambia, na bila kupinga Jaka akaelekea ndani huku akiwa ameshikana mikono na Mnyaga. Kichwani mwake alikuwa akiyafikiria yale maneno aliyokumbushwa na Mnyaga. Zamani sana Mnyaga alimwambia maneno yale, lakini leo aliona ni kama jana tu wakati Mnyaga alipokuwa akimwambia maneno hayo...
Mwanaume kamwe hakabiliani na adui yake kwa machozi, bali hukabiliana naye kwa ngumi na hupigana mpaka mikono yake itumbukie mwilini mwa adui yake...na hapo mwanaume huanza kutumia miguu...
Jaka alikumbuka kuwa siku iliyofuata baada ya kuambiwa maneno yale na Mnyaga, alimtafuta yule mtoto aliyempiga na kumtaka wapigane. Mwisho pambano yule mtoto aliondoka analia akiwa na nundu kubwa kichwani huku akiacha meno mawili kwenye uwanja wa pambano. Jaka alirudi nyumbani akiwa mshindi.
3
Wiki mbili zilikuwa zimeshapita tangu awasili pale Dodoma, na amekuwa akienda kuripoti kituo cha polisi kila asubuhi na kila jioni bila kukosa, ikiwa ni sehemu ya masharti ya kifungo chake kile cha miaka mitano nje ya jiji la Dar. Siku zote anapokwenda kuripoti humkuta askari mmoja mwenye nguo za kiraia katika chumba maalum alichoelekezwa kuwa ndio awe anaenda kuripoti.
Jioni hii alipoenda kuripoti amemkuta askari mwingine kabisa. Huyu alikuwa amevaa mavazi ya kiaskari, na si ya kiraia, ambayo kwa kweli yalikuwa yamemkaa vyema. Mabegani mwake alikuwa ana nyota mbili na hivyo Jaka alihisi kuwa alikuwa ni Luteni, ingawa hakuwa na uhakika. Kwa muda alibaki akimtazama yule askari bila ya kusema lolote.
Sura ya huyu bwana haikumvutia Jaka hata kidogo, kwani alionekana kuwa ni mtu mpenda shari na mkorofi.
Hakukosea katika dhana yake hiyo.
"Wewe ndio Jaka?" Aliuliza yule bwana huku akimtazama kwa dharau. Jaka hakufanya haraka kumjibu. Alikuwa akiendelea kumzama kwa makini.
Sura yake pana haikuwa nzuri. Macho yake makubwa yalikuwa mekundu na yaliyotokeza nje kama ya mtu aliyekabwa, na Jaka alijikuta akijiuliza iwapo macho yale yaliweza kufumba pindi mtu yule alalapo, kwani ngozi zilizo juu ya macho yale zilionekana ndogo kuliko macho ambayo zilitakiwa ziyafunike.
Pua yake pana na fupi ilimtambaa karibu uso wote na chini ya pua ile kulikuwa kuna ndevu zilizolala juu ya mdomo wake wa juu na kufanya mustachi mnene.
Midomo yake ilikuwa minene na mipana, na kutoka kwenye kona ya kushoto ya mdomo wake huo kulitambaa kovu moja baya lililokwenda hadi chini kidogo ya taya lake la kushoto. Wazo jingine lililomjia Jaka ni kwamba hapo nyuma kuna mtu alijaribu kumpanua mdomo wake huo kwa kisu kikubwa na kikali sana.
Moyoni alimpongeza mtu huyo.
Kidevu cha yule bwana kilikuwa kimejaa mapele yaliyotokana na kunyoa ndevu zilizotaka kukitawala kidevu kile, mapele ambayo yalitapakaa chini ya kidevu hicho hadi sehemu ya mbele ya shingo lake nene.
"Naongea na wewe 'apo...! We' ndio Jaka?" Alifoka kwa ghadhabu yule askari baada ya kuona kuwa Jaka hakumjibu haraka kama jinsi yeye alivyotaka. Jaka aligundua kuwa pindi afokapo, pua ya yule askari hutanuka na kuwa pana zaidi, hivyo kufanya nywele ndogo za ndani ya pua ile kutokeza nje.
"Yes Sir...mimi ndio Jaka...nimekuja kuripoti." Hatimaye alimjibu.
Yule bwana alimtazama kwa makini, kisha akaitazama picha ndogo saizi ya pasipoti iliyokuwa kwenye faili lililokuwa mbele yake pale mezani, faili ambalo lilikuwa limeandikwa jina la Jaka juu yake na chini ya jina lile kulikuwa na neno moja tu lililoandikwa kwa wino mwekundu, “Murder”, yaani "Mauaji".
Mwili ulimsisimka Jaka kwa kuliona neno lile likinasibishwa na jina lake pale kwenye lile faili namna ile.
"Mimi naitwa Inspekta Osman Mgunya, na nimekuja Dodoma maalum kutoka Dar es Salaam kwa ajili yako wewe!" Jamaa alimkoromea kwa sauti nene ya kukwaruza. Jaka akapigwa butwaa. Alibaki akimtazama tu, asijue la kusema.
“Kwa hiyo ukae ukijua kuwa nitakuwa nikifuatilia nyendo zako kwa makini sana hapa Dodoma.” Jamaa lilimwambia na kutulia kidogo, kisha likaendelea, “…na nikikupata na kosa tu...” Likapitisha kidole chake cha shahada kutoka upande mmoja wa shingo lake pana hadi mwingine, likikifananisha kidole chake na kisu, huku akitoa sauti ya “Krrrr!” kumaanisha kuwa atamchinja.
Jaka hakuelewa alimaanisha nini kwa kitendo kile.
Alimtazama machoni yule bwana kabla ya kumuuliza kwa upole.
"Kwa nini?"
Osman Mgunya alibaki kimya kwa kama dakika moja hivi huku naye akimtazama Jaka machoni, kama kwamba aliyekuwa akijishauri iwapo amjibu au amchape makofi. Katika dakika moja hiyo Jaka naye hakupepesa wala kukwepesha macho yake kutoka kwa yule askari mwenye sura ya kuchukiza. Hakuna kilichosikikandani mle ndani zaidi ya sauti za pumzi zao tu wakihema, mithili ya majogoo yaliyopigana na kugundua kuwa yote yalikuwa nguvu sawa.
Hatimaye Mgunya aliamua kujibu swali lile. Huku bado macho yao yakiwa yamefungana, alimwambia kwa sauti ya kunong'ona ili kusisitizia uzito wa maneno yake.
"Kwa sababu imegundulika kuwa umepewa adhabu ndogo kuliko kosa ulilofanya Jaka. Na kazi yangu ni kuhakikisha kuwa unafanya kosa jingine moja tu, basi! Umeelewa?" Kisha bila kusubiri jibu kutoka kwa Jaka, alimsukumia Jaka kwa nguvu kile kitabu cha kusaini kuwa alikuwa ameripoti pale kituoni jioni ile.
"Saini hapo na upotee upesi machoni mwangu, muuaji mkubwa wewee!" Alimkoromea kwa hasira.
Taratibu Jaka alichukua kalamu iliyokuwapo pale mezani, akasaini sehemu aliyotakiwa kusaini, kisha akailaza juu ya lile daftari ile kalamu. Baada ya hapo aliinua macho yake na kumtazama tena yule askari mbaya, na bila ya kusema neno lolote aligeuka na kutoka nje ya chumba na hatimaye, jengo lile.
___________________
Imegundulika kuwa adhabu uliyopewa ni ndogo kuliko kosa ulilofanya...
Maneno hayo yalijirudia tena na tena kichwani kwa Jaka usiku ule akiwa amelala chali kitandani kwake. Kwa usiku ule hakuwa na mategemeo ya kupata usingizi, kwani alikuwa amezongwa na mawazo mengi sana na yote hayakuwa mazuri hata kidogo.
Yaani... kweli Mungu anaweza kuangalia tu jinsi waja wake tunavyofanyiana unyonge hapa duniani bila ya kuingilia kati hata kidogo...? Na kisha baada ya yote haya bado tena watu tunakufa na kurudi kwake ili tukahukumiwe kutokana na matendo yetu hapa duniani...! Sasa sisi tunaoanza kupata hukumu hapa hapa duniani tukienda huko tutakuwaje...?
Jaka aliendelea kuwaza kwa unyonge huku bila ya yeye mwenyewe kujua, machozi yakimtoka.
Kwa mbali, ndani kabisa ya akili yake alipitiwa na ile hisia kuwa kuna kitu ambacho kingeweza kumtoa katika janga lile la kusingiziwa...
Lakini ni kitu gani...?
Hakujua ni muda gani ulipita akiwa amejilaza chali pale kitandani akiumiza akili kutafuta njia ya kujikwamua kutoka katika janga lile, bila mafanikio. Alipoanza kusinzia, majogoo yalikuwa yakiwika huko nje.
_____________________
Anakimbia. Pumzi zimemjaa. Amechoka kupita kiasi. Lakini hawezi kusimama.
Lazima akimbie...na anaendelea kukimbia, tena kwa kasi. Hajui anamkimbia nani au anakimbilia wapi, analojua ni kwamba ni lazima akimbie. Anatazama mbele...Kiza. Haoni kitu. Ni kiza totoro! Radi inapiga na mwanga mkali wa radi ile unamuonesha njia kidogo naye anaifuata mbio.
Mvua kubwa inamnyeshea. Moto. Maji ya mvua ile ni ya moto! Yanamuunguza kichwani, mgongoni, mikononi na mwili mzima. Anapiga kelele kwa maumivu ya kuunguzwa na yale maji ya moto huku anakimbia. Radi imetoweka na kiza kimetawala tena, anatumbua macho ili aone vizuri, na maji ya moto ya mvua ile yanamuingia machoni. Ananapiga ukelele mkubwa...haoni mbele.
Ghafla mwanga unajitokeza kwa mbali sana mbele yake. Anaukimbilia. Anaona anaufikia haraka sana ule mwanga...hapana ule mwanga nao unamsogelea. Anasimama ghafla. Ule mwanga ni taa ya Chemli. Msichana mzuri ameishika chemli ile kwa mkono wake wa kulia na kwa mkono wake wa kushoto ameshika mwavuli ambao amejifunika kujikinga na mvua ile ya ajabu. Msichana wa ajabu...
Nuru imemzunguka msichana yule mwenye uzuri wa kuvutia.
Malaika...?
Amevaa gauni refu jeupe na jepesi sana ambalo linaonesha mwili wake wote...hakuwa amevaa nguo yoyote nyingine chini ya gauni lile jepesi. Anatumbua macho kumshangaa yule msichana wa ajabu.
Anayatazama matiti yake yaliyochomoza mbele kiasi cha kutishia kuitoboa nguo ile laini. Kiuno chake chembamba kilitenganisha vizuri sehemu iliyokuwa imebeba matiti yale na sehemu ya chini ya mwili wake wenye kushawishi. Mapaja yake yalikuwa yamejaa vizuri na miguu yake ilikuwa ni yenye kuvutia hasa kwa vile alivyokuwa hakuvaa viatu. Wazo jipya linagonga akilini mwake.
Ni jini...?
Woga mkubwa unamshika. Anataka kugeuka na kukimbia kurudi kule alipokuwa anatokea, lakini macho ya yule binti yanamkataza...anayatazama tena macho yale...
Yule msichana anainama na kuiweka chini ile taa, kisha anainuka huku akiwa amemnyooshea mkono wake wa kulia kwa ishara kuwa amsogelee. Bila ya kujitambua anamsogelea yule msichana wa ajabu. Anapomfikia, yule binti anampa ule mwavuli naye anaanza kunyeshewa na ile mvua ile ya moto. Anauchukua ule mwamvuli na kumsogelea zaidi yule msichana. Wanajifunika pamoja kwa mwamvuli ule, msichana anaichukua ile taa na kwa pamoja wanaanza kuondoka kuelekea kule kule alipokuwa anapakimbia hapo mwanzo.
Mara yule msichana anasimama na kuanza kumuangalia usoni kwa huzuni huku akitiririkwa machozi. Anashangaa. Haelewi, na punde yule msichana wa ajabu anaangua kilio kikubwa na cha uchungu mno!
Anataka ambembeleze lakini hawezi...ananyoosha mkono wake ili amshike lakini mkono wake unamuwia mzito sana.
Woga unamzidi maradufu!
Na mara hiyo anasikia sauti kali ikimwita kwa jina lake kutoka kule walipokuwa wakielekea. Anainua uso wake kutazama ni nani anayemwita. Anamuona Osman Mgunya akiwafuata pale walipokuwa kwa mwendo wa haraka huku amekunja uso kwa ghadhabu zisizo kifani, mkono wake wa kulia ukiwa umeshika upanga mrefu ambao mara ile alipoinua uso wake kumuangalia yule mtu tu ule upanga ukatoa radi kubwa...upanga wa radi !
Osman Mgunya alikuwa akimwendea mbio huku akimwita jina lake mfululizo... Jaka!....Jaka!....Jaka!.....Jaka !
" ... Jaka ! Jaka...! Jaka...amka, utachelewa kuripoti kituoni....saa mbili kasoro sasa!"
Jaka alishtuka kutoka kwenye usingizi na ndoto ile ya ajabu.
Kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka. Alifumbua macho kisha upesi akayafumba pale mwanga wa jua ulipompiga moja kwa moja usoni. Alijikinga uso wake kwa kiganja chake kutokana na mwanga wa jua lile na kuyafumbua tena macho yake taratibu.
Mnyaga alikuwa amemwinamia hali mkono wake wa kulia ukiwa begani kwake, akimtikisa.
"Anko leo umelala sana...nimeanza kukuamsha kitambo!" Mnyaga alimwambia.
" Unnnhh...aaankhh...nilikuwa naota....saa ngapi sasa?" Jaka alibwabwaja huku mwayo ukimtoka.
"Saa mbili kasoro kumi sasa!" Mnyaga alimwambia, naye akakurupuka na kuketi kitandani.
Jambo la kwanza lililomjia akilini mwake baada ya usingizi kumtoka ni kwamba sura ya yule binti aliyemuota kwenye ile ndoto haikuwa ngeni akilini mwake. Alikuwa na hakika kabisa kuwa ilikuwa ni sura ya mtu anayemjua...alishapata kuiona sura ile kabla ya ndoto ile...
Tatizo ni kwamba hakuweza kukumbuka ni wapi au lini. Alijiuliza sana ni nini maana ya ndoto ile katika wiki yote ile bila mafanikio. Jambo pekee alilokuwa na uhakika nalo ni kwamba yule askari aliyejiita Osman Mgunya hakuwa na nia nzuri kabisa naye. Hilo halikuwa na shaka hata kidogo akilini mwake.
______________________
Miezi minne baadaye alikuwa ameisahau kabisa ile ndoto, naye akawa ameshazoea hali ya pale Dodoma. Mara kwa mara alikuwa akienda sokoni pamoja na mzee Mnyaga na kumsaidia katika biashara zake za matunda. Katika moja ya siku hizo alipatwa na msukosuko ambao ulikuwa ni mpango wa Osman Mgunya katika kuhakikisha kuwa Jaka anafanya kosa litakalompa fursa ya kumchukulia hatua kisheria.
Siku hiyo alikuwa akiuza zabibu pale sokoni na mara wakaja jamaa wanne walioonesha nia ya kutaka kununua zabibu. Jaka alijaribu kuwakaribisha kwa uchangamfu na kuanza kuwatajia bei za mafungu mbalimbali ya matunda yale aliyoyapanga vizuri pale mezani.
Cha ajabu ni kwamba baada ya kukaribishwa, mmoja kati ya wale jamaa alichukua chana moja ya zabibu na kuikamua yote pale juu ya meza huku wale wenzake wakicheka kwa dharau na kebehi. Mara moja Jaka akabaini kuwa wale jamaa walikuwa wametumwa. Akaamua kunyamaza kimya.
"Vipi, mbona unagwaya wewe...huna ubavu nini?" Aliuliza kwa kejeli mmoja kati ya wale jamaa.
Kabla Jaka hajajibu, jamaa mwingine akamchapa kofi kali la uso. Kwa ghadhabu Jaka alitaka kumrukia yule jamaa lakini akawahi kujizuia. Mwingine akachukua chana mbili za zabibu na kuzitupa chini. Jaka akatoka nyuma ya meza yake na kwenda kuziokota. Vile anainama tu alipigwa ngwara kali sana kwa nyuma na kuanguka chali pale chini, na wale jamaa wakaendelea kumcheka kwa fujo.
Watu waliokuwa pale sokoni wakaanza kujaa huku wengine wakitaka kujua kulikoni.
Mara hiyo akatokea mzee Mnyaga, ambaye kwa hasira aliwafokea wale jamaa. Mmoja wa wale jamaa alitaka kumletea jeuri na Mzee Mnyaga akamtwanga konde zito lililompeleka moja kwa moja mpaka chini. Basi huo ukawa ndio mwanzo. Wafanya biashara wengine pale sokoni nao wakawavamia wale jamaa na kuwapa mkong'oto wa haja!
Na ni hapo ndipo Land Rover ya polisi ilipowasili kwa vishindo eneo lile huku askari wakiruka chini kwa jazba kuja kutuliza ghasia ile. Osman Mgunya alikuwa ndio kiongozi wa kundi lile la askari. Jaka alimtupia jicho kwa chati huku akendelea kupanga zabibu zake taratibu pale mezani na kumuona jinsi uso ulivyomshuka baada ya kuwaona wahalifu na kubaini kuwa Jaka hakuwa miongoni mwao. Aligeuka huku na kule akijaribu kumtafuta Jaka. Alipomuona, Jaka alikuwa ametulia kimya nyuma ya meza yake ya zabibu akimtazama. Osman alimtulizia jicho la chuki mno, kisha akaingia kwenye gari lile kwa ghadhabu na kubamiza mlango.
Wale jamaa wanne ndio waliotiwa mbaroni baada ya watu wote pale sokoni kuwataja kuwa ndio chanzo cha vurugu ile. Jaka alijua kuwa wataenda kuachiliwa mbele ya safari na bila shaka kupewa na posho yao kwani alikuwa na hakika kabisa kuwa wale jamaa walikuwa wametumwa na Osman Mgunya.
Jioni ile alipoenda kuripoti pale kituoni alimkuta Osman Mgunya akiwa amefura vibaya sana kwa ghadhabu, jambo lililomhakikishia kuwa mawazo yake kuhusiana na tukio lile yalikuwa sahihi. Osman alimsukumia daftari na kalamu ili aweke saini yake kwa jioni ile. Bila ya kusema neno alichukua ile kalamu na kusaini sehemu aliyotakiwa kisha akamsogezea Mgunya daftari lile ili naye asaini.
Mgunya akaweka kiganja chake kinene mithili ya chana ya ndizi juu ya kiganja cha mkono wa Jaka na kukigandamiza kwa nguvu pale juu ya daftari. Kwa mshangao Jaka alimuinulia uso wake uliojaa viulizo kutaka kujua kulikoni, na hapo akakutana na kofi kali sana la uso kwa mara ya pili katika siku ile.
Khah!
Kabla hajatanabahi kutokana kofi lile Osman alikuwa ameshamdaka shingo kwa kono lake la kushoto na kumbana koo.
Ebwana we!
Macho yalimuwiva Jaka kwa kofi lile na akiona vinyota vikielea mbele ya macho yake huku akiuhisi uso ukimtutumka. Aliinua mikono yake yote miwili na kuushika ule mkono uliomkaba koo akijaribu kuutoa bila mafanikio.
Mgunya alimvuta mbele kwa nguvu mpaka sura zao zikawa zimetenganishwa na sentimeta chache mno baina yao. Hali ile ilisababisha Jaka avutwe kutoka upande mwingine wa meza ile na kupandishwa kiwiliwili chake juu ya meza ile hali miguu yake ikining'inia upande wa pili wa meza ile.
Osman alimkazia macho yake mekundu yaliyotokeza nje kama ya mtu aliyekabwa.
"Unajua wewe unajifanya mjanja sana...lakini ambacho hukijui ni kwamba muda wako unazidi kufikia ukingoni kwani hatimaye nitakupatia tu, fisi we! " Alimkoromea kwa sauti ya kunong'ona iliyojaa ghadhabu na vitisho.
Jaka alikunja uso kwa maumivu huku akifinya macho na pua yake kutokana na pumzi za Osman zilizonuka sigara.
Baada ya maneno hayo Osman alimuwekea usoni kiganja cha mkono wake wa kulia kumsukuma nyuma kwa nguvu huku wakati huo huo akimuachia ile shingo yake kwa mkono wake wa kushoto. Jaka alirushwa nyuma huku yowe likimtoka, akipepesuka kinyuma nyuma na hatimaye kujibwaga chali hatua chache kutoka kwenye mlango wa chumba kile.
Alijiinua kwa hasira kutoka pale chini akiwa na wazo la kumparamia Osman pale mezani kwake na kumpa ngumi nyingi tu, liwalo na liwe. Lakini kabla hajafanya hivyo aligundua kuwa alikuwa ameangukia miguuni kwa mtu ambaye alikuwa anaingia katika chumba kile.
Aliinua uso wake na kukutana na mtu wa makamo, aliyepata kiasi cha miaka kama hamsini na tatu au na nne hivi. Alikuwa mfupi na mnene, ingawa unene wake haukuwa ule wa kibwanyenye ila wa mtu mwenye nguvu. Mavazi yake ya ki-askari hayakuonesha alikuwa na cheo gani kutokana na koti refu jeusi alilolining'iniza mabegani mwake juu ya mavazi yale.
Uso wake wa duara haukuwa ukimtazama Jaka bali ulielekezwa moja kwa moja kule alipokuwa Osman Mgunya hali macho yake madogo yakionesha hasira kubwa.
"What's this...What's going on here, Osman?" Yule bwana alimfokea Osman kwa kiingereza, akimaanisha kuwa anataka aeleweshwe kilichokuwa kinaendelea pale ofisini wakati ule.
Wakati huu Jaka alikuwa ameshasimama pembeni akiwatazama Osman Mgunya na yule mtu kwa zamu, akiwa amemakinika na namna yule jamaa alivyomsemesha Osman kwa mamlaka namna ile. Osman alivyobabaika vibaya sana.
Alijikurupusha kutoka nyuma ya meza yake na kupiga saluti hali akiwa amekauka kama ubao, macho yake mekundu yakiwa yamemtoka pima.
"Hivi ndivyo ulivyofundishwa namna ya kuwatendea raia hata kama ni wahalifu?" Badala ya kuijibu ile saluti, yule bwana aliendelea kumuuliza Osman.
"Eeh...Yaani...Hapana afande...! Haitatokea tena afande!" Osman alijibu kwa kubabaika.
"Hii sio namna ya kuwatendea watu, Osman...na nataka leo ndio iwe mwisho. Sitaki kabisa mkoa wangu upate kashfa magazetini kwa unyanyasaji wa raia wowote, wawe wahalifu au vinginevyo, tumeelewana?" Aliendelea kuasa yule mtu ambaye mara moja Jaka alibaini kuwa ndiye mkuu wa polisi wa mkoa.
"Ndi…ndio afande!"
Yule bwana akamgeukia Jaka na kumtazama kwa muda kama mtu anayejaribu kukumbuka alipata kumuona wapi, kisha kama mtu aliyekumbuka akamuuliza, “Unaitwa Jaka Madega, sio?” Na kabla Jaka hajajibu lolote akaendelea, “…nadhani kwa mujibu wa maelezo ya faili lako wewe ni msomi, na hivyo unazijua fika haki zako za kisheria au sio? Sasa nataka hili jambo lililotokea leo ulisahau na nina imani kuwa bwana Osman hapa…” Akamgeukia Osman Mgunya na kumkazia macho, “…atahakikisha kuwa halitokei tena.”
Jaka alibaki akiwa ameduwaa tu. Hakujua iwapo yule mtu alikuwa akimaanisha yale aliyokuwa akiyasema au alikuwa akimkebehi tu. Kwa mambo aliyoyapata kutoka kwa wana-usalama hapo nyuma, hakuwa na imani na askari yeyote hapa nchini. Yule bwana alimtazama Jaka kwa makini zaidi.
“Au kila siku unapokuja kuripoti huwa unapigwa bwana mdogo? Ni mara ya ngapi sasa tukio kama hili linakutokea hapa kituon?” Hatimaye aliongezea kumsaili.
Jaka alimgeukia Osman na kumtazama usoni. Mgunya aligwaya wazi wazi, midomo ikimcheza na nyusi zikimtetema.
“Hapana mzee...jambo kama hili halijawahi kunitokea hata siku moja hapa kituoni.” Jaka alijibu huku akiendelea kumtazama Mgunya usoni kwa macho makavu. Osman alimeza fundo kubwa la mate huku pua zikimtanuka na kumsinyaa haraka haraka. Hakuamini masikio yake.
Jaka alimgeukia yule mzee na kumshukuru.
“Nashukuru sana kwa wema wako mzee...”
“No! Sio swala la wema hilo bwana mdogo. Huu ni wajibu wangu...na ni wajibu wa askari yeyote mzuri...kulinda na kuhudumia umma.” Yule bwana alimwambia.
“Nashukuru sana...”
Yule bwana akamnyooshea mkono wake wa kulia huku akijitambulisha.
“Naitwa Januari Mwakaja, ndio RPC wa hapa Dodoma.”
“Na...nafurahi sana kukufahamu mzee.” Jaka alijibu huku akiupokea kwa heshima mkono wa yule mzee. Januari Mwakaja alitabasamu.
“Twende. Nitakupa lifti mpaka njia ya Makole...naamini unaishi Makole, au sio?” Ilikuwa ni zamu ya Jaka ya kutoyaamini masikio yake kwa siku ile. Yule mkuu wa polisi wa mkoa alionekana kujua kila kitu kuhusu yeye, na hili lilimkosesha amani kidogo Jaka.
“Eeenh...ndio mzee...lakini...nitatembea tu!” Alibwabwaja, na Januari Mwakaja akamcheka kidogo.
“Wacha uoga dogo...twende nikupe lifti. Angalau uone kuwa askari ni watu wema pia.” Alimwambia.
Jaka hakuwa na namna.
Wakiwa garini kuelekea Makole, Mzee Mwakaja alimuuliza Jaka alikuwa akifanya nini pale Dodoma wakati anapokuwa anasubiri muda wa kuripoti kituoni. Jaka alimwelwza kuwa huwa anamsaidia mjomba wake kuuza matunda sokoni.
Mzee Mwakaja aliendelea kuendesha gari lake aina ya Toyota Prado akiwa kimya kwa muda mrefu.
“Unajua si kila mfungwa ni mkosa, na hata huko magerezani wafungwa huwa wanafanya kazi mbalimbali ili kuwaandaa na maisha ya uraiani mara baada ya kumaliza adhabu zao...ili wasije kuwa wazururaji tu baada ya kutoka vifungoni...” Hatimaye yule mzee aliongea.
Jaka aliendelea kumsikiliza bila ya kusema neno, akijaribu kuchambua maana ya maneno yale.
Si kila mfungwa ni mkosa...
Ina maana anajua kuwa sikufanya kosa nililoadhibiwa kwalo ?
“Si...sijakuelewa unamaanisha nini mzee...”
“Ni kwamba na wewe una haki ya kujitayarisha kukabiliana na maisha yako ya baadaye baada ya kumaliza muda wako hapa Dodoma." Januari Mwakaja alimwambia.
Jaka alitikisa kichwa tu kuashiria kuwa alikuwa amemuelewa. Alihisi kuwa mzee Januari Mwakaja alikuwa ni mtu ambaye angeweza kumuamini. Alijiuliza ingekuwaje iwapo angesema ukweli juu ya mambo aliyokuwa akifanyiwa na Osman Mgunya pale kituoni....labda Osman angerudishwa Dar es Salaam....
Hapo Jaka alikumbuka wakati alipokuwa JKT akilitumikia Jeshi La Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria. Jambo moja alilojifunza huko lilikuwa ni kwamba hata kama mtu ukiwa unajuana au unaelewana sana na mkuu wa kikosi au CO, yaani Commanding Officer, haitakusaidia kitu iwapo utakosa kuelewana na Koplo tu, ambaye ni afisa wa cheo cha chini lakini ndiye unayekuwa naye muda wote. Hivyo Koplo anaweza kukutafutia adhabu kadhaa wa kadhaa na kukufanyia visa kemkem na kuyafanya maisha yako kuwa ni ya mashaka makubwa sana, pamoja na kujuana kwako na CO .
Na ni katika misingi hiyo hiyo ndivyo alivyoiona ile hali iliyojitokeza kati yake, Osman Mgunya na Januari Mwakaja.
___________________
Siku iliyofuata hakupata vishindo vyovyote kutoka kwa Osman Mgunya ambaye alimkuta akiwa amepoa sana. Baada ya kusaini kwenye kitabu aligeuka na kuanza kuondoka, lakini Osman alimwita na kutoa bahasha kutoka kwenye droo ya meza yake.
Akaitupia pale juu ya meza.
“Barua yako hiyo.”Alimwambia na kuangalia pembeni.
Jaka aliichukua ile bahasha na mara moja akajua ilikuwa imetoka wapi kwani hati iliyoandika jina lake juu ya bahasha ile kwa anuani ya RPC Dodoma aliijua fika, na kwa nukta ile alipouona mwandiko ule, moyo wake ulifanya kitu kama sarakasi hivi.
Ulikuwa ni mwandiko wa mama yake!
Kwa furaha Jaka alitamani kumshukuru Osman kwa kumpa mkono, lakini hakufanya hivyo. Badala yake aliitazama ile bahasha taratibu na kugundua kuwa ilikuwa imefunguliwa hivyo akajua kuwa Osman alikuwa ameshaisoma. Aliangalia muhuri wa Posta wa siku barua ile ilipofika pale Dodoma, na kugundua kuwa barua ile ilikuwa imefika zaidi ya wiki mbili nyuma.
Alimtazama Osman kwa hasira ya wazi.
“Sasa si bora ungenisimulia tu yaliyoandikwa kwenye barua hii, unaonaje?” Alimwambia kwa hasira, kisha bila kusubiri jibu aligeuka na kuondoka.
Osman alibaki akiwa amefura kwa hasira.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
4
Akiwa amebakiza miezi miwili akamilishe mwaka mmoja mjini Dodoma, Jaka alirejewa tena na ile ndoto ya yule msichana wa ajabu. Kwa muda wote uliopita alisahau kabisa kuhusu ndoto ile. Jambo lililomshangaza ni kwamba ndoto ile ilimrudia vilevile kama ilivyomjia mara ya kwanza.
Hili lilimpa taabu sana kulielewa.
Nini maana ya ndoto hii?
Ni utabiri wa aina fulani au...?
Vyovyote iwavyo hii si ndoto ya kawaida...si ya kawaida kabisa! Sasa kwa nini inanijia namna hii?
Alikuwa akiwaza mambo hayo huku akitembea jioni ya siku iliyoamkia usiku alioota ile ndoto kwa mara ya pili. Ilikuwa inapata saa moja kasoro robo hivi za jioni.
Alikumbuka maneno ya mzee Mnyaga mara alipomueleza habari za ndoto ile baada ya kumrudia tena asubuhi ya siku ile. Mnyaga alibaki mdomo wazi, na kwa muda mrefu alibaki kimya kabla ya kumwambia kuwa alikuwa na uhakika kuwa ndoto ile ilikuwa inambashiria mambo fulani ambayo yangemtokea baadaye au yaliyomtokea hapo awali. “...ila kwa hakika hiyo ndoto inakubashiria mafanikio fulani...” Mnyaga alimalizia huku akionyesha kuwa na mawazo mengi.
“Mafanikio? Kwa vipi anko?” Alimuuliza huku akionyesha kutoamini kabisa maneno yale.
Mnyaga aliguna kidogo kabla ya kumjibu.
“Kwanza kuna mwanga katika ndoto yako, ambayo ni ishara ya ufumbuzi fulani...halafu kuna mwamvuli...mwamvuli unaashiria kinga au ushindi wa aina fulani...” Mnyaga alisita kidogo, kisha akaendelea “...sijui lakini...ila nadhani vitu vyote hivyo vinaashiria mafanikio...ushindi dhidi ya matatizo, ambayo humo ndotoni yamekuja kama mvua ya maji moto na yule khabithi Osman Mgunya laana za manani zimuangukie milele!”
Jaka alimcheka sana kwa majibu yale, akimtania Mnyaga kuwa ni vyema angeanzisha biashara ya kutabiri ndoto.
Lakini sasa kila alivyozidi kulifikiria swala lile ndivyo lilivyozidi kumtia wasiwasi kwani lilionesha uhusiano fulani na jambo jingine ambalo kwa muda mrefu limekuwa likimkosesha raha. Kwa namna fulani amekuwa akipatwa na hisia kwamba kuna kitu au jambo fulani hivi, ambacho kingeweza kumtoa katika janga lile alilotumbukizwa...
Ni kitu gani basi?
Hakuweza kukiweka sawa akilini mwake kitu hicho, ingawa uwepo wake ulizitawala sana hisia zake. Ni kitu ambacho kilikuwepo muda wote tangu mwanzo.
Sasa na hii ndoto tena...
Mungu wangu ! Ni nini kinanitokea mimi?
Kwa nini mimi... ?
___________________
Maisha ya binadamu huweza kubadilika kwa namna ya ajabu kabisa na kwa namna ambayo hata binadamu mwenyewe hawezi kufanya lolote katika aidha kuyazuia yasibadilike au kuyafanya yabadilike na kuingia kwenye hali hiyo yanayobadilikia.
Ni sawa na jinsi alivyoeleza mwanafalsafa mmoja wa Ujerumani aliyeishi karne kadhaa zilizopita aliyeitwa Hegel. Yeye alisema kuwa binadamu hawezi kubadilisha au kuongoza matukio katika historia, bali mwanadamu huishi maisha yake kutekeleza yale ambayo matukio ya historia yametayarisha yamtokee mwanadamu katika maisha yake mafupi hapa duniani.Hivyo kadiri matukio yanavyobadilika na binadamu nae hulazimika kubadilika.
Sio watu wengi waliokubaliana na Hegel wakati ule alipokuwa akiandika falsafa zake hizo katika karne ya kumi na nane. Na pia sio wote wanaokubaliana nae leo hii katika karne hii tuliyonayo sasa.
Lakini bila shaka katika wale wachache watakaoweza kukubaliana na falsafa hii ya marehemu Geog Wilhelm Friedrich Hegel katika karne yetu hii, Jaka atakuwa ni mmoja kati yao hasa ukizingatia jinsi maisha yake yeye yalivyobadilika kwa namna ya ajabu kabisa kwanza bila ya yeye mwenyewe kutaka na pili bila ya yeye kuwa na lolote aliloweza kufanya kuzuia mabadiliko hayo na hatimaye akajikuta Dodoma.
Na bila ya yeye kutaka au kujua, ilifika siku akiwa pale Dodoma ambapo mlolongo mzima wa maisha yake ulibadilika kwa namna ya ajabu kabisa na bado asiwe na la kufanya zaidi ya kupigwa na butwaa tu. Ni siku ambayo hakujua kama ingefika na hata ilipofika hakutegemea kwamba ndio ingekuwa mwanzo wa kufungua ukurasa mpya kabisa katika hadithi ya maisha yake...kama jinsi alivyosema bwana Hegel.
Tofauti pekee ni kwamba ni wazi kuwa Jaka na watu wengi wa karne hii wangesema kuwa kila jambo hupangwa na Mungu...
________________________
Jaka alikuwa ameegemea nguzo ya jengo la Benki Ya Taifa Ya Biashara (NBC) tawi la Mtendeni pale Dodoma mjini akiangalia vijana wenzake wakipita kwa mbwembwe na furaha kuelekea ndani ya ukumbi wa disko wa NK ambao jengo lake lilikuwa linatazamana na lile jengo la Benki.
Ilikuwa ni siku ya jumatano na muda ulikuwa ni kama saa tatu na robo hivi za usiku. Vijana wengi waliokuwa wakielekea ndani ya ukumbi ule, wake kwa waume, walikuwa wamejipendezesha kwa mavazi ya kileo ambayo mengi yao yalivaliwa kufuatia mitindo ya uvaaji ya wanamuziki maarufu duniani.
Kile alichokuwa akikiona pale nje ya ule ukumbu wa disko usiku ule kilimkumbusha wakati akiwa Dar es Salaam ambapo naye alikuwa ni mhudhuriaji mzuri wa maeneo kama yale, pamoja na matamasha mbalimbali ya muziki. Pia hali ile ilimkumbuka mtu ambaye mara nyingi alikuwa akiambatana naye katika matukio kama yale. Mtu ambaye yeye aliamini kuwa walikuwa wanapendana sana...mpaka ilipofikia siku ile aliposhuhudia maisha na ndoto zake zote zikisambaratika mbele ya macho yake...na ndipo alipogundua kuwa kama ni penzi, basi lilikuwa la upande mmoja tu...
Kila alipomfikiria yule binti ambaye yeye aliamini kuwa baina yao kulikuwa kuna upendo wa hali ya juu, roho ilimuuma sana. Hakutaka kuendelea kumfikiria, hivyo alihamishia mawazo yake kule walipokuwa wale vijana wenzake na jinsi walivyokuwa wakisherehekea ujana wao.
Akiwa anaendelea kutazama matukio ya kufurahisha pale nje ya ule ukumbi maarufu wa disko, gari aina ya Nissan X-Trail lilifika eneo lile na kuegeshwa hatua chache kutoka pale alipokuwa amesimama. Yeye aliamua kuondoka eneo lile akiwa na wazo moja tu la kwenda kulala. Kwake siku ilikuwa imeisha salama. Aliangaza kulia na kushoto na kuamua kuchukua njia iliyokuwa kulia kwake ambayo ingempeleka mpaka chuo cha biashara cha CBE, huko angekata kushoto na kuingia Makole.
Alikuwa anageuka kulia ili aanze hiyo safari yake.
Na hapo ndipo alipomuona.
Moyo ukamlipuka na hapo hapo ukaanza kumuenda mbio. Na hata pale alipokuwa amesimama akimkodolea macho yule mtu aliyeteremka kutoka kwenye ile X-Trail, bado ilimuwia vigumu kuamini macho yake. Pamoja na mtu yule aliyemduwaza Jaka pale nje ya ule ukumbi wa disko, waliteremka vijana wengine watatu, wawili wakiwa wasichana. Haikuwa na shaka kuwa nao walikuwa wamekwenda kujiburudisha kwa disko usiku ule pale NK.
Alibaki akiwa amekodoa macho kuwatazama.
Yule mtu aliyemfanya moyo ulimpuke alikuwa amesimama nje ya lile gari hali akiwa ameegemeza mkono wake juu ya paa la gari lao wakati mkono wake mwingine ameuzungusha kiunoni kwa mmoja kati ya wale wasichana wawili wazuri sana waliofika nao eneo lile. Uso wake alikuwa ameuelekeza kwenye lango kuu la kuingilia kule ukumbini, na kutokea pale alipokuwa, Jaka alikuwa akiuona upande wa kushoto wa sura ya yule mtu.
Hivi ni yeye kweli au nimemfanaisha? Atakuwa amekuja kutafuta nini huku?
“Duh! Inaelekea mambo yameshaanza hapa, you know what I'm sayin' ?” Yule jamaa alisema kwa sauti ya mbwembwe za kimarekani kuwaambia wenzake huku akiendelea kutazama kule kwenye jengo lenye ule ukumbi wa disko.
Ah! Ile sauti...Ni ile ile!
Na yale maneno....you know what I'm sayin' ....
Hapo Jaka ndipo haswa alipopata uhakika juu ya mtu yule.
Ni yeye bloody swine!
Hasira zilianza kumpanda kwa kasi ya ajabu.
Alimfahamu fika yule jamaa...kwani ndiye hasa chanzo cha matatizo yote yaliyomkumba.
Sasa wamekuja kukutana tena huku Dodoma!
Bila kufikiri zaidi alijikuta ameshamsogelea yule jamaa na alimwita kwa jina huku akinyoosha mkono wake ili amshike bega.
“Aisee, Tony...”
Hapo ndipo alipoishia, kwani yule jamaa alipouona mkono wa Jaka ukimjia kwa pembe ya jicho lake, alishtuka na kugeuka ghafla huku akifikiria kuwa Jaka alikuwa ni mwizi aliyetaka kumpora cheni yake ya dhahabu aliyokuwa ameivaa shingoni. Masikini Jaka hakufikiria kuwa kwa muonekano aliokuwa nao wakati ule, hata vijana wenzake walimuona mzee, kwani uso ulimjaa ndevu, nywele zake hazikuwa zimenyolewa kwa muda mrefu kiasi cha kunasibishwa na uchafu, na zaidi ya hapo, mavazi yake yalikuwa tofauti kabisa na hadhi ya eneo lile.
Hivyo mtu yeyote angeambiwa kuwa Jaka alikuwa mwizi, asingekataa.
Basi yule jamaa ambaye Jaka alimtambua kwa jina la Tony na ambaye ki-umri hawakutofautiana sana, alimgeukia Jaka kwa ghadhabu na mara ile ile yule kijana mwingine aliyekuwa safari moja na yule mtu ambaye Jaka aliamini kuwa ndiye chanzo cha matatizo yote yaliyomkuta, alipiga yowe la mwizi kwa woga.
Na katika sekunde ile ambayo yule mtu alimgeukia Jaka kwa ghadhabu, macho yao yalikutana. Mara moja Jaka akaona kuwa na yule mtu alikuwa amemtambua, kwani alipigwa na butwaa na kubaki akimtazama kwa kutoamini.
Walibaki wakitazamana.
Kama jinsi walivyowahi kutazamana hapo nyuma.
Lakini kabla ya yeyote kati yao hajasema lolote, vurumai ilianza.
Ule ukelele wa "mwizi" uliwavuta vijana wengine waliokuwa pale nje ya ule ukumbi ule ambao walifika kwa kasi pale kwenye ile X-Trail huku wakipiga mayowe ya jazba. Jaka akagundua kuwa tayari maisha yake yalikuwa hatarini. Haraka alimgeukia yule jamaa aliyepiga kelele ya "mwizi" ili amfahamishe kuwa yeye sio mwizi.
Ile anageuka tu alikutana na kofi kali sana la uso. Mmoja kati ya wale wasichana waliokuja na yule mtu aliyejulikana na Jaka kama Tonu akapiga kelele wawoga. Jaka alijishika uso wake na kuinama kwa uchungu. Mara alishtukia miguu yake ikichotwa ngwara kali naye akaenda chini kwa kishindo huku yowe likimtoka, akisikia matusi kemkem yakivurumishwa dhidi yake. Alijitahidi kuinuka kutoka pale chuni huku akijinadi kuwa si mwizi, na hapo alianza kupokea mvua ya mapigo kutoka kila upande. Mateke, fimbo, ngumi, mawe...
Alipiga kelele za kujitetea huku akijitahidi kuinuka kutoka pale chini bila mafanikio. Ilikuwa ni vipigo vya mfululizo. Damu ilimtoka puani, mdomoni na sehemu nyingine za mwili kutokana na mapigo yale.
Matusi yaliendelea kumuangukia sambamba na mapigo yale, naye akahisi alikuwa anaanza kurukwa na akili. Kwa mbali aliweza kusikia sauti za akina dada wakilia na wengine wakimuombea msamaha bila mafanikio.
Aliamini kuwa mwisho wake hapa duniani ulikuwa umewadia.
Sura ya mama yake ilimjia akilini huku akihisi macho yake yakiingia kiza...
"Jamani mmeua!"
"Bado 'uyo...! 'uoni bado anahema 'uyo?"
"'Uyo dawa yake kuchomwa moto tu...!"
"Kwani pale benki si kuna askari? Apelekwe tu kituoni akafie huko huko!"
"Aaah...yule askari kasema tumwache aende zake tu...unajua ye' 'awezi kuacha lindo lake aje 'uku kuangalia vibaka, benki ikiibiwa kazi hana..."
Jaka aliyasikia maongezi hayo kwa mbali huku akiwa amelala akitweta pale chini. Alikuwa akisikia maumivu makali mwili mzima na macho yake yalikuwa yanaingia kiza na kuacha mara kwa mara. Alijiona akibebwa kimabavu kutoka pale chini na kupelekwa sehemu ambayo hakuijua.
“Sio mwiz...sio mwizi miye jam...mani...!” Alijitahidi kujieleza huku akijaribu kujigeuza kumtafuta yule mtu aliyemwita kwa jina la Tony. Alimuona kwa mbali akiwa amesimama kando ya gari lake akiwa bado amepitisha mkono wake kiunoni kwa yule msichana mzuri sana aliyekuwa naye, akiangalia wakati yeye akibebwa kuondolewa katika eneo lile.
Jaka alimnyooshea mkono kwa namna ya kumuita, au kumuomba msaada, au kumtaka aseme kitu kuthibitisha kuwa yeye hakuwa mwizi, lakini yule jamaa alibaki akimtazama tu vile vile.
“Aaah, niachieni ndugu zangu...sio mwizi mim...”
“Kelele!” Alikemewa na hapo hapo akachapwa bakora kali mgongoni, na yowe la uchungu likamtoka.
Baada ya mwendo mfupi alibwagwa chini na kutandikwa bakora nyingine ya mgongo. Alijaribu kujiinua lakini akapigwa teke kali la mbavu, naye akarudi chini kwa kishindo.
"Lete petroli!" Alisikia sauti ikiagiza kwa jazba.
Oh, Mungu wangu...!
Mara alihisi akimwagiwa petroli mwili mzima.
Hah! Nachomwa moto hivi hivi sasa!
Alijikurupusha na kusimama kutoka pale chini, lakini akapigwa ngwara iliyorudisha tena ardhini kwa kishindo huku akisikia lile kundi la watu likiendelea kumpigia mayowe ya jazba. Akajua kuwa sasa mwisho wake ulikuwa umedhihiri. Hakuwa tayari kulikubali hilo. Kwa nguvu zake zilizosalia alijitahidi kujiinua kutoka pale chini ili aukwepe umauti ule uliokuwa ukimkabili. Hapo ikawa kama ndio amechokoza nyuki, kwani aliangushiwa mapigo makali kutoka kila upande. Alipigwa rungu la nguvu kichwani na akahisi fahamu zikimpotea taratibu.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Lete kibiriti upesi tumuwashilie mbali kimburu huyu!” Sauti yenye jazba iliamuru.
Na mara hiyo lilitokea gari na kumulika lile eneo kwa taa zake kali. Jaka alihisi kuwa aliweza kuusikia mvumo wa gari hilo ila fahamu zilikuwa zinamhama kwa kasi. Taa za gari lile ziliwamulika wale watu waliokuwa tayari wameshawasha mwenge kwa makaratasi na kipande cha mti ili wamchome moto "kibaka" yule. Walipoona kuwa wamemulikwa na taa za lile gari, wale watu walitimua mbio na kumuacha Jaka pale chini akipigania fahamu zake zisimtoke.
Ukungu mzito ulitanda mbele ya macho yake. Alijitahidi kutambaa kwa tumbo kuliendea lile gari lakini hakujua iwapo alikuwa anafanikiwa au alikuwa akiendelea kujigaragaza tu pale pale alipokuwa. Aliona mlango wa lile gari ukifunguka karibu sana pale alipokuwa na akashindwa kuelewa kuwa hiyo ilitokana na juhudi zake za kulisotea lile gari au ni kutokana na lile gari kumsogelea yeye pale alipokuwa akigaragara.
“Msss...aaadah!”
Aliona miguu ya mtu ikikimbia kuelekea pale alipokuwa amelala...hakuweza kuelewa iwapo ilikuwa ni miguu ya mwanamke au mwanaume, lakini hakujali. Kiza kilikuwa kinazidi kuyafunika macho yake naye alikuwa akijitahidi kutazama kule ile miguu ilipokuwa inatokea...au alipohisi kuwa inatokea, lakini ilikuwa ni kazi ngumu mno.
Kitu cha mwisho alichoweza kukisikia, au kwa lugha fasaha, alichoweza kukinusa, kilikuwa ni harufu nzuri ya uturi, na baada ya hapo alijihisi akitumbukia kwenye shimo refu lenye kiza kinene....
Alipoteza fahamu.
____________________
Clara Wilfred Mashauri Zaza alikuwa ni mwanadada aliyeumbwa, akaumbika. Si kama hakukuwa na wasichana wengine ambao wangeweza kupewa sifa kama hiyo. La hasha. Bali Clara alikuwa ni miongoni wa wale waliokuwa matawi ya juu kabisa katika kundi hilo.
Alikuwa mrefu. Urefu ambao ni athari ya kizazi chake ambacho hakikuwa cha kitanzania halisi bali chenye mchanganyiko wa damu ya kitanzania na ya kizungu. Ni mchanganyiko wa mbali kidogo na Clara mwenyewe hakupenda kabisa kujinasibisha na mchanganyiko huo. Badala yake alipenda kutambulika kama mtanzania halisi, na hivyo ndivyo alivyojitahidi kuyaweka maisha yake.
Mama yake Clara ndiye hasa aliyekuwa na mchanganyiko huu wa mzungu-mtanzania.
Joanna Salvatori alikuwa ni mwanamke ambaye baba yake alikuwa mzungu wa damu kabisa kutoka Italia aliyeitwa Rocco Salvatori. Rocco aliamua kuoa binti mzuri wa kizaramo na kuhamia kabisa Tanzania.Wakati huo Tanzania ilikuwa bado iko katika makucha ya wakoloni na mzee Rocco Salvatori alikuwa akimiliki shamba kubwa la mkonge kule Tanga. Jinsi alivyokutana na binti huyo wa kizaramo haijulikani, lakini alimpenda na kumjali sana mke wake huyo.
Hawa ndio waliomzaa mtoto Joanna ambaye ndiye akaondokea kuwa mama yake Clara.
Joanna alijaaliwa vitu vitatu; urefu, ambao aliurithi kutoka kwa baba yake mzee Rocco Salvatori, weupe ambao uliuzidi hata ule wa baba yake, na busara ya hali ya juu.
Wazazi wake hao walifariki katika ajali mbaya ya ndege wakati wakirejea Tanzania kutoka Uingereza ambako mzee Rocco Salvatori alikwenda kwa matibabu ya ini, na Joanna akajikuta ameachiwa utajiri mkubwa sana, utajiri ambao uliambatana na jukumu la kumlea mdogo wake wa kiume aliyeitwa Deogratius.
Pamoja na huzuni kubwa iliyowakumba yeye na mdogo wake kutokana na vifo vya wazazi wao, msichana Joanna hakutetereka hata kidogo. Hekaheka za kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi zilipokuwa zinazidi kupamba moto nchini Tanzania, Joanna alimuuuzia tajiri mmoja wa kiarabu shamba la marehemu baba yao ambalo lilikuwa ni sehemu ya urithi wao kwa pesa nyingi mno kisha akamchukua mdogo wake na pamoja wakaenda Uingereza ambako ndiko alipokuwa akipatia elimu yake kabla ya kuondokewa na wazazi wao.
Joanna alitunisha akaunti aliyofunguliwa na baba yake kule Uingereza alipokuwa akisoma katika benki maarufu ya Barclays kwa kuweka fedha nyingi alizopata baada ya kuuza shamba lao la urithi. Baada ya hapo yeye na mdogo wake wakaondoka Uingereza kuelekea Parlermo, mji mkuu wa kisiwa cha Sicily, kilichopo Italia ya kaskazini, kwa jamaa za baba yao.
Baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi kuisha na hali kuonekana kuwa shwari Joanna alirejea Tanzania na kuanza biashara ya madini kutoka Tanzania kwenda nchi mbali mbali za ulaya na uajemi. Ni katika kipindi hiki ndipo alipokutana na kijana wa kisukuma aliyeitwa Wilfred Mashauri Zaza ambaye pia alikuwa akijishughulisha na biashara hiyo. Wilfred Mashauri Zaza alikuwa akitoa madini kama dhahabu, rubi na almasi kutoka sehemu za Magu, Nyarugusu na nyinginezo na kuziuza kwa wahindi na wafanya biashara wakubwa ambao waliziuza nje ya nchi.
Baada ya kukutana na Joanna, Wilfred alianza kuwasilisha madini yote aliyokuwa akikusanya huko vijijini kwenye machimbo na kuikabidhi kwa Joanna ambaye aliyasafirisha nje ya nchi. Biashara hiyo ilikuwa na kuwapatia faida kubwa wote wawili.
Mwaka huo huo Joanna na Wilfred waliacha biashara ile ya madini ambayo ilikuwa imeshaingiliwa na wafanyabiashara wengi zaidi na kuifanya biashara hiyo kuwa ya mazingira ya hatari. Ni katika mwaka huo huo ndipo walipofunga ndoa na kufungua kampuni nyingine iliyojishughulisha na usafirishaji wa bidhaa mbali mbali ndani na nje ya nchi .
Wakiwa na utajiri wa kutosha na hamu ya kutulia katika maisha ya raha kama mke na mume, Joanna na Wilfred walipagawa kwa furaha pale Joanna alipopata ujauzito mwaka mmoja baada ya ndoa yao. Ujauzito ule nusura umpotezee uhai Joanna kwani ulimpa taabu sana. Kutokana na matatizo ya ujauzito ule Joanna alijifungua mtoto wa kiume kwa taabu mno, mtoto ambaye alijaaliwa kuishi kwa siku nne tu kabla ya kufariki dunia.
Hilo lilikuwa ni pigo kubwa sana kwao.
Tangu hapo afya ya Joanna haikuwa nzuri tena. Kutokana na ukubwa wa tatizo la afya yake ya uzazi, madaktari bingwa kadhaa waliwashauri kuwa ni bora Joanna afunge kizazi kabisa kwa usalama wa maisha yake, kwani kulikuwa kuna uwezekano mkubwa sana wa kupoteza maisha iwapo angejaribu kuzaa tena.
Wilfred alikubaliana moja kwa moja na wazo la daktari. Hakuwa tayari kumpoteza mke wake kipenzi, hata kwa gharama ya kukosa mtoto maishani.
Joanna hakukubaliana asilani na wazo hilo.
Ndoto yake kubwa maishani ilikuwa ni kuchuma mali ya kutosha kisha apate watoto wa kutumia na kuiendeleza mali ile. Kwa sababu mali tayari walikuwa nayo, lililobaki ilikuwa ni kupata watoto, na hili ndilo Joanna alilolitaka kuliko kitu kingine chochote hapa duniani kwa wakati ule.
Ingawa hiyo pia ilikuwa ndiyo ndoto ya Wilfred, hakuweza kabisa kuvulia wazo la kumpoteza mke wake mpenzi, hivyo alijaribu bila ya mafanikio kumshawishi Joanna kutekeleza ushauri wa daktari.
Joanna hakubadili msimamo wake juu ya hilo.
Miaka mitatu baadaye Joanna alifanikiwa kwa taabu sana kujifungua mtoto wa kike waliyemwita Clara. Kinyume na moja ya hofu zao, mtoto Clara alikuwa na afya nzuri na kila dalili za kuishi zaidi. Ila hofu yao ya pili hawakuweza kuitoa. Afya ya Joanna ilikuwa mbaya sana baada ya kujifungua mtoto yule.
Joanna Salvatori alifariki dunia miezi miwili baadaye, akimuachia Wilfred mtoto Clara akiwa na miezi miwili tu tangu aje duniani.
Kifo cha Joanna kilikuwa ni pigo kubwa sana kwa Wilfred, kwani Joanna alikuwa ndiyo familia yake pekee. Wakati alitarajia kukuza familia hiyo kwa kuzaliwa kwa Clara, matarajio hayo yalifutwa kabisa na kifo cha mkewe mpenzi. Na ni hapo ndipo kwa uchungu mwingi alipoamua kuwa familia yake iliyobaki itakuwa ni shemeji yake Deogratius ambaye walielewana sana, na mwanae Clara.
Hakutaka tena kuoa maishani mwake.
Mwaka mmoja baadaye Wilfred alibadili jina la kampuni yao kutoka The Continental Freighters na kuwa Zaza Cargo Movers na kuhamishia makao makuu ya kampuni hiyo Dodoma ambapo alinunua nyumba nzuri katika eneo la uzunguni.
Yeye alihamia Dodoma na mwanae Clara na shemeji yake Deogratius Rocco Salvatori alibaki jijini Dar es Salaam ambako alikuwa meneja wa tawi la kampuni yao ya Zaza Cargo Movers.
Wilfred Mashauri Zaza alibaki kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo.
____________________
Mtoto pekee na kipenzi cha mzee Wilfred Mashauri Zaza alikuwa ni msichana mpole na mara nyingi alionekana mpweke, kitu ambacho kwa namna ambayo haikuwa rahisi kuielezea, kilimfanya azidi kuonekana mrembo. Sura yake nyembamba ilikuwa na macho madogo yenye kope ndefu na za kupendeza. Pua yake ndogo na nyembamba ilikuwa ndefu zaidi ya pua za wabantu wengi, ila mdomo wake mdogo ulikuwa umejaa kibantu hasa na hivyo kumfanya awe na sura ya kuvutia mno.
Kidevu chake kilikuwa kimechongwa mithili ya ncha ya yai. Kichwa kilichobeba urembo wake ule kilikuwa kimebebwa na shingo ndefu na nyembamba, shingo ambayo ilikiunganisha kichwa kile na kiwiliwili ambacho kilimfanya awe na umbo la namba nane.
Ingawa Clara hakuwa mnene, mwili wake ulikuwa umejaa vyema. Matiti yake ya wastani yaliyoweza kuwapendeza mwanaume wengi yalitulia vyema kifuani kwake na tumbo lake la ubapa lilitambaa vizuri na kuishia kwenye kiuno chake chembamba kilichotenganisha sehemu ya juu na ile ya chini ya mwili wa kiumbe huyu mrembo.
Mapaja yake yaliyojaa vizuri na yalifanya miinuko ya kuvutia katika kila upande wa nje wa miguu yake, kama kwamba alikuwa ameshindilia bastola kubwa kila upande wa mapaja yale.
Wengi wangeweza kusema kuwa Clara alikuwa mweupe kwa rangi, weupe uliofanywa utokeze zaidi kutokana na nywele zake ndefu, laini na nyeusi mno.
Basi huyo ndiye Clara Zaza.
Elimu yake yote, tangu chekechea hadi Chuo Kikuu aliipatia Nairobi nchini Kenya, ambapo alisomea katika shule za kimataifa katika madarasa ya chekechea, msingi na sekondari kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi.
Baada ya kufaulu vizuri shahada yake ya Uongozi na Uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Nairobi, aliamua kurudi Tanzania kumsaidia baba yake kuongoza Kampuni yao.
Akiwa na umri wa miaka ishirini na sita, Clara ndiye alikuwa meneja mkuu mdogo kuliko wote, wa kampuni maarufu ya usafirishaji katika afrika ya mashariki yenye makao yake makuu mjini Dodoma, nchini Tanzania. Kampuni ya Zaza Cargo Movers.
____________________
Clara alikuwa akitabasamu peke yake huku aliendesha gari lake kubwa na ghali aina ya Jeep Cherokee.
Alikuwa akirejea nyumbani kwake eneo la uhindini akitokea kwenye tafrija ya kuwaaga wafanyakazi wa Zaza Cargo Movers waliokuwa wanastaafu kutokana na umri mkubwa. Tafrija hiyo ilikuwa imefanyikia katika ukumbi wa maarufu wa Dodoma Hotel naye kama meneja mkuu wa Zaza Cargo Movers aliwajibika kuhudhuria hafla hiyo.
Hata hivyo hilo silo lililomfaya awe akitabasamu peke yake garini usiku ule. Ni mawazo yaliyokuwa yakipita kichwani mwake ndiyo yaliyomfanya ajikute akitabasamu namna ile.
“Well...that's my daddy!” Hatimaye alisema kwa sauti na kuangua kicheko kikubwa, akikumbukia vituko vya baba yake.
Kila anapofikiria jinsi baba yake alivyokuwa akijitahidi kumlea kama yai hadi wakati ule ambao yeye ameshafikia umri wa kujiamulia mambo mengi mwenyewe hujikuta aidha akitabasamu peke yake au akicheka kabisa.
Alicheka tena kwa sauti ya chini na kutikisa kichwa huku akiendelea na safari yake.
Baada ya kukabidhi zawadi na hundi za fedha kwa wastaafu wa kampuni yao usiku ule, yeye aliaga na kuwaomba wafanyakazi na wageni waalikwa waliohudhuria hafla ile waendelee na sherehe waliyoandaliwa kisha yeye na baba yake wakatoka kurejea nyumbani.
“Una hakika hutaki kulala nyumbani kwetu leo, dear?” Mzee Zaza alimuuliza bintiye huku wakishuka ngazi za pale hotelini taratibu kuyaelekea magari yao.
“ery sure...baba, si nimekwambia kuwa leo n’talala nyumbani kwangu?" Clara alimjibu baba yake huku akitasamu.
"Sawa...lakini pale pia ni nyumbani kwako dear, unaweza kuja wakati wowote."
"Na pia naweza nisije wakati wowote vile vile, au sio dad?" Clara aliendelea kumkorofisha baba yake.
"Clara dear, unajua jinsi gani najisikia nikifikiria..."
"Yeah, yeah, najua...mtoto wa kike, peke yangu kwenye nyumba, sijaolewa, blah,blah,blah...Baba! Si nimekwambia tangu mwanzo tu kuwa leo nitalala nyumbani kwangu?"
"Sawa...lakini na mimi pia si nimekwambia kuwa nyumbani kwangu kwa hakika ni nyumbani kwako, Clara...?"
"I know dad, lakini na wewe lazima ukubali kuwa sasa mimi ni msichana mkubwa na I can take care of myself! Besides, sehemu kubwa ya maisha yangu nimekuwa nikiishi peke yangu tu, yaani boarding school tena nje ya nchi, you shouldn't worry about me that much dad..." Clara alimbishia baba yake, akimsisitizia kwa kizungu kuwa kwa umri aliofikia anaweza kujitunza.
“Yeah…labda hiyo ndiyo sababu sasa nataka niwe karibu na wewe dear, nifidie kwa muda wote huo uliolazimika kukaa peke yako nje ya nchi ukiwa masomoni...?” Mzee Zaza alimwambia bintiye kwa kimombo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Aah, hiyo imeshapita tena baba…na unajua mie nashukuru sana kwa hilo? Kuweza kuishi peke yangu ugenini.... kujifunza kufanya maamuzi mengi mwenyewe. Hiyo ni zawadi kubwa kwangu baba. Just you be happy for me dad, okay?” Clara alimjibu babiye, akiongezea kwa kimombo kuwa awe na furaha kwa ajili yake.
“Okay, okay...ni sawa dear, nimekuelewa....nitajitahidi kuelewa, okay?” Mzee Zaza alisalimu amri kwa shingo upande.
“Okay...Goodnight dad." Clara alikatisha mazungumzo yale huku akimbusu shavuni baba yake.
“Goodnight baby... sleep tight."
Clara aliendelea kutabasamu peke yake huku akikumbukia mjadala ule baina yake na baba yake, akiwa ndani ya ile Jeep Cherokee yake yenye rangi nyekundu.
“Mnhu! Yaani baba mpaka leo bado ananiona mimi mtoto mdogo tu!” Alijisemea peke yake huku akiizungusha Jeep Cherokee yake kiufundi kwenye mzunguko wa Jamatini pale Dodoma mjini. Alifuata barabara inayoelekea Dar es Salaam na kukata kushoto kuingia kwenye mtaa mfupi uliopo baina ya ofisi ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na hoteli maarufu ya Nooreen. Mtaa ule mfupi ulimpeleka mpaka kwenye njia panda ya msikiti maarufu wa Nunge pale mjini. Hapo aliingia kulia ili atokee kwenye barabara inayoelekea Uhindini ikitokea maeneo ya ukumbi wa disko wa NK ambapo angekata kushoto na kuelekea zake Uhindini.
Na hapo mawazo yake yote yalikatika ghafla mara alipoona kundi la watu likiwa katikati ya barabara mbele yake, wengine wakiwa wameshika mienge na silaha mbali mbali. Roho ilimlipuka na wazo lililomjia kichwani mwake wakati ule ni kwamba wale walikuwa ni majambazi waliojaa barabarani makusudi ili asimame wapate kumpora gari na mali nyinginbe zozote atakazokuwa nazo mle garini.
Woga mkubwa ukamshika, akikumbukia tukio jingine baya la kuvamiwa na vibaka lililowahi kumtokea maishani mwake.
Alianza kujilaumu kwa nini hakukubali kulala nyumbani kwa baba yake usiku ule huku akipata wazo la kugeuza gari kwa kasi na kutokomea kwa njia nyingine. Lakini kabla hajatekeleza wazo lake hilo alishangaa kuona wale watu wakitimua mbio, wakimuacha mtu mwingine akigaragara pale barabarani.
Mara moja alielewa kilichokuwa kimetokea. Bila shaka yule mtu alikuwa amepigwa na kaporwa pesa zake zote na majambazi wale.
Sijui wamemuua...?
Bila kujishauri zaidi alisogeza gari lake hadi karibu na pale alipokuwa yule mtu na akaona kuwa yule mtu alijaribu kujiinua kutoka pale chini lakini alishindwa. Akiwa amepata imani kuwa yule mtu alikuwa hai, Clara alizidi kumsogelea kuona kama angeweza kumsaidia kwa angalau kumpeleka hospitali. Alisimamisha gari karibu na yule mtu na kuchungulia huku na huko kutokea mle garini. Kote kulikuwa kimya, hakukuwa na dalili ya wale watu waliokuwa wakimpiga yule mtu. Aliteremka haraka na kukimbilia pale chini alipolala yule mtu.
Alipiga goti moja kando yake na kumtazama kwa makini zaidi. Alimuwekea mkono kifuani na kusikiliza mapigo ya moyo, na hapo harufu kali ya petroli ikazishambulia pua zake na akagundua kuwa nguo za yule mtu zilikuwa zimemwagiwa petroli.
Walitaka kumchoma moto! Ndio maana walikuwa wameshika ule mwenge, wauaji wakubwa!
Mwili ulimsisimka kwani alielewa kuwa asingetokea eneo lile wakati alipotokea, basi yule mtu angechomwa moto!
“Loh! watu wanawezaje kuwa wakatili kiasi hiki jamani!” Aliwaza kwa mshangao ulichanagnyika na huzuni.
Hapo wazo jingine likamjia. Ni wezi tu ndio waliokuwa wakichomwa moto siku hizi hapa nchini.
“Au huyu mtu ni mwizi?"
Aliamua kumuangalia kwa makini zaidi kama aliyetaka kujihakikishia kuwa yule mtu hakuwa mwizi. Alimgeuza uso wake uliokuwa umelalia upande mmoja na kumtazama usoni.
Khah!
Moyo ilimlipuka vibaya sana alipoiona sura ya yule mtu. Mara moja alijua kuwa aliwahi kuiona sura ile sehemu fulani, wakati fulani. Lakini kwa nini moyo ulimlipuka kiasi kile? Kwa pale alipokuwa amepiga goti alikuwa ameupa mgongo mwanga wa taa za gari lake na hivyo sura ya yule mtu ilikuwa imezibwa na kivuli chake. Alisogea pembeni na mwanga wa taa za gari lake ukammulika moja kwa moja usoni yule jamaa.
Naam. Sasa alimkumbuka yule mtu, na hakuwa na shaka kabisa juu ya hilo.
Alikuwa ni yule mtu wa ajabu aliyemsaidia na kuokoa maisha yake siku nyingi zilizopita katika jiji la Dar es Salaam.
E bwana we!
Ingawa sasa alionekana mwembamba zaidi, Clara aliweza kumkumbuka bila shaka hata kidogo. Asingeweza kuisahau kabisa sura ya yule mtu hata angemuona wapi na katika mazingira gani. Tangu siku ile alipomuacha pale kituo cha polisi akigaragazwa na wale askari, akili yake haikuweza kuacha kumfikiria yule mtu.
Mara kwa mara amekuwa akirejewa na mawazo kuhusu yule mtu, akijaribu kujiuliza ni masahibu gani yaliyomkuta yule kijana bila ya kufanikiwa kupata jibu maridhawa. Naye hakutegemea kabisa kuonana naye tena maishani.
Na sasa bila ya kutegemea kabisa anamuona tena yule jamaa, tena katika mazingira yale yale ya ajabu kama jinsi alivyokutana naye kwa mara ya kwanza kiasi cha mwaka moja uliopita kule jijini Dar!
Akili ilikuwa ikimzunguka kwa kasi sana. Ilibidi apitishe uamuzi haraka kabla wale watu hawajarudi kuja kummalizia kabisa kijana yule wa ajabu.
Wazo alilokuwa anajitahidi kushindana nalo ni la kumuacha pale pale alipo nae ashike hamsini zake akamwombee tu kwa mungu labda atamjaalia kuokoka kutokana na madhila makubwa ya kidunia yaliyoelekea kumuandama kijana yule.
Akili yake ilimwambia kuwa kwa vyovyote yule kijana naye alikuwa ana mambo yake ambayo si mema. Yule Sajenti wa polisi siku ile mwaka mmoja uliopita alisema kuwa kwa kosa alilofanya adhabu ya kunyongwa tu ndiyo ingemfaa. Clara hakuwa mjinga, hivyo alijua kuwa kuna makosa machache sana hapa nchini yanayostahili adhabu ya kunyongwa, na kubwa miongoni mwa hayo ni kosa la mauaji...
Sasa niondoke au...?
Moyo wake ulimuwia uzito sana kumuacha yule jamaa namna ile pale barabarani.
Kwani mimi amenifanyia ubaya gani?
Hakuna alichonifanyia ila ni wema tu...tena kwa kujihatarishia maisha yake katika kujaribu kuniokoa mimi kutoka mikononi mwa wauaji ambao bila shaka wangeweza hata kunibaka!
Na kama na yeye pia alikuwa ni muuaji, angeshindwa nini kuwaacha tu wale watu wanifanye watakavyo naye akashika hamsini zake?
Tena kwa sababu ya kunisaidia mimi, mtu ambaye hanijui nami simjui, ndio akashikwa na wale polisi ambao bila shaka alikuwa ameshawatoroka...nao wakampa kipigo kizito na sijui amekutwa na mambo mangapi mengine hadi leo hii nakuja kumkuta hapa katika hali kama hii...!
Hata!
Haiwezekani, lazima nimsaidie. Kama yeye alikubali kunisaidia mimi bila kujali iwapo angeweza kupoteza maisha yake katika kufanya hivyo, basi na mimi leo ndio nafasi yangu ya kumlipa kwa wema alionifanyia....
Bila kuchelewa zaidi, Clara alijitahidi kumzoazoa yule jamaa kutoka pale chini na kumburura kuelekea kwenye gari lake. Alipofika usawa wa mlango wa nyuma wa gari lile alimlaza chini na haraka akawahi kufungua mlango ule. Kwa taabu aliweza kulaza kichwa na sehemu ya juu ya kiwiliwili cha mtu yule, ambaye muda wote huo alikuwa amepoteza fahamu, kwenye kiti cha nyuma cha gari lile na kuacha sehemu ya chini ya kiwiliwili chake ikining'inia nje.
Huku akitweta na moyo ukimwenda mbio alikimbia kuzungukia upande wa pili wa gari lile na kufungua mlango wa nyuma wa upande ule na kuingia kwenye kiti cha nyuma cha gari lile. Akiwa kwenye kiti kisafi cha gari lake aliyoipenda sana, alipitisha mikono yake chini ya makwapa ya yule mtu na kuuvutia ndani ya gari mwili wote wa yule mtu na kumlaza chali pale kitini.
Aliteremka mbio-mbio na kuufunga ule mlango na moyo wake ukapiga sarakasi aliposikia sauti za watu zikielekea pale alipokuwa. Aligeuka kule zile sauti zilipokuwa zinatokea, na akaona kundi la watu likitokea upande wa ukumbi wa disko wa NK likielekea pale aliposimama huku wakiwa wameshika kitu kama mwenge. Miguu ikamwisha nguvu na akatamani atimue mbio aache gari na yule mtu pale pale, lakini alijipa moyo kuwa bado wale watu walikuwa mbali naye. Alikimbia haraka na kuzunguka upande wa pili wa gari na kuubamiza kwa nguvu mlango wa pili wa nyuma wa gari lake na kujitupa nyuma ya usukani na kutazama mbele.
Wale watu walianza kutimua mbio kuelekea kule kule alipokuwa huku wakimpigia kelele!
Duh!
Huku akitetemeka aliingiza gia na kukanyaga mafuta kwa nguvu zake zote. Gari lilivuma kwa nguvu lakini halikusogea hata kidogo!
Heeeh!
Clara alichanganyikiwa. Kwa nini gari halitaki kwenda tena? Aliinua macho na kuwatazama wale watu waliokuwa wakimwendea kwa kasi huku wakipiga mayowe yaliyoashiria kuua watu tu. Sasa aliwaona kwa ukaribu kuwa walikuwa wameshika marungu, fimbo, mapanga na wengine wakaanza kumrushia mawe.
Alikanyaga tena mafuta na kwa mara nyingine gari likavuma bila kwenda popote.
Jiwe kubwa likatua juu ya boneti la gari lake na yowe kubwa likamtoka, taharuki ikimtawala.
"Let's go goddammit! Move! " Alifoka kwa kuchanganyikiwa huku akijaribu tena kukanyaga mafuta ili gari liondoke, na gari likazidi kuvuma tu bila kusogea hata kidogo. Wale watu walizidi kuwakaribia huku wakizidi kupiga mayowe na jiwe jingine likajikita juu ya paa la gari lake.
Clara aliona nguvu zikimwishia hivi hivi. Jasho lilikuwa likimtiririka usoni na makwapani huku moyo wake ukitishia kuchomoka kutoka kifuani kwake kwa jinsi ulivyokuwa ukirukaruka kwa kasi isiyo ya kawaida.
"Sasa ni nini tena...jamaniii !" Alilalama huku akikanyaga tena mafuta. Gari bado liliendelea kuvuma likiwa palepale!
Alianza kulia kwa sauti kama mtoto. Aliinama na kutazama chini ya usukani kuhakikisha iwapo ufunguo ulikuwapo lakini alijua kuwa hilo si tatizo kwani taa za gari zilikuwa zinawaka na hivyo gari lilikuwa linafanya kazi vizuri. Sasa ni nini? Alipeleka mkono kwenye gia, na hapo moyo wake ukanywea alipogundua kosa lake.
Ah, bloody fool me!
Katika kiherehere cha kutimua mabio kutoka eneo lile, alikuwa ameweke gis kwenye “neutral” badala ya kwenye “drive”!
"Pumaaaaaaaaavvvv!" Alipiga kelele huku akihamishia gia kwenye sehemu ya “drive” na akikanyaga
breki na kuiachia huku akihamishia mguu kwa nguvu kwenye ile pedeli ya mafuta. Wale watu walikuwa kiasi cha hatua zipatazo kumi kutoka pale alipokuwa. Jeep Cherokee iliruka mbele kwa kasi kama jiwe lililoachiwa kutoka kwenye manati iliyovutwa kisawa sawa. Iliwaelekea kwa kasi mbaya wale watu waliokuwa na nia ya kuua. Jamaa walitawanyika na kuruka pembeni, kila mtu kwa uelekeo wake wakihofia kugongwa huku wakipiga mayowe ya woga na ghadhabu.
Clara alisikia mayowe na kelele zao alipowapita kwa kasi, wakimtukana na kumlaani kwa hasira. Yeye hakujali, aliongeza kasi huku machozi na kamasi vikimvuja bila mpangilio na moyo ukimdunda kwa mguvu. Alikata kona kwa kasi na kutimua vumbi zito, gari ikaserereka huku tairi zikitoa mlio wa malalamiko kabla ya kutulia barabarani sawia.
Kwa mara nyingine jiwe likatua juu ya paa la gari lake, naye akakanyaga mafuta zaidi. Jeep Cherokee iliunguruma kwa nguvu na wale watu waliokuwa wamepandwa jazba ya kuua waliambulia kukodolea taa nyekundu za gari lile zikitokomea katikati ya vumbi na kiza cha usiku ule.
_____________________http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jaka alifumbua macho taratibu na hapo hapo akayafumba baada ya kukutana na mwanga mkali wa taa. Kichwa kilikuwa kikimgonga kwa mbali na alihisi maumivu kwenye ubavu wake wa kulia. Aliendelea kulala kimya huku akiwa amefumba macho akijaribu kukumbuka kilichokuwa kimemtokea hata akawa amelala pale.
Kwamba pale hapakuwa nyumbani kwa mjomba wake Mnyaga lilikuwa wazi kabisa akilini mwake, kwani kitanda chake cha Makole hakikuwa na godoro laini namna ile. Aidha, kwa mzee Mnyaga hakukuwa na taa ya umeme hata moja kama ilivyo pale alipojikuta akiwa amelala muda ule.
Aliweza kukumbuka kuzongwa na watu wengi...na kumuona tena yule jamaa aliyeitwa Tony...
Ndiye haswa.
Tony...mzee wa You know what I am sayin'?
Tony...mshenzi wa tabia!
Alihisi maumivu mengine kwenye ugoko wake wa kushoto, na taratibu aliukunja mguu wake na kuupapasa ugoko wake, na kugundua kuwa ulikuwa umefanya uvimbe kidogo.
Kipigo.
Alikumbuka kuwa alipigwa sana. Hakuweza kukumbuka ni nani hasa aliyempiga...ila alikumbuka kuchezea kipigo kikali, na kumwagiwa petroli yenye harufu kali...
Hakukumbuka kitu kingine zaidi kuhusiana na tukio lililosababisha yeye kuwa pale wakati ule...
Hapana. Alikumbuka kuona taa za gari zikielekea kumgonga wakati yeye akiwa anagaragara barabarani, kisha akakumbuka kufikiwa na harufu nyingine, sio ya petroli, bali ya uturi mzuri wa kupendeza... kisha kote kukawa kiza.
Taratibu alifimbua macho na kuanza kukichunguza kile chumba alichokuwamo.
Kilikuwa na ukubwa wa wastani chenye dari nyeupe ya zege. Kwenye dari la chumba kile taa ndefu ya muanzi ilikuwa inawaka. Kuta za chumba kile zilikuwa zimepakwa rangi ya buluu bahari na ufito mwembamba wa rangi nyekundu kwa chini. Kitanda alichokuwa amelalia kilikuwa kimewekwa kwenye kona ya chumba kile, kikiwa chini ya dirisha moja kushoto kwake, wakati dirisha jingine likiwa kwenye ukuta uliokuwa upande ambao kichwa chake kilikuwa kimeelekea. Madirisha yote yalikuwa yamefunikwa kwa mapazia mazito ambayo yalisababisha mle ndani kuwe na kiza kilichoufanya mwanga wa ile taa iliyokuwa inawaka mle ndani uonekane kuwa ni mkali sana.
Ukuta uliokuwa mbele yake ulikuwa umepambwa kwa picha za wasanii mbali mbali wa filamu na muziki wa ndani na nje ya nchi. Mbele ya ule ukuta uliotapakaa picha za wasanii wale maarufu kulikuwa kuna meza ya kuandikia na kiti, ambapo juu ya meza ile Jaka aliona kompyuta mpakato na vitabu kadhaa.
Jaka akaguna, na wasiwasi ukampanda.
Muda wote ule alikuwa akihisi kwamba alikuwa kwenye wodi ya hospitali fulani, lakini zile picha pale ukutani na ile meza iliyokuwa na komyuta juu yake vilimhabarisha kuwa pale hapakuwa hospitali bali ni nyumbani kwa mtu.
Ni nani?
Ni mtu mwema au mwovu?
Ana nia gani na yeye hata akamuweka kwenye chumba kile kizuri na kisafi namna ile?
Ni wapi?
Akapeleka macho yake kwenye ukuta uliokuwa kulia kwake ambako ndiko kulikuwa kuna mlango wa kuingilia na kutokea ndani ya chumba kile na kuachia mguno wa fadhaa huku moyo ukimlipuka, kwani saa kubwa ilikuwa imetundikwa juu ya mlango ule ilikuwa inamwambia kuwa muda ulikuwa ni saa tano na robo!
Alitakiwa akaripoti kituo cha polisi!
Mungu wangu, leo Mgunya ataua!
Alikurupuka kutaka kutoka pale kitandani lakini alipambana na maumivu makali kifuani na kwenye mbavu. Alitoa mguno wa maumivu na kujilaza tena chali pale kitandani huku akigeuzia kichwa chake kwenye ukuta uliokuwa pembeni ya mlango wa chumba kile.
Na ndipo alipomuona.
Alikuwa amekaa kwenye kochi lililokuwa kando ya mlango ule hali miguu yake akiwa ameikunja na kuipandisha kwenye kochi lile na kuilaza kulia kwake na hivyo kufanya kiwiwliwili chake cha juu kulalia kushoto huku uzito wake ukiuegemea mkono wake wa kushoto ambao ulifanya "mbinu".
Alipomuona tu Jaka alijua kuwa alishawahi kumuona yule msichana mara kadhaa hapo kabla na alijua alimuona wapi.
Alikuwa ni yule msichana wa kwenye ile ndoto iliyokuwa ikimrudia mara kwa mara!
Mshituko alioupata safari hii ulikuwa mkubwa mno. Bila kujali maumivu yake alijiinua tena kutoka pale kitandani na kuketi huku akiwa amemtumbulia macho pima yule msichana. Midomo ilimcheza, pua zilimtanuka. Alijaribu kumeza mate akashindwa kwani ghafla koo likamkauka kwa namna ya ajabu kabisa, huku moyo nao ukimwenda mbio haijawahi kutokea.
Mawazo mengi sana yalipita kichwani mwake ndani ya zile sekunde chache ambazo yeye aliziona kama masaa. Alikuwa anaota...? Au alikuwa anaanza kupatwa wazimu?
Au yule mwanamke ni jini?
Yaani ameanza kumjia ndotoni na sasa ameamua kumchukua kabisa na kumleta nyumbani kwake?
Ina maana hapa ndio ujinini au...?
Hapana. Haiwezekani.
Kama haiwezekani hapa ni wapi basi?
Alijua kuwa ile haikuwa ndoto, lakini yule mwanamke....!?
Muda wote huo yule binti alikuwa akimwangalia tu huku akitabasamu.
"Naona umeamka hatimaye...karibu tena duniani kaka..." Hatimaye yule binti aliongea huku akiendelea kutabasamu na kuteremsha miguu yake sakafuni kutoka kwenye kochi.
Sauti!
Ile sauti!
Jaka aliikumbuka ile sauti...!
Alishawahi kuisikia...wapi?
Sasa aliamini kuwa yule msichana alikuwa jini. Alikumbuka kusikia simulizi kwamba miguu ya majini wa aina ile huwa sawa na kwato za punda au farasi. Haraka aliitupia macho miguu ya yule binti.
Ilikuwa ya kibinadamu.
Sasa ni kitu gani?
"Usiwe na wasiwasi wala usiogope..." Yule binti alimwambia kwa upole huku akimsogelea pale kitandani. Jaka aliendelea kumkodolea macho akiwa mdomo wazi.
Naikumbuka hii sauti ...na hii sura...kwa nini?
"Wewe!" Jaka alimaka ghafla, na yule binti akisimama kwa mshituko.
Naam, Jaka alimkumbuka yule binti. Sasa mambo yote yalikuwa yakimjia vizuri akilini mwake.
Yule ndiye haswa binti wa kwenye ile ndoto ya ajabu.
Lakini pia aligundua kitu kingine. Kwa nini siku zote alikuwa akipatwa na hisia kuwa yule binti wa kwenye ile ndoto, aliyekuwa akimuota akimjia na taa na mwamvuli katika usiku wa kiza kizito na mvua kubwa ambayo maji yake ni ya moto, alikuwa amewahi kumuona sehemu fulani kabla ya ndoto ile ingawa hakuweza kukumbuka ni wapi.
Sasa alipata jibu.
Akiwa pale kitandani akimkodolea macho yule binti, akili yake ilirudi nyuma siku nyingi zilizopita, katika mji mwingine kabisa.
Alikumbuka kupamiana na yule msichana kwenye kichochoro kimoja ndani ya usiku mmoja wenye kiza kizito na mvua kubwa. Alikumbuka jinsi yule binti alivyokuwa akimuomba msamaha asimdhuru usiku ule, kabla hawajavamiwa na vibaka wanne na pamoja kujikuta katika wakati mgumu sana...
Ndiye huyu binti aliyejaribu kumsaidia usiku ule wa kiza kizito ndani ya jiji la Dar, na matokeo yake nusura na yeye auawe. Ni huyu msichana ambaye kama asingejitolea kumsaidia usiku ule, hata yeye asingekamatwa tena na polisi na kujikuta akihamishiwa Dodoma chini ya ulinzi mkali na kulazimika kuishi maisha ya kikimbizi ndani ya nchi yake mwenyewe.
Na ndiye huyu huyu aliyekuwa akimuona kwenye ile ndoto ya ajabu.
Sasa tena ni huyu huyu msichana leo hii, kiasi cha kilomita zisizopungua mia nne kutoka kwenye mji aliokutana nae kwa mara ya kwanza, tena katika mazingira ambayo hakuyategemea kabisa, anakutana nae tena kwa namna ile ile ambayo yeye hakuweza kutegemea...na bila shaka ni huyu binti ndiye aliyemuokoa kutoka kwenye kile kipigo kikali cha usiku uliopita...
"Wewe...wewe, una...fanya nini hapa...yaani mbona mimi niko hapa....aa..aaa...namaanisha...nimefikaje... hapa...yaani hapa ni wapi...?" Jaka alibaki akibwabwaja huku akizidi kumkodolea macho yule binti kutoka ndotoni.
"Tulia tu kaka’angu, tulia. Hapa uko salama. Unahitaji kupumzika." Yule binti alimwambia kwa upole huku akimuwekea viganja vya mikono yake laini kifuani na kumlaza tena kitandani. Ndipo Jaka alipogundua kuwa alikuwa amefunikwa shuka zito ambalo alipojiinua liliteremka na kuacha kifua chake kikiwa wazi, lile shuka lilimfunika sehemu ya kiuno kuteremka chini.
"Shati langu liko wapi?" Alimuuliza yule binti kwa wasiwasi huku akifumbata mikono yake kifuani.
"Nguo zako zote zilikuwa hazitamaniki kabisa na wala hazifai tena kuvaliwa..." Yule binti aliendelea kumjibu kwa upole huku akitabasamu.
Nguo zako zote?
Haraka Jaka alipeleka mkono wake chini ya ile shuka na kujipapasa ili kuhakikisha iwapo alielewa sawasawa. Naam, alikuwa ameelewa sawasawa, kwani suruali na nguo yake ya ndani vyote havikuwapo! Alikuwa uchi wa mnyama chini ya lile shula!
Aka!
Alimuinulia uso wa mshangao yule msichana.
“Umenifanya nini kingine wewe, eenh?” Alimuuliza kwa ukali.
Binti hakuonesha kubabaika wala kuwa na wasiwasi juu ya ukali wake.
"Sijakufanya chochote kingine zaidi ya kukuosha mwili mzima...”
“Mwili mzima...?”
“Of Course! Mtu ulikuwa umetapakaa damu, vumbi na umemwagiwa petroli mwili wote... nisingeweza kukulaza hivyo hivyo bila kukusafisha, au we’ unaonaje?" Alimjibu, na kabla Jaka hajaongea lolote aliendelea, "Umepoteza fahamu kwa saa takriban kumi na matatu hivi tangu nilipokukuta umetupwa pale barabarani. Nilidhani hutaamka tena...lakini daktari niliyemleta alisema kuwa ungeamka tu. Ila itabidi upumzike sana..."
Akili ya Jaka ilikuwa inafanya kazi kwa kuruka ruka na hakuweza kuzingatia maneno yote aliyokuwa akiambiwa na yule binti. Alimkumbuka Osman Mgunya.
"Sasa mimi inanibidi niondoke...ni lazima niende....nipe nguo zangu sasa hivi!" Alimaka huku akizidi kujitahidi kuinuka kutoka pale kitandani.
"Uende wapi? We' unahitaji kupumzika sana na unahitaji ule vizuri...huwezi kwenda popote katika hali hiyo. Unaweza kuanguka njiani!" Binti alimpinga vikali.
Jaka alitamani amfokee, amueleze kuwa binti kama yeye hawezi kuelewa kwa nini ni lazima Jaka aende kuripoti kituo cha polisi, na tena asizoee tena kumuuliza kuhusu anataka kwenda wapi.
Lakini alijizuia.
Alijua kuwa yule binti ndiye akiyeokoa maisha yake kutokana na kifo kibaya usiku uliopita.
"Anti sikiliza...kwanza samahani sana kwa kukutolea ukali. Halafu naomba nikushukuru sana kwa msaada wako..."
"Bila samahani kaka. Mimi naelewa kuwa imekuwa vigumu sana kwako kuelewa mambo yote haya...hasa kwa jinsi ambavyo tumekuwa tukikutana kiajabu-ajabu, na kwa nini mimi niamue kukuchukua na kukuleta hapa wakati hatujuani kiasi hicho....nadhani sasa umenikumbuka? Mimi nilikukumbuka jana nilipokukuta ukiwa umetupwa barabarani ndio maana niliamua kukuchukua na kukuleta hapa..." Binti alidakia kabla Jaka hajamaliza kutoa maelezo yake, na kuendelea huku akitabasamu, "...bila ya wewe kujitolea nafsi yako kunisaidia mimi siku nyingi zilizopita kule Dar, bila shaka mimi nisingekuwa hai leo hii."
Jaka alimtazama yule binti na moyo wake ulijaa shukurani. Hakuona kuwa alilolifanya yeye kwa yule binti siku nyingi zilizopita kuwa lilikuwa na umuhimu wowote kulinganisha na yale aliyofanyiwa na binti yule usiku uliopita.
"Asante sana dada...lakini nasikitika kwamba mimi ni lazima niondoke...natakiwa niwe sehemu fulani...ni muhimu sana. Sasa...naweza kupata nguo zangu tafadhali?" Alimwambia kwa upole ili kumfanya yule binti aelewe.
"Ni matatizo yako na polisi, sio?" Binti alimuuliza huku akimkazia macho kwa makini.
Jaka alimtazama machoni kwa muda, kisha akaafiki kwa kichwa.
"Basi nitakupeleka." Binti alimwambia huku akiinuka kujiandaa na safari.
Jaka alilipinga vikali swala hilo lakini yule binti alitoka nje ya chumba kile bila kujali, kama kwamba alikuwa hamsikii. Aliporudi alikuwa ameshavaa viatu vya raba na suruali ya jeans iliyomkaa vyema na fulana kubwa nyeupe iliyokuwa na nembo ya bendera ya Tanzania kifuani. Alipendeza sana. Alimuwekea nguo kando yake pale kitandani.
"Vaa nguo hizi halafu nikupeleke huko unapotaka kwenda, okay?" Alimwambia.
"Sio Okay, kwa sababu sidhani kama ni vyema kwa mtu kama wewe kujihusisha na mimi...We' hujui nimefanya nini mpaka nikapatwa na yale uliyoyaona na kuyasikia pale kituo cha polisi kule Dar...na hujui ni kwa nini nipo Dodoma hivi sasa..." Jaka alimpinga.
"Fanya upesi usije ukachelewa zaidi huko unapotakiwa kwenda." Binti alimhimiza kama kwamba hakuwa amemuwekea pingamizi.
"Sawa, lakini naenda peke yangu...kwani hata nikianguka njiani wewe utaweza kunibeba?" Jaka alimjia juu. Badala ya kumjibu, yule msichana alianza kutoka nje ya chumba na alipofika mlangoni alimgeukia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kwani hujajiuliza jana niliwezaje kukufikisha hapa? Vaa upesi twende mwanamume...mi' nakusubiri hapa nje." Kisha akatoka na kufunga mlango.
"Shit!" Jaka alilaani huku akiinuka na kuanza kuvaa zile nguo. Hazikuwa nguo zake. Zilikuwa ni nguo nyingine kabisa.
Sijui hizi ni nguo za mumewe?
Alijiuliza huku akivaa chupi ambayo aligundua kuwa ilikuwa ni mpya kabisa, kwani bado ilikuwa ndani ya mfuko wake wa nailoni. Alivaa suruali ya jeans ambayo ilimkaa vizuri ila ilikuwa fupi kidogo. Akamalizia na fulana nyeusi ambayo ingeweza kuwa ya msichana na ilimbana kidogo. Aliona viatu vya raba pale chini ya kitanda, akavijaribu. Vilimkaa, lakini kiasi vilimbana.
Alitoka nje ya chumba kile akijua wazi kuwa alikuwa hakupiga mswaki.
Hakujali.
5
Maisha ya Jaka yalibadilika kwa kiasi kikubwa sana baada ya kukutana tena na yule binti wa ajabu aliyekutana naye kwa mara kwanza jijini Dar katika usiku wa kiza kinene na mvua kubwa. Bila ya kuamini ukweli wa mambo yale, alijishuhudia akibadilika kutoka kuwa mtu hohehahe asiye na mbele wala nyuma, na kuwa mtu mwenye mwelekeo mzuri wa maisha na matumaini ya maisha mazuri zaidi kwa siku za mbeleni. Ilikuwa ni ajabu na vigumu kwake kuamini, lakini ndivyo ilivyokuwa.
Miezi mitatu baada ya kukutana tena na Clara katika yale mazingira ya ajabu pale Dodoma, Jaka alikuwa amekwisha kutana tena na binti yule mara kadhaa na walikuwa wameongea mambo mengi ya kimaisha. Ingawa Jaka hakutaka kumwelezea ukweli juu ya matatizo yake, Clara alionesha kujali zaidi kuwa naye kuliko kujua matatizo yake, na hilo lilimpa Jaka wepesi katika kuendelea kuonana na kuongea na yule binti.
Matunda ya makutano yao hayo ya mara kwa mara yalikuwa ni Clara kufanikiwa kumshawishi baba yake kumpatia Jaka ajira kwenye kampuni yao ya ZazaCargo Movers kama msaidizi wa afisa ugavi wa kampuni ile. Alipatiwa mshahara mzuri na hivyo katika muda wa miezi miwili tangu apatiwe ajira ile, Jaka aliweza kurudia muonekano ule ule aliokuwa nao kabla ya kukutana na masahibu yaliyomkutanisha na yule binti kwa mara ya kwanza kule jijini Dar.
Lakini Clara hakuishia hapo. Baada ya Jaka kumtambulisha kwa mzee Mnyaga, Clara alimpatia yule mzee ajira katika ile kampuni yao kama utingo kwenye magari yao yaliyokuwa yakisafiri kuelekea nchi mbali mbali barani Afrika. Hivyo na maisha ya mzee Mnyaga pia yalibadilika na kuwa bora zaidi, kwani mshahara aliokuwa akilipwa na posho za safari za nje ya nchi vilikuwa ni vikubwa kuliko alivyowahi kutarajia. Nyumba yake ilibadilika na kuwa nzuri na imara zaidi, ingawa mwenyewe alikuwa safarini muda mwingi.
Ingawa Jaka alikuwa na uwezo wa kupanga chumba na kuishi mwenyewe, au hata kuishi nyumbani kwa Mnyaga, Clara alimuomba sana aendelee kukaa naye ndani ya nyumba yake, jambo ambalo lilipingwa vikali na Jaka pamoja na mzee Wilfred Mashauri Zaza, baba yake Clara, lakini lilitetewa kwa nguvu na Clara mwenyewe pamoja na mzee Mnyaga. Hatimaye Clara alifanikiwa na Jaka akaendelea kuishi mle nyumbani kwake kwenye chumba kile kile alichokuwa amelazwa baada ya kuokolewa na Clara kutoka kwenye kipigo kikali.
Jaka alipewa ruhusa ya kutumia magari ya kampuni kwa kazi za kiofisi na hata kwa safari zake binafsi. Hali hii ilimfanya ajisikie vizuri sana, kwamba ingawa hakuwa nyumbani kwao kama ambavyo angetaka, angalau alikuwa akiishi kama binadamu wengine. Hata hivyo, bado hakusahau sababu za kuwepo kwake pale Dodoma na bado alikuwa akihesabu siku zilizobaki kabla hajarudi tena kwenye maisha yake ya hapo awali, ingawa sasa alianza kupata mashaka kama alitaka tena kurudi huko.
Lakini asubuhi ya siku hii, ikiwa ni miezi mitatu tangu akutane tena na Clara pale Dodoma, Jaka hakuwa akijisikia vizuri hata kidogo. Alikuwa akiendesha gari la Zaza Cargo Movers aina ya Suzuki Vitara kuelekea kazini akitokea kuripoti kituo cha polisi kama kawaida huku kichwani akiwa amezongwa na mawazo mazito. Mawazo yaliyomzonga yalitokana na ukweli kwamba jambo alilokuwa akilihofia siku zote tangu akubali kuhamia nyumbani kwa Clara, sasa kilikuwa linajitokeza.
Clara alikuwa akimtaka kimapenzi.
Hilo aliligundua mapema mno na hilo ndilo jambo alichokuwa akilihofia siku zote. Yeye hakuwa tayari kabisa kujihusisha kimapenzi sio tu na Clara, bali na msichana yeyote maishani mwake. Alishajihusisha na mapenzi hapo nyuma, tena mapenzi mazito kabisa, lakini yaliyompata...!
Alikata kona na katika mtaa mfupi ambao ndio ofisi za Zaza Cargo Movers zilikuwepo. Baada ya kufunguliwa geti kubwa na kuingia ndani ya uzio mpana wa eneo la ofisi zile, aliegesha gari na kuelekea moja kwa moja kwenye jengo kubwa ambamo ofisi yake ilikuwamo. Kabla hajalifikia lango kuu la kuingilia ndani ya jengo lile, yule mlinzi aliyemfungulia geti alimwita huku akimkimbilia. Jaka alisimama na kumsubiri.
"Samahani sana mista Brown..." Alisema huku akitweta yule mlinzi, kwa lafudhi ya kigogo.
"Bila samahani Chonya, unasemaje?" Jaka alimjibu. Pale ofisini watu wote walimjua kwa jina la Brown Madega.
"Hapana mzee...ila kuna jambo tu nilitaka nikueleze. Juzi usiku nilikuwa zamu hapa. Kiasi cha saa tatu usiku hivi, alikuja mtu mmoja hapa getini nami nikamwambia kuwa haukuwa muda wa kazi hivyo aje asubuhi. Yeye akasema ana shida na mimi, ya kwamba alitaka nimjulishe iwapo kuna mtu yeyote hapa ofisini anayeitwa Jaka, unaona bwana?" Yule mlinzi alimwambia, na Jaka akauhisi moyo ukimpiga chogo chemba ndani ya kifua chake, lakini alijitahidi kuendelea kusikiliza.
"...Sa' mi' nikamwambia kuwa wafanyakazi wote wa humu ndani nawajua, na hakuna hata mmoja mwenye jina hilo, au vipi bwana? Jamaa akaondoka zake akidai kuwa labda alikuwa amepotea." Chonya akaweka kituo.
Jaka alianza kufikiri haraka haraka. Ni kweli kwamba pale ofisini yeye alijulikana kwa jina la Brown Madega, lakini hakuna mtu yeyote zaidi ya Clara aliyelijua jina la Jaka. Alishakubaliana na Clara kuwa jina hilo lisitumike kabisa pale ofisini, kwa sababu za kiusalama. Maswali mengi yalipita kichwani mwake katika muda ule mfupi aliobaki kimya akitafakari maelezo yale. Ni nani huyo aliyekwenda kumuulizia pale ofisini, akimtaja kwa jina la Jaka? Kwa nini aende usiku wakati akijua fika kuwa yeye hatokuwepo? Ofisi ya RPC ilikuwa ina taarifa na kuwepo kwake pale Zaza Cargo Movers, naye alikuwa ana ruhusa maalum kutoka kwa mzee Januari Mwakaja ya kufanya kazi pale, kwa hivyo haiwezekani huyu mtu awe ametoka polisi...
"Uliweza kumuona sura yake huyo mtu?" Hatimaye alimuuliza yule mlinzi.
"Enhee.. sasa hilo ndilo jambo jingine la ajabu kuhusu yule mtu, kwa sababu alikuwa amevaa kofia kubwa ya pama iliyoficha uso wake, halafu alikuwa amevaa koti refu jeusi lililofika mpaka magotini...unajua mi' nilimuona kama jambazi tu..." Chonya alimjibu, na kumchanganya zaidi.
"Hakutaja jina lake au sehemu anayotokea...? "
"Hapana...hakunipa nafasi ya kumuuliza maswali mengi. Nilipomjibu vile tu, akadai kuwa amepotea njia, akaondoka."
Jaka aliyatafakari kwa muda maelezo yale kabla ya kuuliza, "Hebu subiri kidogo, we' si umesema alikuja usiku? Sasa ulijuaje kuwa koti lake lilikuwa jeusi? Lingeweza kuwa la buluu au kahawia!"
"Sawa kabisa, ila unajua kwa nini? Kwa sababu leo asubuhi amekuja tena na nguo zile zile kama za siku ile."
Hapo Jaka alizidi kupata wasiwasi.
"Sasa...Dah! Sasa kwa nini unadhani mimi napaswa kujua juu ya hilo? Si ulishamwambia kuwa hapa hakuna mtu anayeitwa Jaka...?"
Yule mlinzi alimtazama Jaka kwa macho makavu na taratibu alimwambia huku akiendelea kumtazama
"Kwa sababu leo asubuhi ameniuliza kama kuna mtu aitwaye Brown Madega...Jaka Brown Madega.
“Eeenh?"
“Ndiyo bosi!" Chonya alithibitisha habari ile, na kuendelea, “Sasa mi' najua kuwa wewe unaitwa Brown Madega....sasa aliposema Jaka Brown Madega moja kwa moja nikahisi kuwa ni wewe!"
Ingawa sasa moyo wa Jaka ulikuwa anaenda mchaka-mchaka ndani ya kifua chake, alifyatua tabasamu la ghafla usoni kwake.
"Ah! Basi lazima huyo atakuwa ni mmoja kati ya jamaa niliosoma nao sekondari....hilo jina niliacha kulitumia zamani sana baada ya kumaliza sekondari..." Alijikausha na kumjibu yule mlinzi huku akitabasamu. Aliona uso wa yile mlinzi ukisajili mshangao tu. Hakumpa muda wa kufikiri wala kuongea zaidi.
"Ahsante sana Chonya kwa taarifa hii. Basi akija tena usisite kunieleza...na nitahitaji kuonana naye, sawa?" Alimwambia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Bila shaka mzee...!" Chonya alijibu na Jaka akaondoka haraka kuelekea ofisini kwake huku akimwachia noti ya shilingi elfu mbili yule mlinzi ambaye alifurahi sana na kuahidi kuwa pindi yule jamaa akitokea tena atampa taarifa.
Ni kitu gani tena kinataka kujitokeza sasa?
Alikuwa akijiuliza huku akifungua mlango wa ofisi yake iliyokuwa ghorofa ya pili ya jengo lile la ghorofa tatu.
Sasa kichwabi mwake kulikuwa kuna mgongani wa mawazo.
Kwanza kuna swala la Clara ambalo bado alikuwa hajalipatia ufumbuzi, sasa tena anatokea na huyu mtu mwenye makoti marefu na kuanza kuulizia habari zake...
Ni nani huyu mwenye kuvaa koti refu jeusi na kofia kubwa ya pama?
Na kikubwa zaidi...anamtakia nini?
Alijikuta anarudi pale pale. Hakuna jibu.
Na bado kuna tatizo la Clara.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment