Search This Blog

Monday 24 October 2022

MKONO WA SHETANI - 3

 

    Simulizi : Mkono Wa Shetani

    Sehemu Ya Tatu (3)





    * * *



    Wakati Jacob anaegesha gari eneo la kuegeshea magari la kituo cha kati, ni wakati huo huo ambapo gari aina ya land cruiser ilikuwa inapaki mbele ya lango kuu la kuingilia nyumbani kwa Inspekta Ezron.

    Ndani ya gari walitoka vijana watatu wote wakiwa ni vijana wa kazi walioiva. Mmoja wa nne alibaki ndani ya gari huyu alikuwa ni dereva. Mmoja ambaye alionekana kuwa ni kiongozi wao aligonga lango wakati wengine wa kikimbilia upande wa nyuma.

    Mlinzi alipokuja na kufungua lango ghafla alianguka chini huku damu zikimtoka. Alikuwa amepigwa risasi na mmoja kati ya wale vijana wawili waliokimbilia nyuma na kuruka ukuta na kumwacha mwenzao akigonga lango. Haraka haraka walivuta ile maiti mpaka lilipokuwepo banda la mlinzi na kuifungia humo ndani.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nyie pitieni mlango wa nyuma, wakati mimi nagonga mlango wa mbele”

    Aliamuru kiongozi wao na wote walitawanyika huku yeye akiuendea mlango wa mbele wa jumba hilo.



    Wakati yule jamaa anagonga mlango wa mbele wa kuingilia ndai kwa Inspekta Ezroni, ni wakati huo huo ambapo mpelelezi Jacob Matata alikuwa akipiga hatua za haraka haraka kuelekea ilipo mapokezi ya kituo cha Polisi kati.

    “Habari yako Afande” alisalimia alipofika mapokezi

    “Hivi wewe kijana huoni foleni hii yote we umekuja tu. Ina maana hawa sio watu au umefikiri hawana haraka. Au unadhani nani ana shida na salamu yako? alifoka askari aliyekuwa zamu ya kuwa mapokezi, mara baada ya kumwona Jacob amevunja utaratibu, ambapo watu walikuwa katika foleni ili kuhudumiwa.

    “aah bosi nikusaidie nini…. Samahani..” hatimaye huyo askari alisema kwa kubabaika mara baada ya kuona kitambulisho alichoonyeshwa na Jacob.

    “Nataka kuonana na mkuu wa kituo”

    “Mkuu wa kituo hajafika ila yupo msaidizi wake”

    “Nahitaji kumwona” yule askari aliharakisha ili Jacob aingie kumwona mkuu wa kituo. Muda mfupi baadae Jacob alikuwa anagonga mlango wa chumba ambamo ndio ofisi ya mkuu wa kituo msaidizi.

    “Ingia ndani” Ilinguruma sauti tokea ndani ambayo ndio ya huyo mkuu wa kituo msaidizi.

    Kabla ya kusalimiana naye Jacob alitoa kitambulishoa chake na kumwonyesha.

    “Ndio mzee nikusaidie nini? Hatimaye huyo mkuu wa kituo msaidizi alisema mara baada ya kuona kitambulisho cha Jacob.

    “Je umewahi kuongea na yule dada aliyehudumia wakati wa tuko la wizi wa pesa hiyo jana pale Benki? Jacob alimwuliza huyo afisa Polisi.

    “Hapana ila mkuu ndiye aliyemuhoji”

    “Je huyo dada na yule meneja bado wako hapa kituoni au mliwaruhusu kuondoka baada ya mahojiano?

    “Mahojianao yalimalizika usiku wa manane kuamkia leo, hivyo mkuu wa kituo Inspekta Ezron amewarushu kuondoka leo alfajiri.”

    “Mkuu wa kituo yuko wapi wakati huu?

    “Yuko nyumbani kwake”

    “Je unapafahamu anapishi yule dada wa Benki?

    “Ndio”

    “Anaishi wapi?

    “Mwananyamala mtaa wa bonge nyumba namba S521K.”

    “Asante” Jacob alishukuru na kuondoka.

    Alirudi mpaka pale alipoacha gari lake. Alipoingia ndani alitoa simu yake na kutafuta namba za Inspekta Ezron. Alipoipata alibonya kitufe cha kupigia, mara simu iliita upande wa pili ambapo ni nyumbani kwa Inspekta Ezron.



    * * *



    Ile simu haikupokelewa na Inspekta Ezron kwani yeye tayari alishakuwa maiti. Mwili wake ulikuwa umelala chini kutokana na shambulio la kareti, ambapo mpigaji alimjia kwa nyuma kama ilivyokuwa imeelezwa na kiongozi wao kuwa wale vijana wawili wapitie nyuma. Hivyo wakati Inspekta anafungua mlango wa mbele, wale vijana wengine wawili tayari walikuwa wamefanikiwa kuingilia mlango wa nyuma.

    Pigo la kareti lililotolewa lilipigwa ipasavyo halikumpa hata nafasi ya kugeuka alikuwa tayari maiti.

    Wakati wauaji hawa walipokuwa wanataka kutoka ndipo ile simu iliyopigwa na Jacob Matata ilipoita ndani ya nyumba hii. Yule kiongozi wao alikimbilia mezani na kunyanyua mkonge wa simu

    “Insipeka Ezron hapa naongea” aliongopa yule jamaa.

    “Jacob Matata hapa ninahitaji kukuona kabla sijaenda kumhoji yule dada wa Benki naomba unipe nafasi ya maongezi kwa dakika tano tu kabla hujaenda huko kikaoni” alisema Jacob upende wa pili pasipo kujua ni nani alikuwaanaongea nae.

    “Sawa nina kama dakika kumi na tano zimebaki ili niende kikaoni hivyo ni vema ukaja haraka maana nikisha toka si rahisi kuonana kwa leo.” Aliongopa tena huyo jamaa ambaye alijifanya ndiye Inspekta Ezron.

    Alipoweka mkonga wa simu chini tu, aliwageukia wenzie na kuwaambia.







    “Mimi na Isaack tutaenda nyumbani kwa yule binti mhudumu wa Benki, wewe Chacha utabaki hapa kumpokea Jacob Matata kama atakuja kabla hatujarudi”

    Alisema yule kiongozi wao huku akianza kuondoka.

    “aah Jacob anakuja” aliongea yule aliyeitwa Chacha na ndiye aliyetakiwa kubaki.

    “Unamwogopa? alihoji yule kiongozi wao.

    “aah wapi, tena msipokaa sawa mtaikuta maiti yake tu “ Chacha alijigamba.

    “Hapana kama atakuja kabla hatujarudi basi muhifadhi vizuri ili nije nimmalize kwa mkono wangu mwenyewe” alisema yule kiongozi.

    “sawa” Chacha aliitikia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ila kuwa makini sana maana ‘bosi’ amemsifia sana yule kiumbe kuwa si wa kawaida”

    “aah bwana, mimi ndie Chacha ” alijigamba yule jamaa aliyetakiwa kubaki.

    “Isack twende tukammalize yule kiumbe wa kike kisha turudi hapa kumwondoa Jacob duniani, nafikiri mpaka hapo tutakuwa tumecheza vizuri sana” alisema yule kiongozi wao. Hao wawili walitoka huku wakimwacha mwenzao akivuta mwili wa Inspekta Ezron ambaye sasa ni marehemu na kupeleka kwenye chumba kimoja wapo ndani ya nyumba hiyo. Baada ya zoezi hilo akawa tayari kumsubiri Jacob Matata.



    * * *



    Baada ya kuwasiliana na mtu aliyedhania kuwa ndiye Inspekta Ezron, Jacob Matata aliamua aende kumwona Inspekta Ezron kwanza, kisha ndipo angeenda kumwona yule mhudumu wa DE EURO LINKAGE. Uharaka aliokuwa nao Inspekta Ezron wa kwenda kikaoni ndio uliomfanya Jacob aamue kwenda huko kwanza. Bila kujua kuwa alikuwa anasubiriwa na adui zake.

    Wakati gari ikiwa kwenye kasi kuelekea kwenye mitaa aliyokuwa akiishi Inspekta Ezron, kitu kimoja tu ndicho kilichomtatanisha Jacob Matata. Kila alivyoongeza kasi ya gari ndivyo nywele zilivyomsimama hali mapigo ya moyo yakizidisha kasi ya kupigia kite. Hisia za kwamba kule alikokuwa anakwenda kuna hatari zikaanza kumtawala akili kichwani mwake.

    Jacob aliamua kupaki gari mbali kidogo na eneo ilipokuwepo nyumba ya Inspekta Ezron. Kwa hatua za mtu anayeenda kupanda daladala ambayo haina abiria saa saba mchana pale Posta, alianza kuelekea upande ule ilipokuwepo nyumba. Baada ya kuvuka nyumba mbili tatu, hatimaye aliiona nyumba iliyokuwa na lango kuu la kuingilia lenye rangi nyekundu. “Bila shaka ndio hapa” alijisemea.

    Kabla hajalisogelea geti, alipapasa sehemu aliyokuwa ameficha bastola yake ili kuhakiki kama ilikuwa sawa, baada ya kuona yuko sawa kwa lolote. Alilisogelea lango kuu la ua wa nyumba hiyo. Wakati huo kwa haraka haraka Jacob aliruhusu macho yake kuangalia mandhari ya nje ya nyumba hii. Hii ilikuwa ni moja kati ya tabia za Jacob.

    Alipofika langoni alibonyeza kengele ya kubishia hodi. Mara geti lilifunguliwa na kijana mmoja. Aliyevalia sare ambayo ndiye Chacha japo Jacob hakujua hilo.

    Macho ya Jacob na yale ya Chacha yalipogongana, Jacob tayari akawa ameshaona kitu. Kwa uzoefu na ujuzi wake, Jacob aliweza kugundua kuwa macho ya Chacha yalikuwa ni zaidi ya mlinzi wa kawaida kwani yalionyesha ni macho ya ‘mtu wa kazi’ kweli.

    “Habari za hapa”

    “Nzuri nikusaidie nini” aliuliza yule kijana huku akijifanya kutomjua Jacob

    “Mzee nimemkuta?

    “Ndi…ndi…ndio” Chacha alijibu kwa kubabaika. Hali ya tahadhali kichwani mwa Jacob iliongezeka.

    “Karibu ndani”

    “Asante” Jacob alijibu huku akivuka lango hilo na kumwacha huyo mlinzi wa bandia afunge lango.

    Chacha alimwelekeza Jacob mpaka sebuleni ambapo alimwelekeza kiti cha kukaa. Lilikuwa ni kochi la mtu mmoja na mbele yake kulikuwa na meza ndogo. Upande mwingine wa sebule kulikuwa na kochi kubwa la kutosha kukalia watu wanne. Baada ya kuhakikisha kuwa Jacob amekaa alivyotaka, Chacha alitoka nje kwa njia ambayo Jacob alikuwa ameipa mgongo.

    Dakika ya kwanza, ya pili ya tatu lakini hakuna mtu aliyetokea wala Chacha hakurudi pale sebuleni. Mara mlio wa simu ya mkononi ukavuma sebuleni hapo haikuwa simu ya Jacob. Kwa vile ni yeye peke yake ndiye aliyekuwa sebuleni hapo, Jacob alitupa macho yake hapa na pale ili kuona hiyo simu ilikuwa wapi. Ndipo aliposhangaa kuona kuwa simu hiyo ilikuwa chini ya kochi kubwa lililokuwa mbele yake upande mwingine wa sebule.

    Bila hadhali yoyote, Jacob aliinama chini ya kochi ili aichukue simu. Alidhani kuwa mwenyewe atakuwa alikuwa amekalia kochi hilo na kuidondosha.

    Ghafla alikuwa chini kutokana na teke alilokuwa amepigwa wakati akinama ili kuiokota hiyo simu Alipotaka kukaa sawa alipigwa ngumi nyingine ya kisogoni iliyomfanya aone nyota nyota.

    Mambo haya yote yalifanywa na Chacha kwa ufundi mkubwa na kasi ya ajabu.

    “Simama taratibu na ukifanya ujanja wowote, nitasambaratisha ubongo wako” alifoka Chacha.

    Jacob akageuza macho yake ili aone umbali ambao Chacha alikuwa amesimama, ili aangalie uwezekano wa kujitetea. Alimwona Chacha akiwa amesimama umbali wa kama hatua sita huku akiwa ameshikilia bastola kuelekea kisogo chake.

    “Weka mikono yako kichwani kisha kaa taratibu kwenye kiti” Chacha aliamuru na Jacob akatii bila ubishi wowote. Jacob hakuwa anaamini macho yake kuona alikuwa ametekwa kirahisi namna hiyo. Ni wakati anakaa kwenye kiti ndipo alipoweza kuhisi maumivu aliyokuwa nayo kwenye kiuno kutokana na pigo la teke alilokuwa amepigwa.

    Jinsi mambo yalivyoanza ilitosha kabisa kumthibitishia Jacob kuwa alikuwa anapambana na mtu aliyekamilika. Jambo jingine lililomfanya Jacob aanze kumhusudu yeyote aliyekuwa nyuma ya mambo hayo ni jinsi alivyokuwa hodari wa kufuta ushahidi wowote ambao ungepelekea yeyé kufikiwa. Hadi sasa ilionyesha ni jinsi gani ingekuwa vigumu kupata ‘nyayo’ za mtu huyo.

    Mara ile simu iliyokuwa bado chini ya kochi ilianza kuita. Ni simu hii ndio iliyopelekea Jacob apate kipigo kwa urahisi zaidi. Kochi hilo ndilo ambalo amekalia wakati huu. Jacob Matata akili yake ilikuwa ikifanya kazi kwa haraka sana. Alitulia tuli huku mikono yake ikiwa juu kama alivyoamriwa. Alisubiri aone yule jamaa atachukuwa hatua gani.

    Simu iliendelea kulia. Yule jamaa alitoka pale mlangoni alipokuwa amesimama. Alipiga hatua taratibu huku akiwa bado bastola yake kailekeza kwenye paji la uso wa Jacob, nyumba nzima ilikuwa kimya kabisa. Kunyata kwa yule jamaa kulimfikisha karibu kabisa na lile kochi alilokuwa amekalia Jacob. Akasogea upande wa kushoto wa kochi. Muda wote huo ile simu pale chini ya kochi iliendelea kupiga kelele.

    Alifanya kitendo ambacho Jacob alikuwa akiomba kitokee. Aliinama ili aichukue ile simu. Kama radi, Jacob alimzoa judo kali sana ambayo ilivunja shingo ya yule jamaa palepale. Wakati yule jamaa anakata roho, mlio wa ‘breki’ za gari ulisikika nje ya jumba hilo. Mara moja Jacob akajua mambo yamekuwa mambo. Aliivuta maiti ya yule mlinzi hadi chumba cha jirani ili kuwasubiri wanaokuja. Wakati anaingiza ile maiti ndipo alipokutana na maiti nyingine ambayo mara moja akatambua kuwa ni ya Inspekta Ezron. Hakuwa na muda wa kupoteza kwani alisikia lango la mbele la nyumba hiyo likifunguliwa. Alikimbia hadi sebuleni akaiokota ile simu. Alipoangalia namba ya mpigaji macho yake aylikutana na jina la Amosi Bugingo. Mara moja akajua simu ile ilikuwa imepigwa na mkuu wa Polisi Inspekta generali Amosi Bugingo. Bila shaka ni wakati ule mkuu wa Polisi alipotaka kujua sababu za kuchelewa kwa Inspekta Ezron kupeleka taarifa ya mahojiano kule kikaoni. Jacob aliifutika mfukoni ile simu. Akakimbilia kule chumbani zilikokuweko maiti.

    “Chacha” sauti tayari ilikuwa sebuleni walikuwa wakimwita mwenzao ambaye tayari alikuwa kwenye ulimwengu wa marehemu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Uko wapi na huyo mbwa wa kiume tummalize na kuondoka zetu” vicheko vilifuata. Walifurahia kazi yao ambayo mpaka hapo ilikuwa ikiashiria ushindi na wangepewa dau kubwa na Dr. Don kwa kazi hiyo.

    “Uko wapi” sauti iliuliza tena.

    “Huku chumbani” Jacob alijibu ili kuwaondoa wasiwasi.

    “kwa nini umejificha naye huku…? alisema yule jamaa huku akitaka kuingia ndani ya chumba alichokuwemo Jacob. Hivyo kabla hujamalizia kusema swali lake mikono yenye nguvu kama ya chuma ilikidaka kichwa chake na kumvutia ndani ya chumba kwa kasi. Kabla hajatambua nini kilikuwa kinatokea mikono hiyo hiyo ilimtia konde zito la usoni na kumpeleka chini.

    Yule mwingine ambaye alikuwa nje ya chumba akawa ameshashtiukia, hivyo akaingia kwa sarakasi ya aina yake. Wakati anatua ndani ya chumba Jacob alikuwa ameshusha mguu mara baada ya teke alilotaka kumpa yule wa kwanza kukwepwa. Alimwona huyo aliyeingia kwa sarakasi. Akamkwepa naye akamparamia mwenzie.

    Sasa Jacob akawa anapambana na watu wawili. Akajifanya kana kwamba anataka kukimbia, wote wakamfuata mbio. Kwa kasi ya ajabu aligeuka na kuachia mateke mawili kwa miguu yote miwili. Wote wakaenda chini. Mwingine alianguka karibu kabisa na alipokuwa amesimama Jacob. Jacob alikuwa tayari kuachia kipigo pale miguu yake yote miwili ilipovutwa kwa nguvu na yule aliyekuwa ameangukia karibu yake. Akaenda chini wakati anatua chini yule mwingine ambaye sasa alikuwa tayari aliruka ili ammalize Jacob kwa kareti pale chini. Jacob alijipinda kama chatu, pigo lake likakutana na sakafu tupu kwani tayari Jacob alikuwa ameshakwepa. Kwa vile yule jamaa alikuwa ameinama wakati alipopiga lile pigo lilokwepwa na Jacob pale chini. Jacob alitumia nafasi hiyo kuidaka shingo yake na kuivunja kwa kasi mno.

    Yule mwingine alipoona mwenzie amevunjwa shingo kwa namna ya kutisha, akajua mambo yamekuwa magumu. Aliiwahi bastola iliyokuwa imeanguka chini akamimina risasi kuelekea pale alipokuwepo Jacob. Jacob alijiviringa na kumkumba huku akiwa amekwepa risasi zote. Wote walianguka chini huku zile risasi zikimmalizia yule jamaa aliyekuwa amevunjwa shingo.

    Mle chumbani sasa ikawa ni vita kati ya yule jamaa na Jacob tu. Walibingirishana pale sakafuni kwa muda huku kila mmoja akitaka kumwai mwenzie. Jacob alibanwa kwenye kona sawa sawa. Aligeuza kichwa na kumpiga yule jamaa kichwa cha kinyume nyume ambacho kilimtia kiwewe. Kutokana na pigo hilo la kichwa, yule jamaa akalegeza mbano wake. Jacob akaelekeza miguu ukutani na kumsukuma kwa nguvu, wote wakaruka huko kila mmoja akitua upande wake.

    Kwa bahati yule jamaa aliangukia jirani na mlango, akasimama haraka ili akimbie. Jacob akaiona bastola iliyokuwa jirani kabisa na yeye. Alilenga mguu wa yule haramia wakati unaishia kwenye pazia la mlango. Kishindo cha mtu kuanguka kikasikika. Jacob akakimbia ili kumfuata, akamkuta ameanguka kwenye varanda ya nyumba hiyo iliyokuwa imetenganisha vyumba vya upande huu na huu.

    Jacob alimtia teke moja la mbavuni jamaa akaguguma kama mbuzi pori anayeiba mahindi shambani. Akamvuta mpaka kile chumba walichopambania mwanzo.

    Jacob akaona huo ndio wakati muafaka wa kumuhoji huyo jamaa.

    “Jina lako nani?

    “Naitwa Donito”

    “Nani aliyewatuma kuja kumwua Inspekta Ezron na kwa nini?

    “Simjui? Alijibu huku akionyesha kiburi

    “Bosi wako ni nani?

    “Sijui”

    “Aah unajifanya mjanja sio ngoja uone dawa ya watu kama wewe” Jacob aliingiza mkono mfukoni, wakati anatoa kisu kidogo ambacho ni maalumu kwa ajili ya kutesea watu wa aina hii, yule jamaa kwa haraka sana alitoa sindano ndogo sana na kujichoma nayo kwenye mshipa mkubwa wa damu na baada ya sekunde kadhaa tayari alikuwa njiani kuelekea ulimwengu wa marehemu. Bila shaka ile sindano ilikuwa ya sumu. Kwa hasira Jacob alimwongezea risasi nyingine tatu na kutoka mle chumbani.

    Ghafla kitu kilidondoka kama umeme Jacob alianguka chini na kuachia risasi kuelekea kule kulikotokea kishindo. Alishangaa pale alipoangalia upande ule na kukuta paka akiwa amebeba panya. Kumbe ilikuwa ni harakati za paka katika kusaka panya.



    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Macho yake hayakuwamchia yule paka haraka. Hisia nzito zilimwingia kichwani kwa picha hiyo ya paka na panya. Alimwonea wivu yule paka kwani tayari alikuwa ameshafanikisha windo lake tofauti kabisa na yeye ambaye mpaka hapo alikuwa ndani ya sitofahamu kubwa.

    Mlio wa ‘breki’ ya gari pale nje ya jumba hili ndio uliotoa fikira za Jacob kwa yule paka. Alizikagua zile maiti zote na kukimbia kuelekea ndani alichungulia kwa makini ili aone ni nani angeingia. Watu waliovalia sare za Polisi ndio walikuwa wameingia. Hawa ndio wale waliokuwa wametumwa toka kikaoni na mkuu wa Polisi Inspekta generali Amosi Bugingo. Kwa kupitia ukuta wa nyuma, Jacob aliruka na kuelekea alipoiacha gari yake.

    Akili ya Jacob sasa ilikuwa ni kumhoji yule dada mhudumu wa Benki. Aliongeza spidi ya gari lake wakati alipoishika barabara ya kuelekea mwananyamala. Inaonekana kuna habari ambazo Inspekta alipata toka kwa huyo dada ambazo hawa maharamia walijua zingefanya wafikiwe na vyombo vya dola. Ndio maana wakaamua kuutoa uhai wake.

    Dakika tatu baadae, Jacob alikuwa anaegesha gari jirani na nyumba aliyokuwa anaishi huyu mhudumu.

    Baada ya kuwa ameingia ndani aliusogelea mlango wa chumba amnacho ndicho alichouwa amepanga huyo dada. Kabla ya kugonga alisikiliza kwa pozi. Haikuonyesha dalili za kuwapo mtu yeyote. Aligonga mlango mara kadhaa pasipo jibu lolote.

    Alipojaribu mlango alikuta uko wazi.

    “Ingia tu labda ametoka kidogo” ilishituliwa sauti ya mama mwingne ambaye bila shaka alikuwa ni mpangaji mwenzie. Mama huyo aliingia chumba cha jirani.

    Bastola ikiwa mkononi aliusukuma mlango na kuingia ndani.

    “Washenzi kweli hawa, sidhani kama ni watanzania hawa” alisema Jacob huku akiwa amekunja ngumi. Maneno hayo yalimtoka baada ya macho yake kuonana na maiti ya msichana mrembo ambaye hakustahili kufa kabisa japo hakuna anayestahili kufa lakini uzuri wa yule dada ulimfanya Jacob asahau falsafa hiyo.

    “Ama kweli Kichaa akiona jalala anadhani utajiri kumbe uchizi ndio unaongezeka” Jacob alinong’ona. Alishangaa jinsi pesa inaweza ondoa ubinadamu wa mtu. Alipousogelea na kuugusa mwili wa marehemu ndipo alipogundua kuwa mauaji au wauaji wamefanya kazi hiyo si muda mrefu uliopita. Hasira kali zilimpanda Jacob. Ila wakati huu ilimbidi kutulizana zaidi maana huu ulionekana kuwa mchezo wa ujanja zaidi.

    Macho ya Jacob yalivutwa na kijikaratasi kidogo kilichokuwa juu ya meza. Kwa tahadhali kubwa alikichukua. Maneno yaliyoandikwa ndani ya karatasi hiyo yalizaa mambo mawili ndani ya kichwa cha Jacob.

    Karatasi hiyo ilisomeka JACOB NILIKWAMBIA YAACHE KAMA YALIVYO, LAKINI UMEKUWA MZALENDO ZAIDI, BAADA YA HUYU DADA NI WEWE.

    Jambo la kwanza alilopata ni kuwa ilionyesha mwandishi wa ujumbe huu ni yule aliyeandika ile karatasi aliyoikuta ndani ya ‘briefcase’ kule Hoteli ya Fortune Inn. Wakati anafukuzana na yule mzungu. Pili ilikuwa hakika kuwa yule mzungu na genge lake ndio waliohusika na wizi wa mabilioni ya pesa. Ile ‘briefcase’ aliyoiiba ndani ya ndege siku ile ndiyo iliyokuwa na nyaraka muhimu. Jacob aliwaza huku akiwa bado ameshikilia ile karatasi. Lakini namna gani aliweza kumrudishia mkurugenzi zile karatasi? namna gani alibadilisha briefcase tofauti na ile ambayo yeye Jacob aliichukua? Kichwa kilijiuliza maswali mengi lakini hakuna jibu lolote. Aliamini ipo siku atampata Dr. Don na kutaka majibu ya maswali yote hayo. Na mara hii ndipo alipoona kuwa kazi hii ingekuwa ngumu maradufu tofauti na alivyoitarajia.

    Kama ingetokea ukamwuliza Jacob Matata akutajie siku ambayo aliwahi kuhisi akili yake imeshangaa basi angekutajia leo. Akili yake iliduwaa, huku fikira zake zikiwa zimedumaa. Kwa jinsi alivyokuwa alishindwa kupambanua kama kilichomsumbua ni hasira au aibu. Mara baada ya kutoka kwenye kile chumba cha yule dada aliyekuwa mhudumu wa Benki ya DE EURO LINKAGE na ambaye sasa ni marehemu, Jacob alikaa takribani dakika tano ndani ya gari huku akiwa ameacha inaunguruma. Alishindwa kuiamuru iende wapi. Hakujua aelekee wapi na kufanya nini.



    * * *



    Hali ilikuwa tofauti kabisa kwa mtu huyu mwingine. Yeye akiwa ametulia juu ya kiti chake huku moyo wake ukiwa umejaa furaha Don aliendelea kuvuta sigara yake taratibu. Dr. Don alishindwa ajiweke kwenye kundi gani la washindi. Akili yake ilikuwa ikirudia rudia picha za namna alivyofanikiwa kuendesha “oparesheni” yake hiyo ya wizi wa mamilioni ya dola. humba alichokuwepo wakati huu, kiko katika jengo moja la ghorofa katikati ya jiji. Chumba hiki kilikuwa na hadhi sawa kabisa na ile ya Dr. Don mwenyewe. Anapoingia ndani ya chumba hiki, huwa huitaji huduma ya aina yoyote nje ambayo haimo humu. Dr. Don hakuwa mtu aliyependa ubabaishaji. Hii ndiyo iliyopelekea atumie mamilioni ya shilingi kukifanya chumba hiki kuwa na chochote alichohitaji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alitakiwa kutekeleza mambo mengi siku hii. Lakini matatu aliyapa kipaumbele. Moja alitaka kusikia taarifa za vifo vya watu alioamuru wauawe. Taarifa hii alitarajia kuipata saa tatu na nusu kama alivoamuru. Pili aliamua kumtaarifu Mr. Peari Robert juu ya hatua aliyofikia katika operesheni yao hii. Tatu alihitaji kuweka mkakati wa kumwondolea uhai Jacob Matata. Hapo ndipo angekuwa huru kutorosha toka ndani ya Tanzania pesa zote alizokuwa amefanikiwa kuziiba.

    Badala ya kupokea simu iliyokuwa ikilia, macho ya Dr. Don yalielekea kwenye saa yake. Alipoona bado alikuwa haijafika saa tatu na nusu, akahisi simu hiyo inatoka sehemu nyingine tofauti na vijana wake wa kazi. Ilikuwa ni simu toka kwa wale jamaa waliokuwa wameenda kwa Inspekta Ezron.

    “Bosi, Inspekta Ezron tayari ni maiti, lakini tumepokea simu toka kwa Jacob Matata ambaye anataka kuja hapa nyumbani kwa Inspekta ili waongee, je tummalize?

    Kidogo aruke kwa furaha. Kwa mara ya kwanza yule kijana alimsikia Dr. Don akicheka.

    “Sikiliza, inabidi muwe makini sana, yule kiumbe si wa kawaida. Nitafurahi sana, nikisikia mmemmaliza”

    “Bado yule dada wa mhudumu tukitoka hapa tunaenda huko” ulijibu upande wa pili.

    “Sawa kuweni makini na kazi sitaki makosa yoyote. Mkisha mmaliza Jacob, nitaarifu haraka” Dr.Don aliongea.

    Dr.Don aliona mambo yamekuwa rahisi tofauti na alivyokuwa amefikiria. Hivyo akili yake akaihamishia kufikiri namna ya kutorosha hayo mapesa. Taarifa ya kuuawa kwa Jacob, ingekuwa ni robo tatu ya ushindi kwake. Dakika kumi baadaye tayari alikuwa amepata wazo jingine. Alisimama kama aliyemriwa. Aliindea simu yake maalumu iliyokuwa imeunganishwa kwenye satelite. Baada ya kuwa ameunganisha nyaya fulani na kuinua antenna ya simu hiyo Dr. Don alibonyeza namba fulani.

    ‘Hellow, Dr. Don hapa” alijitambulisha

    “aah, nimepata taarifa juu ya kazi yako” ilisikika sauti ya Mr. Peari Robert, ambaye alionekana mwenye furaha.

    “Vipi pesa unazo? Aliuliza Mr. Peari Robert.

    “Mambo yamekwenda vizuri sana. Ndani ya chumba nilichopo ndimo ambamo pesa zote zipo” alisema Dr. Don kwa furaha wakati anataka kuendelea alikatishwa na mlio wa simu iliyokuwa mezani.

    “Ok subiri kidogo niongee na vijana wana habari muhimu” Don alimtaka radhi Mr. Peari Robert. Aliweka chini kifaa alichokuwa akiongelea na kuelekea mezani.

    Taarifa aliyopokea ilikuwa kama pigo la mshale moyoni.

    “Kwa hiyo amuwaua wote? Dr.Don aliuliza kwa hasira.

    “Ndiyo bosi, ila hakufanikiwa kumhoji yeyote kwani yule dada wa Benki, tayari tulikuwa tumeshammaliza” ulisema upande wa pili huku sauti ikionyesha dhahiri hofu na woga wa msemaji.

    “Mshenzi Jacob, lazima nimmalize hata hivyo” Dr. Don alisema huku akiweka chini mkonga wa simu.

    Pamoja na kusema hivyo, alibakia akiwa amesimama. Hakutaka kukubali na kuamini kile alichokisikia. Ilikuwa ni simu ya tahadhali na ya kuashiria kuanza kwa mapambano. Mapambano ambayo kwa hakika haikuwa rahisi kutabiri mshindi wake. Kitendo cha kusikia Jacob yu hai kiliivuruga kabisa akili yake. Hisia za hofu, kitu ambacho kwa kawaida hakimo kabisa katika damu yake, zilikuwa zikimnyemelea.

    Alitaka ajilaumu, lakini hakuona kosa lake. Alitaka awalaumu vijana wake kwa kukubali kushindwa mbele ya Jacob, lakini alipokumbuka kipigo na jinsi alivyomkimbia Jacob kule hoteli ya Gardenia, nafsi yake ilimsuta.

    Wazo la kuwa Mr.Peari Robert alikuwa bado amemsubiri lilimfanya atembee kizembe kuelekea kwenye vifaa vyake vya mawasiliano. Japo hakuwa mzoefu sana lakini Mr. Peari Robert hakushindwa kutambua mabadiliko katika sauti ya Dr. Don. Ndipo alipomwuliza Dr. Don ambaye alimweleza kila kitu kuhusu Jacob Matata na jinsi anavyohatarisha mpango wao.

    Baada ya kusikia maelezo ya Dr. Don, Mr. Peari Robert aliona kuna kila sababu ya kumwongezea nguvu Dr.Don.

    “Kuna wale mafundi wetu wa kupigana watano ambao wako mapumzikoni kule mbuga a wanyama Mikumi. Jiandae kuwapokea jioni hii ya leo. Utawaongoza katika kuhakikisha pesa hizo zinafika hapa Marekani” alisema Mr. Peari.

    “Pamoja na hayo kuna jambo naomba ulifanye”

    Dr. Don alisema huku sauti yake ikiwa ile ile ya “kazi ipo”

    “Leo au kesho safirisha watu kumi. Watu hao tafuta toka mitaani watu wasiojiweza. Kisha walipie gharama zote za kuja huku kama watalii. Kampuni letu ndilo litakuwa wenyeji wa watalii hao. Ila hakikisha umechukua watu walioshindwa na maisha huko “ Dr. Don aliagiza, kama kawaida Mr. Peari mara nyingi kuwa haelewi mipango ya Dr. Don. Lakini ilimlazimu kutekeleza kama ametaka kufanikisha ndoto zake za kutaka hayo mapesa.

    “Sawa nitawatuma huko siku yoyote na kukutumia taratibu na taarifa zote kuwahusu. Kuna jambo Dr. Don alitaka kufanya na hao watu. Lakini haikuwa rahisi kujua kuwa jambo hilo ni lipi. Baada ya kuamaliza maongezi na bosi wake, Mr. Peari Robert, Dr. Don aliagiza vijana wake wengine kwenda kuwapokea hao mapiganaji toka Mikumi.

    “Jeshi hili nitaliongoza mwenyewe, Tanzania itageuka uwanja wa mapambano, mchezo utakuwa mtamu bila shaka! Dr. Don aliwaza wakati akikusanya vifaa vyake na kuvitia katika briefcase yake. Alizima taa za chumba hicho na kusimama kwa muda wa kama dakika tatu hivi kabla ya kutoka na kukifunga. Alipitia njia zake za siri kuelekea nje.

    Alipofika nje mahali lilipo gari lake, iliingia na kulitia moto. Akatokomea kusikojulikana. Bila shaka kwenda kupanga mipango ya kumsaka Jacob.



    * * *

    Jacob mwenyewe alikuwa ametulia tuli juu ya kiti kwenye mgahawa mmoja nje kidogo ya jiji la Dar es salaam. Hii ni baada ya kuwa ametoka nyumbani kwa msichana aliyekuwa muhudumu wa Benki, ambaye alikuta ameuawa. Aliamua kuja kwenye mgahawa huu ili kuipa akili yake nafasi ya kufikiri. Macho yake yalikuwa kwenye mshale wa saa yake ambao ulikuwa ukiyakimbiza majira bila mafanikio. Kila mshale ulipofika ulikuta majira yameshaondoka hivyo ilibidi uruke tena kwenda mbele. Hivyo Jacob aliweza kusoma saa na dakika bila kufanikiwa kuusoma mshale wa sikunde.

    Akili yake ambayo inasemekana ina uwezo wa kufikiri zaidi ya vichwa ishirini vya watu wenye akili timamu wakikusanywa pamoja, ilikuwa ikipitia mlolongo wa matukio. Alishangaa pale alipofika mwisho bila hata ya kupata ufa wowote wa kuingilia ndani kwa wahusika. Wahusika wa tuko hili walikuwa wamefanikiwa kufunga kila mlango ambao ungemruhusu kuwafikia. Kila tukio alilowaza aliona linafikia kikomo. Hakuwa na tukio hata moja ambalo liliacha nyayo za wahusika. Kila walipopita wahusika walikuwa wakifuta kila nyayo nyuma yao.

    Ujumbe wa kutisha ambao siku hiyo ni mara yake ya pili kukutana nao, haukuwa na chochote cha ziada. Ujumbe huu ulimwonyesha tu kuwa adui alikuwa amejitahidi kumfuatilia. Jambo moja lilikuwa bayani kichwani kwake. Yule mzungu ni mhusika katika mchezo huu! Ni namna gani atamfikia hilo ndilo swali ambalo halikuwa na jibu mpaka wakati huo, na lilihitaji jibu. Alitoa miwani yake mweusi usoni na kutoa kitambaa ili aifute.

    “Magazeti” Jacob aliita alipomwona kijana mmoja mtembeza magazeti.

    “Nipe alasiri na Mwananchi”

    Alipoangalia gazeti la alasiri ndipo alipozikuta habari za mauaji ya siku hiyo. Alisoma kwa makini kama kuna jipya ambalo angelipata katika magazeti hayo. Hakuona jipya. Mwandishi wa habari hizo bila kusita alihusisha mauaji ya Inspekta Ezroni na wizi wa mamilioni ya shilingi.

    “Mzee pesa zangu” sauti hii ilimshitua. Ndipo alipogundua kuwa taarifa hiyo ilikuwa imemgusa kiasi gani mpaka akawa amesahau kumlipa yule kijana pesa zake.

    “Samahani alisema na kumpa pesa zake wakati huo huo akiwa tayari amesimama. Alipofika sehemu aliyokuwa ameegesha gari yake, aliingiza mkono mfukoni ili kutoa funguo za gari. Hapo ndipo alipokutana na makaratasi kadhaa ambayo aliyachukua mifukoni mwa wale jamaa aliowaua kwa Inspekta Ezron.





    Aliingia ndani ya gari, badala ya kuondoa gari alianza kuvisoma hivyo vikaratasi, alisoma kimoja baada ya kingine lakini hakuna habari ya maana aliyoipata. Aliviweka sehemu ya mbele ya gari, akawasha gari na kuondoka taratibu.



    Dakika chache baadaye tayari alikuwa ameshafika nyumbani kwake ambapo alilakiwa na mpenzi wake.

    “ooh karibu mpenzi” Regina alisema mara baada ya Jacob kuwa ameingia ndani.

    “Asante sana” alisema huku akimkumbatia Regina “vipi umeshafanya fanya maana tumbo linadai kweli”

    “Usitie shaka ndio wajibu wangu, umepata”

    Alisema Regina huku akielekea jikoni kuandaa chakula. Jacob alikaa hapo sebuleni.

    Pamoja na njaa iliyokuwa ikimsumbua, akili ya Jacob haikumruhsu aache kufikiria juu ya kazi yake.

    “Karibu mezani” sauti ya Regina ilimgutua toka kwenye mawazo yake. Regina alimkumbatia na kumnyanyua toka kwenye kiti alichokuwa amekali. Hivyo akampeleka mpaka mezani.

    Wakati Jacob anakula, Regina alitoka nje. Akafika pale Jacob alipokuwa ameegesha gari. Alifungua na kuchukua magazeti yaliyokuwa ndani. Regina ni mpenzi sana wa magazeti. Kwa vile muda mwingi huwa nyumbani, huona kuwa magazeti ndio rafiki ambao wanaweza kumwambia juu ya kitu gani kilikuwa kinaendelea nchini. Wakati anataka kufunga mlango wa gari ndipo macho yake yalipoona vikaratasi ambavyo Jacob alivipora toka kwa jamaa aliokuwa amepambana nao. Regina alivichukua na kuingia navyo ndani ya nyumba.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Na hiki ndio nini? Regina alimuliza Jacob

    “Karatasi zangu hizo, naomba uniweke juu ya meza ndogo hapo” Jacob alisema

    Alipomaliza kula, alikaa kutafakari hali ya mambo. Baadaye aliamua kuutumia kuangali tena vile vikaratasi.

    “Hivi kuna ‘network’ kweli” aliuliza Jacob mara baada ya kuona anuani ya tovuti moja katika hivyo vikaratasi.

    “Ndiyo. Asubuhi ilikuwepo, ngoja niangalie” alisema Regina ambaye alikuwa amekaa pembeni ya Jacob wakati anaangalia hivyo vikaratasi. Regina alimpenda sana Jacob alimwona kuwa ndiye kila kitu kwake. Hii inatokana pia na jinsi walivyokutana katika ule mkasa ambao umeandikwa kwenye kitabu kimoja cha riwaya kiitwacho HEKA HEKA. Hivyo hakuchelewa kutambua kuwa Jacob alikuwa na jambo lililokuwa likimtatiza.

    “eeh ipo” alijibu huku akisogeza kiti ambacho kingetumiwa na Jacob hapo kwenye ‘computa’.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog