Search This Blog

Monday, 24 October 2022

MTUHUMIWA - 5

 











    Simulizi : Mtuhumiwa

    Sehemu Ya Tano (5)





    Wakati Moze akijibu maswali ya yule askari, Jaka naye alikuwa kwenye chumba kingine ndani ya jengo lile lile akitoa maelezo yake kuhusiana na tuhuma zilizomuangukia. Sasa aliinua uso wake taratibu kuwatazama wale askari wawili waliokuwa mbele yake ambao walikuwa wakimtazama kwa hasira, meza kubwa ikiwa imekaa baina yake na wake askari. Mmoja kati ya wale askari wawili, ambaye alikuwa mnene, mfupi na mwenye macho makubwa sana, alimsukumia Jaka karatasi iliyokuwa na maelezo yake huku akimfokea.

    “Nasema haya maelezo hatuyataki! Andika mengine!”

    Jaka aliendelea kumtazama kwa mshangao.

    “Mimi nimeshasema hapo mwanzo na ninasema tena...sina maelezo mengine zaidi ya hayo kwa sababu huo ndio ukweli wenyewe! Sasa kama nyie...” Jaka alianza kujibu kwa ukali, lakini hakuwahi hata kumalizia jibu lake, kwani yule askari aliinuka na kumzaba kofi kali la uso na mara ile ile alimkamata nyuma ya shingo yake na kuubabatiza uso wake kwa nguvu pale mezani, yowe la maumivu likimtoka Jaka bila kutarajia.

    “Pumbavu! Unataka kuleta mchezo hapa! We’ unaua mtu halafu unategemea sisi tuamini huu upuuzi ulioandika hapa? Unataka kutuchanganya sisi, eenh?”

    “Mi’ sina maelezo mengine zaidi ya hayo ndugu zangu, mtaniumiza bure tu jamani!” Jaka alijibu huku akiwa amekandamizwa uso wake pale juu ya meza. Yule askari alimuinua kwa nguvu na kumkwida fulana yake kwa mbele na kumvuta hadi pua zao zikagusana.

    “Sikiliza we’ dogo, tena sikiliza kwa makini...tumeshakabiliana na wababe zaidi yako sisi, na wote walianza na msimamo kama wako lakini hatimaye walisalimu amri!” Alimkoromea.

    Jaka alimtazama yule askari bila ya kusema neno, na yule askari aliendelea, “Sasa kwa nini usiseme tu ukweli wako kabla hatujakuchakaza zaidi?”

    “Ukweli tayari upo hapo kwenye hiyo karatasi afande...au ukweli gani zaidi unaoutaka wewe?”

    Yule askari alimsukuma kwa hasira, na Jaka alipepesuka kwa nyuma, akaangukia kwenye kiti alichokuwa amekalia na kupinduka nacho mpaka sakafuni kwa kishindo kikali.

    “Ukweli wa kwamba umemuua Joakim Mwaga kwa sababu unazozijua mwenyewe...na sisi tunazitaka hizo sababu!” Yule askari alimbwatia.

    Akiwa amelala chali pale sakafuni, Jaka alihisi mchirizi wa damu ukimtoka puani baada ya kupigizwa uso wake kwenye ile meza. Alijipangusa damu ile kwa mgongo wa kiganja chake huku akijizoazoa kutoka pale sakafuni. Yule askari mwingine alimsaidia kuinuka kutoka pale chini na kumuweka tena kitini. Kisha alichukua ile karatasi iliyokuwa na maelezo ya Jaka na kumueleza, “Sawa, sasa tuanze tena kupitia haya maelezo yako.”

    Jaka alikuwa akitazamana na yule askari mnene kwa hasira, na yule askari mwingine akaanza kuongea.

    “Kwa mujibu wa maelezo yako uliyoandika...” Alisema yule askari wa pili huku akisoma kutoka kwenye ile karatasi. “...ni kwamba wewe uliletewa ujumbe na mtoto usiyemfahamu leo hii, muda wa saa nane kasoro mchana, kuwa Joakim alikuwa anaomba mkutane juu ya jengo la bweni namba tano, sawa?”

    “Sawa.”

    “Na kwamba ulipofika kule juu ndio ukamkuta Joakim akiwa tayari ameuawa...”

    “Ndiyo.”

    “...na kabla hujafanya lolote, askari walitokea na kukuweka chini ya ulinzi.”

    Jaka aliendelea kusikiliza.

    “Na umeandika kwamba Joakim alikuwa ameuawa na watu wengine ambao walitaka wewe ukamatwe na kuhukumiwa kwa kosa hilo badala ya wao, ili kukufunga mdomo...”

    “Ndiyo hivyo...” Jaka alidakia na kutaka kusema zaidi, lakini yule askari alimnyamazisha kwa kumnyanyulia mkono. Aliendelea kusoma.

    “Kwamba hata glovu zilizokutwa chumbani kwako zilikuwa zimewekwa makusudi ili kuhakikisha kuwa ni wewe ndiye unayehukumiwa kwa kosa hilo.”

    Jaka alikubaliana na maelezo yale kwa kichwa, yule askari aliendelea.

    “Kwa hiyo, unaandika, hata huyo mtu aliyepiga simu polisi kutaarifu kuwa kulikuwa kuna mauaji juu ya jengo unaloishi pale chuoni, ni ushahidi tosha kuwa mambo yote hayo yamepangwa, ndio maana huyo mtu aliyepiga simu alijua kuwa wewe ukienda kule juu utaikuta maiti ya Joakim hivyo akaiarifu polisi ili wewe ukamatwe.”

    Jaka aliendelea kusikiliza.

    “Mwisho unamalizia kwa kuandika kuwa haya yote yamepangwa yakukute kwa sababu wewe umegundua njama za biashara ya madawa ya kulevya, na ili kuhakikisha kuwa hupati nafasi ya kuzitoa njama hizo kwenye vyombo vya dola, wamekupakazia mauaji haya ili kukuharibia sifa yako na kupoteza imani ya Jamhuri juu yako ili kila utakalosema lisitiliwe maanani.”

    “Na tayari wameshaanza kufanikiwa katika hilo afande...si unaona hata nyie hamniamini?” Jaka alidakia kwa uchungu.





    Yule askari alimtazama tu bila ya kusema neno, kisha akaendelea kusoma.

    “Pia, hapa chini umeandika kuwa mtu ambaye unadhani kuwa anahusika na njama hizo za kukutia wewe hatiani bila makosa ni Anthony Athanas Wanzaggi, au Tony, na washirika wake.”

    Askari aliinua macho yake na kumtazama Jaka.

    “Una hakika na habari hii?” Alimuuliza.

    “Nimeandika nadhani atakuwa anahusika kwa sababu yeye ndiye anayehusika na njama za biashara ya madawa ya kulevya nilizozibaini.”

    “Afande huyu anatupotezea muda tu na porojo zake...” Yule askari mnene alidakia. Jaka akamtolea uvivu.

    “Oh, Yeah? Sasa kwa nini msiyafanyie uchunguzi mambo ninayowaeleza? Kwa nini msimfuatilie huyo mtu ninaewatajia halafu mkahakikisha iwapo ninasema ukweli au vinginevyo? Au mnamuogopa kama walivyoogopa wenzenu?” Alimfokea.

    Loh!

    Mara ile ile mkono wa yule askari aliyekuwa akimsomea maelezo yake ulichomoka na kumdaka koo kwa nguvu.

    “Kwa sababu hatuelewi ni kwa nini wewe usitoe taarifa juu ya njama hizo za biashara ya madawa ya kulevya mapema, na uje uamue kuzitoa sasa, baada ya kuwa umekamatwa kwa kosa la mauaji...” Alimwambia kwa sauti ya upole huku akiwa amemkaba koo namna ile.

    Jaka alibaki akiwa ametumbua macho.

    “Na kwa nini hao watu wamuue Joakim na wasikuue wewe ?” Yule askari mnene naye alidakia.

    “Sasa hilo ndilo mngepaswa muwaulize hao watu ninaowatajia, mimi nitajuaje?” Jaka alijitutumua kumjibu. Yule askari wa pili alimuachi koo na kurudi kuketi kitini.

    “Utetezi wako unanuka Jaka...unasema Joakim alikuandikia huu ujumbe ndio maana ukaenda kule juu, tutahakikisha vipi kuwa huu ni mwandiko wake?”

    Jaka aliwatazama wale askari mmoja baada ya mwingine.

    “Njia ya kuhakikisha hilo ni ndogo sana sidhani kama mnahitaji mimi niwaelekeze namna ya kulihakikisha hilo…na kama si Joakim mnadhani ni nani atakuwa ameandika ujumbe huo...?” Aliwajibu na kuwauliza.

    “Mimi nadhani ni wewe ndiye uliyeandika huu ujumbe Jaka, ili utupoteze maboya...” Yule askari mnene alimjibu kwa jeuri.

    Aka!

    “Unaongea nini wewe?” Jaka alibwata, kisha akaendelea, “Yaani nijiandikie huo ujumbe ili mkija kule juu mnikute nao halafu niwambie kuwa nimebambikiwa? Hivi kweli inakuingia akilini hiyo afande? Au hutaki tu kukubali maelezo yangu?”

    “Ati!? Ongea kwa adabu wewe!” Alifoka yule askari mnene huku akimtupia Jaka kofi kwa nguvu. Safari hii Jaka alikuwa macho, kwani alishaona kuwa wale askari hawakuwa na nia ya kumuelewa makusudi, hivyo kwa mkono wake wa kulia alimdaka mkono yule askari kabla lile kofi halijamfikia.

    “Swala la maelezo yangu kuwa hayafai au yanafaa si juu yenu, hiyo ni juu ya hakimu kuamua hapo mtakapoifikisha hii kesi mahakamani. Kwa namna moja mnaogopa kuwa nikifika mahakamani nitatoa siri za biashara haramu na kuhusika kwa huyo mtu niliyewatajia...au na wengine mnaowafahamu...katika biashara hiyo...” Alimwambia huku bado akiwa amemshika ule mkono, na hapo yule askari akamtupia kofi la pili, Jaka akalidaka kwa mkono wake mwingine, na kuendelea,“... mnataka kesi hii ya kufungua na kufunga pindi ifikapo mahakamani siyo? Mnatarajia nikiri kuwa nilimuua Joakim ili iwe open and shut case sio? Basi eleweni kuwa kazi yenu ni kulinda na kutumikia jamii, na jamii hailindwi na haitumikiwi kwa kupigwa makofi na mateke!” Baada ya kusema hayo aliitupa pembeni mikono ya yule askari ambaye muda wote ule alikuwa amepigwa na butwaa. Hajawahi kuona mtu akijiamini kiasi kile akiwa chini ya ulinzi hata baada ya vitisho kama vile.

    “Mimi nimeshaandika maelezo yangu, na sababu ya mimi kuwa kule juu ya lile jingo tayari iko wazi kwenye huo ujumbe nilioandikiwa…sasa sioni kwa nini muendelee kuniweka tu hapa kituoni wakati nina mambo kibao ya kufanya...” Jaka alikuwa anaendelea kuwapa vipande vyao, na wale askari ambao kwa sekunde kadhaa hivi walikuwa wamepigwa bumbuwazi. Yule askari aliyemkamata kule juu ya ghorofa alikichukua kile kijikaratasi alichoandikiwa na Joakim.

    “Kwa hiyo huu ndio ushahidi unaokutia kiburi, sio?” Alimuuliza huku akimtazama kwa hasira.

    “Sio kunitia kiburi..ndio unaeleza kwa nini nilikuwa pale wakati ule…”

    “Huu?” Jamaa alimuuliza tena huku akimuoneshea kile kijikaratasi.

    “Of Course!” Jaka alimjibu huku amekunja, na hapo hapo uso ulimsawajika pale alipomshuhudia yule askari akikitumbukiza kinywani kile kikaratasi chenye ujumbe kutoka kwa Joakim na kuanza kukitafuna tarattibu huku akiwa amemkazia macho ya hasira.

    Hah!

    “Pumm-Baaaaaavvvvvv!!!” Alimaka na kukurupuka kutaka kumrukia, na hapo wale askari walimrukia yeye na kumuangushia kipondo kizito. Makofi, mateke, ngumi. Alijaribu kusimama na kujitetea lakini hakuweza. Kipigo kilikuwa kikimuangukia kutoka kila upande na kila kilipokuwa kikiendelea, ndivyo kilivyozidi kuwa kizito.

    Hatimaye aliishiwa nguvu na kulala chini huku akimtazama yule askari akimalizia kuutafuna ule ushahidi na kuumeza kabisa.

    “Aaaah wanaharamu mmenipotezea ushahidi wangu (akawatukania mama zao) nyieeeee!” Aliwakemea kwa nguvu hafifu. Mapigo yaliendelea kumuangukia kama mvua.

    Alipoteza fahamu...http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    __________________



    Mama Jaka alizipokea habari za kukamatwa na kuhusishwa mwanaye na mauji kwa mshituko mkubwa sana. Raymond Mloo ndiye aliyempelekea habari zile za kushtusha na kutatanisha. Mara baada ya kupata habari za kukamatwa kwa rafikiye, Raymond alienda moja kwa moja hadi pale kituoni na kuomba kuonana naye. Alikataliwa kabisa kumuona, lakini kitu kilichomshangaza ni kuona kuwa polisi hawakutaka kumuuliza maswali yoyote hata pale aliposema kuwa yeye alikuwa akiishi chumba kimoja na Jaka.

    Kama kwamba walikuwa wakimtaka Jaka tu, na sasa wameshampata.

    Jioni ile ile alikwenda kumpasha habari mama Jaka.

    Kitu kilichomuuma zaidi yule mama ni kule kuzuiliwa kumuona mwanaye siku ile alipoenda pale kituoni baada ya kupata taarifa za kukamatwa kwake.

    Siku iliyofuata magazeti yalipambwa na habari za mauaji yale. Picha za Jaka na Joakim zilitokea kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti maarufu nchini likiyanadi mauaji yale kwa kichwa cha habari kilichosomeka: Mauaji ya kutisha Chuo Kikuu: Mtuhumiwa mbaroni.

    Habari iliyofuatia kichwa cha habari kile ilielezea jinsi mtuhumiwa alivyokutwa katika eneo la tukio na kutiwa mbaroni “katika harakati za kutoroka kutoka eneo la tukio”, na polisi ambao walipigiwa simu na “msamaria mwema” kuwaarifu juu ya tukio lile “la kinyama” muda mchache kabla ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.

    Pia kulikuwa kuna habari ambazo mwandishi wa habari ile alizipata baada ya kuwahoji baadhi ya wanafunzi wa pale chuoni waliowafamu marehemu na mtuhumiwa, kuwa kumekuwa kuna uhasama wa muda mrefu baina ya marehemu na mtuhumiwa na kwamba walishawahi kufanyiana “vitendo vya kiadui” kabla ya tukio hilo la kutisha.

    Gazeti la “Daily News” pia liliandika juu ya habari ile chini ya kichwa cha habari kilichosomeka: Terrible murder at the Hill: Suspect under custody.

    Haikuwa mpaka siku mbili baada ya tukio ndipo Jaka alipopata nafasi ya kuonana na mama yake. Alikuwa amekonda sana kwa siku mbili zile na uso wake ulikuwa umevimba kutokana na kipigo. Huku akibubujikwa na machozi mama yake alimuuliza iwapo yale aliyoyasikia na kuyasoma kwenye magazeti yalikuwa yana ukweli wowote.

    “Hayana ukweli mama...ninasingiziwa tu, na najua ni kwa nini...” Jaka alijibu kwa uchungu.

    “Ni kwa nini unasingiziwa jambo kama hili mwanangu? Itakuwa ni yale yale ya akina Tony?” Mama alimuuliza kwa simanzi.

    “Ni yale yale tu mama…ni mazito sana mama’angu. Nikipewa nafasi ya kuyaeleza mahala muafaka, nitayaeleza. Ni mazito sana kwa kweli!”

    Yule mama alimtazama mwanaye kwa muda.

    “Basi usiwe na wasiwasi mwanangu, mimi nilijua kuwa huwezi kufanya jambo kama hilo...na nitahakikisha kuwa sheria inafanya kazi yake nawe unapewa nafasi ya kusikilizwa. Utaachiwa tu.” Alimwambia mwanaye.

    Jaka alimtazama mama yake huku akijitahidi kuyazuia machozi yaliyokuwa yakimuelemea.vAlijua kuwa kwa hali aliyoiona mpaka kufikia pale, uwezekano wa yeye kutoka mikononi mwa “sheria” ulikuwa mdogo sana.

    “Mimi nataka wewe usiwe na wasiwasi mama...” Alimwambia.

    “Wasiwasi lazima niwe nao mwanangu. Kesi ya mauaji sio jambo dogo na najua kuwa hao waliofanya njama ya kukufikisha wewe hapa watafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa unabaki hapo na unapotea kabisa...hivyo na sisi ni lazima tutafute sheria...nina ahadi ya kuonana na wakili mmoja mzuri sana mchana huu, na nadhani jioni ya leo hii atakuja kukuona.”

    Jaka alimtazama mama yake na kujaribu kutabasamu.

    “Asante sana mama...”

    “Unadhani ni nini ambacho mama ataacha kukifanya kwa ajili ya mwanaye?”

    Tabasamu la Jaka likatanuka zaidi. Mama na mwana walikumbatiana, kisha mama akaondoka.

    Saa mbili baadaye Moze alifika pale mahabusu kumuona.

    Walitazama kwa muda bila ya kusemezana lolote, Moze akionekana mnyonge na aliyekata tamaa kabisa. Jaka alijaribu kutafuta maneno ya kumliwaza mpenziwe lakini hakuyapata.

    “Kwa nini Jaka?” Hatimaye Moze aliuliza kwa sauti ya chini.

    Jaka alimtazama kwa mshangao bila ya kuelewa alikuwa anamaanisha nini.

    “Kwa nini...? Unamaanisha nini Moze?” Alimuuliza.

    Moze alimtazama kwa muda na Jaka akahisi kuona kitu kama hasira machoni kwake, hakujua hasira ile ilikuwa ni kutokana na mambo yaliyomkuta yeye au ni kitu kingine.

    “Kwa nini umemuua Joakim, Jaka? Hicho ndicho ninachomaanisha...”

    Hah!

    Moyo ulimlipuka Jaka na hapo hapo akaingiwa na unyonge wa hali ya juu.

    “Mungu wangu, Moze! Huwezi kuamini kuwa nitakuwa nimemuua Joakim! Ndivyo unavyoamini hivyo? Hata wewe?” Alimuuliza kwa fadhaa kubwa, kisha akaendelea,“Sikumuua Joakim Moze…siwezi kufanya kitu kama hicho kabisa! Na wewe unajua hilo...!”

    “Sasa ilikuwaje hata ukakutwa eneo la mauaji?” Moze aliuliza kwa hasira. Jaka alizidi kupigwa na butwaa.

    Hata mpenzi wangu naye haniamini!

    Kabla Jaka hajajibu swali lile Moze alimtupia swali jingine.

    “Na ilikuwaje glovu zilizotumika kwenye mauaji hayo zikutwe chumbani kwako? Tena chini ya godoro la kitanda chako, sio cha Raymond?”

    Yaani hadi mpenzi wangu naye anashindwa kuniamini katika hili!

    “Moze, we’ unajua kuwa watu tuliokuwa tunapambana nao ni watu aina gani...vyote hivyo vimetegwa makusudi ili nionekane mimi ndiye muuaji, lakini...” Jaka alijaribu kumuelewesha mpenzi wake huku akihisi nguvu zikimwishia kwa kila pumzi aliyokuwa akiitoa katika kufanya hivyo.

    “Wacha kusema uongo Brown! Wewe umemuua mwenzako...umemuua kwa sababu siku zote ulikuwa unataka kulipiza kisasi kutokana na mambo waliyokufanyia na wenzake...” Moze alibwata huku akitiririkwa na machozi.

    E bwana we!

    Jaka aliona kama vile yuko ndotoni.

    “Moze…”

    “...sikutegemea Jaka, sikutegemea kabisa kama itafikia siku utafanya kitu kama hiki...unamuua mwenzio! Kisa nini? Kisasi? Mapenzi?”

    Jamani!

    “Moze! Usiwe na mawazo hayo mpenzi...” Jaka alimwambia kwa kuomboleza huku akipeleka mikono yake ili amshike mabega kumpoza. Moze aliisukuma pembeni mikono ile na kusimama kutoka kwenye benchi alilokuwa amekalia, akarudi nyuma kujiweka mbali naye.

    “Usinishike!” Alimaka huku akilia.

    “Moze, Please!”

    “Brown uliposema kuwa unaniandalia zawadi ambayo sitaisahau maishani mwangu kumbe ulikuwa unamaanisha zawadi hii? Zawadi ya kuniulia mtu?”

    “Heeeh!”

    “Kwani nilikwambia kuwa nataka damu ya mtu ndiyo niamini kuwa unanipenda Brown...?”

    Looh!

    “Moze...you are over-reacting...” Jaka alijitahidi kumpoza mpenziwe, akimaanisha kuwa alikuwa amepandwa jazba bila sababu tu. Ile kauli ikaonekan kumkera Zaidi Moze.

    “N’na over-react miye? N’na Over-React? Kweli? Brown...umemuua mtu in cold blood, for God’s sake, halafu unasema n’na over-react!”

    “Moze, unajipandisha jazba bila sababu juu ya hili mpenzi, na ndio maana unashindwa kunielewa...mimi siwezi kuua mtu, na wala sijamuua Joakim...hizo ni njama tu ...kuna mambo nimeyajua ambayo...”

    “Sasa nimekuwa nashindwa kukuelewa...kwa nini usisubiri kutoa maelezo yako kwa hakimu Jaka...? Haitosaidia kitu kunieleza mimi hayo maelezo...penzi langu lote kwako...na mambo yote yaliyotupata kwa ajili ya penzi letu, leo hii umeona zawadi ya kunipa kwenye Birthday yangu ni kuniulia adui yako? Sasa ona faida yake...!” Moze alisema kwa masikitiko huku akilia.

    Lah!

    Mshangao uliomvaa Jaka wakati akimtazama mpenzi wake aliyedhani kuwa alikuwa akimjua vizuri sana ulikuwa ni mkubwa kuliko. Hakuamini kabisa yale aliyokuwa akiyasikia. Sasa hivi ndio alikuwa akiuhitaji sana msaada wa Moze, msaada wa upendo, huruma na kuelewa kutoka kwa mpenzi wake. Badala yake, mpenzi wake mwenyewe ndiye anakuwa wa kwanza kumtupia lawama na kutomwamini! Ni nani tena zaidi ya mama yake na Raymond atakayemuamini?

    Nguvu zilimwisha.

    “Moze...mbona hiyo siyo zawadi niliyokuwa nimekuandalia? Zawadi yako ilikuwa tofauti kabisa...mimi sikumuua Joakim, na naapa kwa jina la mola wangu kuwa sikumuua...nakuomba sana uniamini mpenzi wangu, kwani imani yako wewe ni nguvu kubwa sana kwangu katika kipindi hiki...naomba uniamini mpenzi...”

    Lakini Moze alikuwa kama aliyepagawa. Ilikuwa vigumu sana kwake katika mazingira yaliyokizunguka kifo cha Joakim, kuamini kuwa Jaka hakuhusika na kifo kile.

    “Jaka, mimi siwezi kukupenda tena maishani mwangu kutokana na jambo ulilolifanya...kila kitu kinaonesha kuwa ni wewe ndiye uliyemuua Joakim...na mimi najua kuwa unazo sababu nyingi za kutaka kufanya hivyo, nitakachoweza kufanya Jaka ni kukuombea kwa Mungu tu akusamehe, lakini sidhani kama nitaweza tena kuwa na wewe kama nilivyokuwa nawe hapo mwanzo...” Moze alimwambia kwa masikitiko, kasha akageuka na kuanza kutoka nje ya chumba kile.

    Jaka alichanganyikiwa.

    “Lakini Moze...Joakim alikuwa ni rafiki yangu...tulishapatana siku chache kabla ya kifo chake…wakati nilipokuwa nimelazwa pale hospitali!” Jaka alimambia kwa hamaniko.

    Moze alisimama ghafla na kutulia tuli. Kisha aligeuka taratibu na kumtazama kwa macho yaliyokuwa na mchanganyiko wa mshangao, kutoamini na fadhaa.

    “Joakim alikuwa rafiki yako tangu lini, Jaka?” Alimuuliza kwa sauti ya upole huku akimshangaa waziwazi.

    Jaka aliguna na kutikisa kichwa kwa kukata tamaa. Aliona wazi kuwa hakuna atakalosema ambalo Moze atalielewa katika hali ile.

    “Sasa kama rafiki yako ndiyo umemfanya vile...haya mie unayeniita mpenzi wako utanifanya nini...?” Moze alimuuliza kwa uchungu.

    Heh!





    Jaka alibaki akimtazama yule binti kwa simanzi, hakuamini kama ni kweli mpenziwe alikuwa amemgeuka ghafla namna ile.

    “Jaka unataka kunifanya mimi mjinga...? Unasema uongo hivi hivi bila haya? Joakim angekuwa rafiki yako mimi nisingejua? Leo hii unategemea mimi nikuamini ukiniambia kuwa alikuwa rafiki yako...?”

    Hata wakati akiyasikia maneno yale ya kunyong’onyeza moyo yakitamkwa, majuto na simanzi vilimshukia Jaka kutokana na uamuzi wake wa kutomueleza Moze tangu hapo awali kuhusu yale maongezi yake na Joakim ya siku ile Joakim alipokwenda kumtemebelea pale hospitali.

    Laiti angejua kuwa haya yangekuja kutokea!

    Ama kweli usilolijua, usiku wa kiza.

    Sasa ni nani atamuamini akisema kuwa Joakim hakuwa adui yake wakati wa kifo chake?

    Chuki aliyoiona machoni kwa Moze wakati akimueleza maneno yale ya kukatisha tamaa ilikuwa ni kubwa sana, na hilo lilimtisha pasina kifani. Na wakati akimuangalia yule binti akimsemesha yale maneno ya kunyong’onyeza moyo kwa chuki kubwa namna ile, ilimfunukia wazi kuwa kitu kilichokuwa kikiwaunganisha na kuwaweka pamoja siku zote, kilikuwa kimekatika, hakikuwepo tena. Alichokiona wakati ule machoni mwa yule msichana kilikuwa ni chuki iliyoelekezwa kwake yeye...macho ambayo siku zote yalikuwa yakimuangalia kwa upendo, sasa yalikuwa yakimuangalia kwa chuki ya hali ya juu. Hakukuwa na penzi hata kidogo kwenye macho yale! Ilikuwa ni chuki, chuki, chuki...

    Mungu wangu! Jaalia hii iwe ndoto tafadhali...

    “Moze...” Jaka alitaka kusema zaidi lakini Moze alimkatisha kwa kutikisa kichwa chake kwa nguvu kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

    “Jaka...kila mtu anajua kuwa wewe na Joakim hamkuwa marafiki...lakini tulishakubaliana kuwa hakuna haja ya kutaka kulipiza kisasi wala kuendeleza uhasama…”

    “Na hivyo ndivyo ilivyokuwa Moze…hebu nisikilize basi kwanza nikueleweshe kilichotokea…”

    “Kilichotokea ni kwamba umemuua Jaka…umeua mtu wewe! Kuna nini tena cha kuelewesha hapo, eenh?” Moze alimkatisha kauli kwa jazba huku akitikisa kichwa na akifumba macho kama kwamba alikuwa hataki hata kuendelea kumuona.

    Jaka alibaki akimshangaa. Moze akafumbua macho na kumtazama Jaka kwa muda.

    Walitazamana.

    “Unanidanganya Jaka! Unanidanganya...kwamba Joakim alikuwa rafiki yako...!

    “Moze wewe huelewi...inabidi unisikilize, la sivyo hutaelewa kabisa...”

    “Haitosaidia kitu Jaka! Kuelewa au kutoelewa hakutobadilisha ukweli wa jambo hili Brown...sina haja ya kuelewa tena! Sina haja ya kuelewa kwa sababu huu ndio mwisho wa mapenzi yangu kwako! Sina tena upendo na wewe na sitaki kukuona tena maishani mwangu kwa sababu wewe ni muuaji Jaka...muuaji mkubwa!” Moze alifoka kwa hasira huku macho yake yakionesha kuumia kwa kiasi kikubwa sana.

    “Ndio maana Rose alikuwa akijaribu kunitahadharisha kwenye ile barua yake…kumbe alijua kuwa wewe ni mtu wa namna gani! Je, na Joakim ulimuua kwa sababu alikugundua kuwa u- muuaji Jaka?” Moze aligongelea msumari wa moto kidondani.

    “Eeenh?” Jaka alibaki mdomo wazi. Alihisi kitu kama msumari wa moto kikichoma kati kati ya moyo wake. Alitaka kusema kitu zaidi lakini sauti haikutoka tena. Alijaribu kumeza mate lakini mate yalikuwa yamemkauka. Alifumba macho kwa nguvu na kuyafumbua.

    “Moze...!” Ndilo neno pekee lililotoka kinywani mwake baada ya hapo.

    “Wewe ni muuaji Jaka. Tena muuaji wa watu wasio na hatia! Siwezi kupendana na muuaji Jaka, samahani sana...na naomba kuanzia sasa tusijuane!” Moze alifoka na kukimbia kutoka kwenye chumba kile huku akibubujikwa na mchozi. Jaka alikurupuka kutoka kwenye benchi alilokuwa amekalia na kujaribu kumsimamisha.

    “Subiri Moze! Usiondoke tafadhali...tafadhali usiniache...sio sasa hivi! Unakosea sana Moze...yote unayoamini sivyo yalivyo...!” Alimpigia kelele, lakini Moze alikuwa ameshatoka nje ya chumba kile. Akabaki akiwa amesimama katikati ya chumba kile asijue la kufanya. Alijishika kichwa na kuinua uso wake kutazama juu, kisha akaachia ukelele mkubwa sana uliokuwa chanzo cha kilio kikubwa cha uchungu na kuomboleza. Alijibwaga pale sakafuni na kubaki akiwa amepiga magoti huku akiwa amejishika kichwa chake kwa mikono yake yote miwili kabla ya kujiangusha sakafuni kwa kishindo akitanguliza mikono na uso wake.

    Mwili wake ulikuwa ukirukaruka kwa kilio cha kwikwi hali akiwa amesujudu pale sakafuni. Maneno ya Raymond Mloo yalimrudia tena na tena kichwani mwake huku akilia kwa sauti.

    “...msichana anaweza kukupenda sana, lakini pia anaweza kukuchukia sana...na hapo ndipo utakapojuta kuzaliwa...”

    Machozi yaliendelea kumbubujika akiwa pale chini huku akihisi uchungu usio kifani. Hakujua afanye nini. Maneno ya kwenye shairi alilomtungia Moze kwa ajili ya siku yake ya kuzaliwa yalimjia na kumzidishia uchungu maradufu.



    ... When your love is gone, my tears will flow.

    …Siku penzi lako litakapoisha, machozi yatanibubujika...



    Hajui alikaa pale kwa muda gani. Hatimaye alijizoazoa na kukaa pale sakafuni akiwa ameegemea ukuta. Kwa namna fulani maneno kutoka kwenye ule wimbo wa Roxette ambao siku zote ulikuwa ukimliza Moze yalimjia kichwani.

    It must have been love, but it’s over now...

    Bila shaka lilikuwa ni penzi, lakini sasa limekwisha...

    Alianza kulia upya.



    __________________



    Sehemu nyingine ya jiji, Raul aliinua uso wake na kumtazama Kamishna Msaidizi wa Polisi Albert Bangusillo kwa macho yake ya kuogofya.

    “Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa huyo kijana anajua juu ya biashara inayofanyika hapa?” Alimuuliza, na Albert Bangusillo hakufanya haraka kumjibu. Alipeleka kinywani sigara iliyokuwa mkononi mwake na kuvuta moshi wa tumbaku kutoka kwenye sigara ile na kuupuliza juu kwa madaha.

    Walikuwa nyumbani kwa Raul, maeneo ya Upanga, jijini Dar.

    “Kwa mujibu wa maelezo yake, hiyo ndiyo maana yake…na kwa vyovyote atataka kutumia hilo kama njia ya kujisafishia jina lake na kuachiwa huru.” Hatimaye alimjibu.

    Raul alimkazia macho kwa hasira.

    “Lakini si tayari ana kesi ya mauaji? Sio rahisi kwake kuachiwa hivi hivi tu eti kwa kuwa amegundua njama za biashara ya kulevya…” Alimwambia.

    “Yeah…ni kweli, lakini yule kijana siye aliyeua Raul…sheria ina namna ya kutambua jambo kama hilo. Unadhani akipata wakili mzuri itakuwa vigumu kumkwamua kutoka kwenye tuhuma feki kama hizo?”

    Raul Pinto Garcia alimtazama kwa jicho la ghadhabu zaidi.

    “Hapati wakili wa kumkwamua! Ataangamia tu!” Alikoroma.

    “Hivyo ndivyo tunavyotarajia…lakini iwapo itatokea vinginevyo, italazimisha uchunguzi wa kina ufanyike kwenye hayo madai yake na pia kwa kumtafuta muuaji halisi…jambo ambalo litaleta usumbufu mkubwa kwa biashara yote. Hiyo haitasaidia lolote katika biashara, na mambo yakifika hapo Raul, sio siri…sitaweza tena kuyadhibiti!” Bangusillo naye alimkoromea.

    Raul aliguna na kubaki akimtazama kwa muda bila ya kusema neno, na alipoongea ilikuwa dhahiri kuwa mjadala ule ulikuwa umefikia mwisho.

    “Huyo kijana atazibwa mdomo milele Albert, iwe kabla au baada ya hukumu, it doesn’t matter….vijana wangu watahakikisha kuwa anapatwa na maafa fulani, na wewe kazi yako kama kawaida itakuwa ni kuhakikisha kuwa polisi hawaingilii mipango yangu, Okey?”

    Albert Bangusillo aliafikiana naye kwa kichwa.

    “Usiwe na shaka na upande wangu…ila sasa na wewe usipomdhibiti huyo Tony atakuja kututia wote kwenye balaa…” Alimwambia.

    “Sipendi mtu yeyote anifundishe nini nifanye na nini nisifanye…shughuli hizi sikuzianzia hapa! Kitu pekee kinachonifanya nimtumie Tony ni kuwa popote anapokwenda anajulikana yeye ni mtoto wa nani na hivyo huwa hakuna maswali, na wewe unaelewa hilo!” Raul alimjibu kwa ghadhabu.

    “Hilo liko wazi Raul, ila ni lazima nikukumbushe kuwa tatizo sio Jaka tu kwa hapa tulipo…na Tony naye pia ni tatizo…na wote wawili ni juu yako kuwadhibiti. Mimi mchango wangu kwako uko pale pale…n’taendelea kuhakikisha kuwa polisi haiingilii mipango yako, mengine ni juu yako!” Bangusillo alimjibu.

    “Basi tuko sawa. Fanya jukumu lako…nami niache nifanye yangu!” Raul alimkoromea.

    Waliagana, Bangusillo akiondoka na bahasha nene iliyosheheni noti nyingi.



    _________________



    Muda mfupi baada ya Moze kuondoka pale kituo cha polisi, Raymond Mloo alifika na kumkuta Jaka akiwa katika hali mbaya sana. Baada ya kumbembeleza sana, hatimaye kwa uchungu na taabu kubwa Jaka alimueleza kila kilichojiri baina yake na Moze pale mahabusu. Habari ile ilimsikitisha sana Raymond.

    “Yaani…Dah! Moze huyu huyu…?”

    “Ndiyo rafiki yangu…Moze kanigeuka kaka!”

    “Yaani, aisee!” Raymond alijikuta akiishiwa na maneno ya kusema.

    Walikaa kimya mle ndani kwa muda mrefu sana mpaka yule askari aliyekuwa zamu alipokuja na kumtaka Raymond aondoke kwani Jaka alikuwa ametembelewa na wageni wengine. Raymond alimtazama rafiki yake kwa huzuni, kisha walikumbatiana, na bila kuongea lolote akatoka huku akijipangusa machozi.

    Baada ya Raymond kutoka, Mama Jaka aliingia akiwa ameongozana na msichana mmoja ambaye Jaka alikisia kuwa na umri wa kati ya miaka ishirini na nane ua thelathini hivi. Alikuwa amevaa suti nzuri nyeusi iliyokuwa na sketi fupi sana iliyoonesha mapaja yake mazuri na miguu yake mirefu. Mkononi alikuwa amebeba mkoba maalum wa kiofisi, maarufu kama briefcase.

    “Naitwa Abiah…Abiah Byabato…nimeajiriwa na mama yako nikutetee kwenye kesi inayokukabili. Unajisikiaje?” Yule msichana alijitambulisha huku akimpa mkono na kumuwashia tabasamu zuri sana. Jaka alijitahidi kutabasamu kidogo huku akiupokea mkono ule laini. Alizitazama kucha ndefu na nzuri za vidole vya yule binti zikiwa zimepakwa rangi ya damu ya mzee na kukumbuka vidole vya mpenzi wake Moze.

    “Sijambo…wewe ni wakili?” Jaka aliijibu salamu ya yule binti na kumtupia swali. Abiah aliafiki kwa kichwa huku akitabasamu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unadhani utaweza kunisaidia dhidi ya tuhuma hizi?”

    “Hakuna kisichowezekana kaka’angu…vipi huo uso wako, umepigwa?” Abiah alimjibu na kumtupia swali, akimakinika ghafla.

    Jaka aliafiki kwa kichwa. Abiah alimtazama na kumuuliza tena.

    “Umepigwa ukiwa chini ya ulinzi?”

    Jaka akaafiki tena kwa kichwa. Umakini uliojengeka usoni kwa yule binti uliongezeka. Alimwita yule askari wa zamu, na kwa dakika kumi zilizofuata, alimtetemesha vibaya sana yule askari kwa kumnukulia vifungu kadhaa vya kisheria vinavyopinga mtuhumiwa kupigwa akiwa chini ya ulinzi bila ya sababu maalum. Yule askari alibabaika mno na alijitahidi kujitetea kuwa yeye hakuwa zamu wakati mambo hayo yanatokea.

    “Basi mkuu wako wa kituo atajibu shutuma hizo mahakamani, kwani mimi na mteja wangu tutawafungulia kesi ya police brutality, halafu ndio utajua nani alikuwa zamu na nani hakuwepo!” Abiah alimchachamalia zaidi yule askari huku akiandika kwenye kijitabu kidogo alichotoa kwenye mkoba wake, akimaanisha kuwa atalifungulia jeshi la polisi kesi ya “ukatili wa kipolisi” huko mahakamani.

    Jaka alivutiwa na jinsi yule binti alivyokabiliana na yule askari na akajua kuwa angalau alikuwa amepata wakili makini na mwenye kuielewa kazi yake.

    “Jambo la kwanza tunalotakiwa kufanya kaka Jaka ni kukupatia dhamana ili utoke katika makazi haya mabaya. Halitakuwa jambo rahisi kutokana na uzito wa tuhuma zenyewe, lakini kutokana na mazingira haya ya kupigwa kwako, tunaweza kushawishi hadi ukapata dhamana, Okay?” Abiah alimwambia huku akirudisha tena ile sura yake nzuri yenye tabasamu.

    Jaka aliafiki kwa kichwa.

    “Sasa naomba unieleze mkasa wote ulivyokuwa hata ukajikuta katika tuhuma hizi…na naomba unieleze ukweli wako wote. Mimi ni wakili wako na ndiye msiri wako mkuu kuanzia sasa mpaka mwisho wa kesi hii.”

    Jaka alikaa kimya kwa muda, kisha akaanza kumueleza. Alimuaelezea kisa chote tangu mwanzo hadi mwisho wakati Abiah akimrekodi maelezo yake kwa kutumia redio kaseti ndogo aliyokuja nayo. Jaka alipomaliza kutoa maelezo yake, Abiah alikaa kimya kwa muda huku akimtazama.

    “Mnh! Pole sana Jaka…lakini naomba nikuhakikishie kuwa hii sio kesi ngumu kwako kama inavyoonekana. Kwanza lazima tuhakikishe unafunguliwa mashitaka…au unaachiwa huru bila kushitakiwa, ila huwezi kuendela kuwa mahabusu tu hapa bila sababu. Kesi ikiwa mahakamani ndio inakuwa rahisi kwetu kuivunjavunja na kuibuka washindi…”

    “Nakubaliana nawe, lakini…unadhani kesi iliyo na vidhibiti kama hivi, japo vya kupandikizwa…itakuwa rahisi kuivunjavunja kama unavyodai?” Jaka alihoji, na mama yake akitikisa kichwa kukubaliana na swali lile.

    “Oh, Yes…ila…itanibidi nipitie vifungu kadhaa vya sheria na nionane na baadhi ya wanasheria wenzangu, na baada ya hapo tutakuwa tayari kupambana mahakamani…kama wataifikisha mahakamani.” Abiah alimwambia huku akitabasamu.

    “Kwa hiyo ndiyo kusema…” Jaka aliuliza kwa matumaini kidogo, na Abiah alirudisha tena ile sura yake ya umakini.

    “Sitaki kukupa matumaini hewa Jaka, lakini kutokana na maelezo yako, hii ni kesi nzuri sana kwetu. Tuna nafasi kubwa sana ya kushinda na kudai fidia ya mamilioni baada ya hapo, ila kuna vipengele fulani vya sheria ambavyo nahitaji kuvihakiki kwanza kabla sijawa na uhakika juu hilo…” Alimwambia kwa uangalifu. Jaka alimtazama na kuafiki maelezo yale kwa kichwa.

    Muda mfupi baadaye Abiah aliaga na kuahidi kurudi tena siku iliyofuata saa nne asubuhi akiwa na maelekezo juu ya dhamana na uhakika juu ya vile vipengele muhimu vya sheria.

    Jaka alibaki na mama yake kwa muda zaidi, kabla naye hajaondoka na kumuacha na majonzi yake pale mahabusu.



    __________________



    Wakili Abiah Byabato alitazama saa ya ukutani pale sebuleni kwake na kupiga mwayo. Ilikuwa ni saa nane za usiku na alihisi uchovu mkubwa. Alishusha miguu yake mirefu kutoka juu ya meza ndogo iliyokuwa imetapakaa vitabu na makabrasha kadhaa ya sheria na kusimama huku akijinyoosha.





    Ile kesi ya Jaka ilikuwa ni kesi nzuri sana. Sasa alikuwa na uhakika kuwa alikuwa ana uwezo wa kushinda kesi ile iwapo itafikishwa mahakamani. Mwili ulimsisimka kwani alijua kuwa kushinda kesi ile kungempatia umaarufu mkubwa na kumfanya kuwa miongoni mwa mawakili wa kutumainiwa nchini.

    Na maisha yake yatabadilika.

    Akiwa amevaa suruali ya kulalia ya kitambaa cha hariri hali akiwa kifua wazi, alichukua ile redio kaseti yake ndogo iliyorekodi maelezo ya Jaka na kupachika visikilizio vya redio ile masikioni. Alizima taa ya pale sebuleni na kuelekea chumbani kwake ambako alizima taa ya kawaida na kuwasha taa ya rangi ya buluu, akajibwaga kitandani huku akisikiliza kwa mara nyingine tena yale maelezo ya Jaka. Aliyasikiliza upya yale maelezo hadi mwisho, kisha akayarudia tena. Kabla ile kaseti haijafika mwisho katika ile mara ya pili, alipitiwa na usingizi mzito.

    Muda mfupi baada ya kupitiwa na lile lepe zito la usingizi, alihisi kitu kikimbana kwa nguvu mdomoni. Alishtuka kutoka usingizini na moyo ulimlipuka vibaya sana alipoona sura ya mtu asiyemjua ikiwa imemuinamia karibu sana na uso wake. Alitaka kupiga kelele lakini mkono wa yule mtu ulikuwa umembana mdomo kwa nguvu. Alijaribu kujiinua kutoka pale kitandani huku akitupa mikono na miguu, lakini vyote vilikuwa vimebanwa kwa nguvu. Alibaki akiikodolea macho ile sura ya duara uliyokuwa ikitabasamu.

    Nani?? Unataka nini…?

    Ingawa ile sura ilikuwa ikitabasamu, macho mekundu yaliyokuwa na nyama zilizolegea chini ya macho yale yalikuwa hayatabasamu hata kidogo. Yalikuwa ni macho maovu na wakili Abiah Byabato aliishiwa nguvu kwa woga.

    “HuSsshhh, mwanasheria…kimya!” Yule mtu alimnong’oneza, halafu akaendelea huku akimuwekea mdomo wa bastola fupi kwenye paji la uso, “Nitatoa mkono wangu mdomoni mwako taratibu, nawe utaendelea kubaki kimya hivyo hivyo…la sivyo natawanya ubongo wako…sawa?”

    Abiah aliitikia kwa kichwa haraka haraka huku akiwa ametumbua macho vibaya sana.

    Yule mtu alimuachia mdomo wake taratibu huku akimdidimizia ile bastola kwenye paji la uso. Abiah alibaki kimya huku akifumba macho yake kwa nguvu, kisha aliyafumbua taratibu akitaraji kujikuta peke yake pale kitandani, lakini bado yule mtu alikuwepo, akiendelea kumtazama huku akitabasamu.

    Heh!

    “Un…unataka nin…we’ nani….?” Abiah aliuliza kwa kitetemeshi.

    Yule mtu aliendelea kumtazama tu huku akiwa amemuwekea bastola kwenye paji la uso. Na hapo ndipo Abiah alipomuona mtu mwingine akitokea nyuma ya mtu yule.

    Wako wawili!

    Ingawa taa ya rangi iliyokuwa ikiwaka chumbani kwake haikuwa na mwanga wa kutosha kuona vizuri, aliweza kuona kuwa sura nyembamba ya yule mtu wa pili ilikuwa imetapakaa alama nyingi za ndui. Yule mtu mrefu mwenye sura ya ndui alianza kumfunga mikono na miguu yake kwa kamba. Abiah hakuthubutu kupiga kelele kwani bastola bado ilikuwa kwenye paji lake la uso. Baada ya kumfunga kamba kwa nguvu pale kitandani, yule mtu mwenye sura ya ndui alitoa plasta kubwa kutoka kwenye mfuko wa suruali yake na kumbandika mdomoni.

    Yule mtu mwenye tabasamu aliondoa bastola usoni kwa Abiah na kuanza kutembeza macho yake kwenye sehemu ya juu ya kiwiliwili cha yule msichana. Aliyatazama matiti mazuri na madogo ya yule binti kwa muda, kisha akateremsha macho yake taratibu hadi kwenye kitovu cha yule binti.

    Mungu wangu…wanataka kunibaka…!

    Wakili Abiah aliwaza kwa kihoro huku akitokwa na machozi.

    “Hapana mrembo wangu…hatuna haja ya kukubaka….” Yule mtu mwenye tabasamu la kuogofya alimwambia kwa sauti ya kuchobeza, kama kwamba alikuwa ameyasikia mawazo yake.

    Oooh, sasa mnataka nini jamani? Mmeingiaje humu ndani…?.

    “Abiah…Abiah…Abiah…kwa nini unataka kujiharibia maisha yako bure? Mtoto mrembo kama wewe…” Yule mtu mwenye tabasamu alimnong’oneza huku akivuta meza ndogo iliyokuwa mle chumbani na kuiweka kando ya kitanda na kuketi. Abiah alibaki akitembeza macho huku moyo ukimdunda kwa woga na kihoro.

    Kwani nimefanya nini jamani…? Mmejuaje jina langu…?

    Wale jamaa walikuwa wakifanya wayafanyayo kwake kimya kimya, na Abiah alipandwa kihoro pale alipomshuhudia yule mtu mwingine akimpandia pale kitandani na kumpigia magoti juu yake, akikiweka kiwiliwili chake katikati ya miguu yake.

    Ooh, mungu wangu! Mnanibaka nyieee…!

    Abiah alibaki akilia kwa kukata tamaa, akitembea macho tu kufuatilia kile alichokuwa akifanyiwa. Na hata pale lile wazo lilipokuwa linapita akilini mwake alimuona yule mtu mwembamba akimuwekea ncha ya kisu chembamba na kirefu katikati ya matiti yake mazuri. Mwili ulimsisimka, taharuki ikamtawala. Huku akimtazama usoni kwa macho ya kutisha, yule jamaa alitembeza ncha ya kisu kile taratibu kutoka kifuani kwa yule binti hadi kitovuni. Hapo kisu kile kilitulia na yule jamaa akijiweka vizuri pale kitandani. Kufikia hapo Abiah alikuwa akilia kama mtoto mdogo huku akitoa miguno hafifu kutokana na kuzibwa mdomo na ile plasta aliyobandikwa mdomoni. Alizungusha macho kule kwa yule mtu mwingine, na kuona kuwa alikuwa akitazama mambo yale huku akitabasamu. Mwili ulimuingia baridi. Lilikuwa ni tabasamu la kutisha kuliko yote aliyowahi kuyaona maishani mwake.

    Ghafla alihisi yule mtu aliyekuwa pale kitandani akiishika kwa nguvu suruali yake ya kulalia na kwa tendo moja la haraka sana aliichana ile suruali kwa kisu chake kikali. Mguno wa woga ulimtoka huku akijitahidi kupiga kelele bila mafanikio. Yule mtu alivuta kwa nguvu mabaki ya suruali ile na kuitupa kando bila kujali.

    Wakili Abiah Byabato alibaki uchi, kwani huwa havai chupi wakati wa kulala.

    Eeeh, Mungu wangu…!

    Yule jamaa alimtazama kwa dharau akiwa amelala uchi wa kuzaliwa pale kitandani, na Abiah alijihisi anakaribia kufa.

    Ni nini hasa mnachokitaka jamani…kwa nini mnanidhalilisha namna hii?

    Yule jamaa alikitembeza tena kile kisu taratibu kuelekea kwenye sehemu ya uuke wake, na Abiah alihisi ubaridi ukimtambaa mwili mzima, akawa analia waziwazi huku kamasi zikimvuja. Kile kisu kilisimama kwa muda katika lile eneo la uuke wake, kisha yule jamaa akafanya kama kwamba alikuwa akijaribu kumnyoa nywele zilizokuwa eneo lile kwa kisu kile.

    Abiah akajikojolea bila ajizi.

    Jamaa hakuonekana kujali hali ile, badala yake alikipandisha tena kisu kile taratibu na kukituliza kwenye titi la yule binti na kumtazama usoni kwa macho yake yaliyojaa unyama wa hali ya juu.

    Huku akilia kwa uchungu Abiah alijikukurusha pale kitandani kujaribu kujikomboa, lakini kila alivyofanya hivyo ncha kali ya kile kisu ikawa inamcoma kwenye titi, akabaki akijinyonganyonga tu pale kitandani huku akimtupia macho ya kuomboleza yule mtu mwenye tabasamu lisilokauka, machozi yakimbubujika, akitoa sauti za kilio kilichobanwa.

    Ndipo yule mtu mwenye tabasamu alipoinama na kumuwekea mdomo wake sikioni, kisha akamnong’oneza kwa ile sauti yake ya kubembeleza huku akimchezea rasta zake kimahaba.

    “Mambo yote haya umejitakia mwenyewe Abiah…huyu bwa’ mdogo hapa alisema kuwa tuje tukuue tu halafu twende zetu…lakini mi’ n’kamwambia kuwa haitakuwa busara kulipotezea taifa rasilimali-mtu kama hii, Abiah…au wewe unaonaje? Kukuua si kutalipunguzia taifa idadi ya rasilimali-watu, eeeennh?”

    Abiah alijikuta akiitikia kwa kichwa haraka haraka huku akiwa ametumbua macho, moyo ukimwenda mbio.

    “Safi sana! Mi’ n’lijua kuwa tutaelewana tu Abiah…” Mzee wa matabasamu alimwambia huku akimpigapiga kichwani kwa namna ya kumbembeleza, kisha akaendelea, “…kwa hiyo tukakubaliana kuwa badala ya kuja kukuua, tuje tukueleze tu mawazo yetu halafu tukuachie wewe uyatekeleze, na…ukiyatekeleza basi hutatuona tena maishani mwako na utaendelea kuishi…”

    Kufikia hapo mzee wa matabasamu alipiga kimya na kubaki akimtazama tu, tabasamu likiwa limeganda usoni kwake. Alikaa vile kwa dakika nyingi kiasi cha kumjaza wahka Abiah.

    Mnataka kunieleza nini kwani ndugu zangu…? Nielezeni basi muende zenu…!

    Yule mtu mwingine alimtembezea tena ncha kali ya kisu chake tumboni, na Abiah alijihisi kupoteza fahamu huku mkojo aliojikojolea ukimuwasha mapajani.

    “…lakini ukiamua kuwa mkaidi, basi…itabidi tufanye kama bwa’ mdogo hapa alivyopendekeza….” Hatimaye yule mzee mwenye tabasamu lisilokauka akamalizia kauli yake, na safari hii lile tabasamu lake likaishia kwenye kicheko chepesi, kisha akapiga kimya tena, akawa anajishughulisha kuisafisha-safisha bastola yake kwa kutumia shuka ya kile kitanda.

    Abiah alimtazama kwa woga akamgeukia yule mtu mwembamba aliyemkalia juu yake pale kitandani, ambaye sasa alikuwa anatumia kile kisu chake kujikunia kidevu chake, kama kwamba hana habari naye tena.

    Abiah alitamani awasemeshe wale watu lakini alikuwa amezibwa mdomo. Walibaki katika hali ile kwa dakika kadhaa, ambazo Abiah aliziona ni masaa.

    Sasa mnataka nini kwani jamani??? Semeni basiii!!!

    Aliwakemea nyuma ya miguno aliyokuwa akiitoa huku akihangaika pale kitandani. Nahapo ayule mtu mwenye tabasamu la mfululizo alimgeukia ghafla na kuwambia huku akimazama moja kwa moja usoni na tabasamu lake likiwa imara usoni kwake.

    “Jaka ni habari mbaya sana Abiah!”

    Khah!

    “Na mtu yeyote anayejihusisha naye anakutwa na mabaya zaidi ya haya unayoyaona hapa sasa hivi Abiah…so kaa mbali na Jaka bi mdogo. Hayo ndiyo mawazo tuliyokuja kukupa usiku huu wakili.” Mzee wa matabasamu alimalizia kwa sauti yake ya kuchombeza huku akimvutavuta zile rasta zake.

    Haa! Kumbe ndio hilo! Jaka…!? Oh, Mungu wangu…!

    Wakili Abiah Byabato alilia kama mtoto mdogo. Matabasamu aliendelea tu kumueleza kwa ile sauti yake ya kuogopesha, japo mwenyewe ndio alikuwa anaifanya iwe ya kuchombeza.

    “Kama umetuelewa juu ya hilo Abiah, sisi tutaondoka nawe utaendelea kuishi. Ila ukijitia kupiga simu au kutoa taarifa polisi tu, ujue huo ndio mwisho wako…tutakutokea popote pale ulipo na tutakuua taratibu sana hadi utatubembeleza tukuue haraka haraka, upo hapo?”

    Doh!

    Abiah aliitikia kwa kichwa huku akiwa amemtumbulia macho yule mtu. Macho ya yule mtu sasa yalikuwa makatili kweli kweli na bado lile tabasamu lake lilikuwa palepale.

    “Lazima ukumbuke juu ya mawazo yetu kuhusu Jaka Abiah, sawa?”

    Kwa mara nyingine Abiah aliitikia kwa kichwa haraka haraka, macho yakimtembea, machozi yakimbubujika, akili ikimzunguka. Matabasamu alimkazia macho, na alipotaka kugeuza uso wake alimkamata kidevu kwa nguvu na kumgeuza ili waendelee kutazamana, kisha akamgeukia yule mwenzake mwenye sura ya ndui.

    “Hebu muoneshe Abiah mfano wa yatakayompata iwapo atasahau haya mawazo yetu juu ya Jaka.” Alimwambia, na kwa mara ya kwanza tangu wamuibukie mle chumbani mwake, Abiah aliona tabasamu likichanua usoni kwa yule mtu mwenye uso wa ndui, kisha kwa kihoro kikubwa alimshuhudia yule mkatili akimkamata kidole cha shahada na kumuwekea kile kisu kwenye pingili ya kidole kile kwa muda.

    Mungu wangu, ananikata kidole!

    Kisha kama aliyebadili mawazo, yule jamaa alikihamishia kisu kile kwenye kucha ya kile kidple na kuanza kuikata taratibu sana kama kwamba kile kisu kilikuwa ni wembe.

    Oooooh!

    Alipomaliza kumkata ile kucha alihamia kidole kingine…na kingine…na kingine. Kile kisu kilikuwa kikali kuliko wembe. Yalikuwa ni mateso makubwa sana kwa Abiah, ambaye alibaki akilia huku akiziona kucha zake za mikononi alizozipenda na kuzitunza sana zikikatwa na yule mtu ambaye sasa alijihakikishia kuwa alikuwa mwehu. Na kila kucha iliyokatwa mwili ulimsisimka kwa kuhofia kukatwa kidole na kisu kile kikali. Alipomaliza vidole vyote vya mikononi, yule mtu alihamia miguuni na kumkata kucha zote za miguuni. Aliifanya ile kazi kwa utaratibu wa hali ya juu kiasi kwamba Abiah alitamani kumpigia kelele kuwa afanye haraka amalize ili apate kupumua.

    Ilikuwa ni hali ya kuogopesha sana.

    Hatimaye yule mtu alimaliza.

    “Vizuri sana dogo!” Matabasamu alisema baada ya yule jamaa kumaliza kazi yake, kisha akamgeukia Abiah. “Na huo Abiah, ni mfano tu wa kuhakikisha kuwa hutasahau juu ya haya tuliyokueleza…kaa mbali na Jaka…kaa mbali sana na Jaka…Jaka ni habari mbaya sana kwako!” Alimwambia. Abiah alianza kutulia kwani alijua kuwa karibu wale watu wataondoka. Lakini mambo yalikuwa bado. Yule mtu alibaki akimtazama tu baada ya kumwambia yale maneno.

    Sasa mbona hamuondoki…?

    “Sasa tunataka kukuonesha kuwa hatutanii juu ya haya tuliyokuja kukueleza Abiah. Utakapokwenda kinyume na maelekezo yetu, utapatwa na madhila makubwa kuliko haya utakayoyapata hivi punde.”

    Nhah? Nini tena…? mbona sielewi…kuna madhila gani tena zaidi ya haya ndigu zangu? Eeh Mungu wangu nisaidie mie….!

    Abiah alipagawa.. Na hapo yule jamaa mwembamba aliyemkata kucha kwa namna ya kutisha kabisa, alimkamata kidole chake cha shahada cha mkono ya kushoto na kuanza kukikeremsha taratibu kisu cha kuelekea kwenye kidole kile.

    Oooh, sasa nd’o wanan’kata kidole!

    Alijikukurusha kwa nguvu pale kitandan huku akigumia kwa taabu, mate yakimpalia kooni kutokana na kuzibwa mdomo na ile plasta kubwa. Alilia kwa uchungu na maumivu ya hali ya juu wakati yule jamaa akimng’oa kucha yake ya kidole kile kwa kutumia kile kisu.

    Lilikuwa ni tendo lililohitaji roho mbaya sana kulitekeleza, lakini yule jamaa alikuwa akilitekeleza kama kwamba alikuwa akimpaka rangi ya kucha tu, uso wake ukiwa mtulivu, usioonesha hisia yoyote.

    Lah!

    Mwanamama alilia kwa sauti iliyokuwa ikitoka kwa miguno isiyoeleweka huku mate yakizidi kumpalia, alishuhudia kucha yake iking’olewa huku damu ikimwagika kwa wingi sana. Alifumba macho lakini bado uchungu ulikuwa palepale.

    Jamani si bora nife tu…!

    Maumivu yalikuwa ni makali mno kuvumilika. Wakili Abiah Byabato akapoteza fahamu.



    ____________________



    Alipozinduka wale watu hawakuwepo. Huku akihisi maumivu makali mkononi, alijitahidi kujiinua kutoka pale kitandani na kukaa. Zile kamba alizokuwa amefungwa hazikuwepo na ile plasta aliyobandikwa mdomoni ilikuwa imetolewa. Redio kaseti yake ilikuwa imetupwa sakafuni ikiwa wazi, kaseti iliyokuwa na maelezo ya Jaka haikuwemo.

    Shuka lake pale kitandani lilikuwa limetapakaa damu.

    Wakili Abiah Byabato alijikunyata pale kitandani na kuanza kulia kwa sauti. Alilia kwa muda mrefu sana huku akitetemeka.

    Wale ni watu gani?

    Kwa nini walitaka Jaka aadhibiwe kwa kosa ambalo hakulifanya?

    Iwapo wameweza kumnyofoa ukucha bila hata ya kuonesha kujali hata kidogo, watashindwa kumuua?

    Alijikongoja hadi bafuni ambako alijisafisha na kujifunga kile kidole kilichoathiriwa kwa bandeji iliyokuwa mle ndani mwake, kisha usiku ule ule aliwasha gari na kujipeleka hospitali, machozi yakimbubujika njia nzima.

    Kulipopambazuka na akiwa tayari ameshapata matibabu ya lile jeraha aliloachiwa an wale watu, alimuelekeza katibu muhtasi wake kuandika barua ya kujitoa uwakili wa Jaka kwa sababu za matatizo ya kiafya.





    Pamoja na barua ile, aliambatanisha maelekezo yaliyopata kurasa tatu ambayo yalimpa Jaka kipengele muhimu cha kutumia katika utetezi wake dhidi ya tuhuma zinazomkabili, iwapo kesi yake itafikishwa mahakamani. Alimpa maelezo juu ya kipengele alichokielezea kuwa kinahusiana na Evidence beyond reasonable doubt.

    Ushahidi usio na shaka hata kidogo.

    Ingawa yaliyomkuta usiku uliopita asingeweza kuyasahau kamwe, alijua kuwa yatabaki kuwa siri yake maisha yote.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ___________________



    Mchana wa siku ile barua iliwasilishwa kwa Jaka, na baada ya kuisoma alichanganyikiwa vibaya sana. Kila kitu kilionekana kumong’onyoka mikononi mwake. Ilikuwa ni wazi kuwa alikuwa amekamata njia kuu kuelekea kwenye maangamizo, na hilo lilimuuma sana. Alielewa wazi kuwa swala la wakili Abiah kujitoa kwenye utetezi wake lilikuwa ni matokeo ya njama za akina Tony, hususan wale washirika wake aliomuona nao kule kwenye lile jengo la St. Stanza, kwa lengo la kuhakikisha kuwa anatiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya Joakim.

    Masikini wakili Abiah…sijui naye amekutwa na yepi huko. Mungu amsaidie!

    Alikubali matokeo.

    Siku iliyofuata, alifunguliwa rasmi mashitaka ya mauaji na siku hiyo hiyo akahamishiwa gerezani Segerea.

    Siku tatu baadaye alifikishwa mahakama ya Kisutu kusomewa rasmi shitaka lake. Siku hiyo aliteremshwa kutoka kwenye gari la kubebea mahabisu na washitakiwa kutoka kule gerezani pamoja na washitakiwa wengine, yeye akiwa amefungwa pingu mikononi. Alilishtushwa na umati wa watu waliojaa nje ya mahakama ile. Wapiga picha wa magazeti mbali mbali walianza kumpiga picha bila ya mpangilio naye akalazimika kujiziba uso kwa mikono yake yenye pingu. Wengi wa waliokusanyika pale walikuwa ni wanafunzi wenzake, naye aliweza kuwatambua baadhi yao wakati akipitishwa kuelekea ndani ya jengo la mahakama, ambamo aliwekwa pamoja na mahabusu wengine kwenye chumba maalum kusubiri muda wa kesi yake kuitwa.

    Hatimaye kesi yake iliitwa naye akapandishwa kizimbani na kusomewa shitaka lake. Kutokana na mahakama ile kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuendesha kesi za mauaji, hakutakiwa kujibu lolote kwenye shitaka lile na akafahamishwa kuwa kesi ile itahamishiwa mahakama kuu ambako itapangiwa siku ya kusikilizwa. Kabla ya kurudishwa kwenye kile chumba cha kusubiria kurejeshwa Segerea alipata nafasi ya kutembeza macho yake ndani ya kile chumba cha mahakama kilichofurika. Alimuona rafiki yake Raymond Mloo akiwa ameketi kwenye safu za mbele kabisa ndani ya korti ile. Macho yao yalipokutana, Raymond alitabasamu. Naye alijitahidi kutabasamu kidogo na kiasi alifarijika kwa tendo lile. Mama yake alikuwa nyuma kidogo ya Raymond. Walitazamana kwa huzuni na mama yake kwa muda, na hatimaye Jaka alifanikiwa kumtupia tabasamu hafifu. Yule mama alijibu tabasamu lile kwa tabasamu hafifu zaidi huku akibubujikwa na machozi.

    Pamoja na wanafunzi wengi wengine aliwatambua pale mahakamani, Tony na wale wenzake wawili pia walikuwepo, wakiwa wamevaa nguo nyeusi tupu kwa ishara ya kuomboleza msiba wa “rafiki” yao.

    Wanafiki wakubwa.

    Jaka aliwatazama mmoja baada ya mwingine bila ya kuficha hisia zake dhidi yao. Aligonganisha macho na Tony, wakatazamana kwa chuki huku Jaka akitamani amrukie kutoka pale alipokuwa amesimama, lakini hakuweza kufanya hivyo. Alibaki akimtupia chuki kwa macho yake. Tony akamchanualia tabasamu la kejeli. Jaka alihamisha macho yake uapnde mwingine wa chumba kile cha mahakama.

    Ndipo alipomuona Sajenti John Vata.

    Alikuwa amekaa kwenye kona kabisa ya chumba kile akiwa katika mavazi ya kiraia miongoni mwa raia wengine waliokusanyika ndani ya mahakama ile. Walitazamana, na Jaka akaona huzuni kubwa machoni mwa yule askari ingawa alikuwa kijitahidi kuficha hisia zake. Walizidi kutazamana kwa muda, na Jaka hakujua iwapo alitakiwa atabasamu au akasirike. Alihamisha macho yake kutoka kwa yule askari na ndipo yalipotua kwa Moze. Moyo ulimlipuka na kuanza kumwenda mbio. Alihisi koo likimkauka na machozi yakimchonyota.

    Walitazamana kidogo sana ilitosha kumfanya ajutie kitendo kile kwani katika sekunde zile chache walizotazamana, aliona chuki kubwa machoni mwa Moze. Chuki ile ilikuwa imeelekezwa kwake.

    Iliuma sana. Ilikuwa haivumiliki.

    Aliinamisha macho.

    Hakuyainua tena hadi alipotolewa nje ya mahakama ile…





    ___________________



    Kesi yake iliunguruma mahakama kuu wiki mbili baadaye, na kudumu kwa miezi mitatu. Ilikuwa ni miezi mitatu ya machungu na madhila mazito sana kwake wakati akisota gerezani Segerea huku akizidi kuendelea na kesi. Mama yake na Raymond walishamtembelea mara kadhaa akiwa kule Segerea, pamoja na baadhi ya rafiki zake wachache kutoka kule chuoni. Si Moze, wakili Abiah wala Sajenti Vata aliyeenda kumtembelea kule gerezani katika kipindi kile…



    MATUKIO YALIYOFUATIA HAPA YATAONEKANA KWA UKAMILIFU KWENYE KITABU CHA RIWAYA HII AMBACHO KITATOKA HIVI KARIBUNI. ILA NI KWAMBA KESI ILIUNGURUMA KWA MIEZI MITATU, NA NDANI YA MIEZI MITATU HIYO JAKA ALIJITETEA, AKATETEWA LAKINI PIA AKADIDIMIZWA NA KUSHUTUMIWA VIKALI NA UPANDE WA MASHITAKA. NA PIA ALIJARIBIWA KUUAWA…LAKINI MWISHO WA KESI HUKUMU IKATOKA KUWA AHAMISHIWE DODOMA.



    Ni nini kilijiri hapo kati hadi Jaji akafikia kupitisha hukumu hii?



    Basi hicho utakijua ndani ya kitabu cha riwaya hii ambacho hivi sasa tayari kipo mtamboni.



    (Tunaomba mtuwie radhi, ila hii ni moja ya mbinu zetu katika kuwadhibiti wale wanaoingia humu kwa lengo la kuiba riwaya na kwenda kuziuza kwa bei ya kutupa kwenye page nyingine wazijuazo, kwenye Instagram na/au kwa kuwauzia watu wengine inbox wakitumia email za uongo).



    SASA TUTAENDELEA NA YALE YALIYOJIRI, BAADA YA HUKUMU…



    ___________________



    Gari la magereza aina ya Land Rover lilikuwa likienda kwa mwendo wa kasi sana, kuelekea Dodoma. Sehemu ya nyuma gari lile, Jaka alikuwa ameketi kwa kujiinamia kwenye benchi lilikuwa mle garini, akiwa amefungwa pingu mikononi na miguuni. Pamoja naye kule nyuma safari hii kulikuwa kuna askari wawili wa magereza ambao hakuwa amewatilia maanani tangu anapakiwa ndani ya gari lile. Alijua tu kuwa mmoja wa wale askari alikuwa ameketi pembeni yake, wakati yule mwingine alikuwa ameketi mbele yake. Roho ilimuuma sasa, kwani ingawa aliona kuwa hakimu alijitahidi kutoa hukumu kwa haki kadiri alivyoweza, bado kulikuwa kuna walakini kwa kuwa yeye alikuwa anaadhibiwa kwa kosa ambalo hakulifanya. Mama yake alishukuru kuwa angalau atakuwa hai, lakini kwake lile bado lilikuwa ni tatizo.

    Kwa nini muuaji aachiwe hivi hivi tu?

    Kwa nini madai yake yasifanyiwe uchunguzi na akina Tony wakatiwa mbaroni?

    Alijua sasa hatoweza tena kuendelea na masomo yake na hilo ndilo lililomuuma kuliko vyote.

    Akiwa amejiinamia pale kando ya yule askari, aliweza kuiona bastola fupi na nene ikiwa inaning’inia kwenye mkoba maalum uliopachikwa kiunoni kwa yule askari, na hivyo ile bastola ilikuwa katikati yake na yule askari.

    Alipeleka macho yake kwa yule askari aliyekuwa mbele yake na hapo hapo moyo wake ukamlipuka na akahisi ubaridi ukimtambaa kwa kasi mgongoni. Yule askari alikuwa akimtazama kwa makini hali uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu pana!

    Lile tabasamu na macho ya yule askari havikuwa vigeni kwake.

    Jaka alikumbuka siku ile alipokuwa akichungulia kwenye dirisha ndani ya jengo la St. Stanza Canned Fish Company na kumuona Tony akiwa amekaa kando ya mtu mfupi, mnene, aliyekuwa amevaa tai iliyompendeza sana ambaye alikuwa akitabasamu bila ya sababu maalum.

    ...smiling face...

    Ni yeye! Tabasamu ni lile lile!

    Jaka alibaki akimtazama yule askari aliyekuwa akitabasamu mbele yake na aliyaona tena yale macho. Ni macho yale yale yaliyokuwa yakimchungulia kutoka kwenye vitundu viwili vilivyotobolewa kwenye soksi iliyouficha uso wa mtu yule siku moja tu iliyopita.

    Ah! Huyu ni yule yule muuaji aliyetaka kuniua jana...! Vipi leo yumo ndani ya gari hili akiwa kama askari...?

    Mungu wangu! Jana alinikosa, sasa ndio amekuja kunimaliza kabisa!

    Woga wa ajabu ulimgubika.

    Yaani hawa watu walikuwa wamedhamiria kumuua kiasi hiki? Waliwezaje kupata nafasi ya kuwa naye ndani ya lile gari pamoja naye namna ile? Yule mtu aliendelea tu kumtazama huku mdomo wake ukiwa umeachia tabasamu pana. Yaani alikuwa analiona tabasamu la kifo mbele ya uso wake na hakuwa na la kufanya.

    Alishusha macho yake taratibu na kumgeukia yule askari aliyekuwa pembeni yake na moyo ukamtumbukia nyongo.

    Uso wa yule askari aliyeketi pembeni yake ulikuwa umetapakaa alama nyingi za ndui!

    Oh, Mungu wangu…Klaus Kinski!

    Hapo alielewa kuwa wale jamaa hawakuwa askari wa kweli na kwamba walikuwa naye mle garini kwa lengo moja tu la kumuua.

    Watamuuaje? Na wapi?

    Na hata wakati mawazo haya yakipita kichwani kwake, alimuona yule jamaa mwenye uso wa ndui akitoa sigara na kuanza kuipeleka taratibu mdomoni mwake. Akili ilimcheza, macho yalimtembea. Alizungusha jicho na kuitazama ile bastola iliyokuwa katikati yake na yule askari.

    Ghafla, kabla yule “askari” hajaifikisha kinywani ile sigara yake, alijitia kupiga chafya kwa nguvu huku akiinua mikono yake kujiziba mdomo. Kiwiko cha mkono wake kilimgonga kwa nguvu kidogo yule askari na kumfanya aiangushe ile sigara. Haraka alijitia kuomba samahani kwa woga huku akiinama kutaka kuiokota ile sigara taratribu.

    “Hebu tulia wewe!” Yule mtu mwenye tabasamu pana alimkaripia na kumuamrisdha atulie kama alivyokuwa. Ndilo jambo alilokuwa akilitaka. Alitulia na yule askari aliyekuwa pembeni yake aliinama na kuanza kuiokota ile sigara. Hiyo ndiyo nafasi aliyokuwa akiitarajia.

    Haraka sana Jaka alijigeuza na kuichomoa ile bastola kutoka kiunoni kwa yule askari kabla hajainuka. Don Sibazosi aliliona tendo lile na kutoa tusi kali huku akipeleka mkono wake kiunoni kutoa bastola yake, lakini alichelewa.

    Jaka alikuwa ameikamata ile bastola kwa mikono yake yote miwili na kuikandamiza kwa nguvu kisogoni kwa Puzo Vurumai, yeye akimjua kama Klaus Kinski.

    “No! Nyie nd’o mtulie!” Jaka alifoka kwa kitetemeshi huku akiwa amemkazia macho Don Sibazosi na bastola bado ikiwa kisogoni kwa Puzo ambaye alibaki akiwa ameinama vile vile, mkono wake mmoja ukielea juu ya ile sigara iliyolala pale chini ndani ya gari. Don Sibazosi alibaki akiwa ameduwaa na bastola yake mkononi.

    “Unafanya kosa kubwa kijana...sisi ni askari...na hapa tunaiwakilisha Jamhuri...” Alisema huku akimtazama Jaka machoni kwa makini na mdomo wake bado ukiwa na tabasamu pana.

    “Kimya!” Jaka alimfokea huku akiwa amekunja uso wake kwa ghadhabu, kisha akaendelea kwa kitetemeshi, “Weka chini hiyo bastola yako...taratibu mno!”

    Don Sibazosi alitii huku macho yake yakionesha ghadhabu zisizo kifani na mdomo wake ukiwa una tabasamu pana. Jaka alikiri kuwa yule jamaa alikuwa ni mtu hatari na wa ajabu sana.

    “Sasa…Sasa nataka…unifungue pingu za miguuni...kwa utulivu mno! Nikihisi mtikisiko wowote usiohitajika natawanya ubongo wa huyu mwenzako hapa, sawa?” Jaka alimuamuru tena kwa ukali, safari hii bila kitetemeshi.

    Bila ya kujibu kitu, Don Sibazosi alitoa funguo kutoka kwenye mfuko wake wa shati na kuanza kumfungua zile pingu taratibu mno. Alipomaliza alibaki akimtazama kwa hasira kubwa huku bado mdomo wake ukiwa una tabasamu pana. Jaka alimwamuru arudi mahala alipokuwa amekaa hapo mwanzo na aziache zile funguo pale chini. Yule muuaji alitii.

    Gari liliendelea kwenda tu.

    Taratibu Jaka aliitembeza ile bastola mwilini kwa Puzo Vurumai na kuikandamiza ubavuni kwa yule jamaa.

    “Sasa wewe nataka uokote hizo funguo hapo chini na unifungue pingu za mikononi...ukitetereka kidogo tu, nakushindilia marisasi!” Alimwambia huku bado macho yake yakiwa yamemuelekea Don Sibazosi.

    Puzo Vurumai alitekeleza amri ile huku akitetemeka kama bwege. Baada ya kumaliza Jaka alimwamuru naye aende kukaa kule alipokuwa yule mwenzake.

    Sasa wakawa wanatazamana, Jaka kwenye benchi la upande mmoja wale wauaji la uoande mwingine, huku safari ikiendelea.

    “Nyie sio askari wala nini...ni wauaji tu nyie!” Aliwaambia. Jamaa walibaki wakimtazama tu. Alimnyooshea Don Sibazosi ile bastola.

    Don Sibazosi alibaki akimtazama kwa macho ya ghadhabu huku kinywa chake bado kikiwa kimechanua kwa tabasamu pana. Jaka alikuwa akifikiri haraka haraka afanye nini baada ya kufikia hatua ile. Alikuwa akiuliza yale maswali kwa kupitisha muda wakati akifikiri. Alitupa jicho kwenye dirisha dogo lililozibwa kwa wavu na nondo, na kuona kuwa walikuwa wameshafika maeneo ya Manzese. Alijua kuwa Manzese kulikuwa kuna msongamano mkubwa wa watu, hivyo kama alitaka kufanya kitu ni vyema afanye akiwa katika eneo lile.

    Huku akiwa amewaelekezea wale watu ile bastola kwa mkono wake wa kulia, aliokota mkoba wake uliokuwa chini ya miguu yake na kuupachika begani.

    “Hutafika popote kijana...” Don Sibazosi alimwambia.

    “Kimya!” Jaka alimkemea, na hapo hapo aligeuka na kuipiga risasi loki ya mlango wa nyuma wa gari ile, bastola ikitoa mlipuko mkubwa mle ndani, lakini aliikosa. Akapiga risasi nyingine na loki ikisambaratika vibaya, mlango ukafunguka na kujibamiza tena kwa nguvu.

    Don Sibazosi na Puzo Vurumai walikurupuka kutaka kuiwahi ile bastola iliyokuwa pale chini, lakini Jaka aliwageukia na kuwanyooshea ile bastola iliyokuwa mkononi mwake.

    “We! Weeee! Tulia kama mlivyo, pumbavu!”

    Jamaa walisita, na hapo gari lilianza kupunguza mwendo likielekea kusimama baada ya dereva kusikia ile milipuko ya bastola kutokea kule nyuma. Bila ya kufikiri zaidi Jaka alimtupia Puzo ile bastola kwa nguvu. Puzo aliikwepa na wakati huo huo Don Sibazosi alijirusha chini kuiwahi ile bastola nyingine wakati Jaka akijitupa nje ya gari lile na kudondokea barabarani. Gari lililokuwa nyuma ya ile Land Rover lilifunga breki ghafla baada ya dereva wake kuona mtu akidondoka barabarani kutokea kwenye gari lililokuwa mbele yake, na wakati huo huo Jaka alijibiringisha pembeni huku akisikia mayowe ya watu na honi za gari zikiambatana na misuguano ya matairi kwenye lami na baadaye kishindo kikubwa. Lile gari lililomkosa liliigonga kwa nyuma ile Land Rover ya Magereza.

    Tafrani!

    Jaka aliinuka kutoka kando ya barabara na kutupa jicho kule yale magari yaliyogongana na kuona watu wengi wakikimbia kuelekea kule. Alimuona Puzo Vurumai akiwa ameinua juu bastola yake akijaribu kupenya kwenye ule msongamano wa watu kumfuata kule alipokuwapo. Aligeuka na kuanza kutembea kwa mwendo wa haraka kuondoka katika eneo lile, akipishana na watu waliokuwa wakikimbia kuelekea kule ilipotokea ajali.

    “Simama! Mkamate huyo…mfungwa anatorokaaa!” Amlisikia Don Sibazosi ikipaaza sauti nyuma yake. Aliongeza kasi huku akigeuka na kuwaona wale wauaji wawili wakikimbilia, bastola zao zikiwa zimeinuliwa juu ya vichwa vyao na vya watu wengi waliokuwa wamesongamana katika eneo lile, kelele za kishabiki na honi za magari zikirindima kutokana na msongamano uliotokana na ajali ile.

    Alianza kukimbia kurudi kule lile gari lao lilipokuwa limetokea.

    Don Sibazosi na Puzo Vurumai, wakiwa katika mavazi ya kiaskari wa magereza, bastola mikononi, walimkimbiza huku wakipamiana na watu waliokuwa wamezagaa eneo lile.

    Jaka aliongeza mbio.

    “Simama we! Kamata huyooo!”

    Jaka alizidi kutimua mbio kwa kasi zaidi.

    “Kamata huyooo! Mwiziii!”

    Oh, Mungu wangu!

    Jaka aliongeza kasi.

    Wapita njia na wachuuzi wa bidhaa mbali mbali waliozagaa eneo lile walianza kumtafuta mwizi, huku wengine wakijiunga kupiga kelele za “mwizi...mwizi...” bila hata ya kujua ni nani hasa anayekimbizwa. Jaka aliendelea kutimua mbio, akilini akijua kuwa tayari alikuwa mdomoni kabisa mwa mauti, kwani kuitiwa mwizi katika eneo la Manzese ni kifo cha wazi wazi. Mbele yake aliliona daraja la Manzese naye alitimua mbio kulielekea.

    “Jakkaaa! Simamaaaa! Tutakupiga risasi!” Don Sibazosi alimpigia kelele huku akimkimbiza, na Jaka akazidisha kasi. Puzo Vurumai alisimama na kutanua miguu yake huku akichukua shabaha kumlenga Jaka kwa bastola aliyoishika kwa mikono yake yote miwili. Watu wengi waliokuwa wakikimbia hovyo katika eneo lile huku wakipiga kelele za “Mwizi…! Mwizi…!” walimkinga asiweze kupata shabaha vizuri. Alisonya kwa sauti na kuteremsha mikono yake. Alitazama uelekeo aliokuwa akichukua Jaka, kisha akatimua mbio huku akiikata ile barabara kuelekea upande wa pili.

    “Toka njianiii! Polisi..!” Alibwata huku akikimbilia upande wa pili wa ile barabara akiwa ameinua bastola yake hewani.

    Kule alipokuwa Jaka alibakiza hatua chache tu kulifikia lile daraja, na hapo alitokea mtu mmoja mbele yake aliyetaka kumdaka huku akipiga kelele za mwizi. Jaka alimpiga kibega na kumuacha akisambaratika barabarani naye akaendelea kutimua mbio. Yaani sasa alikuwa kama jogoo anayekimbizwa ili achinjwe...kukamatwa kwake kulimaanisha kifo.

    Hatua kadhaa mbele yake jamaa mwingine alijitokeza akimwendea kasi huku akiwa ameinua fimbo kubwa tayari kumtandika. Bila kufikiri Jaka aliruka juu na kumshidilia soli ya kiatu chake kifua, na yule mtu akatupwa nyuma huku akitoa yowe na ile fimbo ikimtoka. Lile pigo lilimpoteza uelekeo Jaka na alipepesuka vibaya, akisota kwa mikono huku miguu yake ikiendelea kujisukuma mbele ili aendelee kukimbia kisha akafanikiwa kisimama tena wima na kuendelea kutimua mabio.

    Aliziparamia kwa pupa ngazi za lile daraja huku Don Sibazosi akiwa mbali nyuma yake. Juu ya daraja lile alitimua mbio kuelekea upande mwingine wa barabara huku akipishana na watu kadhaa waliokuwa wakipita juu ya daraja lile. Don Sibazosi alifika juu ya daraja na kumuona Jaka akikimbia kuelekea upande wa pili wa barabara. Aliinua bastola yake na kupiga risasi mbili hewani.

    “Wote lala chiniii!” Alipiga kelele kuwambia watu waliokuwa wakipita pale darajani baada ya kuachia ile milipuko miwili iliyozua taharuki isiyosemekana pale juu ya daraja.

    Mara ile ile watu wote waliokuwa wakitembea juu ya daraja lile walijitupa chini huku wakipiga kelele kwa woga. Mlio wa risasi si jambo la kawaida kwa wakaazi wa jiji la Dar, na hakuna aliyetaka kuwa wa kwanza kupigwa risasi.

    Jaka alisimama ghafla aliposikia ile milio ya risasi, na wakati huo huo aliona watu wote wakilala chini huku wakipiga kelele za woga. Aligeuka nyuma haraka, na kumuona Don Sibazosi akimsogelea taratibu huku akiwa amemnyooshea bastola, akitweta kwa nguvu na jasho likimtiririka hali macho yake yakiwa yamemwiva kwa hasira na mdomo wake ukiwa umepambwa na tabasamu lake pana, pua zikimtanuka na kumsinyaa kila alipopumua.

    Jaka naye hakuwa katika hali tofauti sana na ile ya Don Sibazosi, kwani alikuwa amelowa jasho huku akihema kwa taabu kutokana na kutimua mbio. Alimtazama Don Sibazosi na akajua kuwa mwisho wake ulikuwa umewadia. Aligeuka nyuma na kutazama kule alipokuwa akijaribu kukimbilia hapo awali.

    Kutokea upande ule, alimuona Puzo Vurumai akimsogelea huku akiwa amemnyooshea bastola kwa mikono yake yote miwili, naye alikuwa ametota jasho huku akihema kwa nguvu.

    Dah!

    Alichanganyikiwa.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Taratibu aliinua mikono yake juu na kumgeukia Don Sibazosi huku akitamani kulia na kupiga kelele.

    “Utafanyaje sasa Jaka?” Don Sibazosi alimfokea huku akimsogelea,“ Unataka kukimbia? Kimbia tu...kimbia!”

    Jaka alibaki akiwa amesimama huku mikono yake ikiwa juu. Kando yake alisikia vilio vya akina mama na watoto waliokuwa wamelala chini pale darajani. Aliangalia kulia kwake chini

    ya lile daraja. Magari yalikuwa yakipita chini ya daraja lile. Hakuwa na njia yoyote ya kujiokoa kutoka katika mtego ule. Alikuwa amenasa.

    Alitazama kushoto kwake.

    Kingo za daraja lile zilikuwa karibu sana naye kwa upande wake wa kushoto kuliko kulia. Aligeuka tena kulia. Kutokea upande wa magari yatokeayo Ubungo aliliona lori kubwa la mchanga likija taratibu mno huku likipiga kelele nyingi. Lile Lori lilikuwa wazi nyuma na kutoka pale alipokuwa amesimama, Jaka aliweza kuona jinsi mchanga ulivyokuwa umejirundika kule nyuma. Lile Lori lilikuwa likikaribia kupita chini ya daraja.

    “Nyie sio askari! Ni wauaji tu nyie!” Jaka alimpigia kelele Don, na yule muuaji aliachia cheko ya kebehi.

    “Piga magoti hapo chini mafungwa! Mbinu yako ya kutaka kutoroka imegonga mwamba!” Don alimkoromea kwa sauti ili watu wote pale wamsikie.

    Haraka haraka Jaka alipima umbali uliokuwepo kabla lile lori halijapita chini ya lile daraja, moyo ukimwenda mbio, na mabango makubwa ya matangazo pale juu ya daraja yakimkinga asione vizuri.

    “Mnataka kuniua!” Alibwata kumjibu Don, huku taratibu akianza kutembea kuelekea kule alipokuwa Puzo, akiwa ameinua mikono yake juu. Don Sibazosi nae aliendelea kumsogelea huku akimtazama kwa makini, bado akiwa amemlengeshea bastola. Kutokea pale aliposogea, Jaka aliweza kuona vizuri zaidi kule chini barabarani. Lile Lori sasa lilikuwa chini ya daraja, na kwa kadiri alivyopimia, lilikuwa moja kwa moja chini ya pale alipokuwa amesimama. Alisimama akimtazama Don Sibazosi huku akijitahidi kutomfikiria Puzo Vurumai aliyekuwa nyuma yake.

    “Sasa huna ujanja mfungwa...utakwenda na sisi kwa upole au kwa mabavu? Uamuzi ni wako!” Don Sibazosi alimwambia huku akimuashiria kwa ile bastola kuwa akae chini. Wala Jaka hakumtilia maanani. Akili yake ilikuwa ikifanya kazi kwa kasi sana, moyo wake ukimuenda mbio kwa kasi zaidi. Alijua ni jambo gani alikuwa anataka kulifanya na alihisi miguu ikimwishia nguvu, naye akajitahidi kutoitilia maanani hali hiyo.

    Aligeuka kidogo kushoto kwake, na kutokea pale juu alikiona kichwa cha lile Lori kikitokeza upande wa pili wa daraja kule chini, barabarani.

    Mungu nisaidie!

    Ghafla alishusha mikono yake, akapiga hatua moja kushoto na kukamata kingo za daraja lile kwa mikono yake na kujirusha juu, akiitupa miguu yake juu ya kingo za lile daraja huku akiiachia mikono yake.

    Alielea hewani kudondokea upande wa pili wa lile daraja, ambako, kiasi cha futi zisizopungua kumi na tano kwenda chini, ililala ile barabara ya Morogoro na magari mengi yakipita juu yake.

    E bwana we!

    Kilikuwa ni kitendo cha haraka na cha hatari sana, kilichohitaji udiriki kwa hali ya juu.

    Don Sibazosi hakuamini macho yake wakati akimshudia yule kijana akijirusha kutoka juu ya lile daraja, na tusi kubwa kwa mshangao lilimtoka huku akimtupia risasi.

    Alichelewa kwa sekunde tu na risasi yake ikaambulia patupu.

    Puzo Vurumai naye aliliona tendo lile lisilotarajiwa, na aliachia ukelele wa kutoamini huku hapo hapo naye akimtupia Jaka risasi mbili za haraka haraka, lakini naye pia alichelewa. Risasi zake zilipita sehemu ile wakati Jaka akiwa tayari ameshapotelea upande wa pili wa ukingo wa daraja lile.

    Jaka alipiga kelele huku akidondoka kutoka juu ya daraja lile, akisikia milio ya bastola na mayowe ya taharuki kutoka kwa watu, na kwa sekunde chache alipata hisia kuwa ule ulikuwa ndio mwisho wake.

    Hesabu zake zilikuwa sahihi.

    Alidondoka kwa kishindo kwenye rundo la mchanga nyuma ya lile lori, vumbi jingi likitimka na kupeperuka hewani, maumivu makali yakimtabaa mwilini kutokea ubavuni alipoangukia pale mchangani, lakini hakujali. Lile lori lilikuwa likiendelea tu na safari yake polepole huku likipiga kelele nyingi. Jaka alijigeuza haraka pale mchangani na kutazama kule darakani.

    Kutoka pale alipokuwa, aliweza kuwaona wale wauaji wawili wakiwa wamesimama nyuma ya kingo za kushoto za daraja la Manzese wakilitazama lile Lori likitokomea taratibu, yeye akiwa ndani yake.

    Na hata alipokuwa akiwatazama wale wauaji wakizidi kuonekana wadogo kadiri lile lori lilivyokuwa likizidi kutokomea, alijua kuwa alikuwa ameshinda pambano tu, lakini sio vita. Wale jamaa wangeendelea kumfuatilia tu.

    Sasa aende wapi…?



    _____________________



    Lile lori liliposimama kwenye taa za kuongozea magari zilizokuwa kwenye makutano ya barabara ile ya Morogoro na ile ya Kawawa, aliruka nje kutoka nyuma ya lile Lori bila ya hata dereva wa gari lile kuelewa kilichokuwa kimeendelea. Alianza kutembea haraka bila ya uelekeo maalum kando ya ile barabara ya Kawawa.

    Kichwa chake kilikuwa kimezingirwa na mawazo huku akijiuliza ilikuwaje hata akapata ujasiri wa kujirusha kutoka pale juu ya daraja namna ile. Mwili ulimsisimka alipojaribu kufikiri matokeo yangekuwaje iwapo angelikosa lile Lori.

    Ingawa mvua ilikuwa ikinyesha kwa nguvu na watu walikuwa wakikimbia huku na huko kujikinga na mvua ile, yeye alikuwa akitembea tu kama kwamba ile mvua haikuwepo au ilikuwa haimhusu. Aliangalia saa yake na kuona kuwa ilikuwa ni saa kumi na moja na nusu za jioni.

    Ilikuwaje hata wale wauaji wakafanikiwa kuingia pamoja naye ndani ya lile gari la magereza bila ya kugundulika kuwa hawakuwa askari wa kweli?

    Au ina maana kuwa jambo hili linahusisha watu wengi katika ngazi za juu kiasi kwamba hakuna namna ya yeye kujikwamua katika balaa hili…? Au ndio maana hata hakimu aliamua kunipa adhabu hii, akijua kuwa hata huko Dodoma sitafika…?

    Mawazo hayo na mengine kama hayo yalikuwa yakipita kichwani mwake wakati akitembea kuifuata ile barabara, sasa akitembea kwa mwendo wa taratibu sana huku akihisi uchovu wa hali ya juu.

    Aliamua kwenda nyumbani kwa mama yake huko msasani bila ya kujali kuwa huenda huko akakutana na balaa likimsubiri, lakini aliona ni lazima aonane na mama yake, kwani alijua kuwa muda mfupi tu ulikuwa umebaki kwa yeye kuendelea kuwa hai.

    Alipoifikia nyumba yao alikuwa amechoka na ametota kwa mvua vibaya sana. Akili yake ilimtuma afungue tu mlango na aingie ndani ajibwage kitandani huku akijua kuwa ataonana tena na mama yake. Wazo la kumuona tena mama yake wakati hakuwa na matarajio ya kumuona tena kwa siku nyingi zijazo nusura limtie tena mikononi mwa polisi, kwani alikuwa akipeleka mkono wake kufungua mlango ule, kisha katika sekunde ya mwisho kabisa alisita. Alinyata kuzungukia ubavuni mwa nyumba ile na kuchungulia sebuleni kwao kupitia dirishani.

    Moyo ulimlipuka kwa mshituko na kihoro, kwani kupitia pale dirishani aliweza kuwaona askari wa jeshi la polisi wawili wakiwa wamekaa kwenye kochi kubwa wakitazamana na mama yake aliyekuwa amekaa kwenye kochi ndogo mbele yao. Askari mwingine alikuwa amesimama kando ya lile kochi alilokalia mama yake. Wale askari walionekana kuwa walikuwa wakimuuliza maswali fulani mama yake, ambaye alikuwa akitikisa kichwa chake kutoafikiana na yale waliyokuwa wakimueleza huku machozi yakimtiririka. Aliwatazama wale askari kwa makini, lakini hakuwa amepata kuwaona kabla na hakuwa na njia yoyote ya kuweza kujua iwapo walikuwa ni askari wa kweli au ni miongoni mwa wale wa bandia wanaotaka kumuua.





    Alijiondoa pale dirishani na kuanza kukimbia kwa kasi kutoka pale nyumbani kwao bila ya kujua ni wapi hasa alikuwa akielekea. Ilimfunukia kuwa hakuwa na mahala pa kukimbilia. Mvua iliongezeka na radi zilikuwa zikipiga kwa nguvu na kutisha. Bila shaka watu waliomuona waliamini kuwa alikuwa akiikimbia ile mvua, ingawa yeye haikumshughulisha hata kidogo. Alikimbia na kukimbia. Hatimae alishindwa kukimbia zaidi. Pumzi zilimwishia na alisimama akitweta, akabaki akiangaza huku na huko. Kiza kilikuwa kimetanda na bado mvua ilikuwa ikipiga kwa nguvu sana. Mbio zake zilimfikisha ufukweni mwa bahari. Bila shaka ilikuwa ni pwani ya msasani, hakuwa na hakika.

    Alijivuta kwa uchovu kukiendea kichaka cha miti iliyokuwa kando ya bahari ile na kujibwaga kama mzigo. Akiwa amejilaza pale mchangani alihisi unyevu uliotokana na maji ya bahari na mvua, lakini kwa uchovu aliokuwa nao hilo lilikuwa ni jambo dogo sana. Usingizi ulimpitia. Hakujua alilala kwa muda gani, ila usingizi ule ulikuwa mzito na mrefu.

    Alipozinduka, mvua ilikuwa ikinyesha kwa rasha rasha tu. Alijiinua kwa taabu na kuanza kutembea kuelekea barabarani. Kibegi chake bado kikiwa kinaning’inia mgongoni, alianza kuelekea tena nyumbani kwa mama yake akiwa na uhakika kabisa kuwa kwa muda ule wale askari watakuwa wameshaondoka. Ulikuwa ni umbali mrefu kidogo, na kabla hajafika kwao, mvua ilianza kunyesha tena kwa nguvu.

    Hakujali.

    Hatua chache kutoka mlango wa mbele wa nyumba yao alishtuka ule mlango ukifunguliwa ghafla na mmoja kati ya wale askari aliowaona sebuleni kwao hapo mwanzo akitoka nje.

    Walionana uso kwa uso.

    “Huyu hapa!” Yule askari alibwaka huku akitoa bastola yake iliyokuwa ikining’inia kiunoni mwake na kumfyatulia risasi.

    Jaka alijitupa chini upesi sana na kujibiringisha pale chini ili kuongeza umbali baina yake na yule askari, ile risasi ikamkosa. Risasi nyingine mbili zilifyatuliwa haraka haraka wakati akijibiiringisha pale chini, nazo zilimkosa na kuchimba ardhi huku zikirusha tope.

    Alijitupa wima kutimua mbio, nyuma yake akisikia vishindo vya wale askari na sauti ya mama yake akipiga kelele kutokea kule nyumbani kwao. Alikata kona kwa kasi na kutokea mtaa mwingine. Wale askari walimkimbiza huku bastola zikiwa wazi mikononi mwao. Akakata kona nyingine kwa kasi na kuibukia mtaa mwingine hali wale askari wakiwa hatua kadhaa nyuma yake. Mlio mwingine wa bastola ulisikika na risasi ikachimba ukuta wa nyumba iliyokuwa kwenye kona aliyopotelea. Aliendelea kutimua mbio kwa kasi zaidi.

    Alipotokeza kwenye ule mtaa wa pili alijikuta akimulikwa na mwanga mkali wa taa za gari. Gari aina ya Toyota lililokuwa katika muundo wa pick-up lilikuwa likipita kwa kasi kwenye ule mtaa aliokuwa ameuingia. Na hata pale taa zile zilipommulika alikuwa ameshafika katikati ya barabara. Dereva alipiga honi kwa nguvu huku akikanyaga breki ghafla. Gari lilisota mbele na Jaka akaturusha mbele kwa nguvu na kuangukia upande wa pili wa ile barabara, akinusurika kugongwa. Sasa lile gari likawa katikati yake na wale askari waliokuwa upande wa pili wa ile barabara.

    Na mara hiyo hiyo risasi nyingine ilivuma na kupasua moja ya taa za mbele za ile gari. Dereva kakanyaga tena mafuta kwa nguvu na lile gari likairuka mbele na kuondoka kwa kasi kutoka eneo lile.

    Kwa mara ya pili katika siku ile Jaka alijikuta akifanya jambo lisilotarajiwa.

    Alikamata upande wa sehemu ya mizigo ya lile gari kwa nguvu na kujaribu kulidandia wakati lilipoondoka kwa kasi kutoka eneo lile. Alirusha mguu wake kuuingiza kwenye ile sehemu ya kubebea mizigo, mguu ukateleza naye akabaki akining’inia ubavuni mwa lile gari kwa mikono yake huku miguu yake ikiburuzwa.

    Wale askari waliona taa za nyuma za lile gari zikitokomea kizani kwa kasi. Waliangaza huku na kule katika eneo ambalo walitarajia Jaka angekuwepo bila mafanikio. Hawaelewa kabisa Jaka aliwatokaje pale na hawakutaka kabisa kuamini kuwa angekuwa amedandia lile gari kutokana na ile kasi iliyokuwa nalo. Kwa kasi iliyoondoka nalo kutoka eneo lile, mtu yeyote mwenye akili timamu asingeweza kudiriki hata kufikiria kulidandia lile gari.

    Dereva wa lile gari alikata kona kwa kasi kuingia mtaa wa tatu kutoka ule zilipotokea risasi, na msukumo wa kasi ya kukata kona ile ulimtupa Jaka hewani na kumbwaga kwa kishindo kando ya barabara na kumgaragaza vibaya kwenye matope na majani. Alijiinua kutoka kando ya barabara na kuanza kukimbia kwa kuchechemea kuelekea kule lile gari lilipokuwa limepotelea. Wakati huu mvua ilikuwa inanyesha kwa nguvu zaidi na mji ulikuwa kimya na kiza kinene kilitawala. Jaka alihisi kuwa umeme ulikuwa umekatika, kama kawaida ya jiji la Dar katika kipindi cha mvua kubwa.

    Aliacha kukimbia na kuanza kuifuata ile barabara iliyompeleka hadi akatokea kwenye barabara ya Old Bagamoyo road. Aliifuata barabara ile hadi kwenye eneo la maduka mengi ya Namanga. Bila ya kujali aliendelea na safari yake ambayo kwa kweli hakujua ingeishia wapi. Alitokea kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Akaivuka na kuingia mitaa ya maeneo ya Block 41. Kwa namna ya ajabu begi lake dogo bado lilikuwa likining’inia mgongoni kwake pamoja na misukosuko yote ile iliyotokea.

    Alikuwa akitembea katika ile mitaa ya Block 41 bila ya uelekeo maalum katika usiku ule wa kiza kizito na mvua kubwa bila ya kujua kuwa mtaa wa pili kutoka pale alipokuwa, kulikuwa kuna msichana mmoja ambaye naye pia alikuwa matatani usiku ule. Msichana aliyekuwa akijitahidi kuwakimbia watu wanne waliokuwa na dhamira mbaya dhidi yake.

    Ni katika usiku huu wa kiza kinene na mvua kubwa ndipo Jaka alipokutana na msichana yule, na pamoja wakajikuta wakikabiliana na wale watu wanne wenye dhamira mbaya.

    Mmoja alikuwa ameshika rungu refu na zito.

    Mwingine alikuwa ameviringisha mnyororo mnene kwenye ngumi yake.

    Wa tatu alikuwa mikono mitupu, lakini mikono yake ilikuwa mikubwa yenye misuli minene.

    Na yule wa nne alikuwa ameshika kisu kilichotoa mng’ao katika kiza kile cha usiku.

    Na huo ndio ukawa mwanzo wa matukio mengine mengi katika maisha yake…



    ______________________



    Saa ya ukutani iliyokuwa ikining’inia kwenye moja ya kuta za pale sebuleni ilionesha kuwa muda ulikuwa ni saa moja na nusu za jioni. Jaka alikuwa amekaa kwenye kochi kubwa la pale sebuleni huku akiwa amejishika tama na uso wake umekunjamana kwa mawazo mazito.

    Alikuwa akitafakari matukio yaliyotokea siku ile.

    Baada ya mlipuko wa lile bomu asubuhi ile pale sokoni, walichukuliwa na gari la polisi hadi kituo cha polisi cha mkoa ambako walimkuta mzee Januari Mwakaja akiwasubiri ofisini kwake. Baada ya kuwauliza juu ya hali zao na wao kumthibitishia kuwa walikuwa salama aliwatupia maswali mengi ambayo hawakuwa na majibu ya moja kwa moja.

    Waliulizwa iwapo kuna mtu yeyote waliyekuwa wakimhisi kuhusika na tukio lile la kuogopesha.

    Hawakuwa na mtu yeyote waliyekuwa wakimhisi kuhusika na tukio lile.

    Januari Mwakaja alisisitiza sana juu ya uwezekano wa kuhusika kwa yule mtu ambaye Jaka na Clara walimjua kama John Doe na tukio lile. Kwa hilo Jaka alisema kuwa ingawa naye alikuwa akihisi hivyo, hakuwa na hakika. Alikumbuka onyo alilopewa na yule mtu mwenye koti refu na kofia pana kuwa pindi akihojiwa na polisi, asiseme lolote kuhusu kuonana kwao.

    Muda wote huo Clara alikuwa ametulia kimya.

    Walitolewa pale kituoni na kupelekwa hospitali ya mkoa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi iwapo walikuwa wamepata madhara yoyote kutokana na mlipuko ule. Uchunguzi ulionesha kuwa hawakuwa na madhara yoyote ya kutisha hivyo wakarudishwa nyumbani.

    Muda mfupi baada ya kufika pale nyumbani, Mzee Wilfred Masahuri Zaza, baba yake Clara, alifika akiwa amejaa wahka mkubwa baada ya kupata taarifa ya mlipuko uliotaka kuondoa maisha ya mwanaye kipenzi na pekee hapa duniani.

    Baba na mwana walikumbatiana kwa upendo na kufarijiana huku wakitokwa na machozi. Jaka waliwatazama wakiwa katika hali ile na moyo ulimuuma sana. Wazo kuwa yeye ndiye chanzo cha mashaka yale kwa baba na mwanye lilimuumiza roho sana.

    Mzee Zaza alimgeukia na kumtazama kwa huzuni.

    “Jaka…unajua kuwa sina chuki yoyote juu yako, lakini sasa ni dhahiri kuwa kuendelea kwako kuwa pamoja na binti yangu ni hatari kubwa kwa maisha yake.” Alimwambia huku akijifuta machozi. Jaka alimtazama tu yule mzee bila ya kumjibu, moyoni mwake akikubaliana naye moja kwa moja. Yule mzee alimgeikua binti yake.

    “Clara mwanangu, nikiwa kama baba yako, kwa usalama wako nakuomba sana uhamie nyumbani kwangu mara moja. Huko utakuwa salama zaidi…lakini hutakuwa tena na huyu …mwenzio…hali halisi imejionesha kuwa si salama kwako.” Alimwambia.

    Clara hakukubaliana kabisa na baba yake. Pamoja na Jaka kuingilia kati na kumsihi akubaliane na ushauri wa baba yake kuwa ndio wa busara zaidi kwake kwa wakati ule, bado Clara alishikilia msimamo wake.

    “Hivi mnataka mimi niwe mtu wa aina gani?” Clara aliuliza kwa hasira baada ya kuona kuwa Jaka na Mzee Zaza wanazidi kumshawishi awe mbali na Jaka japo kwa muda tu mpaka hali itakapokuwa shwari.

    Wote wawili walibaki wakimtazama.

    “Tumekaa na Jaka kwa heshima na furaha kwa siku zote hizi, muda wote tukijua kuwa Jaka alikuwa anakabiliwa na tuhuma nzito…kabla ya hapo yeye alijitolea maisha yake kunisaidia wakati nilipokuwa nakiona kifo waziwazi machoni mwangu, sasa leo hii yeye afikwe na tatizo mimi niondoke niende kwa baba, naye nimwache peke yake? Hapana jamani. Siwezi kabisa kufanya kitu kama hicho!”

    “Lakini mimi niko radhi Clara…ni bora iwe hivi!” Jaka alidakia.

    “Na mimi pia nina maamuzi na maisha yangu Jaka, na uamuzi wangu kwenye hili ndio huo!” Clara alimjia juu, na akaondoka kwa hasira akiwaacha pale sebuleni.

    “Clara!” Jaka na Mzee Zaza waliita kwa pamoja, lakini Clara alipitiliza na kujifungia chumbani kwake. Jaka na Mzee Zaza walitazamana, kisha wakainamisha nyuso zao. Baada ya muda mfupi Jaka aliinua uso wake na kumtazama yule mzee.

    “Nimekuelewa sana mzee na wala sikulaumu kwa uamuzi wako…mimi nitaondoka leo hii hii hapa nyumbani, lakini naomba sana uendelee kumshawishi Clara ahamie kule kwako kwa usalama zaidi. Wema ambao wewe na yeye mmenifanyia ni mkubwa sana na mimi sina haki kabisa ya kutaka chochote zaidi kutoka kwenu…” Alimwambia.





    “Hapana Jaka…” Mzee Zaza alimjibu, “…mimi namjua sana mwanangu. Akiamua jambo huwa haamui kipumbavu, huwa amelifikiria…na akishaamua, ni vigumu sana kumshawishi vinginevyo...ni tabia aliyoirithi kutoka kwa mama yake…marehemu mke wangu.” Alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu. Jaka alitaka kusema kitu lakini mzee Zaza akamuashiria anyamaze.

    “Mama yake Clara alijua kuwa iwapo atapata ujauzito na kujifungua, basi maisha yake yangekuwa hatarini na angeweza kupoteza maisha kutokana na afya yake kuwa dhaifu. Lakini alipopata ujauzito alikataa katakata ushauri wa daktari kuwa ile mimba itolewe ili aokoe maisha yake…kwa sababu alikuwa anataka sana kupata mtoto. Na kweli…baada ya kuzaliwa Clara mke wangu mpenzi akaaga dunia…na tangu siku hiyo Clara amekuwa ndiye amekuwa familia yangu…” Aliongea yule mzee kwa huzuni, na Jaka alibaki akimtazama yule mzee tajiri bila ya kujua aseme nini.

    “Wacha nikaongee naye tena.” Yule mzee alisema huku akielekea chumbani kwa Clara.

    Nusu saa baadaye, mzee Wilfred Mashauri Zaza alirejea pale sebuleni na kusimama kwa muda mrefu kabla ya kuanza kuongea.

    “Najua kuwa binti yangu anakupenda sana Jaka, lakini sijui kama amefanya uamuzi wa busara au wa kipuuzi kwa kukupenda. Ninachojua ni kuwa hivyo ndivyo mapenzi yalivyo. Wakati mimi naanza mapenzi na marehemu mama yake, sikuwa tofauti sana na wewe…kwamba Joanna, mama yake Clara alikuwa tajiri sana wakati mimi nilikuwa mfanyabiashara wa kawaida tu, sikuwa na ndugu wala jamaa na sikuwa tajiri kama yeye. Lakini Joanna hakufanya jambo la kipuuzi alipoamua kupendana nami…mimi sikuwa na nia mbaya juu yake.”

    Jaka alitulia kimya akimsikiliza.

    “Nadhani usalama wa mwanangu unategemea sana na nia yako kwake, Jaka. Kwa sababu yule ni msichana tu aliyetokea kukupenda, I can understand that …sasa wewe ukija kumfanya yeye bwege kwa hilo sitakuelewa kabisa. Usije ukamfanya ajutie uamuzi wake Jaka. Kwa sababu ukimfikisha katika hatua hiyo hutakuwa umemuumiza yeye tu bali na mimi vilevile…”

    Jaka aliendelea kumsikiliza kwa makini huku yale maneno yakimwingia vizuri mno.

    “Clara ameamua kuendelea kukaa na wewe hapa hapa…hivyo ndivyo mwanangu anavyokupenda Jaka. Yuko tayari kuhatarisha maisha yake kwa ajili yako…sio jambo la mchezo hata kidogo hilo. Mimi nimemkubalia kwa sharti kwamba nitaweka askari wa kuhakikisha usalama hapa nyumbani saa ishirini na nne…na kila atakapokwenda, atasindikizwa na askari. Namna hiyo nadhani kidogo kutakuwa kuna amani japo kidogo, moyoni mwangu.”

    “Nashukuru mzee…na sitamfanya ajute hata kidogo.” Jaka alisema, na yule mzee alimtikisia kichwa tu kuafikiana naye, kisha akaiendea simu na kuanza kufanya taratibu za ulinzi kwa kuwasiliana na mkuu wa polisi wa mkoa. Baada ya kufanya hivyo walikaa kimya pale sebuleni hadi dakika ishirini baadaye wakati askari wawili waliporipoti kuanza kazi ya kulinda usalama wa nyumba ya Clara pale Uhindini. Hapo Mzee Zaza alienda chumbani kuagana na mwanaye, kisha akarudi pale sebuleni na kuagana na Jaka.

    “Zingatia maneno niliyokueleza kuhusu binti yangu kijana.” Mzee alimwambia.

    “Bila shaka mzee…” Jaka alijibu.

    Yule mzee akaondoka, akimuacha akiwa amekaa peke yake pale sebuleni.



    _____________________



    Sasa Jaka aliinuka kutoka pale kwenye kochi na kuchungulia dirishani. Askari mmoja alikuwa amesimama mbele ya nyumba ile. Bastola moja ilikuwa imening’inizwa kiunoni kwake na radio ya mawasiliano ya kipolisi ilionekana kuchungulia kutoka kwenye mfuko wa shati lake. Begani alikuwa amening’iniza bunduki aina ya SMG. Alienda kuchungulia dirisha la nyuma. Nako kulikuwa na hali kama ile ya kule mbele. Alirudi sebuleni na kurudia kujiinamia pale kwenye kochi, bado mawazo mazito yalikitawala kichwa chake.

    Ina maana hawa jamaa wamenifuata mpaka huku Dodoma? Kule Dar wamenikosakosa mara mbili bloody fools…kule njia ya Segerea na pale darajani Manzese…sasa hii hali itakuwa hivi mpaka lini?

    Alisonya.

    Mwishowe wataniua kweli hawa, yaani walikuwa tayari hata kumuua na Clara ambaye hana makosa yoyote? Aaah mi’ naona sasa wakati wa wao kulipa kwa matendo yao umefika…na watajuta! Hivi lini John Doe atatokea? Nina hakika jamaa atakuwa na msaada fulani kwangu, kinyume na nilivyomdhania hapo mwanzo.

    Muda huo Clara aliingia pale sebuleni kutokea chumbani kwake na kwenda kuketi naye kimya pale kochini. Jaka alimtazama na kukumbuka maneno ya mzee Wilfred Mashauri Zaza. Moyo wake wote ukamuendea yule binti na alijihisi kumpenda zaidi na zaid. Kitendo cha kuamua kuendelea kuwa naye hata katika kipindi kile kigumu na cha hatari kabisa kilimtia moyo sana Jaka. Alikumbuka jinsi Moze, mpenzi wake wa awali na aliyewahi kumpenda kwa moyo wake wote, alivyomkana na kumuacha katika kipindi ambacho ndio alikuwa akimhitaji sana kutokana na matatizo makubwa aliyokuwamo wakati huo…matatizo yaliyomkuta kutokana na kulitetea penzi lao wenyewe.

    Sasa leo huyu binti aliyekaa pembeni yake amekuwa radhi kujitolea maisha yake kuliko kumuacha peke yake katika dimbwi la madhila yale yasiyosemeka…

    Alibaki akimtazama tu yule binti kwa upendo uliojaa shukurani.

    Clara alimgeukia na wakatazamana. Macho yao yaliongea na kuelewana vizuri sana. Walikumbatiana kwa upendo, na kubaki wakiwa wamekumbatiana pale kwenye kochi kwa muda mrefu.

    “Asante sana Clara.” Hatimaye Jaka aliongea.

    “Kwa nini…?”

    “Kwa kutoniacha peke yangu katika matatizo haya…”

    Clara aliinua kichwa chake na kumtazama usoni.

    “Kwani kama ungekuwa wewe ungeniacha?”

    “Hapana…hata kidogo.”

    “Sasa kwa nini unadhani mi’ ningeweza hata kufikiria kukuacha?” Clara alimuuliza, na kuendelea, “Matatizo hayana mwenyewe Jaka, yanaweza kumpata mtu yeyote…na umuhimu wa rafiki…wa mpenzi…unaonekana zaidi pale ambapo mtu uko kwenye matatizo. Mi’ n’takuwa mpenzi wa aina gani kama nitakuacha mpenzi wangu katika kipindi kama hiki Jaka? Halafu matatizo yakiisha nitafanyaje..nitarudi tena kukwambia ‘haya mpenzi sasa tuanze kupendana tena’? Haiwezekani.”

    Jaka aliafikiana naye kutikisa kichwa taratibu, akilini akijiuliza ilikuwaje hata Moze akashindwa kuelewa jambo kama lile. Waliendelea kukaa kimya huku wakiwa wamekumbatiana kwa muda mrefu zaidi.

    “Ni mambo gani yaliyokutokea huko nyuma hata ukalazimika kuja kizuizini huku Dodoma, Jaka?” Hatimaye Clara alimuuliza.

    “Mengi sana Clara…”

    “Naomba leo unielezee juu ya mambo hayo mpenzi…ni nini kilitokea mpaka tukakutana siku ile ya mvua kubwa na kiza kizito kule Dar es Salaam, na pia ilikuwaje hata tukaja kukutana tena hapa Dodoma…na mara zote hizo tumekuwa tukikutana katika mazingira ya kutatanisha. Ni wazi kuwa tukio la leo linatokana na mambo yaliyokutokea huko nyuma…”

    Jaka alitulia kimya kwa muda kabla ya kumjibu.

    “Clara, mi’ naona ni salama zaidi kwako kutoyajua mambo yaliyotokea huko nyuma kuliko kuyajua…”

    Clara alijiinua taratibu kutoka kifuani kwake na kuketi huku akimtazama usoni.

    “Jaka, tangu tuanze kujuana kwa ukaribu, sijawahi hata siku moja kukuuliza kuhusu maisha yako ya huko nyuma, hasa kuhusiana na mambo yanayohusiana na matatizo haya uliyonayo. Ni kwa sababu nilijua kuwa yaliyotokea huko nyuma hayakunihusu, nami nikaamua kujihusisha na maisha yako niliyokukuta nayo na kuendelea mbele huku nikiamini kabisa kuwa wewe hukufanya hilo kosa linalosemekana kuwa umelifanya hadi ukapewa adhabu ya kufukuzwa jiji la Dar…”

    “Clara…”

    “Subiri nimalize…mi’ nilishawahi kukueleza kuwa huwezi kuukimbia ukweli Jaka, kwani kuukimbia ukweli ni sawa na kujikimbia mwenyewe. Sasa ukweli umeshadhihirika mpenzi wangu…nao ni kuwa kuazia sasa hauko peke yako kwenye jambo hili…tuko pamoja. Mimi na wewe. Na kama tuko pamoja, basi sasa na mimi nastahili kabisa kuelewa juu ya jambo ambalo saa kadhaa tu zilizopita lingesababisha wewe na mimi tuwe marehemu, kwa sababu lile bomu lisingechagua Jaka..tungekufa sote!”

    Duh!

    “Dah! Ni kweli Clara, lakini…”

    “Lakini nini Jaka? We’ kama unaona kuwa hayo matatizo ni yako peke yako basi hali hiyo ilibadilishwa na ule mlipuko wa bomu asubuhi ya leo. Ule mlipuko umenipa haki ya kujua kila kitu kuhusu yaliyokutokea kule Dar, Jaka. Sasa matatizo haya ni yetu sote, na tunatakiwa tushirikiane katika kukabiliana nayo…na njia nzuri ya kufanya hivyo ni kuanza kueleweshana hali halisi ilivyokuwa tangu mwanzo hadi hapa tulipo…halafu tuone tutaenda vipi huko mbele katika kukabiliana na hali hii.” Clara alimwambia kwa msisitizo.

    Jaka hakuwa na hoja tena.

    Akamueleza kisa chote cha maisha yake tangu mwanzo. Alimueleza kuhusu Moze, Joakim Mwaga na wenzake na mambo yote yaliyotokea hadi kuuawa kwa Joakim na yeye kutuhumiwa na hatimaye kuhukumiwa kwa mauaji yale. Alimalizia kwa kuelezea matukio yaliyotokea siku ile ambayo usiku wake ndio walikuja kukutana kwa mara ya kwanza kule Dar katika usiku ule wa mvua kubwa na kiza kinene…



    _____________________



    Clara alibaki mdomo wazi huku akimkodolea macho kwa huruma na mshangao.

    “Aisee! Pole sana…dear…yaani, Ah! Hayo mambo huwa nayaona kwenye sinema tu, sikutegemea kabisa kuwa yanaweza kumtokea mtu kikweli kweli, na mtu mwenyewe awe ndiyo wewe…!”

    “Yametokea dear…na yamenitokea mimi…nadhani sasa unaelewa ni kwa nini hao watu wataka kuniua.”

    “Naelewa sasa…naelewa kabisa!”

    Jaka alishusha pumzi ndefu na kutazama pembeni. Walibaki kimya kwa muda, kisha Clara aliuliza, “Kwa hiyo mtu aliyemuua Joakim hajajulikana mpaka sasa…?”

    “Sijui kwa kweli…kwa sababu mtu pekee ambaye ningeweza kumhisi ni Tony, lakini Tony na Joakim walikuwa marafiki…” Jaka alijibu kwa mashaka.

    Bado Clara alionekana kulitafakari kwa makini lile swala.

    “Sasa…na zile glovu zilifikaje chumbani kwako…yaani inawezekanaje mtu aingie chumbani kwako na kupandikiza kitu kama kile bila ya wewe kujua?” Clara aliuliza kwa wasiwasi.

    “Mmnh, Clara…! Hapo ndipo panaponishinda…kwa vyovyote vile yeyote aliyeingia na kupandikiza zile glovu chumbani kwangu siku ile, alifanya hivyo katika muda ule ambao mimi nilikuwa kule juu ya jengo nilipomkuta Joakim akiwa tayari ameuawa.” Jaka alijibu huku uso wake akiwa ameukunja kwa kutafakari.

    “Kwani ulipotoka hukufunga mlango?”

    “Mnh! Sikumbuki sawa sawa…”

    “Mnh, Jaka! hebu rudia tena kunielezea kuanzia pale ulipoanza kujirekodi…” Clara alimwambia huku akijiweka vizuri pale kwenye kochi, uso wake ukionesha bashasha ya hali ya juu. Jaka alimtazama kwa mshangao kwani hakuelewa ingesaidia nini au Clara alikuwa na mawazo gani. Hata hivyo, alifanya kama alivyoombwa na kurudia kumuelezea ile sehemu.

    Alipomaliza, Clara alibaki akiwa amekunja uso kwa mawazo huku akiangalia upande ule aliokuwapo Jaka ingawa Jaka aliona kabisa kuwa alikuwa hamuoni. Akili yake ilikuwa inafanya kazi kupita uwezo wake, na Jaka alizidi kushangaa ni nini kilikuwa kinapita kichwani mwa yule binti wakati ule.





    “Jaka, ulipotoka kwenda kule juu ya jengo siku ile, ulitoka na ile simu yako uliyokuwa ukiitumia kujirekodi?” Clara alimuuliza baada ya kufikiri kwa muda mrefu. Jaka alimtazama Clara kwa mshangao huku akionesha wazi kuwa hakuona umuhimu wa swali lile.

    “No, sikutoka nayo…niliiacha…” Alimjibu kw auhakika kabisa.

    “Una hakika…?” Clara alizidi kumuuliza.

    Bila ya kuelewa Clara alikuwa ana nia gani, Jaka alimjibu tena kuwa ana hakika kabisa na hilo.

    “Mnh…haya…na sasa hili ninalokuuliza ni la msingi sana…uliizima ile sehemu ya kurekodia pale kwenye simu yako kabla hujatoka?” Clara alimuuliza tena, na Jaka akakunja uso.

    “Aaa sasa ilikuwa ni muda mrefu sana Clara…sikumbuki iwapo…”

    “Kumbuka Jaka…hebu fikiria kwa makini na urudishe kumbukumbu zako hadi siku ile ulipokuwa ukijirekodi…ulizima ile sehemu ya kurekodia ulipotoka…?” Clara alizidi kumhimiza, uso wake ukionesha umakini uliomfanya Jaka pia amakinike. Bila ya kuelewa Clara alikuwa anaelekea wapi na swali lile, alikunja uso na kufumba macho akijitahidi kukumbuka. Alikaa katika hali ile kwa muda mrefu huku Clara akimtazama kwa makini. Kichwani mwake, matukio ya siku ile ambayo alishajipiga marufuku kabisa kuyafikiria au kuyakumbuka, yalijirudia haraka haraka kichwani mwake, bila ya mpangilio maalum.

    Na mara ikamjia.

    Ilitokea tu kama kama kitu kilichoshushwa na mwenyezi Mungu kutoka mbinguni na kumuingia kichwani mwake.

    Ghafla alifumbua macho huku akimgeukia Clara taratibu, akimtazama kwa mshangao na kutoamini.

    “Umekumbuka!” Clara alimwambia kwa bashasha.

    “Sikuizima ile simu, Clara!” Jaka alimwambia kwa sauti ya kunong’ona huku naye macho yake yakionesha bashasha kubwa.

    Clara aliinuka kutoka kwenye kochi na kusimama mbele yake.

    “Una hakika Jaka?”

    “Ndio, aisee…ndio! Nina hakika kabisa sikuizima, Clara!”

    “Oh, My God!” Clara alisema huku akimtazama kwa hamasa kubwa kabisa.

    Siku zote amekuwa akitawaliwa na hisia kuwa kuna kitu fulani ambacho kingeweza kumpatia ufumbuzi wa kitendawili kikubwa kilichoizunguka ile kesi aliyoangushiwa na ambayo imemchafulia jina lake kwa kiasi kikubwa sana. Alikuwa akijua kabisa kuwa kuna kitu fulani lakini hakuweza kukigundua mara moja ni kitu gani…ni kitu kilichokuwa nyuma kabisa ya ubongo wake ambacho siku zote kilikuwapo, lakini hakuweza kukivuta kutoka nyuma ya ubongo wake na kukiona wazi katika fahamu zake.

    Mpaka leo.

    Leo kitu kile kimemjia wazi wazi akilini mwake. Fahamu ile ilimjia kama muujiza kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hapo Jaka alikubali kabisa kuwa kumbe kweli Mungu yupo.

    “Jaka! Unaelewa ni nini inamaanisha hiyo…?” Clara alimuuliza huku akiketi tena pale kochini kando yake.

    Jaka alitikisa kichwa kwa mastaajabu.

    “Kwa hakika kwanza nilikuwa sielewi kwa nini ulikazania kuulizia iwapo niliizima ile simu au la…lakini kama na wewe unafikiria lile ninalolifikiria hivi sasa, basi jibu ni kwamba ninaelewa ni nini inamaanisha…”

    Walitazamana.

    Alipopigiwa hodi chumbani mwake siku ile alipokuwa akijirekodi akiimba shairi kwa ajili ya Moze, yeye alikurupuka na kwenda kusikiliza ni nani aliyebisha hodi pale mlangoni na kuiacha ile simu ikiendelea kurekodi. Baada ya hapo alikurupuka kwenda kusubiri lifti baada ya kusoma ule ujumbe wa Joakim, na kuacha mlango wazi na ile simu ikiendelea kujirekodi pale mezani…

    Mawazo yake hayo yalikatishwa na sauti ya Clara iliyojaa hamasa.

    “Jaka! Hiyo inamaanisha kuwa ile simu itakuwa imerekodi sauti zote zilizotokea mle ndani muda mchache baada ya wewe kutoka, na mtu yeyote aliyeingia chumbani mwako siku ile na akatoa sauti yoyote ile, atakuwa amerekodiwa…”

    “Sawa sawa kabisa!” Jaka alikubaliana na yule binti, kisha akiongezea, “kama atakuwa ametoa sauti, lakini kama aliingia na kutoka kimya kimya…”

    “Hiyo itajulikana baadaye…lakini najua lazima watakuwa wamesema kitu Jaka…si umesema kundi lao wako watatu…?”

    “Kama ni wao ndio waliohusika na kifo cha Joakim, na kunibambikia ule ushahidi, watakuwa watatu tu…Tony, Ng’ase na Muddy…na huwa hawaachani.”

    “Jibu liko kwenye ile simu yako Jaka!” Clara alimwambia kwa wahka.

    Jaka alimtazama yule binti kwa upendo na heshima kubwa.

    “Clara you are a genious! Yaani sijaona msichana mwenye akili kama wewe! Bila ya wewe kufikiria juu ya simu niliyokuwa natumia kabla ya kutoka nje ya chumba changu sijui kama ningeweza kuigundua siri hii…!” Alimwambia kwa shukrani.

    “Ndio uzuri wa kujadili matatizo pamoja dear…lazima kutapatikana ufumbuzi tu…” Clara alimjibu huku akimkumbatia.

    “Oh, Clara…”

    “Sasa swali kubwa zaidi mpenzi wangu ni je, ile simu bado ipo? Na tutaipataje?” Clara alimwambia huku akijichomoa kutoka kwenye kumbatio lake na kumtazama usoni.

    Jaka aliafikiana naye kwa kichwa huku akikunja uso kwa kutafakari.

    “Nakumbuka rafiki yangu niliyekuwa naishi naye pale chuoni aliniambia kuwa alikusanya vitu vyangu vyote na kuviweka kwenye boksi…ambalo alilipeleka nyumbani kwa mama yangu…sa’ sijui kama na ile simu itakuwa ni miongoni mwa hivyo vitu au hata kama bado inafanya kazi…ni muda mrefu sana unajua!” Alisema.

    “Itabidi tulipate hilo boksi basi ili tujihakikishie…hatuwezi kumpigia simu mama’ako tumuombe aangalie kwenye hilo boksi?” Clara alisema. Jaka alisita.

    “Mnh! Mimi sasa sina imani kabisa na hawa jamaa wanaoniwinda, vipi kama watakuwa wanafuatilia hadi mawasiliano yetu ya simu? Wanaweza kutuvurugia hata hili, unajua hiyo simu inaweza kubadili kabisa kila kitu kilichosemwa juu yangu kwenye kesi hii? Wale jamaa hawawezi kabisa kupenda hilo litokee.”

    “Mnh, ila kweli aisee. Sasa itakuwaje? Maana we’ kwenda Dar kufuatilia huwezi…vipi tukimtumia mama ujumbe wa simu kumuagiza aatutizamie kwenye hilo boksi alilokabidhiwa na huyo rafikiyo?”

    “Yote yale yale tu mi’ naona Clara…wanaweza kupata machapisho ya mawasiliano yetu ya meseji kutoka kwenye makampuni ya simu pia! Watu wameweza kujifanya maaskari wakasafiri nami gari moja bila kutiliwa mashaka, watashindwa hilo? Hapo ni mtu kwenda tu mpaka Dar…” Jaka alisema kwa kuchanganyikiwa.

    Walikaa kimya kwa muda mrefu. Katika muda ule, Jaka alikuwa akifikiria ni jinsi gani watalitatua tatizo lile. Akilini mwake alikuwa akiikumbuka vizuri sana ile simu yake aliyokuwa akiitumia kujirekodia pale chumbani kwake siku ile. Ile simu ilikuwa imerekodi lile shairi kwa muda wa kama dakika mbili tu kabla yule mtoto hajabisha hodi mlangoni kwake siku ile. Ukitoa dakika zipatazo tano hivi alizotumia kuongea na yule mtoto pale mlangoni na kujishauri iwapo aende kule alipotakiwa kwenda kwa mujibu wa ujumbe wa Joakim, alibakiwa na dakika nyingine nyingi sana ambazo ile simu ingeweza kurekodi sauti nyingine yoyote ambayo ingesikika mle chumbani mwake. Katika dakika hizo zote, mtu aliweza kabisa kuingia mle ndani, akaweka zile glovu chini ya godoro, na kutoka.

    Mara wazo lilimjia.

    “Unajua…mimi siwezi kwenda Dar sasa hivi, lakini wewe unaweza…” Alimwambia mpenziwe. Clara alimtazama huku akiafikiana naye kwa kutikisa kichwa chake taratibu.

    Hatimaye walikubaliana juu ya hilo. Jaka alimuelekeza nyumbani kwa mama yake na akaandika barua ambayo alimtaka ampe mama yake pindi akionana naye ili aweze kumpatia kile walichokuwa wakikihitaji.

    Walipanga safari ya Clara iwe siku iliyofuata.

    “Sasa naomba unihadithie mambo yote yaliyotokea baada ya mimi kuondoka kule Dar na kukuacha na wale askari pale kituo cha polisi cha OysterBay siku ile.” Clara alimwambia baada ya kukubaliana juu ya safari ile.

    Usiku ule wakiwa wamelala kitandani Jaka alimsimulia mambo aliyokutana nayo tangu siku ile, miezi kadhaa iliyopita, alipomuacha pale kituo cha polisi cha Oyster Bay jijini Dar, hadi pale alipoamka na kujikuta chumbani kwa Clara pale Dodoma baada ya kupoteza fahamu kutokana na kipigo kwa kudhaniwa mwizi pale nje ya ukumbi wa Disko wa NK.



    __________________



    Wakati Jaka anamsimulia Clara mambo aliyopambana nayo tangu waachane jijini Dar miezi kadhaa iliyopita, Mzee Januari Mwakaja, mkuu wa Polisi wa mkoa wa Dodoma alikuwa akizungusha gari lake kwenye mzunguko wa Jamatini taratibu huku akipiga mwayo mrefu. Alikuwa amechoka na akilini mwake alikuwa anajaribu kuyatafakari matukio ya siku ile huku mara kwa mara mawazo yake hayo yakimfikiria mkewe huko nyumbani ambaye siku zote huwa hapendi kabisa mumewe achelewe kurudi kutoka kazini.

    Huyu Jaka alifanya nini kule Dar? Hadi anategeshewa bomu!

    Alipita ofisi ya mhandisi wa mkoa na kuzunguka mzunguko wa pili uliokuwa karibu na chuo cha biashara, akikata kushoto na kuchukua barabara ielekeayo Area C kupitia Makole.

    Kitendo cha faili la kesi yake kutoweka katika mazingira yasiyoeleweka kinamaanisha kuwa jambo hili lilipangwa toka zamani…sasa leo angekufa katika mlipuko ule kusingekuwa na kumbukumbu yoyote ya mambo ambayo yeye alihusika nayo hapo mwanzo au uwezekano wa kugundua iwapo alisingiziwa mauaji ili kuficha ukweli fulani…ambao nadhani yeye Jaka atakuwa anaujua…

    “Endelea kuendesha hivyo hivyo na utekeleze maelekezo yangu afande!” Sauti nzito ilimshitua kutokea kwenye kiti cha nyuma mle garini.

    “AAAAARRGHH…!” Alipiga kelele kwa mshituko na kwa muda gari liliyumba kabla hajatulia na kuliweka sawa barabarani. Mara ile ile alihisi akiwekewa kitu cha baridi nyuma ya shingo yake naye akajua kuwa alikuwa amewekea mdomo wa bastola. Aliendelea kuendesha taratibu huku akili yake ikifanya kazi haraka haraka.

    “Wewe ni nani bwana, na unataka nini? Unajua kuwa mimi ni nani?” Aliuliza huku akiendelea kuendesha kwa mwendo mdogo sana.

    “Wewe ni RPC Januari Mwakaja, na kisogoni kwako kuna mdomo wa bastola aina ya

    Graz-Burya. Ni silaha makini yenye uwezo wa kufanya uharibifu usiotengenezeka katika mwili wa binadamu, kwa hiyo ningekuomba utulie tu afande na unisikilize…” Ile sauti ilimkoromea kutokea kule nyuma. Mzee Januari Mwakaja alitulia huku akiendelea kuendesha, kisha akajaribu kutia jeuri huku akiongeza mwendo wa gari.

    “Nadhani unaelewa kuwa ukiitumia hiyo silaha sasa hivi sote tutakufa, kwa sababu gari litapinduka na hutakuwa na uhakika kama wewe utatoka salama…” Alimwambia.

    “Unataka tujaribu?” Ile sauti ilimuuliza, na Mzee Mwakaja akajua kuwa hakuwa na ujanja.



    Alibaki kimya huku akijaribu kumtazama yule mtu kwa kutumia kioo cha kutazamia magari yatokayo nyuma kilichokuwa mbele yake mle garini. Hakuweza kumuona vizuri kutokana na kiza, lakini aliweza kuona kofia pana iliyofunika sehemu kubwa ya uso wa yule mtu. Hapo hapo alikumbuka maelezo ya Jaka juu ya mtu aliyekuwa akimfuata fuata anayevaa koti refu na kofia ya pama.

    Ndiye huyu…?

    “Unataka nini?” Hatimaye alirudia swali lake la kwanza.

    “Endelea kuendesha!”

    Mzee Mwakaja alitii amri ile. Baada ya mwendo fulani, ile sauti ilimwamuru aegeshe gari kando ya barabara na atulize mikono yake kwenye usukani. Januari Mwakaja akatii amri ile huku akibaini kuwa yule mtu alimwamuru asimamishe gari sehemu ambayo ilikuwa mbali sana na nyuma za raia.

    “Maongezi ninayotaka kuongea nawe ni ya siri sana ndio maana imenibidi nitumie njia hii ya kijasusi, bila shaka utaelewa.” Ile sauti ilimwambia kutokea kule nyuma huku muongeaji akimkabidhi kitambulisho kutokea kule nyuma. Mzee Mwakaja alikipokea na kuwasha taa ya ndani ya gari kukiangalia. Haikuwa mara yake ya kwanza kuona kitambulisho cha aina ile. Kilikuwa ni kitambulisho cha afisa wa usalama wa taifa.

    “Sawa bwana Jeff Bijhajha…nimekiona kitambulisho chako, lakini sijui kuwa sura iliyoko huko nyuma ndiyo haswa ya huyu mtu anayeonekana kwenye hiki kitambulisho.” Alisema huku akirudisha kile kitambulisho bila ya kugeuka nyuma.

    “Unaweza kugeuka nyuma taratibu sana kuniangalia.” Jamaa alimwambia huku akikipokea kile kitambulisho chake. Januari Mwakaja aligeuka na kumtazama. Walitazamana. Hakuwa amepata kumuona kabla ya wakati ule, lakini sura iliyokuwa kwenye kitambulisho kile ilikuwa ndiyo haswa aliyokuwa akitazamana nayo wakati ule.

    “Umeridhika?” Jeff Bijhajha aliuliza, na mzee Mwakaja aliafiki kwa kichwa.

    “Nadhani sasa unaweza kuzima taa ya gari ili tuongee.”

    Mzee Mwakaja alizima taa ya ndani ya gari na yule afisa wa usalama wa taifa alianza kueleza.

    “Sasa hivi kumetokea wimbi kubwa la biashara ya madawa ya kulevya hapa nchini, na katika miaka miwili iliyopita serikali, ikivitumia vyombo vyake vya dola, imekuwa ikijitahidi bila ya mafanikio kukabiliana na wimbi hili…

    “…tatizo kubwa limekuwa kwamba pamoja na kuwa inajulikana wazi kuwa biashara hiyo inafanyika humu nchini, kiini cha bidhaa hiyo haramu kimeendelea kuwa kitendawili…swala la nani hasa anayehusika na kuyaingiza hapa nchini na kwa kutumia njia gani ndilo limekuwa gumu mno kwa serikali na idara zake zote za kudhibiti madawa ya kulevya.”

    “Ah, Lakini mbona kuna watu, hasa vijana, wengi tu wanaokamatwa na madawa hayo kila kukicha? Ina maana imeshindikana kuwabana wote hao hata wakataja ni wapi wanapata bidhaa hiyo?” Mzee Mwakaja alidakia.

    “Hao unaowasema wewe ni wale wasambazaji wadogo wadogo tu ambao hawakuwa na msaada wowote wa maana mpaka sasa. Wengi wao wamekuwa wakitoa mtiririko wa habari zilizoishia hewani tu, hazifikii hasa pale kwenye shina kuu la biashara hii nchini…yaani hizi mbinu za kuendesha biashara hii ni za uficho sana kiasi kwamba ni vigumu kuwatia mkononi wale mapapa na manyangumi wa biashara hii. Tunaishia kukamata vijidagaa tu…wale watekelezaji wa mwisho kabisa ambao huwa hata hawaelewi hao mabosi wa biashara hii ni akina nani hasa…it’s very complicated…”

    “Yote nayajua hayo…inahusu nini kuniinyatia garini mwangu usiku wote huu na kunieleza hayo?” Januari Mwakaja alitia hoja.

    “Isitoshe, wengi wa hao wanaokamatwa ni watumiaji wadogo wadogo tu ambao huwa hawajali ni nani anayewaletea bidhaa hiyo, wanachojali wao ni kupata tu hiyo bidhaa, basi...” Jamaa aliendelea kama kwamba hakulisikia swali la yule mkuu wa polisi wa mkoa, na akaendelea, “…na wengine ni wale wanaokuja na bidhaa hiyo moja kwa moja kutoka nje ya nchi, kama vile Pakistan, Uturuki na nchi za Afrika ya Kusini na magharibi, wale wanaomeza paketi za unga huo na kukamatwa hapa uwanja wa ndege. Hawa mara nyingi huzitaja nchi walizotoka na unga huo kuwa ndio chanzo cha biashara hiyo. Wote hawa hawakuwa na msaada wa maana katika kuwafikia yale manyangumi ya biashara hii humu nchini.”

    “Nimekuelewa. Lakini bado hujanielewesha ni jinsi gani swala lote hilo linahusika na mkoa wangu hadi ifikie hatua ya sisi kuongea katika mazingira kama haya.”

    “Swali zuri…hapa ndipo utakapoelewa ni jinsi gani wewe unaingia…” Jeff Bijhajha alimjibu kisha akavuta pumzi na kutulia kidogo kabla ya kuendelea, “Kiasi cha kama mwaka mmoja uliopita, ujumbe maalum kutoka kikosi cha kupambana na madawa ya kulevya cha marekani, kijulikanacho kama D.E.A…”

    “Drug Enforcement Agency…” Januari Mwakaja alidakia.

    “Yeah…Drug Enforcement Agency…ujumbe kutoka D.E.A. ukiongozwa na balozi wa Marekani hapa nchini ulimtembelea Rais Ikulu na kumkabidhi ripoti kuhusu biashara ya madawa ya kulevya hapa nchini. Ripoti hiyo ilionesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kushiriki kwa viongozi wa ngazi za juu aidha serikalini au ndani ya jeshi la polisi katika uendeshaji wa biashara haramu ya madawa ya kulevya hapa nchini. Ingawa taarifa hii ilikuwa ngumu kukubalika mara moja, lakini ilileta maana kutokana na ukweli kwamba jitihada zote za serikali za kupambana na biashara hii zimekuwa zikigonga mwamba, na mara nyingi ilionekana kama kwamba hao wanaoendesha biashara hii, walikuwa wanapata taarifa zote za nini serikali ilikuwa inapanga na hivyo kuwawia rahisi kwao kukwepa mitego ya serikali.”

    Mzee Januari Mwakaja alikaa vizuri huku akisikiliza kwa makini maelezo yale. Ile sauti nzito iliendelea kueleza kwenye kiza cha mle garini.

    “Ni kutokana na ripoti hii ndipo rais alipounda tume maalum kuchunguza undani wa swala hili. Hii ni tume ya siri sana kiasi kwamba hata watu wa ngazi za juu kabisa serikalini hawajui juu ya uwepo wake. Mimi ni mmoja kati ya watendaji wa tume hii, na mpaka sasa tuna orodha ya baadhi ya askari wakubwa wanaoshukiwa kujihusisha na biashara hiyo, ingawa bado hatujafanikiwa kukitambua kiini cha uendeshaji wa biashara hiyo hapa nchini mpaka sasa.”

    “Sasa bwana mdogo mbona unaniambia yote haya?” Januari alidakia tena.

    “Hewaa! Nakueleza haya kwa sababu tume imenielekeza nije nikueleze habari hii, na nimetakiwa nikueleze habari hii ili uone umuhimu wa kunipa ushirikiano kwenye jambo lililonileta hapa Dodoma…”

    “Mnh, okay. Ni jambo gani hasa lililokuleta hapa Dodoma bwana Bijhajha?” Januari Mwakaja aliuliza huku akiwa makini sana .

    “Kijana aitwaye Jaka Brown Madega.”

    “Whaat? Jaka…! Jaka si mhalifu aliyeletwa hapa kutumikia kifungo cha nje kwa kosa la mauaji!” Januari Mwakaja aliuliza kwa mshangao.

    “Inaweza ikawa kweli amefanya hayo makosa…lakini pia inawezekana ikawa amepakaziwa tu kwa sababu ya kulinda maslahi ya watu fulani…” Jeff alimjibu.

    “Kwa hiyo…?”

    “Bila kutafuna maneno mzee kuna kila sababu za kuamini kuwa Jaka anaweza kuwa na taarifa nyeti zinazoweza kutusaidia kwenye kulifikia shina la biashara hii haramu hapa nchini.”

    Mzee Januari Mwakaja aliduwaa.

    “Kwa hiyo…?” Aliuliza tena, akili ikimzunguka, kile alichokuwa kikihisi kuhusu Jaka kikijidhihirisha katika zile taarifa alizokuwa anapokea wakati ule.

    “Nimepewa kibali maalum cha kumtumia Jaka Brown Madega kwa namna yoyote ile nitakayoona inafaa katika kutekeleza uchunguzi wa tume niliyokuelezea, ili kuhakikisha kuwa tume inatimiza kazi iliyotumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano.” Bijhajha alimalizia na kutulia.

    Kwa mara nyingine Januari Mwakaja alilazimika kuwasha taa ya ndani ya gari ile na kusoma karatasi aliyokabidhiwa na yule mtu ambaye kitambulisho chake cha kazi kilimtambulisha kama Jeff Bijhajha. Ile karatasi ilikuwa inatoa kibali kwa Jeff Bijhajha kumtumia Jaka Brown Madega katika kutekeleza majukumu aliyokabidhiwa na tume ya siri ya kuchunguza uhusikaji wa maafisa wa polisi na viongozi wa juu serikalini katika uendeshaji wa biashara ya madawa ya kulevya nchini.

    Kile kibali kilikuwa kina nembo ya rais na kusainiwa na waziri wa mambo ya ndani kwa niaba ya rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.

    Januari Mwakaja alijikuta akipiga mbinja kwa mshangao na kustajaabia jambo lile.

    “ Dduh! Imetoka moja kwa moja Ikulu hii!” Alisema kwa mastaajabu.

    Jeff Bijhajha hakujibu. Aliichukua ile karatasi na kuihifadhi kwenye mfuko wa ndani wa koti lake refu.

    “Kwa hiyo unadhani kuwa Jaka anaweza kuwa na msaada kwako?”

    “Tukio la leo asubuhi pale sokoni linazidi kunihakikishia hivyo.”

    “Kwa hiyo, wewe ndiye uliyekuwa ukimfuatilia nyendo zake yule kijana?” Mwakaja aliuliza, na kabla Bijhajha hajajibu, akaendelea, “Sasa kwa nini ulimtwanga mangumi kule uwanja wa sabasaba siku kadhaa huko nyuma?”

    Badala ya kumjibu, Jeff akacheka kidogo, kasha akwamwambia, “Tuachane na hayo. Nadhani sasa umeshaelewa kuwa siko hapa kwa ubaya dhidi yake. Sasa, Mi’ nitahitaji kwenda Dar kwa siku mbili kabla ya kuja kuongea rasmi na Jaka. Katika siku mbili hizo, nakuomba sana mzee uhakikishe kuwa Jaka anaendelea kuishi hadi hapo nitakaporudi. Baada ya hapo atakuwa chini yangu.”

    Alifungua mlango, akateremka na kuanza kutokomea kizani.

    “ Hey! Jeff!” Januari Mwakaja alimwita, na Jeff akarudi na kuchungulia dirishani.

    “Unasemaje?”

    “Sasa tutaonana vipi tena? Huu utaratibu wa leo si mzuri bwana…”

    “Nikikuhitaji nitakupata tu mzee…si unaona nilivyokupata leo?”

    “Hii sio namna nzuri ya kukutana…”

    “Lakini ndio salama zaidi…”

    Akatoweka.

    Januari Mwakaja alitia gari moto na kuondoka eneo lile huku akiwa na mawazo tele kichwani.

    Siku iliyofuata, Clara alisafiri “kikazi” kuelekea Dar es Salaam kwa gari la kampuni. Dereva aliyekuwa akimuendesha na wafanyakazi wengine wote pale ofisini kwao, walijua kuwa ile ilikuwa ni moja kati ya safari zake nyingi za kikazi kuelekea Dar es Saalaam. Kama jinsi ambavyo wale askari waliowekewa kuwalinda pale nyumbani kwao walivyoelewa.

    Ni wao pekee ndio walioijua dhima ya safari ile.



    ___________________



    Akiwa ofisini kwake siku ile Jaka alikuwa akifanya kazi huku akili yake ikiwa kwa Clara tu aliyekuwa safarini wakati ule. Alikuwa na wahka mkubwa wa kujua iwapo atafanikiwa kuipata ile simu yake na iwapo ile simu itakuwa na ufumbuzi walioutarajia. Mawazo haya yalikuwa yakimjia na kuondoka huku akijitahidi kufanya zile kazi kadiri alivyoweza.

    Hatimaye akili yake ikazama moja kwa moja kwenye zile kazi na kusahau kuhusu safari ya Clara kwa muda. Mlango wa ofisini kwake ulifunguliwa taratibu na kufungwa tena, naye akiwa na uhakika kuwa aliyefungua mlango ule alikuwa ni mhudumu wa ofisi akileta barua za kikazi au vocha za malipo ya madereva wa ile kampuni ya usafirishaji, aliendelea kushughulika na kazi zake kwa muda kabla hajainua uso wake kumsikiliza.

    La Haula!

    Moyo ulimlipuka na hapo hapo ukaanza kumwenda mbio huku akili ikikataa kabisa kuamini alichokuwa akikiona mbele ya uso wake.

    Mbele yake mle ndani walikuwa wamesimama watu wawili ambao aliamini kuwa hatowaona tena maishani mwake.

    Don Sibazosi, ambaye yeye alimtambua kama “mzee wa matabasamu”, alikuwa amesimama katikati ya ofisi ile hali akiwa amemuelekezea bastola ambayo alishawahi kuiona mikononi mwa muuaji yule hapo awali. Llama Automatic ilikuwa imemuelekea moja kwa moja usoni. Nyuma ya yule mtu mwenye tabasamu la kutisha kabisa alilopata kuliona, Puzo Vurumai, ambaye yeye alikuwa akimtambua kama “Claus Kinski” mwenye sura yenye alama za ndui, alikuwa amesimama akiwa ameegemea ukuta kando ya mlango hali mikono yake ikiwa imezama kwenye mifuko ya koti la suti nyeusi aliyovaa huku akimtazama kwa macho makali.

    Jaka alibaki mdomo wazi.

    Wale jamaa walikuwa amevalia suti ghali sana zilizowafanya waonekane kama aidha ni wafanyabiashara wenye mafanikio au ni maafisa wa maana sana kiasi kwamba Jaka hakuwalaumu walinzi waliowaruhusu kupita hadi pale ofisini kwake. Wakati Puzo alikuwa amepiga suti kali nyeusi, Don Sibazosi alikuwa amevaa suti safi sana ya kijivu iliyomkaa vyema sana.

    Don Sibazosi alikuwa akimsogelea pale mezani huku akimlengeshea ile bastola iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti hali mdomo wake ukiwa umefanya tabasamu na wakati huo huo macho yake yakionesha chuki ya hali ya juu.

    Heh!

    “Unadhani unaweza kuwakimbia Don Sibazosi na Puzo Vurumai halafu uishi kwa raha mstarehe hapa duniani Jaka?” Don Sibazosi alimuuliza, na ndio kwa mara ya kwanza Jaka alipoyasikia majina ya wale wauaji, ingawa kwa pale alipokuwa hakuwa na namna ya kujua yupi ni yupi kati yao. Alibaki ameduwaa.



    ***DAH, Wapi Jeff Bhijhajha...mzee wa mapama?





    “Ulijiona una bahati sana ulipoponea chupu chupu siku ile tulipolipua lile gari la magereza kule Dar, eeenh?” Don alizidi kumuuliza huku bado akiwa amemlengeshea ile bastola.

    Bado Jaka alikuwa amepigwa na butwaa.

    “Halafu ukatutoka tena kwa namna ya ajabu kabisa pale darajani Manzese…” Don alizidi kumsimanga, na alipofikia hapo aliguna na kutoa sauti ya mfyatuko wa ulimi, kisha akaendelea, “…ila kwa hapo lazima nikupe sifa aisee…lile lilikuwa ni tendo la mwaka Jaka. Sijui kwa nini hujawa miongoni mwetu wewe, ungetufaa sana…sijui kama nitaona tena tendo la kudiriki kama lile!”

    Sasa Jaka alianza kutembeza akili yake haraka haraka kutafuta namna ya kujinasua kutoka kwenye mtego ule, ingawa alijikubalisha kuwa hakika pale alikuwa amepatikana. Alitembeza macho huku na huko mle ndani kwa taharuki.

    “Hebu fanya lililotuleta tuondoke, bwana!” Yule mwenzake alimhimiza, lakini Don bado alikuwa anataka kumpa Jaka maneno yake kabla hajamuua.

    “Halafu ukawatoka vibaya sana vijana wetu wengine waliokukurupusha usiku ule ulipotaka kurudi nyumbani kwa mama yako baada ya kututoroka sisi kule darajani…Mungu wangu, Jaka! Yaani hadi leo wale vijana hawaelewi uliwezaje kuwaacha kizani namna ile!”

    “Bosi nauweka bwana, akh!” Puzo alimkoromea tena mwenzake, na hapo hapo Jaka naye akaongea.

    “Kwa…kwani nyie mnataka nini hasa kwangu?”

    “Funga bakuli lako!” Don alimfokea, kisha akaendelea, “Sasa sijui leo umetuandalia mbinu gani ya kututoka…maana ulitaka kujiona mjanja sana ulivyonusurika kutawanywa vipande vipande kwa bomu pale sokoni…”

    “Ha! Kumbe ni nyie? Yaani kweli mlikuwa tayari kuua na watu wengine wasio na hatia…?”

    “Shut Up!” Don alimfokea tena na kumsogelea pale mezani kwa hatua moja kubwa huku bado akimlengeshea ile bastola. “Ulifikiria ni nani wengine, eenh? Huwezi kutukimbia namna ile halafu utegemee kuishi kwa amani tu…”

    “Kwa nini…”

    “Tulia kimya! Sasa umeshagundua kuwa huwezi kutukimbia? Nataka ujue hivyo kabla hujaaga dunia leo hii!”

    “Don…hatuna siku nzima na hatukuja kutoa risala hapa! Fanya tuondoke!” Puzo Vurumai alimhimiza mwenzake na hapo ndipo Jaka alipojua jina la kila mmoja kati yao.

    Hapo Don Sibazosi alimwamuru Jaka asimame na atoke nyuma ya meza ile. Jaka alitekeleza huku akiwa amenyoosha mikono yake juu, mwili ikimtetema. Don Sibazosi alimuwekea mdomo wa ile bastola kwenye paji la uso.

    “Omba sala yako ya mwisho, sukununu we!” Alimkemea kwa hasira.

    “Sala za nini lakini Don? Muwashe tutambae bwana…” Puzo alimfokea mwenzake na Jaka akafumba macho kwa woga huku akijua kuwa alikuwa anakabiliana na mauti.

    Na hapo simu yake ya mezani iliita na wote mle ndani walishituka, Don akipeleka macho yake kule ulipotokea ule muito.

    Jaka hakufanya ajizi.

    Kwa nguzu aliupiga ngumi ule mkono uliokuwa umemshikia bastola naye akajikwepesha pembeni. Ile bastola ikaatupwa hewani huku akimsikia Don akipiga ukelele wa ghadhabu uliofuatana na mhemko wa hamaniko kutoka kwa Puzo. Alijirusha haraka kuiwahi ile bastola huku na Puzo naye akikurupuka kutoka pale alipokuwa amesimama kuiwahi ile bastola. Lakini Don alikuwa mwepesi zaidi.

    Alijigeuza kistadi na kumtandika Jaka ngumi nzito iliyojikita sawia katikati ya mwamba wa pua na Jaka alibweka huku akijishika pua na kuinama kwa maumivu. Hapo hapo Don alimkamata ukosi wa koti lake kwa nyuma na kumshindilia futi la uso, na Jaka alitupwa chali mle ndani huku damu zikichuruzikaa kutoka puani na mdomoni. Don alimuinamia na kumkamata ukosi wa koti lake kwa mbele na kumnyanyua kimabavu huku akimtukania mama yake na kumbebesha kichwa kizito cha mdomo na Jaka alilia kama mfiwa huku akienda tena chini kama gunia.

    Simu aliacha kuita.

    Puzo akarudi kusimama pale pale ukutani kando ya mlango baada ya kuona kuwa Don alikuwa amelimudu pambano, Jaka alibaki akipapatika pale chini kwa maumivu na kiwewe cha kipigo.

    “Inuka smart boy…nataka uone hasara ya kufanya mchezo na Don Sibazosi leo!” Mzee wa matabasamu alimtambia huku akimzunguka akiwa amelala pale chini akitweta kwa maumivu.

    “Kwani nimewakisea nin…AAAAARGH!” Jaka alianza kuuliza lakini hapo hapo Don alimtandika teke kali mbavuni, kisha yule adui alimkwida na kumnyanyua tena kutoka pale chini, akamsukumia ukutani kwa nguvu, ambapo alijibamiza vibaya na na kabla hajaenda tena chini yule muuaji akamrukia na kumshindilia soli ya kiatu chake kifuani.

    Jaka alilia kwa uchungu na kujibwaga sakafuni akiwa hoi.

    “Sasa nenda ukasimulie hizo siri ulizoona jehannam, mpumbavu mkubwa!” Don Sibazosi alimwambia huku akitoa kamba ya nailoni kutoka kwenye mfuko wa suruali yake. Jaka alijaribu kuinuka kutoka pale chini lakini alipoinua kichwa tu, Don alimpitisha ile kamba shingoni na kuanza kumkaba kwa nguvu. Jaka alikurupuka na kujitupa na kufurukuta akijaribu kujinasua kutoka kwenye kitanzi kile, lakini Don aliyekuwa amemkaba kwa nguvu, alizidi kukikaza kile kitanzi na kuzidi kumkata pumzi.

    Pumzi zilimuisha Jaka. Mapafu yakawa kama yanayomuwaka moto. Uso ukaimvimba. Alitupa mikono yake kwa nyuma akijaribu kumkamata Don lakini hakufanikiwa. Alijiinua kutoka pale chini na kusimama na Don akasimama pamoja naye huku akizidisha kumkaba kwa ile kamba. Alijaribu kupiga kelele lakini hilo halikuwezekana kabisa. Macho yalimtumbuka na mishipa ya kichwa ilimtutumka. Mikoromo ikamtoka na ulimi ukamtutumka na akajua kuwa pale uhai ulikuwa unamtoka.

    Hakika hiki ni kifo kibaya kabisa…

    Kwa nguvu zake zote alizodhani alikuwa amebakiwa nazo, alijitupa kwa mbele kuliendea dirisha, na akaangukia magoti karibu na lile dirisha, Don Sibazosi akiwa amemng’ang’ania kwa nguvu mgongoni huku akizidi kumkaba kwa ile kamba.

    Aaa kwa heri mama…kwa heri Clara!

    Akiwa amepiga magoti pale chini ya lile dirisha pana la kioo, aliweza kuwaona baadhi ya wafanyakazi wakipita kule chini lakini hakuweza kuwaita. Alikipigapiga kioo cha lile dirisha kwa matarajio kuwa wale waliokuwa kule chini wangeweza kusikia na kwenda kumsaidia, lakini mikono yake ilikuwa inaishiwa nguvu haraka sana na fahamu zilianza kumpotea.

    Ah, jamaa ndio ananiua hivi…!

    Alijikurupusha kutoka pale chini na kufanikiwa kusimama tena huku akitweta na akimsikia Don Sibazosi akigumia wakati akizidi kuikaza ile kamba shingoni kwake. Ile kamba ilianza kumkata shingoni na damu ikaanza kumchuruzika.

    Ah, Kifo hiki sasa!

    Alipiga ukelele na kwa nguvu zilizobakia alitupa juu miguu yake kwa nia ya kukipiga kile kioo na kukivunja, akiamini kuwa tendo hilo lingesababisha wafanyakazi walioko kule chini waje kuangalia kulikoni na hatimaye kumuokoa, lakini Don aliigundua mbinu hiyo na kabla miguu yake haijakifikia kile kioo, alimvuta nyuma kwa nguvu. Miguu yake ikatua kwenye ukingo wa lile dirisha na kukikosa kile kioo. Hapo hapo alijisukuma nyuma kwa nguvu kwa kutumia miguu yake iliyokuwa kwenye ukingo wa lile dirisha na wote wawili walijibwaga kwa kishindo juu ya meza, ile kamba ikamtoka Don naye akipindukia upande wa pili wa meza ile na kumuacha Jaka akiangukia sakafuni baina ya ile meza na lile dirisha. Jaka alikurupuka kutoka pale chini na kutambaa kwa pupa kuelekea dirishani huku akitweta kutafuta pumzi. Aliegemeza mikono yake kwenye kingo za dirisha na kujaribu kulifungua ili apate hewa huku akikohoa na machozi yakimtiririka akiwa amepiga magoti nyuma ya dirisha lile. Lakini mikono yake ilikuwa mizito, hivyo akabaki amejiinamia pale chini ya dirisha huku akitapatapa.

    Puzo Vurumai aliyekuwa akifuatilia purukushani ile kwa makini alitoka mbio kutaka kumuwahi Jaka pale alipokuwa, lakini Don Sibazosi alikurupuka kwa ghadhabu kutoka pale alipoangukia huku akitoa tusi kali. Aliwahi kuiparamia ile meza na kudondokea upande ule aliokuwako Jaka hali kamba yake ikiwa mkononi.

    Tukio lilifuatia hapo lilikuwa la haraka sana kiasi kwamba Puzo Vurumai aliyekuwa akikimbilia pale walipokuwa, hakuweza kufanya lolote zaidi ya kukodoa macho tu kwa kutoamini.

    Don Sibazosi alimrukia Jaka akiwa ametanguliza mikono yake iliyoikamata ile kamba akitaka kumzungushia tena shingoni kwa Jaka, aliyekuwa amemgeuzia mgongo akitweta pale kwenye ukingo wa lile dirisha pana la kioo. Aliposikia vishindo vyake, Jaka aligeuka haraka kadiri alivyoweza huku akijitahidi kusimama wima. Na hapo ndipo alipoiona mikono ya Don ikimuendea usawa wa shingo yake ikiwa imeshika ile kamba. Bila ya kutarajia Jaka alijikuta akiinama kumkwepa, na mikono ya Don Sibazosi ikampitia juu ya kichwa, ile kamba ikiikosa shingo yake na kiwiliwili cha yule muuaji kikamkumba na kumsukuma kinyuma nyuma kuelekea kule dirishani, na hapo bila ya kujua kitakachofuatia, Jaka alimshika Don sehemu za mbele za mapaja yake, akarudisha nyuma mguu wake na kujizuia kwenye ukuta uliokuwa chini ya dirisha lile, na kwa nguvu zake zote alimtupa juu yule adui aliyemuiwa mwepesi kutokana na ile kasi aliyokuwa amekuja nayo.

    Don Sibazosi alitupwa hewani huku akipiga kelele akiwa ametanguliza mbele mikono yake, alijiona wazi wazi akikiendea kwa kasi kioo cha lile dirisha. Macho yalimtumbuka na mdomo ukampanika sio kwa kutabasamu tena, bali kwa yowe kubwa la woga.

    Ulisikika mlio wa kioo kikipasukia sanjari na ukelele wa Don Sibazosi ukipotelea nje ya lile dirisha lililokuwa ghorofa ya kwanza ya jengo lile.

    “Doooonn!” Puzo Vurumai aliita kwa sauti iliyokuwa na mchanganyiko wa mshituko na woga mkubwa, akimuona mshirika wake akipotelea nje ya dirisha lile akifuatiwa na mapande ya vioo.

    Na hata pale alipokuwa akimsikia Puzo ikiita jina la mshirika wake kwa hamaniko, Jaka alisikia kishindo kikubwa kutokea chini, nje ya lile dirisha. Aligeuka na kuona uwazi mkubwa pale dirishani ambapo awali kulikuwa kuna kioo. Vipande kadhaa vya kioo kilichokuwa pale dirishani vilibaki vikining’inia kwenye mbao za dirisha lile. Upepo ulivuma kwa nguvu na kuingia mle ndani kupitia kwenye uwazi ule na kupeperusha hovyo makaratasi kutoka pale mezani kwake. Mayowe ya wafanyakazi yalisikika kutokea kule chini naye akalisogelea lile dirisha na kuchungulia kule alipopotelea Don Sibazosi. Aliwahi kuuona mwili wa Don Sibazosi ukijitikisa kwa mara ya mwisho kabla ya kutulia ukiwa hauna uhai. Kutoka pale alipokuwa alihisi kuwa Don Sibazosi alikuwa amevunjika shingo.

    Hapo alimkubuka mshirika wake na haraka akageuka nyuma na kumuona Puzo Vurumai akimuendea kwa kasi huku akiwa umekunja uso kwa hasira na dhamira ya mauaji. Na hata pale alipogeuka, Puzo alimrushia kisu kwa mkono wake wa kulia, na hapo hapo alihisi maumivu makali kwenye bega lake la kushoto, kilekisu kikijikita mwilini mwake. Yowe lilimtoka bila kupenda.

    Puzo bado alikuwa akimuendea kwa kasi, naye bila ya kufikiri zaidi wala kujali maumivu, alikichomoa kile kisu na kumtupia. Puzo aliyumba na kile kisu kikamkosa, lakini tendo lile lilimpoteza lengo kidogo, na hapo hapo Jaka alijitupa sakafuni kuiwahi ile bastola ya Don Sibazosi. Puzo aliliona tendo lile na akajua kuwa usalama wake ulikuwa mdogo. Aligeuka na kutoka mbio kuuelekea mlango wa kutokea nje ya ofisi ile.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jaka aliikamata ile bastola na kumtupia risasi mbili za haraka haraka, ile Llama Automatic ikitoa sauti kama ya chafya ya mtoto mchanga wakati. Risasi zilichelewa kwani Puzo alikuwa ameshatokomea nje ya ofisi ile, risasi zikijikita ukutani, naye akisikia vishindo vya viatu vyake wakati akishuka ngazi kwa kasi huko nje.

    Alijibweteka chini huku damu zikimtoka shingoni na puani hali mikono ikimtetemeka vibaya sana. Muda mfupi baadaye wafanyakazi wenzake walifika na kumkuta akigaragara pale zuliani mle ofisini kwake. Walianza kumpa msaada huku wakihoji kulikoni na Jaka akishindwa kuwaeleza lolote la kueleweka. Baadaye walinzi wa kawaida wa pale ofisini na askari wa jeshi la polisi waliingia, na hapo alijua kuwa alikuwa salama. Alijua kuwa Puzo atakuwa ametoroka bila ya kutiwa mbaroni, lakini kwa wakati ue hilo hakulijali.

    Baada ya hekaheka na maswali mengi, hatimaye alitolewa na kukimbizwa hospitali kwa kutumia moja ya magari ya pale ofisini. Huku nyuma, wale askari wa jeshi la polisi waliubebea mwili wa marehemu Don Sibazosi na kuuondoa kutoka eneo lile.





    MWISHO





0 comments:

Post a Comment

Blog