Search This Blog

Monday, 24 October 2022

BALAA ! - 2

 





    Simulizi :Balaa !

    Sehemu Ya Pili (2)



    Askari Selo alisema maneno hayo huku akiranda mle ndani ya Selo, ukiwa ni utawala wa Kimahabusu, kulikuwa hakuna ubishi, watu wote walilala ubavu, watu waliopangwa pale kati kati ya Selo pakiitwa Maandazi road, au Mchongoma! Hali ilikuwa mbaya sana, hakika ulikuwa ni mchongoma! Mahabusu walikuwa ni wengi sana kuliko uwezo wa chumba/Selo ile kiasi kulikuwa hakuna nafasi ya mtu kulala chali au kifudifudi, kwani wengine wangekosa kulala, kwa hiyo ilikuwa ni kulala ubavu! Hali ya hewa ilikuwa nzito sana, harufu kali ya majasho na watu wasiooga na kupiga mswaki ilienea ndani ya Selo ile, Athumani Dobe alikuwa amepangwa katikati pale kwenye mchongoma! Machozi yalikuwa yakimtoka akikumbuka mbali! Alikumbuka nje nyumbani kwake, alikuwa akilala katika kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita, Siyawezi akiwa pembeni ubavuni kwa huduma aitakayo, lakini leo amelazwa katika godoro dhaifu, akiwa anatizamana na miguu iliyokosa maji kwa muda, miguu iliyojaa vipele vya ukurutu. Pia watu wakitoa harufu kali ya jasho. Njaa ilikuwa ikimsakama sana, kwani walipoingia pale gerezani hawakuwa na lesheni ya mlo, kwa hiyo walilala na njaa! Ni kawaida ya magereza yote nchini fresh hawana hesabu ya kula kwa siku ile wanayoingia gerezani. Ama kweli lililopangwa na mungu likupate, halikosi kukupata!



    *******

    Katika hospitali ya mnazi mmoja iliyopo Unguja imepelekwa maiti na polisi, baada ya polisi wale kupigiwa simu na raia wema asubuhi ile ya saa moja waliokuwa wakifanya mazoezi katika viwanja vya Maisara. Pale katika viwanja vile jirani yake kulikuwa na fukwe ya bahari ya hindi jirani na msikiti wa pale Maisara. Mwili wa mtu wa jinsia ya kiume ulikuwa umelala chali hauna uhai! Polisi waliupeleka mwili ule katika hospitali ya mnazi mmoja kwa uchunguzi zaidi!

    Mkuu wa upelelezi wa kituo kikubwa cha polisi Unguja pale Madema, alikuwapo wakati mwili ule ukipakiwa katika gari yao aina ya Toyota land cruser pickup. Mkuu yule wa upelelezi aliuchunguza mwili ule kwa makini, akiwa amevalia glovu katika mikono yake, aliupekuwa mwili wa marehemu lakini hakufanikiwa kupata kitu chochote kwani hakupata simu, wala kitambulisho au ujumbe wowote kutoka katika mifuko ya nguo alizovaa marehemu yule.

    Mkuu wa upelelezi akatikisa kichwa kukubali hisia zake, na matokeo ya uchunguzi wake katika mahali pale kuwa, ule mwili wa marehemu uliokuwa pale ulipolala au kulazwa, pamoja na kuwa kulikuwa na mchanga, lakini hakukuonesha kama kulikuwa na rabsha yoyote!

    Hata kama upepo wa pwani uliokuwa ukivuma asubuhi ile utakuwa umepeperusha alama zozote mahali pale, lakini mkuu Yule alikuwa na hisia zaidi zilizojificha nyuma ya ubongo wake kuwa, maiti ile ilipelekwa mahala pale, na haikufia sememu ile! Hisia zile zilimtawala sana, na aliziamini kiasi hata akaagiza mwili ule, lazima dakitari wa jeshi la polisi ndiyo aufanyie uchunguzi kwanza kabla ya dakitari mwingine! Kwa kuwa mwili ule ulikuwa ni wa baridi sana, kiasi kila mwenye uzoefu wa kukagua maiti, angekubaliana kuwa mwili ule ulikufa muda mrefu siyo chini ya saa nane nyuma!

    Hisia zake zilimuelekeza kuwa, mbali na ubaridi mkubwa wa mwili wa maiti yule, lakini pia bahari ya hindi wakati ule ilikuwa inajaa usiku kuanzia saa tatu, na kupwa saa nane baadae ambayo ingekuwa ni saa kumi na moja alfajiri! Kama hivyo ndiyo basi maana yake mwili ule kama ungekuwa asubuhi ile ndiyo umepoteza uhai, basi ungelikuwa bado una joto hasa katika maeneo ya kichwani! Kwa vile uzoefu wa kazi yake ya upelelezi imeshamkutanisha na masuala ya uchunguzi wa kuchunguza maiti zaidi ya mia moja! Hivyo anaijua maiti ipi imekufa muda huu, na maiti ipi imekufa muda mrefu! Kwani uzoefu na utaalaamu wake ulimuongoza kuwa maiti anaanza kupoa katika miguu sehemu ya nyayo! Kisha baridi inapanda juu kichwani kwa kadiri muda utakavyokwenda!

    Lakini pia alijiuliza kama mwili ule ungelikuwa pale wanapouona umelala/kulazwa, kama ungelikuwapo tangu usiku, basi mwili na nguo za marehemu zingekuwa zimerowana kwa maji chumvi ya bahari iliyokuwa imejaa maji yake usiku! Ila kinyume chake nguo za marehemu pamoja na mwili wake zilikuwa ni kavu kabisa, hazikurowana na maji chumvi ya bahari! Japokuwa pale ulipo mwili ule, alama ya maji ilionekana dhahiri kuwa bahari ilipokuwa imejaa maji yake yalipita pale alipo maiti yule, na kuendelea hadi katika kingo! Ndipo Yule mkuu wa upelelezi wa kituo cha madema akaona kuna jambo kubwa linalotakiwa kufanyiwa kazi katika mwili ule.

    Baada ya kutafakari hili na lile, akaupiga picha mwili ule wa marehemu na simu yake ya mkononi, akipiga picha uso na mwili mzima. Kisha akapiga picha zile alama za maji zinazoonekana babari ilipokuwa imejaa, pamoja na maeneo ya jirani ya eneo lile.

    Askari wale waliipeleka maiti ile katika hospitali ya Mnazi mmoja pale Unguja. Hospitali ile ilikuwa ipo katika fukwe ya bahari ile ya hindi. Na askari wanaoshughulika na uchunguzi wa vifo, wakaingia kazini wakitafuta sababu za kifo cha marehemu yule. Na mkuu wa upelelezi baada ya kukabidhi jukumu kwa madakitari, yeye alirudi ndani ya gari yake ndogo aina ya IST nyeupe, akawa katika tafakuri nzito! Na saa moja baadae akaamua kurudi ofisini kwake hiyo ikiwa ni majira ya saa tatu asubuhi.

    Mkuu wa upelelezi alirejea ofisini kwake, mara akakuta kuna mgeni akimsubiri pale katika benchi, mgeni Yule alikuwa amejiinamia kwa huzuni, akionekana ametoka kulia siyo muda mrefu, alikuwa hana raha kabisa nae akamkaribisha ndani ya ofisi yake, kwa mazungumzo baada ya kutambuana hali.

    “Afande mie naitwa Salma Machano, mume wangu tangu jana jioni ametoka kumsindikiza mwanetu mtoto wa kaka yake kwenda bandarini, akienda Dar es salaam, hadi hivi sasa nizungumzapo na wewe, hajarudi nyumbani wala simu yake toka jioni ile hadi hivi leo saa mbili ya asubuhi nilipoipiga simu yake bado ikawa haipatikani! Ndipo nilipoona niwasiliane na watu wa Dar es salaam kujua kama mume wangu nae aliamua kwenda huko. Lakini taarifa niliyoipata imeniliza sana na inanipa wasiwasi mkubwa. Kwani mume wangu kule Dar hayupo, lakini hata yule mwanetu Mauwa ambae mume wangu alimsindikiza jana bandarini kwenda Dar, hakufika nyumbani kwao! Hivi ninavyoongea na wewe amekutwa amefariki katika fukwe ya bahari huko Dar es salaam, Polisi walimpigia simu Shemeji baba wa Mauwa, kuwa kuna mwili umekutwa umekufa hivyo aende hospitali ya Muhimbili ili akautambue. Alipokwenda kule, hakika akamuona Mauwa bintie ameuwawa! Ndiyo nikaona nije kutoa taarifa ya kutoweka kwa mume wangu, lakini pia nipate kusikia kutoka kwenu kama kuna ajali yoyote iliyouwa watu labda mume wangu anaweza kuwamo, kwani mume wangu hana kawaida ya kulala nje!”

    Yule dada Salma Binti Machano, alijitambulisha kwa mkuu wa upelelezi, kisha akasema azma yake iliyomfanya awe pale kwa wakati ule! Habari ile ilimuingia na kumsisimua yule Mkuu wa upelelezi wa kituo kile.

    “Pole sana dada kwa kutoweka kwa mumeo, je unaweza kuniambia hiyo jana mumeo alikuwa amevaa nguo za aina gani, nikimaanisha rangi ya nguo zake pia?!” Yule Mkuu wa upelelezi alimsaili yule dada huku akiwa na wahaka mkubwa wa kutaka kufahamu jambo lile!

    “Mume wangu jana alikuwa amevaa suruali ya kodrai nyeusi na fulana ya kijivu.” Salma Machano alimjibu. Yule Mkuu wa upelelezi alikiinua kichwa chake juu, alipokishusha chini akashusha pumzi ndefu kisha akamuuliza tena, huku akitoa kijitabu kidogo na kuwa tayari kwa kuandika.

    “Mumeo anaitwa nani, na mnakaa wapi, na kama ni mfanyakazi basi anafanya kazi wapi?!”

    Salma Machano, alimjibu askari yule kwamba. “Mume wangu anaitwa Haruna Makupa, tunakaa Miembeni Sheha wetu ni Makame. Kuhusu kazi alikuwa akifanya kazi katika shirika moja lisilokuwa la kiserikali, linalojihusisha na masuala ya kupokea na kutuma mizigo ndani na nje ya Zanzibar, lakini hivi sasa ana wiki ya pili tangu aachishwe kazi, na amepewa stahiki zake zote! Kwani pale alikuwa akifanya kazi kwa mkataba, na alikuwa amebakisha miezi mitatu, ili mkataba wake wa miaka miwili umalizike, ila jamaa wamemlipa pesa yake yote ya miezi mitatu, na kumuachisha kazi!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Salma Machano alijibu, na yule Mkuu wa upelelezi wa kituo kile kikubwa pale Madema, aliandika katika kikaratasi chake, jina kamili, mahali anapoishi, na mahala alipokuwa akifanyia kazi. Kisha akamwambia yule mwanamke, Salma bint Machano kwamba.

    “Kuna picha katika simu yangu, nakuonesha sasa hivi naomba uitambue kama unamfahamu mtu huyu!” Baada ya kusema maneno yale, Mkuu wa upelelezi alitoa simu yake, na kutafuta picha alizopiga leo muda si mrefu kule Maisara, akatafuta ile picha aliyoipiga katika uso wa marehemu aliokuwa amelala chali, akamuonesha na kumuuliza. “Je?! Unamfahamu mtu huyu?!”

    Salma Machano, aliitazama ile picha kwa makini sana, huku yule askari akimtazama yeye usoni mwake, Salma machozi yakaanza kumtoka, uso wake ukawa mwekundu, midomo yake ikaanza kugongana, na mara akaachia ukelele mrefu wa kilio, “Mume wangu eeeeeeeeeeeeee!” akaanguka chini macho yamemtoka pima, akatulia kimya akiwa amepoteza fahamu!

    Yule Mkuu wa upelelezi, aliinuka na mara askari watatu waliingia kwa haraka baada ya kusikia ukelele wa Salma, na kabla hawajainua vinywa vyao, wakiwa katika salamu ya utii, kiongozi wao akawapa majukumu. “Toa uwani huyu kamlazeni apate hewa, kwani amepoteza fahamu! Na bado ninamuhitaji kwa mahojiano zaidi” Wale askari walitii huku wakijiuliza kulikoni?!

    Mkuu wa upelelezi, alikwenda kwa mkuu wa kituo kile ofisini kwake. Alitoa salamu ya utii kwa mkuu wake wa kazi, akakaribishwa kitini akaketi kitako. Baada ya kuketi akaanza kumpa taarifa kuhusu maiti, waliempeleka hospitali ya mnazi mmoja, na kuwa sasa amemtambua yule marehemu kwa jina la Haruna Makupa, mkazi wa Miembeni Unguja. Ila kutokana na taarifa ya Mke wa marehemu, alitaka mkuu wake wa kazi aithibitishe, Je?! Tanzania bara ni kweli kuna mtu ambae leo nae amekutwa ufukweni akiwa maiti?!

    Mkuu wa kituo cha Polisi cha Madema, aliwasiliana na msemaji wa jeshi la polisi Zanzibar, akamuelezea kila alichoelezwa na mkuu wa upelelezi, kisha akataka kujua ukweli wa taarifa zile kwa hatua zaidi za kikazi.

    Msemaji wa jeshi la polisi Zanzibar, nae akawasiliana na Kamishina wa polisi Zanzibar, akampa taarifa ile kama alivyoelezwa na mkuu wa kituo cha polisi madema. Nae akaahidiwa kupata majibu sahihi ya jambo lile!





    Kamishina wa polisi Zanzibar, akawasiliana na IGP akatoa taarifa ile, na hakika akapewa majibu aliyoyataka, ila alitakiwa mchana wa saa sita apande ndege haraka aende makao makuu ya jeshi la polisi yaliopo Dar es salaam. Kwa kikao cha kujadili na kupeana mikakati ya kuikabili. Kwani imeonekana ni mambo yenye uhusiano hivyo nilazima ifanyike kazi kama timu, ili kuwatambua wauwaji na wafikishwe katika mikono ya sheria. Lakini pia zijulikane sababu za vifo vile, na kuzuia vifo vingine zaidi visitokee ili kuwafanya raia na mali zao waishi kwa amani. Kamishina wa polisi Zanzibar, alitakiwa katika kikao kile ahakikishe ripoti ya dakitari kuhusu mwili wa Haruna Makupa anakwenda nayo kikaoni akiwa nayo mkononi mwake! Baada ya kupokea agizo kutoka kwa IGP simu ilikatwa na Kamishina wa polisi Zanzibar, akamwita msemaji wa polisi Zanzibar aende ofisini kwake. Alipofika walizungumza yale majibu kutoka Bara, na kuhusu safari yake mchana ule, pia akamtaka awe na subira kusema chochote hadi atakaporudi kutoka Dar es salaam kwa (Inspekter General of police) IGP.

    *******



    Katika ofisi ya mkuu wa polisi nchini, pale makao makuu jijini Dar es salaam, katika majira ya saa saba mchana kikao kikubwa kilikuwa kinafanyika, kikao kile kilikuwa cha watu sita wazito katika jeshi la polisi wakipanga na kupangua. Kiongozi wa kikao kile alikuwapo Mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP akiwa katika kiti chake akiongoza kikao, pamoja nae alikuwapo Kamishina wa polisi wa Zanzibar upande wa kulia kwake. Pia alikuwapo Mkurugenzi wa makosa ya jinai wa jeshi la polisi ambae pia ni Kamishina, kwa upande wa kushoto kwake. Akifatiwa na kamishina wa Oparesheni za jeshi la polisi nchini. Akifatiwa na Kamishina wa utawala nchini. Akifatiwa na Kamishina wa Fedha wa jeshi la polisi nchini. Akitimiza idadi ya viongozi sita madhubuti, wakiwa katika dhamana kubwa ya kujenga, kulinda na kutetea amani na utulivu nchini kwa raia na mali zao.

    IGP alikuwa amevaa kofia yake kichwani, na wale Makamishina watano kwa sababu za kiitifaki, wao walivua kofia zao wakawa makini na kikao kile cha dharula namna ile, kutokana na matukio yaliotokea asubuhi ya siku ile!

    IGP alifungua kikao kile na kuwaeleza wale makamishina watano wa jeshi la polisi. “Makamishina nimeitisha kikao hiki cha dharula, baada ya kutokea matukio ya mauwaji, mawili leo asubuhi hii, yote yakiwahusisha watu wawili wa familia moja waliokufa au kuuwawa katika miji tofauti, Dar es salaam na Unguja. Yapo mambo yalionifanya nilipe uzito jambo hili hata kuamua kuwaita nyie nyote katika kikao hiki!”

    IGP alisema maneno yale kisha akasimama kuzungumza, akachukua gilasi ya maji na kupiga funda kadhaa, kisha akaendelea na kueleza. “Mazingira ya vifo hivi, kuna utata mwingi sana unavyovigubika! Kwani Marehemu wote wawili, wakati wa uhai wao siku ya jana, walikuwa pamoja kwa mujibu wa Kamishina hapo wa Zanzibar. Na leo hii wote wamekutwa wamekufa asubuhi, tena wote wakiwa katika fukwe za bahari! Hivyo hatuna yakini kama hawa wauwaji makazi yao ni bara au visiwani. Mbaya zaidi ripoti za dakitari wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania pale muhimbili, inafanana na ripoti ya dakitari wetu pamoja na dakitari wa hospitali ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ambayo alinikabidhi Kamishina wa Zanzibar hapo muda mfupi kabla sijaingia katika kikao hiki. Lakini pia Hatujui kama vifo hivi vitaendelea au vitakoma, hivyo nikaona ni vyema niitishe kikao hiki cha dharula, ili tujipange zaidi kwa vifo hivi. Kikosi kazi kiundwe ili kupata majibu ya vifo hivi, na hatimae wahalifu watiwe mikononi na wapelekwe katika chombo cha sheria ili sheria ifate mkondo wake, mmenipata mpaka hapo?!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    IGP alimaliza usemi wake kwa swali, na makamishina wale wote walijibu kwa pamoja “Ndiyo Afande”. IGP akaendelea. “Nitamkabidhi Mkurugenzi hapo, ripoti za vifo vya watu hao atusomee sote tusikie, mtajua kwa nini nimeitisha kikao hiki!” IGP alivuta mtoto wa meza, akatoa ripoti tatu akaziweka mbele ya Mkurugenzi wa makosa ya jinai, na kumpa idhini ya kusoma ripori zile.

    Mkurugenzi wa makosa ya jinai, alizipokea kwa heshima ripoti zile, na kuanza kuzisoma;

    “Ripoti ya dakitari wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, hospitali ya taifa Muhimbili. Mwili wa mwanamke huyu anaekisiwa kuwa na umri wa miaka thelasini hadi thelasini na mbili, vipimo vinathibitisha alikata roho saa mbili ya usiku kwa kuvuta hewa yenye sumu, aina ya ETHEL kwa kiasi kikubwa! Pia usoni mwake imeonekana alivuta au kupuliziwa dawa ya usingizi iitwayo LADY GUARD FORSVARSSPRAY, kabla ya mauti kumfika. Pia marehemu nyuma ya shingo yake, alikandamizwa na kitu butu. Mwisho wa ripoti.”

    Mkurugenzi ma makosa ya jinai nchini, alimaliza kuisoma ile ripoti ya maiti ya Mauwa Simba Makupa. Na wale Makamishina wote wakatikisa vichwa vyao kusisitiza kuwa wamefahamu kwa upana taarifa ile! Kisha IGP akamuashiria azisome na zile taarifa mbili zote zinazomuhusu Haruna Makupa. Ripoti moja ikiwa ni ya dakitari wa jeshi la polisi Zanzibar, na ripoti ya pili ikiwa ni ya dakitari wa serikali ya mapinduzi Zanzibar. Mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini, nae akaanza kuisoma ripoti ya dakitari wa jeshi la polisi Tanzania Zanzibar. Ripoti yake ilikuwa haina tofati sana na ile ya dakitari wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania. Ongezeko lake ni jinsia tu, na mikwaruzo katika shingo ya marehemu. Ripoti ile ilifafanua na ilionesha kuwa mwili wa marehemu wa kiume, anaekisiwa kuwa na miaka arubaini na tano, hadi hamsini, roho iliacha mwili saa mbili usiku, kwa kuvuta hewa ya sumu kwa wingi aina ya ETHEL iliyosababisha kifo chake! Kabla ya kifo marehemu pia alilazwa na dawa ya usingizi yenye sumu aina ya LADY GUARD FORSVARSSPRAY. Muuwaji au wauwaji hawakuacha alama zao za vidole, katika mwili wa marehemu inaonekana walikuwa wamevaa glovu mikononi mwao! Ripoti ile ilimaliza na kuwekwa saini na dakitari wa jeshi la polisi Tanzania Zanzibar.

    Makamishina sasa walitazamana kwa pamoja, kisha wote wakawa wanatikisa vichwa safari hii walitikisa kwa nguvu zaidi, kuonesha hakika haya matukio yana uhusiano na wauwaji hawa. Pia inaonekana walikuwa wamejipanga vya kutosha! Ila hakuna hata askari mmoja kati ya wale sita waliokuwa katika kikao kile, aliekuwa na hakika kwa nini mauwaji yale yametokea! Kwa nini katika familia ile, nani anaehusika na mauwaji yale, kwa nini wauwaji wauwe familia ile, je wauwaji wapo wapi?! Bara au visiwani?! Ndipo kwa wakati huu wale makamishna na wao ikawafungukia kuwa lazima kikao kilihitajika kwa wakati ule, ili kuona ufumbuzi wa jambo lile unapatikana haraka iwezekanavyo! Kwani vifo vile vinaweza kuendelea na kuleta taharuki kwa wanachi, na wanaweza kupoteza imani na jeshi lao!

    IGP alimtaka pia Mkurugenzi wa Makosa ya jinai nchini, aisome na ripoti ya dakitari wa hospitali ya serikali ya Mnazi mmoja Zanzibar, alivyoona katika uchunguzi wake! Mkurugenzi nae akafanya hivyo.

    “Ripoti ya mwili wa mwanaume, mwenye umri upatao miaka hamsini, vipimo vinaonesha, marehemu alivuta sumu kwa kiasi kikubwa sana aina ya ETHEL, na ndiyo iliyoyakatisha maisha yake! Dawa hiyo ambayo inaweza kuwa sumu kama utaitumia kwa kiwango kikubwa, huwa tunaitumia katika hospital zetu kule Thieta kwa ajili ya kuwalaza wagonjwa wa upasuaji, na huwa tunaiweka kwa kiasi kidogo tu, na mgonjwa atalala hadi tunamaliza kupasua na kurejesha hali yake sawasawa. Hivyo mwili huu inaonekana imevuta au kuvutishwa kwa kiasi kikubwa sana! Lakini pia katika uso wa marehemu kuna mabaki ya rangi ya dawa ya usingizi iitwayo LADY GUARD FORSVARSSPRAY. Hii inathibitika kabla mwili huu roho haijaacha mwili, ilivuta au kupuliziwa dawa hiyo! Mwili wa marehemu katika shingo yake, nyuma kuna michubuko iliyosababishwa na kusuguliwa au kubanwa na kitu! Mwisho wa ripoti. Ilimaliza ripoti ile, ikawafanya askari wale wazame katika lindi la fikra chanya ili kupata utatuzi wa lile lililoonekana kuwa ni Balaa, lililojitokeza kwa siku ile.

    IGP alitoa uzoefu wake wa kazi kwa Makamishina wale watano, Kisha kikosi kazi kikaundwa. Kamishina wa Fedha akapewa jukumu, la kukiwezesha kila kitakachohitajika kwa kikosi kile, ilimradi ndani ya wiki mbili IGP apewe ripoti ofisini kwake kwa taarifa. Kamishna wa utawala alipewa jukumu lakupangua askari kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine, ilimradi kazi ile ifanyike kwa ufanisi. Kamishina wa Oparesheni, jukumu lake ndilo lilikuwa kupanga kikosi kazi kwa namna anavyoona vijana ambao watafanya kazi ile kwa haraka na usahihi mkubwa, bila kumuonea mtu yeyeto Yule! Lakini pia bila kumchelea mtu yeyote awae ilimradi ushindi wa kishindo upatikane! Baada ya nusu saa hivi IGP alifunga kikao, na kila mtu akapewa jukumu lake, kikosi kile kitafanya kazi chini ya Kamishina wa Oparesheni wa jeshi la polisi.



    *****

    Tanzania Bara waliteuliwa askari watatu wakushughulikia kesi ile ambao ni Staf Sajenti Kubuta, kutoka makao makuu, na Sajenti Magane kutoka kituo cha kati. Pamoja na Coplo Uzegeni, kutoka kituo cha Sarenda. Hawa watafanya kazi na kuripoti kwa kamanda wa kanda maalum ya Dar es salaam. Wakati Zanzibar napo waliteuliwa askari watatu, ambao wote watafanya kazi chini ya Mkuu wa upelelezi wa kituo cha Madema ambae nae atatoa taarifa kwa mkuu wa kituo, na mkuu wa kituo atatoa taarifa kwa Kamishina, ambae yeye ataziwasilisha kwa IGP moja kwa moja. Askari walioteuliwa Unguja ni Staf Sajent Wastara, Sajenti Evodi, pamoja na Koplo haji. Kamishina wa utawala, aliwafahamisha wakuu wao wa kazi uteuzi wao wa kazi maalum kuanza mara moja! Na Kamishina wa Oparesheni, akapanga timu yake sawasawa, nusanusa zikaanza, watoa taarifa wa polisi au wasiri, wakajulishwa kutoa taarifa mara wapatapo fununu ya mauwaji yaliyotokea, kama kawaida zawadi zikatangazwa watu wakaingia kazini.



    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ****

    Mkuu wa upelezi wa kituo cha polisi Madema, alimpa pole Salma Machano baada ya kuzinduka, na kukaa nae pale uani kwa uangalizi zaidi, baada ya kama saa moja hivi akamwambia; “Bi Salma, nitakupa askari akusindikize nyumbani kwako, ili ukaandae mazingira ya sehemu ya msiba. Ama kwa hahika kazi ya mungu haina makosa! Mumeo ameshatangulia mbele ya haki. Hivyo jipange vyema, na sisi tutahakikisha wauwaji wanapatikana, haraka iwezekanavyo! Ili walipwe kwa waliyoyatenda.” Mkuu wa upelelezi alijitahidi kumrai mke wa marehemu kwa kadiri ya uwezo wake, na hatimae Salma akashuka katika hali aliyokuwa angalau, sasa akawa anajielewa.

    WP Monica alipewa jukumu la kumsindikiza Salma nyumbani kwake, akapewa funguo za gari la mkuu wa upelelezi, akampakia Salma akampeleka nyumbani kwake kwa msaada wa maelekezo ya Salma. Walipofika Miembeni wakiwa wapo katika nyumba ya tatu kabla hawajafika nyumba waliyokuwa wanakwenda, Salma alimfanyia ishara Wp Monica asimamishe gari! Kwani aliona kitu ambacho si chakawaida katika macho na fikira zake. Vespa nyekundu ilikuwa imeegeshwa usawa wa nyumba yake ikiwa na dereva aliekuwa akitazama usawa wa nyumba ya Salma. Mara bwana mmoja wa makamo alitoka katika nyumba ya Salma huku akizungumza na simu, na kupanda katika ile Vespa, ikaondolewa kwa mwendo kasi katika eneo lile, ikigeuzwa na kulipa mgongo gari alilokuwa Wp Monica na Salma! “Vipi mbona umeniashiria nisimame, kisha unaitazama sana ile Vespa?!” Wp Monica alimsaili Salma.

    “Afande wale jamaa walioondoka na Vespa, walipotoka ni nyumbani kwangu. Sijui wamefata nini lakini hawaonekani kama ni watu wema! Kwani wasingeondoka kwa mwendo ule!” Salma alijibu, kisha akamtaka WP Monica wafike nyumbani kwake, ili wakajionee wenyewe hali halisi ilivyo! Wp Monica aliindesha ile gari hadi pale nyumbani kwa Salma, wakateremka wote kwa pamoja. Walipoufikia mlango waliuona umefungwa. Salma akatoa ufunguo wake na kuufungua ule mlango. Walipofika ndani, hawakuyaamini macho yao kwa walichokiona! Salma huku wahaka ukimpanda, aliuwendea mlango wa chumba chake, akaukuta upo wazi, sivyo alivyouwacha wakati alipoondoka. Kwani alipoondoka alikuwa ameufunga na funguo! Haraka akajichoma ndani huku WP Monica akimfata kwa karibu, nae akiwa ametaharuki vibaya sana! Huko ndani napo pia kuliwaacha midomo wazi. Ilikuwa ni chakuchaku ya nguvu kuanzia pale sebuleni, hadi chumbani, kumepekuliwa hovyo, vitu vimetupwa shaghala bagala! Kabati la milango mitatu, milango yake yote ilikuwa ipo wazi, nguo zote zilikuwa zimetupwa hovyo chini, hasa upande ule wa nguo za Marehemu Haruna Makupa, ndipo kulikuwa kumepekuliwa sana! “Yaani hii hali niionayo ni kazi ya mtu mmoja tu Yule alietoka humu?!” Wp Monica aliuliza swali ambalo hakupata majibu yake! “Hakika humu kutakuwa kuna kitu muhimu, kama siyo hatari kwa huyu bwana kitakuwa kimewekwa. Isingewezekana kuwe hakuna kitu cha maana kisha kupekuliwe namna hii! Ila nadhani kwa upekuzi huu, bila shaka watakuwa wamekitia mkononi!” Wp Monica alikuwa akiongea kimoyomoyo.

    Wp Monica alitoa simu yake ya mkononi, akampigia mkuu wa upelelezi kumjulisha hali tete waliyokumbana nayo. Mkuu wa upelelezi akamwambia tunakuja sasa hivi hapo ili kujionea hali halisi nipe mwelekeo wa kufika hapo, Wp Monica alitoa maelekezo na simu ilikatwa. Baada ya dakika kama mbili hivi mara walisikia mlio wa gari ikisimama nje ya nyumba. Wp Monica akiwa katika sare zake za polisi, akiwa amevalia shati jeupe, na sketi ya buluu, Viatu vyeusi vinanyong’aa mbele ya kiatu kuliko nyuma, Sox nyeusi, na kofia yake yenye craun. Alitoka nje ili aangalie ugeni uliokuja. Ile anatoa uso wake nje akawaona watu wawili warefu weusi, wakifungua milango katika gari aina ya Suzuki Eskudo nyeupe, mikononi mwao wakiwa wameshikilia silaha kali za kivita AK 47 iliyotengenezwa Urusi mwaka 1947.

    Mara watu wale wakazikoki zile silaha na kuelekea katika nyumba ile. Wp Monica hakuwa na silaha, hivyo haraka bila ya ajizi alikimbilia ndani akamkuta Salma amejibweteka chini analia! Haraka akaufunga mlango kwa ndani na funguo, kisha akazizungusha funguo upande ili mtu akitaka kutumbukiza funguo nyingine katika tundu la funguo lile, ufunguo ule usiweze kutoka mahala ulipo! Kisha kwa nguvu zake zote akakivuta kitanda na kukiweka pale usawa wa mlango huku akihema kwa nguvu! Akatoa simu na kuipiga simu ya Mkuu wa upelelezi, ili haraka apate msaada, lakini simu ya Mkuu wa upelelezi ikawa inatumika! “Mtumiaji wa simu unaempigia kwa sasa, anaongea na simu nyingine, tafadhali jaribu tena baadae!” Wp Monica alisonya na haraka akamrukia Salma aliekuwa amekaa usawa wa mlango akamuamrisha walale chini, huku akimvuta pembeni aondoke mahala pale alipokuwa! Mara wakasikia kitasa cha mlango kikizungushwa, mlango ukawa haufunguki! Wakiwa wamelaliana pale chini, simu ya WP Monica ikaanza kuita kwa sauti. Wp Monica aliichukua ile simu iliyokuwa inatoa mlio, akaitazama namba ya mpigaji, akaona ni namba ya Mkuu wa upelelezi. Haraka aliipokea simu ile lakini hakufanikiwa kusema jambo! Kwani risasi zilirindima katika usawa wa mlango, na Mkuu wa upelelezi akawa anasikia milio ile ya risasi katika simu yake, akapigwa na butwaa!

    Salma pale alipokuwa amelala, mikojo ilikuwa inammwagika hana habari, anapiga kelele kwa woga anachokiongea hakijulikani! Wp Monica alimziba mdomo kwa mkono wake akamnyamazisha! Baada ya sekunde kadhaa risasi zile zikasimama, na kiasi cha dakika moja hivi walisikia milio ya tairi za gari ikisuguana kwa nguvu, na kuacha hali ya ukimya kwa muda katika eneo lile lililokuwa linanuka baruti.

    Wp Monica aliitazama ile simu, na kuiona ilikuwa bado imeunganishwa katika simu ya Mkuu wa upelelezi, akaisemesha ile simu kwa sauti ya chini akinong’ona.

    “Halow Afande, nguvu tafadhali!” Upande wa pili wa simu ile, alisikia sauti ya Mkuu wa upelelezi ikimjibu. “Wp mmesalimika? Sie dakika tatu tutakuwa hapo, kutoa msaada!” Simu ilikatwa.

    Wp Monica akamtazama Salma aliekuwa hajijui hajitambui kwa woga! Akamuona amefumba macho amejikunja amekuwa kama mtoto mdogo! “Ama hakika hili ni Balaa! Kwani humu ndani kuna nini, inaonekana pia wale jamaa walikusudia kuja kumuua na huyu bibie!” Wp Monica alikuwa katika tafakuri nzito, na mara simu yake ikaita kwa fujo, nae akaipokea. “Mpo wapi sie tumeshuka tupo kwa miguu, kwani adui angetuona tukiwa katika gari, ingempa wepesi wa kushambulia na isingekuwa wepesi kupambana!”

    Wp akamjibu kiongozi wake. “Sie wote tupo salama kabisa, ila tumeshambuliwa na adui, lakini kupitia MK (MBINU ZA KUJIHAMI) tumefanikiwa ‘kuklow’ tupo chumbani ndani ya nyumba!” Wp Monica aliongea kwa ukakamavu, kumjuza kiongozi wake, hatua walizozichukua kujiokoa, lakini pia mahali walipo! Simu ikakatwa.

    Baada ya takribani dakika tatu hivi Simu ya Wp Monica iliita akaipokea nakusikia “Ok mnaweza kutoka nje tumeshafika hapa ingawa adui amefanikiwa kuondoka pia amefanya uharibifu mkubwa sana huku!” Mkuu wa upelelezi alimwambia Wp Monica, huku wakiimarisha ulinzi nje ya nyumba ile!

    Wp Monica alikivuta kile kitanda kutoka pale mlangoni, akashindwa kukirejesha nyuma akashangaa! Mwanzo aliwezaje kukivuta kwa urahisi, na sasa kinaelekea kumshinda? Akagungua mwanzo aliweza kuyafanya yote yale kwa kuwa alikuwa ananusurisha roho yake na ya raia asie na hatia Salma Binti Machano. Kwa kuwa sasa hakuna tena uzito ule wa awali ndiyo maana nguvu zimepungua!

    Wp Monica akamwambia Salma wakivute wote kile kitanda, lakini Salma aliona kama ndiyo wanataka kuwaruhusu wale wauwaji waje kuwamaliza, hivyo aliendelea kulala pale chini kama sanamu asiesikia lolote!

    Wp Monica aliushuhudia mlango ule ukiwa umetobolewa vibaya sana na risasi za silaha ile yenye nguvu ya kivita AK 47.

    Mkuu wa upelelezi na askari wengine saba sita wakiwa na silaha aina ya SMG, waliizunguka nyumba ile na kulifanya eneo lile lijaliwe na ulinzi! Wp Monica alitumia nguvu ya ziada akafanikiwa kukisogeza kitanda kwa sehemu ndogo, akaufungua ule mlango kwa funguo iliyokuwa ikining’inia pale mlangoni katika sehemu yake. Alipotoka nje ya chumba kile, akayaona maganda ya risasi kwa hesabu za haraka yanafika kumi na tano! Alipotoka nje ya nyumba ile, akaishuhudia gari ya Mkuu wa upelelezi, ikiwa tairi zake zote nne, zimekaa chini kwa risasi, vioo vimevunjwavunjwa bibaya sana vimekuwa chenga tupu!

    “Afande hili ni Balaa hivyoo, leo ilikuwa niwe maiti wallahi hee! Wale jamaa nilivyowaona sura zao, hawafanani na wanzazibar hata kidogo!” Wp Monica alimwambia kiongozi wake, huku akilikagua lile gari la kiongozi wake, lilivyochakazwa!

    Mkuu wa upelelezi, aliongea kupitia radio ya upepo akaita breck down, na gari yao ya kazi, huku yeye akizama ndani ya chumba na kustaajabu namna alivyoona vitu vilivyopekuliwa na kutawanywa hovyo namna ile. Akaingia kazini katika kuchunguza na kutazama ndani ya nyumba ile! Kiasi ya kama dakika tano hivi, gari ya polisi ilifika eneo la tukio, na dakika mbili baadae Breck down ilifika katika eneo lile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mkuu wa upelelezi alitoka ndani ya nyumba ile, akiwa ameyachukua yale maganda ya risasi, na kuyaweka katika mfuko maalum. Pia walishashughulikia kuchukua alama za vidole katika kitasa cha mlango wa chumbani. Kwani Wp monica alimwambia Mkuu wa upelelezi kuhusu kitasa kile kutaka kufunguliwa kwa nje na wale madui walipofika pale!

    Wp Monica alimtaka Salma abadilishe nguo ili waondoke wote. Hivyo Salma akaenda msalani akajisafisha, kisha akabadilisha nguo na kuchukua nguo kadhaa, akapanda katika gari ya polisi na kuelekea kituo cha polisi Madema.

    Ile gari ya Mkuu wa upelelezi ilifungwa na gari la Breck down, ikavutwa kupelekwa kituoni. Na pale katika nyumba ile waliachwa askari wawili na silaha, wakiilinda nyumba ile, ili asiingie mtu kutoa kitu chochote kile.

    *******





    Jijini Dar es salaam, katika majira ya alasiri makaburi ya kisutu yalijaa uma wa watu Makaburi mawili yalikuwa yamechimbwa jirani jirani! Watu waliguswa sana hasa baada yakusikia wale maiti ni mtu na baba yake mdogo! Makachero walimwagika katika mazishi yale. Maiti zikazikwa, dua zikafanywa kila aina, mwisho watu wakashukuriwa kwa kuzika, na hatimae wakapewa ruksa. Mzee Simba Makupa, alikuwa anahuzuni kubwa sana, lakini pia moyoni mwake alijawa na hofu kuwa watu waliomuua mwanawe na mdogo wake, kama walitaka kumuua na shemeji yake watashindwajwe kumuua na yeye?! Akiwa yupo katika tafakuri nzito pale makaburini mara alihisi bega lake likiguswa! Mzee Simba Makupa aligeuka kumtazama mtu aliemgusa lile bega, akamuona mtu asiemfahamu akimwambia. “Pole sana Bwana Simba kwa msiba mzito, sie ni wenzake Marehemu Haruna kutoka Unguja, tulikuwa tunafanya nae kazi, hivyo tunaomba twende kwenye gari ili tukurudishe nyumbani, lakini pia tukupe mchango wetu wa ubani na sanda.”

    Mzee Simba Makupa aliinuka na kuongozana na yule bwana aliekuwa amevaa kanzu safi nyeupe. Alipofika kwenye gari yao akajipakia ndani yagari katika siti ya nyuma ambayo Yule mtu alioongozana nae alimfungulia ule mlango! Gari ile nyeupe aina ya Toyota Cresta ilikuwa na vioo vya kiza. Yule bwana aliekuwa amevaa kanzu, alipanda katika siti ya mbele ya abiria, na mle ndani ya gari wakaingia watu wengine wawili. Dereva na mtu mwengine aliekuwa amevaa suti safi ya rangi ya kijivu ambae alipanda nyuma, akakaa na Mzee Simba Makupa. hivyo ile gari ikawa na watu wane pamoja na dereva wa gari ile!

    Gari ile iliwashwa na kutoka eneo lile kwa mwendo wa taratibu, huku magari mingine yakiwa katika msururu wa kutoka katika barabara ile ya ALLY KHAN, kuelekea makutano ya barabara ya morogoro. Gari ya tatu kutoka gari aliyokuwamo Mzee Simba Makupa, kulikuwa na watu wawili, dereva na abiria wake, wakiwa wanaifata ile gari aliyokuwamo Mzee Simba Makupa! Na gari ya tano kutoka katika gari zile, ilikuwapo Pick up Toyota Hilux Double Cabin nyeupe ikiwa katika msafara ule!

    Gari ile aliyokuwamo Mzee Simba Makupa, ilipofika pale katika makutano ya barabara ya Morogoro na Ally Khan, ilipinda kulia kuelekea faya. Gari ya nyuma yake ikapinda kushoto kuelekea eneo la Makutano ya barabara ya Bibi Titi Mohamedi, na barabara ya Morogoro. Hivyo ile gari ya tatu iliyokuwa inalifatilia lile gari alilokuwamo Mzee Simba Makupa nalo likapinda kulia likawa nyuma ya gari ile Toyota Cresta. Taa za pale umoja wa vijana na barabara ya Lumumba, ziliruhusu magari kutoka mjini, hivyo magari yale yakapita kwa wepesi, hata walipofika katika makutano ya barabara ya Msimbazi na Morogoro, taa ya kijani bado ilikuwa inawaka, gari zile zikapita! Ile gari ya nyuma, wale watu wawili waliokuwamo mle ndani wakashangaa kuona ile Cresta, ikikaa upande wa kulia wa barabara ile badala yakukaa kushoto na kuingia mtaa wa Swahili ambapo ndipo msiba ulipo, na ndiyo nyumbani kwa Mzee Simba Makupa! Lakini badala yake ile Toyota Cresta ikanyoosha na barabara ya Morogoro!

    Wale watu wawili waliokuwa katika gari aina ya Toyota Noah nyeupe, wakatizamana wakakosa majibu ya msingi! Wakaamua waendelee kufatana na gari lile!

    Walitembea kwa kasi wakiacha magari mawili mbele yao kabla ya ile gari aliyokuwamo Mzee Simba Makupa. Walipofika katika taa za Magomeni pale katika makutano ya barabara ya Kawawa na Morogoro, ile Cresta ikawasha taa kuashiria kupinda kulia kuelekea Kinondoni! Mara baada ya taa kuwaruhusu kupinda, walikata na safari yao ikawa inaendelea! Wale watu waliokuwa katika gari ya nyuma Toyota Noah, yule bwana aliekaa katika kiti cha abiria, alitoa simu yake ya mkononi, akawasiliana mahala kisha akawa na wahaka sana moyoni mwake! Safari ile iliendelea ikapita Kinondoni Studio pale kona ya Mwananyamala na Kawawa, ikapita katika taa za Barabara ya Kinondoni na Kawawa maarufu Manyanya, ikasonga mbele. Ikaipita kona ya kituo cha Kanisani pale Kinondoni Hombozi. Walipofika Moroco pale katika taa za barabara ya Ally Hassani Mwinyi na Kawawa, taa zakuongozea magari zilikuwa zimezuwia gari za Barabara ya Kawawa, na kuruhusu magari yanayotoka mjini katika barabara ya Ally Hassan Mwinyi. Lakini pia walikuwapo askari Polisi wakiwa na silaha zao wakaisimamisha ile gari Toyota Cresta ambayo ilikuwa inasubiri taa ziiruhusu ili iondoke inapopajua, kwani ilizingwa na gari moja tu mbele yake! Wale watu waliokuwa ndani ya ile Cresta, wakashushwa mmoja baada ya mmoja, lakini Mzee Simba Makupa hakushuka! Wale watu waliokuwa katika ile Noah, wakatazamana tena kisha yule bwana aliekuwa amekaa katika kiti cha abiria alishuka chini akapiga hatua hadi pale walipokuwa wale askari katika ile gari. Akajitambulisha “Naitwa Staf Sajent Kubuta, majukumu maalumu!” Kisha akatoa kitambulisho chake, kwani hakuwa amevaa sare zake za kazi! Wale askari wakatoa heshima ya utii kwake, kwani katika wale askari watatu waliokuwa pale hakukuwa na askari mwenye cheo kumzidi yeye!

    Staf Sajenti Kubuta akaufungua mlango wa nyuma wa gari ile na kutizama ndani ya ile gari, moyo wake ulipiga sarakasi kwa alichokiona! Mzee Simba Makupa, alikuwa amelala fofofo hana habari, wala hatikisiki! Usoni mwake alikuwa na rangi ya Buluu! “Shit tia pingu wote hawa” Staf Sajenti Kubuta alisema huku akijipapasa kiunoni kutaka kutoa silaha. Lakini alishindwa! Milio ya risasi ilisikika, wale jamaa pamoja na askari wote wakalala chini kwa ghafula. Mara Toyota Hilux Double cabin iliyokuwa makaburini, Ilitanua kushoto ikapanda kikuta na kusimama pembeni karibu na ile Toyota Cresta, huku jamaa wawili wakiwa na silaha aina ya AK 47, wakirusha risasi kama hawana akili vizuri! Wale jamaa watatu waliinuka na kuirukia ile gari haraka! Gari ile ikachimba tairi zake, na kuondoka mahala pale! Wale askari walirusha risasi na kutua kichwani kwa yule jamaa aliekuwa amesimama akipiga risasi kule walipokuwa wamelala wale askari! Akadondokea ndani ya ile gari, na kuwahiwa na wenzake waliokuwa wamelala chini wakamshika yuke bwana miguu yake asidondoke nje ya gari ile. Lakini silaha yake ilimdondoka na kutua chini ikafyatua risasi kadhaa na kujeruhi raia wema kadhaa na kuharibu magari yaliyokuwa barabarani yakitembea!

    Balaa lililotokea hapo siyo dogo, kwani kila mtu alikuwa anakimbia hovyo kwani hakuna aliethubutu kubaki eneo lile! Hata wale walemavu waliokuwa pale barabarani wakiomba, hakuna hata mmoja aliesalia mahala pale!

    Staf Sajent kubuta, haraka aliinuka kutoka pale alipolala, na kumtizama Mzee Simba Makupa, kama amepatwa na majeraha ya risasi, akamuona yupo salama kwa majanga ya risasi. Tena bado anapumua ila alikuwa katika usingizi mzito! Haraka akaanza kulikagua lile gari, na katika droo ya gari ile akaliona kopo dogo la Lady guard Forsvarsspray, likiwa na picha ya Mbwa mkubwa! Mara moja akatambua mzee Simba alishapuliziwa dawa ya usingizi, Na bila shaka wale jamaa wao wakati wanamspay Mzee Simba Makupa, wao walikuwa wamejifunika pua zao kwa vitambaa vya mkononi ili wasivute hewa yake na wao wakalala! Kwani walimtaka huyu bwana waende nae mahali walipotaka wao!

    Lakini pia kitendo cha ile Toyota Hilux kutokea pale, na kuwatorosha wahalifu wale, ilimuingia akilini kuwa walikuwa wanapambana na wahalifu wakubwa waliojipanga kutekeleza azma yao! Akajipa moyo kuwa mradi gari ya wale mazabania imebaki, basi kazi kwao itaweza kuwa nyepesi kuwafikisha kwa wahalifu wale mara baada ya kulifatilia gari lile usajiri wake na kugundua mmiliki wake halali wa gari ile!

    Mzee Simba Makupa alipelekwa hospitali ya taifa ya muhimbili, kunusuru maisha yake yaliyokuwa yanachungulia kaburi! Lakini pia polisi walimuhitaji sana, kwani inaonekana ana jambo muhimu alijualo! Bila shaka kwa kumtuma mwanawe Unguja, itabidi ijulikane nini alifata kule?! Kwa nini mwanawe auwawe? Lakini pia kwa mtu aliemtuma ambae ni mdogo wake wa tumbo moja na baba mmoja nae auwawe! Kisha na yeye alikuwa auwawe! Mke wa Marehemu Haruna nae alinusurika kuuwawa! Hapana kuna jambo kubwa limejificha nyuma ya pazia ambalo linasababisha Balaa lote hili!!!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ile gari ya wale jamaa Toyota Cresta kwa kuwa iliachwa na funguo zake ndani ya gari, polisi walichukua alama za vidole katika Gia, usukani, vitasa vya milango vya ndani ya gari na kila pahala walipodhani kuwa wale jamaa watakuwa wameshika kwa mikono yao! Kisha gari ile ikapelekwa kituo cha polisi Ostabei kwa upekuzi zaidi!

    *******

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog