Search This Blog

Monday 24 October 2022

WIMBO WA GAIDI - 4

 

    Simulizi : Wimbo Wa Gaidi

    Sehemu Ya Nne (4)





    Milango ya lifti ikafunguka.

    Akamuona mbaya wao akiwa amesimama hali akiwa ameweka mikono mfukoni ndani ya ile lifti pana. Jamaa alikuwa amevaa vazi aina ya overall lililompitisha kuonekana kuwa alikuwa ni fundi. Bila shaka wa lifti, lakini sura yake ilikuwa ni ile ile.

    Bila kujijua akapeleka haraka mkono wake mgongoni, akitaka kuchomoa bastola aliyoifutika kiunoni na kuiziba kwa jaketi alilovaa juu ya fulana yake, lakini akawahi kusita katika muda ule ule ambao Brey naye alimsemesha.

    “Utanipiga risasi mbele ya kadamnasi hii Mukri?” Aliulizwa huku akimtazamwa kwa makini na yule jamaa, ambaye bado alikuwa amefutika mikono yake kwenye mifuko mipana ya lile vazi alilokuwa amevaa. Wakabaki wanatazamana.

    “Naweza kukuua kwa mikono yangu, fala we!” Mukri alimkoromea kwa hasira huku akiwa amesimama kwenye mlango wa ile lifti, na Brey akamcheka kwa dharau.

    “Sasa unasubiri nini…?” Brey alimuuliza kwa bezo, huku akichomoa mkono wake taratibu kutoka mfukoni, akamuonesha kuwa mkono ule uliokuwa umevishwa glovu za mpira, haukuwa umeshika kitu chochote, na akijisogeza pembeni kidogo. Mukri akamakinika kidogo na hali ile, na Brey akabofya sehemu ya kufungia milango ya ile lifti nayo ikaanza kujifunga.

    Mukri akarukia mle ndani kwa hatua moja kubwa, na Brey akajigeuza haraka kutoka pale alipokuwa amesimama kiasi wakawa wanatazama ilhali milango ya ile lifti pana ikimalizikia kujifunga.

    Lifti ikaanza kupanda juu ya jengo lile, na Brey akarudisha mkono wake mfukoni huku akimtazama kwa makini yule jamaa.

    Ebbo!

    Mukri alimrukia kwa teke kali huku akiunguruma kwa ghadhabu na akipeleka mkono wake mgongoni kuchomoa bastola yake, akilini akiwa ameshajiwekea lengo la kuua tu na si vinginevyo.

    Badala ya kulikwepa au kujikinga na teke lile, Brey Jabba alitanua miguu na kujiwekea zege pale pale alipokuwa, macho yake makali yakiwa kwenye ule mkono uliokuwa ukichomoa bastola. Teke ambalo Mukri alitarajia limsukume pembeni Brey na kumpa nafasi ya kumdunga risasi mle mle kwenye lifti, likadunda ubavuni mwa Brey na kumpepesusha yeye pembeni.

    Hapo hapo Brey akajizungusha kwa ule wepesi usiozoeleka huku akichomoa mikono yake kutoka mifukoni, na akitembeza mapigo ya kuchanja kwa mikono yake ile iliyovikwa glovu kwa uharaka wa ajabu ilhali akijigeuza huku na huko lakini akiwa amesimama pale pale alipokuwa.

    “WAAAARGHH!” Mukri alilia kwa uchungu na mshituko, pale maumivu yakatayo yalipoutawala mkono wake wenye silaha, akihisi maji ya fukuto yakiutambaa mkono wake. Bastola ikawa haikamatiki vizuri vidoleni mwake.

    HAH!

    Brey akaruka nyuma kwa hatua moja na kumfyatua teke zito la kwapa kwenye ule ule mkono uliokuwa umeshika bastola, na ghafla bastola ikamuwia nzito Mukri.

    Kanifanya nini huyu?

    Aliukodolea macho mkono wake na kuona ulikuwa ukitiririkwa damu nyingi.

    Oooh!

    Aliinua uso na kumtazama kwa mshangao yule jamaa, ambaye sasa alikuwa amesimama hatua chache tu kutoka pale apokuwa huku akimtazama kwa makini, mikono yake akiwa ameitawanya kimakabiliano huku kwa mara ya kwanza Mukri akiviona visu viwili vyembamba na virefu vikiwa kwenye kila mkono wa yule jamaa.

    Hah!

    “Umesafiri kutoka mbali kuja kuniua wewe, sio?” Brey alimnong’oneza kwa hasira. Lifti ilikuwa inaendelea kupanda juu, na hapo hapo Mukri akatumia uwezo aliokuwa nao mkononi mwake na kumfyatulia risasi yule mtu, lakini muda wote Brey alikuwa akisubiri jambo kama hilo. Alijizungusha haraka huku akibonyea na kumtelezea kama achezaye “charanga”, kisha haraka akainuka huku mikono yake iliyoshika vile visu vikali ikifanya matendo ya kucharanga mithili ya manamba wa kwenye shamba la miwa, na kwa kila mcharango ulioenda hewani Mukri alihisi maumivu makali yakiuchimba mkono wake. Bastoka ikamtoka pamoja ni kidole chake kimoja huku akiachia mayowe ya uchungu.

    “UMENIKATA KIDOLE (AKAMTUKANIA MAMA YAKE) WEWEE!” Alimaka kwa kutoamini huku akiwa amejishika mkono, damu ikimmwagika kwa wingi.

    Brey akaruka nyuma, akabofya sehemu kwenye ile lifti na lifti ikasimama katikati ya safari yake. Akaruka tena mbele kwa wepesi wa unyoya na kuishindilia kwa nguvu soli ya kiatu chake kifuani yule muuaji, na Mukri akababatizwa vibaya kwenye ukuta wa ile lifti, kisha Brey akaruka nyuma hadi pale kweye ile sehemu ya kuongozea lifti, akabofya sehemu ya kuizuia ile lifti isiende juu tena wala isishuke chini tena.

    “Unakuja vitani halafu unalia kwa nini umepigwa?” Brey alimuulia kwa hasira.

    Mukri akabaki akiukodolea macho mkono wake uliocharangwa vibaya kwa visu huku akiishuhudia damu ikimchuruzika kama maji kutoka pale kilipokuwa kidole chake cha shahada.

    Alitweta kwa mbwa koko aliyetoka kukoswa-koswa kumezwa na chatu.

    Alijua kuwa alikuwa ana kisu kwenye ala aliyoichimbia mguuni kwake, ikiwa imefichwa na ile suruali yake ya jinzi, lakini alishauona wepesi wa yule jamaa na akajua kuwa akijitia kuinama tu ili akichomie kile kisu jamaa atamfanya kachumbari.

    Alimtupia tusi jingine zito la nguoni kwa hasira yule jamaa.

    “We tukana matusi yote uyajuayo, lakini ujue kuwa leo humu nakucharanga kidogo kigogo mpaka ukate roho, paka we!” Brey alimkoromea huku akimtazama kwa makini, hali bado akiwa ametawanya mikono yake tayari kumcharanga zaidi.

    Mukri alipiga ukelele wa hasira huku akimrukia kwa teke jingine ilhali wakiwa amejishika ule mkono wake ulioishiwa nguvu. Brey akasimamia ncha za viatu vyake, na kujizungusha kistadi pale pale alipokuwa kama “el matador”, huku kwa mara nyingine mikono yake yenye visu ikicheza haraka haraka na kwa nguvu mithili ya “conductor”, yule muongozaji muziki wa “Symphony”, na Mukri akapitiliza na kujipigiza vibaya kwenye ukuta wa bati gumu la ile lifti huku mlipuko mwingine wa maumivu ukimtawala mgongoni, unyevu uliojaa fukuto la damu yake ukimtambaa mwilini.

    “Aaaarghh…!” Alilia kwa uchungu na hapo hapo akajitahidi kugeukIa kule ambao akili yake ilimtuma kuwa yule adui yake mwenye wepesi wa ajabu alikuwapo, lakini Brey alishajiepusha kutoka mahala pale na akawa sehemu kulia kwa yule muuaji mle liftini.

    “Unadhani utakuja hapa nchini kwangu na uniue kirahisi-rahisi tu, fisi koko wewe?” Brey alimkoromea.

    Mukri akapiga ukelele wa gadhabu na kumtupia ngumi kali ya upande- upande, na pale pale alipokuwa, Brey akapiga msamba huku kwa mara nyingine akitembeza mikono wake harakaharaka mwilini mwa yule muuaji kama anayepiga piano.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Dooh!

    Maumivu makali sana yalimtambaa Mukri kutokea chini ya kwapa lake na kushuka ubavuni kwake kwa kasi ya ajabu,yakashuka tumboni, kiunoni, pajani hadi chini kidogo ya goti lake, naye akalia bila kupenda, damu zaidi ikimchuruzika kutoka kwenye yale maeneo aliyocharangwa.

    Akiwa pale chini Brey akajigaragaza huku akijisukumia pembeni na kubaki akiwa amepiga goti moja kwenye kona moja lifti ile huku akiwa amechanua mikono yake yenye visu, mithili ya tai anayetaka kupaa au kushambulia, huku akimtazama kwa makini sana yule muuaji.

    Mukri alienda chini kwa goti moja bila kupenda hali akiwa amejishika ubavu wake ulioraruliwa vibaya kwa visu. Sasa machozi yalikuwa yakimtoka wazi wazi muuaji yule. Hii aliyokutana nayo haikuwa ligi ya daraja alilolizoea, na aliijutia nafsi yake.

    “Vipi muuaji…huwezi kuniua ukiwa wima?” Brey alimhoji huku akizidi kumtazama kwa makioni sana. Mukri akaitupia jicho bastola yake iliyokuwa hatua fupi kutoka pale alipokuwa.

    “Nilikuona tangu ukiegesha gari lako hapo nje, nikiwa juu kabisa ya hili jengo…nikaja kukusubiri hapa…nilijua utakuja tu…ajabu sasa washindwa kufanya lile lililokupandisha ndege kuja kulifanya…” Brey alimwambia huku akiendelea kumtazama kwa makini.

    Mukri alipiga ukelele mkubwa huku akiirukia ile bastola pale chini, na Brey akajizungusha kwa goti moja pale chini, na kujikunjua kwa teke kali sana lililombabatiza usoni yule jamaa kabla hata hajaifikia ile bastola. Mukri alitupwa pembani huku yowe likimtoka na meno kadhaa yakisambaratika kutoka kinywani mwake.

    Brey akajipindua pale chini na kumlalia mgongoni yule muuaji aliyesambaratika pale chini, hali akiwa amemuwekea makali ya kisu kilichokuwa kwenye mkono wake wa kulia kooni, hali kile kilichokuwa kwenye mkono wake wa kushoto kikiwa kimelala sehemu ya nyuma ya shingo ya muuaji yule.

    “Furukuta zaidi nikuchinje, muhindi koko wee!” Alimkoromea kwa ghadhabu akiwa amemlaLia mgongoni namna ile.

    Mukri alilia kama bwege. Damu nyingi ilikuwa imemvuja, nguvu zilikuwa zimemuishia. Hakuthubutu kujitikisa hata kidogo, kwani vile visu vilikuwa vimemkalia sehemu tete sana.

    “Weh...wew..wee nih…nin…nani…?” Mukri aliuliza huku akilia na kutweta.

    “Unachukua kazi ya kuua mtu usiyemjua?”

    Mukri hakuwa na jibu.

    “Kwa nini hukujiuliza hao waliokutuma walishindwa nini kuifanya hii kazi wao wenyewe, eenh?”

    “Niach…e…nih...en…niende! Nitakupa hela…na n’takwambia ni nani…aliyetutuma!” Mukri alitweta.

    Brey aliguna.

    “Sina shida ya hela tena mimi hapa duniani wewe! Na hao waliokutuma…? Wala usihangaike kunitajia…nawajua sana tu!” Alimkoromea.

    Mukri alilia kwa muda, kisha akajitutumua.

    “Kama unaniua niue…vinginevyo niache niende…sitakusumbua tena!” Alimwambia kwa taabu.

    Brey alianza kudidimiza vile visu taratibu kooni na nyuma ya shingo yake.

    Mukri akaanza kulia upya…





    _______________



    “Fasta, Sam…Fasta!” Sandra alibweka garini huku akiwa ametumbua macho kwa wahka, akimshinikiza mshirika wake wa muda, Sam Kiranga, aongeze kasi ya gari alilokuwa akiendesha.

    “Come ooon, Sandra! We huoni foleni hii lakini?” Sam alimkoromea huku akibamiza honi kwa hasira, kumshinikiza mwendesha daladala aliyekuwa mbele yake aongeze mwendo. Jamaa akamtolea mkono kwa dirishani na kumuashiria kuwa apaishe gari lake hewani ili awahi huko aendako.

    “Ooh Shiiit!” Sam, alilalama, na Sandra akasonya huku akizidi kujichua kisogoni alipopigwa kwa kitako cha bunduki ya Brey, akiwa amejawa michubuko kadhaa kichwani na usoni kutokana na kuangukiwa na lile li-chandelia lililokuwa mle ndani kwa Brey.

    “Tanua basi Sam, tumuwahi jamaa…” Sandra alisema kwa kukereka huku akitazama kwenye kifaa kilichokuwa pale kwenye gari la Sam, chini kidogo ya ile sehemu ambapo redio ya kwenye lile gari ilipokuwa, kikiwa mithili ya skrini ya luninga ndogo ya kwenye gari. Pale kwenye ile skrini, ramani ya jiji la Dar ilikuwa ikionekana, ilhali kiduara chekundu kikionekana kikiwaka na kuzimika kikiwa kimetulia sehemu moja tu ya jiji.

    “…bado inaonekana kuwa yuko ndani ya Quality Center huyu…lazima tumuwahi pale! Sijui kaenda kuzua tafrani gani tu kule sasa…!” Akamalizia.

    Sam Kiranga akalichomoza gari lake aina ya Prado na kulipita lile daladala kwa upande wa kushoto na kurudi tena barabarani mbele ya lile basi, akimchomkea dereva mwingine ambaye alitupia tusi zito.

    “Hizi sio kazi zangu Sandra, na wewe unajua hilo…! Nilifanya wema tu kukuchukua kwa gari langu kukupeleka nyumbani kwa yule steringi kule…” Sam alianza kulalama na Sandra akamkatisha.

    “Aliyekwambia yule steringi nani? Tumetumia gari lako kwa vile lina mfumo wa kuweza kumfuatilia nyendo zake yule jamaa, ndio maana nikakwambia tutumie gari lako wewe!” Sandra alimjia juu.

    “Na sasa ona tuliyokutana nayo…kwanza tumepigwa kama watoto kule…halafu tukafungwa pingu kama vibaka. Dharau kubwa hii! Sijui mke wangu akijua ukweli wa hii kazi yangu atasemaje tu, kwa kweli!” Sam alizidi kulalama huku akizidi kuyachomekea magari mengine pale barabarani, na akijiongezea mzigo wa matusi kutoka kwa madereva wengine.

    Sandra akasonya tena.

    “Hebu acha kulalamika bwana! Hapa ndio unaufanyioa kazi mshahara unaolipwa…fanya tumuwahi yule fala huko!”

    “Aka! Sa’ kwani mi’ kazi yangu ni hii ya makabiliano? Mi’ zangu ni kucheza na mawasiliano, mitandao na vifaa vya kieletroniki tu…lakini ona mnavyoniingiza kwenye mambo ya shuruba kama haya sasa!” Sam akamjibu huku akiendesha kwa kasi kadiri hali ya barabani ilivyoruhusu, nayo ilikuwa mbaya. Walikuwa wanakaribia mataa ya Tazara wakielekea barabara ya Nyerere.

    Sandra hakumjibu. Akili bado ilikuwa inamtembea akikumbuka namna Brey alivyoweza kuwatoka pale kwake, kwa namna alivyowatoka.

    Walikuja kushitukia wakimwagiwa maji na kundi la watu mle ndani ya nyumba ya Brey. Wakajikuta wakiwa wanakodolewa macho na askari wa jeshi la polisi wenye silaha, wakiwa pamoja na meneja wa utawala wa zile nyumba za pale Mlimani City. Jamaa waliwaeleza kuwa walisikia milipuko ya bunduki kutokea kwenye nyumba ile, hali iliyoeneza taharuki eneo lote lile, kabla ofisi ya utawala haijapata akili ya kufanya mawasiliano na jeshi la polisi.

    Sandra alipata kazi ya ziada kuwaelewesha wale askari juu ya ilikuwaje hata wakakutwa wakiwa wamelaliana bila fahamu mle ndani ambamo sio kwao, huku wakiwa wamefungwa pingu mikono yao kwa nyuma.

    Haikuwa mpaka walipomruhusu kufanya mawasiliano na mkuu wake wa kazi, ndipo wakaja askari wengine waliojitambulisha kwa kwa wale askari waliowakuta mle ndani kuwa ni kutoka kwenye kikosi maalum, na kuwachukua kutoka kwenye ile nyumba baada ya mkuu wa kazi wa wale askari kuongea na vijana wake waliokuwa wamewang’ang’ania akina Sandra.

    Walipotoka tu mle kwa Brey, Sandra akamuamuru Sam waendelee kumfuatilia kwa kutumia njia ile ile iliyowawezesha kumfuata hadi pale Mlimani City baada ya Sam kucheza na teknolojia na kuweza kukinasa kimawasiliano kile kifaa kilichokuwa mwilini mwa yule jamaa, ambacho alipata picha yake kutoka kwa Sandra.

    Na sasa ndio walikuwa barabarani kumfuatilia mtu yule hatari na muhimu sana.

    “Hivi kwa nini Brey haelewi kuwa yeye hatakiwi kabisa kujiletea udadisi kutoka kwa watu na hususan wana usalama lakini? Anaifanya kazi yangu kuwa ngumu sana kwa kweli!” Sandra alijikuta akijisemea mwenyewe kwa sauti. Sam hakumjiubu, alimakinika na taa zilizokuwa zikiwaita, na alitaka awahi kuifikia kona ya pale Tazara kabla magari hayajasimamishwa, ili akunje kushoto aitafute Quality Center…http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ________________



    “Sasa nataka unieleze jambo moja tu paka wewe…” Brey alimnong’oneza yule muuaji aliyemcharanga kwa njia isiyotarajiwa, na bila kusubiri jibu kutoka kwa yule jamaa akaendelea, “…ni vipi mliweza kupata namna ya kunifuatilia nyendo zangu…ni nani aliyewapatia hicho kifaa cha kunifuatilia?”

    Mukri alihema kwa shida, na Brey akalegeza kidogo kukididimiza kile kisu kilichokuwa kooni kwa yule bazazi wa kigeni.

    “Nih…kikwambia, utaniachia?”

    Kwa kitendo cha haraka sana Brey akamchanja kwa nguvu kooni, na Mukri akalia kwa maumivu na woga.

    “Huna nafasi ya kuweka masharti hapa wewe! Mi’ nakuuliza, nataka jibu, na ukishanijibu nakuchinja tu vile vile…” Alimkoromea, kisha akafoka, “Nani kawapa?”

    Mukri akalia kama mtoto.

    “Ukweli siwezi kujua! Huwa…tunapata maelekezo kwa njia ya mtandao!”

    “Kutoka kwa nani?”

    “Yo…yote anayehitaji huduma zetu…niachie tafadhali!”

    “Kwa hiyo waliokutumeni mje kuniua, ndio waliowapa na hii namna ya kunifuatilia?”

    “Ndi…ndiyo, ndiyo…tulielekezwa tu kwenda mahala ndio tukakuta hayo maelekezo na hicho kifaa…niachie tafadhali!”

    Uso wa Brey ukaingia kiza kidogo kwa habari ile. Hakuipenda.

    “Umeingia kwenye biashara ya mauaji…kwa hiyo lazima utakuwa unajua kuwa kwenye biashara kuna faida na hasara…kwa hii biashara uliyochagua, kifo ni sehemu ya hasara…” Alimwambia na hapo hapo akamkata koo kwa nguvu, kisha akajibiringisha kutoka juu ya mwili wa yule muuaji na kusimama wima.

    Mukri aliachia ukelele mbaya sana wa kuongofya.

    “Utakufa pole pole Mukri…mimi namuendea yule mwenzako sasa…na usiniulize nitampataje. Nitampata tu!” Alimwambia kwa hasira huku akimtazama wakati akitapatapa kwa woga huku akijaribu bila mafanikio kuizuia damu isimtoke pale kooni kwa mikono yake. Haraka akaichukua ile bastola ya yule jamaa, kisha akamsachi mifukoni. Akamchukulia funguo za gari lake, na akakichukua na kile kifaa walichokuwa wakikitumia kumfuatlilia kutoka kwenye mfuko wa jaketi lake, kilichokuwa mithili ya simu pana ya kiganjani. Na zaidi ya hapo akakuta pochi ya hela iliyokuwa na leseni ya kimataifa ya kuendeshea gari iliyombulisha kwa jina la Mukri Sudeiss, ikiwa na hela za kitanzania kama laki mbili hivi. Akaipekua zaidi lakini hakuona alichotarajia kukikuta kwenye ile pochi. Hakujali. Akairudisha mle mle mfukoni kwa yule mfu mtarajiwa. Akaviweka pembeni vile vitu vingine alivyochukua kutoka kwa yule jamaa. Kisha akatoa mfuko mkubwa wa plastiki kutoka kwenye moja ya mifuko mipana ya ile nguo ya kazi “overall” aliyokuwa amevaa, halafu akaivua haraka ile nguo. Akabaki na nguo nyingine safi zilizokuwa chini ya lile overall. Alivifuta damu vile visu vyake kwa kutumia ile ile nguo aliyokuwa ameivaa hapo awali, kisha akaliweka lile ovaroli ndani ya ule mfuko wa plastiki pamoja na zile glovu alizokuwa amevaa, akiishindilia na ile bastola ya yule muuaji ndani ya ule mfuko. Akabonyeza sehemu maalum na vile visu vikazama ndani ya mipini yake, naye akavishindilia kwenye mifuko ya suruali yake ya jinzi aliyokuwa amevaa.



    _________________



    Nje ya jengo la Quality Center Sam Kiranga aliegesha gari lao kwa fujo, na kabla hajalizima vizuri Sandra alikuwa amesharuka nje, akiwa makini sana.

    “Twende!” Alimpigia kelele mwenzake.

    Sam Kiranga alizima na kuloki gari lake, kisha akatoka mbio kumfuata akiwa na simu yake mkononi. Alimuwahi Sandra kwenye lango kuu la kuingilia ndani ya jengo lile.

    “Sasa sijui atakuwa kwenye kona gani tu ya jengo hili mshenzi yule…” Sandra alisema huku akiangaza huku na huko.

    “Lakini panaonekana pako salama tu hapa Sandra…hajafanya maafa yoyote hapa huyu…” Sam alimwambia huku akibofya simu yake.

    “Mnhu! Yule sio mjinga kuja huku…lazima atakuwa…”

    “Kwenye lifti!” Sam alimaka huku akimpita na kuongoza njia kuelekea kule kwenye lifti.

    “Whaa…umejuaje?” Sandra alimaka huku akimfuata.

    “Hizi ndio anga zangu Sandra…simu yangu inaweza kuungana na mfumo uliokuwa kule kwenye gari kumfuatilia huyu jamaa…” Alimjibiwa huku akichekwa.

    “Seriously?”

    “Jamaa yako yumo humu ndani, Sandra…” Sam alimwambia huku akiioneshea ile lifti kwa ile simu yake. Sandra alisoma kile kibao pale kwenye mlango wa lifti.

    “Ah, huyu kweli yumo humu…” Alisema huku akiipapasa bastola yake iliyokuwa kwenye mfuko wa jinzi yake…







    Na hata pale walipokuwa wakiitazama ile lifti iliyoonekana kuwa ilikuwa imetulia tu mahala pamoja, ghafla ikaanza kutembea. Wakaona taa za pale juu ya mlango wa ile lifti ikionesha kuwa ilikuwa ikipanda kwenda ghorofa za juu zaidi za jengo lile.

    “Ah, yupo humu!” Sandra alimaka huku akibonyeza kitufe pale kwenye mlango wa lifti akijaribu kuirudisha chini ile lifti.

    Lifti haikurudi, ikazidi kuonekana ikipanda juu tu.

    “Heh, huyu jamaa atakuwa anafanya nini humo? ” Sam aliuliza kwa wahka huku akiangaza huku na huko.

    “Twende!” Sandra alibwata huku akitimua mbio na kuanza kuziparamia ngazi zilizokuwa pembeni mwa ile lifti kuelekea kule juu. Sam Kiranga alisita. Akaangalia tena ile simu yake na kuona kweli bado Brey alionekana kuwa yumo ndani ya ile lifti. Akatoka mbio kumfuata Sandra huku akiwa makini kutazama iwapo ile lifti bado ilikuwa ikiendelea kupanda juu kila wanapofika kwenye ghorofa inayofuata, lakini ile lifti ilikuwa imeanza safari wakati tayari ikiwa kwenye ghorofa za katikati ya jengo lile, ilhali wao waliaza kuikimbiza wakitokea chini kabisa ya jengo lile, tena kwa miguu….



    ____________



    Akiwa mle ndani ya lifti Brey Jabba alibonyeza vitufe na ile lifti ikaendelea na safari yake kuelekea ghorofa za juu za jengo lile, muda wote huo akimsikia Mukri akikoroma kwa uchungu wakati akijitahidi kuipokonya roho yake mbaya kutoka mikononi kwa Ziraili. Lifti ikafika mwisho wa safari yake naye akatoka nje ya lifti ile na kusubiri mpaka milango ilipojifunga. Aliangaza huku na huko. Kulikuwa kuna ngazi kama tatu zinazofika pale juu kutokea kwenye korido tatu tofauti za jengo lile. Aliifuata korido iliyokuwa moja kwa moja mbele yake, na kuzifuata ngazi zilizokuwa zikiteremka chini, kutokea kwenye korodo ile. Akaziteremka zile ngazi kwa miguu kurudi kule chini huku akipiga mbinja hali akiwa amening’iniza mfuko wake wa nailoni begani, lengo likiwa ni kujifanya aonekane kuwa ni raia mwema tu aliyefika pale Quality Centre kufanya manunuzi, na ameridhishwa na manunuzi yake. Ingawa machoni mwa watu aliokuwa akipishana nao ndani ya jengo lile alionekana hivyo, akili yake ilikuwa ikifanya kazi haraka sana, akizipangilia hatua ambazo zingefuatia baada ya kile alichokitekeleza kule kwenye lifti.



    ____________



    Iliwachukua muda, wakiziparamia mbio zile ngazi huku wakiwa makini kuwatazama watu waliokuwa wakipishana nao kwenye zile ngazi au waliowakuta wakizikwea zile ngazi, wakimtafuta Brey. Hawakumuona yeyote mwenye kufanana na naye, na hatimaye walipofika mwisho wakawa wanatweta huku miguu ikiwapwita. Kule juu palikuwa kimya sana. Si watu wengi waliokuwa wakifika hadi kule juu. Waliangaza huku na huko na hawakuona mtu yeyote. Wakausogelea mlango wa ile lifti kule huku wakiwa makini sana. Sandra akabonyeza kitufe cha kufungua milango ya lifti ile kisha akaruka nyuma akiwa tayari kwa lolote, akiwa ameelekeza bastola yake kwenye ile lifti.

    La Haula!

    Walichokiona ndani ya ile lifti kiliwaduwaza kwa sekunde kadhaa, kisha kila mmoja akazinduka kwa mshituko wa namna yake. Sam Kiranga mtaalamu wa mawasiliano na kompyuta aliishiwa nguvu za miguu na akaachia matapishi kwa kile alichokiona. Sandra aliyumba kidogo na kujiegemeza kwenye mlango wa ile lifti huku akimkodolea macho yule mtu aliyelala kwenye sakafu iliyotapakaa damu ya ile lifti.

    “Holy Shiit, Brey Jabba!” Alimaka kwa kutoamini.

    Mukri alikuwa katika hatua za mwisho za kutaka roho, akishituka-shituka huku sauti za kwikwi hafifu zikimtoka, damu yake ikiwa imemlevya kiasi cha kutoweza kujielewa.

    Sandra aliruka haraka ndani ya ile lifti na kumuinamia yule muuaji aliyerambishwa ladha ya kifo na Brey Jabba.

    “Nani aliyekufanyia hivi, wewe?” Alimuuliza yule mtu, akitaka kupata uhakika tu wa kile alichokuwa tayari anakijua.

    Mukri alikoroma tu, macho yakimrembuka bila kujijua. Alimsachi haraka haraka, akakuta ile pochi yake yenye hela na leseni yake ya kuendeshea gari. Akaiweka mfukoni mwake haraka.

    “Mwezako yuko wapi…?” Alimuuliza tena yule mtu, lakini sasa Mukri alikuwa ameshakia kwenye ile ambayo ma-ulamaa wanaiita “Sakaratul-Maut”, alikuwa ameshakamata njia kuu kuelekea kwenye mlango wa kifo.

    Alisonya na kuinuka. Akatoka nje ya lifti ile, akaacha milango ijifunge lanini akabonyeza kitufe kuishikilia ile lifti isishuke chini. Alimuona Sam akiwa hajiwezi pale nje ya lifti, na hakumjali. Akatoa simu na kuwapigia simu wakuu wake wa kazi.

    “Shetani aliyejificha ndani ya nafsi ya Brey ameamka! Hawa wauaji wameyaamsha mashetani yaliyolala kwa kweli. Brey amefanya mauaji ya kutisha sana hapa Quality Center…hii ni mbaya sana…” Aliripoti simuni kwa wahka mkubwa. Akasikiliza kwa muda, kisha akaendelea, “Yaani huyu mtu hajafa, lakini hana zaidi ya robo saa ya kuendelea kuwepo duniani…ni mmoja kati ya wale wauaji waliokuwa wakimsaka…sasa nimeelewa ni kwa nini Brey hakutaka kuondolewa kile kifaa cha kumnyatia…alijifanya chambo ili aje awafanyie yake…na kawafanyia kweli!” Aliendelea, na kusikiliza tena maelezo ya upande wa pili.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Okay, mi naondoka hapa…ila huu mwili haupaswi kukutwa na na raia hapa aisee...Ukikutwa, na habari zikizagaa, hofu itatanda jijini…fanyeni hima muwahi kuja kumuondoa huyu jamaa hapa!” Alisema kwa msisitizo, kisha akakata simu. Akamgeukia Sam.

    “Tuondoke hapa! Huyu Brey kichaa kweli kweli!” Alisema huku akiziendea ngazi za kushuka kule chini. Sam alijizoazoa kutoka pale chini.

    “Dah, mi siwezi kabisa mambo haya jamani…”! Alilalama.

    “Twende huko!”

    “No subiri basi…” Sam alisema huku akiiendea ile lifti. Akatoa bastola yake na kuibondabonda ile sehemu yenye vitufe vya kuendeshea ile lifti.

    “Kama huhitaji watu wasiotakiwa waje waukute huo mwili humo ndani…inabdi lifti iwe imeharibika kiukweli!” Alisema huku akiendelea kuibondabonda ile sehemu, na kile kibati kikafyatuka. Akazingo’a kwa fujo nyaya zilizokuwa chini ya kile kibati kinachoshikilia vile vitufe vya kuongozea lifti.

    “Okay…sasa lifti imeharibika kiukweli…tuondoke!” Sam alisema huku akijifuta mdomo kwa mkono wa shtati lake, akiondoa sehemu ya matapishi aliyotoa.

    “Safi sana, Okay sasa twende…naamini Brey atakuwa anaenda kumfuata yule muuaji mwingine…tukiharakisha huenda tukamuwahi…”



    *** Watamuwahi?





    _____________



    Nje ya jengo Brey alienda moja kwa moja hadi pale ambapo alimuona yule muuaji akiegesha gari lake aina ya Range Rover, wakati huo yeye akiwa juu ya paa la jengo lile akiwasubiri wale wauaji wamfuate pale kwa kutumia kile kifaa kilichopandikizwa mwilini mwake. Kufikia muda ambapo alimuona yule jamaa akiteremka kutoka kwenye lile gari, yeye alikuwa ameshakuwapo pale Quality Center kwa zaidi ya saa moja, ambayo ilimtosha sana kuuandaa vyema uwanja wake wa mapambano dhidi ya wale adui zake na pia dhidi ya akina Sandra iwapo wangetokea.

    Nje ya ile Range Rover ghali aliuweka chini ule mfuko wake mkubwa wa nailoni, akaingiza mkono kwenye moja ya mifuko ya suruali yake na kutoa glovu nyingine za mikononi kama zile alizokuwa amevaa wakati akimpaa kama samaki yule muuaji aliyemuacha kwenye lifti. Akainama tena akiwa ameingiza mikono yake ndani ya ule mfuko kama anayetafuta kitu ndani ya mfuko ule, na kuzivaa zile glovu huku mikono yake ikiwa ndani ya ule mfuko, kisha akainuka na mfuko wake, akalifungua lile gari na kujifungia ndani yake.

    Akaanza kufanya upekuzi alioukusudia ndani ya lile gari.

    Kitu cha kwanza alichokuwa akikitafuta alikiona kikiwa wazi tu kwenye sehemu ya kuhifadhia vitu vidogovidogo iliyokuwa kwenye dashibodi ya gari lile.

    Simu.

    Akaichuku ile simu ya kisasa ambayo alikuwa ana uhakika ni ya yule muuaji na kuishidilia mfukoni mwake. Kisha akatafuta kadi ya gari. Akaikuta kwenye sehemu ambapo wamiliki wengi wa magari huwa wanaweka kadi za magari yao. Akaitazama kwa makini ile kadi, akitaka kumjua mmiliki wa lile gari. Alijua kuwa kwa kuwa wale jamaa walitoka nje ya nchi kuja kumuua, wasingeweza kuja na gari kutoka huko. Lazima kutakuwa kuna mwenyeji aliyewapatia lile gari. Ndiye aliyekuwa akimtaka kwa wakati ule.

    Ile kadi ikaonesha kuwa lile gari lilikuwa ni mali ya kampuni ya kukodosha magari. Akaikunja ile kadi na kuishindilia mfukoni. Muda wote aliokuwa akifanya mambo hayo alikuwa akichugulia huku na huko nje ya lile gari na kule kwenye jengo la Quality Center. Akapekuwa zaidi ndnai ya lile gari, na zaidi ya vishungi kadhaa vya sigara mle garini, alikuwa vijitiketi kwa kulipia maegesho ya gari vingi tu kwenye moja ya droo za mle garini. Akachukua viwili na kuvichinguza. Akamakinika. Akachukua viwili vingine na kuvitazama kwa ukaribu. Akaguna. Akachukua kimoja kilichobakia na kukitazama pia.

    Akatabasamu.

    Na mbele yake akamuona Sandra akichomoka kwa kasi nje ya lile jingo lilikuwa mbele yake, akifuatiwa na yule mshirika wake muoga.

    Akakunja uso.

    “Huyu mwanamke haswa king’ang’anizi jamani, Lah!” Alijisemea peke yake huku akijituliza mle garini akitawatazama…



    _____________



    Sehemu nyingine ya jiji, Jarraar Bakhtiyar alishituka kutoka kwenye usingizi mzito na kuguna kwa mnung’uniko wa kiusingizi. Aliangaza huku na huko mle ndani, na ukimya ukamsalimu. Mkojo ulikuwa umembana sana, na ndio uliomuamsha kutoka kwenye usingizi ule mzito.

    “Mukri..!” Aliita, lakini hakupata itikio lolote. Akakunja uso.

    “Mukrii…aheee Mukri!” Aliita tena kwa mtindo wa kikwao, lakini bado Mukri hakumuitika.

    Akasonya na kuinuka. Akajikongoja kwa shida kuelekea chooni kutokana na maumivu ya pale kwenye jeraha la mguuni aliloachiwa na risasi ya Sandra. Kimoyomoyo alijikumbusha tena ahadi ya kumtembezea maumivu makali sana yule mwanadada pindi atakapokutana naye tena, kabla hajaondoka nchi hii aliyoondokea kuichukia sana.

    Alipotoka kujisaidia akachechemea hadi jikoni ambako kulikuwa kuna jokofu, ili anywe maji. Na ndipo alipouona ujumbe kutoka kwa Mukri ukiwa umebandikwa pale kwenye mlango wa jokofu lile kwa kutumia moja ya vijisanamu vya urembo vibandikwavyo kwenye majokofu vikiwa vina sumaku chini yake.

    Akiwa amemakinika aliichomoa ile karatasi na kuisoma, na alipomaliza alipiga ukelele wa ghadhabu peke yake mle ndani.

    Ujumbe wa Mukri alikuwa unamwambia kuwa alikuwa ameenda kummaliza yule mtu aliyewasumbua sana kabla mtu yule hajapata muda wa kujipanga zaidi, na kwamba atakarejea pale nyumbani, atakuwa ana kidole cha yule jamaa kama ushahidi na kumbukumbu ya kazi ile iliyowasumbua sana.

    “Aaaah, Mukriiiii! Kwa nini usifanye kama tulivyokubaliana lakini Mukri???” Jarraar alibwata peke yake mle ndani, kisha haraka akaiendea simu yake, na kuanza kumpigia mwenzake.

    Laiti angejua!

    ________________



    Sandra aliangaza kulia na kushoto nje ya jengo lile na biashara, akiwapangua watu wengi waliokuwa wakiingia na kutoka kwenye jengo lile. Jasho lilikuwa likimvuja na alikuwa akihema kwa nguvu kutokana sio tu na ule mwendo wa mbio alioutumia kuzishuka zile ngazi, bali pia kwa kumbukumbu ya kile alichokiona mle kwenye lifti.

    “Jamaa yuko hapa!” Sam alibwata huku akigeuka huku na huko hali akitazama kioo cha ile simu yake.

    “WAPI SASA, KIRANGA?? AAAH!” Sandra alibwata.

    Badala ya kumjibu, Sam akatimua mbio kuelekea kwenye sehemu ya maegesho ya magari iliyokuwa mbele ya jengo lile, ambapo nyuma ya magari mengi yaliyokuwa yameegeshwa eneo lile, barabara ya Nyerere ilikuwa ikipitisha magari mengi kwenda na kutoka maeneo ya uwanja wa ndege. Sandra alimfuata mbio huku akiyatembezea macho yale magari pale nje. Sasa baadhi ya raia nao wakawa wameanza kumakinika nao. Kwa hali ilivyokuwa, Sandra wala hakujali. Brey alikuwa amefanya jambo la hatari sana kule kwenye lifti, naye ilibidi akabiliane naye na ku badili kabisa mbinu ya kucheza na yule jamaa.

    “Yuko hapa hapa huyu mtu Sandra!” Sam alisema kwa wahka, huku akiielekezea ile simu kule kwenye yale magari. Yaani sasa ile simu ilikuwa kama mbwa anusaye madawa ya kulevya kule uwanja wa ndege, na yale magari ndio mabegi ambapo moja wapo ndilo lilikuwa lina hayo madawa yasakwayo ya huyo mbwa.

    “Hey Sam…cheki hii!” Sandra alimpigia kelele mwenzake huku akimuoneshea gari mojawapo pale. Sam akachanganyikiwa. Akaitazama tena simu yake, kisha akageukia kwenye lile gari alilokuwa akioneshewa na Sandra.

    “Nini sasa?”

    “Hili gari…ni la Dokta Muro hili!” Sandra alisema, na Sam akaangusha mdomo.

    “Ndilo alilotoroka nalo jamaa kule hospitali?” Alihoji, akiwa alishapata maelezo kutoka kwa Sandra jinsi Brey alivyowatoroka usiku uliopita.

    “Ndio! Atakuwa mle ndani….”

    “Hayumo mle Sandra…!” Sam alimpinga huku akimuonesha ile simu yake.

    “Khhhh! Sasa atakuwa wap…” Sandra aliuliza huku akigeuka upande mwingine wa maegesho yale, kauli yake ikaishia njiani.

    Alijikuta macho kwa macho na Brey Jabba, aliyekuwa akiwaangalia kutokea nyuma ya kioo cha mbele cha Range Rover ghali sana iliyokuwa imeegeshwa kama magari manne kulia ya lile la Dokta Muro, lakini likiwa nyuma ya gari jingine.

    “There he is!” Sandra alimaka huku bila kujijua mkono wake ukienda kwenye ule mfuko ambamo bastola yake ilikuwapo lakini akaghairi. Sam anaye akageuka, akamuona.

    “Woow! Range Rover new model! Dah huyu jamaa ana mbwembwe kweli kweli ku—nina zake!” Sam aliropoka kwa kusifia, lakini Sandra hakuwa na mawazo hayo. Alikuwa amemnyooshea viganja Brey kuonesha kuwa hakuwa na silaha yoyote, huku akimfuata pale alipokuwa, na nyuma yake mlipuko mkubwa ukasikika kutokea kule Quality Center.

    Heh!

    Aligeuka kwa wahka huku ukulele ukimtoka, na kuona raia wakitimua mabio hovyo kule mjengoni huku wakipiga mayowe, kutokea nyuma ya vioo vya lile lango kuu la lile jengo aliona kitu kama moto mkubwa ukiruka hewani.

    EBBO!

    Akageuka kule kwa Brey, na kumuona yule jamaa akiwa ametulia vile vile mle garini, akimtazama.

    “Nini tena hii!” Sandra alifoka, akaanza kuikimbilia ile Range Rover, wakati Sam Kiranga akitimua mbio kujiweka mbali zaidi na lile gari. Na mle ndani ya ile Range Rover, Brey akabonyeza kitufe kingine kutoka kwenye kilipulizi alichokitoa kwenye mfuko mwingine wa suruali yake, na mlipuko mwingine mkubwa sana ukasikika kutokea kule kwenye jengo, safari hii ikiwa ni kutokea kwenye moja ya mapipa ya taka yaliyokuwa nje ya lile jengo, na moto mkubwa ukaruka hewani sanjari na mlipuko ule, mayowe na taharuki vikizagaa kwa wananchi waliokuwepo. Sandra akajitupa chini huku akimtazama yule jamaa kwa kutoamini, na Brey akaivurumisha ile Range Rover mara moja, mbili, tatu, kisha akaichomoa taratibu kutoka eneo lile, akageuza kama raia tu wa kawaida aliyemaliza shughuli zake eneo lile na kuondoka. Sandra alitoa bastola yake, lakini hapo tena akasikia ving’ora vya magari ya polisi vikiekea kule kule walipokuwa. Akajua kuwa wale wenzake aliowapigia simu walikuwa wamefika. Akainuka, bastola ikiwa wazi mkononi mwake na kuitokea mbio ile Range Rover.





    “Simama Brey! Umezingirwaaa!” Alimpigia kelele, na hapo hapo mlipuko mwingine ukarindima kutokea sehemu fulani pale nje, na magari mengi yaliyokuwa na ving’ora vya tahadhari yakaanza kupiga ving’ora, watu wakajua tayari Al-Shabaab ndio wamevamia Quality Center kama walivyofanya kule Westgate, jijini Nairobi, takriban miaka miwili na nusu nyuma. Sandra akaenda chini bila kupenda. Akatupa macho kule ambako ule mlipuko wa mwisho ulitokea, na kuona kuwa ulikuwa umetokea jirani na pale ambapo lile gari la Dokta Muro lilikuwapo, wingu kubwa la moto likiruka hewani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tafrani ikapanda chati Quality Centre.

    Magari yakaanza kuchomoka hovyo kutoka eneo lile, raia wakawa wanakimbia bila mipangilio wala mielekeo, mayowe yakazagaa, na ile Range Rover ya Mukri ikazungushwa kwa kasi ya ghafla, ikiyakwepa magari mengine kiufundi wa hali ya juu, kisha ikaunga msururu wa magari mengine yaliyokuwa yakichomoka kwa kasi kutoka eneo lile.

    “Oooh noo, Brey Jabbaaa, nooo!” Sandra alipayuka kwa hamaniko pale alipoishuhudia ile Range Rover ikichomoka kwa kasi kuelekea usawa wa mataa ya keko kwa kutumia njia ya ziada (service Road) iliyokuwa pale mbele ya Quality Center, wakati vile ving’ora vya yale magari ya wenzake vikizidi kukaribia eneo lile kutokea upande wa mataa ya Tazara. Aliinuka na kuichomokea kasi huku akiwa ameielekezea bastola yake, lakini magari mengine yalikuwa nyuma ya ile Range Rover na hivyo hakuweza kupata shabaha vizuri. Hapo hapo akakoswakoswa kugongwa na gari jingine lililokuwa likichomoka kutoka eneo lile. Sam Kiranga akachomoka haraka na kumdaka kiuno, akamvutia pembeni.

    “Acha aende Sandra…utagongwa bure! Jamaa hatumuwezi aisee!” Alimbwatia kwa wahka huku akiyatazama yale magari, Range Rover ya Brey ikiwemo, yakitokomea kutoka eneo lile, honi, ving’ora na mayowe vikirindima eneo lote.

    Ama hakika habari ya kifo cha gaidi Nouman Fattawi, ilikuwa imezua kizaazaa jijini Dar.



    _________________



    Kwa saa mbili zilizofuatia pale Quality Centre palibadilika na kuwa eneo la harakati za kiusalama. Magari ya polisi wa kawaida na wale waliojitambulisha kuwa ni wa kikosi maalum yalizingira eneo lile. Raia wote walitokewa nje ya mashinikizo makubwa kabisa, ingawa hata wao wenyewe hawakuwa na hamu wala nia ya kuendelea kubaki ndani ya jingo lile. Ile milipuko ya mabomu ilikuwa imewatikisa wote waliokuwepo pale kwa kiwango kikubwa kabisa.

    Sam na Sandra waliwaongoza wale askari waliotoka kwenye kitengo chao hadi pale kwenye ile lifti, kisha wakati wale wenzao wakifanya kazi yao ya kuuondoa ule mwili usio na mwenyewe hapa nchini kwa namna yao ya uficho wa hali ya juu, wao waliondoka na kurudi kule kwenye gari lao.

    “Huyu jamaa si wa kawaida aisee!” Sam Kiranga alimnong’oneza Sandra wakiwa wanaelekea kwenye gari lao.

    “Mjinga tu yule, hana lolote! Yeye anaona sifa hii? Hakutakiwa kabisa kujianika namna hii bwana! Hebu cheki maafa aliyoacha hapa…” Sandra alilaumu.

    “Si ndio maana nikakwambia kuwa si kawaida? Yale mabomu…ni milipuko tu inayofuka moshi wa moto…si mabomu wala nini yale….” Sam alisema. Sandra akasimama.

    “Whaat?”

    “Ndio. Yaani yule aliweka vile vitu kama geresha bwege fulani tu…hakuna dhara lolote zaidi ya kuwapagwawisha watanzania tu hapa…hakujapasuka kioo wala hapajateketea gari la mtu kwa milipuko ile!” Sam alisema huku akizidi kuliendea gari lake. Sandra akamkimblia.

    “Lakini ni kweli aisee!”

    “Ooh, mi nakwambia huyu mtu bora umuachie tu afanye yake, akitosheka yeye mwenyewe atakutafuta!” Sam alisema.

    Sandra akagoma.

    “Mn-MH. Huwa hatuendi hivyo aisee…mi nnaye tu huyu mpaka tuelewane. Siwezi kumuacha tu aendelee kuupaka mji rangi ya damu namna ile…ni mbaya sana kwa swala zima la usalama wa nchi. Unadhani sisi tutaweza kuendelea kuficha mauaji yake mpaka lini?”

    “Kwani si kabakisha mtu mmoja tu Sandra? Muache ammalize tu na huyo kisha muendelee na mipango yenu!” Sam alisema, na Sandra akamkata jicho baya.

    “Oh, okay..sorry. Fanya sijasema hivyo basi…” Sam aliomba radhi haraka, kisha akaendelea, “Okay, nini kinafuata sasa?”

    “Bado unaweza kuona nyendo zake?” Sandra alimuuliza.

    “Of course…yuko mitaa ya katikati ya jiji hivi sasa…” Sam alimjibu haraka.

    “Twende!” Sandra aliamuru.

    Wakari wao wanayaongea haya, sehemu nyingine ya jiji, simu iliyokuwa mfukoni mwa Brey Jabba ikaita. Akiwa amemakinika na uendeshaji wa lile gari ambalo alijua Mukri hatakuwa na kazi nalo tena sasa, aliichimoa ile simu na kutazama.

    “Jarraar” ilionekana kwenye kioo cha ile simu, na Brey akaachia tabasamu baya.

    “Oho, kumbe wewe unaitwa Jarraar, sio? Basi sawa…jaa upepo kwanza!” Aliisemesha ile simu na kuiweka pembeni, akiiacha iendelee kuita tu vile vile. Ikaita hadi ikakatika. Na kama dakika moja baadaye ikaanza kuita tena.

    “Usiwe na haraka Jarraar…nitakufikia soon enough!” Brey alijisemea peke yake mle garini, akimaanisha kuwa atamfikia ndani ya muda mfupi kiasi cha kutosha tu yule mshirika wa marehemu aliyemuacha kule kwenye lifti.

    Simu iliendelea kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa, na dakika chache baadaye ujumbe mfupi ukaingia kwenye ile simu…



    ______________



    KATIKA KUKABILIANA NA TATIZO LA WADUKUZI WA RIWAYA ZETU TUZIWEKAZO HAPA KONANI AMBAO HUZIKOPI NA KWENDA KUZIWEKA KWENYE MAGRUPU YAO YA WHATSAPP NA HATA KWENYE KURASA ZAO ZA FACEBOOK, KIPANDE HIKI TUMEKIONDOA HAPA KONANI NA KITAKUWA KITABUNI PINDI KITAKAPOKUWA TAYARI. KWA HAPA ITOSHELEZE TU KUELEWEKA KUWA BREY NA NAMNA YA KUFUATILIA NYENDO ZAKE. NDIPO ALIPOMKABILI SANDRA…



    _________________



    Sandra alishitushwa na muito wa simu yake kutoka kwenye usingizi mzito wa mchoko. Ilikuwa ni saa tisa za usiku na alisonya kwa hasira huku akiinuka na kuiendea simu yake aliyokuwa ameibwaga bila kujali kwenye meza ya kujirembea iliyokuwa mle chumbani mwake.

    Alitazama mpigaji wa simu ile katika muda ule na usingizi ukamkauka.

    “Ni nini tena, Kiranga? Mkeo yuwapi hata unanipigia muda kama huu wewe?” Alibwata simuni huku moyo ukimuenda mbio sana.

    “Brey katoweka, Sandra!” Sam Kiranga alimwambia simuni kwa wahka mkubwa.

    “What do you mean Brey katoweka? Si ulikuwa unafuatilia nyendo zake mwanzo mwisho wewe?” Sandra alifoka.

    “Na si ndio maana nimeweza kujua kuwa katoweka? Yaani jamaa haonekani tena hewani! Simsomi! Simuoni kwenye rada zangu…hayupo tena himayani mwangu huyu mtu Sandra…gone, disappeared, vanished…yaani kuch ney , wahindi wanasema aisee, dah!” Sam Kiranga alimjibu kwa hamaniko lililokithiri, kila neno analotumia kumfahamisha kuwa Brey hayupo tena kwenye himaya yao akiliona halifai.

    Loh!

    Sandra alichanganyikiwa.

    “Sasa…sasa inawezekanaje hiyo lakini? Si mpaka afanyiwe upasuaji ndio kile kitu kitoke?” Alihoji.

    “Ndio hivyo nijiavyo, lakini haina maana kuwa ni Dokta Muro wako tu ndiye awezaye kufanya upasuaji huo!” Sam alisema, na Sandra akatukana tusi zito nguoni, bila kubanisha ni nani hasa aliyekuwa akimtukana.

    “Ah, sasa ina maana yule muuaji mwingine…kawaje sasa?”

    “Mi’ ntajuaje?”

    Wote walikuwa wamechanganyikiwa. Kimya kikapita kidogo, kisha Sandra akauliza, “Sasa tunafanyaje?”

    “Ah,mi’ hapo simo sasa. Na kwa kuwa hicho kifaa hakipo tena, na mimi sasa najitoa rasmi kwenye kesi hii Sandra…sina tena sababu ya kuendelea kushirikishwa kwenye swala hili…”

    “Akh, sio kirahisi namna hiyo wewe!” Sandra alimchachamalia.

    “Ni rahisi namna hiyo Sandra…mkimuwekea kifaa kingine na kumnyatia niiteni tu, anytime.” Sam alimpasha.

    “Oh Come on, Sam! Au unajifanya haonekani ili usiendelee kuwepo kwenye kesi hii wewe? Unaogopa mapambano yatamuacha mkeo mjane?”

    “Tuheshimiane Sandra! Nimehatarisha sana maisha yangu kwenye kumfuatilia huyu jamaa na hata mara moja sijataka kujitoa, lakini sasa hali ndio imeshakuwa hivi nikwambiavyo. Brey Jabba kaingia kizani, kwa hiyo taaluma yangu haitahitajiki tena sasa.” Sam alijazibika.

    “Dah, samahani aisee. Nilipagawa tu. Najua huwezi kufanya ujinga kama huo, I am sorry , Sam…”

    “Poa, sio ishu. Pole sana Sandra…bado una kazi kubwa na huyo jamaa. Na bado nasisitiza kuwa Brey siyo daraja letu aisee…”

    “Daraja letu tu huyu wewe! Ila huwa ana namna ya kutuzidi kete kiajabu ajabu tu…!” Sandra alimkatisha, na kumkatia simu.

    “Oh, Okay…” Sam aliijibu simu iliyokuwa imeshakatwa.

    Saa tano baadaye Sandra alikuwa amefura vibaya sana ofisini kwake. Taarifa kuwa amempoteza Brey kutoka kwenye rada zao haikupokewa vizuri kabisa na wakuu wake wa kazi.

    “Kwanza tumempoteza Benson, halafu tumelazimika kwenda kusafisha matapishi yenu mliyoyaacha kule Quality Center, kisha tukalazimika kutoa maelezo ya uongo-uongo kwenye vyombo vya habari na kwenye sekta zisizohitajika kuelewa kinachoendelea serikalini kuhusu ile milipuko ya kule Quality Center…na sasa umempoteza kabisa?” Mkuu wake alimsimanga kwa hasira asubuhi ile.

    “Mkuu naona kama unanibebesha mzigo usio kuwa wangu sasa…mimi nilikuwa namsaidia Benson tu. Yeye ndiye hasa aliyekabidhiwa kaz…”

    “Na ikakabidhiwa kwako rasmi baada ya Benson kuuawa!” Mkuu alimjia juu.

    “Na nikaifanya kwa nguvu zangu zote…”

    “Kweli kabisa. Inaonekana nguvu zako ndio zimeishia hapo. Umempoteza mtu muhimu sana. Unajua kuwa hatuwezi kuingiza maafisa wengi kwenye kazi hii kutokana na unyeti na usiri wake. Wewe na Benson mlionekana mnatosha kabisa. Na kazi ilikuwa nyepesi tu. Mchukueni huyu mtu mumfikishe sehemu salama…basi! Hivyo tu! Ona kilichotokea sasa!”

    “Mkuu hatukuwa tumetarajia kuwa kutakuja wauaji wa kukodiwa kutoka nje ya nchi kumuua huyu mtu…tena wakiwa na kifaa cha kumfuatilia nyendo zake zote...nimefanya kazi ya ziada hadi na sisi tukawa tunaweza kumfuatilia nyendo zake…nahitaji kupongezwa kwa hilo, lakini..”

    “Nitakupongeza ukiniletea Brey Jabba hapa, na kumpeleka anapotakiwa kwenda. Nakupa siku tatu Sandra, vinginevyo naidhinisha ripoti iende kwa washirika wetu kuwa tumeboronga…tumeshindwa kumlinda Brey Jabba na sasa hatujui alipo!” Mkuu alimkemea kabla ya kumuamuru atoke ofisini kwake.

    Sasa alikuwa amefura vibaya sana mle ofisini na wala hakujua aanzie wapi kumtia tena mikononi Brey Jabba. Akayakumbuka kwa uchungu mkubwa maneno ya Sam Kiranga…

    “Hodi Sandra…”

    Alishitushwa kutoka kwenye mawazo yake, na alipoinua uso wake alimuona dokta Muro akiingia mle ofisini mwake akiwa ameongozana na mwanamke aliyejitanda khanga mwili nzima, akiwa amebandika miwani kali sana ya kike usoni na amepaka rangi nzuri ya mdomo hali akinukia uturi mzuri sana.

    “Oh, Dokta Muro…karibu. Whats up?” Alimkaribisha na kumuuliza huku akimtazma yule mwanamke aliyeongozana naye. Dokta Muro akabaki akimkodolea macho bila ya kusema neno.

    “Dokta Muro…mbona hiv…”

    “Funga mlango huo dokta, halafu kaa hapo pembeni, tuna kazi ya kufanya!” Yule mwanamke aliongea.

    Isipokuwa sauti yake haikuwa ya kike. Sandra alitoa macho huku akiiwahi bastola yake kutoka kwenye droo yake pale mezani.

    “Acha hizo Sandra, na unisikilize!” Brey Jabba alimkoromea akiwa ndani ya muonekano ule wa kike.

    Lah!

    Sandra akanywea kama puto. Akabaki akimkodolea macho kwa kutoamini yule jamaa aliyejitanda khanga.





    “Huyu jamaa yako…” Brey alianza huku akimuoneshea Dokta Muro kwa kidole chake cha gumba, “…anatakiwa kujua lolote zaidi kuhusu mimi?”

    Sandra akapepesa macho, bado alikuwa hajazinduka kutoka kwenye kile kilichomshukia pale ofisini kwake muda ule. Ametoka kugombezwa na mkuu wake wa kazi si zaidi ya nusu saa iliyopita, akilaumiwa kwa kumpoteza Brey Jabba, kisha akapewa siku tatu awe amempata na kumpeleka kutakiwapo ama sivyo utendaji wake wa kazi utaingizwa dosari kubwa…na wakati anafura kulalamika na nafsi yake namna asivyojua hata pa kuanzia kumpata huyo Brey, jamaa anamuibukia ofisini kwake akiwa kwenye nguo za kike.

    “Jibu swali basi Sandra…vipi wewe?’ Brey alimshitua, naye akazinduka…pamoja na Dokta Muro.

    “Ah mi’ sihitaji kujua lolote zaidi…naweza kujiondokea kiroho safi tu kama mna maongezi ya siri zaidi…sikuja kwa ridhaa yangu hapa ujue Sandra…nimeshinikizwa.” Dokta Muro akadakia, na Brey akamkata jicho kali kutokea nyuma ya ile miwani ya jua aliyovaa ambayo hata hakuivua ingawa alikuwa ndani ya jengo.

    “Okay, Muro naelewa…” Sandra alimjibui mwenzake, kisha akamgeukia Brey, “Er, ukweli hapana. Muro hakuhitajika na wala hahitajiki kujua lolote zaidi juu yako. Aaam…nililazimika kumshirikisha ili kwanza achunguze iwapo ulikuwa una “tracking Device” mwilini mwako…na kama ndivyo akutoe…lakini wewe…”

    “Kwa hiyo aende zake basi, tuendelee na yetu!” Brey alisema, na alipoona Sandra amepigwa butwaa, akaendelea, “Nilimshinikiza anitoe kile kifaa baada ya kuwa kazi yake imeisha…”

    “Kazi yake ipi? Na imeisha kivipi?” Sandra akadakia, lakini wakati huo huo na Muro naye akaamua kutoa lake la moyoni.

    “Kwa mtutu wa bastola, Sandra!” Muro akadakia kwa jazba, na Sandra akamgeukia yule tabibu kwa mshangao.

    “Kakulazimisha umtoe kile kifaa…kwa mtutu wa bastola?” Alimuuliza huku akimgeukia Brey kwa mshangao.

    “Sasa kumbe? Tena bila ganzi wala nusu kaputi, shenzi taipu! Huyu mtu mmetoa wapi lakini, Sandra?” Muro alimaka zaidi, na Brey akamgeukia kwa hasira.

    “Unataka mbata zaidi? Hapa tuna mambo mazito zaidi ya huko kuumia kwako nafsi eti kwa kuwa nimekushinikiza vitu wewe! Fanya uende huko, na kazi yako hii pia imeisha sasa. Nilitaka unifikishe kwa Sandra, na umnenifikisha. Nice doing business with you, sir!” Brey alimkoromea, na Dokta Muro akafura kwa hasira zaidi, baada ya kukumbushwa madhila aliyopitishwa na Brey Jabba.

    “Uliniotea vibaya sana wewe, kwa kujitia mwanamke, laa sivyo…” Alianza, lakini Sandra akamkatisha.

    “Hebiu fanya uende, Muro…vipi wewe?” Akamkaripia. Muro akamkata jicho baya Brey, kisha akatoka kwa hasira. Brey akabaki akitikisa kichwa, kisha akamgeukia Sandra.

    “Nilikuwa nina maelekezo kamili kuwa watu watakaonipokea, ambao nataka kuamini kuwa walikuwa ni wewe na marehemu Benson Kanga, ndio wangekuwa na maelekezo ya wapi natakiwa niende…sawa?”Alimueleza na kumuuliza.

    “Ngoja kwanza Brey…nini kimemtokea yule muuaji mwingine…?” Sandra alimuuliza.

    “Sio tatizo tena yule hapa duniani…tuangalie lililo mbele yetu.”

    “Umemuua?”

    “Aa-a. Nimemuozesha binti yangu. Unaanza kuuliza maswali ya kibwege sasa, eenh? Nataka tuzungumize safari yangu ya kulihama hili jiji sasa…”

    “Mwili wake uko wapi?”

    Brey akasonya na kujiegemeza kitini huku akikunja nne. Akapiga kimya.

    “Come on, Brey…nataka kujua kuhusu yule muuaji mwingine, maana ulivyomfanya yule wa kwanza nimeona, na kwa kweli...”

    “Sandra. Tosheka na kwamba hatokuwa tatizo tena kwangu na kwako pia. Nataka maelekezo sasa ya kulihama hili jiji …” Brey alimbishia na kumrudisha kwenye hoja yake ya msingi.

    Sandra akasalimu amri japo kwa shingo upande.

    “Okay. Itabidi nikukutanishe na mkuu…”

    “Sihitaji kuonana na yeyote ambaye hahusiki Sandra, tayari nimeshajiweka wazi sana hadharani…nahitaji kuondoka hapa jijini sasa.”

    “Oh, kumbe unalijua hilo? Sasa mbona ulikuwa unajitia huelewi?”

    “Ilikuwa ni lazima iwe vile. Huyo mkuu ndiye mwenye hayo maelekezo, au unataka kwenda kujipa sifa tu kuwa umenifikisha hapa. Mi nimekuja mwenyewe hapa, in case umesahau!” Brey alimwambia.

    “Hapana…maelekezo tutapewa tukiwa angani…na yeye atawasilaiana na mtu atakayekupokea huko uendako ambaye atamthibitishia kuwa umefika huko…au hujafika, vyovyote itakavyotokea.”

    “Ambako ni wapi?”

    “Mimi sijui…nijuacho ni kwamba ni kijijini tu…ndani ya nchi yetu hii hii…”

    “Nani anayejua?”

    “Maelekezo ni kwamba tutapanda helikopta pamoja mimi na wewe sasa, kwa kuwa Benson ndio hayupo…maelekezo yatafikishwa kwa rubani wetu kwa njia ya simu…tutakapofika huko tuendako, tutagawana njia. Utachukua usafiri mwingine ukiwa na maelekezo ya sehemu ambako utakutana na mwenyeji wako…na huyo ndiye utakayekuwa naye kwa maisha yako yaliyobakia, na huko ndiko kutakuwa maisha yako yaliyobakia…uoe huko, uzae watoto huko…uishi huko…ufie huko.” Sandra alimjibu. Brey akamkata jicho kwa muda, kisha akaguna.

    “Ni nani atakayepiga hiyo simu?”

    “Mimi simjui…yaani hii operesheni imevunjwavunjwa kiasi kwamba hakuna mtu mmoja anayejua kila kitu. Kila mtu anajua sehemu tu ya operesheni, na sio wote wanaojua sehemu nyingine ya operesheni inajulikana na nani…watendaji hatujuani…yote ni kw ausalama wako wewe tu!”

    “Of course…kwa kuwa niliyoyafanya yanastahili nifanyowe hivyo. Fanya tundoke sasa.” Brey alimjibu.

    “Itabidi ifanye maadalizi…”

    “Nakusubiri hapa hapa ofisini kwako…”

    “No, kuna chumba cha faragha humu humu mjengoni…njoo.” Sandra alimjibu, na kwa saa mbili zilizifuata, Brey Jabba akiwa ndani ya mavazi ya kike, alisubiri wakati Sandra akifanya maadalizi yaliyokusudiwa.



    _______________



    “Okay, tunaelekea morogoro jamani, sawa?” Rubani wao aliwaambia baada ya kuwa ameshaongea na simu aliyokuwa akiisubiri mle kwenye helikopta baada ya kuwa Sandra na Brey Jabba wameshapanda. Walikuwa kwenye eneo maalum la kuegeshea ndege za aina ile kwenye jengo ambamo ndimo ofisi za akina Sandra zilikuwepo. Bado Brey alikuwa kwenye mavazi yale yale ya kike.

    “Morogoro?” Brey alihoji, na Sandra akambetulia mabega. Dege likaenda hewani, na safari ya kumuondosha mtu aliyetambulika kama Brey Jabba kutoka jijini ikawa imeanza…

    Wakiwa angani, Brey Jabba akatoa zile khanga alizojitanda na kubaki na nguo za kawaida, ambazo zilikuwa ni fulana ya kawaida tu na suruali ya jinzi, akijifuta na kujiosha ule urembo aliojiweka usoni ili aonekane kuwa ni mwanamke.



    ________________



    Morogoro waliteremkia kwenye kambi ya jeshi iliyokuwa eneo la Dakawa, nao wakapokewa na mkuu wa kambi ile. Pale Brey alikabidhiwa kibegi cha wastani.

    “Vitu muhimu utakavyohitaji huko uendako vitakuwa humo…” Yule mwenyeji wao alimwambia, na Brey akalipekua haraka haraka lile begi. Kulikuwa kuna bastola mbili, kitita cha fedha zipatazo kama laki saba hivi, pasi ya kusafiria, vyeti kadhaa vya ngazi mbali mbali za kielimu, na baadhi ya nguo. Wakatolewa nje ya ile kambi kwa gari la jeshi hadi eneo la msamvu, ambako wakateremka kama watu tu waliokuwa wamepewa lifti na lile gari la jeshi.

    “Itabidi mchukue basi la Iringa hapa!” Dereva aliyewateremsha aliwaambia, nao wakatazamana. Sandra akabetua mabega.

    “Si nilikwambia kuwa kila mtu anajua sehemu tu ya operesheni nzima? Twende tu Brey” Alimwambia. Brey hakutia neno. Saa moja baadaye walikuwa kwenye basi wakielekea Iringa, wakiwa ni mongoni mwa abiria wengine wa kawaida basini.

    Ilikuwa jioni sana walipoigia Iringa mjini.

    “Okay nini kinafuata sasa?” Brey aliuliza.

    Sandra akatoa bahasha kutoka kwenye mfuko wa suruali aliyokuwa amevaa, akamkabidhi.

    “Okay Brey Jabba...au yeyote uwaye...mimi na wewe tunagawana njia hapa. Maelekezo ya wapi uende, nini ufanye kutokea hapa, yamo humo kwenye hiyo bahasha…kazi yangu imeishia hapa Brey…na siwezi kusema kuwa imekua ni furaha sana kufahamiana nawe.” Alimwambia.

    Brey alimtazama yule dada kwa muda. Kisha akatabasamu.

    “Ahsante sana kwa yote Sandra…be safe!” Alimwambia huku akimpa mkono. Sandra alimtazama kwa muda, kisha akaupokea ule mkono.

    “Hivi wewe ni nani lakini, Brey Jabba?” Alimuuliza kwa hisia iliyojaa udadisi.

    “Brey Jabba.” Jamaa lilimjibu, kisha likageuka na kuondoka likiwa limening’iniza kibegi chake mgongoni, likiwa limeishika ile bahasha mkononi.

    Sandra alibaki akimkodolea macho hadi alipojichanganya miongoni mwa raia waliokuwa wamezagaa pale kituo cha basi na kutoweka….

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Alitikisa kichwa huku akitoa simu na kupiga namba fulani.

    “Special Agent Sandra hapa…nimeshaufikisha mzigo mahala nilipotakiwa…” Aliongea simuni baada ya mtu wa upande wa pili kupokea, akasikiliza kwa muda kisha akakata simu bila kuongea zaidi. Alitoka pale alipokuwa amesimama na kuchukua usawa wa barabara kuu, kisha akaenda kusimama chini ya bango moja kubwa sana la matangazo lililokuwa kando ya barabara. Hakusimama muda mrefu pale. Kama dakika kumi baadaye, gari aina ya Landrover 110 likafika na kusimama hatua kadhaa mbele yake, naye akalifuata, akalipanda.

    “Nina maelekezo ya kukufikisha Dar es Salaam usiku huu huu, ni sawa?” Dereva wa lile gari alimwambia, na Sandra akaafiki kwa kichwa.

    “Okay, njia moja to Dar hii tena.” Jamaa alisema.

    “Yeeaaap. Mi’ najilaza hapa kama hutajali…” Sandra alimjibu huku akijifunga mkanda vizuri na akikilaza nyuma kiti alichokuwa amekalia.

    “Sweet dreams!” Dereva alimwambia, akimtakia njozi njema, huku akiliingiza gari barabarani.

    Kutokea upenuni mwa moja ya maduka kadhaa yaliyokuwa yamekizunguka kituo kile cha mabasi, Brey Jabba aliitazama ile Land Rover ikikamata kasi kufuata uelekeo wa Dar. Aliendelea kujiegemeza pale kwenye ukuta wa duka lile kwa dakika kama tatu zaidi, kisha akajisukuma kutoka ukutani na kujichanganya zaidi mitaani.

    Kiza kilikuwa kimeshaufunika mji wa Iringa.



    _____________

    Baada ya kuzunguka mitaa ya Iringa kwa muda huku akiwa makini kuhakikisha kuwa hakukuwa na yeyote anayemfuata au kumfuatilia, Brey Jabba akaingia saluni na kumuelekeza kinyozi amnyoe ndevu zake zote za kidevuni na zile za mashavuni, akabakisha mustachi tu. Akatoka hapo akiwa na muonekano tofauti kiasi na ule aliotoka nao Dar.

    Akazunguka zaidi mjini, kabla ya kuingia sehemu ya chakula cha “Mama Ntilie”, akaagiza wali wa maharagwe, ambao aliula kwa hamu sana. Kutoka hapo akazunguka zaidi mjini na kuingia saluni nyingine. Hapa akamuagiza kinyozi amnyoe upara, na alipotoka kwenye saluni hii alikuwa na muonekano tofauti na ule aliotoka nao kwenye ile saluni ya kwanza, na tofauti kabisa na ule aliokuwa nao wakati anatoka Dar. Alienda moja kwa moja hadi kwenye hoteli moja ya kawaida tu aliyoiona wakati alipokuwa akikata ile mitaa ya mji wa Iringa. Alichukua chumba kwenye ile hoteli na akiwa amejifungia chumbani kwake, aliamwaga kitandani vitu vyote vilivyokuwa mle kwenye lile begi alilopewa kule kwenye kambi ya jeshi, na kuanza kuvitathimini.

    Pamoja na vile alivyoviona hapo awali wakati analipekua haraka haraka lile begi, aligundua kuwa kumbe kulikuwa kuna simu ya kiganjani pia. Mpya kabisa, ikiwa na chaja yake ilhali hiyo simu yenyewe ikiwa imeshajaa chaji. Akaangalia vile vyetiu vya shule, kikubwa katia vile vikimnadi kuwa kuwa ni mhitimu wa chuo kikuu cha sokoine akiwa ni mtaalamu wa kilimo. Miaka mitano iliyopita.

    Akakunja uso.

    Zaidi ya hapo kulikukwa kuna barua iliyotoka makao makuu ya jeshi la wananchi wa Tanzania, ikiwa inamkubalia ombio lake la kujiuzulu jeshi nakufanya kazi binafsi, hii nayo ilikuwa imeandikwa miaka mitano nyuma.

    Akakunja uso zaidi.

    Pia kulikuwa kuna wasifu wake wa ajira kadhaa, yaani curriculum Vitae, au “CV”, ulioonesha kuwa alishahudumia jeshio la wananchi kwa miaka kumi, na baada ya akjpo ameshawahiun kuw amkuu wa usalama kwenye makampuni kadhaa makubwa ndani na nje ya nchi.

    Mwisho kulikuwa kuna barua iliyokuwa ikimtaarifu kuwa ombi lake la kazi ya ukuu wa usalama kwenye kampuni ya “ANAND Timber Mill” iliyokuwa Kilolo, yalikuwa yamekubaliwa na kwamba pindi afikapo Iringa mjini awasiliane nao kwa namba ambayo ilikuwa kwenye ile barua, nao watampa maelekezo ya namna ya kukifikia kiwanda hicho kilichokuwa kilometa zipatazo thelathini kutoka Kilolo.

    Brey akaguna huku akitabasamu.

    Haya yote yalikuwa mageni kwake, lakini aliyaelewa sana…na aliyatarajia kwa namna fulani. Alielewa ni nini kilichofanyika pale. Watu aliofanya nao kazi tayari walikuwa wameshamjengea historia mpya maishani mwake. Kama walivyokubaliana. Huu ndio ulikuwa mwanzo wa yeye kama yeye kutoweka kabisa kwenye uso wa dunia, na Brey Jabba, mwanajeshi mstaafu, na mtaalamu wa kilimo na mkuu wa usalama kwenye makampuni kadhaa, kuzaliwa.

    Akaichukua ile simu na kuipiga ile namba iliyokuwa kwenye ile barua ya kumpa ajira, yenye nembo ya kampuni ya ANAND Timber Mill, kiwanda cha mbao, na ile simu haikuita kabisa. Alijaribu mara mbili zadi, na kupata ujumbe kuwa ile namba anayoipiga, haipo.

    Akakunja uso.

    Akaitoa ile bahasha aliyopewa na Sandra, ambayo kufikia pale alikuwa ameishindilia kwenye mfuko wake wa suruali, na kuifungua.

    Akakuta kipande kidogo tu cha karatasi ndani yake, kikiwa kimeandikwa namba moja tu ya simu. Akacheka, akielewa ni kwa nini alikuwa haipati ile namba ya kwenye barua, lakini zaidi ni kwa nini alikuwa amewekewa ile simu mle kwenye lile begi dogo.

    Akaipiga ile namba iliyokuwa kwenye bahasha aliyopewa na Sandra.

    Simu ilipokelewa na sauti nzito kutokea upande wa pili.

    "Brey Jabba?"

    "That's me. Nani mwenzangu?"

    "Mjombaako hapa...Zibadu.Zidadu Mgina..." Sauti ilijitambulisha na Brey akamakinika.

    "Okay. mjomba...mi ndo nshafika Iringa hapa...sasa sijui tunaonanaje?"

    "Uko stendi?"

    "Hoteli..."

    "Okay...nitajie jina la hiyo hoteli na nitakuwa hapo usiku huu huu..."Mtu aliyejinadi kuwa ni mjomba wake aendaye kwa jina la Zidadu Mgina alimwambi. Brey akamtajia jina la ile hoteli.

    "Nakuja..." Zidadu alimwambia na hapo hapo akakata simu.

    Brey Jabba akabaki akiwa amekunja uso kwa tafakuri.Alizikagua zle silaha alizokuta kwenye lile begi lake. Zote zilikuwa vizuri. Akaingia bafuni kuoga. Akabadili nguo na kujilaza kitandani akiwa na moja ya zile bastola karibu kabisa ubavuni kwake.

    Alimsubiri Zidadu Mgina...mjomba wake.





    ______________



    Saa mbili baadaye simu ya chumbani kwake ikaita, na mhudumu wa mapokezi akamfahamisha kuwa kulikuwa kuna mgeni wake aliyejitambulisha kwa jina la Zidadu Mgina.

    “Mwambie asubiri…nakuja.” Brey alijibu, kisha akatoka nje ya chumba kile hadi pale mapokezi, akiwa makini sana, bastola yake ikiwa imetulia kiunoni kwake, kwa nyuma.

    Aliona watu kadhaa wakiwa pale mapokezi, lakini alipojitokeza tu eneo la pale mapokezi, aliona mtu mmoja wa makamu, mfupi na aliyejengeka kimazoezi akiinuka huku akitabasamu kwa furaha halisi ya mjomba aliyeonana na mpwaye waliyepoteana kwa muda mrefu, akimfuata huku akimnyooshea mkono.

    Ni nani huyu?

    “Oooh Brey, mwanangu! Imekuwa ni mkiaka mingi sana…” Yule bwana alisema kwa sauti huku akimfikia na kumpa mkono. Brey aliupokea ule mkono huku akiwa makini, lakini yule bwana alimvuta na kumkumbatia.

    “Tunahitaji kuongea faragha, Brey…inabidi uniamini kwa hili!” Alimnong’oneza.

    “Kuna kitu inabidi nikione kutoka kwako kwanza…hapo tutaweza kuongea…” Brey alimjibu kwa kumnong’oneza huku naye akimkumbatia kwa namna ya kuendelea kujenga ile picha ya kuwa wao ni mtu na mjombawe walikutana baada ya muda mrefu.

    Yule bwana alimshika mabega na kujirudisha nyuma huku akimtazama usoni kwa namna ya kumstaajabia mpwa wake aliyemkosa muda mrefu.

    “Doh uko vizuri sana…muonekano huu muafaka sana kwa “head of security” aisee” Zidadu alimwambia, akimaanisha kuwa muonekano wake ulikuwa unaendana sana na ile kazi aliyoandikiwa barua kuwa ameipata kule Anand Timber Mill, ya ukuu wa usalama; na hapo Brey akapata sehemu ya uhakika kuwa huyu ni mtu anayejua kuhusu mambo yanayomhusu.

    “Okay, tukae pembeni basi hapo kidogo, mjomba…” Brey alisema kwa sauti huku akimuelekezea sehemu ya mgahawa wa kawaida tu wa pale hotelini. Wakaketi. Brey akaagiza kahawa. Zidadu akaagiza chai ya rangi.

    “Okay, michezo ya kuigiza basi sasa…sina mjomba aitwaye Zidadu na wala sihitaji wajomba maishani…una nini kwa ajili yangu?” Brey alimkoromea kwa upole yule bwana, na Zidadu akatabasamu.

    “Najua…lakini huko tuendako, hivyo ndivyo nitakavyokutambulisha kwa jamii. Mpaka hapa elewa kuwa uko kwenye mikono salama. Jipange kisaikolojia kuishi maisha ya kijijini sasa…jiji ulisahau kabisa…” Zidadu alimwambia.

    “Nahitaji kuona kitu kutoka kwako mzee! Vinginevyo siwezi kukuami…” Brey alianza kumkoromea zaidi huku akiwa makini sana, lakini hata yeye alishangaa alipoona amewekewa kadi ya benki pale mezani. Yaani alichoona ni wakati ule mkono wa Zidadu ukirudi kule ulipokuwa, na sio wakati ukiipeleka pale mezani ile kadi.

    Mnh!

    Alimtazama yule bwana kwa udadisi mpya. Ule ulikuwa ni wepesi wa hatari sana. Alijijua kuwa yeye ni mwepesi lakini pale kama ingekuwa ni kudhurika basi yule bwana angeshamdhuru. Ndio maana alitaka kuongea naye sehemu ya wazi. Akawa makini naye maradufu, na Zidadu akamchekea.

    “Najua una kasi nzuri sana Brey…lakini hukudhani kuwa kuna anayeweza kuwa na kasi kuliko wewe?” Alimuuliza.

    Akili ikamtembea Brey. Alimtazama kwa makini zaidi yule mtu. Alitamani amuulize yeye ni nani, lakini alikumbuka jinsi yeye alivyomjibu Sandra alipoulizwa swali kama lile saa chache tu zilizopita. Akapiga kimya.

    “Nadhani hicho hapo ndicho kitu ulichohitaji kukiona…ili uniamini?” Zidadu alimuuliza. Brey akaafiki kwa kichwa.

    “Okay, there it is…” Zidadu akamwambia tena, akiwa ametulia kabisa, akimaanisha kuwa kile alichokitaka ndio tayari kilikuwa mbele ya macho yake.

    Brey akainuka.

    “Nisubiri hapa…” Alimwambia yule bwana, na Zidadu akamuashiria kwa mikono yake kuwa hilo halikuwa tatizo. Brey akatoka nje ya ile hoteli na kuvuka barabara hadi kwenye kituo cha kujazia mafuta kilichokuwa ule upande mwingine wa barabara. Pale palikuwa pana mashine ya kutolea pesa ya VISA, yaani ATM. Hiyo ilikuwa ndio sabau kuu iliyomfanya akae kwenye hoteli ile, maana alijua mtu aliyetakiwa kuonana naye angetakiwa aje na ile kadi ya benki ikiwa kwenye jina lake. Akaichomeka ile kadi, akaingiza namba za siri ambazo alikuwa akizitambua kwa kichwa, akaangalia salio.

    Moyo ukamlipuka.



    _______________







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog