Search This Blog

Monday 24 October 2022

PATASHIKA - 3

 

    Simulizi : Patashika

    Sehemu Ya Tatu (3)







    SIKU ILE AMBAYO MAGANGA NA HELLEN waliruhusiwa kuondoka kwa Mzee Mwasumbi, na Maganga alipofika nyumbani kwao kisha akaanza kumtafuta Mzee Paul huku akilia kwa uchungu. Dakika chache kabla ya kuwasili kwa Maganga na Hellen nyumbani hapo Mzee Paul alikuwa shimoni kwenye nyumba yake hiyo. Watu wakiwa wamejaa nyumbani kwake kufuatia kifo cha mke wake. Mzee Paul aliingia ndani kwake kwenye chumba cha kulala akiwa anatembea kwa taabu sana kwa vile mguu bado ulikuwa umefungiwa muhogo. Lakini baada ya kuwa amejifungia chumbani kwake. Haraka sana aliufungua ule muhogo. Baadaye aliinua kitanda chake cha miti na kukisukumia pembeni. Ule uigizaji wake kuwa mguu umevunjika akawa ameshaachana nao. Aliyekuwa akishughulika sasa ni Mzee Paul kamili ambaye alionekana kuwa alikuwa akiharakisha kutaka kufanya kitu. Baada ya kuwa amekisukumia kile kitanda pembeni, alisogea sehemu moja ya ukutani karibia na sakafu akapapasa kisha akashika kitu kilichokuwa kama kisiki, akakivuta kama anayetaka kuking’oa. Kikabanduka kama kifuniko. Baada ya kufunuka likaonekana kufuli dogo likiwa limeshikamanisha vyuma viwili bapa. Haraka, Mzee Paul kwa kutumia funguo alizochukua mfukoni mwake alifungua lile kufuli. Alichukua upanga uliokuwa chumbani humo na kuuingiza katikati ya vile vyuma viwili vilivyokuwa vimeshikanishwa na kufuli akaanza kupindua mithili ya mtu afunguaye mfuniko wa ndoo ya plastiki ya maji. Mfuniko ulipofunguka, kukawa na shimo kubwa kiasi cha kuweza kumtumbukiza mbuzi wa miezi tisa. Mzee Paul kabla ya kutumbukia ndani alipanga vitu mle chumbani na kuwa kama hapo awali. Baada ya kujiridhisha, aliingia uvunguni mwa kitanda chake kilichokuwa kimechoka na kuchakaa, uvunguni alikutana na shimo likiwa linamwangalia, alitumbukia kwa kutumia kamba aliyoukuwa imefungwa kwenye chuma cha mviringo kilichofanya ukingo wa lile shimo.

    Wakati Maganga anachukuliwa na Askofu Alphonso, kamba ilimpeleka Mzee Paul hadi tumboni mwa lile shimo, sakafu ikampokea huku mlio wa nyayo ukionyesha kuwa kulikuwa na uwazi wa kutosha. Alitembea taratiibu hadi sehemu ambayo alijikwaa kwenye kengele, mlio wa kengele hiyo ulifanya taa kuwaka. Mwanga wa taa ukafanya macho yake yaweze kuona kila kitu kilichokuwa ndani ya kile chumba.

    Kilikuwa chumba kizuri cha wastani. Kulikuwa na viti viwili na meza moja ambayo juu yake kulikuwa na computer laptop. Kwenye kona moja ya chumba hicho ambacho kuta zake zilioneka kuwa zimejengwa kwa matofali mazito kulikuwa na kabati moja ndogo ya chuma, ambayo ilionekana kuwa ya miaka mingi. Mzee Paul alielekea ilipokuwa ile kabati, katika rundo la funguo alizokuwa nazo ambazo katika hizo moja aliitumia kufungua kufuli lililokuwa kwenye mlango wa kwenda kwenye chumba hicho.

    Kwa muda wa saa moja na kama dakika arobaini, Mzee Paul alifungua na kusoma mafaili mbali mbali yaliyokuwa kwenye compyuta iliyokuwa kwenye hicho chumba. Betri moja kubwa ya kisasa iliyokuwa chumbani humo ambayo ilikuwa imeunganishwa kwenye mlango wa mabati wa kuingilia nyumbani kwa Mzee Paul, iliwezesha utoaji wa umeme kwa vifaa vichache vilivyokuwa chumbani humo. Mlango wa kuingilia nyumbani kwa Mzee Paul, ambao ni wa bati ulikuwa ni mashine maalum ya kukusanya nguvu za jua na kuzifanya kuwa umeme. Mtu yeyote angeiona nyumba ya Mzee Paul, ambayo ilikuwa imeezekwa kwa nyasi asingeweza kudhani kuwa mlango ule mbovu ulikuwa na kazi maalum kama hiyo. Mzee Paul, mara kwa mara alikuwa akigombana na mkewe juu ya kuhakikisha anaezeka vizuri sehemu ya mlangoni maana ilikuwa wazi kiasi kuwa wakati wa mvua maji ya mvua yaliweza kupitia sehemu ile na wakati wa jua, basi mionzi ya jua iliweza kulifikia barabara eneo lile. Mzee Paul, alikuwa akitoa visingizio mbalimbali ili mradi asiezeke lile eneo, alifanya makusudi maana alihitaji mionzi ya jua iweze kuufikia mlango ambao ulikuwa na kazi maalum. Mlango huo wa bati kwa usiri sana ulikuwa umeunganishwa na waya mmoja ambao ulikwenda moja kwa moja kwenye betri iliyokuwa kule shimoni. Hivyo betri hiyo ilikuwa ikipata nguvu kila siku.

    Wakati huu Paul alipokuwa kwenye shimo, hakuwa na wasi wasi juu ya umeme, ile betri ilifanya kazi. Kwa jinsi Mzee Paul alivyokuwa akifungua na kufunga mafaili mbalimbali ndani ya ile kompyuta na jinsi alivyokuwa akitumia keyboard kwa ustadi mkubwa usingeweza amini kuwa ndiye yule Mzee aliyeonekana wa kawaida tu pale kijijini. Sehemu nyingi alizotembelea ndani ya ile kompyuta, mafaili mengi aliyofungua yalihitaji neno la siri, lakini ilikuwa ajabu namna ambavyo aliweza kukumbuka maneno mengi ya siri, ya aina tofauti na mafaili kwa kasi na usahihi mkubwa.

    Aliporidhika na alichokuwa amefanya na kuona kwenye ile compyuta, Paul aliizima kisha akabaki amekaa kimya kama mtu anayesubiri kuingia kwa Daktari.

    Baadaye kama aliekurupushwa, alisimama na kuelekea upande mwingine wa shimo. Alifikia kwenye ukuta wa upande huu, hapo kulikuwa na kibuyu kilichokuwa kinaning’inia kwenye kamba moja iliyokuwa imefungwa toka darini mwa lile shimo. Alikichukua kile kibuyu, ndani yake alitoa kitu kama simu, simu ya upepo ambayo askari polisi hupenda kuzitumia wanapokuwa kwenye operesheni mbalimbali.

    Aliifungua ile simu, akaiwekea kitu kama betri, baada ya kuifunga akaifutafuta kisha, akaminya kitufe cha kuiwasha. Baada ya sekunde kadhaa, simu iliwaka na makelele mengi kusikika. Alirudi kwenye kile kiti kilichokuwa pembeni ya meza yenye compyuta. Makelele yalipopungua sasa alisikia sauti kama ya radio ambayo kituo cha matangazo kimewekwa hewani.

    “Hallo, Mr M hapa wa oparesheni TAFUTA, Over!” Mzee Paul alisema huku akiwa anasubiri majibu toka upande wa pili.

    “Ooooh! Mr. M, long time men, Captain hapa naongea, over!” Ulijibu upande wa pili.

    “Always on time Captain, najua leo jioni ndiyo siku ambayo mzigo unahitajika, Over!’ Mzee Paul alisema.







    “Ndiyo ndiyo, tumekusubiri sana kuanza kwa hii operesheni, hasahasa kuwasili kwa huo mzigo maana shughuli nzima inategemea uwepo wake.” Upande wa pili ulisema.

    “Vipi umeshatuma wasafirishaji, over?” Mzee Paul alihoji.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wameingia tangu juzi, walipowasili walinitaarifu na nikawaambia wawe maeneo hayo kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa maana mara nyingi mambo huharibika dakika za mwishoni kama umakini usipokuwepo, wapo hapo kijijini, nitawasiliana nao muda mfupi ujao ili ifikapo saa kumi na nusu jioni hii wafike hapo nyumbani kwako kuchukua mzigo na kuondoka, over.” Upande wa pili ulijibu.

    “Safi sana Captain, hata mimi nimechoka pia, nimekuwa hapa kwa miaka mingi sasa, nimekuwa kama mfungwa, ningejua hii kazi ingekuwa ndefu kiasi hiki wala nisingeichukua. Mzigo uko kwenye hali nzuri sana, utafurahi pindi utakapouona, haujaingiziwa uchafu wowote kichwani, bado uko safi. Over.” Mzee Paul alisema kwa sauti ya mtu aaliyetua mzigo mzito mabegani.

    “Hamna shida Mr. M, baada ya leo utakuwa huru kwa muda wakati ukisubiri hatua ya mwisho ya oparesheni hii. Baada ya kazi hii, nchi itakuhitaji kwa ajili ya kuandaa vijana wetu ambao watachukua nafasi zenu. Ila hilo tutaliongea baadae. Over.” Ulisema upande wa pili kwa sauti iliyoonyesha furaha.

    “Maagizo mengine Captain?” Mzee Paul aliuliza.

    “Maagizo mengine na njia za mawasiliano utazikuta sehemu ya mapokezi ya Hoteli Tilapia Mwanza. Ukifika sema unatoka kwa Captain, utahudumiwa. Hela ya kutosha wewe kwenda nchi yoyote na pia, Diplomatic Passport ya kukupa uwezo wa kwenda nchi yoyote. Hapo vipi Mr M? Over.” Upande wa pili ulisema kwa sauti ya kujigamba kidogo.

    “Imekaa vizuri sana Captain, hawakukosea waliokupa kuendesha hii oparesheni. Over!”

    “Asante Mr M”

    “Asante Captain.”

    “Over.”

    “Over.”

    Dakika ishirini baadaye, Mzee Paul alitokea ndani ya nyumba yake huku akichechemea kama mtu aliyekuwa na maumivu makali sana. Watu waliokuwa wamekusanyika pale mbele ya nyumba yake walimwangalia. Wapo waliomuonea huruma na wapo waliomuona yeye kama mdogo wake shetani. Alipofika chini ya mti waliokuwa wamekaa wazee wenzie aliketi. Wazee wengine ambao walikuwa bado hawajaonana naye waliendelea kumpa pole kwa msiba. Baada ya dakika kadhaa viongozi wa kijiji walimwita kutaka kuwa na maongezi naye.

    Walimweleza nia yao ya kutaka mazishi yafanyike siku hiyo, kwani isingekuwa busara kuendelea kuweka ndani ule mwili. Mzee Paul aliafikiana nao hasa ikizingatiwa kuwa alishaambiwa kuwa Maganga alikuwa ameshaonekana. Kusikia kuwa Maganga ameondoka na Askofu Alphonso kwa maongezi kulimfanya Mzee Paul afarijike. Alikubaliana na wazo la wazee wa kijiji. Mara moja vijana wakaelekezwa sehemu ya kuchimba kaburi.

    Kaburi lilipokuwa tayari, mjira ya jioni, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tayari kwa mazishi. Watu wote walikuwa wameshakuwa eneo la tukio isipokuwa Maganga, Vivian, Hellen na Askofu Alfonso.

    * * *

    Vivian na Hellen walikuwa wanatoka nyumbani kwa Askofu Alphonso. Walimwona wakati Askofu Alphonso anamchukua Maganga. Kutokana na hali aliyotoka nayo Maganga pale nyumbani na muda aliokaa kwa Askofu Alphonso viliwapa wasiwasi hivyo kwa pamoja wakajikuta wanakubaliana kwenda kuangalia kulikoni.

    Walipofika walipokelewa vizuri na Askofu Alphonso ambaye alianza nao maongezi. Walishangaa kutomkuta Maganga eneo lile.

    “Kutokana na hali aliyokuwa nayo Maganga, nimemwambia afanye sala maalum. Ila itakwisha muda si mrefu kutoka sasa. Inaonekana ana hasira sana juu ya baba yake, hilo si jambo zuri, ni kweli Mzee Paul anaweza kuwa amekosea lakini yeye kama mwanaye na pia, mtumishi wa Bwana anatakiwa kuwa na moyo mstahimilivu na wa kusamehe.” Aliongea Askofu huku macho yake yakiwa mapajani kwa Vivian.

    “Vivian ulifanyaje hapo?” Askofu Alphonso alihoji huku macho yake akiwa ameyaelekeza kwenye paja la mguu wa kushoto wa Vivian.

    “Wapi?” Viviani alijibu kwa aibu kiasi huku akijaribu kuivuta khanga iliyokuwa imeacha wazi sehemu ya paja lake. Alikuwa amevaa sketi fupi sana lakini kwa sababu ya msiba alikuwa amevaa khanga kwa juu. Kwa Vivian kuvaa nguo fupi ilikuwa jambo la kawaida japo wazee kijijini pale walijaribu kupiga kelele dhidi ya tabia yake hiyo lakini, hawakufanikiwa kumbadilisha. Mazingira ya watu aliyokuwa akiishi wakati akiwa shuleni huko Ulaya yalikuwa yameshambadilisha kwa kiasi kikubwa.

    “Unajua hiyo alama imenikumbusha kitu.” Alisema Askofu Alphonso huku akiwa anameza mate.

    “Kitu gani?” Vivian aliuliza kwa mshangao. Hakutegemea Askofu angeendeleza mazungumzo yale. Vivian alimwangalia Hellen usoni na kukutana na mshangao usoni kwa binti huyo kadhalika.

    “Ulizaliwa Hospitali gani?” Askofu alihoji huku akiwa anamwangalia Vivian usoni.

    “Bugando Mwanza.” Vivian alijibu kwa sauti ya kukereka kidogo.

    “Aiseee!, umewahi kumuuliza mama yako kama kuna kisa chochote cha kushangaza kiliwahi kutokea wakati wa kuzaliwa kwako?” Askofu Alphonso alizidi kuwashangaza wale mabinti kwa maswali yake.

    “Mmmmmmh! hapana, ila siku moja niliwahi kutembelea hospital ya Bugando kutaka kujua sehemu niliyozaliwa. Nilipotaja tarehe niliyozaliwa, nilielekezwa kumuona Daktari mmoja mzee. Yule Daktari aliponiona na nilipomweleza shida yangu aliangalia paja langu la mguu wa kushoto. Alipoangalia akasema, sitoweza kuangalia wodi niliyozaliwa kwa vile, asubuhi iliyofuata baada ya kuzaliwa kwangu, kulitokea mlipuko kwenye ile wodi, na Daktari wa kiyahudi ambaye ndiye alikuwa daktari pekee aliyekuwa amebaki katika hospital ya Bugando inasemekana aliuawa katika mlipuko huo. Mwili wa Daktari huyo haukuwahi kuonekana hadi sasa, hivyo serikali ya Israel ikaiomba serikali ya Tanzania kuifunga ile wodi hadi watakapo kamilisha uchunguzi wao. Ni miaka mingi sasa, hicho chumba kimefungwa na hairuhusiwi mtu kuingia wala kutoka.” Vivian aliema huku sasa ile hali ya kukereka ikiwa imeondoka usoni na badala yake mshangao ulichukua nafasi.

    “Sasa, na wewe nini kimekufanya uunganishe hii alama yangu na siku yangu ya kuzaliwa. Maana yule Daktari naye aliunganisha kuzaliwa kwangu na alama pajani.” Vivian alihoji.

    “Ndiyo maana nimekwambia hiyo alama imenikumbusha kitu. Any way, tutaongea kwa mapana zaidi siku nyingine. Ila nadhani kwa sasa twende msibani. Tangulieni mimi nitakuja na Maganga.” Askofu Alphonso alisema huku akiwa anasimama. Vivian na Hellen nao walisimama. Macho ya askofu Alphonso yalikuwa mwilini mwa Vivian muda wote.

    Walipofika nje ya mlango, Alphonso aliita.

    “Vivian!”

    “Bee!, Baba Askofu!

    “Naomba nikuone kidogo.” Alphonso alisema huku akiminya jicho la kushoto.

    “Makubwaaaa!” Hellen alinong’ona.

    Vivian alirudi ndani.

    “Vivian tutaongea zaidi msiba ukiisha, hakikisha unaniona ili nikupe habari vizuri. Ila ukifanikiwa kuingia ndani na kufunua ile maiti ya mama yake Maganga, na ukaona ana alama kama yako pajani, ujue ni mama yako pia. Baadae.” Askofu alisema kwa kunong’ona. Kauli hii ilimchanganya sana Vivian. Lakini alijua wazi hakuwa na muda wa kuuliza zaidi. Ila alidhamiria kufanya alichoambiwa na Askofu Alphonso.





    *********

    Kukosekana kwa Hellen, Maganga, Vivian na Askofu Alphonso kulifanya minong’ono kuzagaa eneo hilo. Toafauti na kawaida yake, Mzee Paul alikuwa mpole huku akisikilizia kilichokuwa kinaendelea.

    “Jamani, naomba tutulie. Nimepewa taarifa hapa kuwa Maganga alichukuliwa na Askofu Alphonso wakaelekea nyumbani kwa askofu. Baadaye Vivian na Binti mwingine wameenda kuwaita.” Alisema Mwenyekiti wa Kijiji katika hali ya kupooza minong’ono iliyokuwa ikiendelea.

    Wakati watu bado wakiwa katika ile sintofahamu, mara ulisikika muungurumo wa gari. Haukuwa muungurumo mpya, wengi walishauzoea, ulikuwa wa gari la Askofu Alphonso. Na kweli, gari lilitokezea, lakini tofauti na matarajio ya wengi hailikuwa limetokea upande yaliko majengo ya kanisa na nyumba za watawa. Lilitokea upande mwingine iliko barabara ya kuelekea madukani. Watu wakashikwa na mshangao.

    Si watu waliokuwa kwenye eneo la kaburi tu, hata Vivian na Hellen walishikwa na mshangao. Walikuwa wanatoka nyumbani kwa Askofu Alphonso, walikuwa wamemwacha kwa makubaliano kuwa angekuja muda mfupi ujao baada ya Maganga kumaliza sala maalum. Sasa iweje wanamwona Askofu Alphonso akiwa anatokea upande mwingine. Walichanganyikiwa.

    Askofu Alphonso alishuka kwenye gari na kuanza kutembea taratibu pale walipokuwa wanakijiji. Watu walizidi kushangaa. Alipofika kwa wanakijiji, alienda alipokwa Mzee Paul, alimkumbatia kwa upendo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Pole sana baba Maganga, habari ya msiba huu imenisikitisha sana. Nilikuwa Mwanza mjini lakini imebidi nije haraka ili kuhakikisha nahudhuria huu msiba…”

    “Hebu acha mzaha Askofu, unasema ulikuwa Dar es salaam wakati tulikuwa hapa wote muda wote huu!?’ Mzee Paul aliongea kwa jazba na hamaki kubwa.

    “Baba Maganga najua inawezekana labda umechanganyikiwa kwa msiba wa ghafula wa mkeo mpenzi. Tuliza akili. Mungu atakusaidia…” Kabla hata Askofu hajamaliza, Mzee Paul alirusha ngumi kali iliyompata.

    “Haya niambie haraka sana Maganga yuko wapi?” Alifoka Mzee Paul kwa jazba, huku watu wakishangaa jinsi mtu aliyekuwa mgonjwa wa mguu akiwa anatembea sawa sawa.

    “We! Askofu, hivi unataka kusema kweli siye wewe tuliyekuwa tukiongea wote kule nyumbani kwako sasa hivi?” Vivian aling’aka kwa hasira.

    Hapo ikatokea taharuki kubwa sana. Ikabidi watu waelekee nyumbani kwa Askofu Alphonso. Walipofika walikuta mlango uko wazi. Kundi la watu likavamia ile nyumba, wakaanza kukagua sehemu zote mule ndani lakini hawakuona mtu.

    “Mamaaaaa!” Sauti ya kike ilitokea upande ambako kulikuwa na jiko na bafu. Watu wote wakaelekea huko. Yule mama alitoka anakimbia.

    “Vipi mama?” Askofu aliuliza kwa fujo.

    “Hebu pisha huko!” Yule mama hata kabla hajajibu, Mzee Paul alielekea bafuni kwa kasi na kumsukuma Askofu Alphonso apishe njiani.

    Mzee Paul alipofika kwenye mlango wa choo, aligutuka kidogo.

    “Shiiiiiit!” Ilimtoka. Lakini wakati watu wakija alifaulu kuinama na kuchukua karatasi iliyokuwa sakafuni pale. Aliiangalia kwa mshangao kidogo. Karatasi ilikuwa imeandikwa “Operesheni TAFUTA imeanza, muulizeni Mzee Paul!” Mara moja Paul alielewa nini kilikuwa kikiendelea. Hakutaka kupoteza muda wake na wale watu wala Askofu. Alishaelewa kuwa amezidiwa hesabu na watu asiowajua. Hivyo wakati umati wa wanakijiji ukisukumana kuja pale ulipo mlango wa choo, Mzee Paul yeye alikuwa akisukuma watu wampishe ili atoke eneo lile. Hakuwa na makelele tena. Yule mama aliyekuwa ameona kitu kilichokuwa bafuni alizidi kupiga kelele kwa nguvu.

    “Maiti za watu jamani, zimevimba, uuuuuuwi watu wana dhambi!”

    “Wewe kweli…Askofu ndiyo kafanya hivyo au?” Walizidi kuropoka hili na lile. Askofu akajikuta kwenye wakati mgumu sana. Hakuwa anajua nini kilikuwa kikiendelea.

    Hebu Vivian na yule msichana ninyi ndiyo mlikuwa wa mwisho kuonana na Askofu, tuelezeni kilichotokea.” Hatimaye Mwenyekiti wa Kijiji aliongea kwa hamaki.

    “Yule msichana na Vivian mko wapi?” Mwenyekiti aliuliza kwa sauti ya kupaa.

    “Niko hapa!” Hellen alijibu kwa hofu kubwa.

    “Njoo hapa!” Mwenyekiti aliamuru. Umati wa watu ukatulia tuli. Hellen akajongea alipokuwa amesimama mwenyekiti.

    “Vivian yuko wapi?” Mwenyekiti aliunguruma huku watu wakiwa wanageuza macho huku na kule katika kumtafuta Vivian.

    Vivian hakuwepo eneo lile. Alijionea mambo yalivyokuwa yakienda kwa kasi, alishaona maji ya mto yalikuwa yakielekea wapi, hivyo hakutaka kuoegelea yalipokuwa yakitokea, akaona ni busara kuogelea yalipokuwa yakielekea huenda angeweza kuona mti wa kushika na kujiokoa. Alipoona watu wote wamekimbilia nyumbani kwa Askofu Alphonso, yeye aliona ndiyo mwanya wa kuangalia kile alichoambiwa na yule Askofu Alphonso mwingine. Maana hadi sasa ilikuwa dhahiri kichwani mwake kuwa kulikuwa na Askofu Alphonso wawili.

    Haraka sana alielekea walipokuwa wameweka jeneza lililokuwa na mwili wa mke wa Mzee Paul, kiu ya kutaka kujua ilikuwa imemjaa kifua na kichwa chake kiasi kuwa hofu na kinyaa vikawa mbali sana na hisia zake. Alipekuwa, japo mwili ulikuwa umeshavimba. Alipofika kwenye sehemu ya paja la kushoto la ile maiti, macho yalimtoka. Aliona alama kama ile aliyokuwa nayo kwenye paja lake la mguu wa kushoto.

    “Ina maana mama yake Maganga ni mama yangu? Ina maana Mzee Paul ni baba yangu? Na wazazi nilionao sasa, je?”

    Maswali mengi yalifumuka kichwani mwa Vivian, akajikuta kichwa kinakuwa kizito. Mara akaona kama anga linazunguka kwa kasi. Akaona kiza usoni. Fahamu zikamtoka.

    Paul alimwona Vivian akiwa anaanguka lakini hakuwa na muda wa kushughulika naye kwani aliweza kuliona gari moja la kifahari jeusi liliokuwa imeegeshwa mbele ya nyumba yake. Alielewa kuwa wale ndiyo wasafirishaji waliokuwa wametoka kwa CAPTAIN, mtu aliyekuwa ameongea naye shimoni chini ya nyumba yake.

    “TAFUTA?” Mzee Paul alisema alipowafikia watu waliokuwa kwenye gari.

    “TAFUTA.” Walisema huku wakimwangalia Mzee Paul kwa macho yao yaliyokuwa kama ya paka.

    “Mzigo umetoweka, inabidi tufukue kila sehemu mradi upatikane. Mimi nitaenda kushugulika kule upande wa kanisa. Wewe utahakikisha kila nyumba inafukuliwa hapa kijijini. Wewe utahakikikisha hakuna mtu anatoka hapa kijijini. Sitaki makosa, tutapekua kila mahali ili mradi Maganga apatikane.” Alisema Mzee Paul kwa amri. Ile mipande ya watu ilitii amri na kuanza kushughulika.





    TILAPIA HOTEL, chumba namba nane kilikuwa kimewekwa picha ya samaki mlangoni. Juu ya kitanda kwenye chumba hicho Mzee Paul ndiyo kwanza alikuwa ameshtuka toka usingizini. Hakuamka, aliendelea kujigaragaza kwa muda juu ya kitanda hicho pasi kufungua macho. Mlio wa saa kuashiria ukamilifu wa wakati ulilia, Mzee Paul aliusikia lakini aliendelea kujigaragaza kwenye hicho kitanda kikubwa na kizuri. Baadaye huku akiwa amefumba macho alijivuta hadi kwenye ukingo wa kitanda hicho kwa juu upande wa kulia. Hapo kulikuwa na kimeza kidogo ambacho kilifanya sehemu ya kitanda hicho. Akiwa bado umefumba macho alinyanyua mkono wake kivivuvivu akauelekeza juu ya kile kimeza. Kiganja na vidole vikawa vinacheza kama vile ambavyo mtu aliye katika hatua za kukata roho ambaye yuko katika kuachia pumzi ya mwisho ya uhai wake hufanya. Akiwa amelala kifudifudi huku kichwa akiwa amekifukia kwenye mito miwili alipapasa hivyo kichovu hadi pale mlio wa saa iliyodondoka chini uliposikika. Alikuwa akitaka kuchukua saa, kivivu kivivu.

    “Shiiit!” Ilimtoka aliposikia mlio wa saa kudondoka chini. Bila kufungua macho alijivuta zaidi hadi pale kichwa ckake sasa kikawa kinaning’inia kwenye ukingo wa kitanda. Akafungua jicho moja, alilifumbua kidogo sana, aliiangalia ile saa. Aliona uvivu kuiokota.

    “Mmmmmh!, saa mbili tayari. Daaaah!” Alinong’ona kwa sauti ya kichovu. Akafumba jicho lake, akajisogeza katikati ya kitanda huku akiwa ameiacha ile saa pale chini. Akaendelea kujigaragaza kama chatu aliyemeza ndama. Safari hii alikuwa chali lakini akiwa bado amefumba macho yake. Alifanya hivyo kwa dakika kadhaa. Halafu taratibu akaanza kutulia. Mwishowe alitulia na kuyafungua macho yake taratibu. Aliliangalia dari, fikira zake zikiwa mbali toka chumbani humo. Aliyaruhusu macho yake kusafiri toka upande mmoja wa dari hadi upande mwingine kama ambaye alikuwa akisanifu namna fundi aliyetengeneza lile dari alikuwa amefanya kwa ubora kiasi gani. Macho yake yalipofika upande wa kushoto wa chumba kile ambamo pia, kulikuwa na dirisha kubwa, yalidakwa na mionzi michanga ya jua la mashariki ambalo lilikuwa likitoa uhai wake na kuvigawia viumbe mbalimbali vilivyohitaji mionzi hiyo. Mionzi hiyo ilimfanya afumbe tena macho yake kana kwamba yalikuwa yameshindwa vita na mionzi ya mwanga wa jua tamu la asubuhi. Dirisha lilikuwa limefunikwa na pazia zuri jeupe, lakini mionzi ya jua iliweza kupenya katikati ya muunganiko wa vipande viwili vya pazia hilo. Alifikicha macho yake huku akiwa anaupitisha ulimi wake juu ya meno ya juu na chini kinywani mwake kwa namna ya kuuzungusha ulimi huo. Ladha aliyoipata ilimfanya aone kuna umuhimu wa kuamka na kuianza siku yake alihitaji kuswaki. Kama aliyekurupushwa, alijibiringisha hadi upande wa chini wa kitanda sehemu ambayo alikuwa ameelekezea miguu yake wakati amelala. Huko alikisogeza kifua chake ukingoni mwa kitanda. Upande huo kulikuwa na meza ndogo ya mviringo.

    Huku akiwa bado amefumbua macho safari hii aliunyoosha mkono wake hadi ilipokuwa meza ndogo ya mviringo. Meza hiyo pamoja na mambo mengine ilikuwa na simu ya mezani. Mzee Paul aliichukua ile simu kizembezembe tena. Aliitua kitandani, akanyanyua mkonga wa simu, akaminya namba kadhaa huku akiwa amefumba macho. Lakini ni ajabu ambavyo aliweza kuminya namba alizozitaka. Kwanza aliminya namba sifuri na kuongea na mapokezi.

    “Nataka kupiga simu nje ya hoteli tafadhali.” Paul aliongea na mtu wa mapokezi.

    “Hamna shida Mzee, bonyeza 472 ikifuatiwa na namba unayotaka kupiga. Kama ni nje ya nchi anza na 972 kisha endelea kama kawaida. Gharama utazikuta kwenye bili yako.” Alisema mtu wa mapokezi. Mzee Paul hakuwa na muda wa kujibu, aliuweka chini mkonga na kuminya namba nyingine huku akiwa bado amefumba macho.

    “Hallo, je, hapo ni Katunguru hospitali ya misheni?” Mzee Paul alisema.

    "Ndiyo penyewe, naongea na nani na nikusaidie nini?”Upande wa pili ulijibu.

    “TAFUTA, naitwa TAFUTA. Nahitaji kuongea na Daktari Masaga tafadhali". Mzee Paul alisema.

    “Subiri kidogo tafadhali nikuunganishe ofisini kwake kama atakuwepo.” Ulijibu upande wa pili. Mzee Paul alisubiri hivyo kwa sekunde kadhaa.

    “ Hallo, naitwa Daktari Masaga, sijui mwenzangu?”

    “TAFUTA.” Mzee Paul alisema.

    “TAFUTA.” Upande wa pili ulisema.

    “Sikiliza, mambo yameharibika kiasi. Maganga ametoweka, jana ilikuwa patashika pale kijijini. Tumeteketeza karibuni Kijiji chote katika jitihada za kumtafuta. Nadhani utakuwa umepata taarifa. Hadi dakika hii naongea na wewe bado hatujafanikiwa kumpata…” Mzee Paul alisema kabla kauli yake haijakatishwa

    “Nimezipata, hivi hapa kuna askari kila kona ya Kijiji, unasakwa ile mbaya. Ila na nyie ni balaa watu watatu tu mmeweza kuteketeza kile Kijiji na raia bila kujali! Ama kweli!, hii ni Operesheni TAFUTA. Sasa nani atakuwa ameuchukua mzigo wetu, maana inauma sana baada ya kusubiri kwa miaka yote hiyo na mipango ya muda mrefu mambo yanataka kuharibika mwishoni jamani?” Ulisema upande wa pili.

    “Hilo ndilo linatuumiza vichwa, wakuu bado wanasubiri tuupeleke mzigo ili awamu ya pili ya mpango ianze. Nina wasiwasi wakisikia hili limetokea wanaweza chukua kichwa changu. Unajua nimekuja kugundua kuwa inawezekana Mwasumbi bado yuko hai. Hii nimeipata jana, inasemekana Maganga na msichana mwingine ambaye ni damu yangu walishinda kwake kwa siku zaidi ya nne. Sasa wasiwasi wangu inawezekana Mwasumbi anahusika au kuna upande ambao hatuujui nao uko kwenye huu mpango…hapo ndiyo sijui na natakiwa nijue ndani ya saa chache zijazo kama kweli nayapenda maisha yangu...”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Khaaaa! unamaanisha Mwasumbi yule Kipusa hatari…basi kazi ipo! Vipi Askofu huyu anajua lolote? Maana inasemekana anahojiwa hapa na Polisi lakini inasemekana hataki kusema chochote.” Ulisema upande wa pili wa simu.

    “Hapana, inavyoonekana kuna mtu alikuja akajibadilisha na kujifanya Askofu Alphonso, cha kusikitisha alifanikiwa kunihadaa hata miye. Unajua kwa jinsi nilivyokuwa nimetengeneza mazingira sikutegemea ingekuja julikana na yeyote kuwa tuko kwenye operesheni. Na ndiyo maana nikachagua sehemu ya mbali na ya kijijini ili kuweka haya mambo. Hivyo huyo mtu alivyoingia na kuondoka na Maganga ni kama mzimu tu. Ila kwa gharama yeyote, ili mpango huu ufanikiwe lazima nimpate Maganga.” Alisema Mzee Paul huku akiwa bado amefumba macho pale kitandani.

    “Nakuaminia Mr M. Wewe tena ukiamua hakuna la kushindikana. Nakumbuka siku ile umekuja hapa hospitali unajiliza mguu, tofauti na miye, hakuna mwingine aliyehisi kuwa ule ulikuwa mchezo kama michezo yetu mingi ambayo tuliwahi kuifanya pamoja…” Ulisema upande wa pili kabla kauli yake haijakatishwa.

    “Hilo ndiyo limefanya nikupigie. Najua uchunguzi unaweza kufika mbali, hivyo si ajabu watu wakajiuliza nilipona muda gani na kuweza kufanya yale mambo. Kwa kifupi lazima watajua kuwa kuna namna nilidanganya kuwa nimevunjika mguu, na kwa jinsi ule uongo ulivyokuwa lazima watashawishika kuja kuulizia hospitali zote nilizopita…nadhani unajua. Itajulikana ulishiriki uongo. Hivyo nashauri utoweke hapo Kijijini. Unaweza kwenda popote kati ya vituo vyetu…” Alisema Mzee Paul kwa sauti yenye mkazo.

    “Hilo ni kweli aisee, nitaondoka leo leo, sina haja ya kuchukua chochote. Nitaenda kujizika kokote kule, bila shaka akaunti yangu iko njema?”Ulihoji upande wa pili wa simu.

    “Hilo usitie shaka. Wewe tu!” Paul alisema.

    “Sawa, Mr M, nimefurahi kufanya kazi na wewe. Imekuwa kazi nzuri hadi hiyo jana na naamini ipo siku tutafanya kazi pamoja. Miye ninatoweka muda mfupi kuanzia sasa” Ulisema upande wa pili.

    “TAFUTA.” Paul alisema.

    “TAFUTA.” Upande wa pili ulijibu. Kisha, Paul akaweka simu chini kabla ya kuinyanyua tena. Safari hii akiwa amefumbua macho.

    “Hallo, je, hapo ni Hospitali ya Wilaya Sengerema?”

    “Ndiyo Mzee wangu, je, naongea na nani na nikusaidie nini?” Ulijibu upande wa pili.

    “Sihitaji msaada, nahitaji kuongea na Daktari Hassan wa kitengo cha mifupa tafadhali. Mwambie Mr TAFUTA, ninashida naye ya muhimu sana.” Mzee Paul alisema.

    “Sawa, subiri, usikate simu tafadhali nikuunganishe naye kama yuko ofisini.” Ulisema upande wa pili. Kisha ukafuata ule mlio wa simu inayounganishwa.

    “Hallo! Asante kwa kusubiri. Tafadhali ongea na daktari yuko hewani.”

    Ulisema upande wa pili.

    “Naitwa Hassan, nani mwenzangu na nikusaidie nini?” Ulisema upande wa pili.

    “Mr M hapa, TAFUTA!”

    “TAFUTA!” Upande wa pili ulijibu mara baada ya utambulisho wa Mzee Paul.

    “Sikiliza, mambo yameharibika, mzigo wetu ambao tumeuandaa kwa muda mrefu umetoweka. Sasa kazi ndiyo imeanza, badala ya kusonga mbele na hatua ya pili inabidi tuanze kuushughulikia mzigo ulipo. Maana kama ujuavyo bila Maganga mpango wetu kamwe hauwezi kutimia. Sasa kilichofanya nikupigie simu ni juu ya usalama wako. Unajua juzi nilikuja hapo, kwa hila na ukaniwekea ule mhogo. Sasa kwa hali ilivyo najua Polisi na watu wowote wa usalama watakufikia kuulizia kulikoni mgonjwa wako aonekane akifanya vitu kama vile nilivyofanya pale Kijijini. Hivyo unatakiwa utoweke muda wowote kuanzia sasa.” Mzee Paul alieleza huku akipiga mwayo.

    “Nimekuelewa Mr M. Ila nadhani ushauri huu umpe na Masaga maana ulipitia pale kwake kabla huajaja huku.” Upande wa pili ulishauri.

    “Unatilia mashaka utendaji wangu nini?” Mzee Paul alifoka. Alichukia pale alipogundua kuwa mtu wa upande wa pili alionyesha kuwa yeye hawezi kufikiria jambo dogo kama lile.

    “Hapana Mzee!” Ulijibu upande wa pili kwa sauti iliyojaa hofu mara hii.

    “Fanya kama nilivyokwambia, mengine niachie mimi.” Mzee Paul alisema kisha akaibamiza chini simu. Alipoweka simu chini alisikia mlango wa chumba alichokuwemo ukigongwa.

    “Nani?” Aliuliza kwa sauti ya juu kiasi. Lakini hakupata jibu. Kwa vile alikuwa bado hajaamka, alisimama huku akiwa uchi wa mnyama. Alitembea hadi upande kulikokuwa na bafu, alivuta taulo moja jeupe. Akajizungusha kiunoni, kisha akatembea kuelekea mlango wa chumba.

    “Nani wewe unayenikatisha usingizi wangu?” Aliuliza tena huku akiwa amekaribia mlango. Lakini mara akasita akaelekea kwenye kitanda alichokuwa akijigaragaza hapo awali. Alinyanyua mto mmoja na kuchomoa Bastola yake ya automatic.

    “Room service!” Sauti ya kike ilisikika mlangoni. Mzee Paul alivyosikia hivyo. Aliirudisha ile Bastola alipokuwa ameitoa. Kisha akauendea mlango. Alizungusha ufunguo, akaufungua malango. Akatoa kichwa nje ili amwangalie mhudumu aliyekuwa akibisha mlango. Hapo ndipo mara akajikuta amerushwa ndani chumbani kwa teke kali lililokuwa limetolewa na mtu tokea mlangoni. Kabla hata hajainuka, mara akaingia Kijana mmoja mwembamba akiwa amevalia sare za jeshi.





    Huyo ndiye aliyekuwa amepiga lile teke. Mzee Paul hakutaka kuamini kuwa uzito wa lile teke ulitoka kwa yule Kijana. Hivyo akasimama ili akabiliane naye, akashangaa kuona yule Kijana akiwa anamngoja tu. Mzee Paul kwa kasi sana alilivuta taulo na kulirusha kwa yule Kijana halafu akalifuata lile taulo. Wakati yule Kijana anatafuta namna ya kulikwepa lile taulo, alipokea teke zito la shingo akapepesuka. Baadaye alisikia kitu kama nyundo kinatua kichwani mara baada ya kichwa cha karibu kilichopigwa na Mzee Paul kutua upande wa sikioni. Kijana akajaribu kujiweka sawa, lakini Mzee Paul hakumpa hiyo nafasi. Alimwandama kwa vipigo vikali, halafu teke la paji la uso likawa limechukua uhai wa yule kijana. Wakati Mzee Paul hajakaa sawa aliingia binti mmoja mdogo tu na yeye alikuwa na sare za jeshi. Alikuwa akitabasamu huku akimwangalia Mzee Paul. Mzee Paul alimwangalia akamfananisha lakini hakuwa na muda wa kukumbuka alimwona wapi. Yule binti alikuwa ameshika ua jekundu mkononi. Alimrushia Mzee Paul.

    “Binti Ua Jekundu, kuna nini mbona mnanifanyia hivi?” Mzee Paul alisema baada ya kumbu kumbu kumjia

    “Unahitajika!” Yule binti alijibu huku tabasamu bado likiwa usoni.

    “Sasa kwa nini mnanijia namna hii?” Mzee Paul alihoji.

    “Shiiii!, sina muda wa kujibu maswali yako. Ama unakwenda na mimi kwa hiari au nakupeleka kwa nguvu.” Alisema yule binti huku akiangalia maiti ya yule mwenzie. Mzee Paul kuona, yule binti ameelekeza macho pembeni akataka ajaribu bahati yake. Akarusha mateke mawili makali, lakini akaambulia patupu, kisha akapokea vipigo vitatu tatanishi sana.

    “Naona umenisahau baada ya kuwa likizo ya muda mrefu siyo Mr M?” Yule binti alisema.

    “Unajua kawaida yangu, huwa naweka ua la heshima kwa mtu kabla hajafa ili aone kile nilichoweka kwenye maiti yake akiwa bado hai…” Kabla yule binti hajamalizia, Mzee Paul alirusha taulo lake tena kama alivyomfanyia yule Kijana mwingine ambaye sasa alikuwa marehemu.

    Yule binti kwa kasi ya ajabu sana alitoa kitu kama cheni akalipiga lile taulo na kulizungusha kisha akalirudisha usoni kwa Mzee Paul. Mzee Paul ambaye mara baada ya kurusha lile taulo akawa anamfuata yule binti huku akiwa ameshajiandaa kutoa kipigo alishangaa lile taulo linatua usoni kwake kisha mvua ya vipigo ikafuata.

    “Haya Ua Jekundu, nimekubali twende!” Mzee Paul alisema kwa sauti ya kusalimu amri. Lakini hilo halikumfanya yule binti aache kushusha kipigo. Yule binti alikuwa fundi wa kupiga. Baada ya muda, Mzee Paul alikuwa chini hoi hajitambui.

    “Nasikitika sana kuwa sitokuua, si kawaida yangu na unajua hilo, nikishamrushia mtu ua jekundu hakuna namna anaweza pona. Wewe unanijua vizuri.” Yule binti alisema. Lakini Mzee Paul hakuweza kujibu maana hakuweza hata kusikia sauti, alikuwa ameshazimia. Kuona vile yule binti alitoa simu yake ya upepo. Akaiwasha na kuminya kitufe.

    “Kapteni, Ua Jekundu hapa, Over!”

    “TAFUTA.” Upande wa pili ulisema.

    “TAFUTA.” Yule binti alisema.

    “Mr M tumempata ila wakati tunaingia kumuona kamuua Mika. Mr M, bado yuko vizuri sana huwezi amini. Vipi bado unamhitaji au nimalize? Over!” Yule binti alisema.

    “Mwache hapo nitatuma watu wamhifadhi, nahitaji ufanye kila namna uwatafute Vivian na Hellen. Maana kwa taarifa nilizo nazo hao wana habari ambazo zinaweza kuvuruga mambo yetu. Mwasumbi niachie mimi mwenyewe maana huyo hahitajiki haraka kiasi hicho. Ukiweza kuwapata hao watu wawili utakuwa umetuliza hali ya mambo wakati tukiendelea kujua mzigo uko wapi na kutafuta harufu ya Mwasumbi. Over!” Ulisema upande wa pili.

    “Nimekuelewa Kapten, Over!

    “TAFUTA, Over!” Ulisema upande wa pili.

    “TAFUTA, Over!” Alisema yule binti. Kisha akazima ile simu. Akatengeneza vizuri mavazi yake. Kisha akatoka mle chumbani tayari kwa kuanza msako wa Hellen na Vivian.

    ********http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    VIVIAN ALIPOZINDUKA alijikuta amekaa ndani ya gari ambalo lilikuwa kwenye mwendo wa kasi sana. Alikuwa amekalishwa kwenye kiti cha abiria pembeni ya dereva. Aligeuza shingo na kumuangalia dereva ambaye alikuwa akiendesha gari kwa kasi sana.

    “Askofu unanipeleka wapi? Tunaenda wapi? Mazishi yameshaisha? Tuko wapi? Ile alama uliyosema niingalie kwenye maiti ya mama Maganga niliiona je, inamaanisha nini? Mbona hunijibu, na kwa nini unaendesha gari langu kwa fujo kiasi hiki?” Maswali mengi mfululizo yalimtoka Vivian pasi kumpa nafasi muulizwa kujibu.

    Dereva aliendelea kuendesha huku akiwa kama mtu ambaye hajamsikia Vivian. Vivian akaanza kushikwa na mshangao juu ya hali hiyo ya Askofu Alphonso.

    “Sikiliza Vivian, unatakiwa utulie kwa usalama wako na wengine ambao maisha yao yanakutegemea wewe.” Alisema yule dereva huku akiendelea kukanyaga moto ili gari iongeze mwendo zaidi.

    “Mazishi yaliisha jana jioni na nitakueleze vizuri tukifika mahali pazuri na salama. Ila kwa sasa nakuomba tulia, hapo kwenye kiti cha nyuma kuna mfuko, ndani yake kuna boksi mbili za juice, chukua unywe maana hujala tangu jana ulivyoanguka na kuzimia.”

    “Ennnhe! ilikuwaje maana ninachokumbuka mara ya mwisho nilikuwa kwenye jeneza nikikagua mwili wa mama Maganga?” Vivian alihoji kwa shauku.

    “Nitakueleza yote, nitakueleza wewe ni nani, hiyo alama inamaanisha nini. Pia, nitakueleza kwa nini niliihusisha na yule daktari wa Kiyahudi kule kwenye Hospitali ya Bugando. Ila kwa sasa tuko hatarini, lazima tufanye namna ya kujiokoa kama kweli tunapenda maisha yetu na ya wale tuwapendao. Najua unampenda Maganga, lazima tumsaidie katika mazingira magumu aliyonayo.” Alisema Askofu Alphonso huku akijaribu kukwepa korongo moja lililokuwa mbele yao.

    Vivian aliangalia vijiji vilivyokuwa pembeni ya barabara na kugundua kuwa walikuwa kwenye barabara itokayo Kijiji cha Katunguru kwenda kilipo kivuko cha Kamanga. Aligundua kuwa walikuwa kwenye Kijiji cha Nyamatongo. Dereva alishindwa kukwepa korongo na wakawa wameliingia, gari ikayumba lakini kwa namna ya ajabu sana dereva alifanikiwa kulitoa gari na kuendelea na safari.

    Walipofika kijiji fulani, dereva alikatisha gari na kuingia nyumba za ndani Kijijini hapo. Kijiji hicho kilikuwa upande wa kushoto mwa barabara. Aliendesha gari hadi jirani na shamba moja lililokuwa na miwa.

    “Haya shuka!” Dereva aliamuru.

    “Ndiyo tumefika? Hapa ni wapi? Kwani hapa ndiyo kuna usalama sasa? Miye nilidhani tunaenda Kituo cha Polisi Kamanga?” Maswali yalimtoka Vivian. Alipomwangalia dereva usoni na kukutana na lile jicho akashituka.

    “Wewe ni Askofu Alphonso kweli, mbona macho yako yako tofauti.” Vivian aling’aka kwa sauti iliyojaa wasiwasi, mshituko na hofu.

    “Macho yangu yakoje?” Dereva aliuliza.

    “Yako kama ya ndama wa mwezi mmoja.” Vivian alisema huku safari hii akiwa hana hamu ya kumwangalia tena yule dereva.

    “Shuka!” Sauti ilisema tena, ila safari hii ikiwa na chembechembe za amri.

    “Mmmhhh!” Alipumua huku akiwa ameshafungua mlango wa gari na kushuka. Alikuwa ameshikilia boksi la juisi mkononi.

    “Simama pale!” Aliamuru tena.

    “Wewe ni mwanajeshi?” Vivian alihoji huku akichukua ujasiri wa kumwangalia usoni.

    “Simama pale binti, hatuna muda wa kupeana majibu hapa!” Aliamuru yule dereva kwa sauti ya hadhari.

    Vivian alipoenda sehemu aliyoambiwa asimame, yule dereva alikanyanga mafuta na kuiingiza ile gari kwenye shamba la miwa. Aliendesha hivyo hadi alipopotelea kwenye msitu wa miwa. Baada ya dakika kadhaa akaja akiwa anatembea.

    “Gari lako utapewa nyingine, ila kwa sasa sahau.” Alisema yule dereva huku akiwa anatembea kurudi upande wa barabarani. Wakati huu na yeye alikuwa na boksi la juisi mkononi.

    “Nifuate!” Alisema mara baada ya kugeuka na kukuta Vivian bado akiwa amesimama pale mahala pa kwanza kwa bumbuwazi. Alivyosema hivyo hakugeuka aliendelea kutembea, kuona hivyo, Vivian alianza kumfuata. Hakuwa na hiari maana hakuwa na mbadala wa yale maamuzi.





    Walitembea hadi walipofika barabara kuu.

    “Twende tukasimame kwenye kile kichaka, tusubiri basi, tukifanikiwa kupata basi itakuwa vema zaidi. Maana nimeona si salama kuendelea kusafiri kwa lile gari lako. Kutumia gari lako itawapa urahisi wa kutupata haraka.” Alisema yule dereva huku akimuonesha Vivian kichaka alichotaka waende. Yule dereva alikimbia hadi kwenye kile kichaka, kuona hivyo Vivian na yeye alikimbia kizembe huku akiwa anakunywa juisi yake kuelekea pale alipoenda yule dereva. Vivian hakuelewa kwa nini alikuwa akitii kila alichoambiwa na yule dereva, lakini pia, hakuona sababu ya kutotii mradi awe na uhakika wa usalama wake.

    “Wakati tukiwa hapa, nitajaribu kukuelezea kwa kifupi kuhusu mimi na wewe. Maana sina hakika nini kitafuata dakika chache kutoka sasa. Nimekaa miaka mingi nikiwa nasubiri muda kama huu ili niweze kufanya hiki nikifanyacho sasa kwa faida yenu na Taifa hili…” Alisema yule dereva huku akiwa anavua sura ya bandia aliyokuwa amevaa. Vivian aliweka chini boksi la juisi aliyokuwa anakunywa.

    “Naitwa Mwasumbi, Luteni Mwasumbi.”

    “Ooooh my God!, kwa hiyo muda wote ule tulikuwa tukiongea na wewe kule kijijini tukidhani kuwa u Askofu Alphonso kumbe haikuwa kweli! Kwa nini umeamua kufanya hivi?” Vivian alisema kwa mshangao mkubwa. Huku sasa akitazamana na sura ya mtu mwingine tofauti na ile ya Askofu Alphonso. Kabla Mwasumbi hajajibu walisikia mlio wa gari ukija kwa kasi. Vivian alitaka kukimbilia barabarani ili kulisimamisha.

    “Stop!, usifanye hivyo Vivian, nimekwambia tutapanda basi, huo mlio wa gari si wa basi ni wa gari ndogo tu tena wanaweza kuwa wenyewe!” Mwasumbi alisema huku akimshika mkono Vivian na kuukandamiza chini, Vivian akaanguka chini kutokana na ule mkandamizo.

    “Wewe vipi sasa tusipopata hilo basi tutalala hapa? Si bora tukaomba msaada kwenye magari madogo yanayoelekea Kamanga.” Vivian aling’aka kwa hasira na mshangao. “Sikiliza we mtoto, si muda mrefu utajua uko kwenye kisa gani na kwa nini unatafutwa san…” Kauli ya Mwasumbi ilikatishwa na mlio wa gari lilokuwa likija kwa kasi. Mlio ulionyesha kuwa lilikuwa karibu sana na pale walipokuwa wamejificha na lilikuwa kwenye mwendo wa kasi. Mwasumbi alisogea na kuchungulia barabarani kupitia matawi ya kile kichaka walichokuwepo. Macho yake yaliweza kuliona gari aina ya Land Rover 110 rangi ya kijani likiwa na alama kubwa nyeupe, alama hiyo ilikuwa herufi T ubavuni.

    “Oooh yeah!, unaona sasa ndiyo wenyewe, wanatutafuta!” Mwasumbi alisema kwa kunong’ona. Vivian alibaki ametoa macho wala hakuwa anajua kinachoendela.

    “Vivian, naomba nikueleze kwa kirefu kuhusu kisa hiki. Mwaka 1967 kulikuwa na harakati kubwa sana hapa nchini. Ilikuwa ni wakati ambao Mwalimu Nyerere alikuwa katika harakati kubwa za kutaka kuonyesha kuwa nchi ilikuwa huru kutoka katika mikono ya wakoloni. Mambo mengi yalifanyika, nuruni na gizani, ya kusemeka na ambayo hatuwezi hata kuyatamka. Mengi yalitokea, machache yaliandikwa na ambayo mnaweza kuyasoma leo. Harakati ziliendelea sana hadi mwaka 1976 ambapo wazungu wengi walikuwa wameshaondoka nchini na Nyerere akaikoleza zaidi ile sera ya Ujamaa na misingi ya Kujitegemea. Kama nilivyosema, kulikuwa na harakati nyingi sana ila ukweli ulikuwa wazi sana kuwa, wazungu waliokuwa hapa nchini walikuwa wakiijua nchi yetu kuliko tulivyokuwa tukiijua wenyewe. Walijua nini kiko wapi na kina faida gani. Wazungu wengi walibaki kulinda maslahi yao kwa kutumia dini. Kanisa Katoliki kwa upande wake walianza ujenzi wa Hospitali ya Bugando mnamo mwaka 1968. Ujenzi huo ulifanywa na kampuni ya Kiyahudi iliyoitwa COSATA. Wayahudi hao walijenga Bugando kwa ustadi mkubwa kama ambavyo walifanya kwa majengo mengine muhimu hapa nchini kama vile KCMC, jengo la Usalama wa Taifa, UDSM na Hospital ya Taifa ya Muhimbili. Lakini hata kabla hawajamaliza ujenzi wake sawasawa, Mwl. Nyerere aliwafukuza Wayahudi hao.

    Ufunguzi wa hospitali hiyo ulifanyika rasmi tarehe 3 Novemba 1971. Na baadaye hospital hiyo ilitaifishwa na Serikali mwaka 1972.

    Wengi hawakuelewa kwa nini Nyerere aliwafukuza Wayahudi hao. Kulikuwa na uvumi mwingi, lakini kwa sababu mimi kama mwanajeshi nilikuwa jirani sana na mkuu mmoja wa jeshi ambaye alining’ata sikio. Sababu ya kwanza ni ya kisiasa na msimamo wa Nyerere juu ya uhusiano wa Wayahudi na Wapelestina. Lakini pia, kulikuwa na sababu nyingine ya siri ambayo ndiyo inasumbua hadi leo. Nitakueleza sababu zote mbili zilizo sababisha Nyerere akosane na Wayahudi; ya kisiasa yaani uhusiano wa Wapalestina na Wayahudi na hiyo nyingine. Ila hiyo nyingine ndiyo ambayo inanifanya mimi na wewe tuwe tumejificha hapa hii leo.

    Wewe ni msomi najua umesoma historia. Kama ujuavyo kuwa Ujerumani ilikuwa ikiitawala Tanganyika tangu mwaka 1885 mara baada ya Carl Peters kusaini mkataba wa kitapeli na viongozi wa kiafrika. Mtu huyo baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro – Moshi mnamo mwaka 1891. Jamaa alikuwa mkatili kiasi kuwa watu wa maeneo hayo walimwita Mkono wa Damu. Nadhani wajua mengi yaliyofanywa na Carl Peters hadi pale majaji wa Kijerumani walipotuma taarifa Ujerumani juu ya ukatili wa huyo jamaa na mwaka 1897 aliondolewa katika shughuli za kikoloni. Ujerumani ikaendelea kutawala Tanganyika huku wajerumani wakiongezeka kumiminika Tanganyika.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nadhani unajua yaliyotokea kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambapo baadaye Ujerumani ilishindwa lakini wakati huohuo ikiacha wakimbizi wengi wa Kiyahudi ambao walikuwa wameikimbia Ujerumani. Hapo kabla Waingereza walikuwa wamenunua kama heka 50,000 ndani ya Tanganyika na kuwapangisha Wayahudi. Mara kwa mara Uingereza ilikuwa ikipendekeza kuwa ili kukabiliana na shida ya wakimbizi wa Kiyahudi ni vema Tanganyika, British Guiana, Kenya, Zimbabwe ya wakati huo na Nyasaland zikatengwa na kuwa makazi ya Wayahudi hao. Kwa hivyo baada ya Ujerumani kushindwa vita, nguvu ya chama cha NAZI na shughuli zake zikaathirika sana. Na sasa Tanganyika na Palestina zikawekwa kwenye mchakato wa kuzifanya kuwa makazi ya Wayahudi. Nchi kadhaa za Ulaya na Wamarekani wakawa kwenye kampeni kubwa kuhakikisha hilo linafanikiwa. Mapango huo haukufanikiwa kwa Tanganyika lakini ukafanikiwa kwa Palestina.

    Haiko wazi sana kama Nyerere alipata taarifa za ule mpango wa mwaka 1930 wa kuifanya Tanganyika na Palestina kuwa makazi ya Wayahudi. Maana kwa wakati huo Nyerere alikuwa na miaka kumi na tano tu na ni wakati wakati vijana wa NAZI walipofanya maandamano kupinga Wayahudi kupewa Tanganyika. Maandamano hayo yalifanyika Moshi katika Shule ya Kijerumani ya Mweka. Hata hivyo, haina ubishi kuwa Nyerere alikuwa akijua vema historia ya Palestina wakati alipokua akiamua Sera ya Tanzania, kuhusiana na Palestina ule mwaka wa 1977 ambapo alisema anaitambua Palestina na kuwa anaunga mkono Palestine Liberation Organization (PLO). Ngoja nikueleze ili ulewe suala hili kwa upana, japo linaoneka la kisiasa lakini ni muhimu kwako kujua. Tanganyika muda wote ilikuwa mstari wa mbele katika kutaka Palestina ijitawale. Kumekuwa na mivutano mingi sana juu ya suala hili hadi leo. Lakini chanzo chake ni cha kihistoria zaidi. Sasa kuna watu wanaoamini kwa sehemu kubwa kuwa Nyerere hakupenda huduma ya Wayahudi na kuwaondoa kwenye miradi yote kwa sababu ya matashi yake kwa Wapalestina ambayo hayakuja hivi hivi bali yaliletwa na hisia kuwa Palestina na Tanganyika zingekuwa kwenye mkondo mmoja kama mambo yangekwenda kama ilivyopangwa kuwa zote ziwe makazi ya Wayahudi. Japo mpango huo haukufanikiwa kwa Tanganyika…” Kabla hajaendelea na maelezo walisikia mlio mwingine wa gari. Safari hii mlio uliashiria kuwa lilikuwa gari kubwa.

    “Daaah! historia yako inasisimua lakini bado haijanipa picha yote ya hili tunalopitia.” Hatimaye Vivian alisema huku akiwa anasimama. Mzee Mwasumbi alijipenyeza hadi sehemu ambayo aliweza kuona upande lilikokuwa linatokea lile gari.







    “Twende, ni Basi linakuja.” Mwasumbi alisema. Wote wakawa wanaelekea barabarani Walisimamisha gari na kuingia ndani. Basi lilikuwa limejaa sana hivyo kulikuwa na nafasi ya kusimama kwa shida. Gari lilitembea kwa dakika kama ishirini kisha, Mzee Mwasumbi akapiga kelele.

    “Tushushe hicho Kijiji cha mbele hapo!”

    Kweli gari lilipofika hicho Kijiji alichokusudia kushuka, lilisimama, wakashuka.

    “Upande huu kuna ufukwe wa Ziwa Victoria, kutakuwa na watu wanatusubiri hapo.” Alisema huku wakiwa wanavuka barabara kwenda upande mwingine wa barabara.

    Huko kulikuwa na makazi machache ya watu. Walianza kufuata barabara ndogo ya vumbi iliyokuwa ikitelemka kwenda sehemu ambayo Mwasumbi alisema wangekutana na ufukwe.

    “Sasa hayo maelezo yako yanahusiana vipi na haya yanayotokea?” Vivian alihoji wakati wakitembea.

    “Huyo mkubwa wangu wa jeshi anasema kuna sababu nyingine ya kiusalama ambayo ilisababisha Nyerere asitake Wayahudi waendelee kuwa hapa nchini. Wakati wa Vita ya Pili ya Dunia, Marekani na washirika wake walikuwa wanaelekea kushindwa, hadi pale Marekani walipofanikiwa kutumia lile bomu la Atomic na kuipiga Hiroshima na Nagasaki, Japan. Ili kulipua mabomu hayo, ilihitajika neno la siri ‘password’. Maneno ya siri ya kufyatulia mabomu hayo yalitengenezwa na kuwekwa na mtengenezaji ambaye ni Myahudi. Myahudi aliyevumbua bomu hilo, Bwana J. Robert Oppenheimer alitengeneza maneno ya siri. Neno la siri la lile bomu lililolipua Hiroshima lilikuwa ni ‘Little Boy’. Wakati lile neno la siri la lile bomu lililolipua Nagasaki ilikuwa ‘Fat Man’.

    Baada ya kwisha vita hiyo, huku Marekani na washirika wake wakiwa wameshinda, ilikuja kugundulika kuwa, baada ya Bwana J. Robert Oppenheimer kulazimishwa kutoa kanuni za kutengeneza bomu hilo kwa Serikali ya Marekani, aliona kuna umuhimu wa kutengeneza bomu jingine ambalo likipigwa kwa wakati mmoja na lile la Atomic huondoa madhara yanayoweza kuletwa na bomu hilo la Atomic. Ikiwa na maana kuwa hilo bomu jingine lina uwezo wa kulidhibiti lile la Atomic. Inasemekana wazo hilo alikuwa nalo akiwa katika hatua za mwisho za kutengeneza bomu la Atomic. Hivyo alitengeneza kanuni ya kutengeneza hilo bomu jingine, lakini hadi leo haijulikani mahali ambapo kanuni hiyo imewekwa. Kumekuwa na harakati kubwa za kutafuta mahali ambapo Myahudi huyo alificha karatasi zenye kanuni hiyo. Mashirika ya ujasusi yanaamini kuwa kuna siri kubwa katika maneno ya siri aliyoyatoa Bwana J. Robert Oppenheimer kulipulia yale mabomu mawili ya Atomic. Maneno ‘Little Boy’ and ‘Fat Man’ inasemekana yana siri na ufunguo wa kujua sehemu na mtu ambaye ana kanuni ya kuwezesha kutengeneza hilo bomu jingine la kulidhibiti lile bomu la Atomic. Katika kuchimba na kufuatilia wapi hiyo kanuni inaweza kuwa, ilikuja kugundulika kuwa mjomba wake na Bwana J. Robert Oppenheimer aitwaye Eud Benjamin, ambaye aliingia Tanganyika miaka hiyo kama walivyoingia wakimbizi wengine ndiye Fat Man. Myahudi huyo alikuwa mtaalamu wa mambo ya utabibu wa binadamu. Hivyo akajikuta anaishia kuwa Daktari katika hospitali ya Bugando.

    Daktari huyo alikuwa maarufu sana hadi pale alipouawa katika usiku ambao wewe, Milka na Maganga mlizaliwa. Wakati huo yaani mwaka 1981 alikuwa na umri wa miaka 41 na inaaminika wakati bomu la Atomic lilipotumika kwa mara ya kwanza kule Japan mwaka 1945 yeye alikuwa na miaka 5 tu.

    Neno ‘Fat Man’ lilikuja kutambuliwa kuwa ndiyo huyo mjomba wa Bwana J. Robert Oppenheimer. Lakini neno Little Boy halikuwa limegundulika hadi hapo baadaye baada ya kifo cha huyo mjomba wake na mgunduzi wa bomu la Atomic, hapa namaanisha kifo cha Daktari wa Kiyahudi Eud Benjamin katika Hospitali ya Bugando …” Kabla hajaendelea Mwasumbi alikatishwa na swali la Vivian

    “Kwa hiyo usiku ule tuliozaliwa una nini sasa?”

    “Jambo la kwanza ninalotaka ujue ni kuwa wewe ni Milka na Milka ni wewe. Nikiwa na maana kuwa mama Maganga alienda kujifungulia Mwanza katika Hospitali ya Bugando. Alifanya hivyo kwa vile mama yake mzazi alikuwa akiishi Mwanza hivyo kama wafanyavyo wanawake wengi wa Ki-tanzania, huenda kujifungulia kwa mama zao. Maana hilo huwapa haueni ya kisaikolojia kuwa watapata msaada wa uzoefu toka kwa mama zao na hali ya kujaliwa itakuwa juu. Na kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopatikana wakati wa kuzaliwa wewe na Maganga huduma ilitolewa na yule Daktari wa Kiyahudi. Kwa vile tayari mashirika mengi ya kimataifa ya Kijasusi yalikuwa yameshapata fununu kuhusiana na mahali alipokuwa huyo mjomba wake yule mgunduzi wa bomu la Atomic, walikuwa wameshaweka majajusi kufuatilia nyendo za huyo Myahudi kwa vile walikuwa wakitafuta maana ya neno Litle Boy na wapi zilipokuwa kanuni za kutengeneza bomu la kudhibiti bomu la Atomic…” Kabla Mwasumbi hajaendelea zaidi, mlio wa risasi ulisikika. Wote wakashtuka!

    “Pancha au nini?” Vivian alihoji, hakuwa anajua mlio wa risasi. Hakuwahi kusikia wala kuona risasi ikipigwa.

    “Hapana ni risasi!”

    “Sikiliza, Vivian, sitaki watukamate wote, maana wewe sasa ni wa muhimu kuliko mimi, najihisi kama nimeshamaliza kazi yangu. Ufukweni si mbali toka hapa, ukifika huko, utakuta kuna boti ndogo ya kijani, waambie mimi nimekuelekeza kwenda pale, waambie Luteni Mwasumbi ameniagiza kuja, wao ni wanajeshi, hawajui wewe ni nani ila watakupeleka sehemu salama. Najua utaonana na Hellen, msimulie haya na yeye atakusimulia yote niliyomsimulia yeye na Maganga.

    Ukiona mambo yanaharibika na unahitaji msaada wa haraka na uhakika basi utapiga hizi namba +255785975443…” Hata kabla Mwasumbi hajamaliza maelezo yake mara walisikia gari likiunguruma kuja upande waliokuwepo.

    “Vivian, I love you so much and I always wanted to see you, nashukuru nimekuona. Jitahidi sana kuificha hiyo alama hapo pajani asiione mtu yeyote. Kama unataka kujua ukweli kuhusu hiyo namba na wakati huohuo uendelee kuwa salama, basi kuna watu wanne tu ambao unaweza kuwauliza. Mtu niliyekupa hiyo namba ya simu, Maganga, mimi au yule Daktari wa Kiyahudi japo na yeye anaweza kukudhuru akigundua kuwa umeshagundulika na unatafutwa….haya nenda…mimi nitajitahidi kuwazuia hapa ili kukupa wewe nafasi ya kufika ufukweni….tafadhali kuwa makini na kinywa chako.” Mwasumbi alisema hayo maneno kwa hisia kali kisha akamvuta Vivian na kumbusu. Wakati huu mlio wa gari ulikuwa jirani zaidi, Mwasumbi alimvuta Vivian hadi pembeni ya barabara, wakabana nyuma ya nyumba moja ya nyasi eneo hilo.

    “Haya nenda, pita kwenye hayo mashamba hadi ufike ufukweni, ukiwapata nendeni, kama nitatoka hai najua nitakapokupata. Kama sitotoka hai nakutakia kila la heri mwanangu!”

    “Mbona sikuelewi, unanitisha, unanihuzunisha, unanichanganya na kuniweka kwenye sintofahamu!” Viviani alimudu kusema huku akiwa anasukumwa na Mwasumbi kama ishara ya kumhimiza aondoke eneo lile.

    “Natamani ningekusimulia kisa chote ila nachelea wote tutakuwa maiti hapa au twaweza kuangukia kwenye masahibu mazito na mateso. Chukua hii…” Hatimaye Mwasumbi, aling’oa nywele chache zilizokuwa kichwani kwake akampatia Vivian.

    “Ipo siku utazihitaji hizi.” Mwasumbi alisema huku safari hii akichomoa bastola iliyokuwa mgongoni kwake.

    “Go, go, go!” Alipiga kelele. Kusikia hivyo, Vivivan alikurupuka kuelekea kwenye vichaka vilivyokuwa kwenye mashamba yaliyokuwa jirani na eneo hilo. Alitembea kwa shida, maana hakuwa mtu aliyezoea taabu. Mawazo mengi yalikuwa kichwani. Kwa mara ya kwanza akajikuta anafanya kitu asichokielewa, ila hakuwa na namna zaidi ya kufanya hivyo. Alimfikiri Mwasumbi, alimfikiria Maganga na Milka kwa wakati mmoja huku akiwa bado anakatiza vichaka kueleke upande kulikokuwa na Pwani ya Ziwa Victoria.





    Aliwafikiria wazazi wake ambao walikuwa mapumzikoni Brazil halafu, akafikiria simulizi ya Mzee Mwasumbi kuwa yeye na Maganga ni mtu na kaka yake. Akakumbuka kauli ya Mwasumbi, “Wewe ni Milka na Milka ni wewe.” Hapo akachanganyikiwa. Akakumbuka kuhusu alama aliyokuwa nayo pajani ambayo kwa mujibu wa Mwasumbi ndiyo chanzo cha yeye kutafutwa. Vivian alihisi kuna ukweli kwenye hayo maelezo kwani aliyalinganisha na tukio aliloliona wakati ameenda Hospitali ya Bugando ili kujua wodi aliyozaliwa, maana yule Daktari alimuuliza ile alama kwanza. Hivyo aliona kuna kitu katika ile alama na mtu pekee ambaye anaonekana kujua hadi sasa ndiyo huyo ameachana naye dakika chache zilizopita, huku sababu iliyotolewa ni usalama wake yeye Vivian. Alishangaa jinsi hayo mambo yalivyotokea kwa kasi. Alishangaa kuona kama ni kweli mtu aliyehangaika naye siku chache zilizopita pale Hospitali ya Sengerema alikuwa ni mama yake mzazi. Hilo lilimuuma zaidi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sasa alikuwa amekaribia zaidi Pwani na kwa mbali waliweza kuiona boti ambayo Mwasumbi alikuwa amemwambia. Aliziangalia zile nywele alizopewa na Mwasumbi, akafikiria ujumbe aliopewa kuhusu hizo nywele. Kama kweli siku moja angezihitaji kama Mwasumbi alivyosema basi aliona kuna sababu ya kuzihifadhi vema. Alifikiria sehemu sahihi ambayo angeweza kuzihifadhi hizo nywele. Alifungua saa yake ya mkononi aliyokuwa ameivaa, akafungua sehemu ya kuwekea Betri, akaziweka zile nywele kisha akaifunga na kuivaa tena. Mara akasikia mrindimo wa risasi kule alikokuwa anatokea. Mara hii aliweza kujua ni risasi maana hakukuwa na tofauti na ile aliyoambiwa na Mwasumbi. Japo alikuwa amechoka lakini akajikuta anatumia nguvu zilizobaki kwa kutimua mbio kuelekea upande ule alioiona Boti.

    ***************************





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog