Search This Blog

Monday, 24 October 2022

WIMBO WA GAIDI - 3

 

    Simulizi : Wimbo Wa Gaidi

    Sehemu Ya Tatu (3)





    “Shiiit…” Mukri alimaka, na hapo hapo taa ya mle ndani ikawaka, naye akajirusha pembeni ilhali akijigeuza akiwa na bastola yake mkononi, akimsaka Brey.

    PBaaaaah!!

    Mlipuko wa bastola ulivuma mle ndani kutokea kule mlangoni sanjari na yowe la taharuki kutoka kwa Mukri aliyetupwa hewani kwa msukumo wa risasi iliyojikita kifuani kwake.

    “Mukriii…!” Jarraar alipayuka huku naye akiigeuzia bunduki yake kule ulipotokea mlipuko ule wa bastola, na vitu viwili vikatokea kwa wakati mmoja.

    Kutokea kwenye kiti alichokuwa amekalia kikiwa kando ya ule mlango wa kuingilia mle ndani kikitazama kule kitandani ambako Sandra alikuwa amelala hapo awali, Brey Jabba alifyatua risasi nyingine kumuelekea Jarrar aliyehamanika…na katika nukta ile ile, kutokea pale chini alipokuwa, Sandra alijizungusha na kumchota ngwara kali sana Jarraar huku naye akijibiringirishia uvunguni mwa kile kitanda.

    Jaraar alimaka kwa ukelele huku akienda chini kama mgomba, na risasi ya Brey ikamkosa kwa bahati tu. Lakini mithili ya paka anapoangushwa kutanguliza mgongo, Jarraar alijigeuza haraka sana na kujiinua kwa goti moja akiwa ameelekeza bunduki yake kule ambako Brey alikuwapo.

    Kosa.

    Kama aliyetarajia tendo lile, Brey Jabba alikuwa ameshajitupa wima kutoka kwenye kile kiti alichokuwa amekalia na kuruka kwa hatua moja mpaka sehemu baina ya pale alipokuwa amejibanza kwenye kiti na kile kitanda, akadunda sakafuni mithili ya mcheza dansi ya “ballet”, akaenda tena hewani na kutua pale juu ya kile kitanda katika nukta ile ile ambapo Jarraar ndio alikuwa amejiinua kutoka sakafuni upande wa pili wa kile kitanda, na kuifyatua kwa teke kali ile bunduki kutoka mikononi kwa yule muuaji wa kukodiwa.

    Lah!

    Jarraar alimaka kwa hamaniko, na hapo hapo Brey akajirusha hewani juu pale kitandani na kumshidilia miguu miwili ya kifua yule jamaa ambaye alitupwa nyuma na kubingirika vibaya sana sakafuni, naye akadunda pale kitandani na kujirusha tena sakafuni. Akajigeuza kwa wepesi wa kama vile wa kimaskhara tu, sasa macho yake yakiwa kwa Mukri. Akamuaona bado amesambaratika kibwege sakafuni. Kwa wepesi ule ule wa kimaskhara alijegeuza huku akibonyea chini kidogo kumgeukia yule muuaji mwingine. Jamaa ndio alikuwa akijiinua kutoka kule alipoangukia huku akipeleka mkono wake nyuma ya kiuno chake.

    “Don’t!” Brey alimkoromea huku akiwa amemnyooshea bastola.

    Jarraar akaganda kama alivyokuwa. Wakabaki wakitazamana kwa ghadhabu. Muda huo Sandra akajibiringisha kutoka kule uvunguni na kuiwahi ile AR-15 ya Jarraar iliyokuwa imetupwa pale sakafuni. Sasa kutokea kwenye vyumba vingine ndani ya nyumba ile ya wageni watu walisikika wakipiga kelele ingawa hakuna aliyetoka nje ya chumba chake.

    Jarraar alimtupia jicho mwenzake na kuona kuwa alikuwa amelalia ubavu huku ameelekea ukutani, akiwa amewageuzia mgongo.

    “Kaa chini…taratibu mno!” Brey alimkoromea, na Jarraar akabaki akimkodolea macho kwa hasira ya mbichi, wazi kuwa hakuwa amemuelewa.

    “Nasema kaa chini kwa upole sana!” Brey akamkoromea tena, safari hii akitumia lugha ya kiingereza, na jamaa likamtupia tabasamu la ghadhabu.

    “Ningekuwa mimi hapo wala nisingehangaika kukuambia ukae chini pusi wewe…ningekiwasha risasi tu!” Alimwambia huku akimtazama kwa ghadhabu, na hapo hapo AR-15 ikapiga chafya na kuchimba sakafu milimita chache sana kutoka kwenye miguu yake, na Jarraar aliruka kwa mshituko huku akimgeukia yule mwanadada aliyekuwa na chupi tu mle ndani.

    “Kama hivyo?” Sandra alimkoromea kwa kiingereza vile vile huku akiwa amemlengeshea ile bunduki itishayo.

    Jarraar alimtumbulia macho kwa hasira, kisha akainua mkono wake mmoja juu kwa ishara ya kusalimu amri huku akianza kuchutama ili akae.

    “Mikono yote ioneka…” Brey alianza kufoka lakini hakumaliza, kwani ghafla Jarraar aliuchomoa ule mkono wake uliokuwa mgongoni kwake na kutupa kwa nguvu kitu sakafuni huku naye akijirusha pembeni, sanjari na mlipuko mkubwa mithili ya bomu uliombatana na moshi mwingi sana mle chumbani.

    “Heey!” Brey alimaka huku akijirusha pembeni na hapo hapo akamtupia risasi yule jamaa aliyoenekana kupotelea kwenye ule moshi mzito. Kutokea sehemu nyingine ya chumba kile Brey alimsikia Sandra akiachia yowe la uchungu likifuatiwa na kishindo kizito.

    Akachanganyikiwa. Taa iliyokuwa ikiwaka mle ndani haikusaidia kabisa kwa uzito wa moshi uliotanda mle ndani. Haraka alijitupa chini na kulala sakafuni, akihofia kurusha risasi bila uelekeo na kumdhuru Sandra ambaye alikuwa kimya isivyo kawaida. Hatua za yule muuaji zilisikika zikiruka kutoka kona moja ya chumba kile kwenda nyingine, miguno mizito ikasikika kama kwamba muuaji yule alikuwa akibeba kitu kizito, naye akajaribu kuelekeza bastola yake kule ambako vishindo vya mtu yule vilikuwa vikitokea, lakini sasa kitu kingine kikajitokeza. Ule moshi ukawa unamuwasha machoni.

    Shiit!

    Akaelewa mchezo aliochezewa, na akajua pale alikuwa mbioni kufanywa asusa bila hata ya kujiona.

    No way!

    Akaanza kumimina risasi hovyo kuelekea usawa wa alikohisi kuwa ndiko mlango wa kuingilia mle ndani ulikuwako, huku akiwa amefinya macho kujinusuru na moshi ule uchonyotao.

    Alisikia vishindo vya yule muuaja akikimbia kutoka mle ndani sanjari na mayowe ya woga wa wazi kutoka kwa wapangaji wengine mle ndani.

    Huko nje akasikia mlango wa gari ukifunguliwa na kubamizwa, kisha akasikia mvumo wa gari kubwa au lenye nguvu sana, ukiutangulia msuguanao wa matairi na ardhi, kisha sauti ya gari likiondoka kwa kasi.

    “Sandra!” Aliita kwa hamaniko.

    Hakukukwa na jibu.

    “Sandraaa!” Aliita tena, na bado hakukuwa na jibu.

    “Pumbaavu!” Alimaka huku akisota kwa tumbo kuelekea upande ambao alijua kuwa choo kilikuwepo ndani ya chumba kile. Alijitupa mle chooni na kuiwasha taa ya huko. Macho yalimchonyota naye akawahi kujiosha uso kwa maji, akijua fika kuwa muwasho ule ndio ungezi maradufu, lakini pia ungepungua baada ya muda mfupi. Alizidimkujiosha uso wake huku wazo moja tu likiruindima akilini mwake.

    Wale wauaji wamejuaje kuwa wako kwenye ile nyumba ya wageni?



    ____________

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alirudi mle chumbani akiwa na matarajio ya kukuta watu wawili, Sandra na yule muuaji wa kwanza aliyemchabanga risasi vizuri sana kifuani. Ule moshi ulikuwa umepungua, na alipigwa butwaa alipoona kuwa yule muuaji aliyempiga risasi hakuwemo mle ndani, ila Sandra alikuwa amesambaratika chali sakafuni, akiwa hana fahamu.

    “Shit!” Alilaani huku akiruka na kuurudishia ule mlango, kisha akaketi kitandani, akili ikimtembea. Safari hii alifanikiwa kuiona vizuri sana sura ya yule muuaji wa pili, na hakuwa na kumbukumbu ya kuwahi kukutana na mtu yule mahala popote hapo kabla.

    Ni kwa nini wale watu walikuwa wanataka kumuua hakuhitaji kujiuliza mara mbili, maana jibu alikuwa nalo wazi kabisa kichwani mwake. Walikuwa ni akina nani ndilo ambalo hakuwa akilijua mpaka kufikia pale.

    Alisonya huku akiinuka na kuchukua chupa ya maji ya kunywa iliyokuwa mezani mle chumbani na kummwagia Sandra kwa fujo. Baada ya kummwagia mara kadhaa binti alikurupuka kwa wahka na kutapatapa.

    “Tulia…tulia. Uko salama.” Brey alimwabia.

    “Hah…ni…nini kimetokea…?” Sandra alihoji.

    “Vaa nguo tuondoke upesi hapa…askari wanaweza kutokea muda wowote hapa.” Badala ya kumjibu, Brey alimwambia.

    Sandra alitukana tusi la nguoni na kuanza kuvaa haraka haraka.

    “Ilikuwaje? Nakumbuka ulisema utalala sakafuni…what happened?” Sandra alimuuliza.

    “Uliamini kuwa ningeweza kulala wakati najua tunawindwa?”

    “Dah! We’ kiboko…umakini wako umetuokoa leo. Mimi nilichoka sana…nikalala wakati we umeingia kuoga bafuni…” Sandra alimwambia.

    “Siamini kuwa katika mazingira kama haya ulidiriki kulala na chupi tu kama uko kwa mumeo namna hii wewe!” Brey alimkoromea.

    “Sina mume, kama ndilo ulilokuwa unataka kulijua…lakini kama ikitokea nalala na mwanaume basi hata chupi huwa sivai!” Sandra alimjuibu kwa kiburi, na kuishia kuguna kwa maumivu huku akijishika taya. Brey akaishia kutikisa kichwa tu.

    “Dah, yule mshenzi kaniotea ngumi nzito sana ya taya (akamtukania mama yake)” Alisema.

    “Na ile bunduki yake kaichukua…” Brey alisema. Sandra akazungusha macho mle ndani.

    “Inaelekea aisee…” Alisema.

    “Na ameweza kumbeba na yule mwenzake, akakimbia naye…mshenzi mkubwa!” Brey alisema.

    “Kafa…? Yule mwenzake?” Sandra aliuliza.

    “Mnh…sioni damu pale alipoangukia…” Brey almjibu.

    “Hawa ni watu gani lakini? Na wamewezaje kutuibukia hadi huku leo hii hii?” Sandra aliuliza kwa mshangao.

    “Hata mimi hilo ndilo linalonitatiza…lakini tuondoke kwanza hapa. Tutaulizana mbele ya safari…” Brey alisema.

    Walitoka nje ya nyumba ile ya wageni iliyojaa wateja waliogubikwa woga, kwa tahadhari kubwa.

    “Wapi sasa…?” Sandra aliuliza huku akionekana kuwa na mawazo mengi.

    “Sijui kwa kweli…lakini lazima tuwe kwenye mwendo, hatuwezi kukaa tu sehemu moja…”

    “Turudi kwenye gari letu basi…hatuwezi kuzurura tu mitaani kwa miguu usiku wote huu…”

    “Ongoza njia…”

    Walipofika sehemu waliyoegesha vyombo vyao vya usafiri, Sandra alimtaka amsubiri nje ya lile eneo la maegesho naye akaingia ndani kufuata gari. Dakika chache baadaye alitoka na gari lake, akaliegesha jirani na alipokuwa amejibanza Brey, kisha akateremka.

    “Nimemwambia mlinzi tutairudia pikipiki yako asubuhi kabla ya saa mbili…” Alimwambia huku akimkabidhi funguo za gari kwa mkono wake wa kushoto. Brey akamtazama kwa macho ya kuuliza.

    “Nini sasa…?” Alimuuliza.

    “Itabidi unisaidie kuendesha aisee…siko vizuri kabisa!” Sandra alimwambia.

    Bila ubishi Brey aliupokea ule ufunguo, lakini bahati mbaya Sandra akawahi kuuachia kabla hajaukamata vizuri nao ukaanguka chini. Brey akainana kuuokota.

    Akapokea pigo zito sana la kisogoni, mguno hafifu ukamtoka, na kiza kizito kikatanda mbele ya uso wake.

    Fahamu zikamhama bila kupenda.

    Sandra alimtazama akiwa amelala bila fahamu pale chuni huku akiwa ameshika spana nzito ya kufungulia matairi ya gari ambayo muda wote alikuwa ameishika kwa uficho nyuma ya mguu wake, kwa mkono wake wa kulia.

    “Samahani sana Brey…lakini imenibidi nifanye kazi yangu…” Alinong’ona huku akimtazama yule shababi aliyelala bila fahamu chini ya miguu yake.





    ________________



    Hakujua ni muda gani ulikuwa umepita pale ambapo hatimaye alifumbua macho. Alikuwa amelazwa chali kitandani kwenye chumba ambacho kilikuwa kinanukia harufu ya mchanganyiko wa dawa, jambo lililomjuza kuwa alikuwa hospitali.

    Mnh!

    Aligeuka huku na huko mle ndani lakini hakuona mtu. Akajaribu kuinuka akashindwa.

    Aka!

    Akainua kichwa chake kutazama sehemu ya miguu yake pale kitandani, na akamuona Sandra akiwa amejiegemeza kwenye kiti kilichokuwa moja kwa moja mbele ya kile kitanda ilhali miguu yake ameinyooshea juu ya kiti kingine kilichokuwa mbele yake, akiwa amejitanda shuka kiwiliwili chake.

    Alijaribu kuinuka tena, na akashindwa tena, na ndipo alipogundua kuwa alikuwa amefungwa pale kitandani kwa mikanda maalum iliyokatisha kifuani kwake, kiunoni kwake na miguuni kwake.

    Ebbo!

    Ina maana nimekuwa sina fahamu kwa muda wa kutosha kusafirishwa hadi mahala hapa na kufungwa namna hii bila hata kujijua? Sio kawaida hii!

    Alijiwazia, huku akijihisi kichwa kikiwa kizito, na kama ambaye alikuwa amelala na kilevi usiku kucha.

    Kumbukumbu ya kilichomtokea ikamrudia…ikazaa swali.

    Kwa nini?

    Hakutaka kupoteza muda kwenye kutafuta jibu la swali lile, kwani alijua fika kuwa katika mkondo wa fani aliyoingia…no, aliyojikuta ndani yake, usaliti, kugeukana na kulaghaiana ni mfumo wa maisha…ni sehemu ya utendaji kazi. Ilikuwaje Sandra akaweza kumlaghaika kirahisi namna ile hilo ndilo labda akipata wasaa atajaribu kulifanyia kazi. Anapoteza umakini wake? Alichukia.

    Pia hakutaka kupoteza muda kwenye kuchukia sababu ya kumfanya awe kwenye hali ile kwa wakati ule, bali alitaka kuangalia ni namna gani atajinasua kutoka kwenye hali ile…yoyote iwayo…aliyojikuta kuwamo baada ya kupoteza umakini ambao daima ndio umekuwa ngao yake muhimu.

    Kichwa kilimuuma sana sehemu ya kisogo.

    “Shit…” Aliwaza tena, “ …nimebondwa kichwani mara mbili ndani ya masaa machache tu siku hii…tena na huyu huyu mwanamke (akamtukania mama yake)”.

    Alijaribu kujigeuza pale alipokuwa huku akipeleka mkono wake kisogoni ili ajipapase pale alipobondwa.

    Hakuweza.

    Khah!

    Pamoja nakuwa alikuwa maefungiwa pale kitandani kw aile mikanda mipana, mikono yake pia ilikuw aimefunguwa pingu kwenye kile kitanda Dah!

    Alijikurupusha klwa hasira, zile pingu zilizokamata mikono yake pale kwenye kile kitanda cha huma zikatoa sauti ya kugongana na chuma cha kitanda kile na hapo hapo Sandra alikurupuka pale kwenye kile kiti, akilitupa pembeni lile shuka alilokuwa amejifunika na kuonesha bastola kubwa iliyokuwa mkononi mwake chini ya ile shuka.

    Akabaki akimtazama jinsi alivyokuwa amelala bila namna pale kitandani, akimtazama kwa ghadhabu.

    “Oh, umeamka…? Good!” Hatimaye alimwambia huku akimtazama kwa makini.

    Brey akajikukurusha tena kwa hasira pale kitandani.

    “Hebu tulia hapo, Brey Jabba!” Sandra alimtupia kauli huku bado akimtazama kwa makini.

    “Hebu fanya unifungue haraka sana, wewe!” Brey alimkoromea huku akigumia kwa hasira.

    “Kila kitu kwa wakati wake Brey…ndio maana nilipokufikisha hapa, hatukufanya papara, tulikusubiri uamke ndio tufanye yetu…”

    “Niamke? Nilikuwa nimelala mimi? Kama umesahau labda nikukumbushe…ulinipiga na kitu kizito kisogoni nikapoteza fahamu…na sio matra yako ya kwanza kunifanyoa hivi mimi wewe!” Brey alimkoromea kwa hasira.

    “Of course nilikugonga kichwani…lakini unadhani ungeweza kuwa umepotezxa fahamu kwa muda wote huu kwa vile nilivyokugonga kisogoni tu? Nilijaribu hivyo mara moja kule hotelini na nikaona ulivyotufanya…ilibidi nikudunge na sindano ya kukulaza pia…na ndio maana tulikuwa tukikusubiri uamke kwanza…”

    “Oh, okay mnisubiri, sio? Ukimaanisha wewe na jamaa zako akina Mukri, eenh?” Brey alimchachamalia.

    Sandra hakumjibu.

    “Siye wewe uliyekuwa ukijinadi mara kwa mara kuwa uko upande wangu, wewe…? Sasa what happened?” Brey alimuuliza tena huku akizidi kujikukurusha pale kitandani.

    “Shut-Up, Brey!”

    “Mlikuwa na nafasi nzuri ya kuniua, lakin mkaona mnifungefunge hivi na msubiri niamke, kwa hiyo kuniua sio lengo lenu kwa sasa…kwa hiyo nifungue tu!”

    “Okay…endelea tu kujichosha kwa kupiga mayowe.” Sandra alimjibu huku akitoka nje ya chumba kile.

    “Unafanya kosa kubwa sana wewe…hujui tu!” Brey alimkoromea zaidi huku akizidi kujikurupusha pale chini.

    “Potelea mbali!”

    “Ntakufanya kitu mbaya sana ujue wewe?” Brey alizidi kumkoromea, na hili lilimfanya Sandra afyatue kicheko kifupi.

    “Poa tu!” Alimjibu na kupotelea nje ya chumba kile ambacho kilionekana kuwa ni wodi ndogo ya hospitali.

    Brey akasonya.

    Alizidi kujikurupusha pale kitandani kwa muda, kisha akatulia. Akaamua kuwa mpole kusubiri hatima.



    _______________



    Jarraar alilitazama baka dogo jekundu lililojisajili kifuani kwa Mukri, akasonya kwa mara nyingine na kupiga ngumi kwa hasira ndani ya kiganja chake.

    “Hivi unajua kama si “Bullet Proof vest” uliyokuwa umevaa ungekuwa marehemu leo hii Mukri?” Alimwambia mwenzake kwa jazba iliyopea, akimaanisha kuwa kama si fulana ya deraya ambayo Mukri alikuwa ameivaa wakati wanakabiliana kwa mara ya pili na Brey Jabba basi muda ule angekuwa marehemu, na kabla mwenzake hajajibu lolote, akaendelea kwa jazba ile ile, “…yaani ngedere wa kitanzania angekuondoa wewe, Mukri Sudeiss, mwamba wa mauaji, duniani?”

    Mukri Sudeiss, muuaji mrefu na mwembamba sana, aliuma meno na kutazama pembeni, kisha akamgeukia mwenzake.

    “Sio mara ya wanza kwangu wala kwako, kunusuriwa na bullet proof vest kutokana na kifo cha wazi, Jarraar…” Alimwambia, lakini Jarraar alimkatisha kwa jazba ile ile.

    “Lakini kunusuriwa na bullet proof vest kutokana na risasi ya ngedere mweusi? Hapana aisee…hapana. Hili sasa limekuwa la kibinafsi zaidi kwangu. Huyu mtu sasa nataka mimi ndio nimuue…!” Jarraar alizidi kujazibika.

    “Hatuendi hivyo Jarraar…hii ni kazi na sio jambo lolote la kibinafsi…tunahitaji kujipanga upya na tuumalize huu mchezo turudi nyumbani…”

    “Na inatubidi tufanye hivyo haraka sana kabla hatujaipoteza na hii turufu tuliyonayo…inayotujuza kila anapokuwa. Tukiipoteza na hii basi ni vyema tu tukapanda ndege na kurudi nyumbani, tukarudishe hela za watu, na tukiri kuwa kazi hii imetushinda, bloody fools sisi!” Jarraar alizidi kupayuka kwa jazba.

    Mukri alifunua kinywa kutaka kusema kitu lakini akakosa cha kusema. Akaishia kutukana kikwao.

    Wauaji hatari wa kukodiwa walikuwa wameshikwa pabaya na kiumbe kitembeacho kwa jina la Brey Jabba…



    ______________



    Ambacho kwa wakati ule kilikuwa kikitumbua macho huku kikimtazama Sandra akirudi tena mle kwenye ile wodi ndogo akiwa ameongozana na mwanaume mwingine mmoja aliyekuwa amevaa mavazi ya kidakitari.

    “Mteja wetu ndio huyu kamanda…nadhani hatuna muda wa kupoteza sasa, madhali ameshaamka…” Sandra alikuwa akimwambia yule bwana.

    “Na wewe ndio nani bwana?’ Brey alimuuliza yule bwana ambaye kiumri alikuwa akilingana naye.

    “Niite dokta Muro…na niko hapa kwa kazi maalum tu ambayo ni wewe…” Jamaa alimjibu na hapo hapo akaanza kukisukuma kile kitanda ambacho Brey alikuwa amelalia, kilichokuwa kina matairi na kuelekea kwenye chumba kingine kilichofikiwa kwa kupitia kwenye mlango mwingine uliokuwa kwenye ukuta mmoja wa ile wodi ndogo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni nini kinaendelea hapa?” Brey alimaka kwa hasira.

    “Tulia Brey…hii inaweza ikachukua muda mfupi sana…” Sandra alimjibu.

    “Ni nini sasa hiyo ambayo inaweza kuchukua muda mfupi sana malaya wewe?” Brey alimkemea huku akibaini kuwa walikuwa wameigia kwenye chumba cha uchunguzi wa kitabibu, kikiwa na mitambo kadhaa.

    Hakuna aliyemjibu.

    Dokta Muro alikisukumia kile kitanda hadi kwenye mashine moja ambayo ilikuwa katika mfumo wa pipa refu la kioo. Akamdunga sindano fulani ambayo ilimfanya Brey awe kama amekufa ganzi maungo yote. Kisha akasaidiana na Sandra kumfungua ile mikanda aliyofungiwa pale kitandani. Sasa Brey alikuwa anaona kila anachofanyiwa lakini hakuwa na namna yoyote ya kujitetea. Hakuweza kuinua kiungo chochote. Hakuweza kuongea. Alibaki akitazama tu kila kinachofanyika dhidi yake bila ya yeye kuwa na namna yoyote ya kupinga au kubisha. Dokta Muro na Sandra walimbeba na kumlaza kwa taabu kidogo ndani ya lile pipa la kioo.

    “Okay Brey, tulitaka uone kinachofanyika kwako, ndio maana tulikusubiri mbaka uamke…naomba utazame kwenye ile skrini pale ukutani…” Dokta Muro alimwambia huku akipitisha mikono yake ndani ya lile pipa la kioo na kumgeuzia uso wake kule ambako luninga kubwa ilikuwapo.

    Brey akauona mwili wake pale kwenye ile luninga, lakini hakuweza kusema lolote.

    “Tunaanza sasa…” Dokta Muro alimwambia Sandra.

    “Okay…twende kazi!” Sandra alisema huku akimtazama Brey.

    No! Sandra, NOOO!

    Brey alimaka akilini, lakini kiywani hakuna kilichotoka.

    Dokta Muro akaanza kubonyeza vitufe kwenye kifaa kilichokuwa mithili ya kompyuta-mpakato kilichoungwa kwenye lile pipa pa kioo, na hapo miale ya ajabu ikaaanza kutembea mwilini kwa Brey aliyekuwa ndani ya lile pipa, huku vijimbinja vidogo vidogo vikisikika.

    OOH… NOOOOO!

    Brey alibwata kwa fadhaa akili mwake…





    ____________________



    Dokta Muro alikuwa amemakinika na kikichokuwa kikitokea kwenye ile skrini ndogo iliyokuwa kwenye kompyuta-mpakato iliyounganishwa na ile mashine iliyokuwa kwenye umbo la pipa la kioo, wakati miale ya rangi za buluu, nyekundu na ya mwanga ulioonekana kuwa kama ule utokao kwenye taa za kawaida za "energy saver", ikitambaa kwa kupanda na kushuka mwilini mwa Brey Jabba aliyedhibitiwa matendo na ile sindano ya kudumaza mwili.

    Brey na Sandra walikuwa wamemakinika na kilichokuwa kikionekana kule kwenye ile skrini kubwa iliyokuwa ukutani, ambayo ilikuwa inaonesha kile kile alichokuwa akikiona Dokta Muro kwenye ile kompyuta yake ya kupakatika.

    "Haileti maana hii kamanda Sandra..." Dokta Muro alisema huku akizidisha umakini kwenye kile alichokuwa akikitazama pale kompyutani, na kabla Sandra hajasema lolote, akaendelea, "...hakuna chochote kisicho cha kawaida mwilini mwake mpaka sasa...na kwa kawaida ndani ya dakika tano tu tungeweza kubaini iwapo ana kitu kama hicho ambacho unakihisi kuwa anacho..."

    Sandra akafyatua sauti ya kukereka.

    "Ni kweli haileti maana kamanda...lakini usemalo wewe ndilo ambalo halileti maana...huyu atakuwa ana tracking device mwilini mwake nakwambia! Hawezekani kila nilipokuwa naenda naye jamaa wanatuibukia..." Alimwambia kwa ubishi, akimaanisha kuwa Brey alikuwa ana kifaa cha kuweza kuonesha nyenendo zake zote, ambacho ndicho kilichokuwa kikiwawezesha wale wauaji kuweza kuwaibukia popote pale wanapokuwa naye.

    "Sasa jibu si sote tunalo hapa...? Kama angekuwa na hicho kitu dakika tano tu zingetosha kubaini..." Dokta Muro naye akazid kutetea hoja.

    "Tafuta hicho kitu kamanda Muro...!” Sandra alimkatisha kwa kukereka, kisha akendelea, “…wale maponjoro watatuibukia hapa hapa tusipokuwa fasta...kwani hiyo sindano uliyomchoma itaendelea kumdumaza kwa muda gani zaidi?” Sandra alimwambia kwa msisitizo na kumuacha na swali.

    “Ah, si zaidi ya dakika kumi…” Dokta Muro alimjibu huku akimgeuza kwa shida kidogo Brey pale kitandani na kumlaza kifudifudi.

    "Wacha tujaribu mara nyingine..." Alisema huku akibofya sehemu kwenye ile mashine yake na ile miale ikaanza tena kuivinjari sehemu ya nyuma ya mwili wa Brey.

    Miale ilitambaa mara ya kwanza, ya pili…na umeme ukakatika. Kiza kikatawala.

    “AAAAH K---NINA ZAO TANESCOOOO!” Sandra alimaka kwa ghadhabu huku akitupa mikono hewani.

    “Noo, lakini kuna jenereta…lingepaswa liwake mara mo…”

    KBBAAAM!

    “Aaaah…wamefika bloody vultureeees!” Sandra alimaka kwa hamaniko huku akijirusha pembeni, pale mlango wa kile chumba walichokuwamo ulipobutuliwa kutokea nje, na kwa mwanga hafifu uliokuwa ukitokea nje ya jengo lile kupitia kwenye moja ya madirisha ya mle ndani, akashuhudia vibomu viwili vikitambaa mle ndani huku vikifuka moshi.

    Kutokea alipokuwa, bastola ikachomoza ghafla mkononi mwa dokta Muro naye akajirusha pembeni huku akikisukuma na kile kitanda alicholalia Brey aliyedumazwa.

    Sandra alijipindua sakafuni, akaona mtu mmoja wenye mavazi ya kitabibu huku akiwa amejivika kifaa cha kujikinga na moshi usoni na machoni akiingia kwa kasi mle ndani huku akiwa ameinama na ametanguliza bastola mbele yake.

    “Pumbaaff!” Sandra akajirusha mzima mzima juu ya kile kitanda alicholalia Brey na kumlalia mgongoni yule jamaa huku kwa wakati huo huo akijisukuma mbele na kile kitanda.

    Kitanda kilisererekea kule kule mlangoni, Brey akiwa juu yake naye akiwa juu ya Brey, na kwa bastola mbili zilizokuwa mikononi mwake, moja kwenye kila mkono, Sandra akawai anaachaia mmiminiko wa risasi bila kuangalia. Kitanda kilimkumba yule jamaa naye akaenda chini kama zigo.

    Bastola ya Dokta Muro ikabanja mara moja, lakini yule mtu aliyekumbwa na kitanda hakuwa na haja naye. Alijiinua haraka kutoka pale chini na kutoka mbio kukifuata kile kitanda, akimuacha Dokta Muro akitapatapa kwa shida kutokana na ule moshi mkali.

    Sandra akajibamiza na kile kitanda kwenye ukuta uliokuwa kwenye kile chumba cha kwanza walichokuwa na Dokta Muro kabla ya kumuingiza Brey kule kwenye ile maabara. Akajigeuza haraka na kukisukuma kile kitanda nje ya kile chumba wakati akimuona yule muuaji akirudi mbio pale alipokuwa kutokea kule kwenye maabara. Akamtupia risasi mbili za haraka na jamaa akaenda chini bila kupenda, akijinusuru na zile risasi. Sandra akaenda hewani na kutua tena juu ya kile kitanda na kuserereka nacho kwenye korido ndefu ya hospitali ile iliyojificha maeneo ya Mbezi. Ndipo alipomuona muuaji wa pili akiwa amepiga doria pale kwenye ile korido. Jamaa hakuwa ametarajia kuona kitanda kikivurumishwa kutoka kule wodini namna ile, na kabla hajatanabahi, Sandra akamtupia risasi mbili, akamuona yule jamaa akisukumwa upande na kutupwa ukutani.

    “Kufa mwana kufa!” Alimaka kwa hasira. Kitanda kikajipigiza ukutani, kikayumba kabla ya kubingirika vibaya sana kwenye ngazi fupi zilizokuwa mwisho wa ile korido. Sandra alijipindua haraka na kumsukumia Brey nyuma ya nguzo ya zile ngazi naye akamlalia juu yake akiwa amekamata vizuri bastola zake, akiwa hana hakika amebakiwa na risasi ngapi. Akawa anasuburi yeyote ajitokeze kule kwenye mwanzo wa zile ngazi amuwashe.

    Kimya.

    Nhah?

    Alichugulia huku akitweta, tayari kuweka mkabala wa mwisho na wale wauaji kutoka mbali, lakini hakuna aliyetokeza.

    Mtego?

    Mtego gani huu…?

    “Sandra…!” Sauti iliita kutoka kizani kule juu.

    Dokta Muro?

    Akapiga kimya, akiwa makino sana, mayowe ya wahudumu wachache waliokuwa mle hopitalini muda ule wala hayakumsumbua. Alikuwa amemakinika na kile kilichokuwa kule mwanzo wa zile ngazi fupi.

    “Sandra…Dokta Muro hapa…uko…sal…salama?” Sauti ya dokta Muro ikamfikia, naye bado akapiga kimya. Alijua ule ni mtego. Wauaji walikuwa wamembana Dokta Muro…sasa walitaka wamtumie kumpata na yeye. Na hata lile wazo lilipokuwa likipita kichwani mwake, alimuona Dokta Muro akipepesuka pale juu ya zile ngazi na akizishuka kwa mwendo wa kusua-sua. Alikuwa peke yake.

    Ati??

    “Wamekimbia wale jamaa…mmoja kajeruhiwa…nahisi vibaya sana…!” Dokta Muro alisema kwa taabu huku akikohoa-kohoa. Sandra alizidi kumtazama. Dokta Muro alifika mpaka karibu na pale alipokuwa na bado alikuwa hajamuona.

    “Shit, where are you Sandra…?” Dokta alisema kwa hamaniko.

    “Right here, kamanda!” Sandra alimjibu huku akiinuka kutoka pale alipokuwa amejibanza.

    “Wamekimbia wale jamaa…!” Muro alisema.

    “Una hakika?”

    “Yeah…nimewaona wakibururana…mmoja amejeruhiwa…”

    “Yeah…nimemtwanga risasi (akamtukania mama yake)” Sandra alijibu.

    “Doh, afadhali…sasa hapa hapafai…tuondoke haraka!”

    “No…tumalizie zoezi letu kwanza…hichi kimeo alichokuwa nacho Brey kitatuua hiki…lazima kitoke leo hii hii!” Sandra alisema.

    Dokta Muro alimtazama kwa taabu kwenye kiza cha alfajiri ile.

    “Are you serious?” Alimuuliza.

    “Dead serious kamanda…! Fanya utaratibu wa kurejesha umeme hapa tumalizie hii kazi…!” Sandra alimwambia.

    “Dah, huyo jamaa…yu mzima huyo kweli?” Dokta Muro alimuuliza huku akimuoneshea Brey aliyelala pale chini kwa kidole.

    “Natumaini hivyo…” Sandra alimjibu huku wakisaidiana kumuinua Brey kwa shida. Brey alichezesha vidole tu vya mkono wake, akini bado hakuweza kujimudu.



    _____________



    Dakika ishiri baadaye hali ilikuwa imerudi kama ilivyokuwa hapo awali, ingawa taharuki ilikuwa bado imetawala maeneo mengine ya jengo la hospitali ile. Umeme ulirudishwa na Brey alikuwa ameamka lakini hakusema neno hata moja, pamoja na Sandra kujaribu kumsemesha mara kadhaa. ALikuwa amefura kwa hasira isiyosemeka.

    Pamoja na hivyo, alimuacha Dokta Muro aendelee na uchunguzi wake kwenye mwili wake, na ile miale ilipoipitia tena sehemu ya nyuma ya mwili wake milio ya mbinja ikabadilika na kuwa ya mfululizo, huku ile miale ya buluu na myekundu ikizungukia eneo moja tu kwenye mwili ule…sehemu ya nyuma ya mkono wake wa kushoto.

    “Bingo!” Dokta Muro alipayuka kwa furaha huku akiikuza ile sehemu ambayo ile miale ilikuwa imesongana, pale kwenye kioo cha ile kompyuta yake.

    “Si nilisema? Washenzi walikuwa wanamnyatia kila alipokuwa anaenda huyu jamaa kwa kutumia hicho kifaa…kitoe upesi!” Sandra alimwambia.

    “Sio kirahisi namna hiyo Sandra…” Dokta Muro alimwambia, akaendelea, “…hapa tumejua kuwa ni kweli ana hicho kifaa…sasa bado kujua ni kifaa cha aina gani, kiliwekwa vipi, na kitaweza kutolewa vipi…na iwapo kukitoa hakutakuwa na madhara kwake…bado sana hapa!”

    “Na muda huo hatuna…chunguza haraka tujue aisee…mi’ n’na jukumu la kutimiza kwake huyu bwana, kisha nirudi kwenye maisha yangu…” Sandra alisema.

    Hata pale alipokuwa akiongea namna ile, Dokta Muro alikuwa ameshalichana shati la Brey sehemu ya mkono, na ile miale ikawa inalimuika kovu moja dogo la mshono ulioonekana kuwa ni wa kawaida tu, uliokuwa sehemu juu kidogo ya kiwiko chake kwa nyuma na kuishia sehemu ya ndani ya sehemu itunayo ya msuli, maarufu kama “kiazi”, ya mkono ule.

    “Washenzi wamemshonea kifaa kwenye hili kovu…” Dokta Muro alisema huku akimsogezea Brey kwenye mashime ya x-ray. Akalisanifu kwa ukaribu zaidi lile jeraha, na kutokea kwenye skrini nyingine ya ile mashine ya x-ray, waliweza kuona kitu kidogo sana mithili ya punje ya mchele, ambacho kilikuwa kikimweka-mweka ndani ya mwili wa Brey Jabba.

    Sandra aliwatukana waliokiweka kile kifaa mwilini mwa yule jamaa wa sauti ya kunong’ona.

    “Kinaweza kutolewa?” Alimuuliza Dokta Muro, ambaye hakumjibu haraka…alizidi kukitafiti kwa muda kile kipunje cha ajabu kupitia kwenye skrini ya ile x-ray maalum.

    “Oh, yeah…kinatoka hiki. Itabidi niuchane tena huu mshono, kitolewe kisha ashonwe upya.

    “Okay, fanya hivyo sasa hivi dokta.” Sandra alisema.

    “No…kiache hapo hapo kilipo!” Kwa mara ya kwanza Brey aliongea, na wote dokta Muro na Sandra wakabaki wamepigwa na butwaa.



    ***DUH!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sandra alimtazama yule shababi aliyefura, kisha akamgeukia Dokta Muro.

    “Ana wazimu kidogo huyu?” Alimuuliza huku akimuoneshea Brey kidole. Dokta Muro akashawishika sana kukiri kuwa jamaa hakika alikuwa ana wazimu, lakini akajua vile sivyo hali ilivyokuwa. Brey hakuwa na wazimu, ila alihitaji kuufafanua ule msimamo wake.

    “Ah...wazimu sidhani, ila…” Alisema kwa mashaka na kumgeukia Brey, “…itabidi ufafanu…”

    Brey alichomoka kama mshale kutoka pale kitandani alipokuwa amekaa na kutembezea mapigo mawili mazito sana na Dokta Muro akaenda chini kama puto lililodungwa sindano.

    “Heeeeyy-khkkkk…!” Sandra alianza kumaka kwa kuona kitendo kile, lakini naye hapo hapo akaishia kukoroma huku ametumbukwa macho na akitapatapa hovyo.

    Brey aliporuka kutoka pale kitandani alimtandika Dokta Muro pigo lisilotarajiwa kwenye koo kwa ubapa wa kiganja chake kigumu, na Dokta Muro akabweka kama mbwa aliyeshtushwa wakati akipata haja huku akiinamisha kichwa bila kupenda, akipeleka mikono yake kooni, hapo Brey akamshushia pigo jingine zito zaidi sehemu nyuma ya shingo yake, mahala ambako shingo ilikuwa inaishia na kichwa kinaanzia, kwa ubapa wa kiganja chake kingine, na wakati yule tabibu akienda chini yeye alimrukia Sandra , akijua fika kuwa dokta Muro hatoinuka angalau kwa dakika zipatazo tano au saba zijazo. Sandra alishtukia akizabwa kofi kali sana la uso lililomuachia vimulimuli usoni, na kabla hajatanabahi, Brey akashika bega na kumzungusha kama anayetaka kucheza naye dansi, na kumpiga kabali kali sana kwa mkono wake wa kushoto huku akiwa ameibana shingo yake kwa nyuma kwa mkono wake wa kulia. Mawasiliano kwenye mishipa inayopitisha pumzi na oksijeni kwenda kwenye ubongo na kurudi yakamkatika ghafla Sandra. Moyo ukampoteza mapigo, akabaki akimkodolea macho dokta Muro aliyesambaratika bila fahamu pale chini huku akili ikimuwanga.

    Brey kawaje???

    “Inawezekana ulilolifanya lilikuwa ni la lazima na muhimu Sandra, lakini kunifanya nishindwe kujitetea mbele ya maadui wakubwa kama wale lilikuwa ni kosa kubwa sana…naona unataka kuniletea kiza kwenye maisha yangu wewe…siwezi kukupa nafashi hiyo kwa kweli. Kutokea hapa itanibidi niwe peke yangu kwanza!” Brey alimnong’oneza kutokea mgongoni kwake kwa sauti ya kuogofya.

    No! Brey, No! Usifanye hivyo…ilikuwa kwa faida yako mwenyewe…

    Sandra alimjibu…lakini ni kwa fikra tu, maana sauti haikumtoka asilani, na alihisi kichwa kikimuwia kizito.

    Brey alizidi kumkaba kwa kama dakika moja zaidi, na Sandra akatepweta mikononi mwake. Fahamu zikamhana.

    Akamlaza chini taratibu, kisha haraka sana akamsachi dokta Muro mifukoni na kuchukua funguo zake za gari. Akafurahi kuona kuwa zilikuwa zina “sensor” ambayo ilikuwa ina uwezo wa kuiloki gari hata kama akiwa mbali nalo. Aliwaruka wale washirika wake wa muda aliowapoteza fahamu na kutoka taratibu nje ya wodi ile.

    Akiwa nje, alienda haraka hadi kwenye eneo la maegesho ya magari ya pale hospitali. Akabofya sehemu kwenye kile kitufe kilichokuwa kwenye ufunguo wa dokta Muro, na kutokea sehemu fulani kwenye eneo lile la maegeshpo gari moja likapiga king’ora kifupi huku taa za njano za gari lile zikiwaka na kuzima mara kadhaa.

    “Okay, dokta Muro…ahsante kwa usafiri…” Alijisemesha peke yake huku akiliendea lile gari, na hapo alisikia ving’ora vya gari la polisi vikielekea upande ule ule wa ile hospitali. Bila kujali, aliingia kwenye lile gari na kuondoka kwa mwendo wa wastani.



    _____________



    “Una hakika na unayosema? Kuwa kuna majambazi yasiyojulikana yalivamia humu huku yakitupiana risasi…kisha yakatimua mbio kutowekea kusikojulikana?” Askari wa jeshi la polisi alikuwa akimuuliza dokta Muro kwa kutoamini. Dokta Muro alijichua nyuma ya shingo yake na kufinya sura kwa maumivu.

    “Ndivyo ilivyokuwa afande. Yaani yalivamia tu humu ndani, na mimi na mteja wagu hapa tukapigwa vikumbo vibaya sana…hata sijui ilikuwaje hata wakaingia humu ndani…” Dokta Muro alimjibu yule askari. Askari akamgeukia Sandra.

    “Hivyo ndivyo ilivyotokea bibie?” Alimuuliza.

    Sandra aliafiki kwa kichwa.

    “Ndi…ndio hivyo…ilikuwa ghafla sana…hata sikuelewa ni nini kilikuwa kinaendelea kwa kweli…nilipigwa kumbo tu nikajibamiza ukutani halafu nikaona kiza…nilipoamka ndio nikawa nasikia heka heka huko nje na mara na nyie mkaingia humu ndani…” Sandra alijibu. Hakutaka kujinadi hadhi yake kwa wale askarI ambao aliwaitakidi kuwa ni wadogo sana, kutoka kituo cha polisi cha kimara.

    Yule askari akajishika kiuno na kuwageukia wenzake wane aliofika no mle wodini. Nao hawakuwa na msaada wowote kwake. Akamgeukia tena Dokta Muro.

    “Sasa ni nani aliyepiga simu polisi…akidai kuwa hapa pamevamiwa na majambazi?” Akamuuliza.

    “Sijui, lakini hii hospitali ina wahudumu wengi…yeyote anaweza kupiga hiyo simu…”

    “Lakini wewe si ndiye mkuu hapa?”

    “Ndiyo..lakini kama nilivyosema, sikuwa kwenye hali ya kuweza kupiga simu…nahisi nami nilipoteza fahamu baada ya kupigwa makumbo na wale watu…nilipoamka nikaona huyu mteja wangu bado yuko chini bila fahamu…nikaanza kumhudumia.” Dokta Muro akadanganya zaidi.

    Askari wakagunaguna kwa muda, wakawapiga maswali mengine machache, wakaondoka.

    Muro na Sandra wakatazamana.

    “Nini kinafuata sasa?” Dokta alimuuliza mwenzake.

    Sandra akasonya.

    “Itabidi kumsaka huyu Brey sasa…sijui nitampataje tena sasa…atakuwa kwenye hatari zaidi yule, hajui tu!” Alisema kwa hasira.

    “Nadhani anataka akabiliane na wale watu yeye mwenyewe…”

    “Na hilo ni kosa! Sio swala lake kupambana na wale watu…sisi tungewapoteza wale watu kirahisi tu kwa kukitoa kile kifaa kutoka mwilini mwake, kisha tungemhamisha mji, basi…wasingeweza hata siku moja kujua ni wapi alipo. Lakini yeye….” Sandra alisema na kuiacha kauli yake ikielea tu hewani.

    “Anywy, Sandra…huko sasa ni kwenye idara yako. Mimi idara yangu ni hapa, ukimpata na kama akiwa tayari kuondolewa hicho kifaa, unajua pa kunipata. Naenda nyumbani mimi saa hizi…haya ya leo yamenitosha…” Dokta Muro alimwambia. Sandra akaguna.

    “Unajisahau kuwa na wewe ni afisa wa usalama, Muro? Huo utabibu unakupanda kichwani sasa, eenh?” Alimuuliza kwa maskhara.

    Muro alitabasamu kwa huzuni.

    “Hata kama nikitaka kujisahaulisha juu ya hilo sitafanikiwa, Sandra…good night!” Alimwambia huku akitoka nje ya wodi ile akimuacha peke yake mle wodini.

    “Unaendaje nyumbani sasa…na Brey ndo keshachukua gari lako…si umeona kuwa amekuchukulia ufunguo wa gari?”

    “N’taenda tu…hata kwa bajaji, gari najua litarudi tu…”



    ________________



    Saa moja baadaye Brey aliliegesha gari la Dokta Muro kwenye maegesho ya Mlimani City jijini Dar. Muda ulikuwa ni kama saa moja kasoro robo za asubuhi. Alijua kuwa kwa yale waliyokutana nayo usiku ule uliopita, wale wauaji wasingekuwa na uwezo wa kuibua zahma yoyote nyingine katika muda ule. Baada ya kuwa wameshashindwa kumuua mara tatu ndani ya ule usiku mmoja, hakukuwa na namna yoyote ambayo wangeweza kujifaragua kuyajaribu tena maisha yake ndani ya muda ule mfupi tangu kushindikana kwa lile jaribio lao la mwisho. Na kwa mujibu wa maelezo aliyoyasikia kutoka kwa Sandra na Muro, mmoja wao alikuwa amejeruhiwa, alishindwa kujizuia kumpongeza kimoyomoyo yule mwanadada kwa hilo, na ushahidi wa damu aliuana pale hospitali. Hivyo kwa vyovyote sasa watakuwa kwenye heka heka za kujiganga.

    Na yeye aliona ule kuwa ni muda muafaka wa kujiweka sawa kukabiliana nao, washenzi wakubwa.

    Aliliacha gari lile pale kwenye maengesho ya wateja wa pale mlimani city naye akatembea kwa mwendo wa kujiamini bila kujali nguo zake zilizochafuka, na kupita ubavuni mwa lile jengo, akazunguka hadi nyuma kabisa ya jengo lile ambako kulikuwa kuna nyumba kadhaa za kupangisha kwa kodi ya bei mbaya.

    Akifuata maelekezo aliyopewa awali, alienda moja kwa moja hadi kwenye nyumba iliyokuwa kwenye kona kabisa miongoni mwa zile nyumba za kupangishwa. Akaenda moja kwa moja hadi kwenye mtungi moja wa maua na kuubinua, akatoa ufunguo chini yake na kuutumia ufunguo ule kuingia ndani ya nyumba ile.

    Akajikomea kwa ndani.

    Aliivinjari ile nymba yote na kuona kuwa kila kitu kilikuwa sawa kama alivyoambiwa kuwa atakikuta. Akaingia bafuni na kuoga kwa muda mrefu. Kisha akainga jikoni na kukuta vyakula vya haraka vilivyokuwa kwenye jokofu kule jikoni. Alijiandalia mlo, akala. Kisha akafungua sehemu ya siri kwenye kabati la nguo lililokuwa mle ndani, akatoa bunduki moja fupi na nene. Aliizungukia tena ile nyumba na kuhakikisha kuwa milango yote na madirisha vilikuwa vimekomewa. Akiwa amevaa suruali ya pajama tu, alipanda kitandani na ile bunduki yake, akategesha saa yake imuamshe saa sita kamili mchana.

    Akalala.

    Wala saa sita haikufika…





    __________________



    Sandra hakuwa na ari ya kwenda kulala kama dokta Muro. Yeye alishapata lepe zito kabla ya ule uvamizi wa wale wauaji kule kwenye ile nyumba ya wageni iliyokuwa kule Kigogo, hivyo usingizi haukuwa tatizo kwake. Aliirudia ile skrini ya kompyuta ya dokta Muro ambapo bado ule uso wa kompyuta ile ulionesha kile ambacho dokta Muro alikikopi kutoka kwenye ile mashine ya x-ray maalumu, ikionesha kile kifaa cha kufuatilia nyenendo za Brey Jabba kilichokuwa ndani ya mwili wake. Alitoka haraka nje ya maabara ile hadi kule nje alipokuwa ameegesha gari lake. Alichukua mkoba wake mdogo na kurudi nao kule maabarani, ambako alitoa simu yake ya kisasa kutoka kwenye mkoba ule na kwa kutumia waya maalum wa simu ile, aliiunganisha kwenye ile kompyuta na kuinakili ile picha ya kile kifaa kikiwa mwilini kwa Brey, kwenye simu yake. Hapo hapo, kwa kutumia mfumo wa kutuma picha wa telegram, alimrushia mtu ambaye namba zake alikuwa nazo kwenye simu yake, kisha akampigia.

    Sam Kiranga, mtaalamu wa mambo yote yanahusiana na teknolojia ya mawasiliano na kompyuta kwa ujumla kwenye kitengo kidogo, cha siri na muhimu sana kwa usalama wa nchi na mataifa mengine, aliipokea simu ile akiwa bado amelewa usingizi.

    “Yah!” Aliropoka kivivu simuni, na Sandra akamchangamsha.

    “Angalia telegram yako wewe! Kuna picha nimekutumia…naomba uifanyie kazi halafu tukutane ofisini kwako baada ya saa moja…hili ni swala zito sana!” Alimwambia.

    “Acha hizo Sandra, in case huna habari, huku nchini kwetu saa hizi ni usiku…sa cjui huko kwenu wewe saa hizi ni mchana…? Hilo moja, halafu la pili, huku kwenye hii nchi niliyopo mimi huwa tunaoa wanawake ujue… kwa hiyo mimi ni mume wa mtu, huwezi kunikurupusha tu usiku-usiku na kunipangia miadi isiyo na kichwa wala mig…”

    “Hebu acha masihara huko saa hizi Kiranga! Hili swala ni priority red, ujue…” Sandra akamjia juu, na pamoja na kupenda kwake maskhara, Sam Kiranga akamakinika.

    “Priority Red?”

    “Sasa kumbe? Agana na mkeo uje tukutane ofisini kwako wewe…!”

    Sam Kiranga akacheka kwa sauti, na mkewe aliyekuwa amelala ubavuni mwake akagutuka, akamuuliza kulikoni.

    “Ah, ofisi imekumbuka kuwa eti na miye ni muajiriwa wao…natakiwa niende haraka sana, mke wangu…” Sam alimjibu mkewe huku akiinuka. Mkewe alisonya na kugeukia upande wa pili.

    “Wana wazimu ka’a nini hao nao!” Alisema.

    “Na mi’ kila siku huwa nawaambia lakini hawaamini…” Sam alimjibu mkewe huku akicheka, muda wote akijua kuwa Sandra bado alikuwa hewani na akiwasikia, kisha akaiweka simu mdomoni kwake, “Okay, wacha niicheki kwanza hiyo picha, kisha nitakuwa hapo in one hour, boss!”

    “We na mkeo wote hamnazo!” Sandra alimjibu na kukata simu. Sam Kiranga aliachia kicheko kingine.

    “Hebu kachekee huko bwana…nini?” Mkewe alikoromea, na jamaa likacheka zaidi huku likielekea sebuleni likiwa na simu yake mkononi.

    Ingawa alikuwa ni mtu muhimu sana kwenye kitengo nyeti cha mawasiliano na kompyuta kwenye idara ya siri na muhimu sana ndani ya usalama wa taifa, mkewe na jamaa zake siku zote waliamini kuwa Sam Kiranga alikuwa ni muajiriwa wa kituo cha utabiri wa hali ya hewa nchini, akiwa mtaalamu wa mawasiliani na kompyuta …

    Mara baada ya kumalizana na mtundu Sam Kiranga, Sandra alifanya mawasiliano na wakuu wake wa kazi, akieleza kwa ufupi lakini kwa undani, kile kilichotokea. Alilazimika kukiri kwa uchungu kuwa Brey Jabba aliwapotea akiwa kwenye himaya yake. Hili lilimuuma sana, lakini hakuwa na namna. Aliwahakikishia kuwa alikuwa anafanya kila liwezekanalo kurekebisha ile hali kabla haijawa mbaya zaidi.

    Baada ya hapo alirudi kwenye gari lake na kuelekea nyumbani kwake kwa ajili ya kujiandaa kwenda kukutana na mtaalamu wa Tehama, Sam Kiranga…



    _______________http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Wakati yote haya yanaendelea, Mukri naye alikuwa ana mashaka yake. Alimtazama mwenzake aliyekuwa amelala kwenye kochi refu mle ndani mwao kwa hasira. Jarraar alikuwa akigumia kwa maumivu makubwa hata baada ya kuwa alikuwa amefanikiwa kumtibia jeraha alilopata. Risasi ya yule mwanadada mkorofi ilikuwa imemchimba vibaya sana pajani na ilikuwa imeondoka na kipande cha nyama, ikimsababishia kupoteza damu nyingi.

    “Itabidi nikupatie daktari Jarraar…hii hali siyo nzuri, kwa kweli!” Alimwambia kwa msisitizo, na Jarraar akaguna kwa hasira iliyochanganyika na maumivu.

    “No…hamna haja ya daktari Mukri…! Madhali risasi haikukaa mwilini, na jeraha limeshasafishwa na kufungwa vizuri kama nilivyokuekeza…nitakuwa vizuri tu!”

    “Mnh! Sasa na unavyogumia namna hiyo kweli? Uko kwenye maumivu makali wewe, na…”

    “Ni ya muda tu haya. Kuwahusisha madakitari wa kitanzania hapa tutajianika bila sababu kwenye jamii Mukri…acha tu. Nitakuwa vyema baada ya muda…nipe vidonge vya kupunguza maumuvu tu, nilale kwanza!” Jarraar alisema.

    “Dah, sasa hapa ina maana itabidi tutulie kwa muda kwanza…” Mukri alisema.

    “Ndivyo ambavyo inatakiwa iwe…lakini sidhani kama wale watu wataendelea kuwa wajinga kiasi wasigundue kuwa tuna namna ya kuweza kunyatia nyenendo zote za yule mcheza ngoma mweusi aisee…wakilishitukia hilo na kuondoa kile kifaa mwilini mwake tutakuwa tumecheza pata-potea kubwa kabisa!” Jarraar alisema.

    “Kwa hiyo unaniambiaje…?” Mukri alihoji.

    “Ah, nadhani itabidi tuimalize tu hii kazi kwa taabu hivi hivi. Nadhani mimi mpaka kesho nitakuweza kutembea japo kwa kuchechemea…tutamuendea na kummaliza kiukweli this time, ila itabidi wewe ndio ufanye kazi kubwa, maana mimi ndio nimeshakwazika hapa…”

    “Tulishapitia hali kama hii huko nyuma Jarraar, kwa hiyo hilo sio tatizo sana…” Mukri alimjibu mwenzie.

    “Okay…nipe vidonge hivyo miye nilalale kwanza…ila usiache kufuatilia nyenendo za yule mcheza ngoma…”

    “No problem…” Muri alimjibu huku akimpatia zile dawa alizotaka, akilini akiwa ameshapitisha uamuzi wake binafsi…



    ________________



    Brey alishitushwa na mlio wa simu usiokoma. Mara moja akawa makini, akajibiringisha sakafuni kutoka pale kitandani akiwa makini na bunduki yake mikononi. Akautikisa usingizi kutoka mwilini mwake na kugeuza kichwa chake huku na huko.

    Simu iliyokuwa kando ya kitanda chake ilikuwa inaita kwa nongwa.

    Ah, ni nani huyu anayejua kuwa niko humu ndani muda huu?

    Kwamba walikuwa ni wale wauaji hilo halikumuingia akilini…wampigie simu ili iweje…kumtahadharisha kuwa akae mkao wa kufa wauaji waja? No way!

    Sasa ni nani?

    Alibonyeza kitufe kilichomuwezesha kuongea na mpigaji wa simu ile kwa sauti bila ya kulazimika kuunyanyua mkono wa simu ile ya mezani na kusikiliza.

    “Amm, mista Jabba…” Sauti nzuri ya kike ilimsemesha simuni.

    “Yah…nani mwenzangu?” Alihoji.

    “Aamm…utawala hapa…kulikuwa kuna mgeni wako hapa alitaka kuja kuonana nawe, ila tulitaka kujua kuwa ulikuwa una miadi naye ili tumuelekeze hapo kwako…” Mwanadada alimwambia. Brey akazidi kumakinika.

    “Sina ahadi na mtu yeyote kwa kweli…” Alianza kujibu.

    “Amesema nikwambie kuwa ana salamu zako kutoka kwa Mukri…” Yule dada alimwambia na Brey akamakinika mara dufu.

    “Mukri…?”

    “Yeah…amesema ukisikia hivyo utamkumbuka…”

    “Mpe simu niongee naye…” Brey alisema, akili ikimzunguka. Kimya kikapita kidogo, akisikia sauti zikiongea kwa mbali, kisha dada akarudi tena simuni.

    “Samahani mista Jabba…huyu mtu hata sielewi kwa kweli…”

    “Kwa nini?” Sasa Brey alikuwa ameshapandwa mzuka wa umakini.

    “Eti anasema kama huwezi kumruhusu aje kuonana nawe uso kwa uso anaondoka…”

    Wala Brey hakuwa akiendelea kumsikiliza…aligeuka nyuma haraka huku akijirusha pembeni baada ya kusikia sauti kali ya kioo cha dirisha la nyumba ile kikipasuka na jiwe likiangukia mle ndani. Akijua ni bomu, alijigaragaza sakafuni kuelekea kwenye kona moja ya chumba kile, na wakati huo huo kishindo kingine kikasikika kutokea mlangoni, akajitupa wima, akibaini kuwa kilichotupiwa mle ndani kilikuwa ni jiwe tu, akajibingirisha tena sakafuni kuwahi usawa wa jikoni ili awe mbali na chumba kile, lakini hata pale alipokuwa akijibingirisha namna ile alisikia sauti ya bunduki ikikokiwa kutokea kushoto kwake, naye akapiga goti huku akijigeuza na bunduki yake kuelekea upande ule.

    Akajikuta akiukodolea macho mdomo wa bunduki kubwa sana…na saa ya ukutani mle chumbani ikagonga saa tatu kamili asubuhi…





    _______________



    Mukri alimtazama Jarraar akitopea kwenye usingizi mzito baada ya kumeza vile vidonge vya maumivu na usingizi. Alimuacha akiwa amelala pale kochini naye akaelekea bafuni na kuoga. Kisha akaingia jikoni na kujitengenezea chakula, ambacho kilikuwa ni mikate tu na mayai ya kukaanga.

    Kwisha kupata mlo ule wa haraka, alitoa kompyuta yake mpakato na kuingia kwenye sehemu ya mawasiliano ya email, na kukuta email mbili kutoka kwa muwakilishi wa watu waliowapa kazi ile ya kumuangamiza mtanzania Brey Jabba. Email ya kwanza, ambayo wao hawakuwa wameijibu ilikuwa ikiulizia maendeleo ya kazi ile, ikiwakumbusha kuwa waalikuwa wameahidi kuikamilisha ndani ya wiki moja tu.

    Akasonya.

    “Sasa kwani hiyo wiki moja si bado haijaisha?” Aliikoromea ile email kwa hasira, ile ikiwa ni siku ya tano tu tangu waingie tanzania kwa ajili ya kazi ile tata.

    Email ya pili ilikuwa imeingia kiasi cha kama saa mbili tu zilizopita, ambayo ilikuwa inahoji kwa nini hawajamjibu email yake ya mwanzo, na ikaendelea kuhitaji majibu iwapo “mzigo” ulikuwa umesharudishwa kwa mwenyewe, ili awaingizie sehemu iliyobakia ya malipo yao kwenye akaunti yao, baada ya wao kumtumia ushahidi wa picha kuwa kweli “mzigo” ulikuwa umefikishwa “mahala pake”. Ulikuwa ni ujumbe wenye msimbo, ambao ni yeye tu na Jarraar ndiyo wangeweza kuusimbua kwa kuelewa ni nini yule muajiri wao alikuwa anaulizia.

    “Mzigo bado tunao…tutaufikisha mahala pake ndani ya siku mbili hizi.” Mukri aliijibu ile email kwa ufupi, akazima kompyuta yake na kubaki akiwa amekunja uso peke yake mle ndani.

    Huyu jamaa ni nani lakini? Kwa nini amekuwa mgumu sana kwetu kumuangamiza hivi?

    Hakuwa na jibu wala wa kumjibu. Aliiendea ile simu yao pana na kuibofya kwa utulivu uliomaanisha alikuwa ameshapitisha uamuzi…



    __________________



    “Hello loverboy…remember me?” Sandra alimuuliza Brey Jabba aliyeghadhibika, kwa maskhara huku bado akiwa amemuelekezea mtutu wa bunduki kubwa iliyokuwa mikononi mwake, akiwa amepiga goti moja pale ndani bila ya kujali kuwa na yeye alikuwa ameelekezewa mtutu wa bunduki kubwa iliyokuwa mikononi mwa Brey.

    “Inaelekea una uhaba mkubwa wa mabwana wewe (akamtukania mama yake), tangu lini mi’ nikawa loverboy?” Brey alimkoromea kwa hasira.

    “Hukufanya vyema kunizimisha namna ile kule hospitalini Brey…na hukufanya vyema kabisa kudhania kuwa sitaweza kukupata tena…hell, wameweza kukupata watu kutoka nchi za mbali huko, nishindwe mimi…?”

    “Kwa hiyo na wewe unafuatilia nyenendo zangu sasa kwa kutumia kifaa kilichopo mwilini mwangu?”

    “Hata bila hicho kifaa ningekupata tu wewe! Watu waliokufikisha hapo ulipo…waliokuwekea hadi hii nyumba…lazima wapate ushirikiano wa watu wengine kama sisi…huwezi kuwakimbia waliokuumba Brey!” Sandra alijitapa na kumsimanga. Brey akasonya.

    “Hakuna aliyeniumba mimi hapa duniani wewe…! Muumbaji wangu hawezi kuwa mtu kama wewe au hao unaowatumikia wewe…”

    “Hiyo yote ni kujidanganya tu Brey…ukweli ndio huo. Mungu kakuleta hapa duniani, sawa. Lakini hivyo ulivyo sasa…? Hivyo umetengenezwa na watu, Brey. Nami niko upande wa hao hao…kwa hiyo…”

    “Sema shida yako Sandra…nilikuwa ninalala mimi saa hizi…unataka nini?” Brey alimkoromea kwa hasira, akilini akijua kuwa yule binti hakuwa peke yake pale, kwani asingeweza kupasua kioo cha chumba chake kwa jiwe, na kisha hapo hapo awahi kuja kuupasua ule mlango wake kwa risasi na kuingia mle ndani namna ile.

    “Nataka nimalize kazi yangu Brey…nayo kwa sasa ni kukutoa hicho kifaa kinachoripoti nyenendo zako, na kisha kukuondoa hapa jijini kwenda mahala salama kwa uhai wako uliobakia hapa duniani…”

    “Nilipokwambia kuwa nataka niwe peke yangu kwa sasa…hukunielewa?” Brey alimuuliza.

    “Nilikuelewa…ila sikukubaliana na wewe…”

    KpBBAAH!

    “Ayyy…!”

    KbbBBUUM!

    Chhwaaaarrrr-Ttih!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yalaaa!”

    Ni mambo yaliyotoke haraka sana na yalipoisha Sandra alijikuta akiwa amedhibitiwa pasi kupenda, baada ya Brey kufyatua risasi na kulidungua chandelia lililokuwa likining’inia darini usawa wa pale alipokuwa amepiga goti, huku yeye akijitupa pembeni. Sandra alimaka huku naye akiachia risasi bila kutarajia, lakini kwa kuwa Brey alilitarajia hilo akawa ameshajirusha pembeni, na kabla Sandra hajalizamisha vizuri akilini tendo lililotokea, lile chandelia likamporomokea pale chini huku vile vijishanga vingi pamoja na balbu ndogo ndogo nyingi vikimmiminikia kwa fujo pale sakafuni, naye akalia kwa maumivu na mshituko, bunduki ikimtoka.

    Na Brey akawa ameshamrukia na kumbana pale chini, akiwa amemuwekea goti mgongoni na amemuwekea mtutu wa bunduki kisogoni.

    “Unachonga sana wewe!”

    “Aaaah…Brey…!”

    Brey alikuwa anatembeza macho yake huku na huko mle ndani.

    “Uko na nani mwingine hapa wewe?” Alimkoromea.

    “Tuko upande wako Brey sisi…”

    “Mko wangapi?” Alikoromewa.

    “Ah, acha hizo, Brey…aaauch!” Sandra alianza kumjibu lakini Brey akampiga kwa nguvu kisogoni kwa kitako cha ile bunduki yake, na Sandra akapoteza fahamu.

    Brey akaruka haraka hadi kando ya mlango wa kuingilia mle ndani, akajibanza. Mlango ulisukumbwa na mtu mwingine akaingia mle ndani huku amejikunja na ametanguliza bastola. Brey alimuwekea mtutu wa bunduki yake kichwani kutokea ubavuni kwa ule mlango.

    “Tupa chini hiyo kitu, wewe!” Alimkoromea.

    Bila ubishi Sam Kiranga akatii, akamgeukia taratibu huku akiwa amenyoosha mikono juu.

    “Wangapi wengine huko nje?” Brey alimkoromea.

    Sam akaachia tabasamu pana.

    “Man! Kumbe wewe ndiye mzee wa priority red? Amazing, man! Nimefurahi kukuona…mambo si ya kitoto mzee...”

    “WANGAPI??”

    “Hakuna! Hakuna…ni mimi na Sandra tu hapo…” Alipayuka huku akimuoneshea kidole mwenzake aliyelala bila fahamu pale chini.

    “Mi…mi ni mtu wa IT tu kaka….ndiye niyekitathmini hicho kifaa walichokuwekea mwilini mwako…hadi tukaweza kujua kuwa uko hapa…na hatukuwa na nia mbay...”

    “Shut up!”

    “Okay…” Sam aligwaya.

    Brey akaliendea lile kabati lake kwa uangalifu huku bado akiwa amemuelekezea mtutu wa ile bunduki, akatoa pingu mbili na kumrushia.

    “Mfunge pingu mikono kwa nyuma huyo…fasta!” Brey alimkoromea.

    “Oh, najua na mimi utaniambia nijifunge…lakini…”

    “Shut-Up!”

    “Okay, Okay…” Sam alimjibu huku akimfunga pingu Sandra, na wakati akiwa amemuinamia Sandra namna ile, Brey aliruka kwa hatua kubwa ya kimya na kumshushia kitako cha ile bunduki yake kwa nguvu kisogoni. Sam Kiranga akatoa mguno laini huku akimuangukia Sandra pale chini…



    _________________



    Saa mbili baadaye Mukri aliingia ndani ya jengo kubwa la biashara maarufu kama Quality Center, eneo la Nyerere Road. Kila kitu kilimuonesha kuwa mtu wao alikuwa ndani ya jengo lile. Alikuwa amedhamiria kuumaliza mchezo ule peke yake…akiwa amemuacha Jarraar kule nyumbani kwao amelala bila fahamu. Katika muda ule uliokuwa unaelekea mchana, eneo lile lilikuwa limechangamka kwa pirika za watu waliokuwa wakipita huku na huko. Aliitoa simu yake na kuitazama. Kidoa chekundu kilikuwa kimetulia sehemu moja tu, na kutokea pale alipokuwa amesimama ile hali ilimwambia kuwa mhusuka, au “mzigo”, kama anavyojulikana kwao na kwa muajiri wao, ulikuwa si zaidi ya mita kumi kutoka pale alipokuwa.

    Damu ikamchemka na mwili ukamsisimka.

    Alijigeuza taratribu huku na huko akijaribu kutafuta mahala windo lake lililopokuwa miongoni mwa raia wengi waliokuwa wakirandaranda katika eneo lile.

    Alienda hatua chache kulia huku akiiangalia ile simu yake, na kile kiduara kikafifia. Akarudi alipokuwa, nacho kikang’aa.

    Akaenda hatua chace kushoto, kikafifia. Akarudi alipokuwa na kwenda moja kwa moja mbele yake, nacho kikazidi kung’aa.

    Uko wapi wewe?

    Alijinong’oneza huku akiwa amemakinika. Kiduara kikawa kinamweka-mweka haraka haraka. Akajua mtu wao alikuwa karibu sana na pale alipokuwa. Akainua uso wake na kuona kulikuwa kuna lifti za kupandia juu ya jengo lile, moja kwa moja mbele yake. Akaisogelea, na kiduara kikazidi kuwaka na kuzimika haraka haraka.

    Yuko humu!

    Akasita. Lifti ilikuwa imebandikwa kibao kuwa haifanyi kazi, kwa lugha ua kiingereza.

    Lakini…inawezekanaje?

    Akaisogelea na kuibonyeza.

    Milango ya lifiti ikafunguka.

    Akamuona mbaya wao akiwa amesimama hali akiwa ameweka mikono mfukoni ndani ya ile lifiti pana…









    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog