Search This Blog

Monday 24 October 2022

SIRI ILIYOTESA MAISHA YANGU - 1

 

    IMEANDIKWA NA : ERIC SHIGONGO



    *********************************************************************************





    Simulizi : Siri Iliyotesa Maisha Yangu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Harry Robertson

    Arusha Secondary School,

     1979:

    “Sababu ya kumpiga tunayo! Nia ya kumpiga tunayo! Na uwezo wa kumpiga Nduli   Idi Amin tunayo, ni lazima tumpige!”

    Ilikuwa ni sauti ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiongea na wapiganaji wa Jeshi la Wanachi Watanzania katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

    Hofu ya vita ilikuwa   imetanda  Tanzania nzima, watu wote hasa wakazi  wa mikoa ya kanda ya ziwa kama Mwanza, Kagera na Mara ambayo ipo jirani na nchi ya Uganda walikuwa na hofu kubwa mno!Wengi walishaanza kuikimbia mikoa yao  kwenda  mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Tanga, iliyokuwa mbali na nchi ya Uganda, walifanya hivyo kuyaogopa makombora ya Nduli.

    Miongoni mwa watu waliokimbia alikuwemo mwanamke  wa Kihaya aliyeitwa Agripina Rwechungura na mtoto wake mdogo wa kiume Harry Robertson, alikuwa mtoto mzuri sababu ya mchanganyiko wa damu aliokuwa nao, baba wa mtoto huyo alikuwa Mwingereza aliyekuja mkoani Kagera kufanya utafiti  wa zao la Kahawa.

    Alikutana na Agripina  mwaka 1973 na wakawa na uhusiano wa  kimapenzi ndipo akazaliwa mtoto huyo ambaye kwa pamoja waliamua kumwita jina la Harry, alikuwa mtoto mzuri kuliko jina lake! Kila mtu alimfurahia mtoto huyo, mchanganyiko wa damu ya kizungu uliifanya ngozi yake iwe  na rangi ya  senti tano! Rangi adimu ya ngozi.

    “Huyu mtoto akikua atakuwa tishio, wenye binti zao ni lazima wawe waangalifu sana, atapiga mimba sana huyu!” Alisema mzee mmoja  Harry na mama yake walipoteremka katika mabasi mjini Arusha.

                   *****************

    Mkoani  Kagera waliishi mjini Bukoba ambako mzungu Robertson alimnunulia Agripina nyumba kabla ya kuondoka nchini kurejea  nyumbani kwao Uingereza mkataba wake ulipokwisha, mjini Arusha Agripina alitegemea kuishi nyumbani kwa dada yake mkubwa Dk. Swai aliyefanya kazi katika hospitali ya mkoa wa Arusha Mount Meru kama daktari wa magonjwa ya wanawake.

    Agripina na mwanae walipokelekwa vizuri na Dk. Swai aliyeishi maeneo ya Uzunguni mjini Arusha ambako yeye na mume wake Eric Swai mfanyabiashara maarufu mjini humo waliishi katika nyumba ya kifahari waliyojenga wenyewe, ilikuwa nyumba kubwa mno na waliamua kuwakaribisha Agripina na mtoto wake kuishi nao bila wasiwasi wowote.

    Jioni ya siku hiyo waliongea mengi kuhusu nyumbani, Agripina alimweleza Dk. Swai kila kitu kilichotokea Bukoba, pia alimfahamisha kuhusu kuondoka kwa mzungu Robertson nchini na kumwachia mtoto lakini akiwa amemnunulia nyumba kubwa ya kifahari.

    “Kama kakununulia nyumba basi inatosha, ukiongeza na hilo toto la nguvu alilokuachia huna wasiwasi huu ni utajiri tosha! Mtoto wako ni mzuri sana Agripina niamini, sijapata kuona mtoto mzuri kama huyu  hapa Afrika  labda kwenye televisheni, unachotakiwa kufanya sasa  ni kuhakikisha   unampa  Harry elimu bora!”

    “Ahsante nitafanya kila kinachowezekana kumtafutia shule nzuri, huko Bukoba alisoma katika shule ya kimataifa ya Rugambwa, alifanya vizuri sana katika masomo yake ya darasa la kwanza!” Alijibu Agripina na waliongea mengi sana Harry akimsikia.

    Harry alikaa kimya kwenye kochi pembeni akiwa amekuja nne na mdomo wake ukiwa amechomekewa vizuri  kuingia ndani, hiyo ilimfanya apate vishimo katika mashavu yake, ambavyo watu huviita ‘Dimpos’ sifa za kwamba Harry  alikuwa mtoto mzuri zilimfanya ajisikie vizuri na aone yeye alikuwa bora kuliko watoto wengine wote duniani.

    “Sijui na yeye anajua kuwa ni mzuri  ona mapozi yake!” Dr Swai alimtania Harry huku akimchezea shavu lake la kulia, Harry alitabasamu na kuifanya sura yake ionekane ya kuvutia  zaidi, Agripina alijisikia vizuri kuwa na mtoto kama Harry! Alifurahi kukutana na mzungu Robertson kwani alimpa alichokitaka.

            ********************

    Mwezi mmoja baada ya kufika mkoani Arusha, vita ilikuwa imepamba moto mpakani mwa Tanzani na Uganda! Harry alikuwa tayari katika shule  ya kimataifa ya Arusha darasa la kwanza! Siku alipopelekwa  kuandikishwa katika shule hiyo waalimu na wanafunzi walipigwa butwaa kwa uzuri wa  sura ya mtoto huyo,  walimu walivutana kila mwalimu akitaka asome katika darasa lake! Baada ya mvutano wa muda mrefu  hatimaye Harry aliandikishwa katika darasa la kwanza E.

    “Mwalimu darasa lako lina wanafunzi wazuri wawili!”Mwalimu mmoja alimuuliza mwalimu wa darasa la kwanza E.

    “Yupi mwingine?”

    “Si Caroline!”

    “Ah!Ndiyo nilitaka kusahau, kwa hiyo ninao Mr na Miss Arusha School au siyo?”

    “Mshindi  ni wewe bwana!” Walitaniana walimu lakini huo  ndio ulikuwa   ukweli, Harry na Caroline walilifanya darasa la kwanza E kuwa darasa la aina yake, watoto hao wawili walikuwa na uzuri wa ajabu! Ili mwalimu  alipendezeshe zaidi darasa lake  aliwapanga Caroline na Harry katika  dawati moja!

    Harry na Caroline walitokea kuwa marafiki wakubwa na uwezo wao wa  darasani pia ulikuwa mkubwa   kuliko wanafunzi wengine, ushirikiano  wao katika masomo ndio uliowafanya wawe hivyo, wanafunzi  wengine waliwaonea wivu!

    Ni urafiki wao  ndio uliowafanya hata wazazi wao wafahamiane, Cynthia na Agripina walitokea kuwa marafiki wakubwa sababu ya kuzaa watoto wazuri, mara kwa mara walitembeleana nyumbani kwao na kuongea mipango mingi juu ya watoto wao baadaye.

    Pamoja na uzuri wote aliokuwa nao Caroline bado tatizo la kifafa lilimsumbua kwa kiasi kikubwa na lilimuumiza sana akili yake, alitamani angekuwa na ugonjwa mwingine wowote lakini si kifafa! Alianguka kila mwezi mara moja kati ya tarehe 26 hadi 28 za kila mwezi.

    Wazazi wake walijitahidi kumtafutia tiba lakini hazikusaidia dawa nyingi alitumia bila mafanikio yoyote!  Caroline alikuwa mzuri mno kuwa na kifafa na wazazi wake hawakutaka kabisa jambo hilo lijulikane, waliendelea kuufanya ugonjwa wa mtoto wao siri ya familia! Hata mtumishi wao wa ndani   hakulifahamu jambo hilo.

    Ili kuhakikisha kuwa Caroline haanguki mbele za watu na kuaibika ililazimu kila tarehe 26 hadi 28  ya kila mwezi   afungiwe ndani ya chumba chake cha kulala, ni wazazi wake  ndio walioruhusiwa kuingia ndani ya chumba hicho! Alisubiriwa mpaka aanguke kifafa ndio aendelee na masomo yake shuleni, chumba hicho hakikuwa na kitu chochote cha chuma au mbao kwa kuogopa kumuumiza wakati wa kuanguka.

           ********************

    Mpaka   anamaliza darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza Caroline alikuwa bado ni tishio kwa uzuri shuleni kwao  kasoro pekee aliyokuwa nayo ni   siri yake ya kifafa ambayo hakutaka kabisa  igundulike, watu wengi akiwemo Harry walijiuliza ni kwanini  kila tarehe 26 hadi 28 ya kila mwezi Caroline  hakwenda shule! Hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kutoa  jibu la swali hilo isipokuwa Caroline mwenyewe na hakuruhusu   swali hilo liulizwe na mtu yeyote!

     Kila aliyediriki kudadisi juu ya   kutokuja kwake shuleni  alibadilika na kuwa adui mkubwa wa Caroline! Lakini swali hilo hilo liliendelea kumuumiza Harry moyoni mwake hatimaye siku moja alifunga mkanda na kuamua kumwita Caroline na kumuuliza baada ya kumwona akiwa amevimba usoni! hakujua kama jana yake alianguka na kujipiga ukutani.

    “Caroline vipi mbona una ngeo?” Aliuliza Harry na swali hilo lilimuumiza sana moyo Caroline.

    “Jana nilianguka bafuni wakati naoga!”

    “Aisee, pole sana!”

    “Ahsante!” Alijibu Caroline.

    “Lakini Caroline kuna kitu kimoja nataka kufahamu!”

    “Kitu gani Harry!”

    “Mbona kila tarehe 26-28 ya kila mwezi huwa hauji shule?”

    “Harry ni mambo ya wanawake siwezi kukueleza!” Alijibu  Caroline akijaribu kudanganya kuwa  tarehe hizo hakwenda shule sababu ya hedhi! Harry aliamini na kujikuta akimwomba msamaha!

    “Samahani sana kwa kuingilia mambo yako ya ndani!”?“Hakuna shida!”

    Hata walipoingia kidato cha kwanza waliendelea kusoma darasa moja na kukalia dawati moja! Urafiki wao ulizidi kukomaa na utaratibu wa Caroline kutokuja shuleni kila mwisho wa mwezi uliendelea kuwepo, matibabu pia yaliendelea kufanyika lakini bado hakupona kifafa kiliendelea kumsumbua.

    Ugonjwa huo ulimnyima Caroline raha ya maisha, hakuwa kama watoto wenzake shuleni, kila siku alihofia kuanguka mbele za watu na alishindwa kuelewa kama ingetokea   akaanguka mbele ya wanafunzi wenzake waliomchukulia kama malkia wa uzuri ingekuwa vipi! Alijua ingekuwa aibu na hakutaka aibu hiyo itokee ndio maana alikuwa makini na tarehe.

    Urembo wake ulizidi kutisha  si kwa wanafunzi peke yao  bali hata walimu, watu walizidi kuchanganyikiwa na uzuri wa msichana huyo! Caroline alizidi kupanuka chini na kuwa mwembamba zaidi juu kadri siku zilivyozidi kwenda!  Wavulana wengi walimtaka mapenzi lakini Caroline aliendelea kuwakatalia, hakutaka kuwa na uhusiano na mvulana   kimapenzi kwani alijua ukaribu wao ungefanya siri  yake ijulikane!

    “Sitaki nitakaa hivi hivi!”Huo ndio ulikuwa uamuzi wake kila siku, hofu yake kubwa ilikuwa  kwa maisha yake ya baadaye, pamoja na umri wake kuwa mdogo bado alifikiria nini kingetoka siku za usoni, alijua yeye kama mwanamke   alitakiwa kuolewa na kuwa na watoto!

    “Ni mwanaume gani atakubali kuoa mwanamke mwenye kifafa?” Hilo ndilo lilikuwa swali lake la kila siku na lilimuumiza sana moyo, hakuogopa kuolewa tu bali pia aliogopa sana kuzaa watoto kwa  sababu alijua kifafa hurithishwa hadi kwa watoto!

    “Sitaki pia kuzaa sitaki mtoto wangu aje kuwa na matatizo kama yanayonikuta mimi!”

               *******************

    “Kwa nini mimi?” siku moja alijikuta akitamka maneno hayo yeye na Harry walipokuwa  wakisoma pamoja darasani.

    “Unasemaje Caroline?”

    “Hapana nilikuwa nawaza mambo fulani tu!”

    Siku zote Harry alihisi   kulikuwa na kitu kilichomsumbua Caroline lakini hakukifahamu kitu hicho kilikuwa ni kitu gani, mara kwa mara aliyaona macho ya Caroline yakiwa mekundu, ishara   alikuwa amelia muda mfupi kabla lakini alipoulizwa Caroline hakuwa tayari  kueleza ukweli.

    Waliendelea kuwa na urafiki wao hadi kidato cha tatu wote wawili mpaka  wakati huo walikuwa bado hawajajua tendo la ndoa lilikuwa kitu gani! Harry alisumbuliwa sana na wasichana lakini siku zote hakukubali.

    “Huyu ni wa Caroline bwana!” hivyo ndivyo wasichana walivyosema kwa fikra kuwa kulikuwa na uhusiano kimapenzi kati ya Harry na Caroline! Kitu ambacho hakikuwa kweli hata kidogo.

    Wakiwa kidato cha nne ghafla hali ya ajabu ilianza kujitokeza kati yao, Harry alijisikia kumpenda Caroline na Caroline alijisikia vivyo hivyo   lakini hakuna shujaa kati yao aliyeweza kuzieleza hisia zake! Mioyo yao  iliendelea kuteseka kwa miezi kadhaa bila kutoboleana ukweli, ndipo Harry alipoamua kuusema ukweli wake.

    “Caroline nimeishi na wewe kama dada yangu na rafiki  kwa muda mrefu lakini siku za hivi karibuni nimeanza kujisikia tofauti kidogo!”

    “Tofauti gani?”

    “Nakupenda Caroline! Sikudanganyi,  ninataka uwe mpenzi wangu na ikiwezekana tufunge ndoa siku moja!”

    Caroline hakuyaamini masikio yake alifikiri yamemdanganya, alitaka kukubali lakini alipoufikiria ugonjwa wake alisita kusema ndiyo! Alibaki kimya kwa muda akijaribu kutafuta kitu cha kusema!

    “Tafadhali nijibu Caro!”

    “Harry, hata mimi ninakupenda lakini nafikiri hutaniweza!”

    “Kwa nini?”

    “Nina matatizo!”

    “Matatizo gani?”

    “Siwezi kukueleza ila wazazi wangu hawafurahi kuona mimi na wewe tunakuwa wapenzi!” Caroline alificha lakini alitaka kuuelezea ugonjwa wake!

    “Nakupenda Caroline ina maana wazazi wako hawapendi mimi na wewe tuwe na familia siku moja?”

    “Basi nipe muda Harry ili nifikirie vizuri!”

    Baada ya kuachana Caroline alizidi kufikiria juu ya uamuzi wa Harry! Moyo wake ulimwambia akubali lakini akili yake iliogopa, kila  alipoifikiria picha ya kuanguka mbele ya Harry na kukakamaa alizidi kuogopa zaidi! Lakini wiki mbili baadaye alifikia maamuzi ya kukubali.

    “Sawa nimekubali Harry lakini katika siku zote za mwezi sitakuwa na wewe tarehe 26-28 kwani siku hizo huwa nipo katika hedhi!”

    “Sawa lakini…………!”

    “Lakini nini?”

    “Au basi tu hilo lisiwe kikwazo!” Harry alitaka kusema kuwa sikukuu yake ya kuzaliwa katika kila mwaka ilikuwa ni tarehe 26 mwezi wa saba!

               ****************

    Penzi lao lilichipuka na kukua kwa kasi ya ajabu   na kufikia kiwango ambacho wote wawili hawakukitegemea kabisa!

    Harry na Caroline walizidi kuchanganyikiwa katika mapenzi lakini Harry alichanganyikiwa zaidi kumzidi mwenzake, walitembea wakiwa wameshikana mikono kila walikokwenda! Walipigana mabusu mbele za watu bila kujali, Caroline alishindwa kuelewa siku ambayo Harry angegundua alikuwa na kifafa kingetokea nini! Alikuwa na uhakika angemwacha na alishindwa kuelewa angeishi vipi bila Harry!

    “Ni heri kufa kuliko kumkosa Harry!”

    Mpaka miezi michache tu kabla ya kufanya mitihani yao  ya kidato cha nne penzi lao lilikuwa juu mno! Karibu kila mtu shuleni alifahamu juu ya uhusiano wao    hata wazazi wa Caroline walilifahamu jambo hilo na lilisababishia   ugomvi mkubwa kati yake na mama yake mzazi Dk. Cynthia!

    “Umeyasahau matatizo yako siyo? Shauri yako utaaibika mwenyewe na ugonjwa wako!”

    “Nafahamu mama lakini nampenda sana Harry na  siwezi kumwacha tena ni heri kufa kabisa kuliko kumkosa  yeye nitajitahidi kumficha siri hii asifahamu!”

                   ************

    Mahafali ya kumaliza kidato cha nne yalipangwa kufanyika tarehe 27 mwezi wa saba ikiwa ni siku moja tu baada ya   sikukuu ya Harry ya kuzaliwa!  Harry alimpa Caroline taarifa hizo ili ajiandae na alisema   ilikuwa ni lazima ahudhurie sikukuu hiyo.

    “Tutafanya hiyo ndiyo siku  ya mimi na wewe kupongezana kwa  kumaliza shule pamoja na siku itakayofuata yatakuwa mahafali yetu itakuwa babu kubwa au sio?”

    Caroline alikaa kimya kwa muda na baadaye kuanza kulia machozi, alijua siku hizo zilikuwa ni mbaya sana kwake! Ni katika siku hizo ndiyo alianguka kifafa, alijua angeharibu uhusiano wake kimapenzi na Harry! Alijua wazi kama Harry angefahamu Caroline alikuwa na kifafa asingekubali kuwa naye tena maishani! Aliomba Mungu azibadilishe siku na kuzirudisha nyuma  jambo ambalo halikuwa rahisi hata kidogo kufanyika.

    “Harry sitahudhuria sikukuu yako na hata mafahali!”

    “Kwanini darling?”

    “Kwa sababu nilizokwishawahi kukueleza kuwa nitakuwa kwenye hedhi!” Caroline alidanganya.

    “Hilo mbona dogo utavaa padi za kutosha nina hakika hutajichafua mpenzi lakini lazima uwepo!”

    “Sawa lakini…..!”

    “Lakini kitu gani tena Caroline au hunipendi nini?”

    “Nakupenda Harry lakini hapana!” Caroline alizidi kuweka msimamo.

    “Usipohudhuria pati yangu mimi na wewe basi!” Alisema Harry akinyanyuka kutoka darasani walimokuwa wakisoma pamoja na kuanza kutoka nje.

    Caroline alimfuata nyuma huku akilia machozi, hakuwa tayari hata kidogo kumpoteza Harry! Hakuwa tayari kuachwa na mtu aliyempenda kiasi hicho, alimtupia lawama Nyingi Mungu na kuruhusu ugonjwa huu umpate yeye!

    “Kwa nini sikuugua ugonjwa mwingine wowote zaidi ya kifafa?” Alijiuliza Caroline huku akitembea kwa kasi.

    “Harry! Harry! Harry! Tafadhali simama unisikilize, nakupenda Harry!”

    Harry hakusimama alizidi kutembea kwenda mbele zaidi, Caroline alianza kukimbia akimfuata kwa nyuma  na alipomfikia Harry alimshika begani.

    “Nisikilize mpenzi!”
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimekwishasema kama hutakuja kwenye bethidei yangu mimi na wewe basi tena!”

    “Basi nitakuja darling lakini nitawahi kuondoka kurudi nyumbani!” Alijibu Caroline, alikuwa tayari kufanya lolote lakini asimpoteze Harry.

    “Sawa ili mradi ufike tu!”

    “Nitakuja darling usichukie eh!”

    “Sijachukia darling nakupenda Caroline!” Walicheka na kukumbatiana.

            *********************

    Siku ya Julai 26 watu walifurika ndani ya ukumbi wa Sunflower kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Harry Robertson! Caroline alikuwa ndani ya ukumbi huo akiwa mwenye wasiwasi mwingi, alikaa karibu kabisa na Harry, alivaa  gauni la kung’aa lililompendeza pengine kuliko  wasichana wengine wotte ndani ya ukumbi huo! Aliletewa gauni hilo na baba yake aliporejea kutoka Uingereza, ni siku hiyo ndiyo alilivaa kwa mara ya kwanza.

    Aliondoka nyumbani kwa kutoroka, hakumuaga mtu yeyote, wazazi wake waliamini alikuwemo ndani ya chumba   amejifungia, baadaye mama yake alipokwenda chumbani  alikuta hayupo! Alichanganyikiwa na kumpa taarifa hizo mumewe!

    “Yupo wapi?”

    “Kwa kweli sifahamu kabisa! Nimekuta chumbani hayupo jamani mtoto huyu anataka kutuaaibisha masikini!” Alisema mama yake. Walihisi  alikuwa amekwenda kujiua baada ya kukata tamaa  ya maisha ilibidi watoe taarifa polisi na   alianza kutafutwa kila  mahali.

                ******************

    Mpaka sa nne za usiku tafrija ilikuwa bado ikiendelea, watu walikuwa wakifurahia ndani ya ukumbi wa Sun flower lakini Caroline hakuwa na furaha hata kidogo, alihisi wakati wowote angeweza kuanguka.

    “Harry nataka kuondoka! Baba na mama watakuwa na wasiwasi sana!”

    “Kuondoka  kwenda wapi wewe kula starehe bwana, au hunipendi!”

    “Nakupenda!”

    “Basi kaa hapa na mimi nitakurudisha baadaye!”

    “Hapana!” Caroline alizidi kukataa hakuamini mpaka saa hizo alikuwa hajaanguka.

    “Sasa ni wakati wa kufungua muziki na watakaotufungulia muziki wetu ni mr na mrs watarajiwa, Harry na Caroline!” Dj alitangaza na Harry alinyanyuka na kumwomba Caroline amfuate katikati ya ukumbi.

    “No! No!No! Sitaki”

    “Kwanini?” Harry aliinama na kumuuliza.

    “Sitaki kucheza muziki! Nasema sitaki kama ni kuniacha basi uniache Harry!” Alisema Caroline ambaye tayari alishaanza kuona kizunguzungu machoni pake!

    Harry alimshika mkono na kumnyanyua kwa nguvu huku watu wakishangilia, ilibidi Caroline ajikaze na kwenda hadi katikati! Muziki ulipigwa kwa ajili yao.

    Wakiwa wamekumbatiana ghafla Caroline alianza kupoteza nguvu  miguuni na kuanguka chini! Akageuza macho yake kuangalia juu,  akaanza kutoa povu mdomoni, mwili wake  ulikakamaa na mkojo  mwingi ukamtoka!

    Watu wote ukumbini walishangaa kuona hali hiyo Harry alijishika mikono yake yote miwili kichwani hakukiamini kilichokuwa kikitokea  mbele yake! Hakuamini kama aliyelala sakafuni akitupa mikono na miguu  hewani alikuwa ni mpenzi wake aliyempenda Caroline! Harry alihisi ni ndoto.

    “Kha! Kumbe kujidai kote huko  shoga yetu ana kifafa, lo!” Alisema msichana mmoja nyuma ya Harry!

    “Masikini msichana mzuri huyu ana kifafa jamani!” mama mwingine alisema.

    Agripina mama yake Harry alisonga mbele ya watu na kumuingizia Caroline kijiko  kilichofungwa na kitambaa cheupe mdomoni ili asiume ulimu wake,  alikuwa akilia machozi.

    Nusu saa baadaye Caroline alizinduka na kuangaza huku na kule kama mtu aliyetoka usingizini, alishangaa kuona watu wote wamemzunguka yeye, nguo zake zililowa mkojo na mdomoni alikuwa na mapovu, alijua tayari amekwishaanguka!

    “Harry unaona sasa mambo yako ya kulazimisha?” Alimlaumu Harry.

    “Caroline kwanini hukuniambia una kifafaa?”

    “Niliogopa  Harry, nilijua ungeniacha! Nakupenda sana Harry hata mimi sikupenda kuwa hivi tafadhali usiniache”

    Badala ya  kujibu   Harry alianza kulia machozi, kuona hivyo Caroline alinyanyuka na kuanza kukimbia hadi  kwenye jiko la shule  ambako alichukua kamba iliyofungia kuni na kuanza kukimbia nayo kwenda msituni!

    “Ni heri nife tu!”

    Dakika tano baadaye Harry, alitoka mbio kwenda msituni kumfuata, alijua ni lazima Caroline alikuwa amekwenda kujiua! Hakumwona mahali popote msituni, alihisi bado alimpenda Caroline pamoja na kifafa alichokuwa nacho! Alitaka kumuokoa!

    “Caroliiiiiiiiiiiiiiiiiiiine! Caroliiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiine!Upo wapi, tafadhali  usijue bado ninakupenda hivyo hivyo ulivyo!” Alizidi kuita Harry akitembea katikati ya msitu lakini hakuna mtu aliyemwitikia alijua lazima Caroline amejiua! Sauti yake iliitikiwa na mwangwi.

    Je Caroline atakufa? Fuatilia wiki ijayo!













    U

    likuwa ni usiku wa giza ?nene lililotanda kila mahali ?lakini  Harry  hakuogopa  aliendelea kulia machozi  akipita katikati ya vichaka vyenye miiba chini ya miti mingi ya mikorosho, alikuwa akiliita jina la Caroline lakini  hakusikia sauti ya  kuitikiwa kutoka sehemu yoyote katika msitu huo! Sauti yake ilijibiwa na mwangwi uliomfanya ahisi ilikuwa ni sauti ya Caroline na kuzidi kuzama msituni akifuatilia! Kwa hakika kwa ukimya uliokuwepo alijua Caroline alikuwa amekufa!

    “Ni lazima atakuwa amejinyonga! Masikini Caroline wangu kwanini hakusubiri kidogo? Amechukua uamuzi wa haraka mno ni vyema angenisikiliza kwanza akasikia uamuzi wangu ungekuwa upi!” Alisema peke yake Harry huku akilia.

    Wakati akiwaza hayo upande mwingine wa  akili yake  haukulipitisha hilo kama jibu moja kwa moja  uliendelea kuamini   Caroline alikuwa hai na alikuwa mahali fulani akitafuta mahali pa kujinyongea, hilo lilimtia nguvu Harry na kumfanya azidi kuita akiamini muda mfupi uliofuata angeitikiwa lakini bado hapakuwa na jibu lolote.

    Moyoni mwake Harry  aliamini kifafa au ugonjwa wowote ule  kisingeweza kuwa kitu cha kumtenganisha yeye na msichana aliyempenda Caroline, roho ilimuuma   na alishindwa kuelewa angeishi vipi shuleni  katika muda waliobakiza bila kuwepo Caroline na alishindwa pia kuelewa angefanya nini kuzuia kifo kisitokee muda wote alihisi yeye ndiye alikuwa chanzo cha kifo cha Caroline kama kweli angefanikiwa kujinyonga!

    “Sikutakiwa kuonyesha mshangao hata kidogo si ajabu hiyo ndiyo ilimfanya Caroline afikiri nitamwacha!” aliwaza Harry.

    Ghafla wakati akitembea alishtuka aliposikia kwikwi za kilio  cha mtu zikitokea juu ya mti mkubwa wa mkorosho uliokuwa pembeni mwa njia!   Haikumchukua muda mrefu kugundua  sauti aliyoisikia  ilikuwa ya Caroline bila kuchelewa alianza kunyata akitembea kwenda chini ya mti huo.

    Alipoufikia alianyanyua  uso wake na kuangalia juu  kwa sababu ya giza lililokuwepo na majani mengi ya mti huo yaliyotanda kila mahali hakuweza kuona kitu chochote lakini kwikwi za mtu akilia ziliendelea na ndani ya kwikwi hizo alisikia jina lake likitajwa mara kwa mara.

    “Ee Mu....ngu kwanini ulini...umba mimi hivi? Kwani..ni ume..ninya...nga...nya Harry?” Sauti hiyo iliendelea kusikika kutoka  juu  ya mti.

    “Caroline, nakupenda tafadhali sana usijaribu kujiua!  Nakupenda kwa jinsi ulivyo tafadhali   usidiriki kuutoa uhai wako nakupenda Caroline! Kifafa si kitu cha kututenganisha mimi na wewe hata siku moja na hata ungekuwa Ukimwi bado tusingetengana! Tafadhali nipe nafasi nyingine ili uone kama nitakuacha au la! Siwezi kufanya hivyo mpenzi!”Harry alisema huku akipanda mtini   kujaribu kumuwahi Caroline  aliyekuwa amevaa kamba shingoni tayari kwa kujinyongakabla hajajirusha mtini!

    Machozi yalikuwa bado yakiendela kumbubujika  Harry kwa wingi, alikuwa akimlilia Caroline hakutaka afe! Ni wazi alimpenda na hakutaka kumpoteza katika maisha yake.

    Ingawa hakuwa na uhakika kama angeweza kuwahi kabla hajajirusha, Harry  alizidi kutembea juu ya tawi la mti  akimwomba Mungu amduwaze Caroline mpaka amfikie! Lakini akiwa hatua kama mbili hivi  kabla hajamgusa  alishangaa kwa macho yake kumshuhudia Caroline akijirusha na kuning’inia mtini! Kamba ilimkaza shingo na macho yakaanza kumtoka.

    “Caroliiiine don’t do it! (Caroline usifanye hivyo!) Alisema Harry lakini alikuwa amechelewa kwani tayari Caroline alikuwa   akining’inia mtini ulimi wake ulianza kutoka nje!

    Harry alilia kwa uchungu na kujaribu kuivuta ile kamba kwa juu akifikiri angeilegeza shingoni kwa Caroline lakini kwa kufanya hivyo ndiyo alizidi kuikaza! Hakuwa na la kufanya tena mwili wake ulikufa ganzi! Alipoangalia saa yake ya mkononi aligundua tayari ilikuwa saa nne na nusu ya usiku.

             ********************

    Msako wa Caroline:

    Polisi kwa kushirikiana na wazazi wa Caroline bado waliendelea kumtafuta  kila mahali mahali mpaka wakajikuta wamefika katika hoteli ya Sunflower  baada ya kuelezwa na watu kuwa uwezekano wa Caroline kuwa katika hoteli hiyo ambako rafiki yake mpendwa Harry alikuwa akifanya sherehe ya kuzaliwa  ulikuwa mkubwa.

    “Sasa si ni heri angesema  tu kuwa anakwenda kwenye tafrija  kuliko  kutoroka na kutuhangaisha kiasi hiki!” Alisema baba yake Hollo

    “Wewe baba Caro hivi umesahau kuwa  hizi tarehe kuwa ni mbaya kwake?” Aliuliza  Dk. Cynthia mamaye Caroline.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo nakumbuka  lakini….” Profesa John Kadiri alishindwa kuimalizia sentensi yake alijua tarehe hizo huwa hazifai  kwa Caroline kutoka nje!”

    Walipofika  mbele ya  hoteli ya Sunflower walishangazwa  na idadi kubwa ya watu waliokuwepo  pamoja na  ukimya  uliotawala! Watu walionyesha  kuwa na masikitiko makubwa! Ghafla  Agripina mama yake Harry alitokeza  na kuwafuata waliposimama kabla hawajasema lolote.

    “Jamani karibuni sana!”

    “Ahsante!”

    “Nani kawapa habari za matatizo yaliyotokea hapa?”

    “Matatizo? Matatizo gani?” Dk. Cynthia aliuliza kwa mshangao.

    Agripina alikaa kimya baada ya kugundua  walikuwa hawajui lolote, lakini baadae aliamua kujipa moyo na kusema ukweli  hakuona sababu ya kuendelea kuficha.

    “Tulikuwa hapa katika sherehe ya kuzaliwa  mwanangu Harry, kila mtu alikuwa  na furaha!  Lakini ghafla wakati wa kufungua muziki Caroline alipatwa na tatizo!”

    “Tatizo gani?”

    “Alianguka kitu kama kifafa lakini sidhani kama ni kifafa!” Agripina alijaribu kupunguza uzito wa tatizo ili asimuumize sana Cynthia akiamini alikuwa hafahamu.

    “MUNGU   WANGUUUUUU! UNAONA SASA MTOTO HUYU ALIVYOTUAIBISHA!” Alisema Dk. Cynthia kwa sauti kubwa, kila mtu alishangazwa na kauli hiyo.

    “Sasa hivi  yuko wapi?” Baba yake Caroline aliuliza!

    “Alipozinduka dakika kama kumi zilizopita  alichomoka na kukimbia kuelekea  msituni na muda mfupi baadae Harry nae aliondoka kumfuata hapa tulipo  tunajiandaa kwenda kuwatafuta huko huko msituni!”

    Bila  kusita wala kusema lolote wazazi wa Caroline, polisi na  watu waliowakuta kwenye hoteli ya Sunflower waliungana   kwenda msituni   kuwasaka Harry na Caroline ilianza, kila mtu aliamini Caroline alikwenda msituni  kujiua baada ya kuaibika! Mama na baba yake walilia machozi kwani  Caroline alikuwa mtoto wao pekee.

    Dakika chache   baada ya kuingia   msituni walianza kusikia mwangwi wa sauti ya Harry akiliita jina la Caroline na wote walikimbia kuelekea  mahali mwangwi huo ulikotokea, mbele kidogo sauti ilipotea lakini  walizidi  kusonga  mbele  kila mtu aliamini wangewapata wote wakiwa hai.

    Ghafla hatua kama mia tano  hivi katikati ya pori wote wakitembea katika njia ndogo  huku miili yao ikiwa imelowa umande  kutokana na ukungu uliokuwepo usiku huo walisikia minong’ono     chini ya mti mkubwa wa mkorosho uliokuwa pembeni  ya njia, ilikuwa ni sauti ya mtu akimbembeleza mtu mwingine asijinyonge tayari ilikuwa saa 4:28.

    “Jamani wapo humu!” alinong’ona mmoja wa maaskari na watu wote walianza kunyata kuingia chini ya mti huo huku tochi zao zikiwa zimezimwa ili kuepusha kuwashtua, walipofika chini ya mti waliziwasha tochi zao ghafla  na kushangaa kumuona msichana akijirusha kutoka mtini na kuning’inia huku akitupa miguu yake huku na kule.

    Harry alipoangalia chini aliona kundi kubwa la watu akajua walikuwa wamekuja kumsaidia, hakumtambua  hata mtu mmoja kati yao!

    “Jamani nisaidieni kuokoa maisha ya mpenzi wangu!” Alisema Harry baada ya kuwaona watu hao chini!

    Mmoja wa askari waliokuwepo aliinyosha bunduki yake na  kwa kutumia  singe  kali  ya bunduki hiyo alianza kuikata kamba  na Caroline alianguka   na kufikia mikononi mwa mmoja wa   Maaskari, alikuwa kimya kabisa na hakuonekana kuhema  hakuna mtu aliyekuwa na  uhakika Caroline  alikuwa hai au amekufa.

    Walikimbia  mbio hadi Sunflower hoteli ambako walichukua gari na kuondoka kwa kasi kuelekea hospitali ya Mount Meru!  Ndani ya gari  la polisi  walipanda  baba na mama yake Caroline na gari lao lingine liliendeshwa na askari mwingine na ni katika gari hilo ndilo walipanda Harry na watu wengine akiwemo mama yake Agripina!

    Mpaka wanafika hospitali   Caroline alikuwa bado kimya na hakuonyesha dalili yoyote ya kuhema wala moyo wake kudunda.  Baada ya kupokelewa alikimbizwa hadi chumba cha wagonjwa mahututi ambako aliwekewa mashinde ya hewa   safi ya oksijeni na akafungiwa  mashine nyingine ya kuushitua moyo wake daktari alidai  kulikuwa nafasi kubwa ya kuokoa maisha yake. Dripu za kupandisha mapigo zilichomekwa kwenye mishipa yake nazo zikawa zinakwenda kwa kasi kuingia ndani ya mishipa yake.

     Wazazi wake waliendelea kulia wakiwa wamekata tamaa kabisa ya maisha ya mtoto wao kurejeshwa! Waliumia zaidi kwa sababu Caroline   alikuwa mtoto wao pekee na ndiye alikuwa tegemeo lao kwa kila kitu ikiwemo kurithi mali zote waliokuwa nazo! Hawakuwa na uwezo wa kuzaa mtoto mwingine tena.

             ******************

    Kwa polisi  ilikuwa si rahisi kuamini   Caroline alijinyonga mwenyewe! Kitendo cha  kumkuta  Harry  juu ya mti kiliwafanya wafikiri alikuwa akimnyonga!  Waliamua kuanzia upelelezi wao kwa Harry, walimkamata na  kwenda nae moja kwa moja hadi kituo cha polisi cha kati Mjini Arusha ambako walichukua maelezo  yake na kumweka rumande!

    Aliingia rumande akilia kwa uchungu kwa sababu alijua wazi hakuwa na hatia, alijaribu kadri alivyoweza kuwaelewesha askari  ni kiasi gani  alimpenda Caroline na asingeweza kumuua lakini hakuna mtu aliyeonekana kumwamini!

     Baadhi ya watu walianza kufikiri labda  kweli Harry alifanya  kitendo hicho  baada ya kubaini Caroline alikuwa  na kifafa, lakini kwa umri wake na jinsi alivyoonekana   wengi waliamini isingekuwa rahisi kwake kufanya hivyo.Alilala mahabusu kwa siku mbili mfululizo akiwa amefunguliwa jarada la mauaji na upelelezi ulikuwa bado ukiendelea.

    Baba yake Caroline alijua wazi Harry asingeweza kufanya hivyo lakini aliamua kunyamaza kwa kuamini Harry alichangia matatizo ya mtoto wake, hivyo hata kuwekwa ndani ilikuwa ni adhabu tosha kwake. Agripina alijaribu kufanya kila aliloweza  kumwekea  mwanae dhamana lakini ilishindikana  kwa  sababu kesi  hiyo iliitwa ya mauaji! Roho ilimuumakwa sababu alijua mwanae hakufanya kosa lolote lile!

                ****************

    Masaa  48 baada ya kuingizwa wodini  ndiyo Caroline alizinduka! Neno la  kwanza alilotamka baada ya kurejewa na fahamu lilikuwa Harry!  Aliliita jina hilo kama mara mbili hivi kisha akafumbua macho yake na kuangaza huku na kule na  kuwaona wazazi wake, mama yake alikuwa  bado akilia machozi.

    “Mama mbona unalia?”

    “Kwanini ulitaka kujiua Caroline mwanangu wakati unajua  wewe ndiye mtoto  pekee tunayekutegemea  na hatuna uwezo wa kupata mtoto mwingine!”

    “Mama nimeaibika mno  sina mahali pa kuificha sura yangu ni heri nife?”

    “Yaani ndiyo ujiue? Ni wangapi walio na matatizo kama yako  na wengine makubwa ziadi lakini wanaishi?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo mama, lakini najua kabisa Harry ataniacha na mimi siwezi kuishi bila yeye ni heri nife tu  mama! Kwanza Harry yupo wapi”

    “Polisi walimchukua!”

    “Polisi walimchukua!Kwanini?”

    “Walidhani eti ndiye aliyetaka kukunyonga!”

    “Baba!”

    “Naam mwanangu!”

    “ No! Haiwezekani, Harry hawezi kufanya hivyo, Harry  hawezi kuniua, ni mimi mwenyewe niliyetaka kuitoa roho yangu! Tafadhali nendeni mkawaambie polisi wamwachie haraka iwezekanavyo vinginevyo nitautoa uhai wangu!” aliongea Caroline akilia.

    Baba yake hakuyachukulia maneno hayo mzaha pale pale bila kuchelewa alitoka hadi nje na kuingia ndani ya gari lake na kwenda moja kwa moja kwenye ofisi ya mkuu wa polisi wa mkoa aliyekuwa rafiki yake mkubwa.

    “Vipi mbona unahema?” Kamanda wa polisi wa mkoa aliuliza.

    “Bwana mtoto wangu amezinduka na anadai kuwa huyu kijana mnayemshikilia hakuhusika kabisa na kitendo hicho, yeye alikuwa akijaribu kumuokoa na amesema kama hatutamwachia basi atajiua tena!”

    “Lakini huyu binti yako vipi? Hivi anajua  kweli kuwa kitendo cha  kujiua ni kosa katika nchi hii, shauri yake atafungwa!” alisema kamanda na baadae alimwita askari mmoja wa kike na  kumwagiza amletee faili la kesi ya Harry na amwite pia askari aliyekabidhiwa kupeleleza kesi hiyo!

    Muda kama dakika kumi baadae askari aliingia ofisini akiwa na faili na  kumkabidhi kamanda na alianza kuyapitisha macho yake akilisoma  faili hilo, alipofika mwisho alimwamuru askari  wa upelelezi  kumtoa Harry ndani ya mahabusu na wakaondoka nae kwenda hospitali ya Mount Meru, hata kamanda wa polisi pia aliongozana nao.

     Harry alipoingia wodini, Caroline alinyanyuka kitandani na kwenda kumkumbatia kwa furaha, watu wote walishangaa na baada ya kukumbatiana wote walianza kulia   machozi.

    “Harry  tafadhali usiniache!”

    “Nakupenda Caroline siwezi kufanya hivyo tafadhali niamini ingawa nimeteseka sana mahabusu! Walifikiri eti nilitaka kukunyonga, kweli naweza kukuua wewe kwa ninavyokupenda Caroline? “

    “Huwezi kufanya hivyo!”

    Watu wote waliokuwemo ndani ya chumba hicho waliendelea kushangazwa  na   waliamini kweli vijana hao walipendana na hapakuwa na jinsi ya kuwazuia  wasiendelee na mapenzi yao!  muda mfupi baadaye Caroline na Harry walianza kutembea kwenda nje ambako Harry alitaka kufahamu ukweli.

    “Nilizaliwa  kwa  matatizo  kwani wakati wa kuzaliwa nilikuwa mkubwa kuliko njia ya mama yangu ya uzazi  ikabidi madaktari wanivute kwa kutumia vyuma!  Ni madaktari hao ndio walionisababishia kifafa!  Tangu utotoni nimeugua ugonjwa huu!   kila mwezi tarehe kati ya 26-28 ni lazima nianguke kifafa, uliponiuliza juu ya jambo hilo  nilikudanyanga kuwa huwa nipo katika  siku zangu za hedhi  hiyo si kweli bali huwa nafungiwa ndani  ya chumba mpaka nianguke ndio niendelee na masomo!” Alisema  Caroline akilia machozi  kichwa chake kikiwa kimeegemezwa begani kwa Harry na kulowanisha shati lake.

    “Kwanini hukuniambia ukweli tangu mwanzo Caroline?”

    “Niliogopa!”

    “Uliogopa nini?”

    “Nilijua ungeniacha!”

    “Lakini ulifanya vibaya sana kunificha ningejua nisingekulazimisha uje kwenye tafrija ingeendelea kubaki siri yetu wawili lakini sasa wanafahamu watu wengi!”

    “Nisamehe Harry lakini naomba usiniache!”

    “Kwanini unaongelea sana swala la kuachwa?”

    “Harry ni mwanaume gani anayeweza kukubali kuwa na mpenzi mwenye kifafa?”

    “Mimi naweza!”

    “kweli?”

    “Ndiyo Caroline!”

    “ Kumbuka Harry  hata mimi sikupenda kuwa hivi  basi angalau univumilie mpaka tumalize shule huko mbeleni unaweza kuoa mwanamke mwingine  na sitakuzuia lakini kwa sasa  maisha yangu ni bure bila wewe!” alimaliza Caroline huku akilia.

    Baadaye maaskari waliondoka kurejea makazini kwao, hapakuwa na kesi tena  faili lilifutwa.

              *******************

    Jioni ya siku hiyo Harry alirejea nyumbani kwao ambako ugomvi mkubwa uliendelea kati yake na mama yake akizuia uhusiano wake na Caroline.

    “Sitaki kukuona tena na yule msichana usije kutuletea watoto wenye kifafa kwenye ukoo wetu!”

    “Mama kwani kifafa kinaweza kwenda kwa watoto?”

    “Wewe hujui kuwa kifafa kinarithiwa?”

    Moyo wa Harry uliuma na ghafla akili yake ilibadilika, alianza kujisikia tofauti juu ya Caroline

    Siku ya tatu  hali ya Caroline ilikuwa  nzuri na wazazi wake waliamua kumpeleka  shule ili aendelee na masomo yake!  Alikwenda shuleni akiwa na hamu kubwa ya kuonana na Harry kwa sababu tangu waachane alikuwa hajampigia simu jambo ambalo halikuwa kawaida katika maisha yao ya urafiki alitaka kufahamu ni kitu gani kilitokea ingawa tayari alishaanza kuhisi kulikuwa na tatizo. 

    Wakati anaingia shuleni alimwona Harry  akiongea katikati ya kundi la wasichana walioonekana kumuuliza juu ya kilichotokea.  Bila kufahamu ambacho kingempata Caroline aliamua kumfuata kwenye kundi hilo.  Habari zake za kuanguka kifafa zilishaenea shule nzima!  Kila alikopita  vidole vilimfuata nyuma, Caroline alijisikia vibaya  na alitakani ardhi ipasuke aingie ndani yake kukimbia aibu.

    “He! Michana mzuri hivi ana kifafa!”

    “Alikuwa anaringa sana  huyu   tutamwona sasa kila tarehe 26-28! Tutakuwa tunamfuatilia!” walisema wasichana wawili  aliopishana nao njiani, maneno hayo aliyasikia na yakamtia simanzi kubwa sana moyoni mwake  lakini alijitahidi asilie.

    Alipolifikia kundi hilo la wasichana Harry alikuwa bado yupo katikati akijaribu kusimulia yaliyotokea tena kwa sauti alijifanya hajamwona  Croline ingawa alikuwa  nyuma yake! Wasichana wote waliokuwa wakicheka  walinyamaza ghafla,  Caroline aliwasalimia lakini hakuna aliyeitikia.

    “Harry!” Caroline aliita lakini Harry hakuitika. Akaita tena lakini bado alikuwa kimya akiendelea kuongea na wasichana kwa sauti ya chini!  Ikabidi Caroline asogee na kumgusa mgongoni ndipo Harry akageuka na kumwangalia,  sura aliyoivaa usoni siku hiyo haikuwa sura ya kawaida hata kidogo! Caroline hakuwahi hata mara moja kumwona Harry   katika sura hiyo.

    “Darling vipi?” Caroline aliuliza.

    “Caroline it is history now! (Caroline yaliyotokea kati yetu hivi sasa ni historia tu!)

    “He! Unasemaje Harry!”

    “Naomba uchukue hii barua ukaisome kwa wakati wako!”  Harry alimkabidhi Caroline barua hiyo na kuondoka zake kurudi katikati ya kundi la wasichana na kuendelea na maongezi yake.

      Wasichana wote walimcheka Caroline kwa sauti, huku akilia Caroline alitembea kwa unyonge na kwenda hadi nyuma ya darasa lao na kuanza kuisoma barua hiyo, kabla hata hajafikia mwisho wake aliangua kilio, barua hiyo iliandikwa:-  

     Je barua hiyo imeandikwa nini? Na nini kitampata Caroline? Fuatilia wiki ijayo.















    Mpendwa Caroline,

    Nakubali kwa asilimia mia moja kuwa  wewe ni msichana mzuri pengine kuliko msichana mwingine yeyote niliyewahi kumwona maishani mwangu!

    Na ninakiri kukupenda   Caroline na sikutegemea hata kidogo kuwa maneno   ninayotaka kuyasema hapa ningeyasema maishani mwangu lakini nimelazimika kufanya hivyo ingawa sipendi.

    Caroline   ulifanya vibaya sana kunificha tangu mwanzo kuwa wewe ni mgonjwa wa kifafa kwani ungeniambia  mara tulipofahamiana  labda ningekuwa na maamuzi tofauti  na niliyoyachukua! Kuanguka kwako mbele ya watu siku ya sherehe yangu ya kuzaliwa kuliniaibisha na kunifedhehesha sana! Kwa hivi sasa kila ninakopita nazomewa na kuambiwa natoka na msichana mwenye kifafa, mama yangu hataki hata kukuona na ametishia kujinyonga kama mimi na wewe tutaendelea kuwa wapenzi!

    Caroline nashindwa nitafanya kitu gani ili niendelee kuwa na wewe! Kwa sababu hiyo napenda kutamka wazi kwamba tangu dakika unapoisoma barua hii   sitaki tena uhusiano wa kimapenzi! Unaweza kutafuta mvulana mwingine yeyote anayeweza kuvumilia fedheha ya kuwa na  mwanamke mwenye kifafa!

    Sina mengi nakutakia kila la kheri katika maisha yako!

    Ahsante,

    Ni mimi,

    Wako wa zamani,

    Harry Robertson.

    Ilikuwa asiimalize barua hiyo hadi mwisho lakini alijikaza akiamini labda mistari ya mwisho ingeweza kusema “Hata hivyo nitakuwa na wewe wakati tukitafuta matibabu” Lakini haikuwa hivyo mpaka anamaliza  kuisoma barua hiyo  shati lake la shule lilikuwa limelowa kwa  machozi! Alihisi mwili wake kuishiwa nguvu na alifikiri angezirai wakati wowote! Moyo wake uliuma sana na alishindwa kuelewa ni kwanini mwanaume aliyempenda kiasi hicho, mwanaume aliyemwonyesha jinsi dunia ilivyo alikuwa ameamua  kuumiza moyo wake!

    Maneno ya mwisho aliyoyasema  Harry msituni kuwa asingemwacha hata kama angekuwa mgonjwa wa Ukimwi  yalimtia moyo na   kumfanya ajisikie bado alipendwa na Harry!  Alishindwa kuelewa maneno hayo yalipotelea wapi! Harry hakuwa mtu wa kubadilibadili maneno hivyo ndivyo alivyomfahamu.

     Alipoangalia kwenye kundi la wasichana alimwona Harry akiwa katikati bado akiendelea kuongea  tena bila kujali! kama vile kilikuwa hakijatokea kitu chochote!  Moyo wa Caroline ulizidi kuumia, alitamani ardhi ipasuke na aingie ndani yake kukwepa aibu na maumivu  yaliyokuwa mbele yake.

    “Now I know boys tell sweet words superficially  but hurt badly inside!(Sasa nimeelewa kweli wavulana husema maneno matamu juu juu lakini huumiza vibaya sana kwa ndani!)  Alisema Caroline wakati  akinyanyuka kutoka kwenye msingi aliokuwa amekaa.

    Hakutaka kuendelea kubaki shuleni tena kwani asingeweza kuelewa kitu chochote darasani, machozi yalizidi kumbubujika  bado hakuamini kama maneno katika barua hiyo yaliandikwa na Harry mvulana aliyezoea kumtamkia   mara zisizopungua kumi  kwa siku kuwa  alimpenda kupindukia na alitaka kuwa mume wake baadaye! Caroline alimtupia lawama nyingi Mungu kwa kumpa sura nzuri lakini akaruhusu apate ugonjwa mbaya wa kumdhalilisha!

    Huku akilia aliendelea  pia kuwalaumu wazazi wake  kuwa kuruhusu madaktari wamvute kwa vyuma wakati wa kuzaliwa na kuuharibu kabisa ubongo wake kitu kilichomsababishia kifafa!

    “Kwanini hata sikuzaliwa kwa operesheni badala ya kuvutwa?” Alijiuliza Caroline.

     Pamoja na lawama zote hizo bado ukweli ulibaki palepale kuwa Caroline alikuwa mgonjwa wa kifafa na tayari  suala hilo halikuwa siri tena kila mtu shuleni na hata mitaani alielewa pamoja na uzuri wake Caroline alikuwa mgonjwa.

    Akiwa mwenye mawazo mengi kupita kiasi  alinyanyuka na kuanza kutembea taratibu kuelekea kwenye lango la kuingilia shuleni kwao, hakuwa na haja ya kwenda ofisini kwa walimu kuomba ruhusa ya kuondoka shuleni tena! Alishafikia uamuzi wa  kuacha shule, hakutaka kusoma tena kwa sababu ya kuogopa kuzomewa na wanafunzi wenzake kila siku na si kusoma tu  bali hakutaka kuishi tena Caroline alitamani kufa kuikwepa aibu na maumivu.

    “Kama Harry asingenikataa ningefikiria kuishi lakini hivi sasa sitaki tena, ni bora nife!” Aliwaza Caroline wakati akitembea kwa miguu  kutoka shuleni.

    Kidogo  agongwe na  daladala lililokuwa likija kwa kasi wakati akijaribu kukatisha barabara kutoka shuleni kwao kwenda upande wa pili,kama si dereva wa gari hilo kufunga breki mambo yangekuwa mengine.

    “Wee msichana unaleta uzuri wako siyo? Utakwenda ahera au umechoka kula pilau?” alifoka dereva wa daladala  lililotaka kumgonga Caroline bila kujua kuwa huko ahera ndiko hasa Caroline alikotaka kwenda siku hiyo!

    “Ee bwana Suka umekiona lakini kifaa chenyewe?”   konda wa  daladala hilo alimwambia dereva wake na abiria wengine  ndani ya gari walitoa vichwa vyao kuchungulia nje! Kila mmoja wao alitingisha kichwa akikiri kuwa Caroline alikuwa mzuri kupita kiasi.

    “Hivi kumbe wasichana wanaochorwa kwenye magazeti wapo? Mimi nilifikiri ni michoro tu! Huyu msichana anafanana kabisa na picha ambazo huchorwa kwenye gazeti la Bongo!” Alisema abiria mwingine na gari lilizidi kwenda kwa kasi.

    “Konda hebu nilegezee  hapo kwenye tuta!” Sauti ya mvulana mmoja ilisikika  kutoka kiti cha nyuma na dereva alipunguza mwendo wa gari  badala ya kupitia mlangoni kijana huyo aliruka  na kutokea dirishani na kuanza kumkimbilia  Caroline aliyekuwa upande wa pili wa barabara!

    Caroline alitembea kuelekea kwenye duka lililoandikwa Manyilizu Chemist! Lilikuwa ni duka la madawa, mita kama mbili hivi kutoka alipokuwa Caroline kijana huyo aligundua Caroline alikuwa akilia machozi.

    “Anti mambo?” Kijana huyo alianza kumsemesha  lakini Caroline hakujibu kitu alizidi kububujikwa na machozi huku akitembea  kwa kasi kuelekea kwenye duka dawa lililokuwa mbele yake.

    Kijana  huyo hakukata tamaa alizidi kumfuata kwa nyuma na alipofika dukani Caroline aliingia na kijana alibaki nje akisubiri.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Vipi dada mbona unalia?” Muuza duka aliuliza.

    “Naumwa sana na kichwa kaka!”

    “Pole sana dada yangu  nikusaidie nini?”

    “Nisaidie vidonge kumi vya klorokwini najua hii ni malaria!”

    “Sawa kidonge kimoja ni shilingi 20 kwa hiyo ni shilingi 200!”

    “Sawa nipe!” Alisema Caroline wakati akimkabidhi muuza duka noti ya shilingi 5000 aliyokuwa nayo mfukoni, alipokabidhiwa dawa hakutaka hata kusubiri chenji yake alitoka nje na kuanza kukimbia! Ilibidi mwenye duka amkimbilie hadi akampata.

    “Dada chenji yako hii hapa!” Alisema  muuza duka na Caroline alipokea chenji na  bila hata kutoa shukrani alianza kuondoka mbio.

    Kijana aliendelea kumfuata kwa  nyuma bila kuchoka, alikuwa amevutiwa kiasi cha kutosha na sura ya Caroline naye katika maisha yake hakuwahi kuona msichana mwenye sura nzuri kama ile!

    “Lazima nimwambie shida yangu, sijui anaishi wapi   Arusha hii? Mtoto wa nguvu kiasi hiki bado sijamwona na mimi ndiye bingwa wa ……….!” Aliwaza kijana huyo akimfuatilia Caroline kwa nyuma mbele alimshuhudia akiingia katika duka jingine  la madawa alisimama  nje akimsubiri.

    “Dada una klorokwini hapa dukani kwako?”

    “Cheti cha daktari kiko wapi?”

    “Sina ila huwa natumia dozi ya 4/4/2/2!”

    Maneno hayo ya Caroline yalimridhisha dada muuza duka na kujikuta akimuuzia Caroline vidonge vingine kumi vya klorokwini! Maongezi yao yote  aliyasikia na kushtuka, aligundua lengo la msichana huyo halikuwa jema hata kidogo na kwa hali aliyomwona nayo alielewa wazi  msichana huyo alitaka kujiua kwa vidonge.

    “Lakini kwanini msichana mzuri kama huyu ajiue?” Alijiuliza kijana huyo bila kujua suluhu!”

    Alipotoka dukani Caroline alishangaa kukuta kijana huyo aliyevaa nguo za kupendeza, kichwani kwake akiwa amenyoa panki na chini amevaa viatu aina ya mokasini nyeupe  akimsubiri. Alimwangalia kwa jicho la chuki na  kuonyesha kabisa hasira yake waziwazi! Caroline aliwachukia wanaume wote duniani kwa sababu ya kitendo alichofanyiwa na Harry, aliwaona wanaume wote duniani ni wanyama na  hakutaka tena uhusiano wowote na mvulana yeyote!

    “Hivi wewe unanitafuta kitu gani au wewe ni kibaka nini?”?“Hapana dada mimi naitwa Richard Nelson nimemaliza kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Umbwe  sijui mwenzangu unaitwa nani?”

    “Jina langu siyo shughuli yako, tafadhali naomba uniache ufuate mambo yako sitaki unifuatefuate na  ukizidi kunisonga nitakupigia kelele za mwizi!” Alisema Caroline huku akilia.

    “Sawa dada lakini naomba usifanye unavyotaka kufanya kwani mimi nitaumia sana   sababu nimekuona kwa macho yangu!”

    “Ninavyotaka kufanya? Yaani kitu gani?”

    “Najua unataka kujiua! Tafadhali usifanye hivyo hebu nieleze tatizo lako labda ninaweza kukusaidia!”

    “Kunisaidia? Utanisaidia nini wewe sitaki kukuona  mbele ya uso wangu ondoka sasa hivi!” Alisema Caroline kwa ukali na kuanza kuondoka akitembea kwa kasi, Richard alizidi kumfuata kwa  nyuma hakuwa tayari kuona roho ya  msichana mzuri kama Caroline ikipotea  alitaka kufanya kila kilichowezekana kuokoa maisha yake.

    Mbele kidogo Caroline aliingia tena katika duka jingine na kutoka na chupa ya maji akiendelea na safari yake  Richard akiwa nyuma yake akizidi kumbembeleza asifanye alichotaka kufanya!

    Katika hali ambayo Richard  hakuitegemea na katika kasi ya ajabu walipofika pembeni mwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid,  alishuhudia Caroline akitupia vidonge  mdomoni mwake, wala hakujua ni muda gani alivitoa vidonge hivyo  kutoka kwenye vifuko vyake na kwa haraka aliinamisha chupa ya maji mdomoni  na kuanza kumeza.

    Kama upepo Richard aliruka na kumwangusha Caroline chini na  kumkaba    shingo ili asimeze vidonge hivyo! Watu waliokuwa jirani na eneo hilo  walipoona kitendo hicho walifikiri mwanafunzi anakabwa na kibaka!  walitoka mbio na kwenda hadi eneo hilo  na mmoja wao bila kuchelewa alirusha jiwe kubwa  lililotua   moja kwa moja kichwani kwa Richard na kumpasua! Damu nyingi zilivuja ikabidi amwachie  Caroline aliyetumia nafasi  hiyo  kuvimeza vidonge vyote alivyomwaga mdomoni mwake.

    “Jamani mimi siyo mwizi najaribu kuokoa maisha ya huyu dada amekunywa vidonge vingi vya klorokwini anataka kujiua!” Alipiga kelele Richard.

    “Wewe muongo tu nyie ndio vibaka mnaotusumbua mitaani leo lazim ufe maana kila tunapowapeleka polisi  mnaachiwa!”

    “Ndiyo!Ndiyo! Ndiyo! Huyu ni kibaka anataka kuniibia mkoba wangu wa pesa!”Alisema Caroline baada ya kumeza vidonge alionekana  kuwa na  nguvu.

    Watu wengi walianza kuwasili na kumpiga Richard kwa mawe, marungu na matofali huku Caroline akishuhudia  kitendo kile cha kikatili, alijua Richard alipigwa kwa kuonewa lakini kwa hasira aliyokuwa nayo dhidi ya wanaume wote duniani hakujali wala kumwonea huruma! Richard alizidi kushambuliwa Caroline akiwa amesimama pembeni akishuhudia.

    “Nipisheni!Nipisheni!” Alisema mtu mmoja akiwa na tairi la gari pamoja na galoni ya mafuta ya petroli akiwa na ameuma kiberiti mdomoni kwake alikuwa  ameamua kumchoma   Richard kwa moto kama walivyofanywa vibaka wengine!

    Wananchi wote walimpisha akaanza kummwagia Richard mafuta mpaka akalowana kabisa! Kabla hawajamtia kiberiti walishangaa kuona Caroline akiyumba na kuanguka chini   kisha  kupoteza fahamu zake.

    “jamani vipi au kweli kanywa vidonge nini?” Walijiuliza  wananchi na walipompekua katika mfuko wake wa shati walikuta vifuko viwili vilivyoandikwa chloroquine 4/4/2/2 kila kimoja na   vyote havikuwa na kidonge ndani! Hiyo ilimaanisha  kweli binti huyo alikunywa klorokwini kwa lengo la kujiua!

    “Jamani mimi siyo mwizi jamani! kitambulisho changu  cha shule hiki hapa!” Alisema Richard akiwa amenyanyua kitambulisho chake mkononi, mmoja wa watu alikichukua na   alipokisoma kweli kilionyesha alikuwa mwanafunzi aliyemaliza  kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Umbwe mwezi mmoja kabla.

    Wananchi waligundua makosa yao na kwa kuogopa polisi   walianza kusambaa  taratibu  mpaka wote wakaisha na kuwaacha Caroline na Richard wakiwa  wamelala  chini peke yao! Damu nyingi ziliendelea kuvuja katika mwili wa Richard! Mwili wake ulipasuliwa pasuliwa kwa mawe na matofali, nguo zake zote zililowa lakini  pamoja na hali  hiyo mbaya  alimsogelea Caroline na kuanguka juu yake.

    “Nina..kufa  saba..bu ya kuo..koa mai..sha ya..ko! Haina shi..da Mun.gu ana..jua!” Alisema kwa tabu Richard.

    Hapakuwa na msaada wowote ule watu wote walishakimbia kutoka eneo hilo kuogopa polisi! Hakuna aliyejitokeza kulisogelea eneo hilo,kila mtu aliogopa kuhusishwa na  kosa la kujichukuliwa sheria mkononi.

    Kadri msaada ulivyozidi kuchelewa  ndivyo vidonge vya klorokwini vilivyozidi kuingia   katika damu ya Caroline na kumwathiri zaidi! Macho yake  yalikuwa mazito sababu ya athari za dawa hizo, kizunguzungu kilimtawala! Alijitahidi kufungua macho yake lakini alishindwa na  alipogusa juu yake alishika mwili wa mtu alijua mtu huyo hakuwa mwingine bali Richard!

    “Ninaitwa Caroline ni vyema unifahamu kabla sijafa samahani kwa kukusababishia kifo Richard  ni hasira iliyonifanya hivyo! Nisamehe Richard kabla hatujafa ninajua hauna makosa aliyestahili kufa ni Harry” Alisema Caroline kwa taabu!

    “Usijali lakini tatizo lako ni nini!”

    “Siwezi kukuambia ila naomba samahani kwa yote yaliyokupata!”

    Hakuna mtu aliyejitokeza kuwapa msaada wowote! Kwa Caroline ilikuwa furaha lakini kwa Richard ilikuwa huzuni kubwa kukutana na kifo mahali ambapo hakutegemea!

    Je watapona? Futilia wiki ijayo.













    B

    inadamu wote duniani ?hawawezi kuwa na mioyo ?na tabia ya aina moja kwani wakati  Richard anamwagiwa mafuta ya petrol, msichana mmoja aliingiwa na huruma sana na kupiga simu polisi.

    “Ni eneo gani hilo?”

    “Hapa ni karibu kabisa na uwanja wa Sheikh Amri Abeid njia ya kwenda kituo cha mabasi!”

    Baada ya simu hiyo maaskari walingia ndani ya gari na safari ya kuelekea eneo waliloelezwa na mpiga simu hiyo ilianza, walipofika  eneo  waliangalia mahali kuliko kuwa na mkusanyiko watu lakini hawapakuona na kuzidi kusonga mbele.

    “Afande nafikiri ni pale!”

    “Wapi?”

    “Pale walipolala watu wawili  ardhini!”

    “Inawezekana!” Alijibu dereva wa gari hilo aliyekuwa na V mbili begani na kukata kona haraka kuelekea mahali alipoonyeshwa. Msichana mmoja aliwafuata mbio.

    “Afande ni mimi ndiye niliyewapigia simu!”

    “Binti wamekuwaje hawa watu lakini?”

    “Huyu kijana amepigwa na wananchi wenye hasira  baada ya huyu msichana   kudai alitaka kumpora mkoba wake! Lakini yeye  alidai alikuwa  akimuokoa huyu msichana  baada ya kunywa vidonge vya klorokwini kwa lengo la kujiua!”

    “Ilikuwaje huyu msichana akafikia hatua hii sasa?” Maaskari waliendelea kuuliza maswali wakati wakiwapakia ndani ya gari.

    “Alianguka  peke yake na alipochunguzwa mfukoni alikutwa na vipakiti viwili vilivyoandikwa juu yake  Chloroqwine 4/4/2/2!”

    “Vilikuwa na vidonge?”

    “Vyote viwili havikuwa na kidonge hata kimoja!”

    “Aisee inawezekana kweli huyu binti alikunywa vidonge!”

    Wote wawili walipakiwa ndani ya gari  na kuondoka kwa kasi  kuelekea hospitali ya Mount Meru, hakuna hata raia mmoja aliyejitokeza zaidi ya msichana huyo! Watu wote waliogopa sababu waligundua waliua kimakosa.

    Mapokezi walipokelewa vizuri,Richard alikimbizwa chumba cha upasuaji na Caroline alikimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi ambako tumbo lake lilisafishwa na   kuwekewa dripu za maji katika mishipa yake ili kuyapunguza nguvu madawa yaliyokuwa kwenye mishipa yake ya damu! Hakuna mtu aliyekuwa na uhakika  Caroline na Richard wangepona!

    “Mama yangu wee! Ni Caroline!” Alipiga kelele mmoja wa wauguzi baada ya kumchunguza vizuri Caroline usoni.

    “Caroline gani?”

    “Mtoto wa mzee John Kadiri anayesifika kwa uzuri Arusha nzima!”

    “Nasikia ni msichana  hana boyfriend sasa imekuwaje akaamua kunywa sumu?”

    “Ah! Wapi! Si anatoka na mwanafunzi mwenzake aitwaye Harry!”

    “Sasa tufanye kitu gani?”

    “Tupige simu nyumbani kwao ili tuwajulishe wazazi wake!”

     Richard aliporudishwa kutoka chumba cha upasuaji sehemu nyingi za mwili wake zilikuwa zimeshonwa, chupa za damu na maji zilikuwa zikimiminika kuingia katika mishipa yake.Muuguzi mmoja alimwangalia kwa makini na kumtambua.

    “Ha! Kumbe huyu naye ni mtoto wa jaji Lushinga!”

    Simu zilipigwa kwa familia zote mbili  za  Caroline na Richard na katika muda wa dakika arobaini na tano tu hospitali ilijaa idadi kubwa ya ndugu na marafiki huku wengi wakilia! Haikuchukua muda mrefu sana taarifa hizo zilifika katika shule ya sekondari ya Arusha! Wanafunzi wengi walimiminika kwenda hospitali ya Mount Meru kumwona Caroline, mtu mmoja muhimu hakujitokeza naye ni  Harry! Hakujitokeza kabisa hospitali na wala hakuumizwa na taarifa hizo.

    Wanafunzi wengine katika shule ya sekondari ya Arusha walipopewa taarifa kuwa Caroline alikunywa vidonge vya klorokwini kwa lengo la  kujiua  walisikitika  sana, walipoonyeshwa barua ambayo Harry alimwandikia  Caroline walisikitika zaidi  na walimtupia lawama Harry  kwa tatizo lililojitokeza.

    Si wanafunzi  peke yao waliofikiria hivyo  bali polisi pia!  Harry alikamatwa jioni ya siku hiyo akiwa shuleni na kupelekea kituoni ambako alifanyiwa mahojiano na baadaye  kuwekwa rumande! Akiwa ndani alijilaumu kwa kitendo alichokifanya! Kwa ndani alihisi  bado alimpenda Caroline lakini alimwogopa mama yake na wanafunzi wenzake.

    Dk. Cynthia na mumewe  walisikitishwa na kitendo cha mtoto wao  kutoka kujiua na walimchukia  Harry wakiamini barua yake ndiyo ingesababisha kifo cha mtoto wao, walikuwa na uhakika ni yeye aliyemshawishi mtoto wao kuingia katika uhusiano  wa kimapenzi! Kitendo cha kumkatia mapenzi ghafla waliamini ndicho kilichomsababishia matatizo.

    “Labda apone   lakini mwanangu akifa sijui kitakachotokea kwa kweli?” Baba yake Caroline alifoka hospitalini.

                  **************

    Masaa arobaini na nane  baadaye mapigo ya moyo wa Caroline yaliyokuwa yameshuka kiasi cha kutishia maisha yake yalianza kupanda taratibu  na hatimaye kurejea katika hali ya kawaida kabisa!  Alipofumbua macho yake na kukuta baba na mama yake wapo pembeni mwa kitanda chake.

    “Nani ameniokoa? Nataka kufa mimi? Niacheni nife nimekwishasema sitaki   kuishi!” Alisema Caroline huku akijaribu kuketi kitako kitandani,  mwili wake ulikuwa na nguvu za ajabu lakini baba na mama yake walimkandamiza kitandani na kubaki amelala chali.

    “Mama!”

    “Naam mwanangu!”

    “Niache nife mama, Harry hawezi kitendo alichonifanyia!”

    “Msamehe mwanangu maisha yako ni bora kuliko huyo Harry, tufikirie mimi na baba yako wewe ndiye mtoto wetu pekee ukifa tutafanya nini?  Tafadhali usijiue mwanangu!”

    Caroline aliendelea kulia kwa uchungu hakuuona kabisa  umuhimu wa kuendelea kuishi duniani, alihisi kufedheheka vya kutosha, uzuri wake haukuwa na maana  yoyote kwake Harry alikuwa  amefanya kitendo  cha kumuumiza moyo  wake ambacho hakuwahi kutegemea  kufanyiwa maishani mwake.

    “Harry! Harry! Harry! Kweli unanitenda hivi  mimi, sawa tu!”

    “Mwachie Mungu  mwanangu” Dk Cynthia alimwambia Caroline.

    “Sawa mama lakini nimefanya kosa moja baya sana!”

    ‘Kosa gani?”

    “Nimesababisha kifo cha  mtu asiye na hatia!”

    “Nani?”

    Caroline alimsimulia kila kitu kilichotokea mpaka Richard akishambuliwa na mawe na watu akidhaniwa ni mwizi!

    “Nilikuwa na hasira mama!”

    “Ni mtoto wa jaji Lushinga baba yake alikuja hapa  jana kukuona, akasema hali ya mtoto wake ilikuwa ikiendelea vizuri alisikitika sana kwa kilichotokea!”

    “Atapona lakini mama?”

    “Baba yake alisema matumaini yapo!”

    “Ee Mungu wangu, mama nipelekeni nikamwombe msamaha huyo kaka sasa hivi, nimemkosea sana!”

    Wazazi wake walikataa na Caroline alikubali kwa shingo upande na kubaki kitandani kwa wiki kama tatu   akipatiwa matibabu,  siku ya kwanza  ya wiki ya nne alishtukia mlango  wa chumba alicholazwa ukifunguliwa na  kuingia  kijana mwembamba mrefu akiwa amefungwa bandeji sehemu kubwa  ya uso wake, mikono  yake yote miwili ilikuwa imefungwa na piopii!

    Kijana huyo alitembea kwa kuchechemea kuelekea kwenye kitanda cha Caroline na  alipomwangalia  usoni  aligundua  kijana huyo ni Richard! Alinyanyuka kitandani na kumfuata, alipomfikia alipiga magoti chini na kuanza kumwomba msamaha.

    “Nisamehe sana Richard ilikuwa ni hasira dhidi ya wanaume!” Aliongea Caroline huku akilia machozi.

    “Nilikusamehe tangu siku hiyo Caroline, kitu kimoja ninachotaka kukueleza ni kwamba  pamoja na yaliyojitokeza bado nakupenda Caroline  na penzi langu ni la kweli tafadhali nikubalie  niwe mpenzi wako, nina hakika Mungu ametunusuru kutoka katika kifo ili tuwe wapenzi!”

    “Naogopa Richard!”

    “Unaogopa kitu gani?”

    “Siwezi kukueleza ila ni hicho ndicho kilinifanya nitake kujitoa roho, hutaniweza Richard!’

    “Kwanini nisikuweze?”

    “Basi tu!”

    “Na kwanini ulitaka kujiua sasa?”

    “Siwezi kusema!”

    Wiki mbili tu baadaye wote wawili waliruhusiwa kutoka hospitali hali zao zikiwa nzuri, wazazi wa pande zote mbili waliketi pamoja na kuyamaliza  mambo hayo wakimshukuru Mungu kwa kuokoa maisha ya watoto wao, polisi walipofuatilia ili Caroline afikishwe mahakamani kwa  kosa la kutaka kujiua mambo yalizimwa kimya kimya!

    Caroline na Richard waliendelea kuwa marafiki wakubwa! Kwa sababu ya mapenzi aliyokuwa nayo Caroline alimshinikiza baba yake  amwachie Harry kutoka mahabusu.

    “Mwachie tu baba yote anayajua Mungu hata ukimfunga haitasidia kitu!”

    ‘Hapana ni lazima nimpe somo maana hii ni dharau sasa, nakumbuka  huko nyuma  pia ulisema hivyo hivyo tukamwachia!”

    “Sawa baba lakini hatutakiwa kuhesabu makosa!” Maneno hayo yalimfanya profesa John Kadiri kukubali kumsamehe Harry.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

               *************

    Hali ya Arusha haikuwa nzuri kwa Caroline tena, alizidi kukonda sababu ya mawazo juu ya Harry, alitembea  njiani akiongea peke yake, kila alipomwona Harry  akipita alilia machozi, alimpigia simu mara kwa mara kumbembeleza waendelee lakini kila mara Harry alikata simu.

    “Inabidi Caroline ahamishwe Arusha vinginevyo atakuwa mwehu!” Ulikuwa ni ushauri wa mtaalam wa magonjwa ya akili wa hospitali ya Mount Meru.

    Dr Cynthia na mumewe John Kadiri walikubaliana na ushauri wa daktari ikabidi mwezi mmoja baadaye  utaratibu wa haraka kumhamishia Caroline  Dar es Salaam kwa shangazi yake  ulifanyika huko aliendelea  na masomo katika shule ya sekondari ya wasichana ya Jangwani.

              ****************

    “Paaaaaaaa!” Ulikuwa ni mlio mkubwa katika makutano ya barabara ya Morogoro na Swahili eneo la zimamoto, daladala mbili zilikuwa zimegongana uso kwa uso! Abiria walikuwa wakiwashambulia madereva wa magari hayo kwa kusababisha ajali kizembe!  Ajali hiyo isingetokea kwenye mataa kama  madereva hao wangefanya kazi yao vizuri!

    Msichana mrembo alikuwa akipita kandokando ya barabara ya   akielekea shule ya sekondari ya Jangwani ni msichana huyo ndiye aliyesababisha ajali hiyo kutokea kwani badala ya  madereva wa daladala   kuendesha magari walibaki kumshangaa binti huyo alivyotembea na kutingishika kwa nyuma.

                      *************

     Jiji la Dar es Salaam ni  kubwa  na lenye idadi kubwa  sana ya watu   ni kitu kigumu sana kujulikana  ndani ya  jiji hilo! Lakini kuingia kwa Caroline kulilitingisha jiji zima la Dar es Salaam, alikuwa gumzo midomoni mwa watu. Kila   aliyemwona  hakuamini  kama kulikuwa na wasichana wazuri kiasi kile! Kila dereva aliyepita na  kumwona Caroline   ilikuwa ni lazima akanyage breki na kumwangalia  angalau  kidogo ndiyo aondoke! Waalimu wa kiume katika shule ya  sekondari ya Jangwani walichanganyikiwa kwa uzuri na sura ya mwanafunzi huyo mgeni kutoka Arusha.

    Jambo hilo lilimkera sana Caroline ambaye kwa  donda alilosababishiwa   na Harry   ambalo lilikuwa bado halijapona  aliuahidi moyo wake kutompenda mwanaume mwingine tena maishani! Aliwachukia wanaume kuliko kitu kingine chochote.

     Pamoja na yote aliyotendewa na Harry bado aliendelea kumkumbuka kama mwanaume aliyemwonyesha dunia ilivyokuwa kwa mara ya kwanza, bado alihisi  upande mmoja wa moyo wake  ulimpenda Harry na  aliamini kama ingetokea siku moja akaja  kwake na kumuomba waendelee asingesita kukubali, zaidi ya Harry hakutaka mwanaume mwingine zaidi.

              ******************

    Miaka mitatu baadaye:

    Ratiba ya maisha ya Caroline jijini Dar es Salaam  ilikuwa ni ileile! Kila tarehe 26-28 ya kila mwezi alijifungia ndani  akisubiri kuanguka kifafa! Alikuwa mwangalifu sana na tarehe hizo kiasi kwamba hakuna mtu hata mmoja aliyegundua tatizo lake.

    Watu wote waliendelea kumpa heshima  ya  msichana mrembo kuliko wote jijini Dar es Salaam, waandaji wa mashindano ya urembo walimfuata mara nyingi ili ashiriki  mashindano hayo lakini  hakukubali kwa  sababu sheria za shule hazikumruhusu.

    Caroline alipomaliza kidato cha sita miaka mitatu baadaye aliwashangaza wazazi wake alipofaulu na kupata divisheni 1!! Kwa furaha Dk. Cynthia na  mumewe profesa Kadiri walimwambia achague nchi yoyote aliyetoka kwenda ili wampeleke kupumzika, Caroline alichagua Uingereza.

    Kwa  miezi miwili  alikaa Uingereza kama zawadi kwa ushindi  alioupata!  Huko Uingereza aliishi na familia moja iliyokuwa na  uhusiano na wazazi wake, akiwa huko alimfikiria Richard   lakini hakujua  mahali pa kumpata kwani alishapoteza anuani zake na hata jina la chuo alichosoma!

                    ***************

    Akiwa ndani ya ndege ya British Airways akirudi  Tanzania alishtukia  kijana amesimama mbele yake na kumwita kwa  jina.

    “Hee! Richard!” Alijiitikia kwa mshangao.

    “Vipi?” Unatoka wapi huku wewe chaurembo?” Richard aliuliza.

    “Nilikuwa hapa UK kwa miezi miwili!”

    “Bila hata kunitafuta?”

    “Sikujua kama uko hapa!”

    Waliongea mengi  na Richard alimweleza Caroline  juu ya mapenzi yake kwake na alimtakia wazi kuwa alitaka kumuoa, kwa mara ya kwanza Caroline alihisi kumpenda Richard lakini kila alipoufikiria ugonjwa wake wa kifafa kisichopona alizidi kuchanganyikiwa! Alijichukia mwenyewe.

    “Nitafikiria lakini kuna kitu itabidi nikueleze kwanza!” Alijibu Caroline.

    “Sawa tu!”

    Uwanja wa ndege wa Dar es Salaam walipokelewa na kijana mmoja aliyeitwa Dickson akiwa na mpenzi wake Mariam!  Dickson alipomwona Caroline alipigwa na butwaa  kwa uzuri aliokuwa nao na Richard alipomwona Mariam alibaki mdomo wazi kwa uzuri wa msichana huyo.

    Shangazi yake Caroline alimpokea na kumpakia ndani ya gari na Dickson, Richard na Mariam waliondoka ndani ya  gari walilokuja nalo hadi Mikocheni nyumbani kwao na Dickson. Kwa sababu Mariam alikuwa mwanafunzi wa chuo cha Usimamizi wa fedha (IFM)   baada ya kufika nyumbani  aliondoka kurudi chuoni  na kuwaacha Dick na Rich peke yao.

    “Mshikaji kile kifaa vipi?” Dickson alimuuliza Richard.

    “Si ndiye yule mtoto wa Arusha aliyenisababishia matatizo kipindi kle umesahau?”

    “Aisee ndiye yule?”

    “Ndiyo bwana ila sasa hivi kazidi kuwa mzuri!”

    “Aisee usimwachie mshikaji kaza kamba angalau ufidie kidogo maumivu uliyoyapata!”

    “Safari hii sikubali lazima nimpate na akikubali nitaka nimuoe  kabisa ili nikiondoka kurudi Uingereza niondoke naye!”

    “Poa tu, lakini kati yake na Mariam nani zaidi?”

    “Caroline zaidi!”

    “Ah! Wapi ni Mariam zaidi huuoni usafiri wake!”

    Yalitokea mabishano makali kati yao  na hawakufikia muafaka kila mmoja wao akisema wa kwake ni zaidi.

                   ************

    Miezi mitatu baadaye mambo yalishakolea kati ya Caroline na Richard! Caroline alihisi kuchanganyikiwa na penzi la Richard hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angechanganywa na  mwanaume kiasi hicho baada ya kuapa kuwa asingempenda mwanaume tena. Kilichomsumbua akilini mwake kilikuwa ni tatizo la kifafa, siku zote hakuzisahau tarehe 26-28! 

    “Siku akijua itakuwaje? Au  yakitokea kama yaliyotokea kwa Harry?” Swali hilo lilimsumbua sana kichwani mwake! Lakini bado hakuwa tayari kuisema siri iliyosema moyoni mwake.

           *****************

    Mashindano yalikuwa yamefikia hatua ya tano bora.

    “Mshiriki anayefuata sasa ni mwakilishi wa Ilala, Mariam Hassan!”Ukumbi mzima ulishangilia kwa vigelegele.

    Richard na Dickson walikuwa nyuma kabisa ya ukumbini wakiangalia kwa chati! Alipotajwa Mariam, Dick aliruka juu na kushangilia lakini Richard alinyong’onyea na kukosa raha kabisa! Dick alianza kumzomea.

    “Nilikuambia mshikaji kuwa Caroline siyo kitu! Ukabisha unao sasa hata kwenye tano bora hayumo!”

    “Anayefuata ni Caroli…..!” Kabla hata Jaji  hajamaliza sentensi yake Richard aliruka juu na kuanza kushangilia huku akikimbia kwenda jukwaani! Hakuamini kama alikuwa amelisikia jina la mpenzi wake likitajwa.

    Ilikuwa siku ya tarehe 27/12/1999 watu walifurika ndani ya ukumbi wa Diamond  Jubilee kushuhudia kinyang’anyiro cha Miss Tanzania! Ni mabishano ya “nani zaidi” yaliwafanya Richard na Dickson kuwashinikiza Mariam na Caroline washiriki mashindano hayo.

    Awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika tarehe 14/10/1999 lakini yaliahirishwa sababu ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere! Ni tarehe hizo  zilizomfanya Caroline akubali kushiriki mashindano lakini yalisogezwa mbele hadi tarehe 27/12/999! Alikataa lakini Richard alimlazimisha   kwa kitisho cha kuacha kumuoa na kwenda naye Uingereza.

    “Mbona Mariam  anashikiri yeye siyo msomi?”

    “Siyo hivyo Richard najua ni kwanini sitaki kushiriki siku hiyo ingekuwa siku nyingine yoyote sawa kwani hawawezi kufanya mwezi wa kwanza? Au tarehe 30/12/1999?” Aliuliza hakuwa tayari kushiriki  lakini badala ya kushawishiwa sana na Richard  alikubali kwa shingo upande akitegemea labda siku hiyo isingekuwa mbaya kwake, alitamani aanguke tarehe 26 au 28!

                     ************

    Kipindi cha kuulizwa maswali kwa washiriki wa tano bora kilimalizika na Jaji maarufu  jijini Dar es Salaam Bw. Manjit alisimama wima kutaja majina ya washindi wa Miss  bongo

    Gari aina ya benzi lililokuwa zawadi ya mshindi wa Miss Tanzania lilikuwepo ukumbini hapo!   Minong’ono  ya chinichini ilisikika   Caroline akitajwa karibu na watu wote ukumbini kuwa ndiye alistahili kuwa mshindi! Wakati huo Caroline alikuwa nyuma ya pazia akitetemeka hali yake aliisikia si nzuri alihisi kizunguzungu.

    Jaji alitaja majina ya washindi  namba nne na tatu, ukumbi wote ulipiga kelele na kushangilia kwa furaha,  nyuma ya pazia walibaki watu wawili tu mariam na Caroline.

    “Haya mzee mwenzangu nani anaibuka dume kati yangu mimi au wewe!” Dick aliuliza lakini Richard hakujibu kitu alisubiri sauti ya jaji Mkuu.

    “Mshindi wa pili ni Mariam Hassan!” Ukumbi wote ulipiga kelele na kushangilia baada ya kujua Caroline ndiye alikuwa ameibuka mshindi wa Miss Tanzania! Richard alilia kwa furaha.

    “Nilikueleza mzee mwenzangu Caroline ni kifaa cha nguvu ukabisha unaona sasa!” Richard alimwambia Dickson.

    “Miss Tanzania mwaka huu ni Caroline John Kadiri!”

    “Nyanyuka twende wewe ndiye Miss Tanzania!” Wasichana wenzake walimwambia lakini hali ya Caroline haikuwa nzuri.

    “Sitaki kwenda jukwaani!” Alikataa Caroline.

    “Kwanini?”

    “Najua mwenyewe!” Alijua wakati wowote angeanguka kifafa muda mfupi baadaye Richard na Dickson pamoja na mwaandaaji walipokwenda na kumleta hadi jukwaani ambako kizunguzungu kilizidi.

    “Richard! Richard! Richard!”

    “Naam Darling!”

    “Nirudishe nyuma ya pazia upesi!”

    “Kwanini?”

    “Wewe nirudishe tu!”

    “Hapa....!” kabla Richard hajakamilisha sentensi yake Caroline alianguka sakafuni, akageuza macho na povu likamtoka mdomoni! Watu wote ukumbi mzima walishika mkono kichwani na wengine kuzomea.

    “Miss Tanzania ana kifafa!”

    Richard alimwaga machozi ya huzuni.

     Je nini kitatokea? Fuatilia wiki ijayo.













    Caroline ni msichana mrembo kupita kiasi mwenye siri kubwa moyoni mwake, siri ya ugonjwa wa kifafa! Siri ambayo hataki mtu mwingine yeyote zaidi ya wazazi wake aifahamu lakini inakuwa vigumu kufanya hivyo kwani tayari amekwishaanguka mara mbili mbele za watu! Mara ya kwanza alianguka mbele ya mpenzi wake Harry na akaachwa! Mara ya pili ameanguka baada ya kutangazwa tu kuwa mshindi wa Miss Bongo zawadi yake ikiwa gari aina ya Benz! Ameanguka mbele ya mpenzi wake mpya, Richard. Je nini kitampata na siri yake hiyo? Endelea............

    Watu wote waliokuwa ukumbini walipigwa na butwaa sababu ya hali iliyojitokeza,  mikono ya watu wengi ilikuwa kichwani kwa uchungu! Wachache hasa wasichana waliowashangilia washindani wengine waliotupwa na Caroline  wakisikika wakizomea kwa sauti ya juu! Lilikuwa ni jambo la kusikitisha kupita kiasi, hakuna mtu aliyekuwa tayari kuamini kuwa msichana mrembo kama Caroline alikuwa ameanguka kifafa tena mbele ya watu baada ya kutangazwa ni mshindi wa Miss Tanzania.

    “Karogwa! Karogwa!” Sauti ilisikika  kila sehemu ukumbini, watu wasijojua siri ya ugonjwa  wa Caroline walipiga kelele.

    Caroline alikuwa amelala  chali jukwaani  akiwa amezungukwa na watu wengi, kila mtu alitaka kumwona mrembo aliyeanguka kifafa! Wapiga picha wa magazeti mbalimbali walikuwa bize wakipiga picha zake kwa ajili ya magazeti yao siku iliyofuata.

    Richard alisimama mbele ya Caroline akilia machozi, hakuwa tayari kuamini kilichokuwa kimetokea usiku huo,  kwa uzuri aliokuwa nao Caroline hakutakiwa kabisa kuwa na kifafa! Hiyo ilikuwa kasoro mbaya sana, kwa Richard yaliyotokea usiku huo yalikuwa ni kama ndoto!

     Dickson na Mariam  walimpigapiga Richard mgongoni kumfajiri kwa yaliyojitokeza lakini  alizidi kulia,  alimpenda mno Caroline lakini alihisi asingeweza kuendelea na  msichana mwenye kifafa! Kwake ilikuwa ni bora aishi na msichana  kikojozi kuliko mwenye kifafa!

    Upande mwingine  kichwani mwake  alihisi  kulikuwa na kitu  kilichofanya kwa lengo la kumharibia Caroline ushindi wake. “Kuna mtu amefanya uchawi ili   achukue ushindi” Aliwaza Richard.

    Dakika kama arobaini na tano baadaye Caroline alishtuka na kuketi kitako jukwaani, alifungua macho na kuangalia kila upande, alishangaa kukuta idadi kubwa ya watu wamemzunguka! Hakuwa na kumbukumbu juu ya kitu chochote kilichotokea na hakukumbuka pia alikuwa  mahali pale kufanya jambo gani! Kumbukumbu zote juu ya mashindano ya Miss Bongo aliyokuwa akishiriki zilikuwa zimepotea.

    Alipoangalia vizuri kati ya watu waliomzunguka alimwona Richard akilia  moyo wa Caroline ulishtuka na kujikuta akisimama wima kutaka kujua kilichotokea!

    “Richard kimetokea kitu gani hapa mbona watu wamejaa?”

    Richard hakujibu kitu  bali aliendelea kutokwa na machozi  jambo lililozidi kumtia wasiwasi zaidi Caroline, hakuwa na kumbukumbu hata kidogo juu ya kilichompata! Alipounyanyua mkono wake wa kulia kwa lengo la  kujikuna  usoni alikumbana na mapovu mdomoni! Aliushusha tena ukatua kwenye gauni lake zuri la kutokea jioni alilovaa kwenye maonyesho hayo lililobuniwa na mbunifu maarufu wa mavazi  jijini Dar es Salaam Bw. Merinyo,nalo pia lilikuwa limelowa!

    Aliunyanyua mkono wake na kuuweka puani  na kugundua nguo yake ililowa na mkojo ni hapo ndipo kumbukumbu zilimwijia kichwani mwake kuwa alianguka kifafa!

     Machozi yalianza kumbubujika, aligeuka na kutaka kumshika Richard begani, lakini mikono yake ilitupwa na Richard alianza kuteremka ngazi  haraka kutoka jukwaani, ilionyesha wazi   alikuwa akiondoka ukumbini  kwenda nyumbani! Nyuma yake walifuata Dickson na mpenzi wake Mariam.

    Waliamua kuondoka kumwacha Caroline  peke yake ukumbini! Hakukubaliana na jambo hilo na   kuteremka  mbio jukwaani,  aliwafuata hadi nje ambako kulikokuwa na kiza kinene, alipita katikati ya magari kuelekea mahali lilipoegeshwa gari  la Dickson walilokuja nalo lakini  kabla hajalifikia   liliondoshwa kwa kasi na kumwacha peke yake.

    “Richard! Richard! Richard please don’t leave me here”(Richard!Richard! Richard! Tafadhali usiniache hapa) alipiga kelele Caroline lakini gari halikusimama liliondoka kwa  mwendo wa kasi, maumivu aliyoyapata Caroline moyoni mwake   hayakuwa na kitu cha kulinganishwa nayo.

    Hakuelewa mahali pa kwenda baada ya kutoka hapo lakini pia hakuwa na sababu ya kurudi tena ukumbini ambako watu waliendelea kuzomea wakiwaomba waandaaji wamtangaze mshindi wa pili wa mashindano hayo  Mariam kuwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho.

    Muandaaji hakuwa na namna nyingine yoyote zaidi ya kukubali na   Mariam akatangazwa  Miss Tanzania usiku huo huo bila hata yeye mwenyewe  kuwepo! Kifupi mashindano   yalivurugika.

                    ***************

    Muda mfupi baadaye watu walianza kuondoka na magari yao, Caroline hakuwa na usafiri wa kumpeleka nyumbani kwao, alitamani sana achukue teksi   lakini alishindwa kufanya hivyo kwa sababu hakuwa na pesa na pochi yake ilikuwa ukumbini nyuma ya pazia mahali ambako kwa uhakika asingeweza kwenda tena kwa sababu ya aibu aliyokuwa nayo! Alishindwa kuelewa angeondoka vipi ukumbini hapo.

    Alisimama nyuma ya mti mkubwa na kuendelea kulia bila kujua  cha kufanya, alihisi dunia imemgeuka tena na kuichukua furaha yake! Alijilaumu kuzaliwa na ugonjwa usiopona, aliona ni heri hata uzuri aliokuwa nao usingekuwepo maana ndiyo uliowafanya wanaume wamfuate.

     Yakiwa yamebaki magari kama matano kwenye maegesho nje ya ukumbi huo,  aliliona gari la Dickson likiingia kwenye maegesho, alijua wazi kuwa walikuwa wamemrudia, Caroline alianza kutembea akilifuata gari hilo  alishangaa kumkuta Dickson peke yake ndani ya gari.

    “Pole sana Caroline!”

    “Ahsante sana kwanini mliamua kuniacha lakini?”

    “Ni Richard  sio mimi alipatwa na aibu sana na amesema hakutaki tena maishani mwake!”

    “Kweli?” Aliuliza Caroline kwa mshangao.

    Mambo aliyofanyiwa na  Harry yalikuwa tayari yamemrudia tena, maumivu aliyoyasahau yalikuwa yamerejea, alijiona ni binadamu mwenye mkosi kuliko binadamu wengine wote duniani kwa mara nyingine tena uamuzi wa kifo ulianza kumfuata kichwani mwake, alianza kutamani kifo, hakuwa tayari hata kidogo kupambana na aibu iliyokuwa mbele yake, aibu ya kuzomewa sababu ya ugonjwa.

    “Lakini nilimwambia Richard kuwa tarehe 26-28 huwa siyo nzuri kwangu akalazimisha!” Alisema Caroline huku akilia.

    “Hivi ina maana huwa unaanguka kila mwezi?”

    “No! No! No! Nilitaka kusema hivi ....... tarehe hizo huwa si nzuri kwangu!” Alidanganya Caroline lakini alikosa namna ya kuitetea hoja yake na kujikuta akirudia  maneno yaleyale.

    Sentensi hiyo ya Caroline ilimfanya Dickson aelewe  jambo tofauti,  hisia kuwa Caroline alikuwa amelogwa zilianza kumtoka  na alianza kuamini Caroline alikuwa na kifafa kwa muda mrefu!

    “Ulianza lini kuugua?”

    “Kuugua nini?”

    “Kifafa?”

    “Nani kakuambia  mimi nina kifafa?”

    “Si ulianguka ukumbini?”

    “Kwani kuanguka ni kifafa?Mimi sina kifafa Dickson ila nilikunywa dawa za malaria aina ya Halfan halafu sikula chakula zikanizidi nguvu!”

    “Ahaa! Pole sana!”

    “Ahsante sana  lakini unanipeleka wapi Dickson?”

    “Ninakupeleka hotelini kwa Richard ukalale au?”

    “Nitafurahi sana ukifanya hivyo kwani ninahitaji kumwelewesha Richard kuhusu jambo hili sitaki kukosana naye!”

    “Sawa!”

    Badala ya kupelekwa Sunshine hoteli aliyofikia Richard, alipelekwa hoteli Bridge side hoteli!

    “Na huku tumekuja kufanya kitu gani?”

    “Richard alisema nikulete hapa halafu nimfuate!”

    “Sawa basi fanya haraka!”

    Wote wawili walipanda hadi   ghorofa ya tatu kulikokuwa chumba namba 222! Dickson alikaa kitandani na Caroline alikaa kwenye kochi, ilikuwa hoteli nzuri yenye kila kitu ndani!

    “Mfuate basi!”

    “Subiri dakika chache nipumzike!” Alisema Dickson lakini badala ya kukaa dakika chache  alizosema alikaa zaidi ya saa nzima! Caroline alianza kuingiwa na wasiwasi na kumkumbusha tena ndipo alipoondoka na hakurejea tena mpaka masaa matatu baadaye ikiwa tayari saa tisa ya usiku alipoingia chumbani peke yake bila kuongozana na Richard, mkononi mwake alikuwa na kopo kama la dawa ya  mbu ya Doom!’

    “Yupo wapi Richard?”

    “Amekataa kuja! Amesema hana shida na wewe tena na usimfuatefuate!”

    “Mungu wangu nitafanya kitu gani mie!” Alisema Caroline huku akilia.

    “Lakini usijali sana kama amekuacha  poa tu  msichana mzuri kama wewe, nipo tayari kumwacha Mariam niwe na wewe!” Alisema Dickson huku akijaribu kumpapasa Caroline kifuani, ni kitendo hicho ndicho kilifanya aielewe nia yake.

    “Koma! Nimesema koma na kama umenileta hapa kunifanyia fujo basi umeshindwa, niachie mimi niondoke zangu nikafie mbele!” Aliongea kwa ukali Caroline huku akisimama wima  na kuanza kuufuata mlango uliokuwa bado haujafungwa kwa ufunguo.Kabla hajaufikia mlango Dickson alimdaka na kumuangusha chini

    “Dickson  nitakushtaki na kwa uhakika utafungwa maisha kwa kunibaka!”

      Dickson hakujali na bila kusita alilichukua kopo la dawa lililokuwa pembeni yake na kumpulizia Caroline usoni  bila kujali kiasi  cha madawa aliyopuliza, yalikuwa ni madawa ya usingizi ambayo hutumiwa chumba cha upasuaji kufanya upasuaji.

    Caroline alilegea na kuanguka sakafuni Dickson akambeba na kumtupa kitandani  kisha kumvua nguo zote alizovaa akabaki kama alivyozaliwa yeye pia alifanya hivyo hivyo.

                 ***************



    Nusu saa baadaye kazi aliyodhamiria kuifanya alikuwa ameikamilisha na akili yake ilimrejea na kumkuta  Caroline  amelala pembeni yake akiwa kimya, alionekana kuwa katika usingizi mzito, hakuelewa kitu chochote kilichoendelea chumbani hapo! Kila alipouangalia uzuri  na ulaini wa ngozi  ya Caroline kwenye taa Dickson alizidi kuhemuka na hivyo  kuzidi kumfanyia ukatili  Caroline  bila yeye kufahamu.

    Mpaka saa kumi na moja alifajiri Caroline alikuwa bado hajazinduka usingizini, Dickson alianza kuingiwa na wasiwasi  na  hakuelewa   angemtoa  hotelini na wazo jingine lililomwijia kichwani ni juu ya kifungo kilichokuwa mbele yake, alijua kwa vyovyote baada ya kuzinduka   Caroline angeyasema yote yaliyompata na ni lazima angemwingiza Dickson jela!

    “No! No! Huyu ni lazima afe kwani nani anajua nipo naye hapa?”Aliwaza Dickson.

    Baada ya kuwaza hayo alitoka hadi nje kwenye gari lake ambako alichukua guni tupu alilotumia kubebea mkaa siku moja kabla  na kuingia nalo hadi ndani ya chumba, alihangaika lakini hatimaye alifanikiwa kumwingiza Caroline ndani ya gunia hilo akiwa bado usingizini na kutoka  akiwa amebeba gunia hilo begani na kwenda  kumtupa ndani ya gari lake!

    Baada ya kazi hiyo Dickson aliingia katika gari lake na kuondoka  kwa mwendo wa kasi akifuata barabara ya Morogoro, aliendesha, nusu saa baadaye na alifika  Kibaha! Ambako alikata kulia kufuata   barabara  iendayo Msata mbele kilometa kama ishirini hivi katikati ya pori alilishusha gunia na kulitupa vichakani!

    “Tutaonana ahera!” Alisema Dickson huku akiondoka kurejea mahali alipoliacha gari lake! Kabla ya kuondoka aligeuka na kuliangalia gunia roho ilimuuma kugundua alikuwa amemuua msichana mzuri asiye na hatia.

                    *************

    Dakika ishirini na tano baadaye tayari alikuwa nyumbani kwake akioga na kuvaa nguo safi, hakutaka kukaa nyumbani alitoka  kwenda moja kwa moja hadi hotelini kwa rafiki yake Richard, alimkuta akilia machozi.

    “Vipi mshikaji?”

    “Caroline hajaonekana tangu jana usiku nimemtafuta  mno  nampenda  sana Caroline, yaliyotokea  jana  yalikuwa ni hasira tu!”

    Moyo wa Dickson ulilipuka  kwa hofu! Alijisikia mkosaji na hakujua ni kwa jinsi gani angeificha siri aliyokuwa nayo.

    “Mbona umeshtuka sana?” Richard alimuuliza rafiki yake.

    Dickson alishikwa na kigugumizi.

    Je nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo.











    R

    ichard alionyesha wazi  ?kumkubali Caroline  ?pamoja na tatizo alilokuwa nalo, jambo hilo lilimshangaza sana Dickson. Alijua wazi Caroline alikuwa mfu. 

    “Kwanini umeonyesha mshangao mkubwa  kiasi hicho Dickson?”

    “Nimeshangaa sana sababu jana tulimwacha palepale nje ya ukumbi sasa atakuwa amekwenda wapi?” Dickson alimjibu Richard  huku akitetemeka.

    “Hata mimi sifahamu mahali alipo  nimemtafuta  sana, sehemu pekee ambayo sijafika wala kuulizia ni nyumbani kwao na  ninaogopa kufanya hivyo!” Alisema Richard, mwili wake ulijaa hisia kuwa Caroline alikuwa katika matatizo.

    “Labda atakuwa nyumbani kwao?” Dickson aliuliza ingawa ukweli aliufahamu

    “Kwa kweli sifahamu labda tupige simu!”

    “Namba yao ya nyumbani unayo?” 

    “Ninayo!”

    Richard kishujaa kabisa   alijikakamua na kunyanyua simu  na kupiga namba ya nyumbani kwao na Caroline   jibu  alilopewa lilimkatisha tamaa zaidi, aliyepokea simu hiyo alikuwa mtoto mdogo na alimtaarifu kuwa baba na mama yake hawakuwepo nyumbani.

    “Wamekwenda wapi?”

    “Wamekwenda kumfatuta dada!”

    Jibu  la mtoto huyo lilizidi kumchanganya  akili Richard na kumfanya abaki akijilaumu moyoni mwake kwa kitendo kibaya  cha kumuacha Caroline ukumbini usiku.

    “Nilifanya makosa sana kwani huo ndio ulikuwa wakati wa kumuonyesha Caroline mshikamano zaidi! Nahisi atakuwa amejinyonga au kujiua kabisa na kama itakuwa hivyo sijui mimi nitafanya nini!” Aliwaza Richard huku akionyesha huzuni kubwa, Dickson alimuwekea Richard mkono begani na kumbembeleza.

             ****************

    Kushiriki kwa Caroline katika kinyang’anyiro cha Miss Bongo kulifanywa siri kubwa sana kwa sababu katika tarehe  za mashindano hayo zilikuwa ni zile tarehe za hatari kwake ambazo hakutakiwa kutoka nyumbani hata dakika moja.

    Ni mpango wa uongo uliofanyika kati ya Mariam Hassan na Caroline ndio ulimwezesha kushiriki mashindano hayo, Mariam alitoka chuoni IFM  na kwenda nyumbani kwao Caroline  na kumdanganya shangazi yake kuwa   alikuwa na sherehe  ya kuzaliwa kwake nyumbani kwao  na alitaka Caroline awe kwenye sherehe  hiyo na wasingechelewa kurudi.

    Mara ya kwanza shangazi alikataa katata lakini baadaye Caroline alimwita chumbani kwake na kuanza kumbembeleza   akimhakikishia kusingekuwa na  tatizo lolote  siku hiyo na asingechelewa kurudi nyumbani. Caroline alikuwa tayari kusema uongo wowote ili mradi amridhishe Richard.

    “Shangazi kwanza siku hizi sianguki mara kwa mara, mfano mwezi uliopita sikuanguka kabisa! Hizi dawa za Wachina zinanisaidia sana, naomba tu uniruhusu niende shangazi!” Caroline alizidi kumbembeleza shangazi yake hatimaye akakubali lakini akamwomba anywe kwanza dawa na alimwomba Mariam amwachie namba yake ya simu.

    “Ahsante sana Mariam bila wewe nisingeruhusiwa!” Alisema Caroline kabla ya kuondoka nyumbani.

    “Mbona kuna siku nyingine tarehe 26 inapita bila mimi kuanguka kawnini iwe leo?” Aliwaza  Caroline  wakati wakipanda ndani ya gari kwenda ukumbini.

                        ****************

    Mpaka saa kumi na moja alfajiri   Caroline alikuwa bado hajarejea nyumbani! Jambo hilo lilimtia wasiwasi mkubwa sana shangazi yake Caroline, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mtoto huyo kuchelewa nyumbani kiasi hicho,  fikra ya kwanza kumwijia kichwani mwake ilikuwa ni kifafa! Alihisi Caroline alichelewa kwa sababu alianguka kifafa katika sherehe aliyokwenda.

    “Atakuwa ameanguka kifafa na wamempeleka hospitali  lakini kwanini wasinitaarifu? Hebu ngoja kwanza nimpigie simu yule rafiki yake!” Aliwaza shangazi  na kuchukua simu  ya mkononi iliyokuwa pembeni kwenye meza ndogo  na kuanza kubonyeza  namba  za Mariam  sekunde ishirini tu baadaye alisikia simu  ikiita.

    “Hallow shangazi yake Caroline anaongea sijui ninaongea na Mariam?”

    “Ndiyo!”

    “Caroline ameamua kulala huko huko nini?”

    Mariam alikosa jibu la kumweleza  kwani aibu  waliyoipata  ukumbini ilikuwa  kubwa mno na isitoshe  kitendo cha kumwacha Caroline ukumbini kilikuwa kibaya zaidi na mpaka wakati huo hakufahamu ni wapi alikokuwa, sababu ya hofu hiyo aliamua kukata simu!

    Kukatika  kwa simu kulitafsiriwa na shangazi kama ubovu wa mawasiliano  na aliamua kupiga kwa mara nyingine! Safari hii simu yake haikupokelewa kabisa.

    “Labda simu yake imeishiwa chaji  acha nisubiri nitampigia tena baadaye!” Alijisema shangazi yake lakini hata alipojaribu  kupiga tena baadaye hali iliendelea kuwa hiyo hiyo.

    Hali hiyo ilizidi kumchanganya zaidi  shangazi  alishindwa afanye kitu gani ili  kuwa fahamu mahali aliokuwa Caroline mpaka alfajiri hiyo! Alishindwa kuelewa angewaeleza nini wazazi wake kama angekuwa amepatwa na matatizo yoyote.

    Kilipokucha asubuhi  bila Caroline kurudi  hakuwa na jambo jingine la kufanya zaidi ya   kuendesha gari lake  hadi chuo cha usimamizi wa fedha  kumtafuta Mariam aliyekuja nyumbani kumchukua Caroline, bado aliamini walikuwa wote mpaka asubuhi hiyo.

    Aliendesha gari lake kwa mwendo wa kasi akipitia barabara za Ali Khan upanga na baadaye kuingia barabara ya Ali Hassan Mwinyi hadi  kwenye mataa ya hoteli ya Sheraton ambako alikata kushoto kuingia mtaa wa Ohio hadi  alipokutana na barabara ya Samora, hapo alikata kulia na kunyoosha moja kwa moja hadi  chuo cha usimamizi wa fedha.

    Aliegesha gari lake  na kushuka kisha akatembea kuelekea  kwenye lango la kuingilia, alipokelewa na mlinzi na kumweleza  shida yake.

    “Subiri kidogo nikamwangalie  sina uhakika kama amerudi maana  jana alikwenda kwenye mashindani ya urembo  Diamond Jubilee!” Alisema mlinzi na kuanza kutembea akimwacha  shangazi amekaa kwenye kiti akiwa mwenye mawazo mengi.

    Neno ‘Mashindano ya urembo’ lililosemwa na mlinzi lilifungua fikra mpya kichwani mwa shangazi, aligundua alichoambiwa jana yake hakikuwa kweli.

    “Hivi inawezekana nilidanganywa eh!” Aliwaza mama huyo lakini alishindwa kulikubali wazo hilo moja kwa moja na kuliweka pembeni.

    “Kuna mgeni wako nje dada Mariam!”

    “Mgeni?”

    “Ndiyo!”

    “Yukoje?”

    “Ni mama mweusi, mnene!”

    Maelezo hayo  peke yake yalimtosha kueleza ni nani aliyekuwa akisubiri nje, alipochungulia dirishani alimwona shangazi yake Caroline ameketi akiwa amejishika tama. Hakuwa na jibu la kumpa  juu ya mahali alikokuwa Caroline, alichofanya ni kuchukua pochi yake na kutoa noti ya shilingi 10,000 akamkabidhi mlinzi.

    “Afande huyo mama ananidai,  na mimi hivi sasa sina pesa hebu chukua hii  mwambie sipo sawa?”

    Kwa pesa hiyo aliyopewa neno ‘sawa’ halikuwa gumu kutamkika mdomoni kwa mlinzi.

    Mlinzi alirejea getini na kumpa mama jibu kama aliloelekezwa na Mariam.

    “Una uhakika hayupo!”

    “Asilimia mia tano mama!”

    “Nisaidie kitu kimoja basi!”

    “Kitu gani mama?”

    “Ulimwona Mariam na msichana mmoja mrefu jana?”

    “Ndiyo!Waliondoka wote usiku kwenda kwenye Miss Bongo!”

    “Kwenda wapiiiiiii?” Shangazi aliuliza kwa mshangao.

    “Kwenye Miss Bongo lakini aliporudi hapa alirudi peke yake sijui mwenzake alimwacha wapi!”

    “Kweli?”

    “Ndiyo!”

    “Kwa hiyo kumbe alirudi mbona umenidanganya?”

    “Alirudi lakini nafikiri ameondoak tena asubuhi!”

    “Basi akija  mwambie shangazi yake Caroline alikuja na amesema umpigie simu haraka, sawa kijana?”

    “Sawa mama!”

    Shangazi yake Caroline aliingia ndani ya gari na kuondoka    kurejea nyumbani  kwake ambako alitulia akisubiri simu ya Mariam iingie lakini   na haikuwa hivyo mpaka saa  tatu na nusu,  alishindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kimempata Caroline.

    Baada ya kufikiria kwa muda mrefu nini kifanyike hatimaye alifikia uamuzi wa   kwenda ofisini kwa Muandaaji wa  shindano hilo  kujaribu kuulizia mahali alipokuwa mwanae! Wakati mwingine alifikiri labda waandajai waliwapa washiriki mahali pa kulala.

    Alikuta makundi ya wasichana wengi wakiwa wamesimama nje ya ofisi hiyo, wengi walionekana miongoni mwa wasichana warembo kwani walikuwa wembamba na warefu! Alipoteremka ndani ya gari lake wasichana wote waligeuka kumwangalia! Walionekana kuongea kitu fulani kwa chini chini lakini katika maongezi  neno kifafa lilisikika! Wasiwasi ulianza kuingia.

    Wasichana wote walimwamkia  akiingia ofisini kwa Muandaaji,   ndani alikaribishwa vizuri na  kuketi kitini, hakutaka kupoteza muda kwani baada ya salamu alieleza shida yake.

    “Baba mimi shida yangu ni ndogo tu!”

    “Ndiyo mama!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mtoto wangu Caroline nasikia alishiriki mashindano ya urembo jana ingawa mimi sikuwa na  taarifa na mpaka hivi sasa sijui mahali alipo!”

    “Kweli mama?”

    “Ndiyo!”

    “Sijui nianzie wapi kukueleza lakini ukweli ni kuwa Caroline aliibuka mshindi tena kwa pointi nyingi  lakini kabda hajakabidhiwa zawadi yake alianguka   jukwaani na kuanza kutoa mapovu mdomoni huku mwili wake ukiwa umekakamaa, watu wote walishangaa sana na hatukuelewa kama ulikuwa ni ugonjwa wake siku zote au vipi?

    “Hapana!”Shangazi alijaribu kudanganya, alijua tayari aibu imekwishawapata.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog