Search This Blog

Monday 24 October 2022

MKONO WA SHETANI - 2

 

    Simulizi : Mkono Wa Shetani

    Sehemu Ya Pili (2)







    Masaa mawili mara baada ya Jacob kuwa ameshaondoka ofisini hapo, simu ya mkurugenzi wa ofisi hiyo, Bi. Anita iliita kwa fujo. Kabla ya kuipokea, Bi. Anita aliangalia ukutani, saa ilionyesha kuwa ni saa sita na dakika ishirini na moja.

    Aliingalia simu hiyo kwa nukta kadhaa kabla ya kuinua mkono wa simu.

    “Fukuzi hapa, nikusaidie nini” Alisema Bi. Anita kwa sauti ya barafu kidogo.

    “Nakuhitaji ofisini haraka iwezekanavyo” Ilisema sauti hiyo huku mnenaji wake akiwa hajajitambulisha.

    “Sawa mzee, nakuja” Alisema Bi. Anita, safari hii kwa sauti ya kike. Alikuwa ameshaitambua sauti.

    Dakika tano baadaye, Bi. Anita alikuwa ameshafika Ofisi moja muhimu ya umma. Hapo alikuta ‘Mkubwa’ aliyemwita akiwa katika hali ambayo asingesubiri kuambiwa kuwa kulikuwa na jambo baya likiwa linamtatiza. Baada ya kukaribishana na salamu, ‘Mkubwa’ alimweleza Bi. Anita kilichomfanya amwite.

    “Leo asubuhi, muda mfupi uliopita kumetokea tuko ambalo ni aibu kwa taifa” alianza kusema ‘Mkubwa’, Sauti yake ikishindwa kuficha huzuni, hasira na wasiwasi aliokuwa nao. Bi Anita alitabasamu, tabasamu ambalo ‘Mkubwa’ alilielewa kuwa ni la kumtaka aeleze kilichomsibu. Hivyo ‘Mkubwa’ akaendelea na maelezo.

    “Kama miezi nane imepita, ambapo nilipokea taarifa toka umoja wa nchi za Ulaya na Marekani ya kunieleza juu ya uamuzi wa nchi hizo kulipatia shirika la JEPA msaada wa kipesa ili kusaidia katika vita dhidi ya umaskini. Umoja wa nchi za Ulaya pamoja na Marekani walikuwa wameamua kulipa Shirika hilo mamilioni ya dola za kimarekani kama msaada”. ‘Mkubwa’ alimeza mate na kuendelea.

    “Kama ujuavyo kuwa shirika hilo ni moja kati ya mashirika ya Umma ambayo yanajihusisha kwa kiasi kikubwa katika vita dhidi ya umaskini kwa kuwawezesha watu binafsi na vikundi vidogo vya biashara kujiendeleza. Hivyo nchi hizo ziligundua mchango na umuhimu wa shirika hili na kuamua kuwafikia wananchi maskini kwa njia yake. Tarehe ishirini na moja mwezi huu, ambayo ni juzi juzi tu. Mkurugenzi mtendaji wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa alikwenda jijini New York Marekani ili kutia sahini nyaraka za makabidhiano ya pesa hizo. Nyaraka hizo ndizo zingetuwezesha kuchukua fedha hizo hapa nchini kupitia Benki ya DE EURO LINKAGE tawi la Tanzania. Imezoeleka kuwa, mkataba ukisha sainiwa nchi au mashirika wafadhili hutoa fedha hizo kwa mafungu mafungu huku wakiwa wamewekamasharti nataratibu ili kuyapata mafungu hayo. Lakini kwa sababu za kiufundi, mojawapo ikiwa nikuja kwa uongozi mpya katika Umoja wa Ulaya na uchaguzi mkuu ujao nchini Marekani, ikaamuliwa kuwa fedha hizo zitachukuliwa hapa nchini na kuhamishiwa kwenye akounti ya shirika hilo kwa mkupuo. JEPA ikipewa sharti la kuhakikisha kuwa, Ofisi ya mkaguzi mkuu wa serikali inahusishwa kwa karibukila wanapochukua pesa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

    Tarehe ishirini na mbili makabidhiano yalifanyika katika jiji la New York, ambapo kwa nchi yetu aliyewakilisha ni Mkurugenzi mkuu wa shirika la JEPA bwana Makia Kimisa, Waziri wa fedha na uchumi Bwana Mwaitete, na Balozi wetu nchini Marekani. Baada ya shughuli nzima ya utiwaji sahini na makabidhiano ya nyaraka za msaada huo Kimisa aliondoka Marekani siku iliyofuata. Jana alifika hapa nchini akiwa na nyaraka zote ambazo shirika hilo lingezitumia kwenda DE EURO LINKAGE BANK kuhamisha pesa zote tulizopewa kwenda kwenye akaunti ya shirika hilo. Leo asubuhi, Mhe Makia Kimisa kwa kushirikiana na maafisa wengine wa ofisi yake, walipitia nyaraka hizo na kuziandaa kwa ajili ya kwenda nazo Benki ya DE EURO LINKAGE kwa ajili ya kuzihamishia kwenye akaunti ya shirika. Walizihakiki na kuona kuwa hazikuwa na mapungufu wala kasoro yoyote. Saa tano na nusu asubuhi leo hii msafara wa mkurugenzi na maafisa wengine ulielekea zilipo ofisi za Benki ya DE EURO LINKAGE. Jambo la kushangaza mara walipofika ofisi za DE EURO LINKAGE waliambiwa kuwa zilikuwa zimepita kama dakika thelathini tu tangu ambapo watu wapatao wanne walikuwa wameenda hapo Benki wakiwa na nyaraka zote na kufanya utaratibu wa kuzichukua pesa hizo, walifanikiwa kuzichukua baada ya taratibu zote kutimizwa. Kwa hiyo mamilioni ya dola za kimarekani yamechukuliwa na watu wasiojulikana.

    Pamoja na kuwa taarifa za kupewa msaada huo mkubwa wa kipesa kuwahi kutokea katika historia ya nchi yetu zilienea katika vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya Afrika, lakini hakuna mwingine aliyejua juu ya makabidhiano na utiwaji sahini wa fedha hizo. Mimi kama kiongozi wa nchi, na maafisa wachache wa ngazi za juu wa umoja wa nchi za Ulaya na Marekani ndio tuliokuwa tukijua juu ya tarehe na mahali pa makabidhiano ya nyaraka za pesa hizo.”

    ‘Mkubwa’ alimaliza maelezo yake huku akimwangalia Bi. Anita kwa jicho la ‘naomba msaada’. Bi.Anita alishusha pumzi ndefu na kuachia tabasamu.Tabasamu lililoashiria kuwa kazi ipo. Tofauti na lile tabasamu aliloachia pale mwanzoni.

    “Nimekuelewa mheshimiwa, kwa hiyo unataka ofisi yangu ifanye nini? Ikuletee waliochukua pesa, au ikuambie imekuwaje nyaraka zikawa mbili? Bi.Anita aliuliza.

    “Swali zuri; jambo la kwanza nataka hizo pesa zipatikane ndani ya muda mfupi kadiri inavyowezekana. Pili ningependa kujua ni namna gani hizi nyaraka zikawa katika sehemu mbili” ‘Mkubwa huyo wa nchi’ alisema huku akimkabidhi Bi. Anita lundo la karatasi lilokuwa katika mafungu mawili.

    “Kati ya hizi nyaraka nashindwa kuelewa ipi ni halisi na ipi ni ya kughushi. Hili faili nililoandika namba ‘1’ juu yake ndilo lenye karatasi ambazo Makia Kimisa alienda nazo Benki, na faili la pili ndilo lenye nyaraka ambazo zimetumiwa na wahalifu katika kuchukua pesa Benki ndilo hilo nililoandika namba ‘2’ juu yake” ‘Mkubwa wa nchi’ alisema huku akimwangalia Bi.Anita kwa makini kisha akaendelea.

    “Nahitaji ofisi yako itafute ukweli juu ya nyaraka hizi. Nataka kujua ni vipi ziwe katika sehemu mbili na tena zote zifanane. Lazima kutakuwa na Mkono wa Shetani hapa?!!! Alimaliza kuongea na kusubiri lolote toka kwa Bi. Anita.







    “Baada ya tukio hilo ni hatua gani ambazo nchi imechukua tofauti na kuieleza ofisi yangu? Bi. Anita alimwuliza ‘Mkubwa’.

    “Mipaka yote imefungwa ukaguzi katika vituo mbalimbali vya usafiri ni mkali sana ili kuhakikisha waliochukuwa pesa hizo hawapati nafasi ya kuzisafirisha pesa hizo nje ya jiji na nchi. Tumesambaza namba za noti za pesa zilizoibiwa katika Benki zote katika bara la Afrika ili kuzuia ubadilishwaji wowote wa pesa hizo. Pia Polisi wanaendelea na msako mkali wa kuwatafuta maharamia hao.

    Nimeamua kukupa jukumu hili kutokana na unyeti na uharaka wake. Nchi za umoja wa Ulaya na Marekani wanataka taarifa juu ya ukweli wa mambo ndani ya siku kumi na tano tu. Naamini ndani ya nchi hii hakuna ofisi inayoweza kutuondolea aibu hii isipokuwa ofisi yako tu. Unapaswa kujua kuwa hakuna ajuaye kuwa nimeikabidhi ofisi yako kufuatilia jambo hili. Hii inamaanisha hata baraza langu halijui juu ya uamuzi wangu huu wa kuipa ofisi yako kazi ya kuutafuta ukweli juu ya jambo hili”.

    Baada ya maelezo mengine na kushauriana, Bi.Anita aliondoka Ofisi muhimu ya umma huku akiwa amebeba jukumu hilo kama mtu anayevuka mto wa maji mengi yaendayo kasi huku akiwa amebeba gunia la sukari.



    **************



    Hali ya mawingu mazito iliyoandamana na manyunyu ya mvua ilikuwa imetanda anga lote la jiji la Dar es salaam. Kwa wakazi wa jiji hili ambao si wazoefu wa hali ya hewa kama hii, kwao ilikuwa kama adhabu. Kwani hata wale waliokuwa wamezoea kwenda kwenye shughuli zao pasipo kutumia usafiri wa moto, iliwabidi waingie gharama ya nauli ili waweze kufika sehemu zao za kujipatia ridhiki.

    Wakati hali ikiwa hivi asubuhi hii, katikati ya jiji la Dar, gari nyeupe aina ya Land Cruser Prado ya kisasa ilikuwa inaegesha mbele ya jengo moja kubwa la ghorofa. Mara baada ya gari hiyo kuegesha akatelemka mwanamke mmoja wa makamo, kwa kukadiria mwanamke huyo alikuwa na umri wa kati ya miaka hamsini na sitini. Lakini ilibidi mtu unayemtazama uwe na ujuzi wa kukadiria ili aweze kujua ukweli kuhusu umri wa mama huyo, kwani macho yanaweza kukuambia kuwa unayemwona ana umri kati ya miaka thelathini na tano tu hivi.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuwa ameshatoa faili moja toka ndani ya gari na kuufunga vizuri mlango wa gari, mwanamke huyu alipiga hatua za kikakamavu kuelekea ulipo mlango wa kuingilia ndani ya jengo hilo.

    Saa mbili ya asubuhi iligonga wakati mwanamke huyu akiwa mbele ya mlango wa ofisi yake. Juu ya mlango wa ofisi hiyo palikuwa na maandishi yaliyosomeka “MKURUGENZI”. Huku akionekana kuwa na jambo lililokuwa likimtatiza, alipoingia tu ofisini badala ya kuelekea kwenye kiti kama ilivyo kawaida yake, mwanamke huyo alielekea upande wa kushoto wa ofisini akiwa unaingia ndani. Hapo macho yake yaliongoza mpaka ukutani. Ukutani hapo kulikuwa na ramani nyingi za sehemu mbalimbali Duniani. Macho yake makali yalifikia kwenye ramani ya bara la Afrika yalitembea kwa muda wa kama nusu saa hivi, kisha akahamia kwenye ramani ya bara la Marekani hapo ilimchukua takribani dakika kumi na tano. Hatimaye alirudi kwenye ramani ya bara la Afrika kabla ya kuchukua ramani ya jiji la Dar. Alipofika hapo akajikuta akiropoka kwa hasira “haiwezekani hii ni aibu na uonevu mkubwa, lazima utakuwa ni mkono wa shetani”

    Aliichukua hiyo ramani ya jiji la Dar na kuiweka juu ya meza.Kisha akavuta kiti na kukaa. Kwa jinsi alivyokuwa akiiangalia ramani hiyo ungefikiri ndio kwa mara ya kwanza leo anaiona. Hali ya mambo ilimlazimu ainone ramani hii ni mpya. “Hivi inawezekana mtu au watu waliofanya zoezi hili wawe wanatoka ndani ya jiji hili? Alifoka huku akipiga ngumi yake juu ya meza. Tangu alipopata taarifa za kuyeyuka kwa mamiilioni ya dola za kimarekani, Bi. Anita amekuwa kama mtu ambaye amebebeshwa gunia la maharage ambalo hajui mahali pa kulitua. Jambo hilo ndilo lilikuwa bado likiitafuna akili yake asubuhi hii ambayo amefikia kuangalia ramani zilizoko kwenye kuta za ofisi yake. Kwani baada ya kuwa amelitakafakari jambo hili jana yote tangu aambiwe na mkubwa, Bi. Anita alikuwa bado hajaamua ni nani kati ya vijana wake alistahili kupewa kazi hii.



    Macho ya Bi.Anita yaliendelea kuiangalia ramani ya jiji la Dar kwa makini zaidi. Ni miaka ishirini imeshapita tangu Bi. Anita alipoteuliwa ili awe mkuu wa idara ya siri ya ujasusi ya nchi. Idara hii ni ya siri kabisa kiasi kuwa hata vigogo wengine hawakuwa wanajua juu ya utendaji wake. Hata miye nayeandika habari hii ilitokea bahati tu kuweza kunasa habari za kuwepo kwake. “Ofisi Fukuzi” ndio jina hasa ambalo kitengo hiki kilipewa. Hii ilitokana na kazi za Idara hii kuwa ni za kufukua mambo ambayo si rahisi kuyafukua katika hali ya kawaida. Ilifukua mambo ambayo watu wengine wasingependa yafukuliwe. Kuna visa vingi ambavyo vimeshawahi simuliawa ambavyo vimewahi fukuliwa na kitengo hiki kupitia mpelelezi Jacob Matata. Visa kama vile HEKA HEKA na NI ZAMU YAKO KUFA.

    Bi. Anita ni mtaalamu wa juu katika masuala ya upelelezi na ujasusi. Sifa hizi ndizo zilizomfanya Rais mmoja wa wakati huo kutosita kumpa kazi ya kusuka na kusimamia kikosi cha Idara ya siri ya “Ofisi Fukuzi”.

    Ofisi hii ambayo majengo yake ndimo alimoingia Bi. Anita asubuhi hii, imesheheni vijana waliopikwa na kupikika katika masuala ya upelelezi. Ikulu imekuwa ikitenga fungu maalumu kama matumizi ya ofisi hii. Hali hii imesababisha “Ofisi Fukuzi” kuwa na vifaa vya kisasa na vijana ambao wana mafunzo ya juu kabisa na kisasa toka nchi zilioendelea katika masuala ya ukachero.

    Lakini kazi aliyokuwa amepewa jana na ‘Mkubwa’ ilimfanya Bi. Anita akose raha. Kwanza kisa cha wizi huu hakijulikani mwanzo wala mwisho wake. Pili ni muda mfupi sana ulikuwa umetolewa ili kukabidhi kazi hiyo. Hii ilimtaka Bi. Anita kutafuta mtu ambaye angeweza kufanya kazi hii kwa kuzingatia mambo yote hayo.

    Alipomaliza kuangalia ramani ya Dar – es – salaam, Bi Anita alisimama. Alipiga hatua chache mpaka lilipokuwepo dirisha na kuanza kuangalia nje. Wakati huo wote akili yake ilikuwa ikichambua ni kijana gani alikuwa akifaa kwa kazi iliyokuwa inalikabili Taifa.



    * * *



    Wakati kichwa cha Bi. Anita mkuu wa “Ofisi Fukuzi” kikiwa kinawaka moto juu ya nani ampe mzigo huu mzito wa kusaka ukweli kuhusu upotevu wa mabilioni ya dola za kimarekani, ni asubuhi hiyo hiyo ambapo kikao fulani nyeti kilikuwa kikiendelea.

    Kikao hicho kilijumuisha washika dau wa ngazi za juu wa masuala ya usalama. Wadau hao walikuwa wamekutana kwa malengo makuu mawili. Moja ni kutafuta kauli na msimamo wa pamoja juu ya upotevu wa pesa hizo za misaada. Kauli hiyo ndiyo ambayo ingetolewa na Rais kwa wananchi na nchi wafadhili ambazo kwa wakati huo zilikuwa zimepamba katika kutoa shutuma juu ya Shirika la JEPA ya Tanzania.

    Pili Rais pamoja na viongozi wa juu wangependa kupokea taarifa rasmi toka kwa mkurugenzi wa shirika la JEPA, ndugu Makia Kimisa. Katika taarifa hiyo bwana Kimisa alitarajiwa kusema nini kilikuwa kimetokea tangu mwanzo hadi mwisho. Wakati huo huo, mkuu wa Polisi Inspekta Amosi Bugingo alitegemewa kutoa taarifa juu ya mahojiano yaliyofanywa na jeshi la Polisi kwa mhudumu wa Benki aliyehudumia siku ya tukio.

    Kikao hicho kilikuwa kimeanza majira ya saa mbili na nusu asubuhi. Ndani ya chumba cha kikao hali ilikuwa ni ya huzuni na simanzi kubwa. Hakuna aliyekuwa anajua kilichotokea na jinsi mchezo huu wa wizi wa mamilioni ya dola ulivyochezwa.

    Mkurugenzi wa shirika la JEPA, ndugu Makia Kimisa hakuwa anaamini kinachotokea, tangu jana yake ambapo ndio siku ya tukio alikuwa kama mtu aliye ndotoni tu. Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kutakiwa kueleza kikao hicho juu ya yote tangu safari yake ilivyoanza hapa Tanzania, namna makabidhiano ya nyaraka za kupokelea msaada yalivyofanyika jijini New York, mpaka ikatokea wakakuta pesa zimechukuliwa.



    Makia Kimisa alisimama na kueleza hatua kwa hatua jinsi mambo yote yalivyofanyika. Kikao chote kilimsikiliza kwa makini sana. Mpaka anamaliza, Makia Kimisa aliamini kuwa aliweza kueleza kila kitu kilichofanyika kwani hata jinsi alivyoingia kulala nyumbani kwake alisimulia.

    “Kuna mtu yeyote aliye na jambo ambalo anataka kumwuliza Makia Kimisa kwa ufafanuzi zaidi? Aliuliza Rais baada ya kuona chumba chote kiko kimya pale Kimisa alipomaliza kusoma ripoti yake. Ukumbi wa kikao ulikuwa kimya kabisa pale ambapo mkuu wa Polisi Inspekta Amosi Bugingo aliposimama na kuuliza

    “Mheshimiwa, ningependa kujua kuwa tangu ulipoingia nchini briefcase iliyokuwa na nyaraka hizo uliiweka wapi? Pili, je hakukuwahi kuingia mtu ndani ya chumba hicho?

    Baada ya kufikiri kwa muda Makia Kimisa alijibu,

    “Mara baada ya kushuka ndani ya ndege hiyo juzi nilipitiliza moja kwa moja mpaka zilipo ofisi zangu, pale kwenye majengo ya shirika la JEPA. Hapo ndipo nilipoiweka hiyo briefcase ndani ya kabati la chuma na kufunga. Jana nilipofungua nilikuta ikiwa ndani ya kabati kama kawaida. Na hapo kwa kushirikiana na maafisa wengine tukazifanyia uhakiki na kukuta zikiwa sawa kama nilivyozichukua kule New York”. Makia Kimisa aliongea kwa kujiamini na kwa uhakika.

    “Juu ya mtu yeyote kuingia ofisini hapo sikupata taarifa hizo na wala sijauliza kwa katibu mhutasi wangu. Labda kama akiulizwa sasa…”

    Kabla Makia Kimisa hajamaliza, Rais aliamuru mtu wa mapokezi wa ofisi ya Makia na katibu mhutasi wake waitwe mara moja kikaoni hapo.

    “Na wakati tukiwasubiri watu hao, naomba mkuu wa Polisi Inspekta Amosi Busingo atupe taarifa juu ya mahojiano ya jeshi hilo na wahusika wa Benki ya DE EURO LINKAGE waliohudumia siku ya tukio” Alisema m.

    Wakati huo Inspekta Amosi Bugingo alikuwa ametoka nje. Kwa vile kikao kilikuwa ni cha dharula, na mahojiano kati ya Polisi na dada aliyehusika na utoaji wa pesa katika Benki ya DE EURO LINKAGE yaliendelea mpaka usiku wa manane. Inspekta Amosi Bugingo alikuwa amemwamuru Inspekta wa Polisi wa kituo cha kati, Inspekat Ezron kuleta taarifa hiyo moja kwa moja kikaoni asubuhi hiyo. Kabla ya kikao Inspekta Amosi alimpigia simu Inspekta Ezron ili kujua kama taarifa ilikuwa tayari, ambapo Inspekta Ezron alimtaarifu mkuu Polisi Inspekta Amosi kuwa ripoti ilikuwa tayari. Na kuwa kuna mambo machache aliyokuwa amegundua na kupendekeza baada ya mahojiano hayo. Hivyo Inspekta Ezron akamwambia mkuu wa Polisi kuwa angefika nje ya jengo la kikao mnamo saa tatu na robo asubuhi hiyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lakini mpaka wakati mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa ameanza kuongea saa tatu na nusu, Inspekta Ezron alikuwa hajatokea na mkuu wa Polisi hakuwa na taarifa yoyote ya kutoa mbele ya Mkubwa na baraza lake. Hali hii ilimfanya mkuu wa Polisi, Amosi, kutuma vijana wake ili kumfuata Inspekta Ezron nyumbani.

    Hivyo wakati Rais anamtaka mkuu wa Polisi kutoa taarifa waliyonayo Polisi kutokana na mahojiano kati yao na wahusika wa DE EURO LINKAGE, mkuu huyo wa Polisi ndio kwanza alikuwa anatokea nje ambako alitegemea vijana wake waliorudi toka kwa Inspekta Ezroni wangempa taarifa hiyo. Lakini katika hali ya kushangaza katika kikao hicho, mkuu huyo wa Polisi alipopita mbele ili kutoa taarifa yake hakuwa na karatasi hata moja. Huku akionekana mwenye wasiwasi na aliyebadilika ghafla tofauti na kawaida yake mkuu wa Polisi Inspekta Amosi Bugingo alianza kuongea.

    “Mheshimiwa, pamoja na washika dau wengine, nasikitika kusema kuwa sitakuwa na taarifa ya kuwapa katika kikao hiki. Kwa sababu mkuu wa kituo cha kati ambaye ndiye aliyefanya mahojiana na meneja wa Benki ya DE EURO LINKAGE na mhudumu wa Benki hiyo ndiye aliyekuwa na taarifa hizo mpaka asubuhi ya leo. Kwa vile mahojianao hayo yalifanyika mpaka usiku wa manane usiku wa kuamkia leo. Baada ya kuona amechelewa kuniletea taarifa hiyo asubuhi hii nilituma watu waende kuangalia ni nini kimesababisha asifike kuniletea taarifa hiyo kwa muda niliomwamuru..” Hapo alitua na kisha huku akiwa amekunja ngumi yake aliendelea.

    “..Vijana wamerudi na kunitaarifu kuwa wamefika nyumbani kwa Inspekta Ezron na kukuta ameuawa, maiti yake ikiwa imeachwa ndani huku taarifa aliyokuwa ameandaa ikiwa haionekani!!!





    Alipofika hapo mkuu wa Polisi Inspekta Amosi Busingo aliuma meno yake kwa hasira na kupiga ngumi yake juu ya meza iliyokuwa mbele yake.

    “Sasa nimetuma vijana wangu wakamchukue meneja wa Benki ya DE EURO LINKAGE na yule mhudumu, ili tuwahoji tena maana inaonekana wanataarifa ambazo hawa wahalifu hawataki tazipate, ndio maana wameamua kumuua inspekta Ezroni!!! Kikao chote kilishikwa na baridi iliyochanganyika na hofu. Mkuu wa Polisi alirudi kukaa sehemu yake na kisha Rais akafunua kinywa chake na kusema, “Inaonekana watu waliofanya kazi hii si wababaishaji, ila watake wasitake ukweli utajulikana tu. Hivyo wakati tunasubiri meneja wa Benki ya DE EURO LINKAGE na yule mhudumu waje, fursa hii tuitumie kusikia maelezo toka kwa mtu wa sehemu ya mapokezi na katibu mhutasi wa ofisi ya mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa.”

    Mpaka wakati huu kikao hiki kilikuwa kinabadilika sura yake taratibu toka ile ya huzuni na aibu ya kuibiwa kwenda kwenye sura ya hofu na aibu ya kudhalilishwa. Tofauti na ilivyotarajiwa kuwa mtu wa sehemu ya mapokezi wa ofisi ya mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa na katibu mhutasi ndio wangesimama, badala yake mkurugenzi wa JEPA alisimama huku machozi yakimtoka.

    “Mheshimiwa, nasikitika kuwataarifu kuwa hata hawa watu tuliowahitaji wamekutwa wameuawa asubuhi hii sehemu mbili tofauti. Hivyo hawapo. Hii inatuweka katika njia nyembamba na kitendawili zaidi. …”

    Wakati Rais anataka kusema kitu kutokana na taarifa hiyo ya mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa, mkuu wa Polisi naye akasema, “Taarifa ninazopokea hivi punde ni kuwa meneja wa Benki ya DE EURO LINKAGE na yule mhudumu ambao ndio waliowahudumia wahalifu wa tukio hili wote wamekutwa wameuawa katika sehemu tofauti tofauti”.

    “Ok!! naomba kazi hii ya kuutafuta ukweli tuwaachie vijana wetu wa Polisi na kitengo cha upelelezi wafuatilie kisha tutaueleza umma na nchi wahisani kuwa tutatoa tamko rasmi baada ya siku kumi na tano kama walivyotaka nchi wahisani katika barua yao ya pamoja. Tukumbuke kuwa Baharini hawaogi na kopo na wala mguu wa bandia hauoti vinyweleo. Tuwaachie wataalamu wetu”.

    Baada ya maneno hayo kikao kiliahirishwa katika hali ya sitofahamu mioyoni mwa waliohudhuria kikao hicho. Ulinzi uliongezwa kwa viongozi hao wa nchi, hii ilitokana na hofu iliyotanda mioyoni mwao baada ya kusikia taarifa za vifo hivi vya kutatanisha.



    *************

    Wakati uso wa Bi. Anita, Mkuu wa Ofisi Fukuzi unapambwa na tabasamu, tabasamu la matumaini ndio kwanza ilikuwa inagonga saa tatu kasorobo. Kama utakumbuka huu ni wakati ule ambapo ndani ya chumba cha mkutano mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa alikuwa ameanza kutoa taarifa yake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Furaha iliyoleta tabasamu usoni kwa Bi Anita si kwamba ilikuwa inatokana na kuwa amemwona mtu aliyekuwa ameiba hizo pesa. Mpaka wakati huu hakuwa na taarifa zozote za wapi zilipo pesa wala wahalifu wenyewe. Bi. Anita hakuwa amemwaona mtu aliyekuwa amehusika na wizi wa mabilioni ya pesa, bali tabasamu lake la matumaini lilitokana na kuwa amempata mtu ambaye bila shaka angeweza kumfikia mhusika wa tukio hili na kurudisha mabilioni ya pesa.

    Zilikuwa zimepita dakika kadhaa akiwa amesimama sehemu ya dirishani huku macho yake kayaelekeza mita kadhaa nje. Uso wake ulikuwa uking’aa wakati alipokuwa akisogea juu ya meza, toka pale alipokuwa amesimama. Aliichukuwa ile ramani ya jiji na kuiweka ndani ya droo ya meza yake. Akanyanyua mkono wa simu na kubonyeza namba kadhaa kabla ya kusema.

    “Bi Anita hapa” alijitambulisha kisha akasema

    “Vipi Jacob Matata bado umelala saa hizi? Ok nakuhitaji hapa ofisini mara moja. Ukichelewa sana iwe nusu saa” aliongea kwa sauti iliyojaa mamlaka na kukata simu.

    Macho yake yalielekezwa darini. Kisha akajisemea “Jacob Matata ataweza, ataweza kufumbua kitendawili hiki na kuliondolea taifa aibu hii.”alisema maneno hayo huku picha ya Jacob Matata ikimwingia kichwani mwake.



    ******************

    Siku nne nyuma kabla ya ile ambayo alikutana na Jacob Matata ndani ya ndege akielekea Dar, Dr.Don alipokea simu toka kwa bosi wake iliyomtaka aende New York Marekani haraka iwezekanavyo.

    Siku hiyo kama kawaida yake alikuwa ndani ya ofisi yake ya siri iliyoko katikati ya jiji la Dar es salaam. Akiwa amekaa na kutulia huku akitathimini juu ya utendaji wake wa kazi katika bara la Afrika. Mara simu iliyokuwa mezani ilipata uhai. Kama mtu aliyekuwa akiisubiri simu hiyo aliinyanyua haraka

    “Don hapa”

    “Mr. Peari Robert” ulijibu upande wa pili

    “Ohh bosi habari za USA? aliuliza Don

    “Nzuri tu, ila si sana”

    “Kuna nini tena? Don alihoji

    “Naumwa sana, na dawa ya ugonjwa wangu unayo wewe” ulijibu upande wa pili

    “Unaweza kukaa na ugonjwa kwa muda gani kabla hujapata tiba yangu? Dr. Don alijua kuwa tatizo alilonalo Mr. Peari si ugonjwa

    “Ukichelewa sana iwe keshokutwa jioni la sivyo utakuta maiti yangu” Jibu hili liliashiria kuwa Dr. Don alihitajika kwa kazi ya haraka.

    “Okay nitegemee hapo muda wowote kuanzia kesho”.

    Kwa mtu mwingine ambaye angekuwa amesikiliza maongezi hayo angeweza kudhani Dr.Don ameuguliwa ghafla. Lakini hali halisi haikuwa hivyo maongezi hayo yalimaanisha kuwa kuna kazi ambayo Don alitakiwa kwenda kuifanya kwa haraka.



    * * *

    Siku mbili baadae Dr. Don tayari alikuwa ndani ya jumba moja la kifahari nje kidogo ya jiji la Washington DC, Marekani. Jumba hili ni maskani ya bosi wa Dr. Don aitwaye Mr. Peari Robert.



    Ilivyo ni kwamba, mara baada ya kuisha kwa vita ya pili ya Dunia mataifa mengi barani ulaya, Asia na Marekani yaliingia katika mbio za kujipatia maendeleo ya haraka. Kila nchi iliamini kuwa ili iweze kuwa na sauti duniani ni lazima iwe na maendeleo ya hali ya juu kiuchumi na kijeshi. Ni ushindani huo ndio ulioleta mabadiliko ya haraka katika mfumo wa uchumi duniani. Neno “Soko huria” na “ubinafsishaji” yalitawala ghafla katika vinywa vya nchi mbalimbali. Maneno hayo mawili “Soko huria” na “ubinafsishaji” yalitaka uhuru zaidi wa kibiashara kati ya watu wa nchi na nchi, bara na bara, na wakati huo huo yakitaka serikali kujiondoa kwa kiasi kikubwa katika biashara na kuacha kazi hiyo kufanywa na watu binafsi.

    Kupitia “Soko huria” na “ubinafsishaji” ilikuwa wazi vichwani mwa wazungu kuwa wangeweza kuingia tena Afrika na kufanya wanachokata. Waliamini kuwa nchi za Afrika hazikuwa zimejiandaa vya kutosha katika mfumo huo. Nchi za Afrika hazikuwa na bidhaa za kuweza kushindanisha katika “soko huru”, pia pindi ikitokea ubinafishaji wa mashirika ya Umma, waafrika wengi hawakuwa na uwezo wa kununua mashirika hayo ya umma. Hivyo ingekuwa ni nafasi nzuri kwao wazungu kuyachukua na kuyaendesha walivyokata wao.

    Hivyo makampuni mengi ya kibeberu ambayo yalifukuzwa na viongozi shupavu wa Afrika kama vile Mwl. J.K.Nyerere, Kwame Nkuruma na wengineo wengi, yaliona ndio wakati mzuri wa kurudi Afrika. Makampuni hayo yaliamini kuwa Afrika haitakuwa na uwezo wa kujitetea pindi wakianza kuinyonya kupitia sera hizo mbili za “Soko huria” na “ubinafsishaji”

    Mr.Peari Robert ambaye ni mingoni mwa maafisa wa ngazi za juu katika Umoja wa mataifa, aliamua kuanzisha makampuni mbalimbali ndani ya Afrika. Pamoja na kufanya biashara nyingi barani Afrika, lakini shughuli nyingi zilizokuwa chini ya Mr. Peari Robert zilikuwa ziko katika mkondo wa unyonyaji na udhulumaji wa mali za Afrika.

    Mr.Peari Robert ndiye aliyefanikiwa kumwondoa Dr. Don katika kazi yake ya ujasusi. Mr. Peari alimfanya Dr. Don kuwa mtendaji na msimamizi mkuu wa shughuli zote ndani ya Afrika. Kutokana na maslahi ambayo angeyapata tofauti na yale aliyokuwa akipata katika kazi yake ya ujasusi, Dr.Don alikubaliana na Mr. Peari Robert.

    Dr. Don alitumia ujuzi wake katika masuala ya ujasusi katika kufanikisha kazi mbalimbali za siri ambazo alitakiwa kufanya. Mr. Peari katika uchaguzi wake juu ya mtu wa kusimamia na kutekeleza mipango yake ndani ya Afrika alihitaji mtu kama Dr.Don na si vinginevyo, kwani alijua fika kuwa kazi zake zingehitaji mtu wa kutumia mbinu za uhalifu wa kimataifa ili afanikiwe.

    Kwa kutumia cheo chake ndani ya umoja wa mataifa Mr. Peari Robert hakuchelewa kupata taarifa za shirika la JEPA kukabidhiwa mamilioni ya Dola za Marekani kama msaada. Tangu alipopata taarifa hizo, Mr. Peari alizimezea mate pesa hizo. Hasa ukizingatia nchi iliyokuwa imepewa msaada ndiyo ambayo yeye na Dr.Don wameifanya kuwa makao yao makuu ya kiutendaji ndani ya Afrika. Tanzania ni moja ya nchi zilizokuwa zikiwaingizia faida kubwa. Hapa walikuwa na makampuni mawili. Moja ni la utalii na jinginine ni la usafishaji wa madini. Mr. Peari alianza kufuatilia kwa makini taarifa zote zilozohusiana na msaada huo wa pesa kwa shirika la JEPA.

    Wakati amempigia simu Dr. Don alikuwa amepata taarifa za kufanyika kwa hafla ya utiwaji sahini na makabidhianao ya nyaraka muhimu za msaada huo wa kipesa. Yeye Mr. Peari Robert alikuwa ni mmoja kati ya watu walioalikwa kwenye hafla hiyo ambayo ingefanyika katika jiji la New York.

    Hivyo ujio wa Don ulimpa matumaini Mr. Peari Robert kuwa pesa hizo angezipata, kwani tangu wameanza kufanya kazi na Don hakuna ambalo limewahi kushindikana kwao.

    “Mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa wa Tanzania kesho atasahini hati za makubaliano ya kupokea msaada toka nchi za Ulaya na Marekani” alianza kueleza Mr. Peari Robert baada ya kuwa wameshapata chakula cha jioni ndani ya jumba lake hilo la kifahari.

    “Msaada huo ni wa kulisaidia Shirika la JEPA la Tanzania katika vita yake dhidi ya umaskini, hivyo kiasi cha mamilioni ya dola za ki-Marekani kitatolewa kama msaada. Katika hafla hiyo ya kesho mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa wa Tanzania atapewa nyaraka na cheki za kumwezesha kuchukua pesa hizo pindi akifika nchini kwake.” Mr. Peari alipiga fundo jingine la kahawa kabla ya kuendelea.

    “Kwa kawaida na kitaalamu Pesa za msaada huwa hazitolewi kwa cheki wala kwa mkupuo, mkataba husainiwa na shirika husika hupata hizo pesa kwa mafungu. Lakini kwa sababu maalum, JEPA watapewa pesa zote kwa mkupuo, hivyo itakuwa kazi ya JEPA kuzihamisha pesa hizo toka kwenye akaunti maalumu ya Umoja wa Mataifa ambayo iko Tanzania na kuziweka kwenye akaunti yao. Hapo ndipo napoona mwanya wa kuweza kuziiba hizi pesa. Tukiweza kupata cheki na nyaraka muhimu za kuchukulia pesa hizo, itakuwa rahisi kwako kuweza kuziiba na kutoweka nazo.

    Nilichokuitia hapa si kukueleza habari hizi njema kwa Tanzania, bali kuzigeuza habari hizi ziwe njema kwetu na kilio kwa Tanzania. Kwa kusema hivyo nina maanisha kuwa ninazitaka pesa hizi Don, ili nipanue utajiri wangu. Naomba utumie mbinu yoyote unayoijua mradi tu nizipate pesa hizo”

    Maneno hayo huwezi kuamini kuwa yalikuwa yanatoka ndani ya kinywa cha mtu ambaye ni afisa ndani ya umoja wa mataifa.

    Baada ya kupokea maelezo hayo ya Mr. Peari, macho ya Don yaling’aa na kuwa makubwa zaidi. Uchu wa pesa tayari ulishamwingia. Na kwa kutumia mbinu zake za kijasusi za muda mrefu, haikumchukua muda mrefu kujua nini cha kufanya.

    “Sawa nimeelewa inabidi twende wote kwenye hiyo hafla ili niweze kuchunguza mambo kadhaa ya kunisaidia katika zoezi hili”. Don alisema huku tayari mkono wake ukiwa ameshashikilia bastola yake na kuichezea. Kwa tabia ya Don, hii iliashiria tayari akili yake ilikuwa kazini na kuua mtu wakati huo kwake ilikuwa sherehe.



    * * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndani ya ukumbi mdogo ambapo makabidhiano ya msaada wa umoja wa nchi za Ulaya na Marekani kwa Shirika la JEPA la Tanzania yalikuwa yamefanyika, kulikuwa na watu wachache tu. Lakini watu hao walikuwa ni wengi kiasi cha kumwezesha Jasusi Don kujipitisha bila kushitukiwa na mtu yeyote. Alipopita hakupata shida kumtambua mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa wa Tanzania, kwani yeye peke yake na mtu mwingine ambaye Don alikuwa anamjua kuwa ni waziri wa fedha na uchumi ndio walikuwa waafrika wanaume, mwafrika mwingine alikuwa ni mwanamke ambaye baadaye alitambulishwa kuwa alikuwa ni balozi.

    Saa tatu usiku iliwakuta Don na Mr. Peari Robert tayari wakiwa ndani ya jumba lile la kifahari la Mr. Peari jijini Washington, walikuwa wameshatoka kwenye hafla ya makabidhiano.

    “Haikuwa shida kwangu kupata nafasi niliyoitaka ndani ya ndege” alisema Don.

    “Ulifanyaje? alihoji Mr. Peari.

    “Nilijua fika kuwa yule mkurugenzi angekuwa na tiketi ya kuja hapa na kumrudisha Tanzania hivyo nilienda moja kwa moja kwenye ofisi ya shirika la ndege la Uingereza ambapo kwa mbinu nilifanikiwa kupata orodha ya wasafiri wa kesho na namba za viti vyao. Hapo haikunipa shida kupata kiti kinachopakana na kile cha bwana Kimisa” Don alieleza.

    “Lengo la kuwa karibu naye ni nini? Alihoji Mr. Pear Robert.

    “Leo wakati mnamalizia makabidhiano niliona aina ya briefcase ambayo mkurugenzi aliweka hati za makabidhiano na cheki. Hivyo nilipotoka pale tayari nimeshanunua briefcase ya namna hiyo na kuijaza makaratasi mengi ndani yake” pamoja na maelezo hayo ya Don lakini bado Mr. Peari alikuwa mbali

    “Bado sijaelewa unataka kufanya nini?

    “Nitakachofanya nitahakikisha nambadilishia briefcase tukiwa ndani ya ndege na yatayofuata hapo nitakutaarifu baada ya siku mbili tatu tokea kesho” Sauti ya kujiamini na utulivu aliyoitoa Don, ilimuaminisha kabisa Mr. Peari Robert kuwa pesa zilishakuwa zake.





    Alipomponyoka Jacob Matata pale Guardenia hotel, jasusi Don alikwenda moja kwa moja mpaka kwenye moja ya ofisi zake. Hapa alifanya kazi ya kutoa kopi zile nyaraka zote alizopora kwa mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa.

    Ni kile chumba chake cha ‘siri’ ambayo pia ni ofisi aliyofanya kuwa makao yake makuu ya kiutendaji. Hakuna mtu mwingine zaidi yake aliyewahi kugundua wala kuhisi kuwa kwenye ghorofa ya pili ya jengo hili kungeweza kuwa na ofisi ya kutisha kama hii.

    Mbali na kabati la chuma chumba hiki kilikuwa na vitu vingine vingi tu. Simu ya ‘satelite’, seti ya video, computer iliyounganishiwa ‘Internet’, ‘fax’ mashine ya photocopy na vingine vingi sana ambavyo ni yeye Don aliyejua ni nini na vina kazi gani.

    Ni mashine hiyo ya kutolea kopi ambayo Don aliitumia kutolea kopi zile nyaraka alizoziiba toka kwa Makia Kimisa. Mashine hizo zimetengenezwa maalumu kwa shughuli za kijasusi. Mwisrael aliyetengeneza mashine hizi Wolfgang Lotz ni moja kati ya majasusi walioacha historia ya kutisha duniani kwa kazi zao.

    Mashine hii inaweza kutoa kopi ikawa sawa kabisa na ile nakala halisi. Vitu kama sahini, nembo mbalimbali, alama za dole gumba hutoka kama ndio ziliwekwa kwenye hiyo karatasi ya kopi.



    Ilipofika asubuhi tayari alikuwa na pea mbili za nyaraka kamili. Usingeweza kutofautisha ipi ilikuwa nakala halisi na ipi ni kivuli. Asubuhi ya siku ya tukio, Dr. Don alikuwa na kazi moja tu ya kufanywa kwa haraka.

    Kuhakikisha anairudisha ile briefcase halisi ya mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa ndani ya ofisi ya mkurugenzi huyo bila kugundulika.

    Kwa mtu kama Don hilo halikuwa tatizo sana kwake. Alishuka na ile briefcase halisi toka chumba chake cha siri mpaka chini aliokuwa ameegesha gari lake. Alitia gari moto na kuanza safari ya kuelekea zilipo ofisi za shirika la JEPA.

    Saa mbili kasoro dakika tano, tayari alikuwa karibu kabisa na ofisi hizo. Baada ya kuegesha gari sehemu aliyohakikisha usalama wake, Don alitoka na ile Briefcase. Alizungusha macho yake huku na huko, hakukuwa na yoyote aliyemtilia shaka. Bila wasiwasi wowote alianza kupiga hatua kuelekea ndani ya ofisi hizo. Hii ni moja ya tabia za majasusi wa aina hii, hupenda kujiamini hata sehemu ambayo ni ya hatari kubwa.



    Dakika chache baadaye, tayari alishakuwa sehemu ya mapokezi ya ofisi za JEPA. Hapo alimkuta yule mama aliyekuwepo jana wakati ameacha ile briefcase nyingine aliyomdanganyia Jacob. Lakini kwa jinsi alivyobadilika asubuhi hiyo isingekuwa rahisi kwa mtu wa kawaida kama huyo mama kugundua kuwa sura hii ndiyo iliyofika jana.

    “Mzee ameshafika? Aliuliza Don bila kutoa salamu. Alifanya hivyo akijua hii ndio tabia ya watu wenye vyeo - alitaka aonekane hivyo.

    “Nani? mkurugenzi? Alihoji yule mama ambaye alionyeshwa kukerwa na tabia ya Don ya kutosalimia. Lakini hakusema neno. Aliogopa

    “Kwani kuna mzee mwingine zaidi yake hapa? Dr.Don alijibu kwa jeuri ili kumtia hofu huyo mama wa mapokezi, kweli sasa alionekana kumwogopa Don.

    “Bado huwa anafika hapa saa mbili na robo au na nusu, kama anakuja ofisini siku hiyo”.

    “Okay, kuna sehemu nahitaji kufika haraka, je naweza kumwona katibu wake mhutasi ili nimwachie maagizo ya Mkurugenzi?

    “Sawa pita tu hapo, ukifika mlango ule upande wa kushoto utaona mlango umeandikwa mkurugenzi, ingia hapo ukutane naye”

    “Haya asante” Dr. Don alisema huku akiwa tayari anaelekea upande alioelekezwa.

    Hakutaka kupoteza muda hakupenda kuvuruga kitu chochote. Hakupata shida kuona ofisi iliyoonyeshwa kuwa ndiyo ya mkurugenzi husika. Hapo wakati anajiandaa kubisha hodi alipapasa bastola yake na kuona mambo yote yako sawa.

    Alibisha tena na tena, kujibiwa. Ukimya uliokuwepo ulionyesha kuwa hapakuwa na kiumbe hai eneo hilo. Alipojaribu mlango akakuta uko wazi akaingia ndani. Kwa jinsi ilivyoonekana katibu mhutasi wa mkurugenzi alikuwa ametoka, ila hakuwa mbali, maana ‘computa’ ilikuwa imewashwa na simu yake ya mkononi ilikuwa mezani.

    Kwa haraka ya ‘kichomi’, Dr. Don alitumia mwanya huo. Alichomoa lundo la funguo malaya alizokuwa nazo na kuzijaribu kwenye mlango wa kuingilia ofisi ya mkurugenzi. Ufunguo wa kwanza, wa pili, alipojaribu wa tatu tayari mlango ukasalimu amri. Haraka haraka aliangaza macho yake hapa na pale hakuona kitu alichokihitaji. Kwa kutumia funguo zake malaya alijaribu vitasa vya kabati la chuma lililokuwa kwenye kona moja ya chumba hicho. Vitasa hivyo pia havikutaka kumwangusha viliitikia. Ile kutupa tu macho ndani ya kabati akakutana na alichokuwa akikitafuta. Ni ile briefcase bandia aliyombadilishia mkurugenzi ndani ya ndege jana yake. Aliichukua na kuiweka ile halisi. Wakati anamalizia kufunga mlango wa kabati, alisikia vishindo vya mtu vikija upande ule alikuokuweko. Mara moja akajua kuwa kama si katibu mhutasi wa mkurugenzi basi anaweza kuwa mkurugenzi mwenyewe.

    Badala ya kuchacharika Dr. Don aliongeza utulivu na kasi ya vitendo vyake. Kwa jinsi ofisi ilivyokuwa imepangiliwa ukitoka ndani ya chumba cha ofisi ya mkurugenzi unaingia ilipo ofisi ya katibu wake mhutasi, ukitoka hapo ndiyo unakutana na varanda ya kuelekea ilipo sehemu ya mapokezi.

    Vile vishindo vya mtu vilisikika kwa karibu zaidi wakati huo, ilionyesha kuwa mtu aliyekuwa anakuja alikuwa amekaribia mlango wa kuingilia ofisi ya katibu mhutasi. Wakati huo Dr. Don alikuwa anahangaika na namna ya kuufunga mlango wa ofisi ya mkurugenzi huku briefcase yake ikiwa mkononi. Wakati amemalizia, kitasa cha mlango wa kuingili kwa katibu muhtasi kiliguswa. Haraka haraka Dr. Don alifutika funguo zake malaya mfukoni na kurukia kilipo kiti cha kukalia mtu aliyekuwa akisubiria kumwona mkurugenzi hapo ofisini kwa katibu mhutasi. Ni wakati anajituliza tu, tayari aliingia dada mmoja mrembo wa kutosha.

    “Samahani kwa kuingia bila kukaribishwa” Dr. Don alitaka radhi.

    “Nikuombe wewe samahani kwa kukuchelewesha, maana yule mama wa mapokezi ameniambia kuwa umepita kitambo” alisema yule dada bila kutambua chochote kilichokuwa kimetokea.

    “Usihofu hii ni hali ya kawaida kwenye ofisi zetu hizi. Sitakaa sana ila naomba nikuachie ujumbe ili umpe mzee”Alisema Dr. Don huku akisimama.

    “Naomba usahini kwenye kitabu cha wageni kwanza, ndipo uache huo ujumbe” alisema yule dada huku akimkabidhi Dr. Don sehemu ya kusahini. Hakumpa kalamu na badala yake akaanza kutafuta kwenye droo ya meza yake.

    “Aah huo mtindo wa kuazimana kalamu unaboa kweli ona…” kabla huyo dada hajamalizia malalamiko yake, Don alimdakia

    “Usipate taabu sana, acha nitumie yangu maana nina haraka” Dr. Don alitoa kalamu yake kuandika jina lake halisi na sahini bila kuficha chochote.

    “Naomba karatasi ili nimwachie ujumbe”

    Wakati yule dada anamchukulia Don karatasi, Don alifunga kile kitabu cha wageni. Alipokea karatasi na kuandika ujumbe ndani yake. Aliikunja vizuri ile karatasi na kumpa yule dada.

    Mpaka Don anaaga na kuondoka yule dada hakujua kuwa alikuwa ameingizwa mjini. Kalamu iliyotumiwa na Don ni maalumu kabisa. Inapoandikiwa baada ya dakika moja kupita tangu wino ulipotua kwenye karatasi, maandishi hufutika na karatasi huwa kama ilivyokuwa kabla ya kuandikia. Hivyo kitendo cha Don kutoa kalamu yake haraka na kufunga kile kitabu cha wageni haraka ilikuwa ni katika harakati za kuhakikisha yule dada hasomi jina lake wala kuona chochote kilichoandikwa.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati mkurugenzi alipofika ofisini, yule dada alitaka kumpa taarifa za mgeni yule wa asubuhi. Alishangaa alipoangalia sehemu zote alizoandika yule mgeni kuwa hazikuwa na maandishi. Alipofungua ile karatasi iliyokuwa na ujumbe kadhalika ilikuwa karatasi tupu. Akashindwa kuelewa nini kilichokuwa kimefanyika. Kwa aibu akaamua kutompa mkurugenzi taarifa za mgeni aliyeingia hapo asubuhi hiyo.

    Hivi ndivyo Dr. Don alivyofanikiwa kurudisha briefcase iliyokuwa na nyaraka halisi za kwenda kuchukulia pesa. Baada ya kutoka hapo alikuwa na kazi moja tu ya kuwahi Benki kabla mkurugenzi na kundi lake hawajaenda. Alikuwa na hakika ya kutumia zile nyaraka alizotoa kopi kwa mashine yake maalumu ya kutolea kopi.



    * * *



    Zilikuwa zimepita dakika kadhaa tangu alipokuwa ametoka kule ofisini kwa mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa kurudisha ile briefcase halisi. Na sasa alikuwa tena ndani ya ile ofisi yake ya siri akisubiri muda wa kwenda Benki kujichukulia mipesa. Moyo wake ulikuwa na furaha japo si kamilifu kwani kila alipomfikiria Jacob Matata, akili ya Dr.Don ilikuwa ikishituka.

    “Hauko peke yako! Wazo lilimnong’oneza Dr. Don.

    “Sawa lakini hii ni fani yangu! Don aliijibu ile sauti.

    “Jacob ni makini, anaweza na yuko mbioni utamzuiaje? Sauti ile ilimwuliza tena Dr. Don. Kabla hajapata jibu ndipo alipokumbuka kuwa huu ni muda aliotakiwa kwenda Benki. Aliandaa watu wake na vifaa ambavyo angehitaji kuvitumia wakati akichukua pesa.



    * * *



    Saa sita kasoro dakika tano mchana Dr. Don alikuwa tena ndani ya ofisi hii ya ‘siri’. Safari hii akijihesabu ‘mshindi’. Tayari alikuwa amefanikiwa kuendesha operesheni ya kuchukua pesa Benki. Pesa hizo zilikuwa ndani ya hicho chumba kwenye kabati la chuma.

    Baada ya kuwa amefanikiwa kuchota mamilioni ya Dola za kiMarekani, jambo ambalo alilokuwa akilishuku ni akili ya Jacob Matata iliyojaa maajabu. Badala ya kufurahia kwa jinsi alivyokuwa amefanikiwa kuiba pesa, Dr. Don alikuwa ameshikilia picha ya Jacob mikononi mwake.

    Alipenda afanye sherehe. Alitamani kuwapa likizo wafanyakazi wake wote. Alitamani kumtaarifu bosi wake, Mr. Peari Robert. Lakini jambo moja aliona bado ni kikwazo. Kitendo cha Jacob Matata kuwa hai aliona kana kwamba mambo yake yote yangekuwa matatani. Alikunywa fundo mbili za kinywaji chake. Kisha akaitazama saa yake mkononi, saa kumi na mbili jioni.

    Yalikuwa yameshapita masaa kadhaa tangu pale yeye na kundi lake walipokuwa wameenda Benki ya DE EURO LINKAGE. Kwa vile walikuwa na kitu kilichohitajika kuchukulia pesa hizo, walizichukua bila kushitukiwa. Ni katika ofisi hii ya siri ambapo ndipo alipozihifadhi pesa hizo. Ndani ya kabati kubwa la chuma lililojengewa ukutani upande wa kushoto kabisa wa chumba hicho.

    Ili kuhakikisha tena usalama wake aliiruhusu akili yake kumpa taarifa zozote. Alihitaji kujua kama mpaka hapo kuna kasoro yoyote aliyoifanya. Je kuna mwanya wowote ambao Shirika la JEPA na Polisi wanaweza kuutumia kumfikia? Alitafuta ili kujua kama kuna adui mwingine ambaye anaweza kumkaribia kwa haraka zaidi ya Jacob. Mara macho yalimtoka. Akasimama na kuweka mikono yake kwenye mifuko ya suruali. Alikumbukua jambo! Tena la hatari.

    Akili yake ilizunguka haraka zaidi.

    Tayari alishapata jibu.

    Mkono wa kulia ulitoka mfukoni na kunyanyua mkonga wa simu. Baada ya kubonyeza namba hadhaa.

    “Nikuagizayo sihitaji kosa hata moja. Kama ungependa chukua kalamu na karatasi ili uyaandike haya maagizo” alisema Dr. Don huku sauti yake ikiwa haina hata harufu ya utani.

    “Kesho saa tatu na nusu nitakuwa hapa nilipo ili kupokea simu toka kwako. Simu hiyo initaarifu kuwa yule meneja wa Benki pamoja na yule dada mhudumu waliotuhudumia ni marehemu. Mtawapata wapi na wakati gani hiyo si juu yangu. Kazi njema” hii ndiyo iliyokuwa kawaida ya Don kwa vijana wake. Alijua fika kuwa uhai wa hawa watu wa Benki ungekuwa tatizo kwao.

    Hivi ndivyo Don alivyoamuru mauaji ya wote aliowahisi kuwa wangekuwa vyanzo vya kufikiwa na Shirika la JEPA . Ndivyo alivoamuru mauaji ya Inspekta Ezron baada ya kugundua kuwa alikuwa amemhoji wahusika wa Benki. Hakuchelewa pia kuamuru mauaji ya yule mama wa mapokezi na katibu muhtasi wa ofisi ya mkurugenzi wa shirika la JEPA, Bwana Makia Kimisa.





    “Hivi sasa ni saa moja kamili asubuhi”.

    “Ifuatayo ni taarifa ya habari na msomaji ni John msingi. Kwanza ni muhitasari wake;

    Mabilioni ya fedha za kitanzania yameyeyuka katika hali ya kutatanisha hapo jana…”

    Mwanzo aliisikia sauti hii kana kwamba yuko ndotoni lakini baadae Jacob Matata alibaini kuwa sauti hii ilikuwa ikitokea pembeni ya kitanda chake ambapo kulikuwa na radio ndogo. Taarifa hii iliishitua akili ya Jacob Matata asubuhi hii ambapo ni masaa machache tu tangu hapo jana alipokuwa amepewa likizo ya wiki mbili.

    Ni katika taarifa hiyo ya habari ambapo Jacob alisikia juu ya upotevu wa mamilioni ya dola, ambazo shirika la JEPA lilikuwa limepewa kama msaada toka nchi wahisani.

    Saa tatu kasoro robo ilimkuta Jacob kishamaliza kupata kifungua kinywa alichoandaliwa na Regina mpenzi wake. Wakati amejipumzisha sebuleni, ndio ile simu iliyopigwa na Bi. Anita ilipomfikia.

    Laiti angejua ujio wa simu hiyo na kuwa inatoka ofisini kwao, angefanya namna ili kuhakikisha kuwa haipokei. Hali hii ilitokana na jinsi alivyokuwa anahitaji kupumzika na mpenzi wake, Regina.

    Jacob Matata hakufahamu kama alistahili kuifurahia au kuichukia simu hiyo ya Bi. Anita, ambayo aliipokea yeye mwenyewe. Kule kusikia tu sauti ya Bi. Anita kulimfanya Jacob ahisi wajibu alionao katika taifa hili, ingawa ujumbe uliokuwa ndani ya sauti hiyo uliashilia shari.

    Ofisini?

    Ina maana amesahau kuwa ni jana tu amenipa likizo ya wiki mbili?

    Kuna nini kilichomsibu bosi? Haya ni baadhi ya maswali aliyojiuliza Jacob mara baada ya kupata wito wa Bi. Anita.

    Dakika Ishirini baadae Jacob Matata, alishazifikia ngazi za kuelekea ofisini kwa Bi.Anita na kuzipanda kwa haraka.

    “Ingia ndani”Bi Anita alimkaribisha ndani Jacob Matata mara baada ya mlango wa ofisi yake kugongwa.

    “Asante Jacob alisema huku akivuta kiti na kukaa. Jacob alipoiona sura ya Bi. Anita alishaiona shari iliyo mbele yake.

    “Imebidi nikatishe mapumziko niliyokueleza jana” Alianza kuongea Bi. Anita ambaye sauti yake ikionyesha huzuni na kukerwa na jambo.

    “Hamna tatizo mkuu maadamu sababu ni maslahi ya nchi yangu au wapenda haki Duniani!! Lilikuwa ni jibu la Jacob ambalo liliisisimua damu ya Bi. Anita.

    “Ndio maana nakupenda kwa vile wewe una moyo wa uzalendo licha ya kuwa hii ni kazi yako. Naomba unisikilize kwa makini sana” Bi. Anita alijitengeneza kisha akavuta yale mafaili mawili aliyokuwa amepewa na mkuu wa nchi akamkabidhi Jacob.

    “Jacob angalia haya mafaili kwa makini moja baada ya jingine”. Muda wote huo Bi. Anita alikuwa akimwangalia Jacob wakati akiyapitia hayo mafaili.

    “Kuna nini katika haya mafaili? Maana naona karatasi zilizoko ndani ya faili moja ni sawa kabisa na zile zilizoko ndani ya faili jingine. Ila tofauti ni kuwa hili faili liloandikwa ‘1’ juu yake karatasi zake inaonyesha zimeshatumika kwani kuna mihuli ya Benki tena yenye tarehe za jana…..” Kabla Jacob Matata hajaendelea zaidi Bi. Anita alidakia.

    “ndio ni jana ndio hizo karatasi zimetumika kuibia mamilioni ya dola za kimarekani toka DE EURO LINKAGE……….” Bi Anita alimweleza Jacob kila kitu alichokuwa ameelezwa na Rais jana.

    “Ni hatua gani zilichukuliwa tangu kugundulika wizi huu hiyo jana? Alihoji Jacob.

    “Polisi walichukua hatu zote za kuhakikisha wahusika wa tuko hilo hawapati nafasi ya kutoka ndani ya jiji la Dar es salaam na wala kusafirisha pesa hizo kwa aina yoyote.

    Pili walimchukua mhudumu aliyehusika kuwahudumia wateja hao katika Benki ya DE EURO LINKAGE. Mhudumu huyo wa Benki hiyo alianza kuhojiwa jana jioni na mkuu wa kituo cha kati. Meneja wa Benki hiyo pia alitarajiwa kuhojiwa hiyo jana ili kuona kama kuna lolote ambalo lingepatikana kama kianzio katika kufuatilia mkasa huu.

    Hivi ninavyoongea na wewe kikao ambacho kinaongozwa na mheshimiwa Rais mwenyewe na kuwajumuisha maafisai wote na mkuu wa Polisi ndio kimeanza muda mfupi uliopita. Ni katika kikao hicho ambapo Polisi inatarajiwa kutoa taarifa ya mahojiano kati yao na yule dada mhudumu na meneja wa Benki hiyo ya DE EURO LINKAGE.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jana mchana niliitwa na Rais na ameitaka ofisi hii fukuzi kutafuta ukweli juu ya jambo hili na kuwatia mbaroni wote waliohusika. Yote haya yanatakiwa kufanyika ndani ya siku kumi tu ambazo zimeanzia leo nami nakupa wewe siku nane tu kuhakikisha jambo liko wazi.

    Nikiwa mkurugenzi wa ‘Ofisi Fukuzi’. Nimekuteua wewe na ndie utakayebeba jukumu hili. Ofisi itakuwa nawe bega kwa bega katika kukupa msaada wowote utakaohitaji. Nchi yote na wananchi wa Tanzania wako mabegani mwako bwana Jacob. Naamni ni nafasi nyingine ya kuudhirishia ulimwengu na maadui wa haki juu ya uwezo wa haki. Thibitisha uwezo wako na nchi na ‘Ofisi Fukuzi’ katika fani.

    Ni imani yangu kuwa utafanya kazi kwa kasi, umakini na uchungu Mkubwa. Umepewa ruhusa ya kumchunguza yeyote katika nchi hii ambaye utahisi kuwa anaweza kuwa amehusika au ni chanzo cha mkasa huu.Nakutakia kazi njema Jacob, naomba unipe tarifa ya kila linaloendelea maana Rais atakuwa anapenda kujua nini kinaendelea” alimaliza mkurugenzi huyu wa ofisi pekuzi na kusimama kisha akampa mkono wa heri Jacob Matata ambaye wakati huu naye tayari alikuwa ameshasimama.

    Walishikana mikono na kubaki hivyo kwa sekunde kadhaa, Bi. Anita aliweza kuisikia damu ya Jacob ambayo ilikuwa ikikimbia kwa kasi wakati huo.



    Saa nne kasorobo asubuhi hii, Jacob Matata tayari alikuwa ameshatoka ndani ya ofisi ya mkurugenzi wa ‘Ofisi Fukuzi’ Bi. Anita. Alirudi mpaka pale alipoegesha gari lake. Baada ya kuwa ameingia ndani ya gari na kukagua vizuri vifaa vyake vya kazi, Jacob akatekenya stata ya gari, likawaka na akaingiza gia na kuliondoa kwa kasi. Tayari akili yake ilimnong’oneza kuwa alikuwa kazini tena kazi yenyewe ya hatari.



    Baada ya kutoka kwa Bi. Anita na kukabidhiwa ile kazi, Jacob Matata aliingia ndani ya mjadala mkali. Lakini tofauti na mjadala uliokuwa ukiendelea kati ya Rais na baraza la mawaziri na wakuu wa Usalama, mjadala wa Jacob ulikuwa baina yake na nafsi yake mwenyewe. Alikuwa akijaribu kuhusishanisha taarifa alizozipata leo na tuko alilokabiliana nalo jana wakati akitokea New York. Alihitaji kujua kama kweli yule Mzungu anahusika na mkasa huu. Je kama kweli anahusika pesa ameziweka wapi na atampataje mara baada ya kumtoroka hiyo juzi usiku pale Gardenia hotel chumba namba 11.

    Akaruhusu ubongo wake kuileta picha ya yule mzungu, aliiangalia kwa makini kisha akaihifadhi kwenye ubongo wa nyuma. Akaruhusu ubongo umletee kumbukumbu za namna yule mzungu alivyokuwa fundi wa kupigana. Alitaka kulinganisha na Kiroboto katika mkasa wa HEKA HEKA ambao una kitabu chake. Hapo Jacob alikiri kwa nafsi yake kuwa katika suala la kupigana yule mzungu hakuwa mpiganaji wa kawaida. Jacob hakupata kuona mtu mwepesi kama yule mzungu. Mwenye mikono ya chuma na shabaha ya mzimu ambayo ndiyo iliyopelekea mama Wambura kumtilia shaka juu ya jicho lake kuwa jekundu kuliko kawaida asubuhi ya hiyo.

    Hata hivyo Jacob Matata alifurahi kwa vile mkasa huu ulitakiwa kutatuliwa na yeye. Kwa vyovyote vile mkasa kama huo ulimhitaji mtu wa aina yake katika kuutatua. Mtu aliyejiamini, aliyefuzu na kujaa mbinu zote katika fani hii.



    Jacob aliazimia kuanzia kazi kwa Inspekta Ezron pale kituo cha kati cha jiji la Dar. Japo alifahamu fika kuwa Inspekta Ezron alitakiwa kupeleka taarifa za mahojiana yake na meneja wa Benki ya DE EURO LINKAGE pamoja na yule dada mhudumu, lakini alionelea si vibaya akimwona kwanza na ikiwezekana apewe nafasi ya kumhoji yule dada mhudumu wa Benki.

    Huku gari ikiwa kwenye kasi ya wastani, alitupia macho saa yake na kugundua kuwa zilikuwa zimebakia dakika arobaini tu kabla Inspekta Ezron hajaenda kupeleka taarifa yake kule kikaoni. Aliongeza kasi ya gari.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog