Search This Blog

Monday, 24 October 2022

PATASHIKA - 1

 

    IMEANDIKWA NA : JAPHET NYANG'ORO SUDI



    *********************************************************************************





    Simulizi : Patashika

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    ALISHTUKA TOKA USINGIZINI. Akajituliza pale kitandani kwa sekunde kadhaa, masikio yake yaliweza kusikia moyo wake ulivyokuwa ukidunda kwa kasi. Naam! Baada ya kujituliza kwa muda, sasa akaweza kusikia dhahiri kuwa mlango wa sebuleni ulikuwa unagongwa na hicho ndicho kilichomkatisha usingizi wake mtamu. Kwa kukereka kidogo, alijiinua pale kitandani kisha kivivuvivu alinyoosha mkono wake kuelekea ilipokuwa swichi akawasha taa.

    Baada ya kuwasha taa na mwanga kuwa umelishinda giza kwa kutawala kile chumba alichokuwemo, alipepesa macho yake ambayo wakati huu yalikuwa yakijitahidi kuuzoea mwanga. Hii hutokea mara zote mtu anapokuwa kwenye giza kwa muda mrefu au anapokuwa ametoka usingizini kisha akakutana na mwanga mkali kama hivi. Baada ya sekunde kadhaa tayari macho yake yalikuwa yameshauzoea mwanga wa taa, hapo aliyaelekeza hadi ilipokuwa saa iliyokuwa imesimama kama boksi juu ya meza ya kitanda. Saa ilimwonyesha majira kuwa ilikuwa saa nane na dakika kumi usiku. Alishangaa nani angekuwa anagonga usiku wote ule ambao mvua kubwa iliyoambana na radi za ajabu ilikuwa bado inanyesha? Ulikuwa ni msimu wa masika katika eneo hili la Katunguru wilayani Sengerema mkoani Mwanza. Hivyo wakazi wa eneo hilo walikuwa kwenye wakati wa kilimo, kilimo cha mpunga ndicho hasa kilichokuwa kikifanywa na watu wengi. Alitembea hadi sebuleni, hapo akaelekea ulipokuwa mlango wa kutokea nje. Kabla hajafanya lolote mlango huo uligongwa tena, ikabidi achungulie kwanza kwenye tundu la mlango. Mwanga wa taa ya kibarazani ukamwezesha kumwona mtu aliyekuwa anagonga.

    “Milka mdogo wangu pole, kuna shida gani usiku wote huu? Ona ulivyonyeshewa na mvua!” Hatimaye Maganga alisema kwa mshangao baada ya kumwona mdogo wake wa damu akiwa amejikunyata pale nje huku akiwa ameloa chepechepe, nguo zikiwa zimemng'ang'ania mwilini kama manyoya ya kuku aliyeloa maji. Badala ya kujibu, Milka aliingia ndani huku akiwa anatetemeka kwa baridi iliyotokana na mvua iliyokuwa imemnyeshea.

    “Kaka Maganga…” Milka alianza kuongea kwa shida huku sauti yake ikitetemeka pia.

    "Naam, Milka mdogo wangu!” Maganga aliitika.

    “Nimeficha kwa muda mrefu sana.” Milka akasita huku akiwa anamwangalia Maganga ambaye wakati huu alikuwa amekwisha ufunga mlango na kuuegemea. Alikuwa na hamu ya kujua nini kilikuwa kimemsibu mdogo wake yule. Badala ya kuendelea, kwikwi ya kilio ilisikika toka kwa Milka. Kusikia hivyo Maganga alimsogelea mdogo wake na kumshika mabegani.

    "Niambie Milka, nini kinakutatiza?. Najua umekuja hapa kuniambia, niambie sasa!” Maganga aliongea kwa sauti ya huruma, msisitizo na iliyokuwa na mashaka. Alijua kuna jambo kubwa limemfika mdogo wake huyo.

    “Maganga!” Milka aliita na kusita.

    "Weee, Milka, hebu acha kufanya hivyo, niambie kuna tatizo gani?” Badala ya kuitika Maganga sasa aliongea kwa sauti ya kufoka kidogo.

    "Unanipenda?” Milka alihoji huku akiwa bado kajikunyata huku sakafu aliyokuwa amesimama juu yake ikiwa imeloa maji yaliyokuwa yakiteremka toka mwilini mwake. Maganga hakuweza kuona hilo, kwani muda wote huo walikuwa gizani, taa ya sebuleni haikuwa imewashwa. Mwanga wa taa ya barazani ndiyo iliyokuwa ikipenyeza miale yake kupitia dirishani, miale ambayo hata hivyo haikuwa ya kutosha kuwawezesha kuona vema kila kitu. Mshtuko aliokuwa nao haukumpa nafasi Maganga ya kuwasha taa.

    “Swali gani hilo wewe? Wewe wajua!”

    “Acha kujibu ki-kasisi, nataka kujua Maganga!” Milka alisema huku akiinua mikono yake kushika viganja vya Maganga ambaye alikuwa amesimama nyuma yake na mikono yake ikiwa imeshika mabega ya Milka huku na huku.

    “Unamaanisha nini Milka? Nitaachaje kukupenda na wewe ni ndugu yangu? Kama maandiko yanasema umpende adui, je si sana ndugu yako wa damu?!!

    "Simaanishi hivyo Maganga. Oooh! Nasikia baridi. Una chai hapa?” Milka alisema huku akijitoa mikononi mwa Maganga kaka yake.

    Japo Maganga alikuwa na hamu ya kujua nini hasa kilikuwa kimemsibu mdogo wake lakini pia hakushindwa kuona jinsi mdogo wake huyo alivyokuwa akiteseka kwa baridi ambayo ilimfanya atetemeke mwili na sauti. Hivyo ombi la Milka kuhusu chai alilipokea kwa uzito uliostahili. Alitembea kuelekea chumbani kwake. Aliingia na kuucha mlango wa chumba hicho wazi. Wakati mkono wa Maganga ukiwa unaifikia chupa ya chai iliyokuwa pembeni mwa kitanda chake chini ya meza ndogo ya kujisomea, alihisi kama kuna nyayo za mtu nyuma yake.

    Akiwa bado ameinama pale ilipokuwa chupa ya chai, alitupia macho yake nyuma kupitia katikati ya miguu yake na aliweza kuona miguu. Macho yake yalipanda taratibu toka miguuni mwa Milka kwenda juu, alipofika juu kidogo ya mapaja Maganga alishtuka.

    "Milka!” Aliinuka mara huku akipiga kelele. Wala hakuichukua tena ile chupa ya chai. Aligeuka, macho yalimtoka pima.

    “Hivi wewe, umechanyikiwa nini? Hiki ndiyo kimekufanya uje usiku wote huu hapa kwangu?” Maganga aling'aka.

    “Kaka Maganga, acha kujifanya hutaki. Najua unataka sana usiniambie mafunzo ya Utawa uliyonayo ndiyo yamekufanya usiwe mwanaume kamili...” Milka alisema huku ile sauti ya kutetemeka sasa ikiwa haipo tena. Maganga akabaki amesimama kwa shangao akimwangali Milka.

    "Maganga, najua una kiu na unanipenda kama ulivyosema. Hivyo basi, kilichonileta hapa usiku wote huu ni kukwambia kuwa nakupenda sana, na nataka tufanye walau mara hii moja tu kiu yangu ikatike, naomba." Milka aliendelea kusema huku akiwa anatetemeka japo wakati huu sauti yake haikuwa ikitetemeka. Wakati akiongea akawa anamalizia kuvua blauzi toka mwilini mwake. Maganga akajishika kiuno huku macho yake yakiwa yanauangalia mwili mbichi wa mdogo wake. Japo alikuwa haamini kinachotokea lakini, aliendelea kuutalii mwili wa mdogo wake. Alijikuta yuko katikati ya maamuzi. Milka alikuwa amebaki kama alivyozaliwa, akaanza kumsogelea kaka yake, Maganga akaingiwa na huruma iliyochanganyika na tamaa. Wazo kuwa yuko ndotoni likamjia, hakutaka kuamini kuwa jambo lilokuwa linatokea mbele yake lilikuwa ni kweli. Akajaribu kujifinya ili aamke, lakini akajikuta kuwa Milka yuko karibu yake zaidi, wakati huu akaanza kuisikia harufu ya mwili wa Milka. Damu ya mwili wake ikaanza kukimbia kwa kasi mwilini. Mawazo kuwa alikuwa ni Padri mtarajiwa na wakati huu alikuwa kwenye nyumba ya kanisa kama Padri mwanafunzi yalishaondoka kichwani mwake. Lakini hata hivyo ghafula akamudu kusema,“Milka, hebu subiri kwanza mdogo wangu!” Alisema kwa hadhari huku akipepesa macho.

    “Kaka Maganga, najua si halali, lakini sina namna nyingine ila kufanya hivi.”

    “Unakosea mdogo wangu na kamwe siwezi kukubaliana na hili.” Maganga alisema.

    “Sogea hapa ili unione vizuri.” Milka alisema kama anayenong’ona.

    “Kaka Maganga, kwani nina kasoro gani au upungufu gani kwenye huu mwili wangu?” Milka alihoji huku safari hii machozi yakiwa yanamtoka tena.

    “Milka na...” Kauli ya Maganga ilikatishwa na sauti ya mlango kugongwa. Mlango wa nje uligongwa tena!
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakuna aliyeitikia, walitazamana. Mlango ulipogongwa mara ya tatu, wote wakatazamana tena. Akili ya Maganga ikafanya kazi haraka haraka, hakuwa na hakika mgongaji angekuwa nani na alikuwa anataka nini. Hivyo alimsogelea Milka, akamnong’oneza, “Baki hapa, sina hakika atakuwa nani. Haitakuwa picha nzuri akikukuta hapa ukiwa katika hali kama hiyo. Unajua miye ni nani na Kanisa linanichukuliaje. Mbona wanifanyia hivi Milka mdogo wangu? Halafu usisahau wewe ni mdogo wangu pia”

    Wakati Maganga ananong’ona alikuwa jirani sana na Milka, zile pumzi za Maganga sikioni kwa Milka, na ile hisia ya ukaribu ikamfanya Milka amkumbatie Maganga. Miili yao ikakutana. Maganga akaweza kusikia jinsi mwili wa Milka ulivyokuwa wa moto utadhani hakuwa amenyeshewa mvua. Vitu kama umeme viliamsha mishipa yake ya mwili.





    Wakati akiwa amechanganyikiwa hajui nini cha kufanya huku Milka akiwa anafanya vitu ambavyo Maganga hakuelewa vina lengo gani, mlango wa sebuleni uligongwa tena, safari hii kwa fujo zaidi. Maganga akatumia nguvu zilizobaki mwilini, kumsukuma Milka. Milka akaangukia kitandani, Maganga akatoka chumbani kuelekea sebuleni. Milka akabaki kitandani, ameduwaa. Sasa mgongaji alikuwa amekazana kugonga.

    “Nani na unataka nini usiku huu?” Hatimaye Maganga aliuliza.

    “Paul.” Sauti nzito ilijibu. Maganga mara moja akaitambua sauti hiyo kuwa ni ya baba yake mzazi. Kwanza alichanganyikiwa, lakini akajipa moyo kuwa hakuna baya lilikuwa limefanyika. Ila akajiuliza baba alikuwa anatafuta nini pale usiku huo.

    “Ooooh! baba karibu sana. Kuna nini mbona usiku sana kiasi hiki?” Alitoa karibu iliyoambatana na swali huku akifungua lango. Alijitahidi kuweka akili yake sawa.

    “Imebidi nije tu, maana nimeona asubuhi ni mbali sana.” Alisema Mzee Paul baba kwa sauti nzito iliyojaa kitu kama ghadhabu huku akiwa anaketi kitini.

    “Kuna nini baba?” Maganga alihoji. Maganga aliwasha taa ya sebuleni ambayo hakuwa ameiwasha kipindi Milka alipokuwa amekuja. Mzee Paul alianza kuzungusha macho pale sebuleni baada ya kuwa ameweka pembeni mwamvuli aliokuwa ametumia kujikinga mvua ambayo bado ilikuwa ikiendelea kunyesha. Macho ya Mzee Paul yaliweza kuona alama za miguu pale sebuleni, tena uzoefu wake ulimwambia kuwa ilikuwa alama ya miguu ya kike. Hakutaka kuuliza wala kufuatilia sana, hakutaka kugombana na Maganga, maana aliweza kuona zile nyayo zikiwa zimelekea chumbani. Aliweza kuona kwa vile mwenye nyayo alikuwa ameloana. Si hivyo tu aliweza pia kuona khanga na sketi vilivyokuwa vemelala pale sakafuni. Moyo ulimwenda mbio. Hakutegemea mwanawe ameshaanza mambo ya wanawake. Maganga alikuwa mtu mzima sasa lakini kwa jinsi alivyolelewa kidini na ambavyo Paul amekuwa akihakikisha anakuwa Padri, ilikuwa hakika Maganga hakuwa mtu wa wanawake. Hali hii sasa ilikuwa inampa ujumbe mpya.

    “Sikiliza Maganga, nimegombana sana na mama yako, nimemwacha huko nyumbani akiwa katika hali mbaya…”

    “Tatizo nini baba?”

    “Tatizo ni lile lile Maganga.”

    “Lipi hilo? Maana kama ni kuhusu mimi na Milka nadhani tulishakubaliana na limekwisha.”

    “Halijaisha mwanangu, mama yako bado hajakubali wewe kuwa Padri na Milka kuwa Sista wa kanisa. Madai yake ni kuwa anataka awe na wajukuu. Yuko radhi mmoja wenu aendelee na wito wa kanisa lakini si nyote…”

    “Lakini baba sijaelewa hilo limesababishaje ninyi mpigane usiku huu?” Maganga alizidi kuhoji.

    “Kama ujuavyo dada yako Milka yuko hapa kwa mapumziko toka kwenye shule ya Utawa. Tangu amefika kuna mambo yamekuwa yakifanyika kati ya Milka na mama yako ambayo kwa kweli miye siyaelewi au kama nayaelewa basi siko radhi nayo. Ni wazi kuwa mama yako yuko tayari Milka aolewe wakati wowote. Hivi ninavyoongea na wewe Milka hayupo nyumbani, na ugomvi wetu ndiyo umeanzia hapo. Tangu saa tatu usiku nimekuwa nikimuuliza mama yako ili nijue mahali alipokuwa Milka, akawa ananiambia yuko kwa rafiki ake hapa Kijijini. Imeendelea hivyo hadi ilipofika saa saba usiku huu, nilipomuuliza mama yako, akaniambia Milka ni mtu mzima ana uhuru wa kufanya aonalo jema. Hapo ndipo ugomvi wetu ulipoanzia.” Mzee Paul alisema huku akionyesha hasira kuu.

    “Baba, umesema mama ana hali mbaya nadhani, twende tukamwone kwanza, tumpeleke hospitali halafu haya mengine tutaongea kesho.”

    “Maganga, naomba uongee na mama yako, ajue kuwa siwezi kubadili msimamo wangu na kwa hili niko tayari kulipa gharama yoyote.” Alisema mzee Paul huku akiwa anainuka toka kitini alipokuwa ameketi. Maganga aliingia chumbani akavaa shati kisha akatoka akiwa na ile ile Kaptula aliyokuwa nayo alipompokea Milka. Mwamvuli mkononi, hakutaka kupoteza muda zaidi. Wakatoka nje na safari ya kuelekea nyumbani ikaanza huku mvua ikiendelea kunyesha.

    Walipofika nyumbani Maganga aliingia ndani na kupitiliza hadi chumbani ambako mzee Paul alikuwa amemwacha mkewe akiwa hajiwezi kwa kipigo. Kwa mshangao, hakukuta mtu yeyote chumbani humo. Walijaribu kuangalia kila kona.

    “Mama ni miye mwanao Maganga, nimekuja, usijifiche, nataka nikupeleke hospitali.” Maganga alipiga kelele akihofia kuwa huenda mama yake alikuwa amejificha kwa woga wa kipigo. Dakika kadhaa zilipita wakiwa wanatafuta bila mafanikio.

    Dakika thelathini zilizofuata zikawa za kutafuta na kuuliza kwa majirani kama mke wa Mzee Paul alikuwa huko. Saa nzima ilipita na walikuwa wameshazunguka kijiji kizima bila mafanikio.

    “Mwanangu, nenda kapumzike, usije pata matatizo hapa nikashindwa namna ya kumjibu baba Askofu, kumbuka wewe sasa ni Padri mtarajiwa na sherehe yako ya upadirisho ni mwezi ujao.” Mzee Paul alimwambia Maganga kwa sauti nzito ya kubembeleza. Lakini sauti hiyo ilikuwa kama radi masikioni kwa Maganga na mkuki wa moto katika moyo wake. Hakutegemea baba yake angeongea hivyo katika wakati huo ambao mama yake mzazi ambaye ni majeruhi kwa kipigo ikiwa haijulikani alipo. Maneno hayo yalimuumiza moyo wake. Alitembea taratibu kuelekea ilipokuwa nyumba yake ambayo alikuwa amepewa na Kanisa. Moyo wake ulikuwa umekufa ganzi kwa simanzi, na akili yake ilikuwa imejaa wasiwasi. Aliomba kimoyo moyo kuwa Mungu amlinde mama yake popote alipo.

    Alipofika nyumbani kwake, alifungua mlango akaingia. Mara hii ndiyo akakumbuka kuwa alikuwa amelowa chepechepe, hakukumbuka mwamvuli wake alikuwa ameuacha wapi. Alipoingia chumbani ndipo tena alipokumbuka kisa cha Milka baada ya kuona mtu amelala kitandani akiwa amejifunika blanketi. Alimwangalia kwa sekunde kadhaa bila kusema neno. Alifikiria kuwa kwa hali ilivyo isingekuwa busara kumwambia Milka aende nyumbani. Hivyo alikata shauri kumwacha Milka alale hapo kwake kwa ajili ya usalama. Maana kama Milka angetokea mbele ya Mzee Paul saa hizi, angemfanya kitu kibaya sana.

    “Milka, umesikia habari ya mama na baba?” Maganga aliuliza kwa sauti iliyotoka kwenye koo lililokuwa limeshambuliwa na baridi.

    “Nimesikia yote.” Milka alijibu huku akijinyonga nyonga ndani ya blanketi.

    “Umesikia?” Maganga alishangaa.

    “Ndiyo!”

    “Mbona huonekani hata kushtuka Milka.” Maganga alihoji kwa sauti ya mshangao.

    “Nilishituka wakati baba anaongea kukutaarifu, ila kwa sasa najua mama yuko salama sina shida.”

    “Yuko salama! Kivipi wakati tumetafuta kijiji kizima hatujafankiwa kumpata?”

    “Baba alivyosema amempiga mama, mara moja niliwasiliana na Vivian, yule rafiki yangu anayesomea utabibu Ujerumani, ambaye kwa sasa yuko likizo, kama mimi, akaenda kumchukua mama na amempa huduma tayari kwa hivyo mama yuko salama.”

    “Nadhani tulale sasa Maganga, acha kujikunyata hapo baridi.” Milka aliongea kisha ghafla akaruka toka kitandani akamrukia Maganga...





    Maganga hakutarajia, hivyo mwili wake ukawa himaya ya Milka kwa sekunde kadhaa kabla hajatumia nguvu kujinasua na kumsukuma Milka pembeni.

    “Hivi Milka umeingiwa na nini?” Maganga alihoji kwa hasira, “Huko kwenye mafunzo ya Utawa ndiyo mnafundishwa hivyo?” Aliongeza swali ambalo lilijibiwa kwa tabasamu tu toka kwa Milka. Maganga alimwangalia Milka kwa upya tena safari hii akawa kama anayekiona kwa upya kila kiungo cha mdogo wake, kisha akakumbuka ule mwili wa moto uliomkumbatia kwa sekunde chache kabla hajausukumia mbali. Akainamisha macho chini kukwepa macho ya Milka ambayo safari hii yalikuwa kama yanamsoma baada ya kugundua jinsi alivyokuwa anauangalia mwili wake.

    * * *

    Katika Maisha yake yote, Maganga hakuwahi kukutana na mtihani kama huu uliokuwa mbele yake. Akiwa na umri wa miaka takribani ishirini na tisa, Maganga alikuwa muadilifu mno kuweza kumtongoza msichana na alikuwa mwaminifu sana kuweza kufikiria kitu kama hicho. Wakati huu sasa, kufuatia vituko alivyokuwa amefanyiwa na Milka mbele ya macho yake, aliweza kuhisi dhahiri jinsi moyo ulivyokuwa ukimwenda mbio. Kadiri alivyokuwa akiungalia mwili wa dada yake macho yake yakawa kama yanakosa nguvu zake za kawaida. Alisikia kama nguvu zinaongezeka mishipani na damu inakimbia kwa kasi. Mambo mengi yakamjaa akilini mwake. Uwezo wa kutafakari mambo kwa kina ukaanza kupungua. Ni kweli ilikuwa imebakia mwezi mmoja tu apate upadirisho, kitu ambacho si tu kuwa alikuwa anakipenda sana, ila anajua fika hiyo ndiyo zawadi pekee ambayo angeweza kumpa baba yake katika maisha yake. Baba yake, Mzee Paul, hakuna kitu alikuwa anasubiri kama kuona mwanae amekuwa Padri. Alishamsikia baba yake akisema mara kadhaa kuwa siku mwanawe akiwa Padri na yeye akishuhudia tukio hilo kwa macho yake, basi ni siku ambayo atakuwa tayari kusubiri kifo chake.

    Si kwamba Maganga alipenda kuwa Padri, ila alijikuta akichukua njia hiyo kwa shinikizo la baba yake ambaye amekuwa Kateskista kwa muda mrefu sasa. Kazi yake ya uanajeshi aliyoifanya akiwa kijana na kuicha katika mazingira ya kutatanisha haikumfanya asahau kuwa karibu na kanisa. Maganga alimwangalia Milka, safari hii ile hali ya kuwa ni dada yake ikawa inaanza kufifia, kikubwa ikawa anafikiria kuwa hajawahi kufanya jambo lile. Hivyo akawa anajiuliza atafanyaje. Tofauti na Mzee Paul alivyokuwa akimdhania Maganga kuwa hakuwa mpenda wasichana, jaribu kubwa la Maganga siku zote ni pale anapokutana na wasichana wazuri. Mwili wake umekuwa ukimpeleka kasi sana na mara kadhaa amekuwa akijiridhisha mwenye kitandani. Hivyo huu ulikuwa ni zaidi ya mtihani kwake, hakuwahi kuwa karibu na msichana chumbani namna hii.

    Milka akawa amemsoma kaka yake, maana kwake hayo mambo hayakuwa mageni. Kama kaka yake, Milka alishinikizwa na Mzee Paul awe mtawa, jambo ambalo si kwamba lilipingwa na yeye tu bali hata mama yake hakuafikiana nalo. Hivyo akajikuta ameingia kwenye mafunzo ya utawa bila ridhaa yake. Lakini kwa vile haikuwa hiari yake, Milka akajikuta mchezo wa kutembea na wanaume umeshamkolea mwilini na akilini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Milka alisimama taratibu akasogea pale alipokuwa amesimama kaka yake. Akasogeza mkono wake akaushika ule wa kaka yake ambaye wakati huu alikuwa anatetemeka.

    “Milka kwa nini unafanya hivi?” Maganga alihoji kikondoo kwa sauti ya kutetemeka, huku akishindwa kupinga mkono wake usinyanyuliwe na Milka.

    “Maganga na….” Milka hakumalizia, kengele ya saa iliyokuwa juu ya meza pembeni mwa kitanda cha Maganga ililia, hiyo iliashiria kuwa saa kumi na moja alfajiri. Wakati huo huo wakasikia mlango ukigongwa. Maganga alichomoa mkono wake toka kwa Milka, akapiga hatua kuelekea mlango wa kutoka chumbani. Huku moyo wake ukiwa unapingana vikali na uamuzi wa akili yake kuamua kuachanisha mkono wake na ule wa Milka, ilikuwa burudani jinsi joto la Milka lilivyokuwa likipenya kupitia kwenye ule mkono. “Miye ni mwanaume, natakiwa kuitii akili zaidi kuliko moyo, we always use logic rather than feelings.” Maganga alijiwazia kuipa nguvu akili yake katika maamuzi yake yaliyokuwa yakipingwa na moyo.

    “Karibu!” Alijibu huku akifungua mlango, safari hii hakuuliza kujua mgongaji alikuwa nani. Maana ilikuwa alfajiri tayari.

    “Aaaaah Vivian, karibu ndani.” Maganga alisema.

    “Mmmmh asante, miye naogopa kuingia nyumba ya Padri mtarajiwa akiwa pake yake nisije nikamtia majaribuni.” Vivian alisema kwa kutania lakini uso wake haukuonyesha hivyo.

    “Maganga hali ya mama yako si nzuri, hivyo amenituma nije nikuite uende haraka.” Vivian alibadili mada haraka na ujumbe ulithibitisha kile uso wake ulikuwa ukionyesha. Maganga hakutaka kusubiri, alitoka nje na kufuatana na Vivian. Hakukumbuka kufunga mlango wala kumuaga Milka ambaye wakati huo alikuwa bado ndani.

    “Vivian kwanza nashukuru kwa kukubali kumhudumia mama yangu. Unataka kuniambia mama ameumia sana?” Maganga alihoji baada ya kushukuru.

    “Maganga, siwezi amini kama baba yako ndiye aliyefanya kitendo kile, labda kwa vile aliwahi kuwa mwanajeshi. Amempiga mama kama mtu aliyekuwa anapiga nyoka aliyeingia ndani!” Vivian alisema kwa sauti ya mshangao. Wakati huo walikuwa wameshafika nyumbani kwa akina Vivian. Vivian ni binti anayetoka katika moja ya familia zenye uwezo pale kijijini, kwa kifupi ndiyo familia tajiri zaidi. Haikuwa ajabu kwa Vivian kuwa anasoma Ujerumani. Wakati huu wazazi wake walikuwa wamekwenda mapumzikoni Brazil, alitakiwa awepo kwenye msafara, ila alikataa. Sababu kubwa ya kukataa aliwaambia wazazi wake kuwa amewakumbuka rafiki zake pale kijijini na angejisikia vema kama Krismas angekula akiwa pale nyumbani. Hivyo wakamwachia nyumba wakaenda zao Brazil.

    Vivian na Milka ni marafiki tangu utotoni wakiwa majirani Dar es salaam, wakati huo wazazi wao wote wakiwa wanajeshi kwenye kambi ya Ruvu. Urafiki wao ulichangiwa na mambo mengi. Wakiwa wadogo Vivian na Milka walikuwa wakicheza pamoja. Ki-umri wote walikuwa sawa, Milka alikuwa pacha wa Maganga, japo Maganga ndiye Kulwa. Kingine ni kuwa watu hawa walizaliwa siku moja katika hospitali ya Bugando mjini Mwanza. Japo wakati wanazaliwa wazazi wao walikuwa ni Askari jeshi katika chuo maalumu cha kijeshi Monduli. Ambapo baadaye wote walihamishiwa Ruvu na kibahati-bahati wote sasa wanaishi katika kijiji hiki. Hili limekuwa likiwashangaza lakini wamekuwa hawana majibu kwa nini imewezakana wao kuwa wakihamia sehemu moja kila mara. Tofauti yao kubwa kimaisha ilitoka na ukweli kuwa baba yake Vivian alikuwa ni Daktari Mwanajeshi, hivyo amekuwa akijipatia hela nyingi kwa kazi ya utabibu ambapo kiinua mgongo chake alitumia kufungua hospitali binafsi. Hata walipoanza shule, Vivian alipelekwa shule ya misheni ambayo walikwenda watoto wa watu waliokuwa na uwezo pale kijijini ambao pia walichanganyika na watoto wa kizungu wa wamisionari waliokuwa katika kanisa Katoliki pale kijijini.

    Walipoanza kukua, licha ya kumpenda Milka, Viviana alijikuta anaanza kuvutiwa na kaka yake Milka yaani Maganga. Hilo likawa limetia mafuta katika urafiki wao, nyumbani kwao na Milka kukawa na harufu nzuri kwa Vivian kama ile ya ua zuri puani kwa nyuki. Kila mara Vivian alijikuta akiwa nyumbani kwa akina Milka ili walau awe anamwona tu Maganga, hata kama asingeweza kuongea naye. Hii ilidhihirisha kuwa Mbegu haichagui pa kuota

    “Karibu ndani Maganga, tafadhali usivue ndala, kuna baridi sana wakati huu haifai kukanyaga sakafu, simenti ni ya baridi sana.” Vivian aliongea kwa sauti iliyojaa ukarimu, ndala za Maganga zilikuwa na matope hivyo hakukubaliana na wazo la yeye kuingia na ndala. Akazivua mlangoni na kuingia ndani. Wakaingia chumba alichokuwa mama yake.

    “Oooooh mama yangu!” Maganga alisema baada ya kuuona uso wa mama yake. Uso wake ulikuwa umeharibika vibaya kama vile gari ndogo iliyogongana na gari kubwa ya mizigo. Pua yake ilikuwa imevimba vibaya kama gari iliyofunguliwa boneti yake ya mbele. Macho yake yalikuwa yamevimba kiasi kuwa hakuwa anaweza kuyafungua.

    “Siwezi amini kama baba yangu ndiyo amemfanyia mke wake kitu kama hiki...” Maganga alisema huku akiwa ameinama kumkumbatia mama yake ambaye alisikika akipumua kwa shida.

    “Maganga, nadhani tumpeleke mama hospital ya Wilaya Sengerema huko anaweza kupatiwa matibabu zaidi maana hali yake inatia shaka sana, gari ina mafuta ya kutosha. Tusipoteze muda zaidi.” Vivian alisema huku akitoka na kuelekea chumbani kwake. Kwa Vivian ilikuwa ni huzuni lakini pia ilikuwa ni nafasi ya kumwonyesha Maganga ni kiasi gani alivyo msichana anayejali. Alikusudia kutumia nafasi hiyo kujiweka jirani na Maganga na ikiwezekana kupata muda wa kuwa naye na kumzoea.

    “Haya tusipoteze nafasi tumbebe, tumpeleke kwenye gari.” Vivia alisema wakati huu alirudi toka chumbani akiwa tayari kwa safari.

    “Sawa.” Maganga alisema kwa sauti ambayo alijishangaa kama ilikuwa yake. Wakati wanambeba ndipo mama yake Maganga alijaribu kusema kitu, alipokufungua mdomo wake ndipo Maganga akaweza kuona jinsi kinywa chake kilivyokuwa kimeharibiwa vibaya. Maganga nguvu zikamwishia chozi likamdondoka. Vivian alimkaribia Maganga, akamshika mabegani na kumpigapiga katika ile hali ya kumbembeleza.

    “Jikaze Maganga wewe mtoto wa kiume, mama yako anakuhitaji sasa, fanya tumpeleke hospitali.” Sijui kama ndo maneno ya Vivian yalifanya kazi au Maganga alijikaza tu, maana aliinuka wakambeba mama yake kwenda nje. Walimwingiza kwenye gari, wakaingia kisha Vivian akalitia gari moto. Ni wakati wanataka kuondoka, waliona mkono unagonga kioo cha dirisha la nyuma. Wote wakageuka kuangalia. Mzee Paul alikuwa amesimama nje ya gari, macho yamemtoka huku akitetemeka kwa hasira. Maganga akafungua mlango ili kumkabili baba yake ambaye tayari alikuwa ameanza kutukana pale nje ya gari.

    “Maganga, unaonaje kama tukienda tu, najua hawezi kufukuzana na gari.” Vivian alisema huku mkono wake wa kushoto ukiwa shingoni kwa Maganga unamminyaminya katika hali ya kumtuliza.

    “No, this is too much Vivian, its unacceptable…” Maganga alisema huku akifungua mlango. Kabla hajamaliza kufungua mlango, sauti ilisikika toka kiti cha nyuma walikokuwa wamemlaza mama yake Maganga.

    “Maganga mwa mwa mwa ma ….na nangu, nyu..nyu....nyumbani, chi…chi….chi…..oooh aaaah…chini…..ya…..ya…ya…..mtungi…..wa…..maji……chimba……usome siri…Zingatia sana…. Kauli ya mama yake na Maganga haikwisha mlango wa upande wa dereva ulivutwa. Mzee Paul alimvuta Vivian na kumsukumia kofi kali la usoni. Kuona hivyo Maganga alitoka nje ya gari kama Swala aliyekurupushwa mafichoni na mwindaji. Alienda ule upande aliokuwa Mzee Paul na Vivian. Vivian alikuwa akilia kwa sauti wakati huo.

    “Baba huwezi kufanya hivyo, hivi wewe ni mtu wa namna gani usiyekuwa na hisia. Mbona una moyo wa shaba na akili za gundi?”







    Maganga alisema huku akimvuta baba yake amwachie Vivian. Kweli alifanikiwa. Vivian alikurupuka, akakimbilia kwenye gari na kuliondoa kwa kishindo huku akiacha watu wakiwa wanakimbilia eneo la tukio. Vivian hakusimama akatokomea. Mzee Paul alijizoa zoa pale chini, akamwangalia Maganga kwa jicho kali huku mikono, midomo na pua zikitetemeka kwa hasira. Maganga alimwangalia baba yake kwa jicho la kukata tamaa na uso ulioshuka. Wakiwa wanatazamana hivyo mara Milka akatokea.

    “Na wewe mjinga utaniambia ulikuwa wapi, muda wote huo…wewe ndiye chanzo cha haya yote.” Mzee Paul alisema huku akimfuata Milka. Milka alisimama huku akitetemeka kwa hofu, alishahisi hatari mbele yake, lakini kwa wakati huo hakuwa na namna ya kujitetea, alikuwa kama Kinyonga aliye katikati ya barabara mbele ya gari lijalo kwa kasi. Aliuanda mwili wake kupokea kipigo. Mzee Paul alimfikia Milka, wakati anajiandaa kutoa kipigo mara akasikia sauti inaita.

    “Mzee Paul!” Ilikuwa ni sauti anayoifahamu na kuiheshimu kuliko sauti ya mtu yeyote pale kijijini. Nguvu za kupiga zikaisha, akatamani yale mambo yasingekuwa yanatokea muda ule ambapo Askofu alikuwa ameingia eneo lile.

    “Naam baba askofu!” Alijibu kwa heshima zote kama si yule aliyekuwa anakwenda kutoa kipigo kwa manawe wa kike na aliyekuwa ametoa kipigo kikali kwa mke wake usiku. Watu walikuwa wameshajaa aneo la tukio, wakubwa kwa wadogo, wanawake kwa wanaume. Baridi ilikuwa kali sana. Maganga alipomwona Askofu Alphonso ndipo alipokumbuka kuwa kumbe alikuwa amevaa kaptula na miguu yake ilikuwa imechafuka kwa tope huku shati lake likiwa lina matone ya damu yaliyosalia wakati anambeba mama yake. Alijiona kama yuko uchi, familia iliyotakiwa kuwa mfano sasa ilikuwa balaa. Alimwangalia dada yake akamwonea huruma kwa jinsi alivyokuwa amesimama. Alienda hadi alipokuwa amesimama akamkumbatia. Milka akaangusha kilio cha uchungu.

    **********

    MKONO WAKE WA KULIA ulikuwa ukichezea kifua cha msichana huyu ambacho wakati huu kilikuwa wazi na kufanya mwonekano mzuri uliodhihirisha kuwa alikuwa bado ni msichana mdogo sana na aliyejaaliwa uzuri wa kutosha, lakini mkono wa kushoto wa mwanaume huyu ulikuwa umeshikilia sigara ambayo ilikuwa ikiteketea taratibu bila kuvutwa. Wote walikuwa wameridhika na kitu walichokuwa wamekifanya hapo kwa masaa kadhaa. Wakati huu kila mmoja alikuwa kwenye ulimwengu wake baada ya kutoka kwenye ule wa pamoja ambao, Hellen alikuwa akilia kwa raha aliyokuwa akiipata na Machumu alikuwa akigugumia kwa sauti yake ya kiume kutokana na utamu aliokuwa akihisi. Walikuwa wameingia katika hoteli hiyo iliyoko uswahilini kabisa mwa jiji la Dar es salaam maeneo ya Sinza Kumekucha, majira ya saa tatu asubuhi. Walifanya kile walichotaka na sasa walikuwa wanapumzika huku kila mmoja akiwa anawaza lake.

    Siku nne zilizopita Hellen alikuwa ametimiza umri wa miaka ishirini na moja. Hakuwa mwanafunzi, hakuwa mfanyakazi, hakuwa anaishi na wazazi, hivyo mishemishe za mjini zisizo na majina wala mahali maalum ndiyo ilikuwa mpango wake. Kwa kifupi alikuwa akifanya kazi zisizo maalum ila na watu maalum. Tofauti na wasichana wengine waliokuwa wakijiuza kwa bei chee maeneo hayo ya Sinza kumekucha, yeye alikuwa wa watu maalum. Uzuri wake, umri wake na dalali wake vyote kwa pamoja vilimfanya asiwe wa bei nafuu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maisha yake haya yalianza siku ile aliposikia mama yake na baba yake kwa mara ya kwanza wakigombana chumbani. Mwanzoni hakujua chanzo cha ugomvi lakini baadae alikuja kugundua kuwa chanzo ilikuwa ni yeye. Maana alisikia baba yake akisisitiza kuwa kama kweli yeye ni mwanae basi waende wakapime vinasaba na ijulikane. Hilo ndilo lilopelekea yeye na mama yake kufukuzwa nyumbani na mtu ambaye yeye aliamini kuwa alikuwa ni baba yake.

    Maisha yao mtaani hayakuwa rahisi, mama yake alifanya kila awezalo ili kunusuru maisha yao. Lakini katika kufanya kila awezalo akajikuta anaishia kwenye UKIMWI na kumfanya Hellen abaki peke yake. Baada ya kifo cha mama yake, Hellen hakuwa na namna ya kuishi hivyo akajikuta analazimika kutafuta namna. Kazi pekee aliyokuwa anaifahamu ni ile aliyomwona mama yake akiwa anafanya ni kuuza mwili wake. Na yeye akaanza. Huyu ndiye Hellen ambaye alikuwa amejilaza kwenye chumba cha hoteli hii ya Gwama iliyoko Sinza Kumekucha.

    “Machumu nadhani wakati umefika wa mimi kwenda Mwanza na kuujua ukweli kunihusu.” Hellen alisema huku akichezea misuli iliyokuwa imefungamana kifuani kwa Machumu.

    “Mbona kama maamuzi yako hayo yamekuja ghafla sana, kuna tatizo lolote?” Machumu aliuliza huku akiachia kipande kifupi cha sigara iliyokuwa bado inateketea mkononi kidondokee kwenye sahani ya sigara iliyokuwa jirani na kitanda walichokuwa wamelalia.

    “Wiki hii nimekuwa nikiota ndoto za ajabu ajabu tu na moyo wangu umekuwa mzito sana, nadhani natakiwa niende nikajue ukweli kuhusu mimi. Mama alinisisitiza sana katika dakika zake za mwisho kuwa lazima niende katika Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza kuna mtu nikaonane naye.” Alisema Hellen huku akijiinua toka pale kitandani. Alielekea bafuni huku nyuma macho ya Machumu yalikuwa yakimsindikiza na kuhusudu jinsi msichana huyo alivyokuwa ameumbika. Machumu alimeza mate, huku hamu ya kufanya tena ikiwa imeshamjaa. Alimfuata Hellen bafuni huko wakaanza tena. Kwa vile wote walikuwa mafundi, wote walikuwa na uwezo, mchezo wao ulikwenda vema. Vilio na miguno ya raha na utamu vikasikika tokea bafuni.

    * * *

    Saa kumi na mbili na dakika tano ya siku iliyofuata ilimkuta Hellen akiwa ameshakaa kwenye kiti cha basi la Zuberi tayari kwa safari ya kuelekea Mwanza. Kiu ya kutaka kujua chimbuko lake ilimzidi na hivyo kuyashinikiza maamuzi yake, maamuzi yalitii na akakata shauri aende.

    Walifika Mwanza kituo cha mabasi Nyegezi majira ya saa tatu na robo usiku. Hapo alikodi taxi iliyompeleka hadi hoteli Lakairo maeneo ya Kirumba. Siku iliyofuata majira ya saa kumi na mbili na nusu tayari alikuwa ameshafika kwenye kivuko cha Kamanga Feri, huku akiwa ameshakata tiketi kweye basi la Nyehunge Express. Kutoka Kamanga Feri upande wa Mwanza mjini hadi Kamanga Feri upande mwingine iliwachukua kama dakika kumi na tano wakiwa majini. Ambapo safari ya kwenda Wilaya ya Sengerema ilianza.

    “Konda, miye siyo mwenyeji sana maeneo haya ila nashukia sehemu inaitwa Katunguru.” Hellen alimwambia konda wakati basi likiwa limeshatoka kwenye kivuko na kuanza safari. Safari yao ilichukua saa moja na nusu hadi pale konda alipomwambia Hellen kuwa sehemu aliyotakiwa kushuka ilikuwa ni kituo kinachofuata. Kwa vile mabasi yalikuwa yanafukuzana, ilitakiwa asogee mlangoni ili wasipoteze muda mwingi kituoni.

    Aliposhuka kituoni ilikuwa tayari saa tatu kasoro dakika ishirini na moja.

    “Habari za leo kaka?” Hellen alisabahi.

    “Nsuri tu dadayango, pole na safali!” Alijibu kijana huyo kwa ile lafudhi ya Kisukuma ambapo kwenye 'r' wao huweka 'l' huku wakiwa wanakandamiza maneno.

    “ Samahani, nahitaji kwenda sehemu inaitwa madukani.” Hellen alisema baada ya kuwa amesoma maelekezo toka kwenye kitabu chake cha kumbukumbu.

    “Aaaha, haina shida tu, nenda pale, chukua baiskeli mwambie akupeleke, ni kama nusu saa hivi kufika kule”.

    “Haya asante!” Hellen alisema huku akijifunika mtandio, mvua ilikuwa ikinyesha sana tangu walipotoka Mwanza. Alishukuru kwani hapo mvua likuwa imeshaacha kunyesha japo kulikuwa na tope jingi.

    Alipofika madukani, Hellen aliulizia kwa Mzee Paul, akaelekezwa. Hapo tena akachukua mtu wa baiskeli ampeleke. Haikuwa mbali sana toka madukani.

    “Hapa ndiyo kwa Mzee Paul.” Mwendesha baiskeli alisema walipokuwa wamefika kwenye nyumba moja iliyokuwa imezungukwa na michungwa mingi. Hellen alishukuru baada ya kuwa amelipa. Hapo aliusogelea mlango wa hiyo nyumba, aligonga kwa muda mrefu bila majibu mpaka pale mtu mmoja alipopita na kumwambia Mzee Paul alikuwa nyumba ya tano toka hapo japo kulikuwa na ugomvi.

    “Ugomvi wa nini tena?”Hellen alihoji.





    “Ugomvi wa kifamilia wewe nenda ukaone.” Alisema huyo mzee huku akionyesha kutotaka kuongelea zaidi habari hiyo. Alimwelekeza sehemu ambayo angempata Mzee Paul, nyumbani kwa akina Vivian. Alipofika umati wa watu ndiyo ulikuwa unatawanyika, huku Maganga na Milka nao wakiwa wanaondoka eneo hilo. Njia aliyokuwa anakuja nayo Hellen ndiyo njia ambayo Maganga na Milka walikuwa wakija wanatembea taratibu wakiwa wamejaa majonzi yaliyochanganyika na hasira kufuatia vitendo vilivyoonyeshwa na baba yao. Walikutana na Hellen, mara ya kwanza walipomwona wote walidhani ni Vivian. Maana msichana aliyekuwa hatua chache akija mbele yao alifanana kila kitu na Vivian ambaye waliongea naye dakika chache zilizopita akawahakikishia kuwa alikuwa amefika salama hospitali na kuwa mama yao alikuwa ameshaanza kutibiwa. Wote wakashikwa na bumbuwazi jinsi msichana huyo alivyofanana na Vivian. Walipokaribiana, wakasalimiana huku kila mmoja akiwa kajikunyata.

    “Habarini za asubuhi?” Hellen alisabahi.

    “Nzuri.” Maganga na Milka wakajibu.

    “Je tunaweza kukusaidia, maana unaonekana mgeni hapa kijijini?” Maganga aliongeza huku akijilazimisha kutabasamu.

    “Ndiyo, naitwa Hellen, namuulizia bwana mmoja anaitwa Paul, nimepita nyumbani kwake kuna mtu akaniambia yuko upande huu...na ....halafu...” Hellen akasita huku akijaribu kutafuta maneno.

    “Oooh wala usijali, bila shaka Mzee Paul utampata tu dada yangu. Miye naitwa Maganga....”

    “Na miye naitwa Milka...” Milka akadakia kwa sauti ya kutetemeka kutokana na baridi. Ilikuwa inaelekea saa sita mchana, lakini kutokana na hali ya mawingu na mvua iliyokuwa imenyesha usiku na mapema asubuhi ungedhani bado ni saa moja asubuhi.

    “Siye ni watoto wa huyo Mzee Paul unayemtafuta...” Maganga akasita kisha akaendelea.

    “...kwa sasa ametoka na nadhani atachelewa kurudi, basi karibu ukapumzike wakati tukimsubiri.” Maganga alisema huku akijitoa kwenye mkono wa Milka uliokuwa umemshika kwapani na kuomba mzigo wa Hellen. Hellen alimkabidhi Maganga begi lake dogo alilokuwa amekuja nalo. Walitembea kimyakimya hadi walipofika nyumbani kwa Maganga. Wote wakaingia ndani.

    “Karibu sana Hellen hapa ni nyumbani kwangu, jisikie uko nyumbani. Karibu kiti ukae...” Maganga alisita, wakati anamwonyesha Hellen akae kwenye kochi upande wa kulia mwa sebule, ndipo macho yake yalipogongana na ushungi ukiwa sakafuni jirani na kochi hilo.

    Wote watatu waliviangalia, Milka akajikausha maana alitambua kuwa ile ilikuwa nguo yake, alisahau kuichukua alipotoka. Jukumu likabaki kwa Maganga.

    “Daaah!, jamani wamama wa kazi hawa, sasa ndiyo mambo gani haya inamaana alivyomaliza usafi hakuweza kuona hii kitu yake...” Maganga alijitia kudanganya, alidanganya kijinga, hakuwa amezoea kudanganya. Milka na Hellen waligundua jinsi Maganga alivyobabaika.

    “Aaah!, huwa hawako makini wale..ha ha ha.” Hellen alisema huku akijilazimisha kucheka. Milka alichukua zile nguo na kuzipeleka bafuni.

    Kila alipokuwa akiwaangalia vijana wenzake hawa Hellen akawa anapata hisia mchanganyiko. Kama kweli yeye ni mtoto wa Mzee Paul kama mama yake alivyomwambia kabla ya kufa, basi inamaana hapo yuko na kaka yake na dada yake, kama si kweli basi angependa kuwa rafiki wa hawa vijana maana walioneka wacheshi na wenye upendo. Milka alionekana mtulivu, Maganga alionekana mcheshi na alikuwa na mvuto pia, kila macho yao yalipogongana na yale ya Maganga kuna kitu alihisi kinaruka ndani yake.

    "Ndiyo mgeni wetu, karibu sana kwa mara nyingine. Hatukuwa tumepata kifungua kinywa. Hivyo karibu mezani ujumuike nasi.” Maganga alisema huku kwa mikono miwili akimwonyesha Hellen meza ilipokuwa. Kwa kawaida chai hundaliwa sehemu moja na kusambazwa kwenye nyumba za Watawa. Hivyo Maganga aliikuta imeshaandaliwa mezani. Ilikuwa ni viazi vya kuchemshwa na chai ya maziwa.

    “Asanteni sana...” Hellen alisema huku akijiinua kuelekea mezani.

    Wakiwa wanapata kifungua kinywa japo walikuwa wamechelewa, waliongea mengi ikiwa ni pamoja na kutambulisha, mambo ya shule na mengineyo.

    “Kwa hiyo kilichokufanya ufunge safari toka Dar hadi hapa Mwanza halafu Katunguru ni kuja kumwona Mzee Paul ambaye umeambiwa ni mganga wa kienyeji maarufu?” Maganga alihoji kwa mshangao baada ya Hellen kuwadanganya kuwa alikuwa amekuja kwa sababu za kitabibu.

    “Haswaa!” Hellen alijibu huku akiangalia pembeni.

    “Basi ngoja tumsubiri huyo Mzee Paul bila shaka anaweza kuwa na namna ya kukusaidia.” Maganga alisema huku akibetua midomo. Hakuwahi kusikia wala kumwona baba yake akitibu watu kwa uganga wa kienyeji. Hilo lilimshangaza.

    “Hellen umefanana na rafiki yangu mmoja anaitwa Vivian, yaani mmefanana sana kwa kweli, ngoja akija utamwona...'”Milka alisema huku akitabasamu.

    “Kweli?”Hellen alijitia kushangaa.

    “Saana!” Milka alisisitiza.

    “Basi safari hii itakuwa bahati yangu kwani sijawahi fananishwa na mtu yeyote wakati wowote huko nyuma. Nina hamu nimwone huyo mtu ninayefanana naye ili nijione nilivyo.” Hellen alisema wote wakacheka.

    * * *

    “Ndiyo binti, Maganga amenielezea kuwa kilichokuleta hapa ni kutafuta tabibu wa afya yako je, ni kweli?” Mzee Paul alihoji kwa sauti mzito iliyojaa wasiwasi.

    “Hapana, si kweli baba, mimi naitwa Hellen Tino....” Helleni alijieleza kwa kirefu yeye ni nani na alikuwa ametoka wapi!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hivyo kabla mama yangu hajafariki siku moja alinielezea kuwa anaona ni haki yangu kujua ukweli kuhusu mimi...akasema siyo rahisi kunielezea nikaelewa ila akasema katika maisha yangu nijitahidi kuja hapa Kijijini nikutafute maana wewe ndiwe baba yangu mzazi.” Hellen alisema huku akijitahidi kumwangalia Mzee Paul usoni. Kumbukumbu nyingi zilimjia kichwani lakini Mzee Paul alijua kukubaliana na hilo ni kujivunjia heshima yake kijijini pale. Alikuwa anaelekea kuwa baba wa mtu ambaye ni Padri, kisha mwanawe mwingine angekuwa Mtawa muda si mrefu, habari kuwa alikuwa na mtoto wa nje ingemvurugia maisha yake. Ni kweli alimkumbuka Theresia, mama wa msichana aliyekuwa mbele yake.

    “Inawezekana usemalo, ila ili kuhakiki kuwa wewe kweli ni mwanangu inabidi nikathibitishe hilo. Jioni hii itabidi twende wote kuna shamba langu liko Kasomeko, huko kuna waheshimiwa tutawauliza na watatuambia ukweli. Kama ni kweli itakuwa shangwe na vifijo kwelikweli.” Alisema Mzee Paul huku akitabasamu kinafiki. Hellen alikubaliana na mpango huo.

    Ilipogonga saa kumi na mbili na nusu jioni Mzee Paul na Hellen walikuwa wameshafika kwenye shamba alilosema Mzee Paul.

    “Hii ni njia ya kiutamaduni ya kujua kama mtoto ni wako au la. Wewe utasimama hapa chini ya mti miye nitapanda juu. Ukihisi kuna kitu kinakugusa kichwani tulia tu, ukiona kina zunguka shingoni na kukubana ujue wewe kweli ni mwanangu, basi utasubiri hivyo na miye kitakuja kunibana nitajua u mwanangu.” Alisema Mzee Paul huku akiwa anamwangalia Hellen usoni.

    Hellen aliafikiana na utaratibu, akafumba macho, dakika chache baadae akasikia kitu kinamgusa kichwani, baadae akashitukia kinamzunguka shingoni kilipombana alisikia maumivu. Wakati bado anasikilizia, akashangaa anakabwa na kunyanyuliwa juu akafumbua macho wakati kitu hicho kikimnyanyua. Alipoangalia vizuri na kupapasa kwa mikono ndipo akagundua kuwa kamba ilikuwa imemzunguka shingoni. Alikuwa ananyongwa. Alitamani kusema kitu hakuweza, alitaka kupiga kelele akashindwa pumzi zikaanza kumbana.

    “Karibu nyumbani Hellen!” Ilikuwa sauti iliyojaa dhihaka ya Mzee Paul, mtu aliyeamini kuwa ni baba yake. Wakati huo huo akamwona Mzee Paul akikimbia na kupotelea kichakani. Alianza kupigapiga miguu huku pumzi zikianza kumtupa mkono.

    ***************************

    Macho yalimtoka pima, Maganga hakuamini kitu ambacho baba yake alikuwa anafanya. Mwanzo alitetemeka kwa woga, lakini mwishoni alipomwona Hellen ananing’inia kwenye kamba, Maganga alitetemeka kwa hasira. Alitaka kukurupuka aende lakini kuna kitu kilimzuia akasita. Mzee Paul alipoanza kukimbia kuondoka eneo la tukio alipita jirani na kichaka ambacho Maganga alikuwa amejificha.



     Macho ya Maganga yalimsindikiza baba yake hadi alipopotelea kwenye miti ya mihogo shamba la jirani na pale alipowakuta Hellen na baba yake mzazi.

    Aliporudisha macho kuelekea kwenye mti ambao Hellen alikuwa ananing’inia alishangaa kuona Mzee mmoja akiwa anahangaika namna ya kumshusha Hellen. Hapo tena akapigwa na bumbuwazi. Mzee huyo makamu yake yalionekana kutotofautiana sana na Mzee Paul, baba yake. Hakuwa anamjua Mzee huyo. Baada ya dakika chache yule Mzee alifanikiwa kumtoa Hellen katika kile kitanzi, japo mwili wa Hellen ulionekana kuwa umetulia kabisa. Maganga alitilia shaka kama bado uhai ulikuwemo ndani ya mwili huo. Mzee huyo alimbeba Hellen na kuanza kuondoka naye.

    Maganga alimfuata Mzee huyo kwa siri hadi safari yao ilipoishia kwenye nyumba moja nzuri iliyokuwa mbali kiasi toka sehemu ambayo tukio lilikuwa limetokea. Nyumba hiyo ilikuwa nzuri ukilinganisha na nyumba nyingine kijijini pale huku ikiwa imezungushiwa ukuta wa matofali. Mzee huyo alipofika getini aligonga, geti likafunguliwa akaingia ndani. Hapo Maganga hakuweza kujua nini kiliendelea. Alikaa kwenye kichaka takribani nusu saa huku akiwa amejawa na mawazo tele. Wazo la kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi lilikuja lakini alilipinga haraka sana. Hakuna mwanajamii yeyote pale kijijini ambaye angemuelewa pindi angesikia kuwa amekwenda kumshitaki baba yake kwa mauaji. Maganga alijikuta akiishangaa siku hiyo, ilikuwa siku ambayo ilianza kwa visa na vituko tangu saa nane usiku alipoamshwa na Milka mdogo wake. Maganga hakuwahi kumwona wala kujua kuwa baba yake ni mganga wa kienyeji. Hilo lilimfanya awe na hamu ya kujua ukweli. Hivyo kwa siri sana alikuwa akifuatilia nyendo za Paul na Hellen. Hicho ndicho kilichomfanya aandamane nao kwa siri walipokuwa wakielekea kule shambani.

    Alitaka kuondoka eneo la hiyo nyumba aliyoingia yule mzee akiwa amembeba Hellen, lakini sauti nyingine ikamwambia si vema kuondoka bila kujua hali ya Hellen. Pia, akajikumbusha kuwa Hellen alikuwa ni mgeni wao. Huruma ilimjaa, ikamsukuma kufanya kitu, akatoka kichakani alipokuwa amejificha huku akiwa amejawa na wasiwasi akapiga hatua taratibu kuelekea lilipokuwa lango kuu la nyumba hiyo. Alipofika langoni akangonga kama alivyofanya yule Mzee. Aligonga mara ya pili na ya tatu lakini hakukuwa na dalili ya mtu kuja kumfungulia. Aliendelea kubisha namna hiyo kwa dakika ishirini nyingine bila mafanikio. Ndipo wazo la kujaribu kuingia likamjia. Akaanza kuungalia ukuta wa nyumba hiyo, katika kuhangaika huko mara akaona mawe yaliyokuwa yamekusanywa kuegemea ukutani. Alikwenda hadi mahali pale, akasimama juu ya rundo la mawe hayo, akachungulia ndani. Mbwa wakubwa kama ndama wakawa wamemwona wakaanza kubweka kwa fujo na kufanya eneo hilo kulipuka kwa kelele. Alijua kuwa haingekuwa rahisi kwa yeye kuingia ndani bila mwenyeji kumruhusu kufanya hivyo.

    Wakati anaondoka sehemu hiyo yenye mawe mara simu yake ya kiganjani ikaita.

    “Hallo Milka!”Alisema baada ya kuminya kitufe cha kupokelea.

    “Maganga uko wapi, nimekutafuta kila mahali hupatikani.” Milka alisema kwa sauti iliyokuwa na jazba iliyochanganyika na wasiwasi.

    “Kuna nini Milka? Nipo nakuja.” Maganga alisema kwa sauti ya kichovu.

    “Usiniambie uko na yule msichana mgeni.” Milka alisema tena.

    “Sikiliza Maganga, baba ameteguka mguu, watu wamemleta hapa nyumbani baada ya kumkuta huko akiwa amelala hajiwezi. Halafu Vivian kanipigia simu, kasema hali ya mama imebadilika usiku huu.” Milka alisema huku akipumua kwa kuchanganyikiwa kama mtoto wa ndama ambaye hajamwona mama yake wakati kundi la Ng’ombe likiwa limerejea toka malishoni.

    “Heeeh, Milka niko njiani nakuja!” Maganga alisema huku akiwa anaondoka eneo hilo. Kwa kifupi alikuwa amechanganyikiwa. Taarifa kuwa baba yake ameteguka, mama yake hali imekuwa mbaya, Hellen yuko ndani ya jumba lile ambalo ameshindwa kuingia, zote zilikuwa kama ndoto tu kwake. Akiwa ameshapiga kama hatua kumi na tano toka kwenye lango kuu la nyumba ile mara akasikia mlango wa chuma ukitoa mlio wa kufunguliwa. Alisimama akageuka kuona kama kuna mtu anatoka. Mara akamwona yule mtu aliyekuwa amembeba Hellen akiwa anachungulia. Maganga aligeuka akatembea haraka kuelekea kwenye lile lango.

    “Shikamoo Mzee wangu!” Maganga alisema alipokuwa amefika pale langoni. Hakujibiwa. Yule Mzee alibaki anamwangalia tu Maganga kama mtu aliyeona kichwa cha nyoka nje kupitia dirishani mwa chumba cha kulala.

    “Shikamoo Mzee wangu!” Maganga alirudia tena.

    “Nani Mzee wako?” Hatimaye huyo mwanaume alisema kwa sauti ya kukwama kwama. Maganga alimwangali huyo mtu kuanzia juu hadi chini. Kisha akajikuta anakosa la kusema. Kama nilivivyosema, alikuwa mtu wa makamo, kati ya miaka arobaini na nane hadi hamsini na tano. Alikuwa na nyewle nyingi huku chache zikionekana kuwa na weupe. Alikuwa na mwili uliojengeka vema na kimo cha kupendeza. Si mweusi si mweupe.

    “Una shida gani hapa kwangu usiku huu?” Alihoji, tayari ilishatimia saa mbili kasoro dakika kumi na saba. Kiza kilikuwa kimeshatanda kote, huku ndege aina ya Popo wakisikika kushangilia asubuhi yao. Maganga akakosa la kujibu.

    “Ahh….ha..ha..nilikuwa nataka kujua kuhusu yule msichana uliyemchukua kule shambani.” Maganga alisema kwa kubabaika kiasi.

    “Ahhhhh! kumbe wewe ndiyo uliyetaka kumuua?”

    “Haya mikono juu na ingia ndani!” Yule Mzee alisema huku mdomo wa bastola aliyokuwa ameishikilia ukiwa unatazama paji la uso wa Maganga. Kwanza Maganga alisikia kizungu zungu, halafu akasikia kama damu imekauka mwilini halafu mwili umekuwa wa baridi, halafu mwishowe akahisi kama suruali yake imelowana, huku miguu ikiwa inagongana. Katika maisha yake hakuwa amewahi kuona bastola na hakuwa na mpango wa kuja kuwa nayo.

    “Siyo mimi Mzee wangu, haki ya Mungu vile!” Alipomaliza kuapa ndipo akakumbuka kuwa kuapa ni dhambi tena hasa kwa yeye kama Padri mtarajiwa.

    “Nimesema ingia ndani!” Alisisitiza yule Mzee. Maganga hakuwa na namna, alitii. Alipoingia yale majibwa yalianza kumnusanusa huku yakitoa miguno ya uchu.

    “Tafadhali kijana usijifanye mjuaji hata kidogo.” Mzee alionya huku wakiwa wanatembea kuelekea ulipo mlango wa kuingilia ndani. Wakati huo huo mvua ilikuwa imeshaanza kunyesha.

    “Haya niambie vizuri nini kimekuleta hapa?” Alihoji huku akiwa anakaa kwenye kiti na kumwacha Maganga akiwa bado amesimama. Alimimina mvinyo akanywa mafunda mawili, kisha akamkazia macho Maganga.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nilikuwa maeneo ya shambani kwako…”

    “Ulikuwa unafanya nini kule peke yako jioni yote ile?” Mzee alimkatisha Maganga kwa swali. Hilo swali lilimkera Maganga.

    “Kwani wewe ulikuwa unafanya nini? Nadhani hilo si swali la kuniuliza, kama wewe ulikuwa kule basi na mimi naweza kuwa kule. Cha msingi hapa nataka kujua kama yule dada yuko salama au la?” Maganga alijibu kwa ukali kiasi.

    “Unajitia mbogo siyo, haya twende huku ukamsubiri huyo mwenzio.” Alisema yule Mzee kwa sauti yake iliyokuwa imekauka. Alisimama na akamwonyesha Maganga ishara kuwa atangulie. Walitembea wakapita vyumba kadhaa kabla ya kufika kwenye chumba kilichokuwa mwisho wa ukuta kwenye kona upande wa kulia.

    “Ingia ndani!” Iliamuru sauti ya yule Mzee. Maganga akatii.









    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog