Simulizi : Mvuvi Bruno (Bruno The Fisherman)
Sehemu Ya Tano (5)
Maxwell alikuwa nyumbani kwake, moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, kitendo cha vijana wake kushindwa kumteka mzee Todd kilimuhuzunisha kupita kawaida.
Alichanganyikiwa, alijua hatari ambayo ilikuwa mbele yake, alijua kabisa kwamba kama asingefanya kila liwezekanalo kuhakikisha mwanaume huyo anatekwa basi mbele yake kungekuwa na hatari kubwa mno.
Hakutaka kutulia, kila wakati alikuwa akiwasiliana na vijana wake lakini walichokuwa wakimwambia ni kwamba hawakuwa wamefanikiwa kumpata mwanaume huyo.
Hakutaka kuona akikubali, bado aliendelea kuwasisitiza vijana wake kumpata mzee Todd lakini mpaka siku hiyo ambayo alikuwa sebuleni kwake mwanaume huyo hakuwa amekamatwa.
Baada ya dakika kadhaa kukaa sebuleni, macho yake yakatua kwenye taarifa ambayo ilimshtua sana. Kupitia kituco cha televisheni cha CNN kulikuwa na habari ambayo iliyokuwa imefika hivi punde kwamba mzee Todd alikuwa amekamatwa nchini Kenya na muda huo alikuwa amefikishwa makao makuu ya CIA kwa ajili ya kujibu kesi yake iliyokuwa ikimkabiri.
“Amekamatwa! Mungu wangu!” alisema Maxwell huku akisimama na kuangalia vizuri televisheni ile.
Hakuamini alichokuwa akikiangalia, hapohapo akampigia simu mmoja wa vijana wake aliyeitwa Dragon na kumwambia kuhusu taarifa ile kwamba mzee Todd alikuwa amekamatwa hivyo walitakiwa kufanya kila kitu kujua namna kesi hiyo ilivyokuwa ikiendeshwa.
Hilo halikuwa tatizo, vijana wakaanza kufanya kazi yao kufuatilia, walihitaji kujua mambo mengi kuhusu huyo wakili ambaye angemsimamia, walijua kuwa kama kulikuwa na kesi ilikuwa ni lazima kuwa na mashahidi wa kumtetea mzee huyo.
Hao ndiyo waliotaka kuwajua, walitaka kuhakikisha wanawatafuta mashahidi wote na kuwamaliza ili mzee Todd ashindwe kesi hiyo iliyoonekana kuwa ngumu kwa upande wake.
Siku ambayo kesi ilikuwa ikisikilizwa, walikuwa mahakamani hapo, lengo lao lilikuwa ni kuhakikisha wakili anakamatwa na kupelekwa sehemu kwa ajili ya kuulizwa maswali kadhaa.
Hilo likafanyika na muda huo walikuwa na Harry ndani ya gari lao. Walimwambia anyamaze kwani vinginevyo wangeweza kummaliza.
Walikuwa wakizunguka naye tu huku wakimuuliza baadhi ya maswali kuhusu kesi hiyo na hata mashahidi ambao walitakiwa kwenda mahakamani. Harry hakutaka kuwaambia ukweli, alichokisema ni kwamba bado kesi ilikuwa mahakamani na hata mashahidi hawakuwa wamejulikana hivyo walitakiwa kusubiri.
“Unatudanganya! Hebu kifumue kichwa chake,” alisema mwanaume mmoja maneno yaliyomfanya Harry kuogopa.
“Naomba msiniue! Naomba msiniue, mimi ndugu yenu,” alisema Harry huku akianza kulengwa na machozi.
“Muue bwana, anatuchelewesha,” alisema jamaa huyo na mwenzake kukoki bunduki.
“Subiri nawaambieni ukweli,” alisema Harry.
“Tatizo unahisi kwamba tumekuja hapa kucheza na wewe. Sikiliza mshikaji wetu, tumekuja kufanya kazi, ukituzingua, tunakuzingua,” alisema jamaa aliyeshika bastola.
Harry hakutaka kunyamaza, ilikuwa ni lazima awaambie vijana wale kila kitu kilichokuwa kimetokea hasa upande wa mashahidi ambao walitakiwa kwenda mahakamani kutoa ushahidi wao kuhusu kile kilichokuwa kimetokea.
Mtu wa kwanza aliyemtaja alikuwa Innocent, huyo walimfahamu, kummaliza halikuwa jambo gumu hata kidogo na mtu wa pili aliyemtaja aliiitwa Bruno ambaye waliambiwa kuwa alikuwa nchini Kenya.
Walipoambiwa hivyo hawakutaka kumshikilia Harry, wakamuacha na kumuonya kwamba hakutakiwa kumwambia mtu yeyote yule kuhusu kile kilichokuwa kimetokea.
Wakampigia simu Maxwell na kumwambia kila kitu kwamba katika kesi ile kulikuwa na watu wawili ambao kama asingehakikisha wanamalizwa basi angeweza kufungwa.
Akatajiwa majina ya watu hao, alimfahamu Innocent, kwake, huyo hakumsumbua ila mtu ambaye alikisumbua kichwa chake alikuwa Bruno, mwanaume ambaye hakuwahi kumuona na hakujua alifananaje.
“Alisema anaishi Kenya?” aliuliza.
“Ndiyo!”
“Sehemu gani?”
“Mombasa!” alijibu.
Hilo halikuwa tatizo, kwa sababu walijua mahali pa kumpata walihakikisha wanafanya kila liwezekanalo kabla ya wiki mbili na kumuua.
Alichokifanya ni kuwalipa vijana hao kiasi cha dola laki mbili na kuwatuma kwenda nchini Kenya huku wakijifanya watalii na wengine kutakiwa kumuua Innocent hapohapo Marekani.
Baada ya siku mbili, vijana watatu, Kelly, Adson na Tim walikuwa ndani ya ndege wakielekea nchini Kenya. Walipewa maelezo yote juu ya kile walichotakiwa kufanya, kwa Mombasa, hawakujua eneo hilo lilikuwa na ukubwa gani lakini walikuwa na uhakika wa kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku chache kabla ya kurudi nchini Marekani.
***
Kama kudharaulika, Bruno alidharaulika sana, alikejeliwa kila kona, hakupendwa kutokana na umasikini uliokuwa umemtafuna.
Kipindi hicho kila kitu kilionekana kubadilika, hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba mwanaume aliyekuwa ameagiza boti mpya kutoka jijini Nairobi alikuwa Bruno yule ambaye alionekana kuwa si lolote lile.
Mzee Juma alijisikia aibu moyoni mwake, hapokuwa Bruno alimuonyeshea kutokujali lakini hakuwa na raha hata kidogo.
Alihisi kila mtu alikuwa akimcheka baada ya kumpuuza kijana huyo na mwisho wa siku kutaka kumuozesha binti yake kwa mtu mwingine na wakati Bruno alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.
Alizipokea boti zile, machozi yalikuwa yakimtoka, hakuweza kuvumilia, hapohapo akaanza kububujikwa na machozi, hakukuwa na kitu kilichomuuma kama hicho, akaanza kumuomba msamaha Bruno ambaye bila kupepesa macho alimwambia kwamba alimsamehe.
Jina la Bruno likaanza kukua, kila mtu aliyesikia kile kilichotokea alitaka kumshuhudia Bruno mwenyewe, walitaka kuona alifananaje kwani taarifa walizozisikia ni kwamba alikuwa kijana mdogo aliyekuwa na utajiri wa kutisha.
Hakutaka kuishia hapo, alichokifanya ni kuanza kujenga nyumba kubwa hapo kijijini na kuwawekea bomba maji ya kunywa na kufulia, akawa na mipango ya kununua magari lakini pia akanunua jumba kubwa jijini Nairobi na kuanzisha biashara zake nyingi.
Maisha yake yalionekana kama kulala masikini na kuamka tajiri. Hawakujua sababu iliyomfanya mzee Todd kumpa pesa nyingi Bruno ambaye alikuwa akiziendesha kwa kufanya biashara nyingi na kubwa.
Ndani ya wiki moja tu tayari jina lake likawa kubwa na wengi kutabiri kwamba angekuwa bilionea mkubwa sana hapo baadaye.
Kwa kuwa alikuwa masikini na alijua jinsi masikini walivyokuwa na maumivu mioyoni mwao hasa katika kupata matibabu, akaanzisha taasisi yake ya kusaidia wagonjwa wasiojiweza kujilipia aliyoiita Bruno & Sharifa Foundation.
Aliwekeza kiasi kikubwa cha pesa, akaanza kuwaita madaktari kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa waliokuwa wakihangaika kupata matibabu.
Alitumia kiasi kikubwa cha pesa lakini hakujali, kwake, moyo wake ulijitolea kumsaidia kila mtu. Hilo likamfanya kujulikana nchini Kenya, watu wakatamani kumuona kwani kwa masikini wasiokuwa na uwezo alionekana kama Mungu.
Umaarufu wake ukawa mkubwa, kwa jinsi alivyokuwa na pesa, alivyosaidia watu kwa kipindi kifupi cha wiki moja na nusu tayari kila kona alikuwa akisikika yeye tu.
Magazeti yakamuandika yeye na mkewe, jinsi walivyokuwa wameyabadilisha maisha ya watu wengi kwa kipindi kifupi. Hawakuringa, hawakujiona, kwao, ni upendo wa dhati tu ndiyo uliokuwa umetawala mioyoni mwao.
Bruno hakuacha kufuatilia kesi ya mzee Todd, tangu siku ya kwanza ilipoanza kusikilizwa, alipokuwa akihojiwa na hata mashahidi walipokuwa wakihitajika alikuwa akifuatilia kila kitu.
Alisahau kabisa kama alitakiwa kuwa shahidi katika kesi hiyo hivyo kuendelea na maisha yake huku akimuomba Mungu ampiganie mzee huyo ili ashinde kesi ile.
Baada ya wiki moja, akapokea ugeni kutoka nchini Marekani. Watu hao walikuwa madaktari kutoka katika Hospitali ya St. Andrew iliyokuwa jijini New York na lengo lao kubwa la kufika nchini Kenya ni kusaidia watu waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa mbalimbali.
Watu hao walikuwa ni Tim na wenzake. Walipofika Nairobi, kitu cha kwanza kilikuwa ni kulisikia sana jina la Bruno. Hawakujua kama mwanaume huyo ndiye waliyekuwa wakimtaka au alikuwa mwingine.
Walifuatilia na kugundua kwamba alikuwa mwenyewe kwani alikuwa akiishi katika Kijiji cha Guolduvai kilichokuwa Mombasa.
Mbali na kulisikia jina lake, wakapewa taarifa nyingi kuhusu mwanaume huyo, taasisi aliyokuwa ameifungua ambayo ilionekana kuwa gumzo kila kona.
Hilo likawasadia na kuona kwamba kama wangejifanya madaktari kutoka nchini Marekani basi ingesaidia sana kukutana na mwanaume huyo na kutimisha lengo lao.
Wakasafiri kutoka Nairobi mpaka Mombasa. Walipofika huko, haraka sana wakamuulizia mwanaume huyo, kumpata halikuwa tatizo hata kidogo, wakaelekezwa na kuanza kumfuatilia kwa ukaribu.
Siku iliyofuata, walikuwa mbele yake. Bruno alipowaona, alifurahia kwa sababu aliamini kwamba watu hao wangemsaidia mno kuwatibu wagonjwa wengine.
Akawakaribisha nyumbani kwake, akawatambulisha kwa mpenzi wake, kwa kifupi akatokea kuwaamini kupita kawaida.
Walizungumza mambo mengi kuhusu matibabu, walimwambia kuhusu ujio wao nchini Kenya, hawakuwa wamefika kwa kuwasaidia watu bali walifika kwa ajili ya kutembelea nchi hiyo kama watalii ila kwa sababu walisikia kuhusu taasisi yake basi nao wakaona kulikuwa na umuhimu wa kutoa msaada ili wachangie baraka.
“Hakika ni Mungu!” alisema Bruno huku akionekana kuwa na furaha kupita kawaida, hakujua kama watu hao walitumwa nchini Kenya kwa lengo la kummaliza kama maagizo kutoka kwa Maxwell..
Kitendo cha Bruno kuwaamini Wazungu wale kilionekana kuwa kosa kubwa kwa kuwa hawakufika nchini Kenya kutangaza dini au kutoa msaada, walifika mahali hapo kwa kufanya kitu kimoja tu, kumuua yeye na kurudi nchini Marekani.
Kumpata Bruno na kumuua lilionekana kuwa jambo gumu mno, mara nyingi hakuwa akishinda nyumbani, kwa kuwa alikuwa na mambo mengi ya kufuatilia, kazi yake kubwa ilikuwa ni kwenda huku na kule na kuhakikisha hakuna kitu chochote kile kinachoharibika.
Tim na wenzake wakawa kwenye wakati mgumu, kila walipopanga wamteke na kwenda naye sehemu kwa lengo la kufanya mauaji, jambo hilo lilionekana kuwa gumu mno.
Mtu waliyekuwa wakibaki naye alikuwa Sharifa. Yeye ndiye walisaidiana naye kuhakikisha huduma ya afya ilikuwa ikiendelea vizuri na kila mtu kuhudumiwa kama ilivyotakiwa kuhudumiwa.
“Tufanye nini?” aliuliza Adson.
“Hivi kweli imeshindikana kumteka kabisa?” aliuliza Tim huku akiwaangalia wenzake.
“Ni suala gumu sana! Yaani kumuua ni vigumu kuliko hata tulivyokuwa tunajifikiria,” alisema Kelly.
“Kwa hiyo?”
“Kama vipi tumteke mkewe!”
“Halafu?”
“Tumuonye asiende Marekani kwa ajili ya kutoa ushahidi vinginevyo tutamuua mke wake,” alisema Adson.
Hawakutaka kufanya jambo hilo kwa haraka, walitakiwa kusubiri mpaka siku mbili kabla ya kesi ile kuunguruma tena nchini Marekani.
Kumteka Sharifa halikuwa jambo gumu, lilikuwa jepesi mno ambalo lingefanyika ndani ya dakika chache tu na kufanya mambo mengine.
Wakakubaliana na hatimaye kwa pamoja kuanza kuhesabu siku. Hawakumuonyeshea Sharifa tofauti yoyote ile, nyuso zao zilikuwa na tabasamu pana na kila wakati walipokuwa wakiongea waliongea kwa mbwembwe kiasi kwamba msichana huyo akawaona kuwa watu muhimu sana.
“Una mimba?” aliuliza Tim huku akimwangalia Sharifa.
“Umejuaje?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unavyoonekana tu! Kweli au uongo?” aliuliza.
“Kweli!”
“Ooh! Safi sana!”
Hiyo ikawa sababu nyingine kwao kufanikisha kile walichokuwa wakikihitaji, walijua kabisa kwamba mwanamke anapokuwa na mimba ya kwanza, mwanaume huwa anachanganyikiwa na anakuwa radhi kufanya lolote lile lakini si kumpoteza mke wake.
Wakaambiana kilichokuwa kikiendelea na hivyo kusuka mipango yao vizuri. Tim akaanza kuangalia ramani, ilikuwa ni lazima kumteka mwanamke huyo na kukimbia naye mbali kabisa na kijijini hapo.
Sehemu ambayo aliiona kuwa nzuri kukimbilia ilikuwa ni ni Tanga ambapo huko kulikuwa na mapango ya Amboni, wangekaa huko mpaka kipindi ambacho kesi ile inamalizika pasipo Bruno kuelekea nchini Marekani.
“Ni mpango mzuri sana, naamini kama tutafanikiwa, basi tutakuwa tumeshinda vita kubwa mno,” alisema Adson huku akitoa tabasamu pana.
Wakati wao wakiendelea kujadiliana na kupanga mipango yao, upande wa pili watu walizidi kumiminika katika kila kituo ambacho taasisi ya Bruno na mkewe ilianzisha. Madaktari waliokuwa na uwezo waliendelea kufanya kazi yao kama kawaida huku wakipata usimamizi wa karibu kutoka kwa Sharifa.
Kila siku Bruno alikuwa na kazi ya kumpigia simu mke wake na kumuuliza kuhusu maendeleo yake. Kipindi hicho ndicho msichana huyo alipomwambia mpenzi wake kwamba alikuwa mjauzito.
Bruno aliposikia hivyo, hakutaka kuendelea kubaki Nairobi, haraka sana akaondoka na kuelekea Mombasa kwa lengo la kumuona mpenzi wake huyo.
Alipofika, akapokewa kwa mabusu kemkem na kukumbatiwa. Alimwangalia Sharifa machoni na kumuuliza kama kile alichomwambia kilikuwa kweli au alikuwa akimtania tu.
“Ni kweli! Nilikwenda kupima,” alisema Sharifa huku akimwangalia mpenzi wake huyo.
“Wa kike au wa kiume?”
“Bado sijajua! Ila ninachojua atakuwa mtoto mzuri sana,” alisema Sharifa na kumkumbatia Bruno.
Ujauzito huo ulimchanganya Bruno, hakuamini kama naye alikuwa akikaribia kuitwa baba. Kila alipomwangalia Sharifa, msichana huyo alionyesha tabasamu pana huku muda mwingi akilishika tumbo lake.
Mapenzi aliyokuwanayo Bruno ni kama yalikuwa yamechochewa na kuchipuka upya moyoni mwake. Alizidi kumpenda mpenzi wake na kumwambia kwamba angempenda milele hata kama kingetokea kitu gani. Hakukaa sana Mombasa, siku iliyofuata akarudi Nairobi huku Tim na wenzake wakiendelea kupanga mipango yao.
***
Wakati akina Tim wakiwa nchini Kenya, huku Marekani Maxwell alitakiwa kufanya jambo jingine la msingi, kwa kuwa kati ya mashahidi waliokuwa wametajwa alikuwepo Innocent, ilikuwa ni lazima kuhakikisha kijana huyo anauawa mara moja.
Akampigia simu na kumwambia kwamba anataka kuonana naye, kwa kuwa Innocent hakuwa na hofu na alishirikiana na Maxwell kwa mambo mengi, akakubali na kwenda kuonana naye.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ambayo Maxwell alitakiwa kummaliza kijana huyo, hakutaka kuona akiendelea kuishi, ili kwenye kesi ile ionekane kwamba kweli mzee Todd alifanya mauaji hayo, hakuwa na jinsi kuanza na kijana huyo.
Baada ya dakika arobaini na tano Innocent akaibuka nyumbani hapo na kuanza kuzungumza. Hakutaka kumficha, alimwambia ukweli jinsi kesi ilivyokuwa ikiendelea mahakamani na ilitakiwa wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba mzee huyo hachomoki.
Hilo halikuwa tatizo kwa Innocent, akakubaliana naye lakini kwa upande mwingine, akajua kabisa kwamba angeweza kusalitiwa.
Akachukua simu yake na kumtumia ujumbe mfupi kijana aliyekuwa nje, ujumbe ambao alimwambia kuwa alitakiwa kuhakikisha anamchukua Innocent na kwenda naye sehemu kumuua akiwa na wenzake.
Hilo halikuwa tatizo, wakakubaliana na wakati wakiagana na Innocent kutoka nje, wanaume wawili wakamsogelea na kuanza kumzongazonga huku wakiwa na bastola.
Alishangaa, lilikuwa jambo geni kabisa kwake, akahoji lakini akajibiwa kwa kupigwa na kitako cha bastola kichogoni hapohapo akaanguka na kupoteza fahamu.
Wakambeba na kumuingiza ndani ya gari. Hawakutaka kupoteza muda kusubiri mahali hapo, wakaondoka na kuelekea katika jumba moja lililokuwa Manhattan hapohapo jijini New York.
Huko, hawakutaka kuchelewa, wakamuingiza katika chumba cha mateso na kumuweka kitini kisha kumfunga kamba. Aliporudiwa na fahamu, alishangaa kuona akiwa kwenye chumba hicho kilichoonekana kutisha kupita kawaida kutokana na mazingira yake yalivyokuwa.
Hakujua kosa lake lakini hakuwa na budi kuomba msamaha, wanaume hao waliokuwa na miili iliyojazia hawakutaka maswali wala maelezo walichokifanya ni kutekeleza kazi ya bosi wao na hivyo kumpiga risasi kadhaa kifuani na kumpigia simu Maxwell.
“Kazi imekamilika,” alisema jamaa mmoja.
“Amekufa?”
“Kama ulivyotuagiza.”
“Sawa. Ahsanteni! Ngoja niwasiliane na akina Tim nione wamefikia wapi,” alisema Maxwell na kukata simu, hakutaka kupoteza muda, hapohapo akampigia simu Tim kwa lengo la kumuuliza mahali walipofikia.
“Kila kitu tayari,” alisikika Tim kutoka upande wa pili.
“Mmemuua?”
“Hapana! Ila tumemchukua mke wake, hapa tupo tunaelekea nchini Tanzania,” alisema.
“Kufanya nini?”
Tim akaanza kumuelezea kile kilichokuwa kimetokea, walimwambia hali aliyokuwanayo Sharifa kwamba alitakiwa kuchukuliwa na mumewe kupigiwa simu na kuambiwa kwamba hakutakiwa kwenda nchini Marekani kwa gharama yoyote ile.
“Kazi nzuri! Na akija Marekani tu, hakikisheni mnamaliza huyo mke wake, sawa?” alisema na kuuliza.
“Ndiyo mkuu!”
“Kazi njema,” alisema na kukata simu.
***
“Today is the day,” (leo ndiyo siku yenyewe) alisema Tim huku akiwaangalia wenzake.
Walikaa nchini Kenya kwa siku kadhaa wakisubiri kufanya mipango ya kumteka Sharifa na kuondoka naye. Kwao, kazi hiyo haikuonekana kuwa ngumu tena kwa kuwa waliaminika na kila mtu aliyekuwa akiwaangalia aliwaamini kwamba walikuwa madaktari kutoka nchini Marekani.
Siku hiyo ambayo ndiyo waliyotaka kufanya tukio wakamwambia Sharifa kwamba lingekuwa jambo jema kujiunga nao kwani kesho yake wangeweza kuondoka kurudi nchini Marekani kuendelea na kazi zao nyingine.
Hilo lilimshtua Sharifa kwani kitu alichojua ni kwamba watu hao wangeendelea kukaa nchini Kenya kwa siku kadhaa. Kuhusu kuungana nao na kula chakula cha mchana halikuwa tatizo hata kidogo, akakubali na hatimaye kwenda sehemu fulani iliyokuwa na hoteli na kuanza kunywa.
Kichwa cha Sharifa hakikuwaza ubaya wowote ule, aliwaamini watu hao kwamba walikuwa wema kwa kuwa tangu walipofika nchini humo na kutoa msaada wa kuwasimamia wagonjwa wengine katika vituo vya afya walivyokuwa wamevianzisha.
Walikula na kunywa, walizungumza mambo mengi, walifurahia mno na kugongesheana mikono lakini vichwa vyao vilikuwa vikifikiria kitu kimoja tu, kumteka msichana huyo na kuondoka naye kuelekea Tanga.
Walipomaliza, wakaingia ndani ya gari. Humo ndipo Sharifa akagundua kwamba watu aliokuwanao hawakuwa wa kawaida, walibadilika, vile vicheko walivyokuwa wakicheka, vikapotea, sura zao zikawa na muonekano mwingine na kuanza kumtia hofu.
“Kuna nini?” aliuliza.
“Tulia hivyohivyo,” aliambiwa na kutolewa kisu, Tim akakishika na kumwamuru anyamaze kwani vinginevyo angemchoma tumboni, msichana huyo akafanya kama alivyoambiwa.
Gari likawashwa mahali hapo na kuanza kuondoka kuelekea katika barabara inayoelekea nchini Tanzania. Njiani, Sharifa alitakiwa kunyamaza kwani vingine angeuawa kama alivyoambiwa.
Hakukuwa na tatizo lolote lile barabarani, waliendelea na safari yao huku kila mmoja akitarajia kufika nchini Tanzania pasipo kupata kipingamizi chochote kile njiani.
Muda wote huo Sharifa alikuwa na hofu, hakujua kilichokuwa kikiendelea, aliwaamini watu hao lakini ghafla walibadilika na kuwa watekaji.
Kila alichokuwa akijiuliza juu ya kile kilichokuwa kimetokea alikosa majibu. Kila alipotaka kuuliza kitu, aliambiwa kunyamaza, hakutakiwa kuzungumza jambo lolote lile kwani kama angekaidi basi angechomwa kisu kama alivyokuwa ameambiwa. Hivyo akanyamaza.
***
Muda ulikuwa ukienda, kila mmoja nyumbani alijua kwamba muda wowote ule Sharifa angerudi nyumbani hapo na kuendelea na majukumu lakini msichana huyo hakutokea.
Nyumbani kwake, wafanyakazi walikuwa na hofu, wakahisi kwamba alipitia sehemu fulani hivyo kuendelea kumsubiri lakini kitu cha ajabu kabisa msichana huyo hakutokea mahali hapo.
Mpaka inafika majira ya saa mbili usiku, bado hakuwa amefika. Hilo likawatia wasiwasi na kuhisi kwamba kulikuwa na jambo lilikuwa limetokea, haikuwa kawaida na mbaya zaidi kila walipokuwa wakimpigia simu haikuwa ikipatikana.
Walichokifanya ni kumpigia Bruno na kumwambia kilichotokea. Alipoambiwa hivyo, hakutaka kuendelea kubaki jijini Nairobi, ni kweli alikuwa bize lakini kwake, familia ilikuwa ni zaidi ya pesa na mali hivyo akarudi haraka sana Mombasa ili kuangalia ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
Njiani, alijaribu mara kadhaa kumpigia simu Sharifa, hazikuwa zikipatikana, Hilo lilimtisha na kumfanya kuogopa, akahisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, akapiga simu zaidi na zaidi lakini majibu yaliendelea kuwa yaleyale.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuripoti polisi na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea. Kila polisi alishangaa, hawakuamini kama Wazungu waliokuwa wametajwa wangeweza kushirikiana kumtena msichana huyo.
Wakamuuliza maswali kadhaa kuhusu Wazungu hao, akawaambia kwamba walitoka nchini Marekani na walifika huko kwa kuwa walitaka kuwasaidia wagonjwa waliokuwa wakiteseka na magonjwa mbalimbali nchini humo.
“Mh! Sasa Wazungu wamemteka au kuna watu wamewateka na hao Wazungu?” aliuliza polisi mmoja huku akionekana kushangaa.
“Hatuna jibu. Naomba mfuatilie,” alisema Bruno huku akionekana kuchanganyikiwa.
Hilo ndilo lililofanyika, mtu ambaye mchumba wake alikuwa ametekwa alikuwa Bruno, mwanaume aliyeibuka ghafla na pesa na kuwa mtu mwenye heshima kubwa mno.
Polisi hawakutaka kusubiri, hawakutaka kuona suala hilo likifika mbali zaidi mpaka rais kujua, ili kuwe na amani, waokoe vibarua vyao ilikuwa ni lazima kupambana kuhakikisha msichana huyo anapatikana mara moja.
Simu zikapigwa katika vituo vya polisi na kuambiwa kilichokuwa kikiendelea, walitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha Sharifa na Wazungu wale wanapatikana haraka iwezekanavyo.
Bruno hakuwa na furaha tena, moyo wake ulinyong’onyea na kuona kabisa kwamba asingeweza kumuona tena mpenzi wake. Hakulala, usiku mzima alikuwa akiongea na wakubwa wa vituo kuhusu mpenzi wake kama alikuwa ameonekana sehemu au la.
Wakati hayo yote yakiendelea, zilikuwa zimebaki siku mbili kabla ya kesi ya mzee Todd kuendelea nchini Marekani. Akiwa katika hali hiyo, akapigiwa simu kutoka moja kwa moja nchini Marekani na kuambiwa kwamba alikuwa akihitajika nchini Marekani kwa ajili ya kutoa ushahidi katika kesi ya mzee Todd.
Alipoambiwa hilo tu, akaanza kupata picha, akaunganisha tukio lililotokea la kutekwa kwa mchumba wake na kesi ile ya mzee Todd, akahisi kabisa vitu hivyo vilikuwa vimepangwa, kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Huku akiendelea kuwa katika hali hiyo, akapigiwa simu tena, akaichukua na kuangalia kioo, mpigaji hakuwa mwingine bali ilikuwa ni namba ya mchumba wake, muda huo ulikuwa ni saa sita usiku.
“Halo! Sharifa upo wapi?” aliuliza mara baada ya kuipokea simu ile.
“Unatakiwa kufanya kitu kimoja tu,” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja kutoka upande wa pili, alikuwa Tim.
“Unasemaje?”
“Sikiliza maelezo yetu kwanza,” alisikika Tim.
Akamwambia kilichokuwa kikiendelea, alikuwa akihitajika nchini Marekani kwa lengo la kwenda kutoa ushahidi katika kesi ya mzee Todd, hapo, Tim alimwambia kwamba alitakiwa kutokwenda nchini humo kwani kama angekwenda, mchumba wake angeuawa kwa kuchomwa visu kwa kuwa alikuwa mikononi mwao.
Bruno aliposikia maneno hayo, akaogopa, akahisi kabisa mwanaume huyo hakuwa akitania kwani hata sauti yake ilivyokuwa ikitoka, ilionyesha ni kwa jinsi gani alikuwa siriazi kwa kile alichokuwa akikizungumza.
“Naomba msimuue mpenzi wangu,” alisema Bruno huku machozi yakianza kumtiririka mashavuni mwake.
“Hatutomuua kama tu hautokwenda nchini Marekani, vinginevyo, tutamuua yeye na hata hicho kiumbe kilichopo tumboni mwake,” alisikika Tim, maneno aliyokuwa ameyazungumza yalimfanya Bruno kuogopa kupita kawaida.
***
Mzee Bruno alitulia huku masikio yake yakiwa kwa wakili wake, Harris. Mwanaume huyo hakumwambia kitu chochote kuhusu kutekwa kwake, alijua kwamba kama angemwambia ukweli basi hali ingekuwa mbaya zaidi na inawezekana watu wale wangemrudia tena na kumteka kama walivyofanya.
Alizungumza naye kwa utaratibu, hakutaka kumuonyeshea dalili kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea, alimpa matumaini kwamba angeshinda kesi ile pasipo kumwambia kuwa mashahidi waliokuwa na nguvu ya kumtoa walikuwa njiani kuuawa.
Yeye ndiye aliyekuwa akimwambia hali ilivyokuwa ikiendelea. Hakumficha, alimwambia kuwa Wamarekani walimchukia na kila mmoja kwa kipindi hicho alikuwa akitaka kuona akihukumiwa kifo kama watu wengine.
Hilo lilimuhuzunisha mzee huyo kwani hakuwa amefanya jambo lolote baya, hakuwa ameua wala yale madawa ya kulevya yaliyokutwa ndani ya nyumba yake hayakuwa yake.
Kila alipokuwa akimuuliza kuhusu mashahidi wake kama walipigiwa simu, Harris alikuwa akijiumauma kana kwamba kulikuwa na jambo baya sana ambalo mzee huyo hakutakiwa kulijua.
“Waliwasiliana nao,” alisema.
“Ikawaje?”
“Waliniambia kwamba watakuja!”
“Watakuja? Washaanza safari? Serikali ndiyo inatakiwa kuwasafirisha! Wameanza hiyo safari?” aliuliza.
“Hata sijajua!”
“Harris! Inakuwaje usijue na wakati wewe ndiye wakili wangu ninayekutegemea?” aliuliza mzee Todd.
Harris hakuwa na cha kujibu, hofu ilimtanda moyoni mwake. Mpaka kufikia hatua hiyo, tayari mzee Todd akahisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea ambacho mtu huyo aliyemtegea hakutaka kumwambia ukweli.
Siku hazikuwasubiri, zikaendelea kukatika kama kawaida. Mpaka siku ya kupanda tena mahakamani, bado mashahidi hawakuwa wamefika mahakamani na kwa taarifa ambazo zilianza kuzagaa ni kwamba mtu aliyetajwa kama shahidi namba mbili, Innocent alipotea katika mazingira ya kutatanisha, na hakukuwa na mtu aliyejua mahali alipokuwa.
***
Ilikuwa ni lazima kwa Tim na wenzake kuondoka Mombasa na kuelekea Tanga nchini Tanzania. Hawakuona kabisa kama kungekuwa na watu wangeweza kuwasumbua njiani kwa kuwa walikuwa na kiasi kikubwa cha pesa ambacho wangekitumia kwa polisi yeyote yule ambaye angediriki kuwazuia.
Njiani, walikuwa wakiendelea na safari yao, hakukuwa na mtu aliyekuwa na wasiwasi, waliwapigia simu wenzao waliokuwa nchini Marekani na kuwaambia kwamba walifanikiwa kumpata mchumba wa shahidi namba mbili ambaye kwake alikuwa hanywi, hali wala hafanyi kitu chochote kile, kwa mapenzi aliyokuwa akimpenda msichana huyo, alikuwa tayari kufanya jambo lolote lile.
Walichukua saa kadhaa wakaanza kukaribia Horohoro huku ikiwa ni saa nne usiku, mahali kulipokuwa na mpaka wa Kenya na Tanzania. Mpaka kufikia hapo wakawa na uhakika kwamba wangeingia nchini Tanzania kwa kuwa kusingekuwa na mtu yeyote yule ambaye angediriki kuwasimamisha.
Ndani ya gari Sharifa alipewa masharti kwamba hakutakiwa kuonyesha hali yoyote ile ya kuwatia wasiwasi watu wengine, kama alivyokuwa ndivyo alivyotakiwa kuwa, yaani sura yenye tabasamu ambayo ungeonyesha kwamba hakukuwa na jambo lolote baya ambalo lilikuwa likiendelea.
Baada ya kubakiza mita mia mbili kabla ya kuingia mpakani hapo wakaanza kuyaona magari kadhaa yakiwa yameweka foleni na kwa kuwa hawakutaka kusababisha jambo lolote ambalo lingewafanya kugunduliwa, nao wakaweka foleni kwa ajili ya upekuzi.
Magari yalikwenda taratibu sana mpaka baada ya saa moja nao ndiyo wakafanikiwa kufika mahali pa kuvuka ambapo hapo wakatakiwa kuonyesha vibali vyao kabla ya kuendele.
“This is our passports,” (hizi ni hati zetu za kusafiria) alisema Tim huku akimwangalia polisi aliyekuwa akikagua hati za kusafiria.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“What about hers?” (vipi kuhusu yake?) aliuliza akimaanisha Sharifa.
Tim hakutaka kuzungumza sana, alichokifanya ni kuchukua kibunda cha dola kilichokuwa na dola mia moja kama ishirini na kumuonyeshea polisi yule kisiri.
“We have no time friend,” (hatuna muda rafiki) alisema Tim huku akimwangalia polisi huyo ambaye naye kwa siri kubwa akakichukua na kukichikichia chini ya kitabu chake cha maelezo na kuwaambia jamaa waliokuwa wameshikilia vyuma vya kuzuia magari kuliruhusu gari hilo, na kwa kuwa ilikuwa ni usiku, hakukuonekana kuwa na tatizo lolote lile.
Wakaondoka huku wakiwa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, pesa zile walizozitoa zilibadilisha kila kitu na kuonekana kwamba walikuwa watu wema.
Walipofika kama umbali wa miaka mia tano kutoka mpakani pale, simu ikapigwa na taarifa kutolewa kwamba kulikuwa na Wazungu watatu walikuwa ndani ya gari na mwanamke mmoja, Wazungu hao hawakutakiwa kuvuka mahali hapo.
Polisi yule aliposikia tangazo lile, akajua kabisa kwamba watu waliokuwa wakiuliziwa ni wale ambao aliwaruhusu mpakani hapo lakini hakutaka kusema kitu chochote kile kwa kuhofia kuharibu kila kitu na hata zile pesa alizokuwa amepewa, mwisho wa siku zingeweza kugundulika na kumletea matatizo.
Safari ilikuwa ikiendelea huku kila mmoja akijiona kuwa bingwa kwa kile kilichokuwa kimetokea. Kutoka hapo Horohoro mpaka Tanga Mjini ilikuwa ni umbali wa kilometa 172, Tim hakutaka kuendesha kwa mwendo wa taratibu, ilikuwa ni lazima kuwahi hivyo kuendesha kwa mwendo wa kasi kana kwamba walikuwa wameliiba gari hilo.
Walitumia dakika arobaini na tano mpaka kufika tanga Mjini ambapo moja kwa moja wakaenda uswahilini na kuchukua vyumba katika gesti moja na kujificha huko huku wakiwasiliana na wenzao ambao walikuwa wakihitaji kujua kile kilichokuwa kimeendelea nchini Kenya.
Ilipofika saa sita usiku, Tim akachukua simu ya Sharifa na kumpigia simu Bruno na kumwambia kwamba hakutakiwa kwenda Marekani kwani vinginevyo mpenzi wake ambaye walikuwanaye wangeweza kummaliza.
“Umemwambi?” aliuliza mwenzake.
“Ndiyo! Akibisha basi hatutokuwa na jinsi! Tutamuulia mbali,” alisema Tim maneno yaliyomtisha Sharifa.
***
Polisi walichachamaa, kila kona walikuwa wakiwaulizia Wazungu hao walioonekana kuwa mwiba mkali kwa Bruno. Alichanganyikiwa, usiku huo alikuwa akiwatafuta lakini mpaka asubuhi inaingia hawakuwa wamefanikiwa kwa lolote lile.
Hilo liliwachanganya polisi, walichokiamini ni kwamba watu hao walikuwa hapohapo Mombasa hivyo kuendelea kuwatafuta kwa nguvu zote.
Asubuhi hiyo walipoona kwamba hawakufanikiwa, wakawapigia simu polisi waliokuwa mipakani na kuwaulizia watu hao kama walikuwa wamepita huko au la lakini kwa bahati mbaya, kila walipokuwa wakiuliza waliambiwa kwamba watu hao hawakuwa wamepita hivyo kuendelea kuwatafuta ndani ya Kenya tu.
“Hawa watu watakuwa wameondoka Kenya, haiwekani kila kona hawapo japokuwa tumehakikisha ulinzi kila sehemu,” alisema mkuu wa kituo kikuu cha polisi cha hapo Mombasa, kwa jinsi alivyoongea alionekana kuchanganyikiwa kwani suala la mchumba wa Bruno kutekwa halikuwa la kawaida hata kidogo, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria rais endapo tu angepata taarifa hiyo.
Wakati polisi wakiendelea kumtafuta Sharifa, Bruno alikuwa akijua kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Moyo wake ulitamani sana kumsaidia mze Todd lakini kila alipofikiria upande wa pili kwamba mpenzi wake angeuawa mara baada ya kwenda nchini Marekani akabaki akiwa hajui ni kitu gani alitakiwa kufanya.
“Hii haiwezi kuwa siri tena, ni lazima nimshirikishe Bartazar,” alisema Bruno.
Hilo ndilo alilolifanya, haraka sana akampigia simu mkuu wa polisi nchini Kenya, Bartazar na kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea. Mkuu huyo wa polisi alipoambiwa, alichanganyikiwa, akauona ugumu wa kazi uliokuwa mbele yake, hakutaka kuchelewa, kwa kuwa alikuwa na namba za rais, akampigia na kumuhadithia kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
“Yaani ilikuwaje?” alisikika rais akiuliza hivyo kuanza kuhadithiwa tena.
Hakuwa akijua kitu chochote kile, kwake, jambo hilo lilionekana kuwa geni kabisa. Bartazar alichokihitaji kilikuwa ni kitu kimoja tu, rais huyo wasiliane na ubalozi wa Marekani kwa lengo la kuwapa taarifa maofisa wa CIA ambao walitakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha Sharifa anapatikana kwani wao kama wao wasingeweza kuwapata.
Rais hakusubiri, kama alivyoambiwa ndivyo alivyofanya, haraka sana simu ikapigwa mpaka ubalozini na kuwaambia kilichokuwa kimetokea. Balozi wa Marekani nchini Kenya, akapiga simu nchini Marekani na kuwaambia kila kitu.
Haraka sana maofisa wa CIA waliokuwa nchini Kenya, wakapigiwa simu na kuambiwa kila kitu na walitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha huyo msichana anapatikana kwa udi na uvumba ili mpenzi wake asafirishwe na kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kutoa ushahidi wa kesi hiyo.
“Ila tumechelewa, kesi yenyewe ni kesho,” alisikika jamaa mmoja.
“Itaahirishwa. Tutapeleka taarifa mahakamani,” alisema mkuu wa CIA nchini Marekani.
***
Siku ya kesi ambayo ilitarajiwa kusikilizwa kwa upande wa mashahidi ilikuwa imefika. Watu wengi walifika mahakamani hapo kwa kuwa walitaka kusikia kile kilichokuwa kimetokea mpaka mwanaume huyo kuamua kuyaficha madawa ya kulevya nyumbani kwake na mwisho wa siku kuhusishwa katika vifo vya familia yake.
Watu wengi waliohudhuria kesi hiyo siku hiyo walikuwa na hamu kubwa kusikiliza kwa upande wa mashahidi. Wale waliokuwa wakitakiwa kusimama kwa upande wa jamhuri walikuwa tayari lakini kitu cha ajabu mpaka siku ya kesi inafika jaji hakuwa amepokea taarifa yoyote kuhusu mashahidi kwa upande wa mshtakiwa.
Mahakamani kukaanza kuzuka minong’ono, hakukuwa na mtu aliyejua kilichokuwa kikiendelea, walikuwa wakiangalia huku na kule kuona kama mzee Todd alikuwa na mashahidi mahakamani hapo.
Yeye mwenyewe alishangaa, hakujua kama kweli Bruno alikuwa na taarifa au la. Alimsaidia sana kijana huyo na alikumbuka kabisa kwamba siku ya mwisho kuzungumza naye alimwambia kuwa angependa sana siku ya kesi yake aende Marekani na kusimama kama shahidi lakini kitu cha kushangaza kabisa kijana huyo hakutokea.
Hilo lilimsikitisha sana, upendo wote aliokuwanao kwa Bruno ukapotea, akahisi kugeukiwa na mtu ambaye hakumtarajia kufanya jambo kama hilo. Moyo wake ukaanza kuwa na chuki dhidi ya Bruno, japokuwa kijana huyo alimsaidia sana lakini muda huo hakuwa hakuona thamani ya msaada alioutoa kwake kwa kuwa alihitaji kusaidiwa zaidi katika hali ngumu kama aliyokuwanayo kipindi hicho.
“Bruno! Why do you do this to me?” (kwa nini unanifanyia hivi Bruno?) aliuliza mzee huyo kwa sauti ya chini huku machozi yakimtoka kwani aliamini kwamba Bruno alikuwa mtu muhimu hata zaidi ya alivyokuwa Innocent.
Baada ya dakika kadhaa, jaji akapokea kikaratasi kutoka kwa mwanaume mmoja, akaanza kukisoma, alipomaliza, akayainua macho yake na kuielezea mahakama kwamba kesi hiyo iliahirishwa mpaka baada ya wiki mbili kwani mashahidi wawili waliokuwa wakitarajiwa kusimama kizimbani kumtetea mzee Todd hawakufika mahakamani hapo.
“What? Just hung him,” (nini? Nyie mnyongeni tu) alisikika mwanaume mmoja mahakamani hapo.
CIA watatu, Andrew Putt, Gilbert Michael na Richard Bull wakaianza kazi yao nchini Kenya kuhakikisha Sharifa anapatikana haraka iwezekanavyo.
Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda Mombasa katika kijiji cha Goulduvai alipokuwa akiishi Sharifa kwa muda huku akiwahudumia wanakijiji kwa afya zao.
Walipofika huko, kila kona watu walikuwa wakilizungumzia tukio hilo. Hakukuwa na mtu aliyekuwa na furaha, kila mmoja alihuzunika kwani kwa kile kilichokuwa kimetokea hawakukitegemea hata kidogo.
Hapo, wakazungumza na Bruno na kumuuliza maswali kadhaa. Aliwasimulia kila kitu alichokuwa akikifahamu kuhusu Wazungu wale na mwisho kabisa akawaambia kwamba lengo la watu hao ni kwamba hakutakiwa kwenda nchini Marekani kutoa ushahidi kwa yaliyokuwa yametokea kwa mzee Todd.
“Someone is behind this,” (kuna mtu yupo nyuma ya hili) alisema Bull huku akiwaangalia wenzake.
Wakahitaji simu ambayo Bruno aliwasiliana na Tim, walipopewa, wakachukua namba, wakasogea pembeni hidogo huku Putt akichukua tablet yake na kufungua sehemu ya ramani na kuanza kuangalia.
Bruno alitulia pembeni, alibaki akiwaangalia Wazungu hao walioonekana kuwa hatari katika kumtafuta mtu yeyote waliyekuwa wakimtaka. Walikaa huko kwa zaidi ya nusu saa huku wakizungumza na wakati mwingine wakiangalia tablet ile kwa lengo la kujua zaidi kuhusu watu hao walikuwa mahali gani.
“Hivi kweli wanaweza kwenda Nairobi?” aliuliza Putt huku.
“Sidhani! Haiwezekani mtu afanye tukio kama hili halafu akaelekea Nairobi,” alisema Bull huku akiwaonyeshea wenzake ramani katika table.
“Kwa maelezo ya mumewe alisema kwamba alipigiwa simu, lakini haikuwa ya kawaida, ilipigwa kwa mtandao wa WhatsApp, mnajua kwa nini mpigaji alifanya hivyo?” aliuliza Gilbert.
“Hapana!”
Gilbert alikuwa miongoni mwa maofisa wa CIA waliokuwa na utaalamu mkubwa wa kumtafuta mtuhumiwa yeyote yule. Alikuwa mtaalamu wa hisia ambaye kama kulikuwa na tukio limetokea ndani ya nyuma na mtuhumiwa kutoweka, aliweza kusimama na kukwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea ndani ya nyumba hiyo.
Alikuwa mtaalamu na makao makuu walimpeleka nchini Kenya kwa lengo la kuhakikisha kwamba Kundi la Al Shabaab linateketezwa haraka sana kwa kuwaambia kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Kwa akili yake, akagundua kwamba watu hao hawakuwa nchini Kenya, walikuwa wameondoka na kuelekea katika nchi nyingine na ndiyo maana waliamua kupiga simu kwa kutumia Mtandao wa WhatsApp.
“Kivipi?” aliuliza Bull.
“Ni kwa sababu hawakutaka kupatikana katika minara ya simu za mkononi. Kama wangetumia simu ya kawaida, tungejua wapo wapi, ila kwa WhatsApp, bila shaka watu hawa wameamua kuficha mawasiliano ili tusijue wapo wapi,” alisema Gilbert huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikizungumza.
Alichokisema ndio ulikuwa ukweli wenyewe kwamba watu hao waliondoka na kuelekea nje ya Kenya. Hakukuwa na maswali mengi kwamba ni nchi gani walikuwa wameelekea, moja kwa moja wakagundua kwamba ilikuwa ni Tanzania na hivyo ilikuwa ni lazima waende huko.
“Kwa nini isiwe Somalia?”
“Ni kwa sababu kuna mapigano huko. Kwa akili ya kawaida tu, ungeweza kukimbilia Somalia?” aliuliza Gilbert.
“Haiwezekani!”
“Kama haiwezekani, basi watu hao watakuwa wamekimbilia Tanzania,” alisema.
Hawakutaka kupoteza muda, ilikuwa ni lazima kuondoka na kuelekea nchini humo. Hawakuaga bali walimwambia Bruno kwamba watakaporudi watarudi wakiongozana na mpenzi wake hivyo alitakiwa kuwasubiri hapohapo Mombasa.
Njiani, walikuwa wakizungumza mambo mengi, kwao, kazi ile haikuonekana kuwa ngumu tena, waliamini kwamba kwa namna moja ama nyingine wangefanikiwa kwa kuwa tu walijiona kuwa na uwezo mkubwa kuliko hata hao watu waliokuwa wamemteka Sharifa.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika mpaka wa Horohoro kwa upande wa Kenya. Wakateremka na moja kwa moja kuelekea katika ofisi ya kiongozi wa maaskari hapo mpakani, mzee Hamidu na kumuuliza kuhusu watu hao waliokuwa wamepitia mahali hapo kuingia Tanzania.
“Hakuna watu waliopita,” alisema mzee Hamidu huku akimwangalia Bruno.
“Si kweli!”
“Huo ndiyo ukweli, au kama mmekuja na ukweli wenu mwingine,” alisema mzee Hamidu huku akisimama kwenye kiti, yote hayo ilikuwa ni kutaka kuwaonyeshea watu hao kwamba alikuwa mwanaume imara na kile alichokuwa akikisema ndicho kilikuwa sahihi.
“Hapana! Bado tunajua kwamba walipita hapa, ila walipitaje? Inawezekana wewe hufahamu lakini kuna mtu hapa atakuwa anafahamu,” alisema Gilbert.
“Kwa hiyo kuna mtu alichukua rushwa?”
“Huwezi kujua!”
“Hizo ni dharau,” alisema mzee huyo.
Gilbert hakutaka kubaki ndani ya ofisi hiyo, kwa jinsi mzee Hamidu alivyokuwa akiongea, alihisi moyo wake ukipatwa na hasira kali, na ili kuepusha matatizo, akaamua kutoka ndani ya ofisi ile.
Pale nje akasimama na kuanza kuangalia huku na kule, aliwaangalia jinsi ambavyo askari walivyokuwa wakipekua magari, alikuwa na uhakika kwamba watu hao walipita mahali hapo kwani hata upekuzi ambao ulikuwa ukifanyika, ulifanyika kizembe sana.
“Tuingieni nchini Tanzania, bado moyo wangu una uhakika kwamba watu hawa walipita mahali hapa,” alisema Gilbert, wakaingia ndani ya gari lao na kuingia nchini Tanzania, hapo wakaanza kuitafuta Tanga Mjini.
***
Kila kona katika Tanga Mjini kulikuwa na stori moja tu iliyokuwa ikianza kuzagaa kila kona. Wazungu watatu ambao walichukua chumba kimoja katika nyumba ya wageni iliwashangaza kila mtu aliyekuwa ameisikia.
Watu walijua kwamba Wazungu walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na pesa, watu ambao mara baada ya kufika barani Afrika basi wangekuwa wakiishi katika hoteli nzuri lakini Wazungu waliokuwa wameingia Tanga kwa siku hizo walionekana kuwa tofauti na wenzao kabisa.
Hali hiyo ikaanza kuwatia wasiwasi watu wa hapo Tanga kiasi kwamba wengi wakahisi kwamba kulikuwa na kitu cha siri kilichokuwa kikiendelea ambacho kingeweza kuwa hasara au hata kupoteza maisha kwa wakazi wa hapo.
Walichokifanya siku iliyofuata ni kuwasiliana na polisi. Waliwaambia kila kitu kilichokuwa kimetokea kwamba inawezekana kabisa Wazungu wale hawakuwa watu wazuri na ndiyo maana hawakutaka kupanga katika hoteli kubwa kwa kuogopa kukamatwa.
Polisi walipoambiwa, hawakutaka kusubiri, wakaondoka na kuelekea huko kwa lengo la kuwaona Wazungu hao. Walipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuzungumza na mmiliki wa gesti hiyo na kumuuliza maswali mengi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakuwaficha, aliwaambia kila kitu kuhusu Wazungu hao na hivyo kuhitaji kuzungumza nao. Hilo halikuwa tatizo, alichokifanya ni kuwaita, wanaume hao, wakatoka chumbani, wakafunga mlango kwa ufunguo ili Sharifa asitoke, wakawafuata polisi na kuanza kuzungumza nao.
Waliwaambia kwamba walifika hapo Tanga kwa lengo la kuingia katika mapango ya Amboni lakini kabla ya kwenda huko walijikuta wakiibiwa kiasi cha pesa walichokuwanacho cha dola elfu themanini, laptop na saa zao za mikononi na vijana wa mitaani ambao waliwafuata na kuwatolea visu.
“Poleni sana! Kwa nini hamkutoa taarifa polisi?” aliuliza polisi mmoja, kwa jinsi Tim alivyokuwa akielezea, ilikuwa ni vigumu kuamini kwamba alikuwa akidanganya.
“Tulichanganyikiwa! Hatupo sawa, hata nauli ya ndege kurudi nyumbani hatujui tutaipataje, hapa mnapotuoni, tupo hivihivi pamoja na msichana wa nchini Ghana ambaye tumekuja naye, hatuna kitu,” alisema Tim.
Polisi wakaangaliana, kile alichokuwa amekisema kilionekana kuwagusa kupita kawaida hivyo kuwaambia kwamba wanaondoka na kurudi baadaye huku wakiwa tayari wamejua ni kitu gani walitakiwa kufanya kuwasaidia Wazungu hao.
Walipoona polisi wameondoka, hawakutaka kuendelea kukaa kwenye gesti hiyo, ilikuwa ni lazima waondoke kwani walihisi kwamba mara baada ya kuondoka, wangekwenda kupata ukweli wa wao kuwa hapo na kurudi huku wakiwa na sura nyingine.
Wakaufungua mlango na ufunguo, wakaingia ndani, kilichowashtua ni kwamba Sharifa hakuwemo chumbani humo. Hilo liliwatia hofu kwani walipokwenda nje kuzungumza na polisi walimuacha humo ndani na zaidi ni kwamba waliufunga mlango kwa ufunguo, sasa kama ameondoka, atakuwa amepitia wapi?
“Kwenye dari! Tuangalieni kwenye dari,” alisema Adson na kwa kuwa pale kulipokuwa na mlango wa dari kulikuwa na meza, wakajua kabisa msichana huyo alipanda juu ya meza hiyo na kuingia humo kwa lengo la kuwatoroka hotelini humo.
“Jamani! Ili tuwe salama, huyu msichana ni lazima apatikane,” alisema Kelly, wakautoa mlango wa dari na Tim kuingia huko kumtafuta Sharifa.
***
Sharifa alikuwa ndani ya chumba kile huku akiwa na wasiwasi tele, hakujua ni kitu gani kingeendelea kama tu watu hao wangeendelea kumshikilia kama ilivyokuwa.
Hakutaka kuona akiwa mikononi mwa watu hao, alitamani kuona akiondoka na kurudi kwa mpenzi wake. Kama kulia, alilia sana lakini muda huo haukuwa wa kulia tena, ilikuwa ni lazima kufanya kila liwezekanalo kuondoka ndani ya chumba hicho.
Alikuwa humo, Tim na wenzake walikwenda nje walipokuwa wakihitajika na polisi, yeye mule ndani ilikuwa ni lazima afanye kila linalowezekana kuhakikisha anatoka ndani ya chumba hicho.
Akaufuata mlango, akakishika kitasa na taratibu kuanza kukitekenya kwa lengo la kukifungua. Mlango haukufunguka kuonyesha kwamba ulifungwa kwa nje.
Haraka sana akaacha. Akaangalia huku na kule, akafanikiwa kuuona mlango wa dari ukiwa umefungwa. Kichwa chake kikamwambia kwamba hiyo ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuweza kuondoka ndani ya chumba hicho.
Akachukua meza, akaiweka chini ya mlango wa dari na kupanda, akaanza kuufungua mlango huo kwa kuusukuma, ukafanikiwa kufunguka.
Kazi kubwa ilikuwa ni kupanda juu ya dari. Ilikuwa ni kazi ngumu ambayo aliamini kwamba asingeweza kuifanya hata kidogo lakini kitu cha kushangaza kabisa ambacho hata yeye kilimwachia maswali ni kwa namna ambavyo alipanda na kuingia darini, akaurudishia mlango ule wa dari.
Ndani kulikuwa na giza, hakuwa na simu, hakuwa na kitu chochote kile ambacho kingemfanya kumulika mule ndani lakini hilo halikumfanya kubaki mahali pale, kwa kutumia magoti yake akaanza kusonga mbele, sehemu ambayo aliamini kulikuwa na mlango mwingine.
Humo darini, alisikia milio ya panya, hakuoga hata kidogo, kitu alichokuwa akikimbia kilikuwa ni hatari hata zaidi ya panya aliokuwa akiwasikia. Baada ya dakika mbili akafika katika mlango mwingine wa dari na kuufungua.
“Mungu nisaidie,” alisema huku akiangalia ndani ya chumba hicho.
Alisikia sauti za watu wakiongea bafuni kwa furaha, hakutaka kujiuliza kuhusu watu hao, akahisi kabisa kwamba walikuwa wapenzi waliokwenda kuyafurahia maisha yao na muda huo walikuwa wakioga tayari kwa kuondoka.
Bahati ilikuwa upande wake kwani pale kulipokuwa na mlango wa dari kulikuwa na kitanda, haraka sana akaruka mpaka juu ya kitanda.
Akaondoka na kuufuata mlango, akaufungua na kuanza kuangalia nje. Alipoona koridoni hakuna mtu, hakutaka kusubiri, hara sana akatoka na kuelekea nyuma ya gesti hiyo na kuanza kukimbia.
Mule ndani, Tim aliendelea kutambaa ndani ya dari na kufanikiwa kuuona mlango wa kushukua katika chumba kingine. Haraka sana akaufuata, haukuwa umefungwa hivyo akarukia ndani ya chumba hicho.
“She was passing through this room,” (amepitia chumba hiki) alisema Tim na kuufungua mlango na kutoka ndani.
Kichwa chake kilimwambia kwamba msichana huyo alikuwa ameondoka kupitia katika mlango wa nyuma na hivyo kuanza kukimbilia huko.
Alichanganyikiwa, msichana huyo alikuwa mtu muhimu mno, aliwafanya kufika nchini Kenya, wakatoroka mpaka Tanzania na walikuwa wamelipwa kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kuhakikisha mpenzi wa msichana huyo, Bruno haondoki kuelekea nchini Marekani.
Kule nje aliwakuta watu wakiwa wamepigwa na taharuki, kilichokuja kichwani mwake ni kwamba walimuona Sharifa akiwa amekimbia na hawakujua sababu iliyomfanya kukimbia na ndiyo maana walikuwa kwenye hali hiyo.
Akaanza kuelekea katika njia iliyokuwa na watu wengi waliokuwa wamesimama kwa kuamini kwamba msichana huyo alipitia njia hiyo. Watu wote wakaanza kumwangalia na yeye, ni kweli walimuona msichana mmoja akiwa amekimbia lakini ghafla, baada ya sekunde kadhaa wakamuona mwanaume wa Kizungu naye akikimbia kuelekea kule alipokimbilia mwanamke yule.
“Jamani! Kuna nini tena?” aliuliza jamaa mmoja aliyekuwa amevaa msuli kama mtu aliyekuwa na busha.
“Hata mimi nashangaa! Hawa watoto wetu siku hizi wana visa sana, utakuta huyo Mzungu kamtoa Instagram halafu anamkimbia,” alisema mzee mwingine.
Tim alikimbia mpaka katika barabara kuu kabisa lakini hakuweza kumuona Sharifa. Alichanganyikiwa, kwa wakati huo msichana huyo alikuwa muhimu kuliko kitu chochote kile.
Akamtafuta na alipoona hajafanikiwa, akarudi kule gesti na kuwaambia wenzake kile kilichotokea. Kila mmoja alichanganyikiwa, kitendo cha kumkosa msichana huyo kilimaanisha kwamba Bruno angekwenda nchini Marekani na kuweka ushahidi juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
“Ni lazima tuondoke kurudi Marekani haraka sana,” alisema Tim huku akiwaangalia wenzake, yeye alionyesha kuchanganyikiwa zaidi ya wenzake.
“Tukiulizwa?”
“Tunakwenda kimyakimya!”
“Halafu?”
“Huyu mtu tutamvizia uwanja wa ndege, najua tutajua siku ambayo atakwenda nchini Marekani, nadhani hapo ndipo tutakapofanya utekaji hukohuko mbele ya safari! Mnaonaje?” alisema na kuuliza.
“Linaingia akilini! Hakuna kuchelewa, kama vipi kesho tuondokeni,” alisema Kelly.
Hivyo ndivyo walivyokubaliana, hakukuwa na sababu ya kuendelea kubaki nchini Kenya na wakati kulikuwa na kazi kubwa ambayo walitakiwa kuifanya haraka iwezekanavyo.
Usiku huohuo wakaondoka na kuelekea katika hoteli ya kifahari ya Jumanji iliyokuwa Tanga Mjini na kuchukua vyumba hapo. Siku iliyofuata, wakapanda ndege na kuelekea Dar es Salaam ambapo huko wakaunganisha mpaka nchini Marekani.
Ndani ya ndege kila mmoja alikuwa akifikiria lake, mbele yao kulionekana kuwa na kazi kubwa lakini ilikuwa ni lazima kuhakikisha wanaikamilisha kwa haraka sana.
Hawakutaka kuzungumza mambo mengi kuhusu jambo hilo ila walipanga kuzungumzia zaidi mara baada ya kufika nchini humo.
Baada ya saa ishirini na tano, wakaingia nchini humo. Wakafikia hotelini, hawakutaka kuwasiliana na Maxwell, walitaka kukamilisha kila kitu haraka sana pasipo mwanaume huyo kufahamu jambo lolote lile.
Wakajipanga na baada ya siku tatu tangu wafike nchini Marekani wakapata taarifa kwamba Bruno alikuwa njiani akielekea nchini Marekani. Kwa kuwa walitakiwa kukamilisha mpango wao haraka sana, wakajipanga kwa kwenda uwanja wa ndege na kufanya uchunguzi ili wagundue ni ndege ipi ambayo ingemfikisha hapo nchini Marekani.
Wakapewa taarifa kwamba Bruno alipanda ndege ya Shirika la American Airlines na angeingia mahali hapo majira ya saa 05:43 usiku, hivyo walitakiwa kusubiri.
***
Gilbert na wenzake waliingia nchini Tanzania katika jiji la Tanga na kuanza kufanya upelelezi kugundua kile kilichokuwa kikiendelea. Walianza kuzunguka katika vituo vya polisi kwa lengo la kupata ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea.
Huko, wakaambiwa kwamba hakukuwa na taarifa yoyote ile juu ya mtu waliyekuwa wakimtafuta lakini kama wangewapa muda, basi bila shaka wangejua kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Japokuwa walikuwa katika kituo kikuu cha Tanga, wakaondoka na kuelekea katika vituo vingine vidogo, walikuwa na uhakika kwamba kama Sharifa alikuwa amepelekwa nchini humo basi ilikuwa ni lazima kupatikana hata kama kungetokea jambo gani.
Huko, wakapewa taarifa kuhusu Wazungu waliokuwa wamefika hapo Tanga na kuchukua chumba katika gesti moja ya uchochoroni ambapo huko walionekana wakiwa na mwanamke mmoja kutoka nchini Ghana.
“Mwanamke kutoka nchini Ghana?” aliuliza Gilbert.
“Ndiyo!”
“Ulimuona huyo mwanamke?”
“Hapana! Ila tuliambiwa na mwenye gesti kwamba walikuwa watalii,” alisema polisi aliyekuwa akijibu maswali kwa niaba ya mkuu wa kituo ambaye hakuwa mahali hapo.
Hapo hakukuonekana kuwa msaada tena, wakahisi kabisa kwamba watu hao ambao waliambiwa kuhusu stori zao na kwamba walikuwa na mwanamke kutoka nchini Ghana iliwezekana kabisa wakawa watu waliokuwa wakiwatafuta, wakaelekea katika gesti hiyo huku wakisindikizwa na polisi, walipofika, wakaingia ndani.
Wakakutana na mhudumu na kumuuliza kuhusu Wazungu hao, aliwaambia kwamba walikuwa ndani hivyo kwenda katika chumba walichokuwa wamechukua huku Gilbert na wenzake wakiwa na bastola mikononi mwao kwa ajili ya jambo lolote baya lile ambalo lingetokea huko.
Walipokifikia chumba, wakaufungua mlango na kuingia ndani huku wakiwa na bastola zao. Walipofika, hakukuwa na mtu yeyote yule, Wazungu wale ambao waliambiwa kwamba walikuwa humo na mwanamke mmoja, hakukuwa na yeyote yule, chumba kilikuwa kitupu kabisa.
“Wapo wapi?” aliuliza polisi.
“Mmh! Walikuwa humu! Sijui wapo wapi!” alisema jamaa mwenye gesti.
Wakatoka kwa kuhisi kwamba watu hao walikuwa wamekwenda sehemu fulani hivyo walitakiwa kuwawahi. Nje, kila kona hawakufanikiwa kuwaona watu hao zaidi ya wananchi kuwashangaa tu kwani kwa tukio lililokuwa likitokea siku hiyo kila mtu lilimshangaza kwani haikuwa na kawaida kwa Wazungu kuwa katika hali kama waliyokuwa wale wa mwanzo na hata hao wa kipindi hicho.
“Wametoroka! Wamekwenda naye wapi?” aliuliza Gilbert, kwa kumwangalia tu usoni alionekana kuwa na hasira kupita kawaida.
***
Sharifa alikuwa akikimbia huku akiangalia nyuma, kila mtu aliyekuwa akipishana naye alimshangaa, hawakujua kitu kilichokuwa kimetokea mpaka msichana huyo kukimbia huku akionekana kuwa na hofu kubwa.
Alikimbia mpaka alipofika mahali kulipokuwa na nyumba nyingi zilizokuwa milango wazi, hakutaka kuendelea kukimbia tu kwa kuona kwamba angekamatwa kwa kuwa hakuwa na kasi, hivyo akaingia ndani ya nyumba moja na kuomba msaada.
Watu walikuwa vyumbani mwake, wakatoka na kumwangalia Sharifa aliyekuwa ukumbini, aliwaambia watu hao kwamba alihitaji msaada kwa kuwa alikuwa akikimbizwa.
Wakati akiwa hapo ukumbini, akamuona Tim akipita nje kwa kasi huku akikimbia, Sharifa akajificha kwani hakutaka kuonekana na mwanaume huyo. Watu wote wakabaki wakimshangaa, kwao, alionekana kama mtu aliyekuwa na matatizo fulani, yaani kama changudoa aliyemkimbia mteja gesti.
“Bibie vipi?” aliuliza mwanamke mmoja.
“Kuna mtu ananikimbiza anataka kuniua,” alisema Sharifa huku akiangalia huku na kule, kwa kifupi alikuwa na wasiwasi.
Kwa lafudhi yake tu, kwa jinsi alivyokiongea Kiswahili chake hakukuwa na swali kwamba msichana huyo alikuwa Mkenya. Mwanamke mmoja akamchukua na kumuingiza chumbani mwake na kumuuliza tatizo alilokuwanalo ambapo akaanza kumwambia kila kitu kilichotokea.
Alishangaa, hakuamini kama kweli kungekuwa na watu ambao wangetoka nchini Marekani mpaka Kenya kwa lengo la kumteka mtu fulani, haikumuingia akilini, wakati mwingine aliona kama alikuwa akidanganywa na msichana huyo lakini akaamua kukubaliana naye.
“Nikusaidie nini?” aliuliza mwanamke huyo baada ya kusikiliza maneno ya Sharifa.
“Nataka kuwasiliana na mume wangu! Naomba unisaidie,” alisema.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, akampa simu na msichana huyo kumpigia Bruno aliyekuwa nchini Kenya, baada ya sekunde kadhaa alikuwa akiongea naye.
Alimwambia mahali alipokuwa, Bruno aliposikia hivyo, alichanganyikiwa, hakuamini kama mpenzi wake alitoroka mikononi mwa watu hao na hivyo kuanza safari ya kuelekea Tanga.
Hakuwa akienda peke yake, aliwasiliana na polisi na kuwaambia kila kitu kilichotokea kwamba mpenzi wake alikuwa salama kabisa nchini Kenya hivyo alitakiwa kwenda huko na kumchukua.
Njiani, Bruno alikuwa na presha kubwa, moyo wake ulikuwa umekwishakata tamaa na alihisi kabisa kwamba huo ungekuwa mwisho wa kumuona mpenzi wake huyo akiwa mzima, kitendo cha kumwambia kwamba aliwatoroka watu wale kilimfanya kuwa na furaha kupita kawaida.
“Ila kawatoroka kweli au wanamtumia ili kunipata mimi?” alijiuliza Bruno, upande wake mwingine ulionekana kuwa na wasiwasi.
“Haiwezekani! Kama ingekuwa wanamtumia, wangemwambia aniambie niende peke yangu,” alijijibu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Polisi hao wa Kenya walichokifanya ni kuwasiliana na polisi wa Tanzania kupitia Interpol na kuwaambia kile kilichokuwa kikiendelea.
Wao, yaani polisi wa Tanzania walitakiwa kwenda mahali alipokuwa Sharifa na kumchukua lakini baada ya Bruno kuambiwa hivyo, hakutaka kabisa hilo litokee, alichohitaji ni kwenda yeye mwenye mpaka alipokuwa mpenzi wake na kumchukua.
Baada ya saa kadhaa, wakafika Tanga. Akampigia simu Sharifa ambaye alimpa mwenyeji na kumuelekeza mahali nyumba yake ilipokuwa. Kutoka hapo walipokuwa mpaka kulipokuwa na nyumba hiyo hakukuwa mbali sana kwani ni mwendo wa dakika ishirini kwa gari wakawa wamekwishafika.
Wakamkuta mwenye nyumba nje, wakamfuata na yeye kuanza kuwapeleka ndani ambapo huko Bruno akakutana na Sharifa, kwa furaha aliyokuwanayo, akamsogelea na kumkumbatia.
“Walitaka kuniua,” alisema Sharifa huku akilia, alikuwa amekumbatiana na Bruno tu.
“Wasingeweza. Nipo pamoja na wewe, kukumaliza wewe inamaanisha walihitaji vita na mimi,” alisema Bruno huku akiwa amemkumbatia mpenzi wake huyo.
Wakamchukua na kuanza safari ya kurudi Mombasa. Njiani, kila mmoja alionekana kuwa na furaha, mioyo yao ilifurahia kuungana tena kwa mara nyingine tena.
Baada ya saa kadhaa wakafika Mombasa ambapo huko, kitu cha kwanza kilikuwa ni kwa Bruno kuwasiliana na akina Gilbert na kuwaambia kile kilichotokea na hivyo kukutana na kuzungumza.
Wao wenyewe walifurahi lakini bado walionekana kuwa na hofu na usalama wa maisha ya Bruno. Walijua kabisa kwamba kama lengo la kumteka Sharifa lilikuwa ni kuhakikisha kwamba Bruno haendi nchini Marekani basi ingekuwa ni lazima watu hao wafanye jambo lolote lile kuhakikisha mwanaume huyo hatoi ushahidi katika kesi hiyo.
“This is not the end,” (huu si mwisho) alisema Gilbert huku akimwangalia Bruno.
“What do you mean,” (unamaanisha nini?)
“They are going to look for you,” (watakutafuta)
“And kill me?” (na kuniua?)
“That what they want. Bruno, we have to take you to USA by ourselves,” (Hicho ndicho wanachokitaka. Bruno, tutakupeleka Marekani sisi wenyewe) alisema Gilbert.
Hicho walichokifanya, baada ya siku mbili wakaanza safari ya kuelekea nchini Marekani. Kwa kuwa walikuwa na uhitaji wa kuwapata watu hao, hawakutaka kujionyesha, ilikuwa ni lazima na wao wajifanye abiria ili iwe rahisi kwao kufanikiwa kwa kile walichokuwa wakikitaka.
Ndege ilichukua saa zaidi ya ishirini angani na ndipo ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK. Abiria wakaanza kuteremka akiwemo Bruno. Walitembea kwa mwendo wa taratibu kuufuata mlango uliokuwa ukielekea katika jengo la uwanja huo.
Hakuonekana kuwa na hofu hata kidogo, alijiamini mpaka alipochukua begi lake lililokuwa limechunguzwa na kuanza kutoka nje ya jengo lile.
Alipofika, harakaharaka mwanaume mmoja akamfuata na kumwambia kwamba alikuwa dereva teksi ambaye alitumwa na mwanaume aliyeitwa Todd kwa lengo la kumpokea.
“Alikuagiza?” aliuliza Bruno.
“Ndiyo! Au nimekuchanganya?”
“Ni mimi! Nilidhani ungekuwa na bango lililokuwa na jina langu,” alisema Bruno huku akiachia tabasamu pana.
“Hapana! Alinionyeshea picha yako. Karibu,” alisema mwanaume huyo huku akimpa mkono, wakaanza kuifuata teksi iliyokuwa maeneo hayo.
Bruno akaingia ndani ya teksi ile, hakuonekana kuwa na hofu hata kidogo, aliamini maneno aliyoongea mwanaume yule kwamba alitumwa na mzee Todd kwenda kumchukua hapo uwanjani.
“Ni mara yako ya kwanza kufika hapa?” aliuliza mwanaume huyo.
“Ndiyo! Ni mara yangu ya kwanza, nimekuja kutoa ushahidi kwenye kesi yake kisha nitarudi Kenya,” alijibu huku tabasamu likiwa usoni mwake.
“Ooh! Sawasawa! Nadhani atafurahi sana akisikia umefika salama,” alisema dereva, safari ikawa inaendelea kama kawaida.
Tim na wenzake wakajipanga vilivyo, ilikuwa ni lazima Bruno atekwe uwanjani na kupelekwa sehemu kwa lengo la kuuawa na kisha mwili wao kuutupa.
Hilo likapangwa na hivyo kuanza kumtafuta dereva ambaye walimwambia kuwa ingekuwa vizuri kama angekwenda uwanjani hapo na kumchukua Bruno na kujifanya kwamba alikuwa ametumwa.
Siku ilipofika, Tim akaenda na dereva huyo mpaka uwanja wa ndege, akachukua namba yake ya simu na wakati abiria wanatoka ndani ya jengo la uwanja huo, alikuwa akizungumza naye na alipomuona Bruno, akamwambia kwamba alikuwa mwenyewe na ndipo dereva huyo alipoanza kumfuata.
Alifuatilia kila hatua mpaka alipoingia ndani ya teksi na kuanza safari ya kuondoka mahali hapo. Mipango yao ilikuwa ni kwenda katika jengo moja lililokuwa hapohapo New York.
Hawakuchukua muda mrefu, wakafika, dereva akasimamisha gari, hapohapo akateremka na Kelly na mwenzake, Adson kutokea na kuanza kuifuata teksi ile, walipoifikia, wakaufungua mlango na kumtoa kwenye gari.
“What is going on?” (nini kinaendelea?) aliuliza Bruno huku akionekana kushangaa.
“Shiiiiiiiiii!” alimnyamazisha Kelly huku akiwa na kipande cha nondo mkononi mwake.
Wakambeba na kuondoka naye, wakamuingiza ndani ya jumba hilo, kitu kilichokuwa kikitakiwa kufanywa haraka ni kumuua na kisha kuuacha mwili wake hapohapo na wao kuondoka.
“Don’t kill me, please,” (tafadhai, msiniue) alisema Bruno lakini hakukuwa na mtu aliyejali, kila mmoja alichokuwa akikihitaji mahali hapo ni kuona mwanaume huyo akifa haraka sana.
***
Gilbert na wenzake walikuwa wakifuatilia kila kitu, waliteremka kutoka ndani ya ndege huku wakimwangalia Bruno, walikuwa makini naye na waliamini kwamba kwa namna moja ama nyingine ilikuwa ni lazima watu wamfuatilie kwa sababu kile alichokuwa akienda kukifanya nchini Marekani kilionekana kuwa kitu hatari.
Waliingia ndani ya jengo la uwanjani hapo huku wakiwa pamoja naye, walijifanya abiria na ilikuwa vigumu kwa watu wengine kugundua kwamba watu hao walikuwa pamoja kwani walijitenga naye kupita kawaida.
Walipofika nje, wakamuona akiongea na dereva teksi, kwa jinsi walivyoongea, walionekana kama watu waliokuwa wakifahamiana, akaambiwa aingie ndani ya gari, akafanya hivyo.
Gilbert na wenzake hawakutaka kuchelewa, walikuwa na uhakika kabisa kwamba dereva teksi yule alikuwa ametumwa hivyo kuanza kuifuatilia teksi ile.
Walikuwanayo kwa umakini kabisa, hawakutakiwa kuwa na presha yoyote ile, ila walitakiwa kuwa makini kwa kuwa kama wangekosea hatua moja basi Bruno angeweza kuuawa.
Waliifuatilia teksi ile mpaka ikafika mahali fulani, nje ya nyumba moja, kwa jinsi walivyoangalia huku na kule, haikuwa vigumu kugundua kwamba eneo hilo lilikuwa la hatari sana, wakazima taa za gari lao na kisha kulisimamisha kwa mbali kidogo huku macho yao yakiwa katika teksi ile iliyokuwa imesimama.
“Tufanye nini? Tupige risasi?” aliuliza Putt.
“Hapana! Subiri kwanza!” alisema Gilbert.
Hapohapo wakamuona Kelly akielekea ilipokuwa teksi ile, akaufungua mlango huku akiwa na kipande cha nondo. Hakuwa peke yake, alikuwa na Adson ambapo wakambeba Bruno na kuingia naye ndani ya jumba lile.
“Tuwafuate?” aliuliza Bull.
Wakati wakiwa wamejiandaa, wakashtuka kuliona gari jingine likifika mahali hapo, mlango ukafunguliwa na mwanaume mmoja kuteremka.
Alikuwa Tim ambaye alikwenda uwanja wa ndege kuhakikisha kwamba Bruno anakamatwa. Alipofika maeneo yale, akasimamisha gari na kuteremka, naye akaingia ndani ya jumba lile.
Haraka sana Gilbert na wenzake wakateremka na kuanza kuelekea lilipokuwa jumba lile. Walikuwa na bastola mikononi mwao ili kuhakikisha wanafanya mauaji pale ambapo ingewabidi kufanya hivyo.
Walipofika katika dirisha la jumba lile wakaanza kuchungulia ndani. Wakawaona vijana wale wakiwa wamemuweka Bruno chini tayari kwa kuanza kumpiga.
Hawakuwa na bunduki, kama kumuua ilikuwa ni lazima wafanye hivyo kwa kutumia vipande vya nondo walivyokuwanavyo.
Kilichotokea ni kuanza kumshambulia Bruno na vipande vya nondo walivyokuwanavyo. Gilbert na wenzake walikuwa wakiangalia na kila walipotaka kuingia, Gilbert alikuwa akiwazuia kwa kuwaambia kwamba hawakutakiwa kuwa na presha hata kidogo.
“Watamuua!” alisema Putt huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Tunakusanya ushahidi, subiri!”
“Tunakusanya ushahidi?”
“Ndiyo! Subiri!”
Bruno alizidi kupigwa na vipande vya nondo ile mpaka akawaida hoi. Wakati wakijiandaa kummalizia, haraka sana Gilbert akanyoosha mkono wake uliokuwa na bastola, zilitoka risasi tatu mfululizo, kila mtu akapigwa, wakaanguka chini.
Gilbert na wenzake wakatoka kule walipokuwa na kuingia ndani, wakawafuata wanaume wale, wote watatu walikuwa chini wakiugulia maumivu, Gilbert hakutaka kuchelewa, hapohapo akawapiga risasi za vichwa Adson na Tim kisha kumuacha Kelly akiwa peke yake huku akiugulia maumivu.
Wakamshika Bruno pale alipokuwa, alikuwa amepasuliwa, alipigwa vibaya, hawakutaka kumuacha, wakamchukua na kumpeleka ndani ya gari huku wakiwapigia simu polisi na kuwaambia kwamba walitakiwa kuelekea katika jumba lile kuchukua maiti za waharifu ambao waliwashambulia kwa risasi.
“Na huyu?” aliuliza Putt huku akimaanisha Kelly.
“Tunaondoka naye!”
Japokuwa alikuwa na maumivu makali, hawakutaka kujali, walimchukua kwa kumshika hovyohovyo mpaka ndani ya gari na kuliondoa mahali hapo.
Njiani Kelly alikuwa akilia, alisikia maumivu makali katika paja lake la kulia, damu zilikuwa zikimtoka lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyejali. Walimchukua mpaka hospitalini na kumtaka kutibiwa huku akiwa chini ya ulinzi mkali.
Kwanza risasi ikatolewa na kuendelea na matibabu mengine. Wakati huo, pia Bruno alichukuliwa na kupelekwa katika chumba kingine na madaktari kuambiwa kwamba walitakiwa kuhakikisha mwanaume huyo anapona haraka iwezekanavyo kwa kuwa walikuwa na kazi naye.
Wakati hayo yote yakiendelea, mzee Todd alikuwa selo, kama kawaida yake alikuwa akilia mno, moyo wake ulimuuma kwa kuwa aliona kama Bruno alimsaliti kwa kile kilichokuwa kikiendelea.
Hakupokea taarifa yoyote ile, moyo wake uliumia kwani miongoni mwa watu aliokuwa akiwaamini alikuwa Bruno, na yote hiyo ni kwa sababu alikuwa naye kwa kipindi kirefu na hata kumpa kiasi kikubwa cha pesa.
Siku zikaendelea kukatika, baada ya siku ya kusikiliza tena kesi hiyo kwa upande wa mashahidi ilipofika, Bruno akachukuliwa na kupelekwa mahakamani huku akiwa amefungwa bandeji katika sehemu kubwa kichwani mwake kwani alikuwa amejeruhiwa mno.
Watu wengi hawakujua sababu ya mwanaume huyo kufika mahakamani, wengi walihisi kwamba inawezekana alikuwa na kesi kama watuhumiwa wengine ambao walikuwa wakifika hapo huku wakiwa wamejeruhiwa.
Baada ya dakika kadhaa, gari lilobeba watuhumiwa ambao walitakiwa kusimama kizimbani na kujibu mashtaka yao wakafika mahali hapo.
Haraka sana waandishi wa habari wakaanza kusogea na kuanza kupiga picha. Mtu waliyekuwa wakimtaka alikuwa mzee Todd, waliihitaji picha yake mno kwa kuwa ndiye mtu aliyekuwa akijulikana kuliko wote ambao walikuwa wakifikishwa mahakamani katika kipindi hicho.
Kwa kumwangalia tu isingekuwa vigumu kugundua kwamba moyo wake ulivunjika nguvu, mwili wake ulipungua kwa sababu ya kuwa na mawazo mengi. Alikuwa akiifikiria familia yake lakini pia aliifikiria kesi hiyo ambayo ilikuwa ikimuelemea.
Akaingia ndani, akawekwa katika kiti kimoja na kuambiwa kutulia hapo. Hakujua kama Bruno alikuwemo mahakamani, alichohisi ni kwamba alikuwa amesalitiwa na mwanaume huyo.
Wakili wake alikuwa mbele kabisa, yeye mwenyewe alionekana kuwa na hofu moyoni mwake, kila alivyokuwa akiiangalia kesi ile alikuwa na uhakika kwamba mteja wake angeshindwa kesi ile.
CIA walifanya kila kitu kwa siri kubwa, hakukuwa na mtu aliyetakiwa kujua kilichokuwa kikiendelea kuhusu mashahidi kwani walimficha Bruno kwa nguvu zote na ndiyo maana hata mzee Todd hakuambiwa kitu chochote kile, alitakiwa kumuona Bruno kwa kushtukiza mahakamani hapo.
Hakimu alipokuwa akiingia, watu wote wakasimama kama kumpa heshima na alipokaa, wakakaa na kutulia. Kesi ikaanza, kama kawaida ikaanza kusomwa kwa dakika chache, ilipoanzia mpaka siku hiyo ambapo mashahidi walitakiwa kusimama na kusema kile kilichokuwa kimetokea.
“Shahidi namba moja anaitwa Bruno,” alisema hakimu, mzee Todd akashtuka kulisikia jina hilo, alikuwa ameinama, akauinua uso wake.
Akamuona mwanaume mmoja akisimama na kuanza kuelekea kizimbani, kwa kumwangalia tu ilikuwa ni rahisi kugundua kwamba alikuwa kwenye maumivu makali, alitembea kwa msaada wa Gilbert ambaye alikuwa pembeni yake na kumpeleka mpaka kizimbani.
Kila mtu aliyekuwa mahali pale alikuwa akishangaa, hawakumjua mwanaume huyo, alikuwa amezungushiwa bandeji, na kwa usoni yalionekana macho tu kwani alikuwa amejeruhiwa vibaya.
Akanyoosha mkono wake wa kulia na kisha kujitambulisha na kuiambia mahakama kwamba kila kitu ambacho angekwenda kukizungumza mahali hapo kilikuwa cha kweli kabisa na asingezungumza uongo hata kidogo.
“Naitwa Bruno Mike Onyambe!” alijitambulisha na mahakama kuanza kusikiliza ushahidi wake.
Alianza kusimulia kila kitu baada ya yeye kutoswa ndani ya maji na baadaye kuokolewa na watu waliokuwa katika meli ambayo aliikumbuka kwa jina lake, iliitwa Britannian Cargo P56 kwani iliiandikwa ubavuni.
Mule ndani, akaepelekwa ndani ya chumba ambacho akakutana na mzee huyo akiwa amefungwa huko na hivyo kuanza kuzungumza.
Hakutaka kuishia hapo, alisimulia kila kitu mpaka mzee huyo alivyokuwa akitafutwa na vijana ambao walipokea maelekezo kutoka nchini Marekani na hata wakati familia yake ilipokuwa ikiuawa, walikuwa Afrika Kusini na waliiona taarifa hiyo kwenye televisheni.
“Hakukuwa na kipindi kigumu kwa mzee Todd kama kipindi hicho. Alilia sana, hakuamini alichokuwa akikiona, iliniumiza sana moyoni mwangu, kwa nilivyokuwa nikimwangalia, niliyaona mapenzi yake makubwa aliyokuwanayo kwa familia yake. Mara nyingi aliniambia kitu kimoja tu kwamba kuna mtu anaitwa Maxwell ndiye aliyekuwa amesababisha yote hayo, alitaka kumuona akiingia gerezani ili afanye biashara zake kwa uhuru zaidi,” alisema Bruno, mahakama nzima ilikuwa kimya.
Alitumia dakika arobaini na tano, alipomaliza, akashuka kizimbani. Mzee Bruno alikuwa akilia, hakuamini kilichokuwa kikitokea. Ushahidi wa Bruno ulimkumbusha mbali kabisa, ulimkumbusha familia yake na mateso makubwa aliyoyapata alivyokuwa ndani ya meli.
Alipomaliza, akanyamaza. Akaanza kuulizwa maswali kutoka upande wa jamhuri na kila alipokuwa akiulizwa, alijibu kama ilivyokuwa ikitakiwa.
Alipomaliza, akateremka na kisha hakimu kusema kwamba kulikuwa na ushahidi kutoka CIA ambao ulikuwa ni wa kina kwa kuwa ulifuatiliwa kwa hatua zote.
Akaanza kuusoma ushahidi huo ambao ulieleza mambo mengi kuhusu mchezo ulivyokuwa na moja kwa moja ulikuwa ukimuweka hatihani mzee Maxwell.
“Vijana walifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Ni kweli mzee Maxwell alikwenda Afrika, alipofika huko, akatekwa na kuingizwa katika meli iitwayo Britannian Cargo P56 ambayo ina usajili wa jina la Maxwell anayemiliki kampuni kadhaa nchini Marekani,” ulisema sehemu ya ushahidi huo na kuendelea:
“Nchini Afrika Kusini kulikuwa na kijana aliyekuwa akishirikiana naye, huyu aliitwa Xuso ambaye aliuawa siku chache zilizopita. Pale bandarini, Pretoria ndipo alipotaka kumalizia kazi yake kwani aliamini kuwa endapo angemuua Todd pale ingekuwa ni rahisi kwao kuupoteza mwili huo kwa kuwa walikuwa na watu wengi.”
“Walifanikiwa kwa kila kitu. Baadaye baada ya kugundua kwamba mzee Todd amekamatwa, alichokitaka ni kupoteza mashahid, hapa tunapoongea, kijana ambaye alikuwa karibu na Todd, Innocent, ameuawa na tulivyofuatilia tukagundua kwamba kijana huyo alianza kuweka ukaribu na Maxwell na alihusika katika kuweka madawa ya kulevya ndani ya nyumba ya Todd.”
“Yeye alifanikisha kutekwa kwa familia ya Todd, alihakikisha anashirikiana nao kwa ukaribu lakini waliposikia kwamba naye alitakiwa kuwa shahidi, wakamuua na mwili wake kuutupa baharini.”
“Bruno ambaye ni raia wa Kenya alipitia vikwazo vingi. Kwanza hakutakiwa kufika Marekani kwa kuwa Maxwell alijua kwamba mtu huyu alikuwa mwiba hatari sana. Wakamteka mchumba wake ili baadaye atishwe kwamba angeuawa kama tu angekanyaga nchini Marekani, bahati nzuri baadaye msichana yule alitoroka walipofika nchini Tanzania.”
“Hiyo haikutosha, wakapanga mipango wamteke uwanjani, walifanikiwa ila kwa kuwa maofisa wetu ni watu hatari, walifanikiwa kumuokoa katika mikono yao na kuwaua vijana wawili na kumbakiza mmoja,” ulisema sehemu ya ushahidi huo.
Mahakama nzima ilikuwa kimya ikisikiliza ushahidi uliotolewa na Shirika la Kijasusi la CIA. Kila mtu alikuwa makini kusikiliza, kile ambacho kilizungumzwa mahali hapo kilionekana kumshangaza kila mmoja.
Baada ya kutolewa kwa ushahidi huo mrefu ambao ulichukua saa moja, ndipo mahakama ikasimamishwa kwa muda kwani baraza la wazee lilitakiwa kulizungumzia jambo hilo kabla ya kutoa uamuzi wa kukamatwa kwa Maxwell.
Muda huo mzee Todd alikuwa akitokwa na machozi ya uchungu, hakuamini kile alichokiona kikiendelea, mbali na Bruno, hata CIA walikuwa upande wake kumtetea kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Alitamani kusimama na kumfuata Bruno na kumkumbatia kwani kwake, alikuwa mwanaume shujaa ambaye alimtetea mpaka pumzi ya mwisho kabisa.
Baraza hilo la wazee lilikaa kwa nusu saa nzima ndipo likatoka na mahakama kuendelea. Kitu cha kwanza kabisa kilichoamuriwa na mahakama ni kuachwa huru kwa mzee Todd lakini vilevile Maxwell alitakiwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani huku akitakiwa kusomewa mashtaka ya kushiriki katika mauaji ya familia ya mzee Todd na hata kifo cha Innocent.
Kesi ilipofungwa, mzee Todd akamsogelea Bruno na kumkumbatia, hakuamini kama alishinda kesi hiyo ambayo iliibua chuki kubwa mioyoni mwa Wamarekani kwa kuwa waliamini kwamba aliua na kukimbia nchini humo.
Akamshukuru sana kiasi cha kutokwa na machozi, walizungumza kidogo na kisha kuondoka ndani ya mahakama hiyo huku Bruno akiwa chini ya ulinzi mkali kwani hakukutakiwa kuachwa hata kidogo kwa ajili ya usalama wake.
Siku hiyohiyo Maxwell akakamatwa na siku iliyofuata kupelekwa mahakamani. Kesi yake ilikuwa nzito na iliyonguruma kwa miezi miwili na mwisho wa siku kukutwa na hatia na kuhukumiwa kifo kwa kuchomwa sindano ya sumu ya cynaide.
Kwa Bruno, aliendelea kutibiwa hospitalini nchini Marekani huku akiwa chini ya ulinzi mkali. Hakukutakiwa mtu yeyote kuingia ndani ya chumba chake zaidi ya daktari, mzee Todd na Sharifa ambaye alisafirishwa mpaka Marekani kwa ajili ya kumuona mpenzi wake.
Mzee Todd hakuacha kumshukuru Bruno, kwake, mwanaume huyo alionekana kuwa mkombozi aliyemuokoa katika mdomo wa kifo, hakutaka kumuacha hivi hivi kwani hata alipopona, akamuingizia kiasi cha dola bilioni moja kwenye akaunti yake ambapo kwa pesa za Kitanzania ilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni mbili.
Maisha ya Bruno yakabadilika, alikuwa masikini, aliyedharauliwa lakini mwisho wa siku alikuwa bilionea aliyeheshimika sana nchini Kenya.
Hakuacha kuwasiliana na mzee huyo, kwake, alikuwa kama baba yake kwani ndiye mzee ambaye alikaa naye kwa kipindi kirefu na kumfundisha maisha kuhusu umiliki wa pesa, biashara na mambo mengine mengi.
Baada ya miezi tisa kutimia, hatimaye Sharifa akajifungua mtoto wa kike na kumpa jina la Grace, yaani Rehema akiwa na maana kwamba kwa kile alichokuwa nacho, maisha aliyokuwa akiishi ni kama alipewa rehema tu kutoka kwa Mungu wa mbinguni.
Kutoka katika maisha ya dhiki, kuishi katika kijumba kibovu alichoachiwa na wazazi wake mpaka kuishi kwenye bangaloo kubwa, hakika ilikuwa ni ndoto moja ya kusisimua kupita kawaida.
“Kila kitu kilipangwa na Mungu. Mtu wa kwanza kumshukuru ni baba yako, bila yeye, nisingekutana na mzee Todd, bila yeye nisingekuwa hapa nilipokuwa,” alisema.
Aliendelea kufungua kampuni nyingi, kwa kuwa aliamua kuwekeza kwenye uvuvi pia, akanunua meli kubwa iliyokuwa ikisafiri mbali kwenda kuvua huku akimuweka Abdul kuwa kiongozi lakini pia hakuangalia ubaya, akamchagua James na mwenzake ambao ndiyo waliomtosa baharini na kuwapa vyeo kwa kuamini kwamba pia watu hao wawili walichangia kuyabadilisha maisha yake.
Hakuangalia kisasi, alisahau kila kitu, nguvu ya upendo ilikuwa na uwezo wa kubadilisha kila kitu, hicho ndicho alichokikumbuka ambacho alihubiriwa mara kwa mara kanisa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Upendo unapozidi, kisasi kinakufa, namshukuru Mungu kwa kuyabadilisha maisha yangu na kuniweka hapa. Tulimuomba Mungu sana siku moja tuishi pamoja, na hapa tunaishi pamoja, siku si nyingi kuanzia leo tutafunga ndoa,” alisema Bruno huku akimwangalia Sharifa.
“Nakupenda sana, nakupenda zaidi kwa kuwa umekuwa mtu wa msamaha kwa kila aliyekutendea ubaya,” alisema Sharifa.
“Hilo ndilo ambalo Mungu anatuagiza kila siku. Tunatakiwa kusamehe hata kama tulikasirishwa na kupata maumivu makubwa kiasi gani,” alisema Bruno, hapohapo akamkumbatia mpenzi wake huyo na kujifunika shuka, kilichoendelea, hakifai kuandikwa mahali hapa.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment