Search This Blog

Monday, 24 October 2022

WIMBO WA GAIDI - 1

 







    IMEANDIKWA NA : HUSSEIN ISSA TUWA



    *********************************************************************************





    Simulizi : Wimbo Wa Gaidi

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Ni miaka mitatu tangu kuuawa kwa Osama bin Laden nchini Pakistan. Wanamgambo wa Al-Qaida wamesambaratika. Wengi miongoni mwao wameuawa, wengine wamekamatwa na majeshi ya marekani nchini Pakistani…na kikundi cha wachache wengine kimefanikiwa kutoroka na kukimbilia eneo la Waziristan lililo kaskazini mwa Pakistan, hususan kwenye kitongoji cha Miramshah kinachodhibitiwa na wapiganaji wa Taleban, ambao walikuwa ni washirika wao wakuu na huko wakapata hifadhi baada ya kifo kile kichungu cha kiongozi wao.

    Na tangu wakati huo, hali ya wakaazi wa kijiji kilichokuwa kiasi cha kilomita saba kutoka kwenye ile ngome ya wa-Taleban iliyowahifadhi wale wanamgambo wachache wa Al-Qaida, imekuwa ni ya mashaka makubwa. Njaa ilikuwa imetawala, mahitaji yote muhimu yametoweka, maradhi hayakuwa na wa kuyatibu, ilhali magonjwa ya mlipuko na yatokanayo na lishe duni yakishamiri…na roho za wanakijiji kile zikiwa sio mikononi mwao tena, bali mikononi mwa wapiganaji wa taleban waliokidhibiti kijiji kile.

    Kwa nini?

    Kwa kuwa Osama Bin Laden alikuwa ameuawa na wamarekani…na taarifa ziliwafikia wa-Taleban kuwa tabibu aliyefika mahala ambapo Osama alikuwa amejificha kwa ajili ya kumtibu binti wa mpiganaji yule mwenye msimamo mkali ndiye aliyetoa siri ya mahala Osama alipokuwa, kwani wamarekani walivamia eneo lile siku mbili tu baada ya tabibu yule aliyeaminika kuwa alikuwa akiiunga mkono Al-Qaida kufika eneo lile. Kwa kuwa Al-Qaida ilisambaratika kwa muda baada ya kifo cha Osama, Taleban wakachukua jukumu la kulipiza kisasi kifo cha mshirika wao mkubwa kwa niaba ya Al-Qaida.

    Hivyo basi, pale binti wa Osama aliyekuwa akishikiliwa na wanajeshi wa Pakistani kabla ya kukabidhiwa kwa wamarekani, alipofanikiwa kupenyeza taarifa kwa watalebani kupitia kwa mmoja wa watendaji wa jeshi la Pakistani aliyekuwa akiiunga mkono Al-Qaida kwa siri, kuwa tabibu huyo alikuwa akiongea kwa lugha ya ki-pashtuni, lakini kwa lafudhi ya watu watokao kwenye kijiji kile, ilitosha sana kuwajulisha watalebani kuwa dakitari aliyemchomea utambi Osama kwa wamarekani hadi akauawa, alikuwa ametokea kwenye kijiji kile kilichokuwa kiasi cha kilometa saba tu kutoka pale kwenye ngome yao.

    Kilichofuatia kilikuwa ni kizazaa kikubwa pale kijijini.

    Mauaji, mateso, na utekaji nyara viliwaandama wanakijiji, ikitafutwa familia ya tabibu aliyemchoma Osama kwa wamarekani. Msako wa nyumba hadi nyumba uliondeshwa ukazaa matunda. Familia ya tabibu aliyehusika kumchomea utambi Osama ilipowekwa kizuizini kwa wiki nzima na kuwekwa kwenye wakati wa mateso na vitisho visivyosemeka ikiwamo kubakwa, kupigwa mijeledi na baadhi yao wakiuawa huku wengine wote wakishuhudia, siri ikabidi itolewe. Tabibu wa Osama akatajwa na wanafamilia wake mwenyewe, wakati huo yeye akiwa jijini Islamabad.

    Wataleban wakamfuata huko huko kwa lengo la kumuua. Lakini sio kabla ya kumtesa na kumhoji kikatili. Tabibu akakiri kuwa hakuwa peke yake…alikuwa na mwenzake kutokea kwenye kijiji kile kile ambaye alikuwa ni miongoni mwa wapiganaji wa Al-Qaida waliokimbilia kule kwa Wataleban na kuhifadhiwa.

    Hah!

    Wateleban wakahamanika. Ni nani huyo?

    Tabibu akafa na siri yake kwa kujitia kumpora silaha mmoja wa watesaji wake ili awateketekeze.Wakamuwahi na kummiminia risasi. Kifo cha Osama kikalipizwa… miezi mitatu tu baada ya kifo chake. Lakini sasa wataleban wakabakiwa na kitendawili kikubwa. Ni nani miongoni mwa wale maswahiba wao wa Al-Qaida waliowahifadhi kule kwenye ngome yao jirani na kile kijiji walichokibatiza jina “kijiji cha wasaliti”, aliyekuwa akishirikiana na yule tabibu msaliti?

    Sasa huyu ndiye alikuwa anasakwa na kijiji kile kikawekwa chini ya karantini kabambe na watalebani.

    Na mpaka msaliti huyo na wengine kama yeye watakapobainishwa na kuuawa, hakuna atakayetoka wala kuingia kwenye kijiji kile.

    Kijiji kikawa kimetengwa na dunia.

    Jitihada za majeshi ya Pakistani kukiokoa kijiji kile hazikufua dafu asilani, kwani Waziristan ilikuwa ni ngome kuu ya wataleban, na hakukuwa na namna ya kuiangusha isipokuwa kwa kuipenya kijasusi kama jinsi alivyopenyezwa yule tabibu mzaliwa wa kijiji kile ndani ya kundi la Al-Qaida.

    Na hilo lilikuwa haliwezekanin tena sasa. Watalebani wlaikuwa wkimshuku kila aliyewaendea na kila waliyemuona kuwa si miongoni mwao.

    Na sasa hali ilikuwa imefikia pabaya.

    Wapiganaji wote wa Al-Qaida waliokuwa wamehifadhiwa kwenye nyumba salama ya uongozi wa wa-Taleban. Miongoni mwao alikuwamo msaliti. Talebani walidhamiria kumtia mikononi na kumuangamiza. Ilikuwa ni mahojiano ya mara kwa mara, mitihani ya hapa na pale kwa wale Al-Qaida waliokimbilia mikononi mwa washirika wao wa ki-Taleban.

    Amani ikapotea. Ndani nan je ya nghome ile kubwa ya watalebani.

    Jumuia ya kimataifa ilifanya bidii za kila namna kuwaokoa wakaazia wa kijiji kile bila mafanikio yoyote. Serikali ya Pakistani pamoja na kulaani kwake kuuawa kwa Osama ndani ya nchi yake bila ya wao wenyewe kushirikishwa, haikufua dafu, kwani Taleban siku zote wamekuwa wakiamini kuwa serikali ya Pakistani ilikuwa ni kibaraka wa wamarekani.

    Marekani ikatoa tamko. Talebani iwaachie huru wana kijiji wale waondoke kijijini pale na kwenda kwenye kambi za wakimbizi nje ya kitongoji kile cha Waziristan, na iwasalimishe wapiganaji wote wa Al-Qaida iliowahifadhi, ama si hivyo ndege za maangamizi zinazoruka bila ya rubani, yaani “drones”, zitatumwa kuisambaratisha ngome yao.

    Taleban wakagoma.

    Na wao wakatoa tamko.

    Wamarekani wakituma hizo ndege ijue pia itaua raia wa kijiji wasio na hatia…na watalebani watakuwa wanaua kila mmarekana watakayemuona, popote pale duniani.

    Ngoma nzito…



    ______________



    SEHEMU YA KWANZA



    Kijiji cha Dargah Mandi, kilomita saba magharibi mwa kitongoji cha Miramshah, Waziristan ya Kaskazini, Pakistan.



    Ni saa saba za usiku. Baridi kali ilikuwa ikipambana na mashuka mazito yaliyokuwa yakijaribu kuihifadhi miili ya wanakijiji waliorundikana upande mmoja wa eneo pana la tambarare lililokuwa mpakani kabisa mwa kijiji kile kilichojaa madhila makubwa na mashaka mazito.

    Ni kijiji cha Dargah Mandi kilichokuwa ndani ya kitongoji cha Waziristan ya Kaskazini, ambayo ilikuwa ni ngome kuu ya wapiganaji wa Taleban, nchini Pakistani.

    Wanakijiji walikuwa wamejikunyata wakisubiri msaada waliokuwa wameutarajia kwa muda mrefu bila matumaini ya kuupata. Wapiganaji wa Taleban wenye silaha walikuwa wamewazingira wanakijiji wale kutoka pande zote za eneo lile, nao wakiusubiri msaada ule ambao kwa hakika na wao walikuwa wakiuhitaji, maana hali kijini Dargah Mandi ilikuwa tete kila upande.

    Mbele yao, kiasi cha kama mita mia tatu hivi kutoka pale ambapo wale wanakijiji walikuwa wamejikunyata huku wakiwa wamewekewa mitutu ya bunduki za wapiganaji wale wenye roho zisizosita kutekeleza mauaji, kulikuwa kuna uwanja mpana wa wazi wenye majani mafupi, na kwenye maeneo sita tofauti ya uwanja ule, kulikuwa kuna mioto iliyokuwa ikiwaka kutokana na marundo ya kuni zilizowashwa kwa kusudio maalum, ikitupa miale yake hewani na kuleta mwanaga kiasi eneo lile na wakati huo huo ikiacha baadhi ya maeneo ya uwanja ule kuwa na kiza kizito.

    Dakika zilisonga na baada ya muda ulioonekana kuwa ni mrefu kuliko uhalisia wa muda wenyewe, miungurumo ya ndege ilisikika ikitokea angani upande wa mwisho kabisa wa eneo lile la wazi lililowekewe mioto, eneo ambalo liliiishia kwenye korongo refu sana lililoanguka umbali wa mita zipatazo mia nne kwenda chini, ambako kulikuwa kuna mto mkubwa sana uliokuwa ukipeleka maji kwa ghadhabu isiyosemekana hadi kwenye bahari ya Arabia (Arabian Sea), kilometa nyingi kusini mwa Pakistani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Dargah Mandi haikuweza kabisa kuingilika kutokea upande ule hatari, ambapo hakuna binadamu ambaye angeweza kukiingia kijiji kile kwa kulikwea korongo lile kutokea kule chini kwenye mto ule mkali.

    Na ni kutokana na uhatari wa eneo lile ndipo watalebani waliojaa hila na shuku zisizo ukomo, walipoelekeza kuwa ndege zile za misaada ziangushie marobota makubwa ya chakula na madawa kwenye eneo lile, kisha ndege zitakazoangusha misaada ile zigeuzie huko huko angani na kwenda zake. Hakukuwa na ruhusa kabisa kutua pale kijijini wala sehemu yoyote ya eneo walilolidhibiti vilivyo, la Waziristan ya Kaskazini.

    Ndege ya kwanza ikatokeza kutokea nyuma ya milima mingi iliyolizunguka eneo lile, na mining’ono ya viherehere ikazagaa miongoni mwa wanakijiji. Ndege ikazidi kukurubia na ikazidi kushuka. Watalebani wengi wa shuku wakajiweka makini kwa bunduki na makombora yao…





    Na ni kutokana na uhatari wa eneo lile ndipo watalebani waliojaa hila na shuku zisizo ukomo, walipoelekeza kuwa ndege zile za misaada ziangushie marobota makubwa ya chakula na madawa kwenye eneo lile, kisha ndege zitakazoangusha misaada ile zigeuzie huko huko angani na kwenda zake. Hakukuwa na ruhusa kabisa kutua pale kijijini wala sehemu yoyote ya eneo lile walilolidhibiti vilivyo, la Waziristan ya Kaskazini.

    Ndege ya kwanza ilitokeza kutokea nyuma ya milima mingi iliyolizunguka eneo lile, na minong’ono ya viherehere ikazagaa miongoni mwa wanakijiji. Ndege ikazidi kukurubia huku ikizidi kushuka. Watalebani wengi wa shuku wakajizatiti kwa silaha makini wakiwa miongoni mwa wanakijiji ambao sasa waliwakusanya kuwafanya kama ngao zao dhidi ya shambulizi lolote kutoka kwenye ndege ile. Na hata pale walipoanza kujizatiti namna ile, ndege nyingine tatu zilioneka kutokeza juu ya vilele vya milima iliyolizunguka eneo lile, na dakika kumi baadaye marobota makubwa yalionekana kuanguka kutoka angani. Mayowe yalizagaa, wanakijiji wakazidi kujirudisha nyuma ili kuwa mbali na eneo lile la wazi lililokuwa likimulikwa kwa ile mioto kutoka pembe sita tofauti. Lakini muda si muda, maparashuti yakafunuka kutoka kwenye marobota yale makubwa, nayo yakaanza kushuka taratibu huku yakinesanesa hewani kwenye anga ile ya usiku. Wanakijiji na watalebani walijitahidi kwa kadiri walivyoweza kufuatilia ushukaji wake kwenye kiza cha usiku ule wenye mbalamwezi hafifu, lakini haikuwa rahisi. Marobota yalizidi kushuka, kila moja kwa uelekeo wake…kila moja likiwa na shehena muhimu kwa wanakijiji wa Dargar Mandi ndani yake…lakini pia juu ya kila mgongo wa robota la vyakula vile, kulikuwa kuna siri kubwa….



    ________________



    Makomando wanne walishuka kwa maparashuti wakiwa wamelala juu ya migongo ya yale marobota makubwa ya chakula cha msaada yaliyokuwa yakiangushwa na ndege za msalaba mwekundu kwenye kile kijiji cha Dargar Mandi. Wote wanne walikuwa wamevaa nguo maalum za kuzamia mbizi majini bila ya kulowa.

    Lengo lao lilikuwa ni moja tu. Kumkomboa mtanzania aliyenaswa ndani ya kijiji kile, akiwa ni mmoja wa wapiganaji wa Al-Qaeda aliyetajwa kutafutwa na FBI baada ya shambulizi la kutisha kwenye ubalozi wa Marekani jijini Dar mnamo mwaka 1998. Sasa ngome iliyosalia ya Taleban ilikuwa inawahifadhi baadhi ya wapiganaji wa Al-Qaeda waliobakia, yeye akiwemo, ilikuwa imezingirwa na majeshi ya ushirika wa Marekani na Pakistani. Upinzani wa Taleban ulikuwa unaelekea kushindwa, na wamarekani wakiingia ndani ya ngome ile hakutakuwa na garantii ya mtanzania yule kunusurika.

    Isipokuwa kama atatolewa mle ngomeni kabla majeshi ya washirika hayajavamia.

    Lakini kivipi?

    Ndipo nafasi ilipojitokeza pale Taleban walipokubali wanakijiji waletewe vyakula vya msaada kwa njia ile.

    Marobota yanatua kwa vishindo ardhini na kuviringika shaghala baghala, kila moja upande wake. Makomando wanagaragazwa vibaya na yale marobota makubwa, lakini kwa kuwa walikuwa mahiri kwenye kazi zao na kwa kuwa walishalifanyia mazoezi mara kadhaa tukio lile kabla ya siku ile, kila mmoja alifanikiwa kujirusha pembeni na kubaki akiwa amejilaza kimya kwenye majani mafupi ya eneo lile, macho yao yakitafuta uelekeo ambao kila mmoja aliamini kuwa ni kusini ya pale walipoangukia, wakiyaacha yale marobota makubwa kabisa yakiendelea kubingirika huku yakijizonga na yale maparashuti yaliyoyashusha.

    Kule kwa wanakijiji wenye njaa, watalebani walikuwa wakiyafuatilia yale marobota kwa umakini kwa kadiri walivyoweza. Kwa namna fulani ambayo sio bahati mbaya, marubani waliokuwa wakiyadondosha yale marobota waliyaangusha mbali na ile mioto mikubwa iliyowashwa kuwaelekeza ni wapi yale marobota yaangushwe, na hii iliwapa nafasi makomando walioshuka na marobota yale kuweza kutumia kiza kilichopo, mbali na ile mioto, ili kijiweka mbali na marobota yale na kwenda kwenye jukumu lililokuwa mbele yao. Jukumu kubwa na la hatari sana…wenyewe waliliita ni jukumu la kujitoa muhanga…suicide mission. Kwa ajili ya mtu mmoja ambaye hata hivyo hawakuwa wakimjua kiukaribu wowote zaidi ya kuwa alikuwa akihitajika sana na nchi kubwa duniani, na kwamba malipo yao kwa kujitoa kwao kwenye kulitekeleza jukumu lile, yalikuwa ni makubwa sana kiasi cha kuhalalisha lolote ambalo wangekutana nalo ndani ya eneo lile lililoshindikana kabisa hata kwa mataifa makubwa yenye uwezo mkubwa wa kivita…

    Kila mmoja alibaki akiwa amelala mahala pake, akitafuta ishara aliyoandaliwa kuitafuta mara baada ya kutua ndani ya eneo lile kusudiwa. Wakaiona. Kutokea kwenye kona moja ya eneo lile, hatua kadhaa kutoka kwenye moja ya marundo ya mioto iliyokuwa ikiwaka eneo lile, taa nyekundu ilikuwa ikiwashwa na kuzimwa kwa kufuata utaratibu maalum. Iliwaka mara nne kwa kuacha kiasi cha kama sekunde moja baina ya muwako mmoja na mwingine, kisha ikafuatiwa na miwako mingine mitatu ya haraka haraka. Ilikuwa ni mbinu maridhawa kwani kwa pale ile toch maalum yenye mwanga mwekundu ilipokuwa ikiwakia, haikuwa rahisi hata kwa mtalebani mwenye macho makali kiasi gani, kuweza kuutofautisha mwanga ule kutoka kwenye mwanga wa moto uliokuwa ukiwaka hatua chachekutokea pale.

    “Mmeona?” Mmoja alisaili kwa mnong’ono mkali.

    “Yah!” Mwingine alijibu, na wengine wawili nao walituma majibu yao kuwa wameiona ile ishara. Lakini hakuna aliyetoka pale alipokuwa amelalia tumbo, akiwa na silaha yake mgongoni.

    Kule kwa wanakijiji, watalebani waliendelea kujificha huku wakiyatazama yale marobota yakiendelea kubiringika huku wakiwa wamewaamuru wanakijiji wote kutulia mahala walipokuwa. Marobota yalipotulia kila moja upande wake, bado watalebani waliojaa shuku na wasiyemuamini yeyote isipokuwa wao wenyewe, wanawazuia wanakijiji kuyasogelea. Wanayatazama kwa umakini mkubwa yale marobota kutokea kule walipokuwa, wakitaraji jambo baya kutokea. Lakini halitokei. Hatimaye wanatoa amri kwa wanakijiji kuyaendea yale marobota. Kelele za shangwe zasikika pale wanakijiji wanapokurupuka na kuyakimbilia marobota yale, na ndipo kule walipokuwa, wale makomando wanatambaa kwa kasi sana kuelekea kule ile ishara ilipotokea. Wakati watalebani wako makini kufuatilia harakati za wanakijiji kule kwenye yale marobota ya vyakula, hawatakuwa makini kufuatilia kitu kingine na hawataweza kuona wakati wale makomando wakitambaa kwa uficho namna ile kuelekea sehemu tofauti na kule yale marobota yalipokuwa.

    Makomando wanafika pale ishara ilipotokea, na hapo wanakutana na mshirika wao, mwenyeji wao, raia wa Pakistani aitwaye Imraan Gopang. Naye akiwa amevaa nguo kama walizovaa wao, ila akiwa amebeba begi mgongoni na akiwa amening’iniza bunduki mbili mgongoni kwake, Imraan anawaongoza kwa usiri bila ya kuongea lolote hadi kwenye shimo la wastani mithili ya yale mashimo ya vyoo yatumikayo kwenye jamii nyingi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Haraka haraka wanaufunua mfuniko mzito wa zege wa shimo lile, na tochi zilizounganishwa kwenye bunduki zao zinawaonesha ngazi za chuma zilizojengewa kwenye ukingo wa shimo lile, ambazo zingewateremsha hadi kwenye kichanja kikubwa cha chuma kizito ambacho kilikuwa kinakatisha kutoka upande mmoja wa mtaro mkubwa kabisa wa chini ya ardhi, hadi mwingine, na kuwa kama daraja la aina fulani..

    Wale makomando wanne na yule mwenyeji wao wanaingia ndani ya shimo lile na kuufunika ule mfuniko wake kwa ndani. Wateremka hadi pale kwenye kile kichanja kirefu cha chuma kizito, sasa wakiwa ndani ya mtaro mkubwa wa chini ya ardhi. Kiasi cha kama mita tatu hivi chini ya daraja lile, maji machafu ya kitongoji kile cha Waziristan yalikuwa yakitiririka kuelekea kwenye mdomo mpana wa mtaro ule, ambao ulichomoza kutokea kwenye uso wa jabali refu sana, kiasi cha kama kilomita moja zaidi kutokea pale walipokuwa. Njia nyingi kutoka pande mbali mbali za nchi ile zilikuwa zikimimina vinyesi na majitaka kwenye mtaro ule mkubwa kabisa, ambao nao ulisafirisha shehena ile ya uchafu kwa hiyo kilometa moja zaidi kutokea pale wale makomando walipokuwa na hatimaye kwenda kuitiririsha kwenye mto mkubwa kabisa uliokuwa umbali wa mita zipatazo mia saba kwenda chini kutokea kwenye uso wa jabali refu ambalo juu yake ndipo kijiji kile cha Dargah Mandi kilikuwepo.





    Njia nyingi kutoka pande mbali mbali za nchi ile zilikuwa zikimimina vinyesi na majitaka kwenye mtaro ule mkubwa kabisa, ambao nao ulisafirisha shehena ile ya uchafu kwa hiyo kilometa moja zaidi kutokea pale wale makomando walipokuwa na hatimaye kwenda kuitiririsha kwenye mto mkubwa kabisa uliokuwa umbali wa mita zipatazo mia saba kwenda chini kutokea kwenye uso wa jabali refu ambalo juu yake ndipo kijiji kile cha Dargah Mandi kilikuwepo.

    Wanajitosha kwenye maji yale machafu na kuufuata ule mtaro kuelekea kule vinyesi vinapotokea, zile nguo zao za kupigia mbizi majini zikiwakinga dhidi ya uchafu ule uliowafika viunoni, puani wakiwa wamevijisha viziba pua kujikinga na harufu mbaya na kali ya maji yale machafu.

    Ikiwa ni wazi kuwa alishafika eneo lile peke yake hapo kabla, Imran Gopang anawaongoza hadi kwenye ngazi za chuma zilizoegeshwa kwenye ukuta wa mtaro ule, ambapo kwa lugha za ishara anawaelekeza kumulika paa la mtaro ule kwa kurunzi zao kali. Baka la unyevunyevu lililo kwenye dari lile linawajuza kuwa pale ndio mahala walipopakusudia.

    Wanaangalia saa zao. Muda bado. Wanasubiri. Wote kimya kabisa. Dakika ishirini na tano zinapita wakiwa wima kwenye mtaro ule mkubwa, wakiwa wamezama hadi viunoni kwenye maji ya vinyesi.

    Muda unawadia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wanapeana ishara na kuanza kutekeleza jukumu lao. Wanaisimamisha ile ngazi kwa kuishikilia usawa wa lile baka lililokuwa kule darini. Mmoja wao, mtaalamu wa milipuko, anapanda kwenye ile ngazi iliyoshikiliwa wima na wenzake na kubandika milipuko maalum, kitaalamu ikijulikana kama “plastic explosives”, kwenye ile sehemu yenye lile baka la unyevu. Anateremka haraka, na yeye na wenzake wanajisogeza pembeni, mbali na lile baka lililowekewa milipuko. Imraan anatoa wavu maalum kutoka kwenye begi lililokuwa mgongoni kwake, na haraka haraka makomando wanashirikiana kuukunjua ule wavu mpana, mgumu, na mahsusi kwa kazi waliyokuwa wanataka kuufanyia.

    Wawili wanakamata upande mmoja wa wavu ule wakiwa ubazi mmoja wa mtaro, ilhali makomando wengine wawili wakishikilia upande mwingine wa ule wavu, wakiwa ubazi mwingine wa mtaro. Ule wavu ukawa umewamba mithili ya kitanda cha kamba moja kwa moja chini ya lile baka. Imraan Gopang anatupia lile begi alilokuwa nalo pale juu ya ule wavu na kuliacha pale.

    Wanatulia, wanasubiri. Kimya kabisa. Maji machafu yanasafiri chini yao kuelekea kwenye mdomo wa mtaro ule, mapanya buku yakiogelea kwenye maji yale na kuwagonga gonga miguu yao. Hawajali. Wanatupiana macho kwenye ule mwanga hafifu, wakiutaraji muda muafaka wa kutekeleza wajibu wao ule wa hatari, ilhali yule mtaalamu wa vilipuzi akiwa makini maradufu na kifyatulio chake mkononi.

    Hatimaye muda unawadia. Mtaalamu akawaashiria wenzake kwa kichwa kuwa alikuwa anatekeleza lililowafikisha pale muda ule na wenzake wakajizatiti kila mmoja mahala alipokuwa, tahadhari kubwa ikiwavaa wote.

    Akabonyeza kifyatulio, na wote wakaficha nyuso zao huku wakigeukia kwenye kuta za ule mtaro mkubwa.

    Mlipuko mkubwa ulisikika mtaroni ilhali kuta na sakafu za mtaro ule wa chini ya ardhi vikitikisika kana kwamba kulikuwa kuna tetemeko la ardhi lililokuwa likipita. Ile sehemu iliyotegewa mabomu ilipasuka, mapande ya zege na plasta yaliporomoka kutoka kule juu na kuanguka kwenye yale maji machafu yaliyorushwa huku na huko na kuzilowesha zile nguo za kuzamia mbizi walizovaa wale wapiganaji mahsusi.

    Kisha kukawa kimya.

    Makomando wakaelekeza kurunzi zao kali pale ambapo palitegwa yale mabomu kutazama matunda ya kazi yao, lakini walichokiona sicho walichokitarajia. Lile eneo lililokuwa na unyevu hapo awali sasa lilikuwa limeharibika na kumegeka vibaya. Nyufa nyingi zilikuwa zimetawanyika kila upande kutokea pale palipokuwa pamezungushiwa vile vilipuka, maji yakichuruzika kutokea kule juu kupitia kwenye baadhi ya nyufa zile.

    Lakini bado lile eneo lilionekana madhubuti. Mabomu yaliyotegwa hayakufanya madhara yaliyotarajiwa kwenye eneo lile.

    Doh!

    “Ina maana hukuweka vilipulizi vya kutosha?” Mmoja wa makomando alimuuliza mtaalamu wa vilipuzi.

    “Naijua kazi yangu jamani...” Mtaalamu wa vilipuzi alinong'ona kwa msisitizo.

    “Unajua huu mtaro umejegwa ndani ya jabali lililochongwa tangu enzi na enzi...ni jiwe la mwamba mgumu sana hili. Hata sijui hao mababu na mababu wa zamani waliwezaje kuuchimba mtaro huu... " Imran Gopang alidakia kwa hamaniko, akaendelea, “...ni kama yale mashimo ya tora bora...ya tangu enzi za Nabii Suleiman! Serikali ilikuja kuongezea tu kujengea hili liji-karavati kubwa ndani yake…”

    “Sasa muda unazidi kwenda...mashambulizi ya anga yataanza muda si mrefu. Nashauri tufanye la kufanya sasa...kabla nasi hatujaangamizwa pamoja na watalebani humu, demshitt!” Mwingine alikoroma kwa kunong'ona.

    “La kufanya kama nini kwa mfano...? Misheni yote ilitegemea kuilipua hii sehemu, na sasa...”

    “Hatuwezi kulipua tena…?” Alidakia mwingine.

    “NO! Kiwango cha vilipuzi nichoweka kilikuwa sahihi...ila nadhani huu mtaro kama alivyosema kamanda hapa, umekuwa imara kuliko tulivyodhania...kama ningezidisha viwango, mtikisiko ungekuwa mkubwa kiasi cha kuwashitua mapashtuni na watalebani huko juu...hatutaki iwe hiv...” Mtaalamu wa vilipuzi aliipinga hoja kwa wahka, lakini hakumaliza kauli yake.

    Kishindo hafifu kilisikika kutoka pale juu ya paa la mtaro ule. Wote wakamakinika mara moja, wale wanne wakauvuta kwa nguvu ule wavu kila mmoja kutokea upande wake. Kikasikikika kishindo kingine kikubwa zaidi. Imraan Gopang akaweka silaha yake sawa kuelekea kule juu, na ghafla mapande ya mawe, udongo, vumbi na beseni la choo cha kuchutama vikaporomoka kutoka kule juu palipowekewa vilipulizi hapo awali, sanjari na ukelele wa hamaniko, maji yenye kinyesi, na mtu mmoja aliyeporomoka na vitu vyote vile kutoka kule juu.

    E bwana we!

    Jamaa alidunda kwenye ule wavu, akatupwa tena hewani na kuangukia tena kwenye ule wavu, akatupwa tena mara tatu zaidi kabla hajaagukia tena pale wavuni na kubaki akiwa amelalia tumbo.

    "Yeeeah! Kazi imetimia! Hakuna muda wa kupoteza tena!" Mmoja wa wale makomando walioushikilia ule wavu alipayuka wakati yule mtu akijiinua kutoka pale kwenye wavu ambao bado ulikuwa umeshikiliwa kwa nguvu na wale makomando wanne...mmoja kwenye kila kona ya wavu ule maalumu.

    Kurunzi kali ikammulika usoni yule mtu aliyeporomoka na mawe kutoka kule juu...naye haraka akajiziba uso kwa mikono yake, lakini sio kabla kurunzi ile haijawaonesha wale makomando kuwa alikuwa amevaa nguo za kitalebani na uso wake ulikuwa umezingirwa na madevu mengi.

    "Toa mikono usoni hiyo!" Imraan Gopang, ambaye ndiye pekee aliyeweza kushika bunduki wakati ule, alimkemea kwa ukali huku akiikoki bunduki yake tayari kumchabanga risasi yule mtu kama ikibidi.

    Jamaa akashusha mikono na kubaki akiwa amefinya uso akiuacha mwanga mkali wa ile kurunzi iliyounganishwa na bunduki ya Imraan Gopang ummulike usoni, lakini hakubaki kimya.

    "Sa...samahani jamani! Mimi ndiye muhusika...huko juu sio salama sana...kishindo cha mlipuko kimesikika kiasi. Wakigundua kilichotokea tutakutwa hapa..." Jamaa kutoka juu alisema kwa mashaka, akiongea kwa lugha ya kipashtuni fasaha.

    Makomando walimtazama kwa sekunde chache tu zaidi, wakiionanisha sura yake na picha yenye sura ya mtu ambaye ndiye walikuwa wamefika pale mtaroni kwa njia ile ya hatari kabisa kumuokoa; picha ambayo wote waliitazama na kuikariri kabla ya kuianza ile misheni yao ya hatari.





    “Ndiye yeye...lets get out of here!” Mmoja wa makomando alisema, akimaanisha kuwa waondoke eneo lile haraka, muda wa kuwa tayari wameshathibitisha kuwa aliyeporomoka kutoka kule juu ndiye mlengwa wa misheni yao ile ya kifo.

    "Toa hizo nguo…vaa zilizomo humo kwenye hilo begi hapo...haraka!" Imraan, ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa operesheni ile aliamuru. Haraka sana jamaa akatekeleza. Kutoka kwenye lile begi lililokuwa pale juu ya ule wavu alioangukia, alitoa nguo za kupigia mbizi kama zile walizovaa wale makomando, ambazo ziliuganika moja kwa moja kutoka unyayoni hadi kichwani kuwa kama kofia iliyobana na kuacha sehemu ya uso tu, na kuzivaa kwa pupa. Alipomaliza, Imraan akachomoa bunduki nyingine kama zile walizokuwa nazo yeye na wale wenzake iliyokuwa ikining’inia mgongoni kwake na kuitupia pale juu ya ule wavu.

    “Kamata hiyo tuondoke hapa kabla maonesho ya fataki hayajaanza!”Alimkoromea. Jamaa kutoka juu ya paa la mtaro aliiokota ile bunduki na kujirusha mtaroni kwenye yale maji ya kinyesi bila hata ya kuambiwa. Wale makomando wanne walioshuka Dargah Mandi kwa yale marobota ya chakula cha msaada waliuacha ule wavu ukiangukia majini na kwa pamoja wale wanaume sita wakaanza kukimbia kwa haraka yenye tahadhari kueleka kwenye mdomo wa mtaro ule, wakifuata mkondo wa yale majitaka yaliyowafika viunoni.

    Hawakuwahi kuufikia mdomo wa ule mtaro…

    ***********

    Kule uwanjani baadhi ya wanakijiji wa Dargah Mandi walikuwa wakiyapandisha kwa taabu magunia mengi yenye uzito wa kilo mia kila moja, kwenye malori matatu ya watalebani chini ya ulinzi mkali wa wale wanamgambo wenye roho mbaya. Hii ilikuwa ni baada ya kurarua mikanda maalumu ya khaki ngumu kabisa iliyokuwa imeyabeba yale marobota makubwa yaliyotengenezwa kwa mbao maalumu ambazo ndani yake ndio kulikuwa kumepangiliwa yale magunia makubwa...yakiwa yamesheheni mchele, ngano, sukari na madawa mbali mbali ya binaadamu hususan kwa kutibu maradhi ya milipuko na yale yatokanayo na utapiamlo.

    Ilikuwa ni taswira ya kusikitisha kwa kweli, kwani walionekana wazee na vijana waliokondeana kwa njaa ambayo pia iliwafanya wasiwe na nguvu, wakijitutumua kuburura na kuyapandisha kwenye malori yale magunia, ilhali wale wanamgambo wenye afya kuliko wao, wakiwa wamewasimamia kwa mitutu ya bunduki huku wakiwashinikiza kwa ukali na kelele, kuwa wafanye haraka kupandisha chakula kile kwenye yale malori; chakula ambacho wanakijiji wale waliokondeana wala hawakuwa na matumani ya kukipata, pamoja na kwamba kilikuwa kimeshushwa pale kijijini kwa njia ile ya hatari kabisa, kwa ajili yao.

    Pembezoni kabisa mwa uwanja ule, akina mama na watoto walikuwa wamejikunyata wakiwa na mabakuli, makapu na masinia mapana kabisa, wakishuhudia namna tumaini lao la mlo walioukosa kwa kipindi kirefu, likishehenezwa kwenye yale malori ya watalebani, wakitaraji na wao kugawiwa chakula kile na kukipeleka majumbani mwao kikiwa kwenye vile vyombo vyao na kunusuru maisha yao kutokana na kifo cha unyonge kabisa duniani...kifo cha njaa.

    Na katikati ya harakati zile zilizokuwa zikiendelea pale uwanjani usiku ule, mtoto mmoja wa kike aliushika na kuutikisa kwa nguvu mkono wa mama yake, wahka uliomkumba ukijidhihirisha kwenye nguvu aliyoiweka kwenye mtikiso ule. Mama aliyekuwa amemakinika na kilichokuwa kikiendelea kule kwenye magunia ya chakula alimgeukia kwa kukereka huku akiwa amekunja uso tayari kumkaripia, lakini hofu aliyoiona usoni kwa bintiye ilimfanya ageuzie uso wake angani kufuatisha kule ambako kidole chenye kutetema cha mwanaye kilikuwa kinaoneshea...na ndipo sanjari na kile alichokiona kule angani, miungurumo ya kwanza wa zile ndege za ajabu ilipoyafikia masikio yake pamoja na ya wanakijiji wenzake aliokuwa nao pale uwanjani.

    "Eee Khuda!" Mama alimtaja mola wake kwa woga mkubwa na punde hiyo hiyo sauti za wanakijiji wenzake walioona kile ambacho yeye na bintiye walikiona, zilimezwa na sauti kali mithili ya mbinja ndefu kabisa ikisindikizwa na mwale wa moto uliopasua anga ya usiku ule kutokea kwenye moja ya ndege zile za kivita zilizoshindikana. Wanakijiji walijitupa chini kwa taharuki na mayowe makubwa wakiogopea uhai wao duni...na hapo hapo kishindo na mlipuko mkubwa vilisikika umbali wa mita kadhaa kutoka pale walipokuwa. Watalebani waliokuwa wanawalinda wale wanakijiji walihamanika vibaya, na kuwah-kika vilivyo.

    "Tunashambuliwaaaaa!" Mmoja wao alipayuka huku bila ya kufikiri akifanya lile ambalo mafunzo yao ya kijeshi yalimuelekeza, kwa kumnyakua mmoja wa wanakijiji aliyekuwa karibu naye na kumuweka mbele yake kama ngao huku akigeuka huku na huko na bunduki yake macho yakiwa yametumbuka.Wenzake walijitupa chini ya yale magari yao huku wakitapatapa na bunduki zao pasina kuelewa ni wapi shambulizi lilikuwa limetokea na nani alikuwa anashambulia.

    Mbinja nyingine mbili zilirindima angani zikifuatiwa na ile miale mirefu na mikali ya moto iliyopasua anga mithili ya vimwondo...na sekunde ile ile milipuko mingine miwili ilisikika kutokea sehemu mbali na pale walipokuwa...mioto mikubwa kabisa ikiruka hewani na vumbi kali likijichanganya na hewa ile ya ubaridi wa usiku.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "AAAH ni mashambukizi ya droni! Wanashambulia kambi yetu… wanaharamu!" Mtalebani mwingine alibainisha kilichokuwa kinatokea kwa hamaniko lililobadilika na kuwa ghadhabu.

    "Nguruwe weupe! Yaani wamarekani wametutega kwa msaada wa chakula kwa raia kumbe walikuwa wana lao jambo??! Ua wanakijiji wooot..." Mwingine alidakia lakini kabla hajamaliza mbinja nyingine fupi ilisikika na muda huo moja ya yale magari yao pale uwanjani likasambaraishwa vibaya kwa kombora kutoka kwenye moja ya zile ndege zisizotumia rubani.

    Loooh…Mtafaruku!

    Watalebani na wanakijiji kadhaa waliokuwa kwenye lile gari walisambaratishwa vibaya na bomu lile. Bomu la pili likalisambaratisha lile lori la pili...ambalo safari hii halikuwa na mtu lakini hata hivyo lilijeruhi watalebani na baadhi ya wanakijiji waliokuwa wakikimbia kwa woga na mayowe mengi.

    Vita haina macho.

    Hekaheka ikashamiri...watalebani na wanakijiji wote wakawa wanakimbia sasa, kila mmoja akiwaza "yarabi nafsi yangu…!"

    Zile ndege zisizo na rubani maarufu kama "drones" zikaachana na yale malori na kuendelea kutupa makombora kule katikati ya kijiji, hususan kwenye jengo moja tu ambalo vipimo vya satelaiti vilionesha kuwa ndimo ambamo wafuasi waliobakia wa hayati Osama Bin Laden walikuwa wamehifadhiwa na wale washirika wao hatari, wataleban.

    Mzizimo wa usiku ule wenye baridi ulibadilika na kuwa mrindimo wa milipuko ya makombora na fukuto la hofu.

    **********

    Kiasi cha kama dakika moja kabla yule mtoto wa kike kule uwanjani hajaziona zile ndege za kuvizia na kumgutusha mama yake, kule mtaroni makomando waliokuwa wakitembea haraka na kwa tahadhari kuelekea kwenye ndomo wa karavati lile kubwa kabisa la chini ya ardhi waligutushwa na kishindo cha mtumbukio wa kitu kizito majini, sanjari na ukelele wa ghadhabu.

    "Ah! Tumeshitukiwaa!" Jamaa aliyeporomoka na beseni la choo kutoka kule juu ya paa la ule mtaro aliropoka huku akijirusha pembeni na kujibabatiza kwenye ukuta mnyevu wa ule mtaro, na hapo hapo milipuko ya risasi ikasikika kutokea nyuma yao.

    "Pumbaaavvvv!" Mmoja wa makomando alilaani huku akigeuka na kumimina risasi kule walipotokea ilhali wale wenzake nao wakijitupa pembeni huku nao wakitupa risasi. Na hata pale alipokuwa akitupa macho kule alipotokea huku naye akiwa ameshikilia imara bunduki yake, mpiganaji aliyeshuka na beseni la choo kutoka kule juu aliona watalebani kadhaa wenye silaha wakirukia pale mtaroni kutokea kwenye lile tundu alilolitoboa kwa taabu sana kwenye sakafu ya choo cha lile jumba alilokuwamo kwa masiku kadhaa, sakafu ambayo kutokea kwa pale alipokuwa ilikuwa ndio sehemu ya paa la ule mtaro unukao.

    "Tusonge mbeleee!!" Imraan Gopang alibwata huku akitupa risasi kuwaelekea wale watalebani ilhali akirudi nyuma akiwa amejibaza kwenye ukuta wa mtaro. Milipuko ya risasi ndani ya ule mtaro ilirindima kwa kelele kubwa isivyo kawaida, sauti za milipuko ya bunduki zao zikitupwa huku na huko mtaroni na kubaki mle mle bila ya kuwa na mahala pa kutokea. Kurunzi kubwa iliwamulika makomando...watalebani walikuwa wakiwakimbilia kwa jazba mle mtaroni...wawili walidunguliwa na kupiga mieleka huku wakiachia mayowe. Risasi ilichimba ukuta wa mtaro sentimeta chache kutoka pale jamaa alipojibanza...naye akazinduka. Akatupa risasi mbili...watalebani wawili zaidi wakaenda chini. Mmoja wa wale wenzake akamkamata kiwiko na kumvuta kibabe kuelekea kwenye mdomo wa ule mtaro...ambao ulikuwa kiasi cha kama mita hamsini hivi kutokea pale walipokuwa.

    "Achana nao...twende!" Jamaa alimkoromea. Hapo hapo mwenzao mmoja akaachia yowe la uchungu...risasi moja ilimpata begani naye akatupwa vibaya kwenye ukuta wa mtaro na kuangukia majini.



    Akatupa risasi mbili...watalebani wawili zaidi wakaenda chini. Mmoja wa wale wenzake akamkamata kiwiko na kumvuta kibabe kuelekea kwenye mdomo wa ule mtaro...ambao ulikuwa kiasi cha kama mita hamsini hivi kutokea pale walipokuwa.

    "Achana nao...twende!" Jamaa alimkoromea. Hapo hapo mwenzao mmoja akaachia yowe la uchungu...risasi moja ilimpata begani naye akatupwa vibaya kwenye ukuta wa mtaro na kuangukia majini. Imraan Gopang akamnyanyua haraka.

    "Tukingenii!" Alipiga kelele huku akimburura yule mwenzao aliyejeruhiwa. Makomando waliobaki wakajipanga pamoja na yule mwenzao waliyekuja kumkomboa kutoka kwenye ngome ile ya watalebani iliyojengwa juu ya ule mtaro mkubwa na kujibu mapigo ya watalebani kwa kuwamiminia risasi za mfululizo huku wakizidi kurudi kinyumenyume kuuelekea mdomo wa mtaro ule waliokuwamo, na katikati ya majibizano yale ya risasi, kurunzi kubwa ya watalebani ilikuwa ikiranda huku na huko mle mtaroni, ikimsaka mtu aliyeshuka na beseni la choo kutoka kule juu, ambaye sasa watalebani walijua kuwa ndiye msaliti wao...ndiye msaliti wa Osama bin Laden. Ikammulika.

    "Yuleee...!" Yowe kutoka kwa mtalebani mwenye kurunzi lilienda sambamba na mwanga wa kurunzi ile uliomnasa yule jamaa, na hapo mmiminiko wa risasi za watalebani ukamgeukia yule jamaa aliyekuwa akibururwa na yule mwenzake. Upesi sana jamaa akamsukuma yule mwenzake katikati ya mtaro huku naye akijitupa huko huko kutoka kule ukutani walipokuwa wamejibanza huku wakikimbia. Ukuta wa mtaro kwa pale walipokuwapo nukta moja tu iliyopita ukachabangwa marisasi bila mpangilio. Akiwa kwenye yale maji ya kinyesi katikati ya mtaro jamaa akajigeuza na kutupa risasi mbili za haraka na ghafla kiza kikatawala mtaroni sanjari na yowe la uchungu kutoka kwa yule mtalebani aliyekuwa ameishika ile kurunzi kubwa baada ya risasi ya kwanza ya yule jamaa kumdungua yule mtalebani na ya pili kuipasua vibaya ile kurunzi.

    Mayowe yasiyo mpangilio yalisikika miongoni mwa watalebani walioachwa kizani.

    "Safi sana bro!" Yule mwenzake alimpongeza jamaa, ambaye hakujisumbua kumjibu.

    "Kila mtu awahi kule mbele gaddemmit...mashambulizi yataanza muda wowote sasaa!" Imraan Gopang alibwata huku akizidi kumburura yule mwenzao aliyejeruhiwa. Bila ya kusubiri kuhamasishwa zaidi jamaa aliyeshuka na beseni la choo alivuta pumzi nyingi mapafuni na kupiga mbizi kwenye yale maji ya kinyesi.

    Na hapo kishindo hafifu kilisikika kutokea juu ya ule mtaro, ukifuatiwa na mtikisiko mkubwa kabisa ulioyatikisa yale maji machafu mle mtaroni kiasi cha kufanya mawimbi hafifu.

    "OOOH! Tayari yameanza huko juu!" Mmoja wa makomando alimaka huku naye akichupa mbizi kwenye yale maji machafu. Watalebani walipigwa butwaa kwa kutoelewa kilichokuwa kikitokea, lakini butwaa yao haikudumu sana kwani hapo kombora jingine lilishuka kule juu kwanye ngome yao na kupitiliza moja kwa moja hadi kwenye paa la mtaro ule, likaupasua vibaya na kujikita mtaroni kutokea kule juu.

    Hatari!

    Watalebani kadhaa waliokuwa karibu zaidi na usawa wa jengo la ngome yao kule juu walisambaratishwa vibaya wakati mapande ya mawe, udongo na matofali ya ngome yao kule juu vilipoporomokea mle mtaroni. Maji yale machafu mle mtaroni yalisukumwa kwa nguvu kuelekea kule kwenye kinywa cha mtaro ule mkubwa huku yakifanya wimbi kubwa kabisa lililokaribia kugusa paa la mtaro ule.

    Na ndipo wale makomando waliokuwa wamekaribia kuufikia mdomo wa mtaro ule waliposombwa kwa nguvu na maji yale na kutupwa vibaya sana nje ya mtaro ule...kila mmoja akipiga mayowe kwa woga na wahka, kwani

    ingawa tangu awali walikwa wamepanga kutoroka kutoka kwenye mtaro ule kwa njia ile...hili la kusukumwa kwa nguvu namna ile kwa wimbi zito la maji yale halikuwa sehemu ya mpango wao...

    ***********

    Yale maji machafu yalitupwa kutoka kwenye kinywa cha mtaro ule kilichochomoza kutoka kwenye uso wa jabali kali na kuanguka kwenda chini kwa umbali wa mita mia saba kutoka kwenye uso wa jabali lile lisilopandika. Makomando walianguka kutoka kule juu pamoja na maji yale huku wakipiga mayowe na roho zikiwapaa, kwa muda ambao ulionekana kuwa ni milele, ingawa kwa hakika iliwachukua dakika zisizozidi kumi tu kutoka kule juu hadi pale walipotoswa kwa kishindo kikubwa sana kwenye maji ya mto mkubwa uliokuwa ukipita chini ya jabali lile, ambapo majitaka ya mji mzima kutoka kule juu yalichanganyika na maji mengi zaidi ya mto ule mkubwa na kusombwa yakiwa yamechanganyika na maji ya mto ule kuelekea kaskazini zaidi ya kijiji kile cha Dargah Mandi ambacho kutokea kule mtoni, kilikuwa umbali wa mita mia saba juu kutoka usawa wa bahari.

    Pamoja nao ilianguka miili isiyo hai ya watalebani waliokuwa wakikabiliana nao kule mtaroni.

    Kila mmoja aliibukia upande wake pale mtoni huku akitweta na kutapatapa hali akisukwasukwa na mkondo wa ule mto wenye nguvu. Kwenye kiza kizito cha usiku ule, jamaa aliona vijitaa vyekundu viking’aa kutoka sehemu mbali mbali mle mtoni. Aliinama na kujitazama kifuani, akagundua kuwa ile nguo aliyovaa nayo ilikuwa ina kitufe kilichokuwa kikitoa mwanga mwekundu mara baada ya kuwa kimekutana na maji. Hapo akajua ni kwa nini wale waokozi wake walimshurutisha kuvaa nguo zile.

    "Wote salama?" Imraan Gopang alipiga kelele ili asikike juu ya sauti ya mfoko wa maji ya mto ule huku akigeuka huku na huko kuwasaka wenzake. Kila mmoja aliitika kutokea alipokuwa, akiwemo yule mwenye ndevu nyingi.

    “Tuna majeruhi mmoja! Yu-hali gani?” Imraan alimaka.

    “Nitaishi kamanda! Twenden’zetu!” Komando aliyejeruhiwa aliwatoa hofu wenzake.

    “Okay, tuongelee kufuata mkondo wa maji…tutakutana na mwenzetu huko mbele!” Imraan alibwata, na kuanza kuogelea. Wenzake wakafuata, na kiasi cha kama dakika kumi na tano baadaye waliona tochi ikiwashwa na kuzimwa kutokea mbele yao.

    “Tulieni!” Imraan aliamuru na wote wakatulia walipokuwa, wakijitahidi kutosombwa na mkondo wa ule mto mkubwa. Waliitazama ile tochi ikiwashwa na kuzimwa kufuatisha ishara fulani ambayo walitakiwa waitambue. Baada ya kuitazama ile tochi ikiwashwa na kuzimwa mara kadhaa, wakajiridhisha.

    “Okay, mtu wetu yule. Twendeni… ila tahadhari ni muhimu!” Imraan alisema, na kwa ukimya wa hali ya juu makomando na yule mtu waliyetoka kumkomboa waliogelea kuifuata ile tochi na hatimaye kulifikia lile boti maalum.

    “Misheni imetimia?” Sauti nzito kutoka kwenye boti ilisaili.

    “Misheni gani?” Imraan aliuliza, na jamaa mwenye ndevu nyingi aliguna kwa mshangao.

    “Safi! Ingeni tuondoke eneo hili…mbwembwe ndio kwanza zinaaza huko juu…” Sauti kutoka kwenye boti ilisema, na jamaa aliyekombolewa akashusha pumzi za ahueni. Kumbe majibizano yale ilikuwa ndio ishara yao ya kutambuana. Hapo taa hafifu ziliwaka kwenye lile boti na makomando wakashudia watu wengine watatu wakiwa na silaha nzito, ihali yule aliyekuwa akijibizana na Imraan akiwa anatabasamu.

    “Kama kawaida yako Imraan…kazi imeenda vizuri!” Yule mtu ambaye alikuwa ni mmarekani mwenye asili ya Afrika alisema huku akimshika mkono Imraan na kumsaidia kupanda ndani ya lile boti, wakati wale makomando na yule mtu waliyetoka kumtorosha wakiparamia kwa pupa ndani ya lile boti, ambalo muda huo huo liliwashwa na kuondoka eneo lile kwa mwendo wa kasi. Nyuma yao, ndege zaidi zilikuwa zikielekea Dargah Mandi kupelekea mashambulizi zaidi…na wakati huo huo ndege nyingine mbili zilikuwa zikipeleka marobota mengine ya vyakula vya msaada. Safari hii, yale marobota hayakuwa na komando yoyote aliyejilaza juu yake…





    Nyuma yao, ndege zaidi zilikuwa zikielekea Dargah Mandi kupelekea mashambulizi zaidi…na wakati huo huo ndege nyingine mbili zilikuwa zikipeleka marobota mengine ya vyakula vya msaada. Safari hii, yale marobota hayakuwa na komando yoyote aliyejilaza juu yake…





    _______________



    Wakati boti ikipasua maji kufuata mkondo wa mto ule, makomando walibadili zile nguo za kupigia mbizi na kuvaa za kawaida. Wawili kati yao waliokuwa na asili ya kiasia walivaa "salwan khameez", nguo maarufu za ki-pakistani, ilhali yule mwingine aliyejeruhiwa kwa risasi aliyekuwa wa asili ya afrika, alikuwa akisaidiwa kutolewa zile nguo kabla ya kupatiwa huduma haraka haraka na tabibu mmoja waliyemkuta mle botini. Ile risasi ilimkwaruza tu sehemu ya bega hivyo haikuwa na madhara makubwa sana kwake. Yule mmarekani mweusi alimtupia nguo za kipakistani yule jamaa aliyechoropolewa kutoka kwenye ngome ya watalebani.

    "Vaa hizo nguo!" Alimkoromea.

    Jamaa akatii bila kutia neno, ingawa muda wote akili yake ilikuwa ikimtembea kwa kasi sana. Aliona wale watu wengine kama watati hivi waliokuwa pamja na yule mmarekani mweusi mle botini wakiwa makini sana na bunduki zao, na mara moja alibaini kuwa umakini wao wote ulikuwa umeelekezwa kwake yeye, na si kwa wale wenzake alioibuliwa nao kutoka mle mtoni. Upande mwingine wa boti ile, mpakistani Imraan Gopang naye alikuwa akivaa kanzu safi ya kijivu juu ya suruali nyeupe ya "panjabi", baada ya kutoa zile nguo za kuzamia mbizi alizokuwa amevaa. Akiwa makini sana bila ya kujionesha kuwa yuko kwenye hali ile, jamaa alivua fulana mchinjo aliyokuwa ameivaa chini ya zile nguo za kuzamia mbizi...na ndipo wale wenzake aliokuwa nao mle ndani walipouona mwili wake kuwa kutumia mwanga wa taa zilizokuwa ndani a lile boti.

    "Eeh...!" Mmoja wa wale makomando wa kiasia alimaka huku kama wale wenzake na wale walinzi waliowakuta mle botini, akilikodolea macho kovu baya kabisa lililotambaa kutokea upande wa kushoto wa kifua cha yule jamaa, hadi ubavuni kwake. Lilikuwa ni kovu lenye michirizi mitatu mizito iliyotokea kwenye vishimo vitatu vilivyochimbwa pale kifuani na kuacha makovu yenye vishimo. Yaani ni kama vile kuna mtu katika siku za nyuma alimshindilia kwa reki la kukusanyia majani kifuani, na kujaribu kuzikusanya ngozi yake kutokea pale kifuani hadi chini kabisa ya ubavu wake wa kushoto. Hakika lilikuwa ni kovu baya sana.

    "Nini?" Jamaa aliuliza huku akiwatembezea macho wote mle botini, hali akiwa kidari wazi, ameshikilia shati la kipakistani alilotupiwa na yule mmarekani mweusi, ambaye ndiye pekee aliyeonekana kutolishangaa kovu lile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Umekutwa na nini hapo komredi? Hilo kovu...." Imraan Gopang akawasilisha swali ambalo bila shaka lilikuwa likirindima vichwani mwa wale wenzake. Jamaa aliinama na kujitazama pale penye kovu, kisha akawatazama wale wenzake kwa uso uliosajili hali ya kutokuwa na jibu kwa swali aliloulizwa.

    "Nyie ni wapiganaji halafu mnaogopa makovu?" Aliwauliza badala ya kuwajibu, huku akilivaa lile shati refu la kipakistani, na kulificha kovu lake. Jamaa walichanganyikiwa kiasi kwa jibu lile.

    "Ah...mimi nimepitia makabiliano ya kila namna komredi...lakini sisi ni watu tunaocheza kwa bunduki, risasi na mabomu kaka...hilo ulilo nalo? Si kovu litokanalo na chochote kati ya hivyo aisee..." Imraan Gopang alimjibu.

    Kwa mara ya kwanza jamaa akaachia tabasamu, na alivyofanya vile, sura yake ngumu ikabadilika na kuwa ya kuvutia kwa namna fulani ya ugumu.

    "Basi bado hujapitia makabiliano ya kila aina komredi..." Alimjibu bila kujali.

    "Okay...imetosha jamani..." Yule mmarekani mweusi alidakia, akaendelea, "Tumalize hii biashara Imraan..."

    "Nyie ni kina nani kwani....?" Jamaa akauliza lililokuwa likimtatiza kichwani mwake tangu aporomoke kutoka kwenye dari la ule mtaro wa majitaka.

    “Hutaki kujibu maswali yetu, unataka tukujibu ya kwako?” Komando mwenye asili ya kiafrika alimuuliza, sasa akiwa amefungwa bandeji kitaalamu begani. Alikuwa amevaa suruali ya jinzi huku akiwa kidari wazi. Jamaa akamtupia jicho fupi, kisha akageukia Imraan Gopang.

    “Nilitaka niwashukuru tu kwa kunitoa mle ndani kwa namna mlivyonitoa…sasa nisingependa kushukuru watu nisiowajua, pamoja na kuwa ndio mlioniokoa.” Alimueleza mpakistani yule ambaye alishajua tangu kule mtaroni kuwa ndiye kiongozi wa wale jamaa waliomuokoa. Jamaa walitazamana.

    “Okay sio mbaya…” Imraan Gopang alisema, na kuendelea, “tuchukulie sisi kama matarishi tu komredi.”

    “Matarishi?”

    “Yah…kazi yetu kubwa ni kusafirisha vifurushi kutoka sehemu moja kwenda nyingine…kwa malipo, of course….”

    “Na kwenye swala hili la leo, kifurushi chetu kilikuwa ni wewe…wajibu wetu ulikuwa kuhakikisha kuwa tunakutoa kwa watalebani na kukufikisha kwenye hili boti…ukiwa hai.” Yule komando aliyemvuta mkono kule mtaroni wakati wanashambuliwa na watalebani alidakia.

    “Oh? Kwa hiyo nyie ni mamluki…mercenaries?” Jamaa alisaili.

    “Matarishi ni sahihi zaidi…” Imraan akasisitiza, kisha akaendelea, “Hatujui umefanya nini na wala ni kwa nini umejipatia umuhimu wa kulazimisha sisi tupewe kazi ya kwenda kukuchoropoa kule ulipokuwa, kwa namna ya hatari namna ile…na hatujali. Ndivyo matarishi walivyo. Wao hulipwa kwa kubeba na kuifikisha bahasha mahala patakiwapo pasina kujua ndani ya bahasha ile kuna ujumbe gani…”

    Jamaa akaafiki kwa kichwa na kumgeukia yule mmarekani mweusi.

    “Ina maana wewe ndiye uliyeandaa mkakati huu wa kunitoa mle ndani kwa kuwatumia hawa…matarishi.” Alimwambia, na bila kusubiri uthibitisho kutoka kwake akaendelea, “Basi ahsante sana. Nilijua tu kuwa msingeweza kuniacha mle ndani…ingawa mmekawia sana. Hali ilikuwa ngumu sana kule…hasa baada ya kuuawa kwa yule mwenzangu…sikujua kama hangenitaja, ilikuwa ni hali tete kwa kweli…”

    “Ni kweli. Ilitubidi tubahatishe kufuata ile ile kanuni mliyowekewa na mwenzako aliyewahiwa na watalebani…kuwa siku ya kuja kuwachomoa mle ndani itatangazwa sana maredioni hapa Pakistani kwa wiki nzima…kuwa idara ya hali ya hewa inawatahadharisha wananchi wote dhidi ya kimbunga kikali…kitakachoipiga pwani ya Pakistani kwenye siku, tarehe na saa maalumu…tulitaraji tu kuwa utakuwa umesikia tangazo hilo ukiwa mle ngomeni mwa watalebani, na utajua kuwa hiyo ndiyo siku na saa ambayo tutakuja kukuchomoa mle ndani…” Mmarekani alimjibu.

    “Ni kweli…na ndipo nilipoanza kujinadi kushikwa na tumbo la kuhara…nikawa naenda chooni mara kwa mara, nikikichimba kidogo kidogo kile choo ambacho tangu awali nilishaelekezwa na mwenzetu aliyeuawa kuwa ndio ingekuwa njia yangu ya kutokea mle ndani pindi hali ikifikia pabaya…”

    “Okay, tutaongea zaidi mimi na wewe…kwanza wacha nimalizane na matarishi wetu hapa…” Mmarekani alisema.

    Kwa dakika kumi na tano zilizofuatia jamaa alimshuhudia yule mmarekani mweusi akihamishia pesa kwenye akaunti za wale mamluki wanne waliokuwa wakiongozwa na mpakistani Imraan Gopang, kwa kutumia kompyuta mpakato maalum aliyokuwa nayo mle botini. Alipomaliza alipeana mikono na wale jamaa mmoja baada ya mwingine, akimalizia na Imraan Gopang.

    "Ilikuwa ni faraja kufanya tena biashara na wewe, Imraan." Alimwambia, na kwa mara nyingine jamaa akaelewa kuwa ile haikuwa mara ya kwanza kwa wale jamaa kufanya pamoja kazi kama ile.

    "Na mimi vile vile, kamanda! Ukija tena kwenye nchi yetu hii ya majanga usisite kunipigia...tukutane japo kwa kikombe cha kahawa..." Imraan alimjibu.

    "Ha ha ha haaaa...Okay poa, Imraan haina shida.Ila unue umipokea simu yangu haitakuwa kwa ajili ya kuoanga miad ya kupata kikombe cha kahawa kaka...itakuwa ni kwa kazi tu". Imraan akacheka pamoja naye, na walipomaliza kucheka, mmarekani mweusi akamwambia, "Basi sasa nyinyi na sisi tutagawana njia baada ya kama dakika kumi hivi...helikopta maalum itawafikisha Karachi...na pale kila mmoja atatawanyika kivyake...mimi na ninyi hatujaonana kabisa jamani...na siku hii haipo kabisa katika historia zenu...sawa?"

    "Kama kawaida..." Mmoja wale makomando alini u wakati Imraan akiafiki kwa kichwa tu swala lile.

    "Good. Basi mpaka hapo tutakapohitajiana tena...kama ikibidi." Mmarekani mweusi alisema.

    "Poa."

    ______________



    Dakika kama saba baadaye boti liliegeshwa kwenye ukingo wa pili wa mto ule, likiwa limesafiri kiasi cha kama kilometa kumi na tano kutokea pale ambapo lilipokuwa likiwasubiria wale makomando. Kutokea mle kwenye boti zilionekana helikopta mbili zikiwa zimeegeshwa umbali fulani kando ya mto ule.

    “Okay Imraan…nyie mtaingia kwenye ile helikopta ya kushoto…itawafikisha Islamabad na huko kila mtu ataangalia ustaarabu wake…sisi tutaingia kwenye ile ya kulia na kuelekea Karachi …” Mmarekani mweusi alisema.

    Lakini haikuwa hivyo...





    “Okay Imraan…nyie mtaingia kwenye ile helikopta ya kushoto…itawafikisha Islamabad na huko kila mtu ataangalia ustaarabu wake…sisi tutaingia kwenye ile ya kulia na kuelekea Karachi…” Mmarekani mweusi alisema.

    Lakini haikuwa hivyo...



    ________________



    Kutokea kwenye lile boti, jamaa aliwashuhudia Imraan Gopang na wenzake wakiikwea ile helikopta waliyoelekezwa kuwa itawapeleka Ismalabad.

    “Kwa hiyo sisi tunaondoka muda gani kutoka hapa…?” Jamaa aliuliza huku akimgeukia yule mmarekani mweusi, lakini akashangaa akijikuta akiwa ameelekezewa mitutu ya bunduki na wale walinzi wa yule mmarekani mweusi.

    Khah!

    “Hii nini sasa…?” Aliuliza kwa mashaka, macho yakimtembea.

    “Uko chini ya ulinzi Nouman Fattawi…” Mmarekani Mweusi alimwambia huku akimtazama moja kwa moja usoni, ilhali akiwa ameweka mikono yake mifukoni, wale walinzi wake wakiwa wamemuelekezea mitutu ya bunduki zao yule jamaa aliyeshuka mtaroni na beseni la choo.

    “Ebbo! Hii ni nini sasa…who are you?” Jamaa aliyetambuliwa na Mmarekani mweusi kuwa ni Nouman Fattawi alimaka, akitembeza macho kwa wote mle botini. Huko nyuma yake alilisikia lile heliokopta la akina Imraan Gopang likianza kuunguruma tayari kwa kupaa.

    “Derrick Appiah…CIA!” Mmarekani mweusi alijitambulisha huku akizidi kumtazama moja wka moja machoni.

    Kabla hajajibu, Nouman alijikuta akipigwa teke kwa nguvu nguma ya goti na mmoja wa wale walinzi wa Derrick, na bila kupenda akaenda chini kwa goti moja. Mitutu ya bunduki ikamuinamia pale pale chini.

    “What the…?” Alijaribu kuuliza kwa hamaniko, lakini mikono yenye nguvu ikambana kutokea nyuma na hapo hapo akapigwa pingu mikononi, kwa nyuma. Akainuliwa kibabe kutoka pale chini na kubaki wima, akitazamana tena na Derrick Appiah wa C.I.A.

    “Wewe ni Gaidi, Nouman…na daima serikali ya Marekani huwa haishirikiani na magaidi…Guantanamo Bay bado haijafungwa rasmi kama kaka Obama alivyosema, hivyo kwa sasa inakuhusu sana tu…” Jamaa alimjibu bila kupepesa.

    Nouman alichanganyikiwa.

    “Seriously? Tumekuwa tukifanya kazi pamoja miaka yote hii? Leo unaniita gaidi?” Alihoji.

    “Sasa kumbe we’e nani?” Mmoja wa wale walinzi wa mtu aliyejiita Derrick alimuuliza kwa kejeli, lakini Nouman hakumjali.

    “Ulifanya kazi na mimi? Lini?” Derrick alimuuliza.

    “Sio wewe...lakini C.I.A…nimeshakutana na watendaji kadhaa wa C.I.A. hapo nyuma ambao ndio tuliopanga nao mikakati yote hii…!”

    “Uliokutana nao hawakuwa C.I.A. Nouman…bila shaka kilikuwa ni kikundi tu cha wahuni kilichokuwa kikinufaika na vita kati ya Marekani na Osama…na Al-Qaida. Sasa vita imekwisha….tunawatia mbaroni nyote!” Derrick alimkoromea.

    Duh!

    Akili ilimzunguka Nouman. Hakuona namna ambavyo angeweza kujiokoa kutoka pale.

    “Sasa nini kinafuata, Derrick Appiah wa C.I.A.?” Alimuuliza kwa hasira.

    “Tunaenda kwenye helikopta ile na kupaa moja kwa moja mpaka kwenye kambi maalum ya kijeshi nje ya Pakistani…hatuendi Karachi kama nilivyowaambia wale matarishi.

    “Halafu…?”

    “Utarataibu wa kukufikisha Guantannamo Bay utafanyika na huko utakutana watu wengine watakaokuhoji…mimi kazi yangu ni kukufikisha kwenye hiyo kambi yetu ya kijeshi tu, kutokea hapa…lets go!” Derrick alimjibu, na kuamuru.

    Nouma alitolewa na wale walinzi wa Derrick hadi ukingoni mwa ule mto. Akaongozwa kuelekea kwenye ile helikopta iliyobakia, wakati huo akiiona ile ya akina Imraan ikiwa imeshaanza kupaa. Aliona kuwa safari yao ya kuelekea kwenye ile helikopta ilikuwa imeongezeka mtu mwingine mmoja, ambaye alihisi kuwa ndiye aliyekuwa akiendesha ile boti. Yule tabibu aliyekuwa akimtibia yule mamluki aliyejeruhiwa naye alikuwa pamoja nao kwenye msafara wa kuiendea ile helikopta.

    Akili akazidi kumzunguka.

    “Sasa lile boti vipi…mbona linabaki tu pale?” Aliuliza, akijaribu kumchimba zaidi yule mmarekani mwenye sura mbili.

    “Si kazi yako…songa mbele huko!” Alikoromewa.

    “Mi najua unafanya kosa kubwa sana wewe…na kama si kingine, basi ni kwamba ninyi ndio nilikuwa nikishirikiana nanyi tangu awali, sasa kama hamkuwa C.I.A. tangu awali hilo ni siri yenu…lakini usiniambie kuwa niliokuwa nikipanga nao mkikakati hii walikuwa wahuni fulani tu…na kwamba ninyi ndio C.I.S., siamini hilo!”

    “Inaelekea una hamu sana ya kuOngea Nouman Fattawi, gaidi kutoka Tanzania, eenh? Basi usiwe na pupa…utaongea sana tu kule Guntannamo!” Derrick alimjibu.

    Nouman Fattawi, akaishiwa namna. Akapiga kimya, akiijutia nafsi yake kuamini kile alichokiamini wakati anaingia kwenye kujihusisha na watu wale…



    _________________



    Wakiwa kwenye ile helikopta ambayo ingewafikisha Islamabad, Imraan Gopang na wale wenzake walipongezana kwa kazi nzuri iliyowaacha wakiwa na vitita vya fedha kwenye akaunti zao.

    “Kaka ilifika siku ulitaraji kuwa tutakuja kuwa tunatafuna dola za mmarekani kwa kazi hizi?” Mmoja wa wale wenzake alimuuliza yule mwenzao mwenye asili ya Afrika.

    “Aaa, hapana kaka. Hii ni kama ndoto kwa kweli. Tulikuwa tunauana wenyewe kwa wenyewe kule Afrika kwa vitu vya kijinga tu...ng’ombe, mashamba, wanawake…wakati kumbe huku unaweza kuua au kuuawa kwa pesa ya maana kiasi hiki?” Jamaa alijibu, na wote wakaagua vicheko.

    Helikopta yao ilizidi kwenda hewani na kukamata uelekeo wa Islamabad.

    “Kwa hiyo kaka wewe unaishije hapa kwenu, na hali kama hii…? Hawa watalebani wakikushtukia si watakufanya asusa wewe?” Moja wa wale wenzake ambaye alikuwa raia wa Bangladesh alimuuliza Imraan. Imraan akacheka.

    “Mimi ni mwalimu wa madrasa tu huku kwetu…ni kazi inayoheshimika na kutotiliwa mashaka kabisa…hakuna anayejua ninafanya nini nyuma ya pazia, na ndio maana mawasiliano yetu huwa ni ya siri sana…”

    “Sasa hela yako unaifaidije kaka…?”

    “Oh, hiyo nitaifaidi tu kaka…sina mpango wa kubaki hapa milele…nikishakusanya pesa ya kutosha naondoka hapa na familia yangu…natafuta nchi moja iliyotulia nafungua hoteli moja maridadi, nawaonyesha wenyeji mapishi ya kipakistani…” Imraan alimjibu.

    Kimya kikatawala.

    “Dah, bora hivyo aisee…hii sio nchi ya kujengea maisha kabisa kwa kweli…” Mwingine alisema.

    “Yah, lakini kuna tunaonufaika na hali hii hapa Pakistani…” Imraan alijibu.

    Kutokea pale angani waliweza kuiona ile helikopta nyingine nayo ikiwa hewani.

    “Oh, naona jamaa nao wameshakamata anga…” Moja wa wale wenzake alisema.

    “Yah…Naombea tu isipite muda mrefu kabla jamaa hajanitafuta tena kutupa kazi nyingi…HOLLY SHHHIITT!!” Imraan alianza kujibu, lakini jibu lake likaishia kwenye apizo la mshangao, pale yeye na wale wenzake walipoishuhudia kwa kihoro ile helikopta nyingine ikilipuka vipande vipande hewani, wimgu kubwa la moto likiambatana na mlipuko ule.

    Laah!

    “Haaah, watalebani wameidungua!” Mwingine alimaka.

    “Ina maana na sisi tutadunguliwa anytime, gadddemmit!” Mwafrika alimaka, na hata pale aliposema maneno yale, rubani wao aliilaza ubavu ile helikopta na kuanza kuishusha chini.

    “HEEEEYY, Unaishusha chini tena??” Imraan alimaka, lakini hapo hapo jamaa akaiinua juu zaidi ile helikopta, kwa kasi sana, kisha akailaza ubavu mwingine, yaani kama mtu anayejaribu kuikwepesha ile helikopta ili isidunguliwe kama ile nyingine.

    “Eee Mungu wangu…ina maana wale jamaa wote ni marehemu kule hivi sasa? Si pa kupona mtu pale!” Mwenzao mmoja alipayuka.

    “Haponi mtu pale…” Imraan alisema huku akiwa amehamanika vilivyo, helikopta yao ikizidi kupasua anga.

    “Loh…kazi bure sasa hii…bidii yote ya kumchomoa yule jamaa kutoka kwa watalebani…ndio ameishia hivi?” Mwafrika alisema.

    “Sio kazi bure komredi…akaunti zetu zimenona…tuombe tunusurike tu hapa…” Imraan alimjibu.

    “Kweli kaka…”

    Safari yao iliendelea bila ya tukio lolote…



    ______



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog