Search This Blog

Monday 24 October 2022

BALAA ! - 5

 







    Simulizi :Balaa !

    Sehemu Ya Tano (5)











    “Upulizapo sumu hii kwa kawaida hukaa na kufanya kazi kwa muda wa saa mbili, baada ya hapo huwa haina madhara tena, hata kama utaivuta hewa yake baada ya hizo saa mbili huwezi kupata madhara. Ila kwa mtu alieivuta hewa yake wakati ikiwa inafanya kazi, basi itamdhuru na kumlaza, usingizi wake utamchukua zaidi ya saa nne, pia itategemea na afya ya mtu ipoje. Kama afya ya mtu imeimarika vizuri itamchukua saa nne kuanza kurejewa na fahamu, na kama afya ya mtu ikiwa ni mgogoro itaweza kumchukua hadi saa sita ili kurejewa na fahamu”Askari wale wakautumia muda ule kuupoteza kwa kumueleza kiongozi wao, juu ya Balaa walilokutana nalo kule St Monica’s, na hatua walizozichukua hadi wakati ule.

    Lakini pia kuvuta wakati usonge, ili wakaokote watu. Yule dereva wa taxi alikuwa mara atoke nje afute gari yake, mara akae juu ya boneti, mara kwenye buti, ilimradi saa zilikuwa zinakwenda na abiria wake hawakuwa na dalili za kutokea.

    Namba za simu zao hakuwa nazo kwa kuwa hakika alikuwa hawatambui watu wale. Alikaa kwa muda wa saa moja akaamua kuwasha gari yake akaondoka taratibu kwenda kutafuta riziki yake mahala pengine.ASP Jamila alizungumza mengi na askari wale hadi ilipotimu saa nane na robo, wakiwa wameshapigwa sana na upepo wa baridi wa pwani, katika eneo lile, hatimae wakapanda ngazi kupitia ule mlango wa nyuma na kabla hawajaenda mbali, walisikia sauti nyuma yao ikisema.

    “Tulieni hivyohivyo kwa nini mnapita huku saa hizi, saa nane yoye hii nyie ni wezi eee?” sauti ya mlinzi wa Hoteli ile aliwaweka chini ya ulinzi askari wale waliokuwa wamevaa nguo za kiraia.Askari wale huku wakiwa wameinua mikono yao juu, Inspekta Ussi Makame akamwambia Yule mlinzi aliekuwa na bunguki mikononi mwake.

    “Sie siyo wezi ni wapangaji wa Hotel hii, tulikuwa tunapunga hewa sasa tunarejea vyumbani kwetu, kama wewe husadiki basi tusindikize” Yule mlinzi akawauliza tena

    “Kama nyie kweli ni wapangaji wa humu ndani, mpo vyumba vipi?” ASP Jamila alimjibu “Chumba namba 205.” Yule mlinzi akawaambia haya twendweni hadi katika hicho chumba nione kama mnafunguo yake, na nyie wote mpo katika chumba kimoja?”ASP Jamila akajibu “Mimi na mume wangu ndiyo tumepanga na huyu ni rafiki yake, alikuwa anatupa ushirikiano ila yeye ataondoka punde tu” Askari wale walikataa kujitambulisha kama wao ni askari, kwa wakati ule kwa kuwa hawakujua kama wanae zungumza nae, kama ni mlinzi kweli, au ndiyo walewale anataka kuwachota akili tu. Hivyo walikuwa wanamchekecha kama hayupo upande ule kule.Yule mlinzi aliwaambia askari wale,

    “Mnaweza kunionesha funguo ya chumba?” ASP Jamila alitoa funguo akamuonesha, na yule mlinzi akaruhusu waendelee na safari yao, lakini ASP Jamila akamwambia Yule mlinzi. ”Samahani baba yangu, wewe ni mlinzi wa Hotel hii na mimi chumbani kwangu, nina wasiwasi huenda nikawa nimeingiliwa na watu, hivyo nakuomba tuwe sote hadi katika chumba changu ili niingie nithibitishe vitu vyangu usalama wake, lakini na wewe pia uwe shahidi kwa upande wangu, hasa kwa vile wewe ni mlinzi wa Hotel hii”

    Yule mlinzi akaongozana nao hadi katika chumba namba 205, walipofika pale ASP Jamila akamwambia Yule mlinzi “Chumba changu nilikiacha nikiwa nimekifunga wakati natoka nje kwenda kupunga upepo, sasa hebu fungua huo mlango kama bado umefungwa hata kabla sijatumbukiza ufunguo wake.” Yule mlinzi aliujaribu kuufungua mlango ule na mara mlango ukafunguka. Alitangulia kuingia ndani ya chumba kile akakutana na Balaa zito.Watu wawili wakiwa wamelala chini wametawanya mikono na miguu yao pale chini, bastola ndefu zikiwa na viwambo vya kuzuia sauti zikiwa chini pamoja na simu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maganda ya risasi yalikuwa yametapakaa pale chini tele, sufi zilikuwazimemwagika chini kwa wingi, pamoja na vipade vingi vya godoro. Wakati Yule mlinzi akiwa anashangaa, ASP Jamila aliichukua ile simu akaikagua akaitumbukiza katika mkoba wake. Yule mlinzi alipoona simu imewekwa katika mkoba, akataka kusema jambo lakini hakuwahi kwani ASP Jamila alijitambulisha kwa kitambulisho chake, na Inspekta Ussi nae akafanya vile, pia Staf Sajenti Kubuta nae akajitambulisha, mlinzi akabaki kuwa mpole na mdogo kama nukta.Askari wale walizichukua zile silaha za wale jamaa, wakazitoa risasi zilizokuwa chemba, wakazirudisha katika megazini kisha silaha zile wakazitunza. Waliyaokota yale maganda ya risasi yote yakapata idadi yake maganda kumi na mbili, yaani wale jamaa walipiga risasi idadi ya maganda yale. Waliwapekuwa wale jamaa mifukoni mwao, wakawakuta na wallet zenye pesa, na ndani ya wallet kulikuwa na vitambulisho vyao vya kazi. Vitambulisho vile vilikuwa vinafanana na kile kitambulisho cha Yule adui walichomkuta nacho kule kulipokuwa na mapambano ya risasi kule katika maeneo ya Kiponda. kwa uzito wa jambo lile wamekubaliana kitambulisho kile apewe Kamishina wa Zanzibar ili yeye pekee au pamoja na IGP ndiyo wafatilie suala la vitambulisho vile kwa wahusika.

    Wakati suala lile bado halijafanyiwa kazi, kwa mara nyingine wanakutana na vitambulisho vilevile, tena safari hii vikiwa ni viwili. Askari wale walitikisa vichwa vyao kwa masikitiko, walitazamana kwa muda kila mmoja alikuwa haamini fikira zake kama kweli wale jamaa walikuwa wanafanya kazi inayosomeka katika vitambulisho vyao. Wakawachukua wale jamaa wakiwa bado wangali wameuchapa usingizi mzito, wakashuka nao chini huku Yule mlinzi akisaidia kuwabeba wale jamaa, akishirikiana na Staf Sajenji Kubuta. Walipowafikisha ndani ya gari kule uwani, ASP Jamila alirudi chumbani akatoa vifaa vyake vya kunasa sauti, akachukua na kila kilicho chake, akashuka chini kuja kuungana na wenzake ikawa kwa heri Bwawani Hotel wakaelekea kituoni Madema. Walipofika kituoni wale jamaa waliingizwa katika chumba kimoja wakalazwa wakawa wanasubiriwa waamke, ili wapambane na nguvu ya dola. Askari wale wakiwa katika chumba cha mkuu wa upelelezi Inspekta Ussi Makame, ASP Jamila alitoa simu ya Yule jamaa aliyoichukua kule ndani ya chumba chake, akaikagua akaiona simu ile namba ya mwisho kutumika, pamoja na muda uliofanya mawasiliano. Akaiandika namba ile ambayo mle katika simu ilikuwa haikuhifadhiwa na jina bali ilitoka namba tupu. Kisha akatoa vile vifaa vyake vya kunasia sauti, akaviwasha wakawa makini kuvisikiliza. Ilisikika milio ya “psiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii” ASP Jamila akasema “Hapo nilipokuwa napuliza dawa” mara ikasikika sauti ya mlango ukifungwa na ASP Jamila akasema tena “Hapo nilipokuwa natoka nje” baada ya mlio ule wa mlango kikapita kimya kirefu mara kukasikika sauti hafifu zilizokuwa zikisikika mfululizo “puh puh puh puh puh” mara ikasikika sauti ya swichi ikiwasha taa, mara kukawa kimya sekunde kadhaa mara ilisikika sauti ikiongea.

    “Kiongozi huyu Malaya hakulala humu chumbani. Kwani tumeingia chumba namba 205 kama ulivyotuambia kuwa yupo chumba hiki, lakini usiku huu wa saa sita hayumo chumbani kwake, tumepoteza risasi za bure kwa kupiga mito na godoro.” Askari wale walitazamana usoni kwa muda kisha wakayarudisha macho yao katika kile kifaa cha kunasia sauti, na mara wakaisikia sauti ambayo ASP Jamila pamoja na Inspekta Ussi Makame, ilibidi watizamane kwa fadhaa. Kwani sauti ile haikuwa ngeni masikioni mwao, sauti ile ilisikika kutoka katika kile kifaa cha kunasia sauti, ikiijibu ile simu kwamba.

    “Hiyo ndiyo Hotel aliyopangiwa na hicho ndicho chumba chake kwa mujibu wa mtu wetu alietupa taarifa ambazo ni sahihi taarifa zake.” Inspekta Ussi Makame akampa mkono kiongozi wake kuwa wamepata picha halisi ya watu wale na wapi wanapotumwa. Wakiwa katika kuendelea kusikiliza kifaa kile mara ikasikika sauti nyingine ikisema “Sasa!” Kisha ikasikika sauti ya awali ikijibu. “Hapa hakuna cha sasa, tumsubiri humu ndani kwa nusu saa kama atakuja sasa hivi tumalizane nae, kama akiwa hajaja basi tuchomoke”Kifaa kile kiliweza kutoa kila kilichohifadhi, hata sauti zao wakati wanaingia mle ndani ya chumba kile wao pamoja na Yule mlinzi, kikasikika kila kitu hadi mwisho wa kuhifadhi kwake pale vilipozimwa kuendelea kuhifadhi na kutolewa na ASP Jamila. Hakika askari wale walikuwa na ushahidi ulionyooka kwa sauti zile zilizonaswa na kifaa kile cha kunasia sauti. Inspekta Ussi Makame akamwambia kiongozi wake.

    “Itabidi Yule bwana asubuhi tukamkamate, kwani hii sauti yake hatoweza kuipinga, lakini pia wale jamaa tuliowakamata watasema wale tukishawafanyia kibano cha sawasawa watatwambia tu wale, hivyo pia nao watakuwa washitakiwa.” Kinyume na matarajio ya Inspekta Ussi Makame alivyofikiri, ASP Jamila akamjibu kwamba. “Bado mapema sana Inspekta, kwani hadi sasa kuna jambo la msingi hapa ambalo ndilo lililotufanya tuwe wote huku Unguja katika wakati huu. Mimi nashauri kukishapambazuka twendeni nyumbani kwa Haruna Makupa, ili tukapate kitu muhimu ambacho nadhani hata hawa jamaa kwa kitu hicho ndiyo wanasababisha Balaa lote hili.” Askari wale walitazamana kwa muda kama vile walikuwa hawajamuelewa kiongozi wao anachokimaanisha, ASP Jamila alilitambua jambo lile jambo alifungua mfuko wake akatowa ile karatasi iliyokuwa imeandikwa kwa mkono aliyoipata katika sakafu chumbani kwa marehemu Haruna Makupa, akaiweka mbele ya askari wale na kuwatazama kwa makini huku akiwaambia

    “Tukifumbua fumbo hilo hakuna shaka hata chembe, tutakuwa tumefika katika Balaa lenyewe”Wale askari nao wakapitisha macho yao katika ile karatasi iliyokuwa imeandikwa katika fumbo. Muhimu zaidi ya sana.Kabati Jeneza, Kitanda Kaburi.Maisha yangu yapo mikononi! Si ajabu kukatishwa! Kurejea Mapinduzi, hapana ninakataa!!!Ng’amua uikomboe Zanzibar! Asante sana. Marehemu mtarajiwa Haruna Makupa.Askari wale waliisoma tena na tena karatasi ile, hatimae Staf Sajenti Kubuta alitoa mawazo yake katika fumbo lile kwa namna alivyotafakari. “Mimi nadhani hapo, kabati jeneza, kitanda kaburi, hapo itakuwa kwenye kabati kuna kitu muhimu na kitanda kaburi, basi bila shaka tukirejea na maneno ya mke wa marehemu Haruna Makupa, Bi Salma Machano nilivyomsikia kule ofisini DSM kupitia ile card maalum ya kunasa sauti ya kiongozi aliyoitoa katika miwani yake, alisema Mumewe ameweka sakafu mpya chumbani kwake tu, pia amepiga rangi chumbani kwake tu! Hii inanipa ushawishi wa kuvunja ile sakafu ili kuona chini kuna kitu gani? Kama kutakuwa hakuna kitu basi tujenge sakafu ya watu, tuendelee na mapambano hadi kieleweke mzizi wa Balaa lililomkuta Haruna na Mauwa.”Askari wale walimsikiliza mwenzao kwa mawazo yake, kisha Inspekta Ussi Makame, nae akamkosoa kidogo Staf Sajent Kubuta. “Siyo kama hakuna kitu basi tujenge sakafu ya watu, hata kama tukifanikiwa kukipata hicho kitu pia tunawajibika kujenga”ASP Jamila alimuuliza Inspekta Ussi Makame “Inspekta na wewe unakubaliana na mawazo ya Staf Sajeti Kubuta ya kwenda kuvunja sakafu ya chumba kile?” Inspekta Ussi Makame akamjibu kiongozi wake, “Naam Afande hata mimi nahisi huenda kukawa kuna kitu si bure”ASP Jamila aliwasikiliza wale askari maongezi yao, lakini yeye alikuwa yupo tofauti na mawazo yao, lakini hakutaka kuwaonesha pale aliona kwanza awasikilize, labda huenda mawazo yake yakawa siyo sahihi bali ya wenzake yakawa ndiyo sahihi, hivyo aliwafikiana na wenzake watafutwe watu wa kwenda kuvunja sakafu ile na wao wakiwepo ili waweze kuona hicho kitu ambacho wenzake wanadhani kinaweza kuwa kimezikwa chini ndani ya chumba kile.

    *******

    Watu watatu mashababi, vifua vipana misuli yenye nguvu, walikuwa wanapiga sululu katika sakafu ya chumba cha marehemu Haruna Makupa, kila kitu kilikuwa kimetolewa sebuleni, kuanzia kitanda kilichobebwa na kupitishwa mlangoni upande bila kufunguliwa, kabati la milango mitatu nalo lilitolewa pale sebuleni kulipokuwa na zulia tu na mito mingi iliyokuwa imeegemezwa ukutani, pale sebuleni hakukuwa na kiti hata kimoja. Sebule ile ilikuwa imepambwa kiarabu zaidi.Wale wanaume majasho yakiwatoka walivunja sakafu ile ngumu huku mchanga wake uliochanganyika na kokoto ukirushiwa upande mwengine wa chumba kile, kwani walikuwa wanavunja kwa upande upande.Zoezi lile liliendelea hadi kina cha kwenda chini, kikafikia futi sita kwa upande ule, lakini zaidi ya mchanga na kokoto na mfano wa yale hakukuwa na kitu chochote chenye maana.

    Askari wale wakasema wao kwa wao, haiwezekani ndani ya chumba mtu afukie kitu kwa urefu zaidi ya futi sita. Hivyo mawazo, fikira, na matumaini yakahamia upande wa pili wa sakafu ile mle chumbani. Inspekta Ussi Makame ambae ndiye aliewatafuta mafundi wale, akawaambia basi kule imetosha wachimbe na upande wa pili nao waone kuna nini?Wale jamaa waliopewa kibarua kile cha kuvunja na kujenga, hawakuwa na ubishi, walitoka mle ndani ya shimo na kwa msaada wa mwenzao aliekuwa nje ya shimo lile akisogeza mchanga, aliwavuta wenzake juu. Baada ya wote kutoka kwa pamoja wakaanza kulifukia lile shimo, ili kupata nafasi ya sehemu ya pili kuchimba. Kibarua kile kilihitaji nguvu nyingi zaidi na maarifa machache.Majagi ya maji yalikatika, kwa kunywewa kazi ikafanyika chini ya askari wale, lakini hata na upande wa pili nao ulipofika shimo lake urefu wa futi sita, hakukuwa na kitu chochote unachoweza kusema kuwa ni cha maana. Inspekta Ussi Makame akiwa na Staf Sajenti Kubuta pamoja na ASP Jamila, wote walishuhudia shimo lile likiwa udongo wake kwenda chini ukiwa umeshikamana madhubuti, ikionesha kwamba haikuwahi kuchimbwa kule chini, kwani udongo uliokuwa ukitoka kule chini ulikuwa ni udongo mpya.

    Hakika ilikuwa ni kazi ya bure ambayo haikuwapa mafanikio yoyote. Ila kwa matokeo yale ASP Jamila yeye fikira zake zilizidi kupata nguvu kuwa fumbo lile hakika ndivyo lilivyomaanisha.

    Hatimae mafundi wale walipewa kazi ya kuurejesha ule udongo na kuijenga ile Sakafu kama ilivyokuwa awali. Wale mafundi wakafukia tena udongo wa shimo lile kwa udongo waliokuwa wameutupia katika sehemu ile waliyokuwa wamechimba awali.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    . Kwa kuwa Udongo Ulaya ‘Cement’ ilikuwa imeshaandaliwa kwa kazi ile, mafundi wale huku wakifanya kazi ile kwa ushirikiano mkubwa, walifanikiwa kulifukia lile shimo. Walisawazisha shimo lile wakawa wanashindilia huku wanasawazisha hadi walipopata usawa uliokuwa ukihitajika, wakachangaya udongo Ulaya na mchanga mlemle ndani, kisha wakausambaza ule udongo Ulaya uliochanganywa na mchanga na maji, wakashindilia vyema wakasakafia na kumwaga niru ya udongo Ulaya, wakapiga pasi ya kibati sakafu ikawa inang’aa ndani kama kioo.Wale mafundi walilipwa ujira wao wakashika njia, hiyo ikiwa ni majira ya saa saba kamili Adhuhuri.

    ASP Jamila alikuwa amekaa kitako katika zulia akiwa na WP Monica pale sebuleni, Inspekta Ussi Makame na Staf Sajenti Kubuta walikuwa nao wapo pale wakimtazama kiongozi wao aliowaita kwa pamoja.

    “Mimi nilikuwa na fikira tofauti baina yangu na yenu, ila nilikataa kuyapinga mawazo yenu. Sasa nataka kufata mawazo yangu juu ya ujumbe uliokuwa katika karatasi aliyoiandika Marehemu Haruna Makupa. Marehemu katika ujumbe wake, hakutaja ardhi, au sakafu kuwa ndiyo kaburi hasha wa kala. Bali aliandika kabati jeneza kitanda kaburi. Mimi nataka tucheze na kitanda na kabati. Kwa kawaida jeneza huwekwa maiti, na kaburi pia huzikwa maiti. Hivyo nashauri kwanza hilo godoro la kitanda hapo livuliwe hiyo nguo yake iliyoveshwa, kisha tuone kuna nini ndani yake.” Askari wale hawakutaka kufanya ajizi waliivua folonya ya godoro lile, wote kwa pamoja macho yao yaliwatoka pima, walipigwa na butwaa isiyosemeka. Wale askari watatu walimtazama ASP Jamila, na ASP Jamila alikuwa akiwatazama wao, wakawa wanatazamana.Kila mtu aliekuwapo pale alipatwa na shauku ya kujua katika lile gadoro lililokuwa lina alama ya kukatwa na kisu, kuonesha ndani ya godoro lile kuna kitu kimewekwa kwa makusudi. Inspekta Ussi Makame, aliingiza mkono wake pale katika sehemu ile ya godoro iliyokatwa, akatoa mkono wake ukiwa na bahasha ndogo ya khaki.

    Bahasha ile juu yake ilikuwa imeandikwa Siri.

    Kwa maandishi ya kalamu nyekundu. Askari wale wakiwa na wahaka mkubwa, waliichana ile bahasha na ndani yake wakakutana na karatasi ukubwa wa A4 ikiwa imechorwa. Kulikuwa na mchoro wa mji wa Unguja, uliochorwa kwa mkono, ukionesha ramani ile inavyoonekana. Kulikuwa na mshale mwekundu ukiwa unatambulisha maelekezo ya kufata njia hadi sehemu iliyokuwa imezungushiwa duara kwa wino mwekundu ikisisitiza kuwa pale ndiyo sehemu lengwa. Moyo wa ASP Jamila ulipiga sarakasi hasa baada ya kuona ramani ile pale mahala ilipokuwa ikielekezwa ilikuwa ni maeneo ya Maisara. Lile eneo ambalo Haruna Makupa ndipo ulipokutwa mwili wake, akiwa maiti. Pembeni ya alama ile muhimu ya duara ilikuwa inaonesha kuna msikiti kwa upande wa kaskazini, na pia imechorwa Bahari kwa upande wake wa Magharibi. Mchoro ule ulionesha upande wa kusini kuna minazi mitatu iliyokuwa kwa pamoja, minazi ile yote ilikuwa imepigiliwa misumari ya jahazi iliyokuwa imetokeza kwa nje.

    Chini Katikati ya minazi ile ndipo duara lilipochorwa kuwa hapo ndipo kuna kitu adhimu sana ambacho kitatatua kila Balaa lililojiri. Damu za askari wale zilikuwa zikichemka sana hivyo ilibidi waondoke pale Miembeni, ili kuelekea Maisara kwa mujibu wa ramani ile, kwenda kujaribu bahati yao kama wataweza kuona kitu cha maana kwao, kitakachowafikisha katika mafanikio.

    *******

    Wakiwa katika eneo la Maisara, askari wale walikuwa wamesimama pale katika ile minazi mitatu, ambayo ilikuwa ikionekana Misumari ya jahazi ikiwa imetokeza. Askari wale wakiwa makini waliimarisha ulinzi eneo lile, Staf sajenti Kubuta akiwa na jembe na kulega alikuwa akifukuwa kwa makini sana eneo lile, huku moyo wake ukiwa unapiga kwa kasi mapigo yake. Alipiga jembe na kutowa mchanga, kiasi ya jembe kama Ishirini na tano hivi, ndipo jembe likagonga katika kitu ambacho siyo udongo, wala siyo mchanga. Mlio wa jembe ulikuwa umegonga katika kitu chenye asili ya chuma au bati gumu.Askari wale waliisikia kwa uwazi sana sauti ile ya chuma iliyolia pale ardhini, hivyo walifukuwa kwa mikono na mara kitu ambacho siyo cha kawaida kilionekana dhahiri shahiri machoni mwao. Ilikuwa ni Selfu la chuma, halikuwa kubwa wala halikuwa dogo sana, bali lilikuwa la wastani, lilionekana wazi pale katika mchanga laini wa ukanda wa pwani. Askari wale kwa pamoja walijikuta wameinama pale shimoni na kufukua kwa mikono yao. Walifukua kwa mikono hadi lile Selfu likaonekana lote.

    Walijipinda pale chini na kulitoa nje likiwa limefungwa madhubuti. Halikuwa zito sana ila lilikuwa ni imara sana. Walilipakiza ndani ya gari na kwenda nalo kituoni.Walipofika pale kituoni askari wale waliliingiza ofisini kwao wakiwa na shauku kubwa sana, yakutaka kufahamu ndani yake kuna kitu gani. Selfu lile halikuwa lakufungua kwa namba laa, bali lilikuwa linafunguka kwa kutumia funguo.

    Askari wale wakiwa wanatizamana ili kujua watalifunguaje Selfu lile, ASP Jamila akasema.

    “Hapa itabidi turudi katika ujumbe wa marehemu Haruna, ndiyo kila kitu kitafunguka na kueleweka.” Askari wale wote wakakubaliana na mawazo ya kiongozi wao, mara simu ya Inspekta Ussi Makame ikaita, nae aliipokea simu ile kwa nidhamu ya hali ya juu.

    “Ndiyo Afande, sawa kiongozi nakuja sasa hivi.” Simu ile ilipokatwa Inspekta Ussi Makame akawaambia wenzake, “Jamani ninahitajika haraka kwa mkuu wa kituo, hivyo nawaacha mara moja”Alitoka katika chumba kile nakuelekea katika ofisi ya mkuu wa kituo kile cha Madema. Askari wale kabla hawajakaa sawa mara simu ya WP Monica nayo ikaita. WP Monica aliipokea simu ile akawa anaongea kwa ukakamavu.

    “Sawa Afande naenda kufata sasa hivi.” Mara simu ile ikakatwa na WP Monica akawaambia askari wale ASP Jamila pamoja na Staf Sajenti Kubuta kuwa; Nimeagizwa mjini mara moja na mkuu wa kituo, hivyo nawaacha mara moja” Baada yakusema maneno yale akaaga na kuondoka ndani ya ofisi ile.ASP Jamila alimtazama Staf Sajenti kubuta, kisha akamwambia “Unajuwa sielewi kabisa?” Wote kwa pamoja walitazamana na ASP Jamila akafanya kitu ambacho Staf Sajenti Kubuta hakukitegemea kama kingefanyika.

    *******

    Inspekta Ussi Makame akiwa kwa mkuu wa kituo kuitikia wito, alimkuta jamaa mmoja ambae yeye alikuwa hamfahamu, alikuwa ni mtu wa makamo ambae alikuwa amevaa kinadhifu sana, alivaa miwani yenye kioo cheupe, alikuwa katika ofisi ya Mkuu wa kituo akiwa miguu yake ameipachika katika mtindo wa namba nne.

    Mtu Yule alikuwa akimtazama usoni Inspekta Ussi makame tangu alipoingia katika ofisi ile. “Inspekta huyu muheshimiwa amekuja hapa muda kidogo ana jamaa zake wawili anasema wapo hapa kituoni mmewashikilia tangu usiku, hivyo nataka kujua kama mmeshawafungulia jalada” Mkuu wa kituo alisema maneno yale huku akimtazama usoni Inspekta Ussi Makame aliekuwa amesimama wima mara baada ya kupiga saluti kwa kiongozi wake.. “Afande bado hatujawafungulia jalada, ila tulikuwa na masuala ya kesi ya MarehemuHaruna tunayafatilia, ndiyo maana hawa jamaa hatukuwafungulia jalada, lakini piatulipowaleta hapa wale jamaa walikuwa wamelala usingizi wa madawa, hivyo isingewezekana kuwahoji wakati hawakuwa na fahamu, ndiyo maana tuliwasubiri waamke ili tufanye nao mahojiano.” Inspekta Ussi Makame alimjibu kiongozi wake, lakini Yule mgeni aliposikia yale maneno ya Mkuu wa upelelezi, alikuwa makini zaidi ya awali. “Sawa nimekuelewa na ulisema kuwa mlikuwa mnafatilia masuala ya kesi ya Marehemu Haruna, je mmefikia wapi?”Mkuu wa kituo kile alimdadisi Inspekta Ussi Makame, na kwa udadisi ule Yule mgeni alishusha mguu wake katika ule mtindo wa namba nne aliokuwa amekaa awali na kuushusha chini ya zulia mguu wake.Inspekta Ussi Makame alimtazama Yule mgeni kisha akahamishia macho yake kwa mkuu wake wa kazi akamjibu.

    “Tumefanikiwa kupata mzigo ambao nadhani utakuwa ndiyo una ushahidi wote, upo ofisini kwangu tulikuwa tunafikiri namna ya kuufungua, na kuukagua ili tuone kilichomo ndani” Inspekta Ussi Makame alimjibu kiongozi wake, na Yule mgeni aliivua miwani yake, akatoa kitambaa na kuisafisha ingawa haikuwa na vumbi hata kidogo.“Ok nimekuelewa nenda kaulete huo mzigo hapa sasa hivi, Mwambie ASP Jamila kuwa nautaka huo mzigo. Na huyu bwana hapa ni wakili amekuja kuwafatilia hao jamaa, hivyo mpe fursa aongee na wateja wake, ili asiseme huko mahakamani kuwa hatukuwapa haki zao za kimsingi wateja wake.” Mkuu wa kituo alisema maneno yale, na Inspekta Ussi Makame, alipiga Saluti huku akisema;

    “Sawa Afande” Baada ya kusema maneno hayo alitoka nje ya ofisi ile na Yule bwana alietambulishwa kuwa ni wakili akatoka nae nje, sanjari na Inspekta Ussi Makame.“Askari naomba nionane na wateja wangu muda huu, ili nizungumze nao.” Yule wakili alimwambia Inspekta Ussi Makame aliekuwa na mawazo tele. “Nisubiri pale kaunta nakuja” Inspekta Ussi Makame alimjibu Yule jamaa na kuelekea ofisini kwake, akamkuta ASP Jamila na Staf Sajenti kubuta wametulia makini wakimsubiri.“Afande mkuu wa kituo anataka huu mzigo uende ofisini kwake mara moja, pia kuna wakili amekuja alikuwa nae, amewafatilia wale jamaa tuliowakamata chumbani kwako kule Bwawani Hotel, anataka kuzungumza na wateja wake, sijui nani aliowaambia kama wapo hapa!” Inspekta Ussi makame, alimwambia kiongozi wake aliekuwa akimtazama yeye na kugeuzia macho yake kwa Staf Sajenti Kubuta.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sawa kama mkuu anautaka huo mzigo, hakuna shida mpelekee na huyo wakili nani aliempa habari hilo ni jambo jepesi sana, kwani Yule mtu aliewatuma wale jamaa waje kwangu ili kunimaliza, baada yakupigiwa simu na wale vibaraka wake na kuelezwa sikulala mle chumbani kama tulivyosikia wote katika kile kifaa cha kunasa sauti, na kwa kuwa mimi nilipoichukua simu ya Yule jamaa niliizima ili isipatikane, basi hakuna shaka kuwa atakuwa Yule mtu ameshaipiga sana ile simu ili kujua kinachoendelea na haikuwa na majibu, wala jamaa zake pia hakuwaona, nadhani ndiyo maana jamaa akafahamu kuwa mambo yameharibika kwa upande wao haraka wakaamua kuweka wakili.”ASP Jamila alimjibu Inspekta Ussi Makame, na kumuamuru Staf Sajenti Kubuta alibebe lile Selfu, nae akafanya hivyo likapelekwa kwa mkuu wa kituo likiwa limefungwa vilevile.Wakati Yule wakili pale alipokuwa amekaa, aliliona lile selfu likiwa limebebwa, na kuingizwa ofisini kwa mkuu wa kituo, yeye alitowa simu katika mfuko wake wa shati na kuwasiliana sehemu.

    Staf Sajenti Kubuta alilitua lile Selfu kwa mkuu wa kituo, kisha akatoa heshima kwa mkuu wake.

    Inspekta Ussi Makame alimwambia kiongozi wake. “Mkuu huo ndiyo mzigo wenyewe ambao tumeupata kutokana na upelelezi wetu, tunadhani kuwa utakuwa ndani yake kuna kitu cha muhimu zaidi ya sana.”Mkuu wa kituo alitikisa kichwa kuafikiana na maneno ya Inspekta Ussi Makame, kisha akamwambia.

    “Vizuri Inspekta kazi nzuri sana mmefanya, huu mzigo nataka niufungue mimi mwenyewe kisha nitawasiliana na viongozi, hivyo ninachotaka sasa hakikisheni tunaimaliza kesi hii haraka sana. Mimi nitawaita vijana wa karakana watakuja na gesi mara moja, na kulikata hili Selfu ili kuona hicho kilichokuwa ndani. Ingawa si kawaida kuwe humo ndani hakuna kitu cha maana halafu mtu atie ndani ya Selfu nakataa, ni lazima kuwe na vitu vya maana tena maana kubwa.” Mkuu wa kituo alimaliza kauli yake, wale askari wakapiga saluti na kutoka nje ya ofisi yake. Mkuu wa kituo alitowa simu yake akabonyeza tarakimu kadhaa na kusikiliza upande wa pili simu ikawa inaita.ASP Jamila akiwa na mkoba wake alitoka nje ya ofisi ile ya mkuu wa upelelezi, akakutana na askari wenzake wanatoka katika ofisi ya mkuu wa kituo, akawafata na kuwaeleza. “Hebu kawachukulieni maelezo wale jamaa, mimi jana sikulala kabisa hivyo ninakwenda kutafuta Lodge ambayo nitalala kwa amani, Mkuu atatufahamisha mara baada ya kufunguwa lile Selfu ili tufahamu kilichojiri”Staf Sajenti Kubuta alimtazama kiongozi wake kwa makini, akawa anatikisa kichwa kuafikiana na maelezo ya kiongozi wake.

    “Sawa Afande, hakika hukulala jana, unahitaji kupumzika sisi tutawahoji hawa jamaa na tutakwenda pia hospitali ya mnazi mmoja, ili kuwahoji na wale wahalifu wawili halafu tutakupa taarifa.” Inspekta Ussi Makame, alimwambia kiongozi wake, na ASP Jamila akatoka nje ya jengo lile la polisi na kusimamisha Taxi iliyokuwa inaelekea maeneo ya Miembeni. ASP Jamila alipanda katika ile gari, akamuamuru dereva wa taxi ampeleke pale katika kituo cha Ukipinda, ile njia ya kutokea uwanja wa Amani, mkabala na njia ya Mwanakwerekwe, na kulia kwake kulikuwa na njia inayokwenda Kibanda maiti, na uwanja wa ndege, na kushoto kwake ikielekea Skuli ya Mto pepo, njia ya kwenda Bububu. Yule dereva alimpeleka hadi pale akamshusha na ASP Jamila alimlipa pesa zake, dereva akenda zake.ASP Jamila alipoiona ile taxi iliyomleta imeshaondoka, alisimamisha Taxi nyingine na kumwambia derive wake “Nikimbize uwanja wa ndege haraka iwezekanavyo” Yule dereva wa Taxi akataja pesa ya kumpeleka uwanja wa ndege, huku akibadilisha gia kuitafuta uwanja wa ndege.



    *******



    Isnpekta Ussi Makame, akiwa na Staf Sajenti Kubuta, pamoja na Yule wakili walikwenda pale ubaoni, Inspekta Ussi Makame akaamrisha askari wa pale akawatowe watuhumiwa waliokuwa katika chumba cha peke yao ili waje kuonana na wakili wao. Wale jamaa wawili waliokutwa chumbani kwa ASP Jamila, walitolewa Selo na kuingizwa katika chumba kingine, wakawa wapo wao pamoja na askari. Yule wakili akawaambia wale askari;

    “Nipeni nafasi niongee na wateja wangu, kwani mkiwepo nyinyi na kusikiliza mazungumzo na wateja wangu, tambueni kwamba wateja wangu watakuwa hawapo huru katika mahojiano yao. Sheria inanipa fursa ya kuzungumza na wateja wangu kwa uwazi na uhuru.”

    Wale askari walitazamana na kumwambia Yule wakili, “Tunakupa dakika ishirini kuzungumza.”

    Yule wakili akagomba “Hapana dakika hizo ni chache sana, kwani kila mmoja nahitaji kupata maelezo yake kwa kina, kwa hiyo naomba nizungumze nao kwa nafasi”

    Inspekta Ussi Makame, alimtazama Yule wakili akamuashiria Staf Sajenti Kubuta watoke nje, ili kumpa nafasi wakili ya kuongea na wateja wake.

    Askari wale walitoka nje ya chumba kile, wakakaa nje ili kusubiri na wao wawachukulie maelezo yao.

    Yule wakili aliingiza mkono mfukoni mwake na kutoa kijitabu kidogo, akawatazama wale wateja wake kwa makini, na wale jamaa wakawa wanamtazama vilevile, Yule wakili akasema.

    “Mmefanya uzembe wa mwaka wajinga wakubwa nyie! Yaani mnaokotwa wazima kabisa, nyie askari gani sasa?! Hivi mnajuwa kwamba jambo hili likivuja kisiwa hiki kitakuwa hakikaliki?”

    Yule wakili aliwaambia wale jamaa na wale jamaa walipoisikia sauti halisi ya Yule wakili, macho yaliwatoka pima kwa mshangao, na mmoja wa wale jamaa akasema kwa fadhaa “Smart Boy?! Leo umekuwa wakili nakuamini mkuu”

    Yule wakili wa mipango akawajibu “Naam ndiyo mimi, tulieni msikubali lolote, kadiri mtakavyoulizwa, kila kitu kinakwenda vizuri tutawachomoa iwe isiwe.”

    Wale jamaa walizungumza na Smart Boy, kisha Yule wakili akawapa vidonge viwili kutoka katika mfuko wake wa suruali kila mmoja, akawaambia;

    ”Vidonge hivi mkila mara baada ya saa moja kutoka sasa, mtajisikia vibaya, kichefuchefu, na mapovu yatawatoka mdomoni, kwa hiyo jamaa kwa vyovyote vile watataka kuwapeleka hospitali basi wakifanya hivyo tu, itakuwa ni ushindi kwetu kwani sie tutamaliza kesi hii njiani na kuwachukua sawa? Ila msisubiri hadi saa moja ifike, badala yake mie nikishaondoka kiasi ya nusu saa kutoka sasa nyie ombeni kupelekwa Hospitali, na msikubali kuhojiwa chochote semeni afya zenu siyo nzuri, na kwamba maelezo yenu mtayatowa mbele ya wakili wenu ambae ni mimi mmenielewa?”

    Wale jamaa wakaitika kwa kutikisa kichwa juu chini, kuwa wamekubaliana na jambo lile, na mara moja akawakabidhi vidonge vile na wale jamaa kwa kupitia mate yao, wakafanikiwa kuvimeza vile vidonge. Yule wakili aliwatizama kwa muda akatabasamu, nakuwaambia. “Natoka tunawasubiri njiani kuwachukua.” Wale jamaa waliitika kwa kichwa, kuwa sawa wameelewa.

    Mazungumzo yale na vitendo vile vilikuwa vinafanyika kwa sauti ya chini, na hata askari aliekuwa nje ya mlango ule hakuweza kusikia kwani walikuwa wakinong’ona. Yule wakili au Smart Boy, aliwaaga wale jamaa akatoka nje ya chumba kile. Alipotoka nje ya chumba kile alimkuta askari akiwa anaimarisha ulinzi akamwambia askari Yule.

    “Mimi nishamaliza kazi yangu, nishawahoji na wameshanipa maelezo yao, hivyo naomba wateja wangu wapewe dhamana ya polisi”

    Yule askari aliekuwa nje ya mlango ule baada ya kuwekwa pale na Inspekta Ussi makame kuwalinda wale wahalifu, alimwambia Yule wakili.

    “Waone viongozi, wale ndiyo wanaoshikiria kesi hii, muone Afande Ussi kwani yeye ndiye mpelelezi wa shauri hili”

    Yule wakili alikwenda kwa mkuu wa kituo, akabisha hodi akaingia ndani, akakutana ana kwa ana na lile Selfu, likiwa limewekwa sakafuni katika ofisi ile. “Karibu wakili umewaona watuhumiwa tayari, au una jambo gani tena?” Mkuu wa kituo alimuuliza Yule wakili huku akimtazama usoni.

    “Asante Afande, ninashukuru sana nimewaona wateja wangu, ingawa hali zao wamenambia siyo nzuri ki afya, hivyo sikuweza kuongea nao kwa kina kutokana na hali zao. Bila shaka wateja wangu watakuwa wamepata athari kubwa sana, hivyo naomba wapelekwe Hospitali kwa uchunguzi zaidi na matibabu. Ikibidi pia ninahitaji kuwadhamini kwani hali waliyoniambia kama wataendelea kukaa mahabusu inaweza kuleta madhara makubwa zaidi.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakili alimwambia Mkuu wa kituo, na yule mkuu wa kituo akamjibu

    “Jukumu la kumpeleka mtuhumiwa hospitali ni jukumu letu sie baada ya kuthibitisha kuwa kweli mtuhumiwa ni mgonjwa, hivyo wewe nenda uje kesho hapa utajuwa kinachoendelea. Na sie kama tukithibitisha hali zao ni wagonjwa wanaohitajika kupelekwa hospitali, tutawapeleka hiyo ni haki ya binaadamu yoyote kutibiwa hasa akiwa yupo mikononi mwetu”

    Yule wakili wakujitegemea, alitoka pale akiwa na furaha kiasi. Alitembea kwa miguu akavuka barabara, akaifata gari yake aliyokuwa ameiegesha ng’ambo ya barabara ile pale Madema. Alipofika garini alifungua mlango akajitoma ndani, akatowa simu na kupiga sehemu, mara baada ya simu kupokelewa akasema kwa kujiamini.

    “Nimemaliza kazi iliyokuwa muhimu sana, kwani wale wazembe wawili, hivi niongeavyo na wewe wanahesabu dakika za kuwa marehemu. Wale watu ni wazembe na kifo ndiyo stahiki yao pumbavu sana wale, yaani wanaokotwa kama kuku mdondo wakati wao ni askari!”

    Yule wakili hewa alizungumza na yule bwana katika simu kisha akamtupia swali.

    “Vipi umeifanyia kazi kuhusu ile taarifa niliyokupa kuwa Yule mwanamke Kirusi kibaya zaidi ya Ukimwi, kuwa alitoka pale kituoni na haijulikani kama amekwenda wapi?”

    Upande wa pili katika simu ile ukamjibu Smart Boy kwa utulivu mkubwa sana.

    “Ondoa wasiwasi wowote kuhusu Yule mwanamke, ambae wewe unamwita ni kirusi, tumepata jina na cheo chake anaitwa ASP Jamila, Yule leo ndiyo mwisho wake hatathubutu kuiona kesho. Nishafanya mawasiliano na watu wetu tuliowapandikiza katika Hoteli na Lodge zote kubwa hapa Unguja, kama atakapokwenda ili kupanga chumba, basi tutapewa habari kuwa yupo chumba gani, kwani nimeshawaeleza wasifu wake na watamtambua lazima na safari hii hata ikibidi kuilipua Hoteli nzima ikiwa hakuna budi ili Yule mwanamke afe, basi tutafanya hivyo. Kwani lisilo budi hutendwa”

    Alimaliza kuzungumza Yule wakili wa mipango au Smart Boy, simu ikakatwa akawasha gari, akatokomea zake mitaani.

    Inspekta Ussi makame, akiwa na Staf Sajenti Kubuta waliwafata wale wahalifu pale chumbani walipokuwa baada ya kuondoka Yule mtu mbaya sana aliejitambulisha kama wakili, akiwa pia na kitambulisho kinachomuonesha hivyo, ambacho ndicho alichojielezea kwa mkuu wa kituo, hadi akaaminiwa na kupewa fursa yakuonana na kuongea na watuhumiwa.

    Kwani kisheria wakili anayo haki yakuzungumza falagha na wateja wake, bila kusikilizwa anaongea nao nini, na kwa njia hiyo ndiyo ikamfikisha karibu na watuhumiwa wale. Ingawa lengo lake lililompeleka pale, halikuwa dhamana hata kidogo, bali ilikuwa ni kwenda kupoteza ushahidi wa watu wale muhimu kutoka katika kitengo nyeti cha serikali, hakika kwa Balaa walilojiingiza hawakustahili kuishi. Kwani kifo kilikuwa ndiyo njia sahihi kabisa kwao, kuliko kuwa na kesi halafu wakaharibu jina la kitengo kile. Hasa kwa mazingira waliyokamatiwa.

    Inspekta Ussi Makame alimwambia Staf Sajenti Kubuta kuwa, “Hakikisha maelezo yao unayachukuwa muda huu, kwani kesi hii ishaingia mawakili sasa hivi italeta matatizo ya kisheria kwani wale jamaa wanajua sana. Mimi nipo ofisini kama utahitaji msaada utanambia“

    Inspekta Ussi Makame alisema maneno yale akatoka nje ya chumba kile akimuacha Staf Sajenti Kubuta na wale watuhumiwa.

    Staf Sajenti Kubuta aliwaambia wale watuhumiwa, “Nataka kuwachukulia maelezo yenu, hivyo naanza na wewe nataka uniambie jina lako kamili, umri wako, dini yako, kazi yako, kabila yako, na sehemu unayoishi.”

    Alikuwa akimwambia mmoja kati ya wale jamaa wawili waliokuwa chumbani pale. Wale jamaa walimtazama kama watu waliokuwa hawamuelewi nini anachokikusudia, hivyo walikaa kimya hawakumjibu kitu chochote.

    Staf Sajenti Kubuta alichukia kukaliwa kimya akapiga ngumi katika meza kuwastua wale jamaa waliokuwa wamemtumbulia macho bila kusema chochote, kisha akawaambia tena. “Naongea na nyinyi mnaojifanya hamsikii hivyo msinilazimishe kuongea na nyie mkiwa mnavuja damu, sawa?”

    Wale jamaa walimtizama Staf Sajenti kubuta katika hali ile ile ya awali. Askari Yule alisimama wima akageuka kama alieuwa anatazama nje kupitia dirishani, mara akageuka kwa kasi na kumchapa kofi kali la shavu Yule mtuhumiwa aliekuwa anamuhoji.

    Yule jamaa akashika shavu lake kwa maumivu makali yaliokuwa yakimchonyota katika shavu lake, huku alama la vidole vikiota katika shavu lile.

    Staf Sajenti Kubuta huku akiwa amechukia akamwambia “Umeshaamka tayari naona sasa utajibu maswali yangu.”

    Yule mtuhumiwa huku akiendelea kushika shavu lake, alisema kwa shida “Nipelekeni hospitali najisikia vibaya sana.”

    Kauli ile iliungwa mkono na mtuhumiwa wa pili, na hakika hawakuwa wanatania, wala kufanya dhihaka hata kidogo, kwani vidonge vile huwa vinafanya kazi ndani ya dakika kumi tangu kumezwa kwake.

    Ikifika muda huo vinaanza kufanya kazi. Vidonge vile vilikuwa vinaharibu mfumo mzima wa vitu tumboni, yaani ilikuwa kama mtu aliekunywa tindikali, hivyo kila kitu tumboni kilikuwa kinaungua.

    Staf Sajenti kubuta hakuwa kabisa na habari ile, kinyume chake yeye alidhani wale watuhumiwa wanamletea usanii wa mjini. Kwa hiyo na yeye ilikuwa ni mwendo wa makofi na ngumi za chembe, mbavu na tumbo, hadi wale jamaa wakawa wanavuja damu.

    Ila pamoja na hali ile waliyokuwa nayo awali ya kuzungumza kuwa wapelekwe hospitali, sasa wakawa hawazungumzi chochote, kwani hata sauti mfumo wake ukawa umeshakata kwa dawa zile hatari walizopewa kumeza.

    Staf Sajenti Kubuta akiwa amejawa na hasira, alitoka nje ya chumba kile akiwa ameghazibika sana, akaenda kukaa nje akiwa anatafakari ni adhabu gani afanye ili wale watuhumiwa waweze kuongea?

    Akiwa pale nje anatweta kwa hasira kiasi ya dakika zisizozidi tatu, mara akatokea Inspekta Ussi Makame, akamuuliza “Vipi umeshawachukulia maelezo yao hao watuhumiwa?”

    Staf Sajenti Kubuta alisaluti kwa Mkuu wake, akamwambia “Jamaa viburi sana, pamoja na kuwavujisha damu lakini hawataki kuzungumza kabisa, wanataka wapelekwe Hospitali hivyo nafikiria kitu cha kufanya ili nipate maelezo yao.”

    Inspekta Ussi makame, alimuashiria Staf sajenti Kubuta amfuwate mle chumbani, wote wakaingia katika chumba kile walichokuwamo watuhumiwa wale. Hali waliyoiona mle ndani kwa wale watuhumiwa hakika iliwastua sana.

    Watuhumiwa wale walikuwa wamelala chini damu nzito nyeusi zikiwatoka masikioni, puani, machoni, na mdomoni, lakini pia walikuwa ngozi za miili yao, zilikuwa zinabambuka ngozi kama watu walioungua moto.

    Inspekta Ussi Makame akawatazama wale jamaa akamgeukia Staf Sajenti Kubuta na kumuuliza.

    “Umefanya nini sasa Staf Sajenti? Mbona ulichokifanya ni kinyume na maelekezo niliyokupa? Hivi unafikia kupiga mtuhumiwa hadi anakuwa katika hali hii! Unajuwa hawa jamaa walikuwa wazima na wakili wao amewaona hivyo? Sasa tutamwambiaje wakili Yule kwa hali ya watuhumiwa kuwa hivi ilivyo sasa? Laini pia mkuu wa kituo huwa hataki watuhumiwa wapigwe kwa kiasi hiki, sasa hapa si unawauwa hawa jamaa wewe?!”

    Staf Sajenti Kubuta alichanganyikiwa sana kwa hali ile, ingawa hakuwa na hakika kama zile ngumi na makofi yake, ndizo zingeweza kuwafanya wale jamaa wawe katika hali ile anayowaona nayo. Kwani yeye ameshawapiga watuhumiwa wengi sana ambao hujifanya viburi, lakini hawakuwahi kuwa katika hali ile waliyokuwa nayo hawa jamaa.

    Hakika hili ni Balaa linamuangukia yeye. Staf Sajenti kubuta alitaka kusema jambo lakini alishindwa. Wale jamaa waliokuwa wakihangaika kuyanusuru maisha yao pale chini, sasa kwa pamoja walitulia tuli kama magogo pale chini, walikuwa hawatikisiki, wala hawana uhai, ndipo jumba bovu na Balaa likamuangukia Staf Sajenti Kubuta, kuwa amepiga hadi kuwauwa watuhumiwa.

    *******http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mkuu wa kituo cha Polisi Madema, akiwa ofisini kwake aliwakaribisha maaskari wawili kutoka karakana ya Polisi, wakiwa na mitungi ya Gesi ili waje kulifungua lile Selfu. Mkuu wa Kituo alimwita kwa simu Inspekta Ussi Makame, ili ashuhudie mle ndani ya lile Selfu kilichomo, wale askari wataalamu wakufungua lile Selfu walilikagua kwa makini, wakawasha gesi, na kuanza kuunguza ile sehemu ya kutilia funguo.

    Walifanya vile kwa muda mara ikasikika sauti ya loki kuachia “Tap” wakalifungua Selfu lile na likawa wazi. Mkuu wa kituo, Inspekta Ussi Makame, pamoja na wale askari wawili kutoka karakana, wote kwa pamoja walikuwa wamepigwa na butwaa. hawayaamini macho yao.

    Lile Selfu ndani yake mlikuwa patupu hakuna kitu. Mkuu wa kituo alimgeukia mkuu wa upelelezi huku akiwa amejazibika akamuuliza. “Nyie mmelifungua hili Selfu? Mbona humo ndani hamna kitu, yaani Selfu likafukiwe chini ndani yake liwe halina kitu? Hapana niambie vipo wapi vitu vilivyokuwamo humu ndani?”

    Inspekta Ussi makame, akamjibu kiongozi wake kwa utulivu. “Hapana Afande sie hatukufungua kwani hatuna funguo zake, hapa kwenyewe limefunguliwa kwa Gesi, kwa dakika kama tano sie tungefungua na nini Afande?! Hivyo lilivyokuwa ndivyo tulivyolikuta, na ndivyo tulivyolileta hapa kwako Afande”

    Yule Mkuu wa kituo alitafakari kisha kama mtu aliegutuka hivi akasema, “Wewe na Wp Monica mlipotoka mle ofisini kwako walikuwamo kina nani?”

    Inspekta Ussi Makame, alimjibu kiongozi wake. “Alikuwapo Afande Jamila, na Staf Sajenti kubuta Afande.”

    Yule mkuu wa kituo alitikisa kichwa kukubali akamtazama usoni kijana wake, akamwambia “Niitie ASP Jamila na Staf Sajenti Kubuta sasa hivi” Inspekta Ussi makame alipiga saluti na kutoka mle ofisini, akaingia ofisini kwake akatowa simu yake akampigia simu ASP Jamila, lakini aliipiga simu ile zaidi ya mara kumi, lakini simu ile ilikuwa haipatikani, wasiwasi ukamuingia, fadhaa ikampanda, akawa anatembea afisini mwake kutoka pembe moja hadi pembe nyingine, akiwa katika lindi la mawazo.

    Alikuwa akiwaza na kuwazua kuwa ASP Jamila hapatikani katika simu, wakati mkuu wa kituo anamuhitaji, pili kuhusu wale watuhumiwa, wameshakuwa maiti wakati hawakuwahi kuchukuwa maelezo yoyote kutoka kwa wale jamaa, Wakili wao alizungumza nao wakiwa wazima, lakini pia kifo chao wale jamaa kimesababishwa na kipigo kikubwa kilichoelekezwa sehemu mbaya na Staf Sajenti kubuta hadi kupelekea kifo chao. Mzigo katika lile Selfu haukuwamo ndani yake.

    Kifupi Inspekta Ussi Makame, alikaribia kudata kwa mawazo yaliokosa ufumbuzi wa haraka. Akiwa yungali amezama katika lindi la mawazo mara simu yake ya mkononi ikaita Alipoitazama namba ya simu ya mpigaji, moyo wake ukaongeza kasi mapigo yake ya moyo, mapigo yake ya moyo yakawa yanakwenda mbio kuliko kawaida yake. Hatimae akaipokea ile simu kwa fadhaa.



    *****



    ________



    MWISHO

    Pseudepigraphas

0 comments:

Post a Comment

Blog