Sehemu Ya Pili (2)
Clara...ina maana amemfanyia mambo yote haya....wema wote huu...kwa vile alikuwa na matakwa yake binafsi?
Jaka aliliona hilo ni gumu kuamini, kwani kadiri alivyokuwa akilitafakari, alishindwa kujiridhisha kuwa halikuwa hivyo.
Kwanza yule binti alijihatarishia maisha yake alipojitolea kumuokota pale alipopigwa na kutupwa barabarani usiku ule alipoonana tena na yule mshenzi wa tabia, Tony. Zaidi ya hapo alijitolea kumtibu na kumhudumia ndani ya nyumba yake, bila ya kujali kuwa angeweza kuwa mwizi au muuaji na kumdhuru. Asiishie hapo yule binti, akajitolea kumkaribisha ahamie nyumbani kwake, ampe chumba ndani ya nyumba yake aishi, bure....!
Kama hiyo haitoshi, bado binti yule alimfanyia wema wa kumpatia kazi kwenye kampuni ya baba yake, kazi iliyompatia kipato kizuri, na gari la kuendea kazini na kutembelea kampa!
Haya yote hayawezi kuwa bure...na ingawa Clara mwenyewe alisisitiza kuwa hayo yote hayawezi kufikia wema ambao Jaka alimfanyia kwa kujitolea kuokoa maisha yake usiku ule wa mvua kubwa kule Dar es Salaam zaidi ya mwaka mmoja uliopita, bado Jaka hakuamini kuwa hiyo ndio sababu pekee.
Na sasa mashaka yake hayo yalikuwa yamethibitishwa. Ni kweli kulikuwa na sababu nyingine zaidi ya hiyo. Aliingia kwenye ofisi yake ndogo na nzuri, akaketi nyuma ya meza ya mninga iliyokuwa ikiutazama mlango. Mbele ya meza ile kulikuwa kuna viti vingine viwili ambavyo viliwekwa kuitazama ile meza. Baada ya muda mfupi aliinuka na kutembea taratibu juu ya zulia zito la rangi ya zambarau lililonakshiwa kwa maua mekundu na kwenda kusimama nyuma ya dirisha kubwa lililokuwa nyuma ya kiti chake likitazamana na mlango. Alifungua pazia zito la rangi ya zambarau lililokuwa limefunika dirisha lile. Lilikuwa ni dirisha la kioo kitupu ambacho aliweza kukifungua na kukifunga pindi atakapo. Hakutaka kukifungua.
Kutokea pale dirishani aliweza kuiona Jeep Cherokee ya Clara ikiwa imeegeshwa kule chini, kando ya gari alilokwenda nalo yeye pale ofisini. Alielewa kuwa Clara alikuwa ameshafika pale ofisini. Ilikuwa ni kawaida kuwa ingawa walikuwa wakiishi pamoja, siku zote Jaka alikuwa akitangulia kuondoka na kumwacha Clara akiwa bado amelala au ndio anaamka. Ilibidi iwe hivyo kwa sababu wote walielewa kuwa Jaka alilazimika kupitia kituo cha polisi kuripoti kabla ya kufika ofisini. Vilevile hawakupenda kwenda pamoja ofisini ili kuepusha kupandikiza mawazo potofu kwa wafanyakazi wa pale ofisini zaidi ya yale ambayo tayari yalishapandikizwa kutokana na wao kuishi nyumba moja, kwani ingawa walilala vyumba tofauti, watu wa nje hawakujua hilo.
Aliaendelea kusimama pale dirishani akiangalia kule nje huku akiwa katika lindi la mawazo, kisha alishusha pumzi ndefu na kurudi kuketi pale kwenye kiti chake nyuma ya ile meza na kuendelea na mawazo yake huku akiwa amejishika tama na uso ameukunja kwa uzito wa mawazo aliyokuwa nayo.
__________________
Tangu akutane tena na Clara pale dodoma, wamekuwa marafiki wakubwa sana. Kitu ambacho Jaka alikitilia mkazo sana akilini mwake siku zote ni kwamba urafiki ule usivuke mipaka na kuingia kwenye hatua ya mapenzi. Kwanza Clara alikuwa tajiri sana na hivyo aliamini kuwa asingekuwa na haja ya kutaka kujihusisha na mtu kama yeye kimapenzi; kwa hiyo vile Clara kuweza kuwa na urafiki wa heshima tu na yeye ni jambo lililomfanya Jaka amheshimu sana. Angekuwa ni mtu asiye na heshima wala shukurani iwapo pamoja na yote yale ambayo Clara amemfanyia, na heshima yote ambayo Clara amemuonesha, bado tena angemtaka binti yule kimapenzi. Hilo halingewezekana asilani, na Jaka hakuwa na wasiwasi hata kidogo kuwa angeweza kumvunjia Clara heshima hata siku moja.
Ni kweli Clara alikuwa ni msichana mwenye sura ya kuvutia na umbo la nzuri, lakini pia Jaka hakutaka kujidanganya kuwa atakuwa amekaa miaka yote hiyo aliyokaa na uzuri ule asipate mtu yeyote wa kumpenda mpaka aje atokee yeye ndio ampende...kwani yeye ni nani? Katika watu wote Dodoma ile, akae bila mpenzi hata mmoja mpaka atokee Jaka, mtuhumiwa na hatimaye mhukumiwa wa kosa la mauaji, ndio aje apendane naye?
Hapana, hiyo halikuwezekana, na Jaka alikuwa na akili timamu kuelewa hivyo.
Sasa cha ajabu ni kwamba, ni Clara mwenyewe ndiye ambaye anaonesha kumtaka Jaka kimapenzi! Alishafanya visa kadhaa wa kadhaa vya kumuonesha Jaka kuwa alikuwa tayari kumridhia kwa lolote atakalo...
Kuna siku alimuuliza iwapo Jaka alikuwa na mpenzi kabla ya kuja kwake Dodoma.
"Ni ajabu mtu handsome kama wewe kukosa girlfriend...." Clara alijibu baada ya Jaka kumueleza kuwa hakuwa na mpenzi kabla ya kuja Dodoma. Hakutaka kumueleza ukweli juu ya maisha yake yaliyopita, kwani alikuwa ana nia ya kufunua ukurasa mpya katika maisha yake na hakutaka kujikumbusha yale yaliyopita. Walikuwa wamekaa sebuleni kwa Clara usiku ule wakiangalia video. Clara alikuwa amevaa suruali ya mazoezi na fulana kubwa, wakati Jaka alikuwa amevaa suruali yake ya Jeans na sweta zito, miongoni mwa nguo nyingi alizoweza kununua kutokana na fadhila za ajira aliyopatiwa na Clara.
Kwa hiyo wewe unadhani mimi ni handsome.
Jaka alijiwazia kichwani siku ile lakini hakusema kitu, alibaki kimya.
Taratibu Jaka alianza kujishughulisha na kazi za pale ofisini huku mawazo yale yakimrudia mara kwa mara.
Siku nyingine wakati Jaka akiwa amekaa kwenye kochi refu pale sebuleni akiangalia runinga, Clara alikuja na kujilaza kwenye kochi lile huku akilaza kichwa chake mapajani kwa Jaka. Kwa mshangao Jaka aliinamisha uso wake na kumtazama. Kwa kweli ilikuwa ni picha ya kuhamasisha hisia za mapenzi kwa kiasi kikubwa, kwani nywele zake ndefu na laini alikuwa amezitimua kivivu na gauni lake la jioni la kitambaa chekundu cha hariri, liliongezea mvuto wa hisia zile za mapenzi na Jaka alihisi moyo wake ukibadili mapigo.
Wakati Jaka alipoinamisha uso wake kumtazama kwa mshangao namna ile, Clara naye aliinua uso wake na kumtazama huku akitabasamu, na ilimchukua Jaka sekunde kadhaa kabla hajakumbuka kuwa alitakiwa ashangazwe na kitendo kile.
"Vipi...nikupishe ulale vizuri nini...?" Hatimaye alimuuliza huku akijaribu kujisogeza ili kumpa Clara nafasi ya kujilaza vizuri pale kwenye kochi.
"Kwa nini...mi' napenda tukae hivi hivi tu..." Clara alijibu huku akijilaza vizuri zaidi mapajani kwake.
Usiku ule Jaka hakulala kwa mawazo. Jambo ambalo aliazimia kutolianzisha baina yake na Clara lilikuwa linaanza kujitokeza, na siyo yeye aliyekuwa analianzisha.
Ataweza kulizuia?
Baada ya kutafakari hali ile kwa muda mrefu, alipitisha uamuzi usiku ule kuwa ifikapo asubuhi, angefungasha virago vyake na kuihama nyumba ile, na ikibidi kufukuzwa kazi kwa kufanya hivyo potelea mbali...
Kumbukumbu zake hizo zilikatishwa na hodi iliyobishwa kwenye mlango wa ofisi yake. Alipaza sauti kumkaribisha mgongaji, na Clara akaingia na kumsalimia kwa uchangamfu.
"Hey! Mambo ?"
Jaka alimtazama yule binti. Kwa hakika alikuwa amependeza sana.
"Ah, safi tu Clara..." AliMjibu, lakini si kwa uchangamfu kama jinsi Clara alivyomsalimia. Hali hiyo ilimfanya Clara asimame mbele ya meza yake pale ofisini kwa muda huku akimtazama kwa macho ya wasiwasi.
"Hey, what's the matter with you? Mbona umechukia?" Alimuuliza kwa mashaka, akimaanisha kutaka kujua alikuwa ana tatizo gani.
"Eeenh? No!...sijachukia...niko sawa..." Jaka alimjibu, ingawa ilionekana wazi kuwa hali haikuwa sawa.
Clara alimwangalia kwa sekunde kadhaa.
"Samahani, nilikuwa nimekuja kukusalimia tu." Hatimaye alimwambia kwa kisirani, kisha akageuka na kutoka nje ya ofisi ile.
"Clara..." Jaka alijaribu kumuita kabla hajatoka nje, lakini Clara hakusimama wala hakugeuka.
Hakuweza kufanya kazi vizuri siku yote ile kutokana na kutawaliwa na mawazo mengi. Ilikuwa ni kawaida pale ofisini kuwa kila ifikapo saa nne asubuhi, wafanyakazi wanaelekea kantini pale pale ofisini kupata chai. Alitegemea kuwa angemkuta Clara kantini, kwani walikuwa na mazoea ya kukaa meza moja kila siku na kunywa chai huku wakiongea, na baada ya hapo kila mmoja alielekea ofisini kwake.
Siku ile hakumkuta.
Alitembeza macho huku na kule ndani ya ile kantini bila kufanikiwa kumuona. Aliagiza chai na kuanza kunywa taratibu akitarajia kuwa Clara angefika na kumkuta pale kantini. Wakati akinywa chai ile taratibu, mawazo yake yalirudia tena kwenye matukio mbalimbali yaliyotokea baina yake na Clara...
____________________
Alikumbuka kuwa baada ya tukio la usiku ule ambao Clara aliamua kujilaza mapajani mwake, asubuhi yake aliamka akiwa na wazo la kuhama upesi sana kutoka kwenye nyumba ile kabla mambo hayajaharibika. Na asubuhi ile Clara aliamka akiwa na homa kali sana. Hakuwa na namna, akalazimika kuahirisha mpango wake ule kwa muda mpaka Clara atakapopona.
Ikawa anamhudumia kwa kumkorogea chai, kumtengenezea juisi na kumhimiza kunywa dawa, kwani Clara alikuwa mwoga sana wa kumeza dawa.
Katika wiki moja ile aliyougua, ukaribu wao ukaongezeka maradufu. Na Clara alivyojua kujidekeza sasa! Ikawa halali usingizi mpaka alale mapajani mwa Jaka, ambaye alilazimika kukaa naye hivyo hivyo mpaka alale, ndipo alipomlaza kitandani taratibu na kutoka kwenda kulala chumbani kwake.
Jaka alijiuliza ingekuwaje iwapo akiondoka halafu binti yule akapata ugonjwa wa ghafla wakati yuko peke yake mle ndani. Alijipa moyo kuwa kabla ya ujio wake si alikuwa akiishi peke yake?
Alikumbuka jinsi alivyolijadili swala la Clara na mjomba wake Mnyaga.
"Kwani we' wasiwasi wako nini mjomba?" Mnyaga alimuuliza.
"Aakh! Anko...mi' siwezi kujihusisha naye kimapenzi..."
"Kwa nini?"
“Kwanza sijui kama hana au hakuwa na mpenzi mwingine kabla yangu.
“Si umuulize? Si uulize watu wanaomjua kabla yako? Si uchunguze? Acha hizo anko!”
“Akh, sasa yote hayo ya nini na mi’ sina nia naye? Isitoshe, iwapo anaweza kufanya hivi kwangu, ni watu wangapi kabla yangu ambao amewahi kuwanasa kwa kutumia utajiri wake?” Jaka alimjibu. Mnyaga alimcheka sana kwa jibu lile kiasi cha kumkera.
“Sasa Anko we’ unaona hili ni jambo la kuchekesha?”
“Hapana. Hili si jambo la kuchekesha, ila wewe ndio kichekesho.”
“Khaa!”
“Ndio.”
“Sasa ndio majibu gani hayo mjomba!”
“Mimi nimeanza kumuona yule binti kabla yako, Jaka. Na kama angekuwa ana tabia kama hizo ambazo wewe unamdhania kuwa anazo, basi mimi ndio ningekuwa wa kwanza kukueleza kuwa huyo binti si mwema...”
“We’ ungejuaje Anko? Wanawake hawatabiriki hata kidogo mjomba! Niulize mimi bwana...achana nao kabisa!”
Jibu hilo lilimfanya Mnyaga acheke kwa mara nyingine. Kwa mara nyingine Jaka alikereka kuchekwa namna ile.
“You think this is funny? We’ Anko hili jambo lote unaliona mzaha tu, eenh?”
“Sio hivyo msomi wangu...lakini kama ungekuwa umekaa hapa duniani kwa muda mrefu kama mimi ungeelewa...lakini wewe bado mgeni na mambo mengi sana hapa duniani anko; bado kijana sana wewe, na ndio maana hutakiwi kukimbia mambo kama haya,unatakiwa uyaelewe halafu uyapeleke jinsi utakavyo...utajificha mpaka lini?”
Jaka alibaki akimkodolea macho tu. Mnyaga akaendelea, “Jaka yule msichana anakupenda! Tena anakupenda kwa nia nzuri tu. Na hili sio swala la ajabu au geni hapa duniani, kwa mtu mmoja kutokea kumpenda mwingine...sasa wewe badala ya kuchangamkia nafasi hiyo unachukia? Au umesahau?"
Jaka aliendelea kumtazama Mnyaga kwa mshangao.
"Nimesahau...? nimesahau nini tena!"
Mnyaga alimkazia macho na kumwangalia Jaka moja kwa moja machoni kwa muda kabla ya kumjibu.
"Ndoto Jaka....ile ndoto uliyokuwa ukiiota tena na tena...huoni kuwa ndio maana yake inazidi kujidhihirisha? Haya mambo yalishajionesha kwako kwa njia ya ile ndoto. Sasa wewe unataka kushindana na ukweli, unataka kubadili hali ambayo tayari historia imeshaamua kuiweka...utashindwa tu!"
Jaka alibaki mdomo wazi wakati ukweli wa maneno yale ulivyokuwa ukiingia kichwani mwake.
"Kwa hiyo...?"
"Kwa hiyo wewe huna haja ya kuhama kwa sababu hizo ulizozitoa, labda utafute sababu nyingine. Endelea kukaa naye tu pale nyumbani. Iwapo mwenyewe amekuamini kiasi hicho, na baba yake anajua juu ya uwepo wako pale nyumbani, sioni sababu ya wewe kujitia wasiwasi wa bure..."
"Tatizo sio kukaa tu pale nyumbani kwa Clara Anko, tatizo ni kwamba, nikiendelea kukaa pale ndio itabidi nikubaliane na matakwa yake..."
"Ndivyo alivyokwambia?"
"Hapana...ila..."
"Ila hayo ni mawazo yako! Ambayo sio lazima kila wakati yawe sahihi. Sikiliza anko, mi' nakushauri usifanye papara ya kuondoka pale nyumbani, kwani muda ukiwadia mtapata ufumbuzi wa swala hilo. Mbona tangu mwanzo mambo yote yalivyokuwa yakitokea hukuweza kuyazuia? Iweje uanze sasa?"
Ni baada ya mjadala ule ndipo Jaka akaendelea kuishi na Clara ndani ya ile nyumba.
Aligeuka na kuangaza tena mle kantini. Clara hakuwepo. Alikumbuka kuwa alikuwa hajamaliza kunywa chai aliyoagiza. Alichovya kidole kwenye ile chai na kugundua kuwa ilikuwa imeshapoa sana. Alishusha pumzi ndefu huku akiinuka na kurejea ofisini kwake. Kabla hajafika ofisi kwake aliamua kupitia ofisi kwa Clara ili kujua kulikoni, ingawa alijua kuwa Clara alikuwa amekasirishwa na hali aliyomkuta nayo pale ofisini kwake asubuhi ile.
Sasa yeye alitegemea nini!
Sekretari wa Clara alimjulisha kuwa Clara alikuwa ameenda nyumbani kujipumzisha kutokana na maumivu ya kichwa. Taratibu Jaka aligeuza na kuelekea ofisini kwake.
Kitu kilichomkosesha raha asubuhi ile ni kwamba usiku wa kuamkia siku ile Clara alitupa mipaka katika vituko alivyokuwa akimfanyia pale nyumbani.
Jioni ya siku ile kama kawaida yake Jaka aliingia nyumbani baada ya Clara kuwa amesharudi. Yeye siku zote huchelewa kutoka ofisini kwani hulazimika kubaki mpaka saa kumi na moja na nusu ili kufunga mahesabu ya ugavi ya siku. Na akitoka kazini hupitia kituo cha polisi kusaini kama kawaida, ndipo huelekea nyumbani.
Alipoingia chumbani kwake alishangaa kusikia harufu uturi ghali sana ambayo mara moja aliitambua kuwa ni harufu ya uturi ambao Clara hupenda kujipulizia. Na ndio harufu aliyokumbuka kuinusa mara ya mwisho kabla hajapoteza fahamu siku ile aliyoambulia kipigo kizito pale nje ya ukumbi wa disko wa NK kabla ya kuokolewa na Clara. Alizungusha macho mle ndani ili kuona iwapo kuna kitu chochote kilichobadilishwa, kwani Clara hakuwa na mazoea ya kuingia chumbani kwake kabisa.
Kila kitu kilikuwa kama alivyokiacha.
Alivua shati na kulitupia juu ya kiti kilichokuwa nyuma ya meza ya kusomea mle chumbani, na alikuwa analiendea kabati dogo lililokuwa kando ya ile meza ili achukue taulo ndipo alipoiona.
Katikati ya kitanda chake kulikuwa kuna kadi nzuri na kubwa iliyonakshiwa kwa michoro ya maua mazuri kwa rangi ya dhahabu. Akiwa amemakinika aliichukua na kuitazama kwa karibu zaidi, na hapo alihisi mlipuko fulani moyoni mwake, kisha ubaridi akamtambaa mwilini. Hali hiyo ilimpitia kwa kama nusu sekunde hivi halafu joto la mwili wake likarudi kama kawaida na akahisi kijasho kikimtiririka kufuata uti wake wa mgongo.
Juu ya ile kadi kulikuwa kuna maandishi makubwa yaliyocharangwa kwa rangi ya dhahabu.
I Love You With All My Heart.
Heh!
Nakupenda kwa moyo wangu wote.
Ni maneno yaliyomtoa kijasho Jaka. Kama mwenye kutaka kuhakikisha, aliifungua ile kadi na hapo kipande cha karatasi kilichokunjwa vizuri kilidondoka kutoka ndani ya ile kadi. Hakufanya haraka kukiokota,bali alibaki akikodolea macho kile kilichokuwa kimeandikwa ndani ya kadi ile.
“Dear Jaka,” ilikuwa imeandikwa kwenye kona ya kushoto kwa juu ndani ya ile kadi. Halafu katikati yake kuliandikwa maneno kwa lugha ya kiingereza yaliyotafsirika kama:
Pokea ujumbe wa dhati kutoka ndani kabisa ya moyo wangu.
Na kwenye kona ya kulia kwa chini, kadi ile ilikuwa imeandikwa kwa lugha ile ile ya kiingereza:
Ni mimi, pamoja na upendo wa dhati, Clara.
Alishusha pumzi ndefu na kuketi taratibu pale kitandani. Naam, ama kweli sasa mambo yalikuwa yameanza. Hakujua afanye au aseme nini. Alibaki akiwa amepigwa na butwaa tu. Kabla hajajua ni hatua gani ifuate, akakiona kile kijikaratasi kilichoanguka pale sakafuni kutoka kwenye ile kadi. Alikiokota na kukifungua. Kwa lugha ile ile iliyotumika kwenye kadi, kilikuwa kimeandikwa maneno yaliyotafsirika:
Nimekuonesha kila kinachohitajika,
Nimekufungulia kila kilichofungwa,
Lakini wewe, wewe hutaki kuangalia,
Na mimi sasa, sasa nakupasulia,
Moyo wangu uko radhi,kwako kutulia,
Iwapo utaridhia, kwangu kutulia.
Akupendaye, Clara.
Nguvu zilimwisha.
Hivi huyu msichana ana akili sawasawa kweli...? Hajui chochote kuhusu maisha yangu, hajui iwapo naweza kuwa mtu hatari kwake au la, halafu ana...
Alishindwa kumalizia mawazo yake na akaishia kusonya. Alisikia vishindo laini vya Clara akipita nje ya chumba chake. Alitamani amtokee na ampe mawazo mawili matatu kuhusu swala la mapenzi baina yao na jinsi lilivyokuwa ni wazo la kipuuzi kuliko yote aliyowahi kuyasikia maishani mwake, lakini aliamua kutulia kwanza.
Baada ya kuoga Jaka alienda kukaa sebuleni akiwa tayari ameamua kumueleza kwa utaratibu kuwa hawawezi kuwa wapenzi. Clara alikuwa akijishughulisha na mapishi jikoni, jambo ambalo si la kawaida kwani kila siku msichana wa kazi huwa anakuwa amewapikia kabla ya kuondoka na kurudi tena asubuhi ya siku iliyofuata.
Aliamua kumfuata kule kule jikoni ili ajaribu kuongea naye juu ya swala lile.
"Yap! Mambo?" Clara alianza kumsalimia kwa uchangamfu alipoingia mle jikoni.
"Safi..." Jaka alijibu kwa mashaka kidogo, lakini kabla hajasema lolote zaidi,Clara aliongezea, "Umekuja kunisaidia kupika nini?" Alikuwa katika hatua ya kugeuza vipande vya kuku alivyokuwa akikaanga. Pembeni Jaka aliona viazi vilivyokaangwa, hivyo akajua kuwa Clara alikuwa anatayarishwa mlo wa chipsi kwa kuku. Pia aligundua kuwa Clara alikuwa anajitahidi kukwepa kumtazama usoni. Kabla Jaka hajajibu lile swali aliloulizwa Clara akamtuma.
"Naomba ukaniletee sahani pale kabatini."
Shit!
Jaka alilaani kimoyo moyo huku akitekeleza.
"Naona leo uliamua kutembelea chumbani kwangu" Alimwambia huku akimkabidhi sahani. Clara aliipokea sahani ile na kuendelea na upishi wake kama kwamba hakumsikia. Jaka aliendelea kumtazama, akisubiri jibu.
"Hukupendezewa?" Hatimaye Clara alimjibu kwa swali.
Aan-haa, kumbe ulisikia swali langu.
"Si hivyo, ila tu nilikuwa..."
"Ah, jamani! Basi Jaka naomba unisaidie kukata vitunguu ili tupate kachumbari, mi' n'takata nyanya na karoti." Alimkatiza kabla hajapata fursa ya kujieleza.
Jaka akajikuta anakata kachumbari na Clara jikoni badala ya kumwelezea ukweli aliodhamiria kumweleza. Wakati Jaka akiwa amekereka na hali ile, Clara alionekana kuifurahia sana. Jaka alijaribu tena kuuanzisha ule mjadala wakati wakiwa mezani wanakula.
"Clara...nilikuwa naomba tuongee kidogo kuhusu jambo ambalo nadhani linatuhusu sote..."
"Mmmnh! Sasa si tunakula jamani Jaka? Huwezi kusubiri hadi tukamaliza?" Clara alimkatisha huku akitabasamu, na kuendelea, "kwanza mbona husifii upishi wangu, au sijui kupika ?"
"Ah, chakula kizuri sana..."
"Na kadi yangu?" Aliuliza kwa sauti ya chini huku akiinamisha uso wake. Jaka hakusikia vizuri, akamwomba arudie tena. Clara akauliza tena huku ameinamisha uso, bila shaka kwa aibu.
Ilitakiwa uone aibu kabla ya kuniandikia kadi ile bibie...sio baada!
"Ni nzuri...asante...na nilikuwa nataka kuongelea juu ya swala hilo hilo Clara..."
"Tule kwanza basi."
Waliendelea kula wakiwa kimya. Baada ya kula na kuondoa vyombo, Clara aliaga kuwa anaenda kulala kutokana na uchovu. Jaka alishangaa, kwani walikubaliana kuongea baada ya kula.
"Hey! Tuna maongezi mimi na wewe Clara, umesahau?"
"Ah! Bwana mi' nimechoka...tuongee kesho basi, eeenh?" Clara alimjibu kivivu huku akijinyoosha. Kisha aligeuka na kuelekea chumbani kwake bila kumwangalia wala kusubiri mjadala zaidi.
Jaka alifura kwa hasira. Alitamani amrukie na amtikise kwa nguvu sana mpaka akili yake ikae sawa ndani ya bichwa lake, na kisha amueleweshe kuwa iwapo alikuwa anampenda, basi yeye alikuwa hampendi na hivyo hawawezi kuwa wapenzi na pia ni kinyume cha uungwana.
Lakini alibaki akiwa ameduwaa tu pale mezani, akiikodolea macho sehemu ambayo yule binti alikuwa amesimama sekunde chache zilizopita.
Hiyo ilikuwa jana usiku.
Na sasa akiwa amekaa nyuma ya meza yake pale ofisini alikuwa akijiuliza maswali mengi.
Ni kweli alikuwa hampendi yule msichana?
Alikumbuka siku ile alipojikuta chumbani kwa yule binti baada ya kupoteza fahamu kutokana na kipigo ambacho kilikuwa kinampeleka moja kwa moja kwenye himaya ya ziraili. Yule binti alimtoa nguo zote na kumsafisha mwili wake uliotapakaa damu na petroli.
Ni kweli kuwa yule binti haujui undani wake?
Alikumbuka maneno ya mzee Mnyaga.
Jaka, yule msichana anakupenda! Tena anakupenda kwa nia nzuri tu...
Ni kweli?
Je, hii itakuwa heshima kweli kwa mzee Zaza, baba yake Clara?
Isitoshe, kwa tabia iliyojengeka ya vijana wengi kupenda kulelewa na akina mama au akina dada wenye pesa, ni dhahiri kuwa ataonekana kuwa ni yeye ndiye aliyemshawishi yule binti kimapenzi ili apate kufaidi matunda ya utajiri wake.
Jaka hakupenda kabisa kunasinishwa na tabia hiyo chafu.
Lakini ni nani atakayeamini kuwa ni Clara, na sio yeye, ndiye amekuwa chanzo cha penzi hilo?
Roho ilimuuma. Alijiona kuwa amenswa kwenye mtanziko mkubwa sana.
Kwa nini kila linapokuja swala la uhusiano wa kimapenzi baina ya mvulana na msichana, ni mvulana ndiye ambaye siku zote anabebeshwa lawama iwapo penzi hilo litaingia vipingamizi fulani?
Sasa kabla hajajua hatima ya swala lile tete baina yake na Clara, limezuka swala jingine ambalo bila shaka ni tete zaidi!
Ni nani huyu anayevaa koti refu na kofia pana anayepita akiulizia habari zake? Anataka nini?
Mawazo haya yalimsakama siku nzima pale ofisini pasina kuyapatia ufumbuzi wowote.
__________________
Jioni ile aliporudi nyumbani alimkuta Clara akiwa amejiinamia pale sebuleni. Ingawa runinga ilikuwa imewashwa, Clara hakuwa na habari nayo kabisa. Alikuwa amekaa kwenye kochi refu huku miguu yake yote miwili akiwa ameipandisha juu ya kochi lile na kufanya magoti yake kuwa sawa na kidevu chake. Alikuwa amevaa gauni jepesi la usiku lililokuwa limemkaa vyema sana. Weupe wa gauni lile ulimkumbusha Jaka ile ndoto aliyokuwa akiiota mara kwa mara huko nyuma, na moyo wake ukapiga mshindo.
Hakuwa ameifikiria ile ndoto kwa muda mrefu, sasa kwa nini ameikumbuka wakati ule?
Clara aliinua uso wake na kumtazama, na Jaka akaona kuwa yule binti hakuwa mwenye furaha kabisa. Walitazamana kwa sekunde kadhaa kisha Clara alirudia kujiinamia bila ya kumsemesha. Akajua kuwa Clara bado alikuwa amekasirika kutokana na yale yaliyotokea baina yao asubuhi ile kule ofisini.
Sasa kwani ye’ alitegemea nini? Alitaka nishangilie kwa kuniletea ile kadi?
"Clara, vipi...niliambiwa uliondoka mapema ofisini kutokana na maumivu ya kichwa..." Alimsemesha.
"Kwani we' unajali chochote hata kama nikiumwa?" Baada ya kimya kifupi Clara alimjibu kwa swali.
"Come on, Clara, unajua kuwa mi' n'najali..." Alianza kumjibu, lakini hapo Clara aliinua uso na kumtazama kwa macho ya hasira na yenye kukata tamaa. Yalikuwa yamejaa machozi ingawa bado yalikuwa hayajaanza kutiririka kutoka kwenye macho yale ya kuvutia. Jaka alijikuta akipiga hatua tatu za haraka kumsogelea pale kochini akitaka amshike, amfute yale machozi ambayo hakuwa na uhakika kuwa yalitokana na maumivu ya kichwa au hasira. Kabla hajamgusa Clara alimnyooshea mikono yake yote miwili kumwashiria kuwa asisogee zaidi.
"Usiniguse, Jaka!"
Jaka alisimama na kuduwaa.
Sasa yale machozi yalianza kumtiririka Clara.
"Clara...kwani vipi...?"
Akiwa amekaa vile vile pale kwenye kochi, Clara aliikumbatia miguu yake kwa mikono yake huku akimtazama Jaka kwa macho makali.
"Hivi we' unanionaje mimi?" Clara alimuuliza taratibu.
Kabla Jaka hajajua cha kujibu, binti aliendelea, "Leo nimekuja ofisini kwako ukajitia kuninunia...kisa nini? Eti nimekuandikia kijibarua na kadi vilivyokuwa na ujumbe kuwa nakupenda..!"
Jaka bado aliendelea kuduwaa, akijaribu kuitathmini ile hali.
"Kwa hiyo umeniona kuwa mimi najipendekeza na najirahisi mno kwako, sio? Siku zote nikikuonesha kuwa nakupenda wewe unajifanya huelewi, au unajitia huoni. Kwa vile umeshajua kuwa nakupenda basi ndio unaamua kunidharau na kunitesa...mimi nilidhani kuwa wewe ni mtu muwazi na mwenye kuelewa, kumbe nilidhani vibaya!" Clara aliendelea kumtupia maneno yaliyomkaa moyoni.
"Sio hivyo Clara...wewe ndio huelewi..." Jaka alijaribu kujitetea, lakini hapo Clara aliinuka kutoka pale kwenye kochi na kupiga hatua mpaka pale alipokuwa amesimama. Alimuinulia uso wake na kumuuliza huku machozi yakiendelea kumtiririka, “Sielewi nini Jaka...hebu nieleze ni nini nisichokielewa mimi, eenh? Au unataka nikueleze ninachoelewa? Unataka kujua ni nini ninachoelewa ambacho wewe unadhani sikielewi....?” Sasa Clara alikuwa anaongea huku akisaidiwa na kichwa pamoja na mikono yake yote miwili, hali sauti yake bado ikiwa kali lakini ya chini.
Jaka alibaki amebutwaika. Hajawahi kumuona Clara katika hali kama ile na wala hakutegemea kuwa angeweza kumuona katika hali kama ile.
“No! Nilichotaka kukuelewesha ni…”Jaka alijaribu kuongea, lakini Clara hakutaka kumsikiliza.
"Huna lolote la kunielewesha Jaka! Mimi naelewa kuwa unanipenda! Unanipenda, na unanitaka. ila unaogopa...!"
Khah!
"We' una wazimu nini?" Hii ilikuwa kali kuliko, na Jaka alijikuta akifoka bila kuelewa kwa nini alikuwa anafoka.
"Ndio! Mimi n’na wazimu, tena n’na wazimu sana...!" Clara naye alianza kufoka.
"Mimi jana nilitaka niongee na wewe juu ya mambo haya, lakini we’ ukajitia kunikwepa ukaenda kulala...ulitegemea mimi niichekelee hali hiyo?"
"Eti kuongea na mimi! Mimi nilishaongea na wewe kabla ya hiyo jana Jaka...na niliongea kwa sauti ambayo wewe ulishindwa kuielewa, na ndio maana ikabidi nikuandikie...!”
"Hatujawahi kuongea juu ya swala hili mimi na wewe hata siku moja Clara, na we' unajua hilo!”
"Mimi nimeongea nawe kwa sauti ya moyoni! Na nimelisikia penzi lako kwangu kutoka moyoni mwako, na si kinywani mwako. Sauti ya moyoni husikiwa na moyo, sio na masikio, na huwa inatoka moyoni na sio mdomoni...sauti ya moyoni huhitaji kueleweka zaidi kuliko kusikiwa; ni wewe ndiye huelewi Jaka, sio miye!”
Heh!
Jaka alibaki kinywa wazi. Hakutegemea kusikia maneno kama yale kutoka kwa Clara. Mshangao huo ulipita upesi sana, kisha nae akajibu huku akitikisa kichwa.
“Usitegemee kuwa moyo uliokwisha kufa unaweza kufufuka tena ili kuja kusikia sauti iliyochelewa Clara...”
“There is never too late for love Jaka and you should know that!” Clara alimfokea kwa jazba, akimaanisha kuwa kwenye penzi hakuna kuchelewa, na kwamba Jaka alitakiwa awe analijua hilo.
“Hiyo dhana ya moyo uliokufa ni njia yako ya kujidanganya tu juu ya swala hili...inaweza kuwa uliumizwa kimapenzi huko nyuma but so what? You can always love again, and I am giving you that chance, god damn it! Nipe nafasi uone!” Clara aliendelea kwa ukali, akimaanisha kuwa si hoja iwapo alishawahi kuumizwa katika penzi huko nyuma, kwani anaweza kupenda upya tu wakati wowote, na kwamba yeye alikuwa anampa nafasi ya kupenda upya…basi na aichukue hiyo nafasi ajionee.
Duh!
Kwa mara nyingine tena Jaka alipigwa na butwaa kwa maneno yale makali kutoka kwa Clara. Ilikuwa wazi kwamba alikuwa anaelekea kushindwa kwenye malumbano yale makali.
“Ni wewe ndiye unayejidanganya kuwa tunaweza kuwa wapenzi...sisi ni watu tulio pande mbili tofauti Clara. Sijui kwa nini hulioni hilo..maana halihitaji digrii...liko wazi kabisa!" Alimjibu kisha akageuka kuelekea chumbani kwake bila hata ya kujua alikuwa anaenda kufanya nini.
"Siwezi kuliona hilo kwa sababu moyo unapozidiwa hutoa sauti yake kwa njia yoyote ile ili usikike...mimi nakupenda Jaka...nakupenda wewe kama ulivyo....sijali kuwa umehukumiwa kwa kosa la mauaji kwa sababu najua kuwa wewe si muuaji na wala hukuua..." Clara alimjibu kwa sauti ya chini akiwa amesimama pale pale alipokuwa.
Jaka alisita kwenye hatua zake. Kisha akageuka taratibu na kumtazama kwa kutoamini yule msichana. Clara alikuwa amesimama pale sebuleni, shingo yake ameilaza upande na mikono yake ameiacha ikining'inia kila upande wa mwili wake. Uzito wake wote alikuwa ameuegemeza kwenye mguu wake wa kushoto ilhali mguu wake wa kulia akiwa ameukunja kwenye goti na umesogea mbele kidogo. Machozi yalikuwa yakimtiririka naye wala hakuonesha kujua kuwa alikuwa akitokwa na machozi.
Ilikuwa ni picha mtu aliyekata tamaa na mwenye huzuni kubwa kabisa, na kwa hakika alimtia simanzi kubwa sana Jaka.
Na alipokuwa akimtazama yule binti akiwa amesima kwa simanzi isiyosemeka huku akibubujikwa machozi namna ile, taswira ya yule binti kama alivyokuwa akimlilia kwenye ile ndoto ikamrudia, na sanjari na mlipuko wa kumbukumbu ya ndoto ile, ukweli aliokuwa akipingana nao ukamshukia na kumvaa kama joho fahamuni mwake.
Ni kweli alikuwa akimpenda yule binti!
Huo ni ukweli ambao siku zote amekuwa akishindana nao. Siku zote amekuwa akihisi kuwa kuuruhusu ukweli ule umtawale kungekuwa ni kosa kubwa sana kwake kwani kusingemletea isipokuwa majuto tu...
Lakini sasa mtoto ndio ananililia huyu jamani…sio kwenye ndoto tena, bali wazi wazi mbele ya macho yangu! Ameridhia mwenyewe huyu! Kanitamkia kwa maandishi na kwa kinywa bloody hell…nafanyaje sasa?
"We’ unajaribu kuukimbia ukweliJaka...hutaki kukubali kuwa mambo yaliyokutokea yamekutokea wewe na kwamba una nafasi ya kuikubali hali iliyopo na kuishi nayo..." Clara aliendelea kumweleza taratibu huku machozi yakimtoka.
Akilini mwake Jaka alikumbuka maneno ya mzee Mnyaga.
...wewe unataka kushindana na ukweli, unataka kubadili hali ambayo tayari historia imeshaamua kuiweka...
Akili ilimzunguka.
Sauti ya Clara ilizidi kumfikia masikioni mwake.
“...yule Jaka wa zamani ni wewe, na huyu wa sasa pia ni wewe Jaka, huo ni ukweli ambao huwezi kuufuta. Unapojaribu kuukimbia ukweli huu Jaka, unakuwa ni sawa na unayejaribu kujikimbia wewe mwenyewe, na hivyo unakuwa hujijui wewe ni nani na unataka nini hapa duniani! Amini usiamini Jaka, huwezi kufika huko unapokimbilia mpaka kwanza ukubali kujitambua na kujikubali...”
“Dah, Clara…”
“…mimi nakupenda kama ulivyo sasa Jaka. Sijui huko nyuma ulikuwaje au ulifanya nini, hilo kwangu si tatizo, na nipo tayari kuwa na wewe mwanzo-mwisho katika matatizo yote unayohofia kuwa yatatokea huko mbeleni..."
Sasa hii ilikuwa imezidi.Jaka hakuweza kuvumilia zaidi. Aliziba masikio yake kwa viganja vya mikono yake huku akimaka kwa kelele.
"Basi! Basi! Basi....inatosha....!"
Clara aligutuka na kumshangaa pale alipomuona akatoa mikono yake masikioni na kupiga ngumi ndani ya kiganja chake kwa hasira.
"We' unataka nini kwangu lakini mimi, eenh? Nimeshakwambia kuwa mimi siwezi...siwezi, tena siwezi kabisa!" Alifoka kwa hasira na kuchanganyikiwa.
Clara nae akamjibu, sasa machozi yakiwa yanambubujika kama maji na akiongea kwa uchungu mkubwa.
"Hivi wewe unafikiri mimi napenda sana wanaume...? Au unadhani ni kwa nini najidhalilisha na kujiangusha kwako kiasi hiki, eeenh...?"
"Hayo yote yako Clara...mimi ninachosema ni kwamba sitaki hicho kitu unachotaka wewe, na sitaki kwa vile moyo wangu hauko tayari...mi' niko tayari kuondoka hapa nyumbani kwako Clara, na hata kufukuzwa kule kazini, lakini heshima yangu kwako na kwa mzee Zaza kwangu ni kitu cha maana sana..."
"Ndio! Moyo wako hauko tayari kwa sababu hutaki kutembea na janamke malaya, huni...lenye kupapatikia kila mwanaume limuonaye, sio? Laiti ungejua...!" Clara alipandisha sauti kwa jazba.
“Hayo yote yako Clara, mimi sijasema hivyo! Ninachosema ni kwamba…”
"Kwa taarifa yako mimi pia nina heshima zangu na ninaujali sana usichana wangu! Hii kukupenda wewe ni moyo wangu tu ndio umeamua kunishusha chini na kunidhalilisha kiasi hiki..lakini nilifanya hivyo nikijua na nikiamini kuwa na wewe unanipenda na ni mtu mwenye kuelewa...Ni mara ngapi nimekufuma ukinitazama kwa matamanio? Sa’ sijui unaogopa nini! Hujui maana ya kupendwa masikini...!" Hapo Clara hakuweza kuendelea kwani kwikwi zilimzidi. Uchungu wa maneno yake ulimkaba na alianza kuangua kilio. Kama kwamba alikuwa ameelemewa na uchungu ule, alidondokea magoti huku akiendelea kulia akiwa amekalia visigino hali kiwiliwili chake amekiegemeza nyuma. Alijiziba mdomo kwa viganja vya mikono yake miwili akijaribu kila mafanikio kuzuia sauti ya kilio chake
Alilia kwa uchungu sana, na kilio kile kilisababisha mabega na kichwa chake kutikisika kwa kila kwikwi aliyopiga. Katika zile sekunde chache kabla hajadondoka na kupiga magoti pale sakafuni, Jaka alimkumbuka tena yule msichana kama alivyomuona kwenye ndoto ile iliyokuwa ikimjia mara kwa mara. Na katika sekunde zile Jaka alipata wasiwasi iwapo na ile pia haikuwa ndoto. Hakika aliomba sana iwe ndoto, lakini alijua kuwa haikuwa ndoto. Alitafuta maneno ya kusema, hakuyapata. Aliendelea kumtazama yule binti tajiri akilia pale chini na lile joho la ukweli aliokuwa akishindana nao lilizidi kumbana kila kona ya mwili, hisia na fahamu zake.
Nampenda huyu msichana jamani...haki ya Mungu nampenda!
Sasa mateso yote haya ni ya nini?
Alipiga hatua mpaka pale Clara alipokuwa na kumwinamia huku akimshika mabega.
"Clara...Clara..." Alianza kuongea lakini alishinndwa kuendelea. Clara aliikung’uta mikono yake kutoka mabegani mwake huku akitupa mikono na kutikisa kichwa chake kwa nguvu.
"Don't touch me! Don't touch me at all Jaka! Just leave alone damn it!" Alibwata kwa hasira huku akilia, akimaanisha kuwa hakutaka Jaka amguse kabisa, amuache tu kama alivyo.
"Hapana Clara, hapana. Naomba unisikilize tafadhali...tafadhali sana hebu tulia kwanza!" Jaka alijitahidi kumshika mikono ile ambayo sasa ilikuwa ikimpiga kila sehemu.Usoni, kifuani, mabegani…kila mahali kwani sasa Jaka nae alikuwa amepiga magoti mbele ya yule binti. Lakini Clara aliendelea tu kutupa mikono na kutikisa kichwa huku akilalamika.
"Sitaki! Niachie..don't you dare touch me goddamn it! Just Don't! "
Jaka alijitahidi kumzuia hatimaye alifanikiwa kumkamata mabega na na kumvutia kwake, na hivyo kuibana mikono ya yule mwanadada baina ya vifua vyao viwili. Clara aliendelea kufurukuta lakini Jaka alikuwa amembana kwa nguvu huku akimuongelesha kwa kubembeleza.
"Clara naomba unisikilize basi..."
"Leave me alone Jaka..." Clara alimbishia huku akizidi kufurukuta. Hapo Jaka alimtikisa kwa nguvu sana huku akifoka, "Clara tulia basi unisikilize!”
“Sitaki!”
“Sikia basi kwanza wewe!”
“Niache nimesema na umalaya wangu, fala we!”
“Nakubali nilikuwa mjinga...tena fala kweli kweli! Lakini sasa...lakini...Oh, I love you! Clara, I love you...!"
Kimya!
Ilichukua kama sekunde tatu hivi kwa maneno yale kuzama akilini mwa Clara. Alitulia kimya na kubaki akimkodolea macho ya kutoelewa au kutoamini yule rijali aliyemkumbatia pale sakafuni, kama kwamba ndio anamuona kwa mara ya kwanza. Alishangaa kuona kuwa na Jaka naye alikuwa akitiririkwa machozi. Jaka aliyaangalia macho ya Clara yaliyokuwa yamemkodolea na aliona jinsi yalivyokuwa yanajitahidi kuamini maneno yake. Walibaki wakitazamana kwa muda kabla Jaka hajauvunja ukimya ule.
"Ndio Clara, nakupenda, nakupenda sana, Clara. Tafadhali nyamaza kulia...hakika nilikuwa bonge la fala!"Alimwambia kwa sauti ya upole sana huku akimtazama moja kwa moja machoni.
Loh!
Clara alimtazama Jaka kwa mshangao mkubwa kabisa. Hakika alikuwa haamini aliyokuwa akiyasikia. Jaka alimtikisia kichwa chake taratibu kumuashiria kuwa aliyoyasikia ni haki kabisa. Hapo midomo ilianza kumcheza huku kwa mikono iliyotetemeka akianza kumfuta Jaka machozi.
“Oh, Clara…” Jaka naye alianza kumfuta machozi.Clara aliangua kilio kipya.
"Sikukuona malaya wala muhuni Clara...nakubali kuwa nilipata mawazo mabaya juu yako, lakini ukweli ni kwamba wewe ni msichana mzuri sana. Kwa sura na tabia. Sikupenda nije nikuharibie maisha yako...kwa sababu mimi ya kwangu yalishaharibika zamani na sina uhakika na maisha yangu ya baadaye! Wewe una kila sababu ya kujitengenezea maisha bora zaidi ..."
Kilio kilizidi kuongezeka kwa Clara.
"...lakini vile vile lazima nikiri kuwa ni kweli nilikuwa nashindana na ukweli Clara, na ukweli wenyewe ni kwamba nakupenda sana Clara...nakupenda na sitaki nikuache kwa hata dakika moja..."
Hapo ndio ilikuwa kama ametoa idhini rasmi, kwani Clara aliachia kilio cha sauti huku akimzungushia mikono yake shingoni na kumkumbatia kwa nguvu.
"Oh! Jaka...Jaka...jamani…." Alibwabwaja huku akilia kwa furaha yule mwanadada. Jaka nae alimkumbatia kwa upendo yule huku akitiririkwa machozi, donge kubwa likiwa limemkaba kooni. Alijihisi kama aliyetua mzigo mzito uliokuwa ukimuelemea kwa muda mrefu.
Wakiwa wamekumbatiana huku wamepiga magoti pale chini namna ile, wote wawili walijua kuwa ule ulikuwa ni mwanzo wa penzi lililokuja baada ya vikwazo kadhaa.
Na kwa wakati ule hakuna aliyejali ni nini kingetokea baadaye.
6
Mapenzi baina yao yalishamiri upesi sana. Jaka alijiona kama mtu aliyezaliwa upya katika ulimwengu wa wapendanao. Katika muda huo aliokuwa na Clara kama mpenzi, rafiki na mshirika wake wa karibu, Jaka aliweza kumeelezea Clara mambo yote yaliyomtokea wakati akiwa Dar es Salaam mpaka alipojikuta pale Dodoma; ingawa bado kulikuwa kuna mambo machache ambayo alidhani haikuwa lazima kwa Clara kuyajua.
Siku kadhaa baada ya lile tukio lililoishia kwenye ahadi ya mapenzi mazito baina yake na Clara pale sebuleni Jaka alikuwa akiendesha gari la kampuni ya Zaza Cargo Movers kuelekea ofisini huku akikumbukia matukio ya siku ile, matukio ambayo yaliishia kwa wao kuamka asubuhi iliyofuata wakiwa kitandani kwa Clara. Na baada ya usiku ule hakika aliazimia kumpenda kwa moyo wake wote yule binti, kwa kadiri atakavyojaaliwa.
Tangu mapenzi yao yaanze, walikuwa wametembelea sehemu mbali mbali za starehe pale mjini na mara nyingi wamekuwa wakienda picnic nje ya mji, kwenye vilima tulivu vya pale Dodoma. Ilikuwa ni furaha sana kuwa pamoja, na hili Jaka alilithamini sana.
Aliegesha gari nje ya kituo cha polisi na kuingia mle ndani ili kusaini kama ilivyo ada. Alimkuta Osman Mgunya pale ofisini naye alisaini bila ya kumsemesha neno na kuanza kuondoka.
“Naona sasa umesahau kabisa kuwa unatumikia adhabu kwa kosa la mauaji, eeenh?” Osman alimtupia kauli ya kichokozi. Hakumjibu wala hakusimama. Alitoka nje na kufungua mlango wa gari lake kwa nia ya kuondoka eneo lile, lakini akajikuta akisita na kukunja uso huku mguu mmoja tayari ukiwa ndani ya gari. Upande wa pili wa barabara kulikuwa kuna mtu mmoja aliyesimama chini ya mti kama anayesubiri kuvuka barabara. Alitoa miwani yake ya jua usoni, kisha akatoa kitambaa kwa mkono mmoja huku ule mwingine bado ukiwa umeshikilia ile miwani. Alianza kuifuta ile miwani taratibu. Muda wote aliokuwa akifanya matendo hayo, macho yake yalikuwa yakimtazama yule mtu aliyekuwa upande wa pili wa barabara, kwani kuna kitu kilimvutia kuhusu yule mtu.
Jamaa alikuwa amesimama upande wa pili wa barabara akiangalia kule kule ambako Jaka alikuwepo, na kwa muda wa dakika kama tatu hivi barabara ilikuwa tupu kiasi cha kutosha mtu yeyote kuvuka, lakini yule mtu hakufanya bidii yoyote ya kuvuka barabara ile. Hapo Jaka akajua kuwa yule jamaa alikuwa akimtazama yeye. Naye aliendelea kumtazama.
Alijitahidi japo kupata muundo tu wa sura ya yule mtu kwa umbali ule lakini alishindwa, kwani sehemu kubwa ya sura ya yule mtu ilikuwa imefunikwa kwa kofia pana kama zile uzionazo kwenye filamu za kimarekani za Cowboys au Westerns.
Chini ya uzio wa kofia ile Jaka aliweza tu kuona sehemu ya mdomo na kidevu chake kilichozungukwa na ndevu zilizochongwa vizuri katika umbo la herufi “O”.
Chini, yule mtu alikuwa amevaa koti refu lililoteremka mpaka chini ya magoti yake, ambapo Jaka aliweza kuona suruali ya rangi ya kahawia ikitokeza chini ya koti lile na viatu vyeusi vilivyopanda juu kidogo kama vya jeshi. Kola za koti lile jeusi alikuwa amezisimamisha kama vile aliyetaka kujikinga na baridi na mikono yake yote miwili alikuwa ameizamisha kwenye mifuko ya koti lile.
Jaka alirudisha miwani yake usoni taratibu kisha akaingia garini nakufunga mlango. Yule mtu alikuwa amesimama pale pale alipokuwa, akiendelea kuangalia upande ule lilipokuwa gari lake. Jaka alipata wazo la kumfuata yule mtu pale alipo na kumuuliza kwa nini alikuwa akimfuata-fuata, kwani alikuwa na hakika kabisa kuwa huyu ndiye yule mtu aliyekuwa akiulizia habari zake kwa mlinzi kule ofisini kwake. Lakini aliamua kutofanya hivyo, kwani aliamini kuwa iwapo yule mtu alikuwa ana haja ya kuonana naye, basi ni yeye na sio Jaka ndiye anayepaswa kufanya jitihada ya kukutana naye uso kwa uso. Aling’oa gari na kuondoka eneo lile, akimuacha yule mtu alikuwa amesimama pale pale.
Jioni ya siku ile alimuelezea Clara kuhusu yule mtu, na wote walikuwa na mawazo kuwa mtu yule, ambaye waliamua kumpachika jina la John Doe, angeweza kuwa ni kibaraka wa Osman Mgunya aliyetumwa kumfuatilia Jaka ili kuhakikisha kuwa Jaka anapata balaa pale Dodoma. Jambo lile liliwakera sana.
“Kwa nini usimshitaki kwa mkuu wake wa kazi?” Clara aliuliza.
“Nimshitaki nani?”
“Osman Mgunya.”
“Aaah, bado hatuna ushahidi wowote kuwa ni kweli yule mtu ametumwa na Osman....” Jaka alijibu kwa kukata tamaa.
“Mnh! Ila kweli. Sasa...?” Clara aliafiki na kuhoji.
“Hebu tusuiri tuone kama ataendelea kunifuatilia...na iwapo ataamua kuweka wazi dhamira yake kwangu.” Jaka alimwambia.
John Doe alikuja kuonekana tena siku mbili baadaye.
Ilikuwa ni siku ya Jumamosi nao waliamua kwenda kwenye ukumbi wa disko kujiburudisha. Ni Clara ndiye aliyetoa wazo hilo baada ya kuona kuwa Jaka alikoseshwa raha sana na swala la John Doe.
Kwa siku mbili Jaka alikuwa na mawazo mengi kuhusu yule jamaa. Alijiuliza sana kuwa iwapo John Doe hakuwa ametumwa na Mgunya, atakuwa ametokea wapi? Na anataka nini? Alijaribu kukumbuka matukio yote yaliyomtokea kule Dar kabla ya kuletwa kwake pale Dodoma na kadiri alivyotafakari ndivyo alivyozidi kuamini kuwa John Doe atakuwa ametokea Dar es Salaam japo hakuwahi kabisa kukutana naye huko. Hili lilizidi kumkera, kwani alijua matukio yaliyotokea Dar hayakufikia mwisho na siku zote alikuwa akihofia kuwa yangemrudia tena tu, kwa namna moja au nyingine.
Je, sasa ndio yalikuwa yanamrudia?
Hili jambo lilimfanya aanze kujutia uamuzi wake wa kuingia kwenye mapenzi na Clara, kwani sasa na Clara atakuwa ameingizwa rasmi kwenye matatizo yanayomuandama.
Kitu kingine kilichomkosesha raha ni ukweli kwamba John Doe aliweza kumpata Jaka wakati wowote atakao, wakati yeye hakuwa na namna yoyote ya kumpata iwapo angehitaji kufanya hivyo. Mawazo haya yalimsumbua sana kiasi Clara akaona ni bora waende disko jumamosi ile ili kidogo apumzishe akili yake. Na kwa kweli hilo lilisaidia, na Jaka alifurahi sana.
Walikuwa wanarudi nyumbani kwao kiasi cha saa saba za usiku ule ndipo alipomuona.
Wakiwa kiasi cha kama mita kumi hivi kutoka kwenye geti la nyumba yao huku Clara akiwa nyuma ya usukani, taa za gari lao zilimmulika mtu akiwa amesimama upande wa pili wa barabara akitazama kule ilipokuwa nyumba ya Clara. Mara moja Jaka aliyagundua mavazi ya mtu yule.
“Simamisha gari!” Alimaka huku akiangalia kule alipokuwa amesimama yule mtu.
“Kuna nini...?” Clara aliuliza huku akipunguza mwendo na kusimamisha gari kama alivyoambiwa, lakini Jaka alikwisha ruka nje ya gari kabla hata halijasimama sawasawa. Yule mtu alipoona vile aligeuka na kuanza kuondoka taratibu. Jaka alianza kumfuata kwa hatua za haraka.
“Hey, Jaka vipi? Unaenda wapi...” Clara alimsemesha kwa hamaniko huku akimfuata kwa gari kwa mwendo mdogo.
“Tangulia nyumbani!” Jaka alimjibu huku akianza kumkimbilia yule mtu. John Doe naye akaanza kutimua mbio.
“Simama wewe! Simama laa sivyo nakupigia kelele za mwizi!” Jaka alimpigia kelele huku akizidisha kasi kumfuata. John Doe akaongeza kasi akishika njia ya kuelekea kituo cha kurushia matangazo ya redio cha TBC kanda ya kati, Jaka akimfuata kasi nyuma yake huku Clara naye akiongeza mwendo wa gari kuwafuata. Mbele kidogo John Doe akakunja upenuni mwa ukuta wa kituo cha redio kanda ya kati na kukata kulia kuelekea kwa kasi sana kwenye kichochoro kingine kilichotokezea kwenye uwanja ambao kwa nyakati maalumu huwa unatumika kwa sherehe za mbali mbali za kimkoa, maarufu kama uwanja wa sabasaba. Jaka nae akakunja kona ile kwa kasi huku akiwa hatua chache sana nyuma yake kiasi aliweza kuzisikia pumzi za yule mtu akihema kwa nguvu.
Alipofika usawa wa jengo la ofisi ndogo ya posta tawi la uwanja wa sabasaba, John Doe alitaka kukata kushoto ili apotelee kwenye uchochoro mwingine mdogo. Jaka alijua kuwa akifanikiwa tukuingia kwenye uchochoro ule hatoweza tena kumpata. Pia alihisi kuwa huenda John Doe akawa ana wenzake kule upande wa pili wa uchochoro ule ambao wangeweza kumdhuru.
Hakumpa nafasi hiyo.
Alijirusha mzima mzima na kumdaka kiunoni kwa mikono yake yote miwili. John Doe aliachia yowe la hamaniko huku akipepesukia mbele, na kwa sekunde kadhaa aliendelea kukimbia kwa kuyumba yumba huku akimburura Jaka nyuma yake.
Huku akigumia, Jaka alihisi mikono yake ikianza kuteleza. Akawa amemng’ang’ania koti yule jamaa huku miguu yake ikiendelea kubururwa kwenye ardhi ile iliyojaa kokoto. John Doe akazidi kupepesuka, kasi yake ikaanza kupungua, naye akijitahidi kujitikisa na kujikung’uta ili Jaka amwachie. Akafanikiwa kumchomoa mkono mmoja, na Jaka akabaki akiwa amemng’ang’ania kwa mkono mmoja huku akibururwa vibaya.
“Sim…ma…ma we…wweee!” Alikuwa akimshinikiza yule mtu mwenye koti refu huku akisota vibaya ardhini akiwa amemng’ang’ania kwa mkono mmoja ilhali kwa ule mwingine akijitahidi kujiinua bila ya kupunguza mwendo.
Ilikuwa ni tafrani ya aina yake.
Ghafla John Doe alimgeukia na kofi kali lililomkosa Jaka na kupitia inchi chache juu ya kichwa chake. Kitendo kile kilisababisha lile koti lichanike ule upande ambao Jaka alikuwa ameung’ang’ania kwa mkono wake wa kulia huku John Doe akizidi kukukuruka kwa nguvu ili ajinasue kutoka mikononi mwake. Jaka akamng’ang’ania mguu kwa nguvu na hapo wote wawili wakapiga mweleka mzito. Jaka hakuuachia ule mguu hata kidogo. Sasa John Doe alikuwa anagaragara pale chini huku akijaribu kuunasua mguu wake, wakati Jaka akizidi kuung’ang’ania huku akiutumia kama nyenzo ya kujivutia juu ili amlalie yule jamaa pale chini na kumdhibiti kikamilifu.
Katikati ya rabsha ile John Doe alimfyatulia teke kali sana la uso kwa mguu wake uliokuwa huru. Yowe la maumivu lilimtoka Jaka huku akisukumwa pembeni na mikono ikamlegea. John Doe akajichomoa na kumshindilia kwa soli ya kiatu chake kifuani akiwa bado amelala pale chini, na Jaka akagaragazwa hovyo pale chini huku akigumia kwa maumivu na hasira.
John Doe alikurupuka kutoka pale chini na kutaka kukimbia, lakini Jaka nae alikuwa ameshainuka na aliwahi kumdaka ukosi wa koti lake kwa nyuma kabla hajafika mbali.
“Tulia weweee! Unan’natakia nini mim...” Alianza kumfokea, lakini hapo John Doe alimgeukia kwa konde zito lilitua sawia kwenye “solar plexus”, sehemu nyeti sana iliyopo baina ya pale kifua kinapoishia na tumbo linapoanzia. Jaka alienda chini bila kupenda na kupiga goti moja ardhini huku akipatatapa kutafuta pumzi bila mafanikio. Lilikuwa ni konde zito sana lililomlegeza maungo yote na hakuelewa kwa nini pigo lile lilimfanya vile.
Kwa mbali aliweza kumsikia Clara akiita jina lake huku akikimbilia pale walipokuwa. Aliinua uso wake kumtazama yule jamaa, na kuona kuwa John Doe alikuwa amemsimamia katika ile “honor stance” ya kibondia, kama kwamba alikuwa akimsubiri ainuke ili waendelee na pambano iwapo Jaka angekuwa tayari kuendelea. Lakini ile ngumi ilikuwa kali sana na Jaka hakuwa na nguvu kabisa ya kujiinua kutoka pale chini. Alibaki akiwa amejikunja kwa maumivu huku akimtumbulia macho ya kukata tamaa yule jamaa.
“Wew…we nin…nah…nahh…nannii?” Alimbwabwajia kwa taabu yule mtu huku bado akiwa amejikunja pale chini.
“Jaka! Jak…Ni nini tena hiki lakini? Umekuwaje?” Sasa Clara aliwafikia pale walipokuwa na alikuwa akisaili kwa sauti iliyojaa hamaniko.
“Uh…usingekuja huku Clar…” Jaka aligumia kwa taabu, lakini Clara hakumtilia maanani.
“Who are you, mwanaharamu mkubwa wewe? Umemfanya nini huyu wewe, Eeenh?” Clara alimfokea yule jamaa kwa ukali huku akijitahidi kumuinua Jaka kutoka pale chini.
“No, Clara…ondoka ha…hapa! Ni hatari!” Jaka alijilazimisha kuongea huku akishindana na pumzi zilizoonekana kumbana kwa namna ya ajabu kutokana na pigo alilopokea.
John Doe alimtupia macho yule dada, kisha akamtazama Jaka aliyekuwa akihangaika kuinuka kutoka pale chini huku akisaidiwa na Clara, kisha bila ya kujibu akaruka nyuma hatua tatu, akageuka na kutokomea kichochoroni.
Clara akamtupia tusi la nguoni kwa hasira, kisha akamgeukia mpenziwe.
“Jaka! Jaka...vipi, uko salama...? Ni nani yule?” Alimuuliza huku akitweta.
“Yeah! Niko fiti....” Jaka alijibu kwa kujikakamua huku akiyumba. Mate yalimpalia na akakohoa kwanguvu sana, Clara akimpa pole kwa mashaka makubwa. Alitikisa kichwakwa nguvu kamamtu atakaye kuiweka akili yake sawa.
“Pole mpenzi…lakini…ilikuwaje kwani?”
“Ni John Doe yule!” Jaka alimjibukwa taabu huku wakiwa wameshikana mabega wakirudi kule ambako Clara alikuwa ameliacha gari lao, mbele ya jengo la TBC kanda ya kati.
“John Doe?”
“Yeah, ndiye yeye…mshenzi ana ngumi nzito sijapata kuona, bloody fool!”
Hakuwa na namna ya kujua kuwa yule mtu waliyempachika jina la John Doe alikuwa amempiga ile ngumi mahala pale makusudi, akijua kuwa ingemfanya ashindwe kabisa kumbughudhi. Ilikuwa ni ngumi iliyopigwa kwa uzito uliokusudiwa na ikatua mahala ilipokusudiwa.
Clara aliguna.
Hatua chache mbele yao Jaka aliiona kofia ya John Doe ikiwa imeanguka pale chini. Aliiokota na kuikumbatia kwapani kwake huku akiyumba kuelekea nje ya ule uwanja akisaidiwa na Clara.
Kwa nini umekimbia John Doe…?
Unataka nini kwangu wewe lakini…?
___________________
RPC Januari Mwakaja alishusha pumzi ndefu na kubaki akimtazama Jaka aliyekuwa ameketi kwenye kiti kilichokuwa upande wa pili wa meza yake pale ofisini huku akiigonga gonga meza ile taratibu kwa kalamu iliyokuwa mkononi mwake.
“I see...” Hatimaye alisema huku akiendelea kumtazama yule kijana, uso wake ukionesha kuwa bado alikuwa anajaribu kuyatafakari yale aliyokuwa ameambiwa na Jaka muda mfupi uliopita, kisha akaendelea, “...sasa wewe binafsi ulikuwa una mawazo gani hasa juu ya swala hili?”
Ikawa zamu ya Jaka kushusha pumzi ndefu kabla ya kuingea.
“Kitu ninachoomba kieleweke mzee ni kwamba, ingawa mimi nimeletwa hapa kama mhalifu niliyekuja kutumikia adhabu, bado kuna haki ninazopaswa nitendewe. Wakati nasomewa adhabu yangu sikusikia neno lolote kuhusu kuwekewa watu wa kufuatilia nyendo zangu kinyemela, halafu nikijaribu kuuliza kwa nini wananifuata wanipige...”
“Lakini mpaka sasa hakuna ushahidi wowote kuwa mtu huyo ametumwa na vyombo vya dola, kijana! Kama ingekuwa hivyo basi mimi ndiyo ningekuwa wa kwanza kujua...” January Mwakaja alimbishia.
“Sasa kama hivyo ndivyo, basi hiyo inathibitisha kauli yangu ya mwanzo kuwa maisha yangu yamo hatarini hapa Dodoma! Jambo lolote linaweza kunitokea hapa na wewe usiwe na habari mzee.” Jaka alizidi kuweka wazi mashaka yake.
Mzee Januari Mwakaja alimtazama kwa muda mrefu akiwa kimya. Hatimaye alimuuliza swali ambalo siku zote limekuwa likimsumbua kichwani mwake.
“Ni kweli uliua mtu huku ulipotoka?”
Ni swali ambalo Jaka hakulitegemea kabisa. Alipiga kimya kwa muda, akilini akitafakari iwapo lile swali halikuwa mtego.
“Unajua...kuna jaji mmoja huko Marekani aliwahi kusema kwamba, sisi sote tuko chini ya sheria, lakini sheria ni kile ambacho Jaji amesema kiwe...sasa kwa mtazamo huo mzee, iwapo bwana hakimu alisema kuwa mimi nastahili kifungo hiki kutokana na kuhusishwa na kifo cha mtu, kuna haja gani tena kutaka kujua iwapo ni kweli au si kweli niliua?” Hatimaye Jaka alimjibu kwa hisia kali.
Mzee Mwakaja alibaki akimtazama tu kwa muda.
“Oh! I see... Hivi ulifanya nini kule wewe...? Au uliona nini kule mpaka uwe mtu wa kufuatiliwa hivi?” Hatimaye alimuuliza kwa sauti yenye kukwaruza. Jaka aliachia tabasamu dogo la huzuni huku akiguna. Uso wake ulimbadilika na kuwa kama anayevuta kumbukumbu iliyomgusa sana, na ingawa alionekana kumuangalia yule mzee, hakika alikuwa hamuoni na badala yake alikuwa akiona mambo mbali mbali aliyokumbana nayo kabla ya kuletwa kwake pale Dodoma yakipita kwa kasi mno kichwani mwake.
“Ni mengi yametokea mzee...na mengi nimeyaona...tatizo ni kwamba waliotakiwa kuyasikia hawakutakana kufanya hivyo...”
Januari Mwakaja alizidi kumtazama. Tangu akutane na yule kijana, amekuwa akipata hisia kwamba kuna kitu hakikuwa sawa katika kuletwa kwake pale Dodoma. Aliwahi kuhisi kuwa pale alikuwa ameletwa ili apatwe na maafa ya kumtoa duniani, kwani kama ni kweli angekuwa amefanya kosa alilosemekana kuwa amelifanya, ile haikuwa hukumu sahihi.
“Unaweza kunieleza baadhi ya hayo uliyokutana nayo huko?”
Jaka alitikisa kichwa kwa masikitiko.
“Hapana mzee... ni hakika nimeona mengi sana, ila siwezi kukuelezea kwa sasa. Ni machungu sana...”
Mzee Mwakaja alimtazama kwa muda.
“Okay. Ila nina hakika kuwa katika hayo mengi uliyoona, kuna moja au mawili ambayo hukutakiwa kuyaona...” Hatimaye alihitimisha yule mzee.
Kimya kilipita kidogo, kisha Jaka akamuuliza yule mzee swali lililokuwa likimnanga kichwani mwake.
“Sasa baada ya kukuelezea mkasa ulionikuta jana usiku kutoka kwa huyu mtu mwenye koti refu na kofia pana...unaweza kunihakikishia vipi usalama wangu hapa mjini kwako?”
“Hilo swala niachie nilifanyie kazi kwanza kijana. Ninasikitika sana na yaliyokukuta hapa dodoma mpaka sasa ila elewa kuwa usalama wa raia wote wa hapa mjini uko chini yangu, hivyo na wewe pia uko katika himaya yangu. Nitalifanyia kazi kwa karibu sana hilo. Ila nawe saa upunguze kutembea tembea usiku na ujitahidi kuwa kwenye maeneo yenye majumuiko ya watu zaidi kuliko kuwa meneo pweke na peke yako...sawa?” Alimjibu.
Jaka aliafikiana naye kwa shingo upande, kisha akaaga na kuondoka.
Nyuma yake Mzee Januari Mwakaja aliinua mkono wa simu iliyokuwa pale mezani kwake na kumpigia mkuu wa polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam. Kuna mambo kadhaa ambayo alihitaji kufahamishwa.
Wakati ile simu ikiendelea kuita, Osman Mgunya aliingia mle ofisini nayeakairudisha ile simu mahala pake na kumtazama kwa macho ya kuuliza.
“Ulikuwa unahitaji kuniona afande ?” Osman aliuliza.
“Hapana...nikikuhitaji si nitakuita Osman?” Mwakaja alimjibu kwa mshangao.
“Ndio...nilikuwa nimetoka kidogo ofisini, na nilipokuwa narudi nikamuona Jaka akitoka ofisini kwako na simu ya ofisini kwangu ikawa inaita, lakini ilikatika kabla sijawahi kuipokea...hivyo nikadhani ni wewe ndiye uliyekuwa ukinipigia...” Mgunya amlijibu kwa kubabaika kidogo.
“Hapana, endelea na kazi zako.”
“Ndiyo Afande!” Osman alisaluti na kutoka.
Januari Mwakaja alikunja uso kwa mawazo huku akiendelea kukodolea macho pale mlangoni alipotokea Osman Mgunya sekunde kadhaa zilizopita.
Ni kweli alikuja kuulizia alichokuja kukiulizia pale ofisini, au alikuja kuhakikisha kitu...? Kwa nini ameamua kuja pale ofisini baada ya kumuona Jaka akitokea ofisini kwake?
Alikumbuka siku ile alipomkuta akimpiga Jaka kule ofisini kwake na akazidi kukunja uso kwa tafakuri. Alishusha pumzi taratibu, akainua tena mkono wa simu na kuanza kupiga namba za mkuu wa polisi wa kanda maalumu ya Dar es Salaam.
__________________
Dakika arobaini baadaye, Mzee Mwakaja alibaki akiwa ameduwaa na simu yake sikioni hata baada ya mtu aliyekuwa akiongea naye kule Dar kukata simu yake. Akiwa bado ameduwa na simu yake sikioni, aliweza kusikia mtu wa upande wa pili wa simu ile akiweka simu yake chini. Alikuwa anataka kuirudisha simu yake chini aliposikia tena mlio wa simu nyingine ikiwekwa chini. Alikunja uso na kuitoa haraka simu ile sikioni mwake na kuitazama, kisha akaiweka tena sikioni.
Kimya.
Aliurudusha mkono wa simu ile mahala pake huku sura yake ikisajili mikunjo mingi kwa mawazo. Alikuwa na hakika kabisa kuwa alisikia simu ya pili ikiwekwa chini baada ya simu ya RPC wa Dar kuwekwa chini...
Januari Mwakaja alikuwa mzoefu sana katika kazi kipelelezi, na ingawa alijua kuwa muda wake wa kustaafu ulikuwa unakaribia, bado alikuwa na imani kubwa sana katika uwezo wake wa kazi.
Kwa hali hiyo, mara moja alijua kuwa kuna mtu mwingine, mtu wa tatu, aliyekuwa akisikiliza mazungumzo kati yake na Kamanda wa Polisi wa kanda maalumu ya Dar es Salaam.
Kitu kingine alichojua ni kwamba ile simu ya tatu iliyotumika kusikiliza mazungumzo yale ilikuwa katika jengo lile lile ambamo ofisi yake ilikuwepo. Hiyo inamaanisha mtu aliyekuwa akisikiliza mazungumzo yale alikuwa ndani ya jengo lile lile alilokuwamo.
Ni nani?
Na kwa nini afanye vile?
Aliweza kujijibu swali la “nani” mara moja, au alidhani aliweza. Lakini swali la “kwa nini” bado lilihitaji uchunguzi wa kina.
Mawazo yake yalirudi kwenye maongezi yake na kamanda wa polisi wa kanda maalumu ya Dar es Salaam, ambapo alitaka ajulishwe mambo fulani kuhusiana na swala zima la mhalifu Jaka Brown Madega...
Tangu awali kesi ya huyu mtu aitwaye Jaka imekuwa ikimuachia maswali mengi kichwani, na alishindwa kuielewa. Cha ajabu ni kwamba baada ya kuongea kwa zaidi ya dakika arobaini na yule mwenzake wa Dar es Salaam, amejikuta ndio ameongezewa maswali zaidi kuliko majibu kuhusiana na kesi ya Jaka na hivyo kuzidi kutoielewa.
Samson Ramadhani, kamanda wa polisi wa kanda maalumu ya Dar es Salaam alimpa jibu ambalo hakulitegemea pale alipomuomba amtumie faili la kesi nambari 08/12582/94/800 inayomhusu mtu aitwaye Jaka Brown Madega.
“Faili hilo limetoweka katika mazingira ya kutatanisha kiasi cha miezi miwili iliyopita...”
Ndilo jibu lililomfanya abaki ameduwaa na simu sikioni...
_________________
Sehemu nyingine ya jengo lile lile, Osman Mgunya alirudisha taratibu mkono wa simu mahala pake baada ya kujihakikishia kuwa January Mwakaja na Kamanda wa kanda maalumu ya polisi ya mkoa wa Dar es Salaam, ambao yeye alikuwa akifuatilia mazungumzo yao ya simu bila ya wao kujua, walikuwa wameshaweka chini simu zao. Alibaki kimya kwa muda huku uso wake mbaya ukiwa umekunjamana kwa tafakuri.
Aliyasikia yote yaliyoongewa baina ya January Mwakaja na yule mwenzake wa Dar es Salaam, na aliyoyasikia hayakumpa amani hata kidogo. Lakini kilichomnyima amani zaidi ni kukosa kujua kilichoongelewa baina ya Jaka na yule mkuu wake wa kazi wa pale Dodoma kule ofisini kwake asubuhi ile. Osman hakuwa mjinga. Aliweza kuunga moja na moja na akapata jibu sahihi kuwa ni mbili. Ilifunukia wazi kuwa ni kile kilichoongewa baina ya wawili wale mpe ofisini kwa Mzee Mwakaja ndicho kilimchochea yule mkuu wake wa kazi wa muda apige ile simu kule Dar.
Baada ya kusikia jinsi RPC January Mwakaja alivyokuwa akimhoji yule mwenzake wa Dar juu ya mazingira ya kupelekwa pale Dodoma kwa mtuhumiwa Jaka, na hususan alivyojaribu kuomba apelekewe faili zima la kesi iliyomhusisha yule kijana, alijua kuwa lolote aliloambiwa na Jaka kuhusu mazingira ya kupelekwa kwake pale Dodoma alikuwa ameliamini.
Alianza kumung’unya midomo kwa wasiwasi.
Ni nini Jaka amemwambia huyu mzee kilichomfanya apige ile simu na kuongea yale aliyomsikia akiongea na kamanada wa kanda maalumu ya Dar?
Hakupata jibu zuri. Na kwa kuwa hakupata jibu zuri alijua kuwa wakati wa kuomba msaada wa haraka kutoka kwa watu aliokuwa akishirikiana nao kule Dar ulikuwa umefika, vinginevyo angeweza kushindwa kumtia Jaka hatiani kwa kosa jingine pale Dodoma kama alivyokuwa ameagizwa. Yule mkuu wa polisi wa mkoa ule alionekana kumuamini sana yule kijana. Na hilo lingeifanya kazi iliyompeleka pale Dodoma kuwa ngumu sana.
Akiachana na ile simu ya mezani, alitoa simu yake ya kiganjani na kuanza kubofya tarakimu za namba ya simu ya mtu ambaye alijua kuwa muda ule alikuwa jijini Dar es Salaam...
___________________http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jioni ya siku ile aliyokwenda kumshitakia Mzee January Mwakaja kuhusu tukiio la kushambuliwa na yule jamaa aliyempachika jina la John Doe, Jaka alikuwa amekaa sebuleni akiwa amezongwa na mawazo juu ya yale mambo yaliyokuwa yakimuandama. Alikuwa akifanya hivyo huku akiichezea chezea ile kofia ya yule mtu aliyoiokota kule uwanja wa sabasaba usiku uliopita baada ya kuambulia ile ngumi nzito sana ya chembe.
Clara alikuwa amezama kwenye kutazama tamthiliya aipendayo kwenye runinga, akijitahidi kutombughudhi kwani alijua kuwa Jaka alikuwa kwenye mawazo mazito na alihitaji kuachwa peke yake kwa muda.
Jaka alikuwa akiigeuzageuza ile kofia huku akiwa amezama kwenye lindi la mawazo, hususan namna atakavyoweza kumnusuru Clara na zahma ile ambayo sasa alikuwa ameshamtumbukiza rasmi.
Clara hakutakiwa kabisa aingizwe kwenye matatizo haya!
Alijiwazia huku akiigeuza ile kofia na kutazama ndani yake. Akamakinika. Kitu ndani ya kofia ile kilimvutia jicho lake, naye akamakinika maradufu huku akiisogeza ile kofia karibu zaidi na uso wake.
Mawazo yakatoka kwenye madhila yake na Clara na kuhamia ndani ya ile kofia.
Ukingo wa ndani wa kofia ile ulikuwa umeshonewa ufito wa kitambaa kwa ajili ya kumkinga mvaaji na jasho au mikwaruzo kutoka kwenye ngozi ya kofia ile. Kutoka kwenye ukingo wa ule ufito wa ndani ya ile kofia aliona kipande cha karatasi kikiwa kimechomoza kidogo. Alikichomoa kile kikaratasi na kukikunjua.
Kwa hati nzuri ya kiume aliona jina lake likiwa limeandikwa kwenye kile kipande cha karatasi, likifuatiwa na namba ambazo hakuzielewa, kisha maneno “Uhindini, DOM” yakafuatia. Chini ya maneno yote hayo kulikuwa kuna maneno yaliyopitisha ubaridi mwilini mwake.
MURDERER…OR FG…???
“Heh!” Alimaka kwa sauti huku akiinuka kutoka kwenye kochi akiwa amekishikilia kile kipande cha karatasi, ile kofia ikianguka kutoka mikononi mwake.
“Ni nini Jaka?” Clara alimuuliza huku akimgeukia.
“Mnh! Hata sielewi Clara!” Alimjibu huku akimpa kile kikaratasi. Clara alisoma yale maandishi na kumuinulia uso uliotatizika.
“Imetoka wapi hii karatasi Jaka?”
“Ilikuwa imechomekwa ndani ya kofia ya yule jamaa…John Doe!”
“Seriously?”
“Seriously…na zaidi ya hilo jina langu hapo, na hilo neno “murderer” linalomaanisha kuwa mimi ni muuaji, sielewi maana ya kitu kingine chochote kilichoandikwa hapo, mpenzi!” Jaka alilalama huku akiwa amejishika kiuno.
Clara alikunja uso.
“Subiri…hizi namba kando ya jina lako…ni namba za hii nyumba yetu tuliyomo hapa…” Alisema kwa hamasa.
“Ama?”
“Ndiyo! Ambayo iko hapa Uhindini, mjini Dodoma!” Clara alizidi kutanabahisha.
“Ah! Ndio maana ya hilo neno “Uhindini, DOM”, siyo?” Jaka naye alithibitisha uelewa wake juu ya ile hoja ya Clara.
“Ndiyo!”
Kimya kilipita kidogo.
“Kwa hiyo hii inathibitisha kabisa kuwa John Doe si mkaazi wa hapa Dodoma, ndio maana ameandika au ameandikiwa hiyo anuani ya mahala nyumba ninayoishi ilipo!” Jaka alisema huku akijiegemeza kwenye mgongo wa moja ya makochi ya pale sebuleni.
“Yah, inaonesha hivyo aisee!”
“Na amekuja hapa Dodoma kwa makusudi mazima ya kunifuatilia mimi!”
“Hilo tulishalijua Jaka…kilichobaki kuwa kitendawili ni haya maandishi ya mwisho hapa kwenye hii karatasi, mpenzi…” Clara alisema, na hapo Jaka akadakia.
“Yeah…murderer or FG…”
“Haswa! Muuaji, au FG…sasa hii FG ni nini?” Clara alithibitisha na kuanika hewani swali ambalo pia lilikuwa kichwani kwa Jaka wakati ule.
Kimya kilipita. Hakukuwa na jibu la aina yoyote juu ya swali lile.
“Nadhani hilo litajibiwa na John Doe pindi nitakapokutana naye tena. Hii sasa ni vita ya wazi kati yangu na yeye…!” Jaka alisema kwa sauti ya chini lakini yenye azma thabiti.
“No Jaka. Vita na yule jamaa huiwezi. Inabidi tutafute msaada katika hili!” Clara alimwambia kwa mashaka makubwa.
“Hakuna msaada kwangu katika hili Clara…naona lile jinamizi nililoliacha kule Dar limeamua kunifuata huku Dodoma. Sina jinsi wala namna sasa…ni kukabiliana nalo tu!”
“Kuna Polisi Jaka. Mzee Mwakaja anaonekana kuwa ni mwenye nia ya kukusaidia…mtake tena msaada!”
Jaka alimtupia jicho la pembeni, lakini hakusema kitu. Alijua kuwa asemayo kuhusu Mzee January Mwakaja ni kweli kabisa, lakini pia kuna mengi zaidi ambayo yeye alikuwa anayajua na Clara alikuwa hayajui. Na hayo ndiyo yaliyomfanya asiamini sana kuwa atapata msaada kutoka kwa jeshi la polisi, pamoja na uwepo wa Mzee Mwakaja.
“Nadhani nahitaji kwenda kulala sasa…” Alisema kwa upole huku akilelekea chumbani, akimuacha Clara akiwa amepigwa butwaa pale sebuleni ilhali bado amekishikilia kile kikaratasi.
Siku zilizofuata Jaka alijitahidi kuwa makini sana kila alipokwenda, na alimsisitizia Clara kufanya hivyo hivyo. Alijikuta akijaribu kumtafuta John Doe kila kona, akitaraji kuonana naye tena.
Lakini John Doe hakuonekana tena.
Alijaribu kuwauliza walinzi mbali mbali wa pale ofisini kwao iwapo kuna mtu yeyote aliyekuwa akimuulizia pale getini au ofisini.
Hakukuwa na mtu yeyote aliyekenda kumuulizia pale ofisini.
Hakumuona tena, lakini hakuweza kumtoa akilini mwake. Kitu kimoja alichokuwa na uhakika nacho ni kwamba John Doe hakuwa ametumwa na polisi wa mkoa ule wala wa Dar es Salaam. Hilo alilijua kutokana na maongezi yake na mzee Januari Mwakaja ambaye alishakutana naye mara mbili zaidi kuongelea juu ya jambo hilo. Sasa ilikuwa inakaribia wiki ya pili tangu vurumai ile ya uwanja wa sabasaba imtokee, na ingawa mwanzo RPC Januari Mwakaja alionesha dalili za kumshuku Osman Mgunya kuhusiana na tukio lile, baada ya muda huo kupita alianza kulipuuzia tukio lile na kuamini kuwa yule mtu alikuwa ni mwizi wa kawaida tu.
Wazo ambalo lilipingwa vikali na Jaka. Haikumuingia akilini kwa nini mwizi wa kawaida aanze kumuulizia habari zake ofisini kwanza kabla hajaamua kwenda kumwibia au kumvamia. Zaidi ya hapo, haikuwa rahisi kwake kulipuuzia tu swala lile. Kama John Doe alikuwa ni mwizi, basi kwa hakika hakuwa "mwizi wa kawaida tu".
___________________
Suzuki Vitara ya bluu ilikata kushoto na kuingia Mtaa wa Kuu(Kuu Street) ikitokea Uhindini. Moja kwa moja mwisho wa mtaa ule, jengo la ofisi za makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Dodoma lilionekana likiwa upande wa pili wa barabara ile. Ile Vitara ilipaki kiasi cha hatua kumi hivi za miguu nje ya wigo wa eneo maarufu na Nyerere Square pale Dodoma ambalo lilikuwa linatazama na jengo la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ng'ambo ya pili ya barabara Kuu, upande ule ule ambao ofisi za CCM zilikuwapo. Eneo lile la Nyerere Square lilikuwa maarufu kwa migahawa mingi iliyoandaa maakuli mbali mbali kwa wakaaji wa pale mjini. Na pia kilikuwa ni kituo muhimu cha makutano kwa watu kutoka sehemu mbalimbali za mji wa Dodoma.
Jaka na Clara waliteremka kutoka kwenye gari lile na kuingia ndani ya eneo lile. Ikiwa ni asubuhi ya siku ya jumapili, eneo lile lilikuwa limefurika watu, wengi wao wakiwa ni waumini waliotoka kwenye nyumba za ibada na kuamua kwenda kujipatia staftahi au kujiburudisha kwa vinywaji mbali mbali ndani ya eneo lile. Wengine walienda eneo lile kwa lengo la kukutana tu na marafiki ambao hawakuweza kuonana nao kwa wiki nzima. Ilikuwa ni mazoea ya Jaka na Clara kwenda kupata kiamsha kinywa sehemu ile siku za jumapili badala ya kujipikia chai wenyewe nyumbani.
Pamoja na umakini aliojiwekea tangu siku ya mkabala wake wa mwisho na John Doe, Jaka hakumuona mtu mmoja aliyekuwa ameinama kwa msafisha viatu aliyekuwa pembeni ya mlango wa kuingilia ndani ya eneo lile. Yule mtu aliwaona wakipita mita chache tu kutoka pale alipokuwa amekaa akisafishiwa viatu vyake. Alikuwa amevaa koti refu jeusi lililoishia chini ya magoti yake. Suruali ya kahawia ilitokeza chini ya koti lile na kofia yake ya pama ya rangi ya kahawia alikuwa ameipakata mapajani mwake akiwa amekaa kwenye benchi la yule msafisha viatu...
Ambalo pia Jaka hakuliona ni kwamba dakika chache tu baada ya ile Vitara yao kuegeshwa pale nje ya eneo lile, gari jingine dogo aina ya Toyota Raum lenye rangi nyeupe lilifika na kuegeshwa nyuma ya gari la tatu kutoka pale ilipoegeshwa ile Vitara yao. Watu wawili waliokuwa ndani ya ile Raum hawakuteremka mara moja.Walitulia ndani ya lile gari wakiwaangalia akina Jaka wakiteremka na kuingia ndani ya lile eneo la Nyerere Square.
Kama Jaka na Clara wangekuwa makini zaidi, wangegundua kuwa ile Raum ilikuwa nyuma yao tangu walipotoka nyumbani kwao pale Uhindini kwenye kona ya Mbeya Avenue. Lakini umakini waliodhamiria kuwa nao ulikuwa umeshawatoka.
Yule bwana mwenye koti refu aliinuka kutoka kwenye benchi la mng'arisha viatu na kuondoka taratibu kuelekea kule lilipoegeshwa gari la akina Jaka. Alipofika usawa wa ile Vitara, alianza kuvuka barabara kuenda upande wa pili wa ile barabara ya Kuu, lakini ile Raum nyeupe nayo ikaanza kutoka na kuingia barabarani, hivyo alisimama ili ipite huku akiwa ameipa mgongo ile Vitara.
Ile Raum ilikuwa inakuja taratibu mno na yule mtu mrefu aliona kuwa mtu aliyekuwa kando ya dereva alikuwa akiiangalia sana ile Vitara. Jamaa alikuwa amevaa shati kubwa jeupe na tai pana yenye mchanganyiko wa madoa meusi na meupe. Usoni alikuwa amevaa miwani ya jua iliyoficha sehemu ya sura yake, na nywele zake zilikuwa zimekatwa na kuwa ndogo sana kiasi cha kukaribia kuwa upara. Hakuwa amepata kumuona kabla ya wakati ule yule jamaa. Raum ilipopita akavuka ile barabara na kwenda kusimama ng’ambo ya pili ya ile barabara, kando ya jengo la Benki, mahala ambapo kutokea pale aliweza kuona moja kwa moja kule ambapo ile Vitara ya akina Jaka ilikuwa imeegeshwa.
Dakika chache baadaye alimuona yule jamaa aliyekuwa kwenye ile Raum iliyompita muda mchache uliopita akirudi kwa miguu akiwa upande wa pili wa ile barabara, akielekea kule lilipokuwa gari la akina Jaka. Akamakinika naye huku akihisi msisimko ambao huwa unampata pale tu anapohisi hatari.
Alipofika usawa wa lile gari la Zaza Cargo Movers, yule jamaa aliinama kama anayefunga kamba za viatu zilizomfunguka ghafla. Alikuwa ameinama kando ya tairi la mbele la gari ile kwa upande wa barabarani. Hivyo hakuweza kuonekana na watu waliokuwa kule Nyerere Square. Mara ile yule mwenzake aliyekuwa akiendesha ile Raum nyeupe alipita na kuegesha lile gari upande ule ule aliokuwapo yule mtu mwenye koti refu, mita chache kutoka pale alipokuwa amesimama.
Mnh! Kuna mpango gani hapa?
Alimtazama kwa makini zaidi yule jamaa aliyechutama pale kando ya gari la akina Jaka.
Mbona kama anafunga kamba kwa mkono mmoja? Inawezekanaje?
Alimakinika zaidi na yule mtu, lakini gari lililopita pale barabarani lilimkinga kidogo. Akageuka na kumtazama yule dereva wa ile Raum, ambayo sasa ilikuwa upande ule aliokuwapo yeye. Huyu alikuwa kijana zaidi ya yule mwenzake na alikuwa amevaa kofia ya kepu, miwani myeusi na fulana nyeusi iliyoushika sana mwili wake mwembamba. Hakuwa na ndevu.
Alitupa tena macho upande wa pili wa ile barabara, na kuna gari jingine likawa linapita hivyo hakumuona yule jamaa mwenye tai mpaka lilipopita, ambapo alimuona yule jamaa akiinuka kutoka pale alipokuwa amechutama. Mara moja yule mtu mrefu mwenye koti refu aligundua kitu kisicho cha kawaida. Mkono wa kulia wa yule mtu mwenye tai ulikuwa unatokea nyuma ya bati linalofunika tairi la mbele la gari lile!
Ala!
Yule mtu mwenye tai alisimama kwa sekunde chache zaidi kama mtu anayetaka kuvuka barabara. Kisha taratibu alitumbukiza mikono yake kwenye mifuko ya suruali yake ya buluu, akageuka nyuma taratibu kuangalia upande ambao Jaka na Clara wangetokea, halafu aligeuka tena taratibu na kutazama kule ambapo ilipoegeshwa ile Raum nyeupe.
Hapo yule mtu mrefu mwenye koti refu alijua kuwa yule jamaa alikuwa ni mtaalamu kwenye fani yake kwani alikuwa akigeuka kwa namna ambayo kwa mtu mwingine yeyote angeonekana kuwa ni mtu wa kawaida aliyekuwa akimsubiri rafiki au jamaa aliyechelewa miadi. Katika kugeuka kwake, alikuwa akizungusha mwili wake kutokea kiunoni kuja juu, na wakati akifanya hivyo alikuwa akitupa tupa miguu yake mbele, mara moja au mbili akijaribu kupiga teke vijiwe vidogo vilivyokuwa pale barabarani. Hii ilileta picha kuwa alikuwa akimsubiri mtu, na subira yake ilikuwa inaelekea ukingoni.
Haya yote yaliendelea kutazamwa kwa utulivu wa hali ya juu na yule bwana mwenye kofia pana, kwani naye, kama yule mtu mwenye tai ng'ambo ya pili ya barabara, alikuwa ni mtaalamu kwenye fani yake. Mara ile yule mtu mwenye tai aliinua mkono wake wa kulia na kuangalia saa. Mtu mwenye pama alitabasamu, kwani alielewa ni nini kitafuata baada ya kitendo kile. Yule bwana mwenye tai alishusha mkono wake na kuanza kuvuka barabara taratibu kuelekea kule ilipokuwa imeegeshwa ile Raum.
Jamaa mwenye kofia pana alijua kuwa hakuwa peke yake aliyekuwa akimvizia Jaka siku ile. Yeye
binafsi alijua ni kwa nini alikuwa anamfuatilia Jaka siku ile. Tatizo ni wale jamaa wengine. Wanahusiana vipi na Jaka? Kwa nini hawakutokea siku zote wakaamua kutokea leo? Na jambo alilofanya yule bwana mwenye tai pale kwenye gari la akina Jaka....
Maswali haya yalipita kichwani mwake huku akijaribu kuoanisha matendo ya yule mtu mwenye tai na uwepo wa akina Jaka kwenye eneo lile. Jibu la jumla alilolipata ni kwamba jambo baya sana lilikuwa linaandaliwa...limeandaliwa pale.
Alibaki pale pale alipokuwa amesimama. Jamaa aliingia ndani ya ile Raum na kutulia kando ya dereva. Kinyume na matarajio ya yule bwana mwenye pama, ile Raum iliendelea kubai pale pale, haikuondoka, Aliitazama ile gari na kujikuta akizikariri namba za usajili za gari lile.
Ni jambo gani limefanyika pale?
Kwa nini?
Hakupata jibu. Dakika zilisogea. Nusu saa ilipita. Dakika aribaini na tano. Hakuna badiliko. Ile Raum bado ilikuwa imeegeshwa pale pale na wale watu wawili wakiwa ndani yake.
Sasa wanasubiri nini? Yule mtu alipitisha mkoni chini ya ile Vitara...kwa nini...?
Wakati akiendelea kujiuliza maswali hayo, alizidi kuchanganyikiwa pale alipowaona Jaka na Clara wakitoka nje ya eneo lile la Nyerere Square kuelekea kwenye gari lao huku wakiongea na kucheka kwa furaha, Clara akiwa amebeba kifurushi kidogo bila shaka cha vipochopocho walivyonunua eneo lile.. Aligeukia tena kule kwenye ile Raum. Dereva wa ile gari alikuwa ametoa kichwa nje ya dirisha akiangalia kule ambapo akina Jaka walikuwako. Na hata pale alipokuwa akimtazama, alimuona yule dereva wa Raum akiinamisha uso kutazama saa yake na kuuinua tena uso kuwatazama akina Jaka.
Ina maana gani?
Kama kuna jambo lolote lililoandaliwa pale, basi sasa ndio ulikuwa wakati wa jambo hilo kutokea. Akili ilimwenda mbio...
Kule upande wa pili wa barabara Jaka alikuwa anazunguka mbele ya ile Vitara ili aende upande wa dereva ambao ulikuwa upande wa barabarani. Clara alikuwa amesimama upande wa mlango wa abiria wa gari lile....
Ni nini kitatokea pale?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Na mara alikumbuka.
Ilimjia kichwani mwake kwamba katika nukta moja ya sekunde baina ya kupita gari la kwanza na la pili aliweza kumuona yule mtu mwenye tai akiwa ameinama pale chini, na katika nukta ile macho yake yalikuwa yanautafuta mkono wa kulia wa yule mtu, kwai ilimjia kama anayefunga kamba kw amkono mmoja tu...mkono wa kushoto. Katika nukta moja ile, alihisi aliuona ule mkono wa kulia wa yule mtu ukiwa umeshika tairi la mbele la lile gari...au ulikuwa umefichwa na bati la gari lile linalofunika tairi...?
Aligeuka tena kushoto kwake.
Ile Raum ilikuwa inaondoka taratibu kutoka eneo lile; na sasa alimuona yule mtu mwenye tai, akiwa ndani ya gari akigeuka kutazama pale lilipokuwa gari la akina Jaka. Naye upesi aligeuka tena kutazama kule walipokuwa akina Jaka.
Jaka alikuwa ameegemeza sehemu ya mbele ya mwili wake kwenye boneti la gari lile akipokea funguo za gari kutoka kwa Clara aliyekuwa upande wa pili wa gari lile.
Akili ilizidi kumzunguka jamaa mwenye pama.
Ilikuwa haileti maana....kwa nini yule mtu, ambaye kwa hakika alikuwa akiwasubiri akina Jaka, aamue kuondoka baada ya watu aliokuwa akiwasubiri kutokea...bila ya kuongea nao chochote? Au...?
Hakufikiri zaidi.
Alikurupuka na kutoka kasi kukimbilia kule walipokuwa akina Jaka huku akimwita Jaka kwa kelele na akimpungia mikono ili amuone.
"Jaka...! Jakaaaaaaa! Toka hapoooo....tokeniiiih! Kimbienii....ondokaaaaa...uppeeeesssss!" Yule mtu alikuwa akipiga kelele huku akivuka barabara kuelekea kule walipokuwa akina Jaka.
Jaka aligeuka kwa mshituko aliposikia jina lake likiitwa kwa kelele hadharani. Na hata pale alipogeuka alimuona yule mtu mwenye koti refu akiingia barabarani huku akimkimblia bila kujali magari. Gari moja lilifunga breki kali na kuserereka huku tairi zake zikitoa sauti kali ya msuguano na lami huku honi kali ikirindima. Lile gari lilikuwa linaelekea kumgonga lakini yule mtu aliweka mkono wake wa kulia kwenye boneti la lile gari na kujisereresha juu ya boneti lile na kudondokea upande wa pili wa gari ile. Watu walioshuhudia tukio lile walipiga kelele za woga na mshituko juu ya kitendo kile hali wengine wakibaki midomo wazi na kujishika vichwa. Jamaa hakujali. Aliendelea kuwakimbilia akina Jaka huku akiwapigia kelele kama mwehu.
"Ondoka wewweeeh....! Kimbia...! You are going to die gaddemmiiiitt! Toka...! Hilo gariiii!"
Mara moja alimtambua John Doe. Alimuona alivyokuwa akiwaendea mbio huku akipunga mikono hewani na akipiga mayowe kama mwehu, na alishuhudia kwa mshituko jinsi alivyoruka juu ya boneti la gari lililokuwa kwenye mwendo wa kasi. Alipoona bado John Doe anazidi kuwakimbilia namna ile baada ya kukoswa kugongwa na gari, alijua ni lazima afanye kitu. Alisikia maneno yaliyokuwa yakitoka kinywani mwa yule mtu na aliiona hofu iliyojianika usoni kwa yule jamaa wakati akiwakimbilia namna ile. Jamaa alikuwa hafanyi utani.
Kutokea kule alipokuwa Jaka aligeuka na kuudaka mkono wa Clara na kumvuta pembeni huku na yeye akijisukuma kutoka ubavuni mwa lile gari kuelekea mbele ya lile gari. Clara alipiga kelele za hamaniko bila ya kuelewa kilikuwa kinatokea. Jaka alimkamata kiuno na kujitahidi kumvutia pembeni, mbali na lile gari lao. Walipepesuka vibaya huku raia waliokuwa eneo lile nao wakipiga kelele za kutoelewa.
Sasa John Doe alikuwa karibu sana na walipokuwa wakipepesukia. Jaka alijigeuza mzima mzima na kumkabili yule jamaa mwenye ngumi nzito huku akiwa amemkinga Clara kwa mgongo wake. Alikuwa akijitahidi kuongeza umbali baina yao na John Doe kwa kurudi nyuma huku akimsukuma Clara kwa nyuma. Watu wengi waliokuwa katika eneo lile walitawanyika mbio kila mmoja kwa upande wake bila ya kujua ni nini hasa walichokuwa wanakikimbia.
"Hilo gari hilo weweee...! Gariii! Kaa mbali naloo...ebbo! TOKA HAPOOO! Kimbieniii, Pummm-bbaaavvvv!" John Doe aliendelea kubwata huku akiwakimbilia. Jaka aliduwaa kidogo, na hapo John Doe alienda hewani mzima mzima akiwa ametanguliza mikono yake na kumkumba Jaka kwa kishindo, bega lake la kushoto likijikita tumboni kwa Jaka na wakati huo huo mkono wake wa kushoto uking'ang'ania kiunoni Clara aliyekuwa nyuma ya Jaka. Kwa wahka Jaka alirusha ngumi kwa mkono wake wa kushoto akiamini kuwa jamaa alikuwa anashambulia, lakini yule jamaa jabari aliipangua ngumi ile na hapo hapo akamdaka mkono ule kwa mkono wake wa kulia na wote watatu wakawa wanaelekea kupiga mweleka mzito.
Jaka hakuwa na la kufanya zaidi ya kung'ang'ania koti la yule mtu kwa mgongoni kwa mkono wake wa kulia. Nyuma yake, Clara akajigonga kisigino kwenye ukingo wa barabara na kupoteza kabisa mwelekeo. Alibaki akimng'ang'ania Jaka mgongoni huku akipiga kelele zisizoeleweka.
Msukumo wa yule mtu alivyowaparamia, na kujikwaa kwa Clara, viliwafanya wote watatu waruke hewani na kujibwaga bila mpangilio juu ya meza za wachuuzi wachache waliokuwa kando ya barabara ile. Mayowe yalizagaa wakati wao wakijipigiza chini kwenye vumbi wakisambaratisha meza na bidhaa zilizokuwa juu yake huku wale wachuuzi wakipiga mayowe na kukimbia hovyo. Jaka alikuwa akijaribu kujiinua kutoka pale chini akiwa amemlalia Clara kwa mgongo wake huku yule jamaa akiwa amemlalia kwa tumbo lake juu yake. Lakini kila alivyojaribu kujiinua ndivyo yule jamaa alivyozidi kumkandamiza chini kwa nguvu na ndivyo walivyozidi kumwelemea Clara aliyekuwa chini kabisa akipiga kelele vibaya sana.
Na mara hiyo hiyo mlipuko mkubwa sana ulisikika.
Jaka akiwa amekandamizwa chini na yule mtu aliweza kushuhudia kwa mshituko na kutoamini kukubwa kabisa jinsi gari lao likipasuka kuanzia sehemu ya mbele sanjari na mlipuko ule. Moto mkubwa uliruka hewani na aliliona lile gari likinyanyuliwa zima zima kutoka pale lilipokuwa limeegeshwa na kutupwa hewani huku likisambaratika vipande vipande. Vipande vya vioo vilirushwa huku na huko na kurudi ardhini kama matone ya mvua, vikijeruhi watu waliokuwa wamezagaa eneo lile. Tairi moja lilichomoka na kutupwa angani huku likiwaka moto na kufuka moshi.
Yote haya Jaka aliyaona ndani ya sekunde moja tu.
Macho yalimtoka pima na kinywa kilimchanua pasi sauti kutoka.
Mayowe, vilio na heka heka vilitawala eneo la Nyerere Square asubuhi ile. Watu walikibia huku na kule wakijaribu kuokoa maisha yao bila ya kujua ni wapi hasa palikuwa salama. Katika kelele zao hizo, Jaka alimsikia Clara akipiga mayowe ya woga na maumivu kutokea nyuma yake.
Clara likuwa amelalia mgongo pale chini. Juu alikuwa amelaliwa na mgongo wa Jaka. Juu ya Jaka John Doe alikuwa amelalia tumbo uso wake akiwa ameuficha upande wa kulia wa shingo ya Jaka huku akijikinga kichwa chake kwa mkono wake wa kushoto. Uso wa Jaka ulitokeza juu ya bega la kushoto la yule mtu ukitazama angani.
Na mara nyingine tena kilisikika kishindo kingine kilichotokana na mabaki ya lile gari kujibwaga tena ardhini katikati ya barabara na kulalia ubavu huku likiendelea kuteketea kwa moto. Watu walianza kulikimbilia na kulizunguka, hali wengine wakiwazunguka akina Jaka waliojirundika pale chini.
John Doe alijiinua kutoka pale chini, na haraka Jaka aliyechanganyikiwa naye akakurupuka kutoka pale chini. Alipepesuka na kuanguka tena chini. John Doe alimsaidia Clara kuinuka kutoka pale chini na kumshikilia asianguke kama Jaka. Uso wake ulionekana kutulia na kutokuwa na woga hata kidogo. Hatimaye Jaka aliinuka na kujivuta mpaka pale alipokuwa amesimama Clara huku macho yakiwa yamemtoka pima.
"Oh! Jaka...Jaka...tungekufa leo dear!" Clara alibwabwaja huku akilia. Jaka alimkumbatia kwa nguvu huku akimpigapiga mgongoni.
"Ni kweli. Lakini bado tunapumua...hatujafa...." Jaka alimliwaza huku macho yake yakiangaza huku na kule akimtafuta yule mtu mwenye koti refu ambaye alionekana kuyeyuka kama upepo mara Jaka alipomfikia Clara pale walipokuwa wamesimama. Kwa hakika yule mtu alikuwa amewaokoa kutokana na kifo kibaya sana, na sasa jumla ya maswali yaliyopita kichwani mwake ilikuwa haisemeki. Swali moja lilibaki kuwa kubwa kuliko yote.
Kwa nini?
"Imekuwaje...? Nini kimetokea...?" Alijikuta akibwabwaja peke yake huku akiendelea kutembeza macho kila kona bila ya mafanikio, kundi la mashuhuda liliowazunguka ulilifanya zoezi la kumuona yule mkombozi wao asiyetarajiwa kuwa gumu sana.
"Mlitegewa bomu....na wewe ndiye uliyekusudiwa." Sauti ilimjibu kwa upole kutokea nyuma yake. Aligutuka huku akigeukia kule sauti ilipotokea, na kumuona yule mtu mwenye koti refu. Alikuwa amesimama huku macho yake akiwa ameyaelekeza kule lilipokuwa linateketea lile gari.Yaani jamaa alikuwa amemjibu bila ya kumtazama na hakutaka kumtazama.
"Lakini wewe...? Kwa nini umeni...umetu....mbona... Ah! We' nani kwani...?" Jaka alibwabwaja huku akimkodolea macho yule mtu na akishindwa kabisa kuzipangilia sentesi zake. Mara ving'ora vya magari ya polisi vilisikika, na muda mfupi baadaye magari matatu ya polisi yalifika eneo lile kwa makeke. Askari wa jeshi la polisi waliruka kutoka kwenye magari yale na kuzidi kuwatia hofu wananchi waliojazana eneo lile.
Kwa sauti ya chini huku akiendelea kutazama kule kwenye moto John Doe alimwambia:
"Utakapoulizwa na hao polisi, mimi na wewe hatujaonana. Hujui ni nani aliyekuokoa...tutaonaoena tena." John Doe alimnong’oneza huku bado akiwa ameelekeza uso wake kule kwenye lile gari lililokuwa likiteketea kwa moto. Kisha aligeuka na kujichanganya kwenye umati wa watu.
Jaka alibaki akiwa ameduwaa. Wala hakugeuka kutazama ni wapi alikuwa akielekea yule jamaa. Macho yake yalikuwa yanatazama mbele ambako askari wawili walikuwa wakielekea pale alipokuwa amesimama na Clara.
"Niachie mimi nijibu maswali yote." Alimnong'oneza Clara ambaye hata hivyo hakuwa katika hali ya kuongea hata kidogo.
"Nyie ndio wenye lile gari?" Mmoja wa wale askari aliuliza mara walipowafikia. Jaka aliafiki kwa kichwa.
"Samahani, naomba tungozane." Yule askari aliwaambia.
Bila ya kutia neno, Jaka alimshika mkono Clara na kumuongoza kuwafuata wale askari. Mmoja wa wale askari alikuwa akiwapangua watu waliojaa eneo lile ili kuwapa njia ya kupita. Walielekezwa kuingia ndani ya gari la polisi aina ya Volkswagen Golf, na hapo hapo hilo gari liliondolewa kwa kasi kutoka eneo lile.
Njia nzima kuelekea huko alipokuwa anapelekwa na wale wana usalama Jaka alikuwa amezongwa na mawazo kuhusu yule mtu wa ajabu aliyeokoa maisha yao kutokana na mlipuko ule. Clara alikuwa akiendelea kulia taratibu akiwa ameegemeza kichwa begani kwake, naye alikuwa akimpapasa kichwa kile kwa kumliwaza huku akili yake ikilitafakari lile tukio.
Lile bomu alikuwa ametegewa yeye, na kama si John Doe kujitolea kuwatahadharisha namna ile, ni wazi yeye na Clara wangekuwa marehemu muda ule.
Sasa ni nani anayetaka yeye afe?
Kwa nini atake kumuua sasa hivi na si wakati wowote kabla ya sasa?
Lile bomu lilikuwa limetegwa saa ngapi?
Ni nani aliyelitega?
Maswali haya yalikuwa yakizunguka tu akilini mwake bila ya kujua ni wapi walipokuwa wakipelekwa na wale wana usalama.
Na wala hakujali.
Bila shaka yule mtu aliyewaokoa na kifo kutokana na bomu lile, ambaye amekuwa akifuatilia nyendo zake kwa siri, atakuwa na ufumbuzi kuhusu mengi ya maswali haya.
Lakini nyuma kabisa ya akili yake, Jaka alijua kuwa tukio lile lilikuwa ni muendelezo wa matukio mengine aliyokutana nayo huko nyuma na ambaya alitamani yawe yamefutika maishani mwake.
Ule mlipuko wa bomu ilikuwa unamuanikia wazi ukweli kuwa hakika lile jinamizi la matukio mabaya aliyokutana nayo akiwa jijini Dar sasa lilikuwa limemfuata rasimi pale Dodoma.
Ni ukweli mchungu sana...na usiokwepeka.
Je niko tayari kuukabili ukweli huu?
Eee Mungu! Hebu nisaidie mja wako...!
Kitabu Cha Pili:
Tuhuma-Mwaka Mmoja Uliopita
Nipashe, Novemba 18
Dar es Salaam
Msichana mmoja,mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam jijini,alifariki dunia hapo jana baada ya kumeza vidonge vingi aina ya Chloroquine.
Msichana huyo aliyejulikana kwa jina la
Mwahija Mlawa (21) alikutwa akiwa amekufa chumbani kwake katika bweni namba saba muda wa saa tano za usiku.
Hata hivyo, mpaka tunapoandika habari hizi ilikuwa bado haijajulikana ni nini hasa ilikuwa sababu ya msichana huyo kuchukua hatua hiyo ya kujiua, jambo linalotokana na kutokuwepo hata na barua iliyoachwana msichana, huyo aliyekuwa akisomea fani ya biashara kuelezea sababu za kujiua kwake.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Dar es Salaam bwana Samson Ramadhani alikaririwa akisema kuwa uchunguzi wa kina utafanyawa ili kugundua sababu za msichana huyo kujiua...
Uhuru. 08 Januari
Dar es Salaam.
Msichana mmoja mwenye umri wa miaka Ishirini na mitatu alifariki dunia huko nyumbani kwao maeneo ya OysterBay,Toure Drive, baada ya kunywa sumu kali aina ya Strichnine.
Kutokana na msemaji wa familia ya binti huyo kutoweza kupatikana mara moja, haikuweza kujulikana iwapo kulikuwa kuna sababu yoyote inayojulikana ya binti huyo kujiua.
Msichana huyo, aliyekuwa akiitwa Margareth Mfinanga, alikuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam akisomea shahada ya kwanza ya Sheria...
Jaka alipiga mwayo mrefu huku akifunua ukurasa mwingine wa gazeti lile. Ingawa na yeye pia alikuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, hakuwa akimjua yule binti aliyeandikwa habari zake kwenye gazeti lile. Hiyo vile vile ilichangiwa na ukweli kwamba wakati yule binti alikuwa akisomea sheria, yeye alikuwa akisomea shahada ya Biashara.
Hakuona habari yoyote ya kuvutia kwenye ule ukurasa mwingine aliofunua na hivyo alipiga mwayo mwingine mrefu na kugeukia kwenye ukurasa wa michezo.
Kwa mbali akilini mwake alikuwa akikumbuka kuwa kuliwahi kutokea tukio jingine la binti mwingine wa pale pale chuoni kujiua kwa kumeza vidonge au sumu, katika siku za nyuma.
Hakulitilia maanani zaidi...
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
9
Ufukwe wa pwani ya OysterBay jijidi Dar ulikuwa umefurika watu wa aina mbalimbali katika siku ile ya Jumamosi. Mawimbi yalijitupa kwa mbwembwe zote katika ufuko ule na watu wengi waliokuja kujiliwaza katika pwani ile, wakubwa kwa watoto, walionekana kufurahia sana hali ile.
Miongoni mwa waliokuwepo pale ufukweni siku ile alikuwa ni binti mmoja mzuri mwenye umri uliopata miaka ishirini na mitatu hivi. Yeye alikuwa amevaa suruali ya Jeans nyeusi iliyomkaa vizuri sana, na juu alikuwa amevaa fulana ndogo nyepesi iliyoishia juu kidogo ya kitovu chake. Alikuwa amejilaza juu ya kanga aliyokuwa ameitandika pale mchangani chini ya kivuli mwanana cha mmoja kati ya miti michache iliyokuwa imetawanyika katika pwani ile ya kupendeza. Macho yake mazuri alikuwa ameyaelekeza baharini akiwaangalia watu waliokuwa wakiogelea huku uso wake ukifanya tabasamu dogo na hatimaye kuangua kicheko pale alipomshuhudia kijana mmoja miongoni mwa wale waliokuwa wakiogelea akigaragarazwa na wimbi kubwa na kutupwa kando ya bahari ile kabla ya kuibuka akiwa ameenea mchanga kichwa chote.
Yule mvulana alijiinua haraka na kujitosa tena baharini, kabla ya kurudi nchi kavu dakika chache baadaye na kuelekea pale alipokuwa yule binti huku akitabasamu. Alikuwa kidari wazi na chini alikuwa amevaa bukta iliyoishia juu kidogo ya magoti yake, iliyomkamata mwilini mithili ya soksi. Miguuni alikuwa amevaa viatu vya chachacha vilivyoilinda miguu yake kutokana na mawe makali yanayopatikana kwenye sakafu ya bahari ile.
Alimfikia yule msichana na kumuinamia na kumbusu kwenye paji la uso huku akitabasamu, kisha akachukua taulo dogo lililokuwa pale pembeni na kuanza kujifuta yale maji ya bahari. Yule binti alimpenda sana yule mvulana na hakuwa na shaka kuwa na yeye pia alikuwa akimpenda.
“Naona ulifurahi sana pale nilipotupwa na mawimbi, eeenh?” Mvulana alimuuliza kwa utani huku akiketi kando ya yule binti, ambaye binti alicheka kwa sauti huku akijiinua na kuegemea kiwiko cha mkono wake mmoja ili apate kumuona vizuri mpenzi wake.
“Hapana...unajua we’ unapenda sana kujitia ubingwa katika kila kitu...sasa leo bahari imekutoa ushamba...” Binti alimjibu kisha akamcheka zaidi, na Jaka akajikuta akiangua kicheko pamoja naye.
Yule msichana alikuwa anaitwa Moze.
Moze Mlekwa alikuwa ni msichana mwenye sura ya kuvutia sana na Jaka alijiona ni mtu mwenye bahati kubwa kabisa kuwa mchumba wa binti yule aliyemendewa sio tu na vijana wengi wa rika lake bali pia na watu wazima. Moze hakuwa “mweupe” au maji ya kunde kama Jaka, bali yeye alikuwa na weusi fulani ambao haikuwa rahisi kuubainisha moja kwa moja kuwa ni weusi. Ulikuwa ni weusi ulioelekea kwenye rangi kama ya kahawia kidogo.
Baada ya kuvaa suruali yake aina ya jeans ya buluu, Jaka alinyoosha miguu yake na kuugemeza mgongo wake kwenye mti. Moze alijiinua na kumuegemea mpenzi wake kwa mgongo wake hali kisogo chake akiwa amekilaza kifuani kwa Jaka. Jaka alipitisha mikono yake na kuilaza tumboni kwa mpenziwe yule. Walikaa vile kwa muda mrefu wote wakiwa kimya, kila mmoja akifurahia ukaribu wa mwenzake. Nyakati kama hizi huwa ni nyakati zenye hadhi ya ndoto kwao na kila mmoja alihisi furaha isiyo kifani moyoni mwake.
Wakiwa ni wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wapenzi hawa walikutana kwa mara ya kwanza miaka miwili iliyopita na kuanza mapenzi yao miezi sita baadaye. Wakati Moze alikuwa anasomea shahada ya sheria, Jaka alikuwa anasomea shahada ya uongozi na biashara.
Mapenzi yao yaliota mizizi haraka sana kiasi cha kuwafikishia hatua ya kufunga uchumba rasmi mwaka mmoja baada ya kuanza kwa mapenzi yao.
Wakiwa wamebakisha miezi sita tu kabla ya kumaliza mwaka wao wa pili pale chuoni na kuingia mwaka wa tatu na wa mwisho kwa shahada yao ya kwanza, walikuwa wamedhamiria kufunga ndoa mara tu baada ya kumaliza masomo yao na kuanza maisha mapya kama mke na mume.
Uhusiano wao ule ulikuwa unajulikana na marafiki zao wengi pale chuoni na hata na baadhi ya wahadhiri, na hivyo waliheshimika sana na asilimia kubwa ya wanafunzi wenzao waliowafahamu pale chuoni.
Ilikuwa wakati wakiwa njiani kurejea chuoni jioni ile wakati Moze alipoamua kumueleza Jaka juu ya vituko alivyokuwa akifanyiwa na Joakim Mwaga. Joakim Mwaga alikuwa ni msomi mwenzao pale Chuoni ambaye aliwahi kumtaka Moze kimapenzi hapo awali. Kutokana na tabia yake chafu ya umalaya na uhuni Moze hakumkubalia ombi lake. Joakim hakuwa na mazoea ya kukataliwa na msichana yeyote, na hivyo alikula kiapo mbele ya Moze kuwa ipo siku tu “atamtia mkononi.” Hata habari za urafiki wa Moze na Jaka zilipodhihiri, Joakim aliendelea tu kumfuatafuata kwa kishawishi hiki na kile ili amwache Jaka na awe mpenzi wake.
Moze hakubadilli msimamo wake.
Kwa upande wake Jaka aliyajua yote hayo lakini hakutaka kuyaingilia kwa msimamo kuwa anamwachia Moze mwenyewe aamue ni yupi mpenzi anayemfaa.
Zilipodhihiri habari za uchumba kati yao, ambapo walifanya sherehe ndogo ya kufunga uchumba pale pale chuoni na kuwaalika baadhi ya marafiki zao, wote wawili walitegemea kuwa sasa Joakim Mwaga angekubali kushindwa na kuwaacha waendelee na mapenzi yao bila mashaka yoyote.
Lakini haikuwa hivyo, kwani ndio kwanza Joakim aliongeza vishawishi kwa Moze, na alipoona vishawishi vyake vinazidi kugonga mwamba alianzisha vitisho.
Vitisho vya Joakim vilitokana hasa na uhusiano wake na kundi dogo lenye fujo sana la watoto wa matajiri walioona nyadhifa na utajiri wa wazazi wao kuwa ni sababu ya wao kufanya lolote walitakalo kwa mtu yeyote.
Ingawa baadhi ya wanafunzi wenzao walikuwa wakiwatukuza na kuwanyeyekea Joakim na kundi lake lililoongozwa na kijana mwingine aliyeitwa Anthony Mpoki, au Tony kama mwenyewe alivyopenda kujiita, Jaka hakuwa miongoni mwa haw wenye kuwatukuza wale jamaa. Yeye aliwaona kuwa ni wahuni na wapumbavu waliokwenda pale chuoni kupoteza muda tu. Mara kadhaa aliwahi kujiuliza ilikuwaje hasa hata watu kama wale wakapata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu kama kile, na mara zote jibu lililomjia kichwani mwake halikuwa la kupendeza hata kidogo.
Kutokana na kundi la Tony kuwa na pesa nyingi za kuchezea tu na kwenda pale chuoni kwa magari ya aina mbalimbali na mapikipiki makubwa, baadhi ya wasichana wasomi wa pale chuoni walionekana kuwapapatikia na kuwanyenyekea sana bila ya kujali tabia zao chafu za kuwadhalilisha na kutowaheshimu wasichana wanaotembea nao.
Jaka alijiuliza ni wapi watakuwa wanapata pesa nyingi namna ile, kwani hata kama wazazi wao walikuwa matajiri kiasi gani, hakuamini kuwa watakuwa wanawapa watoto wao pesa zote hizo ili wachezee tu bila ya sababu maalum.
Hali hiyo ilisababisha Joakim na wenzake wajione kuwa walikuwa wana haki ya kutembea na kuchezea msichana yeyote waliyemtaka pale chuoni bila ya kujali kuwa alikuwa ni mpenzi wa watu au la. Kwa hiyo lilikuwa ni jambo la kushangaza sana kwa Joakim Mwaga kuona kuwa Moze alikuwa anamkataa. Na ilipomdhihirikia kuwa kumbe ni Jaka ndiye alikuwa sababu ya yeye kukataliwa, alijenga chuki kubwa sana kwa Jaka.
Moze alimweleza Jaka jinsi Joakim alivyokwenda kumgongea mlango wa chumba chake pale chuoni usiku wa siku iliyopita na kumlazimisha afungue mlango. Baada ya Moze na rafiki yake wanayeishi naye chumba kimoja katika bweni namba tatu kukataa kufungua mlango, Joakim alitishia kuuvunja mlango ule na hakuondoka nje ya mlango ule mpaka Moze alipotishia kupiga kelele za mwizi.
Jaka alisikiliza habari ile na kubaki kimya kwa muda mrefu bila ya kusema neno.
“Basi mi’ n’taenda kuongea naye ili aache upuuzi wake, sawa?” Hatimaye Jaka alisema, na Moze akajua kuwa Jaka alikuwa amechukizwa na taarifa ile.
“Sawa...lakini msigombane...ongea naye kiungwana tu, sawa...?” Moze alionesha wasiwasi kutokana na jinsi Jaka alivyobadilika kutokana na taarifa ile.
“Usiwe na wasiwasi Moze. Mi’ najua n’taongea naye vipi.”
“Hilo sina shaka nalo kabisa babie…mashaka yangu ni iwapo Joakim anajua jinsi ya kuongeleshwa jambo hilo…unadhani atalipokea vizuri kweli?” Bado Moze alionesha wasiwasi.
“Aaam…yeah…ataelewa tu…” Jaka alimjibu, kisha haraka akamua kubadili maongezi.
“Hey...umesoma Uhuru la jana...? Limeandika habari za binti mmoja aliyejiua pale chuoni...eti anasoma huko huko Laws. ”
“Ah...nimesoma bwana...yule msichana namfahamu sana, alikuwa anaitwa Mage. Masikini Mage, sijui ni kwa nini tu aliamua kujiua...” Moze alijibu kwa masikitiko.
Wakaendelea kimya na safari yao. Walipofika barabara ya Haile Selasie Jaka alisimamisha teksi ya kuwarudisha hadi chuoni. Wakiwa ndani ya teksi ile bado Jaka alionekana kuwa na mawazo mengi. Moze alimuuliza kulikoni.
“Ah, unajua nilikuwa najaribu kutafakari...hivi tukio kama hili si liliwahi kutokea pale chuoni hapo nyuma...?”
“Tukio kama lipi?”
“La msichana wa Chuo Kikuu kujiua. Nakumbuka kuna binti mwingine alijiua pale Chuoni...kama kwenye Oktoba au Novemba hivi ya mwaka jana, sikumbuki sawasawa...”
“Kwa hiyo...?”
“Ah, mi’ sitaki kuamini kuwa vifo hivi vinatokea kwa bahati mbaya tu. Lazima kuna kitu fulani kinaendelea pale Chuoni aisee… na bila shaka kuna uhusiano mkubwa baina kifo cha kwanza na hiki cha sasa hivi. We’ unaonaje?”
“Mi’ sioni chochote zaidi ya kwamba mambo hayo wenyewe ni polisi...na kama umesoma vizuri lile gazeti, utagundua kuwa Kamanda wa Polisi mwenyewe amesema kuwa watafanya uchunguzi wa kina kuhusiana na swala hilo.” Moze alimshushua.
“Labda hujanielewa, ninachomaanisha ni kwamba...”
“Wewe ndiye hujanielewa Jaka. Ninachomaanisha ni kwamba usitake kuingilia kabisa mambo kama hayo mpenzi. Utakuja kujitia kwenye matatizo makubwa bure...halafu ikawa balaa kwetu sote. Naomba usirudie tena kusema jambo hilo mbele ya mtu mwingine yeyote pale chuoni aisee! Tafadhali sana, Okay?”
Jaka alitaka kubisha, lakini akaghairi.
“Ahh...Okay...”
Waliendelea na safari yao wakiwa kimya.
________________
Siku iliyofuata, Jaka alimkuta Joakim katika uwanja wa kuchezea Tennis ndani ya eneo la michezo pale chuoni. Muda ulikuwa ni kiasi cha saa kumi na moja za jioni hivi.
Alijipenyeza miongon mwa wanafunzi wachace waliokuwa wakifuatilia mchezo ule kutokea nje ya uzio ule wa senyenge, na kubaki akimtazama kwa muda wakati yule jamaa wakati akicheza mchezo ule uliopendwa sana na baadhi ya wanafunzi wenzao pale chuoni. Joakim alikuwa mwembamba na mrefu kuliko yeye. Jioni ile alikuwa amevaa bukta ya michezo ya rangi nyeupe na fulana kubwa ya rangi hiyohiyo, huku miguuni akiwa amevaa viatu vyeusi aina ya Reebok bila ya soksi, vyote vikiwa ni vivazi ghali.
Aliendelea kufuatilia mchezo ule mpaka ulipoisha. Joakim alichukua mkoba wake mdogo uliokuwa kando ya ule uwanja waliokuwa wakichezea na kutoa kijitaulo kidogo na kuanza kujifuta jasho huku akiondoka eneo lile. Jaka alisogea hadi kwenye ile senyenge ule upande ambao Joakim alikuwapo, na kumwita kwa sauti. Joakim Mwaga aligeuka, na alipoona kuwa ni Jaka ndiye aliyemwita, aliachia tabasamu la upande mmoja na kumfuata pale alipokuwa kutokea upande wa pili wa senyenge ile.
Walitazamana kwa muda bila ya yeyote kumsemesha mwenzake hali Joakim akiwa ndani na Jaka akiwa nje ya seng’enge ile. Aligundua kuwa umbali baina ya jicho moja la Joakim na jingine ulizidi kidogo ule umbali wa kawaida kama unavyokuwa kwa watu wengine.
“Unasemaje?” Hatimaye Joakim aliuliza kwa jeuri, akivunja ukimya baina yao.
Jaka hakutaka kupoteza muda zaidi.
“Joakim, kwa muda mrefu sasa umekuwa ukimfuatafuata Moze kwa vishawishi kadhaa wa kadhaa kwa nia ya kuvunja uhusiano uliopo baina yangu na yule binti, uhusiano ambao wewe unaufahamu fika...”Alianza kumwambia lakini alimuona Joakim akikenua meno kwa tabasamu la kejeli, ingawa hakusema kitu. Sura yake ilimkumbusha Jaka dume la nyani alilopata kuliona zamani katika mbuga fulani za wanyama hapa nchini.
“...lakini sasa naona unaanza kutupa mipaka na kufikia hatua ya kutoa vitisho na kumfanyia fujo yule binti, jambo ambalo mimi nikiwa kama mchumba wake siwezi kukaa kimya tu na kulifumbia macho...”
“Kwa hiyo...utafanyaje sasa, mchumba?” Joakim alimkatisha kwa jeuri kubwa huku akimkebehi kwa kumwita “mchumba”.
Ingawa hakupendezwa na kauli ile, Jaka alijitahidi kuipuuza. Akaendelea, “…kwa hiyo bwana Joakim mimi ninataka tabia hiyo uiache mara moja. Kwa sababu itakuletea aibu na kukuvunjia heshima yako bure tu. After all, sisi hapa ni watu wazima, na litakuwa ni jambo la aibu sana kwa wasomi wazima kufanya vituko vya watoto wa kidato cha pili, au we’ unaonaje?”
“Aah! Ina maana we’ unataka kunipangia maisha mimi?” Joakim alimjia juu huku akionesha wazi kuwa hakutaka tu kuelewa kile ambacho Jaka alikuwa akimwambia.
“Sikiliza bwana…mi’ najua we’ umezoea tabia ya kuchezea-chezea watoto wa watu. Sasa kuna baadhi wanaopenda kuchezewa kama jinsi unavyopenda kuwachezea...lakini pia kuna wengine ambao hawapendi. Kwa hiyo jambo ninalojaribu kukueleza ni kwamba ingekuwa bora kama ungewaacha kama walivyo wale wachache ambao hawapendi hiyo michezo yako na ukaendelea kuchezea wale wanaopenda, ambao ni wengi sana. Sasa katika hao wachache wasiopenda kuchezewa-chezewa, Moze ni mmoja wapo...na hataki umfuate fuate...”
Yale maneno yalionekana kumuudhi sana Joakim.
“Sasa mi’ nakwambiaje (akamtukania mama yake)…mi’ Moze n’taendelea kumtongoza na n’tamchukua! Mchumba, mchumba…mchumba Mlimani? Chukua taimu kule, fala nini?” Alimkoromea kwa ghadhabu.
Jaka akajua kuwa Joakim alikuwa anaupeleka kusudi ule mjadala kwenye mtafaruku. Kwa vile alikuwa ameshafikisha ujumbe wake, aliamua kuondoka.
“Naamini ujumbe umekufika Joakim…kaa mbali na Moze!” Alimwambia na kugeuka, akaanza kuondoka akimuacha Joakim na ghadhabu zake.
Jokaim aliruka mbele kwa hatua mbili kubwa na Jaka akajikuta uso kwa uso na hasimu wake.
“Hivi wewe unajiona kama nani hata unipangie ni mwanamke gani nitembee naye na yupi nisitembee naye, eennh?” Joakim alimkoromea huku akimtomasa-tomasa kifuani kwa kidole chake na uso wake ukionesha hasira nyingi.
“Kama utatumia akili kidogo tu Joakim, utagundua kuwa nilichofanya ni kukupa ushauri wa busara sana...kuwa tembea na kila mwanamke umtakaye iwapo naye anakutaka, na yule ambaye hakutaki, basi achana naye...ni hivyo tu. Sasa sijui ni kitu gani kinachokufanya wewe uje mbogo kiasi hicho!” Jaka alimjibu kwa utulivu huku akiwa ameingiza viganja vya mikono yake miwili ndani ya mifuko ya jaketi lake la michezo alilokuwa amevaa. Kwa jibu lile wasomi wachache waliokuwa pale karibu waliangua kicheko na kumfanya Joakim ajione mjinga.
“Kkha! Yaani unamaanisha mimi situmii...yaani sina...akili?” Joakim alibwata huku macho yakimtembea. Jaka alijua kuwa pale Joakim alikuwa hatumii akili bali alikuwa akiendeshwa na jazba na pupa.
“Mi’ naona huu mjadala tuuahirishe kwa sasa na tutafute wakati mwingine iwapo utaona kuna haja ya kufanya hivyo Joakim…Lakini kwa upande wangu nadhani ujumbe niliokuletea ni mdogo tu na uko wazi sana.” Jaka alimwambia huku akimpita pembeni na kuendelea kuondoka katika eneo lile. Mashuhuda wakazidi kucheka. Joakim akazidi kujazibika.
“Hey! Bado hatujamaliza! Unaniletea kiburi mimi wewe...?” Joakim aliendelea kubwata wakati Jaka akiendelea na safari yake bila kumjali.
Joakim alimrukia na kumsukuma kwa nguvu. Jaka alianguka huku akilaani kwa sauti. Alijiinua kutoka pale chini akiwa amehamanika, na alikuwa akimgeukia Joakim kwa hasira wakati Joakim alipomuwahi na kumkwida kwa kola ya jaketi lake.
“Hata siku moja usijaribu kunitolea jeuri mie...umesikia wewe?” Joakim alimwambia kwa hasira na kumsukuma tena chini kwa nguvu. Lakini safari hii Jaka naye alikuwa tayari. Kama umeme alimdaka mikono yake na kumvuta nyuma pamoja naye, na hapo hapo akamrusha hewani kwa judo kali. Joakim aliachia ukelele wa taharuki kabla ya kuangukia mgongo kwa kishindo. Haraka sana Jaka alijirusha na kusimama wima na kumgeukia pale alipokuwa akigaagaa.
Joakim alijikurupusha kutoka pale chini na kumkimbilia Jaka kwa ghadhabu huku akiwa ametanguliza mikono yake kwa nia ya kumdaka koo, lakini Jaka alipiga hatua kubwa kumuwahi, kisha akajigeuza huku akimzungushia teke kali sana la nyuma-nyuma na kumshindilia kisigino cha chembe yule hasimu wake. Joakim alijipinda huku yowe la uchungu likimtoka. Alienda chini bila kupenda na kubaki akiwa amepiga magoti pale chini huku akiwa amejishika ile sehemu iliyopata dhoruba, miguno ya maumivu ikimtoka na akiwa anamtumbulia Jaka macho ya kutoamini.
Jaka alibaki akimtazama kwa dharau jinsi alivyokua akiugulia bila namna pale chini, kisha bila ya kusema neno aligeuka kuondoka, akimwacha Joakim akitweta hovyo. Kabla hajafika mbali mmoja kati ya wasomi wenzao wachache walishuhudia tukio lile kwa butwaa alimkimbilia.
“Aisee...! Hivi unajua kuwa umechokoza vita kubwa sana wewe? Unajua wash’kaji zake wakiipata habari hii utakuwa katika “trabo” kubwa sana mshikaji wangu!” Jamaa alimwambia, akimaanisha kuwa Jaka atakuwa kwenye matatizo makubwa pindi kundi la marafiki wakorofi wa Joakim likipata habari za tukio lile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nionavyo mimi ni kwamba yeye ndiye ambaye yuko kwenye “trabo” hivi sasa.” Jaka alijibu kwa kutojali huu akiendelea na safari yake.
Ambalo hakukijua kwa wakati ule ni kwamba kulikuwa kuna “trabo”, yaani matatizo, makubwa zaidi yaliyokuwa yakimsubiri yeye huko mbele kutokana na tukio lile.
Ukweli ni kwamba kuzagaa kwa habari za kipigo alimdondoshea mtukutu Joakim kulimpa umaarufu mkubwa sana Jaka pale chuoni. Umaarufu hu ulikuja kwa namna mbili, ya kwanza ikiwa ni ya kuonekana shujaa na mdiriki aliyeweza kusimama imara dhidi ya mtukutu anayehofiwa na wengi, kiasi kwamba baadhi wa wanafunzi walifikia hatua kwenda kumpongeza kwa tendo lile. Lakini namna ya pili ni kwamba aliondokea kupata umaarufu mkubwa sana miongoni mwa washirika wa mtukutu Joakim Mwaga, hususan kwa kijana aliyeitwa Anthony Wanzaggi, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika fani ya elimu ya Kompyuta pale chuoni, ambaye ndiye hasa aliyekuwa kiongozi wa kundi lile ambalo Joakim alikuwa akijihusisha nalo.
Anthony Wanzaggi, au Tony, kama jinsi alivyopenda aitwe, alijulikana sana kutokana na umaarufu na utajiri wa baba yake. Mzee Athanas Wanzaggi alikuwa akimiliki makampuni kadhaa makubwa hapa nchini na ilikuwa inasemekana kuwa Tony alikuwa amewekewa ukurugenzi katika moja ya makampuni hayo.
Kwa upande mwingine, hali ile ilizidisha wasiwasi na mashaka makubwa kwa Moze, ambaye alikuwa anahofia kisasi kutoka kwa Joakim na wenzake dhidi ya Jaka na hata dhidi yake pia.
Jaka alijitahidi kumtoa mashaka kwa kumwambia kuwa Joakim hatarudia tena upuuzi wake kwa kuhofia aibu ya kipigo kingine, na kwamba hakukuwa na sababu ya hao marafiki zake kuingilia katika jambo ambalo wao halikuwa likiwahusu hata kidogo.
“Ah, we Jaka huwajui wale jamaa nakwambia…sijui ni kwa nini, ila jamaa wanapenda sana sifa na kuogopwa. Yaani ningejua hata nisingekwambia kuhusu haya mambo dear…watatusumbua tu hawa. Mi najua!” Moze alilalama.
Jaka alifinya uso kwa tafakuri.
“Ah, okay…basi na tuwe makini tu kuanzia sasa. Hili jambo ilibidi lifikishwe mwisho Moze, na nilitaraji litaisha kwa mazungumzo tu…lakini ndio haikuwa.” Alimwambia.
________________
Anthony Athanas Wanzaggi, au Tony, alifikicha pua yake pana kwa nguvu huku akitikisa kichwa chake kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Alifumbua macho yake mekundu na kuinua uso wake kuwatazama wale jamaa waliokuwa chumbani kwake muda ule. Aliwaona kwa mbali huku akihisi kama kwamba macho yake yalikuwa yameingiwa na ukungu fulani.
Alitikisa tena kichwa chake na kukiinamisha huku akiinua mkono wake wa kushoto na kunusa unga mweupe na laini sana uliobakia kwenye mgongo wa kiganja cha mkono ule kwa mkupuo mmoja na ule unga ukatowekea puani mwake na kusambaa kwenye mishipa yake ya fahamu zake. Kwa kutumia kilekile kiganja aliifikicha tena pua yake pana kwa nguvu zaidi huku akiendelea kutikisa kichwa chake, miguno ya kuridhika ikimtoka huku akivuta pumzi nyingi ndani ya mapafu yake. Safari hii alipofumbua tena macho yake kuwatazama wale jamaa, aliwaona vizuri sana. Wale jamaa wawili waliokuwa pamoja naye mle chumbani walikuwa wakimtazama huku wakitabasamu, naye alitabasamu.
“Ee bwana ee...yaani najisikia poa kishenzi mshikaji wangu, you know what I’m sayin’?” Tony aliwataarifu wale wenzake kisha akacheka sana. Wale jamaa nao wakacheka pamoja naye kisha wakagonganisha viganja vya mikono yao kama kihitimisho cha furaha yao.
Walikuwa chumbani kwa Tony pale chuoni katika bweni namba moja ghorofa ya tatu. Wale jamaa wawili walikuwa ni wanafunzi wa mwaka wa pili pale chuoni na ndio waliounda kundi lile lililoogopwa sana pale chuoni wakiongozwa na Tony.
Joakim alikuwa bado mgeni katika kundi lile potofu.
Kuvuta na kusambaza madawa ya kulevya kwa “wateja” mbalimbali ndani na nje ya chuo kile ilikuwa ndio kazi yao yakua nfasi ya pili tu kwao. Baadhi ya wasomi wachache pale chuoni walikuwa wameingizwa kwenye mkumbo ule wa kutumia madawa ya kulevya, wengi wao ikiwa ni kinyume na matakwa yao. Baada ya kuingia katika mkumbo ule walikuwa ni kama tongwa walionaswa kwenye ulimbo, na mara kwa mara walipohitaji unga ule haramu waliupata kwa bei ghali sana kutoka kwa wale jamaa wawili waliokuwa na Tony mle ndani usiku ule.
Pamoja na kuwa “wateja” walikuwa wakiupata unga ule wa haramu kila walipouhitaji, hakukuwa na hata mmoja kati yao aliyekuwa akijua ni wapi hasa wale wasambazaji wao walikuwa wakiupata unga ule haramu. Ni wale jamaa wawili tu ndio waliojua kuwa Tony ndiye aliyekuwa akiongoza biashara ile pale chuoni na kuwatuma wao kuisambaza kwa “wateja” wachache walioingia katika ulevi ule kwa kulazimishwa na kwa vitisho hata wakajikuta kuwa hawawezi tena kukaa bila kutumia unga ule.
Wengi wa wateja wa Tony walikuwa ni wasichana.
“Sasa Tony unasemaje kuhusu huyu Jaka...unajua katutia aibu sana?” Mohamed “Muddy” Shomari, mmoja kati ya wale jamaa wawili ambaye naye pia alikuwa ni mtumiaji mzuri wa madawa ya kulevya au “bwimbwi” kama watoto wa mjini walivyozoea kuuita unga ule haramu, alisema.
“Yaa...katutoa nishai kichizi mshikaji!” Jamaa wa pili alithibitisha hoja ya mwenzake, huyu aliitwa Alphonce Ng’ase, na alikuwa mfupi na mkomavu. Mwenyewe alipenda sana kujiita “Al Pacino”, labda kutokana na upenzi wake kwenye ile biashara haramu ya madawa ya kulevya aliyokuwa akiifanya pale chuoni.
“Katutoa nishai sisi au kamtoa nishai Joakim bhana?” Tony aliuliza huku akijishughulisha kuchagua CD ya muziki miongoni mwa nyingi zilizozagaa hovyo mezani kwake pale chumbani.
“Aaah...sasa Joakim si mshiriki wetu bwana? Sasa hivi kila upitapo hapa Chuo stori ni hiyo tu! Lazima na sisi tujibu mapigo kwa niaba ya mshiriki wetu bwana, au unasemaje Ng’ase?” Muddy alimjibu huku akitaka kuungwa mkono na yule mwenzake.
“Yaani hilo ndio mpango mzima mwanakwetu...lazima na siye tufanyie ya kwetu fala yule, hawezi kutuaibisha namna ile halafu aachiwe tu hivi hivi, nkhaa!” Ng’ase aliunga mkono hoja ile.
“Ah…Joakim nae laini mno yule...tabu yake ni kuwa hatumii “madope” yule mtoto...kama angekuwa anapata “dope” yule angechangamka kidogo.” Tony alilalamika kwa hasira akimaanisha kuwa Joakim alikuwa laini kwa sababu alikuwa havuti unga na ndio maana akapigwa na Jaka. Sio wote katika marafiki wa lile kundi lao waliokuwa wakitumia madawa ya kulevya, na ukitoa Ng’ase na Muddy, wengine wote walikuwa hawajui kuhusu utumiaji na uuzaji wao wa unga ule haramu. Ilikuwa ni siri kali sana ambayo kujulikana na mtu yeyote asiyetakiwa kulimaanisha kifo kwa mtu yule, na kutokana na ugeni wake kundini, Joakim hakushirikishwa kabisa kwenye siri ile.
“Unajua tatizo ni kwamba inatufanya hata sisi tuonekane mabwege mbele ya “wateja”, na hii inatishia usalama wa biashara yetu Tony.” Muddy alichangia. Kauli ile ilikamata umakini wa Tony. Alinyamaza kimya na kubaki akimtazama Muddy kwa muda, kisha akatikisa kichwa kuafikiana naye huku uso wake ukionesha mawazo mazito.
“Good point, man! Basi jamaa itabidi apewe onyo kali sana, you know what am sayin’?.” Alisema kwa sauti ya chini na kunusa tena ule unga wa haramu.
Muddy na “Al Pacino” wakagongesha ngumi zao kufurahia kupita kwa hoja ile.
_________________
Siku mbili baadaye Moze alikuwa akimweleza Jaka, “Wale ni watu wabaya sana Brown...haikuwa busara kabisa kufanya jinsi ulivyofanya kwa Joakim.” Moze hupendelea kumwita Jaka kwa ubini wake, yaani Brown.Walikuwa chumbani kwa Moze, ambapo Rose, mwanafunzi mwenzao aliyekuwa akiishi pamoja na Moze mle chumbani pia alikuwapo. Ilikuwa ni saa tatu za usiku.
“Kwani wewe wasiwasi wako ni nini Moze?” Jaka alimuuliza huku akiielekeza kinywani bilauri ya juisi kabla ya kupiga funda kubwa na kuirudisha mezani bilauri ile ikiwa tupu.
“Mi’ n’na wasiwasi Brown...kila ninapokutana na wale marafiki wa Joakim huwa wananitazama kwa namna ambayo inaashiria kuwa wana lao jambo...” Moze alijibu kwa mashaka.
“Lakini Moze, mi’ naona Jaka hakuwa na budi kufanya jambo alilolifanya, kwa sababu Joakim asingeacha kukufanyia vituko.” Rose alidakia huku akimtazama Moze kwa makini.
“Ah…najua, lakini...naona kama bado mambo hayajaisha haya...”
“Sasa unaonaje kwa muda huu tukiishi kwa furaha mpaka hapo hayo mambo yatakapoamka tena? Muda huo ukifika tutajua tuchukue hatua gani, unaonaje mpenzi?” Jaka alimwambia Moze kwa utaratibu akijaribu kumtoa wasiwasi. Moze alimtazama kwa sekunde kadhaa, kisha akatabasamu.
“Brown kwa kujifanya Van Damme!” Hatimaye alisema na wote watatu wakacheka kwa sauti.
Jaka aliinua Trampeti yake ndogo iliyokuwa pale juu ya meza na kuanza kupuliza taratibu wimbo ambao alijua kuwa Moze alikuwa akiupenda sana. Trampeti ile ilikuwa ni zawadi aliyopewa na Moze katika kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa miezi sita iliyopita. Jaka alikuwa ni hodari sana wa kupuliza ala ile na ilikuwa ni kiburudisho chake kikubwa.
Taratibu nota za wimbo ule zilianza kusikika na Moze na Rose walibaki wakimtazama huku wakiwa kimya. Alikuwa akiigiza kupuliza wimbo wa zamani lakini walioupenda sana ulioimbwa na Roxette, ulioitwa It must have been Love.
Kadiri wimbo ule ulivyokuwa ukiendelea ndivyo Jaka alivyozidi kupata mori na kujisahau kabisa kuwa alikuwa na watu wengine mle ndani hali akiendelea kupuliza Trampeti yake huku macho yake akiwa ameyafumba kwa mdadi. Moze alimwangalia mpenzi wake huku ule wimbo ukimwingia na alihisi raha sana.
Taratibu Jaka aliumalizia wimbo ule huku akifumbua macho yake taratibu kumtazama mpenzi wake. Macho yao yalikutana na waliangaliana kwa mapenzi huku mlio wa Trampeti ile ukimalizikia kwa sauti ya chini. Moze alionekana kulengwa na machozi kwani siku zote wimbo ule alioupenda sana ulimtia msisimko fulani ausikiapo, na huwa anashindwa kuyazuia machozi kutokana na maana ya maneno ya wimbo ule uliokuwa akielezea hadithi ya simanzi ya penzi lililopotea.
Taratibu Rose aliinuka na kutoka nje ya chumba kile bila ya kusema neno na kuwaachia faragha wapenzi wale wawili. Moze aliinuka na kwenda kumkumbatia Jaka kwa mapenzi huku machozi yakizidi kumchoma machoni. Jaka alimpakata mpenziwe mapajani na kumbusu kwenye paji la uso huku kwa mkono wake mwingine akiining’iniza pembeni ile ala yake ya muziki. Aliyaona machozi yaliyokuwa yakipigania kutoka kwenye macho ya mpenzi wake.
“Unalia.”
“Ndio.”
“Sitaki mtu yeyote atupotezee penzi letu, Moze...si Tony wala si Joakim…yeyote yule.”
Moze alitikisa kichwa kukubaliana naye lakini hakusema kitu.
“Kwa hiyo usiwe na wasiwasi, penzi letu halitapotea…halitaisha.”
Moze alimtazama mpenzi wake kwa huba na kumkumbatia kwa nguvu. Jaka alimkumbatia yule binti kwa mkono mmoja huku akiwa bado ameshikilia Trampeti yake kwa mkono mwingine. Nyuso zao zilikutana na kugusana kwa upendo. Walikutanisha midomo yao katika mvuto wa mapenzi na ndimi zao zilipokutana kila kitu kilionekana kusimama, trampeti ikaanguka juu ya zulia lililotandikwa pale sakafuni...
It must have been love, but it’s over now…
It must’ve been good...but I lost it somehow...
Maana ya baadhi ya maneno ya wimbo ule wa Roxette ilikuwa bado vichwani mwao hali wakiwa wakielea katika ulimwengu wa kipekee katika mvuto ule wa kimapenzi.
Bila shaka lilikuwa ni penzi, lakini sasa limekwisha...
(Ni wazi kuwa) ilikuwa vizuri (kuwa na penzi), lakini kwa namna fulani nimelipoteza...
Ni maneno hayo katika wimbo ule ambayo mara nyingi yaliwakumbusha majuto watakayokuwa nayo pindi wakiliachia penzi lao lipotee.
“Penzi letu halitapotea...” Moze aliyarudia maneno ya Jaka kwa sauti ya kunong’ona sana.
“Mmnnhh!” Ndilo jibu pekee lililomjia Jaka kichwani mwake kwa wakati ule huku akizikutanisha tena ndimi zao...
____________________
Kwa kawaida siku za mwisho wa wiki huwa ni siku za burudani mbalimbali kwa wanachuo. Siku hizo wanachuo hupata nafasi ya kwenda kubadili mawazo kwa kujiburudisha katika kumbi mbalimbali za starehe ndani ya jiji la Dar es Salaam. Wanachuo huwa wanajiandalia utaratibu maalum wa kwenda katika moja ya kumbi hizo za starehe kwa gharama nafuu. Wikiendi hii wanachuo walikuwa wameandaliwa kwenda kwenye ukumbi wa disko wa Club Billicanas, ambapo mmoja wa wanamuziki wa kizazi kipya alikuwa anafanya onesho maalumu la kuzindua albamu yake mpya pamoja na video ya moja kati ya nyimbo zake kutoka kwenye albamu yake hiyo mpya.
Wanachuo wengi waliamua kujimwaga kwenye ukumbi ule ili kwenda kujisahaulisha machovu ya wiki nzima ya kusumbua ubongo pale chuoni au “The Hill” kama wenyewe walivyopenda kupaita, wakimaanisha “Mlimani”. Miongoni mwao usiku ule pale Billicanas walikuwapo Jaka na mpenziwe Moze, pamoja na rafiki yao Rose ambaye alikuwa amesindikizwa na Raymond Mloo, rafiki mkubwa wa Jaka ambaye walikuwa wakiishi chumba kimoja katika bweni namba tano pale chuoni.
Raymond alikuwa ni kijana mkimya na mtaratibu kama Rose, na kinyume cha matarajio ya Moze, hakuonesha dalili yoyote ya kutaka uhusiano wa kimapenzi na Rose ingawa Rose mwenyewe alishaonesha kila dalili za kumridhia katika hilo. Raymond hakuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana yeyote pale chuoni na hakuwa na mpango wa kufanya hivyo ingawa aliuheshimu sana uhusiano uliokuwapo baina ya Jaka na Moze.
Jaka alielewa ni kwa nini Raymond hakupenda kujihusisha na maswala ya mapenzi, kwani mara nyingi alipojaribu kumchokoza kuhusu swala hilo jibu lake lilikuwa ni lile lile siku zote.
“Mi’ nawaogopa sana wasichana...kwa sababu msichana anaweza kukupenda sana halafu akaja kukuchukia ghafla kwa jambo dogo tu...na usiombe msichana unayempenda atokee kukuchukia ghafla rafiki yangu, kwani hapo ndipo utakapojuta kuzaliwa. Sasa mimi sitaki ije itokee siku nije kujuta kwa nini nilizaliwa...ndio maana sitaki kabisa michezo na hawa watoto wa kike...”
Lakini pamoja na msimamo wake huo juu ya mapenzi, Raymond hakuonesha dharau hata kidogo kwa akina dada. Na ni tabia yake hiyo iliyojengwa na msimamo wake huo ndio iliyowafanya akina dada kama Rose wazidi kupata hamu ya kuhusiana naye kimapenzi. Jaka aliwahi kumweleza hilo mara kadhaa lakini jibu lake halikubadilika.
“Wanawake ni viumbe hatari sana rafiki yangu, ukijaaliwa kupata mwanamke mwenye tabia tofauti lazima ushukuru sana. Acha kabisa kunishawishi-shawishi kuhusu mambo ya wanawake bwana, kwa sababu wanawake hawatabiriki...sasa ukinishawishi nami nikakubaliana nawe, siku atakaponibadilikia wewe hutaweza kunisaidia hata kidogo rafiki yangu. We’ niache tu!”
Jaka alicheka sana siku alipojibiwa hivyo. Wakati ule hakuwa na namna ya kujua kuwa kuna siku angekuja kuyakumbuka kwa uchungu sana yale maneno.
Yote kwa yote, ulikuwa ni usiku ya furaha sana pale Billicanas. Jaka na Moze walicheza muziki,waliongea na marafiki zao ambao wengine walikuwa hawajaonana nao kwa wiki nzima ingawa walikuwa wakisoma pale pale chuoni. Nje ya ukumbi ule kulikuwa kuna sehemu ya maakuli, zaidi ikiwa ni chipsi, ndizi choma na nyama choma. Basi ndizi na nyama choma vilitafunwa kwa vinywaji baridi, muziki ulichezwa, nyama na ndizi zikatafunwa tena, muziki ukachezwa tena, maongezi yakapamba moto, vicheko vikatawala. Ilikuwa ni burudani iliyotimia. Moze alicheza muziki na Raymond pamoja na baadhi ya marafiki mbalimbali wa Jaka kwa nyakati tofauti huku Jaka akiongea na marafiki zao kadhaa.
Hatimaye wakawa wamebaki peke yao kwenye meza moja ya pembeni mle ukumbini. Rose alikuwa amejichanganya kwenye ukumbi ule na Raymond halikadhalika. Moze alionekana ni mwenye furaha sana na Jaka alifurahishwa na hali ile kwani alijua kuwa wasiwasi wake juu ya kundi la akina Joakim bado ulikuwa haujaondoka.
Bila ya wao kujua, pamoja na jitihada za Jaka kuangaza kwa chati kila kona ya ukumbi ule bila ya mafanikio, furaha na nyenendo zao zote zilikuwa zikishuhudiwa kwa utulivu mkubwa na Alphonce “Al Pacino” Ng’ase na Muddy waliokuwa wamekaa kwenye meza moja iliyojificha kwenye kona nyingine yenye kiza kidogo pale ukumbini.
Baada ya Raymond kuzunguka sehemu mbalimbali za ukumbi ule akiongea na jamaa kadhaa aliojuana nao huku akiendelea kula maraha, aliangalia saa yake na kugundua kuwa muda wao wa kuondoka ulikuwa umekaribia kwani walikubaliana waondoke pale ukumbini ifikapo saa nane na nusu za usiku. Saa yake ilimwambia kuwa muda ulikuwa ni saa nane na dakika kumi...
Huku nyuma, Jaka aliinuka na kumbusu mpenzi wake shavuni, akamuaga kuwa alikuwa anaelekea chooni kujisaidia haja ndogo. Moze aliafiki na kubaki peke yake pale mezani akimsubiri.
Walipoona kuwa Jaka amechukua uelekeo wa maeneo ya msalani, Ng’ase na Mudy walitazamana, na bila kuongea waliinuka kwa pamoja na kumfuata...
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Raymond alimkuta Moze akiwa peke yake pale mezani, na alipomuulizia Jaka Moze akamfahamisha kuwa ameenda kujisaidia.
“Rose…?”
“Naye pia alitowekea huko huko kwenye muziki na mpaka sasa hajarudi.” Moze alijibu.
Raymond aliokota kipande cha nyama kutoka kwenye sahani iliyokuwa pale mezani na kukitupia kinywani. Alitafuna taratibu huku akiangaza huku na kule akijaribu kumtafuta Rose bila ya mafanikio.
“Mi’ naona nikamtafute Rose ili tukija hapa Jaka atakuwa amesharudi tunatimua, au vipi ?”
“Sawa Ray...wazo zuri.”
Raymond akapotelea ukumbini kumtafuta Rose.
________________________
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment