Search This Blog

Monday 24 October 2022

FEDHEHA - 2

 http://pseudepigraphas.blogspot.com/2019/12/fedheha.html

    Simulizi : Fedheha

    Sehemu Ya Pili (2)







    Akaituliza akili yake na kuiweka kikazi zaidi ili aweze kupokea majukumu kwa ukamilifu. Wakati akiwa anasubiri alichoitiwa akapata nafasi ya kuisanifu ofisi ile. Chini ilikuwa imetandikwa zulia zito jekundu, pembeni upande wa kulia kulikuwa na kabati kubwa la chuma. Meza ya kubwa ya duara ilikuwa katikati ya ofisi huku ikiwa imezungukwa na viti vipatavyo sita. Ni ofisi ambayo haikuwa na vitu vingi zaidi ya hivyo alivyoviona kwani ilikuwa kama ukumbi wa mikutano tu. Ukutani kulikuwa na picha za maraisi wastaafu na waliowahi kuwa wakuu wa jeshi. Picha ya Raisi wa Kwanza ndiyo iliyokuwa kubwa zaidi huku ikita imezungushiwa taji la maua.

    “Karibu sana Luteni.” Alianza kuongea Jenerali. Macho maangavu ya Luteni Taisamo yaliweza kumwona Jenerali Nalinga akifunua jalada pekee ambalo lilikuwa pale mezani. Taisamo akalitazama lile jalada kwa shauku kubwa.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa ni muda muafaka wa kuanza kikao chetu.” Alisikika Jenerali huku macho yote akiwa ameyaelekeza kwenye jalada lililoko pale mezani.

    “Kwa kuwa hiki si kikao cha wanasiasa naona niende moja kwa moja kwenye mada husika, Hali ya nchi kwa sasa si nzuri inaonesha kuna kitu kinafukuta chini kwa chini, hivyo tumeamua kutumia kitengo chetu kutafuta ukweli, kutokana na unyeti wa suala lenyewe na wasiwasi wa kuonekana kuwa huenda kuna maafisa waandamizi wanahusika ndio maana tumekuteua wewe kufanya kazi hiyo. Sababu iliyotufanya tukuteue ni uwezo mkubwa wa mitihani ya kiakili ambao uliuonesha ulipokuwa chuoni Monduli na hata ulipokuwa ukichukua mafunzo maalum hapa Dar.” Akatulia na kumeza mate.

    “Kifo cha makamu wa Rais pekee kisingetosha kutushawishi kufanya kazi hiyo moja kwa moja, tungewaachia wenzetu wa CID au Usalama wa Taifa. Ni kweli kifo cha makamu wa Rais kimetokana na ajali ya gari, lakini pale polisi walipojaribu kufuatilia wameishia kushuhudia Afisa mwandamizi akinusurika kifo. Kinachotia mashaka zaidi ni jinsi zoezi hili lisivyotiliwa mkazo na wenzetu wa polisi na usalama wa Taifa, tunataka tufahamu nini kimejificha nyuma ya pazia, kwa kuanzia utaanza na hili jalada la maelezo kutoka polisi ingawa nafahamu fika halina kitu cha maana sana lakini siku zote safari ya ghorofani huanzia nyuma ya ngazi na si kwenye ngazi.” Aliongea Jenerali kwa sauti iliyojaa utulivu huku akilisogeza lile faili.

    “Pia utatakiwa kuripoti matukio yote kwangu au kwa Luteni Jenerali Nalinga pale ambapo nitakuwa sipo. Zingatia utatumia namba yangu ya kiganjani ambayo nitakupatia pale utakaponihitaji, usithubutu kuja ofisini kwangu sitaki afahamu yeyote zaidi yetu kuwa kuna kazi inaendelea. Kuhusu matumizi umeingiziwa kiasi cha fedha kwenye akaunti yako kama utahitaji msaada zaidi tafadhali wasiliana nami au Luteni Jenerali Nalinga.”

    Kama si ukubwa wa jukumu alilopewa basi hiyo ilikuwa ni siku ya furaha mno kwake, alielewa wazi ugumu wa jukumu alilokabidhiwa hivyo asingeweza kufurahia zile fedha alizoingiziwa.

    “Jambo la kwanza unatakiwa kutafuta ofisi yako binafsi pale unapoona panafaa kufanya shuguli zako kwa usiri na utulivu, jambo la pili hatakiwi kujua yeyote hususani maafisa wako waandamizi juu ya jambo hili. Hivyo huna sababu ya kuaga kwa mkuu wako wa UNIT,nafikiri hii ndio kazi yako ya kwanza ambayo inaendana na mafunzo yako toka upandishwe cheo, kazi njema.” Aliongea jenerali kwa msisitizo.



    MWEZI MMOJA KABLA YA MAUAJI



    Saa 8.30 usiku, ndani ya chumba kidogo kilichowekewa ulinzi madhubuti. Hakutakiwa yeyote asiyehusika kunusa kinachoendelea huko ndani, hata walinzi wake hawakutakiwa kujua lolote. Waliridhika na posho nono waliyoahidiwa mara baada ya kikao hicho, hawakuwa na muda zaidi wa kutaka kujua nini kinaendelea huko ndani. Posho ya kulinda chumba hicho usiku mmoja ilikuwa ni zaidi ya mara kumi ya mishahara yao. Haikuwa mara yao ya kwanza kupewa kazi kama hiyo.

    Meza kubwa ya duara ilikuwa imetawala eneo kubwa la chumba hicho, nafasi iliyobaki ilimezwa na viti ambavyo idadi yake ilikuwa kumi na viwili. Viti vyote vilikuwa vimeenea, hakuna kilichokuwa kitupu. Chumba kilitawaliwa na mwanga hafifu wa bluu kitu kilicholeta ugumu wa kuwatambua walio hudhuria kikao hicho cha aina yake.

    Mwenyekiti wa kikao akakohoa kidogo na kuwakazia macho wenzake kabla ya kuongea lolote.

    “Ni matumaini yangu kuwa nyote hamjambo,” alianza mwenyekiti huku akitembeza macho yake kwa wajumbe. Akakohoa tena kabla ya kuendelea.

    “Kubwa lililotuleta hapa ni juu ya mbio za uraisi.” Akatulia na kuwatazama wajumbe ambao walitulia zaidi huku wakiwa na shauku kubwa.

    “....Kwa taarifa nilizo nazo ni kwamba Bw.Oscar Ole Nunga atatangaza nia ya kugombea urais mwaka huu na ameshaanza mchakato.” Akatulia na kuwatazama wajumbe huku akijaribu kusoma fikra zao, wapo walioonesha mshtuko na wapo ambao walichukulia kama taarifa ya kawaida ambayo haikustahiki kuitana usiku wa manane. Licha ya kuwa mwenyekiti wa kikao hakutaka kuzungumza zaidi, badala yake aliamua kuwapa nafasi wajumbe ajue wameipokeaje taarifa hiyo.

    “Kabla sijaendelea naomba kujua kutoka kwenu mmeichukulia vipi taarifa hii?” Akatulia tena huku akiwatazama wajumbe kama kuna ambaye alitaka kuzungumza. Mjumbe mmoja ambaye kama wenzake nae alionekana kushiba madaraka akanyoosha mkono.

    “Enhe, mheshimiwa hapo nafikiri una mchango!” Ilikuwa ni kanuni ya kikao kutotajana majina.

    “Ndiyo, mkuu.”

    “Haya tunakusikiliza.”

    “Kwa mtazamo wangu hakuna tatizo kwa Bwana Ole Nunga kuwania uraisi kwani ni kada mwenzetu na hana tatizo lolote,” akatulia na kuwatazama wenzake huku akiona wazi jinsi wengine walivyokuwa wanatikisa kichwa kukubaliana nae huku wengine wakipingana naye waziwazi.

    “Mkono mwingine...” alisikika mwenyekiti ambaye kwenye kikao alitumia jina la mkuu.

    Mkono ukanyooshwa na mtu aliyekuwa karibu kabisa na mkuu.

    “Enhe.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mi nafikiri hakukuwa na sababu ya kuitisha mkutano huu wa dharura kwa mtu ambaye anafahamika wazi kuwa ni kada nzuri ambaye hana matatizo!”

    Mkuu ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hakuonekana kuwa na haraka ya kujibu hoja hizo za wajumbe badala yake aliendelea kukusanya mawazo bila kuzungumza lolote. Hata pale wajumbe walipoonekana kupinga kikao kile bado mwenyekiti alionekana kuwa mtulivu na asiye na jazba jambo lililowatisha wajumbe wengine.

    Baada ya kupita muda bila kutokea hoja yoyote mkuu alianza kutembeza macho kwa mjumbe mmoja baada ya mwingine kisha kwa utulivu zaidi akaanza kuongea.

    “Nafikiri tunayo haki ya kuzungumza au kufikiri tunavyofikiri kwa kuwa hatuelewi undani wa mambo, Ole Nunga ni mtu hatari tofauti na baadhi yetu mnavyomchukulia. Ana uhusiano mkubwa na baadhi ya wabunge wa upinzani ambao ni matata na tishio kwa mustakabali wa chama, pia ni mfuasi mkubwa wa sera za marehemu Josi Mkulu muasisi wa chama chetu si hivyo tu Ole Nunga ana ushawishi mkubwa sana ndani ya chama.....” akanyamaza kidogo huku akiendelea kuwa mtulivu zaidi, kisha akaendelea.

    “....Pia taarifa za kiinterijensia zinaonesha kuwa ndiye mtu anayetoa siri za serikali kwa vyama vya upinzani hasa pale unapofanyika uozo, amekuwa na falsafa ya hatari ya Nchi yetu kwanza chama baadae, napenda kuwafahamisha kuwa yeye ndiye aliyetoa siri ya ununuzi wa meli mbovu ya kijeshi jambo ambalo limetupunguzia wapiga kura na kuleta ufa ndani ya chama na kusababisha kukosekana ushindi wa kishindo pia.” Akatulia kwa muda mrefu zaidi na kuongeza shauku ya wasikilizaji ambao sasa walionekana kukubali uzito na umuhimu wa kikao kile.

    “…..Si hivyo tu kwa masikio yangu mwenyewe nimewahi kumsikia akidai kuwa atapambana na wote ambao wana akaunti katika benki za nje, hebu niambieni zile fedha zetu zilizoko uswiswi kweli tutanusurika?” Akatulia tena na kuwaachia wajumbe muda wa kutafakari. Aliwaona wazi wajumbe wale jinsi walivyokuwa wanatokwa na jasho kutokana na woga mkubwa. Bila shaka walianza kumuelewa kwa kina kile alichokuwa anakusudia.

    “Kwanini mmempa madaraka makubwa kiasi kile wakati mnatambua wazi kuwa ni mtu hatari?” Aliuliza mmoja miongoni mwa wajumbe.

    “Jibu lake ni rahisi sana, anafahamu mikataba mingi ya hatari kwa jinsi alivyo na ushawishi angeweza kuanzisha hata chama au kujiunga na upinzani kama angeachwa nje ya serikali na isingewezekana kumfunga mdomo, ingekuwa hatari kwa chama na serikali yetu hivyo hatukuwa na namna bora ya kumfunga mdomo zaidi ya kumpa nafasi ile kubwa, tena uzuri ni kwamba ile nafasi ni ya kisiasa zaidi na si ya kiutendaji, yaani tunachotakiwa kufanya ni kumuwekea boksi la mikasi tu ili akazindue miradi ya barabara na majengo mbalimbali hiyo ndiyo kazi ya makamu wa Raisi.” Akatulia tena na kupisha maswali zaidi.

    “Kwanini asifungwe mdomo kama tunavyofanya kwa wengine?” Aliuliza mjumbe mwingine.

    “Hapo ndipo nilipopataka na ndio hasa maana ya kikao hiki, lakini inatupasa kutambua kuwa Ole Nunga si kama hao wengine, anatofautiana nao kwa kiasi kikubwa kama mbingu na ardhi. Ifahamike kuwa Ole Nunga alishawahi kuwa kwenye system, kabla ya hapo ni kapteni mstaafu. Mbaya zaidi ni mtu mwenye akili timamu anayejua nini anakifanya na wakati gani, si hivyo tu pia anajua anaishi dunia gani na aishi vipi! Si mtu wa kumziba mdomo kikawaida kama watu wengine.....” akasita kidogo baada ya kugundua ameongea mfululizo tofauti na kawaida yake ya kuwaachia wajumbe kuchangia.





    Baadhi ya wajumbe walionekana kuanza kuingiwa na hofu juu ya Ole Nunga baada ya taarifa hiyo fupi lakini nzito.

    “Hivi inashindikana vipi kutafuta watu wa kawaida ambao watamnyamazisha kwa risasi moja tu ya kichwa?”

    “Haishindikani!” Sauti mzito ya mjumbe ambaye alikuwa na nafasi muhimu kwenye kikao hiki lakini muda wote alikuwa kimya ikasikika. Akavuta hisia za wote na kufanya wamgeukia.

    “Bila shaka wengi tuliopo kwenye kikao hiki tumewahi kuwa kwenye system katika wakati mmoja au mwingine.......” akawatazama wajumbe wale ambao kila mmoja alitikisa kichwa kukubaliana na kauli hiyo.

    “..... nafikiri hii ndio sababu ya mkuu kutufanya sisi kuwa wajumbe wa kudumu wa vikao hivi ambavyo vina maslahi makubwa kwa chama na serikali.” Utulivu ukatawala tena.

    “..... Vinginevyo hii kazi ilitakiwa asihusishwe yeyote kati yetu maana kulikuwa hakuna ushauri wa kitaalamu ambao ungetolewa. Nirudi kwenye hoja, kumziba mdomo Ole Nunga kwa mtindo wa kutumia watu wa kawaida kutatuletea shida kubwa sana, Nunga ni mtu wa watu na ana watu kwenye system, CID na jambo la hatari zaidi amewahi kuwa kitengo cha ajira ndani ya idara ya usalama wa Taifa hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa masalia yake. Kinachotakiwa hapa ni kutumia akili ya ziada katika kummaliza vinginevyo tutaangukia pua.” Akatulia na kuwaacha wajumbe wengine wakiwa na nyuso zenye hisia tofauti, kila mmoja akijaribu kutafakari mbinu bora ya kummaliza Ole Nunga.

    “Ok, nimepata wazo,” alisikika mmoja kati ya wale wajumbe.

    “Lazima system itumike, nafikiri mjadala ufungwe.”

    “Ufungwe vipi bila ufumbuzi?” Aliuliza mjumbe mmoja.

    “Ufumbuzi upi?” Sauti nyingine ya mjumbe iliuliza. Ile sauti nzito ya mwanzo ikajibu

    “Jibu ni moja tu... Masharubu..” Ilijibu ile sauti.

    “Who is he!”(Ni nani?) Mjumbe mwingine ambaye hakuwahi kuzungumza hapo kabla aliuliza.

    “He is a P.K” mjumbe mwingine akajibu haraka.

    “P.K?!” Aliuliza mjumbe mwingine kwa mshangao.

    “Yes, Professional Killer!” Sauti ile nzito ikajibu.

    “Safi, Uko sahihi.” Kwa mara ya kwanza tabasamu lilionekana kwenye uso wa Mkuu.

    Kikao kikafungwa.



    * * *

    Muziki mororo uliendelea kurindima kwenye baa maarufu ya Mazda iliyopo maeneo ya Tabata Kimanga. Mtu mrefu mweusi mwenye suti ya nrangi nyeusi ya bei mbaya alikuwa amekaa kwenye moja ya kona ya baa hiyo. Mara kwa mara aliinua mkono wake na kutazama saa huku macho akiwa ameyaelekeza langoni. Alikuwa na miadi na mtu, alikunja sura baada ya kuona muda unayoyoma bila ya kutokea yule mtu waliyeahidiana kukutana hapo.

    Huyo ndiye mtu aliyekuwa na kivuli cha jina la Mjomba Masharubu, mtu mrefu mwenye sura pana akiwa na mwili wa wastani. Alikuwa na kidevu cha ufuto ambacho kilisheheni ndevu zilizotunzwa vema. Kama lilivyo jina lake mtu huyu alikuwa na masharubu ambayo yalikuwa yanatunzwa vizuri. Rangi yake nyeusi, masharubu, mawani nyeusi na suti nyeusi vilimfanya afanane na giza licha ya mwanga hafifu uliokuwa unatoka kwenye taa zilizozunguka eneo hilo.

    Akiwa amekata tamaa ya kuonana na yeyote waliyeahidiana kukutana hapo, mara simu yake ya kiganjani ikaanza kuita. Akaitoa simu mfukoni na kutazama namba ya mpigaji.

    Namba ngeni!

    Akaipokea ile simu na kuanza kusikiliza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hallow P.K, Mr.J hapa naongea.”Sauti nzito ilisikika kwenye simu.

    Ni watu wachache na muhimu sana ndio waliofahamu jina lile la P.K na wakamjua PK mwenyewe ni nani, hivyo kuitwa kwa jina lile kulimaanisha jambo.

    “Ndio mkuu, nakusikiliza!”

    “Njoo namba 3 kuna dharura, tunatakiwa kupunguza mnyama mbugani!”

    “Twiga au.....”

    “No, It is a lion, a king of animals!”(Hapana, ni simba mfalme wa wanyama.) Alielewa.

    Akashusha pumzi, bila kujali kuwa ana miadi na mtu akatembea kwa hatua za haraka kuelekea kwenye lango la kutokea nje ya baa ile.

    “Wapi sasa mbona unaondoka?” Sauti ya kike ilimshtua alipokua anavuka lango la baa ile.

    “Oh! Rose, I’m sorry nina dharura kubwa natakiwa mahali saa hizi nina ujumbe wa msiba!”

    “Mungu wangu, nani tena?”

    “Secretary wangu, amegongwa na gari huko kwao Moshi, chukua hizi nitakutafuta!” Alitoa kiasi cha noti ambacho hakukihesabu na kumkabidhi.

    Rose akapokea kile kiasi huku moyo ukimwenda mbio, ni kiasi kikubwa ambacho hakukitarajia tena kwa mtu ambaye ndiyo kwanza walikuwa wamepanga kukutana kwa mara ya kwanza, hakuwa mpenzi wake labda siku hiyo ndio ungekuwa mwanzo wa mapenzi yao.

    Mjomba Masharubu alitembea kwa hatua za haraka kuliendea gari lake aina ya Toyota etios , akajitoma ndani na kukaa kwa dakika kadhaa kabla ya kuliwasha. Alikuwa ameshikilia usukani kama anayetafakari jambo. Kidogo alipatwa na mshtuko baada ya kuambiwa mnyama anayetakiwa kuuwawa ni simba, tena msemaji akaongeza kuwa ni mfalme wa wanyama. Alishtuka kwa sababu alijua uzito wa kazi iliyoko mbele yake, hakupenda kufanya lolote kabla hofu yake haijapoa, ndio maana aliukumbatia usukani ili akili yake irudi kuwa ya kawaida kabla hajaanza lolote.

    Baada ya kutulia kwa dakika chache akawasha gari na kuliondoa kwa mwendo wa wastani hadi alipoipata barabara Mandela. Hapo akakanyaga mafuta na kuifanya gari iondoke kwa kasi sana.

    Mjomba Masharubu ni mwajiriwa wa idara ya usalama wa taifa akijulikana kwa jina la kikazi kama P.K. Si wengi sana waliomfahamu kwa jina hilo, hata wafanyakazi wenzake walikuwa wanajua kama kuna P.K lakini hawakujua ni nani. Walipishana nae hapa na pale bila kufahamu kuwa ndiye P.K mwenyewe. Katika akili zao walijua ni mtu hatari ambaye Idara inamtumia sana kwenye kashikashi nzito ambazo mauaji lazima yafanyike.

    Wapo waliojaribu kunusa wakitaka kumfahamu huyo P.K ni nani! Lakini gharama ya jambo hilo haikuwa ndogo kama walivyofikiri kwani waliishia kupata barua kali ya karipio na wengine hata kuhamishwa makao makuu.

    Watu maalum, watu wachache walimjua ni nani P.K. Hata Mjomba Masharubu mwenyewe kuna wakati alijifanya kutafiti mbele ya wenzake akitaka kumjua huyo P.K ni nani, ikabaki kuwa P.K ni mtu hatari ambaye hata watu wa system walimuogopa

    Kikubwa kilichoongeza usiri wa kumjua huyo P.K ni kutokana na kuwa na mpasuko ndani ya Idara, baadhi ya wafanyakazi walikuwa wanatoa siri nyeti za nchi kwa viongozi au wabunge wa vyama vya upinzani ambao hujichukulia sifa kubwa pale wanapoenda kuweka mambo hadharani. Wafanyakazi hawa huwa wameahidiwa nyadhifa fulani iwapo chama hicho kitaingia madarakani, wengine huvunja viapo vyao vya kutunza siri kwa sababu ya urafiki tu pia wapo wale ambao hufanya hivyo kwa uzalendo wa kuipenda nchi yao kwa kuona nchi inaenda kombo na wengine hufanya kazi hiyo kwa tamaa ya fedha.

    Idara ilikuwa inajitahidi kwa kiasi kikubwa kuishauri serikali mambo mbalimbali kiuchumi, kisiasa, kijamii na mengineyo mengi lakini ikakutana na kiburi na majivuno ya viongozi ambao walitia pamba masikioni na kufanya mambo kwa matakwa yao. Tabia hiyo ya viongozi ikasababisha wananchi kukosa imani kwa chama tawala cha MMD. Mporomoko huo wa chama ukaonekana kuwa hatari kwa maslahi ya baadhi ya wachache ambao walikuwa wameiweka serikali na chama mkononi. Hatari hiyo ya kuanguka kwa chama ndiyo ikasababisha kuibuliwa kwa mtu huyu Mjomba Masharubu. Ni mtu hatari ambaye alikuwa na mafunzo ya juu ya ujasusi. Kwa mtazamo alionekana kuwa mtu wa kawaida lakini undani wake alikuwa zaidi ya mnyama. wajibu wake kwa mkuu wa kazi ulikuwa ni kutekeleza maagizo bila kuhoji. Kuna wakati alishawahi kusafiri nchi mbali mbali za kiafrika kwenda kukatisha maisha ya watu ambao walionekana kuwa hatari kwa usalama wa nchi hizo. Hizo ni zile zinazoitwa nchi rafiki.

    P.K alishawahi kukatisha maisha ya baadhi ya wafanyakazi wa idara baada ya kubainika kutoa siri au kuacha kazi na kujiunga na vyama vya upinzani, pia amewahi kukatisha maisha ya viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani ambao walionekana kuwa hatari kwa chama tawala. Hii ndio sura ya chama tawala ambayo ilikuwa tayari kwa gharama yoyote kuhakikisha kuwa inabaki madarakani lakini si maendeleo ya wananchi.



    ***

    Namba 3 au ‘kichwa’ ni ofisi maalum inayotumiwa na idara ya usalama wa taifa. Mara nyingi hutumiwa na maafisa waandamizi tena sio wote isipokuwa wale waliochaguliwa na mkurugenzi. Usiri mkubwa wa ofisi hii ulitokana na unyeti wake kwani maamuzi mazito ya idara mara nyingi yalianzia hapo. Ni ofisi hii hii ambayo saa 8 usiku uliopita kulifanyika kikao cha watu kumi na wawili.

    Mjomba Masharubu aliingia ndani ya Ofisi hiyo iliyoko maeneo kariakoo mtaa wa Livingstone. Baada ya kuingia akakutana na mkurugenzi wa usalama wa taifa ndugu Wahuva Kilale. Baada ya kusalimiana akakaa na kumuelekea mzee huyo ambaye mvi zilikuwa zimetawala kwenye kichwa chake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Karibu kijana, sijui utapendelea kinywaji gani?”

    “Sihitaji chochote mzee!”

    “Ok, nafikiri hatuna mazungumzo marefu zaidi ya kuingia moja kwa moja kwenye point ya msingi!”

    “Ndiyo mzee.”

    “Safari hii kuna kazi nzito kidogo tofauti na zilizotangulia!” Akatulia na kufanya kero ya shauku ya kusubiri hilo jina iongezeke kwa Mjomba Masharubu. Hakuna alichohitaji kwa wakati huo kama kumjua huyo mlengwa au windo lake jipya.

    “Safari hii kamati imeamua kufupisha maisha ya Mheshimiwa Oscar Ole Nunga.”

    Akainua macho na kumtazama mkuu wake wa kazi kwa mshangao.

    “Makamu wa Raisi?” Aliuliza akitaka kupata uhakika zaidi kwa alichokisikia.

    “Ndiyo!” Alijibu kwa mkato.

    “Kulikoni?”

    “Umesahau kanuni P.K?”

    “Kutekeleza majukumu bila kuuliza?”

    “Ndiyo.”

    “Napenda nifanye kazi nafsi ikiwa imetulia, maana ninavyofahamu Nunga ni kada mwenzenu!”





    “Sawa. Nyati kwenye kundi la ng’ombe. Anautaka uraisi kwa udi na uvumba wakati anajua wazi safari hii ni zamu ya .........” akasita kidogo kisha akaendelea huku akijutia alichotaka kuzungumza.

    “............. Ona nataka kutoa siri za ndani kabisa, anyway ni mtu hatari kwa usalama wa chama na serikali pia amekuwa ni chanzo cha kuundwa kamati teule za bunge kwa kuvujisha baadhi ya mambo nyeti. Siwezi kupokea maswali zaidi.”

    Ilikuwa ni amri hata hivyo aliridhika kwani alifahamu tatizo.

    “Ok, nimekuelewa mzee.”

    “Naomba unifahamishe kila unachokihitaji kwenye kazi hii!”

    “Nahitaji gari mpya ambayo haijasajiliwa!”

    “Simple aina gani?” Alisikika mkurugenzi.

    “Nissan Patrol.” Alijibu kwa mkato huku sura yake ikiwa imebadilika kwa kubeba tafakari nzito, bila shaka akijaribu kupanga nini cha kufanya.

    “Kesho saa 2.30 njoo uchukue hapa!”

    “Ok.”

    “Unaweza kunidokeza plan yako?”

    “Boss umesahau kanuni?”

    “Ya kutoingilia taratibu zako?”

    “Sawa kabisa.”

    “No, sijakuingilia isipokuwa nimeuliza tu maana mwili unasisimka kwa jinsi ulivyoanza haraka hiyo mipango.”

    “Hapana bado sijaratibu vizuri nahitaji siku nzima ya kutafakari kwa makini ingawa gari mpya isiyosajiliwa tayari ni sehemu ya mpango wangu.”

    Mzee Wahuva hakuongea kitu zaidi ya kutikisa kichwa kukubaliana na kijana wake.

    “Ok kazi njema.” Aliongea mkurugenzi huku akimpa mkono Mjomba.



    * * *



    Taisamo alipofika ofisini kwake, kwenye jengo la Mwalimu house eneo la Ilala boma , ilikuwa yapata saa nne na nusu. Alifungua mlango wa ofisi ile mpya ambayo hakuna yeyote katika watu wake wa karibu aliyeifahamu. Alitabasamu baada ya kukaa kwenye kiti kile ambacho kilikuwa na uwezo wa kuzunguka na hata kusogea sehemu nyingine. Kiujumla ilikuwa ofisi nzuri yenye mahitaji yote muhimu kama computer, printer, kabati kubwa la kuhifadhia mafaili na simu ya mezani. Alitumia siku mbili kuandaa ofisi hii.

    Jambo la kwanza alilolifanya ni kuanza kusoma taarifa za kifo cha Makamu wa Rais kama alivyopewa na Jenerali Nalinga. Akili yake ilimtuma kuwa ni kazi rahisi tu kwani angeanzia pale walipoishia wenzake. Akalifungua lile faili au jalada la Mauaji akaanza kulisoma.

    Muheshimiwa aliuwawa muda mfupi baada ya kutoka kwenye mkutano mkuu wa chama. Chanzo cha ajali yake ni ajali ya gari iliyosababishwa na dereva mzembe aliyeingia ghafla barabarani wakati msafara wa viongozi wa chama na serikali ulipokuwa unatoka ukumbini. Alisoma huku akiyakariri maneno yale kwa sauti ndogo.

    Mwandishi mmoja wa gazeti la Muungwana alilifuatilia kwa karibu tukio lile. Inspekta Tunu Nzowa alipewa jukumu la upelelezi. Alianza kazi kwa kumfuatilia mwandishi wa gazeti la Muungwana ndugu John Oscar. Haijulikani nini kilitokea, kilichoshuhudiwa ni kukutwa Inspekta akiwa amepoteza fahamu kwa kipigo ambacho ni wazi kusudio lake lilikuwa ni kummaliza, mwandishi ambaye alionekana kufahamu vizuri kilichotokea akakutwa ameuwawa kikatili, nukta!

    Alishangazwa na kile kilichoitwa taarifa kutokuwa na msaada wowote kwake, ilitosha kwake kama angeanza moja kwa moja kuifanyia kazi kutoka katika vyombo vya habari au watu wengine. Aliitazama taarifa ile na kugundua kuwa haina msaada wowote kwake.

    Akainua kiwiko cha simu yake ya mezani akapiga namba alizozihitaji.

    Alishanga ile namba kutopokelewa na Jenerali Nalinga kama alivyotarajia.

    “Hallow one fifty Rose hapa, bila shaka unahitaji msaada!”

    “Ndiyo naomba unitengenezee kitambulisho chenye jina la Frank Stefano mwajiriwa katika gazeti la serikali la THIS MONTH.”

    “Ok, baada ya masaa manne kazi yako itakuwa tayari, utakikuta kitambulisho nyumbani kwako una ombi lingine?”

    “Ndiyo.” Alivuta pumzi huku akitafakari jinsi upande wa pili utakavyopokea ombi lake.

    “Naomba tuonane!”

    “Oh, mara ngapi?”

    “Kwani tulishawahi kuonana?”

    Kwa mara ya kwanza akamsikia mwanamke yule mwenye amri za kiume akicheka.

    “Usijali utaniona maana inaelekea hutaki kuzingatia hata maonyo yangu.”

    “Lini?”

    “At the end of your mission.(mwisho wa kazi yako)” Simu ikakatwa.

    Aliamua kutafuta sehemu ambayo angepata chakula kwani alikuwa hajanywa hata chai mpaka kufikia muda huo wa saa nane kasorobo.



    * * *

    Alirejea nyumbani kwake Meneo ya Tandika maghorofani saa moja na nusu. Wakati anafungua mlango wa chumba chake ndipo aliposikia sauti ya mama mwenye nyumba.

    “Baba samahani kuna mzigo wako hapa.” Alisikika yule mama wa makamo huku akiwa na bahasha kubwa ya kaki mkononi.

    “Ahsante mama, naweza kumuona mzee saa hizi.”

    “Hapana mbona toka juzi kasafiri, kaenda Kigoma mazishini kaka yake amefariki kumbe ulikuwa huna taarifa?”

    “Taarifa nilikuwa nayo lakini aliniambia anasubiri kodi yangu ili aweze kusafiri kwani alisema hana pesa kabisa.”

    “Kuna mpangaji kahamia chumba hicho…...” Huku akimuonesha kwa kidole chumba ambacho kilielekeana na kile cha kwake.

    “…… Siku nne zilizopita, alipopata tu kodi yake ya miezi sita akaamua kukimbilia msibani ndio akatuachia maagizo kuwa hela ya kula tutaipata kutokana na kodi yako ya miezi miwili nyingine ni ile ambayo ulimkopesha alisema mnakatana juu kwa juu.”

    “Sawa mama lakini kodi ya miezi miwili itatosha kweli kuendesha maisha ya hapa nyumbani?”

    “Tutafanyaje mwanangu, tutajibanabana hivyohivyo bora tusukume siku.”

    Akaingiza mkono mfukoni akachomoa noti za shilingi elfu kumi kumi.

    “Hizi ni za kodi na hizi zitakusaidia kusukuma siku.”

    “Ahsante baba lo! Umenifaa kweli maana hata hapo dukani nilikuwa nadaiwa naona deni litakwisha leo.”

    Yule mama akaondoka huku akiwa na furaha kwani fedha za ziada alizopewa na Taisamo zilikuwa nyingi kuliko kiasi alichokuwa anamdai.

    “Ah! Samahani mama.”

    “Bila samahani.” Aligeuka yule mama na kusimama.

    “Amejitambulisha kwako aliyeleta hii bahasha.”

    “Hapana baba, ni kijana mmoja ambaye ni dereva teksi kasema mlishawasiliana.”

    “Ahsante.” Akasikika huku tayari mguu mmoja ukiwa chumbani kwake.



    ***



    2

    KUTAFUTA UKWELI



    I

    Asubuhi ya Ijumaa hiyo ilimpambazukia Alex Taisamo kwa ishara tofauti tofauti. Kuku waliopokezana na kutambiana kwa ujasiri wa kuwika walizidi kupoteza usingizi wake. Hisia za jukumu zito alilopewa na hofu ya kufanya vibaya kazi hiyo zilianza kumuandama. ‘This is your first mission Liutenant,Goodluck’ Maneno ya mkuu wa majeshi ya ulinzi yalijirudia kichwani mwake. Kilichomtia hofu zaidi ni kitendo cha Jenerali kufikisha ujumbe yeye mwenyewe ingawa kulikuwa na Mnadhimu wa Majeshi Luteni Jenerali Ruhumbika, kwake hii ilibeba tafsiri ya ukubwa wa jukumu lililoko mbele yake.

    Akayafutilia mbali mawazo hayo ambayo yalikuwa yanakatisha tamaa na kupunguza morari ya kufanya kazi. Siku hiyo hakujisikia kabisa kufanya mazoezi kama ilivyokuwa kawaida yake, badala yake aliamua kuoga mapema. Ili kujiandaa kwa siku ile ambayo mwenyewe aliona kuwa ndiyo anaanza kazi rasmi.

    “Mafunzo ya hapa chuoni pekee hayatoshi, hizi ni kazi ambazo wakati mwingine akili yako ya kuzaliwa inahitajika zaidi.” Maneno ya mmoja wa walimu wake alipokuwa chuoni, Meja Mwita yalijirudia kichwani mwake.

    Wakati anatoka kuoga akapishana na binti mrembo ambaye naye alikuwa anaelekea bafuni akiwa na ndoo yake ya maji. Walipokutanisha macho yao alihisi moyo wake ukilipuka kwa mshtuko.

    ‘Bila shaka huyu ndiye mgeni aliyenieleza mama’ Aliwaza. Alitamani kugeuka lakini akaamua kupiga moyo konde.

    ‘Sijui ana mtu huyu?’ Aliendelea kujiuliza huku akifungua mlango wa chumbani kwake.

    Baada ya kuvaa nguo alikaa dakika kadhaa kitandani kisha akafungua ile bahasha yenye kitambulisho chake. Kilikuwa na mihuri yote muhimu, akatabasamu kwani zoezi lake lilikuwa limeenda jinsi alivyopanga.

    Dakika chache baadae akatoka na kuelekea kituo cha daladala. Ilikuwa yapata saa kumi na mbili na robo. Baada ya kupiga takribani hatua kumi akageuka na kumuona yule dada mgeni akiwa nyuma yake na mkoba begani.

    ‘Nimsubiri?’ Alijiuliza huku akiwa amepunguza mwendo. ‘Bila shaka ni vema nikimsubiri, kazi na dawa bwana?’ Alihalalisha kitendo chake hicho kwa kutumbukiza msemo wa mtaani.

    “Habari yako dada.” Alisalimia baada ya kuona amemsogelea.

    “Nzuri.” Alijibu kwa mkato huku akionesha kuwa na haraka zaidi ya Taisamo.

    “Karibu sana maana nimekuona jana lakini nasikia umeingia siku nne zilizopita.”

    “Ahsante.”

    “Naitwa Alex Taisamo, sijui mwenzangu…..”

    “Suzana Lusungu ukipenda niite teacher Suzy au teacher Lusungu.”

    “Aah, kumbe ni mwalimu nitakuita tu Suzy hilo la teacher mutaitana huko shule.”

    Akacheka na kuruhusu meno yake yaliyojipanga vema kuonekana.

    “Sijui unafundisha wapi Suzy.”

    “Jiandae, ni ya mtu binafsi iko Kinondoni.”

    “kumbe tunapanda gari moja mimi niko pale Ilala Boma. Ni mwandishi wa gazeti la serikali la THIS MONTH niko tawi la Ilala au unaweza kusema mkoa wa kihabari wa Ilala.”

    “Mbona mama mwenye nyumba aliniambia chumba hicho ni cha mwanajeshi?”

    “Hajui kuwa niliacha kazi siku nyingi.”

    Baada ya hapo kila mmoja alikuwa kimya huku akiwa na fikra zake kichwani. Taisamo aliutumia muda huo kulisanifu umbo zuri la Suzy lakini huku akijiuliza jinsi yule msichana alivyoweza kubaini mapema kazi yake.

    “Yaani alimuuliza Yule mama kazi yangu?” Alijiuliza huku akionekana wazi kutatanishwa na kitendo hicho.

    Alikuwa msichana mrembo mwenye uso wa duara, macho yake yalikuwa makubwa yenye kuvutia, kichwa chake kilibeba nywele ndogo ambazo hazikuwekwa dawa yoyote zaidi ya mafuta ya kawaida ya nywele. Kifua chake kilibeba matiti ya wastani ambayo yalimvutia Taisamo. Blauzi yake nyeupe na sketi ya rangi ya kaki yenye mpasuo mdogo ni vitu vilivyomfanya Taisamo ajisahau kwa muda. Miguu yake mizuri iliyojazia vizuri kwa kuumuka kama maandazi ya duara yaliyowekwa hamira ilizifanya fikra za Taisamo zipae mbali zaidi.

    “Karume..Magomeni…Kinondoni…Mwananyamala.” Mpiga debe aliwazindua viumbe wale wawili. Wakajitoma ndani ya gari huku wakiwa kimya, Suzy alikaa mbele kidogo huku Taisamo akikaa siti ya pili nyuma yake. Moyoni aliwalaumu wanaopenda kukaa siti za dirishani kwani kama si wao pengine angekaa siti moja na Mwalimu Suzy.





    * * *

    Saa 2.30 Taisamo alipiga simu kwa Jenerali, kama kawaida Rose akapokea ile simu.

    “Habari Luteni.”

    “Salama Rose, kuna jambo naomba unisaidie kidogo…….” Akakohoa kidogo kisha akaendelea. “Nahitaji kumfahamu daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu.”

    “Anaitwa Dokta Gabriel Kilonzo, yuko taasisi ya mifupa pale Muhimbili.”

    “Duh, uko faster binti au umemeza flash?”

    “Ushaanza vituko vyako.” Alisikika Rose huku akiangua kicheko.

    “Na lile la kufahamiana?”

    “Kwani unataka nini zaidi?”

    “Sura yako mrembo.”

    “Una matatizo Luteni, mimi ni mkuu wako wa kazi halafu nakaribia kustaafu bado unaniita mrembo?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ng’ombe hazeeki maini.” Akasikia kicheko upande wa pili simu ikakatwa.

    Baada ya kupata staftahi aliamua kwenda kuonana na Dokta Kilonzo. Alifika maeneo hayo ya hospitali saa 5.21.

    “Vipi bosi nikusubiri?” Aliuliza dereva wa teksi iliyomleta baada ya kupewa pesa yake.

    “Mpaka saa ngapi?”

    “ukimaliza shuguli zako.”

    “Ingawa ninakusudia kutochelewa lakini inaweza kutokea vinginevyo.”

    “Nitakusubiri bosi wangu kijiweni hakuna dili siku hizi watu wa bodaboda wametuharibia soko……” Hakusikia maneno ya mwisho aliyokuwa anawalani madereva bodaboda. Alipiga hatua za haraka haraka kuelekea kwenye lango la kuingilia hospitali.



    ***



    Ilikuwa yapata saa sita na dakika Ishirini na tano wakati Dokta Kilonzo alipokuwa anakusanya nyaraka zake muhimu ili aondoke akasikia mlango unagongwa.

    “Fungua.”

    Mlango ukafunguliwa kijana mtanashati ambaye alikuwa amevaa shati la pinki na suruali ya kijivu akaingia. Alikuwa amevaa viatu vyeusi ambavyo viling’arishwa vema kwa dawa.

    “Karibu sana.”

    “Ahsante. Habari za kazi dokta” Alisalimia huku akikaa kwenye kiti kilichomuelekea dokta.

    “Marahaba, sijui nikusaidie nini maana ninataka kwenda wizarani mara moja.”

    “Naitwa Frank Stefano, ni mwandishi wa habari za uchunguzi katika gazeti la serikali la THIS MONTH.”

    “Karibu sana Bwana Frank, sijui nikusaidie nini?”

    “Ahsante, ujio wangu ni juu ya kifo cha makamu wa Rais mheshimiwa Ole Nunga, Bila shaka wewe ndiye uliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu.”

    “Labda nirekebishe kauli yako, mimi ni mwenyekiti wa Jopo la madaktari walioufanyia uchunguzi mwili wa marehemu.”

    “Unaweza kunifahamisha sababu za kifo chake.”

    “Ripoti yake tuliikabidhi Polisi na tulizuiwa kuzungumzia swala hilo kwa yeyote kwani tutaharibu uchunguzi wa Polisi.”

    “Ni nani alipokea taarifa hiyo?”

    “Hata hilo pia lilizuiwa.”

    “Kwani kuna kitu zaidi ya ajali ya gari kilisababisha kifo chake?”

    “Naona nimeshakujibu kiasi cha kutosha, hilo swala tulifunge. Nimekwambia tumezuiwa kutoa taarifa kwa yeyote sina la zaidi.”

    “Labda nikuulize swali la mwisho.”

    “Lakini lisihusiane na kifo cha Muheshimiwa.”

    “Sawa. Je! Imewahi kutokea katika maisha yako ya kazi kuwekewa pingamizi namna hii?” Dokta Kilonzo akatulia huku anakuna kichwa.

    “Kijana, nyakati hubadilika kwani katika maisha yangu ya kazi sijawahi kuufanyia uchunguzi mwili wa kiongozi yeyote hivyo inawezekana kabisa kukawa na utofauti katika uchunguzi wa mwili wa kiongozi mkubwa na kiongozi wa kawaida au raia.”

    “Tofauti inakujaje wakati tunahubiri haki sawa?”

    “Kiongozi ni kiongozi kutoa taarifa za kifo chake kunaweza kusababisha maafa hulijui hilo?”

    “Kwa hiyo kuna watu wakigundua kuwa ameuwawa na si ajali kama wanavyofikiri inaweza kusababisha vurugu.”

    “Kwa nini isitokee vurugu wakati ana wafuasi wake.”

    “Kwa hiyo waliomuua ndio ambao wameamua kuzuia hii taarifa kwa kuogopa vurugu?”

    “Kijana, hayo maswali yako naona umekusudia kuniharibia siku yangu. Inatosha, unaweza kuondoka au ukabaki peke yako hapa ofisini umenifanya niongee nje ya mipaka yangu.” Akachukua vifaa vyake na kunyanyuka huku akimwacha Taisamo kaduwaa.



    ***

    Saa 10.43 alasiri; Alilakiwa na sofa ambalo muda mrefu limekuwa na upweke mkubwa, hakukumbuka hata kuvua viatu akaitawanya miguu yake mmoja juu mwingine chini. Aliaziacha fikra zake zitafakari matukio ya siku ile. Swali kubwa alilojiuliza ni kwanini ripoti ya kifo cha mheshimiwa imegubikwa na usiri mkubwa, kilichomshangaza zaidi ni kuona katika taarifa aliyopewa hakuna taarifa ya kidaktari juu ya kifo cha mheshimiwa Ole Nunga.

    Kwanini daktari alikuwa mkali sana alipomuuliza juu ya taarifa? Kwanini hakukuwa na Press conferance kama ilivyo ada.

    Aliliandika jina la daktari Kilonzo kisha akalizungushia alama nyekundu kwa kalamu yake.

    “Atasema tu” alinong’ona kwa sauti ya chini sana.

    Wakati akiwa kwenye lindi la mawazo mara akamsikia Suzy yule mpangaji wa chumba cha pili anaongea.

    “Karibu sana, karibu mpendwa.” Alisikia sauti ya Suzy, moyo ukamlipuka kwa wivu.

    Moyo wake ukaanza kwenda mbio pale alipokuwa anafikiria kufungua mlango ili amuone huyo mpendwa. Akatoka ili aweze kujionea mwenyewe, mshtuko alioupata ulikuwa ni zaidi ya alivyotarajia. Haraka akageuza sura yake na kuielekeza upande mwingine ili asiweze kuonana na yule mtu, hakutaka kabisa yule mtu afahamu kuwa yuko pale. Akatembea haraka haraka kuelekea nje.

    “Dokta! Ina maana dokta na Suzy wana uhusiano?” Alijiuliza huku akiwa amesimama kwenye mlango wa kuingilia chooni. Hakuingia, badala yake akarudi ndani kwani alihisi watakuwa wameshaingia chumbani.

    Dakika kumi na tano baadae aliwasikia tena wakiongea nje ya chumba. Akasimama mlangoni na kuwachungulia kwenye tundu la funguo.



    * * *



    “Naomba ulifuate lile gari.” Alihimiza Taisamo huku akimwonesha dereva wa teksi gari ambalo aliingia dokta Kilonzo.

    “Bosi si tuelewane kabisa.”

    “Unataka ngapi?”

    “Inategemea na urefu wa safari.”

    “Una mafuta ya kutosha?”

    “Full tank.”

    “Mfwate nitakulipa full tank kwanza halafu nyingine tutaongea.”

    “Bosi Ishu kama hizi za kufuatilia watu zinakuwa na malipo ya ziada.”

    “Oyaa anatuacha huyo, au nichukue gari lingine?”

    “Hawezi kutupotea yule dokta nafahamu mpaka nyumbani kwake nishawahi kumpeleka mara nyingi tu si ana dispensary hapo nyuma?

    Taisamo akatulia kidogo na kumwangalia yule dereva.

    “Nyumbani kwake, nikulipe kiasi gani?”

    Alipomtajia kiasi wakakubaliana kisha wakaanza kuifuata gari ya dokta Kilonzo Starlet nyeupe.

    “Kama haelekei nyumbani kwake tutafanyaje?”

    “we mfwate tu.”

    “Halafu kuhusu malipo!”

    “Una wasiwasi na mimi?”

    “Sio wasiwasi bosi ‘some times’ wateja mnakuwa watata.”

    “Ok, shika hizi.”

    Galasa yule dereva teksi alitoa macho ya uchu baana ya kuona akichotewa pesa kutoka katika kibunda cha noti. Akazihesabu na kuziweka mfukoni huku akiwa na furaha.Ni pesa nyingi kwa mtu wa kawaida.

    “Nafikiri hizi zinatosha kufanya kazi zangu za leo na kesho.”

    “Bila shaka mkuu.” Alijibu huku akikenua meno na kumtazama Taisamo kwa jicho la wizi bila shaka akimjumuisha katika kundi la ‘mapedeshee’ wasiofahamika.

    “Haya naomba tumfuate dokta sasa.”

    “Poa.” Alijibu huku akiliwasha gari lake.



    * * *



    Saa 3.30 usiku.Mlango uligongwa tena, safari hii mgongaji alitumia nguvu kidogo. Dokta Kilonzo ambaye alikuwa sebuleni akitazama Runinga akainuka taratibu kwenda kufungua mlango.

    “Karibu.”

    “Ahsante dokta.”

    “Habari yako.”

    “Nzuri , shikamoo.”

    “Marhaba,karibu ukae.”

    “Ahsante, bila shaka unanikumbuka.” Alianza Taisamo huku akijiweka sawa kwenye kiti.

    “Hapana, labda unikumbushe maana kazi zetu hizi zinatufanya tukutane na watu wengi sana.”

    “Naitwa Frank Stefano, ni mwandishi wa haba………”

    “Oooh, Mungu wangu! Ni nani kakuonesha huku nyumbani kwangu?”

    “Hukutaka nipafahamu?”

    “Kabisa, yaani kama suala ulilojia ni kuhusu kifo cha muheshimiwa, nikueleze wazi tu kuwa sina majibu.”

    “Leo utanijibu dokta.”

    “Nimekwambia sina majibu na ni hiyari yangu huwezi kunilazimisha.” Dokta alikunja sura wakati anajibu.

    “Ok, kwanza nataka kujua familia yako iko wapi?”

    “Kama swali ni hilo nitakujibu, wako Kilolo Iringa, sijui una maana gani kuuliza swali kama hilo.”

    “Nisingependa washuhudie jinsi nitakavyokisambaratisha kichwa chako kwa kukataa kujibu swali langu.”

    “Kwani ni lazima?”

    “Ni lazima sana.”

    Dokta akashtuka baada ya kauli ile kwani alikuwa anatazamana na mdomo wa bastola.

    “Sijawahi kusikia waandishi wanatafuta habari kwa mfumo kama huu.”

    “Sema hujawahi kuona sio lazima usikie kila kitu, ok sina muda wa mjadala utajibu maswali yangu la sivyo…”

    “Ni hiyari yangu, kwa sababu nikikujibu gharama yake ni kifo na nisipokujibu pia gharama ni kifo.”

    “Mimi ndiye niliyekuahidi kifo iwapo hutanijibu.”

    “Hata MKUU kaahidi kifo iwapo siri hii itatoka, tofauti yako na mkuu ni kwamba mkuu ana mkono kila kona wewe mkono wako ni mfupi sana.”

    “Mkuu ni nani?”

    “Kumbe umedhamiria kuniua, kwani hata nikikuambia Mheshimiwa alimalizwa kwa risasi itakusaidia nini?”

    “Kwa hiyo kauwawa kwa Risasi na Mkuu, Ni nani huyo?”

    Ghafla, akasikia sauti nzito nyuma yake.

    “Utamjua huyo mkuu muda si mrefu, shusha bastola chini na usithubutu kugeuka….”.

    Taisamo alisisimka kutokana na hisia kali ya adui aliyeko nyuma yake. Kitu kizito mithili ya chuma kikagusa kisogoni kwake. Kitu kilichomshangaza ni hiyo sauti, licha ya uzito wa kuigiza bado haikuwa ngeni sana kwake. Ameisikia wapi? Hilo ni swali gumu ambalo kwa muda huo hakutaka kulipa nafasi.

    “Kabla sijakulipua nataka kwanza ujibu maswali yangu.” Sauti hiyo isiyo na mzaha ilipenya kama mwale wa moto kwenye masikio ya Taisamo.

    “Wewe ni nani, umetoka wapi na umetumwa na nani kwa lengo gani?”.

    “Naitwa Frank, ni mwandishi wa gazeti la THIS MONTH.”

    “Usinitanie kijana, waandishi wa Tanzania hawawezi kutumia hata kisu sembuse bastola.”

    “Si kweli, wengi wamepitia JKT kabla ya kuajiriwa hivyo si jambo la ajabu.”

    “Usinifanye kuwa mjinga, kwa umri wako JKT ilikuwa imeshafutwa.”

    “JKT ipo mpaka sasa na inaendelea kuchukua vijana wazalendo.”

    “Wewe chizi acha kunipotezea muda nataka unieleze ukweli ni nani kakutuma? Pia napenda ufahamu kuwa zimebaki dakika tano tu nitakulipua”

    II



    ***

    Ubaridi wa alfajiri ndio uliomzindua, alifumbua macho na kushangaa mazingira aliyopo. Wakati anafumbua macho alihisi kuwa yupo kitandani kwake, akatumia mkono wake wa kulia kupapasa akiamini kuwa hicho ni kitanda na pembeni yake yupo Tamasha.

    ‘Mchanga?’ Alishtuka baada ya kushika kitu ambacho kilikuwa tofauti na godoro lake, akaanza kuhisi ubaridi ambao si wa kawaida, akashtuka na kuendelea kuutembeza mkono wake wa kulia akashika kitu kingine ambacho kiliendelea kumstaajabisha. ‘Majani?!’ Lilikuwa jambo jingine la kushangaza.





    Macho yake yalikuwa mazito lakini akalazimisha kufumbua, lilikuwa ni eneo geni kwake, alijihisi kama mtu aliyeko kwenye kilele cha mlima kwani kwa mbali aliweza kuona taa zikiwaka kwenye nyumba ambazo zilionekana kwa chini. Alijaribu kadri alivyoweza kuvuta kumbukumbu ya pale alipo lakini akili yake ilikuwa nzito. Baada ya dakika chache akaanza kurudiwa na fikra juu ya kilichotokea.

    James Makabi alikiona kifo mbele yake, hakuamini kama anaweza kupona iwapo gari lile litafika mwisho na kugonga vile vijumba vya wauza gongo, akaamua kufungua mlango na kujichomoa ndani ya gari. Alishuhudia vumbi zito ambalo lilitimuliwa na lile gari, kutokana na kasi ya lile gari alijikuta akiyumba na kusukumwa kwa kasi hadi kichakani. Akaangukia hapo kwenye kichaka na kuliona lile gari likizidi kuserereka kuelekea kwenye zile nyumba zilizoko bondeni. Akili yake ilimfanya aone kama kila kitu kinazunguka wakati huo. Dakika chache baadae akasikia kishindo kikubwa na kushuhudia moshi nzito ukipanda angani.

    “Mungu wangu….” Alitamka dakika chache kabla hajapoteza fahamu, hakukumbuka chochote mpaka muda huo aliozinduka. Fikra za ile ajali zikamkumbusha jina muhimu sana kwake, Mjomba Masharubu. Akajiinua pale kichakani na kujipongeza kimoyomoyo jinsi alivyoweza kufanya mauaji ya mtu ambaye mpaka muda huo hakumfahamu bila kukamatwa na polisi. Akili ya pesa alizo ahidiwa ikajirudia. Akajiinua na kuanza kutembea kwa mwendo wa kuchechemea.

    Alilikumbuka tukio zima kama sinema Fulani ya kusisimua. Akapapasa mifuko ya suruali yake, akatabasamu baada ya kugundua kuwa simu yake bado ilikuwemo. Akaichomoa na kuikagua. Bado ilikuwa mzima na ilimtambulisha kuwa hiyo ilikuwa ni saa 10.30 Alfajiri. Akatabasamu kwa mara nyingine baada ya kuwasikia wanadi swala kutoka misikiti mbalimbali.

    ‘Swalaa…swalaaa…swalaaa, saa kumi na nusuuu.’ Sauti hizo kali za spika zilipenya kwenye masikio yake. Na kumfanya asadiki kile alichokiona kwenye simu.

    Baada ya kujikung’uta vumbi akatembea taratibu kuelekea kule bondeni ambako gari liliangukia. Akayaona mabaki ya lile gari, hakuhitaji uthibitisho kuwa lazima lile gari lilijeruhi au kuua watu kule chini. Nyumba moja ilikuwa imeteketea kwa moto ambao vilevile alifahamu ulitokana na gari. ‘Hivi kulikuwa na haja gani kwa yule mtu kutumia gharama zote zile kumuangamiza mtu mmoja tu? Yule mtu ni nani na ana thamani gani?’

    Alianza kujiuliza maswali ambayo yalimtisha hata yeye mwenyewe.

    ‘Kama yule mtu amethubutu kutumia gharama kubwa kuua hivi kweli hawezi kuniua hata mimi pale nitakapoanza kudai ujira wangu’ Swali hilo lilimshitua na kumfanya aanze kukosa raha. Furaha aliyokuwa nayo ikaanza kutoweka kama giza la usiku lililochomozewa na jua ghafla.

    “Nitanyaje iwapo polisi waliipata picha yangu wakati wa tukio!” Aliongea kwa sauti ndogo ambayo ni yeye mwenyewe aliyeisikia. Alianza kupishana na watu wawili wachache ambao walikuwa wanawahi kwenye shuguli zao.

    Fikra zikamfanya atembee mpaka Magomeni Kagera bila kujijua wakati dhamira yake ilikuwa ni kuelekea Magomeni Mikumi. Akatazama tena saa kwenye simu yake, ilikuwa ni saa 11.45. Akasimama kituo cha daladala cha Kagera na kusubiri gari zinazoelekea ubungo. Haukupita muda mrefu kabla gari aina ya DCM halijawasili.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ubungo, Manzese, Kimaraaa…” Mpiga debe aliendelea kupiga makelele.

    Akajitoma ndani ya gari na kuchagua siti ambayo haikuwa na mtu.

    Akashangaa kuona dada mmoja ambaye alikuwa amekaa siti ya kushoto kwake akimwangalia kwa macho ya wizi kila dakika. Akaja kugundua hata mtu aliyekuwa siti iliyofuata naye alikuwa akimtazama kwa jicho lilelile.

    “Brother vipi mbona umechafuka sana kwa vumbi ulianguka? Halafu upande huu kuna damu kwenye shati inakuwaje?” Swali hilo likamzindua na kumfanya aandae majibu ya haraka.

    “Nilikuwa najenga huko ‘saiti’, tumekesha hukohuko. Hapa kuna kipande kidogo cha tofali kimeniangukia ndio maana nimeamua kurudi nyumbani kwanza halafu nitarudi tena maana tutakuwa huko kwa siku tatu.”

    “Dah, pole sana mimi nilishakufikiria vibaya.” Yule dada ambaye alikuwa anamtazama kwa jicho la wizi naye akaongea.



    ***



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog