Search This Blog

Thursday 27 October 2022

ANGA LA WASHENZI (1) - 4

 











    Simulizi : Anga La Washenzi (1)

    Sehemu Ya Nne (4)





    ***



    Saa saba kasoro usiku …



    Kuna makelele makali ya muziki. Wanaume kadhaa pamoja na wanawake wapo ndani ya mahali hapa ambapo unaweza ukapaita klabu ya usiku, lakini ilikuwa ndani ya nyumba ya mtu! Ndani ya eneo hilo kulikuwa kuna kaunta, na eneo kubwa tu la watu kujimwaya kucheza muziki uliokuwa unapigwa.



    Vinywaji vilikuwa vingi na vya kumwaga. Kila mtu aliyekuwa eneo hili alikuwa amebebelea kinywaji chake, haswa mvinyo ama whisky, katika mtindo wa chupa ama glasi. Na kila mtu alionekana akiwa na mtu wake.



    Mwanga ulikuwa hafifu. Taa zilikuwa mbili tu, nyekundu na ya kijani. Wakati taa moja ikiwa inamulika kushoto, nyingine ilikuwa inamulika kulia. Kwahiyo ilikuwa ngumu kujua watu waliokuwemo humo kwa uso. Labda kwa maumbo.



    Kulikuwa kuna milango miwili maeneo hayo, milango yote hii ikiwa ni ya kioo. Ukutani kulikuwa kumechorwa picha kadhaa za wanawake, maua na silaha.



    Muziki ukiwa unaendelea kukonga nyoyo za watu, kama si vichwa, mlango mmoja ukafunguliwa na mwanaume fulani aliyekuwa amejaza mwili. Mwanaume huyu alitembea kwa kasi kuelekea meza fulani ukutani. Hapo akamnong’oneza mwenziwe sikioni.



    Ghafla huyo aliyenong’onezwa akanyanyuka. Aliangaza kule kaunta akatoa ishara ya mkono, mara muziki ukakata! Akapaza sauti kusema wamevamiwa!



    Haraka wanaume wote wakatoka nje, na hapo ndiyo ikaonekana kumbe mwanaume yule aliyepewa taarifa alikuwa ni Nyokaa, na hayo yalikuwa ni makazi yake. Haraka walielekea kwenye chumba walichokuwa wamemfungia Nade, hawakukuta mtu zaidi ya kiti kitupu na kamba zilizokatwa!



    Nyokaa akatukana na kusaga meno. Akapiga ngumi kiganja chake na kuwatazama wenzake kwa macho mekundu.



    “Mtafuteni huyo hayawani aliyediriki kumchezea simba sharubu! Upesi!”



    Basi isijulikane na hata wanaume wengine walitokea wapi, jumla wakawa ishirini! Wengi wao walikuwa wamebebelea bunduki, na wachache, watatu kwa idadi wakiwa hawana silaha yoyote ile. Msako ukaanza!



    Wakasambaa huku na huko. Wakibeba tochi na wengine wakiyakodoa macho yao kana kwamba matonge ya ugali ili wapate kuona wanachokitafuta. Hawakujua mvamizi ameelekea upande gani, ilikuwa ni kubashiri tu wakiwa wanaamini hatakuwa yupo mbali.



    Uzuri kwao, eneo hili lilikuwa ni kubwa, kwa mtu kuvamia na kutoka, haikuwa rahisi. Ingemchukua muda mrefu, na akili pia kwani eneo lilikuwa limezingirwa na msitu mkubwa na njia fupi fupi zilizokomea mitini!



    Lazima Nade apatikane. Na si hivyo tu, na huyo mvamizi pia apatikane kwa ajili ya adhabu na kueleza ametumwa na nani.



    “Ananitania, hanijui vizuri!” alisema Nyokaa. Pembeni yake alikuwa amesimama Roba. Mkononi mwa Nyokaa kulikuwa kuna chupa kubwa ya kinywaji cha Ciroc, kikihudumia kinywa chake mara kwa mara.



    “Ameuchokoza moto uliokuwa umezima, sasa ataona cha mtemakuni!” aliendelea kunena Nyokaa, alafu akajipooza na kinywaji chake.



    “Tulifanya makosa sana kumwamini yule mshenzi,” alisema Roba. “Hatukuwa na haja ya kufanya naye mazungumzo yoyote yale, bali vitendo.”



    “Nilimpatia nafasi ya kuyamaliza kwa amani,” akasema Nyokaa akitikisa kichwa. “Lakini kaniona fala. Sasa kichwa cha huyu malaya wake, pamoja na huyo mbwa aliyemtuma vitakuwa ni salamu zake tosha. Na kama hatamleta Miriam hapa, tutamfuata mwenyewe huko alipo!”



    Wakati maongezi haya yanaendelea, Jona alikuwa anatazama. Alikuwa amejificha kwa kujibanza kando ya jengo akiusoma mchezo mzima. Kumbe wakati wanaume wametapakaa huku na huko kwenda kumtafuta, yeye alikuwepo pale walipopaacha.



    Mtihani wake ulikuwa ni kutoka ndani ya eneo hilo akikwepa watu waliozagaa huko. Hili halikuwa gumu kwake kabisa kama angelikuwa mwenyewe, ila shida ni kwamba mgongoni mwake alikuwa amembebelea Nade aliyekuwa hoi.



    Macho ya mwanamke huyo yalikuwa yanarembua kwa kuchoka. Mwili wake ulikuwa unanuka damu ukijawa na majeraha. Kama Jona angelimwacha pale, asingeliweza kwenda popote pale kwa maana hakuwa na nguvu hizo.



    Jona akapiga mahesabu, kushoto ama kulia, kaskazini ama kusini. Kwa kuhofia kupotea ndani ya eneo hilo alikuwa ameikariri ramani ya eneo zima kichwani kabla hajafanya kazi yake hiyo. Alikuwa anajua wazi wapi kuna njia na wapi kuna kupotelea msituni.



    Na basi kwa akili zake timamu akaamua kuenenda upande anaoujua hamna njia. Akifanya hivyo kwasababu za kiusalama zaidi akiamini ya kwamba wanaume wale waliotapakaa huko, watakuwa wamejijaza mahala penye njia wakidhani amezitumia.



    Akihema taratibu na akikanyaga hatua fupi fupi za haraka, akasonga. Ndani ya ‘mamiti’ hali ya hewa ilikuwa ni ya ubaridi. Udongo ulikuwa ni wa kutitia ukilowanishwa na unyevunyevu. Kulikuwa ni giza, taa za makazi ndizo zikisaidia kwa mbali.



    Wakati Jona akisonga, Roba akasikia sauti ya kukatika kwa kipande cha mti kaskazini mwake upande wa kushoto. Upesi akatazama eneo hilo. Alilitilia mashaka, ila akapuuzia. Hili likawa kosa lake kubwa mno!



    Baada ya sekunde chache, roho yake ikiwa haijaridhika, akamwomba Nyokaa kurunzi na kumulika kule alipokuwa amepatilia shaka. Kurunzi ilikuwa kubwa yenye mwanga mkali mweupe. Aliipeleka mbele na nyuma akiangaza, lakini hakuona kitu!



    Jona alikuwapo wapi?



    Bada ya kurunzi hiyo kuzima na kiza kurudi ndani ya miti, sauti ya Jona inanong’oneza ndani ya msitu:



    “Amka, twende!”



    Kumbe alikuwa amelala chini, yeye pamoja na Nade. Anamnyanyua Nade na kisha anamuweka tena mgongoni. Wakaendelea na safari.



    Lakini Roba hakukaa na amani tangu pale aliposikia mlio ule wa mti. Hakuchukua muda mrefu sana, akamuaga Nyokaa anataka kwenda kutazama hali kule alipomulikia kurunzi.



    “Twende wote!” Nyokaa akaropoka akisimama kwa shida.



    “Hapana,” akasema Roba. “We kaa hapa, nakuja muda si mrefu.”



    Nyokaa akaleta ubishi kidogo, alikuwa chakari kwa kulewa. Hata kusimama likuwa tabu, Roba akamsaidia kwa kumshikilia. Akamtuliza kitako na kisha haraka akapandisha kwenda kutazama.



    Ndani ya dakika mbili, Roba akaona alama za viatu kwenye udongo. Akachuchumaa na kuzitazama alama hizo vema, kwa kuusoma ulaini wa udongo akagundua adui alipita hapo ndani ya muda mfupi. Na kwa kusoma kina cha alama hizo, akajua adui alikuwa amembembelea mateka wao.



    Basi akatabasamu maana aliona kazi imeshakwisha. Endapo adui huyo amembebelea mateka, basi hatakuwa na kasi ya kutembea wala kukimbia. Na alama zake za miguu zitaonekana kwa urahisi udongoni.



    Akaona hamna haja ya kuita watu wengine, kazi ataimaliza kwa mkono wake mwenyewe. Haraka akaanza kusonga kwenda mbele. Alitumia macho yake kama kurunzi na alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kutembea kimya kimya japo kwa upesi ili asimgutue adui mapema.



    Macho yake yalitazama chini, na akitumia alama za miguu kama ramani. Akafikia mahali ambapo alama hizo zilikata. Akasimama na kumulika na kurunzi aone.



    Mahali hapo ndiyo palikuwa sehemu ambapo Jona alilala punde baada ya kuona mwanga wa kurunzi kwahiyo Roba alipomulika kwa mbele kidogo, akafanikiwa kuona alama za viatu vya Jona vikiendelea, naye akaendelea kuvifuatilia.



    Lakini pasipo kufahamu, akawa ametenda kosa lingine la pili ndani ya usiku huu. Kitendo cha kumulika kurunzi msituni kwa mara nyingine, kikamshtua Jona na kumtaarifu kuwa anafuatwa kwa ukaribu. Anapaswa kuchukua hatua!



    Dakika tano mbele, Roba akafika tena mahali ambapo hakuona alama za miguu. Akasimama na kuangaza. Pembeni yake akaona mwili wa binaadamu. Haraka akawasha kurunzi kumulika. Akamwona Nade amejilaza!



    Kwa tahadhari akasogea. Akamulika kushoto, kulia, mbele na nyuma. Hakukuwa na mtu wala alama za viatu. Alipotaka kumulika juu ya mti, mara vuuup! Jona akashuka kama radi akamparamia na kumwagusha chini!



    Kurunzi ikarukia kando.



    Jona akang’ang’ania shingo ya Roba wakishindana nguvu. Roba akamtupia mwanaume huyo mbali kwa kutumia miguu yake, alafu haraka akasimama. Naye Jona upesi akasimama kwa kujifyatua kama mtego wa panya.



    “Huu ndiyo mwisho wako!” Roba akasema kwa msisitizo kisha akafikicha pua yake kama mtu mwenye mafua. Akamjongea Jona akijiandaa kwa pambano.



    Ngumi na mateke yakarushwa kwa fujo! Kila mtu alikuwa stadi kwenye kukwepa mashambulizi ya mwenzake. Ngumi na mateke ya Roba yalikuwa mazito zaidi, lakini hazikufanikiwa. Jona alikuwa mwepesi mno kukwepa kana kwamba anacheza gemu la nyoka.



    Kwa sekunde chache akausoma mchezo wa Roba, na sasa akaanza kucheza faulo za kuleta ushindi. Kila Roba aliporusha ngumi yake nzito, Jona akawa anaipisha na kuisukumia mbali kuharibu balansi ya adui.



    Akafanya hivyo mara tano. Roba akajaribu kurusha teke, Jona akalikwepa na kugusa kidogo mguu ulioleta shambulizi , Roba akaenda kombo. Kuja kukaa sawa akamkuta Jona yupo hewani. Kabla hajavuta pumzi, akala teke la kibabe, likamnyanyua na kumtupia chini! Hoi!



    Mdomo ulimwaga damu. Macho hayakuona vema, kichwa kikaita kwa miale ya maumivu makali. Lakini hakutaka kushindwa, akajikokota kunyanyuka. Akakunja ngumi apambane tena.



    Lakini kwa mara hii haikumuwia vigumu Jona. Alijua adui yake hakuwa sawa, na basi akamruhusu arushe shambulizi lake yeye awe wa mwisho. Roba akaingia mkenge. Aliruhusu hasira zikamtawala. Akairusha ngumi yake kwa pupa, Jona akaiyeya kama amefungiwa ‘springi’, Roba akakatiza hatua mbili mbele, Jona akamrusiha nyuma kwa teke la kukunjuka lililomkita kifuani. Roba akalala tuli asionekane mwenye dalili ya kuamka!



    Jona akamuweka Nade mgongoni, wakaendelea na safari. Wakatembea kwa hatua kumi na tano, mara wakamulikwa na kurunzi!



    Watatoboa?





    Jona akageuka na kuangaza mwanga huo watokea wapi na kwa nani, hakuona! Mwanga ulimpiga usoni na kumuumiza macho. Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kukazana kukimbia. Alidhani aliyemnyoshea kurunzi ni adui, na yupo karibu.



    Alikimbia kwa muda mrefu pasipo kusikia ama kuona chochote. Alifanikiwa kuchoropoka ndani ya ngome ya Nyokaa salama, mgongoni akiwa amembebelea Nade aliyekuwa hajiwezi kwa lolote.



    Alikuja kugundua mbeleni ya kuwa kurunzi ile iliyommulika, ilikuwa ni ya Roba aliyemlaza chini, akifanya hivyo kuwapa ishara wenzake baada ya yeye kunoa nanga.



    Baada ya nusu saa wafuasi wote wa Nyokaa wanakutana na kutoa taarifa kwamba hawajafanikiwa kumtia mikononi mvamizi wala mateka. Nyokaa ananghafirika, anapasua chupa alikuwa ameibebelea mkononi kisha alaani kwa matusi.



    “Yani himaya hii ilivyo kubwa, mtu anatokaje kirahisi namna hiyo? Ni uzembe mkubwa kiasi gani? … Roba!” akaita. Roba akampatia macho na masikio. Alikuwa ameumia mdomo na upande wake mmoja wa uso ukiwa taabani.



    “Unaweza ukaniambia ni kwa namna gani huyo ms** ametoka humu?!” Nyokaa akafoka. Akaongea na kuongea lakini hakuna hata mtu mmoja aliyesema neno. Wote walibakia kusikiliza kana kwamba mwalimu mkuu yupo ‘asembo’.



    Nyokaa alikuwa ameudhika sana. aliona ni kama vile amevuliwa nguo mbele ya umati. Aliona amedharauliwa na kushushwa kiwango haswa. Inakuaje mtu azame ndani ya nyumba yake na kutawala meza?



    Akachojoa sigara kubwa ndani ya mfuko wake, alafu akaiwasha akipepesuka. Akavuta pafu moja zito kabla hajautema moshi nje kana kwamba treni ya makaa. Akanyamaza kwa muda akiwaza kwa kutumia kichwa chake cha pombe, watu wote wakimtazama na kumngojea atasema nini.



    “Robaa!” Nyokaa akaita. Roba akaitikia kiukakamavu.



    “Nataka kichwa cha Eliakimu hapa. Namtaka na Miriam hapa … Utajua mwenyewe cha kufanya. Anayelikoroga sharti alinywe.”



    Aliposema hayo akaondoka zake kwenda kujipumzisha, akimwachia jukumu zito Roba, ambaye alishusha pumzi ndefu na kuketi chini kwanza kabla hajafungua kinywa.





    ***





    Saa tatu asubuhi …



    Baada ya usingizi kukoma, Nade anaunguzwa na mwanga wa jua usoni. Alikuwa juu ya kitanda kidogo kilichotandikwa vema, ndani ya chumba cha ukubwa wa kati. Pembeni ya kitanda hicho kulikuwa kuna taa ya mwamvuli, na bado ilikuwa inawaka.



    Alipepesa macho yake kukagua chumba kizima kabla hajafanya lolote. Mpaka muda huo hakuwa anajua chumba hicho ni cha nani na amefikaje hapo. Alichokuwa anajua ni kwamba yeye ni mateka, na mara ya mwisho akiwa fahamuni alikuwa amefungiwa kwenye kiti na amegoma kula wala kunywa.



    Mbona yupo kitandani?



    Akatupia shuka lake kando na kujaribu kuketi kitako. Mwili ulikuwa unamuuma sana. uso wake ulikuwa mwekundu, maungio ya mikono yake yalikuwa mekundu. Mgongo wake ulikuwa unatoa jasho la damu.



    Kwa maumivu hayo lakini akamudu kusimama na kutembea kwa hatua chache kwenda ukutani. Aliona picha ya mwanamke hapo na mtoto mdogo wa kiume. Akaitazama picha hiyo kwa umakini akijaribu kushirikisha akili yake. Lakini hakupata kitu!



    Akiwa anachechemea kwa maumivu, akauendea mlango na kuusukuma. Ulikuwa wazi, usifungwe na komeo. Hakuusukuma kwanguvu, akiwa na lengo la kuchungulia, ili basi kama ni adui ajue ni namna gani atakabiliana naye.



    Alivyotupa macho, akaona taswira ya Jona. Mwanaume huyo alikuwa amekaa kwenye kiti akipitia karatasi ya mchoro, ule ambao aliletewa na Panky toka kwa Marwa. Macho yake nyuma ya miwani yalikuwa yanaenda huku na huko. Juu ya meza kulikuwa kuna kikombe cha chai, karatasi tatu nyeupe, kalamu ya risasi na rula ndefu.



    Nade akasimama kwa sekunde kumi na tano akimkagua mwanaume huyo aliyekuwa kifua wazi, ndani ya bukta fupi ‘timberland’.



    “Karibu na pole,” Jona akasema akiwa anaendelea kutazama karatasi yake. Nade akajikuta anatabasamu baada ya kugundua ameonekana, akiwa anajivuta kwa maumivu, akasonga na kuketi kwenye kiti.



    “Kumbe ni wewe,” Nade akasema akimtazama Jona.



    “Nikupatie chai?” Jona akamkarimu Nade.



    “Hapana, nashukuru. Nipo sawa.”



    “Haupo sawa. Najua haujala kwa muda wa siku tatu. kila chakula ulicholetewa ulikuwa unafanya kukimwaga kwa kukipiga teke. Tumbo lako linahitaji kinywaji cha moto kwa sasa kabla ya chakula ... unajua kwanini? Kwasababu unaweza ukajikunja na kukusababishia matatizo.”



    “Umejuaje kama nilikuwa sili?”



    “Sidhani kama ni siri hiyo, Nade.”



    Jona akaamka na kuifuata chupa ya chai akamimina kiasi kwenye kikombe na kumkabidhi Nade. Alafu kwa ukimya, akaendelea kufanya kazi yake ya kupekua ile karatasi, na muda mwingine akiwa anachorachora vitu vyake ambavyo Nade hakuwa anavielewa.



    “Ile picha ni ya mkeo na mtoto wako?”



    Jona akamtazama Nade kama mtu ambaye hakuamini kusikia swali hilo.



    “Picha ipi?”



    “Kule chumbani ukutani.”



    “Ndio,” akajibu kwa ufupi.



    “Wako wapi? Sijawahi kuwaona.”



    “Chai itapoa, hakikisha unamaliza upesi,” Jona akasisitiza. Nade akatabasamu na kupiga mafundo mawili ya chai. Macho yake hayakukoma kuendelea kutazama huku na huko.



    “Umempatia masharti gani mheshimiwa?” Mwanamke huyo akauliza.



    “Masharti? Kivipi?”



    “Najua mpaka umekuja kuniokoa kuna makubaliano mliyoyaweka. Unaweza ukanishirikisha?”



    Jona hakujibu kitu, akaendelea kufanya kazi yake. Nade naye akalipuuzia hilo swali, akaendelea kunywa chai lakini sasa hivi akiwa anazingatia kile ambacho Jona alikuwa anafanya. Kukawa kimya kwa muda.



    Kama dakika kumi na tano hivi mbele, Jona akapokea simu yake. Akaongea maneno machache tu akiahidi kufika ndani ya muda. Akanyanyuka toka sebuleni na kwenda chumbani.



    Nade akanyakua makaratasi ya mwanaume huyo upesi na kuyatazama. Jona aliporejea, akawa tayari ameshamaliza haja yake.



    “Twende kwa bosi wako,” Jona alisema akimwonyeshea Nade mlango. Nade akanyanyuka kwa taabu kabla ya Jona hajamshika mkono na kutoka naye ndani, Huko nje taksi ilikuwa tayari inawangoja, wakajiweka ndani na safari ya kwenda kwa Mheshimiwa ikaanza.



    Ndani ya gari kulikuwa kimya. Jona alikuwa anatazama nje ya dirisha lililokuwa limezibwa na kioo. Pembeni yake Nade alikuwa ametulia tuli kama maji ya mtungi. Mbali na mlio wa gari, kwa mbali sana ndiyo ungeweza kusikia sauti ya redio.



    Redio hii ilikuwa inaimba nyimbo za zamani, miaka ya themanini huko, na kwa uchache miaka ya tisini kipindi hicho muziki ukiwa muziki. Nyimbo hizi zilikuwa zinaendana na dereva wa taksi hii: mwanaume mweusi aliyepambwa na mvi kadha kwa kadha kichwani.



    Derava huyu ndiye pekee anayeaminika na mheshimiwa Eliakimu kwenye mambo ya usafiri, ukimtoa dereva wake anayempeleka ofisini na kumrudisha nyumbani.



    “Jona,” Nade akaita na kumshtua Jona. Jona akamtazama pasipo kusema jambo.



    “Ule mchoro uliokuwa unautazama pale sebuleni, umeutoa wapi?” akauliza. Jona akampuuza, akaendelea kutazama nje.



    “Naujua … naujua ule mchoro,” Nade akasema. Jona akurudisha upesi uso wake kumtazama.



    “Umeujulia wapi?”



    Hapo Nade akawa amekamata atensheni yote ya Jona. Mwanaume huyo alimtazama akiwa na kiu kubwa ya kujua.



    “Nilishawahi kuuona mahali kama sijakosea. Kwenye mojawapo ya vipeperushi ama barua ya mheshimiwa.”



    Jona akashangazwa. Mchoro huo ulikuwa na mahusiano gani na mheshimiwa? Alitaka kujua zaidi lakini hakupata majibu kwani Nade naye alikuwa mtupu asiyefahamu kwa kina.



    “Nakumbuka siku moja niliuona. Sikuuliza kwa kuwa sikuona kama una maana ya kufanya hivyo,” alisema Nade. Akamuuliza Jona kama ana lolote la kumwambia kuhusu mchoro huo, Jona akamwambia pengine majibu yao watapewa na Mheshimiwa.



    Baada ya hapo kukawa kimya tena. Lakini kichwani mwa Jona kukiwa na vurugu kwasababu ya mawazo mapya aliyopewa na Nade. Alijiona ana maswali mengi ya kujibiwa na mheshimiwa. Alijiuliza Eliakimu ni nani haswa asipate jibu.



    Akiwa humo fikirani, anashtuliwa na sauti kubwa! Gari lao linayumba vibaya mno! Dereva anajitahidi sana kulimudu na kuliweka sawa. Jona anakuja kusoma mchezo, walikuwa wamepushiwa na gari moja kubwa jeusi, Toyota Prado. Na halikuwa mbali.



    Bado dereva akihangaika kuweka matairi sawa, prado inashusha vioo, mkono mweupe uliobebelea bunduki aina ya SMG unatoka. Haraka Jona akapiga kelele:



    “Lala chini!”



    Mara risasi zinaanza kumwagwa kama njugu kushambulia taksi waliyomo Jona na wenzake. Dereva anakula risasi nne na kufa papo hapo. Taksi inaacha njia na kufuata fremu za maduka kwa kasi.



    Sasa hakukuwa na namna la sivyo wanaenda kufa wote. Jona akajirusha upesi toka kwenye viti vya nyuma na kuudaka usukani tena huku akipambana na mwili mfu wa dereva. Akajitahidi kuwakwepa watu na mali zao japo hakufanikiwa kwa kiasi kikubwa, akapasua na kubinua nyungo za karanga na kadhalika.



    Lakini hatimaye akafanikiwa kurejesha gari barabarani. Taharuki na makelele yakiwa yametamalaki, magari mengine yakiwa yamesimama ama kuhepa kujiepusha na hasara ama vifo!



    Akiwa mtulivu, macho yake yakatazama gari lile lililokuwa linawashambulia, Prado nyeusi, basi akadhamiria kufanya jambo. Taratibu akaanza kuutafuta mwanya wa kuisogelea gari hilo ambalo kwa muda huo tayari yule mshambuliaji alikuwa ameurejesha mkono wake wenye silaha ndani.



    Akayekwepa magari ya mbele na pembeni yake kwa ustadi. Kufanikisha adhma yake ikamlazimu atumie barabara ya wanaokuja, si wanaoenda kama yeye. Na hivyo basi ikamlazimu tena awe makini kupitiliza. Akifanya hayo Nade akajawa na hofu kubwa, hata akapiga kelele kumtaka Jona asitishe zoezi.



    “Jona, are you crazy!” (Jona, umewehuka!) akawaka akiwa amejishikiza kwenye viti. “Stop the car! Simamisha gari!”



    Lakini Jona hakujali, akaendelea kusaka lengo lake. Si kuwaua wale waliokuwa wanamshambulia, lah! Hakuwa na silaha pamoja naye ila alitaka kulitambua gari hilo vema na hata wale waliomo ndani.



    Akajitengenezea vema kwenye kiti cha dereva baada ya kumsukumia dereva yule mfu kando. Akakanyaga mafuta na kuendesha atakavyo. Lakini bado muda ukawa haupo upande wake, chombo chake hakikuweza kufua dafu kupambana mwendokasi na Prado, akaachwa.



    “Damn it!” akalaani akisaga meno. Akabadili mwelekeo akirejea nyuma kidogo na kisha akachukua njia ya kushoto. Mwendo ukabadilika, akawa anasukuma magurudumu kwa mwendo kati.



    “Watakuwa ni wale watu! – wakina Nyokaa!” Akasema Nade. Bado moyo wake ulikuwa unaenda mbio asiamini kama ametoka salama kwenye yale mashindano.



    “Hapana!” Jona akatikisa kichwa. “Sio hao unaowadhani.”



    “Ni wakina nani basi kama si wao ambao wangefuata roho yetu?” Nade akauliza.



    “Sijajua ni wakina nani ila sio hao unawafikiri. Mosi, hakuna mtu anayenijua kama mimi ndiye nahusika na kukuokoa isipokuwa mheshimiwa peke yake. Niliyatenda yote sura yangu ikiwa nyuma ya kinyago.



    Pili, kabla sijafanya zoezi la kukuokoa nilifanya upekuzi wa mazingira yote, hamna mahali niliona lile gari. Haitaleta maana kusema wao wanahusika, labda tu kama tungekuwa tumetokea nyumbani kwa mheshimiwa, hapo tungesema walianza kutufuatilia tokea huko, maana makazi yake watakuwa wanayajua.”



    “Sasa atakuwa ni nani?” Nade akashupaa kuuliza.



    “Sijui ni nani,” akajibu Jona. “Ila atakuwa anawinda roho yangu, si yako!”





    Baada ya nusu saa …





    “Kwahiyo mwili wake upo wapi?” akauliza Mheshimiwa akiwa ameshikilia kiuno. Alikuwa amevalia kaushi nyeupe nyepesi na bukta iliyokomea juu ya magoti. Usoni akiwa amevalia miwani ya kusomea. Mkono wake wa kuume umebebelea gazeti.



    “Upo ndani ya gari!” akajibu Jona.



    “Kwahiyo hamjafanikiwa kabisa kugundua hao watu? Kabisa yani!”



    “Sijafanikiwa, ila najua muda si mrefu ukweli utajiweka bayana.”



    “Ebu twendeni kwanza ndani … tuingie ndani …” mheshimiwa aliwasukumizia Jona na Nade ndani huku akiperuzi macho yake huku na kule. Baada ya muda mfupi mezani kwao kukawa kumependezeshwa na vinywaji vilaini. Nade alikuwa ameketi kando ya Mheshimiwa, Jona akiwa amejitenga kwa umbali mdogo akiketi kwenye kiti cha kuwatazama.



    “Hapa hapatakuwa mahali salama tena, ni kheri ukachukua tahadhari mapema,” Jona akashauri.



    “Najua hilo na bila shaka umeshaliona. Nimeongeza walinzi sasa maradufu!”



    “Sidhani kama watatosha, bado ni wachache. Adui yako ana jeshi kubwa, kwa idadi na hata nyenzo,” Jona akanguruma. “Nakushauri uwe makini zaidi.”



    “Sasa Jona na ndiyo hapo sasa nami ninapokuja kwenye ombi langu. Najua endapo nikiwa na wewe basi nitakuwa salama salmini, mkishirikiana na Nade hapa. Walionaje hilo?” Mheshimiwa akatia nadhiri.



    Kukawa kimya kidogo.



    “Miriam yupo wapi?” Jona akauliza. Mheshimiwa akamtazama Nade kwanza kisha akaurejesha uso wake kwa Jona na kujibu:



    “Yupo ndani.”



    “Naweza nikamwona?”



    “Ya .. yah! Unaweza ukamwona,” Mheshimiwa akajibu. Kukawa kimya kidogo.



    “Ila si kwa sasa, Jona,” Mheshimiwa akapendekeza.



    “Kwanini si sasa?” Jona akauliza. Mheshimiwa akawa kimya kidogo. Kisha akanyanyuka na kwenda ndani, baada ya dakika mbili akarejea akiongozana na Miriam aliyekuwa mchovu na mwenye huzuni. Alikuwa amevalia dera akitembea kama mwanamke aliyetoka leba.



    Jona akamsalimu, hakuitikia. Akamrushia macho yake makali akiwa ameuvuta mdomo. Hakujalisha Jona ameongea kitu gani, yeye hakutia neno hata moja. Macho yake ndiyo yalibadilika rangi kuwa mekundu, na ndani ya kinywa chake akisaga meno.



    Baada ya muda huo usiokuwa na matunda, mheshimiwa akamnyanyua mwanamke huyo kumrejesha ndani. Hapo sasa akaufungua mdomo wake akimtazama Jona. Akamlaani vikali akimrushia matusi.



    “Sitakusamehe maisha yangu yote kwa kunileta jehanamu!”



    Mheshimiwa akampeleka ndani ya chumba na kumfungia.



    “Naweza nikaambiwa sasa nini kinaendelea hapa?” Jona akauliza akimtazama Mheshimiwa ndani ya mboni zake. Mheshimiwa akashusha pumzi, kisha akashushia na juisi yake ya komamanga.



    “Jona, ni simulizi ndefu sana hii. Ni simulizi ambayo isingependeza kabisa kusikika kwenye masikio ya yeyote yule, haswa mtanzania. Ni simulizi ya kutisha ambayo yaweza kukufanya ukashindwa kulala kwa ndoto za jinamizi!”



    “Nipo tayari kuisikia simulizi hiyo,” akasema Jona. Basi Mheshimiwa akamtazama Nade na kumpandishia kichwa pasipo kutia neno. Nade akanyanyuka, na kwa mwendo wake wa majeruhi, akasonga kuondoka zake.



    “Jona,” Mheshimiwa akaita. “Mimi si kiongozi mzuri, si mfano wa kuigwa wala sistahili kuwepo kwenye kiti hiki. Ni mambo mengi nimefanya, na yote hayo ni kwa ajili yangu si kwa taifa wala wananchi. Kuna muda nafsi yangu inanisuta sana, lakini sina namna maana yaliyopita hayawezi tena kubadilika.



    Nimeshaingia kwenye anga la wenyewe, nikavinjari ninavyotaka, kutua chini ni ngumu …”



    Nade akarejea akiwa amebebelea kiboksi kidogo cha chuma. Akamkabidhi Mheshimiwa aliyekipokea kwa mikono miwili na kisha akakiweka mapajani. Akaendelea kunena akiwa anafungua kiboksi hicho.



    “… maana nimeshazoea hewa ya huko juu kiasi kwamba naona nikitoa naweza nikafa kwa kukosa pumzi. Kutua chini kutaninyima uhuru niliozoea kwenye anga hilo … kwahiyo siwezi, siwezi tena kutua. Siwezi kurudi tena ardhini.”



    Alipomaliza kusema hivyo, mara mkono wake ukatoka ndani ya kiboksi ukiwa umebebelea bunduki ndogo nyeusi. Akamnyooshea Jona.



    “Na hivyo basi, haitakiwi mtu yeyote kujua kama nami ni rubani kwenye anga hilo. Ni siri inayotakiwa kudumu milele, na milele, amin,”



    Akafyatua risasi mbili kutoboa kifua cha Jona. Kisha akaangua kicheko akirejesha bunduki yake ndani ya kiboksi.



    “Kwaheri Jona, kwaheri katuandalie makao.”



    Akamuita mmoja wa walinzi wake waliokuwepo nje, akaunyooshea mkono mwili wa Jona.



    “Beba hiyo na nyingine ndani ya taksi, kaitupie mbali!”



    “Sawa mkuu!”



    “Hakikisha hakuna mtu anayekuona, wala anayekufuatilia. Sawa?”



    “Sawa!”



    Mwanaume huyo mpana na mrefu, akaubeba mwili wa Jona na kutoka nao nje, akautupia ndani ya gari kisha akaubeba na ule wa dereva taksi, alafu akatimka akienda anapopajua yeye kichwani. Kwenda kuitupa miili hiyo isiwahi kuja kujulikana!



    Huko nje ya jiji la Dar akaishusha na kuitelekeza baada ya kuhakikisha yupo mwenyewe, na kweli alikuwa mwenyewe. Akajipaki kwenye chombo na upesi akatimka.



    “Ndio, mkuu. Kazi imeshakwisha!” akaongea mtumishi huyo mwadilifu.





    Baada ya lisaa limoja …





    Mtumishi huyo akafungua mlango wa sebuleni na kuangaza macho. Sura yake imebeba hofu na mazingira yalikuwa tulivu mno. Mkononi mwake alikuwa amebebelea bunduki ndogo. Haikuchukua muda, akaona mwili wa mheshimiwa pamoja na wa Nade ukiwa umelala kwenye kochi, damu zinawatiririka vichwani!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akatahamaki. Akawatazama watu hao kwa macho ya bumbuwazi. Akakimbilia napo chumbani kutazama, Miriam hakuwapo! Chumba kilikuwa kitupu, mlango upo wazi.



    Hakuamini kilichotokea, akarudi tena sebuleni na kumtazama bosi wake, kwa mbali alikuwa anahema na kumbe alikuwa amejeruhiwa na risasi kifuani na hapo kichwani alikuwa amepasuliwa na kitu chenye ncha kali.



    Akamtazama na Nade, mwanamke huyo alikuwa ahemi kabisa. Hakuonyesha dalili yoyote ya uhai! Mara akasikia sauti ya kuguguma toka kwa mheshimiwa, upesi akamtazama.

    "Haaaammm ... "



    "Unasemaje mheshimiwa? ..." akasema mlinzi yule akiweka sikio lake mdomoni mwa Eliakimu. Lakini hakusikia tena kitu, mheshimiwa akanyamaza na kutulia tuli.



    Amekufa? mlinzi akajiuliza. Akamtikisatikisa mheshimiwa lakini hakufanikiwa abadani. Pengine alikuwa ameenda na maji!



    Baada ya muda mchache mbele, waandishi wa habari na vyombo vya usalama vikajaa hapo kila mmoja akitenda kazi yake. Ikabainika wanaume watatu waliovalia vinyago usoni ndiyo walihusika ma mauaji hayo.



    "Sijajua ni wakina nani na kwanini wamefanya haya mauaji!" Akasema Alphonce akimwambia Kamanda wa polisi mkoa.



    "Hivi mtu huyu alikuwa na adui yoyote kisiasa?" Akauliza kamanda.



    "Hapana! Labda pengine, huwezi jua." Akasema Alphonce akiwa anatazama waandishi wa habari wakiwa wanajitahidi kurusha matangazo yao moja kwa moja.





    "Lakini mkuu ..." Alphonce akataka sema kitu. Akamtazama Kamanda kwa uso wa 'kumtonya', wakaelekea ndani ya gari la kamanda huyo wapate kuteta.





    "Unaiona ile gari pale?" Alphonce akasema akinyooshea kidole taksi iliyokuwa imepaki kwenye ndani ya nyumba ya Eliakimu.



    "Ndio, naiona. Ndiyo iliyobeba wauaji?"



    "Hapana, ila ndiyo iliyombeba yule kasuku!"



    "Kasuku? Una uhakika?" Kamanda akatahamaki.



    "Ndio! nina uhakika asilimia mia saba. Ile kazi uliyotupa ya kummaliza ilikuwa inafanyika ndani ya lile gari!"

    "Alphonce, embu acha ngonjera. Nyoosha maelezo!"



    "Lile gari ndilo lilimbebelea Kasuku leo, na kumbe lilimleta hapa. Wakati unahojiwa na vyombo vya habari nikachukua muda wangu na kulipekua. Lina matundu ya risasi na hata damu!"





    "Sasa huyo Kasuku hamkumuua?"



    "Hapana, mkuu! Bila shaka atakuwa hajafa. Asingeweza fika hapa."



    "Na huyo Kasuku mule ndani hayupo?"



    "Hayupo! Yupo mheshimiwa na mwanamke fulani ambaye alikuwa na Kasuku yule ndani ya hilo gari!"



    "Sasa Kasuku atakiwa ameenda wapi? Au unataka kunambia yeye ndo atakuwa anahusika na haya mauaji?





    "Sijajua! Lakini atakuwa ana cha kueleza kuhusu haya mauaji."



    "Lakini Alphonce, unajua unaniangusha sana kwenye hili! Kwanini huyo mtu unashindwa kummaliza? Na kila kitu unacho!"



    "Mkuu, Kasuku ni mjanja mno. Ila itafikia mwisho akaingia tegoni tu."

    "Hakikisha hiyo siku na sisi tutakuwa bado tupo hai."



    "Usijali, mkuu!"



    "Najali. Unadhani Kasuku huyu akija kutambua tumemuweka kwenye rada, huoni tutakuwa tupo hatarini? Kasuku yule ni mwekundu, na wa kijani! Anabadilika rangi kwa mujibu wa miale ya jua!"





    Kukawa kimya kidogo. Mara, Alphonce akashika kitasa cha mlango wa gari.





    "Nakuja!"



    "Unaenda wapi?"



    "Nimemwona mtu ambaye anaweza kutusaidia kumpata Kasuku!"





    Kabla Kamanda hajasema neno, Alphonce akatoka ndani ya gari.





    Kamanda akabaki akimtazama wapi anaenda. Akamwona mwanaume huyo akienda kuongea na yule mlinzi aliyesalimika kwa kwenda kumtupa Jona.

    Akakodoa macho akifuatilia kila nyendo, punde akamwona Alphonce akimtaka mlinzi yule aelekee kwenye gari alilomo.





    Mlinzi huyo akatikisa kichwa ishara ya kukataa, Alphonce akamlazimisha kwa sura ya msisitizo. Mlinzi akaridhia, japo kishingo upande.





    Wakazama ndani ya gari wakiketi kwenye viti vya nyuma.





    "Haya mwambie huyo!" Alphonce akamwamuru mlinzi yule. Alikuwa amejawa na woga, na macho yake yalikuwa mekundu.



    "Tulienda kumtupa!"



    "Ulienda kumtupa wapi? Kwanini mlienda kumtupa?" Akauliza Kamanda.



    "Tuliamriwa na mheshimiwa. Alikuwa tayari ameshakufa kwasababu ya majeraha ya ajali! Alifika hapa akiwa hoi sana. Hakuchukua muda," mlinzi akalaghai. Mheshimiwa akatabasamu na kumtazama Alphonce kwa macho ya furaha.





    "Mheshimiwa, ni mpaka tukihakikisha," akashauri Alphonce.





    Basi muda mchache tu, gari la Kamanda likatoka kuelekea kule ambapo Jona alitupwa wakielekezwa na mlinzi wa mheshimiwa. Ikawachukua kama dakika ishirini wakawasili.





    "Ndipo hapa!"





    Wakashuka na kusonga kwa ndani, wakauona mwili mmoja, haraka Alphonce akaukimbilia na kuchuchumaa kuutazama. Haukuwa wenyewe!

    "Nilijua tu! Huyu mbwa hawezi akafa kirahisi hivi!" Akasema Alphonce akisimamama.





    "Una uhakika ilikuwa hapa?" Kamanda akamuuliza yule mlinzi.





    "Ndiyo, ni hapa kabisa!" Akajibu mlinzi akipepesa macho yake huku na huko.

    "Nakumbuka nilimtupia hapa!" Akanyooshea kidole.





    "Basi atakuwa ameondoka," akajibu Alphonce, "ila nadhani hatakuwa mbali!"

    Wakatafuta pasipo majibu. Jona hakuonekana wapi ameenda. Kumaliza ushahidi, Alphonce akammaliza Mlinzi kwa kumnyonga na kumtupia ndani ya msitu!





    "Hakikisha mtu huyu anapatikana na kuuawa! Hakikisha hilo Alphonce!" Alisema Kamanda aking'ata meno.







    ***









    Usiku wa saa sita, La Palma Pub.









    "Nataka kuhama pale!" Akasema Glady baada ya kupulizia moshi wa sigara kando.





    "Unaenda wapi sasa na kama unavyojua kodi ya pale angalau unaweza kumudu? Au umepata danga jipya mwenzetu?" Mwenzake akauliza. Wote walikuwa wamesimama nje ya pub wakiwa wanavuta sigara. Glady alikuwa amevalia sketi fupi nyeusi na topu nyeupe yenye maneno ya kichina. Mwenzake akiwa amevalia sketi nyekundu yenye mpasuo mpaka kwenye nyonga.





    "Hamna si mambo ya madanga wala nini, sema nataka kubadili mazingira tu!"

    "Umeanza lini hiyo tabia Glady?"

    "Nitaanza hivi karibuni."





    Mara mwenzake na Glady akatazama barabarani na kisha akajinyooshea kidole kifuani. Mara akamtazama Glady na kumwambia kwa sura ya kinyonge:

    "Unaitwa kule!"





    Glady kutazama akaona prado nyeusi. Kioo cha dereva kikashushwa vema, Alphonce akaonekana vema, akamfanyia ishara ya kumwita.





    "Kwaheri shost, baadae!" Glady akaaga na kwendaze. Akapanda gari na kuondoka hilo eneo, mwenzake akimtazama.





    Ndani ya muda mfupi, mwenzake huyo akasikia simu yake ikinguruma. Akaitoa na kutazama:





    "Shosti lazima nipige mshindo kesho tukatumbue!" Ilikuwa ni ujumbe toka kwa Glady. Mwenzake akatabasamu na kuviweka vidole kwenye kioo cha simu, akaandika na kutuma:





    "Kamua haswa shoga angu, nakuaminia!"

    Akausindikiza ujumbe huo na tabasamu. Akatazama na mambo mengine ndani ya simu yake kabla hajairudisha kwenye mkoba na kuendelea kusimama.







    Saa tisa usiku ... Kwachu Best Lodge, Kimara.









    "Mimi siwezi kutumia kondom kabisa," alisema Alphonce. Alikuwa amekaa juu ya kitanda akiwa amevalia bukta fupi na yu kifua wazi. Glady alikuwa amebakia na sidiria na kufuli tu, vyote rangize ya pink. Yeye alikuwa amejilaza kitandani.

    "Hatujakubaliana kavu!" Akaropoka Glady. "Ukitaka kavu basi ongeza pesa!"

    Alphonce akacheka.





    "Na vipi kama nisipokupa hiyo pesa? Utafanya nini?" Akauliza kisha akawasha sigareti yake aliyoiweka mdomoni na kuanza kuifyonza. Macho yake yamelegea ila imara. Mdomo wake ulikuwa mkavu ukipinda mithili ya wa samaki.





    "Kwanini usinipe?" Glady akauliza.

    "Si naamua tu," Alphonce akajibu. Glady akamtazama kwa macho ya hasira pasipo kusema kitu. Ndani yake alishaanza kutengeneza hofu juu ya mwanaume yule. Hakuwa mtu mzuri.





    Lakini kwa mujibu wa fikra zake, ni kama vile aliona kitambulisho cha polisi ndani ya gari la mwanaume huyo. Mwanzoni alijihisi salama, kumbe alikosea.





    Akili yake ikaanza kurukaruka na kutambalia mazingirani. Akiwa anawaza, mara Alphonce akanyananyuka na kumwambia:

    "Nakuja, jiandae!"





    Akaelekea chooni kukojoa baada ya kuweka kipisi chake cha sigara kwenye kisosi cha kioo kilichokuwa kipo juu ya kistuli. Aliporejea, akadaka kwanza sigara yake na kupiga pafu mbili za kumalizia.





    Lakini kabla hajajimwaga kitandani, akaanza kupoteza uwezo wake wa kuona. Alikuwa anaona kama ukungu mbele yake na kichwa kikawa kinamzumguka, akachukua dakika mbili tu, akadondoka chini kama mzigo!

    "Ms*nge wewe!" Glady akasema kwa kebehi kisha akanyanyuka toka kitandani na kumtazama Alphonce.





    Alikuwa anavuja damu sakafuni.

    Haraka Glady akavaa na kisha akatoa chupa ya mafuta na kitambaa.





    Akalowanisha kitambaa mafuta kisha akapaka kwenye nyayo ya kushoto ya Alphonce na mafuta kidogo akayamiminia chini.





    Alafu akaenda zake akiwa kabebelea kila kitu cha Alphonce!





    Saa saba mchana, Tikko Hotel ghorofa ya nne.





    "Niliona hii sehemu itatufaa sana," akasema Boka akitazama huku na huko ingali akiketi. Alikuwa amevalia suti nyeusi ya kujichana ikirandana na mwili wake. Kwenye kamfuko ka koti mkewe alikuwa ameweka kijiua kidogo rangi nyekundu, kikivutia na kunogesha vazi.



    Mbele yake alikuwa ameketi mwanamke mrembo Miranda. Nywele zake akiwa ameritachi na kuzimwagia kushoto. Kope za macho yake zilikuwa zimesimama dede akirembua. Lips zake zilikuwa rangi ya pink akinukia kama bustani ya kando ya mto.



    "Una uhakika?" Akauliza Miranda.



    "Aaaah! Unadhani nakutania?" Boka akajoki, "Hapa pametulia sana na hapana macho ya watu wengi si unajua bana siku hizi kila mtu ni mwandishi wa habari wa kujitegemea!"



    Wakacheka, kabla hawajamaliza mhudumu akawa amefika. Akawauliza ni nini wanataka, wakaagiza chakula na vinywaji.



    "Hivi kuna siku ulisahau kupendeza kweli? Umependeza haswa!" Boka akamsifia Miranda kisha akashushia na kinywaji.



    "Ahsante, ila sijakuzidi wewe," Miranda akapokea sifa kwa sauti ya deko huku akipambana na kisu cha chakula.



    Wakapiga stori kwa muda kidogo kabla hawajazama kwenye lengo la kijikao chao. Boka akasafisha koo na kusema:



    "Bila shaka umeshaingia ubia na mke wangu. Nilipata kuwaona juzi mkiwa mnajinasibu mbele ya vyombo vya habari. Ni hatua nzuri."



    "Ahsante, vipi ulinionaje? Nilikuwa sawa? Maana sikuwa comfortable kabisa!" Akalalama Miranda akiwa ameacha kula na kumkodolea Boka.



    "You were fine! Sikuona tatizo, nilikuwa nawatazama nikiwa ofisini kwangu and felt very proud."



    Miranda akashukuru akitafuna.



    "Nataka kukuoa, Miranda. Nataka uwe mke wangu wa pili," Boka akasema huku anamtazama Miranda kwa jicho lisilo na utani.



    "You must be joking, Boka!" (Utakuwa unatania Boka) akajibaraguza Miranda. "Mie niwe mkeo?"



    "Kwani haiwezekani?"



    "Haiwezekani!"



    "Kwanini?" Boka akaacha kula.



    "Kwasababu siwezi kugombania pakuo na mwanamke mwenzangu," akasema Miranda.



    "Una maanisha nini?" Boka akauliza.



    "Boka," Miranda akaita. "Mafahari wawili hawakai zizi moja. Unadhani msemo huu ulikosewa?"



    "Sasa wataka nifanyaje Miranda na mie ilhali nishazama kwako. Mguu hautaki chomoka kabisa."



    Miranda hakusema kitu. Akatafuna kwanza na kisha akanywa kinywaji chake rangi nyekundu ndani ya glasi yake yenye kiuno chembamba. Kisha akamtazama Boka kwa jicho la kike.



    "You want to have me?" (Unataka kuwa nami?)

    "Yes, I really do." (Ndio, nataka haswa.)



    "But are you ready to do what it takes to have me?" (Lakini uko tayari kufanya namna ukanipata?)



    "Yes, I am. But please don't tell me to abandon my wife." (Ndio, ni tayari. Lakini tafadhali usiniambie nimwache mke wangu.)



    Miranda akacheka.



    "Usijali, ila nikuweke wazi nashindwa kukupa jibu la moja kwa moja."



    "Tena?"



    "Nop! Si hivyo, I mean unajua kama nina mlezi. Nisingependa kufanya jambo hili siri. Ningependa tukamshirikisha."



    Boka akaguna. Akala na kunywa kwanza kabla hajatia neno.



    "It's ok! Ila huoni kama italeta matatizo na wewe hujaafiki kuwa mke kwangu?"



    "Let us give it a try," akasema Miranda. "Mlezi wangu ni mzungu, huwezi jua." Akaongezea: "kama wanipenda kweli, kweli, basi nitajua kwa hatua zako."



    Muda si mrefu, ujumbe ukaingia kwenye simu ya Miranda toka kwa BC. Alikuwa anataka kuonana naye hivi punde. Lakini kabla hajasema dhamira yake ya kuondoka, Boka akapigiwa simu na akamtaka waende maana yampasa afike ofisini.



    "Basi twaweza tumia gari langu hamna shida," Boka akapendekeza. Wakapanda gari na kumpitisha Miranda nyumbani kwa BC.



    "Ndipo hapa?" Boka akauliza.



    ""Ndio, karibu."



    "Ningeingia na kusalimu, sema nahitajika kwa haraka ofisini."



    "Sawa, usijali. Hamna shida," Miranda akasema na kisha akaaga na kujiendea zake ndani. Akamkuta BC akiwa amelisimama ghorofani akiwa anaangaza macho. Mkononi, mzungu huyo alikuwa amekamatia glasi ya mvinyo. Mwili wake akiuhifadhi kwa shati la "beach boy" alilolichomeka ndani ya suruali yake nyeusi ya kitambaa.



    "Hellow, is that the man?" (Habari, yule ndiye yule jamaa?) Akauliza BC akitazama barabara.



    "Yah! He is the one. Very soon he will be here talking to you." (Ndiye mwenyewe, muda si mrefu atakuwa hapa kuongea nawe.)



    "That's nice! You know I called you here to talk about Eliakimu. Have you heard news about him?" (Hilo ni jema! Unajua nimekuita hapa kumuongelea Eliakimu. Umesikia habarize?)



    "No! What is it?" (Hapana! Kuna nini?)



    "He's passed away! Some people ambushed and killed him!" (Amefariki! Watu fulani wamemvamia na kumuua!)



    Miranda akashangazwa. Akauliza zaidi kuhusu hiyo habari, BC akampatia 'full mkanda'.



    "So from now on we'll be free to move on." (Kwahiyo kuanzia sasa tutakuwa huru kuendelea,) akasema Miranda akionyesha kuvutiwa.



    "Yes, but I wonder who killed him. I know he had been involving in several crimes, but his killing will leave us safe?" (Ndio, lakini najiuliza nani kamuua. Najua alikuwa akijihusisha na uhalifu kadhaa, lakini kifo chake kitatuacha salama?"



    Miranda hakuwa na jibu. Akaguna na kuhema akifikirisha kichwa chake. Mara akakurupuka na swali:



    "About the news ... where was he killed?" (Kuhusu hiyo taarifa ... wapi ameuawa?)



    "At his home!" (Nyumbani kwake!)



    "All alone?" (Peke yake?)



    "Yes. Heard only about him." (Ndio. Nimesikia kumhusu yeye tu.)



    "Sure?" (Hakika?)



    "Yes. What's wrong?" (Ndio. Nini shida?) BC akauliza akimtazama Miranda kwa macho ya kina.



    "No - no nothing!" (Hamna kitu!)

    "Are you sure you don't have anything to share?" (Una uhakika hauna kitu cha kushirikisha?)



    "I think somebody may have the answers," (Nadhani kuna mtu anaweza kuwa na majibu,) akasema Miranda akitazama kando kwa mawazo.



    "Who is it?" (Nani huyo?) BC akawahi kuuliza.



    "The girl whom Eliakimu lived with," (mwanamke aliyekuwa anaishi na Eliakimu.) Kisha akaongezea:



    "I think we should look for her." (Nadhani tuna haja ya kumtafuta.)



    "But where? I went there, the house is empty!" (Lakini wapi? Nilienda kule, nyumba ni tupu!)



    "There must be a way. We must find Nade where she is. And if we wont find her, then I will be convinced that she is the one who is responsible." (Kutakuwa na namna. Ni lazima tumtafute Nade alipo. Na kama tusipompata, basi nitaamini kwamba yeye ndiye mhusika.)



    BC akanywa kinywaji chake, akatazama barabarani akiwa amekunja mdomo.





    ***





    "Bosi, una mgeni," akasema mlinzi akimwambia mwanaume wa kichina aliyekuwa ameketi kwenye kochi akisoma gazeti.



    Mwanaume huyu wa kichina kwa jina lake halisi anaitwa Foang. Ni mfanyabiashara mkubwa wa vyombo maeneo ya Kariakoo. Ana miliki maduka matatu makubwa akiwa ameajiri watu kadhaa.



    Mwanaume huyu ndiye yule aliyeletewa nyaraka na wakina Mustapha kwa dhumuni la kuwasaidia tafsiri. Tangu siku ile amekuwa akisaka nyaraka hiyo pasipo mafanikio. Hivyo moyoni amekuwa na kama donda sugu ambalo lilishapewa dawa kisha ikashaisha. Sasa anaisaka kwa udi na vumba!



    Anataka nyaraka hiyo kwa gharama yoyote ile. Kwani ni pesa! Pesa kubwa ambayo inazidi hata mara hamsini ya mtaji wake. Unalalaje sasa? Vipele vya baridi humtoka kila anapofikiria nyaraka hiyo.



    Anafahamu ni kwa namna gani atafanya biashara safi ndani ya mji wa Hongkong. Pasi na shaka alikuwa anajiona karibu kabisa na tajiri namba moja barani Asia - Alibaba!



    "Mwambie aingie!" Akasema Foang pasipo kumtazama. Macho yake yaling'ang'ania kwenye maandishi ya gazeti, ila alikwishajua ni nani mgeni wake huyo. Hakuwa na haja ya kuhangaika.



    Punde, mlango unafunguliwa akaingia mwanaume aliyeshiba. Alikuwa amevalia suti rangi ya brown, koti kubwa kidogo kuvuka mwili wake. Mwendo wake ni wa hatua nzito, akaketi kwa kishindo na kusalimu.



    Alikuwa ni Alphonce! Alikuwa ana bandeji kubwa kichwani kwake kwa nyuma. Uso wake ulikuwa umefuma kwa hasira na pembeni ya jicho lake la kushoto alikuwa amevimba. Macho yake yalikuwa mekundu akitengeneza ndita.



    Foang akaweka gazeti lake pembeni, akamtazama Alphonce. Kwa dakika kama moja hakunena kitu. Bila shaka alishangazwa na muonekano wa Alphonce, ila hakutaka kujisumbua nao akamuuliza:



    "What have you brought on the table?" (Umeleta nini mezani?)



    Alphonce akasafisha koo lake kisha akazamisha mkono wake ndani ya koti na kutoa simu. Akailaza mezani. Foang akatabasamu kabla hajainyaka simu hiyo na kuikagua kwa kuigeuzageuza.



    "Is this the one?" (Hii ndiyo yenyewe?) Akauliza Foang.



    "Yes it is. I got it from the man who was left. I've already finished him!" (Ndio yenyewe. Nimeipata kwa yule jamaa aliyebaki. Tayari nimeshammaliza!)



    Foang akatabasamu zaidi. Ila akakunja sura yake na kuuliza:



    "Are you sure you've finished?" (Una uhakika umemaliza?)



    "He doesn't breath anymore," (Ahemi tena) Alphonce akasema kwa uhakika.



    "And about the police?" (Na kuhusu polisi?)



    "Told you before. I am the only police whom you should worry about." (Nishakuambia hapo kabla. Mimi ndiye polisi pekee wa kumhofia.) Kisha akauliza:



    "Where my money at?" (Pesa yangu ipo wapi?)



    "Where are you rushing at?" (Unakimbilia wapi?) Foang akauliza.



    "Let me inspect the phone first!" (Acha niikague simu kwanza!)



    Kabla hajaifungua simu, Alphonce akamdaka mkono wake na kumwambia:



    "Till I see my money first!" (Mpaka nione pesa yangu kwanza!)



    Macho ya Alphonce yalikuwa hayana utani hata kidogo. Hakuwahi na utani kwenye pesa tangu azaliwe. Kwake pesa ndiyo kitu cha thamani maishani. Amezaliwa atafute pesa! Na kutumia pesa!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kuhusu kiapo cha kazi ya upolisi, uzalendo na mambo ya ujamaa, hayo unaweza ukabaki nayo. Yeye mpe pesa! Kama unataka uendelee kuvuta pumzi ama kuishi kwa amani.



    Foang akamtazama mwanaume huyo machoni. Akajifunza kweli hana utani. Hata akaogopa. Akatabasamu na kupandisha mabega yake:



    "I still depend on you, Alphonce. I can not cheat on you." (Bado nakutegemea, Alphonce. Siwezi kukulaghai.)



    Alphonce hakusema kitu, akaendelea kumtazama na macho yaliyotoa ujumbe tosha. Foang akanyanyuka na kwendaze chumbani, muda si mrefu akarejea na bahasha ya kaki aliyomkabidhi Alphonce.



    Alphonce akatupia macho yake ndani ya bahasha, akatabasamu na kunyanyuka akimpatia mkono Foang.



    "I think I should go." (Nadhani napaswa kwenda.)



    "But I have not yet inspected the phone!" (Lakini bado sijaipekua simu!) Akalalama Foang.



    "Just do it then you will inform me. You know my contacts, right?" (We fanya alafu utanitaarifu. Unajua namba zangu, sio?)



    Hakungoja Foang aseme neno, akaenda zake Foang akimsindikiza kwa macho. Mchina huyo hakuwa anajua cha kufanya, akaishia kumtazama Alphonce akiyoyoma.



    Alphonce akaweka bahasha yake kwenye kiti cha pembeni, akatekenya funguo na kutoka ndani ya nyumba ya Foang kwa kasi. Haikupita punde, simu yake ikaita. Ilikuwa ndani ya mfuko wa koti, akaichomoa na kuitazama kwa kuibia. Alikuwa ni kamanda.



    "Ndio, mkuu ... muda si mrefu sana n'takuwa hapo ... serious? ... sijatazama na wala sijasikia kabisa! ... sawa! ... sawa."



    Simu ikamuacha ameachama mdomo. Alikuwa amekunja sura, macho yake yakiwa yametambaliwa na utashi wa fikra. Habari alizozipokea zilimshangaza, na kumpatia mawazo. Zilimfanya kwa muda asahau kwamba alikuwa ameweka 'manoti' kadhaa kwenye kiti cha pembeni yake akiwa ameziingiza kwa 'kazi ndogo'.



    Akashusha pumzi ndefu. Akasonya na kutikisa kichwa. Lakini ajabu, ghafla akasikia kitu cha baridi shingoni kwake! Akatazama kupitia 'sight mirror' akamwona mchina akiwa amemuwekea 'chuma', macho ameyakaza wakitazamana kiooni.



    Alikiwa ni Lee!



    "Habari za muda mrefu, Alphonce."



    "Hivyo ndiyo namna ya kumsalimu rafiki yako ambaye hamjaonana kwa muda mrefu?"



    "Si hivi, bali kwa kutoboa shingo yake na risasi! Rafiki hawi tena rafiki anapouarua mgongo wa rafiki yake aliyemkabidhi aukune."



    "Una maanisha nini Lee?"



    "Unajua ninachomaanisha. Peleka gari makaoni kabla sijakugeuza nyakati iliyopita ... na unafahamu vizuri kwamba sitanii."



    Alphonce akamtazama Lee kiooni. Lee akamtazama Alphonce kiooni. Macho yao yalikuwa yanasema mengi zaidi ya maneno waliyoyatamka na vinywa. Macho haya yalikuwa ya janja janja! Macho ya kizandiki!



    Macho ya njama!



    Akilini mwa Alphonce kulikuwa kuna mafikirio, kama ilivyokuwa kwenye bongo ya Lee. Alphonce hakuwa tayari kwenda popote pale akiongozana na Lee. Mosi, kamanda anamngojea ofisini. Pili, ilikuwa ni ombwe kwake juu ya anachoenda kukutana nacho huko apelekwapo.



    Akili yake ikabidi ifikirie namna ya kujinasua. Hakuwa na budi kumzidi akili Lee kisha atokomee zake! Basi akakaza mkono kwenye usukani wa gari. Akiwa katika mwendo wake wa kasi, akaanza kuhesabu kimoyomoyo, mdomo wake ukiwa unachezacheza kwa mbali.



    1 ... 2 ... 3 ... 4 ...



    ... 5!



    Akakanyaga breki kwanguvu! Lakini asifahamu kilichotokea, akajikuta hana fahamu baada ya kuhisi amegongwa kwanguvu chini ya kisogo.



    Akazama kizani!



    ---



    Robo saa mbele ...



    Gazeti linatupiwa juu ya meza ya kioo, Kamanda akasonya na kunyanyuka akifuata kabati. Anatazama saa yake alafu anasonya tena. Anachukua faili rangi ya samawati, nalo analirushia mezani.



    Anasimama na kufikiri jambo. Akajirejesha kwenye kiti chake na kunyakua simu yake nyeusi, SONY toleo jipya, akapiga. Simu ikaita pasipo kupokelewa. Akapiga tena, haikupokelewa!



    Akaweka simu mezani na kulaza kichwa chake kwenye kiti. Akazunguka kwenda kushoto na kulia, kulia na kushoto akitazama feni yake darini.



    Lile faili alilolitoa kabatini, hakuonekana kuligusa wala kuwa na mpango nalo. Mezani, kwa mbele yake, ungeweza kuliona gazeti la Habari Leo likiwa na picha ya wanaume wawili waliokuwa wamelala chini, wamejeruhiwa na kutapakazwa damu.



    Kwa juu ya picha hiyo ikisomeka kichwa cha habari chenye maneno meusi:



    *"WATU WAWILI WAMEUAWA KINYAMA NA MTU ASIYEJULIKANA."*



    Chini ya maneno hayo, kwa mtu mwenye macho 'mepesi' angelisoma tena maneno yenye ukubwa wa saizi ya kati yaliyoandikwa kwa wino wa kijani:



    "Watu hao watuhumiwa kuwa majambazi, na wameuawa kwa mkono wa siri."



    Chini ya kichwa hicho, kulikuwa na habari kamili sasa ikiwa imeandikwa kwa maneno madogomadogo, ngumu kuonekana kwa macho ya wazi yaliyo mbali. Na mbele kidogo ya taarifa hiyo ikalekezwa kuendelea ukurasa wa tatu.



    ***



    Usiku wa saa mbili ...



    Baada ya sauti ya vishindo vya miguu, inafuata ya mlio wa mlango kisha Jona anaingia ndani ya makazi yake akiwa anachechemea.



    Anawasha taa na kujitupia kwenye kochi kama mzigo. Akahema kwa mafundo makubwa makubwa mara tano kabla hajavua nguo yake ya juu na kubaki na kaushi ya kuzuilia risasi.



    Akafungua kaushi hiyo kwa nyuma kisha akaiweka mezani. Kifuani kwake kulikuwa kuna majeraha, kwa mbali kulikuwa kuna rangi nyekundu ya kuvilia damu.



    Kabla hajafanya kitu kingine chochote, akanyanyuka na kwenda chumbani akiwa anapepesuka. Alipofika mlangoni, akadondoka chini kama mzigo, akapoteza fahamu!



    Baada ya kama dakika tano akiwa hapo chini, taratibu, kwa mbali akaanza kupata taswira ambazo hakuzielewa. Taswira hizi zilikuwa zinakatiza upesi kichwani kwake mithili ya mwanga wa radi!



    Kulikuwa na sauti ambazo hazikueleweka. Mayowe na nderemo za kifo. Na mara sauti za watu waliomezwa na giza wakiwa wamebebelea maginga ya moto!



    "Amepita wapi?" Sauti moja ya mwanaume ikauliza. Giza lilikuwa pana kiasi cha ginga la moto kutofua dafu!



    "Huku! ... Amepita huku!" Akasema mwanaume mwingine upesi!



    Mara tih! Tih! Tih! Vishindo vikaenda huko na kupotelea gizani.



    Jona hakutikisika. Na hakuonyesha dalili ya kuamka karibuni. Masikioni hakusikia tena kitu, na machoni akawa mpofu.



    ***



    Saa sita usiku.



    "Bosi nadhani kuna mtu getini," akasema mlinzi baada ya kugonga mara mbili mlangoni, Foang akatoka akiwa amevalia taulo.



    "Who is it?" (Nani?) Foang akauliza. Macho yake madogo ya kichina yalikodoa, mkono wake wa kuume ulikuwa umeshikilia taulo lake lisianguke.



    "Bwana mi sielewi! Spiki kiswahili" akalalama mlinzi.



    "Nani? Nani huyo?" Foang akafoka kwa lafudhi ya puani.



    "Sijui nani? Hauna appointment na mtu?"



    "No! No! No appointment!" Foang akatikisa kichwa, kisha akamtaka mlinzi aende, akafunga zake mlango!



    Akiwa ndani ya chumba akasimamisha masikio yake apate kusikia kila jambo linalotukia huko nje. Lakini hakusikia hata lepe. Zikapita mpaka dakika nne ... tano ... sita ...



    Akaulaza mwili wake kwa amani. Akazima taa, na bunduki yake ndogo ambayo alikuwa ameshaisogeza karibu akaisokomezea chini ya mto.



    Kabla hajabebwa na usingizi, akasikia hodi mlangoni. Akalalama na kutusi. Aliona sasa huyu mlinzi ameshindwa kazi, na akaapa kumfunda adabu huko mlangoni aendapo.



    Akajikwamua kitandani na kupiga hatua tatu ndefu. Akafungua mlango kwa hasira na kuangaza. Uso kwa uso akakutana na bomba la bunduki!



    Alikuwa ni Lee!



    Akamwamuru atoke na kumpatia simu aliyopewa na Alphonce. Na akitumia lugha ya kichina, akamuuliza kama amefanya lolote na ile nyaraka. Foang akatikisa kichwa chake upesi, akakana katukatu!



    Kuhakiki, Lee akapekua simu ile kwa haraka. Alipomaliza, akamuaga Foang na kisha akamzamishia chuma cha risasi kichwani! Akatoka zake ndani ya jengo kwa kuchumpa ukuta.



    Dakika kumi na tatumbele ...



    "Ndiyo hii?" Akauliza Lee akimwonyeshea simu Alphonce aliyekuwa amefungwa kamba kitini. Walikuwa ndani ya chumba kidogo ndani ya makazi ya Lee. Kulikuwa kimya sana, kama si maongezi haya ungeliweza dhani hapana mtu.



    "Ndiyo yenyewe!" Alphonce akajibu kwa kiburi. "Nifungilie basi niende!"



    "Bado sijamalizana na wewe," Lee akananga akitikisa kichwa. Akaketi na kumuuliza Alphonce:



    "Niambie ni nani aliyekuwa anawasiliana naye?"



    "Mzee!" Alphonce akaita. "Hilo mimi silijui. Kazi yangu ilikuwa ni kutafuta hiyo simu tu!"



    Kabla Lee hajaongeza kauli ujumbe ukaingia kwenye ile simu, haraka akatazama. Ilikuwa ni barua pepe toka kwa mtu aliyetunzwa kwa jina la Chen Zi. Lee akalazimika kufungua barua hiyo na kuitazama.



    Akajikuta moyo unapiga fundo kubwa! Gibum! Alafu ukaanza kukimbia mbio! Mbio! Mbio!



    Asiamini macho yake, aliona nyaraka ile, anayoipambania iwe siri, ikiwa imeshatumwa kwenye historia ya maongezi. Na huyu bwana Chen Zi alikuwa yupo huko Hong Kong, China!



    Akahisi kuishiwa nguvu. Akapiga moyo konde na kusoma maongezi ya barua pepe ile mwanzo mpaka mwisho. Alipomaliza, akaiweka simu chini akisaga meno. Alipandwa na hasira mno. Alikunja ngumi yake kubwa akifuma ndita.



    Akamtazama Alphonce kwa hasira, na mara akanyanyuka na kuchomoa bunduki yake akamuwekea kwenye paji la uso. Hakusema kitu, macho yake yalikuwa tayari mekundu. Akabinua mdomo na kufyatua kitufe cha bunduki!



    Klick! Hakuna kitu. Klick! Klick! Klick! Hamna kitu, risasi zilikuwa zimeisha. Kwa hasira akaitupia bunduki mbali Alphonce akishusha pumzi ndefu ya neema.



    Akatoka ndani ya chumba na kwenda kuketi sebuleni akiwa ametingwa na mawazo lukuki. Aliwaza, je kuna haja ya kumshirikisha Sheng kwenye mkasa huu?



    Vipi kama Sheng akijua hizi habari, ambazo amejitahidi kuziweka chini ya kapeti akashindwa, atafanya nini na atamfanya nini?



    Akajikuta akitetemeka mikono.





    Kama kuna usiku ambao uliwahi kuwa mgumu kwake, basi ni huu. Hakupata usingizi kabisa. Kichwa chake kilikuwa kinatepeta mawazo. Alijazwa na hofu moyoni.



    Baada ya kufikiria kwa muda, aliona kuna haja ya kushirikisha wenzake, pengine wanaweza kumpatia mawazo mbadala maana aliona kichwa chake hakifanyi kazi tena.



    Akawatafuta kwa kuwapigia simu lakini hakuwapata. Pengine walikuwa wamepumzika vitandani mwao. Akaona afanye kazi hiyo asubuhi na mapema, japo kishingo upande maana aliona kama anapoteza muda.



    Akaendelea kugaragara kitandani, akaichukua ile simu na kuitazama tena. Akapitia zile jumbe za barua pepe kati ya Foang na Chen Zi. Akahisi moyo wampasuka.



    Alitamani kurudisha hali lakini haikuwa inawezekana. Akawaza sana kuhusu yule Chen Zi. Alikuwa ni nani, na kwanini Foang amtumie ujumbe kama mtu wa kwanza.



    Kwakuwa hakuwa na usingizi, akaona si mbaya akautumia muda wake huo kusaka taarifa za Chen Zi ndani ya mtandao.



    Akiwa amekodoa akatafuta jina hilo huku akiwa ameliambatanisha na Hong Kong, punde chache Chen Zi ikaja ikiwa na majibu kadha wa kadha, lakini haswa lililotamalaki lilikuwa ni jina la Chen Zi aliyetambulishwa kama msanii maarufu wa miondoko ya pop nchini China, Hong Kong.



    Lee akafuatilia taarifa za msanii huyo akiwa ameshavunjika moyo kuwa si mtu anayemhitaji. Na kama haitoshi, alipochekechua taarifa za mtu huyo akaja gundua Chen Zi alikwishafariki, tena mwaka jana kwa kuzidisha dozi ya madawa ya kulevya!



    *"CHEN ZI 'THE ROCKER' DOPPED TILL DEATH" (CHEN ZI 'MTUMBUIZAJI' AMEZIDISHA DAWA MPAKA KIFO)*



    Mojawapo ya kichwa cha habari kilisema vivyo. Akatazama na majibu mengine ya Chen Zi akapata kuona watu wa mitandaoni haswa Facebook. Akasonya na kutoka mtandaoni.



    Kitu alichotokea kuamini ni kuwa Chen Zi atakuwa si mtu maarufu mitandaoni. Akawaza sana asilale mpaka asubuhi. Akadhamiria kuwasiliana na Bigo ampe ushauri.



    ***



    Macho ya Jona yalikuja kufunguka akiwa kitandani. Amechoka na mwili ukiwa mzito. Akakohoa na kukunja shingo kutazama kando.



    Hakuelewa nani aliyemuweka hapo kitandani, alipatwa na hofu lakini mwili wake haukumruhusu kunyanyuka.



    Hakumwona mtu kwa muda wa dakika kama mbili. Hatimaye akamwona mwanaume akiingia, akakaza macho kumtazama akagundua ni Panky. Angalau akawa na amani.



    "Unaendeleaje?" Panky akamuuliza akitabasamu kwa mbali. "Ni kama bahati kuja hapa, nilikukuta chini ukiwa hujitambui."



    Jona akamshukuru kwa msaada wake. Akajitahidi sana kuketi wakati Panky akimuuliza nini kilijiri akawa kwenye hali ile. Kabla Jona hajamjibu, akamuuliza kwanza kama kuna habari yoyote kumhusu mheshimiwa Eliakimu.



    Panky akahamaki. Akatikisa kichwa chake na kuanza kueleza juu ya habari ya kuvamiwa na kuuawa kwa mheshimiwa huyo. Habari yake imesambaa jiji zima na kuzua taharuki.



    "Ninavyokuambia mpaka sasa, hakuna mtu aliyekamatwa."



    Jona akatulia kwanza. Alikuwa anawaza juu ya hayo aliyoambiwa akichambua kwanini mheshimiwa aliuawa. Na tena ndani ya muda mfupi tangu aondolewe pale.



    Kichwani akayapata majibu kuwa ahusikaye hapo si mwingine bali wale waliomteka Nade. Kutoonekana kwa mke wa mheshimiwa, kulithibitisha mawazo yake hayo.



    Baada ya muda mfupi wa kuwaza, kwa akili yake timamu, Jona akamwambia Panky kuwa anahitaji kurejea jeshini. Panky akashangazwa na maamuzi hayo, lakini Jona akajitetea kuwa hiyo ndiyo njia sahihi ya kukamilisha anachokitaka.



    "Panky, nahitaji covering. Nahitaji authority kwenye mikono yangu. Nahisi kuna haja ya kurejea kukamilisha mambo kadhaa."



    Aliposema hayo akaendelea kuwaza. Panky akamhitaji apumzike kwani amechoka sana. Lakini kabla ya kupumzika, Jona akamuuliza kuhusu ile picha. Ni wapi amefikia.



    Panky akatabasamu kwanza kabla hajajibu. Akamshika Jona bega na kumweleza kuwa hicho ndicho kilimleta hapo. Na anashukuru kwa maana kama asingelikuja basi angelimpoteza.



    "Nimeshapata zile code. Huwezi amini! Na mpaka sasa nashawishika kuamini kuwa ile picha ni siri kubwa ya Sheng! Si bure alikuwa anaitafuta."



    Panky alisema kwamba Marwa ndiye aliyemsaidia kung'amua code za picha hiyo baada ya kumshawishi sana na kumuahidi usalama wake kwa gharama yoyote ile. Akampatia "x-ray pictures" ambazo alimtaka azihifadhi sana, akiwa ameziiba toka kwenye tarakilishi ya 'administator' wa kitengo chao.



    "Ni kwanini Marwa amekuamini kiasi hicho?" Jona akataka kujua.



    "Marwa, ni zaidi yangu. Ni mjuzi wa mambo makubwa sana na ni mtaalamu sana wa mambo haya, lakini hafanyi kazi ile kwa kupenda bali kulazimishwa. Kila mwisho wa mwezi, mbali na kulipwa pesa, hupewa 'antidote' kwa ajili ya kuwapatia wazazi wake ambao walidungwa sindano na Sheng.



    Kama Sheng asipompatia antidote hiyo wazazi wake hawatachukua hata dakika tano, watafariki dunia!"



    Jona akasisimkwa na hiyo simulizi. Akatamani hata kuonana na Marwa, lakini Panky akamwambia watalifanya hilo taratibu mbeleni kwani hakumwambia Marwa juu yake.



    "Nilichomwambia ni kwamba hii inaweza ikawa namna ya sisi kujikomboa. Kama unavyojua, hatukuwa na muda mrefu sana wa kuteta. Tunapokuwa kazini huwa tunatazamwa kila saa."



    Baada ya maongezi hayo machache, Panky akamwachia Jona bahasha ya kaki ambayo ilikuwa na taarifa zile alizomweleza. Akamwambia anapaswa kwenda kwani kuna mahali anatakiwa kupitia.





    ***



    Saa kumi na moja jioni, Monduli, Arusha.



    "Anapoelekea, atakufa," Roba alisema akiketi chini. Akamtazama Nyokaa aliyekuwa anavuta bangi akitazama zake bustani. Ni ndani ya nyumba ya wastani yenye bati la bluu.



    "Amekula?" Nyokaa akauliza.



    "Hajala, analia tu anataka unga," Roba akajibu kisha akapokea kipisi cha bangi toka kwa Nyokaa naye akawa anakipiga pafu.



    Wakawa wanateta juu ya Miriam - mke wa mheshimiwa. Mwanamke huyo alikuwa hoi chumbani akiwa hataki kula wala kunywa chochote isipokuwa heroine. Amekuwa akitetemeka mwili na kuharisha.



    "Unadhani ni muda wa kuachana naye sasa?" Akauliza Roba.



    Nyokaa akatikisa kichwa chake akikakataa. Akasema hata kama kazi yake ya kuwachomesha 'ma-broker' wa madini, ambao ni majamaa wa Eliakimu imeshafanyika, bado wanamhitaji mwanamke huyo. Watamtumia hata kujaribishia madawa.



    "Akifa tutamtupia huko mtoni!" Akahitimisha Nyokaa kabla ya kumuuliza Roba juu ya kazi yake aliyoifanya kwa mheshimiwa.



    "Vipi yule manzi? Bado hujasikia habari yake?"



    "Bado, sijasikia. Nadhani atakuwa amekufa tu," Roba akajibu kisha akavuta pafu moja.



    "Roba, yule mwanamke haikupasa umuache hai kabisa. Siwezi nikakaa kwa amani chali'angu. Anaweza akatuchoma."



    Nyokaa akataka Roba amtafute Nade na kuhakikisha anakufa kwa njia yoyote ile. Mara ya mwisho alisikia amelazwa Aga khan kwa mujibu wa vyanzo vyake vya habari.



    Alipomsisitizia hilo, akanyanyuka kwenda kumuona Miriam. Akamkuta akiwa amejikunyata. Nywele zake zilikuwa vurugu mwili wake aliokunyata ukiwa ndani ya dera la njano.



    "Miriam, mbona hutaki kula?" Akauliza akichuchumaa. Miriam hakujibu zaidi ya kumtazama kwa jicho la husda.



    "Inabidi ule, sawa?" Nyokaa akamshika Miriam. Mara Miriam akaanza kububujikwa na machozi yasiyo na kikomo. Kifuani mwake alikuwa anaumia. Maisha yake yalikuwa yameharibika na hakuwa na namna tena kuyarejesha kama hapo awali.



    Leo amekuwa mtu wa kuvuta unga! Pua yake haikuwa kawaida asipotia kitu hicho mwilini. Amekuwa mdhoofu na asiyevutia tena. Zaidi ya yote, mwanaume aliyemuingiza huko akiwa ni yule aliyempenda na kumtumaini.



    "Nyokaa," akaita kwa sauti ya chini, kisha akasema:



    "Sitakusahau maishani mwangu. Na Mungu wangu aliye juu atakulipia."



    Nyokaa hakujali hayo maneno. Kwake hilo lilikuwa ni dua la kuku kwa mwewe. Akatabasamu na kunyanyuka akisema:



    "Utakapojisikia kula, utasema sawa? Sina muda wa ngonjera hapa." Kisha akaondoka zake akimwacha Miriam akiendelea kumwaga machozi akimshuhudia mwanaume huyo akiyoyoma.





    ***





    Saa nne asubuhi, ofisini kwa Kamanda wa mkoa.



    "Mkuu, una ugeni," alisema mwanaume mkakamavu ndani ya sare ya jeshi la polisi. Kamanda pasipo kumtazama, akamtikisia kichwa kama ishara huku macho yake yakiwa yameganda kwenye gazeti la MAMBOSASA alilolijaza mkononi.



    Punde kidogo, Kamanda akasikia sauti ikimsalimu. Sauti hii ikamfanya abandue macho yake gazetini na kumtazama mgeni huyo nje ya miwani yake ya kusomea. Akastaajabu ni yule mwanaume aliyekuwa anamtafuta.



    "Ooh Jona! Karibu sana!"



    Jona akashukuru na kuketi. Wakasalimiana, Kamanda akijawa na tabasamu. Lakini haikuchukua muda kwa Kamanda kujua kuwa Jona hakuwa sawa kiafya.



    "Vipi, upo sawa?" Akauliza. Jona akalazimisha tabasamu akijibu:



    "Nipo sawa." Kisha akaeleza haja yake iliyomleta pale pasipo kupoteza muda. Kuwa anataka kurejea kwenye jeshi kama alivyokuwa akisisitiziwa.



    Kamanda akastaajabu kwanza kabla ya kulipuka kwa cheko la furaha. Kwake hizi habari zilikuwa za kufurahisha ambazo hakuzitarajia kabisa! Hatimaye mbuyu ulikuwa umeangushwa chini.



    Akamkabidhi Jona mkono wa pongezi na kusifia maamuzi yake hayo.



    "Hapo sasa, umeamua kiume, Jona!"



    Lakini pia akataka kujua sababu iliyomfanya Jona arejee jeshini ingali alipingana na hoja hiyo kwa muda mrefu.



    "Nimerudi kumalizia kazi zangu nilizoziacha kiporo," hilo likawa jibu la Jona kabla Kamanda hajampatia tena mkono na kumuahidi ushirikiano kwenye kutimiza adhma yake hiyo.



    "We unaweza kwenda sasa, kesho ukarejea hapa majira ya asubuhi. Kuna mambo machache yanipasa kuyakamilisha ili kuweka vitu sawa," alisema Kamanda. Jona akaenda zake.



    Kabla ya kurejea gazetini, Kamanda akatambaliwa na mawazo kichwani. Akalaza kichwa chake kwenye kiti akizunguka kwenda kushoto na kulia huku akitafakari jambo lile la Jona.



    Ingawa alifurahishwa nalo, lilimpatia walakini kwa kiasi chake. Ni 'kiporo' gani hicho Jona anachotaka kuja kumalizia ndani ya jeshi?



    Pengine akawaza Jona atakuwa ameng'amua hila zake za kumtesa ili arejee jeshini na hivyo basi amekuja kumuadhibu? Akawaza. Alitamani sana kufahamu nyuma ya 'kiporo' cha Jona, na basi kujiweka salama kwenye bandari hii, akaona ni vema kumtaarifu Alphonce. Wanatakiwa kuwa makini na nyendo za Jona. Lakini mwanaume huyo hakuwa anapatikana tokea jana yake alivyomuita ofisini!



    Basi akajikuta hana namna zaidi ya kungoja akiwa amedhamiria kama leo hatomwona Alphonce, inabidi juhudi za makusudi zifanyike kumtafuta.



    Akashika gazeti lake, lakini kabla hajaanza kulisoma, akasikia mtu akiingia.



    "Samahani sana, mkuu!" Alikuwa ni Alphonce! Alikuwa amevalia suti rangi ya kahawia, koti limemzidi kipimo. Akasimama kwa ukakamavu kutoa salamu kisha akaketi.



    Kabla ya kuulizwa, akaanza kujitetea kwa Kamanda ni kwanini alishindwa kutimiza agizo lake la kufika ofisini jana yake.



    "Nilipata ajali, mkuu. Sikuwa na uwezo wa kuwasiliana nawe pia kwani simu yangu iliibiwa."



    Kamanda hakuwa na muda wa kupeleleza maelezo hayo ya Alphonce, donge lilikuwa limemkaba shingoni kungoja, akamwambia kuhusu habari za Jona kurejea jeshini.



    "Nimekutana naye huko nje, nikastaajabu kufika kwake hapa," Alphonce akateta akitabasamu.



    "Amekuona?" Kamanda akauliza.



    "Yah! Tumesalimiana tu kila mtu akaenda zake."



    Kamanda akavuta kwanza pumzi akiweka kituo. Alafu akamwambia Alphonce juu ya hofu yake.



    "Unadhani mkono wake utatuacha salama?"



    Alphonce akaangua kicheko. Hakuona sababu ya kuhofia. Akamwambia Kamanda wake kama Jona angekuwa anataka kuwamaliza wala hakuwa na sababu ya kurudi jeshini kwani angeweza kutimiza haja yake hiyo hata huko nje.



    "Tujipongeze maana hila zetu zimefanikiwa," akasema Alphonce na kuongezea: "ametambua kuwa maisha yake hayawezi kuwa sawa akiwa nje ya jeshi."



    Lakini bado Kamanda hakujiona mjinga. Bado aliona kuna haja ya kumtazama Jona kwa darubini ya pekee hivyo akamuagiza Alphonce kutenda hilo.



    Alphonce aliyekuwa hana shaka akalipokea hilo jukumu.



    ... lakini hakujua uzito wake kamili.





    ---





    Akiwa ndani ya daladala kurudi kwenye makazi yake, Jona aliyekuwa ameketi kwenye viti vya nyuma kabisa, alikuwa anawaza juu ya kile alichokiona kule ofisini.



    Macho yake yalikuwa nje ya gari lakini ndani ya mawazo. Kichwani kwake taswira ya gari aina ya Prado nyeusi ilikuwa inamjia. Gari lililomwagia risasi nyingi akiwa anaelekea nyumbani kwa Eliakimu ndani ya taksi.



    Mbona ameliona gari hilo pale ofisini kwa Kamanda? Akakumbuka pia na taswira ya mwanaume anayemtambua akishuka toka kwenye gari hilo. Alikuwa amevalia suti kubwa ya kahawia - suti inayofanana na ya yule aliyeambiwa na shuhuda kuwa ndiye muuaji wa Jumanne, mshirika wake kwenye biashara ya kuchora na kuuza picha!



    Taswira hizo mbili zikamnyima raha. Zikampa ukweli mchungu kuwa Kamanda anahusika na jaribio lake la kumuua, vilevile la kuharibu biashara yake. Haswa kwanini?



    Akakumbuka kauli aliyoambiwa na Kamanda kwa mara ya mwisho alipoonana naye ofisini kwake. MAISHA YAKE KAMWE HAYATAKUWA SAWA NJE YA JESHI. Hatomtafuta tena, bali ni yeye atakayemtafuta.



    Akashtuliwa na kondakta akidai nauli. Akatoa nauli hiyo na muda si mrefu akashuka toka chomboni, akishkuru kondakta kumshtua kwani hakuwa anafahamu kama alikaribia, kisa mawazo.





    "Umeshampatia chakula?" Akauliza Nyokaa akiwa anamtazama kijakazi wake - mwanaume mrefu mweusi aliyevalia nguo iliyombana kifua chake kipana.



    "Bado, mkuu!" Akajibu kijakazi kwa ukakamavu.



    Nyokaa akamtazama kwa ukali na kufoka kwanini kijakazi huyo hajampatia Miriam chakula mpaka muda huo? Kijakazi akajibu kwa unyenyekevu kuwa mwanamke huyo hali hata pale anapompatia.



    "Kutokula siyo kazi yako, bali kumpatia chakula!" Nyokaa akafoka na kumtaka mwanaume huyo haraka iwezekanavyo kwenda kumpatia Miriam chakula, naye akaenda pasipo kupoteza muda.



    Nyokaa akisonya, akaketi chini na kumpigia simu Roba.



    Roba alikuwa yupo Dar es salaam. Kazi yake kama alivyoagizwa ilikuwa ni kumtafuta na kumuangamiza Nade ili kumaliza chembe ya ushahidi iliyobakia. Punde simu ilipokelewa, Nyokaa akaulizia ni wapi Roba amefikia.



    "Nimeshafika hospitali. Ni kitendo cha muda tu kumaliza kazi."



    Nyokaa akamwambia afanikishe hilo upesi arudi Monduli kwani kuna kazi za kufanya. Roba akamuahidi ushindi.



    Alipokata simu, Roba akashusha pumzi na kutazama hospitali iliyokuwa imesimama mbele yake. Alikuwa ndani ya taksi, akalipa pesa ya nauli kisha akashuka.



    Mwanaume huyu alikuwa amevalia tisheti nyeusi yenye alama ya fuvu jeupe, na chini akijisitiri na suruali ya jeans na moka nyeusi.



    Alikuwa na muda mchache wa kumalizana na kazi yake hapo. Alizama ndani ya hospitali na ndani ya muda mfupi akawa ameshafika stoo ya hospitali.



    Mwendo wake akifanya kitu moja kwa moja kilithibitisha kwamba ana ramani ya hospitali kichwani mwake, na alishapanga jambo hilo mapema kichwani mwake.



    Ndani ya muda mfupi, akawa ameshavalia koti jeupe la daktari, shingoni amezungushia kipima mapigo ya moyo, akiwa anatembea kwa kujiamini.



    Akaelekea kwenye wodi za gharama, zikiwa zimegawanywa kwa vyumba vyumba vya wagonjwa binafsi.



    Akafungua mlango wa chumba cha kwanza kabisa kukutana nacho, akazama ndani na kumkuta Nade akiwa amejilaza anasaidiwa na mashine kupumua.



    Akahakikisha mlango umefungwa vema, alafu akachomoa sindano yenye kimiminika rangi ya 'green' na kukidungia ndani ya mfuko wa dripu. Haraka alipofanya hivyo, akatoka ndani ya chumba hicho na kupotea!



    Baada ya muda wa kama dakika kumi, dripu ile ikaishilia mwilini mwa Nade. Zikapita dakika kama tano, mwili wa Nade ukaanza kubadili rangi kuwa wa njano!



    ***





    "Tayari, nimeshakamilisha!" Sauti ya Roba ikavuma kwa simu.



    "Sawa sawa. Rudi sasa nyumbani na ndege ya jioni," Nyokaa akanena na kisha akakata simu kabla hajaja kupokelewa na sauti ya kupaza ya kijakaziwe.



    "Mkuu, yule mwanamke ametoroka!"



    "Mwanamke?" Akastaajabu Nyokaa. "Mwanamke yupi?" Akawahi kuuliza akisimama upesi toka kwenye kiti chake cha kuvinjari.



    Kijakazi akasema ni Miriam. Nyokaa kwa hasira akakimbia mpaka kule Miriam alipokuwa amehifadhiwa, hakumkuta!



    Akalalama na kutusi. Akaamuru Miriam atafutwe akitishia hakuna mtu atakayebaki hai kama asiporudi na mwanamke huyo.



    Wanaume wakazagaa kumtafuta 'teja' huyo kwa udi na uvumba.





    ***



    Saa kumi na mbili jioni.





    "Ameshafika!" Miranda alisema kwa tabasamu pana akiangaza getini. Alikuwa ndani ya nyumba ya BC kwa juu kabisa akiwa anaangaza kama atamwona mgeni wake akiwa anakuja.



    Alikuwa amependeza kwa kuvalia gauni safi linalometameta dhidi ya giza jepesi la jioni. Nywele zake zilikuwa zimerembwa na uso wake ameupara.



    Alikuwa ana hamu sana ya kumwona Boka. Alipoona gari la mwanaume huyo likiwa limefika, moyo wake ukawa wa baridi kwani 'alishampanga' BC vya kutosha.



    Boka anakuja kama alivyomuahidi.



    "He is here!" (Yupo hapa!) Rhoda alimwambia BC aliyekuwa ameketi kwenye kiti cha kaunta ndani ya nyumba yake akiwa anakunywa wiski.



    BC naye kwa kujiandaa na kikao na Boka, alikuwa 'amekula' suti nyekundu na tai nyeusi. Japokuwa kupendeza ni kawaida yake, leo alikuwa zaidi.



    Alimtaka Miranda akampokee mgeni na baada ya utambulisho aende ndani, kila kitu atakifanya yeye.



    "Are you sure you won't need me?" (Una uhakika hautonihitaji?) Miranda aliuliza kabla BC hajamtikisia kichwa kama ishara ya ndio. Miranda akaendaze.



    Lakini kwa kutaka kujua kitakachoongeleka, akajibana mahali ambapo angepata kusikia maongezi.



    "Glad to see you. My daughter's been telling me about you," (Nimefurahi kukuona. Binti yangu amekuwa akiniambia kuhusu wewe,) alisema BC kwa tabasamu akimpatia mkono Boka.



    Wakateta kwa muda kidogo kupeana historia juu ya wapi walikutana na kuanza kutengeneza mahusiano na Miranda. Baada ya hapo BC akaenda kwenye kitovu cha kikao.



    Pasipo kupepesa macho akamuuliza Boka kama kweli yu radhi kuwa na Miranda. Boka akakubali kwa kuwahi kujibu. Lakini BC akarudia kumuuliza mara tatu kabla ya kumwambia:



    "Then there is a little sacrifice you have to make." (Basi kuna sadaka ndogo ya kutoa.)



    Boka akasimamisha masikio yake asikie. BC akamweleza kuhusu biashara yake, akihitaji msaada wa mheshimiwa huyo kuingiza 'madawa' yake nchini.



    Kwa mara ya kwanza Boka akadhani ni madawa ya kulevya. Moyo wake ukaenda mbio mno kabla hajapata angalau ahueni baada ya BC kumwambia ni madawa ya kutibia binadamu.



    "Where are you taking them to?" (Unayepeleka wapi?) Akauliza Boka. BC akamwambia yeye hufanya biashara ya kuuza hayo madawa huko Msumbiji, Zambia na Zimbabwe kwa bei ya juu.



    Lakini Boka alikuwa na hofu na hakuweza kutoa jibu la moja kwa moja kabisa kwa BC. Hata mikono yake ilikuwa inatetemeka akashindwa kubebelea kinywaji. Akaomba aende zake.



    "So what about it?" (Kwahiyo vipi?) BC akauliza. Boka akabanwa na kigugumizi. Akaomba apewe muda kwani jambo hilo ni zito mno. Si la kulichukulia kiurahisi hata kidogo.



    Hakumkubuka hata Miranda, akaenda zake akijawa na mawazo kedekede kichwani.



    "Do you think it will work?" (Unadhani itawezekana?) Miranda akamuuliza BC akiketi.



    "I don't know. Let's see!" (Sijui. Acha tuone!) BC akajibu alafu akashushia na wiski.



    Boka akafika nyumbani akiwa ametingwa na mawazo hata mkewe akafahamu japokuwa hakuwa radhi kumwambia nini kimemsibu.



    Akajilaza akiukosa usingizi akiwaza nini afanye. Katikati ya usiku akapokea ujumbe kwenye simu. Mkewe akawa wa kwanza kuinyaka simu.





    Moyo wa Boka ulikuwa unapiga mafundo makubwa makubwa pindi mkewe alipokuwa anatazama simu yake. Aliwaza atakuwa ni nani amemtumia ujumbe, na kwa haraka akili yake ikaegemea kwa BC.



    Hakutaka mkewe ajue kinachoendelea kati yake na mwanaume huyo, sasa akadhani siri yao imeingia mchanga.



    "Ni nani huyu?" Akauliza mwanamke akimkabidhi simu Boka. Boka akaipokea na kutazama, akajikuta anashusha pumzi ndefu baada ya kugundua si kile alichokuwa anakiwaza.



    Alikuwa ni mfanyakazi mwenzake akimsihi kesho awahi kazini wapate kupangilia mambo ya kikao.



    Lakini haikupita muda, simu yake ikaingia ujumbe. Ilikuwa ni bahati yake kwani kwa sasa ujumbe ulikuwa umetokea kwa Miranda na simu ikiwa kiganjani mwake.



    Kwa muda kidogo akachat na Miranda, muda huo mkewe akiwa anadhani anachati na rafiki yake.



    Mwanamke huyo, Miranda, alikuwa anamjulia hali na akimtaka amwambie ni wapi amefikia kwenye maongezi na 'baba mkwe' wake bwana BC.



    Pasipo kusita, Boka akaonyesha hofu yake juu ya kile alichoambiwa na 'mkwewe' lakini kwa wakati huo akijitahidi kumwonyesha Miranda kuwa anampenda na si kwamba hafanyi jitihada.



    Naye Miranda kwa maringo, akiwa anajua kidonda kipo wapi, akafanya kumtia hamasa Boka kwamba anataka kuwa naye kwa hali na mali.



    "Tafadhali, fanya juu chini mpenzi. Tusiishie njiani."



    Boka akiwa ameshikwa na kigugumizi cha vidole akamwomba ampatie muda kidogo. Na pia mazingira hayakuwa mazuri kuteta kwani mkewe anaweza kumpoka simu muda si mrefu.



    Hivyo, wakakata maongezi. Tena baada ya Miranda kumtumia mwanaume huyo maneno matamu ya kumpa moyo. Na kisha bwana Boka kufuta chati zao za kidhalimu.



    Akaweka simu kando na kumtazama mkewe, alikuwa amelala. Akashusha pumzi ndefu na kutazama paa. Hakujua ni muda gani usingizi ulimnyakua.





    ***





    Saa mbili asubuhi, ofisi ya kamanda polisi mkoa...





    Hodi ndogo iliita kisha ikaruhusiwa kuingia ndani. Alikuwa ni Jona akiwa amevalia suti rangi ya udongo, aliketi kisha akamsalimu kamanda.



    "Naona umefika on time!" Kamanda akasema akitabasamu. Pasipo kupoteza muda akanyanyuka na kwenda kabatini alipotoa kiboksi cha chuma alichokiweka mezani na kukifungua, alafu akamsogezea Jona.



    Ndaniye kulikuwa kuna vitu ambavyo Jona alivikabidhi siku alipoacha kazi.



    "Tulijua utarejea, shida hatukujua ni siku gani haswa," alisema Kamanda akiketi. Akamwambia Jona kuwa kila kitu kipo sawa, na haikuwa shida sana kwani hakuwa amemuondoa kwenye orodha ya watumishi wake, na siku zote hizo alikuwa akihesabu kama anaumwa.



    Lakini kabla ya kuendelea na majukumu yake, Kamanda akamsihi Jona kwamba kila atakachokuwa anafanya hatakuwa na budi kueleza kwa mkubwa wake.



    Naye hakuwa mwingine bali Alphonce!



    Jona akastaajabishwa na hilo, lakini hakuweka bayana. Alifahamu fika, yeye na Alphonce walikuwa sawa kwa cheo, iweje awe chini yake?



    Kabla hajanyanyuka, Kamanda akamwambia kuna kazi kedekede za kuzifanya tangu uongozi mpya uingie madarakani. Wamekuwa wakihofia usalama wa nchi kutokana na kulegalega kwa mahusiano ya kidiplomasia na nchi jirani, kwahiyo atakuwa akisafiri mara kwa mara, haswa mikoa ya mipakani, ajiandae kwa hilo.



    "Unajua mimi ni kama daraja tu la kukufikia wewe ... unahitajika nchi nzima, na kila mtu ndani ya jeshi anatambua mchango wako. Wanategemea makubwa kutoka kwako."



    Baada ya maongezi hayo, Jona akanyanyuka na kwenda zake. Huku nyuma Kamanda akapiga simu na kumtonya Alphonce yaliyoendelea.



    Jona alienda kantini akaketi hapo akinywa kikombe cha chai taratibu, akiwaza. Alikuwa aking'amua na kupanga nini aanze kufanya sasa kati ya yale yaliyomrejesha jeshini.



    Akaona ni busara akifanya kazi ya mikono misafi kwanza, kisha akamalizana na ile itakayomchafua. Aanze kwanza na maadui wa nje, alafu atarudi nyumbani.



    Akiwa hapo anakunywa chai kusindikizia mawazo, akaona gari lile prado nyeusi ikiingia. Kwa macho yake thabiti akafuatilia lile gari, akamwona Alphonce akishuka, amevalia koti refu jeusi akaangaza na kuzama ndani.



    Kifuani mwake alikuwa ana jambo la wazi linalomkereketa kumhusu huyu mwanaume. Aliamini siku yake itafika na atajaa mikononi mwake, akiomba msamaha abakiziwe roho yake.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya Alphonce kupotea, Jona akarejea kwenye mawazo yake ya awali. Akalipia chai na kutoka ndani ya eneo lile la ofisi ya Kamanda, akaelekea Aga Khan hospital kwa lengo la kuonana na Nade.



    Alishapata taarifa kuwa mwanamke huyo yupo huko akiwa hajifahamu tangu tukio la mauaji ya Mheshimiwa lipate kutokea. Alikuwa ana machache ya kuongea naye.



    Akawaza sana kwanini mwanamke huyo alimgeuka ilhali alimsaidia dhidi ya mikono ya mbwa mwitu wasio na huruma. Ilikuwaje upesi wakamgeuka na kulenga kumuua?



    Akakiri na moyo wake kwamba kuna kitu kikubwa ambacho hawakutaka kabisa akifahamu. Na sasa Mheshimiwa ameenda na siri yake kifuani.



    Kama Nade asipokuwa hai, basi hakutakua na masalia yoyote sasa.



    Aliomba Mungu amkute kama alivyodhamiria.



    Akawasili hospitali na basi kwa kutumia kitambulisho chake akapata mwanya wa kumfikia daktari aliyekuwa anahusika ma mlengwa wake.



    Daktari huyu alikuwa mwanaume mnene mwenye asili ya India. Alimtazama kwanza Jona kisha akamwambia ana bahati sana, kwani mgonjwa alikuwa amepitia tundu la sindano kubaki kuwa hai.



    "Alizidiwa?" Jona akataka kujua.



    "Hapana!" Daktari akatikisa kichwa. "Aliwekewa sumu kwenye dripu!"



    Wakati huo walikuwa wanatembea kwenda kumwona Nade.



    "Nani alimtilia sumu?"



    "Hakuna anayejua. Ila kuna videos za CCTV zilizomuonyesha mtu huyo ambaye hatujamtambua mpaka sasa."



    Wakafika kwa mgonjwa, Jona akamtazama kwa ukaribu. Alikuwa ana rangi ya njano kwa mbali ngozini, anahema kwa msaada wa mashine na kucha zake zilikuwa zina michirizi meusi.





    "Kama tungekawia hata kwa sekunde tatu, asingekuwa hai!" Daktari akasema kwa kujiamini.



    Jona akamwomba ampeleke akaone hizo video za CCTV.



    Pasipo kusita daktari akamuongoza mpaka mahala pa kutazamia video alipowakuta wanaume wawili waliomsalimia na kumsaidia kuiona video aitakayo.



    Alipotazama vema, akajikuta anatabasamu mwenyewe na kujisemea kifuani.



    "Nilijua tu," baada ya kumwona Roba akiwa anatoka ndani ya chumba.



    Sasa alikuwa amethibitisha aliyeshiriki tendo la kumuua Nade ni Roba, yaani Nyokaa. Na wao pasipo shaka ndiyo ambao walifanya tukio lile la kumuua Mheshimiwa Eliakimu!



    Akapata mawazo sana alipokuwa hapo. Mosi, wapi Miriam atakuwapo? Wanamfanyia nini na kwanini hao wanaume wanamhitaji kiasi hicho? Pili, wanahusika na biashara gani haswa?



    Akajikuta ana kazi ya kwenda tena kule alipomuokolea Nade akawakute wanaume hao. Lakini pia apate mwanya wa kuonana na Nade, akipata ahueni, ili apate kumweleza anachokijua.



    Akashusha pumzi ndefu kisha akaandikisha baadhi ya maelezo na kwenda zake baada ya kuahidi atarejea. Lakini akasihi juu ya usalama wa Nade, kwa upande wake atahakikisha anapatikana askari wa kuja kumlinda.



    Akatoka ndani ya hospitali na kuangaza magari yakikatiza, akaweka mikono mfukoni na kuambaa akifuata kituo cha magari.



    Lakini kuna mtu alikuwa anamtazama. Mtu huyu alikuwa amevalia koti refu na kofia ya kizee iliyomeza kichwa chake.



    Baada ya Jona kusonga umbali wa kutosha toka hospitali, mtu huyu akatoka alipokuwa amejibanzia, mstimu, kisha akazama ndani ya hospitali akitembea kwa tahadhari.



    Mwanaume huyu alikuwa ni Alphonce!



    Kazi yake hapa ilikuwa moja tu, kujua nini Jona amekuja kufanya hapo? Ndani ya muda mfupi, akitumia nafasi yake, akawa amefika mbele ya kitanda cha Nade akimtazama mwanamke huyo kama mtu aliyemfananisha.



    Kichwani kwake alikuwa anafikiria mambo kadhaa. Alisonya alafu akatoka kuongea na daktari.



    "Kuna kingine?"



    "Hapana, yote tumeshaeleza kwa askari aliyekuja awali."



    "Nataka unieleze na mimi pia hayo yote!" Akaamuru Alphonce. Basi ikambidi Daktari arejelee yale aliyomwambia Jona, na tena zaidi kwani Alphonce alikuwa anataka kila ambacho Jona alikifanya.



    Alipomaliza akatoka zake ndani mpaka kwenye gari lake alipotulia na kupiga simu kwa Kamanda akampa taarifa.



    "Sijajua, ila bado wanamuwinda kumuua!"



    "Na picha umeiona?" Akauliza Kamanda.



    "Ndio, ila sura ni ngeni. Bila shaka ndiyo hao hao waliomuua Eli! ... kuna haja ya kuifuatilia?"



    "Hapana! Anayejua ya kesi hii kwa undani ni Jona. Kuna vitu anavifahamu kuliko sisi, na kama alikuja huko ina maana ameamua kuivalia njuga. Mwache aendelee nayo, cha muhimu ni kumfuatilia tu!"



    Alipokata simu, akakanyaga mafuta na kuyoyoma toka eneoni.



    Ambacho hakukijua ni kwamba, hata wakati anatoka, Jona alikuwa anamuona! Alimwona tangu anaingia ndani ya hospitali na hata pale alipotoka!



    Ni vile alikuwa anajua kwamba atafuatiliwa.



    Akatikisa kichwa chake akibinua mdomo. Gari la Alphonce lilikuwa linaishia machoni. Akakuna kidevu chake na kushusha pumzi ndefu, kisha akajikuta anatabasamu.



    "Keep your friends close, but your enemy closer!" (Waweke marafiki zako karibu, lakini maadui karibu zaidi!) Jona alijisemea kisha akanyanyua mguu kuchukua hatua.





    ***





    "Ameamka!" Mtoto mdogo wa kike alimwambia mama yake. Haraka mama akaamka na kukimbilia ndani kutazama.



    Ndani ya nyumba hii iliyochoka, kulikuwa kuna samani mbovu, mazingira yasiyovutia. Joto na pia kiza.



    Mwanamke huyu akiwa ameongozana na mtoto wake, walifika ndani ya chumba chao kimoja, wakatazama kitandani. Kulikuwa kuna mwanamke amejilaza hapo kitandani kana kwamba mtu asiyejiweza. Mwanamke huyu hakuwa anaonekana vema kwasababu ya giza. Dirisha lilikuwa moja tu, dogo, na limezibwa magazeti na majarida ya zamani.



    Mwanamke aliyeambatana na mwanae akawasha kibatari na kuangaza. Kumbe mwanamke aliyekuwa kitandani alikuwa ni Miriam!



    "Habari yako dada?" Akasalimu mwanamke mwenye nyumba akisogeza kibatari chake auone uso wa Miriam. Macho ya mwanamke huyu yalikuwa makubwa na yenye kujali. Miriam alikuwa anamtazama kwa mbali mdomo wake ukiwa wazi.



    "Habari yako dada? Naitwa Mili, wewe ni nani?"



    Akajitambulisha, kumbe anaitwa Mili. Alikuwa anamtazama Miriam kwa kina akitegemea kusikia lolote toka kwake karibuni. Lakini haikuwa hivyo, Miriam hakuweza kuongea.



    "Tulikukuta shambani kwetu ukiwa hujiwezi. Tungekupeleka hospitali lakini hatuna uwezo huo. Unaweza ukatuambia umetoka wapi? Wewe ni nani?" Akauliza Mili. Lakini Miriam hakuweza kutia neno. Alikuwa anasikia pia kuona lakini akishindwa kusema.



    Mili akakata tamaa. Akamtazama mwanaye na kumwambia inabidi wakatoe taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji. Alikuwa anahofia sasa yule mgeni anaweza kuwafia pale wakakosa la kusema.



    Haraka mtoto akaamka, lakini ghafla Miriam akaanza kuguguma kama mtu anayesikia maumivu huku akitoa ishara kwa kutikisa kichwa! Kwa tabu akamtaka Mili asifanye alivyoadhimia.



    "Msi ... en ... de ... pop...pote!" Akasema kisha akakusanya pumzi kwanza kana kwamba mwanariadha aliyekata utepe wa mwisho wa marathoni.



    Mili akamtaka mwanaye amletee viazi vilivyopo kwenye bakuli kabatini, akamlisha Miriam akimsindikizia na maji ya kunywa. Angalau Miriam akapata nguvu.



    Kwa taabu, akipambana na hisia za maumivu, na kwa ufupi akamweleza Mili wapi alipotokea na yeye ni nani kisha akawasisitizia Mili na mwanaye wasije wakamwambia yeyote juu yake.



    "Hapa ni mbali sana toka huko!" Akasema Mili. "Siku ya kwanza walikuja wanaume wawili hapa wakatuulizia kumhusu mwanamke mwenye sifa zako, lakini tulihofia, tukakanusha kukuona."



    Miriam akamuuliza kwanini alifanya hivyo. Mili akamjibu ni kwakuwa waliwaona wanaume hao wakiwa wameficha bunduki ndani ya nguo zao, wakafahamu si watu wema.



    "Hata jana mwanangu alipata kumwona mmoja wa wanaume wale akirandaranda na kuangaza huku na huko!" Akamalizia Mili, kisha akamtaka Miriam apumzike wataongea zaidi baadae.





    ****



    Alikitazama kioo akatabasamu mwenyewe. Sasa alijiona amependeza na anaweza kutoka. Akajiangalia tena mwili mzima, akajikubali na kujipa ruhusa. Akabeba mkoba wake na kisha akatoka ndani.



    Yalikuwa ni majira ya saa kumi na moja jioni. Jua lilikuwa limepoteza nguvu yake likionekana jekundu linaloadhimia kwenda zake na kuuacha ulimwengu kizani.



    Ndani ya jioni hii, Glady alikuwa ana mipango kadhaa ya kutekeleza na sehemu kadhaa za kwenda.



    Mwendo wake wa madaha na nguo yake ya nusu uchi, zilimfanya awe gumzo barabarani, lakini nani anajali? Sio Glady huyu! Hakuwa anaogopa macho ya watu hata kidogo. Alikuwa anafanya yale yanayopendezesha nafsi yake tu, mengine mtabaki nayo nyie.



    Kwa watu waliokuwa wanamfahamu kuwa anajiuza, hawakustaajabishwa naye, pengine walivutiwa. Glady alikata mitaa kwa hatua zake za maringo mpaka alipowasili mbele ya fremu iliyoandikwa;

    MSUGULI PHONE ACESSORIES



    Alipokutana na fundi, mwanaume mfupi mweusi mwenye nywele pilipili. Akamsalimu na kumuulizia kazi aliyompatia. Mwanaume huyo akatabasamu, kisha akauzamisha mkono wake kwenye kabati la kioo alipotoa simu kubwa nyeusi aliyomkabidhi Glady aipekue.



    "Yani nilimaliza kitambo sana, nikajua umeisusa!" akasema fundi.



    "Ili uiuze sio?" Glady akauliza akiifungua simu aliyokabidhiwa. Akazama kwenye menyu, ikakubali! Huko akakuta kila kitu. Basi akajikuta akitabasamu.



    "Safi sana! Aisee! ... yani nilikuwa siamini kabisa kama ungeweza!" Glady akalipuka kwa furaha.



    "Nilikuambia ni kitu kidogo sana hiko," fundi akajigamba. "Yani kufungua maloki ya simu ndo kazi yangu, chap tu mbona unafurahi mwenyewe na roho yako."



    Glady akatoa pesa kwenye mkoba wake, shilingi alfu kumi akamkabidhi fundi. Wakazoza kidogo kwani fundi alikuwa anataka zaidi kwa kazi alofanya. Glady akaishia kumwongezea alfu tano alafu akaenda zake.



    Njia nzima akawa anatabasamu mwenyewe. Hakuamini kama amefanikiwa kuifungua simu ile aliyoiiba toka kwa Alphonce. Aliona amefanya kazi kubwa na sasa anaweza akaitumia simu hiyo ambayo ipo juu kiteknolojia ukilinganisha na ya kwake.



    Akafika nyumbani na kujimwaga kitandani. Akafungua na kuanza kuipekua simu ya Alphonce, aone kama yaliyomo yamo. Cha kwanza kilikuwa ni kamera, akaridhika nayo, 'akajitwanga' picha kadhaa kabla hajaendelea na upekuzi wake.



    Akawasili sasa kwenye gallery ambako huko ndipo alichukua muda mrefu kuliko mahali pengine. Akatazama kila picha alizoziona huko. Ajabu ni kwamba, akakuta mpaka picha za watu anaowajua!



    Na picha hizi hazikuwa za kawaida, lah! Bali za uchi. Za wanawake mbalimbali, ikiwamo wengine wenye nyadhfa kubwa serikalini ama kwenye mashirika ya umma na yale ya binafsi!



    Kama haitoshi, akakumbana na picha kadhaa za watu waliouawa. Akaona mpaka picha ya Mustapha! Hapa sasa kifua chake kikaanza kukita kwa mapigo kasi ya moyo. Akaweka simu pembeni kwa hofu, akigongwa na mawazo kichwani.



    Ametoa wapi picha za watu hawa? Je, ameshiriki kwenye mauaji? Ni yeye ndiye alikuwa akimfuatilia Mustapha na hatimaye kumuua? Akawaza sana.



    Akaogopa mno kwanini alijihusisha na huyo mtu. Kama amewaua wote hao, je yeye atasalimika? Akajihisi joto, damu inakimbia kwa kasi.



    Lakini baadae akakumbuka kuwa mtu yule ni polisi. Naam! Aliona kitambulisho chake kwa macho yake kabisa. Inawezekana zile picha za wafu ni kwasababu za kipolisi? - yani za kipelelezi? Akawaza. Japokuwa hakupata jibu, lakini wazo hili lilisaidia kumshusha presha aliyokuwa ameitengeneza.



    Lakini vipi kuhusu hizi picha wanawake walio uchi? - nazo zafanya nini?



    Akaelekea kwenye mitandao ya kijamii, huko akapita kila sekta asiache jambo. Ilimgharimu masaa mawili kutimiza haja yake kisawasawa, akikagua kila maongezi ambayo Alphonce aliyoyafanya.



    Mwishowe akaja kugundua kuwa mwanaume yule hakuwa mtu wa kawaida. Alikuwa ni muuaji! Na amekuwa akifanya hivyo kwa malipo makubwa na ustadi mkubwa. Na amekuwa akitumia kofia yake ya upolisi kumaliza mambo 'kirahisi'.



    Ana miradi kadhaa, na kwenye akaunti yake kuna pesa ya maana anazozipata kwa mkono mchafu! Hapa pakamkamata Glady na kumbadili mawazo. Pesa! Pesa! Pesa!



    Hapa akasahau kwamba anaweza akauawa. Hapa hakuona tena hatari ya kifo, bali akijiona yupo Dubai. Akajiona anaendesha magari makubwa na yenye thamani ya hali ya juu!



    Alijikuta anataka kupata mgao wa pesa iliyopo kwenye akaunti ya Alphonce. Abadili mfumo wa maisha yake kabisa.



    Hivyo basi akajikuta hana budi kucheza mchezo huu na simba. Mchezo wa aidha nipate nitoke, ama nikose nife. Akadhamiria kumtafuta Alphonce kwa namna yoyote alafu amfahamishe kuwa ana siri zake zote kiganjani. Na kama anataka ziendelee kuwa salama, atume mamilioni!



    Tabasamu likachipuka usoni. Mara akashtushwa na hodi mlangoni! Haraka akaficha simu na kuuliza:

    "Nanii?"



    "Aaaaah nawe! Embu funguaga hukoo!" Sauti ikamjibu kwa shombo. Akamtambua ni shoga wake katika kazi.



    "Alah! Kumbe muda umeenda!" Akastaajabu. Akasimama upesi na kwenda kumfungulia huyo shoga 'ake - mwanamke aliyekuwa amevalia kikaptula kifupi cha kijani na blauzi nyeupe inayohakisi ya ndani - sidiria rangi nyeusi.



    Wasikae muda, wakatoka kwenda kazini.



    ***



    Saa tatu usiku ...



    Televisheni ilikuwa inaongea yenyewe. Juu ya meza ya kioo kulikuwa kuna chupa ya mvinyo mwekundu na glasi yake kwa pembeni.



    Hakukuwa na nuru ya taa, mwanga pekee uliokuwepo hapa ulikuwa ni ule utokao kwenye televisheni. Na mbali na sauti ya televisheni hii, hakukuwa na sauti nyingine iliyosikika.



    Kwenye kochi alikuwa ameketi bwana Lee akiwa ameinamishia kichwa chake chini. Alikuwa ameelemewa na mawazo. Na chupa hii ya mvinyo juu ya meza, ilikuwa inaelekea kukatika pasipo kumsaidia kabisa.



    Kwanini asiwe na mawazo wakati maisha yake yapo hatihati? Alikuwa amekonda, endapo ukimtazama vema, wala havutii tena. Rafiki yake mkubwa alikuwa ni pombe, na anajifungia ndani.



    Mara kwa mara sauti ya marafiki zake, Nigaa na Mombo, zilikuwa zinamrejelea masikioni zikimtaka asitishe mpango wake wa kwenda Chinakumtafuta Chen Zi.



    Wao hawakuona kama hilo wazo ni jema kwani kuondoka kwake kutamsababisha bwana Sheng kuanza kumshuku. Walipendekeza Lee aachane na mambo ya hiyo Nyaraka. Lolote litakalotokea, akane kuhusika nalo.



    Lakini atawezaje kufanya hilo? Akajiuliza. Sheng anajua kuwa yeye ndiyo alikuwa na nyaraka hiyo, tena ya thamani kubwa, endapo akisikia huko kwengine atamfikiria nani zaidi yake?



    Akajikuta anakataa kabisa wazo la kutokwenda China. Ni lazima aende huko akamaliza alichokianzisha. Akamtafute Chen Zi aliyetumiwa nyaraka hiyo na bwana Foang - mchina aliyemrubuni Mustapha.



    Ila sasa kazi inakuja, atatolea wapi sababu ya kwenda huko China? Akahisi kuchanganyikiwa.



    Akanyanyuka na kwenda kujiandaa, mara akatoka ndani na kujiweka kwenye gari, safari mpaka klabu. Bahati, akiwa huko akamwona Glady. Alikuwa amesimama na marafiki zake mikononi wakiwa wameshikilia bia za kopo.



    Akamfuata mwanamke huyo na kumtaka awe naye kwa usiku huo. Kwa kumtazama tu, Glady akajua Lee hakuwa sawa. Alikuwa na msongo wa mawazo. Basi pasipo kusita, akaridhia kwa kumpa tabasamu.



    Lakini kabla hawajatoka ndani ya klabu, Alphonce akazama ndani akiwa anaangaza. Alikuwa amamtafuta Glady!







    Mwili wake ulivishwa suti nyeusi, lakini kama kawaida yake, haikuwa imemkaa vema. Nguo ilionekana ni kubwa tofauti na umbo lake. Pengine huwa anajiona ana mwili, ama amenenepa kwa ndani, na hivyo basi matatizo ni kwetu sisi tunaomtazama.



    Akaelekea kaunta akaoda wiski moja, aliomba iwe ngeni kinywani mwake. Akiwa anasubiri apatiwe, akawa anaangaza macho yake kutafuta. Lakini shida ni kwamba, mwanga uliokuwemo humo ndani, kumeta-meta kwa rangi nyingi kama pinde za mvua, hazikumruhusu aone watu vema.



    Kwahiyo basi yeye alikuwa anasachi kwa mujibu wa maumbo. Alikuwa amelikariri umbo la Glady ma endapo tu angeliona basi angeling'amua kwa wepesi kabisa, hata kama kizani.



    Ila mpaka muda huo, alikuwa ameshachelewa. Kwa muda huo, tayari Glady alikuwa ndani ya gari la Lee wakiondoka zao.



    "Hii hapa!" Akasema mhudumu akisogeza glasi. Alphonce akaitikia kwa kichwa alafu akapiga pafu moja kana kwamba anakunywa juisi ya machungwa!



    Akasafisha koo lake na kumtazama mhudumu machoni. Kwa sauti yenye stara ndaniye, akamuuliza endapo kama anamjua Glady. Si kwa kumtajia jina, la hasha! Bali kwa kumdadavulia mwanaume huyo mhudumu namna gani Glady aonekanavyo. Kuanzia umbo, mwendo na hata sauti.



    "Hapana, simfahamu!' Mhudumu akabinua mdomo. Na akiwa mwenye haraka ya kuhudumia wateja wengine wanaomngoja. Akashika shelvu, akafungua jokofu na kuwapatia watu vinywaji, punde alipomtazama Alphonce akakutana naye macho kwa macho. Na mezani Alphonce alikuwa ameweka kitambulisho chake cha kazi.



    Ni askari.



    "Pengine unaona haja ya kwenda kujadiliana kituoni?" Akamuuliza mhudumu katika sauti ya kutotaka kuwaogofya wengine.



    Mhudumu akatazama kando na kando upesi. Hakuona kama kuna haja hiyo. Ni kweli hakuwa anamjua Glady, lakini kutokana na uzoefu wake wa kazi ndani ya eneo hilo, alishafahamu tokea awali kuwa Glady atakuwa ni mwanamke anayejiuza ndani ya eneo hilo. Na huyo mwanaume, yaani Alphonce, atakuwa anamsaka kishari, aidha walikorofishana kihuduma.



    Kwahiyo kuepusha zogo, huwa wanajibu sijui. Lakini kesi ya leo haikuwa iliyozoeleka. Alikabwa na hofu. Na kadiri Alphonce alivyokuwa anakaa pale, hakujihisi mwenye amani.



    Akanyooshea kidole upande wake wa magharibi ya mbali kisha akamtazama Alphonce.



    "Anaweza akawa pale."



    "Na kama hayupo?" Alphonce akauliza akiweka kitambulisho chake ndani ya mfuko wa koti.



    "Basi wenzake watakusaidia kumpata ... wale wote ni wenzake!... wote wale!"



    Alphonce akagida mafundo yasiyo na mwisho kumalizia wiski yake kisha akanyanyuka. Hata hakulipa, akaendaze alipoelekezwa. Lakini hilo halikumshtua mhudumu, bali namna mwanaume huyo alivyoweza kunywa chupa ile ya kinywaji kikali kana kwamba chai baridi!



    Akamtazama akiyoyomea mataani. Akaendelea na kazi yake lakini kila dakika akirusha macho kuangaza usalama kule magharibi. Masikio yake hayakuwa yanasikia tena mziki mkubwa uliokuwa unapigwa mule. Muda wowote yalikuwa yamejitenga kusikia yowe ama makelele ya wale madada poa wakimkimbia 'askari'.



    Ila haikuwa hivyo. Baada ya muda kidogo akamwona Alphonce akitoka nje akiongozana na mwanamke ambaye hakumwona vema, japo alifahamu ni miongoni mwa wale wadada wanaojiuza.



    Hapo, angalau sasa akashusha fundo la pumzi alilolikabia kifuani kwa muda.



    ***



    Mlango wa Prado nyeusi ulipofungwa, gari haikuwashwa, badala yake Alphonce akatoa bunduki ndogo na kuipuliza kana kwamba ina vumbi. Akaitazama kana kwamba msomaji wa gazeti apekuae kisa alichosimuliwa. Alafu pasipo kufanya nayo jambo, akairudisha alipoitoa. Akatengenezea 'sight mirror' vema kisha akamtazama mwanamke yule 'aliyeloki' naye ndani ya gari.



    Mwanamke huyu alikuwa ni yule 'shoga' aliyempitia Glady kwenda naye 'kazini' masaa kadhaa nyuma tu. Kama ni upatu, Alphonce alikuwa ameula.



    "Sina shida ya kukupeleka popote, bali mambo mawili. Na katika hayo utachagua mwenyewe lipi linalokufaa. Unipatie taarifa ninayoihitaji ukaenda zako salama, mkononi una pesa, ama nikutoe ndani ya gari hii ukiwa mfu."



    Hata kabla Alphonce hajaendelea, mwanamke huyu alikuwa tayari kusema lolote lile atakaloulizwa. Alishafanya chaguzi. Hakuwa na taarifa ya muhimu kuzidi uhai wake, na wala chungu kutia doa utamu wa pesa.



    Alikuwa anatetemeka mno na kama milango ya gari isingekuwa 'imelokiwa' basi ni wazi angeshachumpa nje kukimbia kadiri ya urefu na uwezo wa miguu yake.



    Bunduki haikuwa kitu alichozoea kukiona.



    Kwa utaratibu kabisa, Alphonce akampembua mwanamke huyo, na akapata alichokuwa anakitaka. Akazamisha mkono mfukoni, akatoa noti kadhaa nyekundu, pasipo kuhesabu, akamtupia yule mwanamke mapajani kisha aka'unlock' milango pasipo kusema kitu.



    Mwanamke akashuka upesi. Hapo ndo' akagundua kumbe alikuwa ameshalowana mapajani na nguo yake ya ndani ilikuwa mbichi. Haraka akakimbilia ndani ya klabu usidhani amevalia viatu vya visigino virefu!



    Akaingia ndani kwa pupa, na kusababisha tahamaki kwa waliomuona. Haswa yule mhudumu wa kaunta!



    ***



    Saaa nne asubuhi ....



    'nitakuwa hapo ndani ya dakika kumi,' Jona alituma ujumbe kisha akaizamisha simu yake mfukoni. Akatazama kando, kando tena, alafu akanyanyuka toka kwenye kituo cha basi na kuanza kutembea kwa ukakamavu.



    Alikuwa amevalia shati jeupe, tai nyembamba nyeusi, suruali nyeusi ya kitambaa na moka. Mabegani mwake alikuwa ametundika koti kubwa la mvua lilikomea magotini.



    Kwa mtu mwenye macho ya 'chujio' ungemtambua huyu mtu hakuwa raia wa kawaida. Alikuwa mtu mwenye mafunzo. Kisigino chake kilikuwa kinaanza kukanyaga chini kwanza kabla ya nyayo, tena kwa ustadi na sare.



    Macho yake yalikuwa hayajatulia, yanakwenda huku na kule kuangaza usalama. Alijua anafuatiliwa. Ilipangwa afuatiliwe. Na anatakiwa afuatiliwe!



    Hiyo ndiyo maana anatakiwa kuripoti asubuhi na mapema kwa Kamanda mkuu wa mkoa, badala ya kituoni kama ilivyo utaratibu wa kazi, kabla ya kutimiza majukumu yake.



    Kufika huku kwa Kamanda kulikuwa ni kwa lengo moja tu, nalo ni kumpachikia 'mkia', na si lingine. Jona alitakiwa kuwa chini ya 'jicho la tai' kwa muda fulani kuhakikisha mienendo yake si 'hatari kwa afya' kwa walioshika mpini.



    Alizidi kutembea na huku nyuma yake, hatua kama kumi na nane akiwa anasindikizwa na mwanaume mpana mweusi aliyevalia kaunda suti ya kijivu.



    Hatua za mwanaume huyu zilikuwa za kiutu uzima. Suruali yake pana ilikuwa inarushwa rushwa kwa hatua zake za nguvu. Alimjaza Jona kwenye mboni na hakusumbuliwa na kingine chochote kilichokuwa kinakatiza machoni.



    Lakini dakika moja ni kubwa sana! Ndani ya dakika moja, yaani sekunde sitini, jambo kubwa linaweza kupangwa, liketekelezeka na kuacha pengo!



    Wakavuka kona ya kwanza ... pili ... tatu ... ndani ya dakika moja tu. Mwanaume yule aliyekuwa anamfuatilia Jona akatambua ameshaachwa solemba!



    Mbele yake bado alikuwa analiona lile koti alilojivika Jona, halikuwa limebadilika, ni lilelile! Lakini suruali haikuwa nyeusi tena, bali rangi ya udongo! Haraka akakimbia na kumnyaka bega mwanaume mwenye koti hilo, kugeuka alikuwa ni mwanafunzi!



    Hakugundua tangu kona ya kwanza, Jona alikuwa ameshamwacha akiendelea kumalizana na kona ya tatu.



    "mkuu, amenipotea," akavuma kwa fedheha akiongea na simu.



    ***



    'Nipo nje ya mlango' Ujumbe uliingia ndani ya simu ya Marwa. Akanyanyuka toka kochini alipokuwa ameketi akauendea mlango na kuufungua. Akakutana na Jona. Hakuwa na koti.



    Wakasalimiana na kumkaribisha kitini.



    "Ungependelea kinywaji gani, mkuu?"



    "Hapana, nashukuru ... umewasiliana na Panky?" Jona akaenda moja kwa moja kwenye 'biashara'.



    "Ndio, amesema anakaribia," Marwa akajibu kwa kujiamini akiketi.



    Nyumba ilikuwa kimya. Hakukuwa na dalili yotote ya kuwa na mtu mbali na wao walioketi sebuleni. Na kwa Jona, kwa muda mfupi alioketi hapo, akagundua Marwa amekuwa akiishi maisha ya kipweke. Nyumba haikonekana kama ina 'mguso wa kike' wala shurba za mtoto.



    Alipokuwa amekaa aliweza kuona jiko, ukuta wa korido, samani, sakafu na kadhalika. Havikuwa katika namna ambavyo vingekuwa endapo Marwa angekuwa anaishi na mtu mwingine mule ndani.



    Hakujali, ila hakukuwa na kingine cha kufanya wakiwa hapo wanamngojea Panky zaidi ya kuperuzi peruzi. Hakutaka kuanza kumpekenyua Marwa kwa kumrushia maswali mapema yote hiyo, kwani hakuonekana kama mtu aliye 'comfortable' mbele ya uwepo wake.



    Akaendelea kutazama tazama pasipo kutia neno, mpaka macho yake yalipotua mezani kulipokuwa na tarakilishi nyeusi HP modeli ya kisasa, makaratasi kadhaa, mengine meupe, mengine ya grafu, zaidi kalamu tatu, penseli nne na rula moja.



    Kwenye makaratasi hayo kulikuwa kuna michoro michoro mingi, na mengine mahesabu mahesabu yakiwa yametapanywa. Bila shaka Marwa alikuwa anayatumia kufanyia zoezi analoendelea nalo kwenye tarakilishi, akawaza Jona.



    Akasafisha koo lake, na kuvunja ukimya.



    "Hata leo haupo off?" Akauliza akitabasamu kwa mbali. Marwa akatabasamu zaidi.



    "Sijawahi kuwa off. In fact, nafanya kazi overtime mara kwa mara. Nadhani n'shazoea!" Marwa alimalizia kwa kupandisha mabega yake.



    "Basi pasi na shaka, mshahara wako ni mnono," Jona akaendelea kuchokoza mada. Macho yake yalikuwa makini kutazama kila kitu toka kwa Marwa.



    "Lah! Nafanya kazi si kwa ajili ya pesa, bali maisha."



    "Pesa ni maisha."



    "Hapana. Pesa si maisha ... pesa haiwezi nunua maisha."



    Hapa Jona akaona kuna cha zaidi Marwa alikuwa anataka kusema lakini aidha anakosa namna bora ya kukisema, ama anajitahidi kuzuia kutokukisema.



    Lilikuwa ni jukumu lake kukijua hiko kitu.



    "Kama pesa kwako si kitu. Unafanyiaje kazi maisha? Wafanya kazi kwa kuwa umezoea?"



    Marwa hakujibu upesi. Alitulia kwanza. Jona hakuona haja ya kumshinikiza ajibu kwani uso wa mwanaume huyo ulimwonyesha jibu lipo karibuni. Ni vile anapanga namna ya kulitamka.



    Marwa akashusha pumzi ndefu. Pasipo kumtazama Jona, akasema kwa sauti iliyotoka chini ya vungu la moyo wake.



    "Output ya kazi yangu, ndiyo pumzi ya wazazi wangu."



    Jona hakupata wasaa wa kuendelea kumdadisi, Panky akawasili. Sasa wakaanza kujadili kuhusu ile picha.



    _Picha ya siri._



    _Picha ya Bite inayotia rehani roho zao wote._



    ***



    Kama vile uonavyo watahiniwa wakiwa kwenye hall la mtihani, ndivyo ilivyokuwa hapa. Palikuwa tulivu, macho yote yakitazama kioo cha tarakilishi ya Marwa.



    Marwa akaelezea kila anachokijua. Tangu alipopewa kazi hiyo na mpaka pale alipoikamilisha kwa Moderator wao. Akaeleza ni kwa namna gani kazi hiyo ilivyofanyika kwa siri, ustadi na mazingatio makubwa.



    Kila 'detail' ilikuwa imepimwa kwa umbali wa sentimita za kuwiana. Na japokuwa hakuambiwa vitu vile vilimaanisha nini, alishatambua zitakuwa 'codes'. Na kwa wakati huo akatokea kuamini aidha ni codes za kufungulia tarakilishi tawala - yani ile 'inayomoderate' tarakilishi zote hizo ndani ya jengo.



    Alipomaliza kuifanya kazi hiyo, akaikabidhi kwa moderator, lakini baada ya muda akiwa amesahau kabisa picha hiyo , Moderator akamrudishia akimwambia kuna mambo alitakiwa kurekebisha. Idadi ya mawimbi baharini!



    "Kitu hichi kikanishangaza, si kwamba zilikuwa ni taarifa ndogo ndogo, lah! Bali kwa sasa aliponipatia alikuwa strict mara tatu ya awali akitazama kila nyendo za mkono wangu, macho yangu.



    Nilipomaliza, akaniagiza nimrushie. Na hapo ndipo ikawa mwisho wa mimi kukutana na hiyo picha mpaka pale Panky alipoiibua na kunishtua."



    "Unamfahamu Bite?" Jona akauliza.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Bite? ... "Marwa akatengua macho kwa kufikiri. "Bite Mayanja?" Akauliza.



    "Sijui jina lake la ubini, namjua kwa jina la Bite tu. Kuna mtu yeyote unayemfahamu, ama wamjua anaitwa Bite?"



    Marwa akafikiri kwa dakika.



    "Sidhani ... ila, ebu ngoja. Bitee? ... Bitee ... Bitee..." akameza lips zake akiendelea kuwazua. Punde akamuuliza Jona juu ya mwonekano wa mwanamke huyo, Bite. Jona akajipambanua kutumia kumbukumbu zake zote kuelezea. Hapa Marwa akapata kitu.



    "Unamwongelea marehemu Bite?"



    "Exactly! Atakuwa ndiye huyo. Unamjua?"



    "Ndio ... ila tuseme kiasi chake ... namjua kiasi."



    "Ulimjulia wapi?"



    "Kazini. Bite alikuwa ni miongoni mwa wafanyakazi wachache niliowakuta. Hakuwa mwanamke muongeaji sana, wala mwepesi kumzoea. Kwa kipindi hicho alikuwa ndiye mwanamke pekee ndani ya chumba cha IT. Lakini hali hiyo haikudumu kwa muda mrefu, akaacha kazi!"



    "Alikuambia ameacha? Au ulijuaje?"



    "Najua tu aliacha kazi, hata kama hakuniambia. Sheng huwa hafuti mtu kazi, anafuta uhai. Unakumbuka nilivyokuambia Bite ni miongoni mwa wafanyakazi wachache niliowakuta? ... wenzake wote niliowakuta hapo, watatu kwa idadi, waliuawa."



    "Umejuaje?"



    "Natazama taarifa ya habari. Najua walitaka kuacha kazi, haswa baada ya Bite kufanya hivyo ila hawakufanikiwa."



    "Na kwanini Bite akafanikiwa?"



    "Akafanikiwa!" Marwa akastaajabu. Akatabasamu kisha akatikisa kichwa. "Bite alichofanikiwa ni kudumu kwa muda mrefu tu, tofauti na wenzake. Yeye aliweza kukaa miaka na miaka akiwa huru!"



    "Lakini iliwezekaje hili?" Jona akauliza. Hapo Marwa hakuwa na majibu. Kila mtu akawa kana kwamba yupo hewani kutafuta tofali hili moja kumalizia nyumba.



    Jona akatabasamu. Akatabasamu kwa upana zaidi. Na mara akacheka.



    "Bite aliweza kudumu muda mrefu kwasababu ya hii picha," akajibu akionyeshea kidole kwenye kioo cha tarakilishi.



    "Ni wazi Bite alikuwa anajua risk ya yeye kuacha kazi. Basi akaondoka na kitu cha thamani toka kwa Sheng. Kitu atakachokitumia kama dhamana ya uhai wake. Nacho ni hii picha!"



    "Lakini mbona Sheng alimuua tu?!" Panky akauliza akistaajabu.



    "Sheng alimmaliza baada ya kupata mbadala wa kile alichokuwa nacho Bite mkononi. Ukiachilia mbali bado Bite alikuwa na pandikizi la Sheng ndani ya kila shughuli aliyokuwa akiifanya. Na kwa akili tu ya kitoto, maana yake ni kwamba Sheng alikuwa anajiandaa kuzipokea shughuli hizi punde atakapomwondoa Bite duniani," Jona akadadavua.



    Marwa akakunja usowe kwa kuchanganyikiwa. Akauliza:

    "Umejuaje Sheng alipata mbadala wa picha aliyokuwa nayo Bite mpaka akaamua kumuua?"



    Jona naye akamuuliza:

    "Ilichukua muda gani kati ya wewe kubadili picha na Bite kuuawa?"



    Marwa akajaribu kufikiri. Haraka akainamisha mgongo wake kutazama chini ya meza, kulikuwa kuna magazeti lukuki huko, akapekua pekua magazeti hayo na kuibuka na mojawapo.



    Lilikuwa na taarifa ya mauaji ya Bite.



    Akalisoma tarehe. Kisha akazama kwenye tarakilishi yake alipopekua mambo kwa muda wa dakika mbili, kisha akasema:

    "Tofauti ya siku mbili tu!"



    Jona akatabasam kwa mbali.



    "Umeona enh?"



    "Lakini," Panky akazuka. "Kama ingelikuwa ni rahisi hivyo, kubadili tu picha mchezo ukaisha, kwanini ilichukua muda mrefu Bite kuwa hai?"



    "Na hapo ndipo tunaporudi pichani," Jona akamjibu. "Hizi zilizopo kwenye picha ni codes. Ni kitu kikubwa. Kuongeza tu mawimbi pichani, si tu kupendezesha mambo bali kumaanisha jambo. Jambo ambalo lilimchukua Sheng muda wote huo akichezewa sharubu na Bite!"



    Sasa mambo yakaanza ku' make sense'. Kuhakiki zaidi mambo, Jona akatoa simu yake mfukoni na kutazama picha ya picha ile aliyoichora toka kwa Bite.



    Kweli ilikuwa na upungufu wa idadi ya mawimbi ukiilinganisha na ile kopi ya Marwa! Upungufu wa mawimbi mawili tu! Lakini ungeliona hili endapo ungeamua kuua muda wako wa kutosha kuchunguza.



    "Wamekuamini sana kukuachia hii kopi," Jona alisema akimtazama Marwa.



    "Hawana hofu kuu nami," Marwa akajibu. "Maana wanajua sina janja kwao. Nikapofanya lolote lile, watakatisha dozi ya antidote kwa baba na mama yangu, nao watakufa ndani ya sekunde thelathini tu!"



    Jona aliona ni namna gani Marwa anaumizwa na hilo jambo. Macho yake yalitamka namna gani anaumia kila akilikiri hilo. Hakutaka kumumiza zaidi, akakengeusha mawazo.



    "Hii picha tukiikokotoa. Sheng atakuwa amejaa kiganjani."



    "Hakika!" Panky akaliunga mkono hilo. Lakini kabla hawajaendelea kuumiza vichwa zaidi, Marwa akapendekeza wapate kifungua kinywa kwanza kwani tumbo limeanza kudai chake kwa fujo.



    "Hli tumbo limetifuliwa na kuumiza kichwa," akasema Marwa akienenda jikoni. Pengine alikuwa sahihi kwani mara hii Jona hakumzuia.



    Alihisi naye anahitaji kitu kujaza utupu wa tumbo lake.





    Chai na vitafunwa kadhaa vikiwa vimewekwa kwenye sinia ya plastiki, nadhifu jeupe lenye nakshi za maua maua, vikawasilishwa mezani. Vikafuatiwa na maji ya kunawa na ya kunywa pia. Marwa akawanawisha wageni wake mikono na kuwakaribisha.



    "Umepika mwenyewe hivi?" Jona akauliza baada ya kung'ata kitafunwa kimoja na kukitafuna. Ladha ilikuwa tamu. Na zaidi, aliona ilikuwa ni fursa adhimu kwake kujua machache toka kwa Marwa.



    "Hapana, sijapika mie ... siwezi kupika hivi!" Marwa akasema akitabasamu. "Si kwamba siwezi, hapana! Ningepika hapa mngejing'ata lakini sina huo muda. Nabanwa sana na kazi."



    "Hakuna wa kukusaidia?" Jona akaendelea kudadisi akitafuna.



    "Atolee wapi?" Panky akawahi kumjibu, kisha akacheka kidogo. "Unavyomuona huyu alivyo ndiyo yupo hivyo hivyo!"



    Kukawa kimya kidogo. Wote walikuwa wametabasamu midomo yao ikicheza kwa kutafuna.



    "Nimechagua haya maisha," Marwa akavunja barafu la ukimya. "Ni ngumu, najua ... lakini sina namna."



    Jona akamtazama kwa macho ya maulizo pasipo kusema kitu. Alitumai Marwa hataishia hapo. Marwa akanywa mafundo mawili ya chai na kufuta mdomo wake kwa mgongo wa kiganja.



    "Kazi yangu ya hatari sana," Marwa akasema kabla hajatia kitafunwa kingine mdomoni. "Kumpata mwanamke siyo shida. Ila nitaweka maisha yake rehani, na huenda akatumika, kama ilivyo kwa wazazi wangu, kunifanya niwe mdhaifu."



    Wote wakaunga mkono hoja yake. Wakaendelea kutafuna kwa muda kidogo kabla Jona hajairudisha tena mada mezani.



    "Lakini unajitahidi... indeed unajitahidi sana kukeep nyumba vizuri."



    "Kiasi chake!" Marwa akapokea pongezi kwa aina yake. "Nikipatapata muda unashika hiki na kile, hapa na pale, nidumishe rangi za vitu, angalau hata mgeni akija asipate picha mbaya ya kusimulia."



    Maongezi hayo yakawasha taa kichwani mwa Jona. Kuna kitu aliwaza. Kuna kitu alikipata. Alitazama sinia ile iliyobeba vitafunwa, ilikuwa ni nyeupe peh.



    Kudumisha rangi ...



    Rangi nyeupe ...



    Rangi nyeupe huonyesha usafi.



    Akilini alikuwa anaonganisha mambo ...



    Ghafla, akalipuka na kuuliza:

    "Vipi kama rangi za ile picha zikawa ndiyo codes zenyewe?"



    "Kusema kwamba?" Panky akatahamaki. Jona akamtazama kwa macho ya uhakika.



    "Kusema kwamba, rangi za vile vitu vilivyopo kwenye picha ndiyo zikawa codes!"



    Hawakutaka kupinga hoja ya Jona kabla hajaithibitisha. Wakamaliza kula na kuchangia maoni yao kwenye hilo wakiwa wanatazama picha ile kwa umakini.



    Lakini wakagundua walikuwa ni wadhaifu kwenye mambo ya rangi. Lakini kabla hawajakata tamaa, Marwa akataka watumie 'Techonological interpretation of colors' - yaani wazichambua zile rangi kwa kuzihusanisha na teknolojia kwani kazi hiyo ilitengenezwa na kitengo cha teknolojia tarakilishi ndani ya mtandao wa Sheng.



    Basi, Marwa akafungua 'application' yake ya siri aliyoitengeneza kwa mikono yake mwenyewe, inaitwa CODAQ. Akaandika namba za siri kwa vidole vyake vyepesi juu ya keyboard. Mara zikaja namba namba nyingi. Akabofya bofya keyboard kwa haraka mno usijue hata aliandika nini, na mara kioo kikawa cheupe.



    "Ni nini hii?" Jona akauliza.



    "Ni app yangu ya kutengeneza Techonological logos kwa ajili ya techonological gadgets."



    "Kwani wataka kutengeneza logo?"



    Marwa akatabasamu. "Hapana. Nataka ku 're-assess' kila rangi na maana yake kwenye techonology field."



    Akabonya bonya keyboard kwa wepesi. Jona hakusumbuka tena kutazama nini Marwa anabofya kwani macho yake hayakuweza kwenda sambamba na kasi ile.



    "Unajua kila rangi ina maana yake kwenye logo ..." Alisema Marwa akiwa anaendelea kufanya mambo yake. Hakuna mtu mwingine aliyeongea, wote walikuwa wanangojea aweke mambo bayana.



    Punde,



    "All right!" Akasema Marwaa akitabasamu. Alikuwa amefika mahali alipokuwa anapahitaji, akashirikisha wenzake kwa kile alichokuwa nacho.



    Mosi, kwenye ile picha kuna rangi ya blue - ambayo ndiyo ilitumika kupambia bahari. Pili, kuna rangi ya kijani kilichoshamiri kisiwani. Tatu, kuna rangi nyekundu na nyeupe iliyotumika kupambia ndege warukao juu.



    Hizo ndo zilikuwa rangi 'dominative' pichani. Sasa wakazianisha kimaana.



    - Blue = security/strength/dependable. (Ulinzi/ nguvu/cha kutegemewa)



    - Kijani = life/growth/freshness. (Uhai/ukuaji/hali nzuri)



    - Nyekundu = communication/energetic. (Mawasiliano/chenye nguvu)



    - Nyeupe = purity/reliable (kisafi ama kitakatifu/kuaminika.)



    Kwahiyo basi kwa maana hiyo, kisiwa kile (kijani) kilikuwa kinamaanisha uhai wa Sheng, ukuaji wa Sheng, hali nzuri ya Sheng. Lakini hicho kisiwa kikiwa kimezingirwa na blue (maji), kumaanisha ulinzi, nguvu na kutegemewa.



    Mpaka hapo, maana yake ni kwamba hakuna ukuaji wala uhai wa Sheng kama hamna ulinzi na nguvu kuzunguka uhai huo. Na kwa tafsiri ya picha, bahari ama rangi blue ndiyo iliyochukua sehemu kubwa.



    Na wale ndege waliopo juu ya kisiwa, wakimaansha utakatifu wa mawasiliano kama moja ya nguzo ya kupendezesha mandhari!



    Nusu ya kazi ikawa imeisha. Sasa mkia uliobakia ukawa ni kujua maana ya idadi ya kila kilichomo ndani ya picha. Kwanini ndege watano? Mawimbi manne? Kwa maana kama yasingekuwa na maana basi Marwa asingepewa kazi ya kuyarudia kuyaongeza.



    "Nguvu ya bahari ni mawimbi yake, sio?" Jona akauliza. Asisubiri majibu akaendelea kuteta: "basi haya mawimbi manne yaliyopo kwenye bahari hii, ndiyo nguvu ya ulinzi wa Sheng. Aidha ni watu ama vitengo."



    "Na basi kama ni hivyo," Marwa akadakia lain. "Nguvu ya mawasiliano ya Sheng ni watu ama vitengo vitano pia!"



    ***



    Saa kumi na mbili jioni, Whitesand Hotel.



    "Nimefurahi sana sana!" Sauti ya kike ya Miranda ilivuma wakati mwanamke huyo akiagana na mheshimiwa Boka kwa kumpatia kumbatio la joto na busu mubashara shavuni.



    "Usijali, nimefanya yote haya kwasababu nakupenda. Nimedhamiria haswa kuwa nawe," Mheshimiwa Boka akajivuna kabla hajatoka zake eneo hilo na kujipaki ndani ya VX yake nyeusi. Akahepa.



    Miranda akarudi ndani ya hotel akiwa anatuma ujumbe simuni. Alipoketi, ndani ya muda mfupi BC akatokea nyuma yake na kuketi. Mwanaume huyo alikuwa anatabasamu usoni.



    Akampongeza Miranda kwa kukamilisha kazi, kisha akamsikiliza amwambie cha ziada.



    "From next month, he will be on trip in South Africa." (Kuanzia mwezi ujao, atakuwa safarini Afrika ya kusini) Miranda akajipambanua. BC akatoa macho ya mshangao.



    "What a coincidence!" (Bahati iliyoje!) Akamsihi Miranda ahakikishe hiyo safari anakwenda na Boka kwani kuna baadhi ya mzigo wao utatua huko, na atakuwa na jukumu la kuuleta hapa nchini.



    Kidogo Miranda akaonyesha hofu.



    "Never mind, it's just small one. It will never get you in trouble," (Usijali, ni mdogo tu. Kamwe hauwezi kukuingiza matatizoni,) BC akampoza akiwa anamkanda bega kwa kiganja chake kipana.



    Hawakukaa hapo sana, wakatimka zao.



    ***



    Wivu ndiyo mapenzi. Lakini pia wivu ni kidonda, ukishiriki utakonda. Walisema waswahili. Na hakika hawakukosea kwa neno hilo, ulikuwa ni ukweli mtupu ulio uchi.



    Punde baada ya mumewe kuingia bafuni, akaiteka simu ya mumewe na kuanza kuiperuzi. Boka mule bafuni asiwe na hofu yoyote, alikuwa anaimba huku akiusugua mwili wake mpana mweusi kwa ujazo wa sabuni.



    Alikuwa anabadili nyimbo hii kwa hii. Wakati mwingine akiwa anagugumia kutengeneza 'beat'. Alikuwa ana furaha moyoni, ungelijua kwa kumtazama tu. Kama mwili wake ungelikuwa unamruhusu kucheza, basi angelijimwayamwaya.



    Lakini laiti angelijua mkewe anaperuzi simuye, nakuhakikishia asingekumbuka hata taulo. Angekimbia upesi kwenda kumpokonya.



    Alipomaliza kuoga, akatoka bafuni akiwa amejifunga taulo jeupe kiunoni. Bado akiwa anaimba, akaketi kitandani na kumtazama mkewe. Alikuwa ameigiza kulala.



    Akajaribu kumuita mara mbili kwa sauti ya chini. Mama hakuitika. Basi asimsumbue, akaenda zake kabatini na kuteka nguo ya ndani apate kulala.



    Bila shaka akijua usiku umeenda salama. Lakini kumbe kifuani mwa mkewe kukiwa kuna vita hatari. Vita inayomtafuna zaidi ya kirusi.



    Akazima taa na kisha kujimwaga kwenye kitanda kipana, maridadi kabisa, apate kulala. Kwa 'kajoto' kalichokuwepo, hakuhitaki kujifunika shuka.



    Alikuwa amechoka mno kwa 'shughuli pevu' aliyopewa na Miranda. Hakudumu macho kwa muda mrefu, akapotelea usingizini akiwa anakumbuka raha alizopewa.



    Raha za karne.



    Lakini mkewe hakuwa amelala. Muda huo alikuwa anatiririsha machozi bujibuji. Alikuwa akisaga meno, kichwa kinamuwaka moto. Likapita lisaa limoja. Akashindwa kuvumilia.



    Akanyanyuka na kutoka ndani ya chumba. Baada ya dakika tatu, akarejea akiwa ameshikilia kisu mkononi.



    ***



    Alikuwa amejawa na hasira kedekede. Hakuwaza tena kama ana watoto aliozaa na huyo mwanaume. Hakuwaza kama ana familia inayomtegemea, wala mambo lukuki waliyoyapanga na kuadhimia na huyo mwanaume. Hakuwaza kifungo cha maisha.



    Aliwaza kuua tu kuridhisha nafsi yake kwa kuua.



    Lakini anawezaje kufanya hili wakati hata kuchinja kuku hajawahi?



    Akamsogelea mumewe aliyekuwa hajitambui, kazamia usingizini. Kifuani moyo wake ukimdunda haswa! Na jasho likiwa tayari limelowanisha gauni lake jepesi la usiku.



    Mikono yake ilikuwa inatetemeka. Kisu kikienda huku na kule, akijitahidi kukituliza.



    "Nitamkita tu tumboni ... hapana, anaweza akapona ... namkita kifuani. Si atakufa? ... Atakufa ndio!" Alikuwa anazoza mwenyewe na nafsi yake.



    Lakini ghafla mwanga wa simu ukammulika usoni. Akashtuka mno! Kama isingelikuwa mbavu, moyo wake angeliukutia nje.



    Ilikuwa ni simu ya mumewe. Kuna mtu alikuwa anapiga. Baada ya simu kutoa mwanga, punde sasa ikaanza kuita kwa wimbo kwanguvu. Mwanamke akachanganyikiwa. Hakujua cha kufanya kwa haraka.



    Alitupia kisu chini kwa kupagawa, alafu upesi akaketi kwenye kingo ya kitanda. Akasikiliza simu ya mumewe ikiita ... ikiita ... ikiita.



    Ikakata!



    Ikaita tena. Lakini ikakata pasipo kupokelewa. Mara hii haikuita tena kwa muda mrefu kama hapo awali. Kwa muda wote huo Boka hakusikia chochote kile. Alikuwa akiendelea kukoroma kana kwamba hakuna kilichojiri.



    Simu ilikata na kunyamaza kwa muda wa dakika kadhaa. Chumba kikarejea katika hali ya kiza, lakini mama hakukifuata tena kisu chake. Akaendelea kuketi kingoni mwa kitanda akifikiria mambo kadhaa kichwani.



    Mara akanyanyuka na kwenda kutazama aliyepiga simu. Alikuwa ni mfanyakazi mwenziwe na mumewe. Akapuuza. Akaelekea kule kwenye jumbe, akainakili namba ya mtu aliyekuwa anachat na mumewe na kuihamishia kwenye simu yake.



    Mara namba hiyo ikatokea na jina! Kumbe alikuwa nayo simuni.



    Alikuwa ni Miranda.



    "Malaya mkubwa!" Akajikuta akitusi. Amekunja ndita na ngumi kwa hasira. "Kumbe ni wewe! ... kumbe ni wewe unanizunguka?"



    Akajiona mpuuzi sana. Kumbe mwanamke aliyeingia naye kwenye mahusiano ya kibiashara, alikuwa anamzonga nyuma ya mgongo!



    Kichwa chake kikampitishia picha za kumbukumbu akiwa na mwanamke huyo, tangu siku ya kwanza kuonana naye. Siku wakiteta na kucheka.



    Akaghafirika mno.



    Akarejesha kisu jikoni kisha akajilaza kitandani akiwa sasa anapiga mahesabu ya kumpata Miranda. Hakujua atamfanya nini. Ila hakika hakitakuwa kizuri, hiko ndicho alikijua na kuwa na uhakika nacho.



    Hakitakuwa kizuri.



    Hakulala usiku wote huo.



    ***



    Saa mbili na nusu asubuhi; ndani ya ofisi ya Kamanda mkuu wa polisi mkoa.



    Kamanda akamtazama Alphonce kwa macho ya nje ya miwani akiwa ameshikilia gazeti la The Guardian mkononi. Kofia yake ilikuwa juu ya meza, amejilaza kuegemea kiti chake cha kunesa na kuzunguka.



    Akamkagua Alphonce aliyekuwa amevalia suti kubwa rangi ya kahawia na mwenye sura ya ukakamavu, alafu akarudisha macho yake gazetini.



    Kwa muda kidogo kukawa kimya kana kwamba hamna mtu ndani ya ofisi.



    Kamanda akashusha pumzi ndefu puani, alafu akasonya kama mtu aliyesikitishwa na jambo. Akatoa macho yake gazetini na kumtazama Alphonce tena.



    Kwa utaratibu akamuuliza:

    "Tumeshindwana?"



    "Hapana mkuu!" Alphonce akajibu kwa ukakamavu. Kamanda akawela gazeti lake mezani kisha akaendea kabati lake akitembea kwa uchovu. Akalifungua na kutoa faili kubwa zito jeusi alilolipekua karatasi kadhaa ndaniye.



    Akaita,



    "Alphonce," akiwa anaendelea kuliperuzi faili lake.



    "Afande!" Alphonce akaitikia.



    "Unajua nina kazi nyingi mno za kuzifuatilia. Kazi lukuki lukuki. Lakini sasa nashindwa kufanya kazi zangu hizo kwa ajili yako, uzembe wako, ubishi na ukaidi wako ..."



    "Hapana, mkuu si ka --"



    "Nyamaza!" Kamanda akageuka na kumtazama Alphonce kwa jicho la bundi. "Sitaki kusikia lolote toka kwako. Lolote! Unajua jana alikwenda wapi? Kufanya nini? Unachukulia haya mambo mepesi, sio?"



    Kamanda akarejesha faili kabatini, akamsogelea Alphonce na kuketi juu ya meza akimtazama.



    "Unajuwa wazi, tulimaliza familia yake. Tulichoma nyumba yake. Tuliharibu biashara yake. Tukaua washirika wake. Kwako ni mepesi hayo?"



    "Lakini mkuu, kwanini tulimrejesha jeshini? Hukuona itakuwa salama yeye ang ---"



    Twaaah! Kamanda akamzaba kofi zito Alphonce!



    "Pumbavu wewe!" Akalaani. "Unadhani nilikuwa siyajui hayo? Jona alikuwa anahitajika kurudi jeshini kwa namna yotote ile. Huo ulikuwa ni msalaba wangu. Jukumu nililopewa kutimiza na IGP. Sikutia sahihi barua yake ya kujiuzulu mpaka leo hii. Jona anahitajika taifa zima. Haswa kipindi kama hiki!"



    Kamanda akashusha pumzi ndefu. Akanyaka chupa yake ya maji makubwa ya Kilimanjaro yaliyokuwa mezani akagida mafundo kadhaa kujipoza.



    "Ni jambo la muda mfupi tu. Nilikuambia umtazame kwa muda mfupi tu maana naamini wewe ndiye unayeweza hilo jukumu. Shida yangu ni kujua nyendo zake. Kujua kama anafuatilia nyayo zetu za damu. Basi!"



    Akanywa tena mafundo kadhaa ya maji. Akamaliza chupa nzima.



    "Sasa hivi, sitakuelewa tena, Alphonce ... sitakuelewa." Akarudia akimtazama mlengwa wake.



    "Ni wewe tu ndiye wa kumfuatilia Jona. Kila hatua ... kila muda ... kila saa!"



    Punde Alphonce akatoka ndani ya ofisi na kwenda kukaa ndani ya gari lake. Macho yake yalkuwa mekundu. Uso wake ulikuwa umevimba kwa hasira. Si kwasababu ya kuzabwa kofi, hapana. Moyo wake ulikuwa umejawa na wivu.



    Wivu juu ya Jona.



    Aliona Jona anathaminiwa kuliko yeye. Jona ni nani haswa? Kwani yeye ndiye jeshi lote la polisi nchini. Hili jambo lilimuuma sana. Lilikuwa linautoboa moyo wake.



    Akiwa humo garini, punde akamwona Jona akizama ndani ya ofisi ya Kamanda kuripoti. Alikuwa amevalia suruali jeans na shati nyeupe aliyoichomekea.



    Baada ya dakika kama tano, akatoka ndani ya ofisi na kwenda zake.



    Alphonce akawasha gari.



    Baada ya nusu saa ... Ocean road hospital



    "Anaendelea vizuri, anaweza akaongea," alisema nesi kwa tabasamu huku akimtazama Jona.



    Walikuwa wamesimama nje kidogo ya chumba alicholazwa mwanamke huyo.



    "Kwahiyo naweza nikamwona?" Jona akauliza akiwa anatarajia kuruhusiwa. Mguu wake ulikuwa tayari umeshajiseti kwendaze.



    "Mmmmh kwa sasa hapana," akasema Nesi. "Nimetoka kumdunga sindano ya usingizi muda si mrefu. Amekuwa halali, kuna mambo anayawaza sana bila shaka."



    Jona akajitengenezea vizuri kumtazama Nesi.



    "Kwahiyo usiku mzima hakulala?"



    "Ndio. Alikuwa anamimina machozi tu na kuvuta makamasi. Sasa anakosa muda wa kupumzika kitu ambacho kinaweza kumpa shida. daktari akaniagiza nimpumzishe kabla sijaondoka maana shift yangu ishakwisha."



    "Oooh!" Jona akatazama kushoto na kulia. "Naweza kuonana na daktari?"



    "Bila shaka," Nesi akamjibu na kuanza kutembea. Jona akamfuata kwa nyuma mpaka ndani ya ofisi ya daktari, kisha Nesi akaenda zake. Jona akaendeleza maongezi na daktari.



    Daktari akampatia maelezo ya kutosha juu ya hali ya maendeleo ya Nade.



    "Anaonekana mwenye mawazo. Tungepata ndugu au wanafamilia wake nadhani wangetusaidia," daktari alisema akimtazama Jona kwa macho ya uhakika. Kisha akatazama tarakilishi yake ya mezani.



    "Kwa ile dawa mliyompatia, atarudi kwenye fahamu zake muda gani?" Jona akauliza.



    "Si muda mrefu in such kwani atahitaji kula chakula chake cha mchana," daktari akamjibu.



    "Ok, then ntangoja," Jona akasema. Kisha kukawa kimya. Daktari alikuwa anatarajia Jona atatoka ndani ya ofisi yake muda si mrefu, ila haikuwa hivyo.



    Akamtazama Jona. Wakakutana macho kwa macho.



    "Dokta," Jona akaita. "Kuna mtu mwingine alikuja baada ya mimi kuondoka siku ile?"



    Dokta akamtazama Jona kwa kukodoa. Jona akatambua swali lake hilo limemshtua mwanaume huyo muhindi. Hakukwepesha macho yake, akamtazama.



    Dokta akahamishia macho yake kwa kioo cha tarakilishi.



    "Watu wanakuja wengi afisa, kila saa na kila muda. Siwezi nikawakumbuka wote waliokuja baada yako," daktari akajielezea. Jona akiwa anaendelea kumtazama machoni, akamuuliza tena:

    "Hakuna mwanaume uliyeonana naye muda mfupi baada ya mimi kutoka? ... Ni polisi."



    "Hapana." Daktari akatikisa kichwa. "Hamna!"



    "Una uhakika?" Jona akauliza.



    "Ndio, hamna polisi aliyekuja hapa baada yako."



    "Nikithibitisha alikuja, sitakuwa na soni nawe. Nitaenda kukulaza ndani kwa juma zima upate akili."



    Daktari akawa kimya. Akamtazama Jona, akamwona ni mtu anayeongea kwa uhakika. Akahofia.



    "Afande, nina kazi nyingi za kufanya muda huu. Tafadhali naomba unipatie nafasi," daktari akajitetea akijikaza kumtazama Jona.



    Jona akatoa pingu ubavu wake wa kulia kisha akasimama.



    "No! You dont have to do that, kaa chini tuongee," daktari akamwomba.



    "Umekataa maongezi, sina tena huo muda wa kupoteza na wewe hapa," Jona akakaza.



    "Si kwamba sitaki, nimeambiwa nisiseme!" Daktari akaropoka. Jona akaketi chini, akarudishia pingu yake.



    "Mnaniweka kwenye wakati mgumu!" Daktari akalalama. "Huyu anakuja ananiambia hivi, mwingine naye anakuja ananiambia hivi. I am confused!"



    Kwa utulivu, Jona akaanza kumdadisi. Daktari akamwambia alikuja polisi aliyemtaka aeleze kila kitu alichofanya pamoja na Jona. Baada ya kuambiwa kila kitu, akatoa kitisho kwa nesi na yeye, wasiseme kama alikuja hapo hospitali!



    Jona alipopata taarifa hizo akashukuru sana, akamuaga daktari na kumwambia anaenda zake nje kupata chakula. Atakuwapo hapo mpaka pale Nade atakaporejea fahamuni wapate kuteta mambo kadhaa.



    Akaenda kantini kula, akiwa hapo akawa anatazama saa yake na huku akitazama njia endapo atabahatisha kumwona Alphonce. Alijua wazi mwanaume huyo anamfuatilia.



    Akawa anakula taratibu kuvuta muda.



    ***

    Saa sita mchana ... ndani ya nyumba ya Miranda.



    Dada wa kazi alimkaribisha Kinoo akiwa ameongozana na wanawake mapacha: Sara na Sasha, wanawake waliowahi kuwa wafanyakazi wa Bite kipindi yu hai.



    Wanawake hawa kwa muda walikuwa wametengana ambapo Sasha alikuwa amesafiri akimwacha dada yake Sara aliyejipeleka mikononi mwa Kinoo kwasababu ya hofu. Sasa Sasha alikuwa amerejea, na jana yake tu wakawa na kikao pamoja na Kinoo juu ya mustakabali wao.



    "Wewe ni mgeni hapa enh?" Kinoo akamuuliza yule dada wa kazi. Dada akatabasamu,



    '"Ndio, nimekuja hapa wiki iliyopita tu."



    "Oooh! Karibu sana," Kinoo akamkarimu kisha akajitambulisha kama rafiki mkubwa wa bosi wake. "Ukiniita Kinoo hutokuwa umekosea."



    Dada akashukuru, kisha akawauliza wangependelea vinywaji gani wakati wakingojea Miranda aje. Wote wakaagiza maji ya kunywa. Dada akawapatia, na punde Miranda akatokea.



    "Kinoo, umenikumbuka sasa! Yani wewe kama huna dili, hun'tafuti sio?" Miranda alisema akitabasamu. Wakakumbatiana na Kinoo na kusalimiana.



    "Nakuona una ugeni."



    "Yah! Huyu anaitwa Sarah na huyu Sasha."



    Wakapeana mikono ya kutambulishana. Kinoo akamtambulisha Miranda na kisha wakateta habari za masiku ya kutokuonana.



    Baada ya habari hizo, Kinoo akaeleza lililo kuu. Akamwambia Miranda kwamba Sara na Sasha wameazimia kuungana nao.



    Jambo hili likamshtua Miranda, lakini hakufanikiwa kulionyesha. Akaomba apate faragha kidogo na Kinoo.



    "Una akili timamu wewe Kinoo?" Miranda akastaajabu. "Umewaamini nini hao wanawake kuwafakamia kuwajaza huku?"



    "Nina akili zangu timamu, Miranda," Kinoo akajipambanua. "Najua ninachokifanya. Mimi sio mwehu mpaka kukuambia hivyo. Ninawaamini kwa asilimia zote. Hawana la kufanya kwa sasa. Wanaweza wakawa asset nzuri sana kutusaidia."



    "Unadhani BC atatuelewa kirahisi hivyo?" Miranda akauliza. Kinoo akamsogelea mwanamke huyo na kumshika bega.



    "Najua BC anakuamini sana. Endapo ukiuweka ulimi wako vizuri, hawezi akakataa."



    "Lakini, Kinoo," Miranda akatia shaka. "Mbona ni haraka hivyo? Mbona ghafla ghafla hivyo? Kuna nini?"



    Kinoo akashusha pumzi ndefu na kutazama chini. Akarudisha macho yake kwa Miranda na kumwambia:

    "Sarah ana mimba yangu."



    Miranda akakodoa. "Wasema?"





    "Sarah ana mimba yangu," Kinoo akasisitizia. Miranda akashusha pumzi ndefu na kuulaza mgongo wake kitini.



    Akatikisa kichwa chake akimtazama Kinoo. Akamlaumu kwa jambo hilo la kipumbavu, kamwe hakulitegemea kwa mtu kama yeye.



    "Unajua wazi situation yetu. And blindly you are about to make a family!" Miranda akalalama. Hawakuongea sana na Kinoo, akamtaka mwanaume huyo aende, amwache peke yake.



    Kinoo akaendaze akiongozana na wanawake wake aliokuja nao. Walijipaki kwenye gari, Escudo ya grey, wakatimka.



    "Umefanikiwa?" Sasha akamuuliza Kinoo baada ya kuacha makazi ya Miranda kwa hatua kadhaa. Kinoo akashusha pumzi ndefu. Macho yake yalikuwa yanatazama mbele lakini akiwa amezama fikirani.



    "Ni jambo la kuchukua muda," Kinoo akajibu. "Lakini litakuwa sawa tu," akawatoa hofu.



    Hawakuongea tena kwa muda. Sauti ya gari tu ndiyo ikawa inavuma na kuita.



    **



    Jona akatazama saa yake mkononi. Muda ulikuwa umeenda sasa. Alishamaliza kula na sasa akaona ni vema akienda kumwona Nade kama vile daktari alivyomwambia kwamba atakuwa macho kipindi cha kula chakula cha mchana.



    Akanyanyuka na kulipia bili yake ya chakula, na kwa hatua nzito akajongea mpaka kwa daktari moja kwa moja. Yeye hakuwa anangojea msururu wa wagonjwa kwa kutumia kofia yake ya kazi.



    Akiongozana na nesi, akaenda mpaka alipolazwa Nade, akamkuta mwanamke huyo akiwa anakula.



    Nade akatabasamu kwa mbali kumtia Jona machoni. Ni kama vile alikuwa anataraji ujio wa mwanaume huyo. Alionekana bado hana nguvu, ila ilikuwa kheri. Akamkaribisha Jona kula.



    "Nashukuru," Jona akasema kwa tabasamu la bati. Kisha "Nimefurahi kukuona," akasema akimtazama Nade machoni.



    Nade akatabasamu kimaumivu. Jona hakumwongelesha tena, akamwacha amalize kwanza kula.



    "Daktari kaniambia umekuwa na mawazo sana hapa karibuni, nini shida?" lilikuwa swali la kwanza Jona kuuliza.



    Nade akajilaza kwanza kitandani. Akawa kimya kwa muda. Mara macho yake yakaanza kulowana na hatimaye kuvujisha machozi.



    Kuna kitu kilikuwa kinamsumbua kifuani. Jona aliliona hilo. Hakutaka kumlazimisha kuongea, akamngojea kwa wakati wake sahihi.



    "Nisamehe sana, Jona," Nade akasema akitazama dari. Macho yake bado yakiendelea kuvuja kama mto.



    "Nimekukosea sana, najua hilo. Umekuwa ukinipa mkono wakati mimi nikikukabidhi kisu. Umetetea uhai wangu lakini mimi nikifanya jitihada kuupokonya wa kwako. Nisamehe sana. Sistahili hata msaada wako."



    Uso wake ukawa mwekundu. Mafua yakaanza kumtambalia, na kwikwi za kilio zikampalia.



    Akamwomba sana Jona msamaha. Jona akamsihi hana haja ya kufanya hivyo kwani alishamsamehe, hata hivyo alifanya hayo kwasababu za ushawishi wa bosi wake, marehemu Eliakimu.



    "Nataka tu uniweke bayana kile ambacho bosi wako alikuwa ananificha. Naomba unisadie kwenye hilo," Jona akampendekezea, lakini hakutaka kumpa presha mwanamke huyo kutokana na hali yake, akamtaka apumzike, na utakapofika muda basi wataongea kwa urefu na mapana.



    Lakini Nade akakataa.



    "Tuongee tu hata sasa," akateta kwa sauti ya chini ya msisitizo. Uso wake ulikuwa mzito ukizongwa na majuto ya kujiona mkosefu. "Huna haja ya kungoja, Jona, ntakwambia hata sasa."



    Kisha akakaa kimya. Bado macho yake yakimwaga machozi.



    Kwa uchungu mkubwa, akaanza kufunguka kinagaubaga. Akamweleza Jona ni kwa namna gani Eliakimu alivyokuwa anacheza mchezo wa damu kwa kutumia mkono wa serikali.



    Namna gani alivyokuwa anashiriki magendo na biashara haramu na vitu hivyo vikamvunisha pesa nyingi mno. Namna alivyokuwa akishirikiana na magenge ya wauaji, madawa ya kulevya, utakatishaji wa fedha na kadhalika na kadhalika nyuma ya pazia.



    Na ni kivipi alivyokuwa anatumkika kama mkono wa kushoto wa bwana Eliakimu akitumwa kuwamaliza maadui zake, na hata wale washirika wake waliomzulumu baada ya kupiga dili.



    Akamweleza Jona yote kumhusu BC na Sheng. Namna anavyowafahamu, na jinsi walivyoshirikiana na hao watu kutimiza kazi kadhaa za kimagendo, ikiwamo kuingiza nchini makemikali yaliyokatazwa, pia hata madawa ya kulevya.



    "Tulifanya hivyo kwa siri sana tukitambua wazi BC na Sheng walikuwa ni maadui wakubwa kibiashara, lakini tukafanikiwa kula na vipofu."



    Akamwambia pia Jona ni kwasababu gani walikuwa wanamuwinda Miriam, na kwanini basi mwanamke huyo alikuwa anatakiwa kuuawa japokuwa ni mke wa Eliakimu.



    "Kwanza Miriam hakuwa anampenda Eliakimu hata kidogo. Eliakimu alikuwa analijua hilo, lengo la mkewe lilikuwa ni kurithi tu mali zake pindi atakapofariki ama kumuua. Ilifikia kipindi Miriam akawa anatembea na mshirika mmoja wa kibiashara wa Eliakimu, mwanaume huyu akiitwa Nyokaa, mfanyabiashara wa madini Arusha.



    Nyokaa alikuwa amekorofishana na Eliakimu kwasababu za kibiashara. Kila mmoja akawa anataka kulipa kisasi kwa mwenzake kwa kutuhumiana kurudishana nyuma, lakini kiuhalisia ni Eliakimu ndiye alikuwa na makosa. Aliingia dili na Nyokaa, mwisho wa siku akamsaliti kwa kuchukua kiasi fulani cha mzigo wake na kumdanganya ulipotelea njiani kwasababu za kiusalama.



    Kulipiza kisasi na kurejesha fedha yake nyingi, akafanikiwa kumlaghai Miriam ili amtumie kunyooshea biashara zake kwa mtandao wa Eliakimu."



    Jona akakuna kidevu chake. Akajikuta anapata kiu ya kutaka kujua zaidi na zaidi kadiri alivyokuwa anaelezwa.



    Akataka kujua kwanini Nade hakutumwa kummaliza Nyokaa baada ya kuyatambua hayo. Nade akamwambia asingeliweza hilo kwani Nyokaa ana jeshi kubwa la watu.



    Si rahisi kumkamata kama kutamka.



    "Tulikuwa tunataka kumrejesha tu Miriam kwani alikuwa anajua mengi kumhusu Eliakimu, kwahiyo kuwa mikononi mwa adui, ilikuwa ni hatari sana."



    Lakini zaidi, Eliakimu asingeweza kutekeleza mipango na mambo yake yote haya akiwa peke yake. Hilo lilikuwa bayana.



    Ni lazima kuna watu vitengo na maeneo mbalimbali aliokuwa anasaidiana nao.



    "Ni watu wengi mno," akasema Miranda. "Kila mtu na eneo lake, kila mtu na kitengo chake. Kila mtu akicheza nafasi yake kutimiza maagizo ya Eliakimu. Na kwasababu alikuwa anatoa pesa nono, haikumuwia vigumu kuwakamata."



    Sasa Jona akaona kuna haja ya kutia nguvuni watu hao wote, lakini ushahidi ni muhimu sana kwenye hili. Ataupataje? Na atawapatia wapi watu wote hawa waliokuwa wanashirikiana na Eliakimu?



    "Usijali," Nade akamtoa hofu. "Eliakimu alikuwa ana orodha ya watu wake wote aliokuwa anafanya nao kazi, pamoja pia na mawasiliano yao."



    Akamwelekeza Jona wapi atavipata.

    "Chumbani kwake, kwenye droo za kitanda, utakuta nyaraka zake zote humo. Ufunguo wa droo hizo huwa anauweka ndani ya moka zake ndefu nyeusi kwenye stendi ya viatu."



    Jona akashukuru kwa taarifa hizo. Lakini kabla hajaondoka, akamsihi mwanamke huyo asimweleze mtu mwingine yoyote juu ya habari alizoongea naye. Nade akamhakikishia hilo kwa kuapia na maisha yake.



    "Sitakusailiti tena kwa sasa."



    Jona akaenda zake.



    Lakini kama ilivyo ada, nje ya hospitali Jona akaonekana na Alphonce aliyekuwa ameketi ndani ya gari lake. Mwanaume huyu akamtazama Jona akiishilia, kisha akashuka garini na kuzama ndani ya hospitali.



    Moja kwa moja akaonana na daktari na kumtaka afanye vile alivyokuwa anataka, amweleze yale yote Jona aliyoyafanya hapo. Kama haitoshi, akambana pia na nesi, ila bahati si kwake nesi wa zamu, yule aliyekuwa na Jona, alikuwa tayari ameshaondoka.



    Akaagiza aonane na Nade.



    Akaongozwa na nesi kupelekwa huko chumbani. Akamkuta Nade akiwa amelala. Akamwamsha.



    "Naweza nikaongea na wewe machache?" Alisema kwa sura ya bati kisha akamtazama Nesi kwa uso wa kumwomba nafasi. Nesi akaenda zake.



    Nade akamtazama Alphonce kwa macho makali akinyanyuka. Akakunja ndita zake na kuuliza:



    "Kumbe ni wewe?"



    Mwanamke huyu alikuwa anamtambua vilivyo Alphonce! Tayari kichwani kwake akajua mambo si shwari.



    Alphonce akatabasamu. Akatoa leso kwenye koti lake la suti kisha akajifuta viganja vyake.



    "Ndiyo ni mimi. Bila shaka ni muda mrefu umepita," akasema kwa sauti nzito.



    "Unataka nini hapa?" Nade akamuuliza. Alphonce akamkazia macho mwanamke huyo.



    "Unajua nataka nini, Nade. Mimi ni polisi, umesahau?"



    "Polisi gani wewe?" Nade akastahamaki. "Wewe ni muuaji tu uliyevaa sare za polisi. Hujawahi kuwa polisi hata siku moja!"



    Alphonce akaguna. Na mara akatabasamu.



    "Sijaja hapa kulumbana na wewe, Nade. Nina mambo mengi ya kufanya, kwahiyo tafadhali jali muda wangu nia--"



    "Sitakuambia kitu!" Nade akamkatiza. "Usitarajie nitakwambia lolote lile, Alphonce. Kwa hilo sahau."



    "Utakuwa unatania!" Alphonce akastaajabu. "Unajua wazi mimi na wewe tupo behewa moja. Unadhani kutokuniambia kitu kutakuweka wewe salama? Embu acha ujinga. Hii ni kwa ajili yetu wote. Niambie nini Jona alikuwa anataka toka kwako na kwanini alikuwapo nyumbani kwa Eliakimu siku ya tukio?"



    Nade akatabasamu. Akatabasamu tena zaidi.



    "Alphonce, naona hunielewi. Nimechoka na haya mambo, nipo tayari kufa lakini siyo kuendelea kufanya makosa yaleyale. Niliyofanya yanatosha, usidhani ntakusaidia wewe ukayaendeleze. Enough is enough!"



    "Acha upumbavu Nade!" Alphonce akafoka. Sura yake sasa ilibadilika na lile tabasamu la mwanzoni halikuwapo tena. "Acha ujinga wewe mwanamke! Unataka kwenda kuozea jela? Do you know how serious this matter is?"



    Nade akatabasamu akimtazama mwanaume huyo. Akamshika mkono na kumwambia kwa upole:



    "Yamekwisha, Alphonce. Kila zama zina mwisho wake. Umeshachelewa. Jiandae kwa anguko lako."

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alphonce akapandwa na hasira kali. Akamkaba mwanamke huyo mpaka alipohakikisha amekufa. Akawaza nini cha kufanya, akawaza ni nini Nade atakuwa amemwambia Jona.



    Kichwa chake kikazunguka kwa msongo wa mawazo. Akanyanyuka na upesi akatoka ndani ya chumba. Hakuonana na daktari wala nesi, akanyookea moja kwa moja ndani ya gari lake..



    Akaliwasha na gari lilivyoanza kwenda ndipo akapata akili juu ya nini cha kufanya. Aliamini Jona atakuwa ameelekea nyumbani kwa Eliakimu. Maneno ya Nade yalimshawishi aamini hivyo.



    Akaamua kueleka huko pasipo ajizi.







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog