Sehemu Ya Pili (2)
“Utakaa humu!” Alisema kisha akafunga mlango. Maganga aliangalia mule ndani kisha akakaa juu ya boksi la vitabu. Jambo moja lilikuwa dhahiri akilini mwa Maganga, huyu Mzee alikuwa ni msomi. Aliangaza macho yake huku na huko humo chumbani, chumba kilikuwa kimejaa vitabu vya aina mbali mbali, huku asilimia kubwa vikiwa katika lugha ya kiingereza. Alitembeza macho yake taratibu huku akisanifu namna chumba kile kilivyokuwa kimepangiliwa vema, kulikuwa na vitabu vya sayansi, vitabu vya hadithi, vitabu ya maarifa mbali mbali. Macho ya Maganga yaliendelea na safari yake hadi yalipogota kwenye vyeti vilivyokuwa ukutani. Havikuwa vyeti halisi bali nakala za vyeti halisi. Maganga alisoma kimoja baada ya kingine, vyote vilikuwa vya mtu mmoja. Kisha macho yake yakafika sehemu ambayo kulikuwa na picha mbalimbali huku nyingi zikiwa za Mzee aliyekuwa amemweka humo ndani. Zilionyesha tangu akiwa kijana, akiwa kwenye majoho mbalimbali ya kuhitimu elimu za juu. Alipomaliza macho yake yakahamia ukuta mwingine. Hapo ndipo akabaki kinywa wazi. Aliona nakala ya cheti cha kuhitimu mafunzo ya kijeshi. Kisha pembeni Maganga akaona picha ya mama yake mzazi akiwa bado msichna,amabaye wakati huu alikuwa hospitali. Anaoneka akiwa na mtu ambaye anafanana na huyo Mzee. Hapo akajikuta udadisi unaongezeka na hamu ya kutaka kujua zaidi kuhusu huyo Mzee inaongezeka.
Akaanza kupekua, kabla hata hajafika mbali mara chumba chote kikawa giza. Hakujua kama ni umeme ulikuwa umekatika au taa ilikuwa imezimwa. Lakini baada ya sekunde chache wazo la kuwa umeme ulikatika lilitoweka pale alipoona mwanga ukiwa unatokea dirishani. Hakuwa na jingine la kufanya zaidi ya kutulia na kungoja majaaliwa yake. Mawazo yalirudi kwa baba yake na mama yake. Mlolongo wa matukio ulimfanya Maganga ahisi kuwa labda alikuwa anaota.
* * *
Hadi jogoo wa asubuhi walipoanza kuwika, Maganga alikuwa hajapata hata lepe la usingizi. Alikuwa amejaa mawazo mengi kiasi kuwa akili yake haikuruhusu usingizi hata kidogo. Ilipotimia saa moja na nusu, chumba tayari kilishakuwa na mwanga wa kutosha. Alisimama, wakati anasimama alipepesuka, ndipo alipogundua kuwa tangu juzi usiku alipoanza kusumbuana na mdogo wake Milka, alikuwa amepata mlo mmoja tu, wakati ule Hellen alipokuwa amewasili kijijini na wakawa wamepata naye kifungua kinywa. Tofauti na hicho hakuwa ametia kitu chochote tumboni. Lakini hata hivyo alijikaza kiume, akajinyosha kama mtu aliyekuwa ametoka kulala ili hali haikuwa hivyo. Akaendelea na zoezi lake la kupekua ndani ya kile chumba hadi ilipotimia saa mbili na dakika ishirini na moja wakati mlango wa kile chumba ulipofunguliwa taratibu. Yule mwanaume aliingiza kichwa chake huku kiwiliwili chake kikiwa nje kama wafanyavyo makonda wa daladala. Macho ya Mzee yule yalimwangalia kwa muda wa dakika nzima bila kusema neno lolote. Maganga naye alimwangalia hivyo kisha akapiga hatua kuelekea pale mlangoni.
“Hivi Mzee unajua kuwa ufanyavyo ni uhalifu mkubwa, sijajua kosa langu kwa nini umenifanya mateka wako?” Maganga alisema akiwa ameshafika pale mlangoni. Yule Mzee hakusema kitu, ila safari hii macho yake yalilegea na akawa kama analengwalengwa na machozi.
“Sikiliza Maganga.” Yule Mzee alianza kuongea. Kitendo cha kumtaja jina kilimshtusha sana Maganga.
“Umejuaje jina langu?” Maganga alihoji kwa namna ya kushangaa .
“Maganga, mimi nililijua jina lako hata kabla wewe mwenyewe hujalijua…”
“Kivipi?” Maganga alihoji huku macho yake yakipepeswa na kuusoma uso wa yule Mzee ambaye wakati huu alikuwa analengwa lengwa na machozi.
“Halafu nimeona picha ya mama yangu imefikaje humu ndani?” Maganga alizidi kuhoji.
“ Naitwa Mwasumbi, Luten Mwasumbi. Jana nilikuwa nakuja nyumbani kwako kuongea na wewe, lakini nilipokuwa jirani na kwako nikakuona unatoka kwa mwendo ambao nilihisi kulikuwa na shida. Hivyo nikakufuata kwa kuvizia hadi ulipofika kwenu. Kilichonishangaza hukuingia ndani na wewe ulijificha mahali. Nikajua kuna kitu kisicho cha kawaida kilikuwa kikiendelea. Baba yako alipotoka na Hellen nilimwona. Lakini nilishangaa Hellen alifikaje hapa kijijini, sikutegemea yeye kufika huku…”
“Kwani wewe unamjua Hellen kama nani, na kwa nini hukutegemea yeye kuja huku kijijini?”
“Tulia nikuelezee ili uelewe, nitakuja huko maana ndilo lililokuwa linanileta kwako.” Alisema yule Mzee na kumfanya Maganga akae chini.
“Baada ya hapo nikaona ulichokiona ila miye nilikuwa mwepesi kwenda kumwokoa Hellen.” Alisema yule Mzee. Wakati anataka kuendelea mlango wa kile chumba uligongwa, maana wakati huu yule Mzee naye alikuwa ameshaingia ndani.
“Subiri kidogo Grace.” Alisema yule Mzee huku akiwa anamwangalia Maganga kama anayemsoma vile.
“Unaonaje kama tukienda kuongelea kwenye chumba kizuri ili hali tukiwa tunapata kifungua kinywa?” Alihoji kwa sauti tulivu kiasi safari hii, bila shaka hiyo ilitokana na jinsi Maganga alivyokuwa ameanza kunywea.
“Mmmmmh!” Maganga alishusha pumzi kisha akainamisha kichwa chini. Hakuwa na sababu ya kukataa.
“Okay, twende. Hellen yuko wapi?” Hatimaye alikumbuka kuuliza.
“Yupo utamwona tu, baada ya tukio la jana, usiku ule ule nilimwita daktari wangu maalum akaja kumwangalia na kumpa huduma ifaayo.” Alisema yule Mzee akiwa anageuka na kufungua mlango. Waliongozana wakafika sebuleni.
“Hapa hapatatufaa kwa maongezi yetu, twende huku.” Alisema yule Mzee na kuongoza upande wa kushoto wa sebule, hapo alifunua pazia na kufungua mlango. Wakajikuta wako kwenye chumba kingine cha wastani tu. Kulikuwa na meza kubwa iliyokuwa imezungukwa na viti sita, kisha pembeni kulikuwa na sehemu ya kunawia mikono. Meza ilikuwa imeshaandaliwa tayari kwa kifungua kinywa, baada ya kuona vilivyokuwa mezani, Maganga akahisi kama njaa aliyokuwa nayo iliongezeka mara dufu.
“Karibu, utanawa pale halafu tutapata kifungua kinywa.” Alisema yule Mzee kwa sauti iliyokuwa na kitu ndani yake, japo Maganga alishindwa kupambanua kitu hicho ni kitu gani. Wakaanza kushambulia chakula, baada ya dakika kama ishirini hivi walikuwa wameshamaliza.
“Haya sasa tuna…” Maganga hakumalizia kuongea kwani macho yake yalitua ukutani na kuganda hapo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Baba!?” Maganga alishangaa huku akisimama kuisogelea ile picha.
“Ndiyo huyo ni rafiki yangu Paul, hapo tulikuwa jeshini mafinga, tulikuwa ni marafiki tulioshibana. Urafiki wetu ulianza tangu tulipokuwa wadogo sana, maana tulikuwa majirani. Baaada ya kumaliza shule wote tukaenda kujiunga na jeshi kwa ajili ya mpango maalum. Tulifanya mafunzo yetu na kumaliza kwa mafanikio makubwa sana. Wakuu wa jeshi wakapendekeza twende tukapate elimu ya juu, hivyo wote wawili tukajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam.” Alipofika hapo Mzee huyo alinyamaza kuruhusu koo lake kupitisha mate. Maganga alikuwa ametulia tuli akimsikiliza huyo Mzee huku macho yake yakiwa hayabanduki usoni kwake.
“Jiji la Dar es salaam lilitupokea, japo miaka hiyo hailkuwa kama lilivyo sasa. Paul alikuwa mkorofi sana, japo alikuwa na akili sana. Mimi nilikuwa mcheshi sana, hiyo ilinifanya kuwa na wasichana wa kutosha hadi wa ziada. Wasichana wengi walikuwa wanamkataa Paul. Ikafikia wakati alipokuwa akihitaji wasichana ilibidi apitie kwangu ili nimfanyie mpango. Katika wasichana wote niliowafanyia mpango kwa Paul, Paul alifanikiwa kujenga urafiki na msichana aitwaye Elizabeth. Japo mara kwa mara nilikuwa nikiingilia kati kuamua ugomvi baina yao. Tulipokuwa mwaka wa mwisho pale chuoni, urafiki kati ya Paul na Elizabeth ulikuwa umefifia sana. Mara nyingi Elizabeth alipenda kuja chumbani kwangu kuongea, na mara kwa mara Paul alipotukuta ulizuka ugomvi mkubwa sana. Hatukuwa na sababu ya kujitetea maana tungekuwa tunachukua masomo yanayofanana tungesingizia kuwa tulikuwa tunajisome, lakini tofauti na sisi ambao wote wawili tulikuwa tunasomea uhandisi, Elizabeth alikuwa anasomea ualimu.
Kitendo cha kusingiziwa kuwa anatembea na miye kilimchukiza sana Elizabeth, mwishowe akajikuta anaanza kunishawishi tufanye kweli ili hata Paul akiwa anatulaumu iwe kweli. Mimi ni mgonjwa, ni mgonjwa kwa kweli, linapokuja suala la kiumbe wa kike. Hivyo sikuwa na nguvu za kupinga. Tukaanza kuwa tunafanya na Elizabeth.
Paul alipokuja kugundua, hapo urafiki wetu ukafa kabisa. Tulipomaliza chuo tukapangiwa kazi maalum, yeye alipelekwa Kagera wakati mimi nilipelekwa Ruvuma.
Miaka sita baadaye nikahamishiwa Arusha, kwa bahati nzuri au mbaya na yeye akahamishiwa Arusha. Hivyo wote tukawa Chuo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi Monduli. Hapo Paul akaamua kuoa, mimi bado nilikuwa sijaamua bado. Urafiki wetu ulipata uhai kidogo, japo mara zote Paul alikuwa akinitaja kama mlafi wa wanawake…”
“Ila wewe unaona ni kweli au si kweli?” Maganga alimkatiza kwa swali. Yule Mzee hakujibu, alitabasamu, huku akiuruhusu ulimi wake uyafute meno ya mbele juu na chini.
“Sijui kwa kweli, jipe jibu mwenyewe. Basi ndani ya miaka mitatu Paul na mke wake hawakuwa wamefanikiwa kupata mtoto. Hii ilianza kuleta ugomvi kati ya Paul na mkewe ambaye alikuwa akiitwa Agatha. Kila mara Paul alipokuwa akilewa, alikuwa anampiga sana mkewe sababu ikiwa ni kushindwa kumzalia mtoto. Paul alidai kuwa dada zake na mama yake walikuwa wakimsumbua kuwa wanataka mtoto.
Basi siku moja kulikuwa na sherehe ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi, kwa kawaidi viongozi wakubwa wa serikali akiwemo Rais walikuwa wakija wakati wa mahafali hayo. Baada ya mahafali kufanyika mchana, usiku zilikuwa sherehe , watu kula, kunywa na kufanya anasa za kila aina.
Siku hiyo Paul kama kawaida baada ya kunywa na kulewa akaanzisha fujo na kuanza kumpiga mkewe. Kwa vile wengi walikuwa wamechoka na vitendo vyake hivyo vya kumyanyasa mkewe, walijitokeza wanaume wachache kumtuliza, lakini akataka kupigana nao, hapo ndipo walipompa Paul kipigo kikali sana, hakuna mtu aliyejitolea kumsaidia, ila miye nikaona nimsaidie kumwondoa mke wake maeneo hayo. Tulipoondoka eneo la tukio, mke wake akagoma kwenda nyumbani kwao usiku huo kwa kuhofia usalama wake. Hapo tena nikaona nimsaidie, nikamchukua mke wake hadi nyumbani kwangu tukalala naye. Alikuwa na mke mzuri, na nadhani unajua ugonjwa wangu...”
“Nimeshakuelewa Mzee, isingekuwa rahisi ugonjwa usipande wakati uko kwenye mazingira hatarishi kama yale!” Maganga alisema huku akionyesha kufurahia simulizi ya huyo Mzee. Kisha akakumbuka kisa chake na Milka usiku wa juzi.
“Eti, Mzee vipi kama una dada yako mzuri halafu akajipendekeza?” Maganga alihoji huku kwa mara ya kwanza katika maisha yake akijisikia huru kuongea hayo mambo. Alijikuta ile hofu aliyokuwa nayo mwanzo imemtoka.
“Maganga, sijajua unamaanisha nini lakini huwa kuna mazingira tata ambayo akili inakuwa na nafasi ndogo sana ya kuweza kupambanua mambo. Na hapo kama una ule ugonjwa kama mimi, utajikuta umeanza kupembua jema au baya wakati ukiwa unapumzika baada ya kumaliza kitendo.” Alisema yule Mzee, tabasamu likiwa limechanua usoni.
“Ha ha ha ha! We Mzee unanifurahisha.” Maganga alicheka.
“Basi asubuhi nikamwambia aamkie kwa mkuu wa kambi na amweleze kilichotokea na akiulizwa alilala wapi aseme kanisani. Basi mkuu wa kambi aliwasuluhisha huku Paul akipewa onyo kali juu ya tabia yake ya kupiga na kumdhalilisha mke wake. Baada ya miezi kadhaa habari zikavuma kuwa mke wa Paul alikuwa na uja uzito. Hatimaye Paul na mke wake wakafanikiwa kupata watoto mapacha wa kiume na wakike. Mke wake Paul alikuwa mwenyeji wa Mwanza, hivyo alikwenda kujifungulia Mwanza katika Hospital ya Bugando. Paul alifurahi sana.
Siku moja nikiwa katika pitapita zangu, nikakutana na mke wa Paul, alinisalimia kwa furaha sana. Lakini pia, akaniambia kuwa anatamani ile siku ingejirudia. Alinisisitiza sana niende nikawaone watoto. Nilijua uhusiano wangu na Paul haukuwa mzuri sana, hasa ambapo angegundua kuwa safari hii tena nimeanza kuwa jirani na mke wake, angeweza hata kunitia risasi. Nilimshukuru mke wake lakini nikamwambia ingekuwa vigumu kwenda nyumbani.
Siku nyingine tulipokutana naye aliniomba tupange tukutane naye mahali ili niwaone na kumsalimia watoto, msisitizo wake ulianza kunipa wasiwasi. Maana ilikuwa wazi alikuwa akijisikia raha zaidi kuwa na mimi na pia ilikuwa wazi kuwa alitaka sana niwe na ukaribu na watoto.
Baadaye ikawa tabia kuwa kila mwezi ilikuwa lazima tukutane na mke wa Paul mara mbili au tatu kwa ajili ya kuhudumiana. Muda ukafika na miye nikaamua kuoa, siku ya harusi yangu ndipo mambo yalipoharibika. Takribani ndugu zangu wote walikuwa wamekuja kwenye harusi yangu. Tukiwa katikati ya sherehe, ndipo bomu lilipolipuka, na kusababisha vifo vingi vya papo hapo huku wengi wakiwa na majeraha ya kutisha.
Kwa kifupi, katika tukio lile nilipoteza ukoo wangu wote wa karibu huku mwenyewe nikiwa na hali mbaya ya majeraha. Ni katika tukio hilo pia nilipoteza uwezo wa kulala na mwanamke kama mwanaume rijali.” Mzee alipofika hapo alinyamaza. Akaangalia chini huku akiminya minya mikono yake ambayo ilikuwa imeanza kutetemeka. Maganga alijikuta akianza kumuhurumia huyo Mzee.
“Bora ningekatwa miguu, lakini ningebaki na burudani yangu.” Alisema yule Mzee kwa masikitiko
“Pole Mzee wangu yote ni mapenzi ya Mungu…”
“Hapana Maganga, siamini kama hayo ni mapenzi ya Mungu….Mungu kweli anapenda kiumbe wake aishi bila furaha!?” Alisema huyo Mzee kwa sauti ya kulalamika. Alitia huruma.
“Basi kwa vile mkuu wa kambi alikuwa rafiki yangu nilipelekwa Urusi kwa matibabu. Nilipomaliza matibabu nilipitiliza huko huko kwa mafunzo mengine maalum. Baada ya miaka mitatu nilirudi, nikapelekwa Makao Makuu ya Jeshi. Baadae, nilipata mawasiliano na Paul, alikuwa ameshahamishiwa Dar es salaam. Kwa kuwa alikuwa amejua nini kimenipata hivyo hakuwa na hofu nami tena. Alianza kunikaribisha kwake, pale kambi ya Ruvu. Wakati mwingine aliniita ili nikashinde pale wakati wa mwisho wa wiki.” Alipofika hapo Mzee huyo alimwangalia Maganga kisha akainuka. Aliporejea, akaja na juisi ya Parachichi.
“Najua unapenda sana hii juisi.” Alisema huku akimkabidhi glasi moja.
“Umejuaje kuwa napenda, japo ni kweli napenda sana juisi ya Parachichi?”
“Wewe jua tu kuwa najua.” Alijibu yule Mzee.
“Najua hata hizi habari ninazokupa hasa za mambo ya wanawake unazipenda sana, maana ndiyo asili yako na siyo huo upadri unaoung’ang’aniza.” Alisema huku akiinua glasi ili anywe juisi.
“Jumamosi moja nikiwa kwa Paul huku yeye mwenyewe akiwa amesafiri kikazi, mwanae aligongwa na gari. Kwa vile alivuja damu nyingi ilitakiwa mtu ajitolee kumwongezea. Kwa vile nilikuwa pale ilibidi utaratibu ufanyike nitolewe damu. Mke wa Paul pia alikuwa akisisitiza kuwa lazima nimsaidie mwanae. Nilimweleza kuwa inategemea kama makundi ya damu zetu yanawiana, lakini yeye alisisitiza tu kuwa lazima yatawiana.
Hilo lilinishangaza mimi na kunipa wasi wasi, Daktari aliyekuwa anamhudumia yule binti, mtoto wa Paul naye akaingiwa na wasiwasi juu ya tabia aliyoonyesha mke wa Paul. Hivyo walipokuta damu yangu inafanana na ya mtoto waliichukua na kumwongezea mtoto. Lakini tukafanya kitu cha zaidi tukapima vinasaba vya damu ya mtoto na yangu. Cha kushangaza, ilibainika kuwa yule mtoto alikuwa wangu. Nilishikwa na mshangao uliochanganyika na furaha.” Hapo alitengeneza koo lake kisha akaendelea.
“Duniani hakuna siri, habari zikamfikia Paul, ikabidi aende kupima damu yake na ya watoto kuona ukweli wa mambo. Alishangaa kukuta ni kweli. Siku moja nikiwa natoka matembezi jioni, ilikuwa ni miezi kadhaa baadae, nilivamiwa na watu ambao naweza kusema walikuwa maalum, kwani pamoja na utaalamu wangu katika kupigana, lakini nilikuta watu hao wananizidi kila idara. Watu hao waliniambia wazi kuwa nimeingilia maisha ya watu na kwa hivyo nilikuwa nakwenda kufa, ili kuondoa ushahidi wowote kuwa nimeuawa, watu hao wakaishia kunitupa katikati ya bahari ili nifie huko. Lakini kwa kudra za mwenyezi Mungu nikiwa katika hatua za mwisho, kama ilivyokuwa kwa Hellen jana, wavuvi waliniokoa baada ya mtego wao wa samaki kunikokota toka vilindi vya Bahari. Sikurudi kambini, niliwasiliana na mkuu wangu wa kazi, akanikubalia kujiuzulu. Na kama zawadi ya jeshi kwangu, ndiyo wakanijengea nyumba hii na kuniwekea vitu vyote unavyoviona humu ndani.
Uchunguzi juu ya kifo changu, ulifanyika, maana hakuna aliyekuwa anajua kuwa bado naishi. Tulikubaliana na mkuu wangu kuwa kwa usalama wangu bora ijulikane kuwa nimekufa. Lakini pia baada ya uchunguzi, Paul aliachishwa kazi huku akipoteza haki zote za msingi. Kufuatia ombi langu, mkuu wa kambi alijitolea kumnunulia Paul mashamba katika kijiji hiki. Lengo ni kuwa pamoja na kuwa nimekufa lakini niwe na uwezo wa kuwaona wanangu.” Alipofika hapo Maganga alishituka.
“Unamaanisha nini? Paul unayemwongelea ni yupi?”
“Paul ninayemwongelea ni baba yako, watoto ninao waongelea ni wewe na Milka.” Alipofika hapo, Maganga akawa kama aliyekufa ganzi. Alishindwa kufikiri, akili yake iligoma kuamini, aliona kama ni hadithi ya kutungwa na kuwa hayakuwa mambo halisi. Alimwangalia yule Mzee katika hali ya bumbuwazi. Mzee alisimama kisha akatoka nje. Akili ya Maganga ilizunguka ikasimama, ikaruka, ikachuchumaa, ikalala kwa muda, ilipokuja kuanza kuzunguka tena. Alijikuta anaongea kwa sauti.
“Haiwezekani, unajaribu kunirubuni tu! Nooooo !” Alipiga ngumi juu ya meza.
Mlango ulifunguliwa, Hellen aliingia huku akiwa na tabasamu usoni. Maganga alipomwona Hellen alisimama, alisikia kama kuna vitu vinamtembea mwilini japo hakujua ni nini hasa.
“Pole Hellen! Maganga alisema huku akiwa ameshamfikia Hellen ili amkumbatie.
“Don’t!” Hellen aling’aka.
“Wewe na baba yako lenu moja, na mtajuta kwa mliyonitendea.” Hellen alisema huku machozi yakimlengalenga. Maganga alijikuta anashindwa namna ya kujitetea.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati maganga akiwa anafungiwa kwenye kile chumba kilichojaa vitabu na maandiko mbalimbali jioni ile, Milka yeye alikuwa akihangaika na baba yake, Mzee Paul, ambaye mguu wake ulikuwa umefura vibaya sana baada ya kuanguka wakati akikimbia toka shambani ambako alikuwa amemning’iniza Hellen kwa nia ya kumnyonga.
Baada ya kumpigia simu Maganga kumwelezea yaliyokuwa yamemkuta baba yao, Milka alikuwa katika harakati za kumpeleka baba yake, Mzee Paul hospitalini. Kwa msaada wa watu wengine pale kijini alifanikiwa kumpeleka hospitali ya misheni, Katunguru.
“Dokta naomba umsaidie baba yangu jamani, mkimwacha akae kwenye foleni wakati ana maumivu kiasi hiki itakuwa ni utesaji.” Milka alimwambia Daktari aliyekuwa anapita kwenda upande kulikokuwa na wamama waliotoka kujifungua. Wakati huu Mzee Paul alikuwa akigugumia kwa maumivu makali, japo mguu ulionekana wa kawaida tu.
"Bila shaka atakuwa amevunjika huyu." Daktari alisema mara baada ya kuwa ameuangalia mguu wa Mzee Paul kwa muda. “Neema, hebu mleteni huyo Mzee huku ndani.” Daktari alimwambia mmoja wa wauguzi aliyekuwa amebeba dawa. Kauli ya Daktari ilionyesha kuwa alikuwa ameafikiana na maelezo ya Milka
“Oooooh mguuu wangu, ooooooh God!” Mzee Paul alipiga kelele kwa uchungu wakati alipokuwa anainuliwa kupelekwa kwenye chumba cha vipimo.
“Pole baba, ngoja wakuhudumie hali itakuwa nzuri” Milka alisema kwa huruma, alishaweka pembeni ugomvi mkubwa waliokuwa nao asubuhi ya siku hiyo. Muda huu ilikuwa ni saa tatu na nusu usiku, ni siku ile ambayo Maganga alikuwa ametekwa na yule Mzee kule shambani.
“Kutokana na hali ilivyo huyu Mzee inabidi apelekwe hospitali ya Wilaya Sengerema, ni dhahiri kuwa kavunjika mguu. Kule ndiyo wapo wataamua ama kuunga au kuukata inategemea na jinsi watakavyoona.” Daktari alimwambia Milka, ambaye maelezo hayo yalimchanganya sana. Alichukua simu yake ili kuuliza Maganga alikuwa amefika wapi, maana tangu alipokuwa amemtaarifu muda ulikuwa umeshapita. Aliijaribu simu ya Maganga lakini haikuwa inapatikana.
“Najaribu, kumpigia Maganga lakini simu yake haipatikani.” Milka alimwambia baba yake katika hali ya kuchanganyikiwa.
“Inawezekana yuko kwenye mambo ya kanisa, haina shida maadam anafanya mambo ya Mungu.” Mzee Paul alisema huku akiwa anauma meno ishara kuwa alikuwa anapambana na uchungu wa maumivu.
“Sidhani kama hiyo ni sababu ya msingi baba, hawezi kukuacha wewe unateseka hapa halafu akasema kuwa yuko kwenye kazi za kanisa. Hata hiyo jamii anayoihudumia sidhani kama atakuwa anaifundisha kwa vitendo. Maana hii ni sawa na wale wanaosema fuata maneno yangu na si matendo yangu. Maganga hawezi kufanya hivyo, nadhani kutakuwa na tatizo limempata maana hata nilivyoongea naye, haikuwa sauti ya Maganga ninayemfahamu.” Milka alisema kwa sauti yenye wasiwasi uliochanganyika na kuchanganyikiwa. Alikuwa anamfahamu Maganga tangu wakiwa wadogo, hakuwa mtu wa kuambiwa baba kaumia halafu awe hajaonekana hadi muda ule. Alijua ingekuwa vigumu kwa yeye Milka, kumsamehe baba yao kwa yote aliyomfanyia mama yao lakini si kwa Maganga. Maganga ni mtu aliyejaa upendo na msamaha na ndiyo maana alimpenda kaka yake huyo.
* * *
Saa sita kasoro dakika mbili usiku, kwa msaada wa gari la AIC misheni Katunguru, Mzee Paul na Milka ndiyo walikuwa wamefika hospitali ya Wilaya Sengerema. Wataalamu waliamuru Mzee Paul apelekwe moja kwa moja chumba cha upasuaji. Wakati wakiwa wanampeleka huko, mara Milka akakutana na Vivian. Vivian alikuwa anatokwa na machozi. Alipomwona Milka ndiyo machozi yakazidi kububujika.
“Milka, mbona mmechelewa sana kuja mpenzi, hali ya mama ni mbaya sana. Amekuwa akilalamika kuwa anataka awaone, ni hakika kuwa uwezekano wa yeye kupona ni mdogo sana. Najaribu kumpigia Maganga lakini simu yake haipatikani, je una taarifa zozote kuwa yuko wapi na ana mpango gani?” Vivian alisema kwa uchungu, huku tayari akiwa ameshamkumbatia Milka.
“Saa mbili kasoro nilimpigia simu Maganga, nilimpata na nikamwambia juu ya maendeleo ya mama kama ulivyoniambia lakini pia, nikamwambia kuwa baba amepata ajali na kuvunjika mguu. Nimejaribu kumpigia tena wakati tulipoambiwa kuwa tunatakiwa kumleta huku baba, lakini simu yake haikuwa inapatikana. Muda ule nilipoongea naye, nilipata wasiwasi kidogo, maana sauti ya Maganga haikuwa ile yake ya siku zote.” Milka alielezea.
“Ilikuwaje?” Vivian alisema kwa kushtuka kama mtu aliyetoneshwa kidonda kilichovunda.
“Alionekana kuwa na wasiwasi halafu ni kama mtu aliyekuwa anataka nimalize kuongea haraka!” Milka alisema huku akiwa anatengeneza sketi yake.
“Unadhani anaweza kuwa wapi?” Vivian alihoji.
“Sijui kwa kweli.” Milka alijibu.
“Duuuh! Mbona haya mambo yanatokea kama vile kuna mkono wa mtu?” Vivia alisema huku akiwa anamvuta mkono Milka kuashiria kuwa amfuate.
“Ni vema twende ukamwone mama sasa hivi!” Vivian alisema huku akiwa anamwongoza Milka kuelekea ilipo wodi ya wagonjwa walio katika hali mbaya. Walipokuwa wanatazamana na mlango wa chumba walichokuwa wanakwenda, mara nesi alitoka huku akiwa anakimbia. Kuona hivyo, Vivian na Milka nao wakakimbia kuharakisha kuingia kwenye kile chumba. Walipoingia walikwenda moja kwa moja kwenye kitanda alichokuwepo mama Milka. Walipomwangalia kila mmoja hakungoja utaalamu wa daktari kumwambia kuwa mgonjwa wao alikuwa katika dakika zake za mwisho.
Milka alimshika mkono mama yake, kisha akainama na kumwambia,“Mama, tafadhali usituache bado tunakuhitaji mama!” Bila shaka mama Milka aliitambua sauti ya mwanawe, alifumbua macho kisha akatabasamu. Akaushika mkono wa Milka kwa mikono yake yote miwili. Alitaka kusema kitu akashindwa maana sauti yake ilikuwa kama anayekoroma vile.
“Milka, mwa mwa mwanangu, ni…i…n i…i..samehe mimi mama yako. Mwambie Ma ma ma ganga naye anisamehe…mwambieni asisahau kuangalia chini ya Mtungi. Nimemsamehe baba yenu….kwa vile…a.a.a.a.a.a.linifichi..ia.siri yangu............................ .Kwa..a.a.a.a.a.a.aher… .....aaaaggggrrrih. Mwasumbi Mwasumbiiiiii...Mwasumbiiii.” Hilo ndilo lilikuwa neno la mwisho la mama yao. Mwasumbi. Akaendelea kukoroma huku macho yake yakigeuka na kuwa meupe. Kilichofuata hapo ni kilio toka kwa Milka na Vivian.
Wakati Agatha mama yake akiwa anapigania uhai wake katika hospitali ya Wilaya Sengerema, Maganga alikuwa kwenye wakati mgumu mbele ya Hellen. Hellen hakuishia tu kukataa kukumbatiwa na Maganga, akaendelea kumshambulia kwa maneno. Bado walikuwa kwenye ile nyumba ya yule Mzee aliyemkomboa Hellen kitanzini, Mzee Mwasumbi.
“Baba yako Mzee Paul ameshaniua, naishi lakini kwenye akili zake miye ni mfu. Amefanya haya yote kwa ajili yako na Milka, anaona nyie mkijua kuwa miye ni mtoto wake hadhi yake kwenu itashuka...”
“Kwa ajili yangu na Milka?” Maganga alihoji kwa hamaki na kumkatisha Hellen ambaye bado alikuwa anaongea
“Ndiyo, anajua kuwa miye ni mwanae!” Hellen alisema huku akijimwaga kitini. Kwa vile alikuwa amevaa khanga moja tu, macho ya Maganga yalibaki yanaangalia mtetemeko wa viungo vya msichana huyo. Alipomwangalia Mzee Mwasumbi, alikutana na macho yaliyokuwa yakimsoma Maganga wakati akiwa anamwangalia Helleni kwa matamanio. Ugonjwa!
“Ina maana wewe ni mtoto wa Mzee Paul!?” Maganga alisema kwa mshangao mkubwa.
“Ndiyo Maganga, na inavyoonekana baba anajua hilo, ila hataki nyie na jamii ijue kwa sababu ya kulinda heshima yake.” Hellen alisema kwa uchungu huku akifuta kamasi ambazo zilikuwa zinachuruzika kwa wingi.
“Heshima, kwani mtu kuwa na mtoto ni kosa? Kwa nini hataki siye tujue? Je, mama anajua hilo? Wewe umejuaje kuwa baba anajua na hataki siye tujue?” Maganga aliuliza maswali mfululizo bila kutoa nafasi kwa Hellen kujibu. Alikuwa amechanganyikiwa na taarifa hizo, si kuwa hakutaka Hellen kuwa ndugu yake, ila ni vile haya mambo yalivyojifunua kwa muda mfupi bila kumpa nafasi ya kufikiria na kuyapokea.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Jana niliongea na Mzee Paul, na kumweleza kile kilichonifanya nifunge safari toka Dar es Salaam kuja huku Katunguru katika Wilaya ya Sengerema.
Ni kufuatia mama yangu kunisisitiza kuwa nije kumtafuta baba yangu katika kijiji hiki cha Katunguru. Mzee Paul hakuoneka kushtuka, na pia aliweza hata kukumbuka jina la mama yangu mzazi kuwa anaitwa Theresia. Lakini akaniambia kuwa ili yeye kuthibitisha kuwa mimi ndiye yule mtoto aliyekuwa amezaa na Theresia inabidi taratibu za kimila zifuatwe. Ndipo akaniambia kuwa twende kule shambani chini ya mti, na nifumbe macho wakati mizimu ya mababu itakapokuwa inanihakiki kama miye ni mwanae kweli au la. Hapo ndipo akaishia kunitundika, kabla huyu Mzee Mwasumbi hajatokea na kuniokoa.” Hellen alielezea huku kilio cha kwikwi kikiwa kinasikika. Maganga alisogeza kiti chake na kukaa jirani na Hellen. Baada ya dakika kadhaa za kubembelezana hatimaye Hellen alinyamaza.
Baada ya Hellen kutulia, Mzee Mwasumbi alikaribia na kuwaambia,“Ukweli ni kwamba miaka ishirini iliyopita Paul alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Theresia ambaye ndiye mama wa Hellen. Nayaita mahusiano kwa vile wawili hawa walitumia kitanda kimoja katika kutafuta mtoto. Haikuwa hiari ya Theresia, lakini kwa Paul ilikuwa ni hiari yake. Kama nilivyokusimulia Maganga, baada ya kugundua kuwa watoto wote aliokuwa nao si wake, Mzee Paul alitafuta chanzo cha tatizo. Ndipo wataalamu walipomwambia kuwa shida ilikuwepo kwa sababu ya muundo wa chembe chembe hai za Paul na mkewe Agatha zilikuwa haziingiliani. Ambapo kutokana na aina ya chembe chembe za uhai alizonazo baba na mama hawawezi kwa pamoja kutengeneza mtoto, hata kama wakitengeneza mtoto hataweza kuishi maana atakufa akiwa mdogo. Paul akaambiwa kuwa anaweza kuzaa na mwanamke mwingine. Hivyo akaamua kwa siri sana kutembea na msichana wake wa ndani, ambaye ndiye Theresia mama yake Hellen. Hapo ndipo ulipopatikana Hellen.” Alisema huyo Mzee huku akiwa amebeba glasi mbili za mvinyo, moja alimpa Hellen na moja akampa Maganga.
“Sasa kwa nini baba hataki kukubali kuwa huyu ni mwanae?” Maganga alihoji.
“Hilo pia ni suala la kihistoria Maganga! Baada ya kugundua kuwa ana uwezo wa kuzaa na mwanamke mwingine, Paul alikusudia kulipiza kisasi kwa mama yenu. Jambo hili alilifanya hata kabla hajafanya jaribio la kuniua. Hivyo alipanga kuzaa na Theresia kisha, angefanya utaratibu wa kutaka mpimwe hadharani kisha angewakataa ninyi. Mpango huu alimwambia mmoja wa marafiki zake wakiwa kwenye baa, bila kujua kuwa rafiki yake huyo ana uhusiano wa kimapenzi na msichana, ambaye ni mdogo wake na mama yenu.
Taarifa zikamfikia mama yenu, ambaye naye aliwashirikisha baadhi ya ndugu zake wa karibu ambao wangeweza kumsaidia pindi angefukuzwa na watoto.”
“Je, mama hakuwasiliana na wewe kama baba wa watoto?” Maganga alimkatiza yule Mwasumbi kwa swali.
“Alinitaarifu maana wakati huo ilikuwa bado sijafanyiwa jaribio la mauaji, nami nikamwambia si mpango wangu wala furaha yangu kuona ndoa yake inavunjika, hivyo nilimwambia ningeingilia kati pale tu ambapo ningeona kuwa sasa msaada wangu unahitajika kwa ajili ya kuwanusuru watoto wangu. Mzee Paul alikuwa akitaka mtoto wa kiume, hivyo hakufurahi pale Theresia alipojifungua mtoto wa kike ambaye ndiye huyu Hellen. Ili kuondoa utata tena, ndipo akaamua kuwaona madaktari ili wampe namna ya kufanya ili apate mtoto wa kiume. Hapo ndipo kaka yake mama yenu, yeye akiwa kama daktari alipotumia mwanya huo kama kutaka kumsaidia Mzee Paul. Ni katika kumsaidia huko ndipo alipomfanyia ‘testosterone injections’ kwa kiwango kikubwa. Hiyo iliondoa kabisa uwezo wa Mzee Paul kupata mtoto, hilo likamkumbusha ule usemi wa waswahili kuwa, usiache mbachao kwa msala upitao. Ili asiharibu heshima yake mbele ya jamii kuwa hana mtoto wa kiume, maana kwake mtoto wa kiume ndiyo mtoto. Akaamua kumfukuza Theresia na kumpa vitisho vizito kuwa asije thubutu kutoa siri. Lakini pia, alimwonya kuwa asimfuatefuate maishani mwake. Miye niliweza kuyajua hayo kwa sababu Theresia alinijia siku moja kuomba msaada na ndipo aliponisimulia yote hayo kwa masharti kuwa nisimsimulie mtu yeyote. Pia, akaniambia kuwa lolote likitokea niwe tayari kumwonyesha Hellen alipo mzazi wake halisi.” Alisema Mzee huyo na kuweka tuo. Wakati wote huo Maganga na Hellen walikuwa wakisikiliza kwa makini sana. “Hellen na Maganga, nadhani tumeongea mengi, tumeulizana mengi na tumejibizana mengi, binafsi naona kama nimetua mzigo niliokuwa nimeubeba kwa siku nyingi sana.” Alisema Mzee huyo.
* * *
Hii ilikuwa siku ya tano tangu siku ile Mzee Mwasumbi alipomwokoa Hellen katika tundu la kifo na kumteka nyara Maganga kwa nia njema kama yeye mwenyewe anavyosema.
“Kukuteka kwangu nyara, niliona ndiyo njia pekee ya mimi kupata muda wa kuongea na wewe mambo haya mazito, na wakati huohuo wewe ungeweza kunisikiliza.
Mnayo haki ya kuyafanyia uchunguzi mambo haya niliyowaambia ili kuthibitisha kama ni kweli au la.
Naomba mniache niendelee kuishi maisha yangu haya ila kama kwa kufanya hivyo mnaona siwadhulumu na kuwanyima haki zenu za msingi. Kwa hivi sasa niko tayari kwa lolote kwani baada ya kuyasema haya maisha yangu hayana thamani kama yalivyokuwa hapo kwanza. Nilikuwa naogopa sana kama ningekufa halafu nyuma yangu akakosekana mtu wa kuufunua ukweli huu. Lakini maadamu nimeshausema, hata nikifa hakuna jambo ambalo litanifanya nitamani kurudi Duniani.” Alisema Mwasumbi huku akiwa anajitengeneza kitini. Walikuwa wameshaongea mengi na ilivyokuwa kila mtu alikuwa ameridhika na hakukuwa na la kuongezea.
“Hivyo mimi leo nawaruhusu kuondoka hapa, ila msimwambie mtu kuhusu maisha yangu. Napenda niendelee kuishi hivi, msalimieni Milka na ningependa nionane naye pia.” Alisema Mwasumbi huku akisimama na kwenda kukumbatiana na Maganga na Hellen, ambao hata hivyo walioneka kana kwamba wamepigwa na bumbuwazi na walihitaji muda kutafakari na kupembua yote waliyokuwa wameyaona na kuyasikia hapo.
**********
UMATI MKUBWA ULIKUWA UMEKUSANYIKA kwa Mzee Paul kufuatia kifo cha Agatha, mke wa Mzee Paul. Msiba huo ulikuwa umebeba hisia tofauti-tofauti miongoni mwa wanakijiji waombolezaji. Wapo waliokuwa wanajua kuwa mke wa Mzee Paul alifariki kufuatia kipigo kikali toka kwa mumewe, Mzee Paul.
Mzee Paul mwenyewe hakuwa anaumizwa kichwa na kifo cha mke wake, sababu za kutoumizwa sana na kifo hicho ni nyingi na zilikuwa wazi kichwani mwake lakini kubwa ni kuwa Maganga alikuwa na umuhimu zaidi kuliko utu na mapenzi. Ni kweli Agatha mkewe walikuwa wameishi naye kwa muda mrefu lakini yeye hakuhesabu kuwa ni kitu kwani hawakuwahi kuwa na mtoto na mwanamke huyo. Kwa sasa kichwa chake kilikuwa kinaumizwa na kutoonekana kwa Maganga.
Katika hali halisi msiba huu ulikwa ‘msiba’ kwa Vivian na Milka. Walikuwa wameona jinsi Aghata mke wa Paul alivyokuwa amefariki. Lakini pia, walikuwa wanaujua ukweli kuwa kifo kile kilikuwa kinatokana na kipigo alichopata toka kwa Paul. Tatu ilikuwa haijulikani Maganga alikuwa wapi. Kingine kilichokuwa kinawaumiza ni kauli ya mwisho aliyokuwa ametoa mama yake Milka dakika za mwisho za uhai wake. Ile kauli kuwa wamsamehe na kuwa amemsamehe baba yao kwa vile amemfichia siri kwa muda mrefu. Ilikuwa inamuumiza Milka kutaka kujua ni ‘siri’ gani ambayo baba yake alikuwa amemfichia mama yake kiasi kuwa mama akawa tayari kumsamehe. Pili, ni kitu gani ambacho mama alitaka wamsamehe, maana hakuweza kukisema wazi.
Mzee Paul alikuwa amegoma mwili wa mke wake kuzikwa ikiwa Maganga hakuwepo.
“Haiwezekani mke wangu kuzikwa wakati mwanangu hayupo. Nimeshaomba hospitali watauchoma sindano mwili ili usiharibike” Alisema Mzee Paul ambaye sasa alikuwa anatembelea gongo.
Jioni hii siku ya tano watu wakiwa wamekaa, wangine wanacheza bao, wangine karata, wengine wako kwenye mabishano ya mpira, wamama washika dini wako wanaimba zile nyimbo za misibani na wengine wakiwa na habari zao za umbea tu, maana penye wengi pana mengi.
Mara kwa mbali wakaona watu wawili wanakuja. Wakiwa kwa mbali hakuna aliyeweza kutambua sura zao, ila ilikuwa dhahiri kuwa mmoja alikuwa mwanaume na mwingine ni mwanamke. Watu hao waliposogea karibu ndipo watu walipoweza kutambua kuwa walikuwa ni Maganga na Hellen. Wengi walimjua Maganga ila hawakuwa wanamjua Hellen. Kutokezea kwa Maganga kulisababisha msiba kuanza moja, watu walilia sana, lakini Milka alilia zaidi huku akionyesha dhahiri kutokumwelewa kaka yake. Katoweka kwa takribani wiki nzima halafu anarejea katikati ya msiba akiwa na msichana ambaye ni mgeni pale kijijini.
Maganga alipoambiwa kuwa ule msiba ulikuwa wa mama yake alikaa chini mavumbini, kisha akalia sana.
“Baba yuko wapi?” Alilia huku akiuliza watu wamuonyeshe baba yake.
Huku akiwa anaomboleza kwa uchungu mkubwa Maganga alilia kuelekea kilipokuwa chumba cha baba yake. Kabla hata hajaingia ndani mara akasikia sauti inamwita kwa nyuma yake usawa wa mlango wa kutokea nje. Aliifahamu sauti hiyo, ilikuwa ya Askofu Alphonso, Maganga aligeuka na kumwangalia askofu kwa macho makali.
“Maganga, naomba tuonane ofisini kwangu, naelewa hali uliyonayo sasa, ila tafadhali sana naomba tuonane sasa hivi.” Askofu alisema huku akimshika na kumkumbatia Maganga.
“Nataka kumuona Mzee Paul kwanza halafu nitakuja baba Askofu.” Maganga alisema kwa jazba na uchungu mkubwa.
“Nakushauri tungeongea kwanza, ni maongezi muhimu sana ambayo yatakusaidia pia, kuonana na baba yako.” Askofu alisema huku akiwa anamwangalia Maganga machoni. Maganga alipoonyesha kutoafikiana na Askofu, ndipo Askofu akamnong’oneza
“Baba yako yuko kule kwangu.”
Kusikia hivyo, Maganga hakubisha tena waliongozana na Askofu kuelekea kanisani ambako pia, pembeni yake kulikuwa na nyumba ya Askofu na watawa wengine.
Maganga na Askofu walikuwa wameshaingia ndani ya nyumba ya Askofu wakati waliposikia mlio wa Bastola. Maganga alishtuka, askofu hakushtuka, alitabasamu. Maganga akainuka kwa haraka ili atoke nje lakini mara Askofu akamwita kwa sauti ya chini. Maganga alipogeuka kumwangalia Askofu akakuta ameshikilia bastola ameielekeza kifuani kwa Maganga. Maganga akabaki ameduwaa. Wakati hajui afanye nini maana hakutegemea kukabiliana na hali kama hiyo, Maganga alihisi anachomwa na kitu kama pini shingoni mwake. Alipotaka kushika sehemu aliyohisi yale maumivu, alishangaa alipohisi kuwa alikuwa amepoteza uwezo wa kunyanyua mkono wake. Wakati huo huo akahisi macho yake yamekuwa mazito kiasi kwamba uwezo wa kunyanyua kope ukamtoka. Giza likamvaa usoni na miguu yake ikashindwa kuubeba mwili. Akaanguka chini huku fahamu zikiwa zinamtoroka taratibu.
* * *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Fahamu zilipomrudia Maganga alijikuta amelala kitandani. Alizungusha macho pande zote, chumba kilikuwa nadhifu sana. Kila kitu ndani ya chumba hicho kilikuwa cheupe; mashuka, mapazia, viti na chochote kilichokuwepo. Ni sehemu chache ambazo vitu hivyo vyeupe vilikuwa vimewekewa alama ya msalaba mwekundu. Alijiinua taratiibu, akairuhusu miguu yake kutoka kitandani na kukanyaga chini. Miguu ikagusa chini, hilo likaruhusu yeye kuubebesha mwili wake kwenye hiyo miguu. Akasimama. Aliposimama ndipo akaona karatasi ndogo ikiangukia sakafuni toka pale kitandani. Inaonyesha karatasi hiyo ilikuwa juu ya mwili wake hivyo alipoinuka ikaanguka chini. Maganga aliiangalia karatasi hiyo ya njano iliyokuwa na maandishi meusi. Akainama kuichukua, wakati anaichukua ndipo alipogundua kuwa vidole vyake vilikuwa vikitetemeka. Hata hivyo aliichukua na macho yake yakakimbilia haraka kusoma maandishi ambayo yalisomeka hivi, ‘RELAX, IT IS FOR YOUR SAFETY. SAFE TRAINING. REV. ALPHONSO.’Kwa Kiswahili yakiwa na maana; ‘TULIA, NI KWA USALAMA WAKO. MAFUNZO MEMA.’ Ilikuwa wazi kuwa mwandishi wa Karatasi hiyo alikuwa ni Askofu Alphonso. Maganga alielewa maneno yale yanasomekaje, lakini hakuweza kuelewa lengo hasa la Askofu Alponso kusema vile. Aliiangalia ile karatasi kama mtu anayetaka kuuliza maelezo zaidi juu ya kile alichosoma. Lakini karatasi haikuwa na jipya. Akaikunja na kuiweka mfukoni. Wakati ameingiza mkono mfukoni ndipo alipohisi uwepo wa kitu kingine mfukoni mule. Vidole vyake vilikivuta kile kitu. Ilikuwa ni karatasi nyingine iliyokuwa chafu. Ndipo alipokumbuka kuwa kabla hajaondoka kumfuata askofu Alphonso siku ile pale nyumbani kwao alikuwa ameenda chini ya mtungi kama mama yake alivyokuwa amemhimiza asubuhi ile wakiwa ndani ya gari la Vivian muda mfupi kabla ya kupelekwa hospitali. Hapo tena Maganga akawa na hamu ya kujua kilichokuwa ndani ya karatasi hiyo. Hamu hiyo ilitokana na jinsi mama yake alivyokuwa ameificha ile karatasi na pia muda ambao mama yake aliamua kumwambia kuhusu hiyo karatasi. Alijua kwa vyovyote karatasi hiyo itakuwa na mambo muhimu ambayo mama yake angependa yeye ajue. Maganga aliifunua karatasi hiyo kisha macho yake yakaanza kutembea kwenye maandishi. Barua ilisomeka
Mwanangu, Maganga!
Sijui ni mazingira gani uliyonayo wakati unaisoma karatasi hii, ila ni dua yangu kuwa upate nafasi ya kuisoma maana ni muhimu sana kwako na kwa ndugu zako.
Maganga, leo siku ambayo tunakuaga hapa nyumbani kwa vile unasafiri kwenda shule kuanza mafunzo yako ya Ukasisi, nimegundua kuwa mbali ya kuwa mama na mwana lakini pia tumekuwa marafiki wakubwa sana. Najisikia furaha na fahari kubwa kuwa mama yako huku wewe ukionekana kuwa na furaha sana.
Lakini hata hivyo, kuna mambo ambayo siwezi kukuambia leo katika umri huu ulionao. Natamani ujumbe huu uupate miaka kumi au kumi na tano toka leo. Lengo langu ni kuwa upate haya ninayoandika humu siku ambayo utakuwa unapata upadirisho. Najua huo ndiyo utakuwa wakati muafaka. Ila kutokana na hali ya maisha niishiyo na Paul lolote linaweza tokea wakati wowote. Hivyo kwa kuwa sasa umeweza kuipata Karatasi hii ina maana nimeshindwa kusubiri hadi wakati huo ambao ningekuambia kwa mdomo wangu mwenyewe. Inawezekana wakati huu unaposoma karatasi hii mimi ni marehemu au ni taabani sijiwezi.
Maganga mwanangu, ningependa ujue haya mambo manne. Ningependa ujue majina yenu halisi kuwa mnaitwa;
1. Maganga Mwasumbi
2. Milka Mwenda
3. Vivian Mwasumbi
4. Hellen Paul
Maganga mwanangu, baada ya kuyajua mambo hayo manne, pia ningependa kukuambia machache ambayo yatakusaidia. Haya niyasemayo ni hisia zangu, naomba ufanye ambavyo hisia zako zitakuongoza na uonavyo kuwa ni vema.
Mwanangu, ni vema kuwa Padri, ila kwa mazingira yanayokuzunguka lazima ujifunze upande wa pili wa shilingi. Zingatia hili, Mwasumbi na Paul wako kazini. Ni mmoja tu kati yao aliye upande wako. Nasikitika kukuambia kuwa kwa kweli sijui ni yupi aliye upande wako. Nimejitahidi sana kwa miaka yote tangu umezaliwa hadi leo ninavyoandika ujumbe huu kutaka kujua nani hasa yuko upande wako lakini sijafanikiwa. Ninachojua ni kuwa wewe ni mtu uliyejaaliwa sana na unahitajika sana. Na kati ya hao niliowataja hawajuani kuwa wako kazini na mlengwa wao ni mmoja.
Nijuavyo ni kuwa ukimaliza mafunzo ya Upadri utakuwa umehitimu nusu ya kile unatakiwa kujifunza. Utakuwa umemaliza nusu ya safari ya mafunzo yako. Itakuja awamu ya pili.
Naomba ushike hii namba kichwani siku ukiona kuwa umefikia sehemu huwezi kuendelea mbele piga hii namba kwa msaada +255785975443.
Maganga, nakupenda sana mwanangu. Naamini utashinda yote yaliyoko mbele yako. Pia, utawasaidia wenzio kujua ukweli.
Umalizapo kusoma karatasi hii, tafadhali sana iharibu kwa kuichoma moto au kuitumbukiza chooni. Mtu yeyote akiiona itakuwa hatari sana, kwa maisha yako na ndugu zako.
Tafadhali kariri sana hiyo namba ya simu.
Akupendaye milele,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Agatha wa Mwasumbi na Paul.
Maganga alibaki akiwa ameiangalia ile karatasi kama Pusi aliyeona shimo la Panya. Wakati anaanza kusoma alikuwa amesimama lakini pindi alipomaliza alijikuta akiwa ameketi kitandani. Barua ile iligusa roho, nafsi na mwili wake. Mambo mengi yaliujaza ubongo wake. Alimtafakari Askofu Alphonso akamuacha, aliwaza mazungumzo yake na Mzee Mwasumbi, alimtafakari Milka akamwacha, aliwaza ujio wa Hellen kijijini kwao na jinsi mtu ambaye yeye alikuwa anajua ni baba yake alivyotaka kumuua binti yule. Alipomuwaza Mzee Paul na visa vyake vyote, Maganga akajikuta anajawa na hasira. Aliwaza namna Milka, Hellen na Vivian ambavyo wangekuwa wanamfikiria wakati huu ambapo yeye ametoweka katikati ya msiba wa mama yake na kuugua kwa baba yake. Wakati akiwa anawaza mara akasikia vishindo vya mtu aliyekuwa akitembea. Vishindo vya hatua za huyo mtu vilionyesha kuwa mtembeaji alikuwa akija upande wa chumba alichokuwa kwani sasa aliweza kuvisikia kwa karibu zaidi. Aliingalia ile barua ya mama yake, haraka haraka akaifutika mfukoni.
Mlango wa chumba alichokuwemo ulifunguliwa. Aliingia binti mmoja mrembo sana, alimtazama kwa nukta chache kisha akaurudisha mlango nyuma yake.
“Naitwa Maganga. Unaitwa nani na hapa ni wapi?” Maganga aliongea kwa haraka haraka. Badala ya kujibu yule msichana alitembea taratibu hadi pembeni ya chumba sehemu iliyokuwa na meza. Akaweka kitu kama daftari lakini kilifanana hasa na kadi za harusi sambamba na hicho akaweka saa ya mkononi iliyotengenezwa kwa plastic. Alipomaliza akageuka na kutoka kwa kupitia sehemu aliyoingilia bila kuaga wala kuongea lolote.
Maganga akabaki anashangaa. Akaenda pale vilipowekwa vile vitu, akachukua ile karatasi na kuisoma. Alishangaa kwa jinsi ilivyokuwa imeandikwa. Ilikwa na kichwa kilichoandikwa, ‘RATIBA YA MAFUNZO’, halafu kikafuatiwa na ratiba ya siku nzima ambayo ilijaa matukio ambayo alitakiwa kuyafanya huku yeye akitajwa kama mwanafunzi. Katika ratiba hiyo hakukuwa na majina ya waalimu wala majina ya mahali alipotakiwa kuwa kwa mafunzo. Kulikuwa na muda kwa kila tukio huku muda wa kulala ukiwa ni saa nne tu kwa siku. Akaichukua ile saa akaangali, ilisomeka 6:05pm, hapo akajua kuwa ilikuwa ni saa kumi na mbili na dakika tano jioni. Kwa ratiba iliyokuwa mbele yake ilikuwa ni muda wa kula na kujiandaa kwa mazoezi ambayo yangeanza saa moja na nusu jioni.
Saa moja ilipofika, Maganga alikuwa amejipumzisha kwenye kitanda mle mle chumbani. Alikuwa amekula chakula katika hali ya kutatanisha baada ya kuletewa na mtu ambaye alikuwa haongei. Alipomaliza aligundua kuwa ndani ya chumba kile kulikuwa na kabati la nguo, bafu na choo. Hivyo tofauti na chakula, kila kitu angeweza kukipata ndani ya kile chumba. Mara taa ya chumbani humo ilizimika, giza likachukua nafasi. Akashtuka kiasi. Ukweli ni kuwa akili yake na hisia vilikuwa vimeshakufa ganzi, mambo yalivyokuwa yametokea kwa siku takribani saba mfululizo yalifanya awe mvivu wa kufikiri na hisia zake zilishamalizwa makali yake. Hivyo alijiona kuwa yuko tayari kwa lolote. Hakuwa anajali tena, aliona maisha yake hayakuwa na maana tena. Yangekuwaje na maana kama ameshindwa hata kumzika mama yake kipenzi, yatakuwaje na maana kama mtu aliyekuwa anatamani kuwa kama yeye ndiye aliyemteka na kumleta hapo. Yatakuwaje na maana kama muda wote amekuwa akiishi bila kumjua baba yake huku akiishi na mtu katili kama Mzee Paul. Yatakuwaje na maana.
“Njoo nifuate!” Sauti iliamuru tokea sehemu ambayo kulikuwa na mlango wa kutokea nje ya chumba kile. “Mbona hunielezi nikaelewa, wewe nani?”
“Njoo!” Ile sauti ilisema kwa ukali kidogo.
“Nieleweshe kwanza.” Maganga alisisitiza.
Hakupewa jibu, alishangaa tu anapokea kofi kali la usoni ambalo lilimpeleka hadi chini, kwa vile wakati aliposikia ile sauti alikuwa amesimama.
“Jesus!”Maganga aligugumia kwa maumivu.
“Njoo!” Ile sauti ilisema tena.
Maganga akatii. Alijikuta anafuata hatua za huyo mtu aliyekuwa mbele yake. Walipita milango kadhaa kabla ya kutokezea nje. Alishangaa kukutana na msitu mkubwa wa miti mikubwa na midogo.
“Hakikisha unanifuata kila ninakokwenda na kwa kasi ninayotumia. Ukishindwa unajua nini kitakupata.” Sauti ilisema. Maganga hakuwa na la kujibu wala hakupata nafasi ya kufanya hivyo kwani alikiona kivuli cha mtu aliyekuwa anamsemesha kilianza kukimbia kuingia kwenye lile pori.
Maganga akaanza kufuata. Sehemu walizopita zilikuwa za taabu na vichaka vilivyojaa miiba, lakini kila alipotaka kupumzika au kupunguza mwendo alishushiwa kipigo ambacho aliona heri kujilazimisha kukimbia kama alivyoamriwa. Hiyo ndio ikawa siku ya kwanza ya mafunzo ya Maganga. Aliporudi kwenye chumba chake alikuwa hoi huku akiwa na majeraha mengi mwilini.
************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment