Simulizi : Muuaji Asakwe
Sehemu Ya Tano (5)
INGAWA kulikuwa na usumbufu wa foleni ya magari barabarani, Kachero Inspekta Malik hakukawia kufika kwenye Kituo cha Polisi Buguruni. Baada ya kufika, akaingia moja kwa moja katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo, ambaye alikuwa ni mtu mchapakazi na anayeijali kazi yake. Kwa bahati nzuri alimkuta amekaa akiendelea na kazi ya kuyapitia mafaili kadhaa.
“Karibu Malik…” Alfred Gonzo alimkaribisha Kachero Inspekta Malik, ambaye alivuta kiti na kukaa huku wanatazamana.
“Nimefika, afande…” Kachero Inspekta Malik akamwambia mkuu wake wa kazi.
“Karibu…na pole na kazi…”
“Ahsante, afande…”
“Nipe taarifa za kazi Malik…” Alfred Gonzo akamwambia.
“Upelelezi wangu unaendelea vizuri afande. Unajua tokea mauaji yale yalipotokea, nimekuwa nimebanwa sana na upelelezi, hasa ukizingatia kifo chenyewe kilivyotingwa na utata mkubwa…” Kachero Inspekta Malik akaendelea kumwambia mkuu wake.
“Ni kweli, kifo hicho kina utata, kwani inaonyesha watu waliotenda kosa hilo wana kitu kingine zaidi ya hicho. Haiwezekani watu hao wakuwinde na wewe kiasi cha kutaka kukuangamiza, ndiyo maana Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum anataka kujua upelelezi huo umefikia wapi…” Alfre Gonzo akamwambia Malik.
“Kwa vile upelelezi huu nilishauanza, niko mbioni kuukamilisha kuanzia muda wowote ndani ya saa ishirini na nne afande!” Kachero Inspekta Malik akamwambia.
“Una uhakika na unachokisema?”
“Ni kweli afande, kama si usiku wa leo, basi ni kesho!”
“Basi, kama itakuwa ni hivyo, nakutakia heri, lakini kumbuka kila mara tuwasiliane ili niweze kukupatia msaada wa askari itakapobidi. Hivi sasa endelea pake yako kwanza kwa kile tunachokwepa kuweka wapeleleza zaidi ya mmoja, kwani tunaweza kuharibu kazi. Sisi tunasubiri wakati wa ukamataji tu!”
“Sawa afande, nitakujulisha kila hatua zinavyoendelea…” Kachero Inspekta Malik alimweleza mkuu wake juu ya upelelezi wake ulivyokuwa unakwenda tokea alivyouanza, na pia angemtia mbaroni muuaji wakati wowote!
Baada ya kumaliza kumpa taarifa Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, Kachero Inspekta Malik aliaga na kutoka. Wakati huo ilikuwa imetimu saa kumi na moja za jioni, hivyo akaona hakukuwa na haja ya kuelekea nyumbani kwake, Shariff Shamba, Ilala, bali aliamua kuelekea katika miadi yake na mwanadada Helen Fataki, walikopanga kukutana, Sarova Pub, majira ya sa kumi na mbili za jioni.
Kwa vile Pub ile haikuwa mbali sana, Kachero Inspekta Malik hakutumia muda mrefu kufika kwa gari lake, ambalo alilipaki sehemu nzuri iliyojificha ikiwa ni kwa usalama zaidi ukizingatia alishamtibua John Bosho baada ya kumfuata nyumbani kwake Ukonga, jioni ile. Kwa vyovyote alijua kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa John Bosho kumwekea watu wa kumwinda na kummaliza kabla hajawatia mbaroni.
Hivyo basi, kabla ya hajaendelea na safari yake, Malik akaangaza macho pande zote kuangalia kama kuna mtu yeyote anayemfuatilia, na roho yake ilikuwa nzito kwa kutomruhusu kuangalia ndani ya Kimicho Bar, iliyokuwa jirani na sehemu anapokwenda, ambapo alishambuliwa mara ya kwanza. Akaongeza mwendo na kupenya kwenye uchochoro mmoja kwa hadhari, na kutokeza upande wa pili ya mtaa, ambapo ndipo sehemu walipoahidiana kukutana na Helen.
Baada ya kufika pale Sarova Pub, Malik aliangaza macho yake kabla ya kutafuta sehemu ya kukaa. Muda wote alikuwa makini sana kwa kila hatua alizokuwa anakwenda, masikio, pua na hisia zake zilikuwa wazi kwa kunusa hatari yoyote itakayotokea mbele yake! Hata hivyo akiwa mawazoni, akashtuka akishikwa bega lake kwa mkono laini!
“Ni nani? Akajiuliza Malik huku akigeuka nyuma haraka sana kwa kutoa shambulizi kama ni adui. Macho yake yakakutana na mwanadada, Helen Fataki, mwanadada mrembo aliyekuwa anatabasamu!
“Oh, ni wewe Helen?” Kachero Inspekta Malik!
“Ndiyo, ni mimi, Malik…” Helen Fataki akamwambia huku akitabasamu.
“Jihadhari Helen, siku nyingine unaweza ukaumia usipokuwa makini! Usije kwa kunivizia!” Kachero Inspekta Malik akamwambia kimasikhara!
“Kwa hivyo ulikuwa tayari kunimaliza?”
“Ni kitu kama hicho!
“Duh, pole sana…”
Wakasalimiana wakiwa bado wamesimama, na baada ya hapo wakatafuta sehemu ya kukaa kwa ajili ya maongezi yao muhimu. Lakini kwa kujihami, Helen akamwambia:
“Tusikae humu ndani.”
“Kwa nini?” Malik akamuuliza baada ya Helen kumwambia vile!
“Ni kwa ajili ya usalama zaidi!”
“Mbona sikuelewi?”
“Utanielewa tu…”
“Tukae wapi sasa?”
“Nifuate mimi…”
Kachero Inspekta Malik akamfuata Helen Fataki alipokuwa anaelekea. Wakapenya katika vichochoro vingine kadhaa vya eneo lile la Buguruni na kutokeza upande wa pili wa Pub ile. Sehemu ile kulikwa na baa nyingine tena, ambapo wanywaji wengi walikuwa wamekaa katika viti vilivyopangwa nje. Hakika Malik akashangaa kuwa mwanadada yule alikuwa amevifahamu vipi vchochoro vyote vile?
“Hapa ndiyo pazuri…panafaa kwa maongezi yetu bila bughudha zozote!”
“Mh, wewe ni kiboko!” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen Fataki huku akivuta kiti cha plastiki na kukaa, akifuatiwa na Helen.
“Kiboko kivipi?” Helan Fataki akamuuliza.
“Yaani unajua vichochoro vingi kama askari?”
“Ndiyo utambue kuwa mpaka sasa uko na mtu wa shughuli, si mchezo!” Helen akaendelea kumwambia Malik kwa msisitizo!
Baada ya kukaa tu, mhudumu, mwanadada mmoja akawaendea pale walipokuwa wamekaa. Akiwa amejiandaa, Helen akaagiza vinywaji, ambavyo kila mmoja alikuwa anatumia. Ni vinywaji ambavyo walipelekewa wakabaki wakiendelea kunywa taratibu. Sehemu ile waliyokuwa wamekaa, palikuwa na giza kiasi, lilifanya wasiwasi kuonekana kirahisi.
“Hapa sasa tunaweza kuongea mambo yetu!” Helen Fataki akamwambia Malik huku akimimina kinywaji chake kwenye glasi.
“Ni kweli, nimeitikia wito wako, naomba unipe michapo!” Kachero Inspekta Malik akamjibu huku akijiweka vizuri pale kwenye kiti walipokuwa amekaa. Helen Fataki akajiandaa kumwelezea!
********
WAKATI Getruda akiendelea kuwaza juu ya kile alichokuwa ameelezwa na John Bosho, yeye John aliwapigia simu vijana wake wa kazi, Robi, Kessy, Chogolo, Muba na Shabani, wakutane Machimbo ya Mawe, baada ya saa tatu. Alipomaliza kuwataarifu, akaingia chumbani huku hasira zake zinaonekana wazi. Getruda naye akamfuata nyuma na kumkuta akifungua kabati la nguo na kuanza kutoa nguo maalum kwa ajili ya kazi hiyo!
John Bosho akachukua fulana nyepesi iliyobana na suruali nyeusi ya Jeans na koti kubwa jeusi la ngozi. Vingine ni kofia kubwa ya pama, na miwani mieusi, lakini iliyoweza hata kuona hata gizani, na kisu aina ya Okapi. Pia, hakuacha kuchukua bastola kubwa, iliyokuwa na risasi za kutosha. Baada ya kumaliza kufanya maandalizi, akavalia zile nguo na kumfanya abadilike na kuwa mtu wa aina yake! Akatisha hata kumwangalia!
Wakati wote ule Getruda alikuwa akimwangalia John Bosho kwa hofu kubwa iliyokuwa imejengeka moyoni mwake. Na pale ndipo alipouhakikisha unyama wake, kiasi cha kujiona kama nusu mfu. Akajiona kama na yeye angeweza kugeukwa muda wowote, kama alivyofanywa rafiki yake mkubwa, Anita, ikiwa ni baada ya kuijua siri ya kifo chake!
Makubwa!
“Getruda…” John Bosho akamwita kwa sauti ndogo.
“Bee…” Getruda akaitikia huku akimwangalia.
“Mbona umenyemeza kimya? Jiandae tuondoke, alah!” John Bosho akamwambia!
“Mimi niko tayari…” Getruda akamwambia huku akijiangalia.
“Yaani hivyo ulivyo? Chukua hili koti kubwa uvae!” John Bosho akamwambia huku akimrushia koti moja kubwa, ambalo alilitoa ndani ya kabati. Getruda akalichukua na kulivaa!
Baada ya kuwa tayari, John Bosho na Getruda walitoka nje na kupanda lile gari aina ya Toyota Harrier, na safari ya kwenda Chamazi ikaanza huku wote wakiwa kimya ndani ya gari. Kila mmoja akiwa na mawazo yake, na hakuna aliyezungumza na mwenzake hadi walipofika Mbagala, kwa mganga wa jadi, mzee Chiloto Bandua. Hata hivyo ili wasijulikane, John akalipaki gari mbali na nyumba ya mganga yule.
“Tumeshafika!” John Bosho akamwambia Getruda ambaye alikuwa mbali kimawazo!
“Mh, tumeshafika?” Getruda akauliza.
“Ndiyo, tumeshafika…”
“Sasa kinachoendelea?”
“Tushuke tumfuate!”
“Haya…”
John Bosho na Getruda walishuka kutoka garini, na kuiendea nyumba ya mganga huyo kwa mwendo wa wastani kama watu waliokuwa wanapita njia tu. Eneo zima lilikuwa limefunikwa kwa giza kiasi, lililomfurahisha John, kwani angeifanya kazi yake kwa wepesi zaidi na kumtia adabu mzee yule ambaye kwa muda ule alikuwa amehesabia kuwa alikuwa amemtapeli na kula fedha zake.
Baada ya kufika katika himaya yake,walimkuta mzee Chiloto Bandua amekaa nje ya kibaraza cha nyumba yake, kwenye kiti cha uvivu, na hakukuwa na wateja kwa muda ule. Alipowaona wageni wale, akawakaribisha ndani ya chumba cha kuhudumia wateja kilichokuwa upande wa pili wa nyumba yake kubwa. Lakini John alikataa na kumwambia wakutane faragha, kwani kuna maongezi muhimu. Hata hivyo mzee Chiloto alishtuka baada ya kuambiwa vile!
“Kwani vipi?” Mzee Chiloto Bandua akauliza!
“Leo hatukuja kwa tiba…nina shida nyingine!” John Bosho akamwambia.
“Oh!” Getruda akaguna kwa mbali!
“Shida gani usiku huu jamani?” Mzee Chiloto akaendelea kusema huku wasiwasi ukimzidi! Ule ugeni wa John Bosho ulimtia wasiwasi, hasa ukizingatia ile dawa aliyomtengenezea majuzi tu, ilikuwa haifanyi kazi!
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni shida ya kawaida tu mzee, mbona huwa unatibu hata usiku?” John Bosho akaendelea kumwambia.
“Lakini si umesema leo huhitaji matibabu?” Mzee Chiloto Bandua akaendelea kumuuliza!
“Wewe njoo tuongee, usiwe na wasiwasi…” John Bosho akamwambia kwa sauti ya upole iliyomridhisha Mzee Chiloto Bandua. Ndipo waliposogea kando nyuma ya nyumba yake kubwa.
“Haya jamani, ni shida gani?” Mzee Chiloto Bandua akawauliza John na Getruda waliokuwa mithili ya giza, kwa ajili ya zile nguo nyeusi walizokuwa wamevalia!
“Mzee Chiloto!” John Bosho akaanza kumwambia.
“Nakusikiliza bwana mdogo…” Mzee Chiloto akamwambia huku akimwangalia kwa makini sana.
“Mimi nimekuja hapa kwa jambo moja tu!”
“Jambo gani hilo?”
“Mimi nilichojia hapa siyo kingine zaidi ya kutaka kujua kwamba ile dawa uliyonitengenezea ni ya kweli ama la!
“Kwani vipi?”
“Uliniambia kwamba unanitibia ili Polisi wasiweze kunigundua kama ni mimi niliyehusika na mauaji ya mchumba wangu,” John Bosho akamwambia na kuendelea. “Sasa hapa ninapoongea na wewe, ninaandamwa kishenzi!”
“Ina maana wanakufuata?” Mzee Chiloto Bandua akamuuliza kana kwamba hakumwelewa!
“Ndiyo jibu lake!” Akasisitiza John Bosho.
“Au ulivunja masharti?”
“Masharti gani uliyonipa?”
“Mh, makubwa!” Mzee Chiloto Bandua akasema huku akianza kuogopa! Alijua fika kuwa John ni jambazi, na kamwe jambazi hana rafiki!
“Ni makubwa kweli!” Akaongeza John Bosho na kuongeza. “Tena umenichimbisha kaburi la marehemu, kumbe usanii mtupu!”
“Aisee, sasa. Haidhuru, ngoja nakuja…” Mzee Chiloto akasema huku akitaka kuondoka ikiwa nia yake ni kukimbia!
“Unakwenda wapi?” John alimuuliza.
“Nakwenda kujisaidia…oh!”
“Jisaidie hapa hapa…leo mpaka kieleweke!”
“Yamekuwa hayo bwana mdogo?”
“Ndiyo, huendi popote!” John Bosho akamwambia huku akimkamata kwa nguvu ili asiweze kumponyoka!
Halafu John Bosho akampiga ngumi moja ya nguvu, iliyompata kwenye taya lake, ambayo iliyomfanya Mzee Chiloto aanguke chini kwa kishindo! Akanusa ardhi na kusikia harufu yake!
“Ooohps! Mhn!” Mzee Chiloto Bandua akatoa mguno ulioambatana na maumivu!
“Nakuua!” John Bosho akamwambia.
“Usiniue tafadhali!” Mzee Chiloto akasema kwa sauti huku amepiga magoti!
“Sasa kwa nini ulinidanganya?”
“Oh…oh…” Mzee Chiloto Bandua akaendelea kugugumia!
“Lazima niitoe roho yako! Nimeshachukia!” John Bosho akamwambia huku amemwekea bastola kichwani! Mzee Chiloto akaendelea kutweta kwa woga! Kifo si mchezo!
“Nisamehe bwana mdogo…”
“Rudisha fedha zangu!”
“Sina n’nshatumia…oooh!”
“Msamehe …naomba umsamehe John!” Getruda akamwambia.
“Wewe unamwonea huruma sivyo?”
“Msamehe tu…” akasisitiza Getruda huku akimwonea huruma mzee yule.
“Haya, toka hapa!” John Bosho akamwambia Mzee Chiloto bandua huku akimsindikiza kwa teke la nguvu!
Mzee Chiloto akachomoka mbio mithili ya Paka mwizi aliyekurupushwa akidokoa nyama jikoni! Akapotea gizani na kuwaacha John na Getruda wakiumia mbavu!
“Bahati yake, twende zetu Machimbo ya Mawe!” John Bosho akamwambia Getruda huku akiichomeka bastola yake kiunoni.
Wote wawili wakaondoka kwa mwendo wa kawaida kuutoka mji wa mganga Chiloto, kuelekea kule walikoliacha gari lao. Hakuna aliyemsemesha mwenzake!
Ni mtafutano!
********
HELEN Fataki alivuta pumzi ndefu na kuzishusha, punde tu baada ya kupiga funda moja la pombe yake na kuiweka glasi chini. Halafu akamwangalia Kachero Inspekta Malik takriban dakika moja hivi, kwani alikuwa ameamua kumtolea ukweli ili kurahisisha kazi yake ya upelelezi iliyokuwa inamkabili.
“Kwanza kabisa napenda kukujulisha kwamba sakata lote unalolifuatilia, mimi nalifahamu fika!” Helen Fataki akamwambia Malik!
“Ina maana hata mimi ulikuwa unanifahamu sivyo?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza huku akimwangalia kwa makini.
“Ndiyo. Mimi nakufahamu, na ndiyo maana nikakufuatilia ili nikusaidie juu ya huyo mtu hatari, John Bosho, na juu ya kifo cha mwanadada Anita. Narudia kusema kwamba ndiyo maana jana nikakufuata nikiwa na nia ya kukupa msaada. Hivyo basi, mpaka sasa elewa hilo!”
“Aisee, basi naomba unipashe vizuri…” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen. Akaona ni mtu aliyempunguzia kazi! Ukweli hakutegemea kitu kama hicho!
“Kwanza kabisa, mimi nimefahamiana na John Bosho kwa muda mrefu sana, kwa upande wa mambo ya kibiashara. Lakini baada ya kugundua vitendo vyake viovu, ndipo nikaamua kuachana naye, ili asije akanipakazia…” Helen Fataki akamwambia, lakini hakugusia kuwa waliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi!
“Mlikuwa mnafanya biashara gani?”
“Ni biashara nyingi, lakini nyingine zilikuwa za haramu, ambazo nimeshaziacha…”
“Hizo achana nazo…hebu tuendelee…” Kachero Inspekta Malik akamwambia huku akimsikiliza kwa makini.
“Basi, yeye John Bosho alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu Anita kwa muda mrefu, kiasi ambacho waliamua kuwa wachumba na kupanga kuoana. Lakini baadaye John akavutiwa na rafiki yake, Anita, aitwaye Getruda. Akatembea naye na kumfanya mpenzi wake. Mwishowe Anita akagundua na kuamua kuuvunja uhusiano kabisa, kiasi cha kuwa maadui kama Paka na Panya…” Helen akanyamaza kidogo huku akimwangalia Malik.
“Aisee, mbona habari hii inasisimua?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza Helen.
“Basi, kwa vile Anita alikuwa ameshazijua siri za John Bosho, kama ni jambazi, ndipo akaamua kumuua kwa stahili ya aina yake ya kumdunga sindano ya sumu ya nyongo ya Mamba, baada ya kumvizia bafuni wakati anaoga. Kwa hivyo tambua mpaka sasa muuaji ni John Bosho!”
“Mungu wangu!” Kachero Inspekta Malik akasema na kuendelea. “Sasa wewe ndiyo umenipa picha kamili. Yeye ndiye muuaji, na pia waliofukua lile kaburi na kuitoa maiti ya Anita. Lakini sidhani kama yuko peke yake!”
“Hayuko peke yake…” Helen akasema na kuendelea. “John Bosho anamiliki Kikosi cha Uhalifu akiwa na vijana wake kadhaa, ambao huwatuma kufanya uhalifu katika sehemu mbalimbali hapa nchini!”
“Unasema kweli?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni kweli, ni vijana hatari ambao wameshatenda maovu mengi sana, na pia wana maficho yao ya siri yaliyoko kule Ubungo Machimbo ya Mawe, ambapo wana bohari kubwa wanalolitumia kama sehemu yao ya kutendea uhalifu…” Helen akaendelea kumwambia na kubaki akimwangalia.
“Hata hivyo,” Helen akaendelea kusema. “Kuna habari njema kwamba usiku wa leo wamepanga kwenda kukutana kwa kikao cha faragha. Kwa hivyo mimi nimejitolea kukusaidia ikiwezekana kukupeleka kuwachunguza. Au unasemaje?”
“Kama umeamua kunisaidia hakuna tatizo, mimi niko tayari. Baada ya kunipeleka huko, nitawasiliana na uongozi wa juu na taratibu za kuwakamata zitafuata mara moja!” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen.
“Naapa kukusaidia…ondoa shaka!” Helen akamwambia.
“Basi, nashukuru, na pia utakuwa umelisaidia Jeshi la Polisi ukiwa kama Raia mwema!”
“Ni jukumu letu sote, na kama wote tungefanya hivyo, hakika uhalifu ungepungua kama siyo kumalizika kabisa!”
“Ni kuupunguza tu, lakini uhalifu hauwezi kwisha…”
Wakati Kachero Inspekta Malik akiongea na Helen Fataki, mara wakaingia vijana wawili waliokuwa wameongozana. Vijana hao walikuwa na maumbile yaliyoshupaa na kuonyesha walikuwa ni watu wa mazoezi, na baada ya kuingia, wakatafuta sehemu ya kukaa, ambayo ilikuwa mbali kidogo na sehemu ile waliyokuwa wamekaa wao.
Mhudumu mmoja wa kike ambaye alionyesha kuwa anawafahamu, alipowaona akawaendea pale walipokuwa wamekaa. Wakamuagiza vinywaji na kuendelea kunywa taratibu. Hata hivyo, Malik hakuwafahamu wala kuwatilia mashaka.
“Umewaona wale vijana?” Helen Fataki akamwambia Kachero Inspekta Malik.
“Si wale waliokaa kule mwisho?” Akauliza Malik.
“Ndiyo wenyewe…” Helen akasema
“Nimewaona…” Kachero Inspekta Malik akamwambia huku akiendelea kuwaangalia ingawa hakuweza kuwaona vizuri kutokana na sehemu ile kuwa na giza.
“Basi, wale ni vijana wa John Bosho, ambao wanaojulikana kwa majina ya Robi na Kessy. Bila shaka wanakwenda kwenye maficho yao kama walivyopanga na bosi wao. Hapa bila wanapata vinywaji tu!” Helen Fataki akamwambia Malik
“Kama wanakwenda kwenye maficho yao, basi tutawafuatilia!” Kachero Inspekta Malik akasema na kuendelea. “Na itakuwa wananisaidia sana kuyafahamu maficho yao! Tutawafuatilia!”
“Hakuna shaka…leo kazi moja tu!”
“Mpaka kieleweke!”
Kachero Inspekta Malik akaendelea kujipa moyo!
********
NI kweli kwamba baada ya vijana, Robi na Kessy kuingia katika eneo lile la baa, hawakuwaona Kachero Inspekta Malik, wala Helen Fataki katika sehemu ile walipokuwa wamekaa, hasa ukizingatia palikuwa na giza kiasi, lililosababishwa na taa yenye mwanga wa kijani iliyokuwa inawaka. Walikuwa wameamua kupitia pale wakiwa safarini kuelekea Machimbo ya Mawe, baada ya kutaarifiwa na bosi wao, John Bosho.
John Bosho aliwajulisha wakati ule alipokuwa anakwenda nyumbani kwa mganga wa jadi, mzee Chiloto, akiongozana na Getruda. Hivyo basi, vijana hao walielekea kule machimboni kiawamu, kwani hawakupenda kuongozana wote kwa kuhofia kujiingiza kwenye mtego wa Jeshi la Polisi, hasa ukizingatia hali ilikuwa imeshachafuka!
Ndipo, Robi na Kessy walipoamua kupitia kwanza katika baa ile, ili kupooza makoo yao. Kwa vile walikuwa bado vijana wabichi na wanaohusudu sana ulevi na wanawake, vijana hao walijihusisha sana na wale wahudumu muda wote waliokuwa pale, na pia kunywa pombe kwa pupa!
Kwa upande wa Kachero Inspekta Malik na Helen Fataki, walikuwa wakifuatilia nyendo za vijana wale, ambapo nao waliendelea kunywa huku mara nyingi wakiwasiliana kwa simu, kudhihirisha kuwa walikuwa na mipango mikubwa iliyokuwa inawakabili. Tuseme kwamba walikuwa hawatulii vitini, mara nyingi walikuwa wakinyanyuka na kuongea kwa simu, kudhihirisha kwamba hawakutaka mtu yeyote asikie yale mazungumzo yao.
Baada ya kutimu saa nne za usiku, wote walikuwa wameshapata nishai ya kutosha, hivyo wakanyanyuka vitini na kuamua kuondoka wakiwa wameongozana. Robin na Kessy wakaelekea kwenye gari lao aina ya Toyota Mark 11 Grande, waliyofika nayo pale, ambalo lilikuwa katikati ya magari mengine.
Baada ya kupanda wakaondoka kuelekea Machimbo ya Mawe, dereva akiwa ni Robi, na Kessy akiwa amekaa upande wa kushoto. Wakaifuata Barabara ya Nelson Mandela kwa mwendo wa wastani, kama vile watu wasiokuwa na haraka yoyote, wakiwa wanaongea mambo yao huku muziki mororo ukitumbuiza ndani ya gari na kutakasa nafsi yao usiku ule.
Tena, vijana hao walikuwa wakivuta sigara kwa pupa na kupuliza moshi ovyo. Kwa ujumla pale walipokuwa walikuwa wamekamilika ipasavyo, wakiwa wamechimbia bastola zao sehemu fulani, kiasi cha kuwafanya wajiamini kupita kiasi. Hawakutishika na chochote!
Mara simu ya mkononi ya Robi ikaita. Kwa haraka akaichukua kutoka katika mfuko wa kushoto na kuipachika sikioni.
Mkono mwingine wa kushoto Robi akawa anaendesha gari. Kessy naye akawa anamkodolea macho Robi, ili kujua kwamba ile simu ilikuwa inatoka kwa nani! Simu ilikuwa imetoka kwa bosi wao, John Bosho!
Na wakati huo ndiyo alikuwa anatokea Chamazi, kwa Mganga, mzee Chiloto!
“Bosi…Robi naongea…” Robi akaipokea.
“Mko wapi saa hizi?” John Bosho akauliza kwa sauti iliyojaa hasira!
“Ndiyo tunaelekea Machimbo ya Mawe bosi…”
“Mko wangapi?”
“Niko mimi na Kessy!”
“Je, wengine…Chogolo, Muba na Shabani…”
“Wameshatangulia bosi.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ok, na mimi nakuja huko.”
“Sawa bosi…”
Wakakata simu baada ya mawasiliano.
“Ni nani? Au bosi?” Robi akamuuliza.
“Ndiyo…ni bosi. Salamu hizo mwanangu!”
“Anasemaje?”
“Anataka kujua tuko wapi! Na yeye yuko njiani anakuja!”
“Mh, basi leo kuna kazi…najua bosi atakuwa amechukia sana. Lakini ni kwanini alimwua Anita, kiasi cha kuleta usumbufu wote huu?”
“Ah, hata mimi sielewi. Yote ni mipango yake mwenyewe! We’ twende huko huko tukamsikilize!”
Robi akaendelea kuendesha gari, ambapo usiku ule magari yalikuwa machache sana barabarani kiasi cha kuwafanya wasipoteane!
********
WALIENDELEA kuwaungia mkia. Kachero Inspekta Malik na Helen Fataki waliendelea kuwafuatilia nyuma watu wale pasipo wao kugundua, hadi walipofika eneo la Tabata na kuendelea na safari mpaka Ubungo Riverside. Hapo Robi alipinda kulia na kuifuata barabara moja ya udongo, iliyokuwa inaelekea katika makazi ya watu eneo lile la Ubungo.
Ni eneo ambalo ndiyo kwanza nyumba mpya zilikuwa zinajengwa katika viwanja vilivyopimwa, na chache zikiwa zimeshakamilika na kuhamiwa. Basi, wakaifuata barabara hiyo, huku wakipanda na kushuka milima, hadi walipofika katika sehemu ya tambarare. Sehemu hiyo pia palikuwa na nyumba mpya zilizojengwa kwa mpangilio maalum.
Ili wasishtuke kama walikuwa wanafuatiliwa, Malik akazima taa zote za gari na kuendesha kwa uzoefu. Hatimaye wakafika katika eneo lililokuwa na nyumba chache, na miti mingi ya mikorosho. Ni eneo linaloitwa Machimbo ya Mawe, ambapo kipindi cha nyuma palikuwa panachimbwa mawe ya ujenzi, na kampuni moja ya ujenzi.
Vilevile palikuwa pamejengwa mabohari kadhaa ya kuhifadhia bidhaa, na mengine ni kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi, makatapila,vidampa vya kubebea mchanga, malori na mitambo mingine inayohusiana na shughuli za ujenzi kwa ujumla. Kwa mbele kama umbali wa mita hamsini hivi, palikuwa na uzio mkubwa wa seng’enge na waya, uliozunguka eneo lote ili kudhibiti watu wenye nia mbaya kuweza kuingia.
Kwa ndani ya uzio palikuwa na jengo kubwa lililiojengwa mjengo wa bohari, likiwa limezungukwa na miti kiasi cha kufanya lijifiche na kutawaliwa na giza kwa upande wa nje. Lakini kwa ndani palikuwa na taa chache zilizokuwa zinawaka kuzunguka hilo bohari, ambazo zilikuwa na mwanga hafifu usiofika mbali.
Gari walilokuwemo Robin na mwenzake, Kessy lilisimamishwa nje ya geti kubwaa la chuma, ambapo upande wa juu hapo nje, palikuwa na kibao kikubwa cha mbao, kilichoandikwa maandishi makubwa yaliyosomeka: ‘J.B.ENTERPISES LTD.’ Ni maandishi yaliyokuwa yanamulikwa na taa yenye mwanga mkali kiasi cha kufanya yasomeke kwa uwazi. Honi ikapigwa mara tatu hivi, halafu akatokea mlinzi mmoja aliyekuwa amevalia koti refu jeusi, na kifuani mwake amebeba bunduki aina ya Automatic Rifle.
Kabla ya kuwafungulia lile geti, mlinzi huyo akatoka hadi nje na kuwakagua kama walikuwa ni watu wao, au ni watu wengine wasiohusika. Baada ya kuhakikisha ni watu wao, akalifungua geti na wao wakaingia ndani na geti likafungwa kama mwanzo. Kama walivyokuwa wametaarifiwa mwanzo na John Bosho, vijana wote walikuwa wameshafika ndani ya lile bohari, wakimsubiri bosi wao, kwani wa mwisho kufika walikuwa ni Robi na Kessy.
Basi, vijana wote wakaingia ndani ya chumba maalum kilichokuwa ndani ya bohari lile, kumsubiri bosi wao kama alivyowaahidi wakutane. Wote wakajiandaa kupokea ujumbe mzito! Na siyo mwingine zaidi ya mapambano!
“Unaona pale waliposimamisha gari?” Helen Fataki akamwambia Kachero Inspekta Malik
“Ndiyo, naona…” Malik akasema.
“Ndipo penye bohari lenyewe, sasa tusubiri mpaka waingie na sisi tupitilize…”
“Sawa,” Kachero Inspekta Malik akasema huku akilisimamisha gari.
Baada ya lile gari walilokuwemo Robi na Kessy kuingia ndani ya uzio wa bohari, Kachero Inspekta Malik na Helen Fataki, waliokuwa ndani ya gari wakiwafuatilia vijana hao, wakapitiliza moja kwa moja ili wasije wakashtukiwa, ambapo Malik akasimamisha mbele kidogo, sehemu ambayo ilikuwa siyo rahisi kuonekana, kwani palikuwa na vichaka na miti midogo midogo iliyokuwa na kiza.
Wote wakashuka na kuanza kurudi walipotokea kwa miguu taratibu na kwa tahadhari ya hali ya juu, huku mkononi mwake, Malik amekamata bastola yake imara, na redio ya mawasiliano (Radio Call) ameipachika kiunoni katika mkanda wa suruali, na pia simu yake ikawa katika mfuko wa shati.Wakati wote huo, Helen alikuwa akimwelekeza jinsi yale maficho yao yalivyokuwa, ukizingatia yeye aliyafahamu yalivyo.
Baada ya kutembea kwa muda, wote wawili wakaamua kujificha kwenye kichaka kidogo kilichokuwa kando ya barabara, chini ya mti wa mkorosho. Ni sehemu ambayo haikuwa mbali sana na bohari lile walilokuwa wanaliendea, ni umbali wa mita mia hamsini hivi. Malik na Helen aliamua kujificha pale kwa sababu waliona mwanga wa taa za gari ukiwamulika kuelekea sehemu waliyokuwa wanaelekea.
Wakabanisha pale hadi gari lile lilipowapita kwa mwendo wa wastani, ambapo lilikuwa ni gari aina ya Toyota Harrier ya rangi ya fedha, ambayo ndani yake palikuwa na watu wawili, John Bosho na Getruda, na baada ya gari lile kuwapita, likaelekea moja kwa moja usawa wa geti la kuingilia mle ndani ya bohari.
Mlinzi yule wa mwanzo aliyekuwa pale getini karibu na kibanda cha ulinzi, akaenda kulifungua geti na kuliruhusu gari hilo kuingia ndani. Baada ya kuingia, gari hilo likaenda kupaki sehemu maalum ya kupaki magari iliyokuwa upande wa mbele ya bohari, na pia yalikuwepo magari mengine machache yanayowahusu wao waliokuwa wamefika kwa ajili ya kikao hicho. John Bosho na Getruda wakashuka kutoka ndani ya gari na kuingia ndani ya bohari lile kwa mwendo wa haraka!
*********
WAKIWA bado wamebanisha kichakani, Kachero Inspekta Malik na Helen Fataki, waliweza kuona jinsi gari lilivyoingia mle ndani, na kisha yule mlinzi alivyofunga geti kama mwanzo, halafu akarudi katika kibanda chake kilichokuwa karibu na geti, wala hakujua kama umbali wa mita chache tu, kulikuwa na watu waliokuwa na kiu ya kuwaingilia mle ndani!
“Umewaona?” Kachero Inspekta Malik akamuuliza Helen.
“Ndiyo, imewaona,” Helen akasema na kuongeza. “Ni kama nilivyokwambia kuwa leo ni siku ya funga kazi, kwani wote wanakutana mle ndani kwa kikao maalum. Hivyo ni wakati muafaka wa kuwakamata!”
“Vizuri sana,” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen na kuendelea. “Sasa wewe nisubiri hapo, mimi nakwenda katika eneo lile kuchunguza zaidi. Halafu nitawasiliana na Kikosi Maalum cha Polisi!”
“Haya, mimi nakusubiri hapa…nakutakia kazi njema!” Helen Fataki akamwambia Malik huku akimpiga busu shavuni!
Kwa bahati nzuri siku ile Kachero Inspekta Malik alikuwa amevalia nguo za rangi nyeusi zilizoshabihiana na lile giza. Baada ya kutoka pale, akaikamata bastola yake vizuri kwa mkono wake wa kulia na kuanza kunyata ili miguu yake isiweze kutoa sauti na kuwafanya watu washtuke kwamba kulikuwa na adui. Hatimaye akaufikia ule uzio wa waya uliozunguka eneo zima la bohari.
Akiwa amechuchumaa chini, Kachero Inspekta Malik akauinua uso wake na kuchungulia mle ndani takriban dakika tatu hivi, lakini hakuweza kuona chochote zaidi ya giza la ukimya. Kwa kutumia nguvu, akaunyanyua ule waya uliotumika kama uzio kwa juu, kiasi kwamba aliweza kupata mwanya wa kuweza kuingia ndani ya uzio ule kwa kupenyeza kiwiliwili chake kizima.
Hatimaye baada ya kufanikiwa kuingia ndani ya uzio, akaanza kutembea kwa tahadhari kubwa kuelekea usawa wa jengo lile kwa upande wa nyuma, ambao ulikuwa na miti mingi. Kila alivyokuwa anatembea, Malik alikuwa akisikia sauti za watu, zikionyesha wazi kwamba zilikuwa zinatokea sehemu aliyokuwepo yeye. Hivyo akaruka na kujificha nyuma ya tanki moja la kuhifadhia maji, lililokuwa karibu na kufanya wasiweze kumwona.
Hata hivyo baada ya kusimama kwa muda, sauti zile zikatoweka na akapata fursa ya kuliendea lile jengo la bohari ambalo halikuwa mbali sana, na pia akijikinga na vivuli vya miti ile iliyozunguka eneo lote. Hatua kadhaa kabla ya kulifikia hilo jengo, Malik akasikia vishindo kikikimbilia sehemu hiuyo aliyokuwa amesimama yeye! Ni kitu gani tena?
Hamad! Malik akawaona mbwa wawili wakubwa mithili ya beberu, wakimwendea kimya kimya bila kubweka, kitu ambacho alikuwa hajakitegemea. Ni Mbwa ambao walikuwa wamepata mafunzo maalum ya kushambulia bila kupiga kelele, basi, akagundua kuwa hawakuweka ulinzi upande wa nyuma! Hata hivyo hakupaniki, akasimama tayari kwa kuwakabili, kwani alijua kama angekimbia tu, wangemshambulia kwa nyuma! Mbwa hao nao wakasimama wakimsubiri akimbie tu, wamrukie na kumng’ata!
Kwa vile bastola yake ilikuwa na kiwambo cha kuzuia mvumo, akakaza mkono na kufyetua risasi mbili kuelekea walipo Mbwa wale, ambao kwa pamoja waliruka juu na kisha kutua chini kwa kishindo wakiwa maiti. Kitendo kile kilikuwa cha haraka sana, na pia hakuzubaa, akajiondoa huku akikimbia kidogo kuelekea upande wa nyuma wa bohari,ambalo lilikuwa limejengwa kama mabohari mengine ya kawaida tu, lakini upande wa kushoto palikuwa na vyumba vilivyotumika kama ofisi, pamoja na ukumbi mdogo wa mikutano.
Ni chumba ambacho Kachero Inspekta Malik alihisi walikuwepo wale watu waliokuwa wanaongea. Kwa bahati nzuri sehemu ile aliyobanisha ukutani, palikuwa na dirisha kubwa lililokuwa na vioo. Akajiinua kidogo na kuchungulia kule ndani! Baada ya kuchungulia, aliweza kuona vizuri watu wote waliokuwa mle ndani, ambao ni John Bosho mwenyewe, aliyekuwa amekaa mbele yao pamoja na Getruda.
Halafu walifuata vijana wale, Robi, Kessy, Shabani, Muba na Chogo. Wote walikuwa wamekaa kwenye viti wakionyesha kuwa na kikao maalum cha siri baada ya mipango yao kuharibika! Hivyo Malik akawa anawasikiliza jinsi walivyokuwa wanapanga mikakati yao. Ndani ya chumba hicho, John Bosho alikohoa kidogo ili kusafisha koo lake, halafu akawatizama vijana wake huku amekunja sura kwa hasira alizokuwa nazo, ambao wote waliweza kuzitambua kwa jinsi walivyomzoea bosi wao. Hasa mipango aliyopanga inakwenda mrama!
“Tumekutana hapa tena usiku huu!” John Bosho akawaambia.
“Ndiyo bosi…” wakasema.
“Ni matumaini yangu kuwa nyote hamjambo!” John Bosho akaendelea kuwaambia!
“Sisi hatujambo bosi!” Wote wakasema!
“Jamani…nimeona niwaite huku kwa ajili ya kikao hiki cha dharura usiku huu,” John Bosho akasema ba kuendelea. “Kwa upande wangu naona mambo siyo mazuri, yanazidi kuwa mabaya mara baada ya kumuua mchumba wangu,!”
Wakaendelea kumsikiliza!
“Na hata kama ningemwacha hai Anita, asingesita kunichoma kwa Polisi kuwa alikuwa anaishi na Mchumba Jambazi! Cha msingi ninachotaka kuongelea ni kuhusu huyu mtu wa pili, Kachero wa Polisi, Inspekta Malik. Ananifuatilia kwa kasi sana, kiasi kwamba ameshapafahamu hata nyumbani kwangu, Ukonga, na mbaya zaidi ameshajua kuwa mimi ndiye muuaji wa mchumba wangu!”
“Mh, ni hatari!” Robi akasema
“Aisee?” Kessy akaongeza kusema!
“Basi, jioni ya leo amekuja nyumbani, Ukonga, na kuanza kunihoji maswali mengi, ambayo kwa kiasi fulani yaliniingiza mtegoni!”
“Mh!” Robi akaguna!
“Mungu wangu!” Kessy akadakia!
“Aisee?” Muba naye akasema kwa kuonyesha mshangao!”
“Tumejaribu kwa hali na mali kummaliza, lakini tumeshindwa, ikiwa ni kumtilia ile sumu kali ya nyongo ya Mamba kwenye kinywaji, lakini akafanikiwa kukwepa! Ina maana tumemshindwa mtu huyo mmoja kiasi cha kuweza kutuchanganya namba hii? Eti jamani!”
Baada ya kutoa maelezo yale, John Bosho akabaki anawaangalia huku kando yake akiwepo Getruda, aliyekuwa akijiona kama mtu aliyekuwa ndotoni. Hakutegemea kwa usiku ule kuwa katikati ya kundi la majambazi, waliokuwa wanajadili kutoa uhai wa binadamu! Na vijana, Robi, Kessy, Muba, Shabani na Chogo, wakawa wanaangaliana kwa zamu. Kwa ujumla walikuwa wamemwelewa!
“Bosi, tumekusikia vizuri…” Robi, kijana anayejiamini akasema na kuongeza. “Sisi hatujashindwa kazi!”
“Hamjashindwa? Sasa mnanipa ushsuri gani?”
“Cha muhimu ni kumsaka tena!” Robi akaongeza kwa msisitizo!
“Ni kweli bosi, tumsake tena!” Chogo naye akaunga mkono.
“Bosi, huyo Malik ni mtu mdogo sana. Tutamsaka usiku wa leo na kummaliza. Kesho asubuhi atahesabika ni marehemu. Na hata ikiwezekana tumchomee ndani ya nyumba yake baada ya kuimwagia mafuta ya Petroli!” Shabani akachangia!
“Vizuri sana…naona mna moyo. Nashukuru sana kwa kuniunga mkono katika wakatui huu mgumu. Kama mko tayari, nawasihi tuingie kazini mara moja na kuhakikisha tunamsaka mtu huyo katika sehemu yoyote atakayokuwa, labda awe mbinguni, ambapo tuna uhakika hatuwezi kufika!”
“Sawa, bosi!” Robi akasema.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hakuna shaka!” Akamaliza Muba!
“Ok, poteeni!”
********
MAMBO yalikuwa magumu kwa upande wa Kachero Inspekta Malik, ambaye alikuwa ameamua kujitosa na kuingia ndani ya ngome ya maadui, ikiwa ni baada ya kuyasikia yale mazungumzo waliyokuwa wanaongea, ambayo yalimtisha. Ni pale ilipotolewa adhabu ya kifo dhidi yake, ambayo ilitakiwa ikamilike baada ya saa ishirini na nne.
Hivyo basi, Kachero Inspekta Malik hakuendelea kukaa pale kando ya dirisha lile alilokuwa amejibanza, bali alijiondoa kwa mwendo wa haraka huku akijikwepesha kwenye vivuli vya miti, na kufanikiwa kutoka nje ya uzio ule kama alivyoingia. Baada ya kutoka, akatembea huku ameinama hadi alipofika katika kichaka kingine na kubanisha ndani yake.
Hakika ilikuwa ni sehemu nzuri ambayo siyo rahisi kuonekana na adui. Akiwa ndani ya kichaka hicho, Malik akatoa simu yake ya mkononi na kumpigia Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, ili amweleze hali halisi ilivyo.
“Nakupata Inspekta Malik…nipe taarifa…” upande wa pili Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo akasema.
“Napenda kukujulisha kuwa bado niko kazini…”
“Uko wapi muda huu?”
“Niko hapa Ubungo Machimbo ya Mawe…”
“Nipe taarifa za hapo, je, kuna mafanikio?”
“Ndiyo afande, nimeigundua ngome ya wahusika tunaowatafuta. Hivi sasa wako ndani ya bohari wakipanga mipango yao, hivyo ni wakati muafaka wa kuwavamia na kuwatia mbaroni…”
“Kazi nzuri sana…hebu nipe ramani ya kufika hapo!”
“Fuata Barabara ya Nelson Mandele mpaka Ubungo Riverside. Halafu unapinda kushoto kuifuata barabara ya udongo moja kwa moja hadi kwenye mabohari ya kampuni ya ujenzi ya zamani….ni hapo…”
“Sawa, basi subiri hapo hapo…tunaandaa Kikosi Maalum cha askari, na tunakuja muda huu!”
“Sawa, afande…nawasubiri…”
Baada ya kumaliza kuwasiliana na Mkuu wa Upelelezi, Kachero Inspekta Malik akajiondoa ndani ya kichaka kile, na kuelekea pale alipokuwa amejificha mwanadada Helen Fataki. Akamkuta akiwa amejikunja na kujikunyata akipambana na mbu wengi waliokuwa wakisherehekea damu yake, ikiwa ni tafrija isiyo rasmi!
“Helen…” Kachero Inspekta Malik akamwita.
“Bee…” Helen Fataki akaitikia.
“Nimefanikiwa kufika eneo lile na kuwasikiliza mazungumzo yao waliyokuwa wanaongea, ambapo wana mkakati wa kunisaka mimi usiku wa leo na kuhakikisha kuwa wananimaliza kwa kunichomea ndani ya nyumba yangu. Hivyo nimewajulisha polisi ambao wako njiani wanakuja, hivyo basi, wewe nenda ndani ya gari ukanisubiri, kazi hiyo tuachie sisi polisi wenyewe!” Malik akamwambia Helen Fataki.
“Hakuna wasiwasi…utanikuta baada ya kazi!” Helen Fataki Fataki akasema huku akiondoka kwa mwendo wa kuinama na kunyata hadi lilipokuwa lile gari. Akaufungua mlango wa nyuma na kuingia, kisha akajilaza kwenye kiti. Kwa kiasi fulani akajisikia raha ilioje kwa kulisaidia Jeshi la Polisi akiwa raia mwema!
Kachero Inspekta Malik naye akajiondoa eneo lile kwa hatua za haraka, na kuelekea mwanzoni mwa barabara inayoelekea sehemu ile yenye mabohari, ili aweze kuwapa maelekezo Mkuu wa Upelelezi na wale askari polisi aliokuwa wanaelekea pale kutoa msaada. Baada ya kufika akabanisha kwenye kona iliyokuwa na miti ya mikorosho iliyofungamana na kufanya kuwe giza.
Baada ya dakika ishirini hivi, magari mawili, moja aina ya Land Rover 110 Deffender, na jingine Toyota Land Cruiser, yaliwasili eneo lile la Ubungo Machimbo ya Mawe, akiwemo Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo, pamoja na timu ya askari polisi maalum waliokuwa na silaha, bunduki aina ya Sub Machine Gun zilizosheheni risasi.
Askari polisi wale walishuka harakaharaka tayari kukabiliana na majambazi wale, huku wakiwa na kiongozi wao, Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo, ambaye naye alishuka haraka akiwa na bastola yake mkononi. Hakika walikuwa wamejiandaa vya kutosha, na hawakutaka kufanya makosa ya aina yoyote na kuwapoteza majambazi yale hatari. Baada ya kushuka tu, akampa maelekezo Malik kuwapanga askari wale, kila mmoja akae katika sehemu yake ili kulizunguka bohari pande zote!
*********
JOHN Bosho na vijana wake bado walikuwa mle ndani ya bohari, wakimalizia kupanga mikakati yao bila kujua kwamba wamezingirwa na Kikosi Maalum cha Askari wa Jeshi la Polisi, waliokuwa na kiu kubwa ya kuwakamata. Kwa ujumla eneo lote lilikuwa kimya kabisa ukizingatia nyumba za wenyeji zilikuwa mbali kidogo na sehemu hiyo iliyokuwa maalum kwa ajili ya mabohari tu.
Hata hivyo yule mlinzi aliyejulikana kwa jina la Boaz, aliyekuwa pale getini tokea mwanzo, alishtuka baada ya kusikia michakacho ya miguu alipokuwa ndani ya kibanda chake. Akatoka nje na kuanza kuchunguza kwa makini na kuhisi hali ya hatari baada ya kuona vivuli vya askari wale waliokuwa wanajipanga kulizunguka bohari taratibu na kwa mpangilio maalum.
Mlinzi huyo akatupa macho yake pande zote, kisha akachomoka mbio kwa kutoka ndani ya kibanda chake, halafu akakimbilia ndani ya chumba cha mikutano huku ameinama wasiweze kumwona. Baada ya kuingia ndani ya chumba kile cha mikutano, akawakuta John Bosho na vijana wake ndiyo kwanza wanataka kutoka nje kwenda kutekeleza kazi yao!
“Wewe vipi?” John Bosho akamuuliza mlinzi yule baada ya kumwona akitweta!
“Hatari bosi!” Mlinzi huyo akasema huku akiendelea kuhema kwa nguvu!
“Hatari ya nini?” John Bosho akamuuliza.
“Tumevamiwa bosi!”
“Tumevamiwa na nani?”
“Nahisi watakuwa ni polisi…”
“Una uhakika na unachokisema?” John Bosho akamuuliza huku wasiwasi ukianza kumwingia! Akasimama!
“Ndiyo…nimewaona!”
“Oh, kazi ipo! Jamani jiandaeni kwa vita!” John Bosho akawaambia watu wake!
“Ni sawa bosi!” Robi akasema huku akijiandaa kuchukua silaha yake.
“Kumekucha!” Kessy akadakia naye akijiandaa.
“Oh, Mungu wangu!” Getruda akasema huku mikono yake ameiweka kichwani!
“Getu…usijali sana. Tupo pamoja na wala hakuna mtu yeyote wa kukutia hata kidole cha macho! Nitapambana nao!” John Bosho akamwambia huku akimshika mkono.
“Ni hatari jamani! Oh!” Getruda akaendelea kusema kwa hofu kubwa!
Vijana wote wakachukua silaha zao na kila mmoja akaruka kuchukua nafasi yake, tayari kukabiliana na askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa wameshajiandaa kule nje ya bohari!
Ni kizaazaa!
*********
UPANDE wa nje wa bohari lile, walikuwepo, Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, na Kachero Inspekta Malik, ambao walikuwa wanawaangalia askari walivyokuwa wanajipanga kulizunguka bohari zima na kuiacha sehemu ile ya getini tu. Gonzo akamwambia Malik atoe amri ya kujisalimisha kwa majambazi yale yaliyokuwa yamejichimbia ndani!
Kachero Inspekta Malik ambaye alikuwa ameshika bastola yake mkononi, akachomoa kile kiwambo cha kuzuia sauti, halafu akafyetua risasi mbili angani na kupasua ule ukimya uliokuwa umetawala eneo lile katika usiku ule! Kisha akatoa amri kali!
“Wote mlioko ndani ya bohari, mko chini ya ulinzi! Jisalimisheni na mtoke huku mikono ikiwa juu!”
Ukatawala ukimya!
Hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kujisalimisha ndani ya bohari lile! Ilikuwa ni wakati huo vijana wa John Bosho walipokuwa wanachukua nafasi za kujificha. John Bosho na Getruda wakabanisha pembeni kabisa kwenye upenyo wa makabati yaliyokuwa mle ndani, wakati huo John akiwa amekamata bastola yake imara mkononi! Getruda alikuwa akitetemeka ovyo!
“Usihofu Getruda…” John Bosho akaendelea kumpa moyo!
“Oh, John umeniponza…” Getruda akamwambia.
“Poa…usijali wala usiwe na wasiwasi…” John Bosho akaendelea kusema huku akiangaza macho yake pande zote.
“Nisijali wakati nje kuna polisi?”
“Polisi hawatuwezi!”
“Hapana…jisalimishe…”
“Usiwe mwoga…yaani kirahisi namna hiyo?”
“Sasa tufanyeje?”
“Tutapambana nao!”?
“Oh, Mungu wangu!”
“Hakuna jinsi Getruda…” John Bosho akaendelea kusema huku uso wake kaukunja!
Milio mingine ya risasi ikasikika kule nje!
Askari polisi wakafyetua risasi kuelekea ndani ya bohari lile kiasi cha kutoboa mabati juu.Vijana wa John Bosho wakazidi kuchanganyikiwa na kujiweka tayari kwa mapambano ya kuokoa roho zao! Hata hivyo hawakupenda kushindwa kirahisi, kwani nao wakaanza kufyetua risasi kuelekea nje walipokuwa wamesimama wale askari polisi, ambao nao hawakukawia kujibu mapigo kwa kuanza kuwamiminia risasi kwa mpangilio maalum, ambao siyo kwa nia ya kuwaua bali waishiwe risasi na kujisalimishe!
Milio ya risasi na moshi wa baruti ikaenea eneo lote na kuchafua hali ya hewa! Ukweli ni kwamba waliona njia ya kuokoka ikiwa finyu sana, kwani baada ya muda wakaishiwa risasi walizokuwa nazo na hawakuwa na za akiba. Hapo ndipo askari polisi walipowasubiri kwa hamu wajisalimishe!
“Sasa jamani, ndiyo tumeishiwa risasi, sijui tufanyeje?” Robi akawaambia wenzake!
“Mh, ngoma nzito!” Muba akasema huku ameegemea ukuta.
“Hapa tutumie akili tu ili tuweze kuwatoka polisi hawa!” Shabani akasema huku akichungulia dirishani, ambapo aliweza kuwaona wale askari walivyokuwa wamejipanga kule nje baada ya kugundua wameishiwa risasi!
“Mimi najiondoa, siwezi kukamatwa kikuku!” Kijana, Boaz, mlinzi yule aliyekimbilia mle ndani mwanzo, akasema. Halafu akachomoka mbio huku ameinama chinichini kuelekea kwenye uchochoro mmoja uliokuwa na giza lililosababishwa na miti iliyokuwa imezunguka. Huku nyuma akafuatiwa na mvua za risasi zilizokuwa zinapigwa na wale askari polisi!
“Mamaa!” Boaz akasema huku akiruka juu! Risasi zote zilimpata kichwani na sehemu nyingine mwilini, zikamrusha mbali na kumfanya afe ndani ya ule uchochoro uliokuwa na giza!
Vijana wengine, Robi, Kessy, Chogolo, Muba na Shabani, wakaamua kutoka mbio kila mmoja na uelekeo wake. Hata hivyo wale askari waliokuwa imara, wakafyetua risasi mfululizo ambazo nyingi zilizowajeruhi na kuwaacha wakigaragara chini kwa maumivu makali na damu nyingi kuwatoka. Ndani ya bohari wakabaki John Bosho na Getruda wakiwa wamebanisha katika sehemu ileile ya mwanzo wakiuona mwisho wao.
Ukweli ni kwamba, John Bosho na Getruda hawakuwa na njia nyingine ya kuweza kupambana na askari wale waliokuwa wamewazingira kote, ukizingatia vijana wake wote walikuwa wamejeruhiwa. Hivyo John akawa anajilaumu kwa upumbavu wa kumuua mchumba wake, Anita, kwa suala la mapenzi tu, ambalo lingeweza kuepukika kama angenyamaza!
“Oh, nimekwama jamani!” John Bosho akamwambia Getruda!
“Hakuna jinsi, ni kweli umekwama! jisalimishe tu!” Getruda akamwambia kwa kumsisitiza!
“Lakini kirahisi namna hiyo?” John Bosho akamuuliza.
“Wewe ulitakaje?’
“Hapana…” John Bosho akasema huku amemata bastola yake iliyokuwa imejaa risasi. Ni bastola iliyokuwa ina uwezo wa kubeba risasi kumi na mbili, ambao ni chache sana katika mapambano na askari waliokuwa na silaha kubwa kama bunduki.
Baada ya kuiandaa bastola yake, ndipo alipomkamata Getruda na kumwambia. “Nataka kucheza mchezo, mimi Komandoo!”
“Mchezo gani?” Getruda akamuuliza kwa hofu, kwani hakuelewa John Bosho alikuwa amepanga kumtumia kama ngao, ili aweze kuwakwepa polisi, ambao wangesita kumpiga risasi kwa kuhofia kumdhuru Getruda asiyekuwa na hatia!
“Watatuua John!” Getruda akamwambia!
“Usiogope! Twende!” Akazidi kutoa amri!
John Bosho akabaki akivuta pumzi na kupanga jinsi ya kuwatoka polisi!
“Tafadhali tokeni nje na mjisalimishe!” Kule nje Kachero Inspekta Malik akaendelea kutoa amri kwao, ambao walikuwa wamebaki wao wawili.
Basi, kitendo bila kuchelewa, John Bosho akamsukuma Getruda mpaka kule nje huku amemkamata kwa nguvu akimtumia kama ngao! Halafu wakatoka naye mbio huku akijaribu kukwepa kwa kujibanza na vivuli vya miti iliyokuwa pale nje. Askari wakaugundua ule ujanja alioutumia. Askari wakajua kwamba John hakuwa na ujanja, hivyo wakamsubiri kwanza ili wapate wasaa mzuri wa kumkamata!
“Hafiki mbali!” Kachero Inspekta Malik akasema. “Nyie mzungukieni kwa mbele, na mimi namfuata kwa nyuma! Nitakapotoa amri tumdhibiti!”
“Sawa afande!” Askari wakasema huku wakimwangalia John Bosho alivyokuwa anakwenda huku akigeuka nyuma ya mti!
Askari polisi waliokuwa mbele yake, wakamfyetulia risasi na kumpa amri ya kusimama.
“Mungu wangu!” John Bosho akachanganyikiwa!
Akamwachia Getruda aliyekuwa kama ngao!
Bunduki za askari pamoja na bastola ya Inspekta Malik zikamwelekea!
Sasa ampige nani? Akashindwa!
“Angusha silaha yako!” Kachero Inspekta Malik akamwambia huku amemlenga kwa bastola yake!
“Sina ujanja!” John Bosho akasema. Halafu akaidondosha bastola yake chini na kunyoosha mikono yake juu!
“Shenzi sana! Umetusumbua sana!” Akasema askari mmoja!
“Mfunge pingu haraka!” Akaongeza askari mwigine!
Askari wakamzingira na kumlaza chini huku wakimfunga pingu baada ya kumpekua tayari kwa kumpeleka kwenye Kituo cha Polisi kwa hatua zaidi. Halafu wale majeruhi wengine, vijana wa John pamoja na maiti ya mlinzi wakachukuliwa kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Baada ya Getruda kuachiwa na John Bosho aliyekuwa akimtumia kama ngao, akabaki amechanganyikiwa na kujiona kama mtu aliyekuwa ndotoni. Milio ya risasi ilikuwa imemchanganya sana kitu ambacho alikuwa hajawahi kukumbana nacho! Kwa haraka Getruda akamkimbilia Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwanamizi wa Polisi, Alfred Gonzo, aliyekuwa karibu naye ikiwa ni katika kujiokoa!
“Oh, nisaidie!”
“Tulia…” Alfred Gonzo akamwambia.
“Mimi sihusiki….majambazi ni hao!” Getruda akasema huku akitetemeka ovyo!
“Sasa ni nani kwako?”
“Ni mpenzi wa John Bosho…”
“Hukujua kama ni jambazi?”
“Sikujua!”
“Basi, tutaongozana wote mpaka kwenye Kituo cha Polisi Buguruni, na utakuwa shahidi muhimu!” Mkuu wa Upelelezi, Alfred Gonzo akamwambia Getruda aliyekuwa bado anatetemeka!
“Sawa…” akasema Getruda huku akiyafikicha macho yake katika kiza kile.
“Panda garini…”
“Sawa…” Getruda akasema huku akijiandaa kupanda kwenye gari la polisi.
Hatimaye askari polisi wakamchukua Getruda aliyekuwa bado anatetemeka ovyo na hata haja ndogo kumtoka bila kipingamizi. Wakampakiza kwenye gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser tayari kwa kumpeleke kituoni kwa hatua zaidi za mahojiano ya kina katika kuupata ukweli. Hakika hakuamini kama alikuwa amepona katika sakata lile baada ya kushuhudia wenzake wakisambaratishwa! Akawa anajuta ni kwanini alikuwa akishirikiana na John Bosho mtu aliyekuwa jambazi!
Kachero Inspekta Malik akapanga askari wengine waliokuwa na magwanda, kwa ajili ya kulinda eneo lile la tukio, ili kesho yake liweze kufanyiwa uchunguzi. Kisha baada ya kuhakikisha kila kitu kimekwenda vizuri, na Mkuu wa Upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Alfred Gonzo wameshatangulia na wale watuhumiwa, Malik akajiondoa kwa hatua ndefu kuliendea gari lake, ambalo alikuwa ameliacha huku mwanadada Helen akiwa ndani yake. Ni Helen Fataki aliyempa mpango mzima wa kuweza kuwapata watu wale, na sehemu walipokuwa wamejichimbia.
Baada ya kulifikia gari, akaufungua mlango wa upande wa dereva; akapokewa na harufu ya mafuta mazuri aliyokuwa amejipulizia Helen Fataki, ambaye muda huo alikuwa amejitandaza kwenye kiti huku akitoa tabasamu zito!
Tabasamu la ushindi!
“Twe’zetu,” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen huku akiufunga mlango wa gari na kuingia.
“Oh, pole sana…” Helen Fataki akasema huku akijiweka vizuri pale kwenye kiti cha gari.
“Sijapoa bado…” Kachero Inspekta Malik akamwambia Helen Fataki huku akitabasamu.
“Vipi tena?”
“Hujanielewa tu?”
“Oh, nimekuelewa…basi subiri tufike nyumbani…”
“Poa, ama kweli kila kazi na dawa, kutokana na uchovu wa wiki nzima, ambayo umenisaidia kuhitimisha na kuwapata wabaya wetu!”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Lilikuwa ni jukumu langu kukusaidia kama raia mwema…” Helen Fataki akamaliza kusema huku akiziweka nywele zake vizuri.
Kacherio Inspekta Malik akalitia gari moto na kuondoka katika eneo lile la Ubungo Machimbo ya Mawe. Na eneo hilo likabaki tulivu tena baada ya pilikapilika zile za mapambano kumalizika. Hapo walibakia baadhi ya askari polisi waliopangwa kulinda eneo hilo la tukio, lililokuwa limezungushiwa utepe wa rangi ya njano ili ushahidi usiharibiwe na wananchi waliofika kushuhudia.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment