Sehemu Ya Nne (4)
ASP Jamila na Inspekta Ussi Makame, walitoka katika ofisi ile, wakaangaza katika maeneo yale lakini hawakuiona gari aliyokuwa akiiendesha WP Monica, ambayo ilikuwa ikiwafatilia wakati wakienda pale Shangani.
ASP Jamila alimtizama Inspekta Ussi Makame, wakaingia katika gari yao, ASP Jamila alitoa simu akampigia Staf Sajenti Kubuta, akaisikia simu yake inaita. Akasubiri kupokelewa huku akiwa na wahaka mkubwa. Mara simu yake ikapokelewa. “Halow my dear, nimekuja kumfata mjomba hapa, nadhani muda si mrefu atatoka nje tuendelee na safari yetu, nipo na wifi yako yupo kwenye gari, mimi nipo maeneo ya Mkunazini, hapa ST MONICA’S HOSTEL!”
Staf Sajenti kubuta alijibu katika simu ile, na mara moja ASP Jamila akanga’amua jambo, nakumwambia. “Nije nikusindikize?” Na Staf sajenti Kubuta akajibu mle katika simu kisha ikakatwa simu ile. “Acha wivu mke wangu, mie kumsindikiza peke yangu mjomba umekuwa lazima na wewe uje? Basi mpigie wifi yako akuelekeze njia!”
Kwa majibu yale, mara moja ASP Jamila, alitafuta namba za WP Monica, alipozipata akampigia simu haraka! WP Monica alimwambia kila kitu, kilichotokea hadi kumfatilia Yule bwana alietoka mle ofisini kwa Marehemu Haruna kwa haraka na kwamba muda ule Staf Sajenti Kubuta, alikuwa amemfatilia ndani katika Hostel ile! Kwa majibu yale Insekta Ussi Makame, akaamriwa aendeshe gari waende Mkunazini, kuwafatilia wenzao, ili ikibidi nguvu iongezwe, na mafanikio yapatikane kwa haraka. Inspekta Ussi Makame, akatii agizo la kiongozi wake! Aliiondosha gari katika eneo lile la Shangani.
Inspekta Ussi Makame akiwa ni mwenyeji wa Unguja wa Kuzaliwa, aliijuwa mitaa ya Unguja vizuri sana. Hivyo alikatisha njia za haraka. Aliingia barabara ya Kaunda, akapinda kushoto katika mtaa wa Pipawaidi, akashika njia ya kulia barabara ya Vuga, alinyoosha hadi katika makutano ya barabara ya Health Office kwa upande wa kulia na mtaa wa Sokomuhogo kwa upande wa kushoto, Pale katika ofisi za shirika la ndege la Kenya. Kenya Airways akapinda kushoto kushika njia ya Sokomuhogo, kisha akapinda kulia kushika mtaa wa Mkunazini. Walipofika mita chache kabla hawajakata kona ya kulia katika barabara ile mpya ya Mkunazini, simu ya ASP Jamila ikaanza kuita. Nae alipoitazama simu ile, akaziona namba za WP Monica zikiwa katika kioo cha simu yake, akaipokea simu ile kwa taharuki kubwa.
*******
Staf Sajent Kubuta, aliuona mlango wa chumba namba nane, kitasa chake kikiwa kinazungushwa chini mlango ukifunguliwa. Baada ya simu yake kuita kwa sauti. Alipoitoa simu ile nakumuona mpigaji ni ASP Jamila, kabla hajaipokea ile simu aligeuka haraka akawa kama mtu anaekwenda kuteremka ngazi ashuke chini. Pia alisikia mlango ukifunguliwa kisha ukafungwa kwa funguo kwa nje. Yuke bwana wa chumba namba nane, alishika uelekeo wa alipokuwa yeye. Staf Sajenti kubuta aliipokea ile simu, huku akijifanya anazungumza na mkewe.
Yule bwana alimpita pale alipokuwa amesimama akamtizama kwa makini. Lakini Staf Sajenti Kubuta hakutaka kumpa nafasi yakukaririwa sura yake, aligeuka nyuma huku akimalizia kuzungumza na ile simu.
Baada ya Yule bwana kumpita, Staf Sajent Kubuta alitembea kumfata kwa nyuma huku akitaka pale mapokezi Yule bwana asiwe peke yake, akaja kuharibu picha. Hivyo pamoja na simu ile kuikata, lakini Staf Sajent kubuta bado alijifanya anazungumza na simu, huku akiwa anashusha ngazi.
Yule bwana aliteremsha ngazi hadi pale mapokezi, akawacha funguo tu nakuondoka bila yakusema neno lolote akaielekea Vespa yake, akaiwasha na kushika njia ya kuelekea barabara mpya ya Mkunazini.
Staf Sajent Kubuta, alipofika pale mapokezi, aliingiza mkono mfukoni kama anaetaka kukabidhi funguo, badala yake akatowa noti ya shilingi Elfu kumi na kumpa Yule mama huku akimwambia. “Utakunywa soda hii mama yangu, binaadamu sie hatufanani hivyo naomba utuvumilie!” Yule mama aliipokea huku asante zisizokuwa na idadi zikimtoka mdomoni mwake. Kisha akasema. “Umeshachukuwa hizo funguo? Sasa mbona mwenzako ametoka kama hakujui, Yule bwana ana dharau Yule?!”
Staf Sajenti Kubuta akaongopa “Amesema funguo hakuchukua. Hivyo nikamwambia kuhusu kutokukusalimia, lakini yeye amekasirika amesema hapa hakuja kusalimia, amekuja kwa kazi zake na hapa amelipa pesa zako tasilimu humdai.”
Yule mama muhudumu alipoambiwa maneno yale, alikuja juu akitoa faida kubwa sana kwa Staf Sajenti Kubuta, pamoja na jeshi la Polisi. “Ana jeuri yakulipa pesa tasilimu kikaragosi kile? Yeye hapa amepangiwa chumba kama mwanamke. Siku ya kwanza walipokuja hapa walikuwa wapo watu watatu, wote wamepangiwa hapa na Bwana mmoja kigogo anaefanya kazi Serikarini, siku ya pili wale watu wawili, waliondoka na kumuacha huyu bwana hadi leo. Pesa ya pango hapa analipa huyo kigogo huyu kapuku tu!”
Staf Sajenti Kubuta akajifanya kustuka, akamsaili Yule mama huku macho yake, yakimtazama Yule bwana ambae kwa hakika alikwenda pale Hostel na kubadilisha nguo tu. Sasa alikuwa ameshaifikia ile Vespa yake na kuikwea akaiwesha na kuiendesha akishika njia ya Barabara mpya ya Mkunazini.
“Mmmm mama yangu wee huyo bosi mwenyewe wewe unamjua aliempangia hapa? Asije akawa labda huyu jamaa analawitiwa na huyo bwana uliemwita Kigogo?!”
Yule mama alitoa kicheko kirefu sana. Alicheka kicheko cha ushangingi. Kisha akasema “Unguja hii, akija kwa macho ya juu, atapakatwa kweli na wanaume wenzie. Ila Yule kigogo inaonekana hana michezo hiyo, kwani hajawahi kuja tena tangu siku alipokuja kuwalipia vyumba hapa na kuwakabidhi, hajaja tena hadi hii leo Hawa watakuwa watwana wake tu anawatuma hawa!”
Staf Sajent kubuta alitungua kicheko. Kisha akamwambia Yule mama; “Haya mama yangu wa khiyari mie natoka ila nitakuja tena wakati mwengine tupigepige story, akachukua namba ya simu ya Yule mama kisha akamuaga Yule mama aliemzowea kwa haraka, na kutoka nje ya Hostel ile akaenda katika gari yao mahala ilipokuwa na kumkuta WP Monica anazungumza na simu!
“Halow Afande, mwenyeji wetu ametoka na sie tunamfata tupo timamu kabisa, tunaelekea barabara mpya ya Mkunazini” WP Monica alimaliza kuzungumza na simu, nae akasikia akijibiwa na kiongozi wake.
“Pamoja sana tupo Mkunazini, jirani na mlipo hapo kwa ajili ya kuongeza nguvu.” ASP Jamila baada ya kusema maneno yale alikata simu, na mara wakaiona gari waliyokuwa WP Monica na Staf Sajenti Kubuta, ikipita kuvuka mtaa ule wa Mkunazini, na kushika Barabara mpya ya Mkunazini.
Inspekta Ussi, aliongeza mafuta mguuni, gari ikaongeza mwendo. Walipofika pale katika kona ya Barabara ya Mkunazini, wakapinda kushoto, na wakawa wanaiona kwa mbali mbele yao ile gari ya askari wenzao, ikiambaa na njia. Inspekta Ussi aliongeza mwendo gari ile, wakaikaribia ile gari na mara wakapunguza mwendo, kwani Vespa nyekundu ilikuwa mbele yao ikionesha endiketa ya kuegesha pembeni kando ya barabara.
Yule dereva wa Vespa alitoa simu yake akazungumza mahali, kisha akaigeuza ile Vespa kurudi njia aliyotoka huku akiwa makini sana na vioo vyake vya pembeni, kwani mishale ya hatari ilikuwa inagonga katika kichwa chake mfululizo.
Naam mara akaiona ile gari ambayo alikuwa anataka kuihakiki kama inamfata yeye, ikigeuza na kuunga kurudi katika njia ile aliyokuwepo yeye taratibu. Kuona vile akatoa tena simu yake akapiga pahala alipokuwa akizungumza napo awali, kisha akawa anatabasamu huku akivuta mafuta kwa mkono, katika Vespa ile nakuongeza mwendo.
WP Monica alipoona jamaa anaongeza mwendo, nae akakanyaga mafuta mgandamizo mkubwa, chombo kikaongeza kasi kuifatilia ile Vespa. ASP Jamila na Inspekta Ussi, nao walikwenda mbele kidogo wakageuza, na wao wakaunga katika kuwafatilia wenzao, ambao sasa walikuwa wameshasonga parefu kiasi.
Ile Vespa dereva wake alikuwa akiendesha huku akitazama vioo vyake vya pembeni. Alipofika pale katika makutano ya Barabara inayokutanisha mitaa miwili ya Mkunazini na Tharia, akapinda kushoto kuelekea mtaa wa Tharia kama anakwenda Mchambawima, aliivuta ile Vespa hadi maeneo ya Mchambawima, akaelekea Hurumzi, huku akitazama nyuma akawa anaiona gari ndogo ikiwa inamfata. Akanyoosha Vespa ile hadi maeneo ya Kiponda. Alipofika pale akasimama na kushuka.
Mara zikatokea gari mbili ndogo zikawa zinatembea kwa kasi kama zinazotaka kupishana lakini hazipishani. Zilitembea vile zikiwa sambamba hadi zikakutana uso kwa uso na ile gari aliyokuwa akiiendesha WP Monica. Ile gari iliyokuwa upande wa kulia ilisimama uso kwa uso na gari waliyokuwamo WP Monica na Staf Sajenti Kubuta. Ile gari iliyokuwa upande wa kushoto ilisimama usawa wa mlango wa gari ya kina afande Kubuta na kwa kasi ya ajabu, milango ya nyuma ilifunguliwa, na wanaume wawili waliokuwa na bastola mikononi mwao, waliteremka kwa haraka na kuwaoneshea wale asakri wawili pale dirishani silaha zile.
Yule jamaa mwengine alieshuka kutoka katika gari ile hakutaka kuzunguka gari ile ndogo saloon, waliyokuwamo WP Monica na Staf Sajent Kubuta. Bali yeye aliruka samasoti akawa yupo upande wa pili wa dirisha la gari ile. Huku bastola ikiwa mbele ya mikono yake. Ikawa asakri wale wawili kila mmoja alikuwa akitazamana na mdomo wa bastola.
Askari wale waliamriwa kutoka nje ya gari ile, wakiwa wanatoka nje, mara Yule jamaa mwenye Vespa Nyekundu, alikuja akiwa katika Vespa yake akasimama na kuwatazama kwa macho yaliojaa shari askari wale. Kisha kwa dharau na kejeli akasema. “Huu siyo wakati wa Simba kuchunga maisha yake, ni wakati wa digidigi kuchunga maisha yake! Vijana mmeingia maji marefu, basi na sie tutawaonesha cha mtema kuni.” Baada ya kusema maneno yale, akawaacha wakidhibitiwa, yeye akaendelea na safari yake.
Inspekta Ussi alikanyaga Breki ya fadhaa, kwani alikuwa katika mwendo kasi, lakini pia aliiona ile gari ya wenzao ikiwa imesimama, milango yake ya kushoto na kulia ikiwa ipo wazi. WP Monica na Staf Sajenti Kubuta, walikuwa nje ya gari ile wakiwa wamechuchumalishwa chini huku mikono yao, ikiwa ipo kichwani kama jinsi walivyotakiwa washike vile na wale jamaa waliowateka.
Wale jamaa waliokuwa gari yao imewazibia njia gari ya kina WP Monica kwa mbele, walishuka nakuifata gari iliyokuwa imepiga Breki haraka. wakaiendea na kuwaamuru wale waliokuwamo ndani ya gari ile ASP Jamila na Inspekta Ussi, washuke ndani ya gari ile. Wale jamaa mmoja mikononi mwake alikuwa ameshika silaha ya kivita mashine gun AK 47. Yule Jamaa aliekuwa na silaha ile alikuwa amesimama upande aliokuwa amekaa ASP Jamila. Na askari wale wakatii amri ile haramu ya wale madhalimu, wakatoka nje ya gari yao mikono yao ikiwa imenyooshwa juu.
*******
Katika gereza la Mahabusu la Segerea, watu walikuwa wengi siku ile ya Jumamosi, waliokwenda kuwatembelea ndugu zao. Siyawezi Binti Gonga alikuwa na kikapu alichojaza mazagazaga kadhaa pamoja na chakula, alichompelekea mume wake pale gerezani. Chakula alitoka nacho nyumbani kwake pamoja na nguo za mumewe za kubadilisha. Lakini maji safi ya kunywa, sabuni, mswaki, dawa ya meno, nyembe, pamoja na Mikate, alinunua katika duka la magereza, lililokuwa nje ya Gereza lile.
Askari walikuwa wakali mtu anapokuja na maji na mikate yake kutoka huko atokako, basi pale Gerezani vilikuwa vinazuiliwa, ikielezwa kuwa huko hakuna usalama wa vitu hivyo, kwani raia wanaweza kuweka vitu vibaya vikamdhuru mlengwa, au vikaleta maafa ndani ya Gereza. Hoja zote hizo zilikuwa na maana moja kubwa tu. Kuungisha kwa kununua vitu kutoka katika Duka la Magereza ili vitu viishe na wao waweze kupata faida. Yaani pamoja na ndugu wa jamaa kuwa ndani ya gereza, na wao walitakiwa wanunue vitu vyao ili kuwapa ndugu zao, kama mtu aliekwenda pale kutaka kuzungumza na jamaa yake kwa maneno matupu bila yakununua kitu, alizuiliwa nakushauriwa aende siku za kazi ili akaonane na jamaa yake kwa utaratibu maalum. Lakini kwa kwenda mwisho wa wiki, ilikuwa ni lazima ununue kitu japo wembe.
Siyawezi alikuwa ameandikisha jina lake katika karatasi ya nne. Karatasi ile iliingizwa ndani ya Gereza na askari aliekuwa katika kitengo kile.
Kule ndani ya Gereza, karatasi ile alipewa Odeli wa kifungwa ili mle gerezani aweze kuita majina ya mahabusu, na wafungwa ambao wamekuja kuonwa na jamaa zao. Karatasi ile iliandikwa jina la mtu mwenyeji uliekwenda kumtembelea. Pia iliandikwa jina lako wewe mgeni uliekwenda, mahali utokako, na uhusiano wako na mtu uliemtembelea pale Gerezani. Watu waliokuwa wameandikisha mapema majina yao, waliitwa kwenda kuonana na jamaa zao.
Odeli kule ndani ya gereza, alikuwa anatembea katika magereza matatu, kati ya mane yaliokuwa ndani ya Gereza lile la Segerea. Akiita majina yalioandikwa katika karatasi ile, na kila ambae amesikia jina lake likitajwa aliitika, Odeli akaweka alama ya pata katika jina lake. Ili asiliite tena jina lile.
Odeli yule alianzia kuita majina yaliyokuwa katika karatasi ile katika Gereza la watoto watukutu, watoto ambao umri wao ulikuwa chini ya miaka kumi na minane, ambapo juu katika mlango wake mle ndani kuliandikwa ‘Special Wing’.
Baadae alienda kule ufungwani ambapo ndipo wanapokaa wafungwa, na ndiyo pia kwenye jiko lakulisha Gereza zima. Kisha akamalizia kule wanapokaa mahabusu watu wazima ‘Rumande Wing’.
Gereza la nne ni la wanawake ambalo mfungwa wa kiume haruhusiwi kuingia kule, pia limetengwa nje ya Gereza la wanaume. Japokuwa wafungwa wa kiume wanaoingia ni wale wapishi tu, wao huingia wakiwa chini ya usimamizi wa askari wa jiko, wakeshapeleka chakula, hukiacha Gadi na wafungwa wanawake huja kuchukua chakula kile pale. Kwani lau kama wafungwa wakiume wangeliachiwa kuingia kule katika gereza la wanawake, hakika wangelibakwa na wanawake waliokuwa wamekaa miaka mingi bila yakukutana na mwanaume kimwili. Ndiyo maana kuzuia hali yakusagana na mambo mengine, katika gereza la wanawake hairuhusiwi ndizi, matango, karoti, soseji, na mfano wa vitu hivyo kuingia katika uhalisia wake, ila zitakatwakatwa katika vipande vidogovidogo na kupewa muhusika. Lengo kubwa lakufanya hivyo ikiwa ni kuzuia wafungwa na mahabusu wa kike, kuvitumia vitu hivyo kama zana zakujipa au kumpa mwenzake burudani. (Kusagana)
“Weee Nyonzo bin Vule weee, wee Mikao kwa janta wee, wee Athumani Dobe wee, wee Miki Densa wee, wee Nagwa stima wee, wee twende mwizi twendee mama kaleta mwizi. Wee uliesikia jina lako uje bwana, dada kauza mama kaleta, wee wameletaa. Wee uliekuwa huko chooni ukigonga Podo, ukigongea Bingili za Rosta, acha uje kupokea cha nje.” (Podo ni sigara spoti. Bingili za Rosta, ni vipisi vya sigara nyota) Ilikuwa ni sauti ya Odeli wa Kifungwa aliekuwa akiita majina ndani ya gereza, ili watu wakaonane na jamaa zao. Na kwamba waache kujificha chooni na kuvuta sigara. (Kiberiti na Sigara, ni marufuku kuingia navyo ndani ya Gereza, ukikutwa navyo adhabu kali huchukuliwa dhidi yako, ikiwemo kupigwa rungu nyingi, na kuwekwa selo ya peke yako, yaani chumba cha adhabu PC. Ukiwa humo hata kama ndugu zako wamekuja kukutembelea huruhusiwi kuonana nao hadi umakize adhabu, unapata robo ya ugali au robo ya wali kutegemea na ratiba ya siku ya chakula gerezani.)
Athumani Dobe, alikuwa amekaa chini ya Mkungu, karibu na Mesi akiwa hana raha, muda mfupi aliokuwa mle gerezani, alikuwa amechoka kama aliekaa mwaka mzima! Mlo mmoja kwa siku aliokuwa anakula mchana wa saa sita, hadi siku ya pili tena saa sita. Ugali wa dona uliojaa mabuja, katika bakuli la bati, na maharage machache na maji ya maharage yaliyojaa katika kikombe cha bati, nasema maji ya maharage, kwa sababu hayana sifa ya kuitwa mchuzi. Tena chumvi siku nyingine iwepo, siku nyingine isiwepo.
Maharage yale hayana kitunguu, wala kiungo chochote unachokijua wewe kinatiwa katika maharage. Mafuta machache yaliotiwa katika maharage yale, yakifika na maharage yake, baadhi ya Manyapara huyaengua na vikombe vyao, wakawa wao ndiyo walaji wanayaweka mafuta yale katika chupa za plastiki, ili wawe kila siku wanakula maharage yenye mafuta, tofauti na watu walioitwa ngulumbili, Viande, walala nje, wajaza jela, majina waliokuwa wakiitwa na watu wenye kesi kubwa kubwa pamoja na baadhi ya Manyapara wale.
Yaani wale wote wenye kesi za mahaka za mwanzo, na mahakama ya City, walidharauliwa sana gerezani na mahabusu waliokuwa wana kesi katika mahakama za wilaya, mkoa au mahakama kuu.
Athumani Dobe na mahabusu na wafungwa wote, kasoro Manyapara. Asubuhi walikuwa wakinywa uji katika kikombe cha bati, tena kikombe kimoja cha uji wa dona ambao sukari yake iliwekwa kama uji ule anakunywa mgonjwa wa Kisukari.
Tangu ameingia Gerezani Athumani Dobe alikuwa hajapiga mswaki kinywani mwake. Angeupata wapi? Meno yake meupe kama theluji, yalibadilika rangi yakawa kama jezi ya Yanga. Chawa walianza kumshambulia, tayari alianza kutokwa na vipele. Maji ingawa yalikuwepo, lakini kwa kuwa hakuwa na chombo cha kuhifadhia maji yale, kulimfanya asioge tangu ameingia Gerezani wiki moja iliyopita. Ukosi wa shati lake ulibadilika rangi, na kuwa mweusi tii kwa jasho. Nguo yake moja aliyoingia nayo Gerezani, ilijikunja na kuchafuka vibaya sana. Athumani dobe tumbo lote lilikwisha. Hakika alitia huruma ukimtazama. Nywele zake kubwa zilizokosa kitana maji na mafuta, zilikuwa kama za punguani.
Suruali yake ilikuwa inampwaya haina mkanda, chini miguu yake alikuwa yupo pekupeku kwani, siku aliyoingia Gerezani, Mkanda na viatu alikabidhi kwa Mfungwa anaetunza Mkanda, viatu. Mahabusu ndani ya Gereza haruhusiwi kuvaa mkanda kwa sababu za kiusalama. Mbali yakuwa inahofiwa mahabusu/mfungwa ataweza kujinyonga hadi akajiuwa, lakini pia mkanda unaweza kutumika kama silaha ukaweza kumpiga nao mwenzako ukamjeruhi, au ukamuua kabisa.
Hata Viatu vya kutumbukiza ambavyo vina kamba kama viatu vya Athumani dobe, ni marufuku kupewa kuvaa ndani ya Gereza kwa kuwa zile kamba zinaweza kuleta madhara. Mkanda na Viatu Mahabusu huruhusiwa kuvaa pale anapokwenda mahakamani. Ila ukiwa na yeboyebo, malapa, au Sandoz, ruksa kuvaa ngani ya gereza.
Athumani Dobe, aliinuka haraka pale chini ya kivuli cha mti wa mkungu, alipokuwa amekaa yeye na mahabusu wengine wengi, ambao walikuwa hawana habari kabisa kama wapo jela. Wapo waliokuwa wanacheza mchezo wa Draft, Bao la kete, na Mpita wa miguu wa makaratasi. Kule katika kiwanja kidogo kilichopo usawa wa selo namba namba tano na sita katika gereza lile. Wapo waliokuwa wanasikiliza miziki katika radio ndogo za mikononi, wapo waliokuwa wanazungumza kukumbushana nje ya Gereza Uraiani. Watu wa jela huku uraiani wanapaita ni Duniani.
Athumani dobe, alimuuliza Yule Odeli. “Kaja nani kuniona?” Yule Odeli wa kifungwa, aliitazama ile karatasi yake katika jina la mtu aliekwenda kumtembelea Athumani Dobe, akamjibu “Kaja Siyawezi mkeo.” Athumani alipata faraja, kiasi alichangamka kuja kuonwa na Mkewe. Kwani alikuwa na hamu kubwa sana yakumuona mkewe, lakini pia kupata kujua taarifa za nje, lakini pia kufahamu juu ya kesi yake mambo yanavyokwenda.
Yule Odeli alitia pata majina yote aliyoyaita, kisha kundi la wale mahabusu walioitika majina yao, wakawa nyuma ya yule Odel wakimfata ili awapitishe pale gadi ya ndani, ili waende pale katika mti wa mzambarau ambapo huwa ndiyo mahabusu na wafungwa, huwa wanasubiri ndugu zao nje waingie pale Gadi kubwa, ili waweze kuonana na kuzungumza nao.
“Meja nipo na wezi hawa, mama zao leo wamewakumbuka wamewaletea chemi cola, nawatobolesha lango wakaonane nao.” Yule Odeli wa kifungwa alimwambia askari magereza aliekuwa gadi ya ndani ya Gereza lile, na yule askari akachukuwa ile karatasi kwa odeli, akasimama mlangoni akaanza kuita majina moja baada ya moja, na kila aliesikia jina lake, aliruhusiwa kutoka pale katika gadi ile ya ndani. Wale mahabusu wote walikuwa wamechuchumaa chini, kila mtu akisikia jina lake anaitika na kupita hadi wote wakesha katika karatasi ile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ile karatasi namba nne ilitolewa nje na askari magereza. kule nje waiitwa majina wale ambao jamaa zao wameitika ndani, wote wakaingia ndani pale Gadi kubwa kwa ajili yakuonana na ndugu zao. Mara baada yakuingia ndani wanandugu wale, mahabusu nao waliinuka pale chini ya mti wa mzambarau, wakaenda pale Gadi kubwa wakapinda kulia wakaingia pembeni ya Gadi ile, Katika chumba maalumu kilichokuwa na wavu madhubuti. Wavu ambao ili kumuona nduguyo, ilibidi utumie nguvu za macho za ziada.
Siyawezi binti Gonga, alipomuona mumewe hali yake, ubalamaki wote ulimwisha machozi yalimtoka kwa uchungu akasema.
“Pole mume wangu pole. Daaah ndivyo ulivyo hivyo Athumani? Ama kweli Jela siyo mahali pazuri dah. Inshaallah utatoka mume wangu. Hakika hukumuua Mauwa nakataa abadani asilani. Utakawia tu humo ndani lakini utatoka. Jela siyo kaburi. Athumani mume wangu kule kupiga tu huwezi, sembuse leo uje kushitakiwa kwa kuuwa?! Huko kaburini kama kweli kuna adhabu, basi namuomba Mungu amzidishie adhabu yule Malaya mtoto Mauwa, mpaka akome. yule ndiyo chango mzaa maradhi yule, afiriti mkubwa asiekuwa na haya wala hajui vibaya. Ndiyo maana akauwawa mwanaharamu yule. Hivyo simu zote hakuziona katika ile boti mpaka simu ya mume wangu? Mwanahizaya Yule Amekwenda kunipotezea Mume wangu mie. Hivyo Siyawezi mie wakulala peke yangu nakukumbatia mito inahusu?!”
Athumani alinyamaza kimya maana hakuwa na kauli alikuwa ameinama tu, machozi yakimlengalenga.
“Oyaa muda umekwisha sasa njooni mtoe vyakula mwende zenu, kwani muda wenu umekwisha, huko nje kuna wenzenu nao pia wanataka kuja kuingia humu kuwaona ndugu zao, haya toka huko.”
Askari Magereza alikuwa anasema huku akiwatoa watu kule ndani ili waje kutoa chakula wapishe na wenzao waweze kuja kuwatembelea ndugu zao.
Athumani Dobe alitaka kumueleza kitu mkewe, lakini wakawa hawasikilizani, kila mahabusu aliekuwa pale katika chumba kile alikuwa akizungumza kwa sauti, ili ndugu yake asikie, matokeo yake ikawa ni mazogo mtindo mmoja, huyu anasema Yule anasema, hakukuwa na mtu wakumuachia nafasi mwenzake, pale ilikuwa kama wapo jandoni, kila mmoja alikuwa anawania uume wake upone. Hivyo hahukuwa na wakumuhurumia mwenzake.
Wale wageni wote walitii amri ya askari magereza. Walitoka kule walipokuwa kwenye uzio madhubuti, walipokuwa wakiongea na ndugu na jamaa zao, wakaenda pale gadi sehemu ya kutolea chakula.
Kila mtu akiwa na chakula chake alikitoa katika chombo alichokwenda nacho, akakitia chakula kile katika mabakuli ya Bati ya Jela. Kisha akakionja chakula kile chini ya usimamizi wa askari magereza. Halafu askari Magereza hukichukua chakula kile na kumpa mlengwa chakula chake.
Siyawezi alionja chakula alichopeleka, kisha akampa askari chakula kile. Askari magereza alikipokea chakula kile, akampa mlengwa Athumani Dobe.
Baada ya Siyawezi kutoa chakula, akamkabidhi vile vitu yule askari magereza. Yule askari alivikagua vile vitu kwa makini, kisha akamkabidhi Athumani Dobe. Nguo, Mswaki, Dawa ya meno, Sabuni, Nyembe, Mikate, pamoja na Maji safi ya Uhai lita sita. Kisha Siyawezi akamwambia Mumewe kwa upendo pale pale kwenye nondo wakitazamana.
“Punguza mawazo Mume wangu, nitatembea mashariki na Magharibi, Kaskazini na Kusini, Mchana na Usiku mpaka nihakikishe unatoka Jela.”
Athumani Dobe alimshukuru Mkewe kwa kwenda kumuona, kumpelekea vitu, lakini pia kumfariji. Kwani mtu akiwa jela anaishi kwa matumaini, hasa akiwa ana kesi nzito kama ya mauwaji inayomkabili yeye.
Athumani alimshuhudia mkewe akitoka nje ya mlango wa gadi kubwa huku akifuta machozi kwa upande wake wa khanga. Nae aligeuza kurudi ndani huku machozi yakimtoka vilevile. Kwani asingekuwa na uwezo wakuondoka na mkewe, Ama kweli Jela Jeraha.
****
Yule jamaa alieshika ile silaha ya moto ya kivita AK 47, alimsogelea ASP Jamila akaanza kumpapasa akimpekua kama ana silaha au kitu chochote cha hatari kwa upande wao. ASP Jamila aligeuka kwa wepesi ambao Yule jamaa hakuutarajia. Alipiga pigo moja takatifu la Karate akapiga mikono ya adui na ile silaha yake ikenda chini bila ubishi. Yule bwana baada yakuona silaha imemdondoka, alirusha teke zembe ambalo lilimgharimu. ASP Jamila aliliona lile teke lililokuwa likimfata kifuani mwake. Haraka akachanuka msamba na teke lile likapita juu hewani. ASP Jamila akiwa pale chini ametanua miguu yake katika mtindo wa msamba, alikuwa anatizamana na adui ana kwa ana. Hivyo alimrushia ngumi jiwe aina ya Gedan Nzuki, ikatua katika korodani za Yule jamaa. Yule jamaa ngumi ile ilimuingia barabara, akatoa yowe kubwa na kujipinda huku mikono yake ikishikilia korodani zake akiwa anaruka ruka kwa maumivu.
Kwa kuinama kule Yule adui alikuwa ameufanya uzembe mwengine wa mwaka, kwani uso wake ulikuwa uwazi hauna kizuizi chochote, nafasi kama ile mpiganaji yeyote angeitaka aipate wakati wa mapigano. ASP Jamila alijiinua kwa haraka pale chini, akasimama huku ameinama kidogo kama mtu aliekuwa katika ulingo wa ngumi. Alipiga Panchi mfululizo kwa haraka kama sita hivi. Ngumi zile za uso zinaitwa Jodan Nzuki. Adui meno yake yalipururuka kinywani mwake, akatema ‘tambuu’. Ngumi zile zilimlewesha adui akayumba yumba na kuanguka chini uso wake ukiwa umetapakaa damu tupu. Akiwa pale chini Yule adui alijizoa zoa kwa tabu akafanikiwa kusimama wima.
Rsisasi zilirushwa na Yule adui alekuwa karibu na WP Monica, zikamkosa ASP Jamila Jirani sana na pale alipokuwa amesimama akimshuhudia Yule jamaa alivyokuwa akisimama.
ASP Jamila alijitupa chini kama mkizi risasi kadhaa zikipita pale pale alipokuwa amesimama, zikampata kifuani adui aliekuwa sawa yake, zikamchakaza vibaya sana na kuchukua uhai wa adui Yule. Yaani laiti kama Afande Jamila asingejilaza chini, hapana shaka wakati huu ingelikuwa tunasema mengine.
Akiwa pale chini ASP Jamila alijizungusha pale chini akagalagala kwa kubimbilika na kuishika ile silaha ya Yule adui iliyomtoka mikononi mwake silaha ya AK 47. Akiwa bado amelala pale chini akiwa kichalichali aliinua silaha ile nakuanza kurusha risasi kwa maadui.
Yule jamaa aliekuwa na Inspekta Ussi, alipigwa risasi za miguu na risasi za ile AK 47, zikamvunja miguu yake yote miwili. Akatupwa chini akawa anaugulia maumivu makali zaidi ya risasi. Huku damu nyingi sana ikimtoka katika majeraha yake ya risasi.
Inspekta Ussi baada yakumuona kiongozi wake amelianzisha, nae haraka alijitupa chini akimuacha Yule adui akiwa peke yake amesimama wima kitendo kilichomsaidia Afande Jamila kumpata Yule adui kwa urahisi, kwani kama nae angelikuwa amesimama, angemkosesha Afande Jamila shabaha kwa adui, kwa kuchelea kumshambulia na yeye. Inspekta Ussi alitoa bastola yake kiunoni huku akiwa amelala chini, akamnyooshea Yule adui aliekuwa amemdhibiti Staf Sajenti Kubuta. Sasa akawa anatazamana nae uso kwa uso wote wakiwa wamelala chini kifudifudi, mikono yao ikiwa ina sihala ndogo za bastola.
Wale jamaa waliokuwa wamewadhibiti WP Monica na Staf Sajenti Kubuta, walilala chini wakichelea ile mashine gun AK 47 iliyokuwa ikikohoa risasi zake kwa mpango. Kwani mpigaji alikuwa anapanga mapigo yake. Alikuwa anapiga risasi mbilimbili kisha anatoa risasi moja moja, mara anakohoa risasi tatu tatu.
Adui alichanganyikiwa vibaya sana, kwani hakutarajia upinzani mkubwa kiasi kile. Wale maadui wawili wenye silaha ndogo za bastola, walikuwa siyo tena wakiwadhibiti wale askari waliowateka laa, bali walikuwa wamelala wakinusurisha maisha yao. Ama kweli maisha matamu.
WP Monica alikuwa amelala kifudifudi, hakuwa na silaha mwilini mwake, wala Staf Sajenti Kubuta pia pale alipo hakuwa na silaha vilevile. Hivyo walitegemea sana mikono yao kuwa silaha, lakini kwa mazingira yale walikuwa hawawezi kusimama wakati risasi za AK 47 zinarushwa. Lakini pia wale watekaji wao wana silaha na wamejitupa chini chache na walipo tena wakiwa wameshika silaha za moto mikononi mwao.
ASP Jamila alikuwa anawatia hofu pia akiwanyima nafasi wale jamaa yakushambulia. Pale alipokuwa alijibinua kutoka kichalichali alichokuwa amelala awali, akawa amelala kifudifudi. Pale aliweza kuwaona adui vizuri sehemu walipo.
Inspekta Ussi, akiwa na Bastola yake mkononi aliwaona wale adui wakimlenga ASP Jamila pale chini ili wampige risasi. Mara ukasikika mlio wa risasi wa silaha ndogo aina ya Baleta, aliyokuwa nayo Inspekta Ussi ikikohoa.
Inspekta Ussi alifyatua risasi ili kuwanyima utulivu wa shabaha wale maadui wawili waliokuwa wamelala katika pande tofauti tofauti.
Yule jamaa aliekuwa karibu na Staf Sajenti Kubuta, aligeuka ili ampige risasi Staf Sajenti Kubuta, lakini alikutana na upinzani ambao hakuutarajia kabisa katika nafsi yake. Staf Sajenti kubuta akiwa amelala kifudifudi, macho yake yeye muda wote yalikuwa yakimtazama Yule adui aliekuwa mbele yake na silaha ndogo ya bastola aina ya Chinise, yenye kubeba risasi nane ndani yake. Hivyo alipomsoma Yule adui kuwa anageuka ili amshambulie, kwa wepesi alijilaza ubavu akarusha teke kwa adui yake aina ya Mawashi Geli, teke lile likaipangusa ile bastola mikononi mwa adui na kudondokea mbali na wao walipolala. Staf Sajenti Kubuta lile teke alilopiga hakuliacha libaki kule kule bali aliurudisha mguu wake haraka akakita usoni kwa adui kwa kutumia soli ya kiatu kile. Teke lile linaitwa Maigeli. Yule adui akatoa yowe la fadhaa. Kwa sekunde chache za pigo lile, uso wa adui uliumka mara moja, ukawa umevimba.
ASP Jamila akiwa amelala kifudifudi, alimuona vyema Yule adui aliekuwa amelala kifudifudi, jirani na alipokuwa WP Monica. Hivyo pale alipo alionesha Mbinu za Medani (MM) na kumshanga adui (MM = Mbinu za Medani) Aligalagala kwenda kushoto mara mbili huku akipiga risasi zile usawa wa juu kwa adui, ili kumfanya adui asirushe risasi, kisha akagalagala upande wa kulia mara tatu, yaani alikuwa akibimbilika na bunduki ipo mikononi, alipokuja kulala kifudifudi, alikuwa yupo katika shabaha nzuri, aliishusha silaha ile huku ikikohoa risasi ikapiga utosi wa adui na kufumua ubongo ukaruka juu pamoja na damu, adui akawa maiti sekunde ileile.
ASP Jamila aliinuka kidogo akapiga goti huku akigeuka huku na kule ili aweze kusafisha uchafu wowote utakaojitokeza, lakini eneo lile lililokuwa likinuka baruti lilikuwa showari hakuna shari. Watu wachache waliokuwa katika majumba yao, hakuna aliethubutu kutoka nje.
ASP Jamila alisimama akawa anakimbia kama hatua kadhaa kasha analala chini, kusikiliza kama kuna upinzani, alifanya hivyo kila aliposikia kimya, hatimae akamfikia WP Monica. Afande Jamila aliichomoa Bastola iliyokuwa ameivaa mbele kwenye kinena, akiwa amelala pale chini, aliirusha bastola ile kumrushia WP Monica. Wp Monica aliidaka silaha ile akaikoki, kisha akamnyooshea Afande jamila alama ya dole gumba, kwa mkono wake wa kushoto, na mkono wake wa kulia, akawa ameidhibiti ile silaha sawasawa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Askari wale walilala vile kwa muda kadhaa, kisha wote wakainuka kwa tahadhari kubwa sana pale walipoona kimya kimetawala. Wote walizizingira zile gari, wakiwa makini sana.
Gari zile hazikuwa na kitu cha ziada, kwani bado zilikuwa mashine zake zikiunguruma, yaani zilikuwa katika ‘Silence’.
Staf Sajenti Kubuta aliifata ile silaha aliyokuwa ameipiga teke mikono ya adui, akaichukua akamrudia Yule jamaa aliekuwa akiugulia kwa maumivu, uso wake ukizidi kuvimba, pua yake mshipa ulipasuka damu ilimmwagika nyingi, ikawa imeganda katika uso wake. Alitikuwa anatisha kumtazama.
Staf Sajenti Kubuta alimpekuwa Yule jamaa mifukoni mwake, akamkuta na simu pamoja na wallet, iliyokuwa na pesa na vitambulisho. Kama kuna jambo lililowakosesha amani askari wale, basi ni vitambulisho walivyomkuta navyo Yule adui. Hakika kila askari aliekuwa akivitazama vitambulisho vile, alitikisa kichwa kwa masikitiko. Kwa vitambulisho vile, askari wale ilibidi wawapekue na wale maadui wengine watatu, ambao wawili kati yao, tayari walikuwa ni maiti. Wawili ndiyo walikuwa majeruhi, kati ya wale wawili mmoja alikuwa mahututi sana. Yule alievunjwa miguu na risasi za AK 47, alikuwa mahututi sana, kwani majeraha ya risasi yalimmwagika damu nyingi sana, hivyo kumfanyanya apoteze fahamu.
Wale maadui wengine, walipopekuliwa hawakuwa na kitu chochote. Hawakuwa na simu, wala vitambulisho, wala pesa. Walikuwa watupu.
Inspekta Ussi Makame, Mkuu wa upelelezi wa kituo cha polisi madema, aliwasiliana na askari wa kupambana na vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha Anti Robary, wafike mahala pale walipo mara moja. Aliwaelekeza mahala walipo na akaahidiwa kufikiwa mahala pale haraka iwezekanavyo.
Watu walianza kusogea eneo la tukio, huku hofu ikikitawala kisiwa cha Unguja katika eneo lile la Kiponda. Kwani wakazi wa Unguja ukiondoa rabsha za kipindi cha uchaguzi, au sekeseke la askari wa mji kupambana na machinga wa pale Darajani, mji ule unaweza kukaa mwaka mzima na zaidi hutasikia milio ya risasi.
Ndani ya dakika kumi, magari mawili aina ya Land lover 110, Defender askari wakiwa wananing’inia na bunduki mikononi mwao waliwasili eneo la tukio, gari moja ikabeba maiti za wale maadui, na gari nyingine ikabeba majeruhi. Askari wale wawili waliingia katika yale magari, waliyokuwa wakiyaendesha maadui wale, na kuyaendesha kuelekea kituoni Madema.
ASP Jamila alikuwa amechafuka kuliko askari yeyote aliekuwa pale, kwani Balaa walilokutana nalo, hakika lilikuwa ni Balaa kubwa. Alikuwa amechafuka vumbi, lakini pia alipatwa na michubuko midogomidogo. Askari wale aliokuwa nao walimpongeza kwa ujasiri aliouonesha kwa wale maadui, na kuwafanya wawe washindi. Kwani kama si juhudi za haraka za Afande Jamila, mambo yangekuwa yanasemeka vinginevyo.
Kila kitu kiliwekwa sawa, wakarejea kituoni ili kwenda kutafakari na kupanga mikakati yenye nguvu ya kuwashika wale wahalifu wa sheria. Inspekta Ussi Makame, aliingia katika gari na ASP Jamila, na WP Monica akiwa bado anajikung’uta mchanga pamoja na vumbi, aliingia katika ile gari yao pamoja na Staf Sajenti Kubuta, akaigeuza ile gari nakuelekea kituoni Madema.
Zile gari ziliongozana kwa pamoja, zikiwa kama zipo katika msafara. Gari zilizobeba maiti na majeruhi, zilikwenda moja kwa moja katika hospitali ya serikali ya mnazi mmoja. Na zile gari mbili zingine zikaelekea kituoni pale Madema.
*******
Walipofika kituoni askari wale wanne, wakiwa wamejaa vumbi hasa ASP Jamila, walijadili vile vitambulisho vya yule adui kwa kina na hatimae suala lile ikabidi liwasilishwe kwa Kamishina wa Zanzibar ili lifatiliwe zaidi suala lile. Baada ya majadiliano na mipango kabambe iliyopangwa na askari wale wakibadilishana uzoefu na ujuzi, hatimae ikaamuliwa kuwa usiku wa siku ile, kuwe hakuna kulala. Ili usiku ule chumba namba nane katika ile Hostel ya St Monica’s kipekuliwe, na kumkamata mtu anaeishi mle ndani. Kwani yule adui baada yakufatiliwa kwa makini, bila ya shaka ndipo akawasiliana na wenzake na kuzusha Balaa kubwa sana. Askari wote waliafikiana na hoja ile mikakati ikaandaliwa. Inspekta Ussi na Staf Sajenti Kubuta waliteuliwa kukifatilia kile chumba namba nane, ili kujuwa mtu aliepanga pale. Kwani Staf Sajenti Kubuta aliwaeleza wale askari wenzake alichokuwa ameelezwa na Yule mama muhudumu wa Hostel ile, kuwa kigogo wa serikali ndiyo aliyepanga vyumba vile, kwa ajili ya watu wale. Hivyo ni lazima ajulikane mtu huyo na kuhojiwa, na kama akionekana anafadhili genge lile basi mara moja sheria ifate mkondo wake. Baada ya mipango yote kukamilika na kupokea taarifa kutoka Dsm juu ya askari waliowekwa kwa siri bila Mzee Simba Makupa kufahamu ili wamfatilie nyendo zake pamoja na kumlinda iwapo wale jamaa waliojaribu kumteka kama wangerudi tena. Mwisho kikao kile kikavunjwa na kuhusu makazi ya wageni, kila mmoja alielezwa wapi ambapo alipatiwa sehemu ya kulala. ASP Jamila alielekezwa chumba alichopangiwa katika Hotel ya Bwawani, na Staf Sajent kuvuta alipangiwa katika Lodge iliyopo mtaa wa Mtendeni.
Wote wakakubaliana wakajipange ili usiku ule kazi ikafanyike sehemu waliyoikusudia. Nusu saa baadae WP Monica akawapeleka katika vyumba vyao kwa ajili ya kujipumzisha na kujimwagia maji ili usiku kazi iendelee. Alimuacha Mtendeni Staf Sajenti Kubuta, kisha akaendelea na safari hadi Bwawani Hotel, WP Monica akajieleza kuwa Yule mgeni ndiye aliyewekewa chumba katika hotel ile chumba namba 205. Hivyo walipewa funguo na ASP Jamila alipelekwa katika chumba chake na WP Monica akamuaga na kuondoka.
ASP Jamila alifunga mlango wake kwa funguo, akaizungusha upande ile funguo ili mtu akiwa kwa nje asiweze kutumbukiza kitu katika tundu la funguo na kuudondosha funguo uliokuwa ndani na kuufungua ule mlango. akakikagua chumba chake kwa makini sana, kila kona hata uvungu wa kitanda kwenye makabati juu ya dari sakafuni, maliwatoni, na kila sehemu, akajiridhisha kwamba chumba kile kilikuwa kina usalama hakukuwa na kitu ambacho sio chakawaida. Baada yakujiridhisha usalama wa chumba kile, alitoa mfuko wake, na kuuweka juu ya kitanda, kisha akaenda kuoga. Aliporudi alijitupa kitandani akapumzika.
*******http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa tano ya usiku Inspekta Ussi Makame, na Staf Sajent Kubuta walikuwa katika Hostel ya St Monica’s. Walipofika pale mapokezi hawakukuta mtu hali ilikuwa ni kimya kabisa. Wakasubiri labda Yule mama muhudumu atakuwa amekwenda chooni, au kufata chakula. Lakini hadi saa sita ya usiku inagonga, Yule mama muhudumu alikuwa hajarudi katika sehemu yake ya kazi. Asakri wale wakakata shauri kwamba Staf Sajenti Kubuta kwa kuwa alichukua namba yake ya simu, ampigie ili wafahamu alipo waonane nae kwanza kabla ya kwenda chumba namba nane. Staf Sajenti Kubuta alitoa simu yake, akazitafuta namba za Yule mama. Baada yakuziona alipiga simu na kusikiliza. Simu ile ilikuwa ikiita upande wa pili, lakini haikupokelewa. Alijaribu tena na tena lakini simu ile haikuleta badiliko lolote bado iliendelea kuwa haipokelewi. Askari wale sasa wakawa na maswali lukuki yaliyokosa ufumbuzi. Vipi mtu awache ofisi yake, wakati wa kazi? Kwa nini hataki kupokea simu? Je pale kama wao ndiyo wangelikuwa wageni wanataka chumba je wangehudumiwajwe? Mara moja Inpekta Ussi akatoa wazo kuwa waangalie na wachukue kitabu cha wageni waliokuwa katika Hostel ile, ili kuwatambua watu waliopanga katika Hostel ile, hasa mtu muhimu waliomfata wa chumba namba nane, kwani hata Yule mama walimtaka ili awape kitabu cha wageni, au awatajie nani aliepanga chumba kile namba nane.
Staf Sajenti Kubuta aliruka ule ubao wa mapokezi pale walipokuwa, akawa upande ule wa muhudumu. Aliangalia Kitabu cha wageni pale juu ya meza katika kaunta ile lakini hakukiona. Akavuta droo za meza ile akakutana na funguo kadhaa za vyumba lakini kitabu cha wageni hakikuwapo. Walizikagua funguo zile ambazo kila funguo ilikuwa na kishikio cha mbao kilichochorwa namba ya chumba inayofungua. Walizitazama funguo zote, lakini funguo ya chumba namba nane haikuwamo katika orodha ya funguo zile, hii alimaanisha kuwa, mwenye chumba namba nane alikuwamo chumbani mwake muda ule.
Askari wale bila yakupoteza muda wakakubaliana kwenda katika chumba namba nane, ili wakamtie mbaroni mpangaji wa chumba kile. Haraka Staf Sajenti Kubuta alirudi kupitia pale juu aliporuka awali na kuwa pamoja na Inspekta Ussi Makame, wakapandisha juu kwenye chumba namba nane, huku simu zao zikiwa zimetolewa milio, na kuwekwa mitetemo kama ndiyo wito wa simu.
Walipandisha ngazi kwa uangalifu mkubwa sana, wakawa wanatazama mbele na nyuma katika usiku ule wa saa sita, Hostel ile ilikuwa kimya sana. Hatimae wakawa wanakitazama chumba namba nane upande wao wa kushoto. Inspekta Ussi alitoa funguo kadhaa mfukoni mwake, akakitazama kile kitasa kilivyo, akachagua funguo moja fupi, akamkabidhi Staf Sajenti Kubuta ili afungue chumba kile, wakati huohuo yeye alichomoa bastola yake na kuiweka sawa kisha akampa ishara ya kichwa Staf Sajenti Kubuta aufungue ule mlango, yeye akiimarisha ulinzi nyuma yake.
Staf Sajenti Kubuta alipokea zile funguo na kwa umakini mkubwa, akaitumbukiza ile funguo katika tundu lake, ufunguo ukaingia mzima mzima bila yakizuwizi kutoka katika funguo ya ndani. Yaani ilionesha kwamba pale mlangoni hakukuwa na funguo. Staf Sajenti Kubuta alipouzungusha ufunguo ule upande wa kushoto, ufunguo ule ulizunguka peke yake, yaani mlango ule ulikuwa haukufungwa. Walitazamana askari wale na lugha ya ishara ikawa ndiyo wanawasiliana kwa wakati ule. Katika ishara aliyoitoa Inspekta Ussi Makame, alitaka ule mlango ufunguliwe kisha wavamie haraka ili wamalize kazi. Naam Staf Sajenti Kubuta, alihesabu kwa vidole moja, mbili, tatu, akaufungua ule mlango kwa kasi sana, na ule mlango ukafunguka bila kupinga. Askari wale haraka walilala chini wakawa wamelala pale kama sekunde tatu hivi wakisikiliza kama watasikia mlio wa risasi au chochote kuelekezwa pale mlangoni, lakini hakukuwa na upinzani wowote. Haraka wakainuka pale chini na kuwa ndani ya chumba kile ambacho kilikuwa kinawaka taa. Hamadi hawakuyaamini macho yao kwa wanachokiona. Huku wakiwa wanageuka huku na kule, lakini bado hawakupata upinzani wowote. Ila kitu wanachokiona hakika kimewatia kiwewe, fadhaa na sintofahamu ya hali ya juu sana.
Mwili wa Yule mama muhudumu wa ile Hostel ulikuwa amelala kitandani kifudifudi, lakini ule mwili upande wa mgongo ndiyo kichwa kilikuwapo kikiwa kinatazama juu ilihali hakioni. Simu yake ikiwa pembeni yake upande wa kulia kwake imebarizi. Inspekta Ussi Makame alikagua chumba kile hadi chooni lakini hamkuwamo na mtu mwengine zaidi ya wao wawili, na maiti moja. Yule mama muhudumu alikuwa amenyongwa shingo yake na kubadilishwa nyuma mbele. Askari wale walitingisha vichwa vyao kulikubali Balaa lakini wakiwa wanastaajabu namna ya yule mama aliyofanyiwa ukatili ule mkubwa. Askari wale walifungua kabati la mle chumbani, lakini kabati lilikuwa tupu ndani yake hamkuwa na kitu. Walipekua kila pahala lakini pote hawakupata kitu cha ziada. Hatimae waliirudia ile maiti na kuanza kuikagua vyema.
Damu nzito iliyoganda ilikuwa imeenea chini ya sakafu na kitanda mle chumbani, macho ya yule mama maiti yalikuwa yametobolewa na kitu chenye ncha kali. Mwili ule haukuwa na tundu hata moja la risasi. Yaani inaonesha muuji ametumia mikono yake katika kutekeleza dhamira yake, bila shaka na kisu, au bisibisi.
Askari wale walijiuliza kwa nini mama yule auwawe Lakini walikosa jibu ikawadhihirikia kuwa wale watu ni zaidi ya hatari, na bila shaka waliamua kumuua yule mama ili kupoteza ushahidi wa mtu aliewapangia chumba wale wahalifu, na ndiyo maana hata kile kitabu cha kuandikisha wageni wote waliopanga katika Hostel ile hakikuwapo pale mapokezi wala katika chumba kile namba nane ambapo muhusika wa kitabu kile, alikuwa ameuwawa.
Inspekta Ussi Makame alipiga simu kituoni ili askari waweze kufika katika eneo lile kwa ajili yakuuchukua mwili wa marehemu. Kisha wao wakatoka pale katika korido na kuwa pale huku wakiusindika ule mlango wa chumba namba nane.
Ndani ya dakika zisizozidi ishirini, askari walifika katika eneo lile ambalo lilikuwa bado lipo kimya kama vile hakuna kitu kilichokuwa kimetokea cha hatari katika Hostel ile. Mara baada yakufika pilikapilka zilianza, askari wale wakiwa na glovu mikononi mwao, walipiga picha maiti ile ilivyolala pale kitandani, kisha wakaibeba ile maiti na kushuka nayo ngazi kwenda nje kwenye gari waliyokuja nayo kwa ajili ile. Mwili ule ulipakiwa ndani ya gari ukapelekwa katika hospital ya mnazi mmoja. Inpekta Ussi makame na Staf Stajenti Kubuta, walirudi kituoni ili kuandaa jalada la maiti ile.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ASP Jamila akiwa chumbani kwake katika majira ya saa tano na nusu za usiku, alikitandika kitanda chake na mito akiiweka pamoja na kuifunika shuka vizuri, mithili ya mtu alielala pale kitandani kisha baada yakuridhika na kazi aliyoifanya aliuchukua mfuko wake wenye zana za kazi akaufungua na kutoa vifaa vyake vya kunasia sauti akavifunga ndani ya chumba kile katika sehemu muhimu za chumba kile. Baada ya kuviweka sawa alitoa maski katika mfuko wake akavaa kuzuia pua na mdomo wake, kisha akatoa kopo dogo mfano wa kopo la dawa ya mbu, akapuliza ndani ya chumba kile akianzia chooni hadi chumbani kisha akauendea mlango akaufungua akatoka nje huku akiufunga mlango ule kwa nje na funguo. ASP Jamila akiwa nje ya chumba kile, alivua ile maski akaiweka katika mfuko wake maalum na kupiga hatua kutoka nje ya Hotel ile. Kile chumba kwa kuwa kilikuwa na madirisha ya kioo kiliruhusu dawa ile kubaki mle ndani bila kutoka nje.
ASP Jamila alitoka nje ya Hotel ile akipitia mlango wa nyuma. Mtu aliekuwa mapokezi hawezi kumuona mtu alietokea kule kwenye mlango wa nyuma. Alikwenda kule uwani kulipokuwa na viti na meza chache kwa ajili ya watu wanaotaka kupunga upepo wa bahari, kwani kingo za mwisho wa Hotel ile ya Bwawani ilikuwa imepakana na Bahari ya Hindi kwa kule uwani. Akiwa pale katika viti vile amekaa sehemu iliyokuwa na taa za rangi, mara aliiona taxi ikiwasili eneo lile, ikawashusha abiria waliokuwamo katika gari ile. Watu wawili waliokuwa wamevalia makoti marefu, wakiwa wamejengeka vyema kimazoezi waliteremka katika ile taxi. ASP Jamila alikuwa amekaa katika mwanga hafifu, katika kingo ya bahari akiwa amekaa usawa ambao anaeingia na kutoka, anamuona vyema kabisa. Hata chumba chake namba 205 kwa pale alipokaa kama ikiwashwa taa ndani ya chumba kile, kwa pale alipo angeweza kuona mwanga wa taa wa chumba kile. Wale jamaa baada yakuteremka ndani ya ile taxi, wakajichoma ndani ya Hotel ile, huku dereva wa gari ile akiiegesha gari ile katika mkao wa kutoka akaizima gari yake na kuwasubiri abiria wake. ASP Jamila aliziona vyema namba za ile gari, akazishika kichwani akaendelea kusubiri lakini akiwa hana amani moyoni mwake.Wale jamaa walizama ndani ya Hotel ile, kisha wakachukua funguo pale mapokezi wakiwa nao ni wageni waliopangiwa Hotel ile, wakaelekea vyumbani mwao. Mmoja wa watu wale alikuwa amepangiwa chumba namba 206 na mwengine chumba namba 207
Wageni wale walikuwa wamepangiwa jirani kabisa na chumba namba 205 chumba cha ASP Jamila. Usiku ule Hotel ile ilikuwa na utulivu wa hali ya juu, ukimya ulitanda sana.Watu wale wawili walikwea ngazi hadi katika usawa wa vyumba vyao, lakini wasiingie katika vyumba vyao badala yake wote walipofika chumba namba 205, wakachomoa bastola zilizokuwa zimefungwa kiwambo cha sauti, ili itumikapo silaha ile isiweze kutoa sauti. Jamaa aliekuwa upande wa kushoto alitoa funguo kutoka mfukoni mwake, funguo zinazojulikana sana kama funguo Malaya au ‘Master Key’ akaiingiza funguo ile pale katika kitasa cha mlango ule, akauzungusha taratibu ufunguo ule na kitasa cha mlango ule kikakubali kutoa loki bila ya khiyana, kikaruhusu mlango kufunguka. Wakiwa katika mwendo wa kunyata wale jamaa waliingia ndani katika chumba kile kilichokuwa kimezimwa taa zake. Wakaurudisha mlango kwa nyuma na kuubana taratibu ukafunga mlango ule bila kelele. Wakanyata na kwa ghafla wakakishambulia kitanda kwa risasi mfululizo hasa pale palipokuwa pakionekana kama mahali kulikotuna ambapo kulikuwa kukionekana kama amelala mtu.Baada yakuridhika kuwa wameshauwa mmoja wa wale jamaa alisogea ukutani akawasha taa ya chumba kile, wakitarajia kuona damu nyingi sana zimemwagika, lakini badala yake walishuhudia sufi tele zimezagaa chini kutoka katika mito waliyokuwa wakiipiga risasi katika usiku ule wa saa sita badala ya kumpiga mtu. Wale jamaa walikuwa hawaamini macho yao. Mmoja wa wale jamaa alitowa simu kisha akabonyeza namba kadhaa simu ilipoita upande wa pili na kupokelewa akasema. “Kiongozi huyu Malaya hakulala humu chumbani. Kwani tumeingia chumba namba 205 kama ulivyotuambia kuwa yupo chumba hiki, lakini usiku huu wa saa sita hayumo chumbani kwake, tumepoteza risasi za bure kwa kupiga mito na godoro.” Yule mtu wa upande wa pili aliekuwa katika line, alishangaa sana akajibu.
“Hiyo ndiyo Hotel aliyopangiwa na hicho ndicho chumba chake kwa mujibu wa mtu wetu alietupa taarifa ambazo ni sahihi taarifa zake.” Sauti ya Yule mzungumzaji kwenye simu ilikuwa ikisikika chumbani mle kwa kuwa Yule bwana aliempigia aliiweka simu yake katika loud Spiker ili mwenzie nae asikie kile kinachoongelewa.“Sasa?” aliuliza yule jamaa mmoja. Na Yule jamaa aliekuwa akizungumza na simu akamjibu. “Hapa hakuna cha sasa, tumsubiri humu ndani kwa nusu saa kama atakuja sasa hivi tumalizane nae, kama akiwa hajaja basi tuchomoke” Wale mabwana walipowafikiana walimudu kukaa mle ndani kwa dakika zisizozidi tatu, miili yao ikawa inaishiwa nguvu kwa kasi kubwa. Walikuwa hawajuwi kitu gani kimewasibu. Yule jamaa aliekuwa akizungumza na simu alitaka kusema kitu lakini mdomo wake ulikuwa kama kabwia ugolo. Kwani mdomo wake ulikuwa mzito na haukuruhusu maneno kutoka katika kinywa kile. Bastola walizokuwa wamezishika mikononi mwao hazikuweza kuendelea kuwa mikononi, kwani mikono yao ilikosa nguvu hata yakushika silaha ile ndogo, bastola zile zikawadondoka chini, ile simu nayo ikaanguka chini hatimae na macho yao yakapoteza nuru yake ya kuona, yakawa mazito mboni zikafumba, wakaingia katika usingizi mzito.ASP Jamila pale alipokuwa amebarizi, hakustaajabu hata kidogo alipoona mwanga wa taa chumbani mwake ukiwaka. Ila alitabasamu na kuzidi kuziamini imani na mbinu zake kuwa zinafanya kazi sawasawa. Simu yake iliingia ujumbe akausoma, kisha akaamua aipigie simu ile. “Nimewaelewa Inspekta, ila njooni Bwawani muda huu, kama hiyo maiti tayari imeshapelekwa kuhifadhiwa. Fanyeni haraka sana kuna wageni wapo chumbani kwangu wananisubiri, hivyo tuje kuwaokota tu na wao ndiyo watatupa kila jambo walijualo ili kufikia mafanikio na mzizi wa Balaa hili.” ASP Jamila alisema maneno yale, na mtu aliekuwa akizungumza nae kwenye simu ile ikamjibu” Sawa Afande sie tupo viwanja vya Malindi hapa tushafika mbona dakika mbili tutakuwa hapo.” Baada ya kusemwa yale simu ile ilikatwa.ASP Jamila aliifata ile taxi pale ilipoegeshwa, na mara akaona mwanga wa gari ukiingia katika geti la ile Hotel, nae mara moja akaitambua gari ile.Alipomfikia Yule dereva wa taxi alimkuta amekunjua kiti cha gari ile amejiegesha huku sauti ya music wa taarabu asilia ukisikika taratibu. “Habari yako kaka yangu vipi una abiria?” ASP Jamila alimuuliza yule dereva taxi.“Naam dada yangu nina abiria wawili nimewaleta wameniambia niwasubiri.” Alijibu Yule dereva bila wasiwasi wowote.“Kwani umewachukua wapi hao abiria wenyewe na unawapeleka wapi pengine huko utakapokuwa unawapeleka, na mie nitakuwa naelekea huko.” ASP Jamila alikuwa yupo kazini, anasaili ili kufahamu kama huyu jamaa na wale abiria wake kama wanauhusiano, kwa maana ya kujuwana au kama walikuwa ni watu waliomkodi tu hawatambui.Ile gari iliyoingia getini ilikuja kuegesha pale karibu na taxi ile aliyokuwa ASP Jamila. Wanaume wawili wakashuka kutoka ndani ya gari ile , wakamfata ASP Jamila huku wakiwa na wahaka mkubwa sana.“Wale mie wamenikodi pale darajani wamenambia niwalete hapa Bwawani, ikisha niwapeleke Bububu maeneo ya Kijichi ndiyo nawasubiri hapa” Yule dereva wa Taxi alimjibu ASP Jamila. “Ahaa kwa hiyo huwafahamu kabisa? Sasa hapa wamekwambia wamemfata nani?” ASP Jamila alikuwa yupo katika kujiridhisha kwa Yule dereva taxi.
“Wale abiria mie siwafahamu yakhe, wamenikodisha tu leo wale, ikisha wamenileta hapa wamenambia hapa waja mtembelea mtu wao, ikisha twenda zetu Bububu, ndiyo mimi wameniwekesha hapa hivyoo, kwani vipi dada mbona waniuliza sana?! Kwani weye wawafahamu wale?” Yule dereva taxi alijibu na kuuliza ndani yake katika lafudhi ya kizanzibar.
“Basi kaka watu niliokuwa nataka niwafate hawa hapa wamekuja wao, hivyo wewe endelea kuwasubiri abiria zako” ASP Jamila alimwambia yule dereva taxi huku akiondoka katika gari yake.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Inspekta Ussi Makame na Staf Sajenti Kubuta, walitoa salamu ya utii kwa kiongozi wao, kisha wakawa wapo tayari kwa maagizo. ASP Jamila aliwavuta pembeni hadi mahali pale alipokuwa awali, akawaonesha wenzake ile gari, pamoja na usawa wa chumba chake, ambapo mwanga wa taa ulikuwa bado ukiendelea kuwaka.“Nina wageni kama nilivyosema katika simu, kwani mimi hujiongeza kila wakati hasa hisia zangu zinaponiamrisha kufanya hivyo. Baada ya kutia shaka kuwa naweza kuuzwa na watu walionitafutia chumba hiki, kwa sababu ya tamaa zao, nikaamua nije kuupitisha usiku mahala hapa, lakini kule chumbani nilipuliza ile sumu ya kulaza mtu mara anapoivuta hewa yake. Na kwa kuwa chumba changu kilikuwa giza mimi mwenyewe ndiyo nilieizima taa, sasa hivi chumba changu kile pale na nyie mashahidi taa zake zinawaka. Na hapa nikiwa nimekaa walishuka jamaa wawili katika taxi ile, ambao kwa muonekano wao tu, mimi mashaka yaliniingia kuwa wale jamaa hawakuwa watu wazuri, na hakika dhana hiyo iliondoka baada ya dakika chache nikiwa hapa, nikaona mwanga wa taa katika chumba changu ukiwaka. Hii maana yake hakuna ubishi kuwa wale jamaa ndiyo walioingia mle ndani kwangu. Kwani wangekuwa siyo wale, muda huu wangekuwa wameshatoka na kwenda katika gari waliyokuja nayo” ASP Jamila aliwaeleza wale askari wenzake, na wale askari wakawa na shauku kubwa ya kutaka kuingia ndani mle na kuwakuta madhalimu wale. Lakini ASP Jamila akawaeleza kuhusu sumu ile namna inavyotenda kazi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment