Sehemu Ya Nne (4)
Dakika tano baadae fax ikaingia kwa meneja. Hakuwa na haraka ya kuisoma kwani alitumia kama dakika nne kumaliza chai ambayo ilikuwa kwenye kikombe. Hakuwa mtu mwenye kupenda kuharakisha mambo, alipenda kufanya kila kitu kwa utulivu.
Alishtushwa na taarifa aliyoisoma kwenye fax ile, dakika hiyo hiyo akasimama huku akishindwa kujua nini la kufanya kwa muda huo.
Taarifa ya dharura Kwa Mameneja wote. Account no. 02042513272432 ya mteja wetu Alex Taisamo imezuiwa, haruhusiwi kuchukua kiasi chochote cha fedha na pindi atakapoonekana, taarifa ifikishwe makao makuu haraka iwezekanavyo. Wataalamu wetu wa IT wanaendelea kufanya kazi ili kuizuia Akaunti hiyo lakini kuna tatizo kidogo kwenye system, Tafadhali wasiliana na Tellers wote walifahamu hili kabla ya kuanza kwa shuguli yoyote ya kibenki, Zingatia system inasumbua lakini kwa sasa tunalazimika kutoa taarifa hii ya dharura.
Ilimaliza taarifa hiyo ambayo ilimtoa jasho meneja huyo wa Tawi la kariakoo. Dakika hiyo hiyo akainua simu na kupiga namba ile ile.
“Frank, yule mteja bado yupo?”
“Ndiyo bosi” Ulijibu upande wa pili.
“Mhhhh!” Alishusha pumzi meneja.
“Vipi, kuna tatizo bosi?”
“Ndiyo, kuna agizo kutoka makao makuu ambalo linatutaka kuzuia akaunti yake, pia tutoe taarifa kuwa yupo hapa umeshampa hizo pesa?”
“Ndiyo, anamaliza kuzipanga kwenye begi.”
“Mungu wangu mzuie.”
“No, Bosi ana bastola, hajatishia maisha yangu lakini anaonekana ni mtu ambaye hana masihara.”
“Mungu wangu, ina maana anakusikia unavyoongea?”
“No, hapa nilipo hanisikii maana nimejifungia, si unajua sauti haitoki humu ndani ingawa unaweza kumuona aliyeko nje.” Aliongea Frank ambaye alikuwa kwenye kichumba kidogo cha vioo.
“Acha maneno mengi Frank, nishauri nifanye nini?”
“Toa Taarifa kuwa huyo mtu yuko hapa Benki na ameshachukuwa hizo fedha kabla ya taarifa ya zuio haijaingia, pia usisahau kuwafahamisha kuwa hajafanya vurugu zozote lakini ana bastola mkononi, nasisitiza tena ana bastola mkononi.”
“Duh....” Alisikika Meneja kisha akakata simu.
“Nasisitiza ana bastola mkononi.....” Yalijirudia maneno hayo katika kichwa cha meneja huyo mwoga ambaye hakuwahi kupitia JKT wakati anarudisha kiwiko cha simu sehemu yake.
***
Ndani ya chumba kidogo ambacho kuta zake zilikuwa zimepambwa kwa picha kubwa za ngono, chumba hiki kilikuwa na harufu ya udi ambayo haikukatika mara zote. Hakikuwa na mvuto mkubwa kutokana na maisha duni ya mmiliki wa chumba hicho kutokuwa na uwezo wa kumiliki samani za gharama, badala yake kulikuwa na ndoo chache, kabati dogo na stuli chakavu ambayo juu yake kulikuwa na boksi ambalo lilikuwa limesheheni kondom ambazo hutolewa bure katika hospitali za serikali.
Kitandani alikuwa amekaa mrembo ambaye alikuwa na fikra nzito, siku hiyo hakuhitaji mteja katika biashara yake hiyo ya kuuza mwili; Taarifa za kwenda kupokea Fedha zilimsisimua Mary ambaye alijiona mwenye bahati kwa kuhisi kuwa wakati wa kuachana na ukahaba umefika. Matukio mengi ambayo alishirikishwa alilipwa fedha kidogo sana licha ya ugumu ambao alikumbana nao, hili la kwenda kupokea fedha kwake lilikuwa jukumu jepesi ambalo lina malipo makubwa. Akiwa na fikra nzito juu ya jambo hilo ndipo alipomkumbuka Mudy Guy, hakumfahamu kwa jina lingine zaidi ya jina hilo.
Mudy Guy alikuwa rafiki yake mkubwa ambaye alimshauri mambo mbalimbali, hata pale wateja wake walipokataa kumlipa mara nyingi alitaka msaada kutoka kwa kijana huyo mbabe ambaye mara nyingi alikuwa akishinda kwenye kituo cha teksi, mara moja moja akipata kazi za muda mfupi maarufu kama ‘deiwaka’. Alipata kazi hizo pale dereva anapokuwa amechoka au ameenda kula.
“Nina mazungumzo muhimu sana Mudy ndio maana nimekuita.” Alianza Mary huku akichezeachezea vidole vya Mudy ambaye hakuonekana kuitilia uzito sana kauli hiyo.
“Unajua nimeshtuka sana nilipoambiwa unatafutwa muhimu sana usithubutu kukosa.”
“Ni kweli Mudy, kama nisingekuona bila shaka nisingelala leo.”
“Kuna mtu kakudhulumu?”
“Sio dhulma ni mpango wa pesa mchizi wangu.”
“Duh, si ungesema tu maana nimeishiwa yaani sina kitu kabisa.”
“Sina maana hiyo, kuna dili la pesa nahitaji ushauri.”
“Sasa ushauri gani unahitaji hapo si unachukua tu halafu tunaingia viwanja kunako vinywaji?”
“Mudy, sizungumzii pesa ya chai. Nakusudia mamilioni ya shilingi.”
Mudy ambaye muda mwingi alikuwa amekaa kivivuvivu akakaa vizuri huku akimkazia macho Mary.
Kisha akamsimulia mpango mzima kama alivyoelezwa na Makabi.
“Duh, hilo dili si mchezo mtu wangu.”
“Ndio maana nikaona ipo haja ya kukutafuta unipe ushauri.”
“Hizo pesa ni zetu, nakuambia huyo bwege kaingia choo cha kike, kama yeye zungu launga basi sisi ni wazungu wa pesa.”
“Kivipi Mudy.”
“Tunakomba zote, hizo haziwezi kuwa chini ya mia.”
“Halafu...”
“Usiwe mjinga mtoto wa kike, kinachofuata ni kusepa na kwenda kutumbua kuku kwa mrija.”
“Tutawezaje?”
“We si umeniita nikupe ushauri.”
“Ndio maana yake.”
“Au unataka kula peke yako?”
“Si hivyo Mudy, mi nimetaka kujua nini tufanye si unajua ninavyokutegemea katika mambo yangu mengi?”
“Subiri kidogo, nahitaji nusu saa nitarudi na jibu” Akainuka na kutembea kwa haraka akikiacha chumba kile.
*******
Baada ya nusu saa akarudi akiwa ameongozana na mtu mwingine jambo ambalo lilionekana kumkera Mary.
“Mary, kutana na Cheusi ni rafiki yangu wa siku nyingi nimeamua kumwalika katika kikao hiki kwa sababu ni mtu muhimu sana kuweza kufanikisha mpango wetu, kwanza ni mtoto wa mjini halafu vilevile ishu kama hizi anaziweza.........” Akatulia na kuwasha sigara ambayo tayari alishaibana kwenye mdomo wake kisha akaendelea.
“.....Unajua hii ishu wewe unaiona nyepesi lakini hatuwezi kufanikisha peke yetu, huyu jamaa ana gari lake ambalo tunaweza kulitumia kufanikisha mpango wetu. Yaani ukishachukua hizo fedha unaingia kwenye gari la cheusi ambalo litakuwa tayari kwa lolote eneo la tukio, kisha tunasepa na kumwachia vumbi huyo Bwege wako.”
“Hapo, nimekubali mchizi wangu.” Aliongea Mary huku akiruhusu meno yake meupe yaliyojipanga vema kuonekana.
***
Ilikuwa yapata saa 9.15 mchana. Akitembea kwa tahadhali kubwa Alex Taisamo alikuwa Kariakoo mtaa wa Narung’ombe. Kwa umakini zaidi akatembea kuelekea kwenye moja ya ghorofa iliyopo pale.
“Habari yako.” Alimsalimia mlinzi aliyeko mapokezi.
“Nzuri, karibu.”
“Ahsante, nahitaji kufika ofisi za MJ Security.”
“Ghorofa ya kwanza upande wa kushoto chumba cha pili kutoka mwisho.”
Akapanda ngazi za jengo lile chakavu kiasi kuelekea Mj security. Alishangazwa na uchakavu wa kuta za jengo lile ambao ungeweza kudhibitiwa vema kwa kupakwa rangi ya mafuta au maji.
“Ngo,ngo,ngo.....” aligonga.
“karibu.” Aliitikiwa huku ikifuata sauti ya kikohozi cha mvutaji mzuri wa tumbaku au sigara.
Akafungua mlango na kuketi kwenye kiti huku akimuelekea mzee wa makamo ambaye alimkuta ofisini humo.
“Karibu, sijui nikusaidie nini?” Aliongea mzee huyo ambaye alionekana kuwa na madaraka katika kampuni hii ya ulinzi.
“Nahitaji kuonana na Meja mstaafu, Silvester Rutakinikwa.”
“Ha, ha, ha..... Karibu sana, yaani wewe umelitamka kwa ufasaha sana jina lake. Hapa wengi wanaita Meja Ruta tu au meja kwa wavivu wa kurefusha maneno.”
“Ahaa, kumbe ana jina fupi hivyo, inafaa maana halipotezi muda.” Yule mzee akaangua kicheko tena, alionekana wazi kuwa mtu mcheshi ambaye alipenda utani.
“Oh, Meja Ruta ingia chumba hicho,lakini kama ni shida ya kikazi hata mimi unaweza kunifikishia.”
“Hapana ni ya binafsi.”
“Alijibu huku akifungua mlango wa chumba kidogo ambacho kiliandikwa DIRECTOR.”
“Karibu kijana.” Alikaribishwa na sauti nzito yenye mikwaruzo wakati anaingia kwenye chumba hicho kidogo.
Akapiga saluti kabla ya kukaa.
“Karibu, keti tafadhali.”
“Ahsante.”
Akakaa na kutulia kidogo kabla ya kuanza kuongea.
“Bila shaka utakuwa umenisahau Meja.”
“Hapana, sina tabia ya kuwasahau watu kama watu ninachosahau huwa ni majina yao. Nakumbuka vema kama mara ya mwisho tulikutana Angola kwenye zoezi la uteguaji mabomu.” Ilikuwa ni wakati wa Alex kupatwa na mshangao jinsi kichwa cha yule mzee kilivyokuwa na kumbukumbu nzuri.
“Ona sasa, nimekukumbuka mpaka jina bila shaka ni Taisamo.... Si hivyo tu nafahamu vema kama unatafutwa na millitary police.” Alikuwa kama aliyepigwa na shoti ya umeme baada ya kusikia taarifa hizo kutoka kwa huyo mzee.
“Ooh, samahani mkuu kabla sijaongea lolote ningependa kujua umefahamu vipi haya yote.”
“Nilikuwa kwenye kitengo ulichopo ndani ya jeshi, napenda ufahamu kuwa ukiwa ndani ya kitengo hicho mara nyingi huwa unaendelea kutumika hata kama umestaafu hasa kwenye maswala ya ushauri. Hivyo leo saa 10.30 Alfajiri nimepokea baadhi ya taarifa zako. Pia saa 3.00 nikapokea taarifa kuwa umekusanya fedha zote ulizopewa kwa ajili ya kazi ni kweli?”
Alex alishusha pumzi kisha akaegemea kiti.
“kabla hujanieleza shida yako naomba unieleze uliwezaje kuchukua fedha pale benki na kisha kuondoka salama?”
“Nitakueleza Meja, lakini kwanza napenda kufahamu kwanini kama umeyafahamu yote hayo hujatekeleza wajibu wako?”
“Kijana, hii kazi yako unatakiwa kuwa na akili inayofanya kazi haraka sana. Kwa tukio ulilolifanya leo ulihitajika kutoroka na kutokomea sehemu ambako jicho la kijeshi lingekuwa gumu kukufikia lakini kitendo chako cha kuja kwangu nimekitafsiri haraka sana kuwa unahitaji msaada inaonesha kuna tatizo hapa.”
“Sawa ngoja nikujibu swali lako. Benki nilitumia kanuni ya kisaikolojia zaidi, baada ya kuchukua kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwenye akaunti yangu mara nikamuona yule keshia akiongea na simu
Nilikuwa simsikii lakini sura yake ilionesha wazi kuwa mimi ndiye ninayezungumziwa hivyo nilichomoa bastola na kuikamata vema mkononi kwa isahara ya kwamba yeyote atakayejaribu kunizuia nitamlipua, si hivyo tu pia nilimkazia jicho la kiaskari.”
“Safi sana sasa niko tayari kusikiliza shida yako.”
“Meja, kuna risasi mbili ambazo zinatofautiana zimetolewa katika mwili wa Mheshimiwa Makamu wa Rais, nataka kujua ni bastola za aina gani zimetumika maana sijawahi kuona aina hizi za risasi.”
“Sawa nitakusaidia lakini nashangaa kuona unaendelea kufanya kazi ambayo umeshaiacha, kwa lengo gani?”
“Ni kweli nimetangaza kuacha kazi lengo kuu likiwa ni kufanya kazi kwa uhuru zaidi kwani kuna hisia za usaliti naanza kuziona sielewi nini kinatokea.” Baada ya kusema hayo akamsimulia Meja mkasa mzima mpaka kufikia hapo.
Meja alimkazia macho Alex huku akiwa ameshangazwa na kilichotokea.
“Oh God, kuna tatizo.”
“nisaidie Meja, mpaka sasa hivi ni wewe tu ndio nimekueleza ukweli wote.”
“Ok, lete hizo risasi.”
Akatoa kifuko kidogo cha karatasi ambacho kilikuwa katika mfuko wa suruali yake akampatia Meja Rutakinikwa.
Akaitazama ile ya kwanza kisha akaitazama ile ya pili. Alex aliyaona wazi macho ya Meja jinsi yalivyotafsiri mshtuko wake.
“Mh, Luteni, Luteni, Luteni...... hii sio mission uliyostahili kuifanya peke yako. Hizi risasi ni mbili tofauti lakini ni ishara ya ukubwa wa tatizo.”
“Kivipi?”
“Usiwe na haraka, acha nikueleze kwa tuo ninachokifahamu juu ya silaha zilizotumika.......” Akakohoa kidogo na kuwasha sigara ambayo ilikuwa kwenye mfuko wa kulia wa shati. Akaanza kuvuta huku akiutazama moshi ulivyokuwa unaelekea angani. Kisha kama aliyezinduka akamgeukia Taisamo.
“Kuanzia sasa, unatakiwa kufahamu kuwa una jukumu zito mbele yako na unatakiwa kuifanya hii kazi kwa umakini zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla, nakuonya usimuamini yeyote mpaka umekamilisha hii kazi. Niko nyuma yako kwa msaada pale utakapohitaji.” Akatulia tena na kuvuta sigara yake kisha akaendelea.
“Hii risasi ya kwanza ni ya bastola ya kisasa aina ya bereta92 ambayo imeanza kutengenezwa mwaka 1975 na kampuni ya Fabbrica d'Armi Pietro Beretta ya Italia lakini kwa sasa imeboreshwa sana, ina wastani wa uzito wa gram 950,urefu wa milimita 217, ina uwezo wa kupiga kwa shabaha nzuri zaidi kwa umbali wa mita 50 mpaka 100 ingawa kwa mtumiaji mzuri anaweza kuitumia hata meta 200 na ikaleta madhara, inatumika kwa matumizi ya kijeshi na nchi za Amerika na zile za mashariki ya kati, Kwa hapa Tanzania zilikuja rasmi kwa watu wa usalama wa Taifa, kumbukumbu yangu inaonesha kuwa ziliingia kumi tu hapa nchini, ingawa nimestaafu lakini bado mambo mengi yanayohusiana na silaha nahusishwa ili kutoa ushauri.” Akatulia kidogo na kumkazia macho Alex ambaye alikuwa anasikiliza kwa makini maelezo hayo.
“Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa kuwa muuaji hakuwa zaidi ya umbali wa mita mia na hilo gari lilitumika kama kisingizio, pia huyo muuaji lazima atakuwa ni mtu wa usalama wa Taifa au si Mtanzania kwani Utoaji wa silaha hizi unatofautiana na zile nyingine.” Akashusha pumzi na kuvuta tena sigara yake huku akitafakari kwa makini zaidi.
“Sasa hii nyingine ndio balaa kabisa,ni FN57 hii ni bastola hatari, bora na ya kisasa zaidi. Hii imetengenezwa nchini Ubelgiji inatumiwa sana na mashirika ya kijasusi ya magharibi kama CIA la Marekani, MOSAD ya Israel pia FSB ambalo lilikuwa likijulikana kama KGB la Urusi. Hapa Tanzania zililetwa tano tu moja ilikuwa kwa ajili ya Jenerali, nyingine alipewa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na tatu zilizobaki walipewa walinzi maalum wa Rais.” Akatulia na kumtazama Alex Taisamo ambaye alikuwa anakuna kichwa.
“Nafikiri tunahitaji mfumo mpya wa Idara yetu ya kijasusi.” Aliongea Alex baada ya kukaa kimya muda mrefu.
“Una maana gani unaposema mfumo mpya wa kijasusi?”
“Nakusudia kuwe na shirika au idara itakayojiongoza yenyewe na kuwasimamia wanasiasa, hii ya kwetu naona inaongozwa na kusimamiwa na wanasiasa.”
“Unaonekana kuwa na mawazo mazuri Luteni lakini kwanza rudi kwenye kazi yako, tafakari kwa kina nini cha kufanya kwani hali ninayoiona ni nzito na inanitisha sana.”
“Ok Meja, tuna mengi ya kujadili lakini nahisi muda hautoshi. Natakiwa kuondoka, naweza kurudi kwako saa na wakati wowote au vinginevyo utatakiwa kushuhudia maiti yangu kwenye Jeneza, kama nitakufa kabla ya kuonana na Jenerali naomba umfikishie kila ambacho sijafanikiwa kukifikisha kwake.
“na iwapo yeye ni miongoni mwa wahusika itakuwaje?”
“Ah, nashindwa kukujibu Meja, utafanya uchunguzi wako ili uweze kubaini kama anahusika au vinginevyo.”
***
Hakufikiria kabla kuwa baada ya kuahidiwa milioni kumi Mary anaweza kuwa na wazo la kutoroka na fedha zake. Akiwa amepigwa na butwaa kwa kitendo cha Mary kukimbia na begi la fedha na kujitoma kwenye gari ambalo ni wazi liliandaliwa kwa ajili ya kazi hiyo akapatwa na mshangao mwingine wa mwaka, alishuhudia gari lile likishambuliwa na watu waliokuwa na sare za polisi wakiwa kwenye defender 110.
Mary ambaye alikuwa anamaliza kuingiza mguu wa mwisho alirushwa juu kabla hajaangukia upande wa pili wa barabara. James alishuhudia begi la fedha ambalo lilishikwa na Mary likifunguka na fedha kutawanyika angani kitendo kilicholeta msisimko mkubwa kwa watu wenye shida zao. Licha ya hali ngumu ya kimaisha hakuna aliyekuwa na muda wa kwenda kuokota noti hizo wakati milipuko ya risasi inaendelea.
Pale aliposimama aliweza kumuona vizuri dereva wa gari lile jinsi alivyoharibika vibaya kifuani kwa risasi ambazo zilifanya kazi yake vema. Hakuwa na shaka kuwa dereva, Mary na yeyote aliyemo kwenye gari lile amekufa.
“Kwanini?” Alijiuliza huku akiongeza utulivu.
Dakika kadhaa baadae hali ikawa shwari, Masharubu hakuwepo tena wakati tukio linaendelea.
Makabi aliendelea kuwa kama mtazamaji wa filamu akaendelea kuganda pale aliposimama huku akiwaangalia watu ambao walikuwa wanarudi eneo la tukio. Polisi ambao walifanya shambulizi lile nao hawakuwa nyuma.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nusu saa baadae baadhi ya watu walianza kuliacha eneo la tukio, akaamua kuwafuata watu wanne ambao walikuwa wanasimuliana tukio lile. Akajiunga nao huku akisikiliza mjadala ule wa kusisimua.
“Ebwana, jamaa anatisha yaani amewatoka palepale!”
“Lakini kakosea, we unaingia vipi eneo la tukio na kitambulisho cha kupigia kura?” Aliongeza mwingine.
“Kwani amefahamika?”
“We hujasikia pale watu wanaulizwa kama wanamfahamu James Makabi?”
“Mi nimechelewa, jamaa alibugi sana we unatembea vipi na kitambulisho cha kura kwenye ishu kama ile.”
“Dah, lakini kawatoka utamu... yaani kama komando!” Aliendelea kusifia jamaa mwingine.
“Lakini Fedha zote zile ni za bandia kwanini?” Aliuliza yule wa kwanza.
“Dah, hapo sasa. Inaelekea jamaa ndio ishu zake, tusubiri taarifa ya habari.”
“Ishu zipi, zakutengeneza fedha za bandia?”
“We hujasikia askari wanasema aliyetoroka ni mtu hatari sana?”
Aliamua kujitoa kwenye kundi hilo. Alijihisi kutaka kupoteza fahamu.
Bado taswira ya Mary ilimjia akilini.
“Nimemsababishia kifo, lakini tamaa yake imemponza pia.” Aliwaza huku akielekea kituo cha daladala.
Aliingia kwenye moja ya daladala ambalo hakuangalia linaelekea wapi.
***
Kwa mtu wa kawaida lilikuwa ni jambo la kustaajabisha kwa Alex Taisamo kujificha kwenye nyumba ya kulala wageni ambayo haikuwa mbali sana na kambi ya Jeshi. Hakukosea, alijua wazi kuwa kuna msako wa siri ambao unaendelea dhidi yake, yeyote aliyekuwa anamtafuta asingeweza kufikiria kuwa Taisamo anaweza kujificha karibu na kambi ya jeshi.
“Ngo,ngo, ngo....” Mlango uligongwa kwa nguvu kitendo kilichomshtua Alex.
“Fungua mwenyewe” Mtu aliyeko nje aliendelea kufoka.
“Unataka nini?” Aliuliza Taisamo huku akiwa na wasiwasi.
“Fungua bwana, ukituzingua tunavunja mlango.”
Taisamo aliingiwa na hofu kwa kujuwa kuwa ficho lake limegundulika.Kijasho chembamba kikaanza kumtoka.
“Ikibidi kuua ua.” Alikumbuka maneno ya mmoja wa walimu wake Kapteni Isack Kihengu. Akapapasa bastola yake aina ya SIG P228.
“Subiri nafungua.”
Kabla hajafungua akachungulia kwenye tundu la ufunguo, akabahatika kuiona sura ya mmoja wa watu walioko nje. Haikuwa sura aliyoitarajia ilikuwa sura ya kawaida ambayo isingeweza kuwa na kile alichokiwaza licha ya kuonesha dalili ya hasira na shari.
Akafungua mlango na kushuhudia watu sita wakiingia ndani kwa fujo.
“Yuko wapi mke wangu?” Alihoji mmoja kwa hasira, wakati huo huo akamuona muhudumu wa Guest naye akiingia.
“E bwana, ndio utaratibu gani huu wa kuingiliana vyumbani?”
“Samahani bro, hata mimi wamenilazimisha tu wanasema wamekuja kufumania.”
“Maelezo mazuri, lakini nafikiri itakuwa ni bora maelezo hayo utakapoyatoa kwa polisi ambao watakuja hapa muda si mrefu baada ya kupata simu yangu.” Alijitutumua Taisamo huku akionesha hasira. Kidogo wale watu walioingia wakaanza kuingiwa na wasiwasi na kupunguza jazba na kelele zao.
“We, una uhakika mkeo kaingia huku?” Aliuliza mtu mwingine ambaye alijifanya kuwa na busara kuliko wenzake.
“Sasa naomba wote msubiri na maelezo yenu yatafuata kituoni.”
“E bwana, njagu huyo hamuoni hata sura yake?” Aliropoka mtu mmoja na kutoka mbio mle chumbani huku akifuatiwa na wenzake. Hakuna aliyekuwa tayari kati yao kukabiliana na Polisi. Wote wakatimua mbio na kumwacha Muhudumu wa guest ambaye aliitumia fursa hiyo kwa kumuomba radhi Taisamo.
Baada ya Muhudumu kuondoka Taisamo akajilaza kitandani huku akishusha pumzi.
“Hii si dalili nzuri, kesho narudisha chumba.” Aliwaza huku akitazama saa na kupuuza njaa ambayo ilishaanza kumsumbua.
Alianza kuyapitia mawazo ya Meja Rutakinikwa kwa kichwa.
“Bereta92, zililetwa kumi kwa idara ya Usalama wa Taifa, kwanini watu wa usalama wa Taifa wamuue Makamu wa Raisi, Je ni mpango wa idara au baadhi ya watu ndani ya Idara?” Alijiuliza huku akitikisa kichwa. Fikra zake akazipeleka kwenye FN57. Aliweza kukumbuka vema maelezo ya Meja mstaafu kuwa hiyo walipewa watu maalumu watano akiwemo aliyemtuma kufanya kazi, au jenerali yuko nyuma ya pazia?
Kwanini zitumike bastola za aina mbili tofauti? Au kuna watu tofauti walikuwa na ugomvi na marehemu? Na yule aliyetumia gari alitumwa na nani? Marehemu alikuwa na tatizo gani kwa Usalama wa nchi? Kwanini yote haya yametokea baada ya kutangaza nia ya kugombea Uraisi?
Alijiuliza maswali hayo kwa haraka na kujikuta akikosa jibu. Akazirudisha fikra zake kwa jinsi alivyokuwa anamfahamu marehemu. Alikuwa ni mtu muungwana, mchapa kazi na asiye na makundi ndani ya chama. Kubwa zaidi alikuwa kipenzi cha wengi.
Inawezekana sababu za kisiasa zimesababisha yote haya. Akaamua kuandika kwenye kidaftari chake, sababu za kisiasa zinaweza kuwa chanzo cha yote haya.
“Sasa nahitaji chakula, angalau nimeweza kupiga nusu hatua.” Aliwaza huku akitazama saa yake ambayo ilionesha kuwa ni saa 4.22 usiku.
Kesho naanza rasmi kazi yangu.
3
HARUFU YA UKWELI
.......... Jambazi mmoja aliyefahamika kwa jina la James Makabi amefanikiwa kutoroka eneo la tukio. Zawadi nono ya dola 2500 za kimarekani itatolewa kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa jambazi hilo Sugu.
Kishindo cha mshituko kilimkuta James alipokuwa anasikiliza taarifa hiyo ambayo aliikuta katikati ya taarifa ya habari ya redio ndogo ya mpenzi wake Tamasha.
“Dear, utafanya nini sasa?”
“Nimechanganyikiwa Tamasha Mpenzi, naomba msaada wako tafadhali.”
“Njia ni tatu tu, kuendelea kujificha kwa umakini zaidi, kutoroka na kwenda mbali kabisa na macho ya polisi au kujisalimisha Polisi.”
“Polisi?”
“Ndiyo Polisi.”
“kujificha kwa zawadi nono iliyoahidiwa ni jambo gumu, kutoroka ni ngumu na hatari zaidi kwani kila kona kuna makachero, kidogo hilo la kujisalimisha Polisi lina unafuu lakini polisi wenyewe nao hawaaminiki.”
“Fanya kitu kimoja dear.”
“Enhe.”
“Ongea na waandishi wa habari kuwa umeamua kujisalimisha. Usiwaeleze ukweli wote isipokuwa wafahamishe wazi kuwa unaomba msaada wa wakili ili uweze kueleza chanzo cha yote hayo.”
“Wazo zuri, lakini kama wameweza kumuua makamu wa Raisi unafikiri kuna urahisi wowote wa kuondoka eneo la tukio nikiwa salama?”
“Una wakati mgumu sana dear, lakini nafikiri ni muhimu kwako ukijisalimisha Polisi.”
“Ok, nakubaliana na wewe kwani kadri nitakavyoendelea kujificha, ndivyo ninavyojitia matatizoni zaidi, nitanya hivyo kesho.
***
“Google, Bi Jesca Ole Nunga,” alitamka Taisamo huku akiandika jina alilolitaja kwenye kiboksi cha google kwenye tovuti hiyo kubwa ambayo ni maarufu kwa utafutaji wa vitu na mambo mbalimbali ikijulikana zaidi kama ‘search engine’ akatulia na kusubiri kwa sekunde chache kabla haijamletea vichwa vya habari vingi. MKE WA MAKAMU WA RAISI AZINDUA MRADI WA KINA MAMA, MKE WA....... Alikutana na vichwa vingi akavutiwa na kile kilichosema. HISTORIA YA MAMA OLE NUNGA. Akafungua na kuanza kusoma. Baada ya kumaliza alikuwa amekipata alichohitaji. “Ni mwalimu, shule ya sekondari ya Wazazi Tabata Kimanga.” Aliandika maneno hayo kwenye kikaratasi kidogo kisha akamlipa muhudumu wa mkahawa ule wa Intaneti ‘Internet cafe’ akaondoka.
Saa 8.43 alikuwa maeneo ya Kimanga mwisho. Akaamua kuingia kwenye mgahawa kwanza kabla hajaenda shuleni hapo.
“Nipatie maziwa na keki tatu.” Aliagiza.
Baada ya muda mfupi akaletewa vitu alivyohitaji. Akala kwa utulivu huku akiwa makini kutazama kama kuna mtu anamfuatilia.
Alikuwa karibu na wanawake wawili ambao walikuwa wanaongea kwa kunong’ona. “Vipi shosti na leo mama hajafika kazini?”
“Mwenzangu, si nimesikia kwa Headmaster kuwa ameacha kazi?”
“Ameacha kazi?”
“Ndiyo, anasema amechoshwa na watu wanaomfuata mara kwa mara.”
“Kwani kuna watu wanamfuata?”
“Yaani toka kifo cha mumewe amekuwa akifuatwa sana ana wasiwasi maisha yake yako hatarini.”
“Mungu wangu, ina maana anawajua waliomuua mumewe?”
“Hapana, kuna wakati alitaka kujua kwa madaktari kile walichogundua kutokana na kifo cha marehemu mumewe, toka hapo amekuwa hana amani kwani anaandamwa mno na watu asiowafahamu na wakati mwingine kupata vitisho.”
“We umewahi kumtembelea toka kuzikwa kwa marehemu mumewe?”
“Mh, shoga. Yaani sina hamu.”
“Kwanini?”
“Yaani ile nyumba ina ulinzi mkali tofauti na kipindi cha marehemu.”
“Usiniambie, sasa kwanini ulinzi uwe mkali wakati Vice ameshakufa?”
“Mh, tuyaache shoga.....” Aliongea dada aliyekuwa anajibu maswali huku akiweka vizuri kitabu chake mkobani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alex aliwatazama vizuri akabaini kuwa ni walimu. Hakuona sababu ya kusitisha uchunguzi wake ingawa alikuwa amepata mambo mengi zaidi ya alivyotarajia.
Akatembea taratibu akiiacha barabara inayoelekea Kisukuru na kufuata ile inayoelekea shule ya sekondari ya wazazi Tabata.
“Hatua moja kamili.” Aliwaza huku akiwa katika mlango ulioandikwa Headmaster.
Akagonga mlango na kuingia baada ya kukaribishwa.
“Habari yako dada.”
Nzuri, salama.” Alijibu dada ambaye alikuwa kwenye meza yenye kompyuta akiandika kwa kutumia kicharazio ‘keyboard’
“Salama kabisa.”
“Sijui nikusaidie nini?”
“Nina shida ya kuonana na mkuu wa shule.”
“Amesafiri kikazi.”
“Msaidizi wake.....”
“huyo kaacha kazi.”
“Aaah, kumbe yule mama kaacha kazi.” Alijifanya kumfahamu.
“Yaani, tunasikitika sana maana alikuwa mchapakazi kubwa.” Aliongezea yule dada na kumpa uhakika wa alichokuwa anahitaji.
****
Saa 2.30 usiku alifika maeneo ya Oysterbay. Aliifahamu vema nyumba ya marehem Ole Nunga. Haikuwa mbali sana kutoka kituo maarufu cha polisi cha Osterbay. Akapita mbele ya nyumba hiyo na kujionea jinsi askari wenye silaha walivyokuwa wameiweka chini ya uangalizi mkali.
“Kwanini?” Alijiuliza wakati akipita kana kwamba hana mpango na nyumba ile.
Ilikuwa nyumba kubwa ya ghorofa moja huku ikiwa imezungukwa na uzio mkubwa wa matofali. Aliweza kuiona miti ya aina mbalimbali ambayo ilipandwa kwa ustadi mkubwa. Baada ya kutembea umbali wa mita kama mia nane akafuata kichochoro kinachoelekea kushoto ambacho kinatokea nyuma ya nyumba ya Marehemu Ole. Akafanikiwa kutokea nyuma ya nyumba bila kufikiwa na jicho la yeyote ambalo lingeweza kunusa dhamira yake.
Akiwa nyuma ya nyumba kadhaa ambazo zilifanana kidogo na ile ya mheshimiwa, alitembea taratibu huku akihofia sana mbwa ambao kama wangethubutu kubweka basi ingekuwa tatizo kwake. Aliposogea karibu na nyumba ya mheshimiwa alikutana na miti ambayo ilimsaidia kujificha akikwepa taa kali ambazo zilizunguka nyumba nzima kiasi cha kuwezesha kuonekana kwa pini au sindano iliyoanguka usiku wa manane. Hofu ilianza kumtawala pale alipokuwa anafikiria namna ya kupanda ukuta ule, sio kwamba ulikuwa mrefu kiasi cha yeye kushindwa kuingia ndani tatizo lilikuwa ni hofu ya kukutana na walinzi wengine.
Akaruka na kukamata sehemu ya juu ya ukuta, mikono ikafanya kazi kama jeki ya gari kwa kuinua sehemu ya mwili iliyobaki, akachungulia ndani na kulakiwa na ukimya. Akauvuta mwili wote na kulala sehemu ya juu ya ukuta ule. Akatulia kwa sekunde chache kisha akaangukia ndani na kufanya kishindo kidogo ambacho kingeweza kumshitua yeyote aliyeko karibu.
Kwa mwendo uleule wa kunyata akatembea taratibu huku akienda upande wa mbele wa jengo lile. Hofu ilianza kuchomoza kadri alivyokuwa anazidi kusogea upande wa mbele wa jumba lile.
“Kwanini wakati marehemu yuko hai hakukuwa na ulinzi kama huu?” Alijuliza swali ambalo alijikuta likimuongezea hamasa ya kazi. Akiwa kwenye kona ya jengo lile alichomoka mbio na kwenda kusimama kwenye mti mmoja ambao ulikuwa usawa wa ngazi fupi ambazo zilikuwa zinaelekea kwenye mlango mkubwa wa kuingilia ndani.
Akatoka kwenye maficho ya mti ule kwa kasi ya mita mia moja hadi kwenye mnazi ambao ulikuwa usawa wa mlango. Aliwasikia walinzi wakiongea kwa sauti za chini. Kizuizi baina yake na hao walinzi kilikuwa ni gari aina ya Toyota Landcruiser ambalo lilikuwa limeegeshwa usawa wa mnazi. Akatulia dakika kadhaa kabla ya kupiga hatua kuelekea mlango wa kuingilia ndani. Akajaribu kufungua, lakini ulikuwa umefungwa kwa funguo. Akachomoa rundo la funguo ambazo zilikuwa mfukoni. Kila alipokuwa anajaribu ufunguo alihakikisha kuwa macho yake ameyaelekeza getini licha ya kuzuiwa na gari. Kijasho chembamba kilikuwa kinamtoka, alihisi kubanwa na pumzi. Mapigo ya moyo wake yalikuwa yanaenda kasi.
Hatimaye moja ya funguo zake ikafanikisha zoezi lile. Akafungua mlango na kuingia ndani taratibu huku akihakikisha anarudisha mlango. Baada ya kufanikiwa hatua hiyo akaanza kutembea taratibu kuelekea ngazi zinazoelekea juu. Akatembea kwa kunyata huku viatu vyake vya mpira vikificha kelele za mchakato wa nyayo zake. Alipofika usawa wa chumba kimoja akasikia sauti za watu waliokuwa wanaongea.
“Sasa utafanyaje mama.”
“Mimi sijui la kufanya mwanangu, wameninyang’anya paspoti wamenilazimisha kuacha kazi na wamenizuia kuongea na mtu yeyote bila ya usimamizi wao.”
“Kwani baba aliwahi kukudokeza wasiwasi wake wa kuuwawa?”
“Hapana isipokuwa aliwahi kunieleza mzozo wake na baadhi ya viongozi ambao walikuwa hawampendi kutokana na kufuatilia na kutaka kuvujisha siri za ufisadi katika wizara mbalimbali.”
“Kwa hiyo waliomuua baba watakuwa mafisadi?”
“Bila shaka na kuna mengi ambayo siwezi kukueleza kwani ni hatari kuyafahamu, sasa ona haya maisha gani tunalazimishwa mpaka kufikia saa 3 tuwe tumelala, ndiyo maana nilikuomba ubaki hukohuko Kyela kwani hapa mambo si mazuri si unaona jumba lote hili nimeachwa peke yangu?”
“Kwanini hakuna hatua zozote za upelelezi zinazoendelea?”
“Sifahamu kama zipo au hazipo, ninachofahamu ni askari ambaye alipewa jukumu hilo, alishambuliwa pale tu alipojaribu kuhojiana na mwandishi wa gazeti la muungwana ambaye alikuwepo eneo la tukio sina uhakika iwapo huyo askari yuko hai au ameshakufa.”
Taisamo alihisi hatari iliyopo kwa kuendelea kusimama pale bila ya kuingia ndani. Akakinyonga kitasa cha mlango wa chumba kile taratibu kisha akaingia ndani kama mtu ambaye hana wasiwasi. Akaufunga ule mlango na kuwageukia mama na mwanae ambao walikuwa wamezama kwenye mazungumzo mazito.
Alikutanisha macho yake na macho yaliyojaa woga ya mke wa marehemu Ole Nunga.
“Samahani mama, sikuwa na namna mzuri ya kuhudhuria kikao chenu zaidi ya hii niliyoitumia.” Alianza kuongea baada ya kuwaona wote wakiwa wanatetemeka kwa woga kisha akaendelea.
“Sikufahamu kuwa upo kwenye wakati mgumu kiasi hiki, pole sana.” Kisha akachomoa kitambulisho chake na kumwonesha yule mama ili kumuondoa hofu.
Yule mama na msichana wote walikuwa wamekaa kitandani. Bado yule mama alionesha kutomuamini Taisamo.
“kwa kifupi, mimi natokea kwenye kitengo maalum cha upelelezi ndani ya jeshi nimekufuatilia kuanzia shuleni kwako Tabata....” Kisha akamueleza yote kuanzia yale maongezi na wale walimu mpaka kule Ofisini.
“Kwa hiyo ulitaka nikusaidie nini?”
“Mama wewe ni sehemu muhimu sana ya upelelezi wangu. Mambo matatu tu nataka kuyafahamu kutoka kwako. Jambo la kwanza ni maadui wa marehemu kama una wafahamu wa ndani nan je ya chama, jambo la pili ningependa kufahamu sababu ya uadui huo mwisho ningependa kufahamu kama kulikuwa na mabadiliko yoyote ambayo marehemu alikuwa nayo kabla ya kifo chake.”
“Mwanangu kabla sijakujibu lolote, kwanza nataka kufahamu umewezaje kuingia humu ndani bila kuzuiwa wakati ulinzi ni mkali?”
“Usihofu mama, najua bado una wasiwasi na mimi, nimeingia kwa njia za panya sijapitia huko getini kama unavyofikiri. Najua unajiuliza jinsi nilivyoweza kupita huko ukutani maana ndio njia pekee iliyobaki, napenda ufahamu kuwa mimi si mwanajeshi tu bali ni mwanajeshi maalum.”
“Lakini si unajua hatari inayoweza kutokea kwa kuongea na wewe mambo mazito kama haya?”
“Ni kweli na nitajitahidi kukulinda kadiri ya uwezo wangu.”
“Utanilinda vipi?”
“kukulinda kwangu ni kwa jambo hili kulifanya kuwa la siri, siwezi kumweleza yeyote kama kuna lolote nimelisikia kutoka kwako mpaka nikishamaliza kazi hii kama kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo sasa naomba unijibu mama.”
“kuhusu maadui alikuwa nao wengi ndani ya chama na si nje ya chama, sababu kubwa za uadui ni mambo mawili tu, Jambo la kwanza ni cheo chake kwani kama unavyofahamu kila mtu mwenye uchu wa madaraka huwa anatamani nafasi kama ile, jambo la pili ni misimamo yake ya kupinga ufisadi, nafikiri unafahamu wazi kuwa chama kimepoteza dira kila mmoja anatamani kuwa kupe badala ya kuona aibu? Kuhusu swali lako la tatu ni kweli marehemu alikuwa na mabadiliko makubwa sana kabla ya kifo chake, mara nyingi alikuwa anaweweseka usingizini. Baadhi ya maneno aliyokuwa anaongea ni..... Sitaki lazima nigombee, demokrasia iko wapi....Yapo mengine mengi ambayo pengine yanatokana na kuufikiria sana uchaguzi. Zaidi ya hapo mwanangu hakuna ninachofahamu kwani marehemu alikuwa msiri sana na hakutaka kunishirikisha katika mambo yake mengi ya kisiasa.” Akatulia na kumkazia Macho Taisamo kama anayetaka kuulizwa swali la ziada.
“Na huyu....” Huku akimnyooshea kidole yule binti.
“Ni binti yangu, mimi na marehemu tumebahatika kupata watoto wawili tu wa kwanza ni huyu Jeska na wa pili ni Zakayo ambaye ameondoka siku chache baada ya mazishi kurudi chuoni Japan.”
“Nilikuwa nakusikia jinsi ulivyokuwa unamsimulia binti yako matukio ya kifo cha baba yake ina maana hakuwepo msibani?”
“Huyu tulichelewa kumpa taarifa kwani naye alikuwa chuoni Uganda, tulisubiri amalize mitihani yake.”
“Pole sana Jesca.” Aliongea huku wakipeana mikono.
“Ahsante.” Alijibu huku akitumia mkono wa kushoto kupangusa machozi ambayo yalianza kutiririka kama matone ya mvua kwenye kioo cha gari.
“Lakini nina wazo mama, naona hapa kama hapakufai nahisi kama uko hatarini. Unaonaje ukiondoka hapa.”
“Mwanangu, nashukuru unaonekana kuwa na mawazo mazuri, hicho ndicho tulichokuwa tunakijadili kabla na mwanangu lakini tatizo tutatokaje hapa ndani? Siruhusiwi kutembea peke yangu pia hata mwanangu naye kazuiwa”
“Nitakusaidieni, hakuna njia zaidi ya kutoroka kwani hatujui hawa jamaa wana dhamira gani.”
“Utatutoaje huko nje wakati kuna askari?”
“Usihofu, kuna ngazi humu ndani?”
“Ipo.”
***
JAMBAZI LAJISALIMISHA POLISI Gazeti moja la kila siku lilikuwa miongoni mwa magazeti kadhaa yaliyotoa taarifa ya tukio hilo la aina yake. Halikuwa jambo la kawaida kwa majambazi kujisalimisha toka muheshimiwa Alphonce Kanyanga atolewe wizara ya mambo ya ndani. Ni waziri ambaye alifanya kazi kwa ustadi mkubwa na kufanikisha majambazi kadhaa kujisalimisha wenyewe polisi huku wakikabidhi silaha zao. Toka aachie wizara hiyo mambo yamekuwa yakienda ovyo na kila kitu kuvurugika.
Leo kwa mara ya kwanza chini ya waziri ambaye si tishio kwa majambazi anatokea jambazi na kujisalimisha mwenyewe polisi. Gazeti moja likaongezea kwa kusema ANA SIRI NZITO AMBAYO ATAITOA MAHAKAMANI. Habari hii ilikuwa gumzo katika jiji hususani baada ya kutokea kwa mauaji kadhaa ambayo hayaeleweki chanzo chake. Kuuwawa kwa Makamu wa raisi, Mwandishi wa habari, daktari na muuguzi kuliamsha hisia za hofu na udadisi kwa wananchi walio wengi. Kujisalimisha kwa jambazi huyo kulizuwa minong’ono kuwa huenda anafahamu siri za mauaji hayo.
***
Simu iliendelea kuita na kumkera Selemani Mahundi mkuu wa gereza la Ukonga ambaye alikuwa amejilaza kwenye sofa pale sebuleni. Hakujisikia kupokea simu hiyo kutokana na uchovu aliokuwa nao.
“We mama Juma, naomba uniletee hiyo simu.”
“Unataka ukate, si useme tu niikate hukuhuku?”
“Niambie kwanza nani anapiga ndipo ukate.”
“Kamishna Mkuu.”
“Nini, ilete haraka.” Usingizi wote na uchovu aliokuwa nao ulikimbia kama mtu aliyesikia simba ananguruma nje ya nyumba yake.
“Halow afande shikamoo.”
“Marahaba Mahundi, nafikiri una taarifa juu ya ujio wa mtuhumiwa muhimu sana kwenye gereza lako.”
“Ndiyo mkuu, amewasili kama nusu saa iliyopita tumeshampokea na tumetekeleza majukumu yote kama ulivyohitaji.”
“Ok, sasa huyo ni mtu muhimu sana na tumepokea maagizo kutoka wizarani kuwa asihojiwe chochote na yeyote, hakikisha kuwa anakaa sehemu ya peke yake asipate fursa hata ya kuongea na wafungwa au mahabusu wenzake.”
“Nimekuelewa mkuu, vipi kuhusu mwanasheria kama atahitaji kuwasiliana nae?”
“Hilo pia limezuiwa hiyo ni special order kutoka makao makuu.”
“Sawa afande nitatekeleza.”
Usingizi wote ulikuwa umetoweka na sasa akaamua kuhamishia macho yake kwenye runinga. Kipindi alichokuwa anaangalia kilikuwa ni cha uchambuzi wa magazeti yanayotoka jioni.
“Familia ya marehemu Ole Nunga aliyekuwa makamu wa raisi yatoweka.”
Alisikika mtangazaji huyo na kumfanya mkuu huyo wa gereza kupoteza kabisa uchovu uliosalia. Akaamua kukaa vema na kuisikiliza taarifa hiyo.
***
Akiwa ndani ya maficho mapya katika nyumba ya kulala wageni inayojulikana kama kusini guest house iliyoko eneo la Temeke mwisho, ndio kwanza alikuwa anamaliza kula ugali na nyama choma ambavyo aliviagiza kutoka mgahawa ulioko nje. Akashushia na juisi baridi ya ukwaju. Hakujisikia kunywa kilevi chochote katika wakati huo mgumu ambao hakujua nguvu ya kumtafuta ni kubwa kiasi gani.
Saa 5.30 simu ya Taisamo ilianza kuita.
“Hallow nani mwenzangu.”
“Teacher Suzzy hapa, mbona huonekani Taisamo uko wapi?”
“Niko safarini nitarudi baada ya wiki mbili.”
“kuna wageni wengi sana huwa wanakuja kukuulizia hapa nyumbani.”
“Huwa wanajitambulisha.”
“Kuna mmoja tu ndiye alijitambulisha, anasema anaitwa Rose.”
“Yaani huyo tu ndiye umemkumbuka haraka?”
“Kwa sababu ni mwanamke halafu alisema mnafanya kazi ofisi moja, sasa nilikuwa nashangaa mtu mnayefanya naye kazi ofisi moja anashindwaje kujua taarifa za safari yako.”
“Suzy, tunaweza kuonana?”
“we si uko safarini tutaonana vipi?”
“Kesho nitakuja Dar mara moja kwa ajili yako tu.”
“kuna nini?”
“Nafikiri tutaongea zaidi tutakapoonana.”
“Nafikiri kama ni maongezi tu basi tuongee kwenye simu.”
“Hapana Suzy, unajua simu inawafaa zaidi watu waoga wasiojiamini.”
“Sikuelewi unamaanisha nini?”
“kuna jambo nataka kukueleza lakini sitopenda kuliongea kwenye simu kwani nachelea kuingia katika kundi la wanaume waoga.”
“Kama jambo lipi?”
“Dah, we mwanamke mbona unachimba sana.”
“We sema tu, mi nitajua ni mwanaume jasiri ambaye umelazimika kutokana na sababu ambazo haziwezi kuzuilika.”
“Nakupenda.”
“Mh, halafu Rose!”
“Huyo Rose ni mfanyakazi mwenzangu na hata hivyo simfahamu.”
“He, Unanishangaza sasa Rose amekuja hapa anaonesha dalili zote za kukupenda we unasema humfahamu unashindwa vipi kumfahamu mfanyakazi mwenzio?’
“Yeye ni mwandishi wa makala za uchumi pale ofisini, na ofisi yetu ni kubwa sana wengine huwa hatufahamiani kama huyo Rose namfahamu kwa kusoma tu makala zake za uchumi.”
“Lakini yeye anakufahamu na anakupenda.”
“Umejuaje?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mimi ni mwanamke naomba uniamini Rose anakupenda.”
“Mimi nimekupenda wewe naomba kesho tuonane.”
“Niko tayari kuonana na wewe lakini kwa swala la mapenzi nakushauri uwe na Rose.”
Baada ya kukata simu Taisamo akazirudisha fikra zake kwa Rose. Ni nani huyu Rose na kwanini bado anamfuatilia? Kwanini Suzy yuko tayari kukutana na mimi wakati anaonesha kutokuwa tayari? Alianza kuingiwa na wasiwasi juu ya usalama wake katika mikono ya Suzy hasa alipofikiria picha alizopigwa na dokta na jinsi zilivyoweza kuingia ndani.
Mawazo mengi yaliyokuwa yamesababishwa na matatizo mazito anayokabiliana nayo kwenye kazi yalikatishwa na usingizi mzito uliomchukua ghafla. Usingizi huo ulitawaliwa na ndoto nyingi za kutisha, zikitawaliwa na mauaji na damu ambayo aliishuhudia. Aliziona maiti za nesi Belinda na msichana wake wa kazi zikiwa zinavuja damu mbichi huku akiwa amesimama nyuma yake, ghafla akatokea mwanamke ambaye alijitambulisha kwa jina la Rose na kumfahamisha kuwa amekuja kumsaidia kumpata muuaji, akapeana naye mkono kwa furaha lakini ghafla yule mwanamke akachomoa bastola na kumuelekezea Taisamo.
“Lazima nikuue mbwa wewe.” Alifoka yule mwanamke.
Akashtuka kutoka usingizini huku jasho likimvuja. Alihema kwa nguvu kutokana na hofu kubwa.
“Ina maana Rose ananisaka aniue?” Alijiuliza huku akiwa amekaa kitandani. Mawazo hayo hayakuchukua muda mrefu kwani punde yalikatishwa na mlio wa simu iliyokuwa chini ya mto.
“Nani tena.” Alilalamika huku akinyoosha mkono wake kivivu vivu.
“Sikiliza Alex, hapa ni makao makuu ya Jeshi la wananchi. Unahitajika ufike hapa sasa hivi kabla jeshi halijaamua kutumia nguvu kukutafuta, hatua uliyofikia ni mbaya zaidi kwani umefanikiwa kuwateka mke wa makamu wa Raisi na binti yake na haifahamiki umewaficha wapi, mbaya zaidi ni kwamba hutafutwi na wapelelezi wa jeshi tu hata wa usalama wa Taifa na wenzetu wa CID pia wanakutafuta ingawa tofauti hapa ni kwamba sisi tunajua tunamtafuta nani lakini wenzetu hawamjui wanayemtafuta.” Akakata simu na kuirudisha pale alipoitoa.
Dakika hiyohiyo usingizi wote ulitoweka, maana alipata simu ya mtu ambaye alikuwa ‘sirias’ kuliko alivyomzoea, mtu asiyemfahamu, mtu anayemwendesha kama rimoti Rose ni nani huyu Rose?
Aliinuka kitandani na kuvaa nguo zake haraka haraka, baada ya kujiona yuko sawa akatoka na kwenda kujichanganya sehemu ambayo ilikuwa na vinywa ji huku watu wachache wakiwa wamekusanyika hapo. Kulikuwa na runinga moja ambayo macho ya watazamaji wachache yalikuwa yameelekezwa hapo huku wale wachache wengine wakiendelea kunywa bia.
“Naona umeshindwa kulala!” Alisikika muhudumu wa nyumba ile ya kulala wageni ambaye alihudumia wateja wa vinywaji pia.
“Aah, kitanda kinachosha, nipatie maji tafadhali yasiwe ya baridi.”
Aliendelea kuikodolea macho runinga ile huku kiukweli akiwa haoni kabisa kinachoendelea.
Ghafla, kama aliyezinduka kutoka usingizini akayaelekeza macho yake kwenye Runinga huku akiwa na umakini unaotakiwa.
Ni taarifa ambazo zilikuwa zinasomwa kwenye ile runinga.
“.... Kwa taarifa tulizonazo ni kwamba hadi hivi sasa Familia hiyo ya marehemu Ole Nunga haifahamiki iliko na wala watekaji wake, sambamba na tukio hilo jambazi aliyeamua kujisalimisha bado yuko katika mikono ya dola na atafikishwa mahakamani baada ya kukamilika mahojiano, habari kamili mtaletewa kesho baada ya kupatikana taarifa ya kamanda wa polisi ambaye ataongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa habari na maelezo.” Ilimaliza sehemu ya taarifa hiyo ambayo ilikuwa inasomwa katika moja.
Baada ya taarifa hiyo aliamua kurudi chumbani kwake huku akisahau kuchukua maji yake ambayo hakuyanywa kabisa. Akili yake ilikuwa imechoka kutokana na kuwaza kupita kiasi. Akafunga mlango na kwenda kujitupa kitandani, hakukumbuka hata kuvua nguo.
***
Msichana mrembo alitembea kwa mwendo wa kinyonga kuelekea kwenye moja ya viti vilivyokuwa wazi katika eneo hilo la hoteli. Hakuonekana kuwa na haraka licha ya kuangaza macho yake huku na huko kwa nia ya kumtafuta mwenyeji wake. Alikuwa amevaa gauni refu la rangi ya dhambarau lenye mng’ao lakini lenye mpasuo wa wastani kwa mbele ambao ulifika usawa wa magotini, ile sehemu ulipokomea mpasuo ilikuwa na ua zuri lenye rangi za bluu bahari na zambarau. Akiwa na kimo cha wastani alikuwa na umbo la kuvutia ambalo lilimfanya awe kivutio kwa jicho la kiume ambalo lingetua kwake.
Wanaume wachache waliokuwa ndani ya ukumbi huo wa vinywaji katika hoteli ya Rovena walishindwa kujizuia kumtazama binti yule, wengine wakashindwa kuzuia hisia zao kwa kumkazia macho yao kwa namna ambayo ingefanya yeyote aliyekuja na mkewe apigwe kofi la uso au shavu.
“Niko hapa malaika.” Sauti ilimshitua.
“Ooh, Jirani.”
“Karibu ukae teacher Suzy.”
“Ahsante.”
“Umependeza saaana.”
“Ahsante, wewe mbona uko hivyo?”
“Nikoje?” Aliuliza Taisamo.
“Ni siku chache tumepoteana lakini unaonekana umekuwa mnyonge na pia umepungua kama ulikuwa unaumwa vile, vipi kuna tatizo?”
“Agiza kwanza unachohitaji Suzy kisha tutaongea.”
“Nahitaji kinywaji chochote ambacho hakina kilevi kama Vitamalt, bavaria chochte kile.”
“Kwanini?”
“Situmii kilevi cha aina yoyote.”
“Ok. Hakijaharibika kitu, chakula?”
“Chips kuku.”
“Ok.”
Wakati wanaendelea kujadiliana muhudumu wa kike ambaye alikuwa nyuma yao alisimama kwa utulivu huku akisubiri wamalize majadiliano yao. Baada ya mjadala huo mfupi wakaagiza vitu walivyohitaji.
“Enhe, tumeshaagiza naomba unijibu maswali yangu.”
“Nafikiri ni ugumu tu wa maisha.”
“Alex Taisamo, kwanini unanifanya kama mtoto mdogo?”
“He, nani kakutajia jina langu lote?”
“Ndio maana nakuambia usinifanye mtoto mdogo, nimekuuliza makusudi hayo maswali ili kama una tatizo ninaloweza kukusaidia nifanye hivyo, niambie ukweli una tatizo gani?”
“Suzy, u mwanamke mwerevu sana nazidi kukupenda lakini nataka kujua kwanini umekuwa na hisia hizo juu yangu?”
“Siku ambayo ulikuwa unaniaga pale nyumbani ulikuwa na kila dalili ya mtu aliyechanganywa na jambo, macho yako hayakuwa na utulivu pia ulikuwa na tabasamu bandia. Si hivyo tu toka umeondoka umekuwa unafuatwa na kuuliziwa mara kwa mara na watu wenye kila dalili za ukachero, hivi ninavyokuambia kuna taarifa ambazo nimetonywa na mmoja wa waliokuwa wanakutafuta kuwa umemteka mke na mtoto wa marehemu muheshimiwa Ole Nunga. Ukweli toka hapo nimekuwa nakuogopa lakini kuna kitu kama siamini vizuri hivi.... ndio maana nataka kutoka kwako maelezo ya kina ili niweze kukusaidia kama inawezekana kwani pale ndani tumeshapewa namba za simu ambazo kama utaonekana tunatakiwa kutoa taarifa mara moja.” Akatulia na kumkazia macho Alex Taisamo ambaye alikuwa mtulivu na hakuruhusu mshtuko muda wote aliokuwa anapewa taarifa hiyo.
“Kitu gani kinakufanya usiwaamini hao makachero?”
“Nasikia hiyo nyumba ya makamu wa raisi ina ulinzi mkali hasa baada ya kifo cha Muheshimiwa, kwa jinsi ninavyokufahamu ingawa ni muda mfupi toka tufahamiane bado siamini kama unaweza kufanya kitendo kama hicho.”
“Ok, nimekuelewa Suzan oh sorry suzy”
“hakuna shida umepatia tu mi naitwa Suzana lakini Suzy ndo limezoeleka zaidi.”
“Vema. Ukweli ni kwamba ninatafutwa, tena sana. Msaada ninaoutaka kutoka kwako ni taarifa za mtu yeyote ambaye atakuja kuniulizia kama......”
“Kwa hiyo ulichoniitia hapa si mapenzi ila ni hilo la kutaka kujua nani anakutafuta?”
“Sikiliza Suzan, hata angekuwa nani lazima angebadilisha mada hivi unafikiri kutafutwa ni jambo zuri?”
“Kwa hiyo hatutajadili tena kuhusu mapenzi yetu?”
“Suzan, nashindwa kukuelewa.”
“Kivipi?”
“Bado hunionei huruma hata kwa hayo matatizo yanayonikabili?”
“Nafikiri hatukukutana hapa kuzungumzia hayo matatizo yako, au ndio ulitumia ujanja huu wa kuniita hapa ili ujue kinachoendelea nyumbani na si mapenzi kama ulivyonieleza? Kama ni hivyo basi nieleze kwa kina bila kutafuna maneno chochote kinachokuhusu juu ya sakata hili vinginevyo utanifanya nikufikirie vibaya.”
“Suzy, ni wewe kweli?”
“Nimekuwaje?”
“Sikuelewi, ghafla umekuwa mkali hutaki mjadala uende kidiplomasia.”
“ni wewe ndio umeanza kuharibu hiyo unayoita demokrasia, umekuwa mwongo sana na hata kama nitakubali ombi lako la kuwa mpenzi wako sijui itakuwaje…. Kumbuka ulinifahamisha kuwa wewe ni mwandishi wa habari pia ulinieleza kuwa uko wapi sijui safarini lakini ninachokiona hapa ni uongo mkubwa, wewe ni mwanajeshi unafahamika hivyo na kila mmoja pale ndani kwanini ulitaka kuniongopea?”
“Mhhhhh.” Alishusha pumzi na kuyaelekeza macho yake juu, ama kwa hakika lilikuwa shambulizi la ghafla sana.
“Suzana.”
“Abee.”
“Naomba kwa leo tuachane, najua unautaka ukweli ambao unaweza kukugharimu.”
“Naomba maelezo ya kina tafadhali.”
“tuonane baada ya mwezi mmoja.”
Alisikika Taisamo huku akiitazama bili yao ambayo ililetwa muda mfupi uliopita.
***
Alifumbua macho yake kabla ya kuyafumba tena kwa haraka kutokana na mwanga mkali ambao ulimpiga moja kwa moja kwenye macho yake. Alihisi kichwa chake kuwa kizito kuliko kawaida. Uwezo wake wa ufahamu ulikuwa mdogo lakini huku ukipata nguvu kadri muda ulivyokuwa unasonga mbele.
Sasa fahamu zake zilianza kupata nguvu, alijijua kuwa yeye ni Inspekta, sasa hapo yuko wapi? Lilikuwa ni swali gumu ambalo liliongeza nguvu ya fahamu yake. Alijikuta akianza kuvuta kumbukumbu ya matukio. Alikumbuka jinsi alivyomuaga mwanawe mtoto wa marehemu mama yake mdogo kuwa anaelekea kazini…. Kisha…
“Ah, kisha nini?” Alijikuta akishikwa na hasira zaidi kwa kushindwa kubaini kilichoendelea baada ya hapo.
Ghafla alijikuta akipatwa na mshtuko baada ya kukumbuka kuwa amepewa jukumu zito la kupeleleza kifo cha makamu wa Rais.
“Hivi nimefikia wapiiii…” swali lilipita kichwani mwake na kumfanya aanze kurejewa na kumbukumbu.
“John Oscar… aah, ameuwawa halafu nikashambuliwa… no it means I’m…. no niko hai…. Kwa hiyo hapa ni hospitali? Na vipi kuhusu kamishna ambaye alikuwa ananipigia simu? Mh …..” Alijikuta akipatwa na wazo jipya baada ya kumkumbuka Kamishna.
Aliinuka na kukaa kitandani huku akianza kuyasanifu mazingira ya chumba kile. Mbele ya kitanda chake kulikuwa na kikabati kidogo chenye magurudumu ambacho hakikuwa na chochote zaidi ya bomba la sindano ambalo lilikuwa kwenye kifungashio chake. Mbele zaidi ya nyuma ya kile kikabati kidogo kulikuwa na kabati kubwa la chuma ambalo lilikuwa na rangi ya kijani mpauko kabati hilo lilikuwa na ‘code number’ ambazo haraka Inspekta alitambua kuwa yupo hospitali ya taifa ya Muhimbili Taasisi ya mifupa MOI.
Sasa hakuwa na shaka kuwa yupo hospitali baada ya kipigo cha kushtukiza ambacho alikipata alipoenda kwa John Oscar ambayea alimkuta akiwa ameuwawa. Ni wazi kuwa muuaji hakutegemea ujio wa ghafla wa Inspekta, lakini kwa nini Kamishna alikuwa kama amemchelewesha?
“Ooh, umeamka mama. Shikamoo!” Muuguzi ambaye aliingia ndani muda huo alimshitua Inspekta kutoka kwenye kina kirefu cha mawazo.
Inspekta alimwangalia yule Muuguzi kwa macho ya mduwao huku akishindwa kujibu salamu yake.
“Nakusalimia mama.”
“Marahaba, nani kanileta hapa hospitali?”
“Umeletwa na askari wenzio.”
“Wako wapi kwa sasa?”
“Huko nje wako wawili ambao wapo zamu, ikifika asubuhi anakuja mmoja tu ambaye anaondoka jioni.”
“Eh, ina maana huu ni usiku?”
“Ndiyo mama ni saa nane na robo sasa.”
“Mungu wangu ina maana nimelala hapa kwa masaa zaidi ya kumi nambili?”
“Pole sana mama lakini hii ni siku ya tatu sasa uko hapa hospitali.”
“What?”
“Ndivyo ilivyo lakini tunamshukuru Mungu kwani umekuwa salama.”
“Mh.”
“Kwa sasa inabidi nikuchome sindano mbili kama nilivyoagizwa na daktari.”
“Ok, fanya kazi yako binti”
Akafungua lile kabati kubwa na kutoa chupa kadhaa za dawa, kisha akamgeukia Inspekta.
“Hii moja ni ya usingizi ambayo itakuchukua masaa sita kutoka sasa, sasa sijui nimfahamishe yule mkubwa wenu kwanza au… maana ni usiku mwingi.”
“Mkubwa yupi ina maana kuna mtu anafuatilia taarifa zangu?”
“Ndiyo, alijitambulisha hapa kuwa ni kamishna nani… sijui nani vileee.. ah nimemsahau kidogo lakini aliniambia kuwa nimfahamishe mara tu utakaporejewa na fahamu.”
“Yukoje?”
“Ni mrefu mweusi.”
“What? Alikupa namba yake ya simu au alikuambia utumie ya ofisini? alikuwa na sare za kazi?” Maswali ya haraka yalimtoka Inspekta.
“Namba alinipa tena ni ya simu yake ya kiganjani, hakuvaa sare za kazi alikuwa amevaa suti nyeusi na kofia nyeusi ya duara kama zile wanazovaa waendesha farasi kwenye Tv.”
“Sikiliza nesi, usithubutu kumfahamisha kuwa nimezinduka kama inawezekana hata hiyo sindano ya usingizi usinichome.”
“Hapana, hii ya usingizi lazima nikuchome kama alivyoagiza daktari.”
“Sawa lakini kwanza niandikie hiyo namba ya huyo mtu kabla ya kunichoma sindano sawa?”
“Sawa nimekuelewa mama.”
Baada ya kuandika akamgeukia Inspekta Tunu.
“Haya mama kaa vizuri nikuchome sindano.”
“Hapana, hutonichoma sindano, siko tayari kuharakishiwa kifo namna hiyo.”
“Ni maelezo ya dokta mama.”
“Sikiliza nesi.. njoo nikudokeze kitu sikioni….” Nesi akasogea nae akamnong’oneza.
***
James Makabi alishangazwa na mienendo ya pale gerezani, tofauti na mara ya kwanza ambapo alikuwa mfungwa alishangaa kuona akiwa chini ya uangalizi mkali tena la kushangaza zaidi ni baada ya kugundua kuwa hata baadhi ya askari magereza walikuwa wanamwogopa. Kwake halikuwa jambo la kawaida.
Kwa upande mwingine alianza kujilaumu kwa kitendo chake cha kujisalimisha kwenye mikono hiyo ya sheria ambayo kiasi fulani alianza kuitilia mashaka. Kama ni ujambazi mbona kuna watuhumiwa na wafungwa wengi mle gerezani lakini kwa nini hawakupewa ulinzi mkali kama ule?
Hofu ya maisha yake kuwa yako hatarini ikazidi kumtawala. Akahisi kuwa njama za Mjomba Masharubu zitakuwa zinaendelea na sasa atakuwa amehamishia huko gerezani. Kama alikuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kiasi cha kuweza kutolewa gerezani kwa msamaha wa Raisi basi anao uwezo mkubwa wa kushawishi hata akauwawa hukohuko gerezani. Wazo hilo lilipopita kichwani mwake akajikuta akijiuliza swali la ghafla.
Huyu mjomba ni nani hasa?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Swali hilo lilianza kumtesa na kumtia mashaka kwani alihisi kuwa Mjomba ni mtu mzito ambaye nyuma yake kuna watu wazito zaidi yake.
Lakini kwanini wamemuua makamu wa Raisi? Kama ni uzito naye si alikuwa mzito mwenzao?
Akiwa kwenye fikra hizo mara mlango wa ule wa chuma wa chumba alichopo ukafunguliwa. Askari mweusi mkakamavu akamkodolea macho kabla ya kumsukumia bakuli la chuma lililojaa uji.
“samahani afande.” Alianza Makabi huku akimkodolea macho askari yule ambaye alionekana kama mwenye haraka.
“Naomba unisaidie kitu kimoja tu.”
“Nikusaidie nini ongea fasta usije kunisababishia majanga hapa!”
“Ahsante afandea angalau wewe umeweza kunisikiliza”
“Punguza ngonjera wewe, sema shida yako si unajua wewe ni mtuhumiwa ghali kuliko watuhumiwa wote kuwahi kutokea.”
“Mtuhumiqwa ghali?” Lilipita swali kichwani mwake.
“Nahitaji kuonana na wakili sijui utanisaidiaje!”
“Wakili?”
“Ndiyo afande.”
Akageuza macho huku na kule kabla hajaendelea kumsaili mtuhumiwa.
“Suala lako limefungwa na wakuu kutokana na uzito wa tuhuma zako.”
“Tuhuma zipi?”
“Mimi sizijui kama hutajali si vibaya ukinidokeza.”
Koplo Rashidi Chande alijikuta akiuliza swali ambalo siku zote alijiuliza yeye mwenyewe tu huku akikosa jibu. Ni zipi tuhuma za huyu mtu? Kwanini wakuu walizuia hata kuongea naye?
“Afande ni mambo mazito, nakudokeza wewe kama wewe na kwa kuwa ni mtu wa kwanza kunisikiliza ni matumaini yangu kuwa utakuwa msiri na kunisitiri kwa jambo hili ambalo limegubikwa na usiri mkubwa”
Akamsimulia kwa ufupi mkasa wake uliomkuta mpaka kufikia pale huku akimalizia na tukio la makabidhiano ya fedha jinsi lilivyogeuka mtego wa panya kwa kuuwawawa watu ambao hawakuwamo.
Koplo Rashidi akajikuta akitetemeka na kijasho chembamba kikimtoka, midomo ilimkauka akajikuta akishindwa kuongea. Alimkazia macho Makabi lakini ukweli alikuwa hamuoni kabisa fikra zake zilikuwa kilomita kadhaa nje ya jengo. Semburi Makwanga jina hilo ndilo lililomjia haraka huku moyo wake ukienda mbio. Alimkumbuka rafiki yake huyo ambaye ni mwandishi wa habari, mara nyingi alikuwa akimpatia taarifa mbalimbali za matukio yanayojiri gerezani naye akimpatia kile kinachoitwa hela ya soda. Tabasamu la hofu likatanda usoni pake huku akiondoka eneo lile bila hata kumuaga Makabi.
“Kuumbe… mh!” Alijisemea koplo huku akimaliza na mguno hafifu, pesa aliitamani lakini bado hofu ilimtawala kwani alijua wazi kuwa anacheza na jambo ambalo linaweza kuitikisa nchi.. Licha ya hatari ya jambo hilo kwa nchi bado ilikuwa ni taarifa nzuri kwa mwandishi wa habari za uchunguzi kwani ingempaisha na kumjengea jina uraiani licha ya heshima ambayo angeipata kazizini kwa wakuu wake wakazi. Si hivyo tu ni habari ambayo ingelijenga gazeti na kulifanya lipendwe hivyo kuliongezea kipato.
Aliinua mkono wake wa kushoto na kuikazia macho saa yake ya mkononi aina ya Seiko5, zilikuwa zimebaki dakika 15 atoke kazini lakini aliona kama yamebaki masaa kumi kutokana na hamu yake ya kukutana na Semburi.
“Hii itavunja rekodi, jamaa lazima wanitoe mshiko wa nguvu.” Aliongea kwa sauti ya chini huku akielekea upande wenye kibanda kidogo cha kukabidhiana kazi.
*****
Eneo Fulani la jiji la Dar es salaam, Alex Taisamo alitembea kwa kasi huku akitazama huku na huko kuhakikisha iwapo yuko salama. Alilifikia lango kubwa linaloingia kwenye moja ya makampuni makubwa ya uuzaji wa magari.
“Habari yako ndugu.”
“Nzuri, sijui nikusaidie nini?”
“Naomba kufika ofisi ya manunuzi ya magari.”
“Ooh, karibu sana tena kuna mzigo umeingia jana tu!”
“Ok, Ahsante wacha niwahi maana hii ni saa nane muda wa kufunga unakaribia.”
“Hapana mkuu, hapa huwa tunafunga saa kumi na mbili jioni.”
“Sawa.” Alijibu huku akiwa ameshapiga hatua kadhaa kutoka eneo lile.
Hakupata shida kuingia ofisi aliyohitaji ndani ya jengo lile kubwa ambalo lilizungukwa na ukuta mrefu wa tofali za saruji, kila mlango alioutazama ulikuwa na maandishi mlangoni. KITENGO CHA MAUZO.
“Habari za kazi.”
Alisalimia huku akivuta kiti ambacho kilielekeana na mkuu wa kitengo cha mauzo ambaye alikuwa ameweka kibao kilichokuwa kinamnadi mbele yake huku kikiwa na jina lake ambalo lilisomeka kwa kifupi Mwita.M.B.
“Salama kabisa, karibu sana.”
“Ahsante.”
“Sijui naweza kukusaidia?”
“Bila shaka, nahitaji kupata kumbukumbu ya uuzaji wa magari aina ya Nissan Patrol”
“Sidhani kama naweza kukusaidia kwa hilo kwa sababu hizo ni taarifa za kampuni na hatupaswi kuzitoa hovyo.”
“Ni vizuri tukitambuana naitwa Luteni Taisamo.” Akachomoa kitambulisho chake na kumkabidhi yule jamaa.
“Ndiyo Luteni, sijaona uhusiano wa kazi yako na hivyo vitu unavyovihitaji hivyo nashindwa kushawishika.”
“Ni uelewa mdogo wa mambo ya ulinzi na usalama wan chi yetu, unaonaje nikikuhusisha wewe na kifo cha makamu wa Raisi muheshimiwa Nunga maana gari lililotumika ni Nissan Petrol ambalo limenunuliwa katika ofisi yako?”
Lilikuwa shambulizi la ghafla kwa mkuu yule wa kitengo cha mauzo abalo lilimfanya ageuke mnyonge ghafla.
“Sasa utanihusisha vipi na kitu ambacho kimeuzwa na kimetumiwa na mtu mwingine huko?”
“Kukataa kwako kutoa ushirikiano ni moja ya dalili nzuri kabisa ya kuwa unahusika na unafahamu mpango mzima.”
“Isiwe tabu mkuu kama jambo lenyewe liko hivyo ngoja nikuangalizie kile unachohitaji.”
“Nitashukuru kwa ushirikiano wako.”
“Sijui unahitaji kumbukumbu ya mwaka mzima?”
“Hapana.” Akainua kichwa juu huku akifumba macho kwa kuvuta kumbukumbu ya kile alichohitaji.
“Nahitaji kumbukumbu ya miezi miwili iliyopita.”
“Unahisi hiyo gari ilikuwa mpya?”
“Ndivyo ilivyo na ingekuwa ni vigumu gari kutembea bila kusajiliwa zaidi ya muda huo bila kuzusha hoja za wazi kwa wananchi.”
“Ok, ngoja niiprint maana ninayo humu kwenye kompyuta.” Aliongea huku akijiuma uma midomo.
Dakika chache baadae ile taarifa aliyoihitaji ilikuwa mezani, akachukua mashine maalumu ya kubania pini.
“Ina maana huna secretary?”
“Yuko likizo.”
Taisamo akautumia muda ule mfupi kusoma taarifa ile aliyopewa kisha ghafla akamgeukia yule mkuu.
“Naomba kujua namba hii ya gari ilinunuliwa na nani?”
“Nakala huwa zinabaki kwenye kitabu cha risiti ambacho kinakaa kwa mkaguzi wa ndani wa hesabu za kampuni.”
“Nakiomba hicho kitabu, nataka kujua gari lenye namba ya injini hii lilinunuliwa na nani.”
“Sawa ngoja nikuangalizie huko kwa mkaguzi.”
****
Saa 7.30 usiku mlango wa chumba kidogo ambacho alifungiwa James Makabi ukafunguliwa, askari magereza wawili wenye sare zenye nembo za sajenti kila mmoja walikuwa mbele yake.
“Tufuate.” Aliamrisha mmoja ambaye alikuwa na macho mekundu na sura ya ukatili kuliko mwenzake.
Akainuka pale kwenye kirago huku moyo ukimwenda mbio na kuanza kuwafuata. Kilichomfanya awe mwepesi kuwafuata ni mazungumzo aliyoyafanya na koplo Rashidi, akili yake ilimtuma kuwa huenda mwanasheria ambaye aliomba kuonana nae amewasili, lakini kwanini iwe usiku wa manane? Swali hilo kidogo lilimtatiza lakini akaendelea kufuata bila kuuliza. Moyo ulizidi kwenda mbio alipoona wanapita kwenye lango la gereza bila kuulizwa na askari wanne ambao walikuwa zamu.
Gari ndogo la kizamani aina ya Toyota Corolla lilikuwa limepaki huku ndani kukiwa na dereva ambaye alikuwa ameegemea usukani bila shaka akiwasubiri. Dereva hakuwa na sare kama wale wengine, alikuwa amevaa shati jeusi la mikono mifupi huku akiwa amechomeka airphone kwenye sikio la upande wa kulia.
“Vipi shwari?”
“Poa kaka.” Alijibu mmoja huku akimuelekeza James kukaa siti ya katikati.
Gari iliondoka taratibu huku kukiwa hakuna mazungumzo yoyote ndani ya gari. Makabi aliitafsiri hali hiyo kuwa ni ya hatari kwake.
Kutokana na giza Makabi alishindwa kuelewa ni wapi walikuwa wanaelekea. Dakika kumi na tano baadae alihisi wakielekea eneo ambalo lilikuwa nje ya mji, wakaacha barabara kubwa na kuingia vichochoroni ambako kulikuwa na nyumba mojamoja tena zikiwa mbalimbali. Baada ya kama dakika kumi wakaifikia nyumba moja ambayo ilikuwa imezungushiwa seng’enge, gari ikapiga honi kama mara tatu kisha lango likafunguliwa. Mwanga wa rangi nyekundu ulikuwa unatoka ndani.
Bado Makabi alishindwa kutafsiri maana ya tukio lile, akaendelea kuwa kimya akisubiri kitakachojiri. Baadae wakatoka watu wawili wenye miili iliyojengeka vema kimazoezi wakiwa wamevaa fulana zilizopanguliwa makusudi huku zikiacha nje mabega yao, zilikuwa na nembo ya fuvu la kichwa cha mtu kifuani. Wote wawili walikuwa wamenyoa kipara huku mmoja akiwa amefuga ndevu ambazo zilichongoka na kufanana na za mchezaji mmoja ambaye anachezea klabu kongwe ya ligi kuu ya Tanzania, hata kwa sura alifanana na mchezaji huyo huyu alizidi kwa umbo kwani alikuwa katika namna ambayo watu mtaani wangemwita ‘Baunsa’.
“Teremka.” Aliamrisha askari wa upande wa kushoto huku akiteremka kumpisha makabi, akarudi kwenye gari na kumwacha Makabi chini ya wale mabaunsa wawili ambao walimbeba kindakindaki kumeleka ndani. Akapelekwa kwenye chumba kimoja ambacho kilikuwa cha mwisho kabisa katika korido ya nyumba ile.
Ulipofunguliwa mlango ndipo alipopatwa na mshtuko wa mwaka, hakuamini macho yake kwa kile alichokiona.
Mpenzi wake Tamasha alikuwa amefungwa kwenye kiti cha chuma ambacho kilikuwa kimechimbiwa ardhini na kujengewa vizuri kwa zege, alikuwa anaonekana wazi kujeruhiwa kwa vipigo, alipoangalia vizuri kile kiti kilikuwa kimeunganishwa na waya uliotoka kwenye swichi ya umeme. Mdomo wa Tamasha ulikuwa umevimba kwa kipigo ambacho Makabi alishindwa kukielewa kilikuwa kinatokana na kosa lipi, alipomuangalia vizuria akagundua kuwa hata jicho la kulia nalo lilikuwa limevimba na kufanya wekundu. Alihisi hasira na kutaka kufanya makeke lakini alipoangalia upande wake wa kushoto na kuwaona wale Mabaunsa akanywea. Alipoangalia kona nyingine akamuona mwanaume ambaye alikuwa amefungwa kamba kama mpenzi wake. Tofauti na mpenzi wake huyo jamaa alikuwa amefungwa kwa umakini zaidi huku akionekana kupata kipigo kikali zaidi ya kile cha mpenzi wake.
“Hebu kaa hapo. Nawe kama hutatoa ushirikiano yatakukuta kama yaliyowakuta hao Mbwa wenzako.” Alisema huku akimnyooshe kiti ambacho kilikuwa kimeelekea kwenye dirisha kubwa. Akakaa na kulielekea dirisha lile ambalo lilikuwa linaonesha mandhari ya nje. Aliweza kuuona vema uzio wa seng’enge ambao ulifuatiwa na miti na vichaka ambavyo vilileta ugumu kidogo kulifahamu eneo lile. Hakukuwa na dalili ya nyumba karibu, alihisi kuwa zile walizozipita wakiwa kwenye gari ambazo zilikuwa takribani kilometa nne au tano kutoka pale zilikuwa nyumba za mwisho na ile ilikuwa eneo la peke yake kabisa.
“Kaa, unashangaa nini?” Ilikuwa ni amri kali iliyofuatiwa na kofi kali la shavu ambalo lilimfanya aone vitu kama nyotanyota hivi. Hakutaka kufanya ubishi kwani alielewa kuwa ubishi wowote ungemsababishia kipigo kikali kama wale aliowakuta, akatulia kama maji ya mtungini akisubiri kuhojiwa.
“Tunataka kujua nani na nani wanafahamu tukio lako na Mjomba Masharubu.”
“Mpenzi wangu Tamasha ambaye ni huyo hapo kwenye kiti na askari magereza ambaye alikuwa zamu juzi mchana kule magereza.”
“Vizuri unaonesha ushirikiano nzuri, ila napenda kukufahamisha kuwa huyo askari anaitwa Koplo Rashidi na kwa sasa ameshatangulia kuzimu kama ulivyomtanguliza jembe letu moyo.” Aliongea jamaa wa mzuzu huku akizunguka zunguka kwa namna ya kutakabari.
“Pili nataka kufahamu picha ya mjomba Masharubu ambayo ilikuwa nayo kwenye simu kama bado ipo au uliifuta.” Makabi akatulia kidogo na kukumbuka jinsi alivyomuongopea Masharubu kuwa alimpiga Picha, akatabasamu kimoyomoyo kwani alifahamu wazi kuwa alimkamata pabaya Masharubu huku akitambua wazi kuwa hiyo ilikuwa ni fursa nzuri kwake kuchelewesha kifo au kipigo.
“Ile picha bado ipo kwenye simu nyumbani kwangu.”
“Usitufanye watoto wadogo, simu ulimwachia huyo mbwa wako na tumeipekua hatujaona picha.” Aliongea baunsa wa ndevu huku kauli yake hiyo ikisindikizwa na teke kali lililomsukuma sakafuni huku akifuatiwa na kiti mgongoni. Akajiinua na kufuta damu kidogo ambayo ilitokana na kuchanika kidogo sehemu ya juu ya mdomo.
*****
Saa 10.30 alfajiri mlango wa chumba alicholazwa Inspekta Tunu ulifunguliwa, akaingia muuguzi aliyekuwa anamuhudumia akiwa na mfuko mweusi wa nailoni. Akampatia Inspekta ambaye aliufungua kwa kiherehere na kuchungulia kilichomo, akatabasamu baada ya kugundua kuwa nesi ametekeleza ombi lake ipasavyo. Ndani ya ule mfuko kulikuwa na koti jeupe ambalo huvaa madaktari. Haraka hara akavaa na kutoka nje ya wodi ile huku akiwapita askari waliokuwa wanasinzia pale nje.
Baada ya kutoka akatembea kwa haraka huku akipishana na wauguzi wachache ambao walikuwa nje ya wodi zao, hakuna aliyejishugulisha kutaka kumtambua hivo ilikuwa rahisi kwake kutoka nje ya eneo hilo. Hofu yake ilikuwa pale getini kwani alihisi angetambuliwa na mlinzi kuwa sio daktari kutokana na kuwazoea madaktari.
Bado alikuwa anahisi maumivu makali ya kichwa lakini hakuona sababu ya kukaa hospitali na kusubiri kitu ambacho alihisi ni kuzidi kuharibika kwa jambo asilolifahamu. Bahati ilikuwa upande wake kwani alipovuka tu getini alidakwa na dereva teksi.
“Wapi dada?”
“Magomeni usalama.” Alijibu kwa mkato huku akikaa kwenye siti iliyokuwa nyuma ya dereva.
Akiwa kwenye gari alivuta fikra na kumbukumbu mbalimbali juu ya matukio yote kuanzia kupigiwa simu na kamishna mpaka kushambuliwa na mtu asiyemfahamu.
Haikuwachukua muda mrefu kufika eneo la magomeni usalama. Aliteremka kwenye gari na kumlipa dereva kiasi alichohitaji kisha akatembea kwa kasi kuelekea kituoni. Alikutana na askari kadhaa ambao hawakuweza kumtambua haraka hivyo akakosa haki yake ya kupata heshima ya kiaskari.
“He, afande!” Alikuwa koplo Peter Mkwabi ambaye alianza kushtuka baada ya kumuona Inspekta Tunu akiwa kwenye mavazi ya kidaktari.
“Nifuate.” Aliongea neno moja tu huku akimuashiria koplo yule kuwa amfuate.
Baada ya kukaa kwenye kiti chake alimkazia macho Koplo ambaye kama askari wengine aliowapita pale kaunta nao walionesha mshangao wa wazi lakini wakashindwa kumuuliza bosi wao nini kilichojiri.
“Nini kinaendelea juu ya mauaji ya makamu wa Rais, uchunguzi umefikia wapi?”
Mkwabi alimwangalia kwa wasiwasi bosi wake huyo ambaye hakutaka hata salamu jambo ambalo si la kawaida.
“Afande Kamishna amezuia kufuatilia lolote linalohusiana na kifo cha makamu wa Rais mpaka wewe utakaporuhusiwa kutoka hospitali.”
“What? Kwa hiyo tunatakiwa kuanza upya?”
“Utaanzia ulipoishia afande.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ah, hii ni sawa na kuanza upya, naomba kuwasiliana na Sajenti Kasweyaga.”
“Huyo kapewa uhamisho, anahamia wiaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma.”
“He, lakini si atakuwa bado hajaondoka.”
“Yaani ni usiku wa siku ile ambayo wewe ulishambuliwa akapokea simu kutoka kwa kamishna kuwa anatakiwa kuhamia Tunduru hivyo ajiandae, siku ya pili akapewa kila kilicho chake.”
“Unakusudia nini unaposema kila kilicho chake.”
“Fedha zote za uhamisho, gari ambalo litasafirisha mizigo yake pia kalipwa pesa za Night ya miezi miwili, yaani jamaa kadondokewa na dhahabu mkononi.”
“Acha ujinga wewe hiyo si dhahabu, kuna mambo mazito hapa yanaendelea hii nchi saa........” Hakumaliza badala yake alijishika kichwa kwa kukata tamaa.
“Nitapambana kufa na kupona.” Alisema kwa sauti ndogo yenye kuonesha hasira huku akiinuka kwenye kiti na kumwacha Koplo akiwa amepigwa na butwaa.
Huku akiwa na mavazi yaleyale ya kidaktari alitoka ofisini na kuelekea eneo la Magomeni mikumi ambako kulikuwa na teksi nyingi.
“Wapi dokta?” Aliuliza dereva huku akimkodolea macho Inspekta ambaye alifikiri ni dokta.
“Nipeleke Kawe”
******
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment