Search This Blog

Monday, 24 October 2022

DHIHAKA - 3

 









    Simulizi : Dhihaka

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Nico aliusikia mlango wa ofisini kwake ukigongwa kwa nidhamu. Moja kwa moja akahisi kifungua kinywa kimeletwa, lakini akawa na mashaka kama mletaji angekuwa ni Hija.

    “Karibu,” alisema kwa sauti ya kujidai.

    Mlango ukafunguliwa, akamwona Hija amebeba tray iliyokuwa na birika yenye kahawa na nyingine ya maziwa na sahani za matunda na mayai.

    “Oh, karibu Hija,” Nico alisema kutoka kwenye meza huku akiyumbayumba kwa maringo kwenye kiti chake. Akanyoosha mkono kuuelekeza juu ya meza. “Unaweza ukaweka hapa,” alisema.

    Hija aliiweka tray yenye vyakula juu ya meza. Akageuka kutaka kuondoka.

    “Subiri!” Nico alisema. Aliacha kuyumba na kuonekana kuwa makini usoni huku akimwangalia Hija.

    Hija alisimama huku sura yake ikiwa na aina ya hofu. Akamwangalia Nico kwa macho yanayouliza, unasemaje?

    “Kaa kwenye kiti,” Nico alisema huku mkono wake ukimwelekeza Hija kwenye kiti anachotakiwa kukaa.

    “Kuna kazi nimeiacha, naenda kuimalizia!” Hija alijitetea.

    “Nimpigie simu Amin nimwambie atafute mtu wa kumalizia hiyo kazi uliyoiacha?”

    Hija akakwama! Akakwepesha macho yake baada ya kugundua uongo wake umegundulika.

    Nico akamwangalia Hija usoni, akawa kama anaiona akili ya msichana huyo inavyohangaika.

    Kama aliyepumbazwa akili, Hija alijivuta taratibu hadi kwenye kiti na kukaa, akamwangalia Nico kwa macho ya mashaka.

    Nico alimwangalia Hija kisha akafanya tabasamu dogo. “Siku chache za nyuma ulikuwa ukiingia kwenye ofisi hii kwa kujiamini na kujidai,” alimwambia Hija. “Lakini angalia sasa ulivyo kwenye mazingira magumu uliyojiwekea. Unaonekana mnyonge, huna amani na siye yule Hija mcheshi mwenye bashasha.”

    Hija hakujibu!

    Nico aliichukua glasi yenye juisi kutoka kwenye tray iliyoletwa na Hija na kuiweka mbele ya msichana huyo. “Kunywa,” alimwambia Hija. “Mimi nitakunywa kahawa na vitafunio vingine ulivyoniletea.”

    Hija alitingisha kichwa kukataa. “Nitaenda kunywa canteen,” alisema.

    “Toka lini chai ya wafanyakazi ikawa na juisi?” Nico aliuliza kwa dharau.

    “Sijisikii kunywa juisi.”

    “Leo unaniogopa?”

    Hija hakujibu!

    Nico aliichukua glasi ile ya juisi na kupiga funda moja kisha akairudisha mezani. “Tuachane na hayo, kuna ya msingi nataka kuyaongelea,” alisema na kujiweka sawa kwenye kiti.

    Hija akaendelea kuwa kimya.

    “Umeamua ghafla kunipiga chini na kumchukua Badi! Mfanyakazi mwenzangu..? Haikupendeza!” Nico alisema, akatingisha kichwa. “Lakini ndio uamuzi wako, inabidi niuheshimu. Awali nafsi yangu ilikataa kulikubali hilo, nikafikia hatua ya kuwa na hasira na wewe. Nakiri nilikudhalilisha na halikuwa jambo jema. Lakini pia nilikaribia kugombana na Badi kwa ajili yako. Nikajiuliza kwa nini nigombane naye wakati yeye ndiye aliyechaguliwa? Naomba msamaha kwa yote niliyokufanyia, nataka amani itawale juu yetu. Nisamehe Hija!”

    Kimya kifupi kilipita kati yao. Kisha Hija akashusha pumzi za mara moja kama mtu aliyechoka. Akaendelea kuwa kimya.

    Nico alimwangalia Hija, kisha bila ya kutarajiwa, Hija naye akayainua macho yake kumwangalia Nico. Yakakutana. Mapigo ya moyo ya Nico yakaanza kupiga kwa kasi, akakiri kwamba alikuwa akimwangalia msichana mzuri mwenye mvuto. Akajikuta akitafuta kwa haraka neno la kuzungumza.

    “Umekubali kunisamehe?” Nico aliuliza.

    Hija hakujibu kwa haraka. Aliendelea kumwangalia Nico kama aliyekuwa akiisoma akili yake.

    “Nimekusamehe!” hatimaye Hija alisema kwa sauti ndogo iliyotoka vizuri kinywani mwake.

    “Nashukuru,” Nico alisema.

    Hija akainuka. “Nakwenda,” aliaga.

    “Nimefurahi ulivyonisamehe, nakuahidi sitokusumbua tena!”

    Hija akageuka na kuelekea mlangoni huku akiwa na uhakika macho ya Nico yalikuwa mgongoni kwake yakimwangalia huku akili yake ikimsukuma atoke haraka humo ofisini.

    Nico alimwangalia Hija alivyokuwa akiukaribia mlango, kisha akaunda tabasamu la kihalifu ambalo halikushuhudiwa na Hija!



    ***



    MENEJA Mkuu wa hoteli ambaye ni raia wa Canada alitoka na wageni wake aliokuwa nao ofisini, akawasindikiza hadi mlangoni na kuagana nao kwa kupeana mikono kisha akarudi ndani. Badi aliyekuwepo meza ya mapokezi alimwona meneja wake akiagana na wageni wake, mara tu baada ya kuagana nao, hakurudi ofisini, akaenda mapokezi.

    Badi aliyekuwa amekaa nyuma ya kaunta ya mapokezi akishughulika kikazi na kompyuta iliyokuwa mbele yake, akamwona meneja wake akija upande wa mapokezi. Akaacha shughuli aliyokuwa akiifanya na kusimama kwa lengo la kumpokea meneja wake.

    “Badi,” meneja alisema kuonyesha lengo lake lilikuwa ni kumwona Badi.

    “Yes Sir,” Badi aliitikia kwa nidhamu.

    “Unayo taarifa ya mabadiliko yanayohusu mali za thamani wanazohodhi wageni wetu wanaokaa hotelini?” Meneja alisema huku akiegemea kaunta.

    “Hapana Mkuu, sina!” Badi alijibu tena kwa nidhamu akiwa amesimama nyuma ya kaunta akimkabili meneja wake..

    “Kuna mwongozo mpya unaotarajiwa kutoka muda sio mrefu. Nimeitisha kikao cha dharura ofisini na viongozi husika, wewe ukiwa mmojawao. Kwa hiyo njoo ofisini!”

    Badi na meneja wake wakaongozana. Wakaingia kwenye korido yenye ofisi za utawala, wakaelekea ilipo ofisi ya Meneja Mkuu. Wakiwa hatua chache kuifikia ofisi hiyo, mlango wa ofisi ya Meneja Msaidizi wa Vyakula na Vinywaji uliokuwa mbele ya ofisi ya Meneja Mkuu ukafunguliwa, wote kwa pamoja wakamwangalia mtu aliyekuwa akitoka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa Hija!

    Macho ya Meneja Mkuu yakamwangalia Badi mara moja! Badi akakiona kitendo hicho! Utazamaji huo kutoka kwa Meneja Mkuu ukamthibitishia kuwa, alikuwa akiujua uhusiano uliopo kati yake na Hija! Lakini pia, kukadhihirisha kuwa, hata uhusiano unaovumishwa kuwepo kati ya Hija na Nico nao ulikuwa ukifahamika na meneja huyo!

    Tafakuri hiyo ikamchanganya Badi! Ilimchanganya kwa sababu tukio wanalolishuhudia lilikuwa likiwathibitishia kuwa, uhusiano uliopo kati ya Hija na Nico ulikuwa ukiendelea! Badi akajiona alikuwa akifanywa zoba na watu hao wawili!

    Tukio la kumwona Badi likamshtua Hija. Likawa kama shambulizi la ghafla asilolitarajia. Mhimili wa kujiamini ukapotea! Lakini pia akagundua kuwa mshtuko wake umeonekana na Badi. Hatia ikauvaa uso wake!

    Wote wawili wakaaangaliana bila ya kusemezana wakati Meneja Mkuu akiufungua mlango wa ofisi yake. Meneja akaingia na kufuatiwa na Badi aliyeonekana kuwa mnyonge ghafla. Hija akapita kimyakimya!

    Akiwa amechanganywa na hali hiyo baada ya kuyasoma mawazo ya Badi kuwa yangekuwa yanamtuhumu kwa kumwona kwake akitoka ofisini kwa Nico ambako aliamini Badi angekuchukulia kuwa alikwenda huko kwa masuala ya kimapenzi, Hija alijikuta akitamani angeiokoa hali hiyo palepale kwenye korido kwa kumwambia Badi kuwa, alikwenda ofisini kwa Nico kumpelekea breakfast yake kwa kuagizwa na mkuu wake wa kazi, Amin. Lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kuwepo kwa Meneja Mkuu eneo hilo.



    ***



    KIKAO cha dharura kilichoitishwa na Meneja Mkuu kilimalizika baada ya dakika ishirini. Badi alirudi eneo lake la kazi akiwa amechanganyikiwa. Hakikuwa kikao alichotoka ndicho kilichomchanganya, bali ni tukio la kumwona Hija akitoka ofisini kwa Nico! Ilikuwaje akaenda ofisini kwa Nico? fikra hizo ndizo zilizokuwa zikimsumbua. Alikumbuka Hija alivyomlia kiapo kuwa asingeweza kwenda ofisini kwa Nico labda kutokee jambo zito la kikazi, lakini hata kama lingejitokeza, Hija alimwahidi angemfahamisha mapema kabla ya kwenda! Alichoshuhudia ni kumwona Hija akitoka huko alikoapa kuwa asingeenda, lakini pia hakuwa alimtaarifu kama alivyoahidi!

    Kitendo hicho cha Hija kwenda kimyakimya ofisini kwa Nico kilimwumiza sana. Kilimwumiza kwa sababu aliuona uso wa Hija ukijengwa na hatia baada ya kumfumania akitoka humo. Badi aliamini, Hija alikuwa amefanya siri kwenda ofisini kwa Nico! Kwa maana nyingine, Hija hakutaka yeye ajue wakati alivyokwenda kuonana na Nico! Ndiyo maana kukutana kwao ghafla wakati akitoka ofisini kwa Nico kulimfanya Hija ashtuke na kutahayari! Kutokana na sababu hizo, Badi akahitimisha kuwa, pamoja na Hija kukanusha hakuwa kwenye uhusiano wa mapenzi na Nico, lakini tukio hilo likawa limemdhihirishia kuwa watu hao wawili walikuwa ni wapenzi na bado wana ushirikiano wa kimapenzi!

    Ukweli huo aliouhitimisha ulimwuma. Akaikumbuka kauli ya Hija wakati akikanusha kuwa hajawahi kutembea na Nico, kauli ambayo sasa aligundua ilikuwa ni ya uongo! Kugundua Hija alimdanganya kulimwumiza, hasa baada ya kuufikiria mgogoro aliouanzisha na Nico na kukaribia kupigana kwa ajili ya msichana huyo!

    Badi alishusha pumzi akiwa peke yake. Wivu ulimwumiza, ukamfanya ashindwe kuyatafakari yaliyotokana na kikao kilichofanyika. Akili iliyojawa na hasira ikamshauri aende kwa Nico akamwombe msamaha kwa rabsha iliyotokea kati yao.

    Akiwa anajishauri kwenda kumkabili Nico kumwomba msamaha, bila ya kutarajia, Badi akamwona Hija akitokeza. Palepale akajua anakuja kumwona yeye! Akajiuliza, aende akazungumze naye? Au amkaushie na kujifanya hamjui? Akili yake ikamtuma amkaushie, lakini uwezo wa kulitenda hilo ukawa utata! Hakujua kama ni mapenzi au ni ustaarabu, lakini moyo wake ulimshauri kuwa, haitokuwa vyema kumfanyia ukatili wa kumwaibisha kwa kuamua kumkaushia. Akakubali kwenda kumkabili huku akiendelea kuumia, akataka amsikilize anachotaka kusema!

    Badi akatoka nje ya kaunta, akamwona Hija akipunguza kasi ya mwendo baada ya macho yao kukutana. Zile bashasha walizokuwa wameamkanazo walipokuwa nyumbani hadi kuja kazini pamoja, zikawa hazipo nyusoni mwao.

    “Umenifuata mimi?” Badi aliuliza kwa sauti iliyodhihirisha kuanza kupoteza mhimili wa uvumilivu.

    “Nataka kuzungumza na wewe!” Hija alisema huku uso wake ukiwa makini na sauti yake haikuonyesha kubembeleza.





    Badi akamwangalia Hija. Wakati akimwangalia, kumbukumbu ya kumwona akitoka ofisini kwa Nico ikawa inajileta. Dalili za jazba zikawa mbioni kumjia!

    “Kwa nini tusionane baada ya kazi?” Badi alisema huku akiangalia saa yake.

    Kama vile hakuridhishwa na kauli ya Badi, Hija akaonekana kuwa mwenye hasira. Akasita kama mtu aliyezuiwa asiongee neno alilotaka kulizungumza.

    “Poa!” hatimaye Hija alisema kwa mkato na kugeuka, hapohapo akaondoka akimwacha Badi akiwa ameshangaa.

    Dalili za kutokuwepo maelewano kati yao zikawa ziko wazi!

    Mara baada ya Hija kuondoka kwa hasira, Badi aligeuka na kuangalia kaunta walipo wenzake. Akawaona wakimwangalia! Akatambua walikwishauona mchezo wote uliotokea kati yake na Hija!

    Hofu ya kuwa, baada ya muda mfupi taarifa za kutoelewana kati yake na Hija zingesambaa hotelini humo ikamwingia!



    Ingawa waliachana katika hali ya kutokuwa na maelewano kati yao, muda wa kazi ulipomalizika, Badi alimpigia simu Hija kumwambia wakutane kwenye gari.

    “Bwana basi!” Hija alisema kwenye simu.

    “Basi nini?”

    “Nilichotaka kukwambia, nimeamua iwe basi!”

    Badi akaingiwa na ubaridi wa ghafla huku akili yake ikiwaza kwa kasi. “Sawa!” alisema. “Lakini mimi nina maongezi ya kuongea na wewe!”

    “Nakusikiliza!”

    “Siyo kwenye simu!”

    “Kumbe wapi?”

    “Nataka kuonana na wewe!”

    “Sikiliza Badi,” Hija alisema kwa utulivu. “Nakijua unachotaka kukizungumza kwangu, lakini maadamu fikra zako zimeamua kufikiria hivyo basi endelea nazo!”

    “Unamaanisha nini?”

    “Namaanisha basi! Kila mmoja aendelee na ustaarabu wake!”

    Badi akapata mshtuko alioweza kuudhibiti. Akasema, “Sasa hivi uko wapi?”

    “Najiandaa kuondoka.”

    “Nakusubiri, niko parking,” Badi alisema na kukata simu.

    Mara tu baada ya kumaliza kazi, Badi alikwenda kwenye gari lake na kumsubiri Hija. Alisubiri kwa zaidi ya dakika ishirini bila ya kuziona dalili za Hija akitokea. Awali, aliamini ndani ya dakika kumi angekuwa amekwishawasili, lakini kuona ikikaribia nusu saa tokea asubiri bila ya kutokea kukaanza kuifanya akili yake ikose utulivu.

    Badi aliwaona karibu wafanyakazi wote wa kike walioingia zamu ya asubuhi kama alivyoingia Hija wakiwa wamekwishaondoka. Yuko wapi? alijiuliza huku akibadilisha mikao kwenye kiti alichokalia ndani ya gari. Ghafla akaingiwa na wazo lililomshtua. Au yuko ofisini kwa Nico ndiyo maana haonekani?

    Wazo hilo likamtia unyonge, akataka kuhakikisha kama mawazo yake yako sahihi. Palepale akamwazia Amin, akaamini huyo ndiye angeweza kumpatia habari za uhakika. Akiwa ameshaikamata simu kumpigia Amin, mara akamwona Hija akija kwa mwendo wa taratibu kama vile askari wa kike wa barabarani akilifuata gari alilolisimamisha!

    Akafika kwenye gari la Badi, akaufungua mlango wa mbele wa abiria, akaingia bila ya kusema lolote. Badi naye akaliwasha gari bila ya kutamka neno.

    Sura yake ikiwa haina furaha, Hija aliuliza, “Tunakwenda wapi?” sauti yake ilikuwa kavu.

    “Nyumbani,” Badi alijibu na kumwangalia Hija mara moja.

    “Nyumbani wapi?”

    “Kwangu!”

    “Niteremshe!”

    “Kwa nini?”

    “Nikafanye nini?”

    “Tukazungumze!”

    “Kuhusu nini?”

    Badi akakosa neno la kuweka wazi! Hakutaka kuonekana akilia wivu, lakini bado alikuwa na dukuduku la kutaka kulizungumzia tukio la kumwona akitoka ofisini kwa Nico. Akawa na mtihani wa neno lipi aanze nalo huku hisia za kusubiriwa na Hija atoe jibu zikimpa karaha.

    “Ilikuwaje ukaenda ofisini kwa Nico?” Badi aliuliza bila kuliandaa swali hilo.

    “Nilimpelekea breakfast aliyokuwa ameagiza!” Hija alijibu kwa kujiamini kama vile jibu hilo lilikuwa sehemu ya kumsuta Badi.

    “Kwa nini hukukataa?” sauti ya Badi ilipanda kidogo kama aliyeanza kupandwa na jazba. “Ungemwambia Amin kuwa huipeleki na ungempa sababu ya kutopeleka. Angekuelewa! Angepewa waiter au waitress mwingine!”

    “Yeye ndiye aliyeniagiza niipeleke!”

    “Nani? Amin?” Badi aliuliza kama hakuamini alichokisikia.

    “Ndiyo!” Hija alijibu kwa kiburi bila ya kumwangalia Badi.

    Badi akanywea. “Sawa,” alisema. “Lakini bado ungekuwa na sababu ya kukataa na yeye angekuelewa!”

    “Asingenielewa!”

    “Kwa nini?”

    “Nico ndiye aliyempa maagizo kuwa niipeleke mimi oda hiyo ofisini kwake!”

    “Eti nini?” sauti ya Badi ilitoka kwenye mhimili wa kujizuia.

    “Usipandwe na jazba,” Hija alisema kwa utulivu. “Nico alikuwa na sababu za kunitaka niende ofisini kwake.”

    Badi akanywea. “Unataka kuniambia nini?” aliuliza.

    “Alitaka niende ili kuniomba msamaha kwa yaliyotokea kati yangu na yake.”

    “Alikuomba?”

    “Ndiyo.”

    Kengele ya hadhari ikalia kichwani kwa Badi!

    “Anataka kukubugisha ili ubugi stepu!” Badi alionya.

    “Una maana gani?”

    “Anataka mrudiane!”

    “Kwani alikuwa bwana wangu?”

    Badi akanywea tena!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sikiliza Badi,” ikawa zamu ya Hija kutawala mazungumzo. “Nataka uelewe kuwa, Nico hajawahi kuwa bwana wangu na wala sina mpango aje awe bwana wangu. Nadhani hili nilikwishakueleza, lakini asubuhi nilikuona jinsi ulivyonuna baada ya kuniona nikitoka ofisini kwa Nico. Nikataka jambo hili nilimalize mapema ili nikueleze kilichojiri. Nikaamua kukufuata reception, lakini mwenzangu ulikuwa na hasira zako na ukaamua ulivyoamua. Kifupi ni kwamba, sikwenda mwenyewe! Kama huamini, wasiliana na Amim atakwambia!”

    Munkari uliokuwa ukimtawala Badi ukapungua baada ya kuambiwa awasiliane na Amin ili kuthibitisha.

    Yeye na Amin waliwahi kufanya kazi pamoja kwenye Idara ya Restaurant kila mmoja akiwa na cheo cha ‘Head Waiter’ kabla ya kuhamishwa kupelekwa Idara ya Mapokezi kuwa mkuu wa idara hiyo na wakati huohuo Amin akipandishwa cheo kuwa Mkuu wa Idara ya Restaurant. Pamoja na kuhamishwa idara, lakini urafiki wao wa kikazi ukaendelea na kuzidi kuheshimiana. Kauli ya Hija ya kumtaka awasiliane na Amin ikamjengea imani kuwa, laiti Hija angekuwa alijipeleka mwenyewe kwa Nico, kamwe asingemtaka awasiliane na Amin!

    Ukimya uliofanywa na Badi baada ya kuambiwa hivyo, ulimfanya Hija agundue jamaa amekosa hoja.

    “Badi,” Hija aliita kwa utulivu. “Nadhani unajua ninavyokupenda, lakini pia najua unavyonipenda. Nataka utambue, siwezi na sitoweza kutembea na wanaume wawili sehemu moja ya kazi! Nifanye hivyo kwa ajili ya kukuumiza au nifanye hivyo kwa ajili ya nini?” baada ya kuuliza hivyo Hija akasita kuendelea na kumwangalia Badi. Kisha akamalizia kwa kusema, “Naomba uniamini!”

    “Ulivyompelekea breakfast yake alikwambia nini?” Badi aliuliza na kuonyesha akili yake bado ilikuwa ofisini kwa Nico.

    “Aliniomba msamaha.”

    “Ulishaniambia alikuomba msamaha, alikwambia kitu gani?”

    “Unamaanisha maneno aliyotamka ya kuniomba msamaha?”

    “Ndiyo!” Badi aliitikia kwa kusisitiza.

    Hija akafanya tabasamu fupi la kuusanifu wivu wa Badi. Akamwelezea jinsi Nico alivyomwambia.

    “Na umemwamini?”

    “Sasa unadhani ningefanya nini? Nimwambie kuwa sikuamini? Halafu iweje?”

    Badi hakujibu!

    “Nakupenda Badi,” Hija aliirudia tena kauli hiyo lakini safari hii aliitamka kwa Kiingereza. “Nakupenda kuliko unavyonipenda!”

    “Mimi?” Badi aliuliza kwa mshtuko kujaribu kuonyesha ni namna gani Hija anavyokosea katika hilo. Kisha akasikitika. “Sijui nikufanyie nini ili ujue nakupenda kuliko unavyonipenda!” alisema.

    “Kwa hiyo tushindane ili tujue nani anayempenda zaidi mwenzake?”

    Kwa mara ya kwanza tokea wawemo kwenye gari, Badi alitabasamu.

    “Tupinge?” Badi aliuliza.

    Hija akakinyoosha kidole chake cha mwisho kukielekeza alipo Badi bila ya kutamka lolote. Badi naye akakipeleka chake, wakavifunganisha kuonyesha upinzani.

    “Kata!” Hija alimwambia Badi.

    “Kata wewe, mimi naendesha gari!” Badi alijibu.

    Hija akakata kwa kutumia kiganja cha mkono mwingine kuvitenganisha vidole vyao. Kisha wote wakatabasamu kama wanaoshangilia utani wao. Macho yao yakazungumza kuonyesha furaha ya mwafaka waliofikia.



    ***





    NICO alimpigia simu mmoja wa ndugu zake wenye nasaba za kiukoo, lakini pia waliwahi kusoma pamoja kwenye shule ya sekondari kutoka kidato cha kwanza hadi cha pili. Ndugu yake huyo anayeitwa Chaza, alikuwa mtundu na nunda shuleni ingawa alitoka kwenye familia yenye kujiweza. Ununda wake ulimsababisha afukuzwe shule baada ya kukamatwa chooni akimlawiti mwanafunzi mwenzake wa kiume. Ingawa alifukuzwa, lakini kutokana na uwezo wa kifedha wa wazazi wake aliweza kuendelea na masomo kwenye shule nyingine ambako alimaliza kidato cha nne akiwa amepata alama ya sifuri.

    Chaza akawa kama kansa kwenye familia yake na kuonekana kushindikana kimalezi. Akafukuzwa nyumbani kwao! Ingawa hakuwa anatumia dawa za kulevya za kubwia na kujidunga kama cocaine na nyinginezo, lakini alivuta bangi. Alijuana na magenge ya kihuni huku akiingia kwenye biashara ya kununua na kuuza simu zilizokuwa zikiibwa na vibaka waliozagaa kwenye vituo vya daladala au kwengineko.

    Kumkumbuka ndugu yake mwenye sifa za aina hiyo, kulimfanya Nico apate wazo la kumtumia ndugu yake huyo kulipizia kisasi chake kwa Badi! Akaanza juhudi za kumtafuta, hatimaye akaipata namba yake ya simu. Ndipo alipompigia! Akajitambulisha baada ya kumpata.

    “Mjomba!” Chaza aliongea kwa sauti ya juu kutoka upande wa pili wa simu. “Leo umekumbuka nini hadi kunipigia mjomba?”

    “Nataka tuonane mjomba, kuna dili nataka nikupe!” Nico alisema.

    “Dili?”

    “Ndiyo mjomba, wapi naweza kukupata?”

    “Tinga maeneo ya Kinondoni Studio. We’ ukija nitwangie.”

    “Basi sawa mjomba, ndani ya siku mbili hizi nitakuja.”

    “Afya mjomba!”

    Nico alikata simu na kutabasamu peke yake. Akaiweka simu juu ya meza yake iliyopo ofisini, kisha akajizungusha kwenye kiti na kujihisi kupiga mruzi ingawa hakufanya hivyo. Alijizungusha na kuipa mgongo meza yake, akawa ameligeukia dirisha lililokuwa likitazama nje ambako kulikuwa na bustani kubwa nzuri iliyokaa mfano wa uwanja wa kuchezea gofu huku mbudu za kijani zilizokatwa vizuri na kunawirishwa na miti midogo ya maua zikisambaa na kuufanya uwanda huo uwe mandhari ya aina yake. Katikati ya uwanja huo wa bustani kulikuwa na mpira wa maji uliokuwa ukimwaga maji yanayochezeshwa na kiwambo cha kumwagia kilichokuwa kikiyatawanya maji hayo.

    Kwa dakika kadhaa, macho ya Nico yalitulia kuyaangalia maji yaliyokuwa yakijimwaga kwenye mbudu kana kwamba hicho alichokuwa akikiangalia ndicho alichokuwa akikiwazia. Kadri alivyokuwa akiendelea kuangalia, ndivyo alivyokuwa akiufikiria unyama ambao angependa Badi afanyiwe!



    ***

    ILIKUWA asubuhi baada ya siku mbili kupita, Nico aliwasili eneo la Kinondoni Studio akiwa na gari lake. Akiwa anawasiliana na Chaza kwenye simu, akaelekezwa wapi pa kukutania. Akayafuata maagizo aliyopewa, akamkuta Chaza amesimama kwenye kibanda kinachouza chips akimsubiri. Akalisimamisha gari mbele ya kibanda hicho. Chaza akalifuata.

    “Kuna mtu kanifanyizia, nataka ukamfanyizie!” Nico alimwambia Chaza aliyekuwa amekaa kando yake kwenye kiti cha abiria.

    “Kakudhulumu?” Chaza aliyekuwa amevaa kapero iliyoandikwa NY aliuliza kwa utulivu.

    Nico akasita. Ni kweli alidhulumiwa na Badi kwa kunyang’anywa Hija, lakini alifahamu hilo silo lililomaanishwa na Chaza katika msingi wa swali lake. Chaza alilenga masuala ya kipesa na si mapenzi. Kukiri kuwa amenyang’anywa mwanamke na mwanamume mwenzake ndicho kilichomleta hapo, kungemfanya aonekane fala!

    “Ndiyo amenidhulumu!” Nico alijibu bila ya kufafanua.

    “Amekudhulumu nini?”

    “Sio lazima kujua, lakini uelewe mtu huyu amenidhulumu!”

    “Unataka akafanywe nini?”

    “Kipigo!”

    Chaza akageuka na kumwangalia Nico. “Basi?” aliuliza.

    Nico alivuta pumzi na kuishusha, akaonekana kusita. “Nataka iwe zaidi ya hapo!” hatimaye alisema.

    “Kama?”

    “Nataka apate kichapo mbele ya bibi yake na ikiwezekana…” Nico akasita tena.

    Chaza akavutiwa na kilichositishwa kuzungumzwa. Akamwangalia Nico kwa shauku ili amalizie alichotaka kukizungumza. Akasubiri akiwa kimya huku akiendelea kumwangalia Nico.

    Nico aligeuka kumwangalia Chaza, macho yao yakagongana. “Lakini basi!” alisema.

    “Kwa hiyo umeamua kutomfanyizia?”

    “Sina maana hiyo!”

    “Mjomba unanichanganya! Mbona huwi wazi?”

    “Nataka mumfanyizie!” Nico alisema kwa haraka. “Lakini…” akasita tena.

    Chaza akamwangalia Nico kwa mshangao. Akapiga kite. “Unanitundika mjomba, nashindwa kukusoma!” alilalamika.

    “Nilitaka…ikiwezekana mmwingilie!” Badi alisema kwa kusita.

    “Bibi yake?”

    “Hapana! Yeye mwenyewe baada ya kumpa kichapo!”

    Chaza akatulia na kumwangalia Nico. Nico naye akamwangalia Chaza huku akihisi shida yake imekwishaeleweka.

    “Siyo wakora wote wanaofanya mambo hayo mjomba!” Chaza alijibu kwa utulivu.

    “Lakini wapo?”

    “Wanaopatikana kirahisi kwa mambo hayo ni vibaka, na vibaka huwezi kuwatumia kwa kazi za suluba za kutoa kichapo kwa mtu. Wao wenyewe unga umewachokesha, uwezo wa kumpa mtu kichapo na kisha wamalizie kwa hayo unayoyataka watautoa wapi? Labda nimuunganishe mmoja awe kwa ajili ya kusubiri kuifanya shughuli hiyo unayoitaka.”

    “Muunganishe!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwani amekudhulumu kiasi gani mjomba mpaka ufike huko?”

    “Hayo niachie mwenyewe, mi’ n’nachotaka akafanyiziwe!”

    “Utatoa shilingi ngapi?”

    “Nina laki tatu!”

    “Hizo ndogo mjomba, siwezi kutuma watu kwa shughuli hiyo kwa kuwapa shilingi laki tatu.”

    “Mjomba fanya kama unanisaidia,” Nico alilalamika.

    “Najua mjomba, lakini shughuli siendi kuifanya mimi. Kuna watu maalum ambao wapo tayari kuifanya kazi hii mradi ukiwapa pesa inayotakata.”

    “Kwa hiyo kama kiasi gani?”

    Chaza hakujibu haraka. Baada ya kutumia sekunde kadhaa za kufikiri, hatimaye akasema, “Wacha kwanza nikaonane nao na kuwatangazia zabuni, wakiikubali na kuniambia kiasi wanachotaka, basi hapo ndipo tutakapoizungumza biashara mimi na wewe.”

    “Utakapokwenda kuwaona, epuka kunitaja wala kutaja jina langu au uhusiano wetu. Umenielewa?”

    “Mbona sana tu, mjomba.”

    “Unadhani mpaka lini utakuwa umeshaonana nao?”

    “Nipe leo na kesho, mambo yakiwa mswano, nitakupigia simu.”

    “Poa mjomba,” Nico alisema na kuliwasha gari.





    “Niachie basi ya kushtua japo supu,” Chaza alisema akiwa ameufungua mlango wa gari.

    Nico akatoa noti ya shilingi elfu kumi na kumpa.

    Wakaagana.



    ***



    SIKU ya pili asubuhi kukawa bado hakuna mawasiliano yaliyofanywa na Chaza, lakini Nico akawa na uhakika angepigiwa hata baadaye siku hiyo. Akiwa kazini asubuhi hiyo, Nico alifuatilia kama Badi angekuwepo kazini. Akagundua yupo. Akamtuma mmoja wa wafanyakazi amwitie.

    Akiwa ofisini kwake, Nico aliusikia mlango ukigongwa. Hakuwa na uhakika angekuwa ni nani kutokana na asubuhi kuwa na shughuli nyingi za kiofisi zinazowafanya wafanyakazi wengi waje kumwona kwa masuala ya kikazi, lakini bado alibuni huenda anayegonga ni Badi.

    “Karibuu,” Nico alisema kwa kuvuta maneno kama sehemu ya majivuno yake.

    Mlango ulifunguliwa, Badi akaingia.

    “Karibu Badi,” Nico alisema akiwa amelilaza bega lake kuegemea upande mmoja wa kiti alichokalia huku mguu wake ameupandisha juu ya mwingine. Alikuwa akiyumba na kiti.

    Badi aliingia na kusimama mbele ya meza. “Nimefahamishwa unaniita,” alisema huku akiwa makini kumwangalia Nico usoni.

    “Karibu kiti,” Nico alisema na kujiweka vizuri kwenye kiti na kuushusha mguu alioupandisha juu mwingine. Akaacha kuyumbayumba wakati Badi akikaa kwenye kiti kilichopo mbele ya meza.

    “Nimekuita Badi,” Nico alisema. “Lengo ni kutaka kukuomba msamaha, ingawa naamini sikuwa na ugomvi na wewe.”

    “Sasa msamaha wa nini wakati hukuwa na ugomvi na mimi?” Badi alisema akiwa makini usoni.

    “Tumegombana kwa ajili ya Hija, umekuja ofisini na kunikunja, ukanikanya nisimfuatefuate Hija. Au sivyo hivyo?”

    Badi alijiona kutokuwa mwepesi kuikubali hoja hiyo. Hakujibu!

    “Eti Badi?” Nico alikumbushia. “Haikuwa hivyo?”

    “Ndiyo ilikuwa hivyo,” Badi alikubali bila ya kumwangalia Nico machoni.

    “Nimekubali niachane na Hija, ingawa imeniuma!” Nico alisema. “Naamini hata ingekuwa wewe ingekuumiza! Nimeamua, simhitaji tena Hija kama yeye asivyonihitaji! Kwa hiyo nataka uwe huru. Moyo wangu hauna kinyongo na wewe na ndiyo sababu ya kukuita na kukuomba msamaha. Kama ulikuwa na kinyongo na mimi nakuomba ukiondoe ili uhusiano wetu urudi kama awali. Nataka tufanye kazi bila ya misuguano. Hilo ndilo nililokuitia!”

    Badi alitulia kimya, kisha aliuinua mkono wake na kumpa Nico ambaye aliupokea.

    “Yamekwisha!” Badi alisema huku akiwa bado ameushika mkono wa Nico.

    “Nashukuru kwa kunielewa,” Nico alisema.

    Badi akainuka, akaaga.

    Nico naye alisimama na kumpa tena mkono Badi. Wakaagana.

    Badi akaondoka kuelekea mlangoni huku akiangaliwa na Nico aliyekuwa akirudia kukaa kwenye kiti chake. Wakati Badi akiufungua mlango na kutoka bila ya kugeuka nyuma kumwangalia Nico, Nico aliendelea kumwangalia Badi huku akili yake ikimfikiria Chaza!

    Kabla fikra zake hazijampoteza Chaza na ikiwa zimepita kama dakika tano tokea Badi alivyotoka ofisini kwake, Chaza akampigia simu!

    “Ndiyo mjomba,” Nico alisema baada ya kuipokea simu ya Chaza.

    “Wanataka ‘M’ na nusu!” Chaza alisema.

    “Una maana milioni?”

    “Usiulize majibu mjomba, fuatilia matokeo!”

    “Milioni moja na nusu nyingi!”

    “Kazi yenyewe nzito mjomba, mbona kung’ang’aniwa kuko nje-nje!”

    “Nataka kazi ifanyike bila ya mtu kukamatwa!” Nico alisihi.

    “Ndiyo sababu ya kutaka ‘M’ na nusu!”

    “Sina uwezo huo.”

    “Unataka kutoa ngapi?”

    “Laki tano. Tatu kabla ya kazi, mbili baada ya kazi.”

    “Uko serious na hii shughuli?”

    “Ndiyo!”

    “Basi nitawabembeleza kwa ‘M’ moja kwa sababu ni washikaji zangu.”

    “Wabembeleze kwa laki tano.”

    “Basi mjomba tuue biashara!”

    Jibu hilo likamshtua Nico. “Sasa biashara itakufaje mjomba?” alilalamika.

    “Kama upo tayari kwa milioni, tuongee biashara!”

    “Sawa mjomba, nimekubali hiyo milioni,” hatimaye Nico alisalimu amri.

    “Watamjuaje?”

    “Nitakapoleta awamu ya kwanza shilingi laki tano, nitakupa maelekezo ya kupatikana kwake huyo mtu.”

    “Unataka kazi ifanyike lini?”

    “Jibu hilo nitakujanalo.”

    “Lini?”

    “Nipe kama siku nne, sasa hivi kidogo kazi zimenibana.”

    “Poa mjomba.”



    ***



    BADI alimwelezea Hija tukio la kuitwa kwake na Nico na kuombwa msamaha. Kujua kuwa Nico amesalimu amri kuliwafanya wacheke walipokuwa wakimzungumza.

    Kusalimiana kwa Badi na Nico kukarudia kama kawaida. Ingawa hawakuwa na maongezi ya kuongea kati yao zaidi ya mambo ya kazi, lakini ile hali ya kuwepo kiwingu cha chuki kati yao ikapotea huku mmoja akiwa ameiondoa kwa dhati na mwingine akifanya maigizo kwa ajili ya kusubiri muda maalum ufike.

    Hali hiyo iliwafanya Badi na Hija wajione wako huru wanapokuwa kazini ndani ya wiki hiyo na wakati mwingine Nico alikuwa akiwakuta wakiwa pamoja kwenye vipenyo vya maeneo ya kazini. Kwenye maeneo kama hayo, Nico alikuwa akikenua meno kuonyesha hakuwa na kinyongo nao tena!

    Uhusiano wa Badi na Hija ukamjenga Hija kwenye mazoea ya kila anapokuwa yupo nyumbani kwa Badi pale inapokuwa mdogo wake Badi hayupo, alijijengea mazoea ya kuvaa mashati ya Badi hasa ya mikono mirefu yaliyokuwa yakimpwaya, akiyavaa akiwa na chupi tu na wakati mwingine kupika jikoni akiwa kwenye mavazi hayo.

    Uvaaji huo ulimkonga sana Badi kwa sababu alikuwa akilifurahia kuliona umbo la Hija likiwa ndani ya shati lake na wakati mwingine kunogeshwa na jinsi matiti yake yalivyokuwa huru kutingishika wakati akitembea. Akiwa ndani ya vazi hilo la shati na chupi, Hija alijua kucheza na akili ya Badi. Kuna wakati alikurupuka ghafla na kumrukia Badi au kwenda kumkalia akiwa amekaa kwenye kochi na kujilaza kwa kuegemeza kichwa kwenye mapaja na kuanza kutomasana. Matukio ya aina hiyo wakati mwingine yalikuwa yakiwaletea ashki na kumalizia kwa kufanya mapenzi kwa eneo watakalokuwa.

    Wakati wawili hao wakizidi kuyaborosha mapenzi yao kwa vionjo tofauti, Nico alikwenda kuonana na Chaza kama alivyokuwa ameahidi. Akalipa shilingi laki tano yakiwa ni malipo ya awali, lakini pia akamkabidhi Chaza picha ya Badi ili amjue. Akamtaka afike hotelini ili aweze kumwona kwa macho yake. Akampa maagizo ya kumwezesha kumtambua kumwona Badi atakapokuwa amefika hotelini.

    Nico akamkumbushia Chaza onyo alilompa, kuwa wasijuane na wala asithubutu kulitaja jina lake kwa sababu yoyote itakayojitokeza pindi atakapofika hotelini!



    ***



    CHAZA alifika hotelini akiwa amevaa kinadhifu, shati la mikono mifupi lenye rangi ya krimu na tai ya pundamilia. Suruali aliyovaa ilikuwa ya kijivu na viatu vinavyong’ara. Wakati akiwa amesimama nyuma ya kaunta ya mapokezi, akabahatika kupokewa na Badi mwenyewe. Kupokewa na Badi na maelekezo aliyopewa, akawa ana hakika anayezungumza naye ndiye mlengwa wao!

    “Kuna marafiki zangu kutoka nje ya nchi wanatarajia kuja nchini kwa muda wa wiki moja, nataka kujua bei zenu za vyumba,” Chaza alimwambia Badi huku akiwa makini kumwangalia usoni, lakini pia alikuwa akifurahia kuiangalia sura aliyokuwa akiiona kwenye picha muda mfupi uliopita alipokuwa akiiangalia kwa mara ya mwisho kabla ya kufika hapo hotelini.

    Badi alijibu maswali ya Chaza na kumwonyesha viwango vya bei ya vyumba na huduma nyinginezo za ziada. Chaza alishukuru na kuondoka. Saa moja baadaye akampigia simu Nico na kumfahamisha kuwa, alishakuwepo hotelini na ameiona vizuri sura ya Badi!

    “Sasa tunataka kujua anapoishi!” Chaza alimwambia Nico kwenye simu.

    Nico akazitaja namba za gari la Badi. “Mkimtegea njiani na kuliandama gari lake, mtapajua kwake!” alisema.

    “Subiri matokeo!” Chaza alisema.

    “Hakikisheni mnafanya mambo kwa mpangilio, asikamatwe mtu!”

    “Usiwe na shaka nalo.”

    Kazi ya kujua anapoishi Badi ilifanyika siku ya pili alasiri wakati Hija na Badi wakiwa wamemaliza kazi na kuondoka na gari lao. Wakaelekea moja kwa moja hadi Tegeta nyumbani kwa Badi. Hadi wanawasili nyumbani, si Badi wala Hija aliyediriki kuitilia shaka pikipiki iliyokuwa nyuma yao ikiwafuata!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwendesha pikipiki aliyeonekana kama dereva wa bodaboda alilipita gari la Badi baada ya kusimama nyumbani kwake na kuliangalia mara moja gari hilo kisha akaendelea na safari yake. Alipofika mbele kiasi cha mita zisizopungua hamsini, akageuza na kurudi tena. Alipoifikia nyumba ya Badi akaiona gari aliyokuwa akiifuatia ikiingia ndani ya geti. Akapata uhakika hapo ndipo anapoishi Badi!

    Kabla ya kulifuata gari la Badi na kulifungia mkia, dereva wa pikipiki akiwa na Chaza walikuwa wametegesha mtego wa kulisubiri gari hilo wakiwa jirani na hoteli anayofanya kazi Badi. Walipoliona gari hilo likitoka kwenye eneo la maegesho ya magari, Chaza alianza kuhakikisha kama mwendeshaji wa gari hilo ni Badi mwenyewe. Akamwona, lakini kando yake kukiwa na mwanamke! Chaza akampa ishara mwenzake mwenye pikipiki kuwa aanze kulifuata gari hilo!

    Saa chache baada ya kumalizika kazi ya kulifuatia gari hilo, Chaza alimpigia simu Nico.

    “Lini unataka tukufanyie kazi yako?” Chaza aliuliza baada ya kumpata Nico.

    “Kila kitu kipo kwenye mikono yenu, ninachosubiri ni matokeo.”

    “Utayapata hivi karibuni!” Chaza alisema na kukata simu.



    8



    “NINA mwaliko,” Hija alimwambia Badi wakati wakinywa supu asubuhi kwenye baa iliyokuwa mita kadhaa kutoka nyumbani kwa Badi. Wote wawili asubuhi hiyo walikuwa hawakwenda kazini.

    “Kutoka wapi?” Badi aliuliza bila ya kuonyesha msisitizo.

    “Mwaliko wa Uzinduzi wa aina mpya ya huduma ya mtandao wa simu za mkononi utakaoandamana na chakula cha jioni.”

    “Wapi?”

    “Hoteli ya Wind’s. Kutakuwepo na baadhi ya vigogo wa serikali.”

    “Ilikuwaje ukaalikwa?”

    “Alialikwa baba, hatokwenda. Amenipa mimi mwaliko huo kama nitapenda niende.”

    “Utakwenda?”

    “Tutakwenda!” Hija alisema kwa kusisitiza.

    “Na nani?”

    “Wewe!”

    “Saa ngapi?”

    “Saa moja jioni.”



    *

    Hoteli ya Wind’s yenye ghorofa nane iko Masaki. Haikuwa ufukoni, lakini ilikuwa karibu na bahari. Eneo lake la mbele ndilo lilionekana kwa uwazi na kuiweka taswira ya hoteli hiyo huku vyumba vilivyopo ghorofani upande wa Mashariki vikitoa nafasi kubwa kwa wapangaji wa vyumba hivyo kuiangalia bahari kwa uwanda mpana na kuufurahia upepo wake wakiwa wamekaa kwenye vibaraza vya nje vya vyumba hivyo.

    Hija na Badi hawakuwa wapangaji wa hoteli hiyo, lakini walifurahia uwepo wao katika mwaliko huo. Badi alikuwa amevaa koti na shati vyote vikiwa na rangi nyeupe inayong’aa kama theluji, lakini suruali yake ilikuwa nyeusi kama ilivyokuwa kwa viatu vyake ambavyo viling’aa. Kola ya shati lake ilikuwa maalum kwa ajili ya kufunga tai ya kipepeo mahsusi kwa hafla za chakula cha jioni. Tai aliyokuwa ameivaa usiku huo ilikuwa nyeusi.

    Hija alikuwa amevaa vazi la usiku lenye ushawishi wa kimahaba umtazamapo, likamjengea taswira ya kuwa naye kitandani. Lilikuwa gauni refu jeusi lenye kitambaa laini lililokaa sambamba na umbile la Hija hasa kwenye eneo la makalio na kuonyesha mwonekano wa mbali wa mchoro wa chupi yake aliyovaa. Kitamba cha gauni lake kilitawaliwa na vidoti vinavyomeremeta. Eneo la mgongoni lilikuwa wazi na kuufanya mgongo wake unaonyiritika kwa ulani wa ngozi yake ulete mvuto kwa mwonekano wa mfereji wa uti wake wa mgongo na kufichwa na gauni hilo ukiwa umekaribia sehemu za makalio. Lilikuwa ni vazi lililoleta tafrani za kishawishi za kimahaba. Lilikuwa vazi lililomfanya aonekane alijipamba, alijikwatua, akajirembesha na akapendeza!

    Ukumbi uliokuwa na hewa ya kiyoyozi ulianza kujaza watu wenye kujiona ni waungwana na wastaarabu. Wengi wa wanaume walikuwa kwenye vazi la suti na wanawake walikuwa wakishindana kwa kuivalisha miili yao nguo za gharama za kutisha na vito vya thamani huku kila mmoja akijitahidi maumbile yake yaonekane vizuri kutokana na vazi alilovaa.

    Vicheko vyenye haiba za kupendeza vilinawiri kila kona hasa kutoka kwa wanaume huku sauti zenye furaha za kufurahia mafanikio ya kuyapatia maisha yao zikitawala kwa ngurumo na wengine kutukuza maringo yao kwa kuzungumza Kiingereza. Ulikuwa mkusanyiko wa wima huku kila mmoja akiwa amekamata glasi yenye kinywaji kwa mkono mmoja na mkono mwingine ukiwa ndani ya mfuko wa suruali.

    Ukumbi ulioandaliwa hafla hiyo nao ulipendeza. Meza kubwa za kulia chakula za duara zilizofunikwa na vitambaa vyeupe zilizungukwa na viti ambavyo navyo vilivishwa vitambaa vyeupe. Juu ya kila meza kulikuwa na jozi nane za nyenzo za kunywea na kulia chakula kama vile visu, uma na vijiko vyenye rangi ya fedha inayong’aa hasa vikipigwa na nuru ya miali taa, vyote vikiwa na chuma isiyoingia kutu.





    Glasi zilizokuwa juu ya meza ziling’aa kwa usafi usiokuwa na doa hata moja. Kulikuwepo na glasi za kunywea maji au bia, mvinyo mweupe au mwekundu huku zikitofautiana kwa maumbo. Kwenye kuta za ukumbi huo kulipambwa na vipeperushi vyenye maandishi makubwa yenye kunadi huduma mpya inayotarajiwa kuzinduliwa usiku huo. Eneo hilo likaonekana ni maalum kwa watu maalum.

    Badi na Hija walikuwa sambamba wakati wote huku wakiwa na vinywaji vyao mikononi. Badi alikuwa na glasi iliyokuwa na pombe ya whisky iliyotumbukizwa barafu wakati Hija alikuwa amekamata glasi ndefu nyembamba yenye mvinyo mweupe. Ndani ya hafla hiyo walikuwepo baadhi ya viongozi wa serikali na mashirika tofauti. Ikawa ni fursa za waliohudhuria kupeana mikono kwa kusalimiana na wengine kujitambulisha.

    Ghafla akatokea mtu mmoja mwanamume aliyeonekana kujuana na Hija, wakasalimiana kwa kutajana majina. Lakini kabla ya Hija kutoa utambulisho kumtambulisha Badi, mtu huyo akawahi…

    “Vipi Badi, habari za jioni?” mtu huyo alisema.

    “Nzuri, za jioni na wewe?” Badi alijibu huku akili yake ikitatizwa kwa kuitwa jina lake na mtu huyo kama vile walikuwa wakifahamiana!

    “Amelijuaje jina langu?” Badi alimwuliza Hija baada ya mtu huyo kuondoka.

    “Nilimwambia,” Hija alijibu na kutabasamu.

    “Sidhani kama nilikusikia ukimjulisha jina langu wakati ukiongea naye.”

    “Nilimfahamisha karibu wiki moja nyuma. Aliwahi kutuona kama mara mbili tukiwa pamoja. Siku tulipokutana akaniuliza, nikamwambia jina lako.”

    “Kulikuwa na sababu ya kumtajia jina langu?”

    “Nilimwambia wewe ni mchumba wangu!”

    Ilikuwa ni mara ya kwanza Badi kumsikia Hija akijitanabaisha kwa utambulisho huo kuwa ni mchumba wake. Moyo wake ukachanuka kwa furaha!

    “Yeye ni nani kwako?” Badi alimuuliza Hija.

    “Family friend. Anajuana sana na mama, ndiyo maana umesikia tukiitana mjomba. Mara kwa mara huwa anakuja nyumbani.”

    “Na yeye amealikwa?”

    “Ninachojua, yeye ni dereva wa Waziri wa Mambo ya Nje, lakini nimemwona Naibu Waziri wa wizara hiyo, sina uhakika kama ndiye aliyekuja naye.”

    “Hata kama amekuja naye, inakuwaje awemo humu? Anatakiwa awepo nje kwenye gari.”

    “Nadhani hilo halipo kwenye uwezo wangu kulijibu,” Hija alijibu huku akigundua Badi hakupendezwa na mtu huyo.

    Badi akaangalia upande alikoelekea jamaa huyo, kisha asiendelee na suala lake.

    Mlio wa glasi inayogongwa ulisikika. Kimya cha ghafla kikajitengeneza humo ndani baada ya watu wote kuacha kuzungumza na kumwangalia mtu aliyekuwa akiigonga glasi. Alikuwa mshereheshaji wa hafla hiyo.

    “Wageni waalikwa mnakaribishwa mwende kwenye meza zenu!” mshereheshaji alisema.

    Mlolongo wa sherehe za uzinduzi ukawa umeanza rasmi.



    ***



    SAA sita na ushei usiku, jirani na nyumba ya Badi kulikuwa na watu wanne wakiwa na pikipiki mbili. Wawili kati yao walianza mapema doria za kuivinjari nyumba ya Badi. Ilipokaribia saa moja usiku wakamwona Badi akiwa na mwanamke wakitoka na gari. Wakaanza kulifuatilia kwa uangalifu huku wakiwa makini wasitambulike kuwa walikuwa wakilifuata gari hilo. Hatimaye wakawasili Hoteli ya Wind’s na kuwaona Badi na Hija wakiteremka na kuingia hotelini humo.

    Doria yao ya kwanza usiku huo ikawa imeanzia hapo baada ya kutambua kulikuwa na hafla maalum iliyokuwa ikiendelea hotelini humo na kuhisi hata Badi alifika hapo kwa ajili ya hafla hiyo. Wakawasiliana na wenzao wengine wawili waliokuwa tayari wako maeneo ya Tegeta ambao nao pia walikuwa na pikipiki.

    Ilipofika saa sita na nusu, watu wawili wanaomfuatilia Badi, wakawaona watu wenye uvaaji wa kinadhifu wakianza kutoka hotelini na kwenda kwenye magari yao. Taswira hiyo ikawajulisha kuwa, hafla iliyokuwepo hotelini humo ama imekwisha au ipo ukingoni kumalizika. Wakaamini, Badi naye angekuwa yuko njiani kutoka.

    Utambuzi huo ukawafanya wasiendelee kuwepo maeneo hayo. Wakawajulisha wenzao waliopo Tegeta wajiandae kurudi maeneo ya nyumbani kwa Badi. Wao nao wakaamua kutosubiri hadi wamwone Badi akitoka hotelini, wakawahi kurudi Tegeta kuungana na wenzao kwa ajili ya kumsubiri rasmi Badi arudi!

    Saa saba na robo mwanga wa taa za gari lililokuwa likipunguza kasi kadri lilivyokuwa likikaribia kwenye nyumba ya Badi likaonekana. Watu waliokuwa wakimsubiri Badi, wakalitambua gari linalokuja ni la Badi. Wakapeana ishara kuwa makini nalo.

    Badi aliwasili na gari lake akiwa na Hija, akalisimamisha nje ya geti. Aliteremka na kuliacha gari kwenye ngurumo ya injini inayozunguka ili Hija aendelee kupata hewa ya kiyoyozi. Akaelekea kwenye geti dogo kwa ajili ya kufungua na kuingia ndani kisha afungue geti kubwa na ndipo angerudi kuliingiza gari.

    Akiwa tayari amelifungua geti kubwa, Badi alirudi kulifuata gari lake, ndipo akashtuka kuwaona vijana wanne waliojigawa mara mbili. Wawili walikuwa ubavuni mwa gari na wengine wawili wakiwa ubavu wa pili wa gari. Wote kwa pamoja walikuwa wakimjia kwa mbele! Palepale akatambua amevamiwa na majambazi!

    Badi akawa makini kuwaangalia watu hao. Akavutiwa na mmojawao aliyekuwa ametangulia kumjia kwa mbele. Huyo alionekana kama ‘teja’. Moja kwa moja Badi akaamua aanze na mtu huyo ambaye alijua ni dhaifu.

    “Hija usitoke!” Badi alionya kwa sauti kubwa ili aweze kusikika na Hija kutokana na gari kufungwa vioo, kisha akamkabili yule aliyemwona ni teja.

    Kijana aliyeonekana ni teja alipomwona Badi akimwendea kwa kasi, akasita kwenda mbele zaidi. Uso wake ukajenga woga, akataka kurudi nyuma. Mwenzake aliyekuwa nyuma akamsukuma kwa mbele na kuishia kwenye mikono ya Badi ambaye alifanya uamuzi wa haraka wa kutupa ngumi iliyodhamiria kuua kama ingekuwa na nguvu hizo. Ikatua usoni kwa yule kijana, sambamba na ngumi hiyo kumpiga, yule kijana akatoa mlio wa kuguna wakati akijibamiza na ukuta kutokana na nguvu ya ngumi iliyompiga na kumsukuma. Badi akaanza kukabiliana na mtu aliyekuwa nyuma ya yule kijana!

    Mtu yule kumwona mwenzake amepata kipigo cha mara moja kilichoshindwa kumwinua tena, akajihami kwa kutoa kisu alichokificha kiunoni. Palepale Badi akaruka na teke aliloliinua juu na kulisukumiza kifuani kwa mtu huyo. Mtu huyo akajaribu kulikinga teke hilo kwa mikono yake, akachelewa. Teke likamwingia kifuani na kumsukuma kinyumenyume, akaanguka chali!

    Badi akageuka haraka kuwaangalia watu wengine wawili waliokwisha izunguka gari na kuwa nyuma yake. Wote wawili walikuwa wamekamata mapanga, mmoja akalitua panga kwenye bega la Badi. Badi akatoa mguno wa maumivu, akajaribu kumvaa mtu aliyempiga panga, lakini kabla hajamkaribia, panga la mwingine likatua kichwani kwake na kumaliziwa na kitu kingine kizito kilichompiga kisogoni. Badi akaanguka. Hakutikisika tena!

    Ukawa mwisho wa pambano!

    Hija aliyekuwa ndani ya gari alifyatuka kama kombora, akatoka nje na kukimbia huku akilia na kupiga kelele kwa kusema, “Majambazi wanamuua Badi, jamani majambazi…Badi anakufa!” na kuishia kuliita jina la Hassani mdogo wake Badi aje kutoa msaada.

    Kelele zake zikasababisha baadhi ya nyumba za jirani ziwashe taa kuonyesha kuwa wameamshwa na kelele hizo. Tukio hilo likaonekana kuwatisha watu waliomvamia Badi.

    “Jamani tuondokeni!” mmoja wao aliwaambia wenzake.

    Kauli ya mwenzao ikawazindua, na wakati huohuo taa ya sebuleni nyumbani kwa Badi nayo ikawaka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kimeshanuka!” mwingine alisema.

    Kauli hiyo ikamaanisha eneo hilo halikaliki tena.

    “Oyaa Kibusta, tunakuacha mwanangu!” mmojawao alimwambia yule mwenye mwonekano wa kiteja ambaye bado alikuwa amekaa amejiinamia huku akishikilia sehemu yenye nundu iliyotokana na ngumi aliyopigwa. Maumivu ya ngumi hiyo yalikuwa bado yakiendelea kumtesa!

    Onyo hilo likamkurupusha Kibusta kutoka pale alipokaa. Kwanza aliyumba na kuonekana kutaka kupoteza mwelekeo kama vile alitaka kuingia getini, lakini baada ya kuwaona wenzake wakielekea barabarani, naye akajiunga nao kwa kutoka mkuku. Dakika chache baadaye zilisikika pikipiki zinazowashwa na kutoa mlio wa kuondoka kwa kasi!







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog