Sehemu Ya Tatu (3)
Staf Sajenti Kubuta akiwa TRA, pale mkabala na ‘Long Room’ Sokoine drive alishangazwa na majibu ya afisa wa TRA pale alipofatilia usajili wa gari ile iliyotelekezwa na wale madhalimu. Kwani taarifa ilisema namba iliyoulizwa, usajili wake halali ni wa Power Tiller siyo Cresta Saloon kama alivyotazamia Staf Sajent Kubuta! Taarifa ile haikuwa njema kwa jeshi la polisi hata kidogo, kwani imezidi kuwaweka mbali na wahalifu wale! Lakini pia kwa Balaa walilolifanya Unguja nyumbani kwa Salma, na lile Balaa lililotokea Moroco alichoka sana! Akaona mtandao wa wale jamaa ni wa hatari zaidi ya sana! Kama wameweza kuweka namba za gari bandia, bima bandia, leseni ya barabara bandia, zote zikiwa katika usajili wa namba ya gari ile bandia! Hakika ni watu wenye dhamira mbaya sana kwa serikali na jamii! Lakini hata cheses namba ya gari ile Toyota Cresta, ilipofatiliwa ili kupata usajili wake halisi, majibu yake pia yaliendelea kutatiza! Kwani gari yenye Cheses namba ile haikuwahi kuingia nchini kupitia bandari yetu! Gari ile itakuwa imetembea na kuingizwa nchini kutokea nchi jirani!
Staf Sajent Kubuta aliona kuna jambo zito sana ambalo limejificha katika familia ya Simba Makupa na aliweka ahadi kuwa lazima aifatilie kwa undani ili kupata makoko na matandu ya usiri ule! Haiwezekani Balaa lote hili liwe ni bure hapana! Lakini hata bwana Simba Makupa tayari alikuwa ameshatekwa, na alishapulizwa dawa ya usingizi, ili waende nae mahala walipotaka, bila shaka kumuhoji na si ajabu kesho angekutwa katika fukwe ya bahari akiwa maiti! Staf Sajenti Kubuta aliwaza na kuwazua, akili yake ilikuwa inakaribia kuganda! Kwani hakuwa na yakini kwamba wale jamaa hasa makao yao makuu yapo wapi Unguja au Bara?! Staf Sajent Kubuta, alichukua ile taarifa akaondoka nayo kwenda kuifanyia kazi.
*******
Waratibu wasaidizi wa jeshi la polisi walikuwa wakipongezana kwa kumaliza vyema kozi zao zilizowachukua takribani miezi sita! Kwani katika muda wote ule wa miezi sita walikuwa chuoni pale Dar es salaam Police Academy (DPA) Chuo cha taaluma ya police Dar es salaam. Wakisomea kozi mbalimbali. Hivyo walihitimu vyema kozi za sheria ambazo ni Criminal Procedure Act (CPA) Law of Evidence (TEA) Penal Code pamoja na Police Adminstratar. Mbali na masomo ya sheria pia walisomea kozi ya Medani za kivita (MK) na mafunzo ya mapambano ya kujihami. Hivyo walijifunza Karate, Kung fu, Judo, Taekondo, Kombat, na aina tofauti za mapigano zisizopungua kumi! Masomo yao yote waliyosoma yatazingatia utendaji kazi katika jeshi la polisi (PGO) Police Jenaral Oder.
Wakiwa wanajipongeza mara akaingia mkufunzi wao, na utulivu ukapatikana. Yule Mkufunzi akawasalimia askari wale wa Nyota tatu, waliohitimu kozi yao na kuwapa taarifa ya kufunga kozi yao kuwa; “Tunamtarajia Mgeni rasmi atakaekuja kuhudhuria maafali ya leo ni Muheshimiwa Waziri wa mambo ya ndani ya nchini. Hivyo na IGP pia atakuwepo kwa hiyo kama desturi yetu nidhamu na ufanisi kwa askari watakaokuwa wanaonesha maonesho kwa viongozi wetu na hata wale watakaokuwa watazamaji, ni lazima iimarishwe!” Askari wale walitikisa vichwa kukubaliana na agizo lile! Kisha askari wale wakajiandaa vyema kwa mapokezi ya viongozi wale wa juu katika jeshi la polisi.
Baada ya muda mara ugeni uliwasili katika eneo lile lililokuwa limeandaliwa rasmi kwa shughuli ile, zulia jekundu lilikuwa limetandikwa, mahema yalikuwa yamepambwa vizuri, blas band ya polisi ilikuwa ikitumbuiza, na mara moja taratibu za kiitifaki zilifata viongozi wale pamoja na makamishina na maafisa wa polisi wa ngazi za juu, waliketi katika nafasi zao. na hatimae maonesho mbalimbali yaliyokuwa yameandaliwa yakaweza kuchukua nafasi yake! Kulioneshwa mambo mengi mbwa wanavyofanya kazi ya kuksaka na kukamata, kulioneshwa maonesho ya farasi anavyofanya kazi na askari, pia maonesho ya mapambano ya kivita yalifanyika. Ilipofika katika maonesho ya mapambano ya mikono ya ana kwa ana viongozi wale walivutiwa sana na umahiri wa askari wa kike aliekuwa akiuonesha mbele yao! Ilikuwa ni Komito, yaani mapambano ya mtu mmoja kupambana na watu wengi! Askari wa kike alikuwa anapambana na askari wenzake wakiume sita! Lakini hadi dakika tano zinamalizika hakuna hata askari mmoja aliefanikiwa kumuangusha askari Yule wa kike au kumdhuru kwa chochote askari yule shupavu, aliewiva vizuri katika sanaa ya mapambano ya kujihami! IGP pale alipokuwa alimuona askari Yule jinsi alivyokuwa shujaa na jasiri akikwepa ngumi na mateke kiufundi kabisa, hadi Muheshimiwa Waziri wa mambo ya ndani, IGP na jopo la viongozi wa jeshi la polisi wa ngazi mbalimbali wakapiga makofi kumkubali mwanadada Yule! Kwani kozi ile, hakika aliitendea haki. Kwasababu alikuwa mwepesi na hodari sana katika kuruka, kujipinda, kujipindua na kuchanganya mbinu tofauti. Yaani alibadilisha mitindo ya upiganaji kiasi ya tisa! Ni kwa vile pale alikuwa yeye anatakiwa ajihami kwa kukwepa tu, wala hakutakiwa kumpiga mtu katika maonesho yale! Lau kama ingekuwa na yeye anaruhusiwa kupiga, basi bila shaka watu wangevuja damu kama siyo kuvunjika kabisa!
Baada ya kumaliza maonesho yale na kufanywa taratibu zote zilizokuwa muhimu kiitifaki, kozi ile ilifungwa rasmi na Muheshimiwa Waziri wa mambo ya ndani ya nchi. Pia askari wale walipewa vyeti vyao vya kuhitimu kozi ile mmoja baada ya mwengine! Ilipofika zamu ya yule mwanamke aliekuwa anafanya maonesho ya mapigano kuchukua cheti chake, IGP akamwambia “ASP Jamila, baada ya hapa nikukute mesi muhimu sana!” ASP Jamila akaitikia “Sawa afande” pia akapiga saluti ya utii, akachukua cheti chake na kuelekea sehemu walipokuwa wamekaa wahitimu wenzake.
Baada ya mambo kufikia ukingoni, IGP aliingia Mesi akamkuta ASP Jamila, akiwa anamsubiri. IGP alizungumza nae kwa utuo, akampa mikakati na maagizo, na akatakiwa mara moja ayafanyie kazi maagizo yale kuanzia muda ule!
*******
ASP Jamila alipofika ofisini kwa IGP, alikaribishwa na kuketi kitako baada ya kutoa heshima kwa mkubwa wake. IGP Alimpongea ASP Jamila kwa umahiri aliouonesha kule katika maafali kisha akamueleza kwa kina kazi inayomkabili na majukumu yake. Akaelekezwa aende kwa Kamishina wa Oparesheni, ili akakabidhiwe vitendea kazi na kuweza kupata maelekezo ya ziada katika majukumu maalumu yaliyopo mbele yake!
ASP Jamila aliingia afisini kwa Kamishna wa Opareshen, akatoa heshima kwa Mkuu Yule. Akaketi kitini baada yakuamrishwa kuketi kitini na Kamishina. ASP Jamila alielezwa kadhia ile na Balaa lililopo mbele yake, lakini akitakiwa kujua kiini cha mauwaji yale, na wauwaji wote watiwe hatiani! Kila kitendea kazi alichokitaka katika kufanikisha kazi yake, alikabidhiwa! ASP Jamila alihoji maswali haya na yale, hatimae akawa amepata mukadima mzima wa kadhia ile ngumu na yahatari! Ila kwa kuwa ndiyo alikuwa ametoka masomoni, ari yakufanya kazi ilimjaa sana, akaapa kuifanya kazi ile kwa ufanisi mkubwa! ASP Jamila akiwa katika kutekeleza majukumu ya kazi ile, alitakiwa afanye kazi Tanzania bara na Tanzania Zanziabar. Mwisho aliagana na Kamishina, akiwa yupo kamilikamili kwa majukumu aliyopewa, mara moja akaingia kazini!
ASP Jamila aliingia katika ofisi yake aliyokuwa akifanyia kazi kabla ya kwenda kozi, akakutana na askari wenzake watatu, ambao ni Staf Sajenti Kubuta, Sajenti Magane, na Koplo Uzegeni. Alipoingia katika ofisi ile wote walisimama na kumpa salam za heshima. Nae akazipokea kisha akaketi katika kiti kimojawapo pale na kuwa tayari kwa kupokea taarifa za kiutendaji kutoka kwa wenzake, ambao tayari walishaianza ile kazi kwa siku chache zilizopita. Staf Sajent Kubuta, alipewa taarifa kutoka kwa mkuu wa Oparesheni kuongezwa jembe muhimu katika kufatilia kesi ile, hivyo hata walipokuwa pale ofisini walikuwa wanamsubiri kiongozi wao ambae yeye Staf Sajenti Kubuta, alishawahi kufanya nae kazi katika ile kazi ya Barua kutoka Jela. Hivyo anamfahamu utendaji kazi wake, kuwa ni mtu muhimu na hatari ambae alikuwa ni lazima kwa opareshen kama ile awemo! ASP Jamila alikabidhiwa jalada la kesi ile na Staf Sajenti Kubuta. Kisha pia akapewa maelezo ya mdomo ya tangu mwanzo mambo yalivyojitokeza hadi kufikia wakati ule! ASP Jamila alisikiliza kwa makini taarifa ile, kuna sehemu ilimsisimua, kuna sehemu ilimsikitisha, mwisho akawa anapicha kamili, ya nini kilichotokea, na kipi kifanyike. Hivyo mara moja akasema.
“Simba Makupa, pamoja na Salma Machano ambae sasa ni kizuka wanapaswa kuhojiwa kwa kina! Kwani kuna sababu za msingi hapa si bure! Pia taasisi aliyokuwa akifanyia kazi Marehemu Haruna Makupa, haitoshi kuwa walimpa mshahara wake wote na stahili zake zote, wakati wamemuachisha mtu kazi kabla ya muda wake kufika, iachwe hivihivi hapana! Lazima tuichunguze na kuifatilia kwa karibu sana ili tuone kama kuna chochote tunachoweza kukipata cha maana!” ASP Jamila alimaliza kauli yake na wale askari wote akawa wanatikisa vichwa vyao kwa kukubali mawazo chanya ya kiongozi wao!
“Mzee Simba Makupa, kwa taarifa ya madaktari anaendelea vizuri, muda wowote anaweza akaruhusiwa kutoka hospitali, kwani amewekewa dripu nyingi za kuweza kumfanya aamke haraka, sanjari na hilo alichomwa sindano ambayo itavunja nguvu ya ile dawa ya usingizi aliyopuliziwa nayo usoni, katika kumzimisha bila shaka asiwape bugudha yoyote wakati wakimpeleka huko walipopataka!” Staf Sajenti Kubuta alizungumza kuhusu hali ya Mzee Simba Makupa inavyoendelea! ASP Jamila akapanga mbinu mpya alizotoka nazo chuoni, kila mtu akakabidhiwa jukumu lake, na kitendo bila kuchelewa wakaingia kazini kwa pamoja, kila mtu akielekea pande yake katika kutimiza kazi iliyopo mbele yao!
Mtaa wa Swahili katika wilaya ya Ilala mkoa Dar es salaam ulikuwa unapitika kwa tabu. Magari ya daladala, yalikuwa yakiibia kupita njia ile inayo kutana na barabara ya Morogoro, na barabara ya umoja wa mataifa, yakitokea mtaa wa msimbazi kutokana na foleni kubwa ya magari katika eneo la Kariakoo. Mtaa ule wa Swahili katika nyumba za kati ukiupita mtaa unaokutana na mtaa wa Swahili ambao ni mtaa wa Rufiji. Turubai bado lilikuwa halijatolewa na pazia ya mlango wa mbele wa nyumba ile iliyokuwa na misiba miwili! Bado ilikuwapo mlangoni. Katika Uwa wa nyumba ile, kina mama walikuwa wanahangaika kuchoma maandazi ya takhtimu, iliyokuwa inatarajiwa kusomwa kwa ajili ya kuwaombea dua marehemu Haruna Makupa, na mwanawe Mauwa Simba Makupa! Wakina mama wengine walikuwa wakipika tangawizi, wengine walikuwa wakiosha vyombo, ilimradi kila mwanamke aliekwenda katika nyumba ile ya msiba, alikuwa katika kufanya kazi za kujitolea kama jirani mwema, au jamaa au ndugu wa familia ile.
Katika chumba cha ndani, upande wa kushoto kulikuwa na mwanamke maashaallah alievalia baibui zuri kutoka Dubai. Kichwani kwake alijifunga kilemba kinzanzibar! Kile kilemba kinachofunika kichwa na kuuwacha uso tu ukiwa wazi, ilihali masikio na nywele vyote vikiwa vimestiriwa! Usoni mwake alikuwa amevaa miwani pambe nyeusi na pana iliyomkaa vyema katika uso wake. Hakika alikuwa akionekana kama halati au banati wa mabanati! Ajabu ya mwanamke huyu hakuwa analia! Wala hakuwapo katika msiba ule wakati wa mazishi! Alikuwa katika chumba ambacho Kizuka mke aliefiwa na mumewe alipo. Yule Kizuka Salma binti Machano, alikuwa amevaa nguo nyeusi tupu! Alikuwa mnyonge kupita maelezo. Alikuwa amejiinamia akiwa na wingi wa tafakuri katika ubongo wake!
“Pole dada kazi ya Mungu haina makosa, sote sie tutakwenda huko. Safari yetu ni moja. Kinachogomba ni utangulizi tu!” Yule dada aliekuwa amevaa miwani na Baibui la bei mbaya, alikuwa akimfariji Salma Machano.
“Asante dada ingawa bado sijapoa! Kwani pamoja na kufiwa na mume, lakini na mimi pia nipo katika hatari ya kuuwawa! Hata Shemeji Simba tumepata taarifa juzi alitekwa walipomaliza maziko, na alikuwa tayari akauliwe! Mie nimekoswa na risasi sa…..!” Salma hakumaliza kauli yake, kwani dada mmoja aliekuwa pembeni yake aliekuwa amevaa dera, WP Monica alimfinya asizungumze jambo lile! “Vipi dada mbona umenyamaza ghafla?! Kuna nini unachochelea kusema?! Yule dada aliekuwa akimliwaza mfiwa alimsaili Salma!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“WP Monica kutoka Zanzibar, mie ndiye niliemzuia kusema hayo! Kwani bado tupo katika upelelezi hivyo si busara kuelezwa kila mtu jambo hili! Tunashukuru kwa pole yako, muache Kizuka apumzike, kwani bado akili yake haijakaa sawa!” WP Monica alisema maneno yale kumwambia Yule dada halati, na kumkazia uso! Lakini kinyume cha Yule dada halati aliekuwa akiambiwa maneno yale, hakuonesha kubabaika, wala kuacha kuendelea kudadisi! Badala yake Yule dada alimjibu WP Monica.
“Naitwa ASP Jamila, hapa nipo kikazi zaidi!” Afande Jamila alisema maneno yale huku akitowa kitambulisho chake na kukionesha! WP Monica alisimama akatoa heshima kwa mkuu wake, kisha akawa mpole mara moja! ASP Jamila aliitikia salamu ile, kisha akasema. “ Samahani wazazi wangu, dada zangu, na wadogo zangu. Nawaomba mtoke nje kidogo nibaki na WP Monica na Mfiwa, kwani kuna mambo ya kiusalama nataka kuyazungumza na Kizuka! ASP Jamila alisema maneno yale huku akiwatizama wale watu waliokuwa wamejazana mle chumbani kwa Kizuka, wakimfariji! Na wote hawakupinga walitoka nje wakawaacha wao ili wafanye mambo yao!
“Bi Salma. Naomba uniambie ni sababu ipi hasa ambayo wewe unadhani ndiyo iliyopelekea balaa lote hili kutokea?!” ASP Jamila alianzisha mahojiano mara moja, huku akiwa ameitoa miwani yake machoni, na kuipandisha juu kichwani, lakini ikiwa usawa wa mzungumzaji Bi Salma Machano!
“Mmmmh wallahi hata mie hapa kichwa kinaniuma sana! Kwani marehemu mume wangu alirudi kazini katika siku yake ya mwisho ya kuwa kazini, akiwa hana raha hata kidogo! Nilipomuuliza kulikoni upo hivyo? Akanijibu kuwa niliyoyaona leo kazini, sina muda mrefu, nitapoteza maisha yangu! Lakini ni bora nipoteze maisha kuliko kuwapa! Kila nikimuuliza kuwapa nini, au umewachukulia kitu chao kipi? Alinijibu kuwa laita kama angekuwa amewaibia, basi wangempeleka polisi! Lakini kinyume chake wamemlipa pesa yake kabla mkataba wake kumalizika, na wamempa stahiki zake zote! Pia akawa anasema kuwa mimi ni mwanamke siwezi kukaa na siri! Hivyo akaamua anipeleke nyumbani kwetu Pemba kwa siku tatu! Yeye akidai kuwa anataka kuhakikisha kuwa Siri aliyokuwa nayo, inafika katika sehemu aliyoikusudia! Hivyo mimi baada ya kurudi kutoka Micheweni Pemba, nilishangaa kuona chumbani kwetu huyu bwana amepiga sakafu mpya! Nilipomuoji akaniambia ametengeza nyumba yake kaamua kuanza na chumba na pengine kutafatia!” Salma Machano alitulia kidogo akameza mate, huku akiwatazama wale askari wawili waliokuwa hawana sare mle chumbani walimokuwa.
“Ok Salma umesema huyu bwana alikuambia kuwa ameona jambo ambalo anadhani hana muda mrefu atauwawa kwani mumeo alikuwa akifanya kazi gani na wapi?!” ASP Jamila alimsaili Yule mke wa marehemu huku akiwa makini zaidi.
“Mume wangu alikuwa akifanya kazi katika taasisi ya kibinafsi, inayoshughulika kutoa na kutuma mizigo duniani, hapa Unguja ofisi yao ipo Shangani. Yeye alikuwa akifanya kazi kama mtu wa IT kwani taasisi ile ina matawi yake Mombasa, Somalia, na Africa ya kusini, panoja na nchi za falme za kiarabu!” Salma alijibu jibu lile, huku akiwa hajui kama moyo wa ASP Jamila alikuwa anaupeleka mbiyo kuliko kawaida!
“Je baada ya kurudi Pemba nakukuta mabadiliko hayo, marehemu mumeo alikwambia kama hiyo siri yake ameshaitoa huko mahala alipopakusudia?!” ASP Jamila alimuuliza Salma huku akimtizama usoni mwake.
“Nilimuuliza ili anipe habari hiyo, lakini akasema huku Unguja, hana mtu anaemuamini kabisa! Ila amewasiliana na kaka yake shemeji Simba, ingawa na yeye pia hakumuambia hiyo siri, akamtaka aende Unguja ili akamkabidhi/kumwambia hilo jambo. Semeji akamjibu ana mambo mengi ila angemtuma Mauwa aende kuchukua! Hata Mauwa alipokuja alilala siku mbili ya tatu akamsindikiza, akimpa na huo mzigo! Ili aulete kwa shemeji, lakini ndiyo hata nyumbani hajafika ameuwawa!” Salma aliposema maneno yale sasa machozi yalimlengalenga! ASP Jamila hakujali machozi yale akamtupia swali lingine.
“Wakati Mauwa akikabidhiwa huo mzigo wewe uliuona huo mzigo? Namaanisha ulikuwepo katika makabidhiano yao?!” ASP Jamila alikuwa yupo makini na mawali anayouliza. Salma akamjibu. “Mimi nilikuwa na shauku kubwa sana yakutaka kuona huo mzigo, lakini Yule bwana alitoka na mauwa akiwa na bahaha mkononi, kitu kilichokuwamo ndani hakika sijakiona, akaniaga kuwa anamsindikiza Mauwa bandarini, na ule mzigo na kwamba akirudi tutakuja kuongea, lakini ndivyo hivyo tena siyo Mauwa wala Bwana Haruna alierudi nyumbani salama!” Salma sasa akawa analia kwa kwikwi, na WP Monica akambembeleza, huku ASP Jamila, akimtazama usoni! Baada yakutulia kulia, maswali yakaendelea!
“Kama mzigo marehemu Mumeo alimpa mwanawe, na mwanawe ameuwawa kabla ya kufika nyumbani, na mumeo nae pia ameuwawa! Hii maana yake ingenipa picha kuwa mzigo ushapokwa! Ila kitu kinachonipa tabu kichwani mwangu, mbona bado hao wahalifu wamekuja kwako, wewe ukiwa polisi wakapekua nyumba yako, na hata kutaka kukuua? Lakini hata Bwana Simba nae alichukuliwa bila shaka nae walitaka kwenda kumuua? Ndiyo maana akili yangu inanambia ni zaidi ya mzigo! Au bado huo mzigo haujapatikana na walengwa! Au kuna watu tofauti wanaoutaka huo mzigo? Sasa maswali yananiandama kemkem, je ni mzigo gani, na upo wapi?!”
ASP Jamila aliendelea kumsaili Yule Kizuka, hadi alipotosheka kwa majibu aliyoyapata, kisha akasema, WP Monica kesho tutakwenda sote Unguja nyumbani kwa Bi Salma, kuna kitu nataka nikahakikishe, hapa ataletwa askari mwengine, ili kumlinda Salma sawa?!” WP Monica akajibu huku akiwa mkakamavu “Sawa afande” Na ASP Jamila akaendelea,
“Salma kesho asubuhi atakuja askari mwengine hapa kuwa na wewe, naomba mpe funguo za nyumbani kwako WP Monica, ili tuweze kuingia na kuona hali halisi , lakini pia kama nilivyosema awali, kuna jambo nataka kwenda kulihakiki!” Salma alitikisa kichwa chake juu chini, kuashiria kukubali jambo lile. ASP Jamila aliwaaga akateremsha miwani yake katika macho yake na kutoka. Huku nyuma macho ya wanawake wenzake, yalimtizama kwa jinsi Maashaallah alivyopendeza, wale watu waliokuwa mle chumbani kwa Kizuka wakati ASP Jamila alipoingia, walisambaza uani kote kuwa Yule dada ni askari, hivyo wanawake wale wakawa makini katika kumtizama.
*******
Hospitali ya taifa ya Muhimbili, watu walikuwa wakipishana huyu anatoka na Yule anaingia, huyu kabeba hiki na Yule kabeba kile, huyu anatoka na kilio, yule anatoka na kicheko! Katika wodi maalum pale Kibasila, Staf Sajent Kubuta alikuwa na Sajent Magane, wakiwa na mgonjwa wao Bwana Simba Makupa, walikuwa wanamsubiri dakitari aje kuwaruhusu, lakini pia awape ripoti ya mgonjwa wao. Nusu saa baadae dakitari aliwafata na kuwapa ripoti, pamoja na kuwaruhusu kuondoka na mgonjwa wao! Mzee Simba Makupa alikuwa anaendelea vyema, ingawa alikuwa amegubikwa na unyonge sana. Walishusha ngazi wakatoka nje walipoegesha gari yao, wakapanda na safari ikaanza ya kwenda ofisini kwao. Walipofika ofisini kwao maswali yakaanza mfululizo kwa Bwana Simba Makupa! “Bwana Simba unaweza kutujuza kuwa Mauwa alikwenda kwa jambo gani Unguja?” Mzee Simba Makupa, alitikisa kichwa chake juu chini kuonesha anajua, kisha akasema.
“Mwanangu Mauwa nilimtuma aende Unguja, baada ya ndugu yangu kunambia kuwa anamzigo muhimu sana, anataka aupeleke katika vyombo vya sheria. Hivyo alinitaka mimi ndiyo niende huko, lakini nami nilikuwa na pilikapilika nyingi, hivyo nikamwambia nitamtuma Mauwa huko ili ampe huo mzigo ili anifikishie, kisha yeye aje ili twende sote huko alipopataka mdogo wangu. Mauwa akenda bila shaka nadhani huo mzigo atakuwa amempa, lakini ndiyo hivyo kwangu hajafika Mwanangu akauwawa, na mdogo wangu pia nae hakurudi nyumbani kwake akauwawa! Bwana Simba Makupa alisema maneno yale huku akiwa na uchungu tele moyoni mwake!
“Labda nikuulize namna hii, je?! Ulikuwa unajua mzigo aliokuwa anakwenda kuchukua Mauwa? Na kwa nini aulete huku, wakati Unguja kuna askari, mahakama, na dola kamili?!” Sajenti Magane alimsaili mzee Simba Makupa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wallahi sifahamu huo mzigo ni mzigo gani! Lakini hata mimi pia niliwahi kumuuliza kwamba, kwa nini huo mzigo au kama ana taarifa asizipeleke polisi kule alipo, akanijibu kuwa lile ni jambo zito sana, hivyo askari wa Unguja amekosa imani nao!” Mzee Simba Makupa alijibu swali lile nakuwafanya askari wale watizamane kwa majibu yale! Wote wakaingia katika tafakuri nzito sana.
“Sawa Mzee Simba, je unaweza kutuambia wale jamaa walipokuchukuwa pale makaburini, walikuwa wakikuuliza nini mkiwa mle ndani ya gari yao?!” Staf Sajenti Kubuta alimuuliza swali lile Mzee Simba huku akiwa makini kusikiliza jibu lake!
“Mie nakumbuka kuwa nilipokuwa mle ndani ya gari, tulipofika pale faya, Yule Bwana alievaa kanzu alisema twendeni hadi Magomeni tukachukue mchele dukani kwake na mafuta, ili vije kutusaidia msibani nami sikuwa na ubishi! Ila tulipofika jangwani wale jamaa wote watatu wakatoa vitambaa vyao mifukoni mwao, kisha wakafunika pua zao. Mie nikiwa nashangaa jambo hilo, Yule bwana aliekuwa amevaa suti, alitoa kopo dogo kama la dawa ya mbu akanambia Simba unaijua hii? Mimi nikageuka ili niitazame vizuri, nilipogeuka na kuitazama Yule jamaa aliibonyeza ikaspray usoni mwangu, pumzi zikakata kwa kweli sijafika hata mapipa nguvu zikaniishia, macho yakawa mazito, mdomo ukawa siwezi kusema neno, hatimae kiza kinene kikatanda usoni kwangu! Kuanzia hapo sikujua tena kitu chochote kilichokuwa kikiendelea, hadi nilipozinduka na kujikuta nipo hospital.” Mzee Simba Makupa, alisema maneno yale huku akiwatizama wale askari waliokuwa wapo makini sana kwa kila taarifa iliyokuwa ikitolewa kwao! Wakaendelea kumuhoji hadi waliporidhika kwa waliyoyapata, wakampa mikakati ya kuishi hivi sasa kwani atakuwa akiwindwa na wale madhalimu, hasa baada yakujua kuwa atawafahamu akikutana nao tena kwa mara nyingine! Mwisho wakampeleka hadi nyumbani kwake mtaa wa Swahili.
*******
*******
Askari wale wakiwa na kiongozi wao ASP Jamila, walikuwa wamekaa ofisini kwao wakijadili taarifa walizozipata kama mikakati yao walivyoipanga. Kuwa yule mtu na shemeji yake wahojiwe kila mtu kivyake, tena kabla Mzee Simba hajarudi nyumbani kwake kutoka hospitali, ili kuondosha uwezekano wa kuyapanga maneno!
Asp Jamila aliwasikiliza wale askari kwa makini, maelezo yao kwa namna walivyomuhoji mzee Simba Makupa! ASP Jamila alitowa miwani yake, pale baina ya kioo na flem ya miwani ile, alichomoa card ndogo mithili ya Memory Card ndogo za simu, akaichomeka card ile katika card Reader, akaipachika katika kompyuta iliyokuwa mle ofisini kwao, na kuifungua ile Card Reader nayo ikafunguka! Yakaonekana mahojiano yote aliyokuwa akimuhoji Salma binti Machano, sanjari na kusikia pia sauti ya mahojiano yale kwa sauti tena ya stereo, isiyokuwa na mikwaruzo! Baada ya kuona na kusikiliza mahojiano yale, sasa wakawa wanayachambua kwa umakini mkubwa ili kupata pa kuanzia! Walijadiliana haya na yale, hatimae wote walikubaliana kuwa kutokana na majibu ya maswali yale, kutoka kwa mtu na shemeji yake, chanzo cha Balaa lote lile inaonekana limeanzia Unguja!
Huku bara limeenea kwa kuwa nayo pia ni familia ileile ya ya Bwana Makupa! Wote wakakubaliana kuwa pamoja na Unguja napo kuna timu ya maaskari inayofanya kazi katika kesi ile, lakini pia na wao lazima waende ili wakabadilishane uzoefu, lakini pia wafike alipokuwa akifanya kazi marehemu Haruna. Waende wakawahoji watendaji wao sawasawa, wachunguze kuna nini katika ofisi zile kisha wakutane kule madema kwa uchambuzi zaidi! Kikao chao kile kiliamua askari wawili ASP Jamila pamoja na Staf Sajenti Kubuta ndiyo waende Unguja, wakati Sajenti Magane, na Coplo Uzegeni wao watabaki wakiwa makini sana pale katika nyumba yenye msiba kwa Mzee Simba Makupa. Naam mawasiliano yakafanyika, Kamishina wa Zanzibar, alifahamishwa ujio wa watu wale, nae akatoa agizo kwa askari wa chini yake, ili zitafutwe Lodge za kufikia wageni wale, na simu zikatembea hatimae vyumba vikapatikana.
ASP Jamila aliandaa vitendea kazi vyake, akawa yupo tayari kwa safari. Alikuwa amebeba nguo kadhaa hasa nguo wanazopenda kuvaa wanawake wa Kinzanzibar, akabeba na vifaa vyake vya kazi, akilalia safari. Akamfahamisha Kamishina wa Oparesheni kuhusu safari ile, na kwenda nae WP Monica kule Unguja, akamfahamisha askari wa kike anaehitajika kwenda kuchukua nafasi ya WP Monica. Kila kitu kiliwekwa sawa na siku ya pili yake asubuhi safari ya Unguja ikawadia.
*******
Mkuu wa upelelezi wa kituo cha polisi Madema, Inspekta Ussi Makame, ASP Jamila, Staf Sajenti Kubuta, pamoja na WP Monica, walikuwa nyumbani kwa Marehemu Haruna! Huku nje ya nyumba ile kulikuwa na askari polisi wawili wenye silaha wakishika doria kila siku wakibadilishana zamu katika nyumba ile! ASP Jamila na askari wenzake walikuwa sebuleni wakikagua taratibu mahala pale, lakini hawakupata kitu cha maana wakaingia chumbani.
ASP Jamila alikitazama chumba kile kwa makini, akaona kitimtim kilivyofanyika. Akaanza kuyaokota makaratasi machache yaliyokuwa yamezagaa mle chumbani, ambayo kabla hayajatolewa na yule mpekuzi asie rasmi, makaratasi yale yalikuwa yamefungiwa katika droo la kabati la chumbani mle!
ASP Jamila aliyakagua kwa makini makaratasi yale, akayaona mengi yake yalikuwa ni ya kodi ya majengo! Aliendelea kuyapitia moja baada ya moja, hamadi akakukata na karatasi ambayo ilimvutia sana! Ilikuwa karatasi iliyokuwa imejifunika maandishi yake kwa chini, wakati anaiokota karatasi ile iliyoandikwa kwa mkono, huku ikionesha tarehe mwezi na mwaka! Ilikuwa imeandikwa mistari sita tu. Karatasi ile ilikuwa ikisomeka hivi.
Muhimu zaidi ya sana.
Kabati Jeneza, Kitanda Kaburi.
Maisha yangu yapo mikononi! Si ajabu kukatishwa!
Kurejea Mapinduzi, hapana ninakataa!!!
Ng’amua uikomboe Zanzibar!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Asante sana. Marehemu mtarajiwa Haruna Makupa.
ASP Jamila aliyarudia kuyasoma maneno yale mara karibu ya tano. Hatimae kwa mbali akawa anapata mwanga wa maneno yale. Akaikunja karatasi ile akaiweka mfukoni mwake. Alikwenda katika lile kabati, akalitazama kwa makini sana. Kabati lilikuwa bado li wazi Salma hakulifunga hata mlango mmoja kati ya ile milango mitatu. Droo la kabati lile lilikuwa wazi, likiwa na funguo kadhaa, zilizokuwa zikionekana. ASP Jamila akazichukua zile funguo zote, huku akiwaonesha wenzake idadi ya funguo alizozichukua. Akazitia katika mkoba wake funguo zile, kisha akakiendea kile kitanda, na kuchungulia uvunguni, huku akitoa tochi ndogo iliyokuwa na mwanga mkali kutoka katika mkoba wake. Akaiwasha tochi ile na kumulika chini ya Kitanda uvunguni, akakukatana na sakafu tupu hakukuwa na kitu chochote mle chini ya uvungu wa kitanda.
ASP Jamila, aliganda pahala pale akitazama kwa makini katika ule uvungu wa kitanda, hatimae akatikisa kichwa juu chini kukubali kitu kilichokuwa kimepita katika ubongo wake. “Vipi Afande kuna kitu umegungua?!” Mkuu wa upelelezi Ussi Makame, alimuuliza ASP Jamila huku akiwa na shauku kubwa. ASP Jamila aligeuka kumtazama Ussi Makame, akamjibu; “Hapana bado nafanyia kazi Inspekta.” Kisha akainuka pale, huku akizima tochi yake, na kuwaambia wenzake. “Turudini Kituoni humu kazi yake itakuwa kesho, twendeni tukajipange ili kuenda kazini alipokuwa akifanyia kazi Marehemu Haruna” Askari wale walikubaliana na kiongozi wao, wakatoka kwa pamoja WP Monica alifunga milango kwa funguo, wakaelekea kituoni Madema.
Walipokuwa kituoni, wakapanga mikakati na hatimae Inspekta Ussi Makame, na ASP Jamila, wakakubaliana waende katika ofisi ile ili wakahoji kwa undani, sababu hasa za kukatishiwa mkataba wake Marehemu Haruna, na kama wataweza kupata majibu ambayo yatawapeleka hatua kadhaa mbele. Hivyo mara moja safari ya Shangani ikaanza na nyuma yao kulikuwapo na gari ndogo ikiwafata kwa mbali wote wakielekea Shangani.
Walipofika pale karibu na Shangani Hotel, walikwenda kidogo na kuegesha gari yao iliyokuwa ikiendeshwa na Inspekta Ussi Makame. Kisha wakateremka na kujitoma ndani ya jengo lile lililokuwa na nakshi nakshi za kizamani milango yake. Mbele kidogo kushoto wakakutana na dada mmoja, aliekuwa amevalia vazi la hijabu, alikuwa amekaa anacheza na kompyuta. Ofisi ile ilikuwa na kiyoyozi safi, kilichokuwa kikipuliza, samani zake zilikuwa zimetengenezwa kwa mti wa mnazi. Zilikuwa zinapendeza sana. Kuanzia meza pamoja na samani kadhaa zilizokuwa mle ndani.
“Cheichei bibie?” Inspekta Ussi Makame, alimsalimia Yule dada, ambae nae akaacha kuendelea na kompyuta yake. Akainua uso wake akajenga tabasamu pana kichwani mwake akajibu; “Chei bwana Karibuni sana, niwasaidie nini jamani?” Inspekta Ussi Makame, akamwambia. “Asante tushakaribia, tuna shida yakuonana na meneja uajiri.” Yule dada aliwatazama wale wageni wake kwa muda, kisha akasema. “Hapa hakuna kazi hivyoo!” Wale askari waliokuwa wamevaa kiraia wote wakatabasamu, kisha ASP Jamila akamwambia “Sie hatuna shida ya kazi kwenu, ila sie tumekuja kuonana na meneja muajiri, tunataka kuzungumza nae kuhusu mizigo yetu!” ASP Jamila alisema maneno yake huku akiipandisha miwani yake juu!
“Mnatokea wapi nyie?” Yule dada wa mapokezi aliendelea kuwasaili. “Dada kuonana na meneja muajiri kunakuwa na maswali yote haya, je tungetaka kuonana na Mkurugenzi itakuwaje?” Inspekta Ussi Makame, alimwambia Yule dada wa mapokezi. Na yule dada akawajibu. “Huo ndiyo utaratibu niliopangiwa na viongozi wangu hivyo siwezi kuupinga!” Askari wale walitazamana kama watu waliokuwa wameelewa kitu, kisha ASP Jamila akamwambia yule dada. “Sisi tunatokea Dar es salaam, tunataka kumuona meneja muajiri leo, ili tukishazungumza nae tupande Boti tuondoke.” Yule dada aliinua uso wake akawatazama kwa mara nyingine, kisha akawaambia, “Meneja ametoka amekwenda bandarini kutoa mzigo, mnaweza kusubiri au mkaja kesho.” Wale askari wakatazamana tena kisha wakamwambia Yule dada kwa pamoja; “Tutamsubiri!” Baada yakusema hayo mara simu ya mezani ya Yule dada ikaita, nae akaipokea na kuiweka simu sikioni.
“Sawa sawa. Ndiyo boss, ahaa haya nitawaelekeza.” Alikuwa Yule dada wa mapokezi akizungumza na simu, kisha akaiweka simu katika sehemu yake, akawageukia wale wageni wake akawaambia “Mkurugenzi anawahitaji ofisin kwake.”
ASP Jamila pamoja na Inspekta Ussi Makame, wakatizamana tena kwa mara ya tatu, safari hii wakijiuliza Mkurugenzi amejuaje kama wao wapo pale kwa ajili ya kuwaona wao? “Piteni kulia hapo pandisheni juu gorofa ya kwanza, kisha upande wenu wa kushoto mtauona mlango wa kwanza, bisheni hodi humo.” Basi hawakutaka kushangaa walipanda juu gorofa ya kwanza, upande wao wa kushoto, mlango wa kwanza wakabisha hodi, na sauti ikasikika kutoka ndani “Karibu Inspekta Ussi!”
Butwaa iliyowakumba askari wale ilikuwa ni kubwa sana, ASP Jamila alimuuliza Inspekta Ussi Makame “Vipi huyo Mkurugenzi mnafahamiana?!” Inspekta Ussi Makame akatikisa kichwa kukataa kumfahamu Mkurugenzi yule ila akasema. “Ngoja tuingie tumuone labda ninamfahamu kwani mtu kidole!” Baada yakusema maneno yale walijitoma ndani ya ofisi ile, iliyokuwa imetandikwa zulia jekundu ndani, pia upande wa kulia kwao, wakaziona tv kama sita hivi zikionesha eneo na ofisi mbalimbali katika nyumba ile.
Kupitia Tv zile ndipo wakapata majibu kuwa Yule mkurugenzi aliwaona kupitia zile Tv zilizounganishwa katika mfumo wa CCTV CAMERA. “Karibuni sana Inspekta Ussi, naona upo na mgeni je salama?! Niwasaidie nini tafadhali?” Yule mkurugenzi aliwakaribisha huku akiwa ametengeneza tabasamu pana usoni mwake. “Asante sana Mkurugenzi, tumekuja katika ofisi yako kuna mambo yanatutatiza hivyo tunataka majibu yake ili huo utata utuondoke Je?! Marehemu Haruna Makupa, alikuwa ni muajiriwa katika taasisi yenu?!“
Inspekta Ussi Makame, alianzisha maswali na ASP Jamila yeye alikuwa akishangaashangaa kutazama huku na kule juu chini kushoto kulia, ilimradi alikuwa anajua nini anachokifanya!
“Naam Haruna kweli alikuwa Muajiriwa wa taasisi yetu, ila kwa sasa siyo tena mfanyakazi wetu, amelipwa stahiki zake zote, hatudai kwa hilo ndilo ninalolifahamu!” Alijibu Mkurugenzi Yule huku akiwa ametulia kwa makini sana.
ASP Jamila miwani yake ikiwa juu, sasa alikuwa akimtazama Yule mkurugenzi moja kwa moja, akamtupia swali la haraka. “Unadhani ni kwa nini mliamua kukatisha mkataba wake, na kumpa pesa yote ya mshahara ya miezi mitatu ambayo hakuifanyia kazi? Kulikuwa na ulazima huo?!” Yule mkurugenzi hakutegemea swali lile, hivyo alizubaa kidogo kama mtu anaetafuta jibu na mara baada yakulipata akajibu.
“Eee unajuwa wafanyakazi wetu, tumewaajiri kwa mikataba, hivyo kama unaona mtu utendaji wake unalegalega, basi unachukua hatua, ndivyo tulivyofanya sisi! Mimi nilidhani mngeuliza kama anatudai, lakini swala la kuachisha au kuajiri, hilo ni khiyari yetu na hatuingiliwi na mtu!” Yule Mkurugenzi alijibu swali lile huku akiwa ameondosha ile hali ya tabasamu usoni mwake.
“Kwani Haruna Makupa alikuwa akifanya kazi gani hapa?!” Aliuliza Inspekta Ussi Makame, na Yule Mkurugenzi akawapa jibu ambalo hawakulitegemea. “Haruna alikuwa tarishi katika taasisi yetu!” Askari wale walitazamana kwa mara nyingine kisha wote kwa pamoja wakasema “Tarishi?!” Sasa ikawa zamu ya Mkurugenzi kuwatazama wao huku akiwashangaa kisha akawauliza.
“Kwani nyie mlikuwa mnajua alikuwa akifanya kazi gani hapa?!” Askari wale hasa ASP Jamila alimkumbuka Salma mkewe Marehemu Haruna alipomwambia kuwa mumewe alikuwa akifanya kazi katika kitengo nyeti cha IT. Sasa mbona huyu Mkurugenzi anawaambia kuwa Haruna alikuwa ni Tarishi? Au Haruna alikuwa akimuongopea mkewe kazi yake? Lakini kwa utarishi kweli ndiyo auwawe na nyumba yake kuwindwa namna ile? Hapana hapa ipo namna! ASP Jamila aliwaza hatimae akamuuliza mkurugenzi Yule. “Unaweza kuniambia mtu wenu wa IT mmemuajiri muda gani sasa?!” Swali lile lilimfanya Mkurugenzi ameze mate kisha akasema. Meneja muajiri ndiyo anaefahamu suala hilo!” Na wale askari wakamuuliza. “Tunaweza kumuona?” Yule Mkurugenzi akawajibu “Ametoka nadhani mlijibiwa pale mapo….!”
Mkurugenzi hakumaliza kauli yake kwani macho yake, yalikuwa yameganda katika moja ya Tv zile ikimuonesha Bwana mmoja wa makamo, aliekuwa amevalia suti, akiwa anaonekana pale mapokezi.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vipi ndiye huyo? Mbona umekatisha maongezi yako?! Kwa kumtizama huyo bwana?!” ASP Jamila alimsaili Yule Meneja ambae sasa uso wake ulionesha mashaka makubwa! Lakini pia nae akamkariri Yule bwana alievaa suti kupitia pale katika kioo cha luninga!
Kupitia pale katika Tv zile za ofisi ya pale kwa Mkurugenzi, walimshuhudia Yule bwana akizungumza neno na Yule dada wa mapokezi, kisha Yule dada alikuwa akioneshea mkono wake juu! Mara Yule bwana alifungua mlango na kutoka nje ya jengo lile kwa mwendo wa haraka!
“Hapana sie Yule, Yule bwana tunamdai pesa zetu pale nilipomuona ndiyo maana nikasita nikawa namtazama labda atatowa pesa zetu, lakini ameondoka bila kutulipa!” Mkurugenzi aliongopa uongo ambao hata askari wale waliung’amua!
“Sawa Mkurugenzi lakini je? Unafahamu kama Haruna Makupa ameuwawa?!” ASP Jamila alimuuliza Mkurugenzi huku akimtazama usoni. Kwa swali lile alimshuhudia Mkurugenzi akibadilika na kujibu katika mfumo wa swali; “Kwa hiyo fikira zenu zinawaambia sie ndie tuliemuua? Tumuue yeye ili iweje?!”
ASP Jamila baada yakumuona Mkurugenzi amehamaki, akafurahi katika nafsi yake kuwa atakuwa akijibu maswali bila uangalifu, na kwamba atapata walau kitu kwa mda ule chakuwafikisha katika ukweli wa Balaa lililomkumba Haruna. Hivyo haraka akamuuliza tena Yule Mkurugenzi.
“Mmemuua ili kujaribu kupoteza ushahidi muhimu, ingawa kwa bahati mbaya tayari ushahidi huo tunao, na ndiyo maana tupo kwako katika muda huu! Unadhani ungesalimika Mkurugenzi?!” ASP Jamila alikuwa akisema kwa dharau huku akimtazama usoni bwana Yule, lakini pia akiwa makini mara dufu!
”Siwaelewi mnachokiongea, ushahidi gani mliokuwa nao nyie?” Mkurugenzi alisema maneno yale huku akiinuka katika kiti chake na kusimama! Uso wake ukiwa umesawajika, lakini alikuwa akijikaza kisabuni! Baada ya kusimama alikaa chini huku akiwa ameghazibika kupita kiasi!
“Mkurugenzi unatuelewa sana yaani. Ila unafanya makusudi! Sasa sisi tutaondoka na wewe kama hutaki kutupa ushirikiano, pia ukizidi kutuongopea na ukaacha kusema ukweli!” Inspekta Ussi Makame, alimtumbukizia kauli ile mkurugenzi huku akimtazama usoni bila kupepesa macho.
Mkurugenzi pamoja na kiyoyozi kilichokuwamo mle ndani, alitoa kitambaa akaanza kufuta kijasho chembamba, katika uso wake halafu akasema kwa sauti iliyokosa kujiamini.
“Mimi nimewaongopea nini? Na mnichukue kwa ushahidi upi huo nionesheni na mimi kama kweli mnao huo ushahidi!”
ASP Jamila alimjibu Yule Mkurugenzi. “Umetuongopea kuhusu kazi aliyokuwa akifanya Haruna hapa kwenu. Haruna hakuwa Tarishi hata siku moja! Tunazo taarifa kuwa alikuwa akifanya kazi katika kitengo nyeti cha IT. Lakini pia wewe ndiye uliyeamuru Haruna auwawe baada ya kuona hawapi kile kitu mlichokuwa mkikitaka, ambacho sasa kipo mikononi mwetu! Na muda ukifika utaoneshwa ushahidi huo, usitulazimishe kukuonesha wakati huu!”
Yule Mkurugenzi alikunja ndita katika uso wake, kukaonekana matuta mengi yameshamiri usoni kwake, huku jasho jingi sasa likiwa linamtoka mwili mzima! Aliwatazama wale askari akawa hana hakika na maneno ya wale askari, kama kweli au sikweli yale wanayoyasema, hatimae akapata kauli nakusema. “Sasa nyie mnasemaje?”
Wale maaskari walimtazama Yule Mkurugenzi kwa muda. Kisha ASP Jamila akamuuliza swali la mkato. “Je kuna ubishi juu ya hili kuwa Haruna hakuwa Tarishi? Hilo ndilo tunalolitaka utuambie kutoka kwako!”
Mkurugenzi aliinamisha uso wake chini, alipokuja uinua akajibu. “Kusema kweli Haruna alikuwa Tarishi, ila pia aliwahi kufanya kazi katika kitengo cha IT, kama afisa muandamizi wa kitengo hicho lakini hakufanya kwa muda mrefu.”
ASP Jamila akatikisa kichwa juu chini, kukubali hisia zake na hikima zake kuwa zinamfikisha katika ukweli! Akasema kumwambia Mkurugenzi. “Haijalishi kama alifanya kazi kwa muda gani, lakini nashukuru umekubaliana na mimi kuwa Haruna alikuwa akifanya kazi katika kitengo cha IT, vizuri sana! Je wewe mkurugenzi ulikwenda kumzika aliekuwa mfanyakazi wenu au kutoa wawakilishi wako katika msiba ule?!”
Swali lile lilijibiwa huku sauti ya Mkurugenzi ikiwa haipo sawasawa. “Mimi nilikuwa safari, ingawa katika taasisi yetu hakuna mfanyakazi yeyeto aliekwenda kushiriki mazishi yake, lakini pia hadi kifo kinamkuta, Haruna hakuwa mfanyakazi wetu!”
Inpekta Ussi Makame aliekuwa amekaa kimya muda mrefu, akamtupia swali la kizushi Mkurugenzi. “Lakini kule makaburini wakati wa maziko, kuna watu walimwambia Kaka wa marehemu kuwa wao ni wafanyakazi wenzake, wamekwenda kumpa pole, taarifa hiyo tumeipata kwa mujibu wa askari wenzetu waliokuwapo makaburini, una neno gani lakusema juu ya jambo hilo?!”
Mkurugenzi huku akionesha jazba alijibu; “Mimi ninachokijua hakuna mfanyakazi wetu hata mmoja aliekwenda kumzika Haruna, sijui labda kama Marehemu Haruna alikuwa amepata kazi sehemu nyingine, na wafanyakazi wenzake wakenda kumzika, hilo mimi siwezi kulisemea!”
Askari wale walimuhoji Mkurugenzi Yule kadiri walivyotaka kujua kitu Fulani, hadi wakaridhika kwa majibu waliyoyapata. Hata Mkurugenzi hakuamini alipomsikia ASP Jamila akimwambia. “Mkurugenzi tunashukuru sana kwa majibu yako. Sie tunakwenda ila hatutosita kuja tena katika ofisi yako. Tunakuwacha uendelee na kazi yako, tukikuhitaji tutakuita!”
Mkurugenzi aliinuka kitini pake akawapa mikono askari wale, akaagana nao akataka kuwatoa awasindikize. Inspekta Ussi Makame akamwambia aendelee na kazi yake wao watatoka tu. Wakati askari wale wakishusha ngazi nakuondoka, Mkurugenzi alitoa simu yake ya mkononi, akapiga pahala nyeti na kueleza ujumbe uliomfikia ofisini kwake, maswali aliyokumbana nayo na kwamba muda wowote, ameahidiwa akihitajika atafatwa au kuitwa!
Ule upande wa pili huku ukijiamini ukamuhakikishia Mkurugenzi kuwa afanye kazi. Yeye analishughulikia jambo lile chapu kwa haraka! Na simu ile ikakatwa Mkurugenzi akashusha pumzi ndefu sana. Amani ikamrejea upya! Akawa anaikodolea macho luninga iliyokuwa ikiwaonesha wale askari wakiwa wanatoka nje ya jengo lile.
*******
Staf Sajent Kubuta, akiwa nje ya jengo lile yeye na WP Monica, walimshuhudia Yule bwana alievaa suti, akitoka kwa haraka katika ofisi ile, akapanda katika Vespa nyekundu na kuondoka eneo lile. Staf Sajenti Kubuta akamwambia WP Monica “Tumfate Yule bwana tuone anaendea wapi? “ Wp Monica hakutaka kuuliza mara mbili akawasha gari, na kuanza kumfatilia Yule bwana alievaa suti anaeendesha Vespa nyekundu.
Yule bwana aliekuwa katika Vespa nyekundu, aliiendesha Vespa ile na kunyoosha mtaa wa Shangani, akaingia barabara ya Kaunda, akapinda kushoto kushika barabara ya Vuga. Akaendesha kwa mwendo wa kasi hadi katika makutano ya barabara ya Benjamin Mkapa, akapinda kushoto kuelekea eneo la Vikokotoni. Alitembea katika mwendo ule hadi alipofika Vikokotoni, akapinda kushoto na kuingia Barabara mpya ya Mkunazini, akatembea hadi St Monica’s Hostel, akaegesha ile Vespa akashuka na kuingia ndani ya Hostel ile huku akitoa simu na kuzungunza akiwa anatembea kwa haraka.
Staf Sajent Kubuta na WP Monica walikuwa makini sana, katika kumfatilia Yule bwana. Walipomuona amewasha endiketa kuonesha kupinda kulia pale katika Hostel ile, wao walipunguza mwendo zaidi na kusogea mbele zaidi ya Hostel ile, hadi pale katika makutano ya Barabara mpya ya Mkunazini. Kwa mbele yao, wakapinda kushoto walipofika katika makutano ya Mtaa wa Mkunazini na mtaa wa Tharia kwa upande wa kulia kama unaelekea maeneo ya Mchambawima! Wakageuza gari yao na kuelekea walipotoka, huku macho yao yakiwa yanaiangalia Hostel ya mtakatifu Monica, pia ile Vespa nyekundu.
Staf Sajenti Kubuta aliteremka katika gari, akashika njia na kujichoma ndani ya Hostel ile. Alipoingia pale mapokezi, alimkuta Muhudumu wake mama mmoja akiwa anaandika katika daftari lake, akamsalimia kisha akamuuliza. “Samahani mama, nina mwenzangu ameingia humu muda si mrefu, ameondoka na funguo za ofisini, hivyo niambie yupo chumba gani ili nikachukue hizo funguo!”
Yule Mama akasema “Unamaanisha huyu Bwana wa chumba namba nane?! Kwani yeye ndiyo alieingia sasa hivi ameshindwa hata kusalimia amepanda juu huko anaongea na simu, wahaka umempata amechukua funguo hapa hata salamu imemshinda. Mwambie jamaa yako, wazanzibar hata ndani ya daladala pia wanasalimiana seuze ndani ya nyumba! Sasa asilete mambo yake ya Bara hapa!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Staf Sajent Kubuta, alishukuru katika moyo wake kwa kusikia Yule bwana anakaa pale, na yupo chumba namba nane. Akamwambia Yule mama huku na yeye akiigiza kuongea sauti kama wazanzibar, “Hana mana hivyo Yule, mijitu ya bara hii ustarabu wao ni mdogo sana! Pole mama yangu na naomba radhi kwa niyaba yake!”
Yule mama akapokea msamaha ule na kusema. “Hapa huwa tuna utaratibu mgeni yeyote anaekuja hapa kwa ajili ya kumtembelea mpangaji wetu, huwa tunampigia simu mgeni wetu, tumwambie mtu aliemfata kama anamiadi nae au anamfahamu, akituambia aende basi tunamruhusu, lakini kwa fataani huyu, nenda tu ukaonane nae hana mana hana adabu!”
Yule mama muhudumu hakika alikuwa amechukia sana. Lakini kuchukia kwake ilikuwa ni faida kubwa sana kwa Staf Sajenti kubuta, kwani vije kama angepigiwa simu Yule bwana kisha akasema hana mtu aliekuwa na miadi nae? Hivyo kwa hasira za yule mama ilikuwa kama hasira ya Mkizi, tijara kwa Mvuvi. Staf Sajent Kubuta alipanda ngazi kwa haraka huku moyo wake ukimpiga haraka haraka, hadi katika korido kubwa, na kuona milango ya vyumba. Jengo lile chini zilikuwa ofisi na juu ndiyo ilikuwa kuna vyumba vya kulala. Staf Sajenti Kubuta alizifatilia zile namba za vyumba, moja ikiwa upande wake wa kulia, mbili upande wake wa kushoto, alikwenda katika utaratibu ule hadi akaufikia mlango namba nane uliokuwa upande wa kushoto, akausogelea ule mlango akashusha pumzi zito! Mara alipokuwa pale usawa wa mlango kabla hajafanya jambo lolote, simu ya Staf Sajent kubuta ikaita kwa sauti pale mahali alipokuwa usawa wa mlango. Akiwa katika harakati za kuipokea ile simu, mara kitasa cha mlango wa chumba namba nane, kilizungushwa mlango wake ukafunguliwa.
*******
0 comments:
Post a Comment