Search This Blog

Monday 24 October 2022

DHIHAKA - 5

 









    Simulizi : Dhihaka

    Sehemu Ya Tano (5)





    ***



    HAKUISHIA hapo! Matukio ya Badi kunyimwa unyumba yakawa kama yameanza rasmi, lakini pia hata kama alipewa, haukuwa unyumba wenye utundu kama ilivyokuwa siku za nyuma. Vikwazo vya hapa na pale na visingizio vilivyoendelea kutolewa na Hija vikazidi kuikoroga akili ya Badi. Akayaona ni mabadiliko yaliyojitokeza ghafla na kumuweka njiapanda. Akashindwa kuelewa kwa nini yamekuwepo na imekuwaje yakaja ghafla!

    Hata hivyo, akasisitiza msimamo wake wa kumtaka Hija anapokuwa anataka kutoka lazima amuage. Hija akafuata masharti ya Badi, kila alipokuwa anataka kutoka ilibidi aage. Hali hiyo ikaleta mabadiliko kwa upande mmoja, kuwa Hija hawezi kutoka bila ya kuaga, lakini kwa upande wa pili, si kumzuia kutoka! Angalau kukawa na mabadiliko kidogo kwani ile tabia ya Hija ya kuchelewa kurudi nyumbani hadi muda wa usiku nayo ikawa haipo tena.

    Pamoja na kuridhishwa na kile alichokiona ni marekebisho aliyofanya kwa mkewe, lakini ile dhana ya kuwa huenda Hija anakwenda kuonana na bwana wake iliendelea kumtafuna. Na hilo akalijengea shaka huenda ni moja ya sababu ya kutopewa unyumba ipasavyo kama mwanandoa!

    Leo hapana! akakumbuka anavyokataliwa na Hija kuhusu haki yake ya kindoa. Akakumbuka kuna siku alijibiwa, Ah, na we’ kila siku!” ilhali mara ya mwisho alipewa unyumba huo karibu wiki mbili au tatu zilizopita! Hali hiyo ilimfanya ajione kama hayawani aliyekosa mwelekeo dhidi ya mkewe. Akatawaliwa na hasira!

    Akiwa ndani ya hasira hizo, Badi akawa anasomeka kirahisi na Hija. Kwanza alikuwa akinunanuna ovyo, lakini pia akawa na kisirani na kuwa mwanzilishi wa kutafuta viugomvi visivyo na sababu za msingi ili kwamba apate nafasi ya kumfokea Hija ili kumwonyesha kuwa yeye ndiye baba mwenye nyumba na ana uwezo wa kumwondoa humo ndani wakati wowote! Hija akagundua hiyo ni mikwara! Na alijua ilitokana na nini.

    Usiku mmoja, wakiwa kitandani. Hija akamwanzishia utundu wake uliokuwa umeshakuwa adimu kwa Badi, lakini pia ndiyo yalikuwa maradhi ya Badi. Akajua wapi pa kuanzia kuzicheza kete zake na wapi pa kumalizia. Akamchezea Badi kama bingwa wa bao anavyozicheza kete zake. Akazicheza kwa ufundi wenye utukutu, hatima ya yote akamsikia Badi akigugumia kwa kelele na kujiachia kama aliyepigwa risasi!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kutulizwa kwa kitulizo hicho, Badi alijikuta akiingiwa na kujiamini kuwa mambo yamerudi kwenye reli. Siku chache tena akaanza kumchokoza Hija kimapenzi ili ikibidi arejeshewe aliyoyafanyiwa kwa mara ya mwisho. Badala ya kufanyiwa, akaishia kukumbana tena na viwiko vilivyotua kwenye mbavu zake. Safari hii akashindwa kukaa nalo moyoni baada ya kukiri umefikia wakati wa kupata msaada wa mawazo. Akamwona Rajabu!

    “Mi” nashindwa kumwelewa mke wangu!” Badi alimlalamikia Rajabu wakiwa baa wanakunywa.

    “Vipi tena?” Rajabu aliuliza na kuwa makini usoni.

    Badi akamlamimikia Rajabu kuhusu visa anavyofanyiwa na Hija, akamwelezea anavyoupata unyumba kwa shida. “Nimekuwa sina furaha na ndoa yangu!”

    Kama vile hakuwa na haraka ya kulijibu hilo, Rajabu alimwangalia Badi mara moja, kisha akainamia meza. Alipomwangalia tena akawa na swali. “Unampenda mkeo?” alimuuliza Badi huku akimwangalia usoni.

    “Mbona sana tu!” Badi alijibu kwa kujiamini. “Ni yeye tu ndiye mkorofi!”

    Rajabu akakivuta kimya kingine.

    “Unadhani kwa nini anakufanyia hivyo?” hatimaye Rajabu aliuliza tena.

    Badi alianzia na kupiga kite, kisha akamalizia kwa kusema, “Au sijui ana bwana yule mwanamke?” hakutaka kukiri, lakini moyoni mwake alikubali kuwa lazima mkewe ana bwana nje!

    Rajabu hakujibu, kwa sababu alimwona mwenzake kama aliyekuwa akizungumza peke yake.

    “Lakini inawezekana akawa na bwana!” Badi alihitimisha, safari hii akiwa amekusudia kumlenga Rajabu.

    “Huoni kama ulifanya haraka kumuoa?” Rajabu aliuliza.

    “Lakini mwenyewe alikubali nimuoe!”

    “Hukulazimisha?”

    Badi akatulia ghafla akamwangalia Rajabu. “Una maana gani?”

    “Siamini kama Hija alikuwa tayari kuolewa. Unakumbuka nilikuuliza kama unamjua vizuri?”

    “Ndiyo nakumbuka.”

    “Ulijiuliza kwa nini nilikuuliza vile?”

    Badi hakujibu, akabaki kumwangalia machoni Rajabu.

    “Sitaki kuingilia ndoa yako Badi, lakini ninachojua ni kwamba ulifanya haraka kumuoa Hija. Ulitakiwa umjue kwa undani kabla ya kufikia uamuzi wa kumuoa.”

    “Nimekuelewa!” Badi alisema.

    Rajabu akawa kama aliyeshangaa, akamwangalia Badi katika hali ya kutomwelewa kwa nini alisema vile.

    “Kwa hiyo umenielewa?” Rajabu aliuliza huku akiwa na shaka na kauli ya Badi.

    “Nimekuelewa Rajabu,” Badi alimhakikishia.

    Rajabu alimwangalia Badi kwa macho ya shaka, lakini kama vile alijua alikuwa anaangaliwa, Badi akawa hayatulizi macho yake usoni kwa Rajabu.

    “Kwa hiyo utafanya nini?” Rajabu aliuliza.

    Badi akaduwaa. Alionekana kutatizwa na swali la Rajabu. “Kivipi?” aliuliza.

    “Si ulisema umenielewa?”

    “Ndiyo nimekuelewa.”

    “Kwa hiyo?”

    “Najua mwenyewe nitakavyofanya!”

    Ingawa Badi alimjia na hoja ya kunyimwa unyumba, lakini Rajabu alikusudia kutaka kumjadili Hija kitabia. Akagundua, Badi hakuwa tayari kulijadili hilo. Palepale akatambua kuwa, hata Badi mwenyewe alikwishaanza kuzigundua tabia za mkewe za kukosa uaminifu kama alivyodai awali kuwa mkewe huenda ana bwana nje! Lakini akashangaa kumwona mtu huyohuyo akikwepa kuendelea kumjadili mkewe!

    Kwa upande wa Badi, akili yake ilikwishalijua lengo la Rajabu, alimwona mwenzake huyo akitaka kuuchambua upungufu wa mkewe ambao hakuwa tayari kuusikiliza. Ingawa alikuwa akiandamwa na dhana ya kiasi kikubwa kwamba Hija anatoka nje ya ndoa, lakini hakuwa tayari kuukabili ukweli huo kutoka kwa mtu mwingine! Na moja ya sababu ya kutokuwa tayari ni kuhofia kupewa ushawishi wa kuja kugombana na mkewe!

    Rajabu akiwa ameligundua hilo, akabadilisha hoja, akaleta hoja ya mpira!



    ***





    ***



    KIKAO hicho ukawa mwanzo wa urafiki wao kuanza kusuasua. Kila mmoja alijikuta akimwangalia mwenzake kwa mtazamo tofauti. Rajabu alimwangalia Badi kama mwanamume aliyewekwa kiganjani na mwanamke, huku Badi akimwona Rajabu kama anayetaka kumgombanisha na mkewe!

    Ingawa Rajabu alianza mapema kupunguza safari za kwenda nyumbani kwa Badi tokea amuoe Hija baada ya kutoridhishwa na tabia za Hija, lakini kikao hicho kikawa kama kimetoa hatima ya urafiki wao. Akaacha kabisa kumtembelea Badi nyumbani kwake, na hilo Hija akaligundua!

    Tokea awali, Hija hakumpenda Rajabu baada ya kugundua kuwa, Rajabu alikuwa akiwachukia shoga zake na alikuwa akiwaangalia pamoja na yeye mwenyewe kama makahaba wenye tabia ya kuiba wanaume wa watu! Hakuwa na uhakika kama Rajabu alikuwa akijua kama anamchukia, lakini alikuwa na uhakika Rajabu hakutaka yeye aolewe na Badi! Na hilo ndilo lililomshangaza siku alipomsikia Badi akimchagua yeye Rajabu awe mshenga wake!

    Kutoonekana ghafla kwa Rajabu kutofika hapo nyumbani kulimfanya Hija ahisi kuna mushkeli uliotokea kati ya watu hao wawili, Badi na Rajabu!

    “Rajabu sijamwona akija?” Hija alimuuliza Badi wakiwa nyumbani.

    Swali hilo likamfanya Badi akumbuke mara ya mwisho alivyokuwa na Rajabu wakimjadili Hija.

    “Sijajua kwa nini,” Badi alijaribu kuficha huku nafsi yake ikimsuta kwa kuijua sababu inayomfanya Rajabu asije.

    “Au mlikorofishana?”

    Swali hilo likamfanya Badi ayakwepeshe macho yake kumwangalia Hija. “Tukorofishane kisa nini?”

    “Ah, sijui wenyewe!” Hija alisema na kuonekana kuupuuzia mjadala huo.

    Badi akajiona kama hamtendei haki mkewe kutomweleza ukweli ambao aliamini ungechukua nafasi ya kumwonyesha ni namna gani anavyompenda.

    “Yule Rajabu naye wakati mwingine anakera!” Badi alianzisha tena mazungumzo hayo.

    Hija akatambua kuna walakini uliotokea kati yao. “Anakukera nini?” aliuliza.

    “Ah..,” Badi alisema kisha hakuendelea kama vile kuukatisha mjadala huo.

    Hija akavutwa na kusita kwa Badi. Akamwangalia machoni bila ya kutamka lolote.

    Kitendo cha kuangaliwa na Hija ikawa kama kichocheo cha kutaka kumwonyesha mkewe anavyompenda.

    “Wakati mwingine huwa anakusemasema, mi’ sipendi!” Badi alisema na kuununisha uso wake.

    Hija akavutwa na kauli hiyo, lakini hakuonyesha mshawasha wa wazi. Akajenga utulivu na kuunda tabasamu lisilotafsirika, kwa upande mwingine alionekana kama akisanifu zaidi.

    “Ananisema mimi?” hatimaye Hija aliuliza kwa sauti iliyoingia uzito kidogo huku mdomo wake akiupindisha kwa dharau.

    “Ah, unajua hakupenda nilivyokuoa!” Badi alibwabwaja.

    “Mbona hilo nalijua!” Hija alisema kama kwamba jambo hilo halikuwa na muhimu kwake. “Kwani alikwambiaje?”

    “Anakuona siyo mtulivu.”

    Akionekana kujua namna ya kucheza na Badi, Hija aliamua kutoijibu hoja hiyo, alijua kwa kufanya hivyo kungemfanya Badi azidi kujieleza kwa undani.

    Kama vile akili yake ilikuwa ikishikiliwa na Hija, Badi akaendelea kubwabwaja. “Mi’ mtu akitaka kuingilia ndoa yangu, hatutaelewana!” aliuweka wazi msimamo wake kwa lengo la kumhakikishia Hija kuwa asiwe na hofu.

    “Wewe si ulimchagua awe mshenga wako? Kisha akawa mpambe wako bwana harusi? Leo ndiyo umegundua hana maana?”

    Badi hakujibu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kugundua kuwa Badi na Rajabu hawapo kwenye maelewano kama ya awali, kulimfanya Hija kutoliona tena tishio la kidudumtu wa kumpika maneno Badi. Akaubariki kimoyomoyo ugomvi huo uzidi kuendelea huku akijipanga vizuri kwenye lengo lake!

    Kwa kuwa alishakuwa na uhakika kuwa alimuweka Badi kiganjani, Hija akawa anajua kucheza na Badi mithili ya paka anavyocheza na panya aliyemkamata. Alijua namna ya kujigeuza kila alivyotaka, na alijua namna ya kumgeuza Badi kila alivyohitaji! Hija akawa mtawala wa nyumba! Alichotaka yeye ndicho kilichofanyika. Shoga zake wakaanza kuja hapo nyumbani kwa mapana na marefu. Kila walipokuja nyumba ilifurika kwa vinywaji vya bia na wakati mwingine hata pombe kali zenye bei ya juu zilinunuliwa.

    Vicheko na mazungumzo ya furaha kuzungumzia uhusiano wao na wanaume maarufu waliopo kwenye ndoa zao ndiyo ikawa ni ajenda zao kila wanapokutana huku Badi akiwa hayupo. Wapo wanaume waliozodolewa, waliosifiwa na kukashifiwa, kila mmoja akisifiwa kwa uwezo wake wa kipesa na matumizi yake au akipondwa kwa ubahili wake, huku wao wenyewe wakijisifu kwa jinsi wanavyowadhibiti wanaume kutokana na kuujua udhaifu wao.

    Kama magwiji waliokutana, shoga zake Hija walijua kuzichanganya na kuzicheza karata kadri na hali ilivyo. Walikuwa wepesi wa kubadilisha hoja na kuunganisha na hoja mpya ambayo haikuwepo! Majigambo ya kijivuni yalikuwa yakikatishwa ghafla pale Badi anaporudi nyumbani na kuwakuta. Hapo ndipo somo linapobadilishwa kwa ufundi wa hali ya juu. Sifa zinazomhusu Badi huanza kutiririshwa, mwanamume huyo akasifiwa jinsi anavyojua kumlea mkewe, na mkewe anavyojua kumlea yeye. Sifa hizo humwacha Badi akizifurahia na yeye mwenyewe kuzirudisha kwa vijembe vya utani wa hapa na pale.

    Sifa hizo alizokuwa akipewa Badi hazikwenda bure! Ulikuwa ni moja ya mkakati aliojipanga nao. Aliuanza kwa kuuandaa wiki nzima, wiki ambayo Badi alionyeshwa thamani ya penzi lililopo ndani ya ndoa lilivyo. Penzi la zamani likarudi kwa kasi kubwa. Wiki hiyo Hija alitoka mara kwa mara na Badi, wakaenda maeneo tofauti yenye mjumuiko wa watu wengi wenye nacho kama kwenye maduka makubwa ya Mlimani City, Msasani na mengineyo na wakati mwingine hata kwenye hoteli maarufu kwa ajili ya kula chakula cha usiku.

    Hija aliyatumia maeneo hayo kwa kudeka, akihakikisha anatembea huku akiwa ameukamata mkono wa Badi na wakati mwingine kuukumbatia. Alikuwa akionyesha jinsi anavyompenda mumewe na hali hiyo kufurahiwa na Badi aliyekuwa akihitaji kitu kama hicho kwa kuamini alikuwa akiwaonyesha watu waliokuwa wanaikosoa ndoa yake kuwa walikosea!

    “Badi, nataka kuchukua mkopo benki ili nifanye biashara ya duka kama da’ Fina,” Hija aliliachia kombora alilokusudia kulifyetua baada ya mikakati yake ambayo aliiona imefanikiwa.

    “Mkopo wa shilingi ngapi?” Badi aliuliza kwa utulivu huku sura yake ikionyeshwa kutokerwa na ombi hilo.

    “Nataka nichukue kama milioni hamsini.”

    “Milioni hamsini? Mbona nyingi?”

    “Kwa duka siyo nyingi, mbona da’ Fina analeta mali hadi za shilingi milioni themanini.”

    “Milioni themanini?” Badi aliuliza kwa mshangao.

    “Kwani wewe unalionaje duka lake? Unafikiri thamani uionayo mle ni ya shilingi milioni tano kama maduka mengine?”

    “Usijifananishe naye, duka lake ameanza nalo kitambo na ndiyo maana limekua na wateja anao. Wewe unayetaka kuanza ni tofauti na yeye. Unatakiwa uanze kidogo kidogo.”

    ‘Maduka ya sasa hivi yanaanza na kasi ya mwendo mdundo, mambo ya zamani kuanza kidogo kidogo utampata mteja gani? Duka sasa hivi linafunguliwa likiwa linang’aa kwa wingi wa bidhaa na hapo ndipo utakapowapata wateja.”

    “Sawa nimekusikia, kwa hiyo unataka nini kwangu?”

    “Unidhamini.”

    “Kivipi?”

    “Benki wanataka dhamana ya kitu kisichohamishika kama hati ya nyumba au shamba, na mimi sina!”

    Badi akanywea ghafla baada ya kuambiwa hivyo. Alijua kinachotakiwa hapo ni hati ya nyumba yake!

    Kama vile alikuwa akiyasoma mawazo ya Badi, Hija alimwangalia Badi usoni na kusema, “Wala usitie wasiwasi mume wangu. Kwa biashara ya duka? Mbona uwezo wa kulilipa deni hilo upo! Hata Fina alianzia kwa kukopa benki vilevile. Amemaliza deni lake, sasa anajilia kuku zake. Nakuomba usitie wasiwasi, niamini naweza. Kwanza duka litakuwa letu wenyewe, hesabu zote utakuwa unasimamia wewe!”

    Badi akakamatika.

    “Umeshazungumza nao huko benki?” Badi aliuliza.

    “Nimeshazungumza nao, Fina ndiye aliyenipeleka kwa Branch Manager,” akalitaja jina la benki. “Tawi la mjini. Anafahamiana naye na ndiye aliyemfanyia mpango wa kupata mkopo wake. Nimekwenda na nimezungumza naye pamoja na wahusika wengine, wameniambia kama ninayo hati ya nyumba yenye hadhi inayokubalika, hilo halina shida. Kwa hiyo wanachotaka ni hati ya nyumba au shamba.”

    Baada ya siku tatu za kumshawishi Badi, siku ya nne Badi na Hija wakaongozana pamoja hadi benki. Baada ya taratibu zote kuzikamilisha, Badi akamdhamini Hija kwa kuiweka rehani hati yake ya nyumba!



    *****



    KITENDO cha Badi kuiwekea dhamana hati yake ya nyumba, kikamwongezea Hija kiburi hasa baada ya fedha hizo kuingia kwenye akaunti yake binafsi iliyofunguliwa kwenye benki hiyo. Hali hiyo ikaleta kutoelewana kati ya Hija na Hassani humo ndani ya nyumba. Chanzo cha kutoelewana ni amri zilizokuwa zikitolewa na Hija kila kukicha hapo nyumbani. Leo anataka kufanyike hiki, kesho kile na nyingine zikimgusa moja kwa moja Hassani. Makabiliano ya mara kwa mara ya kujibizana kati ya Hassani na Hija ukawa mwanzo wa mifarakano kati ya mtu na shemeji yake. Hija akaichukua nafasi hiyo kumlalamikia Badi kuwa Hassani ni kiburi.

    “Mimi nitashindwa kukaa naye!” Hija alimwambia Badi.

    “Nitaonana naye!” Badi alimwahidi Hija.

    “Au mimi nitampisha humu ndani ili afurahi! Si ananifanyia hivi kutokana na nyumba kuwa ni ya kaka yake!”

    “Kote huko kwa nini?” Badi alimtuliza mkewe.

    “Ah, usije ukaona namchukia mdogo wako!”

    “Nimekwambia nitazungumza naye, si usubiri hadi hapo nitakapozungumza naye?”

    “Sawa, lakini mi’ sipendi nionekane mkorofi nikaambiwa nawachonganisha ndugu.”

    Badi akayabeba kichwa kichwa malalamiko ya Hija. Akamwona Hassani ni mkorofi. Akaanza kumchachamalia mdogo wake.

    “Kama unaona huwezi kukaa na shemeji yako bora urudi nyumbani ukakae na wazee!” Badi alimbwatukia mdogo wake.

    “Tatizo kaka unamsikiliza sana shemeji…”

    “Kwa hiyo unamfanya shemeji yako ni mwongo?” Badi aling’aka.

    Uelewano kati ya Badi na Hassani ukaingiwa na dosari. Hassani akaamua kumtafuta Rajabu na kumlalamikia kuhusu adha zimkutazo.

    “Kaka yako kwa yule mwanamke hageuzi! Namsikitikia!” Rajabu alisema. “Wewe siku hizi unaniona nikija pale nyumbani?”

    “Kwa kweli namwonea huruma kaka. Kuna kipindi wale shoga zake shemeji wakija, maneno wanayoyazungumza wakifikiri mimi sipo, wee acha tu! Nyumba sasa hivi kama yao! Lakini ipo siku kaka atakuja kujionea mwenyewe na hapo ndipo atakaposaga meno.”

    “Badi sasa hivi hashauriki lolote kuhusiana na yule mwanamke, nimejitahidi sana kumshauri kabla hata hajamuoa, lakini hakunielewa. Matokeo yake sasa ananitangazia kuwa nataka kumvurugia ndoa yake!”

    “Hata mimi nilimsikia shemeji na shoga zake wakikuzungumza kuhusu jambo hilo.”

    “Nina wasiwasi kaka yako hata yale tuliyokuwa tukiyazungumza kuhusu mkewe nayo kishamwambia!”

    “Mimi naona bora nihame tu pale nyumbani nirudi home kwa wazee, vinginevyo yule mwanamke nitakujamtia vibao! Eti naye kaka’angu kishaniwekea mikwara ya kutaka kuniondoa!”

    Rajabu alisikitika na kusema, “Hassani, siwezi nikauingilia ugomvi wako na kaka yako, nyinyi ni ndugu, mko tofauti na mimi. Mimi ni rafiki tu, lakini pia siwezi nikaingilia ndoa ya kaka yako ingawa mimi ndiye niliyekuwa mshenga na kuwa msimamizi wake kwenye harusi yake. Nina imani ipo siku Mungu atamwonyesha!”

    Kauli hiyo ya Rajabu ikawa kama iliyotabiri jambo kwa Badi!



    ***



    ILIKUWA siku ambayo Badi alikuwa mapumziko ya kazi. Alitoka nyumbani asubuhi akiwa na Hija, wakaingia kwenye gari wakaelekea mjini ambako alimwacha Hija akisimamia mafundi waliokuwa wakifanya matengenezo eneo litakaloanzishwa duka.

    “Si utanifuata kwa Fina jioni?” Hija alimuuliza Badi baada ya kuteremka kwenye gari.

    “Nitakupigia simu,” Badi alisema.

    “Ili iweje?”

    “Ikibidi tuonane maeneo ya Mwenge. Utamwambia Fina akupe lifti, sidhani kama atakukatalia kukuleta mpaka Mwenge kisha naye akarudi nyumbani kwake Kijitonyama.”

    “Kukataa hawezi, lakini itategemea safari zake. Pengine asiwe na mpango wa kurudi nyumbani mapema?”

    “Ndiyo maana nimekwambia nitakupigia simu kufahamu hali ikoje.”

    “Poa. Kwa hiyo ndiyo unakwenda Uhamiaji?”

    Badala ya kuitikia, Badi akaonekana kushtuka, kisha akapekua kwa haraka kwenye dawati la gari. “Hivi zile fomu ulinipa?” alimuuliza Hija.

    “Ah!” Hija alishtuka. “Nimezisahau kwenye kabati langu!” alisema.

    Badi akanyong’onyea. “Sasa tutafanyaje? Yule jamaa wa Uhamiaji ameniambia nifanye itakavyokuwa, lakini fomu ziwe mikononi mwake leo. Itakuwaje?”

    Kwanza Hija alizubaa na kumwangalia Badi. “Itabidi urudi nyumbani ukazichukue,” alisema huku akionekana kutokuwa na uhakika kama wazo lake lingepokewa kwa upole na Badi.

    “Nirudi tena Tegeta?” Badi aliuliza kama vile kitu hicho hakiwezekani.

    “Sasa utafanyaje wakati kila kitu kwenye fomu kimekamilika na leo zinatakiwa, na wewe unajua nahitaji pasipoti yangu itoke haraka. Na mimi ikitoka tu, nasafiri.”

    Badi akapiga kite cha kuudhika. “Lakini ilikuwaje na wewe ukazisahau wakati unajua pasipoti yenyewe unaitaka haraka? Unajua kilichonileta mjini ni kuzipeleka fomu zako kwa yule ofisa wa Uhamiaji, halafu unaniambia umezisahau!”

    “Sasa Badi, unafikiri nilifanya kusudi kuzisahau?”

    Badi akataka kumwambia uliofanya ni uzembe! Lakini hakuwa na ubavu wa kutamka hivyo! Akaishia kupiga kite cha kuhamanika.

    “Kwa hiyo utakwenda kuzichukua?” Hija alimuuliza Badi huku akimwangalia machoni.

    Badi akayahamisha macho yake. “Sasa nitafanyaje?” aliuliza swali linaloonyesha amekubali huku sauti yake ikilalamika.

    “Please darling, usichukie,” Hija alisema kwa sauti ya kudeka.

    Badi hakujibu!

    “Kwa hiyo mpenzi utakwenda kuzichukua?” Hija aliuliza kwa pozi zilezile.

    “Nikifikiria mafuta tuliyoyachoma bure hadi huku, halafu nirudi tena Tegeta, kisha nigeuze!”

    “Nitakutilia mafuta.”

    Badi akageuka kumwangalia Hija bila ya kutamka neno, kisha akaingiza gia kwenye gari. “Baadaye,” alisema.

    “I’m so sorry mpenzi, najua umekasirika,” Hija alisema kwa sauti iliyodeka zaidi kuliko kubembeleza.

    Badi akaliondoa gari.

    Eneo la Tegeta liko nje ya jiji la Dar es Salaam kwa takribani kilomita kumi na nane na Badi alipokuwa akirudi tena huko alijikuta akitaka kuliendesha gari kwa kasi ya kilomita mia moja kwa saa, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na wingi wa magari yaliyokuwa barabarani.

    Alifika nyumbani na kulisimamisha gari nje, kisha akaingia ndani.

    Aliingia chumbani kwake na kwenda kulifungua kabati la nguo lenye milango miwili. Upande mmoja wa mlango ulikuwa ukitumiwa na yeye mwenyewe, na upande wa pili wa mlango ukiwa ni wa Hija. Wote wawili walijenga mazoea ya kila mmoja kutofungua upande wa mwenzake labda itokee dharura kama iliyojitokeza. Kwa kuwa alishaambiwa na Hija kuwa akazichukue fomu hizo alizozisahau ndani ya upande wake wa kabati, Badi akaufungua upande wa Hija.

    Alizikuta fomu alizozifuata zikiwa usoni mwa ndani ya kabati. Akazichukua na kuzihakikisha kama ndizo zenyewe na zimetimia. Baada ya kuhakikisha, macho yake yakaangalia tena kwenye kabati kabla ya kulifunga. Akavutiwa na kiboksi chenye tembe za dawa. Akashawishika kukiangalia ili kujua dawa zake zinatibu nini. Akakifungua na kutoa kikaratasi cha ndani chenye maelezo, akakisoma. Akashtuka alipogundua ni tembe za kuzuia mimba!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Hija anatumia vidonge vya kuzuia mimba? alijiuliza kwa mshangao. Haraka aliyokuja nayo ikamwishia! Kugundua mkewe anatumia tembe za kuzuia mimba kukamchanganya. Kwa nini anatumia hizi tembe bila ya kushauriana? alijiuliza. Nini maana ya kuoana? Ingawa alikiri wakati mwingine suala la kupata mtoto ni maafikiano ya wawili kulingana na mazingira yaliyowazunguka, lakini lazima kuwepo na maafikiano hayo. Sivyo alivyofanya Hija! Badala yake amekuwa akizitumia tembe hizo kisiri! Kwa nini afanye siri? Hataki nijue?

    Akatoka chumbani kwa kasi ndogo, tofauti na ile aliyoingia nayo. Alirudi kwenye gari huku akihisi kichwa chake kutokuwa sawa. Na kadri alivyokuwa akiliendesha gari kurudi mjini ndivyo kasi yake ya uendeshaji ilivyozidi kupungua. Njia nzima aliliwazia tukio la kuziona tembe zile, akawa anawaza hili, anapangua lile. Anaingiza lile, anatoa hili. Hatimaye akarudiwa na dhana yake ya awali kuwa, huenda Hija ana bwana wa nje! Na anatembea naye bila ya kutumia kondomu! Na ndiyo sababu ya kujilinda asipate mimba! Lakini pia, kitendo cha mkewe kutotumia kondomu kulimrudisha kulekule kwenye dhana yake ya mwanzo kuwa, Hija bado alikuwa hajaachana na bwana wake wa zamani!

    Atakuwa nani?

    Lilikuwa pigo lililomwumiza! Dhamira ya kutaka kumkomesha huyo mtu ili asiendelee kutembea na mkewe ikamjia! Lakini kabla ya kumkomesha, ilibidi kwanza amjue! Na alijua vita hiyo asingeweza kupigana peke yake! Kulihitajika msaada kutoka kwa mtu mwingine. Akamfikiria Rajabu, akakiri asingeweza kumtumia. Yeye na Rajabu walishakuwa na ukakasi ndani ya urafiki wao, lakini huyo ndiye angekuwa mtu sahihi wa kusaidiana naye kumjua mtu anayetembea na mkewe!

    Rajabu alikuwa ni mwerevu wa mambo na alimwamini. Pamoja na kuwa ni msomi wa shahada ya Uzamili na aliyemzidi umri, lakini rafiki yake huyo alikuwa mtoto wa mjini mwenye uhusiano na watu tofauti kiasi kwamba angekuwa msaada mkubwa wa kuweza kupeleleza ni mshenzi gani anayemchukulia mkewe wake!

    Kwa mara ya kwanza, Badi alianza kujuta kuingia kwenye mfarakano na Rajabu, ingawa ulikuwa ni mfarakano wa kimyakimya, lakini alielewa mfarakano uliokuwepo kati yao si wa kumalizika kirahisi. Shutuma za hapa na pale alizisikia kutoka kwa watu wengine kuwa Rajabu alikuwa akimlalamikia kwa kumshutumu kumtangazia anaingilia ndoa yake! Angemwingia vipi tena kwa suala hilohilo huku akikiri ni kweli alikuwa akimtangazia hivyo! Badi akanywea!

    Uelewa huo ukamwondolea fikra za kuendelea kumwazia Rajabu baada ya kutambua asingekuwa msaada kwake. Mtu mwingine ambaye aliamini angeweza kumsaidia kwenye sakata hilo la kutaka kumjua mtu anayemchukulia mkewe, angekuwa ni mdogo wake; Hassani! Angeweza kumwomba mdogo wake amfanyie kazi hiyo ya kumpeleleza shemeji yake, lakini huko nako alikuona kukiwa na utata. Yeye na Hassani picha ilikuwa haiendi kati yao! Kisa kikitokana na Hija huyohuyo!

    Alikuwa akiujua mtazamo wa mdogo wake ulivyo dhidi yake. Hassani alikuwa akimtazama yeye kuwa ametawaliwa na mkewe! Lakini kama hiyo haikutosha, mara ya mwisho katika kugombana kwao, mdogo wake huyo alimwahidi angehama wakati wowote kwa madai ya kuchoshwa na lawama zinazotengenezwa na shemeji yake huku yeye akimbeba mkewe! Hilo aliliona ni onyo tosha kuwa asingepata ushirikiano kutoka kwa mdogo wake huyo! Lakini pia kutokana na uhasama uliopo kati yao, ungewezesha mdogo wake achukue nafasi hiyo kuivujisha siri hiyo kwa watu kuwa, mkewe anatembea nje ya ndoa!

    Akiwa ameelemewa na mkanganyiko unaomkabili, Badi aliwasili mjini na kuliegesha gari lake kando ya barabara jirani na jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya maegesho ya magari yaliyomo ndani ya uzio wa jengo hilo kujaa. Hakuteremka palepale! Kwanza alitulia ndani ya gari na kuendelea kuifikiria tuhuma anayomtuhumu mkewe kutembea nje ya ndoa!

    Alishusha pumzi kwa nguvu, akajifungua mkanda wa kiti na kufungua mlango. Aliteremka akiwa amezikamata fomu za Hija mkononi mwake. Akavuka barabara na kuelekea kwenye geti la kuingilia jengo hilo lenye Ofisi za Uhamiaji na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi. Akiwa bado na fikra zinazomchanganya huku akiwazia namna ya kwenda kumwona ofisa anayempelekea hizo fomu, Badi aliendelea kukosa utulivu kichwani.

    Hija! alimwazia tena mkewe. Fikra za kuwa kuna mtu anamchukulia kulimwuma mno!



    ***



    BAADA ya kuzikabidhi fomu za Hija kwa Ofisa wa Uhamiaji na kupewa maelekezo mengine yaliyomhusu Hija, Badi alitoka kwenye jengo hilo na kurudi kwenye gari lake. Akaingia kwenye mitaa ya katikati ya jiji kwa kufanya hili na lile huku akielewa kuwa alitakiwa amjulishe Hija kuhusu maagizo aliyopewa na Ofisa wa Uhamiaji.

    Moyo wake ulikuwa mzito kumwambia maagizo hayo. Hakujisikia kuongea na mkewe, kila wakati alikuwa akilifikiria tukio la kuziona tembe za kuzuia mimba alizozikuta nyumbani na ile dhana ya kuwa mkewe anamkosea uaminifu vikawa vinaendelea kumwumiza.

    Hija akapiga simu!

    Ikawa kama vile hakutarajia kitu kama hicho kingetokea baada ya kuona ni mkewe ndiye anayempigia. Akaiangalia simu yake inavyoita huku akipata kigugumizi cha kuipokea. Akaiacha ikiita hadi ilipokatika. Kupigwa kwa simu hiyo na kutoijibu kukawa kama vile alikuwa akihalalisha usaliti anaofanyiwa na Hija.

    Alitamani kumpata mtu wa kumzungumzia tatizo alilonalo kwa kuamini kufanya hivyo kungemwezesha angalau kulipunguza shinikizo la mawazo linalomkabili. Hata hivyo alijionya kuwa, tatizo alilonalo sio la kumropokea mtu yeyote madhali anamjua, bali ni tatizo linalostahili kuelezwa mtu anayeaminika na anayemwamini kama ilivyokuwa kwa Rajabu au mdogo wake, Hassani. Watu hao wawili wangekuwa ni watu mwafaka kuwaeleza. Kikwazo kikawa, wote hao amekorofishana nao!

    Kumkumbuka Rajabu kulimfanya azikumbuke baadhi ya kauli za rafiki yake huyo zilizowahi kumwonya kuwa, alikuwa akimpa sana Hija uhuru wa kutoka anavyotaka. Akamtaka amzuie asiendelee kuwa karibu sana na shoga zake. Ni maonyo ambayo hakuyasikiliza na yaliyomfanya amwone rafiki yake kuwa anaingilia ndoa yake! Hofu ya kuwa shoga zake Hija ndio waliokuwa wakimpoteza mkewe, sasa ilimwingia na kuukubali ukweli huo!

    Alikuwa na uhakika mtu anayemchukulia mkewe lazima angekuwa anafahamika na shoga zake Hija! Hao ndio waliokuwa wakizijua siri za mkewe kwa sababu wakati anaanzisha uhusiano naye, alimkuta akiwa na shoga zake hao. Uelewa huo ulianza kumpa tabu baada ya kujitambua kuwa, alikuwa akisanifiwa na shoga za mke wake! Wananifanya bwege! aliwaza. Na akaiona hiyo ndiyo sababu iliyokuwa ikimfanya mkewe kila wakati kutaka kwenda kushinda kwa shoga zake hao!

    Tuhuma hizo ambazo alikuwa hana ushahidi nazo, alikiri kuwa, zisingeweza kumpa nafasi ya kumchukulia hatua yoyote Hija kabla ya kuwepo ushahidi. Pamoja na uzito wa tuhuma anazomtuhumu nazo mkewe zingemwezesha kumpa msukumo wa kuanza kufikiria mambo ya kupeana talaka, lakini haikuwa hivyo kwa Badi.

    Mapenzi aliyokuwa akimpenda Hija yakawa mwanzo wa kikwazo cha kuufikiria uamuzi huo. Badala yake akafikiria njia mbadala ya kukabiliana na tatizo hilo. Akajipanga awe mkali! Msukumo wa kuamini kuwa, mkewe alikuwa akiyafanya hayo kutokana na yeye kutokuwa mkali ndiyo chanzo cha matatizo yote hayo, ulimwingia. Akajipa angalizo, anachotakiwa kukifanya ni kumwonyesha Hija ukali ili atambue nani mume, nani mke ndani ya nyumba!

    Aliamini hilo lingefanikiwa kumtuliza mkewe hasa baada ya kuufikiria upendo aliomwonyesha wa kuiweka hati yake ya nyumba kuwa dhamana ya kupata mkopo wa benki. Alikuwa na uhakika hiyo ingekuwa ni silaha ya kumfanya Hija amsikilize.

    Kuziwazia shilingi milioni hamsini za mkopo zilizoiweka nyumba yake rehani, kwa mbali kulimuweka kwenye wasiwasi aliokuwa akijaribu kuukanusha kwamba, hajacheza kamari. Pamoja na kutumia nguvu ya kifikra kukanusha, lakini moyo wake ulielea kwenye kina kikubwa cha mashaka pale alipojiuliza, je, endapo atamjua mtu anayemchukua mkewe, atafanya nini? Ampe talaka mkewe? Hapo ndipo kamari aliyoicheza alipoiona!

    Swali hilo likafanya mapigo yake ya moyo yafanye mshtuko baada ya kubaini kuwa, kumpa talaka mkewe kusingewezekana! Vinginevyo, kungemaanisha awe tayari kuziachia shilingi milioni hamsini alizokopeshwa mkewe zikiyeyuka!

    Hakukuwa na mkataba wowote kati yao zaidi ya makubaliano ya maneno yaliyotamkwa na mkewe kuwa, pesa za mauzo ya dukani zingetumika kuurudisha mkopo huo benki. Hiyo ilimdhihirishia kuwa, mkataba wa hiari uliokuwepo kati yao, ni ndoa. Uwepo wa ndoa yao, ndiyo matumaini pekee ya kulipwa kwa mkopo huo kama Hija alivyoahidi. Lakini endapo atachukua hatua ya kumpa talaka mkewe endapo itadhihirika kuwa ni kweli mkewe anatembea nje ya ndoa, ni wazi Hija hatalilipa deni hilo baada ya kuachwa! Hiyo ndiyo kamari aliyokuwa akiiona na ndiyo iliyokuwa ikiupeleka moyo wake puta!

    Kulikuwa na sababu kadhaa alizoziona kwa Hija kutolilipa deni hilo endapo angeichukua hatua ya kumpa talaka wakati itakapodhihirika ni kweli upo ukosefu wa uaminifu unaofanywa na yeye. Kwanza, ni kule kukubali pesa zote za mkopo kuingia kwenye akaunti binafsi ya Hija. Hiyo ilimaanisha kwamba, ni Hija pekee ndiye mwenye uwezo wa kisheria kuzitoa pesa hizo benki. Hivyo kumpa talaka Hija, kungemfanya aondoke kiulaini na milioni hamsini kibindoni! Pili, ni kule kumwachia Hija kulisajili duka wanalotarajia kulifungua kwa kuandikisha jina lake. Hiyo ingemaanisha kwamba, kumpa talaka Hija, kungemwacha awe huru na duka hilo! Sababu ya tatu ndiyo iliyokuwa ikimrusha roho zaidi. Hakukuwa na mkataba wowote wa maandishi unaomtaka Hija alilipe deni hilo benki! Kwa maana nyingine, dhamana yote ya deni alikuwa amejitwisha nayo mwenyewe Badi! Kwa maana hiyo, kumpa talaka Hija, kungemgharimu yeye mwenyewe Badi kutafuta pesa kwa njia nyingine kuulipa mkopo huo!

    Utambuzi huo ukawa ni gharika ndani ya kichwa chake! Akahisi kijasho chembamba kikitiririka nyuma ya uti wake wa mgongo baada ya kukiri kuwa, kusingekuwa na uwezekano wowote wa kumdai mkewe pesa hizo endapo atateleza kidogo kwenye uamuzi utakaofanya wawe mbali kindoa!

    Hija amekamata mpini wa ndoa yao! alikiri.

    Badi alijaribu kuituliza presha iliyomwingia kwa kujipa matumaini kuwa, Hija asingeweza kumfanyia kitu kama hicho endapo ndoa yao itadumu, lakini pia akakiri wa kuidumisha ni yeye na si Hija!

    Ukweli huo uliojidhihirisha, na ile dhana anayomtuhumu mkewe kuwa anamsaliti vikawa vimemuweka njiapanda! Hali halisi ilikuwa ikijionyesha mbele yake kuwa, hata kama atagundua ni kweli mkewe ana bwana anayetembea naye, bado hakutakiwa hasira hizo azipeleke kwa Hija! Hija alikuwa hagusiki! Alichotakiwa ni kuvumilia kwa kuikubali hiyo hali ili nyumba yake iliyokuwa rehani isije ikapotea!

    Simu yake ikaita tena. Ikamshtua na kumtoa kwenye mawazo yake. Alipoiangalia akaliona tena jina la mkewe. Alikwishasahau kama awali alipigiwa simu na mkewe ambayo hakuipokea. Safari hii akawahi kuipokea!

    “Nimekupigia mara ya kwanza mbona hukuipokea?” Hija aliuliza baada ya Badi kuipokea simu yake.

    “Nilikuwa niki-drive, isitoshe trafiki walikuwepo,” Badi alidanganya.

    “Uliziona?” Hija aliuliza.

    Badi akajua mkewe anaulizia fomu zake za Uhamiaji. “Ndiyo niliziona,” alijibu.

    “Kwa hiyo umeshazipeleka?”

    “Tayari.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Anasemaje?”

    “Kesho asubuhi unatakiwa upeleke picha zako na kuchukuliwa alama zako za vidole. Nadhani tutalizungumza vizuri tutakapoonana,” Badi alisema huku akiiona akili yake haipo kwenye utulivu.

    “Kwa hiyo jioni utanifuata kwa kina Fina?”

    Swali hilo likawa kama limemtonesha kidonda. Akataka kumwambia, kwani lazima uende huko kwa kina Fina? lakini akapata kigugumizi. Akajipa imani kuwa suala hilo asilifanyie haraka kulizungumza kwenye simu, akaamini upo muda ambao angeutumia kulizungumzia na kwa mpangilio mzuri.

    “Nitakupigia simu kukujulisha,” Badi alisema.



    ***





    ***



    KABLA ya kumfuata Hija dukani kwa Fina, Badi alikuwa na uhakika muda huo ambao anajiandaa kwenda, Fina angekuwa ameshafunga duka lake. Taswira ya kumwona mkewe akiwa yuko baa na kundi la kina Fina, pengine wakiwa wamezungukwa na wanaume ikamjia.

    Pamoja na kukiri kuwa Hija alikuwa ameshika mpini katika suala zima la ndoa yao, lakini iliendelea kumwumiza baada ya kutafakari uwepo wa mkewe baa kuuhusisha na uwepo wa bwana wake! Ile hali ya kujiona kuwa hana uwezo wa kumfanya lolote mkewe nayo ikampa hasira ya kutamani kuua mtu! Shinikizo la kutaka kumjua mtu anayetembea na mkewe likawa linampanda kwa jazba.

    Akampigia simu Hija akamwambia kuwa angechelewa kidogo kumfuata kutokana na udhuru ambao ungemchelewesha. Aukataja muda ambao angefika. Hakukuwa na udhuru ambao ungemchelewesha, lakini alipanga hivyo kwa lengo la kutaka kumhadaa Hija aelewe angechelewa kufika. Na angeitumia hadaa hiyo ili afike mapema kwa lengo la kuvamia, akiamini uvamizi wake ungewezesha kumkuta mwizi wake akiwa hajaondoka!

    Awali wakati alipokuwa akimtaarifu mkewe kuwa angechelewa kumfuata, Badi alipatwa na wasiwasi huenda Hija angemlalamikia kwa kuchelewa kwake kwenda. Lakini hali ikawa tofauti. Hija hakufanya manung’uniko yoyote, badala yake akaipokea taarifa hiyo kama kitu cha kawaida. Kwa mazingira hayo, Badi akaamini, mkewe alikuwa akifurahia kuchelewa kwake ili aendelee kuwa huru na bwana wake!



    *

    Badi aliwasili kwenye hiyo baa saa mbili kabla ya muda aliokuwa ameahidi. Kundi la kina Fina na Fina mwenyewe walikuwepo, lakini Hija hakuwepo!

    Kwenye meza aliyokaa Fina akiwa na Ester pamoja na Mahadia, kulikuwepo na wanaume wanne. Kati ya wanaume hao, wawili alikuwa akiwajua. Mmoja alikuwa ni bwana wa Fina na mwingine akiwa bwana wa Mahadia. Wawili wengine ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuwaona.

    Kutokuwepo kwa Hija na kuwasili kwa Badi mapema hakukuonyesha kuwashtua Fina na wenzake. Badala yake walimkaribisha kwa bashasha za hapa na pale!

    Akiwa amejiunga na kundi hilo, Badi akagundua jambo. Kati ya viti vilivyokuwepo, kimoja kilikuwa hakina mtu! Akahisi kiti hicho kilikuwa kimekaliwa na Hija na akachukulia huenda ametoka kwenda chooni kama si kwa shughuli nyingine ya muda mfupi. Mshawasha wa kutaka kuhoji wapi mkewe alipokwenda ukamjia, lakini akahofu kuonekana kuwa ana papara. Akaamua kuujenga utulivu uliokuwa ukimwadhibu ndani kwa ndani. Fina akamwagizia bia.

    “Hija yuko wapi?” Badi aliuliza baada ya kupiga fundo dogo kinywani mwake. Sauti yake alikuwa ameishusha ili iweze kusikiwa na Fina pekee aliyekuwa jirani na alipokaa.

    “Msubiri, atakuja sasa hivi,” Fina alimhakikishia kwa sauti ya kujiamini.

    Badi akamshangaa Fina. Kwani mara tu baada ya kumhakikishia kwamba Hija angerudi baada ya muda mfupi, Fina alimpigia simu Hija.

    “Hebu rudi, mumeo amekuja!” Fina alisema kwenye simu huku sauti yake ikionyesha utawala wa kumdhibiti Hija.

    Ujumbe huo wa kutoka kwa Fina kwenda kwa Hija ukamshtua Badi. Ulionekana kutaka kumwonyesha kuwa, Hija hayuko mbali, au kwa maana nyingine walikuwa naye hapohapo. Kuna mchezo unaochezwa! Badi alijipa angalizo.

    “Kwani amekwenda wapi?” Badi alimuuliza Fina kwa sauti ileile ya chini.

    “Msubiri sasa hivi anakuja,” Fina aliendelea kusema kwa kujiamini.

    Badi akatambua kujiamini kwa Fina ni kutaka kumtuliza ili asiendelee kuhoji.

    Ilikuwa baada ya dakika kumi kupita, bila ya kutarajia, Badi akavutwa kuliangalia gari lililowasili na kusimama kwenye nyumba jirani na baa waliyokuwepo huku taa nyekundu za breki za gari hilo zikiwaka kwa mng’ao unaoonyesha ni jipya au lipo kwenye hali nzuri. Kukawa hakuna aliyeteremka baada ya kusimama. Badi akapuuzia. Lakini baada ya dakika kama mbili macho yake yakavutwa na mlango wa mbele wa abiria uliofunguliwa. Akamwona mwanamke akiteremka. Akashtuka baada ya kujikuta akimfananisha na mkewe!

    Akamtambua kuwa ni mkewe! Alikuwa amevaa nguo ileile aliyokuwa ameivaa asubuhi alipokuwa amemleta mjini. Palepale akaiona sababu ya gari hilo kwenda kusimama nyumba ya jirani; Hija alikwishajua kuwa yeye yuko hapo, na ili asionekane wakati wa kuteremka ndiyo sababu ya kwenda kusimamia huko!

    Baada ya kugundua kuwa ni Hija ndiye aliyerudishwa na gari, Badi alichemkwa na ghadhabu ambayo ilimpa wakati mgumu kuidhibiti. Ili watu waliokuwepo hapo wasitambue kuwa yuko kwenye hali hiyo, ikamlazimu azuge kana kwamba hakumwona mkewe alivyorudishwa na gari.

    Badi aliinua glasi yake yenye bia kutaka kunywa, lakini kabla hajaifikisha mdomoni akagundua mkono wake ulikuwa ukitetemeka! Akairudisha mezani! Akamwangalia Fina kwa kuiba kutaka kujua kama amekishuhudia kitendo cha kutetemekwa na mkono. Akamwona amejiinamia kama mtu anayewaza kitu. Kujiinamia kwa Fina kukamwelewesha kuwa, Fina amemwona wakati akiliangalia tukio la kurudishwa Hija!

    Badi alijaribu tena kuinua glasi ya bia, safari hii kasi ya kuipelekea kinywani ikawa kubwa kuepuka kujimwagia endapo kitendo cha kutetemeka mkono kama kingeendelea kuwepo. Ghafla akaihisi bia ikiwa chungu, ladha yote ya bia ilikuwa imepotea!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Badi akamwona Hija akimjia kwa nyuma kwa mwendo wa kunyata wa kutotaka kujulikana kuwa yuko nyuma yake. Akajua mkewe anataka kuja kumfanyia masihara ya kumziba uso. Lengo la mkewe lilimkera kwa sababu hakuwa kwenye hali ya kutaka masihara!

    Ukawa ni wakati mwingine mgumu aliokuwa anakabiliana nao baada ya kujionya kuwa, kitendo chochote cha kuitumikia ghadhabu inayomchemka kwa wakati huo kingeleta taswira isiyopendeza kati yao ndani ya hadhira iliyokuwepo hapo. Alikuwa na uhakika kama angeiendekeza hasira iliyokuwa ikitokota, angeupoteza mhimili wa kujizua kwa kumpa Hija kipigo cha nguvu, kitendo ambacho aliamini kingemwaibisha yeye na Hija! Watu wangeamulia, lakini pia wangemdharau kwa kumpiga mkewe hadharani!

    Fikra hizo zikamlazimisha awepo kwenye shinikizo la kujizuia asionekane ameghadhibika. Hasira zikazidi kumteketeza kutokana na uvumilivu aliokuwa akiufanya wakati viganja laini vya mkewe vilipomvamia kwa nyuma na kuuziba uso wake huku matiti ya Hija yakiwa yamemlalia kisogoni. Harufu ya manukato ya Hija iliingia kwenye pua zake na kumfanya ajione ameegemewa na mtu aliye karibu yake kimaisha. Hakujihangaisha kumtaja aliye nyuma yake kama ilivyotarajiwa, badala yake, Badi aliiondoa mikono ya mkewe kutoka usoni mwake.

    “Manukato yako yananidhihirishia kuwa ni mke wangu!” Badi alisema huku akiwa bado ameishikilia mikono ya Hija. Ilimwuma kutaja neno ‘mke wangu’ wakati alikuwa na uhakika Hija alitoka kwa mwanamume!

    Hija akainama zaidi na mikono yake kuegemea kwenye kiti alichokalia Badi na kumbusu mumewe shavuni. “Nadhani sijakuweka sweetie,” alisema.

    Ulaini wa mikono ya mkewe na ubaridi wa midomo iliyombusu shavuni, ulimuweka Badi kwenye dhana kuwa, muda mfupi uliopita Hija alitoka kuoga!

    “Kwani ulikuwa wapi?” Badi aliuliza kwa kuidhibiti sauti yake ionekane ni ya kawaida.

    “Wakati anti Fina ananipigia simu, nilikuwa na kama dakika tatu nne tokea nilivyoondoka kwenye ukarabati wa duka. Mafundi walinichelewesha sana kuondoka, ilinibidi niwasubiri hadi wamalize. Mbona hukuniambia kama unakuja?”

    Nadanganywa! Badi aliwaza na kukiangalia kiti kilichokuwa hakina mtu huku akijipa uhakika, kiti hicho kilikuwa kimekaliwa na Hija kabla ya kuondoka na kurudi tena! Akajilaumu kwa kutokuuliza kuhusu kiti hicho. Aliamini kama angemuuliza mapema Fina, ana hakika jibu ambalo angepewa lingekuwa linatofautiana na kauli anayoizungumza hapo Hija! Na angekuwa amemnasa vilivyo mkewe!

    Akijua ameipoteza nafasi ya wazi ambayo angembana nayo mkewe, Badi alijikuta akilijibu swali la mkewe kwa kusema, “Nilijua ningekukuta hapa.”

    Fina akamwita mhudumu. “Tuletee bia mbili, naona shemeji yangu kishamaliza,” alisema huku akimaanisha bia nyingine ipelekwe kwa Hija.

    “Shemeji hapana!” Badi aliwahi kusema. “Nataka kuondoka!”

    “Basi mwache mwenzako anywe hata moja,” Fina alisema.

    “Atakwenda kunywa hata nyumbani,” Badi alisema.

    Wanaume waliokuwepo pale nao wakajaribu kumtaka Badi awepo japo kwa dakika chache zijazo, lakini Badi alisimamia kwenye msimamo wake.

    “Basi shoga kesho,” Fina alimuaga Hija.

    Hija akaagana na watu waliokuwepo kwenye meza hiyo kama alivyofanya Badi, kisha wote kwa pamoja wakaingia kwenye gari.

    “Unawahi nini?” Hija aliuliza baada ya mwendo wa mita chache kutoka eneo waliloondoka. Swali lake lilionyesha kutoridhishwa na uamuazi wa kuondoka.

    Itulize akili yako! Badi alijionya. “Nimechoka sana, akili yangu yote iko nyumbani,” alisema.

    “Basi si ungeniachia japo ninywe hata bia moja!”

    Kitu alichokifanya Badi ni kugeuka na kumwangalia Hija mara moja, kisha asiseme lolote.

    Hija akakiona kitendo hicho. Akajua hoja aliyomwambia mumewe ilimkera! Lakini ili na yeye aonyeshe kuwa hakufurahishwa na uamuzi wa Badi wa kuondoka mapema na kumkosesha kuzungumza na shoga zake, lakini pia kumkatalia kunywa japo bia moja, akaamua kununa ndani ya gari kwa kukaa kimya!

    Hali hiyo ya kununa na kukaa kimya kwa Hija kulimfanya Badi ashukuru. Hakuwa kwenye kujisikia kuzungumza, akili yake ilikuwa imeelemewa na mkusanyiko wa matukio yanayomhusu mkewe kwa siku nzima ya siku hiyo. Ukimya wao ndani ya gari ukawa ni faraja kwake. Hali hiyo ikaendelea hadi walipowasili nyumbani.

    Tukio hilo likawa limeanzisha kisirani kwao. Mara baada ya kufunguliwa geti na mtumishi wao na kuliingiza gari, wote wawili waliteremka bila ya kusemezana. Wakaingia nyumbani kimyakimya huku sauti pekee zilizosikika ni kuitikia ‘shikamoo’ waliyopewa na msichana wao wa kazi.

    Wakati Hija alipokuwa akibadilisha nguo, Badi aliingia kuoga, alipotoka alimkuta mkewe akiwa amekaa mbele ya meza ya kuvalia huku amevaa nguo ya kulalia. Alikuwa akijipaka krimu ya usiku kabla ya kulala.

    Badi alivaa pensi na fulana, kisha akamwangalia Hija.

    “Huogi?” Badi alimuuliza Hija.

    “Nimechoka!” Hija alijibu kwa sauti iliyosikika kwa shida kuonyesha kisirani.

    “Umechoka kuoga?” Badi aliuliza kwa utulivu.

    Hija hakujibu.

    Badi akaduwaa huku akimwangalia mkewe aliyekuwa akiendelea kujipodoa. Mlango ukagongwa. Badi pekee ndiye aliyegeuka kuangalia mlangoni huku Hija akiendelea na shughuli ya kujiremba. Badi akaitikia.

    “Chakula kiko mezani,” msichana wa kazi alisema akiwa nje ya mlango.

    Badi akaenda kuufungua mlango. “Sawa tunakuja,” alimwambia mtumishi wao na kurudi tena ndani huku akiufunga mlango. “Chakula tayari,” alimwambia Hija.

    “Nenda kale!” Hija alijibu bila ya kugeuka kumwangalia mumewe. Alikuwa akiendelea kujitengeneza huku akiangalia kioo cha kuvalia.

    “Na wewe?” Badi aliuliza huku uso wake ukiwa makini kumwangalia mkewe.

    “Sijisikii kula!”

    Badi akaganda kama aliyeishiwa hoja. Akaendelea kumwangalia mkewe kwa sekunde kadhaa. “Hija,” hatimaye aliita.

    Hija aligeuka na kumwangalia Badi aliyekuwa bado amesimama palepale alipomwitia. Hakuitikia, wala kutamka lolote! Akabaki anamwangalia mumewe.

    Wakawa wanaangaliana!

    “Yule aliyekurudisha na gari ni nani?” Badi aliuliza.

    Hija akamwangalia Badi kwa macho makavu bila ya kupepesa kwa sekunde kadhaa pasipo kutamka neno. Hali hiyo ikaonekana kama kutaka kumpa wakati mgumu Badi.

    “Nilipewa lifti!” hatimaye Hija alijibu kwa mwonekano usio na hatia lakini wenye ushari wa kisirani.

    “Nimekuuliza ni nani?”

    Kisirani cha Hija kikalipuka. “Nikishakwambia itakusaidia nini?” aliuliza.

    “Nataka utambue unaongea na mumeo!” Badi nusu alibwata, nusu alilalamika.

    Hija akajenga tabasamu dogo lenye mionekano miwili, dharau na tasnifu! “Kwa nini usiende kula?” alisema.

    Akionekana kujizuia kutokana na jazba iliyomwingia, Badi akajenga ndita kwenye paji lake la uso. “Suala la kula kwangu achana nalo!” alisema kwa sauti yenye mwonekano wa jazaba. “Nataka uniambie, ni nani aliyekuleta na gari pale baa?”

    “Unadhani ni bwana wangu?”

    “You cross the line, Hija!” Badi alionya.

    “Sasa ulitaka nikuulizeje?”

    “Unadhani nitaona ajabu ukiniambia ni bwana wako?”

    “Eti nini Badi?” Hija aliuliza na kuujenga mshangao usoni kwake.

    “Nadhani umenisikia!”

    Hija akaganda kwa hamaki na kumwangalia Badi kwa macho yaliyokaza. “Sawa ni bwana’angu!” hatimaye alisema kwa hasira, kisha akageukia kwenye kioo cha kabati la kuvalia na kuanza kujisugua usoni.

    Badi akapiga hatua hadi kwenye kabati la nguo, akaufungua upande wa Hija. Akatia mkono na kuzitoa paketi zenye tembe za kuzuia mimba na kuzitupa sakafuni. Kitendo hicho kikamfanya Hija aache kujitazama kwenye kioo, akauinamisha chini uso wake na kuziangalia paketi zilizoangukia karibu na miguu yake. Aliziangalia kwa sekunde kadhaa, kisha akayainua macho yake taratibu na kuyatuliza usoni kwa Badi.

    “Hivi vidonge vinafanya nini humu ndani?” Badi aliuliza.

    Hija akaendelea kumwangalia Badi bila ya kujibu!

    “Nakuuliza wewe?” safari hii Badi alisema kwa kufoka.

    “Ilikuwaje ukafungua kabati langu bila ya kuniambia?” Hija alihoji.

    Badi akataka kumkumbusha kuhusu fomu alizomtaka aje kuzichukua kwenye kabati lake, lakini hiyo akaiona siyo hoja kwa wakati huo.

    “Nazungumzia suala la wewe kutumia vidonge vya kuzuia mimba! Hutaki kuzaa na mimi sio? Au unaogopa kupata mimba za nje?” Badi alisema kwa hasira.

    “Kama unaniona ni malaya, sijakulazimisha nikae kwako! Nipe talaka uone kama nitakuuliza kwa nini umenipa talaka!”

    Badi akapoteza mhimili wa kujizuia. Akamnasa Hija kibao cha shavuni!

    Hija akainama akiwa amelishika shavu lililopigwa. Akabaki hivyo kwa muda bila ya kutamka lolote. Baada ya muda akauinua uso na kujipangusa damu iliyokuwa ikitoka kwenye kona ya mdomo wake kwa kutumia mgongo wa kiganja.

    Badi baada ya kumwona mkewe anatokwa na damu, akanywea ghafla. Upendo ukamrudia, huruma ikamwingia.

    “Badi unanipiga?” Hija aliuliza kwa utulivu huku akimwangalia Badi usoni.

    Kwa mara ya kwanza, Badi aliyakwepesha macho yake kuyakwepa ya Hija. “Oh, my God!” alisema na kuonekana kama aliyekuwa akiongea peke yake.

    Hija akateremka taratibu kutoka kwenye stuli aliyokuwa ameikalia, akaelekea bafuni bila ya kuongeza neno huku akimwacha Badi ameduwaa katika hali ya kutahayari. Badi naye akaondoka taratibu kama mgonjwa, akaenda kukaa kwenye kona ya kitanda. Majuto yakamwelemea!

    Badi akayasikia maji kutoka bafuni yakimiminikia kwenye beseni la kupigia mswaki. Akauangalia mlango wa bafu uliokuwa wazi, kisha akajiinamia na kuanza kukifikiria kitendo alichomfanyia mke wake.

    Baada ya muda Hija akatoka bafuni kimyakimya akiwa na taulo mkononi huku akiufuta mdomo wake kwa kugusagusa sehemu yenye jeraha. Akaelekea mlangoni na kutoka huku akiufunga mlango nyuma yake na kumwacha Badi peke yake chumbani.

    Kitendo cha mkewe kutoka kikamfanya Badi asimame. Akaelekea mlangoni kutaka kumfuata Hija nje, lakini kabla ya kufungua mlango, akajipa hadhari ya kuweza kutokea malumbano ya maneno huko nje na kusikiwa na mfanyakazi. Akageuzia palepale mlangoni kurudi huku amejishika kiunoni na sura yake ameiinamisha chini. Akarudi hadi kwenye sofa lililomo humo ndani na kukaa.

    Dakika chache baadaye, Hija alirudi chumbani. Hakumwongelesha lolote Badi, badala yake alikwenda moja kwa moja na kupanda kitandani. Akajilaza na kujifunika shuka.

    Badi akamwangalia Hija aliyempa mgongo. Hatia ilimwingia na kujilaumu kwa uamuzi wake wa kumnasa kibao mkewe. Hisia za kujihisi amemwonea zikawa zinamsulubu hasa baada ya kujiona amemtuhumu mkewe bila ya kuwa na ushahidi wowote. Hata zile tembe za kuzuia mimba alizomtupia Hija miguuni, alikiri bado hakikuwa kigezo cha ushahidi wa kumhukumu nacho. Alitakiwa afanye subira ya kusikiliza majibu ambayo yangejibiwa na Hija ni kwa nini alikuwa amezihifadhi tembe hizo kwenye kabati lake.

    Alikiri hali ilishakuwa ngumu huku akijitupia lawama mwenyewe kwa kuianzisha. Akajipanga aimalize kwa kumwomba msamaha mkewe. Akainuka na kwenda kukifunga kitasa cha mlango kwa ufunguo. Njaa ilipotea, akaamua alale bila ya kula. Alijua asingeweza kula katika hali hiyo ya sintofahamu iliyokuwepo kati yao.

    Akavua fulana na pensi vilivyokuwa mwilini mwake, kisha akavaa bukta aliyozoea kulalia, akapanda kitandani kujiunga na Hija.

    “Hija,” Badi aliita na kumshika Hija begani mara baada ya kupanda kitandani.

    “Usinishike!” Hija alisema kwa ukali huku akilifyetua bega lake lisishikwe.

    Badi akaganda, lakini hakuuondoa mkono wake kwenye bega la Hija.

    “Nimekwambia usinishike!” Hija alirudia onyo lake.

    Badi akafanya ubishi wa kutouondoa mkono wake begani kwa Hija.

    Hija akatulia vilevile kwa sekunde kadhaa, ghafla akajiinua na kuamka kitandani, akawa anateremka bila ya kuongea lolote. Badi akamzuia.

    “Unakwenda wapi?” Badi aliuliza.

    Badala ya kujibu swali aliloulizwa, Hija akamwangalia Badi kwa hasira.

    Wakaangaliana!

    “Sasa unakwenda wapi?” Badi alirudia kuuliza.

    Hija hakujibu!

    Badi akauondoa mkono wake uliomzuia Hija. Hija akainuka kutoka kitandani. Badi naye akasimama!

    Hija akafanya mwelekeo wa kuelekea bafuni, mwelekeo huo ukamfanya Badi amwache.

    Kabla ya Hija kuingia bafuni, awali Badi alihisi mkewe alikuwa anataka kutoka humo chumbani na alijiandaa kumzuia asitoke. Hakuwa na uhakika kama mdogo wake alisharudi, lakini hakutaka mdogo wake na msichana wa kazi wajue kinachoendelea humo chumbani.

    Hija alivyoingia bafuni akajifungia mlango kwa ndani. Kukafuatia ukimya!

    Akiwa amesubiri kwa takribani dakika kumi, Badi alianza kuingiwa na wasiwasi alipoona Hija hatoki. Akaenda kusimama nje ya mlango wa maliwatoni.

    “Hija!” Badi aliita.

    Kimya!

    “Hija!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kimya!

    Akasita kuita. Akazubaa kama aliyekuwa akifikiri jambo. Kisha akaita tena, “Hija!” safari hii akasaidia na kuugonga mlango.

    Kimya!

    Akazidisha sauti ya kugonga huku akiita kwa kuipandisha juu sauti. Ukimya ukaendelea. Hakuna kilichokuwa kinasikika kutoka maliwatoni. Hakukusikika maji wala mwenendo wowote ulioonyesha humo ndani kuna mtu. Hali hiyo ikamchanganya zaidi Badi! Wazo la haraka la kuuvunja mlango likamjia. Akawazia kutafuta kipande cha nondo. Akatoka chumbani kwa kasi na kuufunga mlango kwa kishindo kidogo.

    “Dadaa!” Badi aliita kwa sauti akiwa kwenye korido.

    Dada aliitikia kutoka sebuleni. Wakakutana njiani.

    “Unaweza kunipatia chuma cha nondo?” Badi aliuliza.

    “Hata cha kuvunjia nazi?”

    “Kitafaa!”

    Badi akasubiri palepale kwenye korido wakati msichana huyo aliporudi jikoni. Sekunde chache baadaye akarudi akiwa na nondo ya kuvunjia nazi.



    MWISHO







0 comments:

Post a Comment

Blog