Search This Blog

Thursday 27 October 2022

ANGA LA WASHENZI (1) - 3











    Simulizi : Anga La Washenzi (1)

    Sehemu Ya Tatu (3)





    ***





    Rrrrrrrrrrrrnng! Rrrrrrrrrnnngg! Lee akashtuka na kutazama simu yake. Alikuwa maeneo ya nyumbani kwake na majira yalikuwa ni ya saa nne usiku,



    Jina kwenye kioo halikutokea, bali namna mpya. Aksita kidogo kupokea, ila akapuuza na kuweka simu sikioni. Akanyamaza amsikie kwanza sauti ya aliyempigia. Alikuwa ni mwanaume mwenye sauti nzito.



    “Yes, Lee anaongea.”



    “Wewe ndiye yule mchina, si ndio?”



    Lee hapendi kuitwa hivyo. Ila hakujali, alihisi kuna habari njema inafuata. Akawahi kujibu na kutega sikio.



    “Mimi ni baunsa wa hapa klabu ulipoacha namba yako. Nimemwona yule msichana uliyekuwa unamtafuta.”



    “Una uhakika?”



    “Ndio. Kwa mujibu wa maelezo yako.”



    Lee akanyanyuka upesi. Hakumuaga yeyote yule, akajipaki kwenye gari na kwenda moja kwa moja klabu. Alipofika akapiga namba ile iliyompigia, akaongea na kuelekezwa aende wapi.



    Akakutana na baunsa aliyevalia ‘kibodi’ cheupe aliyemdai pesa yake kwanza kabla hajamuonyesha mlengwa.



    “Tulipane kwanza, vipi ukin’toroka.”



    Lee asifanye ajizi, akazama mfukoni na kumpatia baunsa ‘wekundu’ watatu. Baunsa akatabasamu, akamnyakua Lee mpaka ndani. Akamnyooshea kidole mwanamke fulani kwenye kona ya klabu.



    Alikuwa amekaa na wenzake akifunikwa na nywele ndefu za badia. Alikuwa amevalia gauni fupi, pamoja na wenzake pia. Taa za rangii rangi zilikuwa zinamulika mulika watu wakipata ‘kilaji’ kungoja usiku uwe mzito zaidi.



    Mdundo mzito wa muziki ulikuwa unakita.



    Lee akamsogelea mwanamke yule na kumshika bega kwanguvu. Mwanamke huyo alipomtazama, akagundua siye yule aliyekuwa anamtaka. Akaomba radhi na kurejea kwa bodyguard haraka.



    “Sio yule!” akang’aka. Bodyguard akashadadia kwamba maelezo yake yaliendana na mwanamke huyo. Lee akataka pesa yake, bodyguard hakuwa tayari kumpatia.



    Ugomvi ukazuka.



    Wakavutana nje wapate kuonyeshana. Nyama za bodyguard zikamfanya aamini kwamba anaweza kumdhibiti Lee mwenye mwili wa sisimizi.



    Bahati kabla hawajaanza pambano, Lee akamshuhudia mwanamke yule aliyekuwa anamtaka. Alikuwa yupo na mwanaume fulani hivi wakifuata mlango wa kuzamia klabu. Lee akaachana na baunsa yule, akakimbilia kwa yule mwanamke.



    Akamdaka mkono na kumvuta.



    “Unanikumbuka?”



    Mwanamke akaigiza hamjui Lee. Alimtaka mwanaume huyo amwachie mkono wake kabla hajamuitia mwizi. Lee akajikuta anatabasamu. Wakati huo na yule mwanaume aliyeongozana na mwanamke huyo anataka kuchukua hatua dhidi ya Lee.



    “Sitaki ukorofi wowote. Ninachotaka ni pochi yangu na vile vilivyomo ndani tu. Sina shida na pesa bali nyaraka.”



    Bado mwanamke akang’ang’ania msimamo kwamba hana chochote cha Lee. Yule ‘bwana’ aliyekuwa ameambatana na mwanamke huyo akamtaka Lee aondoke na awaache waendelee na mambo yao.



    “Tumekuja hapa kustarehe, si kupigana.”



    Lee akashindwa kuzuia hasira zake, akamvuta kwanguvu yule mwanamke upande wake kisha akamchakaza mwanaume yule mwambatanizi kwa muda usiozidi dakika moja! Mikono na miguu yake ilikuwa mepesi kana kwamba inaendeshwa na mota.



    Haraka naye baunsa akasonga kukata ngebe. Alichokumbana nacho lazima akahadithie nyumbani kwa mkewe.



    Alijikuta anashikilia shingo yake kwa maumivu makali, mbavu zikiwa zimetepeta na yupo chini! Kama ungemuuliza ni kwa muda gani amepigwa hivyo, asingekuwa na jibu moja.



    Lee akahepa zake kufuata gari watu wakimtazama kwa mshangao. Hakuna aliyethubutu kuhangaika naye.



    Akapeleka gari mpaka nyumbani kwa huyo mwanamke akiamuru apewe pochi haraka iwezekanavyo. Hakuwa na hata tone la utani!



    Mwanamke akiwa analia kwa hofu, akatafuta pochi ndani lakini hakuikuta. Akahisi anauawa. Mbona pochi ilikuwepo jana? Alijiuliza akihangaika na mikono yake inayotetemeka.



    Hakuona kitu.



    Macho yake yakiwa mekundu, akamwambia Lee ya kwamba hajapata kitu.



    “Sitaki ujinga na tusipotezeane muda. Naomba pochi!”



    Katika kuchambua fikira zake, mwanamke akakumbuka jana alimleta mgeni chumbani hapo. Pengine yeye ndiye atakuwa kaichukua.



    “Twende kwake,” Lee akasema haraka. Na pasipo kupoteza muda wakaenda mpaka kwa mwanaume huyo. Uzuri mwanamke alikuwa anapafahamu. Ni mwanaume mteja wake wa enzi, mara zingine huwa anaenda kwake huduma ikiwa inahitajika.



    “Naomba niende kuongea naye,” mwanamke akasema walipofika kwenye chumba cha mlengwa wao. Lee akakataa na kutaka waende pamoja kwa kuogopa kutiwa mchanga wa macho.



    Akiwa yupo nyuma, akaongozana na mwanamke huyo mpaka mlangoni, akagonga na uzuri kuna mtu akawapokea, japokuwa hakuwa mlengwa wao. Alikuwa ni mwanamke mnene mweupe aliyevalia khanga.



    Alitoka usingizini na ugeni ule ulimshtua. Lee akaeleza haja yake, lakini mwanamke yule akamwambia hawezi kumsaidia kwani mwenyewe hayupo.



    Lee hakutaka kungoja, akazama ndani kwa mabavu. Akasaka chumba na kukuta pochi yake mezani. Akaipekua, akakuta hamna kitu! Basi asipoteze muda hapo, akachukua picha moja ya mwanaume aliyoikuta mezani, pasipoti, kisha akamrudia yule mwanamke mnene na kumuuliza:



    “Atakuwa ameenda wapi?”



    “Sijui!”



    “Mimi najua atakapokuwa mida hii,” akadakia mwanamke aliyekuja na Lee. Basi pasipo kukawiza, wakaenda kwenye gari na safari ikaanza.



    “Anapenda kwenda sana viwanja. Kama hayupo Ambiance, basi atakuwa Billicanas.”



    Wakaanzia Ambiance, wakahaha klabu nzima. Hapo ndiyo yule mwanamke akajua namna gani Lee alikuwa anamaanisha kutafuta kile kilichomo ndani ya pochi. Alijiuliza ni nini hicho na thamani yake.



    Mungu alikuwa upande wao, wakampata. Mwanamke alimnyooshea Lee kidole na kumnong’oneza kuwa ndiye wanayemtafuta.



    “Naomba vitu vilivyokuwemo kwenye hii pochi,” Lee alienda moja kwa moja kwenye mada akiwa anamtazama mlengwa wake: mwanaume mwenye mwili kiasi, mweusi na nywele nyingi zilizo hovyo.



    Mwanaume yule akaleta nyodo. Akasema vyote vilivyokuwemo amevitupa maana hakuona kama vina umuhimu. Lee akakasirika sana, lakini mwanamke yule akamvutia kando na kumsihi:



    “Usianzishe ukorofi hapa. Niachie hiyo kazi n’takufanyia pasipo kutoa jasho.”



    “Ndani ya muda gani?”



    “Nipe siku moja tu.”



    Lee pasipo kuaga, akaondoka zake baada ya kumkata jicho mwanaume yule ambaye alikuwa tayari ameshaita jamaa zake kwa ajili ya shari. Alimwacha mwanamke aliyekuja naye hapo asionekane kama aliyepotea.



    Akasonya kabla hajakanyaga pedeli ya mafuta.





    ***





    Saa mbili asubuhi …





    “Nitakuchek baadae,” Jona alituma ujumbe mfupi kwenda kwenye namba aliyoitunza kwa jina la Jumanne. Akaweka simu kando na kupasulia mayai mawili kwenye frampeni.



    Alikuwa amevalia bukta ya bluu akiwa kifua wazi. Akili yake ilikuwa inawaza mambo kadhaa, la kwanza juu ya usalama wake. Na pia juu ya Miriam wa mheshimiwa Eliakimu.



    Alikuwa ametenga siku hiyo mahususi kwa ajili ya kupembua, kupanga na kuamua juu ya hatma ya maisha yake kutokana na yanayoendelea kwani hata kipofu angelijua ya kwamba kwa sasa yupo vitani.



    Alikaanga mayai yake akayala pamoja na sharubati. Bado akiendelea kutafakari. Akatathmini maisha yake na tathmini hiyo akaenda kuirejelea kwenye makaratasi yake meupe anayotumia kuchora. Hapo akaandika na kuchora kila ambalo lilikuwa linazingira maisha yake.



    Kuanzia sakata la kifo cha mke na mtoto wake, biashara yake kufa, picha, Eliakimu, Miranda na Kinoo, Bigo, na mauaji yale yote aliyopata kukumbana nayo. Je vitu hivyo vitakuwa vina mahusiano? Akajiuliza na nafsi yake.



    Akachoropoa chupa kubwa ya mvinyo alafu akagida akiendelea kutafakari. Mwishowe alipomaliza chupa nzima, akapitiwa na usingizi baada ya kichwa kuwa kizito.



    Alipokuja kuamka yalikuwa majira ya jioni, na simu yake ilikuwa na jumbe nne, tatu toka kwa Miriam na moja toka kwa Jumanne. Kabla ya kusoma jumbe hizo akaoga, alafu akavaa na kutoka ndani mpaka baa iliyokuwepo karibu.



    Akaagiza maji makubwa tu, alafu ndipo akatoa simu na kuanza kuhangaika nayo.



    “Am in Dar,” (Nipo Dar) alituma ujumbe kwenda kwa Miriam. “Where are you now? When shall we meet?” (Upo wapi saa hii? Lini tutakutana?”)



    Hakutaka kungoja. Alitaka sasa kufanya mambo haraka aone matokeo yatakuwaje. Hakuona haja ya kungoja ngoja kuumiza tumbo.



    Alipotuma ujumbe huo, akaufungua na ujumbe wa Jumanne.



    “Mbona kimya? Kuna mtu amekuja kukuulizia hapa?”



    “Nani huyo?” Jona akatuma ujumbe kuuliza.



    “Hajajitambulisha,” Jumanne akajibu. “Ni jamaa fulani hivi mwembamba.”



    “Alikuja na usafiri?”



    “Sijajua. Sikumwona na usafir”



    Jona akajiuliza juu ya mtu huyo. Inawezekana akawa ndiye yule anayetaka kummaliza? Akajikuta anatikisa kichwa. Wa kwanza alikuwa Bigo, na sasa huyu.



    Suluhisho siyo kummaliza, bali kuukata mzizi kabisa. Endapo akifanikiwa kummaliza huyo anayemtafuta, bado atatumwa mwingine … na mwingine na mwingine. Basi kwakuwa Miranda na Kinoo wanafahamu kuhusu hawa watu, hana budi kuwawahisha kaburini upesi.



    Akanywa maji yake. Muda si mrefu, akapokea ujumbe toka kwa Miriam. Alikuwa amefurahi sana kusikia taarifa ya ‘mtu’ wake kuwapo Dar es salaam. Wakaongea kidogo na akajieleza wapi alipo, wakapanga pia pa kukutania.



    “I think tomorrow I’ll be free.” (Nadhani kesho nitakuwa huru.) aliandika Jona. Akapata uhakika wa kuonana Miriam.



    Baada ya hapo akampigia simu Miranda na kumtaka waonane kesho yake jioni kwani kuna jambo la kuliongelea na kuliweka sawa.





    -----





    Siku iliyofuata, Lamada hotel, majira ya saa sita mchana.





    Jona alikuwa tayari ameshampanga Miriam kwamba wakutane hapo. Miriam alifika hapo hotelini na gari nyeupe Nissan Murano akiwa amevalia suruali ya kitenge. Karibu na mabwawa ya kuogelea, akaketi hapo na kuanza kuteta na Jona kwa kupitia simu.



    Hakufahamu kwamba Jona alikuwa tayari ameshafika eneo hilo, na alikuwa anamtazama.



    Baada ya muda mchache Jona akajitokeza na kusogea papo baada ya kuhakikisha kwamba Miriam alikuwa mwenyewe, hamna kampani. Akaketi na kujitambulisha kwa jina la Roden, na kitambulisho cha polisi akatoa kotini.



    “Usijali, na wala usihofu. Sina haja wala nia ya kukuumiza,” akasema Jona akimtazama Miriam ambaye uso wake ulikuwa mweusi kwa hofu. Hata mwili wake ukitetemeka.



    Jona akasema ametumwa na Eliakimu na yupo pale kwa lengo moja tu, la kumtwaa na kumpeleka huko. Miriam akatikisa kichwa upesi, akamwomba Jona kumwachia huru kwani kumpeleka kwa Eliakimu ni sawa na kumpeleka kwenye domo la simba mwenye njaa.



    “Nipo radhi kwa lolote ila si kunipeleka huko. Nakuomba, nipo chini ya miguu yako.”



    Hii ikawa fursa adhimu sana kwa Jona kutimiza malengo yake. Akaanza kumpeleleza na kumdadavua Miriam kwa undani. Akahakikisha anapata kile ambacho Eliakimu anamficha.



    Alimtaka Miriam afungue simu yake na kumkabidhi. Miriam akafanya hivyo na kinyume na matarajio yake kwamba Jona ataenda kwenye uwanja wa ujumbe, mwanaume huyo akaenda mtandaoni na kupakua kitu fulani na kukitunza kwenye simu ya Miriam. Kisha akairejesha simu na kuendelea na maongezi.



    Tukio hilo lilichukua sekunde ishirini tu kisha akaendelea na maongezi.



    Lakini wakiwa katikati ya maongezi hayo, Jona akasikia sauti ya kike nyuma yake ikinong’oneza kumwamuru asimame akiwa amenyoosha mikono juu! Haikujulikana ni wapi mwanamke huyo ametokea.



    Kwa ustadi mwanamke huyo aliambaa na ukuta na kuhakikisha hagundulikani na yeyote yule. Nywele zake ndefu za bandia zilizozonga uso wake ukijumlisha pia na miwani ya macho, haikuwa rahisi kumng’amua.



    Miriam alimwona mwanamke huyo ila alidhani ni mpita njia. Kumbe alikuwa Nade, na ndani ya koti la zambarau alilolivaa alikuwa ameweka bunduki yake ndogo ambayo kwa sasa mdomo wake ameuminyia kwenye mbavu za Jona. Bado bunduki akiwa ameifichia ndani ya koti.



    Haraka akampekua Jona na kubeba bunduki yake kisha akamtaka asogee mbali na Miriam asogee upande wake haraka. Matukio hayo yakafanikiwa ndani ya muda mchache mno! Nade akatoka na Miriam ndani ya hoteli.



    Wakajipaki ndani ya gari, wakayoyoma! Jona akawatazama namna wanavyoishilia. Akatabasamu na kusema:



    “Kama ilivyopangwa.”



    Nade pasipo kujua alikuwa ametanguliwa hatua mbili mbele.



    Jona alishatambua mpango wa Nade na alifahamu fika mwanamke huyo atakuwa karibu kwani amekuwa akimfuatilia kisirisiri kwa muda sasa.



    Hivyo kila kitu alichokifanya alifanya akiwa amejiandaa na uvamizi ndani ya muda wowote ule. Na akajipanga kunufaika na uvamizi huo kwa kupandikiza 'application' katika simu ya Miriam itakayomsaidia kutambua wapi mwanamke huyo yupo na pia vile vile kumwezesha kusikia angalau sauti!



    Kwahiyo kuondoka kwa Nade akiwa ameongozana na Miriam, kwa Jona ilikuwa ni mpango ulio kamilika.



    Jona akiwa hapo amesimama na macho yake yakishuhudia gari la Nade likiyoyoma kwenda kujichoma, haraka ya punde toka upande wake wa kulia, nje ya uzio, akaona gari aina ya Altezza, ile ile ambayo ilihusika na tukio la kujaribu kummaliza, ikikatiza kwa mwendo pole na kioo cha upande wa dereva kikiwa kimefunguliwa.



    Akatazama kwa ustadi na karibu zaidi, akamwona dereva akifichamua mkono wake wa kulia! Mara akatoa bunduki na kuonyeshea kule alipo Jona!



    Haraka Jona akachumpa na kujikinga kwenye mojawapo ya magari yaliyokuwa yameegeshwa hapo uwanjani. Risasi tatu zikavuma! zikamkosa na kuishia kutoboa magari ya gharama kubwa yasiyo kuwa na makosa. Kisha gari la yule adui, ambaye ni wazi alikuwa ni Panky, likaongeza mwendo maradufu lipate kupotea tukioni!



    Upesi Jona akakimbia kufuata uzio, akauruka kama kiunzi! Akasimama katikati ya barabara na kuzuia gari moja, Toyota Corola nyeupe, kwa ishara ya kunyanyua mkono, akaonyesha kitambulisho chake bandia cha polisi na kumwambia dereva:



    "Nitahitaji gari lako kusaidia jeshi la polisi."



    Akachumpa ndani ya gari na kulitimua mno kukimbiza gari lile Altezza. Mwendo wake ulikuwa mkubwa mno na hata akatanua kando ya barabara ili apate mwanya wa kujiachia zaidi.



    Dereva wa hilo gari akahofia maisha yake. Aliogopa hata kutazama namna gari inavyoendeshwa kwa kushindwa kustahimili. Alitetemeka kwa kukutana na kifo uso kwa uso. Muda wote alikuwa analia gari ipunguzwe mwendo, huku Jona akimwambia hana haja ya kupata shaka!



    Ndani ya muda mfupi, Jona akawa amejiweka usawa mzuri na lile Altezza anayoikimbiza. Sasa walikuwa wamefika Afrikana kuikuta barabara ya kutokea Bagamoyo kwenda katikati ya jiji.



    Panky akakata kona kushika njia kuelekea Bagamoyo. Naye Jona akaunga mkia! Akamzidi maarifa Panky na kumsogelea karibu zaidi na zaidi. Sasa wakawa wamepeana ubapa.



    Ila kichwani mwa Jona hakuwa amelenga kummaliza Panky. Alikuwa na uwezo kamili wa kupindua gari lake ila alimhitaji akiwa hai. Kifo chake kwake pia ingekuwa hasara.



    Hivyo nini alichokuwa anakifanya? Kumpa presha zaidi Panky wamalize njia hii kukaribia kuitafuta Bagamoyo, kule ambapo magari si mengi. Yaani mbele kidogo, katikati ya Bunju na Bagamoyo.



    Akafanikiwa janja hiyo lakini geji ya mafuta ya gari alilokuwa anatumia ikaonyesha mafuta yanaenda kukauka hivyo muda si mrefu sana chombo hicho kitakuwa na kiu ya kushindwa kufanya kazi!



    Sasa ikabidi atumie nafasi hiyo kabla hajawa amepoteza muda wake bure.



    Huu ukawa ni muda wa kumwonyesha na kumfunda Panky ujuzi wake kwenye uendeshaji wa vyombo vya moto. Akawasha 'full lights' kisha akakanyaga mafuta zaidi. Na kutokana na uhodari wake wa kukwepa magari, punde akawa beneti na adui!



    Ndani ya muda mfupi, Jona akafanikiwa kumtoa Panky kwenye barabara ya lami kwa kumtishia kumparamia na gari. Kisha akageuza gari upesi na kukita mti fulani wa wastani kwa kutumia bodi ya nyuma ya gari, mti ukaangukia Altezza na kuibonyeza paa!



    Panky akapoteza mwelekeo na kujikita kwenye chaka la miti. Akajeruhiwa kichwa na miguu. Alivuta hewa mara moja tu na mara Jona akawa amewasili!



    Akamalizia kupasua kioo akafungua loki na kumtwaa Panky. Alikuwa hajiwezi, hoi asiyejitambua. Kichwa kilikuwa kinachuruzika damu. Macho yamemlegea!



    Jona akamlaza chini baada ya kuhakikisha ameshabeba silaha ya adui, akafanya upekuzi wa haraka ndani ya Altezza alafu akayoyoma na Panky.



    ***



    "Kuna kitu umeelewa?" Akauliza Miranda akimtazama Kinoo aliyekuwa ameketi kando yake. Wote mkononi walikuwa wamebebelea karatasi inayofanana. Ile yenye mchoro wa Bite ambao Jona aliwakabidhi.



    Kinoo akatikisa kichwa. Hakuwa amepata kitu! Ni masaa sasa wamekuwa wakiichambua picha hiyo pasipo mafanikio. Sasa wakaona wanafanya kazi ya ubuyu.



    "Tunafanyaje sasa?" Kinoo akauliza. Miranda akashusha kwanza pumzi na kuiweka kando karatasi apate kunywa sharubati yake ya embe. Akafikiri na akaona kuna haja ya kumshirikisha BC katika hilo, pengine anaweza akawa na maarifa.



    Lakini Kinoo akamtaka awe mwangalifu.



    "Hatujamshirikisha hili tangu mwanzo, huoni linaweza likatusababishia tafrani?"



    Miranda akaona hoja ndani ya kauli ya Kinoo. Lakini wasipofanya hivyo itakuaje na ilhali vichwa vishagoma? Kinoo akapendekeza wajaribu zaidi na zaidi hata kama ikiwachukua mwezi.



    Kwa sasa hakuna habari itakayokuwa njema kwa BC isipokuwa ya wao kufungua fumbo hilo.



    "Nahofia yule mchoraji anaweza akang'amua hili kabla yetu," alisema Kinoo.



    "Unadhani akigundua atafanya nini?" Miranda akawahi kuuliza, lakini kabla Kinoo hajajibu, mwenyewe akajipa maelezo.



    "Alichokipata kinamtosha. Hatakiwi ajue zaidi ya hapo. Inabidi tukumbuke kwamba yule si mshirika wala mtu wetu."



    Wakaona kuna haja ya kummaliza Jona punde tu watakapopata mchanganuo wa picha ile. Aidha utoke kwao ama kwa Jona mwenyewe.



    Hakutakiwa kuwa hai baada ya hapo!



    "Hakikisha leo unawasiliana naye kumuuliza kama amepata chochote," alisema Miranda.



    "Unajua mimi siendani na yule lofa. Kwanini usifanye hiyo kazi wewe?" Kinoo akarusha mpira.



    "Ningekuwa nina muda huo, nisingekusumbua. Ila nina appointment. Sidhani kama n'takuwa huru."



    Ulikuwa umebakia muda mchache kwa Miranda kwenda kukutana na Boka - waziri wa Afya. Muda si mrefu aliwasiliana na mheshimiwa huyo wakapanga miadi ndani ya Kempinski hotel ndani ya majira ya jioni.



    Alishamtaarifu BC na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa wao kutengeneza daraja la pili baada ya la sasa kupiga nyufa.



    Kwahiyo karata ilibidi ichezwe vema!



    ---



    Saa 1:12 jioni, Kempinski Hotel, Posta.



    "I have already arrived," (tayari nimeshawasili) alisema Miranda kwa sauti ya puani. Alikuwa amejivika gauni moja matata sana! Rangi nyekundu lisilo na mabega likijishikiza kifuani mwake.



    Hapo kifuani gauni hilo lilikuwa linametameta. likaenda moja kwa moja na mwili wake uliosimamisha nyonga na kudaka mapaja mpaka chini miguuni lilipojiachia.



    Nywele zake zilikuwa zinawaka zikitiririkia mgongoni. Juu kidogo ya sikio la kushoto alikuwa amepachika ua dogo jekundu. Uso wake ulikuwa umekwatuliwa vizuri kwa viwango vya kimataifa!



    Katika kijiwanja hicho cha kupata chochote kitu kilichomo ndani ya hoteli, hakuna aliyekuwa amependeza kama yeye.



    Punde Boka akatokea. Hakupata shida kuangaza kwani Miranda alikuwa anang'aa. Akajisogeza taratibu akiwa anatabasamu. Nyuma yake alikuwa akiongozana na mlinzi.



    Alikuwa amekula suti moja matata nyeusi toka Italia.



    Akaomba radhi kwa kuchelewa. Akahisi moyo wake unakuwa wa baridi kila alimpotazama Miranda ambaye alijua kucheza na macho na tabasamu lake kumzizima mwanaume.



    Boka akajikuta anatabasamu mara kwa mara. Akisisimkwa vinyweleo!



    "Unajua mke wangu hajui juu ya hili kutano letu, na siku ukikutana naye usithubutu kumwambia," alisem Boka akitabasamu.



    "Usijali, sijawa mjinga kiasi hicho," Miranda akamtoa hofu. Mhudumu akaja na kuwahudumia glasi mbili kubwa za juisi ya Raspberry.



    Wakateta kidogo kukumbushiana ya tafrija ile iliyowakutanisha. Ila Boka akapata hamu ya kumjua yule mwanaume aliyekuwa ameongozana na Miranda siku ile, yani BC.



    Miranda asifanye makosa akamwambia yule ni mlezi wake. Alimuasili na kumlelea tangu mtoto kwahiyo kwake anamuita baba.



    Boka akafurahi na kushukuru kwa taarifa asijue Miranda alikuwa anatengeneza 'makao'. Akaanza kumpeleleza Miranda juu ya maisha yake ya mahusiano. Na Miranda kumridhisha akampatia majibu ambayo mwanaume huyo alikuwa anataka kuyasikia.



    "Mpenzi wangu wa kwanza alikuwa ni mtu toka France, lakini nilishindwana naye tabia. Ni mlevi sana na mtu asiye na 'future'. Nikapata mwingine lakini naye hayupo 'serious' so nikaona inabidi nitulie kwanza kabla ya kuzama tena uwanjani."



    Basi Boka akafurahi mpaka jino la mwisho. Na pasipo kukawia akamtongoza Miranda. Kwanza Miranda akaigiza mshtuko ya kwamba hakuwahi kudhani kama kuna siku anaweza akapendwa na mtu 'mkubwa' vile.



    Pili akaigiza uoga juu ya usalama wake kwa mke wa Boka ambaye anaonekana ni mjawa wa wivu. Boka akamtoa shaka.



    "Hilo niachie mimi. Nikubalie uonje matunda ya nchi, mrembo."



    Miranda, akiwa anaminyaminya lips na kuzimumunya, akaomba apewe muda kwani moyo wake uliojeruhiwa huko nyuma unahitaji kushirikisha akili yake kwanza.



    "Kwahiyo mpaka lini mpenzi?"



    "Nitakutaarifu."



    Baada ya hapo wakateta kidogo juu ya mkewe Boka, Boka akimtaarifu Miranda kwamba mkewe anaweza kumtafuta muda si mrefu kwani alikuwaanamwongelea hivi karibuni.



    Hawakukaa tena sana, wakaagana na kila mtu akaenda zake. Miranda akampigia simu BC na kumtaarifu vile mpango ulivyokwenda.



    Yote yalikuwa mema!



    ***



    Simu iliita kwanguvu! Ilikuwa ni alarm ambayo ilimkurupusha Lee toka kitandani akaangaza. Lah! Ilikuwa ni saa kumi na mbili jioni. Akanyanyuka upesi na kwenda kujiandaa pasipo kuoga.



    Akajipaki kwenye gari lake na moja kwa moja akanyookea mpaka nyumbani kwa yule mwanamke ambaye alimuahidi kumtafutia nyaraka yake toka kwa yule mwanaume aliyelala naye.



    Uzuri akafika na kumkuta akiwa ndani nay u maandalizini akikaribia kuruka viwanja. Mwanamke huyu ni kama popo kwani hulala mchana na usiku kwake ni kazini.



    Alikuwa pamoja na marafiki zake watatu ambao walijikuta wanamwonea wivu mwenzao baada ya kumwona akiitwa na mchina. Hawakujua alikuwa matatizoni.



    “Vipi ile ishu?” Lee akauliza. Alikuwa ameegemea ukuta akimtazama mwanamke kama vile maelekezo ya mtihani.



    “Bado hajanipatia,” Mwanamke akajibu. Lee akajikuta akipandwa na hasira! Akauliza shida ni nini, mwanamke akamwambia wale wanaume wamesema wana hizo nyaraka lakini wanataka pesa kwanza.



    Kama kweli ni za muhimu basi na wao wanataka angalau ‘kamgao’. Lee akastaajabu. Yani kamgao na nyaraka ni zangu! Akamkwida mwanamke shingo na kumkazia macho.



    “Nipeleke kwa hao mabazazi!”



    Mwanamke akamwambia si kwa sasa kwani ana mtoko. Lee akacheka na kumwambia hakutakuwa na mtoko wowote ule mpaka pale atakapohakikisha amepata karatasi zake.



    “Twende ama nikuvunje taya saa hii!”



    Basi kwanguvu Lee akampaki mwanamke ndani ya gari na kwenda mpaka kule kwenye yale makazi ya yule mwanaume. Wakagonga lakini hakukuwa na majibu. Wakauliza pia hata kwa majirani pasipo mafanikio.



    “Sijaona mtu leo hii,” alisema jirani mmoja, mmama mnene mweusi aliyekuwa amevalia khanga aliyoifungia kifuani. Mdomo wake mwekundu akiupindua.



    Siku hiyo ndiyo Lee akatambua jina la mwanamke yule anayesumbuka naye kutafuta vilivyo vyake. Alikuwa anaitwa Glady! Akamtaka ampeleke kwenye viwanja anavyoenda huyo mwanaume akamkute huko. Hapo akiwa anajilaumu kwanini ile jana aliimwacha salama.



    “Nadhani alikuwa anahitaji funzo, na mbaya sikumpatia.”



    Kwahiyo Glady na Lee wakaongozana mpaka viwanja. Lakini Glady alikuwa anasisitizia kwamba ule muda sio. Hawawezi kumkuta huyo mlengwa wao huko labda mpaka baadae, usiku ukiwa umevunja ungo.



    Lakini kwa hamu aliyokuwa nayo Lee, hakuelewa! Bado alitaka kwenda akashuhudie na macho. Kweli wakafika kiwanja cha kwanza, hawakupata kitu. Cha pili vilevile hakukuwa na kitu. Mpaka cha tatu!



    Glady akamwambia:



    “Unaona? Hapa inawezekana bado akawa kwenye mihangaiko yake.”



    Lee akauliza: “Na yule mwanamke tuliyemwona jana kule nyumbani?”



    Glady akaangua kwanza kicheko. Akamjibu kuwa yule alikuwa ni malaya tu kama yeye. Mwanaume yule huwa anabadili wanawake, kwahiyo itakuwa hajaleta malaya siku hiyo.



    Lee akachoka. Kichwa kikagoma kuzalisha mawazo kwa muda. Asikae muda, akasikia simu yake inaita. Haraka akaichoropoa mfukoni na kutazama. Alikuwa mkuu! Alimtunza kwa jina la ‘The Big.”



    Akasita kupokea simu akifikiria. Ila mwishowe akapokea na kuongea kwa sauti ya chini.



    Maongezi yakadumu sekunde tatu tu! Akakata simu. Sura yake ilikuwa imenyong’onyea. Na macho yake yalifumbwa kwa mawazo.



    Ujumbe ukaingia kwenye simu yake. Akautazama. Ulikuwa unatoka kwa Nigaa akimuuliza yupo wapi. Hakujibu akairudisha simu mfukoni na kulalia usukani.



    Glady akamuuliza nini kimejiri. Baada ya muda kidogo akamtazama tena Glady na kumuuliza:



    “Ina maana hamna namna nyingine tunayoweza kumpata?”



    Glady akabinua mdomo na kutikisa kichwa. Lee akawasha gari na kutimka! Akamrejesha Glady nyumbani kwake akimuahidi anaweza kuja baadae, alafu akanyookea mpaka yalipo makao yao kwenda kuonana na mkuu.



    “Vipi, ulikuwa wapi?” Nigaa akamuuliza. Lee, kwa sauti ya unyong’onyevu, akamwambia alipotoka.



    “Mkuu alikuwa anakuulizia kweli. Bado hujapata ile ishu?”



    Lee akamwambia namna mambo yalivyo. Nigaa akafunika mdomo kwa kiganja.



    “Sasa utamwambiaje mkuu?” Akauliza.



    “Nitajua huko huko,” Lee akajibu akaminya lips.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nigaa akapendekeza waende wote, ila Lee akakataa. Ule ulikuwa ni wito wake na ilibidi autimize. Kwahiyo akaenda zake, lakini Nigaa akabaki na moyo mzito, basi akasonga karibu na mlango apate kusikia.



    Maongezi yakachukua kama dakika nane. Mara Nigaa akasikia sauti ya risasi! Pah – pah! Kukawa kimya.



    Lee ameuawa? Nigaa akatoa macho.





    ***





    “Katika siku ambazo umefanya kazi za kiume, basi ndiyo hii!” alisema mheshimiwa Eliakimu alafu akaangua cheko pana. Macho yake yalikuwa mekundu. Mkononi alikuwa amebebelea chupa kubwa ya mvinyo akiipeleka mdomoni kupiga tarumbeta.



    Alikuwa amevalia bukta kaki ya ‘timberland’. Kifua chake kilikuwa wazi na miguuni peku. Pembeni yake tu hapo, alikuwa amesimama Nade akiwa amevalia ‘vest’ ya bluu na suruali ya jeans. Mkononi alikuwa amebebelea bunduki.



    Ndani ya chumba hichohicho, alikuwapo pia Miriam. Yeye peke yake ndiyo alikuwa amekaa. Kiti kilikuwa kimoja tu chumba kizima, Miriam alikuwa amefungiwa hapo na kamba ya katani rangi ya manjano.



    “Unastahili zawadi, tena nono!” alisema Mheshimiwa akimtazama Nade. “Na nitakupatia zawadi hiyo kwa kuniletea kichwa huyu mbwa koko hapa ngomeni.”



    Akanyooshea kidole kwa Miriam aliyekuwa amekaa akimtazama kwa uso wa ghadhabu kali.



    Akamwambia Nade kwamba hakuamini pale alipopokea taarifa ya kukamatwa kwa mkewe. Alimfanya asifanye kazi kabisa na kutazamani kutoka ofisini papo hapo. Amekimbiza sana gari mpaka kufika hapo. Hakutaka hata dereva aangaike.



    Alipomaliza kusema hayo, akamtazama Miriam na kumuuliza alikuwapo wapi siku zote hizo. Na huko alikuwa anafanya nini. Miriam akacheka kwanza. Akimtazama mumewe, akasema:



    “Bwana, nilikuwa kwetu. sikutaka kabisa kuwa na wewe, si uligoma kunipa talaka?”



    Mheshimiwa akabana pua na kurudia maneno ya mkewe. Akamzaba kofi kali na kufoka:



    “Unadhani mimi ni mjinga, sio?”



    Eliakimu alikuwa anaamini kuwa mwanamke huyo alikuwepo mahali na anafanya jambo. anahofia siri zake anaweza akawa ameziweka wazi. Hivyo akamlazimisha sana Miriam aongee kwa kutumia mabavu.



    Miriam akachakaa kwa kipigo asiseme kitu. Alitema meno matatu nje lakini bado akisema alikuwa kwa ndugu ambao Eliakimu alishawauliza na wakasema mwanamke huyo hakuwako.



    “Utasema tu … utajua namna gani nilivyo mafia!”



    Wakiendelea na zoezi hilo, mara simu ya Miriam ikanguruma. Ilikuwa ndani ya mfuko wa bukta ya mheshimiwa Eliakimu. Kabla mheshimiwa hajapokea, akamtazama kwa Nade. Alafu akatoa simu hiyo na kutazama.



    ‘My heart’ Pale’ alikuwa anapiga.



    Eliakimu akasonya. Bila shaka huyo ndiye anayemchukulia na kumzuzua mkewe, akasema. Akamtazama Nade na kumkabizi simu apokee ajifanye Miriam.



    Miriam akatamani kupiga kelele, lakini mdomo ulikuwa hautamaniki. Ulikuwa umevuja damu na kupasukapasuka. Ajabu hata Eliakimu alikuwa anangojea mwanamke huyo aongee. Kwa namna gani sasa!



    “Hallow!” akasema Nade kwa sauti ya utulivu.



    “Vipi, mbona sauti imekuwa hivyo?” sauti nzito ya kiume ikauliza.



    “Mafua mafua tu yananisumbua.”



    “Upo wapi?” mwanaume akauliza. Nade akamtazama Eliakimu akifikiria jibu.



    “Nipo kwa shangazi,” ndilo jibu lililokuja kichwani.



    “Unafanya nini huko? Ina maana hujui kwamba huko ni hatari kwa usalama wako?!” Sauti ikafoka.



    “Nitatoka muda si mrefu,” akajibu Nade na kisha akauliza: “Kwani wewe upo wapi saa hii?”



    Sauti ikaelekeza makazi. Alikuwa hoteli ipi na chumba namba ngapi, kisha simu ikakata. Eliakimu akafurahi sana kwani aliona sasa anaenda kumpata na huyo mwanaume amalize kazi.



    Wakaachana na Miriam kwa muda wapange namna ya kumtia nguvuni ‘mwanahizaya’ huyo. Nade akasema yeye mwenyewe atosha kufanya hiyo kazi, ahitaji msaada. Eliakimu akahofia kidogo kutokana na jeraha alilo nalo mwanamke huyo begani.



    “Ukiona inashindikana kumpata hai, mmalize kabisa!”



    “Sawa, mkuu.”



    “Na usisahau na yule mshenzi pia. Hatuwezi jua amepata nini toka kwa huyu malaya. Hakikisha naye unammaliza haraka iwezekanavyo,” Eliakimu aliagiza. Nade akahepa zake.



    Kama isingelikuwa Jona alikuwa hotelini, mahali ambapo kuna watu wengi na ulinzi pia, mwanamke huyu angemdungua risasi Jona. Na Jona alilifahamu hilo hapo kabla na ndiyo maana hakutaka kukutana na Miriam mahali pa kimya zaidi.



    Na pia alifahamu Eliakimu na Nade wataenda kubwabwaja maneno lukuki mbele ya Miriam, ndiyo maana akaishurutisha simu ya Miriam kumletea mrejesho wa sauti zote zilizokuwa zinasikika karibu kwa kupitia ‘application’ aliyokuwa ameipakua.



    Hawakujua Jona alikuwa ‘amewapelekea’ Miriam, ila wampelekee taarifa pasipo jasho. Na alikuwa anafanikiwa hilo!



    Akiwa ametulia chumbani kwake, alikuwa anasikiliza yatukiayo kwa njia ya ‘earphone’. Akajiuliza, je na yeye azuke eneo ambalo Nade ataenda kukutana na mwanaume yule anayedaiwa ndiye kipenzi cha Miriam kwa sasa?



    Hakupata jibu haraka.





    **





    Ujumbe ukaingia kwenye simu ya Kinoo - kweng! kweng! – kweng! kweng!



    Mwanaume huyo alikuwa amejilaza kitandani akiwa amevaa nguo ya ndani tu. kwa mujibu wa saa yake ya mkononi ambayo alikuwa ameiweka juu ya meza, ilikuwa inasema ni saa nne na robo.



    Na ama kwa hakika, hii ilikuwa ni mojawapo ya siku nadra sana kumwona Kinoo hajavalia kibodi chake cheusi. Kifua chake kilikuwa kipo nje kinahema akiwa amelowea usingizi.



    Hakusikia sauti ya mlio wa ujumbe. Ila ujumbe huo ukajirudia mara mbili, na baada ya muda kidogo simu ikaanza kuita. Kinoo akamka na kutazama. Namba ngeni! Akajivuta kupokea akijiuliza ni nani huyo amsumbuaye.



    “Hallow!”



    “Hallo, Sarah hapa. Unanikumbuka?” sauti ya kike iliuliza kwa pupa. Kinoo akaguna akijaribu kuvuta kumbukumbu. Sarah? … Saraaah…



    “Yule mfanyakazi wa marehemu Bite!” Sarah akamkubusha. Sasa Kinoo akamkumbuka. Alikuwa ni mmoja wa wale mapacha wawili aliwaona kwenye kikao cha siku ile.



    Amepata wapi namba yake na alikuwa anataka kumwambia nini? Akajiuliza upesi akijtengenezea kitako. Sarah akamwambia juu ya mauaji ya Mudy. Kinoo akashtuka sana! Sarah akamwambia na mpaka kuzikwa alishazikwa. Kilichomfanya akampigia ni kutomuona msibani.



    Kisha simu ikakata!







    Kinoo akafanya mpango wa kuongeza salio alafu akamtafuta tena Sarah na kumuuliza juu ya makazi yake. Sarah akamwelekeza na Kinoo akamuahidi kwenda kumtembelea muda si mrefu. Haitazidi lisaa.



    Kinoo akajiandaa, kwa kutinga kibodi chake cheusi na suruali ya jeans, akabebelea bunduki ndogo na kisha kujipaki kwenye pikipiki yake kubwa na safari ikaanza. Huko barabarani kulikuwa kuna magari machache, muda wa foleni ulikuwa umeshapita.



    Hakuchukua muda mrefu sana mpaka kuwasili alipoelekezwa na Sarah, maeneo ya Sinza Palestina. Akakuta gari, VX ya grey, nje ya makazi hayo.



    Gari hili halikuwa jipya machoni. Akatafakari kwa muda mfupi na jibu akalipata, aliliona siku ile ya kikao! La nani?



    Lilikuwa ni gari la Brokoli! Akili yake ikalipuka. Haraka akaficha pikipiki yake ubavni mwa nyumba na kulifuata gari lile karibu. Akatambua limekuja hapo muda si mrefu. Lilikuwa na joto kubwa.



    Basi akasogelea dirishani ambapo angeweza kusikia chochote kitu toka ndani. Alikuwa na hamu ya kujua nini kimemleta Brokoli hapo. Walikuwa na ajenda gani wanayojadili?



    Kwa akili ya Kinoo akafahamu fika kuwa ujio ule wa Brokoli ulikuwa ni wa ghafla. Laiti kama Sarah angelikuwa anaufahamu, basi angelimtaarifu.



    Akatazama ndani asione kitu, ila akasikia sauti ya Brokoli ikinguruma. Maneno mengi hayakuwa anayasikia vizuri. Ila kwa sauti na namna yalivyokuwa yanatamkwa, yalikuwa ni maagizo ama matisho. Akili ya Kinoo ikasema vivyo.



    Kwa dakika kama tano mbele, akasikia sauti ya vishindo vya miguu inasogea. Haraka akajificha na kuchngulia. Akamwona Brokoli aliyekuwa amevalia Kaunda suti ya kahawia akiingia kwenye gari na kuhepa.



    Akatoka mafichoni na kwenda kukutana na Sarah. Alikuwa ameketi sebuleni akilia. Macho yake yalikuwa mekundu na nywele zake hazikuwa mpangilioni. Sasha hakuwepo, yeye alisafiri.



    Kinoo akamuuliza kwanza juu ya ujio wa Brokoli hapo, haswa muda huo na kwanini analia. Sarah akamwambia ya kwamba ameacha kazi, na hataki tena! Akiwa anapaliwa na kilio hakuwa anaongea vema.



    Kinoo akawa ana kibarua cha kumbembeleza.



    “Amesema hataki kuona yeyote yule anasumbuka wala kusema chochote kuhusu kifo cha Mudy. Amefuatilia polisi na amewaachia kesi huko. Nimemwambia naacha kazi, akaniambia niache na kila kitu. Asije akasikia nimesema chochote kinachohusu ofisi. Nikithubutu, nitakiona cha mtema kuni!”



    Kinoo akastaajabu. Na pamoja na Sarah wakamshuku Brokoli kuhusika na kifo cha Mudy. Na hata vile vile mkono wake utakuwemo kwenye kifo cha Bite.



    “Vifo vyao vinafanana. Nahofia nisije nikawa anayefuata,” alisema Sarah akilowanisha macho yake kwa machozi.



    Akamwonya na Kinoo kuwa hayupo salama, inabidi awe mwangalifu sana.



    “Kuna taarifa amesema Mudy alizichukua kule ofisini na kumkabidhi mtu mwingine, jina hakumtaja. Na taarifa hizo ni nyeti. Bila shaka mtu huyo atakuwa ni wewe.”



    Kinoo akakiri. Na akamwambia wamefuatilia nyaraka hizo na kugundua zina mahusiano na shirika fulani, tawi la kampuni kubwa ya kichina. Hapo Sarah akagutuka na jambo.



    “Wachina?” Akauliza.



    “Ndio, wachina. Unawajua?” Kinoo akatia swali.



    Sarah akasema hawajui ila alikuwa anawaona mara kadhaa pale ofisini wakija kuteta na Bite. Na hata kwenye baadhi ya vikao walikuwa wanahudhuria. Ila hawakuwahi kujua wanahusika na nini.



    “Hatujawahi kupewa mrejesho wa vikao vyao. Walikuwa wakivifanya kwa siri,” alisema Sarah. “Kikao cha mwisho wachina hao walikaa pamoja na Bite na Brokoli, ndipo likapita juma moja na Bite akauawa.”



    Kinoo akamuuliza Sarah kama kuna chochote anachokijua baina ya pande hizi mbili, wachina na Bite. Walikuwa wana mahusiano gani na nini kiliwaunganisha. Sarah akasema hajui lolote zaidi ya wachina hao kuwa ‘partners’ wa mbali.



    Kwa usalama, Kinoo akamshauri aondoe makazi yake hapo maana hawezi jua nini Brokoli amelenga kumfanyia. Sarah akasema hana pa kuelekea. Hana makazi mengine mbali na hayo na ndiyo hivyo kazi ameshaikataa.



    Kinoo akapendekeza akakae kwake kama hatojali. Sarah akakubali baada ya mafikirio kidogo. Akabeba nguo zake chache alafu wakaondoka na Kinoo.





    ***





    Baada ya Jona kutoka mezani kwake, alikwapua ndoo moja ya bati iliyojaa maji, akaongozana nayo mpaka stoo iliyopo nje. Akafungua mlango na kuwasha taa, kukawa na mwanga!



    Ndani ya stoo hiyo iliyokuwa na vitu vichache, alikuwa amelala Panky humo akiwa amefungwa miguu na mikono. Kichwani mwake alikuwa na majeraha yaliyoacha kutoa damu.



    Jona akammwagia maji kumwamsha. Panky akakurupuka na kutoa macho kumtazama Jona.



    “Muda wa kulala umeisha,” Jona akasema akichuchumaa na kumtazama Panky kwa ukaribu. Mwanaume huyo alikuwa amevimba upande wake wa kushoto wa uso.



    Jona pasipo kupoteza muda akamuliza ni nini alikuwa anataka kwake na nani amemtuma. Aliyauliza hayo kwa kujua mtu huyo hatasema, na hata mwishowe anaweza akafanya jaribio la kujimaliza kwa kuunyofoa ulimi.



    Kama ilivyotarajiwa, Panky akaleta ubishi. Hakuwa radhi kusema chochote kile na yuko radhi kufa. Jona akaendea kidumu cha maji cha lita tano, alafu akachomoa leso ya kufutia jasho mfukoni na kuifungia usoni mwa Panky.



    Taratibu akaanza kumwagia maji juu ya leso hiyo, akihakikisha maeneo ya pua na mdomo yanapata maji ya kutosha. Panky akahangaika kuhema. Kila alipovuta pumzi akawa anavuta maji puani na mdomoni.



    Akapaliwa na kupata shida mno!



    Jona akabandua leso usoni mwa Panky na kumuliza kama yupo tayari kuongea ama lah. Kabla Panky hajajibu akakohoa sana na kuhaha kutafuta pumzi. Lakini akasema hayupo tayari kusema kitu!



    Jona asiongee sana, akarudia zoezi lake mara tatu. Panky akashindwa kuvumilia na mara akaanza kuhororoja. Akasema ametumwa na mkuu wake kuja kummaliza.



    “Kwasababu gani minimalize?”



    Panky akasema hakuambiwa kwa sabab gani amalizwe, ila agizo tu ya kwamba amalizwe. Zaidi ya hapo hakuna anachojua. Yeye ni mtu wa kuagizwa tu na kwenda kutenda.



    Jona akamuuliza juu ya makao ya mkuu wake na anajishughulisha na nini. Panky akamtaja mkuu wake kwa jina moja la Sheng’ akisema ni mfanyabiashara wa vipuri vya magari.



    Jona akakumbuka jina hilo la Sheng’. Alikuwa ndiye yule mshirika ambaye mke wa Fakiri alimweleza. Akamuuliza Panky juu ya mauaji hayo, Panky akasema hayafahamu.

    Hapa Jona akapata maswali, Sheng’ anajihusisha na biashara ngapi? Na imekuaje Panky akasema mambo hayo kwa wepesi hivyo tofauti na Bigo ambaye aliamua kujiua?



    Mfukoni akatoa kitambulisho cha kura cha Panky, leseni na makaratasi kadhaa. Akayatazama kwa muda kidogo, kabla hajamuuliza Panky kama anajua lolote kuhusu ‘Pumzi ya mwisho’.



    Panky akasema hajui kitu. Jona akahisi anamdanganya. Akamwambia juu ya Bigo na kumgusia juu ya kikundi hicho kuhusika na mauaji. Panky akakiri, lakini akasema yeye afahamu kitengo hicho japokuwa inawezekana kikawa kipo.



    “Kuna vikundi vingi ndani yetu, na kila kikundi kina majukmu yake ya kuyatimiza,” alisema Panky ndani ya kamba.



    “Na wewe upo kikundi gani kati ya hivyo?” Jona akauliza. Panky akamwambia yupo kwenye kikundi cha ‘Space button’. Kikundi kinachohusika na mambo ya teknolojia, haswa udukuzi.



    “Sasa ikawaje ukatumwa kummaliza mtu na ingali si kazi yako?” Jona akauliza.



    “Hii ni adhabu nimepewa kwasababu ya kufeli kufanya vema kazi yangu iliyopita. Punde unapokosea, huwa unauawa. Nimetumwa kukumaliza kama namna ya kusahihisha makosa yangu. Ikishindikana basi nifie huko huko kama adhabu yangu inavyosema.”



    Jona akafahamu kwanini mateka hyo ameongea kwa urahisi tofauti na Bigo. Hakuwa mtu anayehusika na mauaji bali wa kukaa mbele ya kioo cha tarakilishi. Hata mafunzo ya kujilinda hakuwa nayo na ndiyo maana hakumpatia changamoto pindi anamtia nguvuni.



    Lakini Jona akataka kujua ni kosa gani ambalo Panky amelifanya kupelekea kupewa adhabu kama hiyo. Panky akamweleza ni upotevu wa faili moja muhimu sana kwenye mtindo data wao. Faili ambalo hajajua limepoteaje mpaka muda huo.



    “Kwanini unaniambia yote haya?” Jona akauliza. Panky akashusha kwanza pumzi yake, na kusema kwa huzuni.



    “Najua naenda kufa tu. Angalau nimpe mtu mwanga ama mahali pa kuanzia kuukata mbuyu huu … kama si na wewe, basi nitamalizwa na mkuu wangu. Sina haja ya kufa na taarifa hizi.”



    Jona akamwambia hana tatizo naye, atakapopata anachokihitaji, yupo radhi kumwachia. Panky akatabasamu na kutikisa kichwa chake.



    “Hata kama ukiniacha hai, sitadumu. Hamna namna ya kumkimbia Sheng’. Hata uwe wapi atakutia tu mikononi na kukumaliza.”



    Panky akaongezea ya kwamba pindi unapoingia ndani ya mfumo wa Sheng’, familia yako yote anakuwa anaijua. Watu wako wa karibu na marafiki zako. Ni labda ajue umekufa, na si hai akakukosa!



    “Watu kadhaa walishawahi kutoroka, wengine wakitaka kuacha kazi kwa hiyari. Hakuna aliyebakiziwa uhai hata mmoja! Kwa Sheng’ kuna kuingia tu, mlango wa kutokea haupo. Na utakapoulazimisha kuujenga ukutani, basi utalipia gharama zake.”

    .

    Jona hakuona haja ya kuendelea kumweka Panky mule stoo kwa ushirikiano wake alioutoa. Akamfungua kamba na kwenda naye ndani alipomkabidhia nguo kavu na nadhifu. Wakaendelea kuongea kwa muda kidogo Jona akipeleleza baadhi ya taarifa.



    Panky pasipo kumficha akampatia Jona zile azijuazo. Namna gani alikuwa anatenda na kumsaidia Sheng’ kukamata Tanzania nzima, Afriika Mashariki, na hatimaye Afrika nzima. Namna gani wanavyokusanya data toka sehemu nyeti mbali mbali na kumkabidhi Sheng’ kwa ajili ya kazi zake binafsi atakazogawia vitengo vingine.



    Kwa maelezo hayo, Jona akapata uelewa namna gani Panky alivyokuwa na uwezo wa kucheza na tarakilishi kwenye kila kona. Namna gani ujuzi wake ulivyokuwa mkubwa kwenye kunyambulisha taarifa, kutengeneza na kuzipoteza.



    “Kama kuna taarifa ama data hatari kwa Sheng’, na taarifa hiyo ipo kwenye mashine ama tarakilishi ya mtu yeyote yule, basi ni jukumu letu kuipoteza. Tunatengeneza virusi na kuvituma kwa mtandao kama mashine ipo mbali. Virusi hao watakula mafaili yote watakayokuta humo na kiacha mashine tupu!”



    Kitengo hicho hicho cha Space Button ndicho kinahusika na ukusanyaji wa taarifa popote pale ilipo kwa njia za kisasa aidha mwenye taarifa anataka ama hataki. Kama kuna mkataba ambao Sheng’ anautaka, na upo mtandaoni ama kwenye tarakilishi ya mhusika yeyote ule. Wakimtambua wataupata!



    “Sheng’ ana mikataba yote ya ujenzi, madini, ardhi na kila kitu. Ana taarifa za mawaziri, na wabunge. Ana taarifa za taasisi kubwa kubwa, yote hayo yakiwezekana kwa kupitia kitengo hichi cha Space Button.”



    Pia kwa kupitia mkono wa kitengo hicho, huwa wanabambikizia watu kesi kwa kuwawekea vitu ndani ya tarakilishi zao ama kwenye tovuti zao. Kutengeneza ‘application’ mbalimbali kwa ajili ya kufanyia kazi za Sheng’.



    Jona akamuuliza kama kuna uwezekano wowote wa kupata data na taarifa zilizopo kwenye ‘vault’ ya Sheng’. Panky akamwambia kitu hicho hakiwezekani na hakiwezi kufanywa na mhsika yeyote yule wa Space Button kwasababu imewekwa katika usala sana.



    “Kufungua Vault ya Sheng’ utahitaji alama za vidole gumba vya wahusika wote wa Space Button, na utahitaji code nne ambazo ni Sheng’ peke yake anazifahamu.”



    Maelezo hayo yakamvutia sana Jona. Kichwani kwake haraka akapata wazo la kumtumia Panky katika kazi zake. Alitafakari ni kwa namna gani ujuzi wa mwanaume huyo utakavyoweza kukamilisha kazi zake kwa ufanisi zaidi.



    Lakini akahofia, bado Panky hakuwa mtu wa kumwamini kiasi hicho. Bado alihitaji kumpekua na kumsoma zaidi. Na pia kama ataridhia kufanya naye kazi, maana ni jambo la hiari, si lazima.



    “Unaona picha hii?” Jona alimwonyeshea Panky picha ile aliyochora kwa ajili ya Bite. Akamwambia hiyo ndiyo sababu anatafutwa na uhai wake unawindwa. Je ana ufahamu nayo?



    Panky akaiteka picha hiyo kwa mikono yake na kuitazama kwa makini. Kuna jambo alikuwa analifikiria, wapi aliona picha ile. Kumbukumbu ikamjia, alishawahi iona siku moja kule ofisini kwao, mwenzake akiwa anaishughulikia.



    “Sijui ina maanisha nini lakini nakumbuka siku moja niliwahi kuiona picha hii ofisini, na ndiyo ilikuwa inatengenezwa. Sikuwahi kuifuatilia wala kuiona tena.”



    Jona akamuuliza kama anamfaham mtu huyo aliyekuwa anaitengeneza, Panky akasema anamfahamu mpaka na makazi yake. Jona akapanga waende kumtafuta mtu huyo ambaye alitambulishwa kwa jina la Marwa.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lakini kabla ya kwenda huko inabidi akakutane kwanza na yule mwanaume ambaye Nade anataka kwenda kumdhibiti kwa kuhusiana na Miriam – mke wa mheshimiwa. Kazi hiyo ilikuwa ni ya kufanywa kesho yake kwenye majira ya mchana mpevu.





    ***





    Saa tatu asubuhi…





    “Huwezi amini yule mzee ameshammaliza yule jamaa!” Alisema Kinoo aliyekuwa amebebelea kikombe cheupe cha chai. Akiwa amekaa na Miranda ambaye mkononi alikuwa ameshikilia simu yake kubwa akiperuzi.



    Ni ndani ya nyumba ya Miranda, Kinoo akiwa amewasili hapo muda si mwingi. Miranda alikuwa amevalia dera, nywele zake zikifungashwa na kiremba cheusi.



    Kinoo alikwa hapo kumhabarisha juu ya kifo cha Mudy, mwanaume ambaye amewapatia nyaraka zile za kampuni ya umeme wa jua.



    Miranda akashangazwa na taarifa hizo. Kifo cha Mudy kilikuwa ni ishara kwamba na wao, ambao wanamiliki nyaraka hizo, wanaweza wakawa ndiyo ‘tageti’ inayofuatia.



    “Ni kweli,” Kinoo akamwambia. “Inabidi tuwe makini, la sivyo tutaenda na maji.”



    Miranda akasonya na kubinua mdomo. Akamtazama Kinoo kwa macho ya bumbuwazi na kumwambia hawana haja ya kuishi kama digidigi sababu ya Brokoli. Kama ameanzisha vita, basi hawana budi kupambana kabla haijatoka nje ya mikono yao.



    “Tuchunge ngamia huyu asije akawa mkubwa kuliko banda. Endapo tukimwacha Brokoli akaendeleza saga hili, linaweza kuwaamsha majabali yaliyolala. Akuanzae mmalize.”



    Kinoo akasita kiaina. Lakini Miranda hakuona haja yay eye kufanya hivyo kwani aliamini hayo maamuzi ya yeye kumuua Mudy yametoka mikononi mwake. Na kama amemuua Mudy, sababu ya nyaraka, hatakomea hapo.



    Je wapo radhi kuuawa?



    “Lakini sifahamu makazi yake,” akasema Kinoo. Miranda akamuuliza:



    “Umetafuta ukakosa? Mbona unakuwa kama mgeni kazini.”



    Kinoo akakumbuka numbani anaishi na Sarah, pengine atakuwa anafahamu. Akaacha kuulizwa maswali ya ‘kijinga’ kama asemavyo Miranda.



    “Kwahiyo kwa muda gani utakuwa umemaliza hiyo kazi?” Miranda akauliza akimtazama Kinoo na macho yake aliyoyatoa kwenye kioo cha simu.



    “Nahitaji siku moja tu,” akajibu Kinoo na mjadala huo ukaisha. Miranda akamwambia Kinoo kwamba baadae jioni ana miadi ya kwenda kukutana na mke wa Boka nyumbani kwake Upanga kwa ajili ya majadiliano.



    Hivyo atamtaka ampeleke huko kama atakuwa na muda. Ajabu Kinoo akakataa, akimwambia ya kwamba ana kazi ya kufanya usiku. Miranda akataka kjua kazi hiyo.



    “Tangu lini ukawa na kazi usiku nisijue?”



    Kinoo akatabasamu kwanza kabla hajamtaarifu Miranda ya kwamba anaishi na Sarah – aliyekuwa mfanyakazi wa Bite kwasababu za usalama. Miranda akastaajabu. Alihofia juu ya usalama wao.



    “Vipi kama huyo binti akakuchota taarifa?”



    Kinoo akamtoa hofu. Anajua mwanamke huyo hatakuwa na lolote kmdhuru. Miranda akamtaka awe makini na macho muda wote.



    “Najua umewahi kumpa hifadhi kwasababu ni mwanamke. Huna lolote!”



    Kinoo akatabasamu na kukanusha pasipo kumaanisha.





    ***





    Saa nane mchana…





    Gari aina ya Harrier rangi ya fedha inapaki kwenye uwanja wa hoteli, na baada ya punde Nade anashuka. Amevalia miwani meupe ya urembo. Koti dogo jeusi linalobana mwili wake. Suruali ya jeans na raba nyeupe.



    Mkono wake wa kulia umebebelea simu ya Miriam. Na kama ukimtazama vizuri nyuma ya koti lake, utaona amefichama bunduki ndogo. Ila mpaka utazame kwa makini! Kitu ambacho ni kigmu kidogo kutokana na mwanamke huyo anavyovutia, utatazama vingine.



    Akatazama kushoto na kulia. Akaridhia kila kitu kipo sawa. Akanyookea mapokezi, ambapo aliteta kidogo kabla ya kuelekezwa kwenda chumba namba fulani ambacho ndipo mtu anayemhitaji yupo.



    Akabisha hodi.



    Hakukuwa na majibu. Akabisha tena na tena, pasipo majibu. Akatazama simu kwa malengo ya kupiga kumtaarifu ‘mwenyeji’ kuwa ameshafika, yupo nje. Inabidi amfungulie.



    Kwenye simu akakuta ujumbe. Kwasababu simu ilikuwa ‘silent’ hakujua ujumbe umeingia saa ngapi. Ilikuwa ni kama dakika kumi na tano zilizopita. Ina maana akiwa njiani kuja.



    Na ujumbe huu ulikuwa umetokea kwa ‘My Heart Pale’, yaani yule mwanaume mtuhumiwa wa mahusiano na Miriam.



    ‘Jipangeni upya. Sipatikani kwa wepesi kiasi hicho. Mnapolala ndipo mimi naamkia.’



    Shabash! Amejuaje? Nade akajiuliza. Akatazama kushoto na kulia kana kwamba labda mtu huyo anamtazama. Hakuona mtu. Akatoka eneo hilo na kwenda mapokezi kuulizia.



    “Sijui, labda kweli kaondoka maana mie nimeingia zamu muda si mrefu,” alijibu mdada wa mapokezi. Nade akasonya. Itakuwa mwanaume huyo amegutuka na sauti yake, akawaza.



    Lakini mwanaume huyo akampatia mawazo Nade. Atakuwa ni mtu mwerevu, ama mwenye uzoefu na mambo haya. Anajihusisha na nini?



    Akatoka nje ya hoteli akiendelea kutazamatazama na kuwaza kichwani. Akafungua gari na kuzama ndani. Lakini kabla hajawasha chombo, akahisi kitu cha baridi shingoni, na amri:



    “Tulia hivyo hivyo!"



    Sauti hiyo ya kiume ilikuwa ngeni kwa Nade. Hakujua ni nani huyo, akapapaswa na woga. Alikuwa amezidiwa ujanja, akawa mpole kama maji mtungini.



    "Haya washa gari na twende ntakapokuelekeza," sauti ikaamuru. Nade akawasha gari na kutoka eneo la hotelini akipewa maelekezo na mwanaume aliyekuwa amemteka.



    Sura ya mwanaume huyu ilikuwa mpya! Alikuwa ni mbaba mweusi mwenye nywele fupi zilizochanjwa 'ways' nne. Macho yake yalikuwa mekundu na madogo.



    Mikono yake ilikuwa imepitiwa pitiwa na michirizi ya mishipa lukuki. Alikuwa amevalia shati 'beach boy' na suruali ya jeans iliyokoza.



    Mwanaume huyu anajulikana kwa jina la Nyokaa! 'Chalii' wa Arusha maarufu kwa pesa za madini. Kazi ambayo aliianza tokea akiwa mtoto mdogo, 'nyokaa' lakini mpaka leo hii amekuwa mtu mzima, jibaba, bado anajulikana kwa jina hilo hilo maarufu.



    Alimwongoza Nade mpaka nje ya jiji akiwa amenyamaza asiseme lolote. Akamwamuru asimamishe gari na kuanza kumuuliza maswali.



    Akataka kujua Miriam yupo wapi na yupo na nani. Yeye ni nani na ametumwa kuja kufanya nini? Nade akalaghai Miriam yupo polisi, na yeye ni polisi pia.



    Nyokaa akajua janja hiyo. Akamtishia Nade kuwa atamnyofoa uhai wake kama akiendelea na michezo yake ya kitoto!



    "Sina muda wa kupoteza we malaya! Sawa? Najua Miriam atakuwa kwa Eliakimu. Na wewe utakuwa kibaraka wake. Usinifanye mimi mtoto mdogo, najua kila kinachoendelea!"



    "Sasa kwanini unaniuliza kama unajua kila kitu?" Nade akauliza. Nyokaa akamzaba kofi zito lililomchana Nade lips. Akavuja damu.



    "Unifahamu vizuri, mwanamke! Ngoja utanijua vema muda si mwingi na utanipa kila ninachokitaka."



    Baada ya Nyokaa kusema hivyo akamziraisha Nade kwa kumpiga na kitako cha bunduki kisogoni. Kisha akampigia simu mtu aliyemtunza kwa jina la Ninjaa.



    Akamwelekeza mahali alipo na kumtaka afike hapo muda si mrefu kuna kazi wanatakiwa kuifanya. Lakini pia akamtaka ajiweke sawa kwa kuwapasha habari wengineo ya kwamba vita inaweza kuzuka muda wowote.



    Basi haikuchukua muda mrefu, gari moja kubwa Hammer nyekundu ikasogea eneo la tukio. Wakashuka njemba tatu, mmoja wao akiwa ndiyo yule Ninjaa.



    Watu hawa walikuwa wanafanana kwa rangi, weusi, na wenye sura angama za kazi. Miili yao ilikuwa mirefu na iliyojaa.



    Wakateta na Nyokaa kwa muda kidogo, wakamchukua Nade na kumtia kwenye Hammer kisha wakalipua gari ya Nade na kuhepa!



    Kitu ambacho hawakuwa wanajua ni kwamba kuna mtu upande mwingine aliyekuwa anasikiliza kila jambo. Mtu huyu aliona wakati Nade akitekwa na hakufanya jambo lolote.



    Mtu huyu aliachwa kule hotelini, ila bado alikuwa anawafuatilia kwa ukaribu akitumia kifaa cha simu cha Miriam ambacho Nade alikuwa nacho mfukoni.



    Mtu huyu ndiye pekee aliyekuwa anajua kama Nade ametekwa na wapi anapelekwa. Hakuwa mwingine bali Jona!



    Mambo yalikuwa yanazidi kupamba moto, na hakutaka kujishughulisha kuuzima moto huu upesi mpaka aone haswa kina cha maji haya ambayo hayatakiwi kupimwa kwa mguu!



    Baada ya muda mfupi Nade kuziraishwa, Jona akatimka toka mazingirani mwa hoteli kichwani mwake akiwaza mambo kadhaa ambayo hakika hakuwa na majibu nayo.



    Akawaza kama kuna namna zaidi ambayo anaweza akatumia kupata zaidi mambo toka kwenye ile application ambayo ameipakua na kuitunza kwenye simu ya Nade.



    Hapo akapata wazo la kumshirikisha Panky. Huenda mwanaume huyo akawa na mawazo zaidi. Ila kwanza akapitia kazini kwake kuhakikisha kila jambo lipo sawa kabla ya kunyookea nyumbani.



    Huko ambapo alikuwa amemfungia Panky.





    ***





    "Sasa?" Nigaa akauliza baada ya kuchomoa sigara yake mdomoni. Macho yake yalikuwa yanamtazama Lee ambaye alikuwa ameshika tama. Walikuwa ndani ya makazi yao, Nigaa amekunja nne, pakti mbili za sigara zikiwa zimekaa pembeni.



    Lee alikuwa anatazama televisheni ila macho yake yakizama fikirani.



    "Inabidi leo twende. For once and for all, nijue moja!" Akasema Lee.



    "Kazi ndogo sana hiyo Lee. Siyo ya kuumiza kichwa kabisa. Si unajua huyo manzi anapoishi?"



    "Ndio."



    "Na huyo famba?"



    "Ndio."



    "Sasa kuna nini hapo? Tukiwapata tunawanyonya macho! Hawaweza wakatuletea pigo za kifala fala!" Akasema Nigaa alafu akapiga pafu nne za sigara na kuchafua chumba kwa moshi.



    "Kwanini tusiende sasa hivi? Naona kama tunakawia," Nigaa alisema akitabasamu. Lee akatikisa kichwa na kumwambia wavute vute kidogo. Wakiwahi sana wataenda kukawia huko.



    Ulikuwa ni muda wa majira ya saa tatu na nusu hivi, Lee alitaka wavute mpaka majira ya saa nne nne, angalau viwanja vinakuwa vimefunguliwa ama kujaa jaa watu.



    Lee alimtaka Nigaa wanywe na kuvuta kwani hakutarajia kama angalikuwepo hai kwa muda huo. Hakutegemea kama angelitoka salama toka chumba cha mkuu.



    "Sikuamini alipopiga risasi zile pembeni. Niliposikia mlio wa silaha nikajua nimeshakwesha. Niliposikia kauli ya kupewa nafasi ya mwisho ndipo nikajua bado nipo duniani, na ninahema."



    "Una bahati sana, Lee," akasema Nigaa. "Mkuu anajua fika akikumaliza basi naye hatapata karatasi hiyo. Wewe ndiyo njia pekee na kuu ya kupata hiyo karatasi."



    "Sidhani," Lee akasema akitikisa kichwa. "Ni mara ngapi anamaliza watu wakiwa kwenye misheni kubwa na nzito kisha anawaweka wengine? Nadhani siku yangu haikuwa imewadia."



    "Unajua ni mara chache sana Mkuu anampatia mtu nafasi ya pili?" Akasema Nigaa. Lee akakubaliana na kauli hiyo. Kwake ilikuwa kama ngekewa!



    Basi muda ule ambao walikuwa wanaungojea, ukawadia. Muda wa kwenda kufanya tukio. Wakajikusanya na kwenda kwenye gari mpaka kwa yule mwanamke, Glady. Ila hawakumkuta!



    Walikuta mashoga zake wawili ambao walisema Glady ametoka muda si mrefu. Kwahiyo ikabidi Lee aongoze mpaka kule klabu alipomkuta mwanamke huyo.



    Huko napo hawakumkuta. Lee asife moyo akanyooshea usukani kuelekea viwanja vile ambavyo Glady alimpeleka kumtazama yule mwanaume wakianzia na Maisha.



    Bahati huko wakamwona mlengwa wao. Alikuwa na mwanaume fulani hivi mrefu katika mazingira ya kimahaba wakiketi kochini. Lee akasonga na kumnyaka bega mwanamke huyo, akamtaka atimize kazi yake.



    Alah! Kumbe yule mwanaume aliyekuwepo naye ndiye yule yule wanayemtafuta. Lee akajikuta anatabasamu na kuangua kicheko kabla hajamwambia Nigaa kwamba siku hiyo imekuwa nzuri maana wamewakuta walengwa wao wote kwa mkupuo.



    Mwanaume yule kutaka kuonyesha umwamba, akanyanyua chupa ambamizd nayo Lee kichwani. Haki hakuamini kilichotokea! Mkono wake ulidakwa upesi na mguu wa Lee, alafu ukakunjwa na kuvunjwa. Chupa ikadondokea chini!



    Mwanaume yule akapiga sana kelele za maumivu. Na kumbe wenzake hawakuwa mbali. Haraka wakasogea karibu. Wanaume wawili warefu, wakijiandaa kwa kubebelea chupa mikononi.



    Kwa namba ambavyo wanaume hawa walivyokuwa wanaogopeka, hata mabaunsa hawakuthubutu kuwazuia zaidi ya kuwaomba waachane na huyo mchina na mwenzake kabla hawajaaribu mambo.



    Ila hawakusikia. Walitaka kuonyesha ubavu wao. Hawakutaka kudharaulika! Kila mmoja akajigawa kumfuata wake, mmoja akienda kwa Lee na mwingine Nigaa.



    Watu wakapisha uwanja hapo klabu na kubakia wakitazama pambano. Ikiwemo hata na mabaunsa wenyewe wanaohusika na ulinzi.



    Bwana we! Wale wanaume wakaonjeshwa joto ya jiwe! Hawakufurukuta wala kufanya kitu, teke na ngumi zao zilikuwa kama mvua za vuli zikapita! Chupa walizokuja nazo zikawakata wenyewe na kuwaacha wakivujilia damu lukuki!



    Lee akamfuata yule mwanaume kochini na kumuuliza juu ya karatasi yake. Mwanaume yule akiwa bado ameshikilia mkono wake uliokunja nne, akasema ipo nyumbani!



    Lee na Nigaa wakambeba na kwenda naye nyumbani. Wakapata nyaraka yao.



    "Kuna yeyote uliyempatia hii karatasi?" Lee akauliza.



    Mwanaume akatikisa kichwa upesi.



    "Hapana hapana ... hakuna!"

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lee na Nigaa wakaondoka zao. Lee asipoteze muda akanyookea kwa mkuu na kumkabidhi karatasi ile. Mkuu akaikagua na kuridhika. Ila naye akaguswa na swala la usiri wa nyaraka ile.



    Akaulizia. Lee akamwambia bado ni ya siri. Ila bado mkuu akataka akahakikishe jambo hilo kwa ufasaha zaidi. Lee akakubali na kisha akaenda.





    ***





    "Umependeza sana," alisema Mke wa Boka akimtazama Miranda kwa matamanio.



    "Ahsante sana!" Miranda akapokea sifa kwa tabasamu pana huku akijitazama tazama.



    Akakaribishwa kwenye sebule kubwa kama ukumbi. Hapo kulikuwa kuna viti virefu vikiambaa ambaa na sebule. Viti hivi vilikuwa vina rangi ya kupendeza viking'arisha sebule.



    Sebule ilikuwa inametameta kwa samani za bei ya juu! Palikuwa panavutia kuvunja shingo ya mgeni kuangaza angaza.



    Miranda asidhulumu macho yake akatazama na kupekua.



    Kinywaji kikaja na hata chakula cha usiku. Wakiwa wanakula wakaendelea na kuteta mambo yao kuhusu urembo na ulimwende. Wakajadili kwa muda wa kama lisaa limoja.



    Wakakubaliana Miranda kuwa balozi wa kampuni ya urembo ya mama huyo. Atakuwa ndiye msemaji mkuu na atahusika na kuwakilisha kampuni hiyo maeneo mbalimbali.



    "Kesho ama keshokutwa tunaweza tukawa na utambulisho mbele ya vyombo vya habari. Utakuwa na muda na utayari?" Akauliza Mama Boka.



    Kabla Miranda hajajibu, akasita kwanza. Alihofia endapo akijianika kwenye mtandao na kwenye televisheni inaweza ikamletea tatizo. Maadui zake watajua na itakuwa kana kwamba amewachokoza.



    Hapa palihitaji hekima. Na hekima kwasababu ya asili ya kazi zake.





    ***



    Akamwambia mama Boka ampatie muda kidogo. Ila kumbuka interview ilitakiwa kuwa kesho ama keshokutwa. Basi ikalazimika isogezwe mbele kukidhi haja ya Miranda.



    "Kwahiyo itakuwa lini?" Akauliza mama Boka. Miranda napo akakosa jibu la kusema. Bado akarejea kule kule. Nitakwambia.



    Mama Boka akampatia mwanya ila akamtaka awahishe maana hamna muda zaidi. Miranda akaafiki kichwani akipanga kwenda kumwambia BC hilo jambo aone atasemaje.



    Basi wakahitimisha hilo jambo na kwendelea kuongea zaidi na zaidi. Usiku ulikuwa unakua, na kwa Miranda hakuwa na presha kwani nje usafiri ulikuwa unangoja.



    Kwenye majira ya saa tano, waziri akarejea nyumbani. Akastaajabu kumkuta Miranda hapo mpaka muda huo, akamsalimu na kumkonyeza.



    Akatamani sana aupate muda binafsi na mwanamke huyo ila haikuwezekana maana mkewe alikuwa hapo kila sekunde akitazama kila jambo. Ikabidi Waziri awe anamtumia ujumbe binti huyo wakati wakiendelea kuongea.



    Chating zao:



    "Umependeza love."



    "Kweli? Asante..."



    "Karibu. Mpaka nikasisimka."



    "Lol acha uongo bana.."



    "Kweli nakuambia, sasa vipi lile jibu langu mrembo?"



    "Mmmm umeanza nawee..."



    "Niambie bas na mie nile vitamu. Mwenzako nangoja na hutaki kunijibu."



    "Ntakujib usjali."



    "Lini sasa?"



    Kimya kidogo.



    "Kesho tunaweza tukakutana?" Ujumbe wa Boka ukauliza. Ila mara hii Miranda hakutaka kujibu, akajifanya amaeupotezea. Akaaga aende.



    Boka na mkewe wakamsindikiza akajipaki garini na kwenda. Akiwa anatembea barabarani akawa anasoma jumbe za Boka ambazo bado hazikukoma kuingia.



    Akatabasamu na kuzipuuza. Si kwamba hakuwa anaziona, la hasha, bali alikuwa anatengeneza mazingira ya kuonekana si mtu wa 'bei chee'.



    Mpaka anafika kulikuwa kuna jumbe kama nane za Boka. Ujumbe wa mwisho ukiwa ni wa kuingiziwa pesa, Boka akiwa ametuma shilingi elfu hamsini!



    "Nakutumia nauli ya kesho basi tukutane mida ile ile kule kule sawa?"



    Ulisema ujumbe wa pili tokea mwishoni.



    Miranda akajikuta akitabasamu. Napo hakujibu ujumbe huo.





    ***



    Saa saba kasoro, usiku...





    Sauti ya vibofyeo vya tarakilishi inagonga gonga na kuacha. Kutokana na ukimya uliokuwepo ndani ya chumba na majira haya ya usiku, sauti hiyo inasikika vema.



    Mbele ya tarakilishi alikuwapo Jona na Panky.



    Panky alikuwa mbele akikodolea kioo cha tarakilishi kana kwamba anatafuta jambo. Jona yeye alikuwa amesimama kwa nyuma mkononi akiwa amebebelea kikombe cheupe cha chai.



    Hii kazi wameanza tangu muda. Jona alikuwa amechoka, akipiga piga mihayo, ila Panky yeye alikuwa fiti. Uzoefu wake kukaa kwenye viti muda mrefu, mbele ya tarakilishi, ulikuwa unamsaidia.



    Mara Panky akatabasamu na kusema:



    "Tayari! Kila kitu kipo sawa sasa!"



    Akamweleza Jona kwamba kuanzia muda ule wanaweza wakai - trace ile simu ya Miriam na kujua wapi ilipo. Kama haitoshi hata mawimbi ya sauti yatakuwa bora zaidi.



    Na punde ataweza hata kuiwajibisha kuchukua picha ama video!



    Jona akafurahi sana na kumpongeza. Na kuhakikisha hilo akaanza kusoma ramani ya wapi Nade alipo. Akapaona! Akaweka earphone masikioni, mawimbi yalikuwa yametulia kiasi kwamba akawa anasikia kitu kilichokuwa kinafanyika kwa mbali!



    "Itakuwa wana party," alisema Jona.



    "Yah! Kwa nje ya nyumba huko," Panky akajazia taarifa. Mbali na muziki huo uliokuwa unasikika kwa mbali hakukuwa na sauti nyingine mbadala.



    Mazingira yalikuwa yametulia mno.



    "Usijali, hauna haja ya kusikiliza muda wote. Pindi kutakapokuwa na sauti yoyote karibu, itataarifu simu yako kwa njia ya vibration, kwahiyo utasikiliza."



    Utaalamu huo ukamsisimua sana Jona. Alivutiwa nao na akataka kujua historia ya Panky. Ametokea wapi na ilikuaje akajiunga na Sheng'.



    Panky akamjibu kifupi, tamaa ya pesa. Alikuwa ametoka mafunzoni na hakuwa na fedha ya kulelea familia yake maskini. Sheng' akamuahidi mshahara mnono, lakini pia masomo zaidi.



    "Ila hapo mwanzoni sikujua kama Sheng' anajihusisha na biashara haramu. Hata serikali haifahamu. Ni mtu mkubwa na mfanyabiashara wa mambo mengi, mambo ambayo anayatumia kama mwamvuli kukingia biashara zake zimwingiazo pesa zaidi ...



    Hata pale nilipokuja kugundua, nilikuwa tayari nimeshachelewa. Sikuweza kutoka tena."



    Jona akamuuliza kama angelipendelea kupata fursa ya kutoka, Panky akatabasamu na kujibu, haijalishi namna gani anataka kutoka huko, hilo jambo haliwezekani.



    Kwa sasa anamfanyia kazi Sheng' kwasababu ya uhai wake na wa familia yake tu. Isingelikuwa hivyo angeshalifanya mambo mengine ya maana.



    "Hakuna jambo lisilo na kikomo," Jona akamwambia. "Na pengine haukujaribu vya kutosha kuupata mlango. Mimi naamini inawezekana wewe kutoka."



    Panky akataka kujua ni kwa namna gani hilo linawezekana. Akatega masikio na macho. Jona akamwambia wao ndiyo watu wa kufanikisha hilo na si wengine.



    Lakini Panky alikuwa anahofia. Alichokuwa anahofia si yeye, bali mke na mwanaye Nasra.



    "Ndiyo kwanza anatimiza miaka minne. Nisingependa afe kwasababu yangu."



    Jona akamhakikishia hakuna atakayekufa. Lakini inatakiwa wawe werevu mno kufanikisha hilo. Jambo kubwa ni kwamba inawezekana kama wakitia nia.



    "Mimi nina mpango," Jona akasema. "Ili kumdhibiti na kummaliza Sheng' inabidi mtu fulani awepo ndani ya system yake. Mtu huyu ajue yanayoendelea huko. Kila kinachofanyika. Alafu awepo na mtu wa nje, ambaye atakuwa anachanga karata kutengua mipango."



    "Ni hatari," akasema Panky. Alihofia sana lakini Jona akamwambia hiyo ndiyo njia pekee la sivyo atakuwa mtumwa milele, na misha yake na ya familia yake yakiwa rehani.



    "Umetumwa kunimaliza. Wakijua mimi sijafa, watakumaliza wewe. Inabidi uende kwa Sheng' na umwambie umenimaliza. Nami nitapotea kwa muda fulani. Wakati huo wewe ukiendelea kufanya kazi."



    Jona alimwambia Panky kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya yeye kuishi na kuwa salama tangu hajamaliza kazi aliyoagizwa. Lakini pia ndiyo fursa ya wao kufanya jambo kwa urahisi kwasababu mosi, Panky atakuwa amerudi ndani ya system, pili, Sheng' hatahangaika na Jona kwa kujua amemmaliza.



    "Ngoja tuone," Akasema Panky.



    "Kumbuka muda unaenda, inatakiwa urejeshe ripoti kwa Sheng'," Jona akakumbusha.



    Panky akashusha pumzi ndefu.



    ***



    Saa kumi na moja asubuhi ...



    Kinoo anarejelea ujumbe alioundika na kuutunza kwenye simu jana yake wakati anaongea na Sarah.



    'Nyumba moja kubwa nyeupe yenye geti jekundu. Ukuta wake una sinyenge kwa juu zilizosokotwa sokotwa.'



    Aliposoma ujumbe huo akatazama nyumba iliyo mbele yake. Akaona vigezo vilivyomo ndani ya ujumbe vinafanana.



    Mwanaume huyu alikuwa juu ya pikipiki yake kubwa. Kichwani amevalia kofia ngumu, mwilini kibodi cheusi na suruali ya jeans na raba - All star.



    Jana yake usiku, pasipo Sarah kutambua, Kinoo akamchunguza juu ya makazi ya Brokoli. Mwanamke huyo akabwabwaja na kumjaza Kinoo taarifa. Kinoo akarekodi kwenye ujumbe kana kwamba alikuwa anachat na mtu.



    Sasa alikuwa mbele ya nyumba ambayo alihisi wazi ni ya Brokoli kwa mujibu wa maelezo. Akazima pikipiki na kuijongea.



    Kwanini wanapenda majira haya ya asubuhi?



    Majira haya yana uhakika zaidi kumkuta mtu nyumbani. Muda wa kurudi usiku huwa hautabiriki, na muda wa mchana ni ngekewa!



    Lakini asubuhi ya mapema, kwa wafanya kazi huwa ndiyo wanaamka kwenda makazini, wengi wao. Na bado hakujawa zogo.



    Mara kaap! Kinoo akatua ndani ya uzio wa nyumba ya Brokoli. Alikuwa hapo kutekeleza jambo moja tu, mauaji! Akuanzaye mmalize.



    Kabla hajafanya kingine chochote akasoma kwanza mazingira. Akagundua kuna mbwa wawili wakubwa karibia na chumba cha mlinzi!



    Mbwa hao wakampatia ishara ya kwamba pale hapakuwa pa kukaa muda mrefu kwani harufu yake yaweza kusababisha zogo



    Basi mfukoni akatoa mfuko mmoja soseji. Akauchanja na meno na kuuweka chini, alafu haraka akaizunguka nyumba.



    Punde mbwa wakasikia harufu hiyo. Ikawapuuzisha wasisikie ya Kinoo. Wakafakamia soseji zile. Mlinzi akagutuka na kusonga karibu na mbwa apate kuona nini hicho wanatafuna.



    Akaona soseji!



    Kutazama vema akaona alama za viatu juu ya sakafu! Akajua wameshavamiwa. Ila haikusaidia kitu, kwani kabla hajafanya lolote, akajikuta amedakwa shingo na kuvunjwa!



    Chini akadondoka akifuatiwa na mbwa wake. Kinoo sasa akaachiwa mwanya wa kufanya mambo yake taratibu pasipo papara. Akatega kumwona Brokoli akitoka nje.



    Dakika kama kumi mwanaume huyo akatoka nje akiwa amevalia taulo na mswaki upo mdomoni. Kuna kitu alikuwa anaenda kuchukua kwenye gari lake, VX la grey.



    Lakini wasaa huo ukawa wa mwisho kwake! Akajikuta amekabwa na mkono mzito. Pua na mdomo vikabanwa na kitambaa kizito chenye malighafi kama taulo.



    Kuvuta kwake hewa kukawa kosa. Alivuta mara moja tu na mara mapigo yake ya moyo yakasimama! Habari yake ikaishia hapo hapo!



    Kinoo akayoyoma zake akifunga mahesabu...





    Kwa mbali sauti za majogoo ungeweza kuzisikia zikitangaza asubuhi. Kama ilivyo ada, ndani ya jiji la Dar es salaam, magari yalikuwa yamesongamana barabarani watu wakienda makazini. Wale walioamka na kujiandaa saa kumi na moja, wao walikuwa wameshafika na huenda wameshaanza na kazi.





    Lakini kwa Jona haikuwa hivyo. Yeye alikuwa yupo ndani, tofauti kabisa na desturi yake ya kudamka asubuhi na kuwahi kazini. ni siku kadhaa sasa amekuwa akifanya hivyo, na sababu kubwa ikiwa ni kazi za hapa na pale ambazo zimekuwa zikitokea na kumuibia muda. Kuna muda anajikuta amerejea kwenye kazi yake ya upelelezi, maana amekuwa akiumiza kichwa kweli.





    Anachofanya akiamka, ni ‘kumchek’ Jumanne na kumjulia hali, kisha anaendelea na kazi zake zingine alizozikubalia kuzivulia nguo. Kazi ambazo anajitahidi kuzikimbia na kuziepuka pasipo mafanikio.





    Akiwa ameketi na tarakilishi yake, mwenyewe sebule nzima, kwenye majira ya saa mbili asubuhi, akasikia hodi inabishwa getini. Akachungulia kupitia dirisha lake, akaona uso wa mtu mmoja anayemfahamu.





    Alikuwa ni Inspekta Norbert Mlanje, mwanaume polisi aliyeonana na Jona miezi kadhaa iliyopita. Mwanaume huyu akiwa ametumwa na uongozi kwa dhumuni la kumshawishi Jona arejee kazini.





    Kwahiyo Jona akawa ameshabashiri kinachofuatia. Ila si vema kumwacha mgeni mlangoni, basi akaenda kuwafungulia na kuwakaribisha ndani. Walikuwa wamevalia makoti marefu ya kaki na suti za kaunda kwa ndani.

    Kama kawaida uso wa Inspekta Norbert ulikuwa umekatwa na mustachi mpana mweusi. Macho yake ya kijanja yalikuwa yanapekuapekua eneo la nyumba ya Jona akiwa anasonga ndani.





    Wakajitambulisha, yule mpya machoni mwa Jona alikuwa anaitwa Bwire. Ni afisa wa polisi kwa cheo cha koplo.

    “Karibuni, bila shaka mtakuwa mna jipya.”





    Norbert akasema hana jipya bali ni lile lile, ila kwa sasa ameagizwa na Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam. Anahitaji kumwona haraka iwezekanavyo, ana maongezi nyeti naye.





    Jona akasema ana kazi za kufanya kwa muda huo. Bwana Norbert akamsihi sana aende kuonana na mkuu muda huo kwani wametumwa kuja kumchukua. Hakukuwa na muda wa kutafakari.

    Kwa ustaarabu Jona akaridhia. Akajiandaa na kwenda ofisini kwa kamanda baada ya kumuaga Panky ambaye alikuwa amefungiwa ndani ya chumba. Akajipaki kwenye gari la maafisa hao na kuanza safari.





    Wakiwa njiani, Norbert akawa anampeleleza Jona juu ya maisha yake. Alikuwa anataka kujua ni kwanini Jona aliamua kuachana na kazi hiyo aliyokuwa akiitenda vema, ila Jona akawa mfinyu wa taarifa. Hakutaka kujiweka bayana kiasi hicho.





    Akasema ni maamuzi, na maisha aliyoyachagua.





    “Bila shaka utakuwa unafanya vema huko kwenye mambo mengine. Ni wapi ulipojishkiza?” Norbert aliuliza.

    “Kwenye kazi mbalimbali,” akajibu Jona kisha akafunga mdomo wake. Mpaka wanafika Norbert hakuwa amekipata anachokitaka. Moja kwa moja, Jona akaingizwa ofisini kwa kamanda na kuketi, kamanda alikuwa akiongea na simu ya mezani.





    Alipomaliza akamkaribisha Jona na kumjuia hali ya muda mrefu. Akamwambia amemuita hapo kwasababu kuu moja, ya kumtaka arejee kazini kwani wanamhitaji kuliko muda mwingine wowote.





    “Jona, unajua serikali ilitoa pesa yake ukapate mafunzo ili uje kusaidia taifa. Tunaomba urejee na uendelee kutimiza majukumu yako. Huu ni muda ambao Taifa linahitaji ujuzi, juhudi na nguvu yako.”





    Jona akaendelea kushikilia msimamo wake, hapana. Kamanda akashindwa kumshawishi kabisa, na sasa ikabidi ahamie upande wa pili wa kumpa vitisho Jona. Uso wake ulibadilika akiwa anasisitizia kile anachosema.





    “Jona, maisha yako kamwe hayatakuwa sawa ukiwa nje ya jeshi. Huu ndiyo wito wako na hauwezi kuukwepa. Na sisi tutakukumbusha hilo kila uchwao.”





    “Ahsante, Kamanda,” akasema Jona, na kuongezea: “Nitarejea jeshini siku n’takapopata maelezo ya kutosha toka jeshi la polisi juu ya kifo cha mke wangu na mtoto wangu. Siku n’takayopewa maelezo ya kina kwanini biashara yangu ilifungiwa kwasababu sizizo na mantiki. Siku ntakapopewa majibu ya kueleweka, pengine ntashawishika kulamba matapishi yangu.”





    Kamanda akaangua kicheko kabla hajaanza kukohoa mara kadhaa. Akatulia na kumwambia tena Jona kauli yake aliyoisema hapo awali ya kwamba maisha yake hayawezi yakawa sawa akiwa nje ya jeshi.





    Hakutoa maelezo zaidi, akamwambia Jona amehitimisha na siku moja atakuja kukumbuka hicho anachokisema. Jona akaaga na kwenda zake. Lakini kauli ya Kamanda juu ya maisha yake haikumwacha upesi.





    Akawa anaifikiria akiwa garini na mpaka alipofika nyumbani. Kuna mawazo mabovu yalimjia kichwani, ila akayapuuzia kwa kuona muda utaongea.





    Akajikuta anamkumbuka sana mkewe na mwanae kana kwamba wamefariki jana.

    Alipofika nyumbani, akaendea karatasi zile ambazo amemchora mkewe na mwanae. Akazitazama sana akikumbuka ‘memory’ kadhaa. Machozi yakasonga machoni. Panky akamkuta hapo, na asimsumbue akaachana naye akienda kuketi na kutumia tarakilishi.





    Punde Panky akamshtua na kumwambia kuna jambo la kulisikiliza. Kuna sauti ilikuwa inasikika toka eneo la tukio, kule ambapo Nade alikuwa amefungiwa.







    ***







    “Haloo!” Mh. Eliakimu aliongea na simu akiwa amekunja sura. “Nade?”

    Mara akasikia sauti ya kiume.

    “Malaya wako uliyemtuma, tunaye hapa.”

    “Wewe nani?” Mheshimiwa akawahi kuuliza.





    “Mimi ni yule uliyedhani ni fala kwa kumtuma Malaya wako aje kunimaliza.”

    Mheshimiwa akapandwa na hasira. Maneno mabovu na makali yakamtoka.





    Ila aliyeongea naye akiwa ametulia, akamngojea amalize, kisha akamuuliza:

    “Unamtaka malaya wako hai ama lah?”

    Mheshimiwa akanyamaza kwanza. Swali likarudiwa. Akatishishia kummaliza mwanaume huyo endapo akifanya lolote kwa Nade. Vitisho ambavyo havikusaidia lolote lile, kwani mwishowe alinywea na kwenda sawia na mtekaji.

    Hakuwa na namna.





    “Tutabadilishana na Miriam. Utamleta Miriam, nawe utampata mtu wako. Deal?”





    Hapa pakawa pagumu kwa Mheshimiwa. Ila akajikuta hana machaguzi mengine zaidi ya kuridhia, japo kwa shingo upande. Simu ikakata.





    Akabakia akiwaza haswa juu ya namna ya kufanya. Akabakia akiwaza namna gani ya kumkomboa mwanamke pekee anayemuamini.





    Kazi haikwenda kabisa, na kichwa kiligoma. Akaaga na kurudi zake nyumbani. Akamkuta Miriam akiwa ameketi sebuleni anatazama televisheni. Ulinzi ulikuwa mkubwa kuhakikisha mwanamke huyo haendi popote pale.





    Mwanamke huyo alikuwa amechafuka kwa majeraha. Uso wake ulikuwa umevimba, macho yake yakiwa mekundu usijue kama analia ama ameumia.





    Akamuuliza juu ya yule mwanaume ambaye amemteka Nade. Miriam asiseme kitu, akamtazama na kunyamaza akiangalia televisheni. Baada ya Mh. Kurudia swali mara kadhaa akiambatanisha na vitisho, Miriam akamwambia kwa ufupi, akihangaika kuongea:

    “Eli, umeingia kwenye anga la wenyewe.”





    Baada ya hapo hakusema tena lolote.







    ***







    Kang! Kang! Kang!





    Sauti ya chuma kilichopo mlangoni ilisikika ikilia. Mara sauti ya kichina ikatoa ruhusa na mtu akazama ndani, alikuwa Panky. Akasimama kiukakamavu akimtazama mkuu wake aliyekuwa amejaa kwenye kiti kirefu cheusi nyamanyama.





    Juu mezani kulikuwa tarakilishi kubwa iliyokuwa ipo on na kunguruma. Panky aliposalimu akakaribishwa kuketi na kisha mwenyeji wake akampatia atensheni yote. Akamtazama na macho yake nyuma ya miwani.





    “Nimemaliza kazi,” akasema Panky. Mkuu huyu alikuwa hawezi kuongea Kiswahili vema ila alikuwa anakisikia na kukielewa. Aliposikia kauli ya Panky, akapandisha nyusi zake kwa mshangao. Kisha akauliza kazi hiyo imemalizwa lini akitumia lugha ya kichina.





    Uzuri Panky alikuwa anaelewa lugha hiyo, japokuwa naye matamshi yalikuwa yanamshinda. Ana kichwa chepesi cha kujifunza ila lugha ya kichina iligoma kunasa mdomoni.





    Akaweka bahasha ya kaki mezani alafu akamsogezea mkuu wake kwa kuiburuza. Mkuu akaipokea na kufungua kutazama yaliyomo ndani.





    Akaona picha tatu alizozitoa na kuziangaza kwa macho yake. Akamwona Jona akiwa amelala chini akielea kwenye dimbwi la damu. Paji lake la uso lilikuwa linachuruza damu na macho yake yakiwa yametoka nje!





    Picha zilikuwa zinatisha na kusisimua kutazama.





    Mkuu akatabasamu na kisha akamtazama Panky. Akampongeza kwa kazi aliyoifanya huku akiweka bayana kwamba hakutegemea kama angefanikisha hilo. Panky akamwambia alijitahidi ili kufuta makosa aliyoyafanya.





    Mkuu akampongeza tena na kisha akampatia kibali cha kwenda kuendelea na kazi akimsihi Panky abakize picha zile palepale na yeye. Panky akaridhia na kwenda. Mkuu akamwita Nigaa na kumpatia kazi.





    Akamwonyesha picha zile ambazo Panky alimpatia, akamwambia neno moja alilolisema kwa lafudhi ya kichina:

    “Hakikisha.”





    Nigaa akajua nini cha kufanya na pasipo kuuliza akatoka zake nje. Mkuu akalalia kiti na kushusha pumzi. Akatafakari zile picha, ila kwa macho yake zilikuwa sahihi na si za kubandikwa kiteknolojia. Ila hakuamini uwezo wa Panky kiasi hicho.

    Amewezaje kitu ambacho Bigo ameshindwa?





    Alitamani kujua.





    “Tayari, nimefanikiwa.” Ujumbe ulifika kwenye simu ya Jona toka kwa Panky. Jona akaupokea na tabasamu alafu akaujibu ujumbe huo.



    “Basi fanya kama vile tulivyopanga.”



    Panky akaupokea ujumbe huo, na kisha akaujibu:



    “Hamna shida,” huku akielekea eneo lao la kazi. Mbele yake kulikuwa kuna mlango mkubwa wa chuma ukiwa umepachikwa bandiko jeupe lililosomeka ‘SPACE BUTTON’. Pembezoni mwa mlango huo kulikuwa kuna kifaa cha kuandikia ‘password’.



    Panky akabofya hapo mara kadhaa na mara mlango ukafunguka. Akazama ndani na kupokelewa na wenzake ambao walimkumbatia na kumkaribisha kwa bashasha. Hawakutegemea kama Panky angerejea salama.



    Baada ya muda kidogo, na hali kutulia, Panky akamtafuta Marwa ndani ya eneo lao. Eneo lilikuwa kubwa lililotapakaa mashine na tarakilishi. Kwa mbali kwenye kona akamwona mlengwa wake.



    Ndani ya ofisi hiyo kuna vitengo kadhaa: ukarani, graphics, hacking na coding, na Marwa alikuwa kwenye kitengo cha graphics. Yeye na jamaa wawili.



    Marwa alikuwa ni mwanaume mweusi mwenye nywele nyingi na chunusi kadha wa kadha usoni. Vidole vyake vilikuwa katika keyboard akichapa jambo. Macho yake yalikuwa yamezama kwenye kioo cha tarakilishi.



    Kwa kumtazama tu, alionekana yupo bize. Panky akamjongea na kumsalimu. Akajibiwa pasipo kutazamwa. Marwa alikuwa anafanyia kazi picha fulani ambayo Panky aliona inapendeza sana ikikaa ukutani.



    Marwa akasimamisha shughuli yake na kumtazama Panky. Alikuwa anamwona anampotezea muda ingali ana kazi lukuki za kufanya. Akauliza:



    “Una shida gani?”



    Panky akatabasamu. Kisha akamwambia Marwa kuna picha fulani aliiona akiifanyia kazi, ilimvutia na angependa kuiona.



    “Nafanyia kazi picha nyingi Panky, unamaanisha ipi?”



    Panky akajitahidi kuielezea picha yake iliyokichwani. Marwa akamwelewa, ila akamuuliza pasipo kumtazama:



    “Unajua miiko ya kazi?”



    “Najua, Marwa. Usijali, Moderator hatajua,” Panky akajibu.



    Moderator ni msimamizi wa mule ndani. Ni mchina kwa utaifa na kazi yake ni kuhakikisha kila mtu anafanya kazi yake pasipo kuingiliana. Kuhakikisha wafanyakazi hawapangi jambo lolote kwa pamoja mule ndani, aidha kugoma, kuharibu mashine kwa kudhamiria, ama kupanga jambo la kitaaluma likaathiri kampuni.



    Macho ya Moderator yanakuwa yanaambaa muda kwa muda, mahali kwa mahali, na masikio yake yanasikiza muda wote. Ujuzi wake pia kwenye mambo ya tarakilishi na mifumo yake yote, upo juu.



    Kabla Marwa hajasema jambo, akasikia vishindo vya miguu. Na mara vikakoma na sauti ikauliza:



    “Kuna tatizo hapa?” sauti nyembamba yenye lafudhi ya ki-mandarin. Alikuwa ni Moderator, mwanaume mfupi mwenye nywele za wastani. Macho yake yakisaidiwa na miwani maana yameshaharibiwa na mwanga wa tarakilishi kupitiliza.



    Alikuwa amevalia shati jeusi kama vile sweta likimbana mpaka koo. Pamoja na suruali pana ya kitambaa cha rangi ya fedha, na mokasin nyeusi.



    “Hamna tatizo,” Panky akawahi kujibu akitabasamu. “Nilikuwa namuuliza kama angeweza kuhudhuria sherehe ya mdogo wangu.” Akasema kwa haraka akijua fika Moderator hakuwa mzuri kwenye lugha hiyo.



    Kisha akanyanyuka na kurejea tarakilishi yake. Kuna kazi akawa anazifanya ila akifikiria ni kwa namna gani anaweza kumuingia Marwa.





    ***





    Baada ya maongezi yaliyokuwa yanafanyika kwa sauti ya chini chini, Mkuu, ama Sheng’ kama aitwavyo na wachache, akiwa anaongea na mwaname fulani mweusi mwenye nywele ndefu na macho madogo akiwa amevalia suti, akatikisa kichwa na kusema:



    “This must be a plot.” (Huu lazima utakuwa ni mpango.) alisema kwa sauti yake ya kichina kiasi usijue kama ameongea lugha ya kiingereza. Mwanamke naye akatikisa kichwa kwa kukubali.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Watu hawa walikuwa wanaongelea mauaji ya kushtukuza ya Brokoli. Nani aliyeshiriki, na pia sababu iliyopelekea tukio hilo.



    Mwanamke huyu mweusi ambaye yupo hapa, alikuwa ndiye yule ambaye Brokoli alikuwa akiwasiliana naye wakati akifanya tukio la mauaji ya Mudy na hata akiwa njia kumtafuta yule ambaye Mudy amemkabidhi nyaraka, yaani Kinoo.



    “The document should be fetched! Otherwise we may awake the dead demon.” (Nyaraka lazima ipatikane! La sivyo tunaweza tukaamsha jinni lililolala.) alisema Sheng’ kwa msisitizo akimwambia yule mwanamke.



    Punde mwanamke huyu akasimama na kuinamisha kichwa chake. Alafu akaondoka akitembea kikakamavu. Chini alikuwa amevalia viatu vya visigino virefu lakini akitembea kana kwamba amevaa raba.



    Mwanamke huyu akaendea gari lake alilolipaki nje, IST nyeupe new Model, akazama ndani na kuondoa chombo.



    Kwa jina waweza kumwita Gee.





    ***





    Saa moja usiku …





    Simu ilinguruma … ggrrrrrmmmm! Mara mbili kabla Glady hajaipokea na kuweka sikioni. Alikuwa amejilaza kitandani akiwa na mashoga zake wawili wote wakiwa wamevalia nguo za ndani tu.



    “Vipi?” akauliza .



    “Njoo hapa nje,” sauti ya kiume ikamjibu na mara simu ikakata. Wenzake wakawahi kumuuliza kama ni mteja, Glady akatikisa kichwa chake na kusema ni fala fulani aitwaye Mustapha.



    Akajiveka khanga na kutoka nje. Akamkuta huko mwanaume aliyevalia ‘form six’ ya bluu na suruali nyeusi ya kadeti. Mkono wake wa kulia ulikuwa upo ndani ya POP, ameuning’iniza ukibembeshwa na kamba uliyodaka shingo.



    Mwanaume huyu alikuwa ndiye yule aliyezama matatizoni na Lee kwa kushikilia nyaraka isiyo ya kwake. Glady akamtazama mkono wake uliovunjwa, alafu akamuuliza:



    “Unataka nini?”



    Mustapha akamwambia yupo pale kwa ajili ya kupata taarifa za yule mchina, Lee. Kwa alimchofanyia, kamwe hawezi kumwacha salama!



    “Vita aliyoianzisha, kamwe haitaisha. Nitahakikisha ananijua mimi ni nani, na si kila mtu ni wa kumchezea!”



    Glady akaangua kicheko.



    “Mustapa, ulishindwa siku ile. Au unataka uuawe kabisa?”



    Mustapha akamsisitizia apewe taarifa za huyo mchina alafu atakuja kumpatia taarifa baadae juu ya nini alichomfanyia. Glady akamwambia hana taarifa yoyote ya Lee. Alikutana naye klabuni na kuachana huko huko.



    Mustapha hakuamini. Na kwa kutaka taarifa hiyo ya Lee, akamwambia Glady kwamba ile nyaraka ambayo Lee alikuwa anaitaka na kuichukua, wanayo. Na muda si mrefu watajua kuna nini ndani yake.



    Glady akaagua tena kicheko. Alijua Mustapha anaongopa.



    “Unatolea wapi na uliitoa?” akauliza. Mustapha akatoa simu yake kubwa na kumwonyesha Glady picha. Kumbe mwanaume huyo alikuwa amepiga picha ile nyaraka ya Lee, picha zimetunzwa kwenye gallery!



    Glady akashangazwa.



    “Ila we Mustapha una hatari!”



    “Hii lazima itakuwa dili. Kwa namna alivyokuwa anaitafuta vile, itakuwa dili tu!”



    “Sasa utaelewa nini humo na kimeandikwa kichina?”



    “Aaaggh! Unadhani hakuna watu wanaojua kichina? Wachina wapo wangapi Kariakoo?”



    Mustapha akamtaka sasa Glady amsaidie kupata taarifa za Lee, ili na yeye aweze kunufaika na chochote kitu kitakachopatikana humo. Taarifa hizo za Lee si tu kwamba zitamsaidia Mustapha kulipiza kisasi, bali pia zitawasaidia kujua namna gani watanufaika na nyaraka ile endapo wakiona kuna mhitaji wa yule ‘mchina’.



    “Mustapha, kweli sina!” Glady akajibu. “Lakini naahidi kukutafutia. Nipe muda kidogo.”



    Wakaachana kwa ahadi hiyo.





    ***





    Saa tatu usiku…



    Jona amesimama mbele ya karatasi zake za kuchorea, anatazama jambo.



    Anafungua karatasi ya kwanza na kisha ya pili. karatasi hizo zina picha ya mkewe na mwanae. Anazitazama kwa muda kabla hajapindua karatasi nyingine mpya na kuanza kuchora mchoro mpya akitengeneza msingi kwa penseli ya kawaida.



    Ilikuwa ni picha ya mtoto anachora. Na hakuwa anarejelea popote pale isipokuwa kichwani kwake.



    Akiwa anaendelea kuchora mchoro huo, akili yake ipo kwenye amani na macho yake yakizingatia kazi anayoifanya, mara anasikia sauti ya honi huko nje. Anasita na kujiuliza ni nani huyo. Hakuwa na miadi na yoyote, na ule ulikuwa ni muda wa usiku.



    Akaendea dirisha na kuchungulia. Akaona gari kubwa, VX rangi ya fedha. Akiwa hapo hapo anatathmini, akaona kuna mtu mmoja ameshuka toka kwenye gari hilo. Macho yake nyuma ya miwani yakatambuo umbo la mgeni huyo.



    Alikuwa ni Mh. Eliakimu!



    Muda huo! Akastaajabu. Akateka bunduki ndogo na kuikobeka nyuma ya kiuno, alafu akaendea geti na kumkarimu mgeni. Alikuwa amebeba tahadhari zote akiwa tayari kwa lolote linaloweza kutokea.



    Mheshimiwa alikuwa ameongozana na bodyguard, mwanaume mrefu mweusi mwenye misuli mipana. Bodyguard huyo akaamriwa abakie nje wakati Mheshimiwa akiingia ndani na kuketi kochini.



    “Sikutegemea ujio wako, vipi mheshimiwa?”



    Mh. Eliakimu akashusha kwanza pumzi ndefu. Hakuwa anajua wapi pa kuanzia. Kujileta kwake kwa Jona kulikuwa hatari kwake na kwa siri zake, ila ndiyo hivyo hakuwa na namna! Maji yalikuwa yamemfika shingoni.



    “Jona,” Mheshimiwa akaita. “Achana na yote yaliyopita. Najua kuna mambo ambayo yalitokea hapa kati, nisingependa kuyaongelea kwa sasa maana si muda muafaka. Nimekuja hapa maana nina shida na ninahitaji tena msaada wako.”



    Jona alikuwa kimya akimtazama. Mheshimiwa akameza kwanza mate, alafu akasema:



    “Nade ametekwa, naomba unisaidie kumuokoa.”



    Ni kama vile Jona alikuwa anategemea kauli hiyo kwani hakushangazwa hata kidogo. Alikunywa fundo moja la mvinyo ndani ya glasi alafu akaendelea kumpatia atensheni mgeni wake.



    “Utahitaji kiasi gani?” mheshimiwa akauliza akichojoa pochi yake mfukoni.



    “Sitahitaji pesa yoyote toka kwako,” akasema Jona. Na kisha akaongezea: “Ninachohitaji toka kwako ni taarifa tu ya yale unayonificha.”



    “Yapi hayo?”



    “Kwanza kwanini unataka kuniua?” Jona akauliza akimkazia macho Mh. Eliakimu. Swali hilo likamshtua muulizwaji, akajitahidi kulimudu akiwa tayari amechelewa kwani Jona alimshasoma.



    Kama haitoshi, Jona akataka kujua kwanini Nade alikuwa anamfuatilia na kwasababu gani haswa alikuwa anamtafuta mkewe. Maswali hayo yakamfanya mheshimiwa akose cha kunena.



    Hakuwa amejiandaa nayo, na kutafuta ahueni akamwambia Jona kwamba watatafuta siku waongee vizuri kila kitu. Kauli ambayo kwa Jona haikuwa na uzito, ila akaridhia kwa kuona hamna haja ya kulumbana. Mheshimiwa alikuwa ni ndege wake, ahitaji kumshikia manati.



    “Sawa, hamna shida,” Jona akajibu. “Nitafanya.” Ndani ya moyo wake alikuwa ana nia ya kumsaidia Nade, lakini pasipo kumsahau na Miriam kwa wakati huo huo.



    “Na vipi kuhusu Miriam?” akauliza. Mheshimiwa akamjibu kuwa watu waliomteka Nade wanamtaka Miriam kubadilishana na Nade. Jona akataka kujua zaidi juu ya hao watu, ila Mheshimiwa hakuwa na majibu ya kumpa. Yeye mwenyewe hakuwa anajua lolote kuwahusu.



    Kwahiyo Jona akawa amepata kibarua kingine, kuwachambua na kuwajua hao watu. Kutopoteza muda zaidi, akakubali kufanya kazi na kumtaka mheshimiwa akapumzike.



    “Una hakika auhitaji chochote toka kwangu?” Mheshimiwa akauliza tena. Hakuwa anajua ni namna gani Jona atawapata hao watu ukizingatia hajamuuliza chochote, wala kutilia shaka lolote.



    Na akasita kuuliza. Kifuani akizoza kwani yeye shida yake nini wakati ameambiwa kazi itafanywa? Akajikusanya na kuondoka zake akitingwa kichwani. Akajiweka kwenye gari na kuondoka toka eneo hilo.



    “Ni lazima nimpate huyu jamaa,” akajisemea peke yake kifuani. “Endapo nikiwa naye hakika mambo yangu yataenda vema.”



    Safari nzima akawa anawazia kwa namna gani angekuwa na Jona, jinsi mambo yake yangemalizika kwa wepesi na kwa uhakika. Vipi kama akiwa na Nade na Jona kwa wakati mmoja? Hatakuwa na haja ya kumiliki jeshi. Maadui zake wataona cha mtemakuni.



    Basi akajikuta anatabasamu kwa taswira yake hiyo ambayo alitamani iwe uhalisia.





    ***





    Saa mbili asubuhi…





    Bodaboda ilisimama nyuma kidogo ya fremu, akashuka Jona na kuvua kofia ngumu na kumpatia dereva kisha akamlipa. Akaenda zake ofisini na kumkuta Jumanne akamsalimu na kumwambia hayupo hapo kwa muda mrefu, amepita maana ameona ana haja ya kumpasha habari.



    “Sitakuwepo hapa kazini kwa muda, kuna ishu fulani nafuatilia. Sawa?” Jona alisema. Jumanne akastaajabu kidogo, haikuwa kawaida. Akauliza nini shida.



    Jona akasisitizia tu kwamba kuna ishu anafanya ila haitakuwa milele. Atarejea.



    "Hakikisha kila kitu kinakuwa sawa. Tutakuwa tunawasiliana. Sawa?"



    "Poa." Jumanne akajibu kishingo upande. Alikuwa anawazia ni kwa namna gani atakavyokuwa mpweke. Japokuwa hapa karibuni hakuwa pamoja na Jona ila kitendo cha kupewa taarifa rasmi kuwa hatakuwepo tena kwa muda usiojulikana, Jumanne akafadhaishwa.



    Jona asipoteze muda, akayeya! Sasa alikuwa yupo katika hatua nzuri ya kupotea kwenye mazingira yake zoefu. Yote haya kwasababu ya kutengeneza mazingira bandia ya kifo chake.



    Lakini pia kujipa muda wa kutenda mambo yake kwa ufanisi zaidi.

    Alishatafuta mahali pia pa kuishi tofauti na makazi yake ya kila siku. Kila kitu kilikuwa kinaenda kwa mujibu wa mipango karatasini.



    "Karibu," akasema Jumanne akimtazama mgeni wake aliyekuwa amesimama mlangoni. Japokuwa bidhaa zilikuwa zimejaa, nyingi, Jumanne alimwona mwanaume huyu mrefu mweusi.



    Alikuwa amevalia suti ya kahawia iliyomzidi ukubwa kidogo. Alimtazama Jumanne na kisha akazama ndani baada ya kuhakikisha yupo mwenyewe.



    Mwanaume huyu ni nani? Akatazama bidhaa ya kwanza na ya pili, kisha akatazama tena nje. Akasogea akizama ndani ya duka. Jumanne alikuwa pembeni yake akisubiria kutoa maelezo pale yatakapohitajika.



    Lakini mteja huyu hakuuliza kitu! Akaendelea kukagua bidhaa. Alipomalizikia ndani ya duka, akamnyaka Jumanne na kumminyia kwenye mikono yake minene meusi kumkaba!



    Jumanne akafurukuta kutetea uhai wake kwa hali na mali, ila hakufua dafu! Mwanaume huyu aliyemkaba alikuwa mkufunzi wa hili tukio haswa!



    Alikuwa amejawa na nguvu na sanaa ya mauaji. Jumanne akaishiwa na nguvu na mwisho wa siku akatulia tulii kukubali sheria!



    Mwanaume huyo akahakikisha kama amefanikiwa kisha akahepa zake mara moja kupotea eneo hilo. Alijipaki kwenye pikipiki ambayo ni wazi ilikuwa inamngojea yeye.



    Wakayeya!





    ***





    Saa kumi jioni...





    "So what did yo do?" (Kwahiyo ulifanyaje?) BC aliuliza.



    "I did nothing. I asked her to wait," (sikufanya kitu. Nilimwomba angoje,) akajibu Miranda.



    "Thats good of you! But dear, we have nothing to do here except accepting it." (Hilo ni jema! Lakini mpenzi, hatuna cha kufanya hapa zaidi ya kukubali.)



    "And what about th...." (Na vipi kuhusu ....)



    "**** those excuses! Jus do it." (Acha hizo sababu! We fanya tu.) BC akasema kisha akakamata kinywaji chake, John Walker, na kumiminia kinywani.



    "Go do that commercial. I will handle the rest." (We nenda fanya hilo tangazo. Nitashughulikia mengine.) Akasema kwa kujiamini.



    Miranda akatikisa kichwa chake alafu akashika simu yake na kuitazama. Swala hilo lilikuwa limeshaisha. Ilibidi afanye ile interview kama ambavyo mke wa Boka atakavyo.

    Ilibidi akajianike mbele ya kamera na yote hayo kwasababu tu ya kuhakikisha hiyo dili yake na mke wa Boka inatimia.



    Kukawa kimya kidogo. Mazingira ya ufukweni walipokuwepo yalikuwa tulivu. Upepo ulikuwa unapuliza na hakuna kingine chochote kinachosikika.



    Ukimya huo ukavunjwa na sauti ya BC punde baada ya kunywa kidogo kinywaji chake glasini.



    Alimuuliza Miranda kama amesumbuliwa na Eliakimu hapa karibuni. Miranda akatikisa kichwa chake kukataa. Hakuwa na mawasiliano na mwanaume huyo tangu siku wakutane.



    Habari hizo zikamfanya BC awaze kidogo. Eliakimu atakuwa anapanga nini na ukimya wake huu? Akanywa mafundo kadhaa ya Walker akiwa anawaza. Aliona kuna hitaji la kujua Eliakimu ana mpango gani, akamshirikisha Miranda.



    "We don't need to bother. Let us wait for his step first," (Hatuhitaji kusumbuka. Ngoja tuone hatua yake kwanza.) Akasema mwanamke huyo.



    Lakini vipi kama hatua hiyo ikawa na hatari kwao? Swali lilikuja hapo. Tahadhari ikaonekana kuhitajika. Miranda asirefushe mada, akapendekeza kuwasiliana na Eliakimu kama njia ya kumchokonoa.



    Ila swala hilo akapendekeza lifanywe na BC.



    BC akakaa kimya kwa muda. Akaendelea kunywa na kunywa akiyapanga kichwani.



    Fikra zake zilienda mbali sana akiwazia na mzigo wao wa kemikali ambao upo tayari, unangoja tu amri ili upate kuja. Kukaa kwake bandarini kunazidi kuchojosha pesa, na huku bado hakujaeleweka. Afanye nini?



    Akakuna kidevu chake akiendelea kuyapanga. Hamna namna BC, ni kurudi kwa Eliakimu tu! Hapana, sirudi huko kwani gharama zake zinawiana na gharama za mzigo kabisa! Sasa tufanyeje na huku Boka bado hajawekwa kwenye mstari?



    Akaendelea kuyapanga akizoza na nafsi yake.



    Boka lazima akalishwe. Lazima ajaribiwe kama mkono wake utakuwa mwepesi kuenenda na kutenda. Na udhaifu wake ni Miranda.



    Miranda inabidi atumie mwili na akili yake kufyatua bomu hili mara moja! Ila pia na hekima yake ni jambo la msingi hapa.



    "Miranda," BC akaita. "Accept the man, Boka, and tell him that I wana see him," (Mkubalie huyo mwanaume, Boka, na umwambie nataka kumwona.)



    Mchezo ukapangwa namna ya kwenda. Miranda amwambie Boka kwamba amemkubalia ila 'baba' yake angenda amwone na wajadili mambo kadhaa juu ya mahusiano yao.



    Na hapo ndipo BC atakapotumia 'ubaba' wake kumminya na kumkamua Boka kama kweli anamhitaji 'mtoto' wake kama mpenziwe.



    Hapo ndipo Boka ataelezwa juu ya shida za 'mkwe' wake na kuzitimiza iwe ndiyo kama mahari. Kama kipimo cha upendo wake kwa mwanamke huyo mrembo, Miranda.



    Waliamini tamaa ya kimwili ya Boka, itazima uwezo wake wa akili. Hatafikiria kwa kichwa chake cha juu, bali kile cha chini.



    Na hapo, ndipo mcchezo utakapokuwa umeishia.





    ***





    Saa moja jioni...





    "Una uhakika ndiyo hapa?" Akauliza Mustapha akinyooshea kidole getini. Alikuwa ameongozana na mwenzake aitwaye Bilali, mwanaume mfupi ambaye uso wake umejawa na majeraha.



    Mwanaume huyu alikuwa ni miongoni mwa wale waliopokea vichapo toka kwa Nigaa na Lee. Sasa wote walikuwa wamesimama mbele ya nyumba ndogo iliyozungushiwa uzio, yenye rangi nyeupe na kupendezeshwa na bustani.



    "Ndio, ndiyo hapa!" Akasema Bilali akitikisa kichwa. Alafu wakagonga na kutulia hapo. Baada ya muda akafungua mwanaume fulani aliyekuwa amevalia bukta na kaushi ya zambarau. Alikuwa amesokota nywele zake zikisimama kama miba.



    Akawauliza wageniwe namna gani angewasaidia.



    "Tunahitaji kumwona bosi wako," akasema Bilali.



    "Bosi ametoka," wakajibiwa kwa ufupi.



    "Ametoka?" Bilali akastaajabu. "Mbona aliniambia atakuwepo mida hii mzee?"



    "Sijui, ila hayupo. Ametoka," akasisitizia mwenyeji.



    Lakini kabla wakina Mustapha hawajaondoka, ikaja gari hapo, Alphard nyeupe yenye vioo vyeusi. Wakasimama na kutazama. Kioo kikashushwa na akaonekana mchina mmoja mwanaume. Akawasalimu kwa kuwapungia mkono.





    "Ndiyo huyo hapo sasa!" Balali akamwambia Mustapha. Wote wakajikuta wanatabasamu.



    “You are welcome!” (Karibuni!) Mchina huyo ndani ya gari akasema na kisha akazama ndani ya uzio. Nyuma Mustapha na Bilali nao wakaingia na punde wakajikuta wapo sebuleni, na yule mchina akiwa anatazama ile picha ya nyaraka iliyokuwepo ndani ya simu ya Mustapha.



    Kwa umakini akaikagua kwanzia mwanzo mpaka mwisho. Akairudia tena kwa mara ya pili na kisha akauliza:



    “Mmeitoa wapi?” kwa sauti ya puani.



    Bilali akataka kujibu, lakini Mustapha akamuwahi na kumzuia. Akauliza:



    “Kuna ujumbe gani?”



    Mchina yule akashusha pumzi ndefu. Alafu akasema ile nyaraka ilikuwa ina taarifa fulani za koo iliyopo huko China. Koo yenye nguvu na ushawishi. Na kwenye hiyo nyaraka kulikuwa kina kipande kidogo tu cha taarifa yao.



    Yaani kuna taarifa ambayo imekosekana ili ipate kutimia. Na inaonekana taarifa hiyo ni ya siri, na koo hiyo wanaitafuta ipate kutimiza mahesabu.



    “Ona sasa! Tumejisumbua bure asee!” Bilali akalaumu.



    “Hapana,” akajibu yule mchina upesi. “Hii ni mali, mali kubwa sana hii, lakini pia ni damu!”



    “Damu? Kivipi?” Mustapha akauliza.



    “Kwanza ni mali kwasababu kuwa nacho ni pesa. Endapo ikijulikana kama mnacho, mnaweza mkavuta pesa yoyote ile kwasababu tu ya kuifanya ikawa siri…”



    “Na damu kivipi?” akauliza tena Mustapha.



    “Ni damu kwasababu wanaweza kuitafuta nyaraka yao pasipo kuamua kutoa pesa. Yani kwa lazima na hapo ndipo kuna shida!”



    Kukawa kimya kidogo. Kila mtu alikuwa anafikiria lake kichwani. Lakini mchina yule akawatoa hofu akisema:



    “Kuna namna lakini ya kutengeneza pesa kama tukikubaliana.”



    Mustapha na Balali wakatenga masikio yao.



    “Huyu mwenye hii nyaraka anajua makazi yenu? Au mahali anapoweza kuwapata?” mchina akauliza.



    Mustapha akatikisa kichwa chake kuafiki.



    “Ndio anapajua kwangu.”



    “Basi hama,” mchina akashauri. “Tafuta mahali unapojua utakuwa salama, ndipo tufanye hii njia.”



    “Kwanini nihame?” Mustapha akauliza.



    “Kwasababu watakutafuta,” mchina akamjibu. “Kabla hawajatoa pesa watahakikisha kama kuna njia ya kufanyika kukwepesha mfuko wao. Hawawezi wakatoa pesa kirahisi. Watatoa pesa ambapo wameona hamna namna ya ziada – hamna njia nyingine!”



    Mustapha akanyamaza kwa muda. Bilali naye hakuwa na cha kusema. Kukawa kimya wakitazamana. Mchina akaendelea kuongea.



    “Ni hatari lakini ni pesa kubwa sana tunaweza tukaitengeneza. Pesa ambayo kila mmoja wetu ataipata na kuifurahia. Mtanunua majumba na magari. Ila ndiyo hivyo, ina gharama yake. Inabidi tuwe radhi kuilipa.”



    Mustapha akamtazama Bilali, alafu akamtazama mchina na kumwambia:



    “Tupo tayari,” akipandisha kichwa.



    Basi mchina yule akaanza kuwaambia namna ambayo wanaweza wakatengeneza pesa kwa kupitia nyaraka ile. Kwanza wahakikishe wanaipata katika nyaraka ngumu, yani waiprint na kuihifadhi. Alafu wataituma mtandaoni moja kwa moja kwenye tovuti ya watu wao na kuwataka walipie pesa wakiwa wameshaainisha na akaunti yao ya benki.



    “Hakuna kukutana nao bali kuwasiliana tu mtandaoni. Kila kitu kitafanywa mtandaoni na watainunua nyaraka yao mtandaoni. Ni kama vile unavyofanya manunuzi mtandao wa ebay ama amazon.”



    Mustapha na Bilali wakakubaliana na hilo, ila sasa wakawa na kazi ya kwenda kufungua akaunti ya benki na wapate master card. Wakamshukuru mwenyeji wao kwa kuwafungua macho, wakaaga waende.



    Ila kabla hawajenda, mchina yule akawaomba:



    “Mnaweza mkanitumia nyaraka hiyo kwenye simu?”



    Mustapha akakataa. Bado hawakuwa wanamwamini mchina huyo kiasi hicho. Vipi kama akiwazunguka?



    “Its ok, hamna shida. Naelewa,” akasema mchina kwa kutabasamu. akawasindikiza wageni wake mpaka nje ya nyumba, akawaomba awabebe kuwapeleka nyumbani maana hana kazi ya kufanya kwa sasa na angependa kuwasaidia.



    Mustapha na mwenzake wakaona hamna shida katika hilo, wakajipaki ndani ya Alphard na safari ikashika hatamu.



    Wakadumu kwenye gari kwa kama dakika arobaini na tano kabla hawajafika kwa Mustapha ambapo wote walishukia.



    “Nashukuru sana,”



    “Msijali, tutawasiliana,” mchina akasema na kisha akaondoka zake.



    Hili ndilo lilikuwa kosa kubwa alilolifanya Mustapha. Aliweza kuruka viunzi kote huko ila hichi akakisahau. Mchina huyu hakuwa mjinga kuchoma mafuta yake kuwaleta hapa. Kuna kitu alikuwa amekipanga na kukitaka, na alishakipata!



    Akiwa ndani ya gari yake, anawasiliana na mwanaume fulani wakiteta kwa lugha yao ya nyumbani. Mchongo ukawekwa bayana wa kumuua Mustapha pamoja na mwenzake na kisha nyaraka ile ndani ya simu iwe mali yao.



    Kumbuka huna rafiki wa kweli ndani ya dunia hii ya washenzi! Anamalizia kwa kusema kwa Kiswahili:



    “Usibakize hata tone la ushahidi.”





    ***





    Saa nne usiku…





    Akiwa anatengeneza juice, simu yake inaita. Jona anaitazama na kuona jina la ‘Beka’ kwenye kioo. Anaguna na kuivuta simu, kisha anapokea.



    Beka ni nani? Ni mwanaume jirani na fremu na ya Jona huko Mwenge. Sehemu yake ya biashara inafuatia baada ya pale kwa Jona. Kabla Jona hajapokea simu hiyo, anajiuliza kutakuwa kuna nini. Na akili yake inamwambia si salama.



    Si mara kwa mara Beka humpigia.



    “Niambie Beka.”



    Pasipo kupoteza muda Beka anamwambia juu ya kifo cha Jumanne. Wamemkuta amejifia ndani ya fremu wasijue nani anahusika. Wametambua hilo muda si mrefu wakiwa wanafunga maeneo ya kazi, wakastaajabu kuona Jumanne hafungi na muda ushaenda.



    Walipoenda kutazama, wakakutana na kisanga hicho.



    “Beka, ni utani au?” Jona akauliza kwa kuchanganyikiwa.



    “Si utani, brother. Tupo hapa pamoja na mwili.”



    Haraka Jona akajiveka shati na kukimbilia eneo la tukio. Kichwa chake hakikuwa salama kabisa kwa mawazo. Kuna muda akajiuliza kama siku hiyo ilikuwa ya wajinga, ama? La hasha haikuwa!



    Aliona dereva bodaboda anabembeleza pikipiki akamhasa aongeze mwendokasi. Alipofika, akajitupa toka kwenye bodaboda akimkabidhi dereva pesa yake. Moja kwa moja akenda eneo la tukio.



    Hapo akakuta wanaume wanne wakiwa wamejikusanya na kuteta. Akawasalimu akizama ndani alipoonyeshewa mkono na Beka. Akaukuta mwili wa Jumanne ukiwa umejilaza.



    Akatazama mapigo ya moyo, hayakuwa yanapiga. Akahakikisha na pumzi pia, kote hola! Akaamini sasa ni kweli Jumanne alikuwa ameenda. Alikuwa amekufa!



    “Hatujui alikufa muda gani, na nani amemuua. Sijui ni nini kilichotokea!” Alisema Beka. “Lakini Chaz anasema ….” Beka akamtazama Chaz, mwanaume mrefu mwenye mwili, akampatia kijiti cha kutia neno.



    “Mida ya asubuhi asubuhi hivi nilimwona njemba fulani akitoka ndani huku. Alikuwa amevalia suti, mara nikamwona anatembea fasta fasta, akadandia boda na kusepa! … nahisi anaweza akawa anahusika.”



    Jona akaulizia rangi ya suti na mwonekano wa mwanaume huyo, Chaz akamjibu. Akameza taarifa hizo, na kwasababu ule ulikuwa ni mzigo wake, siku hiyo hakulala akaimaliza kwa kuhangaika huku na kule kwa ajili ya marehemu Jumanne.



    Akaenda polisi kutoa taarifa na kisha kufanya utaratibu wa kusafirisha maiti mpaka mochwari, kuwasiliana na familia ya Jumanne na kadhalika.



    Mpaka kwenye majira ya saa sita usiku ndiyo akawa ametulia, tena akiwa kibarazani mwa nyumba ya Jumanne. Alikuwa pamoja na mke wa marehemu aliyekuwa analia pasipo kupumzika.



    Muda si mrefu, majirani wawili nao wakafika hapo kujumuika nao.



    Japokuwa kulikuwa kuna maongezi kadhaa na kilio, Jona hakuwa mwenye habari. Kichwa chake alikuwa amekiegemesha ukutani akielemewa na mawazo mazito sana. Ni nani amemuua Jumanne na amefanya hivyo kwasababu gani?



    Huyo mwanaume ndani ya suti, ni nani? Hakupata usingizi kabisa wala kujihisi njaa. Alishiba mawazo.



    Uwanda wake wa mawazo ukapanuka zaidi, na kuna jambo alipolifikiri likamuwashia taa za hatari kichwani.



    Nini kinafuata baada ya kifo cha Jumanne? Kufunga biashara … ndio … maana hataweza kukaa hapo na huku zile msheni zake zinamtaka asionekane. Hii itakuwa ni biashara ya ngapi anafunga sasa?



    Kwa namna moja kubwa, Jona akajikuta anatilia mashaka ile kauli ya Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Dar es salaam:



    “Jona, maisha yako kamwe hayatakuwa sawa ukiwa nje ya jeshi. Huu ndiyo wito wako na hauwezi kuukwepa. Na sisi tutakukumbusha hilo kila uchwao.”



    Alikumbuka maneno yote hayo kana kwamba ametoka kuambiwa muda si mrefu. Akawaza je yatakuwa yanahusika na kifo cha Jumanne? Na hapo tena akajiuliza, je kauli ile itakuwa ina mahusiano na kufa kwa biashara yake?



    Jona akajikuta anapata mawazo ambayo hakuwahi kuyawaza hapo kabla.



    Je kauli ile ya kamanda itakuwa ina mahusiano na kifo cha utata cha familia yake?



    Ya kwamba maisha yake hayatakuwa salama wala ya amani akiwa nje ya jeshi?



    Akaona ana haja ya kunywa. Akanyanyuka na kuondoka zake akienda kutafuta bar. Alipopata akanunua mvinyo na kunywa kwa pupa. Akanywa kwa pupa … akanywa kwa pupa.



    Aliomba pombe imsaidie kupumzika japo kwa muda. Impeleke mahali ambapo atakuwa salama na mbali na uhalisia.





    ***





    Saa nne asubuhi…





    “Amesemaje ulipochonga naye?” aliuliza mwanaume fulani mweupe. Mrefu na mwenye mwili wa mazoezi. Swali hili akilielekezea kwa Nyokaa aliyekuwa ameketi kwenye kochi akivuta sigara.



    “Atajua mwenyewe atakavyosema, ila najua atamleta tu yule manzi.”



    “Una uhakika?”



    “Asilimia mia nane, nina uhakika. Inaonekana anamzimia sana huyu malaya wake. Atajileta tu.”



    Kukawa kimya kidogo.



    “Ila unajua nini Nyokaa, tukimpata tena yule manzi, tujitahidi kumaliza ile ishu mazee. Unajua yule manzi anaweza akawa ametoboa gunia letu la mchele huko kama alivyotoboa la yule boya?”



    “Sidhani asee. Namwamini sana yule manzi.”



    “Hapo ndipo unapofeli sasa, unamwanijie manzi kiasi hicho Arif?”

    .

    .

    .

    .

    ***



    “Najua Miriam ananipenda na yupo radhi kufanya jambo lolote kwa ajili yangu. We unajua ni mangapi yule manzi amefanya kwa ajili yangu?” akauliza Nyokaa. Kabla hajangoja majibu, akaendelea kumwaga sera:

    “Amenifanyia mbishe mingi sana asee kabla haya mafyoko hayajatokea hapa kati. Unadhani angekuwa manzi mwingine akithubutu?”

    Mwanaume yule mweupe, kwa jina Roba, akatikisa kichwa alafu akashusha pumzi yake akitazama kando. Kuna jambo alikuwa analifikiria, na punde akamshirikisha Nyokaa.

    “Unajua mishe zetu, mwanangu. Za hatari kinoma, inabidi tuwe macho sana kuangaza kama kuna snitch, la sivyo tutaharibu kila kitu.”

    “Najua,” akajibu Nyokaa kwa ufupi. Na hakutia tena neno lingine kukiwa kimya kwa muda wa kama dakika tatu.

    “Umeshandaa kila kitu lakini?” Nyokaa akauliza.

    “Kila kitu kipo tayari yani, ni huyo mgeni tu aje.”

    Baada ya hapo kimya kikawa kingi.



    ***



    Saa sita mchana.

    Chumba SPACE BUTTON



    “Naweza nikapata kikombe cha kahawa?” alisema Panky akimtazama Moderator.

    “Cha ngapi sasa?” Moderator akauliza kwa lafudhi yake ya kichina.

    “Sijui idadi,” akajibu Panky. “Naomba tu uniletee kama hutojali.”

    Moderator akasita kwanza na kumtazama Panky. Panky akatabasamu kabla hajageukia tarakilishi yake na kuendelea na kazi aliyokuwa anafanya. Moderator akatoka nje.

    Basi haraka Panky akamtazama Marwa. Mwanaume huyo alikuwa yupo mbali naye sana, kitu ambacho kilikuwa kinamkera si kidogo. Alinyanyuka upesi akamfuata na kumsabahi, na pasipo kupoteza muda akamwambia asome jumbe zake ambazo amemtumia kwenye mashine.

    Kuepusha kukutwa na Moderator, upesi akarejea kwenye kiti na kuendelea na kazi yake. Na kweli, punde Moderator akatokea akiwa amebebelea chupa kubwa rangi ya bluu. Akaiweka mezani mwa Panky.

    “Hiyo hapo, hautasumbua tena sasa!”

    Panky akashukuru kwa tabasamu, akajimiminia kinywaji na kunywa akiendelea na kazi. lakini akili yake ikiwa inamuwaza Marwa kama kweli ameelewa kile alichomwambia.

    “Kile kichwa kigumu nacho,” alisemea kifuani. Akavizia pale Moderator aliposogea kando, akashusha kazi zake zote chini, alafu akafungua application fulani iliyokuwa na kialama chenye rangi nyekundu, akaandika:

    “Unanipata?” alafu akatuma kwenye tarakilishi aliyoitunza kwa jina la M-Spy.

    Alipotuma ujumbe huo, akamtazama Marwa kwa wizi, punde naye Marwa akamtazama. Alafu akabofya keyboard.

    “Ndio, nakupata. Unataka nini Panky?” Ujumbe ukaingia kwenye tarakilishi ya Panky. Panky akatabasamu kwanza kabla ya kujibu. Alifurahi sasa maana alikuwa amepata ‘chobingo’ ya kuteta na mtu wake. Nafasi adhimu hii.

    Panky: sina ishu mpya, ni kuhusu tu ile picha.

    M-Spy: Imefanyaje? Kwani hukunielewa?

    Panky: Unajua nini Marwa, niliipenda sana ile picha. na nilivyoenda kufanya ile misheni niliyoagizwa, nikajikuta nakumbana nayo. Sidhani kama ni vibaya nikajua maana yake.

    M-Spy: Panky, acha ujinga.

    Panky: Kivipi? Nataka kuuondoa huo ujinga kwa kujua.

    M-Spy: Nikukumbushe mara ngapi kwamba hatutakiwi kushirikiana kwa vyovyote tukiwa kazini mpaka pale Mode atakapokuwa anajua?

    Panky: Marwa, acha kujifanya bingwa wa kufuata sheria. Ni mara ngapi huwa nakusaidia mambo yako? Huwa unamuita Mode?

    Kimya.

    Panky akatazama upande aliopo Marwa, akamwona Moderator akiwa amesimama kandokando ya mwanaume huyo. Moyo ukamlipuka kwa kudhani huenda pamebumburuka. Lakini alivyotazama vema akagundua, Marwa alikuwa tayari ameshatoa yale maongezi yao na yupo bize kufanya kazi.

    Basi naye kwa muda akazama kazini mpaka baada ya dakika kama tano alipopata ujumbe toka kwa Marwa.

    M-Spy: Tukutane wakati wa chakula!

    Panky: Poa.

    Kazi zikadumu mpaka majira ya saa nane, watu wakafunga kila kitu kwa ajili ya kwenda kutia kitu tumboni. Huko Marwa na Panky wakakutana na kuteta mambo kadhaa kuhusu ile picha. Cha kushangaza ni kwamba, hata Marwa mwenyewe hakuwa anajua nini kimo pichani!

    Lakini data alizokuwa amepewa kuzitumia kufuma ile picha zilikuwa ni za kushangaza na zenye kuhitaji mafikira kung’amua.

    “Nashukuru sana, Marwa. Nadhani ingekuwa vema kama ungelinitumia picha hiyo kwenye tarakilishi yangu,” alisema Panky akijua wazi pale hawana muda mrefu wa kujadili.

    Marwa akatabasamu.

    “Unajua hilo jambo haliwezekani, Panky.”

    “Inawezekana.” Panky akamkatiza. “Nimetengeneza code ya kuniwezesha kuwasiliana na kila tarakilishi mule ndani. Nina application za kuniwezesha kutengua security na kupokea ama kutuma faili kwa yeyote ndani ya chumba.”

    Marwa akastaajabu.

    “Umewezaje kufanya hivyo?”

    Panky akatabasamu.

    “Huu si muda wa kujadiliana, Marwa. Unajua muda wetu hapa.”

    “Sawa, ila unajua tarakilishi yangu haina uwezo huo kama wako. Sasa natumaje?”

    “Ngoja n’takuonyesha. Wewe kuwa karibu na messenger tu, sawa?”

    Wakamaliza kula na kuondoka. Wakafanya kama vile walivyoelekezana, na Panky akafanikiwa kupata picha na maelekezo yote ambayo Marwa aliyatumia kufuma picha hiyo. Basi tabasamu likajaa usoni.

    Ila muda si mrefu, akashikwa bega na Moderator, akatazamwa na uso mgumu na kisha akaamriwa:

    “Simama!”

    Utumbo ukamtetemeka na kichwa kikaanza kumgonga! Watu wote ndani ya chumba wakamtazama. Ila Marwa akiwa anatamazama kwa woga zaidi!

    Bila shaka alijua sasa kila kitu kimeanikwa wazi! Mwisho wao ulikuwa umewasili, kifo kinawaita. Marwa akajuta kwanini alifanya ujinga ule.

    Moderator akakaa kwenye kiti cha Panky na kuanza kupekua tarakilishi hiyo. akachukua muda wa dakika tano kabla hajanyanyuka na kumtaka Panky aketi chini. Hakuna alichokigundua!

    “Unaweza ukaendelea na kazi yako!” akasema Moderator.

    Panky akaketi akiwa haamini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lakini baadae akajiona ‘jembe’ kwa namna alivyotengeneza mfumo wake madhubuti kiasi cha kumfanya mtaalamu asipate chochote ndani ya mashine yake.

    Akajikuta anatabasamu akipekua pekua tena tarakilishi yake. Kila jambo lilikuwapo kama alivyoyaweka.

    ----

    Saa kumi jioni:



    Panky anachomoa simu yake mfukoni na kumtafuta Jona. Simu ikaita mara tatu pasipo majibu. Akasonya na kujiuliza atakuwa wapi.

    Alikuwa ameshatoka kazini na akiwa tayari amebebelea flashi ambayo ina faili nyeti la ile picha.

    Alikuwa ameketi nyumbani kwake, sebuleni, akitafakari. Mkewe akaja akitokea dukani.

    "Vipi mbona una mawazo hivyo?" Akauliza mwanamke huyu mweupe mwembamba aliyevalia kofia ya kuziba nywele pamoja na dera la njano lenye maua mekundu mekundu.

    Panky akamlaghai mkewe kwamba yupo sawa na angependa apate muda kidogo wa kutafakari peke yake.

    "Unataka nikuache, sio?" Mke akauliza kwa shari. "Yani hapa nyuma uliniacha peke yangu, sikujua wapi ulipo na unafanya nini, leo upo hapa nakaa na wewe unataka nikuache?!"

    "Si hivyo mpenzi!"

    "Ni vipi? - haya kaa basi mwenyewe!" Mwanamke akanyanyuka na kwenda zake. Panky akabakia kumtazama.

    Ila mara na simu ikaita, kutazama alikuwa ni Jona.

    "Nimekutafuta sana mzee vipi? ... ishu gani hiyo? ... serious? ... pole sana kaka, sasa inakuaje? ... yah! Nimepata ile kitu sasa ndo nikawa nataka tukutane uione kama vipi ... poa, basi utanshtua au sio? ... haya baadae!"

    Simu ikakata. Panky akachomoa flash mfukoni mwake na kuitazama. Akanyanyuka na kwendaze chumbani.



    ***



    Saa moja jioni.



    Ngo! Ngo! Ngo!

    "Naona ameshafika, acha nikachonge naye!" Glady aliwaambia wenzake wawili aliokuwa nao chumbani kabla hajanyanyuka na kwenda mlangoni.

    Alikuwa amevalia gauni fupi la njano lililoacha miguu yake uchi. Nywele zake alikuwa amezikusanyia ndani ya kiremba cheusi cha kulalia.

    Alitoka nje akamkuta Mustapha. Alikuwa amevalia shati la buluu, suruali ya kaki na raba nyeupe. Mwanaume huyo akamtaka wakaongelee ndani.

    "Kuna watu, tuongelee tu hapa hapa!" Glady akasisitiza. Mustapha akatazama kushoto na kulia kwake kama kuna usalama. Uso wake ulikuwa una mashaka.

    "Mustapha, kuna nini?" Glady akauliza. Alihisi kuna mambo hayapo sawia.

    "Naomba niingie ndani!" Akasisitiza Mustapha. "Tafadhali!"

    Kabla hata Glady hajajibu, Mustapha akazama ndani na akaurudishia mlango yeye mwenyewe. Akashika kiuno na kushusha pumzi. Glady akamtazama na kumuuliza nini shida mbona anamtia woga!

    Mustapha akamwambia hayupo salama, kuna mtu anataka kummaliza!

    "Nani huyo?" Glady akawahi kuuliza. "Yule mchina?"

    Mustapha akatikisa kichwa. Akasema muuaji huyu hamjui, amemkosa kosa na risasi akijaribu kujiepusha kwa kupitia mlango wa nyuma!

    "Mustapha, upo serious?"

    "Kabisa! Na hapa ninavyoongea na wewe, Bilali ameuawa tayari!"

    Glady akatoa macho ya mshangao. Na hapo akawa amevaa hofu nyeusi kiasi kwamba akamshangaa Mustapha kuja hapo ilhali ana songombingo la kumwaga damu!

    Vipi kama akiwaambukiza tatizo?

    "Sikuwa na kwengine pa kwenda, Glady. Naomba unisaidie hifadhi," alisema Mustapha kwa huruma. Haraka Glady akaenda dirishani na kutazama huko nje.

    Akateta na wenzake wakiwa katika hali ya taharuki.

    "Mustapha, utakuwa umefanya nini saa hii?"

    "Sijafanya kitu, ila nahisi atakuwa ni yule mchina tuliyempelekea ile nyaraka atutafsrie. Anatuzunguka, anataka kuichukua!" Alisema Mustapha. Jasho lilikuwa linamtiririka.

    Akamweleza Glady kinaga ubaga walivyoenda kuomba msaada kwa yule mchina ambaye aliwapa lifti kuwarejesha nyumbani.

    Wakiwa taharukini, wanasikia mlango unagongwa! Glady anamtazama Mustapha, kisha anawatazama wenzake waliokuwa kitandani.



    Kila mtu akajawa na hofu. Habari zile za Mustapha ziliwatisha na sasa wakadhani mambo yameanza kutiwa chumvi kunoga. Roho ya mtu imeshafuatwa.



    Basi kwa tahadhari, Glady akachungulia dirishani kutazama aliyemlangoni. Akamwona mwanaume fulani mrefu mweusi akiwa amevalia suruali ya kijani na tisheti nyeupe.

    Mwanaume huyu alikuwa amepachika hereni kwenye sikio lake la kushoto akitafuna jojo kwa mapozi.



    Glady akaguna na kisha akamweleza Mustapha juu ya mwonekano wa mwanaume huyo ili ajue kama ndiye yeye anayemtafuta. Kwa kuhakikisha, Mustapha naye akachungulia na akaona si yule ambaye anamuwinda. Ila bado akawa na hofu.



    “Embu msikilize anataka nini,” akamwambia Glady. Glady akatoka na kwenda kukutana na mwanaume huyo. Alisimama mlangoni mkono wake wa kushoto ukiwa umeshikilia mlango ambao hakuwa ameufunga ili lolote litakapotokea, ajue namna ya kujikomboa.



    “Habari, dada,” akasema mwanaume huyo akimtazama Glady kuanzia juu mpaka chini. Glady akaitikia salamu na kisha akamtaka aeleze shida yake ni nini. Mwanaume akalamba lips zake, akashika kidevu na kumwambia anataka kuonana na Rose.



    Angalau hapo Glady akashusha pumzi ya hofu na kuona mambo yapo sawa. Rose ni rafiki yake na yupo ndani. Basi aklichofanya ni kumuita Rose akutane na mgeni wake, alafu yeye akaenda kuteta na Mustapha.



    “Najuta kwanini nimejiingiza kwenye janga hili,” akasema Mustapha. “Naona kuna haja ya kuonana na yule mchina na kumweleza yote haya, pengine anaweza kunisaidia.”

    Glady hakuafiki, wakazoza kwa muda kidogo pasipo kufikia makubaliano.





    ***





    Saa tatu usiku, Mbezi beach: Afrikana ya chini. Ndani ya nyumba kubwa rangi ya kijani yenye uzio mweupe.



    Kamanda akasafisha koo lake, akauliza:



    “Kwahiyo mpaka sasa umejua yupo na move gani?”



    Akiwa ameketi kibarazani kwenye kiti kikubwa kilichofumwa na kambakamba za mbao na kujazwa sponji. Kando yake akiwa ameketi yule mwanaume muuaji wa Jumanne, akiwa amevalia suti rangi nyeusi, ila nayo ikiwa imemzidi umbo. Mbele yao kukiwa kumeketi stuli ndogo nyeusi inayong’aa kama kioo.



    Juu ya stuli hiyo kulikuwa kuna chupa kubwa ya maji ya Kilimanjaro na glasi mbili pembeni.



    “Bado yupo msibani, ni ngumu kujua amepanga kufanya nini, lakini kwasababu msiba utaisha leo, nitapata kujua,” akasema muuaji. Jina lake ni Alphonce Ndebali – afisa wa polisi, mwanaume huyu akihusika na kitengo nyeti cha mateso.



    Kamanda akamhusia:



    “Kuwa makini, hakikisha kila jambo linaenda kama lilivyopangwa. Unamjua vema Jona.”



    “Usijali, mkuu. Sijawahi kukuangusha na wala haitakuja kutokea,” akasema Alphonce. Hii haikuwa kazi yake ya kwanza kwa Jona kwani alishafanikisha kumuua mke na mtoto wake kwa kuchoma nyumba.



    Alishafanikisha pia kufuatilia na kuharibu mipango ya biashara ya Jona. Kwa ujumla, alifanikisha mengi kumfanya Jona aishi maisha ya tabu na dhiki. Na kama haitoshi alikuwa anawinda zaidi na zaidi.



    Kazi yake ilikuwa ni kumfanya Jona arejee jeshini kama sehemu yake ya mwisho ya kupata msaada. Akose mkono wa kumsaidia wala mlango wa kutokea. Na alipewa kazi hii kwakuwa anaiweza na kuimudu ipasavyo.



    Alphonce Ndebali ama Jabali kama wamuitavyo wenzake hakuwa mtu wa mchezo hata kidogo. Alikuwa ni mtu asiye na chembe ya huruma. Anamuua mtu huku akimtazama machoni na kutabasamu! Anapata raha kila anapomwaga damu na kukatisha pumzi ya mtu.



    Hana roho ya binadamu, mishipa yake ya utu ilishakatika muda mrefu sana huko nyuma!



    Na japokuwa ni afisa wa polisi, amekuwa akijihusisha na ‘michongo’ mbalimbali ya biashara haramu. Ni muuza madawa ya kulevya, lakini pia amekuwa akikodishwa na watu mbalimbali kufanya mauaji ama kutishia uhai watu kwasababu binafsi.



    Huo ulikuwa ni upande wake ambao jeshi haufahamu. Huo ulikuwa ni upande wake ambao unamwingizia kipato kikubwa kuliko kile anachopewa kila mwisho wa mwezi na jeshi la polisi.



    “Unajua kuna kitu nawaza,” Kamanda alisema akikuna kidevu chake. Alphonce akamwazima macho na masikio yake. Kamanda akamwambia kama ikishindikana kumrejesha Jona kwa haya yote watakayoyafanya, basi wammalize. Hakuna haja ya kumwacha awe hai kwani itakuwa dharau na ishara ya kufeli.



    Alphonce akatabasamu na kuuliza: hilo tu mkuu? Huo ni mfupa mdomoni mwa fisi.





    ***





    Saa sita mchana, Koko bar …





    Mezani kuna Smirnoff moja pweke, na Jona ameketi akiwa amelaza kichwa chake juu ya tama. Anawaza mambo kadhaa na hana furaha. Jumanne ameshazikwa na kaenda zake, ila kamwachia maswali mengi sana. Anahisi kichwa chake kimevurugika.



    Anachomoa simu yake mfukoni na kutazama, anapiga na kuiweka sikioni. Anaongea na mtu anayemuelekeza mahali alipo na isichukue muda mrefu, mtu huyo anafika. Alikuwa ni Panky akiwa amebebelea begi jeusi, amevalia shati jeupe na suruali ya jeans.



    Baada ya kusalimiana na kujuliana hali, Panky anafungua begi lake na kutoa tarakilishi mpakato, anaiwasha na kuchomeka flash disk. Punde inasoma, anamwonyesha Jona kile ambacho alikipata toka kwa Marwa.



    Kwenye kioo cha tarakilishi kulikuwa kuna mahesabu kadhaa na drafti ya kwanza ya mchoro. Kupata maana vema, Jona aliona kuna haja ya kuwa na mchoro ule pale pale kwa ajili ya kulinganisha. Hivyo basi akanywa kinywaji chake kwa mkupuo alafu wakaenda nyumbani kwake.



    Hapakuwa kule pa zamani, la hasha, bali nyumba nyingine ndogo tu isiyo na uzio. Ina vyumba vitatu na sebule. Humo Jona akatoa picha ile chumbani na kuanza kuirejelea na yale mahesabu ya Marwa na drafti yake ya kwanza.



    Wakaja kugundua kumbe kila kilichochorwa mule kilikuwa kimepangwa kisanii na kimahesabu. Vipimo umbali na upana vilikuwa vinafanana. Kuanzia umbali wa kila ndege aliyekuwa anaruka angani, visiwa pichani, na hata mawimbi baharini.



    Lakini maana yake nini? Walishindwa kuipata. Lakini hata hivyo, akili ya Jona bado haikuwa imetulia. Hakuwa anawaza vema. Akamwomba Panky amwachie picha hiyo, ataifanyia kazi akitulia na kufanya mambo taratibu.



    Panky akaridhia na haikuchukua muda mrefu akaenda zake akimwacha Jona peke yake. Jona akaongeza kinywaji cha pili kisha akalala kwa muda kidogo. Aliikuja kukurupuka akatazama simu yake, saa kumi jioni! Akaoga na kisha kuketi sebuleni.



    Akaendelea kupekua pekua picha ile kwa macho yake mekundu. Lakini hakupata kitu. Akaghafirika. Aliona anapoteza muda na kichwa kinazidi kumuuma. Akaifunga picha ile na kwenda kuificha kabatini.



    Mara simu yake ikaita, alikuwa ni Mheshimiwa Eliakimu. Akapokea na kuiweka sikioni. Mheshimiwa alikuwa anamuulizia lile jambo la kumuokoa Nade. Wale wanaume watekaji wamempigia simu na wamempatia masaa matano tu awe amatekeleza, la sivyo wasitafutane!



    “Yakipita masaa hayo, wamesema watammaliza Nade na sitosikia lolote toka kwao milele!” Akasema mheshimiwa.



    “Hamna haja ya kuhofia,” Jona akamhusia. “Hakuna lolote watakaolifanya kwa Nade kwasababu nao pia wanamhitaji Miriam kwa hali na mali. Ni vitisho tu!”



    “Umejuaje? Na unafahamu wanamhitaji kwasababu gani?”



    “Nitafahamu karibuni, pamoja na wewe kwanini hutaki wampate Miriam.”



    Baada ya kusema hivyo, Jona akamwambia Mheshimiwa kwamba ataifanya kazi yake usiku. Na kabla ya kupambazuka, Nade atakuwa kwenye mikono salama. Kisha akakata simu na kuanza kujipanga kwa ajili ya kazi hiyo.





    ---





    ‘Ukithubutu kuleta ujanja wowote, utajuta!’ Ulisomeka ujumbe ndani ya simu ya Mheshimiwa Eliakimu, ujumbe huo ukitokea kwa watekaji, na ukiingia punde tu Mheshimiwa alipotoka kuongea na Jona.



    Mheshimiwa akaagiza kwanza maji ya kunywa. Aliogopa kwa kudhani huenda watekaji hao wamejua janja yake ya kumwokoa Nade. Ila hapana! Akatikisa kichwa. Watakuwa wanahisi tu, akawaza. Hakuwa na budi kumwamini Jona. Hakuwa na mlango mwingine wa kutokea.



    Mambo yalikuwa tafrani.





    ***





    Saa mbili jioni…





    ‘Napitia hapo, basi nikukute,’ Boka akatuma ujumbe kwenda kwa Miranda. Mwanamke huyo akaupokea kwa tabasamu kabla hajarudisha majibu:



    ‘Sawa, utanikuta nakungoja.’



    Boka akatabasamu mwenyewe nyuma ya gari kama mwehu. Akampatia maelekezo dereva wake apitie nyumbani kwa Miranda, maeneo ya Kawe.



    Miranda naye akaweka mazingira yake safi kwa ajili ya kumpokea mgeni. Aliandaa mvinyo na glasi zake, pamoja na chakula kitamu cha kumfanya mgeni ajilambe na kwenda kusimulia.



    Alafu akajivesha nguo maridadi na kufanya hali ya hewa inukie. Akaketi kumngoja mgeni wake kwa hamu.



    Dakika chache kupita, akasikia sauti ya honi huko getini. Akatabasamu na kujitengenezea vema gauni lake jekundu. Akamwita mlinzi na kumuagiza afungue geti upesi kwani kuna mgeni wake wa maana.



    Geti likafunguliwa, na akastaajabu kuona gari aina ya Murrano nyeupe ikiingia ndani. Kutazama, akamwona mke wa Boka akishuka toka kwenye gari hilo, akamtazama kwa tabasamu akimpungia mkono.



    Kichwani akajiuliza mwanamke huyu ametokea wapi? Kwa namna moja akahisi pengine ndiye aliyekuwa anatumia simu ya mumewe, Boka, kumtumia ujumbe. Basi akawa na hofu.



    Lakini wakati mama huyo anamjongea akiwa anatabasamu, simu yake ikaingia ujumbe. Akatazama upesi. Ulikuwa unatoka kwa Boka.



    ‘Nakaribia kufika.’



    Moyo wa Miranda ukapasuka pah!



    Kwahiyo Boka na mkewe hawakuwa wanajua kama wanakutana sehemu moja! Miranda akajua hilo. Sasa afanyaje? Japokuwa alimpokea mke wa Boka na kumkarimu kwa tabasamu matata, akili yake haikuwa pale kabisa.



    Haraka alitumikisha vidole vyake kuandika ujumbe na kuutuma. Akimtaarifu Boka juu ya ujio wa mumewe eneo hilo. Kama haitoshi, pengine kwa kuhofia Boka anaweza akawa hajaupata ujumbe huo, akaibipu simu yake kumtaarifu.



    Boka akatazama simu yake akikunja uso. Kiooni akaona ujumbe toka kwa Miranda. Ila kabla hajaufungua ujumbe huo, dereva akawa tayari ameshapiga honi mara tatu getini! Na kwakuwa mlinzi alikuwa na taarifa juu ya ujio huo, haraka akafungua geti.



    “Simama!” Boka akampiga dereva begani. “Rudi haraka, tuondoke hapa!” Dereva hakuelewa kinachoendelea. Alipigwa na butwaa, ila kutii amri ya bosi akarudisha gari nyuma upesi, na kuligeuza. Alidhani pengine itakuwa ni kuhusu mambo ya usalama. Wakayoyoma.



    Lakini mama Boka akahisi jambo. Akauliza:



    “Nimeona kama gari ya mume wangu,” alisema akitazama nje kupitia dirishani. Miranda akaigiza kushtukiza. Mama akanyanyuka na kwenda nje. Akaangaza pasipo mafanikio kwani geti lilikuwa limefungwa.



    “Hamna kitu, mama! Utakuwa umeona vibaya,” akasema Miranda akitabasamu kiuongo.



    “Hapana, sidhani. Nimefikia uzee huo!”



    Basi Miranda kumaliza zogo akamwita mlinzi aliyemkonyeza tayari kwa ishara. Akamuuliza eti ni nani yule aliyekuja na kuondoka, kwanini ameondoka, na alikuwa anataka nini?



    “Aaah Madam, ni Kinoo yule!” Mlinzi akasema akijichekesha. “Amesema kuna kitu alikuwa anakuletea ila sasa bahati mbaya amekisahau?”



    “Kwahiyo ndo’ ameenda kukichukua?”



    “Eeeenh! Ndo maana nikaona hamna hata haja ya kuja kukwambia huku … anaweza akarudi muda si mrefu.”



    Angalau Mama Boka akawa ametuliza kifua. Wakarejea ndani na kueleza lile lililonyanyua mguu wake kumleta hapo.



    “Samahani sana, najua nimekuja kwa kukushtukiza. Nilikuwa njiani kuelekea City mall, nikaona kuna haja kama nikikatiza hapa maana nina habari za kupasua kifua.”



    Akaweka kituo akimeza mate.



    “Kuna kampuni kubwa sana ya usambazaji ya huko nchini Kenya, wamevutiwa na kazi zetu na hivyo basi wanataka tuwe na ubia. Maana yake ni kwamba, bidhaa zetu sasa zitavuka mipaka na kwenda Kenya kwa uhakika!”



    “Habari nzuri sana hizo!” Miranda akatahamaki. Ila kinafki. Hakuna wazo lake lolote lililokuwa pale. Alikuwa anamuwaza Boka. Namna alivyomkosa. Akijipa moyo ni kukuwe na hana haja ya kumshikia manati.



    Ila alikuwa anataka kumaliza kazi. Huyu kuku atakaa nje ya banda kwa muda gani? Basi mawazo hayo yakapeleka mbali kichwa chake, yale aliyokuwa anayaongea Mama Boka kwake yakawa kama kelele za chura. Alichokuja kusikia mwishoni ni kile cha kuambiwa lazima interview yake ifanyike kesho kutwa.



    “… Tutakapofanya hicho kitu, hapo ndo’ tutaeleza pia umma kwamba kampuni yetu imetanuka na sasa imefika Kenya.”



    Akaitikia: “Sawa.”



    Na hata hivyo vingine vyote vilivyofuatia, akamkubalia pasipo shida. Alikuwa anataka mama huyo aondoke amwache huru, haikupita muda akaaga na kwenda. Kitu cha kwanza ambacho Miranda alifanya ni kuchukua simu yake na kumtumia ujumbe Boka.



    ‘Ameondoka.’



    Boka akamjibu baada ya muda mfupi:



    ‘Tutaonana siku nyingine mpenzi. Usijali.’





    ***



    Saa tano usiku …





    “Sasa Mustapha? – nataka kuondoka,” akasema Glady. Alikuwa amevalia bukta fupi rangi ya pinki na kaushi nyeupe nyepesi. Hakuwa amevalia sidiria, na hivyo basi chuchu zake zilikuwa zinaonekana vema zikitoboa kaushi. Miguuni alikuwa amevalia raba nyeupe – converse, mkononi akibebelea mkoba mkubwa mweusi.



    “Sawa, we nenda tu,” Mustapha akajibu. Alikuwa ameketi kitandani nyayo zake zikigusa sakafu. Glady akacheka.



    “Unajua unachekesha we Mustapha. Niende wapi na wewe umetuama humu? Au mpaka nikuambie amka uende mie nataka kufunga chumba?”



    Mustapha akawa kimya kwanza. Sijui akitafakari nini, akamtazama Glady kwa huruma akisema:



    “Unajua mikasa yangu ndugu yangu, unadhani n’taenda wapi? Huko nje si salama kwangu,”



    “Leo nimekuwa ndugu yako, Mustapha?” Glady akapiga kofi akiangua kicheko. “Kweli shida kirusi. Sasa na mimi chumba changu hakipo salama nikikuacha humu. Umesikia? Mie n’takufuga humu mpaka lini labda?”



    “Naomba unihifadhi kwa leo tu,” Mustapha akanyenyekea. “Kesho n’tajua mie pa kuelekea.”



    “Sasa Mustaphaa …” Glady akakaa kitandani na kumtazama Mustapha. “Mie nikienda nikapata danga langu huko, n’talipeleka wapi? Mfano halina chumba, au anataka tufanyie kwangu? Ntafanyaje?”



    “Kwa leo tu, Glady.”



    “Mustapha mie n’takula nini?”



    Mustapha akazamisha mkono wake mfukoni, “Basi lala na mimi leo.” Akatoa shilingi alfu kumi na kumwonyeshea Glady. Glady akaangua kicheko kikali. Akakohoa mara kadhaa kabla hajatulia na kumtazama Mustapha kwa macho yake mekundu.



    “Mustapha, yani ulale na mimi kwa shing’ efu kumi!”



    “Ntakupatia zingine bana, Glady. Mbona unakuwa kama hunijui? Unajua kabisa tukipiga ile hela na wewe utapata mgao au umesahau?”



    “Mustapha, mie sio mtoto, sawa?” alisema Glady akiweka pesa yake kwenye mkoba. “Kwanza sasa hivi hakuna cha dili wala nini, ona unavyohangaika hangaika hapa kama digidigi. Pili, hii … hii pesa hii … haiwezi kun’tosha kabisaa! Hii ni pesa niliyolipwa kwa busu tu, upo? … cha kukusaidia, ntakuacha ulale humu, ila haiwezi kun’fanya nikabakia nyumbani.”



    Hata hivyo Mustapha akashukuru, Glady akahepa. Alichukua bodaboda mpaka maeneo ya klabu ya usiku, Maasai, akaanza kufanya doria huko akichangamana na wenzake.





    Baada ya robo saa …





    “Shosti, yule siyo mchina wako uliyeenda naye siku ile?” alisema mwanamke mmoja kandokando ya Glady. Mwanamke huyu alikuwa amevalia topu na sketi fupi. Ilikuwa ngumu kujua rangi ya nguo hizo kwasababu ya ufinyu wa mwanga wa wingi wa taa za rangi rangi zilizokuwa zinakatiza zikienda huku na huko kwa kukimbizana.



    Glady alitazama kule alipoelekezwa, kaunta, akamwona Lee! Mwanga uliokuwepo maeneo hayo ya kaunta uliwawezesha kuona vema.



    “Au nimekosea?”



    “Wala! Ndiye yeye. Acha niende,” akasema Glady akichukua hatua kwa mwendo wake wa madaha.



    Lee alikuwa ameketi na marafiki zake, wakina Nigaa, wakipata kinywaji. Kila mtu alikuwa ameshikilia glasi ama chupa yenye kileo. Walikuwa wanasindikizia vinywaji vyao na soga za hapa na pale pamoja na cheko.



    Mara Lee akasikia mkono begani, kutazama akamwona mwanamke ambaye kwa haraka alimtambua kama malaya. Akampuuzia akimshukuru na kumwambia ahitaji huduma.



    “Ni mimi, unanikumbuka?” Glady alisema kwa sauti ya kubana pua. Hapo ndiyo Lee akatazama na kumgundua sasa Glady. Akamuuliza anataka nini?



    “Naweza nikaongea na wewe kidogo?” Glady alisema kwa unyenyekevu.



    “Glady, sihitaji usumbufu, sawa?”



    “Ni jambo la muhimu, naomba unisikilize.”



    Lee akageuka na kumtazama.



    “Enhe, nini unataka kunambia?”



    Glady akamwambia kumhusu Mustapha na matatizo yake. Yote yakisababishwa na ile nyaraka. Namna Mustapha alivyotaka kuitumia kupata pesa lakini mwisho wa siku ikamdumbukiza matatizoni, anawindwa anyofolewe roho!



    Habari hizo zikamshtua Lee. Hakutegemea kama saga hili la nyaraka lilikuwa linaendelea katika ulimwengu huo ambao alidhani ameuacha. Lakini akajiuliza ni mchina gani huyo aliyepokea nyaraka hiyo na kuanza kumsaka?



    Akamuuliza Glady:



    “Unamjua mchina huyo? Unajua anakaa wapi?”



    “Hapana, sijui lolote lile kumhusu.”



    Lee akamtaka Glady waongozane mpaka kwa Mustapha. Lakini Glady akamuuliza:

    “Sasa ukinitoa hapa, maana yake sitaingiza pesa yoyote. Vipi, utan’lipa?”



    Lee akaukwapua mkono wa mwanamke huyo na kumswaga baada ya kuwatonya wenzake kwa ufupi ya kwamba anatoka.



    “Taratibu basi jamaniii!” alisikika Glady akilalamika.









    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog