*********************************************************************************
Simulizi : Mkimbizi
Sehemu Ya Kwanza (1)
Ulikuwa ni msafara wa watu watano, watatu kati yao, pamoja na mimi mwenyewe, tukiwa ni waajiriwa wa Idara ya Makumbusho ya taifa kitengo cha utafiti wa masalia ya kale. Wa nne alikuwa ni mpiga picha binafsi aliyeajiriwa kwa muda na Idara ya Makumbusho ya taifa maalum kwa shughuli iliyopelekea kwenye msafara huu, wakati mtu wa tano alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye alikuwa anafanya utafiti kwa ajili ya shahada yake ya pili hapo mlimani. Alikuwa anafanya utafiti juu ya masalia adimu ya viumbe vya zama za mwisho za mawe nchini Tanzania, na utafiti wake ulikuwa unawiana kabisa na dhumuni la msafara wetu.
Kutoka katika Idara ya Makumbusho ya taifa alikuwepo mtafiti wa mambo ya kale mwandamizi (ambaye ni mimi), mtafiti mkuu bwana Ibrahim Geresha ambaye ndiye alikuwa mkuu wa msafara na mkuu wangu wa kazi, pamoja na dereva wetu ambaye tangu niajiriwe katika Idara ya makumbusho ya taifa nimekuwa nikimjua kwa jina moja tu la Beka.
Mpiga picha wetu katika msafara huu alikuwa anaitwa Gilbert Kyaro, ambaye alipendelea zaidi kuitwa Gil, na alikuwa akipenda sana kusikiliza na kuimba nyimbo za Johnny Gil.Nadhani ndicho kitu kilichomfanya naye ajisikie kuitwa Gil.
Wakati gharama zote zilizotuhusu katika msafara huu zilikuwa zikilipiwa na idara ya Makumbusho ya Taifa, zile za bwana Ubwa Mgaya, kama nilivyokuja kumjua jina lake hapo baadaye, zilikuwa zikilipwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama sehemu ya fungu lake la utafiti.
Wakati Toyota Landcruiser ikitupeleka kwa kasi kuelekea kwenye eneo la tukio, nilikuwa na matarajio kuwa na hii itakuwa ni safari nyingine ya kuvutia na kunufaisha kama nilivyozoea. Sikuwa na sababu ya kutarajia vinginevyo.
Nikiwa nimehitimu kwa mafanikio makubwa mafunzo yangu ya shahada ya kwanza ya Utafiti wa mambo ya kale (Bachelor’s Degree in Archaelogy) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka mmoja uliopita, nilijihisi kuwa mwenye bahati sana kuweza kuajiriwa na Idara hii ya Makumbusho ya taifa kiasi cha mwezi mmoja tu baada ya kusherehekea kupata kwangu digrii hii adimu, nikiwa naelewa fika jinsi kazi zilivyokuwa ngumu kupatikana hapa nchini hata kwa wahitimu wa vyuo vikuu. Lakini nadhani hii ilitokana na fani niliyochagua kusomea, kwani ni fani ambayo haina upinzani mkubwa hasa hapa nchini.
Marafiki zangu wengi walinishangaa kutokana na uamuzi wangu wa kusomea fani hii, lakini kwa wakati ule nilikuwa nimo ndani ya penzi zito la profesa mmoja kijana wa pale Chuo Kikuu ambaye alinishawishi kuchagua fani hiyo akidai kuwa ilikuwa na nafasi nyingi za kwenda kujiendeleza nje ya nchi. Nilipofika mwaka wa pili nikamfumania mpenzi wangu huyo nyumbani kwake, akifanya mapenzi na mwanafunzi mwenzangu ambaye nilikuwa nikiishi naye chumba kimoja pale chuoni, tena sakafuni jikoni kwake wakiwa kama walivyozaliwa. Nilichofanya ni kuwamwagia maji ya baridi kutoka kwenye jokofu lililokuwapo pale jikoni na kuwaacha wakitapa tapa pale sakafuni nami nikashika hamsini zangu. Matokeo yake penzi la profesa kijana likafa pamoja na ahadi ya kutoka nje ya nchi kwa masomo zaidi katika fani ya utafiti wa mambo ya kale.
Hapo tena ilikuwa haiwezekani kubadilisha masomo, hivyo nikaendelea tu na fani hiyo hiyo.
Baada ya kile kituko cha jikoni kwa profesa kijana, nilibadilishana chumba na msichana mwingine nami nikahamia chumba kingine nilicholazimika kuishi na msichana wa kipemba aliyekuwa akiswali swala tano kila siku, kitu kilichoonekana kumkera yule msichana aliyekuwa akiishi naye awali, ingawa kwangu halikuwa tatizo.
Lakini pamoja na upumbavu wake, profesa kijana hakukosea, kwani nilipata ajira haraka sana baada ya kumaliza masomo yangu, na baada ya kuajiriwa na idara ya makumbusho ya taifa nimekuja kuona kuwa hii hasa ndiyo fani inayonifaa kwani iliniweka njiani muda mwingi kwa safari kuelekea sehemu mbali mbali nchini kufanya tafiti nyingi tu kuhusiana na mambo ya kale na kukusanya mabaki ya kale kwa kuchunguzwa kitaalamu zaidi makao makuu ya idara, Dar es Salaam.
Ila kilichonipendeza zaidi katika kazi yangu hii ni pesa. Kwanza mshahara niliokuwa nikipokea ulikuwa ni mzuri sana, hasa kwa mtu niliyetoka chuoni kama mimi, ambaye hapo nyuma nimekuwa nikishambuliwa na FFU mara kadhaa nikiwa katika maandamano na migomo kugombea kuongezewa posho isiyotosheleza chochote wakati nipo chuoni. Zaidi ya hapo kulikuwa na posho nyingi zinazotokana na safari kama hizi za kikazi, ambazo huwa tunaziita per diem.
Na hivyo wakati mabaki ya kiumbe kisichojulikana yalipogunduliwa wiki chache zilizopita katika msitu fulani huko Manyoni katikati ya kanda ya kati ya Tanzania, kwa mara nyingine tena nikajikuta nikiwa safarini. “Manyoni Expedition” au “Msafara wa Manyoni” kama msafara wetu huu ulivyojulikana ulikuwa ni wa awali, uliotarajiwa kukamilika ndani ya wiki moja ambapo baada ya hapo ingeamuliwa iwapo kilichogundulika huko Manyoni ni kweli kilikuwa mabaki ya kiumbe hai wa kale basi ungekuwa ni mradi maalum ambao ungeweza kudumu kwa kadiri ya muda ambao ungehitajika ili kuukamilisha. Na ikifikia hapo ndipo ningekuwa nazivuna per diem kama sina akili vizuri na wakati huo huo nikifanya kazi ninayoipenda.
Nikiwa nimetulia ndani ya Toyota Land Cruiser kuelekea Manyoni kupitia Dodoma, nilijifariji kuwa baada ya misuko suko na maisha magumu niliyolazimika kupitia wakati nikitafuta digrii yangu pale mlimani, sasa nilikuwa nafaidi nyakati nzuri kabisa katika maisha yangu.
Nyakati nzuri sana.
Nilisahau kabisa msemo tuliowahi kuambiwa na mhadhiri mmoja wakati tuko chuoni kuwa “Ni nyakati nzuri kabisa katika maisha ya binadamu ndizo zinazobadilika na kuwa nyakati mbaya kabisa bila ya kutarajia…”
It is always the very good times of one’s life that normally turns into one’s very bad times in no time…
Ni kwamba kama mtu akiwa katika maisha mabovu hakuna kibovu zaidi kitakachomkuta zaidi ya hicho, lakini akiwa kwenye maisha mazuri ndio ataona mabadiliko pale hali hiyo itakapotoweka.Na kwa kawaida maisha mazuri huwa hayadumu. Kwa wakati ule nilimuelewa sana mhadhiri yule, halafu nikasahau kabisa juu ya ukweli huu.
Sikuwa na sababu ya kuukumbuka tena, kwani tayari nilikuwa nimeshaingia kwenye raha ya maisha mazuri…mpaka hapo yalipokuja kunigeuka.
Tulisafiri kwa saa sita mpaka Dodoma ambapo tulilala kwenye hoteli moja ya bei nafuu kubania pesa zetu za safari kwa makubaliano kuwa tungeaza sehemu ya pili ya safari yetu asubuhi ya siku iliyofuata ili kukwepa jua kali libabualo la nusu jangwa.
Asubuhi ya siku iliyofuata, nikiwa msichana pekee katika msafara wetu, nilijiweka vizuri kwenye kiti changu cha dirishani nyuma ya kiti cha dereva na safari yetu kuelekea Manyoni ilianza. Nilipachika visikilizio masikioni na kuanza kusikiliza muziki wa Bongo Flava kutoka kwenye Walkman yangu ya CD na kuwaacha wasafiri wenzangu wakiburudika na muziki wao wa mayenu kutoka kwenye redio ya gari. Kadiri safari ilipoendelea huku Land Cruiser ikienda kwa kasi kupitia kwenye njia za vumbi na kona nyingi kuelekea kwenye lengo la safari yetu nikabaini kuwa bwana Ubwa Mgaya wa Chuo Kikuu alikuwa akinitupia macho ya mara kwa mara jambo ambalo lilianza kunikera.
Nikavaa miwani yangu ya jua na kuamua kuangalia nje ya dirisha.
Ilikuwa jioni sana tulipoingia Manyoni mjini na kuamua kupata malazi katika nyumba yoyote ya wageni tutakayoiona, ambayo ilitokea kuwa ni nyumba kubwa ya vyuma sita isiyokuwa na umeme na choo cha shimo ambacho pia hutumika kama bafu, na mama mwenye nyumba mcheshi sana. Ilibidi tufanye zamu kutumia choo na bafu na kwa msisitizo wa bwana Ubwa Mgaya nikapewa nafasi ya kuwa wa kwanza kutumia huduma hiyo. Nilipotoka bafuni nikajibwaga kitandani chumbani kwangu kwa lengo la kujipumzisha kabla ya kupata mlo wa jioni, lakini nilipofumbua macho ilikuwa alfajiri ya siku iliyofuata.
Kama jinsi taratibu zinavyotaka, tuliripoti ofisini kwa mkuu wa wilaya, ambaye alitokea kuwa ni mwanamke wa makamu mwenye sura ya kuvutia na tabasamu la kutia moyo. Kwa kuwa alikuwa na taarifa ya ujio wetu, hatukupoteza muda pale ofisini kwake. Baada ya mkuu wa msafara bwana Ibrahim Geresha kututambulisha na mpiga picha wetu Gilbert Kyaro au Gil kutupiga picha ya pamoja tukiwa na mkuu wa wilaya, tulipewa wenyeji wawili kutoka kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ambao ndio wangetuongoza kuelekea huko kulipoonekana hayo mabaki ya kiumbe cha kale kisichojulikana.
Kwa mara nyingine tena tukaingia kwenye Land Cruiser yetu na safari ya kuelekea msituni ikaanza, tukiwa tuna watu wawili zaidi na zana zetu za kazi zilizojumuisha mahema, machepeo maalum, vifaa vya kupikia, chakula cha kuweza kutosha kwa wiki nzima na mabegi yetu binafsi. Tukiwa njiani nilianza urafiki na mpiga picha wetu Gil huku nikibaini kuwa bwana Ubwa Mgaya sasa hakuwa akinitupia macho ya wizi tena bali alikuwa akinikodolea macho wazi wazi kama mvulana ambaye amebaleghe halafu akamwona msichana wa ndoto zake.
Niliamua kutomtilia maanani na kujaribu kuelekeza akili yangu kwenye kazi iliyopo mbele yetu.
Laiti ningejua kilichokuwa kikitusubiri huko mbele…
--
Katika siku yetu ya tatu tukiwa msituni ndipo tulipofanikiwa kufanya ugunduzi tulioukusudia. Ugunduzi wa masalia ya kiumbe hicho cha kale yaligundulika umbali wa kilometa zipatazo mbili kutoka eneo ambalo masalia hayo yalionekana kwa mara ya kwanza na wachimba madini walioshindwa kufanikiwa katika lengo lao la kupata madini waliyoyakusudia na kuambulia kufukua mabaki ya kiumbe hicho.
Zilikuwa ni siku tatu za kazi ngumu lakini ya kufurahisha kwani tulikuwa tukicheka na kutaniana huku tukichimba na kutambaa ardhini tukipima aina za udongo na kulinganisha na aina ya mabaki yaliyogunduliwa hapo awali.Tulichimbua aina mbali mbali za mifupa na kujaribu kuipima kitaalam kugundua aina ya kiumbe kilichobakiza mifupa hiyo.Wakati tukiwa katika harakati zetu hizo, Gil naye alikuwa katika harakati za kupiga picha vitu tulivyokuwa tunavichimbua kutoka ardhini na sisi wenyewe tukiwa katika pozi mbalimbali za kazi. Alikuwa anatumia kamera ndogo aina ya Sony ambayo ilinivutia sana. Gil alinielekeza ni wapi ningeweza kuipata nami nikaweka dhamira kuwa nikirudi tu ustaarabuni nitainunua. Ilikuwa ni kamera iliyoweza kupiga picha za video na wakati huo huo kupiga picha za kawaida. Wakati wa kupiga picha za video, mtumiaji hakutakiwa kuiweka jichoni mwake muda wote, kwani ilikuwa na kiji-runinga kidogo pembeni ambacho mtumiaji aliweza kuwaona watu aliokuwa akiwapiga picha kupitia pale kwenye hicho kijiruninga. Kwa hakika ilinivutia sana na mara kadhaa nilipokuwa najipumzisha katikati ya kazi, Gil alikuwa akinielekeza namna ya kuitumia na nilivutiwa zaidi na mikanda yake ya kurekodia picha za video ambayo ilikuwa midogo sana kuliko hata ile mikanda ya kaseti za redio.
Nyakati za jioni tulipenda kukaa kuzunguka moto na kupata mlo ambao mimi nilijitolea kuwa nawapikia wenzangu na kuongea juu ya mambo mbalimbali kabla ya kila mtu kuingia kwenye hema lake kulala. Ni katika nyakati hizi za jioni baada ya kazi wakati siku moja bwana Ubwa Mgaya aliponiuliza iwapo nilikuwa nimeolewa, wakati huu ikiwa tumezoeana kidogo. Nilimjibu kwa kumwonesha pete yangu ya uchumba ambayo ilikuwa kidoleni mwangu.
“Oh! Aa-Okay…I mean, Hongera sana…” Alijibu kinyonge huku akionesha wazi kuwa alikuwa amekatishwa tamaa.
Nikamshukuru kama kwamba sikuelewa kitu.
--
Ilipofika siku ya nne ilikuwa tayari imethibitika kuwa “Manyoni Expedition” ilikuwa imefanikiwa kwani tuligundua mabaki mengi sana yaliyofanana na yale yaliyogundulika hapo awali ambayo mpaka hapo hatukuwa na namna ya kujua ni ya kiumbe wa aina gani mpaka hapo tutakapoyafikisha Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi. Kwa hali hii, mapema siku iliyofuata tulianza kufungasha virago vyetu tayari kwa safari yetu ya kurudi Dar.
Kwa hiyo wakati wenzangu wanafungasha mahema na vifaa vyetu vya kazi na kupikia, nilimwomba Gil kamera yake ili nijifurahishe kwa kupiga picha mbalimbali za wanyama wadogowadogo pale porini ambao walikuwa wengi. Gil alitoa mkanda wa video aliokuwa amerekodi picha zetu za kazi na akaniwekea mkanda mwingine.
“Haya nenda kachezee huo.” Alisema kwa utani na sote tulicheka. Nilichukua ile kamera na kukimbia porini zaidi kutafuta wanyama wa kuwapiga picha. “Msiniache jamani eenh!” Niliwapigia kelele wenzangu.
“We’ ukisikia honi ujue safari iko tayari!” Ibrahim Geresha alinipigia kelele. Nami nikamnyooshea ishara ya dole gumba kumuashiria kuwa nimemuelewa.
Mara nikaona kundi la tumbiri ambalo lilinivutia na nikaanza kuwapiga picha kwa kutumia ile video kamera ya Gil wakiruka kutoka tawi moja la mti kwenda jingine. Mara nikaona digidigi wakikimbizana nami nikawageukia wao na kamera yangu. Nilikuwa najisikia raha sana. Muda si mrefu likapita kundi kubwa la nyani wakubwa sana ambao kidogo walinitisha kwani nilisikia kuwa nyani wa aina hii huwa wakiona mwanamke msituni lazima wambake. Hivyo nilijificha kwenye kichaka huku nikiwarekodi kwenye video kamera niliyokuwa nayo hadi walipopotea.
Nilijitoa kutoka kwenye kichaka nilichokuwa nimejificha na nilianza kurudi kwa wenzangu taratibu huku nikiangaza huku na huko kutafuta viumbe vingine vya kuvutia wakati ghafla niliposikia mngurumo kama wa ndege kwa mbali lakini ukizidi kuja karibu kila sekunde. Nilitazama juu lakini sikuona kitu kutokana na miti iliyojishona sana juu yangu. Nilianza kurudi tena kwa wenzangu, lakini ile sauti ilikuwa inaongezeka na kuanza hata kupeperusha matawi ya miti iliyokuwa karibu kwa upepo nami nikawa na hakika kabisa kuwa ile ilikuwa ni ngurumo ya helikopta. Niliangaza huku na huko nikijaribu kuitafuta ile helikopta bila mafanikio. Nikaamua kurudi kwa wenzangu.
Nilipokuwa naanza kugeuka ili nirudi kule kwa wenzangu, ghafla helikopta ilijitokeza juu ya uzio wa vilele vya miti iliyokuwa ikinikinga. Bila ya kujua ni kwa nini au ni nini kilichonifanya nichukue hatua hiyo, nilijibanza haraka nyuma ya mti na kuanza kuitazama ile helikopta kubwa wakati ikizunguka kwa madaha mara mbili juu ya eneo lile na kuanza kuteremka taratibu na kwa makelele kwenye ukingo wa msitu ambako katika kuranda randa kwangu sikuweza kufika. Nilijiuliza hii helikopta itakuwa inatafuta nini huku porini katika muda huu. Kwa siku zote nne tulizokuwa tumepiga kambi pale msituni hatukuona harakati zozote za binadamu isipokuwa zile za kwetu tu, ambazo zilikuwa ni za muda tu, hivyo wote tulikubaliana kuwa eneo lile halikuwa na harakati nyingi zaidi ya zile za tumbiri na digidigi.
Niliitazama kwa makini zaidi ile helikopta. Ilikuwa ni sawa na zile za kijeshi ambazo huwa zina sehemu ya rubani yenye vioo wakati sehemu yake ya katikati iko wazi kiasi kwamba kama mtu hauko makini unaweza kuanguka kutoka huko juu.Ilikuwa na rangi ya kijivu iliyochakaa na haikuwa na alama yoyote ya kuitambulisha kuwa ilikuwa ni helikopta ya polisi, jeshi au msalaba mwekundu.
Niligeuka kutazama kule ambapo tulikuwa tumeweka kambi yetu, nikasikia sauti za akina Ibrahim Geresha na Gil zikija kuelekea eneo lile ilipokuwa ile helikopta.Nilitazama tena kule helikopta ilipokuwa inatua lakini sasa ilikuwa imeshapotelea nyuma ya uzio wa miti ile mirefu. Mara nikamwona mmoja kati ya wale wenyeji wawili tuliopewa na ofisi ya mkuu wa wilaya akikimbia kuelekea kule ilipopotelea ile helikopta. Alikuwa kiasi cha hatua kama ishirini hivi kushoto kwangu naye hakuniona. Nilisita kidogo tu, kisha kutokea pale nilipokuwa, nikaanza kukimbia sambamba na yule mwenyeji kuelekea kule ilipokuwa ile helikopta huku nikijiuliza ni nini kilikuwa kinatokea.
Nilikimbia mpaka kwenye ukingo wa msitu ule ambapo niligundua kuwa kulikuwa kuna bonde dogo ambalo chini yake kulikuwa kuna ukanda wa michanga, kama kwamba zamani kulikuwa kunapita mto mpana lakini sasa umekauka. Na hata pale nilipokuwa nikilitazama lile dege kubwa likishuka kwa madaha, niliweza kuona watu wawili wakiwa wamekaa katika lile eneo la wazi wakiwa wamejifunga mikanda maalum ya kuwazuia wasianguke.
Lile dege lilitua ardhini huku likitimua vumbi, nami nikabaki nachungulia nikiwa kwenye ukingo wa msitu lakini nikichukua tahadhari ya kutoonekana. Kwa muda sikuona kitu kutokana na vumbi lililotimuliwa na upepo wa mapangaboi ya dege lile.Nikiwa nimelalia tumbo pale kwenye ukingo wa msitu, nilijaribu kufinya macho ili nione vizuri kule kwenye helikopta.
Kutoka pale nilipolala, ile helikopta ilikuwa umbali wa kama mita arobaini na kwa chini kidogo kiasi kwamba nilikuwa naitazama kutokea juu kidogo. Bado vumbi lilikuwa likitua taratibu sana hivyo kuona ilikuwa vigumu lakini tayari moyo ulikuwa umeanza kuingia wasiwasi. Nilitazama kushoto kwangu ambapo nilitegemea kuwaona akina Ibrahim Geresha na Gil wakitokea lakini sikuwaona.Niligeuka tena kule kwenye ile helikopta na safari hii niliona watu wawili wakiwa wamevaa makoti marefu meusi wakiwa wamesimama nje ya ile helikopta wakiangaza huku na kule wakati mtu mwingine wa tatu akiteremka kutoka kwenye ile helikopta. Sikuweza kuwaona vizuri hawa watu lakini mara moja niligundua kuwa yule aliyeteremka mwisho kutoka kwenye ile helikopta alikuwa akitembea kwa kuchechemea kidogo, kama kwamba alikuwa na ulemavu wa mguu mmoja, na akitembelea mkongojo ulionakshiwa vizuri.
Ni watu gani hawa?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wale watu waliongea kwa muda kisha yule mwenye mguu mbovu alionekana kutoa amri fulani na wale wawili wa mwanzo walirudi ndani ya ile helikopta.Bado nikiwa na mawazo kuwa hapa kulikuwa kuna jambo baya lililokuwa mbioni kutokea, niligeuka tena kushoto kwangu kujaribu kuwatazama wenzangu.
Hamna mtu.
Nikageuka tena kwenye helikopta. Wale watu wawili walioingia tena kwenye ile helikopta walitoka wakiwa wanamburura mtu mwingine ambaye alikuwa kifua wazi! Wazo la kwanza kupita kichwani mwangu lilikuwa ni kwamba yule mtu aliyekuwa anabururwa alikuwa mgonjwa, lakini wazo hilo lilifutwa haraka kutoka kichwani mwangu na nafasi yake kuchukuliwa na woga na hofu kubwa pale niliposhuhudia yule mtu aliyekuwa akibururwa akisukumwa ardhini kikatili na kugaragara vibaya sana kwenye vumbi na michanga huku akitoa yowe ambalo nililisikia wazi wazi kuwa ni la uchungu. Nilitaka kupiga kelele lakini nilijizuia na kabla sijajua nifanye nini, moyo ulinilipuka na kihoro kikanitawala pale nilipowaona Ibrahim Geresha na Gilbert “Gil” Kyaro wakiteremka kibonde kwa kasi kuelekea pale kwenye helikopta wakati ule ule lile tendo la kusukumwa ardhini yule mtu asiye na shati likitokea. Wote wawili walisimama ghafla walipoona tendo lile na kwa sekunde chache hakuna kilichotokea wakati wale watu wenye makoti marefu wakiwatazama akina Ibrahim na akina Ibrahim wakijaribu kuelewa walichokiona. Mara wale watu waliwazingira akina Ibrahim huku wakiwaongelesha na kuwanyooshea bastola! Mwili uliniisha nguvu. Sijawahi kuona bastola hata siku moja ukiachilia mbali kwenye sinema, kwa hiyo yaliyotokea pale chini yalikuwa ni mambo ya kutisha sana kwangu.
Sijui ni nini kilichoniongoza kufanya nilichokifanya, lakini sasa nikikaa na kufikiri, nadhani nilichokifanya kilitokea bila ya mwenyewe kufikiri, ni jambo ambalo unaloweza kusema mtu kalifanya in a spur of a moment - tendo linalofanyika kutokana na hali fulani kwa wakati fulani bila ya mtendaji kupata muda wa kufikiri. Mara nyingi tendo kama hili huwa ni la athari kwa mtendaji, kama vile mtu anaweza kumpiga mtu na silaha fulani in a spur ofa moment bila ya kufikiri halafu akamuua,jambo ambalo kama angepata muda wa kulifikiria asingelifanya. Na jambo nililolifanya lilikuja kuniletea madhara na madhila makubwa sana maishani mwangu .
Nilipoona wale watu wamewaelekezea bastola akina Gil tu hapo hapo niliinua kamera ya Gil iliyokuwa bado mikononi mwangu na kuanza kurekodi matukio yale. Hilo ndilo jambo nililolifanya na sijui ni kwa nini nilifanya vile, kwani wakati nafanya hivyo nilikuwa nimetawaliwa na woga wa hali ya juu.
Sikuweza kusikia yaliyokuwa yakisemwa kule chini lakini kadiri nilivyokuwa nikiliangalia lile tukio kutoka kwenye kiji-runinga kidogo cha kwenye ile kamera yenye nguvu, sikuwa na shaka hata kidogo juu ya kilichokuwa kinaelekea kuwatokea watafiti wenzangu pale chini na hapo hapo moyo ulininyong’onyea. Wale ni watu ninaowafahamu na walikuwa wanaelekea kuuawa na sikuwa na lolote nililoweza kufanya kuwasaidia bila ya mimi mwenyewe kujiongezea kwenye orodha ya watakaouawa.
Yule mtu mwenye mguu mbovu aliwasogelea Ibrahim na Gil taratibu wakati mwingine akiwalengeshea bastola, ilhali yule wa tatu akiwa amemkanyaga mgongoni yule mtu aliyebururwa kutoka kwenye helikopta aliyeanguka kifudifudi mchangani baada ya kusukumwa huku naye akiwa amewaelekezea akina Gil bastola yake.
Kufikia hapa moyo wangu ulikuwa ukipiga kwa kasi sana na akili yangu ilikuwa ikizunguka bila muelekeo maalum na sikupata wazo lolote la kusaidia katika hali ile.Nikabaki nakodolea macho kile kijiruninga cha kwenye kamera ya Gil nikishuhudia yaliyokuwa yakitendeka kule chini.Moyo ulikuwa unapiga kwa nguvu hadi nikahofia kuwa wale watu kule walipo wangenisikia na kuja kunikamata.
Na nilizidi kuchanganyikiwa nilipowafikiria wale watafiti wenzetu waliobaki kule kwenye kambi yetu pamoja na wale watu kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya. Hatimaye nilipata wazo kuwa kwa kuwa sikuwa na namna ya kuwaokoa Gil na Ibrahim pamoja na yule mtu asiye na shati pale chini ambao tayari walikuwa mikononi mwa wale watu wabaya, cha msingi ambacho ningeweza kufanya ni kujaribu kujiokoa mimi mwenyewe na wenzangu waliobaki kule kambini. Nilikuwa nataka kujiinua ili nikimbie kule kambini kuwatahadharisha wenzangu wakati nilipomuona yule mwenyeji mmoja kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya naye akiteremka kibonde kwa kasi kuelekea pale walipokuwa akina Ibrahim naye akajikuta amezingirwa na wale watu wenye makoti marefu na nia mbaya.
Nilibaki nimeduwaa. Sasaitakuwaje?Moyo wangu ulinyong’onyea zaidi nilipogundua kuwa mwili wangu ulikuwa unatetemeka vibaya sana kiasi nilishindwa kujiinua kutoka pale chini. Machozi yalianza kunitoka na nikabaki nimelala kiwetewete pale chini nikitazama wenzangu wakikusanywa kama kundi la kondoo na kupigishwa magoti huku mikono yao ikiwa imewekwa nyuma ya vichwa vyao.
Mtu mwenye mguu mbovu alikuwa akiwauliza maswali na Ibrahim Geresha alikuwa akijitahidi kujieleza ili aokoe maisha yake na wenzake. Lakini hata pale nilipokuwa naangalia matukio yale nilijua kuwa bidii zake hazitazaa matunda.Nilibonyeza kitufe kilichoandikwa “zoom” kwenye ile kamera yenye nguvu na mara picha ilivutwa na kuiona kama vile wale watu wote kule chini walikuwa kama hatua kumi tu kutoka nilipokuwa.Niliielekeza kamera ile usoni kwa yule mtu mwenye mguu mbovu aliyekuwa akiuliza maswali na hapo hapo nilishituka na kufumba macho nikidhani kuwa ameniona kwani wakati ule uso wake ulikuwa umegeuzwa moja kwa moja kule nilipokuwapo.Nilifumbua macho na kuanza kumtazama kwa makini. Haikuwa sura ya mtu mzuri hata kidogo. Jicho lake la kulia lilikuwa kubwa kuliko la kushoto na hapo nikagundua kuwa lilikuwa ni jicho la bandia kwani wakati mboni ya jicho lake la kushoto ikitembea huku na huko wakati akiongea, lile la kulia lilikuwa limetulia tu na mboni yake ilikuwa ya rangi tofauti.
Jicho la mbuzi.
Nilijisikia baridi ikipita mwilini mwangu kwa kumtazama tu yule mtu mbaya.
Taratibu niliielekeza kamera kwa mtu wa pili kati ya wale waliokuwa wameteremka kutoka kwenye helikopta ambaye bado alikuwa amewaelekezea akina Ibrahim bastola yake. Huyu naye hakuwa mtu mzuri. Alikuwa na kidevu kilichochimbika na mdomo wake muda wote ulikuwa umebetuliwa kama mtu aliyechefuliwa na kitu fulani.Alionekana kuwa na umri wa kati ya miaka thelathini na tano na arobaini na usoni mwake alikuwa amevaa miwani ya jua iliyoficha macho yake.
Nikaielekeza kamera yangu kwa yule mtu wa tatu ambaye alikuwa amemkanyaga yule mtu asiye na shati.
Ni nani yule?
Nilipouona uso wake kwenye kamera tu hapo hapo nilihisi ganzi ikipita mwili mzima na nikahisi ubaridi ukitambaa kwenye uti wangu wa mgongo. Huyu mtu alikuwa ni muuaji wa kuzaliwa! Alikuwa na macho ya kutisha kuliko yote niliyowahi kuyaona. Na hata pale nilipokuwa nikiutazama uso wake kupitia kwenye kiji-runinga cha ile kamera ya Gil, macho yake yalinikumbusha macho ya nyoka mwenye sumu kali. Pamoja na kuogofya kwa macho yale yaliyojaa ukatili, nilijikuta nikiendelea kumtazama yule muuaji. Niliweza kuona mdomo wake ukiongea kikatili kuwaeleza jambo akina Ibrahim,na ingawa sikuweza kusikia alikuwa akisema nini, hakukuwa na shaka kichwani mwangu kuwa aliyokuwa akiyaongea hayakuwa na wema kwa wenzangu hata kidogo.
Bila ya kujali jasho lililokuwa likinivuja kwa wingi usoni mwangu, niliteremsha kamera yangu kutoka usoni kwa macho ya nyoka mpaka kwa yule mtu aliyemkanyaga kwa mguu wake.
Mimi sijawahi kuona mtu anayekufa maishani mwangu, lakini muda kamera ya Gil ilipouleta uso wa yule mtu kwenye kiji-runinga chake kidogo nilijua mara moja kuwa nilikuwa nauangalia uso wa mtu anayekufa...uso wa mtu anayejua kuwa anakufa.
Uso wake ulikuwa umevimba na ukivuja damu vibaya, damu iliyochanganyika na michanga.Mwamba wake wa pua ulikuwa umevunjika na kulikuwa kuna jeraka kubwa kuanzia kwenye paji la uso wake lililokata uso ule na kuishia chini ya jicho lake la kulia. Mdomo wake wa juu ulikuwa umevimba vibaya sana. Na pale nilipokuwa namuangalia niliona alikuwa akitiririkwa na machozi ya kukata tamaa. Kwa jinsi nilivyomuona, nilimkisia kuwa alikuwa na umri wa kati ya miaka thelathini na thelathini na tatu, si zaidi ya hapo. Alikuwa ni kijana mwenye sura nzuri ya kuvutia...hiyo ni kabla ya kukutana na hawa watu wenye makoti marefu: sasa hivi alikuwa mbali sana na mtu mwenye sura ya kuvutia na nilimwonea huruma sana. Lakini kitu kilichonipa hisia kuwa nilikuwa natazama uso wa mtu anayekufa haikuwa ile sura yake iliyobondwa bondwa au mdomo uliovimba wala mwamba wa pua uliovunjika. Yalikuwa ni macho yake. Yalikuwa yanatazama kwa kukata tamaa na hayakuwa na ile nuru ya uhai ambayo binadamu huwa tunakuwa nayo, hata kama tunaumwa lakini hatuelekei kufa.
Mikono yake ilikuwa imetawanyika kila upande pale mchangani na miguu yaje ilikuwa imefungwa kwa kamba. Suruali yake ya jeans ilikuwa imechafuka na kuchanika hovyo na miguu yake haikuwa na viatu.
Hawa watu wamemfanya nini huyu jamaa!
Kwa muda akili yangu ilinizunguka na sikujua nifanye nini. Taratibu nilianza kuiweka kamera pembeni nikiwa nimekata tamaa, lakini mara nikahisi kitu kisicho cha kawaida. Nilihisi kama kwamba....lakini haiwezekani!
Taratibu nikairudisha tena ile kamera usoni mwangu na kuielekeza kwa yule mtu aliye kifua wazi pale mchangani na hisia yangu ikathibitika.
Yule mtu anayekaribia kufa ameniona!
Yule jamaa ameniona! Niliona wazi kutoka katika macho yake yaliyokata tamaa na nilijua kuwa ameniona. Ilikuwa kama kwamba alikuwa anajaribu kuniambia kitu kwa macho yake...kama ananiomba kitu kwa macho yake!
Nilijua pale pale kama ninavyojua sasa kuwa taswira ile ya macho ya yule mtu itabakia akilini mwangu kwa muda mrefu wa maisha yangu.
Tulitazamana.
“Usinitazame namna hiyo tafadhali..sina msaada wowote kwako!” Nilijikuta nikinong’ona kumuambia yule mtu na kuweka pembeni kamera iliyokuwa mkononi mwangu na kulaza paji la uso wangu mkononi mwangu.
Anajaribu kunielewesha nini?.
Niliinua tena kamera na kumtazama yule mtu. Bado alikuwa anaangalia kule nilipokuwepo.
“Sasa usifanye hivyo...! Utanikamatisha na mimi!” Nilinong’ona tena peke yangu kama kwamba yule mtu atanisikia na hapo hapo nilirudisha kamera kwa macho ya nyoka. Bado alikuwa ameelekeza uso wake kwa wale mateka wao, akiwa hana habari na yule mtu aliyemkanyaga pale chini, bila shaka kwa sababu alikuwa ana hakika kuwa hakuwa na uwezo tena wa kujaribu kitu chochote. Nilikuwa narudisha kamera kwa yule mtu aliyefikwa na madhila mazito kabisa pale chini wakati ghafla niliposikia purukushani kutoka kule walipokuwa akina Ibrahim Geresha. Niliinua uso haraka na kushuhudia yule mwenyeji aliyekuwa akituongoza katika utafiti wetu akitimua mbio kutoka eneo lile.
“Mamaaa!” Nilijisemea mwenyewe kwa woga huku nikiinua kamera kuangalia kule alipokuwa akikimbilia yule mwenyeji na hapo hapo nilishuhudia yule mtu akitupa mikono yake hewani na kupiga yowe kubwa huku akipiga hatua tatu zaidi za kupepesuka na doa kubwa jekundu likitokea kwenye mgongo wa fulana yake nyeupe iliyopauka.Alianguka chini kama mzigo na kufurukuta kidogo kisha akatulia.
Amekufa!
Yule mwenyeji aliyekuwa akituongoza kule msituni alishikwa woga na kuamua kutimua mbio akiamini kuwa anajiokoa na risasi kutoka kwenye bastola ya macho ya nyoka ilimpata katikati ya uti wa mgongo na kumuua papo hapo. Kwa namna fulani niliweza kuendelea kuielekeza ile kamera kule walipokuwapo lakini mikono yangu ilikuwa ikitetemeka vibaya sana. Nilianza kubwabwaja peke yangu huku nikijitahidi kujizuia kulia kwa sauti. Machozi yalinitiririka huku nikijaribu kuendelea kuangalia yale yaliyokuwa yakitendeka kule chini.
Kwa mtu ambaye hajawahi kuona mtu akiuawa hata siku moja hilo lilikuwa ni jambo la kuogopesha sana kwangu.Mwili ulinifa ganzi na nikahisi kupoteza fahamu. Kule walipokuwa akina Ibrahim kulikuwa kuna kelele nyingi zilizotokana na mayowe ya wale wenzangu waliokumbwa na woga mkubwa kwa kumuona mwenzao akiuawa. Gil alijaribu kukimbia lakini nilimuona Ibrahim Geresha akimkamata mkono na kumvuta chini kwa nguvu huku naye akilala chini ilhali akiinua mikono yake juu. Gil naye alifanya hivyo hivyo huku akisema maneno ambayo sikuweza kuyasikia lakini niliweza kuona kuwa alikuwa amechanganyikiwa. Wale watu wenye makoti marefu walikuwa wakitoa amri kwa makelele huku wakiwapiga mateke akina Ibrahim waliokuwa wamejilaza chini kifudifudi kujisalimisha.
Eeh, Mungu wangu...balaa gani hili tena!
Mara hiyo nikahisi mkojo ukinitoka,ukilowesha suruali yangu ya kodrai na kuchuruzika mchangani.
Oh! Shiit!
Niliweka ile kamera pembeni na kutupa macho kule walipokuwa akina Ibrahim ambapo niliwaona wakiinuliwa kwa nguvu kutoka chini walipookuwa wamejilaza na kusukumwa kuelekea kule walipotokea. Nilimtazama yule mtu aliyebururwa kutoka kwenye ile helikopta na nilimuona akifanya kitu ambacho sikukielewa. Haraka niliichukua tena ile kamera na kuielekeza kwake. Kwa kutumia mkono wake wa kushoto na kwa taabu sana, yule mtu alikuwa akiandika vitu fulani mchangani!
Eeh! Sasa hii ndio nini!?
Sikuelewa kwa nini yule mtu alikuwa anafanya vile na nikaanza kumtilia mashaka iwapo alikuwa na akili timamu muda ule, kwani nilisikia kuwa watu wakiwa wanakaribia kufa -na kwa hakika yule mtu alikuwa anakaribia kufa - huwa wanapoteza akili. Kwa sababu wakati mambo kama yale yanatokea mtu mwenye akili timamu huwezi kufikiria kuchora chora mchangani... Isipokuwa kama akili yako si timamu.
Nilimtazama kwa makini yule mtu kwa kutumia ile kamera. Alikuwa akinitazama bila ya kusema neno wala kufanya kitu kingine zaidi.Lakini kwa mara nyingine tena nikapata hisia kuwa yule mtu alikuwa akinieleza kitu kwa macho yake. Nilitazama kule walipokuwa wenzangu na nikaona kuwa walikuwa wakiongozwa kuelekea kule walipotokea huku wawili kati ya wale majambazi watatu wakiwafuata wakiwa wamewaelekezea bastola zao. Macho ya nyoka alibaki nyuma kwa muda na nilimuona akimwinamia yule mtu aliyekuwa amelala kifudi fudi pale mchangani na kumkemea kwa muda mfupi kisha akampiga teke la mbavu kabla ya kukimbia kuwafuata wenzake waliokuwa wakiwaongoza akina Ibrahim kutoka eneo lile.
Nilihisi kuwa wale watu walikuwa wamewalazimisha akina Ibrahim wawapeleke pale tulipoweka kambi yetu , na nilijua kuwa kama hivyo ndivyo, basi walikuwa wana nia ya kuua watu wote watakaowakuta huko. Moyo ulinipiga kwa kasi na sikujua ni nini la kufanya. Nilijiinua kidogo na kujaribu kuchungulia vizuri zaidi. Wale watu walikuwa wametoweka kutoka eneo lile na kuingia msituni kuelekea ambapo nilihisi kuwa ni kule tulipoweka kambi yetu.
Akili yangu sasa ilikuwa ikijitahidi sana kuelewa mambo yaliyokuwa yakitokea pale msituni ili angalau nipate njia ya kujiokoa. Mambo hayakuonekana kuleta maana kwangu, kwani sikuelewa ni kwa nini wale majambazi - kwani sikuwa na shaka kuwa wale watu walikuwa ni majambazi - waamue kuondoka wote watatu na mateka wao wapya na kumwacha mateka wao waliyekuja naye pale bila ulinzi wowote.
Bila shaka walikuwa wamechagua eneo hili pweke katikati ya msitu ili waje kumuua halafu wamwache huku msituni akioza na kuliwa na fisi.
Lakini kwanini ilikuwa ni lazima huyu mtu aje kuuawa huku msituni?
Kwa nini wasingemuua tu huko walipotoka halafu wakaja kuutupa mwili wake huku msituni? Tena wangeweza kumuua hata mle mle kwenye helikopta na kuja kuutupa tu mwili huku msituni. Kidogo hili lilileta maana kwani katika msitu huu, ingechukua muda mrefu sana kwa mwili wake kugundulika.Lakini sasa hili la kuja kumuulia huku msituni...
Kufikia hapa nilikuwa nalia kwa sauti kama mwehu huku midomo ikinitetemeka na machozi yakinitoka mfululizo huku nikijitahidi kuyafuta bila mafanikio kwa mkono wa shati langu la mikono mirefu la drafti-drafti.
Nilimgeukia yule mtu aliyelala pale mchangani akiugulia na nilishituka nilipoona kuwa alikuwa akijitahidi kusota kuelekea upande niliokuwepo kwa taabu sana. Alipoona kuwa namtazama, aliniinulia mkono wake mmoja kwa ishara ya kuniita. Moyo ulinidunda na woga ukanitawala.
Sasa kaka yangu ukija huku si tutakamatwa wote...? Unataka nini...?
Nilitazama kule walipoelekea wale majambazi na mateka wao ambao ni watafiti wenzangu. Walikuwa wameshapotelea msituni. Nikamgeukia yule mtu aliyekuwa akigaragara pale mchangani. Alikuwa akizidi kuniashiria kwa taabu. Alijitahidi kujiinua kutoka pale chini lakini mara moja alianguka tena chini na kupiga ukelele hafifu wa maumivu. Alibaki akitweta pale chini huku akiwa amejiinamia, akiwa ametuliza paji lake la uso kwenye mkono wake uliolazwa mchangani. Nilimtazama yule mtu huku nikiwa nimechangayikiwa na machozi yakinitoka.
Lakini huu si muhali kaka yangu? Na usichana huu mi’ n’takusaidia vipi hapo...?
Yule mtu aliinua uso wake kunitazama kwa mara nyingine na safari hii niliingiwa na simanzi isiyo kifani kwani jamaa alikuwa analia waziwazi huku akiniangalia. Alipeleka mkono wake wa kushoto na kuanza kupigapiga chini pale alipoandika vitu ambavyo mpaka wakati ule sikuweza kuviona na hivyo kuvielewa.
“What? you want me to see what you’ve written?” Nilijinong’onea mwenyewe kumuuliza yule mtu iwapo alikuwa anataka nione alichokiandika, nikijua wazi kuwa yule maskini ya Mungu alikuwa hanisikii. Na hata pale nilipokuwa nikijisemesha kwa kuchanganyikiwa, yule mtu alijaribu tena kujiinua lakini alishindwa na kuanguka tena mchangani huku akitoa mguno wa maumivu.
Mungu wangu! Huyu mtu anataka kuniambia kitu!
Nilisita.
Nilitazama kule walipoelekea wale majambazi. Kulikuwa kimya kabisa. Moyo ulinipiga kwa nguvu na matumbo yalininyonga. Nikamgeukia yule mtu pale chini, kisha nikatazama tena kule walipokuwa wamepotelea wale majambazi na akina Ibrahim.
Bado kimya.
Niliikwapua kamera ya Gil na kutoka mbio huku nikiwa nimeinamisha mwili wangu kutokea kiunoni kuelekea pale alipokuwa yule mtu aliyekuwa katika mashaka mazito.
Nilipomfikia nilijikuta nikitoa mguno wa woga huku mwili ukinisisimka. Yule mtu alikuwa amechakaa vibaya sana kwa kumtazama karibu kuliko nilivyokuwa nikimwona nikiwa mbali. Mwili wake ulikuwa una makovu mengi mabichi ambayo niliweza kuhisi kuwa yalitokana na kuchomwa kwa ncha ya sigara au kitu chenye moto.
“Oh! Mungu wangu! Mungu wangu! Mungu wangu...” Nilijikuta nikibwabwaja huku nikiutazama mwili wa yule mtu ulivyoharibiwa kwa mateso. Zaidi ya vidonda vilivyotokana na kuchomwa kwa ncha ya sigara, pia mwili wake ulikuwa una majeraha yaliyotokana na kuchanjwa kwa kitu au vitu vyenye ncha kali, kama vile kisu kikali sana. Nilijaribu kumshika lakini nilishindwa kwani nilihisi kuwa kila nitakapomshika nitakuwa namtonesha. Miguu yake ilikuwa imefungwa kamba na ilikuwa ina majeraha makubwa sana yaliyokuwa yakivuja damu. Mguu wake wa kushoto ulikuwa na jeraha kwa nyuma ya paja lake wakati ule wa kulia ulikuwa na jeraha baya sana kwenye ugoko. Pamoja na kwamba sikuwa na uzoefu na majeraha ya aina ile, mara moja nilijua kuwa yalikuwa ni majeraha ya risasi.
Nilianza kutetemeka kwa kihoro na wasiwasi. Kwa hakika hawa watu walikuwa wamemtenda vibaya sana huyu kijana. Nilijaribu kumwinua nikashindwa kwani alikuwa mzito kuliko uwezo wangu. Alijitahidi kujigeuza na kulalia mgongo. Nililaza sikio langu kifuani mwake na kusikiliza mapigo ya moyo wake. Yalikuwa dhaifu sana.
“...the...bas...tard!” Yule mtu alisema kwa taabu na sauti yake ilikuwa ya chini sana.
“Usiongee! Tulia, nitakusaidia” Nilimwambia kwa upole huku nikitupa macho ndani ya ile helikopta. Ilikuwa tupu. Yule mtu alinikamata mkono wangu kwa nguvu na kunivutia kwake. Nilipatwa na woga na kumgeukia. Alipoona nimemgeukia, aliniashiria kwa kidole pale mchangani alipoandika kwa kidole chake. Nilitazama na kuona kuwa alikuwa ameandika namba ambazo sikuelewa zilimaanisha nini. Nilimtazama kwa mshangao na kutaka kumuuliza juu ya zile namba lakini alizidi kunisisitiza kwa macho yake huku akijitahidi kuongea bila ya mafanikio.Nilifikiri haraka haraka. Kwa vyovyote hizi nambazina maana kubwa kwake.Nilielekeza kamera ya Gil kwenye zile namba zilizoandikwa pale chini ili niweze kuzitazama vizuri baadae.
“Sawa...nimeshaona! Hizi namba ni za nini? Na wewe ni nani...kwa nini wale watu wamekufanya hivi? Umewafanya nini? Ni nani wale?” Nilijikuta nikimvurumishia maswali yule mtu huku nikiangaza huku na huko kwa wasiwasi wa kukutwa na wale watu wabaya.
Badala ya kujibu yule mtu alikohoa kwa taabu na kubaki akitweta kama mtu aliyemaliza mbio ndefu..
“Find the Bastard!” Yule mtu alisema kwa kimombo, akimaanisha “mtafute mwanaharamu”, au kitu kama hicho. Mara moja nikamuelewa kuwa alikuwa anamaanisha kuwa anataka niwatafute wale watu waliomfanyia unyama huu ili wawajibike.
“Yes! Usiwe na wasiwasi nitahakikisha wanafikishwa mbele ya sheri...’
“...at the Rickshaw...!” Yule mtu alinikatisha kama vile sijaingilia kati kauli yake ya mwanzo. Sikumuelewa.Alikuwa akitweta sana kila baada ya kusema neno na nikaelewa kuwa kusema kulikuwa kunampa taabu. Na alichokisema kilikuwa hakieleweki.
“Rickshaw? Rickshaw iko wapi ?” Nilimuuliza.
Kwa uelewa wangu Rickshaw ni aina ya mikokoteni inayotumika zaidi kule Taiwan na Thailand kubebea watalii.Hivyo neno lile katika mazingira yale halikuleta maana kabisa kwangu. Badala ya kunijibu yule mtu alianza kutapatapa huku akitupa kichwa chake huku na huko hali akigumia kwa taabu. Moyo ulinienda mbio na woga ukanizidi kwani nilijua kuwa yule mtu ndio alikuwa anakata roho.
Na hata bado sijamjua!
“Wewe ni nani...ndugu zako ni nani?” Niliuliza haraka na kwa wasiwasi.
“Get the key....the bastard!”
“Key…?What key…?”
“At the Rickshaw…!”
“I don’t understand!”
“Please…Go now!”
“Lakini bado sijaelewa…nataka kukusaidia! Au hujui Kiswahili…? Can’t you speak Swahili?”
“Find the bastard!’ Yule mtu asiye na jina sasa alifoka, na hiyo ilionekana kummalizia kabisa nguvu zake hafifu. Alibaki akitweta kwa taabu huku akinitazama kwa macho ambayo kidogo yalionesha matumaini.Nilichanganyikiwa na nikajikuta nikibubujikwa na machozi huku nikimtazama yule mtu kwa huzuni. Yule mtu alinitazama na alitoa kitu kama tabasamu dogo sana.
“Okay...I can speak english....who are you? Who are those people…? Do you have any relatives….? I can help you…I want to help you!” Niliamua kurejea maswali yangu ya awali kwa kiingereza nikitaraji kuwa labda atanielewa zaidi kwa lugha ile.
“Please Go...watakukuta!” Aliniambia kwa sauti hafifu, halafu alipeleka mkono wake na kufuta zile namba alizoziandika pale mchangani.
“Watakuua...wacha nijaribu kukusaidia”
“I don’t care...you go find the bastard!” Halafu alijitahidi kutabasamu tena lakini safari hii hakufanikiwa kwani alishikwa na kikohozi kikali na damu ikaanza kumtoka mdomoni. Nilimwinua kichwa chake ili damu isimpalie na kuanza kumfuta ile damu kwa mkono wa shati langu. Yule mtu alinishika mkono kwa nguvu na kunitolea macho.
“Ondoka hapa mwanamke…they will kill you!”
Ah! Kumbe anafahamu Kiswahili.
“Lakini…”
“Onnn…do….kkka!”
“Akh! Sasa…Ah!” Sikujua niseme nini tena.Nilipagawa.
Huku machozi yakinibubujika niligeuka huku na kule. Hakukuwa na dalili yoyote kuwa wale wauaji wangerudi muda ule, lakini sikuwa na uhakika. Nilimgeukia tena yule jamaa.
“Sasa kaka yangu…sijaelewa chochote katika maelezo yako! Nataka nikusaidie, lakini na wewe lazima unirahisishie kazi hiyo…” Sikuweza kuendelea kwani yule mtu alikuwa ametulia kimya akiwa amefumba macho huku akihema kwa taabu. Hakuwa akitilia maanani kabisa maneno yangu. Nilimshika bega na kumtikisa, lakini hakukuwa na badiliko lolote.
“We’ kaka we’…hebu ongea kitu basi! Sasa uliniitia nini huku? Kwa nini hawa watu wanataka kukuua? Umewafanya nini…?”
Yule mtu aliendelea kubaki kimya bila kufumbua macho wala kutikisika. Hali ile ilizidi kunichanganya. Kabla sijaamua nifanye nini nikasikia sauti kama ya vishindo vya miguu ikitokea kule msituni. Niligeuka haraka huku na huko nisione kitu. Nilimtazama tena yule mtu kwa mara ya mwisho, kisha nikanyakua kamera yangu na kutoka mbio kurudi pale mahala nilipokuwa nimejificha hapo mwanzo. Kiasi cha kama dakika mbili tu baadaye wale wauaji walirejea katika eneo lile. Moyo ulinilipuka nikijua kuwa ningezidi kuchelewa wale watu wangenikuta na sijui wangeamua kuniua kwa mtindo gani tu!
Moyo ukinipiga nilibaki nikichungulia kule alipokuwa yule mtu asiye na jina. Moja kwa moja macho ya nyoka alimwendea yule mtu,alimwinua kikatili na kumkalisha kitako huku miguu yake iliyofungwa kamba ikiwa imenyooshwa mbele.Yule mtu aliangukia ubavu pale mchangani. Macho ya nyoka alimpiga teke la mbavu na kumtolea amri yule mwenzake aliyekuwa amevaa miwani, ambaye alimwinua tena yule mtu na kumshikilia pale chini.
Yule mtu mwenye mguu mbovu alimsogelea yule jamaa asiye na jina na kuanza kusemesha au kumuuliza maswali fulani. Inaelekea yule jamaa aliamua kutojibu kwani mara ile ile macho ya nyoka alimshindilia ngumi kali ya uso na jamaa akatoa yowe kubwa na kuanguka mchangani. Haraka yule jambazi mwingine alimwinua na kumkalisha tena pale chini. Macho ya nyoka alitoa bastola na kumwekea mdomoni huku akimsemesha maneno ya kutisha. Kisha yule kigulu alimsogelea na kumuuliza tena. Jamaa akatikisa kichwa kutoafikiana naye na hapo aliambulia kipigo kingine kutoka kwa macho ya nyoka. Aliulizwa tena, akatikisa kichwa tena kukataa. Macho ya nyoka alimkaba koo kwa mkono wake wa kulia huku akimwekea mdomo wa bastola kwenye paji la uso na kumsemesha kwa ghadhabu. Hapo niliinua tena ile kamera ya Gil na kuielekeza kule kwa lengo la kuona vizuri matukio yale ya kutisha. Na hata pale nilipokuwa naielekeza ile kamera upande ule, nilimshuhudia yule mtu akimcheka macho ya nyoka waziwazi usoni. Tendo lile lilimkera macho ya nyoka na kuanza kumvurumishia kipigo kikubwa yule mtu. Mateke, ngumi, makofi. Hatimaye yule kigulu alimzuia macho ya nyoka na kusukuma pembeni. Macho ya nyoka alipiga teke mchangani kwa hasira na kurusha michanga hewani. Alisogea pembeni na kuweka bastola yake kwenye mfuko wa koti lake refu.
Yule mtu asiye na jina alibaki akigaragara mchangani kwa uchungu na maumivu makubwa. Damu zilimtoka kwa wingi usoni na mdomoni. Kigulu alimkemea macho ya nyoka na kumwinua kichwa yule mtu kumuuliza tena kitu alichokuwa akimuuliza hapo awali. Kwani mnataka nini kutoka kwa huyo mtu ndugu zangu?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yule jamaa badala ya kumjibu alimtemea mate usoni.
Kigulu aliruka kwa hasira na kujifuta mate kwa kiganja cha mkono wake huku akipepesuka pembeni. Muda huo huo yule jambazi mwingine aliyekuwa amevaa miwani ya jua alimrukia yule jamaa kwa teke kali la uso lililomrusha nyuma yule jamaa huku akipiga yowe na kuanguka chali mchangani.
Mungu wangu! Kwani si uwaambie tu wanachokitaka ndugu yangu? Watakuua hao…!
Machozi yalizidi kunibubujika kwa woga na huruma kwa yule mtu huku nikijaribu kufikiri nifanye nini kumsaidia yule masikini ya mungu,lakini kabla sijapata ufumbuzi niliona kitu ambacho sikukitegemea kabisa.
Yule jamaa alimrushia mchanga machoni yule kigulu na hapo hapo alijiinua mzima mzima kutoka pale mchangani hali bado miguu yake ikiwa imefungwa na kumrukia macho ya nyoka aliyekuwa amesimama pembeni bastola yake akiwa tayari ameiweka mfukoni. Kigulu aliruka ruka huku akijipangusa mchanga machoni wakati macho ya nyoka na yule jambazi mwingine walibaki wakiwa wameduwaa kwa sekunde kadhaa, jambo lililomwezesha yule mtu asiye na jina kumfikia macho ya nyoka na kumkamata koo kwa mikono yake yote miwili na wote wawili wakapiga mwereka mkubwa pale mchangani.Wale watu hawakutegemea kitendo kile na hivyo hawakuwa wamejiandaa na tukio kama lile.
Yule mwenye miwani na kigulu walipiga kelele kwa pamoja na kukimbilia pale walipoanguka wale mahasimu wawili ambao walikuwa wakibiringishana mchangani. Macho ya nyoka alikuwa akijitahidi kujikwamua kutoka mikononi mwa yule mtu aliyekuwa ukingoni mwa mauti, na yule mtu asiye na jina akizidi kumkaba koo bila shaka kwa nguvu zote alizobakiwa nazo kwa wakati ule. Vumbi lilitimka na wote wawili wakapotelea kwenye vumbi lile. Hapo hapo yule mwenye miwani aliwafikia na kumrukia mgongoni yule mtu asiye na jina aliyekuwa juu ya macho ya nyoka na kujaribu kumvuta kumtoa kutoka kwa mwenzao, lakini yule jamaa alikuwa amemkamata koo macho ya nyoka vizuri sana. Kilikuwa ni kitimtim kizito kilichodumu kwa dakika zipatazo mbili hivi.
Na mara ulisikika mlipuko mkubwa wa bastola.
Yule jamaa mwenye miwani aliruka na kujitupa pembeni, akainuka na kupiga mweleka tena, kisha akainuka na kupepesuka kabla ya kusimama wima. Kigulu alikuwa ameshajifuta michanga machoni na aliungana na yule jambazi mwingine aliyekuwa akitweta pale pembeni. Walibaki wakiwa wamesimama midomo wazi wakiwaangalia wale watu wawili waliolaliana pale chini nami nikiwa nimekaukwa koo kwa hofu iliyotokana na mambo niliyokuwa nikiyashuhudia pale msituni. Nilibaki nikiwa nimeielekeza kamera yangu kwa wale mahasimu wawili waliolaliana pale mchangani.
Kwa kama dakika moja na nusu hivi walikuwa wametulia tuli na hakukuwa na mwenendo wowote kutoka kwenye ile miili miwili iliyolaliana, kisha niliona mwili wa yule mtu asiye na jina ukiinuka mzima mzima na kuanguka pembeni kando ya macho ya nyoka. Kwa kihoro nilimuona macho ya nyoka akijiinua kutoka pale mchangani na kusimama huku akipepesuka akiwa na bastola mkononi mwake na sehemu ya mbele ya koti lake refu ikiwa imetapakaa damu.
Nilipomtazama yule mtu asiye na jina pale chini, niliona jeraha kubwa kifuani mwake na damu nyingi ikibubujika kutoka kwenye jeraha lile.
Alikuwa amekufa.
Nilihisi mwili ukinifa ganzi na nikaanza kulia upya kumsikitika yule mtu aliyeuawa. Macho ya nyoka alipoona ameelemewa na kabali ya yule mtu aliamua kumpiga risasi ya kifuani na kumuua papo hapo. Kigulu alimjia juu macho ya nyoka, akimfokea na kutupa mikono yake hewani na kuunyoshea kidole ule mwili wa yule mtu aliyelala pale mchangani bila uhai. Hata yule mtu mwenye miwani naye alikuwa akifoka kwa nguvu huku akitupa tupa mikono yake hewani. Macho ya nyoka naye akawa anawafokea wenzake huku akitikisa bastola yake na kumnyooshea mkono yule marehemu pale chini na kujishika koo.
Nikiendelea kutazama mambo yale kwa kupitia kwenye kiji-runinga cha kamera ya Gil, nilishindwa kuelewa maana ya matukio yale na kuzidi kuchanganyikiwa.
Ina maana hawakutaka huyu mtu afe!
Kwa hakika nilichanganyikiwa. Nikawakumbuka wenzangu kule kambini. Mungu wangu! Watakuwa wamewafanya nini wenzangu? Nitawakuta hai kweli…?
Wale wauaji watatu waliacha kugombezana na sasa walikuwa wakiongea taratibu huku yule kigulu akitoa maelekezo. Macho ya nyoka aliutazama mwili wa yule marehemu na kuutemea mate kwa ghadhabu. Kigulu alimshika mabega na kumsukumia kule ilipokuwa ile helikopta yao, na wote wakaingia kwenye lile dege kubwa. Nilibaki nikiwa nimejibanza pale kichakani nikishuhudia ile helikopta ikizungusha mapangaboi yake kwa muda kabla ya kunyanyuka kwa madaha kutoka pale mchangani na kuelea hewani. Ililala kulia kisha ikalala kushoto, na kwa sekunde kadhaa niliweza kumuona yule mtu mwenye miwani akiwa ameshika usukani wa ile helikota, halafu ikalala tena kulia, ikapaa na kutoweka kutoka eneo lile ikiacha mwili wa yule mtu asiye na jina pale mchangani.
Sikusubiri zaidi.
Nilining’iniza mkanda wa ile kamera ya Gil begani na kutimua mbio kuelekea kule ilipokuwa kambi yetu huku nikiita majina ya wenzangu kwa kelele. Mara kadhaa nilijikuta nikianguka na kujiinua tena na kuendelea kukimbia bila kujali kuwa nilikuwa nikipamia miti hovyo na kujiumiza. Nikiwa kama niliyechomoka kwenye mdomo wa mauti,swala la kujipamia kwenye miti lilikuwa ni dogo sana kwangu kwa wakati ule.
Nilipofika kambini kwetu nilipiga mweleka mzito kwa mshituko na kubabaika. Wenzangu wote walikuwa wameuawa! Ni vigumu kuamini lakini ndivyo ilivyokuwa.Ilikuwa ni picha ya kutisha kuliko ile niliyoiona kule ilipokuwa ile helikopta.Huku nikitetemeka na kulia kwa sauti nilijiinua kutoka chini nilipoanguka na kuanza kuwakimbilia wenzangu mmoja baada ya mwingine huku nikiwaita kama kwamba wataitika.
Yalikuwa ni mauaji ya kutisha.
Ibrahim Geresha alikuwa amelala chali mbele ya hema lake huku akiwa ametumbua macho na amekenua meno kwa uchungu.Damu ilikuwa ikichuruzika kutoka kwenye tundu moja lililokuwa katikati ya paji lake la uso.Nilimkimbilia na kujibwaga ubavuni mwake.
“Mista Geresha!Mista Gereshaaa….!” Nilimuita huku nikiutikisa mwili wake kwa nguvu.Ingawa bado mwili wake ulikuwa na joto, Ibrahim Geresha alikuwa ameshakufa. Nililia kwa woga na kuchanganyikiwa kukubwa kabisa. Niliinuka na kuanza kuangaza eneo lile ambalo lilikuwa kambi yetu ya utafiti. Ilitisha sana! Hatua chache kutoka pale alipoangukia bosi wangu Ibrahim Geresha niliuona mwili wa yule mwenyeji mwingine tuliyepewa na ofisi ya mkuu wa wilaya nao ukiwa umeanguka pale kwenye ile ardhi ya mawe ukiwa hauna uhai. Yeye alikuwa amelala kifudifudi huku akiwa na jeraha kubwa sana kisogoni ambalo sikuwa na shaka kuwa lilitokana na risasi.Alikuwa ametawanya mikono yake kila upande na mkono wake wa kulia ulikuwa umekusanya fungu la changarawe kwenye kiganja chake bila shaka kutokana na uchungu alioupata wakati roho ilipokuwa ikimtoka. Nilikimbia kwa kupepesuka kutoka pale nilipokuwa nimesimama na kumuendea bwana Ubwa Mgaya huku nikiita jina lake bila ya matumaini. Alikuwa ameuawa vibaya sana, kwani bila shaka risasi ilimpata akiwa akijaribu kukimbilia ndani ya hema lake. Alikuwa ameshikilia mlingoti wa hema lile kwa mkono wake wa kulia ,ambao kutokana na uzito wake uliangukia juu ya paa la gari yetu iliyokuwa karibu na hema lile. Mgaya akawa ananing’inia kwenye ile nguzo aliyoilalia kwa kiwiliwili chake huku turubai la hema lake likimfunika mwili wake. Kwa pale nilipokuwa, nilikuwa nikiuona uso wake ukiwa umetokeza kwenye turubai lililotapakaa damu nyingi sana naye akiwa ametumbua macho sio kwa uchungu bali kwa mshangao.Ingawa sikuona ni wapi hasa risasi iliyomuua bwana Ubwa Mgaya ilikuwa imeuingia mwili wake, kiasi cha damu kilichotapakaa kwenye lile turubai kilitosha kabisa kunithibitishia kuwa naye alikuwa marehemu. Nilianza kurudi nyuma taratibu huku nikiendelea kuukodolea macho uso wa marehemu Ubwa Mgaya.
“Nisaidieni jamaniiii! Watu nisaidieniii...Ooooh Mama yangu weee! Mambo gani tena haya jamaniii!” Nilikuwa nikilia kwa sauti huku nikimangamanga huku na huku pale msituni nisijue niende wapi. Harufu ya damu ilikuwa inanilevya na nilihisi kichefuchefu kikubwa sana.Nilijibwaga chini na kubaki nikiwa nimepiga magoti huku nimezungukwa na maiti za watafiti wenzangu.Nililia!Nililia sana na kwa muda mrefu.Na kila nikilia niliona haitoshi,kama kwamba nikilia sana angetokea mtu wa kunisaidia.
Lakini bado kuna wenzangu wengine siwaoni! Ingawa nilikuwa nimeona kuwa wenzangu wote walikuwa wameuawa, lakini taratibu akili yangu ilianza kufanya kazi huku nikiendelea kulia.Nilikuwa nimeona wenzangu watatu wakiwa wameuawa pale kwenye ile kambi yetu, na damu nyingi ikiwa imetapakaa eneo lote lile...lakini walitakiwa wawe zaidi ya watatu! Nilinyamaza kulia na kubaki nikigumia kipumbavu huku nikiangaza upya eneo lile.
Wako wapi Beka na Gil?
Taratibu nilijiinua na kuanza kulizuru upya eneo lile huku nikizidi kupata matumaini kuwa kumbe kuna wenzangu waliofanikiwa kuokoka na mauaji yale ya kutisha. “Giiiiill! Giiiiilll! “ Nilianza kuita huku nikiangaza huku na huko kwa matumaini. Hatua chache kutoka pale ulipokuwa umelala mwili wa yule mwenyeji mmoja aliyekuwa akituongoza kule msituni niliona mchirizi mzito wa damu ukielekea kwenye kichaka kidogo kando kidogo ya ile kambi yetu. Nilianza kuufuata ule mchirizi huku moyo ukinienda mbio. Nilihisi kuwa huenda mmoja kati ya wale wenzangu wawili waliobakia atakuwa amefanikiwa kutoroka lakini amejeruhiwa. Ule mchirizi ulipita kando ya gari yetu iliyokuwa imepaki pale na kuelekea sehemu mbele ya gari ile. Nilizidi kuufuata huku nikiita majina ya Gil na Beka kwa zamu. Sikujua ni yupi hasa kati yao ambaye ningemkuta mwisho wa mchirizi ule.
Nilipotokeza mbele ya gari ile tu nilipata mshituko mkubwa na yowe la woga likanitoka. Hapo hapo nilianza kupiga kelele kwa kiwewe huku nikikimbia hatua kadhaa kutoka kwenye gari ile.
Beka alikuwa amelalia boneti la ile gari kwa ubavu wake huku mkono wake mmoja ukiwa umenyooshwa mbele juu ya lile boneti na kichwa chake akiwa amekilaza juu ya mkono ule. Miguu yake ilikuwa imetawanywa vibaya huku pale chini kukiwa kumetifuliwa na kuchimbwa chimbwa bila shaka kutokana na pukushani za miguu yake wakati akihangaika kushindana na roho yake wakati ikimtoka, kwani hakukuwa na shaka kuwa Beka alikuwa amekufa, na alikuwa amefikwa na umauti kwa uchungu mkubwa.
Kwa pale nilipokuwa Beka alikuwa amenigeuzia mgongo lakini niliweza kuona damu nyingi ikiwa imetapakaa kwenye lile boneti na kutiririka ardhini, ikilowesha suruali na viatu vyake.
Huku nikitetemeka na kulia kwa sauti, nilijilazimisha kuzunguka upande wa pili wa ile gari ili niweze kumuona Beka kwa mbele kuhakikisha iwapo kweli naye alikuwa amekufa. Nilichokiona kilinithibitishia hofu yangu na kuzidi kunitisha. Damu nyingi ilikuwa ikimtiririka Beka kutoka kwenye jeraha la risasi lililokuwa chini kidogo ya jicho lake la kulia, ambapo mkono wake wa kulia ulikuwa umepashika kama kwamba alikuwa akijaribu kuizuia damu ile isizidi kutiririka kwa mkono ule. Beka alikuwa na jeraha jingine la risasi ambalo ndilo lililotoa damu nyingi zaidi. Hili lilikuwa katikati ya shingo yake, sehemu ambapo shingo ile ilikuwa ikiungana na kiwiliwili chake.
Eee Mungu wangu! Mauaji yote ya nini haya! Kuna aliyebaki kweli zaidi yangu...?
Hapo nikamkumbuka Gil. Woga ulinizidi kwani ingawa nilijua kuwa naye atakuwa ameuawa, nilijikuta nikiogopa zaidi ukweli kwamba wenzangu wote watakuwa wameuawa kuliko kule kumwona na yeye akiwa ameuawa.Niliita jina lake kwa nguvu huku nikikimbia huku na huko katika eneo lile bila mafanikio. Nilikimbia mpaka kwenye vichaka vya pale jirani, lakini nako pia hakukuwa na dalili yoyote kama Gil alipita huko. Hatimaye nikajiona nimechoka kwa kukimbia hovyo huku nikichosha mapafu yangu kwa kupiga kelele bila mafanikio.Nilijibwaga chini kwa kukata tamaa na kubaki nikiwa nimeduwaa pale chini nisijue la kufanya. Akili yangu ilikuwa kama iliyokufa ganzi.Sikuweza kufikiri kitu.Sikuweza kuelewa kitu.Nilibaki nikiwa nimezubaa pale msituni kwa muda mrefu bila ya kujitambua. Tai walianza kushuka taratibu kutoka angani na kuizungukia ile miili ya wale wenzangu waliouawa. Jambo hili lilinikera na kunihuzunisha sana.Hawa ni binadamu na ni watu ninaowafahamu. Ni masaa machache tu yaliyopita nilikuwa nikiongea na kucheka nao kwa furaha. Nimekuwa nao eneo hili kwa wiki nzima. Sasa wameuawa sijui kwa sababu gani, halafu kama hiyo haitoshi, nashuhudia kwa macho yangu miili yao...mizoga yao...ikidonolewa na tai huku porini! Hii haiwezekani. Haiwezekani kabisa!
Nilikurupuka na kuwafukuza wale ndege wakubwa wenye kucha kali na zenye nguvu na midomo mikali kama mkasi kutoka kwenye miili ya wale marehemu wasio na hatia. “Tokeni hapa! Kwenda ’ukoo! Mnadhani kila kitu ni cha kuliwa tu! Huuuuuush! Huuuuuush!“ Niliwabwatia kwa hasira wale tai, ambao waliruka hewani kwa muda tu na nilipogeuka walirudi tena kuanza kuwadonoa tena wale wenzangu waliouawa. Na hata pale nilipogeuka nilishuhudia kwa kihoro mmoja wa ile midege mikubwa na mibaya akinyofoa jicho la bwana Ubwa Mgaya na kuruka nalo hewani huku likivuja damu! Nilihisi kichefu chefu kizito na nikatamani kufa.Kwa hasira niliwarudia tena na kuwafukuza kwa kelele huku nikitupa mikono yangu hewani na kuwatupia mawe, lakini mchezo ukawa ni ule ule. Walishaona chakula na hawakuwa tayari kukiacha kwa kuniogopa mimi. Mwisho nikachoka kukimbizana na tai na kujibwaga chini kwa kukata tamaa.
Nilibaki nikiwatazama kwa huzuni wenzangu wakiliwa na ile midege mikubwa huku nikilia kwa huzuni.
Lazima nifanye kitu...siwezi kukaa hapa muda wote.
Niliinuka na kuliendea begi langu lililokuwa nje ya hema langu. Nilikumbuka kuwa begi langu nililiacha ndani ya hema lile kabla sijaenda kule msituni kuwapiga picha wanyama. Sasa mbona liko nje? Sikufikiri zaidi. Niliitumbukiza ile kamera ya Gil ndani ya begi langu ambalo nililipachika mabegani mwangu na kulining’iniza mgongoni. Nikaliendea gari letu. Lazima nikatafute msaada, na nisingeweza kurudi wilayani peke yangu kwa miguu. Nilitumaini kuwa ufunguo ungekuwa ndani ya ile gari. Nilifungua mlango wa dereva na kichwa cha Gil kikaniangukia mapajani na kubaki kikining’inia nje ya mlango wa gari ile.
Nilipiga yowe kubwa la woga huku nikiruka nyuma na kupiga mwereka. Nilijiinua na kuanza kujisukuma nyuma huku nikipiga mayowe. Nilipiga mwereka mwingine.Nikabaki nikisota kurudi nyuma huku nikizidi kupiga kelele. Lilikuwa ni jambo ambalo sikulitegemea na la kutisha sana. Na hata pale nilipokuwa nikipiga kelele huku nikiukodolea macho uso wa Gil uliokuwa ukinitumbulia macho bila kuona, kama vile alikuwa amelala kichwa chini miguu juu,nilikiri moyoni mwangu kuwa kwa hakika sasa nilikuwa nimeshindwa. Sikuwa na uwezo tena wa kuendelea kustahamili kushuhudia mambo haya.
Gil alikuwa ameuawa akiwa ndani ya gari, bila shaka akijaribu kutoroka kutoka eneo lile. Mwili wake ulikuwa umelala chali kwenye sakafu ya gari ile, kisogo chake kikiwa kimeegemea mlango wa dereva kwa ndani, ambapo nilipoufungua kichwa kile kiliangukia nje na kubaki kikining’inia wakati kiwiliwili chake kikibaki ndani ya gari.
This is a bloody massacre!
Nilijiinua na kuanza kutimua mbio. Nilikimbia bila ya kuwa na uelekeo maalum huku nikijitapikia mwili mzima, lakini sikujali wala sikusimama. Nilikimbia na kukimbia, huku nikijaribu kufuata njia iliyoachwa na matairi ya gari yetu wakati tukija katika eneo la kambi yetu.Machozi yalinitoka na kamasi zilinivuja lakini sikusimama. Niliendelea kukimbia kwa nguvu zangu zote. Mapafu yangu yalikuwa kama yanawaka moto na nilitamani nikae chini nipate kupumua na kupumzika, lakini miguu yangu ilizidi kukimbia tu. Sikuweza kusimama. Ilikuwa ni mbio moja kwa moja. Akilini mwangu nilikuwa na wazo moja tu: kufika ofisini kwa mkuu wa wilaya.
Kwa wakati ule, huko ndiko mahala pekee nilipoweza kupaona kuwa pa usalama.
--
Baada ya kukimbia kwa muda mrefu, huku nikisimama njiani na kupumzika mara kadhaa hatimaye niliingia mjini. Sijui niliwezaje kukimbia mpaka Manyoni mjini, lakini nilifika. Akili yangu bado ilikuwa na wazo moja tu la kufika ofisini kwa mkuu wa wilaya na kutoa ripoti juu ya mauaji yale ya kinyama na hatimaye kupata msaada. Muda wote niliokuwa nikikimbia kutoka kule porini, picha za miili ya wale wenzangu wakiwa wameuawa, na yule mtu asiye na jina aliyeuawa na wale watu wabaya, zilikuwa zikinirudia akilini mwangu bila mpangilio.Na kadiri zilivyonirudia ndivyo nilivyozidi kutimua mabio.
Nilipojiona kuwa nimeshaingia mjini niliacha kukimbia na kuanza kutembea haraka haraka, lakini nilipoangalia saa yangu na kugundua kuwa ilikuwa ni saa tisa za alasiri, nikaingiwa na woga kuwa huenda nikakuta ofisi ya mkuu wa wilaya imefungwa na yule mama akawa amekwenda nyumbani. Sikuwa na mtu hata mmoja anayenifahamu katika mji ule zaidi ya yule mama mkuu wa wilaya na baadhi ya watendaji wake. Na swala la yale mauaji halikuwa la kumweleza mtu akakuelewa kirahisi, hasa ukizingatia kuwa nilikuwa mgeni kabisa katika mji huu mdogo. Wazo hili lilinifanya nianze kutimua mbio katikati ya mji bila kujali watu waliokuwa wakinishangaa.
Nilipolifikia jengo ilimokuwemo ofisi ya mkuu wa wilaya, ambalo wenyeji waliliita “wilayani”, nilipita moja kwa moja hadi mapokezi.
“Nahitaji kuonana na mkuu wa wilaya tafadhali!” Nilimwambia jamaa niliyemkuta pale mapokezi huku nikitweta. Badala ya kunijibu jamaa alikuwa akinikodolea macho kama aliyeona jini. Binti tuliyemkuta pale mapokezi siku ile tuliyoripoti pale ofisini na wenzangu hakuwepo. Hili halikuwa jambo zuri kwangu, kwani nilikuwa na hakika kama ningemkuta yule binti angenikumbuka na kunipunguzia kazi ya kujitambulisha upya.
Sasa yule jamaa aliinuka taratibu kutoka kwenye kiti chake na kuanza kurudi nyuma taratibu huku macho yakimtembea kwa woga ambao sikuuelewa ulikuwa unatokana na nini.
“Kaka, ninaomba kuonana na mkuu wa wilaya tafadhali, ni muhimu…dharura!” Nilimwambia tena yule jamaa huku nikimkazia macho kuonesha msisitizo. Jamaa alikuwa ananitazama kama kwamba nilikuwa mwehu, huku macho yake yakinitazama kifuani na eneo la tumbo langu na kunirudia tena usoni. “We’ bwana bubu? I said I need to see the God-damn District Commissioner for God’s sake! It’s an emergency, can’t you understand?” Nilijikuta nikimfokea yule jamaa kwa kimombo kusisitiza haja yangu ya kuonana na mkuu wa wilaya huku nikipiga meza kwa kiganja cha mkono wangu. Watu wameuawa kama kuku huko halafu mtu ananikodolea mimacho kama hajawahi kuona mwanamke aliyesuka rasta akiwa amevaa suruali na shati!
Jamaa aliruka nyuma akiwa ametumbua macho kwa woga huku akibwata.
”Kuna kichaa hukuu!”
“Hah! Mi’ kichaa? Hebu nipeleke kwa DC halafu uone kama mi’ kichaa! Kuna balaa kubwa limetokea huko msituni…tulikuwa tunafanya utafi…” Hapo nilimuona yule dada niliyetarajia kumkuta pale mapokezi akiingia pale mapokezi kutoka kwenye chumba ambacho nilikijua kuwa kilikua ndio ofisi ya mkuu wa wilaya, akiwa amekumbatia mafaili. Na wakati huo huo kwa pembe ya jicho langu niliona askari wawili wakiingia pale ofisini.
“Ah! Dada! Afadhali umetokea…si unanikumbuka mimi? Nilikuja na wenzangu...kwa ajili ya utafiti...kutoka Idara ya Makumbusho ya taifa?” Nilimdakia yule dada haraka haraka kabla sijatiwa mikononi mwa wale askari. Yule dada alinitumbulia macho kwa mshangao, kisha nikaona kuwa alinikumbuka. “Yee-ees...nakukumbuka...lakini mbona hivyo? Wengine wako wapi...?” Yule dada alisema huku akiweka yale mafaili mezani haraka na kunisogelea huku naye akiniangalia kifuani na kunitazama tena usoni kwa namna ya ajabu. Hawa watu wanashangaa nini? Niliwageukia wale askari, nikaona wamesimama bila maamuzi baada ya kuona kuwa yule dada ananifahamu. Bila shaka waligundua kuwa kumbe sikuwa kichaa kama alivyopayuka yule bwege niliyemkuta pale mapokezi.
“Ni balaa kubwa...” Nilianza kumueleza yule dada lakini sikumalizia sentesi yangu, badala yake nikafuata macho yake yaliyokuwa yamekodolea sehemu ya tumbo langu, huku nikimsikia yule jamaa niliyemkuta pale mapokezi akisema: “Huyu lazima ni chizi tu...” Niliinamisha uso wangu na kujitazama tumboni na hapo hapo nilihisi mwili ukinifa ganzi. Na nikaelewa kwa nini hata yule bwege aliniona kichaa. Shati langu lilikuwa limefunguka vifungo vyote bila ya mimi kuwa na habari na hivyo nilibaki tumbo wazi! Zaidi ya sidiria iliyoficha matiti yangu madogo, sikuwa na kitu kingine chochote chini ya shati lile ambalo sikuwa nimelichomekea ndani ya suruali yangu iliyosheheni vumbi.
Nilikuwa nimetapakaa jasho lililochanganyika na kamasi, nguo zangu zikiwa zimegandiwa na mabaki ya matapishi niliyojitapikia huku nikikimbia,vumbi limenitapakaa mwili mzima. Kwa hakika walikuwa na haki ya kunishangaa na kuniona kichaa.
Mtoto wa kike unatembea hovyo mitaani kidari wazi isipokuwa kwa sidiria tu hali shati chafu likipeperushwa hewani kwa upepo kama muhuni!
Ile kuonekana sidiria tu ni jambo la ajabu sana, katika mji kama huu, sasa ukichangia na jinsi nilivyochafuka, na jinsi nilivyokuwa nimetumbua macho kwa woga na mirasta yangu ikiwa shaghala-baghala huko kichwani, lazima nionekane mwehu.
“Shit!” Nilifunga vifungo vya shati langu haraka haraka huku nikitamka maneno ya kumtaka radhi yule dada. Na hata nilipokuwa nikihangaika kufunga vifungo vya shati langu lililotapakaa matapishi na damu, nilimuona yule dada akiinua macho yake kuwatazama wale askari na kuwatolea ishara fulani, kisha aligeuka na kuanza kurudi tena kule ofisini kwa mkuu wa wilaya. Kabla sijajua la kufanya au la kusema, wale askari walinikamata kwa nyuma na kunisukumia ndani ya ofisi ile ambako yule dada alielekea.
“Hey! Heeeey! What the…niacheni bwana! Nataka kuonana na mkuu wa wilaya!” Nilibwata kwa nguvu huku nikijitikisa kutoka mikononi mwa wale askari bila mafanikio.
“Tulia bibie! Ndipo tunapoelekea!” Mmoja wa wale askari aliniambia kwa sauti kali. Sikuelewa ni nini kilikuwa kinatokea, lakini nilijua kuna tatizo. Kuna jambo haliko sawa.
Niliingizwa ndani ya chumba ambamo mkuu wa wilaya alikuwamo. Alikuwa ameketi nyuma ya meza yake kubwa kwa utulivu, lakini nyuma ya utulivu ule niliweza kuona kuwa yule mama alikuwa anajitahidi sana kuficha wasiwasi mkubwa. Aliinuka kutoka kwenye kiti chake na kunielekeza niketi kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake. Niliketi nikiwa na wasiwasi mkubwa huku wale askari wawili wakisimama kila upande wa kiti nilichokalia wakati yule dada akifunga mlango kwa ndani na kubaki akiwa amesimama kando ya mlango ule.
“Asante Matilda...nadhani unaweza kwenda kupiga simu sasa.” Mkuu wa wilaya alimwambia yule dada ambaye alitoka huku akijibu kwa sauti ya chini “Yes madam”
“Binti...ni nini kimetokea? Mbona umekuwa hivyo?” Mkuu wa wilaya aliniuliza kwa upole kama kwamba alikuwa anaongea na mtoto mdogo.
“U...unanikumbuka mheshimiwa...? Naitwa Tigga...nilikuja na wenzangu hapa ofisini kwako siku chache zilizopita?” Nilimuuliza kwa mashaka huku nikiwatazama wale askari wawili kwa zamu. Walikuwa wameshikilia bunduki zao aina ya SMG mikononi mwao kama kwamba wako na mhalifu hatari sana. Nilimeza mate kwa woga na kumgeukia tena yule mama mkuu wa wilaya.
“Nakukumbuka binti...ni katika ile Manyoni Expedition...lakini mbona hivi? Kumetokea nini? Wenzako wako wapi?”
“Wameuawa wote...! wenzangu wameuawa kinyama mheshimiwa. Mi’ nimefanikiwa kutoroka...inatisha sana!” Niliropoka.
Badala ya kuonekana kushtushwa na taarifa ile, yule mama mkuu wa wilaya aliketi kwenye kiti mbele yangu na kuwatazama wale askari kisha akanigeukia.
“But are you alright? Nadhani unahitaji matibabu…tukupeleke hospitali kwanza?” Nilitikisa kichwa kwa nguvu. “Mi’ niko salama kabisa mheshimiwa…ila wenzangu wote wameuawa nakuambia! nimekuja kutoa taarifa na kuomba msaada. Wamewaua wote!” Nilimwambia kwa sauti iliyojaa kitetemeshi.
“Wameuawa? Nani amewaua?” Mkuu wa wilaya aliniuliza huku akinitazama kwa namna ambayo sikuielewa kama ilikuwa ni wasiwasi au huzuni.
“Macho ya nyoka…na kigulu…na mwenzao.” Nilimjibu, na hapo nikaona kuwa nilizidi kutoeleweka. Niliona wazi kuwa yule mama aliniona mwehu.
Ee Mungu wangu, hebu nisaidie kiumbe wako!
“Macho ya nyoka? Binti, una uhakika na maneno yako? Ni nini hasa kilichotokea...hebu tulia utueleze kwa kituo.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikaanza kumuelezea mambo yaliyotokea kule msituni kwa kadiri nilivyoweza kuyakumbuka. Na kadiri nilivyokuwa nikimuelezea, ndivyo uzito wa matukio yale ulivyozidi kunielemea na nikaanza kububujikwa machozi. Sijui ni kwa nini, lakini nilikuwa nikimuelezea matukio yale kama jinsi mimi nilivyoyaona, na sio kama jinsi mambo yalivyotokea kule msituni na jinsi mimi nilivyoyachukulia. Badala ya kumueleza kuwa niliona mtu akiteswa nami nikaanza kurekodi matukio yale kwa kamera ya Gil, nilimuelezea tu kuwa niliona jinsi wale watu watatu wakimtesa na kumuua yule mtu, na jinsi nilivyowakuta wenzangu wakiwa wameuawa kule msituni kwenye kambi yetu. Baada ya kumaliza maelezo yangu nilibaki nikilia kwa kwikwi huku nikiwa nimefunika uso wangu kwa viganja vya mikono yangu. Ofisi yote ilikuwa kimya.
“Pole sana binti...” Yule mama aliniambia kwa sauti ya upole. Niliinua uso wangu na kujifuta machozi kwa mkono wa shati langu chafu.”...na nataka nikujulishe kuwa kuanzia sasa uko chini ya ulinzi mpaka hapo maelezo yako yatakapofanyiwa uchunguzi wa kina.”
“Hah?” Nilimaka kwa mshituko huku nikiinuka kutoka kwenye kiti. Mikono yenye nguvu ya wale askari ilinikamata mabega na kunikalisha tena kwenye kiti kile.
“Mama! Yaani huniamini? Kwa nini niwe chini ya ulinzi? Mimi ni mfanyakazi wa Idara ya Makumbusho ya taifa, na wewe unajua hilo...mbona sielewi?” Nilimuuliza kwa jazba yule mama huku nikijaribu kuinuka.
“Tuna taarifa zako zote Tigga...au nikuite Sylvia?” Yule mama alinijibu huku akinikazia macho makali. Hii ilinishangaza, na nikashindwa kuelewa.
Eh! Haya makubwa!
“Mbona sikuelewi mheshimiwa? Kwa nini uniite Sylvia? Mi’ naitwa Tigga! Tigga Mumba! Na ni taarifa gani za kwangu ambazo mnazo?” Nilimuuliza yule mheshimiwa huku moyo ukinienda mbio na akili ikinizunguka. Badala ya kunijibu, yule mama alinikabidhi karatasi iliyokuwa juu ya meza yake. Bila ya kuelewa, niliipokea ile karatasi huku mikono ikinitetemeka na kuanza kuisoma. Yaliyoandikwa kwenye ile karatasi yalibadilisha kabisa maisha yangu. Yalikuwa ni mambo ya ajabu na uongo usio kifani. Moyo ulinilipuka na ukaanza kunienda mbio mara dufu. Akili ilinizunguka na nikashindwa kabisa kuelewa ni nini maana ya mambo yale.
This is ridiculous!
Nilikuwa natazama karatasi iliyokuwa na picha yangu ya ukubwa wa pasipoti kwenye kona ya kulia na maelezo chini yake. Ile picha sio kama ilikuwa imebandikwa, bali ilikuwa imetolewa kivuli moja kwa moja kwenye ile karatasi. Ilikuwa ni sura yangu bila shaka.
Maelezo yaliyokuwa kwenye karatasi ile yalinielezea kuwa mimi nilikuwa naitwa Sylvia Mwamkonda, nikiwa na ummri wa miaka 27, jambo ambalo ni kweli kabisa na hata tarehe yangu ya kuzaliwa iliyotajwa pale ilikuwa ni sawa kabisa!
Yale melezo yalikuwa yanamtahadharisha Mkuu wa wilaya ya Manyoni kuwa mtu huyo aitwaye Sylvia Mwamkonda (yaani mimi) ni hatari sana kwani anasumbuliwa na ugonjwa wa Paranoid Schizophrenia, ambao ni ugonjwa mbaya sana wa akili unaoweza kumpelekea kwenye kufanya vitendo vya hatari vinavyoweza kuhatarisha maisha yake na ya wengine watakaokuwa jirani naye.
Kutokana na ugonjwa huu hatari wa akili, mtajwa hapo juu (yaani Sylvia, ambaye ndiye mimi) ameondokea kuwa hatari kwa wengine na kwake yeye mwenyewe. Kwa hali hiyo basi,anatakiwa awekwe kwenye hospitali maalum za wagonjwa wa akili kwa matibabu na kwa usalama wake na wa wengine.
Kwa mujibu wa maelezo ya barua ile iliyotoka Idara ya Makumbusho ya Taifa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo (jina na saini yake vyote ni sahihi kabisa kama jinsi mimi nilivyovijua) ni kwamba Idara ya Makumbusho imegundua juu ya ugonjwa huu wa Sylvia (ambaye ni mimi) baada ya kupokea ripoti ya daktari aliyemfanyia uchunguzi baada ya uongozi wa Idara hiyo kumpeleka kwa matibabu wakati alipoanza kuonesha dalili za ugonjwa huo. Barua ilieleza kuwa bahati mbaya walipokea ripoti hiyo wakati Sylvia akiwa tayari ameshatumwa kuelekea Manyoni kikazi pamoja na wenzake. Kwa hali hiyo basi, Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho ya Taifa, kwa kupitia barua ile alikuwa anaiomba ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni kumweka chini ya ulinzi mara moja mtu huyo anayeitwa Sylvia mara tu atakapoonekana popote pale katika wilaya ile kwa usalama wake na hasa wa watafiti wenzake aliotumwa pamoja nao kikazi huko Manyoni,na raia wengine wasio na hatia ambao wanaweza kudhuriwa naye.
Pia barua ile ilimuagiza mkuu wa wilaya apige namba ya simu iliyokuwamo kwenye waraka ule mara moja pindi atakapofanikiwa kumuweka chini ya ulinzi mtu huyo hatari aitwaye Sylvia Mwamkonda. Ile namba haikuwa miongoni mwa namba za Idara ya Makumbusho ya Taifa nilizozijua.
Nilikumbuka kuwa wakati mimi nilipoingizwa mle ofisini mwake mkuu wa wilaya alimuagiza yule dada akapige simu...
Ni nini kinatokea hapa?
Nakala ya barua ile ilikuwa imepelekwa kwa wakuu wa vituo kadhaa vya polisi jijini Dar es Salaam, Dodoma na pale Manyoni. Pia nakala ya barua ile ilikuwa imepelekwa kwa mganga mkuu, hospitali ya wagonjwa wa akili ya Mirembe.
Paranoid Schizophrenia! Sikuamini kama mambo yale yalikuwa yanatokea kweli. Nilimtazama yule mkuu wa wilaya kwa hasira.
“Huu ni uzushi mtupu! Is this some kind of a joke?” Nilimwambia na kumuuliza iwapo ule ulikuwa ni utani wa aina fulani. Badala ya kunijibu yule mama aliendelea kunitazama kwa utulivu. Niliitazama tena ile karatasi. Niligundua kuwa ilikuwa imetumwa kwa njia ya fax siku ile ile, kiasi cha saa moja tu iliyopita. Tatizo namba ya fax iliyotumika kutumia ujumbe ule haikuonekana pale juu ya karatasi.
These guys are really good! Yaani wameweza kughushi vitu kama hivi?
“Mheshimiwa, sijui ni kwa nini umeletewa ujumbe huu, lakini nakuhakikishia kuwa huu ni uzushi na uongo mtupu! Mimi sio Sylvia, mimi naitwa Tigga Mumba kama nilivyotambulishwa kwako na bwana Ibrahim Geresha...marehemu Ibrahim Geresha siku ile tulipokuja hapa ofisini kwako kwa mara ya kwanza. Nadhani kuna kitu kinafanyika ambacho bado hatujakielewa hapa...”
“Sasa hapa sio mahala pake msichana. Utaenda kutoa maelezo kwenye vyombo vinavyohusika...wewe ni mgonjwa na unahitaji msaada wa kitaalam, hapa unashikiliwa kwa usalama wako na si vinginevyo...”
“Mimi sio mgonjwa bwana! Nakuambia hii ni njama tu...sijui ni kwa nini, lakini nakuhakikishia kuwa hii ni ghilba kubwa kabisa! Naomba unisaidie mheshimiwa...wenzangu wameuawa, bila shaka na mi’ ningeuawa huko...bila msaada wako nitafanyaje mimi?” Nililalamika kwa kuomboleza.
“Na ndio haswa inabidi tujiulize Sylvia...”
“Mimi sio Sylvia jamani!” Nilimkatisha yule mheshimiwa huku nikifoka na kunyanyuka kutoka pale kwenye kiti. Mara moja mmoja wa wale askari aliruka mbele yangu na kuninyooshea mtutu wa bunduki yake. “Kaa chini mwanamke!” Nilimtazama kwa hasira yule askari huku nikiketi.Aliendelea kunielekezea ile bunduki nikiwa nimeketi pale kitini.
“...inabidi tujiulize kwa makini sana Sylvia ni kwa nini katika watu wote waliouawa, tena wote ni wanaume, uokoke wewe tu Sylvia, mtoto wa kike...lazima tujiulize sana juu ya hilo.” Mkuu wa wilaya aliendelea kunieleza huku akinitazama kwa makini. Ilikuwa kama kwamba anajaribu kunichokoza makusudi. Kwa nini?
“Khah! Unamaanisha nini sasa...?” Nilimuuliza kwa mshangao.
“Labda ulinusurika na kifo kwa sababu ulishindwa kujiua mwenyewe Sylvia...”
“Whaaaat?” Niliropoka kwa sauti. “Yaani...”
“Wewe ni mgonjwa Sylvia…Paranoid Schizophrenia ni ugonjwa hatari sana, unaweza kuwaua wenzako bila kujijua halafu ukaamini kuwa watu walikuja kuwaua na wewe ukafanikiwa kutoroka…vitu hivi vipo…”
Nilibaki nikimkodolea macho yule mama hali nikiwa mdomo wazi. Na hata pale nilipokuwa nikimkodolea yule mama, nilijua kuwa nilikuwa nimenasa. Sasa naonekana mimi ndiye niliyeua! Hii sio kweli…haiwezekani!
“How do you know all this? Just from this piece of rubbish?” Nilimuuliza kwa kebehi huku nikimpungia ile barua kuwa anawezaje kujua mambo yote hayo, na iwapo anayajua kutokana na ile barua ya kughushi ambayo niliifananisha na takataka tu.
“Hapana Sylvia, baada ya kupata hii taarifa nilipiga hiyo namba ya simu nikaongea na dokta wako, dokta Martin Lundi…”
“Dokta wangu? Hivi nyie watu mnapata wapi ujinga-ujinga wa aina hii? Mimi sina dokta yoyote na ndio kwanza leo nalisikia hilo jina…”
“Ni vigumu sana kwako kuelewa Sylvia…”
“Mimi sio Sylvia jamani mbona sieleweki?” Nilimkatisha yule mama mkuu wa wilaya kwa ukali. Alinitazama kama jinsi ambavyo wewe unavyoweza kumtazama mtu unayemjua kuwa ni mgonjwa wa akili, lakini yeye mwenyewe akawa anakuhakikishia kuwa yeye ndiye daktari bingwa wa magonjwa ya akili. Kwa kweli nilichanganyikiwa! Nilijaribu kufikiri haraka sana ni jinsi gani nitafanikiwa kufuta imani hii iliyomkolea yule mama kuwa mimi ni mwehu.Nilijiona kuwa ninaanza kuwa kichaa rasmi.
Nifanyeje sasa Mungu wangu?
Mara nilipata wazo. Nitawahakikishia kuwa huu ni uongo mtupu kwa kuwapa ushahidi kuwa mimi sio Sylvia bali ni Tigga. Nilianza kulivua begi langu kutoka mgongoni kwangu haraka. Lakini kama umeme wale askari walinibana mikono hali yule mwingine akiniwekea mdomo wa bunduki yake kifuani.
“Tulia kama ulivyo! Ukileta ujanja tutakupiga risasi!” Mmoja wa wale askari alifoka.
“Nataka niwaoneshe uthibitisho tu kuwa mimi sio Sylvia bali ni Tigga!” Nilibwata huku nikiuweka chini mkoba wangu.Walibaki wakinitazama. Nilianza kuinama na kupeleka mikono yangu ndani ya lile begi lakini walinizuia tena. Nilimtazama mkuu wa wilaya.
“Mama, naomba nitoe kitambulisho na pasipoti yangu...vitathibitisha kuwa mimi ni Tigga Mumba na sio Sylvia-sijui-nani-sijui-huko kama wanavyodai hao walioandika hiyo barua...” Nilimwambia. Mkuu wa wilaya alinitazama kwa mashaka.Ilionekana kuwa alikuwa akijishauri iwapo anikubalie au la. “Sasa ukinizuia utajuaje kuwa ni kweli unaniweka chini ya ulinzi kama Sylvia-sijui-nani-sijui au Tigga Mumba?” Nilimuuliza.
“Askari atafanya kazi hiyo, wewe tulia kama ulivyo.” Mkuu wa wilaya aliniambia huku akimwamrisha mmoja wa wale askari kwa kichwa aupekue mkoba wangu.
Na hapo nikaliona kosa langu. Vipi wakiikuta ile kamera halafu wakaamua kuuchukua ule mkanda ulio na ushahidi? Mungu wangu! Sasa nitakuwa na uthibitisho gani juu ya kutohusika kwangu na mauaji yale?
Askari alianza kupekua ndani ya begi langu. Kwa moyo uliopiga kwa nguvu nilishuhudia akiitoa ile kamera na kuiweka juu ya meza bila ya kusema lolote. Nilimtazama mkuu wa wilaya. Naye hakuwa akiitilia maanani ile kamera, ila macho yake yalikuwa yakiangalia kwa makini kila kitu kilichokuwa kikitolewa ndani ya mkoba ule. Ulikuwa ni mkoba mdogo, na ndani yake nilikuwa nimeweka nguo zangu za ndani, leso za kujifutia jasho, pedi za hedhi, miwani yangu ya jua, pamoja na simu yangu ya mkononi ambayo ilikuwa imeshaishiwa chaji, pamoja na chaja yake. Pia kulikuwa na walkman yangu ya CD, CD mbalimbali za muziki pamoja na kitambulisho changu cha kazi, kadi ya benki, pasipoti, kijitabu kidogo cha anuani pamoja na albamu ndogo ya picha ambayo mara nyingi huwa nasafiri nayo kwa ajili ya kujikumbusha picha za ndugu na mama yangu pindi nikiwa mpweke safarini.Pia kulikuwa kuna pesa kiasi cha shilingi laki nne hivi, sehemu ya matunda ya per diem za safari, fadhila za Idara ya Makumbusho ya Taifa.
Yule askari alitoa kitu kimoja baada ya kingine na kuviweka juu ya meza ya mkuu wa wilaya, akifinya sura yake pale alipolazimika kuzishika nguo zangu za ndani, hasa zile pedi za hedhi. Alitoa vitu vyote na kudai kuwa amemaliza.
Nilimtazama kwa mshangao. “Mbona sijaona pasipoti na vitambulisho vyangu?” Nilimuuliza huku nikianza kuinuka. Yule askari mwingine alinikalisha tena kitini kwa nguvu huku mkuu wa wilaya akinijibu. ”Kwa sababu havimo na havikuwemo toka mwanzo!”
“What do you mean kwa sababu havim o? Hebu angalia vizuri…” Nilifoka huku nikimtazama yule askari aliyekuwa akipekua begi lile na kumgeukia yule mkuu wa wilaya. Yule mama alionekana kuwa ametosheka kwamba nilikuwa nasema uongo na kwamba mimi kwa hakika ni Sylvia-nani-sijui kama ilivyoelezwa kwenye ile barua feki.
“Hakuna uthibitisho wowote kwenye begi lako Msichana, kwa hiyo acha kupoteza muda wetu.” Alisema kwa hasira.
“Haiwezekani! Kunatakiwa kuwe na kitambulisho changu cha kazi humo…kinaonesha kuwa mimi ni Tigga Mumba!” Nilimaka kwa kitetemeshi.
Na hata pale nilipokuwa nikiongea maneno hayo, yule askari alilikung’uta kwa nguvu lile begi.
Hakuna kitu kilichotoka.
”Hakipo.” Yule askari alisema kama kwamba anaijibu ile kauli yangu.
Akaligeuza nje ndani na kulikung’uta tena.
Hamna kitu.
Nilichanganyikiwa!
“Hah! Yaani…kikadi changu cha benki…?”
“Hakuna!” Mkuu wa wilaya alinijibu kwa kukatisha tamaa.
“Na pasipoti yangu…?”
“Hakuna!”
“Simu yangu ya mkononi…? Sony…”
Yule mama alinitazama na kutikisa kichwa kwa kukatisha tamaa huku akibetua midomo yake.
Oh! Mungu wangu, balaa gani hili sasa?
“Kulikuwa pia kuna albamu yangu ya picha humo…”
“Haimo!” Mkuu wa wilaya alinijibu huku akipekua lile rundo la nguo zangu za ndani pale juu ya meza, kisha akatupia macho yake kwenye ile kamera ya Gil pale mezani kwa muda. Nilibana pumzi huku nikimtazama kwa wasiwasi. Alihamishia macho yake kwenye ile walkman yangu, nikashusha pumzi ndefu, kisha akatazama zile CD chache za muziki kando yake. Alihamishia macho yake kwenye zile pesa zangu zilizokuwa zimefungwa vizuri kwa mpira maalum yaani rubber band, kando yake ikiwapo ile miwani yangu ya jua. Alinitazama.
“Una lolote zaidi la kutueleza Sylvia?”
Sikuwa na jibu. Akili ilikuwa ikinizunguka kwa kasi sana na nilihisi kizunguzungu. Sasa vitakuwa vimekwenda wapi? Nilikumbuka kuwa nililikuta begi langu nje ya hema langu kule msituni, wakati nililiacha ndani. Hapo nilielewa.
“Watakuwa wamevichukua wale wauaji...” Nilisema kwa sauti hafifu. Nilikuwa nikijisemea mwenyewe, lakini wote mle ndani walinisikia.
“Mh! We’ binti acha kufanya mchezo na mimi, umesikia? Ni wauaji gani hao wa kufikirika unaotuambia?” Mkuu wa wilaya alinikemea kwa hasira.
“Kigulu na Macho ya nyoka?” Yule askari mmoja aliniuliza kwa kejeli. Niliona kuwa hapa tayari nilikuwa nimethibitika kuwa mgonjwa wa akili.
Paranoid Schizophrenia!
Nilimtazama, nikajaribu kusema kitu nikashindwa. Niseme nini? Nilikuwa nimekwama. Niliamua kunyamaza kusubiri hatima yangu huku akili ikinizunguka. Lakini kitu kimoja nilichokuwa na uhakika nacho ni kuwa pale hapakuwa mahala pa kutoa ule ushahidi wa mkanda wa video niliokuwa nao. Sijui ni kwa nini, lakini hivyo ndivyo nilivyohisi na ndivyo nilivyoamua.
Yule askari mwingine alianza kuvikusanya vile vitu vyangu na kuvirudisha tena ndani ya mkoba wangu mdogo. Nilimtazama huku moyo ukinidunda akiitumbukiza tena ile kamera ndani ya mkoba ule.Nilishusha pumzi.Alipolifikia lile burungutu langu la pesa alisita kwa muda, kama aliyekuwa akijishauri iwapo azirudishe kwenye begi langu au azihamishie mfukoni mwake. Nilimtumbulia macho kwa hasira naye akaamua kuzirudisha kwenye begi langu. Na hapo yule dada aliyeitwa Matilda alirudi mle ofisini.
“Dokta Martin Lundi amefika Mheshimiwa.” Alimwambia mkuu wa wilaya na moyo ukaanza kunienda mbio. Mkuu wa wilaya aliagiza aingie ndani nami nikaukodolea macho mlango kumtazama huyo daktari wangu Martin Lundi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu watatu waliingia ndani haraka haraka. Wote walikuwa wamevaa makoti marefu meupe juu ya nguo zao, na haikuwa na shaka kuwa walikuwa wauguzi au madaktari. Moyo ulinilipuka na nikataka kupiga yowe lakini sauti ikakwama ghafla. Nilikuwa nikimkodolea macho mmoja wa wale watu watatu walioingia ambaye alionekana kuwa ndiye kiongozi wa jopo lile la matabibu. Mkuu wa wilaya alisimama na yule daktari aliyeonekana kuwa ndiye kiongozi alikwenda moja kwa moja hadi kwa mkuu wa wilaya na kumpa mkono huku akijitambulisha.
“Naitwa Martin Lundi...Dokta Martin Lundi, tuliongea kwenye simu.”
“Nimefurahi kuonana nawe Dokta, nadhani mgonjwa wako ndiye huyu?” Mkuu wa wilaya alimwambia. Yule mtu alinigeukia na uso wake ulifanya tabasamu dogo kama jinsi ambavyo madaktari wengi wanavyofanya pindi wakianza kuongea na wagonjwa wao.
“Hallo Sylvia, unajisikiaje leo?” Aliniuliza taratibu huku akinisogelea, na hapo ndipo nilipopata nguvu ya kusema, muda wote nilikuwa nimepigwa na bumbuwazi, kwani yule mtu aliyejiita dokta Martin Lundi alikuwa ndiye yule muuaji wa tatu, ambaye alikuwa akiendesha ile helikopta kule msituni!
Niliruka ghafla kutoka kwenye kiti changu na kumkimbilia yule mkuu wa wilaya huku nikimkwepa yule muuaji.
“Ndio huyu! Huyu ni mmoja wa wale wauaji mheshimiwa! Usimruhusu anishike!”
Kilichotokea hapo ni kizaa zaa kizito. Wale askari hawakutegemea tendo lile hivyo niliweza kumfikia mkuu wa wilaya ambaye alipiga yowe kubwa la woga, bila shaka kichwani mwake akiamini kuwa mimi nilikuwa ni mgonjwa wa akili hatari na muuaji. Haraka sana mmoja wa wale wasaidizi wa yule jamaa aliyejiita Dokta Martin Lundi alinirukia na kunikamata mkono. Nilimzaba kofi la uso na kuanza kuuendea mlango kwa kasi lakini wale askari walizinduka. Walinielekezea bunduki zao huku wakifoka kuwa nikae chini upesi. Nilisimama huku nikitetemeka nikimtazama yule jamaa.
Ingawa kule msituni alikuwa amevaa miwani ya jua na koti refu jeusi, na sasa alikuwa amevaa miwani ya macho na chini ya lile koti lake refu jeupe alikuwa amevaa shati na tai, bado niliweza kumtambua vizuri sana. Na hata pale nilipokuwa nikipiga mayowe kuwa yeye ni mmoja wa wauaji, niliushuhudia uso wake ukionesha mshangao wa hali ya juu naye akaingia woga mkubwa.Lakini hilo lilipita haraka sana usoni mwake.
Alimgeukia mkuu wa wilaya na kujaribu kufafanua huku akitabasamu.
“Ah! Paranoid Schizophrenia...kila mtu anamu-imagine kuwa ni adui...ndilo jambo baya zaidi katika ugonjwa wa Sylvia...” Akimaanisha kuwa ule ugonjwa ulikuwa unanifanya nimfikirie kila mtu kuwa ni adui. Na nilipomtazama mkuu wa wilaya nilimuona kuwa alikuwa ametishika sana na kitendo changu kile na wakati huo huo maelezo ya yule daktari bandia yakionekana kuleta maana sana kwake.
“Acha uongo wako wewe! Mimi sio Sylvia na we’ unajua hilo! Nyie ndio mmemuua yule mtu kule msituni...” Nilimkemea yule jamaa huku wale wenzake wawili wakinishika kwa nguvu kutokea nyuma na wale askari wakinielekezea bunduki zao. Kwa mara nyingine tena uso wa yule jamaa ulionekana kushtushwa na maneno yangu.
“Ooo, Sylvia, Sylvia...usiwe na wasi wasi.Sasa hivi nitakupa dawa yako na utajisikia vizuri...” Aliniambia huku akinisogelea taratibu.
“Mimi siyo Sylvia wewe! Fala nini? Mimi ni Tigga Mumba na we’ sikujui na wala hatujawahi kujuana hata siku moja!” Nilimpigia kelele huku nikijikukurusha kutoka mikononi mwa wale wasaidizi wake bila mafanikio.
Yule jamaa alimgeukia tena mkuu wa wilaya na kujaribu kufafanua tena hali ile.
“Actually hii ni dalili mojawapo ya ugonjwa huu, mgonjwa kujiamini kuwa yeye ni mtu fulani tofauti na utambulisho wake halisi...eeenh, hii dalili tunaiita kiitalam echolaliaandechopraxia...inaweza kumpelekea hata kwenye kuiga mwendo, sauti au tabia ya mtu fulani na kuamini kuwa yeye ndiye huyo mtu.”
Duh! The guy is really good!
Nilielewa kilichokuwa kinafanyika pale. Yule jamaa alikuwa anatumia kila jambo nililokuwa nikilifanya kujaribu kuthibitisha ukweli wa maelezo yangu na kumbainisha kuwa yeye ni miongoni mwa wauaji, kuwa ni njia ya yeye kuthibitisha kuwa kweli mimi nilikuwa mgonjwa wa akili. Na mkuu wa wilaya pamoja na wale askari walionekana kuamini kila kitu alichokuwa akikieleza na mimi nilizidi kuonekana kichaa.
“Mnh!(nilisonya), eti ekolalia and ekopraksha! We’ acha uongo wewe!” Nilimkemea yule mtu muongo aliyejiita dokta Martin Lundi.
Lakini bado niliona kuwa maneno yake ndiyo yaliyoaminika kuliko lolote nitakalosema. Yule mtu alimuashiria mmoja wa vibaraka wake ambaye alifungua mkoba waliokuja nao na kutoa sindano na kichupa kidogo kilichokuwa na dawa ya maji.Nilijua kuwa walitaka kunichoma sindano wakijidai ni dawa kutokana na hayo maradhi waliyonipakazia.
Oh, Mungu wangu! Hii itakuwa sindano ya sumu tu...nifanyeje?
Mtu aliyejiita Martin Lundi alipokea ile sindano kutoka kwa yule kibaraka wake na kujitia kuangalia kiwango cha dawa kilichowekwa ndani ya bomba la ile sindano.
Niliamua kubadilisha mtindo.
“Mheshimiwa usimwamini hata kidogo huyu mtu. Huyu ni muuaji...yeye na wenzake wawili ndio waliofanya mauaji ya kinyama kule msituni...yaani ukimwachia tu anichukue hapa basi jiandae kuokota maiti yangu katika msitu wa jirani.These guys are killers!” Nilimwambia mkuu wa wilaya kwa kuomboleza huku nikijitahidi kuiweka sauti yangu chini ili nisionekane mwehu. Lakini mkuu wa wilaya alikuwa haambiwi hivyo.
“Wewe ni mgonjwa Sylvia na unahitaji tiba.” Aliniambia kwa msisitizo. Nilitikisa kichwa kwa kukata tamaa. Nilitazama mazingira yalivyokuwa mle ndani. Wale askari wawili walikuwa wamesimama mbele yangu kiasi cha hatua za mtu mzima zipatazo kumi hivi wakiwa wameninyooshea bunduki zao. Kushoto kwangu alikuwa amesimama Dokta Martin Lundi muongo. Mkuu wa wilaya alikuwa amesimama mbele ya meza yake iliyokuwa kulia kwangu. Wale vibaraka wa Martin Lundi muongo walikuwa wamenishika mikono yangu, mmoja kila upande wangu wakiwa kwa nyuma yangu.
Lazima nifanye kitu haraka!
“Mkuu huyu jamaa sio daktari wala nini....muuaji tu huyu, na nakuhakikishia utakuwa na damu yangu mikononi mwako ukimruhusu atoke na mimi hapa kwako mheshimiwa...hebu mwambie akupe kitambulisho chake kama kweli yeye ni daktari, mwongo mkubwa huyu!” Nilimwambia mkuu wa wilaya huku nikimtazama yule mtu aliyejiita Martin Lundi. Wakati huo huo yule jamaa alitoa kitambulisho kutoka mfukoni mwake na kupiga hatua moja huku akinyoosha mkono wake kumpa mkuu wa wilaya kile kitambulisho.
“Sylvia ni mgonjwa sana, na nadhani itabidi nimchome sindano yake hapa hapa...” Alisema huku akimkabidhi kitambulisho mkuu wa wilaya ambaye alisogea na kunyoosha mkono wake kukipokea.
Na hilo ndilo nililolitarajia, na ndio nafasi niliyokuwa nikiisubiri. Sikufanya makosa.
Wakati waliposogeleana kupeana kitambulisho, kwa sababu nilijua kuwa jamaa atakuwa amejiandaa na kila kitu kuonesha kuwa yeye ni kweli Dokta Martin Lundi, wote wawili walijikuta wako mbele yangu na wakati huo huo wakinikinga kutoka kwa wale askari wawili waliokuwa wameninyooshea bunduki zao. Mkuu wa wilaya alikuwa karibu sana nami kiasi kwamba kama nisingekuwa nimeshikwa mikono na wale wasaidizi wa yule mtu aliyejiita Martin Lundi, ningeweza kumshika.
Huku bado mikono yangu ikiwa imeshikwa na wale vibaraka wa Martin Lundi,nilijirusha juu kwa nguvu nikitanguliza miguu yangu na kumbana mkuu wa wilaya kiunoni kwa miguu yangu. Yule mama alipiga ukelele wa woga na wale jamaa waliokuwa wamenishika walivutwa mbele kunifuata hali mikono yangu ikiwaponyoka. Mkuu wa wilaya alipiga mweleka sakafuni nami nikawa nimembana kwa nguvu kwa miguu yangu hivyo wote tukaenda chini kwa kishindo. Nilisikia wale askari wakipiga kelele na dokta Martin Lundi akiropoka neno ambalo sikulielewa. Wakati huo huo wale jamaa waliokuwa wamenishika nao wakilalama kila mmoja kinamna yake.
Vyote hivyo sikuvitilia maanani.
Akili yangu ilikuwa kwa mkuu wa wilaya. Haraka sana nilijiinua huku nikiwa bado nimembana kiunoni kwa miguu yangu na kumtia kabali kwa mkono wangu wa kulia hali kwa mkono wangu wa kushoto nikijiinua kutoka pale sakafuni na kumburura pembeni yule mama aliyekuwa akipiga mayowe kwa woga. Nilijua kuwa wale vibaraka wa Martin Lundi bandia walikuwa nyuma yangu hivyo wangeweza kunivamia. Nilimwinua yule mama kwa nguvu na kuyumba naye hadi kando ya meza yake.
Iilikuwa ni tendo la haraka na lisilotegemewa. Wale askari kutahamaki nilikuwa tayari nimemdhibiti mkuu wa wilaya vizuri sana. Martin Lundi alianza kunisogelea lakini nilimkemea kwa hasira.
“Hatua nyingine moja tu namvunja shingo huyu bi kizee wenu hapa!” Nilikuwa nimemkaba kabali kali sana yule mama nikiwa nimemuweka mbele yangu kama ngao.
Martin Lundi alisimama na kuwageukia wale vibaraka wake, ambao ndio walikuwa wanajizoa zoa kutoka sakafuni. Wale askari walinielekezea bunduki zao huku wakitweta kwa wasiwasi.
“Mwache mheshimiwa sasa hivi msichana ama sivyo tunakupiga risasi!” Mmoja wao alifoka. Nilimcheka kwa dharau.
“Wacha ujinga wewe! Utanipiga risasi hapa bila ya kumuanza huyu bi kizee kwanza?”
“Sylvia, haina haja ya kufanya fujo eeenh? Naomba umwachie mhe...” Martin Lundi alianza kunisemesha kwa sauti ya kubembeleza kama kwamba anaongea na kichaa kweli. Alinichefua!
“Hebu ninyamazie mimi huko! Unadhani unaweza kunihadaa kama ulivyomhadaa huyu mama hapa?”
“Ah! Hebu tumia akili msichana, unadhani utajiokoa vipi hapo wakati umezingirwa na askari?” Martin Lundi muongo aliniambia kwa hasira, akipoteza ule utulivu wake wa bandia.
“Haaa-Loh! We’ mwehu nini? Umesahau kuwa mimi ni mgonjwa wa akili? ParanoidSchizo-nini sijui huko...sasa tangu lini mgonjwa wa akili akatumia akili?” Nilimjibu kwa kebehi huku akili yangu ikifanya kazi haraka haraka. Yule jamaa alikosa jibu alibaki akinikodolea macho.Nilipeleka mkono wangu wa kushoto na kunyakua begi langu lililokuwa juu ya ile meza ya mkuu wa wilaya.
“Waambie mbwa koko wako wateremshe bunduki zao chini mama!” Nilimnong’oneza yule mkuu wa wilaya huku nikining’iniza begi langu begani.
“Unafanya kosa kubwa sana we mtoto...” Alisema kwa taabu yule mama.
“Si kazi yako, we’ si umeamini kuwa mimi mwehu? Kwa hiyo usipoteze muda wako na wangu kumpa mwehu tahadhari...do it!” Nilimnong’oneza huku nikijua kuwa ndio nilikuwa najithibitishia shutuma za wazimu. Mkuu wa wilaya aliwaashiria wale askari waweke chini silaha zao. Wale askari walisita. Nikazidi kumkaba. Yule mama alitoa sauti za kukoroma kutokana na kabali ile. Bado akili ilikuwa ikinitembea.
Baada ya hapa halafu nini sasa?
“Weka chini silaha askari!” Nilifoka huku nikiongeza nguvu kwenye ile kabali. Bila shaka macho yalimtoka pima yule mheshimiwa kwani niliwaona wale askari wakimkodolea macho kwa woga. Nililegeza kabali.
“Tupa chini!” Mkuu wa wilaya aliropoka na kuanza kukohoa kwa taabu.
“Hapana!” Martin Lundi moungo aliropoka, lakini wale askari walishapata amri ya mkuu wao wa kazi. Walizitupa chini zile bunduki na kubaki wakinitazama kwa hasira.
“Vizuri...sasa rudini nyuma, nyote na muegemee ukuta ule!” Nilifoka huku nikiwatazama wale askari, Martin Lundi muongo na vibaraka wake. Hakuna aliyetikisika. Walibaki wakinitazama.Moyo ulikuwa ukinidunda kwa nguvu sana.
“Hamnielewi?” Nilifoka. Wale watu mle ndani hawakutikisika. Walibaki wakinitazama kwa hasira. Bila shaka waliona kuwa tayari wameshadhalilishwa na mtoto wa kike kiasi cha kutosha na hivyo hawakutaka kuendelea kudhalilika zaidi, liwalo na liwe.
Sasa itakuwaje?
Na mara mlango ulifunguliwa na Matilda aliingia mle ofisini. Aliacha mdomo wazi kwa butwa baada ya kuona hali ya mle ndani na wale askari walimgeukia.Kwa sekunde mbili hivi hakuna kilichotokea, kisha nilifanya lililostahili.
Kwa nguvu nilimsukuma yule mkuu wa wilaya kwa wale askari huku nikizirukia zile bunduki pale sakafuni.
Wakati huo huo Matilda alipiga kelele na kurudi mbio kule alipotoka. Wale askari nao waliruka kuziwahi bunduki zao. Wakapamiana na mkuu wa wilaya na wote wakaenda chini kwa kishindo. Kwa kona ya jicho langu nilimuona Martin Lundi muongo akipeleka mkono wake kwenye mfuko wa ndani wa koti lake. Nikaiwahi bunduki moja na kuikanyaga nyingine kwa mguu wangu.
“Wote tulia hivyo hivyo!” Nilifoka huku nikiwa nimeishika ile SMG vizuri sana mikononi mwangu na kuizungusha mle ndani ili kila mtu aone kuwa nina bunduki, na kuituliza kwa Martin Lundi muongo ambaye alibaki akiwa ametumbukiza mkono wake ndani ya koti lake.
“Toa hiyo bastola yako na uitupe chini wewe!” Nilimfokea kwa ukali. Alibaki akinitumbulia macho. Alizidi kunikera.
“Haraka!” Nilifoka kwa hasira na bila kujua nilibonyeza kifyatulio na ile bunduki iliachia mfululizo wa risasi huku ikitoa kelele kubwa. Hekaheka iliyotokea hapo ilikuwa si mchezo. Mkuu wa wilaya alilia kama mjinga, wale askari walipiga kelele hovyo. Martin Lundi aliruka huku akipiga yowe kubwa. Risasi zilichimba sakafu hatua chache kutoka miguuni mwake, hali wale vibaraka wake wawili wakijitupa chini kuokoa maisha yao.
Na mimi mwenyewe yowe lilinitoka.Sikuwa nimekusudia kufyatua risasi, wala sikujua ni jinsi gani ya kutumia bunduki ile. Nilijua nimeua mtu, lakini niliona wote bado wazima. “We kichaa nini? Utaua watu hapa!” Mmoja wa wale askari alibwata akiwa pale chini, huku vilio vya mkuu wa wilaya vikizidi kutawala.
“Kumbe na wewe pia hujui kuwa mimi ni kichaa kama mimi eenh?” Nilimjibu yule askari bila kumtazama, macho yangu yakiwa kwa yule muuaji aliyejiita Martin Lundi.
Tulitazamana na Martin Lundi muongo. Hasira niliyoiona katika macho yale ilitosha kabisa kuniambia kuwa nilikuwa natazamana na muuaji.
“Mara ya pili risasi zinaweza zikakupitia na wewe...tupa bastola yako chini!” Nilimfokea.
“Ee mtoto wee! Huyo daktari bastola aitoe wapi lakini...” Mkuu wa wilaya alilalama akiwa amekaa sakafuni pamoja na askari wake. Na hata pale alipokuwa akisema hivyo, Martin Lundi alitoa bastola yake na kuitupa chini. Kwa pembe ya jicho langu niliona mdomo wa mkuu wa wilaya ukimdomdoka na kubaki wazi kwa butwaa baada ya kuona kumbe “daktari’ wake alikuwa na bastola. Sikupoteza muda kumsuta, kwani alishajionea mwenyewe. Niliipiga teke ile bastola ikapotelea uvunguni mwa kabati la vitabu lililokuwemo mle ofisini. Niliipiga teke na ile bunduki nyingine nayo ikapotelea kule kule uvunguni mwa ile kabati.
Huku nikiwa nimewaelekezea bunduki, nilirudi nyuma nyuma kuelekea mlangoni, nilitoka na kuwakuta Matilda na yule bwege niyemkuta pale mapokezi wakihangaika kupiga simu.
“Wacha!” Niliwafokea na wote waliruka na kuanza kurudi nyuma wakiwa wamenyoosha mikono yao juu. Nilisikia purukushani kutokea kule nilipowaacha mkuu wa wilaya wenzake. Haraka niliwafungia kwa nje kwa komeo , niliisogelea ile simu na kuung’oa waya wake kwa nguvu huku wale watu wawili wakinitumbulia macho kwa woga, nami nikatoka mbio nje ya jengo lile.
Gari aina Ambulance ilikuwa imepaki mlangoni mwa jengo lile na dereva akiwa amekaa nyuma ya usukani naye akiwa na koti jeupe kama wale wenzake niliowaacha ndani.
Nilimwahi kabla hajataharuki na kumwekea mtutu wa SMG shingoni kupitia dirishani.Raia wachache waliokuwa wakipita na kuzagaa nje ya jengo lile walipigwa butwaa huku wengine wakipiga kelele za woga. Sikuwajali.
“Toka!” Nilimfokea huku nikifungua mlango wa gari ile. Nilishaona kuwa ufunguo ulikuwa umechomekwa mahala pake. Jamaa alishituka na sikumpa muda zaidi. Nilimvuta kwa nguvu na kumbwaga chini. Nilirukia ndani ile gari na kuondoka kwa kasi huku nikitimua vumbi na kuitupa nje ile bunduki.
Kwa kupitia kwenye kioo cha pembeni, nilimuona Martin Lundi muongo akitoka mbio nje ya ofisi ile huku akinitupia risasi kwa bastola yake akifuatiwa na wale askari. Nilikunja kona na kuingia kwenye barabara ya vumbi iliyoelekea nje ya mji.
Sikuamini kuwa kweli niliweza kumkaba yule mama namna ile na kuwatoroka wale watu wabaya. Mungu wangu, sasa nimekuwa mtu wa aina gani mimi?
Huku nikitokwa na machozi kwa woga, nilikanyaga mafuta na kuzidi kutokomea kwa kasi bila ya kujua mbio zangu zingeishia wapi.
T
ii.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
reni ya reli ya kati iliingia stesheni ya Dar es Salaam kwa mbwembwe na vishindo, huku ikipuliza honi yake kali kuwajulisha wananchi waliokuja kupokea ndugu na jamaa zao kuwa ilikuwa imeingia jijini. Nilijichanganya na abiria wengine kutoka daraja la tatu ambamo ndimo nilipokuwa nikisafiria na kutoka kuelekea nje ya stesheni ile Iliyokuwa na msongamano mkubwa wa watu, kila mtu akihangaika na mzigo au mizigo yake huku wachukuzi wakikimbia huku na huko kutafuta watu wa kuwabebea mizigo. Wakati huo huo wasafiri wenzangu wakihangaika kutafuta wenyeji wao hali na wenyeji nao wakiwa katika hali hiyo hiyo. Kelele za kila aina zilitawala eneo lote lile. Watoto wadogo walilia hovyo wakiogopa kelele na heka heka za watu waliojazana na waliokuwa wakipita kuelekea huku na huko ndani ya stesheni ile kubwa ya treni nchini. Na ni mchaganyiko na mvurugano huu ndio nilioutaka, kwani uliniwezesha kutoka pale stesheni na kujichanganya mjini kama wasafiri wengine bila ya kugundulika mara moja. ++Ilikuwa ni saa kumi na nusu za jioni siku ya tatu tangu yalipotokea yale mauaji ya kutisha kule msituni.
Nilikuwa nimevaa gauni refu la maua maua ambalo juu yake nilikuwa nimevaa jaketi zito kama jinsi wengi wa wasafiri waliokuwa wakitokea mikoa ya ziwa na kati walivyokuwa wamevaa kutokana na hali ya baridi ya maeneo hayo,na ingawa Dar hakukuwa na mazingira ya baridi kulazimisha watu kuvaa makoti au majaketi, niliendelea kulivaa jaketi lile kwani lillinifanya nionekane kuwa ni msafiri kutoka mikoani kama wengine. Kichwani nilikuwa nimejifunga kilemba kilichofunika kabisa nywele zangu za rasta, na miguuni nilikuwa nimevaa viatu vyepesi vya kamba vilivyoshika miguu yangu vizuri sana. Begi langu dogo la kuning’iniza mgongoni,likiwa na vitu vyangu vichache vilivyobakia pamoja na ile kamera ya marehemu Gil, nilikuwa nimeliweka ndani ya mfuko wa plastiki na juu yake nilikuwa nimesokomeza doti ya kanga.
Usoni sikuwa nimevaa ile miwani yangu ya jua ingawa nilitamani sana kufanya hivyo ili nisijulikane kirahisi. Nilijua kwamba, kama kuna wanaonitafuta; wawe polisi au wale wauaji, kwa vyovyote vile wangetegemea nivae miwani ili nisijulikane. Nilichofanya nilipaka wanja mzito kwenye nyusi zangu, ambazo kwa kawaida ni nyembamba na fupi, kuzunguka juu ya macho yangu na kuleta picha kuwa nilikuwa na nyusi ndefu zilizotambaa juu ya macho yangu kutoka kona moja ya jicho hadi nyingine. Pia nilipaka wanja kwenye kope zangu za chini. Kwa mtu aliyenijua vizuri, ingemchukua muda kunitambua kwani kwa kawaida huwa sina kabisa mazoea ya kupaka wanja namna ile.
Nilionekana wa kuja hasa.
Huku bado nikiwa na wasiwasi na moyo ukinienda mbio, nilitembea haraka kutoka eneo lile la stesheni. Niliangaza huku na huko, nikitegemea kusikia sauti kali ikiiniita kutokea nyuma yangu, ambapo nilikuwa tayari kutimua mbio.
Lakini sikusikia mtu yeyote akiniita.
Nilivuka barabara na kukata kushoto kuelekea kwenye mnara wa saa ambapo kulikuwa kuna teksi zilizokuwa zikisubiri abiria. Niliingia kwenye moja ya teksi zile na kumwamrisha dereva anipeleke sinza, nyumbani kwa mchumba wangu, Kelvin.
Nilijua kuwa kufikia sasa nilikuwa natafutwa na wale watu wabaya pamoja na polisi, kwani kizaa kizaa nilichozusha kule Manyoni kwa mkuu wa wilaya kisingeweza kuachiwa kipite hivi hivi. Yule ni mwakilishi wa rais katika wilaya ile, na kitendo cha kumgaragaza sakafuni na kumkaba namna ile kilikuwa ni kosa kubwa sana. Na kama hivyo ndivyo, kwa vyovyote vile wanaonisaka wangeanzia nyumbani kwangu upanga nilipokuwa nimepanga na kwa mama yangu Tabata,na wangekuwa wakinisubiri huko.Na ndio maana niliamua kwenda kwa mchumba wangu, ambaye nilijua angekuwa na msaada mkubwa kwangu katika janga hili kuliko mama yangu au dada yangu ambao wote walikuwa ni wanawake kama mimi.
Nilitulia kwenye kiti cha nyuma ndani ya ile teksi huku nikiwa nimeukumbatia mfuko wangu wa rambo na kuanza kutafakari matukio ya saa arobaini na nane zilizopita...
Baada ya mwendo mrefu na wa kasi nikiwa na ile gari ya kubebea wagonjwa niliyoiteka kutoka kwa mmoja wa vibaraka wa dokta Martin Lundi muongo, nilifika kwenye njia panda. Njia moja niliielewa kuwa ilikuwa inaelekea Dodoma mjini na nyingine sikujua ilikuwa ikielekea wapi. Nilifuata ile njia nyingine kwa kiasi cha kama nusu kilometa hivi na kulitelekeza lile gari kando ya barabara. Niliteremka na kuanza kukimbia kwa miguu kurudi kule kwenye njia panda nikitumia njia ya msituni sambamba na ile barabara. Kwa mbali nilianza kusikia ving’ora vya gari za polisi na nikajua kuwa msako ulikuwa umeanza.
Baada ya kukimbia kwa muda niliweza kuiona ile njia panda kwa mbali na nilisimama ghafla. Nilijizamisha msituni zaidi na kuanza kutembea taratibu na kwa tahadhari huku moyo ukinidunda. Kutokea kule msituni nilipokuwapo, niliweza kuona magari yapatayo matatu ya polisi yakiwa yamesimama njia panda. Nilizidi kusogea kwa tahadhari kubwa. Nje ya magari yale kulikuwa kuna kundi la askari waliokuwa wakiangaza huku na huko. Bila shaka walikuwa wakijaribu kung’amua ni njia ipi niliyochukua kati ya zile mbili. Nilizidi kunyata kuelekea kule walipokuwapo ili niweze kuona kilichokuwa kikiendelea. Wale askari walikuwa wakiongea na mwanamke mmoja aliyejitanda kanga akiwa amebeba mtoto mgongoni. Nilikumbuka kumpita kwa kasi huyo mama hatua chache kabla ya kuifikia ile njia panda.
Yule mama alionyesha kidole chake kuelekeza kule kwenye ile njia niliyoelekea na ile gari. Wale askari walionekana kubishana naye kwa muda, lakini yule mama alikuwa akizidi kuonyesha ile njia niliyoelekea huku akitikisa kichwa. Wale askari waliparamia magari yao kwa pupa na kuondoka kwa kasi kuelekea kule nilipolitelekeza lile gari, huku wakiacha gari moja na askari wawili pale kwenye njia panda.
Nilijua kuwa kwa pale nilikuwa nimewapoteza, hivyo nilizidi kuambaa na msitu ule sambamba na ile barabara iliyoelekea Dodoma mjini.
Mwendo mfupi baadaye niliona lori la mkaa likiwa limepaki upande wa pili wa ile barabara. Kwa jinsi lilivyokuwa limepaki, ni kwamba lilikuwa likielekea maeneo ya Dodoma mjini. Moyo ulianza kunipiga kwa kasi. Nilijificha nyuma ya miti na kuchungulia. Dereva na utingo wa ile gari walikuwa wakihangaika kubadilisha tairi lililokuwa limepata pancha. Ingawa nilitamani kwenda kuwaomba msaada, niliogopa kufanya hivyo kwa hofu ya kutiwa mbaroni na kukabidhiwa kwenye vyombo vya dola au kufanyiwa uhuni tu na wale watu, kwani mtoto wa kike kuomba msaada kwenye njia pweke kama ile ilikuwa ni kujitafutia kubakwa tu. Niligundua kuwa tairi lililokuwa na matatizo lilikuwa la mbele upande wa kushoto. Kwa hali ile wale watu walikuwa upande wa pili wa gari ile na hawakuweza kuniona,kwani hata mimi nilikuwa nawaona miguu na mikono yao tu wakihangaika kufunga hilo tairi. Niliangaza kulia na kushoto. Kulikuwa kimya, utingo alitoka na kulitupia lile tairi liliopasuka nyuma ya gari ile kuliKokuwa na magunia ya mkaa,kisha akarudi tena kule alipokuwapo dereva wake.
Nilibana nyuma ya miti kando ya ile barabara na kusubiri. Ile barabara ilikuwa kimya sana, na hakukuwa na gari hata moja iliyopita. Wale jamaa walipomaliza waliingia kwenye lori lao na kuanza kuondoka kwa mwendo mdogo kama nilivyotarajia kutokana na uchakavu wa lile gari na mzigo iliyobebeshwa. Nilichomoka mbio huku nikivuka ile barabara, nilidandia lile lori na kujilaza kule nyuma kwenye magunia ya mkaa bila ya kujali masizi yaliyonitapakaa.
Nilisafiri na lile lori hadi kijiji kimoja ambapo ndipo lilipokuwa likielekea. Niliwachungulia dereva na utingo wake wakiingia kwenye mgahawa uliokuwa eneo la sokoni ambapo ndipo tuliposimamia. Niliteremka bila kuonekana na kujichanganya mle sokoni huku nikijikung’uta masizi ya mkaa kutoka kwenye lile lori.
Nilijua kuwa nguo zangu zilikuwa zinatisha, hivyo nilinunua nguo za mtumba zilizokuwa zikiuzwa pale sokoni. Kwa bei ya jioni nilipata gauni na jaketi kwa shilingi elfu na mia tano. Nikanunua na kilemba kwa ajili ya kuficha rasta zangu ambazo nilijua zilikuwa ni alama kubwa ya kunitambulisha kwa polisi na hata wale wauaji niliowatoroka. Nikanunua na viatu vya chini ambavyo ingekuwa rahisi kwangu kukimbia pindi ikibidi. Nilirudi kule kwenye ule mgahawa kama mtu nisiye na hofu yoyote na kupita moja kwa moja mpaka sehemu ya vyoo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikiwa kule chooni nilinawa uso na sehemu muhimu za mwili wangu na kubadilisha nguo, nikiziweka nguo zangu nilizotoka nazo kule kwa mkuu wa wilaya ndani ya mfuko wa nailoni niliokuwa nimebebea zile nilizonunua pale mtumbani. Nilitokea mlango wa nyuma wa ule mgahawa na kurudi kule sokoni nikiwa mtu mwingine kabisa, mfuko wangu uliokuwa na nguo zangu za zamani nikiutumbukiza kwenye pipa la taka lililokuwa nyuma ya ule mgahawa.
Kutoka pale sokoni nilisafiri kwa lori jingine lililokuwa limewabeba wachuuzi waliokuwa wakifanya biashara zao pale sokoni kwa nauli ya shilingi elfu moja hadi Dodoma mjini ambapo tulipofika ilikuwa saa mbili za usiku.
Kwa muda ule hakukuwa na usafiri wowote wa kuweza kunifikisha Dar, hivyo nikabaki nikitembea hovyo mjini nisijue pa kwenda na wakati huo huo nisiweze kutulia popote kwa hofu kuwa polisi walikuwa wakinisaka na huenda wakanikuta na kunitia mbaroni.Nilijua kuwa nikisubiri hadi asubuhi itakuwa hatari kwani kwa vyovyote wabaya wangu walikuwa wanategemea kuwa ningejaribu kutafuta usafiri wa kurudi Dar, na hivyo wangenivizia kituo cha mabasi.
Nilipata wazo la kudandia malori ya mizigo ambayo huwa yanasafiri usiku, lakini pia niliona kuwa hilo lilikuwa gumu kutokana na kwamba nisingeweza kujificha kwenye lori la mtu mpaka Dar bila kugundulika kama nilivyofanya hapo mwanzo. Na hata kama ningesafiri kwa makubaliano na dereva kwa malipo maalum, bado kulikuwa kuna uwezekano wa kuwekwa vizuizi njiani ili kukagua magari yote yatokayo nje ya mkoa ule ili kunikamata. Mambo niliyomfanyia mkuu wa wilaya yalikuwa mabaya sana, na lazima polisi walikuwa wakinisaka kwa nguvu sana.
Ndipo nilipopata wazo la kutumia treni. Nilipitia kwenye kibanda cha urembo na kununua wanja na kuelekea stesheni ya treni ya dodoma huku nikiombea nikute kuna treni. Bahati bado ilikuwa yangu kwani nilikuta treni ndio inapakia na abiria walikuwa wakiparamia gari lile refu la chuma kwa fujo. Bila kuzubaa nami nilijitosa ndani ya gari lile bila tiketi, nikijua kuwa mkaguzi akinikuta nikiwa ndani na safari imeshaanza, hatakuwa na la kufanya. Na nilijiamini kwa kuwa nilikuwa na pesa. Nilipita hadi kwenye mabehewa ya daraja la tatu, nikaingia bafuni ambapo kwa kutumia kioo kilichokuwapo kule bafuni, nilijipaka wanja na kujifunga kilemba changu vizuri. Nilipojitizama, nilikubali kuwa nilikuwa nimebadilika.
Nilibana kwenye kiti cha dirishani kwenye kona nyuma kabisa ya behewa lile, lakini mwenyewe alipotokea, niliinuka na kuketi juu ya ndoo ya plastiki ya mmoja wa wasafiri waliorundikana pamoja nami ndani ya behewa lile. Na hapo ndipo nilipogundua kuwa nilikuwa nina njaa kali sana. Nilinunua mapande ya viazi vya kuchemsha na chupa ya maji kupitia dirishani na kuanza kula kwa pupa, bila ya kujali kuwa nilikuwa nakula katikati ya kundi la watu.
Msafiri kafiri.
Wachuuzi wa vitu vidogo walikuwa wakipita huku na huko kule nje ya behewa kama kwamba haikuwa usiku. Nilinunua machungwa kwa ajili ya kula wakati safari ikianza, kisha nikamtuma yule muuza machungwa anitafutie mchuuzi wa visu.Nikanunua na kisu kidogo kwa ajili ya kumenyea machungwa yangu nikiwa safarini. Baridi ilianza kunishambulia ingawa nilikuwa nimevaa jaketi. Nilinunua doti ya kanga kutoka kwa mchuuzi aliyekuwa akipitisha biashara hiyo kule nje, na kujifunika miguuni.
Baada ya muda treni ilipuliza honi yake kali na safari ikaanza. Nilipiga mbwewe kwa shibe na kuegemea dirishani huku nikitafakari matukio yaliyonitokea siku ile. Mwili wote ulikuwa ukiniuma na miguu niliihisi ikipwita na kuvuta kutokana na kukimbia kwa muda mrefu. Nilikuwa nanuka jasho na nywele zangu zilitoa harufu. Nilijiweka sawa pale kwenye ndoo niliyokalia na kujiegemeza zaidi kwenye kona ya behewa lile.
Muda si mrefu nilipitiwa na usingizi mzito.
--
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment